Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Hawa Mchafu Chakoma (5 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu.
Awali ya yote, nipende kumshukuru Mwenye Mungu, mwingi wa rehema na mwenye kurehemu, lakini pia nipende kuwashukuru wanawake wa Mkoa wa Pwani kwa kuniamini niweze kuja kuwawakilisha. Sambamba na hilo, napenda niwashukuru wanawake wa CCM Taifa na Chama changu cha Mapinduzi kwa kuniteua Mbunge wa Viti Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati naelekea kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu, napenda kutoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na timu yake ya Baraza la Mawaziri inayoongozwa na Jemedari Mkuu, Waziri wetu Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa kazi nzuri wanayoifanya ambayo inavutia moyoni mwa Watanzania, kwa kazi nzuri wanayoifanya ambayo inaleta furaha katika macho ya Watanzania. Hakika Mungu mbariki Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baraza lake la Mawaziri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia hotuba ya Waziri Mkuu kwa kuanza ukurasa wa saba. Katika ukurasa wa saba hotuba hii inajielekeza katika namna ya kuchukua hatua kuhakikisha wanaongeza mapato na wanabana mianya ya ukwepaji kodi. Mimi nipende kuunga mkono jitihada hizi, ni jambo jema sana na I believe for sure kama tuna uwezo wa kukusanya hata zaidi ya shilingi trilioni 1.3 endapo TRA itajizatiti kweli kweli lakini pia kila Mtanzania atimize wajibu wake, anayepaswa kulipa kodi alipe kodi, tudai risiti tunapofanya manunuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuelekea kuongeza mapato kama ambavyo Serikali imedhamiria tuna shida moja, EFD mashine bado kuzungumkuti. Suala zima la EFD mashine ni tatizo. Nimeshashuhudia nimepata risiti za aina tatu tofauti pale unapofanya manunuzi. Kuna risiti ambayo unakuta ina maelezo ambayo kwa mtazamo wangu mimi naweza kusema yamejitosheleza. Kuna TIN namba pale, utakuta jina la ile kampuni ama kile kituo cha kufanyia biashara, kuna VRN pale lakini pia utakuta jumla ya amount uliyonunua, muda, tarehe pamoja na ile amount inayokuwa deducted kwenda Serikalini, lakini zipo risiti nyingine zinazotoka katika hii mashine unakuta zina lack hizo details. Kwa hiyo, naomba sana hili suala la EFD mashine tuliangalie vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia baadhi ya wafanya biashara hawana hizi mashine, wanaendelea kutumia risiti za kuandika. Niseme kwamba hizi risiti siyo afya sana katika ongezeka la ukusanyaji wa mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimewahi kwenda petrol station kuweka mafuta, nimeweka saa tatu asubuhi lakini risiti inaniandikia nimeweka saa tano usiku. Kwa hiyo, inaonekana kwamba hizi mashine watu wanaweza kucheza nazo. Kwa sababu hiyo, nasisitiza tena tuziangalie mashine hizi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kwenye petrol station kuna matatizo makubwa sana ndiyo maana nasisitiza TRA inabidi ijizatiti au ifanye kazi kweli kwenye hili suala la ongezeko la mapato. Utakuta kuna visima viwili, cha dizeli na petroli, vya dizeli viwili na vya petroli viwili, kimoja ni cha risiti ya kuandika na kingine ni cha risiti ya TRA. Kwa hiyo, naomba sana katika suala hilo mnaohusika mliangalie kwa ukaribu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mchango wangu mwingine uko katika ukurasa wa 16 ambao unazungumzia shilingi milioni 50 katika kila kijiji lakini pia umeelezea maandalizi ya namna fedha hizi zitakavyowafikia walengwa ikiwa ni pamoja na kuanzisha vikundi vya kiuchumi vinavyokidhi vigezo. Hii ni ahadi ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo unaikuta katika Ibara ya 57(d) kwa ruhusa yako naomba nikisome na kinasema; “kutenga kiasi cha shilingi milioni 50 katika kila kijiji kama mfuko wa mzunguko (revolving fund) kwa ajili ya kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia ushirika wa kuweka na kukopa (SACCOS) katika vijiji husika.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha kampeni kilichokuwa kinawavuta Watanzania wengi ni pamoja na kifungu hiki cha 57(d) cha shilingi milioni 50 katika kila kijiji. Ukiangalia muktadha wa hiki kifungu hizi shilingi milioni 50 siyo kwamba watu watagawiwa, watakopeshwa then watarudisha. Wakati wa ziara yangu ya kushukuru wapiga kura wa Mkoa wa Pwani nilipata maswali kutokana na kifungu hiki, wazee wanauliza wao watanufaika vipi na kifungu hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi wazee ambao wameshafika umri wa kushindwa hata kufanya kazi huoni moja kwa moja kama kinaweza kuwanufaisha. Isipokuwa naomba Serikali masuala mazima ya mapendekezo ya universal pension, pension kwa wazee wote yaweze kufanyiwa kazi kwa haraka ili yaende sambamba na hii shilingi milioni 50. Wakati watu wenye nguvu zao wananufaika na hii shilingi milioni 50 kukopa na kufanya biashara ama ujasiriamali basi wazee waweze kunufaika na pension ya wazee wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine uko ukurasa wa 23 ambao unazungumzia suala zima la kazi na hifadhi ya jamii. Katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambayo inaelezea mwelekeo wa shughuli za Serikali, nilitarajia kuuona hapa Mfuko wa Fidia (Workers Compensation Fund – WCF). Sikukuu ya Mei Mosi mwaka jana kati ya mambo ambayo Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi alifafanua na kueleza kwamba kati ya mafanikio ya Serikali yake basi ni pamoja na kuanzishwa kwa Workers Compensation Fund.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nipende kusema na niwe mkweli na utakubaliana na mimi kabisa kati ya kitu ambacho Serikali ya Awamu ya Nne imefanya kwa wafanyakazi wa Taifa hili basi ni pamoja na kuanzisha Mfuko wa Fidia Kazini. Ikumbukwe hapo awali ilikuwa inatumika sheria ya zamani, Sheria ya Fidia, Sura Na.263 ambapo mtumishi akiumia kazini, akipoteza kiungo alikuwa analipwa shilingi 108,000 kwa upande wa wafanyakazi wa private lakini kwa upande wa wafanyakazi wa public sector ilikuwa inatumia Sheria ya Public Service Act ambayo mtumishi akiumia ama akipoteza kiungo ama ulemavu wa maisha alikuwa anapewa shilingi milioni 12 na yenyewe ilikuwa inatolewa once.
Kwa hiyo, naomba sana Waziri Mkuu na Waziri mwenye dhamana ya kazi na hifadhi ya jamii kuuangalia mfuko huu kwani umeelezea namna njema ya kuwafidia wafanyakazi wetu wanapoumia ama kupoteza viungo sehemu yao ya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitapenda tena kujikita ukurasa wa tano wa hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambao unazungumzia uwajibikaji na maadili ya viongozi wa utumishi wa umma. Baadhi ya watumishi wa umma walifika mahali walijisahau sana, lakini pia baadhi ya watumishi wa umma wasiokuwa waadilifu hao ndiyo walikuwa wameigharimu Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Hata hivyo, Serikali yetu ya Awamu ya Tano imeamua kuchukua hatua ku-deal na hawa watu ambao walikuwa hawana uadilifu wametumia madaraka yao vibaya ama wametumia nafasi zao vibaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, cha kushangaza wenzetu hawa hawa waliokuwa wanapigia kelele kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi inachelewa kuchukua hatua leo wamekuwa mstari wa mbele kutetea wabadhirifu, wamekuwa mstari wa mbele kutetea mafisadi, wamekuwa mstari wa mbele kutetea watumishi ambao hawana maadili. Wamekuwa vigeugeu, ni wao ndiyo waliokuwa wanasema tunaenda taratibu, sasa tunaondoka na supersonic speed, wanatoka tena mbele na kuanza kuwatetea wale watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine…
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hawa Chakoma naomba ukae, Mheshimiwa Cecilia Paresso...
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema kwamba taarifa yake siipokei nimei-shred, lakini pia nipende kumkumbusha anaweza akaenda YouTube akaona Mwenyekiti wao Mbowe analalamika watumishi wa umma ambao wanasimamishwa anataka wahojiwe kwanza, tayari TAKUKURU imeshatoa ushahidi, anahojiwa kitu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda ukurasa wa tisa unaozungumzia kukua na kuimarika kwa demokrasia. Nchini Tanzania demokrasia imekuwa na ndiyo maana kuna uwepo wa vyama vingi. Pia niseme tunatambua uwepo wa upinzani nchini, tunatambua uwepo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na tunatambua chama kikuu cha upinzani. Wakati tunaelekea kwenye mustakabali wa kuwafanya Watanzania wawe na maisha bora, ukiacha kazi nzuri inayofanywa na Chama Tawala ama na Serikali, pia tunahitaji mchango makini kutoka kwa chama cha upinzani ama Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Kama tunakuwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambayo kwanza haiko makini, mbili inaendeshwa na mihemko, tatu inaendeshwa na sintofahamu, hatuwezi kufika mahali kokote.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hawa Chakoma umemaliza muda wako.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa kuonesha masikitiko yangu kwa mgogoro wa wakulima na wafugaji katika Kata ya Magindu na Gwata Mkoani Pwani katika Jimbo la Kibaha Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ziara yangu ya kushukuru wapiga kura wa Mkoa wa Pwani hususani Kata ya Gwata na Magindu nimepokea malalamiko toka kwa wananchi juu ya mgogoro unaoendelea kati ya wakulima na wafugaji. Mfano katika Kata ya Magindu, Kijiji cha Mizuguni mgogoro huo umeota mizizi kwani wafugaji (Masai) na mifugo yao huvamia mashamba ya wakulima na kula mazao yao suala linalopelekea mapigano baina ya jamii hizo mbili. Mgogoro ambao hata Kamati ya Kijiji cha Mizuguni imeshindwa kuutatua. Hata wakulima walivyokimbilia Mahakamani bado wamekuwa wakishindwa kesi hizo (za kuharibiwa mazao yao kila siku) kwa kuwa wafugaji jamii ya Kimasai huhonga Mahakimu na hatimaye wanashinda kesi hizo. Hali hiyo pia imejitokeza katika Kata ya Gwata, Kijiji cha Mlalazi, mifugo (ng‟ombe) wanamaliza mahindi ya wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa zaidi hapa Mheshimiwa Waziri, wafugaji hawa walishatengewa eneo la kwenda ambako ni Vinyenze, kijiji hiki kiliwekwa ama kutengwa mahsusi kwa ajili ya wafugaji ili kunusuru mazao ya wakulima lakini hadi leo hii ninavyoongea wafugaji hao wamegoma kwenda Vinyeze hali ambayo inaendeleza migogoro baina yao na wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana hili suala si la kuchukulia mzaha kwa kweli maana huu mgogoro unafukuta chini kwa chini, siku ukija kulipuka hapatatosha. Hivi ninavyoongea katika Kata ya Gwata wakulima hawaoani na wafugaji lakini pia wanapigana mapanga na kuumizana ilhali hapo awali walioleana.
Mheshishimiwa Spika, naomba sana Serikali kuingilia kati kunusuru jamii hizi mbili kuacha kupigana na kuhatarishiana maisha. Pia Serikali iingilie kati ili wafugaji ambao wanasemekana ni matajiri waache kuwaonea wakulima wanaosemekana ni wanyonge. Kesi inapokuwa Mahakamani wafugaji wanakimbilia kuhonga halafu mwisho wa siku Mahakimu huwapa ushindi huo wafugaji only because wamepokea hongo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nimeamua kuchangia hoja hii moja tu mwanzo mwisho kwa sababu ya umuhimu na upekee wake. Nikuombe sana Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge hili la bajeti katika ziara zako za kikazi Mkoa wa Pwani uwe kwenye orodha kwa kuipa kipaumbele Kata ya Gwata na Magidu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi hii, naomba kuunga mkono hoja. Niwatakie kila la kheri Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri katika kutimiza majukumu ya kilimo, uvuvi na ufugaji kwa maslahi ya Taifa letu.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka zake tele.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Serikali ningependa kuanza kwa kumpongeza Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Pia kwa niaba ya wafanyakazi wote nchini nipende kuishukuru Serikali, Serikali zote mbili iliyokuwa ya Awamu ya Nne na Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwa wasikivu na kusikiliza kilio cha wafanyakazi cha muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Nne wafanyakazi wote nchini tunaishukuru sana kwa kukubali kuanzisha Sheria ya Mfuko wa Fidia (Workers Compensation Fund) Sheria Na. 8 ya mwaka 2008 na kuachana na ile Sura Na. 263 kwa Private na Public Service Act Na.19 kwa upande wa wafanyakazi wa utumishi wa umma kutumika kufidia once wanapoumia ama kupata ulemavu mahali pa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Awamu ya Tano tunaishukuru kwa kukubali kuwasilisha michango ya mwajiri ya 0.5 percent ya mshahara katika Mfuko huu wa Fidia ili itakapofika tarehe Mosi Julai, mwaka huu wafanyakazi wote watakaoumia ama kupata ulemavu kazini wataenda kufidiwa na Mfuko huu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, narudia tena kwa niaba ya wafanyakazi wote nchini, tunaishukuru sana Serikali tena sana kwa kuja na jambo hili jema la kuanzisha huu Mfuko. Nipende tu kusema kwa kuanzisha Mfuko huu automatically tunaongeza muda mrefu wa wafanyakazi kuwepo kazini, lakini pia tunaongeza uzalishaji, kitu ambacho kitaenda kuchochea ukuaji wa uchumi wetu na hali kadhalika pato la Taifa letu litakua. Ni ukweli usiopingika Serikali inapata kodi yake ya uhakika pasipo kusuasua kutoka katika kundi hili la wafanyakazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nipende kuipongeza Serikali kwa kupunguza kodi ya Pay As You Earn hadi kufika single digit kwa wafanyakazi wa kima cha chini. Napenda kuiomba Serikali na niliuliza hapa swali katika Bunge lako Tukufu kwamba, je, Serikali ina mpango wowote ama ina mpango gani kwenda sasa kupunguza hii kodi ya Pay As You Earn kwa wafanyakazi wa kima cha juu wanaokatwa 30%.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya wafanyakazi au watumishi wa nchi hii Mheshimiwa Angellah Kairuki alitupa majibu mazuri sana kwamba tayari Workers Task Force imeshaundwa na inayafanyia kazi haya mapendekezo na tayari yamepelekwa kwenye Baraza la Majadiliano la Utumishi wa Umma wanayafanyia kazi na muda wowote wataturudishia feedback, naamini feedback itakuwa njema.
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe tu Serikali kwa mwaka 2017/2018, ione sasa umuhimu wa kuwapunguzia kodi hawa watumishi wa umma ama wafanyakazi wanaokatwa kima cha juu ili kuwapunguzia makali ya maisha na kama nilivyozungumza hili ndilo eneo ambalo Serikali inapata kodi yake ya uhakika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu wa tatu ni kuhusiana na afya ama vituo vya afya katika Halmashauri zetu. Kiukweli uwezo ama hali ya Halmashauri zetu katika ujenzi wa hivi vituo vya afya, zahanati ama niseme majengo ya wazazi hali yao haiko vizuri, wanatumia own source na yenyewe wanaipata kwa kuhangaikahangaika. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa ku-windup aweze kutueleza kiukweli kabisa kwa sababu hizi Halmashauri zinajaribu kuingia kwenye huu ujenzi wa hivi vituo vya afya ama majengo ya wazazi wanafikia usawa wa lenta, kupaua wanashindwa, yale majengo yanabakia kama magofu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikitolea mfano katika Halmashauri yangu ya Wilaya ya Kibaha katika Kata ya Magindu kuna jengo la wazazi pale tangu mwaka 2012 mpaka leo hii 2016 ninavyoongea halijakamilika na wala halina dalili ya kukamilika. Tunahitaji shilingi milioni 26 tu ili kuweza kulikamilisha jengo lile, wanawake wa Kata ya Gwata na Kata ya Magindu waweze kutimiza haki yao ya msingi ya kuleta watoto hapa duniani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda sana kumwomba Mheshimiwa Waziri alione hilo, tunazihitaji hizo shilingi milioni 26 ili tuweze kuwasaidia wanawake hawa ambao ni wapiga kura wetu lakini hali kadhalika niseme ni walezi wa watoto wa Taifa hili. Hii shilingi milioni 26 kwa ajili ya kumalizia hiki kituo tumeanza kuiomba tangu mwaka wa bajeti 2014/2015 hakuna kitu, 2015/2016 hakuna kitu, 2016/2017 nimechungulia hakuna kitu. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri atufikirie na atuonee huruma na hili suala lifike mwisho. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu mwingine uko katika hili suala zima la private number. Hapa pengine Mheshimiwa Waziri atakuja anipe shule lakini nikiangalia kwa uelewa tu wa kawaida sasa hivi katika gari yangu nimeandika Mchafu nalipa shilingi milioni tano, lakini anasema kwamba anatutoa kwenye shilingi milioni tano anatupeleka kwenye shilingi milioni 10. Katika hali tu ya kawaida ambayo wala haihitaji akili nyingi, mimi nasema tunaenda kupunguza mapato na siyo kwamba tunaenda kuongeza mapato. Kwa sababu ni hiari ya mtu, naweza nikaamua kuacha jina langu Mchafu na nikaenda nikarudi kwenye Na. T302 BZZ.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapo nitapenda Mheshimiwa Waziri atakapokuja anifundishe kutoka kwenye hii shilingi milioni tano kwenda kwenye shilingi milioni 10 anaongezaje mapato ilhali hili jambo ni hiari na siyo lazima. Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuzungumza nitaomba aje anifafanulie suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni kuhusiana na suala zima la kuongeza tozo ama kuweka tozo kwa bidhaa za mitumba. Nilitoka kuuliza swali hapa asubuhi Watanzania milioni 12 ni maskini wa kutupwa, kila mwaka vijana takribani laki nane wanaingia kwenye soko la ajira, je, Serikali kwa mwaka inatengeneza ajira ngapi?
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna vijana wengi ambao ni hawa tunawaita Machinga, wanafanya kazi ya kutembeza hizi nguo za mitumba ili waweze kupata riziki na familia zao. Leo ukiweka tozo kwa lengo la kuizuia hii mitumba, niulize hivi viwanda vitakavyotengeneza nguo kutuvalisha Watanzania viko wapi? Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri jambo hili alifikirie mara mbili, je, tupo tayari kuongeza hizi tozo kwenye mitumba hivyo viwanda viko tayari? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala lingine ni kuhusiana na CAG, wengi wamesema na mimi lazima nilizungumzie hili. Halmashauri zetu uaminifu wao ni wa kulegalega, CAG ndiye mkombozi mkubwa ambaye ameweza kutusaidia, CAG ndio jicho ambalo limeweza ku-penetrate na kuweza kuona kuna watu wanalipwa mishahara hewa, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri na niungane na wenzangu wote waliosimama hapa kuzungumzia suala zima la CAG kuongezewa pesa, hebu akae afikirie mara mbili mbili.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema bajeti yetu ni shilingi trilioni 29 na hela hizo hatuna in cash, ndiyo tunataka twende tukazikusanye sasa kama CAG tunamwekea hela kidogo namna hiyo atakwenda kufanya kazi gani? Kwa hiyo, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri afikirie tena na tena kuhusiana na suala zima la CAG, aone namna bora ya kuweza kumuongezea pesa ili aweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sitaki unigongee kengele, napenda kusema nakushukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa mchango wangu katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii kwa kujikita katika suala moja.
Kwanza, napenda kuanza kwa kuunga mkono hoja katika Wizara hii ngumu, hususani upande majangili namna yanavyoipa wakati mgumu sekta hii ya maliasili na utalii, kitu ambacho kinapelekea kukosekana kwa watalii na ukosefu wa mapato kwa uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania leo tunazungumzia kukua kwa utalii kwa kuwa na watalii milioni mbili, wenzetu South Africa wanazungumzia watalii milioni 12. Hivyo basi, ni kwa Serikali yetu (Wizara) kuhakikisha inaboresha miundombinu ya maeneo yetu ya watalii. Kwa mfano, utalii wa Mlima Kilimanjaro miundombinu ya majitaka siyo mizuri kabisa hususan upande wa vyoo, vyoo ni vichafu. Mbaya zaidi vyoo ambavyo wanatumia wananchi/wafanyakazi wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro ndiyo hivyo hivyo vinatumiwa na wageni wetu (watalii). Hii si sawa kabisa na ni moja ya sababu ya kufukuza watalii katika chanzo hicho cha Mlima Kilimanjaro. Sote tunafahamu wazungu/wageni ni waungwana na wasafi sana ukilinganisha na Watanzania wa maeneo yale. Hivyo basi, niitake Wizara kuhakikisha inajenga choo mahsusi kwa wageni wetu (watalii) na siyo kuwachanganya na wenyeji. Usafi ni sehemu ya kutangaza utalii wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni kuhusiana na mjusi aliyepelekwa nchini Ujerumani. Wabunge walio wengi wanahitaji mjusi huyo kurudishwa nchini, mimi naomba nitofautiane nao kidogo katika maana ya kwamba kuna gharama kubwa sana katika kumtunza, mjusi huyo aendelee kuwepo na kuingiza faida ya nchi. Kwanza ni mkubwa sana, hivyo anahitaji eneo kubwa sana, ni sawa na viwanja vinne vya mpira, lakini pia anahitaji muda wote kuwepo kwenye AC ili asiweze kuharibika/kuoza. Hivyo basi, kuliko kutaka arejeshwe sasa ilhali hatujajipanga, nipende kuishauri Serikali (Wizara) ni bora tuone utaratibu wa kuweza kupata royalty (mrahaba). Ni vyema Serikali yetu ya Tanzania ione utaratibu bora wa kuitaka Serikali ya Ujerumani kutupatia gawio linalotokana na utalii wa mjusi huyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, mchango wangu ni huo. Naomba kuunga mkono hoja.
The Written Laws (Miscellaneous Amendment) (No.2) Bill, 2016
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Napenda kuipongeza Serikali kwa kuja na huu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.2 ya mwaka 2016. Kikubwa zaidi napenda kuipongeza Serikali kwa kutuletea mapendekezo na maboresho ya kuongeza kifungu kipya cha 45 (a) katika sheria ya Taasisi za Kazi Sura namba 300.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi sina matatizo na uwepo wa hiki kifungu kwa sababu kinaenda kuwasaidia wafanyakazi wa Taifa hili. Kimsingi kifungu hiki kinaenda kuwabana wale waajiri ambao kwa makusudi wanaamua kukanyaga sheria za kazi ikiwemo na hili la kutokupeleka michango ya hifadhi ya jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ambacho sikubaliani katika kifungu hiki, ni ile faini ama tozo iliyowekwa kwa mwajiria mbaye kwa makusudi atakiuka Sheria za Kazi kwamba atatozwa kiasi cha shilingi 100,000/=. Ninasema hivyo kwa sababu nimekaa kwenye Vyama vya Wafanyakazi na nimekaa kwenye Mamlaka ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, nina uzoefu na hawa waajiri. Hizi faini ndogo ndogo, wao wameshafika mahali wamezizoea. Wao imeshafika mahali wanaona ni wanazimudu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ambacho napendekeza, twende tukaifute hii shilingi 100,000/= na twende tukaweke shilingi 500,000/= iwe “not less than TShs. 500,000/=.” Tukiweka hii shilingi 100,000/= ama tunavyosema not less than TShs.100,000/=, mwisho wa siku ile tija ambayo tunaitafuta nia njema Serikali ambayo mnataka kuwasaidia wafanyakazi wa Taifa hii hatutakaa tuipate. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kutoa mfano katika hili suala zima la ucheleweshaji wa michango ya hifadhi ya jamii. Ukienda kwenye sheria zote za mifuko ya hifadhi ya jamii, ama niseme Mifuko ya Pensheni, kuna kifungu ambacho kinasema, “mwajiri yeyote atakayechelewesha michango ya mwanachama katika mifuko ya hifadhi ya jamii, ataenda kutozwa asilimia tano.” Leo hii kuna ucheleweshaji mkubwa wa michango ya hifadhi ya jamii katika mifuko ya hifadhi ya jamii. Ndiyo maana nasema, kwa kuwawekea hiki kiwango kidogo, haitatuletea tija ile ambayo sisi tunaitafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bado nipo hapo hapo katika hiki kifungu kipya cha 45 (a). Kimsingi hiki kifungu kinampa mamlaka Afisa Kazi (Labour Officer) kuweza kuwatoza faini hawa waajiri ambao wanakiuka sheria za kazi ikiwemo na hili la kutokupeleka michango ya hifadhi ya jamii. Sina tatizo na Labour Officer kusimamia hao waajiri ambao wanakiuka hizi sheria za kazi, sina tatizo, isipokuwa wasiwasi wangu upo kwa huyu anayeitwa Labour Officer kupatiwa jukumu la kumtoza faini mwajiri ambaye hakupeleka michango ya hifadhi ya jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, wasiwasi wangu ni kwamba Labour Officer scope yake ya kazi ni kubwa, ana-deal na mambo mengi sana likiwemo hilo la kusimamia hizi sheria za kazi; ana mambo ya OSHA, Vyama vya Wafanyakazi na mambo mengine mengi. Kwa hiyo, kuchukua hiki kipengele cha kutokupeleka michango ya hifadhi ya jamii, kipengele mahususi hiki kumkabidhi yeye naona kwamba impact yake itakuwa ndogo. Kwa nini tunampa Labour Officer na wakati mamlaka ama taasisi mahsusi inayo-deal na hifadhi ya jamii ipo? Kwa nini tusipeleke mamlaka haya ama kazi hii kwa mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, yaani SSRA?
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiliacha hilo la kwamba Afisa Kazi, scope yake ya kazi ipo kubwa sana na hili suala la kutokupeleka michango ya hifadhi ya jamii linaweza likaleta ucheleweshaji, lakini pia SSRA tayari wamesha-advance katika mifumo yao. Wana kitengo cha compliance ambacho kimsingi kipindi niko pale nikifanya kazi, kuanzia asubuhi mpaka jioni wanachama wanamiminika na complain yao kubwa ni kwamba michango yao ya hifadhi ya jamii haijafika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda ieleweke, kwa mujibu wa hizo sheria ni kwamba mtu kuweza ku-qualify kupata pension ukiacha ile umeshafikisha umri miaka 55 kwa hiari na 60 kwa lazima, lakini pia kuna kifungu kinachosema, uwe umechangia miaka 15. Kwa maana hiyo, kama imepelea miezi minne ama mitano hukupeleka michango yako, hu-qualify wewe kupata pension.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tukienda tukasema tunampa huyu, tukaacha kumpa SSRA, ninahofu na wasiwasi kwamba dhamira njema Serikali mnayoitafuta hatutakaa tuipate.
Mheshimiwa Naibu Spika, kingine tena, SSRA wana instrument, wana database management guideline ambayo inawawezesha wao kwa kupitia hii mifuko kuweza kupata details ama taarifa za mwanachama, namba ya mwanachama, majina yake, michango yake nakadhalika. Kwa hiyo, nadhani tukimkabidhi SSRA, itakuwa ni nyepesi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine, wakati naondoka pale SSRA niliacha wanaandaa program ya wao ku-connect mifumo yao na TRA ili waweze kuwajua waajiri wote, walipakodi nchini. Kwa hiyo, kama unawafahamu waajiri wote wanaolipa kodi nchi hii, ni rahisi ni rahisi kama kuna mwajiri analipa kodi kwa kiasi kikubwa, huyo atakuwa na wafanyakazi. Kwa hiyo, ni rahisi ku-trace kwamba kama analipa kodi: Je, wafanyakazi wake amewaandikisha kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii? Je, michango ya hifadhi ya jamii imepalekwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naona tukimpa SSRA itakuwa ni rahisi sana. Pengine kama Serikali itapata ugumu wa moja kwa moja kulipeleka kwa SSRA katika maana kwamba hii kazi apewe SSRA, basi naomba huyu Labour Officer afanye kazi hii kwa kushirikiana na SSRA. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kukushukuru sana, lakini pia naungana na wale wenzangu wote waliokuwa wakizungumzia Sheria ya Elimu. Adhabu ya miaka 30 ni mahsusi kabisa, inawatosha kwa wale wote ambao wanaenda kuwakwamisha watoto wa kike wasitimize ndoto zao ambazo wamekuwa wakizifikiria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naungana na wale wote waliozungumzia marekebisho, I mean kupongeza kifungu hicho, nami niungana nao mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, nachukua nafasi hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya uteuzi wake wa ma-DC. Kikubwa zaidi, kumekuwa na ma-DC vijana wengi sana. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuonesha imani kwetu vijana. Nawaomba vijana wenzangu walioteuliwa u-DC waende wakafanye kazi. Kimsingi tunasema, Hapa Kazi Tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.