Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joseph Kizito Mhagama (8 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda nimshukuru sana Mwenyenzi Mungu aliyenijalia wakati huu kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. Pia kwa unyenyekevu mkubwa sana niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Madaba ambao kwa umoja wao wamenituma nifanye kazi yao wakiamini kwamba nitawatendea haki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kupongeza sana hotuba ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa kwa Bunge lako Tukufu. Hotuba hii imejaa hekima kubwa lakini pia imejaa matumaini makubwa sana kwa wananchi wa Tanzania na hasa kwa wananchi wa Jimbo langu la Madaba. Hotuba ya Mheshimiwa Rais kwa sehemu kubwa imetoa mwelekeo wa Taifa letu kwa kipindi cha miaka mitano. Kwa hakika hotuba yake imeshakwishaanza kutafsiriwa kwa vitendo kupitia utekelezaji wa kazi hizo, lakini pia kwa kupitia Baraza lake la Mawaziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Mawaziri wote wa Awamu ya Tano, wanafanya kazi kubwa kwa ajili ya Watanzania. Kwa namna ya pekee sana naomba sana niwashukuru sana Mawaziri ambao tayari wameshakuja kwenye Jimbo langu na tayari wameanza kufanya kazi na wananchi wa Jimbo langu. Kwa namna ya pekee nimshukuru Mheshimiwa Ummy Mwalimu, tayari amekuja kuangalia changamoto za afya na sasa yupo kwenye mchakato wa kuhakikisha kwamba tunapata hospitali ya Wilaya, tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa heshima kubwa nimshukuru sana Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Nishati na Madini katika mazingira magumu na muda mgumu alifika katika Jimbo langu kuangalia changamoto ya umeme na kuipatia majibu pale pale. Namshukuru na kumpongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika uchangiaji wangu nitajikita katika maeneo machache muhimu yanayohusu maslahi ya Taifa letu. Moja ni eneo la viwanda. Katika hotuba ya Mheshimiwa Rais toka ukurasa wa 13 – 16 anaeleza ni namna gani Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuifanya sekta ya viwanda iwe sekta mama itakayotoa ajira za uhakika kwa Watanzania. Mheshimiwa Rais anakwenda mbali zaidi na kueleza namna gani hiyo sekta ya viwanda inakwenda kujibu matatizo ya masoko ya mazao, mifugo pamoja na uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii kwa uzito ambao Mheshimiwa Rais ameupa na kwa hali halisi ya Tanzania ni sekta muhimu sana. Nitumie nafasi hii kupongeza hatua ya Mheshimiwa Rais kuzingatia viwanda lakini naomba nitoe tahadhari kwa wale ambao wamepewa kusimamia utekelezaji wa jukumu hili. Moja, lazima tujue kwamba sekta ya viwanda ina mahusiano makubwa sana na sekta ya biashara lakini pia kwa sababu hivyo viwanda vinahusu kilimo, uvuvi na mifugo, sekta hizi zote zinafanya kazi kwa karibu sana. Sera ya kuimarisha viwanda ndani ya Tanzania siyo sera ngeni, kigeni katika Awamu hii ya Tano ni mikakati mipya ambayo Mheshimiwa Rais amekuja nayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tujifunze ni nini kilisababisha viwanda vyetu vya miaka ya 1980 na 1990 na kuelekea mwaka 2000 vikafa. Mikakati ya ndani ni mizuri, mitaji ilipelekwa lakini naomba wanaohusika na maandalizi na usimamizi wa eneo hili wakubali kurudi tena kwenye kusoma uzoefu hasa unaogusa sera zetu za nje, mikataba yetu na makubaliano ya kibiashara na mataifa mbalimbali zikiwemo jumuiya mbalimbali zenye maslahi ya kibiashara na Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukifuatilia kwa undani pamoja na jitihada za ndani za kuzalisha mazao ya viwandani, mazao yetu yameendelea kukosa soko kwa sababu tumefungulia kiholela mazao ya viwandani yanayotoka mataifa mengine. Ndani ya Mkoa wa Ruvuma nimepambana sana kwa miaka zaidi ya sita kuhakikisha kwamba sekta ya mazao ya mafuta yakiwemo alizeti inakuwa sekta tegemezi kwa uchumi wa Mkoa wa Ruvuma kwa kuhakikisha kwamba tunazalisha mafuta ya kula ya kutosha yatakayoweza kukidhi mahitaji ya mkoa. Hata hivyo, jitihada hizo zimeangamizwa na mafuta ya bei rahisi yanayoingizwa toka Malaysia na nchi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo eneo halitaangaliwa vizuri, Watanzania tutaenda kuwekeza kwenye viwanda na tutafilisika na tutabaki maskini wa kutupwa kwa sababu Tanzania mpaka sasa imeendelea kuwa soko kubwa la mazao ya viwandani yanayotoka nchi zingine. Kwa hiyo, nashauri sera yetu inayohusiana na maeneo hayo iangaliwe vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo ni mama kwa uchumi wetu ni kilimo na mifugo. Niishukuru sana Wizara ya Kilimo, Mheshimiwa Waziri Mwigulu na timu yake wananchi wa Madaba kwa namna fulani wamefaidika sana na Wizara hii kwa asilimia 75 ya wakazi wake kufanikiwa kupata pembejeo za ruzuku.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu wa ruzuku siyo endelevu. Msimu wa mwaka jana wananchi wa maeneo yale hawakupata pembejeo za ruzuku iliathiri sana uzalishaji wao. Najua mfumo huu umechukua uzoefu kutoka Malawi na maeneo mengine na hapa tunau-apply. Naomba Wizara inayohusika na kilimo na mifugo tuchukue hatua za makusudi kujifunza mifumo mingine inayopendekezwa na wadau mbalimbali wa kilimo. Najua kumekuwa na miradi mbalimbali ya wadau wa kilimo inayojaribu mifumo mbalimbali ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata pembejeo kwa namna endelevu. Naomba sana Wizara hii iandae utaratibu maalum wa kufanya utafiti wa mifumo inayofaa. Mfumo huu hauna uendelevu kwa sababu unategemea asilimia 100 ruzuku ya Serikali, ruzuku ambayo hatuna uhakika nayo. Kuna mifumo ya kuwaunganisha wasindikaji, wanunuzi wa mazao, wasambazaji pembejeo pamoja na vikundi vya wakulima kwa kupitia mfumo wa mikataba ambayo itawasaidia kupata mikopo ya pembejeo, uhakika wa masoko ya kilimo na uhakika wa uzalishaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo mengi nyeti yanayowagusa wananchi wa Jimbo la Madaba, eneo la soko la mazao ni mgogoro sana kwa sababu mpaka sasa tunategemea Serikali pekee kununua mahindi kupitia NFRA. Nashukuru sana Wizara ya Kilimo wamefanya jitihada kubwa sana kukarabati maghala ya kuhifadhia mazao wakati wa mavuno. Hata hivyo, maghala yale yametengenezwa kwa pesa za wakandarasi, wakandarasi hawajalipwa, hawajamaliza na mwezi wa sita wananchi wanaanza kuvuna hawana mahali pa kuhifadhia mazao yao, tunaomba hilo nalo liangaliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini eneo gumu sana kwetu Madaba ni maji. Wananchi wa Madaba hawana maji, Jimbo la Madaba ni jipya, Halmashauri ya Wilaya mpya, Makao Makuu maji ni mgogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunisikiliza. (Makofi)
Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa kwa kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2016/2017 – 2020/2021
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nikushukuru wewe kwa kunipa hii nafasi ya kuchangia Mpango huu wa Maendeleo wa Miaka Mitano. Mpango huu wa Miaka Mitano unaeleweka vizuri iwapo utasomwa katika context yake ya kwamba Mpango huu unatokana na Mpango Elekezi wa Miaka 15. Ukishauweka katika context ya miaka 15 unaelewa kwamba kilicholetwa hapa kwa miaka hii mitano ni hatua ya pili ya utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Miaka 15. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukishaelewa hivyo, unaweza ukapunguza sana kejeli ambazo zinatolewa na baadhi ya Wabunge humu ndani. Hatua ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huu ilikuwa kutanzua vikwazo vya uchumi; ni hatua nzuri ambayo imefikiwa kwa kipindi cha miaka mitano tunachokimaliza msimu huu wa 2015/2016.
Mheshimiwa Spika, tunapokuja na Mpango wa miaka mitano inayoanzia mwaka 2016/2017, tunazingatia pia uzoefu tulioupata miaka mitano iliyotangulia. Ukiangalia katika Mpango huu, miaka mitano iliyopita ilieleza bayana, pamoja na kutanzua vikwazo vya uchumi, pia kipindi hicho cha miaka mitano iliyotangulia kilienda sambamba na kubaini maeneo ya vipaumbele. Maeneo ya vipaumbele yaliyobainishwa ni pamoja na Miundombinu, Kilimo, Viwanda, Rasilimali Watu, Huduma za Kifedha, Utalii na Biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunapotoka kwenye awamu ya kwanza na tunapokwenda kwenye awamu ya pili ambayo itachukua tena miaka mitano, tumechagua eneo la viwanda kama eneo mahususi la kulifanyia kazi. Mpango huu ukiusoma kwa umakini na ukaulewa, utaelewa ni kwa nini sasa tumechukua viwanda na kwa nini Mpango huu umeitwa kama kipaumbele kujenga misingi ya uchumi wa viwanda? Tunapoongelea viwanda, tunaenda sambamba na miundombinu ambayo itafanya viwanda viimarike lakini biashara iimarike. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mpango huu umebainisha vizuri maeneo ya ujenzi wa barabara, reli, bandari, lakini pia umeeleza miradi mahususi ambayo itaifanya Tanzania yetu iwe Tanzania mpya, Tanzania ambayo inakwenda kujibu kero za vijana, akinababa na akinamama wa Taifa hili. Ukiusoma katika context hiyo, unakubaliana nami kwamba Mpango huu wa miaka mitano kama sehemu ya utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Miaka 15, Mpango huu umekaa vizuri kwenda kutatua matatizo ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitumie nafasi hii kwanza kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Serikali nzima ya Awamu ya Tano kwa kujifunza kutokana na uzoefu wa miaka mitano iliyotangulia na kuja na Mpango madhubuti utakaolijenga Taifa letu vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninavyouangalia Mpango huu na namna ulivyokaa, nina maeneo machache ambayo ningependa nishauri. Ukiangalia Mkoa wa Ruvuma ambao lango lake lipo katika Jimbo ninaloliongoza, Jimbo la Madaba unaona kwamba Mkoa wa Ruvuma umejaa fursa nyingi sana ambazo kama zitatumiwa vizuri na Mpango huu, kwa hakika Tanzania itakuwa nchi ya neema sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zipo barabara muhimu ambazo zitatakiwa zijengwe na ziimarishwe ili Mpango huu wa viwanda uweze kuwanufaisha wananchi wa Jimbo la Madaba na wananchi wa Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla ambao kwa asilimia kubwa wanachangia sana pato la Taifa na wanachangia sana chakula kinacholisha Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, Jimbo langu la Madaba linapakana na Wilaya ya Ulanga, lakini kufika Wilaya ya Ulanga nahitaji kufika mpaka Mikumi na baadaye niende Ifakara ndipo niende Ulanga. Wakati wananchi wangu wa Kijiji cha Matumbi wanatumia siku sita kwa mguu au nne kufika katika Wilaya ya ulanga, lakini wanatumia siku mbili kwa mguu kufika mpakani mwa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba na upande wa pili wa Malinyi.
Mheshimiwa Spika, hicho tayari ni kikwazo kikubwa sana cha uchumi kwa maendeleo ya maeneo yote mawili. Pamoja na kwamba Mpango huu bado haujabainisha nini kitafanyika, haujafafanua, nafikiri kwa sababu Mpango huu una sifa ya kujifunza kwa Mipango iliyotangulia, basi tuendelee kuangalia lile eneo ambalo linapakana na Jimbo la Madaba kama sehemu moja muhimu ambayo itachangia sana uchumi wa wananchi wa maeneo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia imeelezwa vizuri sana kwamba Mkoa wa Lindi unapakana na Mkoa wa Ruvuma, nalo ni eneo muhimu sana kama tunataka kuimarisha uchumi wa wananchi wale kupitia viwanda kwa sababu tunazalisha malighafi ya kutosha, tunahitaji kusafirisha, lakini tutazalisha bidhaa nyingi za viwandani, tutahitaji ziende Lindi, Ifakara, Mahenge na maeneo mengine ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa miaka mingi sana Mbunge aliyemtangulia Waziri Mheshimiwa Jenista Mhagama, Mbunge Profesa Simon Mbilinyi, aliyestaafu, alianza kuongea sana kuhusu miradi ya NDC, hususan mradi wa Mchuchuma na Liganga. Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama, Mbunge wa Jimbo la Peramiho, ambaye sasa kipande cha Jimbo lile kimekuwa Jimbo la Madaba, ninaloliongoza sasa, kwa miaka kumi amesimamia ajenda hiyo ya mradi wa Mchuchuma na Liganga.
Mheshimiwa Spika, mradi ule kama utafanikiwa kwa kiwango hiki ambacho umeelezwa katika Mpango huu, kwa hakika utatukomboa sana wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, utawakomboa sana wananchi wa Madaba na Jimbo la Peramiho. (Makofi)
Mheshimwa Spika, ni vizuri sasa, kwa vile maandalizi ya kuanza ku-explore ule mradi wa Liganga Mchuchuma, ni vyema sasa barabara inayotoka Wilaya ya Ludewa kufika Madaba iimarishwe ili kwamba wananchi wa pale waweze kunufaika na ule uchumi, lakini pia ndiyo barabara inayokuja kuunganisha na barabara ya Makambako kuja Dar es Salaam, kwa ajili ya kusafirisha mali na bidhaa zitakazozalishwa katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, tuna usemi wa Kiswahili, Waswahili wanasema, “Siku ya kufa nyani, miti inateleza.” Wakati nipo nje ya Bunge hili, kuna wakati nilikuwa naona kuna baadhi ya hoja zenye mashiko kutoka upande wa pili wa upande wangu wa kulia, lakini kadri ninavyozidi kukaa ndani ya Bunge hili, katika hiki kipindi cha miezi kama sita hivi nimekaa hapa, nazidi kuona kwamba hoja zenye mashiko zinazidi kupungua. Naamini sasa kweli miti inateleza. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna wakati ambapo hoja ya ufisadi ndiyo ilikuwa mhimili mkubwa wa kushikilia. Leo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli alipoisimamia hoja ya kutumbua majipu na kuondoa mafisadi, wale wale ambao walikuwa wameshikilia hiyo nguzo, wanamlalamikia na wanamlaumu. Ama kweli Waheshimiwa Wabunge ni lazima tujipime wakati mwingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, inanisikitisha sana ninapoona mtu anaji-contradict mwanzo hadi mwisho wa hotuba yake. Anaanza na kusema Baraza la Mawaziri halifanyi kazi, halifai. Baraza hili ni lile lile la Awamu ya Nne, wanabadilishana nafasi, halafu baadaye anasema Mheshimiwa Waziri fulani umenifaa sana, unafanya sana kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuishi kwa contradiction. Lazima tuwe na consistent katika hoja zetu. Leo nimependa sana…
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, lazima ni-declare interest, approach aliyoitumia Mheshimiwa Ally Saleh, imetujenga sana na imemsaidia sana Waziri wa Fedha kuweza kuboresha Mpango huu wa Miaka mitano wa Maendeleo. Napenda sana tutumie approach hiyo ili kuisaidia nchi yetu na kuwasaidia Mawaziri waweze kutuletea majibu yanayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunalo eneo lingine muhimu sana kwa Jimbo la Madaba…
TAARIFA
MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa kanuni ya 68 (8)!
SPIKA: Mheshimiwa Joseph, naona kuna taarifa ambayo haivumiliki...
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika ahsante. Taarifa hiyo siipokei kwa sababu wale ambao walileta ushahidi ndani ya Bunge hili, mimi nikiwa nje ya Bunge hili, kwamba Mheshimiwa Lowassa ni mmoja katika mafisadi wakubwa, ndio hao hao waliomkumbatia na kwenda naye katika kampeni ya Awamu hii ya Tano. (Makofi/Kicheko/Vigelegele)
MBUNGE FULANI: Wanafiki wakubwa!
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, kwa namna yoyote siwezi kuipokea hiyo taarifa. (Makofi/Kicheko/Vigelegele)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha
kwa muda wa mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Mhagama, muda wako umekwisha. (Makofi/Kicheko/Vigelegele)
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote naomba nikushukuru wewe binafsi kwa kunifanya kuwa mchangiaji wa pili kwa hotuba hii iliyotukuka ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hii ambayo imebeba maudhui ya Wizara zote, imesheheni mipango na mikakati madhubuti ambayo kama itatekelezwa hivi ambavyo imewekwa, kwa hakika itatutoa Watanzania hapa tulipo leo na kutufikisha kwenye maisha ya uchumi wa kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Wazari Mkuu kwa hotuba hii nzuri, pia niwapongeze sana Wenyeviti wa Kamati zote mbili, ambao pia wameleta hotuba yao mbele ya Bunge lako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika tu kwamba kwa bahati mbaya nilitarajia nipate mawazo mbadala, lakini yameshindikana, hata hivi nadhani tutakwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikubaliane na mipango pamoja na mikakati yote ambayo hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu imebeba. Maeneo ambayo nilipeda nitoe ushauri na niiombe Ofisi ya Waziri Mkuu kuifanyia kazi, katika kipindi hiki cha mwaka 2016/2017, moja ni Kitengo cha Maafa.
Katika hiki Kitengo cha Maafa kwanza nimpongeze sana Mkurugenzi wa Kitengo hiki kwa kazi yake nzuri anayoifanya mpaka sasa, licha ya changamoto alizonazo zinazoendana na ukosefu wa nyenzo za kufanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kupitia makabrasha ya kitengo hiki, nilibaini kwamba pamoja na nia nzuri ya kitengo hiki kukabiliana na maafa, pamoja na jitihada nyingi zilizofanyika kuwajengea uwezo wanaofanya kazi katika kitengo hiki, bado kitengo hiki hakijawa na nguvu ya kutosha kuweza kukabiliana na changamoto za maafa katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe jitihada za makusudi zifanyike kuhakikisha kwamba kitengo hiki, pamoja na kujengewa uwezo wa kinadharia ambao kwa sasa wameendelea kujengewe kupitia miradi mbalimbali ingefaa pia kitengo hiki sasa kiwe na vituo maalumu vyenye nyenzo maalumu za kuweza kukabiliana na maafa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushahidi ni kwamba wakati Dodoma na Kondoa wanalia kwelea kwelea responsiveness ya kitengo kinachohusu maafa ilikuwa ndogo sana, huu ni ushahidi kwamba bado tuna changamoto kubwa kwenye eneo hili, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu atusaidie kuhakikisha kwamba tunafanyia kazi ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nilipenda nichangie ni eneo la elimu. Wakati nachangia jana nilimueleza Mheshimiwa Spika kuhusu hali ya Jimbo langu la Madaba. Jimbo letu la Madaba ni Jimbo changa lina takribani miezi michache sana na Halmashauri ya Wilaya nayo ina miezi michache tu. Lakini upande wa elimu kama ilivyo katika maeneo mengine tuna changamoto nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao walimu zaidi ya 412 ndani ya Wilaya ya Songea, walimu hao Wilaya ya Songea inahusisha pia Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, walimu hawajapandishwa madaraja kwa muda mrefu pamoja na kwamba wana hizo sifa. Nimeomba Chama cha Walimu kiniwasilishie nyaraka mbalimbali ambazo nitaziwakilisha katika Ofisi ya Waziri Mkuu ili mtusaidie kutanzua tatizo hili kwa sababu ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya elimu katika Halmashauri yetu na Wilaya ya Songea kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu ambalo ningependa nitoe mchango wa kina ni eneo la soko la mazao ya mahindi. Kama unavyojua Mkoa wa Ruvuma ni ghala la Taifa la chakula. Mkoa huu kwa miaka mingi umeendelea kuzalisha chakula cha kuwalisha Watanzania, katika Mkoa huu Halmashauri Wilaya ya Madaba, Jimbo la Madaba lina wakulima ambao wanazalisha sana mahindi ambayo yanachangia sana kwenye chakula cha Taifa letu. Kwa bahati mbaya mfumo wa manunuzi wa haya mahindi bado siyo rafiki kwa wananchi wale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa bado tunategemea kituo kimoja cha Madaba, yapo maghala katika kila Kata yanajengwa kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Chakula kwa kupitia mradi wa BRN. Maghala haya mpaka sasa hayajakamilika, na ujenzi wake umesimama kwa muda mrefuwakandarasi bado wanalalamika hawajalipwa.
Naiomba Ofisi ya Waziri Mkuu, wakati tunaendelea na mchakato huu tuhakikishe kwamba ule mchakato ambao umesimama katika vijiji vyote vya Halmashauri ya Wilaya Madaba ya kujenga na kuimarisha maghala ukamilike kwa sababu wananchi wa Jimbo la Madaba wataanza kuvuna mwezi ujao na watahitaji kuhifadhi mazao yao. kama ambavyo ulisema mwenyewe Mheshimiwa Waziri Mkuu ulipotembelea Mkoa wa Ruvuma, ulishauri kwamba NFRA wanunue mahindi katika vituo vilivyoko vijijini ili kuwaondolea Wananchi adha ya kusafirisha mazao haya kuyapeleka katika vituo maalum vya mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri yetu ya Madaba pia inachangamoto kubwa sana ya maji. Mji wa Madaba pekee na Kijiji cha Mkongotema ndiyo wenye maji yanayotiririka, lakini wingi wa mabomba hauwiani na idadi ya wananchi waliopo. Ipo miradi iliyofadhiliwa na World Bank, miradi hii imetekelezwa katika vijiji vitatu vya Mkongotema, Lilondo na Maweso. Kwa bahati mbaya miradi ya Maweso na Lilondo imesimama kwa muda mrefu sana, kwa vyovyote vile jitihada zilizofanyika mpaka sasa kubwa na niishukuru sana Wizara husika kwa kutufikisha pale ambapo tumefika. Ninaomba sana tunapoendelea na mchakato huu zoezi hilo pia la kukamilisha hii miradi ya maji katika maeneo yaliyobaki liendelee, lakini pia niombe sana Mji wa Madaba una kilio sana cha maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii pia kumshukuru sana Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu, pamoja na Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo ambao wamekuja ndani ya Jimbo langu na kushirikiana na wananchi kutatua kero zinazowakabili kwenye eneo la afya na eneo la umeme. Hivi ninavyokuambia Mheshimiwa Sospeter Muhongo yupo kwenye mchakato wa kukamilisha umeme wa maeneo ya Mji wa Madaba na Mungu bariki Disemba tutakuwa na umeme, ninaniomba sana zoezi hili liendelee, wananchi wa Madaba wanatambua sana juhudi za Mheshimiwa Sospeter Muhongo, lakini pia wanatambua sana jitihada za Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ummy Mwalimu za kuhakikisha kwamba Madaba tunapata Hospitali ya Wilaya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho na la muhimu sana ni kwamba tulipokuwa tunaelekea uchaguzi wa mwaka 2015 vipo vijiji vingi vilivyozaliwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba kama ambavyo vilizaliwa katika maeneo mengine ya Songea Vijijini. Vijiji hivi bado havijapata usajili wa kuduma na kama vimepata havija…
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, napongeza sana hotuba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba Madelu. Hotuba hii imesheheni mipango na mikakati madhubuti ya kuliondoa kundi la Watanzania wafikiao asilimia 80 na kuwafikisha kwenye uchumi wa kati. Umadhubuti wa Mipango na Mikakati iliyopo katika hotuba hii ni kielelezo cha umadhubuti wa Mheshimiwa Waziri Mwigulu Nchemba. Napenda nimthibitishie kuwa wananchi ninaowawakilisha, Jimbo la Maduba wanatambua sana umahiri na umadhubuti wa Mheshimiwa Mwigulu Nchemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nielekeze mchango wangu katika maeneo yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ni matumizi ya mbegu bora za kilimo. Kadiri ya Utafiti wa Masalwala (2013), asilimia 93 ya mbegu zinazotumiwa na wakulima katika misimu mbalimbali ni recycled from previous crops. Hii inatokana na gharama za mbegu hizo, upatikanaji, ubora wa mbegu hizo na uelewa wa wakulima juu ya matumizi na umuhimu wa mbegu hizo. Napongeza kuwa Wizara imeliona hilo na tayari imejipanga kuongeza uzalishaji wa mbegu kutoka tani 10,270.86 hadi tani 40,000 ikiwa ni mara nne. Ni hatua kubwa sana. Naomba Wizara isimamie hili, tujipime kwa kiasi hiki na mwaka ujao twende mbali zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ni muhimu katika mikakati ya kufanikisha zoezi hili, makampuni ya ndani yapate kipaumbele kujengewa uwezo wa kuzalisha mbegu. Yapo makampuni yenye nia na yamethubutu kuanza. Ni vema yakapata ruzuku kuyawezesha kuzalisha mbegu za mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili ni mfumo wa upatikanaji wa pembejeo. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mwigulu Nchemba kwa kuamua sasa kupitia upya mfumo wa usambazaji wa pembejeo kwa kuzingatia malalamiko makubwa ya mfumo wa sasa wa ruzuku. Mkakati huu mpya ni mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo yangu ni kuharakisha mapitio haya. Case studies ni nyingi, zipo Asasi na wadau wengi waliojaribisha models mbalimbali. Miongoni mwa wadau hao ni AGRA, SNV, RUCODIA, RUDI, BRTENS na kadhalika. Wadau hawa tayari wana models mbalimbali za usambazaji wa pembejeo. Jambo muhimu ni kwamba mfumo mzima wa usambazaji pembejeo uwe enterprise led. Ni vema Wizara ikakutana na wadau hao na kuchukua uzoefu wao katika suala zima la Agro-Dealers Development.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu ni mazingira wezeshi ya kilimo-biashara. Hotuba ya Mheshimiwa Mwigulu imefafanua vizuri mazingira wezeshi ya kilimo-biashara. Katika aliyosema Mheshimiwa Waziri, ningependa kuongeza yafuatayo:-
(i) Mafanikio ya kilimo yanategemea sana mafanikio ya miundombinu ya barabara vijijini, upatikanaji wa rasilimali fedha na elimu ya kilimo; na
(ii) Model ya mradi wa MIVARF uliopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni nzuri sana ya comprehensive approach ambayo kama Wizara itachukua model hizi, maendeleo ya kilimo chenye tija tutayapata kwa haraka sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nne, Chuo cha Mafunzo ya Mifugo LITA (Madaba). Tunaomba chuo hiki kitoe pia mafunzo ya kilimo na kipandishwe hadhi na kuwa chuo kikuu kwani Mikoa ya Kusini mahitaji yetu katika eneo hilo ni makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. KIZITO M. JOSEPH: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia muda niliopewa niende moja kwa moja, kwanza kutoa salamu za shukurani kwa Waziri, Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo, ambaye majira ya jioni kuelekea saa moja, mvua zinanyesha, amechoka, amefanya kazi kutwa nzima Ludewa, anarudi anakwenda Songea Mjini, alikubali kuendesha mkutano Madaba. Wananchi wa Jimbo la Madaba hawataisahau ile taswira.
Mheshimiwa Naibu Spika, siku ile Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo, alitoa majibu ya moja kwa moja ya tatizo kubwa la umeme la wananchi wa Madaba. Wananchi wa Madaba wanamshukuru na wapo pamoja naye katika safari hii ya kutekeleza majukumu aliyopewa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto katika utekelezaji wa maagizo ya Mheshimiwa Waziri, lakini changamoto hizi zinahusisha zaidi muundo wa utaratibu huo wa utekelezaji. Kwa utaratibu ambao Mheshimiwa Muhongo ameuweka, ni kwamba Madaba ifikapo Desemba tutapata umeme, lakini katika kipindi hiki cha miaka miwili Madaba Mjini patakuwa hub ya umeme unaotoka Makambako kuelekea Songea, lakini pia hub ya umeme unaotoka Mchuchuma na Liganga kulelekea maeneo mengine ya Taifa letu. Maana yake nini? Maana yake Madaba inakwenda kupitia transformation kubwa sana ya uchumi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto inayotupata kwa sasa ni kwamba Serikali bado ina ugumu kidogo wa kuchangia gharama kuweza ku-meet gharama za wafadhili kwenye hilo jukumu na kikwazo kinaonekana kipo Hazina. Naomba watu wa Hazina wasikalie pesa kama zipo. Kama pesa zipo na zimepangwa kwa matumizi hayo, basi zitolewe zikafanye hizo kazi ili hizi Wizara husika ziweze kujibu matatizo ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita kwenye hili tu kwa sababu linanigusa na wananchi wa Madaba lina wagusa sana. Ndani ya Jimbo langu la Madaba ni kijiji kimoja tu cha Lilondo kina umeme na umeme huu ni wa wananchi. Nachukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Mwijage, ambao kwa namna moja au nyingine wamesaidia sana kupatikana ule umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo yote ya Jimbo la Madaba, Vituo vyote vya Afya, saa hizi mimi Mbunge kwa kutegemea posho ninazopata hapa Bungeni, naweka solar. Hata ukiiangalia gari ninayoitembelea ni ya kawaida sana ili niweze kubana matumizi ya kupata solar kwa ajili ya Vituo vyote vya Afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana na wananchi wa Jimbo la Madaba wanaomba sana kwa Mheshimiwa Waziri Profesa Sospeter Muhongo, kwamba yale ambayo ameyapanga wanamwomba Mwenyezi Mungu amjalie nguvu ili ifikapo Desemba na kuendelea changamoto hii iwe imekwisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunayo miradi ya kielelezo ya kiuchumi. Ndugu yangu…
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nakushukuru wewe kwa kunipa hii nafasi. Pili, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa uwasilishi wake mzuri. Pamoja na kazi nzuri aliyoifanya Mheshimiwa Waziri nina mambo mawili, matatu ya kuishauri hii Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza, unajua habari ya viwanda Tanzania siyo habari ngeni. Tumekuwa na viwanda miaka ya 80 kuelekea miaka ya 90 na viwanda vingi vimekufa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri, sehemu pekee au mkakati pekee ambao ameuweka ambao umeonekana wa namna ya kulinda viwanda vya ndani ni kuongeza kodi kwenye bidhaa zinazotoka nje, zile bidhaa ambazo tunaweza kuzizalisha ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maoni yangu huo ni mkakati mzuri, lakini mkakati huu pekee hautatosha kulinda viwanda vya mafuta ya kula, hautatosha kulinda viwanda vya sukari nchini, hautatosha kulinda viwanda vya nguo nchini. kwa sababu kikwazo cha viwanda vya Tanzania siyo tu ushindani wa bei za bidhaa zinazoingia, bali pia mikataba ambayo tunaingia na nchi marafiki ambao tunafanya nao biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vyovyote vile, mikataba ile bado inatubana. Pengine hata kuweka hizo kodi kwenye hizo bidhaa huenda tukagomewa na wadau marafiki tunaofanya nao biashara kwa sababu na wao wanataka kulinda viwanda vyao. Kwa hiyo, naishauri Wizara ya Fedha ifanye kazi ya kina. Mwezi wa Pili nilitoa ushauri huu na sasa narudia tena kwa sababu mpaka sasa sijaona assessment ya kutosha ya ku-assess kwa nini tulifeli miaka ya 1980 na 1990 na kwa nini tunadhani tutafaulu katika kipindi hiki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili, ni suala zima la maji. Sera ya Taifa inatutaka Watanzania wote popote walipo waweze kupata maji katika umbali usiozidi mita 400. Ukiiangalia sera hii na mpango mkakati uliowekwa na Wizara ya Fedha, havifanani kabisa. Kukata sh. 50/= kwenye mafuta ya petrol na diesel pekee, havitoshi. Kamati ya Bajeti imeshauri tuweke angalau sh. 100/= na baadhi ya Wabunge wameshauri tuweke angalau sh. 100/=. Nami naomba tuweke angalau sh. 100/= ili tuweze kusogea mbele kwa haraka zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo langu la Madaba ni moja katika Majimbo ambayo yana tabu sana ya maji. Hivi ninavyoongea, Kijiji cha Lilondo na Maweso toka miradi imeanza mwaka 2015, haijakamilika na Wakandarasi bado wanahangaika kulipwa. Naishukuru Wizara ya Maji, tunawasiliana kwa jambo hili, lakini huu ni ushahidi kwamba kuna matatizo ya kutosha kwenye hili eneo, tulitengee bajeti ya kutosha kwa kuzingatia ushauri wa Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ni ombi kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango avae viatu vya Walimu wa Sekondari na Shule za Msingi ambao katika uhai wao wote wanalitumikia Taifa hili, mishahara yao inakatwa kodi na wanapomaliza kipindi cha utumishi wanalipwa kiinua mgongo na kinakatwa kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri avae viatu vya watumishi wengine wa Serikali na Sekta ya Umma ambao mishahara yao ni ya chini, wanakatwa kodi, wanafanya kazi, lakini wanapomaliza utumishi wao, bado kiinua mgogo kinakatwa kodi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lililopita lilienda hatua mbele, likaiomba Serikali iondoe kodi kwenye hivi viinua mgongo, yaani kwenye mafao ya wafanyakazi. Nilitegemea Wizara ya Fedha ije na mkakati huo sasa wa kuondoa hizo kodi kwenye mafao ya wafanyakazi na kupendekeza njia mbadala ya kupata fedha kwa ajili ya kuendeshea Serikali, kwa sababu hawa wafanyakazi wameendelea kukatwa kodi wakati wote. Kilichonishangaza, tunazidi kurudi nyuma. Tulishapiga hatua mbili mbele, tunarudi hatua nne nyuma, tunaanza sasa kufikiria kukata kodi kwenye mafao ya Wabunge. Tunakwenda wapi? Tutafika lini tunakotaka kwenda kuwatengenezea Watanzania maisha bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri avae viatu vya Wabunge wanaotoka katika Majimbo yenye changamoto kama Jimbo la Madaba. Mbunge wa Madaba akishapata posho humu Bungeni, anakwenda kununua solar kuweka kwenye Vituo vya Afya. Anakwenda kuchangia maji Matetereka ili wananchi wapate maji kwa sababu Serikali bado haijaweza kufikia wananchi hao.…
Nasikitika sana ninapoambiwa kwamba...
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia. Kwanza kabisa nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mpango kwa kuleta mwelekeo wa Mpango huu, ili ujadiliwe na Bunge lako na mimi kupata nafasi ya kutoa mawazo yangu, lakini nasikitika itabidi nitumie sehemu ya muda wangu mzuri kuweza kueleza maeneo ambayo pengine yalikuwa very obvious.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya michango yetu inaonesha kwamba baadhi ya Wabunge tume-panic na Wabunge wengi tulio-panic tunaufanya umma wa Watanzania u-panic. Na ukifuatilia vitu vinavyotufanya tu-panic vinakosa mantiki na leo mbele ya Bunge lako Tukufu nalazimika kuongea kwa kutumia analogia kwa sababu ndio namna pekee ambayo nadhani nitaeleweka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka kadhaa iliyopita hapa Dodoma watu wote wakiwemo Wabunge walikuwa wanakutana pale Chako ni Chako wanakula kuku. Miaka mitatu/minne baadaye sehemu mbalimbali zinazotoa huduma kama za Chako ni Chako zimefunguliwa na wateja wanachagua sehemu za kwenda, it is very natural. Miaka kadhaa iliyopita, labda kabla sijafika huko, kama unaishi mtaani, nasema ninatumia analogia, lugha rahisi kabisa na mifano rahisi, kama unakaa mtaani na katika mtaa wako unapakana na mitaa mingine minne/mitano katika mitaa hiyo mitano hakuna baa, kuna baa moja tu katika mtaa wako watu wote wanaokunywa katika maeneo hayo watakunywa katika baa yako, lakini siku mtaa wa tatu wamefungua baa tabia ya walevi ni kwenda kujaribu katika baa nyingine pia. Lakini wakiwa kule wataweza kulinganisha na ubora wa huduma ya baa yako; hiyo ndio lugha ya analogia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tunaendesha Bandari yetu ya Dar es Salaam bandari nyingine zimefuata baadae na kwa kawaida kwa tabia ya watu hupenda kujaribu. Leo bandari nyingine zipo kwa vyovyote vile huwezi kubaki na wateja wale wale ambao ulikuwanao kwa kipindi chote. Hiyo ni lugha rahisi, Watanzania tusiyumbishwe na kauli za baadhi ya Wabunge kuonyesha kwamba sababu za kupungua mizigo bandarini zinahusiana moja kwa moja na mambo ya kodi, si kweli.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, hilo haliondoi jukumu la Waziri wa Fedha kuendelea kuchunguza sababu mbalimbali za kupungua wateja, lakini sababu nyingine ndio hizo. Lazima kazi ya ziada ifanyike ili kuweza kuvuta wateja zaidi na kuweza kuimarisha bandari yetu ili iweze kuchangia mapato zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikitika sana kuona baadhi ya Wabunge tunawalilia wafanyabiashara makanjanja. Ni ajabu kuona kwamba katika bandari ile ile ambayo tunasema kwamba mizigo imepungua, mapato yameongezeka, mantiki yake ni nini? Mantiki yake ni rahisi tu, wale ambao walizoea ubabaishaji wameenda kubahatisha maeneo mengine labda wakabahatishe kubabaisha. Lakini wafanyabiashara makini wanaendela kutumia bandari yetu na hao ndio wanaotupa mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la msingi kwenye eneo hilo ni upotoshwaji wa mantiki nzima ya kusimamia matumizi na kukusanya kodi. Humu ndani baadhi yetu wametafsiri kama kubana matumizi; sijaona mantiki, bajeti ya mwaka jana tunayoimaliza mwaka huu ni shilingi trilioni 29 na mpango huu unatupeleka kwenye shilingi trilioni 32. Hiyo sio kubana matumizi, Serikali ya Awamu ya Tano inachokifanya ni kusimamia matumizi, kuna utofauti kati ya kubana matumizi na kusimamia matumizi. Serikali inachokifanya ni kuhakikisha inaongeza efficiency katika matumizi ya fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale maeneo ambayo hayana tija Serikali imepunguza kupeleka pesa na badala yake imepeleka maeneo yenye tija zaidi. Kwa hiyo, Watanzania tuelewe kwamba hatujabana matumizi isipokuwa tunapeleka fedha maeneo yenye tija zaidi, maeneo ambayo yatakuza uchumi zaidi na ndio maana bajeti imetoka toka shilingi trilioni 29 kwenda shilingi trilioni 32, hiyo ndio mantiki, ni kusimamia matumizi. Sasa wale waliozoea fedha rahisi, wale waliozoea ubabaishaji hilo nalo linawaumiza. Niwaombe Watanzania makini, wanaolipenda Taifa hili wamuunge mkono Mheshimiwa Rais katika jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakuhakikishia katikati ya giza nene ndipo inakaribia asubuhi, hapa tulipo ndipo wakati sahihi kunakaribia kucha. Mheshimiwa Zitto Kabwe alisema lazima kuwe na maumivu tunapotaka kufanya mabadiliko makubwa kama haya. Tukumbuke miongoni mwetu baadhi ya Watanzania walizoea fedha rahisi, walizoweza leo anaanzisha biashara ya shilingi milioni 10 na kila mwezi anapata faida ya shilingi milioni tano kwa sababu, alikuwa anakwepa kodi. Tumueleze mantiki ya kodi na tumueleze kwamba biashara zinakuwa steadly, hatua kwa hatua. Watanzania makini hawana tatizo na hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimpongeze sana Mheshimiwa Mpango atoe ushirikiano na Mawaziri wengine waendelee kuasimamia matumizi ya Serikali na kuelekeza pesa katika maeneo yenye tija zaidi kwa Watanzania. Hilo lilikuwa kuweka tu mazingira sawa kwa sababu niliona linapotoshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kubwa ambalo leo nilitaka nichangie ni dhana nzima ya kukuza viwanda. Katika Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi tumeweka bayana aina gani ya viwanda vitatutoa Tanzania kwa haraka zaidi. Tulisema tuwekeze kwenye viwanda vinavyosindika zaidi mazao ya kilimo kwa lengo kwanza la kumuwezesha mkulima mdogo apate soko la mazao yake, lakini pia kutoa ajira kubwa zaidi kwa Watanzania. Katika mpango tulioupata hilo halijawekwa bayana, tumeongelea viwanda vya General Tyre, tumeongelea viwanda vingine ambavyo kimsingi havigusi asilimia 80 ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosikitika kwenye mpango huu ni kwamba hatujaoanisha vizuri ile Ilani ya Chama cha Mapinduzi na huu mpango. Tunapowekeza nguvu nyingi kwenye kushughulikia viwanda tumesema ni jambo zuri, Magadi ya Soda - Bonde la Engaruka, tumeongea viwanda chini ya TEMCO na nini, lakini viwanda hivi katika ujumla wake haviendi kutatua tatizo la ajira kwa vijana wetu walio asilimia kubwa na wala haliendi kutatua tatizo la soko la mazao yetu ya kilimo. Kwa hiyo, niishauri sana Serikali kwenye hili lazima turudi tukafanye kazi upya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo jingine kwa haraka haraka, tunahangaika sana na soko la mahindi ni vema katika mpango huu sasa ikawekwa bayana. Kinachomfanya mkulima akalime ni bei ya mazao. Tunatoa ruzuku, lakini bado wakulima hawazalishi kwa tija kwa sababu hawapati faida katika uzalishaji wao. Ipo haja sasa ya kuja na sera madhubuti itakayomfanya mkulima mdogo wa Tanzania awe huru kuuza mazao yake kokote na wakati wowote. Leo ukienda kila mahali pikipiki zimejaa, Serikali imetoa ruzuku sana kwenye power tiller, lakini huzioni kokote kwa sababu hazina manufaa
kwenye kilimo chao, lakini watu wangapi wananunua yebo yebo kwa sababu hizo bodaboda kwa sababu wanajua zinawalipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tutajenga mazingira mazuri kwenye sekta ya kilimo hatutahitaji kugharamia mbolea za ruzuku tena. Tujenge mazingira yenye ushindani kwenye sekta ya kilimo, tuwaache wakulima wadogo wauze mazao yao wanakotaka, anayetaka kupeleka Malawi, anayetaka kwenda Zambia na kama Serikali inataka kununua iingie kwenye ushindani. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumemuwezesha sana mkulima mdogo na wala hatutahangaika habari za kutafuta pembejeo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia muda ninakushukuru sana na ninaunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Upatikanaji wa Habari wa Mwaka 2016
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kukushukuru wewe kwa kunipa hii nafasi ya kuchangia. Pia nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya na siha nzuri kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu kuchangia Muswada muhimu sana, Muswada ambao kama utasimamiwa utageuka kuwa sheria na utasimamiwa vizuri, utatutoa Watanzania toka hapa tulipo na kutufikisha Tanzania bora zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kueleza na namna ambavyo Muswada huu wa haki ya kupata taarifa. Chimbuko la Muswada huu ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ambavyo wengi wameeleza, Ibara ya 18(d) kila mtu ana haki ya kupata taarifa. Kwa hiyo, Muswada huu misingi yake ni universal law na misingi yake ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wale ambao wanabeza Muswada huu wanaikosea haki Katiba ya Tanzania na wanawakosea haki Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona vema pia nieleze kidogo historia ya Muswada wenyewe. Kama ambavyo tayari imeelezwa hapo awali, Muswada huu haujatunguliwa tu hewani, mpaka mwaka 2005 nchi 66 duniani zilishapitisha sheria hii, toka mwaka 2005 nchi 66 wana-practice sheria hii katika nchi zao. Sheria hizi katika nchi mbalimbali zinaweza zikawa zinatofautina kwa majina lakini maudhui ya sheria hii katika hizo nchi zote 66 ni ambayo kwa sehemu kubwa yanafanana na maudhuhi ya hii sheria ambayo tunataka tuipitishe. Hivyo, ni vizuri wale ambao tunabeza hii sheria hebu tujikite pia kwenye historia na tujaribu kuangalia comparative studies za hii sheria zinasemaje na practice za nchi zingine wamewezaje ku-practice.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hii kwa hapa Tanzania imechelewa sana kufika. Nchi ya Sweden tayari walishaanza ku-practice sheria hii mwaka 1766, ni miaka mingi sana iliyopita. Leo Tanzania tunashangaa huu Muswada ni ajabu sana!
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kueleza kidogo historia ili tuweke kumbukumbu zetu vizuri, napenda pia nileleze relevance; mantiki ya huu Muswada. Muswada huu kwa namna ulivyo una mahusiano ya kiutatu na mambo matatu; moja ni uwazi, pili ni uwajibikaji na tatu ni maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa taarifa, utoaji wa taarifa unaleta uwazi na panapokuwa na uwazi unazaa uwajibikaji. Mtumishi yeyote wa umma au mtumishi yoyote wa sekta binafsi, sekta ambayo ina maslahi ya umma pale atakapoona kwamba taarifa zake zinatakiwa ziwe wazi ataongeza sana uwajibikaji, pia kwa kuongeza uwajibikaji dhana nzima ya kuwaletea Watanzania maendeleo itakamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naona relevance kubwa sana ya Muswada huu kufika wakati huu katika Bunge lako Tukufu na niwaombe Waheshimiwa Wabunge tukiulewa Muswada huu katika muktadha huo, kwa hakika tutawatendea haki Watanzania kwa kupitisha kwa kuunga mkono Muswada huu kwa asilimia mia moja. Kwa sababu kwanza unaenda kuleta uwazi, unaenda kuongeza uwajibikaji kwa taasisi zote za umma na binafsi zinazogusa maslahi ya umma, lakini pia kwa kuleta uwajibikaji tunakwenda kupata maendeleo zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeshangaa sana katika Serikali hii ya Awamu ya Tano ambapo tunataka kupiga hatua kubwa ya maendeleo kama tungeweza kwenda bila kupata sheria hii. Hata hivyo, nina mapendekezo ya maboresho kwenye Muswada. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza la mapendekezo linajikita kwenye taarifa zilizozuiliwa Ibara ya 6(6) ya Muswada huu. Ibara ya 6(6) inasomeka kama ifuatavyo:-
“Mtu yeyote anayetoa taarifa iliyozuiliwa kinyume na mamlaka ya umma, kinyume cha sheria hii anatenda kosa na endapo atatiwa hatiani atatumikia kifungo kisichopungua miaka 15 na kisichozidi miaka 20.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia makosa yaliyoainishwa katika Ibara hii yanatofautiana sana. Naona kwamba yale makosa ambayo yana maslahi makubwa kwa usalama wa nchi yetu, yanagusa moja kwa moja eneo la usalama, makosa haya yasiwe na adhabu mbadala isipokuwa adhabu ambayo imependekezwa katika Ibara hiyo. Makosa ambayo hayana athari kubwa kwa usalama wa Taifa letu basi yatafutiwe adhabu mbadala au adhabu ipunguzwe. Kwa hiyo, napendekeza kwamba haya makosa yawekwe kwenye mafungu mawili kulingana na uzito wake na kutegemeana na athari ambayo itakuwa kwa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nahofia kupendekeza adhabu hii ipunguzwe kwenye Ibara ya 6(6) tena kwa sababu kuna tabia ya watu waovu wanaolitakia Taifa letu balaa wanafanya makosa haya na wakishahukumiwa Mahakamani kulipa faini ya pesa wanakwenda mtaani wanachangishana pesa wanaenda kulipa faini. Tusiruhusu jambo hili kwa jambo ambalo lina maslahi mapana kwa Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili ambayo napenda nichangie ni wajibu wa kutangaza taarifa, Ibara ya 9. Ibara ya 9 inasema kila mmiliki wa taarifa siyo zaidi ya miezi 36 baada ya kuanza kutumika kwa sheria hii, baada ya kuombwa atatoa kwenye gazeti, tovuti au gazeti linalopatikana kwa wingi likiwa na maelezo hayo mengi hapo chini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kufikia maendeleo kama nilivyosema katika utangulizi wangu tunahitaji Serikali yenye uwazi na uwajibikaji. Palipo na uwazi na uwajibikaji ndipo tutapata maendeleo. Iwapo tutaacha kipindi hiki cha miezi 36 maana yake miaka mitatu kutoka sasa ni muda mrefu sana. Tutashindwa kujipima katika kipindi hiki cha miaka mitano. Ushauri wangu eneo hilo nalo liboreshwe kwa kuweka kipindi kifupi inavyowezekana ili kukidhi haja ya kupata Serikali yenye uwazi, uwajibikaji na hatimaye kufikia malengo ya maendeleo tuliyojipangia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la mwisho ambalo niliona nichangie ni Ibara ya 11(1) na Ibara zote zinazoendelea Ibara ya 12, 13, 14 mpaka 16. Ibara hii ya 11(1) inaeleza kuhusu notice pale ambapo ombi la kupewa taarifa linapowasilishwa. Ipo haja, tumeona na tunaishi katika jamii hii ya Kitanzania tumeona mara nyingi unakwenda katika ofisi zetu za Halmashauri, unakwenda kwenye Wizara na unakwenda ofisi za Kijiji kuomba taarifa kwa barua, lakini unazungushwa miezi mitatu, minne. Kipindi cha siku 30 kilichopendekezwa hapa ni kirefu sana kwa taarifa ambazo tayari zipo mikononi mwa wamiliki wa taarifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo yangu yangu Ibara hii ya 11 mpaka Ibara ya 16 zifanyiwe maboresho ili kuakisi haja nzima ya kupata taarifa kwa muda mfupi inavyowezekana. Naamini nikileta barua katika Halmashauri ya Wilaya, nataka taarifa ya maendeleo ya mradi „A‟ haitakiwi ichukue zaidi ya siku mbili kunitaarifu kwamba barua hiyo wameipokea na sitegemei ichukue zaidi ya siku saba kunipa hizo taarifa. Zipo tayari good practices katika Serikali yetu. TAMISEMI nimeona wana service charter, ile service charter inaweza ikawa model kwa Wizara, lakini pia inaweza ikawa model kwa maeneo mengine yote ambayo yanatakiwa kutoa taarifa. Imeelezwa vizuri ni lini unataarifiwa kwamba barua yako ya kuomba taarifa imefika na ni lini unapewa taarifa. Kwa hiyo, kila kitu kimeelezwa hivi, hata anayeomba taarifa anapolalamika angalau anakuwa na kitendea kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anatunga Kanuni za utekelezaji wa sheria hii basi aangalie hicho kipengele ambacho kitaboresha na kitaharakisha utoaji wa taarifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana lakini niweke tu tahadhari kwamba watu wasitudanganye na wasiwadanganye Watanzania kwamba sheria hii inakwenda kuondoa haki za Watanzania na kwenda kugandamiza haki za Watanzania. Ni makosa makubwa sana kuoanisha haki ya kupata taarifa na haki ya habari ni vitu viwili tofauti japo vinafanana. Haki ya kupata habari siyo synonym ya haki ya kupata taarifa. Ni vema wakajikita kwenye historia ya nchi mbalimbali wakajua nchi zinavyo-practice hii sheria na sisi namna ambavyo tuta-practice ni vizuri tukashauriana namna nzuri ya kufanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.