MHE. ANTHONY P. MAVUNDE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Kwa mujibu wa kifungu cha 64(2)(c) cha Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2011 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2016, sambamba na Tangazo la Serikali Na.30 la mwaka 2013 inazitaka taasisi nunuzi (procuring entity) zitenge asilimia 30 ya zabuni zake kwa mwaka kwa ajili ya vikundi vya akina mama, vijana na watu wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kumekuwa na ulegelege katika utekelezaji wa takwa hili ambalo linawanyima fursa vikundi hivi muhimu, je, ni mkakati gani sasa ambao Serikali unauweka kuhakikisha kwamba takwa hili la kisheria linazingatiwa ili kuweza kuwapa fursa hizi vikundi vya akina mama, vijana na watu wenye ulemavu? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mavunde, Mbunge wetu wa Dodoma Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli tumeweka sheria inayowezesha kila taasisi kutenga kiwango cha fedha kwa ajili ya kukopesha makundi kama alivyoyataja Mheshimiwa Mbunge lakini tunatambua zipo changamoto kwa baadhi ya taasisi kutotekeleza sheria hiyo huku wakitakiwa kutekeleza sheria hiyo. Serikali inaendelea kusisitiza na kuhamasisha taasisi zetu kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na hasa kwenye eneo hili la mikopo kwa sababu tunahitaji sasa Watanzania wanaotaka kujishughulisha na shughuli mbalimbali za kiuchumi au masuala ya kijamii wapate uwezesho wa kumudu kutekeleza wajibu huo. Maelekezo ambayo tunayo kwa sasa ni kuhakikisha kwamba kila mtumishi wa umma aliyepo kwenye kitengo ambacho kimetakiwa kutoa mikopo hii, lazima afanye hivyo kwa sababu tayari pia Serikali huwa inatenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali na wale wote ambao wanatakiwa kupewa mikopo hiyo ikiwemo wanawake, vijana na walemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, msisitizo wa Serikali kwa kila mmoja kujishughulisha na masuala ya kiuchumi ni msisitizo ambao unatokana na malengo yaliyowekwa na utekelezaji ambao upo kwa taasisi hizo. Kwa hiyo, bado nitoe wito kila taasisi ambayo imetenga fedha hizo na sheria inamtaka kutoa mikopo hiyo bado waendelee kutoa mikopo kwa wahitaji ili kila mkopaji aweze kupata fedha hizo na aweze kuendesha miradi yake kadiri alivyojipanga.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nachotaka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kusisitiza kuhakikisha kwamba kila mmoja anatekeleza sheria ili wanufaika waweze kunufaika kwa utaratibu ambao tumejiwekea. Ahsante sana. (Makofi)