Answers to Primary Questions by Hon. Anthony Peter Mavunde (236 total)
MHE. FELISTER A. BURA (K.n.y. AMINA N. MAKILAGI) aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kutumia rasilimali watu katika kukuza uchumi wa Taifa, hasa ikizingatiwa kuwa rasilimali hiyo ni muhimu sana katika kukuza uchumi wa Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassoro Makilagi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini, matumizi ya rasilimali watu ni muhimu sana. Ili kuhakikisha kuwa rasilimali watu inawezeshwa na kutumika kukuza uchumi wa Taifa, Serikali imeweka mikakati ifuatayo:-
(i) Serikali imeandaa mkakati wa Kitaifa wa kukuza ujuzi nchini ambao umelenga kutoa mafunzo ya vitendo yatakayofanyika maeneo ya kazi (apprenticeship and internship programs). Aidha, ili kuwapa vijana wengi fursa za mafunzo, Serikali imeanzisha program maaalum ya kutambua ujuzi uliopatikana kupitia mfumo usio rasmi na kuurasimisha kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wale watakaobainika kuhitaji na kuwapa vyeti. Utaratibu huu unawapa fursa vijana wetu na kuendelea na mfumo rasmi wa mafunzo na pia kutambulika na waajiri au watoa kazi na hivyo kupata nafasi kuchangia katika kujenga uchumi wa Taifa.
(ii) Kuhamasisha vijana wenye utaalam mbalimbali kushiriki katika shughuli za kiuchumi kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira hususan kilimo na biashara. Aidha, Serikali itajikita zaidi kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji kwenye viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kufikia lengo la asilimia 40 ya nguvu kazi nchini kuwa katika Sekta ya Viwanda ifikapo mwaka 2020, kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali kupitia sekta na taasisi zake mbalimbali inaendelea kuhakikisha rasilimali watu iliyopo nchini inatumika sawasawa ili iweze kuchangia uchumi wa nchi.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Tatizo la ajira nchini kwa wahitimu wa vyuo vya kati na juu ni kubwa sana:-
(a) Je, ni wahitimu wangapi hawana kazi hadi sasa kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu nchini?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa ajira kwa wahitimu au kuwawezesha kujiajiri hasa vijana?
NAIBU WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU – SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WALEMAVU - (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali namba mbili la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2014 vijana wahitimu wa elimu ya juu wasio na ajira wanakadiriwa kuwa 27,614 ambapo kati yao 14,271 ni wanawake na 13,343 ni wanaume. Hata hivyo, Serikali inaendelea na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana wahitimu wa Elimu ya Juu kwa kuweka mazingira wezeshi ya kuajiriwa au kujiari.
(b) Mheshimiwa Spika, jukumu kubwa la Serikali ni kusimamia Sera na Sheria mbalimbali ambazo zinaweka mazingira bora ya uwekezaji katika sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira ikiwemo kilimo na biashara), pia kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili viweze kuajiri sehemu kubwa ya nguvu kazi nchini na wengine kujiajiri wenyewe.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na tatizo la ajira kwa wahitimu wa elimu ya juu, Serikali inatekeleza mipango ifuatayo:-
Kwanza, kuimarisha Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA) ambao una jukumu la kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri wa ndani na nje ya nchi.
Pili, kuandaa Mkakati wa Kukuza Ujuzi Nchini ambao utaanza kutekelezwa mwaka ujao wa fedha wa 2016/2017, Mkakati huu umejikita zaidi katika kuwezesha mafunzo ya vitendo yatakayofanyika maeneo ya kazi ili wawe na ujuzi unaohitajika katika maeneo ya kazi.
Tatu, kuendelea kusimamia utekelezaji wa Program ya Taifa ya Kukuza Ajira kwa Vijana, ambayo imelenga kuwajengea uwezo vijana kwa njia ya mafunzo ya stadi za ujasiriamali, stadi za maisha na stadi za kazi.
MHE. JOHN W. HECHE aliuliza:-
Wakati wa kampeni ya Urais mwaka 2015, Mheshimiwa Rais John Pombe
Magufuli aliwaahidi wananchi wa Mji wa Nyamwaga kuwa ataanzisha
mchakato wa kuwalipa wazee pensheni zao kwa wakati:-
Je, mpango huo muhimu utatekelezwa lini?
MHE. ANTONY P. MAVUNDE - NAIBU WAZIRI (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA,
VIJANA NA WALEMAVU) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali
namba 77 la Mheshimiwa John Wegesa Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini, kama
ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Rais ana dhamira ya dhati ya kuhakikisha Wazee wote nchini wanapata pensheni ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa kwenye mikutano ya kampeni Serikali imejipanga kutekeleza mambo yafuatayo:-
(i) Kuainisha idadi ya wazee nchini watakaohusishwa katika mpango wa pensheni kwa wazee nchi nzima;
(ii) Kuainisha viwango vya pensheni; na
(iii) Kuandaa utaratibu utakaotumika kulipa pensheni pamoja na taratibu za kiutawala na kupokea maoni ya wadau kuhusu mpango wa pensheni kwa wazee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 Serikali ilitenga kiasi cha shilingi milioni 130 kwa ajili ya maandalizi ya mpango huo.
MHE. ESTHER M. MMASI aliuliza:-
Serikali kupitia taasisi za umma zimeweza kufanya tafiti nzuri kujua uhalisia wa suala la ajira kwa vijana waliohitimu vyuo vikuu:-
Je, ni kwa namna gani Serikali inaweza kutumia majibu ya tafiti hizo kupitia convocation office ndani ya taasisi ya umma katika kutatua changamoto za ajira katika nchi yetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Michael Mmasi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara imekuwa ikifanya au kutumia tafiti zilizokwisha kufanywa na taasisi mbalimbali ili kushughulikia changamoto za ajira, upangaji wa mipango na utatuzi wa changamoto za ajira kwa vijana wa vyuo vikuu na wengineo.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa na tafiti hizo zinasaidia Serikali kupanga na kutekeleza mikakati ifuatayo:-
(i) Programu ya Kukuza Ujuzi inayolenga kuwapatia wafanyakazi na vijana maarifa na stadi za kazi ili waweze kuajirika na kujiajiri.
(ii) Mfuko wa wa Maendeleo ya Vijana unaolenga kuwapatia vijana mafunzo na mikopo nafuu ya kujiajiri. Mfuko unawahamasisha wahitimu kuanzisha vikundi vya uzalishaji na makampuni ili wajiajiri na kuajiri wengine.
(iii) Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambalo linadhamini wahitimu wachanga kupata mikopo nafuu katika Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB) kwa njia ya ushindani ili waweze kufanya shughuli za kujiajiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwezeshaji kwa vijana na wahitimu wa vyuo vikuu ili kutatua changamoto za ajira katika nchi yetu kwa kushirikiana na wadau husika kama waajiri, taasisi za elimu, taasisi za kifedha na vijana.
MHE. SAUMU H. SAKALA aliuliza:-
Baadhi ya Waajiri ikiwemo Mashirika binafsi wamekuwa wakiwanyima haki ya msingi wafanyakazi wao kujiunga katika vyama mbalimbali vya wafanyakazi nchini kwa kutishia au kuwatafutia sababu ya kuwafukuza kazi pindi wanapojiunga na vyama hivyo:-
a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka Sheria itakayowabana waajiri wenye tabia ya kuwatishia au kuwafukuza kazi pale wanapojiunga na Vyama vya Wafanyakazi nchini?
b) Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa waajiri na kuwalazimisha kubandika Sheria hii ofisini kwa wafanyakazi ili wajue haki zao?
NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saumu Heri Sakala, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, tayari ipo Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya Mwaka 2004 ambayo kupitia Kifungu cha 9 (1), kinaeleza wazi kuwa wafanyakazi wanayo haki ya kuanzisha au kujiunga na Vyama vya Wafanyakazi pamoja na kushiriki kwenye shughuli halali za Vyama vya Wafanyakazi. Aidha, Kifungu cha 9 (3) cha Sheria hiyo, kinaeleza kuwa ni marufuku kwa mtu yoyote kumbagua mfanyakazi kwa sababu tu mfanyakazi huyo ni mwanachama wa chama cha wafanyakazi au anashiriki katika shughuli halali za chama.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi yangu itaendelea kuimarisha huduma za ukaguzi na usimamizi wa sheria za kazi, pamoja na kutoa elimu kuhusu sheria za kazi ili kuongeza uelewa wa waajiri, wafanyakazi na umma kwa ujumla ili kuhakikisha kuwa wafanyakazi wanatumia haki na uhuru huo ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria hailazimishi mwajiri kubandika Sheria ofisini ili wafanyakazi wasome haki zao. Hata hivyo, Kifungu namba 16 cha Sheria hii kinawataka waajiri kubandika haki za wafanyakazi sehemu za wazi ili wazijue haki zao.
MHE. OMARI M. KIGUA aliuliza:-
Ili kuleta ufanisi wa kimaendeleo na kusogeza karibu huduma za kijamii kwa wananchi, Serikali hugawa Wilaya na Majimbo kwa kuangalia ukubwa wa eneo, idadi ya watu kwenye eneo husika, pamoja na shughuli za kiuchumi na Wilaya ya Kilindi ni miongoni mwa Wilaya chache zinazozalisha mazao ya kilimo na biashara kwa eneo kubwa:-
Je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kuligawa Jimbo hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 6,125?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati tukijibu hoja za Waheshimiwa Wabunge hapa Bungeni wakati wa Hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu kwa Mwaka 2016/2017 tuliainisha vigezo vilivyotajwa na Mheshimiwa Mbunge kama sehemu ya vigezo vinavyotumiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika kugawa Majimbo ya Uchaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vingine ni pamoja na hali ya jiografia, upatikanaji wa mawasiliano, mgawanyo wa watu, mgawanyo wa wastani wa idadi ya watu na idadi ya Kikatiba ya Wabunge wa Viti Maalum pamoja na uwezo wa Ukumbi wa Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia fursa hii kumshauri Mheshimiwa Kigua, kupitia Mamlaka ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilindi kuwasilisha maombi yake kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kupitia vikao husika ili wakati muafaka ulikifika yaweze kufanyiwa kazi kwa kadiri itakavyoonekana inafaa.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO (K.n.y. KHATIB SAID HAJI) aliuliza:-
Kumekuwa na mfululizo wa migomo, misuguano na migongano ya mara kwa mara kwa wafanyakazi wa viwandani na Kampuni binafsi zinazotokana na malalamiko ya mishahara na maslahi ya wafanyakazi:-
Je, ni mfumo upi na viwango gani vilivyowekwa kisheria wanavyotakiwa kulipwa wafanyakazi wa viwanda na Kampuni binafsi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khatibu Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo unaotumika katika kupanga viwango vya chini vya mshahara unasimamiwa na taratibu zilizoainishwa katika Sheria Na. 7 ya Taasisi za Kazi ya mwaka 2004 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine, sheria imetoa madaraka kwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya kazi, kuunda Bodi ya kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi. Bodi hii inaundwa na Wajumbe 17 ikiwa na Wawakilishi wa Wafanyakazi, Waajiri na Serikali. Majukumu ya Bodi hii ni kupanga kima cha chini cha mshahara katika sekta binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kiwango cha chini cha mshahara kilichopangwa na kinachoendelea kutumika hadi sasa katika Sekta ya Viwanda ni shilingi 100,000/= kwa mwezi na viwango vingine vya mshahara katika sekta 12 vimetajwa kwa GN.196 ya mwaka 2013.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI (K.n.y. MHE. JAPHET N. HASUNGA) aliuliza:-
Sheria ya Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 inawataka wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi vya kisekta; walimu na wafanyakazi wengine wamekuwa wakiingizwa kwenye vyama hivyo bila ya wao wenyewe kukubali.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaruhusu wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi wanavyotaka kwa hiari badala ya kuwalazimisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya mwaka 2004 imeeleza bayana kuwa wafanyakazi wanayo haki ya kuanzisha au kujiunga na vyama vya wafanyakazi wanavyovipenda wenyewe pasipo kumlazimisha mtu yeyote. Hivyo ni makosa kwa mtu yeyote, awe ni mwajiri au chama cha wafanyakazi, kumlazimisha mwanachama kujiunga na chama pasipo ridhaa yake. Taratibu ni kwamba mfanyakazi anatakiwa kujaza fomu namba TFN 6 ili kutoa idhini yake kujiunga na chama anachokipenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie tena kutoa wito kwa waajiri wa vyama vya wafanyakazi kuzingatia matakwa ya sheria kwa kutowalazimisha wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi pasipo ridhaa yao. Hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya waajiri na vyama vya wafanyakazi vitakavyokiuka matakwa ya sheria hii ili kuruhusu wafanyakazi kuunda vyama vya wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi. Hata hivyo Serikali inatoa onyo kwa waajiri wanaokiuka sheria za kazi kwa kuwalazimisha wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi wasivyovitaka. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa waajiri wanaokiuka sheria za kazi.
MHE. SAUMU H. SAKALA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza ahadi yake ya kuanza kuwalipa wazee pensheni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saumu Heri Sakala, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaanza kutekeleza ahadi yake ya kuwalipa pensheni wazee mara baada ya maandalizi ya utekelezaji wake kukamilika. Maandalizi hayo ni pamoja na kuunda vyombo vya usimamizi wa mpango huo katika ngazi zote, kuweka mfumo na miundombinu muhimu kwa ajili ya kutekeleza mpango huo, kufanya utambuzi na usajili wa walengwa, kutoa elimu kwa umma na kujenga uwezo wa watendaji wa mpango. Vilevile maandalizi haya yatahusu maandalizi ya ziada kama vile rasilimali fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa mpango huu ndiyo maana inalishughulikia suala hili kwa umakini mkubwa ili tu mara utekelezaji wake utakapoanza uwe endelevu na wenye manufaa kwa wazee nchini.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI (K.n.y MHE. SALOME W. MAKAMBA) aliuliza:-
Wafanyakazi wa migodi ya uchimbaji wa madini hufukuzwa kazi kiholela bila kulipwa fidia stahiki kutokana na ulemavu na magonjwa yanayosababishwa na vitendea kazi hatarishi wakati wakiwa kazini.
(a) Je, Serikali iko tayari kuzuia kuingizwa nchini vitendea kazi hatarishi na kufunga migodi ambayo ina wahanga wengi na ulemavu na magonjwa yatokanayo na shughuli za uchimbaji madini?
(b) Je, ni lini Serikali itaanza kutumia Sheria ya Fidia Na. 20 ya mwaka 2008 ili wafanyakazi wa migodini walipwe fidia stahiki wanapopata ulemavu au magonjwa wanapokuwa kazini badala ya Sheria ya Fidia ya mwaka 2002? na
(c) Je, Serikali inatoa tamko gani kwa waajiri wanaowatelekeza wafanyakazi waliopata ulemavu wakiwa kazini na kukataa kuendelea kulipa gharama za matibabu yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salome Makamba, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia taasisi zake na sheria mbalimbali za nchi inao utaratibu madhubuti wa kudhibiti uingizwaji wa bidhaa zisizo na ubora pamoja na vitendea kazi hatarishi kwa afya za wafanyakazi mahali pa kazi ikiwemo migodini.
Aidha, Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, imeipa mamlaka Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi kukagua vitendea kazi vinavyotumika mahali pa kazi ikiwa ni pamoja na migodi na kupima afya za wafanyakazi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Namba 20 ya mwaka 2008 ilitungwa ili kulipa fidia kwa wafanyakazi wanaoumia au kupata madhara au kufariki wakiwa kazini, ikiwa ni pamoja na wafanyakazi wa migodini wanaopata ajali.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria namba 20 itaanza kutoa rasmi fidia kwa wafanyakazi tarehe 1/7/2016. Kipindi hiki waajiri wote waendelee kutumia Sheria Na. 263 kuhakikisha wafanyakazi wanahudumiwa na kulipwa wawapo kazini. Aidha, Serikali inatoa onyo kwa waajiri ambao hawataki kutenda haki ya kuwalipa fidia kwa mujibu wa sheria.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:-
Nchi yetu kwa sasa ina wataalam wengi katika sekta mbalimbali kama vile uhasibu, uchumi, uongozi, menejimenti, udaktari, utawala na kadhalika.
Je, Serikali haioni haja sasa kwa ajira zote kwenye NGOs na taasisi binafsi nchini kupewa Watanzania na kuacha mpango uliopo sasa wa kuruhusu wageni kuajiriwa hasa kwenye nafasi za juu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wageni wanaajiriwa nchini kwa kuzingatia Sheria ya Ajira ya Wageni Namba Moja ya mwaka 2015. Kabla ya kutoa kibali cha kazi kwa mgeni kamishna wa Kazi anatakiwa kujiridhisha kuwa nafasi anayoombewa mgeni ni adimu na mwajiri amefanya juhudi za kutafuta Mtanzania wa kuajiriwa katika nafasi hiyo. Aidha, sheria inamtaka mwajiri kutengeneza mpango wa kurithisha ujuzi na kuhakikisha mgeni anayeombewa kibali anarithisha utaalamu huo kwa Mtanzania ili muda wa kibali utakapokwisha Mtanzania huyo aweze kuchukua nafasi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa utaratibu wa utoaji vibali vya ajira kwa wageni unazingatiwa ipasavyo kwa kutumia sheria na miongozo iliyopo. Kwa hali hiyo, Serikali itaendelea kuona haki inatendeka kwa mujibu wa sheria ili Watanzania waendelee kupata ajira katika NGOs na taasisi binafsi.
MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:-
Mfuko wa PSPF unachelewesha sana mafao ya wastaafu, watumishi wengi waliostaafu mwaka wa fedha 2015/2016 hawajalipwa mafao yao, hususan walimu wa Korogwe Mjini:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuondoa changamoto hii ambayo imekuwa kero kwa wastaafu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha changamoto ya kulipa wafanyakazi mafao inaondoka, Serikali katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Agosti, 2016 imefanikisha mkakati wa kuweza kulipa kiasi cha shilingi bilioni 511.8 ikiwa ni malimbikizo ya michango ya mwajiri. Pia katika kipindi hicho Serikali imelipa jumla ya shilingi bilioni 83 kama malipo ya deni la kabla ya mwaka 1999 (Pre 1999 Liability). Kwa hali hiyo, Serikali imeendelea kulipa malimbikizo ya madai ya wastaafu na mafao mengine yatolewayo na mfuko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha katika kipindi cha mwezi Januari hadi Julai, 2016 mfuko umelipa mafao ya pensheni ya mwezi kwa kiasi cha shilingi bilioni 117 na kwa sasa mfuko unaendelea na kulipa malimbikizo ya mafao ya mkupuo kwa wastaafu wapya na mafao mengineyo.
MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:-
Masuala ya watu wenye ulemavu kwa kiasi kikubwa yanazungumzwa na kushughulikiwa katika maeneo ya mijini na kusahau maeneo ya pembezoni ambapo kuna watu wa jamii hiyo.
Je, Serikali ina mpango gani kuhusu watu wenye ulemavu waishio vijijini ambapo matatizo yao ni mengi na makubwa kulingana na jamii inayowazunguka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Saleh Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu waishio vijijini. Ili kuwa na mipango mahsusi ya kushughulikia kundi la watu wenye ulemavu vijijini Serikali imefanya ugatuaji wa shughuli zinazohusu watu wenye ulemavu kwenda katika Serikali za Mitaa. Serikali inaendelea kuzijengea uwezo wa Halmashauri na watoa huduma wengine ili kutatua kero zinazowakabili watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Namba 9 mwaka 2010 imeelekeza kuanzisha Kamati za Baraza la Huduma na Ushauri kwa watu wenye ulemavu kuanzia ngazi ya Kijiji, Mtaa hadi ngazi ya Taifa ambazo zitasaidia utoaji huduma kwa watu wenye ulemavu. Katika kusimamia utekelezaji wa matakwa ya sheria hii Serikali imewaagiza Makatibu Tawala wote wa Mikoa kusimamia uanzishwaji wa Kamati za Mikoa, Halmashauri Kata na Vijiji, kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu maana ndiko watu wenye ulemavu wengi waliko.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Moja ya tatizo kubwa nchini ni ukosefu wa ajira kwa vijana. Serikali imeweka vipaumbele vya kuanzisha na kukuza viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa kwa lengo la kuajiri vijana wengi wa Kitanzania:-
Je, Serikali ina mikakati ipi kuhakikisha azma hiyo njema inafikiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ukuzaji ajira ni mtambuka na linahitaji juhudi za wadau mbalimbali katika kukabiliana nalo. Serikali kupitia Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) imekuwa mstari wa mbele kuendeleza sekta ya viwanda vidogo vidogo nchini ili kuajiri na kujiajiri kwa vijana wengi. Shirika hili limekuwa likikuza utaalam katika sekta mbalimbali pamoja na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imepanga yafuatayo kuhakikisha viwanda vidogo vidogo vinatoa ajira kwa vijana:-
(i) Kuanzisha na kukuza viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kwa lengo la kuwaajiri vijana wengi kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021). Mpango huu utawezesha uanzishwaji wa viwanda vidogo kama vile viwanda vya kuunganisha vifaa na bidhaa za teknolojia ya habari na mawasiliano na vya kielektroniki, viwanda vya usindikaji wa mazao ya kilimo na mifugo, viwanda vya kuongeza thamani ya madini na viwanda vya kutengeneza bidhaa za ujenzi.
(ii) Kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Ujuzi katika sekta za kipaumbele ambazo ni chachu ya ukuaji wa uchumi na ajira. Sekta hizo ni kilimo na biashara, nishati, utalii na huduma za ukarimu, usafiri na usafirishaji, huduma za ujenzi na TEHAMA.
(iii) Kuimarisha Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambalo linadhamini wahitimu wachanga kupata mikopo nafuu katika benki kwa njia ya ushindani ili waweze kufanya shughuli za kujiajiri ikiwemo kuanzisha viwanda vidogo vidogo na makampuni.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE (K.n.y. MHE. GODBLESS J. LEMA) aliuliza:-
Hivi karibuni Mheshimiwa Rais ameamuru Wakuu wa Mikoa kuwakamata na kuwaweka mahabusu vijana watakaokutwa wanacheza pool table na draft mitaani kama ishara ya mizaha katika nguvukazi:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza ajira ili vijana waweze kuajiriwa na kuepuka adhabu hiyo itakayotekelezwa na Wakuu wa Mikoa?
(b) Ni dhahiri kwamba Taifa letu linapita katika adhabu kubwa ya umaskini. Je, Serikali haioni kwamba Taifa linaweza kuingia katika vurugu kati ya vijana wasiokuwa na ajira na Jeshi la Polisi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Lema kuwa kazi si adhabu na nia ya Serikali ni kuhakikisha kila mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi na hasa za uzalishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuwezesha vijana wengi kufanya kazi Serikali inatekeleza mipango ifuatayo:-
(i) Kuendelea kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira hususan kilimo-biashara. Aidha, katika hili, Serikali itajikita zaidi kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji kwenye viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kufikia lengo la asilimia 40 ya nguvukazi nchini kuwa katika sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2020 kupitia katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021)
(ii) Kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Ujuzi Nchini ambao umelenga kutoa mafunzo ya vitendo maeneo ya kazi (apprenticeship na internship programs). Pia kutambua na kurasimisha ujuzi uliopatikana kupitia mfumo usio rasmi pamoja na kutoa mafunzo ya muda mfupi ya ujuzi wa kujiajiri na stadi za kazi na ujasiriamali.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha hakuna vurugu kati ya vijana wasio na ajira na makundi mbalimbali, Serikali inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao umejikita zaidi katika kukuza viwanda vidogo na vya kati ili kukuza ajira na kuondoa umaskini. Lengo la Serikali ni kuweka msisitizo wa watu kufanya kazi hususan vijana ili wachangie katika maendeleo ya nchi. Uzoefu umeonesha kwamba Taifa la wachapakazi lina utulivu na hivyo Serikali haitegemei vurugu kutoka kwa vijana wanaochapa kazi.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE (K.n.y MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA) aliuliza:-
Mpango wa NSSF kutoa mkopo kwa bei nafuu kwa Vyama vya Ushirika ili navyo viweze kutoa mikopo kwa bei nafuu kwa wananchi wa Karagwe ulikuwa mzuri lakini umekabiliwa na changamoto na kero kubwa kwa wananchi waliotozwa sh. 280,000/= kama kigezo cha kupata mikopo hiyo, lakini mpaka sasa wananchi hawajapata mikopo hiyo na Serikai haijatoa maelekezo yoyote juu ya hali hiyo:-
Je, ni nini msimamo wa Serikali kuhusiana na jambo hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mbunge wa Karagwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lilianzisha mpango wa kuongeza idadi ya wanachama kutoka sekta isiyo rasmi hasa wakulima ili kuhakikisha wanajiunga na Hifadhi za Jamii. NSSF ilifanya uhamasishaji na wakulima ikiwa ni pamoja na Karagwe wakajiunga na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa hiari na kutakiwa kuchangia kiasi kisichopungua sh. 20,000 kila mwezi na kuweza kupata mafao yanayotolewa na shirika kama vile matibabu, uzazi na hata pensheni ya uzee. Aidha, wakulima walihamasika na kujinga na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kuendelea kuchangia kwenye Mfuko hadi kufikisha viwango tofauti kuanzia sh. 120,000 hadi 280,000 na kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika NSSF ilianzisha utaratibu wa kutoa mikopo kwa wanachama wake kama njia mojawapo ya kuwahamasisha wanachama kujiunga na NSSF. Masharti ya kupata mkopo huo ni pamoja na wanachama kuchangia kuanzia miezi sita na kuendelea, kuanzisha SACCOS chini ya Vyama vya Ushirika vilivyosajiliwa na mkopo kutolewa kwa wanachama wa NSSF, Chama cha Ushirika kiwe kimefanyiwa ukaguzi wa hesabu zake na COASCO, uthibitisho wa Mrajisi kuhusu ukomo wa madeni na mkopo uridhiwe na Bodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya Vyama vya Ushirika ambavyo vilitimiza masharti haya na kupewa mikopo ni Nkwenda Rural Primary Cooperative Society (RPCS), Kakanja (RPCS), Kikakanya SACCOS, Karongo Agriculture Marketing Cooperative Society (AMCOs) UVIKASA SACCOS, Nguvumali SACCOS. Kwa wanachama ambao wapo kwenye Vyama vya Ushirika ambavyo vilishindwa kutimiza masharti, hawakupewa mikopo, lakini nafasi bado ipo wakitimiza masharti wataendelea kupewa mikopo.
MHE. KISWAGA B. DESTERY aliuliza:-
Wazee wa nchi hii walilitumikia Taifa na kuchangia Pato la Taifa:-
Je, ni lini Serikali itaanza kuwapatia kiinua mgongo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kiswaga Boniventura Destery, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya mwaka 2004, kiinua mgongo ni malipo yanayolipwa na mwajiri kama mkono wa ahsante kwa mfanyakazi wake baada ya kumaliza mkataba wa kazi. Hata hivyo, katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 na kuwalinda wazee wa nchi hii na umasikini wa kipato, Serikali inaandaa mpango wa pensheni kwa wazee nchini. Aidha, hadi sasa Serikali imetekeleza mambo yafuatayo:-
(i) Kuainisha idadi ya wazee wote nchini;
(ii) Kuainisha viwango vya pensheni;
(iii) Kuandaa utaratibu utakaotumika kulipa pensheni;
(iv) Kuandaa taratibu za kiutawala za kusimamia utoaji wa pensheni kwa wazee; na
(v) Kushirikisha wadau mbalimbali katika kuandaa Mpango wa Pensheni kwa Wazee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itakapojiridhisha kuwa taratibu zote ziko sawa itatoa taarifa ya kuanza kwa malipo.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO (K.n.y. MHE. STEPHEN J. MASELE) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza ahadi ya shilingi milioni 50 kwa kila kijiji na mitaa ili kutatua tatizo la ajira na mitaji kwa vijana na kina mama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali Mheshimiwa Stephen Julius Masele, Mbunge wa Shinyanga Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 13 Juni, 2016 wakati nikijibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum kuhusu lini ahadi ya shilingi milioni 50 kwa kila kijiji itaanza kutekelezwa nilisema kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 59.5 katika bajeti ya mwaka 2016/2017 kwa ajili ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulitaarifu Bunge lako kuwa tayari waraka wa Baraza la Mawaziri utakaoongoza utoaji wa fedha hizo umeshaandaliwa na kujadiliwa katika Kamati ya Makatibu Wakuu (IMTC) hivi sasa waraka huo unasubiri kujadiliwa na Baraza la Mawaziri ili kuweka mfumo utakaoratibu utoaji wa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Hivyo namuomba Mheshimiwa Mbunge asubiri utekelezaji wake mara baada ya Baraza la Mawaziri kuujadili.
MHE. JOHN P. KADUTU aliuliza:-
Kwa miaka mingi kumekuwa na Sheria mbaya za fidia kwa wafanyakazi wapatao ajali:-
Je, ni lini Serikali italeta Muswada wa mabadiliko ya Sheria ya Workmen’s Compensation ili kwenda na wakati kwa vile Sheria iliyopo haiwasaidii waathirika wa ajali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya mwaka 2008, fidia kwa wafanyakazi zilikuwa zikilipwa kwa mujibu wa matakwa ya Sheria ya zamani ya Fidia kwa Wafanyakazi, Sura 263 na Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 na kanuni zake za mwaka 2003. Sheria hizi za fidia kwa wafanyakazi zilitumika kulipa fidia kwa watumishi wote kutoka sekta binafsi na umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, mabadiliko ya Sheria ya Workmen’s Compensation, Sura ya 263 yalifanyika mwaka 2008 ambapo Bunge lilitunga Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi (Workers Compensation Act) Na. 20 ya mwaka 2008 ili kuondoa upungufu kadhaa ulioonekana katika sheria zilizotangulia ikiwa ni pamoja na kiwango kidogo cha fidia kwa mfanyakazi aliyeumia au kupata maradhi akiwa kazini.
Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hii imeanzisha Mfuko wa Fidia ambao unashughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi waliopo katika Sekta ya Umma na Binafsi Tanzania Bara ambao wataumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi wanazofanya kwa mujibu wa mikataba ya ajira zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mfuko huo umeanza kazi rasmi tarehe 1 Julai, 2016 ambapo waajiri katika sekta binafsi wanachangia 1% na Sekta ya Umma 0.5%. Mfuko huu umeanza rasmi kulipa mafao ya fidia kwa wafanyakazi wanaoumia au kupata maradhi wakiwa kazini kuanzia tarehe 1 Julai, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kupitia Mfuko huu, utaratibu wa kupata huduma za fidia umerahisishwa sambamba na mafao kuboreshwa kwa kiwango kikubwa.
MHE. HASSAN E. MASSALA aliuliza:-
Wilaya ya Nachingwea ina ardhi ya kutosha lakini vijana wengi bado wanakabiliwa na tatizo la ajira:-
Je, Serikali inatoa kauli gani kuwasaidia vijana hawa kujikwamua kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli ya Serikali katika kuwasaidia vijana wa Nachingwea kujikwamua kiuchumi ni pamoja na kufanya yafuatayo: Kuwashauri vijana wa Wilaya ya Nachingwea kujiunga katika vikundi vya uzalishaji mali na kubuni miradi mbalimbali ya uchumi katika nyanja za kilimo, ufugaji na viwanda vidogo vidogo vya usindikaji wa mazao ya kilimo. Hii itasaidia kutengeneza nafasi za ajira kwa vijana na kuwakwamua vijana katika lindi ya umaskini wa kipato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha kwamba mpango huu unafanikiwa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira inaendelea kutekeleza mikakati ifuatayo:-
(a) Kuhakikisha Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Nachingwea zinatenga maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za kiuchumi za vijana.
(b) Kusimamia utekelezaji wa utoaji wa mikopo kwa vijana ya 5% ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
(c) Kukopesha vikundi vya vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ili kuchochea upatikanaji wa mitaji ya kuendeshea shughuli za kiuchumi za vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii adhimu kumwomba Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa yeye ni kijana na amekuwa mstari wa mbele katika masuala ya vijana kitaifa na kimataifa, basi tushirikiane kwa pamoja kuwaongoza vijana wa Wilaya ya Nachingwea katika kubuni miradi mbalimbali yenye tija ili kuwakwamua vijana wa Wilaya ya Nachingwea katika suala zima la ukosefu wa ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kauli ya Serikali ni kuendelea kuunga mkono jitihada zitakazofanywa na vijana wa Nachingwea na nchi nzima kwa kusaidia upatikanaji wa mitaji na mikopo kupitia Mifuko ya Uwezeshaji ya Serikali na pia kwa kuwashirikisha wadau wapenda maendeleo ya vijana kuwasaidia vijana kujiinua kiuchumi.
MHE. DKT. ELLY M. MACHA aliuliza:-
Katika miaka ya 60 na 90, Serikali yetu kwa ufadhili wa nchi rafiki kama Norway na Sweden ilijenga vyuo vya ufundi vilivyotoa mafunzo mbalimbali kwa watu wenye ulemavu hapa nchini kama vile Yombo - Dar es Salaam, Singida, Mtapika – Masasi, Masiwani – Tanga, Mbeya, Ruanzari – Tabora na Mwirongo-Mwanza; hivi sasa kati ya vyuo saba ni vyuo viwili tu vya Yombo na Singida ndiyo vinafanya kazi tena kwa kusuasua:-
(a) Je, ni sababu zipi zilizosababisha vyuo hivyo vitano vifungwe wakati kuna mahitaji makubwa ya watu wenye ulemavu kupata mafunzo ya ufundi?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kufungua haraka vyuo hivyo vilivyofungwa ili viendelee kutoa mafunzo ya ufundi kwa watu wenye ulemavu?
(c) Ili kutoa fursa zaidi za mafunzo ya ufundi kwa watu wenye ulemavu, je, Serikali ina mkakati gani wa kujumuisha watu wenye ulemavu kwenye vyuo vyake vya VETA na FDC?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Elly Marco Macha, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu zilizosababisha vyuo hivi kufungwa ni pamoja na uchakavu wa majengo na miundombinu isiyo rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu; upungufu wa watumishi ambapo baadhi yao wameshastaafu na wengine wamefariki.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu nchini wanapata mafunzo siyo tu ya ufundi, bali ya aina nyingine yatakayokidhi mahitaji ya ajira na kuondoa utegemezi kwa watu wenye ulemavu. Aidha, Serikali imewasilisha maombi maalum Hazina, kuomba fedha za maendeleo kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo fedha hizo zitatumika kufanya ukarabati na kuboresha miundombinu ya vyuo mbalimbali nchini. Vilevile, Wizara imewasilisha ikama ya watumishi ili utaratibu wa kuajiri watumishi ufanyike mapema kuziba nafasi zilizo wazi.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa Serikali katika kuwajumuisha watu wenye ulemavu katika Vyuo vya VETA na FDC ni kama ifuatavyo:-
(i) Kuwa na walimu wenye mbinu za kufundisha watu wenye ulemavu. Katika kozi ya ualimu MVTTC ipo moduli inayohusu mbinu za kufundisha watu wenye ulemavu.
(ii) Ukarabati wa miundombinu ya njia za kutembelea na ukarabati wa majengo ili kuwapa fursa watu wenye ulemavu kushiriki katika mafunzo ya ufundi pasipo kikwazo chochote.
(iii) Kuwashirikisha wakufunzi wenye ujuzi wa lugha ya alama kupitia Chuo cha Watu Wenye Ulemavu – Yombo katika kutoa mafunzo ya ufundi kwa watu wenye ulemavu hasa katika kozi fupi fupi.
MHE. STELLA I. ALEX aliuliza:-
Sheria Na. 9 ya mwaka 2010 Sehemu ya Tatu, kifungu cha 8 kinaelezea uanzishwaji wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu na kifungu cha 13 kinazungumzia vyanzo vya fedha.
(a) Je, ni kwa nini baraza hilo halifanyi kazi kama sheria inavyoelekeza?
(b) Sehemu ya Tatu ya kifungu cha 14 cha sheria hiyo kinaeleza juu ya Kamati za Watu Wenye Ulemavu kuanzia ngazi ya kijiji; je, ni kwa nini Kamati hizo mpaka sasa hazijaundwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Ikupa Alex , Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Baraza la Ushauri la Utaifa la Watu wenye Ulemavu limeanzishwa chini ya Kifungu cha 8 cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010. Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu lilizinduliwa rasmi tarehe 1 Novemba, 2014. Baraza hili limekuwa likifanya kazi ipasavyo kwa kujadili masuala ya watu wenye ulemavu kupitia vikao vyake ambapo kwa mara ya mwisho Baraza lilikutana tarehe 14 Januari, 2017.
Aidha, Baraza limekuwa likitekeleza majukumu yake kwa kuishauri Serikali kuhusu uboreshaji wa huduma za watu wenye ulemavu nchini.
(b)Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Watu wenye Ulemavu, kifungu cha 14(2) inaelekeza kuundwa kwa Kamati za Watu wenye Ulemavu katika ngazi ya Kijiji/Mtaa, Kata, Halmashauri hadi Mkoa.
Kutokana na kifungu hiki cha sheria, Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, imekwishatoa agizo kwa Mikoa na Halmashauri zote chini kuunda Kamati za Watu Wenye Ulemavu kwa mujibu wa Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya mwaka 2010.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kuikumbusha Mikoa na Halmashauri ambazo hazijaunda Kamati za Watu Wenye Ulemavu kutekeleza agizo hilo kwani ifahamike kwamba kutokuunda kamati hizo ni ukiukwaji wa matakwa ya kisheria.
MHE. MBAROUK SALIM ALI aliuliza:-
Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizomo katika Bonde la Ufa pamoja na milima mikubwa; kutokana na hali hiyo, upo uwezekano mkubwa wa kutokea kwa matukio kama tetemeko la ardhi mara kwa mara kama ambavyo imeshaanza kutokea na kuleta athari kubwa kwa Taifa.
Je, Serikali ina mkakati gani iliyojiwekea wa kuzuia au kupunguza athari pale inapotokea?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbarouk Salim Ali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa nchi yetu kama zilivyo nchi nyingine imekuwa ikikumbwa na majanga mbalimbali ya asili na yale yanayosababishwa na shughuli za binadamu na kusababisha athari kubwa kwa Taifa letu. Miongoni mwa majanga hayo ni tetemeko la ardhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua uwezekano wa kutokea kwa majanga haya, imejiwekea mikakati mbalimbali ya kuzuia, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali pindi maafa yanapotokea. Aidha, kwa vile maafa ya asili kama vile tetemeko la ardhi ni vigumu kuyatabiri, Serikali kupitia Wakala wa Jiolojia imekuwa ikitoa elimu kwa umma juu ya kukabiliana nayo kwa lengo la kupunguza athari pindi yanapotokea.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia imeandaa Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ambayo imeainisha aina mbalimbali za maafa ikiwemo tetemeko la ardhi pamoja na jukumu la kila mdau katika kushughulikia masuala ya maafa. Vilevile Serikali imeandaa Mwongozo wa Taifa wa kukabiliana na maafa ambao unaelekeza taasisi ongozi wajibu wao katika kukabili maafa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama mkakati kiongozi wa kudumu katika kuhakikisha kwamba suala la Menejimenti ya Maafa inatekelezwa, Serikali imetunga Sheria mpya ya Menejimenti ya Maafa Na. 7 ya mwaka 2015 ambayo pamoja na kusimamia mikakati ya kudumu ya kukabiliana na maafa, imeelekeza kuundwa kwa Kamati za Maafa katika ngazi mbalimbali. Moja kati ya wajibu wa Kamati hizi ni kuhakikisha zinafanya tathmini za kubaini maeneo ambayo yako katika hatari ya kukumbwa na maafa na zinaweka na kupendekeza mikakati ya kukabiliana nayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile suala la maafa ni mtambuka, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo (development partners), pamoja na Chuo Kikuu cha Ardhi, ilifanya tathmini ya kuainisha maeneo yenye viashiria vya uwezekano wa kukabiliwa na majanga mbalimbali (vulnerability assessment) ambayo ilifanyika nchi nzima. Baada ya kuona ukubwa wa tatizo hili, Serikali iliandaa Mpango wa Taifa wa kujiandaa na kukabiliana na maafa hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue fursa hii kusisitiza kuwa kila mmoja wetu achukue tahadhari kwa kusikiliza ushauri unaotolewa na watalaam wetu katika kukabiliana na maafa. Hii ni pamoja na kujenga nyumba katika maeneo yaliyopimwa na salama kwa kuishi, lakini vilevile kwa kuzingatia viwango sahihi vya ujenzi (building codes) kulingana na maeneo tunayojenga.
MHE. HALIMA A. BULEMBO aliuliza:-
Serikali imeanzisha Benki ya Wanawake na Benki ya Kilimo na kwa sasa asilimia kubwa ya Watanzania ni vijana:-
(a) Je, ni lini Serikali itaona umuhimu na kuanzisha Benki ya Vijana?
(b) Je, kwa nini Serikali isianzishe dhamana kwa vijana kukopa?
(c) Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga mfumo madhubuti wa Hifadhi ya Jamii ili vijana waweze kujiwekea akiba ya uzeeni, kupata Bima ya Afya na kupata mikopo ya kuendesha biashara zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a), (b na (c). kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali inalipa umuhimu sana suala la kuanzisha Benki ya Vijana nchini ili kuwawezesha vijana kupata huduma za mikopo yenye masharti nafuu. Kwa hatua za awali, Serikali imeona ni muhimu kwanza kuwajengea vijana tabia ya kuweka akiba na kukopa kwa kuanzisha SACCOS za vijana katika kila Halmashauri ili baadaye ziweze kuwekeza hisa katika Benki itakayoanzishwa. Hatua hii itawezesha Benki ya Vijana itakapoanzishwa kumilikiwa na vijana wenyewe.
(b) Mheshimiwa Spika, suala la Serikali kuanzisha dhamana kwa vijana kwa ajili ya kukopa ni la msingi. Tunakubaliana na ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na tutaufanyia kazi. Aidha, utaratibu utategemea uwezo wa kifedha wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na ubainishaji muhimu wa nani apewe dhamana ya Serikali kwa lengo la kuwanufaisha vijana wote.
(c) Mheshimiwa Spika, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imeweka utaratibu wa mwanachama kujiunga katika mfuko wa uchangiaji wa hiari pamoja na kujiunga na Bima ya Afya. Serikali kwa kushirikiana na mifuko hiyo imekuwa ikiwahamasisha vijana kupitia mafunzo, mikutano na makongamano mbalimbali ili waweze kutumia fursa hiyo kwa ajili ya ustawi wa maisha yao.
MHE.PETER J. SERUKAMBA (K.n.y MHE. ZAINAB A. KATIMBA) aliuliza:-
Mwaka 1993 Serikali ilianzisha Mfuko wa Maendeleo wa Vijana (Youth Development Fund – YDF) ili kutoa mikopo kwa vijana nchini. Mwaka 2013/2014 Serikali ilitenga jumla ya shilingi bilioni 6.1 na mpaka mwezi Machi, 2014 jumla ya shilingi bilioni mbili zilitolewa na Serikali.
(a) Je, Serikali itakuwa tayari kuwaeleza vijana nchi nzima kuwa ni vijana wangapi na wa maeneo gani ambao wamenufaika?
(b) Je, maisha ya vijana waliopewa fedha hizo yamebadilika kwa kiasi gani ili tuweze kupima haja ya mfumo huo na usimamizi wake?
(c) Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa kuangalia upya mfumo uendeshaji wa mfuko huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Katimba, Mbunge wa Viti Maalum na kutoa maelezo mafupi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ni kuwawezesha vijana wote nchini kupata mitaji kwa njia ya mikopo yenye masharti nafuu ili kuanzisha au kuendeleza miradi yao ya uzalishaji mali. Kupitia utaratibu huu, vijana huwezeshwa kujitegemea, kupunguza umaskini wa kipato na kujiajiri wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya vikundi vya vijana 309 kutoka Hamlashauri mbalimbali nchini vilifaidika kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa kupata mikopo yenye jumla ya shilingi 1,867,899,520 ambako mpaka sasa tayari SACCOS za vijana kutoka katika Halmashauri 94 zimepatiwa mkopo huu.
Vijana hawa pia hupatiwa mafunzo ya uendeshaji na usimamizi wa miradi, utunzaji wa fedha na utafutaji masoko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za mkopo zitokanazo na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana umekuwa msingi mzuri katika kuandaa vijana kujiajiri na kuajiri vijana wengine. Kupitia fedha hizo, vikundi vingi vya vijana vimefanikiwa kukuza vipato vyao kwa kushiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi kama vile kilimo, ufugaji, usindikaji wa mazao na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo. Aidha, shughuli hizo zimefanya vijana waachane na utegemezi na badala yake kutumia muda wao mwingi katika uzalishaji na hivyo kuongeza tija katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vikundi vya mfano ambavyo kupitia mfuko huu vimekuwa kielelezo cha dhati katika kubadili mtazamo wa vijana wa kutegemea kuajiriwa hadi kujiajiri wenyewe na kukuza vipato vyao. Vikundi hivyo ni pamoja na THYROID Group kutoka Halmashauri ya Chunya kinachosambaza taa za solar vijijini, MIRANACO Group kinachomiliki duka kubwa la dawa za binadamu kutoka Halmashauri ya Mbozi, Maswa family kinachoshughulika kutengeneza chaki na Meatu Milk kinachotengeneza maziwa kutoka mkoani Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuboresha uendeshaji wa shughuli za Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, Serikali imekuwa ikifanya ufuatiliaji na tathmini mbalimbali mara kwa mara kwa lengo la kuhakikisha ufanisi unakuwepo na kubaini changamoto za kiutendaji zinazojitokeza. Katika mwaka huu wa fedha, Serikali inapitia upya muongozo wa utoaji fedha kupitia mfuko wa maendeleo wa vijana wa mwaka 2013 ili kuwawezesha vijana wengi zaidi kuanzisha viwanda vidogo katika kuendana na sera ya nchi kwenda kwenye uchumi wa viwanda.
MHE. CONSTATINE J. KANYASU (K.n.y JOHN P. KADUTU) Aliuliza:-
Kampuni binafsi ya migodi zimekuwa zikikiuka mikataba ya kazi na pia zikikandamiza na kuwanyanyasa wafanyakazi:-
(a) Je, ni lini Serikali itafanya ukaguzi wa mikataba kwa kampuni zinazofamya kazi migodini?
(b) Je, kwa nini Serikali isiamue kuwaondoa nchini waajiri wakorofi kwa unyanyasaji wanaoufanya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Peter Kadutu, Mbunge wa Ulyankulu, kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, waajiri wote nchini yakiwemo na makampuni ya madini wanapaswa kutekeleza matakwa ya Sheria za Kazi kwa lengo la kulinda haki za wafanyakazi, kupunguza migogoro isiyo ya lazima sehemu za kazi na kuongeza tija na uzalishaji mahala pa kazi. Ofisi yangu imeendelea kutekeleza majukumu yake ya usimamizi wa sheria kwa kufanya kaguzi sehemu za kazi kwa lengo la kuhakikisha kuwa waajiri wanazingatia matakwa ya sheria. Pia elimu ya sheria za kazi zinatolewa kwa waajiri, wafanyakazi na vyama vyao ili kuongeza uelewa wao katika kutekeleza sheria. Aidha, hatua zinachukuliwa kwa kuwafikisha Mahakamani waajiri wanaokiuka masharti ya sheria za kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ukaguzi wa mikataba wa kampuni zinazofanya kazi migodini, Serikali iliunda kikosi kazi ambacho kilishirikisha Maafisa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, NSSF, SSRA, OSHA, Mamlaka ya Mapato Tanzania na Wakala wa Ukaguzi wa Madini. Kikosi hiki kilipewa jukumu la kufanya ukaguzi wa kina kwenye migodi iliyopo kanda ya Ziwa na Kaskazini kwa lengo la kuangalia hali halisi ya utekelezaji wa sheria za kazi, afya na usalama mahali pa kazi, masuala ya hifadhi ya jamii, fedha na kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha Serikali inatambua umuhimu wa uwekezaji katika kukuza fursa za ajira kwa Watanzania na kuchangia kukua kwa uchumi. Serikali itaendelea kusimamia sheria za kazi ili kuhakikisha kuwa waajiri wote nchini wanatimiza wajibu wao na wawekezaji wanapata nafasi ya kuwekezana kuchangia kukua kwa uchumi wa nchi yetu kwa kufuata sheria zilizoko nchini.
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MHE. ESTER M. MMASI) aliuliza:-
Pamoja na juhudi za Serikali katika kulinda ajira za vijana wa Kitanzania, Serikali kupitia Sheria ya Ajira ya Wageni Na. 1 ya mwaka 2015 ilirasimisha vibali vya kuishi na ajira kwa wageni batili wapatao 317 kati ya 779.
Je, ni vigezo gani vilivyotumika katika urasimishaji wa vibali hivyo wakati vijana wengi wa Kitanzania hususan wahitimu wa vyuo vikuu wanahangaika katika kupata ajira ili wafurahie faida ya taaluma zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Mmasi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Kuratibu Ajira kwa Wageni Nchini Na.1 ya mwaka 2015 ilianza kutumika tangu tarehe 15/9/2015. Sheria hii imeweka utaratibu maalum kwa mtu anayetaka kumuajiri raia wa kigeni kuomba kibali cha ajira kwa Kamishna wa Kazi ambaye ndiye mwenye mamlaka pekee ya utoaji wa vibali vya ajira kwa wageni nchini. Kamishna wa Kazi alianza kazi ya kutoa vibali kwa wageni kuanzia tarehe 1/10/2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, vigezo vinavyotumika kurasimisha vibali kwa wageni vimeainishwa katika kifungu cha 6(1) katika Sheria ya Kuratibu Ajira ya Wageni Na.1 ya mwaka 2015 ambapo masharti mbalimbali yameainishwa kwa mwombaji kukidhi kabla ya Kamishna wa Kazi hajatoa vibali. Mojawapo ya sharti ni kumtaka mwajiri atoe ushahidi wa kuridhisha kwamba ametafuta mtaalam huyo kwenye soko la ajira la ndani na hakupata mtu mwenye sifa husika na vilevile azingatie suala la mpango wa urithishaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa itaendelea kusimamia Sheria hii Na.1 ya mwaka 2015 ili kulinda nafasi za ajira za Watanzania wenye fani na taaluma mbalimbali.
MHE. RHODA E. KUNCHELA aliuliza:-
Ipo changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira kwa vijana wa Mkoa wa Katavi. Na hii ni kutokana na miundombinu mibovu inayosababisha wawekezaji kushindwa kuwekeza.
Je, Serikali ina mikakati gani ya kusaidia vijana hao wapate ajira na kuwa na mazingira ya kuwawezesha kujikwamua kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mikakati ya Serikali kusaidia vijana
wa Katavi pamoja na maeneo mengine kupata ajira na kuwa na mazingira wezeshi ya kujikwamua kiuchumi ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza ni kuzielekeza Mamlaka
za Serikali za Mitaa kuzingatia masuala ya ukuzaji ajira katika mipango ya maendeleo, hususan kutambua na kubaini mahitaji ya nguvu kazi katika maeneo husika. Kutenga na kuendeleza maeneo ya uzalishaji wa biashara kwa vijana, kuwezesha nguvu kazi kuwa na ujuzi wa kujiajiri, kuwezesha upatikanaji wa mitaji na vitendea kazi kwa makundi ya vijana, kukuza soko la bidhaa na huduma za wajasiriamali hasa vijana.
Mheshimiwa Spika, pili, kutekeleza programu ya miaka mitano ya kukuza ujuzi inayolenga kuwawezesha vijana takribani 4,419,074 kupata ujuzi wa kuajiriwa au kujiajiri katika sekta mbalimbali. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 vijana 1,469 wamepatiwa mafunzo ya ushonaji wa nguo kupitia viwanda vya Mazava Fabrics na Took Garment. Vijana 3,900 wametambuliwa na watapata mafunzo ya kurasimisha ujuzi wao kupitia VETA. Vijana 100 kati ya 1,001 wameanza mafunzo ya ujuzi kwa kutengeneza bidhaa za ngozi katika Chuo cha DIT, Mwanza.
Mheshimiwa Spika, tatu ni kuandaa na kuana kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Ajira kwa Vijana katika Sekta ya Kilimo (National Strategy for Youth Involvement in Agriculture) ambao unaweka mazingira wezeshi ya kuvutia vijana kujishughulisha na kilimo kwa kuwezesha upatikanaji wa ardhi, mitaji, pembejeo za kilimo, masoko, mafunzo ya ujuzi wa kilimo na ujasiriamali.
Mheshimiwa Spika, mikakati hiyo itasaidia pia kushirikisha vijana wote wa Tanzania, wakiwemo vijana wa Katavi kupata mazingira wezeshi ya kujikwamua kiuchumi. Aidha, Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya barabara inayounganisha mikoa yote nchini ikiwemo Mkoa wa Katavi kwa lengo la kuchochea uwekezaji na kukuza fursa za ajira nchini.
MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:-
Masuala ya watu wenye ulemavu kwa kiasi kikubwa yanazungumzwa na kushughulikiwa katika maeneo ya mijini na kusahau maeneo ya pembezoni ambapo kuna watu wa jamii hiyo.
Je, Serikali ina mpango gani kuhusu watu wenye ulemavu waishio vijijini ambapo matatizo yao ni mengi na makubwa kulingana na jamii inayowazunguka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mhesimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Saleh Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu waishio vijijini, kwa kutambua hilo Serikali imefanya ugatuaji wa shughuli zinazohusu watu wenye ulemavu kwenda katika Serikali za Mitaa. Serikali inaendelea kuzijengea uwezo Halmashauri na watoa huduma
wengine ili kutatua kero zinazowakabili watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kulingana na Sheria ya Watu Wenye Ulemavu Namba 9 ya mwaka 2010, imeelekeza kuanzisha Kamati za Baraza la Huduma na Ushauri kwa Watu Wenye Ulemavu kuanzia ngazi ya kijiji/ mtaa hadi ngazi ya taifa, ambazo zitasaidia utoaji huduma kwa watu wenye ulemavu. Katika kusimamia utekelezaji wa matakwa ya sheria hii, Serikali imewaagiza Makatibu Tawala wote wa Mikoa kusimamia uanzishwaji wa Kamati za Mikoa, Halmashauri, Kata na Vijiji kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu maana ndiko walipo watu wengi wenye ulemavu.
Mheshimiwa Spika, naomba nitoe rai kwa jamii kuanzisha vyama vya kiraia vikiwemo Vyama vya Watu wenye Ulemavu ambavyo vimekuwa vikifanya kazi kwa ukaribu na wenye ulemavu hadi vijijini.
MHE. FAUSTINE E. NDUGULILE (K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI) aliuliza:-
Sheria ya kuwalinda wafanyakazi wa mahotelini na majumbani imekwama kutungwa Zanzibar na Tanzania Bara kutokana na Azimio lililofikiwa na Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) kutoridhiwa na Bunge tangu Mkataba kusainiwa mwaka 2011, mkataba ambao unataka kila nchi mwanachama kuwa na Sheria ya kulinda haki za wafanyakazi hao:-
(a) Je, ni sababu zipi zinazosababisha azimio hilo kutowasilishwa Bungeni tangu Tanzania iliposaini Azimio la ILO wakati nchi nyingine zimeanza utekelezaji wake zikiwemo za Afrika Mashariki?
(b) Kwa kuwa Zanzibar haiwezi kutunga Sheria zake za kulinda haki za wafanyakazi wa mahotelini na majumbani mpaka azimio hilo lipelekwe na Ofisi yako Bungeni na kuridhiwa ndiyo kila upande utunge Sheria zake kutokana na mambo ya kazi kuwa sio ya Muungano: Je, ni lini Bunge litapokea azimio hilo la kulinda haki za wafanyakazi hao?
(c) Je, Serikali inawaeleza nini Vyama vya Wafanyakazi wa Mahotelini na Majumbani ambao walianza kufanya matayarisho ya utekelezaji wa azimio hilo, lakini wamekwama kutokana na mkataba huo kutoridhiwa na Bunge tangu kuafikiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa mwaka 2011, nchi wanachama wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) ikiwemo Tanzania, zilipitisha Mkataba wa Kimataifa kuhusu kazi za staha kwa wafanyakazi wa majumbani (Convention No.189 on Decent Work for Domestic Workers). Hadi sasa nchi zilizoridhia mkataba huu ni 23 kati ya nchi wanachama 189. Kwa upande wa Afrika ni nchi mbili tu zilizoridhia ambazo ni Afrika Kusini na Mauritius. Serikali inaendelea kupitia kwa makini sana maudhui ya mkataba huo ili kufanya maandalizi ya kuuridhia.
Mheshimiwa Naibu Spika, masuala ya kazi na ajira siyo ya Muungano. Tanzania ina Sheria za Kazi, hali kadhalika na Zanzibar pia wana Sheria za Kazi ambazo zinawahusu wafanyakazi wote wakiwemo wafanyakazi wa mahotelini na majumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nchi yetu inazo sheria mbalimbali zinazotambua na kusimamia maslahi ya wafanyakazi nchini, wakiwemo wafanyakazi wa majumbani, wafanyakazi na vyama vyao waendelee kutambua juhudi za Serikali na kulinda na kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi kupitia sheria, kanuni na taratibu tulizonazo. Serikali itaendelea kuelimisha jamii na wadau mbalimbali kuhusu mifumo, maudhui na taratibu za uridhiaji wa mikataba ili kufanya maandalizi stahiki kabla ya uridhiaji wa mikataba hiyo.
MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI aliuliza:-
Serikali ilibinafsisha viwanda mbalimbali nchini ili kuongeza tija katika uzalishaji na kutengeneza ajira kwa Watanzania:-
(a) Je, Serikali ina mpango wowote wa kuvirudisha Serikalini viwanda vyake vilivyobinafsishwa kwa wawekezaji na wakashindwa kuviendeleza hususan viwanda vya MMMT - NDC na UWOP vilivyopo Mang’ula/Mwaya?
(b) Je, Serikali haioni kama kuendelea kuviacha viwanda hivi kwa wawekezaji walioshindwa kuviendeleza na kuamua kukata mashine za viwanda na kuuza kama chuma chakavu ni uhujumu wa uchumi wa Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Peter Ambrose Lijualikali, Mbunge wa Kilombero, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhamira ya Serikali kuhakikisha viwanda vyote vilivyobinafsishwa vinafanya kazi. Tunataka viwanda vyote vifanye kazi ili rasilimali zile zitumike kikamilifu na kwa tija, tupate ajira kwa wananchi wetu, tuzalishe bidhaa na kuongeza wigo wa kulipa kodi. Kama kasi ndogo ya kurejesha viwanda inavyomsikitisha Mheshimiwa Lijualikali, nasi upande wa Serikali hatufurahiii hali hiyo. Tarehe 22 Juni, 2017 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa mwongozo maalum kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji juu ya kuharakisha ufufuaji wa viwanda hivi. Kabla ya mwezi Septemba, 2017 tutatoa taarifa ya kwanza kuhusu uboreshaji wa viwanda hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vya MMMT - NDC ni moja ya rasilimali ambazo tumeanza nazo kufuatia agizo tajwa hapo juu. Kiwanda cha Ushirika Wood Products Ltd (UWOP) kama vilivyo viwanda vingi vilisimamisha uzalishaji kimekumbwa na matatizo ya mashauri mahakamani na madeni ya benki. Hilo ni moja ya mambo ambayo yamepelekea viwanda viwanda vingi visiendelee, kwani wale waliopewa kwa bei ya hamasa waliuliza rasilimali zile au kuweka dhamana benki na fedha waliyopata kufanyia shughuli tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye sehemu ya kwanza ya swali, umetoka mwongozo maalum juu ya kushughulikia viwanda vya aina hii. Viwanda vilivyobinafsishwa lazima vifanye kazi, yeyote mwenye kiwanda cha aina hiyo awasiliane na Msajili wa Hazina ili apate mwongozo utakaomsaidia kuendesha kiwanda au kuwapa walio tayari ili wakirekebishe.
MHE. HASNA S. K. MWILIMA aliuliza:-
(a) Je, Serikali inawaeleza nini wafanyakazi wa Kiwanda cha Chumvi ambao walistaafishwa bila malipo ya kiinua mgongo?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwabana wamiliki wa kiwanda hicho ili waboreshe mazingira ya kiwanda pamoja na mazingira ya wafanyakazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wafanyakazi wa Kiwanda cha Chumvi ambao walistaafishwa bila malipo ya kiinua mgongo lilishashughulikiwa, ambapo wafanyakazi husika walilipwa mafao yao kwa mujibu wa sheria ikiwemo kiinua mgongo. Aidha, kwa kuzingatia Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 ya mwaka 2016 yaliyopitishwa na Bunge lako Tukufu wakati wa Kikao cha Bajeti, kama kuna mfanyakazi au wafanyakazi wanaoona kuwa hawakulipwa stahiki zao za kupunguzwa kazi ipasavyo, wanayo fursa ya kuwasilisha moja kwa moja madai yao kwenye Tume ya Usuluhishi na Uamuzi pasipo kupitishia kwa Kamishna wa Kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali ni kuendelea kuimarisha mikakati na huduma za usimamizi na ukaguzi kazi kwa kuchukua hatua stahiki kwa waajiri wanokiuka sheria ili kuboresha mazingira ya kiwanda na mazingira ya wafanyakazi. Aidha, kupitia Marekebisho ya Sheria za Kazi ya mwaka 2016, Maafisa Kazi wamepewa mamlaka ya kuwatoza faini za papo kwa papo waajiri wanaokiuka sheria. Kanuni kwa sasa zinaandaliwa ili kuweka mwongozo na utaratibu mzuri wa utekelezaji wa suala hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nivisihi vyama vya wafanyakazi nchini, navyo vitimize wajibu wao wa kutetea na kusimamia haki za wafanyakazi pamoja na kukuza tija na uzalishaji sehemu za kazi.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Hivi karibuni wakati Mheshimiwa Rais akifungua majengo ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PPF aliongelea wazo la kuunganisha Mifuko ya Jamii iliyopo sasa NSSF, PPF, GEPF na LAPF na kufanya ama mifuko miwili au hata mmoja tu kama ilivyo katika nchi nyingine.
(a) Je, mchakato huu sasa umefikia wapi?
(b) Je, Serikali ina malengo ya kuunda mifuko mingapi baada ya muungano huo wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athumani Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ina jumla ya Mifuko Saba ya Hifadhi ya Jamii. Kati ya mifuko hiyo, mitano ni ya pensheni ambayo ni NSSF, LAPF, PSPF, GEPF na PPF, mmoja ni wa fidia kwa wafanyakazi na mmoja ni wa bima ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzishwa kwa mifuko mitano ya pensheni hapa nchini kumetokana na historia ya mfumo wa kiuchumi ambayo nchi yetu imepitia tangu uhuru mpaka sasa. Mifuko hii ilipokuwa inaanzishwa ililenga kutoa huduma za hifadhi ya jamii katika sekta mbalimbali kama vile watumishi wa umma, mashirika ya umma, polisi na sekta binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa kuunganisha Mifuko ya Jamii umefikia hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa tathmini na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (actuarial evaluation) ambayo pamoja na mambo mengine imetoa mapendekezo kuhusu namna bora na mambo muhimu ya kuzingatiwa katika zoezi la kuunganisha mifuko. Aidha, wadau mbalimbali wameshirikishwa wakiwemo vyama vya waajiri na wafanyakazi ili kutoa maoni na mapendekezo Serikalini kwa maamuzi. Kimsingi Serikali imefikia hatua nzuri ya mchakato huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa Serikali haijafanya uamuzi rasmi wa idadi ya mifuko itakayobaki baada ya kuiunganisha mifuko iliyopo hivi sasa. Hata hivyo, Serikali itazingatia maoni na ushauri wa wadau ili kufanya uamuzi muafaka wa idadi na aina ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inayotakiwa kuwepo kwa kuzingatia uwepo na mahitaji ya sekta binafsi na sekta ya umma.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y MHE. JUMA HAMAD OMAR) aliuliza:-
Kumekuwa na utaratibu wa muda wa kulipa malipo ya pensheni kwa wastaafu kama vile kila mwezi, kila baada ya miezi sita na kila baada ya miezi mitatu.
(a) Je, ni utaratibu gani kati ya hizo zilizotajwa hauwasumbui wastaafu?
(b) Je, ni formula gani inayotumika katika kuwaongezea wastaafu pesheni zao ili angalau kwa kiasi fulani ziweze kusaidia kukidhi maisha yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Hamad Omar, Mbunge wa Ole, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu mzuri wa kulipa mafao ya pensheni ni malipo ya kila mwezi. Aidha, malipo ya pensheni yanaweza kutafsiriwa kama malipo mbadala ya mshahara wa kila mwezi kwa mfanyakazi aliyestaafu. Ni wazi kwamba malipo haya yanakuwa na mahusiano makubwa na maisha ya kila siku ya mstaafu kama ilivyo kwa mshahara ama kipatao kingine kinachotokana na maisha ya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kutokana na hali halisi ya mazingira ya nchi yetu kijiografia na gharama za kufuatilia pensheni husika, baadhi ya mifuko ya pensheni iliweka utaratibu wa kulipa kwa mafungu ya miezi mitatu au sita ili kupunguza gharama kwa wastaafu. Aidha, kutokana na maendeleo ya teknolojia natoa rai kwa mifuko yote kuendelea kuboresha mifumo yao ili kuendelea kutoa mafao kwa wakati kadri inavyowezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, utataratibu wa kuhuisha pensheni, indexation umebainishwa katika kifungu cha 32 cha Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii, Sura ya 135, kikisomwa pamoja na kifungu cha 25 cha sheria hiyo ambacho kinaitaka mamlaka kufanya tathmini ya mifuko husika kabla ya kutoa viwango vya mafao, kwa mfano, kufuatia tathmini ya mifuko yote iliyofanywa katika kipindi cha mwaka 2015/2016 mamlaka ilikwishatoa maelekezo ya viwango vipya vya malipo ya kima cha chini cha pensheni ya kila mwezi kwa mifuko yote.
MHE. ALLY SALEH ALLY (K.n.y. MHE. MARYAM SALUM MSABAHA) aliuliza:-
Wafanyakazi wa Kampuni mbalimbali nchini wamekuwa wakipata ajali wawapo kazini na baadhi yao kutopewa huduma ya matibabu na waajiri wao na kuishia kupata ulemavu wa kudumu:-
Je, ni wafanyakazi wangapi wamepata stahiki zao baada ya ajali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu lilipitisha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi Na. 8 ya mwaka 2008 (Sura 263 marejeo ya mwaka 2015). Sheria hii ilifuta sheria iliyokuwa inamtaka mwajiri kumlipia mfanyakazi wake matibabu na fidia ya ulemavu wa kudumu baada ya kuumia, kuungua au kufariki kutokana na kazi na hivyo kuanzisha Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (Workers Compensation Fund).
Mheshimiwa Spika, Mfuko huu wa Fidia kwa Wafanyakazi unashughulikia masuala ya fidia kwa wafanyakazi waliopo katika sekta ya umma na sekta binafsi Tanzania Bara na umeweka utaratibu katika utoaji huduma za matibabu na fidia ya ulemavu wa muda, malipo ya ulemavu wa kudumu, malipo kwa anayemhudumia mgonjwa, huduma za ukarabati na ushauri nasaha, msaada wa mazishi na malipo kwa wategemezi endapo mfanyakazi atafariki.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2017, Mfuko umehudumia jumla ya wafanyakazi 478 waliopata ajali wakiwa kazini. Wafanyakazi hawa wamepatiwa huduma za matibabu katika hospitali mbalimbali nchini zilizoingia mkataba na mfuko na wamepatiwa mafao ya fidia kwa mujibu wa sheria. Aidha, Mfuko pia umerudisha gharama za matibabu kwa waajiri ambao waliwatibu wafanyakazi waliopata ajali na kuhudumiwa katika hospitali ambazo hazijaingia mkataba na Mfuko.
Mheshimiwa Spika, Mfuko ulianza kupokea madai ya fidia rasmi tarehe 1 Julai, 2016 na kuanza kulipa fidia kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 212A la tarehe 30 Juni, 2016.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-
Watanzania wengi hasa wanawake wanaokwenda kufanya kazi za ndani katika nchi za kiarabu kama Oman na nyinginezo wamekuwa wakifanyiwa ukatili mkubwa sana unaosababisha wengine kufariki na wengine kujeruhiwa vikali.
(a) Je, Serikali ina utaratibu gani madhubuti wa kudhibiti safari za Watanzania hao wanaokwenda katika nchi za Kiarabu na pia kuwabana Mawakala na kuwawajibisha inapobidi?
(b)Je, ni wanawake wangapi wa Kitanzania wameuawa katika Nchi za Kiarabu na fidia kutolewa katika familia zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kutoa vibali kupitia mamlaka zinazoshughulikia masuala ya ajira ikiwemo Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TAESA) iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia masuala ya kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu kwa kushirikiana na Wizara inayoshugulikia masuala ya kazi Zanzibar na Balozi zetu zilizoko nchi mbalimbali huko Mashariki ya Kati.
Serikali imeweka miongozo itakayosaidia siyo tu kuwabana mawakala bali pia kuwasaidia Watanzania kutumia fursa za ajira zilizopo nje ya nchi ili kupunguza tatizo la ajira hasa kwa vijana kwa kuelekeza kila mfanyakazi kuwa na wakala rasmi na kupata mkataba kutoka Ubalozini.
Mheshimiwa Spika, Ubalozi unakuwa na taarifa katika kila hatua ambayo Watanzania wanapitia wakati wa maandalizi ya kwenda kufanya kazi hivyo kulinda maslahi yao. Aidha, mwajiri anayetaka kuajiri wafanyakazi kutoka Tanzania atatakiwa kusoma na kuelewa mwongozo na baada ya kukubaliana nao anatakiwa kujaza fomu ya kuomba kumwajiri Mtanzania na kuwasilisha Ubalozini kwa ajili ya kufanyiwa kazi. Maombi hayo yatafuatiwa na mkataba wa kazi.
Mheshimiwa Spika, mkataba huu una vupengele vikuu vitano ambavyo mwajiri na mawakala wanapaswa kukidhi mahitaji yake ili Serikali itoe idhini kwa Mtanzania aliye tayari kufanya kazi aendelee na taratibu za ajira katika nchi hizo. Vipengele hivyo ni kama ifuatavyo:-
(i) Taarifa za mwajiri.
(ii) Taarifa za mwajiriwa.
(iii) Mshahra wa mwajiriwa.
(iv) Masharti ya mkataba.
(v) Maelezo ya mawakala wa Tanzania na Oman.
Mheshimiwa Spika, takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa Watanzania zaidi ya 12,000 ambao Balozi unawatambua wanafanya kazi katika kada mbalimbali nchini Oman. Kati ya hao, wanawake watatu wamepoteza maisha kwa sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa, ajali na kadhalika. Katika vifo vilivyowahi kuripotiwa ambapo Serikali ilifuatilia hadi kujua vyanzo halisi vya vifo hivyo, hakuna taarifa kuhusu vifo vilivyosababishwa na mauaji ya makusudi.
Aidha, mara zote tunapopata taarifa za vifo katika nchi hizo, Serikali huchukua jukumu la kufuatilia kwa kushirikiana na mamlaka za nchi husika kujua hatma za familia zilizopoteza mwenzi wao ikiwa ni pamoja na malipo ya fidia kutoka kwa mwajiri wa marehemu.
Mheshimiwa Spika, wakati wote Serikali imekuwa makini katika hatua za awali za maandalizi ya safari hizo kwa kuwabana mawakala na kuhakikisha kuwa mikataba inakuwa ni mizuri ili kuwezesha kuziba mianya yote ya kukwepa majukumu kwa pande zote inayoweza kusababisha Watanzania wanaokwenda kufanya kazi katika nchi hizo kupoteza haki zao.
MHE. PETER A. LIJUALIKALI aliuliza:-
Wakulima wa miwa kata za Sanje, Msolwa Station, Kidatu na Mkula wanaouza miwa kwa Kiwanda cha Sukari Illovo wamekuwa wakilalamika kuhusu upimaji wa uzito wa miwa na kiwango cha sukari katika muwa.
Aidha, Kiwanda cha Illovo kimehodhi upimaji wa uzito wa kiwango cha sukari na kisha kuwashurutisha wakulima kuamini kuwa vipimo vyao ni sahihi.
(a)Je, Serikali haioni kuwa utaratibu huu unatoa mwanya kwa wakulima kunyonywa na kupewa vipimo batili?
(b)Je, Serikali haioni kuwa hali hii ya kumuachia mwekezaji kuhodhi upimaji wa uzito na kiwango cha sukari katika muwa hutoa mwanya kwa mwekezaji kumnyonya mkulima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali ya Mheshimiwa Peter Lijualikali, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, upimaji wa uzito wa miwa ya wakulima unaotumiwa na wakulima wa Kiwanda cha Kilombero unatumia mizani maalum (weighbridge) ambayo inaratibiwa kwa mfumo wa computer. Mizani hiyo huhakikiwa na Wakala wa Vipimo kabla ya msimu wa uzalishaji wa sukari kuanza. Hivyo, kutokana na taratibu hizo hatutarajii mizani hiyo kutoa vipimo batili.
(b) Mheshimiwa Spika, upimaji wa kiasi cha sukari katika miwa hufanyika katika maabara zilizopo kiwandani. Kiwanda cha Kilombero kinafanya upimaji huo kwa uwazi na kimewaruhusu wakulima kuweka wawakilishi wao katika maabara hizo ili kuona na kuhakiki namna ambavyo upimaji unafanyika. Wakulima pia wamewekewa wawakilishi wao katika eneo la kupokelea miwa kabla ya kupimwa na kuingizwa kiwandani ili kuhakikisha kuwa miwa yao inaingia kiwandani na miwa ya kiwanda kwa uwiano ulio sawa.
Mheshimiwa Spika, katika kushughulikia changamoto ya kutokuaminiana baina ya pande hizo mbili, Serikali kupitia Bodi ya Sukari Tanzania inafanya ufuatiliaji katika viwanda ikiwemo Kiwanda cha Kilombero ili kuona namna ya miwa ya wakulima na ya kiwanda inavyopimwa katika mizani na upimaji wa kiasi cha sukari katika maabara. Katika msimu wa mwaka 2016/2017 zoezi hilo limefanyika katika Kiwanda cha Kilombero na kuonyesha kuwa upimaji wa miwa pamoja na kiasi cha sukari katika miwa unafanyika kwa uwazi na kwa mujibu wa taratibu zilizopo.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza:-
Tanzania imeweka nafasi maalum za uwakilishi wa wanawake katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa makundi ya walemavu, wasomi, vijana na wanawake:-
Je, ni lini Serikali itatunga sheria itakayozilazimisha taasisi za Serikali kutenga nafasi maalum za ajira kwa Watu Wenye Ulemavu ili nao wasiendelee kujisikia kama wategemezi katika jamii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma Mbunge wa Bububu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ni kielelezo cha utu. Kufanya kazi kunamwezesha mwanadamu kujitegemea hivyo kupata heshima katika jamii. Kutokana na hilo Serikali imefanya jitihada za kutunga Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 2004 kwa lengo la kuleta maendeleo, haki na heshima kwa watu wenye ulemavu. Aidha, mwaka 2010 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya Mwaka 2010. Sheria hii inatoa mwongozo wa kisheria wa namna ya kutoa huduma mbalimbali kwa watu wenye ulemavu ikiwemo ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa upande wake imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria hii kwa kuziagiza Taasisi za Serikali na Binafsi kuajiri watu wenye lemavu wenye sifa sawia kila inapohitajika, hivyo tumeendelea kufanya kaguzi kwa kuwatumia Maafisa Kazi ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa sheria hii unafanyika ipasavyo. Aidha, Serikali imeendelea kusimamia upatikanaji wa ujuzi na sifa linganifu kwa watu wenye ulemavu ili waweze kuajirika na kujiajiri kiurahisi kwa kutoa mafunzo kupitia vyuo vya ufundi na vyuo vingine kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na jamii kuamini kuwa watu wenye ulemavu hawawezi kufanya baadhi ya kazi imepelekea baadhi ya waajiri kutowaajiri Watu Wenye Ulemavu. Hivyo naomba nichukue nafasi hii kuagiza waajiri wote nchini kuzingatia sheria kila inapotokea nafasi za ajira zinazoweza kufanywa na Watu Wenye Ulemavu na wamefikia viwango vya sifa zinazotakiwa naomba tuwape kipaumbele.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakifanyia tathmini ya kina (ex-post evaluation) Kituo cha Vijana cha TULU kilichopo Sikonge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Vijana cha TULU kinamilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge chini ya usimamizi wa Serikali ya Mkoa wa Tabora. Kilianzishwa mwaka 2014 kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata mafunzo na stadi za ujuzi mbalimbali kama vile ujasiriamali, kilimo pamoja na ujenzi wa makazi bora. Baadaye vijana waanzilishi wa kituo hiki walikisajili kama asasi isiyo ya kiserikali (NGO) ijulikanayo kama Pathfinder. Baada ya kituo hiki kusajiliwa kama NGO, ilibainika kuwanufaisha vijana wachache tofauti na malengo yaliyokusudiwa ambayo ni kuwanufaisha vijana walio wengi ndani na hata nje ya Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kituo hiki kuendeshwa kwa maslahi ya vijana wachache, Serikali iliamua kuchukua hatua ya kubadili usajili wa kituo hiki kutoka kwenye NGO na kuwa kituo cha vijana kitakachosimamiwa na Serikali kwa lengo la kunufaisha vijana wengi zaidi. Aidha, nyaraka muhimu zimewasilishwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya kubadilisha usajili huo wa awali. Baada ya maamuzi hayo kukamilika, Serikali itafanya tathmini ya kina ili kubainisha matumizi na programu mbalimbali zitakazotolewa katika kituo hiki.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Mafao ya wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Mashirika mengi ya Hifadhi ya Jamii yamekuwa na utata kuhusu fao la kujitoa. Je, Serikali inatoa tamko gani ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kuunganisha mifuko hiyo na kuondoa mkanganyiko kwa wanachama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Na. 102 wa mwaka 1952, fao la kujitoa sio miongoni mwa mafao yaliyoainishwa katika mkataba huo. Kwa hapa Tanzania fao la kujitoa ni utaratibu wa wanachama kujitoa na kuchukua mafao yako katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inayotoa mafao ya pensheni kabla ya kufikisha umri wa kustaafu. Utaratibu huu umezoeleka miongoni mwa wanachama wa mifuko hiyo na hata kuonekana ni mojawapo ya mafao ya hifadhi ya jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua changamoto ya kipato inayowakabili wafanyakazi wale wanaopoteza ajira, Serikali itawasilisha Bungeni mapendekezo ya marekebisho ya Sheria za Hifadhi ya Jamii yatakayoanzisha fao la upotevu wa ajira (unemployment benefit) kwa wafanyakazi watakaokuwa wanapoteza ajira kabla ya kufikisha umri wa kustaafu kazi. Fao hili litakuwa linatolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inayotoa mafao ya pensheni.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya wingi wa mifuko inayoikabili Sekta ya Hifadhi ya Jamii. Ili kukabiliana na changamoto hiyo, mwaka 2015 Serikali ilifanya tathmini ya mifuko yote ya pensheni kwa lengo la kuangalia uwezekano na namna bora ya kuiunganisha. Matokeo ya tathmini hiyo yalionesha kuwa inawezekana kuunganisha mifuko hiyo na kubaki na michache kwa kuzingatia hali halisi ya mahitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na matokeo ya tathmini hiyo, Serikali imeandaa mapendekezo ya kuunganisha mifuko mitano inayotoa mafao ya pensheni na kubaki na michache iliyo imara. Mapendekezo hayo yameshajadiliwa na wadau wa kukubaliwa. Hatua inayoendelea hivi sasa ni kuwasilisha mapendekezo hayo katika vikao maalum vya Serikali ili Serikali itoe kibali. Matokeo ya kuunganisha mifuko hiyo ni pamoja na kupunguza gharama za uendeshaji, kuboresha mafao na kuifanya mifuko kufanya kazi kwa ufanisi na kwa uendelevu katika kipindi cha muda mrefu ujao.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS aliuliza:-
Baadhi ya wafanyakazi wamejiunga na Mfuko wa NSSF na hukatwa sehemu ya mishahara yao kwa ajili ya kuwekeza ili iwasaidie baada ya kustaafu.
Je, mpaka sasa ni wafanyakazi wangapi wamejiunga na Mfuko huo?
Je, ni wafanyakazi wangapi wamestaafu kazi na kulipwa fedha zao na Mfuko huo?
Je, ni nani analipwa faida inayopatikana kwa fedha za Mfuko huo kutoka benki zinakowekwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fakharia Shomar Khamis, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na – kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Spika, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lina jumla ya wanachama wapatao 946,533 ambao ni wafanyakazi kutoka taasisi mbalimbali ambao wamejiunga na Mfuko huu kufikia mwezi Juni, 2017.
• Mheshimiwa Spika, hadi kufika mwezi Juni, 2017, NSSF ina jumla ya wafanyakazi 14,946 ambao wamestaafu na wanaendelea kupata pensheni kutoka Mfuko huu.
• Mheshimiwa Spika, mapato yanayopatikana katika uwekezaji wa michango ya wanachama unaofanywa maeneo mbalimbali kama ilivyoanishwa katika miongozo ya uwekezaji hutumika kuwalipa wanachama mafao kama vile pensheni ya uzeeni, pensheni ya urithi, pensheni ya ulemavu, mafao ya kuumia kazini, mafao ya uzazi na matibabu kupitia Mfuko wa Bima wa SHIB. Aidha, Shirika hutumia sehemu ya mapato haya kulipia gharama za uendeshaji wa Mfuko.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Mahakama ya Mwanzo katika Kata ya Upuge, Wilaya ya Uyui, imetelekezwa zaidi ya miaka kumi na kusababisha miundombinu yake kuanza kuharibika.
• Je, ni kwa nini Mahakama hii imetelekezwa?
• Je, ni kwa nini majengo ya Mahakama hiyo yasitumike na Idara nyingine za Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA - K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimekuwa nikisema hapa Bungeni, uhaba na uchakavu wa majengo ni moja ya changamoto zinazokabili Mahakama katika sehemu nyingi nchini. Wizara yangu ipo bega kwa bega na Mahakama ya Tanzania katika kukabiliana na hali hii ikiwa ni pamoja na changamoto nyingine zinazoikabili Mahakama ukiwepo upungufu wa watumishi.
Mheshimiwa Spika, ni kweli jengo la Mahakama ya Mwanzo Upuge ni chakavu lakini halijatelekezwa kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge. Jengo hili linaonekana kutelekezwa kutokana na ukweli kwamba siku za nyuma lilikuwa halitumiki. Hata hivyo, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa jengo hilo kwa sasa linafanya kazi, yupo Hakimu na huduma za kimahakama zinatolewa kama kawaida. Kwa sasa tathmini inafanyika ili kulifanyia matengenezo jengo hilo kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kazi.
MHE. KHALIFA MOHAMED ISSA aliuliza:-
Wananchi wengi wajasiriamali huwa hawapati mikopo katika taasisi za fedha kwa sababu hawana uzoefu na ujuzi wa kutayarisha andiko la uchanganuzi wa miradi ya kibiashara, pia hawana mali ya kuwawezesha kuweka dhamana.
Je, ni lini Serikali itaweka mpango madhubuti unaotekelezeka ili wananchi hao waweze kukopesheka?
Je, Serikali haioni muda umefika sasa kuzitaka taasisi za fedha kupunguza masharti ya ukopeshaji ili wajasiriamali waweze kupanua miradi yao na kuwapatia ajira watu wengine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khalifa Mohamed Issa, Mbunge wa Mtambwe, lenye sehemu (a) na kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inawawezesha wananchi ili waweze kukopesheka kupitia Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 na Sheria ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Na. 6 ya mwaka 2004. Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi imeiainisha nia ya Serikali ya kuweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa mitaji kwa kuboresha vyanzo vya akiba na kuchukua hatua za kuondoa vikwazo mbalimbali ili kuwezesha mabenki kukopesha kikamilifu amana zilizopo na kwa gharama nafuu kupitia vikundi vidogo vidogo na pia SACCOS na VICOBA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na sera hii, mipango, miradi na mifuko kadhaa imeanzishwa na Serikali ili kuwezesha wananchi kukopa kwa urahisi. Aidha, Serikali inaendelea kusimamia mipango na mifuko ya uwezeshaji nchini na wananchi wengi wanaendelea kunufaika na mikopo inayotolewa ambayo ina masharti nafuu.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wetu wa mabenki na taasisi za fedha kwa sasa unaendeshwa kwa utaratibu wa ushindani, hivyo viwango vya riba pamoja na masharti mengine huwekwa na taasisi husika ili kuhakikisha marejesho. Jukumu la Serikali ni kuweka mazingira mazuri kwa vyombo hivyo kuweza kutoa huduma kwa wananchi.
Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania kulingana na mazingira inaendelea kuangalia viwango vya riba kwa mabenki na taasisi za fedha ili ziweze kumudu kupata fedha kwa ajili ya kukopesha wajasiriamali kwa riba ndogo. Mfano, ni hatua ambayo imechukuliwa na Benki Kuu hivi karibuni ya kupunguza kiwango cha riba kwa mikopo yake kutoka 16% mpaka 12%.
MHE. AIDA J. KHENAN aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani kwa vijana wanaomaliza shule za msingi, sekondari na vyuo kwa kuwawezesha kujiajiri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenan, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inayo mikakati mbalimbali ambayo inawezesha vijana wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu kujiajiri.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya mikakati inayotekelezwa mahsusi kwa ajili ya vijana wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari ni kama ifuatavyo:-
Ni kutekeleza Programu ya Kukuza Ujuzi nchini, ambapo kupitia programu hii tumeanzisha utaratibu maalum wa kutambua ujuzi uliopatikana kupitia mfumo usio rasmi na kuurasimisha kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wale walio tayari kuhitaji na kuwapa vyeti vinavyotambulika. Utaratibu huu unawapa fursa vijana wetu kuendelea na mfumo rasmi wa mafunzo na pia kutambulika na waajiri au watoa kazi.
Ni kuhamasisha vijana wanaomaliza shule za msingi na sekondari kujiunga katika vikundi vya kuzalisha mali na kusajiliwa rasmi kupitia Sheria ya Usajili wa NGO’s . Hadi sasa jumla ya vikundi vya vijana vya uzalishaji mali 10,200 vimekwishakusajiliwa.
Aidha, ipo mikakati ya kuwawezesha wahitimu wa vyuo kujiajiri na kuajiriwa ambayo ni pamoja na:-
– Ni kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi nchini ambayo inawezesha vijana wahitimu wa vyuo kupata ujuzi wa kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa. Programu hii inatoa mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa wahitimu (internship) ili kuwapatia uzoefu wa kazi.
– Serikali imerahisisha utaratibu wa uundaji wa makampuni kupitia BRELA hivyo vijana wengi wanaomaliza vyuo kuweza kuanzisha makampuni na biashara zinazoweza kuajiri vijana wengine.
Mheshimiwa Spika, pia ipo mikakati inayowawezesha wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu kujiajiri ambayo ni:-
(a) Serikali imeendelea kuimarisha utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao unalenga kuwasaidia vijana wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu kuweza kujiajiri kwa kuwapa mikopo ya mashati nafuu na mafunzo ya ujasiriamali. Katika kipindi cha mwaka 2013/2014 hadi mwaka 2016/2017 Serikali kupitia Mfuko wa Mendeleo ya Vijana imetoa mikopo ya masharti nafuu ya shilingi bilioni 5.8 kwa vikundi vya vijana 6,076 vyenye wanachama 30,380 katika Halmashauri za Wilaya 157 kupitia SACCOS za vijana.
(b) Serikali kupitia Halmashauri zinatenga maeneo kwa ajili a vijana wahitimu wa ngazi mbalimbali za elimu kufanya shughuli za uzalishaji mali ili kujipatia ajira. Katika mwaka 2016, jumla ya hekta 271,882 zilitengwa kwa ajili ya shughuli za vijana.
MHE. IGNAS A. MALOCHA aliuliza:-
Katika bajeti ya 2016/2017 Serikali ilipanga kujenga baadhi ya Mahakama za Wilaya na za Mwanzo katika maeneo mbalimbali nchini.
(a) Je, ni hatua ipi imefikiwa katika ujenzi wa Mahakama hizo?
(b) Kwa kuwa Mahakama ya Mwanzo Mtowisa katika Wilaya ya Sumbawanga Vijijini ni miongoni mwa Mahakama iliyopangiwa bajeti ya ujenzi kutokana na uchakavu mkubwa na hatarishi kwa wananchi, je, ni lini ujenzi utaanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU - KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijiibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Mahakama imepanga kujenga na kukarabati majengo yake katika maeneo mbalimbali nchini. Mahakama imejiwekea mpango wa kujenga na kukarabati majengo hayo kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Utekelezaji wa mpango huu unaendelea.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Mahakama imepanga kujenga Mahakama Kuu Kigoma na Mara na kufanya ukarabati mkubwa wa jengo la Mahakama Kuu Sumbawanga. Aidha, kwa upande wa Mahakama za Hakimu Mkazi, kipaumbele kimetolewa katika Mikoa ya Simiyu, Njombe, Katavi, Manyara, Lindi na Geita.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali imepanga kujenga Mahakama za Wilaya na za Mwanzo katika maeneo mbalimbali nchini. Mahakama ya Mwanzo Mtowisa ni moja ya maeneo yaliyopangwa kujengwa na ujenzi utaanza mara moja baada ya upatikanaji wa fedha za maendeleo.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa Mahakama wa kujenga majengo kwenye Mikoa mbalimbali, kikwazo kimekuwa ni upatikanaji wa viwanja pamoja na hati miliki za viwanja.
MHE. MGENI JADI KADIKA aliuliza:-
Mafuta ya ngozi kwa watu wenye Ualbino huingizwa kama mafuta ya kawaida na kutozwa kodi na kufanya watu hao kushindwa kumudu kuyanunua:-
Je, Serikali iko tayari kuondoa kodi katika mafuta hayo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (WATU WENYE ULEMAVU) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Awali ya yote, naomba nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ulinzi na fadhili zake na rehema kwangu. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa nafasi hii ambayo ameniamini katika Taifa hili la Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wenye Ualbino hutumia mafuta kinga (sunscreen lotion) ili kulainisha ngozi zao zisikauke na hutumika kwa maelekezo ya wataalam wa afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto zinazowakabili watu wenye Ualbino na imechukua hatua kadhaa ikiwemo kusambaza vifaa mbalimbali vinavyotumiwa na watu wenye Ualbino. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imesambaza miwani ya jua 50, mafuta kinga boksi 100 na tayari Bohari Kuu ya Dawa Nchini (MSD) imejumuisha katika orodha ya madawa mafuta kinga kwa ajili ya kuzuia miale ya jua kwa watu wenye Ualbino na mafuta hayo hutolewa bila malipo katika hospitali za Serikali hapa nchini. Vilevile, Serikali inaandaa Mwongozo wa Msamaha wa Matibabu (National Health Exemption) kwa watu wenye ulemavu wakiwemo watu wenye Ualbino.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa napenda kuwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini, kuhakikisha kuwa wanaweka katika orodha mafuta haya wakati wanapoagiza dawa nyingine kutoka MSD.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeondoa kodi kwa nyenzo za kujimudu kwa watu wenye Ualbino (Technical Aids/ Appliances) yakiwemo mafuta kinga kwa bidhaa zinazozalishwa nje na ndani ya nchi yetu. (Makofi)
MHE. RASHID ALI ABDALLAH aliuliza:-
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) mara nyingi hutumika kwa kutoa mikopo kwa Serikali kwa ajili ya maendeleo ya jamii.
Je, ni utaratibu gani wa kisheria unaofanyika ili kuhakikisha fedha za wanachama zinalindwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K. n. y. WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Ali Abdallah, Mbunge wa Tumbe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ni mpango wa kisheria wa kuchangia huduma za matibabu ulioanzaishwa kutekeleza sera ya uchangiajia wa huduma za afya ya mwaka 1993 kupitia utaratibu wa wananchi kuchangia gharama za matibabu kabla ya kuugua.
Mheshimiwa Spika, ili kuufanya mfuko huu uwe endelevu, Mfuko huwekeza fedha za ziada katika vitega uchumi mbalimbali vya muda mfupi na mrefu vyenye lengo la kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa ujumla wake. Uwekezaji huu pia unajumuisha mikopo kwa Serikali kwa ajili ya maendeleo ya jamii. Uwekezaji unaofanywa na NHIF ni jukumu mojawapo la kisheria linalotekelezwa chini ya Sheria ya Mfuko wa Bima ya Afya ya mwaka 1999 ambao pia unasimamiwa na Sera ya Mfuko wa Bima ya Afya ya Uwekezaji pamoja na miongozo ya uwekezaji kama ilivyotolewa na Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii ikishirikiana na Benki Kuu ya Tanzania.
Mheshimiwa Spika, kazi mojawapo ya msingi ya mamlaka ya usimamizi wa sekta ya hifadhi ya jamii ikishirikiana na Benki Kuu ya Tanzania ni kutetea na kulinda maslahi ya wanachama kwa kuhakikisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inaelekeza uwekezaji wake katika vyanzo vya uwekezaji vilivyo salama na vyenye tija kwa wanachama na taifa kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa kupitia utaratibu huu nilioueleza, fedha za NHIF zipo salama. Aidha, kwa mujibu wa tathimini ya nne uhai wa Mfuko (actuarial valuation) iliyofanywa mwaka 2013 imeonesha uwezo wa mfuko kifedha na uendelevu wake ni hadi kufikia mwaka 2040.
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Serikali ya Tanzania ilisaini Mkataba Namba 189 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) tangu tarehe 16 Juni, 2011 na Rais Mstaafu Mheshimiwa Dkt. Jakaya Kikwete alishawahi kutamka kuwa, Tanzania haina tatizo na Mkataba huo.
Je, kuna kikwazo gani kinachokwamisha kuridhia Mkataba huo wa ILO Namba 189 wa Kazi za Staha kwa Wafanyakazi wa Majumbani wakati Baraza la Wafanyakazi (LESCO) limeshapendekeza kuridhia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Tanzania kama nchi mwanachama wa Shirika la Kazi Duniani ilishiriki kikamilifu katika majadiliano na upitishwaji wa Mkataba ya Kimataifa wa ILO wa Wafanyakazi wa Majumbani Namba 189 wa mwaka 2011 ambao unalenga kukuza kazi za staha kwa wafanyakazi wa majumbani. Aidha, hadi kufikia tarehe 30/08/2017 mkataba huo umeridhiwa nan chi 24 kati ya nchi wanachama 187 ambapo nchi za Afrika zilizoridhia mkataba huu ni tatu ambazo ni Afrika Kusini, Mauritius na Guinea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha napenda nielezee kuwa Serikali inathamini mchango wa wafanyakazi wa majumbani katika kujenga uchumi wa nchi. Hii ndio maana Bunge lako Tukufu lilitunga Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Namba 6 ya mwaka 2004, ambayo inazitambua haki za wafanyakazi wa majumbani kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine. Vilevile kwa upande wa Zanzibar ipo Sheria ya Ajira, Namba 11 ya mwaka 2005.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuridhia mikataba yote ya kimataifa ikiwemo ya Shirika la Kazi Duniani siku zote Serikali imekuwa ikizingatia maslahi mapana ya nchi na ustawi wa wananchi ikiwemo wafanyakazi kwa ujumla. Endapo Serikali itajiridhisha kuwa mazingira na ustawi wa wafanyakazi kwa sheria zilizopo hakuna ustahimilivu, Serikali itafanya maamuzi stahiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hili naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kuwa kwa kushirikiana na wadau wote vikiwemo vyama vya wafanyakazi na vyama vya waajiri, Serikali itaendelea kuimarisha utekelezaji wa sheria za kazi, ili kulinda haki za wafanyakazi wa majumbani pamoja na kujenga uelewa wa wadau kuhusu matakwa ya mkataba na haki za sheria za wafanyakazi hao.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Sekta binafsi ya ulinzi ilianzishwa mwaka 1980 ikiwa na kampuni mbili tu na ikiwa haina miongozo yoyote.
• Kwa kuwa sasa sekta hii ina kampuni zaidi ya 850 nchini kote, je, Serikali italeta Sheria ya Sekta Binafsi ya Ulinzi ili pia kuanzisha mamlaka ya sekta binafsi ya ulinzi?
• Je, Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) ina mpango gani wa kushirikiana na Chama cha Sekta Binafsi ya Ulinzi ili kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athumani Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba sekta ya ulinzi binafsi imekuwa sana hapa nchini na kwamba Serikali inatambua umuhimu wa sekta hii na ilishaanza maandalizi ya kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Makampuni Binafsi ya Ulinzi. Katika kufanikisha jambo hili Wizara ya Mambo ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliandaa walaka kupeleka Baraza la Mawaziri kwa hatua za awali. Ili kukamilisha hatua hii yanahitajika maoni ya wadau kutoka pande mbili za Muungano. Serikali imeweka utaratibu wa kupata maoni kutoka katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na mara yatakapopokelewa waraka huu utawasilishwa mapema iwezekanavyo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi imekuwa ikishikiana na sekta binafsi ya ulinzi katika nyanja mbalimbali. Kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi Namba 322 Rejeo la mwaka 2002. Jeshi la polisi limekuwa likitoa mafunzo kwa makampuni binafsi ya ulinzi, kufanya ukaguzi kuchukua alama za vidole kwa watumishi, kutoa vitambulisho na kutoa ushauri kwa makampuni hayo ili kuboresha na kuhakikisha huduma ya ulinzi inatolewa katika viwango vinavyostahili.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-
Jitihada za wananchi kukaa katika maeneo yaliyopimwa zinakabiliwa na changamoto ya malipo ya shilingi 150,000 ambayo ni kodi ya zimamoto pale wanapotaka kupimiwa ardhi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kufuta kodi hiyo ili kupunguza ongezeko la makazi holela?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linafanya ukaguzi kwa mujibu wa Sheria Namba 14 Sura Na. 427 (Fire and Rescue Force Act) ya mwaka 2007 kupitaia kanuni zake za ukaguzi na vyeti ya mwaka 2008 ikisomwa pamoja na ya mwaka 2014 [Fire and Rescue Force; (Safety Inspections, Certificate and Fire Levy) Regulalations] za mwaka 2008 na mwaka 2014.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni za Ukaguzi za mwaka 2014 (Fire Levy Category No. 58) kanuni inaelekeza kutozwa tozo ya usomaji na ushauri wa michoro au ramani za majengo. Aidha, kwa mujibu wa Kanuni ya Majengo ya mwaka 2005 [The Fire and Rescue Force, (Fire Precautions in Buildings) Regulations], 2015 Na. 248 Jeshi la zima moto na Ukoaji limekuwa likishiriana na Halmashauri za Miji, Manispaa na Majiji kukagua ramani za ujenzi ili kuhakikisha kuwa nyumba zinajengwa kwa kuzingatia tahadhari na kinga dhidi ya moto na majanga mengine. Kupitia ushauri huu Jeshi la zimamoto na uokoaji hutoza tozo ambapo kiasi cha tozo huzingatia aina ya ramani iliyowasilishwa na kukaguliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa ujenzi unaozingatia tahadhari na kinga dhidi moto, Serikali haikusudii kufuta tozo hii kwa sasa. Aidha, Serikali kupitia Jeshi la Zimamoto na uokoaji inawaasa Wananchi kwa kujenga nyumba zao kwa kufuata Sheria na Kanuni zinazosimamia mipango miji ili kuwa na miji salama hivyo kupunguza athari zitokanazo na moto na majanga mbalimbali na kuwezesha utoaji wa huduma za kijamii kwa urahisi zaidi.
MHE. JUMA S. NKAMIA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya ya Chemba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Suleimani Nkamia, Mbunge wa Chemba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali ni kusogeza huduma karibu na wananchi. Juhudi kubwa zinaendelea kufanyika kuhakikisha kuwa kila Wilaya nchini inakuwa na mahakama. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imepanga kujenga jingo la Mahakama Wilaya ya Chemba.
MHE. SONIA J. MAGOGO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani dhidi ya waajiri ambao hawawaandikishi Watumishi wao katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na kuwasababishia kukosa stahiki zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sonia Jumaa Magogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali katika kuhakikisha waajiri wote wanaandikisha wafanyakazi wao kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii Na. 8 ya Mwaka 2008, Kifungu cha 30 ambacho kimeweka utaratibu unaomtaka mwajiri kuwaandikisha watumishi wake katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Aidha, mwajiri anayekiuka matakwa ya kifungu hiki anastahili adhabu ya kulipa faini ya kiasi kisichozidi shilingi milioni ishirini kwa mujibu wa kifungu cha 55 cha Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuimarisha usimamizi wa Sheria za Kazi, Serikali kupitia Bunge ilifanyia marekebisho ya Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7 ya mwaka 2004 ili kuimarisha mfumo wa kaguzi za kazi mahali pa kazi kwa kuruhusu kutoa adhabu za papo kwa papo kwa waajiri wanaokiuka matakwa ya sheria ikiwa ni pamoja na kutosajili au kuandikisha wafanyakazi katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
MHE. JAMES F. MBATIA aliuliza:-
Sheria ya Maslahi na Mafao ya Majaji Namba tatu (3) ya Mwaka 2007 Kifungu cha 8; inafafanua kuwa Jaji Mkuu, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi au Jaji wa Mahakama Kuu akifariki dunia akiwa madarakani au baada ya kustaafu, Serikali itagharamia gharama za mazishi na Kifungu cha 10 cha Sheria hiyo kinafafanua malipo ya pensheni na huduma nyingine atakazostahili Jaji wakati wa kustaafu kama ilivyo kwenye Kifungu cha 20 na 21 cha Sheria ya Utumishi wa Umma:-
Je, Serikali haioni busara kuifanyia marekebisho sheria hiyo au vinginevyo ili Majaji waweze kupatiwa huduma muhimu na hasa matibabu wakati wanapostaafu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa James Francis Mbatia, Mbunge wa Vunjo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Malipo ya Mshahara na Mafao ya Hitimisho la Kazi kwa Majaji (The Judges Renumeration and Terminal Benefits Act) na Namba tatu (3) ya Mwaka 2007 katika Kifungu cha 10 na Vifungu vya 20 na 21 vya Sheria ya Mafao Katika Utumishi wa Umma (The Public Service Retirement Benefits Act) Sura ya 371 zinaweka utaratibu wa mafao na stahili za Majaji baada ya kustaafu.
Mheshimiwa Naibu Spika, masharti ya kazi na stahili za Majaji, kwa maana ya Jaji Mkuu, Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Kiongozi na Majaji wa Mahakama Kuu yamefafanua kuwa, Majaji hao wamejumuishwa katika utaratibu wa matibabu kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya wawapo kazini na gharama hizo hulipwa na Serikali na hata wanapostaafu wanaendelea kupata huduma hizo kupitia Mfuko huo. Kwa wale waliostaafu kabla ya masharti hayo kuanza kutumika hawanufaiki na Mfuko huo.
MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR (K.n.y. MHE. IBRAHIM MOHAMEDALI RAZA) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itachukua hatua kwa kuwasaidia vijana walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ibrahim Mohamedali Raza, Mbunge wa Kiembe Samaki kama ifutavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua tatizo la matumizi ya madawa ya kulevya na athari yake kubwa kwa nguvu kazi ya Taifa letu ambayo asilimia kubwa ni vijana. Katika kukabiliana na tatizo hili, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imechukua hatua kadhaa kuwasaidia
vijana na makundi mengine walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya. Hatua hizo ni pamoja na zifuatazo:-
(i) Kutoa tiba kwa waathirika ambapo hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2017 jumla ya vituo vitno vya tiba (methadone) kwa waathirika wa dawa za kulevya vilikuwa vimeanzishwa nchini katika Hospitali za Muhimbili, Temeke, Mwananyamala, Zanzibar na Mbeya. Kupitia vituo hivyo, jumla ya waraibu 5,830 walipatiwa tiba na wengine wanaendelea kupatiwa matibabu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mwaka huu wa 2018, Serikali inatarajia kufungua vituo vipya vya tiba katika Mikoa ya Mwanza na Dodoma. Kutokana na utafiti uliofanywa mwaka 2014, Serikali imepanga kufungua vituo vya tiba katika Mikoa ya Pwani, Morogoro, Arusha, Kilimanjaro na Tanga kwa kulingana na upatikanaji wa fedha.
(ii) Kuanzisha kituo kikubwa cha kuwapatia waathirika tiba kwa njia ya kazi (occupational therapy) ambapo mafunzo ya stadi za kazi mbalimbali yatatolewa. Kituo hiki kinajengwa katika eneo la Itega, Mkoani Dodoma.
(iii) Serikali kwa kupitia Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, imetengeneza miongozo mbalimbali kwa ajili ya kusimamia utoaji wa huduma kwa waathirika wa dawa za kulevya kuanzia katika vituo vya afya hadi kwenye huduma za kijamii zinazotolewa na asasi mbalimbali za kiraia.
(iv) Kutoa elimu kwa njia ya redio na luninga ambapo viongozi wa ngazi tofauti wa mamlaka wamekuwa wakitoa elimu katika vipindi mbalimbali. Vilevile elimu imekuwa ikitolewa katika shughuli za Kitaifa kama vile Mwenge, Nane Nane, maadhimisho na matamasha mbalimbali.
MHE. SALUM MWINYI REHANI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawatambua rasmi dereva bodaboda au bajaji kuwaandikia mikataba, kuwekewa akiba na kulipiwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na waajiri wao kwani vijana hao wameshajiajiri kwa zaidi ya asilimia 15 - 25 kwenye kila Wilaya au Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salum Mwinyi Rehani, Mbunge wa Uzini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilikwishakuwatambua rasmi madereva wa pikipiki (bodaboda) au bajaji tangu mwezi Aprili, 2009 ambapo pikipiki na bajaji zilikubaliwa kufanya biashara ya kusafirisha abiria kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili madareva wa pikipiki (bodaboda) au bajaji waweze kutambuliwa kwa urahisi kwa lengo la kupatiwa hduma mbalimbali zikiwemo za Hifadhi ya Jamii kutoka Serikalini na wadau wengine, Serikali imefanya juhudi kubwa ya kuwahamasisha waunde vyama vyao katika ngazi mbalimbali ambapo kwa kupitia vikundi hivyo, elimu juu ya masuala ya sheria za kazi na hifadhi ya jamii hutolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kusimamia matakwa ya sheria yanayomtaka mwajiri kutoka mikataba kwa mwajiriwa wake hasa ikizingatiwa kwamba, mkataba unabeba haki za kimsingi na wajibu wa kila upande.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kutoa maagizo kwa waajiri wote nchini wanaotoa ajira kwa vijana waendesha pikipiki au bajaji kuzingatia sheria ikiwa ni pamoja na kuwa na mikataba ya kuhakikisha kuwa wanapata huduma nyingine muhimu zinazowawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi na kwa kuzingatia usalama wa uhai wao na vyombo vyao.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-
Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatambua uwepo wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
(a) Je, kwa nini ripoti za Tume hiyo hazitolewi kwa muda muafaka kila mwaka kama masharti ya Katiba yanavyosema?
(b) Je, ripoti ya mwisho ya Tume hiyo ilitolewa mwaka gani na lini imewasilishwa Bungeni?
(c) Je, kwa nini harakati za Tume hiyo katika kushughulikia migogoro ya ardhi, ukaguzi wa vituo vya polisi, magereza pamoja na matukio ya uvunjaji wa haki za binadamu umezorota kinyume na miaka ya nyuma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 131(3) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaelekeza Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuwasilisha taarifa zake kwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya haki za binadamu ambaye hutakiwa kuwasilisha taarifa hizo nbele ya Bunge mapema iwezekanavyo. Taarifa hizo ni muhtasari wa masuala yote yaliyofanyika katika mwaka husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa huko nyuma taarifa za Tume zilikuwa zikichelewa kuwasilishwa Bungeni kwa wakati. Hata hivyo, mwezi Desemba, 2017, Tume imewasilisha taarifa zake za nyuma hadi mwaka 2014/2015 kwa Waziri mwenye dhamana ili aziwasilishe Bungeni. Taarifa ya mwaka 2015/2016 ipo katika hatua ya mwisho ya uchapaji na itakapokuwa tayari itawasilishwa kwa Waziri mwenye dhamana. Taarifa ya mwaka 2016/2017 ipo katika maandalizi na inasubiri kukamilika kwa taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Tume.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya mwisho iliyotolewa na kuwasilishwa Bungeni ilikuwa ya kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo, kweli kwamba utendaji wa Tume umezorota, Tume imeendelea kufanya kazi zake kama zilivyoainishwa katika Katiba na Sheria. Aidha, Tume imekuwa ikiongeza jitihada kila mwaka kukagua vituo vya polisi, magereza, vituo vya mafunzo kwa upande wa Zanzabar, kufuatilia migogoro ya ardhi na kufuatilia utekelezaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora kwa ujumla. Lengo kuu la ukaguzi na ufuatiliaji huu ni kutathmini hali ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora na kutoa mapendekezo kwa taasisi husika. Vilevile Tume imekuwa ikifuatilia utekelezaji wa haki za makundi mbalimbali ambayo ni pamoja na watoto hususani watoto walio katika mkinzano na sheria, wanawake na watu wenye ulemavu.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejiwekea mpango mkakati wa kujenga Mahakama katika Mikoa na Wilaya zote nchini kwa awamu. Katika mpango huu, Mahakama ya Mkoa wa Katavi ambalo jengo lake litakuwa pia ni Mahakama ya Wilaya ya Mpanda lilipangwa kujengwa katka mwaka wa fedha wa 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari ujenzi umekwishakuanza na unatarajia kukamilika kabla ya Juni 2018. Aidha, huu ni moja ya miradi ya ujenzi wa Mahakama inayotekelezwa nchini kwa kutumia teknolojia rahisi na ya kisasa ya moladi.
MHE. STEPHEN H. NGONYANI aliuliza:-
Miongoni mwa Mahakama za Mwanzo ambazo Serikali iliahidi na kuamua kuzijenga ni pamoja na Mahakama ya Mwanzo Mkomazi. Je, ni lini Mahakama ya Mwanzo Mkomazi itajengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niba ya Waziri wa Katibu na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stephen Hilary Ngonyani Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mahakama ya Mwanzo ya Mkomazi ni moja ya Mahakama zilizo kwenye mpango wa ukarabati na ujenzi wa Mahakama za Mwanzo nchini. Hivyo, kwa mujibu wa mpango huo Mahakama ya Mwanzo Mkomazi imepangwa kujengwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA (K.n.y) MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inarejesha kasi ya kupambana na dawa za kulevya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mantumu Dau haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeongeza kasi na harakati za kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya nchini baada ya Bunge lako Tukufu kutunga Sheria mpya ya Kudhibiti na Kupamabana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya mwaka 2015. Sheria hii imeipa Serikali Mamlaka ya kuanzisha chombo chenye nguvu cha kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya, ambacho kiliundwa rasmi mwezi Februari mwaka 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mamlaka hiyo imepewa nguvu Kisheria ya kuweza kukamata, kupekua, kuzuia mali na kuchunguza mashauri yote ya dawa za kulevya na makosa mengine yanayohusiana nayo ikiwemo mali zitakazothibitika kupatikana kutokana na dawa za kulevya. Hata hivyo, Serikali katika kuongeza kasi ya kupambana na dawa za kulevya, mwaka 2017 ilifanya marekebisho makubwa ya sheria hiyo na kuipa nguvu maradufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa takribani mwaka mmoja sasa tangu kuundwa kwake hadi kufikia mwezi Februari mwaka 2018, Mamlaka imekwishakamata jumla ya watuhumiwa 11,071; kati ya hao, watuhumiwa 3,486 ni wafanyabiashara wa dawa za kulevya na tayari wameshafikishwa Mahakamani. Kutokana na kuongezeka kwa kasi ya kupambana na dawa za kulevya imesababisha kupungua kwa kiasi kikubwa cha matumizi ya madawa ya kulevya nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote kushiriki kikamilifu katika juhudi za Serikali za kupambana na dawa za kulevya kwani madhara yanayotokana na matumizi ya dawa hizo kwa namna moja ama nyingine yanatuathiri sote kwa njia mbalimbali ikiwemo kuongeza vitendo vya uhalifu, matumizi ya Serikali katika kuwahudumia waathirika pia.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza:-
NSSF ilikuwa na mpango wa kutoa mikopo kwa Vyama vya Ushirika ili viweze kukopesha wanachama wake. Kwa upande wa Karagwe wananchi walitozwa michango ya kujiunga na NSSF lakini hawajapata mikopo hiyo.
(a) Je, ni lini NSSF itatoa hiyo mikopo nafuu?
(b) Je, ni kwa nini wananchi wanailalamikia NSSF kwa muda mrefu lakini hakuna majibu yanayotolewa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mbunge wa Karagwe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) lilianzisha Mpango wa NSSF Hiari kwa ajili ya kuwawezesha wanachama wa Vyama vya Ushirika vya Wakulima (AMCOS) na Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) kujiunga na hifadhi ya jamii. Mpango huu ulilenga kila mwanachama kuchangia kiasi cha shilingi 20,000 kwa mwezi ili aweze kupata mafao ya hifadhi ya jamii.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika kuvutia wanachama kujiunga na mpango huu, shirika lilianzisha utaratibu wa kutoa mikopo kwa mwanachama aliyechangia mizei sita na kuendelea kupitia SACCOS na AMCOS zao. Utaratibu huu haukuwa endelevu kutokana na wanachama kutokurejesha mikopo, kutokuendelea kuchangia na vyama vya ushirika kutokidhi matakwa ya kisheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) limepitia upya utaratibu wa kutoa mikopo kupitia Vyama vya Ushirika na kuja na utaratibu mpya wa utoaji wa mikopo utakaoshirikisha Benki ya Azania. Utaratibu huu utaanza rasmi tarehe 1 Julai, 2017 ambapo wanachama kupitia Vyama vyao vya Ushirika vitakavyokidhi vigezo watapata mikopo kupitia Benki ya Azania.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa juu ya mpango huu wa kujiunga NSSF Hiari na suala zima la mikopo kupitia Vyama vya Ushirika zimekuwa zikitolewa mara kwa mara kupitia ofisi zetu zilizopo nchi nzima ikiwemo Karagwe. Aidha, wanachama kupitia Vyama vya Ushirika watataarifiwa juu ya utaratibu huu mpya wa kunufaika na mikopo yenye masharti nafuu.
MHE. STELLA I. ALEX aliuiliza:-
Je, ni lini Serikali itaanzisha miradi maalum itakayosaidia kupunguza ama kuondoa makali ya maisha kwa watu wenye ulemavu wasio na ajira maofisini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stella Ikupa Alex, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa watu wenye ulemavu kama kundi maalum katika jamii ambao wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kuzifikia haki zao na fursa za maendeleo ikiwemo haki ya kupata mitaji kwa ajili ya kuanzisha miradi au shughuli za uzalishaji mali.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, katika kuwawezesha watu wenye ulemavu kujumuika katika shughuli za maendeleo na maisha ya jamii, Serikali imeweka mazingira yanayoruhusu ushiriki wao katika masuala ya jamii sawa na wasio na ulemavu ikiwa ni pamoja na kupata elimu na mafunzo ya stadi za kazi katika shule au vyuo jumuishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha kuwa watu wenye ulemavu nao wanashiriki katika kuanzisha au kuanzishiwa miradi, Serikali kupitia Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, itaendelea kuhakikisha inaimarisha mifumo iliyopo ya kuhakikisha Watanzania wote wakiwemo watu wenye ulemavu wananufaika na mipango ya Serikali ya kuwawezesha kiuchumi. Hata hivyo, dhana ya kuhakikisha watu wenye ulemavu wanashirikishwa katika shughuli mbalimbali za maendeleo ni ya muhimu sana ili kuondoa unyanyapaa.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya pembejeo kwa njia ya vocha kwa lengo la kuwasaidia wakulima, lakini utaratibu ukiwanufaisha Mawakala wa Mbolea kuliko wakulima ambao ndio walengwa.
Je, Serikali inachukua hatua gani ya kuweza kubadilisha utaratibu huo na kuja na utaratibu mwingine utakaoweza kuwasaidia wakulima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI,VIJANA NA AJIRA (K.n.y WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine, Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya mwisho ya utaratibu wa vocha ulitumika msimu wa mwaka 2013/2014 na mwaka 2014/2015, utaratibu uliotumika ulikuwa wa vikundi na msimu wa 2015/2016 utaratibu wa vocha ulitumika tena kwa kuwa wakulima wengi hawakuwa kwenye vikundi na hivyo kutonufaika na ruzuku. Aidha, Serikali msimu wa mwaka 2016/2017 imetumia Kampuni ya Mbolea ya TFC kusambaza ruzuku ya pembejeo moja kwa moja kwa wakulima kupitia mawakala waliowachagua wao wenyewe na waaminifu na sio kutumia vocha tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeunda Kanuni ya Uingizaji mbolea kwa wingi (Bulk Fertilizer Procurement Regulation 2017) kwa kuanza na mbolea za urea na DAP. Lengo ni kuwa uagizaji huu utasababisha mbolea kushuka bei na hivyo Serikali kutokulazimika kutoa ruzuku ya mbolea hizo. Utaratibu huu utaendelea kutumika kwa aina nyingine endapo zitakidhi kanuni hiyo, hususan uwingi wa mahitaji yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 19/05/2017 awamu ya kwanza uchambuzi wa wazabuni ilifanyika, kati ya kampuni 20 zilizoomba kampuni 17 zimepitia awamu ya kwanza, kati yake kampuni kumi ni za ndani na Saba ni za nje ya nchi. Hii inaonesha muitikio mkubwa wa waagizaji wa utaratibu huu na hivyo matarajio ni bei kushuka na kila mkulima kujinunulia. Utaratibu mwingine ni kuwa Serikali inahimiza ujenzi wa viwanda vya mbolea hapa nchini ili kuondokana na uagizaji wa mbolea kutoka nje ya nchi kwa gharama kubwa.
MHE. ESTER A. MAHAWE (K.n.y. MHE. ESTER M. MMASI) aliuliza:-
Serikali imekuwa na juhudi mbalimbali za kuinua kiwango cha ajira zisizo rasmi nchini.
Je, nini mpango wa Serikali katika kuwawezesha vijana wahitimu waweze kuingia rasmi kwenye sekta ya kilimo na ufugaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Ester Michael Mmasi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali katika kuwawezesha vijana wahitimu waweze kuingia rasmi kwenye sekta ya kilimo na ufugaji ni kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kutekeleza mkakati wa Kitaifa wa kukuza ujuzi nchini ambao umelenga kutoa mafunzo ya kukuza ujuzi kwa wahitimu, wakiwemo wale wanaopenda kujiunga katika kilimo na ufugaji. Kupitia programu hii ofisi yangu imetenga fedha kuwezesha vijana, wakiwemo wahitimu, kupatiwa mafunzo ya kilimo cha kutumia kitalu nyumba (green house). Mafunzo haya yatafanyika katika Mikoa yote Tanzania Bara na tayari tumetoa maelekezo kwa Ofisi za Mikoa kuhamasisha vijana kujiunga katika vikundi kwa lengo la kuwawezesha kupatiwa mafunzo hayo katika maeneo maalum yaliyotengwa na mikoa yao kwa shughuli za vijana.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuboresha mazingira bora ya uwekezaji katika sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira, hususan kilimo biashara. Aidha, katika hili Serikali itajikita zaidi kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji kwenye viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa, ili kufikia lengo la asilimia 40 ya nguvu kazi nchini kuwa katika sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2020. Kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano, mwaka 2016/2017 na mwaka 2020/2021.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuendelea kuimarisha utekelezaji wa mfumo wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na mifuko mingine ya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, ambayo inalenga kuwasaidia vijana kuweza kujiajiri na kuajiri wenzao kwa kuwapa mikopo yenye masharti nafuu na mafunzo ya ujasiriamali kupitia kwenye SACCOS za Vijana ambazo zimesajiliwa. Aidha, Serikali kupitia Halmashauri zote nchini inaendelea kuhamasisha kutengwa kwa asilimia tano ya mapato yake kwa ajili ya kuwakopesha vijana, ili kujiajiri na kuajiri vijana wengine.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza:-
Mheshimiwa Rais amesisitiza sana kuhusu Tanzania ya Viwanda na katika Mkoa wa Dodoma kulikuwa na Kiwanda cha Kutengeneza Mvinyo (DOWICO) ambacho kilikuwa msaada mkubwa sana kwa wakulima wa zabibu:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua kiwanda hicho ili kufanya wakulima wapate tija kwa kuuza zabibu zao kiwandani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU - K.n.y WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mhehsimiwa Fatma Hassan Taufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Dodoma Wine Company Limited (DOWICO) cha hapa Mjini Dodoma kinamilikiwa na Bw. Thakker Singh aliyeuziwa kwa njia ya ufilisi mwaka 1993. Kwa sasa kiwanda hiki kimefungwa tofauti na matarajio ya wakati kinabinafsishwa. Mpango wa Serikali ni kukifufua kiwanda hiki na vingine vilivyofungwa, pia kuendeleza vilivyopo na kujenga viwanda vipya hasa vinavyotumia malighafi za ndani na kuajiri watu wengi kama Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 – 2020/2021 unavyoelekeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kufuata Mpango huo, Wizara yangu kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina tunashauriana na wawekezaji mbalimbali namna ya kuvifufua viwanda vilivyofungwa na ikibidi kuwapa wawekezaji wengine ili wavifufue na kuviendeleza viwanda hivyo.
Mheshimiwa Spika, napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba, Mwekezaji wa Kiwanda cha DOWICO ameingia mkataba na mmiliki wa Kiwanda cha SETAWICO kilichopo Hombolo kwa makubaliano ya kukifufua na kazi hii imeanza kwa kufanya ukarabati. Ni matumaini ya Serikali kuwa kazi ya ukarabati na usimikaji wa baadhi ya mashine utafanyika na kukamilika mapema.
Wizara yangu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma tunaendelea kufuatilia ukarabati wa kiwanda hiki kwa karibu ili kuhakikisha uzalishaji unaanza na kukiwezesha kuchangia katika uchumi wa Taifa hasa kutoa ajira kwa vijana na kuwa soko la zabibu ya wakulima hapa mkoani Dodoma.
MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:-
Mhimili wa Mahakama kama ilivyo mihimili mingine unahitaji kuwa na eneo la uhakika la kufanyia kazi na vitendea kazi vya uhakika:-
(a) Je, ni lini Wilaya ya Korogwe itajengewa Mahakama ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU - K.n.y WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa Mahakama kama Mihimili mingine, wanahitaji mazingira mazuri na muafaka kwa kufanyia kazi zao. Aidha, napenda kukiri kuwa moja ya changamoto kubwa inayozikabili Mahakama zetu ni pamoja na uhaba wa majengo na uchakavu wa miundombinu iliyopo.
Mheshimiwa Spika, Mpango wa maendeleo wa ujenzi wa Mahakama kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ni pamoja na ujenzi wa Mahakama za Mkoa ikiwemo ujenzi wa Mahakama sita za Hakimu Mkazi, ujenzi wa Mahakama 15 za Wilaya na Ujenzi wa Mahakama 10 za Mwanzo.
Mheshimiwa Spika, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Mahakama imepanga kujenga Mahakama ya Wilaya ya Korogwe kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, katika Mkoa wa Tanga Wilaya zilizopewa kipaumbele katika ujenzi ni Kilindi, Korogwe na Mkinga. (Makofi)
MHE. FAUSTINE E. NDUGULILE (K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI) aliuliza:-
Sheria ya kuwalinda wafanyakazi wa mahotelini na majumbani imekwama kutungwa Zanzibar na Tanzania Bara kutokana na Azimio lililofikiwa na Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) kutoridhiwa na Bunge tangu Mkataba kusainiwa mwaka 2011, mkataba ambao unataka kila nchi mwanachama kuwa na Sheria ya kulinda haki za wafanyakazi hao:-
(a) Je, ni sababu zipi zinazosababisha azimio hilo kutowasilishwa Bungeni tangu Tanzania iliposaini Azimio la ILO wakati nchi nyingine zimeanza utekelezaji wake zikiwemo za Afrika Mashariki?
(b) Kwa kuwa Zanzibar haiwezi kutunga Sheria zake za kulinda haki za wafanyakazi wa mahotelini na majumbani mpaka azimio hilo lipelekwe na Ofisi yako Bungeni na kuridhiwa ndiyo kila upande utunge Sheria zake kutokana na mambo ya kazi kuwa sio ya Muungano: Je, ni lini Bunge litapokea azimio hilo la kulinda haki za wafanyakazi hao?
(c) Je, Serikali inawaeleza nini Vyama vya Wafanyakazi wa Mahotelini na Majumbani ambao walianza kufanya matayarisho ya utekelezaji wa azimio hilo, lakini wamekwama kutokana na mkataba huo kutoridhiwa na Bunge tangu kuafikiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa mwaka 2011, nchi wanachama wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) ikiwemo Tanzania, zilipitisha Mkataba wa Kimataifa kuhusu kazi za staha kwa wafanyakazi wa majumbani (Convention No.189 on Decent Work for Domestic Workers). Hadi sasa nchi zilizoridhia mkataba huu ni 23 kati ya nchi wanachama 189. Kwa upande wa Afrika ni nchi mbili tu zilizoridhia ambazo ni Afrika Kusini na Mauritius. Serikali inaendelea kupitia kwa makini sana maudhui ya mkataba huo ili kufanya maandalizi ya kuuridhia.
Mheshimiwa Naibu Spika, masuala ya kazi na ajira siyo ya Muungano. Tanzania ina Sheria za Kazi, hali kadhalika na Zanzibar pia wana Sheria za Kazi ambazo zinawahusu wafanyakazi wote wakiwemo wafanyakazi wa mahotelini na majumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa nchi yetu inazo sheria mbalimbali zinazotambua na kusimamia maslahi ya wafanyakazi nchini, wakiwemo wafanyakazi wa majumbani, wafanyakazi na vyama vyao waendelee kutambua juhudi za Serikali na kulinda na kutetea haki na maslahi ya wafanyakazi kupitia sheria, kanuni na taratibu tulizonazo. Serikali itaendelea kuelimisha jamii na wadau mbalimbali kuhusu mifumo, maudhui na taratibu za uridhiaji wa mikataba ili kufanya maandalizi stahiki kabla ya uridhiaji wa mikataba hiyo.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA (K.n.y. MHE. MGENI JADI KADIKA) aliuliza:-
Mradi wa MIVARF ni wa Muungano na Makao Makuu yapo Arusha ambapo kazi yake kuu ni kujenga masoko, miundombinu ya barabara, kuongeza thamani na kupeleka maendeleo vijijini:-
Je, ni kwa kiasi gani mradi huu umechangia kuleta maendelezo Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mgeni Jadi Kadika, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, MIVARF ni programu inayohusika na miundombinu ya masoko, uongezaji thamani ya mazao na huduma za kifedha vijijini. Miundombinu ya masoko ni pamoja na majengo, barabara, maghala na vituo vya kuongeza mazao thamani. Katika utekelezaji wa programu hii Zanzibar imenufaika kukarabatiwa barabara zenye urefu wa kilometa 144; Unguja kilometa 68; na Pemba kilometa 80.
Mheshimiwa Naibu Spika, Barabara zilizokarabatiwa zimechangia katika kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo pamoja na kushamiri kwa usafiri wa abiria yaani daladala kati ya Kibwegele, Makunduchi, Bwejuu, Vikunguni, Uwandani, Mwachealale na maeneo mengine. Gharama za ukarabati wa barabara hizo ilikuwa ni shilingi bilioni tisa na milioni mia tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu unatarajia kuchangia tena shilingi bilioni nne na milioni mia sita katika kujenga masoko matatu ya ghorofa na yenye vyumba vya baridi kwa ajili ya kuhifadhia mazao. Kinyasini Unguja, Tibirizi na Konde - Pemba, pamoja na ujenzi wa kituo cha mafunzo juu ya uhifadhi na utunzaji wa mazao baada ya mavuno Pujini – Pemba. Mradi unatarajiwa kujenga masoko 16 Tanzania nzima hivyo, Zanzibar imenufaika kwa asilimia 20 ya idadi hiyo ya masoko.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi unashughulikia pia na kuhamasisha na kuimarisha shughuli za vyama vya kuweka na kukopa yaani SACCOSS ambapo kwa kipindi cha mwaka 2013 mpaka mwaka 2016 SACCOSS kwa upande wa Zanzibar zimewezeshwa kukuza mtaji kutoka shilingi bilioni
• zilizokuwepo hadi kufikia shilingi bilioni 10.5. Mikopo nayo imepanda kutoka shilingi bilioni 3.9 mwaka 2013 hadi kufikia shilingi bilioni 15 mwaka 2016. Aidha, idadi ya wanachama hai imepanda kutoka 8,000 mwaka 2013 hadi kufikia 28,000 mwaka 2016.
MHE. AIDA J. KHENAN aliuliza:-
Mara kwa mara Serikali imekuwa ikishindwa kesi mbalimbali Mahakamani:-
Je, Serikali imefanya uchunguzi na kujua sababu za kushindwa kesi mara kwa mara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n. y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aida Joseph Khenan, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge hakutaja aina ya kesi anazomaanisha katika swali lake, nianze kwa kufafanua kwamba, kuna aina mbalimbali za kesi au mashauri yanayofunguliwa Mahakamani na Serikali au dhidi ya Serikali. Mfano, mashauri ya jinai, madai, katiba, uchaguzi na kadhalika. Kwa ujumla mashauri hayo hufunguliwa kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, vilevile Halmashauri, Mashirika ya Umma, Taasisi, Wakala wa Serikali na Idara za Serikali zinazojitegemea zinayo mamlaka ya kuendesha na kusimamia mashauri yanayofunguliwa dhidi yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, mashauri yote yanayofunguliwa na Serikali au dhidi ya Serikali yamekuwa yakiendeshwa kwa weledi na pale inapostahili Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekuwa ikiratibu uendeshaji wa mashauri hayo na takwimu zetu zinaonesha mashauri mengi Serikali inashinda. Kwa mfano, kati ya mashauri 53 ya kupinga Uchaguzi wa Ubunge yaliyofunguliwa Mahakamani baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2015, Serikali ilishinda mashauri 52 na kushindwa shauri moja tu na katika mashauri 199 ya kupinga Uchaguzi wa Madiwani, Serikali ilishinda kesi 195.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama takwimu zinavyoonesha si kweli kwamba, Serikali imekuwa ikishindwa kesi mara kwa mara. Hata hivyo, katika nchi yoyote inayozingatia uhuru wa Mahakama na utawala wa sheria, Serikali haiwezi kushinda kila shauri hata kama haistahili. Ni kweli kuna baadhi ya kesi ambazo Serikali inashindwa, sababu zinazosababisha Serikali kushindwa baadhi ya mashauri ni pamoja na namna ushahidi ulivyokusanywa na vyombo vya Serikali, kutokupatikana mashahidi muhimu, mashahidi kutokutoa ushahidi uliotegemewa, baadhi ya Taasisi, Mashirika ya Umma na Idara za Serikali kutoishirikisha mapema ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, zinapofungua au kufunguliwa mashauri Mahakamani, namna ushahidi unavyochukuliwa Mahakamani, mashahidi kula njama na kutoa ushahidi unaoathiri mashauri ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na changamoto hizo, Serikali imekuwa ikichukua hatua kadhaa ikiwemo kuhakikisha kuwa, mashahidi muhimu wanapatikana, kuwaandaa ipasavyo mashahidi kabla ya kutoa ushahidi, kujiandaa vema katika kila shauri, kuwajengea uwezo Mawakili wa Serikali ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi ipasavyo, kushirikiana na vyombo vya Upelelezi kama TAKUKURU na Jeshi la Polisi katika maeneo yanayosababisha ushahidi kuwa hafifu na kurekebisha kasoro hizo, kukata rufaa na kuendelea kuzishauri taasisi za Serikali kutoa taarifa mapema kwa Mwanasheri Mkuu wa Serikali katika kila shauri lililofunguliwa Mahakamani, ili kwa pamoja kuangalia namna ya kulinda maslahi ya Serikali katika shauri husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kupitia Bunge hili sheria zinazosimamia Mashirika na Taasisi za Serikali zimekuwa zikirekebishwa na kuweka masharti yanayompatia Mwanasheria Mkuu wa Serikali haki ya kuingilia kati shauri lolote lililofunguliwa dhidi ya Serikali au Taasisi ya Umma kwa lengo la kulinda maslahi ya Serikali.
MHE. AMINA N. MAKILAGI aliuliza:-
Zipo sheria nyingi ambazo zimepitwa na wakati na sheria nyingine ni kikwazo katika kufanikisha shughuli muhimu za Taifa letu.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzitambua sheria zote zilizopitwa na wakati na zile zinazochelewesha ukuaji wa uchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassor Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali wakati wote imekuwa na mkakati wa kuhakikisha kwamba sheria zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinapitiwa na kufanyiwa marekebisho kadri inavyohitajika ili kukidhi mahitaji. Mkakati huo unasimamiwa na Wizara kupitia Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria, Sura ya 171. Tume hii ni chombo mahsusi cha Serikali chenye kazi ya kusimamia mpango huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1983, Tume ya Kurekebisha Sheria imefanikiwa kuandaa ripoti 37 za mapitio na marekebisho ya sheria mbalimbali na kuziwasilisha Serikalini ambapo baadhi yake zilishatungiwa sheria na nyingine zinaendelea kufanyiwa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya mapitio ya sheria ili kubaini sheria zilizopitwa na wakati na hatimaye kupendekeza marekebisho, kutunga sheria mpya au kufutwa kwa sheria ni endelevu na imekuwa ikifanyika muda wote ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika nchi yetu.
MHE. MARIAM N. KISANGI (K.n.y. MHE. ISSA A. MANGUNGU) aliuliza:-
(a) Je, Mabaraza ya Wazee katika Mahakama za Mwanzo yapo kwa mujibu wa sheria?
(b) Mahakama ya Mwanzo Kizuiani hulipa posho za Wazee wa Baraza kiasi cha shilingi 5,000 kila wanapomaliza shauri. Je, kwa nini sasa yapata miezi tisa wazee katika Mahakama ya Mwanzo Kizuiani hawajalipwa posho zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ali Mangungu, Mbunge wa Mbagala lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya Wazee wa Mahakama nchini yamehalalishwa na sheria. Kifungu cha 9(1), (2) na (3) cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu, Sura ya 11 ya sheria za nchi kinaeleza kuwa kutakuwa na matumizi ya Wazee wa Mahakama katika Mahakama ya Mwanzo na Mahakama za Wilaya na Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Mahakama ya Mwanzo ya Mbagala kama ilivyo katika Mahakama nyingine, malipo ya posho za Wazee wa Baraza yamekuwa yakipewa kipaumbele kulingana na upatikanaji wa fedha. Malipo haya yamekuwa yakifanyika kwa mkupuo wa miezi mitatu au minne ili kutoa fursa ya kuweka kumbukumbu za malipo baada ya mchakato wa kukokotoa malipo stahiki kwa kila mlipwaji kulingana na idadi ya mashauri yaliyomalizika ambayo mhusika ameshiriki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Wazee wa Mahakama zote za Mwanzo katika Mkoa wa Dar es salaam ikiwemo Mahakama ya Mwanzo Mbagala walilipwa posho zao zote. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Wazee wa Baraza katika Mahakama ya Mwanzo Mbagala wameshalipwa posho zao kwa kipindi cha Julai hadi Novemba, 2017 kiasi cha shilingi 5,760,000. Vilevile kiasi cha shilingi 2,840,000 ambacho ni madai ya wazee hao kwa kipindi cha Desemba, 2017 hadi Februari, 2018, kipo katika mchakato wa malipo na hivyo hakutakuwa na deni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutoa umuhimu wa kipekee katika malipo ya posho ya Wazee wa Baraza ili kutokwamisha mashauri yaliyopo Mahakamani hususan kwa Mahakama za Mwanzo.
MHE. MACHANO OTHMAN SAID (K.n.y. MHE. USSI SALUM PONDEZA) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itachukua hatua dhidi ya wauzaji wakubwa wa dawa za kulevya wanaoingiza na kuuza badala ya kuakamata waathirika ambao wanahitaji misaada na ushauri nasaha wa kuachana na matumizi ya dawa hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imejipanga na inaendelea kukabiliana na wafanyabiashara wakubwa na wadogo wa dawa za kulevya ambao wote wanasababisha madhara kwa jamii kwa kufanya biashara hiyo. Hadi kufikia Februari, 2018 jumla ya wanyabiashara 3,486 wa dawa za kulevya walikamatwa na kufikishwa mahakamani. Kati ya hao zaidi ya asilimia 30 ni wafanyabiashara wakubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wamekimbia nchini kutokana na ukali wa Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba Tano ya mwaka 2015 na marekebisho yake ya mwaka 2017 pamoja na udhibiti unaofanywa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola. Aidha, Serikali imeendelea kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya kwa kutoa elimu ya madhara ya dawa za kulevya kwa watumiaji na jamii kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa wale walioathirika kwa kutumia dawa za kulevya, wanapopatikana Serikalini imekuwa ikijikita zaidi kutoa ushauri nasaha, tiba na kuwahamasisha kupata tiba hiyo kwani hutolewa bure. Hadi kufikia mwezi Februari, 2018 zaidi ya warahibu 5,560 wamendelea kupata tiba katika vituo vya Serikali, mpango wa Serikali ni kusambaza huduma hii nchi nzima ili kuwafikia waathirika wengi wenye uhitaji.
ASHA MSHIMBA JECHA aliuliza:-
Mradi wa Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi Vijijini (MIVARF) katika Mkoa wetu wa Kusini Unguja umeweza kuwakomboa wananchi kwa kuongeza uzalishaji wa mazao na kuboresha mawasiliano ya barabara na kuweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi. Kwa kuwa mradi huu umeonesha mafanikio na wananchi wamehamasika.
Je, Serikali ipo tayari kuwaongezea mitaji na mafunzo wananchi hao ili waweze kufikia malengo yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Mshimba Jecha, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha inaunga mkono juhudi za wananchi kushiriki katika uchumi wa kilimo kwa kusaidia upatikanaji wa mitaji na kuwapatia mafunzo stahiki. Hatua za kuwawezesha wananchi wa Zanzibar kimtaji zilianza kwa kuvijengea uwezo wa kiutawala na kiutendaji Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) na vikundi vingine vya uzalishaji ili viweze kuratibu na kusimamia kwa ufanisi matumizi ya mitaji itakayopatikana kupitia mikopo inayotolewa na taasisi za kifedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matayarisho yanaendelea ili kuvipatia vikundi vya wazalishaji ambavyo tayari vimehakikiwa na uwezo wao baada ya ziara ya uongozi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kutembelea Zanzibar mwezi Mei, 2017. Benki hii ni mshiriki mkubwa wa MIVARF, ambayo huendesha mfuko wa dahamana (Guarantee Fund) wa mikopo utakaofanya benki kuwakopesha wakulima kwa masharti nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekit, tayari Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango na Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) wamesaini makubaliano ya uendeshaji wa mfuko wa dhamana tarehe 3 Novemba, mwaka 2017. Kwa kupitia makubaliano hayo, Serikali tayari imetoa shilingi bilioni 22 kwa TADB ili kuanza utekelezaji kwa kushirikisha benki za biashara kufikisha huduma ya mikopo kwa makundi mbalimbali. TADB walishaanza utaratibu huu kwa kutangaza kwenye magazeti ili kupata benki zitakazoshiriki. Nawashauri wananchi wote watumie fursa hii adhimu kujipatia mikopo ili kupanua shughuli zao za maendeleo na kujiongezea kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa kitoa mafunzo mbalimbali kwa wananchi kupitia mradi wa MIVARF ili waweze kuyafikia masoko yenye tija. Mafunzo hayo ni pamoja mbinu bora za kilimo (good agricultural practice), uongezaji thamani mazao na jinsi ya kuyafikisha masoko yenye tija na kukuza na uimarishaji Vikundi vya Akiba na Mikopo (SACCOS). Programu kupitia kwa watoa huduma (Business Coaches) inaendelea kutoa mafunzo haya kwa wananchi hasa katika Nyanja za kuongeza thamani mazao na kuyafikisha masoko.
MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED aliuliza:-
(a) Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha inashirikisha sekta binafsi ili kufikia dhamira ya kuwa nchi ya viwanda na yenye uchumi wa kati?
(b) Je, Serikali haioni kwamba dhamira hiyo ya kuelekea nchi ya viwanda na uchumi wa kati ni ndoto tu na haiwezi kufikiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima ya mpango wa pili wa miaka mitano ni kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Katika mpango huo, imebainishwa wazi kuwa ni jukumu la sekta binafsi kujenga viwanda. Serikali inabaki na jukumu la kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na ufanyaji biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili Serikali iweze kutekeleza majukumu ya ujenzi wa viwanda kwa ufanisi, Serikali imetekeleza yafuatayo; kwanza, kuboresha mazingira ya uwekezaji na ufanyaji biashara kuhakikisha vikwazo vyote vinaondolewa.
Pili, kupitia Wizara na mamlaka husika kutenga maeneo ya kujenga viwanda kuanzia ngazi ya vijiji mpaka ngazi ya Taifa; tatu, kuweka miundombinu ya umeme, barabara, maji, mawasiliano na usafiri wa anga; nne, kupitia taasisi kama SIDO, TIRDO, TANTRADE na kutoa elimu na mwongozo wa kujenga viwanda na tano, kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza katika maeneo ya kipaumbele.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Dira ya Taifa 2025 ni kuona nchi yetu inakuwa Taifa lenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Ili kutimiza dhamira hiyo, tunatekeleza Mipango ya Maendeleo mitatu ya miaka mitano mitano. Pia upo mkakati wa fungamanisho la maendeleo ya viwanda ukiongoza utekelezaji wa mipangi tajwa hapo juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini ya utekelezaji wa mipango mitatu ya maendeleo ambapo sasa tumefikia nusu, inaonesha dhahiri kuwa Taifa letu litafikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 likiongozwa na Sekta ya Viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati kuna hitaji kubwa la uwekezaji katika viwanda vinavyotegemea malighafi kutoka kwa wananchi, mpaka sasa maendeleo ni mazuri kwa viwanda vinavyozalisha biashara zinazotumika kwa wingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa uchumi wa viwanda ni jambo ambalo limeshaanza na kufikia uchumi wa kati mwaka 2025 ni jambo linalowezekana.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza:-
(a) Je, Serikali inazo takwimu za kuaminika za vijana waliohitimu vyuo mbalimbali ambao hawajaweza kujiajiri au kuajiriwa;
(b) Je, ni taaluma zipi zina fursa nyingi za zipi zina fursa chache za kujiajiri au kuajiriwa baada ya kuhitimu?
(c) Je, kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita ni ajira ngapi zilipatikana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Joseph Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali ina takwimu sahihi na za kuaminika za vijana waliohitimu vyuo mbalimbali, lakini hawajaweza kujiajiri au kuajiriwa ambazo hutumika katika kupanga na kutathmini utekelezaji wa programu zinazohusiana na masuala ya ajira. Takwimu hizo huptikana kupitia tafiti za nguvu kazi na tafiti za hali ya ajira na mapato zinazofanywa na ofisi ya Taifa ya Takwimu, pamoja na zinazofanywa na Taasisi za Elimu, kama vile Tracer Studies. Kwa mujibu wa utafiti wa nguvu kazi nchini, vijana 65,614 ambao ni wahitimu wa vyuo mbalimbali hawakuwa wamejiajiri wala kuajiriwa mwaka 2014.
(b) Mheshimiwa Spika, taaluma zenye fursa nyingi za kuajirika ni pamoja na fani za afya ya binadamu zikiwemo utabibu, uuguzi, ufundi sanifu wa maabara, ualimu na ufundi. Aidha, taaluma zenye fursa chache za ajira ni pamoja na masomo ya utawala, biashara na rasilimali watu. Napenda kuchukua fursa hii kuwashauri wanafunzi kusoma masomo ya sayansi kwa kuwa yana fursa nyingi zaidi za ajira hususani wakati huu ambao Taifa linaelekea kuwa nchi ya viwanda.
(c) Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuanzia mwaka 2015 hadi 2017/2018, jumla ya ajira mpya 1,336,957 zilipatikana kama ifuatavyo:-
Kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Serikali ajira 593,986, sekta binafsi ajira 571,073 na Serikalini ajira 171,898. (Makofi)
MHE. ALI SALIM KHAMIS (K.n.y. MHE. ABDALLAH HAJI ALI) aliuliza:-
Mfumo wa vyama vingi Tanzania ulirudishwa nchini hata baada ya Tume ya Nyalali kubaini ni asilimia ishirini tu ya Watanzania ndio waliotaka mabadiliko.
(a) Je, baada ya miongo miwili na nusu ni faida gani za mfumo huo zilizopatikana?
(b) Je, ni changamoto zipi ambazo zimejitokeza na kuwa mtihani katika suala hili la vyama vingi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Haji Ali, Mbunge wa Kiwani lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa kama ilivyokuwa mfumo wa demokrasia ya chama kimoja cha siasa una faida na changamoto zake. Tangu mfumo huo uliporejeshwa mwaka 1992 kumekuwa na faida zifuatazo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; mfumo umewezesha kupanuka kwa wigo wa demokrasia ya siasa ya vyama vingi ambapo hadi sasa kuna vyama vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; kuongezeka kwa ushiriki wa wananchi katika chaguzi za kisiasa kwa ngazi zote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu; kumekuwepo kwa ongezeko la uhuru wa kuchagua wagombea wa vyama vya siasa vilivyonadi na kushindanisha sera zao wakati wa kampeni za uchaguzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nne; ni kuongezeka kwa uwazi na uwajibikaji katika utendaji wa Serikali.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto zilizojitokeza zikiambatana na mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja; ni kuongezeka kwa gharama za kuendesha chaguzi za kisiasa katika ngazi mbalimbali za uchaguzi. Aidha, kuongezeka kwa gharama za ruzuku ya Serikali kwa vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu na uwakilishi Bungeni na katika ngazi ya Serikali za Mitaa wawakilishi katika Baraza la Madiwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; kuibuka kwa makundi ndani ya baadhi ya vyama vya siasa ambapo viongozi wamekuwa hawafanyi siasa za kistaarabu na kuchochea vurugu katika jamii, hasa nyakati za Kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge, Chaguzi ndogo za marudio pamoja na Chaguzi za ngazi ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu; ni kushuka kwa uzalendo wa wananchi kutokana na baadhi ya wanasiasa kushabikia mitazamo na kampeni hasi dhidi ya Serikali iliyopo madarakani.
MHE. JOYCE B. SOKOMBI aliuliza:-
Wafanyakazi katika Mgodi wa Nyamongo hawalipwi mshahara bali posho tu.
(i) Je, Serikali inasema nini juu ya wafanyakazi hao?
(ii) Je, kwa nini wafanyakazi hao hawalipwi mishahara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA, NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joyce Bitta Sokombi, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Dhahabu wa Nyamongo unamilikiwa na Kampuni ya ACACIA. Kwenye mgodi huo kuna makundi ya aina mbili ya wafanyakazi. Kwanza, kuna wafanyakazi walioajiriwa na Kampuni ya ACACIA na pili kuna wafanyakazi walioajiriwa na makampuni yanayopewa kazi na ACACIA (Sub-Contractors).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa wafanyakazi walioajiriwa na ACACIA wao hawalipwi posho bali hulipwa mishahara kwa mwezi. Kwa wafanyakazi walioajiriwa na makampuni mengine (Sub-Contractors) wao hulipwa mishahara kwa kuzingatia aina ya mkataba wa ajira na asili ya kazi anayofanya mfanyakazi kwa kuzingatia sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ofisi yangu kupitia Idara ya Kazi itaendelea kufanya kaguzi za kazi katika maeneo mbalimbali ya kazi nchini ikiwemo Kampuni ya ACACIA kwa lengo la kuwatambua waajiri ambao hawazingatii matakwa ya sheria za kazi.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-
Liwale ni Wilaya ya zamani hapa nchini lakini hadi leo haina jengo la Mahakama zaidi ya jengo lililorithiwa toka iliyokuwa Mahakama ya Mwanzo Liwale.
Je, ni lini Serikali itajenga jengo la Mahakama Liwale sambamba na nyumba za watumishi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Kuchauka, Mbunge wa Liwale, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakiri kwamba ni kweli Wilaya ya Liwale haina jengo la Mahakama ya Wilaya. Aidha, kama alivyoainisha Mheshimiwa Mbunge ni kweli jengo la Mahakama ya Mwanzo ya Liwale Mjini ambalo linatumika sana kutolea huduma za Mahakama ya Wilaya na ya Mwanzo ni chakavu na hivyo kuhitaji kujengwa upya. Katika mpango wa ujenzi, tumepanga kujenga kujenga Mahakama ya Wilaya ya Liwale kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ambalo pia litatumika na Mahakama ya Mwanzo Liwale Mjini, sambamba na ujenzi wa nyumba ya Hakimu kutegemea upatikanaji wa fedha.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI aliuliza:-
Miongoni mwa matakwa ya Serikali ni kuwawezesha vijana na wanawake kiuchumi. Je, Serikali inatekelezaje suala hilo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kutokana na kutungwa kwa Sera ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 pamoja na sheria mbalimbali zinazohusu uwezeshaji wananchi kiuchumi, Serikali inatekeleza Mpango wa Kuwawezesha Wananchi Kiuchumi kama ifuatavyo:-
Moja, ni kutambua umuhimu wa mafunzo ili kuwawezesha wanawake na vijana kukuza shughuli zao za kiuchumi na kujikwamua kimaisha.
Pili, ni kuhamasisha vijana na wanawake kujiunga na vikundi vya kiuchumi vya Vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS) ili kujipatia kwa urahisi mitaji ya kuanzisha na kuendelez amiradi ya kibiashara.
Tatu, ni kuwekeza katika Sekta ya Ufundi stadi ili vijana wanaohitimu waweze kuwa na ujuzi wa kuweza kujiajiri.
Nne, kuanzisha miradi mikubwa ya maendeleo ambayo ni chanzo cha ajira kwa wanawake na vijana.
Tano, ni kuanzisha Benki ya Wanawake kwa lengo la kutoa mikopo kwa wajasiriamali wanawake na pia uwepo wa mifuko maalum ya uwezeshaji wa akina mama (WDF) na vijana (YDF).
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-
Vijana wengi wanakosa sifa za kuajiriwa kwa kukosa uzoefu kazini.
Je, Serikali haioni haja ya kutungwa kwa Sera ya Mafunzo kwa Vitendo Kazini kwa wahitimu wa elimu ya juu na vyuo vya ufundi (Internship Policy for Higher Learning Institutions and Technical Colleges Graduates) ili vijana waweze kupata ujuzi utakaoendana na mahitaji ya soko la ajira?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha pengo la ujuzi (skills mismatch) kati ya ujuzi walinao wahitimu na ule unaohitajika katika soko la ajira unazibwa. Ni kweli Serikali imeona kuna haja ya kuwa na miongozo ya kisera kama alivyoshauri Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba ambapo kupitia ofisi yangu tumeandaa Mwongozo wa Kitaifa wa Mafunzo kwa Vitendo kwa Wahitimu (National Internship Guidelines). Mwongozo huu unasaidia wadau kuandaa, kutekeleza, kusimamia na kuratibu mafunzo ya uzoefu kazini kwa wahitimu. Mwongozo huu ulizinduliwa mwezi Septemba, 2017 na kuanza kutumika rasmi. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 zaidi ya nafasi 750 zimetolea na waajiri mbalimbali kuwezesha wahitimu kufanya mafunzo kwa vitendo.
Mheshimiwa Spika, kufanya marekebisho ya Sera ya Taifa ya Ajira ya mwaka 2008 ili kuendana na mahitaji ya sasa. Sera mpya pamoja na mkakati wa utekelezaji wake ipo katika hatua za mwisho ambapo inatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Juni, 2018. Miongoni mwa matamko mahsusi ya sera hii ni pamoja na kusisitiza kuwepo kwa mafunzo kwa vitendo kazini kwa wahitimu wa vyuo. Baada ya kupitishwa sera hii, suala la mafunzo ya vitendo kazini kwa wahitimu litawekwa katika Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa wito kwa waajiri wote nchini kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa programu ya mafunzo kazini kwa wahitimu kwa kutoa fursa kwa vijana wahitimu kujifunza katika maeneo yao ya kazi.
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza ajira kwa Watanzania waliohitimu Vyuo bila kujali kada walizosomea ambao mpaka sasa wapo mitaani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha wahitimu wa vyuo wanapata ajira za kuajiriwa na kujiajiri Serikali imeendelea na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuongeza fursa za ajira kama ifuatavyo:-
(a) Kusimamia utekelezaji wa sera ya uchumi wa viwanda kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji katika viwanda nchini kupitia sekta binafsi kwa lengo la kutengeneza nafasi nyingi za ajira.
(b) Utekelezaji wa miradi mikubwa nchini, ikiwemo mradi wa bomba la mafuta, ujenzi wa reli ya kisasa na ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa nishati kupitia miradi mbalimbali ambayo yote kwa ujumla itasaidia kupanua wigo wa nafasi za ajira.
(c) Kutoa elimu kwa vijana kuhusiana na masuala ya ajira kwa lengo la kuongezea ufahamu mpana katika masuala ya ajira na kuongeza uwezo wa kujiamini katika kujiajiri kupitia sekta mbalimbali za kilimo, ufugaji, uvuvi na ujasiliamali.
(d) Kuandaa na kusimamia utekelezaji wa programu ya Taifa kukuza ujuzi nchini ambayo ina lengo ya kutoa mafunzo kwa vitendo sehemu ya kazi kwa wahitimu wa vyuo. Mafunzo haya yatawapatia wahitimu wa vyuo ujuzi unaohitajiwa na waajiri, hivyo kuwawezesha kuajirika.
(e) Kuendelea kuwezesha vijana kujiajiri kwa kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu kupitia Mfuko Maendeleo ya Vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji programu ya Taifa kukuza ujuzi ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kuwezesha vijana kuajirika na kupunguza tofauti ya ujuzi uliopo katika nguvu kazi na mahitaji ya soko la ajira.
MHE. SAADA MKUYA SALUM (K.n.y. ANGELINA ADAM MALEMBEKA) aliuliza:-
Baadhi ya Wabunge wa Majimbo walihama Vyama vyao na kujiunga na vyama vingine hivyo Chaguzi Ndogo zikafanyika na Chama cha Mapinduzi kikashinda Majimbo hayo:-
(a) Je, ni nini hatma ya Wabunge wa Viti Maalum walioingia Bungeni kupitia asilimia za Majimbo yao ya Uchaguzi?
(b) Kwa kuwa Chama cha Mapinduzi kimeongeza idadi ya Majimbo zaidi, je, ni lini Wabunge wa Viti Maalum wapya wa CCM kupitia Viti Maalum wataingia Bungeni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Ibara ya 78(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 imeainisha bayana kuwa vyama vya siasa vilivyoshiriki Uchaguzi Mkuu na kupata angalau asilimia tano ya kura zote halali za Wabunge vitapendekeza kwa Tume ya Uchaguzi majina ya wanawake kwa kuzingatia uwiano wa kura ambazo kila chama kimepata katika uchaguzi wa Wabunge ili Tume iweze kuteua miongoni mwao Wabunge wa Viti Maalum. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa msingi wa sheria hii, idadi ya Wabunge wa Viti Maalum kwa kila chama inapatikana wakati wa Uchaguzi Mkuu ambao hufanyika kila baada ya miaka mitano. Hivyo, mabadiliko yoyote yanayotokea wakati wa Uchaguzi Mdogo hayaathiri idadi ya Viti Maalum vya chama husika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali imeendelea kupokea maoni na ushauri kuhusu jambo hili hivyo kutokana na hali ilivyo hivi sasa, Katiba na Sheria za Nchi vitaendelea kuwa msingi mkuu wa ufafanuzi na mgawanyo wa Viti Maalum Bungeni.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-
Ili kuinusuru amani ya nchi yetu baada ya Uchaguzi Mkuu ni kuwa na Tume Huru ya uchaguzi:-
Je, ni lini itaanzishwa Tume Huru ya Uchaguzi kwa mujibu wa sheria?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeanzishwa kwa mujibu wa Ibara ya 74(1)-(15) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo imeainisha na kufafanua kuhusu muundo, majukumu pamoja na uhuru wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi katika utekelezaji wa majukumu yake ya msingi.
Mheshimiwa Spika, tangu kuanzishwa kwa Mfumo wa Vyama vingi vya Siasa nchini mwaka 1992, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeratibu na kuendesha kwa ufanisi chaguzi tano za Rais, Wabunge na Madiwani pamoja na chaguzi ndogo mbalimbali za Wabunge na Madiwani.
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huu, Tanzania tayari inayo Tume Huru ya Uchaguzi.
MHE. FAIDA MOHAMMED BAKARI aliuliza:-
Kiswahili ndiyo lugha ya Taifa letu na kinapaswa kutumika katika nyanja zote ili kukipa hadhi yake:-
Je, kwa nini baadhi ya Mahakama nchini zinatumia lugha ya Kiingereza wakati zinapoendesha mijadala yake na katika kutoa hukumu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Faida Bakari, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya lugha katika Mahakama zetu yamewekwa kwa mujibu wa sheria. Kwa mujibu wa kifungu cha 13(1) na (2) cha Sheria ya Mahakama za Mahakimu, Sura ya 11 (The Magistrates Courts Act, Cap 11) lugha inayotumika kuendesha kesi katika mahakama za mwanzo ni Kiswahili. Vile vile lugha itakayotumika katika mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya ni Kiswahili au Kiingereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, shauri linaweza kuendeshwa kwa lugha yoyote kwa maelekezo ya Hakimu anayeendesha kesi katika Mahakama hizo, japokuwa kumbukumbu za shauri na maamuzi zinapaswa kuandikwa katika lugha ya kiingereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika kwa mujibu wa Kanuni ya Pili ya Kanuni za Lugha za Mahakama na Kanuni ya Tano ya Kanuni za Mahakama ya Rufani ya Mwaka 2009, lugha itakayotumika kuendesha mashauri katika Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani ni Kiswahli au Kiingereza kutegemea na maelekezo ya Jaji au Mwenyekiti wa Jopo la Majaji japokuwa kumbukumbu na maamuzi ya shauri vinapaswa kuandikwa katika lugha ya Kiingereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuendelea kutumika kwa Kiswahili katika Mahakama zetu na hukumu kuandikwa kwa Kiingereza kunatokana na kwamba Tanzania ni Mwanachama wa Jumuiya ya Madola na inafuata mfumo wa Common Law. Kwa kuandika hukumu kwa lugha ya Kiingereza imewezesha Mahakama za nchi nyingine za Jumuiya ya Madola kutumia hukumu zetu kama rejea na vivyo hivyo Tanzania kutumia hukumu za nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa mashauri katika Mahakama zetu unaruhusu kutumia lugha zote mbili, Kiswahili au Kiingereza na Mahakama zetu zimekuwa zikizingatia hilo.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO aliuliza:-
Baadhi ya Mahakama za Mwanzo kama vile Matemanga, Napakanya na nyingine nyingi ni chakavu na hazipati fedha kwa ajili ya ukarabati hali inayosababisha Mahakimu na watumishi wengine kufanya kazi katika mazingira magumu sana:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa Mahakama hizo?
NAIBU WAZIRI OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sikudhani Yassin Chikambo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Mbunge kuwa kwa baadhi ya maeneo watumishi wetu wanafanya kazi katika mazingira magumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tunduru ina jumla ya Mahakama za Mwanzo tisa ambazo karibu zote majengo yake ni ya zamani sana na mengi yakiwa ni yale yalioachwa na mkoloni. Kati ya Mahakama za Mwanzo tisa zilizopo, majengo ambayo angalau yana hali nzuri ni matatu tu, ya Nandembo, Mlingoti na Ndesa. Mengine yaliyosalia yakiwemo ya Matemanga na Nakapanya ni chakavu sana, hayafai kukarabati na hivyo yamepangwa kujengwa upya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa ujenzi wa mahakama, Mahakama ya Mwanzo Nakapanya na Mahakama ya Wilaya ya Tunduru zimepangwa kujengwa mwaka 2019/2020 kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza ugonjwa wa UKIMWI kufikia mwaka 2030 kama Azimio la Umoja wa Mataifa linavyoelekeza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kumaliza ugonjwa wa UKIMWI ifikapo mwaka 2030 kama ilivyoazimiwa na Umoja wa Mataifa, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali kama ifuatavyo:-
Moja, ni kuendelea kutekeleza mkakati wa nne wa Taifa wa kudhibiti UKIMWI Tanzania wa mwaka 2018 mpaka 2023. Mkakati huu umeainisha maeneo saba ya kimkakati yatayowezesha kufikia malengo ya sirufi tatu ikiwa ni ya kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kuratibu mipango ya sekta zote katika mapambano dhidi ya UKIMWI.
Pili, kuhamasisha upatikanaji na utumiaji wa kondomu; tatu, kutokomeza maambukizi ya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, nne, kuendeleza tohara ya hiari ya kitabibu kwa wanaume kwenye mikoa yenye kiwango kidogo cha tohara; tano, kinga ya tiba, matumizi sahihi na endelevu ya ARV’s na sita ni mkakati wa kuzuia maambukizi mapya ya UKIMWI kwenye makundi yaliyo katika hatari ya kuambukizwa. Makundi haya ni pamoja na wasichina balehe na wanawake vijana, wanaojidunga dawa za kulevya, wasichana wanaouza ngono, wafungwa, wavuvi, wachimbaji wa madini kwenye migodi na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuendeleza usimamizi wa Mfuko wa Dhamana wa UKIMWI (AIDS Trust Fund) ili kuimarisha ukusanyaji wa rasilimali fedha na nyingine kupitia vyanzo vya ndani vya nchi ikiwa ni jitihada za kupunguza utegemezi wa fedha za wafadhili nje. Tatu, kurekebisha Sera ya Taifa ya UKIMWI ya mwaka 2001 pamoja na sera nyingine husika. Vilevile sheria mbalimbali ili zitoe miongozo ya programu na mifumo ya kudhibiti maambukizi mapya ya UKIMWI nchini. Na mwisho ni kuhamasisha wanaume kupima VVU.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge kuwa UKIMWI ni janga linalotukabili zote kama Taifa. Hivyo sisi tukiwa kama wawakilishi wa wananchi tunao wajibu wa kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia katika kupunguza na hatimaye kudhibiti maambukizi mapya ya VVU.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y. MHE. HAMIDU H. BOBALI) aliuliza:-
Kumekuwa na raia wengi kutoka Msumbiji katika Jimbo la Mchinga hasa Vijiji vya Kilangala B, Butamba, Mvuleni, Kitolambwani na Kikonde ambao wamekuwa wakishiriki uchaguzi katika nchi zote mbili Tanzania na Msumbiji.
(a) Je, raia hao ni Watanzania au wa Msumbiji?
(b) Je, Serikali imepitisha utaratibu wa uraia pacha na kuwapa watu maalum?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Ibara ya 5(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 raia wa Tanzania aliyetimiza umri wa miaka 18 anayo haki ya kupiga kura katika uchaguzi unaofanywa Tanzania. Aidha, Ibara ya 5(2) ya Katiba hairuhusu mtu mwenye uraia wa nchi nyingine (raia pacha) kushiriki katika shughuli za uchaguzi ikiwemo kupiga kura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ili mtu aweze kupiga kura lazima awe ameandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura lililoanzishwa chini ya ibara ya 5(3)(a) ya Katiba. Uandikishaji wa wapiga kura unapokamilika, daftari la awali huwekwa wazi kwa mujibu wa kifungu cha 24 cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 ili kukaguliwa na wananchi. Kifungu cha 24(1) cha sheria hiyo kinatoa fursa kwa mtu aliyejiandikisha kuweka pingamizi dhidi ya mtu mwingine aliyendikishwa kwenye daftari ikiwa imebainika kuwa hana sifa ya kuandikishwa kwa kutokuwa raia wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali hii, sheria zetu hazijaruhusu uraia pacha na hakuna watu maalum waliopewa uraia wa aina hiyo.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y. MHE. GODBLESS J. LEMA) aliuliza:-
Mishahara ya taasisi za umma hupangwa na Serikali. Utaratibu huo wa Serikali kupanga mishahara ya watumishi wake huathiri pia upangaji na ukadiriaji mishahara katika taasisi binafsi.
Je, Serikali haioni haja ya kuboresha mishahara yake na kuzielekeza taasisi binafsi kulipa mishahara inayoendana na hali ya maisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema, Mbunge wa Arusha Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuboresha mishahara ya watumishi wake wa kada mbalimbali kila mwaka kwa kutoa nyongeza kulingana na kanuni za kiutumishi ikiwa ni pamoja na muda wa kukitumikia cheo au kupandishwa cheo mtumishi. Sambamba na utaratibu huu Serikali imeunda Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara ambayo hufanya utafiti kwa kuzingatia hali halisi ya maisha na uwezo wa kibajeti wa Serikali na kumshauri waziri mwenye dhamana na masuala ya utumishi wa umma kupanga kima cha chini cha mshahara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7 ya mwaka 2004 kama ilivyoboreshwa mwaka 2015 imeanzisha Bodi ya Mishahara ya Sekta Binafsi ambayo ina jukumu la kufanya utafiti kwa kuzingatia hali halisi ya gharama za maisha na masuala mengine ya kiuchumi na kupendekea kiwango cha kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi. Serikali hivi sasa ipo katika hatua za kuiwezesha bodi hiyo kufanya utafiti ili kuhakikisha utafiti huo unakidhi matakwa ya sheria, kanuni na taratibu zinazokubalika hapa nchini na viwango vya kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika kuhakikisha maslahi ya wafanyakazi na ukuzaji wa tija na uzalishaji sehemu za kazi unaboreshwa kila mwaka, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004 kama ilivyorekebishwa mwaka 2015, imeweka utaratibu kwa waajiri na wafanyakazi katika sekta binafsi kujadiliana na kufunga mikataba ya hali bora mahali pa kazi kwa lengo la kuboresha maslahi yao ikiwemo mshahara na stahiki nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia utaratibu huu wa kisheria waajiri katika sekta binafsi wanaruhusiwa kuwalipa viwango vya mishahara hata zaidi ya kiwango kinachowekwa kama kima cha chini cha mshahara pale ambapo wanaona kwa kufanya hivyo itaongeza motisha kwa wafanyakazi wao kufanya kazi kwa bidii na kujituma kwa lengo la kuongeza tija katika kuzalisha mali au katika kutoa huduma.
MHE. SILAFU J. MAUFI aliuliza:-
Serikali inafahamu kuwa michezo ni afya na ni ajira pia, lakini mikoa kadhaa hapa nchini ina viwanja visivyokidhi hadhi ya kitaifa na kimataifa na hata kasi ya kuibua vipaji vipya imedorora katika Mikoa ya Rukwa, Tabora, Iringa, Kigoma na kadhalika.
Je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kushirikiana na wamiliki wa viwanja hivyo kuvikarabati na kuviboresha kufikia hadhi stahiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE K.n.y. WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Silafu Jumbe Maufi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba ujenzi wa miundombinu ya michezo ni jambo muhimu sana katika kuendeleza vipaji vya wanamichezo na ndiyo sababu ya Serikali kujenga viwanja changamani vikubwa viwili nchini ambavyo ni Kiwanja cha Uhuru na Kiwanja cha Taifa, Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya kazi ya ujenzi wa kiwanja kikubwa cha Ngamani cha tatu Jijini Dodoma yanaendelea. Hata hivyo Serikali haiwezi peke yake kujenga miundombinu ya kisasa kwa michezo yote bila mchango wa Halmashauri zetu, taasisi za umma, asasi na kampuni binafsi na vilevile mashirikisho na vyama husika vya michezo mbalimbali hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, pale penye jitihada bayana za kujenga miundombinu ya michezo, Serikali daima imekuwa mstari wa mbele kusaidia juhudi hizo. Utaratibu mkubwa wa viwanja vya Kaitaba - Kagera na Nyamagana - Mwanza, ni matokeo ya mazingira mazuri ya ushirikishaji yaliyowekwa na Serikali kati ya wadau soka, Shirikisho la Soka nchini na Shirikisho la Soka la Dunia.
Aidha, ukarabati mkubwa wa viwanja vya Namfua - Singida; Samora Machel - Iringa na Majaliwa Stadium - Ruangwa ni matokeo ya mazingira mazuri ya ushirikiano yaliyowekwa na Serikali kati ya wadau, TFF na Wizara yenye dhamana ya michezo. Naomba nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu wetu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mbunge) kwa kuonesha mfano wa kuhamasisha Halmashauri yake na wananchi wa Ruangwa kuunganisha nguvu na kujenga uwanja wa Majaliwa Stadium. (Makofi)
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA (K.n.y. MHE. MHE.ANNA R. LUPEMBE) aliuliza:-
Je, ni lini Redio Tanzania (TBC) itasikika katika Kata za Ilela na Ilunde Wilayani Mlele?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE K.n.y. WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia TBC imeendelea na jitihada za kupanua usikivu katika Mikoa na Wilaya ambazo bado hazina usikivu au kuwa na usikivu hafifu wa redio. Katiba bajeti ya mwaka 2016/2017 TBC ilitengewa kiasi cha shilingi bilioni moja kwa ajili ya upanuzi wa usikivu katika Wilaya tano za mpakani mwa nchi. Maeneo ambayo mitambo imefungwa na matangazo ya redio kuwashwa ni Rombo, Nyasa, Tarime, Kibondo na Namanga. Serikali inaendelea na utaratibu huo wa kuongeza usikivu kwenye maeneo yasiyo na usikivu mzuri katika Mikoa ya Katavi, Njombe, Simiyu na Songwe.
Mheshimiwa Spika, mkakati wa Serikali ni kujenga mitambo ya redio katika Mikoa hii katika bajeti ya mwaka 2019/2020 na katika bajeti ya mwaka 2018/2019 TBC imetengewa kiasi cha shilingi bilioni tano kwa ajili ya ujenzi wa studio za redio na television Makao Makuu ya nchi Jijini Dodoma.
MHE. ANDREW J. CHENGE (K.n.y. MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE) aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta baadhi ya sheria zilizopitwa na wakati Bungeni ili ziweze kupitiwa upya ziendane na wakati uliopo hasa zikiwemo Sheria za Usalama Barabarani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Kavuu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa sheria za nchi zinakidhi mahitaji ya wakati, Serikali imekuwa ikifanya mapitio ya sheria ya kupitia Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania iliyopo chini ya Wizara ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Spika, Tume hii imekuwa ikifanya mapitio na tafiti mbalimbali ambazo zimekuwa ni msingi wa marekebisho ya sheria au kutungwa kwa sheria mpya hapa nchini. Kazi ya mapitio ya sheria ni endelevu na Serikali itaendelea kuwasilisha Bungeni miswada ya sheria ambayo inalenga kurekebisha sheria za nchi au kutunga sheria mpya ili kukidhi matakwa ya wakati.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA (K.n.y. MHE. ZUBEDA H. SAKURU) aliuliza:-
Sherehe za Mwenge wa Uhuru zimeendelea kutumia fedha nyingi za walipa kodi huku Watanzania wengi wakiwa na maisha duni. Je, Serikali haioni umuhimu wa kurudisha Mwenge wa Uhuru katika Makumbusho ya Taifa na kuzifuta
sherehe hizo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zubeda Hassan Sakuru, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenge wa Uhuru ni chombo kilichoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1961 ikiwa ni tunu na ishara ya kuwepo kwa Taifa huru la Tanganyika. Dhana na falsafa ya Mwenge wa uhuru inatokana na maono ya mbali kupitia kwenye maneno yaliyosemwa tarehe 9 Desemba, 1961 nanukuu:-
“Sisi tumekwisha uwasha Mwenge wa Uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, ulete upendo mahali penye chuki na heshima mahali palipojaa dharau”
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni umuhimu wa kuweka Mwenge wa Uhuru katika makumbusho ya Taifa na kuzifuta sherehe zake kwa sababu zifuatazo:-
a) Mbio za Mwenge wa Uhuru huwakumbusha Watanzania falsafa nzito ya Mwenge wa Uhuru inayotoa taswira ya Taifa ambalo Waasisi wetu walitaka kulijenga Taifa lenye amani, linalojitegemea na lenye kuheshimu misingi ya utu na usawa wa binadamu. (Makofi)
b) Mwenge wa Uhuru kupitia mbio zake umekuwa ni chombo cha kuchochea maendeleo ya wananchi, kwa mfano, kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, miradi ya maendeleo 6,921 yenye thamani ya shilingi trilioni 2.5 ilizinduliwa na kuwekewa mawe ya msingi. (Makofi)
c) Kila mwaka, Mbio za Mwenge huambatana na ujumbe maalum unaohamasisha masuala muhimu ya Kitaifa kwa wananchi nchi nzima. Kwa mfano, kwa mwaka jana 2017 ujumbe ulikuwa “Shiriki kukuza uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu”. Mwaka huu wa 2018 ujumbe ni “Elimu ni ufunguo wa maisha, wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu”. Aidha, kila mwaka wananchi hukumbushwa kuendelea na mapambano dhidi ya UKIMWI, malaria, rushwa na dawa za kulevya. (Makofi)
d) Mwenge wa Uhuru unaimarisha Muungano wetu, Mwenge wa Uhuru huzunguka nchi nzima Tanzania Bara na Zanzibar. Wanaokimbiza Mwenge wa Uhuru wanatoka sehemu mbili za Muungano. Kwa kufanya hivyo, Mwenge wa Uhuru unazidi kutuunganisha kama watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, si kweli kwamba Mwenge wa Uhuru unatumia fedha nyingi za walipa kodi. Kwa mfano, kwa mwaka 2017, Serikali ilitenga shilingi milioni 463 kugharamia shughuli za Mwenge wa Uhuru ukilinganisha na kiasi cha miradi 1,582 iliyozinduliwa yenye thamani ya shilingi trilioni 1.1 ni dhahiri kuwa hoja ya gharama kuwa kubwa siyo ya msingi. (Makofi)
MHE. JOHN J. MNYIKA (K.n.y. MHE. JOHN W. HECHE) aliuliza:-
Wilaya ya Tarime ni miongoni mwa Wilaya zinazoongoza kwa wakazi wake kuwa na kesi za kubambikiwa hasa za wizi wa kutumia silaha na mauaji, kitendo kinachokuwa na sura ya kumpa mtuhumiwa wakati mgumu sana kupata msaada wa kisheria.
Je, ni kwa nini Serikali isisaidie upatikanaji wa msaada wa kisheria kwa mahabusu hao ambao kitakwimu ni wengi katika Gereza la Tarime kuliko mashauri mengine yoyote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ATHONY P. MAVUNDE K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Wegesa Heche, Mbunge wa Tarime Vijijii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa utoaji wa msaada wa kisheria kwa watu walioko vizuizini. Kwa kutambua hilo, Sheria ya Msaada wa Kisheria ya mwaka 2017 imetamka wazi kuwa Jeshi la Polisi na Magereza yanapaswa kuweka mazingira ya kuwezesha upatikanaji wa msaada wa kisheria kwa watu walioko vizuizini. Vile vile, kanuni za Sheria hiyo (GN.No. 92018) zimeweka utaratibu wa kufuatwa na Wakuu wa Vituo vya Polisi katika kufanikisha suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kufanikisha upatikanaji wa huduma hii, Wizara imefanya vikao vya mashauriano na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa nyakati tofauti tangu mwaka 2017 kwa lengo la kuweka utaratibu mzuri wa kutekeleza matakwa ya sheria. Hadi kufikia leo tayari rasimu ya mwongozo wa kutoa huduma katika Vituo vya Polisi na Magereza umeandaliwa na utawasilishwa kwa wadau. Pia hivi karibuni Wizara ya Katiba na Sheria itasaini hati ya makubaliano na Wizara ya Mambo ya Ndani kwa ajili ya kushirikiana katika eneo hili. Jitihada hizi za Serikali zinalenga kuondoa changamoto ya upatikanaji wa msaada wa kisheria katika magereza yote nchini pamoja na gereza la Tarime.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kumwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, pindi Mwongozo huu utakapokamilika yamkini Wilaya ya Tarime inaweza kuwa miongoni mwa wilaya ambazo zitanufaika na huduma hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Magereza kwa upande wake yamekuwa na utaratibu wa kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa muda mrefu sasa kwa makubaliano yaliyofanyika kati yao na Shirika la Envirocare ambalo lilikuwa likitoa msaada wa kisheria kwa mahabusu na wafungwa katika baadhi ya mikoa hapa nchini.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Katika Bunge la Kumi kulikuwepo na mjadala kuhusu kuanzishwa kwa kilimo cha makambi ambapo vijana wengi wangepelekwa makambini, wangepewa mikopo ya pembejeo na kuzalisha mazao kwa wingi. Mazao hayo yangeuzwa nje ya nchi na vijana wengi wangejiajiri. Aidha, mpango huo uliingizwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM). Je, ni lini makambi hayo yataanzishwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuwashirikisha vijana katika kilimo kwa ajili ya maendeleo ya uchumi wa Taifa na kuongeza ajira. Katika kufanikisha azma hii Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo Mpango wa Kutumia Makambi ya Vijana ya Kilimo na Mkakati wa Ushirikishaji Vijana katika Kilimo (The National Strategy for Youth Involvement in Agriculture 2016-2021) unaosimamiwa na Wizara ya Kilimo. Katika kutekeleza mkakati huu Serikali inafanya yafuatayo:-
(a) Kutumia vituo vya maendeleo ya vijana vilivyopo Ilonga - Kilosa, Morogoro na Sasanda – Mbozi, Songwe kwa ajili ya kupewa mafunzo ya kilimo cha kisasa na kutumia mashamba yaliyopo vituoni hapo kwa ajili ya shughuli za kilimo ambapo vijana hunufaika kwa kujipatia kipato kupitia mazao yanayozalishwa shambani.
(b) Kushirikisha vikundi vya vijana katika miradi mikubwa ya kilimo kama wakulima wadogo wadogo katika kilimo cha miwa eneo la Mbigiri na Mkulazi, Mkoani Morogoro.
(c) Kutekeleza Programu ya Ukuzaji Ujuzi nchini ambapo vijana wameanza kupatiwa mafunzo ya kilimo cha kisasa na kufundishwa ujuzi wa kutengeneza vitalu nyumba na kupatiwa vitalu nyumba kwa ajili ya kilimo cha mbogamboga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilikwishaagiza halmashauri zote zitenge maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za vijana ikiwa ni pamoja na maeneo ya kilimo. Agizo hilo limeendelea kutekelezwa ambapo hekta 217882.4 zimetengwa katika halmashauri 48 mwaka 2017. Serikali inasisitiza kila halmashauri ihakikishe inatenga maeneo hayo ili vijana wayatumie kwa shughuli za kilimo.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-
Wapo wahitimu wengi sana kutoka Vyuo mbalimbali vya Ufundi nchini ambapo hadi sasa hawajapata ajira wala hawajaweza kujiajiri, ikiwa pia tuko kwenye wakati wa kuanzisha uchumi wa viwanda ambapo taaluma za wahitimu hao zinahitajika sana:-
Je, ni lini Serikali itafanya juhudi za dhati za kushughulikia suala hili kwa lengo la kuongeza tija?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha tatizo hili linapungua kwa kiasi kikubwa, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali kukabiliana na changamoto hiyo kama ifuatavyo:-
(a) Kuhakikisha kuwa vijana wahitimu wa Vyuo vya Ufundi wanapata fursa za ajira katika miradi mikubwa ya maendeleo kama vile ujenzi wa reli ya Standard Gauge, ujenzi wa bomba la mafuta, mradi wa usambazaji wa umeme vijijini, mradi wa kufufua umeme na mingine. Mathalan, katika ujenzi wa bomba la mafuta, uchambuzi umeonyesha kutakuwa na fursa za ajira zaidi ya 11,000 za aina mbalimbali. Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Huduma za Ajira (TaESA) inaratibu upatikanaji wa Watanzania wenye sifa za kuajirika katika miradi hiyo.
(b) Kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini, Serikali imeainisha aina ya ujuzi unaohitajika katika ujenzi wa miradi husika na imetenga fedha za kugharamia kuziba ombwe la ujuzi lililopo kati ya wahitimu na mahitaji ya soko la ajira kuwezesha Watanzania wakiwemo wahitimu wa Vyuo vya Ufundi kupata sifa na kuajirika.
(c) Kuendelea kuhamasisha na kuwawezesha vijana kujiajiri kwa kuanzisha makampuni na vikundi vya uchumi vilivyosajiliwa kisheria ili kutumia taaluma zao kuzalisha na kujipatia vipato halali. Kwa mfano, Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini (REA) umetoa fursa za ajira kwa vijana wengi wenye ufundi. Aidha, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Taasisi nyingine za Serikali, Serikali imeendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa vikundi vya vijana ili kuwajengea mitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri kuwa tunapoelekea katika uchumi wa viwanda taaluma za wahitimu wa vyuo vya ufundi zitaendelea kuhitajika sana kwa ajili ya uendeshaji endelevu wa viwanda vitakavyoanzishwa. Serikali imeona jambo hilo na kwa kushirikiana na vyuo vya ufundi imeanza kutoa mafunzo kwa kuzingatia mahitaji.
MHE. DKT. PUDENCIANA W. KIKWEMBE aliuliza:-
Serikali imekuwa ikiwahimiza wananchi wajiunge kwenye vikundi ili waweze kupata mikopo ya kuwasaidia kuendesha shughuli zao:-
Je, Serikali haoni kuwa sharti hilo linawakosesha fursa baadhi ya wananchi ambao pengine wanahitaji huduma hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Pudenciana Wilfred Kikwembe, Mbunge wa Kavuu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia wananchi wake Serikali imetunga Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2017 ambayo itawezesha kuchochea maendeleo stahiki na ubunifu wa huduma ndogo za kifedha ili kukidhi mahitaji halisi ya wananchi wa kipato cha chini na hivyo kuongeza ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini. Pia Serikali inalenga kutatua changamoto inayowapata wananchi juu ya mtazamo wa mifumo ya ukopeshaji kwa vikundi au mtu mmoja mmoja. Sera hii itapelekea kutungwa kwa sheria itakayoweka utaratibu mzuri wa huduma ndogo ya fedha.
Mheshimiwa Spika, utoaji mikopo kwa kutumia vikundi ni mfumo ambao hutumika kutoa mikopo midogo midogo kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali. Mfumo huu hutumika kutoa mikopo kwa watu ambao uwezo wao wa kiuchumi ni mdogo, hasa kwa wakopaji ambao hawana dhamana. Pia mfumo huu husaidia kuweka dhamana mbadala ya usalama wa mikopo inayotolewa kwa kuwafanya wanakikundi kuwa na uwajibikaji wa pamoja juu ya mkopo huo.
Mheshimiwa Spika, mfumo huu umekuwa ukitumiwa na taasisi nyingi za kifedha ambazo zimekuwa zikitoa mikopo kwa watu wenye kipato cha chini ikiwepo mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi inayomilikiwa na Serikali kutokana na faida yake katika kuhakikisha kuwa usalama wa mikopo hasa kwa wakopaji wasio na dhamana. Mfumo huu pia husaidia kurahisisha ufuatiliaji wa kuwajengea uwezo wanakikundi kupitia mafunzo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mfumo huu kutumika lakini ni pia mwananchi mmoja mmoja wamepatiwa fursa za uwezeshaji kupitia benki na mifuko mbalimbali ya uwezeshaji kama vile Mfuko wa Kuendeleza Wajasiriamali, Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi na Mfuko wa Wajasiriamali wadogo wadogo.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y MHE. GODBLESS J. LEMA) aliuliza:-
Mishahara ya Taasisi za Umma hupangwa na Serikali. Utaratibu huo wa Serikali kupanga mishahara ya watumishi wake huathiri pia upangaji na ukadiriaji mishahara katika taasisi binafsi:-
Je, Serikali haioni haja ya kuboresha mishahara yake na kuzielekeza taasisi binafsi kulipa mishahara inayoendana na hali ya maisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Godbless Jonathan Lema, Mbunge wa Arusha Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuboresha mishahara yake na kuzielekeza taasisi binafsi kulipa mishahara inayoendana na hali ya maisha, Serikali imeunda Bodi ya Kima cha Chini cha Mshahara ambayo hufanya utafiti kwa kuzingatia hali halisi ya maisha na uwezo wa kibajeti wa Serikali na kuwashauri Mawaziri wenye dhamana na masuala ya utumishi wa umma na sekta binafsi katika kupanga kima cha chini cha mshahara.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7 ya Mwaka 2004 kama ilivyorekebishwa mwaka 2015 imeanzisha Bodi ya Mishahara ya Sekta Binafsi ambayo ina jukumu la kufanya uchunguzi na kupendekeza kiwango cha kima cha chini cha mshahara na maslahi ya wafanyakazi kwa ujumla. Serikali itaendelea kuiwezesha Bodi ya Mishahara kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi pamoja na kuhamasisha majadiliano baina ya waajiri na vyama vya wafanyakazi katika kuboresha maslahi na kukuza tija na uzalishaji sehemu za kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa sekta binafsi, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya Mwaka 2004, imeweka utaratibu kwa waajiri na wafanyakazi kujadiliana na kufunga mikataba ya hali bora mahali pa kazi kwa lengo la kuboresha maslahi yao ikiwemo mshahara na stahiki nyingine. Kupitia utaratibu huu wa kisheria waajiri katika sekta binafsi wanaruhusiwa kuwalipa viwango vya mishahara hata zaidi ya kiwango kinachowekwa kama kima cha chini cha mshahara pale ambapo wanaona kwa kufanya hivyo itaongeza motisha kwa wafanyakazi wao kufanya kazi kwa bidii na kujituma kwa lengo la kuongeza tija katika kuzalisha mali au kutoa huduma.
MHE. ZAINAB M. AMIRI aliuliza:-
Daraja la Kigamboni ni kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na mawasiliano.
(a) Je, tangu daraja lianze kutumika Serikali imekusanya kiasi gani cha fedha kinachotokana na malipo kwa wanaovuka na vyombo vya moto?
(b) Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu wa kutumia kadi maalum (smart card) kulipia kwa mwezi malipo kwa wanaovuka darajani hapo kwa vyombo vya moto?
wanaovuka darajani hapo kwa vyombo vya moto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Mndolwa Amiri, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambao ndiyo wanasimamia uendeshaji wa daraja hilo hadi kufikia mwezi Machi, 2018 limeshakusanya kiasi cha Sh.19,734,655,482.70 tangu daraja hilo lilipoanza kutumika rasmi mwezi Mei, 2016. Aidha, katika mapato hayo, shilingi bilioni 15.2 ni makusanyo ya waliovuka na vyombo vya moto na shilingi bilioni 4.7 ni faida na pato la ziada la mtaji lililotokana na upatikanaji wa fedha hizo katika dhamana ya Serikali.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii lipo katika hatua za mwisho za kumpata Mkandarasi wa kuweka mfumo utakaotumia kadi maalum (smart card) kwa malipo ya wanaovuka darajani hapo. Mvukaji atakuwa na hiari yake ya kulipia kwa siku, wiki au mwezi kulingana na uwezo wake.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:-
Mkoa wa Tabora ni moja kati ya mikoa inayokabiliwa na tatizo kubwa la ndoa za utotoni na kusababisha watoto wengi wa kike kushindwa kumaliza elimu ya msingi au ya sekondari. Aidha, hivi karibuni Serikali ilikata rufaa juu ya ndoa za utotoni ikitaka iruhusiwe watoto wa kike kuolewa na umri kuanzia miaka 14 ambapo hii ni kinyume cha Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia watoto wa kike wa Mkoa wa Tabora angalau wengi waweze kwenda kupata elimu ya msingi na sekondari kwa kupunguza ndoa za utotoni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mwaifunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa elimu kwa watoto wote wa kike na kiume wa Tanzania. Hii inadhihirishwa na uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kuifanya elimu ya msingi na ya sekondari kuwa ni elimu ya lazima na kutolewa bila malipo. Lengo la mpango huu ni kuhakikisha watoto wetu wote ikiwa ni pamoja na watoto wa kike wanaipata elimu hiyo bila kikwazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa elimu ya mtoto wa kike Serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Elimu ambayo inalinda haki za mtoto kusoma hadi sekondari. Kupitia marekebisho yaliyofanywa kwenye Sheria ya Elimu na Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 ya mwaka 2016, ni marufuku kwa mtu yeyote na katika mazingira yoyote kuoana na msichana au mvualana anayesoma shule ya msingi au sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ni kosa kumpa mimba msichana anayesoma au sekondari na kwa yeyote anayesaidia msichana au mvulana anayesoma kuoa au kuolewa anakuwa ametenda kosa. Marekebisho haya yameweka adhabu kali kwa yeyote anayetenda makosa haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika kumlinda mtoto wa kike na ndoa za utotoni, licha ya Sheria ya Ndoa kuweka mazingira na vigezo vya mtoto wa kike kuolewa akiwa na miaka 15, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuhakikisha mtoto huyu analindwa. Katika kulisimamia hilo, Serikali imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 ambayo pamoja mambo mengine imeainisha haki za mtoto ikiwemo haki ya kupata elimu na kutoa wajibu wa haki hizo kulindwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwa ujumla kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuzuia vitendo vya kuwaozesha watoto wa kike. Si tu kwa mkoa wa Tabora bali katika nchi yote ili kuwawezesha watoto wetu wa kike kupata elimu ya msingi na sekondari na pale ambapo vitendo hivyo vinajitokeza wananchi wana wajibu wa kutoa taarifa na kushirikiana na vyombo vya Serikali ili kuhakikisha wanaofanya makosa hayo wanachukuliwa hatua za kisheria.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. GRACE V. TENDEGA) aliuliza:-
Kesi za dawa za kulevya na upelelezi vimekuwa vikichukua muda mrefu sana na kusababisha wakati mwingine ushahidi kupotea na watuhumiwa kuachwa huru baada ya upelelezi kukamilika:-
Je, kwa nini Serikali isianzishe Mahakama za Dawa za Kulevya kwenye Viwanja vya Ndege, Bandari na mipakani ili watuhumiwa wafikishwe Mahakamani punde tu ushahidi ukiwa mikononi kama zifanyavyo nchi nyingine ikiwemo India?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba wa Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uanzishwaji wa mahakama katika kushughulikia aina fulani ya makosa, ni suala la kisheria linalohitaji ushirikishwaji mkubwa wa wadau wote husika wa haki jinai (criminal justice). Kwa kutambua hilo, Serikali imeshaanza mazungumzo ya awali na wadau hao wa haki jinai, ukiwemo mhimili wa Mahakama ili kuona uwezekano wa kusikiliza mashauri ya watuhumiwa wa dawa za kulevya wanaokamatwa katika maeneo ya viwanja vya ndege, bandarini na maeneo mengine ya mipaka ya nchi, kwa kutumia Mahakama zinazotembea (mobile courts).
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wawe na subira wakati Serikali ikijadiliana na wadau wa haki jinai kuhusiana na suala hilo.
MHE. KHADIJA N. ALI (K.n.y. MHE. CATHERINE N. RUGE) aliuliza:-
Pamekuwa na wimbi kubwa la ukosefu wa ajira kwa sasa huenda kuliko wakati mwingine wowote tangu nchi yetu ipate uhuru, wahitimu wa tangu mwaka 2015 hawajaajiriwa na Serikali mpaka sasa, sekta binafsi nazo kila kukicha zinapunguza wafanyakazi na kutoajiri wapya:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa dharura wa kuhakikisha ajira zinapatikana kwa vijana hawa ambao hawajapatiwa elimu ya kutosha ya kujiajiri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Catherine Nyakao Ruge, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha tunakabiliana na changamoto za ukosefu wa ajira nchini Tanzania Serikali ina mikakati ifuatayo:-
(a) Kuongeza fursa za wigo mpana wa nafasi za ajira kupita sekta mbalimbali za kiuchumi ikiwemo uwekezaji katika uchumi wa viwanda na utekelezaji wa miradi mikubwa kama ilivyoainishwa katika Mpango wa Pili wa Maendeleo nchini;
(b) Kutekeleza Programu ya Taifa ya kukuza ujuzi inayowezesha Nguvu Kazi ya Taifa kuwa na ujuzi stahiki na kutoa fursa kwa vijana kuwa na sifa ya kuajirika na kujiajiri;
(c) Kuendelea kusimamia vijana kujiunga katika makampuni, ushirika na vikundi vya uzalishaji mali ili kupatiwa fursa ya mikopo yenye masharti nafuu kupitia Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kwa lengo la kuwaongezea mitaji ya kufanya shughuli za kiuchumi.
MHE. RUKIA AHMED KASSIM aliuliza:-
Lengo la Serikali ya Awamu ya Tano ni kujenga Uchumi wa Viwanda ifikapo 2025:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwavutia Wawekezaji wa Viwanda nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rukia Kassim Ahmed, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo 2025 limetafsiriwa vema katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2015/2016 - 2020/2021, wenye dhima ya kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Utekelezaji wa mpango huu unaenda sambamba na utekelezaji wa Mkakati Unganishi wa Maendeleo ya Viwanda (Intergratged Industrial Development Strategy) wa mwaka 2011 mpaka mwaka 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango na mikakati hiyo inalenga katika kuhakikisha uwepo wa mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kunakuwa na amani na usalama wa nchi, kuondoa vikwazo kupitia sera na sheria wezeshi, uwepo wa miundombinu wezeshi na saidizi na upatikanaji wa taarifa muhimu kuhusu fursa za uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutekeleza mipango na mikakati niliyoirejea hapo juu, Serikali inahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kujenga viwanda vidogo, vya kati na vikubwa kupitia TIC, EPZA, Balozi zetu nje ya nchi pamoja na Serikali ngazi za Wilaya na Mkoa. Uhamasishaji huo unaenda sambamba na kutoa vivutio vya kodi na visivyo vya kikodi kupitia sheria za uwekezaji pamoja na zile za uendelezaji maeneo maalum ya uwekezaji (EPZ na SEZ). Aidha, Serikali kupitia Taasisi za SIDO, NDC na EPZA inatoa ushauri wa namna ya kuanzisha viwanda vidogo sana, viwanda vya kati na kuvilea ili vikue na kuwa vikubwa.
MHE. AMINA S. MOLLEL (K.n.y MHE. HAWA M. CHAKOMA) aliuliza:-
Je, Serikali inatekelezaje Mpango wa UKIMWI wa 90-90-90?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mpango wa 90-90-90 kwa kufanya mambo yafuatayo:-
(a) Serikali imeridhia Mkakati wa Shirika la Afya Duniani (WHO) wa kupima VVU na kutibu bila ya kuzingatia kiwango cha kinga mwilini (CD4);
(b) Serikali imetoa Waraka unaoagiza utekelezaji wa mkakati huu tangu Oktoba, 2016;
(c) Utaratibu umewekwa wa kuhakikisha watu wote wanaogundulika kuwa na VVU wanaanzishiwa dawa za kufubaza VVU (ARV) mara moja; na
(d) Serikali baada ya kubaini mapungufu ya wananchi kujitokeza kupima maambukizi ya VVU kupitia utafiti, imeandaa kampeni mbalimbali kwa ajili ya kuhamasisha wananchi kujitokeza kupima VVU ili kujua hali zao na hasa mkazo mkubwa utaelekezwa kwa wanaume ambao utafiti umeonesha kuwa hawajitokezi sana kupima na kujua hali zao. Kampeni hii inategemewa kuzinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu tarehe 19 Juni, 2018 hapa Mjini Dodoma. Aidha, kampeni hii itahusisha kusambaza ujumbe wa uhamasishaji kupitia vyombo vya habari, mabango, vipeperushi na makongamano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa wito kwa wananchi wote kuendelea kupima afya zao ili watambue hali zao na kuchukua hatua stahiki. Pia natoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo mara itakapoanza kwa nchi nzima.
MHE. ESTHER M. MMASI aliuliza:-
Ukosefu wa ajira bado ni changamoto kubwa hasa tunapoangalia takwimu za kidunia na hata katika nchi yetu:-
(a) Je, Serikali imejipangaje katika kulinda ajira za Vijana kupitia Sera ya Ajira?
(b) Kwenye kada ya TEHAMA nchi yetu imekuwa ikipokea nafasi nyingi za ajira kwa Vijana kwenye Taasisi za kifedha kwa kazi nyingi kupelekwa nje ya nchi ikiwemo nchi jirani. Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Michael Mmasi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Sera ya Taifa ya Ajira imeweka mikakati ifuatayo katika kulinda ajira za vijana:-.
a) Kuhamasisha mazingira bora ya uwekezaji katika sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira hususani kilimo, ujenzi, viwanda na biashara;
b) Kuwajengea vijana ujuzi wa fani mbalimbali kupitia programu za ukuzaji ujuzi ili vijana wengi zaidi wapate ujuzi stahiki utakaowawezesha kuwa na sifa za kuajirika, kujiajiri na kuwaajiri wengine;
c) Kusimamia sheria na kanuni za kuwawezesha vijana wazawa wengi zaidi kushiriki katika miradi mikubwa ya maendeleo kama sehemu ya nguvu kazi na watoa huduma; na
d) Utekelezaji wa Sheria ya Uratibu wa Ajira kwa Wageni Na.1 ya Mwaka 2015 ili kulinda nafasi za kazi kwa Watanzania, kwa kuhakikisha Watanzania wanafanya kazi ambazo vinginevyo zingefanywa na wageni.
Mheshimiwa Spika, kada ya TEHAMA ni moja ya Kada ambazo zimewezesha ajira nyingi hapa nchini hivyo Serikali imefanya juhudi kubwa kuhakikisha kunakuwepo naa Wataalam wa kutosha wa sekta hii na kulinda ajira zao kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, moja ni kutoa Wataalam wengi wa fani ya TEHAMA kupitia Vyuo Vikuu na Vyuo vya elimu ya Juu kwa kuhamasisha wanafunzi wengi zaidi kusomea fani za sayansi ikiwemo suala la Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, pili ni kuendesha programu za ukuzaji ujuzi ili kuwajengea uwezo Watanzania katika fani ya TEHAMA kupitia mpango wa kitaifa wa kukuza ujuzi na tatu ni kutoa mikopo ya asilimia 100 kwa wanafunzi wa Elimu ya juu kwa Kada ya TEHAMA.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA aliuliza:-
Tarehe 9 Desemba, 1961, Baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere alisema tutauwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro ili umulike nchi nzima na kuleta upendo, amani na kadhalika:-
Je, utaratibu huu wa kukimbiza Mwenge nchi nzima kila mwaka umetoka wapi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika,kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Ally Mtolea, Mbunge wa Temeke, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tarehe 9 Desemba mwaka 1961, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alisema nanukuu;
“Sisi tumekwisha uwasha Mwenge wa Uhuru na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, umulike ndani na nje ya mipaka yetu, ulete matumaini pale ambapo hakuna matumaini, ulete upendo mahali penye chuki na heshima palipojaa dharau.” Mwisho wa kunukuu.
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kukimbiza Mwenge wa Uhuru nchi nzima kila mwaka ulianzishwa mwaka 1964 baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na Muungano wa nchi mbili zilizokuwa zinaitwa Tanganyika na Zanzibar. Utaratibu huu ulianzishwa kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza, kuanzia mwaka 1964 hadi mwaka 1992 mbio za Mwenge wa Uhuru zilitumika zaidi kueneza na kuwakumbusha Watanzania falsafa inayotoa misingi ya sera ya ndani ya nchi yetu baada ya kupata Uhuru. Misingi hiyoni kujenga Taifa lenye amani, linalojitegemea na lenye kuheshimu misingi ya utu na usawa wa binadamu; na mbio hizi zilihasisiwa na Baba wa Taifa mwenyewe.
Mheshimiwa Spika, pili, katika karne ya 20, kwa kutumia falsafa yake, mbio za Mwenge wa Uhuru zilitumika kumulika hata nje ya mipaka ya nchi yetu ili kuhamasisha vita vya ukombozi dhidi ya ukoloni mkongwe, dhuluma, ubaguzi na hasa katika Bara la Afrika.
Mheshimiwa Spika, tatu, wakati tunaingia katika karne ya 21, mbio za Mwenge wa Uhuru baada ya kutimiza azma yake ya awali ya uhamasishaji wa msingi wa utaifa wetu na ukombozi wa Bara la Afrika, mbio hizi ziliendelea kukimbizwa nchi nzima kwa lengo la kuendeleza mapambano dhidi ya maadui ujinga, maradhi na umaskini katika nchi yetu. Kupitia utaratibu huu Mwenge wa Uhuru umekuwa ni chombo muhimu cha kuchochea maendeleo ya wananchi katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la amani, haki, utu, muungano wetu na maendeleo kwa wananchi halina mipaka ya kijiografia wala muda maalum wa kulishughulikia. Hivyo, Serikali inaona ni muhimu kuendelea na utaratibu wa kuukimbiza Mwenge wa Uhuru nchi nzima kila mwaka ili uendelee kufanya kazi ya kuimarisha misingi ya Taifa letu na kuhamasisha maendeleo ya wananchi.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI (K.n.y. MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB) aliuliza:-
Baadhi ya Kampuni binafsi zimekuwa zikiwafanyisha kazi Watumishi wao zaidi ya muda wa saa za kazi, kutowapa chakula na kuwalipa kima kidogo cha mshahara:-
Je, Serikali ina kauli gani kuhusu suala hilo linalowakandamiza Wafanyakazi hao ambao wengi wao ni vijana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Munira Mustapha Khatibu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inasimamia ipasavyo mahusiano ya kikazi sehemu zote za kazi ikiwa ni pamoja na kampuni binafsi. Kupitia Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya Mwaka 2004, Serikali inasimamia viwango stahiki vya kazi ikiwa ni pamoja na masaa ya kazi, likizo mshahara na kazi staha kwa wafanyakazi wa sekta zote.
Mheshimiwa Spika, ni wajibu wa Mwajiri kutii matakwa ya sheria kwa kumlipa mfanyakazi wake mshahara na maslahi stahiki. Hivyo, mwajiri anayekiuka matakwa ya sheria hii anastahili adhabu.
Aidha, katika kuimarisha uwajibikaji upande wa waajiri, mwaka 2016, Bunge letu Tukufu lilifanya marekebisho katika Sheria ya Taasisi za Kazi Na. 7 ya Mwaka 2004 na kuimarisha mfumo wa kaguzi za kazi mahali pa kazi kwa kuruhusu kutoa adhabu za papo kwa papo (compounding of offences) kwa waajiri wanaokiuka matakwa ya sheria, ikiwa ni pamoja na kutowalipa wafanyakazi malipo ya ziada kwa saa za ziada walizofanya kazi na kulipa mshahara chini ya kiwango cha chini cha mshahara.
Mheshimiwa Spika, Ofisi yangu itaendelea kusimamia sheria na kuimarisha mahusiano kati ya waajiri na wafanyakazi na kufanya kaguzi za kazi sehemu za kazi ili waajiri watimize wajibu wao kwa kuzingatia matakwa ya sheria.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Kwa kuwa tumebakiza mwaka mmoja kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020 na ili Watanzania waliokidhi vigezo wapate haki ya kupiga kura, uboreshaji wa daftari la kupiga kura ni jambo lisiloepukika:-
Je, ni lini Serikali itaanzisha mchakato wa kuboresha daftari la wapiga kura?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, KAZI, AJIRA NA VIJANA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mchakato wa kuboresha Daftari la Wapigakura ulianza mwezi Agosti, 2018 kwa kufanya maandalizi yafuatayo:-
(i) Kuhuisha kanzidata ya Daftari la Kudumu la Wapiga kura; na
(ii) Kuboresha mifumo ya uandikishaji na utunzaji wa kumbukumbu za Daftari
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Uchaguzi, Sura ya 343, Tume ya Taifa ya Uchuguzi ipo katika hatua za mwisho za maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mara ya kwanza na uandikishaji wa majaribio kwa baadhi ya mikoa ili kuona ufanisi au changamoto zinazoweza kujitokeza unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
MHE. MOSHI S. KAKOSO aliuliza:-
Wilaya ya Tanganyika haina Mahakama ya Wilaya.
Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya sanjari na kuboresha Mahakama za Mwanzo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiswa Moshi Selemani Kakoso, Mbunge wa Mpanda Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Wilaya ya Tanganyika iliyo katika Mkoa wa Katavi haina jengo la Mahakama ya Wilaya, wananchi wa Wilaya ya Tanganyika wanategemea huduma ya mahakama ya Wilaya ya Mpanda ambayo ni jirani.
Mheshimiwa Spika, kupitia mpango wa maboresho ya miundombinu wa mahakama katika mikoa yote nchini kwa sasa ujenzi wa Mahakama ya Mkoa wa Katavi na Wilaya ya Mpanda unaendelea. Vilevile Mahakama ya Wilaya ya Tanganyika ipo kwenye mpango wa ujenzi wa mwaka wa fedha 2019/2020 ambapo ujenzi huo utaenda sanjari na ukarabati wa Mahakama za Mwanzo kuendana na upatikanaji wa fedha.
MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH aliuliza:-
Miradi ya MIVARF ina malengo mapana ya kuwaendeleza wakulima wa vijiji kibiashara na kimtaji; na hatua za awali kama vile ujenzi wa barabara za vijijini umekamilika lakini pia masoko ya kuongeza thamani yapo katika hatua za kukamilika:-
Je, ni lini hatua za mwisho za kuwawezesha wananchi kimtaji zitaanza rasmi kwa upande wa Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali kuhakikisha inaunga mkono juhudi za wananchi kushiriki katika uchumi wa kilimo kwa kusaidia upatikanaji wa mitaji na kuwapatia mafunzo stahiki. Mpango wa Kuwawezesha Wananchi Kimtaji umezingatia hatua zifuatazo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mradi wa MIVARF, imevijengea uwezo wa kiutawala na kiutendaji Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) na vikundi vingine vya uzalishaji Tanzania Bara na Visiwani ili viweze kuratibu na kusimamia kwa ufanisi matumizi ya mitaji yatakayopatikana kupitia mikopo inayotolewa na taasisi za kifedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 3 Novemba, 2017, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango na Benki ya Maendelea ya Kilimo Tanzania (TADB) walisaini makubaliano ya uendeshaji wa Mfuko wa Dhamana. Kwa kupitia makubaliano hayo, Serikali tayari imetoa shilingi bilioni 22 kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ili kuanza utekelezaji kwa kushirikisha benki za biashara kufikisha huduma ya mikopo kwa makundi mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania walishatangaza utaratibu wa namna benki mbalimbali za biashara zinavyoweza kushiriki katika Mfuko wa Udhamini ambapo Benki za CRDB, NMB, TPB na PBZ zilionesha nia. Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania ilishakutana na benki zote zilizoonesha nia ya kushiriki katika Mfuko wa Dhamana na kufafanua jinsi Mfuko wa Udhamini unavyofanya kazi. Benki za NMB na TPB wameshakubaliana na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kushiriki katika utoaji wa mikopo kwa vikundi vya wakulima kupitia Mfuko wa Dhamana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hatua ya mwisho ya kuwawezesha wananchi kimtaji imeshafikiwa baina ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania na Benki za NMB na TPB kama ilivyoelezwa hapo juu, napenda kutoa wito kwa Vyama vya Kuweka na Kukopa (SACCOS) na vikundi vingine vya uwezeshaji Zanzibar kuwasiliana na Benki za NMB na TPB kwa upande wa Zanzibar ili kupata utaratibu wa kukopa fedha kwa ajili ya shughuli za kilimo.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Kuendesha bodaboda ni ajira kama zilivyo ajira nyingine nchini:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea uwezo vijana hao ili kuifanya kazi hiyo iwe rasmi na yenye kutambulika kama kazi nyingine zozote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika kutambua bodaboda kama mojawapo ya usafiri wa kubeba abiria nchini kisheria, mwaka 2017 ilifanya marekebisho ya Kanuni za Usafirishaji za Mwaka 2010 ambapo waendesha bodaboda walirasimishwa kwa kupatiwa leseni za usafirishaji. Leseni hizo zinatolewa na Mamlaka za Miji, Wilaya na Majiji kwa niaba ya SUMATRA ili kuhalalisha shughuli za uendeshaji bodaboda.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuwajengea uwezo waendesha bodaboda, Serikali inatekeleza mipango ifuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ni kutoa mafunzo ya udereva kupitia Jeshi la Polisi kwa waendesha bodaboda na hatimaye kupatiwa leseni za udereva. Aidha, kama ilivyo katika vyombo vingine vinavyotoa huduma za usafirishaji, usalama wa waendesha bodaboda na abiria umeendelea kusimamiwa na kulindwa wanapotekeleza majukumu yao barabarani.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhamasisha uundwaji wa vikundi vya waendesha bodaboda ili hatimaye viweze kuwezeshwa kwa mitaji na mafunzo kupitia Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na wadau wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatu ni kuwapatia maeneo ya kuegesha bodaboda na kuyatambua pamoja na kuwapatia vitambulisho na nne ni kuwapatia waendesha bodaboda mafunzo ya ujasiriamali na hatimaye kuwapatia mikopo yenye masharti nafuu na kuwaunganisha na taasisi nyingine za fedha zinazotoa mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, ni kuwapatia elimu juu ya faida ya kujiunga na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii pamoja na kuwaunganisha na mifuko husika.
MHE. MOHAMED O. MCHENGERWA aliuliza:-
Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 ya Mwaka 2018 yamemwondoa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kushitaki kesi zote za jinai nchini, lakini Katiba ya Jamhuri ya Muungano inamtambua Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika mambo ya Muungano:-
Je, kumwondoa moja kwa moja Mwanasheria Mkuu wa Serikali hakuwezi kuathiri makosa ya jinai ya uhaini yanayoweza kutokea Zanzibar kukwama kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka hana mamlaka kwa mujibu wa Katiba na mambo ya Muungano kushitaki Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Omary Mchengerwa, Mbunge wa Rufiji, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ibara ya 59(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na Sheria ya Ofisi ya Mashitaka, Sura ya 430, masuala ya ufunguaji, uendeshaji na usimamizi wa mashitaka ya jinai nchini yako chini ya Mkurugenzi wa Mashitaka na siyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wa Zanzibar, masuala hayo yanaongozwa na Ibara ya 56(a) ya Katiba ya Zanzibar na Sheria ya Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka Na. 2 ya Mwaka 2010. Katika Katiba zote mbili na sheria zake, mamlaka ya mwisho ya kufungua, kuendesha na kusimamia mashitaka ya jinai ni ya Mkurugenzi wa Mashitaka. Hivyo, masuala ya jinai siyo suala la Muungano.
Mheshimiwa Spika, ikumbukwe kuwa tarehe 13 Februari, 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alifanya mabadiliko ya muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambapo pamoja na mambo mengine alianzisha Ofisi Huru ya Taifa ya Mashitaka. Ili kuendana na mabadiliko hayo ya muundo, yalifanyika kurekebisha kwenye Sheria ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (Utekelezaji wa Majukumu) Sura ya 268 kwa kukifuta Kifungu cha 8 na kukibadilisha kupitia Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 2 ya Mwaka 2018.
Mheshimiwa Spika, marekebisho hayo yamemwondoa Mkurugenzi wa Mashitaka na iliyokuwa Division ya Mashitaka kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Hivyo, mabadiliko hayo hayajaathiri kwa namna yoyote ufunguaji, uendeshaji na usimamizi wa mashauri ya jinai nchini. Bado kwa mujibu wa Ibara ya 59(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 Mkurugenzi wa Mashitaka anaendelea kuwa na mamlaka ya juu ya mashauri yote ya jinai nchini.
Mheshimiwa Spika, makosa yote ya jinai yanayotokea katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanaendelea kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria zilizopo na hayawezi kukwama kwa kuwa kuna mifumo mizuri ya kikatiba, kisheria na kitaasisi ya kuyashughulikia.
MHE. PASCHAL Y. HAONGA aliuliza:-
Kuna watumishi katika Halmashauri nyingi za Wilaya nchini walikuwa wanachama wa PSPF wamestaafu zaidi ya mwaka mmoja na hawajalipwa fedha zao za kiiunua mgongo (pension) na kwa sasa wanaishi maisha ya taabu na mateso makali:-
(a) Je, ni lini sasa Serikali itawalipa wastaafu hawa?
(b) Inasemekana kwamba Serikali imetumia vibaya fedha za PSPF ikiwa ni pamoja na kukopesha baadhi ya watu na taasisi: Je, Serikali haioni kwamba hii inaweza kuwa sababu mojawapo ya kucheleweshwa mafao kwa wastaafu?
(c) Fedha za kiinua mgongo ni mali ya Mtumishi anayestaafu: Je, kwa nini Mifuko ya Pensheni isiwakopeshe wastaafu watarajiwa angalau 40% ya fedha hizo bila riba pale inapobaki miaka 10 kabla ya kustaafu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Paschal Yohana Haonga, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka kufikia tarehe 28 Februari, 2019 Mfuko mpya wa PSSF ulikuwa umekamilisha kulipa malimbikizo ya deni la wastaafu lilorithiwa kutoka Mfuko wa PSPF ambapo jumla ya wastaafu 9,971 wamelipwa stahiki zao zilizofikia kiasi cha shilingi bilioni 888.39. Aidha, Mfuko umekamilisha mfumo wa ulipaji mafao utakaowezesha kufanya malipo katika ngazi ya mkoa na hivyo kuwezesha mfuko kulipa mafao ndani ya muda uliowekwa kisheria wa siku 60 tangu mwanachama anapowasilisha madai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inaendeshwa kwa mujibu wa Sheria ya Bunge iliyoanzisha mfuko husika. Sheria hiyo pamoja na mambo mengine inasimamia muundo wa utawala na mfumo wa maamuzi na usimamizi wa uwekaji wa fedha za mifuko. Aidha, sheria inaipa Bodi ya Wadhamini ya mfuko jukumu la kusimamia uwekezaji wa fedha za mfuko kwa uhuru. Hivyo basi, siyo kweli kwamba Serikali inaweza kuingilia uendeshaji wa mifuko au kufanya maamuzi ya uwekezaji ikiwemo kukopesha taasisi au watu binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, imekuwa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanachama wake kupitia vikundi vya kuweka na kukopa (SACCOS) katika maeneo ya kazi. Kwa mujibu wa Mwongozo wa Uwekezaji wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii wa mwaka 2015, Mifuko inaweza kutoa mikopo kwa SACCOS hadi asilimia 10 ya rasilimali za mfuko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii zinaruhusu wanachama kutumia sehemu ya mafao yao kama dhamana kwa ajili ya kujipatia mkopo wa nyumba kutoka katika mabenki na taasisi za fedha nchini ili kuwawezesha kuboresha makazi wakati wa kipindi cha utumishi wao.
Aidha, Kanuni Na. 24 na 25 ya kanuni mpya za Mafao ya Hifadhi ya Jamii za mwaka 2018 zimetoa wigo mpana zaidi kwa wanachama waliochangia kwa miaka isiyopungua 10 kuweza kupata huduma hii tofauti na hapo awali ambapo ni wanachama waliokuwa wametimiza umri kuanzia miaka 55 ndio waliweza kupatiwa mikopo ya kujenga vyumba.
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA aliuliza:-
Watu wenye ulemavu wa macho wanakosa haki ya kuchagua viongozi wanaowataka kutokana na kusaidiwa kupiga kura na watu wengine ambao wanaweza kuwapigia kura kinyume na ridhaa zao, hivyo kura zao kwenda kwa watu ambao si chaguo lao:-
Je, Serikali iko tayari kuchapisha karatasi maalum za kupiga kura kwa kutumia mfumo wa nukta nundu kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa macho?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI,VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Suzana Chogisasi Mgonukulima, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 61(3)(b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343 na Kifungu cha 62H cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Sura ya 292 vinafafanua kuwa ikiwa Mpiga kura ni mlemavu wa macho au ana ulemavu wa viungo (mfano, ulemavu wa mikono), au hawezi kusoma na kuandika anaweza kumchagua mtu anayemwamini amsaidie kupiga kura. Mtu huyo anapaswa asiwe Msimamizi wa Kituo cha kupigia Kura, Msimamizi Msaidizi wa Kituo au Wakala wa Chama cha Siasa. Aidha, Kanuni ya 53 ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za Mwaka 2015 na Kanuni ya 46 ya Kanuni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa za (Madiwani) zimeweka utaratibu kuwa iwapo Mpiga Kura mwenye ulemavu wa macho ataomba kupewa karatasi ya kupigia kura ya nukta nundu (tactile ballot paper), Msimamizi wa Kituo atapaswa kumpatia Mpiga Kura karatasi hiyo ili aweze kupiga kura.
Mheshimiwa Spika, katika Uchaguzi wa mwaka 2015, Tume iliandaa karatasi maalum za kupigia kura kwa mfano wa nukta nundu kwa ajili ya Uchaguzi wa Rais pekee. Hivyo, katika chaguzi zijazo, Serikali kupitia Tume ya Taifa Uchaguzi, itaandaa karatasi hizo maalum wa kutumia mfumo wa nukta kwa ngazi zote za uchaguzi.
MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS aliuliza:-
Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) imeongeza idadi ya Majimbo ya Uwakilishi kutoka 50 hadi 54, kabla ya ongezeko hilo Majimbo ya Uwakilishi na Ubunge yalikuwa sawa kwa ukubwa, mipaka na idadi ya wapiga kura. Ongezeko hili limefanya Majimbo mawili ya uwakilishi kufanywa Jimbo moja la Ubunge:-
Je, ni lini Tume ya Taifa ya Uchaguzi itafanya uhakiki wa Majimbo ya Ubunge Zanzibar?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Haji Khamis, Mbunge wa Nungwi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Ibara ya 75 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imepewa jukumu la kuchunguza mipaka ya kiutawala na kuigawa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Majimbo ya Uchaguzi wa Ubunge. Kwa kuzingatia Ibara tajwa, Tume imepewa jukumu la kuchunguza na kugawa Majimbo ya Uchaguzi ya Ubunge mara kwa mara; na angalau kila baada ya miaka kumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mara ya mwisho Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilifanya uhakiki wa Majimbo ya Uchaguzi wa Ubunge mwaka 2015 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015. Baada ya uhakiki, jumla ya Majimbo 26 yalianzishwa kutokana na maombi 77 yaliyowasilishwa Tume kutoka Halmashauri 37 na Majimbo ya Uchaguzi 40. Hivyo, Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatarajia kuhakiki tena Majimbo ya Uchaguzi wa Ubunge katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar baada ya kutangaza kufanya hivyo kwa mujibu wa Katiba.
MHE. MUNIRA MUSTAPHA KHATIB aliuliza:-
Vyama vya Wafanyakazi nchini licha kuwa na uwezo wa kujitegemea bado vinaendelea kutoza ada kubwa ya Uanachama, mathalan, Chama cha Walimu (CWT) kinatoza asilimia mbili.
Je, Serikali haioni kuwa kuna haja ya kulinda maslahi ya Watumishi kwa kuleta Sheria ya kupunguza makato hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Munira Mustapha Khatibu, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, awali ya yote napeda kueleza kwamba, Serikali imeweka utaratibu chini ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba sita (6) ya mwaka 2004 unatoa uhuru na haki kwa Chama cha Wafanyakazi na Chama cha Waajiri, kuamua na kufanya mambo yao wanayotaka kwa maslahi yao ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusu Katiba zao. Kifungu cha 11 cha sheria hiyo, kimeeleza bayana kuhusiana na haki hizo.
Mheshimiwa Spika, katika kuimarisha na kuboresha maslahi ya Wanachama, Wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wanao uhuru na haki ya kufanya mabadiliko katika Katiba zao ambazo zinasimamia uendeshaji wa shughuli za chama chao. Hivyo, suala la kupunguza makato ya Watumishi kwa Vyama vya Wafanyakazi lipo chini ya mamlaka ya Chama cha Wafanyakazi husika na Wanchama wenyewe kupitia vikao vya kikatiba kwa kufanya mabadiliko katika Katiba ya chama chao.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kusimamia viwango vya michango ya wanachama ni kukiuka Mikataba ya Shirika la Kazi Duniani (ILO) Na. 87 na 189 juu ya uhuru wa kujumuika na majadiliano ya pamoja ambayo Serikali yetu imeridhia na kuzingatia katika Katiba ya nchi na Sheria mbalimbali za Kazi nchini.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutoa elimu juu ya haki na wajibu, uhuru wa kujumuika na mambo muhimu yahusuyo Wanachama na Katiba zao.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA aliuliza:-
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuelekeza taasisi zote nchini kuwa sifa mojawapo ya kuajiriwa iwe ni umri wa miaka 21- 35 ili kuwezesha Vijana wengi wanaotoka vyuoni kupata ajira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kiteto Zawadi Koshuma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mijibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya Mwaka 2004, Kifungu cha 5 kimekataza mtoto chini ya umri wa miaka 18 kuajiriwa isipokuwa katika mazingira maalum yaliyotajwa katika kifungu hiki. Kwa msingi huo, umri wa kuajiriwa ni miaka 18 na kuendelea pamoja na masharti yaliyotajwa katika kifungu cha 5 cha Sheria Na. 6 ya mwaka 2004. Hivyo nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuendelea kuwahimiza waajiri wote kutii Sheria za kazi na kuhakikiahsa vijana wote wenye sifa wanapomaliza mafunzo yao na kutimiza umri wa kuajiriwa wanaajiriwa kwa kuzingatia fursa zilizopo kwa waajiri na masharti ya kazi husika.
MHE. RICHARD P. MBOGO (K.n.y JAMAL KASSIM ALI) aliuliza:
Mwaka 2017, Umoja wa Afrika (AU) ulipitisha Azimio kwa nchi za Afrika la kuhakikisha kuwa nchi hizi zinavuna faida itokanayo na Demografia iliyopo kwa kuwekeza kwa vijana:-
(a) Je, Serikali ya Tanzania imechukua hatua gani katika utekelezaji wa Azimio hilo?
(b) Je, ni mafanikio gani yamepatikana kama nchi baada ya utekelezaji huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI,VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jamal Kassim Ali, Mbunge wa Magomeni kama ifuatavyo;
Mheshimiwa Spika, katika Kikao cha 29 cha Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika kilicofanyika Mjini Addis Ababa kiliweka Azimio Na. 601 lililotangaza mwaka 2017 kuwa ni mwaka wa “Kuvuna Faida itokanayo na Demografia kupitia Uwekezaji kwa Vijana” (Harnessing the Demographic Dividend Through Investments in Youth).
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azimio hilo Serikali imechukua hatua zifuatazo:-
(i) Kutoa mikopo ya kuwawezesha vijana kuanzisha na kuendelea miradi yao ya uzalishaji mali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana, ambapo katika kipindi cha mwaka 2014/2015 hadi 2019 Serikali imewezesha vikundi vya vijana 755 ambavyo vimepatiwa mikopo ya shilingi bilioni 4.2 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi.
(ii) Kurekebisha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290 ya Mwaka 2017 inayozitaka Halmashauri zote nchini kutenga fedha asilimia 10 kutokana na mapato yao ya ndani kwa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kwa ajili ya mikopo.
(iii) Kuibua bunifu 31 za vijana katika Sekta ya Sayansi na Teknolojia. Kati ya hizo, bunifu 11 zimefanyiwa tathmini ya kisayansi na kwa sasa ziko katika hatua mbalimbali ikiwemo kuwekwa kwenye kiota atamizi (incubator) kabla ya hatua ya majaribio ya uzalishaji.
(iv) Kutoa mafunzo ya ufundi stadi kwa vijana 5,875 kupitia taasisi ya Don Bosco Net Tanzania, kurasimisha ujuzi wa vijana 10,000 walioupata nje ya mfumo rasmi ya mafunzo kupitia VETA na Serikali kwa kushirikiana na waajiri imeibua fursa 1,800 za mafunzo ya vitendo mahali pa kazi, ambapo wahitimu 292 wameshapelekwa kuanza mafunzo.
(v) Kutoa mafunzo maalum ya vitalu nyumba kwa Halmashauri zote nchini ili kufikia vijana wasiopungua 18,000, tayari Mikoa 12 imeanza programu hii kwa awamu ya kwanza.
Mheshimiwa Spika, kutokana na utekelezaji wa Azimio hilo mafanikio makubwa yaliyopatikana ni pamoja na:-
(i) Ongezeko la ajira kwa vijana katika sekta binafsi;
(ii) Ongezeko la vijana wanaojitegemea kutokana na kujiajiri wao wenyewe;
(iii) Ongezeko la vijana wenye ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa; na
(iv) Upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa vijana.
MHE. RICHARD M. NDASSA aliuliza:-
Kupitia Mifuko ya Jamii tayari tathmini ya kukijenga Kiwanda cha kuchambua pamba Nyambiti Ginnery kilichopo Kwimba umeshafanyika, kilichobaki ni uamuzi wa Serikali kuliongezea thamani zao la pamba.
Je, ni lini Kiwanda hicho kitaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTHONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri napenda kujibu swali la Mheshimiwa Richard Mganga Ndasa Mbunge wa Sumve kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Jumuiya ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Nchini inayoundwa na Mifuko ya NSSF, PSSSF, NHIF, WCF na ZSSF imekamilisha mapitio mapya ya upembuzi yakinifu ya ufufuaji wa vinu vya kuchambulia pamba vya Ngasamo, Nyambiti na Kasamwa vilivyoko Mkoani Simiyu, Mwanza na Geita baada ya takwimu za uzalishaji wa kilimo cha pamba kuongezeka hususan katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Mifuko inakamilisha taratibu muhimu zinazohusiana na Miongozo ya Uwekezaji kwa kushirikiana na Vyama vya Ushirika vya Mwanza, Simiyu na Geita ili kuwezesha uwekezaji wenye ufanisi na tija taratibu zitakapokamilika.
Mheshimiwa Spika, Utaratibu maalum wa namna ya kuwezesha ufufuaji wa viwanda hivyo unatarajiwa kukamilika ndani ya mwezi Februari, 2020.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-
Wakati akiwaapisha Wakuu wa Mikoa tarehe 15/03/2016 Mhe. Rais alitoa agizo la kuwakamata vijana wote watakaokutwa wakicheza mchezo wa “pool table” na kuwapeleka kambini wakalime:-
(a) Je, Serikali imeandaa kambi ngapi na kujua huduma za kujikimu kwa vijana hao wakati watakapokuwa wakiendelea na shughuli za kilimo na kipindi cha kusubiri mavuno yao?
(b) Je, Serikali ina mpango mkakati gani wa kupunguza tatizo la ajira kwa vijana ili kuondokana na wimbi la vijana kuzurura na kushinda bila kufanya kazi?
(c) Je, Serikali imefanya sensa na kujua ni vijana wangapi wanaofanya kazi usiku na kupumzika mchana au mchana na kupumzika usiku ili kubaini wazururaji wa mchana na wanaocheza “pool table” mchana kwa sababu ya kukosa ajira?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, msingi wa agizo la Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli kuzuia vijana kucheza “pool table” wakati wa kazi umelenga kusisitiza na kuimarisha dhana na tabia ya kila mwenye uwezo wa kufanya kazi anafanya kazi katika sekta mbalimbali za kiuchumi ili kuchangia kukuza pato la Taifa na kupunguza umaskini. Katika kuhakikisha kwamba vijana wanashiriki kwenye shughuli za kiuchumi, Serikali kupitia Tawala za Mikoa na Wilaya imetenga maeneo maalum ya uzalishaji mali kwa vijana ambapo jumla ya ekari 217,882 zimeelekezwa katika kukidhi mahitaji ya shughuli za kilimo, ufugaji, viwanda na biashara ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwepo wa Vituo vya Maendeleo ya Vijana na Majengo ya Viwanda “Industrial Sheds” umesaidia kuwapa mafunzo vijana na kuwajengea uwezo wa kuongeza thamani katika mazao ya kilimo.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kuwa vijana, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati ifuatayo:-
(i) Kuwajengea vijana ujuzi kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini ili vijana kutumia ujuzi wa mafunzo mbalimbali kujiajiri na kuajiri vijana wengine. Kwa mwaka huu wa fedha, Serikali inatekeleza mafunzo ya stadi mbalimbali za kazi ambapo jumla ya vijana 49,265 watanufaika.
(ii) Kuweka mazingira bora ya uwekezaji nchini ili kuvutia uwekezaji mkubwa kwenye sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira hususani kilimo, ufugaji, madini na viwanda.
(iii) Utekelezaji wa dhana ya local content katika miradi mikubwa ya kimkakati ya Serikali katika maeneo ya uchukuzi, nishati na miundombinu ya barabara na reli.
(iv) Kuwezesha vikundi vya vijana kupitia zabuni za manunuzi ya ndani kwenye kila Halmashauri za Manispaa na Wilaya nchini Tanzania kupitia Akaunti Maalum kama mabadiliko ya mwaka 2016 ya Sheria ya PPRA yanavyoelekeza.
(v) Uwezeshwaji kiuchumi kwa vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na mikopo ya asilimia 10 za mapato ya ndani ya Halmashauri.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imelipokea wazo la kujua vijana wanaofanya kazi usiku na wanaofanya kazi mchana. Hivyo suala hili litawasilishwa katika Mamlaka ya Takwimu ili lizingatiwe katika sensa ya watu na makazi itakayofanyika mwaka 2022.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. ANNA J. GIDARYA) aliuliza:-
Kwa muda mrefu sasa Serikali imekaa kimya kuhusu ajira kwa vijana, kumekuwa na wimbi kubwa la vijana mitaani wasio na ajira waliomaliza vyuo mbalimbali takriban miaka mitatu iliyopita.
(a) Je, ni lini Serikali itafungua milango ya ajira kwa vijana wa Kitanzania walioteseka kwa muda mrefu?
(b) Je, Serikali imefanya tathmini ya kiwango cha madhara yaliyotokana na vijana kukosa ajira?
(c) Je, ni vijana wangapi wameathirika na kujiingiza katika makundi mabaya kwa kukata tamaa ya kupata ajira?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anna Joram Gidarya Mbunge wa (Viti Maalum) lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Ajira ya Mwaka 2008, Miongozo ya ILO na Kikanda, Ajira inajumuisha shughuli zinazokubalika kisheria ambazo ni za uzalishaji mali, zenye kufanikisha malengo ya kazi zenye staha na zinazozalisha kipato. Hivyo, ajira ni hali ya mtu kuajiriwa au kujiajiri kwa ajili ya kujiingizia kipato halali.
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali kama mmoja wa waajiri wakuu imeendelea kuajiri kupitia Taasisi zake mbalimbali kila mwaka kwa kuzingatia mahitaji na bajeti. Hata hivyo, kupitia Sera na Mipango mbalimbali ya Serikali katika kuchochea Uwekezaji na Viwanda, shughuli nyingi za kiuchumi zimeongezeka hali ambayo pia imesaidia katika upatikanaji wa nafasi za ajira hasa katika kundi hili kubwa la vijana. Utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati imekuwa ni chachu kubwa katika kuongeza wigo mpana wa upatikanaji ajira. Kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2018/2019 jumla ya ajira Serikalini ikijumuisha Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma zilikuwa 184,141. Aidha, katika ajira za miradi ya maendeleo ya Serikali zilikuwa 787,405, na ajira zilizozalishwa na Sekta Binafsi zilikuwa ni 646,466.
(b) Mheshimiwa Spika, Ni dhahiri kwamba ukosefu wa ajira kwa vijana una madhara kiuchumi na kijamii. Ukosefu wa ajira unapunguza mchango wa nguvukazi isiyo na ajira katika Pato la Taifa pamoja na jitihada za Serikali kupunguza umasikini. Aidha, kunapunguza uwezo wa nguvukazi hiyo kuweza kujitegemea na kuendelea kuwa tegemezi kwa jamii. Ili kupunguza tatizo hilo Serikali imeandaa mikakati mbalimbali za kuwawezesha vijana kuajiriwa au kujiajiri. Mikakati hiyo ni pamoja na utekelezaji wa Programu ya Kukuza Ujuzi nchini ambayo katika kipindi cha Mwaka 2017-2019 jumla ya vijana 47,585 wamewezeshwa kiujuzi na kujiajiri katika sekta mbalimbali.
(c) Mheshimiwa Spika, suala la vijana kujiingiza katika makundi mabaya ni suala la maadili na makuzi. Serikali kupitia Idara ya Maendeleo ya Vijana imekuwa ikiandaa miongozo ya maadili na makuzi kwa vijana na imekuwa ikiendesha mafunzo hayo kwa vijana nchini.
MHE. SIKUDHANI Y. CHIKAMBO (K.n.y. MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI) aliuliza:-
Ubunifu wa kupata ajira ni miongoni mwa changamoto kubwa kwa vijana hapa nchini:-
Je, ni lini Serikali itabuni na kusimamia mkakati wa kuwajengea uwezo wa kujiajiri vijana kuanzia shule za msingi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainabu Nuhu Mwamwindi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa mkakati wa kuwajengea uwezo wa kujiajiri vijana kuanzia elimu ya msingi ni muhimu kutokana na kuwa vijana wanapomaliza elimu ya msingi hususan ambao hawaendelei na masomo wanaingia moja kwa moja katika soko la ajira. Kutokana na umuhimu huu, Serikali imeandaa miongozo ya kufundisha masuala ya ujasiriamali na imeanza kutoa mafunzo ya ujasiriamali kuanzia shule za msingi hadi vyuo vya elimu ya juu. Mafunzo ya ujasiriamali yatawezesha vijana kuweza kuibua miradi na kuitekeleza na hatimaye kuajiri wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeandaa Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Ujuzi nchini pamoja na Programu ya Kukuza Ujuzi. Lengo ni kuhakikisha kuwa vijana wa Kitanzania wanapata ujuzi na stadi za kazi stahiki ili kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa. Kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi nchini wameendelea kupata mafunzo kupitia taasisi na vyuo mbalimbali nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019 jumla ya vijana 32,563 wamewezeshwa kupata mafunzo ya ujuzi wa kujiajiri na kuajiriwa katika sekta mbalimbali. Katika mwaka wa fedha 2019/2020 jumla ya vijana 47,000 watapata mafunzo ya stadi za kazi mbalimbali ikijumuisha mafunzo ya ujasiliamali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuimarisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana kwa kutenga fedha katika bajeti kila mwaka ambazo zinalenga kusaidia vijana kujiajiri na kuwapa mikopo ya masharti nafuu na mafunzo ya ujasiriamali mali. Aidha, kutokana na mabadiliko ya sheria yaliyopitishwa na Bunge lako Tukufu, Serikali za Mitaa zinatenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani katika kuwawezesha vijana ili waweze kujiajiri ambapo asilimia 4 ni vijana, asilimia nne ni wanawake na hata vijana wanawake na asilimia mbili ni kwa vijana wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuimarisha mikakati mbalimbali iliyopo ya kuwajengea uwezo vijana kujiajiri pamoja na kubuni mikakati mingine zaidi ili kuhakikisha kuwa vijana wetu wanapata ajira.
MHE. MARIAM D. MZUZURI (k.n.y. MHE. ESTHER M. MMASI) aliuliza:-
Kutokana na kutimizwa kwa masharti na matakwa ya Kisheria ya kutangaza Mkoa wa Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi ni dhahiri imevutia wadau wengi wa uwekezaji katika nyanja mbalimbali za kiuchumi:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kulinda ajira zisizo rasmi kwa vijana wahitimu Tanzania hasa wa Mkoa wa Dodoma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY PETER MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Michael Mmasi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kutangazwa kwa Mkoa wa Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi, kumevutia uwekezaji katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na za kijamii na hivyo kusababisha ongezeko la ajira rasmi na zisizo rasmi. Katika kulinda ajira za vijana wanaojishughulisha katika sekta isiyo rasmi, ikiwemo Mkoa wa Dodoma, Serikali inatekeleza mikakati ifuatayo:-
Kwanza, ni kuhamasisha vijana wakiwemo wahitimu kuunda makampuni katika Mkoa wa Dodoma, ambapo jumla ya makampuni 12 ya vijana yameundwa.
Pili, kuwezesha vijana kupata mikopo yenye masharti nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Vijana pamoja na mapato ya ndani ya Halamshauri, ambapo katika Mkoa wa Dodoma vijana kupitia vikundi na makampuni 978, wamewezeshwa mitaji yenye thamani ya jumla ya shilingi 2,557,090,486/= kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya kuanzisha au kuendeleza biashara zao.
Tatu, kurasimisha ajira za vijana wanaojishughulisha katika sekta isiyo rasmi kwa kuwatambua na kuwapatia vitambulisho vya mjasiriamali ili kuwawezesha kufanya shughuli zao bila kubughudhiwa.
Nne, kutoa mafunzo ya ufundi stadi katika fani mbalimbali kwa jumla ya vijana 1,240 wa Mkoa wa Dodoma, kwa lengo la kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa katika shughuli za ujenzi na biashara hapa Dodoma kupitia programu mbalimbali.
Tano, kurasimisha ujuzi uliopoatikana nje ya mfumo rasmi wa mafunzo katika kada za ufundi mbalimbali kwa vijana 245 wa Mkoa wa Dodoma ili kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa au kuendelea na mafunzo ya ngazi za juu.
Sita, kutoa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba (greenhouse) kwa vijana 18,800 nchi nzima, ambapo vijana 800 wanatoka Halmashauri nane za Mkoa wa Dodoma.
MHE. FATMA H. TOUFIQ Aliuliza:-
Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inaonesha kwamba asilimia saba ya Watanzania wanaishi vijijini lakini katika miaka ya hivi karibuni watu wengi hasa vijana, wanakimbilia mijini wakidai kuwa maisha ni magumu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kupunguza au kudhibiti hali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 asilimia 70.4 ya Watanzania wanaishi vijijini. Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 imeelekeza Serikali kuboresha na kukuza uchumi wa vijijini ili kuongeza tija ya uzaliashaji mali na kukuza uchumi katika maeneo hayo kwa lengo la kuongeza fursa zaidi za ajira kwa vijana. Katika kupunguza hali hii Serikali inatekeleza mipango ifuatayo:-
(i) Kuboresha miundombinu ya kiuchumi pamoja na huduma za jamii ikiwemo ujenzi wa barabara za vijijini, ili kuwezesha wananchi waishio vijijini kusafirisha malighafi, hasa mazao, kupeleka sehemu zenye masoko, Mpango wa Umeme Vijijini kupitia REA, ujenzi wa miradi mikubwa inayotoa fursa za ajira kwa vijana kama miradi ya ujenzi wa reli, mradi wa uzalishaji umeme Stiegler’s Gorge na kuhakikisha upatikanaji wa huduma za ugani.
(ii) Kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa SACCOS za vijana zilizoundwa katika Halmashauri ili kujenga mitaji yao kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na mifuko mingine ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ambapo katika mwaka 2017/2018 kiasi cha shilingi 783,280,000 kimetolewa kwa vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
(iii) Kutekeleza programu ya ukuzaji ujuzi nchini kwa lengo la kuwapatia vijana ujuzi utakaowawezesha kujiajiri, hususan vijijini. Mafunzo haya ni pamoja na mafunzo ya ufundi stadi kwa njia ya uanagenzi na urasimishaji wa ujuzi unaopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu ambapo katika mwaka 2018/2019 jumla ya vijana 32,563 wamewezeshwa kupata mafunzo hayo katika fani mbalimbali.
(iv) Ni kuandaa na kutekeleza mkakati wa Kitaifa wa kuwezesha vijana kushiriki katika kilimo, hususan vijijini. Mkakati huu unalenga kuwawezesha vijana wa ngazi mbalimbali za elimu kushiriki kikamilifu katika kilimo na hivyo kuongeza fursa za vijana kupitia sekta ya kilimo vijijini.
Katika kutekeleza mkakati huu Serikali inaendesha mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa teknolojia ya kitalu nyumba kwa vijana na takribani vijana 18,800 wamepata mafunzo hayo katika Halmashauri zote.
(v) Kusimamia utekelezaji wa Azimio la Wakuu wa Mikoa mwezi Novemba, 2014 lililotoa maelekezo ya kila Halmashauri nchini kutenga maeneo ya vijana na kuyatumia kwa ajili ya shughuli za uzalishaji mali na biashara katika kila Halmashauri nchini.
(vi) Kutoa fursa za upendeleo kwa vikundi vya vijana wakiwemo wahitimu na wenye ulemavu ili kuwawezesha kupata fursa ya zabuni za Serikali kupitia sheria ya ununuzi wa umma.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI (K.n.y. MHE. ESTER M. MMASI) aliuliza:-
Serikali imeonesha nia madhubuti kupitia mikakati yake ya kuinua ajira kwa Watanzania.
Je, ni kwa namna gani Serikali imejipanga kuinua ajira kwa vijana kupitia makundi maalum kama vile vijana wa kidato cha nne, darasa la saba na waendesha bodaboda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Michael Mmasi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kukuza fursa za ajira kwa vijana kupitia makundi mbalimbali ya ngazi za elimu na waendesha bodaboda, Serikali imejipanga kutekeleza yafuatayo:-
(i) Kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika sekta zote zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira, hususan kilimo na biashara, aidha, katika hili Serikali itajikita zaidi kuhamasisha na kuwezesha uwekezaji wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kufikia lengo la asilimia 40 ya nguvu kazi nchini kuwa katika sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2020 kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
(ii) Kuendelea kuimarisha utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao unalenga kuwasaidia vijana kuweza kujiajiri na kuwapa mikopo ya masharti nafuu na mafunzo ya ujasiriamali.
(iii) Ni kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Ujuzi nchini ambao umelenga kutoa mafunzo ya vitendo yatakayofanyika maeneo ya kazi ili kuwapa vijana wengi fursa za mafunzo Serikali imeanzisha programu maalum ya kutambua ujuzi uliopatikana nje ya mfumo usio rasmi na kurasimisha kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wale watakaobainika kuhitaji na kuwapa vyeti. Utaratibu huu unawapa fursa vijana wetu kuendelea na mafunzo rasmi na mfumo rasmi wa mafunzo na pia kutambulika na waajiri au watoa kazi.
(iv) Mwaka 2017 Serikali ilirekebisha Kanuni za Sheria ya Usafirishaji za mwaka 2010 kwa lengo la kuruhusu bodaboda na bajaji kubeba abiria na kurasimisha ajira ya waendesha bodaboda na bajaji.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kusimamia utekelezaji wa Azimio la Wakuu wa Mikoa la mwezi Novemba, 2014 kuhusu kuongeza fursa za ajira kwa vijana kwa kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za uzalishaji na biashara, lakini pia kutoa kipaumbele kwa kununua bidhaa na huduma zinazotolewa na vijana na kutoa mikopo ya masharti nafuu.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itasimamia na kuhakikisha Madereva wa Malori na Mabasi wanapata Mikataba ya Ajira ili kuboresha maslahi yao na kuongeza ufanisi katika Utumishi wao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Frank George Mwakajoka, Mbunge wa Tunduma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kushughulikia haki na maslahi ya Madereva nchini Tanzania, Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kutatua changamoto zinazowakabili madereva ambapo mnamo tarehe 2 Mei, 2015 Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliagiza iundwe Kamati ya Kudumu ya Kutatua Matatizo katika Sekta ya Usafirishaji chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Uchukuzi. Aidha, Kamati ndogo chini wa Uenyekiti wa iliyokuwa Wizara ya Kazi na Ajira iliundwa kwa ajili ya kushughulikia haki, maslahi na mkataba wa ajira wa Madereva.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi Madereva na Viongozi wa Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji nchini waliufanyia marekebisho na kuuboresha Mkataba wa ajira wa Madereva uliokuwepo. Mkataba ulioboreshwa uliidhinishwa na wadau katika kikao kilichofanyika tarehe 23 Juni, 2015 na ilikubalika kwamba Mkataba huo uanze kutumika rasmi tarehe Mosi, Julai, 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, masharti yamewekwa kwamba kila Mmiliki wa basi au lori anayeomba leseni ya usafirishaji toka SUMATRA ni lazima awasilishe mikataba ya ajira ya Madereva wake ambayo imehakikiwa na Maafisa wa Kazi wa maeneo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kusimamia majadiliano baina ya Vyama vya Wafanyakazi, Madereva na Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Usafirishaji ili kuwawezesha kufikia muafaka wa viwango vya posho za safari na kujikimu wakati Madereva wanaposafiri ndani na nje ya nchi.
MHE. MIRAJI J. MTATURU Aliuliza: -
Je, Serikali ina Mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa skimu ya umwagiliaji Mang’onyi ili kuongeza tija ya kilimo cha mbogamboga kwenye Kata za Mang’onyi na Makiungu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu leo ni mara yangu ya kwanza kusimama hapa, napenda nichukue fursa hii kwanza kabisa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aliyeniwezesha kufika siku ya leo na kwa Ukuu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nachukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kubwa kwangu na kuahidi kwamba nitailinda imani hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Miraji Jumanne Mtaturu, Mbunge wa Singida Mashariki, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Skimu ya Mang’onyi ambayo ipo Mkoani Singida imeendelezwa kwa kujengewa banio linalopokea maji kutoka Bwawa la Mwiyanji na takribani hekta 50 kati ya hekta 450 zimeendelezwa kwa kujengewa miundombinu ya umwagiliaji na sehemu ya shamba lililobaki hufikiwa na maji kwa njia ya asili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kukamilisha ujenzi wa Skimu ya Mang’onyi.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: -
Je, ni Mikoa ipi inaongoza kwa mafanikio katika kampeni ya kuwabadili wakulima kutoka kwenye kilimo cha kujikimu na kulima kibiashara na ni mikoa ipi bado inasuasua?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampeni ya kilimo biashara hapa nchini ilianza katika mazao yenye asili ya biashara ambayo ni pamoja na pamba, korosho, kahawa, pareto, chai, tumbaku na mkonge ambapo uhamasishaji wake ulifanyika kwa kuanzisha Vyama Vikuu vya Msingi vya Ushirika na Masoko (AMCOS).
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikoa inayolima mazao ya kibiashara ni pamoja na Mwanza, Kagera, Geita, Shinyanga, Simiyu, Mara, Tabora, Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Mtwara, Lindi na baadhi ya maeneo ya mikoa ya Arusha, Ruvuma, Mbeya, Songwe, na Iringa. Kufuatia kazi kubwa iliyofanywa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika utoaji wa elimu ya kilimo biashara na utafutaji wa masoko ya mazao, wakulima katika mikoa hii wamebadilika na kwa sasa wanalima kilimo cha kibiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikoa ambayo ilikuwa nyuma katika kutekeleza dhana ya kilimo biashara ilikuwa ni pamoja na mikoa ya Rukwa, Katavi, Kigoma, Dodoma, Singida, Morogoro, Manyara na Njombe. Mazao makuu katika mikoa hii ni yale ya nafaka, mikunde na mazao ya mafuta ambayo yalikuwa yakilimwa zaidi kwa ajili ya usalama wa chakula. Hivyo, kutokana na elimu ya kilimo biashara ambayo imekuwa ikitolewa kwa Maafisa Kilimo na wakulima katika mikoa hii, wakulima wengi wamebadilika na wanalima mazao kwa kuzingatia mahitaji ya soko.
MHE. JACKSON G. KISWAGA aliuliza: -
Je, ni kwa nini Serikali isiwalipe angalau robo ya madai Mawakala wa mbolea za ruzuku katika Jimbo la Kalenga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jackson Gedion Kiswaga, Mbunge wa Kalenga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa madai ya mawakala walioshiriki katika utoaji wa rukuzu ya pembejeo za kilimo kwa msimu wa 2014/2015 na 2015/2016 katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Jimbo la Kalenga. Wakati wa utekelezaji wa Mpango wa Ruzuku, uhakiki wa awali uliofanyika na kubaini kuwepo kwa udanganyifu. Kutokana na hali hiyo, Serikali iliamua kuchukua hatua za kufanya uchunguzi na uhakiki wa kina ili kubaini kiasi halisi cha fedha kinachopaswa kulipwa.
Mheshimiwa Spika, ninapenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa, uhakiki wa madai ya mawakala upo katika hatua za mwisho. Mara uhakiki ukiisha, malipo yatafanyika. (Makofi)
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza: -
Je, Serikali imewezesha kwa kiasi gani Maafisa Ushirika kuweza kufanya shughuli zao kwa ufanisi, ikizingatiwa kuwa kumekuwa na msukumo mkubwa sana wa kuanzisha Vyama vya Ushirika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na jitihada za kuhamasisha uanzishwaji wa Vyama vya Ushirika katika sekta mbalimbali nchini ili kujenga umoja na mshikamano katika ukuzaji uchumi wa Watanzania kupitia Ushirika. Jitihada hizo pia hufanyika sambamba na kuweka mazingira wezeshi kwa maafisa ushirika ambao wanalo jukumu la kuhamasisha uanzishwaji na uendelezwaji wa Vyama vya Ushirika. Lakini pia utoaji mafunzo ya usimamizi na uendeshaji wa ushirika kwa viongozi na wanachama wa Vyama vya Ushirika.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2021/ 2022 Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania ilitenga jumla ya shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya: -
(i) Kununua magari 13 ambayo taratibu za manunuzi zipo katika hatua za mwisho, pikipiki 137 zimenunuliwa ili kuwezesha ofisi za Warajisi Wasaidizi wa Mikoa 26 ya Tanzania Bara kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi;
(ii) Mafunzo ya usimamizi wa Vyama vya Ushirika nchini kwa Maafisa Ushirika 184 yametolewa;
(iii) Kutoa mafunzo ya uendeshaji wa Vyama vya Ushirika kwa maafisa ushirika 100;
(iv) Kuunda Mfumo wa TEHAMA utakaowezesha ufuatiliaji na usimamizi wa Ushirika nchini; na
(v) Kuendelea na kazi za usimamizi na kaguzi za mara kwa mara katika Vyama vya Ushirika 9,185.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba elimu ya kutosha inatolewa kwa viongozi na wanachama wa Vyama vya Ushirika nchini. Aidha, Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali viongozi wote wasio na uadilifu ili kuwezesha wanachama wa Ushirika wananufaika na ushirika wao.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itarejesha utoaji wa ruzuku ya pembejeo za dawa kwa wakulima wa kahawa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kutokana na kukua kwa teknolojia ambako kumewezesha kugunduliwa kwa miche chotara ya kahawa ambayo ina ukinzani na magonjwa makuu ya kahawa ya kutu ya majani na Chole Buni, Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kuzalisha miche bora ya kahawa milioni 20 yenye ukinzani mkubwa wa magonjwa na ambayo hutolewa kwa ruzuku kupitia Taasisi ya Utafiti TaCRI na Bodi ya Kahawa Tanzania.
MHE. CHARLES J. MWIJAGE aliuliza: -
Je, ni kwa nini Serikali isishirikishe sekta binafsi katika kilimo cha umwagiliaji ili kutimiza Ajenda 1030?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Charles Mwijage, Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali katika utekelezaji wa miradi yake mbalimbali katika sekta ya kilimo, imeendelea kushirikiana bega kwa bega na sekta binafsi. Kwa muktadha huo, katika miradi ya umwagiliaji ambayo Serikali inatekeleza kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeendelea kuishirikisha sekta binafsi katika hatua mbalimbali za miradi hiyo ili kufikia malengo ya Agenda 10/30. Aidha, katika mwaka 2022/2023 Serikali imepanga kukarabati na kujenga miundombinu ya umwagiliaji katika eneo la hekta 95,000, ambapo jumla ya kandarasi 55 zimetolewa kwa sekta binafsi. Mpaka hivi sasa jumla ya mikataba 21 ya Wakandarasi imesainiwa na Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha usajili wa wakulima wote nchini hasa wa mazao ya kimkakati ikiwemo pamba, korosho, kahawa, chai na michikichi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikisajili wakulima kupitia mifumo mbalimbali ikiwemo Bodi za Mazao, Sensa ya Kilimo na Vyama vya Ushirika. Hadi Agosti, 2022 jumla ya wakulima 1,499,989 wa mazao ya kimkakati ya chai wakulima 31,093, pamba wakulima 556,384, kahawa 305,261, korosho 483,034, miwa 6,746, mkonge 2,369, pareto 10,846, tumbaku 53,758 na mazao mengine 50,498, wamesajiliwa kwenye Mfumo wa Usajili wa Wakulima (Farmers Registration System) na vyama vitatu vya ushirika wa michikichi wamesajiliwa. Serikali imeanza kupitia upya mifumo ya usajili wa wakulima kwa lengo la kuwa na mfumo mmoja utakaowezesha usajili wa wakulima wa mazao yote nchini ili kurahisisha upatikanaji wa pembejeo, huduma za ugani na masoko.
MHE. DKT.OSCAR I. KIKOYO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa skimu za umwagiliaji Wilayani Muleba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Kamati Shirikishi ya Umwagiliaji Mkoa na Ofisi ya Kilimo Wilaya ya Muleba imekamilisha tathmini ya kina ya mahitaji ya sasa ya skimu za umwagiliaji za Buyaga hekta 120, Kyamyorwa hekta 500, Kyota hekta 120 na Buhangaza hekta 600 na kupata gharama halisi za umaliziaji wa ujenzi wa skimu hizo. Serikali inaendelea na zoezi la kuainisha maeneo mengine yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji Wilayani Muleba likiwemo Bonde la Buligi lenye takribani hekta 5,000.
Mheshimiwa Spika, skimu hizo zitaingizwa katika mpango wa ujenzi na ukamilishaji wa skimu za umwagiliaji katika kipindi cha mwaka 2023/2024 na 2024/2025.
MHE. DEUS C. SANGU aliuliza: -
Je, nini mpango wa kujenga Skimu ya umwagiliaji Kata za Kaoze, Kipeta na Kilangawana kwa kutumia Mto Momba Kwela?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deus Clement Sangu, Mbunge wa Kwela, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Vijijini kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kupima mabonde ya umwagiliaji yaliyopo katika Kata za Kaoze, Kipeta na Kilangawana ili kubaini eneo halisi linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji, pia ulalo wa ardhi, kiasi cha maji kwa ajili ya umwagiliaji na aina ya mioundombinu itakayohitajika.
Mheshimiwa Spika, upimaji huo utahusisha hekta 16,000 katika Kata ya Kaoze, hekta 5,000 katika Bonde la Kata ya Kipeta na hekta 7,000 katika Bonde la Maleza, Kata ya Kilangawana. Kukamilika kwa upimaji huo kutawezesha maeneo hayo kuingizwa kwenye mpango wa uendelezaji wa miundombinu ya umwagiliaji kwa kipindi cha mwaka 2023/2024 na kuendelea.
MHE. ALLY M. KASSINGE aliuliza: -
Je, ni lini Ripoti ya Ukaguzi ya Chama cha Msingi Nanjirinji ‘A’ itatolewa ili hatua zichukuliwe kwa wahujumu wa fedha msimu wa 2021/2022?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Kassinge, Mbunge wa Kilwa Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Ripoti ya Ukaguzi wa Chama cha Msingi cha Ushirika cha Nanjirinji ‘A’ ilikamilika Desemba, 2021 na kuwasilishwa kwenye Mkutano wa wanachama tarehe 23 Mei, 2022. Aidha, ukaguzi ulibaini kuwepo kwa udanganyifu katika nyaraka za mauzo ya ufuta na hivyo kusababisha malipo ya shilingi 93,476,190 kutolipwa kwa wakulima 89 waliouza kilo 39,319 za ufuta.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, Serikali imechukua hatua ya kuvunja Bodi ya Chama hicho na taarifa ya uchunguzi imewasilishwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Lindi kwa ajili ya uchunguzi zaidi na hatua za kisheria kwa waliohusika na ubadhirifu huo.
MHE. FATMA H. TOUFIQ aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza wataalam wa zao la zabibu Dodoma?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fatma Hassan Toufiq, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imepata kibali cha kuajiri watumishi wapya 100 na wengine 68 kuhamia TARI kutoka Wizarani wakiwemo Maafisa Kilimo ambao watapelekwa katika vituo vya utafiti ikiwemo Kituo cha Uendelezaji wa Zao la Zabibu TARI Makutupora. Mkakati uliopo ni kuwajengea uwezo wa kutosha wataalamu waliopo kwa kuwapatia mafunzo mahsusi ya kilimo cha zabibu na kujifunza teknolojia mpya za kilimo ili kuongeza tija katika uzalishaji wa zao la zabibu.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza: -
Je, ni kwa nini wakulima wasianze kujua bei ya kuuzia tumbaku na bei ya pembejeo kabla ya kufunga mkataba wa uzalishaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Tasnia ya Tumbaku Na. 24 ya mwaka 2001 na marekebisho yake ya mwaka 2009 na kanuni za mwaka 2011, wakulima wa tumbaku wanapaswa kufunga mikataba ya uzalishaji wakiwa wanajua bei ya kuuzia tumbaku na bei ya pembejeo za kilimo. Huu ndio utaratibu uliopo unaoendelea kusimamiwa na Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku Tanzania. Katika msimu wa mwaka 2022/2023, tayari wakulima wamepata bei ya tumbaku na pembejeo tangu tarehe 30 Agosti, 2022. Kutokana na masoko yaliyopatikana bei elekezi imepanda kutoka Dola za Marekani 1.65 mwaka 2021/2022 hadi Dola za Marekani mbili mwaka 2022/2023 kwa kilo ya tumbaku, sawa na ongezeko la asilimia 21.
MHE. ZAYTUN S. SWAI K.n.y. MHE. DANIEL A. TLEMAI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kurekebisha miundombinu ya Skimu ya maji katika Kijiji cha Mbuganyekundu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Awack Tlemai, Mbunge wa Karatu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kujenga miundombinu ya umwagiliaji ya skimu zilizopo katika bonde la Eyasi zenye jumla ya hekta 5,000 ikiwemo skimu ya Mbuganyekundu. Taratibu za kuwapata wakandarasi wa ujenzi wa skimu hizo unaendelea ambapo zabuni zimeshatangazwa.
MHE. SOUD MOHAMMED JUMAH aliuliza: -
Je, kuna mpango gani kuboresha The National Herbarium of Tanzania Arusha ili
kuimarisha huduma za utafiti na uhifadhi wa Mimea nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Soud Mohammed Jumah, Mbunge wa Donge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, The National Herbarium of Tanzania ilianzishwa kwa Sheria ya TPRI ya Mwaka 1979. Ili kuimarisha utendaji wa Taasisi za Wizara, Serikali imeunda Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA) iliyoanzishwa kwa Sheria Na. 04 ya Mwaka 2020 kwa kuunganisha Sehemu ya Afya ya Mimea iliyokuwa chini ya Wizara ya Kilimo na Mamlaka ya Utafiti wa Viuatilifu vya Kitropiki (TPRI).
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha The National Herbarium of Tanzania na kuimarisha Huduma za Utafiti na Uhifadhi wa Mimea, Serikali imepanga kuendeleza kuimarisha kanzidata ya mimea ya Tanzania inayohifadhi sampuli kavu ndani ya National Herbarium of Tanzania (NHT) pale Arusha, Mweka, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine na TAFORI. Aidha, Serikali kupitia TPHPA inaendelea Kuorodhesha, kukusanya na kutambua sampuli za mimea katika misitu ya hifadhi nne ambazo ni Mlima Hanang, Chenene, Salanga na Chemichemi, katika mikoa ya Manyara na Dodoma.
MHE. BONIPHACE N. BUTONDO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itawatafutia wakulima wa Kishapu Masoko ya Mazao ya Mtama na Uwele?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Nyangindu Butondo, Mbunge wa Kishapu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la mahitaji ya zao la mtama na uwele kwa ajili ya matumizi ya viwanda vya ndani ya nje ya nchi. Kutokana na ongezeko la mahitaji hayo, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali kuhakikisha wakulima wa mazao hayo wanapata masoko ya uhakika.
Mheshimiwa Spika, mikakati hiyo ni pamoja na kuzalisha mbegu bora zinazokidhi mahitaji ya soko, kuwaunganisha wakulima na wanunuzi wa ndani kama TBL ambao wameanza kununua mazao hayo katika Mikoa ya Dodoma na Manyara na kufungua Vituo vya Mauzo katika Mji wa Juba, Sudan Kusini na Lubumbashi Nchini Congo.
MHE. KASALALI E. MAGENI K.n.y. MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora za alizeti kwa wakulima ili kuzalisha mafuta ya kula?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Askofu Josephat Mathias Gwajima, Mbuge wa Kawe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ili kuhakikisha kuwa, nchi yetu inazalisha alizeti itakayo changia kwa kiasi kikubwa katika kuzalisha mafuta ya kula na kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mafuta ya kula, Serikali imepanga kuongeza uzalishaji wa zao la alizeti kwa kuongeza uzalishaji wa mbegu bora kutoka tani 1,500 zilizokuwepo awali hadi tani 5,000 kwa lengo la kuongeza eneo kubwa zaidi la uzalishaji wa alizeti ili kuweza kufikia malengo; Kuendelea kutekeleza mkakati wa uandaaji wa mashamba makubwa zikiwemo block farms ambayo kwa asilimia kubwa yatatumiwa na wakulima kwa kilimo cha alizeti; na Wakala wa Mbegu (ASA) tayari ameanza usambazaji wa mbegu bora ya alizeti aina ya record ambayo imethibitishwa ubora na inauzwa kwa bei ya ruzuku ili kuhakikisha kwamba inamletea tija mkulima.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha pembejeo za korosho kwa msimu wa mwaka 2022/2023 zinapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya pembejeo za zao la korosho katika msimu wa 2023/2024 ni tani 70,000 za salfa ya unga na lita 3,400,000 za viuatilifu vya maji, mabomba 10,000 na magunia 6,200,000. Wizara kupitia Bodi ya Korosho Tanzania inasimamia upatikanaji wa pembejeo za korosho kabla ya msimu kuanza. Tarehe 15 Oktoba, 2022, Kamati ya Ununuzi wa Pembejeo kwa pamoja ilisaini mikataba na kampuni 14 kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo hizo.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania inaendelea kuratibu zoezi hilo ili kuhakikisha kuwa pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati na bei itakayopangwa kulingana na mahitaji.
MHE. NANCY H. NYALUSI K.n.y. MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza: -
Je, lini skimu za umwagiliaji Ukanda wa joto Ihowanza, Malangali, Idunda, Mbalamaziwa, Itandulu, Nyololo na Maduma zitajengwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi Kusini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika Mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 itatenga fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa skimu za Ukanda wa joto za Ihowanza, Malagali Idunda, Mbalamaziwa, Itandu, Nyololo na Maduma. Baada ya kukamilisha zoezi hili Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza ujenzi wa skimu hizo.
MHE. DAVID M. KIHENZILE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga miradi ya umwagiliaji katika Tarafa ya Malangali ili wananchi waweze kushiriki katika kilimo cha umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa David Mwakiposa Kihenzile, Mbunge wa Mufindi Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Iringa unakadiriwa kuwa na eneo linalofaa kwa kilimo la hekta 54,000. Kati ya hizo hekta 20,017 zinamwagiliwa ambapo hekta 16,789 zinamwagiliwa kipindi cha masika na hekta 3,550 zinamwagiliwa kipindi cha kiangazi.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na uhakiki wa maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji katika Wilaya ya Mufindi ambapo hadi sasa skimu nne (4) zenye jumla ya hekta 1,800 zimehakikiwa na kuwekwa kwenye mpango wa umwagiliaji. Aidha, Tume inaendelea na uhakiki wa maeneo mengine yanayofaa kwa umwagiliaji ikiwemo Tarafa ya Malangali.
Mheshimiwa Spika, zoezi la uhakiki litakapokamilika, Tume ya Umwagiliaji itaandaa mpango kazi utakaoainisha kazi zitakazofanyika katika skimu hizo.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga soko la mazao la Kimataifa katika eneo la Mbimba TACRI Vwawa ili Wananchi wapate soko la uhakika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa kilimo na ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi imetenga ekari 25 kwa ajili ya ujenzi wa soko ambapo eneo hilo limeshafanyiwa upembuzi yakinifu kwa kushirikiana na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA). Aidha, gharama za ujenzi wa soko hilo ni takribani shilingi 14,117,640,924.91. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Skimu za Umwagiliaji katika Jimbo la Mbogwe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicodemas Henry Maganga, Mbunge wa Mbogwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na zoezi la utambuzi na uhakiki wa maeneo zaidi yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe. Hadi sasa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na wananchi wa Mbogwe wameweza kuibua Skimu ya Mugelele yenye eneo la ukubwa wa hekta 300. Aidha, baada ya zoezi hilo kukamilika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itatenga fedha katika bajeti ya mwaka 2023/2024 kwa ajili ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Skimu ya Umwagiliaji ya Igurubi katika Jimbo la Igunga?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nicholaus George Ngassa Mbunge wa Igunga, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya umwagiliaji imepanga kufanya mapitio, upembuzi yakinifu na usanifu kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji katka Skimu ya Igurubi. Aidha, mara baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu na gharama ya ujenzi kujulikana, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itatenga fedha katika bajeti ya mwaka 2024/2025 kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo.
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kufufua kilimo cha zao la muhogo katika Mkoa wa Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ilianzisha Mradi wa Kufufua Zao la Muhogo katika Kanda ya Ziwa Victoria na Kanda ya Pwani ukiwemo Mkoa wa Mtwara mwaka 2015. Awamu ya Kwanza ya mradi huo iliisha mwanzoni mwa mwaka 2021, awamu ya pili imeanza Disemba, 2021 na inategemewa kwisha mwaka 2024. Kupitia mradi huu uzalishaji wa muhogo katika Mkoa wa Mtwara umeongezeka kutoka tani 611,210 kwa mwaka 2016/2017 hadi tani 866,676 kwa mwaka 2019/2020.
Mheshimiaw Spika, kutokana na kuongeza utoaji wa huduma za ugani na uzalishaji wa mbegu za muhogo. Jumla ya vipando bora vya muhogo pingili milioni 30.4 kwa mwaka 2019/2020 hadi pingili milioni 40 kwa mwaka 2020/2021 zenye uwezo wa kutoa mavuno mengi kuhimili mabadiliko ya tabia nchi na magonjwa zilizalishwa na kusambazwa kwa wakulima.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itafanya kilimo kuwa kipaumbele cha kwanza cha Taifa kwa kupunguza bei ya mbolea?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Hebron Mwakagenda Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya kupanda kwa bei ya mbolea katika msimu wa mwaka 2020/2021. Katika kukabiliana na changamoto hiyo, msimu wa mwaka 2022/2023 Serikali inatekeleza mpango wa utoaji wa mbolea za ruzuku kwa wakulima ili kuwaongezea uwezo wa kununua na kutumia mbolea. Hadi kufikia tarehe 31 Januari, 2023 jumla ya tani 246,714 za mbolea zimenunuliwa na wakulima kwa bei ya ruzuku ikilinganishwa na tani 173,957 za mbolea ambazo zilinunuliwa katika kipindi cha mwezi Julai hadi Januari, 2021.
MHE. NEEMA K. LUGANGIRA aliuliza: -
Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha mbegu za asili zenye virutubisho zinatambulika kisheria, zinalindwa, zinahifadhiwa na kusajiliwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Kichiki Lugangira, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanzisha Kitengo cha Taifa cha Hifadhi ya Nasaba za Mimea chini ya Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kwa ajili ya kuzitambua na kuzihifadhi nasaba za mimea ikiwemo mbegu za asili za mazao ya kilimo zilizopo nchini. Hadi kufikia Desemba, 2022, sampuli 10,000 ya nasaba za mimea zimekusanywa kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini na kuhifadhiwa katika Benki ya Taifa ya Kuhifadhi Nasaba za Mimea iliyopo Makao Makuu ya TPHPA - Arusha. Serikali imeanza kutekeleza taratibu za kuandaa mapendekezo ya kutunga Sheria ya Hifadhi ya Nasaba za Mimea ambayo itabainisha taratibu za kisheria za kuzitambua, kuzisajili, kuzihifadhi na kutumia mbegu za asili za mazao zilizopo nchini.
MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO K.n.y. MHE. TIMOTHEO P. MNZAVA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia upatikanaji wa chakula cha bei nafuu kwa wananchi walioathirika na ukame nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava, Mbunge wa Korogwe Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imeendelea kutoa chakula na kukiuza chini ya bei ya soko. Hadi kufikia tarehe 31 Januari, 2023, kiasi cha mahindi tani 24,975 zimepelekwa na kuuzwa katika Halmashauri 60 nchini katika vituo vya mauzo 116. Katika Halmashauri ya Korogwe, kituo cha mauzo kimefunguliwa eneo la Masewa tarehe 27 Januari, 2023. Jumla ya tani 32 zimepelekwa na tani 10 zimeshanunuliwa.
MHE. HAMISI S. TALETALE aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kukuza kilimo cha mazao ya viungo katika Wilaya ya Morogoro Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamisi Shabani Taletale, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeandaa mkakati wa kuendeleza mazao ya bustani (National Horticulture Development Strategy 2021 - 2031) yakiwemo mazao ya viungo. Ambapo mazao ya iliki, karafuu, vanilla, pilipili manga, tangawizi na mdalasini ni kati ya mazao ya bustani yaliyopewa kipaumbele katika mkakati huo unaolenga kuongeza uzalishaji wa mazao, kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza Pato la Taifa linalotokana na mazao hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya ya Morogoro Vijijini Serikali kwa kushirikiana na Sustainable Agricultural Tanzania (SAT) inatekeleza mradi wa kuendeleza mazao ya viungo katika maeneo yanayozunguka Milima ya Uluguru (Uluguru Spice Project) kuanzia mwaka 2017. Mradi huu umenufaisha wakulima 1,668 katika vijiji 27 vilivyopo Kata za Tawa, Kibongwa, Konde, Kibungo, Mtombozi, Kisemu, Mkuyuni, Kinole. Vilevile, katika kuimarisha uendelezaji wa mazao ya viungo, Chama cha Msingi cha Ushirika wa Wakulima wa Viungo (CHAUWAVIMU) kimesajiliwa kwa lengo la kuimarisha uendelezaji wa mazao ya viungo (pilipili manga, mdalasini, karafuu, taangawizi, iliki na vanilla) katika Wilaya ya Morogoro Vijijini.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji Mwakijembe pamoja na bwawa la kukinga maji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dunstan Luka Kitandula Mbunge wa Mkinga kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, skimu ya umwagiliaji inakadiriwa kuwa na jumla ya hekta 450. Hekta 200 katika Kijiji cha Mwakijembe na hekta 250 katika Kijiji cha Mbuta ambazo zinafaa kwa kilimo cha umwagiliaji wa mazao makuu yakiwa ni mahindi, maharage na mbogamboga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeanza kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika skimu zilizopo katika Bonde la Mto Umba ikiwemo skimu ya Mwakijembe kwa lengo la kupata gharama halisi za ujenzi. Baada ya kukamilisha zoezi la upembuzi yakinifu na usanifu wa kina skimu hii itaingia katika mpango wa ujenzi wa mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza: -
(a) Je, ni kwa nini Serikali isiongeze uzalishaji wa mafuta ya alizeti nchini kwa ajili ya Soko la Zanzibar na Bara kuliko kuagiza kutoka nje ya nchi?
(b) Je, hali ya uzalishaji wa mafuta ya alizeti ikoje kwa mwaka na ni mikoa gani inayozalisha zaidi Tanzania Bara?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mkakati wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta nchini kwa lengo la kupunguza uagizaji wa mafuta ya kula na kuongeza uzalishaji kutoka wastani wa tani 700,000 hadi tani 1,500,000 ifikapo mwaka 2025. Utekelezaji wa mpango huo unajumuisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji kwenye mashamba ya mbegu ya Wakala wa Mbegu za Kilimo ambapo kwa mwaka 2022/2023 jumla ya shilingi bilioni 43.03 zitatumika kwa lengo hilo.
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya mafuta ya kula nchini ni tani 650,000 kwa mwaka. Tathmini ya mwaka 2020/2021 inaonesha kuwa uzalishaji wa ndani wa mafuta ya alizeti ni asilimia 75 ya kiasi cha wastani wa tani 300,000 za mafuta ya kula yanayozalishwa nchini kwa mwaka. Mikoa inayozalisha alizeti kwa wingi ni Singida, Dodoma, Manyara, Shinyanga, Iringa, Tabora, Morogoro, Ruvuma, Mbeya, Arusha, Lindi, Mtwara, Rukwa na Mara.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kutoa chakula cha bei nafuu kwa wananchi wa Jimbo la Arumeru Magharibi kutokana na athari za ukame?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Noah Lemburis Saputu, Mbunge wa Arumeru Magharibi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imeendelea kutoa chakula na kukiuza chini ya bei ya soko. Hadi kufikia tarehe 31 Januari, 2023 kiasi cha mahindi tani 24,975.152 zimepelekwa na kuuzwa katika Halmashauri 60 nchini katika vituo vya mauzo 116. Halmashauri ya Arumeru, kituo cha mauzo kimefunguliwa eneo la Kikatiti na jumla ya tani 6.28 zimeshauzwa kwa Wananchi.
MHE. ZUENA A. BUSHIRI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga skimu katika vijiji vya Maore, Mpirani, Kadando na Mheza?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuena Athumani Bushiri, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa skimu zilizopo katika vijiji vya Maore, Mpirani, Kadando na Mheza ili kupata gharama halisi za ujenzi. Baada ya zoezi la upembuzi yakinifu kukamilika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itatenga fedha katika bajeti ya mwaka 2024/2025 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuzalisha Mbegu bora za Parachichi aina ya Hass na kuzigawa kwa wakulima kwa bei nafuu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli miche ya parachichi katika baadhi ya maeneo imekuwa ikiuzwa kwa bei kati ya shilingi 5,000 hadi shilingi 6,000 ambapo baadhi ya wananchi wanashindwa kumudu, kwani ekari moja inahitaji miche siyo chini ya 70 na kwa ekari 10 utahitaji shilingi 3,500,000 kwa ajili ya miche tu iwapo bei ya mche ni shilingi 5,000.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia TARI inatarajia kuanza uzalishaji wa miche ya parachichi milioni 20. Miche hiyo itauzwa kwa bei ya ruzuku ya chini ya shilingi 2,000. Aidha, katika kudhibiti ubora wa wazalishaji binafsi, Serikali kupitia Taasisi ya Uthibiti Ubora wa Mbegu (TOSCI) imeanza usajili wa wazalishaji wa miche ya parachichi nchini. Pia katika kuhakikisha usimamizi bora wa zao hili, Serikali inatarajia kuzindua mwongozo wa uzalishaji wa zao la parachichi.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kutatua changamoto zinazokabili Miradi ya Umwagiliaji ya Mkoga na Kitwiru iliyopo Manispaa ya Iringa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Miradi ya umwagiliaji ya Cherehani Mkoga yenye hekta 750 na Kitwiru yenye hekta 100 iliyopo katika Manispaa ya Iringa inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo uchakavu wa miundombinu ya umwagiliaji iliyojengwa muda mrefu; kutokamilika kwa miundombinu, pamoja na miundombinu kuharibiwa na mafuriko.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Umwagiliaji inaendelea kutafuta fedha kutoka kwa wadau wa maendeleo kwa ajili ya kukamilisha miradi ya umwagiliaji mbalimbali ikiwemo miradi ya Mkoga na Kitwiru.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza bei za mbolea zinazopanda kwa kasi kwenye Soko la Dunia ili kumpunguzia mkulima mzigo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza, Mbunge wa Mbeya Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2021/2022 bei ya mbolea imeendelea kupanda katika Soko la Dunia kutokana na athari za UVIKO-19 na Vita ya Urusi na Ukraine zilizosababisha kupungua kwa uzalishaji na ongezeko la gharama za malighafi zinazotumika kutengeneza mbolea.
Mheshimiwa Spika, kutokana na hali hiyo, Serikali imeanza kuchukuliwa hatua za haraka, muda wa kati na muda mrefu katika kukabiliana na changamoto ya kupanda kwa bei. Hatua za haraka ni pamoja na kudhibiti upandaji holela wa bei usiozingatia gharama halisi za uingizaji mbolea nchini kwa kutangaza bei elekezi zinazopaswa kuzingatiwa na wafanyabiashara katika maeneo ya uzalishaji.
Mheshimiwa Spika, Serikali imekutana na uongozi wa kiwanda cha mbolea cha Minjingu kwa lengo la kuzipatia ufumbuzi changamoto za kiwanda ili kuhakikisha kinaongeza uzalishaji wa mbolea kutoka wastani wa tani 30,000 hadi kufikia tani 100,000 kwa mwaka. Aidha, Serikali inaendelea kuhamasisha wawekezaji wapya wa viwanda vya mbolea ambapo kampuni ya Intracom Fertilizers Limited kutoka Burundi imejitokeza na inajenga kiwanda katika Mkoa wa Dodoma chenye uwezo wa kuzalisha tani 600,000 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, hatua hizo zinazochukuliwa na Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi zitasaidia kupunguza bei ya mbolea.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanzisha Wakala wa kudhibiti Mazao ya Mbogamboga na Matunda nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa, Deodatus Phillip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu mkubwa wa kuwa na Mamlaka ya kusimamia na kuendeleza tasnia ya mazao ya bustani kutokana na mchango mkubwa wa tasnia hiyo kwenye mapato ya fedha za kigeni.
Mheshimiwa Spika, Wizara imeandaa mapendekezo ya kufanya marekebisho madogo Miscellaneous Amendment ya Sheria ya Usalama wa Chakula Na. 10 ya mwaka 1991 iliyoanzisha Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko - Cereal and Other Produce Regulatory Authority, ambapo pamoja na mambo mengine majukumu ya Mamlaka hiyo yatarekebishwa ili kuipa jukumu mahsusi la usimamizi na uendelezaji wa tasnia ya bustani.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mgambalenga Wilayani Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Justine Lazaro Nyamoga, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2022/ 2023, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu ya Mgambalenga yenye hekta 3,000 Wilayani Kilolo. Ujenzi huo utahusisha ukamilishaji wa mfereji mkuu wenye urefu wa kilometa 14 pamoja na maumbo yake.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha Mkoa wa Rukwa unalima zao la maharage ya soya lenye uhitaji mkubwa zaidi duniani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Rukwa ni moja ya mikoa inayozalisha maharage ya soya kwa wingi nchini kwa ajili ya chakula na biashara. Katika mwaka 2020/2021 mkoa ulizalisha jumla ya tani 121,356 katika eneo la hekta 120,432. Mwaka 2021/2022 mkoa umelenga kuzalisha jumla ya tani 128,672 za maharage katika eneo la hekta 121,961.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuendeleza kilimo cha maharage ya soya Mkoani Rukwa, Serikali kwa kushirikiana na wadau imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuimarisha upatikanaji wa mbegu bora za maharage ya soya nchini kupitia sekta binafsi, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI-Uyole) na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) na kupitia vikundi vya wakulima wazalishaji wa mbegu za daraja la kuazimiwa ubora (QDS) na kutoa mafunzo ya uzalishaji wa maharage ya soya kwa Maafisa Ugani 64 katika ngazi ya Halmashauri, kata na vijiji ili kuwezesha wakulima kuzalisha kwa tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, Maafisa Ugani hao wanatumika katika kutoa ushauri na kuandaa mashamba ya mfano ya kilimo cha maharage ya soya katika maeneo yao, kupima afya ya udongo ili kuwezesha matumizi sahihi ya pembejeo za kilimo, kuhamasisha kilimo cha mkataba kati ya wakulima na wanunuzi ili kuwa na uhakika wa soko la mazao ya wakulima wanaolima maharage ya soya nchini.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha mchakato wa kuanza Kilimo cha Umwagiliaji katika Bonde la Mto Luiche Mkoani Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix Mbunge wa Buhigwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji katika Bonde la Mto Luiche lililopo katika manispaa ya Kigoma Ujiji mkoa wa Kigoma. Bonde hilo linauwezo wa kumwagilia hekta 3,000 na kunufaisha wakulima wa vijiji vitatu vya Mahembe, Nyangofa na Kidawe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujenzi wa skimu hii utaanza mwaka wa fedha 2022/2023. Utekelezaji wa mradi huu unafadhiliwa na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait (Kuwait Fund for Arab Economic Development) ambapo litajegwa bwawa lenye mita za ujazo milioni 70, ujenzi wa mfereji mkuu Kilomita 10 na mifumo ya umwagiliaji. Serikali imepata kibali (No Objection) kutoka kwa wafadhili mwezi Aprili, 2022 kwa ajili ya kufanya mapitio ya usanifu na kutafuta mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa Luiche.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaruhusu kampuni zinazonunua tumbaku kwenda kwenye AMCOS kujinadi ili kuongeza ushindani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Jimbo la Ushetu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Hapo awali Serikali iliruhusu kampuni za ununuzi wa tumbaku kujinadi kwa wakulima na kuingia mikataba kwa misimu mitatu ya kilimo. Kilimo cha mikataba kwa misimu mitatu kiliathiri bei ya Tumbaku kwa mkulima kutokana na ongezeko la gharama za uendeshaji kampuni na uzalishaji. Jambo hilo lilisababisha Serikali kubadili mfumo huo na kwenda mfumo wa msimu mmoja ili kuongeza ushindani na ufanisi.
Mheshimiwa Spika, Kilimo cha mkataba kwa msimu ni mbadala mzuri kwa wakulima na kampuni kwasababu kinapunguza gharama zinazotokana na kampuni kujinadi. Vilevile, kilimo hicho kinatoa fursa kwa pande zote mbili kujitathmini kabla ya kuingia mkataba kwa msimu unaofuata.
MHE. ORAN M. NJEZA aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kukabiliana na kupanda kwa bei za pembejeo za kilimo ikiwemo mbolea?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oran Manase Njeza Mbunge wa Mbeya Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepanga mikakati ya muda mfupi, kati na ya muda mrefu katika kukabiliana na kupanda kwa bei za mbolea hapa nchini. Mikakati hiyo ni pamoja na kutekeleza Mpango wa Utoaji Ruzuku ya Mbolea kwa wakulima msimu wa 2022/2023, kuhimiza matumizi ya mbolea mbadala wa DAP na UREA kama vile NPK, NPS, NPS- zinc, Minjingu, mbolea za asili na chokaa, kupunguza gharama za meli kukaa bandarini ambazo pengine mwisho wake hujumuishwa kwenye mjengeko wa bei ya mbolea, kuhimiza wafanyabiashara wa mbolea kutumia njia ya reli ya TAZARA na Reli ya Kati kusafirisha mbolea kwa wingi kwenda mikoani na kuhamasisha uwekezaji katika kuzalisha mbolea ndani ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kupitia mpango wa ruzuku ya mbolea, Serikali imeweka bei elekezi ili kuwawezesha wakulima kununua mbolea za DAP, Urea na NPK kwa Shilingi 70,000 kwa mfuko wa kilo 50, Shilingi 60,000 kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya CAN na Shilingi 50,000 kwa mfuko wa kilo 50 wa mbolea ya SA. Aidha, Serikali inaendelea kushirikiana na Sekta Binafsi vikiwemo viwanda vya Minjingu Mines and Fertilizer Limited na Itracom Fertilizers Limited kuhakikisha uzalishaji na upatikanaji wa mbolea hapa nchini kwa gharama nafuu unaimarika na kupunguza utegemezi wa kuagiza mbolea kutoka nje ya nchi.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE K.n.y. MHE. GHATI Z. CHOMETE aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wakulima wa Tarime wanaolima kahawa aina ya Arabika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ghati Zephania Chomete, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Bodi ya Kahawa inaendelea kukiwezesha na kukiongezea uwezo Kituo Kidogo cha Utafiti wa Kahawa (TaCRI) kilichopo eneo la Nyamwaga Tarime ili kuzalisha miche milioni moja kwa mwaka. Miche hiyo inaendelea kuzalishwa na kusambazwa bure kwa wakulima wa Kahawa Wilaya ya Tarime na Wilaya nyingine za Mkoa wa Mara. Kupitia jitihada hizi kuanzia mwezi Septemba, 2022 hadi kufikia mwezi Machi, 2023 jumla ya miche 173,471 imezalishwa na kugawiwa bure kwa wakulima. Aidha, Serikali imeboresha mfumo wa masoko kwa kuwezesha kuanza kufanya kazi kwa mitambo ya kuchakata kahawa katika maeneo ya Muriba na Nyantira.
MHE. JOSEPH Z. KAMONGA K.n.y. MHE. LUHAGA J. MPINA aliuliza: -
Je, nini kimesababisha mbolea kuadimika na kuleta hasara kwa Wakulima na Wawekezaji nchini katika msimu wa mwaka 2022/2023?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nchi katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/2023 hatukuwa na uhaba wowote wa mbolea. Vilevile Serikali haijapokea malalamiko yoyote kutoka kwa wakulima na wawekezaji yanayohusu kupata hasara kutokana na kuadimika kwa mbolea. Changamoto pekee ilijitokeza ilikuwa ni mwamko mkubwa wa wakulima kuhitaji kununua mbolea kuliko uwezo wa mtandao wa mawakala, ambapo Serikali imeendelea kuipatia ufumbuzi na kuongeza idadi ya mawakala kutoka 1,392 mwezi Agosti, 2022 hadi 3,265 mwezi Machi, 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, makadirio ya mahitaji ya mbolea kwa msimu wa 2022/2023 yalikuwa ni tani tani 667,730 na hali ya upatikanaji wa mbolea hadi kufikia mwezi Machi, 2023 umefikia tani 748,890 sawa na asilimia 112 ya mahitaji ya mbolea ndani ya nchi, ikilinganishwa na kipindi kama hicho kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha mapitio ya kubaini madawa na vihatirishi vinavyosababisha madhara na vinaendelea kutumika katika Kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania hutekeleza utaratibu wa kubaini viuatilifu na vihatarishi vinavyosababisha madhara kwa mazao, mimea na afya ya binadamu na wanyama. Utaratibu huo hufanyika kulingana na kifungu cha 54 cha Sheria Na. 4 ya Afya ya Mimea ya mwaka 2020 kinachompa Mamlaka Msajili wa viuatilifu nchini kufuta usajili wa viuatilifu vinavyosababisha madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2018 hadi 2021, Serikali ilifanya mapitio ya kubaini viuatilifu vyenye madhara makubwa kwa afya ya binadamu na mazingira vijulikanavyo kama Highly Hazardous Pesticides. Mapitio hayo yalibaini aina ya viuatilifu 44 vyenye viambata amalifu vyenye madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia hatua hiyo, Serikali kupitia TPHPA imeanza kuchukua hatua za kusitisha matumizi ya viuatilifu 44 vilivyobainika na inaendelea kufanya kaguzi za mara kwa mara katika maghala na maduka ya viuatilifu ili kubaini uwepo wa viuatilifu vingine vyenye madhara.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatafuta soko la uhakika la zao la vanilla?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Benardeta Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi inatekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha wakulima, wakiwemo wa zao la vanilla, wanapata soko la uhakika. Mikakati hiyo ni pamoja na kuhamasisha kilimo cha kibiashara kinachozingatia mahitaji ya soko, kushiriki makongamano na maonesho ya kibiashara na uwekezaji, ujenzi wa miundombinu ya masoko na kuimarisha mifumo ya kielektroniki ambayo itasaidia upatikanaji wa taarifa za masoko.
Mheshimiwa Spika, Serikali inahamasisha sekta binafsi kuwekeza katika uongezaji thamani wa zao la vanilla ili kupanua wigo wa soko la zao hilo. Aidha, wakulima wa vanilla wanahimizwa kuvuna vanila zilizokomaa ili kukidhi mahitaji ya soko hususani vanillin isiyopungua asilimia 1.8 na unyevu wa wastani wa asilimia 25 hadi 30.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaondoa makato yaliyopo kwenye Vyama vya Msingi kwa Wakulima wa Kahawa Mbozi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, Mbunge wa Mbozi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na mapitio ya makato yaliyopo kwenye vyama vya ushirika kwa wakulima katika mazao mbalimbali ikiwemo zao la kahawa. Kufuatia malalamiko tuliyoyapokea kutoka kwa wakulima wa kahawa Mkoani Songwe, Serikali iliunda Timu kwa ajili ya kufuatilia na kufanya tathmini kuhusu masuala mbalimbali yahusuyo zao la kahawa ikiwemo suala la makato.
Mheshimiwa Naibu Spika, Timu hiyo imekamilisha tathmini na inatarajia kuiwasilisha Wizarani mapema Mwezi ujao. Hivyo, baada ya kupitia taarifa hiyo ya tathmini, Serikali itachukua hatua stahiki.
MHE. SHALLY J. RAYMOND aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kujenga Mabwawa ya kuvuna maji ya Mvua pamoja na mifereji ya umwagiliaji ili kupunguza athari za mvua katika Mkoa wa Kilimanjaro?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Shally Josepha Raymond Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kilimanjaro ni miongoni mwa mikoa ambayo ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya kuvuna maji ya mvua pamoja na ujenzi wa mifereji ya umwagiliaji umeendelea ili kupunguza athari za mvua na kusaidia wakulima kujihakikishia kilimo cha mwaka mzima kupitia umwagiliaji.
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imekamilisha mapitio ya usanifu wa ukarabati wa Bwawa la Ikuini na taratibu za kumpata mkandarasi kwa ajili ya ukarabati wa bwawa hilo unaendelea.
Mheshimiwa Spika, aidha, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa bwawa la Boloti na Yongoma sambamba na mifereji itakayoweza kuhudumia takribani hekta 2,000 ndani ya Wilaya ya Same.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kuwawekea mazingira mazuri Wakulima wadogo wa kilimo cha Umwagiliaji katika Mto Ruvu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Michael Constantino Mwakamo, Mbunge wa Kibaha Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inaendelea na hatua mbalimbali za kuboresha mazingira ya kilimo kwa wakulima wadogo ndani ya Bonde la Mto Ruvu kwa kubaini maeneo yanayofaa kwa ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa Skimu ya Kisere (Nyani), usanifu huu ukikamilika ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji utaanza katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kuwa na Sera ya kuongeza tija katika sekta ya kilimo kwenye Mikoa ya Kanda ya Kati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Kilimo ya Taifa ya mwaka 2013, inatambua umuhimu wa kuongeza tija kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo. Kupitia sera hiyo, maeneo ya
kipaumbele ya kuongeza tija ni pamoja na kuimarisha utafiti, kuongeza upatikanaji wa pembejeo bora za kilimo (mbegu, mbolea na viuatilifu), kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji, kupima udongo, kuimarisha matumizi ya zana bora za kilimo na kuimarisha huduma za ugani katika kanda zote za Ikolojia nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza miradi ya umwagiliaji katika Mikoa ya Kanda ya Kati – Dodoma, Singida na Tabora kwa kujenga mabwawa saba na skimu za umwagiliaji kumi; uimarishwaji wa Vituo vya Utafiti vya Tumbi, Makutupora na Hombolo; usambazaji wa mbegu bora kwa wakulima; na uimarishwaji wa huduma za ugani ikiwa ni mkakati katika utekelezaji wa Sera ya Kilimo ya Taifa ya Mwaka 2013.
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: -
Je, lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kukamilisha Mradi wa Skimu ya Umwagiliaji wa Kyakakera uliopo katika Kata ya Kyaka?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo Mbunge wa Nkenge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Skimu ya umwagiliaji ya Kyakakera ni miongoni mwa skimu zinazounda Bonde la Mto Ngono lenye ukubwa wa hekta 11,700 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ambapo kupitia bajeti ya mwaka 2022/2023 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga fedha kwa ajili ya kufanya mapitio ya upembuzi yakinifu na kufanya usanifu wa kina. Mpaka sasa, Serikali ipo katika hatua za kukamilisha manunuzi ya kumpata mshauri mwelekezi atakayefanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika Mpango na Bajeti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Bonde la Mto Ngono limetengewa bajeti ya ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji ambapo jumla ya hekta 3,000 zimepangwa kuendelezwa katika mwaka wa kwanza wa utekelezaji na Skimu ya Kyakakera itakuwa miongoni mwa skimu za awamu ya kwanza zitakazoendelezwa wakati wa utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika Skimu ya Bonde la Mto Ngono.
MHE. KAVEJURU E. FELIX aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhimiza vijana kushiriki shughuli za kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kavejuru Eliadory Felix, Mbunge wa Buhigwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, azma ya Serikali na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ni kutengeneza ajira milioni nane kwa vijana ifikapo mwaka 2025 ili kutatua changamoto ya ajira kwa vijana. Hatua ya awali ambayo imechukuliwa na Serikali pamoja na mambo mengine ni kufanya tathmini na kutambua sababu kubwa inayofanya vijana wasipende kujishughulisha na kilimo, ambapo imeonekana kuwa kukosekana kwa ardhi, mitaji, miundombinu ya umwagiliaji na masoko ya uhakika ni sababu kuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kuweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inatatua changamoto hizo na kuvutia vijana kushiriki katika kilimo. Moja ya mkakati huo ni Mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora (Building a Better Tomorrow) ambapo Serikali imetenga maeneo ya kilimo na kuwamilikisha vijana, inaweka miundombinu ya umwagiliaji, inawawezesha kupata mitaji na masoko ili wanufaike na shughuli za kilimo.
MHE. VITA R. KAWAWA aliuliza: -
Je, ni kwa nini skimu za umwagiliaji za Liyuni na Limamu – Namtumbo hazijakamiliki ingawa Serikali imetumia fedha nyingi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vita Rashid Kawawa, Mbunge wa Namtumbo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, skimu ya umwagiliaji ya Mtakuja iliyopo katika Kata ya Limamu yenye ukubwa wa eneo la hekta 350 na Liyuni iliyopo katika Kata ya Mchomoro yenye ukubwa wa hekta 140 ni miongoni mwa skimu zilizopo katika Wilaya ya Namtumbo. Katika mwaka 2006/2007 hadi 2012/2013, Serikali iliwekeza kiasi cha shilingi bilioni 1.260 kwa ajili ya ujenzi wa mfereji mkuu mita 3,950, vivuko viwili, daraja moja, kalvati na barabara yenye urefu wa kilomita 25 katika mradi wa Liyuni na ujenzi wa banio, mfereji mkuu mita 3,000 vivuko katika skimu ya Mtakuja kupitia fedha za DADPs, DIDF na MIVARF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa usanifu wa skimu hizi ulifanyika muda mrefu, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika mwaka wa fedha 2023/2024 imepanga kufanya mapitio ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kubaini gharama halisi za kukamilisha miundombinu ya umwagiliaji na kuhakikisha skimu hiyo inakamiliaka na kuleta tija ya kilimo cha umwagiliaji katika kata za Limamu na Mchomoro.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI aliuliza: -
Je, ni lini Wakulima wa Tumbaku watalipwa fedha zao kutoka Kampuni ya JESPAN ya msimu wa mauzo 2021 Jimboni Muhambwe?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Florence George Samizi Mbunge wa Muhambwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msimu wa mwaka 2020/2021, kampuni ya JESPAN Company Limited ilinunua jumla ya kilo 512,426 za tumbaku zenye thamani ya Dola za Marekani 662,651. Kampuni hiyo iliweza kulipa wakulima wa Kibondo, Kakonko na Kasulu kiasi cha Dola za Marekani 471,500 na kubaki deni la kiasi cha Dola za Marekani 191,151.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ucheleweshwaji wa malipo, Serikali imeanza kuchukua hatua za kisheria kwa kampuni zilizonunua tumbaku kwa wakulima na kushindwa kufanya malipo. Hivyo basi, malipo ya wakulima yatafanywa kwa mujibu wa maamuzi ya vyombo vya haki ikiwemo Mahakama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni hiyo iliyoshindwa kulipa wakulima baada ya soko la kuuza tumbaku iliyonunua kuyumba na kutouza kutokana na athari za UVIKO – 19. Aidha, Wizara kupitia Bodi ya Tumbaku na Chama Kikuu cha Wakulima wa Tumbaku Mkoa wa Kigoma (KTCU) na Ofisi ya Mashtaka ya Mkoa wa Kigoma inakamilisha taarifa za kuifungulia kesi ya madai kampuni ya JESPAN Company Limited ili kukamilisha malipo ya wakulima.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE aliuliza: -
Je, lini Serikali itaanza kugawa maeneo ya kilimo kwa njia ya mnada katika Bonde la Mto Rufiji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Bonde la Mto Rufiji ni miongoni mwa mabonde 22 ya kimkakati na linakadiriwa kuwa na eneo lenye ukubwa wa hekta 64,896 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa bonde hilo ili kujua ukubwa wa eneo na gharama halisi za kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji katika bonde hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, baada ya upembuzi yakinifu kukamilika, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Mkoa wa Pwani, zitaandaa Mpango shirikishi wa namna bora ya ugawaji wa maeneo ya kilimo katika bonde hilo ili kuongeza uzalishaji na tija.
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga miundombinu ya umwagiliaji katika mabonde ya mpunga ya Mahenge, Goo na Kwamngumi - Korogwe Mjini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Alfred James Kimea, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mabonde ya umwagiliaji ya Mahenge, Goo na Kwamngumi ni miongoni mwa maeneo ya uzalishaji wa mpunga katika Halmashauri ya Mji Korogwe. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilitenga fedha kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika mabonde hayo. Mwezi Aprili, 2023 Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilisaini mkataba wenye jumla ya Shilingi bilioni 1.85 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa miundombinu katika Bonde la Mahenge na Bonde la Goo.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika Mpango na Bajeti ya mwaka 2023/2024 imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kupata gharama halisi ya kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji katika Bonde la Kwamngumi.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaachia bei ya zao la kahawa kuamuliwa kwa nguvu ya soko?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Muleba Kusini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, bei ya kahawa duniani hutegemea mwenendo wa bei katika masoko ya rejea ya kahawa duniani ambayo ni soko la bidhaa la New York (ICE) kwa kahawa za arabika na euronest LIFFE ya London kwa kahawa aina ya robusta. Mabadiliko ya mwenendo wa bei katika masoko hayo huchochewa na kiasi cha kahawa kilichozalishwa duniani na mahitaji kwa wakati husika.
Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya mwenendo wa bei ya kahawa katika masoko rejea yana athari za moja kwa moja kwenye bei za kahawa katika masoko ya kahawa hapa nchini na duniani kwa ujumla. Hivyo, Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi yanayoleta ushindani wa kutosha ili kuchochea bei ya kahawa nchini.
MHE. FRANCIS I. MTINGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga miundombinu ya Umwagiliaji ikiwemo kuchimba visima virefu katika Bonde la Dominiki, Kata ya Mwangeza?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Isack Mtinga, Mbunge wa Iramba Mashariki kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Bonde la Dominiki lipo katika Kata ya Mwangeza Halmashauri ya Mkalama. Bonde hili ni kati ya maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji yaliyobainishwa na kutambuliwa na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ndani ya Halmashauri ya Mkalama. Bonde la Dominiki lina takribani hekta 800 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Hata hivyo kwa sasa wakulima wa bonde hili hutegemea kilimo cha mvua. Hii ni kutokana na kutokuwa na uwekezaji wa aina yoyote ya miundo mbinu ya umwagiliaji na chanzo cha kudumu cha maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji katika mpango na bajeti ya mwaka 2023/2024 imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kupata gharama halisi za kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji katika Bonde hilo.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua zao la kahawa Wilayani Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya waziri wa kilimo ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Shaban Omari Shekilindi Mbunge wa Lushoto kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanzisha kitalu cha miche ya kahawa katika eneo la Jegestal ili kuwezesha upatikanaji wa miche kwa wakulima wa kahawa Wilayani Lushoto. Hadi kufikia tarehe 15 Mei, 2023 jumla ya miche 227,905 imezalishwa na imeanza kusambazwa kwa wakulima mwezi Mei, 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania imekiwezesha Chama Kikuu cha Ushirika cha Usambara kuingia mkataba na Kampuni ya Mambo Coffee Company Ltd na kupata cheti cha kilimo hai (Organic Certification) kitakachowezesha chama hicho kuuza kahawa yake kwenye soko maalum. Hatua hizo ni sehemu ya jitihada za Serikali za kufufua na kuendeleza kilimo cha zao la kahawa katika Wilaya ya Lushoto.
MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: -
Je, lini Serikali itarejesha utoaji ruzuku ya pembejeo za dawa kwa Wakulima wa Kahawa ili wazalishe zaidi kama awali?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Moshi Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, matumizi ya viuatilifu katika zao la kahawa ni njia ya udhibiti wa visumbufu vya zao la kahawa ili kulinda ubora wa mazao yanayozalishwa dhidi ya magonjwa ya Kutu ya Majani na Chole Buni. Aidha, utafiti wa zao la kahawa umebaini kuwa upandaji wa miche bora ya kahawa ni njia pekee inayowezesha kuzalisha mazao yenye tija nzuri, ukinzani dhidi ya wadudu waharibifu na magonjwa ya zao la kahawa na kupunguza matumizi ya viuatilifu kwenye kahawa kwa takriban asilimia 40.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali haina utaratibu wa kutoa ruzuku ya viuatilifu vya kahawa bali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kahawa (TaCRI) na Bodi ya Kahawa Tanzania imeendelea kuzalisha, kusambaza na kuhamasisha wakulima kubadilisha mikahawa ya zamani kwa kupanda miche mipya ambayo ina ukinzani dhidi ya magonjwa ambapo katika kipindi cha mwaka 2019/2020 hadi 2021/2022 jumla ya miche 41,348,628 imezalishwa na kugawiwa bure kwa wakulima.
MHE. MUHARAMI S. MKENGE aliuliza: -
Je, lini Serikali itaongeza eneo na kuboresha Skimu ya Umwagiliaji ya Mto Ruvu – Bagamoyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muharami Shabani Mkenge, Mbunge wa Bagamoyo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Skimu ya Kisere ambayo ni miongoni mwa skimu katika bonde la mto Ruvu. Aidha, Serikali inaendelea na hatua mbalimbali za kubaini maeneo yanayofaa kwa ujenzi wa mabwawa ili kuhudumia skimu zilizopo katika bonde hili, kwani hii itaepusha changamoto ya ukosefu wa maji kwa wakulima kwa kuwa Mto Ruvu unategemewa kwa matumizi mbalimbali ikiwemo matumizi ya majumbani kwa wakazi wa ukanda wa Pwani na Dar es Salaam.
MHE. ENG. SAMWELI X. HHAYUMA K.n.y. MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kupeleka mbegu za mahindi kabla ya kipindi cha masika katika Jimbo la Mbulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mpango wa kuwafikishia wakulima pembejeo za kilimo kwa wakati ikiwemo mbegu bora za mahindi katika Jimbo la Mbulu Vijijini na maeneo mengine nchini unahusisha kukusanya takwimu za mahitaji halisi na kuratibu usambazaji wa pembejeo hizo kupitia sekta ya umma na sekta binafsi kabla ya msimu wa kilimo kuanza.
Mheshimiwa Spika, katika msimu wa mwaka 2022/2023 na mwaka 2023/2024 Serikali kupitia Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) ambayo ni Taasisi ya Serikali imeendelea kusambaza mbegu bora za mahindi katika maeneo mbalimbali kwa bei nafuu ambayo ina ruzuku ndani yake. Ninaomba nitumie fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu kuzishauri Halmashauri za Wilaya ikiwa ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kutenga fedha zitakazowezesha kuendelea kununua mbegu za mahindi pamoja na mbegu za mazao mengine kupitia Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) ambao huuza mbegu kwa bei nafuu zaidi.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE K.n.y MHE. PROF. PATRICK A. NDAKIDEMI aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kutatua changamoto za wakulima waliowekeza kwenye SACCOS na fedha zao kupotea?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Patrick Alois Ndakidemi, Mbunge wa Jimbo la Moshi Vijijini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa upotevu wa fedha za wanachama wa SACCOS nchini unadhibitiwa ipasavyo, Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika inayo mikakati mbalimbali, ikiwemo kutoa miongozo ya uendeshaji na usimamizi wa Vyama vya Ushirika nchi zikiwemo SACCOS, kuanza kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (MUVU), ambao utasaidia kuongeza uwazi na uwajibikaji katika uendeshaji na usimamizi wa shughuli za Vyama vya Ushirika, zikiwemo SACCOS, kuendelea kutoa elimu ya ushirika kuhusu namna bora ya uendeshaji na usimamizi wa Vyama vya Ushirika kwa wananchi wote, wakiwemo wanachama, viongozi na watendaji wa SACCOS kupitia njia mbalimbali.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza: -
Je, ni lini kutakuwa na kiuatilifu kimoja cha magonjwa kwenye zao la korosho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika zao la korosho kuna magonjwa makuu manne ya ubwiriunga, blaiti, chule na debeki yanayodhibitiwa kwa viuatilifu vyenye viambata amilifu tofauti.
Mheshimiwa Spika, ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa visumbufu vya mazao, Serikali itaendelea kuimarisha utafiti na kushauri wakulima kutumia viuatilifu vyenye tija zaidi katika kilimo. Aidha, Serikali kupitia Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu inaendelea kupitia upya usajili wa viuatilifu vyote ili kubaki na viuatilifu vinavyofaa sokoni kulingana na aina ya zao, eneo na magonjwa yaliyopo.
MHE. ASIA A. HALAMGA aliuliza: -
Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Banio la Maji, Kata ya Endagau, Wilaya ya Hanang?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Asia Abdukarimu Halamga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji Endagaw iliyopo katika Mkoa wa Manyara, Wilaya ya Hanang ulianza mwaka wa fedha 2021/2022. Hadi sasa Serikali imeshakamilisha ujenzi wa baadhi ya maeneo ikiwemo ujenzi wa ukuta wa bwawa wenye takribani mita 270 pamoja na punguza maji (Spillway) na baadhi ya maumbo ya mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kukamilisha ujenzi wa kazi zote zilizobaki, hii ni baada ya kukamilisha mapitio ya usanifu wa mradi huu, ikiwemo mfereji wa Onjae pamoja na maumbo yake.
MHE. FRANCIS K. NDULANE aliuliza: -
Je, lini Serikali itafufua kilimo cha pamba katika Wilaya ya Kilwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Francis Kumba Ndulane, Mbunge wa Kilwa Kaskazini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Kilwa ni miongoni mwa maeneo yaliyo chini ya karantini ya pamba katika eneo la kusini mwa Tanzania kutokana na uwepo au kupakana na nchi zilizoathiriwa na funza mwekundu (diparopsis castenea) ambaye ni mdudu hatari wa zao la pamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2020/2021 Serikali ilifanya tathmini ya hali ya funza mwekundu na kubaini kuwa mdudu huyo bado yupo katika maeneo ya karantini. Aidha, Wizara itaendelea kufanya utafiti kwa kushirikiana na Taasisi za Kimataifa kuhusu namna bora ya kudhibiti mdudu huyo.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha inapata data za bidhaa zote za kilimo zinazosafirishwa nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inaendelea kuboresha mfumo wa Agricultural Trade Management Information System (ATMIS) kwa ajili ya kuufungamanisha na mfumo wa pamoja wa forodha wa Tanzania (Tanzania Custom Intergrated Systems - TANCIS) wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Kufunganishwa kwa mfumo wa ATMIS na TANCIS kutaboresha upatikanaji wa takwimu za mazao na bidhaa za kilimo zinazoingizwa au zinazosafirishwa nje ya nchi.
MHE. FLORENT L. KYOMBO aliuliza: -
Je, lini Serikali itatafuta suluhisho la kudumu la kudhibiti wanyama waharibifu wa mazao na ugonjwa wa mnyauko?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Florent Laurent Kyombo, Mbunge Nkenge wa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo kila mwaka hutenga fedha kwa ajili ya kudhibiti makundi mbalimbali ya wanyama waharibifu wa mazao hususani panya, kweleakwelea, viwavijeshi na nzige.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2022/2023, jumla ya shilingi bilioni 4.9 zimetolewa kwa ajili ya kudhibiti wanyama hao. Aidha Serikali inaendelea kuimarisha timu ya kusimamia kilimo anga ambapo ndege moja iliyokuwa mbovu imesharekebishwa na taratibu za kununua ndege mpya zinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kukabiliana na ugonjwa wa mnyauko katika mazao mbalimbali ikiwemo ndizi, viazi, maharage na kahawa, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzalisha miche bora yenye ukinzani na magonjwa ya mnyauko; kutoa elimu kwa wakulima na Maafisa Ugani kuhusu kukata au kung’oa mashina yote yaliyoathirika na kuyachoma moto ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa na kuzalisha miche bora kutoka mashina yaliyoathirika kutumia teknolojia ya tissue culture ambayo inasaidia kusafisha na kuzalisha miche ambayo haitakuwa na ugonjwa huo.
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutatua changamoto ya bei ndogo za mazao pamoja na ukosefu wa masoko ya uhakika nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wakulima wanapata bei shindani na masoko ya uhakika. Mikakati hiyo ni pamoja na kuongeza tija kwenye uzalishaji kupitia uwekezaji katika miundombinu ya umwagiliaji, pembejeo, utafiti, huduma za ugani, matumizi ya teknolojia na kurasimisha Sekta ya Kilimo Mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha kibiashara kinachozingatia mahitaji ya soko; kushiriki makongamano na maonesho ya kibiashara na uwekezaji kwa lengo la kutangaza bidhaa na maeneo ya uwekezaji katika sekta ya kilimo; kushirikiana na Sekta Binafsi katika ujenzi wa miundombinu ya masoko; kuimarisha mifumo ya kielektroniki ambayo itawezesha upatikanaji wa taarifa za masoko kwa wakati; kutoa mafunzo kuhusu kilimo biashara kwa Maafisa Ugani na Wakulima na kuendelea kufungua masoko mapya katika nchi mbalimbali kwa kufanya tafiti za mahitaji kwa nchi husika.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Je, kuna mpango gani wa kuhakikisha kuwa wakulima wa korosho wanapata mikopo nafuu ili waweze kugharamia kilimo hicho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania inaratibu uwezeshaji wa wakulima wa korosho kupata mikopo ya kuendeleza zao la korosho ikiwemo pembejeo na utunzaji wa mashamba. Uwezeshwaji huo utafanyika kupitia Vyama Vikuu vya Ushirika kuwawekea dhamana wakulima ili waweze kupata mikopo kutoka katika taasisi za fedha
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kuwaunganisha wakulima na taasisi za fedha ili waweze kupata mikopo yenye riba nafuu kuanzia asilimia tisa kushuka chini.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Je, Serikali ipo tayari kuzungumza na wenye viwanda vya mbolea ili kuwe na ujazo wa kilo tofauti na 50?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyeketi, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni ya 32, (4) na (5) pamoja na Kanuni ya 33(1) ya Kanuni za Mbolea za mwaka 2011, wazalishaji au waingizaji wa mbolea wanaruhusiwa kufungasha mbolea katika ujazo unaofaa kwa watumiaji mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbolea zilizo katika hali ya yabisi (solid fertilizers) zinapaswa kufungashwa katika ujazo wa kilo tano, 10, 25 na 50. Mbolea zilizo katika hali ya kimiminika (liquid fertilizers) zinapaswa kuwa katika ujazo wa mililita tano, 10, 20, 50 na 100. Aidha, visaidizi vingine vya mbolea kama vile chokaa mazao (agricultural lime) na jasi (gypsum) hufungashwa katika ujazo wa kilo tano, 10, 20, 50 na 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kusimamia wazalishaji wa mbolea kuzalisha mbolea kulingana na mahitaji.
MHE. DEODATUS P. MWANYIKA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itarejesha kwa wananchi wa Kata ya Luponde Ardhi iliyochukuliwa kwa ajili ya Kituo cha Utafiti wa Kilimo Igeri ambayo kwa miaka mingi imekuwa haitumiki?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deodatus Philip Mwanyika, Mbunge wa Njombe Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haina mpango wa kurejesha shamba la Utafiti wa Kilimo Igeri kwa kuwa kama nchi kuna uhitaji mkubwa wa uzalishaji mbegu. Shamba hilo lina ukubwa wa hekta 816, kati ya hizo, hekta 350 ni misitu ya kiasili, hekta 450 ni eneo linalofaa kwa kilimo na hekta 16 ni eneo lenye barabara na nyumba. Kwa sasa shamba hilo linatumika kwa shughuli za utafiti na kuzalisha mbegu za mazao mbalimbali. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imelima hekta 400 za mbegu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imepanga kusafisha, kuweka fensi, kuchimba visima na kulima shamba lote kwa kuzalisha mbegu za awali na za msingi za mazao ya ngano na pareto kwenye hekta 348 na utafiti hekta 88.8. Lengo ni kujitosheleza kwa mbegu za zao la ngano na pareto kwa wakulima wa Njombe, Makete na sehemu nyinginezo. Aidha, natoa rai kwa wananchi kuacha kuvamia mashamba ya utafiti na uzalishaji wa mbegu.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA K.n.y. MHE. JUSTIN L. NYAMOGA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza tija katika uzalishaji wa zao la Pareto Wilayani Kilolo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Justin Lazaro Nyamoga, Mbuge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tija ya sasa ni kati ya kilo 280 hadi 300 ya pareto kavu kwa ekari. Hata hivyo, tija inayoweza kufikiwa na wakulima wengi ni kati ya kilo 400 hadi 500 kwa ekari moja. Pamoja na mambo mengine tija ndogo inasababishwa na wakulima wengi kwa muda mrefu kuendelea kutumia mbegu ambazo zina tija ndogo na wakulima walio wengi kutopendelea kutumia mbolea katika uzalishaji wa zao la pareto.
Mheshimiwa Spika, aidha, kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo katika mwaka wa fedha 2022/2023 ilitenga fedha kiasi cha shilingi milioni 200 ambazo zilipelekwa TARI kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora na zenye tija. Upatikanaji na usambazaji wa mbegu bora hizo unatarajiwa kuanza msimu 2023/2024. Mbegu hizo ambazo zitakuwa na tija kuanzia kilo 400 na zaidi kwa ekari zitasambazwa kwa wakulima wote wa pareto nchini ikiwa ni pamoja Wilaya ya Kilolo. Usambazaji huo utaenda sambamba na utoaji elimu ya mbinu bora za kilimo cha pareto kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kuendesha tafiti za matumizi ya mbolea kwa zao la pareto. Utoaji wa elimu utafanywa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Sekta Binafsi hususan Wanunuzi na Wasindikaji wa zao katika Wilaya ya Kilolo.
MHE. ALLY J. MAKOA aliuliza:-
Je, lini ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji katika Kata ya Serya utaanza?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Juma Makoa, Mbunge wa Kondoa Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kata ya Serya iliyopo katika Tarafa ya Kondoa Mjini ipo takriban kilometa 20 kutoka Kondoa Mjini. Mwaka 2007, Vijiji vya Mongoroma na Serya vilitenga eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji lenye ukubwa wa hekta 3000. Pia Kijiji cha Mongoroma kilitenga eneo la ujenzi wa bwawa ambalo linapakana na eneo la pori la hifadhi ambalo lilikuwa tayari na aina mbalimbali za wanyama. Skimu inatarajiwa kutumia maji ya mvua pamoja na kuchepusha maji ya Mto Bubu na kuyahifadhi kupitia ujenzi wa Bwawa la Mongoroma. Eneo hili linastawisha mazao mbalimbali yakiwemo mahindi, mtama, mbaazi na mbogamboga zinazolimwa kwa kiwango kidogo pembezoni mwa Mto Bubu kwa njia ya Umwagiliaji wa kutumia pampu.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2010/2011, Serikali kupita Mfuko wa Kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji ngazi ya Wilaya chini ya ASDP 1 ilitenga fedha kiasi cha shilingi milioni 300 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina wa bwawa na skimu, pamoja na maandalizi ya awali ya jamii husika katika kushiriki katika ujenzi wa Skimu na Bwawa la Mangoroma/Serya.
Mheshimiwa Spika, aidha, kutokana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, ongezeko la watu na makazi kufuatia kasi ya kukua kwa Mji wa Kondoa eneo la bwawa kupakana na hifadhi Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, kwa kushirikiana na Halmashauri ina mpango wa kuhuisha tafiti za awali zilizofanyika mwaka 2010/2011 pamoja na kufanya utafiti mpya wa athari za mazingira na jamii, matokeo ya uhuishaji wa tafiti hizo, yataiwezesha Serikali katika mwaka wa fedha 2024/2025 kutega fedha za ujenzi wa Bwawa na Skimu ya Mongoroma/Serya.
MHE. ALOYCE J. KAMAMBA aliuliza: -
Je, lini Serikali itakarabati Skimu za Umwagiliaji za Katengera, Ruhwiti na Muhwazi ili kuboresha kilimo cha umwagiliaji Kakonko?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Aloyce John Kamamba, Mbunge wa Buyungu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Skimu za Umwagiliaji Katengera, Ruhwiti na Muhwazi ni miongoni mwa skimu zilizoko katika Wilaya ya Kakonko zinazounda mabonde 22 ya kimkakati. Katika mwaka wa fedha 2022/2023 Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kupitia mshauri elekezi katika Skimu za Buyungu, Nyakanyezi, Mgunzu, Kayonza, Muhwazi, Ruhuru na Chulanzo zilizoko katika Wilaya ya Kakonko.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga fedha za kuanza ujenzi wa skimu zinazounda mabonde 22 ya kimkakati ambapo Skimu za Katengera, Ruhwiti na Muhwazi ni miongoni mwa skimu hizo.
MHE. FLORENT L. KYOMBO K.n.y. MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO aliuliza: -
Je, kwa nini Serikali isiruhusu wafanyabiashara wazawa wa kusindika kahawa Mkoa wa Kagera kununua kutoka kwa wakulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Oscar Ishengoma Kikoyo, Mbunge wa Jimbo la Muleba Kusini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka utaratibu wa uuzaji na ununuzi wa kahawa za wakulima kupitia vyama ya ushirika ili kuondoa uuzaji wa kahawa katika mifumo isiyo rasmi na kuimarisha biashara ya mazao nchini. Aidha, kupitia mfumo huo wafanyabiashara wazawa waliowekeza kwenye viwanda vya kuongeza thamani na kusindika kahawa Mkoani Kagera wanaruhusiwa kununua kahawa kwenye minada ghafi inayoendeshwa na Bodi ya Kahawa. Kupitia utaratibu huo wanunuzi wazawa wanapata nafasi ya kushindana kununua kahawa moja kwa moja kwa wakulima kama ilivyowasilishwa na vyama vyao vya msingi (AMCOS).
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua skimu ya umwagiliaji katika Kijiji cha Mtitaa Wilayani Bahi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Nollo, Mbunge wa Jimbo la Bahi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Skimu ya Umwagiliaji Mtitaa iliyopo katika Kijiji cha Mtitaa, Kata ya Mtitaa Wilayani Bahi, ilijengwa kupitia Mpango Shirikishi wa Kuendeleza Kilimo cha Umwagiliaji (PIDP) katika mwaka wa fedha 2002/2003 na kuanza uzalishaji mwaka 2003/2004. Skimu hii pia ina miundombinu ya bwawa dogo la kuvuna maji msimu wa mvua na zao linalolimwa ni Mpunga. Skimu ina jumla ya hekta 107 na ina jumla ya wakulima 215.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga fedha za ukarabati wa skimu za Bonde la Bahi ikiwemo skimu ya Mtitaa ambazo zimeharibiwa na mafuriko ili kuzirudisha kwenye uzalishaji.
MHE. DKT. THEA M. NTARA K.n.y. MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI aliuliza: -
Je, mpango wa kuufanya Mkoa wa Morogoro kuwa ghala la Taifa la chakula umefikia wapi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Antipas Zeno Mgungusi, Mbunge wa Malinyi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika kutekeleza mpango wa kuufanya Mkoa wa Morogoro kuwa Ghala la Taifa imeendelea na jitihada za kuendeleza miundombinu ya umwagiliaji ambapo mkoa una jumla ya skimu 233. Aidha, katika mwaka wa fedha 2022/2023 zaidi ya shilingi bilioni 15 zilitengwa kwa ajili ya kuendeleza skimu za umwagiliaji ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, mkandarasi mshauri wa kufanya upembuzi yakinifu wa Bonde la Kilombero na Ifakara amekwishapatikana ili kupitia taarifa hiyo ya miradi mipya ya umwagiliaji iweze kuanzishwa na kuongeza uzalishaji. Sambamba na hilo, Serikali inaendelea kuboresha huduma za ugani, upatikanaji wa pembejeo sahihi ikiwemo mbegu bora na mbolea na uimarishaji wa miundombinu ya uhifadhi wa mazao baada ya mavuno.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwakopesha fedha wakulima wa kahawa ili kuondokana na biashara ya butura?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania kwa kushirikiana na taasisi za kifedha ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), imeendelea kuwaunganisha wakulima kupitia Vyama vya Ushirika na kuwapatia mikopo na masharti nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania imeendelea kushirikiana na Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi Ghalani, Soko la Bidhaa Tanzania pamoja na wadau wengine kuweka mfumo rasmi wa masoko na uuzaji wa kahawa za wakulima Mkoani Kagera ili kuwezesha wakulima wa kahawa kupata masoko ya mazao yao.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Je, lini Mradi wa Umwagiliaji wa Kata ya Ikweha uliopo Jimbo la Mufindi Kaskazini utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Skimu ya Umwagiliaji Ikweha ni miongoni mwa skimu zilizoko katika Wilaya ya Mufindi yenye ukubwa wa hekta 500. Skimu hii ina mchango mkubwa katika kuboresha Maisha ya wananchi katika Wilaya ya Mufindi.
Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga fedha za kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kupata gharama za kukamilisha ujenzi wa bwawa na miundombinu ya umwagiliaji katika skimu ya Ikweha.
MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kufanya mageuzi ya kilimo nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ramadhani Ighondo, Mbunge wa Singida Kaskazini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali wa kuleta mageuzi ya kilimo. Mikakati hiyo inatekelezwa kwa lengo la kubadili kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kuwa kilimo biashara, chenye tija, himilivu kinachoratibiwa na kusimamiwa na Serikali na kushirikisha sekta binafsi ili kuwa na mifumo endelevu ya chakula na kilimo.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia misingi hiyo ya kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo, Serikali kupitia bajeti ya mwaka 2023/2024 inatekeleza vipaumbele mikakati yenye lengo la kuongeza tija na uzalishaji; kuongeza ajira zenye staha na ushiriki wa vijana na wanawake kwenye kilimo; kuimarisha usalama wa chakula na lishe; kuimarisha upatikanaji wa masoko, mitaji na mauzo ya nje ya nchi na kuimarisha maendeleo ya ushirika.
MHE. JONAS W. MBUNDA K.n.y. MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza: -
Je, kuna mpango gani kuboresha utendaji wa Shirika la Mbolea (TFC) ili kusambaza pembejeo kwa wakulima kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika msimu wa mwaka 2022/2023 Serikali imeunda Bodi ya Wakurugenzi na kuajiri Meneja Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania. Vilevile, Serikali imeipatia TFC mtaji wa Shilingi bilioni sita ambao umeiwezesha kununua jumla ya tani 4,500 na kusambaza jumla ya tani 3,851.35 za mbolea kwa wakulima 20,271.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imepanga kuiongezea TFC mtaji wa Shilingi bilioni 40 kwa ajili ya kununua na kusambaza pembejeo za kilimo kwa wakulima. Aidha, mpango wa muda mrefu ni kampuni kujenga kiwanda cha kuchanganyia mbolea na eneo la ekari 14.5 limepatikana kwenye Kijiji cha Visegese, Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani, ambapo ujenzi utaanza katika mwaka wa fedha wa 2023/2024.
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA aliuliza:-
Je, baada ya kuporomoka kwa bei ya korosho katika msimu wa 2022/2023 Serikali imechukua hatua gani kuhakikisha hali hiyo haijirudii?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Issa Ally Mchungahela, Mbunge wa Lulindi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, bei ya korosho Nchini hutegemea mwenendo wa bei katika Soko la Dunia. Mabadiliko ya mwenendo wa bei katika masoko hayo huchochewa na kiasi cha korosho kinachozalishwa Duniani na mahitaji kwa wakati husika. Kwa wastani katika msimu wa mwaka 2022/2023 bei ilishuka kutoka shilingi 2,150 hadi shilingi 1,850 kwa kilo kwa korosho daraja la kwanza na shilingi 1,595 hadi shilingi 1,332 kwa korosho daraja la pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeendelea na jitihada za kuimarisha bei ya korosho nchini kwa kufufua viwanda vya kubangua korosho pamoja na kuanzisha viwanda vipya. Vilevile, Serikali itaanzisha kongani la viwanda vya kubangua korosho ili kuongeza thamani ya korosho na kuuza moja kwa moja katika nchi walaji badala ya kuuza korosho ghafi.
MHE. ABUBAKARI D. ASENGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itakamilisha mradi wa Umwagiliaji wa Kisawasawa – Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abubakari Damian Asenga, Mbunge wa Kilombero, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, skimu ya umwagiliaji Kisawasawa ipo katika Kata ya Kisawasawa, Tarafa ya Mang’ula Wilaya ya Kilombero. Skimu hiyo ipo umbali wa kilometa 43 kutoka Mji wa Ifakara kupitia barabara ya Ifakara - Mikumi. Skimu ya Kisawasawa ina eneo linalofaa kwa umwagiliaji lenye ukubwa wa hekta 500.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga fedha za kwa ajili ya kufanya mapitio ya usanifu ili kupata gharama halisi za uendelezaji wa miundombinu ya umwagiliaji katika skimu hiyo.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza: -
Je ni lini Serikali itaanza kutekeleza mradi wa ujenzi wa bwawa katika Kijiji cha Ichemba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Ulyankulu kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu wa ujenzi wa bwawa ambao upo katika Kata ya Ichemba, Wilaya ya Kaliua unategemewa kukusanya maji ya matumizi ya nyumbani, pamoja na umwagiliaji kwenye mashamba na unategemewa kunufaisha wananchi wapatao 18,000 wa Kata ya Ichemba na maeneo mengine ya Ulyankulu. Zabuni ya kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa bwawa hilo imeshatangazwa na RUWASA na taratibu zingine zinaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2024/2025 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itatenga fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji ambayo zitatoa maji kwenye bwawa na kupeleka mashambani.
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza: -
Je, kuna mkakati gani wa kufanya utafiti ili kubaini mazao yanayoweza kulimwa na kustawi Mkoa wa Mtwara kama mbadala wa zao la korosho?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeendelea kufanya utafiti katika maeneo ya Mtwara ili kupata mazao mengine zaidi ya korosho ambayo mkulima ataweza kuzalisha ili kuondokana na utegemezi wa zao la korosho pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo kupitia TARI imeendelea kuhamasisha kilimo cha mazao ya muhogo, ufuta, karanga, alizeti, njugumawe, choroko, mbaazi, mtama na kunde ambayo tayari yamefanyiwa utafiti na kuonekana yanafaa kulimwa katika Wilaya zote za Mkoa wa Mtwara. Aidha, Wizara imetoa elimu ya kilimo bora cha mazao hayo ikiwemo matumizi ya mbegu bora, udhibiti wa visumbufu (wadudu waharibifu na magonjwa), kupanda kwa wakati na matumizi sahihi ya mbolea kupitia mashamba ya mfano, radio za kijamii na televisheni.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA K.n.y. MHE. STELLA S. FIYAO aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kutafuta masoko ya mazao ya kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella Simon Fiyao, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2023/2024, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo itaendelea kuimarisha upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo ndani na nje ya nchi kwa kujenga masoko ya kimkakati mipakani, ujenzi wa vituo vya masoko na kuboresha miundombinu ya maabara za TPHPA ili ziweze kupata ithibati itakayowezesha kufanya uchunguzi na kutoa vyeti vya ubora vinavyokubalika Kimataifa, kuongeza tija na kupunguza gharama za uzalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali inaendelea na majadiliano na nchi mbalimbali na kufungua masoko ya mazao katika nchi hizo. Hadi sasa tumefanikiwa kufungua soko la korosho nchini Marekani, soko la parachichi China, India na Afrika Kusini na tunaendelea kuhudumia masoko ya nafaka katika nchi mbalimbali za Afrika.
MHE. RASHID A. SHANGAZI aliuliza:-
Je, kuna mkakati gani wa kufufua zao la kahawa nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Mlalo, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ya kufufua zao la kahawa hususan katika maeneo yenye mibuni iliyozeeka, mashamba yaliyotelekezwa na kuanzisha kilimo cha kahawa katika maeneo mapya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati hiyo inajumuisha uzalishaji na usambazaji wa miche bora ya kahawa; kuimarisha maabara za kuzalisha miche kwa njia ya chupa ili kudhibiti magonjwa na kuongeza kasi ya uzalishaji wa miche bora; kuboresha mifumo ya masoko ya kahawa ili kumlinda mkulima; kuwezesha matumizi ya teknolojia za umwagiliaji kwenye mashamba ya kahawa na kuimarisha utafiti na maendeleo kupitia Kituo cha Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI).
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msimu wa mwaka 2022/2023 jumla ya miche 8,784,146 ilizalishwa na kusambazwa kwa wakulima. Kati ya kiasi hicho, miche 5,458,123 ni aina ya arabika na miche 3,326,023 ni aina ya robusta. Aidha, katika mwaka 2023/2024 Serikali imepanga kuanzisha mashamba 40 ya mfano katika wilaya 20, kuratibu uzalishaji na usambazaji wa miche bora 20,000,000 katika wilaya 52 na kufufua mashamba 150 yenye jumla ya hekta 400.
MHE. AGNES E. HOKORORO aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani kupitia SIDO kutoa mashine ndogo na rahisi kwa vikundi vya wanawake vya ubanguaji korosho Mkoani Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Agnes Elias Hokororo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bodi ya Korosho imeanza kuchukua hatua stahiki ili kuhakikisha korosho zote zinazozalishwa nchini zinabanguliwa na kuuzwa nje ya nchi zikiwa zimebanguliwa (kernel). Lengo kuu ni kuongeza thamani katika zao, kipato kwa wakulima na ajira kwa vijana na wanawake.
Mheshimiwa Spika, aidha, katika kutekeleza mpango huo Serikali imenunua mashine 100 za kubangua korosho zilizotengenezwa na wajasiriamali walio chini ya mwamvuli wa SIDO na kuzigawa kwa vikundi 22; vikundi 15 vya Mkoa wa Mtwara na Lindi vikundi saba ambapo jumla ya wanawake 241 na wanaume 18 wamenufaika.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania inaendelea kuhamasisha watengenezaji na wauzaji wa mashine za kubangua korosho ikiwa ni pamoja na SIDO, CAMARTEC na TIRDO ili kurahisisha upatikanaji wa mashine hizo.
MHE. ISSA J. MTEMVU K.n.y. MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuendeleza kilimo cha minazi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha minazi nchini ambapo imeanzisha shamba lenye ukubwa wa hekta 54 katika Kituo Kidogo cha Utafiti cha Chambezi, Wilaya ya Bagamoyo ili kuzalisha miche iliyo bora ya minazi. Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imepanga kuzalisha miche bora 750,000 na kuisambaza kwa wakulima wa zao la minazi ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kuanzisha mashamba makubwa ya pamoja.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imeanza mazungumzo na Kampuni ya Deejay Coconut Farm Private Ltd. ya nchini India katika mashirikiano ya uzalishaji wa miche ya inayozalisha nazi 250 kwa mnazi mmoja kulinganisha na minazi ya kawaida inayozalisha nazi 80 kwa mti mmoja.
MHE. GEORGE R. MWENISONGOLE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawachukulia hatua viongozi wa Vyama vya Msingi waliodhulumu fedha za wakulima wa kahawa Mbozi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Ranwell Mwenisongole, Mbunge wa Jimbo la Mbozi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imefanya uchunguzi kwa Vyama vya Ushirika 20 vilivyopo Wilayani Mbozi ambapo kati ya hivyo, vyama nane vimekutwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wakulima kupunjwa malipo ya mauzo ya kahawa; vyama kutowasilisha makato ya ushuru kwa Halmashauri na watoa huduma; na kampuni ya ununuzi wa kahawa kushindwa kulipa fedha za mauzo ya kahawa.
Mheshimiwa Spika, hatua za stahiki zimechukuliwa kwa viongozi na watendaji waliobainika kuhusika na ubadhirifu uliojitokeza. Hatua hizo ni pamoja na kuondolewa kwa viongozi katika nafasi zao; kufanya uchaguzi wa bodi za mpito; na kampuni ya Taylorwinch kulipa kiasi cha shilingi 26,978,094 iliyokuwa inadaiwa na Chama cha Ushirika cha Isaiso. Vilevile taarifa za uchunguzi kwa Vyama vya Ushirika 20 ziliwasilishwa katika Ofisi ya TAKUKURU Mkoa wa Songwe kwa ajili ya mapitio na kuchukua hatua kwenye maeneo yenye viashiria vya rushwa, wizi na ubadhirifu.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:-
Je, lini Serikali italeta Bungeni Muswada wa Sheria wa kulinda ardhi ya Kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kulinda ardhi ya kilimo kama ilivyobainishwa katika Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013. Kwa msingi huo, Wizara inapitia na kuchambua Sheria Mbalimbali zinazohusiana na usimamizi na matumizi ya ardhi ya kilimo ikiwemo Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Sura ya 114, Sheria ya Ardhi, Sura ya 113 na Sheria ya Mipango ya Matumizi bora ya Ardhi, Sura ya 116 na Sheria ya Utwaaji wa Ardhi, Sura ya 118.
Mheshimiwa Spika, uchambuzi huo utabainisha upungufu uliopo katika sheria hizo na kuainisha maeneo ambayo yatajumuishwa kwenye Sheria ya Maendeleo ya Kilimo inayopendekezwa kutugwa ambayo itakuwa na sehemu ya masuala ya usimamizi wa ardhi ya kilimo. Baada ya uchambuzi huo wa kitaalam, itawasilishwa kwenye ngazi za maamuzi kuhusu mapendekezo ya sheria hiyo.
MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU aliuliza: -
Je, Serikali imejipangaje kutatua changamoto ya upatikanaji wa mbolea nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jesca Jonathan Msambatavangu, Mbunge wa Iringa Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi vikiwemo viwanda vya Minjingu Mines and Fertilizer Limited na ITRACOM Fertilizers Limited kuhakikisha uzalishaji na upatikanaji wa mbolea hapa nchini unaimarika na kupunguza utegemezi wa kuagiza mbolea kutoka nje ya nchi. Kupitia mpango huo, uwekezaji unaofanywa na kiwanda cha ITRACOM unatarajiwa kufikia uzalishaji wa takribani tani 1,000,000 za mbolea ifikapo Desemba, 2024. Vilevile kiwanda cha mbolea cha Minjingu kinafanya upanuzi ili kuongeza uwezo wa uzalishaji kutoka tani 100,000 hadi kufikia tani 300,000 kwa mwaka.
Mheshimiwa Spika, katika msimu wa 2023/2024 Serikali imepanga kuiwezesha Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kwa kuipatia mtaji wa takribani Shilingi Bilioni 40 utakao iwezesha kununua na kusambaza mbolea kwa wakulima. Serikali kwa kushirikiana na kampuni za mbolea na Vyama vya Ushirika imepanga kuongeza vituo vya mauzo ya mbolea nchini ili kuwezesha wakulima kupata mbolea kwa urahisi na kwa wakati.
MHE. AMEIR ABDALLA AMEIR aliuliza: -
Je, kwa kiwango gani TEHAMA inatumika kuboresha sekta ya kilimo nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ameir Abdalla Ameir, Mbunge wa Baraza la Wawakilishi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Kilimo ni mojawapo ya sekta zinazonufaika na maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano hapa nchini. Kwa kutumia TEHAMA sekta ya kilimo imeboresha maeneo mbalimbali ya huduma zinazotolewa na Wizara kwa wakulima, wafanyabiashara na wadau mbalimbali katika sekta na umma kwa ujumla. Baadhi ya huduma zilizoboreshwa kwa kutumia TEHAMA ni pamoja na kutoa huduma za ugani kwa wakulima, masoko ya mazao ya wakulima, kutoa mbolea ya ruzuku, kupata vibali ama leseni za kufanya biashara za mazao ya mimea na vyeti vya afya ya mimea kwa mazao yanayosafirishwa nje ya nchi.
MHE. MASACHE N. KASAKA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha ili kukamilisha ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji katika Kata ya Ifumbo, Chunya?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Masache Njelu Kasaka, Mbunge wa Lupa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Skimu ya Umwagiliaji ya Ifumbo yenye eneo la hekta 250 inayolima mazao ya mpunga, alizeti, ufuta, mbogamboga na mahindi kwa wananchi wa Chunya. Kwa kutambua umuhimu wa skimu hiyo, Serikali ilitenga kiasi cha shilingi milioni 400 kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na shilingi milioni 50 kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo Wilayani katika mwaka wa fedha 2008/2009. Fedha hizo zilitumika kujenga miundombinu ya umwagiliaji ikiwemo banio, vigawa maji 11, vivuko vya miguu 10 na mfereji mkuu wenye urefu wa mita 2,165.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji nchini na hasa ukizingatia mabadiliko ya tabia nchi yanayopelekea mtawanyo wa mvua zisizotabirika. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha Skimu ya Ifumbo na zingine zote za umwagiliaji nchini.
MHE. ALEKSIA A. KAMGUNA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha kilimo cha Mpunga katika Mkoa wa Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aleksia Asia Kamguna, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia imetekeleza mradi wa Kuongeza uzalishaji na tija ya zao la Mpunga katika Mkoa wa Morogoro. Matokeo hayo yamechagizwa na kuongezeka kwa upatikanaji wa mbegu bora za mpunga.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mpunga ulifanyika katika Halmashauri za Wilaya za Mlimba, Ifakara, Kilosa na Mvomero ambapo jumla ya maghala matano yamejengwa.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA aliuliza:-
Je, ni lini Mradi wa Umwagiliaji wa Kijiji cha Arusha Chini utatengewa fedha ili uanze kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdallah Dadi Chikota, Mbunge wa Nanyamba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Umwagiliaji katika Kijiji cha Arusha Chini una jumla ya hekta 120 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji. Kati ya hizo hekta 48 zinamwagiliwa kwa kutumia mifereji ya asili ambayo chanzo chake cha maji ni chemichemi na mvua za msimu. Katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa skimu hii.
MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI aliuliza: -
Mheshimiwa Naibu Spika, je, ni lini Serikali itakamilisha majadiliano na Kampuni ya Tanzania Leaf Tobacco ili iweze kurudi nchini kuendelea kununua tumbaku?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Peter Cherehani, Mbunge wa Ushetu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kulitaarifu Bunge lako tukufu na wakulima wa tumbaku nchini kuwa mwekezaji mpya ambaye ni mzawa Kampuni ya Amy Holdings Limited imekamilisha taratibu za kuchukua shughuli zilizokuwa zinafanywa na Kampuni ya TLTC na ameshapewa leseni. Aidha, Kampuni ya Amy Holdings Limited imeanza kununua tumbaku ambapo inatarajiwa kununua tani 10,000 za tumbaku katika msimu wa mwaka 2022/2023 ambazo itazichakata katika kiwanda kilichopo Morogoro ifikapo mwezi Julai, 2022.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wakulima wote nchini, ninapenda kumshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kufungua milango ya wawekezaji ambayo matokeo yake ni pamoja na kupatikana kwa mwekezaji huyu.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA K.n.y. MHE. KASALALI E. MAGENI aliuliza: -
Je, ni kwa nini Serikali isiyaondoe mazao ya choroko na dengu kwenye utaratibu wa stakabadhi ghalani kwani utaratibu huo umekuwa kero kwa wakulima na wanunuzi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Emmanuel Mageni Kasalali, Mbunge wa Sumve, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mfumo wa Stakabadhi za Ghala unawezesha uuzaji wa mazao kwa ubora na bei ya ushindani, kupata takwimu sahihi za uzalishaji za mauzo na kuchochea uzalishaji. Mathalani, katika msimu wa mwaka 2020/2021 jumla ya kilo 14,394,077 za choroko zenye thamani ya shilingi bilioni 18.7 ziliuzwa kwa mfumo wa Stakabadhi za Ghala ikilinganishwa na kilo 1,130,453 zilizouzwa katika msimu wa mwaka 2019/2020 katika Mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Tabora na Singida.
Mheshimiwa Spika, zao la choroko, dengu na mazao mengine yataingizwa kwenye mfumo wa stakabadhi kwa kuzingatia vigezo muhimu vya uwepo wa ghala, waendesha ghala, elimu kwa wadau wa mfumo na mazingira ya soko kwa wakati husika.
MHE. SLYVIA F. SIGULA aliuliza: -
Je, ni lini Vyama vya Maendeleo ya Ushirika vya zao la mchikichi vitaanza kufanya kazi katika Mkoa wa Kigoma?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Slyvia Francis Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Kigoma una Vyama vya Msingi vya Ushirika wa Kilimo na Masoko 14 (AMCOS) vya zao la michikichi katika Halmashauri za Wilaya za Kigoma vipo tisa, Kigoma Manispaa viwili, Uvinza viwili na Buhingwe kimoja ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuendeleza zao la michikichi.
Mheshimiwa Spika, vyama hivyo vimeshaanza kufanya kazi na kwa sasa vipo katika hatua ya kupata mkopo wa shilingi bilioni 2.9 kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) utakaowezesha kuboresha mashamba ya wakulima, miundombinu ya uhifadhi mikungu ya michikichi, mashine za uchakataji na ukamuaji wa mafuta ya mawese.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha Kilimo katika eneo la Ngongo Mkoani Lindi ambapo tayari hekari 120 zimetengwa kwa ajili hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge Lindi Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuimarisha huduma za ugani iliamua kuanzisha Vyuo Vya Mafunzo vya Kilimo vya Serikali tangu miaka ya 1930 ili kuendeleza sekta hii hapa nchini. Mpaka sasa vimeshaanzishwa Vyuo Vya Mafunzo ya Kilimo 14 ambavyo vinatoa mafunzo ya fani mbalimbali za kilimo ngazi ya Astashahada na Stashahada kikiwepo Chuo cha MATI Mtwara kwa ajili ya Kanda ya Kusini kwa maana ya Lindi na Mtwara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Wizara inaendelea na ukarabati wa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo na kuvipatia vifaa vya kufundishia. Hata hivyo, Serikali kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatekeleza Mradi wa HEET ambapo katika eneo hilo la Ngongo kitajengwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kampasi ya Lindi kitakachotoa programu za kilimo.
MHE. KENNETH E. NOLLO aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya ukarabati kwenye skimu ya kilimo cha mpunga iliyopo Kata ya Bahi, Wilayani Bahi kwani miundombinu yake imechakaa sana na kupelekea upotevu wa maji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Kenneth Ernest Nollo, Mbunge wa Bahi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu katika skimu ya kilimo cha mpunga iliyopo Kata ya Bahi, Wilayani Bahi ili kujua gharama halisi ya ukarabati. Aidha, fedha kwa ajili ya ukarabati huo zitatengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga Bwawa la Umwagiliaji Bonde la Endayaya Tlawi ambapo usanifu wake ulifanyika mwaka 2007?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha usanifu wa kina wa bwawa la kuvunia maji la Tlawi litakalotumika katika kilimo cha umwagiliaji na Skimu ya Tlawi yenye ukubwa wa hekta 650 zilizopo katika wilaya ya Mbulu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Tlawi na skimu ambapo taratibu za kumpata mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo zinaendelea.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itasaidia kukarabati mifereji ya Marwa, Kwasita, Magereza, Gunge na Kirua katika Bonde la Mto Pangani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mathayo David, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Bonde la Mto Pangani katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. Bonde hili ni pamoja na skimu nyingine pia linajumuisha skimu za Kirya, Marwa, Kwasita, Magereza, Gunge, Kirua na Ruvuna kwa upande wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali inaendelea na ujenzi wa skimu ya Kirya ambayo inatarajiwa kukamilika mwaka 2022/2023. Katika mwaka wa Fedha 2023/2024, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Skimu za Marwa, Kwasita, Magereza, Gunge na Kirua ili kujua gharama halisi za ukarabati na ujenzi wa skimu hizo.
MHE. YUSTINA A. RAHHI aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kukamilisha uwekaji wa samani na vifaa vya kufundishia katika Vituo vya Rasilimali za Kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ilijenga Vituo vya Rasilimali za Kilimo vya Kata 289 katika Halmashauri 184 kati ya mwaka 2007 na 2011. Kwa mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imeanza uwekaji wa samani na vifaa vya TEHAMA kwa ajili ya kufundishia katika vituo hivyo na kwa mwaka huu wa fedha Wizara itawezesha Vituo 34 vya Halmashauri 27 za Mikoa ya Dodoma, Singida, Morogoro, Tabora, Simiyu, Mwanza, Geita, Lindi, Mtwara, Mbeya, Songwe na Iringa. Kwa ufupi, Wizara itaendelea kuweka samani na vifaa vya kufundishia katika Vituo vyote vya Rasilimali za Kilimo vya Kata vilivyojengwa nchini na kutumika kama Centre of Excellence.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: -
Je, Serikali ipo tayari kufanya utafiti wa madini katika Kata ya KIA Jimbo la Hai?
WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Jimbo la Hai, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ipo tayari kufanya utafiti wa Jiosayansi katika Wilaya ya Hai. Aidha, GST iko tayari kutoa ushirikiano kwa wadau wa sekta binafsi wenye nia ya kufanya tafiti za madini, kwa kuwapa taarifa za awali kwa kuwa taasisi hii, imefanya utafiti wa awali na kubaini kuwa hadi sasa jiolojia ya Wilaya hiyo inafaa kwa upatikanaji wa mawe ya ujenzi hasa chokaa mfano katika Kata ya Masama Rundugai.
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE aliuliza: -
Je, Serikali ipo tayari kufanya utafiti wa madini katika Kata ya KIA Jimbo la Hai?
WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saashisha Elinikyo Mafuwe, Mbunge wa Jimbo la Hai, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) ipo tayari kufanya utafiti wa Jiosayansi katika Wilaya ya Hai. Aidha, GST iko tayari kutoa ushirikiano kwa wadau wa sekta binafsi wenye nia ya kufanya tafiti za madini, kwa kuwapa taarifa za awali kwa kuwa taasisi hii, imefanya utafiti wa awali na kubaini kuwa hadi sasa jiolojia ya Wilaya hiyo inafaa kwa upatikanaji wa mawe ya ujenzi hasa chokaa mfano katika Kata ya Masama Rundugai.
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakuwa tayari kujenga Bwawa la Yongoma ambalo lilifanyiwa michoro ya awali mwaka 1984?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, usanifu na uandaaji wa michoro ya awali ya Bwawa la Yongoma ulifanyika mwaka 1984 na Serikali kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japani (JICA). Bwawa hili litakapokamilika litaweza kuhudumia wananchi katika Vijiji vya Misufini, Ndungu, Makokane na Mpirani. Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Same ipo katika hatua ya awali ya kufanya mapitio ya upembuzi yanikifu na usanifu wa Bwawa la Yongoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilika kwa mapitio hayo, ujenzi wa bwawa hili utawekwa katika mpango wa ujenzi kwa mwaka wa fedha 2023/2024. Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha Skimu za Umwagiliaji za Same ambapo kwa sasa imepeleka mitambo katika Skimu ya Ndungu kwa ajili ya kufanya ukarabati wa dharura. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO aliuliza: -
Je, Serikali imefanya utafiti kuhusu uwepo wa Madini Mkoani Mtwara?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tunza Issa Malapo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia GST imefanya utafiti wa awali na kuainisha madini yapatikanayo katika Mkoa wa Mtwara. Miongoni mwa madini hayo ni kinywe, vito aina ya ruby, sapphire, rhodolite, amazonite na green tourmaline. Pia madini ya metali aina ya dhahabu, shaba, manganese na chuma. Vilevile madini ya viwanda kama marble na chokaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, madini mengine ni mchanga wenye madini mazito (heavy minerals) kama rutile, titanium, ilmenite, zircon na magnetite, ahsante sana.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -
Je, lini Tume ya Umwagiliaji itatimiza ahadi yake ya kuvuna maji ya mvua katika Mbuga inayozunguka Mji wa Itigi ili kuepusha mafuriko?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu spika, katika Mwaka wa Fedha 2023/24, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya imetenga fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kuweza kuchimba na kujenga mifereji ya kuongoza maji kutoka bonde linalozunguka Mji wa Itigi na kuelekeza maji hayo mashambani.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, utekelezaji wa ujenzi wa mifereji hiyo utasaidia kuepusha mafuriko yanayojitokeza katika Mji wa Itigi.
MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Sekta ya Kilimo inakuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa Taifa?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu Swali la Mheshimiwa Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kujenga msingi imara wa muda mrefu wa ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kiwango cha asilimia 10 ifikapo mwaka 2030. Mpango huo, utaweka msingi wa kukabiliana na athari za majanga ya asili na yasiyo ya asili ikiwemo mdororo wa uchumi ili kulinda sekta hiyo na pia kupunguza utegemezi wa uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi. Ili kufikia dhamira hiyo, Serikali imelenga kujitosheleza katika chakula, kuongeza thamani ya mauzo ya mazao, kuongeza idadi ya mashamba makubwa, kuongeza eneo la umwagiliaji, kujihakikishia upatikanaji wa malighafi, kuimarisha utafiti, kuongeza uzalishaji wa mbegu bora, kuongeza mitaji, kuongeza mauzo ya mazao ya bustani na kuimarisha upatikanaji wa pembejeo.
Mheshimiwa Spika, vilevile Serikali imeongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka Shilingi Bilioni 298 ya mwaka 2021/2022 hadi kufikia Shilingi Bilioni 954 kwa mwaka 2022/2023 kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa maeneo ya kipaumbele kwa ajili ya kufikia lengo kuu la ukuaji wa sekta wa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030. (Makofi)
MHE. ASSA N. MAKANIKA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa Kigoma vijijini katika kukabiliana na Ugonjwa wa Mnyauko unaoharibu migomba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Assa Nelson Makanika, Mbunge wa Kigoma Kaskazini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na ugonjwa wa mnyauko wa migomba, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kutoa mafunzo ya utambuzi na udhibiti wa ugonjwa huo kwa maafisa ugani, ambapo hadi Juni, 2022 mafunzo kwa maafisa ugani 76 wa Halmashauri ya Buhigwe yametolewa, ili kuwafundisha wakulima mbinu za udhibiti ikiwemo matumizi ya miche bora ya migomba yenye ukinzani wa ugonjwa huo ambayo nitaliban 1, Taliban 2, Taliban 3, Taliban 4 na FHIA 23, William 5).
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa tayari wakulima wamepatiwa miche bora 100 ili kuanza uzalishaji wa miche bora ya kupanda mashambani na kazi hiyo ni endelevu. Vilevile, wakulima wameshauriwa kung’oa migomba yote iliyoathirika na Banana Xanthomonas Wilt. Aidha, tunaendelea kusimamia Sheria ya karantini kwa Mkoa wa Kigoma na maeneo mengine nchini ili kuzuia kusambaa kwa ugonjwa huo.
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE aliuliza:-
Je, mchakato wa kuwalipa waliokuwa Wafanyakazi wa Kiwira Coal Mine umefikia hatua gani?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, deni la Wafanyakazi wa Kiwira lilitokana na malalamiko ya mapunjo ya mafao kutoka kwa waliokuwa wafanyakazi wa mgodi huo kabla ya ubinafsishaji. Baada ya Chama cha Wafanyakazi Mgodini (TAMICO) kuwasilisha malalamiko ya mapunjo hayo Serikalini, Serikali ilifanya Ukaguzi Maalum kupitia kwa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Novemba, 2008 na baadaye Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali (Internal Audit General) alihakiki madeni hayo, Agosti, 2021.
Uhakiki wa madeni hayo ulibaini madai ya wafanyakazi yalikuwa ni shilingi 1,240,000,000 kwa wafanyakazi 893; na madeni ya wazabuni, wakiwemo watoa huduma ya ulinzi, yalikuwa ni shilingi milioni 496; na kufanya deni lote kuwa jumla ya shilingi 1,520,000,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya uhakiki huo kukamilika, Serikali ililitambua deni hilo na kulipeleka Hazina kwa ajili ya hatua za kuweza kulipwa. Ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia Wachimbaji Wadogo wa Madini Wilaya ya Ulanga?
WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuwasaidia wachimbaji wadogo nchini wakiwemo wachimbaji wa madini wa Wilaya ya Ulanga unahusisha mambo yafuatayo:-
(i) Kuwekeza zaidi katika utafiti wa kina kugundua uwepo wa madini katika maeneo mbalimbali ili kuwaongoza vizuri wachimbaji wadogo;
(ii) Utoaji wa Leseni za uchimbaji kwa wachimbaji wadogo;
(iii) Kutoa elimu ya matumzi ya teknolojia sahihi ya uchimbaji ili kuongeza tija;
(iv) Huduma ya uchorongaji kwa gharama nafuu kupitia Shirika la Madini Tanzania (STAMICO);
(v) Upatikanaji wa mikopo nafuu kwa wachimbaji; na
(vi) Fursa ya ukodishaji wa mitambo na vifaa chini ya usimamizi wa STAMICO.