Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge tumejadili hoja hii iliyokuwa imeletwa na Mheshimiwa Omari Kigua kwa muda mrefu kidogo na nadhani Wabunge hata wale ambao hamjapata nafasi ya kuzungumza, lakini hawa waliopata nafasi ya kuzungumza bila shaka wamewakilisha mawazo yenu pia. (Makofi)
Waheshimiwa Wabunge ameeleza hapa kwa kirefu Mheshimiwa Waziri mwenye sekta na mambo mbalimbali ambayo yanatarajiwa kufanywa, lakini wakati wa mijadala kwa kawaida, jambo ambalo pengine halitatokea leo, lakini kwa kawaida hoja kama hizi huwa inabidi zifungwe kwa Bunge kuwa na maazimio juu ya jambo hilo ambalo limejadiliwa hapa ndani.
Kwa hiyo, kwa utaratibu mtoa hoja ndiye anayetakiwa kuja na maazimio ili Bunge sasa liyatazame yale maazimio, halafu lione litaendaje na hayo maazimio kama linakubali na vipi huwa ndiyo maana tunahojiwa hapa ndani.
Lakini kwa sababu sote tunakubaliana jambo ni la dharura kwa hiyo hakuna maandalizi ya jambo la dharura kwa hiyo hawezi kuambiwa Mbunge mbona hukuja na maazimio na mambo kama hayo. Lakini kwa mijadala namna ilivyokuwa hapa ndani na kwa maelezo ambayo ameyatoa kwa kirefu kabisa Mheshimiwa Waziri mwenye sekta na Waheshimiwa Wabunge mawazo yenu mliyoyatoa ni dhahiri kwa taarifa ile aliyokuwa ameitoa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kikao alichokuwa amekaa tayari Wabunge mlikuwa mmeshaanza kutoa mawazo sehemu mbalimbali ambazo mnaweza kutoa mawazo na hayo mawazo yenu ndiyo yaliyopelekea kikao kile. Hii ni kwa sababu taarifa iliyotolewa ni dhahiri kwamba mawazo ya Wabunge yamechukuliwa na kile kikao na yanaendelea kufanyiwa kazi.
Lakini pamoja na yale yameongezwa tena mawazo mengine ya Waheshimiwa Wabunge. Sasa, kwa kuwa Serikali ilikuwa imeshaanza kufanya ama kuchukua hatua mbalimbali na sasa Wabunge wamependekeza humu hatua mbalimbali pia zinazoweza kuchukuliwa kwa muda mfupi kwa muda mrefu nadhani zichukuliwe hizo pamoja Waheshimiwa Wabunge ili sasa Waziri; kwa sababu Kanuni yetu ya 56 inatoa fursa kwa Waziri kuja na kauli kuhusu jambo fulani. Sasa kwa sababu jambo hili hatutalimaliza kwa Bunge kuazimia jambo fulani basi mimi nimuagize Waziri alete kauli hapa Bungeni ya mambo haya tuliyoyajadili na hatua mbalimbali ambazo Serikali itazichukua kwenye jambo hili.
Sasa kwa sababu ni jambo la dharura na lazima tulifanye kwa udharura basi nimpe muda kidogo Mheshimiwa Waziri; maana kulikuwa na pendekezo hapa kwamba pengine Bunge liahirishwe litoe fursa kwa Serikali ikajipange na mambo kama hayo; hatutaahirisha Bunge isipokuwa Waziri atapewa fursa siku ya Jumanne ataleta kauli yake hapa ndani namna ya kulifanyia kazi jambo hili. Na kwa sababu mengine tuliyoyasema Waheshimiwa Wabunge yanahitaji muda kidogo kwasababu kabla Serikali haijasema itafanya jambo fulani lazima ifanye utafiti na mambo kama hayo.
Kwa hiyo sisi tunataka, yale ya muda mfupi atatueleza siku hiyo ya Jumanne yale ya muda mrefu tunaendelea kumpa nafasi Mheshimiwa Waziri lakini na Serikali kwa ujumla kuendelea kujipanga. Kwa mfano hoja iliyozungumzwa amezungumza Waziri lakini pia Waheshimiwa Wabunge mmeizungumza hapa, ya kuanzisha mfuko maalum sasa uanzishaji wa mfuko maalum inawezekana unahitaji muda kidogo kujipanga Serikali kabla haijasema jambo. Hata hivyo maadamu limesemwa basi Serikali itakuwa ikilifanyia kazi na mambo mengine yaliyozungumzwa hapo. Pia na hii hoja ya kuleta mafuta pengine kwa njia nyingine na yenyewe inaweza ikawa si jambo la muda mfupi kwa sababu lazima watafutwe hao watu wa kuleta mafuta na tujiridhishe mafuta yanatoka wapi na hayo mafuta je, yatakuwa safi. Ninyi ni mashahidi, TBS huwa inarudisha meli hapa. Kwa hiyo hatutaki mafuta yaje halafu tuambiwe jamani bei iko pale pale kwa sababu mafuta yaliyoletwa tena na kampuni fulani ni machafu. Kwa hiyo hayo yote ya kujipanga. Yako mambo yanayoweza kufanywa kwa muda mfupi ikiwa ni pamoja na yale mengi ambayo Wabunge wameyasema hapa na sina haja ya kuyarejea, mawazo yaliyotolewa ni mengi sana Mheshimiwa Waziri nadhani yote ameyapata na Serikali nzima wataleta hiyo kauli.
Lakini sasa nieleze jambo moja la ujumla Waheshimiwa Wabunge; ndiyo maana huwa nawashauri siku zote hapa pengine kuna watu hawaelewi wataelewa vizuri leo. Ni vizuri sana ukisikia Rais amezungumza mahali fuatilia na sasa hivi tunazo namna nyingi za kufahamu Rais amesema nini na wapi. Kwa nini ni muhimu, kwa sababu kanuni zetu zinamlinda Rais humu ndani kusemwa kwa namna isiyostahili. Kusema kwa namna isiyostahili kwa namna ipi? Rais anaweza kuwa amelizungumzia jambo fulani, ukalizungumza na wewe kwa maana pengine ya wazo lako tofauti na Rais lazima ulete hoja mahsusi hapa. Hii ni kwa sababu hatuwezi kuwa tunajadili jambo ambalo Rais ameshalifanyia maamuzi kila mtu anatakiwa kufanya kazi yake nadhani tunaelewana vizuri. Sasa hapa limezungumzwa jambo moja ambalo ndiyo maana nimelazimika kulisema ili taarifa zetu rasmi za Bunge zikae sawasawa kuhusu tozo ya shilingi 100. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri wa Nishati aliiondoa ile tozo Rais akairejesha mjadala kuhusu hoja hiyo maana yake tena unajiuliza kuhusu maamuzi aliyoyatoa Mheshimiwa Rais na hapa panakuwa si mahali pake labda kama hoja mahsusi imeletwa kuhusu maamuzi ya Rais. Pungufu ya hapo sote ni kazi yetu kufuatilia Rais amesema nini kuhusu jambo gani ili unapotaka kuchangia uwe umejipanga kwa namna ambayo kanuni yetu ya 71 hutaikosea kwa sababu haitaki Rais ajadiliwe humu ndani kwa namna isiyostahili.