MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza niishukuru sana Wizara ya Maji kwa sababu Jimbo letu la Temeke maji yamefika karibu kila kata. Tatizo letu kubwa ni kwamba bomba lile kubwa limepita katika barabara kubwa lakini kuvuta maji kwenda ndani ya nyumba zetu ambapo miundombinu siyo mizuri sana kwenye Kata za Buza na Kilakala na nyumba ziko mbali. Niombe Wizara ya Maji tunapoomba kuvutiwa maji ndani ya nyumba zetu, fedha ile ambayo tunatakiwa kuilipa kidogo ni kubwa, sasa mfikirie tuweze kuvuta kwa nusu ya bei halafu muendelee kutudai ndani ya malipo ya kila mwezi kama vile tunavyofanya luku ili tuweze kuona kila mmoja sasa anapata maji ndani ya nyumba yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU SPIKA: Hilo ni ombi, nadhani utakuwa umeliandika Mheshimiwa Waziri.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kumekuwa na taratibu zile kwa mfano nafasi za majeshi na vitu vingine ambavyo watoto wanapatikana kwenye maeneo yetu ya majimbo. Baada ya usaili kutoka kwenye wilaya, anafika mkoani mkoa wanawarudisha, wanaambiwa huyu ana kovu, sijui ana nini, kumekuwa na vigezo vingi sana watu wa mkoa wanadhulumu watu wa wilaya.
Mheshimiwa Spika, sasa tulikuwa tunaomba nafasi zipelekwe wilayani hasa zile ambazo hazihitaji vigezo zaidi ya Form Four. Wakishatoka wilayani waende moja kwa moja kwenye training kwa sababu wanapofika mkoani, watu wa mkoani wanakuwa na nafasi za kuchomeka watu wao na watu wetu waliotoka kwenye wilaya wanaachwa. Tulikuwa tunaomba hilo lizingatiwe, ni hilo tu. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana, nadhani huo ulikuwa ni ushauri, kwa hiyo, utachukuliwa halafu wakaupime kwa sababu hapo mwishoni umemaliza vizuri, lakini vigezo lazima vizingatiwe. Tukisema kutakuwa hakuna vigezo kwa sababu tu watu wametoka mahali, itakuwa changamoto, ila mwishoni umemaliza kwamba unatoa ushauri wa namna ambavyo wafanye hili zoezi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Naibu Waziri naamini umeupokea huo ushauri.