Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Martin Alexander Mtonda Msuha (5 total)

MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:-
Miaka kadhaa iliyopita Serikali iliahidi kuwa itajenga barabara ya kutoka Kitai Wilayani Mbinga hadi Lituhi Wilayani Nyasa kwa kiwango cha lami, lakini hadi sasa wananchi hawaelewi kinachoendelea juu ya ujenzi huo:-
Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Mbinga na Nyasa juu ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martin Mtonda Msuha, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kitai - Lituhi yenye urefu wa kilometa 84.5 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Mkoa wa Ruvuma. Ili kuhakikisha kuwa barabara hii inapitika muda wote, Wizara inaendelea kutenga fedha za kufanyia matengenezo mbalimbali ambapo mwaka 2013/2014 ilitenga shilingi milioni 440 na mwaka 2014/2015 ilitenga shilingi 682.99. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, jumla ya shilingi milioni 1015.123 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hii ili iendelee kupitika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maandalizi ya ujenzi wa barabara za Kitai - Lituhi kwa kiwango cha lami, Wizara kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) tayari imekamilisha taratibu za ununuzi za kumpata Mhandisi Mshauri kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina barabara hiyo.
MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:-
Wananchi wa Tarafa za Hagati, Mbuji na Mkumbi hawapati matangazo ya Redio ya TBC kutokana na Kituo cha TBC- Songea kutokuwa na uwezo wa kurusha matangazo na badala yake wanapata matangazo ya redio toka nchi jirani ya Malawi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza uwezo wa kurusha matangazo ya kituo cha TBC- Songea ili wananchi wa Tarafa hizo wapate habari kupitia TBC?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Martin Alexander Mtonda Msuha, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, matangazo ya Radio ya Taifa kupitia mtambo wa masafa ya kati yaani Medium Wave yenye nguvu ya Kilowati 100 yalikuwa yakisikika vizuri katika Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Ruvuma wakati mtambo huo ulipokuwa ukifanya kazi. Tangu mwezi Julai, 2013 mtambo huo haufanyi kazi kutokana na uchakavu na hivyo kuathiri usikivu wa matangazo ya TBC katika maeneo kadhaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa wananchi kupata matangazo, TBC ililazimika kuhamisha mitambo yake miwili ya Radio yenye uwezo wa Kilowati moja kwa kila mmoja iliyokuwa imefungwa eneo la Mshangano - Songea na kuifunga eneo la juu la mlima wa Matogoro (Songea) ili angalau usikivu wake usambae eneo kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kufunga mitambo hiyo, matangazo ya TBC- Songea yameboreshwa. Hata hivyo, kutokana na uwezo mdogo wa mitambo ya FM inayotumika kwa sasa mawimbi yake ya sauti hayafiki mbali sana ukilinganisha na yale ya mitambo ya Medium Wave iliyokuwa ikitumika wakati wa awali ambayo yanafika eneo kubwa zaidi la Mkoa wa Ruvuma zikiwemo Tarafa za Hagati, Mbuji, na Mkumbi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kukabiliana na changamoto za usikivu hafifu katika maeneo kadhaa Mkoani Ruvuma, TBC imeshafanya upembuzi yakinifu wa kufunga mitambo ya FM yenye uwezo wa kilowati moja katika eneo la Mbamba Bay lililopo Wilaya ya Nyasa ili kuongeza usikivu wa redio na TBC. Katika bajeti ya mwaka wa 2016/2017, Wizara yangu imetenga fedha za maendeleo kwa ajili ya kufunga mtambo eneo la Mbamba Bay. Kazi hiyo ya uboreshaji wa matangazo katika eneo hilo itaanza mara tu fedha za kununua na kufunga mitambo zitakapotolewa.
MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:-
Wilaya ya Mbinga imebahatika kupata mradi wa kujenga barabara ya lami toka Kijiji cha Longa hadi Kijiji cha Litoha kwa kiwango cha lami kwa ufadhili wa Umoja wa Nchi za Ulaya na mradi huo umeshaanza kutekelezwa:-
(a) Je, ujenzi wa mradi huo unategemewa kukamilika lini?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwalipa fidia wananchi waliotoa mashamba na nyumba zao kupisha ujenzi wa mradi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martin Alexander Mtonda, Mbunge wa Jimbo la Mbinga Vijijini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba wa ujenzi wa barabara awamu ya kwanza kutoka Longa hadi Bagamoyo ulianza tarehe 1/10/2015 na unategemewa kukamilika tarehe 30/6/2016. Hata hivyo, kutokana na mvua kubwa zilizonyesha Wilaya ya Mbinga, Mkandarasi alishindwa kufanya kazi kama ilivyokuwa imepangwa hali iliyolazimu kuongeza muda hadi tarehe 30/9/2016. Sehemu ya pili inaanzia Kijiji cha Bagamoyo hadi Kijiji cha Lutoho chini ya Mkandarasi GS Contractors Limited ambaye mkataba wake ulianza tarehe 1/5/2016 na unategemewa kumalizika tarehe 30/1/2017.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, sharti lilitolewa na Umoja wa Ulaya ili waweze kujengewa barabara ya lami kutoka Longa hadi Bagamoyo lilikuwa ni kutokuwepo kwa fidia. Halmashauri kwa maana ya Madiwani walifanya uhamasishaji wa kutoa elimu kwa wananchi ili kukubali mradi huo na wote waliridhia ndiyo maana barabara hiyo imeanza kujengwa. Serikali inawapongeza viongozi wa Halmashauri na wananchi kwa ujumla kwa kukubali kuupokea mradi huo kwa ustawi wa uchumi wa maendeleo ambayo ni uzalishaji mkubwa wa kahawa.
MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:-
Wananchi wa Mbinga wanaishukuru Serikali kwa mradi wa kusambaza umeme vijijini kwani wana imani mradi huo utasaidia kuinua hali za maisha. Hata hivyo ni vijiji 34 tu ndiyo vimepatiwa umeme kupitia mpango wa usambazaji umeme unaotekelezwa na REA Awamu ya Pili.
Je, lini Serikali itapeleka umeme katika vijiji 118 vilivyosailia?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Martin Alezander Mtonda Msuha, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali itapeleka umeme katika vijiji 118 vilivyobaki vya Wilaya ya Mbinga kupitia mradi kabambe wa REA Awamu ya Tatu. Ujenzi wa mradi huu utaanza mwezi Disemba, 2016 na kukamili katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020. Hatua iliyofikiwa hivi sasa ni kukamilika kwa taratibu za kuwapata wakandarasi watakaohusika na ujenzi wa mradi huu.
Mheshimiwa Spika, kazi ya kupeleka umeme kwenye vijiji hivyo itajumuisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovolti 0.4 yenye urefu wa kilometa 471, ufungaji wa transfoma 246 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 19,185. Kazi hii itagharimu shilingi bilioni 18.1.
MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:-
Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2015/2016 Mawakala wa Usambazaji Pembejeo kwa Vocha katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga wanaidai Serikali jumla ya Sh.824, 000,000/=
Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa deni hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Martin Mtonda Msuha, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika msimu wa kilimo wa mwaka 2015/2016, Serikali ilitoa ruzuku ya pembejeo kwa utaratibu wa vocha kwa mikoa 25 ya Tanzania Bara. Kazi ya kusambaza pembejeo hizo kwa kaya za wakulima wanufaika wapatao 999,926 ilifanywa na makampuni na Mawakala wa Pembejeo katika Halmashauri zipatazo 144 zilizonufaika na utaratibu huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kujiridhisha na uhalali wa madai ya makampuni ya Mawakala waliotoa huduma ya pembejeo katika Wilaya hizo, Wizara imefanya uhakiki wa awali ambao umefanyika katika baadhi ya mikoa yenye kiasi kikubwa cha madai.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya uhakiki wa awali imefanyika katika mikoa nane kati ya mikoa 25 ya Tanzania Bara iliyopata ruzuku. Matokeo hayo yameonesha upungufu mkubwa katika madai hayo. Hivyo, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kufanya uhakiki katika mikoa yote kwa makampuni na Mawakala wote waliosambaza pembejeo katika msimu wa 2015/2016 katika kipindi cha mwezi mmoja. Baada ya uhakiki huo madeni yote halali yatalipwa.