Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Martin Alexander Mtonda Msuha (5 total)

MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na pia nashukuru kwa pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, ni lini sasa hii kazi ya upembuzi yakinifu itakamilika ili ujenzi uanze?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili, wananchi wa Mbinga pamoja na Nyasa wanafurahi na wanaishukuru Serikali kwa kupata mradi wa ujenzi wa barabara wa Mbinga – Mbamba Bay chini ya mradi wa Mtwara Corridor. Je, Serikali haioni haja sasa kwa kutumia fursa hii kuunganisha kipande cha barabara inayotoka Unyoni mpaka Kijiji cha Mango Wilayani Nyasa kupitia Mapera, Maguu na Kipapa? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Martin Mtonda Msuha, Mbunge wa Mbinga Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Martin Mtondo Msuha pamoja na Mheshimiwa Stella Manyanya kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha Wilaya yao ya Mbinga inakuwa na miundombinu ya uhakika ili mazao wanayoyalima hasa kahawa inalifikia soko kwa urahisi na kwa bei nafuu. Mimi niwapongeze sana na nawahakikishieni kwamba nikiwa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na Mheshimiwa Waziri wangu tutahakikisha dhamira yenu inakamilika katika kipindi hiki cha miaka mitano kwa kadri fedha zitakavyokuwa zinapatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjulisha Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hii ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, kwanza naomba tuikamilishe na suala la tunaikamilisha lini kwa maana ya kutoa tarehe sio rahisi sana kwa sababu kwa sasa tupo katika hatua ya kumpata huyo mkandarasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba mtuamini kwamba tuna nia ya dhati, kazi hiyo tutaifanya na tutaisimamia na itakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa swali la pili, naomba niwajulishe Waheshimiwa Wabunge wote wa Wilaya ya Mbinga kuanzia Mheshimiwa Mtondo Msuha, Mheshimiwa Stella Manyanya na Mheshimiwa Sixtus Mapunda kwamba mwaka huu tunaanza kuijenga ile barabara ya kutoka Mbinga - Mbamba Bay.
Naomba mtupe fursa tuikamilishe barabara hii. Mtakumbuka ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kutembea kwa taxi kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay na kutoka Bukoba hadi Mtwara itakuwa imekamilika kikamilifu kabisa. Baada ya hapo, nawahakikishia nguvu zetu zote tutakuwa tunaelekeza katika barabara hizo zingine ikiwa ni pamoja na hii barabara ya kutoka Unyoni hadi Mango kupitia vijiji ambavyo Mheshimiwa Mtondo Msuha amevitaja.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante! Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa umbali wa kutoka Songea na Mamba Bay - Nyasa bado ni mrefu, Serikali haioni haja ya kufunga mitambo angalau kwenye milima ya Mbuji ili kuongeza usikivu katika tarafa hizo zilizotajwa?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upembuzi uliyofanyika, huu mtambo utakaofungwa Mbamba Bay utakuja kukutana na mtambo uliofungwa hapa Matogolo na kwa pamoja usikivu utaongezeka badala ya kufunga kwenye Kata ya Mbuji kama anavyosema. Ni upembuzi wa Kitaalam umefanyika na hili likifanyika tutaongeza usikivu katika eneo lake na kwa sababu ni matokeo ya utafiti tunaamini hili likifanyika basi hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge anayaombea hapa yatakuwa yamefanyika na usikivu utaongezeka.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kuuliza maswali mawili yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mazingira ya Jimbo la Mlimba yanafanana kabisa na mazingira ya Jimbo Mbinga Vijijini, je, Serikali itapeleka maji lini katika Miji ya Maguu, Matiri na wa Rwanda ambao una taasisi nyingi sana zikiwemo sekondari za form five na six?
Mheshimiwa Naibu Spia, swali la pili, katika Jimbo la Mbinga kuna miradi miwili ya maji iliyokuwa ikiendelea katika Kata ya Mkako lakini pia mradi mwingine katika Kata ya Ukata kupitia Kijiji cha Litoho. Ni lini Serikali itakamilisha miradi hii ya Mkako pamoja na Ukata ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata maji salama na safi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Serikali itahakikisha inapeleka maji katika maeneo ya Mbinga Vijijini, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tu kwamba tayari tumeanza Programu ya Pili ya Utekelezaji wa Maendeleo ya Sekta ya Maji Nchini. Kama nilivyokwishatoa majibu kwamba wafadhili wametuahidi dola za Kimarekani bilioni 3.3 ambazo zitatumika kutekeleza miradi ya maji hapa nchini, hii ikiwa ni pamoja na miradi ya Mbinga Vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka huu wa fedha Mbinga Vijijini tumewatengea fedha. Niagize na naomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane tutengeneze mpango mzuri wa matumizi ya fedha hizi tulizozitoa katika hii bajeti ya mwaka wa fedha unaoanza mwezi Julai ili kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo ya Mbinga Vijijini wote wanapata maji safi na salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali la pili umesema kwamba kuna miradi miwili ambayo bado haijakamilika. Tumeshaelekeza kwamba miradi ile ambayo haikukamilika katika Programu ya Kwanza ya Utekelezaji wa Sekta ya Maji ndiyo tunaanza kuikamilisha kabla hatujaanza miradi mipya. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane na Halmashauri yake kuhakikisha kwamba kwanza tunakamilisha miradi hii kabla hatujaanza kuingia kwenye miradi mipya.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nami pia niungane na Serikali kwanza kuwapongeza wananchi wa Kata za Mkumbi, Kata za Kipololo na Ukata ambao walikubali kupisha mradi huu kwa ustawi wa uchumi wa Wilaya yetu. Hata hivyo nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa upana wa barabara hii, barabara hii inaanzia Mbinga Mjini inapita Litowo lakini pia inaunganisha na Wilaya ya Nyasa. Mfadhili amekubali kujenga kutoka Longa hadi Litoho; kuna kipande cha kilomita 15 kutoka Mbinga Mjini haji Kijiji cha Longa. Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kutumia nguvu zetu za ndani ili kukamilisha kipande hiki cha kutoka Mbinga Mjini hadi Longa chenye umbali wa kilomita 15?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, barabara yetu inayotoka Mbinga Mjini kwenda Hospitali ya Litembo kupitia Kijiji cha Tanga – Uyangayanga - Kindimba - Mundeki ni muhimu sana kwa vile Hospitali hii inatumika kama Hospitali yetu ya Rufaa. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuijenga barabara hii inayoelekea Hospitali ya Rufaa ya Litembo ili kurahisisha huduma za afya katika eneo hilo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nami nawapongeza sana wananchi hawa kwa sababu barabara hii ina Euro karibu milioni nne ambayo ukipiga mahesabu inaenda karibu shilingi bilioni kumi na eneo lile nadhani Mheshimiwa Mbunge anafahamu, kwanza kuna changamoto kubwa sana ya milima; lakini tumepata ufadhili mkubwa, kwa hiyo, hata zao la kahawa sasa watu watakuwa na fursa ya kuweza kusafirisha vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, ombi lake ni kwamba hiki kipande cha katikati cha kutoka Mbinga Mjini mpaka Longa ambacho kina kilomita 15 ni jinsi gani tutafanya sasa kipande hiki kiweze kuunganishwa? Mheshimiwa Mbunge, tumelisikia hili, lakini naomba michakato hii sasa ianze katika bajeti kuonyesha kwamba kuna uhitaji kutoka Halmashauri husika, nasi tutaangalia kwa pamoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua kwamba barabara hii, hiki kipande cha kilomita 15 bajeti yake itakuwa ni kubwa, lakini nadhani kwanza muanze kuangalia jinsi ya kufanya kwamba Halmashauri ionyeshe kipaumbele katika eneo hilo. Katika mchakato wa bajeti, Serikali itaangalia namna ya kufanya ili eneo hilo sasa liweze kupewa kipaumbele, angalau kipande cha lami kiweze kuunganishwa na mwisho Nyasa na Mbinga iweze kuunganika vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kusema kutoka Mbinga Mjini mpaka Kihesa ambako kuna Hospitali, wananchi wanapata huduma pale, vilevile naomba nirejee katika jibu langu la kwanza kwamba tuweke kipaumbele na Serikali haitasita kuona kwamba kwa sababu ni maeneo ambayo wananchi wanapata huduma hasa ya afya, nasema kipaumbele hiki lazima tukifanyie kazi.
Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge kwa juhudi ile anayoendelea kuifanya na Madiwani wake, waweke katika mpango, Serikali itaujadili kwa kina na sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI hatutasita kushirikiana na Halmashauri ya Mbinga kuhakikisha maeneo haya yanapata huduma kama maeneo mengine.
MHE. MARTIN M. MSUHA: Mheshimiwa Spika, asante pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, mpango wa REA III una-cover mwaka 2016 mpaka 2019/2020. Serikali ina mpango gani kushirikisha Waheshimiwa Wabunge katika kupanga maeneo ya kupeleka umeme katika miaka hiyo husika kuzingatia kwa bajeti ya kila mwaka?
Mheshimiwa Spika, swali la pili Mkoa wa Ruvuma haujaunganishwa bado na umeme wa Gridi ya Taifa. Ni lini sasa mradi wa umeme wa Gridi ya Taifa kutoka Makambako kwenda Songea utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, nishukuru kabisa Mheshimiwa Mbunge ametukumbusha kwamba tuwaambie Waheshimiwa Wabunge. Kwanza kabisa niwaondoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, mradi wa REA Awamu ya Tatu unaoanza sasa tunatumia utaratibu ufuatao:-
Mheshimiwa Spika, wakandarasi watakapokuwa wanaingia site kuanzia Disemba mwaka huu, hatua ya kwanza itakuwa ni kukutana na kukubaliana na Waheshimiwa Wabunge kabla hawajaanza kazi kwenye maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini nitoe tu angalizo lingine, kwamba tumeweka utaratibu sasa mahali ambako kuna Ofisi zetu za TANESCO tumeandaa kwa kushirikiana na viongozi wa Serikali za Mitaa kuweka vituo rasmi ili wananchi wasiende kwenye Ofisi za TANESCO ila wafanyakazi wa TANESCO wakae kwenye vituo ambavyo Serikali za Mitaa zitakuwa zimetambua.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wabunge pamoja na Diwani watashirikishwa sana kabla ya utekelezaji wa mradi huu kuanza.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na mradi wa Makambako – Songea, mradi wa Makambako – Songea una sehemu tatu za utekelezaji. Sehemu ya kwanza ni ujenzi wa distribution line ambao inachukua urefu wa kilomita 900 kwa maeneo yote ya Mbinga, Songea na maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, mradi huu ulianza mwaka juzi na unakamilika mwakani mwezi Julai. Sehemu ya pili ni kujenga transmission line ambayo imeanza mwaka jana na hivyo itakamilika mwezi Septemba, 2018. Hatua ya tatu ni kujenga substations tatu, moja ikiwa Makambako, nyingine Songea na nyingine eneo la Madaba, kwa ujumla wake kazi zote zitakamilika mwezi Mei, 2018.