Contributions by Hon. Eng. Stella Martin Manyanya (71 total)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kazi zao wote kwa ujumla.
(i) Lini Chuo cha Uvuvi kilichokuwa kinazungumziwa kwenye Wilaya ya Nyasa kitaanza?
(ii) Kwa nini ushuru wa uvuvi unabadilika mara kwa mara kwa madai kuwa unachajiwa kwa dola kwa mujibu wa sheria? Je, ni kweli? Kama ni kweli, hiyo sheria itarekebishwa lini? Kwani ni mateso kwa wananchi.
(iii) Kuna malalamiko makubwa ya watumishi wa uvuvi ambao wapo katika forodha ya Mbambabay hususan Bwana Saleke. Nashauri mkamtumie sehemu nyingine kwa kubadilishwa kituo cha kazi.
(iv) Jimbo langu ni wakulima wa mihogo kama zao kuu la mwambao, tunaomba mbegu za kisasa kwa mfano za kiloba.
(v) Kwa kuwa eneo pia ni zuri kwa ndizi, tunaomba mafunzo ya kilimo cha ndizi.
(vi) Tunashukuru boti ya Doris, iongezwe moja kwa ajili ya Kituo cha Ng‟ombo hasa kwa ajili ya uokoaji.
(vii) Kahawa ipunguzwe ushuru. Naungana na Mheshimiwa Sixtus Mapunda, Mbunge wa Mbinga.
Hongereni na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumpongeze Mheshimiwa Waziri kwa jitihada zake za kuhamasisha viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizo, Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni kuwa kutajengwa kiwanda cha samaki na utengenezaji wa boti: Je, mpango huo ukoje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kufuatilia TBS kwa ajili ya kujenga shades za kukaushia samaki na dagaa, ikiwa ni sehemu ya kusaidia MSMES na SMEs. Napenda kufahamu je, Wizara ina fahamu juu ya hilo ili kuendelea kuwasukuma TBS ikiwa ni sehemu ya mafunzo katika suala la usindikaji wa dagaa na samaki wenye ubora?
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hao wamekuwa waki-process dagaa katika mazingira duni, mbaya zaidi kuondoa sura nzuri ya fukwe za Ziwa Nyasa. Angalau basi tusaidiwe eneo la Mbamba Bay.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini Mheshimiwa Waziri atasaidia kwa kuagiza taasisi zake TBS, SIDO na wengine anaowajua ili kusaidia na kuleta tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri, asaidie kabla wananchi hawajanitumbua.
Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwapongeza Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Nape Nnauye pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Anastazia Wambura respectively. Naipongeza timu yote ya wanahabari hususani TBC, TBC Taifa na wengine wote wa Wizara hii. Nimpongeze pia Dkt. Elisante, mwalimu wangu wa siku moja, I hope nitaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri mdogo, pamoja na kazi nzuri wanazozifanya TBC na TBC Taifa, nashauri kuanzishwe kipindi maalum kama kilivyo kile cha Bango au Chereko, kipindi hicho kiwe cha aidha Mbunge wangu au Jimbo langu au Nimetimiza Ahadi Yangu. Kipindi hiki kiwe cha kulipia badala ya kupata nafasi kwa kubahatisha na pia bure kabisa. Ni vema tuchangie hata kama shilingi 200,000 kwa dakika 30 au hata kama ni kwa dakika 15. Kipindi hicho kituwezeshe Wabunge kuzungumzia utekelezaji wa kazi zetu au kuwapasha habari wananchi wetu. Pamoja na kuchangia bado isiruhusiwe mtu kusema vyovyote anavyotaka, ethics lazima iwe observed. Fedha hizo zitasaidia kupunguza kero ndogo ndogo za wanahabari wetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimwa Naibu Spika, awali ya yote nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo, Mbunge na Waziri wa Nishati na Madini pamoja na Naibu Waziri wake Dkt. Kalemani, Mbunge, kwa kazi kubwa mnayoifanya. Pia nawapongeza watumishi na wafanyakazi waliopo kwenye Kamati hii chini ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa shukrani za pekee kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo la Nyasa na mimi mwenyewe kwa kufikisha umeme kwenye Makao Makuu ya Wilaya, Mbamba Bay/Kilosa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilimwandikia Mheshimiwa Waziri kwenye barua yangu, kimsingi nafahamu jitihada zinazoendelea katika kufikisha umeme kwenye Vijiji vyote 82 vya Jimbo langu kupitia REA III kama ambavyo nilifahamishwa. Natarajia kupitia dhamira hiyo, uwezo wake Mheshimiwa Waziri na ahadi ya Chama cha Mapinduzi iliyonadiwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais siku ya tarehe 8/9/2016 – Tingi, suala hilo litakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, line kuu ya umeme wa Kilowatt 33 Mbinga – Mbamba Bay inapita kwenye msitu lakini pia katika milima na mabonde makali kiasi wakati mwingine kusababisha short na hivyo kukosesha umeme Mbamba Bay.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri kwa kuwa mpango pia ni kuendelea kusambaza line hiyo katika vijiji vingine vya Ziwa Nyasa hadi Lituhi, ni vyema kutengeneza T-off eneo la Kihegere ili kuunganisha line hiyo na ile iliyoishia eneo la Kipape – Chemeni, kiasi cha kusaidia endapo umeme wa upande mmoja kukatika. Kipande hicho ni kama Kilometa 15 – 20 tu. Pia naomba kuweka transformer katika Kijiji cha Mkalole na Makunguru kabla ya kufika Mbamba Bay. Jimbo letu la Nyasa ni changa kimaendeleo naomba lisaidiwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, lakini siyo kwa umuhimu, napenda kuwashukuru na kuwapongeza REA kwa jitihada zao katika kutekeleza majukumu yao. Tunawaomba mwendelee kupokea simu zetu bila kuchoka. Natanguliza shukrani zangu za dhati.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutujalia afya njema, pia nitumie nafasi hii kukushukuru na kukupongeza wewe binafsi, Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na viongozi wote wa Bunge kwa ujumla kwa jinsi ambavyo mnaliongoza Bunge letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa kusimamia vizuri Serikali kwa niaba ya wananchi wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mwaka 2016/ 2017 sikufanikiwa kuchangia bajeti kutokana na kifo cha mama yangu mzazi, hivyo basi naomba nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kuniteua katika nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile namshukuru Makamu wetu wa Rais, Rais wa Zanzibar pamoja na Waziri wetu Mkuu kwa jinsi ambavyo wananiongoza na kunipa maelekezo na ushauri mbalimbali katika kutimiza wajibu wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee kabisa namshukuru sana Waziri wangu Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako kwa ushauri na mwongozo wake kwangu, ambao umekuwa ukiniongezea ufanisi katika utendaji wangu wa kila siku. Nimekuwa nikijipambanua siku zote kama silaha ya msaada kumbe yeye ni rada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niwashukuru watumishi wote wa Wizara na Taasisi zake chini ya uongozi wa Dkt. Leonard Akwilapo, Naibu Makatibu Wakuu Profesa Simon Msanjila na Dkt. Avemaria Semakafu kwa ushirikiano wanaonipa na kutekeleza majukumu yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naishukuru familia yangu na vilevile nimkumbuke mama yangu mzazi kipenzi Bi Xavelia Mbele pamoja na Marehemu wote waliotangulia wakiwemo wale watoto wa Arusha, ndugu na marafiki wote tunawaombea wapumzike kwa amani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyoongea nawaona wapiga kura wangu wa Jimbo la Nyasa wakitabasamu mioyoni mwao kuwa walinichagua Mbunge sahihi, mimi ni mtumishi wao, kwani wao ni bora zaidi, nawapenda sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nijibu hoja za Waheshimiwa Wabunge kama ifuatavyo, na hivyo naanza kwa kuunga mkono hoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianzia na DIT suala la kupeleka wakaguzi maalum kutokana na kuchelewa kwa ujenzi, lakini pia matumizi makubwa ya fedha. Kimsingi tayari barua ilishaandikwa kwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani yenye Kumbukumbu Na. PL/AC.19/119/01 ili afanye ukaguzi maalum wa mradi huo. Taarifa itakapokamilika itawasilishwa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii. Vilevile napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa mradi huo sasa umeendelea vizuri na umefikia asilimia 95.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa pia na hoja ya kutaka kufahamu sifa za kujiunga na Taasisi ya Teknolojia - DIT. Kimsingi hapa nitatamka tu sifa za msingi, lakini ni vyema mkawasiliana na chuo au kupitia tovuti yao kuweza kupata taarifa kamili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kuna ngazi mbili, ngazi ya kwanza ni ya diploma ya kawaida ambayo muombaji anatakiwa awe na sifa za kidato cha nne na awe amefaulu angalau pass nne kuanzia “C” na vilevile kwa upande wa degree awe na diploma ya kawaida na GPA ya tatu au awe na cheti cha kidato cha sita na awe ana point angalau nne.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na dhana kutoka miongoni mwetu ambayo kupitia michango nimeweza kufahamu kwamba kuna hisia kwamba vyuo vya ufundi sasa hivi vimepungukiwa na viwango tofauti na ilivyokuwa awali. Nipende tu kuwajulisha Waheshimiwa Wabunge kwamba hali ya sasa ni kwamba vyuo hivyo vimeboreshwa zaidi kwa kuweka ngazi mbalimbali zinazowezesha unyumbufu katika utoaji kozi hizo. Kwa hali ya mwanzo ilikuwa ni kama unasoma kwa mfano kozi ya ufundi sanifu ilikuwa ni lazima uhakikishe unamaliza kozi nzima na ukikatisha ulikuwa hupati cheti kabisa. Sasa hivi mfumo unakuwezesha kusoma hatua kwa hatua na kila ngazi unayoifikia unapata cheti ambacho kinakuwezesha kufanya kazi zako na pia kuweza kurudi pale inapohitajika kurudi chuoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la VETA, hilo limechangiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi sana juu ya mahitaji ya VETA. Tatizo kubwa ni upatikanaji wa fedha. Niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge, kwa wale ambao maeneo yao yana majengo na yana ardhi za kuweza kutupa ili kuendeleza tunaomba basi mkamilishe upatikanaji wa hati, ili maeneo hayo yanapoletwa kwetu yasiwe na mgongano. Kwa misingi hiyo napenda kuwapongeza Wabunge ambao wameisha chukua hatua kama hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mbunge wa Busokelo ambaye alifuatilia na akafuatilia hati kwa Mheshimiwa Mwandosya na hivi sasa chuo cha VETA kimeishakamilishwa na wanafunzi wanasoma. Lakini pia nawapongeza Waheshimiwa Wabunge wengi ambao wanajituma katika kuchangia katika suala la elimu, wapo wengi. Nafahamu kuna ambao wamechangia uboreshaji wa shule kama Loleza, Mheshimiwa Mbene kwenye eneo lako na wengine wengi naomba tuendelee kushikamana katika hali hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ni kuendelea kuwa na VETA katika kila Wilaya, lakini kwa sasa tutazingatia kuimarisha VETA zilizopo kwa kuziongezea mabweni, walimu pamoja na vifaa vya kufundishia na kujifunzia, lakini vilevile kuhakikisha kuwa tunaimarisha vyuo vingine kama FDC ili viweze kuchukua wanafunzi na kukidhi mahitaji yanayoendana na hali ya sasa. Kwa upande wa FDC ni kwamba FDC nyingi yaani vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vinaonekana kuwa na hali mbaya sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshafanya mkutano tayari na wakufunzi wa vyuo hivyo, tuna vyuo jumla 55, na mwaka huu tumeshatenga shilingi bilioni 12 kwa ajili ya kuanza ukarabati katika vyuo hivyo, lakini pia kufuatilia mitaala itakayowezesha kufanya kozi zitakazosaidia wananchi kwa ujumla kwa mahitaji ya soko hasa katika kwenda katika uchumi wa viwanda, vilevile kuzingatia makundi mbalimbali ikiwemo watoto wa kike ambao hawakupata fursa ya kuendelea na masomo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa COSTECH. COSTECH imekuwa ikiendelea kutengewa fedha, kwa mfano kwa mwaka huu 2016 ilipata shilingi bilioni 45.26 katika fedha hizo kuna ambazo zimetekeleza miradi ya upande wa pili wa nchi (Zanzibar). Kwa mfano SUZA katika mradi wa vifaranga vya kaa, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo cha Mpunga na Viazi Kizimbani, Mwani kwenye Institute of Marine Sciences. Pia kwa upande wa Bara kuna taasisi kama TIRDO na nyingine nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Serikali itaendelea kutenga fedha na kuhakikisha kuwa mfuko huo wa COSTECH unatumika vizuri, ambao tunaita MTUSATE na kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi na kuleta matokeo ambayo yanatarajiwa hasa katika kuongeza thamani ya mazao yetu pamoja na fursa tulizonazo nchini. Vilevile tumeendelea kuongeza nguvu na jitihada katika kituo chetu cha TEHAMA na kiatamizi ambacho kinahusika na masuala ya kuibua vipaji mbalimbali vya vijana wetu ambavyo viko pale katika Ofisi za COSTECH - Kijitonyama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la walimu wa masuala ya sayansi. Nipende tu kukufahamisha kwamba ni kweli tuna upungufu katika eneo hilo, lakini hata hivyo Serikali imeisha jitahidi kwa mwaka huu, imeweza kuajiri walimu wa sayansi na hisabati 4,129 na baada ya uhakiki wa vyeti vya walimu 3,081 basi ajira hizo zitaendelea tena. Nipende tu kusema kwamba Serikali imekuwa ikiendelea na jitihada hizo ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wetu wanapata elimu inayostahili kwa kupewa walimu wenye sifa pamoja na vifaa vya kufundishia na kujifunzia kama vifaa vya maabara.
Vilevile kwa upande wa mafundi sanifu wa maabara Serikali kwa kushirikiana na vyuo vya ualimu kwa kushirikiana na TCU na NACTE wataandaa mitaala na kuanza mafunzo kwa ajili ya kuongeza wataalam wa maabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala linalohusu ya tatizo la ujinga katika nchi yetu. Kama ambavyo nimejibu swali la msingi namba152 la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga tarehe 5 Mei, 2017, ni kweli tuna watu wasiojua kusoma na kuandika yaani vijana na watu wazima asilimia 22.4 kwa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012. Zipo jitihada mbalimbali za kuhakikisha kwamba tunapunguza tatizo hilo kupitia MUKEJA, lakini pia kupitia Mpango wa Ndiyo Ninaweza, kuimarisha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu na vilevile kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanaotakiwa kuanza shule wanakwenda shule ili kupunguza ongezeko la watu hao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba watoto wote wanaotakiwa kwenda shule wanakwenda kuanzia elimu ya awali na hivi tumeanzisha hata shule shikizi pamoja na kuongeza idadi ya walimu wa elimu ya awali na hivyo kuwezesha kupata wanafunzi wengi zaidi katika eneo hilo. Tunatarajia ifikapo mwaka 2022 wakati wa sensa ijayo Taifa letu liwe limepunguza ujinga na kufikia angalau asilimia si zaidi ya 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie juu ya lugha ya alama. Tayari Wizara imeshaanza jitihada za kutengeneza vitabu kwa ajili ya kufundisha lugha ya alama. Tunategemea hali hiyo itawezesha wanafunzi na wazazi wao kupata mawasiliano ya kirahisi lakini pia hata sisi wenyewe kuifahama lugha hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuna jambo ambalo limejitokeza leo na katika siku hizi za karibuni, niombe kuungana na Mheshimiwa Waziri wangu kwa masikitiko makubwa juu ya mapungufu yaliyojitokeza katika uchapishaji wa vitabu. Hivyo tunawaomba radhi kwa niaba ya wananchi kwa mapungufu hayo. Hata hivyo Mheshimiwa Waziri wangu atalizungumzia suala hili kwa kina zaidi. Nomba radhi kwa niaba ya Wizara yangu.
Mheshimiwa Mwenyekit, baada ya maneno haya nizidi tu kusema kwamba tumedhamiria kama Wizara kuona kwamba elimu inaendelea kutolewa ikiwa bora na kila aina ya tatizo tutajitahidi kadri inavyowezekana kulifanyia kazi na kuhakikisha kuwa wananchi wa Tanzania wanapata fursa ya kusoma vizuri na kupata ajira katika soko linaloendana na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba kuunga hoja tena.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia afya na baraka tele zinazotuwezesha kutekeleza majukumu tuliyokasimiwa kwa maendeleo ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kwangu na kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Nathamini sana dhamana aliyonipa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru pia Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwongozo wao thabiti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumshukuru Mheshimiwa Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwongozo na ushirikiano wake mkubwa unaoniwezesha kutekeleza vizuri majukumu niliyopewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uniruhusu pia kuishukuru sana familia yangu kwa sala na ushirikiano wao ambao ni Baraka na nguvu ya kipekee kwamba…
KUHUSU UTARATIBU . . .
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa hekima zako na ndiyo maana tulikuchagua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kumshukuru tena, narudia, Mheshimiwa Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, kwa mwongozo na ushirikiano wake mkubwa unaoniwezesha kutekeleza vizuri majukumu niliyopewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uniruhusu kuishukuru sana familia yangu kwa sala na ushirikiano wao ambao ni baraka na nguvu ya kipekee kwangu katika kutekeleza majukumu haya mapya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua pia fursa hii adhimu kuwashukuru sana wapiga kura wangu wote na wananchi wa Jimbo la Nyasa kwa kuendelea kuniamini na kunipa ushirikiano kama Mbunge wao.
KUHUSU UTARATIBU . . .
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tumelelewa kwa nidhamu kwa upande wa kambi hii ndiyo maana Mwenyekiti akisema neno tunaheshimu. Kwa sababu maelekezo ya Kiti ndiyo ya mwisho. Naomba uheshimu Kiti. Wewe usiteseke, uendelee kuomba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapojenga hoja, kuna namna ya kuvuta pumzi. Mimi ni Yohana, ndiyo naanza utangulizi hapa, kwa hiyo, usiniletee vurugu. Ninachosema ni kwamba Tanzania sasa tunajenga viwanda, endelea kusikiliza hoja.
na kamanda wetu mkuu mnamfahamu, ni Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, namshukuru na tunashukuru kwa mwongozo anaoutoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, hoja zetu zitajibiwa zaidi kwa kadri tunavyoenda, lakini nikianzia na hoja ya tafsiri ya viwanda na suala hilo lilitolewa na Mheshimiwa Aida Joseph. Napenda niseme kwamba kiwanda ni eneo ambapo shughuli ya kiuchumi hufanyika ikihusisha uchakataji wa malighafi (value addition) kwa lengo la kuzalisha bidhaa ambazo hutumika moja kwa moja kwa mlaji au viwanda vingine. Hotuba ya bajeti ya mwaka 2018/2019 ukurasa wa tano, aya ya 15 mpaka 16 imeeleza hayo na imeainisha viwanda hivyo kwa kadiri ya ngazi zake na imefafanua kwa uwazi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nikiunganisha na suala ambalo lilijitokeza kwa upande wa hoja ya Mheshimiwa Cecil Mwambe, viwanda hivyo vinavyozungumzwa ni viwanda gani na ni vipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana Mheshimiwa Waziri alipokuwa akitoa hotuba yake, alionesha kitabu ambacho tuliamua kwa makusudi kuorodhesha viwanda vyote. Hiyo ipo katika soft copy ambayo imekabidhiwa kwa ajili ya gharama, lakini pia muda, tumesema kitabu ni hiki. Kama kweli Mheshimiwa Cecil unatoka kwenu Ndanda na unawajua watu wako wote, njoo chukua kitabu hiki upitie, watu wa Ndanda utawaona wako humu, wale wote wenye viwanda vidogo sana, vidogo, vya kati na vikubwa kwa kadri ya utaratibu uliopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwafahamisha Waheshimiwa Wabunge kwamba viwanda ni sawa na binadamu, vinazaliwa, vinakua na vinakufa. Kwa hiyo, usishangae kuona kwa data hizi ambazo zilitengenezwa na kuhakikiwa na NBS toka mwaka 2014 na pia kuongezeka kwa idadi hii ambayo tunasema kufikia sasa, vingine vinaweza visiwe kwenye kazi kwa sababu hatufanyi uhakiki kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba nikimaliza, njoo uchukue, kama unawafahamu watu wako utawaona humu, mimi wa kwangu nimewaona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kuhusu kuwezesha taasisi za tafiti na teknolojia kuchochea maendeleo ya viwanda. Niseme tu kwamba ni kweli kuna umuhimu mkubwa sana wa kuziwezesha taasisi hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa taasisi hizi, hasa katika kufanya tafiti zinazolenga uongezaji thamani, ubora na kupunguza upotevu wa mazao na malighafi mbalimbali kwa kutumia teknolojia sahihi. Vilevile kupitia tafiti hizi, taasisi hizi zinaainisha maeneo ya uanzishwaji wa viwanda (industrial mapping) ili kuweza kutoa ushauri kwa Serikali na sekta binafsi, kuanzisha viwanda shindani na endelevu. Tafiti hizi zitawezesha kuwa na matumizi bora na yenye tija ya rasilimali zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikitenga fedha kuziwezesha taasisi hizi. Kwa mfano tu, kumekuwepo na ongezeko la fedha za maendeleo zilizotolewa kutoka shilingi milioni 678.95 mwaka 2016/2017 hadi shilingi bilioni 7.511 mwaka 2017/2018 likiwa ni ongezeko la asilimia 1,006 ya fedha zilizotolewa na Serikali kwa taasisi hizi. Jitihada za Serikali za kuwezesha zaidi kifedha zitaendelea kutokana na umuhimu wa taasisi hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna suala lilikuwa limezungumzwa kuhusiana na Kiwanda cha Viuadudu. Kiwanda cha Viuadudu cha Kibaha kilianza uzalishaji wa kibiashara kuanzia tarehe 3 Februari, 2017. Kiwanda hiki kina uwezo wa kuzalisha lita milioni sita za viuadudu kwa mwaka. Hadi sasa kiwanda kimezalisha jumla ya lita 449,503 ambazo zimeuzwa ndani na nje ya nchi kama vile Niger na Angola. Ni kweli kabisa jumla ya Halmashauri 84 zilikuwa zimechukua dawa, yaani viuadudu katika kiwanda hiki na Halmashauri tisa ziliweza kulipa nyingine tunaendelea kuzihamasisha. Kiwanda hiki ni muhimu sana katika vita yakutokomeza ugonjwa wa malaria nchini na hasa katika hili eneo la malaria, tunamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alitoa fedha kwa ajili ya kupeleka kwenye Halmashauri ambazo zilikuwa zina maambukizi makubwa ya Malaria na fedha hizo zililipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala kuhusiana na utekelezaji wa Mkataba wa C2C. Katika hotuba ya mwaka 2017/2018 tulieleza kwa kirefu mikakati tuliyoandaa kwa ajili ya uendelezaji viwanda ikiwepo ya sekta ya pamba hadi mavazi. Hotuba hii imejielekeza katika utekelezaji wa kipindi cha mwaka mmoja, mfano katika aya ya 50 inaeleza uanzishaji Kiwanda cha Vifaatiba vinavyotumia Pamba Simiyu, aya ya 52 inaeleza juu ya ufufuaji wa Morogoro Canvas Mill na vinu kumi vya kuchambua pamba. Aidha, aya ya 51, tumeeleza jinsi tunavyoshughulikia changamoto zinazokabili sekta ya pamba hadi mavazi, jambo ambalo limebainishwa kwenye Mkakati ya C2C. Mambo hayo yaliyotekelezwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa C2C.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulijitokeza suala la ulipaji wa fidia kuhusiana na maeneo tunayotegemea ya uwekezaji, EPZA. Na mimi nikiwa natoka Mkoa wa Ruvuma, niseme tu kwamba ukienda katika kitabu cha randama kama unacho kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro, utakuta pale tayari kuna fedha zilizotengwa kwa ajili ya kulipa fidia. Kwa upande wa Ruvuma, Songea, nafahamu Mheshimiwa Waziri Mkuu tarehe 23 Desemba alikuwa pale na wananchi walilalamika sana juu ya suala hilo. Jumla ya shilingi 2,624,990,000 zimetengwa kwa ajili ya shughuli hiyo. Pia kuna maeneo ya mikoa mingine ambayo wanaweza wakapata taarifa hizo kupitia ukurasa huu wa 210.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kuhusu Serikali kuiwezesha Tanrade, kuhakikisha kwamba bidhaa za Tanzania zinaingia katika masoko ya Kimataifa na kwamba Serikali iwezeshe TanTrade kuwekeza katika miundombinu ya masoko, maghala na viwanja vya maonesho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2017/2018, Serikali ilitenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya uendelezaji wa miundombinu ya Uwanja wa Maonesho ya Mwalimu Nyerere na kwa mwaka 2018/2019 TanTrade imetenga shilingi 2,376,400,000 katika bajeti ya maendeleo ikiwa ni ongezeko la shilingi 1,876,400,000. Ongezeko hili linatarajia kuongeza ufanisi katika utafutaji wa maeneo ya uwekezaji kwa ajili ya kujenga ofisi za kanda, viwanja vya maonesho, miundombinu ya masoko katika kanda mbalimbali nchini, kuongeza huduma karibu na wananchi na kuongeza tija katika biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulijitokeza pia suala la Sheria ya FCC na hali halisi ya mazingira ya biashara. Sheria ya FCC inaonekana inakinzana na mazingira halisi ya kufanya biashara. Tulishauriwa kuhusu Serikali kuwa na teknolojia bora ya kutofautisha kati ya bidhaa bandia na bidhaa halisi na Sheria ya FCC ifanyiwe marekebisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia FCC imekuwa ikifanya utambuzi wa baadhi ya bidhaa bandia kwa kutumia teknolojia miongoni mwa bidhaa ambazo utambuzi wake unatumia teknolojia.Ni bidhaa za kielektroniki na wino wa kurudia (catridge).Serikali inaendelea kushirikiana na wazalishaji wa bidhaa mbalimbali ili kupata teknolojia za utambuzi katika bidhaa wanazozalisha. Utambuzi wa bidhaa bandia hufanyika kwa kuzingatia Sheria ya Alama za Bidhaa ya mwaka 1963 kama ambavyo ilirekebishwa mwaka 2007 na 2012 na Kanuni zake za mwaka 2008.
Vilevile kwa kutumia TEHAMA pamoja na kushirikiana na taasisi za utafiti wa elimu ya juu kuimarisha usimamizi vitumike kuhawilisha (commercialization) matokeo ya tafiti kutoka vituo hivyo ili matokeo ya tafiti hizo yaweze kutumika kutengeneza mifumo, huduma na bidhaa hiyo kusaidia kukuza uchumi. Hiyo ipo katika hotuba ya mwaka 2018/2019 ukurasa wa 161 aya ya 327.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuuza ufuta kwa kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani, maandalizi yameshafanyika ambapo kikao cha wataalam kimefanyika Mkoani Dar es Salaam tarehe 30 Aprili, 2018. Maandalizi ya kikao cha wadau yamekamilika ambapo kinatarajiwa kufanyika Mkoani Dodoma pia tarehe 15 hadi 16 Mei, ili kupata maoni ya mwisho kabla ya utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la kulinda viwanda vya ndani, eneo hilo limechangiwa na Waheshimiwa Wabunge wengi na naomba radhi, sitaweza kuwataja wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Serikali inafanya juhudi kubwa katika kulinda viwanda vya ndani. Juhudi hizo ni pamoja na kuhakikisha kunakuwepo mazingira bora ya uzalishaji viwandani ikiwa ni pamoja na kupunguza gharama za uzalishaji, yaani andiko la blueprint limebainisha masuala yote ya kushughulikia, kuimarisha udhibiti wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kuhakikisha kodi stahiki inalipwa na hivyo kutoa suluhisho la under-invoicing, under-declaration, tax evasion na pia masuala ya njia ya panya, kuongeza kodi kwa bidhaa kutoka nje ambazo viwanda vyetu vina uwezo wa kuzizalisha hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na haya ambayo nimeyaeleza, niseme tu kwamba kuna mambo mengine ambayo yalijitokeza. Mfano, suala la lumbesa. Katika suala hili kumekuwa na manung’uniko mengi kutoka kwa baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kukamatwa magunia yakiwa yamebeba viazi na bidhaa za aina hiyo. Tunachosema ni kwamba gunia linaweza likawa limewekwa lumbesa, liwe gunia dogo au kubwa, lakini tunachosisitiza ni umuhimu wa kuwa na mizani itakayopima kwa kilo. Ukishapima kwa kilo, ina maana kilo 50 itajulikana ni kilo 50. Kama utakuwa hauna mzani, kwa vyovyote vile itakuwa ni vigumu mtu kutambua kwamba hizi ni kilo 50 na hivyo kupelekea kuwaibia wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitoe rai kwa Watanzania wote kuhakikisha kwamba wanapofanya shughuli zao zote za kibiashara za kuuza bidhaa zao, wahakikishe bidhaa zile ambazo zinahusika katika upimaji wa kilo, basi watumie kilo na siyo kutumia magunia pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa upande wa Wizara tunaangalia namna ya kufanya marekebisho ya sheria, hasa kuhusiana na suala la ujazo wa magunia yenyewe. Kama unavyofahamu, ni kwamba gunia la kilo 100 hata kulibeba bado linaweza lisilete afya kwa mbebaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa misingi hiyo, kwa kuzingatia kwamba tunaenda na viwango, tunasema kwamba tuwe na ujazo tofauti tofauti utakaowezesha hata wale ambao wanahusika katika shughuli za ubebaji mizigo, wafanye hivyo katika vipimo ambavyo ni sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kulijitokeza pia suala la Mheshimiwa Mariam Kisangi kuomba juu ya watoto au akina mama kuweza kufanyia shughuli zao za kibiashara katika uwanja wa pale Sabasaba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi suala hilo baada ya kujadiliana, Mheshimiwa Waziri wangu kwa ridhaa yake, lakini pia taasisi ya TanTrade, tumeona ni jambo jema sana kwa sababu litawezesha akina mama hao katika hizo siku watakazoweza kwenda kufanya shughuli zao pale kwanza kupata mapumziko, lakini pia kuwa jirani na familia zao na kufanya biashara ndogo ndogo zitakazowawezesha wao kupata kipato zaidi. Kwa hiyo, utaratibu rasmi utawekwa ili kuwezesha namna bora zaidi ya kushughulikia jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu ujenzi wa uchumi wa viwanda kwamba liendane na kutengeneza ujuzi. Ni kweli kabisa kwamba hilo ni suala muhimu sana. Serikali imekuwa ikifanya jitihada hizo katika kuhakikisha kwamba kupitia Wizara nyingine, kama ambavyo inaeleweka kwamba ujenzi wa uchumi wa viwanda siyo wa Wizara moja, ni wa Wizara mbalimbali; kupitia Wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Elimu lakini pia TAMISEMI, kuhakikisha kwamba mafunzo ya aina mbalimbali yanatolewa, lakini hata Vyuo vyetu Vikuu vimekuwa pia vikitoa mafunzo ya ujasiriamali.
Vilevile kwa upande wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji tunacho Chuo cha Biashara (CBE) ambacho kinatoa mafunzo ya ujasiriamali, lakini pia mafunzo ya vipimo, hayo yote yanawezesha wananchi kufanya shughuli zao kiukamilifu lakini pia kufanya shughuli zao kwa tija. Kwa hiyo, mchango huo ni mzuri na tutaendelea kuufanyia kazi ili kuhakikisha kwamba wananchi wengi zaidi wanaelimika na kuweza kufanya shughuli zao inavyostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la kwamba biashara nyingi kushindwa kufanya vizuri, ilizungumzwa kwamba kutolewe elimu siyo tu katika miji ni mpaka vijijini zitolewe elimu. Nakubaliana kabisa na suala hili, ni kwamba biashara ni sawa na binadamu, biashara zinaumwa kama binadamu, mtu anapokuwa hajui namna ya kufanya biashara inamfanya hata hiyo biashara ikianzishwa isiweze kuendelea. Kwa hiyo, Wizara yetu tumeona kwamba kuna kila sababu
ya kuanzisha vituo ambavyo vitasaidia katika kuwezesha kutoa tiba (business clinics) kwa ajili kusaidia viwanda hivyo vidogo vidogo, pia na biashara ndogo ndogo kusaidia katika kuleta uongozi wa masuala ya kiuwekezaji. Tupo katika mkakati huo na tutapokuwa tumekamilisha taratibu zetu basi tunaamini kwamba masuala hayo yatakuwa yamekaa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno hayo, kuna ambao walizungumzia ili tuweze kuwa na biashara vizuri au uwekezaji vizuri suala la amani ni suala muhimu sana, naunga mkono hoja hii ambayo ililetwa na Mheshimiwa Lwakatare, amani itaanzia humu Bungeni, mwenzako akiongea lazima umsikilize, uwe na uhimilivu, lakini kama hatutakuwa na amani ya kusikilizana hata kama kuna jambo la msingi mtu unakuwa kama tunafanya mchezo wakati watu tunakuwa tumefikiria tunafanya mambo ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, kwa kuwa wote tuna dhamira moja ya kumuunga mkono Rais wetu kuhakikisha kwamba uchumi wa ujenzi huu wa viwanda unakua, basi tumuunge mkono kwa dhati na tuhakikishe kwamba tupitie vizuri vitabu hivi vilivyoandikwa na Wizara yetu ukurasa kwa ukurasa mtapata mambo mengi sana ambayo kwa hakika yatajenga na kuhakikisha kwamba tunajenga vizuri uchumi wetu, tusaidiane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa uhai na mpaka siku ya leo tupo hapa. Kwa namna ya pekee napenda pia nitoe shukrani za dhati kwa Mheshimiwa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Viongozi wote Wakuu wanaomsaidia kwa kuwa na imani nasi na hivyo kuendelea kutuamini katika kuongoza Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao wameweza kuchangia katika hii bajeti yetu kwa azma ya kuifanya Wizara yetu iweze kutekeleza majukumu yake vizuri na pia kuzisaidia sekta ambazo zinapewa huduma na Wizara yetu ya Viwanda na Biashara; na hivyo chini ya uongozi madhubuti wa Waziri wetu Mheshimiwa Joseph Kakunda tunawaahidi kwamba michango yote ambayo imetolewa, yenye tija na nia ya kuisaidia nchi yetu, tunaichukulia kwa umakini mkubwa kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi michango imetolewa katika sura mbalimbali; na unapopewa ushauri lazima utafakari, ushauri huu unapewa na nani? Napewa kwa sababu gani na una malengo yapi? Una manufaa gani? Kwa hiyo, tumeweza kuchambua ushauri karibu wote ambao umetolewa na tumeona asilimia kubwa ya ushauri huu ni mzuri na unalenga kujenga na kuimarisha nchi yetu. Kwa hiyo, tuko pamoja na tutafanyia kazi kadiri inavyowezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi Wizara ya viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara nyingine imejizatiti katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na viwanda na biashara endelevu zinazoakisi rasilimali nyingi ambazo zipo Tanzania; na Tanzania kwa kweli wote tunafahamu imejaliwa rasilimali nyingi sana. Ni dhahiri kuwa sekta binafsi iliyo imara ndiyo itakayowezesha kuchakata na kuongeza dhamani ya rasilimali hizi, halikadhalika kuzitumia bidhaa hizo na ziada yake kwenda kuziuza ndani na nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo, tunategemea kwamba kwa kuwa na sekta binafsi ambayo inaweza kuhimili ushindani, ndipo tutakapoweza kupata manufaa makubwa ya rasilimali zetu. Niseme tu kwamba ni ukweli usiopingika, pamoja na jitihada kubwa ambayo Serikali imefanya katika kuimarisha shughuli za sekta binafsi nchini ambayo ndiyo chimbuko na chanzo cha mapato ya nchi, kwa sababu hata tukisema kwamba mfanyakazi analipa kodi, lakini chimbuko la fedha ni pale inapokuwa imetengenezwa kupitia viwanda au hao hao wafanyabiashara ndio hao sasa kodi zao zinawalipa watumishi fedha na hizo fedha nazo zinarudi tena kuchangia katika mfumo wa kikodi. Kwa hiyo, sekta hii ni muhimu sana. Kimsingi ndiyo moyo wa nchi katika kulifanya Taifa letu liweze kuwa imara na liweze kuchakata hizi mali nyingi tulizojaliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, tunakubali kabisa zipo changamoto ambazo bado zinawakabili wanaviwanda wetu na wajasiriamali au wafanyabiashara kwa ujumla. Kwa kutambua hilo, ndiyo maana Serikali baada ya kukaa na wadau mbalimbali, iliona iko haja ya kusema kwamba sasa tufikie mwisho tutambue, tuainishe changamoto hizi na tuzifanyie kazi. Kwa sababu hizo changamoto zimekuwa karibu katika kila sekta, kwa sababu wafanyabiashara au wachakataji wako katika kila sekta, ilibidi lazima tuangalie kila Wizara, kila mdau ni namna gani anapata tatizo au changamoto kupitia mazingira na mfumo uliopo sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo, tulikaa tukatengeneza hii Blue Print, yawezekana wengine kati yetu bado hawajaiona, lakini wengine wameshaona. Kwa hiyo, niseme tu kwamba Wizara itajitahidi kusambaza kwa wadau wengi zaidi ili tuweze kuona nini lilichopo kwenye Blue Print. Hilo andiko ni hili hapa, lina kurasa nyingi ambalo linataja kila sekta. Kimsingi mambo mengi yaliyokuwa yanachangiwa humu ndani kama changamoto, tayari yalishaainishwa humu, lakini kutokana na teknolojia na namna ambavyo tunaendelea kupata ushindani na hali ya kimfumo wa kibiashara, tunaamini kwamba bado Blue Print haitakuwa ni mwarobaini, bali itakuwa ni kazi endelevu ya kuendelea kuiboresha kwa kadri ambavyo changamoto zinavyojitokeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hiyo iko katika maeneo ya ngozi, tumesikia hapo, pia iko katika maeneo ya taasisi za udhibiti kama OSHA, Workers Compensation Fund na taasisi nyingine kama TFDA, wote kila mmoja amechambuliwa humu. Hali tuliyofikia sasa ni kuhakikisha kwamba tunatengeneza mpango mkakati wa utekelezaji, nini kifanyike wakati gani na watu gani washiriki?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunayo furaha kuliarifu Bunge letu Tukufu kwamba tayari kuna wadau wameshajitokeza wenye nia ya kusaidia utekelezaji wa mpango huu wa Blue Print. Kwa hiyo, naamini kwa dhamira na nia njema ya Serikali, huo upungufu au changamoto zilizojitokeza zitafanyiwa kazi na tunaahidi kufikia mwezi wa Saba tayari huo mpango mkakati wa utekelezaji utakuwa tayari na hivyo Blue Print kuanza kufanyiwa kazi na zile sheria ambazo zinazoonekana kuwa ni za kikwazo, zitaletwa humu Bungeni ili ziweze kufanyiwa kazi. Tunaamini kwamba, baada ya kuanza kufanyia kazi hii Blue Print hatutegemei tena kwamba sisi wenyewe tutaendelea kutunga zile sheria au kanuni kinzani zitakazokwenda tena kinyume na hii Blue Print. Kwa misingi hiyo, labda kutakuwa na kamati maalum ambayo itaweza kuangalia ni nini kinaletwa Bungeni ili kisitengeneze tena tatizo juu ya tatizo kwa nia njema na dhamira ambayo tayari nchi imeshaiweka.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kuhusu hoja pia iliyotolewa na Waheshimiwa Kambi ya Upinzani kuhusu korosho. Niseme tu kwamba kwanza hoja hiyo sisi tumeipokea na tumeiona ni nzuri kwa sababu inatusaidia kufafanua zaidi kwa wananchi nini kilichotokea katika suala la korosho. Korosho kama wote tunavyofahamu, ni zao muhimu na linawasaidia wananchi wengi hususan katika Mkoa wa Mtwara, Lindi, Ruvuma, Tanga na mikoa mingine ambayo sasa hivi inajizatiti katika kilimo cha korosho.
Mheshimiwa Naibu Spika, bei ambayo ilikuwa inatolewa na wanunuzi wa korosho kwa kipindi cha nyuma ilikuwa ni mbaya sana. Kwa mtu yeyote mwenye nia njema na nchi yake, mwenye nia njema na wakulima, kwa vyovyote vile hawezi kukubali kuona hali kama hiyo iendelee.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo, tunao wajibu na heshima kumpa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ambaye hakuiangalia tu faida ya kupata hiyo hela ndogo wanayoileta wafanyabiashara kwa gharama ya kuwatesa wakulima kwa ile bei ndogo, ndipo aliposema kama nchi ibebe huo mzigo. Tukaona kwamba korosho zinunuliwe kwa shilingi 3,300/=.
Mheshimiwa Naibu Spika, hayo ni maamuzi makubwa sana ambayo katika nchi yetu nasema kwamba kwa upande wa wakulima pengine haijawahi kutokea. Kwa hiyo, kwa maamuzi hayo, yamefanya kwamba ule mzigo ambao wangeubeba wakulima urudi sasa kwa Serikali ambayo ina vyanzo vingi vya mapato ukilinganisha na huyu mkulima. Kwa hiyo, sisi tunaendelea na niwapongeza sana Wizara ya Kilimo ambao tayari wameshalipa sehemu kubwa ya fedha na hiyo nyingine tunaamini itaendelea kulipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kampuni ya INDO Power ambayo ilikuwa inunue korosho, jamani kampuni ile nashangaa tunaizungumza sana. Yule ni mdau ambaye alitaka kununua korosho sawa na wadau wengine wowote. Mnapokuwa na makubaliano kwamba nataka labda nichukuwe mali yako hii, tuchukulie kama ingekuwa ni nguo dukani kwako, tunapeana muda; kufikiana muda fulani utakuwa umetekeleza, umelipa. Kama hajalipa, sisi tunamchukulia ni sawa na mfanyabiashara mwingine yeyote ambaye alikuwa hana uwezo, hatuwezi kuendelea kuitunza korosho eti tunamwekea mtu ambaye hana uwezo wa kulipa kwa wakati huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ingekuwa imepata hasara kama tungekuwa tumechukua hizo korosho tukampa yeye, halafu tukamwambia baada ya muda utatulipa. Tulikuwa hatujampa, tulichukuwa precautions zote na hayo ndiyo mambo makubwa aliyofanya Mheshimwia Prof. Kabudi, kuhakikisha kwamba mambo yote ya msingi kwa kushirikiana na Wizara yetu na wadau wote muhimu tunayalinda. Kwa hiyo, hata kama akiwa amepata fedha sasa, anataka kuja kununua, kama hatujamaliza kuuza, sisi tutampa tu, lakini kama hajafika, tunaendelea na wanunuzi wengine. Kwa hiyo, Serikali au nchi haijapata hasara. Sisi tumefanya biashara zetu kwa umakini tukizingatia kwamba hakuna hata senti tano au mali ya Tanzania inayoweza kuliwa na mtu mjanja mjanja, hilo hatukubali.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nichukue nafasi hii kuwashawishi lakini pia kuwaonya, sisi wenyewe Watanzania tunapokuwa na jambo zito kama hili, siyo suala la kufanya la mzaha mzaha, tunapochukua maamuzi mazito, siyo masuala ya kimzaha mzaha, ni masuala ambayo yanagusa mustakabali wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wengine unaweza kukuta wanazunguka zunguka tena wanamfuata mnunuzi, anamwambia unajua hapa bwana, ungefanya hivi, ufanye hivi. Wewe ni Mtanzania? Kwa nini ufanye hivyo? Kwa faida ya nani? Nilitegemea wote tutashirikiana, tutaungana na tena hasa kwa Wabunge wanatoka Mkoa wa Mtwara na Lindi na Ruvuma kwa sababu waadhirika wakubwa walikuwa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba Serikali inaendelea na mikakati, korosho ambayo ilitakiwa kubanguliwa kwa muda mrefu ilikuwa viwanda vingine vimefungwa, havibagui korosho, sasa hivi tunabangua, tumefungasha tunazo katoni zaidi ya 17,427 tayari kwa kuuza na zimekuwa-tested, zipo katika hali nzuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hiyo korosho ambayo bado haijabanguliwa, tumei-test katika maabara yetu ya Tanzania, lakini na maabara nyingine za nje zimedhibitishwa kuwa na ubora wa kiwango cha juu. Kwa hiyo, bado tuko katika hali nzuri. Anayetaka kuja kununua kwa tija, karibu; anayetaka kuja kununua kwa kutuibia au kutufanya sisi manamba, kwaheri. Tanzania siyo jalala, Tanzania ni nchi inayojitambua. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine ambalo limejitokeza kuhusiana na bajeti ya Wizara yetu kuwa ni ndogo. Kwanza niseme kwamba tunapokea kwa kiasi fulani concern za Waheshimiwa Wabunge. Kama ambavyo inaeleweka kwamba kupanga ni kuchagua, nasi Wizara yetu kimsingi ni Wizara ambayo ni coordinator, yaani inashawishi Wizara nyingine ziweze kuweka miundombinu rafiki kwa ajili ya hawa wazalishaji wetu na wafanyabiashara kwa ujumla. Ndiyo maana bajeti nyingine unaona haziji moja kwa moja kwenye Wizara yetu, zinajitokeza katika Wizara nyingine. Mfano mzuri ni kama ambavyo ilielezwa hapo awali na Mheshimiwa Mollel kuhusiana na ujenzi wa umeme, Stiegler’s Gorge kuhusiana na mradi mkakati wa SGR. Nyie mnakumbuka, reli hii ya kati ni ya toka mwaka 1905, mpaka leo ilikuwa haijakarabatiwa kadri ya kiwango kinachohitajika kuweza kubeba mzigo unaostahili.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, tunazo meli kama Liemba ya mwaka huo huo 1905, lakini mpaka leo haijaweza kupata huo ufadhili. Huyo mjomba tunayemsubiri kila siku atufanyie kazi, yuko wapi? Hayupo. Lazima tujifunge mikanda. Katika kujifunga mikanda, kuna maeneo yatakuwa yanaathirika kwa muda, kwa sababu nguvu zote zinakuwa zimeelekezwa huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, Serikali kimsingi inasikiliza ushauri wa Waheshimiwa Wabunge. Naamini michango iliyotolewa haiwezi ikaishia hewani tu, lazima Serikali itafanya kitu katika kuangalia maeneo yale yenye umuhimu na ambayo yanakusudiwa kwa ajili ya kuleta tija kwa haraka ikiwemo na maeneo ya miradi mikubwa ya kimkakati yatazidi kuangaliwa na kutengewa fedha inayotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi niseme tu kwamba dhamira iliyopo ya Serikali ni kubwa sana katika kuhakikisha kwamba tunajitoa katika wimbi hili la kuitwa sisi ni masikini Tanzania wakati tuna rasilimali nyingi nyingi, nyingi. Hapana, muda umefika wa sisi kufanya maamuzi ya liyo sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu baadhi ya viwanda ambavyo havifanyi vizuri kutokana na bidhaa mbalimbali ambazo zinaingizwa kutoka nchi za nje. Kweli suala hilo tunalitafakari, lakini unakuta katika baadhi ya viwanda vyenyewe vinatumia rasilimali (raw materials) kutoka nje. Pia tunataka tujiridhishe hivi viwanda vyetu ambavyo tunasema havina uwezo wa kushindana katika hali iliyopo, kule wanapochukuwa malighafi, wanapata kwa bei halali au pengine kuna mazingira ya urafiki yanayofanya pengine huko wanapochukulia mali ghafi yaongezwe bei kiasi kwamba inapofika hapa hizo mali ghafi zisiweze kuzalisasha kwa tija? Kwa hiyo, tutaangalia pande zote mbili, kwa sababu sisi tusingependa kuishi kama nchi ambayo inajiangalia tu yenyewe bila kuwa na washindani wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba viwanda vya ndani vinalindwa. Kwa misingi hiyo niseme tu kwamba Wizara tumejizatiti, tumejipanga, kuhakikisha kwamba viwanda vyetu vya ndani vinapewa msaada unaohitajika ikiwemo kupunguziwa kodi katika bidhaa maalum au pengine kupewa msamaha au ruzuku katika baadhi ya malighafi na vile vile kuweza kuweka tozo zaidi kwa bidhaa ambazo zinatoka nje ya nchi wakati kuna utoshelezi ndani ya nchi. Tumefanya hiyo katika maeneo mengine. Kwa mfano, cement sasa hivi hatuagizi kutoka nje, tunajitosheleza. Hizo nondo, tumo katika mkakati huo na kwa kweli sasa hivi Tanzania inafanya vizuri sana katika viwanda vyake. Ni vile tu kwamba tulizoea kuviona baadhi ya viwanda vilivyokuwa vinajionesha vyenyewe ndiyo vyenye nguvu, tukavidharau vile vingine vidogo vidogo ambavyo vinaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wapo wawekezaji ambao wako tayari, akina Kilua Integrated Group wako hapo, ni Watanzania. Sio hao tu, tunao wengi ambao wanakuja. Vile vile tumefanikisha kuvutia viwanda vingi ambavyo sasa vimeanzishwa nchini, mfano kiwanda cha Cassava (starch), yaani wanga wa unga wa mihogo ambacho kiko kule Lindi. Juzi juzi hapa Mheshimiwa Rais amezindua tena Kiwanda cha Unga pale Mlale, Kiwanda cha Maparachichi pale Rungwe, Tukuyu na vile vile tumeona hata Unilever pale Njombe; na viwanda vingi vinaendelea kufunguliwa. Tatito labda hatujapata fursa ya kutembelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana Watanzania tupende bidhaa zetu za Tanzania, tupende kutumia bidhaa zetu na tujivunie, vile vile kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wote kwa ujumla. Sasa hivi kitambulisho cha ujasiliamali kimeshushwa ni shilingi 20,000/= tu, huhitaji hata sasa utengeneze mahesabu, sijui ufanye nini; kwa mtu mwenye mtaji wa chini ya shilingi milioni nne, huyu akishakuwa na kitambulisho chake cha shilingi 20,000/= tu cha ujasiliamali, habughudhiwi, anaendelea na shughuli zake popote pale. Hayo ndiyo mambo ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika kuwasaidia wanyonge.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba katika masuala haya ya undelezaji wa biashara, hayawezi kufanyika na mtu mmoja. Hata sisi wenyewe tuwe na positive thinking, tuwe na hali ya kusemea vizuri nchi yetu. Ukishaulizwa swali tu, eh mazingira ya biashara nchini kwako yakoje? Unaanza; unajua tuna taabu nyingi sana, unajua kuna OSHA, kuna nini. Sasa unajiuza hasi wewe mwenyewe, ukishajiuza hasi na yule anayeandika atasema mazingira yako ni magumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani changamoto iliyopo siyo tozo tu, ni kuweka mazingira ambayo yatawafanya wafanyabiashara watengeneze faida ili waweze kumudu kulipa hizo tozo, kwa sababu baadhi ya tozo ndiyo chanzo cha uchumi, chanzo cha kuwezesha kuendeleza miundombinu mbalimbali ikiwemo ya afya, maji na mengine. Hata juzi ilikuwa bahati nzuri Mheshimiwa Dkt. Mpango alipokataa, ilikuwa tuongeze tozo nyingine kwenye mafuta, tulishasahau kwamba tunawadunga tena hao hao wafanyabiashara. Kwa bahati nzuri suala hilo tuliliona kwa mapana, halikuweza kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme kwamba Wizara yetu imejipanga na tutaendelea kutumia ushauri wenu Waheshimiwa Wabunge na wadau wengine na kuhakikisha kwamba taasisi zetu zote zinafanya kazi kiujasiriamali, siyo bora uko kazini. Mimi nimefika kazini, nimewaudumia akina nani na kwa namna gani? Hilo ndilo tunalitaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee niwashukuru wadau ambao huwa wanaturudishia mrejesho wa kupongeza jitihada ambazo tunazifanya. Mfano tu kiwanda cha karatasi Mgololo, walikuwa na changamoto tulipowatembelea, lakini tukamwona Waziri wa Maliasili changamoto zikaondolewa, wakatushukuru. Halikadhalika kulikuwa na wadau waliokuwa na shida ya kupata ardhi, kama hao wa cassava kule Lindi, tayari wanafanya shughuli zao vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia wapo wengi wenye shida kama hizo, tunasema kwamba ofisi yetu Wizara ya Viwanda na Biashara iko wazi na sisi wenyewe tuko ndani, siyo kwamba tu ipo wazi halafu hatuko ndani, tuko tayari kuwasikiliza msihangaike peke yenu, hakuna mkubwa kwenye ofisi yetu, sisi wote ni sawa mfalme ni wewe mteja, mfalme ni wewe mwenye kiwanda, mfalme ni wewe mfanyabiashara ambaye mwisho wa yote unachakata uchumi wetu na kulifanya Taifa letu liwe na uchumi imara na tuweze kulipia mahitaji yetu ya kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno haya, nashukuru sana na niwaombe Waheshimiwa Wabunge kutuunga mkono katika hoja yetu hii na naunga mkono mimi mwenyewe hoja yetu ya Bajeti ya Viwanda na Biashara. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, niko hapa mwisho kabisa. Naomba upaone kabisa, nimesimama. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kukushukuru sana kwa kupata hii nafasi na kwa kweli, wavuvi wana matumaini sana na wewe, hasa baada ya kuona jinsi ambavyo umeweka msisitizo katika Wizara ya Kilimo na leo kwenye Wizara hii ambazo ulisema kabisa zote ziangaliwe kiundani kwa sababu, zinawaajiri wananchi wengi sana wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kuwapongeza Waziri wa Wizara hii pamoja na Naibu wake, lakini pia Makatibu Wakuu wote wa Mifugo na Uvuvi wanajitahidi kwa kadiri inavyowezekana pamoja na timu zao zote.
Mheshimiwa Spika, baada ya maneno hayo niseme pia, nawashukuru sana Wizara hii kwa kusikiliza kilio cha wananchi wa Jimbo langu la Nyasa ambao sisi tunatumia takribani ukanda wa kilometa 150 za Ziwa Nyasa. Kwa muda mrefu zaidi ya miaka 20 tumekuwa tukilia, tunalalamika kwa ajili ya kutuzuwia kuvua samaki wanaoitwa vitui, samaki wadogo ambao hawakui, lakini mwaka jana mwezi wa nane tulipata hiyo ruhusa na wananchi sasa hivi wanafurahi na wanasomesha watoto wao. Kwa hiyo, nafurahi kwamba, wamekuwa wasikivu katika eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwaombe kufanya tafiti kabla ya kutoa makatazo kwa sababu, watu wameteseka zaidi ya miaka 20 kwa sababu tu, kulikuwa hakuna taarifa za kutosha. Hata sasa hivi tulivyoruhusiwa hatujapata majibu kwamba, sasa yule kitui anakua au hakui? Kwa hiyo, tunaomba wakati mwingine tusiwe tunafanya makatazo kabla ya kuwa na taarifa za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kukuunga mkono na kuendelea kusisitiza juu ya umuhimu wa halmashauri ambazo zimeanza hivi karibuni na kipato chake ni cha chini, ziko pembezoni na kipato chake ni cha chini. Sawa na ile Wilaya yangu ya Nyasa, kuweza kuangalia upya namna ya kuziendesha halmashauri hizo. Kwa sababu, bila kufanya hivyo hizo halmashauri badala ya kuwa ni sehemu nzuri ya kuwahudumia wananchi inakuwa ni sehemu ya kuwa na kikwazo, kuwa na manyanyaso, kuwa na mateso kwa wananchi kwa sababu, ya kutafuta fedha za kujiendeshea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, halmashauri nyingine zilizopata uwezo mkubwa kimsingi tumezijenga wote kwa sababu, inapotokea tunakubaliana kwamba, safari hii tutajenga barabara ya mahali fulani au tutajenga fly-over mahali fulani au tutajenga miundombinu mahali fulani, ina maana wengine wote tunasubiri ili kuwezesha hizo halmashauri zipate mapato na hatimaye tufaidike wote. Sasa zinapoenda tu kuhudumia hizo halmashauri zenyewe ambazo zimeshapata uwezo na wengine wakaachwa wanateseka si sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema hayo? Katika uvuvi, Halmashauri kwa mfano ya Nyasa, inakusanya ada ya leseni 20,000/= eti ili uende ukaingie kuvua mle majini ulipe kwanza 20,000/= kwa maana hiyo, kila mvuvi anayeenda kuvua lazima afanye hivyo. Na vijana wetu wengine ambao wako kule na wengi ambao kwa kweli, hawajasoma sana kwa sababu, hata nikiuliza sasa hivi kwenye Wizara wavuvi wangapi wana cheti angalau cha uvuvi, sidhani kama nitapata jibu. Nikiuliza wavuvi wangapi wana degree hatutapata jibu kwa hiyo, ni wale tu ambao wamekuwa wajanja wa kuzaliwanao ndio wanaenda kuvua kule halafu unamwambia ili uingie majini leta kwanza 20,000/= wewe umemsaidia nini mpaka yeye kujua kwenda kuvua? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hakuna tulichomsaidia, wanahangaika tu wenyewe na vimitumbwi hivyo. Na kimtumbwi hata kikawa kidogo kiasi gani nacho kinachajiwa (Charge) leseni ya 20,000/= wakati ni hatari huko anakoenda, anaenda tu ilimradi ameenda. Ndio maana nasema kwamba, hata suala la elimu kwa wavuvi ni muhimu sana, lakini huko hatujaenda.
Mheshimiwa Spika, unakuta kwamba, kimazoea karibu wataalam wengi tunaokuwa tunawaandaa, vyeo vyetu vingi, ni kwa ajili ya kwenda kufanya udhibiti sio wao wenyewe kwenda kufanya ile kazi ambayo inaendelea kama kazi ya uvuvi. Ndio maana mwanafunzi akimaliza anasema sasa kazi iko wapi? Kwa sababu umemfundisha kazi za kudhibiti hukumfundisha kazi za yeye kwenda kufanya shughuli ile kwa mfano ya uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala hilo linaumiza sana na ndio maana hata mara ya mwisho niliulizia kuhusiana na engine za maboti, kwa nini watu wakopeshwe kwenye vikundi? Lazima walazimishwe kuwa kwenye vikundi? Kwa sababu, mtu akiwa peke yake anajisikia acha nifanye hii kazi kufa na kupona niweze kupata faida, lakini unamwambia kwamba, lazima uende kwenye kikundi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, halikadhalika tumeona hapa kwa upande wa kilimo, angalao tunasema kwamba, tani moja mtu apite bila kulipa ushuru, lakini mvuvi akishakuwa hapo na vidagaa vyake vichache, visamaki vichache, basi utakuta kila kona inamdai alipe, kila kona alipe. Huyo mvuvi lini atabadilika akawa ni mvuvi mwenye uwezo? Ndio maana mara nyingi katika maeneo ya fukwe wavuvi wengi bado ni masikini, hawajawa na kipato cha kutosha kwa sababu wanabanwa kiasi kwamba, hawawezeshwi vizuri, lakini nina imani kubwa sana na Wizara hii, nina imani kwa sababu, nyie ni wasikivu. Hata siku ile nimeuliza tu swali naona Naibu mara kwa mara unakuja tuna-share, tunashauriana, basi naamini kwamba, tutaweza kwenda vizuri kwa hiyo, niwaombe sana Wizara.
Mheshimiwa Spika, sitachangia katika mambo ambayo ambayo ni ya macro, macro level hayo ya kisera, sheria, nini, hayo nendeninayo ninyi. Wananchi wangu wamenituma nije nilalamikie hayo madogomadogo wanayoishinayo kila siku. Nachangia kwenye micro level ili ukitatua hilo tatizo lao dogo wao wanaendelea kuishi wakati mikakati mikubwa ya kitaifa inaendelea. Kwa hiyo, sitachangia kuhusu meli ya uvuvi kwa sababu meli ya uvuvi tutapata nne zitakuwa Bahari ya Hindi, hilo ni jambo jema sana kwa sababu, tumelalamika kwa muda mrefu kwa nini watu tunafikia mpaka tunakamata watu kutoka nje wanakuja kutuvulia kwenye maji yetu, lakini sisi wenyewe tunashindwa kuvua, hapo mmepiga hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hilo kwa sababu, najua kwamba, tukipata mapato hayo mapato tena yataondoka asilimia chache kwenda kusaidia kule kwa wavuvi wangu wa Wilaya ya Nyasa. Kwa hiyo, niwaombe sana tufanye hivyo, lakini na hizo ranch ambazo tumeambiwa hapa, ndugu zangu hata nilikuwa kule Rukwa, ranch ilikuwepo pale eneo la Namanyere, Nkasi, ng’ombe wachache tu na hata yule mwekezaji tuliyemuweka pale eneo la Sumbawanga mjini bado na yeye ng’ombe 150 kwenye eneo la zaidi ya hekta elfu kumi kwa hiyo, lazima tuangalie vizuri namna gani tunawekeza, namna gani tunasaidia kuona kwamba, yale tunayowekeza yanakuwa yenye tija. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni pamoja na kuwasaidia hao wananchi tunaosema kwamba, wao sasa sekta binafsi ndio iwe engine katika kuwezesha masuala ya kilimo, masuala ya mifugo, masuala ya uvuvi. Nimegundua kitu kimoja, private sector huwa sisi ni rahisi kumhamasisha aingie katika kutenda, katika kuwa kwenye mfumo tunaouhitaji, lakini akishaingia humo akapata kikwazo sisi Serikali, sisi watunga sera, sio rahisi sana kumsaidia, yaani tunataka aanze aingie likishampata huko atajijua mwenyewe na saa nyingine tunamlaumu kwa nini anafanya hivyo? Ameshindwa yule bwana.
Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu kuna mfano Hai. Hivi kile kiwanda cha pale Sumbawanga cha Mzee Mzindakaya kwa nini kimeshindwa kufanya kazi mpaka leo? Tatizo ni nini? Kama alichukua mkopo na mkopo ulikuwa ni wa Serikali kwa nini sisi Serikali tusichukulie ule mkopo ni sawa na asset yetu tuliyoiwekeza pale tukazungumza na mzee yule ili kukiona kile kiwanda kirudi katika hali yake ya uzalishaji?
Mheshimiwa Spika, kiwanda ni kizuri sana na yule mzee aliwekeza, mimi ninavyoamini aliwekeza kwa hamu kwamba, ngoja nikawekeze Sumbawanga angalao nako na sisi tuwe na kiwanda. Yaani alikuwa na ile kiu ya mafanikio, alikuwa na ile sifa kwamba, Sumbawanga kuwe na kiwanda. Matokeo yake wakati ule anawekeza barabara kutoka Sumbawanga mpaka Tunduma ilikuwa ni ya vumbi, mashimo matupu. Alikuwa anasafirisha hizo nyama mpaka Dar-es-Salaam, hakukuwa na Kiwanja cha Songwe kinachofanya kazi, kiwanda cha ndege.
Mheshimiwa Spika, matokeo yake magari yale na mkopo wake ameutumia wakati akiwa na mazingira magumu ya uwekezaji, ame-fail. Kwa nini sasa hatumnyanyui? Tunaona kwamba, kama lile ni suala la Mzindakaya na sio suala la nchi, hela aliyotumia ilikuwa ni zile ambazo zilikuwa zinasaidia wajasiriamali wadogo wavuke kwenda kwenda kwenye ujasiriamali wa kati. Kwa hiyo, nasema kwamba, pale tutakapomuona huyu private sector ni ndugu, huyu private sector anawekeza kwa manufaa ya nchi, anawekeza kama kichochezi cha uchumi wa nchi, hapo ndipo tutakapoenda vizuri, lakini tukimchukulia yeye ni mtu binafsi, amekwama kodi, huyu ana miaka mingapi sasa halipi, mwizi, matokeo yake inakuwa kwamba, wengi wanakimbia kwenda kwenye private sector.
Mheshimiwa Spika, sisi wenyewe sasa kama Serikali tunarudi, acha tuwekeze na sisi kuwekeza kwetu ni ngumu kwa sababu, kwanza ili tukubaliane kuwekeza au kufanya jambo fulani lazima tukae vikao. Na tukitoka kwenye vikao pengine iundwe kamati na kamati na yenyewe kutoa majibu saa nyingine inaogopa inasema nitaambiwa nimekula fedha. Matokeo yake yote tunatoa majibu ambayo yanakuwa yako kati kwa kati. Haya ikitoka hapo sasa fedha zinapatikana vipi, miaka mitatu hatujafanya. Niwaombe sana Ndugu zangu tuiunge mkono sekta binafsi ili tuweze kuendeleza eneo letu la mifugo na uvuvi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya nchini, pia kwa jambo kubwa ambalo juzi amezindua la kuhakikisha kwamba anaendelea na kazi ya kumtua Mama kuni kichwani, amekaribia kumaliza ndoo kichwani sasa anaendelea kuni kichwani ili akina Mama na akina Baba watumie Nishati safi kwa ajili ya kupikia.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee kabisa naomba nikupongeze sana wewe mwenyewe hasa kwa mjadala huu wa ripoti hizi za ukaguzi kwa kweli umeonyesha umadhubuti na nikiangalia michango inayotokea hapa mikali mikali sijaona ukisema wewe kaa chini, wote waseme kadri wanavyoweza, tunakupongeza sana na sisi tupo na wewe kwa sababu tunajua hili ndio jukumu lako kubwa la msingi kuhakikisha kwamba unalinda maslahi ya watanzania kupitia rasilimali zao.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusikiliza michango ya wenzangu mingi, kama kawaida yangu huwa napenda kukaa upande tofauti kidogo kama kioo. Sasa nikianzia na suala hili la TANROADS kufikia malipo ya Bilioni 68. Kwa ajili ya riba kwa makandarasi, nikasema sawa ni TANROADS wamefanya hivyo lakini kitovu cha suala hilo kiko wapi? Kitu gani kinasababisha wanashindwa kuwalipa hawa makandarasi kwa wakati? Kwa sababu ni lazima tukubali pia upande wa ufanyaji kazi, mtu yeyote yule anayefanya kazi yako na wewe akishakugundua kwamba huna tabia ya kulipa kwa wakati anajilinda, kujilinda anaweka kipengele kwamba ukichelewa kunilipa itabidi na mimi nipate riba kidogo.
Mheshimiwa Spika, ninachouliza, kwa sababu kama ni barabara ili zitangazwe ina maana tunakuwa tumeshatenga bajeti kwa ajili ya kazi hiyo, kitu gani kinasababisha hatulipi kwa wakati? Ni TANROADS wanakuwa na fedha hawataki kulipa? Au hizo fedha wanazipata kutoka maeneo mengine kiasi kwamba yale maeneo hayawapatii fedha kwa wakati? Kwa hiyo, nataka hili tunapotibu tutibu mstari wote mpaka mwisho tupate jambo ambalo ni la uhakika badala ya kuanzia na sehemu tu iliyotokea tatizo tukaacha mzizi ulikoanzia. Kwa hiyo, nadhani hata watu wa Hazina wanalo la kuzungumza hapa kwa maana Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Spika, suala la pili napenda kuzungumzia hizi Halmashauri zetu. Kuna Halmashauri za matajiri na Halmashauri za makabwela, mimi binafsi natoka kwenye Halmashauri za makabwela ambayo kipato chao ni kidogo sana kutokana na makusanyo yao. Sasa kuna hili suala la kula fedha mbichi, siungani kabisa na Halmashauri katika suala la kula fedha mbichi, lakini yawezekana kichochezi cha kula fedha mbichi ni pamoja na mifumo yetu wenyewe tulivyojiwekea. Kwa sababu, kwa mfano tukimaliza kujadili Bajeti yetu mwezi Juni, tunapoingia mwezi Julai mpaka mifumo kuweza kufunguka na kuruhusu Halmashauri kuanza kutumia fedha inachukua muda mrefu wakati mwingine mpaka miezi miwili mifumo haijafunguka.
Mheshimiwa Spika, sasa kuna Sheria zinagongana ukipata msiba wa mtumishi inabidi umsafirishe, umzike, kwa kutumia taratibu zilizowekwa kwenye Sheria. Wakati huo hakuna fedha, Mkurugenzi unategemea atachukua fedha za mfukoni mwake? Ataenda kula hela mbichi kwa kutumia wale watu wake ili mradi aweze kwenda kuzika. Kwa hiyo, nadhani pia na taratibu hizo za kuchelewesha kufungua mifumo ziangaliwe au Halmashauri ziwekewe fedha kidogo za kutumia wakati mifumo hiyo inaendelea labda na taratibu za kiuhasibu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda pia kuzungumzia suala la Kamati katika ukurasa wa romani ya pili ya summary yao ambayo imeshauri kwamba Serikali iongeze mtaji kwa Mashirika kama TANESCO, TPDC na STAMICO, hilo ninawapongeza sana wameliona, hatuwezi kwenda tunalalamika tu lazima tena tushauri na mambo mengine ambayo yanafanya haya mashirika yetu tunayoyategemea yafanye vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia TANESCO na TPDC ni ndugu hawa, wako katika Kamati moja ya Nishati na Madini, lakini unakuta huyu TANESCO kwa sababu anawajibu wa kuhakikisha umeme unapatikana anamkopa ndugu yake TPDC. TPDC naye kwa kuogopa kwamba nitasema nini kwa sababu anategemea ruzuku kutoka Serikalini anaruhusu madeni ya kukopwa na TANESCO, kwa hiyo unakuta ni Shirika moja linamtafuna mwenzake lakini wote wanatekeleza majukumu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa mazingira kama hayo iko haja wakati mwingine tunapoona ukweli na hali halisi Serikali yenyewe ichukue hayo madeni, deni kama la TPDC ichukue yenyewe halafu ile fedha ambayo inalipwa kidogo kidogo na Shirika kama la TANESCO ilipwe Hazina baada ya Hazina kuwa imeshachukua deni lake na imeshamrejeshea TPDC fedha zake ili iweze kuendelea na shughuli zake zinazohitajika hasa za kiutafiti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi tunayo changamoto kubwa ya kuhama kutoka kwenye nishati ambayo inaitwa nishati isiyosafi kwenda kwenye nishati safi. Tunategemea utafiti mwingi ufanyike, tunategemea mambo makubwa ya haraka ya kuhakikisha kwamba tunasonga mbele kiteknolojia na kiujuzi kwa ujumla yanafanyika.
Mheshimiwa Spika, lakini sasa unakuta Mashirika kama TPDC, TANESCO na STAMICO wanakosa fedha za kutosha. Kwa mfano, ukiangalia kazi za STAMICO; na hapa niwapongeze kwa kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwao; wanatakiwa kufanya tafiti mbalimbali kwenye nchi. Maeneo mengine hata hayafikiki kiurahisi, hakuna barabara, kwenye misitu, tunajua kuna rasilimali kama za madini, lakini vifaa wanavyotumia ni duni sana; magari sehemu nyingine hayafiki. Walitakiwa watumie hata ndege au helikopta ziwafikishe huko wafanye kazi za utafiti, lakini unakuta hakuna, kwa hiyo tunazungumzia kugawana gawana kilichopo. Tujipange sasa ili tuweze kupata fedha za kutosha ili taifa liweze kupanga matumizi yake bila kutegemea sana mikopo.
Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo mimi naungana na Kamati iliyopendekezwa kwamba haya mashirika matatu ya kimkakati waongezewe fedha ili waweze kutimiza wajibu wao ipasavyo.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na suala lingine ambalo limezungumziwa, mradi wetu mkubwa sana wa maji wa Mwalimu Nyerere. Mimi nimeamua kuwa balozi wa kujitegemea kwa mradi ule. Nasema hivyo kwa sababu mradi ule Watanzania wote wanauangalia. Mradi ule wote tunajua kwamba tukifanikiwa Tanzania itakuwa imepiga hatua, itakuwa pia imeshiriki kikamilifu katika kupunguza nishati zinazochangia hewa ukaa na kuwa kwenye nishati safi.
Mheshimiwa Spika, Mradi ule mashine yake moja itakayowashwa ambayo itakuwa inatowa mega watt 235, haifanani hata na mashine nyingine zote zinazozalisha maji katika nchi hii. Mradi ule kweli umechelewa lakini unakwenda vizuri; na hivyo nataka Watanzania waelewe hivyo, mama Samia amejitahidi. Hata leo Marehemu Mzee Magufuli angefufuka angemkumbatia dada yake mama Samia, kwamba kazi umeiweza, kazi inaendelea, mradi unaenda vizuri. Sasa, katika kuchelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kweli kuna mmoja wapo lazima akubali lazima kasababisha, sababu ni nini? Na hiyo hatuwezi tukafumba macho, kumbana aliyehusika katiaka kuchelewesha. Hata hivyo tunasema ni bora kuchelewa lakini tupate kazi iliyo sahihi, kwa sababu ule mradi ni very sensitive. Sasa, nilikuwa nasikia hapa kwa nini watoe riba kwa ajili ya kulipa fedha hizo za dola; lakini jamani si ni jambo la kawaida? Hivi leo wewe ukienda kununua dola yako exchange rate kama ni shilingi 2,000 kesho ukaikuta 2,500 utaipata dola kwa shilingi 2,000? Ni jambo lipo. Kwa hiyo mimi najaribu kusema tu kwamba sisemi ufanyike ubadhilifu, isipokuwa sitaki sisi Wabunge tuishi kama mambumbumbu wa kusema dola ukiinunua jana lazima leo itakuwa bei ile ile, tutakuwa hatujitendei haki, lazima tuwe wakweli kwatika haya tunayoshauri.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi nasema kwamba katika hilo hakuna ambaye atakuwa mzembe, aseme kwamba hela yake basi yeye alipwe kwa hasara, hilo jambo halipo jamani, tuambizane ukweli.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kwa misingi hiyo tunapozungumzia kuchukua hatua, kwa maeneo yale ambayo tunasema kwamba yamekuwa na ubadhilifu, basi tuhakikishe uchunguzi wa kina unafanyika na wale wanaostahili wachukuliwe hatua; na si tu kusema halafu tukamgusa ambaye hausiki. Nasema hivyo kwa sababu nimesikiliza michango hii tangu mwanzo, wengi wao wanaongea kwa ujumla jumla, angalau mmoja aligusa akashauri kwamba labda pengine Katibu Mkuu wa Wizara fulani, lakini wengi wanasema tuchukue hatua kwa ujumla jumla. Kwa ujumla jumla tunamchukulia hatua nani?
Mheshimiwa Spika, Kamati mnaficha nini kutuambia ni fulani na fulani? Kwa nini tunaenda kijumla jumla? Tunamwaogopa nani? Kama hatuwezi kusimama tukasema ni fulani na fulani wamehususika basi tusiseme haya ya kujaribu tu kuzungumza kwamba Wabunge tumesema, hapana. Hapa tungekuwa sasa hivi tunazungumza kauli moja, kwamba katika hawa wote safari hii hapana, lazima tuchukue hatua. Lakini sasa kwa sababu tunaongea kwa ujumla tutajikuta kwamba tumeongea tunatoka, hakuna kinachoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi naungana na wanaosema ikiwezekana uunde Kamati Teule ifuatilie kwa kina katika yale maeneo ambayo yamezidi ubadhilifu, ikiwemo hiyo KADCO na maeneo mengine ili tuchukue hatua ya ukweli bila kusingizia na bila uoga, haki haina uwoga. Ahsante sana.
SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Mhandisi Stella Manyanya hebu tusaidie, hapo kwenye jumla jumla ndio sijaelewa hapo. Kwenye, kwamba Wabunge walikuwa wanachangia jumla jumla, hebu fafanua kidogo.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ingekuwa ni mimi ninaposema tuchukue hatua; kwa mfano kwa Shirika kama TANESCO, nitasema kabisa. Katika eneo hili ubadhilifu umefanyika either na Mkurugenzi au na Mhandisi fulani au timu fulani ambayo yenyewe inajulikana kabisa ilihusika na hiyo kazi yaani nisingefichaficha. Ili tunapoenda kushughulikia sasa wa kuwaadhibu tunawapa. Sasa CAG taarifa yake haijamtaja mtu, unakuta huku hivyo hivyo na sisi tunachangia vilevile, lakini ubadhilifu unaonekana. Sasa, mimi naona kidogo hiyo inaleta uzito namna ya kushughulikia hilo jambo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza, niipongeze sana Kamati kwa ushauri mkubwa ambao imetupatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la VETA, napenda kusema kwamba tunakubaliana kwamba lazima tuangalie course zake zinazoendelea kutolewa ili kuendana na hali halisi ya uhitaji wa soko na ujuzi tunaohitaji katika uchumi wa viwanda na biashara. Mfano tu kwa siku za nyuma katika baadhi ya maeneo watu binafsi walikuwa wanaruhusiwa kufanya kazi za umeme wa majumbani tu lakini sasa hivi wanaruhusiwa kufanya kazi hata za kuweka vituo vya umeme, jenereta na hata ujenzi wa laini. Kwa hiyo, na sisi tutarekebisha mitaala yetu kadri tunavyoenda ili kuweza kufikia hali inayoendana na soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusiana na UDOM. Serikali haikuwaondoa wanafunzi wa UDOM ili tuweze kuhamia pale. Nachotaka kusema tu ni kwamba Serikali itaendelea wakati wote kuboresha mambo yote ambayo inaona kwamba yana tija kwa nchi. Kimsingi Chuo cha UDOM tuliweka nia njema ya kupeleka wale wanafunzi pale ili tupate hawa wanafunzi kwa ajili ya masomo ya sayansi na hisabati lakini likajitokeza tatizo kubwa la walimu jambo ambalo liliashiria hata kuleta migomo ya walimu yaani wahadhiri. Nafahamu kwamba hata Mheshimiwa aliyetoa hoja aliwahi kunielezea kuna tatizo gani kuhusiana na hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipotafakari tukaona kwamba wanafunzi hawa wanaweza wakapelekwa kwenye vyuo ambavyo tayari kuna walimu, ndivyo tulivyofanya, vilevile katika vyuo hivyo tulikuja kugundua kwamba hata ada yao ni pungufu kuliko hata ile ambayo ilikuwa inalipwa UDOM kwa kozi ileile. Kwa misingi hiyo unakuta kwamba ada iliyokuwa inalipwa UDOM inatosha kulipia watu wanne. Kwa hiyo, imekuwa ni tija kuwapeleka huko na wanafunzi wenyewe wanakiri kuwepo kule wanapata ufundishwaji unaostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niseme tu kwamba kwa Serikali kuhamia na kutumia majengo yale kwa sasa ni jambo ambalo lina tija, kwa sababu majengo yale yalijengwa kwa mkopo unaolipwa na Serikali na Serikali haioni tija kupanga majengo mengine wakati kuna majengo ambayo kwa sasa hayatumiki yakingojea kuendelea kuongeza walimu wa kutosheleza majengo yote.
Kwa hiyo, niseme tu kwamba pale Serikali ipo kwa muda na tunaendelea kupokea ushauri wa Kamati ya Bunge kwamba baada ya hapo tutaendelea na ujenzi katika maeneo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kidogo suala hili la ufaulu. Nitoe mfano wa maisha ya kawaida. Unaweza ukawa kila siku unamwona mume au mke wako siyo mzuri ukafikiria mume au mke wa jirani mzuri kwa sababu anakula nyama kila siku, ukafikiria wa kwako sivyo. Tumezisema sana na kuzisimanga shule hizi ambazo ni za kwetu za kata kwamba labda hazifanyi vizuri. Nataka tu niwaeleze ukweli na hili nalisema kwa ajili ya kusaidia kuiona Serikali imefanya nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda mnielewe naposema hivi simaanishi kwamba shule hizo zinafanya vizuri sana, hapana, nakubaliana kabisa kuendelea kuboresha. Nachojaribu kusema ni kwamba ukienda ndani katika matokeo ya hizi shule, kwa mfano shule ya Kibaha utakuta watoto waliofaulu division one ni 72, division two ni 22, division three ni nne na division four mmoja.
Kutokana na hiyo division four na one wamewavuta kwenye ufaulu wao kiasi cha kuwaweka ni watu wa 16, lakini ukienda Feza hiyo ambayo tunasema imekuwa ya kwanza yenyewe ina wanafunzi 65 na division one ni 59 na division two ni sita. Kwa hiyo, ukiangalia kwa idadi ya watu utakuta kwamba shule imefanya kazi kubwa. Hali kadhalika ukienda katika shule nyingine, kama shule ya Kilimanjaro utaona hivyo hivyo, inaonyesha hapa division one ni 44, division two ni 44, na division three ni 31 lakini kuna 68 ambao ndio wanawavuta wenzao. Kwa hiyo, si kwamba shule za Serikali hazichangii zina mchango mkuwa sana.
Toka shule za kata zimeanzishwa zimechangia jumla ya watu waliopata division one mpaka three 180,542, hayo ni mafanikio makubwa sana kwa Serikali yetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishukuru Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, chini ya uongozi wake Mheshimiwa Profesa Mbarawa. Pia nampongeza Naibu Waziri Mheshimiwa Engineer E. Ngonyani kwa namna wanavyoshirikiana na Waziri wake. Nawapongeza Watendaji wote Wakuu wa Wizara hii na bila kumsahau Kaimu Meneja wa TANROADS Ruvuma Ndugu Razaq kwa kazi kubwa anayofanya hususan katika Jimbo langu la Nyasa ambalo lina changamoto kubwa sana ya miundombinu ya barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona barabara ya Mbinga – Mbamba Bay ikiwa kwenye mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami. Barabara hii imo katika ahadi za Mheshimiwa Rais, siku anaomba kura alisema itajengwa kuanzia mwezi Aprili, 2016. Naomba sana ijengwe. Vile vile barabara ya Kitai – Lituhi na Lituhi – Mbamba Bay ambazo zilikuwa zimefanyiwa upembuzi yakinifu, sijui zimefikia wapi?
Vilevile nashauri barabara hiyo ichukuliwe ni Chiwindi (mpakani na Msumbiji) – Mbamba Bay - Lituhi badala ya Mbamba Bay - Lituhi kutokana na unyeti wake kuwa ni barabara ya mpakani na pia yenye fursa za utalii wa fukwe za Ziwa Nyasa. Hali kadhalika, naomba kuanza upembuzi wa barabara ya Kingirikiti hadi Liparamba - Mitomoni na kuunganishwa na daraja kuvuka Mkenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aliahidi kusaidiwa kujenga daraja baada ya vifo vya waliozama na boti Mto Ruvuma, kwenye bajeti hii, sijaona chochote! Tumeshawasahau wale watu tisa waliokufa. Mto ule hauna kivuko chochote cha uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Mheshimiwa Jenista Mhagama barabara ya Likuyu Fuso - Mkenda inayounganisha na Msumbiji. Jimbo la Nyasa pia tutanufaika na barabara hii endapo itajengwa kwa kiwango cha lami, pamoja daraja la Mto Ruvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile niliomba kupandishwa hadhi barabara ya Chemeni - Kipapa Matuta – Mengo - Kihagara hadi Bandari ya Njambe kuwa ya TANROADS au Trunk road kwani inakidhi vigezo; pia imeunganisha fursa za kiuchumi kwa Jimbo la Nyasa na Mbinga Vijijini. Vile vile kupandisha hadhi kipande cha barabara ya Mpepo hadi Darpori.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizidi kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kukamilisha ujenzi wa meli mbili na hiyo ya abiria zinazoendelea kujengwa, pamoja na Bandari ya Ndumbi na Daraja la Mtu Ruhuhu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti,naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri pamoja na timu yote ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa jitihada kubwa ya kufanikisha shughuli za Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti,baada ya pongezi, nina mchango mdogo; pamoja na kupanda kwa bei ya mafuta nchini, bado hali ya upandaji wa bei ya bidhaa itafutiwe tiba. Manung’uniko ni mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti,naomba pia niendelee kukumbusha ujenzi wa kituo cha SIDO Ruvuma, Nyasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti,nawasilisha.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumpongeza Waziri, Mheshimiwa Ummy Mwalimu kwa kazi kubwa anayoifanya katika kuiongoza Wizara hii. Pia nampongeza Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwa jinsi ambavyo anamsaidia Waziri wake na kujibu maswali kwa ufasaha kabisa Bungeni. Pia nichukue nafasi hii kuipongeza timu yote ya Wizara ya Afya chini ya Katibu Mkuu kwa jitihada zinazoendelea kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru kwa kushirikiana na TAMISEMI na Wilaya yangu kuwa katika Mpango wa Kuboresha Vituo vya Afya, hususani Kituo cha Afya cha Mkili. Hata hivyo, kuna Kituo cha Afya cha Kihagara ambacho kinaendelea na ujenzi. Nitaomba tupewe jengo moja tu kwa mwaka huu kwa ajili ya wodi ya wanawake kwa kuanzia na upande mwingine wanaweza wakakaa watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nyasa, with a very beautiful land kwa sasa tuna mpango mkubwa wa Nyasa Maridadi, Nyasa iwe safi, Nyasa ipendeze na hivyo kuwa ni mahali pazuri pa kuishi na kutalii. Idadi ya watu wanaotembelea Nyasa imeongezeka sana. Kitu cha kusikitisha ni kuwa hakuna uhakika wa usalama wa wananchi hao na watalii kiafya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya hii haina Hospitali ya Wilaya, tunategemea Kituo cha Afya cha Mbamba Bay ambacho hakina Ultra-sound wala X-ray na kadhalika. Tukipata majeruhi lazima wapelekwe Wilaya ya Mbinga au Peramiho na pengine Hospitali ya Rufaa Songea. Hao wananchi wengi wao ni maskini lakini ili kupata vipimo hivi vikubwa lazima walipe gharama ya nauli na baadaye walipe gharama nyingine zaidi kwa ajili ya kujikimu na dawa. Kwa summary naomba mtusaidie Ultra-sound machine, X-ray machine na ambulance, tafadhali sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimboni kwangu kuna malalamiko makubwa juu ya mikopo ya pikipiki iliyotolewa na Benki ya Wanawake wakati Mbunge wa Jimbo akiwa ni Mheshimiwa Marehemu John Komba. Wanadai kuwa wamekuwa wakichangia lakini kila wakati wanatajiwa deni kubwa zaidi. Vile vile ni kuwa ukusanyaji wa madeni hayo hauleweki na wanapokea simu kutoka kwa watu ambao wanakuwa hawana uhakika nao na kuwatishia kuuza mali zao. Ni vema ufanyike mkutano wa wadeni na ikiwezekana nikaribishwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natanguliza shukrani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumpongeza Waziri wa Maliasili na Utalii, Mheshimiwa Profesa Maghembe pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Engineer Ramo Makani kwa kazi kubwa inayoendelea katika kukuza utalii nchini Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana na kumshukuru Katibu Mkuu, Meja Jenerali Malinzi pamoja na timu yake ya wataalamu kwa kazi nzuri. Nawashukuru kwa tuzo ya uhifadhi wa mazingira ya Jane Goodall kupitia taasisi yake ya Roots & Shoots kwa kushirikiana na Makumbusho ya Taifa. Nawapongeza sana kwa kuendeleza Maporomoko ya Kalambo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nikiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, nilijitahidi kadri ilivyowezekana kuona jambo hilo siku moja linawezekana. Mara nyingi mhamasishaji akiondoka na wazo linakufa, lakini kwa jambo hili imekuwa tofauti, ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza kwa kuibua vivutio vingine kama jiwe la Mbuji na Mapango ya Makolo/ Matiri. Kama nilivyochangia wakati wa semina, ipo haja ya kuviibua vivutio vingine na kuvilinda kwani vivutio kama miamba ya hapa Dodoma, mkichelewa mtakuta watu wameshavivunja na kugeuza kokoto, jambo ambalo hamuwezi kurejesha tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tuache utani, Southern Circuit inayoacha Ziwa Nyasa mmefikiria nini? Kwa hiyo, Nyasa itakuwa ni Southern of Southern? Lengo langu ni kuwaomba kuwa ikiwezekana basi, ijumuishwe humo na utalii na fukwe ni vema upewe uzito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nyasa tumekubaliana kuanza kidogo kidogo, hivyo kila tarehe 30 Desemba ya kila mwaka ni kilele cha Tamasha la Utalii - Nyasa. Nawashukuru kwa support mliyotupatia mwaka huu. Sasa tuko kwenye maandalizi; na kila mwaka lazima tuseme angalau tumefanya nini. Hivyo tusaidiwe katika kuipanga fukwe hiyo, kuipamba (beautification) na kuboresha utoaji wa huduma hasa kwa akina Mama Lishe na waongoza watalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kutembelea Jimbo langu na kutoa ushauri muhimu kwetu. Miundombinu ya barabara ni tatizo, naomba Wizara yenu kuendelea kutusemea katika vikao vya Wizara mbalimbali ili Mbinga - Mbambabay iweze kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jiwe la Pomonda nalo lipewe uzito (lipo Liuli – mchezo wa kuruka majini) litangazwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nawashukuru sana TFS kwa kazi walioyoanza ya kupata miti Nyasa na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Madini
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia Wizara hii ambayo ni muhimu sana kwa ujenzi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya hususani katika Wizara hii. Tumeshuhudia hivi karibuni tu kwa suala la madini ya kinywe kule Songwe na mambo mengine mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nimpongeze Waziri Dkt. Dotto Biteko pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Kihuswa. Vilevile Katibu wetu Mkuu Ndugu Kheri pamoja na wote wanaomsaidia na kwa ujmla Wizara yote ya Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza mchango wangu mwingine nisije nikasahau naomba niwaulize Wizara ya Madini, ni lini yule mwekezaji ambaye alisema anataka kuwekeza katika mgodi wa dhahabu kule Mpepo Wilaya ya Nyasa atakamilisha kulipa fidia zake na kuwaacha wananchi wawe huru wakaendelee na maisha yao maeneo mengine, kuliko hii hali ya kusubiri leo kesho, kesho hakuna kinachoendelea, naomba kwa kweli hilo nipate jibu kwa sababu ni suala ambalo linasumbua katika Wilaya yangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo nirudi katika masuala ya kitaifa. Rais wetu Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema namnukuu “usipokuwa na mjomba jijombeze mwenyewe” sisi Bunge hili hatuna mjomba mwingine wa kutujombeza bali sisi wenyewe, utakuta wadau wengine wanasema Wabunge wanakaa mle wanalala tu hawafanyi nini? Jamani katika Wizara hii kuna kazi kubwa imefanyika. Nakumbuka miaka ya 2009 mpaka 2010 tulivyofikia kutunga sheria ambayo ilikuwa inajaribu kujibu matatizo yaliyokuwa yanawapata wananchi wa Mikoa ambayo inachimba dhahabu hususani Geita, tulipoenda kule Kamati yetu ya Nishati na Madini wakati huo tuliona huruma tulitoka machozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini wananchi ambao maeneo yao zinatolewa dhahabu zinasafirishwa kwa ndege huku na huku watu wanastarehe, lakini watu wake ni maskini sana. Ilikuwa inaumiza yaani ilikuwa haifanani maeneo yanayochimbwa dhahabu na hali halisi lakini leo ukienda Geita, Kahama, Shinyanga maeneo yote ya dhahabu kwa kweli unafurahi, unaona kwamba Wabunge walitimiza wajibu wao wa kutetea nchi hii, kuteteta watu wao katika kipindi chote kuanzia huko mpaka leo hii kupitia taasisi mbalimbali pia zilizokuwa zinatusaidia na leo sasa unaona matokeo ya nini maana ya madini kwa kipato cha mwananchi mmojammoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza sana Wizara kwa usikivu wao ambao waliujenga hatua kwa hatua, kwa sbabu mwanzo walikuwa wabishi ukiwaambia wanakwambia mkataba ni siri, hii haiwezekani, hili halipo lakini sasa hivi tunakaa tunajadiliana na mambo yanafanyiwa kazi yanakwenda vizuri, hiyo ndiyo maana ya Bunge katika kushauri Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo STAMICO pia ilikuwa ni moja ya mashirika ambayo yalikuwa yabinafsishwe, lakini tukasema hapana hebu tuliache tusichulie STAMICO kama ni shirika la faida moja kwa moja, kazi yake inayofanyika inasaidia kujenga uwezo katika nchi kwa kuwajengea uwezo wachimbaji wadogowadogo ambao sasa ni Watanzania na hatimaye watakua, leo STAMICO imekuwa ni kinara inaonyesha mfano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumeshuhudia STAMICO ikiongoza mapambano ya kuondoa uharibifu wa mazingira kwa kupanda miti, kusema kwamba lazima tupande miti katika maeneo ambayo tunachimba na maeneo mengine, lakini siyo hivyo tu imefikia kuweza kusaini mkataba wa Bilioni 55.2 wa uchorongaji, anaingia mkataba mkubwa na GGM ambayo ni kampuni kubwa ya uchimbaji. Huu ni mfano mzuri wa mashirika yetu kuigwa, kwa kweli nampongeza pia Dkt. Venance kwa kazi kubwa inayofanyika katika shirika hili la STAMICO ikizingatiwa na mimi nilianzia kazi STAMICO. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi kilichopita cha bajeti nilishauri nikasema kwa nini TANESCO au Wizara ya Nishati haipeleki umeme STAMIGOLD kwa uwezo wao ili kuondoa hasara inayopatikana ya matumizi makubwa ya nishati ya diesel kwa kutumia generator wakati wangepata umeme wangepunguza hayo matumizi, leo nimefurahi kusikia kwamba Mheshimiwa Waziri anatuambia jana umeme umewashwa, hayo ndiyo tunayoyapenda mashirikiano kati ya Wizara na Wizara, tena nawapongeza sana Wizara ya Nishati lakini nawapongeza ninyi wenyewe STAMICO chini ya Wizara yetu ya Madini kufuatilia na kuhakikisha kwamba mnaondoa hasara hizo kama ambavyo mlishauriwa na Waheshimiwa Wabunge .
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba nizungumzie kidogo juu ya suala la wadau tunaowahamasisha kuanzisha viwanda mbalimbali kwa ajili ya kuongeza thamani ya madini yetu. Mara ya mwisho wakati tumeenda Geita kama Balozi wa Wachimbaji Wanawake, tuliamua kumtembelea mwanakiwanda mmoja, Ndugu Sara kwenye Kiwanda cha GGR. Baada ya kufika pale, kitu ambacho tulikiona, hatupata picha nzuri sana. Yule mama tuliposema tunamsalimia ili tujifunze anachokifanya, alituambia kwamba jamani msinione hivi, mwenzenu saa hizi nipo kwenye tension kubwa sana. Nini? Watu wa TRA na watu wa Tume ya Madini wameenda kumkagua, lakini jinsi ambavyo wanamsemesha, hawataki hata kumsikiliza vizuri. Yaani ni ile hali ya kama Polisi hivi sijui, na Polisi wenyewe sio wa siku hizi, wale wa zamani ambao walikuwa hawafuati ustaarabu. Eeh, nini? Hapana sijui nini! Kila wakati anafikiriwa kwamba mwanakiwanda ni mwizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tuiache hiyo tabia. Sisi wenyewe kama hatuwezi kuwekeza, tunawaita private sector wasaidie kuwekeza, kwa nini hatuwajali? Kwa nini hatutumii lugha ambazo ni sahihi? Sikupenda suala lile, sikuipenda kabisa, na ndiyo maana tumesema lazima tuseme. Wale watu wamewekeza kiwanda kikubwa cha kisasa kabisa, lazima tuwajali, tuwaheshimu. Wawekezaji wote lazima tuwaheshimu, tuwasaidie, tuhakikishe wanapata dhahabu kwa ajili ya kusafisha kama ambavyo viwanda vyao vilianzishwa, lakini tukiendelea na mtindo huu wa kufikiria tu kwamba mimi naenda kukusanya mapato. Akifunga, utakusanya wapi hayo mapato? Utakusanya wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii hatuwezi kukubali. Tunawaambia, Bunge hili msituone sisi sijui tumekuwa wapole, hatuna upole wa kuharibu rasilimali au kazi ambazo tunajua zitaleta manufaa makubwa kwa nchi yetu. Kwa hiyo, tunaomba sana, wale ambao bado wanaendelea kuona kuwa na vile viukiritimba vya kizamani, waache. Sasa hivi wameona mfano mzuri, Mama mwenyewe, Mama yetu, Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, anavyosema namna gani tuwashughulikie wafanyabiashara; namna gani tuheshimu wawekezaji; kwa hiyo, ni lazima tuwe na tabia hizo za kuwaheshimu wawekezaji. Tutamfuatilia, mkiendelea kumfanyia fujo, tutawataja humu humu mmoja baada ya mmoja, hadharani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine naomba GST waongezewe kiasi cha fedha za utafiti. Hawa wachimbaji wadogo wadogo pekee yao hawawezi kuwekeza huko. Kama kweli tuna nia kama ambayo tumeanza nayo ya kuwasaidia, basi tufanye hivyo. Serikali ndio inayoweza kuwekeza fedha yake kwa kuchukua risk iliyopo na kujua kwamba baadaye huyu mchimbaji ataweza kunufaika yeye mwenyewe na pia kuisaidia nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana, GST isijikite katika baadhi ya maeneo tu. Tumegundua kwamba hayo madini yapo katika maeneo mbalimbali, ila haijajulikana. Kule Mbinga na Nyasa, tulikuwa hatujui kama makaa yangetusaidia kiasi hiki. Leo sasa hivi makaa ya mawe yamekuwa ndiyo chanzo kikuu cha fedha katika Mkoa wetu wa Ruvuma, lakini zamani tulikuwa tunaona ni ardhi tu tunaikanyaga. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika, watu wamekuwa wanasema makaa ya mawe hayafai, ni nishati mbaya, tunakubali, lakini inakuwa ni nishati mbaya tu pale ambapo tunahitaji kutumia sisi kwa mambo mengine! Sasa hivi kunahitajika makaa ya mawe huko duniani, mbona sasa hatusikii, wanachukua kwa nguvu zote! Tumegundua kwamba kumbe tunakataa jambo pale tunapoona hatulihitaji sisi, lakini pale ambapo wao wanalihitaji, linakua ni suala la dharura, ni changamoto imetokea, basi leteni tu. Kwa hiyo, nasema kwamba tusiwe na mchezo huo wa kudanganyana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nitoe wito na rai kwa madini mapya ambayo tunaanza kuyachimba, haya wanayaita rare minerals, au critical rare minerals; naomba sana, tusije tukaingia tena kwenye mtego ule ule ambao tulianza nao wakati tunaanza kuchimba dhahabu. Kwa sababu hayo hatujui tabia yake, hatujui gharama zake. Kwa hiyo, tusipofanya utafiti wa kutosha tutajikuta tunaingia mikataba ambayo leo tunafurahi tunasema kwamba mikataba hii ina faida kumbe ni hasara tu. Kwa hiyo, tuwe makini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweke mchango wangu kidogo kwenye Wizara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, chanda chema huvikwa pete, hapa leo tunaona, toka tumeanza kuchangia Waheshimiwa Wabunge wote wanatoa sifa kubwa na shukurani kubwa nikiwemo mimi kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wetu mwalimu wa misemo mbalimbali ya kutufundisha na kutusaidia katika maisha Jumaa Aweso lakini pia Naibu Waziri wake Engineer Maryprisca pamoja na Katibu Mkuu Engineer Kemikimba lakini kiujumla wake kwakweli wizara hii watumishi wake wote wanajitahidi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo mambo mengi mazuri yameishachangiwa na Waheshimiwa Wabunge lakini kwa umuhimu wa wizara hii nashindwa kutoa jina langu inabidi niendelee kuchangia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona kwamba wizara imejitahidi kufanya shughuli mbali mbali za kiuwekezaji wa maji katika maeneo mbalimbali nami kwangu nawashukuru sana kwa mradi wa maji Wangingama, Litui group, Ngumbo group na nikiruka mradi wa Pururu Songa mbele ambao kidogo haujanifurahishwa haujaanza lakini kuna Liuli…
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa inatoka wapi? Mheshimiwa Ester Bulaya.
TAARIFA
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nampa taarifa Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya kwa mchango wako mzuri apitie hapo kwamba Taifa linawakilishwa vyema, Young Africans wameshinda goli mbili bila. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Stella Manyanya unaipokea hiyo taarifa?
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mimi naipokea taarifa hii kwa sababu mimi ni Simba, lakini Yanga wamechukua jersey za CCM, kwa hiyo tunawapenda tu hata kama wakifanya vyovyote vile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba nilikuwa naendelea kushukuru kwa ajili ya mradi ambao utaendela pale Kilosa, Nangombo ambao utaenda mpaka Malinyi na Chihulu na miradi mingine michache itakayoendelea. Lakini kama ambavyo mwalimu amesema, ulitufundisha kwamba pilau la sherehe mvua ikinyesha huliwa wima. Sasa kwa mazingira hayo mimi sasa hivi nanyeshewa naomba nipate maji Mtupale, Chinyindi, Ruhangalasi, kata ya Lumeme, kata ya Mipotopoto, yaani eneo la Uhuru na Mipotopoto yenyewe, na Luhindo leo wamenipigia tena simu na kule Mseto Lipalamba, kote huko kuna shida ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiendelea katika masuala mengine yanayotuhusu kitaifa, pamoja na hizi shukrani nyingi nilizozisema. Tunamaliza Dira yetu ya Taifa ya Mwaka 2025. Dira hii ilisisitiza zaidi katika kuhakikisha kwamba Watanzania wanakuwa na Maisha bora, tuwe na jamii ambayo itakuwa na Maisha bora, lakini pia tuwe na amani, utulivu na umoja; utawala bora, jamii iliyoelimika na uchumi wenye ushindani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia mambo haya pamoja na kwamba tumeshaanza mchakato wa kuandaa dira mpya ya mwaka 2050 bado masuala haya ya msingi siamini kama yatatoka katika mtazamo wa dira hii ambayo tunaiandaa. Mambo hayo yote ili yaweze kutekelezeka kuhakikisha kwamba tunakuwa na uchumi ulio imara na wenye ushindani, kwa vyovyote vile suala la maji haliwezi kuwekwa pembeni. Na ndiyo maana sasa unakuta hata Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia suala la kuwa na Mpango kabambe ambao kwa Kingereza lugha nzuri ni hiyo Water Master Plan.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana kwa sababu Pamoja na kwamba sasa hivi tunatafuta maji hapa lakini bado kuna haja ya kuangalia utoshelezi endelevu wa suala la maji katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisikiliza hapa watu wanavyoshukuru miradi inayotajwa. Utasikia tumepata bilioni arobaini, bilioni hamsini, bilioni ngapi, lakini kule kwangu mimi sihitaji bilioni kumi, nahitaji milioni milioni kwa sababu vyanzo vya maji viko vingi tunahitaji tu kuvuvta maji kufikisha pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo kama Simanjiro tulikoenda mara ya mwisho kukagua mradi. Mradi ni mkubwa sana lakini ukiangalia mradi ule umekuwa mkubwa kwa sababu ya kuhangaika kutengeneza vituo vikubwa, kusafirisha kwa umbali mrefu kwa sababu ya kutokuwa na vyanzo vya maji vya kutosha katika maeneo yanayohusika. Kwa misingi hiyo kwa nini tunataka kuwa na hiyo mpango kabambe wa kuona kwamba ni namna gani tunaangalia maji yetu kwa mbali lakini vile vile namna gani tunaweza kuunganisha hivyo vyanzo, hasa vyanzo vikubwa
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi kuna mikakati mingi ya nchi ambayo yote kila Waziri hapo unaona anakuja anachemka, wa kilimo anachemka anasema anataka mashamba sijui ya aina gani, wa Kifugo anakwambia mimi nachemka anataka sijui ng’ombe wa aina gani. Wote hawa wanagombania maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa humo humo kuna kutumia dawa, humo humo kuna kutumia, kwamba hilo hilo bonde moja mwingine anatafuta maji ya kunywa, mwingine anatafuta maji ya kilimo, mwingine anatafuta maji gani. Matokeo yake tutajikuta kwamba tuna hali ambayo baadaye tutakuja kuanza kupigana sisi. Lakini vile vile tukumbuke kwamba tumeshaingia mkataba na umeanza kufanya kazi wa nchi za Afrika kuweza kufanya biashara pamoja; na ninaamini wengi watakuja kufanyia kazi Tanzania kwa sababu ndiko kwenye amani, kuna furaha na rasilimali nyingi ziko huku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama maji hayataonesha dira ya kuweza kutosha, kama maji hatutayawekea mipango maalumu, kama maji yatakuwa kwamba yoyote yule afanye analojisiskia, hiyo itakuwa ni changamoto kubwa sana. Kwa hiyo tunaona kwamba maadam tumeshtuka mapema, tuwaombe si kwamba walikuwa hawafanyi kitu kabisa, tunaboresha mipango ile ambayo tayari wanayo; tunaomba sasa hata katika mpango huu mkuu wa dira ya Taifa ya 2050 suala la maji lionekane vizuri kinagaubaga ili hata tunapoiangalia dira yetu nyingine pia ya 2063 zote hizo ziweze kuwa pamoja ikihakikisha kwamba Tanzania tunakuwa na usalama wa maji, Tanzania inakuwa ni nchi tuitakayo sawa mabavyo Afrika kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema hayo pia kwa kusisitiza hili suala la mfumo wa grid ya taifa ya maji, hayo yamefanyika. Kwanza Mungu mwenyewe ametuumba kwa mfano ambao hata mishipa ilivyounganishwa ndio hizo grid zenyewe, sivyo? Kwenye umeme tumeshaona, na mambo mengine mengine. Kwa hiyo tunaposisitiza suala la kuchukua maji kwenye maziwa yetu kwenye mito mikubwa na maeneo mengine hatumaanishi kwamba sasa tumpe pressure Waziri, kwamba kesho apate fedha za kufanya mambo yote haya kwa mara moja, tunachohitaji ni kuwa na mipango inayoonesha kabisa kwamba eneo hili nitachukua maji kwa muda fulani, lakini baada ya hapo nitatakiwa nichukue huku na huku. Ikifika muda niwe nimeshajiandaa kwa ajili ya kuingiza maji kutoka katika chanzo fulani, lakini pia kuhakikisha kwamba hata mtumiaji mwingine hajakiharibu kile chanzo. Kwa hiyo hizi Wizara zikae pamoja katika kupanga hiyo mikakati mwisho wa yote tuwe na mapango wa maji endelevu ambao utatuongoza huko katika dira kuu ya mwaka 2050 na maisha yetu yote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hiyo, nilikuwa napenda pia kuwaomba wenzetu wa Wizara ya Maji kuangalia suala la upatikanaji wa maji kwa bei nafuu. Kwa upande kama TANESCO kuna umeme unapataikana wa gesi, kuna umeme unapatikana wa maji, kuna umeme unaptikana wa diesel ukijumlisha pamoja unakuta bei ya umeme inapungua, kwa hiyo wananchi wote wanapata bei ambayo inafanana. Sasa kitendo hiki cha kuwa na sehemu za upatikanaji wa maji kila eneo kivyake, na system ya mapato imekuwa kila watu kivyao matokeo yake kuna maeneo kunakuwa na bei kubwa sana za maji wakati maeneo mengine wana – enjoy maji kwa bei nafuu zaidi. Kwa hiyo iko haja ya kuangalia mfumo wetu wa ukusanyaji mapato iili uweze kutoa unafuu katika baadhi ya maeneo ambayo yanapata maji kwa gharama kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Stella Manyanya ulikuwa unataka kumalizia, muda wako kengele ya pili imelia.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Basi nizidi kushukuru na ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, nyongeza yangu ya mchango wa bajeti Wizara ya Maji ni kuwa naomba pia kuikumbusha Wizara juu ya gari kwa ajili ya RUWASA Wilaya ya Nyasa kama ambavyo nilijibiwa kupitia swali langu la msingi Bungeni. Je, katika magari zaidi ya hamsini mliyogawa Nyasa imo? Jimbo la Nyasa ni kubwa ni vema wawezeshwe katika suala la usafiri.
Mheshimiwa Spika, Mkandarasi wa Puulu, Songambele na Ngeye anaanza lini mradi? Ana zaidi ya miezi saba sasa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA; Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza natoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais, Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote; pili, shukrani kwa vyombo vya habari na mashirika ya mitandao yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, Bunge lisaidiwe katika kuboresha huduma zake za maktaba.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini Mkongo wa Taifa utafika Mbamba Bay?
Mheshimiwa Naibu Spika, mawasiliano ya TBC Nyasa yaendelee kuimarishwa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi.
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini la pili nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, mtalii na muongoza watalii namba moja. Vilevile, naomba nikupongeze wewe mwenyewe na kukushukuru sana, pia nakushangaa una nguvu za ajabu, unakaa Bungeni na sisi kama haupo kwenye kiti unamaliza majukumu yako yote mezani, mambo yetu yote yanaenda vizuri, hakika hutashindwa pia kuongoza hilo Bunge la Dunia. Hutashindwa kwa sababu uwezo wako ni mkubwa sana, tunakuombea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri, Ndugu yetu Mchengerwa pamoja na Naibu wake Ndugu yetu Mary Masanja, wakati huo huo nawapongeza Katibu Mkuu pamoja na timu yao yote siyo rahisi kumtaja kila mmoja sasa hivi kwa kazi kubwa wanayoifanya katika Wizara hii. Kwa namna hiyo pia ninavipongeza vyombo vya habari bila vyombo vya habari mambo ya utalii kwa vyovyote vile yatadorora. Kwa hiyo, nawapongeza Safari Channel wa TBC, wanapongeza Channel Ten, nawapongeza ITV na vyombo vyote kwa kweli, Azam Tv na vyombo vyote ambavyo vinajihusisha katika kuhakikisha kwamba wanahamasisha utalii na hasa katika maeneo yale ambayo bado yapo nyuma ki utalii ikiwemo Wilaya yangu ya Nyasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda pia kuungana na ndugu zangu kule Mwanza kufuatia kifo cha Mwanahabari Magreth Tengule ambaye alikuwa ni mpenzi sana wa uandishi katika nakala za afya na utalii, Mwenyezi Mungu amrehemu. Mheshimiwa Naibu Waziri kuna wakati alikua amekuja kwenye Wilaya yangu ya Nyasa na kule kulikuwa na mgogoro mkubwa sana kwenye Pori la Liparamba na jirani zao ambao ni vijiji vinavyozunguka lakini alivyoondoka alituahidi atalifanyia kazi na kwa kutumia kikundi kazi kilichoundwa cha Mawaziri leo mgogoro ule umeisha, mipaka imeshawekwa, imebakia sehemu moja tu kutokea Ndondo mpaka Liparamba ambayo ninaomba pia wakamalizie, naamini chini ya uongozi madhubuti ya Mheshimiwa Kaka yetu Mchengerwa Mjukuu wa Bibi Titi, Mama yetu jambo hilo pia litaisha salama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hiyo pia nitoe taarifa ambayo siyo nzuri, mamba wetu wa maajabu ambaye tulikuwa tunampenda sana alikuwa mpole akiitwa anakuja, kwa bahati mbaya alinaswa kwenye nyavu na wale ndugu zangu wakamuona ni kitoweo basi hatuna naye tena. Kwa kweli tunashukuru tu kwamba alikuwa ameshakuwa na watoto basi ndiyo habari hiyo kwa sababu alikuwa anajulikana Dunia nzima ni maajabu.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kuzungumzia kuhusu umuhimu wa kupanga maeneo ya ardhi yetu hasa katika Wilaya ya Nyasa. Sasa hivi Wilaya ya Nyasa inakua vizuri kiutalii, tumehamasisha kwa muda mrefu wadau wamekuwa hawajitokezi sana. Sasa hivi wametokea TAWA ambao wamechukua Mlima wa Mbamba Bay, Tumbi na Kile Kisiwa cha Lundo. Tunashukuru wameanza kazi nzuri na hivi juzi nimeambiwa tayari boti limeshaenda kwa ajili ya kuwapeleka wataliii kule Kisiwa cha Lundo. Niwaombe sana Wizara kupita TAWA muendelee kuiangalia Wilaya ya Nyasa kwa sababu vivutio vyake ni vingi sana, vinahitaji uwekezaji. Sisi tunapata wivu sana tunaposikia Ngorongoro kuna jambo hili, Serengeti kuna jambo hili, sijui fukwe za wapi jambo hili na kule sisi kunabaki kumekaa kama vile hakuna wa kutumia hizo fukwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo jitihada zilizoanza tunaomba muendelee nazo na ninazidi kuwasihi wale wote ambao wanatabia ya kuvamia maeneo kwenda kuleta vurugu kusema kwamba mlima huu wanasema na wenyewe ni wa kwao lazima tufuate taratibu na sheria za nchi. Kwa hiyo, ninawaomba sana mtu yeyote anayetaka kuwekeza kwenye milima hiyo basi hii milima yote ambayo tayari imeshakabidhiwa kwa TAWA wahakikishe wanawasiliana nao ili taratibu zifuatwe na uwekezaji ufanyike bila migogoro. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ninalotaka nilizungumzie ni kuhusu asali. Nimeona hapa katika taarifa zetu ukiangalia toka mwaka 2005 asali tulikuwa tunavuna kiasi cha tani 465 ambayo thamani yake ilikuwa tu kama milioni 550. Sasa hivi asili katika miaka kuanzia 2017 mpaka 2022 imeendelea kuongezeka na hata pale ilipokuwa inapungua imekuwa bado thamani yake ni kubwa. Kwa hiyo, niwaombe Wizara kuendelea kulisaidia zao hili la asali pamoja na nta, kwa sababu zao hili linamgusa mwananchi mmoja mmoja ukiacha hayo mambo mengine ambayo fedha yake inaenda moja kwa moja kwenye mifuko mikubwa ya Kitaifa, lakini kwenye asali na nta inaenda moja kwa moja kwa wale wananchi wa kawaida. Kwa hiyo, niwaombe sana kulitilia mkazo zao hili lakini pia linatusaidia sisi katika kuapata afya.
Mheshimiwa Spika, wakati ule ilikuwa ukienda sokoni unataka asali unapewa asali iko kwenye chupa ya konyagi tena hiyo chupa sijui imeokotwa vipi shida tupu na hupati wakati mwingine, lakini sasa hivi asali ni zao ambalo unalipata kiurahisi kila mahali na kwa kweli kwa namna ya kipekee kabisa inaandikwa kwenye historia Mheshimiwa Mzee Pinda, Waziri wetu Mkuu Awamu ya Nne anastahili pongezi katika mdudu huyu anayeitwa nyuki pamoja na asali yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nazidi kuomba kwamba tuwe na utamaduni wa kuandika historia za watu. Kama ambavyo leo tunamuona Mama, Mheshimiwa Rais alivyohangaika na Royal Tour aandikwe historia yake vizuri kwa sababu anayetenda jema apongezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia, nikiendelea katika hili suala la makumbusho, makumbusho ukiangalia ni kama vile eneo la utalii ambalo halipendezi pendezi hivi, lakini sisi wenyewe tunashuhudia kila wakati wanapokuja viongozi wa Kitaifa kutoka nchi mbalimbali sehemu wanayokimbilia kwenda ni kwenye makumbusho. Ina maana wanataka kujua historia yetu wanataka kujifunza mambo mbalimbali lakini pia kupitia historia kama hizo zinatoa kipimo namna gani watu wamepiga hatua za kimaendeleo kutokea wakati huo mpaka sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa misingi hiyo nataka kufahamu Wizara imejipanga vipi katika kuhakikisha kwamba makumbusho haziishii tu ziwe za siku nyingi, kwa sababu kila siku zinazaliwa historia nyingine. Wamejipanga vipi katika kuendeleza masuala ya kimakumbusho. Kuna mwongozo wowote ambao upo kwa ajili ya kuendelea makumbusho? Nasema hivyo kwa sababu hata CAG ameuliza swali hili. Kwa hiyo, nimeona na mimi niongeze mbele lakini pia hata nikifuatilia katika baadhi ya maeneo naona makumbusho ziko maeneo machache sana. Hapa Dodoma sijui lini sasa tutaijenga makumbusho kubwa kabisa ya Kitaifa. Kwa hiyo, niwaombe sana suala la makumbusho ni muhimu kwa sababu watu tunakuja, tunapita, vitu vinakuja vinapita, historia zetu zinakuja zinapita lakini tunapokuwa tumeziweka vizuri zinasaidia hata watoto wetu kujifunza hatua kwa hatua za mabadiliko na maendeleo yetu katika nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na suala la Makumbusho ya Taifa ninazidi kuwaomba kwamba katika makumbusho mojawapo ambayo ni ya Majimaji kule Songea bado pamoja na kwamba sasa hivi tunaona kila mwaka ina adhimishwa inapofikia tarehe 27 mwezi wa Pili lakini ile jitihada ya Serikali ya kuwekeza bado ni kidogo, ndiyo maana hata wenzetu wa kule Nandete Rufiji wanalalamika. Kumbe tungeunganishwa sasa hivi tukawa kama circuit moja, makumbusho kimsingi, kisheria, ikishakuwa imekaa zaidi ya miaka 100 automatically inakuwa imeshaingia kwenye kuwa ni Makumbusho ya Kitaifa. Sasa wale Nandete kwa nini kila siku wanakumbusha jambo hilo hilo? Kwa hiyo, mimi niwaombe sana Wizara katika suala hili la kuunganisha hizi historia zetu hizo hazitaki mjadala mrefu. Kinachotakiwa ni sisi kuhakikisha kwamba tunajipanga na kuona kwamba makumbusho hizo zinawekwa katika historia yake inavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ni kwamba, Wizara hii imepata viongozi vijana, kuna kufanikiwa katika wanayofanya, kuna kukosea kutokana na ujana wao na sisi kila siku tunasema kwamba vijana wapewe nafasi, basi pale wanapokuwa wameteleza tuwaelimishe kwa upole, tuwasaidie ili waendelee kufanya vizuri, hiyo itakuwa ndiyo Tanzania tunayoitaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa maneno hayo nashukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi. Kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini pia namuombea kwa Mwenyezi Mungu ambariki na sisi sote pia atubariki. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pili, nikupongeze wewe mwenyewe kwa kazi kubwa unayoifanya ya kusimamia Bunge hili vizuri na kwa kweli sheria uliyoisoma tunaiona matokeo yake. Nasema hayo kwa sababu wakati ule wa Azimio la Bandari kama hapo angekaa mtu ambaye haelewi elewi sheria yawezekana lile azimio lingerudi nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia nitumie nafasi hii kuwaomba ndugu zangu wa kule Nyasa maana yake na wenyewe wamekuwa wanasema mama vipi huko, mama vipi huko? Hasa kuna dada mmoja anaitwa Angella Mayi kimsingi Bunge lipo imara na linafanya kazi zake kwa kuzingatia maslahi mapana ya nchi na tunashauriwa kupitia Mtume Paulo kwamba tusiwakwaze wenzetu wanapojaribu kufanya mambo mazuri, ni wajibu wetu kusaidia na kushauri kwa upole ili jambo liweze kutekelezwa ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nampongeza pia Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa jinsi ambavyo anaingoza Serikali vizuri humu Bungeni, lakini pamoja na Wabunge wote kama hasa wa CCM kama Mwenyekiti wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Nyasa, Tarafa ya Mpepo tunalima kahawa, safari hii malipo ya Stakabadhi Ghalani yale malipo ya awali yamechelewa sana kiasi kwamba yanaweza kuleta athari. Kwa hiyo, niwaombe wanaohusika washughulikie mapema ili kunusuru hali hayo, lakini pia hata kama kutakuwa na haja ya kufanya mabadiliko namna ya mfumo wa kuuza kahawa basi ni vyema wananchi wenyewe washirikishwe kikamilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha pamoja na Naibu wake na timu nzima ya Wizara ya Fedha kwa kazi kubwa waliyofanya, lakini pia hata elimu waliyotupa katika kipindi cha wiki hizi zilizopita imetusaidia sana kufahamu mambo mengi ambayo yanayohusika katika Wizara hii na kwa namna ya pekee nakupongeza kwa ajili ya suala la uliloliandika katika ukurasa wa kumi kifungu namba 16 kinachohusu watu wenye ulemavu kwa kutenga shilingi bilioni moja itakayoweza kuwasaidia katika kupata vifaa saidizi pamoja na mambo mengine ya mitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watu wenye ulemavu wana changamoto nyingi sana, ni mtu mpaka uishi nao ndiyo utazijua. Mtu mwenye ulemavu ni gharama yaani hata kumuhudumia ni gharama. Sasa hivi kuna mwanafunzi kwa mfano yupo pale Chuo cha IAA, Arusha anachangamoto kubwa kwa sababu ni mlemavu anayesota kwa matako, anatakiwa atembee karibu mita 500 kwenda darasani, wenzake wambebe na wenyewe hawapendwi kubebwa, wanapenda kujitegemea, wanapenda utu wao, wanashida.
Ushauri wangu ni kwamba pamoja na fungu hili uone ni namna gani linaweza kutumika katika kusaidia hasa vile vyuo ambavyo havijaweka sera rasmi ya kusaidia watu wenye ulemavu, kupata vifaa saidizi na kwa hii na kukabidhisha huyu binti Sayuni yuko pale Arusha, naomba umsaidie apate angalau kibajaji hata kama kitakuwa ni cha shule aweze kukitumia atakapomaliza watatumia wenzake, inakuwa ni changamoto kubwa sana, naongea kwa uchungu mkubwa kama mzazi na kwa uzoefu mkubwa wa suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kusema kwamba Serikali inasikiliza, siku zote watu tunafikiria tunasema Wabunge wanaongea tu, wanaongea tu, Serikali ina masikio, masikio ninayoyaona hapa sasa ni jinsi ambavyo Wabunge kwa muda mrefu walikuwa wanazungumzia kusaidia kuchangia wanafunzi wanaosoma katika Vyuo vya Ufundi na Sayansi kwa ujumla. Nimefurahi kupitia ukurasa namba 29 mnasema kwamba mtaondoa ada/mnachopendekeza kuondoa ada katika vyuo hivi vya DIT, MUST, ATC kwa kuanzia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nawapongeza sana, lakini naomba kuongeza Chuo cha NIT hakiko hapa, nacho mkiangalie, sasa hivi tunatengeneza reli, tunafanya mambo ya usafirishaji (logistics) chuo hiki ni muhimu sana katika masuala hayo, naomba kama kilisahaulika kiongezeke. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na ukurasa wa 38 kwenye sensa, matokeo ya sensa tumeyapata na hayo tumeambiwa kwamba idadi za watu zisaidie katika kuhakikisha kuwa mipango ya rasilimali inatumika vizuri. Mimi ninachoomba kuongezea isiwe idadi ya watu tu na umbali wa upatikanaji wa huduma uzingatiwe, ukubwa wa maeneo uzingatiwe, mambo yote tusiende tu kiurahisi rahisi kama yale ambayo tulikuwa tunayasikia pengine haya hapa pateni kumi na tano, kumi na tano ngapi hapana. Tuangalie na mambo mengi ya mapungufu yaliyopo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo niwashukuru sana pia kwa suala hili la ujenzi wa reli ya Mtwara mpaka Mbamba Bay ambayo iko kwenye hatua za manunuzi. Tunashukuru sana sisi wa ukanda ule, lakini hata Taifa kwa ujumla reli hii itakuwa na msaada mkubwa sana katika shughuli za kimaendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda pia kuishukuru Serikali kwa kusikiliza Wabunge kupitia hoja ambayo niliitoa katika bajeti iliyopita juu ya changamoto ya watu kuhamisha ardhi, gharama kubwa za uhamishaji wa ardhi baada ya kununua. Lakini nimefurahi kupitia ukurasa wa 98 mpaka 99 kifungu (b) Sura 332 ya Sheria ya Kodi inazungumziwa kupunguza kodi hiyo kutoka asilimia 10 mpaka tatu na kwa wale ambao wametunza kumbukumbu zao vizuri asilimia 10 ya yale mauzo ambayo yalifanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi naona hii itasaidia sana kufanya masuala ya kiuwekezaji yaende kiurahisi, lakini kuwa na taarifa sahihi ya wamiliki wa ardhi, ndiyo maana mara ya mwisho nimesikia Mheshimiwa Waziri wa Ardhi anakilalamika kwamba kuna hati zimeshatengenezwa zaidi ya 2,000 lakini watu hawajachukua, hawajachukua kwa sababu yawezekana hayo majina hayapo sasa hivi, hayahusiki ndiyo maana watu walikuwa hawajaenda kuchukua. Lakini kwa mabadiliko haya ya sheria hii nayaunga mkono sana na napongeza sana na naamini yataleta mabadiliko makubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikienda pia katika suala ambalo Mheshimiwa Waziri wa Fedha ulitoa commitment kipindi kile kuhusiana na kupata fedha maalum au tozo maalum kwa ajili ya kusaidia afya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa hivi tunahangaika kufanya masuala ya kidigitali ya tusaidie katika kufanya shughuli zetu na mifumo ya afya ni vizuri sana ikaongea, unaweza kukuta sehemu nyingine wanadawa sehemu nyingine hawana dawa, unaweza kukuta sehemu nyingine kuna watumishi wengi sehemu nyingine hakuna watumishi wa kutosha, lakini kupitia mifumo hii ya kidigitali tutaweza kupata mambo mengi ambayo yanatuunganisha na kuweza kuboresha katika hizi huduma za afya.
Kwa hiyo, kwa misingi hiyo nazidi kusisitiza eneo la afya ni muhimu sana labda pengine tulichelewa haijaingia katika bajeti hii, lakini ni muhimu ifikie mahali sasa wananchi hawa wapate matibabu yao vizuri, bila shida, mmefanya kazi kubwa sana kujenga vituo vya afya, zahanati na maeneo mbalimbali ambayo yanatoa huduma za kiafya, lakini changamoto ambayo imebakia ni hiyo ya kuimarisha huduma za msingi pamoja na vifaa tiba.
Mheshimiwa Spika, wengine mpaka wanasema kwamba tumekosea, tumejenga vituo vya afya vingi sana, lakini ukiwafatilia wanaosema hivyo ni wale wanaoishi mjini ambazo huduma zote zipo. Haiwezekani mama mjamzito alazimike kusafiri kilometa 20 anaenda kupata sehemu ya kujifungulia, huyo mama lazima tu ataamua kubaki na kujifungua nyumbani. (Makofi)
Kwa hiyo, wakati mwingine tunasema tupunguze vifo vya kinamama na watoto, tupunguze wanawake wengi wakajifungulie katika sehemu za huduma sahihi, lakini wamekuwa hawaendi kwa sababu tu kwamba kule mnakomlazimisha aende hawezi kwenda kutokana na changamoto kubwa za kiusafiri na wakati mwingine inabidi apande pikipiki, yuko barabara labda ina mashimo, anatembea huko mama wa watu anakaribia kujifungua, hatujui kwa sababu tu kwamba nini wengine akina baba mnatuonea huruma tunajua, lakini hamjaonja uchungu wa kujifungua, mngekuwa mmeonja mngejua kwamba hata kutembea kilometa moja wakati uchungu umeshakushika ni kazi kubwa sana. (Makofi)
Sisi mama zenu tumejitolea sana, yaani tumejitoa kwa hali ya juu kwa kutaka tu kwamba tuwe na watoto na ndiyo tuongeze Taifa na ndiyo maana tunaona kwamba hata sasa hivi Mheshimiwa Rais anapofanya maamuzi yake mengine ni ya uthubutu wa hali ya juu, ni kwa sababu akinamama tumezoea kuthubutu ndiyo maana tunafikia hayo malengo na mafanikio tunayoyafanya. (Makofi)
Kwa hiyo, niwaombe sana, fanya hata kama itabidi kwa miaka miwili tupate hiyo tozo, tuboreshe hivyo vifaa ili kuwe na tiba kamilifu katika maeneo hasa kwa vituo hivi ambavyo tayari tumeishavijenga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini wakati huo huo suala la watumishi wa afya jamani hili lisiwe ni suala la kuzungumza sana, tusaidieni, tusaidieni watu wanaotakiwa kutibu wawepo kwenye maeneo ili watu wapate huduma inayostahili…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Charles Tizeba pamoja na Naibu wake Mheshimiwa William Tate Olenasha kwa kazi nzuri katika Wizara hii. Naomba pia nimpongeze Katibu Mkuu wa Wizara Eng. Mathew Mtigumwe pamoja na timu ya watendaji wa Wizara hii kwa jitihada zao. Hata hivyo ninayo machache:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Katibu Mkuu kwa hatua alizochukua za kuhakikisha kuwa wakulima wangu wa kahawa wanalipwa. Pili, tunapongeza Wizara kwa kuweka kipaumbee katika zao la korosho na hivyo kutoa ruzuku katika pembejeo za madawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Nyasa ni wakulima wa kahawa na uvuvi. Kwa upande wa wakulima Serikali imekuwa ikiwapa support ya kuwajengea maghala na pembejeo za mbolea (ruzuku).
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa wavuvi mazingira yao ya uvuvi ni duni sana. Mialo imekuwa na vibanda duni na hata mitumbwi yao ni duni. Wavuvi hulazimika kumwaga dagaa ziwani wakati wa mvua kwani hawana drying shed. Serikali ina mpango gani wa kuwainua kundi hilo kwa kurekebisha mazingira yao ya biashara?
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la samaki wanaoitwa vituwi, wavuvi wa nyasa wanasikitika kuwazuia kuvua samaki hao kwa kutumia nyavu za saizi ndogo, wao wanadai kuwa samaki hao hawakui. Naomba ufanyike utafiti juu ya suala hilo. Nitanyimwa Ubunge kwa ajili ya vituwi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Zao la mihogo; Wilaya ya Nyasa Kata ya Kihagare bado ina mihogo ya asili (Gomela) ambayo ina ladha nzuri sana. Baada ya kuleta mbegu za kisasa wakulima wengi walihamasika kwa mbegu mpya, lakini katika kuchemsha ladha ya mbegu mpya haina uzuri kama gomela. Matokeo yake Gomela imesababisha utamaduni wa wizi. Ukipanda Gomela iwe katikati, pembeni, vyovyote vile ikikua lazima iibiwe. Mimi pia niliibiwa. Naomba Wizara ifuatilie mbegu hiyo ili isipotee, ni mbegu nzuri sana na inaweza kufaa zaidi hasa kwa kitafunwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ruzuku za injini za boti, utaratibu ukoje? Kwa nini zisitengwe fedha za kuleta maboti ya mbegu ili kuwasaidia wavuvi kununua yakiwa jirani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazidi kuwaomba kutembelea Jimbo langu la Nyasa. Nawatakia kazi njema.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nichukue nafasi hii kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu pamoja na timu yao kwa kazi nzuri inayofanyika katika kuboresha huduma za maji hasa katika Halmashauri nyingine kasoro Halmashauri ya Nyasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa uchungu nina masikitiko makubwa juu ya mwenendo wa miradi ya maji katika Wilaya yangu. Nakumbushia barua yangu kwako Mheshimiwa Waziri juu ya tatizo la maji, katika hotuba yako Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 133, Ziwa Nyasa linaongoza kwa kuwa na ujazo mkubwa wa maji. Mwaka 2015/2016 milimita 1,359.78 na mwaka 2014/2015 milimita 1208.92. Ukurasa 135 Ruhuhu ni wa pili kwa wingi wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Wizara inatoa maji toka Mwanza kupeleka Shinyanga/Tabora zaidi ya kilometa 150, lakini wananchi wa Nyasa wana umbali chini ya kilometa 1- 3 kutoka Ziwa Nyasa na hawapati maji salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la Kingirikiti kulikuwa na mradi mkubwa wa maji uliotekelezwa toka tukiwa Wilaya ya Mbinga, zaidi ya shilingi milioni 600 lakini mpaka leo hakuna maji. Nilitoa fedha zangu shilingi milioni 1.5 kusaidia upimaji wa maeneo ya kuboresha upatikanaji wa maji katika Kata ya Tingi, mpaka leo hakuna chochote kinachoendelea. Kituo cha Afya cha Lupalaba kina hali mbaya, niliomba hata ifanyike kazi ya kunusuru kata hiyo mpaka leo hakuna kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kata ya Mbaha hasa kijiji cha Ndumbi hamna maji, hali ni mbaya. Mji wa MbambaBay Makao Makuu ya Wilaya hakuna maji, lakini maji ya Ziwa Nyasa yapo umbali wa mita 30 tu kutoka makazi na shughuli za watu, lakini bado watu hao wanakosa maji salama. Mheshimiwa Waziri, nadhani kuna tatizo Mhandisi waMaji wa Wilaya yangu nadhani anahitaji kusaidiwa, uwezo ni mdogo, yupo kwenye comfort sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kabrasha sijaona mradi specific kuhusu Wilaya ya Nyasa. Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Naibu Katibu Mkuu, wote hawa ni wanangu kule Rukwa, Katibu Mkuu pia ni mwanangu kule Wizara ya Elimu, mbona hamnihurumii? Leo nimejipanga, kesho kusipoeleweka nitashika shilingi kiaina.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitengewe fedha kisha nipewe wataalam wa kunisaidia, suala la maji halijapata majibu kabisa kwenye Jimbo langu, Mbinga tupewe fedha mpaka waseme fedha za mradi wa Kingirikiti wamepeleka wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitashika kifungu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Nishati
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, lakini pia nimshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutuwezesha kuwa hapa tukiwa salama. Kwa namna ya pekee kabisa naomba nichukue nafasi hii kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoendelea kufanya, hususan katika eneo hili la Wizara ya Nishati, hasa katika kuhakikisha kwamba, miundombinu inaendelea kuimarishwa, lakini pia kupeleka fedha katika miradi ya kimkakati tuliyokwishaianza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Waziri wa Nishati pamoja na Naibu wake, Mheshimiwa Makamba na Mheshimiwa Stephen, lakini pia Katibu Mkuu pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi watendaji wote ambao wako chini ya Wizara hii, Wenyeviti wa Bodi pamoja na watumishi wote ambao wako katika Wizara hii. Kwa kuwa, sio rahisi kumtaja kila mmoja, basi niseme tu kwamba, nawapongeza na hasa ikizingatiwa kwamba, Wizara hii wafanyakazi wengi ni wahandisi wenzangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanasema kwamba, ulimi ni kitu ambacho wakati mwingine kinaponza na ukiangalia Wizara hii tulivyoichukulia wakati inapokea madaraka, yaani wakati Mawaziri hawa wapya wanapokea madaraka, ilikuwa kidogo tuna hali ya wasiwasi itakuwaje? Mambo yataendaje? Kwa hiyo, kukawa kunatokea maneno ya hapa na pale, lakini kusema kweli utulivu ulioendelea na pia viongozi hawa jinsi ambavyo wameendelea kupokea wajibu wao na kuutendea haki, tunaona sasa haya mabadiliko makubwa ambayo yanaendelea. Vilevile tunaona hata Waheshimiwa Wabunge ambao walikuwa wakali sana kwa kipindi cha nyuma, sasa wanaiunga mkono bajeti ya Wizara hii bila kusita na wala sio kwa unafiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru kwa semina mbalimbali zilizotolewa kwa ajili ya kuelimisha zaidi. Semina hizi zilikuwa na lengo la kujenga uelewa zaidi na sio kwa ajili ya kuwapofusha Wabunge, Wabunge wa Bunge hili ni Wabunge makini sana, huwezi kuwapofusha. Ni watu ambao wakisimamia jambo lao wamelisimamia, lakini wakielewa watakuunga mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kidogo kuhusiana na Bwawa la Mwalimu Nyerere. Napenda kuipongeza sana Wizara kwa kazi hii na hapa namkumbuka Mwenyekiti wake wa Bodi ambaye katika Shirika la TANESCO ambaye amekuwa ni muasisi wa masuala ya Matokeo Makubwa Sasa. Hapo ni kwamba, unachagua jambo moja zito na unalifanyia kazi kwa nguvu zako zote ili liweze kuzaa matunda mengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika hili kwa mtu yeyote ambaye ni dereva mzuri anapoachiwa gari lililokuwa lime-park mahali au linaendelea kutembea, hawezi kuchukua tu akaliendesha bila kuangalia lina maji, lina oil, lina kitu gani ili liweze kwenda vizuri. Hilo ndilo lililofanyika, baada ya mabadiliko ya kiuongozi kulikuwa na muda kidogo wa kutathmini mradi huu uende vipi, changamoto ni zipi na mahali labda pengine tuboreshe?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mradi mkubwa kama wa Mwalimu Nyerere, jamani ule mradi tusiuchukulie sawa na kujenga nyumba yako au kufanya tu ni mradi wa kawaida ambao unaufikiria, unahitaji umakini wa hali ya juu. Mabadiiliklo yoyote ambayo yanafanyika au marekebisho yoyote yanayofanyika hapo si kwamba, wale wa mwanzo hawakuwa na maana au hawa wa mbele ndio wanajua zaidi, ni katika kuufanya mradi huu ambao unatumia trilioni za Watanzania zaidi ya sita, uweze kuwa imara, uweze kuwa utakaokuwa na tija na utakaoweza kudumu kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkumbuke kwamba, hata zile mashine nyingine zinaenda kuwekwa chini huko kwenye maji. Kwa hiyo, lazima vitu vingine viwekwe vizuri kiasi kwamba, hata zikishafungwa zile mashine kama turbines hutegemei kwamba, kesho tena utaanza kusema kwamba, ngoja niangalie, sijui tuangalie ilikaa vibaya, sijui kitu gani, lazima uende kwa mahesabu yote na usije ukapotea. Kwa hiyo, nawapongeza sana na nazidi kusisitiza waendelee kuwa watu makini, pale ambapo wanaona kuna dosari wasisite kusema na kufanyia kazi hata kama itatugharimu kuongeza muda kidogo au pesa kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwamba, wamefanya jitihada ya kupeleka wataalam wetu kwenda kufuatilia utengenezaji wa zile mashine umba na turbines ambazo ziko kule, hilo ni jambo jema sana. Niseme tu kwamba, ndugu zetu wote ambao tuko humu na walioko nje sisi Kamati yenu ya Nishati na Madini tuko makini, ndio maana hatupigi kelele nje, tunapigia kelele ndani. Tunapokuwa kule kwenye Kamati kule ni patashika nguo kuchanika, kila jambo lazima tulione na tunatembelea hiyo miradi na tumetembelea, tumeona Mradi wa Mwalimu Nyerere unaenda vizuri. Sasa hivi power house yaani nyumba ya umeme inajengwa inaendelea vizuri, hizo mashine zinaendelea kutengenezwa, sehemu ya station ya kituo cha umeme inatengenezwa, line ya umeme kutoka kule kwa Bwawa la Mwalimu Nyerere mpaka Chalinze na yenyewe inajengwa, lakini pia tumesisitiza kwamba, hata tukizalisha huu umeme mega wati 2,115 kama hakuna viungo vya kupeleka umeme kwa hawa watumiaji itakuwa ni hakuna maana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jinsi ambavyo mfumo huu unafanya kazi hakuna tofauti na mwili wa binadamu. Unaweza ukawa na kichwa, huna shingo, wewe ni hopeless, unaweza ukawa na shingo na mikono huna kichwa, haisaidii. Kwa hiyo, ni lazima mfumo mzima uangaliwe. Nashukuru sana bajeti ya safari hii imeendelea kuwa vilevile nzuri, lakini kubwa zaidi ni kuhakikisha kwamba, sasa ile mifumo mingine ya usambazaji umeme, usafirishaji umeme wa KV 400 na yenyewe inakamilika kwa pamoja, iendelee kufanyiwa kwazi kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nimefurahi ni kuona ni kwa namna gani tulipokuwa tunalalamika umeme unakatikakatika, Serikali imetoa fedha ya kutosha kwa ajili ya kufanya matengenezo na marekebisho muhimu ili umeme uendelee kuwafikia wananchi. Sasa hivi naomba Waheshimiwa Wabunge, ukisema umeme unakatikakatika, malizia kusema ni eneo gani ili tukashughulikie, kwa sababu, ukisema kwa ujumla yawezekana utakuwa hutendi haki, sema kwamba, eneo fulani ili liende likashughulikiwe na mambo yazidi kuwa mazuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo mwaka huu ni mwaka wetu wa sensa. Mwaka wa sensa tutaangalia takwimu za aina mbalimbali, moja ya takwimu itakuwa ni namna gani Watanzania wameweza kunufaika katika nishati za aina mbalimbali. Kwa hiyo, niwaombe, wenzetu watu wa REA ambao wamefanya kazi kubwa sana waendelee kuhakikisha katika hii miezi miwili tuliyonayo umeme usambazwe kwenye majumba ya watu ili itakapofikia kujua ni watu wangapi wana umeme, basi idadi yetu iongezeke na izidi kuonesha nchi hii ni nchi yenye nguvu na yenye dhamira katika kuleta maendeleo ya wananchi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna jambo lingine ambalo napenda nisisitize kuhusiana na hizi mita janja ambazo tutaanza kuzitumia. Niwaombe sana kwamba, mita janja kimsingi ni ghali kidogo na kama ni ghali hatutegemei wote watapewa kwa mara moja. Kwa hiyo, nafikiria kwamba, mita janja waanze kupata wale ambao watakuwa na uwezo wao wa kuchangia, kwa sababu zile zitakuwa na bei kubwa zaidi pengine takribani mara tatu ya mita za kawaida. Sisi wa maeneo ya vijijini acha tupate hata kama ni mita hizi za kawaida, lakini la msingi tupate umeme kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikirudi kwenye upande wa mafuta; napenda kuipongeza sana Wizara kwa jinsi ambavyo imechukua hatua ya kujaribu kupoza makali ya mafuta. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa ile shilingi bilioni 100 ambayo ameitoa kwa ajili ya kusaidia marekebisho hayo. Sasa naona kuna mpishano kidogo, wafanyabisahara wanasema kwamba, ile bei ilivyowekwa sasa mafuta yamepungua wao wanapata hasara kwa sababu, walinunua mafuta mengi. Wafanyabiashara tusameheni, acheni ujanja, wakati ule bei ilipotangazwa ikaongezeka mlikuwa pia na madumu mengi mmeyahifadhi, mbona hamkusema kwamba, ngojeni kwanza tuuze kwa bei ndogo haya madumu mengi tuliyoyahifadhi, halafu badaye tutapandisha bei? Acheni ujanja, (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema hivi hata kama hiyo bahati mbaya ipo, ndio hivyohivyo hata wananchi iliwakuta bahati mbaya kupanda bei kubwa sana. Sasa hivi na ninyi bebeni mzigo kidogo, lakini mwisho wa yote tutaenda wote vizuri. Kwa hiyo, ninachosema ni kwamba, kimsingi nia ni njema, kusiwe huyu anasema hili, anasema hili, huko ni kuyumbisha, hakuna suala la kuyumbisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine niombe kuendelea kusisitiza, najua pengine sitapata tena nafasi ya kuchangia. Bajeti inayokuja ya Serikali ipunguze kama ni kodi wapi kokote itakakojua, lakini katika miradi ya umeme, maji na afya, katika maeneo yale muhimu ambayo tunapeleka fedha za tozo, jamani acha tujifunge mkanda. Kwenye corona tulisema tusijifungie tukavuka na hivyohivyo kwenye masuala haya ya kupanda bei mafuta na nini acha tujifunge mkanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kule vijijini tunahitaji maendeleo...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya kwa mchango wako.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, kaka yangu Mheshimiwa Philip Mpango kwa kazi nzuri na nampa pole kwa changamoto kubwa za kuendesha uchumi wa wananchi. Pia napenda kumpongeza Naibu Waziri, Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kijaji. Napenda kuwapongeza watendaji wote chini ya Katibu Mkuu, Ndugu James Dotto pamoja na Manaibu wake. Jimbo la Nyasa tunawashukuru sana kwa support mnayotupa, tunasema ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo dogo kuhusu kufungwa kwa Benki ya Mbinga, napenda kujifunza tatizo ni nini? Benki ile ilikuwa inasaidia sana wakulima wadogo wadogo hasa katika mikopo. Najua kulingana na hali halisi huenda running costs zilikuwa kubwa au uendeshaji usio na tija (ubadhirifu) sasa sijui ni nini kilichotokea. Kwa kuwa wananchi wameulizia sana, naomba kupata majibu na hasa juu ya hisa zao. Nawaombeni na naamini jitihada zenu zitaendelea kuzaa matunda.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. ENG. STELA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nampongeza kaka yangu Mheshimiwa William Vangimembe Lukuvi, Waziri; na Naibu wake Mheshimiwa Angelina Mabula kwa kazi nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu ni moja tu kwa Mheshimiwa Waziri. Nyasa ni Wilaya changa, lakini ina potential nyingi hasa beach. Tunaomba msaada wa ruzuku ya upimaji wa ardhi ili kuipanga Wilaya yetu vizuri. Gharama za kodi za ardhi ni kubwa hasa kwa taasisi za Serikali ambazo zimehitaji maeneo makubwa na ulipaji wa ardhi hizo ni Serikali yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini maeneo ya Serikali kama Vyuo mfano (UDOM), Sokoine na Vyuo vingine kama FDCs ambavyo maeneo hayo ni muhimu kwa ajili ya shughuli za vitendo kwa nini yasimilikishwe na kupewa hati kwa gharama za upimaji tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri alifikirie hilo kwa niaba ya ombi la Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na nawasilisha.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu shughuli za Kamati kwa mwaka 2017.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Kamati kwa kuona umuhimu wa utalii zaidi ya wanyama pori na maeneo mengine yaliyozoeleka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu alipokuja Nyasa kwenye tamasha la utalii alielekeza Wizara ya Maliasili na Utalii kuongeza kasi ya kuhamasisha na kuwezesha utalii wa fukwe. Hivyo aliagiza iundwe mamlaka ya utalii wa fukwe. Naomba, Kamati isaidie kufuatilia kufanikisha suala hilo. Nami napenda utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutoa pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Waziri Profesa Mbarawa na Naibu Mawaziri wake wote, Mheshimiwa Kwandikwa na Mheshimiwa Engineer Nditiye. Nampongeza sana Katibu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Nampongeza Engineer Mfugale na Mkurugenzi wa SUMATRA kwa msaada mkubwa wa Jimbo langu la Nyasa, pia wa Bandari na Mfuko wa Mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru sana kwa jitihada kubwa iliyofanyika ya kuwezesha kuanza ujenzi wa barabara ya Mbinga – Mbambabay kwa kiwango cha lami na mkandarasi yupo site.
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kukubali ombi letu la dharura la ujenzi wa Daraja la Mitomoni katika barabara ya Nyoni Liparambe – Mkende. Tunashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mto umekula watu wengi sana huu kutokana na watu kuzama kwa vivuko hafifu. Tutaomba ujenzi huo upewe kipaumbele na hata katika utoaji wa fedha uwe first charge, bora tuchelewe kidogo maeneo mengine japo nayo ni muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla mahitaji ni mengi lakini kwa kuwa sungura ni mdogo itoshe kushukuru, bila kusahau mawasiliano katika Kijiji cha Kihurunga na Liparambe Ndondo na kuboresha maeneo ya Ng’ambo na Chiwande. Karibuni Nyasa!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Wizara kwa kazi nzuri iliyofanyika chini ya uongozi wake Mheshimiwa Waziri Profesa Joyce Ndalichako (Mbunge) akisaidiwa na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. William Ole Nasha (Mbunge). Pia niwapongeze watendaji wote chini ya uongozi wake Dkt. Akwilapo na Naibu wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi kwa niaba ya wananchi wa Jimbo langu la Nyasa, natoa shukrani nyingi kwa jinsi ambavyo wamelisaidia na leo nimeona tena Chuo cha VETA Nyasa kikiwa katika mpango wa kujengwa, nawashukuru sana. Naomba pia niwatajie wazee wa P4R, DPP wetu Ndugu Gerald na timu yake, kazi haikuwa nyepesi, nasema hongereni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru pia TEA kwa kuliona jimbo langu. Nawashukuru wote kwa upendo toka nikiwa nao hata nilipoondoka. Hali ya jimbo langu ilikuwa mbaya sana kimiundombinu ya elimu. Hata hivyo, nazidi kuomba juu ya Shule ya Lumalo na Shule ya Sekondari Nyasa kuhusu bweni ambalo halijaisha toka SEDP.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazidi kusisitiza juu ya umuhimu wa kuwezesha R&D Institutions ili kufanya tafiti mbalimbali zitakazowezesha uwekezaji wa tija. Kwa kuwa TIRDO ndiyo jicho la viwanda, kama ilivyo jina lake, niiombe Wizara kupitia COSTECH kuisaidia taasisi hiyo iweze kutimizia majukumu yake na hasa la kufanya mapping ya rasilimali ili hata anapokuja mwekezaji yeyote tuwe tuna taarifa za kutosha. Watafanya kwa kushirikiana na taasisi zetu za vyuo kulingana na aina ya utafiti.
Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi sana kwa Waziri Mheshimiwa Jafo pamoja na Manaibu wake, Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa ujumla.
Nashukuru kwa fedha ya Kituo cha Afya cha Mkoli na kuwekwa kwenye bajeti kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Nyasa kwa kutengewa bilioni 1.5. Naamini zitatolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupatiwa Madaktari kwenye Wilaya yangu. Naomba nimpongeze sana Dkt. Aron Hyera, Ag. DMO kwa kazi nzuri ambayo mimi binafsi naridhika nayo pamoja na wenzake ambao wapo katika Wilaya ya Nyasa. Naamini kuna siku atapitishwa kuwa kamili, mnyonge mnyongeni haki yake apewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Nyasa kupitia Kituo cha Afya cha Mbamba bay wameweza kuokoa maisha ya mama na mtoto; upasuaji 231 mpaka last week, operation nyinginezo 87 kuanza tarehe 19 Mei, 2017. Si kawaida sana lakini imewezekana, ubunifu unaofanyika ni mkubwa tumepoteza mama mmoja tu na sababu ni kuwa alicheleweshwa nyumbani hivyo kwa niaba ya wananchi wa Nyasa, nawashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nazidi kuomba uboreshaji kituo cha Afya cha Lipelambo kipo mbali sana takribani 130 kilometres (isolated); Kukamilishwa kwa jengo la utawala Kituo cha Afya cha Kuhagara pamoja na kupata wodi; na Kukamilisha majengo ya Kituo cha Afya cha Chiwanda na Ntipwili ambayo yalijengwa na wananchi angalau yaweze kutumika kama zahanati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumalizika jengo la utawala la mbamba bay secondary school; kuweka kwenye mpango ujenzi wa Kituo cha Afya Kingerikiti ili kuendelea kupunguza umbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mchango wangu hauwezi kukamilika kama sitawashukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Mbunge, Waziri wetu Mkuu, kwa kazi kubwa na nzuri kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba pia kukumbusha ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja jimboni kwangu, kama nilivyomnakilisha Naibu Waziri Mheshimiwa Josephat Kakunda aliyeongozana naye na kutoa maagizo kwa Mkuu wa Mkoa kuhusu wodi Grade A.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, nawapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake, Makatibu Wakuu na timu yote.
Mheshimiwa Spika, nilishaongea juu ya josho eneo la Linga (Keta), suala la samaki wadogo (vituwi) lifanyiwe utafiti ili Wananchi wanufaike na samako hao, kuboresha mialo, mazingira ya uvuvi, pamoja na umuhimu wa boti.
Mheshimiwa Spika, ukopeshaji/ruzuku ya engine za boti isiwe lazima kwa vikundi kwani katika vikundi wakati mwingine uwajibikaji huwa ni dogo.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, hata kama atanunua mmoja bado hawezi kuvua pake yake na ajira zitakuwa nyingi na uvuvi utaimarika. Ubinafsi ndiyo zana kuu ya kumhamasisha mjasiriamali, ‘kwamba ninanufaika vipi?’
Mheshimiwa Spika, nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Nishati
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, pongezi kubwa kwako Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa REA na TANESCO. Umeme utekelezaji unaendelea, lakini nguzo hakuna na waya. Nimeenda juzi nyumbani mafundi wanakaa wanangoja vifaa. Hata hivyo, nashukuru kwa kuongeza scope, asanteni, ila hiyo ndiyo inayoshusha performance ya utekelezaji wa Ilani.
Mheshimiwa Spika, TANESCO haina hasara kamili kutokana na kulazimika kama shirika la nchi kupeleka umeme hata maeneo yasiyolipa kwa sasa kama kichocheo cha uchumi na si tu kibiashara. Serikali inatimiza jukumu hilo kupitia Shirika lake la TANESCO.
Mheshimiwa Spika, hongereni kwa Stiglers na pia, kuwapa gesi Dangote. Viwanda oyee!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, naomba nichangie pia kwa maandishi mambo machache.
Mheshimiwa Spika, kwanza, hali ya mialo kwa upande wa Ziwa Nyasa si nzuri. Hakuna miundombinu ya barabara kiasi kwamba watu hulazimika kubeba mizigo mikubwa kichwani. Nashauri nanyi msaidie kusemea mnapokuwa na Wizara husika kama sehemu ya kuendeleza sekta hiyo.
Mheshimiwa Spika, Serikali ifikishe umeme kwenye mialo. Pia kuwe na mpango maalum wa kutambua na kulinda maeneo ya mazalio ya samaki, yajengwe madogo kila mualo. Pia kuwe na utaratibu wa kutambua ujuzi wa wavuvi (RPL) ili kuwatia moyo kama ilivyo kwenye ujenzi, useremala na kadhalika.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya fukwe zina mmomonyoko mkubwa wa ardhi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu mifugo; angalau kila kata kuwe na Afisa Mifugo mtaalam mmoja ili kuwashauri wafugaji pamoja na kutoa huduma za kitabibu hali ya sasa ni kuwa kila mfugaji atumie uzoefu wake.
Mheshimiwa Spika, ili kuboresha matumizi ya Ranchi za Serikali wananchi wakatiwe vipande vya hekta 50 hadi 150, wakodishwe kwa bei ndogo lakini Serikali iendelee kumiliki asset yake ya ardhi kwani ni vigumu kupata tena maeneo makubwa kama hayo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Madini
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kumshukuru Mungu kwa siku hii ya leo, lakini vilevile nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Madini pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri ambayo wamefanya na hivyo kuifanya Tanzania kufaidika na madini kama ambavyo imekuwa ikitarajiwa.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia katika maeneo machache kama ifuatavyo na ikizingatiwa kuwa hayo maeneo pia yanahusu Wizara ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Spika, suala la Mgodi wa TANCOL; ni kweli katika maneno ambayo yamezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge kwamba Tanzania tunawekeza na tunawaleta wawekezaji kwa lengo la kuhakikisha kwamba kunakuwa na tija na mafanikio ya kifedha, lakini vilevile mafanikio mapana katika uwekezaji unaofanyika. Katika mradi wa TANCOL, mafanikio tuliyoyapata ni kwamba mpaka sasa makaa ya mawe ambayo yanatumika katika viwanda vyetu hususan vya cement yote yanatoka Tanzania na mengine tumekuwa tukiuza hata nje ya nchi, kwa hiyo yameleta faida katika kuwezesha kupata malighafi katika viwanda vyetu vya cement.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, nikiri tu kwamba taarifa ambayo ilikuwa inazungumzwa ambayo imetokana na taarifa ya CAG, sisi kama Wizara tunayo na hatujaifumbia macho. Tayari tulishaunda Kamati ya kufuatilia namna gani tunatekeleza maoni ya CAG na kupata ni namna gani au kwa kiasi gani yashughulikiwe. Kwa hiyo, kuna mambo ambayo yanatakiwa yashughulikiwe katika mpango wa muda mfupi lakini mengine yalikuwa yanahitaji tafakari pana zaidi kwa muda mrefu. Suala hilo lipo katika mikono salama na niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge pale tutakapokuwa tumekamilisha hayo tunayoyafuatilia watapata taarifa ambayo inakusudiwa.
Mheshimiwa Spika, vilevile niseme tu kwamba, wao wenyewe TANCOL pamoja na kampuni zile ambazo walikuwa wanazitumia katika kuwezesha kutoa huduma wamekuwa na migogoro. Kwa mfano, katika Kampuni ya Caspian walipelekana mpaka mahakamani lakini wakaamua kufanya makubaliano nje ya mahakama na hivyo wakakubaliana kulipa zaidi ya shilingi milioni nane kwa ajili ya hayo makubaliano yao na hasa katika lengo la kuvunja mkataba wa kuendelea kuchukua huduma kwa hao Caspian. Kwa hiyo hayo ni mambo tu ambayo yalikuwa yanajitokeza katika migogoro iliyokuwa inaendelea. Niwahakikishie tu Wabunge kwamba kwa hali iliyopo sasa kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano hatutakubali uwekezaji wowote usio na tija na hivi wote tunaangalia Taifa letu katika mtazamo huo.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mchuchuma na Liganga ni kwamba kweli huyo mwekezaji alipatikana na makubaliano ya awali yalikuwepo na hata kwa upande wa nchi kama Serikali tayari tulianza hata kuwekeza katika miundombinu kama ya barabara ili kuwezesha mradi huo uweze kuanza, lakini kama ambavyo nimezungumza na sheria ambazo tulikuwa tumetunga za kusaidia nchi inufaike zaidi na rasilimali zake, tulikuja kuangalia na tukaona kwamba katika baadhi ya taarifa ambazo mwekezaji alikuwa amezitoa hasa kuhusiana na madini zilizokuwepo zinaonekana haziendani na uhalisia kulingana na taarifa zingine tulizozipata kupitia utafiti wetu wa source nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa misingi hiyo, vilevile hata katika upande wa kuchukua mikopo, mwekezaji alizungumza kwamba ili apate mikopo kwa kupitia dhamana ya mashapo yaliyopo, sasa kama ndivyo yeye amekuja na nini? Kama dhamana inatokana bado na rasilimali ile ile ambayo tunayo sisi wenyewe?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kuna mambo ambayo inabidi tuendelee kuongea na mwekezaji, tuweze kutafakari kama tutakuwa tumekubaliana basi ataendelea na kazi, lakini kama tutakuwa hatujakubaliana na pale Serikali inapoona kwamba hapa hakuna tija ya huo uwekezaji, basi sisi tuwaambie tu kwamba hatutakubali kuendelea nae kwa sababu msiimamo wa nchi utabakia vilevile kwamba kila uwekezaji lazima uwe na tija na manufaa mapana ya wananchi lakini pia na upande wa muwekezaji kuwe na win win situation. Kwa hiyo, hiyo ndiyo hali halisi na sisi hatutakubali kuja kuwajibika hapa kwa sababu eti tuliwekeza tu kwa ajili ya kuwafurahisha watu. Lazima tujipange kwa kupata ufumbuzi wenye tija.
Mheshimiwa Spika, baada ya maneno haya, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, kwanza niwapongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu wake Makatibu Wakuu na timu yote ya Wizara.
Mheshimiwa Spika, hali ya ushirika katika Wilaya ya Nyasa si nzuri. Kuna malalamiko makubwa ya wakulima wa kahawa hasa AMCOS za Nambawala na Luhangalasi.
Mheshimiwa Spika, Bonde la Lituhi lina potential kubwa ya kilimo cha umwagiliaji na ndio eneo linalotegemewa zaidi kwa kilimo. Changamoto ni ukosefu wa miundombinu.
Mheshimiwa Spika, nashauri Serikali isaidie kutatua changamoto hiyo.
Mheshimiwa Spika, eneo nililolitaja la Lituhi kwenye orodha ya skimu mliyotoa kwenye kiambatisno cha bajeti limetajwa kama Ruhuhu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa kupata muda huu wa kuweza kuchangia. Nianze kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa jinsi ambavyo anavyotuongoza. Pia niwashukuru ndugu zetu wa Kenya kwa jinsi ambavyo wamempokea vizuri Mheshimiwa Rais wetu, basi nasi tunafarijika kwa faida ya pande zote mbili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianzie kwanza na Jimbo langu, niishukuru sana Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kutuwezesha kupata Chuo cha VETA ambacho ningeomba sasa kiweze kuanza na kuondoa kero ya ajira hasa kwa vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, naomba kuna shule ya Mbambabei High School ambayo Wizara iliisaidia lakini sasa hivi kuna jengo pale Jengo la Utawala na Maktaba ambalo ni jengo moja kwa muda mrefu halijaweza kukamilika. Niwaombe kupeleka fedha ili jengo hili sasa liweze kutumika na kuwasaidia hawa wanafunzi ikizingatiwa kwamba shule hii toka imeanza imefanya wanafunzi wake wafaulu vizuri na kweli inashika katika nafasi nzuri za kitaifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna maboma ambayo yalikuwa yamepewa fedha ya mabwalo na michoro maalum, lakini imeonekana kwamba zile fedha huwa hazitoshelezi kujenga hayo mabwalo. Kwa hiyo niombe tumalizie hayo mabwalo kwa sababu fedha nyingi za Serikali zimeshatumika na nguvu za wananchi, hivyo ni vema tuyamalizie. Kuna pale Nyasa, kuna shule ya Engineer Stella Manyanya na Liuli ambayo inaendelea sasa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba nimefurahishwa pia na michango mbalimbali ambayo Waheshimiwa Wabunge wenzangu wametangulia kuzungumza. Michango ambayo imekuwa, imetazama kwa kina kiasi kwamba pengine kama itafanyiwa kazi inaweza ikarekebisha sekta hii ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, nipende kuwakumbusha ndugu zangu hawa na wananchi kwa ujumla, si kwamba nchi yetu imekuwa haina mikakati maalum ya elimu, tatizo ninaloliona ni uendelevu na wakati mwingine kufanya maamuzi ambayo yanakuwa, yaani kama vile mmoja hana taarifa za kutosha, kwa hiyo ikifikia kufanya maamuzi akimsikia wa kwanza, wa pili wamezungumza, basi maamuzi yanafanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano katika hili suala la ujuzi linalo zungumzwa siku zote, hili suala si jipya, suala la ufundi si jipya tumekuwa na shule maalum za sekondari za ufundi, lakini shule hizi kwa sababu moja au nyingine, naweza nikasema zilifanyiwa uharamia, vifaa vikauzwa, wanafunzi pale wakawa hawafundishwi tena ufundi. Vile vile unakuta sasa hivi hizo shule zilikuwa kuwachukua sasa wanafunzi wa elimu ya sayansi ya kawaida. Ukifuatilia ni kwa nini? Ndiyo maana nasema pengine kwenye Wizara hii ipo haja sana hata mambo ya usalama yaimarishwe, kwa sababu unaweza ukapewa ushauri mwingine ambao unajua baada ya miaka mitano utaua kabisa ile dhamira ya nchi kuipeleka mahali fulani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano mimi binafsi niseme kwamba nilikuwa kwenye Wizara hii na ninapozungumza sijaribu kusema kwamba hakuna kinachofanyika, Mawaziri wanafanya kazi kubwa na wataalam wanafanya kazi kubwa, lakini hayo ndiyo niliyoyaona kipindi hicho, vyuo havina Walimu wa ufundi. Leo hata ukianzisha vyuo vya ufundi, hawa Walimu wapo kiasi gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna ile hali ya mihemko, kwa mfano kuna wakati ilisemwa kwamba huyu amemaliza Advanced Diploma, ya nini? Labda umeme au ufundi, huyu mshahara wake utakuwa mdogo kuliko yule wa degree. Nani atakuwa mjinga akasome Advanced Diploma ambayo ni competence base aache kwenda kwenye degree na uwezo anao? Kwa hiyo hayo ni mambo ambayo yanasababisha watu kufanya maamuzi yasiyo sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunazungumza kwamba Watoto wengi wakimaliza vyuo hawawezi kujiajiri, ni kweli hata wakikaa chuoni hawataweza kupata ujuzi wote, lakini hayo mazingira ya kujiajiri huko kwenye maeneo yetu yakoje? Nani anafurahia sasa hivi aende kujiajiri kwenye uvuvi ambapo uvuvi bado anatumia kale kamtumbwi ambako hajui kama atapona. Kwa hiyo lazima tujenge mazingira mazuri ambayo yanamfanya huyu mtoto akimaliza chuo aweze kwenda kujiajiri. Bila kufanya hivyo tutakuwa tunazungumza lakini hatutafika. Kwa hiyo ninachoomba, wakati utakapofikia wa kufanya marekebisho au maboresho mbalimbali, ni vema kuangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulianzisha chuo kwa mfano Chuo Mahiri kile cha Nelson Mandela, lakini unapokuja kugawa rasilimali unakuta chuo kile ambacho unakitaka kifanye mambo makubwa ya umahiri kinawekewa bajeti sawa sawa na chuo kingine ambacho kinafanya mambo ya kawaida. Kwa hiyo kama hatutakuwa tunawekeza kulingana na mahitaji halisi ya kumwezesha huyu mwanachuo aliyepo kwenye eneo fulani, tutakuwa tunapoteza muda.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya kiufundi, kisayansi au utafiti mara nyingi tunaona uchungu sana kuyapatia fedha, unaona kama vile unapoteza, ukimpa fedha akanunue sijui ka-resister, ka-transistor unasema mbona hela nyingi hii naenda kununua ka-resister, lakini hatujui kwamba katika mafunzo ya aina hiyo lazima mtu ajue kuharibu, ajue kufanya kitu kikawa sawa. Atajua kitu kimekuwa sawa baada ya kujifunza kwa njia zote. Amekosea, ameharibu lakini baadaye anakuja kupata jambo ambalo ni jambo zuri. Kwa hiyo tusipowekeza kwenye maeneo hayo tuseme tutakavyosema hatutakwenda kufanikiwa. Pia tuhakikishe kwamba tunawekeza kwenye wabobezi wa maeneo hayo ya kazi za vitendo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nitakuwa mchoyo wa fadhila nisiposema kwamba nchi yetu imeweza, imefanya mambo mengi. Siku za nyuma ulikuwa hata nyuma tunazojenga ukiziangalia zipo ovyo ovyo tu, lakini siku hizi baada ya kuwa na hao vijana ambao wengine wametoka VETA, wanajifunza maeneo mbalimbali hali yetu ya kiuchumi na kiujenzi au uwekezaji imekuwa ni tofauti na ilivyokuwa. Kwa hiyo lazima tujipongeze kwa yale ambayo tumeyafanya vizuri, lakini tuendelee kuboresha katika maeneo yale ambayo bado hayajawa vizuri. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niseme tu kwamba…
NAIBU SPIKA: Ahsante sana!
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa nafasi hii, pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa mema yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianzie kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa kwanza Mwanamke Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, michango mingi iliyochangiwa na mimi nimeipenda sana naiunga mkono, mchango wangu ambao nataka niunge mkono kwa jitihada zote ni suala la kuhakikisha kuwa Wizara hii inapewa fedha za kutosha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba jeshi linaweza kufanya tafiti muhimu za kisayansi ambazo zinawezesha kulifanya Taifa hili liwe na nguvu zaidi.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba ulinzi uliokuwepo katika siku za nyuma ni ule ambao hasa tulikuwa tunaenda, tunajipanga zaidi kwenye mipaka yetu kuona kwamba labda adui atakuja kwa njia ya silaha ya moja kwa moja. Atakuja na SMG, atakuja labda pengine na silaha ya aina fulani, lakini vita vya sasa hivi ni vya tofauti, ni vita ambavyo hata adui yako humuoni, lakini upo naye jirani, ni vita ambayo inaweza ikapitia teknolojia au hizi tafiti za kisayansi zikaangamiza Taifa wakati nyinyi wenyewe hamjawa na taarifa za kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jeshi letu limeonesha nguvu kubwa sana katika mambo mbalimbali, mimi ningetamani kuona kwamba hata katika Hospitali hii inayotarajiwa kujengwa katika eneo la Msalato basi Jeshi liweze kupewa na sehemu ambayo itaweza kufanya tafiti kubwa za kibailojia ambazo zitaweza kushirikiana na taasisi nyingine za kimataifa na ndani ya Taifa kuweza kuleta matokeo chanya zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba pamoja na hayo kwa sababu Jeshi letu halijaanza leo, yawezekana katika baadhi ya sheria tulizonazo na sera zilizopo haziwezeshi kufanya hayo, kufanya hizi kazi za mashirikiano na taasisi nyingine ndani ya nchi na nje ya nchi. Kwa hiyo, ni vyema tuziangalie pia sheria zetu ili ziwezeshe kufanya Wizara hii kupitia taasisi zake au majeshi yake kuweza kufanya kazi hizi za kitafiti, kazi hizi za kiuwekezaji na kuwezesha tuweze kupata mafanikio makubwa zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kwanza pamoja na kwamba umetolewa ufafanuzi mkubwa, lakini niseme kwamba hawa ndugu zetu wanajeshi wanatakiwa pia kufahamu namna ambavyo sekta mbalimbali zinafanya kazi ikiwemo masuala ya kisiasa, kwa sababu wakati mwingine unakuta kinachosababisha mpaka vita ikatokea mahali ni masuala ya kiuchokozi tu, au masuala ambayo mengine yangeweza kudhibitiwa mapema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hawa wanapokuwa wanapata nafasi ya kushiriki katika maeneo mbalimbali ya kiuongozi inasaidia pia kurudisha mrejesho kwenye taasisi zinazohusiana na masuala ya kiulinzi ili ziweze kujipanga vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi katika suala la ulinzi mipakani; kwanza nianzie kuzungumzia hili suala la mpaka wa Ziwa Nyasa kwa upande wa Tanzania na ndugu zetu kule Malawi. Hili suala ni la muda mrefu, watu tunakaa tunahofu, hatujui kinachoendelea, uwekezaji unakuwa wa shida basi niombe pengine jitihada zifanyike zaidi ili suala hili la mpaka liweze kukamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini wakati huo huo mimi nafahamu mlinzi wa kwanza katika nchi ni raia mwenyewe ni mwananchi mwenyewe, lakini sasa utakuta katika maeneo ya baadhi ya mipaka ikiwemo mpaka katika eneo la Ziwa Nyasa hali ya barabara siyo nzuri, ukitoka kule Chiwindi ukifika mpaka Lituhi uende mpaka Lipingu, Manda, Lipingu ufike mpaka Matema hali siyo nzuri, afadhali hata sisi tuna barabara ya vivumbi kidogo, lakini wenzetu unakuta wanategemea maji. Kwa hiyo ni vema ile barabara ikapewa kipaumbele na sema hayo pamoja na Wizara ya Ujenzi lakini hao Wizara hii ndiyo wadau wakuu wa kufaidika barabara itakapokuwa imeimarika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile eneo la Mpepo mpaka Dapori nalisemea kila siku, jamani kuna changamoto kule kubwa, hivi ninyi ndugu zetu ninyi hamshauri ninyi si mnashirikiana na hawa wenzetu wa barabara! Kwa nini hali imekuwa mbaya vile? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba katika masuala ya kuimairisha ulinzi eneo lile ni vyema lifanyiwe kazi ikiwemo daraja la Mto Ruvuma pale Mitomoni ili kuhakikishwa kwamba usalama wa maeneo yale unaimarika na unakuwa ni mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niende katika suala la haki za binadamu lakini pia kutoa fursa sawa kwa wote. Kwa siku za nyuma uwe mwanajeshi au uwe polisi ukishakuwa mfupi kama mimi Engineer Manyanya hawakuchukui, lakini siku hizi hatuangalii urefu tu, hatuangalii maumbile tu, hawa ndugu zetu wenye ulemavu mbona hawapati fursa za kuingia Jeshini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hatusemi waende wakapigane mstari wa mbele, lakini kichwa chake na mikono yake yawezekana kina uwezo mzuri katika masuala ya ICT, katika masuala ya kimkakati na wakafanya vizuri tu. Kwa nini sasa Serikali isiangalie kuona namna bora ya kuweza kusaidia hata kundi hilo hata kama hawatawekwa katika nafasi hiyo ya kwenda kwenye mstari wa mbele, lakini waweze kufanya kazi ambazo pia zinaweza kusaidia katika kutoa maarifa na mambo mbalimbali yanayohusiana na kuimarisha Jeshi letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naamini inawezekana, hatuwezi kusimamia tu sheria zile za zamani zinasema kwamba wewe tumekuona mkono wako umekaa hivi basi wewe huwezi kwenda. Hapana, kuna watu tena watu wenye ulemavu Mungu amewapa vipawa vikubwa sana, unaweza kukuta kwamba huyo ndio akawa master mind mzuri sana. Kwa hiyo, mimi nasema hili suala tuliangalie ili hilo kundi na lenyewe liweze kusaidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, katika haya masuala ya JKT hawa vijana ambao wako barabarani wanaomba na wenyewe waweze kuwekewa utaratibu wa kusaidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, si jambo la heshima kuiona Tanzania bado inakuwa na watu wengi barabarani wanaombaomba. Hapana hawa vijana wanaweza wakasaidiwa, huyo anayesemekana labda hana mzazi yawezekana kweli wazazi wake wote wawili hawapo, lakini pengine kuna wale wazazi ambao hawajali hao ni Taifa.
Kwa hiyo, mimi niombe kupitia Jeshi letu tuone pia uwezekano wa kunusuru eneo kama hilo, lakini kwa Serikali kutenga fungu maalum la kusaidia Wizara hiyo kuweza kusaidia masuala kama hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kwa kweli pamoja na yote niliyozungumza mimi nalipongeza sana Jeshi letu, napongeza sana sana Wizara hii inavyojitahidi katika kutekeleza majukumu yake. (Makofi)
Nampongeza sana Mheshimiwa wetu Waziri Ndugu Elias kwa kazi kubwa ambayo anaifanya, kijana mpole, lakini mambo yako makubwa. Mimi nakupongeza kwa kweli, naona kwamba ndio maana hata Jeshi letu linaendelea kutulia, lakini nizidi kusisitiza kuomba kwamba hao ndugu wawezeshwe na kwa sababu wakiwezeshwa watafanya kazi kubwa zaidi ikiwemo kuwasaidia vijana waliopo vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na sio wabakie tu kufundisha migambo kule vijijini, mbali ya mgambo wafundishwe hata hizi shughuli za kujiajiri kule vijijini, isiwe tu kutembea, kukimbia, root matching, hapana; lakini pamoja na masuala ya kiuchumi wakati wanapofundishwa masuala ya mgambo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo niliyozungumza naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi ambayo kwa kweli nilikuwa nimeshakata tamaa kwa ajili ya muda, lakini nashukuru sana kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami pamoja na wenzangu kama walivyotangulia, nianzie kwa kumshukuru Mungu na pia niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri Lukuvi pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Dkt. Mabula na Katibu Mkuu, Mheshimiwa Mary Matondo ambaye tulikuwa naye kwenye Bunge la Katiba, alisaidia sana katika rasimu ile ya Katiba; vilevile Naibu Katibu Mkuu, ndugu yetu Nicolaus Mkapa pamoja na timu yao yote ambayo inawasaidia katika ngazi mbalimbali za kiutendaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee zaidi kuhusu gharama za kuhaulisha ardhi. Suala hili nililizungumza pia kupitia swali langu ambalo niliuliza hapa Bungeni na likapata majibu tarehe 9 Aprili, 2021 na lilikuwa swali Na. 329. Nashukuru sana kwa majibu ambayo nilipewa wakati huo, kwa hiyo, niko katika mwendelezo wa kuendelea kutetea juu ya jambo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna changamoto kubwa sana. Pamoja na kazi kubwa inayofanywa vizuri na Wizara hii, lakini changamoto ya kodi zinazotozwa katika kuhaulisha ardhi, zinafanya kuwe na kikwazo cha watu kuhaulisha ardhi zao au mali wanazokuwa wamezipa, matokea yake wanabaki kuwa na mitaji ambayo ni mfu. Kwa sababu unapokuwa na ardhi uliyonunua, lakini iko kwenye jina la mtu na unashindwa kuihaulisha aidha kwa sababu umekosa fedha za kufanyia hivyo, basi inakufanya uwe na kitu ambacho siku yoyote yule ambaye alikuuzia akigundua pengine hujabadilisha, anaweza akaja kukudai kwamba hii bado ni mali yangu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye majibu nilifahamishwa kwamba kuna ada ya upekuzi 40,000, pia kuna asilimia 0.02 ambayo ni ada ya uthamini wa hiyo mali inayokuwa imepatikana. Ada ya taarifa shilingi 40,000; ada ya kibali shilingi 80,000/=; na ada ya usajili 1% ya thamani ya hiyo mali. Baada ya kulipa hizo, kuna kodi sasa ambayo inalipwa TRA, asilimia 10 ya thamani ya mali uliyoipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka tunaweza tukaona ni jambo la kawaida. Ukisema kwamba unaponunua, basi tenga na fedha ya kulipa hayo yote, lakini siyo rahisi kiasi hicho. Tukumbuke kwamba wakati mwingine mtu anauza kitu chake siyo kwa sababu alitaka kuuza, bali ni kutokana na shida aliyonayo au changamoto fulani inayomkabili. Kwa hiyo, anaweza kuuza hata kwa bei ambayo ni ya chini isiyotarajiwa, sawa na minada inavyofanyika. Hata hivyo unakuta kwa yule aliyenunua, akitaka kuhaulisha, huyu mthamini au mpekuzi anapoenda atatoa thamani inayodaiwa inalingana na hali ya sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna mzee mmoja nilimkuta akilalamika anasema kwamba ameambiwa thamani ya eneo kwa mfano la hapa maeneo ya St. Gasper ni takribani shilingi 80,000/= kwa square mita. Sasa unakuta katika kile kiwanja chake kidogo kilikuwa kinafikia karibu shilingi milioni 80. Mpaka akasema basi, nipeni mimi hiyo shilingi milioni 80 ili niwaachie hicho kiwanja. Kwenda kulipa asilimia 10 ya huo mtaji ambao anasema kwamba ameupata, inakuwa ni gharama ambayo mtu hawezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile siku za nyuma elimu haikutolea kiasi cha kutosha. Unakuta mtu labda pengine mstaafu alinunua kiwanja chake kutoka kwa mtu ambaye wakati huo tuseme alikinunua kwa shilingi milioni moja na baada ya kukinunua, akakaa akapata kiinua mgongo chake akajenga, anasema nikabalishe, anaambiwa ahaa, sasa pamoja na hiyo nyumba uliyojenga, pamoja na hicho kiwanja, sasa gharama imeshakuwa shilingi milioni 150, ulipe asilimia 10 ya huo mtaji uliokaa hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unakuta ni mambo ambayo ni kweli kwa mujibu wa Sheria ya Kodi yako sawa, lakini nadhani ni vema tukayaangilia upya hasa kwa hawa wananchi wanyonge ili na wenyewe waweze kumiliki mitaji yao kihalali. Hata kwenye jibu la Mheshimiwa Waziri wakati ananijibu, alisema katika sehemu kubwa inayopewa malalamiko ni hiyo ya capital gain, yaani mtaji uliopatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, hatusemi kwamba hatujui athari yake kimapato, tunajua, lakini sasa hayo mapato hayakusanywi vizuri, kwa sababu hawa watu wanashindwa kuweza kulipa hizo gharama na matokea yake sasa hata kama anataka kukopa, anakopa vipi ili aweze kuwekeza wakati huo mtaji uko kwa jina la mtu mwingine?
Mheshimiwa Naibu Spika, hili suala ni muhimu na kwa sababu nilijibiwa siku ile kwamba watazungumza na Wizara ya Fedha ili kuweza kupata namna bora zaidi ya kulishughulikia ikiwezekana, sasa nimeangalia kwenye taarifa yao sijaona mahali palipozungumziwa suala hili. Ndiyo maana nikaona kwamba nilikumbushe tena kwamba kuna changamoto kubwa, watu wengi wana viwanja, wana mashamba, wana majengo yako kwenye hayo mashamba, lakini yanasomeka kwa jina lingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya hiyo sasa inatokana na nini? Hata ukitaka kufuatilia, unaweza kukuta hata anuani iliyopo pale ni ya mtu mwingine matokeo yake sasa hata kufuatilia masuala ya mapato kwa ujumla wake inakuwa ni shida. Naomba kama tulivyofanya hayo katika masuala mengine, mfano magari wakati ule yalivyokuwa na kero za kodi zile tukafanikiwa, basi na hili tuliangalie hasa kwa hawa wananchi wanyonge wale ambao wanahitaji kuwekeza, wanaohitaji nao wapate mtaji ambao ni halali kupitia hizi mali za rasilimali ya ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nilikuwa naungana na wenzangu katika suala la Mabaraza ya Ardhi. Katika baadhi ya maeneo hilo suala bado ni tatizo, kwa sababu wale wazee wanaendelea kushughulikia mabaraza hayo unakuta wengine ni ndugu zao, wengine ndio anakuwa mtu ambaye sio ndugu yake. Kuna wakati unakuta wao wenyewe wanakuwa ni sehemu ya mgogoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi binafsi kwenye Kijiji cha Kata ya Kihagana, pale Tumbi na Kihagana, nina migogoro iliyodumu zaidi ya miaka nane, mtu anatoka hapo kwenye Baraza la Kata anaambiwa wewe ndio umeshinda, wakienda Wilayani huyu ndio kashinda; wanaenda Mkoani wanarudi. Mwingine anaanza tena upya kutaka rufaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaomba pia Mheshimiwa Waziri katika ziara zake za Mkoa wa Ruvuma atusaidie kumaliza pia hii changamoto ya kesi hizi; ya kwanza ni ya Bwana Mateso na Binti mmoja Nombo, pia kuna ya akina Ndiu na ya tatu niliisahau ya Mama Lambo, zimedumu muda mrefu, ni kero. Yaani ukifika pale, Mbunge kazi yako ndiyo hiyo. Ukiongea na huyu, anakwambia wewe unataka kumsaidia fulani. Naomba kwa kweli Mabaraza ya Ardhi sasa hivi wasomi ni wengi, kwa nini tusiyaweke sasa yakawa katika sura bora zaidi kuliko iliyopo sasa hivi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba pia nizungumzie suala la mgogoro wa Lipalamba, naomba pia kwenye Hifadhi ya Lipalamba ule mgogoro bado unafukuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo, nakushukuru sana. Ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia. Pia nimpongeze sana injinia mwenzangu Mheshimiwa Ulenge kwa mchango wake mzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianzie kuipongeza sana Wizara hii lakini kuwapongeza watanzania wote kwa jitihada za pamoja tulizofanya kuhakikisha kwamba Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) halipelekwi kuwa ni shirika la mtu binafsi limebakia kuwa ni shirika la Tanzania kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya Watanzania. Kazi nyingi zinazofanywa na shirika hili kwa kweli ni za kuchochea maendeleo na siyo faida kama faida ilivyo. Ndiyo maana kwa muda mrefu limekuwa halizalishi faida kwa ajili ya kuangalia wananchi wote wenye uwezo na wasio na uwezo. Tunafurahi hali inavyokwenda sasa TANESCO wanaanza kutengeneza faida. Kwa hiyo, natoa pongezi sana kwa Wizara pamoja na shirika hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na suala la kwamba mpaka sasa tumeshindwa kufikia malengo tuliyojiwekea ya kupata megawatts 5,000. Niseme tu kwamba mimi naona tumekwenda vizuri nikiwa kama mjumbe wa Kamati hii ni kwamba kwa miaka takriban 60 ya toka Uhuru wetu tulikuwa tukiongeza wastani wa megawatts 26.7 tu katika grid yetu kwa maana kwamba tulikuwa na megawatts 1,605 tulizonazo sasa lakini hizo zimefikiwa baada ya miaka 60 sasa, umri wa mtu kustaafu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kwa sasa kupitia hii mikakati tuliyojiwekea ya kuanza kuzalisha umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere na maeneo mengine tayari mwaka 2022 tunaongeza megawatts 2,115 kwenye Grid ya Taifa. Jambo hili ni kubwa sana, unaweza ukawa na malengo lakini kuyafikia unayafikia kwa kiasi gani. Malengo haya yanatufikisha sisi kwa lengo tulilojipangia kwa asilimia 74 siyo kitu kidogo, ni kitu kikubwa lazima tujipongeze kwa kile ambacho tumeweza kukifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niwaombe TANESCO watu vijijini sasa hivi maendeleo yao yamejiwekeza sana kwenye umeme, haitoshi tu kupitisha laini halafu wananchi hawapati umeme lazima sasa lipatikane fungu la kutosha kwa ajili ya kuweka umeme wa laini ndogo yaani LV lines. Hilo ndilo eneo ambalo sasa hivi kwa kweli halipati fedha za kutosha. Wanakijiji hawapendi tu kuona kwamba line imepita hapa wanataka kutumia umeme. Kwa hiyo, kwa fedha hii inayotengwa lazima fedha za kutosha zipelekwe kwa ajili ya kuongeza wire hizi ndogo yaani LV lines. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine naomba niwasaidie ndugu zangu jana nilimsikia Mheshimiwa Mbunge Joseph wa Ukerewe akizungumzia juu ya vile visiwa vinavyopata umeme kwa bei kubwa sana takriban Sh.2000. Kwa muda mrefu shirika letu lilikuwa ndio shirika pekee linalosambaza umeme mijini na vijijini sasa sehemu moja wanapokuwa wanapata umeme kwa bei kubwa sana nimejiuliza kwa nini? Kumbe ni kwa sababu wale wana-independent power producer yaani wanapata umeme kupitia solar, ni mtu binafsi amewekeza, kwa hiyo, lazima umeme utakuwa ghali. Sasa niwaombe TANESCO kwa sababu wao wana umeme ambao unapatikana kutoka kwenye maji na vyanzo vingine na umeme huo waupe either ruzuku au waununue wao halafu wananchi wauziwe umeme kwa bei sana na watu wa maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho, sheria ya EWURA irekebishwe iweze na yenyewe kuwa na vituo vya mafuta vijijini. Tumechoka kuona chupa za petrol kule vijijini halafu zitakuja kuleta madhara tutakuja kuulizana hapa. Watumie formula hii hii kwa sababu tuna Shirika letu la Kusambaza Mafuta Vijijini ili sasa nao waweze kuwa na vituo vidogo vidogo huko vijijini tuondokane na mafuta ya kwenye chupa kwa sababu pikipiki na fursa nyingi ziko huko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri Engineer Masauni na wasaidizi wake wote.
Mheshimiwa Spika, kuna baadhi ya magereza nchini ni ya zamani sana na ni hatari kwa maisha watu. Mfano ni Gereza la Sumbawanga Mjini.
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Nyasa ni kubwa na ina milima mingi. Urefu wa mwambao ni kilometa 157, umbali ukanda wa juu hadi Mitomoni kilometa140. Pia sisi tuko mpakani na Msumbiji na Malawi.
Kuhusu magari, yaliyopo ni chakavu. Mimi mwenyewe niliona umuhimu nikawachangia pikipiki nne.
Mheshimiwa Spika, tafadhali naomba msaada wa gari na nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kuwapongeza sana Mheshimiwa Jumaa Aweso, Mbunge na Waziri wa Maji na Naibu wake Mhandisi Maryprisca Mahundi, Mbunge kwa kazi nzuri ya kuwahudumia wananchi kupitia Wizara wanayoiongoza.
Mheshimiwa Spika, nawapongeza pia Katibu Mkuu Mhandisi Anthony Sanga na Naibu wake Mhandisi Nadhifa Kemikimba pamoja na watendaji wote wa Wizara akiwemo kijana mdogo Engineer Maduhu anayekaimu Wilaya yangu ya Nyasa.
Nawashukuru kwa miradi ya maji inayoendelea jimboni kwangu, hata hivyo nina maombi yafuatayo; kwanza ni kuhusu ukanda wa chini (mwambao wa Ziwa); Wilaya yangu ina milima na ni kubwa sana. Gari iliyopo ni chakavu sana. Tunaomba gari ili kufuatilia vizuri utekelezaji wa miradi.
Pili, kutatua kero ya changamoto ya maji, utekelezwe mradi wa Ngumbo na Liwundi, kukarabati mradi wa Kihagara, kuongeza upatikanaji wa maji katika Mji wa Mbamba Bay na vijiji vyake.
Mheshimiwa Spika, tatu, kupeleka maji kijij cha Mtupale hadi Chiwindi.
Kwa upande wa ikanda wa juu; kupeleka maji Kijiji cha Malayalam, Kimbango, Litindo Asili na Luhangalasi (Kata ya Luhangalasi); kupeleka maji Kijiji cha Luhindo; kupeleka maji Kijiji cha Uhuru na Mipotopoto na kupeleka maji Kijiji cha Mitomoni.
Mheshimiwa Spika, tunasisitiza matumizi ya maji ya Ziwa Nyasa.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru na naomba kuwasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nianze kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nitumie nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Taifa letu. Taifa la Tanzania limeendelea kuwa imara wakati wote. Lakini tunamshukuru zaidi kwa sababu Mwenyezi Mungu ameendelea kutupa viongozi wazuri toka kipindi cha Uhuru mpaka sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunasema ahsante sana Mwenyezi Mungu kwa sababu pia hata sisi waja wake tumeamua kumtumainia. Na wanasema uchaji wa Mungu ni baraka kuliko vyote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo furaha sana baada ya kuona kwamba tulikuwa na kiongozi shupavu, jemedari, marehemu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Lakini Mungu alimuonesha kumchagua mtu wa kuwa mgombea mwenza wake ambaye pengine Mwenyezi Mungu alifunga tu kauli ile ya kumwambia kwamba huyu ndio atakayekurithi, lakini alihakikisha anapata mtu ambaye ni mwenye maadili, mwaminifu, mchapakazi, mshauri sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hivyo, hata ilipofikia kwenye kubadilisha uongozi, hajapata nafasi kwamba eti aende kozi ya kumfundisha kuwa Rais; kuna mahali amefundishwa jamani? Hakuna. Ameendelea kuchukua kasi ileile, ameendelea kuchukua uthubutu uleule, ameendelea kututia moyo na kuonesha kwamba Taifa liko katika misingi ileile. Tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haitoshi, alivyoingia madarakani amejipambanua wazi akasema suala la rushwa silitaki, na sitaki kusikia… shetani na ushindwe! (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maandiko pia tunaambiwa kwamba rushwa ni udhalimu na utafutwa mbali, bali uaminifu utakaa hata milele. Ndiyo maana rushwa ameikataa toka asubuhi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, niseme kwamba, alisema, sitaki mapato ambayo ni ya dhuluma. Na maandiko pia yanaungana na hilo, yanasema kwamba mapato ya mwovu – maana yake ukifanya dhuluma ni mwovu – yatakauka kama mto, na kama ngurumo penye mvua inayopita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hayo yote napenda tu kuunganisha hali halisi ya viongozi wetu walivyo wanyofu, na hasa huyu sasa tuliyenaye, naye amekwenda katika mstari huohuo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu amesifiwa kwa mambo mengi, lakini mimi napenda sana ile misemo yake, naifuatilia, mara kwa mara anafundisha kwa mifano na kwa misemo. Kuna wakati aliwahi kusema kazi lazima iendelee. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kazi iendelee. Lakini mimi naongezea iendelee na nani, na mama Samia Suluhu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haikuishia hapo, akasema kuwe na upepo kusiwe na upepo, jahazi lazima likafike. Jamani mambo si haya, jahazi linakwenda kufika. Kwa hiyo, baada ya kutafakari haya nimejirejesha pia katika malengo endelevu ya maendeleo ambayo tunatarajia tuondoe umaskini kufikia 2030. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba bado kuna tofauti kubwa sana ya kimaendeleo kati ya watu walioko mjini na walioko vijijini. Ukifuatilia unakuta kwamba hata hali ya umeme bado vijijini ilikuwa iko chini, sasa hivi ndiyo tunakwenda kumaliza. Lakini hali ya maji bado ni changamoto kubwa, hasa katika maeneo ya vijijini; hali ya barabara na miundombinu mingine ni hivyohivyo. Kwa hiyo bajeti hii inalenga kwenda kusawazisha hizi changamoto ambazo zinafanya hali ya vijijini iwe ni ngumu zaidi kuliko hali ya mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna akinamama wako kule vijijini hawajawahi kuona kituo cha afya au kujifungulia hospitali. Bajeti hii inakwenda kuondoa hayo yote; inakwenda kupunguza kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda kuipongeza sana, napenda kumpongeza sana Waziri wa Fedha na Mipango, lakini pamoja na timu yake yote. Siyo rahisi kumtaja mmojammoja, lakini nawapongeza, wamekuja na bajeti iliyotutia moyo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii ni tofauti na wadau wengine walivyokuwa wanashauri, wanasema akiingia kiongozi mpya inabidi na yeye aache legacy yake, kwa hiyo, aache yale ya mwanzo yaliyotangulia aanze ya kwake, matokeo yake kunakuwa hakuna uendelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bajeti hii imejiweka wazi namna gani itakwenda kumalizia ile miradi yetu mikubwa ya kimkakati ambayo ilianzishwa na hawa majemedari wawili; jemedari wetu marehemu, na jemedari mama yetu, Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan. Na kwa misingi hiyo niseme tu kwamba hilo ndilo ambalo tunalihitaji Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala ambalo tulifanya kubwa katika kipindi hiki ni uthubutu wa hii miradi mikubwa ambayo ilikuwa inawezeshwa na fedha yetu ya ndani. Kwa misingi hiyo uthubutu ule umeendelea ambao sasa tunajipangia malengo mengine ya kuhakikisha kwamba miundombinu mingine inapatikana kwa kuhakikisha kwamba kila mwananchi anachangia katika kupata fedha hizo; hatuna mjomba, hatuna shangazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na hatuwezi kuendelea kuusifia umaskini au sisi kufurahia kuitwa maskini kwa sababu eti kuna mtu yuko pale pembeni atatuchangia sisi fedha zake. Lazima sasa tuondoke na tujue kwamba sisi tunao wajibu mkubwa wa kuhakikisha kwamba tunapata fedha kwa ajili ya kuhudumia maendeleo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jambo hilo tunazo fursa. Fursa ninayoiendea sasa ni ya Soko Huru la Afrika ambalo tayari Tanzania tumeshasaini mkataba wake, bado kuridhia. Na ninaamini pengine Wizara husika ya Wizara ya Viwanda na Biashara mtajitahidi kufanyia kazi suala hili ili huu mkataba tuuridhie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na suala hili sasa linapojitokeza, niwaombe Watanzania, kuna mambo hatuwezi kuyakimbia. Ni lazima na sisi tujiweke katika mpango na mstari wa kuhakikisha hiyo fursa tunaitumia vipi. Hata kama sisi hatutataka lakini wenzetu watakuja kutumia fursa zilizopo nchini kwetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hatutawakaribisha wawekezaji kuwekeza hapa nchini basi watawekeza pembeni ya nchi yetu na sisi tutakuwa soko lao, watu wanataarifa kiasi gani kuhusiana na suala hili, mambo gani ambayo yanaweza kuwa ni vikwazo kwa hawa wananchi kuweza kushiriki kwenda katika nchi nyingine kutafuta masoko na kufanya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu tukiwawezesha wanawake wakapata elimu ya kutosha, wanawake najua wao siyo waoga wanauwezo wa kwenda nchi yoyote ile wakafanya biashara na ndiyo maana hata Mheshimiwa Rais amesema katika sehemu anayotaka kufanya ni kuhakikisha kwamba anawezesha wanawake kiuchumi katika kupitia majukwaa mbalimbali ya kwenye mikoa yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe kwa sababu hawa wanawake ni kundi kubwa ni jeshi kubwa na lina uwezo huo na wanawake hatuogopi hata tukiamua kuolewa nchi yeyote tunaenda kuolewa huko na tunajenga mataifa huko. Kwa hiyo, hata biashara ukitaka biashara za nje zifunguke ni pale tutakapowezesha makundi haya ya wanawake. Tukifanya hivyo kweli tunaweza kufanya biashara yaani katika soko la Afrika, lakini pia tutaweza kupata maendeleo tunayo yahitaji kwa wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. kwanza nami niungane na wenzangu kuipongeza sana Kamati yetu chini ya Mwenyekiti wetu, Mheshimiwa Kitandula. Lakini pia kuzipongeza Wizara zetu hizi mbili; Nishati na Madini, kwa kazi kubwa ambayo inafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya pekee kabisa nampongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa jambo kubwa sana ambalo amelisimamia, kwamba miradi mikubwa iliyoanzishwa huko nyuma katika Awamu yao ya Tano atahakikisha kwamba inakamilika. Na hapa nauzungumzia Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania lazima tujitambue. Kuna wakati tunaweza tukawa tuna malengo makubwa, mazuri ambayo yametupa heshima katika nchi yetu. Halafu baadaye kwa sababu moja au nyingine, kwa sababu labda pengine uongozi mmoja haupo umekuja uongozi mwingine, watu wengine wanaweza kufikia kujaribu kutuchezea kwa kutushauri tofauti ili tushindwe kwenda kule tulikotaka kwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Rais amedhamiria na ametangaza hadharani, nawaomba Wizara ya Nishati tafadhali tusimuangushe Mheshimiwa Rais wetu. Tuhakikishe mradi huu wote kwa pamoja tunashirikiana, timu iliyopo sasa na hata ile iliyokuwa mwanzo, kama kuna jambo ambalo wao wanalifahamu mshirikiane kuhakikisha kwamba tunakwenda vizuri. Sisi hatuangalii sura ya mtu, tunaangalia umeme upatikane katika Bwawa la Mwalimu Nyerere.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo tuhakikishe kwamba power master plan inatekelezwa inavyotakiwa, kadri umeme unavyozalishwa wakati huo huo na miundombinu mingine ya ujenzi wa line ikamilike sambamba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza kwa sababu umeme usipozunguka kwenye mita ina maana wizara nyingine pia zitapata shida. Tuwapongeze kupita EWURA, REA inapata fedha, Wizara ya Maji wamenyamaza hapo wapongezwe wanapata fedha, lakini vilevile Mfuko wa Barabara unapata fedha kupitia wizara hizo, kupitia mafuta. Kwa hiyo tusishangae tu kwamba bei za mafuta ni kubwa wakati kuna tozo tumeweka huko ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile hata Wizara ya Ardhi sasa inapata fedha kupitia LUKU, kwa hiyo wote huo ni mchango wa Wizara hizi. Sasa nini ninachotaka kusema. Wizara ya Nishati hasa kwenye masuala ya umeme, Shirika la TANESCO siyo la kibiashara kama tunavyoliona, ni shirika ambalo ni la kihuduma. Kwa hiyo hata tunapopanga bajeti zetu tuhakikishe tunapeleka fedha za kutosha kwa sasa fedha nyingi ukiangalia Wizara inaonekana ina bajeti kubwa sana, lakini nenda kwenye miradi ile mipya katika masuala ya matengenezo fedha inayokwenda ni kidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuhakikisha kwamba TANESCO wafuatilie upotevu wa umeme usio wa lazima ambao siyo wa kiufundi. Kwa mfano, wizi wa umeme, umeme unaopotea kutokana na nyaya chakavu, hilo walifanyie kazi, lakini sisi Wabunge kwa pamoja kama kweli tunataka kufikisha huduma hii kwa watu wetu kwa ukamilifu, Wizara hii itengewe fedha za kutosha kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu. Vile vile kwa ajili ya kuwekeza kwa ajili ya hawa wananchi ambao kwa muda mrefu wamekuwa hawana umeme, hasa vijijini ambako wanaanza kujishughulisha na kutengeneza ajira kupitia viwanda na kazi ndogondogo za kiumeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kukatika kwa umeme kuna sababu nyingi, sababu mojawapo alizosema za kuzidiwa kwa mitambo, ukiangalia system ya umeme haipo kwenye uzalishaji tu yaani generation; kuna uzalishaji, kuna hizi transformer ambazo zinaweza kutoa umeme, kupandisha kwenda juu au kuushusha, lakini vilevile nyaya zenyewe. Pia kuna changamoto hata namna ya kuboresha hiyo miundombinu. Watu wa Ardhi wanapotenga maeneo ya viwanja vyao unakuta ni mara chache sana wanatenga maeneo ya kuweza kujenga vituo vya umeme au njia za kupitishia line za umeme. Kwa hiyo, unakuta hata namna ya ku-improve inakuwa ni shida. Niwaombe Wizara hizi kushirikiana ili kuhakikisha kwamba wote wanatoa support kwa Wizara zingine ikiwemo kupeleka umeme kwenye Stangold, haiwezekani watumie mafuta wakati umeme unaweza ukasaidia. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Afya
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumpongeza sana Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu (Mb) na Naibu wake Dkt. Godwin Mollel (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara pamoja na Naibu wake na timu nzima ya watendaji wa Wizara pamoja na wadau wote wa maendeleo ya afya.
Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo nina ushauri ufuatao; kumekuwa hali isiyo ya kawaida baadhi ya vituo kukosa ARVs na kulazimika kutoa dawa zilizoisha muda wake katika Wilaya ya Nyasa; uangaliwe utaratibu wa kununua dawa kwa kuwa baadhi zinanunuliwa nyingi na kupitisha muda wake wakati nyingine hazipatikani kabisa; kuna upungufu mkubwa wa vitanda na vifaa tiba muhimu katika Wilaya ya Nyasa; ni lini Wizara italeta vifaa vya upasuaji katika Kituo cha Afya cha Kihagara? Pia hali ya watumishi wa afya, madaktari na wauguzi ni wachache sana. Ni 228/800 na pia tunaomba magari ya wagonjwa.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza, nianze kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili ya yote. Pili, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kazi kubwa anayofanya na tunamwombea afya njema ili aweze kuendelea kututumikia. Wakati huo huo, nawaombea Waheshimiwa Wabunge wenzangu na wananchi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mengi yamezungumzwa, lakini kazi yetu sisi Wabunge tuliyopewa kwa mujibu wa Sheria na Katiba, ni kuwasemea wananchi kuwatetea na vile vile kuhakikisha kwamba tunakuwa na sheria nzuri zinazosaidia na mambo yote. Kwa misingi hiyo, kila mtu anapokuwa kwenye nafasi hii ya Ubunge lazima atimize wajibu huo kwa nguvu zake zote. Tunapozungumza, haijalishi jana nilikuwa nani au juzi nilikuwa nani? Leo mimi ni Mbunge, lazima niseme bila kuficha, ndiyo maana tunalindwa katika mazungumzo yote tunayosema humu Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitaanza kuzungumzia hali ambayo binafsi naiona siyo nzuri, inayoendelea katika mitandao mbalimbali. Mitandao naichukulia ni sehemu rasmi ya taarifa, kwa sababu sisi wenyewe tumeshasema kwamba hata ushahidi wa kimtandao unaweza ukatumika hata Mahakamani. Hiyo ni kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, nasema nini?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hii hali ambayo inaendelea katika nchi yetu, nami kama mtu mzima ambaye Mwenyezi Mungu amenibariki nikaishi katika Awamu zote za Uongozi, nashangaa ninavyoona sasa hivi watu wanapenda kuendelea kutupiana maneno, wengine wakijaribu kuwasema viongozi waliopita, wengine wakijaribu kuwasema viongozi waliopo mambo mbalimbali, haileti afya kwa Taifa letu. Tuache. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Taifa hili lisingefika hapa leo bila uwepo wa wale viongozi waliopita. Taifa hili haliwezi kuendelea bila viongozi waliopo sasa. Kwa hiyo, badala ya sisi kushikamana kuangalia mbele tunakoenda, tunaendelea kupigana na tena wanaopigana wengine kuna chawa sijui wa watu wa zamani; kuna chawa wa watu wa sasa. Ukiangalia hawa wanaosema ni chawa, kwanza mimi neno lenyewe chawa linanitia kizunguzungu; maana yake chawa akiingia anaweza akakunyonya zaidi akakuharibia hata maisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nasema hawa chawa wasaidie kuifanya nchi iende mbele. Hatutaki kutupasulia nchi yetu, hatutaki. Wote tunawataka wale wanaosifu yale mazuri ambayo yametufikisha hapa kutokea nyuma, na wanaosifu yale mazuri tunayoendelea nayo kwenda mbele. Hatutaki mambo ya ovyo. Nimeongea kama mtu mzima, ninao wajibu wa kupaza sauti kwa Taifa langu kwamba tunapoenda hatuko sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni la kuhusu watumishi. Wengi wamezungumza. Tunaongezea tu kuonesha uzito wa tatizo. Watu wanaoishi maeneo ya pembezoni wana gharama kubwa za kupata huduma kuliko walioko mjini. Inasikitisha, kama ambavyo tumesikia taarifa mbalimbali, nami kwa Jimbo la Nyasa, kwa mfano, katika afya tuna watumishi 206 tu kati ya watumishi 800 wanaohitajita. Ni kama robo tu. Huyu mtumishi ambaye ataweza kuhudumia wale watu wote atakuwa wa aina gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hawa wananchi wanapokosa zile huduma muhimu wanatakiwa wazifuate mbali zaidi ambapo wanakutana na gharama ya nauli, gharama ya mihangaiko na gharama ya vifo. Hili hatuwezi kulivumilia. Kuna baadhi ya maeneo ya mjini humu kuna watumishi wengi. Kwenye shule kwa mfano, watu wanafikia kugawana vipindi, walimu wanne wanagawana kipindi kimoja, yaani somo moja wakati kule hakuna watumishi, kwa sababu gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tumeambiwa kuna ajira karibu 32,000 zitatolewa, lakini zote zitaishia mjini, hazitakwenda huko vijijini. Naomba kama kulikuwa na nia njema ya kusema kwamba tusiwe na ukabila, tuwe tunaajiri centrally, mimi naona hiyo kuajiri kati na yenyewe imeshakuwa ni tatizo, turudi tutafakari. Kuna wakati tulikuwa tunaajiri kupitia Serikali zetu hizi za Mitaa, lakini wengine wakawa kwenye Serikali Kuu. Baadaye tukasema hapana, tuweke mfumo ambao utawezesha wote kulipwa vizuri, pengine umesaidia kidogo, lakini bado matatizo ni mengi. Hivi kweli hata dereva mpaka unataka umwajiri wapi sijui, tumeambiwa hapa kwamba wataangalia utaratibu vizuri. Naona kuna mambo mengine tunaya-complicate pasipo lazima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hali ya mishahara kwa upande wa madereva ni duni sana. Hata madereva wa kwenye Wizara mishahara yao siyo mizuri. Wakati tunapigia kelele mishahara ya watumishi wengine, hao madereva wanakesha usiku kucha. Naomba nao waweze kusaidiwa, waweze nao kupanda mishahara angalau itakayowezesha kupata pension inayoweza kuwasaidia zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende katika suala la kuondoa umasikini na hapo naiangalia TASAF. Hii TASAF tulikoanzia imefanya kazi nzuri, lakini nadhani sasa hivi tuiangalie zaidi. Kwa mawazo yangu ya kufikirika, nilifikiria kwamba pengine tuwachukulie hawa wanafunzi wanaohitimu, kwa mfano, hata ada walilipiwa, wanatakiwa sasa kwenda kufanya kazi, ajira hakuna. Kwa nini hili kundi la TASAF tusiliangalie upya katika kundi hili ambalo halina ajira na lina elimu tayari ya kuweza kufanya kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nafikiria kwamba wanapomaliza kwa mfano JKT kwa wale walioenda, au ambaohawajaenda; pengine tungewatawanya moja kwa moja kwenye maeneo ambayo wanaweza kutoa huduma, lakini wapangiwe angalau fedha ya kuweza kujikimu wakati wakipata zoezi hilo la kufanya kazi na wakati huo huo ikawa wanachangia katika kutoa huduma na kupata uzoefu ili baadaye waweze hata kama ni kujiajiri wenyewe au kuajiriwa lakini angalau wanakuwa wamekaa hapo kwa muda fulani.
Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kama kutakuwa na mfumo rasmi wa kutoa hizo ajira za muda, hasa katika Halmashauri zile ambazo mimi nasema kwamba ni za Ki- TASAF, maana yake kuna Halmashauri hazina mapato ya kutosha na zenyewe ziingie tu kwenye mfumo wa TASAF, ziweze kupewa huo msaada wa watumishi hata hao wa muda waweze kusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, katika kufanya hivyo, naamini kwamba itasaidia hata kuibua mambo mbalimbali yanayowezesha kutoa ajira zaidi. Kwa mfano, kutengeneza vikundi vya kuweza kutoa ajira katika hao wahitimu wa vyuo mbalimbali. Naona pamoja na kwamba tunasema kuna ajira binafsi, lakini ajira hizo binafsi hazijawa na mvuto. Hazijawekewa mfumo ambao unawasaidia. Hata Mungu akibariki, watu wamechangia hapa, pengine mama ikupendeze kutufikiria, watumishi; na hao je? Itawapendeza katika mfumo gani? Watasaidiwa katika mfumo gani? Angalau sisi tuko ndani, tunapata hizo kidogo tulizonazo, hao hawana kabisa na ndio kundi kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, huyu mtu ambaye ameelimika, akiamua kuingia kwenye uhalifu anaweza hata kutumia integration katika kufanya uhalifu wake. Anajua hesabu zote, naye anaweza kujua kwamba atapata nini? Kwa hiyo, ni mambo ya hatari kuliacha hili kundi kubwa bila kuwa na hali halisi ya kulisaidia ili liweze kuajirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nasisitiza hayo na nikiomba kwamba rasilimali za Taifa hili siyo la kikundi cha watu au watu wachache. Rasilimali za nchi hii lazima zitumike kwa kadri inavyowezekana, kwa watu wote, kwa usawa unaostahili. Haiwezekani! Kwani mimi kuzaliwa kule kijijini kwangu ndiyo imekuwa nongwa? Nami nifikiriwe, watu wa maeneo ya vijijini wafikiriwe, wasaidiwe, wapunguziwe mateso yaliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama tulivyoanza katika masuala ya Vituo vya Afya, shule, twende zaidi, kuwe na fedha maalum ya kusaidia kuibua mambo mbalimbali ya kiuchumi maeneo hayo ili kuongeza ajira na utumishi ulio rasmi na usio rasmi. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Hoja ya Dharura (Changamoto ya Kupanda kwa bei za Mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Nianze kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Kigua kwamba tatizo hili la mafuta ni kubwa na lina athari kubwa kwenye uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kusema kwamba, kwanza naipongeza michango mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge waliotangulia, lakini niseme tu kwamba hatua zozote tutakazozichukua zisiende kuleta athari katika ile mikataba ambayo tumeshaingia na wakandarasi wetu katika maeneo mbalimbali hususan katika maendeleo ambayo tayari tulishajipangia, REA ikiwa ni mojawapo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu tayari walishaingia mikataba na kwa sababu kazi lazima zifanyike, pale utakaposema kwamba simamisha fedha labda ya tozo mahali fulani ina maana utakuwa unasimamisha ule mradi, unless kama tutakuwa na uwezekano wa kutoa fedha kutoka maeneo mengine na kupeleka huko kama ambavyo imesemwa bajeti tayari ilishawekwa.
Mheshimiwa Spika, kulikuwa na suala ambalo tulimsikia Mheshimiwa Waziri, kulikuwa na jitihada ya kwenda kuongea moja kwa moja na wale wazalishaji wa mafuta ili tuweze kuyapata kwa bei ambayo ni rahisi au wao kutuuzia moja kwa moja, huo mpango sijajua ulifikia wapi. La pili ninaloliona ni kwamba suala la uadilifu na lenyewe lazima tulipigie kelele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Tabasam alizungumza siku ile hapa hatuna uhakika, lakini tunasema iko haja ya kufuatilia anapolia mtu yawezekana kuna jambo, iko haja ya kufuatilia ili tuone kwamba taratibu tulizojiwekea zinakwenda sawasawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine niseme tu kwamba athari hizi za mafuta tumeziongelea zaidi kwa ujumla wake. Siku za nyuma tulikuwa na taasisi ambazo zilikuwa zinapanga bei ya bidhaa mbalimbali, sasa hivi ikiongezeka lita moja kwa Sh.100 au Sh.200, kila mtu anapandisha bidhaa mara mbili au mara tatu, huko ndiko wanakoumia wananchi zaidi. Kwa nini huko tumekuacha kunakwenda kiholela?
Mheshimiwa Spika, nimeangalia bei ya bati iliyokuwa inauzwa Sh.19,000 sasa hivi Sh.28,000 gauge 30; ukienda kwenye mafuta hivyo hivyo. Kwa hiyo, kuna maeneo tumeacha kuyasimamia ipasavyo, pamoja na haki ya wafanyabiashara kuweka bei ambayo ni bei huria, lakini… (Makofi)
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: …iko haja ya kufuatilia upatikanaji wa bei hizo.
SPIKA: Mheshimiwa Stella Manyanya kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Kabula.
T A A R I F A
MHE. KABULA E. SHITOBELO: Mheshimiwa Spika, ahsante napenda tu kumwambia kwamba tozo zinazoongelewa ni zile ambazo hazitaathiri mapato ya Serikali. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Stella Manyanya, unaipokea Taarifa hiyo?
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, naomba nisimjibu.
Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba, kimsingi tozo zote ambazo zipo kwenye mafuta ziliwekwa kwa sababu na ndio maana tunaona kwamba namna ya kusaidia watu waweze kuendelea na mfumo ule wa kupata maendeleo tuliyojipangia, lakini pia kuhakikisha hatukwami. Kuna kupunguza matumizi yasiyo ya lazima hiyo ndio ambalo naungana nalo. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Manyanya, kuna taarifa nyingine kutoka kwa Mheshimiwa Khadija Taya.
T A A R I F A
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa mzungumzaji kwamba, leo mabasi ya Shabiby yameongeza bei kutoka VIP shilingi 35,000 mpaka shilingi 45,000 na mabasi yale ya kawaida shilingi 22,000 ni shilingi 28,000, kwa hiyo hali ni mbaya Waheshimiwa. (Makofi)
SPIKA: Sasa ngoja, ngoja, kabla sijaleta hiyo taarifa ili uipokee au hapana hayo mabasi yametajwa mahususi, lakini nadhani bei za mabasi zimetangazwa kwa mabasi yote. Kwa hiyo, tusije tukajikuta hapa kwamba tunazungumzia kampuni moja kana kwamba kampuni nyingine bei ziko kawaida. Bei mabasi yote yametangazwa na chombo chetu cha Serikali kinachoangalia bei za vyombo vya usafiri. Kwa hiyo tusije tukajikuta kwamba tunazungumzia kampuni moja hapa ya mabasi, mabasi yote yametangaziwa bei mpya. Mheshimiwa Stella Manyanya. (Makofi)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunisaidia eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, ninachosisitiza ni nini, tupo katika vita vya kiuchumi na jambo hilo la vita vilivyotokea huko kulikotokea duniani kuna wengine wananufaika humo humo kwa wao sasa kuwa ma-supplier wa mafuta katika nchi nyingine. Matokeo yake tunazuiliwa mafuta yasitoke maeneo fulani au vikwazo vinawekwa sehemu nyingine, lakini kuna wengine ambao wananufaika na mfumo huo kwa sasa hivi. Hilo suala pia liko kidunia na dunia tunaomba ituelewe sisi tupo katika kukuza uchumi wetu sasa hivi, wenzetu wameshatangulia, lakini kila vikwazo vinavyowekwa vinaumiza nchi hizi ambazo zinaendelea sasa hivi. Kwa hiyo, lazima tutupie na jicho huko kwa hiyo mimi nasema kwa ujumla wake dunia hii kwa sababu tunaongea live inatusikia tunaumizwa katika nchi zinazoendelea. (Makofi)
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, Taarifa.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja, lakini iko haja ya kufuatilia kwa karibu kuona kwamba bei za bidhaa mbalimbali zinasimamiwa vizuri na mafuta tutafute fedha itakayopatikana kupitia vyanzo vingine, lakini tozo za msingi…
SPIKA: Sasa kwa sababu unaendelea kuongea basi Mheshimiwa Ighondo, Taarifa. (Makofi/Kicheko)
T A A R I F A
MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nilitaka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba, pamoja na sababu za kidunia, lakini sisi tunazungumzia dharura iliyopo mbele yetu kama Taifa kwa sababu zetu za ndani tuchukue hatua za makusudi hasa kwenye tozo ambazo sio za lazima, ambazo haziwezi kuathiri masuala yetu ya maendeleo ili kunusuru uchumi wetu pamoja na kushusha hali ya maisha kwa wananchi wetu. (Makofi)
SPIKA: Haya Mheshimiwa Stella Manyanya unaipokea taarifa hiyo?
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, hii siipokei kabisa, kwa sababu tumefahamishwa kwamba changamoto mojawapo inayosababisha haya tuliyofikia ni hivyo vita vilivyoko huko kwenye mataifa. Kwa hiyo lazima tu-deal na sababu zinazosababisha, kwa hiyo pamoja na hayo ya kupunguza, haya ni matokeo ya athari zinazoendelea huko duniani. Tunasema kwamba hao wanaoweka hivyo vikwazo, hao wanaosema hili lisifanyike wakati wenyewe pia wanafanikisha kupeleka bidhaa zao maeneo mengine wanatuua nchi zinazoendelea. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa uzima lakini pili nami niungane na wenzangu na Watanzania wengi kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa na jitihada ambayo anaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika niipongeze Waziri hii chini ya kiongozi wetu Mama Angellah Kairuki, kwa kazi kubwa inayofanywa. Kwa sababu Wizara hii ni Wizara ambayo ni kuunganisha cha Wizara nyingine ambazo kama Wizara ya Afya, hata Wizara za Ujenzi. Unakuta Wizara hii ndio kila kitu ndio mama wa kila kitu na ndio maana hata kwenye bajeti yake unaona kwamba ni fedha nyingi sana inatengwa lakini ukiangalia mahitaji ambayo yapo ni hazitoshi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, binadamu ameumba kupenda kusikia neno lile linalomfurahisha ndio binadamu wanafurahi lakini mtu anapenda kusikia neno lenye utu. Neno ambalo linagusa watu na mahangaiko ya watu, shida za watu huyo ndio mtu. Kwa hiyo, naamini Wizara hii chini ya Mama Angellah Kairuki, ninyi ni watu, sasa kwa sababu ni watu mna utu naomba mnisikilize haya nayojaribu kuyasema. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, majimbo yetu yanatofautiana sana, kuna majimbo ambayo yameeanza kupata fursa za kiwekezaji, fursa za migao ya Serikali miaka nenda rudi. Toka wakati huo enzi za mkoloni yalipata hiyo bahati lakini kuna majimbo yalisemwa kwamba haya ni pembezoni tusubiri kwanza. Yakasubiri kwa muda mrefu, sasa hivi ndio yanaanza kuibuka sawa na lile Jimbo langu la Nyasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, majimbo haya au wilaya hizi za aina hii ndizo ambazo zinachangamoto kubwa na siku nyingine nilikuwa naziita Wilaya za TASAF yaani ni maskini. Sasa wilaya hizi ndizo zinazokumbana na changamoto nyingi lakini kwa sasa kwa utaratibu unaoendelea naona pia hizo wilaya au haya majimbo ya aina hiyo itakuwa ni ngumu sana yenyewe kupiga hatua ya kuyafikia hayo majimbo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani nasema hivi? Tuna ile hali ambayo tunaizungumza hasa katika migao yetu ya fedha, kiurahisi tunagawa fedha kila jimbo tupate sawa. Kweli sisi Wabunge ni vizuri tupate sawa lakini mtu mwenye kata 20, vijiji 84, vitongoji 423 kama Wilaya yangu ya Nyasa. Unategemeana kwamba tukipeana kwa mtindo huo sisi tutawafikia lini hawa wenzetu ambao sasa wameshaanza kupata kwenye zile kata au vijiji vinajirudia. Vijiji 84 unahangaika upate angalu zahanati 20 za kukaa angalau kwa umbali umbali watu wapate huduma, unakuta wewe unapata zahanati moja wenzako wengine wanapata zahanati 3, 4. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo hatuwezi kulifumbia macho lazima tuseme, na tunatabia ya sisi wakati mwingine kusema tukishakuwa kwamba yule mtu tunayemfikiria hayupo dunia au hayuko kwenye kiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Mheshimiwa Mama Angellah Kairuki, kwa sababu wewe una utu tunasema hapa hapa sasa hivi. Haturidhiki na mgao unavyokwenda. Kwa mfano, hata hizi shule za sekondari kuna wengine kata zao hazina hata hiyo sekondari lakini pia hata hizo kata ukiziangalia zina hali mbaya sana au zimetengwa kijiografia. Kata kama ya Mipotopoto ukienda kule Mitomoni unavuka katikati kilometa 40 ndo unafikia kijiji kingine cha Mipotopoto. Sasa kwa mazingira kama hayo hao watoto watasomaje? Lakini tumeshaandika barua nyingi ziko kwenye mabenchi yenu, tumezileta, tumelalamika na tunasema kwa dhati lakini unakuja ikija migao inaendelea kwa mtindo ule ule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najiuliza changamoto ni nini? Kwamba sisi Wabunge tunasema uongo kiasi kwamba hatustahili kusikilizwa au ni nini? Lakini pia kuna hali ya kutokuwaamini wale ambao wapo kwenye maeneo. Unakuta jambo la kuweza labda pengine kuifanyia kazi kwa haraka mpaka atoke mtu Wizarani aende huko na yeye kwa sababu ya muda wake ni mfupi ataenda kukagua sehemu fulani atachagua tofauti na kile ambacho pengine hata wewe Mbunge umekipendekeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna shule niliitembelea, mfano inaitwa Songambele, shule ile nilikuta madarasa mawili yapo pamoja yana nyufa yana hali mbaya na mle watoto walikuwa wanaingia wanacheza. Nikaona kwa nini tuunde tume ya kukagua mtu gani amesababisha kifo, nikasema wananchi hali hii si hatari wenyewe tunaiona na walinilalamikia. Nikasema ndio, nikasema tubomoe kwa usalama tutaendelea na masuala ya ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka leo nimeandika barua chungumbovu kwenye Wizara hata sisikilizi hivi mlitaka nifanyaje? Angekufa kwanza mtu halafu ndio niwaambie, ndugu zangu tusiende hivyo. Mama anafanya kazi kubwa ya kutafuta hizo fedha basi tuzitendee wema na kwa haki zaidi lakini kuna majengo. Kuna jengo la Sekondari Mbamba Bay, nimeshasema…
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Stella Manyanya, kuna taarifa.
TAARIFA
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimpe taarifa mchangiaji anayechangia kwamba jambo hili limekuwa likijirudia sana na kwa kuwa jambo hili limekuwa likijirudia na wewe umekuwa ukiomba mara kwa mara na husikilizwi. Unaonaje leo Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya sisi kama Wanaruvuma tuondoke na Siwa hapa mpaka Siwa hili litakapokuja kufuatwa Ruvuma na darasa hili liwe limeshajengwa. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Stella Manyanya.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nasmhukuru sana Mheshimiwa Msongozi, mdogo wangu kwa kunipa hiyo taarifa ambayo imeongeze thamani, isipokuwa Siwa nakusihii tusiondoke nayo maana yake Bunge litakuwa limeshasimama na itakua tumekosa kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba ni mambo ambayo yanahuzunisha kuna majengo yapo. Kwa mfano pale Mbamba Bay Sekondari kuna jengo la ghorofa chini ya ofisi ya utawala juu makataba, kwa sababu ule mradi ulikwisha basi hakuna hela ya kumalizia. Tunaambiwa tutenge mapato ya ndani, mapato ya ndani kwenye wilaya, Halmashauri ya Nyasa ndio hiyo ya Ki - TASAF. Sasa hivi tunaishusia kwamba ipunguze hata hela ya kupeleka kwenye maendeleo, tutakamilisha lini?
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Stella.
MHE. ENG. STELLA MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nisaidiwe, twende tutembelee ile wilaya tuione vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya kuendeleza kilimo na kuwaletea ustawi wananchi. Pili, nimpongeze Waziri Mheshimiwa Hussein Bashe pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Anthony Mavunde, Katibu Mkuu Ndugu Gerald Mweli na Naibu wake pamoja na watendaji wote wa Wizara hii.
Mheshimiwa Spika, nashauri mchango uliotolewa na Mheshimiwa Benaya Kapinga kwa kusema kuhusu utaratibu wa sasa wa kununua kahawa ufanyiwe kazi. Wakulima wanalalamika sana ikiwemo wa Wilaya ya Nyasa kutokana na kukopwa kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, shukrani kwa miradi ya umwagiliaji ya Chiulu, Lundo na Kimbande kuonekana katika mipango ya uendelezaji katika bajeti hii. Kuna mahali katika skimu za ukarabati Kimbande inasomeka kuwa katika Wilaya ya Mbinga. Ili mradi usipotee naomba Kimbande isomeke ipo Nyasa.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri alinidokeza kuwa Skimu ya Lituhi imo kwenye mikakati ya bajeti hii. Nilipoenda kwenye mwenge kwa furaha kabisa nikawaeleza wananchi, wakakushukuru na kukuombea sana Mheshimiwa Waziri na pia Mheshimiwa Rais. Sasa Lituhi ambayo pia niliuliza swali humu Bungeni na ukanijibu wewe mwenyewe, imeyeyukia wapi? Nadhani imekumbana na changamoto za kiuandishi.
Mheshimiwa Spika, Nyasa ipo pembezoni, bado ni maskini lakini ina rasilimali za kuanzia kama hizi. Msimu uliopita hatukupata chochote, tunawaamini mwaka huu hamtatuacha.
Mheshimiwa Spika, namalizia kuwashukuru kwa kutuletea Engineer Faraja, yupo vizuri, akipewa nyenzo atafanya vizuri.
Mheshimiwa Spika, nashauri pia bajeti yenu ishuke chini kiutekelezaji.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Afya
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Waziri wa Afya Mheshimiwa Ummy Mwalimu na wote wanaomsaidia wakiwemo madaktari na wauguzi wote wa Wilaya ya Nyasa.
Mheshimiwa Spika, maoni yangu; kwanza fedha inayotengwa itolewe kama ilivyokusudiwa; pili, Serikali iweke jitihada kubwa katika kutoa kinga na pia kutoa mafunzo ya ujuzi kwa mabwana na bibi afya ili kuifikia jamii kubwa zaidi. Lakini kuhusu kuwatumia waliomaliza kidato cha nne ni vema kuwatumia waliopata ujuzi wa vyeti vya fani za utabibu na afya pamoja na kuwaongezea ujuzi huo unaohitajika. Hao wapo wengi huko vijijini.
Tatu, Wilaya ya Nyasa inaomba vifaa tiba muhimu x-ray, utra sound, ambulance na fedha za vifaa vya vituo vya afya na zahanati zilizikamilika Vituo vya Afya Kingirikiti na liparamba.
Mheshimiwa Spika, nne, Hospitali ya Wilaya ya Nyasa imeshaanza kutoa huduma za afya ya kinywa. Changamoto ni hakuna vifaa tiba kabisa. Tunaomba ahadi ya kupatiwa shilingi 50,000,000 tuliyoahidiwa; tano, Wilaya ya Nyasa ina upungufu mkubwa wa watumishi wa afya, ni vema Wizara iwaongeze watumishi wa afya.
Mheshimiwa Spika, sita, kwa nini Serikali isifikirie kuwa na mfuko maalum wa tozo angalau shilingi mia moja tu kwa ajili ya kupunguza changamoto ya kifedha hasa katika kuboresha huduma za afya vijijini na kwa magonjwa maalum kama saratani, figo na kadhalika, tukubali kukata kupitia mafuta au mawasiliano. Najua changamoto zake, lakini tukiamua inawezekana. Tusijifungie kwenye bima ya afya tu. Afya ya mtu ni utu na heshima ya uhai. Inaumiza sana kuona mtu anapoteza maisha kwa ajili ya kukosa uwezo wa kifedha. Umuhimu wa uhai hauchagui hali ya kiuwezo wa kifedha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Mungu. Pili nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa katika sekta hii.
Vilevile nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hii pamoja na watendaji wote wa Wizara akiwemo Engineer Mlavi kwa ushirikiano mkubwa anaotupa katika Wilaya yetu ya Nyasa.
Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mkurugenzi wa TPA pamoja na timu yake kwa kuanza kuimarisha bandari ya Mbamba Bay, huo ni ukombozi mkubwa sana kwa Taifa na hususan wananchi wa Wilaya ya Nyasa.
Mheshimiwa Spika, katika suala ya uboreshaji huduma bandari ya Dar es Salaam naunga mkono, la msingi masuala ya kimkataba yawekwe vizuri kuangalia flexibility ya revision in case kuna lazima ya kufanya hivyo na pia kuzingatia masuala ya kiusalama.
Mheshimiwa Spika, nashukuru pia kwa hatua zinazoendelea katika kujenga Daraja la Mitomoni. Daraja hilo ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa eneo hilo na wananchi wa Nyasa na Songea, hali kadhalika jirani zetu wa Msumbiji. Kutokuwepo kwa daraja hili ni kikwazo kikubwa kiuchumi.
Mheshimiwa Spika, naomba bajeti ijayo itengwe fedha ya kufanya upembuzi barabara ya Unyoni hadi Mitomoni kwa ajili ya maandalizi ya kujenga kwa kiwango cha lami. Nakumbusha utekelezaji kwa kiwango cha lami barabara ya Ruanda - Lituhi - Ndumbi na Mbamba Bay - Lituhi.
Mheshimiwa Spika, mwisho kutokana na Wilaya ya Nyasa kupokea maji mengi toka milima ya Livingstone hivyo kuhitaji fedha nyingi za matengenezo ya dharura. Ni vema bajeti ya matengenezo iongezwe.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Nishati
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, pongezi za pekee kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiangalia kwa jicho la kipekee Wizara hii na kuisaidia hasa katika miradi ya kipaumbele, LNG, Mwalimu Nyerere Hydro Power na mengineyo. Pongezi kwa Wizara, Waziri Mheshimiwa January Makamba, Naibu Waziri Wakili Mheshimiwa Stephen Byabyato, Katibu Mkuu Engineer Mramba, Naibu Katibu Mkuu Bwana Mbutuka pamoja na watendaji wakuu wote wa mashirika na taasisi mbalimbali bila kusahau watumishi wenzangu kwa kazi kubwa na nzuri inayoendelea.
Mheshimiwa Spika, maombi; kwanza pamoja na shukrani za kutuongezea umeme katika vitongoji (Underline T/F) jambo ambalo litaongeza ustawi, ubunifu na uchumi kwa ujumla. Pamoja na shukrani hizo nina maombi rasmi ya kupeleka umeme katika vitongoji viwili vilivyopo mpakani na nchi ya Msumbiji. Ni muhimu kwa ajili ya usalama, ni muhimu kwa ajili ya uchumi kwani maeneo hayo yana dhahabu na pia ni centers za kibiashara. Vitongoji hivyo ni Nindi na Ngeapori. Kwa kuwa Wizara ya Nishati ni sikivu, basi naomba mnisikilize katika ombi langu hili la kuhakikisha kuwa maeneo haya ya mpakani yanasaidiwa.
Pili, napongeza mradi wa nishati safi ya kupikia. Nashauri pia kuwepo na mradi maalum wa ku-supply mitungi ya kilo 30 katika vituo vya afya na zahanati japo tutaanza na michache tuliyopewa kwa ajili ya uhamasishaji. Nawatakia utekelezaji wenye mafanikio.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nampongeza Mheshimies Rais kwa kuhamasisha michezo, utamaduni wetu na sanaa. Pili nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayofanya. Nampongeza anavyohamasisha, mkononi mwako tumeshuhidia ushindi kwa vijana wetu wa Fountain Gate School, lakini pia hatua iliyofikiwa na timu ya Yanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza pia Naibu Waziri - mtu mwema, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote, niwapongeze pia kwa kuwa na utaratibu wa mikopo kwa ajili ya kukuza utamaduni na sanaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya Wizara ni ndogo mno, ni vyema iongezewe ili kuwezesha maendeleo ya majukumu yaliyokusudiwa. Nyasa tumeanza kujenga uwanja wa mpira, mnatuchangia nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Stergomena Tax (Mb) Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa, Katibu Mkuu pamoja na Mkuu wa Majeshi kwa niaba ya Jeshi letu lote la Ulinzi na Kujenga Taifa nchini. Kipekee kabisa napenda kumpongeza sana Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiweka nchi yetu kuwa salama, yenye amani na utulivu.
Mheshimiwa Spika napenda pia kuwapongeza kwa ushirikiano wanaotoa kwa mamlaka mbalimbali katika kuleta amani na kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi. Nawapongeza pia kwa kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya kijamii.
Mheshimiwa Spika, ombi letu, kama ambavyo nimekuwa nikichangia katika mipango mikakati yenu ni vema barabara za mpakani ikiwemo Mbamba bay – Lituhi; kufungua barabara ya mpaka wa Tanzania na MsumbiIji ikiambaa na mpaka wetu, kama ambavyo miaka 1970 ililazimu kufungua barabara ya Mbamba bay - Lituhi kufuatia chokochoko za Malawi. Ni vema kujiweka sawa; na kuboresha makazi ya kiteule cha Liuli na gari.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nimpongeze Katibu Mkuu pamoja na Naibu Katibu Mkuu na Msemaji Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuendeleza mchango wangu kwa kuwashukuru TBC kutangaza Wilaya yangu ya Nyasa kupitia TBC1 na Safari Channel chini ya uongozi wa Dkt. Ryoba. Navishukuru pia vyombo vingine vyote vya habari kwa kuwa si rahisi kukitaja kila chombo vikiwemo vyombo vva habari mtandao (online).
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia uboreshaji wa mawasiliano katika Wilaya ya Nyasa, eneo la Kata ya Linga, Mbaha, Kijiji cha Ndonga na Njambe, Mpepo, Kihulunga, Ng'ombo na Mtupale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi maalum ni kuwa tulipata ufadhili wa kompyuta kwa ajili ya shule ya Tingi, lakini kutokana na mtandao kuwa chini mradi huo unataka kusimamishwa tumepewa miezi miwili tufuatilie uboreshwaji wa mawasiliano hayo. Aidha, Maafisa Habari wanafanya kazi kubwa lakini hawana vitendea kazi vya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio na Mapato ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianzie kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi kubwa anayoifanya toka amekaa kwenye hicho kiti lakini pamoja na timu yake yote ya Wizara hii pamoja na Naibu wake kwa kweli wanajitahidi sana. Na nakupongeza kwa jinsi ambavyo umesimamia suala la anuani ya makazi, tumekuona ukizunguka huku ukitoa maelekezo hayo ndiyo tunayoyahitaji sisi watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze sana kwa namna ya kipekee Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mkazo wa matumizi ya TEHAMA katika kufanya shughuli zetu mbalimbali. Na hivi sasa kuna shule za Sekondari zinajengwa kila Mkoa tena za wasichana kwa ajili ya kuwezesha katika masuala ya TEHAMA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende pia kuchukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Spika wetu wa Bunge la Tanzania kwa jinsi ambavyo ameamua kuendelea kuboresha huduma za Maktaba ili sasa Wabunge pamoja na wadau wote wanaopenda kufuatilia shughuli za Bunge waweze kupata taarifa mbalimbali za Bunge pamoja na kujisomea majarida mbalimbali au vitabu mbalimbali kupitia mtandao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini kwamba Wizara hii itashirikiana na Bunge letu hili Tukufu kuhakikisha kwamba linakuwa ni kweli Bunge la kimtandao. Kwa sababu hata wakati tunaanza hivi vishikwambi watu walisema hivi itawezekana, lakini imeshawezekana sisi wote tunatumia vishikwambi na shuhguli za Bunge zinaendelea vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina suala moja zito sana kwa kuliangalia linaweza kuwa ni la kawaida lakini ni zito. Waheshimiwa Wabunge wengi wanashindwa kuhudhuria vikao vya Baraza katika halmashauri zetu kutokana na shughuli hizo kugongana na shughuli hizo ambazo zinatakiwa ziendeshwe kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati Mheshimiwa Mbunge analazimika kutembea usiku kucha kwa ajili ya kuwahi kikao cha Baraza na kurudi, jambo ambalo linagharimu lakini pia ni hatari kwa maisha yake kwa sababu anakuwa amechoka hata madereva wanakuwa wamechoka. Sasa nilikuwa najiuliza kwa sababu hii Mihimili ya Dola inafanya kazi kwa ushindani lakini pia kwa kuhakikisha wanatoa huduma zinazotakiwa kwa wananchi. Sisi Wabunge tunapokosa kuhudhuria Mabaraza yetu yanapokaa ni kwamba ni mambo mengi tunashindwa kuchangia na kuweza kusimamia halmashauri zetu inavyopaswa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilikuwa nasema niiombe sana Wizara hii ya Habari, Mawasilinao na Teknolojia ya TEHAMA pamoja na Bunge letu Tukufu kuanzisha kona ya Madiwani nikimaanisha Wabunge hapahapa Bungeni. Sisi tunavyokuwa hapa tuweze kuhudhuria vikao vyetu vya Baraza vya halmashauri wakati tukiwa tunaendelea na shuhguli za Kibunge kwa njia ya Mtandao. Kule kwenye halmashauri zetu bado hazijafungwa zile huduma za kuwezesha hayo mawasiliano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana na hilo leo mchango wangu hasa unajikita hapo. Niwaombe kuna mfuko huu ambao ni wa mawasiliano kwa wote ambao umefanya kazi nzuri sana wa kusaidia kwenye maeneo yetu hata huko Vijijini, nawapongeza sana. Lakini pia vyombo vya Habari vinajitahidi, lakini katika hili naomba Wizara yetu hii chini ya wewe Mheshimiwa Waziri Nape Nnauye pamoja na Mheshimiwa Spika wetu sisi tunahitaji hiyo huduma ili tuhudhurie vikao vyetu vya Mabaraza bila kukosa. Haiwezekani Mbunge inafikia unahudhuria vikao viwili tu au pengine kimoja na pengine usihudhurie kabisa simply kwa sababu unakosa mawasiliano kama haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia inapotekea tatizo ni mwanzo wa kufikiri juu fursa nyingine. Kuna tatizo la upandaji wa bei ya mafuta sasa kwa nini tutembeze gari kutwa, usiku kutwa mara mbili, mara tano, wakati pengine kwa kutumia mtandao tu tungeweza kutekeleza hayo majukumu yetu vizuri kabisa. Na nikisema hivyo simaanishi kwamba sisi Wabunge sasa tutakuwa hatuendi kwenye Majimbo yetu. Tunazungumzia kipindi tunachokuwa Bungeni tunataka tuweze kuwasiliana na watu, tuweze kukaa kwenye vikao vyetu vinavyohitajika ili na sisi tuweze kuchangia na kutoa tija kwa wananchi wetu. Hili nalinzungumza kwa kweli nikiwa serious kwa sababu kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu…
MWENYEKITI: Ahsante sana.
MHE. ENG. STELLA M. MAYANYA: Mheshimiwa Waziri Mkuu anatumia sana mtandao katika kuwasiliana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio na Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Mheshimiwa Makame Mbarawa - Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Naibu Mawaziri wote wawili. Pia nampongeza Katibu Mkuu Engineer Asha na Naibu Makatibu Wakuu kwa kazi nzuri. Naomba pia nimpongeze Meneja wa TANROADS Ruvuma, yupo imara. Nawapongeza pia Mkurugenzi wa Mamlaka ya Bandari - Ndugu Erick Hamish na Mkurugenzi wa Shirika la Reli - Ndugu Masanja Kadogosa kwa semina waliyotupa ilituongezea uelewa wa kutosha kuhusu kazi nzuri zinazofanyika.
Mheshimiwa Spika, nina maombi yafuatayo; kwanza ni kujenga kwa kiwango cha lami barabara za Kitai hadi Lituhi na hadi bandari mpya ya Ndumbi; Mbamba Bay hadi Lituhi; na kukamilisha upembuzi yakinifu/wakina Nangombo hadi Chiwindi.
Mheshimiwa Spika, pia ujenzi wa Daraja la Mitomoni; kuanza upembuzi yakinifu barabara ya Noni, Kingerikiti, Tingi hadi Mitomoni; kujenga barabara ya Likuyufusi hadi Mkenda na kuunga Daraja la Mitomoni.
Mheshimiwa Spika, tunaomba boti la fibre ya kutosha tani mbili ili kuvusha watu na mizigo yao wakati tunasubiri ujenzi daraja la Mto Ruvuma (Mitomoni). Aidha, Wizara itenge fedha za kutosha kwa ajili ya matengenezo ya kina kwa kiwango cha changarawe na strips za zege kwenye maeneo korofi. Wilaya ya Nyasa ina milima na mvua nyingi.
Mheshimiwa Spika, pia kuboresha bandari na majengo ya bandari ikiwemo kuweka navigation marks kwa ajili ya kuongozea meli. Ujenzi wa Reli ya Mtwara hadi Mbamba Bay pia hadi Mchuchuma na Liganga.
Mheshimiwa Spika, kimataifa meli za Ziwa Nyasa ziweze kwenda hadi Malawi tufanye biashara. Pia kasi iongezwe ya kuwezesha usafirishaji wa mizigo baina ya Tanzania na DRC bila kulazimika kupitia nchi nyingine.
Mheshimiwa Spika, iko haja ya kuchochea fursa katika maeneo yaliyoachwa.
Mheshimiwa Spika, nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi. Kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu. Pili, nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi pamoja na Naibu wake kwa kazi kubwa ambayo wamekuwa wakiendelea kuifanya pamoja na changamoto mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa unyenyekevu kabisa, kwanza nawashukuru sana kwa josho ambalo walitupa la kule Iringa, limekamilika na soko ambalo limejengwa pale Mbambabay nalo limekamilika. Nawashukuru sana. Siyo kawaida kwa Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi kuweza kufanya kazi kubwa kama hiyo, kwa sababu tulizoea kuwasikia tu katika masuala ya kukamatakamata nyavu na nini, lakini sasa naona mnaenda kuwezesha hawa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na fedha ambayo imetolewa mwaka huu 2022 katika bajeti yao, lakini bado tunaona kwamba Wizara hii inastahili kuongezewa bajeti ikizingatiwa kwamba asilimia kubwa ya wananchi wanaishi katika miambao ya maziwa yetu ambayo ni makuu matatu, Ziwa Rukwa na pia ukanda wa bahari. Watu hao mara nyingi ukifuatilia, kwa kweli wengi wao bado ni masikini. Kwa hiyo, wanahitaji kuwezeshwa zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo nililoongelea kuhusu suala la soko, lile soko inawezekana lisikidhi matumizi yake kutokana na wananchi wa maeneo yale ya mwambao wa Ziwa Nyasa, ambapo urefu wa ule mwambao ni takribani kilomita 150, lakini zana zao za kuvulia ziko duni sana. Mara nyingi nimekuwa nikiomba kwamba kwa nini hao vijana wasiwezeshwe hasa kupata injini za boti kwa mkopo, siyo bure? Ninachopingana nacho ni jambo moja tu la kuwalazimisha kukaa kwenye vikundi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye masuala ya uvuvi kuna watu wana tabia ya kuwa na mazao ya aina tofauti tofauti. Kuna siku mtu anaweza akaamka akasema mimi leo Hapana, siendi ziwani. Leo sitaingia kwenye maji, na kwa hali ya Ziwa Nyasa linahitaji sana kuwa na chombo ambacho ni madhubuti. Sasa kwa misingi hiyo, akipewa mkopo huyo kijana ambaye amethubu, bado hawezi kuvua peke yake, atakuwa anashirikiana na wenzake. Kwa maana hiyo, ajira nyingi zitatengenezwa na wakati huo tutaweza kupata mazao yanayotakiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mara nyingi sana kunatokea vifo kutokana na mitumbwi duni wanayoitumia ambayo haina injini za boti. Kwa hiyo, naomba sana, kwa unyenyekevu kabisa, katika mwambao wa Ziwa Nyasa kwa kweli hawajapewa zana za kutosha hasa hizo injini za boti. Nimekuwa nikizungumza mara kwa mara, hata ukisikiliza leo katika maelezo ya bajeti hii, mambo mengi yaliyozungumza mazuri, yako kwenye ukanda wa bahari, yako angalau kule Ziwa Victoria, lakini haya maziwa mawili; Tanganyika na Nyasa ni kidogo sana, yaani yanatajwa tu kiujanjaujanja fulani hivi. Huoni kamili kwamba kuna mradi gani madhubuti unaopelekwa huko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, msitake tuwe tunaanza sasa kusema kwa nini unapeleka huko? Kwa nini unapeleka huko? Hii ni nchi moja, na kama ni nchi moja itendewe haki. Haiwezekani bajeti kubwa katika hiyo mliyopewa yote inaenda upande mmoja au sehemu chache wengine wanabakia kuwa masikini. Ukizungumzia sijui mambo gani, huko huko. Hata kaka yangu Mheshimiwa Katani pale, alifikia kusema hivyo akaonywa, lakini bado tunasema ndiyo ukweli. Kwa nini maeneo mengine hayaangaliwi inavyotakiwa? Yanapewa fedha kidogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hayo mliyosema sijui kujenga vizimba sijui vitu gani, ukiuliza vizimba vingapi vinaenda Ziwa Tanganyika au Ziwa Nyasa utakuta pengine ni sawa na hakuna. Ndugu zangu hii nchi ni moja, na pengine maeneo hayo ndiyo yanapiga kura nyingi kuliko hata maeneo mengine. Kwa nini mnatufanyia hivyo? Naomba safari hii kwa kweli nisikie kinagaubaga katika hizo injini za boti zitakuwepo, na zitapelekwa kiasi gani katika upande wa Ziwa Nyasa?
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, niseme tu kwamba vilevile tumezungumzia juu ya kuwawezesha vijana kupata ajira zao, kwa sababu sio wote wanapitia mpaka elimu ya masomo ya juu, lakini hakuna mitaala ile ambayo inaweza ikaelimisha watu kwa vitendo kujua kwamba watajifundisha kuvua au kutengeneza zana mbalimbali kama boti na wakapata vyeti. Unakuta watu kama hao hawatambuliki, kumbe watu siku hizi wanapenda kutembea na vyeti. Ni namna gani Wizara yenu itaunganika na Wizara ya Elimu katika huu mchakato unaoendelea wa kutoa mafunzo kwa vijana hasa wale ambao hawajamaliza masomo yao yaani wale dropouts, wanaweza wakajikita katika maeneo hayo, kwa sababu wao wanapenda kwenda katika masuala ya kiuvuvi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tumeona katika Wizara ya Kilimo wanapima afya ya udongo. Ninyi Wizara ya Mifugo na Uvuvi, hasa kwenye uvuvi mnapima vipi afya ya ziwa kujua kwamba eneo hili lina samaki wengi na eneo hili halina samaki wengi? Ninyi mnatumia mbinu gani kuwaelimisha wananchi ili wajue kwamba eneo fulani usiwe unaenda, nenda eneo fulani ambalo mara nyingi utapata samaki na kuna mazalio, labda muepuke kuvua hapo, vueni hapa ili mradi wapate faida inayokusudiwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama wenzenu wanapiga hatua katika maeneo yao na ninyi vilevile sasa mtusaidie kuweza kuona kwamba mtu asiwe anatembea usiku kucha anavua, usiku kucha anaparaza mtumbwi, anahangaika kutafuta Samaki, mpaka inafika asubuhi hajapata hata samaki mmoja, kumbe amepigananao chenga humo humo kwenye ziwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nirudi kwenye suala la mifugo. Wilaya ya Nyasa hasa maeneo ya mwambao kuna changamoto kubwa sana ya ugonjwa wa mapafu ya ng’ombe. Hawana ng’ombe wengi sana, lakini huyo huyo mmoja au watatu walionao ni muhimu sana kwao. Sasa unakuta mara nyingi utaambiwa ng’ombe alipochinjwa alikuwa na konokono; anaumwa sijui konokono; wanaita konokono, lakini hakuna tiba zinazoeleweka kabisa kwamba kukitokea tatizo fulani wanaenda mahali fulani.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata zile ruzuku zinazotolewa kwa ajili ya ng’ombe, kule sijui kama hata zinafika. Nimefuatilia, hakuna ruzuku iliyofika siku za karibuni, na zile dawa ni ghali, nyingine zinafika mpaka Shilingi 35,000/=, wakati mwingine wanamtibu ng’ombe kwa madawa chungu mbovu, yaani ni ile tu kukisia sasa tumtibu kwa magonjwa ambayo wanahisi ndiyo yatakuwa yenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, wataalam wa mifugo pia ni wachache sana katika Wilaya ya Nyasa. Kwa hiyo, naomba kuiangalia wilaya hiyo ili kuiwezesha sasa kuweza kupata wataalam watakaoweza kusaidia katika maeneo hayo ya mifugo hususan katika ng’ombe na mbuzi vilevile.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijamalizia ya kwangu, nisije nikasahau, nilikutana pia na viongozi wa Chama cha Wavuvi pale Canteen, wamenipa maelezo yao, naomba niwakabidhi na yenyewe, mtayapitia kadiri walivyoandika wao wenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, vilevile kuna kuwezesha vijana katika masuala ya mabwawa ya samaki hasa Ukanda wa Juu katika Tarafa ya Mpepo, yaani Kata ya Kingerikiti, Mipotopoto, Luhangarasi, Tingi na Lumeme; tuseme kata nane za Tarafa ya Mpepo. Naomba wawezeshwe kwa sababu hao wangependa sana kufuga Samaki. Nilileta barua kwako Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo, naamini katika bajeti hii utakuwa pia nao umewakumbuka ili waweze kupata kitoweo na pia afya njema kutokana na samaki.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kimsingi tunaona Wizara hii ikijitahidi kwenda lakini bado tunasisitiza umuhimu wa wavuvi na watu wa mifugo kupewa fedha ya kutosha ili nao waweze kufanya kazi zao vizuri.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Ahsante, kengele ya pili hiyo.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote napenda kumpongeza Mheshimiwa Angelina Mabula (Mb) na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Nampongeza pia Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete (Mb) na Naibu Waziri, Ndugu Allan Kijazi - Katibu Mkuu pamoja na Naibu wake Ndugu Nicodemus Mkapa kwa kazi nzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina maombi yafuatayo; kwanza kumaliza mgogoro wa Lipalamba Game Reserve na Kijiji cha Mseto kilichopo kata ya Lipalamba; pili, Wilaya ya Nyasa ni changa sana kimapato. Tunaomba mkopo ili kupima maeneo ya fukwe yote na Mji wa Mbamba Bay ili usijengwe kiholela.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza Mheshimiwa Dkt. Dorothy Gwajima (Mb), Waziri wa Maendeleo ya JamiII, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum; na pongezi kwa Naibu Waziri Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis (Mb). Pia nampongeza Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara.
Mheshimiwa Spika, kuhusu 10% inayotolewa na Halmashauri kwa ajili ya mkopo, nashauri ipatikane system maalum itakayohusika kusimamia vizuri ukopeshaji na ukusanyaji wa madeni kama ilivyo kwa mabenki. Pia vituo vya ushauri nasaha hakuna. Serikali ifungue dirisha maalum either kwenye vituo vya afya au ofisi za kata ili kusaidiwa. Familia nyingi zina changamoto za kifamilia, zinaumwa lakini hazina pa kukimbilia (counselling centres).
Mheshimiwa Spika, uhamasishaji wa maendeleo ya jamii upewe mwongozo maalum na wafanye mikutano ya hamasaki mara kwa mara. Pia umeanza unyanyapaaji wa wazee hata kuwasemasema bila heshima.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maliasili na Utalii
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Chana, Mbunge na Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Mary Masanja, Mbunge. Vilevile nimpongeze Dkt. Francis - Katibu Mkuu pamoja na Naibu Katibu Mkuu Ndugu Mkome.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nampongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuhamasisha na kuutangaza utalii wetu. Nasi Wilaya ya Nyasa tunamuunga mkono.
Mheshimiwa Spika, maombi, kwanza kumaliza mgogoro wa Lipalamba na wanakijiji wa Kijiji cha Mseto; kusaidia kutengeneza barabara zinazopita kwenye hifadhi ya Lipalamba ambazo zinahitaji kifusi kutoka mbali; tunaomba shilingi 5,000,000 kwa ajili ya kukamilisha zahanati ya kijiji cha Mipotopoto kinachopakana na Hifadhi ya Lipalamba na huo mkakati wa utalii kwenye maziwa makuu ikiwemo Nyasa umetajwa kwa kifupi sana. Naomba ufafanuzi ni kitu gani kitafanyika?
Mheshimiwa Spika, niliomba kujenga hosteli ndogo kwenye hifadhi hiyo ili kuanzisha utalii wa eneo hilo. Hadi leo sikujibiwa; je, Wizara yenu haina utamaduni wa kujibu barua?
Mheshimiwa Spika, nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, nawapongeza Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mheshimiwa Mohammed Mchengerwa (Mb) pamoja na Naibu wake Mheshimiwa Paulina Gekul (Mb). Nawapongeza pia Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu, watumishi wote wa Wizara na wanasanaa na michezo wote.
Mheshimiwa Spika, nawapongeza timu ya wanawake Twiga Stars na kwa namna ya pekee nampongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa ya kujitoa kuhamasisha utalii na michezo ikiwemo kuwafadhili vijana wa Twiga Stars pamoja na kuwapatia viwanja kwa ajili ya maisha yao ya mbele. Napongeza pia kwa kuwaenzi waasisi wetu kupitia sherehe na makongamano mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, maombi yangu; kwanza Wilaya ya Nyasa katika kuimarisha michezo tumeamua kuanza kujenga uwanja wa michezo. Tunaomba support yenu ya hali na mali ikiwemo kusaidiwa nyasi za bandia na michango ya fedha kutoka kwa wadau mbalimbali na pili, tunaomba pia mtutembelee Nyasa ili kutuhamasisha.
Mheshimiwa Spika, nawasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, nianze kwa kumpongeza Waziri wa Fedha na Mipango Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba kwa kazi kubwa anayofanya hasa katika kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi yetu unaendelea kuwa imara. Nampongeza pia Mheshimiwa Hamad Hassan Chande - Naibu Waziri, Ndugu Emmanuel Tutuba – Katibu Mkuu Fedha na Mipango, pamoja na Naibu Katibu Mkuu pamoja na timu yote ya Wizara. Kwa namna ya pekee nimpongeze mwenye fedha mkuu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan - Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, nina maombi yafuatayo; naomba mtupitishie maombi yetu ya fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa ofisi ya Halmashauri ya Nyasa, taarifa za ngazi zote zipo tayari na imebakia ruksa yenu. Hata hivyo natoa shukrani nyingi kwa hatua iliyofikiwa.
Mheshimiwa Spika, ili kuboresha huduma za kikodi tunashauri Wilaya ya Nyasa nayo ijitegemee ki-TRA badala ya kuwa mtoto wa Mbinga.
Mheshimiwa Spika, nawasilisha.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudia Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi. Kwanza niungane na wenzangu kukupongeza sana kwa kuwa na hiki kiti kipya, Rais wa Mabunge ya Dunia, kwa kweli umekuwa ni mfano wa kuigwa na Watanzania tunajivunia sana. Tunamshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili yako wewe mwananunu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuendelea kuwaletea maendeleo wananchi Watanzania wakiwemo Jimbo langu la Nyasa. Pia nawashukuru na kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote wawili wa Mipango, pamoja na Fedha kwa jitihada kubwa wanazozifanya kutika kuhakikisha kwamba nchi yetu inakwenda vizuri kimaendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupongeza pia ni kuwatia watu moyo. Nawashukuru sana, Mheshimiwa Mkuu wangu wa Mkoa wa Ruvuma, Mheshimiwa Kanali Laban Thomas na Mkuu wangu wa Wilaya ya Nyasa Mheshimiwa Sanga, kwa kweli wanajituma sana. Mwenyezi Mungu awasaidie pamoja na wengine wote wanaowasaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo jambo langu litajikita hasa kupitia mipango hii katika eneo la maendeleo jumuishi na hapo naangalia katika maendeleo endelevu ya mwaka 2030 lengo la tatu la afya pamoja na kuleta ustawi wa watu. Katika mipango hii inayoletwa mbele yetu, watu ndiyo kiini, watu ndiyo jambo kubwa kuliko jambo lingine lolote lile. Kwa hiyo, napenda kujikita hapo, na kwa sababu mipango inapendekeza kuangalia maendeleo jumuishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka nijikite katika suala la lishe. Nimejiuliza sana, mimi siyo mtaalam sana katika masuala ya afya, lakini kama mtu ambaye huwa napenda kulisikia jambo na kulifanyia mkazi, napenda kujiuliza sana, katika mikoa ambayo inaongeza kwa udumavu ni ile mikoa ambayo inaongoza kwa kilimo au kutoa chakula katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia mikoa hiyo nauona Mkoa wa Ruvuma upo ndani, Iringa upo ndani, Mbeya upo ndani, Njombe upo ndani, Katavi, Rukwa, hasa maeneo haya ya magharibi, sijui wenzetu wa Kigoma safari hii wameponapona vipi; Mtwara na wenyewe wapo kule kusini japo hawapo nadhani ni kwa ajili ya kula korosho na mbaazi, lakini najiuliza ni kwa nini mikoa ambayo inazalisha sana ndiyo inakua na udumavu uliopitiliza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imeanza kuzungumzwa siyo leo, toka miaka ya 2010 tumeanza kupata taarifa hizo. Nimefuatilia, tunapata majibu tu kwamba hawali mchanganyiko wa vyakula na nini. Najiuliza, mbona nikifika hapa Dodoma tunakula tu vile vile, tunafanana fanana? Tofauti ni nini? Nikaona pengine kuna suala lingine ambalo halijapata majibu na halijafanyiwa kazi. Mimi nimeanza kuunganisha udumavu na ukosefu wa miundombinu ya uhakika kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia upande huu wa magharibi ya nchi yetu kwa muda mrefu suala la miundombinu na mipango ya kimkakati ya kimaendeleo kidogo ilikuwa inaenda siyo sawa na maeneo mengine katika nchi. Kwa hiyo, inawezekana hiyo ikawa ni sababu. Nikiangalia sasa hivi hata tunapozungumzia reli, mchuchuma; reli itoke Mtwara mpaka Mbamba Bay hiyo tunaizungumza na msishangae tukafika miaka bado tunazungumza tu. Bandari ya Mbamba Bay tunazungumza tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukanda huu wa kuunganisha kutokea Mbamba Bay unakuja mpaka Ludewa mpaka Mbeya ambao ni nzuri sana kwa utalii ingeongeza uchumi, upo tu, hakuna barabara huko. Ndiyo maana maeneo hayo yote yamedumaa. Kwa hiyo, nilikuwa napenda kumwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Mipango, hebu tuangalie kwa kina, hili suala la udumavu katika mikoa hii niliyoitaja unatokana na nini? Ni kweli kula chakula tu? Kama ni chakula, ni kwa sababu gani huko tu ambako sisi tunazalisha zaidi? Kwa hiyo, iko haja ya kutafuta mambo mengine ya kina ya kusaidia mikoa hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nategemea katika mpango wa maendeleo unaokuja, suala la udumavu litawekewa mkakati maalum ili kuhakikisha kwamba Taifa hili linatendewa haki kwa watu wote. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nafuatilia hata kwa watu ambao wamebahatika kupata ufadhili wa Benki Kuu wa kwenda kusoma. Nikisikiliza majina, kwa sababu ya ufaulu mkubwa nakuta majina hasa yanakuwa ya upande mmoja. Tunafurahi kwamba wachukuliwe waliofaulu vizuri, lakini yawezekana maeneo mengine huu udumavu ndiyo umechangia hata hawawezi kupata hiyo nafasi. Kwa misingi hiyo, hilo ni suala la hatari katika nchi. Ni lazima tupate jibu la uhakika kwa nini udumavu unaendelea kuwa katika mikoa hiyo hiyo miaka yote na siyo katika mikoa mingine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimejiuliza hata kule Kagera, nao kwenye kiwango cha umaskini kila mwaka wanatajwa, lakini akina ushomire ndio wanatoka huko, kwenye udumavu pia wapo. Sababu ni zipi? Hatuwezi kuendelea kuwa na majibu rahisi. Ni lazima tuangalie kwa kina mikoa hii ambayo kila siku inatajwa kuwa ina udumavu, ipate majibu ya uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, tunasema kwamba tunaanglia wananchi wetu waweze kuwa na ustawi wa afya njema, lakini pengine hizi shida zinatokea toka kwenye kuzaliwa kwao. Tumejitahidi tumejenga vituo vya afya vya kutosha, sasa hivi na watumishi tunapeleka, lakini suala la kujifungua haliishii tu kujifungua salama kwamba mama ana mtoto, mama yuko mzima wakati wa kujifungua. Anajifungua mtoto wa aina gani? Kuanzia tumboni mtoto aangaliwe lakini pia hata kwenye kujifungua, wapo wakunga. Sasa hivi tunapoajiri tunafanya kwa ujumla, nurse anaajiriwa kama nurse, lakini pengine hatuangalii wale wakunga. Ndiyo maana wakunga wa jadi bado wana heshima zao kwa namna wanavyowasaidia akina mama kwenye kujifungua na kuondoa changamoto kama hizo.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Haya, ahsante sana.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba katika mfumo wetu wa utumishi uangalie Mkunga ana nafasi gani katika ajira?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Nyasa nianze na kumshukuru sana sana sana Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake yote na kwa bajeti hii inayoongozwa sasa na Mheshimiwa Waziri Mwigulu kwa jinsi ambavyo wameweza kutekeleza shughuli za kimaendeleo katika Jimbo langu la Nyasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa usimamizi wao kwa kazi zote zinazoendelea. Kwavile siyo rahisi kumshukuru kila mmoja, niseme tu nawashukuru wote waliohusika katika kuleta maendeleo katika Jimbo langu la Nyasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuishukuru Serikari kwa kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami, barabara ya kutoka Kitai kwenda Litui hadi Ndumbi. Pia naomba watusaidie juu ya Daraja la Mitomoni ambalo liko katika Mto Ruvuma ambalo kwa kweli limekuwa ni kilio kikubwa kwa wananchi na wananchi wamekuwa wanapata shida wengine kiasi cha kufariki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati nzuri yalipotokea yale maafa, Serikali ilipeleka timu wakafanya feasibility study kiasi kwamba lile daraja sasa liko tayari kwa kuanza kujengwa. Ni imani ya wananchi kwamba daraja hilo litajengwa ili kuondoa adha iliyopo na pia hata hali ya kimawasiliano ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii napenda nizungumzie kama ushauri kwa upande wa Serikali. Serikali imetufundisha jambo moja kubwa sana kupitia mkopo wa masharti nafuu ambao uliletwa kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa madarasa. Katika hilo nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jinsi ambavyo mkopo huu ulifanyiwa kazi. Fedha iliyotolewa ni Shilingi trilioni 1.3, lakini fedha hii inajulikana na kila Mtanzania, kila mtu anajua kwamba kuna mkopo wa Shilingi trilioni 1.3 umeenda kufanya kazi hii na hii na hii, kiasi kwamba mpaka unaweza kufikiria kwamba ah, hivi ina maana kumbe kwa mwaka mzima yawezekana fedha iliyofanya kazi ni hiyo tu. Kwa sababu zile fedha nyingine tunazokusanya tumeambiwa ni karibu Shilingi trilioni 20 na kitu, hazioneshi moja kwa moja zimeenda katika matumizi yapi? Pamoja na kwamba kweli tunajua zimeenda kwenye wilaya zetu, lakini hazijawekwa kwa uwazi mzuri kama zilivyoweka hizi fedha za COVID-19. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda kuona kwamba, kwa kuwa tunafanya hayo makusanyo na tumekuwa tukipeleka fedha huko, basi kila Wizara iwe inatoa orodha ya vitu ambavyo vinaenda kutekelezwa huko kunakotekelezwa, tuweze kuona kabisa Wizara hii ilipata fedha kiasi fulani na zimeenda mahali fulani ili tuweze kusimamia kwa karibu kama ambavyo tulisimamia haya madarasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulijaribu kuona kwamba kama shilingi trilioni 1.3 ilifanya kazi kubwa hiyo nchi nzima, haya matrilioni mengine je, ukiondoa ile mishahara ya wafanyakazi na vitu vingine! Tukiamua hata Shilingi trilioni tatu tu hizi kwamba sasa zitaenda kufanya hili na hili, nina uhakika na tukijipangia muda tutaweza kupiga hatua kubwa sana katika maendeleo yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ninalopenda kuchangia ni eneo la Wamachinga na ile asilimia 10 iliyozungumzwa kwamba ipunguzwe asilimia tano kwa ajili ya miundombinu. Kwa bahati nzuri eneo hili nimelifanyia kazi kwa kipindi kirefu. Niseme tu kwamba kundi hili la Wamachinga, siyo kwamba Wamachinga ni wale wanaotembea tu. Wamachinga wamekuja kutoa jina hilo kutokana na ule ubunifu wao wa kufanya biashara kiasi kwamba sasa hata wale wajasiriamali wadogo wenye mtaji kuanzia shilingi 1,000 mpaka shilingi milioni 50 wanaangukia katika kundi hilo la Wamachinga. Kimsingi ni wale wajasiriamali wadogo wadogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kuzungumza kwamba ipo haja ya kuiga mtindo tunaowafanyia nyuki. Nyuki unamtengenezea mzinga, yeye anakupa asali. Sasa na hawa Wamachinga wanafanya biashara ambazo ukijumlisha katika ile thamani ya kazi wanayofanya ni fedha nyingi sana na wanatengeneza ajira nyingi sana katika nchi yetu. Ila kwa kuwa kundi hili hatujalitambua kikamilifu na kulipa haki kamili ya maeneo ya kufanyia kazi, ndiyo maana wakati mwingine tunampa pressure hata Mheshimiwa Rais, Wamachinga wetu wapate maeneo ya kufanyia kazi; wote tunachangia humo. Leo linapokuja suala la kusema kwamba tuanze sasa kutengeneza mazingira bora ya hawa watu kufanyia kazi, wote tunaruka. Tunasema ah, bora watu wakakopeshwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaambie ukweli, katika baadhi ya maeneo, hata ufuatiliaji wa hawa watu wanaokopeshwa unakuwa ni mgumu kwa sababu hawajulikani waliko. Unakuta watu wanapewa fedha tu kwenye kikundi wanaganagawana mambo yanakwisha. Imekuwa ni kama fedha za msaada badala ya kuwa ni fedha za kuwawezesha katika masuala ya kibiashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya nasema mimi kama mimi na ninasimama mimi kama mimi. Najua Waheshimiwa Wabunge wengi wamekuwa upande tofauti, lakini kazi ya Bunge ni kila mtu anashauri anavyoona. Nasema wazo hili ni zuri sana, isipokuwa tunaweza tukaamua kuanza na maeneo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano Jimbo langu la Nyasa natamani liwe mfano, nami naunga mkono asilimia tano ikatengeneze miundombinu na asilimia tano wakopeshwe, na wale watakaokuwa wamekosa, waendelee kwenda benki kwa sababu benki zipo. Benki ya NMB ipo, CRDB ipo na mabenki mengine yapo. Hayo ndiyo tuwape sasa kazi ile ya kukopesha zaidi. Isitoshe mifumo yetu ya ukopeshaji inabidi na yenyewe itengenezewe utaratibu kama wa kibenki. Kwa sababu sasa hivi hata ukopeshaji wake saa nyingine hata taarifa haziko sawa sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano. Pale kwangu Bambabay palikuwa hapana mazingira mazuri kabisa ya kupata chakula, nikaamua bora nitafute fedha ili waweze kupewa sehemu ya kufanyia kazi. Nikakaa nao, nikawashawishi, tukavunja mabanda yale ya biashara ambayo yalikuwa ya ovyo kabisa. Baadaye tukajenga mabanda mazuri, sasa hivi kila mtu anaenda pale na shughuli za kibiashara zimekuwa kubwa zinazidi kuongezeka. Huu ni mfano mdogo tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mialo yetu mingi ni mibaya, ya ovyo kabisa. Ninazo picha hapa nitawaonesha. Hawasaidiwi hawa watu, kila siku wanakuwa ilimradi tu, ndiyo maana hawakui. Tunajiuliza kila siku, kwa nini hawa wafanyabiashara wadogo wadogo hawakui? Moja ya sababu ambayo kiutaalam imeelezwa ni maeneo ya kufanyia kazi ni hafifu. Siyo lazima kujenga soko kubwa sana, labda eneo kubwa kama labda tulivyofanikiwa Dodoma, hapana. Hata kama ni maeneo madogo madogo, lakini mtu afanye kazi zake kiunadhifu; na wanapokaa pamoja, wanapeana ujuzi na pia wanasaidiana hata katika mambo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nasimama, nasema Serikali hata kama wazo hili itatokea kwamba wengi wamelikataa, mimi naliunga mkono. Naomba mkafanye pilot, yaani kama sehemu ya kujifunzia; kwenye Wilaya yangu ya Nyasa naliunga mkono. Yaani ninachoomba, tutoe flexibility. Wanaotaka zote kukopesha, hiyari yao; wanaotaka 50 kwa 50, hiyari yao; ilimradi taarifa ziwe wazi na watu waweze kusaidiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi. Nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa rehema zake, lakini pia nikushukuru wewe mwenyewe kwa namna ambavyo unaongoza Bunge letu vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hatuwezi kuchangia kabla hatujamsemea Mheshimiwa Rais na wanaomsaidia. Kimsingi Mheshimiwa Rais pamoja na timu yake inayomsaidia, tukianza na Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu lakini na sisi tukirudi kwenye Bunge letu, Mheshimiwa Spika, tuko vizuri na ninaona tunakwenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuwapongeza Waheshimiwa Wenyeviti wetu wote ambao wamewasilisha taarifa zao hapa. Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Maji na Mazingira pamoja na Mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama. Nawapongeza sana kwa taarifa zenu zote ambazo zinalenga kuisaidia nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri ambao wnasimamia sekta ya maji pamoja na mazingira kwa ujumla wake kwa kweli wanajitahidi. Wanajitahidi sana pamoja na wale wote wanaowasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo naomba nirudi kwenye suala linalohusiana na Sheria Na. 11 ya mwaka 2009, kifungu namba 23 ambacho kinahusisha Sheria ya Usimamizi wa Matumizi ya Rasilimali Maji. Pia, hapo naomba kwa kweli nirudie kusema ambayo pengine wengine walisema. Hata hivyo, kwa unyeti wa suala hili inabidi lazima nirudie tena. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kufahamu mimi kama Mbunge ninayesimamia sekta ya maji, lakini kama Mhandisi wa umeme; nataka kufahamu kwa nini Bwawa la Mtera halina maji? Tunahitaji majibu ya uhakika kwa nini Bwawa la Mtera halina maji? Nikizungumzia Bwawa la Mtera inamaana ni Mtera itaambatana na Kidatu, itaambatana na Kihansi, kwa sababu wote hawa wako kwenye mstari mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili ni suala muhimu sana kulitafakari. Ni muhimu sana kwa sababu gani? Nchi yetu tumekwishapitia changamoto nyingi za kupatikana kwa umeme, na chanzo chake ni ukosefu wa maji kwa sababu tumekuwa tukitegemea sana umeme wa maji. Kwa bahati nzuri Mwenyezi Mungu ametupatia maji kwa kiasi cha kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, inashangaza, inashangaza sana. Mara ya mwisho nimepita pale Mtera tarehe 9, ilibidi nisimame nipige picha. Niliomba kama Mjumbe wa Kamati japo hawaruhusu. Niliomba, nikasema kwamba hivi ni kitu gani? Maana mpaka sasa magugu yameanza kuota yanaingia mle kwenye bwawa. Ni kitu gani hiki? Mvua zinanyesha kote kabisa na zinanyesha kila siku. Hivi kweli ukame uko Mtera tu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hatuwezi kuendelea kupeana majibu rahisi rahisi, haiwezekani. Tunategemea sasa hivi nchi nzima iwashe umeme kupitia vijiji vyetu tunavyovisambazia umeme. Vile vile tunawahamasisha wawekezaji wa aina mbalimbali waje kuwekeza Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huu umeme tunaouzungumzia wa Bwawa la Mwalimu Nyerere megawatt 2,100 haziingii leo kwa mara moja. Zitaingia awamu kwa awamu. Tumeambiwa hapo kwamba, zitaanza megawatt 235, zitafuatia megawatt 235, jumla yake 470 na kadhalika. Sasa, wakati huo unapofanya hiyo kazi, unaingiza megawatt 470 lakini una-phase-out (unazitoa kwenye system megawatt 473), yaani ukijumlisha 80 ya Mtera, 204 Kidatu, 189 ya kule Kihansi unazitoa kutokana na upungufu wa maji halafu unasema unaingiza nyingine. Hii hesabu ya kutoa na kujumlisha inatupatia kitu gani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naifikiria nchi hii kuna watu wanatuchezea. Hata hawa watu ambao wanaokuja kutusaidia kwa mfano kwenye suala la utafiti au uandaaji wa miradi lazima tuwe nao makini. Mbona tunao wasomi wengi kwa nini kila siku tunarudi kwenye tatizo hilo hilo? Tutasema haya tusubiri Malagalasi nayo tunaijenga, sawa tunajenga labda megawatt kama 70 mpaka 80, Rusumo imeingia, lakini kwa sababu ya kutokutunza hivi vyanzo vya maji, kutokuwa na mawasiliano katika utekelezaji wa miradi yetu ya maendeleo, matokeo yake hata hiyo itakauka hivyo hivyo. Ni nani huyu aliyeamua kutuangamiza?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naongea haya kwa uchungu. Nimesema hili na nilisema siku ile nisichangie siku ya Kamati ya Nishati kwa sababu niliona kwanza nisimuonee Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, ameingia juzi japo ni sekta anaendelea nayo. Nimesema nianzie na hawa watu wa maji tunaowasimamia, kwa nini hawasimamii matumizi bora ya maji? Kwa nini wanaleta hii changamoto?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunafurahia hapa. Wizara ya Kilimo na yenyewe inasema nitachimba mabwawa, nitapeleka umwagiliaji na nini inatoka, wa mifugo anasema vya kwake vinatoka. Kwa nini hakuna usimamizi wa pamoja tukajua wewe wa kilimo utachukua maji kiasi fulani na utachukulia eneo fulani, huyu hapa anayehusika na mifugo atachukulia eneo fulani lakini sasa tumekuwa tunakwenda na kila mtu anapambana kwenda kivyake. Hii hatuiweki vizuri nchi yetu katika hali inayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni namna ambavyo tunavilinda hivi vyanzo. Kwa mfano, Dar es salaam kila mwaka mafuriko, mara sijui mafuriko, mara sijui madaraja yamebomoka. Hivi nyie mnataka hela yote iwe inakwenda kujenga Dar es salaam tu? Sisi huku tunasubiri mpaka lini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ukiangalia mahali kama mle Vigunguti kwenye mabonde hapakuwa na nyumba, zinajengwa tu, kwenye mabonde; usimamizi ni mdogo, matokeo yake kila mwaka sisi ni watu wa kulia sijui nyumba zimechukuliwa. Watu kwa akili zao wanakwenda kujenga kwenye mifereji ya mito halafu wanalia maji yanawaondoa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nadhani, wizara inayohusika na Mazingira na tena bahati nzuri iko chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, ichukue nafasi yake katika kuongoza mapambano katika kuhifadhi mazingira yetu. Si hivyo tu, tunashauri kwamba, iwe sasa ndiyo msimamo. Wizara hiyo ipewe meno ya kutosha katika kuhakikisha kwamba Wizara zote zinawajibika na kutoa taarifa maalum kabla haijafanya mradi wowote ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo nikirudi upande wa maji. Tunasema kwamba, maji vijijini karibu tunafika asilimia 75, mjini asilimia 85. Hata hivyo, hizi taarifa za ujumla zinaumiza baadhi ya maeneo. Juzi jumamosi iliyopita tulikuwa Tabora. Nilipata huzuni kujua kwamba Wilaya ya Urambo pale Urambo Mjini mpaka sasa asimia ya maji ni 24.5 tu. Watu wa Nyasa wanisamehe, mimi ni Mbunge wa Nyasa na wa kitaifa, lazima pale tunapoona kuna mapungufu tuwasaidie wenzetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Urambo ina hali mbaya, Sikonge ina hali mbaya. Pamoja na kuwa na huu Mradi tunaoutegemea wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka huku, Mradi huu uharakishwe na usaidiwe. Hata kama pesa zinakuwa hazitoshi, basi hawa wapewe jicho la kipekee ili waweze kupata maji. Yako maeneo kama hayo katika nchi yetu yafikiriwe na yapewe Kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukienda kwa ujumla ujumla kweli kuna watu wanaumia lakini tunafikiria kwamba tuko nao kumbe wenzetu wana hali mbaya sana. Mimi binafsi siku ile nilitaka kutoa machozi niliposikia kwamba kule walipoanzia machifu, kwa akina Mama Sitta, akina Mzee Sitta aliyesimamia Bunge hili, Jimbo lile halina maji kabisa, maana yake nini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mimi ninaomba sana, nafahamu Wizara inajitahidi sana lakini kusema kweli katika hili sisi tutakuwa mstari wa mbele kuanza sasa kufuatilia kwa karibu, kuona kwamba maeneo yale ambayo yana changamoto kubwa yaweze kusaidiwa. Jambo lingine tunasema kwamba katika ulinzi huo basi ni vyema ushirikishwaji uwe mpana zaidi hata kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno yangu haya nakushukuru sana naunga mkono hoja ya Kamati ya Maji na Mazingira. (Makofi)
Taarifa ya Kamati Maalum iliyoundwa Kuchunguza Mgogoro wa Ardhi kati ya Mwekezaji kwenye Shamba la Malonje na Vijiji Vinavyolizunguka Shamba hilo Kikiwemo Kijiji cha Sikaungu katika Jimbo la Kwela
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa hii nafasi. Nami niungane na wenzangu kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu.
Mheshimiwa Spika, pili, nakushukuru wewe mwenyewe kwa kuniamini na kuniweka katika Kamati hii japo kwangu mwanzo ilikuwa ni jambo gumu sana ikizingatiwa kwamba nami niliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na baadhi ya mambo niliwahi kuyaona toka kipindi hicho na nikaja kushtuka kuona kwamba mambo hayo bado yanaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sisi wote humu ndani tumeapa kuilinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katiba yetu mpaka leo haijabadilika kwamba sisi ni wananchi tunaofuata misingi mojawapo ikiwa ni misingi ya ujamaa inayozingatia udugu na amani. Nikisema ujamaa wengine wanashtuka. Msishtuke, ndiyo misingi iliyotujenga na ndiyo maana hata mpaka leo tunapofanya mambo yetu tunazingatia huyu mwananchi ana hali gani? Anapata nini? Tupange mambo yetu kwa haki ili wote tuweze kunufaika na tuwe na nchi moja yenye amani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa dhati kabisa Mheshimiwa Mwenyekiti wetu kwanza tunampongeza kwa taarifa ambayo ameisoma kama tulivyoshaurina, lakini kwa unyenyekevu mkubwa na kwa kutoa taarifa za wale wananchi kukushukuru wewe kwa kuthubutu kuunda Kamati hii ili iweze kuchunguza zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, binafsi nimewahi kuwa Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji. Kwa hiyo, nathamini kabisa uwekezaji na hasa Mtanzania au Watanzania wanapothubutu kuwekeza. Tunatarajia sasa uwekezaji wa hawa Watanzania uwe ni mfano na alama ya uwekezaji tunaoutaka katika nchi yetu kwa sababu wanafahamu vizuri shida za Watanzania wenzao, wanafahamu vizuri mazingira yetu, wanafahamu vizuri nini maana ya ardhi na kila linalotakiwa.
Mheshimiwa Spika, Katiba yetu kama ilivyosemwa Ibara ya nane inazungumzia lengo la Serikali ni kuleta ustawi wa wananchi. Ibara ya tisa ndiyo imefafanua kwa kirefu mno mambo mbalimbali tunayopaswa kufanya. Hapa ningependa kuinukuu hii 9(i) inayosema kwamba matumizi ya utajiri wa Taifa yatilie mkazo maendeleo ya wananchi na hasa zaidi yanaelekezwa kwenye jitihada ya kuondoa umaskini, ujinga na maradhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, masuala haya yanayoendelea pale Rukwa, kuna wenzetu tunawaacha waendelee kuwa kwenye dimbwi la umaskini, wataendelea kuwa na changamoto nyingi, kwa hiyo, hao maadui wakuu watatu hawataondoka. Hili jambo lina muda mrefu. Kama ni mtoto amezaliwa mpaka ameenda shule, tufikie mahali liishe.
Mheshimiwa Spika, nafahamu wengine wanakuwa na hofu, Serikali italipa hela nyingi sana, Serikali itakuwaje? Jamani hawa mbona wanaamua tu hiyo hawaangalii! Hakuna gharama katika kuondoa shida za wananchi na hakuna gharama katika kutoa haki kwa wananchi. Tumesema haki haikujengwa katika misingi sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nchi hii ni yetu, na kama ni yetu lazima wote tunufaike nayo kwa uzuri kabisa. Nisingependa nizungumze zaidi, lakini tukumbuke, Taifa hili sasa hivi lina vijana wengi kuliko sisi watu wazima. Pale Sikaungu kote tulipopita vile vijiji ni vijana wenye nguvu wanaotakiwa kupata ajira zao kwa kutumia rasilimali msingi ambayo ni ardhi. Hawana ajira nyingine, lakini wapo. Hata watoto wameshajenga roho ile ya uadui, ya chuki, ya kuhuzunika kwamba hapa tunanyanyaswa. Kwa hiyo, ni kizazi kinaendelea kukua katika misingi kwamba hatuwasikilizi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yawezekana kuna gharama zitahitajika, lakini Serikali hii imeshawahi kulipa fidia za barabara ili tupate barabara, Serikali hii imeshawahi kulipa fidia kwa mambo mbalimbali ya msingi ilimradi wananchi wake wawe na ustawi. Katika hili, Serikali isimame pamoja na Bunge kuhakikisha mgogoro huu unaisha kwa kutatua tatizo hili kama ilivyopendekezwa, iwe ni mwanzo na mwisho.
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri wangu mpendwa Mheshimiwa Mzee Lukuvi leo ni Waziri wetu wa Sera, Bunge na Uratibu, tunashukuru kurudi tena kwenye nafasi hiyo na tunampongeza. Tuliongozana wote tukaenda kule Rukwa na alikuwa ameanza vizuri. Kama siyo kesi ile kusimamishwa, alikuwa ana nia njema. Basi Mungu amemrudisha, amalizie tena jambo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme kwamba wawekezaji wamepitia na wenyewe changamoto nzito nyingi kwa sababu jambo hili hata hili la kubaka na vitu gani siyo kwamba vyote vimefanyika leo, ni hatua za safari yote hii tunayoizungumza.
Mheshimiwa Spika, sasa mambo kama hayo, watu wanaongea na tunazo hata video zao ila hatuwezi kuziweka hadharani. Kwa hiyo, ni mambo ambayo ni mazito, siyo nchi hii ya Tanzania. Tanzania haina tabia hii. Hatuwezi kuendelea kuishi kama hivi.
Mheshimiwa Spika, pia kuna wadau wamenifuata hapa wanasema, mama sema tena basi waangalie na mengine. Mimi nasema hii iwe ni mfano na iwe ni kutukumbusha tufanye vipi masuala yetu ya kiuwekezaji? Tunajali vipi wananchi wetu? Tuangalie na maeneo mengine ambayo pengine yana changamoto kama hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, Nami naungana na wenzangu kwanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu. Pili, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Naibu Katibu Mkuu, na kwa ujumla wake, viongozi wote wa taasisi ambazo zipo chini ya Wizara hii. Kwa kweli wanajitahidi sana na tunazidi kuwatia moyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wizara hii imepata wachangiaji wengi ambao wanaonekana kuifahamu vizuri Wizara hii na shughuli zake, wanatoa hoja ambazo kimsingi ndizo zinazoendelea katika maisha yetu ya kawaida.
Mheshimiwa Spika, leo napenda kutoa mchango wangu katika maeneo hayo ya kawaida kwa sababu pengine ndiyo nitaeleweka kiurahisi zaidi. Suala la umuhimu wa kuimarisha elimu msingi, hilo kwa kweli halina ubishi, kwa sababu Wizara hii ndiyo inayosimamia udhibiti wa ubora wa elimu, hilo lazima tuendelee kulisisitiza.
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo tuliona jinsi mitaala yetu inaonekana kuwa haiko sawa, tukafanya jitihada ya kukaa pamoja na kushauriana nini kifanyike, vivyo hivyo, ningetamani sasa suala la wanafunzi au watoto wanaotoka kule vijijini, kwenye Majimbo hasa ya vijijini ambayo hayana wafanyakazi au watumishi wa kutosha, hususan walimu kwa kweli lifikie mahali lipate jibu.
Mheshimiwa Spika, sioni kwa nini Wizara iwe na furaha ya kuendelea kutoa mtihani mmoja kwa wanafunzi wote wakati wengine hawana walimu. Mimi naona hiyo siyo kuwatendea haki na hapo mwishoni na pengine tutashika shilingi, watufahamishe ni namna gani wanawasaidia hawa wanafunzi, hasa ambao hawako vijijini, kwa sababu wanakosa hiyo elimu iliyo sahihi na bora.
Mheshimiwa Spika, pia inavyokuja kwenye kupata nafasi za kuendelea juu wanazikosa; na inapokuja kwenye fursa za ajira watazikosa. Kwa hiyo unakuta kuna maeneo ambayo yataendelea kuwa maskini na duni, wakati tumeshasema kwamba elimu ndiyo msingi wetu wa maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zaidi ya hapo, napenda kuona katika haya mabadiliko tunayoendanayo ni kuona sasa hizi shule za amali zinatusaidia katika kulitoa Taifa hili kuondokana na ukosefu wa ajira. Sasa nataka nijue, tumeshasema kwamba tutajenga shule za kutosha zaidi ya 100 kwenye maeneo, tumejipanga vipi? Kwa sababu naogopa. Mwaka 2016/2017 nilitembelea Shule ya Ufundi Mtwara, nikakuta ile shule karakana zake zinatumika kwa ajili ya mfanyabiashara mmoja wa ufundi na magari yake, pale hakuna mwanafunzi anayechukua hiyo fani.
Mheshimiwa Spika, nikaenda Ifunda, nikakuta mambo ni hivyo hivyo. Nilipoenda Bwiru nikakuta mfanyabiashara kapewa karakana ile, anaitumia kwa mambo yake. Sijui wapo wanafunzi 0wawili watatu wanaenda kujifunza wanavyotaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia imeenda mpaka Chuo cha Ualimu kilikuwa pale Mkwawa ambacho kilikuwa kinafundisha masuala ya ufundi, nikakuta kinafundisha mambo tofauti. Sasa hofu yangu ni kutokujidanganya kwamba tunaanzisha hizo shule nyingi ambazo zitahitaji vifaa vingi vya ufundi, halafu tusiviweke na tuseme kwamba tayari tumeshaanza, kwa sababu kwenye ufundi haya mafunzo ya amali hayana uwongo, lazima tu ufanye lile ambalo linafanana na kumwezesha huyu mwanafunzi kufahamu inavyotakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba kwamba, pamoja na jitihada hizi ambazo tayari zimeshafanyika na tunazoendelea kuzifanya, basi tusiwe waoga katika kufanya maamuzi ya kuzisadia hizo shule au hivyo vyuo vya ufundi.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano pia mwaka 2023 tulikuwa tumeona kwamba wale wanafunzi wanaochukua diploma za kawaida kwenye vyuo vya ufundi, wasaidiwe nao kupata mikopo. Wanafunzi hao ndio tunaotegemea watakuja wengi sasa kutoka kwenye hizo shule za amali ambazo tutazianzisha, lakini waliopata mikopo ni wachache mno.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, DIT wanafunzi kama 116, kule Mbeya MUST wanafunzi 114, na vyuo vingine, hiyo idadi ni ndogo sana. Kwa misingi hiyo inakuwa kama vile maamuzi yetu tunaenda nayo kwa uwoga fulani hivi. Naomba tuliangalie eneo hili ili tuwawezeshe wanafunzi wengi zaidi kuhitimu wakiwa wamepata hizi fursa za kiufundi vizuri na waweze kwenda kulisaidia Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile nashukuru sana Mheshimiwa Mhandisi mwenzangu ameyazungumza vizuri tu kuhusiana na masuala haya ya kusaidia practical. Ukishakuwa kwenye maeneo ya ufundi, lakini maabara zake haziwezeshwi (siku hizi tunasema kuna teaching factory, ziweze kumsaidia huyu mwanafunzi kulingana na mazingira yale ambayo ameshasema hapa, tupate suluhisho la tatizo fulani), itakuwa haisaidii.
Mheshimiwa Spika, mimi naona kwamba, vyuo vyetu vimekuwa vikijitahidi sana kubuni mambo mazuri ya kuweza kusaidia nchi yetu, lakini inapokuja kwenye kuviwezesha, mara nyingi utoaji wa fedha umekuwa ni mdogo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa inawezekana fedha zetu ni kidogo, basi niombe taasisi zetu na vyuo vyetu vikuu ambavyo vinafanya tafiti mbalimbali, siyo tu katika kugawana hivi vilivyopo, tuongeze jitihada katika kubuni vyanzo vya mapato ili sasa tunaposema tunaenda kwenye haya maeneo ya kuimarisha na kuboresha, basi fedha isiwe ni tatizo tena; kwa sababu tutazungumza lakini fedha hatutapeleka.
Mheshimiwa Spika, kwa kweli, nashauri sana, vyuo hivi viweze kusaidiwa, vipewe fedha za kutosha, vijengewe maabara za kutosha, vijengewe viwanda vya kujifunzia vya kutosha, ili sasa mwanafunzi anapotoka hapo awe amekomaa na aweze kwenda kuonesha kwa vitendo kazi zake. Hata mwajiri atakuwa na furaha kumwajiri, kwa sababu anamwona kabisa huyu sio kwamba nachukua mzigo, bali anakuja kunipa faida. Mwajiri yeyote yule anampenda mtu anayemsaidia kumpa faida. Hampendi mtu wa kumlea kama mtoto. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa misingi hiyo, nasema hivi kwa sababu nimefuatilia, kwa mfano Chuo cha Mwanza cha Ufundi (DIT), wale waliamua kuona kwamba eneo la Mwanza kuna faida ya wanyama wengi, kwa mfano ng’ombe wako wengi, basi tuanzishe mitaala yetu na kazi zetu zitakazoendana na kutoa jibu au suluhisho la matengenezo ya ngozi mpaka viatu. Kweli wale wanafunzi wanafanya kazi nzuri sana na mlezi wao ni Mkuu wa Mkoa wa Mwanza. Hiyo sasa iendelee katika maeneo mbalimbali.
Mhshimiwa Spika, kila chuo kinyang’anyane, kiseme kwamba mimi naenda mkoa fulani kulingana na ile kazi ambayo wao wanaifundisha pale kwao. Hatutaki tena kuendelea kuona tunatafuta fedha kupeleka kwenye vyuo. Vyuo vyenyeye haviturudishii fadhila, ni lazima vipeleke fedhili ya moja kwa moja, ukiacha ile ya ujumla kwamba tumesomesha wanafunzi kadhaa, lakini sasa iwe hata mwananchi wa kawaida anaona matokeo.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa kwenye kile chuo kule Chondiem, kile chuo kinatoa suluhisho kubwa sana katika masuala ya uhandisi, ni kikubwa mno. Ikitokea kuna jambo lolote lile, mfano sijui watu wanataka kupeleka cable, kwa mfano hizi marine cables kuvusha labda kupeleka sehemu fulani, utakuta kile Chuo ndiyo kinaenda kufanya tafiti, kinatoa suluhisho za aina mbalimbali. Kwa hiyo, hata sisi hapa Tanzania inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunazo workshops zetu nyingine nzuri tu, kwa mfano pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hivi tunawatambua vipi? Tunawasaidia vipi ili kuweza kusaidia jamii zetu inavyowezekana? (Makofi)
(hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, basi ninashukuru lakini naona kwamba, kama ambavyo tuliujadili mtaala huu, basi hata namna ya kuutekeleza tutengeneze utaratibu maalum wa kushauriana ili twende vizuri pamoja. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi, wa Mwaka 2016
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nikushukuru kwa kunipa nafasi na niseme kwamba naunga mkono hoja. Napenda kuchangia katika Muswada wa Mamlaka ya Utafiti ya Uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na timu yao yote kwa kuleta Muswada huu ambao ni muhimu sana kwa maendeleo ya wananchi wa Tanzania hususani katika sekta ya uvuvi. Kwa muda mrefu nimekuwa pia nikijiuliza sana kwa nini maeneo ya uvuvi watu wake bado ni maskini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hilo nimekuwa nikilichangia hata humu Bungeni mara nyingi, kwa hiyo naona kwamba kupatikana kwa mamlaka hii ambayo sasa itakuwa ni imara kutafanya wananchi hawa sasa wabadilike. Wote tunafahamu asilimia kubwa ya Watanzania ni wakulima na wavuvi, kwa hiyo, iko haja kabisa Serikali kuongeza nguvu katika eneo hili kama ambavyo sasa tunafanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikubaliane na wachangiaji mbalimbali kwamba kuna umuhimu sana wa sisi Serikali kuongeza bajeti katika eneo hili la utafiti. Kwa sababu bila kufanya utafiti tutashindwa kugundua mambo mengi na sisi tutabaki kuwa watumiaji wa matokeo ya watu wengine bila sisi kuchangia katika matokeo ya utafiti ambayo yatasaidia nchi yetu pamoja na nchi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hayo naomba nirudi katika kifungu cha 19 kufuatia hotuba ya Upinzani na wadau wengine ambao wamelizungumzia. Malalamiko ni kwamba kwa nini wale wanaofanya utafiti walazimike kupeleka maandiko yao katika mamlaka hii ili ndiyo waweze kupata fedha au wakati mwingine wanakuwa na fedha zao binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi pamoja na kwamba niko katika sekta ya elimu ambayo pia inajihusisha sana na masuala ya utafiti ikiwemo COSTECH, nipende kusema kwamba iko haja ya kufanya hivyo kwa sababu tumekuwa na fedha nyingi zinaenda kwa wadau mbalimbali wanaofanya tafiti lakini wakati mwingine coordination ya matokeo inakuwa haipo. Sasa hawa kwa sababu ndiyo wenye sekta yao na wanapenda kuona maendeleo ya sekta yao ni vema wale wadau wote wanaokuwa wamepewa fedha kwa ajili ya utafiti wajulikane na ili kujua kwamba fedha zilizokuwa zimetolewa zinatumika sawasawa na zinaleta matokeo chanya katika sekta ya uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasisitiza hata kama mtu ana fedha zake, fedha zile zinakuwa ni zake pale ambapo anafanyia kazi zake binafsi, lakini anapoenda kufanya utafiti katika masuala ambayo yanahusu nchi na jamii lazima wote tufahamu nini kinachoendelea na matokeo yake ni nini, athari zake ni nini. Pia hata utangazaji wa matokeo hayo, yale matokeo yanayotangazwa yana faida au athari katika nchi, kwa hiyo lazima yawe coordinated.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, naona ni muhimu sana katika eneo hilo kuhakikisha kwamba hao wenye mamlaka wanakuwa ndiyo custodian wa matokeo yote hata kama taasisi nyingine zitakuwa zimesaidia kufanya hivyo. Kwa hiyo, niwaombe washirikiane na wadau wote ambao wanataka kufanya tafiti katika maeneo haya, wasione tabu kushirikiana na hii mamlaka ambayo ndiyo kisheria inao wajibu wa kuona kwamba sekta ya uvuvi inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo napenda nichangie kidogo katika jambo ambalo jana limenishtua sana kuona kwamba Mamlaka hii ya Utafiti wa Uvuvi inaambiwa kwamba inajilimbikizia kazi halafu ikalinganishwa na Wizara ya Elimu tena kwa maneno mabaya kutokea Kambi ya Upinzani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kimsingi sekta husika ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ya sekta hiyo, kwa hiyo Wizara haiwezi kujitoa. Kwa mfano, katika suala la elimu ambapo imezungumziwa vyuo inaonekana kwamba elimu ambayo inatolewa Tanzania haina manufaa kabisa, naomba tusifanye hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini aliyekuwa anazungumza alikuwa hana taarifa za kutosha kwa sababu kama angekuwa na taarifa za kutosha angeweza kuona jinsi ambavyo Tanzania imepiga hatua kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha kwamba sasa elimu inapatikana kiurahisi nchi nzima na matokeo yake ndiyo haya ambayo yanaonekana sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, katika udahili wa kuingia chuo kikuu sasa hivi malalamiko yamekuwa makubwa sana watu wana point 11, 12 hawajachaguliwa kwenda vyuo vikuu si kwa sababu wamenyimwa bali wanafunzi wengi wamefaulu kwa ufaulu wa juu kiasi kwamba nafasi zimekuwa chache, hiyo ndio kazi sahihi ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukisema kwamba sekta binafsi ndiyo inafanya vizuri kuliko Serikali wakati wewe unapima tu matokeo labda kwenye rank shule hii ilikuwa ya kwanza na shule ya Serikali inaonekana ilikuwa ya 200 lakini hiyo shule ya Serikali unakuta ina wanafunzi 300 hapo hapo division one labda wako 100 na wakati shule isiyokuwa ya Serikali ina wanafunzi 40 tu ndiyo maana labda ikawa na rank ya juu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hivi vitu vyote lazima tuvifanyie analysis. Ndiyo maana sasa hivi unakuta wanafunzi wakishatoka katika elimu ya msingi mpaka sekondari kidato cha sita hawataki tena kuendelea kwenye vyuo vya binafsi wanakimbilia vyuo vya Serikali kutokana na ubora unaoboreshwa kila siku, hata sasa hali ndiyo hiyo.
Kwa hiyo, niwaombe sana ndugu zangu tusitumie nafasi zetu tunapochangia kujidharau wenyewe kwa sababu unaweza ukaongea jambo hata wewe mwenyewe ukaonekana hujui unachoongea. Kwa hiyo, lazima tujivunie kazi kubwa tulizofanya pamoja, kwa kushirikiana Upinzani na Chama cha Mapinduzi kuona kwamba sekta yetu ya elimu inazidi kuwa nzuri na kuimarika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizidi kusisitiza utafiti huu uwe na manufaa. Mara nyingi sana tafiti zinafanyika katika ile hali ya ugunduzi lakini inapokuja kwenye commercialization yaani sasa iweze kutumika kwa wananchi watafiti wengi hawataki kusindikiza utafiti. Research nyingi zinazofanyika ni zile za kuandika lakini action research zinazofuatilia nini kimefanyika, wapi tuboreshe, wapi twende mbele zimekuwa ni chache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anataka akifanya moja amemaliza anachukua fedha zake anaondoka, tunataka mtu asindikize utafiti wake mpaka mwisho ili tuone matokeo na tuweze kupima fedha zinazotolewa sambamba na matokeo tunayoyatarajia. Mimi binafsi kwenye Wizara yetu tutakuwa wakali katika eneo hilo na tunasema kwamba kila mtu anapofanya utafiti lazima usajiliwe vizuri na tufuatilie matokeo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maneno yangu haya, nazidi kukushukuru kwa muda wako, nasema ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Kulitangaza Jiji la Dodoma kuwa Makao Makuu ya Nchi wa Mwaka 2018
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niungane na wale wanaopongeza Muswada huu na kwa kweli kwa heshima kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa maamuzi makubwa na mazito anayoyafanya katika kuhakikisha kwamba nchi yetu inapiga mchaka mchaka wa maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kwa wale wanaomheshimu Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, hawawezi kuwa kinyume na Muswada huu. Vilevile Muswada huu unatokana pia na maamuzi mazito ambayo yalifanyika siku ya kishujaa wakati Mheshimiwa Rais wetu tarehe 25 Julai, 2016 alipotoa maagizo ya Serikali kuhamia Dodoma. Hakuachia hapo, vilevile tarehe 26 Aprili, 2017 alitoa tena maamuzi ya kishujaa ya kindugu ya kusema kwamba sasa Dodoma liwe ni Jiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitanukuu kamili lakini ni kwamba nakumbuka alisema hivi: “Tanzania tuna Majiji matano, lakini Makao Makuu ya nchi siyo Jiji, kwa sababu zipi?” Kwa hiyo, ina maana ni mtu ambaye amekuwa akifikiria akiona ni kwa nini mambo yamekuwa tofauti wakati Dodoma ilikuwa inastahili toka siku nyingi iweze kupewa hadhi yake kama Makao Makuu ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, huwa najiuliza, hivi ni wivu kwa sababu sasa Dodoma inapewa haki yake au ni nini? Kama siyo wivu, basi wote tutaungana mkono kuhakikisha kwamba haya mambo mazuri ambayo yamepangwa yanafanyika vizuri na tunayatekeleza ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata mimi siku tulipoambiwa kwamba tunahamia Dodoma kama Serikali niliogopa kidogo na mpaka tuliulizana na wenzetu, hivi inawezekana? Kumbe imewezekana, Serikali iko Dodoma, wafanyakazi wapo Dodoma na huduma zimezidi kuwa nzuri na wananchi wengi wanafurahia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kwamba ndugu zangu hebu tuacheni mambo ambayo kila wakati tuwe kama tunavutana tu. Siyo vibaya kuchangia katika kuboresha, lakini kukataa mambo ambayo ni ya msingi nadhani pia inatuvunjia heshima yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba maandalizi kama ambavyo imezungumzwa yalianza siku nyingi. Sisi kweli Serikali baadhi yetu tupo pale Chuo Kikuu cha UDOM, lakini na yenyewe ilikuwa ni katika mchakato huo huo wa kuhamia Dodoma. Tatizo liko wapi? Kwa hiyo, nilitegemea kwamba wote tutaungana mkono katika kutoa mbinu mbalimbali ya kufanya Jiji hili la Dodoma, Makao Makuu yetu ya nchi yawe mazuri, yapendeze, yavutie na yawe na urembo kama ambavyo sisi wenyewe tunapendeza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kwanza nisije nikasahau, niwahamasishe wawekezaji mbalimbali wa viwanda na biashara kuja kuwekeza Dodoma. Dodoma ni mahali pazuri kwa kufanya biashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefuatilia sana, kuna watu ambao ni wagumu sana katika kufanya maamuzi. kwa upande wa sisi Wanasayansi tunasema kuna emitter na followers, kwa hiyo wenyewe kazi yao ni ma-follower, mpaka kwanza wengine waanze ndiyo wao wafuate. Ukifuatilia hata kwenye jambo hili, nafananisha na suala la umeme.
Kwa muda mrefu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2018
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nianze kwa kuunga mkono muswada huu wa PPP. Vilevile nikianzia katika masuala ambayo yalijitokeza kwa wazungumzaji, niseme tu ukienda kwenye Katiba yetu sehemu ya pili, inazungumzia kwamba malengo muhimu ya mwelekeo wa shughuli za Serikali, ukienda kwenye kifungu cha 9, itakuwa ni ujenzi wa ujamaa na kujitegemea. Nasema hivyo kwa sababu gani? Ni kwamba kila suala ambalo tunajaribu kulifanya ni kwa manufaa ya wananchi wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ukienda kwenye kifungu cha 20 inazungumzia juu ya uhuru na haki ya mwananchi yeyote yule kuweza kukutana au kushirikiana na watu wengine katika kufanya shughuli zao. Katika kifungu cha 25 kinazungumzia juu ya kazi pekee ndiyo izaayo utajiri wa mali katika jamii na chimbuko la ustawi wa wananchi na kipimo cha utu; na kila mtu anao wajibu wa kwanza kushiriki kwa kujituma na kwa uaminifu katika kazi halali za uzalishaji mali. Vilevile (b) inazungumzia kutimiza nidhamu ya kazi na kujitahidi kufikia malengo ya uzalishaji mali ya binafsi na yale malengo ya pamoja yanayotakiwa au yaliyowekwa na sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa misingi hiyo niseme tu kwamba vifungu vyote ambavyo vimeletwa na Serikali vina dhamira hiyo njema kabisa. Vilevile tunatambua kwamba katika PPP tunaenda kutumia rasilimali za nchi na za watu mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono pia kifungu cha 13 ambacho tumeongeza sasa kifungu cha 25 kinachotambua sheria ambayo ilipitishwa hivi karibuni juu ya utajiri wa nchi. Hivyo basi, napenda kusisitiza sasa, kwa sababu sheria hii imetoa nafasi kubwa kwa wadau mbalimbali kushiriki katika uwekezaji wa PPP na hasa kwa hawa wananchi ambao ni wananchi wa kawaida ambao pengine tulikuwa tunafikiria siku za nyuma wanaotakiwa kushiriki katika PPP ni Serikali pekee au wadau wenye fedha nyingi peke yao, nawaomba kutumia taasisi zetu za kitafiti ili waweze kusaidiwa katika kupata michanganuo na kuweza kupata namna bora ya kuingia katika ubia na kuleta faida ambayo itakuwa kwao katika hao wajasiriamali lakini halikadhalika kwa nchi yetu kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema hivyo kwa sababu kuna uzoefu umejitokeza, unakuta pengine wadau au wabia wanaotaka kuja, anasema pengine anataka government guarantee au anasema kwamba nimeshapita mahali huku nimeshaona kwamba naweza nikawekeza katika eneo hili. Kwa upande wa Serikali au upande wa yule mtu ambaye anataka kushirikiana naye unakuta hana taarifa za kutosha na hivyo kufanya ule mradi kwa ujumla wake kutokutoa faida za pamoja au kuweza kunufaisha upande mmoja mmoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ilishapata matatizo hayo. Nchi yetu ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazozungumza kwamba utajiri wake umetumika kunufaisha nchi nyingine. Kwa misingi hiyo, napenda kuomba taasisi zote zitakazoshiriki katika shughuli hizi za ubia, pia watu binafsi kujielekeza kupata taarifa za msingi kuhusiana na ubia wanaoingia ili kuona kwamba ubia huo unakuwa ni wa haki na wa faida kwa pande zote. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia. Kwanza nianzie kumshukuru tena Mwenyezi Mungu, lakini kwa namna ya pekee kabisa niendelee kumshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu Waziri pamoja na wadau wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri iliyofanyika hasa katika kuangalia maeneo muhimu ambayo yakiboreshwa kupitia Muswada huu yatawezesha Taifa kukusanya mapato yaliyokusudiwa na kutekeleza miradi mbalimbali ambayo imekusudiwa katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo nilikuwa na michango michache katika baadhi ya maeneo. Ukienda katika sehemu ya tano nimetumia mchango ambao Mheshimiwa Waziri ulikuwa unawasilisha kwa ajili ya Muswaada huu.
Kwa hiyo ukichukua sehemu ya tano ambayo inahusu sheria ya mikopo, dhamana na misaada sura ya 134 ambayo ulikuwa unapendekeza sasa kuongeza kifungu 13 (b) kitakachosaidia Serikari kuweza kutoa dhamana kwa kampuni ambayo itahitaji kukopa kwa kiwango kisichozidi asilimia ya hisa za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa napenda kujiridhisha zaidi na kushauri kwa sababu imeonekana katika uzoefu ulijitokeza katika miaka hii ya hivi karibuni baadhi ya dhamana hizi zimetumika vibaya, kwa hiyo nilikuwa nashauri, kwa sababu CAG sasa hivi amepata mamlaka ya kuweza kukagua makampuni ambayo Serikali ina hisa zaidi asilimia 50, basi nilikuwa nashauri hata pale Serikali inapokuwa imetoa dhamana kwa kampuni pamoja na kwamba ni kwa kiwango cha hisa zake basi CAG aweze pia kukagua.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu gani? inawezekana tukaona pengine hisa zilizopo ni kiwango kidogo labda asilimia 20, lakini inaweza ikawa ni asilimia 20 ya mabilioni ya hela au matrilioni ya hela kulingana na mradi ulivyo, tuchukulie kama Mchuchuma na Liganga pale kuna fedha nyingi, sasa unaweza kukuta kwamba fedha kama hizo badala ya kutumika kwenye mradi husika nyingine zikatumika ndivyo sivyo. Kwa hiyo, nilikuwa nashauri aidha tuongeze pale kwa CAG kwamba atatakiwa kukagua kwenye hisa hizo zinazozidi asilimia 50 pamoja na sehemu ambayo Serikali imeweka dhamana yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa pia naomba nichangie sehemu ya 24 kama ilivyorekebishwa kuhusu sheria ya kodi ya ongezeko la thamani sura 148(8) ambacho kinahusu kuondoa ongezeko la thamani kwa ajili ya vyumba vya baridi. Lakini imewalenga zaidi wauzaji wa mbogamboga, sasa nilikuwa nafikiri kwamba nila wale watu ambao tunahitaji kuwainua wakiwemo wavuvi hata wanaohusika na masuala ya nyama kwa hiyo nifikirie pengine tusiwaangalie hao tu, tuangalie makundi hayo yote ili kuwezesha sasa hawa wananchi wetu kupata unafuu katika uwekezaji wa vyumba vya ubaridi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini vilevile nilikuwa nashauri kwa upande wa mamlaka ya bandari kutenga line maalum inayohusika na bidhaa za aina hiyo kwa sababu wakati mwingine unakuta kwamba wanasubiri mpaka bidhaa hizo ziwe za kutosha ndipo ziweze kusafiri sasa bidhaa za mbogamboga au nyama au Samaki siyo sawa na chuma. Kwa hiyo, nafikiria kwamba ni vema sasa Mamlaka ya Bandari kuwezesha kabisa kuhakikisha kwamba bidhaa hizo au mazao hayo yanaweza kusafirishwa kwa haraka zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa pia napenda kuchangia kidogo kwenye eneo hili la, kwanza kwenye kuongeza idadi ya kutoza kodi kwa waajiriwa zaidi ya nne mpaka kumi, jambo hili limekuwa ni jema sana na linawezesha kusaidia uwekezaji hata katika maeneo ya vijijini. Lakini kubwa zaidi nimeshukuru kwa jinsi ambavyo tumeondoa kodi ya mafunzo kwa taasisi za kidini hususani hospitali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda maeneo mengine kwa mfano kwenye Jimbo la Nyasa pale tuna hospitali ya Litui, tuna hospitali ya Liuli hayo maeneo yamekuwa ndiyo yakisaidia sana katika kupunguza changamoto za matibabu. Lakini sasa hivi kutokana na hizi gharama za kiuendeshaji na hivi Serikali sasa inavyokuwa imeanza tena kuangalia katika vituo vya afya vilivyojengwa na Serikali yenyewe katika maeneo sasa ni mbali na maeneo hayo unakuta kwamba hizo hospitali zimekuwa zinashindwa kujiendesha kiasi kwamba hata wale wananchi wanaoenda kutibiwa pale, kwa sababu walishajenga kichwani mwao kwamba sehemu ile ndiyo sehemu ya kuponea imekuwa kwa kweli wanapata changamoto kubwa na vifo hata vya wakinamama vimekuwa vikiongezeka, wakinamama inamaana kwenye kujifungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, jambo hili limekuwa ni msaada mkubwa sana na ninaomba kwa kweli tuzidi kuziangalia hospitali hizi ambazo zinatoa mchango mkubwa wa kipekee katika kuendelea kuisaidia Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya michango hiyo naendelea kuunga mkono hoja na ninaamini kwamba Sheria hii sasa ikishakuwa kamili itasaidia sana kuleta mabadiliko katika nchi yetu. Nazidi kumshukuru Waziri pamoja na Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa anayoifanya. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na.3 wa Mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia katika Miswada hii ya Marekebisho ya Sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, umuhimu wa sheria yoyote ile inayotungwa ni hasa pale inapokuwa na nia au dhamira njema. Kwa hiyo, marekebisho ya sheria hii naamini yana nia njema na yanalenga katika kuwezesha utekelezaji bora wa miradi mikubwa ya kimkakati na hivyo kuwezesha kutoa hali ya kuaminika baina ya nchi na nchi au wadau wanaoingia katika mikataba hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika mradi huu unaotajwa wa Bomba la Mafuta, kimsingi una faida nyingi sana za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Kwa misingi hiyo, mradi huu ambao umeanza kujadiliwa toka mwaka 2016 kwa kumbukumbu zangu, kwa kweli sasa unastahili uwezeshwe ili uweze kuanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu kwa jitihada kubwa anayoifanya katika kuona kwamba taifa hili linaendelea kusonga mbele. Niseme tu kwamba binafsi kama ilivyo kawaida yangu napoziona sheria kama hizi zikija hasa zinapogusa maslahi mapana ya nchi yetu, nimekuwa nikiwa na jitihada sana za kutafuta huko na huko japo sio mwanasheria, hiki maana yake nini au hiki hakina athari? Niseme tu kwamba nimejiridhisha na dhamira njema iliyopo katika mabadiliko haya ya sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi kama ambavyo wenzangu wamesema, hivi vifungu vilivyojirudia mara kwa mara kwamba mikataba hii ya kimkakati itakapokuwa imeingiwa au kupitishwa na Baraza la Mawaziri, nikajiuliza Baraza la Mawaziri ni nani, nikakuta pale kuna Mawaziri lakini Mwenyekiti wake ni Rais wetu, Makamu wake na yeye pia ni kiongozi msaidizi katika Baraza hili. Kwa hiyo, nikajiridhisha kwamba kama Rais mwenyewe ndiye Mwenyekiti wa chombo hiki na huyu Rais pia ni sehemu ya Bunge lakini pia Katiba inatoa mamlaka kwa Bunge kwamba Rais akiwa ameenda tofauti, lakini hatua hiyo hatuitamani sana, kuweza kupiga hata kura ya kutokuwa na Imani, si ndiyo jamani, sasa nani ambaye anaweza kuwa ameshikilia majukumu haya mazito zaidi ya Mheshimiwa Rais? Kwa hiyo, mimi nimeona kwamba tuko salama. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama ilivyo ni kwamba Rais ni taasisi na Baraza la Mawaziri halianzii hapo lina watendaji wake wanaoanzia toka huko kwenye sekta mpaka jambo linaweza kufika sasa kwenye Baraza la Mawaziri. Kwa hiyo, niombe wale wadau ambao wanahusika katika kuchakata mikataba hii wawe makini lakini wajitahidi kuwa na uzalendo kwa nchi yao. Wakishakuwa na uzalendo ina maana watachakata mikataba hiyo kwa uhalisia na tutahakikisha kwamba tunaingia kwenye mkataba ukiwa salama na nchi yetu inatendelea kwenda mbele vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu mkataba ni kitu kimoja na hii mikataba kwa sasa kama tulivyoipa mamlaka ina nguvu sana, sasa kama itakuwa haijachukua maslahi mapana ya wananchi, tumeshuhudia kuna nchi nyingi ambazo watu wananung’unika baadaye wanajikuta wameingia barabarani. Kwa misingi hiyo na kwa sababu marekebisho haya hayahusu huu mkataba mmoja tu ambao ni Bomba la Mafuta na mingine ambayo tutaingia, niombe sana Serikali kujipanga zaidi, kuwa na wataalamu ambao wamebobea katika maeneo hayo, tusomeshe watu wetu katika maeneo mbalimbali ili tuwe na watu ambao wanaweza kutoa ushauri mzuri zaidi. Ukiacha tu wale wanaoingia kwa nafasi zao za ki-cheo, tuweze kuwa na wataalamu wabobezi wazuri katika maeneo yetu. Naamini tukifanya hivyo nchi yetu itazidi kusonga mbele na tutakuwa tumenufaika zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niseme tu kwamba kama ambavyo Mwenyekiti wetu wa Kamati ametoa maoni kuna umuhimu wa kuwa na sheria maalum kwa ajili ya hili Bomba la Mafuta. Hii ni kutokana na kwamba baadhi ya rasilimali tunazozizungumzia zinatofautiana sana kiasi kwamba hata sheria moja haiwezi kukidhi, pengine ipo haja ya kulipatia hili Bomba la Mafuta sheria yake maalumu ili iwe rahisi katika ufuatiliaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba mimi binafsi naunga mkono hoja, nikitegemea kwamba na mambo mengine yatakayoendelea katika mikataba mbalimbali yatakuwa yanaangalia maslahi mapana ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)