Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Eng. Stella Martin Manyanya (86 total)

MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-

(a) Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha wanafunzi hawarudishwi shule kwa sababu ya michango ya mlinzi, madawati na chaki?

(b) Je, Serikali ina mpango wa kuanzisha Chuo cha Ufundi (VETA) kwenye Jimbo la Ndanda?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Sera ya Elimu bila malipo, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi imetoa Waraka wa Elimu Na. 6 wa mwaka 2015 unaofafanua majukumu ya kila mdau katika utekelezaji wa elimu msingi bila malipo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa utoaji wa elimu msingi bila malipo ambapo jumla ya shilingi bilioni 15.71 zimepelekwa katika Shule za Msingi na Sekondari za Umma kwa mwezi Disemba, 2015. Fedha hizi ni kwa ajili ya ruzuku ya uendeshaji shule, fidia ya ada kwa shule za sekondari za bweni na Kutwa na chakula kwa wanafunzi wa bweni.

Mheshimiwa Spika, Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule wamepewa Mwongozo wa matumizi ya fedha hizo ambazo zitatumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, zikiwemo chaki, gharama za ulinzi, mitihani na chakula. Aidha, Serikali kupitia Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji itahakikisha inatenga fedha kila mwaka kwa ajili ya ununuzi wa madawati. Sambamba na hilo, wananchi na wadau wengine wa elimu wataendelea kusaidia kuchangia katika upatikanaji wa madawati kwa kadiri watakavyoona inafaa.

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo hayo, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba hakuna Mkuu wa Shule au Mwalimu Mkuu yeyote ambaye atamrudisha mwanafunzi nyumbani kwa kutolipa michango ya mlinzi, madawati na chaki kwa sababu, majukumu hayo ni ya Serikali. (Makofi)

Serikali ina dhamira ya kuendelea kuboresha utekelezaji wa mpango huu kadiri ya tafiti zitakavyoonesha, pamoja na maoni ya wadau mbalimbali yakiwemo ya ninyi Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika Wilaya zote zisizo na Vyuo vya Ufundi Stadi vya Serikali au visivyo vya Serikali. Wakati utafiti wa kubaini Wilaya zisizo na Chuo unafanyika, Wilaya ya Masasi ilikuwa na Vyuo viwili vya ufundi stadi kikiwemo Chuo cha Ufundi Stadi Ndanda, chenye uwezo wa kudahili wanafunzi 180 na Lupaso chenye uwezo wa kudahili wanafunzi 38, vinavyomilikiwa na madhehebu ya dini. Kwa kuzingatia kigezo hicho, Jimbo la Ndanda ambalo lipo katika Wilaya ya Masasi, haipo katika mpango huu.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo katika kutekeleza azma hii ya kila Wilaya kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi, Serikali imeviwezesha Vyuo 25 vya Maendeleo ya Wananchi vilivyopo katika Wilaya mbalimbali ili kutoa mafunzo ya ufundi stadi kikiwemo Chuo cha Maendeleo cha Wananchi Masasi kwa kuwajengea uwezo Walimu, kuboresha miundombinu na ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Utekelezaji wa utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi katika chuo hicho ulianza mwaka 2012/2013. Napenda kumshauri Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Ndanda kutumia Vyuo hivyo vilivyopo Wilayani Masasi ili kupata mafunzo ya ufundi stadi.
MHE. RASHID ALI ABDALLAH aliuliza:-

Kwa mujibu wa Sheria, Wizara ya Fedha inatoa Mikopo kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini Tanzania.

Je, ni utaratibu gani mzuri wa kuondoa usumbufu kwa wanafunzi kupata mikopo yao kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Ali Abdallah, Mbunge wa Tumbe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, utoaji wa mikopo na ruzuku kwa wananafunzi wa elimu ya juu nchini unazingatia Sheria ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu Na. 9 ya mwaka 2004 kama ilivyorekebishwa, Kanuni za Utoaji Mikopo za mwaka 2008 na Mwongozo wa Utoaji Mikopo na Ruzuku kwa mwaka 2015/2016 ili kuweka vigezo, uwazi na urahisi katika utoaji wa mikopo.

Mheshimiwa Spika, fedha za mikopo zinalipwa kwa wanafunzi kupitia vyuo wanavyosoma ili kuhakikisha kuwa fedha zinawafikia walengwa kwa wakati. Tangu kuanza kwa utaratibu wa kuwalipa wanafunzi fedha za mikopo kupitia vyuoni, malalamiko yamepungua kwa takriban miaka minne sasa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kuwepo kwa mafanikio katika utekelezaji wa utaratibu huu, bado kuna changamoto katika ulipaji wa fedha hizo kwa wananfunzi kwa wakati kwa baadhi ya Vyuo Vikuu. Changamoto hizo husababishwa na ufinyu wa bajeti. Baadhi ya Vyuo Vikuu vyenye matawi kuwa na akaunti moja ya benki hali ambayo huchelewesha fedha kufika katika matawi; uongozi wa Chuo husika kutowapa wanafunzi taarifa ya kwenda kusaini kwa wakati ili walipwe mikopo yao; pamoja na baadhi ya wanafunzi kutosaini wakidhani wasiposaini hiyo mikopo hawatadaiwa watakapomaliza masomo yao.

Mheshimiwa Spika, ili kuondokana na changamoto hizi, Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango, itaendelea kulipa kipaumbele suala la mikopo ya wanafunzi kwa Bodi ya Mikopo kupewa fedha kwa wakati. Serikali kupitia Bodi ya Mikopo, imeagiza Vyuo Vikuu vyote vyenye matawi kuhakikisha kuwa kila tawi linafungua akaunti ya benki ambayo fedha za wanafunzi wanaosoma katika matawi hayo zitaingizwa.
Mheshimiwa Spika, Bodi ya Mikopo pia imetoa Waraka wa kuagiza vyuo vyote kuhakikisha wanafunzi wanalipwa ndani ya siku saba baada ya kupokea fedha kutoka Bodi ya Mikopo, kwani fedha hizo siyo za kuwekeza, bali ni kwa ajili ya wanafunzi.

Aidha, Wizara yangu imeiagiza Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kufuatilia kwa karibu fedha zinazopelekwa Vyuoni zinawafikia wanafunzi wa kati. Sambamba na hilo, ili kuratibu upatikanaji wa taarifa za wanafunzi kwa wakati, kila Chuo kimeelekezwa kuwa na dawati maalum la Mikopo pamoja na Afisa Mikopo mwenye uwezo wa kushughulikia changamoto mbalimbali za mikopo ya wanafunzi katika chuo husika.

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA aliuliza:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeamua kujenga Vyuo vya VETA kwa Wilaya zote nchini na Chunya ni kati ya Wilaya 10 za mwanzo kupata chuo hicho:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia majengo yaliyokuwa kambi ya ujenzi wa barabara ya lami pale Chalangwa kwa ajili ya Chuo cha VETA, ili kuokoa gharama kubwa za ujenzi wa majengo mapya.
NAIBU WAZIRI ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa, Mbunge wa Lupa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na Ufundi, imebaini kwamba baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara husika kampuni ya ujenzi iliacha majengo yaliyokuwa yanatumika kama ofisi na makazi.
Mheshimiwa Spika, aidha, ukubwa wa ardhi iliyokuwa imetolewa na kijiji kwa kampuni hiyo ni hekari 25, taarifa ya kitaalamuimebainisha kwamba eneo ilipo kambi hiyo ni zuri kwa maana ya kufikika na kuwa na huduma za umeme na maji. Hata hivyo, majengo yaliyoachwa na kampuni hiyo ya ujenzi wa barabara hayakidhi viwango vya kutolea mafunzo ya ufundi stadi kutokana na ukweli kwamba majengo hayo siyo ya kudumu.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwa na Chuo cha VETA katika Wilaya ya Chunya tayari ilikwishafanya maandalizi ya awali ya ujenzi wa chuo cha VETA. Maandalizi hayo ni pamoja na kufanya utambuzi wa stadi zinazohitajika kutolewa katika chuo hicho. Aidha, Wilaya ya Chunya imekwishatenga eneo la ujenzi wa Chuo hicho katika Kijiji cha Mkwajuni na tayari Halmashauri ya Wilaya imekwisha pima eneo hilo, lenye ukubwa wa hekari 10.1 Kiwanja nambari 1 kitalu (B) na hati ya kiwanja ilikwishapatikana. Katika mwaka huu wa fedha 2015/2016, Wizara yangu kupitia Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi imeshateua wataalam elekezi watakaoshindanishwa kutayarisha andiko la jinsi ya kufanya kazi ya kubuni majengo na gharama ya kazi hiyo. Mtaalam elekezi wa kubuni majengo ya Chuo cha Ufundi Stadi cha Chunya anatarajiwa kupatikana mwezi Februari, 2016.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI aliuliza:-
Serikali imedhamiria kuanzisha mfumo wa utoaji wa elimu ya msingi mpaka kidato cha nne bure, jambo litakaloanzisha wahitaji wa elimu ya kidato cha tano, sita na kisha chuo kikuu. Mkoa wa Katavi kwa dhamira safi ulianzisha zoezi la ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo, lakini kwa bahati mbaya zoezi zima la ujenzi wa chuo hicho limegubikwa na sintofahamu na suala zima kuwa na usiri na utata:-
a) Je, ni lini ujenzi huo muhimu utaanza?
(b) Je, ni kwa nini jambo hili lisiwekwe wazi kwa wananchi ili kuondoa sintofahamu kutokana na usiri uliopo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sebastian Simon Kapufi, Mbunge wa Mpanda Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Mkoa wa Katavi kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, iliridhia kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kilimo katika Mkoa wa Katavi. Uamuzi huo ulifanyika mnamo 11 Februari, 2011, kupitia vikao vya kisheria vya Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda kwa kuzingatia Sheria ya Serikali za Mitaa Na. 8 ya mwaka 1982, Sehemu ya Tano, kifungu Na. 53 na 54(1)(b) na (c) na 2(b) na (c).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume ya Vyuo Vikuu ilitoa hati ya usajili wa awali ya uanzishwaji wa chuo kikuu hiki kwa barua yenye kumbukumbu Na. TCU/A/40/1A/VOL.III/4 ya tarehe 31 Januari, 2012, kwa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda ambaye ndiye mmiliki wa chuo. Kuanzia wakati huo, mmiliki alishirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Chuo cha Kilimo cha Uingereza (The Royal Agricultural University), Baraza la Madiwani la Manispaa ya Mpanda na African Trade Insurance Agency ili kukamilisha masharti yaliyoainishwa katika hati ya usajili wa awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Chuo Kikuu hiki ungeendelea kama mmiliki ambaye ni Manispaa ya Mpanda angefanikiwa kupata mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 2.5 kutoka Benki ya Biashara ya Afrika kwa udhamini wa African Trade Insurance Agency. Hata hivyo, mmiliki amefanikiwa kupata eneo la ekari 500 kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Uongozi wa Mkoa bado una nia ya kuendelea na mradi huu, Wizara yangu itaendelea kutoa ushauri wa kitaalam na kiufundi ili mmiliki aweze kukamilisha azma ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Katavi. Aidha, ili kuondoa sintofahamu kuhusu mchakato wa ujenzi wa chuo hicho, nashauri mmiliki wake achukue hatua za kulifahamisha Baraza la Madiwani ili kuondoa sintofahamu hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO (K.n.y. MHE. HALIMA J. MDEE) aliuliza:-
Serikali ilitoa kauli kuwa itapanga gharama za karo elekezi kwa shule zote za binafsi hapa nchini:-
(a) Je, Serikali imegundua kiwango cha gharama kwa kila mwanafunzi (unit cost) kwa shule za bweni na za kutwa ni kiasi gani?
(b) Je, kiwango hiki hakitasababisha kuporomoka kwa ubora wa elimu ambayo ilikuwa ikitolewa hapo awali na shule binafsi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima James Mdee, Mbunge wa Kawe, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi imefanya utafiti kuhusu gharama za kumsomesha mwanafunzi wa elimu ya msingi na sekondari. Kupitia utafiti huo, imebainika kuwa ada zinazotozwa katika shule za binafsi zinatofautiana kwa kiasi kikubwa kulingana na huduma zinazotolewa, aina ya shule na miundombinu iliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya utafiti huo, Wizara yangu ilifanya mazungumzo na baadhi ya taasisi zinazosimamia shule zisizo za Kiserikali na kukubaliana namna ya kufikia viwango vya ada elekezi.
Mheshimiwa Naibu Spika, taasisi ambazo tumefanya nazo mazungumzo ni pamoja na Umoja wa Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo visivyo vya Serikali (TAMONGSCO), Kamisheni ya Huduma za Jamii za Kikristo (CSSC) na Baraza la Sunna Tanzania (BASUTA). Kutokana na tofauti za ubora na idadi ya huduma zinazotolewa na shule, Wizara sasa imeanza zoezi la kupanga shule hizi kwa makundi ili kuweka viwango vya ada kwa kuzingatia ubora na huduma na hivyo kutoathiri kiwango cha elimu inayotolewa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inatarajia kuwa utaratibu wa ada elekezi hautaathiri ubora wa elimu katika shule binafsi kwa sababu ada hiyo itapangwa kulingana na ubora na huduma na miundombinu iliyopo shuleni.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Mkoa wa Kagera hauna Chuo cha VETA chenye hadhi ya Chuo cha Mkoa na kwa sababu hiyo wananchi wa Mkoa huo hawapati elimu inayostahili. Hivyo, Serikali iliamua kujenga Chuo cha aina hiyo Bukoba kwenye Kata ya Nyakato ambako kiwanja kilipatikana na mipango yote ilifanywa na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi kutembelea mara kwa mara eneo hilo, lakini ni muda mrefu sasa umepita hakuna chochote kinachoendelea:-
Je, ni lini ujenzi huo utaanza na kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Kagera unategemea kuanza baada ya hatua za maandalizi ya msingi zitakapokamilika. Serikali kwa sasa imeshalipa kiasi cha shilingi 4,779,896 kwa ajili ya kupata Hati miliki kwa eneo lenye hekta 40.9 lililopo katika Kijiji cha Burugo, Kata ya Nyakato ambapo chuo kitajengwa. Aidha, uchambuzi wa stadi zitakazofundishwa katika Chuo hicho umekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuandaa michoro kwa ajili ya majengo na miundombinu ya chuo, kuandaa mitaala kulingana na stadi zilizotambuliwa, kuandaa mipango ya ukarabati wa miundombinu hasa kiliometa nne mpaka tano za barabara kutoka barabara kuu na kuhakikisha maji na umeme yanapatikana katika eneo hilo. Aidha, Serikali inaendelea na mazungumzo na Serikali ya Watu wa China kuhusiana na ufadhili wa ujenzi wa Chuo hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inategemea kukamilisha ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Kagera kutegemeana na upatikanaji wa Fedha na juhudi mbalimbali ikiwemo ushirikishwaji wa Wafadhili wa ndani na nje ya nchi kama sehemu ya kuchangia juhudi za Serikali.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Wanafunzi wanaomaliza kidato cha sita na kupata fursa ya kujiunga na vyuo mara tu wamalizapo masomo yao, huruhusiwa kutumia National Examination Results Slip kwa ajili ya taratibu za kujiunga na chuo.
Je, kwa nini wanafunzi wanaomaliza stashahada katika vyuo mbalimbali na kutaka kujiunga na elimu ya juu wasiruhusiwe kutumia academic transcripts badala ya kutakiwa kuwasilisha vyeti halisi ambavyo huchukua muda mrefu kutolewa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kiujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua kuwa vyeti vya kuhitimu stashahada huchelewa kutolewa, wanafunzi wanaomaliza stashahada katika vyuo mbalimbali na kutaka kujiunga na elimu ya juu wanaruhusiwa kutumia hati ya matokeo yaani academic transcripts ili kupata usajili wa muda yaani provisional registration mpaka hapo wanapopata vyeti vyao ili kupatiwa usajili kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa udahili wa wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya elimu ya juu hufanyika kupitia mfumo wa udahili wa pamoja yaani central admission system.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu unaratibiwa kwa pamoja kati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Tume ya Vyuo Vikuu na hutumia matokeo ya mitihani ya ngazi ya stashahada yaliyohifadhiwa kwenye Hazina data ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi. Hivyo, waombaji udahili hawatumii vyeti kuomba udahili kwa kuwa baadhi ya taasisi zinazotoa mafunzo ya Stashahada huchukua muda mrefu kutoa vyeti hivyo katika jitihada za kudhibiti udanganyifu wa vyeti.
Kwa hiyo, wanafunzi hawa wanapo-report vyuoni hupewa usajili wa muda na baada ya kupata cheti ndipo huwasilisha taarifa hizo na kupata usajili kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchukua fursa hii kutoa wito kwa wanafunzi wanaopata tatizo la kutumia hati ya matokeo kusajiliwa vyuoni watoe taarifa ili Wizara yangu iweze kufanyia kazi ipasavyo suala hili.
MHE. SUSAN A.J. LYIMO aliuliza:-
Mwaka 2015 Haki Elimu walitoa tathmini ya utafiti wa elimu kwa kipindi cha miaka 10 ya Awamu ya Nne na kugundua ongezeko kubwa la udahili kwa ngazi zote na kuporomoka kwa ubora wa elimu:-
(a) Je, ni kwa kiasi gani utafiti huo umeakisi uhalisia wa hali ya elimu hususan ile ya sekondari?
(b) Je, Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati gani ya kuinua ubora wa elimu hapa nchini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba udahili umekuwa ukiongezeka katika ngazi zote za utoaji elimu kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu. Ongezeko hili linatokana na utekelezaji wa Mipango ya Maendeleo ya Elimu katika ngazi mbalimbali ikiwemo Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES). Sanjari na ubora wa elimu, lengo kuu la mipango hiyo lilikuwa ni kuwezesha watoto wote wenye rika lengwa kuandikishwa darasa la kwanza na idadi ya wanafunzi wote waliofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (darasa la saba) kuchaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mafanikio ya MMEM na MMES yalisababisha ongezeko kubwa la shule za msingi na sekondari, sanjari na ongezeko la wanafunzi na kuleta changamoto ya utoshelevu wa mahitaji muhimu ikiwemo Walimu, miundombinu pamoja na vifaa vya kufundishia na kujifunzia na hivyo kuathiri ubora wa elimu kwa namna moja au nyingine hasa katika kipindi cha awamu mbili za mwanzo za mipango hiyo (2002 – 2010). Hivyo, kwa kiasi fulani utafiti wa Haki Elimu umeakisi uhalisia wa hali ya elimu nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ubora wa elimu unahusisha mambo mengi ikiwemo mazingira ya utoaji wa elimu ambayo yalianza kuboreshwa katika kipindi hicho. Kwa mfano, idadi ya Walimu wa shule za msingi wenye sifa iliongezeka kutoka Walimu 132,409 mwaka 2005 hadi 180,565 mwaka 2014 na Walimu wa sekondari iliongezeka kutoka 20,754 mwaka 2005 hadi kufikia 80,529 mwaka 2014. Aidha, morali wa Walimu hao kupenda kwenda kufanya kazi katika maeneo mbalimbali ya vijijini imeongezeka kutokana na Serikali kuimarisha miundombinu wezeshi kama vile barabara, upatikanaji wa umeme, maji na mawasiliano ya simu.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa nchini inakuwa na ubora wa hali ya juu, Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mbalimbali kama ifuatavyo:-
(i) Kuimarisha na kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji kwa kujenga na kukarabati miundombinu ya shule, ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, maabara, maktaba, vyoo, nyumba za Walimu na ununuzi wa madawati.
(ii) Kuendeleza mafunzo ya Walimu tarajali hususan kwa masomo ya sayansi, hisabati, lugha na elimu ya awali.
(iii) Aidha, Serikali inaendesha mafunzo kazini kwa Walimu kuhusu matumizi ya stadi za TEHAMA, sayansi, hisabati na lugha ili kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji kwa Walimu wa shule za msingi na sekondari.
(iv) Katika kuimarisha stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) mafunzo yanatolewa kwa Walimu wa darasa la kwanza na la pili.
(v) Vile vile ili kuimarisha ufuatiliaji wa tathmini ya ubora wa elimu itolewayo, Ofisi za Udhibiti Ubora wa Shule, Kanda na Wilaya zinaendelea kuimarishwa kwa kuongeza idadi ya Wadhibiti Ubora wa Shule na vitendea kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI (K.n.y. MASHAKA MAKAME FOUM) aliuliza:-
(a) Je, tangu Serikali ilipoanza kutoa mikopo ya Elimu ya Juu, ni kiasi gani cha fedha kimetolewa mpaka bajeti ya mwaka 2015/2016?
(b) Je ni kiasi gani kimerejeshwa ndani ya kipindi hicho?
(c) Je, Chuo gani kinaongoza kwa wanafunzi wake kupata fedha nyingi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Makame Mashaka Foum, Mbunge wa Kijini, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, tangu Serikali ilipoanza kutoa mikopo ya Elimu ya Juu mwaka 1994/1995 hadi mwezi Machi, 2016, kiasi cha shilingi trilioni 2.44 kimetolewa kwa wanafunzi 378,504 kwa kusudi hilo.
(b) Mheshimiwa Spika, urejeshwaji wa mikopo kutoka kwa wanufaika ulianza mwaka 2006/2007 na hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2016 kiasi cha shilingi bilioni 93.9 kilikuwa kimerejeshwa kati ya shilingi bilioni 256.2 ambazo zilikuwa zimeiva kwa kurejeshwa.
(c) Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015, Chuo kilichoongoza kwa wanafunzi wake kupata fedha nyingi za mikopo ni Chuo Kikuu cha Dodoma.
MHE. MWITA M. WAITARA aliuliza:-
Kumekuwa na utaratibu mbovu na Mawaziri wa Elimu kuingilia shughuli za mitaala kwa kubadilisha mitaala, mfumo wa madaraja na hata aina ya mitihani hasa kuweka maswali ya kuchagua katika somo la hisabati:-
Je, ni lini Serikali italeta marekebisho ya Sheria ya NECTA ili Bunge libadili Sheria ya Baraza kifungu cha 30 ili kuondoa nguvu ya Waziri ya kutoa maelezo bila kuhoji na hata bila kushirikisha wataalam wa elimu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Baraza la Mitihani Tanzania haina kifungu cha 30 kama alivyouliza Mheshimiwa Mbunge. Hata hivyo, Wizara inaona kuwa maudhui ya swali hili yanapatikana katika kifungu cha 20 cha Sheria ya Baraza la Mitihani Tanzania. Kifungu hiki kinampa mamlaka Waziri mwenye dhamana ya Elimu kufanya maamuzi kwa niaba ya Serikali pale inapolazimika kufanya hivyo kwa kuzingatia mahitaji ya jamii kulingana na wakati, mazingira halisi na matokeo ya tafiti mbalimbali kutoka kwa wataalam pamoja na maoni ya wadau wa elimu. Kwa kuzingatia matakwa ya sheria hii, Baraza la Mitihani Tanzania hutakiwa kuyatekeleza maamuzi hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali haina mpango wa kukifanyia marekebisho kifungu cha 20 cha Sheria ya Baraza la Mitihani Tanzania kwa kuwa kinamwezesha Mheshimiwa Waziri kufanya marekebisho mbalimbali kutokana na mahitaji ya jamii yanayojitokeza kwa wakati husika.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-
Wilaya ya Ileje haina vyuo vyovyote vya Serikali vya ufundi zaidi ya vile vichache vya taasisi za dini na chuo cha ufundi ambacho kinamaliziwa kujengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Japan:
Je, Serikali ina mpango gani wa kumalizia ujenzi wa chuo hicho cha ufundi ambacho bado kinahitaji jengo la utawala, vyoo, mabafu, kantini ya chakula, vifaa vya kufundishia pamoja na fedha ya kuwalipa wanafunzi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA MAFUNZO YA UFUNDI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Ileje, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kwamba uongozi wa Wilaya ya Ileje mwezi Februari, 2016 uliiomba Wizara yangu kuangalia uwezekano wa kukabidhi kwa Serikali kupitia VETA Chuo cha Ufundi Stadi kilichopo Ileje kinachomaliziwa kujengwa ili kiwe cha Wilaya. Wizara yangu kwa kutambua juhudi zilizofanyika hadi sasa iliagiza wataalam wa VETA Makao Makuu na VETA Kanda ya Kusini Magharibi kwenda Wilaya ya Ileje na kufanya tathmini ya majengo na kutoa ushauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya wataalam kufanya tathmini na kutoa ushauri wameiwezesha Wizara tarehe 17 Machi, 2016 kutoa maelekezo kwa uongozi wa Wilaya ya Ileje kupitisha suala la kukabidhi chuo hicho kwenye vikao vya kisheria ikiwemo DCC na RCC ili liweze kuridhiwa. Uongozi wa Wilaya ya Ileje pia ulielekezwa kuongeza eneo la ardhi kulingana na miongozo iliyopo ya VETA juu ya ujenzi wa chuo cha ufundi stadi. Pia halmashauri imeshauriwa ilipime eneo hilo na hatimaye kupata hati ya kiwanja kilipo chuo hicho na kisha makabidhiano rasmi yafanyike.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ridhaa ya vikao vya kisheria na kupatikana kwa hati ya kiwanja kilipojengwa chuo hicho Wizara itakuwa tayari kukipokea. Napenda kumuomba Mheshimiwa Mbunge kuhimiza viongozi wa Wilaya ya Ileje kutimiza maelekezo ya Wizara yangu ili makabidhiano ya chuo hicho cha ufundi cha ufundi kwa Serikali yafanyike kwa wakati na mapema iwezekanavyo.
MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:-
Watu wenye ulemavu wanapitia changamoto nyingi sana katika safari zao za kimaisha na mojawapo ni miundombinu isiyo rafiki kwa ajili ya kupata elimu:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kutatua matatizo hayo ili kuwawezesha watu wenye ulemavu kufurahia matunda ya elimu kwa kuweka mazingira mazuri yatakayowasaidia kupata elimu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Saleh Molel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Wanafunzi Wenye Ulemavu wanahitaji mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia pamoja na miundombinu rafiki katika maeneo yote ya kutolea elimu ikiwa ni pamoja na madarasa, jengo la utawala, maktaba, maabara na vyoo. Ili kuhakikisha kuwa miundombinu inaboreshwa kukidhi mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu, Wizara imechukuwa hatua zifuatazo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, imeandaa na kusambaza miongozo ya namna ya ujenzi wa majengo ya shule za msingi na sekodari pamoja na utengenezaji na ununuzi wa samani. Miongozo hiyo imeainisha mambo ya kuzingatia katika ujenzi wa majengo yote ya shule ili kupunguza vikwazo kwa wanafunzi wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika ujifunzaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua nyingine iliyochukuliwa na Wizara ni kuendelea kuhamasisha uanzishwaji wa shule na vitengo maalum vyenye mabweni kwa ajili ya kuandikisha wanafunzi wenye kiwango kikubwa cha ulemavu kwa lengo la kukabiliana na changamoto ya kutembea umbali mrefu na kuwapunguzia wazazi adha ya kuwapeleka na kuwarudisha nyumbani.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutoa mafunzo ya elimu maalum kwa Walimu katika ngazi mbalimbali ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa Walimu katika eneo hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kununua na kusambaza vifaa vya kielimu na visaidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wanaosoma katika shule za misingi na sekondari nchini. Sambamba na mikakati hiyo, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu imekuwa ikitoa kipaumbele katika kutoa mikopo kwa wanafunzi wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kutumia fursa hii kupitia Bunge lako Tukufu kuwakumbusha wale wote wanaojenga majengo maalum yakiwemo ya maghorofa kuweka miundombinu rafiki ili kuwawezesha wanafunzi wenye ulemavu kupata huduma za kielimu pasipo vikwazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, nawaomba Waheshimiwa Wabunge kuendelea kuhamasisha jamii kushirikiana na Serikali katika kujenga mazingira rafiki ya utoaji wa elimu kwa wanafunzi wenye ulemavu.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-
Serikali imepanua wigo wa uandishi na usomaji wa vitabu vya ziada na kiada mashuleni na kuna wakati tunapokea vitabu mbalimbali kutoka kwa wahisani.
(a) Je, ni utaratibu gani uliopo wa kudhibiti vitabu visivyo na maadili mema kwa watoto?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha Kitengo cha Udhibiti na Usimamizi wa Vitabu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliandaa Waraka wa Elimu Na. 4 wa mwaka 2014 unaoipa Mamlaka Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kuandika vitabu vyote vya kiada kwa ngazi ya elimu msingi, sekondari na vyuo vya ualimu. Wizara kupitia TET imeandaa na kutoa mwongozo wa kutathmini maandiko ya kutekeleza mitaala ikiwa ni pamoja na vitabu vinavyoandikwa na waandishi binafsi, vinavyotolewa na wahisani pamoja na vitabu vya kiada vinavyoandaliwa na TET unasisitiza masuala ya maudhui yanayotakiwa kwa kuzingatia muhtasari wa ngazi ya elimu husika pamoja na utamaduni na maadili ya Kitanzania.
Aidha, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia TET imeanzisha somo la uraia na maadili kuanzia darasa la tatu mpaka la sita ili kuwajengea uwezo watoto wa Kitanzania wa kuyafahamu ipasavyo maadili na utamaduni wetu mapema. Pia TET hutoa mafunzo kwa walimu ili kusisitiza suala la maadili kwao wenyewe na kwa watoto wanaowafundisha.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuimarisha Kitengo cha Tathmini na Udhibiti wa Ubora wa Maandiko yanayotumika kutekeleza mitaala, Wizara kupitia TET imeanzisha kitengo maalum chini ya Idara ya Utafiti, Habari na Machapisho, ambacho moja wapo ya majukumu yake ni kuratibu na kusimamia shughuli za kutathmini vitabu na maandiko ya kutekeleza mitaala ikiwa ni pamoja na vitabu vilivyoandikwa na waandishi binafsi pamoja na vitabu vilivyoandikwa na TET.
Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini ya maandiko ya kielimu hufanywa na wataalam kutoka vyuo vikuu, vyuo vya ualimu, shule za sekondari, shule ya msingi pamoja na makampuni mbalimbali ya uchapishaji wa vitabu na makala za kielimu. Aidha, hadi sasa TET imeshatathmini jumla ya miswada ya vitabu 160 vilivyochapishwa na wachapishwaji binafsi.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza:-
Vipo baadhi ya vyuo binafsi vinalipisha wanafunzi ada kwa kutumia pesa za kigeni badala ya pesa za Kitanzania. Je, Serikali inachukua hatua gani kudhibiti usumbufu huo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka ya nyuma yalikuwepo malalamiko kuhusu baadhi ya vyuo vya binafsi kutoza ada kwa fedha za kigeni. Kifungu cha 48(1) cha kanuni zinazosimamia utoaji wa elimu katika vyuo vikuu yaani The Universities General Regulations, 2013 kinakataza kuwatoza ada wanafunzi wa Kitanzania kwa fedha za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vinaruhusiwa kutoza ada kwa fedha za kigeni kwa wananfunzi wasio raia wa Tanzania kama inavyobainishwa katika kifungu cha 48(2) cha kanuni tajwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa misingi hiyo napenda kuchukua fursa hii kuwakumbusha wamiliki wa vyuo binafsi kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao ikiwa ni pamoja na kupewa onyo, kuvifungia na kutoruhusiwa kudahili wanafunzi.
MHE. SALUM MWINYI REHANI aliuliza:-
Kamisheni ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE) na Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) ni Taasisi za Muungano na zina Ofisi Zanzibar.
(a) Je, kuna Wazanzibari wangapi watendaji katika taasisi hizo?
(b)Kama hakuna, je, Serikali haioni kuwa hakuna uwiano kwa vile taasisi hizo ni za Muungano na kwa nini kusiwe na watendaji wa pande zote mbili za Muungano baina ya pande mbili?
(c) Je, kuna mipango gani ya kufanya taasisi hizi kuwa na watendaji wa pande zote mbili hasa Ofisi ya Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Salim Rehani, Mbunge wa Uzini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, watendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Elimu ya Ufundi (NACTE) huajiriwa kwa mujibu wa kifungu 13, 14 na 15 cha Sheria ya Vyuo Vikuu Sura ya 346 na Sura 129 ya sheria ya Baraza la Elimu ya Ufundi Tanzania pamoja na kanuni na miongozo mbalimbali ya utumishi wa umma.
Kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi yaani Staff Regulatiaons pamoja na muundo wa utumishi yaani Scheme of Service wa taasisi hizo, Watanzania wote wenye sifa stahiki wanayo fursa sawa ya kuajiriwa bila kujali upande anakotoka muajiriwa. Hivyo Wizara haijaweka utaratibu wa kuwabaini watumishi kwa misingi ya maeneo wanayotoka. Aidha kwa mujibu wa sheria ya Bunge Namba 21 ya mwaka 1973 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 iliyoanzisha Baraza la Mitihani, inabainisha kuwa muundo wa bodi ya baraza inajumuisha wajumbe watatu wanaotoka upande wa Zanzibar kati ya Wajumbe wote ambao ni kumi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia utaratibu huo na kwa kutambua kwamba TCU na NACTE ni miongoni mwa taasisi zinazoshughulikia elimu ya juu na ufundi ambayo ni kati ya masuala ya Muungano na kwa kuwa Watanzania wote wana fursa na haki sawa, Serikali itaendelea kuajiri watumishi kwa vigezo vya sifa za kitaalamu ili kukidhi malengo ya utoaji huduma bora kwa jamii kama inavyostahili bila ubaguzi.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa taasisi hizi zinatoa ajira kwa Watanzania wa pande zote za Muungano bila upendeleo wowote kwa kuzingatia sifa na mahitaji ya nafasi za ajira husika.
MHE. AMINA S. MOLLEL (K.n.y. MHE. RAISA ABDALLAH MUSSA) aliuliza:-
Mfumo wa Elimu ya Tanzania kwa kiasi kikubwa haimwandai mwanafunzi kuwa mbunifu na kuweza kujiajiri:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kubadili mfumo wetu wa elimu ili kuchochea mwanafunzi kuwa mbunifu na kuwa na uwezo wa kujiajiri?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mtaala wa elimu utakaotoa mafunzo yanayozalisha ajira?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raisa Abdallah Mussa, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Dira ya Elimu ni kuwa na Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mtazamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa. Mitaala inayotumika katika elimu ya awali, misingi na sekondari kwa sasa inaweka msisitizo katika kuwajengea uwezo wanafunzi kiutendaji na utumiaji wa maarifa wanayopata darasani.
Mheshimiwa Naibu Spika, mitaala hii ni ya kujenga umahiri ambapo katika tendo la kufundisha na kujifunza mwanafunzi anakuwa ndiye kiini cha somo na mwalimu anawajibika kutumia mbinu shirikishi wakati wa kufundisha. Matumizi ya mbinu shirikishi yanamfanya mwanafunzi ajifunze kwa kina na kujenga udadisi ambao unamwezesha kuwa mbunifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mafunzo kazini kwa Walimu yanafanyika ili kuwajengea uwezo, ikiwemo mafunzo ya KKK yanayozingatia kuwashirikisha wanafunzi kwa njia ya zana za kufundishia na michezo, mafunzo ya sayansi kwa nadharia na vitendo na mbinu shirikishi kwa masomo mengine pamoja na matumizi TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji. Pia mafunzo kwa Walimu tarajali unazingatia mbinu zinazojenga umahiri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maboresho katika mtaala wa elimu msingi na sekondari, Serikali imeandaa mkakati wa kujenga stadi na ubunifu kwa vijana kupitia Mkakati wa Kitaifa wa Kuendeleza Ujuzi (Skills Development Strategy). Kwa utekelezaji wa mkakati huo, katika mwaka 2016/2017, mradi ujulikanao kama Education and Skills for Productive Jobs (ESP) utaanza. Lengo la mradi huo ni kupanua fursa na kuboresha stadi za kazi katika ngazi za ufundi stadi, ufundi na elimu ya juu pamoja na vijana nje ya mfumo rasmi wa elimu kwa kushirikiana na taasisi binafsi, waajiri na sekta binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu kubwa ya mradi italenga kuwapatia wanafunzi ufadhili ili kujipatia fursa za stadi za kazi katika taasisi za mafunzo na pia katika sehemu za kazi (apprenticeship and internship). Aidha, vyuo vikuu mbalimbali nchini vinatekeleza programu za kuwaandaa wahitimu kuweza kujiajiri. Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, Nelson Mandela Arusha na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam vimeanzisha vituo viatamizi (incubators) katika fani mbalimbali. Vilevile Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili kitaanza kutoa mafunzo katika fani ya afya na sayansi shirikishi kwa kampasi mpya ya Mlonganzila kuanzia Oktoba, 2016.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ilifanya ongezeko la fedha za kujikimu kwa wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu kwa shilingi 1,000 kutoka shilingi 7,500 mpaka shilingi 8,500 katika mwaka wa fedha 2015/16 ongezeko ambalo haliendani na kasi ya mfumuko wa bei uliorekodiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kutoka aslimia 4.2 Februari, 2015 mpaka kufikia asilimia 5.6 Februari, 2016:-
Je, Serikali iko tayari kuongeza fedha hizo kufikia shilingi 10,000 kwa siku ili kuendana na kupanda kwa gharama za maisha?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikifanya utafiti juu ya gharama halisi za maisha ya wanafunzi ambazo hujumuisha gharama za chakula na malazi. Katika mwaka wa fedha wa 2014/2015 Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ilifanya utafiti katika vyuo vyote nchini ili kujua gharama halisi ya chakula na malazi. Utafiti huo ulionesha kuwa gharama hizo zilikuwa kati ya shilingi 8,000 mpaka 8,500.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa utafiti huo hufanyika kila baada ya miaka miwili, Wizara yangu itafanya utafiti mwingine, ili kubainisha gharama halisi za chakula na malazi. Matokeo ya utafiti huo yatatumika kupanga viwango vya fedha atakazolipwa mwanafunzi kwa kuzingatia gharama halisi pamoja na upatikanaji wa fedha.
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI aliuliza:-
Baadhi ya vyuo vikuu nchini vinaendelea kufanya tafiti mbalimbali zenye manufaa kwa wananchi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuviwezesha vyuo vikuu vyote hapa nchini, vikiwemo vya Tumaini na Mkwawa kufanya tafiti zitakazosaidia jamii kubwa ya wananchi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Zainabu Nuhu Mwamwindi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia mwaka wa fedha 2010/2011, Serikali iliazimia na kuanza kutenga kiwango kikubwa cha fedha za utafiti ikilinganishwa na miaka ya nyuma ili kuhakikisha kuwa tafiti zinafanyika kulingana na vipaumbele vya kitaifa. Serikali imekuwa ikitenga fedha hizi kupitia Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji wa Sayansi na Teknolojia (MTUSATE) unaoratibiwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kulingana na Sheria Namba 7 ya mwaka 1986 iliyoanzisha Tume hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha za utafiti kutoka kwenye mfuko huu zimekuwa zikitumiwa na watafiti wa ndani ya nchi wakiwemo watafiti kutoka vyuo vikuu. Utaratibu ni kwamba miradi hii ya utafiti hufadhiliwa kwa misingi ya ushindani kupitia ubora wa maandiko ya miradi ya utafiti. Hivyo basi, vyuo vikuu vyote vikiwemo Vyuo Vikuu vya Tumaini na Mkwawa vinayo nafasi ya kupata fedha hizo iwapo vitaomba na kukidhi vigezo husika vya ushindani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, vyuo vikuu vyote vinatakiwa kutenga fedha kupitia bajeti zao pamoja na kutafuta wafadhili, wadau wa maendeleo kwa ajili ya kuendeshea shughuli mbalimbali za maendeleo, ikiwemo kufanya utafiti.
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-
Baada ya ukarabati wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vya FDC – Njombe na kile cha Ulebwe kilichopo Wanging‟ombe.
(a) Je, ni fani zipi zitaanza kutolewa katika vyuo hivyo?
(b) Je, ni wananchi wangapi wanatarajia kufaidika na vyuo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya ukarabati wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC) Njombe na kile cha Ulebwe kilichopo Wanging‟ombe, Serikali itaendelea kuimarisha na kutoa mafunzo yale yale yaliyokuwa yanatolewa hapo awali, yaani mafunzo ya ufundi stadi katika fani za ufundi magari, ufundi chuma, useremala, uashi, umeme wa majumbani, ushonaji, kilimo na mifugo katika Chuo cha Njombe na fani za useremala, ushonaji, uashi, umeme wa majumbani, kilimo na mifugo katika Chuo cha Ulebwe.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na uwezo na vyuo hivyo, Chuo cha Mendeleo ya Wananchi Njombe kina uwezo wa kunufaisha wananchi 180 wa kukaa bweni na wananchi 70 wa kutwa, wakati Chuo cha Wananchi Ulebwe kina uwezo wa kunufaisha wananchi 80 wa kukaa bweni na 40 wa kutwa na hivyo kufanya jumla ya wananchi wanufaika 370 kwa mwaka.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALOSS aliuliza:-
(a) Je, katika bajeti ya mwaka 2015/2016, Serikali imepeleka wanafunzi wangapi kusoma nje ya nchi?
(b) Je, kada gani ambazo zilipewa kipaumbele?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Galoss, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa masomo 2015/2016, Serikali ilipeleka jumla ya wanafunzi 159 katika nchi za China 84, Algeria 57, Urusi wanne (4), Misri wawili (2) na Uingereza kupitia Jumuiya ya Madola 12.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inapeleka wanafunzi nje ya nchi kwa kuzingatia vipaumbele vya Taifa ambavyo ni masomo ya sayansi, teknolojia na TEHAMA. Hivyo wanafunzi wanaopelekwa nje ya nchi husoma shahada ya kwanza, uzamili na uzamivu katika fani za nishati na madini; mfano masuala ya gesi na mafuta, mazingira na mabadiliko ya tabia nchi, uhandisi, afya na sayansi shirikishi, usanifu majengo, elimu, uchumi na mawasiliano.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha vijiji vya Mlembwe, Kimambi, Lilombe, Mirui, Mpigamiti, Kikulyungu na Mtungunyu vinapata miradi ya mawasiliano ya simu za mkononi?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha usikivu hafifu wa matangazo ya Redio Tanzania (TBC – Taifa) katika Wilaya ya Liwale?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa Liwale kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vya Mlembwe, Lilambwe, Mirui, Mpigamiti na Mtungunyu vimo katika orodha itakayofikishwa huduma ya mawasiliano na kampuni ya simu ya Halotel katika Awamu ya Nne inayotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2017. Aidha, kijiji cha Kikulyungu katika Kata ya Mkutano kitafikishiwa huduma ya simu na kampuni ya simu ya TTCL kupitia mradi wa Awamu ya Kwanza B, kwa jumla ya ruzuku ya dola za Kimarekani 143,280. Mradi huu unategemewa kukamilika mwezi Machi, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Utangazaji Tanzania lina mitambo ya kurushia matangazo ya redio katika Mkoa wa Lindi kwa kutumia mitambo yake iliyopo Nachingwea eneo la Songambele na Lindi eneo la Kipihe. Hivi sasa mitambo ya redio ya masafa ya kati kilowati 100 iliyopo eneo la Songambele Wilayani Nachingwea haifanyi kazi kutokana na uchakavu. Mitambo ya Lindi eneo la Kipihe ni ya FM ambayo ni kilowati 2. Hali hii inasababisha maeneo mengi ya Mkoa wa Lindi na Mtwara kutopata usikivu mzuri wa matangazo ya redio ikiwemo Wilaya ya Liwale na mengine kutopata matangazo kabisa. Mtambo uliopo Kipihe, Lindi una uwezo wa kurusha matangazo katika maeneo ya Lindi Mjini na baadhi ya maeneo ya Lindi Vijijini. Shirika limeandaa mpango mahsusi wa kupanua usikivu nchi nzima ambao utekelezaji wake utategemea upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kujenga mitambo yenye uwezo wa kurusha matangazo maeneo yote yaliyoathirika na kutofanya kazi kwa mtambo wa Nachingwea wa kilowati 100. Mpango wa muda mrefu ni kuhakikisha kuwa TBC inanunua mitambo inayolingana na teknolijia ya kisasa katika tasnia ya utangazaji. Mpango huu utahusisha pia maeneo mengine ya nchi ambako mitambo ya masafa ya kati haifanyi kazi.
MHE. ALLY M. KEISSY aliuliza:-
Mheshimiwa Rais alipokuwa Wizara wa Ujenzi wakati wa Awamu ya Nne aliahidi kwamba baada ya barabara ya Sumbawanga - Mpanda kukamilika kwa lami majengo yaliyopo katika kijiji cha Paramawe, Wilayani Nkasi yatatumika kwa ujenzi wa VETA, hasa ikizingatiwa kuwa Wilaya ya Nkasi haina chuo hicho.
(a) Je, Serikali iko tayari kutumia majengo hayo kwa ajili ya chuo cha VETA?
(b) Je, Serikali, iko tayari kwenda kuyaona majengo hayo mara barabara itakapokamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ally Mohamed Keissy, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, (a) napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ipo tayari kutumia majengo yaliyopo katika kijiji cha Paramawe, Wilayani Nkasi ambayo ni kambi ya ujenzi wa barabara ya lami ya Sumbawanga - Mpanda kwa ajili ya Chuo cha Ufundi Stadi chini ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA) ili kuweza kutoa mafunzo ya ufundi stadi baada ya kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, (b), Serikali pia ipo tayari kutuma wataalam kutoka wa VETA kutoka Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kwenda kuyaona majengo hayo mara barabara hiyo itakapokamilika kwa lengo la kufanya tathimini na kujiridhisha juu ya ubora wake kwa ajili ya kutoa mafunzo ya ufundi stadi. Hata hivyo, majengo hayo tatatumika kutolea mafunzo ya ufundi stadi baada ya kukamilika kwa taratibu za kupata idhini kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ambao ni wamiliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa ushauri kwa wananchi wa Wilaya ya Nkasi waendelee kutumia Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Chala, kuwapatia ujuzi vijana wakati juhudi za Serikali, za kuwatafutia chuo cha ufundi zikiendelea.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA aliuliza:-
Ni Sera ya Taifa kuwa na Chuo cha Ufundi katika kila Wilaya:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha Ufundi katika Wilaya ya Geita?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Lolesia Bukwimba, Mbunge wa Busanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza maandalizi ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Standi cha Mkoa wa Geita kitakachohudumia Wilaya zote za Mkoa huo pamoja na maeneo mengine ya nchi. Mnamo tarehe 6 Agosti, 2016 nilifanya ziara katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa, moja ya maeneo niliyotembelea ni eneo la Magogo katika Mji wa Geita mahali ambapo chuo hicho kitajengwa. Lengo lilikuwa ni kutoa msukumo wa upatikanaji wa hati miliki ya eneo hilo ili hatua za ujenzi zianze mapema kama ilivyopangwa katika bajeti ya mwaka huu wa 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo furaha kukuthibitishia kuwa hatimiliki ya kiwanja Namba 177 kitalu E, chenye ukubwa wa hekta 27.27 yaani ekari 68.17 kwa umiliki wa miaka 99 imepatikana. Kazi inayofuata ni kumpata Mshauri Elekezi na Mkandarasi ili ujenzi uweze kuanza mapema iwezekanavyo.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI aliuliza:-
(a) Je, ni wanafunzi wangapi walifuzu kwa kiwango cha Diploma na Digrii katika Sekta za Sanaa na Ubunifu, Habari, Teknolojia na Sayansi, Elimu ya Afya kwa Mwaka 2010-2015?
(b) Je, Serikali imefanya tathmini katika maeneo ya utumishi yenye uhaba wa taaluma tajwa hapo juu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Immaculate Sware Semesi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, wanafunzi waliofuzu kwa kiwango cha stashahada kwa kipindi cha kati ya mwaka 2010 hadi 2015 katika sekta za Sanaa na Ubunifu (Fine and Perfoming Arts) ni 254, Habari yaani waandishi ni 1,565, Teknolojia ya Sayansi ni 12,538 na Elimu ya Afya ni 14,177, jumla walikuwa 28,534. Aidha, kwa upande wa wanafunzi waliofuzu kwa kiwango cha shahada kwa kipindi tajwa, takwimu zinaonesha kuwa katika sekta za Sanaa na Ubunifu ni 136, Habari 2020, Teknolojia na Sayansi ni 11,953 na Elimu ya Afya ni 5,043 ambapo jumla yao walikuwa ni 17,334
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba inaeleweka kuna upungufu wa wataalam katika baadhi ya fani, kama vile Uandishi wa Habari, Afya, Ualimu wa masomo ya Sayansi, Uandishi wa Teknolojia na Gesi, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora tayari imeandaa Andiko(Concept Note) kwa lengo la kufanya tathmini ya kina katika sekta mbalimbali, zikiwemo zilizotajwa kwenye kipengele (a) cha swali la msingi ili kuainisha mahitaji na upungufu wa Rasilimali watu, kiidadi na kiujuzi katika Utumishi wa Umma na hatimaye kuweza kuandaa mkakati wa namna ya kushughulikia upungufu utakaoonekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati utakaoandaliwa ambao unatarajiwa kukamilika mwaka wa fedha 2016/2017 utaiwezesha Serikali kuwa na matumizi mazuri ya Rasilimali iliyopo ili kufikia Malengo na Mipango ya Taifa ya Maendeleo.
MHE. ESTER M. MMASI aliuliza:-
Changamoto nyingi kwa upande wa kada za waendeshaji Vyuo Vikuu unatokana na uteuzi usio na tija katika nafasi za Wakuu wa Vitengo, Rasilimali Watu na uongozi chini ya Mwongozo wa Universities Charter.
Je, nini msimamo wa Serikali kuhakikisha kada za watumishi wa umma, Taasisi za Elimu ya Juu zinaheshimika na nafasi za Wakuu wa Vitengo, Rasilimali Watu, zinatumika kiufasaha kulingana na miongozo ya kiutumishi.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ester Michael Mmasi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uteuzi wa kada za waendeshaji pamoja na Wakuu wa Idara na Vitengo katika vyuo vikuu vya umma hufuata muundo wa utumishi wa wafanyakazi waendeshaji ambao pamoja na mambo mengine, unazingatia miongozo inayotolewa na Serikali kupitia Msajili wa Hazina na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
Mheshimiwa Spika, nina imani kwamba tatizo siyo taratibu, sheria au miongozo iliyopo ya uteuzi kama hati idhini za vyuo vikuu (universities charter), bali ni ukosefu wa maadili ma ubinafsi kwa baadhi ya wahusika kwenye michakato hiyo. Serikali imeshachukua hatua ya kuchunguza malalamiko kama hayo katika vyuo na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Elimu, Sanyansi, na Teknolojia ili kujua ukweli na ikibainika kuwa kuna wahusika walivuruga utaratibu na kupelekea kuteuliwa viongozi wasiostahili watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB aliuliza:-
Kumekuwa na malalamiko ya wanafunzi wa elimu ya juu Tanzania ambao ni wazawa kulipishwa ada ya masomo yao kwa fedha za kigeni badala ya fedha za Kitanzania wakati wao ni Watanzania na vyuo hivyo viko hapa nchini licha ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kulipigia kelele sana jambo hilo:-
(a) Je, Serikali inatambua kuwa kuna tatizo hili na kama inatambua imechukua hatua gani dhidi ya tatizo hilo?
(b) Kwa kuwa kilio hiki kipo kwenye taasisi mbalimbali kama vile bandarini, uwanja wa ndege, hoteli na taasisi za fedha na kadhalika, je, Serikali inatoa tamko gani juu ya jambo hili?
(c) Je, kuna sheria yoyote ya nchi inayomtaka mwanachuo wa Kitanzania kulipa ada kwa pesa ya kigeni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, kutoka Baraza la Wawakilishi, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa swali kama hili lilijibiwa Bungeni mnamo tarehe 7/9/2016 na lilikuwa ni swali namba 24. Baada ya maagizo yaliyotolewa kwa wamiliki wa vyuo kuzingatia kanuni na taratibu zilizowekwa hakuna malalamiko kuhusiana na vyuo kutoza ada kwa Watanzania kwa fedha za kigeni yaliyowasilishwa. Hivyo, kama kuna chuo chochote kinachotoza ada kwa Watanzania kwa fedha za kigeni naomba tupate taarifa rasmi ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, sarafu inayotakiwa kutumika Tanzania ni Shilingi ya Kitanzania kwa mujibu wa kifungu cha 25 na 26 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ya mwaka 2006. Aidha, kwa Tanzania malipo ya kitu au huduma yoyote inapaswa kulipwa kwa Shilingi ya Kitanzania kama ilivyoainishwa kwenye Kifungu cha 28 cha Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu ni hakuna.
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA aliuliza:-
Chuo Kikuu cha Mzumbe ni chuo kikongwe chenye historia tangu mwaka 1953 kipindi cha ukoloni na mwaka 1972 kupandishwa hadhi kuwa Chuo cha Uongozi wa Maendeleo (IDM) kikiwa na miundombinu ya kukidhi wanafunzi wasiozidi 1,000. Kwa sasa chuo hiki kina jumla ya wanafunzi 11,282 ambapo idadi hii ni sawa na ongezeko la 874.3% wakati hali ya majengo na miundombinu kwa kiasi kikubwa bado ni ile ile ya mwaka 1972:-
Je, ni lini sasa Serikali itaanza kujenga miundombinu mipya ikiwemo madarasa, mabweni, ofisi za Wahadhiri, jengo la utawala na kadhalika ili kukidhi mahitaji ya ongezeko kubwa la wanafunzi na Wahadhiri waliopo na watakaokuja na kukifanya chuo hiki chenye historia kubwa kiwe na taswira ya chuo cha kisasa na hadhi ya kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasmine Tiisekwa Bunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali imeshaanza kujenga miundombinu mipya kwa ajili ya kuongeza uwezo wa kudahili na kuleta tija kwa Chuo Kikuu cha Mzumbe. Kati ya mwaka 2010/2011 hadi 2015/2016, Serikali ilitenga na kutoa jumla ya Sh. 8,075,490,199 fedha za maendeleo kwa ajili ya ukarabati na kujenga majengo na miundombinu mipya katika Kampasi za Mzumbe, Mbeya na Dar-es-Salaam. Aidha, kwa mwaka 2016/2017, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu na majengo katika Kampasi Kuu ya Mzumbe na shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mipya katika Kampasi ya Mbeya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilidhamini chuo kujenga jengo jipya la ghorofa tano lenye thamani ya shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya kumbi za mihadhara, maktaba, ukumbi wa mikutano na ofisi katika Kampasi ya Dar-es-Salaam ambalo limekamilika na linatumika. Katika Kampasi ya Mbeya jengo jipya la ghorofa mbili la maktaba lenye vyumba vya maabara ya computer na ofisi limekamilika na limeanza kutumika mwaka 2015/2016. Vilevile ujenzi wa jengo la taaluma na utawala lenye ghorofa mbili unaendelea na unafadhiliwa na Serikali pamoja na mkopo kutoka kwa Mamlaka ya Elimu (TEA) kwa thamani ya shilingi bilioni 2.7.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa juhudi hizi za ukarabati, ujenzi na mipango inayoendelea kutekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Mzumbe ni dhahiri kwamba Serikali ina nia ya dhati ya kuinua hadhi ya chuo hiki na hivyo kuweka mazingira stahiki ya kufundishia na kujifunzia.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED aliuliza:-
Wasichana wanaohitimu kidato cha sita wanakuwa na ufaulu mzuri lakini wanapojiunga na vyuo vya elimu ya juu ufaulu wao huanza kushuka hadi wengine hufikia kusimamishwa masomo kwa sababu ya ufaulu hafifu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wasichana katika elimu yao ya juu ili ufaulu wao uweze kuongezeka na kufikia malengo yao?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Ali Mohammed, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufaulu wa wanafunzi wanaosoma katika vyuo vya elimu ya juu wa jinsi zote kwa kiasi kikubwa hutegemea juhudi binafsi katika kuzingatia masomo kwa kadri ya maelekezo ya uhadhiri wao. Hata hivyo, mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wa kike kwa baadhi ya vyuo vikuu yana changamoto mbalimbali ikiwemo upungufu wa hostel na hivyo kusababisha wanafunzi hao kupanga nyumba za kuishi mitaani na hivyo kutumia muda mwingi katika kutafuta usafiri na mahitaji yao muhimu ya kujikimu. Hali kadhalika, katika mazingira kama hayo, kwa namna moja au nyingine baadhi ya wasichana hujiingiza katika vitendo vinavyoweza kuchangia kushuka kwa ufaulu wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo, Serikali imekuwa ikifanya jitihada za makusudi katika kuweka mazingira stahiki kwa wanachuo zikiwemo ujenzi wa hostel katika vyuo vikuu ambazo umuhimu wa pekee unatolewa kwa wanafunzi wa kike na watu wenye ulemavu.
Kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali imetoa shilingi bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa hostel zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na utaratibu huo wa kuongeza mabweni utaendelea pia katika vyuo vingine.
Aidha, katika vyuo vikuu vya umma na binafsi kunatolewa huduma za ushauri na unasihi Dawati la Jinsia na Dawati la Malalamiko kwa nia ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kuathiri ufaulu wa wanafunzi wa kike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kuwashauri wanafunzi wa kike kuzingatia masomo kwa umakini wa hali ya juu na kujiepusha na vitendo ambavyo vinaweza kusababisha ufaulu duni na hivyo kushindwa kufikia malengo waliyojiwekea.
MHE. DEO K. SANGA aliuliza:-
Serikali iliahidi kujenga Vyuo vya VETA kwa kila Wilaya ili kuwasaidia vijana
kujifunza stadi za kazi mbalimbali:-
(a) Je, hadi sasa ni Vyuo vingapi vya VETA vimeshajengwa katika nchi
nzima?
(b) Je, ni lini Chuo cha VETA kitajengwa katika Wilaya ya Njombe?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,
napenda kujibu swali la Mheshimiwa Deo Kasenyenda Sanga, Mbunge wa
Makambako, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa Serikali kupitia Mamlaka ya
Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi VETA imeshajenga na kumiliki vyuo 29 vya
ufundi stadi vya ngazi ya Mkoa, Wilaya na vyuo maalum vya ufundi. Vyuo hivyo
orodha yake ni Mikoa ni Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Lindi, Mtwara, Moshi,
Manyara, Dodoma, Kigoma, Mbeya, Iringa, Mwanza, Kihonda na Tabora. Vyuo
vya Wilaya ni Dakawa, Mikumi, Singida, Songea, Mpanda, Shinyanga, Kagera,
Mara, Makete, Ulyankulu na Arusha ambapo vyuo maalum vya ufundi ni pamoja
na Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro, Chuo cha Mafunzo ya TEHAMA
Kipawa na Chuo cha Mafunzo ya Hoteli na Utalii -Njiro.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa sasa haina mpango wa
kujenga chuo cha ufundi stadi katika Wilaya ya Njombe, badala yake
itaviboresha Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi - Njombe na Ulembwe na
kuvijengea uwezo ili viweze kutoa mafunzo ya ufundi stadi sanjari na mafunzo ya
maendeleo ya wananchi. Aidha, Mkandarasi wa ujenzi wa Chuo cha VETA cha
Mkoa wa Njombe ameshapatikana ambaye anaitwa Herkin Builders Limited na
yupo katika eneo la kazi, Kijiji cha Shaurimoyo Wilaya ya Ludewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo hicho kinajengwa katika eneo hilo
kimkakati kutokana na miradi ya chuma na makaa ya mawe ya Mchuchuma na
Liganga. Vilevile, Wizara kupitia bajeti ya mwaka 2016/2017 imetenga fedha kiasi
cha shilingi milioni 450 kwa ajili ya kujenga bweni katika chuo cha VETA Makete ili
kuongeza udahili kwa wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali.
MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:-

Mwaka 2014 katika Chuo cha Ualimu Korogwe yalifanyika mabadiliko ya udahili, udhibiti ubora na tunu yaliyofanywa na Baraza la Elimu ya Ufundi la Taifa – NACTE lakini chuo kimekuwa kikipata wanachuo wachache kuliko miundombinu na rasilimali watu waliopo; na kwa kuwa chuo hiki kwa sasa kimepelekewa wanachuo wapatao 827 kutoka Chuo Kikuu UDOM kwa mafunzo ya Stashahada ya Kawaida ya Elimu:-
Je, Serikali itaendelea kuwapeleka wanachuo wa kutosha ili kuendana na miundombinu na rasilimali watu waliopo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Ualimu Korogwe kina uwezo wa kudahili wanachuo 1,200 kwa wakati mmoja na ndiyo sababu wanachuo wapatao 827 kutoka Chuo Kikuu UDOM walidahiliwa kwa mafunzo ya Stashahada ya Kawaida ya Elimu. Hata hivyo, chuo hicho kimekuwa kinadahili wanachuo wachache kuliko uwezo wake hususan mwaka 2015/2016 kilidahili wanachuo 234 kutokana na kuhuishwa sifa za kujiunga kuwa ufaulu wa daraja la I - III na kuwepo kwa ushindani wa wahitimu wa kidato cha IV kuwa na fursa nyingine za kujiunga na kidato cha V na wahitimu wa kidato cha VI kujiunga na vyuo vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa dhamira ya kuwapokea wanachuo wa kutosha katika Chuo cha Ualimu Korogwe ili kuendana na miundombinu na rasilimali watu waliopo.
MHE. ZAYNAB M. VULLU aliuliza:-
Serikali imeona umuhimu wa kuchukua hatua kali zaidi kwa mwanaume anayempa mimba mwanafunzi wa shule kwamba apatiwe kifungo cha miaka 30:-
Je, Serikali itamhakikishiaje mwanafunzi aliyepewa mimba kuwa ataweza kuendelea na masomo baada ya kujifungua?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zaynab Matitu Vullu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 pamoja na mambo mengine, imeweka mkazo juu ya kuhakikisha upatikanaji wa elimu kwa wote. Aidha, sera inatamka wazi kuwa Serikali itaondoa vikwazo vinavyozuia fursa ya wanafunzi kuendelea na masomo na hivyo kukamilisha mzunguko wa elimu katika ngazi husika na kwamba itahakikisha kuwa usawa wa kijinsia katika elimu na mafunzo unazingatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sehemu ya utekelezaji wa sera hiyo, Serikali imeandaa Rasimu ya Mwongozo utakaofuatwa na wadau mbalimbali ili kuwawezesha wasichana waliopata ujauzito kurudi shuleni na kuendelea na masomo yao baada ya kujifungua. Mwongozo huu pia, baadhi ya mambo yaliyowekwa ni utaratibu utakaofuatwa kwa wasichana waliojifungua kuendelea na masomo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na nia ya Serikali kuondoa vikwazo kwa mtoto wa kike ili kuendelea na masomo, wito unatolewa kwa wadau mbalimbali wakiwemo wazazi, walimu, viongozi wa elimu pamoja na dini na jamii kwa ujumla kwa pamoja kuchukua hatua za makusudi za kuzuia na kudhibiti tatizo la mimba shuleni na katika umri mdogo kwani kwa kiwango kikubwa inamvunjia heshima mwanafunzi mwenyewe na kuwa chanzo cha upotevu wa maadili na pengine kupoteza dira yake ya mafanikio katika maisha.
MHE. SOPHIA M. SIMBA aliuliza:- Lugha ya Kiingereza ina umuhimu mkubwa katika majadiliano na wenzetu wa nchi nyingine na pia hutumika kufundishia katika shule zetu kuanzia sekondari hadi vyuo vikuu, lakini lugha hii imekuwa changamoto kubwa kwa wanafunzi katika masomo yao. (a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kufundisha lugha ya kiingereza kuanzia shule za awali na kuendelea ili Watanzania wawe na lugha ya pili inayotumiwa na watu wote? (b) Je, Serikali haioni kuwa wananchi wengi wanapenda kuongea kiingereza hivyo ione namna ya kuwawezesha?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sophia Mattayo Simba, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mfumo wa elimu wa Tanzania zipo shule za msingi za Serikali zipatazo 11 na zisizo za Serikali zinazotumia lugha ya kiingereza kuanzia darasa la awali ambapo lugha ya kiswahili hutumika kama somo. Vilevile sehemu kubwa ya shule za msingi za Serikali hutumia lugha ya kiswahili kama lugha ya kufundishia tangu awali na lugha ya kiingereza kama somo kuanzia darasa la tatu na kuendelea. Aidha, lugha ya kiingereza ni lugha inayotumika kufundishia shule za sekondari na vyuo vikuu kwa masomo yote isipokuwa komo la kiswahili. (b)Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inathamini mchango wa matumizi ya lugha ya kiingereza kwani hutumiwa na wananchi kama lugha ya pili katika kupata maarifa na ujuzi katika nyanja za uchumi, siasa, utamaduni, sayansi na teknolojia. Katika kuimarisha matumizi ya lugha ya kiingereza kwa walimu, kati ya mwaka 2014 hadi 2016 Serikali iliendesha mafunzo ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa somo la kiingereza kwa walimu wapato 14,054 kupitia mpango wa Student Teacher Enrichment Programme (STEP). Pia kati ya mwaka 2015 hadi 2017 iliendesha mafunzo ya mitaala mipya kwa walimu wapato 82,186 ili kumudu stadi za ufundishaji wa masomo yote ikiwemo kiingereza. Aidha, kwa watu wazima wanaopenda kujifunza lugha ya kiingereza zipo taasisi ambazo hutoa mafunzo ya muda mfupi
MHE. MATTAR ALI SALUM Aliuliza:-
Kuna malalamiko makubwa kwa upande wa Zanzibar kuhusu idadi ndogo ya wanafunzi wanaopata Mkopo wa Elimu ya Juu jambo ambalo linapunguza idadi ya wataalamu kwa upande wa Zanzibar, hivyo kuingia katika soko la ajira katika Afrika ya Mashariki na Kati na kuijenga nchi yetu kwa ujumla.
(a) Je, Serikali haioni kuwa Bodi ya Mfuko wa Elimu ya Juu inatakiwa kutenga asilimia maalum kwa wanafunzi kutoka Tanzania Zanzibar?
(b) Je, bajeti iliyotengwa kwa mwaka huo wa 2015/2016 ni kiasi gani?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Matta Ali Salum, Mbunge wa Shaurimoyo, lenye Sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu huzingatia matakwa ya sheria, kanuni, vigezo na miongozo itolewayo mara kwa mara na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu. Vigezo muhimu vinavyozingatiwa ni pamoja na kwamba muombaji awe ni raia wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, awe mhitaji, mlemavu au yatima. Aidha, muombaji anatakiwa kuwa amedahiliwa katika taasisi ya elimu ya juu na awe anachukua programu za vipaumbele vya taifa ambavyo ni ualimu wa sayansi na hisabati, uhandisi wa gesi na mafuta, sayansi za afya na uhandisi wa kilimo na maji.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2015/2016 kiasi cha shilingi 480,599,067,500 kilitumika kwa ajili ya kugharamia mikopo pamoja na ruzuku kwa ajili ya wanafunzi 124,358.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI (K.n.y. MHE. MARY P. CHATANDA) Aliuliza:-
Serikali imekuwa ikitoa majibu ya upandishwaji wa madaraja na fedha za likizo kwa walimu nchini na katika Chuo cha Ualimu Korogwe kuna walimu na watumishi ambao wanadai kupandishwa vyeo na fedha za likizo.
(a) Je, Serikali ina mpango gani kuwapandisha daraja wale wanaostahili?
(b) Je, ni lini Serikali italipa madai yao ya fedha za likizo ambazo hawajawahi kulipwa?

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini,
lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imekuwa ikiwapandisha vyeo watumishi wake wenye sifa kila mwaka. Kwa mfano, katika mwaka wa 2015/2016, Wizara iliwapandisha vyeo watumishi 2,272 kati yao watumishi 71 ni wa Chuo cha Ualimu Korogwe.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kulipa madeni mbalimbali ikiwa ni pamoja na fedha za likizo kwa walimu/watumishi katika sekta ya elimu, ambapo katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016 hadi mwezi Juni, 2016 jumla ya shilingi 22,629,352,309.99 zililipwa kwa walimu 63,814. Aidha, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/2017 hadi kufikia Machi, 2017 jumla ya shilingi 10,505,160,275.80 zimelipwa kwa walimu 22,420 na hivyo kufanya jumla ya walimu waliolipwa katika kipindi hicho kufikia 86,234. Katika malipo haya, jumla ya shilingi 13,415,410 zimelipwa kwa ajili ya madeni ya fedha za likizo kwa watumishi sita wa Chuo cha Ualimu Korogwe. Uhakiki wa madeni ya miaka ya nyuma unaendelea kuratibiwa na mamlaka husika na taratibu za malipo zitakamilishwa kwa wale watakaostahili.
MHE. MARY P. CHATANDA aliuliza:-
Mwaka 2001, Chuo cha Ualimu Korogwe kwa kushirikiana na wananchi, walianza ujenzi wa maktaba ambayo bado haijakamilika; na kwa kuwa wanachuo na wananchi wa Korogwe wanahitaji sana maktaba hiyo:-
Je, Serikali itakuwa tayari kusaidia juhudi zilizokwishaanza ili kukamilisha jengo hilo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, Mbunge wa Korogwe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa maktaba hiyo kwa Wanajumuiya wa Chuo cha Ualimu Korogwe na wananchi kwa ujumla, Wizara yangu iko tayari kusaidia ujenzi wa maktaba hiyo na hivyo itatuma wataalam kwenda kufanya tathmini ya hatua iliyofikiwa na msaada unaohitajika ili ujenzi huo uweze kukamilika katika mwaka wa fedha wa 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kutokana na jinsi wananchi wa Korogwe wanavyoshirikiana vizuri na Mbunge wao, Mheshimiwa Mary Pius Chatanda, kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha elimu.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Kujua kusoma na kuandika ni nguzo muhimu sana katika maendeleo ya demokrasia na kudumisha umoja na amani nchini.
Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua elimu ya watu wazima kwa vijana wote walio chini ya miaka 40?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kujua kusoma na kuandika ni nguzo muhimu sana katika maendeleo ya demokrasia na kudumisha umoja na amani nchini. Takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 kwa Tanzania Bara zinaonyesha kuwa watu wenye umri wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ambao hawajui kusoma na kuandika ni asilimia 22.4.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa kujua kusoma na kuandika Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kutekeleza programu mbalimbali za kuwapatia vijana na watu wazima stadi za kujua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Programu hizo ni pamoja na mpango wa uwiano kati ya elimu ya watu wazima na jamii (MUKEJA)unaojumuisha programu ya ndiyo ninaweza inayoendeshwa kama tarajali katika Wilaya tisa za majaribio ambazo ni Halmashauri za Wilaya za Bagamoyo, Mwanga na Mkurunga, pamoja na Manispaa za Ilemela, Dodoma, Songea, Kinondoni, Temeke na Ilala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuimarisha elimu ya watu wazima na kuiwezesha jamii kuwa na stadi za KKK, Wizara yangu imeandaa miongozo ya wawezeshaji na vitabu ambavyo vimekwisha sambazwa katika Halmashauri zote nchini. Aidha, kila Mamlaka ya Serikali ya Mitaa imeelekezwa kutenga fedha katika bajeti zake kwa ajili ya kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia, kutoa mafunzo kwa wawezeshaji, kulipa honoraria kwa wawezeshaji, kufanya ufuatilia na kuhamasisha jamii ili watu wazima na vijana wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu wajiunge kwenye madarasa ya kisomo.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH (K.n.y. MHE. SEIF K. S. GULAMALI) aliuliza:-
Serikali ina mpango wa kujenga vyuo vya ufundi katika kila wilaya nchini:-
(a) Je, shirika lisilo la Kiserikali linaweza kujenga chuo hicho katika Kata ya Chuma, Chakola Makao Makuu ya Tarafa ya Manonga na kuikabidhi Serikali?
(b) Je, ni lini Serikali itajenga chuo hicho ili kiweze kutoa msaada katika Wilaya za Igunga na Nzega?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Seif Khamis Said Gulamali, Mbunge wa Manonga, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika Lisilo la Kiserikali linaweza kujenga chuo cha ufundi stadi katika Kata ya Chuma, Chakola, Makao Makuu ya Tarafa ya Manonga na kuikabidhi Serikali. Ili Serikali iweze kupokea chuo hicho, ni vema kabla ya kuanza ujenzi mawasiliano yafanyike kati ya taasisi hiyo kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Igunga na Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA) ili kwa pamoja masuala yote ya kisheria yaweze kuzingatiwa.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inashauri kwamba wakati juhudi mbalimbali za kutafuta fedha na wafadhili wa kujenga vyuo hivyo vya wilaya zinaendelea, wananchi wa Wilaya ya Igunga waendelee kutumia vyuo vya ufundi stadi vilivyopo Mkoani Tabora ambavyo ni Chuo cha VETA Tabora kilichopo Mjini Tabora na Ulyankulu kilichopo Wilayani Kaliua, pamoja na Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Nzega na vyuo vingine vilivyosajiliwa na Mamlaka ya Ufundi Stadi.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA (K.n.y. MHE. MARGARET S. SITTA) aliuliza:-
Kwa mujibu wa takwimu za Serikali kumekuwa na ongezeko kubwa la Taasisi za Elimu zikiwemo shule za Serikali na zisizo za Serikali za msingi na sekondari, shule maalum, vyuo vya ualimu na vituo vya elimu ya watu wazima; na kwa kuwa suala la ubora wa elimu ni kipaumbele kwa Watanzania walio wengi.
Je, kwa nini Serikali isiunde chombo kinachojitegemea
cha ukaguzi wa elimu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Idara ya Ukaguzi wa Shule iliundwa kwa mujibu wa Sheria ya Elimu Sura ya 353 ya sheria za nchi ikiwa na jukumu ka kufuatilia ubora wa elimu ya msingi, sekondari na vyuo vya ualimu kwa kuzingatia viwango vya utoaji wa elimu vilivyowekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Idara ya ukaguzi wa shule ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Elimu, kwa sasa wizara yangu inafanya mabadiliko ya sheria ya mfumo mzima wa elimu ili iende sambamba na Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014. Suala la ukaguzi wa shule kuwa chombo kinachojitegemea litaangaliwa kwa mapana katika hatua za kufanya mabadiliko ya sheria hiyo, pamoja na nyingine ambazo zitaweza kuongeza ufanisi katika ukaguzi wa shule.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itarekebisha mitaala ya elimu ili elimu
ya ujasiriamali na stadi za maisha ziweze kufundishwa kwa wanafunzi wanaohitimu darasa la saba na kidato cha nne ambao hawatabahatika kuendelea na masomo na hatimaye waweze kuwa na uelewa wa kujiajiri na kujitegemea?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa na utaratibu wa kuboresha mitaala ili kuendana na mahitaji ya jamii kwa wakati husika. Mwaka 2005 Serikali iliboresha mitaala ya elimu ya msingi na sekondari ambapo masuala ya ujasiriamali yaliingizwa ili kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiajiri. Uboreshaji huu ulihusisha pia kuingiza maudhui ya stadi za maisha kama suala mtambuka. Kwa ujumla mitaala imezingatia kutoa elimu ya ujasiriamali kupitia maudhui na mbinu za kufundishia na kujifunzia ambazo zinawafanya wanafunzi kuwa watendaji wakuu au kitovu cha kujifunza.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakiboresha Chuo cha Maendeleo ya Jamii yaani FDC Sikonge ili kilingane na Vyuo vya VETA kwa kuogeza idadi ya walimu na mafunzo yanayotolewa?
NAIBU WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya vyuo 55 vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) kuhamishiwa katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2016/2017 Wizara imeanza kufanya tathmini kwa vyuo vyote ili kujua mahitaji halisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutimiza azma hiyo, katika bajeti ya maendeleo kwa mwaka fedha 2017/2018 zimetengwa kiasi cha shilingi bilioni 12 kwa ajili ya kukarabati majengo na miundombinu ya baadhi ya Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi. Wizara pia katika bajeti ya maendeleo ya mwaka 2017/2018 imetenga shilingi bilioni 10 kupitia Mradi wa Kukuza Stadi za Kazi (ESPJ) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na ambao utadumu kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2017 imepanga kuviboresha kwa awamu vyuo hivyo 55 vya Maendeleo ya Wananchi, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Sikonge kitatembelewa ili kuona uwezekano wa kukiboresha.
MHE. EDWARD F. MWALONGO (K.n.y MHE. PROF. NORMAN A. SIGALLA KING) aliuliza:-
Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika Wilaya ya Makete hakina mabweni hivyo kunufaisha kata moja tu wakati watoto wanaotoka Tarafa za Matamba, Ikuwo, Magoma, Bulongwa, Ukwama na Kata za Lupila na Tandala hawawezi kunufaika na Chuo hicho kwa sababu ya umbali uliopo.
Je, ni lini Serikali itakipa chuo kipaumbele cha kujengewa mabweni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Norman Adamson Sigalla King, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa fedha za maendeleo kiasi cha shilingi 250,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili katika Chuo cha VETA cha Makete. Mkandarasi Tanzania Building Agency (TBA) anategemewa kuanza ujenzi kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2017 baada ya kukamilisha hatua za kusaini mkataba.
MHE. STELLA I. ALEX aliuliza:-
Kutokana na umuhimu wa elimu jumuishi Tanzania (inclusive education).
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa kila mwalimu anapatiwa mafunzo maalum yatakayomuwezesha kufundisha wanafunzi wenye ulemavu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stella Ikupa Alex, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imeandaa mtaala mpya ambao umeandaliwa katika misingi ya elimu jumuishi na ulianza kutumika kuanzia mwaka wa masomo 2014/2015. Hadi sasa wahitimu wa ngazi ya Stashahada ya Elimu Maalum wapato 158 wamehitimu Oktoba, 2016 na wanachuo 248 wanaendelea na masomo katika Chuo cha Ualimu Patandi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhumu wa walimu hawa, Wizara katika mwaka wa fedha 2016/2017 iliendesha mafunzo kwa walimu kazini 519 wanaofundisha darasa la kwanza na la pil kuhusiana na mtaala ulioboreshwa ili kumudu ufundishaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalum. Vilevile tarehe 20 mpaka 28 Juni, 2017 walimu kazini 712 wanaofundisha wanafunzi wenye ulemavu wa akili na wenye usonji walipatiwa mafunzo katika vituo vya Mwanza, Arusha, Mbeya na Morogoro ili kuwajengea uwezo wa kumudu ufundishaji wa wanafunzi wenye ulemavu wa akili na usonji.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, walimu 600 wanaofundisha darasa la tatu na la nne watapatiwa mafunzo ya mtaala ulioboreshwa kuanzia tarehe 10 hadi 30 Julai, 217 lengo ni kuwafikia walimu wengi zaidi.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Serikali iliahidi kujenga vyuo vya VETA kwa kila Wilaya ili kuwasaidia vijana kujifunza stadi za kazi mbalimbali:-
Je ni lini Chuo cha VETA kitajengwa katika Wilaya ya Lushoto?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shaaban Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaanza ujenzi katika Wilaya ya Lushoto mara baada ya kukamilisha miradi ya Vyuo vya VETA iliyoanzwa. Vyuo hivyo ni pamoja na Ludewa, Namtumbo, Kilindi, Chunya, Ukerewe, hiyo ni kutokana na tatizo la upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inashauri kwamba wakati juhudi mbalimbali zinaendelea za kutafuta fedha na ufadhili wa kujenga vyuo, wananchi wa Lushoto waendelee kutumia Chuo cha VETA kilichopo katika Mkoa wa Tanga na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) vilivyopo Muheza na Handeni na vyuo vingine vilivyosajiliwa na Mamlaka ya VETA nchini.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:-
Serikali kwa sasa ina Sera ya Elimu Bure kuanzia chekechea hadi kidato cha nne:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu bure kwa kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Destery Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Serikali haina mpango wa kutoa elimu bila malipo kwa wanafunzi wa kidato cha tano na cha sita na badala yake imejikita zaidi katika kuboresha miundombinu ambayo ni pamoja na upungufu wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, majengo ya utawala pamoja na kumalizia changamoto za uhaba wa Walimu wa sayansi na vifaa vya kufundishia na kujifunzia ikiwa ni pamoja na masuala ya TEHAMA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kukamilika kwa miundombinu hiyo itasaidia kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wenye sifa ya kuingia kidato cha tano wanapata fursa ya kuendelea na masomo yao.
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA aliuliza:-
Mji wa Tunduma una vijana wengi wanaohitimu kidato cha nne lakini wanakosa nafasi za kuendelea na masomo ya juu:-
Je, Serikali inasema nini kuhusu kujenga Chuo cha Ufundi VETA ili vijana wengi waweze kupata ujuzi na kujiajiri na kuongeza kipato chao?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Frank George Mwakajoka, Mbunge wa Tunduma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haitaweza kujenga Chuo cha VETA katika Halmashauri ya Tunduma kwa sasa kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Wakati juhudi mbalimbali zinaendelea za kutafuta vyanzo vya ufadhili wa kujenga Vyuo vya Ufundi Stadi kupitia VETA, wananchi wa Mji wa Tunduma waendelee kutumia vyuo vilivyopo katika mikoa jirani hususan Mkoa wa Mbeya wenye Chuo cha VETA cha Mkoa na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) vya Nzovwe kilichopo katika Manispaa ya Mbeya na Katumba katika Wilaya ya Rungwe. Aidha, wananchi wanashauriwa kuendelea kutumia vyuo vingine vilivyosajiliwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) katika mikoa mbalimbali nchini ili kupata mafunzo ya ufundi stadi.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO aliuliza:-
Sera ya Elimu ya mwaka 2014 inaeleza wazi kuhusu mitaala na utaratibu wa masomo katika elimu ya msingi (kidato cha kwanza - nne) na inasema watoto wa kidato cha kwanza – pili watasoma masomo yote ya sayansi na wanapoingia kidato cha tatu watachagua masomo wayatakayo kutokana na uwezo wao.
(a) Je, Waziri alipata wapi mamlaka ya kutangaza kuwa vijana wote wa elimu ya msingi hada kidato cha nne kusoma masomo yote ya sayansi?
(b) Je, kuna utafiti gani uliofanyika na matokeo kuonesha haja ya vijana wote kusoma sayansi yaani kemia na fizikia?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Susan Anselm Lyimo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya Pili kipengele cha 4(1) na 5(f) cha Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1995 inampa Mamlaka Waziri mwenye dhamana ya Elimu kutangaza jambo lolote lenye maslahi kwa Taifa kutokana na hali halisi iliyopo kwa wakati huo. Kwa sasa kuna haja kubwa ya kuhamasisha ongezeko la wanasayansi kulingana na hali halisi ya mahitaji. Kwa mfano, kuna upunfufu wa walimu wa sayansi na hisabati 24,716, upungufu wa walimu 355 wa masomo ya ufundi katika shule za sekondari za ufundi na mafundi sanifu wa maabara wa shule takribani 10,000. Moja ya jukumu kuu la Waziri ni kuhamasisha wanafunzi katika elimu ikiwa ni pamoja na kuchukua masomo ya sayansi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika sehemu (a) taarifa mbalimbali zikiwemo za kimazingira halisi (evidence based) zinathibitisha juu ya upungufu wa wataalam wa sayansi, mfano kwa upande wa afya, ili kupunguza vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua inatakiwa kina mama hao wahudumiwe na matabibu wenye ujuzi lakini hawapo wa kutosha, Wizara imekuwa ikihamasisha wanafunzi kuchukua masomo ya Sayansi ili kupunguza tatizo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia haijatoa waraka wowote unaowataka wanafunzi wote kusoma masomo ya sayansi, badala yake imejikita katika kuimarisha miundombinu ya maabara, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na kupeleka walimu wa sayansi shuleni.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI (K.n.y. MHE. JUMANNE
K. KISHIMBA) aliuliza:-
Mfumo wetu wa elimu unaonekana kuchangia mfumuko wa matatizo ikiwemo kujenga mazingira ya udanganyifu na wizi wa mitihani hali inayopelekea baadhi ya wanafunzi kufutiwa matokeo.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kumpima mwanafunzi kwa kutathmini tangu shule ya msingi na kuoanisha na mtihani wake wa mwisho ili kupata uhalisia na uwezo badala ya kumpima mwanafunzi kwa kigezo cha mtihani wa siku moja?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jumanne Kibera Kishimba, Mbunge wa Kahama Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa tathmini unaotumika kwa sasa unajumuisha alama za upimaji wa mwanafunzi awapo shuleni yaani alama za upimaji endelevu pamoja na mtihani wake wa mwisho. Mfano, katika matokeo ya mtihani wa mwisho wa kidato cha nne, kidato cha sita na ualimu yaani cheti na diploma, alama za upimaji wa mwanafunzi awapo shuleni zinachangia asilimia 30 na mtihani wa mwisho unachangia asilimia 70.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kufanya utafiti zaidi kwenye mifumo ya utahini inayotumika katika nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kuboresha mfumo wa utahini kwa kadri inavyowezekana na inavyoonekana inafaa na kwa kuzingatia mazingira ya utoaji wa elimu bora nchini. (Makofi)
MHE. MUSA R. NTIMIZI aliuliza:-
Serikali inahamasisha upatikanaji wa elimu kwa maana ya ujenzi wa shule nyingi zaidi karibu na makazi ya wananchi wetu yaani satellite schools na Waheshimiwa Wabunge na Madiwani wameitikia wito na viongozi tumezichangia sana.
Je, ni kwa nini Serikali haizisajili shule hizo na kupeleka walimu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kuanzishwa kwa satellite schools au shule shikizi ni kuwezesha watoto wadogo wa darasa la kwanza mpaka la tatu ambao hawana uwezo wa kutembea umbali mrefu kufuata shule mama kusoma karibu na makazi yao. Sababu nyingine za kuanzishwa shule hizi zinajumuisha kuwepo vituo vya msimu vya wavuvi, wafugaji wanaohamahama na kuwepo mazingira yanayosababisha maafa kama mafuriko na misitu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu za shule hizo kutosajiliwa na kupangiwa walimu ni kuwa ni za muda mfupi ambazo ziko chini ya shule mama husika. Kwa mfano, ikianzishwa kwa sababu ya mafuriko, mafuriko yakiisha na shule hiyo itakuwa imekufa. Vilevile shule hizi hazikidhi vigezo vya kusajiliwa ambavyo ni uwepo wa ofisi ya mwalimu mkuu, mwalimu mkuu msaidizi, ofisi za walimu, vyoo, vyumba vya madarasa, maktaba na store.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU) kilichopo Lushoto kwa mafanikio makubwa kimeweza kutumia teknolojia rahisi inayoitwa Grapho Game, kwa kiswahili ni Grafo Gemu kupunguza idadi kubwa ya wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika darasa la kwanza na la pili katika shule kadhaa zilizopo Wilaya ya Lushoto na Bagamoyo na pia SEKOMU kwa kutumia teknolojia hiyo imewezesha watu wazima kujua kusoma na kuandika katika kijiji cha Kwemishai – Kibohelo – Lushoto.
(a) Je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka sasa kuwatumia wataalam walioko SEKOMU akiwemo mtalaam aliyeshiriki kutayarisha maudhui katika teknolojia ambayo imeweka msisitizo katika mbinu za kufundishia kusoma ya kifoniki ambayo hujikita katika utambuzi wa sauti za herufi zinazounda maneno?
(b) Je, Serikali haioni ni jambo muhimu kabisa kwa kupitia mpango huu muhimu na maalum kama walivyofanya nchi ya Zambia na Finland kuidhinisha matumizi ya teknolojia hiyo iwe kama teknolojia suluhisho (IT Solution) kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa madarasa ya mwanzo ya elimu ya msingi wenye changamoto ya kujua kusoma na kuandika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Seriakli inatambua umuhim,u wa kuimarisha stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa wanafunzi wanaosoma madarasa ya chini hususan elimu ya awali, darasa la kwanza hadi darasa la nne na watu wazima wasiojua kusoma na kuandika kwa kuwa stadi hizo zinawawezesha kupata umahiri katika stadi za KKK.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itawasiliana na mtaalam wa Grafo Gemu (kiswahili) ili kufahamu jinsi teknolojia hiyo inavyofanya kazi. Wizara itakapojiridhisha na ufanisi wa matumizi ya teknolojia hiyo, itafuata taratibu stahiki na kuidhinisha matumizi ya teknolojia hiyo shuleni.
MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:-
Serikali iliwahi kuliahidi katika Bunge hili kuwa inafanya mapitio ya Sera ya Elimu Bure na kwamba ingeleta Bungeni mambo yanayohitaji kuboreshwa:-
Je, ni lini mapitio hayo yatakamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wangu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Phillip Gekul, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iliamua kuondoa malipo ya ada kwa elimu msingi inayojumuisha elimu ya awali pamoja na darasa la kwanza hadi kidato nne kama utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Ibara ya 3.1.5 na Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 Ibara ya 52(a). Lengo la Sera hii ni kuhakikisha kuwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule wanapata fursa hiyo bila kikwazo chochote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na umuhimu wa maamuzi hayo ya Serikali kwa ustawi wa wananchi na Serikali kwa ujumla mwezi wa Februari mwaka 2017 Wizara ilifanya ufuatiliaji kuhusu utekelezaji wa Sera hii ili kubainisha mafanikio na changamoto kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kuwa Serikali itatumia matokeo na mapendekezo ya ufuatiliaji uliofanyika kutatua changamoto zilizojitokeza ili kuhakikisha lengo la Serikali la kutoa fursa kwa watoto wote wenye umri wa kwenda shule linafikiwa.
MHE. GIMBI D. MASABA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika Mkoa wa Simiyu na kukijengea uwezo wa kutengeneza vifaa vya baiskeli, pikipiki na magari?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Gimbi Dotto Masaba, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia mradi unaofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa mkopo wa masharti nafuu imeendelea na maandalizi ya ujenzi wa chuo kipya cha mafunzo ya ufundi stadi cha Mkoa wa Simiyu ambapo kwa sasa Wizara imempata mtaalam wa kusanifu majengo na kusimamia ujenzi wa chuo hicho. Usanifu wa majengo hayo unatarajiwa kukamilika Novemba, 2017. Baada ya usanifu wa majengo hayo, zabuni ya ujenzi itatangazwa na ujenzi wa chuo hicho unatarajiwa kuanza Februari, 2018.
Mheshimiwa Spika, sambamba na kuanza kwa ujenzi wa chuo hicho, Serikali inaendelea kuandaa mahitaji halisi ya rasilimali watu, mitaala itakayotumika, mashine na mitambo, samani na vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Maandalizi hayo ni kwa ajili ya kujengea chuo uwezo wa kutoa mafunzo ya ufundi stadi na kuwapata wahitimu wenye stadi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutengeneza vifaa vya baiskeli, pikipiki na magari.
MHE. MOSHI S. KAKOSO (K.n.y MHE. SULEIMAN J. ZEDI) aliuliza:-
Serikali imejitahidi sana kupeleka umeme vijijini jambo ambalo litaongeza ajira kutokana na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vya kusindika mazao ya kilimo maeneo ya vijijini kama vile usindikaji wa mafuta ya alizeti, kukoboa na kupaki mpunga na kusaga na kupaki unga wa mahindi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa vijijini kupata elimu, mitaji na masoko ili shughuli za kuanzisha usindikaji wa mazao ya kilimo kiwe tija?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Suleimani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Zedi kwa kutambua juhudi za Serikali za kupeleka umeme vijijini ambao ni kichocheo muhimu katika uanzishwaji wa viwanda vidogo vya usindikaji wa mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa viwanda katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi, Wizara yangu kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) inatekeleza mkakati wa Wilaya moja, bidhaa moja (One District, One Product – ODOP) ambao SIDO kwa kushirikiana na wadau katika Halmashauri walichagua bidhaa moja katika Wilaya kwa lengo la kuiendeleza. Kwa upande wa Bukene wao walichagua zao la mpunga.
Mheshimiwa Spika, hivyo, SIDO ina jukumu la kutoa huduma mbalimbali ikiwemo mafunzo juu ya usindikaji mazao ya kilimo, kuendeleza teknolojia rahisi za uongezaji thamani mazao ya kilimo na kuandaa maonesho ya kikanda ili kuwasaidia wajasiriamali waweze kupata masoko ya bidhaa zao.
Mheshimiwa Spika, aidha, kupitia Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Ujasiriamali (National Entrepreneurship Development Fund) wananchi wa vijijini wamekuwa wakikopeshwa fedha kwa masharti nafuu ili waweze kuanzisha miradi midogo na ya kati kwa lengo la kujipatia ajira na kuongeza kipato.
Mheshimiwa Spika, tunatambua tatizo la SIDO kutowafikia wananchi walio wengi zaidi vijijini kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa rasilimali fedha na mtandao wa shirika kuishia ngazi ya Mkoa katika Mikoa yote ya Tanzania Bara. Hivi sasa changamoto hizo zitatazamwa kwa kina katika hatua ya kupitia upya sheria iliyoanzisha shirika hilo kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa shirika katika kuhudumia jasiriamali ndogo na za kati nchini.
MHE.BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-
Kupitia vikao vya Jumuiya ya Afrika Mashariki, mwaka 2015 Serikali ya Kenya iliruhusiwa na Jumuiya hiyo kuuza ndani ya nchi hiyo bila kutozwa kodi bidhaa za ngozi na nguo zinazozalishwa nchini humo kwenye maeneo huru ya uwekezaji (Export Processing Zones [EPZ]).
Je, ni sababu zipi za msingi zilizotumika kufanya uamuzi huo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Itifaki ya Umoja wa Forodha ya Afrika Mashariki ibara ya 25 inahusu kanuni zinazosimamia uzalishaji kwenye maeneo huru ya uwekezaji kutoka nje, teknolojia na kutengeneza ajira. Ibara ya 26 inaeleza kuwa viwanda vilivyopo kwenye maeneo haya havipaswi kulipa kodi hata kidogo…

…havipaswi kulipa kodi hata kidogo wanapoingiza malighafi kwa ajili ya uzalishaji. Aidha, viwanda hivi vinaanzishwa kwa ajili ya kuongeza mauzo nje na kupata fedha za kigeni na wanaweza kuuza kwenye soko la ndani asilimia 20 ya kiwango kinachozalishwa kwa mwaka huska na kulipa kodi kiasi hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia Mkutano wa 17 wa Viongozi Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ulizungumzia suala la mitumba ya na viatu, Serikali ya Kenya iliwasilisha ombi la kuuza asilimia 20 ya bidhaa zinazozalishwa katika maeneo huru ya uwekezaji yaani EPZ bila kulipa kodi. Sababu ya msingi iliyowasilishwa na Kenya na kukubaliwa na nchi wanachama ni kuwa kwa kuuza bidhaa hiyo bila ushuru wananchi wangenunua bidhaaa mpya kutoka maeneo huru ya uwekezaji badala ya mitumba. Pamoja na kukubali ombi hilo iliamuliwa kuwa bidhaa kutoka maeneo huru ya uwekezaji yaani EPZ ikiingia katika nchi za jumuia itatozwa kodi zote pamoja na ushuru wa forodha.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH aliuliza:-
Pamoja na jitihada za Serikali na mmiliki wa Kiwanda cha Nyuzi Tabora (TABOTEX) ambazo zimewezesha kiwanda hicho kuwa katika hali ya kufanya kazi bado kiwanda hicho kinakabiliwa na ukosefu wa soko la bidhaa zake:-
Je, ni kwa nini Serikali isikipatie kiwanda hiki hadhi ya EPZ ili kipate vivutio vitakavyokiwezesha kupata ushindani katika masoko ya nje?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Munde Tambwe Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda cha Nyuzi cha Tabora kilisajiliwa na Serikali tarehe 17 Agosti, 1977 kwa lengo la kusokota nyuzi za pamba ili kuuza kwenye viwanda vya nguo vya ndani ya nchi na ziada kuuzwa nje ya nchi. Kiwanda hiki kilianza kazi rasmi tarehe Mosi Januari, 1990 kikiwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni 6.22 kwa mwaka na kuajiri zaidi ya watu 1,000. Kiwanda hiki baadaye kilibinafsishwa kwa mtindo wa kuuza mali (disposal of assets) kupitia Loans and Advances Realization Trust (LART) hadi mwaka 2004 kilipopata mnunuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mnunuzi huyo Ms Rajan Indusrties alinunua kiwanda hicho kwa thamani ya dola milioni 1.5 ambapo baadaye pia alishindwa kuendesha kiwanda hicho. Mwezi Julai hadi Septemba, 2017 alijitokeza mwekezaji na kufunga mitambo midogo na kwa ajili ya kutengeneza kamba na vifungashio kwa mazao kama tumbaku na korosho. Aidha, ameanza mchakato wa kufufua kinu cha kuchambulia pamba cha Manonga ambacho Rajan ni mmiliki mbia na chama cha Igembensabo Corporation Union kwa asilimia 80 na mwenzake asilimia 20.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kiwanda kusajiliwa chini ya Mamlaka ya EPZ nawashauri wawekezaji wawasiliane na EPZA. Hata hivyo, ili kiwanda kiweze kusajiliwa chini ya mamlaka ya EPZ kinatakiwa kukidhi vigezo vifuatavyo:-
• Kuwa na uwekezaji mpya ikiwa ni pamoja na mashine;
• Kuwa na mtaji usiopungua dola za Kimarekani milioni 500;
• Kuwa na uhakika wa soko la nje;
• Kuuza asilimia 80 ya bidhaa zake nje ya nchi; na
• Kuwa na uhakika wa kutoa ajira mpya zisizopungua 500 tofauti na ajira zilizopo sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo nawashauri wawekezaji kupitia vigezo hivyo kutathmini na hatimaye kuwasilisha maombi ya kusajiliwa kwenye mamlaka ya EPZ.
MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:-
Mkataba wa Kimataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu (UNCRPD) wa mwaka 2006 Ibara ya tisa (9) unazungumzia haki za watu wenye ulemavu kupata habari kwa kuwa kumekuwa na changamoto za kisheria hususani katika nyaraka zenye hati miliki:-
Je, ni lini Serikali itaridhia Mkataba wa Kimataifa wa mwaka 2013 Marrakesh Treaty ambao unalenga kuondoa vikwazo mbalimbali vinavyozuia walemavu wasioona waweze kupata habari katika mifumo inayokidhi mahitaji yao?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Saleh Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkataba wa Marrakesh ni mkataba wenye lengo la kuwawezesha watu wenye matatizo ya kuona, kupata nakala za maandishi yenye hati miliki na vifaa vya kuwasaidia kuweza kupata elimu kwa urahisi kwa kutumia vitabu, magazeti, burudani na shughuli mbalimbali za kijamii, hivyo kuwasaidia katika maisha yao ya kila siku na kuwawezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiuchumi na kuondoa umaskini hatimaye kuchangia katika pato la Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania kupitia COSOTA ilisaini itifaki ya Marrakesh tarehe 28 Juni, 2013. Wizara inaandaa mapendekezo ya kuridhia Itifaki ya Marrakesh kulingana na taratibu zinavyoelekeza na hivi sasa inakusanya maoni ya wadau kuhusu mkataba huo. Baada ya kukamilika kwa hatua hiyo, waraka wa mapendekezo utawasilishwa Baraza la Mawaziri na hatimae kuletwa Bungeni kwa lengo la kuridhia.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Wizara ni kuleta Itifaki ya Marrakesh Bungeni haraka iwezekanavyo mara baada ya kukamilisha taratibu zinazotakiwa kufuatwa ili kuridhia Mkataba wa Kimataifa.(Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano imejipambanua kama Serikali ya viwanda na kuna Shirika la Serikali lililoanzishwa kwa ajili ya kuanzisha na kuimarisha Viwanda Vidogo Vidogo vya SIDO .
(a) Je, kwa kiasi gani Serikali imeliwezesha Shirika hilo katika kufikia malengo yake na malengo ya Serikali kwa Tanzania ya viwanda?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa Shirika hilo linakuwa na matawi katika kila Wilaya tofauti na sasa kuwa na Ofisi katika ngazi za Mikoa tu?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuliwezesha Shirika la SIDO kutoa huduma za kujenga uwezo kwa wajasiriamali kupitia programu za mafunzo, ushauri, teknolojia, masoko na utoaji wa mitaji. Katika kufanikisha hilo Serikali imekuwa ikiimarisha bajeti za SIDO kila mwaka na kwa mwaka wa fedha 2018/2018 SIDO ilitengewa shilingi bilioni 14.2 kwa ajili ya kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya viwanda na kuongeza mtaji kwenye mfuko wa NEDF. Kati ya fedha hizo Serikali imekwishatoa shilingi bilioni tano kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Ofisi na Industrial Sheds katika mikoa ya Simiyu, Geita, Kagera kwa hatua ya kwanza na utaratibu unakamilika kwa hatua ya pili katika mikoa ya Mtwara, Manyara, Dodoma na Katavi.
Pia Serikali kwa kushirikiana na wabia na maendeleo ikiwemo Serikali ya Japan kupitia JICA, Serikali ya Canada kupitia CESO na Serikali ya India zimeendelea kuipatia SIDO uwezo ikiwemo kuanzisha vituo vya viatamizi vya kuonyesha na kufundishia teknolojia mbalimbali, kuendesha makongano ya wanaviwanda vidogo nchini na kushirikiana na SIDO kutambua mahitaji halisi ya wajasiriamali na kuwasaidia kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni dhamira yetu kuwa karibu na wananchi katika dhama hizi za kuhamasisha ujenzi wa uchumi wa viwanda kwani viwanda vidogo na vya kati ni muhimu katika kujenga uchumi ulio jumuishi. Kutokana na ufinyu wa bajeti kwa sasa tunahudumia ngazi ya kata mpaka Wilaya kwa kupitia Halmashauri za Wilaya.
MHE. RASHID M. CHUACHUA aliuliza:-
Serikali imekuwa ikiahidi kusimamia Sera ya Viwanda ili Tanzania iwe na uchumi wa kati, lakini hakuna jitihada za wazi za kufufua viwanda vya korosho ili kuongeza thamani halisi ya zao hilo na kutengeneza ajira.
(a) Je, ni lini Serikali itahakikisha Kiwanda cha Korosho cha Masasi kinafanya kazi?
(b) Kwa kuwa utaratibu wa ununuzi wa korosho hauruhusu viwanda kununua korosho kutoka kwa wakulima; je, ni lini Serikali itafungua mlango ili kukuza viwanda hivyo ili vipate fursa ya kununua malighafi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Mohamed Chuachua, Mbunge wa Masasi lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Korosho cha Masasi ni moja ya viwanda vilivyobinafsishwa na kuuzwa kwa Kampuni ya BUCCO Investments Holdings Limited ambayo ilishindwa kukiendesha kutokana na benki ya CRDB kuzuia mali za kiwanda baada ya kiwanda kushindwa kurejesha mkopo waliokopa. Hatimaye kiwanda kiliuzwa na CRDB kwa Kampuni ya Micronix Export Trading Co. Ltd., kwa njia ya mnada. Kwa kuwa BUCCO hawakuridhika na utaratibu uliotumika kuuza kiwanda hicho, walifungua kesi mahakamani na kuishtaki benki ya CRDB.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kesi iliyopo mahakamani uendelezaji wa kiwanda hicho umeshindikana hadi hapo mahakama itakapotoa uamuzi wa kesi husika. Serikali inaandaa mazungumzo na wadau wa viwanda vyote ambavyo vina kesi mahakamani kikiwemo Kiwanda cha Korosho Masasi ili kuharakisha utatuzi wa migogoro iliyopo na hatimaye kuwezesha uwekezaji kuendelea ili vianze uzalishaji haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haijakataza viwanda kununua korosho kutoka kwa wakulima, bali imekataza ununuzi wa korosho kufanyika kiholela kutoka kwa wakulima. Kwa kuwa lengo ni kusimamia maslahi ya wakulima na wadau wengine wa zao la korosho, Serikali ilianzisha utaratibu wa kuuza korosho kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani. Mfumo huo haulengi kuvififisha viwanda bali kuwanufaisha wakulima na wadau wengine ikiwa ni pamoja na wenye viwanda. Kutokana na mfumo huo, korosho zilizohifadhiwa kwenye maghala huweza kutumika kama malighafi ya viwanda kwa mwaka mzima. Aidha, wakulima wanafaidika na bei shindani na udhibiti katika ubora wa korosho unakuwa ni wa uhakika.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-
Serikali imetenga maeneo kadhaa kwa ajili ya uwekezaji nchi nzima:-
Je, ni lini Serikali itatafuta fedha za kutosha kuweka miundombinu muhimu katika maeneo haya ili kuvutia uwekezaji?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Janet Mbene, Mbunge wa Ileje, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia EPZA na halmashauri za wilaya na mikoa imetenga maeneo ya uwekezaji sehemu mbalimbali nchini. Kama alivyosema Mheshimiwa Janet Mbene maeneo ya namna hii ni muhimu katika kuvutia uwekezaji katika sekta ya ujenzi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika uendelezaji wa maeneo hayo kwa kuweka miundombinu wezeshi na miundombinu saidizi, Serikali imebuni mpango wa kushirikiana na sekta binafsi kuendeleza maeneo hayo kama ilivyofanyika kwa Eneo Maalum la Kiuchumi la Bagamoyo. Kwa maeneo yatakayokuwa na uhitaji wa haraka wa kuendelezwa kupitia Mfuko Mkuu wa Hazina tutayatengea fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa viwanda vidogo katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga shilingi bilioni saba kwa ajili ya kujenga miundombinu ya SIDO kwenye mikoa mbalimbali nchini.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani kukamilisha ujenzi wa masoko ya kimataifa ya Nkwenda na Murongo ambayo yamekaa miaka mingi bila kukamilishwa wakati yangekamilishwa yangewapatia soko la uhakika wananchi wa Kyerwa na Mkoa mzima wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Sebba Bilakwate, Mbunge wa Kyerwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Masoko ya Kimkakati ya Kimataifa ya Nkwenda na Murongo ni miongoni mwa masoko matano yaliyokuwa yanajengwa kama sehemu ya utekelezaji wa Program ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) kupitia mradi wa uwekezaji katika sekta ya kilimo ngazi ya Wilaya (District Agriculture Sector Investment Project – DASIP).
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa masoko hayo mpaka sasa umekamilika kwa hatua za awali. Katika soko la Nkwenda ujenzi umekamilika kwa asilimia 25 hadi 30 na soko la Murongo ujenzi umekamilika kwa asilimia 40 hadi 50.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa masoko haya ulisimama baada ya mradi wa DASIP kufikia ukomo wake mwaka 2013 na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) iliyokuwa ikifadhili ujenzi huo kusitisha utoaji wa fedha kwa ajili ya mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukamilisha mradi wa ujenzi wa masoko hayo, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inayoratibu Program ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo katika bajeti ya mwaka wa 2017/2018, imetenga Sh. 385,914,778 kwa soko la Nkwenda na Sh.561,232,364 kwa soko la Murongo. Ujenzi wa masoko hayo utaendelea pindi fedha hizo zitakapotolewa.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua Kiwanda cha SONAMCU kilichopo Songea Mjini?
(b) Je, Serikali ipo tayari kuwaongezea gawio la uzalishaji wa tumbaku wananchi wa Wilaya ya Namtumbo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania ambayo ni msimamizi wa vyama vya Ushirika Tanzania imewezesha kukamilisha mkataba kati ya mnunuzi mwingine wa Tumbaku Kamouni ya Premium Active Tanzania Limited na Chama Kikuu cha Ushirika cha Wilaya za Songea na Namtumbo (SONAMCU Ltd.) wa miaka saba na mkataba huu umeboreshwa zaidi kwa kuweka kipengele cha tumbaku yote inayozalishwa Songea lazima isindikwe katika Kiwanda cha Tumbaku kilichopo Songea Mjini. Mkataba huu tayari umeshasainiwa na umeshaanza msimu huu wa mwaka 2018/2019 ambao utadumu kwa miaka saba hadi mwaka 2025/2026. Vyama vyote vya msingi vimeingia mkataba na Chama Kikuu cha Ushirika (SONAMCU) ili kudhibiti tumbaku yote itakayozalishwa Songea na Namtumbo kusindikwa katika kiwanda cha tumbaku kilichopo Songea Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwezi huu wa Februari, kampuni hii itawaleta wahandisi wawili kutoka nchi ya Italia ambao watafika Songea na kushirikiana na Mkoa ili kuandaa gharama halisi za ukarabati na mtambo mwingine utakaoagizwa Italia ili tumbaku yote itakayozalishwa kuanzia msimu huu wa 2018/2019 isindikwe katika Kiwanda cha Songea Mjini. Serikali ina matumaini kuwa kiwanda hiki kitafunguliwa na kuanza upya kazi ya usindikaji wa tumbaku ifikapo mwezi Julai, 2018 hivyo kuwezesha kutoa ajira kwa wananchi zikiwemo ajira za kudumu na za msimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkataba wa ununuzi wa tumbaku uliopo sasa kati ya SUNAMCU na Premium Active Tanzania Limited umeanza kuongeza uzalishaji wa tumbaku kwa wananchi wa Wilaya ya Namtumbo kutoka kilo 250,000 za mwaka 2017/2018 hali kufikia kilo milioni moja kwa mwaka 2018/2019. Aidha, mkataba unaonesha kila mwaka kutakuwa na ongezeko la uzalishaji wa tumbaku kutoka kwa mnunuzi aliyeingia mkataba kufuatana na ubora na mahitaji ya soko la nje ya nchi.
Hata hivyo, Serikali inaendelea kuboresha mazingira na fursa ya wanunuzi wengine watakaojitokeza wenye mahitaji ya tumbaku. Ikumbukwe kuwa ongezeko hutokea endapo tu kuna mwenendo mzuri wa biashara katika soko na ongezeko la uzaishaji. Ahsante sana.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI aliuliza:-
Kila mwaka Tanzania inaagiza tani laki nne za mafuta ya kula wakati tuna malighafi za kutosha kama vile alizeti, ufuta na kadhalika kwa ajili ya kuzalisha mafuta hayo.
Je, Serikali haioni haja ya kuchukua hatua za makusudi za kutumia malighafi hizo ipasavyo na kuokoa fedha za kigeni zinazopotea nchini?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khadija Nassir Ali, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Khadija kuwa nchi yetu imebarikiwa kuwa na mazao ya aina nyingi ambayo ni vyanzo vya mafuta ya kula. Ni kweli kuwa kama Taifa, Tanzania tunaagiza zaidi ya tani laki nne za mafuta hali inayotugharimu fedha nyingi za kigeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua fursa ya kuwa na malighafi pamoja na soko la bidhaa zitokanazo na mazao hayo. Katika uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda, tuna mkakati wa uhamasishaji wa kilimo na ujenzi wa viwanda vinavyosindika alizeti ili kupata mafuta ya kula. Mkakati wa pamba mpaka mavazi utekelezaji wake utatuwezesha kupata mafuta ya kula yatokanayo na mbegu za pamba. Pia kupitia Shirika la NDC, mradi wa mfano unaandaliwa Mkoani Pwani ambako shamba la mchikichi litaanzishwa tukilenga kuzalisha tani 60,000 za mafuta ghafi ya mawese kila mwaka. Ni maoni yetu kuwa sekta binafsi itaazima uzoefu wa Mkoa wa Pwani na kuanzisha mashamba kama hayo katika mikoa ya Mbeya, Kigoma na Kagera kwa kutaja tu baadhi ya maeneo yanayostawisha michikichi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kuomba Mikoa, Wilaya na Mamlaka ya Serikali za Mitaa zinapohamasisha suala la ujenzi wa viwanda sekta ya mafuta ya kula pia ipewe kipaumbele. Vilevile wananchi wahimizwe kuongeza uzalishaji wa malighafi kama alizeti, mawese na pamba kadri zinavyopatikana kwenye maeneo yao.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-
(a) Je, ni lini Serikali itajenga viwanda kwa ajili ya malighafi ya karafuu?
(b) Je, Serikali haioni kuwa kwa kujenga viwanda hivyo hapa nchini itapunguza kusafirisha karafuu nje ya nchi kinyume na utaratibu?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum, kwama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la karafuu huzalishwa kwa wingi Zanzibar kwa wastani wa tani 5,500 kwa mwaka na Tanzania Bara kwa Mikoa ya Morogoro na Tanga kwa wastani wa tani 364.4 kwa mwaka. Sehemu kubwa ya zao hili huuzwa nje ya nchi hasa nchini India, Singapore, Indonesia, Umoja wa Nchi za Kiarabu na Ulaya. Kwa sasa kuna kiwanda kimoja cha kuzalisha mafuta ya makonyo kwa kutumia malighafi zitokanazo na karafuu ambacho kipo Kisiwani Pemba. Kwa mwaka 2016/2017 kiwanda hicho kiliweza kuzalisha mafuta ya makonyo jumla ya tani 974.714 yenye thamani ya shilingi milioni 974.714 yaliyouzwa ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa viwanda ni jukumu la sekta binafsi Serikali inabaki na jukumu la uhamasishaji na kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji. Kutokana na fursa iliyopo kwenye zao la karafuu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda tutaongeza jitihada ya kuhamasisha sekta binafsi kujenga viwanda vya kuongeza thamani zao la karafuu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nikubaliane na Mheshimiwa Angelina Malembeka kuwa kwa kujenga viwanda nchini kutapunguza kusafirisha karafuu nje ya nchi kinyume na taratibu. Pia ujenzi wa viwanda nchini utatengeneza ajira kwa wananchi wetu na kuongeza thamani ya karafuu hali itakayowezesha wazalishaji kupata bei nzuri na kutokana na kuwa shuguli hizi zinafanyika kwa utaratibu rasmi tutaongeza wigo wa walipa kodi.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA aliuliza:-
Miradi ya Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na Chuma Liganga imekuwa ikizungumzwa na Serikali kwa Awamu hii ya Tano na imewekwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016-2021).
(a) Je, ni lini miradi hii itaanza?
(b) Je, ni lini Serikali italipa fidia kwa wananchi wa Mundindi na Mkomang’ombe waliotoa maeneo yao kupisha miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Deogratias Francis Ngalawa, Mbunge wa Ludewa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa miradi unganishi ya Mchuchuma na Liganga inazungumziwa sana na Serikali na imeainishwa katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano kama moja ya miradi ya kipaumbele. Kutokana na umuhimu wa miradi katika uchumi wa Taifa, Serikali imejipanga kuhakikisha miradi hii inaanza kwa kufuata utaratibu sahihi na kwa kuzingatia manufaa mapana ya Taifa wakiwemo wananchi wa Mkoa wa Njombe, hususan Wilaya ya Ludewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, utakumbuka kuwa mwezi Mei, 2017 wakati nikijibu swali la Mheshimiwa Ngalawa kuhusu miradi hii, nililieleza Bunge lako Tukufu kuwa Kamati ya Wataalam ilikuwa imekamilisha kupitia vivutio alivyoomba mwekezaji ili viwasilishwe Serikalini kwa lengo la kuhakikisha Taifa linapata faida zaidi.
Hata hivyo, mwezi Julai, 2017 Bunge lako Tukufu lilifanya marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 pamoja na kutunga sheria mbili mpya za The Natural Wealth and Resources Permanent Sovereignty Act, 2017 na The Natural Wealth and Resources Contract (Review & Re-Negotiation of Unconscionable Terms) Act, 2017. Maelekezo ya sheria rejewa hapo juu yanakinzana na baadhi ya vifungu vya mikataba ya ubia (joint venture agreement) na mgawanyo wa hisa (Shareholding Subscription Agreement-SSA) iliyokuwa imeingiwa kati ya mwekezaji na NDC mwaka 2011.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na ukinzani wa kisheria uliojitokeza, Serikali imeunda timu ya wataalam ya kufanya majadiliano na mwekezaji ili kutafuta ufumbuzi. Timu hiyo iliyokwishaanza kazi imepewa jukumu la kufanya mapitio ya mikataba yote na vivutio alivyoomba mwekezaji ili kuainisha maeneo yenye ukinzani na kujadiliana na wabia wenza ili kuepuka kutekeleza miradi kinyume na maelekezo ya sheria za nchi. Ni imani yangu kuwa baada ya makubaliano ya mwekezaji mwenza kwenye maeneo kinzani, Serikali itatoa baraka za mwisho na mradi utaanza mara moja ikiwemo kulipa fidia kwa wananchi.
MHE. ASHA ABDULLAH JUMA aliuliza:-
Baadhi ya majengo na mabweni katika campus ya Chuo Kikuu Mzumbe, Morogoro yana uchakavu mkubwa sana ikiwemo miundombinu ya maji vyooni.
Je, kuna utaratibu gani wa kuyafanyia ukarabati majengo haya na hasa kuwapunguzia shida wasichana wanaohitaji matumizi zaidi ya maji kuliko wengine?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Asha Abdullah Juma, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu swali namba 22 tarehe 1 Februari, 2017 Serikali imeshaanza ukarabati wa Miundombinu na majengo katika campus kuu ya Chuo Kikuu Mzumbe kwa gharama ya shilingi bilioni mbili. Hadi kufikia terehe 31 Mei, 2017 jumla ya shilingi milioni 884,634,366 zilizotengwa zilikwishatolewa na Wizara yangu inaendelea kufuatilia fedha zilizobaki ili zitolewe kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa juhudi hizi za ukarabati unaoendelea kutekelezwa chuoni hapo ni dhahiri kwamba Serikali ina nia ya dhati ya kuinua hadhi ya chuo hiki na hivyo kuweka mazingira stahiki ya kufundishia na kujifunzia pamoja na kuwapunguzia shida wasichana wanaohitaji matumizi zaidi ya maji.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanzisha Chuo Kikuu katika Mkoa wa Tabora hasa ikizingatiwa kuwa Mkoa huo hauna Chuo Kikuu hata kimoja cha Serikali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kuna marekebisho madogo sana nadhani atakuwa aliyapata Mheshimwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Munde Abdallah Tambwe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kutokana na gharama kubwa ya uwekezaji inayohitajika katika kuanzisha vyuo vikuu, ni vigumu kwa sasa Serikali kuanzisha Chuo Kikuu katika Mkoa wa Tabora. Hata hivyo, katika Mkoa wa Tabora kuna Tawi la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambacho ni cha Serikali, pia kuna Chuo Kikuu cha Theophil Kisanji Kituo cha Tabora na Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu Mihayo. Uwepo wa Vyuo hivi na hasa vyuo binafsi ni matokeo ya Serikali kutekeleza sera ya ushirikishwaji wa Sekta binafsi kutoa elimu ya juu nchini
Mheshimiwa Spika, naomba niendelee kutoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza na kushirikiana na Serikali katika kuanzisha Vyuo Vikuu katika program za vipaumbele vya Taifa kama vile Uhandisi, Teknolojia, Afya, Kilimo na Ualimu wa Sayansi na Hisabati na maeneo mengine ambayo yataonekana yanafaa.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA aliuliza:-
Mitihani ya Taifa kidato cha nne na sita hufanyika kwa pamoja kwa wanafunzi wa Tanzania Bara na Visiwani.
• Je, Serikali haioni umuhimu wa kutumia mitaala na vitabu vya aina moja ili kuwapa wanafunzi wa Zanzibar fursa ya kujisomea na kufanya vizuri katika mitihani yao?
• Kwa kuwa mitaala na vitabu vya elimu ya awali na ya msingi kwa upande wa Zanzibar ni tofauti na Tanzania Bara, je, kwa nini Zanzibar wasiruhusiwe kutunga mitihani ya Taifa tofauti na Bara kwa kidato cha nne na sita, na mitihani hiyo ikapata hadhi sawa na ile inayotungwa Tanzania Bara?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Angelina Adam Malembeka, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mitaala na vitabu vinavyotumika kufundishia na kujifunzia kwenye ngazi ya elimu ya sekondari (kidato cha kwanza hadi cha sita) kwa Tanzania Bara na Zanzibar ni vya aina moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mitaala na vitabu vinavyotumika katika ngazi ya elimu ya sekondari kwa upande wa Tanzania Bara na Zanzibar ni vya aina moja, Sheria ya Bunge namba 21 ya mwaka 1973 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 inalipa mamlaka Baraza la Mitihani la Tanzania ya kuendesha mitihani ya Taifa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, kwa kuzingatia kuwa mitaala na vitabu vya elimu ya awali na msingi vinavyotumika kwa upande wa Zanzibar ni tofauti na vinavyotumika Tanzania Bara, mitihani ya elimu ya awali na msingi kwa upande huo huendeshwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Zanzibar.
MHE. EDWARD F. MWALONGO (K.n.y MHE. PROF. NORMAN A. SIGALLA KING) aliuliza:-
Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika Wilaya ya Makete hakina mabweni hivyo kunufaisha kata moja tu wakati watoto wanaotoka Tarafa za Matamba, Ikuwo, Magoma, Bulongwa, Ukwama na Kata za Lupila na Tandala hawawezi kunufaika na Chuo hicho kwa sababu ya umbali uliopo.
Je, ni lini Serikali itakipa chuo kipaumbele cha kujengewa mabweni?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Norman Adamson Sigalla King, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa fedha za maendeleo kiasi cha shilingi 250,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa mabweni mawili katika Chuo cha VETA cha Makete. Mkandarasi Tanzania Building Agency (TBA) anategemewa kuanza ujenzi kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2017 baada ya kukamilisha hatua za kusaini mkataba.
MHE. JULIANA D. SHOZA aliuliza:-
Mkoa wa Songwe ni mpya na unakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa Vyuo Vikuu hata vile vya Ufundi.
Je, ni lini Serikali itakuja na mpango wa kujenga hata kampasi ya Chuo Kikuu kimojawapo pamoja na vile Vyuo vya Ufundi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT) hivi karibuni itaanza kutoa mafunzo katika kampasi yake ya Myunga iliyopo Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe. Vilevile kutokana na gharama kubwa ya uwekezaji inayohitajika katika kuanzisha Vyuo Vikuu pamoja na Vyuo vya Ufundi Stadi, wananchi wanashauriwa kuendelea kutumia Vyuo Vikuu na Vyuo vya Ufundi Stadi vilivyopo nchini.
MHE. ABDALLAH A. MTOLEA (K.n.y MHE. MUHAMMED AMOUR MUHAMMED) aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo la kuvuja kwa mitihani ya Taifa hapa nchini hususani ile ya kidato cha nne (CSEE) hali inayoondoa ufanisi hasa ikizingatiwa matokeo yanayotoka yamejaa udanganyifu. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Muhammed Amour Muhammed, Mbunge wa Bumbwini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweza kudhibiti na kuondoa tatizo la kuvuja kwa mitihani ya kidato cha nne, ambapo kwa mara ya mwisho ilikuwa ni mwaka 2008 katika somo la hisabati pekee. Changamoto inayoendelea kujitokeza ni kwa baadhi ya watahiniwa kujihusisha na udanganyifu wakati mitihani inapofanyika kwa kuingia katika chumba cha mtihani na vitu visivyoruhusiwa kama vile notes na simu ya mkononi kwa ajili ya kufanya mawasiliano ndani ya chumba cha mtihani.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeendelea kujidhatiti na kuikabili changamoto ya udanganyifu katika mitihani kwa kuimarisha usimamizi na kutoa elimu kwa watahiniwa kuhusu madhara ya kufanya udanganyifu. Wizara imekuwa ikitoa adhabu ikiwa ni pamoja na kufutiwa matokeo ya mitihani pale inapothibitika kuwepo kwa udanganyifu huo. Mfano, watahiniwa waliofutiwa matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2011 ni 3,303, mwaka 2012 ni 789,
mwaka 2013 ni 272, mwaka 2014 ni 184, mwaka 2015 ni 87 na
mwaka 2016 ni 126.
MHE. JORAM I. HONGOLI aliuliza:-
Katika Jimbo la Lupembe, Halmashauri ya Njombe, Tarafa ya Lupembe, hususan Kijiji cha Madeke kinazalisha matunda aina ya nanasi, parachichi na matunda mengine, lakini hakuna soko la matunda hayo na hii ni kutokana na kutokuwa na kiwanda kikubwa cha matunda.
• Je, Serikali inasaidiaje upatikanaji wa masoko ya mazao hayo?
• Je, ni lini Serikali italeta kiwanda katika eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joram Ismail Hongoli, Mbunge wa Lupembe, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia taasisi yake ya Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) wakati wa Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yaliyomalizika mwezi Julai, 2017 iliwaunganisha wakulima wa nanasi, parachichi na matunda mengine ambao wana uwezo wa kuzalisha wastani wa tani 6,000 kwa mwaka na kampuni ya Tomoni Farms Limited iliyopo Jijini Dar es Salaam. Mwakilishi wa Kampuni ya Tomoni na mwakilishi wa Kikundi cha Wakulima wa Matunda kutoka Kijiji cha Madeke walitiliana saini ya mkataba usiofungani wa kununua wastani wa tani 3,000 za matunda kwa mwaka zenye thamani ya shilingi bilioni 1.5.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tomoni Farms Limited ni kampuni kubwa inayonunua matunda na mbogamboga kutoka kwa wakulima mbalimbali nchini. Aidha, wakulima hao pia wameunganishwa na wanunuzi wa matunda kutoka nchi za uarabuni kwa ajili ya soko la nje.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa ujenzi wa kiwanda kwa ajili ya kusindika matunda katika eneo hili, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Njombe imeanzisha kiwanda kidogo cha kukausha chips za nanazi. Kiwanda hiki kinamilikiwa na wanakijiji wa Madeke kupitia mradi uliobuniwa na mpango wa maendeleo wa kilimo wa wilaya (District Agriculture Development Plans – DADPS), hata hivyo kiwanda hiki bado hakikidhi mahitaji ya usindikaji wa zao hili na jitihada zimeendelea kufanyika, ili kupata wawekezaji, hususan katika Kijiji cha Madeke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto iliyopo katika kijiji hicho ni kukosekana kwa umeme. Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ilishawaandikia barua TANESCO kuweka katika mipango yao kufikisha umeme katika Kijiji cha Madeke, ili uwekezaji uweze kufanyika na vilevile nimefuatilia hata REA watafikia kijiji hicho.
MHE. DAVID E. SILINDE aliuliza:-
Katika kutekeleza azma ya Tanzania ya viwanda.
Je, Halmashauri ya Momba inatarajiwa lini kujengewa kiwanda na cha aina gani?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa David Ernest Silinde, Mbunge wa Momba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa uchumi wa viwanda umeainishwa katika Mpango wa pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017-2020/2021). Lengo kuu la Mpango huo ni kuiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Katika ujenzi wa uchumi wa viwanda, jukumu la Serikali ni kuweka mazingira wezeshi ikijumuisha sera na mikakati rafiki kwa wawekezaji pamoja na miundombinu wezeshi na miundombinu saidizi wakati shughuli za biashara na ujenzi wa viwanda zikiwa ni jukumu la sekta binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza hili Serikali imeendelea kuhamasisha ujenzi wa uchumi wa viwanda kwa kuelekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa kupitia Mikoa na Wilaya kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda ikiwemo Halmashauri ya Momba ambao wametenga ekari
• kwa ajili ya viwanda. Lengo la mpango huo ni kuwa na maeneo ya kutosha kujenga viwanda sasa na baadaye. Kuelimisha wananchi juu ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, kuvutia wawekezaji na kuboresha mazingira ya kufanya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Halmashauri ya Momba na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) itaongeza juhudi ya kuhamasisha wawekezaji wa ndani na wa nje kujenga viwanda Wilayani Momba kutegemeana na fursa za uwekezaji zilizopo.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-
Katika Jiji la Dar es Salaam kuna Viwanda vingi ambavyo vimebadilishwa matumizi yake na kugeuzwa kuwa maghala ya kuhifadhia vifaa mbalimbali. Je, Serikali ina mpango gani wa kuvirejesha viwanda hivyo kwenye matumizi yake ya awali?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kati ya Mashirika ya Umma 341 yaliyobinafsishwa hadi mwaka 2007 viwanda vilikuwa 156. Madhumuni ya ubinafsishaji wa viwanda yalikuwa ni pamoja na kutoa ajira, kuzalisha bidhaa zinazokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa na kuongeza mchango wa viwanda katika uchumi wa Taifa. Ufufuaji wowote wa viwanda ambao unaleta matokeo hayo ni sahihi kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, katika Jiji la Dar es Salaam, ni kweli kuna baadhi ya viwanda vilivyobadili matumizi ya awali na kuanza shughuli nyingine za kiuchumi. Baadhi yake ni vile vilivyouzwa kwa utaratibu wa ufilisi na mali moja moja na hivyo kutokuwa na mikataba ya mauzo inavyowalazimisha wamiliki kuendeleza shughuli za viwanda za awali.
Mheshimiwa Spika, Viwanda hivyo ni pamoja na TANITA One ambacho kwa sasa kinatumika kama maghala; Tanzania Publishing House Limited Investment ambacho kwa sasa ni duka la vitabu, Tractors Manufacturing Company Limited ambapo kwa sasa kuna jengo la biashara la Quality Centre, Light Source Manufacturing ambapo TATA Holding) pamoja na Tanganyika Packers Ltd ya Kawe (Kawe Meat Plant) ambapo eneo lilinunuliwa na National Housing kwa ajili ya ujenzi wa makazi.
Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuhamasisha na kuwezesha viwanda visivyofanya kazi, vifanye kazi. Mpaka sasa uhamasishaji huu umewezesha viwanda 18 vikiwemo vya Dar es Salaam kama vile kiwanda cha UFI kilichokuwa kinatengeneza zana za kilimo, kilibadilishwa na kuwa Tanzania Steel Pipe Limited na kuanza kutengeza mabomba ya maji na vingine vinaendelea kufanyiwa ukarabati na vingine tayari vinafanya kazi.
Hivyo, chini ya Kamati Maalum yenye wataalam toka sekta mbalimbali, tunafuatilia utendaji wa kiwanda kimoja hadi kingine mpaka vyote viweze kufanya kazi kwa tija.
MHE. LUCIA M. MLOWE aliuliza:-
Ardhi ya Njombe inahitaji mbolea kwa wingi zaidi kuliko mikoa mingine.
Je, Serikali ina mkakati gani wa uanzishaji wa Kiwanda cha Mbolea Mkoani Njombe?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Lucia Michael Mlowe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbolea ya viwandani inatokana na malighafi za madini. Aina za mbolea hizo ni nitrogen inayotengenezwa kwa kutumia ammonium inayokana na gesi asilia, mbolea ya phosphorous na ile ya phosphate. Tanzania ina kiwanda kimoja kikubwa cha mbolea cha Minjingu Mkoani Manyara kinachotengeneza mbolea aina ya phosphate kutokana na malighafi husika kupatikana mkoani humo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na upatikanaji wa soko la mbolea Mkoani Njombe, tafiti za kijiolojia zinaonesha kuwa malighafi za phosphate, phosphorous na gesi asilia hazipatikani mkoani humo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kujenga viwanda vingine vya mbolea, majadiliano na wawekezaji wa kampuni za HELM na FERROSTAAL ya Ujerumani zinaendelea kwa ajili ya ujenzi wa viwanda viwili katika Mikoa ya Mtwara na Lindi kutokana na upatikanaji wa gesi asilia. Hivyo ni vyema Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na mkoa na halmashauri kuhamasisha uwekezaji unaolenga zaidi kujenga viwanda vya kuongeza thamani ya malighafi zinazopatikana kwa wingi katika mkoa huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kufanya hivyo mkoa mmoja utakuwa soko la bidhaa za mkoa mwingine kama itakavyokuwa kwa mbolea kutoka Lindi na Mtwara wakati Mkoa wa Njombe ukitoa mazao ya chakula, matunda na mazao ya mbao. Serikali inaendelea kuvutia wawekezaji katika viwanda vya mbolea ili kutosheleza mahitaji ya nchi nzima.
MHE. SALOME W. MAKAMBA (K.n.y. MHE. MARWA R. CHACHA) aliuliza:-
Kiwanda cha Nguo cha MUTEX cha Musoma Mjini amepewa mwekezaji lakini mpaka sasa hakifanyi kazi vizuri:-
Je, ile ahadi ya Rais kurudisha viwanda visivyofanya kazi ipo katika hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Musoma Textile Mills Limited kilianza uzalishaji mwaka 1980 kikiwa na uwezo uliowekezwa wa mita milioni 22 kwa mwaka. Bidhaa zilizokuwa zinazalishwa kwa kutumia pamba inayolimwa nchini ni kanga na kitenge. Kiwanda hiki kiliwekwa kwenye utaratibu wa kufilisiwa mwaka 1996.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na madeni makubwa ya benki, zoezi la ufilisi lilichukua muda mrefu na kukamilika mwezi Juni, 2006 ambapo kiwanda husika kilibinafsishwa kwa utaratibu wa ufilisi kwa Kampuni ya Lalani Group 2006.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Lalani Group ilifanya ukarabati wa kiwanda na kuanza uzalishaji ambao haukudumu kwa muda mrefu. Mwezi Mei, 2008, Kampuni ya Lalani Group iliuza mali za MUTEX kwa Tanzania Commodities Trading Company ambayo ni Kampuni tanzu ya Kampuni ya Mohamed Enterprise Limited. Mauzo hayo yalifanyika kati ya makampuni hayo mawili katika utaratibu ambao haukuhusisha Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda kilifanyiwa ukarabati na uzalishaji wa kanga na kitenge ukaanza mwaka huohuo wa 2008. Uzalishaji umekuwa siyo wa kuridhisha kutokana na kuwepo kwa ushindani mkubwa katika soko la bidhaa kama hizo zinazozalishwa na zinazotoka nje ya nchi. Ilipofika mwaka 2016, kiwanda cha MUTEX kilisitisha uzalishaji kutokana na ushindani kuwa mkubwa na hivyo kutokufanya vizuri katika soko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua changamoto hiyo, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Kilimo, ziliandaa Mkutano wa Wadau wa Nguo na Mavazi tarehe 20 Aprili, 2018 ili kujadili changamoto zinazoikabili sekta hiyo ambayo ni muhimu sana kwa ajira na uchumi kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, muafaka ulifikiwa kuhusu suala la ushindani usio wa haki katika soko kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania iimarishe udhibiti wa bidhaa za nguo kutoka nje na kutoza kodi stahiki kwa mujibu wa sheria na viwango vilivyowekwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza agizo la Rais, tumekubaliana na mmiliki wa kiwanda cha MUTEX na ameahidi kuwa katika kipindi cha miezi miwili uzalishaji utaanza. Aidha, kiwanda kimeandaa mpango wa kupanua shughuli zake kwa kuwekeza kwenye mitambo ya kuzalisha vitambaa vya aina ya Denim (Integrated Denim Manufacturing Facilities) vinavyotumika kutengeneza mavazi aina ya jeans katika kukabiliana na ushindani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu itaendelea kumfuatilia mwekezaji huyu na kuhakikisha kuwa anazalisha kama alivyoahidi.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:-
Mkoa wa Kagera unazalisha matunda ya aina mbalimbali kama vile ndizi, nanasi, parachichi, embe na kadhalika. Kwa kuwa kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha uchumi wa viwanda nchini.
Je, Serikali inaweza kuweka wazi mikakati madhubuti iliyoandaliwa ya ujenzi wa viwanda vya kusindika matunda katika Wilaya ya Ngara, Karagwe na Bukoba katika kipindi cha kuanzia mwaka 2016/2020?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima ya Mpango wa Pili wa Miaka Mitano ni kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Katika mpango huu imebainishwa wazi kuwa ni jukumu la sekta binafsi kujenga viwanda na Serikali ibaki na jukumu la kuweka mazingira bora ya uwekezaji na ufanyaji biashara. Pia katika mpango huo tunalenga kuanzisha viwanda vinavyotumia malighafi zitokanazo na mazao ya wananchi, viwanda vinavyoajiri watu wengi na viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotumika kwa vingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumueleza Mheshimiwa Oliver Semuguruka, Wabunge wote wa Kagera na Wana Kagera wote kwa ujumla kuwa Serikali inasimamia mikakati ifuatayo katika ujenzi wa viwanda vinavyosindika matunda Mkoani Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni kuimiza Serikali ngazi ya Kijiji, Kata na Wilaya kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, kuhakisha maeneo hayo yanawekewa miundombinu wezeshi na saidizi; tatu, kupitia SIDO kutoa mafunzo ya kusindika malighafi za shamba ikiwemo matunda; nne, kujenga majengo ya viwanda (industrial sheds) ambapo wajawasiamali watapata mafunzo ya kuchaka na kusindika mazao yao ya shamba; na tano kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia uwekezaji Mkoa Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa mwitikio ni mzuri kwani viwanda vinavyosindika matunda vimeanza kujengwa, hii ni pamoja na kiwanda cha Mayawa kilichopo Bukoba Mjini, kiwanda cha kusindika nyanya kilichoko Ibwera kinachomilikiwa na Mheshimiwa Dkt. Samsoni Rweikiza Mbunge wa Bukoba vijijini, kiwanda cha mvinyo wa ndizi cha Salum Said Seif kilichoko Mulemba na kiwanda cha mvinyo cha ndizi kilichopo Karagwe kwa kutaja baadhi.
MHE. LATHIFAH H. CHANDE aliuliza:-
Kiwanda cha Kubangua Korosho cha Mtama (Cashewnut Factory) kilichopo katika Jimbo la Mtama kilikuwa chini ya Bodi ya Korosho na kiliuzwa kinyemela kwa Kampuni ya Lindi Farmers ambayo ilikodishwa kwa kampuni ya Kichina ya Sunshine Industries Limited, kampuni ambayo inawalipa wafanyakazi ujira wa shilingi 70 hadi 80 kwa kubangua kilo moja ya korosho.
(i) Je, Serikali ina taarifa ya kukodishwa kwa kiwanda hiki?
(ii) Je, Serikali inachukua hatua gani juu ya mazingira magumu ya wafanyakazi ambao hawana mikataba ya kazi katika kiwanda hiki ambacho kinamilikiwa na wageni?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lathifah Hassan Chande lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kiwanda cha Kubangua Korosho cha Mtama kilibinafsishwa kwa kuuza hisa asilimia 100 kwa Kampuni ya Lindi Farmers Association ambayo inakimiliki. Kufuatia umiliki huo, kiwanda hicho kilikodishwa kwa makubaliano maalum kwa Kampuni ya Sunshine ili iweze kukiendesha.
Mheshimiwa Spika, Serikali inayo taarifa kwamba Kampuni ya Sunshine Industrial Company Limited inaendesha kiwanda hicho kwa kubangua korosho kwa mkataba wa miaka mitano kuanzia mwaka 2013 hadi 2018 ambapo unahusisha kujenga, kuendesha na kuhamisha. Baada ya mkataba kumalizika mashine na mitambo vitakuwa mali ya Lindi Farmers Association. Uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni moja umefanyika tangu mkataba huo wenye gharama ya dola 100,000 kwa mwaka uliposainiwa.
Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali ni kuona viwanda vinafanya kazi na kuleta manufaa kwa Watanzania ikiwemo kutoa ajira, kulipa kodi na kuongeza thamani ya malighafi. Hata hivyo, msimu wa mwisho mwaka huu kiwanda hicho hakikupata korosho za kutosha kutokana na ushindani wa bei ya korosho ghafi na hivyo kupelekea wanunuzi kugombania korosho.
Mheshimiwa Spika, kuhusu usalama wa wafanyakazi viwandani, Serikali inaendelea kutoa wito kwa waajiri wote kuzingatia sheria za usalama kazini. Aidha, nitumie fursa hii kuzihimiza mamlaka zinazohusika na ukaguzi wa usalama kazini kusimamia kwa karibu sheria hizo. Pamoja na hatua hizo, waajiri wote wanapaswa kujiunga na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (Workers Compensation Fund – WCF) ulioanzishwa hivi karibuni na sheria yake kupitishwa na Bunge lako tukufu. Hii itawawezesha kunufaika pale wanapoumia kazini kutokana na majanga mbalimbali. Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu tutaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa sheria hiyo.
MHE. ALLY K. MOHAMED (K.n.y MHE. JAKU HASHIM AYOUB) aliuliza:-
Pamoja na kuwepo viwanda vingi vya sukari hapa nchini bado kuwekuwa na uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo kususan kwa upande wa kilo 50 ni shilingi 65,000 kwa upande wa Zanzibar ambako kuna kiwanda kimoja tu cha sukari, lakini kwa Tanzania Bara mfuko huo wa kilo 50 ni shilingi 120,000:-
• Je, kuna tatizo gani linalofanya sukari iuzwe kwa bei juu kiasi hicho kwa upande wa Tanzania Bara?
• Je, Serikali itachukua hatua gani ili kuweza kuwapatia wananchi unafuu katika upatikanaji wa bidhaa hiyo?
• Kwa upande wa Zanzibar katika kipindi ambacho matumizi ya sukari kwa wananchi yanaongezeka mfano, mwezi wa Ramadhani Serikali inahusisha ushuru wa kuingiza sukari nchini, je, kwa nini Serikali ya Muungano isizingatie utaratibu huu mzuri ili kuleta unafuu kwa Tanzania Bara?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub, Mbunge wa Zanzibar lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
(i) Mheshimiwa Mwenyekiti, ukaguzi wa maafisa masoko katika masoko ya Dar es salaam na Zanzibar unaonyesha kuwa bei ya sukari kwa gunia la kilo 50 ni shilingi 101,000 hadi 105,000 kwa Dar es salaam na shilingi 71,000 hadi 77,000 kwa uzito huo huo upande wa Zanzibar. Mapitio ya bei hizo na kama Mheshimiwa Mbunge alivyoeleza kwenye swali hili kipengele (c) tofauti ya bei katika eneo la Dar es salaam na Zanzibar kwa kiasi kikubwa inatokana na utozaji wa ushuru na kodi. Inaonekana dhahiri kuwa kiasi cha kodi inachotozwa kwenye gharama ya mfuko wa kilo 50 Zanzibar ni kidogo wakati Dar es Salaam ushuru na kodi ni asilimia 25 na 18 vyote kwa pamoja.
(ii) Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya sukari nchini kwa wastani vinazalisha tani 320,000 kwa mwaka wakati mahitaji ya sukari ya mezani ni tani 455,000. Chini ya utaratibu maalum Serikali huagiza upungufu katika uzalishaji (gap sugar) ili kutosheleza mahitaji ya soko. Katika kipindi hiki cha Februari – Mei ambapo viwanda vyetu vimefungwa kwa ajili ya matengenezo na kupisha msimu wa mvua za masika kiasi cha tani 135,000 kimeagizwa kuziba pengo na sehemu kubwa ya shehena hiyo imeshawasili nchini.
Aidha, chini ya utaratibu wa maalum wa kulinda na kuhamasisha viwanda vya sukari ni viwanda vya sukari nchini vinaruhusiwa kuagiza upungufu wa sukari. Utaratibu wa wenye viwanda unaambatana na masharti ya kupanua mashamba na viwanda vyao ili katika kipindi cha miaka mitatu tuwe na uzalishaji wa kutosha mahitaji ya ndani na kuuza ziada nje.
(iii) Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza katika sehemu (b) ya swali hili zimeagizwa tani 135,000 ili kuhakikisha kuwa tunakidhi mahitaji ya soko. Kulingana na sheria za kodi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, sukari inayoagizwa toka nje ya Jumuiya hutozwa ushuru kwa kiwango cha 100% na 18% ya gharama (CIF) ila kwa kulenga kuwapa nafuu walaji sukari hapo juu inatozwa kwa kiwango cha 25% na 18% ya gharama.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-
Katika kuelekea uchumi wa viwanda Tanzania, Serikali imedhamiria kuwepo kwa viwanda vya kimkakati.
Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha Kiwanda cha Kuchakata ao la Tumbaku kinajengwa katika Mkoa wa Tabora?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamisi Sakaya, Mbunge wa Kaliua kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ina viwanda viwili vya kuchakata Tumbaku vilivyopo Mkoani Morogoro. Viwanda hivyo ni Tanzania Tobacco Processing Company Limited na Alliance One Tobacco Processing Limited. Viwanda hivyo vina uwezo uliosimikwa wa kusindika tani 120,000 za tumbaku kwa mwaka lakini vinatumia wastani wa asilimia 50 tu ya uwezo huo kwa sasa. Uwezo unaotumika ni mdogo kutokana na mahitaji ya tumbaku kuendelea kupungua katika masoko ya nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, usindikaji wa tumbaku una uhusiano wa moja kwa moja na tumbaku inayolimwa ambayo kwa sasa ni wastani wa tani 60,000 kwa mwaka. Uzalishaji umepungua kutoka tani 126,000 mwaka 2010/2011 hadi tani 54,000 mwaka 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya tumbaku yamepungua kutokana na kampeni zinazoendelea duniani za kuzuia kutumia tumbaku na bidhaa zake kutokana na athari za afya na mazingira. Kwa upande mwingine, kampeni hizo zimeathiri uwekezaji katika viwanda vya tumbaku na ajira ikiwemo Mkoani Tabora, takribani wafanyakazi 7,000 wamepunguzwa kazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa zao la tumbaku bado lina mcahngo mkubwa katika uchumi wa Taifa, Serikali inaendelea kuwahamasisha wawekezaji kutafuta teknolojia bora zaidi ya kuwekeza katika Mkoa wa Tabora.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA aliuliza:-
Je, Kiwanda cha Sukari Kagera tangu kimepata mwekezaji mpya baada ya kile cha mwanzo kushindwa kuendelea na uzalishaji kimetoa mchango gani kwa Wilaya ya Misenyi, Mkoa wa Kagera na Taifa kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Diodorus Buberwa Kamala, Mbunge wa Nkenge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu Kiwanda cha Sukari cha Kagera kibinafsishwe, faida na michango mbalimbali imepatikana kama ifuatavyo:-
a) Uzalishaji wa sukari umeongezeka kutoka tani 15,362 mwaka 2004/2005 hadi tani 75,568 mwaka 2017/2018, uzalishaji huu umesaidia kuokoa fedha za kigeni ambazo zingetumika kuagiza bidhaa hii toka nje ya Nchi.
b) Pia kiwanda kina utaratibu wa kuwatumia Wakulima wa nje (outgrowers) katika kulima Miwa inayotumika kuzalisha sukari. Mpaka sasa kuna wakulima 500 wanaolima eneo la ekari 5,019 za miwa. Kwa mwaka 2017/2018 tu wakulima hao waliweza kuzalisha tani 60,000 za miwa ambazo ziliwapatia kipato cha shilingi bilioni tatu.
c) Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwaka 2018 kiwanda kimetoa ajira 6000 ikilinganishwa na ajira 124 zilizokuwepo mwaka 2006. Aidha, kiwanda kimejenga Hospitali yenye vitanda 78 vyenye uwezo wa kufanya operation kwa kutumia Madaktari Bingwa. Hospitali hiyo sasa ndiyo ya Rufaa kwa zahanati 11 katika eneo hilo.
d) Katika juhudi za kuchangia elimu, kiwanda kimechangia vifaa vya ujenzi, ujenzi wa madarasa, kuchimba visima vya maji, kujenga vyoo, kujenga nyumba za walimu, kuchangia madawati, kujenga maabara na kuchangia vifaa vya kufundishia kwa shule 23 katika Wilaya ya Misenyi.
e) Aidha, katika juhudi za kuhifadhi mazingira, jumla ya miti 20,000 imepandwa katika eneo la kiwanda, pia kiwanda kimejenga mtandao wa barabara zenye urefu wa kilometa 1,250 kwa kiwango cha changarawe ambazo pamoja na kutumika kwa shughuli za kiwanda hutumiwa pia na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka mitatu iliyopita kuanzia 2015/2016, 2016/2017 mpaka 2017/2018 Kiwanda cha Kagera Sugar kimelipa jumla ya shilingi 44,461,815,798 kama kodi Serikalini.
MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA (K.n.y MHE. FREDY A. MWAKIBETE) aliuliza:-
Tanzania imebarikiwa kuwa na madini mbalimbali na Jimbo la Busokelo pia limebarikiwa kuwa na madini hayo.
Je, ni lini Serikali itapeleka wawekezaji wa kiwanda cha marumaru katika Kata ya Lufilyo kwenye Mto Makalya?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji napenda kujibu swali la Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete Mbunge wa Busokelo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Atupele kwa jinsi ambavyo amekuwa akishirikiana na Serikali kufuatilia ili kuona madini ya eneo tajwa yanapata mwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano ambao moja ya sekta ya kipaumbele ni sekta zinazotumia malighafi zinazopatikana nchini ikiwa ni pamoja uonezaji wa thamani madini ikiwemo madini aina ya granite. Katika Jimbo la Busokelo Kata ya Lufilyo, Kijiji cha Kikuba eneo la Mto Makalya kuna mashapo ya madini aina ya granite ambayo ni malighafi ya kutengeneza marumaru zenye ubora wa kimataifa. Kampuni ya Marmo Granite Ltd. ya Jijini Mbeya ilikuwa ikichimba mawe ya granite kutoka eneo hilo na kutengeneza marumaru na baadae ilisitisha shughuli hizo kwa madai kubwa barabara ya kwenda kwenye machimbo ni mbovu hivyo kutowawezesha kupata faida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kushirikiana na Wizara ya Madini inaendelea kuhamasisha upatikanaji wa mwekezaji mwingine katika mradi huo. Nimuombe pia Mheshimiwa Fredy Atupele Mwakibete aendelee kutupa ushirikiano mpaka hapo mwekezaji mwingine atakapopatikana. Vilevile Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI itawasiliana na TARURA ili barabara hiyo iweze kurekebishwa.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuandaa rasilimali watu ili kufanikisha azma nzuri ya uchumi wa viwanda kwa nchi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kutoa fursa sawa ya elimu kwa wote Serikali mpaka sasa inatumia takribani shilingi bilioni 23.85 kwa mwezi sawa na shilingi trilioni 1.14 kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2018/2019 kwa ajili ya kuwaandaa vijana kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne yaani elimu bure. Pia kutoa ruzuku pamoja na mikopo ya takribani trilioni 1.81 kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2018/2019 kwa wanafunzi wa taasisi ya elimu ya juu ili kuwandaa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kwa Sekta za Vipaumbele kwa Vijana ambapo kwa sehemu kubwa mafunzo hutolewa kwa vitendo mahali pa kazi. Programu hii hutekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau wa utatu yaani Serikali, vyama vya waajiri na sekta binafsi na vyama vya wafanyakazi. Utekelezaji wa programu hiyo ulianza mwaka wa fedha 2015/2016 kwa kutumia mifumo ifuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mifumo kwa vitendo mahali pa kazi kwa njia ya mafunzo ya kukuza ujuzi kupitia wanangezi (apprenticeship), kurasimisha ujuzi uliopatikana nje ya mfumo usio rasmi wa mafunzo (recognition of prior learning skills), mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi kwa wahitimu (internship) na mafunzo ya kukuza ujuzi kwa walio makazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Zanzibar pia kupitia Kituo cha Kulelea Wajasiriamali (Entrepreneurship Incubation Centre) kilichopo chini ya Wizara ya Kazi baadhi ya vijana, makundi ya walemavu na watu wenye uhitaji maalum, hupatiwa mafunzo ya ujasiriamali, ambapo Taasisi ya COSTECH iliwawezesha jumla ya shilingi milioni 206 ili kuanzisha kituo hicho na mpaka sasa jumla kimewanufaisha wajasiriamali 875 wengi wao wakiwa ni vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutoa mafunzo ya ujuzi mbalimbali kulingana na mahitaji ukiwepo ujuzi wa uzalishaji viwandani kuhakikisha nchi yetu inajitosheleza hatua kwa hatua katika eneo hili. Napenda kutoa wito kwa vijana kujitokeza na kushiriki katika fursa hizo za mafunzo.
MHE. ALLAN J. KIULA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga soko la kimataifa katika Kata ya Mwangenza kwa ajili ya kuweka katika madaraja vitunguu vinavyolimwa maeneo hayo ili kuvisafirisha katika masoko ya ndani na nje ya nchi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Allan Joseph Kiula, Mbunge wa Iramba Mashariki kama ifuatavyo:-
Mheshimniwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wakulima wa zao la vitunguu katika Wilaya ya Mkalama na Iramba wanakabiliwa na ukosefu wa miundoimbinu rafiki ya soko. Katika hatua ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto hii, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama imetenga eneo la ukubwa wa mita za mraba 19,600 kwa ajili ya kujenga soko maalum la vitunguu. Eneo hilo lipo katika Kijiji cha Dominic na linamilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mpango wa bajeti wa mwaka 2017/2018 kupitia fedha za ruzuku ya maendeleo (Capital Development Grants), Halmashauri ilipewa jumla ya shilingi milioni 40 ambazo zimetumika kuanza ujenzi awamu ya kwanza kwa kujenga uzio wa soko, vyoo kwa ajili ya wafanyabiashara na sehemu maalum ya kuanikia vitunguu yaani vichanja kwenye soko hilo. Kwa sasa eneo hilo linaendelea kutumika kama soko la vitunguu na Halmashauri hiyo imenunua mzani mmoja kwa ajili ya kupima uzito wa bidhaa hizo hivyo kusaidia wakulima kuachana na vipimo vya lumbesa ambavyo vimekuwa vikiwakandamiza kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukidhi matakwa ya masoko makubwa na maalum ya ndani na nje ya nchi, Wizara yetu kupitia wakala wa vipimo imeshauri Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI wanapoanza ujenzi wa soko awamu ya pili uhusishe sehemu ya vifaa vya kuweka madaraja na kufungasha vitunguu kwa viwango vya kimataifa.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-
Kumekuwepo na mkanganyiko wa elimu ya msingi nchini ambapo kuna sera inasema Elimu ya Msingi ni kuanzia darasa la kwanza mpaka darasa la saba na nyingine inasema elimu ya msingi ya Mtanzania ni kuanzia darasa la kwanza mpaka la kumi na mbili. Je, Serikali inasema nini juu ya suala hilo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa elimu Tanzania ni utaratibu uliowekwa ili kufikia malengo na dira ya elimu katika maeneo husika. Mfumo unajumuisha elimu ya awali ambayo ni miaka miwili, elimu ya msingi miaka saba, elimu ya sekondari miaka minne na elimu ya juu miaka miwili na miaka mitatu au zaidi elimu pia ya ya juu. Aidha, kwa sasa mfumo wa elimu wa Tanzania unasimamiwa kwa Sheria Na. 25 ya mwaka 1978 Sura Namba 353. Sheria hii inabainisha wazi kuwa elimu ya msingi ni kuanzia darasa la awali hadi darasa la saba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kusisitiza kuwa kwa sasa Serikali inaendelea kutekeleza na kusimamia elimu kwa kutumia sheria hiyo ambapo elimu ya msingi ni kuanzia darasa la awali hadi darasa la saba.
MHE. USSI SALUM PONDEZA aliuliza:-
a) Je, katika kipindi cha mwaka 2016/2017, ni vijana/ wanafunzi wangapi walikosa vigezo vya kupata mkopo wa elimu ya juu?
b) Je, Serikali inatumia utaratibu gani kuwatambua wanafunzi wanaotoka katika familia maskini katika utaratibu wa utoaji wa mikopo ya elimu ya juu?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI (K.n.y. WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA
TEKNOLOJIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ussi Salum Pondeza, Mbunge wa Chumbuni lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa masomo 2017/2018, jumla ya wanafunzi 46,131 waliomba mikopo. Maombi ya mkopo ya wanafunzi hawa yalichambuliwa ili kupima uhitaji wao kwa kuzingatia Sheria ya Bodi ya Mikopo Sura ya 178 na mwongozo wa utaoji wa mikopo kwa mwaka 2017/2018.
Baada ya uchambuzi wa maombi hayo kukamilika, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo iliwapangia mikopo wanafunzi 33,920 wa mwaka wa kwanza ambao maombi yao yalikidhi vigezo na sifa zilizoainishwa katika sheria na mwongozo uliotolewa 2017/2018. Waombaji wengine 12,211 hawakupangiwa mkopo kwa sababu hawakukidhi vigezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu na sifa za utoaji mikopo ya elimu ya juu unaongozwa na sheria iliyoanzishwa na Bodi nya Mikopo ya Elimu ya Juu, Sura namba 178. Kwa mujibu wa sheria hii mikopo ya elimu ya juu inapaswa kutolewa kwa Watanzania wahitaji na wenye sifa yaani need and eligible.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu namba 17 cha sheria ya Bodi ya Mikopo kimetaja sifa kuu kuwa ni Utanzania, aliyedahiliwa katika Taasisi ya Elimu ya Juu inayotambulika na Serikali, asiwe na vyanzo vingine vinavyogharamia masomo yake na kwa wanafunzi wanaoendelea na masomo wawe wamefaulu mitihani yao kuwawezesha kuendelea na mwaka unaofuata
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, sheria inaipa mamlaka Serikali kupitia Bodi ya Mikopo kuandaa utaratibu na mwongozo wa utoaji mikopo kwa wahitaji wenye sifa. Katika mwaka wa masomo 2017/2018, Serikali kupitia Bodi ya Mikopo iliandaa mwongozo unaopatikana katika tovuti ya Bodi ya Mikopo (www.heslb.go.tz).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwongozo pia ulitoa kipaumbele kwa makundi maalum kama yatima, wenye ulemavu, au wenye wazazi wenye ulemavu na wale ambao masomo yao ya sekondari ya stashahada yalifadhiliwa na wafadhili mbalimbali.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Vijana na Akinamama wengi kwa sasa wamewekeza katika kilimo cha mboga mboga, lakini wanakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa masoko ya uhakika kwa bidhaa zao:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia wakulima hao kupata soko la uhakika la bidhaa zao?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha matunda na mboga kinakadiriwa kuajiri wananchi milioni 2.4 wengi wao wakiwa akinamama. Kutokana na umuhimu huu, Serikali imekuwa ikiweka kipaumbele katika kutambua fursa za masoko ya matunda na mbogamboga ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na Tanzania Horticulture Association imewapatia wakulima wa matunda na mbogamboga kutoka Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Morogoro, Iringa, Njombe, Mbeya na Zanzibar mafunzo ya kilimo bora cha matunda na mbogamboga ili kukidhi matakwa ya masoko ya ndani na nje ya nchi. Mafunzo haya yatafanyika pia katika mikoa iliyobaki ili kuwasaidia wakulima wananchi nzima kupata soko la ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutafuta ufumbuzi zaidi wa soko, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Uswiss inatekeleza mradi wa kukuza soko la mboga na matunda kwa kukusanya na kusambaza kwa wadau taarifa za masoko hususani uzalishaji, bei, mahali lilipo, zao na mnunuzi anayehitaji. Mradi huu umewezesha taarifa hizo kukusanywa na kusambazwa kwa wadau kwa kutumia simu za viganjani. Lengo kuu lilikuwa kuwaunganisha wakulima na soko maalum na hoteli za kitalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi hizi, wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama Wizara ya Kilimo na Taasisi nyingine za Umma, inahamasisha sekta binafsi kuwekeza katika viwanda vya kusindika matunda. Uwekezaji huo umelenga katika uendelezaji wa viwanda vidogo, vya kati na vikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafanikio yaliyopatikana kutokana na uhamasishaji huo ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha Bakhresa Food Products kilichopo Vikindu, Wilayani Mkuranga, Mkoani Pwani; Sayona Fruits Limited kilichopo Mboga, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoani Pwani; Dabaga kilichopo Iringa; Sayona Fruits Limited kilichopo Mwanza; Elven Agri Company Limited kilichopo Bagamoyo Mkoani Pwani; na Iringa Vegetables Oil and Related Industry Limited (IVORY). Kwa hiyo, ni matumaini yetu kuwa viwanda hivi na vingine vinavyofuatia vitakuwa soko la uhakika la mazao ya wakulima hali itakayochochea ari ya kuzalisha zaidi. (Makofi)
MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani juu ya wawekezaji walioshindwa kuendeleza Viwanda vya Kukamua Mafuta vya Ilulu na Kiwanda cha Mamlaka ya Korosho Wilayani Nachingwea?
NAIBU WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kulitaarifu Bunge lako tukufu kwamba Serikali inafuatilia kwa karibu ili kuhakikisha kuwa waliobinafsishiwa viwanda wanatimiza wajibu wao ipasavyo na kwamba viwanda hivyo vinafanya kazi kama ilivyokusudiwa kwa mujibu wa mkataba wao na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kiwanda cha Mafuta Ilulu, kiwanda hicho kiliuzwa kwa njia ya ufilisi. Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina imekuwa ikimfuatilia mwekezaji ili kiwanda kilichonunuliwa kichangie katika uchumi wa Taifa letu. Kutokana na ufuatiliaji huo, tarehe 6 Juni, 2018, mmiliki wa Kiwanda cha Mafuta cha Ilulu, alitoa taarifa rasmi kurejesha kiwanda hicho cha Serikalini kwa kuwa ameshindwa kukiendeleza. Taratibu za kisheria zinafuatwa ili kukamilisha makabidhiano hayo rasmi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Msajili itaendelea kuona matumizi bora zaidi ya kiwanda au eneo hilo. Aidha, kwa upande wa Kiwanda cha Korosho Nachingwea, kilibinafsishwa kwa kuuza hisa asilimia 100. Hivyo, uendeshaji wote wa kiwanda upo chini ya mwekezaji binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda kinaendelea na zoezi la kufunga mitambo ya kubangua korosho na sehemu ya maghala inatumika kuuzia na kuhifadhia korosho za wakulima na wanunuzi. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa kiwanda hicho kinakamilisha ufungaji mitambo na kuanza uzalishaji haraka ifikapo msimu ujao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nilikuwa nimeahidi hapo awali, narudia kusema tena mara baada ya Bunge hili nitatembelea viwanda vyote vilivyobinafsishwa Mkoani Lindi na Mtwara pamoja na maeneo mengine kwa ajili ya ufuatiliaji na tathmini ya viwanda hivyo.