Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Eng. Stella Martin Manyanya (107 total)

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri sana yameniridhisha sana, lakini pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza. Serikali mwaka juzi ilitangaza kwamba itaweka vyuo vya VETA kwenye Wilaya zote nchi, lakini itaanza na Wilaya 10 ambapo Wilaya ya Chunya ni mojawapo naishukuru sana Serikali kwa kuiweka Chunya katika moja ya Wilaya 10 za kuweka Vyuo vya VETA.
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri sana tena Wilaya ya Chunya inagawanyika kuwa Wilaya mbili, Wilaya ya Chunya na Wilaya ya Mkwajuni Wilaya ya Songwe ambako sasa ndiyo kuna heka kumi zimetengwa za kujenga Chuo cha VETA. Sasa swali, kama Serikali ilisema inaipa Chunya Chuo cha VETA, Chunya imegawanyika ziko Wilaya mbili siyo bora tu zote Wilaya zote mbili Chunya na Songwe zipate Chuo cha VETA? Hilo la kwanza na naona Mheshimiwa Mulugo ambaye ni wa Wilaya ya Songwe amefurahi sana. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, la pili, pale kwenye kambi ya ujenzi wa barabara ya Mbeya - Chunya kwa kiwango cha lami Serikali imesema majengo yale ni ya muda siyo ya kudumu. Je, kwa kuwa, eneo lililotengwa ni heka 25 haiwezi ikaanzia kwa majengo hayo ambayo siyo ya kudumu lakini ikajenga Chuo cha VETA kwa eneo kubwa ambalo limebaki?
NAIBU WAZIRI ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimwa Spika, ahsante sana. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mwambalaswa Mbunge wa Lupa kwa jinsi ambavyo amelifuatilia sana jambo hili. Pia niseme tu kwamba, kwa mujibu wa sera tuliyojipangia na mpango tuliojipangia Wizara yetu imedhamiria kuanza kujenga Vyuo vya VETA katika Wilaya zote ambazo hazina kabisa Chuo chochote cha Ufundi au VETA kwa ujumla. Kwa hali hiyo, kwa sababu ya bajeti ambayo kimsingi inahitajika katika maeneo mengi siyo rahisi kuvijenga vyuo vyote kwa siku moja.
Mheshimiwa Spika, nikuombe Mheshimiwa Mbunge kushirikiana Halmashauri yako hilo eneo ambalo umeliangalia ni vema likatengwa na likapimwa na hati zake zikawasilishwa katika Wizara yetu ili liwe katika mpango.
Mheshimiwa Spika, pia nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote, Wizara yangu inapata tatizo kubwa sana inapofikia kuanza mipango ya maandalizi ya ujenzi wa vyuo hivyo kutokana na ardhi hizo kutokupatikana na kupimwa, ni vema Halmashauri zote ambazo ziko katika mpango huu zihakikishe zinatenga maeneo hayo ili isiwe ni kikwazo tunapofikia kufanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, pili, nadhani nimejibu yote kwa pamoja kama ambavyo nimeelekeza kwamba ukishapima tutafanya hivyo kwa kuwa sasa Wilaya ya Songwe inajitegemea, lakini itakuwa ni baada ya kumaliza zile ambazo tumeanza nazo. Ahsante sana.
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Baada ya majibu hayo, nitakuwa na swali moja tu la nyongeza

Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na malalamiko makubwa sana hasa kwa baadhi ya wanafunzi wenye familia masikini na wenye sifa za kupata mkopo huo, lakini wameshindwa kupata mikopo hiyo na kuendelea na masomo yao jambo ambalo linawadhoofisha wanafunzi wenyewe, lakini pia, linadhoofisha familia zao na Taifa kwa ujumla. Mheshimiwa Naibu Waziri anawaeleza nini wananchi kuhusiana na madai haya?
NAIBU WAZIRI ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ni kweli kabisa mikopo inayotolewa kwa sasa haiwezishi kuwapa wanafunzi wote wakiwemo watoto wa masikini. Hiyo ni kutokana na uhalisia kwamba nchi yetu inayo mahitaji mengi katika sekta mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, nachukue nafasi hii pia kumshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutambua tatizo hilo. Katika mwaka huu wa fedha tulikuwa na bajeti ya shilingi bilioni 306 tu, lakini baada ya kuingia kwake madarakani ameweza kuongeza shilingi 132, 299,067,500/= ambazo zimewezesha sasa kuwapa mikopo wanafunzi ambao walikuwa wanaendelea na wale ambao wanaanza mwaka wa kwanza. Mpaka sasa, jumla ya wanafunzi takribani 121,000 watafaidika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge kwa kutumia nafasi yetu hii ambayo sisi ndio tunaopitisha bajeti, nawaomba wakati wa bajeti ukifika tulipe kipaumbele eneo hili. Ahsante sana.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini ningependa kuuliza swali la nyongeza lenye sehemu (a) na (b).

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa tufahamu wazi kwamba Serikali sasa hivi imeamua kutoa elimu ya bure, lakini hata hivyo haikujipanga nayo. Naweza nikatoa ushahidi katika hili kwa sababu katika Jimbo la Ndanda kuna shule inaitwa Liloya, wamepelekewa pale shilingi 86,000/=. Hii ni shule yenye idadi ya wanafunzi 600, na hiyo ni sawasawa na shilingi 146/= kwa kila mwanafunzi kwa mwezi mmoja. (Makofi)

Je, Serikali haikuona kwamba jambo hili ingeliacha kwanza mpaka pale itakapokaa Bunge la Bajeti na kupitisha bajeti ambayo itakidhi mahitaji ya wakati badala ya kukurupuka kufanya jambo ambalo haijajipanganalo? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili la msingi niliuliza kwamba lini Serikali itakuwa tayari kupeleka ruzuku katika Chuo cha Ufundi Ndanda ili kiweze kudahili wanafunzi wengi zaidi kwa sababu kile ni Chuo kilicho bora kuliko vyuo vyote vya Serikali vinavyotoa elimu ya ufundi vilivyopo katika Mkoa wa Mtwara na Lindi? Naomba kuwasilisha maswali yangu.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, naomba nijibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali haijakurupuka. Haijakurupuka kwa sababu Serikali hii ndiyo inayoishi na wananchi na kufahamu matatizo yao. Ndiyo inayofahamu hali halisi ya mazingira tuliyonayo na ndiyo maana ikajiwekea mpango kupitia Ilani yake ya Uchaguzi wa CCM kwamba itatoa elimu bure kuanzia Chekechea mpaka kidato cha nne. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo basi, kama ambavyo tumejionea katika mipango mingine tuliyokuwa tumeianza, ikiwemo na Mipango ya MMEM, Mipango ya MMES na mipango katika sekta nyingine, kila wakati tumekuwa tukianza na tunaboresha kadiri tunavyoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo, kama ambavyo nimesema, kimsingi tunafahamu hata baadhi ya shule, tulipowaambia walete idadi ya wanafunzi pamoja na mahitaji kulingana na uhalisia, kuna wengine walileta sawa, kuna wengine hawakuleta vizuri. Pamoja na hayo, tumeshadhamiria kuona ni namna gani tunaendelea kufanya uchambuzi na kuboresha kadiri itakavyowezekana.

Hivyo tunasema kwamba katika majukumu yale yanayoihusu Serikali kwa sababu elimu inaendeshwa kwa ubia baina ya Serikali na wananchi; wazazi kwa ujumla, kwa hali hiyo, katika yale majukumu yote ambayo tumejipangia, tutahakikisha Serikali inatimiza wajibu wake. Huo ndiyo msimamo wa Serikali yangu. Katika swali la pili…
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Najibu swali la nyongeza la pili. Katika swali la nyongeza la pili la Mheshimiwa Cecil, kimsingi swali la mwanzo ulikuwa unahitaji ujenzi wa Chuo na sasa hivi umezungumzia juu ya utoaji wa ruzuku.

Kwa sasa hivi bado hatujafikiria kutoa ruzuku katika Chuo hicho ambacho kipo Ndanda. Hata hivyo, ni suala la kuangalia, kama kuna uwezekano na itaonekana lina faida kufanya hivyo, basi tutazidi kushauriana na kuona suala hilo linaweza likafanyika.

MHE. PHILLIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Kwanza na-declare interest, mimi ni mmiliki wa shule.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyoongea, kuna vikao kadhaa vinaendelea kati ya Wamiliki, Mameneja na Serikali, Ofisi ya Kamishna Wizara ya Elimu, lakini mpaka sasa hatujafikia muafaka kwa sababu ya hiki ambacho amekiongea Mheshimiwa Naibu Waziri. Tunaonekana kama vile tunafanya mchezo, lakini jambo hili ni gumu sana. Shule zimetofautiana, wapo wamiliki wamewekeza na wamekopa fedha benki. Zipo shule zina utofauti wa vijijini na mjini. Menu ya chakula huwezi kulinganisha menu ya chakula shule za Dar es Salaam na shule za Rukwa, Mbeya ama Mwanza. Hata hivyo, mpaka wiki iliyopita, tumekutana na Serikali kwamba hata hawajafanya utafiti kwenye shule za msingi lakini ada elekezi inataka kutolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niulize swali, ni lini Serikali itaita tena kikao cha mwisho TAMONGSCO pamoja na Serikali wakae pamoja waweze kufanya utafiti wa pamoja? Serikali ifanye utafiti na shule binafsi zifanye utafiti ili wakae pamoja waweze kufanya negotiation ili ada elekezi itolewe si kwa upande mmoja tu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama ambavyo ameeleza Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeshawahi kukaa na wadau hao, lakini niseme tu kwamba ni msingi huo huo ambao Serikali haitaki kuwanyanyasa wawekezaji wake ambao ni Washirika wakubwa wa elimu na ndiyo maana tumefanya tafiti katika maeneo mbalimbali. Mfano, tumeshakwenda katika maeneo hata ya vijijini, kuna shule za Sekondari kama Fingwa kule Rukwa, Idigima-Mbozi na Kitunda kule Kalambo, hizo zinatoza laki moja kule vijijini kabisa kwa Sekondari lakini ukienda kwenye shule nyingine, kama Feza yenyewe inatoza shilingi milioni 9.4, ukichukua St. Joseph shilingi milioni 5.9, ukichukua Mwanza Alliance shilingi milioni 4.8 na ndiyo maana tunafanya utafiti ili kuona kwamba bei zitakazotolewa kwanza zitapangwa kutegemeana na madaraja na shule mahali ilipo na uhalisia wa utoaji wa hiyo elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo siyo lengo la Serikali kuwatesa au kuwanyanyasa wawekezaji, bali ni kutoa bei inayofanana na uhalisia na hiyo itachochea utoaji wa elimu bora, lakini vilevile uwekezaji ulio sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kikao napenda niwafahamishe Waheshimiwa Wabunge, si kwamba Wamiliki tu wa shule ndiyo wanaostahili kukaa vikao, vikao hivi vitawashirikisha hata walezi pamoja na wazazi, pamoja na wananchi wengine ikiwemo Wabunge ili tupate bei zenye uhalisia.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu suala la elimu na TAMISEMI tunaguswa sana na bahati nzuri Naibu Waziri wa Elimu ametoa maelezo ya kutosha, kulikuwa na suala lini litafanyika hili, maana yake hili ndiyo suala la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba Naibu Waziri ameshazungumza kwamba, hicho kikao kitaitwa na hili naomba nikiri wazi, kwa sababu nchi yetu ni pana sana, lengo kubwa la Serikali ni kui-support private sector, lakini pia kuangalia na watu hao wanaopata huduma hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni kwamba, mchakato huu ni mpana kwa kushirikiana na wadau wote, imani yangu ni kwamba, tutakapofika mwisho wa siku hasa wamiliki wa shule na ndugu yangu Mulugo akiwa mmojawapo, tutafika maeneo ambayo Mtanzania wa kawaida wa kila level ataweza kuguswa kwa maslahi mapana ya nchi yetu.
MHE. JASSON S. RWEIKIZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pia nishukuru kwa majibu ya Serikali, lakini nina maswali wawili ya nyongeza.
La kwanza, nasikitika kwamba swali langu halijajibiwa, suala la Chuo cha VETA Kagera limezungumziwa muda mrefu sana humu ndani na nje ya humu ndani. Mkoa wa Kagera mzima hauna Chuo cha VETA cha hadhi ya Mkoa. Kwa hiyo, vijana wote wanaomaliza kidato cha nne au darasa la saba hawana fursa ya kupata mafunzo ya ufundi kuweza kujisitiri kwenye maisha yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, waliaminishwa kwamba chuo hiki kingejengwa mwaka jana, tukatoa ardhi na mipango mingine ikaendelea na Waziri amefika pale mara mbili, tatu, ameangalia na kusema kwamba ujenzi unaanza, lakini hadi leo kwenye majibu tuliyopewa hapa hakuna matumaini hata kidogo chuo hiki kuanza kujengwa wakati wowote. Kwa hiyo swali langu halijajibiwa, ningependa kujua ni lini hasa kinakwenda kujengwa? Hilo ni la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tupo humu ndani kwa ajili ya Bajeti ya mwaka ujao, ningependa kujua ni kiasi gani kimeombwa kwenye Bajeti hii kwa ajili ya chuo hicho, hayo mambo ya barabara , miundombinu, michoro na chuo chenyewe, ni kiasi gani kimeombwa kwenye Bajeti hii kwa ajili ya Chuo hicho? Asante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niungane na Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza kwa jitihada kubwa ambazo anazifanya juu ya chuo hiki, nami naona umuhimu wa chuo hiki katika Mkoa wa Kagera.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli anaweza kusema kwamba hatujajibu swali lake kwa sababu yeye anataka ni lini, lakini ujenzi wa chuo unaanza baada ya kupitia hatua mbalimbali na baadhi ya hatua zilizopitiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba eneo litakalojengwa chuo hicho limepimwa na ndiyo maana Serikali tayari imeshatoa fedha. Vilevile kushirikisha wadau wengine na baada ya kukamilika jitihada hizo, ndipo sasa tunaweza tukasema tukishakuwa na fedha tuanze kujenga.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu uzito juu ya chuo hicho lakini kimsingi niseme tu kwamba kwa sababu tulishapata hali ya mwelekeo ya baadhi ya wadau kutaka kukisaidia chuo hicho ndiyo tumekuwa tukiendelea nao na mazungumzo yeye mwenyewe ni shahidi, walishawahi kutembelea mpaka huko Kagera. Kwa hiyo naomba tu kwa sababu amekuwa na imani nasi atuamini na ajue kwamba muda wowote tutampa taarifa kadri tunavyoendelea na jitihada za ujenzi wa Chuo hicho.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante, tatizo la watoto au wanachuo wanaohitimu elimu ya diploma au stashahada ni kubwa mno. Haya mambo hayakuanza leo, toka mwaka 2007 wanafunzi wa Vyuo Vikuu kwa Taasisi ya TAHLISO wanadai hili suala halipo vizuri sana.
Kwanza vyuo vyenyewe vinapomaliza muda wake, muda wa kuhitimu masomo unakwepana na muda wa kusajili. Wanafunzi wanapopata ile wanaita supplimentary, kiswahili sijui; lakini na hawa wanachelewa kufanya mitihani yao kujiunga nao chuo. Sasa kama kweli majibu haya yako sahihi, kwanini bado wanapata matatizo haya?
Swali la pili, tatizo hili la kudahili wanafunzi wa diploma, wanapata shida sana kupata mikopo yao kwa maana vyuo vyao vinachelewa sana kupata vile vyeti na wao watu wa Bodi ya Mikopo hawapokei transcript ya mwanafunzi wa diploma. Sasa tunauliza, kwa kutumia hii Taasisi ya Elimu na kwa umaarufu wa Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Ndalichako na kwa kutumia ma-engineer…
NAIBU SPIKA: Naomba uulize swali Mheshimiwa.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Naam!
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la msingi ni kwamba naomba wanafunzi wanaomaliza stashahada wapewe nafasi ya kupata mikopo ya elimu ya juu, nalo ni tatizo. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli kwa siku za nyuma kulikuwa na usumbufu kidogo ambao ulikuwa unajitokeza hususan kwa hawa wanafunzi ambao wanamaliza stashahada. Tatizo ambalo lilikuwa likijitokeza ni kwamba kwa upande wa wale ambao ni wanafunzi kwa mfano form six, wao matokeo yao yanakuwa moja kwa moja yanapitia Baraza la Mitihani ambalo ni moja, lakini kwa upande wa vyuo kumekuwa na utaratibu kati ya chuo na chuo kiasi kwamba baadhi ya vyuo vikuu vimekuwa haviamini kwa uharaka kwamba matokeo tunayoletewa ni sahihi. Kwa hiyo, walikuwa wanatafuta namna ya kufuatilia zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukaa pamoja na kuelezana uhalisia na kwa sababu matokeo hayo ya vyuo vilevile yanaenda kuhifadhiwa katika Hazina data za NACTE, kwa misingi hiyo hakuna huo usumbufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali hiyo, napenda nitoe agizo kwa vyuo vyote kwamba hakuna sababu ya kufanya usumbufu kwa wanafunzi hao ikizingatiwa kwamba matokeo yao yapo na yanaongea moja kwa moja na system ambayo inafanya shughuli ya udahili.
Kwa upande wa suala la udahili wa Stashahada kusababisha wanafunzi kushindwa kuingia katika nafasi za mikopo, kwasababu suala hili linalohusiana na mfumo, ni vyema tulichukue tuendelee kulifanyia kazi na hivyo tutashirikaiana na wewe mwenyewe Mheshimiwa Mbunge kupitia Kamati. Ahsante

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu wangu wa Elimu, ningependa kuchangia kidogo tu katika suala hili.
Kwanza napenda kutoa ufafanuzi kwamba mwanafunzi ambaye ana supplementary bado hajamaliza chuo. Mwanafunzi anakuwa amemaliza chuo pale ambapo anakuwa ame-clear mitihani yake. Kwa hiyo, mwanafunzi ambaye ana supplementary hawezi akadahiliwa kwenda katika chuo kwa sababu bado hajakamilisha masharti ya kumaliza elimu yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kulizungumzia kuhusiana na mikopo kwa wanafunzi wenye stashahada ya ualimu. Mwanafunzi anapata mkopo kulingana na vigezo vinavyowekwa na hivyo basi, kama mwanafunzi wa stashahada amekidhi matakwa ya kujiunga na elimu ya juu na anakidhi matakwa ya mikopo, hakuna usumbufu wowote unaotokea katika upatikanaji wa mkopo.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na jiografia ya Wilaya ya Nkansi, naomba hilo swali labda angesaidia kujibu Mheshimiwa Stella Manyanya, Naibu Waziri wa Elimu, Teknolojia na Elimu ya Juu. Inaonekana hilo swali halikujibiwa jinsi inavyotakiwa na aliyeandika hilo jibu, hajui Wilaya ya Nkasi ilivyo; Kipili iko wapi, Namanyere iko wapi, Kala iko wapi, Itindi iko wapi, Kabwe iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na majambazi katika mwambao wa Ziwa Tanganyika, hilo gari haliwezi kuhudumia vijiji vya mwambao wa Ziwa Tanganyika. Kwa hiyo, lini Serikali, itawapatia mgawo wa mafuta wa kutosha Wilaya ya Nkasi?
Mheshimiwa Naibu Spika, gari lenyewe liko Wilaya ya Nkasi, hata mafuta halina! Lini itaongeza mgao wa mafuta katika Wilaya ya Nkasi? Lini itawapatia pikipiki vijana wa Marine Kipili, ili kuondoa tatizo la usafiri ambako unatokea ujambazi katika vijiji vilivyopo jirani jirani na mwambao wa Ziwa Tanganyika ili kupunguza uharamia katika mwambao wa Ziwa Tanganyika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli kwamba Wilaya ya Nkasi kijiografia imekaa na changamoto nyingi sana hasa ikizingatiwa kwamba baadhi ya vijiji vyake kama Kipili, Kala, Wampembe na vijiji vingine kama Samazi, vimekaa mbali kidogo, vinahitaji mwendo mrefu kuvifuata. Kwa hiyo, vinahitaji mafuta ya ziada. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali imefanya jitihada kubwa sana katika Mkoa wa Rukwa na Nkasi kwa ujumla. Kwanza kuna maboti ya kutosha ambayo yalipelekwa kwa ajili ya Jeshi la Wananchi ambao wamekuwa wakishirikiana kwa karibu sana na Jeshi la Polisi.
Vilevile kuna vituo ambavyo vimeanzishwa katika maeneo hayo na hivyo, kuwezesha kuwa na urahisi wa kuwafikia wananchi wanapokuwa na tatizo, hususan katika kijiji cha Kipili. Kwa hali hiyo, naamini kwamba pamoja na jitihada ambazo zimekuwa zikiendelea kufanyika hali ya Nkasi kwa sasa ni bora kuliko ilivyokuwa hapo awali. Ahsante sana.
MHE. SUSAN A.J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi, lakini lazima ni-admit kwamba nimefedheheshwa sana na majibu ya Wizara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni wazi kwamba elimu imeporomoka kama ambavyo amekiri lakini hajatupa mikakati. Katika majibu yake ya msingi anasema kwamba Walimu wamekuwa na morali, ni wazi kwamba Serikali labda haijui maana ya motivation theories na hawa Walimu wanapata motive gani. Ni wazi hilo suala la umeme miaka ya 60, 70 hapakuwa na umeme lakini nyumba za Walimu zilionekana. Sasa hivi mtoto anaona aibu kusema yeye ni mtoto wa Mwalimu, anaona afadhali hata aseme ni mtoto wa Mmachinga.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunavyoongea Walimu...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Susan, naomba uende kwenye swali tafadhali.
MHE. SUSAN A. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwenye swali, nataka kujua kama tuna tatizo kubwa la Walimu, Walimu wame-graduate toka mwaka jana mwezi wa tano mpaka leo tunapoongea hawajaajiriwa, hiyo ndiyo motisha? Kwa hiyo, naomba kujua ni lini Walimu waliomaliza masomo yao wanapata ajira zao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, moja ya mikakati ni kuhakikisha kwamba Walimu wanapata mafunzo, lakini ukisoma ripoti ya CAG inaonesha Walimu hawajakwenda mafunzo, ni asilimia 11 ya Walimu wa sekondari ndiyo tu wanapata in-service program na Walimu wa primary ni asilimia 30. Ni lini Walimu hawa watapata in service training ili waweze kuendana na mazingira halisi ya ualimu na hasa kuhakikisha kwamba elimu yetu haiporomoki?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli tulivyoeleza kwamba Walimu wameanza kupata motisha kwa sura mbalimbali hasa za mazingira wezeshi na ni jambo endelevu. Hata hivyo, katika suala la ajira huwezi kuajiri mtu kabla hujamwekea bajeti yake. Katika mwezi huu unaoanza mpaka mwishoni kuna mpango wa kuajiri Walimu. Kwa misingi hiyo, mimi nafahamu kwamba kumaliza ni namba moja na kuajiriwa ni namba mbili, lakini kwa taratibu ambapo lazima uwe umeshamwandalia stahiki zake zote ili kupunguza malalamiko yasiyo ya lazima. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuhusu Walimu kutopewa mafunzo ya ziada kama ambavyo imeelezwa katika taarifa ya Mkaguzi Mkuu, niseme tu kwamba, hili suala ni endelevu, hata hivi tunavyoongea sasa hivi kuna mafunzo yanayoendelea huko Mwanza na wiki iliyopita kuna mafunzo yalikuwa Iringa. Kwa hiyo, suala hilo haliwezi kukamilika kwa siku moja lakini kimsingi Wizara imedhamiria.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunachosema ni kwamba, fedha inayotengwa kwenye bajeti haendi katika Wizara ya Elimu peke yake, inaenda katika Wizara mbalimbali na kila Wizara kama tulivyojionea ina umuhimu wake. Kwa hiyo, tutakwenda hivyo hivyo kutokana na kiasi kile kinachopatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. MASHIMBA M.NDAKI: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina swali moja tu la nyongeza. Kwa kuwa wananchi walionufaika na fedha hizi za mikopo wanakatwa kupitia waajiri wao, lakini hawapati taarifa kwamba ni lini deni lao hilo litaisha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza kutoa taarifa hizo kwa wanufaika hao wanaokatwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza napenda kuwashukuru na kuwapongeza sana hao ambao tayari wameshatambua wajibu wao wa kurudisha mikopo, kwani heshima ya mtu ni kukopa kwa staha, lakini pia dawa ya deni ni kulipa.
Mheshimiwa Spika, kwa misingi hiyo, napenda kusema kwamba katika mfumo wetu wa kulipa kupitia sheria zilizopo, tumegundua pia kulikuwa na upungufu wa aina mbalimbali ikiwemo na baadhi ya maeneo mengine, badala ya kukata kwa kutumia 8% ya mshahara, wamekuwa wakikata aidha kwa kusema ni shilingi nane au vinginevyo. Pia hizo taarifa zimekuwa hazipatikani siyo kwa wale ambao wanakatwa, lakini pia hata kwa bodi katika kuhakikisha kwamba watu wote wanalipa.
Mheshimiwa Spika, kwa misingi hiyo, tunashukuru kwa ushauri, lakini pia na sisi wenyewe tumekuwa tukifanyia kazi ili kuona kwamba wanufaika wanaolipa na sisi Serikali, wote tunakuwa na taarifa zinazostahili.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nadhani kuna shida ya mawasiliano, wakati nilipoletewa nifanye marekebisho niliandika ni kifungu namba 20 na nikazungushia na sheria ninayo.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, naomba niseme tu kwamba nasikitika sana kwa majibu niliyopewa. Haya majibu, nimeuliza kuhusiana na mitaala utamsikiliza katika majibu Mheshimiwa Naibu Waziri hakugusa kabisa mitaala. Nimeuliza juu ya maswali ya kuchagua ya masomo ya hesabu, hakugusia. Nimeuliza kipengele cha tatu cha Waziri kutoa maelekezo, Sheria inasema The Minister may give the Council directions of a general or specific character and the Council shall give effect to every such direction, hakuna kushauriana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nitaomba niulize maswali mawili ya nyongeza wakati anajiandaa kunipa majibu sahihi kwenye swali hili.
Swali la kwanza, kwa nini Waziri wanang‟ang‟ania na kipengele cha kutunga mambo yao wao yaani kusema leo watu watumie GPA au watumie division, yaani leo waseme tufanye sayansi, hesabu na physics pamoja, biology na kemia. Haya wanakubali yawepo lakini hii ya ushauri na wataalam hawataki kwa nini naomba tujibu?
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kwa nini Wizara hii inakataa kushirikisha Wataalam katika maamuzi ya kupima wanafunzi wetu, atueleza hapa wale watoto ambao walipimwa kwa kiwango cha kutumia GPA na wakapewa vyeti, sasa hivi Waziri ametoa tamko lake hapa anasema sasa ni division, hivi vyeti anavi-compromise namna gani katika elimu? Naomba atusaidie mambo hayo.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa amelalamika kwamba hatujazungumzia masuala ya kuchagua majibu ya hesabu na mambo mengine. Kimsingi najibu kadri ya swali lilivyowekwa, kule uliweka utangulizi lakini swali lako ulisema kwa nini kifungu hiki kisiondolewe na ndicho nilichokujibu.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo kimsingi lazima ieleweke Mheshimiwa Waziri hafanyi maamuzi kwa kukurupuka bila kupata taarifa mbalimbali zinazomwezesha kufanya maamuzi hayo. Hata hivyo si kwamba kila jambo linalofanyika kwenye Wizara linakuwa limetangazwa, lakini hatua mbalimbali zinakuwa zimechukuliwa, ikizingatiwa kwamba Wizara hii inazingatia sana masuala ya kitaalam.
Mheshimiwa Spika, katika maswali ya kuchagua majibu ya hesabu, siku za nyuma wanafunzi walikuwa hivyo hivyo wanachagua, lakini walikuwa na sehemu ya kufanyia kazi halafu wanachagua. Hata sasa hivi wanapewa karatasi wanazofanyia kazi, lakini wanachagua kwa ku-shade kwa misingi kwamba kwa siku za nyuma kwa sababu walikuwa wanasahihisha karatasi kwa mikono, sasa hivi inasahihisha mashine, ndiyo maana baada ya kuchagua lile jibu lake sahihi anakwenda ku-shade na kuweka ili mashine iweze kusahihisha.
Hiyo imepunguza kazi iliyokuwa inatakiwa kufanyika na watu 3000, sasa inafanyika na watu 300. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lingine Mheshimiwa amezungumzia kwamba kwa nini tumeking‟ang‟ania hicho kifungu. Siyo suala la kuking‟ang‟ania, kifungu hiki kikitumika vibaya ndipo kina kasoro, lakini kama kinatumika vizuri kinaharakisha utendaji na maamuzi ya Wizara.
Kwa hiyo, nasimamia katika sura hiyo kusema kwamba, Waziri aliyeaminiwa na Serikali kutekeleza majukumu yake ipasavyo, naamini atakitumia kifungu hiki inavyostahili. Hata hivyo, baada ya kubadilisha GPA kuweka katika division, kimsingi hakuna athari zilizopatikana kwa sababu bado kuna uwiano katika hizo alama na wanafunzi hawa bado wanaendelea kupata haki zao kama kawaida.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi ili niulize swali moja dogo la nyongeza. Ukiangalia katika majibu amesema kwamba, mabadiliko haya yanafanywa baada ya utafiti, baada ya wataalam kuleta taarifa mbalimbali. Naomba kujua GPA imetumika kuanzia mwaka 2013 na sasa 2015 tayari imebadilika imekuwa madaraja, yaani ilikuwa madaraja ikaja GPA within a year, sasa naomba kujua huo utafiti ulifanywa lini hasa ikizingatiwa wataalam walioko Baraza la Mitihani ni wale wale kuanzia Mtendaji Mkuu? Kwa hiyo, naomba kujua huo utafiti umefanywa wapi na mazingira ya jamii ni watu gani walitaka hasa wabadilishwe kutoka madaraja kwenda GPA na kurudi tena kwenye madaraja?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kimsingi wakati huu mfumo wa GPA unaanza kutumika ulikuwa pia uanze katika misingi ya majaribio. Lengo lilikuwa ni kufanya kwamba, toka mwanafunzi anapokuwa katika hatua za awali yaani katika sekondari na kuendelea aweze kuwa na mfumo mmoja unaokwenda mpaka vyuo vikuu. Kwa sababu unakuta vyuo vikuu tunatumia GPA, lakini huku chini tulikuwa tunatumia division na kwa kweli lilikuwa ni jambo jema tu, lakini kukawa na maneno tena ya malalamiko mbalimbali kupitia vyombo, kama jana ulivyoona Mheshimiwa Susan Lyimo ulisema kwamba hata magazeti na yenyewe pia ni nyaraka sahihi kutumika katika Bunge letu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, maneno haya yamekuwa yakitoka katika pressure mbalimbali na hata hivyo baada ya kupitisha huu mfumo wa division hii juzi, nafahamu kuna magazeti mengi hata Waheshimiwa Wabunge walipongeza. Sasa mjue tu kwamba ni hayo mawazo yetu tunayoyatoa na Serikali ni wajibu wake kufanyia kazi. Ahsante sana.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri ametoa ufafanuzi mzuri, ningependa tu kuongezea pale alipojibu Mheshimiwa Naibu Waziri, kwamba kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri hata huu mfumo wa GPA ulitokana na maoni ya wadau. Hata hivyo, baada ya Serikali kutekeleza, wadau tena wakawa wameleta malalamiko, kwa hiyo, lazima Serikali tuweze kuyafanyia kazi kadri mahitaji yanavyojitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwasihi Watanzania tunapopewa nafasi ya kutoa maoni, tuitumie nafasi hiyo kutoa maoni ya dhati kabisa. Kwa sababu tunatoa maoni, Serikali inapotekeleza halafu tena kuna kuwa na malalamiko kama ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri amesema. Vilevile ningependa pia kuchukua nafasi hii kumwambia Mheshimiwa Ndugu yangu Mwita Waitara kwamba hii Sheria ya Baraza la Mitihani akisoma kifungu cha nne, kinatoa fursa kwa wananchi kutoa maoni kwa Baraza la Mitihani kuhusiana na masuala ya uendeshaji mitihani na maoni yao yanazingatiwa. (Makofi)
Kwa hiyo, siyo kwamba tu imempa mamlaka Waziri wa Elimu, lakini vilevile imetoa fursa kwa maoni kutolewa na naomba kama kuna maoni yoyote ambayo yana tija, basi wahakikishe na yatafanyiwa kazi.
MHE. JANET Z. MBENE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na kwa kuitikia wito wetu wa kusaidia kupokea hiki chuo kiwe cha Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo letu kubwa Ileje na maeneo mengi ya pembezoni ni upimaji wa ardhi kwa ajili ya kuweka taasisi muhimu kama hizi za vyuo na masuala mengine. Naomba Serikali kwa ujumla itusaidie kwa sababu kupima viwanja muhimu kama hivi kwanza ni gharama lakini vilevile hatuna wataalam katika maeneo yetu wa kutupimia kwa haraka ambayo tungeitegemea. Je, Serikali ipo tayari kupitia Wizara nyingine yoyote ambayo inahusika na mambo haya kusaidia Wilaya ya Ileje tuweze kupima viwanja vyote muhimu tulivyoviainisha kwa ajili ya taasisi kwa mfano viwanda, elimu kama hivyo, vyuo vya unesi na vyuo vingine mbalimbali vya ualimu ili tuweze kupata maendeleo haraka zaidi? La sivyo tukiendelea kungojea tu mpaka sisi wenyewe tuwe na uwezo wa kupima tutachelewa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lingine, kwa kuwa sasa hivi tumeshaanzisha mkakati wa kuwa na chuo cha ufundi, tungeomba sasa tunapoendelea na mipango basi hiki chuo kiwe na mitaala ambayo itatusaidia kuzalisha vijana watakaokuja kufanya kazi katika viwanda kwa sababu sasa hivi tunalenga kwenda kwenye uchumi wa viwanda. Ahsante
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA MAFUNZO YA UFUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli kama ambavyo amezungumza Mheshimiwa Mbunge Janet Zebedayo Mbene kwamba kuna tatizo kubwa katika baadhi ya halmashauri kushindwa kumudu kupima viwanja hususani vile vinavyohitajika katika maendeleo ya vyuo na taasisi mbalimbali za kiuchumi. Suala hilo linatokana na hali halisi ya uchumi katika halmashauri hizo. Sisi pia kwa upande wetu Wizara kwa kupitia VETA imekuwa ikicheleweshwa sana katika upatikanaji wa viwanja kutokana na halmashauri husika kushindwa kuleta hati za viwanja au maeneo ambayo yameshapimwa kwa ajili ya shughuli hizo. Hilo suala tumeliona na nadhani linahitaji pia kuangaliwa kwa mapana zaidi.
Katika hili nachukua nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha alivyozungumzia kuangalia mapato katika halmashauri kwa upana zaidi na kuweza pia kuangalia namna ya hizi halmashauri nyingine ambazo zipo katika hali ngumu ya kiuchumi nazo ziweze kupata mitaji hasa katika upimaji kadiri itakavyowezekana.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia katika suala la kuangalia mitaala inayoendana na shughuli za viwanda, ni kweli kwamba kabla Chuo cha VETA hakijajengwa mahali popote, kitu kinachofanyika ni kuangalia mitaala na kozi ambazo zitaweza kutolewa katika maeneo hayo tukiwa na lengo la kuwanufaisha hata wananchi wengi wa maeneo hayo kutegemeana na shughuli mbalimbali zinazofanyika katika maeneo hayo. Kwa hali hiyo ni kwamba kabla hiki chuo hatujaweza kukichukua na kuanza kukiendesha, suala hilo la kuangalia mitaala litakuwa ni mojawapo ya shughuli zitakazozingatiwa. Nachoomba Mheshimiwa Mbene jitahidi kadiri inavyowezekana kumalizia angalau hasa zile taratibu za awali za makabidhiano rasmi kupitia vikao vya kisheria wakati masuala mengine yakiendelea.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Vilevile, naipongeza Serikali kwa jitihada za kutatua matatizo hasa changamoto zinazowakabili watoto wenye ulemavu. Nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Lugha ya alama ni changamoto kwa watoto viziwi ambao wengi wao huishia elimu ya sekondari na kushindwa kuendelea na elimu ya juu kutokana na Wahadhiri wengi kutokujua lugha ya alama. Je, Serikali haioni ni wakati muafaka sasa wa kuingiza lugha ya alama katika shule za msingi, sekondari na katika Vyuo vya Ualimu hapa nchini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, ni Vyuo vingi hasa vyuo binafsi, mazingira yake sio rafiki kwa wanafunzi wenye ulemavu. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwepo mwongozo utakaoviongoza vyuo vyote kuzingatia mahitaji na hasa miundombinu kuwa rafiki kuwatimizia majukumu yao hasa watoto hawa wenye ulemavu ili waweze kusoma vizuri? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ni kweli kabisa lipo hilo tatizo, kutokana na kwamba kama inavyojulikana kwa muda hawa watu wenye ulemavu wamejikuta hawapati elimu za aina mbalimbali kutokana na mahitaji yao. Sasa hivi Wizara inachofanya, kwanza imetambua hayo mahitaji maalum ya aina mbalimbali na kupitia bajeti hii, tumeshatenga fedha kwa ajili ya kuandaa mitaala kwa ajili ya kutoa mafunzo maalum kwa ajili ya Walimu pamoja na wanafunzi wenyewe katika shule husika, vile vile, kwa ajili ya kununua vifaa ambavyo vitatumika katika kufundishia.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la pili, juu ya miundombinu rafiki, niseme tu kwamba, hilo suala limekuwa likijitokeza. Ninayo mifano mingi ambayo nimeishuhudia mwenyewe kwamba, watu wanapojenga shule au taasisi maalum, wanasahau kabisa kwamba kuna siku wanaweza wakawa na mwanafunzi ambaye ni mlemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, unakuta hata mtu anapojenga iwe ni ghorofa, iwe ni choo, haangalii kama atakuja mwanafunzi mwenye wheel chair, atafika vipi huko au angalau kuwashusha wale wanafunzi badala ya kusoma ghorofani waweze kusoma katika madarasa ya chini ili nao waweze kupata hiyo fursa. Kwa hiyo nitoe wito, tujue kwamba, ulemavu siyo jambo la kujitakia bali ni mapenzi ya Mwenyezi Mungu katika kuonesha kazi za uumbaji wake. Ni vyema tuwafikirie na kuwajali watu wenye ulemavu.
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa elimu ndiyo ufunguo wa maisha, je, Wizara imechukua hatua gani kuwahamasisha wazazi wenye watoto walemavu kutoa kipaumbele kwa watoto hao kupata elimu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kweli Wizara yetu imekuwa ikizungumza katika nyakati mbalimbali kupitia vyombo vya habari, lakini pia kupitia Wizara nyeti sana hii ya Sera, Bunge, Watu wenye Ulemavu na mambo yote yaliyoko kule, kwamba tumekuwa tukishirikiana pamoja na Waheshimiwa Mawaziri wenzangu kuhakikisha kwamba tunahamasisha jamii kwa kupitia makongamano, mikutano na kupitia Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hivi tunavyoona, kwamba tuna Waheshimiwa Wabunge wenye ulemavu, mtu anaanza kuona kwamba kumbe mwanangu nikimsomesha, kumbe nikimsaidia, kuna siku ataweza kuwa Mbunge, Waziri au kiongozi yeyote yule. Kwa hiyo, kwa hali hiyo niwaambie sana Waheshimiwa wazazi mlio huko, naomba muwatoe watoto wenu wenye ulemavu barabarani, msiwape kazi ya kuomba, hiyo sio kazi yao. Ninyi ndiyo kazi yenu mfanye kazi na hatimaye iweze kuwasaidia watoto hawa wenye ulemavu.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ina shule ya viziwi kule Dongobesh na pia ina Kitengo cha Elimu ya Watoto Walemavu katika Shule ya Msingi Endakkot na kwa kuwa kundi hili ni kubwa katika jamii; je, Serikali haioni umuhimu mkubwa wa kuweka Kitengo cha Elimu kwa Walemavu katika kila halmashauri kwa shule mojawapo ili kundi hili lililokosa nafasi wapate huduma stahiki?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ni kweli kuna umuhimu mkubwa sana kwa kila halmashauri kuwa na shule yenye kitengo cha watu wenye ulemavu. Hata hivyo, niseme tu kwamba, kuwa na kitengo ni kitu kimojawapo, lakini kuangalia hivyo vitengo vikafanya kazi iliyokusudiwa ni hatua ya pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningetamani kuona kwamba, kwanza kila halmashauri iwatambue hawa watoto wenye ulemavu pamoja na mahitaji yao yanayohusika. Baada ya hapo, katika hizo shule zinazotengwa, naomba ziwasilishwe kwenye Wizara yetu pamoja na Wizara ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili kuona kwamba vinawekwa vifaa vinavyohusika na kukidhi mahitaji yanayostahili, tukifanya hivyo tutakuwa tumetatua matatizo makubwa ya watu wenye ulemavu.
MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwanza, nilitaka nifahamu kwa wale waandishi na wachapishaji ambao wamechapisha vitabu vyenye maadili mabovu au wametoa taarifa za uongo kupitia vitabu hivyo wamepewa adhabu gani?
Pili, ninataka kujua kwa kuwa wananfunzi wanaotoka Visiwa vya Unguja huwa wanafanya mitihani ya Kitaifa sambamba na wenzao wa Tanzania Bara; je, Wizara inafanya utaratibu gani kuhakikisha kwanza mihtasari na vitabu kwa maana ya mitaala na vitabu inawafikia wanafunzi wa Zanzibar mapema ili na wao waweze kujisomea na kufanya vizuri katika mitihani ya Taifa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi vitabu vyote kabla ya kupitishwa vinatathminiwa na baada ya kutathminiwa, vinaangaliwa katika suala la maadili inayoendana katika misingi ya kwamba huyu mwanafunzi atafundishwa vipi. Lakini vilevile siyo maadili tu hata uchapishaji wake kitabu kilivyochapishwa kinaleta uhalisia wa yale yanayokusudiwa kufundishwa au laa! Kwa mfano, kama tuna lengo la kumfundisha mtoto kwamba haya ni mayai, basi tunategemea kwamba na kitabu hicho hata picha itaonyesha mayai ambayo ni meupe na itaonyesha kweli yale ni mayai, hayataonyeshwa mayai wakati hapo imechorwa embe. Kwa wanaokuwa hawajatekelza wajibu wao ipasavyo vitabu hivyo vinakuwa haviruhusiwi kupelekwa au kusambazwa au kuchapishwa kwa maana hiyo wanatakiwa kurekebisha hayo makosa. Hayo yalishafanyika hata katika vitabu ambavyo sisi wenyewe tulikuwa tukivishughulikia na tulivizuia visiweze kuendelea.
Pili; kwa upande wa Zanzibar kimsingi Zanzibar wao wanayo mamlaka yao ya elimu ambayo inashugulikia masuala yote hayo ya mitaala pamoja na vitabu. Lakini kwa kuwa sisi wote ni ndugu na tuna masuala ya ushirikiano wa kielimu huwa pia tunaweza kusaidiana katika masuala ya kitaalam lakini pia hata kuchukua best practice katika kutoka upande wowote wa nchi kwa faida ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, ningependa kuongezea kidogo majibu mazuri aliyoyatoa Naibu Waziri wa Elimu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka nitoe tu ufafanuzi kuhusiana na mitaala ya elimu ya sekondari kwa upande wa Zanzibar. Kama alivyoelezea Mheshimiwa Naibu Waziri kwa upande wa elimu ya msingi mitaala inatengenezwa na upande wa Zanzibar, lakini kwenye upande wa sekondari mitaala inatengenezwa na Taasisi ya Elimu Tanzania ambayo utaratibu ni shirikishi wakati wa mitaala inapotengenezwa tunawashirikisha upande wa Zanzibar na vilevile hata katika Bodi ya Taasisi ya Elimu Tanzania kunakuwa na uwakilishi wa Wajumbe wa kutoka Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na utaratibu wa usambazaji wa vitabu ili vifike Zanzibar kwa wakati, utaratibu ni kama unavyotumika Bara kwamba kwanza zoezi ni shirikishi la vinapokuwa tayari Wizarra ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar huwa inafanya hilo jukumu.
MHE. JORAM I. HONGOLI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa shule zetu nyingi bado zinaendelea na utaratibu wa matumizi ya vitabu vingi vya kiada; na kwa kuwa vitabu hivi vimekuwa vikitofautiana kwenye baadhi ya maudhui yaliyomo kwenye vitabu hivi na kuleta mkanganyiko kwa wanafunzi. Je, lini sasa Serikali itaanza kutekeleza utaratibu wa kutumia kitabu kimoja nchi nzima ili kuleta usawa na kuondoa mkanganyiko wa wananfunzi hao?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa baada ya Serikali pamoja na wananchi kugundua kwamba kuna vitabu vingi ambavyo vinatumika mashuleni kiasi cha kushindwa kutoa mwelekeo halisi hasa katika usimamiaji wa maarifa yanayopatikana, Serikali iliamua kwamba kuwe na vitabu vya kiada na ziada, mpaka sasa imekuwa inasimamia katika zoezi hilo la upatikanaji wa hivyo vitabu kadri ya fedha tunavyozipata. Hivyo naamini tukishakuwa tumekamilisha hali hiyo ya kuwa na vitabu ambavyo ni vya aina tofauti tofauti itaondoka.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
16
Kwa kuwa hapo awali Serikali ilikuwa na chombo ambacho kinadhibiti education materials yaani EMAC na kwa kuwa ilivunjwa rasmi huko nyuma na kutamka kwamba wataunda chombo kingine kwa ajili ya kudhibiti vifaa vinavyoingia katika mfumo wa elimu pamoja na vitabu.
Je, Serikali inaukakasi gani wa kuunda chombo hicho maana mpaka leo hakijaundwa bado?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hapo mwanzo Wizara yenyewe ilikuwa inahusika katika kudhibiti kwa kutumia Kitengo hiko cha EMAC, lakini baadaye kupitia Waraka Na. 4 ambao niliutaja kulikuwa kumeundwa Taasisi ya Elimu Tanzania ambayo kwa sasa ndiyo inashughulikia masuala hayo.
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mwenyekiti ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba kuuliza swali moja fupi la nyongeza. Malalamiko haya ni ya muda mrefu sana na kila siku yanazidi kwa wananchi. Je, Wizara imewahi angalau kuwaonya wamiliki wangapi angalau kwa barua mpaka kufikia mwaka uliopita?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu imeshawahi kuwaonya wamiliki IMTU na mwenzao KIU kwa kukiuka masharti hayo na hivyo tunazidi kusisitiza wamiliki wote wachukue fedha ambayo ni ada kwa kutumia fedha za Kitanza ni ana pale inapobidi iwe tu kwa wananfunzi ambao wanatoka nchi za nje
MHE. SALUM MWINYI REHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimuulize swali moja la nyongeza.
Kwa Zanzibar suala hili limekuwa na manung‟uniko sana na hasa kwa kutokuweko watendaji katika hizi taasisi na hili limetokana kwamba wanafunzi wengi wanaopata huduma kupitia TCU, NACTE na NECTA wamekuwa wanahisi hakuna uwiano na hakuna haki inayotendeka kwa vile hakuna watu ambao wanaohusiana wanaotoka upande ule kule. Je, Waziri au Wizara ina mpango gani wa kuweza kupata angalau maana yake watu wawili, watatu kuweza kuingia katika taasisi hizi ili kuepusha manung‟uniko ya kila siku hasa yanayohusiana na masuala ya vyeti na mengineyo ambao wanataka kujiunga katika vyuo mbalimbali vya huku Tanzania Bara?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwaombe Watanzania tusifanye mambo kwa masuala ya hisia. Lazima twende katika misingi na misingi iliyopo ni hiyo ya kufuata sifa stahiki kwa nafasi zinazohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende tu kusema kwamba pamoja na kwamba hakuna hivi vigezo vilivyowekwa, kimsingi ukiangalia katika hizo taasisi zote wapo Wazanzibari ambao wanafanya hizo kazi na isitoshe kwa mfano kwa Baraza la Mitihani nafahamu hata Mkuu wa Kitengo kile kule Zanzibar anatoka Zanzibar. Lakini ukiacha hiyo nataka tu niseme kwamba sisi tumekuwa na mahusiano ya karibu sana na Serikali ambayo iko kwa upande wa Zanzibar na tunawasiliana katika masuala yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tarehe 11 Agosti, huu tulitembelewa na Mheshimiwa Waziri wa Elimu pamoja na Naibu wake na Katibu Mkuu na tuliweza kujadili mambo mablimbali ikiwemo ya kushirikiana na kusaidiana pale tunapoona upande mmoja haujakaa vizuri na kila jambo linalofanyika huwa tunashirikishana. Kwa hiyo, ninachoomba ni kwamba Mheshimiwa Mbunge tusiende kwa hisia. Kama nafasi zitaonekana kwamba Watu walioomba wenye uwezo wengi wanatoka Zanzibar basi itabidi wapewe kwa sababu tunachohitaji ni uwezo na siyo tu kuangalia upande wanakotoka.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa mwenyekiti, napenda kuongezea katika majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa taaisis za Muungano kuwakilishwa kwa uwiano sahihi na muafaka kwa watu wa pande zote mbili, Serikali iliamua kwamba kuwe na quota kwa watumishi kwenye taasisi za Muungano na quota iliyokubalika ni asilimia 79 kwa asilimia 21 na sisi ofisi yetu tuliwaandikia taasisi na viongozi wote ambao wanahusika na masuala ya Muungano kwanza watuletee idadi ya watumishi waliopo, lakini pili watuletee mpango kazi wa kufikia quota iliyokubalika ya taasisi za Muungano ziwe na uwiano sahihi wa kimuungano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu na mwisho ni kwamba Serikali ilishafanya uamuzi wa kufungua Ofisi ya Tume ya Ajira Zanzibar kwa sababu moja ya changamoto ilikuwa ni kwamba Tume ya Ajira ambayo inaajiri hawa watendaji na watumishi wengineo ipo Bara peke yaake na hizi nafasi wakati mwingine hazifahamiki au hazifikiwi na watu wa upande wa Zanzibar, kwa hiyo, ofisi hii sasa imefungua ofisi yake Zanzibar na nafasi zitatangazwa kwa upana wake kwa watu wa Zanzibar na wenyewe wataziomba ili waweze kupata fursa za kushiriki katika taasisi za Muungano.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza ni kwamba zipo shule za ufundi ambazo zipo katika majengo ya shule za msingi na shule za sekondari ambazo zilikuwa zikijulikana kama shule za ufundi na sekondari. Shule hizi katika miaka ya nyuma zilikuwa maarufu sana, lakini katika miaka ya hivi karibuni shule hizi umaarufu wake umepungua. Je, Serikali haioni kuwa ni wakati sasa wa kuboresha shule hizi na vyuo vya ufundi hapa nchini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Tanzania inaelekea kwenye uchumi wa viwanda na ili kuwapata vijana wenye ujuzi kukabiliana na ajira zitakazokuwepo katika viwanda hivyo tunavyovitarajia na kwa kuwa vyuo vingi vya watu wenye ulemavu vilisaidia kwa kiasi kikubwa kuwapa mafunzo watu wenye ulemavu na katika makundi hayo ya ajira tunatarajia pia kwamba kundi la watu wenye ulemavu nao pia watakuwemo katika uchumi huu wa viwanda na biashara. Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha vyuo vya ufundi mfano kama Chuo cha Yombo Dovya na vyuo vingine ili watu wenye ulemavu waweze kujiandaa kukabiliana na ajira tunapoelekea kwenye uchumi wa viwanda? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. La kwanza, ni kweli kwamba kumekuwa na upungufu kidogo katika baadhi ya shule zetu hasa shule za ufundi zikiwemo zile ambazo zimekuwa ni za ufundi primary pamoja na ufundi sekondari. Sisi kama Wizara suala hilo tulishaliona na kupitia bajeti yetu ya mwaka 2016/2017, Wizara imetenga fedha kwa ajili ya kuboresha shule zote za ufundi zile za zamani ambazo ni pamoja na Mtwara, Iyunga, Ifunda, Moshi, Bwiru na Musoma, nadhani nimezitaja zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo tunategemea kwamba baada ya hapo na ukarabati utakaoendelea pamoja na kuweka vifaa itasaidia kuboresha. Pia tunazipitia hata zile shule za msingi ambazo zimekuwa zikitoa mafunzo ya ufundi hasa kwa vijana wanaomaliza darasa la saba ili pia waweze kupata stadi ambazo zitawasaidia katika kumudu maisha yao. Kwa hiyo, naamini kwa bajeti ya mwaka huu, kuna marekebisho mengi ambayo yatafanyika katika eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili katika suala linalohusu watu wenye ulemavu, ni kweli ulemavu siyo maana yake kushindwa kufanya kila kitu. Mimi binafsi nilishawahi kutembelea Shule ya Yombo na nikajionea matatizo wakati huo bado sijawa Naibu Waziri. Kimsingi Waziri wangu pia yuko katika msukumo mkubwa sana kuhusiana na shule za ufundi hasa zinazowahusu watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulichoamua kukifanya katika Wizara kupitia bajeti yetu ni kuona kwanza mitaala inaboreshwa kuona inakidhi kufundisha watu wenye ulemavu na kuweza kuelewa yale wanayofundishwa kwa kutumia lugha inayoendana na hali yao, lakini vilevile vifaa saidizi vinavyoendana na hali yao. Pia kuhakikisha kwamba tunaweka vifaa ambavyo vitahusika katika mafunzo. Kwa hiyo, kwa kuwa sisi wenyewe pia ni wadau wa watu wenye ulemavu naamini kuna mambo mengi yataboreshwa katika eneo hilo.
MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu maswali vizuri, lakini tunajua kabisa kwamba kuna tatizo kubwa sana la walimu wa sayansi katika Wilaya zote. Sasa je, Serikali ina mkakati gani wa kuchagua chuo kimoja kuweza kusomesha walimu wa sayansi tu? Kwa mfano, Chuo Kikuu cha Mkwawa pale, tungeamua kitoe masomo ya sayansi ili tuweze kupata walimu wengi?
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kwa nini Serikali sasa isitoe mkopo kwa asilimia mia moja kwa wale wanafunzi ambao wanasomea masomo ya sayansi ili kuwavutia wanafunzi waweze kujiunga na ualimu wa sayansi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la mkakati wa kuwapata walimu wa sayansi, kama unavyofahamu kwamba tayari Serikali ilishachukua hatua na kama mnavyokumbuka kwamba tulikuwa na wanafunzi zaidi ya 7,800 ambao walikuwa katika Chuo cha UDOM ambao kwa sasa tumewatawanya katika vyuo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale ambao wana vigezo sasa hivi kwa kufundisha shule za sekondari ni zaidi ya walimu 6,305 wakishamaliza masomo yao wataweza kwenda kwenye hizo shule. Kwa hiyo, Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kufundisha walimu wa sayansi na wakati huo huo kuhakikisha kwamba maabara kwa ajili ya shule za sekondari ili kupata wanafunzi wengi zaidi katika maeneo ya sayansi yaweze pia kukamilika na kupewa vifaa vinavyostahili.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na nitambue kazi kubwa inayofanywa na Wizara hii katika utekelezaji wa majukumu yake, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mkakati gani wa kudhibiti mfumo wa uhakiki wa vigezo vinavyotumika kutoa mikopo kwa wanafunzi, ili kuhakikisha wanaopata mikopo ni wenye sifa na uhitaji na sio wale ambao wanafanya udanganyifu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha mfumo huu wa utoaji mikopo utaendelea kuwa himilivu na endapo idadi ya wanafunzi itaendelea kuongezeka?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Bodi inatakiwa kuhakikisha kuwa kumbukumbu za wote wanaoomba mikopo zinakuwa kamilifu kwa kushirikiana na vyuo ambavyo vina wanafunzi wanaopewa mikopo hiyo. Kila chuo kinatakiwakuwa na dawati maalum ambalo linashughulikia mikopo, lakini pia katika kutoa mikopo ni lazima kuzingatia vigezo na sifa ambazo zimewekwa. Hivi karibuni Wizara imepitia vigezo hivyo na vigezo vinazingatia hasa uhitaji, uraia, lakini pia uombaji lazima upitie kwenye mtandao na vilevile kwa kuzingatia mahitaji ya nchi, yaani kipaumbele katika taaluma ambazo zinahitajika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kuona kwamba, mikopo hiyo inakuwa endelevu ni kwamba, Wizara baada ya kuangalia matatizo yaliyokuwa yakijitokeza katika ulipaji wa mikopo, imeangalia upya Sheria ya Bodi ya Mikopo na hivyo tuko katika kutaka kuileta Bungeni, ili kuona kwamba, inarekebishwa kuweka mikopo kuwa ni deni la kipaumbele kwa mwombaji ambaye ameshamaliza chuo. Lakini vilevile kuhakikisha kuwa waajiri wanahusika nao moja kwa moja katika kuhakikisha mikopo hiyo inalipwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika sambamba na hiyo tunaangalia namna ya kuboresha upya mifumo mizima ili kuona mfumo huo unaweza kuongea na taasisi nyingine zinazohudumia raia, ikiwemo ya Vitambulisho vya Taifa. Ahsante.
MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante ka kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa zipo tafiti nyingi muhimu zilizokwishafanyika, ikiwemo tafiti ya uyoga pori kwa matumizi ya chakula, je, Wizara imejipanga vipi kufikisha matokeo ya tafiti hizo kwa wananchi walio wengi, hasa ambao wako vijijini?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri anaweza kuahidi nini kwa vyuo vikuu vilivyoko mkoani Iringa kuhusiana na ongezeko la bajeti yao ya tafiti katika mwaka ujao wa fedha?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimshukuru sana Mheshimiwa Mwamwindi kwa kuweka kipaumbele katika maeneo haya ya utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa tafiti inapofikia katika nafasi ya uendelezaji (commercialization) inakutana na changamoto kubwa ya kuendeleza kutokana na kutokuwa na fedha zinazoweza kuondoa utafiti huo katika awamu ya awali na kufikisha katika hatua ambayo sasa inaenda kwenye matumizi. Vilevile Wizara imeliona hilo, lakini pia, hata wanasayansi wengine wa nchi za SADC wameliona hilo na hivi jitihada iliyopo ni kuona kwamba katika kila nchi, fedha za utafiti angalau ziwe ni asilimia moja ya bajeti ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa upande wa Chuo cha Iringa kwanza niwapongeze kwa hatua mbalimbali wanazozifanya, lakini niwasisitize kuwa wanachotakiwa ni kuandika hayo maandiko mazuri, ili sasa Wizara iweze kutoa kipaumbele katika ku-support bajeti za utafiti za chuo hicho.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha Ulebwe ni chuo ambacho kina eneo linalozidi hekta 94 na kwa sasa hivi ninavyoongea, kina wanafunzi 64 tu.
Je, Serikali haioni kwamba sasa kutokana na mazingira mazuri ya Ulebwe kuna ulazima wa kubadilisha mifumo katika chuo kile na kuimarisha fani za kilimo na mifugo ili kusudi vijana wa Njombe waweze kunufaika na chuo kile? (Makofi)
Swali la pili, vijana wengi wamekuwa hawasomi hivi vyuo kwa sababu ya mfumo wanautumia kufundishia ambao ni wa VETA ambao sasa unatumia zaidi lugha ya Kiingereza katika mitaala pamoja na mafunzo yote na vijana wengi hawana uwezo wa lugha hiyo ya Kiingereza; je, Serikali iko tayari kuandaa mitaala ya Kiswahili ili iweze kuwasaidia vijana wadogo wanaomaliza elimu ya msingi na sekondari waweze kunufaika na haya mafunzo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia kubadilisha mafunzo katika chuo hicho, napenda tu kumfahamisha Mheshimiwa Mwalongo kwamba kwa mujibu wa Katiba yetu kifungu cha 9(i) kinazungumzia kwamba utajiri wa nchi na rasilimali utaelekezwa zaidi katika kuhakikisha kwamba unatoa umaskini, maradhi na ujinga katika maeneo yetu yote. Vilevile inaendelea kwa kusema kwamba haki ya kupata mafunzo au elimu ni ya Watanzania wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, vyuo hivi vya FDC vilianzishwa kwa lengo la kuhakikisha kwamba wananchi wote hata wale ambao hawajafika kidato cha nne au darasa la saba wanapata mafunzo na kuweza kuwasaidia kukimu katika maisha yao ya kila siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni mtazamo wangu kuona kwamba vyuo hivyo viimarishwe ili kuweza kutoa mafunzo kwa wananchi wengi zaidi ambao bado tunao katika maeneo yote. Sio wote kwamba wamefika darasa la saba au kidato cha nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile suala la kufanya mafunzo haya lazima yafanane na VETA, Wizara inaona kwamba iko haja ya kuona kwamba mafunzo yanayotolewa katika vyuo hivi vya FDC yanakidhi uwezo wa wananchi hao kuweza kuyatumia kikamilifu kwenye kazi zao na hivyo siyo lazima yafundishwe kama ilivyo Vyuo vya VETA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hali hiyo, naona kwamba kwa siku za nyuma kulitokea na mkanganyiko kidogo wa kuona kwamba Vyuo vya VETA ni bora kuliko FDCs, lakini tungependa kuona kwamba FDCs zifanye kazi kwa malengo yake na VETA zifanye kazi kwa malengo yake, lakini vyuo vyote viimarishwe na kuweza kutoa mafunzo stahiki kwa walengwa wanaohusika.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALOSS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa suala la elimu ya juu ni suala la Muungano, je, wanafunzi wangapi katika idadi ya hao aliowataja wametokea Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, je, wanafunzi hawa wanaporudi masomoni hukuta ajira tayari au wanaachwa wanazurura mitaani?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kimsingi nafasi hizi za kusoma nje mara nyingi zinapotolewa zinatangazwa kupitia Balozi husika ambazo zimepanga kutoa masomo hayo, lakini wakati mwingine pia kupitia vyuo vyetu vikuu. Wakati wa uombaji suala linalozingatiwa zaidi ni sifa ikizingatiwa kwamba masuala ya elimu ya juu ni masuala ya Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia wakati mwingine inawezekana kabisa Ubalozi ukaamua kama umependa watu wa Zanzibar, basi utaelekeza moja kwa moja kupitia masuala ya kimahusiano kwa upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kimsingi kwa sasa sitaweza kukupa taarifa kamili na ikizingatiwa kwamba linahitaji data. Kwa upande wa ajira, hawa wanafunzi wakirudi, kwa sababu wengi wanakuwa wamepelekwa kwa ajili ya jambo mahsusi, kwa mfano, upande wa gesi, kwa hiyo wanapofika yale maeneo ambayo yanawahitaji ndiyo ambayo yanakuwa yametangaza kazi na wakati huo huo wenye sifa wanakuwa wanachukuliwa kupitia taratibu zetu za kiutumishi.
MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Suala la idadi ya wanafunzi ambao wametokana na bajeti linaendana na sifa za wanafunzi wanaotakiwa kujiunga na vyuo vikuu. Ningependa kuuliza swali dogo tu, kwamba, sasa hivi Serikali imetoa kauli mbili tofauti, mwezi Julai iliweka vigezo vya wanafunzi kujiunga na Chuo Kikuu vya GPA ya 3.5 kwa watu wa diploma, si zaidi ya hapo. Hata hivyo, juzi wametoa tena tamko lingine la GPA ya 3.0 kwa watu wa ordinary diploma. Je, Serikali itueleze hapa, ni kwa nini inawasumbua wanafunzi katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wengi walikuwa wameshakata tamaa na hawaku-apply katika Vyuo Vikuu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, kama ambavyo siku Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania analihutubia Bunge; alisisitiza kwamba Awamu hii ya Tano, jukumu lake kubwa litakuwa ni kuongeza ubora. Vile vile lazima ikumbukwe kwamba, Serikali kwa kushirikiana na wananchi imefanya kazi kubwa ya kuwezesha wanafunzi wengi kusoma na kiasi kwamba tunao wengi wenye sifa za ufaulu wa juu. Hiyo imejidhihirisha wazi hata katika udahili wa mwaka huu wa Vyuo Vikuu, waombaji ni wengi na waliofaulu ni wengi sana kiasi cha kupandisha zile points ili tuweze kuendana na haki katika kuwachukua.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika suala hilo katika maeneo hayo pia kuna ushindani mkubwa, lakini Wizara kila wakati inaangalia kama hao watu wenye sifa hizo itaonekana kwamba hawapatikani hapo ndipo tunaweza tukafikiria zaidi namna ya kusema tushuke chini, lakini kama wanapatikana basi hamna haja ya kumchukua mtu ambaye ana ufaulu wa chini ukamuacha mtu ambaye ana ufaulu wa kiwango cha juu.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri naomba niulize swali moja la nyongeza.
Pamoja na kufanya kazi nzuri ya kupatikana kwa wafanyakazi hewa ambao takribani wataokoa zaidi ya shilingi bilioni kumi na Serikali inapaswa ijazie hizo nafasi kutokana na watumishi wengine. Lakini walio wengi ni wale wanavyuo ambao sasa wanakwenda kuanza vyuo, lakini mpaka leo tunavyozungumza hawajapata mikopo wanahangaika. Je, kuendelea kutokuwapa mikopo hatuoni kwamba tunaweza tukazalisha hewa nyingine zaidi? Sasa Serikali iseme mpango mzima kwa nini mpaka leo mikopo ya wanafunzi baadhi hawajapata?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo imekuwa ikisisitizwa katika nyakati tofauti tofauti ni kwamba kimsingi fedha kwa ajili ya mikopo kwa awamu hii zilishatolewa jumla ya shilingi bilioni 80 na tayari bajeti yake ipo sawa. Suala lililokuwa limetuchelewesha lilikuwa ni suala la uhakiki kwa misingi kwamba watu wanaohitaji mikopo sio wote watakaoweza kupata kwa sababu fedha ambayo inatolewa ni kwa ajili ya watu wale ambao hasa wana uhitaji wa kupita wenzao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikisema hivyo nina maana kwamba tumeangalia mikopo tu, lakini Serikali kupitia Wizara ina majukumu mengine makubwa sana ya kuangalia mfano tumeona vijana wetu wengi walikuwa wanakaa katika maeneo ambayo walikuwa wakijipangia wenyewe, mabweni yalikuwa yanakuwa hayapo, vitendea kazi vingine vilikuwa viepungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi tunavyoangalia katika utoaji wa elimu tunaangalia Nyanja zote na haswa katika kuona kwamba elimu inatolewa kwa kiwango kinachostahili na kwa haki inayostahili mwanafunzi kuipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa misingi hiyo wale wote ambao wanastahili kupata mikopo kutokana na uhitaji uliopimwa, mikopo yao itapatikana, lakini hata hivyo lazima tuzingatie kwamba mikopo hiyo inamfikia mlengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naamini ndani ya wiki hii tutakuwa tumefikia mahali pazuri zaidi. Ahsante
MHE. ALLY M. KEISSY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa mara ya kwanza Serikali kutoa jibu zuri la kuridhisha kwa wananchi wa Nkasi.
Kwa kuwa aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa John Pombe Magufuli aliniahidi mimi humu Bungeni kwamba mara baada ya kukamilika ile barabara yuko tayari kutoa yale majengo kwa Chuo cha Ufundi VETA. Na sasa barabara yetu inakwenda speed ya ajabu, imebaki kilometa 10 au 12 na wakandarasi wameniahidi Januari au Disemba kipande cha barabara hiyo kitakamilika.
Je, lini sasa mazungumzo kati ya Wizara ya Elimu na Wizara ya Ujenzi yataanza haraka iwezekanavyo wananchi wapate kile chuo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wake tumeupokea, na mara baada ya kumaliza Bunge hili, tutawasiliana na wenzetu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ili tuweze kuona suala hili kabla hata barabara hazijaisha.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, kuna majengo ambayo yalikua yanatumika na Halmashauri ya Karatu, na sasa Halmashauri imehamia kwenye majengo mapya na huku nyuma kulishakuwa na azimio la Baraza la Madiwani kwamba majengo yale yatumike kama Chuo cha VETA.
Je, Serikali iko tayari sasa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kutumia yale majengo ya zamani ili kuweza kufungua chuo cha ufundi VETA?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi, nilipokuwa najibu swali la Mheshimiwa Keissy nilijibu kwa confidence kwa sababu majengo hayo ninayafahamu, nikiwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa na mimi mwenyewe pia nilishiriki kuona kwamba yangefaa kutumika hivyo. Sasa katika hili ambalo umenifahamisha kuhusu majengo ya Karatu, naomba tuweze kuyaangalia kwanza kabla sijatoa majibu. Kwa hiyo, tutafanya utaratibu wa kuja kuyaona.
MHE. OMARY A. BADWEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa yalikuwepo makubaliano kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi miaka minne iliyopita ya kufungua Chuo cha VETA katika Wilaya ya Bahi, katika kijiji cha Kigwe na yako majengo yaliyokuwa ya Chuo cha Kilimo ya Halmashauri na Wizara iliomba ipewe majengo yale ili iweze kufungua chuo cha VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Bahi kupitia kikao cha Madiwani miaka mnne iliyopia iliyakabidhi majengo yale kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, na Naibu Waziri wakati huo Mheshimiwa Mulugo alikwenda kutembelea majengo yale na akayakubali kwamba yanafaa kufunguliwa Chuo cha VETA. Lakini hadi sasa miaka mnne imepita majengo yale yamekaa bure, Wizara haijarudi tena.
Je, ni lini sasa Wizara itarudi pale kuendelea na mchakato wake wa kufungua chuo cha VETA katika Halmashauri ya Bahi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu kwa pamoja kwa Waheshimiwa Wabunge wote ambao wanaona kuna majengo yanayostahili kuweza kutumika kama sehemu za kuweza kutolea mafunzo ya ufundi, wanipe taarifa hizo ili tuweze kuyatathimini kwa pamoja na hivyo kuwezesha sisi kupanua wigo wa kuongeza vyuo vya kutolea mafunzo ya ufundi katika nchi yetu, ikizingatiwa kwamba hata hivyo uhitaji ni mkubwa lakini imekuwani ngumu kwetu kuweza kujenga VETA kwa Wilaya zote kwa wakati mmoja.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nianze kushukuru kwa ajili ya majibu, vilevile maandalizi ya ujenzi wa hiki Chuo cha VETA, Mkoa wa Geita ni wa muda mrefu, ni tangu awamu iliyopita, lakini mpaka sasa ujenzi haujaanza. Ningependa kujua Mheshimiwa Waziri amesema utaanza hivi mapema, ni lini? Je, ni katika mpango wa mwaka huu wa 2016/2017?
Swali la pili, kwa kuwa tunaelekea kwenye viwanda, Awamu ya Tano ni awamu ya viwanda na vijana wetu hasa katika Mkoa wa Geita na Wilaya ya Geita hawana ujuzi kabisa, Serikali inasemaje kuanzisha program maalum kupitia SIDO, kwamba vijana wetu sasa waanze kuelimishwa ili viwanda vikianza waweze kuajiriwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kumshukuru kwa shukrani alizotupa. Pili, nikubaliane naye kwamba mchakato huu umeanza muda mrefu, hata hivyo tunapozungumzia kuanza kwa ujenzi, nina maana ni hatua zote zinazohusika ili kuwezesha ujenzi huu. Kama ambavyo tumekuwa tukizungumza hapo awali, chuo hiki kinategemewa kujenga kwa fedha za mkopo kutoka ADB, kwa hiyo, kuna taratibu ambazo lazima zifuatwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza la muhimu ilikuwa ni kupata hati na kiwanja ambacho kiko mahali pazuri ambapo wanachuo wengi watapenda kwenda hapa na pia itakuwa rahisi kufikika kazi hiyo imekamilika, sasa hivi tunaendelea na hatua za kumpata mshauri elekezi, tunaamini hatua hizi hazitakuwa na utata mkubwa kwa sababu ziko wazi na zinakwenda kwa taratibu zilizopo tukishakamilisha ndipo tukakapoanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kuhusiana na tatizo la upungufu wa wataalam hasa katika azma ya kwenda uchumi wa viwanda. Ni kweli kabisa vijana wetu wengi wanamaliza darasa la saba, form four na vyuo, wanahitaji ujuzi. Kupitia ziara hiyo niliweza kutembelea maeneo mbalimbali vikiwemo Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi ambavyo navyo vinaonekana kuwa na mchango mkubwa katika kutoa mafunzo haya ya ufundi. Wizara tumeshajipanga kuona kwamba vyuo hivyo vinakarabatiwa na kuongezewa vifaa ili vijana wengi zaidi waweze kunufaika.
MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Matatizo yaliyopo kwenye hii Wilaya ya Busanda yanafanana kabisa na yale yaliyoko katika Wilaya ya Liwale. Wilaya ya Liwale hatuna Chuo cha Ufundi, je, ni lini Serikali itatujengea Chuo cha Ufundi Wilayani Liwale?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Liwale wanahitaji chuo, lakini kwa bajeti ya mwaka huu Liwale haimo katika vyuo vitakavyojengwa. Ninachoshauri kwa sasa ,wale wanafunzi wote wanaohitaji kupata mafunzo haya ya ufundi waende pale katika vyuo vyetu ambavyo viko tayari na chuo ambacho kina uwezo wa kuchukua wanafunzi wengi pale Mtwara na watapata mafunzo yanayostahili.
MHE. JUMAA H. AWESO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa, tatizo la ukosefu wa Chuo cha Ufundi katika Wilaya ya Geita inafanana kabisa na Wilaya yangu ya Pangani. Je, ni lini Serikali itahakikisha kwamba inatujengea Chuo cha Ufundi kwa sababu vijana wa Pangani wanashindwa kunufaika na rasilimali zilizopo katika Wilaya yangu ya Pangani?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwa Wilaya nyingi, ambazo zina uhitaji mkubwa wa kuhitaji kupata vyuo hivi vya VETA, niseme tu kwamba, tayari bajeti ya mwaka huu Waheshimiwa Wabunge wote mnayo na vyuo vitakavyotekelezwa vimo. Kwa hiyo, kama Wilaya yoyote ile imo katika orodha ya vyuo vinavyoanza kutekelezwa, basi ajue kwamba tupo katika kutekeleza mpango huo na kama haipo basi tunaendelea na michakato ya kupata ardhi ili na vyenyewe viweze kuwa katika mpango.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tumegundua kwamba kwa muda mrefu fedha ambazo zimekuwa zikitengwa kwa ajili ya vyuo imekuwa ni kidogo, mwaka huu baada ya kutembelea na kuona huu uhitaji mkubwa tulichojifunza ni kuongeza maeneo hayo ya bajeti katika vyuo vyetu hasa hivi vyuo vya ufundi vya Wilaya.
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na swali langu ni hivi, wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne, darasa la saba kwenye nchi hii na hata wanaomaliza kidato cha sita na wakashindwa kuendelea ni wengi mno na Serikali yenu hii imesema inataka kujenga viwanda, japo ni viwanda vya akina Bhakresa na tunajua tunahitaji ma-technician wengi sana kwenda kufanya kazi kwenye viwanda, makampuni na hata migodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri hebu atuambie ni lini kwa mipango yenu nchi nzima hii kutakuwepo na vyuo kwenye Wilaya, kwa sababu siyo kila siku tunasimama hapa tunauliza kwamba swali hili linafanana na la kwangu, lini mnataka muwe mmefikisha vyuo angalau kwenye Wilaya au tuvipeleke kwenye Kata kama shule za sekondari?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo amezungumzia katika suala lake, maudhui yake ya msingi kwamba kuna tatizo kubwa la mahitaji ya vijana kubakisha ujuzi. Ujuzi unapatikana katika staili za aina mbalimbali, mojawapo ni hiyo ya kuwa na vyuo maalum ikiwemo Vyuo vya Ufundi pamoja na Vyuo hivi vya Maendeleo ya Wananchi, pia tunavyo Vyuo Vikuu, ambavyo vyote vinatoa mafunzo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa kutambua mahitaji haya yalivyo mengi, kuna vijana wengine pamoja na watu wazima ambao siku zote wamekuwa wakifanya shughuli za ufundi, lakini wamekuwa hawatambuliwi. Tayari kwa kutambua hilo tunao mpango wa kutambua wale ambao wana ujuzi ambao hawakupitia katika maeneo rasmi na hiyo tukishawatambua wanapewa mafunzo ya ziada ya ujasiriamali na kuwawezesha kutambulika.
Vilevile kupitia mpango ambao ni wa kuwezesha vijana katika mafunzo mbalimbali ya ufundi, hivi juzi tarehe 28 nimezindua tena mpango wa pili wa kuwezesha vijana mbalimbali ambao wataweza kupata mafunzo, yakawezesha kujiajiri na kuwezesha kuhudumia hivi viwanda vidogovidogo kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wa Viwanda jana alivyoeleza ili waweze kufanya shughuli zao. Mpango huo utanufaisha vijana zaidi ya 22,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwa staili mbalimbali ambazo tunatumia tutaweza kuwafikia vijana wengi zaidi na kwa muda mfupi zaidi.
MHE. DKT. IMMACULATE S. SEMESI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa, kuna uhusiano chanya kati ya elimu na maendeleo katika sekta za kijamii na kiuchumi; je, ni lini Serikali au Wizara itaona umuhimu wa ku-link elimu na maendeleo ya Taifa letu au katika mipango ya maendeleo ya Taifa letu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuwa, tayari Serikali imeshachelewa kutathmini; je, tuna upungufu wa aina gani au tunahitaji watu wenye elimu ya aina gani ili kuleta maendeleo katika sekta fulani? Wameji-commit kwamba mpaka mwisho wa mwaka huu wa fedha watakuwa tayari wamekamilisha huo mkakati.
Je, huu mkakati watau-link vipi na Mpango wa Maendeleo wa Taifa hili?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kimsingi Serikali inatambua mahusiano kati ya elimu inayotolewa na ustawi wa jamii au katika kuleta maendeleo. Ndiyo maana msisitizo uliopo sasa hivi ni kuhakikisha kuwa, course zote zinazoanzishwa hasa katika vyuo vyetu, ni zile zinazojitahidi kujibu changamoto zilizopo katika jamii zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo basi, baada ya kukamilisha mpango huu ambao umeandaliwa, unaoangalia kwa kina sasa kwa jinsi ambavyo Mpango wetu wa Maendeleo wa Miaka Mitano lakini pia Dira yetu ya Taifa ya mwaka 2020 - 2025, kwamba tunataka kwenda wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, sasa hivi tunataka kwenda kwenye uchumi wa viwanda. Katika uchumi wa viwanda tutahitaji wataalam mbalimbali watakaoendesha viwanda vyetu, vilevile katika hao watakaoendesha viwanda tunategemea humo kutakuwa na mambo ya aina mbalimbali. Kwa mfano, afya zetu ili hao watumishi waweze kufanya kazi zao vizuri. Pia tunategemea kupunguza madhara kwa akinamama waweze kujifungua salama. Kwa hiyo, kutokana na matatizo kama hayo, ndiyo maana hata sisi sasa mitaala yetu lazima ijibu changamoto ambazo zipo katika jamii.
MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo kimsingi yamejikita kwenye suala la msingi.
Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ni dhahiri kwamba kupitia miongozo ya Serikali juu ya mishahara na posho za waendeshaji na hata walimu wa vyuo vikuu Tanzania, ni kwamba iko mikondo mathalani PGSS 13, PGSS 14, PGSS 15, hizi ni kada ambazo zinapaswa kuongozwa na waendeshaji kwa maana ya kwamba siyo academicians. Practice iliyopo sasa hivi ni kwamba viwango hivi vya mishahara havitumiki kwenye kada husika kwa kuwa nafasi hizi za uongozi wa juu ni kwamba unaongozwa na academicians.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kutafsiri kiwango cha mshahara PGSS 13 ambayo inashikiliwa na Wakurugenzi ambao ni wanataaluma PGSS 14 na PGSS 15 ili viwango hivi viweze kutumika kwa waendeshaji wa vyuo vikuu au taasisi za elimu ya juu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi niende tu katika ufafanuzi wa ziada kwamba baada kuona kwamba kuna malalamiko aina hiyo na mengine kwa kweli katika vyuo vyetu mbalimbali hasa vyuo vikuu, Wizara kwa kuzingatia hilo, mwezi huu wa kumi ulioisha tumeunda vikundi kazi (team) kwa ajili ya kufuatilia hayo mambo yote katika vyuo vyetu vyote vikuu vikiwemo vyuo binafsi ili kuona kwamba kwanza vinaendeshwa kwa mujibu wa sheria, lakini pili uongozi unapangwa kutokana na taratibu na sifa zinazostahili, vilevile kuangalia miundombinu na maslahi kwa ujumla yanayohusu viongozi wa ngazi hizo kama yapo sahihi au hayapo sahihi. Bila kusahau hata watumishi wengine ambao hawaonekani kama ni watumishi muhimu (supporting staffs), kama wapishi, kuona kwamba je, chuo kinaweza kujiendesha kiuhalali au laa!
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nizidi tu kusema haya mapendekezo yako, unayozungumza nayo yatazingatiwa katika kutafakari masuala hayo.
MHE. DKT. ELLY M. MACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kusema tu kwamba sikuridhika kabisa na nina hakika watu wenye ulemavu hawakuridhika kabisa na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo ameyatoa. Ina maana kwamba kwa kutokuwa na miundombinu au kutokuwa na watumishi ni sababu ya kutosha ya kusababisha vyuo vifungwe kwa miaka mingi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la kwanza. Naomba Mheshimiwa Naibu Waziri atupe concrete sababu kwa nini vyuo vimefungwa na vitafunguliwa lini, atupatie time frame.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, hawa watumishi ambao anasema wanatayarishwa, tunahitaji muda gani kuwatayarisha hawa watumishi kwa sababu watu wenye ulemavu wamekuwepo na vyuo vimekuwepo miaka mingi lakini vimefungwa kwa miaka mingi na inaonekana kama ni business as usual but it is not business as usual. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kimsingi, pamoja na kufungwa kwa vyuo hivyo jambo ambalo tayari limeshatolewa ufafanuzi namna gani litafanyika, kupitia mfumo wa elimu jumuishi sasa hivi vyuo vyote vya ufundi ikiwemo VETA, FDC lakini hata shule zinazotoa mafunzo ya ufundi tunahakikisha kwamba tunazingatia namna tunavyoweka miundombinu na namna ya kufundisha kwamba watu wenye ulemavu wanazingatiwa. Hao nawazungumzia hasa wale vijana wenye umri wa kuweza kuingia katika vyuo hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niseme tu kwamba, kwa hali ya sasa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia lakini pia kupitia ngazi zetu za juu kama tulivyoona Ofisi ya Waziri Mkuu, tunahakikisha kwamba walemavu wanapewa kipaumbele cha hali ya juu na yeye atakuwa shahidi hata sasa tunapotoa kwa mfano karatasi zetu humu Bungeni au taarifa zozote lazima tuzi-print kwa nukta nundu na mambo mengine. Kwa hiyo, walemavu wanapewa fursa nyingi na tunawajali kupita kiasi katika kila ngazi. Naomba atuvumilie aone namna ambavyo tutaweza kuendelea katika kuhakikisha tunarekebisha hali ambazo zipo.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa changamoto katika suala zima la elimu na hasa elimu jumuishi kwa watu wenye ulemavu ni kutokana na uhaba wa walimu katika vyuo mbalimbali hasa vyuo vikuu hapa nchini. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba katika vyuo vyote vikuu hapa nchini vinakuwa na programu mahsusi kabisa kwa ajili ya kuwafundisha walimu watakaokwenda kuwafundisha wanafunzi wenye ulemavu hapa nchini ili tuondokane na tatizo hili la uhaba wa walimu pamoja na kuhakikisha kwamba ajira zinakuwepo kwa watu wenye ulemavu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza ili kufanikisha hilo, kwa mfano ukiangalia katika utoaji wa mikopo safari hii watu wenye ulemavu wote kwa ujumla wake bila kujali fani anayochukua wamepewa mikopo. Pili, tunacho chuo maalum, Chuo cha Patandi - Arusha ambacho ni kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa walimu ambao wanaenda kuwafundisha wanafunzi wenye ulemavu. Hali kadhalika, kwa upande wa vyuo vikuu tunayo maeneo ambayo yanahusika katika kuzingatia ufundishaji wa walimu kwa ajili ya watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla wake niseme tu kwamba eneo hili ni pana sana kwa sababu linahitaji walimu wa aina tofauti tofauti kwa ajili ya kufundisha watu wenye ulemavu wa aina tofauti tofauti. Kwa hiyo, ukiwachukua kwa ujumla wake useme kwamba walimu wenye ulemavu labda 200 ukafikiria ni wengi, hawatakuwa wengi kwa sababu mahitaji ya wale wanaoenda kuwafundisha inakuwa wanafunzi ni wachache katika eneo fulani lakini yale maeneo ni mengi sana. Kwa hiyo, juzi tu mimi mwenyewe nimefuatilia pale Patandi na kuona ni jinsi gani tutaweza kurekebisha hasa miundombinu na kuwawezesha walimu wengi zaidi. Ahsante.
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mawaziri, kuna hivi vyuo viwili Chuo cha Yombo na Chuo cha Singida, pamoja na uwepo wa vyuo hivi viwili lakini bado kuna changamoto nyingi sana ambazo zinavikabili vyuo hivi. Naomba niongelee specific Chuo cha Yombo kwa sababu ni chuo ambacho nimekitembelea. Chuo hiki kina changamoto ya deni kubwa la umeme, miundombinu chakavu pamoja na vifaa vya kujifunzia na kufundishia. Naomba nisikie kauli ya Serikali ni hatua gani za haraka na za makusudi za kunusuru vyuo hivi ili visije vikafungwa kama ambavyo vimefungwa hivi vyuo vingine? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa upande wa chuo hicho nikiri pia hata mimi nimewahi kukitembelea kilikuwa na upungufu fulani lakini kama ilivyozungumzwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ni kwamba kimewekwa kwenye bajeti. Hata hivyo, kwa mwaka huu wa fedha tayari Wizara ya Elimu tulikuwa tumeagiza vifaa kwa ajili ya watu wenye ulemavu vya gharama ya shilingi takribani bilioni tatu na tayari vimeshawasili. Kwa hiyo, tutaangalia katika ugawaji na wao waweze kufikiriwa. Ahsante.
MHE. JAKU HASHIM AYOUB: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na kutotaka kuniona naomba niulize maswali madogo sana mawili ya nyongeza na niombe Waziri wa Fedha awe tayari kumsaidia Naibu Waziri. Ninachozungumza ni Kiswahili wala si Kihindi. Waziri wa Fedha ningeomba akainuka yeye maana hili swali linamhusu yeye. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge ni chombo kizito cha Tanzania na Watanzania wametutuma ili tuyasemee matatizo yao. Mheshimiwa Naibu Waziri au Waziri atakuwa yuko tayari kujiuzulu pindi nikimletea ushahidi wa kutosha juu ya suala hili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kujiuzulu pindi nikimletea ushahidi wa kutosha juu ya kadhia hii kwa vijana wa Tanzania kutozwa fedha za kigeni katika vyuo hivyo na anajibu hapa hamna? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, je, amefanya utafiti kwenye vyuo gani mpaka akatueleza hakuna utaratibu wa kutoza fedha za kigeni ili Bunge lako liweze kuridhia tatizo hili? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, swali la tatu, hakuna sheria…
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu yeyote anayekuwa hatendewi haki kwa mujibu wa sheria anayo fursa ya kuchukua hatua. Hatua mojawapo ni pamoja na kutoa taarifa kwa ngazi zinazohusika. Ndiyo maana nimesema kwamba kwa kipindi chote hiki Wizara yetu haijaweza kupata taarifa na hata wewe ulivyoendelea kuuliza umeshindwa hata kutuambia mfano wa chuo ambacho kinafanya hivyo. Kwa misingi hiyo, mimi nachukulia hilo suala halipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusiana na kufanya utafiti, ni sawa, ni jambo jema, hilo nalichukua kuendelea kulifanyia kazi.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili limekuwa likijirudia mara nyingi na naomba nitoe maelezo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Kigeni ya mwaka 1992 inamruhusu mtu yeyote kupokea na kumiliki na kutumia fedha za kigeni kwa shughuli za kiuchumi. Kwa hiyo, hao wenye shule siyo kwamba hawaruhusiwi, hilo la kwanza tuelewane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Sheria ya Benki Kuu ya mwaka 2006 inaweka bayana kabisa kwamba legal tender ya nchi yetu ni Shilingi ya Kitanzania. Nilikwishalieleza Bunge lako Tukufu kwamba ni makosa kwa mtu yeyote kukataa Shilingi ya Tanzania kwa malipo hapa nchini. Kwa hiyo, narudia tena, pale ambapo kuna Mtanzania yeyote anakwenda kulipa ada au malipo mengine akadaiwa kwa dola lakini yeye akatoa Shilingi za Kitanzania akakataliwa, atoe taarifa mara moja ili tuchukue hatua za kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine Benki Kuu tumeshafanya utafiti na nilikwishalitolea taarifa hapa ni 3% tu ya shughuli mbalimbali ambazo wana-quote bei zao kwa dola. Kwa hiyo, kosa ni kukataa shilingi kosa sio ku-quote bei zao kwa dola.
MHE. ALLY SALEH ALLY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Zama hizi si rahisi kukataa kuja kwa wawekezaji kuwekeza katika shule za kigeni na vyuo vikuu mfano ni Shule za Sekondari kama Feza na nyinginezo. Serikali haioni kuna haja kwa utata huu unaotokezea, kwa mfano Chuo cha KIU, Chuo Kikuu cha Zanzibar kiliwahi kutoza kwa dola na Serikali inasema haijui kuwa na sera ya vyuo au shule zinazokuja hapa ili waelewe nini wafanye na nini wasifanye ikiwa ni pamoja na kutolazimishwa na nchi za kigeni kufunga shule kwa sababu ya maslahi yao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi vyuo vyote vimeshaelekezwa na vimejua nini wajibu wao kufuatana na kanuni na taratibu na sheria hizi. Labda jambo ambalo naweza nikalichukua ni kuendelea kuvikumbusha vyuo kama ambavyo tumekuwa tukifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutumia nafasi hii niombe tu kuvisisitiza vyuo pamoja na kwamba wanao uhuru huo wa kuweza kutumia fedha za kigeni lakini suala liwe ni kwamba mwananchi wa Tanzania sarafu yake ni Shilingi ya Kitanzania. Kwa hiyo, hiyo ipewe kipaumbele badala ya kutoa kipaumbele kwa fedha za kigeni.
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukarabati unahitaji fedha za kutosha na Chuo Kikuu cha Mzumbe kwa muda mrefu kina madai halali sana kutoka Serikalini ambapo chuo kinaidai Serikali kama vile fedha za ada kutoka Bodi ya Mikopo. Fedha hizi zingeletwa mapema zingeweza kusaidia kufanya ukarabati. Je, ni lini sasa Serikali itaweza kulipa madeni haya ili Chuo Kikuu cha Mzumbe kiweze kufanya marekebisho haya madogo madogo na kukifanya chuo hiki kiweze kuwa na muonekano mzuri kuliko ilivyo sasa hivi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kama ambavyo amezungumza Mheshimiwa Mbunge Dkt. Jasmine ni kweli kuna umuhimu mkubwa sana wa kufanya marekebisho katika chuo hiki, lakini pia katika suala la ada kuna wakati tulikuwa tumeagiza vyuo vyote kufanya uhakiki hasa kwa wale wanafunzi ambao walikuwa hawastahili kupata mikopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, Mheshimiwa Waziri wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako, alishatoa maagizo kwamba Bodi ya Mikopo ipeleke fedha hizo wakati uhakiki ukiwa unaendelea ili wasikwamishe shughuli zinazoendelea. Kwa hiyo, naamini muda wowote ule hizo fedha watakuwa wamezipata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imedhamiria kuona kwamba vyuo vyote vikuu vinaongezewa fedha ili kuongeza udahili unaostahili kwa wanafunzi ili kwenda kusoma kwenye chuo binafsi iwe ni hiyari zaidi ya mwanafunzi kuliko kuwa ni sababu ya kukosa nafasi katika vyuo vyetu vya Serikali. Kwa hiyo, naamini mpango huu ukikamilika hali itazidi kuwa nzuri zaidi kwa vyuo vyote ikiwepo Mzumbe.
MHE. SUSAN J. A. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Katika siku hizi za karibuni, Tanzania tumepata sifa kubwa sana ya kuwa na chuo kikubwa sana Afrika Mashariki na Kati, Chuo Kikuu cha Dodoma; na chuo hiki kinaweza kuchukua takribani wanafunzi 40,000. Kwa mshangao mkubwa sana, leo Serikali ya Chama cha Mapinduzi imeamua kufanya Chuo Kikuu cha Dodoma kuwa sehemu ya majengo ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua, Serikali kwa kuleta utaratibu wa kubadili au wa kuchanganya wanafunzi na majengo ya Serikali (Wizara), maana yake ni kwamba tunachukua wanafunzi wetu kuwapekeleka kwenye simba. Nataka kujua huu ndiyo utaratibu wa kuhamia Dodoma kwa maana ya kubadilisha miundombinu ya elimu kuwa Ofisi za Serikali? Naomba majibu.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumfahamisha Mheshimiwa Suzan Lyimo kwamba pamoja na hayo aliyoyazungumza, ukweli ni kwamba chuo maana yake siyo majengo peke yake. Chuo maana yake ni majengo, Walimu pamoja na vitendea kazi vingine vya kufundisha na kufundishia. Kwa hali hiyo Chuo cha UDOM kilipojengwa kilijiwekea utaratibu wa namna gani kitakuwa kinakua sambamba na majengo. Kwa hiyo, kwa taasisi au Wizara kuhamia katika majengo haya ni kwa vile ni suala la muda mfupi na kwa sababu majengo hayo yalitokana na…
Kulingana na utaratibu na mipango yake ya kukua yalikuwa kwa sasa hayatumiki. Wizara zinatafutiwa maeneo yake ya kujenga, CDA wakishakamilisha kuleta viwanja hivyo, kila Wizara itakuwa na majengo yake katika eneo lake.
Kwa hiyo, niwaombe tu kwamba suala la kuhamia Dodoma, sisi kwetu tunaona ni suala lenye tija na litaongeza ufanisi mkubwa hasa kwa wananchi wetu kwa sababu sasa watakuwa wanapata huduma kiurahisi zaidi, ikizingatiwa kwamba Dodoma hata foleni hakuna na ni Makao Makuu ya nchi. Kwa hiyo, sisi Wizara tumejipanga na tutahakikisha kwamba tutahamia kwenye maeneo yetu muda ukifika.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa hapa ndani ya Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba nia ya Serikali katika kukiendeleza Chuo cha Dodoma ilijidhihirisha kutokana na nia njema ya Chama cha Mapinduzi kutoa ukumbi wake na kubadilisha matumizi kutoka kwenye matumizi ya Chama kuwa Chuo Kikuu cha Watanzania wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hatua hiyo hiyo ya nia njema ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi, tunaendelea na mpango wa Taifa wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya kuhamishia Serikali Dodoma. Naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge Majengo yatakayotumika na Serikali ni majengo ambayo Serikali ya Chama cha Mapinduzi ilishayajenga na yakawa mengi. Kwa sababu majengo yale ni mengi na yamejengwa na Serikali hii, badala ya kuyaacha yaharibike bila kutumika, yatatumika na baadhi ya Wizara za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, majengo yale hayaingiliani na shughuli zozote za elimu pale UDOM. Nawahakikishia Watanzania wote, nazipongeza Wizara hizo kwa kuyalinda kwa kuyatumia majengo hayo.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwanza, naishukuru Wizara ya Elimu iliweza kutoa fedha kwa ajili ya ukarabati wa Chuo cha Ualimu pale Korogwe ambapo kilileta wanachuo karibu 800 na kitu kwa ajili ya mafunzo pale. Hata hivyo, naiomba Serikali, kwa kuwa chuo kile kina maktaba ndogo na sisi wananchi tumeweza kujenga maktaba kubwa ambayo ingeweza kuwasaidia wanachuo ambao ni wengi sasa pale chuoni, pamoja na wananchi wa Korogwe kwa ujumla: Je, Serikali itakuwa tayari kutupa fedha ili tuweze kukamilisha lile jengo la maktaba?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Chatanda kwa kufuatilia masuala ya kielimu na Mheshimiwa Mbunge anapofanya jitihada kama hizo sisi Serikali tunao wajibu wa kusaidia. Kwa hiyo, tutachukua hilo jukumu la kusaidiana nao kuhakikisha maktaba hiyo inakamilika vizuri.
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi, nami naomba niulize swali dogo la nyongeza kuhusu Chuo Kikuu cha Mzumbe. Kwa kuwa Serikali inaongeza wanafunzi kila mwaka; na kwa kuwa kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipokuja Mzumbe kwamba Serikali itatoa fedha kwa ajili ya Ofisi za Walimu na nyumba za wafanyakazi; na kwa kuwa ahadi hiyo hadi leo haijatekelezwa.
Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne pamoja na kuongeza nyumba za watumishi pale main campus Mzumbe?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo ilielezwa hapo awali, niseme tu kwamba katika Vyuo Vikuu ambavyo vina kipaumbele katika uongezaji wa miundombinu kwa mwaka huu unaokuja wa fedha 2017/2018 ni pamoja na Chuo Kikuu cha Mzumbe. Kwa hiyo, naomba ajue hilo.
MHE. HALIMA ALI MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri.
Kwa kuwa kuna malalamiko makubwa yanayohusiana na kubainika kwamba kuna rushwa ya ngono katika vyuo vyetu, jambo ambalo linapelekea wasichana wengi kupata ufaulu mdogo, lakini vilevile wasichana wengine kutoroka shule, lakini kama haitoshi kuna wasichana ambao wamefanya maamuzi ya kujiua na ushahidi upo. Sasa je, Serikali ina mkakati gani wa kufanya utafiti ni kiasi gani wasichana wameathirika na rushwa ya ngono?(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wasichana wetu wanapatiwa elimu kuhusiana na rushwa ya ngono?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli taarifa hizo za rushwa za ngono zimekuwa zikisikika na hata hivi karibuni ilijitokeza taarifa ya aina hiyo kwa mwalimu mmoja ambaye ameendelea kuchukuliwa hatua na niseme tu kwamba suala la kufanya utafiti ni suala jema, mimi nichukulie kwamba ntalichukua ili kujifunza tatizo hilo kwa undani zaidi. Lakini niwaombe pia wanafunzi wa kike kutoa ushirikiano, lakini pia hata wanafunzi wa kiume wanaweza kusaidia kutoa ushirikiano kwa mambo ambayo yanajitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili katika suala la elimu, sisi wenyewe tumekuwa tukiongea na wanafunzi kupitia wakati tofauti tofauti tunapowatembelea, lakini pia nafahamu kuna taasisi mbalimbali zinazoshughulika na masuala ya kijinsia zimekuwa zikiendelea kuelimisha. Niwaombe pia hata Waheshimiwa Wabunge mnapopata nafasi muweze pia kuongea na wasichana hao ili kuweza kusaidiana kwa pamoja kuona kwamba wote tunakuwa pamoja katika kupigana na kupambana kwamba rushwa za ngono zisipatikane katika shule na hata katika maeneo ya kazi.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Suala la ufaulu wa watoto wa kike elimu ya juu inategemea na ufaulu wa watoto haohao wa kike kwenye shule za chini (O-Level na A-level), sasa kumekuwa na tatizo la watoto wa kike wanaobeba mimba wakiwa shuleni kuachishwa masomo, na hili tumekuwa tukilizungumza muda mrefu; ni lini Serikai italeta utaratibu hapa Bungeni, sheria itungwe ili watoto wa kike wanaobeba mimba shuleni wakishajifungua waruhusiwe kuendelea na shule?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hilo limezungumziwa katika nyakati tofauti tofauti, hivi karibuni pia tulipitisha mpango wa kushughulikia masuala yoyote yanayohusika na unyanyasaji kwa watoto wa kike na suala hilo limekuwa likishughulikiwa mia na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na tayari rasimu ya mwanzo ya mwongozo imeshatoka namna gani tufanye na pia niliweza kwenda kutembelea Zanzibar kuongea na Mheshimiwa Waziri kule kuweza kujua wenzetu wamekuwa wakifanya vipi katika eneo hilo, tukajifunza changamoto ambazo zilikuwa zinajitokeza kwa upande wao kwa mfano mwingine anaweza akasema anapata mimba na aliyempa mimba akasema anataka kumuoa katika mazingira kama hayo. Lakini mwisho wa yote tunaamini kwamba tutaweza kutekeleza kuona kwamba fursa zinatolewa kwa mtoto wa kike aliyepata mimba kuweza kurudi shuleni.
Changamoto tu ni namna gani, je arudi kwenye shule ileile, je unyanyapaaji utakuwepo au apewe shule maalum, ndiyo hayo ambayo wadau mbalimbali wanaendelea kutoa mawazo lakini mwisho wa yote tutatekeleza mapema iwezekanavyo.
MHE. AMINA S. MOLELL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Katika vyuo vikuu suala la miundombinu kwa watu wenye ulemavu ni tatizo, na mfano katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni moja ya changamoto inayochangia wanafunzi wengi hasa watoto wa kike katika kwenda madarasani na hata katika suala zima la mitihani ni tatizo kwao kutokana na changamoto mbalimbali zilizopo. Je, Serikali inatoa kauli gani na hasa kwa kuzingatia chuo hiki ni kikongwe, lakini mpaka leo miundombinu bado ni tatizo na ni kikwazo kwa watu wenye ulemavu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa mujibu wa sera kwa ajili ya watu wenye ulemavu, inazungumzia kuwawekea mazingira bora ya kujifunzia na kufundishiwa. Kwa hali ya sasa ni kwamba tunayo majengo ambayo yamejengwa zamani na unakuta kweli yana changamoto ya miundombinu, lakini tunachofanya ni kwamba tunashauri madarasa yale yenye wanafunzi wenye ulemavu wahakikishe yanakuwa ni yale yanayofikika, kwa mfano kama darasa lina mwanafunzi mwenye ulemavu ni vyema likachaguliwa lile ambalo liko katika ground floor ili mwanafunzi yule aweze kufika darasani bila usumbufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa majengo yote mapya yanayojengwa tumeagiza kwamba lazima kila jengo liwekewe miundombinu inayomuwezesha mtu mwenye ulemavu kufikia katika eneo lolote analohitaji kuishi au kujifunzia na hivyo imekuwa ikifanyika na ni rai yangu kusema kwamba hata hiyo miundombinu inayowekwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu iwe ni ile inayozingatia viwango vinavyohusika, kwa sabau sasa hivi unakuta kwamba kuna shule zinapokaguliwa ili zionyeshe miundombinu yenye ulemavu zinaweza zikaonesha tu kwamba kuna lile tuta (rump) limewekwa pale lakini unakuta jinsi ambavyo limewekwa lina msimamo mkubwa kiasi kwamba hata huyo mtu mwenye ulemavu anapata shida, kwa hiyo lazima kuzingatia viwango vinavyohusika katika kuweka miundombinu ya watu wenye ulemavu ikiwemo kuweka lifti. ahsante.
MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kupewa
nafasi niweze kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu
mazuri ya Serikali nina maswali mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, kwa kuwa lengo la Serikali ilikuwa ni
kujenga VETA kila Wilaya ili vijana wetu waweze kupata mafunzo, vijana ambao
wanakuwa wameshindwa kuendelea na vyuo vikuu na kadhalika. Je, sasa
Serikali imejipangaje kuhakikisha inakamilisha azma yake iliyopanga ya kujenga
chuo cha VETA kila Wilaya?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, pamoja na majibu mazuri kama
nilivyosema ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali kwa majibu yake imesema kule
Njombe tuna Chuo cha Ulembwe pale ambacho kinamilikiwa na Wilaya yetu ya
Njombe. Je, Serikali sasa kwa majibu haya imejipangaje kuhakikisha chuo hiki
kinaboreshwa kama walivyosema ili wananchi wa Wilaya ya Njombe hususan
pamoja na Jimbo la Makambako, vijana hawa waweze kwenda kusoma chuo
hiki cha VETA ambacho kiko pale Ulembwe?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika,
ahsante sana. Serikali imeendelea na hiyo mikakati, lakini niseme tu kwamba
kujenga chuo kimoja cha VETA ni gharama. Kwa hiyo, kwa kutumia fursa hii
kwamba Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDC’s) navyo sasa hivi
vimerudishwa katika Wizara yetu. Tunaangalia katika Wilaya ile ambayo ina chuo
cha aina hiyo basi kiweze kuboreshwa na kiweze kuchukua nafasi ya mafunzo
ambayo yatakuwa yanatolewa yanayowahusu wale wananchi wote bila kujali
sifa zao ili mradi wana akili timamu lakini hali kadhalika kwa wale ambao
wanahitaji mafunzo yale yanayofanana na yanayotolewa katika VETA yaweze
kupatikana, tayari tumeshaanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika Mkoa wa Kagera, chuo cha
Gera tayari sasa hivi kimeshafanyiwa ukarabati, lakini pia Rubondo tumeshaanza
kufanya ukarabati, kuna Kibondo, Kasulu na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwa upande wa Ulembwe tutahakikisha
kwamba chuo hicho kinaboreshwa. Niwafahamishe tu kwamba ili tusifanye kazi
ambazo hazina tija, tayari Wizara imeshapanga kukutana na Wakuu wa Vyuo
vyote vya FDC’s ili kuweza kukaa pamoja na kufahamu kwa undani changamoto
zilizowakabili kabla hatujatoa fedha za kwenda kukamilisha au kuanza uboreshaji
wa vyuo hivyo.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana
kwa kunipa fursa hii ili niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Serikali iliwahi
kutoa orodha ya Wilaya za kipaumbele za ujenzi wa vyuo vya VETA na katika
orodha ile Wilaya ya Mkinga ilikuwa ni miongoni mwa Wilaya hizo. Je, ni lini sasa
Serikali itatekeleza ahadi yake ya kujenga chuo kile kule Mkinga?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu
Spika, ni kweli Serikali inatambua hilo na hata tunapojibu maswali ya VETA
tunajua tutapambana nna swali la Mkinga. Nimfahamishe tu kwamba katika
vipaumbele vya Serikali bado Mkinga iko pale pale. Tukipata fedha tunaamini
kwamba tutatekeleza.
MHE. ANTHONY C. KOMU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Kwa kuwa, wananchi wa Moshi Vijijini kule Tarafa ya Kibosho katika Kata sita,
Kata ya Kirima, Kibosho Kati, Okaoni, Kibosho Magharibi na Kibosho Mashariki
wameshaitikia huu wito na kujenga chuo ambacho kwa kweli kina hadhi kubwa
sana na kinaweza hata kubeba Wilaya kama mbili, tatu. Waziri atakuwa tayari
kwenda na mimi kule kwenda kuona hiki chuo na kukiwekea utaratibu mzuri,
maana naamini akienda kule ataweza kukiwekea utaratibu mzuri wa kukipa
ruzuku kama Walimu na kadhalika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu
Spika, kwanza nawapongeza wananchi kwa kutambua umuhimu wa stadi za
kazi kwa wanafunzi wa vyuo hivyo.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa
kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la uhaba wa vyuo vya ufundi
na ahadi imekuwa ni ya muda mrefu na tatizo ni la muda mrefu. Katika
Halmashauri ya Wilaya ya Msalala tumekwishaanza juhudi za kufanya au
kutekeleza jambo hili. Kwa bahati nzuri kwa mazingira yetu tuna mgodi wa
Bulyanhulu ambao vijana wengi sana wanakosa fursa za kufanya kazi pale kwa
sababu ya kukosa elimu fulani ya ufundi na mgodi umeonesha nia ya kushirikiana
na Serikali kuutekeleza mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kumwomba au kumuuliza swali
Mheshimiwa Waziri kwamba anaonaje akitusaidia katika kutia chachu
mazungumzo kati ya Halmashauri ya mgodi ili kuweza kutekeleza mradi huu kwa
yeye mwenyewe kufika na kukaa na watu wa mgodi ili kuona namna gani
tunaweza tukatekeleza mradi ambao tayari eneo lilishapatikana muda mrefu
kwenye Kijiji cha Bugarama?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu
Spika, ahsante. Niseme tu kwamba kwanza nawapongeza hao wadau wa
madini kwenye migodi wanavyotu- support katika masuala ya elimu kwa Mkoa
wa Shinyanga na Msalala nadhani ikiwa ni wanufaika wamojawapo. Kwa hiyo,
kama kuna jitihada za aina hiyo Wizara pia tuko tayari. Hata hivyo, niseme tu
kwamba Msalala mtakuwa hamjapungukiwa sana kwa sababu tayari kuna chuo
cha VETA kiko Shinyanga ambacho pia kinajihusisha na masuala ya madini.
Vilevile tunategemea kujenga chuo ambacho kitakuwa ni cha Mkoa katika
Mkoa wa Geita ambapo pia ni jirani zenu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hizo jitihada nitakuwa tayari kushirikiana
nanyi kuweza kuomba kama kuna huo uwezekano.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kama ambavyo Naibu Waziri amesema kwamba chuo kile kina uwezo wa kudahili wanachuo 1,200 na ameeleza mwenyewe kwamba 2015/2016 kilidahili wanachuo 234. Kutokana na miundombinu na rasilimali iliyopo pale, kuwa na wanafunzi 234 kati ya 1,200 hatuoni kwamba hatukitendei haki chuo hiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kuna utaratibu ule wa kuwadahili kupitia mtandao na huko vijijini hakuna mitandao kwa nini isirejee utaratibu wa kuandika barua pamoja na kutumia hizo internet kwa wenzetu walioko mijini ili watoto wa wanavijiji na wenyewe waweze kupata hizi nafasi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, zamani utaratibu ulikuwepo wanafunzi ambao wako shuleni walikuwa wakiomba nafasi za ualimu wakiwa shuleni. Je, kwa nini wasirudishe utaratibu huo mtu aweze kuomba akiwa shuleni ili tuweze kupata wanachuo wa kutosha kuliko kuwa na chuo ambacho kinataka wanafunzi 1,200 halafu wanadahili wanachuo 234?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli baada ya kuboreka kwa miundombinu hiyo, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba chuo hicho kinachukua wanafunzi wanaostahili kuwepo. Ieleweke kwamba baada ya kubadilisha hizo sifa kwanza hali ya ufaulu wa wanafunzi katika shule zetu ulikuwa uko chini lakini pia kutokana na mambo ambayo yalikuwa yanachangiwa humu Bungeni juu ya sifa za Mwalimu, kwa sababu ilikuwa inaonekana kwamba ualimu anapelekwa mtu mwenye sifa hafifu, kwa hiyo, Wizara ilifanya marekebisho na kuona kwamba sasa sifa ziwe mwisho ni daraja la III.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hali hiyo, kwa mwaka wa kwanza tulikuwa na wachache lakini kwa sasa hali ya ufaulu imeboreka kutoka katika shule zetu za Serikali na zisizo za Serikali kwa hiyo, tunao wanafunzi wengi ambao wanaweza kupelekwa huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halikadhalika niseme tu kwamba katika suala la udahili tunaliangalia na Kamati yetu ya Huduma ya Jamii imelizungumza sana. Tunaangalia namna bora ya kudahili bila kupoteza dhamira ya Serikali ya kuhakikisha kuwa ubora unalindwa. Kwa hiyo, tutafikia maamuzi baada ya tafiti zinazoendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kuwapeleka wanafunzi moja kwa moja kutoka shuleni ni kwamba wanafunzi hao ni mpaka wawe wameshafanya mitihani na wengine wanachukuliwa kutoka katika ngazi mbalimbali za uombaji, kwa hiyo, matokeo yao ndiyo yanayowapeleka huko siyo tu ilimradi yuko pale shuleni na aanze kujaza. Kwa hiyo, suala ni kuhakikisha kwamba wanafunzi wanaopelekwa katika Chuo cha Korogwe na vyuo vingine vyote ni wale wenye vigezo vya ubora unaohitajika.

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nitaongea kwa kifupi. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na napenda tu kuongezea jambo dogo kwamba, suala hili la vyuo vya ualimu kuwa na wanafunzi wachache kuliko uwezo wake lilitokana na uamuzi wa kuwapeleka wanafunzi UDOM ambapo ilisababisha mlundikano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kulihakikishia Bunge lako Tukufu yale mambo yaliyokuwa yanasemwa kwamba Serikali iliwaondoa wanafunzi UDOM ili ipate nafasi siyo kweli kwa sababu iliona ni vizuri, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba Vyuo vya Ualimu vichukue wanafunzi kulingana na uwezo wake. Nashukuru.
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami nataka kuuliza swali la nyongeza kuhusiana na elimu Mkoa wa Katavi. Ukosefu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Mkoa wa Katavi umeleta usumbufu kwa wananchi wa Katavi. Serikali ilitenga pesa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Kilimo lakini chuo hicho kimeyeyuka. Ni nini mkakati wa Serikali kufuatilia zile pesa zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Kilimo Mkoa wa Katavi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Chuo kikuu kilichokuwa kinategemewa cha Mkoa wa Katavi kilikuwa kinadhamiriwa kujengwa kwa ushirikiano wa Halmashauri ya Mpanda pamoja na wawekezaji ambao walikuwa ameingia nao ubia. Kwanza katika taratibu zilizokuwa zinaendelea kulikuwa na suala la mbia kutaka kupewa dhamana ya Serikali katika kujenga chuo hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hilo tuliona kwamba, kama mtu anahitaji kujenga chuo, wakati yeye tunategemea kwamba ni mwekezaji kwa maana kwamba atakuja kuwekeza katika kile chuo, dhamana ya Serikali inaweza ikasababisha mtu kuchukua deni mahali na kukimbia na kazi isiwe imefanyika. Ni vema mwekezaji awe ni mwekezaji wa kweli na awekeze kadri inavyotakiwa. Hata hivyo, kwa fedha zilizotolewa Halmashauri ya Mpanda inafahamu juu ya mambo yake na hivyo kwa kutumia Baraza lao wafuatilie na kuona kwamba fedha zao hazipotei.
MHE. ZAYNAB M. VULLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwanza niseme nilitarajia angeniambia Mwongozo huo utaanza lini ukizingatia Wizara inaongozwa na Waziri mwanamke, Naibu Waziri mwanamke na Katibu Mkuu mwanamke. Je, Sheria ile ya SOSPA haoni kwamba inakinzana na sera ambayo wanaleta na vipi mtawasaidia hao watoto waweze kuendelea na utaratibu ambao mmeuweka? Hilo ni swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa mtoto wa kike na wanawake wote kibaiolojia kuna siku ambazo lazima tuzitumikie. Watoto wa shule wengi wanaacha kwenda shule kati ya siku sita mpaka saba, ukipiga kwa mwaka mmoja mtoto wa kike anapoteza zaidi ya siku 60 au 70. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kuweza kupeleka mataulo ya kuweza kuwasaidia na kutenga chumba maalum kwa ajili ya wao kuweza kujihifadhi wakati wanapohitaji?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nikiri kwamba ni heshima kubwa sana Wizara yetu ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupewa sisi wanawake kuiongoza ambao tuko jirani sana na mahitaji au matatizo ya wanawake na ndiyo maana tunasema kwamba mwongozo tayari umeshaandaliwa. Kama mazungumzo yote tunayoendelea kuyafuatilia yatakuwa yamekamilika, tunatarajia tarehe Mosi, Machi, 2017 mwongozo huo uwe umekamilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wanawake ni mtambuka. Tunapozungumzia kuwawezesha vijana katika demokrasia na katika kushiriki shughuli mbalimbali za kiuongozi, tunachozungumzia ni kwamba lazima watoto wa kike wasiachwe nyuma. Kutokuwa na sehemu za kujihifadhia wanapokuwa shuleni ni tatizo. Mwongozo ulishatolewa kwamba kila shule lazima itenge chumba maalum kwa ajili ya wanafunzi hao kujihifadhia wakati maalum lakini hali kadhalika tunasema kwamba hata hizi fedha za elimu bure zinazotolewa ni vema ikatengwa sehemu ndogo kwa ajili ya kuwasaidia hawa watoto wa kike pale inapotokea mambo yametokea kwa dharura.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nasema bila kuficha wapate pedi zao kwa sababu tumekuwa tukificha mambo haya ya wanawake, matokeo yake hata kwenye bajeti hayawekwi. Tuseme wazi kwamba mahitaji ya mwanamke ikiwemo pedi ziwekwe kwenye bajeti ili hawa watoto wa kike waweze kusaidiwa.

WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niongezee jibu zuri la Naibu Waziri. Napenda nitoe taarifa kwa Bunge lako Tukufu kwamba imekuja teknolojia ambapo taulo nzuri za bei nafuu zitatengenezwa. Zaidi nitoe taarifa kwamba kuna Wabunge wawili wamejasiria, tunawaongoza kusudi watengeneze viwanda hivyo.
MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Nami niulize swali la nyongeza kutokana na swali la msingi la Mheshimiwa Zaynab Vullu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imalize tatizo la watoto wanaopata mimba kuendelea na masomo. Tunajisikia vibaya sisi Watanzania wanawake, kwa mfano, chukua Zanzibar, Zanzibar mtoto wa kike akipata ujauzito wanaruhusu anaendelea na masomo. Zambia, Kenya, sisi ndiyo tumebaki peke yetu wa mwisho kwa nini? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashangaa, kwa kifupi tu, taarifa zinatolewa kila siku watoto 30 wamepata mimba, watoto 20 wamepata mimba, hivi mnaona ninyi raha kutangaza kila siku na wasababishaji mnawajua ninyi wenyewe? Iliyobaki hawa watoto waruhusiwe wakasome, hakuna mjadala hapa.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lolote lile linapotekelezwa ili litekelezwe kikamilifu ni vema wadau wote wakawa pamoja. Sisi wanawake pamoja na hao wanafunzi wa kike hatuishi kwenye jamii peke yetu. Katika utekelezaji wa suala hili si tu kwamba maadam tukisema wanafunzi warudi shuleni basi unakuwa unasema umesema wakati hujui utekelezaji utakuwaje. Ndiyo maana tumewashirikisha…

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Tulieni. Kama majibu ninayo mimi basi sikilizeni. Nasema hivi suala hili linahitaji Wabunge wote kuwa on board kwa misingi kwamba…

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Na msisahau sisi wenyewe tulitunga sheria ya kuhakikisha kwamba yule anayetoa ujauzito kwa mtoto wa shule achukuliwe hatua.

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Sasa kama ndivyo tumetunga hiyo sheria bila kuwa na ushirikishwaji na utaratibu maalum wa kuwapata hao wanaoendelea kutoa ujauzito kwa watoto wa shule, utaratibu vipi? Ndiyo maana tunataka sekta zetu zote, wadau wote, tuwe na uratibu wa kuweza kukabiliana na mambo yote mawili.

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Kwa hali hiyo, wanafunzi watarudi shuleni lakini wakati huo huo lazima taratibu zetu za msingi za kufanya uratibu katika maeneo yote ikiwemo utoaji wa adhabu hasa wale akinababa ambao wanawanyemelea watoto wa shule uweze kuendelea.
MHE. SOPHIA M. SIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi alivyojibu kwa umakini sana na hususani pale alipozungumzia kwamba walimu wanapata mafunzo zaidi, refresher course ambazo kwa kweli wengi wanazihitaji. Lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiuliza Serikali je, haioni kwamba kuanza kutumia kiingereza kama lugha ya kufundishia kuanzia masomo ya sekondari inasababisha kuleta ugumu sana kwa wanafunzi na matokeo yake wanakuwa wanakariri hasa katika masomo ya sayansi na teknolojia, kitu ambacho kinapelekea wasifanye vizuri sana katika masomo hayo wakati wa mitihani yao, na wale ambao wapo kwenye shule za private wanafanya vizuri zaidi? Sisemi shule zote, lakini hii ni sababu mojawapo ya shule za sekondari za private kufanya vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je, Serikali haioni kwamba upo umuhimu wa kipekee kabisa kuhakikisha kiingereza kinatiliwa mkazo kwa sababu kwenye soko la ajira mara nyingi unaona inatokea kwamba interview zinafanywa kwa kiingereza. Hata mashirika mengine ya umma wakienda vijana interview unawauliza mmefanyiwaje anasema ni kwa kiingereza. Isitoshe sisi tunawakaribisha wawekezaji lakini wale wawekezaji wanahitaji wale ambao wana lugha ya pili ambayo ni kiingereza ili ku-communicate. Je, Serikali haioni kwamba tunapoteza ajira nyingi kutokana na ukosefu wa kujiamini wa kuongea lugha ya kiingereza na matokeo yake uakuta hata kwenye EPZ wako Wakenya, Waganda na Wazimbabwe wameajiriwa na mashirika haya ya uwekezaji. Naomba anijibu hilo tunafanya nini, ajira zinapotea. Ahsante sana
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda ifahamike lugha ya kiswahili ni lugha ambayo ni lugha ya taifa, na ni lugha ambayo inafahamika na wananchi wengi toka wakiwa wadogo. Mwanafunzi anapofundishwa lugha ambayo ameiozoea na amezaliwa nayo ni rahisi zaidi kupokea mitaala anayowekewa kuliko pale ambapo unamfundishia lugha mpya kabisa. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa misingi hiyo tunasema kwamba, sisi kwa kuzingatia kwamba kiswahili ndiyo lugha yetu ya msingi tunasema kwamba mtoto aanze kufundishwa kwa lugha hiyo, lakini mara anapofika darasa la tatu dozi ya kiingereza inaanza kuongezeka kama nilivyosema mpaka kufikia vyuo vikuu. Kwa siku za nyuma kulikuwa na upungufu zaidi kwa sababu unakuta kwamba walimu walikuwa wanaweza kufundisha somo la Kiingereza hata kama alikuwa hana ufaulu wa kutosha. Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile unakuta mwalimu mmoja alikuwa anafundisha masomo mengi. Kadiri tunavyoenda na kuimarisha sifa za walimu na kuongeza idadi ya walimu kutakuwa na specialization kiasi kwamba sasa mwalimu atakuwa anafundisha somo husika na somo alilofaulu na hivyo kiingereza kitazidi kuimarika. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa upande wa suala la kukosa ajira nipende tu kusema ukweli kwamba kiingereza kimekuwa kikiendelea kuzingatiwa; na niseme tu kwamba kwetu Watanzania yawezekana pengine unyanyapaaji wetu nao unachangia katika kuwafanya watoto waogope somo la kiingereza; na kila wakati kutokujiamini na kutokuzungumza kiingereza kwa hofu kwamba nitaambiwa sijui kiingereza. Mimi nasema kwamba kiingereza ni lugha sawa na lugha nyingine, mtu zungumza bila uoga sawa na ambavyo wengine wanaweza kujaribu kuzungumza kiswahili bila uoga na watu tunaelewana. Mheshimiwa Mwenyekiti, serikali itaendelea kuweka mikakati ya kuboresha somo la kiingereza katika shule na kuongeza mijadala katika shule au midahalo, lakini vilevile kupata hata wataalam mbalimbali wanaopenda kuja kujitolea katika nchi yetu kutoka nchi mbalimbali. Kwa hiyo, niwaombe wote tushikamane kuona kwamba lugha hii ya pili ambayo itatusaidia zaidi katika masuala ya mawasiliano hasa ya kibiashara ili nayo iweze kupata nguvu sawa na ambavyo tunasisitiza katika lugha yetu nzuri lugha ya kiswahili, lugha ambayo ni ya upendo na upole. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini hali kadhalika tunasema kwamba bado lazima tuongeze jitihada hata katika lugha za alama kwa sababu huyu mwanafunzi si kiingereza peke yake, ni pamoja na lugha ya alama…
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika,
nashukuru. Pamoja na majibu ya Serikali, lakini naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, kwa mfano tu Wilaya ya Same mwaka 2016, wasichana wadogo waliopata mimba na kufukuzwa shule ni 64 ambao hawa ni wa O-Level ikiwa ina maana mimba hizi ni za utotoni. Mwaka huu 2017 mwezi wa Kwanza, wa Pili na wa Tatu, miezi mitatu tu wamefukuzwa wanafunzi wa shule kwa mimba za utotoni 42 na kati ya hao akiwepo mtoto wa darasa la sita ikiwa ina maana ni kati ya miaka 12 mpaka 14.
Mheshimiwa Spika, hivi Serikali haioni kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa kuwa na mitaala ambayo itawafundisha watoto hawa kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari, ambayo itawafanya waelewe athari za kupata mimba utotoni ambazo ni muhimu sana? Mitaala hii itaweza kuwasaidia watoto hawa kujitambua na kufahamu umuhimu wa kutokukubali kupata mimba utotoni.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali
inafanya jitihada kubwa sana kupambana na madawa ya kulevya sasa hivi na naiunga mkono, nai-support na tunashukuru sana. Jitihada hii ni kwa sababu Serikali imeona athari hasa inayowapata vijana wa kiume na wa kike kwa
kutumia madawa ya kulevya, lakini watoto wa kike
wanapata athari mara mbili, kwanza athari ya madawa ya kulevya na mimba za utotoni.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuleta mkakati
mkubwa kama ule wa madawa ya kulevya ili tupunguze athari za mimba za utotoni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali linalohusiana na masuala ya mitaala kama ifuatavyo:-
Kimsingi katika elimu ya Msingi na elimu ya Sekondari wanafunzi wanapewa maarifa kuhusiana na masuala ya Kibaiolojia na sayansi yanayohusisha hata masuala ya maumbile ya miili yao, kwa hiyo kimsingi suala hilo linafanyika labda tunaloweza kuahidi hapa ni kutoa msisitizo wa kuona kwamba wanafunzi hao wanapewa dozi zaidi hasa kwa kuwachukua hawa watoto wa kike na kuwapa elimu ya ziada kwa ajili ya kuwanusuru katika mazingira hayo.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, kwanza tunao mpango wa kudhibiti ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambao ni jumuishi kwa sekta takribani tisa za Serikali yetu na mpango huu umezinduliwa mwaka jana mwezi Desemba na Mawaziri tisa wa Serikali hii ya Awamu ya Tano na Mawaziri wameonesha comittment kubwa sana ya kuweka utaratibu
wa kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ndoa za utotoni lakini pia mimba za utotoni na vitendo vyote vinavyohusu ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike.
Mheshimiwa Spika, tunachokihitaji kwa sasa ni
kupewa fedha kwa ajili ya kutekeleza mpango huo na kwenye mpango huu tunalenga kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto kwa kiwango cha asilimia isiyopungua 50 kufikia mwaka 2022. Kwa hivyo, mpango huu kama tutapangiwa fedha, tunapanga kuanza kuutekeleza mwezi Julai mwaka 2017. Kwa hivyo, mpango tunao pia tuna mikakati mbalimbali inayoendelea kama ya elimu ya malezi chanya (Positive Parenting Education) kwa watoto ambao umefanyika kwenye Wilaya 72 za Nchi yetu
na tunawalenga zaidi viongozi wa kimila, wazazi pamoja na watu mashuhuri wenye kufanya maamuzi kwenye jamii.
MHE. MATTAR ALI SALUM: Mheshimiwa Mweyekiti, ahsante sana kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nisawazishe jina langu, mimi naitwa Mattar Ali Salum, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri akilijibu alijibu vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake ambayo ameyatoa.
Mheshimiwa Waziri, wapo wanafunzi wanaendelea kupata mikopo ya Serikali kwa kima kidogo hadi sasa, husababisha kukosa kukidhi mahitaji ya vyuo husika ambavyo wamepangiwa. Je, Serikali ni kwa nini isiwaongezee fedha wanafunzi hawa ili waweze kukidhi mahitaji ya vyuo husika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wako wanafunzi walikuwa wakipata mikopo kwa kipindi kirefu, ghafla Serikali imewafutia mikopo yao, sijui ni kwa nini. Je, Mheshimiwa Waziri, Serikali ina mpango gani wa kuwarejeshea mikopo hawa wanafunzi ili waweze kukidhi na kuendelea na masomo yao vizuri? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama alivyorekebisha jina lake, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba kiuhalisiatulingependa kutoa mikopo kwa wanafunzi wengi zaidi, lakini vilevile ingewezekana hata kila mwanafunzi akapata mkopo kwa kadiri ya mahitaji ya chuo anachosoma; lakini kwa sababu fedha hazitoshi inakuwa ni vigumu kufanya hivyo na tunaangalia zaidi ni uhitaji wa kiasi gani upo.
Kwa hiyo, kwa misingi hiyo niseme tu kwamba, Serikali itaendelea kutenga fedha ya kuona kwamba, inawasaidia wanafunzi wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusu kufuta mikopo. Ni kweli kuna baadhi ya wanafunzi walifutiwa mikopo kutokana na kutokuwa na vigezo vinavyostahili. Hata hivyo Serikali imeendelea kulifanyia kazi suala hilo ili kuona kwamba, anayefutiwa mkopo iwe kweli ni mtu ambaye hana uhitaji. Kwa yule mwenye uhitaji na kwamba vigezo vyote vimetimia basi, baadhi yao tumeweza pia kuwarejeshea.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza na nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, nini commitment ya Serikali juu ya kuwapandisha madaraja watumishi hawa kwa wakati?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, katika bajeti ya mwaka huu, Serikali imetenga kiasi gani cha fedha ili kuondoa adha hii wanayoipata walimu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, kimsingi ni kwamba kama ambavyo tumekuwa tukizungumza kila wakati ni kwamba madaraja ya watumishi husika ikiwemo walimu yatakuwa yanapandishwa mara baada ya zoezi la uhakiki ambalo pengine wengine hawapendi kulisikia lakini ni zoezi muhimu sana litakapokamilika. Kwa hiyo, nikuhakikishie tu kwamba mara zoezi hilo likishakamilika tutafanya hivyo.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili kuhusiana na kiasi gani cha bajeti kimetengwa, naomba tusiiwahishe
shughuli, siku yetu ya bajeti mtapata majibu mazuri zaidi. Ahsante sana.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika majibu yake ya msingi amesema kwamba ziko fedha ambazo zimelipwa kwa madai ya walimu lakini ni kidogo sana kuendana na madai halisi ya walimu wa Tanzania kwa miaka karibu mitatu iliyopita. Kwa Wilaya ya Kaliua tu walimu wa sekondari wanadai shilingi 221,347,561 kwa mwaka 2015/2016 tu. Ni lini sasa madai haya ya walimu kwa Wilaya ya Kaliua yatalipwa kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, kimsingi tunatambua kwamba kuna madeni ya walimu lakini naomba pia mnikubalie kwamba kweli kuna baadhi ya madeni sio madeni halali. Uzoefu unaonesha kwamba baada ya uhakiki kuna baadhi ya madeni yanashuka mpaka kufikia moja ya tatu kitu ambacho kinasikitisha na kimekuwa kikichelewesha kuwalipa walimu kwa wakati pamoja na watumishi wengine.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ni rai yangu kwa watumishi wote waone jambo la kulipwa ni haki yao lakini vilevile ni vyema madai yakawa halali ili kuepusha usumbufu usio wa lazima. Haipendezi sana mtu umedai halafu baadaye unaambiwa hayo madai hayastahili kwa sababu taratibu na kanuni zetu tunazijua na hivyo unaweza ukajua ni kipi unastahili na kipi hustahili.
Kwa hiyo, niseme tu kwamba kwa maneno ya Mheshimiwa Mbunge tutajitahidi kufuatilia katika Wilaya au Jimbo lako kuona kwamba hawa watumishi wanaostahili kulipwa waweze kulipwa kwa wakati baada ya uhakiki.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa swali la msingi linaulizia vitendea kazi vya elimu, ubora wa elimu, pamoja na mazingira yake yote ambayo ni elimu kwa wote, shirikishi na yenye ubora; mwaka 2013 tarehe 2 Machi siku ya Jumamosi, Mheshimiwa Rais aliunda Tume ya Sifuni Mchome ya kuangalia vigezo vyote hivi. Tarehe 31 hoja binafsi ilikuwa Bungeni kuhusu vigezo vyote hivi. Je, ni lini Serikali italeta ile ripoti ya Tume ya Sifuni Mchome hapa Bungeni ili Wabunge tuweze tukaishauri vizuri Serikali kuhusu ubora wa elimu Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni kweli nafahamu kuna hiyo Tume ilikuwa imeundwa na kuna baadhi ya mambo ambayo yalikuwa yameelezwa kwenye ile Tume; lakini baada ya hapo kuna team mbalimbali ziliundwa ambazo pia nyingine zilikuja kuona hata baadhi ya mapendekezo pengine hayako sawa; yaani hayaendani sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Wizara tumekuwa tukiendelea kufanya marekebisho kulingana na mahitaji, kwa mfano katika suala la utoaji wa tuzo. Mwanzo zilikuwa zinatumia GPA, sasa hivi tumerudi tena kwenye division. Kwa hiyo, kuna mambo mengi tu ambayo yamekuwa yakifanyiwa kazi kila wakati. Hata hivyo, siyo tatizo kuweza kuwaonesha Waheshimiwa Wabunge nini kilikuwa kimezungumzwa kwenye Tume, lakini pia mabadiliko yanayoendana na uhalisia wa sasa yaliyofanyika.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza nampongeza Waziri wa Elimu na Naibu wake na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa basi, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari kufuatana nami ili aweze kuangalia lile jengo ili kusudi waweze kutoa kitu ambacho kinalingana na kazi ambayo inakusudiwa kumaliziwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, jibu ni ndiyooo! (Makofi)
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Kwa kuwa takwimu za mwaka 2016 zinaonyesha kwamba Watanzania ambao ni zaidi ya miaka 15 na ambao hawazidi miaka 54 wako takribani milioni 25 na kuendelea; na kwa kuwa asilimia 22.4 ni kubwa sana, maana yake ni kwamba karibu takribani watu 5,813,066 hawajui kusoma na kuandika.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kurudisha sasa vituo vya kufundishia kama ilivyokuwa zamani katika kila kijiji, kwa sababu tatizo hili ni kubwa sana na hasa katika Jimbo la Vwawa na maeneo mengine nchini?
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri umesema kwamba mmeziagiza Halimashauri kutenga fedha ili wahakikishe kwamba huo mfumo wa KKK unatekelezwa.
Je, mmeweka mkakati gani wa kuhakikisha kwamba kutakuwa na uwajibikaji na ufuatiliaji wa utekelezaji wa agizo hili?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Hasunga kwa kuridhika na majibu yetu ya awali, pia kwa majibu yanayofuata ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi ni kwamba kila mahali kwenye taasisi ya elimu, iwe ni shule ya msingi, iwe ni sekondari, iwe ni chuo ni kituo halali cha watu wasiojua kusoma na kuandika kuweza kupata elimu au mahali pa kujifunza.
Vilevile Wizara baada ya kutembea na kuona kwamba eneo hilo bado lina uhitaji mkubwa, tumeshaweka mikakati ya kuona kwamba elimu ya watu wazima inapewa kipaumbele na kuona kwamba wananchi wetu wa Tanzania tupungue ikiwezekana angalau tufikie asilimia tano mwaka 2025.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na ufuatiliaji katika Halmashauri ili kuhakikisha kwamba wanatimiza wajibu wao, niwaombe tu Waheshimiwa Wabunge kwa kuwa sisi sote ni Madiwani kwenye Halmashauri zetu, basi tuone umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya shughuli hiyo ya kuhakikisha wenzetu wote wanajua kusoma, kuandika na kuhesabu.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swlai dogo la nyongeza. Kwa kuwa kukua kwa soko huria katika utoaji wa huduma ya anga nchini, hivyohivyo naweza nikaambatanisha na kukua kwa elimu yetu kuwa huria na nilikuwa nataka tu kupata maelekezo ya Wizara juu ya huria hii ya kutokana na elimu yetu ya Tanzania kuwa huria, hali iliyosababisha baada ya kutoka kwa uhakiki wa vyeti feki imepelekea baadhi ya Madaktari, Walimu, Watumishi, taarifa zao kuonekana ni incomplete. Hii ni kwa sababu ya elimu yetu kuwa huria. Sasa naiomba Serikali itoe maelekezo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninapozungumza,
kuna watumishi sasa wanaelekea Dar es Salaam kwenda kuhakiki incomplete zao…
Mheshimiwa Mwenyekiti,
swali langu ni kwamba nakata kujua: Je, Serikali inatoa kauli gani juu ya wafanyakazi ambao taarifa iliyotoka juzi ya uhakiki wa vyeti vyao, hasa wale wote walioandikiwa incomplete? Serikali hasa Wizara hii ya Elimu ituelekeze, maana leo hii watu wanasafiri wengi kwenda kuhakiki vyeti vyao vya Form Four. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni hilo nalielekeza kwa Mheshimiwa Waziri kwa sababu hapa ni mada huria na elimu yetu ni huria, naomba Wizara ya Elimu itoe tamko juu ya kadhia hii ya elimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni kweli kwamba tumekuwa tukitoa elimu huria ili kuwezesha maeneo mbalimbali ya ajira kuweza kupata wataalam wanaohitajika. Katika suala hili la watu kusafiri kuhusiana na kuhakiki vyeti vyao, napenda tu kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna makundi makuu matatu ambayo yameendana na uhakiki uliofanyika. Kuna kundi la kwanza la vyeti feki au vyeti vya kugushi, kundi hili kama kuna yeyote anayeona kwamba hajaridhika, anachotakiwa kufanya siyo kusafiri, bali ni kukusanya vyeti vyake halali na kumwona mwajiri wake ambaye ni DED (Mkurugenzi wa Halmashauri) au Katibu Tawala wa Mkoa ili apeleke huo ushahidi wake na viweze kuwasilishwa. Vitawasilishwa kwa Katibu Mkuu, Utumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna kundi lingine,
hili analolizungumza la incomplete (vyeti visivyokamilika). Yawezekana wakati wa kuwasilisha, mtu aliwasilisha labda vyeti vya Chuoni, vyeti vya Kidato cha nne au cha sita hakuwasilisha; au vyeti vingine vinavyohusiana. Kwa hiyo, anachotakiwa kufanya ni vilevile, kupeleka vile vyeti ambavyo vilikuwa havijawasilishwa kwa hao waajiri wake ambao ni Mkurugenzi wa Halmashauri au RAS (Katibu Tawala wa Mkoa).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kundi la tatu la vyeti vyenye utata. Vyeti vyenye utata unakuta kwamba cheti kimoja kimetumika na watu zaidi ya mmoja. Kwa hali hiyo inabidi lazima kumfahamu ni yupi mwenye cheti halisi. Wanachotakiwa kufanya ni kila mtu anayeamini ndiye mwenye cheti hicho, hao ndio wanaotakiwa kusafiri, waende NECTA ili sasa wakahakikiwe na kujulikana mwenye cheti chake ni yupi kwa sababu haiwezekani cheti kimoja kikatumika na mtu zaidi ya mmoja. Huo ndiyo ufafanuzi wangu. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo hayaridhishi kabisa, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; Mheshimiwa Waziri haoni Serikali kushindwa kumalizia majengo haya na kutoa majibu haya ni kuwavunja moyo wafadhili tuliowabembeleza na kuwaomba watujengee majengo haya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; wafadhili kujenga majengo na kuyamalizia au kutoyamalizia ni jambo la kawaida kabisa kwenye nchi yetu; na kwa kuwa Serikali imesema kwamba haiukufuata sheria wakati majengo yale yamesimamiwa na Engineer wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga. Je, Mheshimiwa Waziri haoni anawanyima haki wananchi wa Igunga kwa kukosa kuwa na VETA yao ambayo wameihangaikia kutafuta wafadhili, bado tu kumalizia lakini wanasema kwamba sheria haikufuatwa wakati Engineer wa halmashauri ndiye aliyesimamia majengo haya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, nadhani hakunisikia vizuri katika jibu langu. Nimesema kwamba shirika linaweza likajenga chuo na kuikabidhi Serikali, lakini kwa sababu katika swali la msingi haikuzungumzwa kwamba chuo hicho kimeshakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachosisitiza ni kwamba, kwa sababu mwisho wa yote hicho chuo itabidi kiendeshwe kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizopo, ndiyo maana tunasisitiza kabla ya wadau wetu wa maendeleo kuanza kufanya shughuli ya ujenzi, ni vema kuwasiliana na taasisi husika ili kile wanachokifanya kiendane na viwango na kiweze kuwa na tija kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, sijasema kwamba wao wamejenga bila kufuata sheria. Katika jibu langu la msingi nilisema kwamba ni vema kabla ya kujenga yawe yanafanyika mawasialiano kupitia halmashauri na VETA ili kwa pamoja kuweza kuzingatia masuala ya kisheria. Kwa misingi hiyo, ninachosema ni kwamba, kwanza hicho chuo hatujakitembelea na hatuwezi kukiamuru kama ilivyo, lakini niseme tu kwamba nazidi kuwaomba wadau wa maendeleo, wanapofanya shughuli yoyote ya kimaendeleo kuhusiana na Wizara fulani, ni vema kushirikisha Wizara husika ili kile kinachofanyika kiwe na tija ili fedha zao zisipotee bila utaratibu ambao pengine usingekuwa wa lazima.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa hitaji la vyuo vya ufundi kwenye nchi yetu liko juu sana na uwezo wa Serikali unaonekana kwamba ni mdogo kuwezesha kujenga vyuo vya VETA nchi nzima kwa wakati mmoja. Je, Serikali iko tayari kutumia fursa tulizonazo kwenye shule zetu za sekondari kujenga karakana ya fani angalau moja kila shule ya sekondari ili kuwezesha vijana wengi kupata elimu ya ufundi na kurejesha elimu hiyo katika shule za sekondari?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba kupitia Sera yetu ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ya Mwaka 2014, Wizara inaangalia kwa umakini uwezekano wa kuongeza nafasi za udahili kwa wanafunzi wa vyuo vya ufundi ili kuwezesha wanafunzi wengi zaidi kupata fursa hizo. Kisera ni kwamba tungehitaji kuona mwanafunzi akisoma moja kwa moja mpaka kidato cha nne na kwa misingi hiyo kuna mambo mbalimbali ambayo yanaangaliwa ili kwa pamoja tuone kwamba ni jinsi gani tutaweza kuangalia mafunzo ya kawaida na vilevile mafunzo ya ufundi ili kuwezesha fursa hizo kupatikana.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa tatizo lililopo Manonga linafanana kwa ukaribu kabisa na tatizo lililopo katika Mkoa wa Songwe na kwa kuzingatia kwamba Mkoa wa Songwe ni mpya, lakini mpaka sasa Wilaya za Mbozi, Ileje, Momba pamoja na Songwe hazina vyuo vya ufundi. Je, ni lini Serikali itajenga vyuo vya ufundi katika wilaya hizo ili kuwasaidia vijana wa Mkoa wa Songwe kuweza kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninavyofahamu ni kwamba Wilaya ya Songwe ni miongoni mwa maeneo ambayo yamo kwenye mpango, nafahamu kuna kiwanja kilishatengwa eneo la Makutano, kwa hiyo, muda ukifika tutafanya hiyo shughuli ya ujenzi.
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nami kwa kifupi tu ni kwamba, mwezi wa kwanza mwaka huu nilikuwa nchini Uswisi na kuna wadau nilizungumza nao na wakaonesha nia kwamba wako tayari kutujengea chuo cha ufundi pale kwenye Jimbo letu la Arumeru. Swali langu kwa Wizara; naomba commitment ya Serikali, kwamba wadau watakapokuja na watakapokuwa tayari kutujengea ninyi mtakuwa tayari kutusaidia utaalam na vifaa pale ambapo chuo kitakamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Nassari na naomba niunganishe na maeneo yote ambayo wamejenga Vyuo vya VETA kwa kutumia taasisi binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba, katika kujenga vyuo vya ufundi kuna njia mbili za kuviendesha; kuna njia ya kwanza, watu wanajenga wenyewe na wanaendesha wenyewe katika sura zote za vifaa na Walimu. Njia ya pili, kujenga na kuikabidhi Serikali ili iweze kuviendesha. Sasa tatizo ninaloliona ni kwamba halmashauri zinashirikiana na wadau kujenga hivyo vyuo lakini baadaye wanakuwa hawawezi kufikia muafaka katika kupeleka Walimu pamoja na vifaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwombe tu
toka mwanzo, ni vema ushirikiano uanzie toka mwanzo ili tujue wadau watakaokuja kusaidia ujenzi wa chuo hicho wajibu wao utakuwa ni nini na upande wa Serikali wajibu wetu utakuwa ni nini ili suala hilo litekelezwe kwa ukamilifu kama inavyostahili.
MHE. DEOGRATIAS F. NGALAWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa ruhusa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na changamoto nyingi za ukaguzi kwenye shule zetu za sekondari, msingi na vyuo vya ualimu, je, Serikali haioni sasa imeshafika wakati wa kuunda mamlaka au taasisi itakayosimamia ubora wa elimu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Idara zetu za Ukaguzi wa Elimu, shule za sekondari na msingi zimekuwa zikipata changamoto nyingi hasa za vyombo vya usafiri na watendaji. Je, Serikali ina mpango gani wa kuiwezesha Idara hiyo ya Ukaguzi ili iweze kufanya kazi yake katika ubora unaotakiwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema awali ni kweli Idara yetu ya Ukaguzi inakabiliwa na changamoto mbalimbali hususan katika ukuaji wa sekta ya elimu kama ilivyo sasa hivi.
Mheshimiwa Mwenyemiti, mwanzo idara hii ilikuwa inakaguliwa kupitia kwenye kanda zetu, lakini kwa sasa ni kanda pamoja na Wilaya, hata hivyo tunaona kwamba kuna mapungufu kidogo katika mfumo mzima, na ndio maana kupitia mabadiliko haya ya sheria tutaangalia namna bora zaidi ya kuendesha shughuli ya ukaguzi katika shule zetu za primary, sekondari na vyuo. Hali kadhalika kwa upande wa uwezo wa Idara za Ukaguzi, ni kweli kuna mapungufu hasa yanayotokana na vifaa kama vitendea kazi kama magari, ofisi na Wizara imeshaona hilo na tayari tumeshaanza kufanyia kazi, tayari kuna magari yamekuwa yakipelekwa kwenye Wilaya na mwaka huu tumeagiza magari mengine kwa ajili ya kupeleka kwenye Wilaya nyingine na wakati huo huo tunatarajia pia kwa mwaka huu kuanza kujenga angalau ofisi 100 kwa ajili ya wakaguzi katika Wilaya zetu.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa suala la udhibiti wa elimu huwezi kutofautisha na udhibiti wa vitabu vinavyoingia kwenye mfumo wa elimu na kwa kuwa imeonekana wazi kwamba taasisi ya elimu ambayo imepewa jukumu la kuthibiti ubora wa vitabu vinavyoingia kwenye mfumo wa elimu imeonekana kuna dosari kubwa. Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha chombo cha ithibati kama ilivyokuwa EMAC huko nyuma ili kudhibiti vitabu vinavyoingia katika mifumo yetu ya elimu na kuacha madudu yanayoendelea sasa hivi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kurudisha mamlaka zilizokuwa zinafanya juu ya utungaji wa vitabu za wakati huo ni suala ambalo linabidi kuangaliwa zaidi. Kimsingi mapungufu yaliyojitokeza kwa mwaka huu Wizara ya Elimu imeanza kutunga vitabu kwa mara ya kwanza. Kwa hiyo, chombo kama hicho inabidi lazima kijengewe uwezo na ndio maana katika kufanya tathmini ya matatizo yaliyojitokeza, moja ya mambo yatakayoangaliwa ni uwezo wa chombo chenyewe, vilevile hata ushirikishwaji mpana wa wadau mbalimbali ikiwemo watu binafsi na wataalam kutoka katika maeneo mbalimbali.
Kwa hiyo, mimi nadhani kiujasiriamali tunasema kwamba kujifunza ni pamoja na kufanya makosa, lakini yasiwe ya kudhamiria yawe ni ya bahati mbaya. Kwa hiyo, tutaendela kuboresha na kushirikisha wadau wengi zaidi ili kuona kwamba tunapata vitabu vilivyo sahihi.
MHE. JAPHET N. HASUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata hii nafasi. Kwa kuwa Mheshimiwa waziri amesema kwamba wana mpango wa kupeleka vitendea kazi na magari katika Ofisi za Ukaguzi wa Elimu, lakini kwa muda mrefu kumekuwa na matatizo makubwa ya ukosefu wa fedha za uendeshaji, unaweza ukapeleka magari kama hakuna fedha za uendeshaji bado hawataweza kufanya kazi; na kwa kwa muda mrefu wakaguzi wamekuwa wakifanya ukaguzi katika shule ambazo ziko jirani tu kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapelekea OC ofisi hizo zote za kanda ili ziweze kufanya kazi yao sawasawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimesema awali ni kwamba kimsingi Wizara imedhamiria kuboresha eneo hili la ukaguzi. Suala la OC limekuwa likiimarishwa kila wakati na ndio maana tunataka kuangalia mfumo mzima, hata ikiwezekana mafungu yao ya upatikanaji wa OC yaende moja kwa moja bila kupitia katika ngazi nyingine.
Vilevile ukaguzi tunaotaka kuuzingatia si tu ule wa kuangalia masomo peke yake, mpaka miundombinu, shule iko wapi? Inafundisha vipi na imesajiliwa katika sura ipi? Kwa hiyo, tunataka kwenda kwenye ukaguzi kwa njia ambazo ni pana zaidi ili kuwezesha kuona kwamba mambo ambayo tunaagiza kupitia sera zetu na miongozo yanatekelezwa pia katika shule zetu za Serikali.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Serikali yetu ya awamu ya tano imedhamiria kuifanya Tanzania kuwa Taifa la viwanda je, Serikali haioni muda muafaka sasa wa kuandaa mitaala ya stadi za kazi na ufundi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa kuwa mahitaji ya dunia sasa yamebadilika, je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya marekebisho makubwa ya sera yetu ya elimu ya juu na elimu ya kati ili wahitimu waweze kushindana kimataifa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sera zetu mpaka sasa zimekuwa zikizingatia masuala ya kuwezesha stadi za kazi. Suala linalojitokeza katika ugawaji wa rasilimali na kuboresha ili ziendane na uhalisia hiyo ndio inakuwa ni changamoto. Kwa mfano suala la kujifunza kwa vitendo ni jambo muhimu sana, lakini wakati mwingine unakuta kwamba bajeti inapokuwa finyu ule muda wa vitendo unapunguzwa.
Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuongeza jitihada katika maeneo hayo ikiwemo kuboresha vyuo vya ufundi kama vile vyuo vya wananchi ambavyo tumeshavichukua kwenye Wizara yetu pamoja na VETA, lakini pia kufungua vituo mbalimbali vya kujifunzia ukiacha katika mfumo rasmi hata mfumo usio rasmi ili baadaye hata wale wanaokuwa wanajifunza kupitia mifumo isiyo rasmi waweze kupata hizo stadi za kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa elimu ya
juu hivyo hivyo, wanafunzi wamekuwa wakifundishwa, lakini pia tumekuwa tukiangalia nchi mbalimbali zinaenda vipi kupitia workshops ambazo tunabadilishana mawazo, vilevile hata kupitia mitaala yetu. Kwa mfano siku nyuma elimu ya ujasiriamali ilikuwa haipo vyuoni, ilikuwa haifundishwi lakini sasa hivi tunazo degree, masters mpaka Ph.D za ujasiriamali. Kwa hiyo, tumekuwa tukifanya hivi na naamini tutaendelea kuzingatia kadiri tunavyopata mawazo mbalimbali ikiwemo ya kwenu Waheshimiwa Wabunge.
MHE. KITETO Z. KOSHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
Kwa kuwa mitaala ya elimu Tanzania inazingatia misingi na mahitaji ya kijamii hususan masuala ya utandawazi. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuweka somo la computer katika shule za sekondari na msingi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi tayari Serikali ilishaanza kuweka masomo ya computer au TEHAMA kwa ujumla katika shule zetu, isipokuwasiyo shule zote ambazo tayari zimeshapata hizo fursa kutokana na miundombinu halisi. Lakini kupitia hii miradi ya REA ambayo sasa karibu kila kijiji kinakuwa na umeme, vilevile karibu taasisi zote za umma ikiwemo shule zitakuwa na umeme. Kwa hiyo, tunaamini kwamba eneo la TEHAMA litaweza kupata nguvu zaidi na tayari wizara inafanyia kazi kuhakikisha kwamba wanafunzi wengi wanapata fursa ya kupata mafunzo hayo.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa takribani miaka miwili iliyopita kumekuwa kuna uhitaji mkubwa sana wa mafunzo ya ujasiriamali, lakini kumekuwa kuna walimu wanaofundisha chini ya kiwango. Serikali inasema nini kuwadhibiti walimu hao kwa kupunguza bei lakini pia kufundisha katika viwango ambavyo vinaweza kusaidia walaji ambao wengi ni wanawake?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, somo la ujasiriamali ni somo ambalo linaweza likafundishwa katika ngazi mbalimbali kama ambavyo wengi tunafahamu, ujasiriamali upo katika sura mbalimbali. Kuna ule ambao unakuwa informal ndio wajasiriamali hawa wadogo wadogo wanaanza, lakini kuna ule ambao unakuwa katika ngazi kubwa zaidi. Kwa hiyo kunaile kupata mafunzo ya awali na kupata mafunzo makubwa zaidi. Jambo kubwa ambalo ningependa leo Waheshimiwa Wabunge mlifahamu ni kwamba katika suala zima la ujasiriamali wengi tunafikiria ni ile kufanya biashara, kuuzauza labda vitu au maduka na vitu kama hivyo. Lakini ujasiriamali tunachotamani hasa watu wakifahamu, ni ile namna gani mtu anafanya shughuli zake kwa njia tofauti ili kuongeza thamani, kiasi kwamba hata Waheshimiwa Wabunge kufanya Ubunge pia ni ujasiriamali wa aina yake. Kwa hiyo, naomba tulizingatie katika sura hiyo.
MHE. RIZIKI S. MNGWALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na nishukuru kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri ameweka vizuri swali ambalo nilitaka kuuliza, ni hiyo hiyo kwamba kuja na misamiati ambayo mwisho wake tunaona kama tunakwama na pale mwanzo akazungumzia mpaka suala la bajeti. Lakini ni vipi Serikali sasa itarudisha katika shule za msingi na sekondari yale mafunzo au taratibu za elimu ya kujitegemea ambapo watoto walikuwa wanajifundisha kupika maandazi, kufuga kuku, kutengeneza mifuko na kazi kama hizo, hizo hazihitaji bajeti wala hazihitaji misamiati lakini watoto wakitoka pale wana ujuzi. Ni lini Serikali itafanya hivyo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba kupitia stadi za kazi wanafunzi wamekuwa wakipata muda wa kujifunza masomo kama hayo. Lakini kuna wakati sera zetu huwa zinakuwa kama zina mgongano kidogo. Kwa mfano kuna wakati tulisema kwamba wanafunzi wasipewe kazi, watoto wasipewe kazi, watu wakachukulia hiyo ni kufuta mpaka hizo stadi za kazi. Lakini kwa kuacha kufanya hivyo, tumejikuta tumerudi nyuma. Kwa mfano, katika shule tunazosema kwamba wazazi wachangie chakula, kwa kweli kupitia mashamba hasa kwa shule zile ambazo zina maeneo huko vijijini wangeweza kulima mashamba yao na wakapata chakula, watoto huku wakiwa wanajifunza na wakati huo wanapata chakula.
Kwa hiyo, mimi nitoe rai yangu kwa shule zote kuona kwamba stadi za kazi hasa kulingana na mazingira yetu ni ya muhimu sana nawapongeza sana shule kama sekondari ya Rugambwa, wao wanafanya vizuri sana.(Makofi)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Ni lini Serikali itarudisha mitaala ya shule za upili ili iweze kuzalisha mafundi mchundo na mafundi sadifu kama ilivyokuwa zamani watu hawa walizewa kujitegemea? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi binafsi nikiwa ni mnufaika katika eneo hilo niliweza kutembelea katika shule nyingi ambazo zinatoa mafunzo ya ufundi, ikiwemo Ifunda, Mtwara, Bwiru na kadhalika. Lakini kitu nilichojifunza ni kwamba zile shule baada ya kuzichanganya na wanafunzi ambao wanasoma kidato cha tano na cha sita imejikutwa kwamba kwa upande wa ufundi ni kama vile ufundi haupo. Vilevile baada ya kuwa VETA ina uwezo wa kuingiza wanafunzi moja kwa moja katika masomo ya ufundi sanifu.
Kwa hiyo, ilionekana lile eneo kama linakuwa reduntant, sasa baada ya hapo tuliita timu kutafakari namna gani tunaweza tukaendelea na shule hizo. Jambo tuliloliona ni kwamba kwa hali ya sasa ambayo elimu imeongezeka na shule nyingi zinatoa wanafunzi wanaofaulu vizuri mpaka kidato cha nne, tunafikiria kwamba hizo shule zirejeshwe katika kutoa mafunzo ya ufundi sanifu, lakini baada ya kujenga shule ambazo zitawachukuwa wale waliokuwa wanasoma kidato cha tano na sita ili kusiwe na upungufu katika eneo hilo, kwa hiyo hali halisi ndio hiyo.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha FDC Sikonge kinatakiwa kutoa mafunzo katika fani za useremala, uashi, uchomeleaji, ushonaji na ufundi umeme. Kutokana na upungufu wa walimu uliopo na uchakavu wa majengo, chuo kwa sasa kinatoa mafunzo kwenye fani ya umeme peke yake. Maswali yangu mawili, je, Serikali aione kuwa chuo hiki kinahitaji jicho la kimkakati ili kukiokoa?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, katika jibu la msingi ameahidi kwamba Chuo hiki kitatembelewa, kitatembelewa lini na nani? Ahsante sana.
NAIBU WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inatambua umuhimu wa kuviimarisha vyuo hivi ili kuweza kuchukua wanafunzi wengi zaidi na kutoa mafunzo yaliyo bora zaidi kulingana na uhitaji wa soko, lakini vilevile kuhakikisha kwamba wananchi wengi zaidi wanaweza kujiajiri wenyewe. Kwa upungufu alioainisha Mheshimiwa Mbunge tutatembelea chuo hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ujumla wake Waheshimiwa Wabunge ili tu-save muda, kimsingi mkakati ni kutembelea vyuo vyote vya FDCs ili kuona namna bora zaidi ya kuviendesha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la kwenda Sikonge nitakufahamisha Mheshimiwa, kimsingi tutaenda na kwa sababu Mheshimiwa Mbunge ni muhimu kuwepo, tutakujulisha twende wote ikiwezekana katika kipindi hiki cha bajeti katika weekend mojawapo.
MHE. EDWARD F. MWALONGO: Ahsante Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la nyongeza ninalo. Je, Serikali ina mpango gani ya kuwasaidia vijana wanaohitimu mafunzo ya ufundi kama hao wa Makete kupata angalau vifaa tu vya kuanzia kazi?
Swali la pili, Halmashauri ya Mji Njombe ina shule za sekondari 22 na zoezi hili la kujenga Vyuo vya Ufundi linaonekana sasa kwa Serikali limekuwa gumu sana na linakwenda pole pole sana.
Je, Serikali ipo tayari kupokea ushauri, sasa ianze kuzibadilisha baadhi ya shule za sekondari kuwa shule za ufundi ili kusudi vijana wetu walio wengi watakaokuwa wanahitimu Kidato cha Nne waweze kuwa mafundi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Kimsingi ni kwamba VETA imekuwa ikifanya hivyo baada ya kumaliza mafunzo ya ufundi kwa baadhi ya wanafunzi wanaohitimu wamekuwa wakipewa vifaa kwa ajili ya kuanzia shughuli zao za kiufundi, pia kusaidia kutengeneza clusters za hao wanaokuwa wamehitimu pamoja na wengine ambao wamekuwa wamehitimu mafunzo ya ufundi siyo tu kupitia VETA hata kupitia kwa wananchi wa kawaida, tunawatambua na kuweza kuwapa vifaa, vilevile kuwatambua rasmi na kuweza kuwapa vyeti.
Swali la pili la kuweza kubadilisha shule ziwe za ufundi, Wizara tayari tumeshaliona hilo na tunafikiria kubadilisha baadhi ya shule za sekondari hasa zilizokuwa shule za ufundi kama Ifunda, Mtwara, Tanga, Bwiru na shule ya Musoma ili ziweze kuwa vyuo vitakavyoweza kutoa mafunzo kwa ajili ya technicians.
Kwa hiyo, muda ukikamilika tutafanya hivyo na kwa mwaka huu tunategemea tuanze kujenga shule mbadala kwa sababu shule hizi zinachukua wanafunzi wa sayansi kwa kidato cha tano na sita na form one mpaka form four tunawajengea shule yao ili hayo majengo ambayo ni muhimu sana kama workshops yaweze kutumika kwa Vyuo vya Ufundi.
MHE. STELLA I. ALEX: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninaomba niendelee kutambua juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali kupitia Wizara hii na hasa pale ilipotamka wazi kwenye hotuba yake kwamba imetoa kipaumbele cha elimu kwa watoto wenye ulemavu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapoongelea elimu jumuishi tunamaanisha kwamba watoto wenye ulemavu wasome na wasio na ulemavu. Sasa Serikali inaonaje hii elimu maalum ikafundishwa kwenye vyuo vyote vya ualimu nchini tofauti na ilivyo sasa hivi kwamba ni walimu wachache wanaopata ujuzi huu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili katika hii mitaala mipya inayoandaliwa Serikali inaonaje ikaingiza lugha ya alama kuwa miongoni mwa masomo ambayo yatafundishwa ili kizazi kijacho kiweze kuwasiliana na viziwi kwa urahisi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stella Ikupa kama ifuatavyo; ni kweli ili wanafunzi hawa waweze kupata haki yao ya msingi ya kuweza kujifunza vizuri popote walipo ni pale tutakapokuwa na walimu wa kutosha ambao wana uwezo wa kuwasiliana na kutoa elimu husika kwa watoto hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii ni muhimu sana, lakini kwa sasa tunachoangalia ni kuona kwamba ni namna gani tunafanya hivyo, kwa mfano katika suala la lugha ya alama, Wizara tayari inaliangalia jambo hili ili kuwezesha walimu wote angalau wawe na msingi wa lugha ya alama ili kuweza kuwasaidia wanafunzi hao. Kwa hiyo, jambo hilo mimi naona tulichukue tuone ni namna gani tutalifanyia kazi. Kwa msingi huo nimejibu maswali yote mawili kwa pamoja, ahsante.
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa Waziri kunijibu majibu mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijauliza maswali mawili ya nyongeza, nitoe pole kwa wananchi wa Jimbo la Lushoto na Wilaya ya Lushoto kwa ujumla kwa mvua zinazoendelea kunyesha maana mpaka sasa hakuna mawasiliano kati ya Dar es Salaam - Lushoto, Arusha – Lushoto na Tanga - Lushoto. Nimeongea na Meneja wa TANROADS Mkoa akaniambia kwamba atashughulikia suala hilo. Hata hivyo, nikiangalia tatizo lile ni kubwa sana, madaraja yamekatika zaidi ya kilometa 32. Kwa hiyo, nipaze sauti Serikali ipeleke msaada maeneo yale haraka iwezekanavyo ili kunusuru maisha ya wananchi wa Lushoto na uchumi unaotegemea barabara ile. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kutoa pole hiyo kwa wananchi wangu wa Wilaya ya Lushoto na mkoa mzima kwa ujumla basi niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri amenijibu kwamba kwa kuwa Serikali itaanza ujenzi katika Wilaya ya Lushoto mara baada ya kukamilisha miradi ya Vyuo vya VETA vilivyoanza. Je, Serikali haioni kwamba itaendelea kulimbikiza vijana wengi wa Wilaya ya Lushoto bila kupata elimu ya VETA?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tayari kuna majengo ya kuanzisha Vyuo vya VETA je, Waziri yupo tayari kuongozana nami ili kwenda kuona majengo yale kama yanafaa na kutoa tamko la kuanzisha Chuo cha VETA? Hata kama VETA hiyo itaanzishwa chini ya mti, lakini naomba wananchi wangu hususani vijana wangu waweze kupata elimu hiyo ya VETA, hiyo ndio shida kubwa. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, si lengo la Serikali kudidimiza Jimbo la Lushoto na kimsingi Serikali imekuwa ikijitahidi kuhakikisha kuwa vyuo vilivyopo vinaweza kudahili wanafunzi wengi zaidi na ndiyo maana kwa sasa badala ya kusubiri tu kujenga chuo kipya, tunaona kuna haja pia ya kuongeza idadi ya mabweni katika vyuo vilivyopo ili kuchukua hata wanafunzi wa mbali. Kwa hiyo, lengo ni kuweza kujenga Chuo cha Lushoto muda muafaka utakapofika na fedha zitakavyopatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kuongozana naye kwenda kuona majengo yaliyopo, kwa moyo mkunjufu kabisa niko tayari na endapo majengo haya yataweza kufaa aidha kwa kutumiwa kama VETA au Chuo cha Maendeleo ya Jamii tutafanya hivyo.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali pamoja na mikakati mizuri ambayo Serikali inaiweka lakini ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa nina imani kwamba Waziri na Maprofesa wote mlioko ndani humu mmesoma bure A-Level na kwa sababu watoto hawa wanachaguliwa, wengine wanashindwa kuendelea na masomo haya kwa kukosa fedha, kwa sababu bado ni watoto wa maskini na wengine wamefaulu vizuri masomo ya sayansi pamoja na hesabu, je, Serikali haioni kwamba inapoteza vijana wazuri ambao wanaweza kusaidia Taifa?(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa hawa watoto wanaochaguliwa kuendelea na A-level ni wachache kuliko wale ambao wanahudumiwa na Serikali kwa maana ya O-Level, je, Serikali haioni kwamba ni wakati muafaka sasa wa kuleta bajeti ili tuweze kuwasaidia watoto hawa wa maskini ili waweze nao kusoma bure wafaidi matunda ya Serikali hii? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi Serikali ingependa kusomesha wanafunzi katika ngazi zote za elimu bure endapo uwezo ungekuwa wa aina hiyo. Kama nilivyosema ni kwamba awamu ya mwanzo tuliongeza shule za msingi lakini tukaja tukaongeza shule za sekondari kila kata na sasa hivi tunaendelea kuongeza shule za kidato cha tano na sita (A-level) kwa sababu ni chache ukilinganisha na wanafunzi wanaofaulu na hasa baada ya Serikali kuchukua jitihada za makusudi za kuongeza ubora wa elimu, imekuwa sasa wanafunzi wanaofaulu ni wengi na hivyo hatuwezi kuwaacha bila kupata elimu hiyo. Kwa hiyo, kabla hatujaweza kutoa fedha kwa kuwalipia hiyo ada, ina maana kama hawana sehemu ya kusomea itakuwa bado hatujafanya jambo la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili la kuongeza bajeti, hilo ni suala letu sote kama Wabunge. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais lakini pia Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye tukonaye humu, Wizara yetu ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ni kati ya Wizara ambazo zinapewa kipaumbele cha hali ya juu kwa kupewa bajeti kubwa kuliko Wizara nyingine. Kwa hiyo, naamini Serikali itaendelea kufanya hivyo.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Mheshimiwa Waziri, mimi kama mtaalam wa misitu, naomba hili swali lijibiwe tena, halikujibiwa, la kwanza hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na majibu haya ambayo wataalam wa Mheshimiwa Waziri wamejaribu kuzunguka, unaposema FITI ni Chuo Cha Misitu, Chuo cha Nyuki kwa nini umekiacha? FITI ni consumers siyo misitu. Tukisema foresters ni yule ambaye unampa mbegu anakupa product ama ya timber ama ya log, huyo ndiyo mwanamisitu, sio unayempa ubao akafanya processing. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo, hivi kweli Watanzania tunajiangalia kwamba misitu ina umuhimu kwa maisha yetu na vizazi vyetu na viumbe vingine vilivyomo katika ardhi? Hekta 5,000 kuhudumiwa na mtu mmoja, tuko serious kweli? Hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, unaposema katika kipindi cha miaka 10…
Mheshimiwa Naibu Spika, sawa. Swali la pili, unaposema una wanataaluma 3,500 katika kipindi cha miaka 10, ni wastani wa 350 kwa mwaka. Hebu tupe mchanganuo kwa sababu katika vyuo vyote darasa halizidi watu 40 na ni madarasa mawili tena ya certificate, wanaochukua degree hawazidi watu 50 kwa siku. Kwa hiyo, mnatoaje watu 350 kwa mwaka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza, pamoja na maelezo mengi ya utangulizi aliyotoa, nililoweza kulinukuu kama swali mahsusi ni kwamba, inawezekanaje hekta 5,000 zikahudumiwa na mtaalam mmoja wa misitu. Dunia inaendeshwa kwa sayansi na teknolojia, wataalam na miongozo mbalimbali. Mawazo na maoni ya mtu mmoja-mmoja yanaheshimiwa lakini yanatakiwa yakae ndani ya utalaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, wakati nasoma jibu langu nimenukuu kwamba takwimu hizi au viwango hivi vimewekwa kimataifa na vimewekwa na Shirika la Chakula Duniani la FAO. Sasa inawezekana Mheshimiwa Mbunge ana maoni mazuri zaidi kuliko yale ya Shirika la Kimataifa la Dunia, basi nafikiri maoni yake hayo afuate channels zinazofaa ili kuweza kwenda kuboresha hali hiyo kwa namna ambavyo ataona inafaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, nalo pia ni la takwimu. Anasema inampa mashaka kidogo kuona kama kweli tuna wataalam hao 3,500 kwa kuwa, kwa mujibu wa taarifa alizonazo yeye watalaam wanaozalishwa kwa mwaka kwa vyuo vyote ni 350, sasa ni muda gani utakuwa umepita huo kuweza kupata idadi ya watalaam hawa 3,500. Kwa sababu, hili ni swali linalohusiana na takwimu, swali lake hilo ili niweze kuwa kwenye nafasi nzuri zaidi ya kuweza kumwambia namna gani tumefikia hapo, basi anione kwa wakati muafaka, hata mchana huu nitaweza kumpa mchanganuo mzuri. (Makofi)
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kutokana na majibu ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kauli mbiu ya Serikali sasa ni viwanda, lakini viwanda havitakuwepo katika nchi hii kama hatutoweza kuzalisha mafundi mchundo wengi ili waweze kutekeleza majukumu mbalimbali ndani ya viwanda hivyo. Je, Serikali haioni kwamba inapoteza muda wa kutamka kwamba itakuwa ni Serikali ya viwanda wakati haitaki kuzalisha mafundi mchundo wengi ili waweze kutekeleza wajibu wao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika hali halisi
ya majibu ya Mheshimiwa Waziri jana wakati anajibu hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge alisema kwamba Serikali imejipanga kujenga Vyuo vya VETA nchi nzima na maeneo mbalimbali katika Taifa hili. Leo katika majibu yake anatuambia kwamba Serikali haina mpango wa kujenga Chuo cha VETA katika Mji wa Tunduma. Je, jana alikuwa akiwadanganya Wabunge katika majibu yake ya msingi aliyokuwa akiyatoa ndani ya Bunge hili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi Serikali inatambua juu ya umuhimu huo wa kuendelea kuzalisha mafundi sanifu na mafundi mchundo pamoja na wahandisi, lakini njia za kuzalisha mafundi hao haziko tu kupitia VETA, zipo pia kupitia vyuo binafsi lakini pia kupitia mafunzo ya muda mfupi ambayo wanafundishwa na kuweza hata kujitegemea katika viwanda vidogo vidogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huo upo, kwa mfano mwaka huu, kuna mafunzo ya vijana wapatao 23,000 ambayo yanaendeshwa na VETA ambayo ipo chini ya Wizara yetu lakini pia kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira, Vijana na watu Wenye Ulemavu kuhakikisha kwamba vijana wengi wanapata fursa hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusiana na majibu yangu kwamba jana nimesema tutajenga vyuo nchi nzima. Kwanza naomba nipende kuliomba Bunge lako Tukufu, naona kuanzia jana hiyo kama ulivyosema na pengine siku zote Waheshimiwa Wabunge pengine huwa hawanisikilizi vizuri ninapotoa majibu yangu kiasi kwamba wameanza kuniwekea maneno ambayo sijazungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema ni hivi Serikali ina dhamira ya kujenga Vyuo vya VETA katika kila Wilaya lakini vilevile kuhakikisha kwamba inaimarisha Vyuo vya Wananchi kila mahali vilipo ambapo vipo 55. Hata hivyo, kwa sasa kutokana na hali halisi ya kibajeti tumesema tutaimarisha kwanza vyuo vilivyopo na vile ambavyo vilishakuwa vimeanza mchakato wa kuanza kuvijenga. Kwa hiyo, sio kwamba tutajenga tu kila mahali bila utaratibu au bila fedha, naomba nieleweke hivyo tafadhali. (Makofi)
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Swali la msingi linaulizia kupata ujuzi na kujiajiri na ifikapo mwaka 2030 kwenye Maendeleo Endelevu ya Dunia, Lengo la Nne ni elimu bora sawa kwa wote. Je, Serikali imejipangaje kuwa na uendelevu wa kutoa masomo kwenye sekondari zetu yaani kwenye mitaala ya sayansi, biashara na kilimo badala ya kulazimisha watoto kuchukua sayansi tu ili iweze ikawa ni endelevu watoto wakaweza kujikita kwenye uelewa wao na stadi ambazo wanazipenda zaidi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru pia kwa swali zuri. Kimsingi hata sasa hivi kwenye baadhi ya maeneo tunazo shule hata za msingi ambazo zinatoa pia mafunzo ya ufundi, lakini vilevile tunaona kwamba kuna haja ya kuwapandikiza watoto wetu ujuzi kuanzia katika ngazi za elimu za msingi, sekondari na kuendelea ikiwemo masuala yanayohusiana na sayansi na mazingira au kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachokiona tu ni kwamba, kuna ugumu wa kusema kwamba kila jambo tunalolihitaji litawekwa kwenye mtaala kwa ajili ya huyo mwanafunzi. Kupitia vipindi vyetu vya elimu ya kujitegemea na mafunzo nje ya vipindi vya kawaida bado hawa wanafunzi wanaweza wakapata pia mafunzo kama hayo.
MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Ilani ya Chama cha Mapinduzi moja ya ahadi kubwa iliyotolewa ilikuwa ni kujenga VETA katika kila Wilaya Tanzania nzima. Kwa kuwa Mkoa wa Kagera unaongoza kwa idadi kubwa ya wanafunzi wanaomaliza darasa la saba na kidato cha nne lakini wanashindwa kujiendeleza kutokana na ukosefu wa vyuo hivyo. Je, ni lini sasa Serikali itahakikisha vijana hawa wanajengewa vyuo hivyo angalau hata katika Wilaya tatu za Mkoa wao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa Mkoa wa Kagera ni kweli kuna uhitaji wa fursa hizo, lakini tayari kuna Chuo cha VETA pale Makao Makuu ya Mkoa. Vilevile kuna Chuo cha Wananchi Karagwe (KVTC) ambacho tunaendelea kukifanyia ukarabati na sasa hivi tayari tupo kwenye hatua za mwisho ili kiweze kuchukua wanafunzi wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Gera ambacho nacho kilikuwa katika hali mbaya sasa hivi kimeshafanyiwa ukarabati na tutaendelea kukiboresha ili kiweze kuchukua wanafunzi wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa niseme kwamba, kwa Mkoa wa Kagera kuna fursa kubwa ambapo tuna chuo tunategemea kukijenga kule Muhengele ambacho kitakuwa kinatoa mafunzo ya ujuzi wa juu zaidi kidogo kulingana na mahitaji ya soko kwa kushirikiana na ndugu zetu wa China.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Chuo Cha Maendeleo ya Wananchi Tarime miundombinu yake ni mibovu sana na haina hadhi ya kuwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi. Kwa bajeti ya mwaka jana 2016/2017, Serikali iliahidi hapa kwamba Vyuo vyote vya Wananchi vitapandishwa hadhi na kuwa VETA. Napenda kujua sasa ni lini Serikali itaenda kutimiza azma yake ya kupandisha Vyuo hivi vya Wananchi kuwa VETA kwa kuanzia na Chuo cha Wananchi cha Tarime? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kuna dhana ya kufikiria kwamba labda mafunzo yanayotolewa na VETA ni bora zaidi kuliko yale yanayotolewa na Chuo cha Wananchi. Nitake tu kusema kwamba Vyuo vya Wananchi vina uwezo mzuri na mkubwa sana katika kutoa mafunzo isipokuwa kwa muda mrefu vilikuwa havijapewa haki yake ya kuendelezwa na kufanyiwa ukarabati unaostahili pamoja na kuwekewa miundombinu na vitendea kazi vya kufundishia kama inavyostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka huu Wizara imetenga jumla ya shilingi bilioni 12 kwa ajili ya kufuatilia vyuo hivyo na kuvirekebisha. Kwa hali hiyo, tutafuatilia pia Chuo cha Tarime kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbunge ili kiweze kusaidiwa.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikitishwa sana na majibu ya Wizara. Suala kwamba tuna wataalam wachache wa sayansi, sikubaliani nalo kwa sababu hivi karibuni tu Mheshimiwa Rais alikuwa ameishatoa kibali madaktari wetu 500 kwenda kufanya kazi nchini Kenya. Vilevile tunatumbua kwamba kuna manesi wengi wako mitaani hawajaajiriwa kwa sababu ya kukosa vibali.
Mheshimiwa Naib Spika, kwa hiyo, swali langu la msingi ninataka kuuliza ni kwamba ni kweli kwamba Mheshimiwa Waziri alitoa tamko na mimi nashukuru kwamba umesema waraka bado haujatoa na ninajua kwamba government moves with papers. Kwa kuwa masomo ya sayansi najua ni muhimu sana na kwa kuwa kwa bajeti ya mwaka huu ukiangalia tuna upungufu wa maabara nyingi sana, vilevile ili kumfanya mtoto asome sayansi inabidi kuwe na madarasa mazuri. Kwa mwaka huu tuna upungufu wa madarasa 158,000 na Serikali imesema inaweza ikajenga madarasa 2,000, hii ina maana itachukua miaka 79 kuweza kukamilisha hayo madarasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama lengo la Serikali ni kufanya watoto wetu wasome sayansi, nini mpango mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wanajenga mazingira mazuri na sio tu kutoa matamko wanafunzi wasome sayansi?
Swali la pili, kwa kuwa tunatambua kwamba nchi hii haihitaji tu wanasayansi bali pia inahitaji wengine, kwa mfano mameneja wanahitajika watu waliosoma, lawyers kama Mheshimiwa Naibu Spika na wengine, ni kwa nini sasa Serikali isihamasishe pia wanafunzi wasome masomo mengine kwa bidii?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba nijibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Waziri Kivuli wa Wizara yetu Mheshimiwa Susan Lyimo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ieleweke bajeti zote za Wizara zinapitishwa na Bunge lako Tukufu na Bunge hili linao uwezo mkubwa sana wa kusema jambo hili lipewe kipaumbele au jambo hili lisubiri kidogo, kama ambavyo tumeona kwenye Wizara ya Maji wote kwa pamoja tumesema iongezewe fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imekuwa ikijitahidi sana kuhakikisha inatafuta wafadhili kila kona ya dunia kuhakikisha kwamba tunapunguza tatizo hilo. Mfano ni madarasa ambayo yamejengwa mwaka huu zaidi ya madarasa 2,000, vyoo tulivyojenga na hali hiyo itaendelea kufanyika hivyo. Pamoja na kwamba kwa upande wako Mheshinimwa Waziri Kivuli unaona hakuna upungufu wa wanasayansi, nataka nikuhakikishie kutokana na mikakati ya Serikali ya kutaka uchumi uwe uchumi wa viwanda, uchumi wa viwanda unaendeshwa na sekta tofauti tofauti, kwenye kiwanda utahitaji watu wa afya, kwenye kiwanda utahitaji watu wa ujuzi wa ufundi, kwenye kiwanda utahitaji mambo mengi, lakini hali kadhalika kwenye sehemu zetu za kuhudumia afya zinahitaji wataalam wa aina hiyo. Kwa hiyo, ukiangalia kwa mapana yake huwezi ku-plan kwa kuangalia leo unaangalia kwa mapana, sisi tunaona iko haja kubwa sana ya wanafunzi wetu kuchukua masomo ya sayansi kwa wingi zaidi ili kukidhi maeneo ambayo bado yana upungufu.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni pamoja na hiyo ya kusema kwamba tunatamka tamka, niseme tu kwamba suala siyo kutamka, unapohamasisha lugha unayotumia ni yoyote inayowezeshwa kutoa hamasa kwa wale vijana na wakafanya maamuzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, samahani swali la pili la nyongeza yako naomba limenitoka kidogo, kama unaweza ukarudia.
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba labda awe pia anaandika wakati mtu anauliza ili isimletee shida. (Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili niliuliza kwamba kwa sababu nchi hii nadhani pia ameshalijibu amechanganya kwamba kwa sababu tunahitaji wataalamu mbalimbali ni kwa nini pia Serikali isihamasishe masomo mengine, kwa sababu hatuhitaji tu wanasayansi tunahitaji variety ya watu.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi mbali ya hayo niliyomjibu ninayo ya kumuongezea na nilikuwa nataka nijue kama na wewe bado unakumbuka swali lako vizuri. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la wanafunzi katika maeneo mengine Wizara yetu haijajikita kwenye sayansi peke yake. Kwa mfano sasa hivi tunaendelea kuona namna ambavyo tunaweza hata tukaingiza somo la kuwezesha wanafunzi katika masuala ya moyo (mindset). Unakuta mtu anao uwezo wa kufanya jambo lakini kwa sababu tu kimoyo hajawa tayari anashindwa hata kusoma. Kwa hiyo, kuna masomo mengi pamoja na hilo, lakini haya ya sayansi tumeyapa kipaumbele kutokana na uhaba wake mkubwa.(Makofi)
MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, napata taabu kidogo maana yake na mimi ni mwalimu, iwapo Serikali tutaacha kwenda kwenye specialization na tukafanya watoto wote wakasoma sayansi. Mimi nina wasiwasi kwamba tutapata wanasayansi wabovu zaidi.
Je, Serikali haioni kwamba specialization ni important kuliko ambavyo sasa tunakwenda kumfanya kila mtoto asome sayansi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, specialization inaanza na msingi na niseme tu kwamba tunawahitaji wataalam wa aina tofauti tofauti. Kuna hao specialization ambao wanakuwa wamekuwa vertical yaani anajikita katika eneo moja pia tunawahitaji wale ambao wanakua kimapana (wide knowledgeable people) ambao wanaweza wakaoanisha upande huu na upande huu. Kwa hiyo, katika ku-specialize kupo lakini lazima kuwe na msingi ni wa eneo gani ambalo huyu mtu atafanya specialization. (Makofi)
MHE. JOSHUA S. NASSARI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona.
Swali langu lilitaka kufanana kidogo na Mama Anne Kilango na nikichukulia mwenyewe kuwa mfano, lakini kwa sababu Mheshimiwa Naibu Waziri amekwishajibu labda nilisogeze mbele kidogo kwamba kama kweli lengo letu ni kuongeza idadi ya wanasayansi kwenye nchi hii na hususan walimu wa masomo ya sayansi kwenye shule zetu, ni kwa nini basi ile Programu ya Serikali ya Awamu ya Nne, Serikali ya Chama hiki cha Mapinduzi ambayo ilianzisha program maalum kwa ajili ya watoto, Chuo Kikuu cha Dodoma kwa ajili ya kutengeneza walimu wengi wa sayansi kwenye nchi hii, ni kwa nini basi watoto wale walifukuzwa mwaka jana tena kwa polisi na mbwa?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TAKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, wanafunzi wale hawakufukuzwa kwa sababu wako kwenye vyuo kumi ambavyo wanaendelea na masomo yao na bado Serikali inaendelea kuwalipia. (Makofi)
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Elimu imerithi Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi na Vyuo vya Maendeleo ya Jamii kutoka Wizaraya Afya. Je, kwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Msaginya kilichoko Jimbo la Nsimbo, Mkoa wa Katavi, kuna mkandarasi miaka miwili amesimama kazi anaidai Serikali. Je, Serikali ina mpango gani wa kumlipa ili kukamilisha ukarabati wa majengo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama Mkandarasi anadai, kimsingi kama ambavyo mnafahamu vyuo hivi vimeletwa kwenye Wizara yetu katika kipindi cha mwaka huu wa fedha unaoishia. Tunachofanya ni kwanza kuvitembelea na kuweza kuviangalia viko katika hali gani, kama kuna Mkandarasi alikuwa anafanya kazi eneo hilo na hakulipwa, Wizara tunao wajibu wa kumlipa lakini baada ya kufanya uhakiki na kujua kwamba kazi aliyoifanya inafanana na uhalisia na aweze kulipwa kwa kadri ya kazi yake.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu, hoja ya swali la Mheshimiwa Kishimba ni kwamba kumekuwa na utaratibu wa kumtahini mwanafunzi kwa mtihani wa mwisho na wakati mwingine unakuta mwanafunzi pengine zile siku za mwisho anakuwa na matatizo ambayo yanamfanya ashindwe kufaulu vizuri.
Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuangalia maendeleo ya mwanafunzi huyu ili kusudi maendeleo yake yawe ni sehemu ya mtihani wake wa mwisho ili kuondoa mchanganyiko huu?
Swali la pili, kwa vile kumekuwa na wizi wa mitihani mara kwa mara na hii inachangiwa kwa sababu wanafunzi wanajiandaa kwenda kushinda mtihani badala ya kujua namna ya kujibu mtihani.
Je, Serikali inatafuta mbinu gani mbadala za kuwasaidia vijana badala ya kukariri kufanya mtihani, wafanye mtihani kwa kuelewa namna ya kushinda mtihani?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, Serikali imekuwa ikifanya hivyo kwa kutumia matokeo endelevu yaani mwanafunzi amekuwa akipimwa katika muda wake anaokuwa darasani, vilevile hata wale wanaofanya shughuli za vitendo, kwa mfano wale wanaosoma masomo ya ufundi wamekuwa wakienda kwenye mazoezi wanafuatiliwa na pia shughuli za vitendo zimekuwa zikichangia asilimia 30 niliyosema katika mitihani ya mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mtihani wa mwisho ni kweli ndiyo unakuwa na nafasi kubwa zaidi kwa ajili ya hiyo asilimia 70; endapo mwanafunzi amepata tatizo siku ya mwisho ya mtihani, taarifa huwa zinatolewa na kuweza kuangalia kwamba alikuwa kwenye mazingira gani. Wakati mwingine mwanafunzi anashauriwa asifanye mtihani kama hali yake kwa mfano itakuwa ni ya ugonjwa ili aweze kurudia na kufanya mtihani wakati mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa wizi kwa kiwango kikubwa Serikali imeweza kudhibiti tatizo hilo, nanyi mtakuwa mashahidi katika kipindi hiki, hasa toka tumeingia halijawahi kutokea tatizo la wizi wa mitihani. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na ningependa kuweka msisitizo kwenye suala la wizi wa mitihani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kulihakikishia Bunge lako kwamba Serikali imedhibiti suala la wizi wa mitihani na kinachotokea ni udanganyifu katika mitihani, ambapo baadhi ya Walimu ama huwa baada ya kufungua zile karatasi za mitihani wanaenda pembeni wanawaandalia wanafunzi majibu na kuyapeleka katika chumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Serikali imekuwa pia makini katika kuhakikisha kwamba inaangalia kwa karibu usimamizi wa mitihani na wote ambao wanakuwa wanajihusisha na udanganyifu katika mitihani hatua zimekuwa zikichukuliwa na zitaendelea kuwa zinachukuliwa.(Makofi)
MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa swali la Mheshimiwa Kishimba linafanana kabisa na changamoto ya udanganyifu wa mitihani yaani thesis and dissertation kwa wanafunzi wa shule ya Uzamili na Uzamivu elimu ya juu.
Je, Serikali imejipangaje kuwa na mfumo mahsusi katika kudhibiti ubadhilifu wa mitihani kwa maana ya kuwa na mfumo mathalani central system plagiarism test? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika masuala haya ya kuhakikisha kwamba wanafunzi wanafanya mtihani na wanapimwa kwa kiwango wanachostahili kwa kadri ya kuwapima uelewa wao, Serikali tumeendelea kufanya hivyo. Kwa upande wa vyuo vikuu hasa kwa upande wa wanapofanya maandishi yao, niseme thesis kwa mfano, kweli kumekuwa kunajitokeza udanganyifu wa watu kuomba ama kufanyiwa na watu, wakati mwingine kunakili maandiko ya watu wengine waliopita kiasi kwamba mtu anakuwa hajafanya kazi yake na kupimwa kwa haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali imeshaliona hilo na tumeshaandaa mfumo kiasi kwamba kila mtu akishamaliza andiko lake litakuwa linapitishwa humo kiasi kwamba likioanishwa litajulikana kwamba huyu ameiba kutoka kwa andiko la mtu mwingine. Ikizingatiwa katika mfumo huu wa digital watu ni rahisi kuiba. Kwa hiyo tumeshaona namna ya kudhibiti eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa elimu ya sekondari ngazi mbalimbali tunafanya uhakiki. Kwa mfano, mara hii ya mwisho hata sisi wenyewe Mawaziri tumekuwa tukitembelea baadhi ya shule za kidato cha sita kuona kwamba taratibu na sheria zinazingatiwa katika sehemu za mitihani. Mfano, safari hii nimeenda shule ya Ifunda na shule ya Iringa Girls. Hivyo tunasimamia kikamilifu.
MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Pamoja na kuwa lugha yetu ya Taifa ni kiswahili lakini kumekuwa na mkanganyiko katika mfumo wetu wa ufundishaji wanafunzi. Shule nyingi za Serikali kuanzia darasa la kwanza mpaka la saba wanafundisha kwa kiswahili lakini wakifika sekondari wanaambiwa wazungumze lugha ya kiingereza. Sambamba na hilo, tatizo hili liko kwenye vyuo vyetu vya Serikali ya Mitaa hususan Hombolo. Masomo yote yanafundishwa kwa kiingereza ilhali watu hawa wanaenda kusimamia watu ambao hawajasoma.
Je, Serikali haioni ni muhimu kubadilisha mitaala hii kuondoa mkanganyiko huu katika sera ya ufundishaji?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza tunamshukuru kwa kuwa ni mdau wa kiswahili na kwa namna ya pekee nimpongeze Mheshimiwa Mama Salma Kikwete kuwa Balozi wa Kiswahili Afrika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika elimu ya msingi kiswahili imekuwa ndiyo lugha ya kufundishia na kiingereza inakuwa kama somo. Tunafanya hivyo kwa sababu tunaamini Watanzania wengi lugha ya kiswahili japokuwa ni lugha ya pili, lakini wana uelewa zaidi na hivyo kuwawezesha kuelewa vizuri elimu yao ya msingi katika lugha ambayo wamekuwa nayo. Hali kadhalika tunapokwenda kwenye sekondari ndipo sasa wanapotumia lugha ya kiingereza kama lugha ya kufundishia na kiswahili kama somo na hiyo sasa inaenda vilevile kwa upande wa zile shule zinazotumia lugha za kiingereza toka awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwalimu hakatazwi kuweka msisitizo katika lugha ile ambayo anafahamu inaeleweka na wanafunzi kwa uzuri zaidi ili kumfanya yule mwanafunzi kile kilichofundishwa aweze kukitafsiri katika lugha yake iliyo rahisi na kukielewa vizuri zaidi. Ieleweke kwamba lugha pekee siyo maarifa. Lugha pamoja na yale maarifa unayofundishwa ndiyo yanayomfanya mwanafunzi kuwa imara na kuweza kutumika katika nyanja mbalimbali zinazohitajika. (Makofi)
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nazungumzia shule hizi ambazo tunazijenga kutokana na umbali wa shule mama. Kuna maeneo ni zaidi ya kilometa 20 watoto wanatembea, hata hawa kuanzia darasa la nne mpaka darasa la saba wanatembea zaidi ya kilometa 20 kwenda na kilometa 20 kurudi, tunasababisha wasichana kukatisha masomo yao kutokana na kupata mimba, lakini pia tunasababisha wavulana kuona hakuna umuhimu wa kwenda kusoma kwa sababu ya umbali wa shule hizi.
Je, kwa nini sasa Serikali haioni umuhimu wa kutumia kigezo hicho kuzisajili shule hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili Mheshimiwa Waziri amesema moja ya sababu ya vigezo vinavyoweza kufanya shule hizo zisisajiliwe ni kutokuwa na ofisi za Walimu Wakuu na kadhalika kama alivyovitaja. Baadhi ya shule zetu nyingi hizo tunazoziita za satellite zimeshajengwa kwa asilimia zaidi ya 80 zimekamilika lakini bado hazisajiliwi. Wakaguzi wakija wanatoa kila siku sababu mpya. Kwa nini shule hizi ambazo zimetimiza zaidi ya 80% ya vigezo zisijaliwe? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni lengo la Serikali kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaotakiwa kusoma wanasoma, kwa hiyo shule hizi zinapoanzishwa ni vema kukawa na ushirikishwaji vizuri. Kwa mfano kuanzisha shule katika maeneo ambayo yanatambulika rasmi, kama ni vijiji ni vijiji rasmi isiwe ni yale maeneo ambayo watu wanaenda labda pengine kwa shughuli za kilimo za msimu tu halafu wakasema kwamba wanaanzisha shule kwa sababu shule inatakiwa iwe endelevu.
Sasa kama kuna shule ambazo zimeanzishwa kwa mujibu wa kamati za shule zinatambua na kwa jinsi ambavyo wananchi walioko huko ni wengi wa kutosha na kuna hiyo miundombinu ya kutosha na bado haijasajiliwa, basi mimi nashauri wafuate tataribu na mimi nitakuwa tayari kusaidia kama hizo shule zinakidhi vigezo husika.
MHE. ALEX R. GASHAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Pamoja na jitihada za Serikali kudhibiti taasisi ambazo zinatoa elimu na mafunzo ambazo hazijakidhi vigezo kwa maana ya kusajiliwa bado kuna taasisi ambazo zinaendelea kufanya hivyo, kwa mfano ni Chuo kimoja ambacho kinaitwa Dodoma College of Business Management ambacho kiko hapa Dodoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe au niseme Mheshimiwa Waziri anaweza kufuatilia na kujiridhisha kuona kwamba Chuo hiki cha Dodoma College of Business Management hakijasajiliwa? Kwa sababu kinasababisha hasara kwa watoto, kwa miaka minne mfululizo chuo hiki kimekuwa kikitoa vyeti ambavyo havitambuliwi na NACTE wala VETA yuko tayari kufuatilia na kujiridhisha?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kusema kwamba ni marufuku Chuo ambacho hakijasajiliwa rasmi kuanza kutoa mafunzo na kuanza kukusanya ada kwa wazazi kiasi cha kusababisha usumbufu baadaye. Vilevile kwa hicho chuo ambacho unakizungumzia nitaomba nipate taarifa ili tuweze kukifuatilia.
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Kwa sababu katika Wilaya ya Mkalama ziko shule shikizi ndio hizo satellite schools za Ilangida, Songambele, Ilama pamoja na Mkola ambazo zinafanya kazi lakini hazijasajiliwa. Na TAMISEMI tuliona udahili au uandikishaji unakuwa ni wa kiasi kidogo kwa sababu wanafunzi wengine wadogo wanashindwa kwenda mbali.
Je, Waziri yuko tayari kuingilia suala hili na kuhakikisha shule hizo nne zimesajiliwa, ambapo zimeshajengwa na miundombinu ipo kwa asilimia 80 kama alivyosema muuliza swali?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi kama nilivyosema hapo awali kama shule inakidhi vigezo na inastahili kupata usajili basi ni suala la kuwasiliana tuweze kufanya hivyo.
MHE. SHABANI O. SHEKILINDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, wakati Waziri anaendelea kufanya utafiti juu ya Grafo Gemu, je, Serikali ina mpango mkakati gani wa haraka wa kuweza kuwapatia baadhi ya vifaa ili wataalam wetu hao waendelee kuwasaidia watoto wetu pamoja na kwamba suala hili litakuwa ni suala la Kitaifa?
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni ya hapa kazi tu; je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuongozana na mimi wakati Bunge likiahirishwa ili akaone juhudi za wataalam hawa watokao SEKOMU wanaofanya kazi kubwa kuwasaidia watoto wetu hasa mama yangu mtaalam anaitwa mama Gorosho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimezungumza kwamba Wizara ingependa kujiridhisha namna gani teknolojia hiyo inavyofanya kazi na namna gani inavyoweza kuwanufaisha wanafunzi wengi zaidi na wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyo kawaida yetu sisi Waheshimiwa Mawaziri wengi tumekuwa tukiambiwa kutembelea maeneo na tunafanya hivyo. Kwa hiyo, nimwambie tu kwamba nitakuwa tayari kutembelea katika eneo la Mheshimiwa Mbunge ili kujiridhisha lakini vile vile kuona uwezekano wa kutoa vifaa ambavyo vitahitajika kama ambavyo ameomba. Namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake. (Makofi)
MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwanza ni vizuri Serikali ikakiri kwamba imeshindwa katika Sera hii ya Elimu Bure na nitatoa mfano. Fedha wanazopeleka katika shule zetu asilimia 35 ni fedha kwa ajili ya utawala na chini ya utawala kuna mambo matano yafuatayo: Kuna stationery, maji, walinzi, umeme na dharura. Nitoe mfano katika sekondari moja ya Babati, sekondari ya Bagara – wanapeleka milioni moja na laki saba asilimia 35 ni 302, 4716.55. Katika 324,000 mlinzi analipwa 150,000, maji 200,000 acha stationery, acha dharura, kwa hali ya kawaida walinzi wameshaondoka katika shule zetu. Maji yamekatwa katika shule zetu za msingi na sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini hawataki kueleza ukweli kwamba wameshindwa kutekeleza sera hii kwa sababu shule zetu zimeachwa sasa na hakuna maji. Naomba majibu ya Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa wamefanya uchambuzi huu tangu Februari, 2017 mpaka sasa hawajarekebisha haya, ni kwa nini sasa wasiruhusu wazazi wachangie maji na walinzi katika shule zao kwa sababu sasa ukitaka kuchangia tu wanasema Serikali inapeleka fedha wakati Serikali haipeleki. Watoe mwongozo tuchangie kuliko watoto wetu wakose maji na walinzi waache shule zetu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Serikali haijashindwa! Narudia tena kusema, Serikali haijashindwa! Kwa nini nasema Serikali haijashindwa? Nimeshatembelea mikoa mingi sasa hivi, nimeshatembelea shule nyingi sasa hivi, kimsingi wanashukuru sana kwamba sasa kuna utaratibu wa wazi wa kupeleka fedha hizo kwenye shule. Wao wenyewe wanapanga, isipokuwa, lazima nikiri bado yapo matatizo machache yanayohitaji kurekebishwa. Tatizo mojawapo lilikuwa ni kutokuwa na ubora wa takwimu. Kuna baadhi ya shule zilikuwa hazijaweza kuleta takwimu zilizo sahihi na hapo ndipo tulipoweza kubaini hata wanafunzi hewa na hivyo tukaweza hata ku-save baadhi ya fedha takriban shilingi milioni 720 zilizokuwa zinaenda zikiwa hewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mheshimiwa Rais na sisi kupitia Wizara hizi mbili tumekuwa tukisema kila wakati kwamba, wazazi wasijitoe katika kuendelea kusaidia elimu nchini. Pale panapoonekana kuna mahitaji ya msingi zipo taratibu zimeshatolewa mwongozo, Kamati za Shule kushirikiana na wazazi kuweza kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nadhani nimejibu yote kwa ujumla. Kwa hiyo, ninachomwomba tu Mheshimiwa kule kwenye jimbo lake aendelee kuhakikisha anashirikiana na Kamati za Shule lakini pia na uongozi kuona kwamba elimu hii tunaishughulikia wote kwa pamoja na hili sio suala la kusema nani afanye, nani asifanye! Mzazi anao wajibu wa kwanza katika kuhakikisha mwanafunzi wake anasoma vizuri. (Makofi)
MHE. GIMBI D. MASABA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Waziri alivyosema kwamba usanifu wa majengo utakamilika mwezi Novemba 2017, swali langu linauliza, ni maeneo gani yaliyobainishwa kujengwa chuo hicho? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, wakati Serikali inaendelea na mpango wa kujenga Chuo cha VETA Mkoa wa Simiyu, Serikali ina mpango gani kuwasaidia vijana wanaomaliza kidato cha nne wanaokosa sifa ya kuendelea na kidato cha tano? (Makof)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Spika, Chuo cha Mkoa cha Simiyu kinategemewa kujengwa eneo ambalo lipo umbali wa takribani kilometa tisa mpaka kumi ambapo kilikuwa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC), eneo linalojulikana kama Kinamhala, nashindwa kidogo kutamka jina hilo, lakini ni eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, vilevile katika swali lake la pili juu ya Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na hawajafanikiwa kidato cha tano. Kwanza ni kwamba tunavyo vyuo mbalimbali vinavyoweza kuchukua wanafunzi wa aina hiyo lakini vilevile Serikali kupitia mpango mpya wa ESPJ, mpango ambao unajipanga katika kuzalisha ajira nyingi kwa vijana wetu wale waliomaliza darasa la saba, kidato cha nne na ngazi nyingine zote ili waweze kupata ujuzi kamili wa kuweza kujiajiri. Kwa hiyo, kuna fedha tumeshapata nyingi kabisa, niwafahamishe tu Waheshimiwa Wabunge, Waziri wangu ameshatoa maelekezo kuwa kutakuwa na semina kwenu ya kuwapitisha juu ya mpango huo ambao utakuwa na manufaa makubwa sana katika nchi yetu.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa SIDO ndio wanaohusika kutoa elimu kwa wajasiriamali wadogo lakini imeonekana wanachaji pesa kubwa sana hasa mafunzo ya vifungashio. Ninaomba Mheshimiwa Waziri atusaidie ni jinsi gani SIDO itapunguza bei na kusaidia hao wajasiriamali wadogo waweze kufanikiwa katika biashara zao? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, kimsingi bei iliyokuwa inakuwa-charged ilikuwa inategemeana na gharama halisi za upatikanaji wa vifungashio hivyo. Jambo ambalo tunaweza tukafanya ni kuendelea kuangalia uwezekano wa kuipatia SIDO ruzuku ya kutosha lakini pia kuwakaribisha watu binafsi katika kutengeneza vifungashio hivyo kwa kadri itakavyowezekana.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa majibu ya Serikali, kwa kuwa wananchi wa Bukene wamepata fursa nzuri ya kupata umeme na wananchi wa Bukene wamejipanga katika shughuli nzima ya ujasiriamali na tatizo kubwa wao wana ukosefu wa mitaji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwawezesha wananchi wa Bukene ili waweze kupata mitaji na waweze kuanza shughuli za ujasiriamali?
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Katavi una fursa nyingi za uwekezaji na vivutio vya kutosha hasa kwenye sekta ya kilimo, uvuvi na eneo la maliasili. Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara wana mpango upi wa kusaidia Mkoa huu ili kuweza kupatiwa wawekezaji waje kuwekeza katika maeneo hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, la kwanza katika suala la mitaji, nipende tu kuwahamasisha wananchi wote wakiwemo wananchi wa Bukene kwamba mtaji wa kwanza ni mtu kuamua kufanya shughuli ya uzalishaji, mtaji wa pili ni huo wa kupata taarifa na mafunzo, lakini vilevile kufuatilia taasisi kama za benki na kwa upande wetu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupitia SIDO kama nilivyosema awali, tunao mfuko ambao unawezesha wajasiriamali pale ambapo wapo serious katika kufanya shughuli zao.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Katavi niwaombe kupitia Serikali ya Mkoa na Halmashauri na wananchi kwa ujumla kuendelea kuhamasisha fursa zilizopo katika Mkoa wa Katavi ili wawekezaji wengi wa ndani na wan je waweze kupenda kuwekeza katika Mkoa huo. Kwa siku za nyuma mmekuwa mkifanya makongamano mbalimbali ya kukaribisha wawekezaji, nashauri muendelee kufanya hivyo.
MHE. BALOZI DKT. DIODORUS B. KAMALA: Mheshimiwa
Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu lakini ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa Kenya iliruhusiwa kuuza bidhaa zake zinazozalishwa EPZ asilimia 20 bila kodi jambo ambalo alitakiwi, lakini kwa nini wakati huo huo baada ya muda mfupi Kenya hiyo hiyo ikaruhusiwa mitumba inayotaka nje badala ya kutozwa senti 40 kwa kilo watoze senti 20 kwa kilo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa nchi za Ethiopia, Afrika ya Kusini, India, Morocco na nyinginezo zinatoa mkakati maalum wa kusaidia viwanda vya nguo na ngozi ili watu waweze kuwekeza kwenye sekta hizo kwa kutoa garantees walau ya miezi ya sita na baadaye Serikali inajiondoa na wazalishaji wanaendelea na kwa kufanya hivyo Ethiopia na nchi nyingine zimefanya vizuri Je, Tanzania tuko tayari walau kujifunza kidogo kutoka katika nchi hizo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza suala la nguo pamoja na mitumba ni suala ambalo ni nyeti na suala ambalo linahusu viwanda vyetu vya Afrika Mashariki kwa ujumla. Kimsingi ni kwamba kufuatia maombi hayo kumekuwa na mambo mengine ambayo yameendelea ambayo yameendelea kujadiliwa na nchi. Lakini kubwa zaidi ni kama nilivyosema awali kwamba swala hilo lilikuwa limejadiliwa na Wakuu wetu wananchi.
Kwa hiyo, mabadiliko mengine yoyote yale ni muhimu lazima yarudi tena kwa wakuu wetu wa nchi na misingi hiyo naamini kwamba Serikali kwa kushirikiana na nchi ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kwa ujumla wake tutapata ufumbuzi wa mambo ambayo yanayoonekana labda pengine yanakuja kuwa ni kikwazo hasa katika kuhakikisha kwamba bidhaa zinazotoka kwenye nchi zetu zinalindwa vilevile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili kuhusiana na kujifunza kutoka nchi nyingine za Morocco na kadhalika. Kimsingi wajasiriamali hawa wawekezaji wanapokuja kwenye nchi wanakuja na mitaji lakini wanakutana na sheria mbalimbali ambazo kwa upande mmoja zinakuwa zinasaidia kuwezesha uwekezaji huo, lakini upande mwingine inaweza ikatokea kwamba kuna vikwazo na sisi tumekuwa tukiendelea kujifunza na kuona namna bora zaidi ya kuwasaidia wawekezaji wetu ili waweze kukua na kuendeleza viwanda vinavyowekezwa na ajira kwa ujumla.
Kwa hiyo, ni wazo jema tutaendelea kujifunza na vilevile kuona namna bora kadri inavyoonekana kila siku ya kuweza kuwasaidia wawekezaji wetu.
MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. Pamoja majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Viwanda napenda kuuliza maswali kama ifuatavyo.
Swali la kwanza; kiwanda cha Nyuzi cha Tabora kinazalisha vifa tiba ambavyo vinatangenezwa na pamba yetu inayolimwa hapa hapa nchini. Inazalisha vifaa kama pamba, bandage na nyuzi. Je, kwa nini Serikali kupitia MSD isimuunge mkono Mheshimiwa Rais maneno yake aliyotamka Mwanza na kununua vifaa tiba kwenye viwanda vyetu vya ndani hususan Tabora badala ya kuagiza nje ya nchi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kiwanda hicho kina uwezo wa kutengeneza sare za wanafunzi (uniform). Kwa nini sasa Serikali isitoe agizo, badala ya kununua sare za shule sehemu tofauti, sare za shule zinunuliwe kwenye viwanda vilivyopo nchini? Kwanza, ili kuchochea uchumi pia kupanua ajira hususan katika Mkoa wetu wa Tabora ambao kwa kweli hauna viwanda vya kutosha. Naamini vijana wetu wa Tabora watapa ajira za kutosha kama sare zitanunuliwa katika kiwanda hicho cha nyuzi cha Tabora.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ni kweli kabisa iko haja ya kuunga mkono jitihada zinazofanywa na viwanda vyetu nchini ikiwemo vifaa tiba. Kimsingi viwanda hivi wakati vinaanzishwa vilikuwa na lengo la kusaidia kutoa malighafi katika viwanda vingine, lakini baada ya kuanza biashara huria na mikataba mbalimbali tuliyosaini Kimataifa, tumejikuta kwamba baadhi ya viwanda vyetu vinashindwa kuzalisha kutokana na wadau waliokuwa wanunue vifaa hivyo kutoka kwetu wanaamua kuagiza kutoka nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, hilo ni suala ambalo Wizara tayari tumeshaliona na tunalifanyia kazi. Vilevile kuimarisha masoko ya ndani na nje kwa hiyo kitengo chetu kitaendelea kufanyia kazi eneo hilo na hivyo niwaombe MSD waweze pia kufuatilia na kuweza kununua pamba na bandage zinazozalishwa katika kiwanda hiki nasi tutafutilia.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusu uniform; naomba vilevile kuwashawishi wadau mbalimbali ambao wanatumia uniform zinazofanana na zile zinazozalishwa katika kiwanda hiki waweze kukipatia kipaumbele pamoja na viwanda vingine ambavyo viko humu nchini. Niwaombe pia Watanzania wote kupenda bidhaa zetu kwanza. Tufahamu kwamba viwanda hivi vinapokufa vinakosesha ajira kwa watu wetu na kwa kweli uzalendo ni kutumia mali zetu za ndani. (Makofi)

WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nichukue fursa hii kumshukuru na kumkaribisha Naibu wangu mpya. Napenda nitoe jibu la nyongeza kuhusu bidhaa tiba za Tabora Textile.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Mbunge Munde Tambwe kwa jinsi alivyopigana kufufua kiwanda hiki, watu wa Tabora watamkumbuka. Nataka nisisitize tamko la Mheshimiwa Rais, Wawekezaji wa Tabora Textile na wote mnaozalisha vifaa tiba nendeni sasa hivi MSD, msisubiri MSD iwafuate. Ni agizo la Rais kwamba MSD kwanza inunue vifaa vinavyotengenezwa hapa ndiyo maana ya kutenga bilioni 269 kwa ajili ya tiba. Kwa hiyo wote nendeni mkanunuae vifaa pale, mkauze vifaa vyenu pale kwa kufuata taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hili la uniform, hili wazo la uniform namshukuru Mheshimiwa Tambwe, maamuzi yetu sasa tutaleta mapendekezo kwenu na watu wasituletee mambo ya WTO. Tukiweza kununua uniform kutoka kwenye viwanda vyetu vya nguo, tutaweza kuchochea viwanda vyetu kufanya kazi na kutumia pamba yetu badala ya kununua nguo zisizofaa zinazotoka nje ya nchi. Hiyo italeta kelele tunategemea ninyi Wabunge mtusaidie kutetea viwanda vyenu vya ndani. Ahsante. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na nashukuru kwa majibu hayo yanayoonesha jitihada za Serikali katika kusaidia watu wenye ulemavu. Pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza. Kama alivyoeleza Mheshimiwa Naibu Waziri, ningependa kujua sasa (time frame) ni lini mchakato wa kukusanya maoni ya wadau utakamilika na kwa kuwa ni miaka minne sasa na wenzetu wa Kenya tayari wameshasaini mkataba huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kutokusainiwa kwa mkataba huu wa Marrakesh kumesababisha watu wenye ulemavu wasioona kushindwa kwenda na wakati na kuendelea kuwa maskini na hasa kutokana na kukosa fursa mbalimbali za kujiongezea kipato, fursa hizo ambazo zinapatikana kwenye maandishi zinazohusu maendeleo ya nchi lakini pia ulimwengu kwa jumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba majibu hayo.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Mollel kwa jitihada kubwa anayoifanya lakini pia yeye mwenyewe atakuwa shahidi, Mheshimiwa Rais wetu amekuwa ni mdau mkuu namba moja katika masuala yanayohusu watu wenye ulemavu na ndiyo maana unaona hata kwenye Baraza tayari kuna watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa misingi hiyo jambo hili tunalichukua kwa uzito mkubwa na tutahakikisha kwamba mapema iwezekanavyo baada tu ya kumaliza hili zoezi wanaloendelea nalo lipelekwe kwenye vikao vya wataalam na kikao cha Makatibu Wakuu na hatimaye liende kwenye Baraza la Mawaziri. Mheshimiwa Waziri wangu amekuwa akilifuatilia sana suala hili na najua nadhani umeona hata anakuja kusisitiza kwamba tutafanyia kazi haraka iwezekanavyo ili watu wenye ulemavu wapate haki zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nikijibu swali la pili ni kwamba, tunatambua watakapoweza kupata machapisho ya aina mbalimbali bila vikwazo itawasaidia pia hata wao kuona namna ya kuweza kuondokana na umaskini. Kwa hiyo, naomba sana ajue kwamba suala hili tumelichukua kwa uzito mkubwa ikizingatiwa kwamba wote sisi ni walemavu watarajiwa. (Makofi)