Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Jenista Joackim Mhagama (8 total)

MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN aliuliza:-
Kuna idadi kubwa ya vijana wa Tanzania ambao wanafanya kazi nje ya nchi zikiwemo kazi za ndani (house girls):-
(a) Je, kuna utaratibu gani unatumika kwa vijana hao kwenda kufanya kazi hizo nje ya nchi?
(b) Je, vijana wangapi wanafanya kazi hizo nje ya nchi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ili kuratibu ajira za Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi, Serikali imeweka utaratibu wa kutumia Wakala wa Serikali wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA) na kurasimisha wakala binafsi wa huduma za ajira ambao wana jukumu la kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri wa ndani na nje ya nchi. Kabla wakala binafsi hajampeleka mfanyakazi nje ya nchi anapaswa kuwasiliana na TaESA kwa lengo la kuhakiki mikataba ya kazi na kupeleka taarifa za mfanyakazi kwa Balozi wetu katika nchi husika.
Mheshimiwa Spika, aidha, sheria haikatazi Mtanzania kujitafutia kazi na kwenda kufanya kazi nje bila kupitia utaratibu huu. Hivyo, wapo baadhi ya Watanzania wanaokwenda nje kufanya kazi kwa utaratibu wao binafsi. Napenda kuchukua nafasi hii kuwaomba wananchi wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi kufuata utaratibu mzuri uliowekwa na Serikali ambao utawawezesha kusaidiwa na Serikali hususani wakati wanapopata matatizo kupitia Balozi zetu.
Mheshimiwa Spika, jumla ya Watanzania wapatao 4,992 waliopitia utaratibu rasmi uliowekwa na Serikali kupitia TaESA wanafanya kazi nje ya nchi yetu ya Tanzania.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:-
Katika Ilani ya CCM 2016/2017 Serikali imeahidi kuinua kipato cha mwananchi mmoja mmoja:-
Je, ni lini Serikali itaanza kutoa fedha kiasi cha shilingi 50,000,000 kwa kila Kijiji au Mtaa ili kuwasaidia wananchi kuboresha mitaji yao?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Ruvuma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imetenga shilingi bilioni 59.5 katika bajeti ya mwaka 2016/2017 chini ya Fungu 21, kwa ajili ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 ya kupeleka shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Fedha hizo zitatolewa baada ya kukamilisha taratibu mahususi zinazolenga kuhakikisha uwepo wa tija, katika matumizi ya fedha hiyo. Hivyo namwomba Mheshimiwa Mbunge Jacqueline, asubiri utekelezaji wake kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017. Mara baada ya kukamilika kwa mfumo na muundo wa utekelezaji wa zoezi zima, ambapo kazi hii imeshaanza kufanyika.
MHE. KHATIB SAID HAJI aliuliza:-
(a) Je, bado kuna faida kwa Watanzania kuendelea kukimbiza Mwenge wa Uhuru kila mwaka, kama zipo ni faida gani?
(b) Kama hakuna faida, je, ni lini Mwenge huo wa Uhuru utasitishwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE,
KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze muuliza swali leo kwa kukaa upande ule alioulizia swali. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Khatib Said Haji, Mbunge wa Konde, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida za Mwenge wa Uhuru Kitaifa na Kimataifa ni pamoja na kuendelea kuhamasisha ari ya wananchi kujitegemea na kuwekeza katika maeneo mbalimbali katika Taifa letu; kuwa ni chombo pekee cha kujenga umoja, mshikamano na kudumisha amani pale ambapo Mwenge unapita bila kujihusisha na itikadi za kisiasa; kuendelea kuhamasisha na kuimarisha umuhimu wa Muungano kwa Watanzania wa pande mbili za nchi yetu; na kila mwaka hufungua na kuweka mawe ya msingi kwenye miradi mbalimbali ya wananchi na kuhamasisha uzalendo wa kuendelea kujitolea. Mfano mzuri ni kutokana na takwimu zilizopo ambazo zinaonyesha miradi ya maendeleo iliyozinduliwa pamoja na kuwekwa mawe ya msingi kupitia Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2015/2016 ni pamoja na miradi 1,342 yenye thamani ya shilingi 463,519,966,467.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Kimataifa Mwenge
wa Uhuru umeendelea kusimamia dhana na maudhui yake ya kumulika hata nje ya mipaka yetu kwa kuwa msuluhishi wa amani katika Bara la Afrika na mfano wa kuigwa kwa mataifa mengine ya Afrika duniani kote. Umoja, mshikamano, upendo na ukarimu wa Watanzania ni matunda pia ya Mwenge wa Uhuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na faida na mafanikio makubwa yanayopatikana kupitia mbio za Mwenge wa Uhuru, Serikali inaamini kuwa zipo faida za kuendelea kukimbiza Mwenge huo wa Uhuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, Serikali haina mpango wowote wa kusitisha mbio za Mwenge wa Uhuru. Dhana hii itakuwa ni endelevu na tungependa kuiendeleza kutoka kizazi kimoja hadi kingine kwa kusisitiza misingi hii bila kuchoka.
MHE. AZZA H. HAMAD aliuliza:-
Kituo cha Watoto wenye ulemavu cha Buhangija kimekuwa kikijiendesha kwa kusuasua:-
Je, Serikali ipo tayari kupeleka fedha kwa asilimia mia moja katika kituo hiki hasa ikizingatiwa kuwa kinachukua
watoto kutoka Kanda yote ya Ziwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Azza Hillal Hamad, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Buhangija ni Shule ya Msingi jumuishi inayochukua watoto wasio na ulemavu na wenye ulemavu wa aina mbalimbali na siyo kituo cha kulelea Watoto wenye ulemavu. Shule hii huchukua watoto wenye ulemavu kama vile wasioona, bubu, viziwi, weye ualbino, ulemavu wa viungo na pia watoto wasio na ulemavu kama nilivyosema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la uendeshaji wa kusuasua kwa utoaji wa huduma katika shule hii kulitokana na ongezeko la ghafla la watoto na vijana wenye ualbino kukimbilia shuleni hapo kuanzia miaka ya 2009 kutokana na sababu za vitendo vya ukatili, mauaji, unyanyasaji na unyanyapaa uliokithiri dhidi ya watu wenye ualbino katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa. Hali hiyo ilisababisha ongezeko la watoto na watu wazima hapo shuleni kufikia 407 kutoka 200.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule ya Buhangija kama shule nyingine nchini zenye mahitaji maalum, itaendelea kupatiwa mgao wa fedha na Serikali pamoja na mahitaji mengine ya kimsingi kwa mujibu wa taratibu za Serikali. Naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa kwa sasa wanafunzi wanapata elimu bila mashaka yoyote kwa kuwa tatizo la msongamano limepungua sana na kufanya wanafunzi kubaki 228 tu, idadi ambayo shule inamudu kuwahudumia.
MHE. CECILIA D. PARESSO aliuliza:-
Wananchi wengi wa Tarafa ya Eyasi katika Wilaya ya Karatu wanajishughulisha na kilimo cha vitunguu maji, hata hivyo mavuno yanayotokana na kilimo hicho hupimwa kwa debe yanapouzwa badala ya kilo.
Je, ni kwa nini Serikali isihakikishe na kusimamia uuzwaji wa mazao haya kwa kutumia kilo badala ya vipimo vya debe?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Namba 340 ya mwaka 2002 na mapitio yake ya mwaka 2016, vipimo sahihi ni kutumia mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo na siyo vinginevyo ambapo kipimo chake ni kilo kwa bidhaa za aina hii yaani vitunguu vikiwa ni mojawapo vinavyostahili kupimwa kwa kilo.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Wakala wa Vipimo inaendelea kutoa elimu kwa umma juu ya matumizi sahihi ya vipimo kwa njia ya redio, luninga, makala za magazeti na kwa kushiriki katika maonesho mbalimbali. Vilevile Wakala wa Vipimo wametoa elimu kwa wadau wa biashara hiyo ya vitunguu huko Mang’ola Tarafa ya Eyasi wakiwemo wakulima, viongozi wa vijiji, kata, tarafa, halmashauri ya wilaya kwa lengo la kuwaelimisha kuhusu matumizi sahihi ya vipimo vinavyoruhusiwa kisheria.
Mheshimiwa Spika, ili kurahisisha utekelezaji wa Sheria ya Vipimo ilipitiwa na Bunge lako Tukufu mwezi Novemba, 2016 ili kuruhusu Mamlaka za Serikali za Mitaa kuwa na Sheria Ndogo (by-laws) za kuwawezesha kuanzisha vituo vya ununuzi wa mazao na bidhaa katika eneo la mamlaka husika vitakavyokuwa na mizani iliyohakikiwa na Wakala wa Vipimo. Hali kadhalika, Serikali inaendelea kuhamasisha ujenzi wa vituo maalum vya ununuzi wa mazao (buying centres) vyenye nafasi ya maghala ya kuhifadhia mazao, ambapo kwa Tarafa ya Eyasi, Halmashauri ya Wilaya ya Karatu kwa kushirikina na wadau wa maendeleo tayari imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa kituo katika kijiji cha Mang’ola chenye maghala matatu kwa ajili ya kuhifadhi vitunguu. Kituo hiki kinatarajia kuanza kutumika katika msimu wa mwaka huu wa ununuzi wa vitunguu. Vituo vya aina hii vitasaidia wakulima kuwa na nguvu ya pamoja kujadiliana na wanunuzi na kutumia vipimo sahihi ili kupata bei yenye ushindani na haki katika soko.
Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako Tukufu ninapenda kuwatahadharisha wakulima na wafanyabiashara wote wanaojihusisha na biashara ya vitunguu na mazao mengine yote kuhakikisha kuwa wanatumia vipimo sahihi. Aidha, Serikali itaendelea kufuatilia kuchukua hatua za kisheria pale inapobidi kufanya hivyo kwa wanaokiuka sheria hiyo.
MHE. DKT. THEA M. NTARA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaboresha Sheria ya Ajira na kuweka mazingira mazuri ili maprofesa wa kigeni waweze kufanya kazi nchini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Thea Medard Ntara, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali katika kuboresha utoaji ajira kwa wageni ilitunga Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni, Namba 1 ya mwaka 2015 pamoja na Kanuni za Kuratibu Ajira za Wageni za mwaka 2016 ili kuratibu ajira za raia wa kigeni wanaokuja kufanya kazi nchini ikiwa ni pamoja na kulinda ajira za wazawa na kuruhusu ujuzi adimu kutoka nje kuingia na kurithishwa nchini. Serikali kwa sasa inaendelea na mapitio ya sheria ili kuifanyia maboresho kwa kuzingatia mazingira ya sasa.

Mheshimiwa Spika, ili kuweka mazingira mazuri ya kuruhusu uwepo wa wafanyakazi wa kigeni nchini, Serikali imeanzisha mfumo wa kielektroniki wa kushughulikia maombi ya vibali vya kazi na ukaazi kwa raia wa kigeni wanaokuja kufanya kazi nchini na mfumo husika umeanza kutumika kwa majaribio (piloting) kuanzia tarehe 23 Aprili, 2021. Mfumo huu utaongeza Ufanisi katika kushughulikia maombi husika.

Mheshimiwa Spika, mfumo huu pia utaondoa changamoto ya upatikanaji wa taarifa unganishi za kisekta za kurahisisha upatikanaji wa vibali vya wageni wakiwemo Maprofesa kwa wakati kwa kuzingatia uhitaji.

Mheshimiwa Spika, kulingana kwa taarifa zilizopo mpaka sasa jumla ya vibali vya kazi 74 vimetolewa kwa Maprofesa na Wahadhiri wa Vyuo Vikuu nchini vikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma, Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (St. Augustine University) na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Tanzania na vinginevyo.
MHE. MOHAMED SULEIMAN OMAR aliuliza:-

(a) Je, ni hatua gani zilizofikiwa kwenye mapambano dhidi ya madawa ya kulevya nchini?

(b) Je, ni watu wangapi wamekamatwa kuanzia mwaka 2019 – 2020 na wangapi wamehukumiwa kifungo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mohamed Suleiman Omar, Mbunge wa Malindi lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Spika, Katika kukabiliana na changamoto ya matumizi na biashara ya dawa za kulevya nchini, hadi sasa Serikali imechukua hatua zifuatazo;

Mheshimiwa Spika, kwanza imetungwa kwa sheria mpya ambayo ilipitishwa na Bunge lako Tukufu, Sheria ya Kudhibiti Dawa za Kulevya Na.5 ya mwaka 2015. Sheria hiyo, ilianzisha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kama chombo maalum chenye nguvu ya kisheria ya kukamata, kupekua, kuzuia na kupeleleza makosa yote yanayohusiana na dawa za kulevya.

Mheshimiwa Spika, pili; kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama kama vile Jeshi la Wananchi wa Tanzania kitengo cha Wanamaji na Jeshi la Polisi, Serikali imeimarishaji operesheni za nchi kavu, anga na majini hasa katika viwanja vya ndege, maziwa na Bahari ya Hindi, ikiwa ni mkakati kwa kudhibiti njia na vipenyo vyote. Pamoja na kuendelea kutoa elimu ya athari za matumizi na biashara ya dawa za kulevya.

Mheshimiwa Spika, vilevile, Serikali kupitia mamlaka imetambua mitandao mikubwa ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini na kubaini njia mbalimbali za usafirishaji. Mkakati huo, umechangia kwa kiasi kikubwa kuziba mianya ya uingizaji wa dawa za kulevya na ukamataji wa dawa hizo.

Mheshimiwa Spika, kwa majibu ya swali (b) kutokana na hatua hizi zilizochukuliwa na Serikali, katika kipindi cha mwaka 2019 hadi 2020, jumla ya dawa za viwandani (Cocaine na Heroin) zilizokamatwa ni kilo 426 na gramu 363. Jumla ya dawa za asili bangi na mirungi zilizokamatwa ni tani 28 na kilo 34. Aidha, katika kipindi cha Januari - Desemba 2020, na Januari - Mei 2021, jumla ya watuhumiwa 124 walikamatwa, kati yao 23 wametiwa hatiani na usikilizaji wa mashauri 40 unaohusisha watuhumiwa 83 unaendelea.
MHE. JACQUELINE K. ANDREA K.n.y. MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha Taasisi ya TAKUKURU katika uwajibikaji wake?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Adamson Mwakasaka, Mbunge wa Tabora Mjini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha Wananchi wa Tanzania wanakuwa na maendeleo endelevu, Serikali imefanya yafuatayo katika kuimarisha uwajibikaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

i. Kuongeza idadi ya watumishi wa Taasisi ya TAKUKURU ikiwa ni pamoja na kufanya mapitio ya uwajibikaji wa watumishi waliopo;

ii. Kuongeza bajeti ya matumizi mengineyo (OC) ya TAKUKURU kwa asilimia 51.7 kutoka shilingi bilioni 20.54 mwaka 2021/2022 hadi shilingi bilioni 31.16. Aidha, bajeti ya maendeleo nayo imeongezeka kwa asilimia 33.3 kutoka bilioni 1.5 kwa mwaka 2021/2022 hadi bilioni mbili kwa mwaka 2022/2023;

iii. Kuwajengea uwezo watumishi 984 wa TAKUKURU ambapo watumishi 976 walipata mafunzo ndani ya nchi na watumishi nane nje ya nchi;

iv. Kutoa fedha za ujenzi wa majengo ya TAKUKURU katika mikoa na wilaya ambazo hazina majengo kulingana na bajeti itakavyo ruhusu.

v. Kuanzisha program za kusaidia kuzuia zaidi rushwa kama TAKUKURU Rafiki

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati hii inalenga zaidi kuisaidia TAKUKURU kuzuia zaidi rushwa na pale inapo bidi itaendelea kupambana na vitendo vya rushwa.