Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Jenista Joackim Mhagama (54 total)

MHE. DKT. ELLY M. MACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri swali moja dogo la nyongeza, je, Waziri anaweza kulihakikishia Bunge hili kwamba katika hii bajeti ya 2016/2017, kutatengwa bajeti kwa ajili ya kuliwezesha Baraza la Ushauri kwa Watu Wenye Ulemavu kuanza kazi na programu zake kuwafikia watu wenye ulemavu? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza kabisa nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa uwakilishi wake mahiri na hasa katika kundi hili la walemavu katika nchi yetu ya Tanzania na swali lake ni swali lenye msingi wa hali ya juu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni azma ya Serikali sasa kuhakikisha kwamba pamoja na utungaji wa Sheria namba 9 ya mwaka 2010 ambayo imetoa maelekezo ya namna gani kundi hili muhimu katika nchi yetu ya Tanzania litaweza kuzingatiwa katika nyanja zote za maendeleo katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Ofisi ya Waziri Mkuu inathamini na kuona umuhimu wa kundi hili maalum na hakika katika bajeti ya mwaka huu unaokuja wa fedha itazingatia kuona Baraza la Watu Wenye Ulemavu linatengewa fedha na linafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria iliyotungwa, Sheria namba 9 ya mwaka 2010.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Hii nafasi ni ya Mwalimu.
Mheshimiwa Spika, nina swali dogo kuhusiana na fedha hizi zinazotarajiwa kutolewa vijijini za Sh. 50,000,000 kwa kila kijiji. Sasa hivi imeanza mizengwe kwamba fedha hizi zitatolewa kwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi. Naomba Serikali itoe kauli fedha hizi zitatolewa kwa utaratibu gani ili kuepuka kwenda kwa wanachama wa Chama cha Mapinduzi peke yao?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza niseme fedha hizi za Sh. 50,000,000 ilikuwa ni ahadi ya Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kupitia kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini Watanzania ambao walichagua Serikali ya Chama cha Mapinduzi na Serikali hii iliamua kuwatumikia Watanzania wote bila kujali itikadi ya vyama vyao wala jambo lingine lolote. Katika majibu yetu ya msingi tumesema Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Tanzania wameshaanza kutengeneza utaratibu wa namna ambavyo fedha hiyo ya Sh. 50,000,000 itaweza kuwafaidisha wananchi wetu kule vijijini wakiwemo vijana, wanawake lakini vilevile na Watanzania wengine wote. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mbunge jambo hilo analolisema ni hofu tu, lakini Serikali ipo imara na itazingatia utaratibu wa kisheria wa kuhakikisha fedha hizi zinawafikia Watanzania.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri. Katika paragraph ya pili ya majibu yake ndiyo nitajenga maswali yangu ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, siku ya tarehe 9 Desemba, 2016, nilikuwa nasafiri kutoka Dubai kurudi Tanzania nikakutana na binti wa Kitanzania anaitwa Zuhura Yussuf Manda, mkazi wa Tegeta Kibaoni, Dar es Salaam. Binti alipelekwa kufanya kazi na agent wa Kitanzania anayeitwa Amne, akafanya kazi Oman kwa miezi mitatu kwa Anna na badala yake Anna akampa dada yake ambaye anaishi Dubai anaitwa Zahra akafanya kazi kwa muda wa miezi mitatu. Huyu Zahra hawakuridhiana kwa hiyo ikabidi binti atoroke akutane na Mzungu ambaye alimchukua akampeleka kwenye Ubalozi wa Tanzania.
SPIKA: Sasa swali.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, hapo ndiyo swali langu linakuja. Alikaa katika Ubalozi wa Tanzania kwa kipindi cha miezi sita bila ya kupatiwa passport yake ambayo aliizuia mwajiri wake, bila ya kupatiwa vifaa vyake ambavyo alivizuia mwajiri wake hadi alipokuja Mtanzania mwingine kwa wiki moja ndiyo akatengenezewa safari ya kurudi Tanzania. Swali linakuja, je, ni utaratibu gani ambao Serikali imeweka sasa kwa wale ambao wameshafikishwa kwenye Balozi zetu kuweza kuwarudisha Tanzania kwa muda mfupi ili kuipunguzia Serikali gharama za kimaisha kwa kubeba mzigo wa watu wale ambao wako pale katika Balozi zetu? Hilo swali la kwanza.
SPIKA: Aaaah kaka! Kama kila mtu atachukua muda mrefu kiasi hiki kwa kweli kwa muda wa saa moja maswali hayawezi kwisha.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, nashukuru, nilikuwa najenga hoja ili Waziri…
SPIKA: Tafadhali jielekeze moja kwa moja kwenye swali.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Ahsante! Nilikuwa najenga hoja ili Mheshimiwa Waziri akijibu ajibu vizuri…
SPIKA: Hapana usijenge hoja, nenda kwenye swali moja kwa moja. Kanuni zinataka uulize swali moja kwa moja.
MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN: Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, hawa ma-agent ambao wanaopeleka watu kufanya kazi nje ya nchi linapotokea tatizo kama hili wao wanawajibika vipi kurudisha gharama kwa Serikali kwa wale watu wao ambao hawakuwatendea vilivyo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Spika, katika jibu letu la msingi tumesema Serikali imeweka utaratibu rasmi ambao utawasaidia Watanzania wanapofanya kazi nje ya nchi na kupata matatizo waweze kusaidiwa kwa haraka. Kwa hiyo, katika jibu langu la kwanza kwa swali la kwanza la nyongeza ili kupunguza gharama kwa Serikali, naomba kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu niendelee kuwaarifu na kuwaomba Watanzania wote wanapokwenda nje ya nchi watumie utaratibu ulio rasmi ambao utawasaidia wao kuwa salama na kupunguza gharama kwa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, linasema hawa ma-agent ambao wanawapeleka nje Watanzania halafu kunatokea matatizo wanaweza kutozwa kiasi gani kulipia gharama za fidia kwa waathirika? Majibu ni yale yale kama hukupitia kwenye utaratibu wa Serikali, Serikali itakuwa ni ngumu sana kufuatilia hizo haki zako. Ukipitia kwenye utaratibu wa Serikali, Serikali kupitia sheria tulizonazo tutasimamia na tutaweza kuchukua hatua kwa hao ma-agent ambao wanafanya mambo hayo kinyume cha sheria.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Swali langu la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri, kuna wastaafu wengine baada ya kupewa pensheni wanapewa kila baada ya miezi mitatu na ukitazama kuna walimu wengine wastaafu na wafanyakazi wengine, kila baada ya miezi mitatu wanapewa kiasi cha shilingi 150,000/=.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kauli ya Mheshimiwa Waziri kwamba je, pesa hizi wana mpango wowote wa kuwaongezea na je, anaonaje kama ikawa kila mwezi mkawapatia kila mwezi badala ya kuwapatia miezi mitatu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake la nyongeza. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu,naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimwia Mwenyekiti, dhana ya pensheni inatawaliwa na mifumo ya utekelezaji wa dhana ya hifadhi ya jamii kwa kuzingatia sheria mbalimbali za Kimataifa, sheria za nchi lakini na taratibu pia ambazo tumejiwekea ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo, katika kila hatua ya ulipaji wa pensheni mifumo ya uchangiaji na mifumo yote ya hifadhi ya jamii, ni lazima kuwe na ushirikishwaji wa kutosha wa kuona nani afanye nini na nani awajibike katika jambo gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili kuhakikisha kwamba pensheni zinaongezeka ama mafao ya aina yoyote yanaongezeka kupitia suala zima la hifadhi ya jamii, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau na itaendelea kutoa taarifa, ni namna gani inaboresha ama kuongeza mafao kwa namna moja au nyingine ili kuhakikisha kwamba dhana ya hifadhi ya jamii inatekelezwa ipasavyo katika nchi yetu ya Tanzania.
MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali
la nyongeza.
Pamoja na njaa iliyowakumba wananchi wa Mpwapwa, Kongwa, Bahi, Chemba,
Kondoa na maeneo mengine ya ukame katika Mkoa wa Dodoma, lakini mvua iliyonyesha na
inayoendelea kunyesha imeleta mafuriko makubwa kwa baadhi ya vijiji na vyakula ambavyo
wananchi walikuwa navyo vimesombwa na maji, mahitaji ya ndani, magodoro, vitanda,
vyombo vimesombwa na maji.
Je, Serikali iko tayari kuwasaidia wananchi hao kwa kushirikiana na Wabunge?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, VIJANA, AJIRA NA WALEMAVU:
Mheshimiwa Spika, nchi yetu imekumbwa na mabadiliko ya tabianchi na kusababisha majanga
ya mafuriko katika maeneo tofauti katika nchi yetu ya Tanzania. Sisi wenyewe kama Serikali
tumekuwa tukitembelea maeneo hayo nakuona madhara yaliyopatikana.
Mheshimiwa Spika, inawezekana tukaweza kufanyakazi ya kuwasaidia Watanzania kwa
namna ile ambayo Serikali ina uwezo kwa sasa. Kwa hivyo, naomba niwahakikishie
Waheshimiwa Wabunge, tutajitahidi kuendelea kufanya tathmini na kuona tunafanya nini
kutoka eneo moja hadi jingine, lakini ninaziomba kamati za maafa kwenye ngazi ya Kata, ngazi
ya Wilaya, ngazi ya Mkoa kuona yale yanayoweza kufanyika ndani ya uwezo wao, na
yanayoshindikana wayalete Serikalini ili tuweze kushirikiana kwa pamoja.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza mimi nasikitika kwa sababu Serikali inaonekana haina nia njema juu ya jambo hili. Mimi nikiwa Mbunge mwaka 2004 Serikali ilitoa majibu haya haya, mwaka 2008 Serikali ikatoa majibu haya haya, mwaka 2012 Serikali ikatoa majibu haya haya. Mimi ni Mbunge kwa kipindi cha nne sasa, nasikitika sana juu ya majibu yenu ambayo … (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa swali kwa ufupi naomba tafadhali.
MHE. MASOUD ABDALLAH SALIM: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni moja tu, uzee na kuzeeka nani ataukwepa, hakuna na kila mmoja ni mzee mtarajiwa. Serikali ituambie sasa ina mkakati gani wa ziada na kama mlivyosema kuwa hatua chache zimebakia, hizo hatua chache ni zipi? Je, ndani ya miezi mitatu mnaweza kumaliza suala hili ili wazee wapate pensheni zao hasa ukizingatia na wale baadhi waliopigana Vita vya Kagera?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE WALEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Masoud, lakini nikiendelea kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina nia ya dhati ya jambo hili na ndiyo maana katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 jambo hili limewekwa na kutafsiriwa vizuri sana. Kipindi cha nyuma jambo hili halikuwa limechukua picha ya kutosha kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi. Hiyo tu kwanza ni nia ya dhati ya Serikali kuhakikisha jambo hili linatekelezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri hapa ameeleza vizuri sana na naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba suala hili sio la kulala na kuamka ndani ya miezi mitatu halafu ukasema unaanza tu kulipa pensheni, hapana.
Narudia kusema Serikali imeshaanza kutengeneza miundombinu ya kulifanya jambo hili liweze kutekelezeka.
Sheria inayompa mamlaka Mdhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, kifungu cha 5(1)(e), kimemuagiza na kumwelekeza Mdhibiti kuhakikisha anasimamia suala zima la kuona namna gani Watanzania wengi wanafikiwa na sekta ya hifadhi ya jamii ikiwemo wazee.
Kwa hiyo, naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu Serikali inalifanyia kazi suala hili na mara litakapokamilika litaanza kuchukua nafasi yake na wazee watapata pensheni.
MHE. DANIEL E. MTUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa muda niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa hali ya maji Manyoni ni tete kwa watu na kwa mifugo. Tunajua bado taratibu za mkopo zinaendelea. Wakati wa Mkutano wa Tatu, aliyekuwa Mheshimiwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba wakati anawasilisha hotuba yake ya bajeti alisema analitambua suala la ukame na hasa kwenye maeneo yale kame na kuna utaratibu Wizara ya Kilimo itawasiliana na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa waweze kupata kibali…
MHE. DANIEL E. MTUKA: Nakuja kwenye swali. Barua ile ilikuwa imeshaandikwa kwa maana ya mawasiliano ya Wizara mbili ya Kilimo na Wizara ya Ulinzi. Sasa swali, Wizara ya Ulinzi au Serikali inatoa majibu gani kuhusiana na mawasiliano ya Wizara ya Kilimo ili kuweza kuruhusu yale magreda kwenda kutuchimbia mabwawa kwa ajili ya watu na mifugo kwa ajili ya umwagiliaji? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, naona Mheshimiwa Mbunge pamoja na kuuliza swali la nyongeza anajaribu kutushauri Serikali kutumia Wizara na taasisi zilizopo ndani ya Serikali kushughulika tatizo hilo. Ningeshauri tu tuwasiliane naye halafu tuweze kujua tunaweza kuunganishaje hizo taasisi katika kutatua tatizo lake. (Makofi)
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Chama cha Mapinduzi ndicho kilichoshinda katika uchaguzi mkuu uliokwisha hivi karibuni mwaka 2015; na kwa kuwa Serikali iliyoko madarakani sasa inatakiwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi iliyojinadi kwa wananchi wake; na kwa kuwa ziko nchi ambazo uchaguzi ukishamalizika vyama vya siasa vingine havipaswi kwenda kufanya mikutano ya hadhara, je, hatuoni sasa ni wakati muafaka wa kufanya marekebisho ya sheria ili chama kilichoko madarakani kiweze kuachiwa nafasi ya kuendelea kutekeleza Ilani ya Uchaguzi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na kuendelea kuwakumbusha wanasiasa kwamba madaraka ya Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa yako kwa mujibu wa Katiba na waendelee kutii madaraka na pale wanapovunja sheria, sheria zitaendelea kuchukua mkondo wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Mary Chatanda ameleta ushauri kwa Serikali na ninachoweza kusema kwa niaba ya Serikali ni kwamba, kwa kuwa Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na sheria mbalimbali zilizowekwa ndizo zinazofuatwa kwa sasa kuongoza misingi ya utawala bora na hasa pale chama kinaposhinda kuendelea kutekeleza Ilani yake ya Uchaguzi, hivyo ndivyo ilivyo sasa. Kwa hiyo, kama nchi hii itaona kwamba kunatakiwa kufanya mabadiliko na michakato ya Katiba inaendelea, basi mambo hayo mengine mapya yanaweza kuzingatiwa katika michakato ya Katiba inayoendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tunaendelea kuwakumbusha Watanzania wote chama kilichoshinda na kushika hatamu ya kuendesha nchi hii kwa mujibu wa Ilani ya Uchaguzi ni Chama cha Mapinduzi na Watanzania
wote wataendelea kushughulikiwa kupitia Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi, sheria na Katiba iliyopo sasa.
MHE. KAPT. GEORGE H. MKUCHIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa ni taratibu dunia nzima katika mfumo wa vyama vingi Ilani ya Chama kilichoshinda uchaguzi ndiyo inayotekelezwa. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba elimu hiyo au uelewa huo unawafikiwa viongozi wa vyama vyote vilivyosajiliwa katika nchi hii?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Mkuchika, naomba nimpongeze sana kwa kushinda kesi yake ya uchaguzi na kuwabwaga wale wapinzani ambao walikuwa wanafikiri kwamba Mheshimiwa George Mkuchika hakushinda kihalali. Kwa hiyo, naomba nimpongeze sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Gerge Mkuchika ameomba kujua ni kwa kiasi gani Serikali itajitahidi kuhakikisha inatoa elimu na hasa kwa vyama ili viweze kutambua umuhimu wa kutii na kuamini kwamba Katiba inayotutawala inaelekeza ilani inayotekelezwa katika nchi ni Ilani ya chama kilichoshinda.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa kadri tunavyoendelea katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya Serikali, Serikali imeendelea kuwafahamisha Watanzania wote, vyama vya siasa vilikuwa vikipata elimu hiyo kabla ya uchaguzi na hata baada ya uchaguzi kwamba waendelee kuamini chama kilichoshinda ndicho kitakachotekeleza Ilani yake ya Uchaguzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie Bunge hili lako Tukufu kuendelea kuvikumbusha Vyama vyote vya Siasa vipitie Sheria ya Uchaguzi, vipite Katiba na vilevile viendelee kusikiliza na kupata maelekezo yanayotolewa na viongozi mbalimbali tukiendelea kusisitiza kwamba chama kilichoshinda, Chama cha Mapinduzi ndicho chenye Ilani ya Uchaguzi na Serikali itapanga mipango kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na siyo vinginevyo.
MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwanza, Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa mikoa yenye wananchi wengi sana na katika vijiji ambavyovimeainishwa kwa ajili ya kupewa mikopo hiyo, kila kijiji kina wastani wa wananchi 5,000 ambao wana uwezo wa kufanya kazi za uzalishaji. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapa mikopo yenye tija wananchi hao?
Swali la pili, kama wanakijiji watapata shilingi 1,000 kila mmoja itakayotokana na shilingi milioni 50. Je, watawekeza kwenye biashara gani ili wapate faida kwenye uwekezaji huo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kumpongeza sana huyu Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Ruvuma kwa kazi nzuri na jitihada kubwa anayoifanya ya uwakilishi ndani ya Bunge na hasa kuwawakilisha Watanzania wote, lakini hasa hasa wanawake wa Mkoa wa Ruvuma nampongeza sana. Mheshimiwa Mbunge ameniuliza maswali mawili la kwanza ameonyesha idadi ya watu jinsi ilivyo, katika maeneo mbalimbali kwenye Vijiji vya Mkoa wa Ruvuma, akitaka kujua kama tuna mpango mahususi katika Serikali wa kuhakikisha vijiji hivyo vinapata mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, wakati tukipitisha bajeti ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, Fungu 65 mradi namba 49, 45 pamoja na hiyo milioni 50. Hata hivyo, Serikali imetenga fedha nyingine bilioni moja kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vijana na akina mama wanapata mikopo katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania. Hata hivyo, Serikali pia kupitia Halmashauri zetu itaendelea kutenga asilimia tano ya mapato kwa ajili ya akinamama na vijana. Kwa hiyo, namhakikishia kwamba nguvu hizo zote zitasaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili la nyongeza amesema, pia anakadiria wastani wa shilingi 1,000 kama Mfuko huo utakopeshwa kwa wananchi, kwa idadi ya wananchi ambao wanaweza kuifanyia kazi. Namwomba Mheshimiwa Mbunge asubiri kama nilivyosema, tunatengeneza utaratibu na mfumo mzuri ambao utasaidia kuhakikisha kwamba wakopaji watapata fedha yenye tija na wataweza kufanya kazi na biashara ambazo zitainua kipato kwa familia zao na Taifa zima kwa ujumla.
MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Kwenye taarifa ya Waziri wa Fedha aliyoiwasilisha hii ya bajeti, imezungumzia tu suala la milioni 50, kwamba zitakwenda kwenye vijiji, haikuzungumzia Mitaa, kama ambavyo Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan walizungumza walipokuwa wakipita kwenye kampeni kwamba watahakikisha Mitaa na Vijiji vinapata mikopo ya milioni 50. Je, Serikali inatuambia nini juu ya wananchi wanaoishi mijini, ambao wana mitaa badala ya vijiji?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Mary Chatanda, Mbunge mwanamke wa Jimbo pia kwa kazi nzuri za uwakilishi anazozifanya na nina imani kule Korogwe Mjini wako salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyokuwa najibu katika swali langu la msingi, kwamba kazi kubwa ambayo tunaendelea kuifanya sasa hivi ili kufanya maandalizi mazuri ya Mfuko huu, kuweza kutumika kwa Watanzania wote. Kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, ni pamoja pia na kutafsiri maana ya Mitaa na Vijiji kwa kuzingatia Sheria ya Local Government kama ilivyoweka mipaka katika maeneo ya mijini na vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie Wabunge wawe na amani, watulie. Serikali yao inafanya kazi na utaratibu utawekwa wazi na tunahakikisha kwamba Watanzania hawa watanufaika na fedha hizi kama vile tulivyoainisha kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa muda wa kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ametoa majibu mazuri sana, kwanza nampongeza. Pili kwa kuwa kundi la walemavu limekuwa likisahaulika sana hasa katika suala hili la mikopo, ukizingatia wapo vijana wa kike na wa kiume, lakini je, kwenye mpango huu wa milioni 500, kundi la walemavu limekuwa considered namna gani. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kunithibitishia hilo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Massay kwa kazi nzuri anayoifanya Bungeni ya kuwawakilisha wananchi wake wa Jimbo la Mbulu na hata walemavu pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria Namba Tisa ya mwaka 2010 ambayo inaongoza na kuratibu shughuli zote za watu wenye ulemavu nchini, zinatutaka na kutukumbusha kwamba, katika kila suala tunalolifanya kwenye nchi yetu ya Tanzania, lizingatie pia kwamba walemavu wanatakiwa wapewe haki sawa katika nchi yetu ya Tanzania. Kwa hiyo, tunapoandaa taratibu na miongozo kwa ajili ya fedha hizi, Sheria Namba Tisa ya mwaka 2010 itachukua nafasi yake, kuhakikisha pia walemavu wanakumbukwa katika mpango huu mzima.
MHE FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa
Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imeanzisha Mfuko wa Udhamini wa UKIMWI na imetenga kiasi cha shilingi bilioni 5.6 kwa ajili ya mfuko huo, je, Serikali haioni umuhimu wa kutumia sehemu ya pesa za mfuko huo kwa kutoa ruzuku kwa kiwanda hicho?
Swali la pili, je, Serikali ina mkakati gani kuhakikisha kuwa uzalishaji unaanza mapema zaidi ili kupunguza gharama za kuagiza dawa za ARV kutoka nje? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ambaye Mfuko huu wa UKIMWI kwa mujibu wa sheria uko chini ya Ofisi hiyo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba nijibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Waziri mwenzangu, Mheshimiwa Ummy Mwalimu ambaye ni mdau mkubwa tunayefanya naye kazi kwa pamoja kushughulikia masuala haya ya tatizo la UKIMWI nchini kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfuko huu ambao unashughulikia matatizo ya UKIMWI (ATF) umeanzishwa kwa mujibu wa sheria na sheria imeweka mamlaka kwa bodi inayosimamia mfuko huo kutoa miongozo na kuangalia ni kwa namna gani fedha zitakazopatikana kwenye mfuko
zitatumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali zinazoendana na tatizo la UKIMWI katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bodi imeshagawa utaratibu wa matumizi ya fedha hizo kwa asilimia 60 kutumika kwenye matibabu, dawa na vitendea kazi na asilimia nyingine 25 na 15 kwa kazi nyingine.
Kwa hiyo, kwa utaratibu ama ushauri ambao ameutoa Mheshimiwa Mbunge, tutarudi kuwasiliana na bodi kuona kama katika zile asilimia 60 zinaweza pia zikatumika katika kusaidia utengenezaji wa dawa kwenye nchi yetu ya Tanzania kama mfuko utakuwa umeshajitosheleza kwa kiasi kikubwa na kiasi cha kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge, tutaendelea kupokea ushauri wa kuboresha matumizi ya fedha ya mfuko huo kadiri inavyoonekana inafaa.

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru
Mheshimiwa Jenista kwa kujibu sehemu ya kwanza ya swali hili, kati ya maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Fatma Toufiq.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya pili, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha tunawekeza katika uzalishaji
wa dawa za ARV nchini Tanzania? Nataka kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge kwamba hadi sasa tuna viwanda
vitano, wawekezaji watano ambao wameonesha nia ya kutaka kuwekeza katika uzalishaji wa viwanda vya dawa
nchini na wiki iliyopita tulikuwa pale Bagamoyo, Zinga Phamaceutical Company na moja ya dawa ambayo
watazalisha ni pamoja na dawa za kupunguza makali ya UKIMWI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitaka tu kumthibitishia tunafanya kazi pia pamoja na Mheshimiwa
Charles Mwijage kuhakikisha kwamba tunazalisha dawa zetu zote ndani ya nchi badala ya kununua dawa nje ya nchi kama tunavyofanya sasa hivi.
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Swali la kwanza, malengo, dhamira ya kuanzishwa Mwenge wa Uhuru yameonekana kutotimizwa ikiwemo badala ya kueneza upendo Mwenge wa Uhuru umekuwa unaeneza chuki. Mfano, katika Mkoa wa Rukwa hivi karibuni Wenyeviti na Watendaji waliwekwa ndani kwa kosa la kutochangisha wananchi kuhudumia Mwenge wa Uhuru.
Je, kama ni mfano wa kuigwa na katika Afrika na Dunia hakuna nchi iliyotuigiza wakakimbiza Mwenge huu hamuoni kwamba kukimbiza Mwenge sio kuleta maendeleo katika nchi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali pili, nataka nimuombe Mheshimiwa Waziri kwa sababu Mwenge wa Uhuru historia yake ni kuupamba Uhuru wa Tanganyika na Zanzibar ina historia yake ya kupata Uhuru kutokana na Mapinduzi. Kwa sababu Mwenge sio jambo la Muungano, hamuoni sasa iko haja ya kuacha kuuleta Mwenge huu kule Zanzibar ambapo hatuoni maana yake yoyote?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango, uratibu na utekelezaji wa kimfumo na wa kifalsafa wa ukimbizaji wa mbio za Mwenge, huratibiwa kwa kufuata kanuni na utaratibu wa maandalizi uliowekwa kwa nchi nzima ya Tanzania. Hivyo basi, kama ziko dosari ambazo zimekuwa zikijitokeza eneo moja hadi lingine hazitaki kumaanisha kwamba historia ya falsafa ya Mwenge ile ambayo imejengwa katika misingi ya uhuru wa nchi yetu, eti sasa ndiyo iondolewe kwa sababu ya dosari hizo ndogo zinazojitokeza. Naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Serikali kwenye dosari ndogo tutaendelea kuzipitia na kuziondoa ili falsafa ya Mwenge wa Uhuru iendelee kubaki kama ilivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Mheshimiwa Mbunge anasema Zanzibar si sehemu ya Mwenge huu wa Uhuru. Nataka kumkumbusha Mheshimiwa Mbunge kwamba kati ya matunda mema ambayo yalizaliwa kwa sababu ya falsafa ya Mwenge wa Uhuru ni pamoja na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Azimo la Arusha na ukombozi wa Bara la Afrika. Hivyo, kwa sababu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni matunda ya Mwenge wa Uhuru, Mwenge huu utaendelea kukimbizwa Bara na Visiwani na utaendelea kuenziwa na Watanzania wote Bara na Visiwani ukiwemo wewe Mheshimiwa Mbunge Haji kutoka Visiwani kama Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo linaenzi falsafa ya Mwenge wa Uhuru.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi nataka kuuliza kwa mtu ambaye ni Mtanzania aliyezaliwa katika nchi yetu, anayehoji juu ya Mwenge…
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Badala ya kuhoji juu ya mambo mabaya yanayotokea kwenye Mwenge, anayehoji juu ya Mwenge unafanya nini huyu unaweza kumkabidhi hii nchi akaendelea kukaa nayo? Nataka tu kupata ufafanuzi huo.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake zuri ambalo linaonyesha jinsi alivyokomaa katika kujua historia ya nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu niwaambie Watanzania, falsafa ya Uhuru wa nchi yetu ya Tanzania haiwezi kutenganishwa na Mwenge wa Uhuru. Naomba niwakumbushe, wakati wa Uhuru tarehe 9 Desemba 1961, Marehemu Baba wa Taifa alisema, sisi tutawasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro umulike ndani na nje ya mipaka yetu ulete amani, tumaini, upendo, uondoe chuki na dhuluma, sasa jambo hili si dogo. Kwa Mtanzania anayemuenzi Marehemu Baba wa Taifa itashangaza sana kama hatataka kuenzi falsafa ya Mwenge wa Uhuru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napenda tu kuwaomba Watanzania kwa kweli hatuna haja ya kuchukuliana hatua ya namna moja au nyingine lakini wote tutambue Mwenge wa Uhuru ni tunu kubwa ya Uhuru wa nchi yetu na unapaswa kuenziwa na Watanzania wote.
MHE. DKT. SULEIMAN ALLY YUSSUF: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kama ziko dosari katika kukimbiza Mwenge basi zitarekebishwa. Mimi nachotaka kumwambia hakuna dosari, dosari ni huu Mwenge wenyewe. Kwa sababu kwanza unapoteza fedha nyingi kupita kiasi na wakati na kwa kule kwetu tunaamini kukimbiza Mwenge ni ibada. Kwa nini tuendelee kulazimishwa kuabudu moto?
Swali langu ni hilo kwa nini tulazimishwe kuabudu moto? Sisi tunaamini ni ibada ya moto hiyo.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimia Mwenyekiti, labda tu nianze kwa kumnukuu mwanafalsafa mmoja ambaye nilimsoma anasema, vipo vitu vingine vinahesabika lakini huwezi kuvihesabu. Unaweza ukawa na vitu vinavyohesabika lakini ukashindwa kuvihesabu na nataka nikuambie hata wewe unaweza kuwa na mtazamo ambao ni hasi kuhusu Mwenge wa Uhuru lakini utashindwa kutekeleza mtizamo huo wa kuufuta Mwenge wa Uhuru katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nakuambia hivi Mheshimiwa Mbunge, mwaka jana wakati tunahitimisha mbio za Mwenge Mkoani Simiyu, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Simiyu, kwa kutumia Mwenge wa Uhuru Mkoa wa Simiyu umeweza kuzindua viwanda vitatu ambavyo vimeongeza maendeleo ya kiuchumi na vimeongeza ajira kwa Watanzania. Kwa hiyo, ukiangalia faida za Mwenge huu ni kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu tumezindua
mbio za Mwenge wa Uhuru Mkoani Katavi. Mkoa wa Katavi haukuwa na uwanja mkubwa wa michezo wa Mkoa. Nje ya bajeti ya maendeleo ya mkoa, Mkoa wa Katavi umeweza kuanza ujenzi mkubwa wa kiwanja cha mpira katika mkoa huo. Nimeeleza hapa miradi ya kujitegemea ambayo imebuniwa na wananchi ambayo imeongeza chachu ya maendeleo na uchumi wa wananchi katika Tanzania nzima. Mwenge wa Uhuru utadumu, utaendelea kusimama kama tunu ya nchi yetu ya Tanzania.
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mwaka jana Mwenge ulizimwa Simiyu, Mtukufu Rais John Pombe Magufuli alizuia misafara ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na baadhi ya Wakurugenzi na kuokoa kiasi cha pesa sijui zaidi ya shilingi bilioni sita.
Nataka kujua kwa mwaka mzima kukimbiza Mwenge wa Uhuru kunagharimu Taifa hili shilingi ngapi? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Keissy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nimpongeze Mheshimwa Keissy kwa kutambua namna ambavyo Mwenge huu wa Uhuru kwa maagizo ya Mheshimiwa Rais uliweza kuokoa fedha nyingi sana ambazo zilikuwa zikitumiwa na Wakuu wa Mikoa na viongozi wengine kuhudhuria katika mbio hizo za Mwenge. Tumekubaliana kwamba ni lazima tuendelee kuthamini namna nzuri ya matumizi ya fedha katika kukimbiza Mwenge wa Uhuru. Kwa hiyo, hilo halina shaka Mheshimiwa Keissy na sisi tunalisimamia vizuri kwa maagizo ya Mheshimiwa Rais wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti ya Mwenge wa Uhuru ambayo Mheshimiwa Keissy anataka kujua ni kiasi gani zimekuwa zikiandaliwa kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine. Hivyo kama anataka kujua ni kiasi gani bajeti zinatumika katika kila Halmashauri moja kwenda nyingine nitamuomba aonane na mimi na tutawasiliana na hizo Halmashauri.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Naipongeza Serikali kwa jitihada zake za kupambana na dawa za kulevya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa mara ya pili tena.
Ni kwamba naipongeza Serikali kwa jitihada zake.
Na vijana hawa wanapoathirika na hizi dawa za kulevya moja kwa moja tayari wanaingia katika kundi letu, kwa maana ya kundi la watu wenye ulemavu. Na kwa sababu wimbi ni kubwa kwa hivi sasa, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inaongeza Madaktari Bingwa kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa hawa walioathirika na dawa za kulevya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nijibu maswali haya mawili, Mheshimiwa Waziri wa Nchi atamalizia kwa ujumla yanayohusu supply reduction.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la kwanza la Mheshimiwa Amina Mollel, kwanza nimpongeze siku ya jana aliniletea wageni kutoka Chama cha Wananchi ambao wanajihusisha na Afya ya Akili Nchini na katika mazungumzo tuliyoyafanya ni pamoja na hili suala la Madaktari Bingwa wa Afya ya Akili kwenye Mikoa nchini. Mkakati tulionao na ndio taarifa niliyowapa wale wananchi wenzetu ni kwamba Serikali ina-scale up huu mkakati wa kuwa na hizi kliniki kama iliyopo Muhimbili, Temeke na Mwananyamala kwa mwaka huu kwenye mikoa kumi ya Tanzania Bara na kwa mwaka ujao tutaongeza mikoa mingine kumi, tunakwenda kwa awamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, kila tutakapoanzisha hii kliniki ya methadone ni lazima awepo Daktari Bingwa anayehusika na ku-administrate hiyo dawa kwa sababu methadone inalindwa kwa taratibu maalum za kuitunza na kuitoa kwa wagonjwa. Kwa hiyo, ni lazima awepo Daktari Bingwa anayeweza kufanya hivyo kwa hivyo, kwa mwaka huu nimhakikishie Mheshimiwa Amina Mollel kwamba tutakuwa na Madaktari Bingwa kwenye mikoa kumi ncjini, pindi kliniki za methadone zitakapoanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ni la Mheshimia Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kuhusu hizi kliniki na rehabilitation centres kwenye Mikoa; kwa sasa kweli, tuko Dar es Salaam peke yake, lakini kwenye mkakati wetu tunakwenda kwenye mikoa kumi kama nilivyosema. Na kwenye kila kanda tunakwenda kuanzisha rehabilitation centre ambapo tutakuwanazo nne sasa katika nchji nzima. Kwa hivyo, hii ni mikakati ambayo tunayo katika siku za usoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ruzuku, Serikali haina utaratibu wa kutoa ruzuku kwenye taasisi mbalimbali za binafsi, kwa sababu wao wanafanya kwa hiyari na tunawaomba na kuwatia moyo waendelee kufanya hivyohivyo kwa hiyari, lakini sisi kama Serikali tuna mikakati yetu ya kuwasaidia wenzetu ambao wameathirika na dawa za kulevya.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ninaomba nijibu maswali ya nyongeza yaliyoulizwa kwa umoja wake, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwanza nianze kumpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya, kwa majibu mazuri aliyokwishakuyatoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze tena kwa kulipongeza Bunge letu Tukufu kwa sababu mwaka 2015, ndilo lililosababisha kufanyika kwa mageuzi makubwa ya mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini kwa kutungwa kwa sheria mpya ambayo imeunda hiyo mamlaka sasa ambayo tumemuona Kamishna Jenerali akifanya kazi kubwa sana kwa kushirikiana na makamishna wenzake kuhakikisha kwamba tunapambana na tatizo la dawa za kulevya nchini.(Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba niliarifu Bunge
lako Tukufu Kamishna Jenerali baada ya kuteuliwa na mamlaka kuanza kazi rasmi, ameshahakikisha ametengeneza Mpango Mkakati Maalum wa Taifa wa kuhakikisha kwamba tatizo hili la dawa za kulevya nchini linaondoka. Na mpango mkakati huo unashirikisha pande zote mbili za Muungano, upande wa Zanzibar na upande wa huku Bara. Kwa hiyo, Mheshimiwa Khatib wala usiwe na wasiwasi, tunafanya kazi hizi kwa pamoja, vyombo hivi vyote viwili vinafanya kazi kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumegundua kwamba, wenzetu wa private sector wanafanya kazi nzuri sana kwenye mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini. Na hivyo nichukue nafasi hii kwanza niwapongeze wale wote ambao wameamua kujitolea kusaidiana na Serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania, tunawashukuru sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika mwaka huu wa bajeti, Ofisi ya Waziri Mkuu imeamua kuweka bajeti kidogo ambayo itasaidia kushirikiana na hao wenzetu ambao wameonesha kwamba, wana nia ama ya kuanzisha sobber houses kwa ajili ya kuwasaidia hawa walioathirika na dawa za kulevya, lakini vilevile kufanya kampeni na kuleta uhamasishaji mkubwa wa kuwasaidia vijana wetu kuwaondoa kwenye tatizo hili.
Kwa hiyo, tuko pamoja tunafanya kazi hii kwa pamoja, mapambano yanaendelea na tunataka kuona kwamba tunaondoa tatizo hili katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kumekuwa na changamoto kubwa ya vijana ambao wanaajiriwa kwa mikataba ya muda mfupi kuzungushwa pale wanapoenda kwenye Mifuko ya Pensheni kudai mafao yao ili waweze kuyatumia kama mitaji ya kujiajiri. Kwa mfano, kule Karagwe Kampuni ya Ujenzi ya Chico iliajiri vijana kwa utaratibu wa mikataba ya vibarua, mpaka hivi sasa wanazungushwa vijana hawa.
Je, Serikali inawasaidiaje vijana hawa kudai mafao
yao ili waweze kutumia hela hii kama mitaji ya kujiajiri?(Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi ya pekee sana kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu amekuwa mstari wa mbele sana kufuatilia haki za wananchi katika Jimbo lake na hilo ni jambo jema.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba tumekuwa na malalamiko ya namna moja ama nyingine ya wafanyakazi wa namna hiyo ambao wamekuwa wakiajiriwa kwa mikataba, mikataba yao inapoisha walizoea kuwa na fao ambalo si fao sahihi lakini lililokuwa linaitwa fao la kujitoa. Baada ya kupitia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kifungu cha 11, lakini kupitia Sera ya Hifadhi ya Jamii katika nchi yetu na sheria tulizonazo, Serikali pamoja na wafanyakazi wenyewe na vyama vya wafanyakazi, tumekubaliana sasa kuna haja ya kuangalia namna nzuri ya kuwasaidia wafanyakazi wote ambao wamekuwa wakikumbwa na jambo hilo kwa kuanzisha fao lingine ambalo litaitwa ni Bima ya kukosa ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hiyo tumeshaanza kuifanya vizuri kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi, niwaombe wafanyakazi wote nchini ambao walikuwa wanaelekea katika fao hilo wavute subira ili matakwa ya kisheria yafanyiwe kazi na ndipo fao hilo litaanza kutolewa kwa mujibu wa sheria ambayo itakuwa imetungwa na Bunge.
Pia ni maagizo ya Mheshimiwa Rais siku ya Mei Mosi alipokuwa pale Moshi ameendelea kusisitiza kwamba sasa tushughulikie suala hilo na liweze kufungwa kisheria na Wafanyakazi waweze kupata haki zao. (Makofi)
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliitaka mifuko kusitisha fao la wafanyakazi ambao wanataka kuchukua mafao yao mpaka wafikishe miaka 60. Ningependa tu kufahamu kwa sababu kwa hivi sasa sakata la wale wafanyakazi waliopatwa na vyeti fake ni dhahiri kabisa watapenda kuchukua mafao yao ili wajiingize katika shughuli nyingine.
Nini kauli ya Serikali katika kuhakikisha kwamba wafanyakazi hao na wale wengine ambao wana ajira fupi wanachukua mafao yao ili waweze kuendelea na shughuli nyingine? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kuhusiana na mafao ya waliokumbwa na kadhia ya vyeti vya kughushi, kwa sasa niseme ni suala ambalo hatuwezi kulitolea maelekezo hapa, pindi taratibu zote zitakapokamilika basi taarifa itaweza kutolewa na watajua hatima yao. (Makofi)
MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna taasisi au makundi katika jamii ambayo yanaajiriwa ajira za mkataba. Kwa mfano, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wabunge wanakuwa na ajira ya miaka mitano na mkataba wao baada ya hapo unakuwa umekwisha. Kama alivyo Mheshimiwa Rais, nembo ya Taifa hili ndivyo alivyo Mbunge nembo ya Jimbo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuwaacha Wabunge baada ya kustaafu bila kuwapa pensheni na tunajua maisha yalivyo, hamuoni kwamba Wabunge wanadhalilika na makundi ya aina hiyo kiasi ambacho wanashindwa kumudu maisha. Je, ni lini Serikali itafikiria kuliona hili ili Wabunge wanapostaafu nao waweze kupatiwa pesheni? Ahsante.(Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, malipo yote ambayo yamekuwa yakifanywa kwa Waheshimiwa Wabunge yanalipwa kwa mujibu wa sheria, yanalipwa pia kwa kuzingatia masharti ya kazi ya Mbunge ambayo yanakuwa yameandaliwa pia kwa kufuata sheria za nchi tulizonazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Waheshimiwa Wabunge wana ushauri, wana jambo linalohusu masuala ya kisheria ya haki na mafao yao Tume ya Huduma za Bunge inafanya kazi kwa niaba ya Waheshimiwa Wabunge wote. Kwa hiyo, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge tuone namna ya kuwasiliana na tume ya huduma ya Bunge ili kuangalia ni kwa kiasi gani yale yanayohusu Wabunge yaweze kushughulikiwa ipasavyo na Tume ya Huduma ya Bunge, ambayo tumeiweka kwa mujibu wa sheria.(Makofi)
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya watumishi ambao fedha zao hazijapelekwa kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ninaomba kuuliza swali moja la nyongeza. Hapa nina barua ya mtumishi ambaye anatarajia kustaafu tarehe 15 Juni; mpaka leo makato yake ya miezi 18 hayajapelekwa jambo ambalo litaathiri pensheni yake.
Je, Serikali haioni haja sasa ya kuwa na takwimu ya watumishi ambao wanatarajia kustaafu ili kusudi makato yao yaweze kupelekwa kwenye mifuko na watakapostaafu wapate kile kinachostahili kwa wakati? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma na matakwa ya Serikali yetu kuhakikisha kwamba watumishi wote ambao wamekuwa wakichangia katika Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kulipwa mafao yao ya pensheni kwa wakati. Hivyo, tumekuwa tukitoa maelekezo na maagizo mbalimbali ili taasisi zote zinazoshughulikia malipo ya pensheni kwa wafanyakazi wa Serikali pia kwa wafanyakazi wa private sector wahakikishe kwamba watumishi wanalipwa mafao yao kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa tukichua hatua pale mafao ya watumishi yanapochelewesha. Ninamuomba Mheshimiwa Chumi atuletee taarifa za mtumishi huyo ambaye amecheleweshewa nasi tutachukua hatua. Niendelee kuwaagiza wale wote wenye jukumu la kusimamia malipo ya pensheni kwa wastaafu, watekeleze wajibu wao na wastaafu waweze kupata mafao yao kwa wakati unaotakiwa bila kucheleweshwa na tukizingati kwamba hata Mheshimiwa Rais amesisitiza na ameagiza sana suala hilo lisimamiwe vizuri na sisi tutaendelea kulisimamia.
MHE. JAMES F. MBATIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa nchi ya Tanzania imejengwa na tabaka
zote hasa wakulima na wafanyakazi; na kwa kuwa Serikali ya awamu iliyopita kwenye bajeti ya mwaka 2013/2014 - 2014/ 2015 walitoa ahadi kwenye Bunge hili kwamba watalipa wastaafu wote (wazee wote wenye miaka 60) bila upendeleo wa aina yoyote, wawe wafanyakazi au wakulima.
Nataka kupata kauli ya Serikali ni lini watatekeleza ahadi yao hii ya kuwalipa wazee wote nchi nzima ambao wana zaidi ya miaka 60?(Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimjibu Mheshimiwa James Mbatia, mzee mtarajiwa swali lake ambalo ameliuza kwa niaba ya wazee.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, imetoa ahadi ya kushughulikia suala zima la ulipaji wa pensheni kwa wazee katika nchi yetu ya Tanzania. Naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu mchakato huo umeshaanza na tayari tathmini na study zimeshafanyika za kuona ni utaratibu gani utafanyika wa kuweza kuwalipa pensheni wazee hao, michakato hiyo yote ikishakamilika basi Bunge lako Tukufu litaarifiwa ni lini utaratibu huo wa malipo ya pensheni utaanza. (Makofi)
MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kama ambavyo Wabunge wengi wanaliona tatizo hili, limekuwa tatizo kubwa sana. Mheshimiwa Waziri anaposema kwamba ni suala la kumiliki, gari halimilikiwa kila mwaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunalipa kwa ajili ya matumizi ya barabara, lakini watu wengi wamepata tabu katika hili, kwa nini Serikali isitoe tamko kwamba hili suala italifuta ili wananchi tulipe hiyo road license kutokana na matumizi ya barabara.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika,kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, lakini kwa niaba ya Serikali kwa ujumla.
Swali hili limeonyesha kuwa na interest kubwa kwa Waheshimiwa Wabunge na simaanishi kwamba ni kwa ajili yao wenyewe ni kwa ajili ya nchi nzima na watu wanaowawakilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu vizuri sana, utaratibu tunaoutumia ndani ya Serikali Waheshimiwa Wabunge mnafahamu. Kwanza sheria iliyopo ndio inayotumika mpaka sasa, lakini Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza hapa kwa niaba ya Serikali tumesikia na kama tumesikia ina maana ni process ambayo inayotakiwa ya kurudi na kwenda kulitazama suala hili kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Naibu Waziri hawezi sasa hapa ndani akatoa commitment ya kubadilisha sheria akiwa hapa ndani ya Bunge bila kuzingatia utaratibu wa kisheria wa kubadilisha sheria.
Mheshimiwa Spika, tunakuomba sana kwa heshima ya Bunge lako, haya yote yaliyoelezwa na Waheshimiwa Wabunge Serikali imesikia lakini kwa pamoja tutajadiliana tujue namna nzuri ya kuweza kulishguhulikia jambo hili. Tunakuomba sana uielewe nia njema ya Serikali. (Makofi)
MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa Waraka wa SSRA Namba 1 wa mwaka 2006 unasema kwamba mstaafu atakayecheleweshewa mafao yake, Mfuko husika wa Hifadhi ya Jamii utatakiwa kumfidia, waraka huo unaonekana kutokuwa na nguvu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni nini sasa mkakati kabambe wa Serikali kuhakikisha tabia ya ucheleweshaji wa mafao ya wastaafu inakoma? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha kwa majibu yake mazuri na nampongeza sana.(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa waajiri wengi lakini na mifuko kwa maana nyingine wamekuwa wakichelewesha ulipaji wa mafao ya wastaafu wetu kwa namna moja ama nyingine. Kupitia SSRA tumeweka sasa mkakati maalum na kupitia maboresho pia ya Sheria za Kazi ambayo yalifanyika ndani ya Bunge lako hili Tukufu, tumewapa nguvu pia Maafisa Kazi wetu ambao sasa wamepata ya kukagua, wanapokwenda kukagua masuala ya kazi, wanakwenda pia kukagua compliance ya mifuko na waajiri katika kushughulikia pensheni za wastaafu na michango ya waajiri kwenye mifuko ya pensheni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mbunge kwamba Serikali inalisimamia hili kupitia SSRA lakini pia kupitia ofisi zetu za kazi tutaendelea kuhakikisha kwamba waajiri na mifuko ya pensheni inafanya compliance katika sharia zote tulizonazo na wastaafu wetu wapate mafao yao kwa wakati na waajiri wapeleke michango yao kwa wakati.
MHE. KASUKU S. BILAGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili mfanyakazi aliyemaliza kazi kwa kustaafu au kupoteza kazi aweze kulipwa mafao yake katika mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ni pamoja na kupata barua yake ya mwisho. Wafanyakazi waliopatikana na vyeti fake hawajapata mafao yao kutoka kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwa sababu hawana barua za kumaliza huo ufanyakazi fake.
Je, Serikali iko tayari kuwapa barua zao ili wakahangaike kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na majibu fasaha na huo ndiyo utaratibu wa Serikali katika kushughulikia yale ya awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jibu la Mheshimiwa Bilago, swali hili la mafao ya watumishi ambao wameonekana kwamba ni watumishi wenye vyeti fake na ambao wamepatikana na masuala kadha wa kadha katika utumishi wao, limekuwa likijibiwa na Serikali mara kadhaa ndani ya Bunge lako Tukufu na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma. Ninaomba Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine wote waendelee kuvuta subira, yale ambayo yamekuwa yakijibiwa na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma hayo ndiyo ambayo yatakuja kutekelezwa baada ya Serikali kufikia maamuzi yale ambayo Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma amekuwa akieleza humu ndani ya Bunge lako Tukufu kila siku.
MHE. ZAINAB M. AMIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na mimi napenda kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, ni lini Serikali itasitisha tozo katika Daraja la Kigamboni ili liweze kutumika kama madaraja mengine yalivyo ya Ruvu na Wami?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kwanza niwashukuru Waziri wa TAMISEMI na Naibu Waziri kwa majibu mazuri yaliyoulizwa na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Daraja la Kigamboni limejengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa NSSF. Ni kivuko ambacho kinafanya kazi kama vivuko vingine tulivyonavyo nchini na vivuko vingine vilivyopo nchini pia vimeweka mfumo wa utozaji wa tozo kidogo ili kuhakikisha kwamba vivuko vile vinaendelea kulindwa na vinaendelea kukarabatiwa viweze kuendelea kufanya kazi.
Kwa hiyo, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge tozo iliyowekwa kwenye Kivuko cha Kigamboni na NSSF imefuata utaratibu wa kisheria na wa kikanuni na hivyo, itaendelea kuwepo, lakini itaendelea kuwa ikibadilishwa kulingana na mazingira na taratibu za kisheria ambazo zinaongoza tozo zote katika nchi yetu ya Tanzania katika vivuko vyote nchini.
MHE. JOSEPH L. HAULE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nisikitishwe sana na majibu haya ya Serikali ambayo wamekuwa wakiyajibu mara kwa mara, kiukweli yanakatisha sana tamaa. Kwa sasa huu utaratibu wa Serikali wanaosema ni kifuta jasho kwa wananchi ambao wanakuwa wameuliwa na tembo au mazao yameharibiwa kiukweli haina uhalisia na haileti haki kwa wananchi ambao wamekaa kwenye mazingira hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hii yote inatokana na sheria ya wanyamapori ambayo imeonekana kuwa na usumbufu na upungufu mkubwa sana. Ni lini Serikali itaileta sheria hii hapa Bungeni ili iweze kubadilishwa ili iweze kwenda na uhalisiana kurudisha fidia na hili neno la kifuta jasho libadilishwe iwe fidia iliyokuwa imetathiminiwa kutokana na matatizo ambayo wamepata wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili juzi kuamkia jana katika Kijiji cha Kikwaraza pale Mikumi ambapo Mbunge wa Mikumi anaishi, simba alivamia zizi la mfugaji anaitwa Agrey Raphael na kuua ng’ombe mmoja pamoja na kujeruhi ng’ombe wawili.Sasa hayo matatizo na changamoto kama hizi zimekuwa nyingi sana kule Mikumi kwenye Kata kama Mikumi, Luhembe, Kidodi, Kilangali, pamoja na maeneo ya Mhenda. Je, Naibu Waziri yuko tayari kuambatana na mimi kuelekea kule mikumi ili akasikilize changamoto nyingi za wananchi ambao wamekuwa na kilio cha muda mrefu kutokana na matatizo kama haya ya wanyamapori kabla hawajaamua kuchukua sheria zao mikononi kwa kutumia silaha za jadi? Ahsante. (Makofi) [Maneno haya siyo sehemu ya Taarifa Rasmi za Bunge)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba….
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu iko sasa hivi inafanya kuiisha tunapitia upya sera na sheria pamoja na taratibu mbalimbali ambazo zinatumika katika kutoa hiki kifuta jasho na machozi, ni hivi karibuni tu tutaileta hii sheria hapa ndani Bungeni ili Bunge lako Tukufu liweze kushauri na liweze kuipitisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la kuambatana naye, nataka nimwambie tu niko tayari mara baada ya shughuli za Bunge kukamilika, nitaambatana naye kwenda kuangalia maeneo hayo yote yalioathirika. Ahsante.
MHE. KANGI A. N. LUGOLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza.
Majibu ya Serikali kwa kweli yanawakatisha tamaa walemavu na hasa ambao wako vijijini. Kwa sababu Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba hii Sheria Namba 9 ni tangu mwaka 2010, lakini leo katika majibu yake ya msingi ndiyo anatamka mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba Serikali sasa inawaagiza watendaji waharakishe kuunda Kamati za Walemavu Vijijini.
Je, kama Mheshimiwa Amina Mollel asingeuliza swali hili leo ina maana Serikali haikuwa na mpango wa kuwaagiza watendaji kwa ajili ya uharakishaji wa uundaji wa hizi Kamati za Walemavu kule Vijijini?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE WALEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwanza kabisa naomba nimshukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa katika swali la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kweli kwamba Serikali haijaanza kutekeleza Sheria Namba 9 ya mwaka 2010 ambayo inasimamia huduma kwa watu wenye ulemavu. Naomba nikuhakikishie wewe binafsi na Bunge lako Tukufu kwamba haya yote ambayo mnaona yamekuwa yakiendelea, yanayowagusa watu wenye ulemavu katika nchi yetu ya Tanzania ikiwemo upunguzaji wa gharama ya vifaa vyao; ikiwemo namna tofauti ya kuhakikisha kwamba elimu inakuwa inclusive kwa watu wenye ulemavu katika nchi yetu ya Tanzania, ikiwemo namna ya kuunda Mabaraza hayo kwenye maeneo yetu ya Halmashauri zetu ndani ya Serikali za Mitaa. Ni utekelezaji wa sheria hiyo, ninaomba tu niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge mipango yote ipo na imeshaanza kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu cha msingi hapa wote kwa pamoja sasa na hasa tunapokaa katika vikao vyetu vya Mabaraza ni kuendelea kuona kwamba yale maagizo ambayo tumeshayaweka na kuyateremsha kwenye Serikali za Mitaa ni kuhakikisha kwamba yanatekelezeka na kama mnaona kuna tatizo mtupe taarifa ili tuweze kusimamia zaidi. Lakini naomba niwathibitishie kwamba sheria hiyo hiyo imeanza kufanya kazi na sisi kama Serikali tumekuwa tukiisimamia na siyo tu tumesubiri swali hili la Mheshimiwa Amina Mollel. Nakushukuru.
MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naishukuru Serikali kwamba hii Awamu ya Tano imeagiza kwamba hii mifuko ya hifadhi ya jamii iweze kuwekeza katika viwanda na katika hivi vyama vya ushirika.
Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru pia Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wetu, alipokuja Mkoani Iringa katika ziara yake, alitembelea kile kinu chetu cha National Milling na aliahidi kwamba NSSF ingeweza kutoa mtaji ili kiweze kufanya kazi vizuri, pamoja na kutoa ajira nyingi kwa wananchi wa Iringa. Sasa nataka tu kujua: Je, agizo lake lile limeshafanyiaka? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza niendelee kumpongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi anavyojibu maswali ya Waheshimiwa Wabunge vizuri sana ndani ya Bunge lako la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba nchi yetu inaingia katika uchumi wa viwanda na hivyo basi Serikali kwa makusudi mazima imeiagiza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ianze sasa kuhakikisha na yenyewe inaunga mkono nguvu za Serikali na mpango wa maendeleo wa Serikali wa kuingiza nchi yetu kwenye uchumi wa viwanda kwa kuhakikisha wanafufua baadhi ya viwanda ambavyo vilikuwa vimekufa na kuanzisha viwanda vingine vipya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana dada yangu, Mheshimiwa Rita Kabati, kwa karibu sana amefanya kazi na Serikali kwa kupitia Mfuko wa NSSF kuhakikisha kinu cha National Milling pale Iringa kinafufuliwa na kinafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Dada Ritta Kabati kwamba NSSF kwa kushirikiana na Bodi ya Mazao Mchanganyiko wameshafikia hatua nzuri ya ununuzi wa mashine na vifaa vinavyotakiwa katika kufufua kinu chetu cha Iringa. Baada ya muda siyo mrefu, uzalishaji utaanza kwa nguvu sana na ajira zitaongezeka na hivyo basi, wananchi wa Mkoa wa Iringa na Mji wa Iringa wajue kwamba Mbunge wao amefanya kazi nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kushirikiana na Serikali na Mfuko wetu wa NSSF na Mifuko mingine ya Hifadhi ya Jamii, tuna mpango wa kufungua viwanda visivyopungua 25 na kuongeza idadi ya ajira zisizopungua 200,000 katika nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)
MHE. AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri ambayo amejibu lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa kituo hiki cha Buhangija kimekuwa na msongamano kutokana na wimbi kubwa la mauaji ya Albino na kukifanya kituo hiki kuwa na watoto wengi zaidi na hatimaye watoto wale kuweza kuishi pale shuleni. Je, ni lini Serikali itakiangalia kituo hiki na kukipelekea fedha ya kutosha ili kiondokane na tatizo kubwa la chakula linalokuwa linakikumba kituo hiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini Serikali itapeleka Walimu wa kutosha kwa ajili ya watoto wasioona, wasiosikia na wasiosema? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimpongeze sana dada yangu Mheshimiwa Azza kwa kazi nzuri anayoifanya na tumekuwa tukishirikiana sana katika kuhudumia watoto katika kituo hicho. Kwa kweli namshukuru sana Mheshimiwa Azza na nadhani wananchi wa Shinyanga wanasikia pongezi hizi za Serikali kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini maswali yaliyoulizwa na Mheshimiwa Azza Hilal ni maswali ya msingi na swali la kwanza angependa kujua ni kwa namna gani sasa Serikali itaendelea kuhudumia vizuri kituo hicho na hasa kuhakikisha wale watoto wanapata chakula kinachotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali la msingi, tulipata shida kubwa sana wakati ule ambapo mauaji ya wenzetu wenye ualbino yalipokuwa yamekithiri katika nchi yetu ya Tanzania, wengi wenye ualbino waliona pale ni mahali pekee na salama kwao, kwa hiyo wengi walikimbilia hapo haikuwa shule tena, ilikuwa ni kituo cha kuwahifadhi wenye ualbino watu wazima, vijana pamoja na hao watoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, baada ya Serikali kufanya kazi nzuri ya kudhibiti mauaji hayo, tumeshafanya utaratibu na tumeweza kuwaondoa wale watu wazima na vijana ambao siyo wanafunzi kutoka hiyo idadi ya 407 mpaka idadi hiyo ya 228 na sasa basi huduma hizo nyingine zinapatikana vizuri na sisi kama Serikali tutaendelea kusimamia chakula na mahitaji mengine yapatikane sawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha kwamba kituo hicho kinapatiwa fedha za kutosha, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu na Mheshimiwa Azza Hillal tumeshaanza mkakati wa kuhakikisha pale panakuwa mahali salama na mahali panapostahili. Kwa kuanzia tumeshapeleka fedha kwa ajili ya ukarabati wa kituo hicho na tutaendelea kupeleka mahitaji mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi juzi mmeona Mheshimiwa Waziri Mkuu amepokea vifaa mbalimbali kwa ajili ya mafunzo ya wenye ulamavu kwenye taasisi zetu, kwa hiyo na kituo hicho tutazingatia kukipa huduma zote zinazostahili kwa mujibu wa taratibu za Serikali.
MHE. CATHERINE N. RUGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri maswali mawili ya nyongeza.
Swali langu la kwanza, natambua halmashauri zetu zote Tanzania zinatakiwa kuwapatia asilimia mbili vikundi vya ujasiriamali vya watu wenye ulemavu. Swali langu, je, ni kiasi gani cha pesa kilitolewa kwa mwaka wa fedha 2017/2018 kwa vikundi vya watu wenye ulemavu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunapoelekea kwenye uchumi wa viwanda Serikali imewaandalia mazingira gani watu wenye ulemavu ili waweze kushiriki moja kwa moja kwenye uchumi huo kwa kupata fursa ya ajira, fursa ya kujiajiri kwa kuanzisha viwanda vidogo vidogo na fursa ya kupata masoko kwa ajili ya bidhaa zao? Ahsante.
WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Catherine Ruge kama ifuatavyo, nikianza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kazi na nzuri na majibu mazuri aliyoyatoa leo Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati tukiendelea na hotuba ya Bajeti ya Waziri Mkuu jana suala hili la asilimia 10 katika mifuko ya Halmashauri za Wilaya ilijitokeza. Ninaomba nikubaliane na maelekezo ama kauli ya Serikali iliyotolewa na Waziri wa TAMISEMI jana kwamba maeneo yote yanayohusiana na asilimia 10 yatatolewa maelezo katika bajeti itakayoanza leo inayohusu Ofisi ya Rais, TAMISEMI na hivyo tutaweza kuwa na maelezo fasaha.
Lakini la pili, kuhusu namna nzuri ya kuwafanya watu wenye ulemavu kuingia nao katika uchumi wa viwanda, kama tulivyotoa maelezo jana wakati tunahitimisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, suala hili ni suala la kisheria liko ndani ya sheria ya watu wenye ulemavu namba tisa ya mwaka 2010. Kwa hiyo, sisi sasa tunachokifanya ni kusimamia sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tu kutoa rai kwa watu wote na wawekezaji wote ambao wanaanzisha viwanda katika nchi yetu ya Tanzania kuona kwamba wenye ulemavu nao wanaouwezo wa kutoa mchango katika ujenzi wa taifa kupitia auchumi wa viwanda hivyo basi wawape fursa kwa kuzingatia sheria ambayo tuko nayo na sisi kama Wizara tutaendelea kusimamia kuona jambo hili linatekelezwa.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika Mkoa wa Kigoma ipo NGO ambayo imezunguka kwa muda wa wiki mbili katika Wilaya zote saba ikiwatoza wanawake shilingi 10,000 na kuwapigisha picha kwa kuwaahidi kwamba Serikali itatoa mikopo kupitia Mfuko wa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu. Ninataka Serikali inieleze, je, mpango huo wa kutoa pesa kupitia Mfuko wa Mama Samia upo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli zote za uwezeshaji wananchi kiuchumi katika nchi yetu ya Tanzania zinasimamiwa na Sera ya mwaka 2004 na Sheria ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya mwaka 2004 ambayo inaruhusu uanzishwaji wa taasisi mbalimbali kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa kuhusu taasisi hiyo zilishapatikana ndani ya Serikali na Ofisi ya Makamu wa Rais ilishatoa tamko la kuikana taasisi hiyo kwamba haihusiki nayo. Ninaomba nichukue nafasi hii kuagiza uongozi wa mkoa wa Kigoma kuifuatilia taasisi hiyo na kuikana na kuipa maelekezo kwamba Ofisi ya Makamu wa Rais haihusiki na jambo hilo. Kama wanaendesha shughuli hizo kwa kutumia sheria na taratibu nyingine, wanapaswa kujieleza kwa kutumia sheria na taratibu nyingine walizozifuata, lakini siyo Ofisi ya Makamu wa Rais. Kama wataendelea kuwadanganya wananchi kwa kutumia Ofisi ya Makamu wa Rais, Serikali haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya taasisi hiyo. (Makofi)
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kumekuwa na Mifuko mingi ya Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi, mingine iko Ofisi ya Waziri Mkuu na mingine iko TAMISEMI; na kwa kuwa sheria/ takwa hili la kutaka kutengwe asilimia 10 kwenye Serikali za Mitaa, muda mwingi katika ripoti za CAG imeonekana ufanisi ni hafifu, kama kweli mna lengo la kuwawezesha wananchi kiuchumi, kwa nini msifikirie kuunganisha mifuko hii uwe mfuko mmoja ili kuwepo na ufanisi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, naomba nitoe majibu ya nyongeza kwenye swali la msingi sana aliloliuliza Mheshimiwa Paresso.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa ndani ya Serikali tumeanza kutafakari na kuona ni kwa kiasi gani tunaweza kuitazama kwa kina mifuko hii yote takriban kama 16 ama 19 hivi tuliyonayo, tukaiunganisha na kuipunguza ikajenga nguvu kubwa zaidi na ikawa na impact kubwa zaidi kwa Watanzania wengi na hasa wale ambao wako vijijini. Kwa hiyo, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kazi hii imeshaanza na Ofisi ya Waziri Mkuu inaishughulikia vizuri na baada ya muda mfupi nadhani tunaweza tukaja na sheria ya kuunganisha baadhi ya mifuko na kuibakiza michache ambayo itakuwa na impact kubwa kwa maendeleo ya Watanzania. (Makofi)
MHE. JUMA OTHMAN HIJA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake marefu lakini ambayo hayakujibu swali langu la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la msingi ni kwamba nilikuwa naulizia matayarisho ya rasilimali watu ambao watakuja kuendesha viwanda vyetu. Mheshimiwa Waziri amenijibu mambo ya mikopo, elimu na kadhalika. Nilichokuwa naulizia hapa ni kwamba sisi sasa hivi tuna siasa ya kuendesha viwanda. Je, tuna matayarisho gani ya kuja kuendesha hivi? Tuna matayarisho kwamba kwa mfano, mtu anaweza akawekeza viwanda lakini baadaye viwanda vile vikaja vikaendeshwa na watu kutoka nje ya nchi. Je, sisi Watanzania tuna matayarishoi tgani ya kuja kuendesha viwanda hivi? Hilo ndiyo swali langu lilikuwa la msingi lakini siyo suala hili ambalo Mheshimiwa Waziri amenijibu.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ya msingi aliyoanza nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014/2015 Serikali ilifanya tafiti kubwa mbili muhimu sana kwneye nchi yetu. Utafiti wa kwanza ni kujua aina ya nguvukazi tuliyonayo na utafiti wa pili ni aina ya ujuzi uliopo katika nguvukazi tuliyonayo wa kuweza kukidhi uchumi kwenye sekta za vipaumbele ambavyo vimewekwa kwenye mpango wa maendeleo, na hasa kwenda kwenye uchumi huo wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya tafiti mbili hizo kubwa kufanyika mpaka sasa ndani ya nchi yetu tunajua mahitaji ya ujuzi katika uchumi wa viwanda yanapungukiwa kwenye maeneo yapi. Ndiyo maana Ofisi ya Waziri Mkuu baada ya kugundua hayo mahitaji ya ujuzi unaohitajika kwenye viwanda na Waheshimiwa Wabunge kila mwaka mmekuwa mkitutengea bajeti ya shilingi bilioni 15; sasa bilioni 15 hizo ndizo zinazotumika kwenye programu tano alizozisema Mheshimiwa Naibu Waziri na nyingine za kujenga ujuzi kwa mahitaji ya viwanda vilivyoko katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie Wabunge jambo hilo tunalielewa na tunalifanyiakazi vizuri sana.
MHE. HAMIDU H. BOBALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kumekuwa na changamoto ya wazazi wanaopata watoto ambao ni pre-mature babies, hawa watoto njiti, kupata leave inayofanana na wazazi waliojifungua kawaida. Serikali haioni kuna haja sasa akina mama watumishi wanaojifungua watoto ambao hawajatimiza muda wao wakaongezewa ile leave ili waweze kuwalea vizuri wakiwa bado ni wadogo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu mbalimbali ya kusimamia haki na maslahi ya wafanyakazi kwenye maeneo tofauti ikiwemo eneo hili la afya pamoja na hili la afya ya uzazi tumekuwa na sheria mbalimbali zinazotuongoza. Sheria hizo zimekuwa zikifanyiwa mabadiliko kwa kuzingatia hali halisi ya namna nzuri ya kuweza kuwahudumia wafanyakazi. Tumeshapokea maombi ya kuangalia ni namna gani wafanyakazi wanaokumbana na hasa wanawake wanaopata matatizo ya namna moja ama nyingine kwenye kujifungua wasaidiwe.
Mheshimiwa Spika, naomba kulihakikishia Bunge lako Tukufu pamoja na Mheshimiwa Mbunge hayo ni mambo ambayo yanaendelea kujadiliwa na kufanyiwa kazi ili kuweza kuwasaidia wanawake. Hii pia ni hata kwa wanaume ambao wake zao wamejifungua watoto ambao wamezaliwa kabla ya umri wao ili waweze kupewa haki na kusaidia malezi ya watoto na malezi ya familia kwa ujumla. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nini mpango kabambe wa Serikali kwa maeneo yale ambayo UKIMWI uko chini ya asilimia moja, kuhakikisha kwamba tatizo hili linaondolewa kabisa kwa maeneo hayo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Salma Kikwete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzindua Taarifa ya Takwimu za UKIMWI tarehe 1 Desemba, 2017 nchi kwa ujumla tumeweza kujua hali ya UKIMWI katika mikoa yote. Tumeiagiza Tume ya Kudhibiti Ukimwi Nchini (TACAIDS) kuhakikisha kila mkoa unatengeneza mkakati wao kulingana na hali ya UKIMWI ilivyo katika mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wale ambao maambukizi yao ni machache, viongozi wa mkoa na taasisi zinazohusika wahakikishe wana-retain ile hali ama kuhakikisha maambukizi hayapandi ama yanaondoka kabisa na ile mikoa ambayo maambukizi yako juu mikakati ya mkoa huo ni kuhakikisha maambukizi yanashuka chini. Kwa hiyo, kila mkoa unatengeneza mkakati kutokana na hali halisi katika mkoa husika. Kwa hiyo, Serikali inalisimamia sana suala hili na lengo letu ni kufika hiyo 90-90-90, ama huko mbele tuendane na matakwa ya kiulimwengu ya kufika 00-00-00. Kwa hiyo Serikali inazingatia sana suala hilo.
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wafanyakazi hawa hawakulipwa kama ambavyo jibu linasema lakini walikuwa wakikatwa mishahara yao kila mwezi na pesa hazikuwasilishwa kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kinyume na utaratibu wa kisheria na ni wajibu wa Serikali kuhakikisha makato ya wafanyakazi yanawasilishwa kwenye mifuko na si wajibu wa wafanyakazi. Je, Serikali inatoa tamko gani?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa madai ya wafanyakazi ambao wamekuwa wakidai mafao yao yamekuwa mengi sana ikiwepo hata iliyokuwa Hoteli ya Sabasaba ya Mkoani Arusha mpaka leo hawajaliwa mafao yao na nimekuwa nikifuatilia kwa mrefu sana. Je, nini tamko la Serikali?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali hilo lakini naomba nichukue nafasi hii kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Catherine Magige, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Catherine Magige katika maswali yote mawili ya nyongeza amelihakikishia Bunge hili kwamba bado lipo tatizo kwanza la kulipwa kwa pensheni kwa wafanyakazi hao lakini lipo tatizo la mwajiri kutopeleka michango ya wafanyakazi katika mifuko iliyokuwa inachangiwa na hao wafanyakazi. Naomba nitumie nafasi hii kuagiza viongozi watendaji wa Mifuko iliyokuwa inahusika na wafanyakazi wa taasisi zote hizi mbili na kwa mujibu sheria mpya tuliyonayo ni wajibu wa Mfuko wenyewe kuhakiksha michango ya mwajiri inapelekwa kwenye mifuko husika, hivyo basi mifuko hiyo ifanye haraka kukutana na wafanyakazi hao na zilizokuwa taasisi zinazosimamia mafao ya wafanyakazi hao ili tuweze kujua nini kilichojiri na kama wanazo stahili zao kwa mujibu wa sheria waweze kulipwa mapema sana na kuweza kuondoa adha kwa wafanyakazi wote katika Taifa letu.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni muhimu wa kuwakumbuka wazee hawa ambao wamelipigania Taifa hili kama zawadi kwao kufuta jasho kwa kile walichokifanya bila ya kuwasahau wazee waliopigana vita ya pili ya dunia?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze na nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa majibu mazuri ambayo yanatokana na historia ya Taifa letu na wazee wa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ibara ya 11(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeshaweka utaratibu wa mamlaka ya nchi kuweka mifumo na sera ambazo zitawajali Watanzania waliokwishakutumikia Taifa hili katika nyanja mbalimbali na kulifanya Taifa lifike mahali lilipofika kwa kuwahifadhi kutumia sheria na sera mbalimbali. Kwa muktadha wa wazee wote nchini na Watanzania wote ambao wamehudumu katika Taifa hili kwa namna moja ama nyingine, Katiba imeshatuwekea utaratibu na ndiyo maana tunazo sera na sheria nyingi tu ambazo zinashughulikia masuala ya ustawi wa wazee kwa ujumla wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha msingi cha kufanya ni sisi kama Wawakilishi wa Watanzania kuendelea kushauriana na Serikali katika kuboresha eneo moja ama lingine ili kuwahifadhi wazee wote ndani ya Taifa letu kwa kuzingatia mchango wao kwenye Taifa hili katika maeneo mbalimbali na maeneo tofauti.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante awali ya yote naishukuru Serikali kwa majibu mazuri na juhudi zote ambazo zimeshafanyika na zinaendelea kufanyika. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina taasisi zake ambazo zinashughulikia matatizo yao ikiwemo mirembe hapa Dodoma na Lushoto na kituo kilichopo Lushoto. Lakini taasisi hizo zina mapungufu katika rasilimali watu, je, Serikali imejipanga vipi sasa kuwezesha taasisi hizo ili wanapozidiwa na wagonjwa hao waweze kupatiwa matibabu hayo kwa haraka?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili , madawa ya kulevya yana urahibu na pia yanaleta msongo wa mawazo ambayo yanapelekea vijana hawa au wote waliotumia kuwa katika hali ngumu sana ya kimaisha hata pale wanapotoka nje ya vituo ambavyo walikwenda kwa rehab.

Sasa Serikali ina mpango gani kuwezesha Chuo chetu cha Ustawi wa Jamii Tanzania ili waweze kupata wataalam ambao watakuwa wanapita au wanasambazwa katika mikoa yote kwenda kuwashughulikia vijana hawa ambao wameshapata shida hiyo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niungane na Watanzania wote lakini vilevile niungane na Waheshimiwa Wabunge wote na hasa Kamati ya UKIMWI na Mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya kuwashukuru wadau wote ambao wameshirikiana na Serikali katika kuhakikisha vita dhidi ya dawa za kulevya nchini inafanikiwa kwa kiasi kikubwa, ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nichukue hatua nyingine kumpongeza sana Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa nia yake ya dhati na dhamira ya dhati ya kuhakikisha kwamba nchi yetu inaondokana na tatizo la dawa za kulevya nchini. Mapambano haya ambayo yameongozwa na mamlaka yamesaidia kwa sasa kwa mujibu wa takwimu na tafiti tulizozifanya mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchi tumeweza kufanikiwa kudhibiti uingiaji wa dawa za kulevya nchini kwa asilimia 95, baada ya kufikia hatua hiyo sasa tunakabiliana na hayo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyazungumza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza tunakabiliana na suala zima la harm reduction kuhakikisha tunawarejesha katika hali nzuri waraibu wote ambao walikubwa na matatizo hayo. Yapi ambayo ni mpango wetu?

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ambalo tumelifanya Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia mamlaka ni kufungua kituo kikubwa cha tiba hapa Dodoma katika eneo la Itega ili warahibu wote ambao wataonekena wanahitaji matunzo ya ziada kupitia nchi nzima waweze kufanikiwa hapo, lakini kupitia madirisha ya hospitali zetu za rufaa katika maeneo mbalimbali kwenye mikoa, madirisha ambayo yanahudumia wagonjwa wa matatizo ya akili yatatumika pia kutoa tiba ya methadon ili kuwahudumia warahibu wote ambao watapatikana kwenye mikoa mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la tatu tumegundua warahibu wakitoka kwenye urahibu wanatakiwa wapatiwe shughuli mbalimbali za kufanya ili wasahau shughuli ile ya utumiaji wa dawa za kulevya, lakini waende katika shughuli ambazo zitawaongezea kipato. Ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu tunayo programu ya kukuza ujuzi, sasa tunataka kuwachukua na warahibu wote waliotengemaa tuwafundishe ujuzi, waweze kujiajiri, waondokane na matumizi ya dawa za kulevya, wawe raia wema na wachangie uchumi na maendeleo ya Taifa lao na maendeleo yao wao wenyewe. Kwa hiyo, nalishukuru sana Bunge na Watanzania wote kwa kazi nzuri ya kupambana na dawa za klulevya nchini. (Makofi)
MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka pia kujua, kwa kuwa nchi yetu tuna watumishi wa umma na watumishi katika sekta binafsi na siku zote tumekuwa tukihamasisha PPP, Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba kama kuna hilo tatizo waajiri wawasiliane na Katibu Mkuu Utumishi.

Je, wale wafanyakazi au watumishi wanawake wenye matatizo hayohayo lakini wanafanya kwenye sekta binafsi, wao watasaidiwaje kwa sababu nchi ni moja? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwanza, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa niaba ya Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma kwa majibu mazuri aliyoyatoa.

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2004, kifungu cha 33 kimeweka masharti ya kuhakikisha kwamba huduma bora kwa akina mama wote wajawazito, wanaojifungua na wanaume kwa maana ya waume wa akina mama hao kwenye private sector na wao wanapewa haki sawa na stahili katika kuhakikisha kwamba suala la uzazi linapewa kipaumbele pia kwa watumishi wa sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa wito kwa waajiri wote nchini kuhakikisha wanatekeleza matakwa hayo ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Na. 6 ya mwaka 2014 na hivyo kuwafanya wanawake wote wa Tanzania waweze kuthaminiwa katika suala hili muhimu sana la kukuza uhai katika dunia hii. Ahsante.
MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, watu wenye ulemavu hasa wanaoishi vijijini hata hizo fursa ni vigumu sana kuzipata. Naomba kujua mkakati wa Serikali hasa kwa walengwa wenye ulemavu kule vijijini ambako hawajui hata wapi pa kwenda ili basi hizi huduma zinazotolewa na wao waweze kupata? Mkakati rasmi ndiyo ninaoutaka.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya, kwa majibu ya kimsingi kabisa ambayo yanaonesha ni kwa namna gani Serikali imejikita kuwahudumia watu wenye ulemavu na kuhakikisha afya zao zinakuwa bora, tunaishukuru sana Serikali lakini hasa Wizara ya Afya.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la pili la uwezeshaji wananchi kiuchumi Ofisi ya Waziri Mkuu imepewa dhamana ya kuhakikisha kwamba masuala yote ya uwezeshaji wananchi kiuchumi yanakuwa inclusive, yanawagusa pia wenye ulemavu wote nchini. La kwanza ni hilo ya Mifuko hiyo ya Vijana, Wanawake na Wenye Ulemavu, lakini tunazo program za mkakati wa kukuza ujuzi katika nchi ya Tanzania. Program hizo ziko tano na zimeanza kutekelezwa.

Naomba nimthibitishie Mheshimiwa Amina Mollel chini ya ushauri wa Naibu Waziri anayehudumu kwenye eneo la wenye ulemavu, dada yangu Ikupa na Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ujumla program zote ambazo zitakwenda kutekelezwa mpaka vijijini za kuwawezesha wananchi kiuchumi, tunasimamia kuhakikisha na wenye ulemavu wanakuwa ni part ya program hizo. Jambo hili limeweza kuanza kuonekana kwa mfano, sasa hivi tuna program maalum ya green house tumeamua na wenye ulemavu wanakuwa ni sehemu ya matunda hayo ya uwezeshaji wananchi kiuchumi katika Taifa letu.
MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibuyake, lakini niseme tu kwamba mpaka sasa vyuo vikuu vina shida sana ya wahadhili na mfumo huo unachukua muda mrefu mno, yaani mtu anaomba kibali inachukua miezi sita na zaidi.

Ni lini watarekebisha na kuona kwamba huo mfumo unakuwa mwepesi ili tupate wahadhili wa kutosha katika vyuo vikuu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nimpongeze sana Dkt. Thea Ntara ni mwakilishi wa vyuo vikuu hapa ndani ya Bunge na kwa kweli anaitendea haki sana nafasi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tulitambua kwamba mifumo ambayo tulikuwa nayo nyuma ndiyo iliyokuwa ikileta matatizo na kusababisha ucheleweshaji mkubwa sana wa upataji wa vibali vya wageni. Mfumo ambao ninauzungumza ambao upo kwenye piloting kwa sasa ni mfumo mpya na tulipoanza kufanya majaribio kibali kina uwezo wa kutoka ndani ya siku moja ama siku mbili.

Naomba tu Mheshimiwa Mbunge awe na amani, tutausimamia vizuri mfumo hu una kuondoa tatizo la upatikanaji wa vibali kwa maprofesa, wahadhili, lakini na wageni wote wanaotaka kupata vibali hapa nchini. (Makofi)
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, katika siku za hivi karibuni tumeshuhudia kuona wasomi, wahadhiri, maprofesa wakiondoka katika taasisi za kufundisha na kuingia katika utumishi mwingine tofauti.

Je, upi umekuwa mkakati wa Serikali kama succession plan kwamba ikimuondoa profesa fulani mwenye uzoefu fulani katika chuo anaweza kuwa replaced ili kuondoa lile pengo ambalo linakuwa linajitokeza?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, ndani ya Serikali na hasa kupitia Sheria za Utumishi wa Umma ipo mipango ya succession plan kuhakikisha kwamba ikama za utumishi wa umma zinazingatia mahitaji tuliyonayo nchini.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi, tutaendelea kusimamia mifumo tuliyoiweka ya kuzingatia na kulinda ikama ya utumishi wa umma nchini ili kuhakikisha kwamba mapungufu hayapatikani pale ambapo wataalam wanahamia katika masuala mengine ya kiutendaji. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, suala la barabara hii ya Kusini liko serious kuliko namna ambavyo Serikali wanafanya kulijibu hapa na niwasihi sana Serikali hayo majibu mnayoyatoa hapa si sawa; ni kuwakejeli wananchi wa Kusini. Hii barabara imeharibika sana, kuna fedha mnapeleka kwa kweli ni uhujumu wa uchumi wa watu wa Kusini. Mtakumbuka mpaka ilifikia wakati Rais Magufuli akaja akafukuza watu yaani mpaka Rais anakuja anapita anaona ubovu anafukuza watu.

Mheshimiwa Spika, kinachoendelea kwenye ukarabati ni kuongeza ubovu ndani ya ubovu yaani kwa kweli Kusini kwa sasa kumefungika.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ni kwamba ni lini Serikali watakuwa serious waache kutumia rasilimali za nchi hii kuharibu zaidi ile barabara badala yake waende kufanya jambo la kuonyesha wako serious na kukarabati hii barabara badala ya majibu haya mnayotoa? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nimesikiliza sana, sana hoja zilizojengwa na Wabunge na hasa katika eneo la Ujenzi wa barabara hii inayokwenda huko Kusini (Mtwara - Lindi) na inafika mpaka huko kwenye Mkoa wa Ruvuma kwa jiografia yake.

Mheshimiwa Spika, na ninaendelea kukumbuka na kurejea maelezo ya Serikali na hasa viongozi wa juu ambavyo walikuwa na concern kubwa na barabara hiyo na hiki ambacho Waheshimiwa Wabunge wanakieleza kwa sasa ndani ya Bunge lako tukufu, ninaomba sana jambo hili tulichukue turudi ndani ya Serikali, tukafanye majadiliano na kwenda kufanya tathmini ya kina ya kujua nini kinachofanyika na hii itatusaidia kuokoa fedha za wananchi wa Tanzania walipa kodi katika kutekeleza miradi ambayo hailingani na thamani ya fedha na uhalisia unaotakiwa katika eneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hapa hatuwezi kupata nafasi ya kufanya haya majadiliano ya kina na kutoa tathimini ya uhakika naomba uridhie tulichukue Serikali na tukalifanyie kazi. (Makofi)
MHE. NAPE M. NNAUYE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, suala la barabara hii ya Kusini liko serious kuliko namna ambavyo Serikali wanafanya kulijibu hapa na niwasihi sana Serikali hayo majibu mnayoyatoa hapa si sawa; ni kuwakejeli wananchi wa Kusini. Hii barabara imeharibika sana, kuna fedha mnapeleka kwa kweli ni uhujumu wa uchumi wa watu wa Kusini. Mtakumbuka mpaka ilifikia wakati Rais Magufuli akaja akafukuza watu yaani mpaka Rais anakuja anapita anaona ubovu anafukuza watu.

Mheshimiwa Spika, kinachoendelea kwenye ukarabati ni kuongeza ubovu ndani ya ubovu yaani kwa kweli Kusini kwa sasa kumefungika.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ni kwamba ni lini Serikali watakuwa serious waache kutumia rasilimali za nchi hii kuharibu zaidi ile barabara badala yake waende kufanya jambo la kuonyesha wako serious na kukarabati hii barabara badala ya majibu haya mnayotoa? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE KAZI, AJIRA, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, nimesikiliza sana, sana hoja zilizojengwa na Wabunge na hasa katika eneo la Ujenzi wa barabara hii inayokwenda huko Kusini (Mtwara - Lindi) na inafika mpaka huko kwenye Mkoa wa Ruvuma kwa jiografia yake.

Mheshimiwa Spika, na ninaendelea kukumbuka na kurejea maelezo ya Serikali na hasa viongozi wa juu ambavyo walikuwa na concern kubwa na barabara hiyo na hiki ambacho Waheshimiwa Wabunge wanakieleza kwa sasa ndani ya Bunge lako tukufu, ninaomba sana jambo hili tulichukue turudi ndani ya Serikali, tukafanye majadiliano na kwenda kufanya tathmini ya kina ya kujua nini kinachofanyika na hii itatusaidia kuokoa fedha za wananchi wa Tanzania walipa kodi katika kutekeleza miradi ambayo hailingani na thamani ya fedha na uhalisia unaotakiwa katika eneo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa hapa hatuwezi kupata nafasi ya kufanya haya majadiliano ya kina na kutoa tathimini ya uhakika naomba uridhie tulichukue Serikali na tukalifanyie kazi. (Makofi)
MHE. MOHAMED SULEIMAN OMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri, ningeomba tu niwe na swali moja tu la nyongeza kwa sababu majibu yake kwa kweli yamekamilika lakini ninalo swali moja tu la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, nimepata malalamiko kutoka kwa wananchi wanapokwenda kutoa mashirikiano kwenye kitengo hiki cha madawa ya kulevya kwa kuwataja wanaohusika, baadhi ya maofisa hutoa taarifa zao za siri na kuwafikia wenyewe. Je, ni hatua gani mtakazozichukua endapo mtawabaini maofisa hawa ambao sio waaminifu ili wananchi warejeshe imani ya kwenda kusaidia Serikali? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika,
kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, najua ni miongoni mwa Wabunge ambao wamekuwa mstari wa mbele kushughulikia tatizo hili la dawa za kulevya nchini na hasa kwa pande zote mbili za muungano, nakushukuru na nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko ya uongozi wa Mamlaka na kama mlivyoshuhudia kilogramu takribani kama 895 kwa mara ya kwanza mzigo mkubwa umekamatwa mwaka huu kwenye Pwani ya Mkoa wa Mtwara ambayo ilikuwa inatoka Mashariki ya Mbali huko kwa hiyo ninawapongeza wote na Rais wetu tunampongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa tumekuwa na tatizo kubwa, baadhi ya watendaji na maafisa ndani ya Mamlaka lakini na vyombo vingine wamekuwa wakitoa siri, sio za watoa habari tu, hata siri ya mipango na mikakati ya kwenda kudhibiti na kuzuia matumizi na biashara hii na matumizi ya dawa za kulevya. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge mara zote tunapowabaini tumekuwa tukichukua hatua kali na wakati mwingine kuwafungulia mashtaka na kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili waweze kuondoa kabisa tatizo hilo la ufichaji wa mianya ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini.

Mheshimiwa Spika, niendelee kutoa onyo kwa watendaji wote wa Mamlaka na watendaji wengine wote kutokuthubutu kabisa kuwa ni sehemu ya biashara hiyo haramu ya dawa za kulevya nchini kwa ustawi wa vijana wetu na Taifa letu kwa ujumla. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami nitakuwa na maswali mawili ya nyongeza kwanza kwa takwimu tu za Serikali inaonyesha ni kwa jinsi gani ukatili dhidi ya watoto ni mkubwa sana kwenye nchi yetu ya Tanzania ambayo inaenda kinyume na mkataba wa kimataifa ambao tumeingia wa haki za watoto.

Mheshimiwa Spika, takwimu ambayo Serikali imetoa ni za kuanzia januari tu mpaka Septemba, 2021. Sasa asikwambie mtu kama angetoa uanzia za miaka mitatu au minne nyuma inamaana ni janga kubwa sana na hii inaonyesha dhahiri kwamba kuna changamoto ya uratibu ya takwimu maana hapo umetoa sources moja tu kutoka polisi wakati najua kuna sehemu kama Kamati MTAKUWWA, ukienda kwenye ustawi wa jamii, ukienda kwenye mashirika ya siyo ya Kiserikali lakini hata zile familia ambazo zinamalizana juu kwa juu ukikusanya haya matukio mengi takwimu ni kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ninataka kujua ni utaratibu gani Serikali imeuweka ya kuhakikisha kwamba inatoa takwimu halisia na kwa wakati kutoka kwenye vyanzo vyote hivi ili kuweza kuwasaidia watoto wa Kitanzani kujua ukubwa wa tatizo ni nini kuliko ku-base kwenye polisi tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kumekuwepo na kusua kusua kutokutenga au tukitenga kupeleka fedha kwenye utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA). (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilataka kujua ni nini mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba wanatenga bajeti ya kutosha na wanaitekeleza kuhakikisha kwamba kuna kuwa na madawati ya kijinsia ya kutosha kuanzia ngazi ya mitaa, wanawawezesha kuwa na Maafisa Ustawi wa Jamii, Kamati ya MTAKUWWA inapata fedha za kutosha ili kutokomeza hii tatizo kubwa la unyanyasaji wa watoto wa Kitanzania ambao wanabakwa, wanalawitiwa, wanauwawa, wanachomwa moto, ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika,
nimpongeze kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri na ninadhani liko suala linalohusu takwimu za unyanyasaji ataendelea kuzijibia.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ninaomba tu nitoe maelezo mafupi kuhusu mkakati huu wa kitaifa wa mapambano dhidi ya unyanyasaji kwa wanawake na watoto kwa sababu Ofisi ya Waziri Mkuu imepewa jukumu la kuratibu na kuziunganisha sekta na utekelezaji wake ukifanywa na Wizara yenye dhamana ya Afya Maendeleo ya Jamii, Wazee, Wanawake na Watoto.

Mheshimiwa Spika, ni kweli tumekuwa na mkakati wa kwanza ambao ulizinduliwa mwaka 2016 mkakati huo wa MTAKUWA na lengo kubwa ilikuwa ni kukidhi matakwa ya kimataifa lakini matakwa ya Taifa vile vile kuhakikisha kwamba tunaweka sawa masuala haya ya unyanyasaji wa wanawake na Watoto na mkakati huo wa kwanza ndiyo unafikia mwisho, unaelekea kufikia mwisho mwaka 2021/2022 tutakuwa tumeumaliza.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni hivi majuzi tu, wiki mbili zilizopita, nilikuwa kwenye kikao cha wataalam kufanya tathmini ni kwa kiasi gani MTAKUWWA I imeweza kufanikiwa. Masuala yaliyoelezwa na Mheshimiwa Mbunge tumeyaona kwamba ni masuala ambayo yameleta utatanishi kidogo kwa namna moja ama nyingine katika utekelezaji wa MTAKUWWA.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo namhakikishia kwamba kwenye mkakati wa pili sasa masuala ya bajeti, masuala ya madawati na ya rasilimali watu katika kuhakikisha MTAKUWWA II inafanikiwa na inafikia malengo ambayo yalikusudiwa yanazingatiwa sasa katika mkakati huu uliopita ambao unafanyiwa tathmini, lakini mkakati utakaokuja haya yote yatazingatiwa.

Mheshimiwa Spika, naomba niwape pongezi sana wenzetu wa Jeshi la Polisi. Wameanzisha madawati mengi ya kutosha katika maeneo mbalimbali kwenye vituo vyao vya polisi kwa ajili ya kusaidia kuhakikisha wanawake na watoto wanapata haki zao. Hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa MTAKUWWA kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tutakuja muda ukifika tutaomba ushauri, maoni na hata kwa Waheshimiwa Wabunge ili MTAKUWWA II uweze kufanikiwa kwa kadri ya mpango tuliokusudia kuwaokoa wanawake na watoto dhidi ya unyanyasaji katika nchi yetu. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, changamoto ya ajira kwa wahitimu wa Vyuo Vikuu wa sekta ya kilimo, zipo pia changamoto zingine kwa sekta mbalimbali. Tumeona kuna changamoto ya wahitimu wa Vyuo Vikuu kwa ajira za Ualimu;

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba hawa Wahitimu wa Vyuo Vikuu wa sekta ya elimu wanapata nafasi za kuajiriwa kwa sababu tumeona wananchi wanachangishwa kwa ajili ya kuweka Walimu katika sehemu mbalimbali, Walimu wa kati wapo wahitimu wengi wamekaa idle? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri ya awali.

Mheshimiwa Spika, maelezo yanayotoka katika Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Serikali inatambua mahitaji ya Watumishi katika sekta mbalimbali nchini. Naomba niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Mheshimiwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Sita toka alipoingia madarakani aligundua mahitaji ya ajira mpya kwa ajili ya sekta mbalimbali na hivyo mara moja alifanya maamuzi ya kuanza kutoa ajira mpya na mpaka sasa kwa takwimu za mpaka mwezi Januari mwaka 2022 tayari tumekwishaajiri watumishi wapya 11,901 ambao wameshaingia katika sekta mbalimbali mtambuka.

Mheshimiwa Spika, tunajua kwamba ajira hizo 11,901 ni kati ya ajira 40,000 ambazo zilikuwa zimeahidiwa na Mheshimiwa Rais. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge tunaendelea kufanya mazungumzo kuangalia Ikama, kuangalia jinsi fedha za ajira ambazo zimeweza kutengwa kwenye Wizara ya Fedha na kama tutakuwa kwenye position nzuri kabla ya kumaliza mwaka huu wa fedha tunataka kuhakikisha kwamba tunaongeza ajira nyingine mpya ili kukidhi mahitaji ya Watumishi katika sekta mbalimbali nchini. (Makofi)
MHE. ZAYTUN S. SWAI: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kuniona. Naomba kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sababu kubwa ya matokeo mabaya kwa wanafunzi wetu hususan kwa masomo ya hisabati na sayansi yanachangiwa kwa kiasi kikubwa kutokana na uhaba wa Walimu wa Kada hizo. Je, Serikali ina mpango gani wa kuajiri na kuongeza ajira hususan kwa Walimu wanaofundisha masomo ya sayansi na hisabati. Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, tunaendelea kupitia Ikama ya mahitaji ya Walimu na hasa kwenye sekta ya sayansi ili kukidhi mahitaji katika shule zetu.

Mheshimiwa Spika, tumeshafanya mazungumzo na Ofisi ya Rais TAMISEMI ili waweze kutuletea mahitaji na tukishayapata tutapitia tena mahitaji hayo tukilinganisha na bajeti tuliyonayo pia umuhimu wa Walimu hawa wa sayansi.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo tutalipa kipaumbele, ukizingatia kwamba kwenye kampeni ya Mheshimiwa Rais ya UVIKO tumejenga madarasa mengi, tumejenga vituo vya afya, tumejenga zahanati, kwa hiyo mahitaji haya yote ni muhimu. Na ninaomba niwahakikishie ni dhamira ya Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan kuondoa tatizo la Watumishi katika kuhudumia Watanzania na umma mzima wa wananchi wa Tanzania.
MHE. YUSTINA A. RAHHI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pia kuna kada kama za Maafisa Ugani wa Mifugo hawajaajiriwa kwa muda mrefu: -

Je, Serikali katika mwaka huu fedha itatoa ajira hiyo? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, naomba kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge, kama nilivyosema toka mwanzo, tunaendelea kuangalia ikama ya Utumishi kwa kuzingatia misingi ya ugawaji wa watumishi katika sekta zote ili kuondoa uhaba wa watumishi nchini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa sasa tunachokifanya, tunaendelea kupokea maombi kwa Mawaziri, kwenye sekta zao na kwa kuangalia ni kwa namna gani upungufu na uhitaji uliopo kwa zile nafasi ambazo tumeshazigawa. Kwa zile ambazo hatujazigawa mpaka sasa, hao watumishi 7,792 niliowasema, tutaendelea kuzingatia mahitaji ya watumishi nchini na kuhakikisha kwamba utendaji wa kazi Serikali kwa kupitia Utumishi wa Umma unaendelea kuwa na usawa kwa kuzingatia mahitaji halisi. (Makofi)
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Suala la Katiba Mpya ni kilio cha muda mrefu sana kwa Watanzania wote, tukiondolewa sisi wanasiasa. Ni lini Serikali italeta Sheria ya Vyama vya Siasa kuhakikisha hii Katiba Mpya tunapokwenda kwenye hilo tamko ambalo Rais ameliridhia, ataenda kulizungumzia na Watanzania wakafahamu, ni lini tunaanza na tutatumia mbinu gani na mipango gani ambayo Serikali imejipanga kuhakikisha Katiba hii inakuwa ya wananchi jumuishi na maoni yanachukuliwa kwa ujumla wake? Tunaomba commitment ya Serikali iseme itaanza lini na itatumia mbinu gani kuhakikisha Katiba hii inaenda kusimama upya tena?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuungana na Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote ambao wamempongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Muungano wa Tanzania kwa kukubali sasa mapendekezo ya kikosi cha Baraza la Vyama vya Siasa na wadau wengine kuhakikisha tunaanza mchakato wa Katiba Mpya, ikiwa ni pamoja na kuhuisha na kutungwa kwa sheria zinazohusu uchaguzi hapa nchini Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba, kwa kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais, tayari Baraza la Vyama vya Siasa linashirikiana na wadau mbalimbali na limeshaweka mpango kazi kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, lakini na ofisi nyingine zinazohusika ili kuhakikisha kabla mwaka huu wa 2023 sheria zote zinazohusu uchaguzi Bunge lako tukufu lipate nafasi ya kuzipitia, kuzitunga na kuzifanyia marekebisho kama itabidi kufanya hivyo. Kwa hiyo, naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Serikali imezingatia sana maoni hayo na tayari tumeshajipanga kwa utekelezaji wa mabadiliko ya sheria hizo. (Makofi)
MHE. KHADIJA S. TAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa watu wengi hawafahamu uwepo wa Sheria ya Manunuzi ya asilimia 30 kwa makundi maalum. Sasa je, Serikali ina mkakati gani kueneza uelewa juu ya uwepo wa sheria hii ya asilimia 30 ya manunuzi kwa makundi maalum ambayo ni wanawake, vijana na watu wenye ulemavu? Ahsante.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, labda kwa kuwa linakwenda kwenye sekta zote ninaomba tu niseme kwamba kwa sababu Serikali inafahamu umuhimu wa makundi hayo tutajipanga ndani ya Serikali ili sekta zote zihakikishe zinasimamia jambo hili na makundi hayo maalum ambayo yamekwisha kutamkwa kwenye sheria hiyo waweze kunufaika. Hiyo ni fursa muhimu sana kwa maendeleo na ustawi wa Taifa. (Makofi)

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, kitu pekee cha kuwatoa wanawake wa Tanzania waendelee haraka, ni mifugo midogomidogo ikiwemo kuku, mbuzi na ng’ombe. Wanawake wa Kilimanjaro wanasubiri sana msaada huo kutoka Serikalini.
Je, ni lini sasa ile mitamba niliyoahidiwa hapa Bungeni itatolewa? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, wakati tunasoma Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2023/2024, Wizara ya Mifugo ilitoa maelezo ya namna gani tunakwenda kuboresha sekta ya mifugo kwa ujumla. Kwa hiyo, kwa sababu Mheshimiwa Shally ameuliza swali hili ambalo ni specific kwenye eneo hilo la mitamba, tunaomba tulichukue na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo atapatiwa taarifa hii na atampatia majibu Mheshimiwa Shally Raymond. (makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, ahsante sana kwa majibu yako kwa maswali ya Waheshimiwa Wabunge. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wa Nchi, majibu yatatolewa kwa Mheshimiwa Shally bila kuwa swali la msingi kama nimekuelewa vizuri. Mtampelekea wenyewe majibu?

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, ndiyo kwa sababu hapa limeletwa kama swali la nyongeza na siyo swali la msingi.

SPIKA: Ni sawa. Mimi naweza kuagiza mambo mawili, moja, ninyi mumpelekee ama lije kama swali la msingi. Kwa hiyo kwa maelezo yako kama nimekuelewa vizuri ni kwamba badala ya kuja kama swali la msingi, ninyi Serikali mtampelekea majibu Mheshimiwa Shally Raymond.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, tuko tayari kupata Mwongozo wa Kiti chako.

SPIKA: Sawa. Mpelekeeni majibu, kama hakuyapata atauliza tena.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)