Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Leonidas Tutubert Gama (11 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua nafasi hii na kwa sababu nasema kwa mara ya kwanza, nawashukuru sana wananchi wangu wa Songea Mjini kwa ushindi mkubwa walionipatia. Ninachotaka kuwahakikishia ni kwamba, nimekuja kama Mwakilishi wao na sitawaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sikupata bahati ya kuchangia Hotuba ya Mheshimiwa Rais, lakini labda nianze na hilo kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais katika ukurasa wa 20, pamoja na hotuba nzuri sana aliyoitoa, lakini ukurasa wa 20 alikuwa amezungumzia kero kwa wananchi, hasa wafanyabiashara ndogo ndogo kuhusiana na ushuru wanaoutoa. Naungana na Mheshimiwa Rais na kwa kweli naomba wenzetu wafanye utaratibu wa kuhakikisha ushuru huu unafutwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nijue, kwa sababu ninachokumbuka, ni miaka ya nyuma hivi karibuni walifuta ushuru wa kero kwa wananchi wote kwa maana ya kwamba ushuru uliokuwa unakusanywa kwa njia ya kero ulifutwa na Serikali ilikuwa inatoa ruzuku kwenye Halmashauri za Wilaya ili kufidia ushuru huo wa kero. Sasa sielewi ule ushuru wa kero umeishia wapi. Kwa nini Halmashauri zetu zimeingia tena kuwa-charge wafanyabiashara ndogo ndogo wa mchicha, vitumbua, Mama Ntilie ambapo sasa imekuwa ni kero kubwa mno! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kitu kimoja hapa, inachekesha kweli! Ukiangalia leseni za biashara zinazotoa Sh. 70,000/= kwa mwaka, ukalinganisha na ushuru wanaotoa akinamama Nntilie, unakuta Mama Ntilie anagharamia gharama kubwa zaidi kuliko mtu anayelipa ushuru wa Sh. 70,000/=. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hesabu za haraka haraka, ni kwamba anayelipa leseni ya Sh. 70,000/= maana yake ukigawanya kwa miezi 12 na ukagawanya kwa siku 30 maana yake mfanyabiashara huyu wa duka au wa mgahawa analipa kwa siku Sh. 194/=. Wakati huyu Mama Ntilie anayelipa Sh. 400/= kama ushuru, ukifanya hesabu za siku maana yake unamkuta analipa ushuru kwa mwaka 144,000/= akimzidi mfanyabiashara wa kawaida wa duka au mgahawa.
Kwa hiyo, ni kitu kinachoshangaza sana. Ni vizuri tukiangalie vizuri; na kwa kweli kama alivyosema Mheshimiwa Rais, nadhani umefika wakati sasa tuwafutie ushuru huu ili wananchi wafanye biashara zao vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mpango, kwanza nami naungana na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. Mpango kwa kazi nzuri aliyoifanya. Mpango huu umezungumzia sana mahusiano ya kibiashara, ya kiuchumi kati ya Tanzania na nchi jirani, lakini katika Mpango ule umezungumzia sana mipaka ya Kenya, mipaka ya Uganda na mipaka ya nchi nyingine. Haujazungumzia kabisa mpaka wa Kusini mwa Tanzania, Mkoa wa Ruvuma ukihusika na hasa kwa nchi ya Msumbiji na nchi ya Malawi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mpango huu utambue kuwapo kwa barabara inayounganisha Tanzania na Msumbiji, kupitia Songea Mjini kwenye eneo la Likuyufusi kwenda kwenye eneo la Mkenda, Kaskazini ya Msumbiji. Barabara hii haijaingizwa na wala haijazungumzwa. Ni vizuri iingizwe na izungumzwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile upanuzi wa uwanja wa ndege wa Songea Mjini ambao ungeweza kusaidia sana suala la wafanyabiashara na wananchi kutoka nchi jirani wanaopenda kutembelea Tanzania, hasa kutoka Msumbiji na Malawi, kuweza kutumia ndege zitakazotoka Songea kwenda Dar es Salaam kufanya shughuli mbalimbali za kibiashara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru vilevile kwa kazi nzuri ya Serikali inayofanywa hasa ya kutengeneza barabara ya kutoka Mtwara kwenda Mbambabay. Barabara hii bado kuna maeneo mawili haijakamilika na wala haijashughulikiwa. Ukitoka Namtumbo kwenda Tunduru kuna Makandarasi wanashughulikia, lakini kati ya Luhira na Ruhuiko, Mjini Songea, wananchi wamewekewa „X,’ wamefanyiwa tathmini, lakini mpaka sasa hawajalipwa fidia zao na kwa hiyo, wanaishi katika maisha ya kutokuwa na uhakika watahama lini. Kwa hiyo, naomba Serikali ifanye utaratibu wa haraka ili watu wanaostahili kulipwa fidia katika eneo hilo waweze kulipwa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile bado kuna kipande kimoja hakijajengwa kati ya Mbinga na Mbambabay. Naomba Serikali ione namna ya kufanya katika hiyo sehemu ili kuhakikisha inatengenezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona kuna mwenzetu mmoja amezungumza habari ya reli; nashukuru kwa mpango kabambe wa Serikali wa kujenga reli ya kati kwa kiwango cha Standard gauge, lakini vilevile kwa mpango kabambe ambao upo katika Kitabu chetu cha Mwelekeo wa Uchumi kuhusu barabara ya Mtwara – Mbambabay.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba basi, Serikali ione namna ya kufanya utaratibu wa kuhakikisha reli hii inajengwa ili kuweza kuimarisha uchumi katika Mikoa ya Kusini, hasa kutokea kule Mbambabay. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala lingine. Kwa muda mrefu sana wananchi wa Mkoa wa Ruvuma na Songea kwa ujumla tumekuwa tukiahidiwa kupatiwa umeme wa Grid ya Taifa kutoka Makambako kuja Songea, lakini sasa kila mwaka linazungumzwa hili suala, lakini bado halijapatiwa ufumbuzi.
Kwa hiyo, naiomba Serikali ifanye utaratibu na itupe uhakika hili suala la umeme kati ya Makambako na Songea litakamilika lini na kwa hiyo, lini utaanza utekelezaji wa suala hilo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho, naomba nizungumzie juu ya suala la EPZA. Katika Taarifa ya Mheshimiwa Dkt. Mpango, amezungumzia EPZA katika maeneo mengi sana, lakini Jimboni kwangu Songea kuna wananchi katika maeneo ya Mwenge Mshindo, Luhila Kati, Kilagano, Ruawasi na Ruhuiko, hawa watu wamechukuliwa maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa ni zaidi ya 2,200 na wamechukuliwa ekari zaidi ya 5,000 kwa ajili ya kuweka EPZA, lakini nasikitika kwamba mpaka sasa watu waliolipwa ni wachache sana, hata kiwango cha fedha walicholipwa ni mwaka 2008. Wamelipa 2015, kiwango kile hakilingani na hali halisi ya sasa na vilevile wanatakiwa kuhama kwenye maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo inasababisha kero kwa wananchi wangu na vilevile kuhakikisha kuendeleza umaskini, kwa sababu hawawezi kujiendeleza kiuchumi, hawawezi kujenga nyumba, lakini hawana mahali pa kwenda palipoandaliwa na Serikali na pesa waliyopata haiwawezeshi kuweza kwenda kuweka makazi katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwa kutumia nafasi hii naiomba sana Serikali, hebu imalize tatizo hili la wananchi hao niliowataja katika eneo la Mwenge Mshindo ili tuweze kupata maendeleo, wananchi waweze kujiendeleza wakiwa na uhakika wanakwenda wapi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii niseme, kwa jinsi taarifa ilivyoandaliwa na kama tutazingatia haya ambayo tumeyaomba Waheshimiwa Wabunge, basi nachukua nafasi hii kuunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu kumpongeza sana Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri sana aliyoianza ambayo imetupa matumaini Watanzania wote ya kuona kwamba sasa tunakwenda kule tunakokuhitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa maelezo yake mazuri sana. Sisi sote tuna imani mno na yeye binafsi na tuna imani sana na timu yake ya Mawaziri ambao nashukuru wote wanakwenda kwa kasi ile aliyoanza nayo Mheshimiwa Rais. Tunaomba basi Mheshimiwa Waziri Mkuu kama ulivyoanza uendelee hivyo kuhakikisha unasimamia yale yote ambayo umewasilisha katika Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, nina maeneo machache ya kushauri. Eneo la kwanza, naomba nishauri juu ya wastaafu. Kwenye Majimbo yetu tuna wastaafu wengi sana. Mimi kuanzia nilipochaguliwa kuwa Mbunge moja kati ya watu wengi sana waliokuja kwa malalamiko mbalimbali ni wale ambao wamestaafu kutoka maeneo mbalimbali kwenye taasisi za umma na binafsi. Imeonekana dhahiri kwamba wastaafu wengi wanachelewa kupata malipo yao au wengine wanalipwa malipo kwa kupunjwa au wengine hawapati kabisa malipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ifanye zoezi la makusudi la kuwatambua wastaafu wote na jinsi walivyoshughulikiwa na taasisi zao ili tuweze kuona namna ya kupunguza na kuiondoa kero hii na matatizo ya wastaafu. Wastaafu hawa wamefanya kazi kubwa sana ya kutumikia nchi hii, kwa hiyo, wanapoteseka maana yake hatuwatendei haki. Ni imani yangu tukifanya zoezi la kuwatambua wote na maeneo ambayo wamestaafu na kile wanachokidai itakuwa rahisi zaidi kutoa maelekezo na miongozo ili kuhakikisha wastaafu wote wanapata haki zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Ilani yetu ya Uchaguzi ya CCM ilivyosema, tunao wastaafu kutoka kwenye taasisi mbalimbali za umma, lakini vile vile tunao wazee ambao hawakuwa watumishi katika maeneo mbalimbali, nafikiri sasa ni muda muafaka wa Serikali kujenga utaratibu wa namna ya kuwalipa pensheni wazee wote, kwa wale ambao walikuwa watumishi wa umma na wale ambao wamezeeka wakiwa wanafanya kazi za kujenga nchi yetu hasa kwenye eneo la kilimo na mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunafahamu kwamba wazee hawa waliokuwa wanafanya kazi kwenye taasisi za umma na wale waliokuwa wanafanya kazi za kujenga nchi kwa kutumia sekta binafsi, wote wamesaidia sana kuichangia nchi hii kufika hapa tulipofika. Kwa hiyo, kama ilivyosema Ilani yetu ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ni vizuri ukatayarishwa utaratibu ili pensheni iwe kwa wazee wote waliostaafu kwenye mashirika ya umma na wale waliostaafu kwenye shughuli binafsi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia maeneo mengi ya wastaafu ni zile taasisi au Mifuko ya Jamii ndiyo wengi wanatoka huko. Ukienda kwenye historia ya Mifuko ya Jamii unakuta tuna Mifuko ya amii mingi sana kiasi kwamba hata watumishi wamekuwa wanayumba, wengine hawajui waende Mfuko gani, wengine wanakwenda kwenye Mifuko kwa sababu ya kushawishiwa bila kuijua vizuri Mifuko hiyo na kuna utitiri wa Mifuko ya Jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri hebu tuangalie uwezekano wa kuwa na Mifuko ya Jamii michache ambayo inaweza kuwafanya wafanyakazi na vikundi mbalimbali vikajiunga na Mifuko michache na tukaweza kuisimamia vizuri zaidi. Nashauri tuwe na Mifuko ya Jamii katika sekta kama nne hivi. Tunaweza kuwa na Mfuko wa Jamii kwa ajili kuhudumia sekta binafsi, tunaweza kuwa na Mfuko wa Jamii kuhudumia sekta ya umma, tunaweza kuwa na Mfuko wa Jamii kuhudumia sekta ya afya na tunaweza kuwa na Mfuko wa Jamii kwa ajili ya kuhudumia sekta ya kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ifanye kazi ya ziada ili kutoa elimu ya kuhakikisha kwamba watu wote wanaelewa na wanajiunga na Mifuko hii ya Jamii kwa maana ya watu katika makundi yao. Kuna akinamama lishe au mama ntilie, bodaboda, wafanyabiashara ndogondogo, wakijiunga na Mifuko hii itasaidia sana kuweza kujiwekea akiba ya uhakika wa maisha yao baada ya kufikia umri wa utu uzima. Tunajua tatizo la ajira lilivyo pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali bado vikundi vya wajasiriamali ni sehemu moja muhimu sana ya ajira binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba tuna Baraza la Taifa la Uwezeshaji, Baraza hili lingeweza kabisa kuona namna gani tunaweza kuwezesha vikundi hivi vya akinamama wajasiriamali, vijana wajasiriamali na bodaboda, tuone namna gani Mfuko huu au Baraza hili linaweza kujikita katika suala hili kuona namna gani tunawasaidia ili kuondoka kwenye umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali kuwa na maamuzi thabiti. Hivi sasa wote tunajua vijana wa bodaboda au vijana kwa ujumla. Kulikuwa na kundi kubwa sana ambalo lilikuwa halina mwelekeo. Katika Bunge hilihili kipindi kilichopita tumeruhusu kuanzisha usafiri wa bodaboda. Usafiri wa bodaboda ndiyo msaada mkubwa sana kwa shughuli mbalimbali za kimaendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na watu wa bodaboda kusaidia sana kupunguza kundi kubwa la wazururaji lakini mpaka sasa haieleweki, hivi tuna tatizo la kutokuwataka bodaboda? Maana kila ukisikia habari unasikia Dar-es-Salaam wamekamatwa, pikipiki 100 zimekamatwa, Songea wamekamatwa wako Polisi, mahali fulani wamekamatwa. Kwa nini hatufiki mahali tukaweka utaratibu mzuri wa kuyashughulikia matatizo katika uendeshaji wa bodaboda badala ya kuwanyanyasa hawa vijana bila kujua sababu za msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina hofu kubwa sana kwamba kama tutaendelea kuwanyanyasa hawa vijana, tunakamata pikipiki zao zinakaa Polisi, maana yake tutatengeneza kundi lingine ambalo litakuwa kundi kubwa tusiloweza kulimudu wakiingia mitaani kwa nia mbaya. Kwa hiyo, nashauri Serikali hii ijipange vizuri kuona namna gani tunashughulikia kundi hili na makundi mengine ili yaweze kujitegemea na vijana waweze kuendesha maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nataka nishauri. Tuna mahusiano mazuri sana kati ya Tanzania na nchi nyingine. Sote tunajua kwamba tuna mahusiano mazuri na jirani zetu wa Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Zambia, Msumbiji, Kongo na kadhalika. Hata hivyo, naona mwelekeo wa Serikali umebana sana Kaskazini, upande wa Kusini kasi siyo nzuri sana. Sisi tutakumbuka mahusiano yetu mazuri yalivyo kati ya sisi na ndugu zetu wa Msumbiji. Tuna mahusiano mazuri sana ya kihistoria lakini tumewasahau ndugu zetu wa Msumbiji kwa maana ya kufungua mpaka kati ya Tanzania na Msumbiji kupitia Kijiji kile cha Mkenda kule Songea.
Mheshimiwa Spika, kama tutafungua mahusiano yale tutaimarisha sana mahusiano ya kibiashara kati ya Tanzania na wenzetu wa Msumbiji kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma, lakini vilevile wananchi wetu wataweza wakafanya kazi nzuri ya biashara kati ya sisi na Msumbiji na hivyo kuinua kipato cha wananchi. Kwa hiyo, naomba Ofisi ya Waziri Mkuu ione namna gani inafanya utaratibu wa kufungua mpaka ambao upo na kuna barabara ambayo ipo lakini haishughulikiwi. Barabara ile Ikishughulikiwa inaweza kutusaidia sana katika shughuli nzima za kuongeza na kupanua uchumi wa wafanyabiashara wa eneo lile la Songea na Mkoa wa Ruvuma kwa jumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na mengine lakini naona muda wangu hauniruhusu, basi nichukue nafasi hii niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja. Niitakie Serikali yangu ya Awamu ya Tano utekelezaji mzuri wa Ilani ya CCM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi naomba nichukue nafasi hii kama walivyofanya wenzangu nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri na uwasilishaji wake mzuri. Mimi nilikuwa na tatizo moja ambalo niliomba Serikali iangalie kwa jicho la huruma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vyuo vilivyofungwa ni pamoja na chuo changu cha St. Joseph, Songea ambacho kilikuwa na maeneo mawili; eneo la kwanza ni eneo la campus ya kilimo na eneo la pili ni campus ya teknolojia. Hiki chuo kimefungwa, lakini sina tatizo na sababu za msingi ila nilichokuwa nakiona ni kwamba uamuzi huu umechukuliwa mkubwa mno, haulingani na mazingira halisi, sisi sote tunataka vijana wetu wapate elimu na kwa sisi Songea kile chuo cha St. Joseph ndio chuo kikuu pekee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo zipo sababu za msingi zilizosemwa na kubaliana nazo lakini vilevile ningeomba nishauri, kwa mfano suala la udahili wa wanafunzi ambao hawajafikia viwango, Mheshimiwa Waziri ametuambia hapa kwamba vijana 424 wamefutiwa udahili wao. Lakini hawa vijana 424 ni kati ya vijana 3,585. Ukiangalia takwimu hizi maana yake waliokiuka taratibu ni asilimia 11.8; kwa hiyo vijana asilimia 88.2 hawana tatizo lolote. Kwa hiyo, haiwezi kufika mahali hiyo ikawa moja ya sababu ya kufunga vyuo au kuvifuta vyuo. Ukiangalia sababu hizi sio sababu zinazotokana na vijana ni sababu zinazotokana na utawala wa chuo, utawala wa uongozi wa TCU na viongozi wengine wa Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo huwezi ukafika mahali makosa ya kiwizara yakaenda kutoa adhabu kwa chuo ambacho chenyewe kilikuwa haina kosa. Lakini yako matatizo ambayo yamesemwa kutokana na vyuo hivi na hasa chuo changu; matatizo ya uongozi, matatizo ya utawala na matatizo ya kitaaluma. Sitaki kubishana na Mheshimiwa Waziri ni kweli makosa hayo yanajitokeza lakini ufumbuzi wa makosa hayo sio kufuta chuo, ufumbuzi wa makosa hayo ni pale ambapo una kitaka chuo au taratibu zilizokosewa ziweze kurekebishwa. Na kama kurekebishwa hakuwezekani zipo taratibu za kudhibiti uongozi uliopo; lakini sasa ukiangalia uamuzi wetu wa kufuta hivi vyuo umekuja kuwahukumu moja kwa moja wahusika kwenye vyuo ambao ni wanafunzi wetu na utawala kwa ujumla wa chuo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie kwamba siku zote wanasema ukiwa na mtoto umemuogesha kwenye dishi (beseni), maji yakichafuka unachofanya ni kuyatupa maji, huwezi kuondoa dishi na mtoto ukaenda kuwamwaga kwa sababu maji yamechafuka, huo sio utaratibu.
Kwa hiyo, kama makosa yalifanywa na uongozi na kama makosa yalifanywa na Wizara yenyewe kwa kutumia vyombo vyake kule kilichotakiwa ni kuona namna gani tunaadhibu wale waliohusika na wala sio vijana waliokuwa wanasoma au utawala wa chuo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi taratibu zilizotumika kukifuta kile chuo maana kimefutwa, sio kimefungwa, kimefutwa usajili wake, hati yake ya kuongoza kile chuo imefutwa rasmi. Kwa hiyo, uaratibu uliotumika katika kukifuta chuo hiko haukuwa sahihi na kuna sababu kadhaa. Kwanza uamuzi wenyewe wa kukifuta chuo ni wa ghafla mno haukuwa na taarifa yoyote, notice yoyote ya kuwajulisha kwamba baada ya hapa tunafuta chuo, ni uamuzi ambao umetokana na taarifa walizozipokea, wakaamua hata uongozi umepata taarifa za kufutwa chuo kutokana na vyombo vya habari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, tumewaadhibu watu wengine ambao hawana hatia, kulikuwa na wanachuo kutoka makundi mbalimbali, tumeamua kuwahamishia vyuo vingine, lakini kuna watu walikuwa wanasoma kama part time pale anatoka kazini anakwenda kufanya masomo, kwa hiyo maana yake kumuhamishia maeneo mengine kwanza unamuingiza kwenye migogoro ya kulipa ada, vilevile unamuingiza kwenye migogoro ya kiutumishi kati yake yeye na ofisi yake.
Kwa hiyo, nilikuwa nafikiri maeneo hayo yote yangeangaliwa kabla ya kutoa uamuzi huo. Athari yake ni nini? Kwanza sisi wenyewe kama Kanda ya Kusini tumeathirika sana, tumeathirika sisi kama Mkoa wa Kusini lakini vilevile na wanafunzi hawa wameathirika sana kisaikolojia, kiuchumi na kijamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, matokeo yake huwezi ukategemea vijana hawa wanakohamishiwa wakaenda kufanya vizuri katika taratibu zao za kimasomo kwa sababu athari hiyo imekuwa kubwa sana na imewaumiza sana vijana wale. Lakini vilevile kimkoa sisi tumekosa mambo mengi sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, chuo hiki pamoja na shughuli nyingine walizokuwa wanafanya, lakini vijana hawa ndio walikuwa wakiwa kwenye field wanakwenda kwenye taasisi zetu mbalimbali za kielimu; walikuwa wanajitolea kwenye vyuo, wanajitolea kwenye shule, wanafanya tafiti mbalimbali ambazo zilisaidia kuwezesha mkoa kuinua kiuchumi.
Lakini sio hilo tu, hata hali ya kiuchumi ya wananchi katika maeneo yale ilikua kutokana na kuwepo kwa chuo hiki, wananchi wengi walifanya shughuli zao, wananchi wengi walijenga nyumba mbalimbali ambazo kuwepo kwa wanachuo hawa kulisaidia sana kuinua uchumi wa wananchi na kusababisha mzunguko wa fedha kwa jamii ya Songea Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, athari hizi zimetukuta wote, kwa hiyo tunaomba Serikali kwa sababu mmeshatoa adhabu kwa TCU, nilikuwa naiomba Serikali ione uwezekano wa kuamua kukirudisha chuo hiki cha Songea pamoja na masharti ambayo mnaona yatafaa ili waweze kuyarekebisha. Lakini kukifuta moja kwa moja naona sio sahihi na haitakuwa kuwatendea haki wanafunzi na ndugu zetu wa Songea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na tuna maswali ambayo tunajiuliza, je, kwa nini TCU iliamua kutokutoa notice kwa chuo? Lakini la pili kwa nini TCU haikutoa muda na nafasi ya chuo kufanya marekebisho yale ambayo waliyapata?
Vilevile tunajiuliza je, kwani Serikali haina namna bora nyingine ya ufungaji wa chuo lazima kukifunga chuo kwa ambush maana kimefungwa kile chuo utafikiri tupo jeshini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri tuangalie. Lakini vilevile tunajiuliza sana sisi Songea kwamba kile chuo kilichokuwa na matatizo kwa mujibu wa maelezo ya Wizara na TCU, ni kile chuo cha campus ya kilimo lakini chuo cha TEHAMA hakikukuwa na tatizo, kwa nini katika kufuta vimefutwa vyuo vyote viwili wakati campus ya TEHAMA haikuwa na matatizo.
Kwa hiyo, nilitaka niiombe Serikali yangu tukufu ione utaratibu wa kufanya ukaguzi, kutoa ushauri, kutoa maelekezo ili ifike mahali yale ya msingi yaweze kuondolewa na wakati huo huo kutoa haki kwa kile chuo kiweze kuanza tena usaili ili kuwarudisha wanafunzi katika chuo kile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya uongozi wa chuo kile na kwa niaba ya uongozi wa Songea kwa ujumla tupo tayari kupokea.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami naungana na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri na kwa mpango mzuri. Labda nianze mwanzoni tu niseme naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimefurahishwa sana na mpango mzima wa ujenzi wa viwanda kwa kuzingatia na uzalishaji na hasa dhamira ya Serikali ya kutumia viwanda kwa ajili ya kuinua kilimo. Ukiangalia kwenye mpango ni kwamba, viwanda hivi vinatazamiwa vijengwe ili kuwawezesha wakulima wazalishe zaidi na malighafi ya mkulima ndiyo itumike katika uendeshaji wa viwanda hivi. Kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii kuipongeza sana programu hiyo. Nafikiri itasaidia sana kwa wakulima wetu ambao kwa muda mrefu ama wamekuwa wakizalisha wasipate masoko au wanapozalisha, uzalishaji unapungua kwa sababu ya kukosa masoko hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa sisi Songea, Jimbo langu la Songea Mjini na Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla tunazalisha sana mahindi. Kwa takwimu za mwaka 2015 tu inaonyesha wananchi wa Mkoa wa Ruvuma walizalisha zaidi ya tani 685,000, lakini uwezo wa NFRA wa kununua mazao hayo ulikuwa ni chini ya tani 50,000. Kwa hiyo, maana yake wakulima walibakiwa na zaidi ya tani 600,000. Ukichukua tani ambazo wametumia kwa chakula, hazivuki tani 300,000 na kwa maana hiyo tani 300,000 za mahindi yao zimepotea, hazina soko. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka niungane na Serikali, niombe rasmi kwamba, Serikali ifanye juhudi za makusudi kwa wakulima kama wale kuwawekea viwanda vya usindikaji. Kwa hiyo, naomba Serikali ione umuhimu wa kuweka viwanda vya usindikaji Songea ili uzalishaji wa mazao ya mahindi uweze kupata vile vile soko la usindikaji kutokana na viwanda vitakavyowekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, usindikaji unahitaji umeme, viwanda vinahitaji umeme. Mji wetu wa Songea na Mkoa wetu wa Ruvuma kwa ujumla hauna umeme wa uhakika. Kwa hiyo, sambamba na hilo, Serikali ione umuhimu wa kuhakikisha umeme wa grid ya Taifa unafika Songea ili uweze kusaidia juhudi hizi za kuanzisha viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Songea tulikuwa na uzalishaji mkubwa sana wa zao la tumbaku. Kama ilivyo Tabora, vivyo hivyo Songea, lakini uzalishaji wa tumbaku umepungua sana hasa baada ya kiwanda pekee ambacho kilikuwa kinasindika tumbaku katika Mji wa Songea kufungwa kutokana na kuhamishwa, usindikaji kwenda Mkoani Morogoro. Kwa niaba ya wananchi wa Songea, naomba Serikali isimamie kurejesha kiwanda kile ili kuongeza uzalishaji wa tumbaku ambao umepungua sana baada ya kiwanda kile kusimama.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Songea kwa kukosa kiwanda cha tumbaku hauna kiwanda cha aina yoyote. Kwa hiyo, Songea maana yake mzunguko wa pesa ni mdogo, hali ya upatikanaji wa pesa ni mdogo, wananchi wanategemea kilimo tu na kilimo ambacho hakina viwanda vinavyoweza kusindika. Kwa hiyo, maana yake wananchi wa Songea ni wananchi maskini sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, alipofanya ziara mwezi wa 12 katika Mkoa wa Ruvuma, alipata nafasi ya kutembelea kiwanda hiki na ametoa maelekezo rasmi kwamba kiwanda kile kiangaliwe ili kiweze kufufuliwa. Naomba nichukue nafasi hii kumwomba sana Mheshimiwa Waziri anayeshughulikia Viwanda, ndugu yangu Mheshimiwa Mwijage, aone namna ya kufufua kile kiwanda ili uzalishaji wa zao la tumbaku urudi upya. Hivi sasa bado uzalishaji upo, lakini kwa kiwango kidogo sana; hasa ndugu zetu wa Namtumbo, zao kubwa la biashara walilokuwa wanategemea ni zao la tumbaku; na vile vile Songea kuna maeneo ambayo yanalima zao la tumbaku. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mwijage afanye juhudi hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba Mheshimiwa Waziri Mwijage kama kuna uwezekano aone namna ya kufuta ile kauli yake. Kuna kauli moja aliitoa hapa, nadhani tarehe 19 ile mwezi uliopita; alisema, anawaomba wananchi wa Lindi wazalishe muhogo kwa wingi, umepata soko China. Sasa kwa maelezo haya ambayo ameyatoa, tukipeleka muhogo China, maana yake tunahamisha ajira kuzipeleka China. Kwa nini tusifanye utaratibu, kama viwanda vya kuchakata muhogo vipo China, visije Tanzania vikajengwa kule Lindi au Songea ili mchakato wa usindikaji wa muhogo ufanyike Tanzania badala ya kufanyika kule China? Kwa hiyo, niseme simuungi mkono Mheshimiwa Mwijage katika hilo la kusafirisha muhogo kwenda China badala yake muhogo usindikwe hapa hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naomba sana Mheshimiwa Mwijage, tunaomba viwanda Songea, lakini viwanda hivi haviwezi kuja endapo hatutakamilisha zoezi la kukamilisha ulipaji wa fidia katika eneo la EPZA ambapo pale Songea Mjini lipo eneo la Mwenge Mshindo, eneo limeshatengwa, wananchi zaidi ya 1,015 hawajalipwa fidia zao, lakini wananchi hawa wamefanyiwa tathmini mwaka 2008, mpaka sasa ni miaka nane. Nina imani kwamba gharama walizokuwa wanadai 2008, leo zitakuwa zimepanda zaidi. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri afanye juhudi ya hali ya juu ili wananchi walipwe fidia zao ili nafasi ile ipatikane kwa ajili ya kuwekeza viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibuni wananchi wale wamefanya mikutano kule, wana wasiwasi kweli juu ya maeneo yao; wanashindwa kuyaendeleza, wanashindwa kufanya shughuli zozote za maendeleo. Juzi walikuwa wameamua kufanya maandamano ya kuja Dodoma. Nikiwa hapa Bungeni nimejulishwa hivyo na nimefanya juhudi za kuwazuia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapohitimisha hoja yake, anipe uhakika wa lini wananchi wangu wa Songea, hasa eneo la Mwenge Mshindo na maeneo mengine yanayozunguka pale, watalipwa fidia zao ili waweze kuondoka katika eneo lile? Kama kuna uwezekano, Serikali ifanye utaratibu wa kuwapatia maeneo mengine ili watakapokuwa wametoka pale, wawe na uhakika wanakwenda wapi na wanakwenda kuendesha maisha yao katika maeneo gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba nirudie kuunga mkono hoja na naomba hizo hoja zangu ambazo nimezisema, namtaka Mheshimiwa Waziri anijibu pale atakapohitimisha. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongelea kuhusu usafirishaji wa makaa ya mawe kutoka machimbo ya Ngaka – Mbinga kupitia Songea Mjini. Makaa ya mawe ni moja ya madini yanayochimbwa katika eneo la Ngaka lililopo Wilayani Mbinga. Uchimbaji wa madini haya ni muhimu sana kwa uchumi na maendeleo ya nchi yetu. Uchimbaji huu unasababisha makaa yasafirishwe kwa njia ya magari makubwa aina ya malori.
Malori haya ni mengi sana na yanasafirisha makaa haya kupitia Mji wa Songea, matokeo ya malori haya kwa Songea Mjini ni:-
(i) Uharibifu wa miundombinu ya barabara ambayo unafanya mazingira kuwa mabovu na mabaya hasa katika maeneo ya Lilambo, Ruhuwiko, Lizaboni, Mjini, Mfaranyaki, Bombambili, Msamala, Mshangano na Shule ya Tanga.
(ii) Magari haya yanapopita huangusha makaa na hata yanapopata ajali. Hali hii inaharibu mazingira ya kiafya ya wananchi wa Songea. Hii ni athari ya kiafya ya wananchi wangu wa Songea Mjini.
(iii) Magari haya yanasababisha msongamano mkubwa wa magari Mjini Songea na makelele kwa mingurumo mikubwa ya malori haya ambayo ni kero kwa wananchi wangu.
(iv) Songea Mjini hakuna eneo maalum la kuegesha magari haya ama yakiwa yamebeba makaa ya mawe au yakiwa yanajiandaa kwenda kubeba makaa ya mawe. Madereva hulazimika kuegesha kwenye maeneo yasiyostahili kama kwenye vituo vya mafuta na kadhalika na hivyo kusababisha kero kwa wananchi wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote haya, je, Manispaa ya Songea ambayo ndiyo inayofanya kazi zote za marekebisho ya matatizo yanayosababishwa na malori haya inanufaika vipi na machimbo haya ya makaa ya mawe?
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niishauri Serikali iamue kujenga njia ya mchepuko ili kuepusha madhara hayo kwa kupita nje ya Mji wa Songea. Zipo barabara za asili zinazotoka eneo la Peramiho na kuunganisha na barabara kuu ya Songea – Dar es Salaam kupitia Njombe ambazo ni barabara ya Peramiho – Shule ya Tanga na barabara ya Peramiho – Madaba. Aidha, ufumbuzi wa kudumu ni mpango wa utengenezaji wa reli ya Mtwara – Mbambabay kupitia Liganga na Mchuchuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kidogo kwenye eneo hili la viwanda na uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka nichukue nafasi hii niwashukuru sana na kuzipongeza Kamati zote kwa kazi nzuri walizozifanya ambazo zinatupa matumaini. Vilevile nataka niipongeze sana Serikali yangu kwa dhamira nzuri ya kwenda kwenye nchi ya viwanda Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niombe sana, tunapozungumza viwanda nadhani tuna tatizo moja kubwa sana la mikoa ya kusini, hasa hasa Mkoa wa Ruvuma. Hivi sasa tunazungumza habari ya viwanda, lakini Mkoa wa Ruvuma mwaka 2008 ulitenga eneo maalum kwa ajili ya kuweka viwanda. Eneo hili toka mwaka 2008 hadi leo na liko Songea Mjini wale wananchi hawajalipwa fidia, wanaishi maisha ya shida na Serikali haina dalili ya kuonesha lini wataanza kulipa fidia za wananchi wale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo wenzangu hapa Waheshimiwa Wabunge wanavyozungumza viwanda katika maeneo yao mie mwenzenu mnaniacha gizani kwa sababu hata hilo eneo la viwanda halipo. Kwa hiyo, nataka niiombe sana Serikali ione umuhimu wa kuhakikisha wale wananchi ambao wanafikia 1,085 wanalipwa fidia zao ili waweze kupisha eneo la kujenga viwanda na ili mipango ya Serikali iweze kufanikiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, EPZA imechukua zaidi ya heka 5,000 na Waheshimiwa Wabunge hebu fikirieni mjini kuwa na heka 5,000 kwa ajili ya shughuli za uwekezaji ambazo hazijalipwa mnaona jinsi wananchi wa maeneo yale wanavyoteseka sana na shughuli hiyo. Kwa hiyo, naomba sana, Serikali ione umuhimu wa kuwalipa wananchi hawa. Nitatoa hoja kama haitakuja bajeti ya kulipa watu fidia na basi safari hii nitakwenda sambamba na Mheshimiwa Waziri ili kuhakikisha shilingi ile ya kwake naikamata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili nataka niombe sana. Wenzetu wengi katika mapinduzi ya viwanda walijali sana wazawa wao. Sisi tunazungumza sana viwanda lakini tunawahamasisha watu na sidhani kama tumejiandaa vilivyo ili kuhakikisha Watanzania wenyewe ndio wanapata nafasi kubwa zaidi ya kuingia kwenye uwekezaji katika viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maandalizi ya kuwafanya Watanzania waingie katika viwanda yako mambo mengi; lazima tuwe na program maalum ya kuwafanya Watanzania wajiandae kisaikolojia kwamba sasa tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda. Lazima tufike mahali tuwe na mitaala maalum ya kuwafundisha wanasayansi na watafiti ili ifike mahali watakaoendesha viwanda hivyo na watakaoweza kuvihudumia viwanda hivyo iwe ni Watanzania wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wenzetu katika nchi nyingine kama China wanafikia mahali wananchi wao wanapewa mikopo ya kuweza kuanzisha shughuli za viwanda kwa ajili ya kujenga uchumi kwa wananchi wenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Tanzania lazima tujiandae, tunajua mabenki yetu yalivyo, ni vizuri tukajiandaa tuweke programu maalum ili Watanzania wapewe kipaumbele katika kuanzisha viwanda na wapate mikopo ya kuweza kuanzishia viwanda hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunavyo viwanda vidogovidogo SIDO na VETA tuna wataalamu wetu, ingawaje hawajapata elimu ya kutosha lakini viwanda vile tuna uwezo kabisa wa kutengeneza program za kuhakikisha tunawapandisha viwango na uwezo wataalam wetu SIDO na VETA ili waje kuwa wawekezaji wazuri katika shughuli za viwanda. Kwa hiyo, nataka niombe sana Serikali iwe na utaratibu mzuri wa kuwafanya Watanzania wenyewe wapate uwezo wa kuwekeza katika viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilitaka niombe sana Serikali iwe na utaratibu mzuri wa kuwafanya Watanzania wenyewe wapate uwezo wa kuwekeza katika viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nilikuwa nataka niangalie upande wa pili vilevile, tumekubaliana kimsingi kwamba hivi viwanda vyetu rasilimali yake kubwa ni kilimo. Lakini tujiulize hivi tumejiandaa vipi kilimo chetu kingia kwenye uzalishaji wa viwanda? Maana hata mtu akianzisha kiwanda cha parachichi leo nina uhakika hatuna uwezo wa kuzalisha maparachichi ya kutosheleza kiwanda cha parachichi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni vizuri kujiandaa kikamilifu kwamba, je, wakulima wetu wanaandaliwa vipi kuweza kuviwezesha viwanda viweze kufanya shughuli zao za uzalishaji? Na kwa maana hiyo, lazima tufike mahali tuangalie mfumo wa benki zetu namna utakavyoweza kuwakopesha wakulima wazalishe mazao ya kutosha mengi, ili mazao hayo yatumike katika kuingiza kwenye shughuli za uchumi wa viwanda; vinginevyo tunaweza tukajikuta tunatengeneza viwanda ambavyo malighafi unaitafuta kutoka nje ya nchi yetu na hii haitakuwa na faida kubwa kwa Watanzania wenyewe. Mwenyekiti, Maana viwanda hivi tunavitazamia vizalishe ndani ya nchi, lakini viwanufaishe wananchi kwa maana ya kutafuta raw materials, lakini vilevile viweze kupata soko la uhakika la matumizi ya viwanda hivyo.
Mheshimiwa Nilikuwa naomba Serikali iweke programu maalum na itengeneze mazingira mazuri ya kuwafanya wakulima waweze kuingia kwenye uzalishaji wa mazao ambayo yatakuwa ndiyo malighafi katika shughuli za viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishukuru. Nizishukuru Kamati zote na niipongeze sana Serikali kwa kazi nzuri inayoifanya katika shughuli za kuandaa mazingira ya viwanda; naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba kuchangia juu ya umuhimu wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro. Mlima Kilimanjaro kimekuwa chanzo kikuu cha utalii katika nchi yetu hivyo ni vizuri Serikali ikaamua kwa makusudi kuhakikisha mazingira yanayotunza Mlima Kilimanjaro ni mazuri. Yapo matatizo yafuatayo ambayo ni hatari kwa hifadhi ya mlima:-
(i) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni tatizo la moto. Mara kwa mara hutokea moto katika Mlima Kilimanjaro, ni vyema Serikali ikadhibiti vyanzo vya moto na tabia zinazosababisha moto. Lakini pia ni vyema Serikali kufuatilia kwa makini juu ya tuhuma za watumishi na baadhi ya wafanyakazi wasio waaminifu kujihusisha na tuhuma za kusababisha moto kwa sababu zao binafsi za kujinufaisha kimaslahi.
(ii) Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, lipo tatizo kubwa la mifugo kuwapo ndani ya hifadhi na kuharibu sana mazingira na uoto wa asili wa Mlima Kilimanjaro ambao husababisha ukosefu wa mvua, pia katika vyanzo vya mito vinavyoanzia kandokando ya Mlima Kilimanjaro.
(iii) Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, lipo pia tatizo kubwa la ukataji wa magogo na upasuaji wa mbao katika misitu inayozunguka Mlima Kilimanjaro. Aidha, ukataji mkubwa wa magogo na upasuaji miti unatokana na matumizi makubwa ya chainsaw ambazo nyingi zilitoka Kenya mara baada ya udhibiti mkubwa wa upasuaji mbao na magogo uliofanywa ndani ya nchi ya Kenya.
Aidha, yapo mahitaji ya badhi ya viwanda vinavyohitaji magogo, mbao na kadhalika na matokeo yake wananchi wa kawaida wanachukua tender ya kusambaza/kutoa magogo na mbao ambayo wanalazimika kuingia katika misitu ya hifadhi. Naishauri Serikali kwa nguvu zinazostahili izuie kwa nguvu zoezi hili la ukataji wa magogo na mbao katika maeneo ya Mlima Kilimanjaro ambapo inaharibu na kuuwavyanzo vya mito na chemchemi za maji.
(iv) Mheshikiwa Mwenyekiti, tatizo la kilimo pia ni moja kati ya vyanzo vikubwa vya uharibifu wa mazingira. Bado hatujawa na udhibiti mkubwa wa watu wanaolima na kuharibu mazingira katika vyanzo vya maji na maeneo ya ardhi oevu. Ni vyema Serikali ikajipanga vizuri na kusimamia Sheria za Kilimo zikiwepo zinazozuia kulima katika kingo za mito, vyanzo vya maji, na kadhalika. Sheria ya mita 60 ni muhimu izingatiwe.
(v) Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo la nusu maili (half mile)ambalo ni buffer zone kwa ajili ya Mlima Kilimanjaro. Dhamira kubwa ya eneo hili la kuwa kinga ya Mlima Kilimanjaro imepotea kwa watu kuvamia eneo hili kwa kilimo, ujenzi na upandaji wa miti usio rafiki na mazingira ya Mlima Kilimanjaro. Ni vyema Serikali ikafanya maamuzi ya makusudi ya kulinda eneo hili kwa ajili ya hifadhi ya Mlima Kilimanjaro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni na mapendekezo yangu ya jumla:-
(a) Juhudi za upandaji wa miti katika eneo lote linalozunguka Mlima Kilimanjaro, ni vyema Serikali ifanye juhudi ya hali ya juu ya suala hili.
(b) Ufanyike udhibiti madhubuti katika kuzuia kilimo holela na hifadhi ya ardhi.
(c) Udhibiti wa ukataji miti uwe wa kina na kuzisimamia sheria zote.
(d) Udhibiti wa mifugo inayoingia msituni uwe wa nguvu zaidi na adhabu kali kwa wanaovunja sheria zichukuliwe.
(e) Uaminifu na uadilifu na kufanya kazi kwa weledi ni muhimu kwa watumishi wa KINAPA na TANAPA kwa ujumla, Serikali ione namna ya kuimarisha na kuhakikisha weledi kwa watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri maalum ni kuwa utalii wa Mlima Kilimanjaro ni muhimu na unakubalika sana duniani, lakini lazima tufikiri zaidi. Wapo ambao wangependa kuupanda Mlima Kilimanjaro, lakini wanashindwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwepo afya ya mtu, umri wa mtu, mapenzi ya kutembea/interest, uwezo wa kutembea kwa kupanda mlima kwa siku tano na kadhalika, ili watu wengi waweze kupanda na kuona Mlima Kilimanjaro. Upo uwezekano wa kutengeneza mnara/tower au reli/treni ya juu ya mlima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema Serikali ikaandaa mazingira haya kwa kuweka vitu vitakavyowawezesha watalii wengi wanaovutiwa na Mlima Kilimanjaro kuja kutalii kwa njia nyingine na si ya kuupanda mlima kwa kutembea; njia hii itawezesha kuongeza watalii wengi zaidi ya mara mbili ya watalii wanaokuja kupanda Mlima Kilimanjaro. Uzoefu wa China kutengeneza tower ndefu ungeweza kutumika kujenga tower katika maeneo yanayozunguka Mlima Kilimanjaro na watalii kuja kwenye tower na kutembelea mlima kwa kutumia tower hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Manispaa ya Songea ni kuuingiza Mji wa Songea katika sekta ya utalii ili kuweza kuufanya uwe mji wa utalii. Songea ina vivutio vingi vya utalii ambavyo inabidi viendelezwe na kutangazwa; mambo kama:-
(i) Vita vya Majimaji, watu/mababu zetu walionyongwa katika mapambano na ukoloni wa Kijerumani.
(ii) Kumbukumbu za mashujaa na mapambano ya Wajerumani na mababu zetu.
(iii) Maeneo ya mapango na maporomoko ya maji.
(iv) Mila na desturi za makabila mbalimbali ya Songea, vyakula, malazi, mavazi, zana za kazi, uwindaji, utunzanji wa chakula, ngoma, tamaduni za malezi bora na kadhalika.
(v) Michezo ya jadi; mieleka, mashindano ya mila, ngoma za kivita, michezo ya kishujaa na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara ione uwezekano wa kutuma ujumbe Songea, tutakaokaa nao pamoja ili kupanga na kuchambua mambo yanayoweza kutangazwa na kuanza kazi ya kutangaza utalii wa Songea na kuanzisha utalii katika Mji wa Songea. Aidha, ni vizuri kwa Wizara kwa kushirikiana na Manispaa ya Songea kuanzisha Kituo cha Taarifa za Utalii (Tourism Information Centre) ili baada ya kuvibainisha vituo hivyo vya utalii na mambo ya utalii kuwe na kituo cha kupokelea na kutolea taarifa za utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa ushirikiano kati ya Serikali Kuu na Manispaa ya Songea tuweze kuvitangaza vivutio hivyo kwa njia mbalimbali. Dhamira kuu ni kukuza utalii na kuupelekea Mji wa Songea kuwa mji wa utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami nichukue nafasi ya kwanza kabisa, kwanza kukushukuru wewe na kukupongeza sana kwa kazi nzuri unayoifanya. Tunakupa moyo usife moyo, chapa kazi, sisi tutakuunga mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nichukue nafasi hii nimshukuru Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kwa hotuba yake nzuri aliyoitoa. Nataka nimpe moyo, kwa kawaida hakuna anayependa kulipa kodi, wote tunachukia kodi, lakini ni ukweli usiopingika kwamba bila kodi hakuna maendeleo. Kwa hiyo, endelea kuchapa kazi, yale tutakayokushauri, tutakushauri na yale mengine ambayo utaona ni muhimu kuyatekeleza basi yasimamie utekelezaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme maeneo mawili makubwa. Eneo la kwanza ni eneo la utalii. Sote tunafahamu kwamba utalii ni moja kati ya maeneo yanayoingizia sana pesa nchi mbalimbali. Na hivi sasa duniani Sekta ya Utalii ndiyo sekta kubwa ya kuingizia fedha nchi nyingi duniani. Bahati nzuri mazingira ya Tanzania ni mazuri sana kiutalii. Tunavyo vivutio vingi vya utalii, lakini naomba niseme kwamba sisi Tanzania pamoja na kuwa na vivutio vingi vya utalii, lakini bado hatujavitumia kikamilifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania tunatumia sana maeneo mawili kwa utalii. Eneo la kwanza ni eneo la Mlima wa Kilimanjaro na eneo la pili ni la Mbuga za Wanyama, lakini ukienda nchi nyingine duniani, hazina milima wala mbuga za wanyama, lakini zina utalii mkubwa sana. Kwa hiyo, nashauri kwamba tujaribu kujikita kwenye maeneo mengine ya utalii ili kuikuza nchi yetu katika eneo la utalii. Yapo maeneo mengi sana kama tutaamua kujikita tutapata watalii wa kutosha sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni mmoja kati ya watu waliopata bahati ya kutembea nchi mbalimbali na nimekwenda kujifunza maeneo mbalimbali jinsi wenzetu wanavyofanya utalii katika maeneo tofauti na yale tunayofanya sisi. Yako maeneo ya upandaji wa milima yenye miamba. Wanasema milima yenye miamba watu wa technical mountain climbing. Wanaipanda milima ile na sisi bahati nzuri tuna milima mingi sana yenye miamba, kule Songea tuna Mlima wa Matogoro ambao hauna utalii lakini tunaweza tukaingiza utalii wa kupanda milima yenye miamba tukapata nafasi kubwa sana ya kuingiza watalii nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ipo sehemu nyingine ya utalii wa historia (Historical Sites). Tuna maeneo mengi sana ya kihistoria; kule Songea tuna maeneo ya Majimaji, Vita ya Majimaji ina historia yake kubwa, ukienda Kalenga kuna historia kubwa, kuna maeneo mbalimbali nchini, lakini hatujafika mahala tukayatangaza vya kutosha na tukayatumia kama maeneo ya utalii. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba tujikite kwenye maeneo mengine ya utalii, ili kuikuza nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini uko utalii wa mila na desturi. Nilipata bahati ya kwenda nchi inaitwa Nepal, kwenye Mji Mkuu wao pale Kathmandu kuna maonesho ya mila. Kuna nchi nyingi zinakwenda kuona mila za Kihindi, historia za Kihindi; wanaingiza pesa nyingi sana kwa sababu ya utalii wa kimila. Sisi Tanzania tuna mila nyingi sana, tuna historia nyingi sana lakini hatuzitumii kwa ajili ya kuingiza watalii ndani ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, yako maeneo mengine mengi, kwa mfano kuna utalii wa Samaki (Acquarium) huu utalii umekua sana, ukienda Dubai saa hizi, wana samaki zaidi ya 33,000 kwenye eneo moja ambalo watalii wanakwenda kuwaona. Kuna nchi mbalimbali zina utalii wa namna hii, nenda Canada, Japan, Ujerumani sisi tuna aina nyingi sana za samaki ambazo tunaweza kuzifanyia utaratibu zikawa ni eneo moja la utalii. Kwa hiyo, naomba Serikali hebu ijaribu kuchambua, maeneo muhimu kwa ajili ya kuweka utalii katika vyanzo vingine tofauti ili kuipatia nchi yetu mapato ya kutosha yanatokana na utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, uko utalii wa wanyama; kule Kilimanjaro kuna sehemu inaitwa Ndarakwai, kuna tembo ambaye ukimweleza anakusikiliza, unampa maelekezo yoyote yale, lakini wale tembo hawatumiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kathmandu kuna tembo ambao wanafanyiwa utalii duniani, watu wanakwenda kupanda tembo; unapanda tembo anakupeleka kwenye maonesho mbalimbali, kwenye misitu unalipa gharama za utalii. Kwa hiyo, nafikiri bado tuna wanyama ambao tunaweza tukawatumia wakasaidia kuweza kuimarisha na kuukuza utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, vitu muhimu; ndugu yangu Shonza alikuwa ananiambia hapa, kule Mbozi kuna jiwe linaitwa Kimondo ambalo tunaweza tukalitangaza kwa nguvu sana tukaimarisha utalii. Nilikuwa nataka nilisisitize hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni juu ya Mlima Kilimanjaro. Mlima Kilimanjaro una sifa duniani kote na unatuingizia pesa nyingi sana, lakini nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri mlima ule unaingiza watu ambao hata moja ya kumi ya watu wanaotaka kuja kuuona hawaufikii kileleni. Tuna uwezo wa kuupanua ule mlima ili ufanye utalii wa watu wengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kuja Mlima Kilimanjaro ni lazima uupande, katika kuupanda zipo sifa za kupanda. Kwanza lazima upende kutembea, lakini lazima uwe na umri unaoruhusu kutembea. Kwa hiyo, watu wengi wanapenda kuja Mlima wa Kilimanjaro hawana uwezo wa afya, ama umri wake hauruhusu. Kwa hiyo tunachoweza kukifanya, kwa sababu Mlima Kilimanjaro unajulikana duniani, ni kuwahakikishia watalii kwamba watu waweza kuja kuutalii ule mlima hata bila kuupanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimjulishe, Mheshimiwa Waziri, labda niliseme na hilo kwamba nilishakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, nilifanya ziara China. China nilizungumza na kampuni ya Serikali kwamba watujengee mnara. Mnara ambao wangetujengea watu ambao afya au interest zao haziruhusu kupanda mlima wangekuja kupanda kwenye mnara huo na tulishakubaliana wajenge mnara wa mita 600, ambapo ukishapanda una uwezo wa kuu-view mlima wa Kilimanjaro kwenye kiganja chako; na kwa hiyo unatembelea Mlima wa Kilimanjaro kwa kutumia mnara huo. Kwa hiyo tunaweza tukafanya hivi na tukapata watalii wengi sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda China iko minara ya namna hii, inajaa watu wengi sana, inatumika kwa utalii wa mjini na inasaidia sana hata kufanya shughuli za utafiti. Bado kwa kutumia mnara huo unaweza ukatengeneza sky train ya kukufanya ufike Mlima wa Kilimanjaro bila kupanda kwa utaratibu wa kawaida uliopo sasa. Kwa hiyo, tunaweza kuona hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana hebu Serikali ijaribu kujikita chini kuangalia namna tunavyoweza kuikuza Sekta ya Utalii ndani ya nchi yetu ili iingize mapato zaidi ya hivi sasa yanayoingia.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuzungumza, kwanza kabisa nianze kwa kushukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, wiki hii ndiyo nimeingia Bungeni baada ya kuwa kwenye matibabu nchini India kwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja. Kwa hiyo, naomba nichukue nafasi hii nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia matibabu mema, afya njema na sasa kurudi salama. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, nashukuru sana Uongozi wa Spika, Naibu Spika, Katibu wa Bunge, pamoja na timu nzima ya Watumishi wa Bunge kwa huduma nzuri walizotupatia za kwenda matibabu India na kurudi salama. Mwisho, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kukubali maombi ambayo vile vile yalipitia Wizara ya Afya, yalipitia pia kwa wataalam kutoka Hospitali ya Taifa, Muhimbili ya kunipa kibali kwenda kupata matibabu na sasa nathibitisha kwamba nimerudi salama na niko tayari kuitumikia nchi yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nifanye kazi moja ya kuwaomba Waheshimiwa Wabunge; pamoja na maombi yenu ya kuniombea, nataka nishauri Waheshimiwa Wabunge wote tujenge tabia ya ku-check afya zetu, kwa sababu ni kweli ukinitazama nilivyo, huwezi kuamini kama afya yangu ilitetereka, lakini ni kwa sababu ya kujenga tabia ya kuangalia afya yako, wataalam wanaweza kukwambia bwana wewe unajiona mzima, lakini sio mzima. Kwa hiyo, napenda nichukue nafasi hii niwaombe Wabunge wote tujenge tabia hiyo ili kuhakikisha afya zetu zipo katika mazingira mazuri zaidi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, naomba nichukue nafasi hii niunge mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali yangu ya Awamu ya Tano chini ya Rais wetu mpendwa, Dkt. John Pombe Magufuli na Wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Maji. Kazi inayofanywa na Serikali ni nzuri sana, inatia moyo na inaonesha dhahiri kwamba tunakokwenda inaelekea tunakwenda vizuri. Nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri; kazi yao wanayoifanya ni nzuri sana, tunawapongeza, tunaomba waendelee hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme kidogo upande wa maji hasa kwa upande wa Wilayani kwangu. Wilayani Songea nina Kata 21. Katika Kata 21 kuna SOUWASA wanahudumia Kata 11 na Kata 10 zinahudumiwa na Halmashauri, ukiangalia mazingira ya Songea huwezi kutazamia kwa nini tuwe na tatizo la maji? Kwa sababu tuna mito ya kutosha, tuna mabonde ya kutosha, hali nzuri ya hewa na mvua ya kutosha. Kwa hiyo, maana yake naiomba sana Wizara ya Maji, hebu tujipange vizuri tuone namna gani tunaweza kuboresha huduma za maji katika Mji wa Songea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa Halmashauri inatoa asilimia 46 tu ya kiwango cha maji kinachotakiwa kwa wananchi wa Songea, lakini wenzangu wa SOUWASA walijenga bwawa kubwa kwa ajili ya kukusanya maji, kwa ajili ya kuhudumia Mji wa Songea. Lile bwawa bahati nzuri limekamilika, lakini mpaka sasa kuna watu wanadai fidia zaidi ya miaka sita hawajapata fidia zao, naomba Wizara iniambie kuna mpango gani wa kuwalipa fidia hawa wananchi ambao wametoa maeneo yao na kuwezesha kuweka bwawa la maji na hivi sasa bwawa lile limeshaanza kufanya kazi?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli siyo busara kwa watu ambao wametoa eneo ambalo linachangia huduma za maji Mjini Songea, lakini hawapati haki yao waliyostahili. Naomba Wizara…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Ahsante sana. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nitumie nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Kamanda wake Mahiri Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi nzuri na ya wazi ya kupeleka nchi yetu katika uchumi wa viwanda. Juhudi za wazi zinajionesha, kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu wa uongozi wake, viwanda vimeanza kuchipuka, SIDO imekua sana na wananchi wamekuwa wakijitokeza kuanzisha viwanda katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza sana Serikali kwa kazi nzuri inayofanyika. Mheshimiwa Waziri, pamoja na juhudi zote hizi zinazofanyika, bado Mkoa wa Ruvuma, Serikali na Wizara yake, haijatoa msukumo wa kuingiza Mkoa wa Ruvuma katika viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujua Serikali ina mpango gani wa kuingiza viwanda Mkoani Ruvuma? Kipo Kiwanda cha Tumbaku ambacho mwezi Januari, 2016 Mheshimiwa Waziri Mkuu, alikitembelea na kujionea mwenyewe hali ya kiwanda hicho na alitoa maelekezo ya namna ya kufufua kiwanda hicho. Je, ni mipango gani ya Wizara ya kufufua kiwanda hicho?

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Songea hawana kiwanda chochote na hivyo kukosa ajira na manufaa yatokanayo na uwezo wa viwanda. Tegemeo letu kubwa ni pale ambapo Serikali ilionesha dhamira ya kuanzisha viwanda kwa kutenga eneo la EPZA pale Songea Mjini, lakini ni masikitiko makubwa kwamba hadi sasa eneo la EPZA limepimwa na watu wamehamishwa, lakini hawajalipwa fedha zao za fidia kutokana na ardhi na mali zao katika eneo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi hawa hadi sasa, hawana mahali pa kwenda, umaskini umewapata, maana hakuna ardhi ya kilimo, hawana makazi wala hawana maendeleo wanayoweza kuyafanya kutokana na kushindwa kupata maeneo ya kufanyia shughuli za maendeleo. Pia wanazuiwa kuendeleza maeneo waliyokuwa wakiishi na kutakiwa kupisha shughuli za EPZA.

Mheshimiwa Naibu Spika, inatukatisha tamaa sana kwa namna tunavyoona wale wananchi wakipata shida katika eneo ambalo walikubali kulitoa kwa dhamira nzuri ya shughuli za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, tunawapatia lini wananchi hawa fidia zao wanazozidai? Ni imani yangu kuwa kuwalipa fidia wananchi hawa kutafuatia juhudi za kazi za Serikali kuanza kulitangaza eneo hili la Songea Mjini kwa wawekezaji waanze kuwekeza viwanda katika Mkoa wa Ruvuma.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. LEONIDAS T. GAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba niungane na wenzangu kuipongeza sana bajeti ya Serikali ya mwaka huu, ni bajeti ambayo tumeona wote, ni bajeti ya karne, bajeti ambayo haijawahi kutokea, ni bajeti ambayo imegusa kila mahali, bajeti ambayo imegusa wakulima, bajeti ambayo imegusa wafanyabiashara, bajeti ambayo imegusa wafanyabiashara wadogowadogo na akinamama lishe, bajeti ambayo imegusa viwanda, bajeti ambayo imegusa wafanyakazi, bajeti ambayo ina vipaumbele vinavyoonesha mwelekeo wa Taifa letu. Vipaumbele kama ujenzi wa reli, vipaumbele kama uanzishaji wa makaa ya mawe, vipaumbele vya ndege, vipaumbele vingi ambavyo vinaonesha mwelekeo mzuri kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza uzuri wa bajeti hii hatuna jinsi lazima tumsifu Rais wetu. Nataka niwakumbushe tu ndugu zangu, mwaka 2015 wakati tunajiandaa na uchaguzi Mkuu, watu wote tulikwenda kwenye Makanisa yetu, tulikwenda Misikitini, tukaomba tupate Rais mzuri ambaye atasaidia nchi hii. Hakuna aliyemtazamia Mheshimiwa Magufuli. Mheshimiwa Magufuli aliibuka alikoibuka na tumefika mahali tumeona. Tunaweza tukasema Mheshimiwa Magufuli ni chaguo la Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama anavyosema mwenyewe na kama tulivyosema hapa, tumuombee. Tufike mahali tumpe moyo. Anavyovifanya havijawahi kufanyika nchi hii, tulitaka Rais wa namna gani? Kwa hiyo, nachukua nafasi hii nimpongeze sana Mheshimiwa Rais na mipango yote ya maendeleo ambayo ameipanga kwa ajili ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme kitu kimoja, Mkoa wa Ruvuma ni moja kati ya mikoa inayozalisha kwa wingi sana mazao ya chakula. Wakati fulani ulikuwa kwenye the big four, ile the big four imepungua sana sasa hivi. Nafikiri niiombe Serikali tuone namna gani tunaweza kuifanya the big four iwe kweli the big four ili tuweze kuzalisha chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza kwa Serikali, kama kuna uwezekano hebu tukusanye nguvu zetu zote badala ya kusambaza kwenye mikoa tofauti ili kujiletea uhakika wa chakula, twende tuwekeze kwenye mikoa ile yenye hali nzuri ya hewa ikiwa ni pamoja na Mkoa wa Ruvuma. Tuangalie namna ya kupeleka mbolea ya uhakika ili watu walime bila wasiwasi, tuangalie namna ya kupeleka ununuzi wa mazao ili watu wauze kwa uhakika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo hatuna sababu ya kuhangaika na njaa katika nchi hii. Tukitumia mikoa miwili, mitatu au mikoa hiyo minne, tukaamua nguvu zetu zote za uzalishaji tuzipeleke kwenye mikoa ile, nina uhakika kabisa nchi hii itaondokana kabisa na tatizo la njaa, badala ya kuhangaika, mbolea tunapunguza, tunatafuta njia tunapeleka kwenye mikoa ambayo mvua haina uhakika, tusifanye hivyo. Kwenye mikoa ambayo mvua haina uhakika tupeleke mazao ambayo yanavumilia ukame, mbolea, matunzo na shughuli zote za kilimo cha mazao ya chakula tukipele kule kwenye maeneo ambayo yanaweza kutuzalishia mazao kwa wingi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo pendekezo langu hilo la kwanza tuangalie mikoa ile ambayo ina uzalishaji mzuri, tuipeleke uzalishaji ili kuhakikisha ghala ya chakula linapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tumezungumza kwenye bajeti hii juu ya suala zima la kupunguza asilimia tano za mazao ya mkulima mpaka asilimia tatu au mbili, lakini tumeweka vilevile kwamba usafirishaji wa mazao kutoka Wilaya moja kwenda Halmashauri nyingine yanayozidi tani moja tuweze kuya-charge. Nashauri kwamba kwa vile tumeshatoa punguzo na tayari wakulima wanakwenda kulipa asilimia tatu au mbili kwenye eneo ambalo wamezalishia basi hii tozo ya tani zaidi ya moja tuifute, tuifute ili mazao yasafiri bure, asilimia watakazolipa za CESS kwenye eneo ambalo wamezalisha iwe imetosheleza kulipa gharama zote za uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano kwangu Songea ni wakulima. Tuko Songea Mjini lakini hatuwezi kulima mjini kwa mujibu wa Sheria za Mjini, kwa hiyo wakulima wa Songea Mjini wanakwenda kulima maeneo ya Halmashauri za karibu. Wanakwenda kulima Madaba, Namtumbo na Peramiho. Akishalima anatakiwa kutoa mazao yake kuyasafirisha kurudisha mjini. Sasa ukimtaka huyu alipe mara mbili atalipa CESS asilimia tatu, wakati huo huo atalipa na tani zaidi ya moja anayoisafirisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nafikiri ili tuweze kumfanya mkulima huyu apate faida kutokana na kilimo chake, basi tum-charge mara moja na kwamba aweze kusafirisha mazao kwenda Halmashauri yoyote. Napendekeza pendekezo hili lifanywe kwa mazao yote ndani ya nchi. Mtu akiwa na mahindi anataka kuyaondoa Songea kwenda kuyauza Shinyanga, aruhusiwe kupita na mahindi hayo mpaka Shinyanga, anatoka Tabora anakwenda Kigoma aruhusiwe kwenda mpaka Kigoma bila kulipa gharama yoyote zaidi ya ile asilimia ya CESS ambayo tumeiweka. Itawasaidia sana wakulima wetu kuwapa moyo katika shughuli za uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nataka nizungumze katika bajeti hii, Mkoa wa Ruvuma ni Mkoa ambao bahati mbaya sana sio mkoa wenye viwanda. Ukienda pale Songea Mjini hakuna kiwanda chochote ukiacha kiwanda kilichoko Mbinga cha Kahawa na Kiwanda
kilichoko Tunduru cha Korosho, lakini Songea Mjini hakuna kiwanda chochote. Kwa hiyo maana yake mzunguko wa fedha ni mdogo sana kwa wananchi wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu alifanya ziara mwezi Januari mwaka jana kule Songea na alipofanya ziara alitembelea kiwanda cha Ngomati, kiwanda cha tumbaku. Kile kiwanda kimekufa katika mazingira ya ajabu sana, hebu tuangalie; Waziri Mkuu alisema angalieni mazingira haya ili muone namna gani tunaweza kukifufua kile kiwanda. Kwa sababu kuna tatizo kubwa la tumbaku kwa sasa kama kiwanda kile hakiwezekani kuzalishwa kwa ajili ya kuzalisha tumbaku, basi tufanye utaratibu wowote wa kupata kiwanda ambacho kitakuwa mbadala wake, maana mashine zipo, mitambo ipo, kiwanda kipo lakini kimekufa katika mazingira ya ajabu kidogo na hivyo mzunguko wa pesa ni mdogo sana kwa sababu hakuna ajira Songea Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna utaratibu ambao tumekubaliana na Serikali wa kutafuta eneo la EPZA ambalo bado halijakamilika. Naomba katika bajeti hii tukamilishe eneo la EPZA kwa ajili ya kutafuta wawekezaji ili waje kuwekeza viwanda Songea Mjini. Hii itasaidia sana kuweza kuinua uchumi na kusaidia ajira kwa wananchi wa Songea na Mkoa mzima wa Ruvuma kwa ujumla. Kwa hiyo, naomba sana Serikali iweke kipaumbele kwanza suala hili la kufufua kiwanda cha Ngomati lakini la pili ni hili la kufungua EPZA, ukanda wa viwanda ambao bahati nzuri Serikali imeshaamua, imetafuta eneo lipo pale, watu hawajalipa tumalize tatizo la kulipwa ili watu waje kuwekeza pale Songea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uhakika kabisa viwanda vitasaidia sana hali ya uchumi ya wananchi wa Songea. Sisi tuko pembezoni sana, hatuna viwanda, hatuna shughuli zote zaidi ya kilimo, hakuna shughuli zozote za kiuzalishaji. Kwa hiyo, tukifanya hivi tutasaidia wananchi wa Songea ili wapate ajira waweze kupata uzalishaji huo utakaosaidia maeneo yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tuna tatizo kubwa sana la suala la makaa ya mawe Ngaka kule Mbinga. Tuna makaa ya mawe lakini usafirishaji wa makaa yale ya mawe ni mgumu sana, unafikia mahali unaharibu barabara zetu unaharibu mazingira. Tunaomba tuone uwezekano wa kupata reli, reli ile ambayo ingejengwa kati ya Mbamba bay na Mtwara naomba iharakishwe kwenye mpango ili iingie kwenye mpango wa maendeleo ili iweze kutengenezwa reli. Reli ile itasaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono mkono hoja.