Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Leonidas Tutubert Gama (6 total)

MHE. LEONIDAS T. GAMA aliuliza:-
Kilimo cha mahindi ndiyo shughuli kubwa ya kiuchumi kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma, lakini kumekuwa na bei kubwa ya mbolea na ruzuku hutolewa kwa wakulima wachache tu.
(a) Je, Serikali haioni utaratibu huu wa ruzuku kwa wakulima wachache umekuwa na changamoto kubwa ya kupotea kwa vocha kunakofanywa na watumishi wasio waaminifu?
(b) Je, kwa nini Serikali isitoe ruzuku kwa wakulima wote kupitia taasisi maalum kama TFC na kuacha mfumo huu wa vocha?
(c) Je, Serikali haijui wakulima walio wengi ni maskini na ndiyo wanaowalisha Watanzania wote?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leonidas Tutubert Gama, Mbunge wa Songea Mjini, lenye sehemu (a) b) na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kumekuwepo na changamoto ya upotevu wa vocha za ruzuku ya pembejeo, unaofanywa na watumishi wasio waadilifu kwa kushindwa kusimamia ipasavyo utaratibu huu katika Halmashauri zao. Serikali inaendelea na taratibu za kuwachukulia hatua watumishi wanaohusika na ubadhirifu katika mfumo wa ruzuku za pembejeo; hii ni pamoja na kupelekwa mahakamani wahusika, na baadhi ya kesi zimeishatolewa hukumu ambapo wahusika wanatumikia adhabu mbalimbali ikiwemo vifungo, kushushwa vyeo na kufukuzwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili mpango wa ruzuku uweze kunufaisha Wakulima wote nchini, Wizara yangu inaandaa mapendekezo ya mfumo wa ruzuku ya pembejeo ambao utawafikishia wakulima wote pembejeo zikiwa na ruzuku na zipatikane popote nchini na kwa wakati wote na hivyo kuongeza tija na uzalisha na kuwa na uhakika wa usalama wa chakula katika ngazi ya Taifa na kaya. Kwa kupitia mpango huu ni wazi kuwa bei ya mbolea itapungua na hivyo kuwezesha wakulima wengi zaidi kumudu kununua mbolea na kuzitumia ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali ina mpango wa kuwezesha ujenzi wa kiwandakikubwa cha kuzalisha mbolea nchini katika Wilaya ya Kilwa. Tayari wawekezaji wa ujenzi wa kiwanda hicho, wameishapatikana na kwa sasa majadiliano kati ya wawekezaji hao na Serikali yanaendelea. Kama kiwanda hicho kitafanikiwa kujengwa, kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mbolea tani milioni 1.2 kwa mwaka, vilevile kampuni ya Live Support System inatarajia kujenga kiwanda cha mbolea katika Wilaya ya Kibaha, kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha tani 500 kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa ujenzi wa viwanda vya mbolea hapa nchini, utawezesha upatikanaji wa mbolea kwa gharama nafuu, hivyo kuwezesha wakulima wengi kutumia mbolea na kuongeza tija na uzalishaji. Serikali inatambua mchango wa wakulima wadogo katika kuhakikisha kunakuwa na chakula cha kutosha nchini na inapongeza sana juhudi zinazofanywa na wakulima hao. Aidha, Serikali inatambua umaskini wa kipato walionao wakulima hao na ndio maana inakuja na mipango mbalimbali ya kuwasaidia ikiwa ni pamoja na ruzuku katika pembejeo za kilimo.
Umeme ni muhimu sana kwa maisha bora ya wananchi, lakini wananchi wa Songea Mjini hawana uhakika wa umeme kutokana na kutegemea zaidi umeme wa jenereta na ule kidogo unaozalishwa na Shirika la Masista Chipole:-
(a) Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa Gridi ya Taifa toka Njombe/Makambako?
(b) Je, Serikali inafahamu kuwa watu wengi wanashindwa kuja kuwekeza Songea kutokana na kukosa umeme wa uhakika?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Leonidas Tutubert Gama, Mbunge wa Songea Mjini, lenye sehemu a na b kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango wa kufikisha umeme wa Gridi ya Taifa mkoani Ruvuma kupitia mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 220 kutoka Makambako hadi Songea. Kazi za mradi huu na utekelezaji wake umeshaanza na zimegawanyika katika sehemu kuu mbili:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya kwanza inajumuisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 yenye urefu wa kilometa 250 kutoka Makambako hadi Songea. Kazi hii pia inahusisha pia upanuzi wa kituo cha kupooza umeme kutoka Makambako, lakini pia ujenzi wa vituo vipya vya kupooza umeme katika Mji wa Madaba pamoja na Mji wa Songea. Kazi hii inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2018 naitagharimu dola za Kimarekani milioni 34.68 lakini pia shilingi bilioni 15.41.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili inahusisha ujenzi wa njia ya kusambaza umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 900. Lakini pia wateja wa awali 22,700 katika vijiji 120 vya Wilaya ya Ludewa, Njombe Mjini, Njombe Vijijini, Wanging‟ombe katika Mkoa wa Njombe wataunganishiwa umeme. Kadhalika kazi hii itajumuisha pia katika wilaya za Mbinga, Namtumbo, Songea Mjini na Songea Vijijini katika Mkoa wa Ruvuma. Kazi hii inatarajiwa kukamilika mwezi Disemba 2017 na itangarimu dola za Marekani milioni 37.63 na shilingi bilioni 6.51.
Mheshimiwa Naibu Spika, upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Ruvuma umeimarika kwa siku za hivi karibuni. Na hii ni kutokana na kufunguliwa kwa vituo mbalimbali vya kuzalisha umeme, ikiwa ni pamoja na vituo vya umeme vya Donya (megawatt 0.5), Mbinga (megawatt 2.5), Namtumbo (megawatt 0.4) Songea (Megawatt 4.5) na Tulila (megawatt 5) vilivyofikisha jumla ya megawatt 12.4.
Mheshimiwa Naibu Spika, mahitaji ya juu ya umeme kwa Mji wa Songea ni megawatt 4.7, na uwezo wa uzalishaji ni megawatt 9.5, hivyo kuwa na ziada ya umeme wa megawatt 4.8. Ni matumaini ya Serikali kuwa kukamilika kwa
mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya Makambako kwenda Songea kutamaliza kabisa tatizo la changamoto za umeme na kufufua fursa za uwekezaji katika Mkoa wa Ruvuma kwa ujumla wake.
MHE. LEONIDAS T. GAMA aliuliza:-
Zahanati zetu zilizopo vijijini ambako ndiko walipo wazee walio wengi wakiwemo wastaafu ambao mara kwa mara hukabiliwa na magonjwa yanayotokana na utu uzima ikiwemo shinikizo la damu zinazokabiliwa na ukosefu wa dawa za magonjwa hayo na inasemekana pia zahanati hazitakiwi kuwa na dawa za shinikizo la damu hivyo wazee kutakiwa kwenda ngazi za vituo vya afya na au hospitali hali inayopelekea wazee hao kupewa dawa za kukojoa tu (Lasix) badala ya dawa za shinikizo la damu kwa ajili ya matibabu. (a) Je, Serikali haijui kuwa wazee wengi wanaosumbuliwa na magonjwa hayo wanaishi vijijini ambako kuna zahanati pekee na siyo hospitali? (b) Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu wa kuhakikisha dawa za aina mbalimbali za shinikizo la damu zinazowekwa katika zahanati zetu zilizoko vijijini ambako ndiko wazee wengi walipo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Leonidas Tutubert Gama, Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua uwepo wa wazee wengi sehemu za vijijini ambao wanasumbuliwa na magonjwa mbalimbali ya utu uzima ikiwemo shinikizo la damu. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imeboresha mgao wa fedha utakaowezesha upatikanaji wa dawa zikiwemo za shinikizo la damu katika ngazi zote za kutolea huduma za afya kuanzia hospitali hadi vituo vya afya na zahanati kulingana na miongozo iliyopo ya utoaji huduma za afya nchini. (b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inao mwongozo wa utoaji tiba za dawa unaojulikana kama Standard Treatment Guideline ya mwaka 2014 ambao umeambatanishwa na orodha ya taifa ya dawa muhimu (National EssentialMedicines List of Tanzania). Orodha hiyo imebainisha dawa mbalimbali ambazo zinatumika katika ngazi mbalimbali za vituo vya kutolea huduma za afya, ikiwemo vituo vya afya na zahanati. Dawa za shinikizo la damu zilizopo kwenye orodha hiyo ni kama Propranolol,Methyledopa, Frusemide, Hydrochlorthiazide na Bendrofuazide. Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, vituo vya kutolea huduma za afya vinayo mamlaka ya kuagiza dawa nyingine za kutibu shinikizo la damu nje ya hizi tulizozitaja hapo juu kulingana na uwezo na kiwango cha elimu cha wataalam waliopo kwenye kituo husika. Hii ina maana kuwa Wizara hauizuii kituo chochote kuagiza dawa mahali popote za kutibu shinikizo la damu ikiwa kituo husika kitaona kina uwezo wa kufanya hivyo kwa kutoa huduma kwa viwango vinavyostahili. Sanjari na hilo, kulingana na mfumo uliopo wa ugavi na usambazaji wa dawa za Serikali, ni jukumu la watendaji wa vituo husika kuainisha mahitaji ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi na kuagiza mahitaji yao kutoka Bohari ya Dawa (MSD) kwa kutumia fomu maalum ya taarifa na maombi (Report and Request – R&R).
MHE. LEONIDAS T. GAMA aliuliza:-
Wananchi wa Songea Mjini wamekuwa wakiitumia Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma kama Hospitali yao ya Wilaya hivyo kufanya kuwepo na mgongano wa kiutendaji kati ya Mamlaka ya Mkoa inayoitambua Hospitali hiyo kama Rufaa ya ngazi ya Mkoa na Mamlaka ya Wilaya. Tarehe 10 Januari, 2016, Mheshimiwa Waziri wa Afya alifika kuona hali halisi na juhudi za wananchi wa Songea Mjini za kujenga Kituo cha Afya Mji Mwema ambacho kimefikia hatua kubwa, hivyo wakamwomba Waziri kituo hicho kipandishwe hadhi kuwa Hospitali ya Wilaya, Songea Mjini.
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuiacha Hospitali ya Mkoa ifanye kazi ya Rufaa Kimkoa?
(b) Je, Serikali haioni haja ya kupunguza msongamano katika hospitali hiyo kwa kuanzisha Hospitali ya Wilaya Songea Mjini?
(c) Je, ni lini basi Serikali itakipa hadhi Kituo cha Afya cha Mji Mwema, Songea Mjini ya kuwa Hospitali ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leonidas Tutubert Gama, Mbunge wa Songea Mjini, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma inatakiwa kutoa huduma za rufaa kama inavyofanyika kwa Hospitali zote za Mikoa nchini. Hata hivyo, mahali ambapo hakuna Hospitali ya Wilaya, wagonjwa hawazuiliwi kwenda katika Hospitali ya Mkoa kwa ajili ya matibabu. Mpango uliopo ni kuimarisha Zahanati na Vituo vya Afya ndani ya Halmashauri ili viweze kutoa huduma kwa wagonjwa wengi ili kupunguza msongamano katika Hospitali hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inakusudia kuboresha Kituo cha Afya cha Mji Mwema ili kiweze kutoa huduma bora za matibabu kwa lengo la kupunguza msongamano katika Hospitali ya Mkoa kwa sasa. Serikali itatoa kipaumbele kwa mpango wowote wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea juu ya uanzishwaji wa Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya cha Mji Mwema kimeshaombewa kibali kuwa Hospitali. Timu ya Wataalam kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeshakagua kituo na kuelekeza yafanyike maboresho ya miundombinu inayohitajika ili kiweze kukidhi vigezo vya kuwa hospitali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Fedha na Mipango ya Halmashauri ya Manispaa ya Songea, imepanga kukutana tarehe 17 Mei, 2017 ili kujadili utekelezaji wa maelekezo ya Wizara ya Afya.
MHE. LEONIDAS T. GAMA aliuliza:-
Wananchi wangu wa Jimbo la Songea Mjini katika eneo la Matogoro, Mahiro, Lihira na Chemchem walitoa maeneo ya kilimo na makazi kwa SOUWASA ili kutengeneza bwawa la maji kwa Mji wa Songea toka mwaka 2003 na jumla ya wananchi 872 walifanyiwa uthamini wa mali na nyumba zao. Mwaka 2015 uthamini ulifanyiwa marejeo (review) na jumla ya kiasi cha shilingi 1,466,957,000 iliidhinishwa na Serikali kama madai halali ya wananchi hao lakini hadi leo ni miaka 14 imepita wananchi hao hawajapewa stahili zao.
(a) Je, Serikali haioni kuwa kitendo hiki cha kutowalipa wananchi haki zao ni kuwaongezea umaskini wa kipato, malazi na kukosa uwezo wa huduma za matibabu na elimu?
(b) Je, ni lini Serikali itawalipa wananchi hao stahiki yao waliyotakiwa kulipwa miaka mingi iliyopita?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leonidas Tutubert Gama, Mbunge wa Songea Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mwaka 2006 Serikali ililipa kiasi cha shilingi 20,695,051 kwa wananchi 64 kwa ajili ya fidia ya Wananchi waliopisha ujenzi wa miundombinu ya Bwawa la Ruhila. Wananchi hao ni wale ambao walikuwa nje ya mita
60. Wananchi 872 ambao walikuwa ndani ya mita 60 kutoka kwenye chanzo cha Mto Ruhila walifanyiwa tathmini mwaka 2003. Kwa mujibu wa Sheria ya mazingira ya mwaka huo wa 2004 wananchi hao hawastahili kulipwa fidia.
Mheshimiwa Spika, wananchi hao walitoa malalamiko yao kwa Serikali ambapo Serikali imepitia Sheria ya mazingira ya mwaka 2004 na kuona kwamba ilitungwa wakati Wananchi wameshafanyiwa tathmini. Aidha, tathmini hiyo ilipitiwa upya mwaka 2015 na kubaini jumla ya shilingi 1,466,957,000 zinahitajika kulipwa fidia. Serikali imepanga kulipa fedha hizi fidia katika mwaka wa fedha 2018/2019.
MHE. LEONIDAS T. GAMA aliuliza:-
Mji wa Songea ni kati ya Miji yenye matatizo makubwa ya maji katika nchi yetu na katika utoaji wa maji, Halmashauri ya Mji wa Songea inategemea visima virefu na vifupi na maji ya mtiririko. Mji huo una jumla ya vituo 187 ambavyo havitoi maji ambapo kila kituo kinagharimu wastani wa shilingi milioni tatu (3) kwa ajili ya ukarabati, gharama zote ni jumla ya shilingi milioni 561.
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kumaliza tatizo hilo?
(b) Je, Serikali haioni kuwa ikondoa tatizo hilo itakuwa imemaliza kero kubwa kwa wananchi zaidi ya 30,000 ambapo kila kituo kitakuwa kinahudumia watu 250?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leonidas Tutubert Gama, Mbunge wa Songea Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Manispaa Songea una wastani wa watu wapatao 230,000, ambapo Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea inatoa huduma katika maeneo ya mji yanayokadiriwa kuwa na jumla ya wananchi 194,000 na pembezoni mwa mji kuna wastani wa wakazi wapatao 36,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya pembezoni mwa mji kuna vituo vya kuchotea maji 187 vilivyogawanyika katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni visima vifupi 89 na kundi la pili ni vituo vya kuchotea maji kutoka katika mradi wa maji wa mtiririko.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilikwishaona umuhimu wa kumaliza tatizo la maji katika Manispaa ya Songea na kwa mwaka wa fedha 2016/2017 kiasi cha fedha shilingi milioni 314 kilitengwa kwa ajili ya ukarabati wa visima vifupi 89 ambavyo ufanisi wake umepungua. Taratibu za kumpata mzabuni wa kufanya kazi hiyo zimekamilika na tayari mkataba umesainiwa mwezi Mei 2017 na Mkandarasi ataanza kuleta pampu hizo mwishoni mwa mwezi Juni, 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali itakarabati vituo vingine 98 vilivyobaki, hivyo huduma ya maji itakuwa imeboreshwa na wananchi zaidi ya 30,000 waishio pembezoni mwa Mji wa Songea watapata huduma ya maji. Vilevile Serikali imetenga Dola za Marekani milioni 50.89 zitakazopatikana toka mkopo wa Dola za Marekani milioni 500 toka India ili kuboresha huduma ya maji katika Mji wa Songea.