Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Juma Hamad Omar (1 total)

MHE. JUMA HAMAD OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa ufafanuzi wa swali langu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba Serikali inapoteza kiasi cha shilingi za Kitanzania trilioni 1.18 kila mwaka. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Idara ya Afrika ya IMF kuhusu effect ya hizi exemptions kwa uchumi wa nchi ambazo ziko Kusini mwa Jangwa la Sahara, imebainika katika ripoti hii kwamba Tanzania ikiwa ni moja ya nchi hizo inapoteza kiasi cha Dola bilioni 1.2 hadi Dola bilioni 2.2 kwa wastani kwa mwaka ambapo hiyo ni sawasawa na kiasi cha shilingi za Tanzania trilioni 2.2 mpaka kwenda kwenye shilingi trilioni 4.6. Nataka kujua ni takwimu zipi sahihi za Waziri au za utafiti huu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ripoti hii ya uchunguzi imebainisha kwamba kivutio cha misamaha ya kodi sio tena kivutio kikubwa kwa maana ya kuwa-attract wawekezaji kuingia katika nchi. Yako mambo matatu ambayo sasa hivi wawekezaji wanaangalia sana yakiwa ni kipaumbele. Kwanza, ubora wa miundombinu. Pili, sera sahihi za fedha zinazotabirika (predictable financial and monetary policies). Tatu, utawala bora na utulivu wa kisiasa (good governance and political stability). (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri, kwa sababu tax incentive siyo tena kipaumbele au vigezo wanavyoviangalia wawekezaji, haoni kwamba time imefika sasa ya kubadilisha ile Sheria ya Uwekezaji hasa Kifungu cha 38 na kubadilisha sheria zinazoanzisha Maeneo Tengefu (Economic Processing Zone, Sspecial Economic Zone and Export Processing Zones) ili misamaha hiyo itolewe kidogo sana kuliko ilivyo sasa ambapo inachukua karibu asilimia 8.3 ya bajeti yote ya Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza, naomba nisema takwimu nilizozisema mimi ni halali kabisa kwa sababu zimetoka katika takwimu za Serikali na naomba aziamini. Hatuna sababu ya kudanganya takwimu hizo kwa sababu tunajua madhara ya mishamaha hii ya kodi kwa uchumi wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, nakiri kwamba ni sahihi kivutio cha kodi sio kivutio tena lakini nimwambie tu Tanzania yetu ni nchi ya mfano katika Bara letu la Afrika na dunia kwa ujumla kwa sera zake za monitory pamoja na fiscal policies ndiyo maana wawekezaji wanaongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nilikumbushe Bunge lako, ni juzi tu wakati tunapitisha bajeti ya Wizara ya Viwanda pamoja na bajeti ya Wizara ya Fedha, Waheshimiwa Wabunge hawa hawa walikuwa wakilalamika kwamba zipo tax incentive ambazo tunashindwa kuzitoa na wawekezaji wanashindwa kuja nchini kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii napata shaka kidogo na swali hili la Mheshimiwa Omar, lakini kama Serikali tunajua na tunafahamu misamaha hii ya kodi tunaitoa kisheria na tunaangalia mazingira ya kiuchumi ya Taifa letu, nani anakuja na kufanya nini katika uchumi wetu, lakini pia kijamii ana impact gani mtu huyu tunayempa msamaha huu na sheria zetu pia tunaziangalia kwa uhakika kabisa.