Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Daimu Iddi Mpakate (60 total)

MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini katika miradi miwili aliyosema imekamilika, mradi wa Nandembo na Nalasi tarehe 22 Julai, 2014, Rais wa Awamu ya Nne alifungua miradi ile, lakini cha kusikitisha hadi leo maji hayatoki katika miradi yote miwili. Je, yuko tayari kufuatana na mimi kwenda kuangalia miradi ile kama alivyosema imekamilika wakati maji hayatoki? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, mradi wa Mbesa umesimama kwa takribani kwa mwaka mmoja na nusu na vifaa viko pale, vina-hang hovyo bila usimamizi wowote. Je, ni lini Serikali itapeleka mkandarasi mwingine ili aweze kumalizia mradi ule?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, miradi miwili niliyoitaja amesema kwamba miradi hiyo haitoi maji. Nitafanya mawasiliano na Mkurugenzi wa Halmashauri husika ili aweze kutupatia maelezo kwa nini miradi hiyo haitoi maji ili tuweze kuhakikisha kwamba tunakamilisha pale ambapo pamepungua kuhakikisha hiyo miradi inatoa maji. Pia kwa ridhaa yako, ridhaa ya Mheshimiwa Spika na Waziri wangu wa Maji na Umwagiliaji, hatuna matatizo kabisa, tukimaliza Bunge tunaweza tukaambatana naye ili kwenda kuangalia utekelezaji wa hii miradi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la nyongeza kuhusu mradi wa Mbeso. Mradi huu ulikosa chanzo cha maji lakini kama mnavyofahamu Waheshimiwa Wabunge ni kwamba tumeanza Programu ya Pili ya Maendeleo ya Maji ambayo imeanza Januari, 2016, baada ya kukamilisha programu ya kwanza. Ile miradi yote tuliyoi-earmark kwenye Programu ya Kwanza ambayo ilianza mwaka 2007 na haikukamilika ndiyo tutaanza nayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata katika bajeti ambayo itasomwa na Mheshimiwa Waziri mwezi huu kwanza tunalenga kukamilisha miradi ambayo tulianza na haikukamilika na miradi ambayo pengine haikuanza lakini ilikuwa imependekezwa itekelezwe katika Programu ya Kwaza tutahakikisha kwamba miradi hii tunaikamilisha kabla hatujaenda kwenye miradi mipya. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hii miradi yote 11 katika Programu ya Pili tutahakikisha kwamba inakamilika kabla hatujaingia kwenye miradi mingine.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa mazingira ya Mchinga yanafanana kabisa na Wilaya ya Tunduru yenye kilometa za mraba 18,776; na kwa kuwa tayari kuna majimbo mawili na taratibu zote za kuigawa Wilaya ile zilishafanyika siku za nyuma; na kwa kuwa zilitolewa ahadi za viongozi wa Awamu ya Nne kuigawa Wilaya ile na Mkoa kwa ujumla. Je, ni lini taratibu za kuigawa Wilaya ile na Mkoa mpya wa Selous zitafanyika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika kumbukumbu zangu nilizokuwanazo ni kwamba eneo analozungumzia Mheshimiwa Mpakate ni kweli jambo hili liko ofisini, lakini nadhani kuna baadhi ya vitu vingi zaidi ya hapo hata kuna suggestion ya kugawa kupata Mkoa mpya wa Selous, kama sikosei katika eneo hilo! Na Mheshimiwa Ngonyani alikuwa akizungumza jambo hilo na hata Mheshimiwa Ramo Makani alikuwa katika mchakato huo wa pamoja kuhakikisha kwamba maeneo hayo, kutokana na jiografia yake, tunapata Mkoa mpya wa Selous.
Kwa hiyo, sasa kama Ofisi ya TAMISEMI itafanya uhakiki jinsi gani, aidha hizo Wilaya, Halmashauri au Mkoa mpya, mwisho wa siku tutakuja na majibu sahihi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kubwa ni kwamba kupeleka utawala katika eneo hilo kwa sababu, ni kweli, kuna wananchi wengine saa nyingine ukitoka huku Tunduru kwenda hata kule Ruvuma kuna changamoto, lakini uko karibu hapa karibu na Masasi. Kwa hiyo, walikuwa na maombi mengi kwa pamoja na viongozi waliopita walitoa ahadi mbalimbali.Ofisi ya TAMISEMI italifanyia kazi na mwisho wa siku ni kwamba, eneo hilo ki-jiografia litagawanywa vizuri kwa suala zima la kiutawala ilimradi wananchi wapate huduma ya karibu katika maeneo yao
MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa matatizo ya ushirika yameenea katika maeneo yote ya nchi yetu ya Tanzania, na kwa kuwa Sheria Na. 6 ya Mwaka 2013 ilianzisha rasmi Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania. Je, ni lini Serikali itaifanya Tume hii iwe na uongozi wa kudumu kwa kuteua Mwenyekiti wa Tume pamoja na Makamishna wa Tume ili ushirika usimamiwe vizuri?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa anavyosema kwamba Tume ya Ushirika bado inakabiliwa na changamoto ya uongozi, nimhakikishie tu kwamba mapendekezo kuhusu uongozi tayari yapo mezani kwa Waziri, kwa hiyo muda mfupi tutasikia kukamilika kwa uteuzi wa viongozi wote wa Tume ya Ushirika.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara ya Makambako - Njombe - Songea, ilijengwa tangu mwaka 1984, na sasa ina hali mbaya sana kila siku inawekwa viraka lakini hali imekuwa ni mbaya sana.
Je, ni lini Serikali itajenga barabara ile upya ili kuwahudumia watu wa Mkoa wa Ruvuma na Njombe kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kutoka Makambako hadi Songea na hususani Njombe hadi Songea imetengewa bajeti ya kufanyiwa ukarabati katika mwaka huu wa fedha. Na mimi nimhakikishie ukarabati huo utakaofanyika tutahakikisha ile kampuni itakayopewa kazi hiyo ya kufanya ukarabati inafanya kwa kiwango ambacho barabara hiyo inakuwa imara na kutumika kwa muda mrefu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimuhakikishie Mheshimiwa Mpakate na Wabunge wote wanahusika katika barabara hii, ikiwa ni pamoja na Mheshimiwa Leonidas Gama ambaye alinisumbua sana ofisini kuhakikisha kwamba hili eneo linakaa vizuri ili anapopita kule asipate matatizo anayoyapata sasa. Namhakikishia na wengine wote kwamba tutahakikisha mkandarasi atakayepata kazi hii ya ujenzi ambayo bajeti mmeshaipitisha anajenga kwa kiwango kinachotakiwa.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini naomba nimuulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo la Tunduru Kusini kama alivyozungumza, kuna kata 15 kati ya hizo ni vijiji vinne tu vya Kata ya Chiwana na Kata ya Mbesa ndivyo vimepata umeme. Je, kati ya kata hizi zifuatazo ni lini watapatiwa umeme wa REA, Kata za Mtina, Nalasi, Mchoteka, Malumba, Mbati, Ligoma, Namasakata, Mchesi, Lukumbule, Chiwana na Msechela?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na tabia ya mkandarasi anayejenga laini ya Mbesa kuwadai wananchi wetu Sh.200,000/- mpaka Sh.300,000/- kwa ajili ya kupelekewa nguzo na kuunganishiwa umeme katika nyumba zao. Je, ni hatua gani imechukuliwa ili mkandarasi huyu asiendelee na tabia hiyo kwani umeme huu ni haki yao wananchi kupewa bure kwa kulipa Sh.27,000/-? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikubaliane na Mheshimiwa Mpakate kwamba kwa kweli ni vijiji vinne tu ambavyo vimepata umeme kwenye jimbo lake lakini vijiji vingine vilivyosalia ambavyo jumla yake kwa kweli ni 67, vikiwemo Vijiji vya Semeni, Angalia, Jiungeni na vijiji vingine vya Mwenge vyote vitapata umeme kwenye REA Awamu ya III inayoanza mwezi Julai, 2016. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mpakate pamoja na wananchi wa Tunduru Kusini kwamba vijiji vyote vilivyosalia vitapata umeme kuanzia mwezi Julai 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusiana na gharama ya nguzo ambayo wananchi wanatozwa, napenda kutumia fursa hii kuwaomba sana Waheshimiwa Wabunge na kuwahakikishia wananchi kama ifuatavyo: Kwanza kabisa, katika Mradi wa REA mteja yeyote hatakiwi kutozwa gharama ya nguzo, si Sh.200,000/- wala Sh.300,000/-. Naomba niwahakikishie wananchi wa Tunduru Kusini na Watanzania wengine, gharama za nguzo kwenye miradi ya REA Serikali imeshagharamia, kwa hiyo, mwananchi hatakiwi kutozwa gharama yoyote ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, niendelee tu kusema kwamba kwenye miradi mingine ya TANESCO, gharama za nguzo ni kama ifuatavyo: Kwa mteja ambaye yuko umbali wa mita 30 -70, gharama yake ni Sh.177,000/- tu kwa vijijini na kwa mijini ni Sh.272,000/- tu. Kwa hiyo, napenda kutoa kabisa hili angalizo kwa wananchi, wasitozwe gharama zaidi ya hiyo kwa umbali ambao nimeutaja hata kwa miradi ya TANESCO.
MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri, lakini katika vivuko vilivyotajwa; Kivuko cha Chaulesi kilichopo Makande na Chamba kilichopo Wenje kinaunganishwa na barabara mbili za mkoa ambazo zipo chini ya barabara ya ulinzi: Je, Serikali ina mpango gani wa kuzitengeneza barabara hizi kwa kiwango cha changarawe ili ziweze kupitika muda wote wa mwaka kwa ajili ya kutoa huduma hiyo ambapo watu wa Msumbiji na Tanzania wanatembeleana kwa ajili ya kupata huduma kutoka Tunduru Mjini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa eneo la Chaulesi na Chamba watu wengi wanapita sana kutoka Msumbiji kuja Tanzania kufuata huduma za mahitaji ya muhimu kutoka Tunduru Mjini: Je, Serikali haioni haja ya kuweka Kituo cha Uhamiaji katika maeneo hayo mawili ili kuondoa kero ya Watanzania ambao wanapata tabu wanapovuka Msumbiji kwa ajili ya kukosa hati na kusumbuliwa na askari wa Msumbiji?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali ni kuhakikisha kuwa barabara zote za mkoa tunazitengeneza kwa kiwango kizuri ili ziweze kupitika wakati wote wa mwaka. Kwa hiyo, nitaongea na Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba tutaona mpango gani barabara hii tutaweza kuishughulikia, hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kuhusu utaratibu wa kuweka Kituo cha Uhamiaji, tutaongea na Wizara ya Mambo ya Ndani kuona kama kuna uwezekano wa kuweka kituo hicho ambacho kitapunguza matatizo kwa wananchi wetu wanaovuka sehemu hizo mbili.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa mazingira ya Tarime yanafanana kabisa na mazingira ya barabara zilizopo katika Jimbo la Tunduru Kusini kutoka Mtwara Pachani, Msewa na Rasi mpaka Tunduru Mjini iliahidiwa na Makamu wa Rais wakati wa kampeni kwamba itajengwa kwa kiwango cha lami. Je, ni lini mchakato wa ujenzi wa barabara hii utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni ngumu sana unapokaa hapa kujibu swali linalohusu barabara yako, kwa hiyo, naomba nijibu kwa niaba ya Waziri wangu wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ya Mtwara Pachani, Lusewa, Lingusenguse hadi Lalasi ni barabara ambayo iliahidiwa na Mheshimiwa Makamu wa Rais wakati wa uchaguzi, ndiyo kiongozi pekee aliyepita barabara hii. Kwa kweli baada ya kuiona na kuona idadi ya watu walivyo katika maeneo hayo akaahidi kwamba ataijenga kwa kiwango cha lami alipokuwa Lusewa na aliahidi vilevile barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami alipokuwa na Lalasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mpakate na wananchi wake wote wa Jimbo la Tunduru Kusini pamoja na wananchi wa Jimbo la Namtumbo na hasa Sasawala kwamba barabara hii kama ilivyoahidiwa tutaijenga, lakini naomba tu wananchi wetu waelewe kwamba ahadi tulizonazo za viongozi ni nyingi, zote tunazo tunazitekeleza kwa awamu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka ujao wa fedha barabara hii imetengewa milioni 100 kwa ajili ya kufanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika nia ya kutekeleza ahadi ya Makamu wa Rais. Naomba nimhakikishie kazi hii itakapokamilika nitaweza kuwa na jibu sahihi lini barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa chuo kile hakikukidhi haja ya kukikarabati na kwa kuwa katika majibu ya msingi yamesema kwamba eneo la chuo lilikuwa dogo. Je, Serikali haioni haja ya kujenga chuo kipya kwa sababu Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina maeneo mengi ambayo yangeweza kujengwa chuo hicho? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina upungufu mkubwa sana wa wafanyakazi katika Idara ya Afya kwa zaidi ya 70%. Ni kwa nini sasa Serikali isitoe upendeleo maalum kwa ajili ya Wilaya ya Tunduru na kwa vijana wa Tunduru ili waweze kuhudhuria mafunzo hayo katika vyuo ambavyo vimefufuliwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inayo haja ya kujenga vyuo vipya kwa ajili ya kutoa mafunzo ya watumishi kwenye sekta ya afya, si tu kwa Tunduru lakini ni kwa nchi nzima. Bahati mbaya sana Mpango wa MCH Aider Training ulipoanzishwa mwaka 1973 ulilenga kuzalisha wataalam wa kutoa huduma za uzazi kwa akinamama vijijini kwenye zahanati ambazo zilikuwa zinaanzishwa kwenye mpango ule kutokana na Azimio la Alma-Ata miaka hiyo na Azimio la Afya kwa Wote enzi za miaka ya 70.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango ule umebadilika na hatuwezi kujenga tena chuo kwenye kila mkoa kwa sababu mpango wa kujenga Vyuo vya MCH Serikali iliazimia kujenga chuo kwenye kila mkoa ili kuwazalisha hawa MCH Aider kwa kuwapa kozi ya mwaka mmoja na nusu kwa haraka ili tuwapate kwa wingi zaidi waweze kuwahi kwenda kuokoa maisha ya akinamama wajawazito na watoto. Mpango ule haupo tena na kwa maana hiyo vyuo vya afya sasa hivi haviwezi kuwa ni vyuo vya afya kwa kila mkoa bali vinakuwa ni vyuo vya afya vya kitaifa na utaratibu sasa hivi tunashirikisha pia sekta binafsi ambao nao wanaanzisha vyuo kwa ajili ya kutoa mafunzo ya taaluma mbalimbali za kwenye sekta ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni kwamba Tunduru wapate watumishi kwenye sekta ya afya, hili ni katika mipango ya Serikali ambayo ni endelevu. Kadri ambavyo tutapewa vibali vya kuajiri watumishi kwenye sekta hii ndivyo ambavyo tutaendelea kuajiri watumishi wapya na kuwatawanya si Tunduru peke yake bali ni kwenye wilaya zote hapa nchini.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Mazingira ya barabara ya Mtwara yanafanana kabisa na mazingira ya barabara ya kutoka Masasi – Mangaka – Tunduru - Songea - Mbinga kutokana na machimbo yanayoendelea ya makaa ya mawe pale Ngaka, Mbinga. Makaa yale yanasafirishwa kwa malori makubwa yenye zaidi ya tani 30 kupitia barabara ya Tunduru – Mtwara
- Lindi - Dar es Salaam. Je, Serikali ina mpango gani wa muda mrefu wa kujenga reli ili makaa yale yaweze kusafirishwa kwa njia ya reli kwa sababu magari yale yanahatarisha usalama wa barabara yetu?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara hiyo inasafirisha mzigo mkubwa lakini kila kwenye barabara tumeweka mizani ambayo kazi yake kubwa ni kuhakikisha kwamba magari hayo hayazidishi mzigo ili kuhakikisha kwamba barabara hizo zinadumu kwa muda mrefu. Kwa hiyo, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kuitumia barabara hiyo lakini tutahakikisha kwamba magari hayo hayazidishi mzigo ili kulinda barabara yetu.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Kwa kuwa Serikali imetambua urefu mkubwa uliopo kutoka Ofisi ya Uhamiaji ilipo mpaka Wenje, Makande na Kazamoyo; na kwa kuwa wananchi hawa wa maeneo haya hawana uwezo mkubwa wa kuweza kufuata huduma hii ya uhamiaji zaidi ya kilometa 90 ziliko ofisi; na kwa kuwa Serikali inakosa mapato kutokana na tozo zinazotolewa kwenye hati hizi ya kusafiria; je, kwa nini Serikali haioni umuhimu kwa sasa wa kuweza kutoa huduma hii kwa njia ya mobile ili wananchi hawa waweze kupata huduma hii kwa haraka?
Swali la pili, katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru
Ofisi ya Uhamiaji ina gari ambalo kwa muda mrefu ni bovu halina huduma yoyote katika maeno yote yaliyopo. Je, Serikali ni lini itatoa gari kwa ajili ya kurahisisha huduma hii ili wananchi wale wahudumiwe kwa urahisi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kukosa mapato Serikali si hoja ya kukosekana kituo karibu na mpaka. Kwa sababu kwa mujibu wa Sheria ya Uhamiji namba 54 pamoja na Kanuni zake mwaka 2015, inaeleza kabisa kwamba ili mtu aweze kuvuka kutoka nchi yetu na kwenda nchi nyingine anahitaji kuwa na nyaraka za aina tatu.
Nyaraka hizo aidha ni passport ama hati ya dharula ya kusafiria ama kibali maalum. Kwa hiyo, kwa mwananchi yoyote anahitaji kuvuka lazima apitie katika njia hizo whether ofisi ipo katika mpaka, ofisi ipo katika Wilaya ama ofisi iko katika Mkoa, kwa hiyo hiyo naona ni hoja ambayo siyo sahihi, ninaomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwasisitiza wananchi wake juu ya umuhimu wa kuweza kutii sheria za nchi yetu ili kuepusha uvukaji wa mipaka kiholela na kuikosesha Serikali mapato.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na gari, hili naomba Mheshimiwa Mbunge atuachie tulichukue, kwa sasa hivi hatuna gari za kutosha kwa Uhamiaji, pale ambapo gari zitapatikana tutaangalia na changamoto zingine za maeneo mengine na vipaumbele vilivyopo ili tuzingatie na kuchukua hatua stahiki.
MHE. MPAKATE D. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba niulize swali la nyongeza, kama ifuatavyo. Tatizo la Manyoni linafanana kabisa na mazingira ya tatizo la barabara ya Mtwaro - Pachani - Lusewa - Mchoteka - Nalasi - Mbesa - Tunduru Mjini ambayo iliwekewa alama za ‘X’ zaidi ya miaka saba iliyopita. Je, ni lini ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona Mheshimiwa Mbunge ameanza kutaja maeneo ambayo yako katika Jimbo langu katika kuongeza umuhimu wa swali lake. Naomba tu niseme masuala ya fidia ni ya Kitaifa na wakati ambapo tutaanza kujenga na sasa hivi siwezi kusema tunaanza lini kwa sababu fedha zilizotengwa kwa sasa ni za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa sababu kazi hiyo bado haijakamilika. Naomba kwanza tuikamilishe kazi upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kabla hatujaanza kutafuta fedha za kujenga hiyo barabara.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Makaimu Watendaji wa Vijiji karibu maeneo mengi ya Tanzania hawapewi posho. Je, Serikali haioni haja ya kuwapa posho Makaimu Watendaji wa Vijiji ili waweze kufanya kazi zao vizuri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, anachosema Mheshimiwa Mpakate ni kwamba katika maeneo mbalimbali ya vijiji vyetu watu wengi wanakaimu na kuna maeneo mengine walimu ndiyo walikuwa wanakaimu kama Watendaji wa Vijiji na tumetoa maelekezo katika Kurugenzi zetu kuacha kukaimisha Watendaji wa Vijiji hasa wale walimu kwa sababu wanaondoa nguvu kubwa sana ya ufundishaji. Katika jambo hili, kila Halmashauri tumeipa maelekezo na kila Mkurugenzi anajua ana watu wangapi wanakaimu sasa kupitia own source zao wataangalia utaratibu gani wa kufanya lakini lengo kubwa tunataka katika kila kijiji kazi ziweze kufanyika.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu aliyotoa Naibu Waziri, lakini Jimbo langu la Tunduru Kusini vituo vyake vya afya vimechakaa na vina hali mbaya na vina matatizo lukuki pamoja na uhaba wa wafanyakazi,hakuna gari, wala chumba cha upasuaji.
Swali langu, ni lini Serikali itahakikisha vituo hivi vya afya vinapata watumishi wa kutosha ili viweze kuhudumia wananchi wa Tunduru?
Swali la pili, katika kampeni ya uchaguzi mwaka 2010, Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga kituo cha afya katika Mji wa Nalasi ambao una zaidi ya watu 25,000. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hii ya kujenga kituo cha afya pale Nalasi ili kuweza kuwahudumia wananchi wale ambao wako katika vijiji sita katika Mji ule wa Nalasi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, katika suala zima la kuongeza watumishi, Serikali hivi sasa iko katika mchakato wa kuajiri watumishi mbalimbali. Katika hilo Jimbo la Tunduru tutalipa kipaumbele katika suala zima la mgawo wa watumishi kwa sababu Tunduru ina changamoto kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, eneo la pili nashukuru Mheshimiwa Mpakate alini-accompany vizuri sana wakati nimeenda katika Jimbo lake. Ni kweli watu wasioijua Tunduru, ukitoka barabarani mpaka Jimbo la Mheshimiwa Mpakate kuna changamoto kubwa sana. Ndiyo maana Mheshimiwa Mbunge alipoleta request, tukaamua kipaumbele cha kwanza twende tukamjengee kurekebisha Kituo cha Afya cha Mkasare.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba leo ninavyozungumza tayari tumeshaingiza shilingi milioni 500 kwa ajili ya kituo kile. Katika kituo kile tutajenga jengo la upasuaji, mortuary, wodi ya wazazi na tutafanya ukarabati mwingine halafu tutawawekea vifaa. Vilevile eneo hili la pili tutaliangalia kwa sababu lengo letu kubwa ni wananchi wa Tunduru waweze kupata huduma nzuri ya afya kwa sababu tunafahamu Wilaya ya Tunduru kwa jiografia yake, changamoto ya afya ni kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mpakate kwamba ahadi na maombi yake tulipokuwa katika mkutano, tumeyatekeleza na tunaendelea kuyafanyia kazi kwa kadri iwezekanavyo.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, asante na Mheshimiwa Naibu Waziri asante kwa majibu mazuri. Kwa kuwa kituo hiki kinahudumia zaidi ya Kata Tano, Kata ya Mtina, Lukumbulem Mchesi, Masakata na Tuwemacho.
Je, ni lini sasa Serikali itaona umuhimu wa kuboresha kituo hiki ili kiweze kutoa huduma za upasuaji kwa wakina mama na wajawazito?
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kampeni ya mwaka 2010 Rais wa Awamu ya Nne alitoa ahadi ya kujenga kituo cha afya katika Kata mbili za Nalase ambazo zipo katika Mji mmoja na Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imekuwa inatenga kila mwaka na mpaka sasa imeishia kujenga msingi tu. Je, ni lini Serikali itaona haja ya kutimiza ahadi ile ya Rais wa Awamu ya Nne ili wapate kituo cha afya pale Nalasi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba uniruhusu nimpongeze kwa dhati jinsi ambavyo Mheshimiwa Mpakate anapigania kuhakikisha kwamba wananchi wake wanapata huduma ya afya iliyo bora. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la kwanza ameuliza lini, na unaweza ukaona nia njema ya Serikali jinsi ambavyo inahakikisha huduma ya afya inapatikana na hasa katika ujenzi wa vituo vya afya katika kata husika. Hii ndio maana katika Halmashauri yake tumeanza na hiyo Kata ya kwanza na hiyo kata nyingine kwa kadri pesa itakavyopatikana. Nia njema ya Serikali ni kuhakikisha vituo vya afya vinajengwa katika kata zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili, ni kweli kwamba kuna ahadi iliyotolewa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne kwamba vingejengwa vituo vya afya katika kata mbili alizozitaja na yeye mwenyewe amekiri kwamba katika hizo kata mbili kazi ambayo imefanyika mpaka sasa hivi ni ujenzi wa msingi. Naomba nimuombe Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na wananchi aendelee kuwahimiza ujenzi sio msingi tu, hebu waendelee kujenga mpaka kufikia usawa wa lenta na Serikali itaenda kumalizia ujenzi huo.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naitwa Mheshimiwa Mpakate. Napenda kuuliza swali la nyongeza. Katika maeneo yanayozalisha korosho, mfumo wa stakabadhi ghalani umesaidia sana wakulima kuongeza kipato, lakini moja ya changamoto inayokumbana nayo ni matatizo ya maghala katika vijiji vyetu katika maeneo yote ambayo yanalimwa korosho. Mradi wa MIVARF ungeweza kusaidia kujenga maghala kila Kata angalau ghala moja moja ili kuwapunguzia wakulima gharama ya kusafirishia korosho. Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi wa kujenga angalau ghala moja kila kata katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ili kuwapunguzia wakulima wa Tunduru gharama ya kusafirisha korosho.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika mradi huu jambo kubwa ambalo linaangaliwa ni miundombinu ya masoko, barabara, lakini vile vile na huduma za kifedha kijijini. Katika eneo la miundombinu ya masoko jambo ambalo linaangaliwa pia ni suala la ujenzi wa maghala. Sasa katika programu hii yako maeneo ambayo tayari maghala yamejengwa lakini siwezi kutoa ahadi ya Serikali hapa kwamba tutajenga katika kila Kata.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mikoa ile ambayo inazalisha zao la korosho, kwa mfano, Ruvuma na Mtwara tayari maghala haya yapo, lakini kutoa ahadi ya kwamba tutajenga kila Kata Mheshimiwa Mbunge hii inategemeana pia na bajeti na programu jinsi tulivyojiwekea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanzia katika ile mikoa ambayo tuliona umuhimu huo na ndiyo maana katika Mikoa ya Ruvuma na Mtwara tayari maghala haya yamekwishajengwa. Kwa hiyo, tunaamini kabisa labda baadaye fedha ya ziada ikipatikana hiyo inaweza ikawa sehemu ya consideration, lakini kwa sasa kama Serikali na kupitia programu hiyo hayo ndiyo maeneo hasa ambayo tumeanzia.

WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na ya msingi kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kusema hapa, Waheshimiwa Wabunge waielewe programu hii ya MIVARF, programu hii ni shirikishi, Mheshimiwa Mbunge anaomba ni kwa nini programu hii isiwe inajenga maghala tu. Tunachokifanya sisi Ofisi ya Waziri Mkuu, tunatafuta fedha na tunatengeneza plan ya nini kitafanyika kwenye fedha hiyo. Jukumu la kuamua aina ya mradi utakaotekelezwa kwenye Halmashauri husika ni jukumu la Halmashauri yenyewe na sio jukumu la Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunachokifanya sisi, tunapeleka aina za miradi, Halmashauri kupitia vikao halali vya kikanuni inaamua aina ya miradi katika Halmashari yao. Kwa hiyo, tunachotaka kusema hapa kama fedha hii itapatikana tena kwa sababu ni mradi ambao unaenda kwa phases, kama fedha itapatikana tena, Halmashauri zikishapelekewa miradi hii basi waamue aina ya miradi kwa kuzingatia hali halisi ya mazingira waliyonayo na shughuli wanazozifanya na Ofisi ya Waziri Mkuu tutakubaliana nao lakini sio wajibu wetu kuwaamulia wao nini kikafanyike kwenye mradi katika Halmashauri yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge, katika maeneo ambayo miradi imefanyika wametupa ushirikiano wa kutosha. Nawapongeza sana na kama kuna tatizo lolote tunaomba tuendelee kuwasiliana ili miradi hii itekelezwe kwa viwango vinavyotakiwa huku ikisimamiwa na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Madini lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, naishukuru Serikali kwa kutenga eneo la Mbesa kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Je, Serikali ina mpango gani ya kuwasaidia wale wachimbaji wadogo kwa maana ya kuwawezesha kimtaji na kuwajengea mtambo wa kuchenjulia madini ya shaba ili waweze kusafirisha yakiwa yamechenjuliwa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Halmashauri ya Tunduru kama alivyojibu kwenye swali la msingi ina mabango mengi sana. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka mtaalam wa kufanya valuation ya madini haya ya sapphire ili Halmashauri ipate takwimu sahihi za usafirishaji wa madini? (Makofi). Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wachimbaji wengi wa madini wanahitaji kusaidiwa kimtaji kama alivyosema na hasa kwenye mnyororo mzima wa uongezaji thamani wa madini (value addition). Nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hii Serikali inaifanya kwa umakini kwa sababu tuna historia mbaya hapo nyuma.
Mheshimiwa Spika, wachimbaji wadogo walivyopatiwa mitaji kupitia ruzuku fedha nyingi sana hazikutumika kwa malengo yaliyokuwa yamekusudiwa. Kwa hiyo tunaangalia utaratibu mzuri zaidi kupitia mradi wetu wa SMRP kuona kwamba tunawasaidia wachimbaji wadogo nchini wakiwemo wachimbaji wa Tunduru.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kwamba tupeleke Mtaalam wa valuation Tunduru kwa ajili ya kufanya uthamini wa madini ya vito, tunalichukua jambo hili na tunalifanyia kazi. Vile vile tutaandaa watu baada ya Tume ikishakuwa imekamilisha kazi zake za kuchukua watalaam ili tuweze ku-station mtu mmoja kwa ajili ya kufanya valuation pale Tunduru.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa Serikali imekiri kwamba mgogoro upo katika eneo hili, je, haioni haja ya kuharakisha kufuta eneo hili ili wananchi wale wapate maeneo ya kulima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wananchi wale wana mahitaji makubwa ya ardhi, Serikali haioni haja sasa kupitia mipaka ya eneo lile ili kuongeza eneo la kijiji?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mpakate, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika swali langu la msingi atakubaliana na mimi kwamba hukumu ndiyo imepatikana Februari, 2018 na bado kuna tetesi kwamba huyu ambaye ameshindwa ni kama vile tayari ametuma application kwa ajili ya kukata rufaa. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wale ambao wanahitaji eneo wanapatiwa lakini kwa kufuata sheria. Naomba tuvute subira taratibu zote zifuatwe ili wananchi wapate haki lakini na yule mwingine ambaye alikuwa anamiliki asije akasema kwamba haki yake imeporwa.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri aliyotoa Naibu Waziri, nina maswali mwili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada hizo za kuimarisha maeneo yaliyokuwepo sasa kuna tatizo la Watendaji Kata maeneo mengi katika Jimbo la Tunduru Kusini na Tunduru kwa ujumla walio wengi wanakaimu.
Je, Serikali itapeleka lini watendaji wa kudumu ambao wameajiriwa katika nafasi ya Kata, Vijiji na Katibu Tarafa?
Swali la pili, kwa kuwa majukumu mengi yaliyopo kwa sasa Vijijini yanafanywa na Watendaji wa Vijiji wakishirikiana pamoja na Wenyeviti wa Vijiji; na kwa kuwa Halmashauri nyingi zimeshindwa kutoa posho kwa maana ya asilimia 20 kwenye Vijiji husika.
Je, Serikali haioni haja kwa sasa kutoa posho kwa viongozi wa vijiji kwa maana ya Wenyeviti wa Vijiji ili waweze kufanya majukumu yao vizuri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba katika nchi tunao upungufu mkubwa wa Watendaji wa Kata, kwa kweli siyo Watendaji wa Kata peke yake bali kada nyingi na Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kuhakikisha kwamba tunamaliza au tunapunguza kwa kiasi kikubwa upungufu wa watendaji wetu katika kada mbalimbali. Kwa upande wa Watendaji wa Kata, mwaka jana tuliajiri nafasi chache lakini mwaka huu tunao mpango wa kuajiri Watendaji wa Kata 1,000 nchi nzima. Ninaamini watakapoajiriwa hao watapunguza sana upungufu wa uwepo wa Watendaji Kata katika Kata nyingi hapa nchini ikiwemo Kata za Wilaya ya Tunduru.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili kwamba Watendaji wa Vijiji na Wenyeviti wa Vijiji ndiyo wanaofanya kazi kubwa huko kwenye vijiji vyetu. Napenda nikubaliane sana na Mheshimiwa Daimu Mpakate kwamba ni kweli Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Vitongoji wanafanya kazi kubwa kwa kuwaongoza vizuri watendaji wa vijiji walioko huko kufanya kazi za Serikali kwa niaba ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, amesema kwamba posho hawapati, natoa hapa agizo ambalo lilishatolewa na Serikali tayari kwamba suala la kushusha asilimia 20 ya mapato ya ndani kupeleka kwenye Kata, Vijiji na Vitongoji kwa ajili ya posho za Waheshimiwa Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji, hilo ni suala la kikanuni na kisheria.
Kwa hiyo Wakurugenzi wa Halmashauri ni lazima watekeleze agizo hilo kikamilifu. Pale ambapo tutagundua kwamba mtu hatekelezi kwa sababu tu ya ujeuri au ukaidi itabidi tuchukue hatua za kiutawala na kiutumishi. Kuna wale ambao ni Wakurugenzi wanapata shida kidogo kutokana na makusanyo hafifu, tunawaomba sana Mabaraza ya Madiwani waridhie mapendekezo ya wataalam kuhusu kupanua wigo wa vyanzo vya mapato ya ndani ambavyo vitasaidia kuweza kupatikana fedha ambazo hatimaye zitapelekwa kwa viongozi hawa kwa ajili ya posho.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Tatizo la Handeni linafanana kabisa na tatizo lililopo katika Jimbo la Tunduru Kusini, kwamba wananchi wanapata shida kubwa ya maji, visima vilivyopo havitoshi. Je, ni lini Serikali itachimba visima katika Jimbo la Tunduru Kusini hasa katika Kata ya Mchoteka, Malumba, Tuwemacho, Lukumbule na Mchesi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri kabisa kwamba eneo lake sijafika na baada ya bajeti hii mwezi wa Saba ndio eneo litakalokuwa la kwanza. Pia ninayo taarifa kwamba, utekelezaj wa baadhi ya miradi haukutekelezwa vizuri, haukusimamiwa vizuri na halmashauri ambapo waliuchelewesha mradi na kufanya wananchi wasipate hiyo huduma ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaambatana na Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge hili, ili twende tukatatue changamoto zote zilizoko kule. Kwa sababu, kuanzia sasa utekelezaji wa miradi utasimamiwa moja kwa moja na Wizara yangu mpaka ngazi ya halmashauri. Nimhakikishie kwamba, tutachimba visima vya kutosha, tutatafuta vyanzo vya kutosha ili wananchi wetu waweze kupata huduma ya maji kama walivyoahidiwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri wa TAMISEMI, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; kwa kuwa eneo la Sasawala ndiyo eneo ambalo linategemewa kuanzisha Wilaya Mpya na Makao Makuu yake kuwa Lusewa; je, ni kwa nini Serikali isianzishe Jimbo jipya la Uchaguzi katika eneo hilo la Sasawala?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ilifuata utaratibu wote wa kuanzisha Wilaya mbili, kwa maana Wilaya ya Tunduru Kusini na Tunduru iliyopo sasa na kwa kuwa Halmashauri hiyo iliendesha vikao vya kuanzisha miji midogo miwili, katika Vijiji vya Nalasi na Mchoteka; je, Serikali haioni haja kwa sasa kuanzisha miji midogo katika eneo la Nalasi na Mchoteka? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, majibu yangu katika maswali yake mawili ya nyongeza, hayawezi kutofautiana sana na jibu langu la swali la msingi. Kuhusu kuanzisha Jimbo jipya, utaratibu wake uko tofauti kidogo na utaratibu wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuanzisha Jimbo jipya linahusisha sana Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Tume ya Taifa ya Uchaguzi kabla ya michakato yoyote ya mikutano haijaanza, inatakiwa itangaze nia ya kuanzisha Jimbo jipya katika eneo fulani, baada ya hapo ndiyo vikao viridhie na baadae Mheshimiwa Rais aridhie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili kwamba michakato ya kuanzisha Wilaya mbili kutoka katika Wilaya moja ya Tunduru, kwa maana Tunduru na Tunduru Kusini na miji aliyoitaja kwamba iwe miji midogo, utaratibu wake ni sawasawa na jibu langu kwenye swali la msingi kwamba hii miji midogo ni maeneo mapya ya utawala, kwa maana kwamba ukishakuwa na mji mdogo utakuwa na Halmashauri ya Mji, Mkurugenzi na utakuwa na vikao vinavyohusika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maeneo hayo yote ya utawala yamesitishiwa kuanzishwa hadi hapo tutakapoimarisha zaidi maeneo tuliyonayo sasa hivi. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, mwaka 2014 alipotembelea Jimbo la Tunduru Kusini alitembelea katika Kijiji cha Mbesa ambapo kuna Hospitali ya Mission pale. Hospitali ile inatoa huduma kubwa kuliko Hospitali ya Wilaya na Mheshimiwa Rais aliahidi kuipandisha daraja hospitali ile kuwa Hospitali Teule. Je, ni lini hospitali ile itapewa hadhi ya kuwa Hospitali Teule ili iweze kuendelea kutoa huduma vizuri?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni Hospitali ya Mission ya Mbesa.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimekuwa nikijibu na ambavyo nimejibu leo, ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo ambayo hakuna Hospitali za Wilaya zinakwenda kujengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni azma ya Serikali kwa kushirikiana na Taasisi za Dini na Mashirika mengine pale ambapo sasa hivi hatuna Hospitali Teule, tunatumia zile ambazo zipo ili zifanye kazi kwa muda tu kama Hospitali Teule. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba tunakuwa na hospitali zetu za Serikali na zile za Mashirika ya Dini pale ambapo tutakuwa tumejenga za Serikali wabaki wakiendesha kwao na sisi Serikali tuwe na za kwetu tukifanya kazi kama Serikali. (Makofi)

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka tu kumshauri Mheshimiwa Mpakate, ili hospitali binafsi au ya Shirika la Dini ifanywe kuwa DDH sasa hivi tumeshusha madaraka haya kwenye Halmashauri husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Halmashauri ndiyo itafanya majadiliano na makubaliano na hospitali ile na tumeelekeza kuwe na mkataba wa muda maalum, kwamba Halmashauri ya Tunduru inaamua kuingia makubaliano na hospitali hii ili iwe Hospitali Teule ya Halmashauri na mkishakubaliana ndiyo mnaleta taarifa hizi TAMISEMI na Wizara ya Afya. Kwa hiyo, tutazitambua rasmi sasa kuwa ni Hospitali Teule ya Halmashauri husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, niseme tunatoka kwenye Hospitali za Wilaya, tunakwenda kwenye Hospitali ya Halmashauri. Kwa hiyo, sasa hivi kila Halmashauri itakuwa na Hospitali badala ya kuwa Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama kuna Wilaya zina Halmashauri mbili, zote zinapaswa kuwa na Hospitali ya Halmashauri ambayo ni ngazi ya kwanza ya Hospitali. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa ujenzi wa kituo kile cha afya ulitokana na ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne alipotembelea katika Kata zile mbili za Nalasi zilizoko katika kijiji kimoja na kuagiza kwamba kipatikane Kituo cha Afya; na kwa kuwa Halmashauri imekuwa ikipanga kila mwaka bajeti ya kujenga kituo kile kwa shilingi milioni 80 na shilingi milioni 75, lakini mpaka leo hii bado wameshindwa kujenga kituo kile. Je, Serikali haioni haja sasa ya kutimiza ahadi ya Rais wa Awamu ya Nne kwa kutoa fedha kwa ajili ya kujenga kituo kile cha afya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ina gari moja ambalo ni bovu tangu 2007, mpaka leo ni zaidi ya miaka 11; na kwa kuwa eneo la Tunduru ni kubwa sana, lina Majimbo mawili (Kusini na Kaskazini), je, Serikali haioni umuhimu sasa kutoa gari mbili za wagonjwa upande wa Kaskazini na Kusini ili kuweza kuhudumia wananchi wa Wilaya ya Tunduru ambao eneo lao ni zaidi ya square kilometer 18,000? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mpakate, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza anaulizia Serikali kutoa nguvu ili kumalizia hicho kituo cha afya. Pesa ambayo imepelekwa, shilingi milioni 400 na shilingi milioni 500 inaashiria dhamira njema ya Serikali ya kuhakikisha kwamba vituo vya afya vinajengwa hususan katika Halmashauri ya Tunduru. Halmashauri nayo ina vyanzo vyake, kwa bajeti ambayo inaisha mwaka 2017/2018 wameweza kukusanya wastani wa shilingi bilioni 2.78 na katika bajeti inayokuja, wanatarajia kukusanya shilingi bilioni 3.1, ni wazi kabisa hakika wakiweka kipaumbele cha kumalizia hicho kituo cha afya na kwa sababu wamesaidiwa na Serikali, wanaweza kumaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili kuhusu kupeleka ambulance, ni kweli tangu mwaka 2007 ile gari itakuwa imeshakuwa chakavu kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi. Ni vizuri tukashirikiana na Halmashauri kwa kutumia vyanzo vyao wakati Serikali Kuu tunahangaikia, tukipata, tutakuwa tayari kuwafikiria lakini siyo vizuri nao wakabweteka kwa sababu wana chanzo kizuri na wanakusanya vizuri. Ni vizuri kiasi hicho ambacho kinapatikana wakatenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya kununua ambulance, sidhani kama itaathiri sana Halmashauri. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Serikali, ila nina maswali mawili ya nyongeza. moja ya Kampuni zilizoomba kujenga mtambo wa kuchenjua shaba pale Mbesa ni Metalicca Commodities Corporation ya Marekani ikishirikiana na Minerals Access System Tanzania (MAST) lakini ni muda mrefu toka wameomba na majibu hayatolewi kutokana na kuchelewa kwa mwongozo. Je, Serikali mpaka sasa imefikia wapi kutengeneza mwongozo mzuri ukizingatia shaba ina tabia tofauti na madini mengine ili kuwezesha wawekezaji hao walioomba kupata kibali cha kuweza kujenga mitambo yao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kumekuwa na leseni nyingi sana za utafiti zilizotolewa na Serikali kwa kampuni tofauti mbalimbali kwa muda mrefu na wamekuwa wanakaa kwa muda mrefu bila kuweza kuendeleza maeneo hayo:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwanyang’anya au kufuta leseni zile za utafiti kwa yale makampuni ambayo yamekaa muda mrefu na badala yake maeneo yale kupewa wachimbaji wadogo ili waweze kujikimu na kujitafutia riziki kwa njia ya kuchimba madini katika maeneo hayo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba Serikali imetoa mwongozo na mwongozo wenyewe umetoka tarehe 25, Januari, unaoonesha aina zote za madini yanaweza yakachenjuliwa katika kiwango gani na baada ya kuchenjuliwa yanapewa sasa ruhusa (permit) kwa ajili ya kusafirisha kupeleka nje ya nchi. Kwa hiyo, kwa kila aina ya madini tumetoa mwongozo huo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge afuatilie tu na aone kwamba sasa wale wawekezaji wanaokuja ambapo sisi tumejipanga kutafuta mwekezaji ambaye kweli yuko serious na kampuni zimekuja zaidi 11 wameonesha nia ya kuwekeza kwenye smelter, tunataka tuwawekee kampuni ambazo tuna uhakika nazo kwamba zinaweza kuwekeza kwenye kuchenjua au kuyeyusha zile shaba kwa maana ya smelter.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuhusu hizi leseni za utafiti za makampuni mbalimbali, ni kwamba mpaka sasa hivi, katika meza zetu tunapitia leseni zote ambazo zinaonesha ni leseni zilizotolewa mwaka gani. Tunataka kuangalia status zake zikoje? Tunapitia leseni ambazo zinafanyiwa kazi; lakini zile leseni ambazo ni za PL walipewa makampuni mbalimbali, wengi tumeona wameshikilia maeneo na hawafanyi kazi yoyote. Sasa hivi Wizara yetu tunapitia leseni zote. Kwa kampuni ambayo haifanyi chochote katika leseni ambazo tumewapatia, tunakwenda kuzifuta.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa leseni ambazo tumewapa watu kwa ajili ya uchimbaji kwa maana ya Primary Mining License, Mining License, Special Mining License na zenyewe tunaangalia kwa mujibu wa sheria na taratibu. Kama umekuwa na leseni huwezi kuifanyia kazi, sisi Wizara ya Madini muda siyo mrefu tutawapa default notice na tunakwenda kuzifuta leseni zote.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri kutoka kwa Naibu Waziri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba itatoa mafunzo kwa wafugaji na Maafisa Ugani katika Halmashauri zetu, je, ni lini itatoa mafunzo hayo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ambayo wafugaji wanaongezeka kwa kasi kubwa sana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru imetenga maeneo kwa maana ya vitalu vya wafugaji mbalimbali vinavyofikia 100; na kwa kuwa wakulima wengi wameshapewa maeneo hayo lakini mpaka sasa hawajaenda. Nini kauli ya Serikali kuhusu hawa wafugaji ambao wameshindwa kwenda kwenye maeneo yale ya wafugaji na kuendeleza migogoro na wakulima mbalimbali kwa mifugo yao kula mazao ya wakulima? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mpakate, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ni lini tutakwenda kupeleka mafunzo haya Wilayani Tunduru? Naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba timu yetu iliyoko Kaliua ikitoka huko itakwenda Tunduru na Halmashauri zingine katika nchi yetu kwa ajili ya kutoa elimu hii kwa wafugaji na Maafisa Ugani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili analotaka kujua ni namna gani na tunatoa kauli gani kwa wale waliopata vitalu. Kwanza nataka niwapongeze sana viongozi wote wa kule Wilayani Tunduru kwa kazi kubwa waliyoifanya ya mfano ya kuandaa vitalu wao wenyewe Halmashauri na kuvigawa kwa wafugaji kwa ajili ya kufanya kazi ya ufugaji iliyo na tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kauli ya Serikali ni kama ifuatvyo: Wafugaji wote waliopewa vitalu hivi na wakaacha kuvitumia kwa wakati, tunawapa tahadhari kwamba watanyang’anywa na watapewa wafugaji wengine walio tayari kufanya kazi hii kwa ufanisi.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Katika Vijiji alivyovitaja kuwa vilipata umeme awamu ya kwanza na ya pili vya Azimio, Chiwana, Mkandu na Mbesa umeme ulipita barabarani ndani ya mita 100 kutoka barabara kuu ilikopita nguzo kubwa. Je, ni lini mradi wa kujazilizia mitaa iliyobaki katika Vijiji hivyo vya Azimio, Chwana, Mkandu na Kijiji cha Airport itaanza?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, mwaka 2017 nilipeleka maombi maalum kuongeza vijiji katika Mradi wa REA katika Vijiji vya Tuwemacho, Chemchem, Ligoma, Makoteni, Nasia, Semeni, Mtina, Angalia, Nalasi, Mchoteka, Kitani, Mkolola pamoja na Masakata. Nini kauli ya Serikali kuhusu uwekaji wa awamu ya tatu ya umeme katika Vijiji hivyo?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi la Mheshimiwa Mpakate, lakini vilevile nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Mpakate jinsi anavyofuatilia umeme katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Spika, ni kweli vijiji vingi tuliviweka kwenye round II ya awamu ya tatu inayoendelea, lakini baada ya kuona changamoto kubwa sana katika Jimbo la Tunduru Kusini tulifanya mapitio mapya na vijiji 13 tuliviingiza kwenye round inayoendelea. Kwa hiyo katika utaratibu tunaojenga line kwa sasa kutoka Tunduru Mjini mpaka Msingi umbali wa kilometa 20 tumechukua vijiji vingine 13 vikiwemo vijiji ambavyo anavisema vya Angalia, Semeni ambako Mheshimiwa Mbunge anatoka lakini mpaka Tuwemacho, Chemchem mpaka Chilundundu kwa vijiji vyote hivyo viko kwenye mpango. Pia Wakandarasi kupitia TANESCO sasa wanavifanyia kazi, kwa hiyo nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge pamoja na kumpongeza, vijiji 13 vya nyongeza tayari vimeshaanza kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu nyongeza ya vijiji vya ujazilizi; mradi umeshaanza na utekelezaji wa maeneo ya kujaziliza, maeneo ya vitongoji unaanza mwezi huu utachukua miezi 12, lakini maeneo ya Azimio pamoja na Mbesa ambako tayari umeme upo kwenye Vitongoji 17, tayari pia TANESCO wameanza kuvifanyia kazi.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo lililopo kwenye Tarafa ya Mgeta linafanana kabisa na tatizo lililopo kwenye katika Tarafa ya Namasakata, katika Jimbo la Tunduru Kusini. Barabara ya Chemchem - Ligoma inazaidi ya miaka 10 tangu 2007 haijawahi kutengenezwa.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutengeneza barabara ile ili wananchi waweze kufaidika na Uongozi wa Awamu ya Tano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge ni mashuhuda kwamba tangu tulivyoanzisha chombo chetu kwa maana ya TARURA, wengi wamekuwa wakipongeza ufanisi ambao umetokana na chombo hiki. Kwa hiyo, ni vizuri sasa tusiishi kwa historia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwmaba ni vizuri tukawasiliana na Meneja wa TARURA ili atupe uhalisia katika barabara hii ambayo anaongelea na hiyo miaka 10 ambayo iliahidiwa, hakika kwa Serikali ya Awamu ya Tano tunaahidi na kutekeleza.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Na ninamshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kutembelea katika kijiji cha Mbesa aliahidi kisima kirefu amechimba, amekwenda kuangalia na sasa ameahidi kutoa milioni 200 kwa ajili ya kufanya ule mradi kukamilike vizuri. Vilevile tunawashukuru wafadhili wetu waliojenga visima 72 na wengine wamejenga visima 90 katika Jimbo la Tunduru Kusini. Na nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa mradi wa Mbesa, mradi wa Lukumbuli ambao ulikamika miaka mitatu iliyopita na mradi wa wanalasa ambao ulikamilika zaidi miaka 9 iliyopita haufanyi kazi kutokana na tatizo la kutumia mafuta ya diesel ambayo wananchi wameshindwa kutumia.

Je, Serikali ina mpango gani wa kufunga solar ili wananchi waweze kutumia kwa ukamilivu?

Kwa kuwa katika mradi wa Kijiji cha Mtina uliokamika mwaka moja uliopita umeshindwa kufanya kazi vizuri kutokana na panel solar zilizopo pale kutokutosheleza kusukuma maji kwa ajili ya kupeleka kwa wananchi.

Je, Serikali haioni haja yakuongeza solar panel katika mradi ule ili uweze kuhudumia wananchi wa Mtina ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kiukweli ni miongoni mwa Wabunge wanafanya kazi kubwa sana, na niseme hili ni baba lao kwa eneo la Tunduru Mungu akubariki sana. Lakini kikubwa ninachotaka kukisema watalamu wetu kwa maana ya WARUSA pamoja na wizara hawana kisingizio tena, utekelezaji wa miradi ya maji inategemeana na fedha, tumepata fedha kwa mikoa 17 zaidi ya bilioni 119. Hata katika Jimbo lako la Tunduru tumeshapeleka bilioni 1.3 hizi fedha ni kwa ajili ya kwenda kutatua changamoto za miradi ya maji. Ni mtake mhandishi wa maji wa Tunduru Kusini katika kuhakikisha anatumia changamoto hizi ili kukarabati na wananchi wako waweze kupata huduma ya maji safi na salama na yenye kutosheleza. Ahsante sana.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza Kijiji cha Misiaje kilichopo katika Kata ya Malumba na Kijiji cha Imani na Kaza moyo kilichopo Kata ya Lukumbule havina mawasiliano. Je, ni lini Serikali itajenga minara katika vijiji hivyo ili kuwapa mawasiliano wananchi hao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naompongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu nilivyofanya ziara Mkoani Ruvuma tulikuwa na mawasiliano mazuri sana kulikuwa na changamoto nyingi sana na hasa hasa maeneo haya ambayo yapo mpakani. Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge avute subira kama nilivyosema tunaorodha ndefu sana, aje tu tupitie kwa pamoja halafu tutakapoweka minara hii katika maeneo ambayo yameainishwa tutaangalia tena tuone kama kuna maeneo bado yanachangamoto Serikali itakuwa ipo tayari kuendelea kupunguza tatizo ambalo lipo katika maeneo yetu.

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Katika Jimbo langu la Nkasi Kusini kuna Vijiji sita vya Kisambala, Ng’undwe, Mlalambo, Kasapa na Izinga, mara nyingi nimepeleka orodha Wizarani ili vipatiwe mawasiliano. Je, ni lini Serikali itavipatia mawasiliano vijiji hivi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante sana. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu changamoto zilizoko katika maeneo haya sababu ya jiografia yake, naona ndiyo maana amekaa na jirani yake pale Mheshimiwa Malocha. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo hili ambalo analizungumzia tutaweka msukumo wa kipekee ili tuone changamoto hizi zinakaa vizuri kwa sababu nafahamu kwamba kuna changamoto nyingi sana kwenye eneo lake, kwa hiyo, avute subira. Pia, naomba tuonane na Mheshimiwa Mbunge ili aweze kuona kwenye orodha namna ambavyo tumejipanga ili aweze kwenda kusema kwa wananchi kwamba Serikali hii imejipanga kuhakikisha kweli mawasiliano yanakuwa mawasiliano kwa wote.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Barabara ya Mitema Upinde kwenda Msinji iliyopo upande wa Tunduru ni sehemu ya barabara hiyo ya ulinzi katika upande wa mto Ruvuma. Barabara hiyo ilitolewa madaraja yake wakati wa vita vya Nduli Iddi Amin, na tangu yametolewa madaraja yale mpaka leo bado hayajaweza kurudishwa. Ni lini Serikali itarudisha madaraja yale ili barabara hiyo iweze kupitika kwa urahisi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Barabara ya Tunduru na Masakata Liwanga mpaka Misechela ni barabara ya ulinzi ambayo inaunganisha Msumbiji na Tanzania kupitia katika Kijiji cha Misechela. Je, Serikali haioni haja ya kukichukua kipande hicho kiwe Barabara ya Mkoa kwa sababu mchakato wote wa kufanya barabara hiyo ichukuliwe na TANROADS ulishafanyika kwa ngazi ya Mkoa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, anafuatilia sana hususani mtandao wa barabara katika maeneo yake. Niseme tu kwamba hii barabara ya Itema Msinji ilitolea madaraja. Utaratibu wa kwetu kawaida ni kwamba madaraja yaliyowekwa kwa wakati wa dharura huwa tunayatoa na kuyahifadhi kama asset; pale ambapo itahitajika sasa kuyaweka madaraja haya sehemu zingine tutaenda kuyaweka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge nielekeze tu wataalamu waangalie maeneo haya kama yanastahili kurudishia madaraja haya yaliyotolewa tutafanya utaratibu huo, lakini kama tutakuwa na mahitaji ya kujenga upya maeneo hayo ili kutoa huduma nzuri kwa wananchi pia tutafanya hivyo. Kwa hiyo nielekeze tu TANROADS Mkoa wa Ruvuma waangalie sehemu hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme tu kwamba tunafanya upembuzi yakinifu wa barabara hii kutoka Mtwara – Pachani – Lusewa – Ligusenguse kwenda Nalasi (km 211), na tumetenga fedha za kutosha. Kwa hiyo wakati wa zoezi hili la kutambua changamoto zilizoko katika maeneo haya pia tutatazama kwa macho mawili maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu barabara hii ya Misechela kuwa Barabara ya Mkoa tumeanzisha chombo hiki cha TARURA. Sisi juhudi zetu ni kuhakikisha TARURA inapata fedha za kutosha, lakini kama kutakuwa na mahitaji mahsusi ya kupandisha Barabara hii tutaiangalia kwa nia hiyo ambayo Mheshimiwa Mbunge umeomba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini chanzo cha kituo kile kuchomwa ni mgogoro wa ugomvi wa usalama barabarani kati ya Askari pamoja na bodaboda, hii ndiyo imekuwa tabia ya Askari wasiokuwa wa usalama barabarani kuwakamata bodaboda na kuwapiga bila kuwaeleza makosa yao.

Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na tabia hiyo ya Askari wasiokuwa wa usalama barabarani kuwakamata bodaboda na kuwapiga bila kuwaeleza makosa yao?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Jimbo la Tunduru Kusini limepakana na Msumbiji likiwa na Tarafa tatu. Tarafa ya Namasakata tangu imeundwa haijawahi kuwa na Kituo cha Polisi. Je, Serikali haioni haja sasa ya kupeleka Kituo cha Polisi Misechela na Namasakate yenyewe kwa kituo cha polisi ili kuwahudumia wananchi wa Jimbo la Tunduru Kusini na Tarafa ya Namasakata kwa ujumla.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza hatuwezi kuhalalisha jambo lolote na vitendo vya uchomaji vituo vya Polisi, kwa hiyo hata kama kulikuwa kuna matatizo kati ya bodaboda iwe na Askari wa Usalama barabarani ama awe Askari yeyote basi haihalalishi uchomaji wa kituo cha polisi, hilo moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na hoja yake kwamba kuna watu ambao siyo Askari wa Usalama Barabarani wanawapiga bodaboda. Niliwahi kujibu swali hili siku chache zilizopita na nilieleza kwamba hatujapata taarifa ya kuona Askari Polisi wakipiga bodaboda na kama kuna taarifa hizo basi ni vema tukapatiwa ili tuzifanyie kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Mbunge amekiri kwamba wanaofanya hivyo siyo Askari wa Usalama Barabarani, kwa sababu tunaamini askari wa usalama barabarani wamepata mafunzo na weledi wa kutosha katika kutekeleza majukumu yao, Askari wa aina nyingine yoyote ama watu wa aina nyingine yoyote ambao wanafanya vitendo kama hivyo kama wapo kauli ya Serikali ni kwamba ni kinyume na utaratibu hivyo watumie weledi katika kuhakikisha kwamba wanawakamata wanaovunja sheria ikiwemo hawa waendesha bodaboda.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu maeneo hayo mawili aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge ambapo anataka kujua ni lini tutajenga kituo cha polisi. Jibu ni kwamba katika maeneo yote nchini tutajenga kuanzia kwenye wilaya hata ngazi ya kata ikiwemo maeneo ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge pale ambapo hali ya kifedha itaruhusu.
MHE. DAIMU IDDI MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Jimbo la Tunduru Kusini lina tarafa tatu, Tarafa ya Nalasi, Lukumbule na Sakata na zote zimepakana na Mto Ruvuma, kwa ng’ambo ni Msumbiji, lakini katika Jimbo hilo Kituo cha Polisi kiko kimoja tu kipo kwenye Tarafa ya Nalasi peke yake. Swali la kwanza, je, Serikali haioni ni muhimu sana kwa sasa kukamilisha Kituo cha Polisi Lukumbule ili kiweze kutoa huduma kwa wananchi wa mipakani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Lukumbule ni sehemu ambayo watu wengi wanapitia kwenda na kutoka Msumbiji katika harakati za kufanya biashara. Wananchi wa Msumbiji wakija Tanzania hamna mahali popote wanapopita tunawapokea kiurafiki, lakini sisi Watanzania tukienda Msumbiji tunakamatwa wanapigwa, wananyanyaswa na kunyang’anywa mali zao. Je, Serikali haioni sasa ni muhimu kuharakisha mazungumzo ya kuanzisha Kituo cha Uhamiaji katika kijiji au Makao Makuu ya Tarafa ya Lukumbule?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Tunduru Kusini kulikuwa kuna vituo vitatu, Kituo cha Nalasi, Masuguru na Lukumbile lakini kwa bahati mbaya hiki kituo kimoja kilikuja kikatiwa moto baada ya kutokea machafuko ya wananchi. Hata hivyo, baada ya Serikali kuona umuhimu sasa wa kuwepo kituo ili sasa kuimarisha hali ya ulinzi pale, Serikali ikashusha Waraka kwa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ili sasa watusaidie kujenga kile kituo hili eneo la Lukumbile. Hivi ninavyokwambia tayari kituo kimeshaanza kujengwa na kimeshafikia katika hatua ya lenta. Sasa kikubwa tu nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara tunaenda kutengeneza mazingira sasa ya kuona namna na kupitia umuhimu wa kuwepo kituo hiki ili sasa tuweze kuweka kituo hiki ili wananchi waweze kuishi katika mazingira ya usalama zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa swali la pili, hakuna Serikali yoyote duniani ambayo inapenda wananchi wake wapate tabu; wanyanyaswe, wapigwe, wadhulumiwe. Sasa kitu ambacho nataka nimuahidi Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, kutokana na umuhimu wa suala hili tunakwenda kuona namna ambavyo tutakapotengeneza bajeti yetu hii Wilaya ya Tunduru hasa katika hii sehemu ambayo wanahitaji Kituo hiki cha Uhamiaji tutaipa kipaumbele ili tuone namna ambavyo tunaweza tukapata kituo cha uhamiaji hapa ili wananchi waweze kuepukana na huo usumbufu. Ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tunduru tuna Kiwanda cha Kubangua Korosho kilichojengwa miaka ya 1980 ambacho alipewa mwekezaji kwa muda mrefu na mwekezaji yule alikuwa anaendelea kubangua korosho bila kufikisha lengo la makubaliano na Serikali. Kufikia mwezi Agosti, 2020, kubangua korosho wamesimama kabisa na korosho za Tunduru zinalazimika kununuliwa na kupelekwa nje. Je, kwa nini Serikali haioni haja ya kumnyang’anya mwekezaji yule Kiwanda cha Tunduru cha Korosho na kupewa mtu mwingine ili uzalishaji wa korosho uendelee? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mpakate kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali ni kuhamasisha uwekezaji wa viwanda mbalimbali hapa nchini ikiwemo viwanda vya kubangua korosho. Ni kweli kiwanda cha kubangua korosho cha Tunduru (Tunduru Cashew Factory) ambacho kilinunuliwa na Kampuni ya Micronics ambaye amewekeza katika maeneo mengi, bado kuna changamoto kidogo katika ufanyaji wake wa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema, lengo la Serikali ni kuona tunaendelea kuhamasisha uwekezaji katika viwanda. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mpakate kwamba tutakaa na mwekezaji huyu, tuweze kujadiliana naye, tuone ni changamoto gani ambazo alizipata katika uendeshaji wa kiwanda hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, suala la kumnyang’anya kiwanda litakuwa baada ya kujihakikishia kwamba kweli ameshindwa kutekeleza kuwekeza katika kiwanda hicho halafu tuweze kuona namna bora ya kupata mwekezaji mwingine. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini Lukumbule ni lango kubwa ambalo wafanyabiashara wanapita kupeleka bidhaa zao Msumbiji na wale wanaotoka Msumbiji wanapita Lukumbule kuleta Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imekubali kufanya tathmini na kwa kuwa wananchi wa Tanzania wanaopeleka bidhaa Msumbiji mara nyingi hunyang’anywa mali zao kwa kukosa documents za kusafirisha mizigo yao kwenda Msumbiji.

Je, Serikali haioni haja ya haraka kufanya tathmini hiyo ili kuhakikisha wananchi wetu wa Tanzania wanaoenda Msumbiji hawanyang’anywi mali zao mara kwa mara? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Jimbo la Tunduru Kusini lina miji mitano mikubwa; Nalasi, Mchoteka, Malumba, Lukumbule pamoja na Misechela ambayo ina wafanyabiashara wengi na miji hiyo iko zaidi ya kilometa 80 kutoka ilipo Ofisi ya TRA Tunduru Mjini.

Je, Serikali haioni haja ya kupeleka agencies katika maeneo hayo ili wafanyabiashara wale waweze kulipa kodi zao wakiwa katika maeneo yao ya biashara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeona umuhimu wa ushauri wa Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo, ushauri tumeupokea na tutaufanyia kazi kwa mujibu wa sheria na miongozo iliyowekwa na pale tutakapopata majibu basi tutamfikishia majibu kwa haraka sana. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri kwa kufanikisha kufanya upembuzi yakinifu na kutengeneza zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ile kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Serikali imesema inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kiwango cha lami barabara hiyo na wananchi walio katika maeneo au waathirika wa barabara hiyo bado wanakiu ya kupata fidia yao kwa ajili ya maeneo hayo. Je, ni lini Serikali itaanza kutoa fidia kwa waathirika wa barabara hiyo kutoka Mtwara Pachani, Lingusenguse, Nallasi mpaka Tunduru mjini?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali imetenga shilingi bilioni 2.2 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida kwenye barabara hiyo; na kwa kuwa madaraja manne kwenye barabara hiyo yamezolewa na mvua, Mto Sasawala, Lingusenguse, Mbesa pamoja na Lukumbule. Je, Serikali haioni haja ya haraka kupeleka hizo shilingi bilioni 2.2 ili kukamilisha kurekebisha madaraja hayo yaliyoharibika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la fidia litaanza pale ambapo barabara itaanza kujengwa. Awamu ya kwanza ilikuwa ni kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambao kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi umeshakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa nini fedha ya matengenezo iliyotengwa kwa kuwa madaraja yameshazolewa isipelekwe huko. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge wa Tunduru kwamba mpaka leo asubuhi madaraja yote ya kutokea Tunduru daraja la kwanza la Mbesa, Mchoteka sasa yanaweza yakapitika na hivi leo wameanza daraja kubwa la Mto Sasawala na tunaweka ndani ya muda mfupi daraja hili litaanza kupitika ili kuweza kuunganisha Tunduru na eneo la Mtwara Pachani. Ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Tunduru Kusini lina matatizo makubwa sana ya umeme hasa vijiji vyake zaidi ya asilimia 70 bado havijapata umeme. Je, ni lini Mradi wa REA Awamu ya Tatu B utaanza katika Jimbo la Tunduru Kusini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Tunduru kwa kusema ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili inazo jumla ya Lot 37 za kupelekeza umeme katika maeneo yetu ya vijiji. Katika hizo Lot 37, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote kwamba tayari maeneo yote yaliyotakiwa kupelekewa umeme ambayo hayakuwa na umeme yamechukuliwa katika hizo Lot 37 na tayari tumeshazindua kuanzia Machi 15, pale Manonga na tunaendelea kuwatuma wakandarasi kuripoti katika maeneo yetu husika.

Mheshimiwa Natibu Spika, nikumbushie tu, agizo ambalo tumeshalitoa kwamba wakandarasi wote wanaenda kupeleka umeme katika maeneo hayo pamoja na maeneo mengine watakayopiga ripoti. Wapige ripoti kwa Waheshimiwa Wabunge ili kuwaonesha maeneo ambayo yanahitaji umeme kwa haraka na kwa ufasaha zaidi ili kuweza kushirikiana kwa pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya hivyo, itapunguza yale maswali ambayo tunaulizwa kwa sababu Waheshimiwa Wabunge watakuwa wamepata uhakika kwamba katika eneo lake mkandarasi anafika. Kwa hiyo, niwasisitize wakandarasi wafike katika maeneo ya Waheshimiwa Wabunge na kutoa taarifa ili Waheshimiwa Wabunge wapate hiyo taarifa na sasa kazi iweze kuendelea vizuri.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Moja ya changamoto inayosababisha Tunduru kukatika umeme mara kwa mara ni ubovu wa miundombinu ya kutoka Namtumbo kuja Tunduru na kutoka Tunduru kwenda Nanyumbu mpaka Masasi.

Je, Serikali haioni sasa ni muhimu kuweka nguzo za zege kutoka Namtumbo mpaka Tunduru na kutoka Tunduru mpaka Masasi ili kudhibiti uharibifu wa nguzo za umeme unaotokea mara kwa mara na kufanya umeme kukatika katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Daimu na muuliza swali mwenyewe Mheshimiwa Hassan, kwa nia ya kuendelea kuhakikisha kwamba miundombinu inaendelea kuboreshwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mkoa wa Ruvuma kwa mwaka huu wa fedha umetengewa shilingi 1,200,000,000 kwa ajili ya marekebisho ya miundombinu mbalimbali ya umeme ikiwemo nguzo, transfoma na waya. Lakini kabla sijasema kuhusiana na uwepo wa nguzo za zege kwanza niwaombe Waheshimiwa Wabunge wote watusaidie katika kuhakikisha miundombinu yetu ya umeme inalindwa kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, huko huko Tunduru jana kuamkia leo na upo Mwenge, lakini wananchi wamechoma miundombinu ya umeme na kusababisha umeme kukatika katika maeneo hayo. Na ni kweli kwamba tunatoka kwenye nguzo za miti kwenda kwenye nguzo za zege kwenye maeneo yenye matatizo korofi. Maeneo ambayo kuna wadudu waharibifu kama mchwa, maeneo ambayo ni oevu yana majimaji, lakini pia kwenye maeneo ambayo ni ya kwenye hifadhi ambako hakuwezi kufikika mara kwa mara na wanyama waharibifu wanakuwa wanaiharibu ile miti yetu ya kushikilia umeme.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye maeneo ambayo hayana matatizo hayo tunawaomba Waheshimiwa Wabunge, waendelee kuwa mstari wa mbele kuhamasisha ulinzi wa miundombinu yetu ili isiharibiwe.

Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Daimu kwamba maeneo ambayo nimeyataja yanayohitaji nguzo za zege yatapelekewa nguzo za zege na tayari tumeshaanza. Wazabuni wanaotengeneza nguzo za zege tumeshawapata na kwenye baadhi ya maeneo kama mnavyoona Waheshimiwa Wabunge, tayari tumeshazipeleka na tutahakikisha miundombinu inaboreshwa zaidi. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa kuwa Jimbo la Tunduru Kusini lina vituo vya afya vitatu kimojawapo ni kituo cha Afya Utina ambacho kinahudumia kata nne kata ya Lukumbule, Mchesi, Utina yenyewe, Tuwemacho, pamoja na Msicheo.

Je, ni lini Serikali itaboresha Kituo cha Afya Utina?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kituo cha Afya cha Utina ni miongoni mwa vituo ambavyo Serikali imeendelea kuvifanyia tathmini na kuona namna bora zaidi ya kukiongezea miundombinu ya majengo, lakini pia vifaa tiba kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba tayari Serikali inafanya tathmini lakini pia kutafuta fedha kwa ajili ya kukiboresha Kituo cha Afya cha Utina, ahsante sana.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru Serikali kwa kupeleka mkandarasi amesharipoti tarehe 11 Mwezi huu. Kwa kuwa Serikali inaenda kutekeleza mradi huu katika vijiji vyote vya Jimbo la Tunduru Kusini na Tunduru kwa ujumla na tatizo la Umeme Tunduru kukatika katika ni jambo la kawaida.

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga substation pale Tunduru Mjini ili kutoa huduma hii kwa vijiji vyote kwa sawasawa? (Makofi)

Swali la pili, kwa kuwa REA imeanza kutekelezwa katika vijiji vyote vilivyopo Jimbo la Tunduru Kusini pamoja na vijiji vya Azimio, Semeni, Angalia Je, Serikali sasa haioni kuna haja sasa ya kuweza kutoa tamko la kuweza kuisaidia TANESCO kwa asilimia 100 ili waweze kutoka huduma hiyo kwa shilingi 27,000?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Daimu Mpakate Mbunge wa Tunduru kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza kuhusu hoja ya kupeleka substation tuichukue tukaifanyie mkakati na upembuzi yakinifu na kuona kama ujenzi wa substation peke yake ndio utasaidia kutokatika kwa umeme katika maeneo hayo au njia nyingine inaweza ikaboresha kwa sababu pengine kama umeme unaofika ni mkubwa wa kutosha maana yake tunatakiwa kuboresha miundombinu badala ya kujenga substation. Tunalichukua tutaenda kulifanyia kazi na tutaweza kufikisha huduma nzuri kabisa kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili tayari Serikali imeshatoa maagizo na maelekezo ya kuunganisha umeme kwa wateja wote kwa shilingi 27,000, katika bajeti iliyowasilishwa na Wizara ya Nishati kwa niaba ya Serikali ilisemwa hapa wazi na Mheshimiwa Waziri kwamba maeneo yote itakuwa ni shilingi 27,000 isipokuwa Dar es Salaam City Centre. Tayari wenzetu wa TANESCO wametoa circular kwa Meneja wa Wilaya na wa Mikoa kuhakikisha kwamba agizo hilo linatekelezwa na tunafahamu linaendelea kutekelezwa, lakini pale Waheshimiwa Wabunge ambapo bado mnaona changamoto basi tuwasiliane ili tuweze kuchukua hatua kwa sababu mambo mengine yanahitaji kusimamiwa kwa ajili ya manufaa ya wananchi. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Changamoto iliyopo kwenye barabara ya Liwale -Nangurukuru inafanana kabisa na changamoto iliyopo kwenye barabara ya Mtwara Pachani, Lusewa kwenda Nalasi mpaka Tunduru Mjini. Mwaka, 2015 aliyekuwa mgombea mwenza ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, alitoa ahadi barabara ile kutengenezwa kwa kiwango cha lami. Nashukuru Serikali imekamilisha upembuzi yakinifu mwaka jana 2020: Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hii ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI – (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mtwara - Pachani hadi Nalasi ni barabara ambayo tayari imeshafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Kwa hiyo, kinachosubiriwa sasa hivi ni Serikali kutafuta fedha kwa ajili ya kuijenga hii barabara. Kwa hiyo, tayari taratibu zimeshaanza, tunachosubiri tu ni fedha ipatikane. Katika Awamu hii ya miaka mitano, kama fedha itapatikana, basi itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kutekeleza hiyo ahadi ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri wa Nishati na ni kweli mkandarasi yupo site anaendelea na kazi.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa vijiji 11 vya awali vilivyopata umeme awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu umeme ule ulipita barabarani bila kupita mitaa yote katika vijiji hivyo kama ville ilivyo Azimio, Chiwana, Mbesa pale Tuwemacho na Ligoma. Ni lini sasa Serikali itaona haja ya kupeleka kuanza mradi wa ujazilizi katika vijiji hivyo ili vitongoji vyote vilivyopo kwenye vijiji hivyo vipate umeme.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba plan na maelekezo ya Serikali ni kuhakikisha kwamba vijiji vyote 12,268 vinapata umeme ifikapo Desemba mwakani na hilo sisi kwa kutekeleza maelekezo ya Serikali tunaiahidi umma kwamba tutakamilisha maelekezo hayo kwa kadiri ilivyoelekezwa na ilivyoazimiwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la vitongoji, upelekaji wa umeme kwenye eneo la vitongoji ni zoezi endelevu ambapo wenzetu wa TANESCO wanaendelea kupeleka umeme katika maeneo hayo lakini pia vipo vitongoji vingi ambavyo vitaguswa na Mradi huu wa REA III round two. Lakini specifically upo mradi wa vitongoji ambao ni wa densification yaani umeme jazilizi ambao tunatarajia uanze mwenzi wa 10 mwishoni ambao utahusika pia katika kupeleka umeme kwenye vitongoji alivyovitaja katika Jimbo la Tunduru Kusini. Nashukuru.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Serikali imesema inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa barabara ile kwa kiwango cha lami na kuna maeneo ambayo hivi sasa magari hayapiti yanakaa siku mbili, tatu kufika mwisho wa safari, kama maeneo ya kutoka Mkandu mpaka Mbesa, eneo la Lusewa mpaka kufika Ligunga na eneo la Majiwe mpaka Milonji ambayo yamekuwa ni maeneo korofi kwa muda mrefu. Je, Serikali haioni sasa haja ya kuweka lami laini katika maeneo hayo ili magari yaweze kupita kwa urahisi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa barabara hii haijawahi kukanyagwa na Naibu Waziri wala Waziri wa Ujenzi, naomba anipe commitment ya yeye na mimi kufuatana kwenda kukagua barabara hiyo ili aone adha wanayoipata wananchi katika maeneo hayo. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, maeneo aliyoyataja ya Lusewa, Mbesa, Malonji nadhani ni jana magari mengi yamekwama. Jana tulitoa maelekezo kwa Mameneja wote wa TARURA Mkoa, naamini watakuwa wananisikia na watakuwa pengine wako site eneo hilo ili waweze kukwamua magari hayo.

Mheshimiwa Spika, hii barabara sasa hivi mwaka huu tumeitengeneza kwa changarawe barabara yote ya kilometa hizi 320. Kwa hiyo nimhakikishie Mbunge kwamba Mhandisi wa Mkoa ninavyosema hivi yuko site kukwamua hayo magari yaliyokwama.

Mheshimiwa Spika, swali la pili; naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na naamini pamoja na Mheshimiwa wa Namtumbo, kwa sababu barabara hii ndiyo barabara muhimu sana kwa watu wa Tunduru na Namtumbo niombe baada ya hapa tupange ziara tutembelee hiyo barabara. Ahsante. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ni kweli barabara hii kwa muda mrefu imekuwa na shida na haipitiki, ni barabara ambayo ni ya ulinzi, inaunganisha kati ya Msumbiji na Tanzania. Kwa mazingira yaliyoko Msumbiji, barabara hii ni muhimu itengenezwe kwa sababu kipindi cha kifuko haiptiki kabisa: -

Je, ni lini sasa Waziri wa TAMISEMI, au Naibu wake wataenda katika eneo hili kuangalia hii kero ambayo inapatikana katika eneo lile? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Kwa kuwa barabara hii iliweza kupitishwa kwenye michakato mbalimbali kabla TARURA haijaanzishwa; na baada ya TARURA kuanzishwa, barabara hii ikabaki kwenye TARURA peke yake; na maombi yale yalifika mpaka kwenye RCC: Je, lini Serikali itaangalia ma-file yake kuona mapendekezo yale ili yaweze kupitishwa kwa haraka kunusuru hali iliyoko pale Msumbiji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Daimu Idd Mpakate, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tuko tayari Kwenda katika jimbo lake muda wowote na tuko flexible kwa sababu huo ndiyo wajibu wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kwamba, jukumu la kupandisha hadhi hizi barabara liko chini ya TANROADS kupitia Wizara ya Ujenzi. Kwa hiyo, nafikiri kwa sababu Serikali tunafanya kazi kwa pamoja, tutaendelea kushirikiana kuhakikisha kwamba jambo hili linafanyika kwa haraka. Ahsante sana.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Jimbo la Tunduru Kusini lina Tarafa Tatu. Tarafa ya Namasakata haina Kituo cha Polisi na ndiyo iliyopo mpakani na Msumbiji.

Je, ni lini Serikali itapeleka Kituo cha Polisi katika Tarafa hii ya Namasakata?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mpakate, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ninamshauri Mheshimiwa Mbunge ikiwa Tarafa hii haina kituo cha kwanza tutafute ardhi. Ardhi ikishapatikana tuipime tukabidhi Jeshi la Polisi hatimaye tuweze kuingiza eneo hilo kwenye mpango wetu wa ujenzi wa Kituo cha Polisi. Kwa vile anasema kiko mpakani inahitaji kwa kweli ulinzi eneo hilo na tutakupatia kipaumbele iwapo upatikanaji wa ardhi utatekelezwa mapema. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Swali la kwanza; kwa kuwa, Waziri amesema tayari mipango ya kufufua Kambi ile inaendelea na sasa hivi hali ya usalama upande wa kusini hasa upande wa Msumbiji sio nzuri katika Vijiji vya Wenje, Lukala, Nasomba, Makandi na Kazamoyo watu hawa wanaishi kwa kutokuwa na amani. Je, haoni sasa ni muhimu kuweka angalau makambi ya temporary ili kurejesha amani ya wananchi wa vijiji hivyo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa vijiji hivyo kwa sasa ulinzi umekabidhiwa kwa mgambo ambao wako 30 katika vijiji hivyo na wanapewa sh.50,000/= kwa mwezi na Halmashauri.

Je, Serikali haioni sasa ni muhimu kuwalipa mshahara mgambo wale ili waweze kuendelea kulinda mipaka?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nijibu maswali ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua hali ilivyo katika mipaka yetu yote ikiwa ni pamoja na mpaka wa Kusini na tayari hatua mbalimbali zimechukuliwa kuimarisha ulinzi, hatukai tu tukisubiri kambi. Kambi itakuja lakini hatua za kuimarisha ulinzi katika mipaka hiyo zinaendelea na ulinzi umeimarishwa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu malipo, kwa mgambo kuwa na mishahara upo utaratibu unaotumika kulipa Jeshi la Mgambo na utaratibu huo utaendelea kutumika. Ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Tunduru Kusini lina shule za sekondari kumi, katika hizo zote hamna high school na Shule ya Sekondari Mchoteka ina maabara tatu, ina mabweni mawili na moja linajengwa, ina vyoo 20, kumi na moja vya kike na tisa vya kiume, halafu ina madarasa 16; kati ya hayo manne hayatumiki. Kigezo kilichobaki ni bweni pamoja na jiko.

Kwa nini sasa Serikali kwa kutilia umuhimu wa kutokuwa na high school katika Jimbo langu isitilie mkazo wa kupewa fedha kwa haraka ili Jimbo la Tunduru Kusini lipate high school?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimthibitishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba moja tumepokea ombi lako, kwa sababu kwa kuizingatia hiyo shule itatupunguzia gharama za kwenda kuanzisha high school mpya, kwa hiyo tumelipokea na tutalifanyia kazi ili sasa tulete shule ya Kidato cha Tano na Sita katika Jimbo lako, ahsante sana.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Suala la makaa ya mawe kutoka Ngaka kupita Songea – Tunduru mpaka Mtwara kuna baadhi ya madereva wamekuwa na tabia ya kusambaza yale makaa ya mawe barabarani, aidha kwa magari kuanguka au kwa kutokufunika. Hii imekuwa ni hatari sana kwa wananchi wanaokaa karibu na barabara hizi. Je, Serikali iatoa kauli gani kwa hawa madereva wanaofanya tabia hii ya kusambaza makaa ya mawe barabarani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daimu Mpakate, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hii ni changamoto, tumeiona na mara kadhaa tumekuwa tukikaa na wafanyabiashara hawa pamoja na vyombo vingine au taasisi nyingine zinazohusika ili kuwaeleza hawa wafanyabiashara kwamba wasiyatawanye ama wasiyaweke makaa ya mawe haya katika maeneo tofauti, bali wawe na vituo maalum vya kuweka ili kuepusha athari zinazojitokeza zikiwemo hizo za uchafuzi wa mazingira.

Mheshimiwa Spika, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea kutoa taaluma na kuwaambia wananchi wasiyasambaze haya mwisho wa siku yakawa yanaleta athari. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Jimbo la Tunduru Kusini kuna miradi miwili ambayo ilifanyiwa kazi na imechukua hela nyingi zaidi ya shilingi bilioni tatu kutengenezwa pamoja na barabara, lakini miradi ile haifanyi kazi. Je, Serikali inampango gani wa kuweza kukamilisha miradi ile, mradi wa Mishaji pamoja na mradi wa Madaba, uliopo Azimio?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Daimu Mpakate, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya awali, tumejipanga kuhakikisha miradi yote hii inafanya kazi. Hivyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba katika uhakiki ambao tutaufanya, tutapitia pamoja na maeneo yake ili kuona miradi hii changamoto yake ni nini; na mwisho wa siku tuweze kuikwamua na wananchi waweze kufanya kilimo cha umwagiliaji.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa Wilaya ya Tunduru ilianzishwa mwaka 1905 na mpaka leo bado ni kubwa kulinganisha na wilaya zingine; na kwa kuwa vikao vyote vinavyohusu kugawa halmashauri ile limefanyika mpaka ngazi ya mkoa; na kwa kuwa Tunduru Kusini ndilo jimbo ambalo linaathirika sana kwa kutokuwa na halmashauri. Je, Serikali itaanzisha lini halmashauri ya Wilaya ya Tunduru Kusini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA
MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Idd Mpakate, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, kwamba halmashauri ambazo zimeshamaliza mchakato, bado Serikali inaendelea kupitia vigezo na kutathimini, ili kuona kama haja ya kutangaza kwa wakati uliopo ama tuendelee kuboresha zile halmashauri ambazo ni changa. Kwa hiyo jambo hilo lipo katika ofisi zetu na wasubiri wakati ambapo itakuwa tayari kufanya hivyo, tutafanya hivyo.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante, Jimbo la Tunduru Kusini lina maboma saba yako katika hatua mbalimbali katika Vijiji vya Mkapunda, Chuwala, Ukandu, Nazya pamoja na Lupanji; je, Serikali ina mpango gani sasa wa kupeleka fedha kumalizia maboma hayo ya zahanati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Iddi Mpakate, Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kusini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tumekwisha elekeza na nirudie kuwakumbusha Wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha wanaweka vipaumbele vya ujenzi na ukamilishaji wa maboma ya zahanati katika maeneo yenye uhitaji mkubwa. Kwa hiyo, maboma haya saba ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja, Ofisi ya Rais TAMISEMI tutachukua lakini tutafanya mawasiliano na Wakurugenzi ili tuone yapi tuanze nayo kwa awamu lakini tutaendelea kutenga fedha kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kituo cha Afya Mtina kilichopo katika Jimbo la Tunduru Kusini kilitegewa shilingi milioni 250 katika bajeti hii ambayo ipo 2022/2023. Je, ni lini Serikali itapeleka pesa hii kwa ajili ya kuboresha huduma ya Mama na Watoto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Tunduru Kusini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie kwamba kwa sababu ipo kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha, naamini kwamba ifikapo Juni 30, fedha zitakuwa zimepelekwa kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu hiyo. Ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa kuwa wananchi wako tayari kukamilisha majengo ya madarasa ambayo Serikali imetoa shilingi milioni 260 na uwezekano upo ndani ya miezi miwili majengo haya yakakamilika.

Je, anihakikishie Naibu Waziri mwezi Julai ujasili na uanzwaji wa kidato cha tano utakuwa tayari?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Shule ya Sekondari Mchoteka ina walimu watano tu wa sayansi.

Je, kukamilisha kidato cha tano na sita Serikali itapeleka walimu wa sayansi zaidi ili watoto wale wawe na ufaulu mzuri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, shule hii kama nilivyokwishakusema kwenye majibu yangu ya msingi imeombewa usajili kutoka Wizara ya Elimu. Na kuona kama itakuwa tayari mwezi wa saba kuweza kupokea wanafunzi tutalifanyia kazi hili kwa haraka sisi Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu kuweza kupata usajili na kuona kama itaweza kupokea wanafunzi mwezi huu wa saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili la ukosefu wa walimu wa sayansi. Bunge lako tukufu ni mashahidi kwamba Serikali imetoa ajira zaidi ya 21,000 ambapo katika hizo zipo za walimu na zipo za Idara ya Afya. Hivyo basi katika ajira hizi tutaiwekeza kipaumbele Shule hii ya Sekondari ya Mchoteka.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Jengo la Tunduru Kusini, Kata ya Marumba, ni moja ya kata ya kimkakati kwa ajili ya kujenga kituo cha afya, ambayo ina umbali wa kilometa 80 kutoka Makao Makuu ya Halmashauri: Je, ni lini Serikali itapeleka pesa kwa ajili ya kujenga kituo cha afya katika Kata ya Marumba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilisema hapo awali, tayari Serikali imetafuta fedha kwa ajili ya kujenga vituo vya afya vya kimkakati katika maeneo mbalimbali nchini. Tutaangalia pia Kata ya Marumba kama ipo imetengewa bajeti kwenye mwaka wa fedha unaokuja, kama haijatengewa, basi tutaitengea fedha kwenye ule mwaka mwingine wa fedha wa 2024/2025.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Katika barabara ya Tunduru – Nalasi, kipande cha kutoka Chiwana mpaka Mbesa kina matatizo ya kupitika wakati wa mvua: Je, ni lini Serikali itaweka lami nyepesi kwenye kipande hicho wakati wanasubiri fedha za kujenga kipande hicho?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi na barabara hii niliitembelea, Waziri alishaahidi na mimi nilipita. Maeneo yote korofi tumeyaainisha na tumetoa maelekezo kwa Meneja wa Mkoa wa Ruvuma kwamba barabara hii yenye urefu wa kilometa 300 maeneo yote ayafanyie kazi kwa maana ya kuainisha maeneo korofi na pia kujenga kwa kiwango cha zege ama lami maeneo yote korofi ili barabara hii iweze kupitika kwa mwaka mzima, ikiwa ni pamoja na eneo alilolitaja Mheshimiwa Mbunge, ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naishukuru Serikali kwa majibu mazuri sana, na tunaomba waendelee kumalizia hiyo Mahakama. Nina swali moja tu la nyongeza. Kwa kuwa maeneo ya Lukumbule na Masakata na Nalasi yamekosa kabisa huduma za kimahakama: Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kuweka Mobile Court katika tarafa hizi ili ziweze kupata huduma za kimahakama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tunashukuru kwa pongezi na shukrani hizo. Kwa sasa Mhimili wa Mahakama una magari mawili (mobile courts) ambazo zinafanya kazi Mkoa wa Dar es Salaam na Mkoa wa Mwanza. Katika bajeti yetu tunategemea kuongeza hizi mobile courts sita Mikoa ya Kagera, Tanga, Dodoma, Arusha, Mara na Morogoro. Tunafanya hivi kwa maeneo ambapo population ni kubwa. Tunatamani tungefika kwa kila Kata, lakini mwenendo wetu wa huu mpango wa Mahakama ni kujenga Mahakama hizo kwa sababu hizi mobile courts ni gharama kuziendesha na wakati mwingine management ya mahabusu na mambo mengine yanaweza yakawa yanaleta gharama kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Kata zake hizi ambazo amezitaja, tutaingiza katika mwaka ujao wa fedha, na tutafikia Kata zake na tutazijenga kwenye maeneo ambapo uhitaji upo, ahsante.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, je, ni lini Serikali itapeleka minara katika Kijiji cha Misyaje, Kata ya Malumba?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kwanza kabisa nipokee changamoto hii ya mawasiliano kutoka kwenye hiyo kata, lakini nimwombe Mheshimiwa Mbunge kwa sababu sina taarifa za kina kuhusu kata hiyo ili tuweze kuitazama na kwenda kuchukua hatua stahiki, nakushukuru sana.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante; je, ni lini Serikali itapeleka pesa kwa ajili ya kukamilisha miradi ya umwagiliaji katika Kijiji cha Misyaje na Madaba kilichopo Jimbo la Tunduru Kusini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ni mkakati wa Serikali kuhakikisha tunakamilisha skimu zote za umwagiliaji ili wananchi wafanye kilimo cha umwagiliaji. Nitakaa na Mheshimiwa Mbunge kuangalia skimu alizozitaja kama hazipo kwenya mpango wa mwaka wa fedha unaokuja basi tuziingize kwenye mpango ili wananchi waweze kushiriki kwenye kilimo cha umwagialiaji.

MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kituo cha Afya Mtina kilitengewa milioni 250 katika bajeti tunayoendelea nayo ili kujenga jengo la akinamama na watoto. Je, ni lini pesa hiyo itaenda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nitakaa na Mheshimiwa Mpakate ili kuona katika mwaka wa fedha huu 2023/2024 tunaoenda kuanza kutekeleza kama Kituo hiki cha Afya cha Mtina kimetengewa fedha na kama hakijatengewa fedha, basi tutaangalia ni namna gani tunaweza tukakiweka katika mipango ya mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa kuwa miradi mingi ya Halmashauri inasimamiwa na walimu wakuu, waganga pamoja na walimu wakuu shule za msingi.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapa semina hao walimu wakuu baada ya sheria hiyo mpya kupitishwa upya?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mpakate kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali taratibu, kanuni na miongozo itatoka mara tu baada ya Bunge lako Tukufu kupitisha Sheria hii. Naomba Mheshimiwa Mbunge awe na subra itakapopita Sheria hii basi hayo yote anayoyatarajia yatapatikana.
MHE. DAIMU I. MPAKATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali; kwa kuwa Kituo cha Afya Mtina kinahudumia zaidi ya kata nne na changamoto ya kituo kile ni pamoja na kutokuwa na huduma ya upasuaji.

Je, Naibu Waziri anaweza kunihakikishia baada ya Bunge hili atembelee kituo kile ili aweze kuona changamoto za wananchi wa kata ile?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa Jimbo la Tunduru Kusini lina kata 15, vituo vya afya vinavyopatikana mpaka sasa ni vitatu ambavyo vyote havituoi huduma ya upasuaji kutokana na tatizo la kutokuwa na vifaa vya upasuaji, lakini kwa kuwa tunahitaji vituo vya afya vingi.

Je, Serikali ina mpango gani ya kuongeza angalau vituo vya afya viwili katika Kata ya Malumba na Kata ya Msechela ambazo zipo mpakani mwa Msumbuji ili kutoa huduma kwa wananchi wale ambao wanahudumiwa kutoka mbali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Daimu Iddi Mpakate, Mbunge wa Jumbo la Tunduru Kusini kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Kituo cha Afya cha Mtina, Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la upasuaji. Kwa hiyo, katika mwaka ujao wa fedha tuna uhakika sasa changamoto hiyo tutakuwa tumeondokana nayo, lakini nipo tayari kuambatana na Mheshimiwa Mpakate kwenda kutembelea kituo cha afya hiki na vituo vingine katika Jimbo lake ili kuona utoaji wa huduma lakini pia kuweka mipango ya pamoja kuhakikisha tunaboresha huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na ujenzi wa vituo vya afya katika kata zake 15 tunachukua kata zake mbili na bahati njema Waheshimiwa Wabunge walileta kata tatu za kipaumbele na Serikali inapitia huko kuandaa mpango wa utekelezaji wa ujenzi wa vituo vya afya kwenye kata tatu za kipaumbele kwa kila jimbo. Kwa hiyo, tutafanya hivyo katika jimbo hili la Tunduru Kusini. Ahsante.