MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu yasiyoridhisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za vipimo ni kubwa mno kwa wananchi wetu maskini ambao tunawawakilisha. Nafikiri ni vizuri Waziri akatamka ni lini ataruhusu watu binafsi kuweka x-ray na vipimo vingine kwenye hospitali za binafsi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii x-ray ziko madukani, Waziri yuko tayari kwenda kufunga hospitali ya mtu lakini hayuko tayari kuamrisha x-ray zilizoko madukani ziende kwenye hospitali za Serikali ili zihudumie wananchi wetu wanaokufa kila siku.
Kama kwa nchi nzima suala hili haliwezekani, namuomba Mheshimiwa Naibu Waziri lifanyiwe majaribio kwenye Halmashauri ya Mji wa Kahama ambapo hospitali hiyo inahudumia zaidi ya Halmashauri 15 ikiwemo na Halmashauri ya kwake mwenyewe. Naomba majibu.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru kaka yangu Mheshimiwa Jumanne Kibera Kishimba kwa swali lake la nyongeza na nimpongeze kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya kuwahudumia wananchi wa jimbo lake la Kahama Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ubunifu anaouzungumzia wa kutumia watu binafsi kutekeleza miradi mbalimbali ya kufunga vifaa na vifaa tiba vya kutolea huduma za afya hususani vya uchuguzi wa magonjwa kama x-ray na ultra-sound kwenye hospitali za Serikali ni ubunifu ambao tunaukubali. Anasema ni lini mimi nitaruhusu kwenye Wizara yetu; napenda kumtaarifu tu kwamba Serikali tayari inaruhusu ubia wa sekta binafsi na Serikali (Public Private Partnership – PPP) na ina sheria mahususi ambayo ilitungwa na Bunge hili miaka kadhaa iliyopita kwa hivyo siyo jambo jipya; sema modality ya mikataba hii iweje na nani afunge lini na mkataba na nani na kwa sababu zipi ndizo taratibu ambazo tunazitazama siku hata siku na tunazitazama kwa kesi kadri zinavyokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo kama Halmashauri ya Kahama Mjini inapenda kufanya mikataba ya namna hiyo Mheshimiwa Mbunge azungumze na wataalam kwenye Halmashauri yake, wafuate taratibu za ndani ya Serikali za kuingia mikataba ya PPP ili waweze kupata vibali kutoka Hazina, Wizara ya Afya na TAMISEMI waweze kutekeleza mipango hiyo ila ni jambo ambalo tunalikubali.