Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Stanslaus Haroon Nyongo (13 total)

MHE. HASSAN E. MASALA aliuliza:-
• Je, Serikali kupitia REA III ina mpango gani wa kusambaza umeme katika kata zilizobaki Wilayani Nachingwea?
• Je, nini mpango wa Serikali kutatua tatizo la kukatikakatika kwa umeme Wilayani Nachingwea?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu, nimshukuru pia Mheshimiwa Rais kwa imani yake na nikushukuru wewe pia Mheshimiwa Spika kwa uongozi wako.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hassan Elias Masala, Mbunge wa Nachingwea, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa vijiji vyote visivyo na umeme vinapata umeme kupitia mradi kabambe wa kupeleka umeme vijijini Awamu ya Tatu (REA III) unaotegemewa kukamilika mwaka 2020/2021. Mradi huu utajumuisha vipengele vitatu vya Densification, Grid Extension na Off-Grid Renewables. Mkoa wa Lindi chini ya Mradi wa Uendelezaji wa Gridi mzunguko wa Kwanza unatekelezwa kwa muda wa miezi 24 na Kampuni ya State Grid & Technical Works Ltd. Katika Wilaya ya Nachingwea Mpango wa Awamu ya Tatu utavipatia umeme vijiji 30. Kazi za utekelezaji wa mradi zilianza mwezi Julai, 2017 na zitakamilika Juni 30, 2019. Aidha, vijiji vilivyobakia vitapatiwa umeme katika mzunguko wa pili wa REA III utakaoanza Aprili, 2019 hadi Disemba 2021.
Mheshimiwa Spika, kazi ya kupeleka umeme mzunguko wa kwanza itajumuisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 380, ufungaji wa transfoma 180, ujenzi wa njia za msongo wa kilovoti 0.4 zenye urefu wa kilometa 360 na uunganishaji wa wateja wapatao 5,710 katika Mkoa mzima wa Lindi. Aidha, kwa Wilaya ya Nachingwea jumla ya wateja wapatao 1,200 wataunganishwa. Mkandarasi anaendelea na upimaji wa njia za umeme ambapo amefikia asilimia 30 na kazi za upimaji zitakamilika mwishoni mwa Novemba, 2017. Gharama za miradi hiyo ni jumla ya shilingi 24,636,112,764.82 na dola za Kimarekani 5,657,471.30 pamoja na VAT.
(b) Mheshimiwa Spika, umeme unaotumika katika Wilaya ya Nachingwe unatoka katika kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia kilichopo Mtwara Mjini ambapo njia ya kusafirisha umeme kutoka Mtwara ina urefu wa kilometa 210 na pia hugawa umeme katika maeneo ya Mkoa wa Mtwara kabla ya kufika Nchingwea. Hivyo, pakitokea tatizo lolote mwanzoni au katikati ya njia basi, umeme hukatika katika maeneo mengi ya Mkoa wa Lindi, ikiwemo Nachingwea. Ili kukabiliana na tatizo hilo Serikali kupitia TANESCO imejenga njia mpya ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 kutoka Mtwara hadi Mnazi Mmoja, Lindi na kujenga kituo cha kupoza umeme chenye uwezo wa MVA 20, 132/33kV ambapo ujenzi wake umekamilika na mradi mzima umegharimu jumla ya shilingi bilioni 16.
Mheshimiwa Spika, umeme utapozwa katika msongo wa kilovoti 33 na kusafirishwa kwenda katika Wilaya za Ruangwa, Nachingwea na badae Liwale. Ujenzi wa njia ya msongo wa kilovoti 33 ya Wilaya ya Ruangwa unategemewa kuanza Januari, 2018 baada ya kupatikana kwa fedha za utekelezaji. Pamoja na ujenzi huo, ukarabati wa miundombinu iliyopo unaendelea ili kuboresha mfumo mzima wa usambazaji katika Wilaya ya nachingwea na Lindi kwa ujumla.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO aliuliza:-
Kuna taarifa zilizotolewa na Wizara ya Nishati na Madini za kugunduliwa kwa gesi ya Hellium yenye ujazo wa takribani futi bilioni 54 za ujazo nchini.
Je, Serikali imejiandaaje kimkakati kuhusu ugunduzi huo na uchimbaji wa gesi hiyo hasa ikizingatiwa kuwa mataifa makubwa kama Marekani yalishatangaza kukosekana kwa gesi hiyo ifikapo 2030?
NAIBU WAZIRI WA MADINI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Tauhida Cassian Gallos Nyimbo, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Kampuni ya Hellium One Ltd. imegundua kiasi cha gesi ya Hellium yenye ujazo wa cubic feet 54 billions katika maeneo ya Ziwa Rukwa. Ugunduzi huo ulitokana na uchunguzi wa sampuli tazo za Mavujia yaani gas seeps ya gesi ya Hellium katika maeneo hayo kiasi ambacho kinakadiriwa kuwa kikubwa zaidi ya mara sita ya mahitaji ya dunia kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya Hellium One Ltd. imegundua madini ya hellium kupitia Kampuni zake tanzu za Gogota Tanzania Ltd., Njozi Tanzania Ltd. na Stahamili Tanzania Ltd. zinazomiliki leseni z utafutaji wa gesi ya hellium katika Mkoa wa Rukwa ikiwemo maeneo ya Ziwa Rukwa. Kampuni hizi zilipewa leseni za utafutaji wa hellium katika maeneo mbalimbali kuanzia mwaka 2015. Shughuli za utafutaji wa kina wa gesi ya helium unaendelea kwa kukusanya taarifa zaidi za kijiolojia, kijiokemia, kijiofizikia na 2D Seismic Survey ili zitumike kwa ajili ya uchorongaji wa visima vya utafiti yaani exploratoty wells. Kazi ya uchorongaji ikikamilika itawezesha kuhakiki kiasi halisi cha gesi ya hellium kilichopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchimbaji wa gesi ya hellium utaanza mara baada ya kazi ya utafiti wa kina, upembuzi yakinifu na tathmini ya athari za mazingira, kukamilika kwa leseni ya uchumbaji wa gesi hiyo kutolewa. Matokeo ya gesi hizo ndiyo yatakayoonyesha kama kiasi cha gesi kilichopo kinaweza kuchimbwa kibiashara kwa kipindi gani na taifa litanufaikaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kufundisha wataalam stahiki yaani wajiolojia, wahandisi wa migodi na wachumi wa madini kusudi wawe na ujuzi wa kutosha na hadi sasa Serikali ina jumla ya wataalam 454 wenye fani za mafuta na gesi katika viwango mbalimbali na elimu. Pia kuna wanafunzi 137 walipo katika mafunzo ya mafuta na gesi katika ngazi za shahada za uzamivu katika vyuo mbalimbali nje ya nchi na wanafunzi 455 katika ngazi ya diploma na shahada ya kwanza ndani ya nchi.
MHE. KISWAGA B. DESTERY (K.n.y. MHE. NJALU D. SILANGA) aliuliza:-
Maeneo mengi yamefanyiwa utafiti na kampuni za kigeni kwa muda mrefu bila kufikia hatua ya kufungua migodi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuzifutia leseni kampuni hizo na kuwapatia wachimbaji wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza kabisa na mimi kwa sababu nimesimama hapa kwa mara yangu ya kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii kufika hapa leo. Vilevile nimshukuru pia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kuniamini na kuniweka katika Wizara hii mpya. Vilevile nimshukuru Mheshimiwa Spika, Wabunge wote na Wajumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara kwa malezi yao mazuri na kunifikisha hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga lililoulizwa na Mheshimiwa Kiswaga ambaye ni Mbunge wa Magu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na kanuni zake inatambua umiliki wa leseni za utafutaji mkubwa wa madini na uchimbaji mdogo wa madini inayotolewa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kama ilivyorekebishwa mwaka 2017, leseni za utafutaji wa madini aina ya metali, viwandani na nishati (makaa ya mawe na urani) hutolewa kwa muda wa miaka minne ya awali na kuhuishwa kwa mara ya kwanza kwa miaka mitatu na mara ya pili kwa miaka miwili. Hivyo leseni ya utafutaji mkubwa wa madini ya aina hizo hubaki hai kwa kipindi cha miaka tisa. Aidha, leseni za utafutaji wa madini na vito na ujenzi hutolewa kwa mwaka mmoja na haziwezi kuhuishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iwapo mmiliki wa leseni atashindwa kuendesha shughuli za utafutaji wa madini, leseni yake hufutwa kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na Marekebisho yake ya mwaka 2017. Aidha, katika kipindi cha mwaka 2014/2015 hadi 2016/2017 jumla ya leseni 423 za utafutaji wa madini zilifutwa ambapo mwaka 2014/ 2015 zilifutwa leseni 2013, mwaka 2015/2016 zilifutwa leseni 155 na mwaka 2016/2017 zilifutwa leseni 65.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la leseni lililofutwa hutathminiwa na Wakala wa Jiolojia yaani Geological Survey of Tanzania (GST) kwa ajili ya kutengwa kwa wachimbaji wadogo endapo litaonekana kuwa na mashapo yenye tija. Katika kipindi cha mwaka 2014/2015 hadi 2016/2017 jumla ya maeneo 19 yenye ukubwa wa jumla takriban hekta 69,652.88 yalitengwa kwa wachimbaji wadogo katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Serikali itaendelea kufuatilia na kujadiliana na kampuni zilizomiliki leseni za utafutaji wa madini ili kuona uwezekano wa kuachia baadhi ya maeneo yanayofaa kwa uchimbaji mdogo.
MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:-
Madini ya Tanzanite yanachimbwa Mkoani Manyara katika Wilaya ya Simanjiro, lakini madini hayo huchakatwa na kuuzwa Mkoani Arusha hali inayosababisha wananchi wa Manyara kutofaidika kiuchumi.
(a) Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu kujenga kiwanda cha kuchakata madini hayo Mkoani Manyara?
(b) Je, ni kiasi gani cha fedha kimeshachangiwa na madini haya katika mapato ya Mkoa wa Manyara?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Manyara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha kuwa madini ya Tanzanite yananufaisha wananchi wa Simanjiro, Serikali imetoa tamko la kutaka shughuli zote zinazohusu madini ya Tanzanite ikiwemo uendeshaji wa minada na ujenzi wa viwanda vya uchakataji wa madini hayo zifanyike katika eneo la Mererani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali imetenga eneo katika Kijiji cha Naisinyai, Mererani ili kuwa eneo maalum kiuchumi kwa ajili uanzishaji wa viwanda vya uchakataji (Economic Processing Zone - EPZ) ili kuvutia uwekezaji katika eneo hilo kwa kutoa vivutio mbalimbali kwa wawekezaji. Hivyo Wizara itaendelea kuhamasisha wawekezaji wa viwanda vya kuchakata madini ya Tanzanite kujenga viwanda katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza hilo kwa vitendo, Wizara ya Madini imepata kiwanja katika eneo la EPZ ili kujenga Kituo cha Umahiri (Center of Excellence), sehemu ya jengo hilo itakuwa na taasisi mbalimbali zinazosimamia shughuli za madini ili kutoa huduma kwa wafanyabiashara wa madini ya Tanzanite kwa haraka (One Stop Centre). Pia baadhi ya ofisi katika jengo hilo litatumika kutoa huduma za uthaminishaji wa madini na kuendesha minada.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2017 madini ya Tanzanite yamechangia kiasi cha shilingi 140,954,229.37 kutokana na kodi ya tozo ya huduma (Service Levy) inayotozwa mujibu wa Sheria ya Ushuru wa Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, manufaa mengine yaliyopatikana kwa Wilaya ni pamoja na fursa za ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kutokana na kuwepo kwa migodi katika eneo husika na huduma za jamii zinazotolewa na mgodi ambapo mgodi umetoa ajira kwa wafanyakazi 674 ambapo asilimia 93 ya walioajiriwa ni Watanzania na asilimia saba iliyobaki ni wageni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya waajiriwa hao, asilimia 21.81 ya wafanyakazi wameajiriwa katika vijiji kutoka vijiji vinavyozunguka mgodi vya Naisinyai na Mererani. Katika kipindi hicho mgodi wa Tanzanite One umefanikiwa kuchangia jumla ya dola za Kimarekani 429,664 katika utoaji wa huduma mbalimbali za kijamii ukilenga kuimarisha mahusiano na jamii zinazozunguka mgodi pamoja na kuchangia maendeleo ya Taifa kwa ujumla. Huduma hizi zinahusisha masuala ya elimu, afya, lishe, ujenzi na sanaa.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE aliuliza:-
Wananchi wa Msalala hususan wakazi wa Bulyanhulu wamefanyiwa dhuluma nyingi sana na Mgodi wa ACACIA, Bulyanhulu ikiwemo kuondolewa kwenye maeneo yao bila fidia mwaka 1996 na kwa wale wanaopata kazi mgodini kufukuzwa kazi bila kufuata utaratibu, kupata madhara makubwa ya kiafya na hata kusababishiwa vifo; na Serikali ya Awamu ya Tano imesimama kidete kutetea wananchi na kuwaepushia dhuluma hizi.
Je, ni hatua gani imefikiwa katika mazungumzo kati ya ACACIA na Serikali kuhusu ulipaji fidia kutokana na dhuluma hizo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa madini, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Ezekiel Magolyo Maige, Mbunge wa Msalala, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Bulyanhulu unamilikiwa na Kampuni ya ACACIA na unaendelea shughuli zake za uchimbaji madini tangu mwaka 2000. Kabla ya kuanzishwa kwa mgodi huo fidia stahiki kwa ardhi ya wananchi iliyotwaliwa ililipwa. Kwa sasa mgodi hauna madai yoyote ya wananchi wa Bulyanhulu yatokanayo na fidia ya ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2007 wafanyakazi wapatao 1,331 wa Mgodi wa Bulyanhulu walifanya mgomo kinyume cha sheria hivyo wakaachishwa kazi. Hata hivyo wafanyakazi 643 walirudishwa kazini. Tarehe 6 Novemba, 2007 wafanyakazi 658 waliogoma kurudi kazini walifungua kesi mahakamani na kuomba kufanyiwa uchunguzi wa kiafya ili kubaini hali za afya zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uchunguzi huo wafanyakazi 78 walionekana kuwa na matatizo ya kiafya. Kwa sasa kampuni ya ACACIA inajadiliana na Serikali kupitia OSHA na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kuhusiana na madai yao ya matibabu na fidia kulingana na sheria za nchi. Ili kupunguza magonjwa yanayohusiana na kazi za migodini Wizara inaendelea kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ili kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa kuzingatia usalama, afya mahali pa kazi, pamoja na utunzaji wa mazingira.
MHE. VICKY P. KAMATA aliuliza:-
Kampuni kubwa za uchimbaji madini kama vile GGM, Buzwagi Gold Mine na North Mara Gold Mine licha ya kulipa kodi kwa Serikali kuu pia zinawajibika kuhudumia jamii inayozunguka migodi kwa utaratibu wa uwajibikaji kwa jamii kwa kutoa fedha au kufadhili miradi ya kijamii au maendeleo:-
• Je, kwa mwaka 2017 Kampuni hizo kila moja ilitoa fedha kiasi gani?
• Je, hadi kufikia Januari mwaka 2018, Kampuni hizo zimetoa kiasi gani.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini, napenda nijibu swali la Mheshimiwa Vicky Kamata, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 105(1) na (2) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017, kinamtaka mmiliki wa leseni kuandaa mpango wa mwaka wa utaratibu wa uwajibikaji kwa jamii (corporate social responsibility). Mpango huo lazima ukubalike kwa pamoja na Mamlaka ya Serikali ya Mtaa husika kwa kushauriana na Halmashauri ulipo mgodi kwa kuzingatia vipaumbele vya Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, maandalizi ya mpango huo yanapaswa kumshirikisha Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kabla ya kuidhinishwa na Baraza la Madiwani la Halmashauri husika. Aidha, kila Halmashauri ulipo mgodi inapaswa kuandaa mwongozo wa uwajibikaji kwa jamii kwenye Halmashauri yao, kusimamia utekelezaji wake na kutoa elimu kwa wananchi wa Wilaya husika juu ya huduma hizo.
Mheshimiwa Spika, kwa takwimu zilizopo, migodi ya Geita Gold Mine, Buzwagi Gold Mine na North Mara Gold Mine imekuwa inatekeleza jukumu hili la kutoa huduma za jamii zinazozunguka migodi hiyo. Huduma ambazo zimekuwa zinatolewa ni kwa maeneo ya afya, elimu, maji, mazingira, ujasiriamali, miundombinu na jamii kama vile barabara, majengo na masuala ya sanaa na utamaduni.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2017, mgodi wa North Mara ulitumia dola za Marekani 1,837,495, sawa na takribani shilingi bilioni 4.25 kwenye huduma za jamii. Mgodi wa Buzwagi ulitumia dola za Kimarekani 595,658.47, sawa na shilingi bilioni 1.38 na mgodi wa Geita Gold Mine, dola za Kimarekani 6,358,542.24 sawa na shilingi bilioni 14.45.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kumekuwa na changamoto za gharama halisi za miradi hiyo. Kunaonekana ziko juu sana ukilinganisha na gharama halisi ya kile kilichotekelezwa. Marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 yaliyofanyika yanataka sasa Halmashauri zihusishwe katika kufanya maamuzi kuhusiana na mipango ya uwajibikaji kwa jamii.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2018, migodi hiyo mitatu imekwishaandaa mpango kazi wa utekelezaji wa uwajibikaji kwa jamii. Maandalizi ya mpango yameshirikisha Serikali za Mitaa kama sheria inayowataka na kuwasilishwa kwa Halmashauri husika kwa ajili ya utekelezaji. Hadi kufikia Juni, 2018 mgodi wa Geita Gold Mine unatarajiwa kutumia kiasi cha dola za Kimarekani 1,932,142 na mgodi wa North Mara jumla ya dola za Kimarekani 333,111.39 na mgodi wa Buzwagi jumla ya Dola za Kimarekani 224,215.24
MHE. FRANK G. MWAKAJOKA aliuliza:-
Je, ni kwa nini Serikali haiwapatii wananchi wa Mji wa Tunduma ruzuku ya asilimia 0.3 kama ilivyo kwa wananchi wanaoishi katika maeneo yenye kuchimbwa madini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Frank George Mwakajoka, Mbunge wa Tunduma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa ya mwaka 1982 yaani Local Government Finance Act, Cap. 290, kifungu cha 6(1)(u), Halmashauri ulipo mgodi hutoza asilimia 0.3 ya mapato yote kabla ya kuondoa gharama za uzalishaji wa madini kama ushuru wa huduma yaani service levy. Aidha, kabla ya kuanza kutoza ushuru huo, Halmashauri husika inatakiwa kutunga Sheria Ndogo ya Halmashauri yaani District Council By-Laws ambazo zinaidhinishwa na Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa yaani TAMISEMI kwa mujibu wa kifungu cha 153(1) cha Mamlaka ya Serikali Mitaa yaani Local Government District Authority Act, Cap. 287.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, eneo la Halmashauri ya Tunduma hakuna leseni ya uchimbaji iliyotolewa. Hivyo, tunaendelea kuhimiza wawekezaji wa ndani na nje ili wawekeze katika utafiti na hatimaye kuanza kuchimba madini katika maeneo mbalimbali yenye madini nchini na Tunduma ikiwa mojawapo. Ahsante.
MHE. MARTHA M. MLATA – (K.n.y. MHE. JESCA D. KISHOA) aliuliza:-
Je, Serikali imejipangaje kuwatengea eneo la kuchimba madini katika Mgodi wa Shanta ulioko Mang’onyi (Singida), wachimbaji wadogo wadogo wa Wilaya ya Ikungi na Mkoa wa Singida wanaotegemea kupata kipato kwa shughuli hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nitoe pole kwa Mheshimiwa Jesca David Kishoa kwa ajali mbaya aliyoipata juzi na kupata maumivu, basi tumwombee kwa Mwenyezi Mungu ili aweze kupata unafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hivyo, naomba sasa kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini, nijibu swali la Mheshimiwa Jesca David Kishoa, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya tarehe 10, Novemba, 2004 na tarehe 1, Aprili, 2005, wachimbaji wadogo wa madini wa Wilaya ya Ikungi waliwasilisha maombi 34 ya leseni ya uchimbaji mdogo wa madini ya dhahabu katika eneo la Mang’onyi. Hata hivyo, maombi hayo yalikataliwa kutokana na kuombwa juu ya leseni ya utafutaji mkubwa wa madini yenye namba PL 2792/2004 ya Kampuni ya Shanta.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kifungu cha 14(1) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017, kinaeleza kuwa mwombaji ambaye maombi yake yalipokelewa kwanza ndiye anayestahili kupewa leseni na hairuhusiwi leseni kutolewa juu ya leseni nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa mujibu wa kifungu cha 7(2) cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na marekebisho yake ya mamlaka ya utoaji wa leseni, kwa ridhaa ya mmiliki wa leseni, inaweza kutoa leseni zaidi ya moja katika eneo moja la uchimbaji madini iwapo leseni inayoombwa ni ya madini tofauti na leseni iliyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo mwezi Mei, 2014, Kampuni ya Shanta ilifanya mazungumzo na Kampuni ya Mang’onyi Company Limited ili iachie baadhi ya maeneo ya leseni inayomiliki na kukubali kutoa leseni tatu za uchimbaji wa madini ya dhahabu kwa wachimbaji wadogo wa Vijiji vya Sambaru, Mang’onyi na Mlumbi vilivyopo katika Kata ya Mang’onyi, Wilayani Ikungi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji hivyo vitatu vinazunguka leseni ya Mgodi wa Shanta. Pia kampuni ya Shanta imetoa kwa kikundi cha Aminika Gold Mining Co-operative Society Limited chenye wanachama 193 ambao ni moja ya wanufaika wa leseni hizo, kiasi cha dola za Marekani 25,000 kama fedha za mtaji wa kuendesha shughuli za uchimbani zilitolewa. Aidha, kampuni hiyo imepanga kutoa elimu ya usalama migodini ikifuatiwa na elimu ya uchimbaji ukiwemo uchorongaji wa miamba ili kuwezesha kikundi hicho kufanya shughuli za uchimbaji wenye tija.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya mazungumzo na kampuni ya uchimbaji wa madini Shanta na kampuni hiyo imekubali kuachia eneo lote la leseni yake ya utafutaji mkubwa wa madini ya dhahabu iliyoko Muhintili Wilaya Ikungi yenye ukubwa takribani kilometa za mraba 71.3 ili itengwe kwa ajili ya uchimbaji mdogo wa madini. Kiasi cha leseni 714 zinatarajiwa kutolea kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa leseni 92 zimekwishatolewa kwa vikundi vya watu binafsi hivyo Wizara inawahimiza wachimbaji wadogo wa madini kuwasilisha maombi yao ili waweze kupatiwa maeneo ya uchimbaji. Hata hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Madini itaendelea kutenga maeneo zaidi kwa ajili ya wachimbaji wadogo kwa madini kadri yanavyoweza kupatikana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipekee niishukuru Taifa kubwa Simba Sports Club kwa ushindi walioupata, ahsante sana. (Makofi)
MHE. MHE. AJALI R. AKBAR aliuliza:-
Madini aina ya Coltan yamegundulika katika Wilaya za Ruangwa, Masasi na Newala, lakini Wizara ya Madini imeweka beacon katika Kijiji cha Nandimba, Kata ya Chilagala.
(a) Je, ni utaratibu gani umetumika kuweka beacon katika Wilaya nyingine?
(b) Je, Serikali haioni kupora rasilimali ya wilaya nyingine kunaweza kusababisha migogoro?
(c) Je, ni lini Serikali itamaliza mgogoro huo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rashid Akbar Ajali, Mbunge wa Jimbo la Newala Vijijini lenye sehemu (a), (b)na (c) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Ruangwa, Masasi na Newala hakuna uthibitisho wa uwepo wa madini aina ya Coltan yaliyogunduliwa. Madini yaliyogunduliwa katika Wilaya hizo ni aina ya Graphite yaani madini ya Kinywe ambapo baadhi ya Kampuni zimepewa leseni za utafiti na uchimbaji wa madini hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 na Kanuni zake, mmiliki wa leseni anatakiwa kuweka alama (beacon) zinazoonesha mipaka ya leseni yake ili jamii inayozunguka maeneo hayo ijue mwisho wa leseni husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, beacon zilizopo katika Kijiji cha Namlimba ziliwekwa na Kamuni ya Natural Resources Limited wakati wa ukusanyaji wa taarifa muhimu. Kampuni hii ya Natural Resources Limited ina umiliki wa leseni ya utafiti wa madini ya Graphite yenye nambari PL 10644/2015 ambayo mipaka yake inaingia kwenye Wilaya za Masasi na Newala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haina lengo la kupora rasilimali ya Wilaya nyingine bali lengo lake ni kuhakikisha kuwa rasilimali madini zinazopatikana katika eneo husika, zinanufaisha wananchi wake na taifa kwa ujumla. Hadi sasa kampuni hiyo inaendelea na shughuli za utafiti wa madini ya graphite (kinywe). Pindi itakapogundulika uwepo wa mashapo ya kutosha, taratibu za kuvuna rasilimali hiyo kwa manufaa ya Watanzania wakiwemo wananchi wa Wilaya ya Newala zitafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa Kampuni ya Natural Resources Limited haina mgogoro wowote na wananchi wa maeneo hayo. Namwomba Mheshimiwa Rashid Akbar Ajali kama kuna tatizo la mipaka ya kiutawala katika Wilaya za Masasi na Newala suala hilo liwasilishwe kwenye Wizara husika kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.
MHE. LOLESIA J. BUKWIMBA (K.n.y. MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA) aliuliza:-
Katika kutekeleza Mkataba wa Corporate Social Responsibility (CSR), Mgodi wa GGM unatumia bei za manunuzi kutoka nchi ya Afrika Kusini, mfano bei ya bati moja ni shilingi 81,000 na bei ya mfuko wa saruji ni shilingi 48,000.
Je, kwa nini Serikali isiziite pande hizi mbili, Mgodi wa GGM na Halmashauri ili iweze kumaliza mgogoro huo na kuweka utaratibu mzuri?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita Vijijini kama lilivyoulizwa na Mheshimiwa Bukwimba, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza matakwa ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017 kifungu cha 105, Halmashauri ya Mji wa Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita pamoja na Mgodi wa Dhahabu wa GGM zimeandaa Mpango wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii wa mwaka 2018 (Corporate Social Responsibility Plan, 2018).
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuandaa mpango huo uliokuwa shirikishi, GGM iliwasilisha bei ya bati la geji 28 kwa kipimo cha mita za mraba ambapo bei ya mita moja ya mraba ilikuwa ni shilingi 81,000 na bei ya mfuko wa saruji ilikuwa ni shilingi 48,000 kwa mfuko mmoja. Aidha, baada ya bei hizo zilizopendekezwa na mgodi kuonekana kuwa ni kubwa, pande zote mbili ambazo ni Halmashauri ya Mji wa Geita na Halmashauri ya Wilaya ya Geita pamoja na Kampuni ya GGM walikaa na kufanya majadiliano ya pamoja na kukubaliana bei zilizopendekezwa na GGM zirekebishwe kwa kuweka bei ya bati moja na siyo bei ya bati kwa mita za mraba ambapo bati moja geji 28 ilikubalika kuwa shilingi 27,000 na mfuko mmoja wa saruji kuwa shilingi 18,000.
MHE. JANET Z. MBENE aliuliza:-
Wilaya ya Ileje imejaliwa kuwa na rasilimali ya makaa ya mawe ya Kiwira na Kabulo na STAMICO imekaririwa kuanza rasmi kuuza makaa hayo kwa kasi ili kukidhi mahitaji ya viwanda vya saruji na kukuza pato la Taifa, aidha, STAMICO ilianza uzalishaji wa majaribio ya makaa ya mawe katika Mgodi wa Kabulo tarehe 30/04/2017.
(a) Je, Mgodi wa Kabulo utaendelea kuchimba baada ya majaribio hayo na ni nani anayefanya uchimbaji huo?
(b) Je, kuna makubaliano gani na Wilaya ya Ileje juu ya mrahaba na uchumi kwa wana Ileje?
(c) Je, ni lini Mgodi wa Kiwira utaanza kufanya kazi na ni nini hasa kinachokwamisha?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Madini, naomba sasa nijibu swali la mama yangu, Mheshimiwa Janet Zebedayo Mbene, Mbunge wa Jimbo la Ileje, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) lilianzishwa mwaka 1972 likiwa na jukumu la kushiriki na kusimamia maslahi ya Serikali katika sekta ya madini pamoja na rasilimali ya madini. Aidha, mwaka 2005 Mgodi wa Kiwira ulibinafsishwa kwa kampuni binafsi ya wazawa ya Tan Power Resources Ltd. (TPR) kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa umeme na kufikia megawati 200. Mnamo tarehe 30, Juni, 2014 Serikali iliikabidhi STAMICO Mgodi wa Kiwira kutokana na mbia mwenza kukosa mtaji wa kuendesha mgodi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, STAMICO ilianza uchimbaji wa majaribio katika leseni yake ya makaa ya mawe ya Kabulo mnamo mwezi Aprili, 2017 ambapo katika kazi hiyo jumla ya tani 8,674 za makaa ya mawe zilichimbwa. Baada ya kukamilisha majaribio ya awali STAMICO imeanza mchakato wa kumpata mkandarasi atakayefanya uchimbaji. Lengo ni mkandarasi huyo aanze kazi ya uchimbaji utakaozingatia taratibu zote za uchimbaji, mazingira na usalama mgodini katikati ya mwaka huu wa fedha yani 2018/ 2019.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, STAMICO kama ilivyo kwa wamiliki wengine wenye leseni za uchimbaji wa madini inawajibika kulipa ushuru wa huduma kwa Halmashauri wa asilimia 0.3 ya mapato ghafi yatokanayo na mauzo ya makaa ya mawe. STAMICO tayari imeanza kulipa ushuru wa huduma kwa Halmashauri ya Wilaya hiyo kutokana na mauzo ya makaa yaliyofanyika ambapo kiasi cha shilingi 57,600 kimelipwa. Aidha, jumla ya shilingi 1,735,900 zimelipwa kama ushuru wa barabara kwa Halmashauri. Manufaa mengine ni pamoja na kutoa ajira kwa wananchi wa Wilaya ya Ileje na kuchangia huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo afya, elimu na maji.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, STAMICO ilikabidhiwa Mgodi wa Kiwira mnamo mwezi Juni, 2014 ili kuendesha na kuusimamia kufuatia Kampuni ya Tan Power Resources kuurejesha Serikalini. Aidha, STAMICO imeendelea na jitihada mbalimbali za kutafuta fedha ikiwa ni pamoja na kutafuta wabia wenye uwezo watakaoshirikiana na shirika katika uendeshaji wa mradi huu.
MHE. DKT. DALALY P. KAFUMU aliuliza:-
Wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza kwenye Sekta ya Nishati na Madini wamepungua sana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita:-
(a) Je, ni nini kimesababisha hali hiyo?
(b) Je, Serikali inachukua hatua gani kuhakikisha kuwa Wawekezaji wanaendelea kuja ili kukuza uwekezaji kutoka nje (Foreign Direct Investment] (FDI)?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Dalaly Peter Kafumu, Mbunge wa Igunga, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, vichocheo vikuu vitatu vya uwekezaji katika Sekta ya Madini katika nchi yoyote, cha kwanza ni jiolojia inayoashiria uwezekano wa uwepo wa madini (prospective geology). Pili ni mwenendo wa bei ya madini husika kwenye Soko la Dunia na tatu Sera za Uchumi Mkuu (Macroeconomics) za nchi husika. Ilani ya CCM tunayoitekeleza hivi sasa ilizingatia vigezo hivi kwa kuhimiza kujenga uwezo wa Geological Survey of Tanzania ili waweze kugundua mashapo ya madini, kupunguza gharama za uzalishaji kwa kuboresha miundombinu na kuongeza thamani ya madini ili yawe na bei nzuri kwenye soko la dunia na kubadili Sheria ya Madini ili kuongeza uwazi na manufaa kiuchumi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi cha miaka mitano nchi yetu imeendelea kupokea wawekezaji kwenye sekta ya madini. Jumla ya leseni 102 za uchimbaji mkubwa (Special Mining Lenience) na wa kati (Mining License) zimetoelewa kati ya mwaka 2012/2013 hadi 2016/2017, ikiwa ni wastani wa leseni 20 kwa mwaka. Aidha, mwaka wa fedha 2012/2013 hadi 2016/2017 leseni 3,136 za utafutaji wa Madini (Prospecting License) zilitolewa, hii ikiwa ni wastani wa leseni 627 kwa mwaka. Mwaka 2017/2018, tumepokea maombi 26 ya Special Mining License na Mining License, yaani uchimbaji wa kati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumepokea maombi 818 ya leseni za utafiti wa madini (Prospecting License). Tume ya Madini iliyoundwa hivi karibuni inaendelea kupitia maombi hayo na iwapo yatabainika kukidhi vigezo vya kisheria leseni hizi zitatolewa na hivyo kuendelea kuchangia kuongezeka kwa Foreign Direct Investment (FDI). Kwa takwimu hizi, bado wawekezaji wanaonesha nia ya dhati kuwekeza nchini kwani nchi yetu inakidhi sifa tatu nilizoainisha hapo awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuchukua hatua za makusudi kuandaa mazingira rafiki ya kuvutia wawekezaji na kutangaza fursa zilizopo nchini. Hatua zinazochukuliwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu wezeshi kama vile ujenzi wa barabara, reli, kupanua bandari, kujenga miundombinu, maji, umeme, gesi na mawasiliano kuelekea maeneo yanayotazamiwa kuanzishwa migodi. Aidha, Serikali imeendelea kuimarisha uwezo wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kwa kuwapatia wataalam vitendea kazi ili kuwawezesha kuongeza kasi ya kufanya tafiti za kina za maeneo yenye madini nchini. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA aliuliza:-
Je, ni lini Mgodi wa GGM utawasilisha bajeti yake ya kuhudumia jamii katika Baraza la Madiwani la Geita ili tuweze kuangalia kipaumbele chao na kuwapa vipaumbele vya Halmashauri ya Geita?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Madini, napenda sasa nijibu swali la Mheshimiwa Joseph Kasheku Musukuma, Mbunge wa Geita Vijijini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kifungu cha 105(1)(2) cha Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na mabadiliko yake ya mwaka 2017 kinamtaka mmiliki wa leseni chini ya kifungu cha 7 cha Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 kuandaa Mpango wa Mwaka wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR). Mpango huo lazima ukubalike kwa pamoja na Mamlaka ya Serikali za Mtaa husika kwa kushauriana na Waziri anayehusika na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Waziri anayehusika na Fedha.
Mheshimiwa Spika, mpango huo unapaswa kuzingatia masuala ya mazingira kijamii, kiuchumi na shughuli za tamaduni zilizopewa kipaumbele katika Mamlaka ya Serikali za Mtaa ya jamii inayozunguka mgodi.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 105(3), mmiliki wa leseni anapaswa kuwasilisha kwa Mamlaka ya Serikali za Mtaa husika mpango huo aliouandaa kwa ajili ya kufanyiwa tathmini na kupata idhini kutoka kwa Baraza la Madiwani wa Halmashauri. Aidha, kila halmashauri uliopo mgodi inapaswa kuandaa mwongozo wa utoaji wa huduma kwa jamii kwenye Halmashauri yao, kusimamia utekelezaji wake na kutoa elimu kwa wananchi wa wilaya husika juu ya huduma hizo.
Mheshimiwa Spika, hadi sasa Mgodi wa GGM, kwa kushirikiana na halmashauri mbili za Geita Mji na Wilaya ya Geita, umeweza kutekeleza mchakato wa kuandaa mpango wake wa kusaidia jamii (CSR) kwa mwaka 2018 kama sheria inavyotaka. Mchakato huo umehusisha wataalam kutoka halmashauri zote mbili na wataalam wa Sekretarieti ya Mkoa.
Mheshimiwa Spika, mpango wa miradi iliyotambuliwa na halmashauri hizo kama vipaumbele umeshawasilishwa kwenye Mgodi wa GGM na umesharidhiwa na mgodi. Mgodi wa GGM unatarajia kutumia takribani shilingi bilioni 9.124 katika kutekeleza miradi iliyo chini ya mpango wa CSR. Kiasi cha shilingi bilioni moja kitatumika kutekeleza miradi katika Halmashauri ya Wilaya ya Geita, takribani shilingi bilioni 6.824 zitatumika kutekeleza miradi katika Halmashauri ya Mji wa Geita na takribani shilingi bilioni 1.3 zitatumika kutekeleza miradi katika Halmashauri za Bukombe, Chato na Mbogwe.
Baada ya taratibu zote kukamilika, mpango huo utawasilishwa katika Baraza la Madiwani ili uweze kuidhinishwa. Miradi iliyokubaliwa na wadau wote kwa mwaka 2018 itaanza kutekelezwa kabla ya mwezi Juni, 2018.