Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Stanslaus Haroon Nyongo (13 total)

MHE. DKT. RAPHAEL M.CHEGENI (K.n.y. MHE. STANSLAUS H. NYONGO) aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Maswa ina uwezo mkubwa wa kuhudumia wananchi wa Mkoa wa Simiyu:-
Je, ni lini hospitali hiyo itapandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Rufaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali ya Wilaya ya Maswa inatoa huduma za afya kwa wagonjwa wa Wilaya ya Maswa na miundombinu yake haitoshelezi kuwa hospitali ya mkoa. Mkoa wa Simiyu umeandaa makubaliano (memorundum of understanding) ya kuifanya Hospitali ya Wilaya ya Bariadi kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu kwa muda ambapo inatarajiwa kuanza kutoa huduma zenye hadhi hiyo kuanzia tarehe 1/7/2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa muda mrefu, mkoa umeshaanza kujenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa kufuata vigezo vinavyostahili ambapo hadi sasa jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje (OPD) limeanza kujengwa. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa shilingi bilioni 1.4 ili kuendelea na ujenzi huo.
MHE. KEMILEMBE J. LWOTA (K.n.y MHE. STANSLAUS S. MABULA) aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana inahudumia zaidi ya wakazi 300,000 wakiwemo wanaotoka Wilaya za jirani lakini haina vifaa tiba kama vile x-ray, ultrasound na kadhalika huku ikiwepo ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne mwaka 2013 lakini mpaka sasa ahadi hiyo haijatekelezwa.
Je, ni lini sasa ahadi hiyo itatekelezwa na kuipatia hospitali hiyo vifaa tiba vya kutosha ili kuokoa maisha ya watu wengi wanaopoteza maisha kwa sababu ya kukosa huduma hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Mabula, Mbunge wa Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa mashine ya x-ray katika utoaji wa huduma za afya, Halmashauri ya Jiji la Mwanza katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 imetenga shilingi milioni 133.14 kwa ajili ya ununuzi na kufunga mashine ya x-ray katika Hospitali ya Nyamagana. Aidha, ultrasound ipo katika hospitali hiyo na inafanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri pia katika mwaka wa fedha 2016/2017 imetenga shilingi milioni 33.9 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba kwenye vituo mbalimbali vya afya vinavyotoa huduma za afya ndani ya Wilaya ikiwemo Hospitali ya Wilaya ya Nyamagana. Aidha Halmashauri imetenga shilingi milioni 10.5 kwa ajili ya matengenezo ya vifaa vya hospitali.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO aliuliza:-
Mkoa wa Simiyu ulianzishwa kisheria na Makao Makuu yake kuwa kwenye Mji Mdogo wa Bariadi badala ya Mji wa Maswa:-
(a) Je, ni vigezo gani vilitumika kuamua Makao Makuu ya Mkoa na shughuli zake yawe Bariadi badala ya Maswa ambako kuna majengo ya kutosha ya Serikali; badala yake Serikali inaingia kwenye matumizi makubwa ya kupanga ofisi toka nyumba za watu binafsi huko Bariadi?
(b) Je, Serikali inaweza kufikiria kubadilisha maamuzi haya kwa manufaa ya Taifa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, maamuzi ya Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu kuwa Bariadi Mjini siyo Maswa yalipitishwa na wananchi wenyewe kupitia vikao vya kisheria ambavyo ni Mkutano Mkuu wa Vijiji, Kamati za Maendeleo ya Kata, Mabaraza ya Madiwani, Kamati za ushauri za Wilaya (DCC) na Mkoa (RCC). Uamuzi wa mwisho ulifanyika katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa tarehe 10 Mei, 2010 ambapo Wajumbe wote waliridhia pendekezo la Bariadi Mjini kuwa Makao Makuu ya Mkoa wa Simiyu. Hivyo, kigezo kikubwa kilichotumika kuamua Makao Makuu kilikuwa ni maamuzi ya pamoja kupitia vikao halali vilivyoshirikisha wadau kutoka Wilaya zote, wakiwemo kutoka sekta binafsi.
(b) Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika sehemu ya (a) ya jibu hili, maamuzi hayo yalifanywa na vikao halali vya kisheria, ikiwahusisha Wajumbe wa vikao hivyo, hivyo kitendo cha Serikali kubadilisha maamuzi hayo itakuwa ni kuwanyang‟anya madaraka wananchi yaliyowekwa kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 145.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO aliuliza:-
Mheshimiwa Rais Mstaafu Dkt. Jakaya M. Kikwete aliahidi kujenga barabara za Mji wa Maswa zenye urefu wa kilometa tatu ndani ya Halmashauri ya Mji Mdogo wa Maswa.
Je, ni lini barabara hizo zitaanzwa kujengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi ya Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Nne kuhusu ujenzi wa barabara kilometa tatu kwa kiwango cha lami imeanza kutekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ambapo katika bajeti ya mwaka 2016/2017 zimetengwa shilingi milioni 20 kwa ajili ya kazi ya usanifu wa kina (detailed design).
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua hiyo itawezesha kujulikana kwa gharama za ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Hivyo, Serikali itaanza ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami baada ya kukamilika kwa usanifu wa kina na bajeti kutengwa kwa kazi hiyo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha ahadi hii inatekelezwa pamoja na ahadi nyingine zilizotolewa na viongozi kwa manufaa ya wananchi wetu.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO aliuliza:-
Kutokana na athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea hivi sasa duniani pamoja na uharibifu mkubwa wa mazingira Mkoa wa Simiyu ni moja kati ya maeneo yaliyoathirika kwa kiwango kikubwa na kuna uwezekano mkubwa wa Mkoa huo kugeuka kuwa jangwa:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi wa kuunusuru Mkoa huo na hali hiyo;
(b) Kwa kuwa, hali hiyo inaathiri shughuli za kilimo hasa cha umwagiliaji; je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha mazingira ya mito na mabwawa yanatunzwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia athari kubwa ya mabadiliko ya tabianchi katika Mkoa wa Simiyu, Serikali inatekeleza programu ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi ijulikanayo kama Simiyu Resilient Development Programme. Programu hii ina lengo la kuwezesha jamii kuhimili mabadiliko ya tabianchi, hasa ukame kwa kujenga mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda Wilaya zote za Bariadi, Meatu, Maswa na Itilima. Programu hii itatekelezwa chini ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji na utekelezaji wake utagharimu Euro milion 313 kutoka Mfuko wa Dunia wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund) na Serikali ya Ujerumani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kunusuru Mkoa wa Simiyu pamoja na maeneo mengine nchini kutokana na athari ya mabadiliko ya tabianchi na uharibifu mkubwa wa mazingira, Serikali imeweka Sera, Sheria na Mikakati mbalimbali ikiwemo Sera ya Taifa ya Mazingira 1997; Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004; Mkakati wa Hatua za Haraka za Kuhimili Mazingira ya Bahari, Ukanda wa Pwani, Maziwa, Mito na Mabwawa ya mwaka 2008, Mkakati wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2012; na kampeni ya Kitaifa ya Upandaji Miti. Sera, sheria na mikakati hii inazitaka Halmashauri zote nchini kuandaa sheria ndogo za mazingira zitakazowezesha hifadhi ya mazingira ili kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi zikiwemo Halmashauri za Mkoa wa Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inahimiza viongozi wa Mkoa, Wilaya na Halmashauri zote za Mkoa wa Simiyu kuhuisha mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika mipango ya maendeleo ili kunusuru Mkoa huo kugeuka kuwa jangwa.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO aliuliza:-
Naibu Waziri wa Maji alipotembelea Mji wa Maswa alipata nafasi ya kutembelea bwawa lililobomoka la Sola na kuahidi kutoa fedha ya ukarabati wa bwawa hilo kiasi cha shilingi milioni 900.
(a) Je, ni lini fedha hizo zitatolewa ili kukamilisha ujenzi wa bwawa hilo ambalo ni muhimu kwa wakazi wa Mji wa Maswa?
(b) Kuna mabwawa 35 katika Wilaya ya Maswa, je, ni lini Serikali itatoa kiasi cha shilingi bilioni 1.9 ambazo zilikadiriwa kwa ajili ya kukarabatiwa mabwawa hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, bwawa la New Sola lina uwezo wa kuhifadhi maji meta za ujazo 4,200,000 na maji hayo ndiyo yanayotumika kuhudumia Mji wa Maswa na vijiji 11 vinavyozunguka mji. Bwawa lililobomoka ambalo ni la Old Sola liko kwenye dakio lilelile la bwawa la New Sola na liko upande wa juu (upstream). Kwa hivyo, ukarabati wake utapunguza maji katika bwawa la New Sola ambalo tayari lina miundombinu ya kusambaza maji. Wizara itafanya uchunguzi zaidi kuhusu faida za ukarabati wa Bwawa la Old Sola.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa mabwawa manne na malambo 31 yaliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa. Aidha, mpango mkakati wamiaka mitano umeandaliwa kwa ajili ya kufanya ukarabati wa mabwawa ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa vyanzo vya maji katika Halmashauri zote nchini. Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji, kwa kushirikiana na Halmashauri zote nchini imeanza zoezi la kuainisha mabwawa (inventory) ambayo yatakidhi viwango vya kiufundi, hatimaye kufanyiwa tathmini ili kujua idadi na gharama halisi ya ukarabati wa mabwawa hayo.
MHE. STANSLAUS S. MABULA aliuliza:-
Jimbo la Nyamagana lina ukubwa wa kilometa za mraba 256, kati ya hizo kilometa za mraba 71.56 ni eneo la maji ya Ziwa Victoria lakini bado wananchi wake hawapati maji ya uhakika ya bomba hasa kwa zile Kata zilizoko nje ya Mji.
Je, ni lini Serikali itahakikisha kuwa wananchi wa Nyamagana wanapata maji ya uhakika hasa ikizingatiwa kuwa wamezungukwa na Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Shing’oma Mabula, Mbunge wa Jimbo la Nyamagana, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma ya maji katika Wilaya ya Nyamagana, Jijini Mwanza inatolewa kwa asilimia 90 ya wakazi wote wa Wilaya hiyo. Hata hivyo baadhi ya wakazi ambao wanaishi sehemu za mwinuko pamoja na wanaoishi pembezoni mwa Jiji wanakosa huduma ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua hilo imepata mkopo wa masharti nafuu kutoka European Investment Bank (EIB)kiasi cha Euro milioni 54 sawa na shilingi bilioni 110 ili kuboresha huduma ya maji katika Jiji la Mwanza kwa kuhusisha Wilaya za Nyamagana na Ilemela. Mkandarasi wa utekelezaji wa mradi huo amepatikana na ujenzi umeanza. Kazi zinazotekelezwa ni pamoja na kuboresha huduma ya majisafi katika maeneo ya milimani hususani yaliyo juu ya matenki ya maji ambayo hayapati huduma kwa sasa, kubadilisha mabomba ya zamani yaliyochakaa na kuongeza mtandao wa mabomba pamoja na upanuzi na kuboresha miundombinu ya majitaka na mabwawa ya kutibu majitaka. (Makofi)
MHE. STANSLAUS H. NYONGO aliuliza:-
Walimu Wilayani Maswa wana uhaba wa nyumba za kuishi; pamoja na juhudi za wananchi kujenga nyumba za walimu wa shule za msingi na sekondari lakini walimu hao bado wanahitaji kujenga nyumba zao wenyewe za
kudumu.
Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu maalum wa kutoa mikopo kwa walimu hao ili wajenge nyumba zao binafsi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ina uhitaji wa nyumba za walimu 1,358. Nyumba zilizopo ni 479 na hivyo upungufu ni nyumba 879.
Mheshimiwa Spika, kutokana na upungufu huu Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Maswa ina mpango wa kujenga nyumba 16 katika mwaka wa fedha 2017/2018. Aidha, kati ya nyumba hizo, nyumba nane zitajengwa kwa bajeti ya 2017/2018 (CDG) na nyumba nyingine nane zitajengwa kwa kutumia mapato ya ndani y (own source) ya Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia kuwa tatizo la upungufu wa nyumba halitaweza kumalizwa na Serikali peke yake, Serikali inawashauri walimu wa Halmashauri ya Maswa na walimu wote nchini wanaohitaji kujenga nyumba zao binafsi kukopa fedha kutoka katika taasisi za fedha zinazokubalika Kisheria.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali inatoa wito kwa walimu nchini kote kujiunga na vyama vya kuweka na kukopa (SACCOS) ili waweze kukopa kwa riba nafuu kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za binafsi. Pia Serikali inawashauri walimu kutumia mikopo ya nyumba inayotolewa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaweka taa katika barabara kuu ya Mji wa Maswa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki, kama ifuatavyo:- Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) ilishaanza kazi ya uwekaji taa katika barabara kuu ya Mwigumbi hadi Maswa eneo la Maswa Mjini katika mwaka wa fedha 2020/2021. Jumla ya taa za barabarani 18 zimeshawekwa ambazo zimegharimu jumla ya Shilingi milioni 81.

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara nchini TANROADS, imepanga kuendelea na uwekaji wa taa katika barabara kuu katika Mji wa Maswa katika mwaka wa fedha 2021/2022. Ahsante.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Maswa hadi Lalago?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Haroun Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Maswa – Lalago yenye urefu wa kilometa 34 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Barabara hii ni sehemu ya Mradi wa Serengeti Southern by-pass ikianzia Maswa – Lalago – Mwanhuzi – Sibiti hadi Karatu yenye urefu wa kilometa 338. Mradi huu ulihusisha kazi ya Upembuzi Yakinifu chini ya ufadhili wa Serikali ya Ujerumani na umeshakamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza usanifu wa kina na ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali sehemu hii ya Maswa – Lalago na inapitika majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya Bypass ya Mji wa Maswa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mkataba wa kazi ya ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara ya mchepuo katika mji wa Maswa (Maswa Bypass) yenye urefu wa kilometa 11.3 ulisainiwa tarehe Mosi Juni, 2021 kati ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Kampuni ya M/S CHICO ya China kwa gharama ya shilingi 13,446,688,420.00 na muda wa ujenzi ni miezi 15 ambapo ujenzi wa barabara hii unatarajiwa kuanza mwanzoni mwa mwezi Julai, 2021. Ahsante.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Kolandoto hadi Meatu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninapenda kujibu Swali la Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Kolandoto – Mwanhuzi (Meatu) yenye urefu wa kilometa 117.57 ni sehemu ya Mradi wa Barabara ya Kolandoto – Lalago – Mwanhuzi – Sibiti – Oldeani B Junction yenye urefu wa kilometa 328 usanifu wake ulikamilika mwaka 2017. Serikali inaendelea na jitihada na juhudi za kutafuta fedha ili kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Serikali ikiendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya shilingi milioni 1,240.246 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo, ahsante. (Makofi)
MHE. STANSLAUS H. NYONGO aliuliza: -

Je, lini jengo jipya la X-Ray litajengwa katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo, Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia fursa ya mikopo inayotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) inakamilisha taratibu za kupata mkopo wa shilingi milioni 190, kwa ajili ya ujenzi wa jengo la X–Ray katika Hospital ya Wilaya ya Maswa.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kutokana na uchakavu wa baadhi ya majengo Serikali katika mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga kiasi cha shilingi milioni 900, kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa majengo katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa. Ahsante.