Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Stanslaus Haroon Nyongo (12 total)

MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ambayo ameyatoa Mheshimiwa Naibu Waziri, nilikuwa naomba kupata ufafanuzi katika maeneo mawili yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, ni takribani miezi minne sasa imepita toka Mkataba wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu usainiwe pale Chinongwe, lakini mpaka leo nazungumza, pamoja na majibu aliyoyatoa, kazi kubwa iliyofanyika ni kuweka tu vijiti. Sasa nilikuwa nataka kujua Serikali imekwama wapi kutoa fedha mpaka sasa hivi kwa ajili ya kuanza kazi hii ya kusambaza umeme vijijini?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, nilikuwa naomba nimuulize Naibu Waziri, pamoja na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme pale Mahumbika ambacho tuliamini kingekuwa ni tiba kwa tatizo la kukatika umeme kwa Mkoa wa Lindi na Mtwara. Ni jitihada gani za makusudi au za dharura ambazo Serikali itakwenda kuchukua, ili kuwaondoa wananchi wa Mkoa wa Lindi na Mtwara gizani, ukizingatia maagizo ya kufunga mashine yalishatolewa na Mheshimiwa Waziri alipofanya ziara Mkoani Mtwara na aliwapa siku kumi, mpaka leo bado hakuna kilichotekelezwa, naomba kufahamu nini kinaendelea?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, mpaka sasa ni kweli wakandarasi wa REA walishaanza kazi kama anavyosema miezi minne iliyopita na ninaomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge pamoja n Bunge lako Mamlaka ya Umeme Vijijini (REA) wameshalipa kiasi cha takribani bilioni 28 kwa wakandarasi wote kama advance. Nimeongea pia na Mkandarasi wa Mkoa wa Lindi ambaye ni State Grid, yupo anafanya kazi na alikuwa katika Wilaya ya Ruangwa na kati ya vijiji 34 alikuwa amevifikia vijiji 19 mpaka jana na akitoka Ruangwa ataelekea Wilaya ya Nachingwea. Nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kweli Serikali imedhamiria kabisa kwamba vijiji vyote vilivyosalia na kwa awamu hii ya kwanza ni vijiji 3,559 mpaka 2019 umeme vitakuwa vimepeta.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili aliuliza namna gani Serikali inachukua jitihada kumaliza tatizo la umeme Mikoa ya Mtwara na Lindi. Naomba nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge, mkandarasi anayefanya matengenezo ya mashine tisa za kuzalisha umeme Mkoa wa Mtwara ameanza hizo kazi. Vipuri vimewasili kama ambavyo Mheshimiwa Waziri alielekeza na kazi inaendelea. Na mpaka jana mashine sita zenye uwezo wa kuzalisha megawati 12 zilikuwa zinafanya kazi, lakini pia Serikali imechukua hatua imeagiza mashine mbili mpya kwa ajili ya kuzalisha megawati nne kwa thamani ya bilioni nane ambazo zitafika mwakani mwezi wa tatu na zitakuwa zimefungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo pia Serikali kupitia TANESCO inafanya matengenezo ya mtambo wa kuzalisha umeme Somangafungu ambao unazalisha megawati 7.5. Tuna uhakika, naomba niwathibitishie wakazi wa Mkoa wa Mtwara na Lindi itakapofika Disemba, 31 hali ya upatikanaji umeme Mtwara na Lindi itaboreka. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kunijibu swali langu kiufasaha kabisa, lakini vilevile nina maswali mawili madogo.
Je, Serikali inaweza kutuambia nini uchorongaji utafanyika wa kazi hiyo?
Swali langu la pili, je, nje ya Mkoa wa Rukwa kuna Mkoa mwingine wowote umeweza kugundulika kwa gesi hii?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya uchorongaji itaanza pale taarifa za kijiolojia zikishakamilika na kwa mujibu wa taratibu zilivyokuwa zimepangwa katika Kampuni hii ya Hellium One Tanzania Ltd. wamepanga kuanza shughuli ya uchorongaji kuanzia mwaka 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile swali la pili, ni sehemu gani ambapo hii hellium inapatikana. Kwa kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge ni kwamba gesi ya hellium vilevile inapatikana katika Ziwa Eyasi lililoko Mkoa wa Manyara na sehemu nyongine ni sehemu ya Singida ambapo na penyewe inapatikana hii gesi ya hellium. Ahsante sana.
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali.
Kwa kuwa Serikali imekiri kufuta leseni 423 yenye eneo la hekta 69,652.88; je, Serikali iko tayari kuwapatia wachimbaji wadogo wadogo eneo hili ambalo limefanyiwa utafiti ili waweze kujiajiri na kujipatia ajira na waweze kulipa kodi stahiki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, je, Serikali iko tayari kuwanunulia vifaa vinavyohusiana na wachimbaji wadogo wadogo ili waweze kukodisha kuliko ilivyo sasa wanachimba bila utaalam na vifaa vinavyostahili?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza ni kwamba Serikali iko tayari kuwasaidia wachimbaji wadogo. Imekwisha kutenga maeneo 11 ambayo yana jumla ya hekari 38.9 kwa ajili ya wachimbaji wadogo wadogo. Kwa hiyo, kwa maeneo haya ambayo yamesharudishwa Serikalini, Serikali itaendelea kufanya mpango wa kuweza kuwapatia wachimbaji wadogo wadogo ili waweze kuchimba na wao waweze kupata faida na waweze kunufaika na madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wachimbaji wadogo kupitia ruzuku iliyokuwa inapitia SMMRP ambayo ilikuwa inatoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo na wadau wengine wa uchimbaji iliweza kutoa fedha ili kuweza kuwasaidia wadau waweze kununua vifaa kwa ajili ya uchorongaji, kufanya utafiti na kuweza kusaidia wale wachimbaji wengine wadogo wadogo kwa kukodisha. Lakini vilevile STAMICO ambayo iko chini ya Wizara ya Madini pamoja na GST na yenyewe ina juhudi za dhati kabisa kununua vifaa ambavyo wachimbaji wadogo watakuwa wanakodisha ili waweze kujua mashapu yaliyopo ni mashapu ambayo yana faida ambayo wanaweza wakachimba na wakapata uchimbaji wa tija ili kujiondoa katika ule uchimbaji ambao wanachimba kwa kubahatisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo Serikali iko pamoja na wachimbaji wadogo. Ahsante sana.
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba uniruhusu nimshukuru sana na kumpongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuamua kujenga ukuta katika eneo lote ambalo Tanzanite inachimbwa katika Mkoa wa Manyara hususan eneo la Simanjiro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niruhusu nimshukuru na kumpongeza sana Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Mheshimiwa Job Ndugai ambaye alimua kwa dhati kabisa kuunda Kamati Maalum kwa ajili ya kuchunguza upotevu wa fedha kupitia madini hayo ya Tanzanite yanayopatikana peke yake duniani eneo la Simanjiro.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maswali yangu ya nyongeza ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uzoefu unaonesha kumekuwa na upotevu wa pesa kwa sababu wageni wanaotoka nje wanaokuja kununua Tanzanite hawalipi VAT, lakini wazawa waliopo pale eneo la Simanjiro, ama Arusha na Manyara wao ndio wanaolipa VAT. Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusu jambo hili?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa muda mrefu kumekuwa na mgogoro unaohusiana na mitobozano hususan kwa wachimbaji wadogo wadogo katika eneo hilo la Mererani, ni nini sasa kauli ya Serikali ili kuzuia migogoro hiyo isiyo ya lazima? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza linalohusiana na VAT, kwa kawaida VAT huwa hatozwi mtu mgeni. Vilevile ni kweli kabisa kwamba katika mnada huu, wageni walikuwa wanunua Tanzanite kwenye mnada bila kutozwa VAT, lakini kwa wale wenyeji walikuwa wanatozwa VAT. Mfano ukienda sehemu nyingine ni kwamba VAT unatozwa kule unakonunua bidhaa, kisha unaenda kurudishiwa kwenye kituo cha ndege (airport).
Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi kama Serikali tunaangalia namna mpya ya kuhakikisha kwamba katika mnada ule, watu wote wanaonunua Tanzanite, sasa hivi tutaanza kuwatoza kodi ya VAT halafu mgeni aende akarudishiwe kule airport. Huo ndiyo msimamo wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa suala la pili, kuhusu mitobozano. Ni kwamba mitobozano ni mgogoro wa muda mrefu pale Mererani na kuna kamati nyingi zimeundwa kuhakikisha kwamba wanakwenda wanatatua tatizo la mitobozano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie kwamba sasa hivi Umoja wa Wachimbaji wa Tanzanite pale pale Mererani wameweka mkakati wa namna wa kutatua mgogoro wa mitobozano. Kuna mkakati wameutengeneza na wamekubaliana kwa pamoja. Kwa hiyo, mkakati huo, ambao tuna hakika kwamba tukiufuata na utataribu ambao wameuweka mgogoro wa mitobozano utakwisha. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. CATHERINE V. MAGIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa mbali na madini ya Tanzanite kuwa chanzo cha mapato kikubwa kwa wafanyabiashara wa mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara, lakini pia kuna madini ya aina ya Rubi yanapatikana katika Kijiji cha Mundarara, Wilayani Longido Mkoani Arusha.
Ningependa kujua Serikali, inajipanga vipi ili madini haya aina ya Rubi iweze kuwanufaisha wananchi wa Longido? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa namshukuru na ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kutetea wachimbaji wadogo wadogo Mkoani Arusha na kazi nzuri anayoifanya na wananchi wa Arusha wanaiona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, madini ya Rubi yanapatikana katika Kijiji cha Mundarara katika Wilaya ya Longido Mkoani Arusha. Madini hayo yanapatikana na eneo hilo kwa pembeni yake kuna leseni ya mtu anayeitwa Mheshimiwa Mareale. Sasa hivi ni kwamba kuna wachimbaji wadogo wanavamia eneo lile. Sisi kama Serikali tunawapenda wachimbaji wadogo, lakini tunataka wafuate taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachokitizama sasa hivi ni kwamba lile eneo ambalo ni la mtu ambaye anayelimiliki na haliendelezi, tutaangalia namna bora ambayo tunaweza tukawatafutia wale wachimbaji wadogo waweze kuchimba na tuwatambue na wachimbe katika vikundi ili tuweze kuwatambua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia wanapochimba, basi tuweze kama Serikali kupata kodi zetu pale, tupate mrahaba pale, Halmashauri ya Longido ineemeke na Serikali kwa ujumla ineemeke na zile fedha tupeleke kwa wananchi wengine ambao wako nje na maeneo ya uchimbaji, waweze kuneemeka kupata huduma za maji, barabara na huduma za afya. (Makofi)
MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kabla sijauliza maswali ya nyongeza naomba nioneshe tu masikitiko yangu kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri kimsingi hajaenda kwenye thrust ya swali langu.
Swali langu nimeuliza je, ni hatua gani imefikiwa katika mazungumzo kati ya ACACIA na Serikali kuhusu ulipaji wa fidia na athari nyingine ambazo wananchi wa msalala wamezipata?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika majibu yake pia, amesema kwamba hakuna fidia inayodaiwa, jambo ambalo si kweli kwa sababu kwa miaka 22 Serikali inafahamu kwamba watu walioondolewa mwaka 1996 Bulyanhulu, hakuna shilingi moja iliyolipwa. Mbaya zaidi kwa hawa wagonjwa Serikali imesema wamepatikana wagonjwa 78, lakini haijasema hatua gani zinachukuliwa kuhakikisha wanatibiwa, kwa sababu tayari kuna watu 49 wameshafariki na hawajalipwa fidia yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niulize maswali mawili yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa sababu uharibifu au wizi uliofanywa na ACACIA kwa Tanzania haujafanywa kwa Tanzania peke yake, umefanywa hasa kwa wananchi wa Bulyanhulu pia; na kwenye ripoti ya Profesa Ossoro ilionesha mabilioni mengi ambayo Tanzania ilipaswa kupata na mimi nilishasema kwamba wananchi wa Msalala wanastahili kulipwa shilingi bilioni 973 kama service levy.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilitaka kujua kwa sababu ACACIA walisha-concede hivyo na tayari walishatoa kishika uchumba kwa Serikali, kile cha dola milioni 300. Nilitaka kujua kwa wananchi wa Msalala wanaodai bilioni 973, je, Serikali inaweza ikawasaidia sasa ili angalau katika hii mitambo inayotaka kuuzwa na ACACIA ikabidhiwe kwa Halmashauri kama sehemu ya fidia ya service levy ambayo haijalipwa kwa miaka yote? Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili,...
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Swali la pili, katika uwasilishwaji wa taarifa ya mazungumzo Mheshimiwa Rais aliagiza kwamba uchunguzi ufanyike kwenye migodi mingine kuhusu utoroshwaji wa madini, ukiacha makinikia peke yake, utoroshwaji wa vitofali vya dhahabu na Wizara iliagizwa kwamba ifanye uchunguzi kwenye migodi mingine. Nilitaka kujua uchunguzi kwenye hilo eneo umefikia hatua gani?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la msingi imeonesha kabisa Mheshimiwa Mbunge ameuliza kuhusiana na masuala ya fidia. Kwa taarifa tulizonazo katika Wizara yetu ni kwamba Mgodi ule wa Bulyanhulu ulivyokuwa unaanzishwa na kuanza kufanya kazi zake mwaka 2000 hakukuwa na madeni yoyote ambayo mgodi unadaiwa. Isipokuwa kama Mbunge ana hao watu ambao anawafahamu wanadai fidia katika yale maeneo kwa sababu yale maeneo ya Mgodi wa Bulyanhulu waliyapata kutoka Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kweli kuna watu ambao wanadai fidia zao, basi tunamuomba Mheshimiwa Mbunge awalete hao watu na madai yao, sisi kama Wizara tuko tayari kuwasimamia na kuhakikisha kwamba hakuna mwananchi yeyote anayedhulumiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile ni kwamba ile taarifa ya ACACIA ambayo waliji-committ kutoa kishika uchumba, Serikali inaendelea na mazungumzo na uchunguzi ambao uliweza kutolewa, kama vile yalivyoweza kutolewa yale maoni na zile kamati mbili teule za Mheshimiwa; Rais ni kwamba yale mashauriano au ushauri uliotolewa wa uchunguzi, uchunguzi unaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama itaonekana katika vile vitofali kuna wizi wa dhahabu ulitokea kwa sababu, kulikuwa kuna under declaration. Kama kweli ilitokea ni kwamba wale wa ACACIA wako tayari kuweza kutoa au kulipa fidia zote ambazo wameji-committ na walitoa kishika uchumba cha dola milioni 300, kwa maana ya kwamba waliji-committ kwamba kama kutakuwa na pesa nyingine za kutoa basi wataendelea kufidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge ni kwamba maongezi yanaendelea na uchunguzi unaendelea na kama kuna upungufu wowote au kama kuna fedha yoyote ambayo inatakiwa ilipwe katika Halmashauri, kama service levy, na wewe mwenyewe umetaja kwamba kuna bilioni 973 kama kweli ni haki ya Halmashauri haki hiyo italetwa katika halmashauri hiyo. Uchunguzi unaendelea na maongezi yanaendelea. Nashukuru sana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Naomba kuuliza swali dogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto nyingi zinazoikabili sekta hii ya madini kwa wachimbaji wadogo wakiwemo wachimbaji wa Jimbo la Mbulu Mjini, ni kwamba wanakosa mitaji, lakini pia uchimbaji wao ni wa kubahatisha. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia fursa za uwezeshaji, lakini pia na vifaa vya kubaini madini yako wapi na njia rahisi ya uchimbaji?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kwamba, wachimbaji wadogo wanakumbana na tatizo kubwa la kuwa na mitaji midogo. Sisi kama Serikali tumejipanga vizuri kuhakikisha kwamba, wachimbaji wadogo tunakwenda kuwasaidia, ili waweze kupata mitaji ya kuweza kuchimba na waweze kuchimba kwa kupata faida, na sisi kama Serikali tuweze kupata maduhuli na kodi kutokana na uchimbaji huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wachimbaji wadogo wengi wanachimba kwa kubahatisha. Sisi kama Wizara kwa kushirikiana na Geological Survey of Tanzania taasisi ambayo chini ya Wizara ya Madini, tuna mkakati kabambe wa kuhakikisha tunafanya tafiti mbalimbali. Tafiti ambazo zitaonesha ni wapi kuna madini ya kutosha na kuweza kuwapa ushauri wachimbaji wadogo kuchimba maeneo ambayo yana madini ili kuepukana na tatizo la kuchimba kwa kubahatisha. Wanatumia fedha zao za mfukoni, wengine wanauza hadi mali zao, ili waende wakachimbe maeneo ambayo hayajafanyiwa utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Wizara tumejipanga vizuri, tunafanya tafiti za kutosha na tutaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo, ili waweze kuchimba maeneo ambayo yana madini na waweze kuchimba kwa teknolojia nzuri ya kisasa na nyepesi, ili waweze kupata tija na waweze kuendesha maisha yao vizuri zaidi, ahsante.
MHE. UPENDO F. PENEZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kutokana na swali la kwanza la msingi mazingira hayo pia yanafanana na kule kwetu Geita ambako wananchi wa Geita wamekuwa wakiathirika kwa kiasi kikubwa na shughuli za Mgodi wa Geita Gold. Serikali kipindi cha Waziri Muhongo na Naibu Waziri Kalemani waliunda tume kwenda kuchunguza matatizo hayo kule Geita na kubaini nyumba ambazo zimeathirika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini sasa suala hili litaisha? Kwa sababu, wananchi wanaishi katika maeneo yenye mitetemo, wanaathirika na vumbi, wanapata hata madhara ya kiafya. Ni lini sasa Serikali itasimamia huo Mgodi wa Geita Gold Mine kuhakikisha ya kwamba, inawaondoa wananchi katika maeneo ya Compound na maeneo ya Katoma ili kupisha shughuli za mgodi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kuna watu ambao wanaishi ndani ya maeneo ambayo ni square kilometer 290,000 ambazo zinamilikiwa na GGM. Kwa mujibu wa sheria ilivyo ni kwamba kuna watu ambao bado wanamiliki zile surface area, yaani kwa maana ya eneo la juu la ardhi, na maeneo ambayo ni ya chini yanamilikiwa na mgodi wa GGM, kwa hiyo, kuna wananchi ambao bado wanaishi maeneo ambayo yako ndani ya leseni ya GGM.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niliwahi kufika pale mwezi wa pili na nilitoa tamko kwamba kuna Kamati ziliundwa na Waheshimiwa Mawaziri waliotangulia na ilionesha kabisa kwamba kuna watu ambao wameathirika katika maeneo yale. Nikatoa tamko kwamba wale ambao wako ndani ya maeneo ya GGM, GGM kama kampuni ikae nao iwalipe fidia iwaondoe yale maeneo ambayo wale wananchi wanaathirika na mgodi huo.
Vilevile kuna watu ambao wako maeneo ya Katoma, wameathirika na matetemeko kutokana na milipuko inayofanywa na GGM. Kulikuwa kuna taarifa mbili ambazo zilikuwa zimetolewa moja ikiwa ya GST kuangalia ni namna gani yale matetemeko yalikuwa yanaathiri zile nyumba. Majibu yaliyokuwa yanatoka yalikuwa yanakizanzana kwamba kuna wengine walisema milipuko ilisababisha nyufa katika nyumba zile na kuna taarifa nyingine inasema kwamba ile mitetemeko haikusababisha zile nyufa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tumeamua kwa pamoja kwamba wakae waangalie tena upya na vile vile wafanye tathmini ya kutosha kwenye zile nyumba zilizoathirika wawalipe wale wananchi. Ikiwezekana wale wananchi walimo ndani ya hiyo leseni ya GGM waondolewe, wawalipe fidia, ikiwemo na watu wa Nyakabare, walipwe fidia waondoke yale maeneo ya uchimbaji. Kwa hiyo, hiyo tumeshawapa GGM na tunaendelea na maongezi na tunaendele na mikakati kuangalia namna gani ya kuweza kuwalipa fidia wananchi hawa. Ahsante sana.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa Halmashauri ya Geita inaudai mgodi wa GGM zaidi ya dola milioni 12; tumekaa tukakubaliana watulipe kwa awamu. Awamu ya kwanza ilikuwa itekelezwe mwezi wa pili, lakini utekelezaji huo haujafanyika na Halmashauri haina nguvu tena ya kuudai Mgodi wa GGM. Je, Wizara inaisaidiaje Halmashauri ya Geita ili tuweze kulipwa pesa hizo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Halmashauri ya Geita inaudai GGM service levy. Tulitoa ushauri kama Wizara kwamba wakae kwa pamoja na waangalie ni namna gani Kampuni ya GGM inaweza ikawalipa wale Halmashauri ya Geita, yaani wakae kwa pamoja waelewane ili wangalie namna bora ya kuweza kulipa kidogo kidogo deni hilo na wameshakaa na nilipokwenda mara ya mwisho mwezi wa pili walisema kwamba wanakwenda kukaa na Halmashauri, ili waweze kusaini memorandum of understanding, namna ya kuweza kulipa deni hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama hawajalipwa mpaka sasahivi, naomba nishirikiane na Mbunge kwamba nifuatilie. Sisi kama Wizara tuko pamoja tutahakikisha kwamba haki ya Halmashauri ya Geita italipwa kama inavyostahili. Ahsante sana.
MHE. VICKY P. KAMATA: Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Pamoja na majibu mazuri, nina swali moja dogo la nyongeza. Kwa kuwa, GGM imekuwa ikitoa hili fungu la CSR kila mwezi kwa ajili ya kuhudumia hayo maeneo ambayo ameyataja katika maelezo yake ya msingi kwa maana ya elimu, afya, mazingira pamoja na wajasiriamali.
Mheshimiwa Spika, pia kwa kuwa, wamekuwa wakitoa kila mwezi hili fungu la CSR na kwa majibu haya inaonekana kwamba tangu Januari mpaka sasa GGM hawajatoa fungu hilo la CSR kwa maeneo hayo, nataka kujua kauli ya Serikali kwa wakati huu wa mpito kuhusiana na hawa waliokuwa wakisaidiwa na GGM kwa mfano, kituo cha Watoto Yatima cha Moyo wa Huruma wamekuwa wakisaidiwa pesa kila mwezi kwa ajili ya malazi ya wale watoto yatima, chakula, kuna mradi wa maji ambao kimsingi ni wa Serikali lakini GGM walikuwa bado wanaendelea kuutunza pamoja na ile hospitali inayotembea majini inayosaidia wanawake na watoto katika Visiwa kwa kuwa tangu Januari mpaka sasa pesa hazijatoka na imezoeleka kila mwezi huwa inatoka. Je, ni nini kauli ya Serikali katika kipindi hiki cha mpito?. Mheshimiwa Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba baada ya marekebisho ya Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na marekebisho yake ya mwaka 2017, tulisimamisha utoaji wa fedha hizi mpaka pale Baraza la Madiwani katika Halmashauri husika wakae, wakubaliane utekelezaji sawasawa wa miradi hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo GGM, pia nimeongea na RAS wa Mkoa wa Geita, ule mpango wa kupitia kwa Madiwani umeshakamilika na kuanzia leo wanaanza kuzitumia zile fedha kutokana na jinsi walivyokubaliana na Halmashauri husika. (Makofi)
MHE. JOHN W. HECHE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuniona. CSR ipo kwa mujibu wa sheria, lakini hii migodi wamekuwa wakionyesha kama ni hisani fulani wanawapatia wananchi. Kwa nini sasa Serikali isiwaagize hizi pesa zipelekwe moja kwa moja kwenye Halmashauri na zisimamiwe na Madiwani wetu katika kutekeleza miradi hii, kwa sababu unaona gharama zinazoandikwa ni kubwa kweli ukilinganisha na kazi halisi ambazo zinakuwa zinafanyika, yaani ziende kama vile kodi zingine zinavyoenda lakini zikiwa specific kama CSR ili zisimamiwe na Baraza la Madiwani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO): Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kwamba hesabu zinazoonekana ni hesabu kubwa sana zilizotumika kuliko miradi yenyewe ilivyo, hilo tunakubaliana kabisa. Nimepita baadhi ya maeneo kwa mfano, GGM na North Mara tumewaagiza kwanza watupe taarifa ya utekelezaji wa zile fedha zilizotengwa kwa miaka miwili iliyopita ili tujiridhishe tuone zile fedha zilizotengwa na wamepeleka wapi na nini kimefanyika. Hilo la kwanza.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, kwa sababu hizi fedha za corporate social responsibility huwa zinatolewa kutokana na jinsi wao wanavyotengeneza faida na kwa sasa hivi ni sheria lazima watoe zile fedha. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na Madiwani husika wakakae na zile Kampuni waamue kwamba watekeleze miradi ile kwa jinsi wao walivyoweka kipaumbele chao.
Mheshimiwa Spika, vilevile kuna fedha ambayo inakwenda moja kwa moja kwenye Halmashauri, fedha hiyo ni service levy ambayo ni asilimia 0.3 ya mauzo ya madini wanayoyapata. Kwa hiyo, nadhani tu kwamba tuendelee kutoa ushirikiano na sisi kama Wizara ambayo tunasimamia Sheria ya Madini tutahakikisha kwamba zile fedha zinazotengwa zinakwenda zinavyostahili na Madiwani wasimamie utekelezaji wa miradi ambayo wamejipangia. Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Napenda kuongezea majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Madini. Napenda kusema kwamba sheria ya sasa na kanuni kuhusiana na uwajibikaji kwa jamii ziko wazi.
Mheshimiwa Spika, niombe tu ushirikiano Waheshimiwa Wabunge pamoja na Halmashauri zetu za Wilaya na Miji waweze kutoa ushirikiano na kutupatia taarifa endapo wanaona kuna miradi imetekelezwa ipo chini ya viwango, lakini kiwango ambacho kimekuwa-declared ni kidogo kuliko fedha halisi ambayo inatamkwa kwamba imetumika.
Mheshimiwa Spika, pili; pamoja na maelezo aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba tumewataka GGM waweze kutoa maelezo na taarifa zao za miaka miwili, tutaenda kwa migodi yote ambayo imekuwa ikifanya uwajibikaji kwa jamii na tutapitia na kukagua na yeyote ambaye ataonekana alifanya udanganyifu, hatua kazi za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Ni hivi juzi tu siku mbili, tatu zilizopita Wabunge wa Geita tumeletewa barua inayoonesha CSR iliyotolewa na GGM 2017/2018 dola 9,600,000 lakini katika majibu ya Waziri amesema ni dola milioni 6.5 na hizi barua ambazo tumeletewa tayari ziko kwa Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na baadhi ya wananchi wameshazipata, lakini kwa majibu ya Wizara ina maana tunachanganyikiwa tujue ipi ni sahihi na ipi siyo sahihi.
Mheshimiwa Spika, sasa ni nini kauli ya Wizara kuweza kuisaidia Halmashauri angalau kufanya auditing kujua uongo uko Wizarani au uongo uko mgodini. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ni kwamba GGM tuliwaeleza tarehe 27 Februari, 2018 watuandikie breakdown ya kuonesha ni jinsi gani wametumia fedha za CSR na majibu waliyonipa ni kwamba kwa mwaka 2017 wametumia kama nilivyosema katika jibu la msingi dola 6,358,000. Mheshimiwa Musukuma anachosema dola milioni 9.7 ni jumla ya miaka miwili yaani mwaka 2016 na 2017 kajumlisha kapata 9.7 lakini swali la msingi limeuliza mwaka 2017 jibu ni milioni 6.358. Mheshimiwa Spika, ahsante.
Waheshimiwa Wabunge, tunaendelea na Wizara ya Maliasili na Utalii. Swali linaulizwa na Mheshimiwa Hawa Mchafu.