Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Stanslaus Haroon Nyongo (44 total)

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini napenda kujua, kwa sababu maendeleo hayana utengemano yaani ni maendeleo kwa jumla bila kujali mipaka na itikadi ya kisiasa, miradi hii inakwenda kwa wananchi wote. Baada ya kutandaza mabomba mpaka maeneo ya Kishapu, je, mradi huu mnaweza kuupeleka mbele zaidi hadi vijiji vya Mwamashindike mpaka Lalago wakapata maji? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Wilaya ya Maswa nayo inasubiri Mradi wa Maji ya Ziwa Viktoria ambao utakuja katika phase two ya ule mradi wa maji kutoka Lamadi. Je, Wizara ina mpango gani kuwasaidia wananchi ambao hawana maji hivi sasa kwa kutumia mabwawa yaliyopo katika Wilaya ya Maswa kwa mfano Bwawa la Sola, Nyangugwana, Mwantonja kwa kuyasafisha na kuyafanya kuwa chanzo cha maji katika Wilaya ya Maswa ili wananchi waweze kupata maji kwa sasa wakati wanasubiri mradi wa Ziwa Viktoria ukamilike? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stephen Nyongo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Mbunge, mwenyewe amesema kwamba miradi hii haina mipaka ndiyo maana tunatoa maji kutoka Ziwa Viktoria Mwanza yanakuja Shinyanga yatafika mpaka Tabora yatakuja mpaka Singida. Kwa hali hiyo, vijiji alivyovitaja kama ile pressure itaweza kufika tutaweza kuvifikia.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, amezungumzia kuhusu Wilaya ya Maswa ambayo itafikiwa na awamu ya pili ya mradi wa maji kutoka Ziwa Viktoria lakini kwa hatua za dharura, tufanye nini kwenye mabwawa? Tumetenga fedha kwenye halmashauri zote, zihakikishe kwamba zinapeleka fedha hizo kwenye miradi ya kipaumbele ambayo itahakikisha kwamba wananchi wanapata maji kwa uharaka.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Swali langu la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri, kuna wastaafu wengine baada ya kupewa pensheni wanapewa kila baada ya miezi mitatu na ukitazama kuna walimu wengine wastaafu na wafanyakazi wengine, kila baada ya miezi mitatu wanapewa kiasi cha shilingi 150,000/=.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kauli ya Mheshimiwa Waziri kwamba je, pesa hizi wana mpango wowote wa kuwaongezea na je, anaonaje kama ikawa kila mwezi mkawapatia kila mwezi badala ya kuwapatia miezi mitatu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake la nyongeza. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu,naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimwia Mwenyekiti, dhana ya pensheni inatawaliwa na mifumo ya utekelezaji wa dhana ya hifadhi ya jamii kwa kuzingatia sheria mbalimbali za Kimataifa, sheria za nchi lakini na taratibu pia ambazo tumejiwekea ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo, katika kila hatua ya ulipaji wa pensheni mifumo ya uchangiaji na mifumo yote ya hifadhi ya jamii, ni lazima kuwe na ushirikishwaji wa kutosha wa kuona nani afanye nini na nani awajibike katika jambo gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili kuhakikisha kwamba pensheni zinaongezeka ama mafao ya aina yoyote yanaongezeka kupitia suala zima la hifadhi ya jamii, Serikali itaendelea kushirikiana na wadau na itaendelea kutoa taarifa, ni namna gani inaboresha ama kuongeza mafao kwa namna moja au nyingine ili kuhakikisha kwamba dhana ya hifadhi ya jamii inatekelezwa ipasavyo katika nchi yetu ya Tanzania.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ningependa kujua ushirikishwaji wa vikao vya Wilaya ya Maswa, kwa sababu jibu lake la mwanzo ameeleza kwamba vijiji vilishirikishwa, lakini nina hakika kabisa ushirikishwaji wa vijiji hivi na Kamati hizi zilizoorodheshwa hapa sina hakika navyo. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuniridhisha kwa kunionesha vikao hivi vilifanyika lini na wapi ili watu wa Maswa waweze kulitambua hilo?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Mwenyekiti wa RCC ni Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Mkoa wa wakati ule alikuwa ni Dkt. Balele ambaye naye anatokea Bariadi, huoni naye alikuwa labda ni sehemu ya kufanya Serikali iingie kwenye matumizi makubwa, kupeleka sehemu ambapo hakuna majengo mengi ikilinganishwa na Maswa ambayo ni Wilaya kongwe iliyozaa Bariadi na Meatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya awali, kwa sababu suala la michakato ya kuanzisha Wilaya, kuanzisha Halmashauri, kuanzisha Mkoa mpya yote haya hayaanzii katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, haya ni maoni ya wadau ambao wameona kwamba kuna haja ya kufanya hivyo, wanakaa katika vikao halali na kufanya maamuzi.
Mheshimiwa Spika, nimesema pale awali kwamba kikao hiki kilipitishwa na wajumbe, tarehe 10 Mei, ndiyo walifanya maamuzi hayo. Sasa nikisema nirejee kuthibitisha vikao kwa sababu suala hili nadhani DCC zote kabla hujafika katika maeneo mbalimbali; kuna vikao vya Mabaraza ya Madiwani, kuna Vikao vya Ushauri vya Wilaya, then kuna Vikao vya Ushauri vya Mkoa.
Kwa hiyo, nasema kwamba tukitaka kupata reference vizuri, tunapokutana katika RCC yetu inayokuja hapo tuitishe mihtasari ambayo ilipitisha, haya naamini tutayaona na ninyi ni wajumbe wa Kamati ya RCC. Kwa hiyo nadhani hili halina shaka.
Mheshimiwa Spika, suala la kusema kwamba Mwenyekiti wa Kikao hicho ambaye alikuwa Mkuu wa Mkoa lakini asili yake alikuwa anatokea Bariadi. Naomba niwaambie ndugu zangu, tunapofanya maamuzi siku zote tusisukumwe na maamuzi ya mtu mmoja. Mimi kwa akili yangu siamini kama mtu mmoja ataburuza Kamati yote ya RCC na Wilaya yote na yakafuatwa maamuzi yake. Kikubwa zaidi tunapojipambanua katika mikutano yetu ni lazima tuwe imara kujenga hoja kujua jambo hilo linafanyika vipi.
Naamini kama kulikuwa na upungufu RCC yenu mtakaa na kufanya maamuzi sasa kwa mujibu wa sheria. Jambo hili bahati nzuri watu walileta pingamizi, lakini kutokana na vigezo vilivyoletwa, pingamizi lile baadaye ikaonekana kwamba kwa sababu maamuzi hayo yalifanyika halali kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 145, kurudisha madaraka kwa wananchi, ikaonekana ni halali. Ndipo jambo hili limekuja na Ofisi ya Rais, TAMISEMI ikaona kwamba ni sawa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge najua kwamba hoja yake ina msingi, lakini inawezekana wakati huo yeye hukuwepo katika RCC, lakini wenzake waliokuwepo kipindi hicho waliona kwamba jambo hilo lifanyike hivyo. Ahsante sana.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri, swali la nyongeza. Kwa kuwa Wilaya ya Maswa imekwishatenga eneo zaidi ya heka 110 na tumekwisha kuandika barua kwa EPZA kuja kuwekeza Maswa. Je, Mheshimiwa Waziri ni lini atatusaidia Maswa, EPZA kuja ku-facilitate maeneo ya uwekezaji ili tuweze kukaribisha wawekezaji kwa maana ya kuwekeza viwanda vidogo vidogo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Mbunge wa Maswa kama Wabunge wengine ambao wamejitolea kutoa maeneo yao ili kusudi kujenga viwanda vidogo lakini na Special Economic Zone. Naomba nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi Mkuu wa EPZA watafute hii barua ya Maswa, waende Maswa na Mkurugenzi wa SIDO wabainishe ni kitu gani kinachoweza kufanyika pale na wanipe jibu ili kusudi nimridhishe Mbunge kabla ya Bunge hili kumalizika.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Napenda kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri swali. Kwa kuwa tunataka kwenda kwenye nchi ya viwanda na tunataka kuwawezesha kimtaji wafanyabiashara na wakulima, je, Wizara ina mkakati gani wa haraka kuhakikisha kwamba mashamba ya wakulima hasa wa Mkoa wa Simiyu na Mikoa ya jirani yanapimwa na kupatiwa hati ili kusudi wakulima waweze kwenda kwenye mabenki na kukopa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Stanslaus ametaka kufahamu ni lini Wizara itapima mashamba hayo na kuwamilikisha watu ili waweze kupata hati. Naomba niseme tu kwanza suala la kuanza kupima viwanja katika maeneo ni lazima Halmashauri yenyewe husika iweze kuyatambua na kuyabaini maeneo ambayo sasa yameiva kwa ajili ya upimaji kwa sababu siyo maeneo yote ambayo yanahitaji kupimwa kwa sasa. Kwa hiyo, tunachosema ni kwamba yale ambayo yameiva na yanahitaji kupimwa na ili kweli tuweze kupata maeneo ya kuweka viwanda kama tunavyosema nchi inaelekea kwenye viwanda lazima Halmashauri ilete mashamba hayo ambayo tayari yatakuwa yamepitia katika taratibu za kawaida za kubainishwa katika Kamati zao za Mipango Miji ili tuweze kujua sasa eneo hili linahitaji kupimwa kwa ajili ya matumizi ya viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima iende sambamba na mpango kabambe wa maeneo hayo kwa sababu hatuwezi kupima tu kwenye maeneo ambayo hayana plan ambayo imekaa katika utaratibu wa mpango wa muda mrefu wa maeneo hayo. Kama haya mashamba anayoyasema tayari yako katika mpango kabambe wa Jimbo lake, basi ni vizuri tukayajua ili Wizara iweze kuchukua hatua hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tulivyosema, tumetenga pesa shilingi bilioni 8.8 kwa ajili ya kununua vifaa vya upimaji na vifaa vitakwenda kila kanda. Kwa hiyo, vitakapofika Kanda ya Ziwa ni wazi na Simiyu vitafika ili kuweza kupima mashamba haya ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa, ahadi nyingi zinazotolewa na Mheshimiwa Rais, kuanzia Awamu ya Nne na mpaka sasa awamu ya Tano, tunavyotambua ahadi ya Mheshimiwa Rais ni kama amri.
Je, ni kwa nini ahadi zinazotolewa na Rais wetu hazitekelezeki mapema? (Makofi)
Swali la pili, kuna ahadi vilevile ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne katika Halmashauri ya Mji wa Maswa, ilisemekana kwamba zitajengwa kilometa tatu ilitolewa ahadi na Mheshimiwa Rais, Jakaya Mrisho Kikwete; je, ni lini ujenzi huu utaanza? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, viongozi wetu wakuu wanapotoa ahadi huwa wanaonesha dhamira na baada ya hapo utaratibu wa kutafuta fedha kwa ajili ya kutekeleza dhamira hiyo unafuata. Kuchelewa kujenga au kutekeleza ahadi ni kutokana na kukosekana kwa upatikanaji wa fedha na kwa kawaida mara fedha zinapopatikana ahadi huwa zinatekelezwa. Ninamhakikishia hata hiyo barabara analiyoongelea maadamu dhamira ilishaoneshwa ni wajibu wetu tuliopo katika sekta ya ujenzi kuhakikisha dhamira hiyo iliyooneshwa na viongozi wetu wakuu inatekelezwa.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwa mpango huu wa hizi nyasi bandia zinazotolewa, je ni mpango wa kila Mkoa na kama ni kila Mkoa, je, ni lini Mkoa wa Simiyu mtatupa uwanja wa namna hii? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na uwanja wa Simiyu vigezo ni kama nilivyovitaja kama uwanja huu ni wa Halmashauri na unakidhi vigezo vya kuwa wa Kimataifa, goal project inaweze ikasaidia, lakini utaratibu ni kwamba TFF inaandika orodha ya viwanja vitano na kuandika details zake na vinapofika FIFA wao wanateua kulingana na ushindani wa kukidhi vigezo vya kutoa msaada. Ahsante.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na nina maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza napenda kujua usanifu huu wa kina umeanza lini na utaisha lini?
Swali la pili ningependa kujua kwa sababu nimefuatilia kwa muda mrefu ahadi hii ya Mheshimiwa Rais kumekuwa na mkanganyiko wa kutokujua, kwamba fedha za ujenzi wa barabara hizi kilometa tatu zitatoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Maswa au zitatoka katika Serikali Kuu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesema katika jibu langu la msingi kwamba bajeti ya fedha hii imetengwa katika mwaka huu wa fedha 2016/2017 ambayo bajeti tumepitisha si muda mrefu sana katika Ofisi ya Rais TAMISEMI. Lengo kubwa ni kwamba fedha zile sasa zitatoka ilimradi detailed design iweze kukamilika, mara baada ya hapo sasa tutajua gharama halisi ya ujenzi wa barabara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Stanslaus avutea subira tu na kwa sababu unajua kwamba ofisi yetu, imejielekeza sasa imejipanga jinsi gani tutafanya kutatua tatizo la miundombinu katika Halmashauri mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, jambo la kwamba hizi fedha zitatoka wapi aidha Halmashauri au zitatoka wapi hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ambaye ni mstaafu regardless hizo fedha kama zitatoka Halmashauri lakini lengo kubwa ni kwamba kazi hii lazima itekelezwe. Na ndio maana hata kama ukifanya rejea bajeti yetu ya mwaka huu tumetenga takribani bilioni 245 na bilioni hizi maana yake kulikuwa na mgawanyiko wa maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna takribani shilingi bilioni 43 kwa ajili ya miradi ile ya kuondoa vikwazo maeneo mbalimbali zingine ni kwa ajili katika Halmashauri mbalimbali. Lakini ukifanya rejea sana katika hiki kipindi cha miaka mitano, kupitia mradi wetu wa uboreshaji wa miji mbalimbali, unaona Miji mingi sasa hivi imebadiika, lakini tunaenda hivyo maana yake tunaenda katika hatua sasa za Halmashauri. Lengo langu na jukumu letu kubwa ni nini kama Serikali, tutahakikisha miradi hii ambayo ni kipaumbele ambayo imetolewa ahadi na viongozi wetu wakuu wa nchi tutahakikisha kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI inasimamia na miradi hii iweze kutekelezeka. Kwa sababu lazima tulinde imani ya viongozi wetu wameifanya na jambo hili tumejipambanua wazi kwamba ahadi zote zilizopangwa lazima tuzitekeleze kwa kadri tulivyowaahidi.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Na mimi siridhiki kabisa na majibu ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, mazingira ya ushindani yanayosemwa kwanza hajawekewa mazingira mazuri ya ushindani na nauli kwa tunaosafiri kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam mara kwa mara, nauli kwa mfano za Shirika la FastJet, wanapoaihirisha safari wewe abiria hawakulipi na ukichelewa ndege unalipa zaidi ya nauli. Je, TCAA na Mheshimiwa Waziri wanalijua hili na kama wanalijua wana mpango gani wa kuliondoa? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ni kweli pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, alivyoliweka ndivyo hivyo lilivyo. Tanzania ni mwanachama wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (IATA) na sisi kama nchi mwanachama tunao wajibu wa kufuata taratibu za Kimataifa za usafiri wa anga. Moja ya taratibu zilizopo katika IATA ni kwamba ushindani ndiyo utatawala bei za tiketi katika usaifirishaji wa anga. Lakini ushindani huo umewekewa masharti, ikitokezea kwamba route iliyokuwa na ushindani sasa ushindani huo umekwisha kumetokeza monopoly ya msafirishaji mmoja; sheria za IATA na kwa maana hiyo sheria zetu za usafiri wa anga zinairuhusu mamlaka ya usimamizi wa usafiri wa anga kuweka ukomo wa bei kwa huyo msafirishaji ambaye anayo monopoly wakati huo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa nizungumzie case ya Fast Jet na route za Mwanza au Songwe. Ni kweli kwamba hizi route ya Dar es Salaam – Mwanza imekuwa inaendeshwa kwa ushindani kwa sababu zipo scheduled flights za kampuni zaidi ya moja. Precision Air bado wameendelea kuwa wana-operate kati ya Dar es Salaam na Mwanza ingawa siyo kwa frequency kubwa kama ilivyo ya FastJet. Na jambo hili limesababishia sana usumbufu kule mamlaka ya usimamizi wa usafiri wa anga kwa sababu linawafanya washindwe kuingia saa kwenye hiyo hatua ya kuwawekea ukomo FastJet wa nauli kwa sababu bado route inaonekana ina ushindani, kwamba Precision Air wapo wana-operate kwenye hiyo route.
Mheshimiwa Spika, lakini ikifika mahali kwamba Precision Air wamesimamisha kabisa safari zao za Dar es Salaam kwenda Mwanza basi mamlaka ya usimamizi wa usafiri wa anga itakuwa ina uwezo wa kisheria sasa wa kuweka ukomo wa bei kwa msafirishaji aliyebaki kwenye route hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na pili usafiri wa ndani wa kawaida kimataifa bado huwa hauwezi kulinganishwa na usafiri wa nje kwa maana ya kuangalia umbali, hii ni practice ya dunia nzima ndivyo ilivyo, sio Tanzania pekee tu.
Mheshimiwa Spika, nitatoa mfano wa Dar es Salaam – Dodoma; Dar es Salaam – Dodoma ndege zinazokuja ni ndege ndogo na hizi ndege ili iweze kuja na kurudi kwa faida lazima bei per seat iwe ni kubwa kidogo kuliko ndege kubwa zaidi ambayo ingefanya route ya namna hii. Ndiyo maana sasa hivi upanuzi huu wa uwanja wa Dodoma ndege za size kubwa zikianza kuja kwa vyovyote vile bei za kusafiri kutoka Dar es Salaam kuja hapa Dodoma kwa ndege zitashuka sana. (Makofi)
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri.
Swali la msingi linauliza kwamba pesa hizi zitaanza kutolewa maana yake toka mpaka sasa ni kwamba uchaguzi umeshapita, mwaka mzima umeisha quarter ya kwanza ya bajeti imeisha ni lini? Swali la msingi linauliza.
Swali la pili la nyongeza ni kwamba hili Baraza la Mawaziri litakaa lini kupitisha hii pesa kwa sababu tayari ilishajulikana pesa hizi zinakwenda kwa kila kijiji, ni nini kinakwamisha Baraza hili kukaa na kupitisha pesa hizi au mpango huu ili wananchi waweze kupata hizi pesa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake kauliza ni lini, na katika majibu yangu nimesema kabisa ya kwamba katika bajeti ya mwaka 2016/2017 tayari kiasi cha shilingi bilioni 59.5 zimetengwa kwa hiyo kinachosubiriwa hivi sasa ni waraka ule kupelekwa Baraza la Mawaziri na ukishajadiliwa, baada ya hapo katika jibu langu nimesema utekelezaji utaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tu nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba jambo hili ni jambo kubwa kidogo na linahitaji maandalizi ya kutosha hasa ukizingatia kwamba tunakwenda kuvigusa takribani vijiji 12,545 vya nchi hii na utaratibu wake huu unawekwa sawa kiasi kwamba tusije tukarudia yale makosa ambayo yalijitokeza pale awali katika usimamizi wa fedha ambao zilitoka ambapo walengwa wale hawakuweza kufikiwa na ndio maana waraka huu unaweka utaratibu mzuri na hatukutaka jambo hili kulifanya kwa uharaka kwa kuzingatia umuhimu wa ukubwa wa jambo hili na ndio maana imeshajidiliwa katika level hiyo na mkumbuke kwamba bajeti hii imepitishwa mwezi wa saba tu, kwa hiyo ni miezi mitatu tayari hapa taratibu zimekwisha kuanza nimwondoe hofu kwamba tunalipa uzito mkubwa na baada ya muda sio mrefu waraka huu utajadiliwa na utaratibu utatolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Baraza la Mawaziri litakaa, Mheshimiwa Mbunge atupe nafasi tu baada ya kukamilisha taratibu hizi za Bunge hapa natumaini wahusika wa kuandaa utaratibu huu utafanyika na tutarudi tena kwa ajili ya kutoa taarifa.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Pamoja na mikakati na Sheria na Sera za Kitaifa za Mazingira ya Mwaka 1997, Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, Mkakati wa Hatua za Kuhifadhi Mazingira 2008, pamoja na Mkakati wa Kitaifa wa Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka 2012. Swali langu la nyongeza dogo, Serikali ina mpango gani maalum kwa Mkoa huu wa Simiyu kwa sababu hizi sheria na mikakati yote inaonekana ni ya Kitaifa zaidi? Ninachotaka ni kupata commitment ya Serikali maalum kwa Mkoa huu wa Simiyu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mkoa wa Simiyu kweli unategemea kupata maji kutokana na huu mradi wa Simiyu Resilient Development Programme wa kutoka Ziwa Victoria, lakini katika Mkoa huu Maswa itapata maji katika mradi huu katika phase ya pili. Vilevile jibu la Mheshimiwa Naibu Waziri linasema kwamba utekelezaji wa kupata maji maeneo haya kutoka Ziwa Victoria unatekelezwa na Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba commitment ya Wizara ya Maji, ni lini itafufua mabwawa ya Wilaya ya Maswa kwa sababu itachelewa kupata maji. Kuna mabwawa mengi zaidi ya mabwawa 35 na yamefanyiwa upembuzi yakinifu yanahitaji shilingi bilioni 1.2 tu kufufuliwa ili watu waweze kupata maji na waweze kuotesha na kumwagilia miti yao. Nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri. Mradi huu pia unapita kwenye jimbo lake la uchaguzi na vilevile unapita kwenye jimbo langu la uchaguzi. Napenda kuwahakikishia wananchi kwamba, mpango maalum ambao Mheshimiwa ameuzungumza hapa, ambao nataka kumwambia mpango maalum wa kunusuru Mkoa wa Simiyu ndiyo huu sasa wa mradi mkubwa kabisa wa Kitaifa ambao utagharimu Euro milioni 313. Serikali tunatarajia kuanza ujenzi huu ifikapo mwanzoni mwa mwaka 2017, tunatarajia tuwe tumeanza ujenzi wa mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia kwamba mradi huu umo ndani ya Ilani ya uchaguzi, lakini commitment ya Serikali na Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba lazima utekelezwe katika kipindi hicho. Mipango mingine ya Serikali inaenda yote kwa pamoja, tulizungumza hapa katika mpango wetu kwamba tumeanzisha Mfuko wa Mazingira sasa ambao tuna uhakika kwamba tutapata fursa nzuri ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi lakini tutapata fursa tena nyingine nzuri sana ya kuhakikisha kwamba tunapambana na uharibifu wa mazingira na kwamba tutaziimarisha taasisi zinazohusika katika usimamizi wa mazingira ili ziweze kusimamia mazingira vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo Mheshimiwa ameuliza hapa, ni kwamba, kuna mabwawa ya maji katika Wilaya ya Maswa ambayo kwamba hayako kwenye hali nzuri na kwa kweli yanahitaji kufufuliwa. Katika hatua hii ninachoweza kusema kwamba wataalam wa ofisi yangu ya mazingira pamoja na wa Wizara ya Maji watakwenda kufanya tathmini na kuona namna bora ya kufufua mabwawa haya ili kuhakikisha kwamba wananchi wa Wilaya ya Maswa Mashariki la Mheshimiwa Nyongo wanapata maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na ya uchumi.

WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongeze majibu ya nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri kuhusu commitment ya Serikali kwa Mkoa wa Simiyu kwa ajili ya kuendeleza yale mabwawa ambayo tumeainisha mabwawa 35.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukirejea bajeti yetu tumeweka bilioni sita, fedha za ndani kwa ajili ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, yapo mabwawa ambayo tumeyaainisha katika Mkoa wa Simiyu ambayo yatashughulikiwa na bajeti hii katika mwaka wa fedha wa 2016/2017.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa nikazie kusema kwamba, Mradi wa KASHUWASA wa Shinyanga sio mamlaka ni mradi na vilevile wananchi wa Mji wa Maswa leo sasa wanakwenda wiki ya tatu wanakosa maji kisa TANESCO imewakatia umeme kwa sababu hawajalipa bili ya umeme na wananchi wa Maswa wanalipa bili zao kwa muda unaostahili na maji wamekatiwa kwa sababu ya makosa sio ya kwao. Je, Mhesimiwa Waziri unawahakikishia ni lini wananchi wa Maswa na Shinyanga watapata maji? Ahsante.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu swali la Mheshimiwa Masele, tunaposema Mamlaka za Maji, KASHUWASA ni Mamlaka ya maji katika daraja la kwanza ambalo kwamba, linatakiwa lisipate ruzusu ya kulipa bili ya maji kutoka Serikalini, anatakiwa alipe kutokana na makusanyo ya madeni, yaani ya watu wanaotumia maji yale. Kwa hiyo, huo ndio utaratibu ambao tumepanga, tunazisaidia hizi mamlaka za daraja la C ambazo
hazina wananchi hawawezi kuhumili gharama za uendeshaji wa miradi ile. Kwa hiyo, katika hii miradi midogo midogo, hii tunatoa ruzuku na kwenye bajeti tunatenga fedha na mwaka
huu wa fedha tulitenga fedha, lakini na mwaka unaokuja tutatenga fedha kwa ajili ya kulipia ruzuku katika hizi mamlaka ndogo za daraja la C na B ambazo hazina uwezo wa kuweza kujiendesha.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi nimuulize Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Maswa imekwisha kutenga eneo kwa ajili ya uwekezaji (EPZA) zaidi ya heka 110, na Mheshimiwa Waziri tulishakuja kuleta barua na EPZA walishakubali kuwekeza hapo, lakini mpaka sasa hivi hakuna mkakati wowote unaoendelea. Naomba kauli yako na commitment ya Serikali, je, ni lini Serikali sasa au EPZA watakaa na Halmashauri ya Maswa na kuweza kuanzisha mradi huu katika maeneo haya? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Nyongo kuhusu eneo la uwekezaji la Maswa na tunashukuru tumelipata eneo la Maswa na Mheshimiwa Nyongo nimshukuru ni miongoni mwa Wabunge ambao wamejasiria kutafuta maeneo ya uwekezaji bila vikwazo. Kuna wengine maeneo yao yanakuwa na vikwazo vikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kitakachofuata, kama nilivyofanya kwa Bunda, Bunda nimeishaitangaza kuwa special economic zone; nitaitangaza Maswa halafu sasa tutaanza kutafuta wawekezaji.
Nirudie Waheshimiwa Wabunge Wawekezaji wanatafutwa dunia nzima na Tanzania si destnation peke yake, wana-move kutoka Asia kuja Afrika, Afrika si Tanzania peke yake. Kwa hiyo, tuweke mazingira wezeshi tuwe wakalimu waje kusudi tutengeneze ajira.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mji wa Maswa umekosa maji kwa mara nyingine tena kwa muda zaidi ya wiki moja baada ya operesheni kata umeme. Kata umeme imeathiri hadi mamlaka ambazo ziko daraja la tatu ambapo kama Mamlaka ya Maji ya Mji wa Maswa iko daraja la tatu kwa hiyo bili zake zinalipwa na Wizara, hawajilipii bili wao wenyewe. Kwa hiyo Wizara haijalipa TANESCO …
TANESCO wanakata. Swali langu, napenda kupata commitment ya Serikali ni lini Maswa watarudishiwa umeme katika Mamlaka ya Maji ili wananchi wa Maswa waweze kupata maji katika Mji wa Maswa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo hilo nakiri kweli lipo lakini Serikali tumekaa kikao Wizara ya Maji na Hazina pamoja na TAMISEMI tumekubaliana. Vilevile tarehe 8 Mei Makatibu Wakuu wa Wizara ya Nishati na Wizara ya Maji watakaa kukamilisha suala hili ili kuhakikisha tatizo la malipo lililokuwepo tukishakaa na Hazina tutalimaliza ili maeneo yote umeme uweze kurejeshwa.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimuulize Waziri maswali ya kwamba tunatambua Bwawa la New Sola yaani Bwawa la Zanzui linapokea maji kutoka mito mitatu, Mto Mwashegeshi, Mto Sola na Mto Mwabayanda na bwawa hili lilikuwepo wakati Bwawa la Old Sola likiwepo na lilikuwa linatunza maji ya ziada. Je, hamuoni kwamba kuna umuhimu wa kulijenga hili Bwawa la Old Sola ili kuhifadhi maji na kukabiliana na ukame wa maji katika Wilaya yetu ya Maswa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nimejibiwa kama Mbunge wa nchi nzima, mimi ni Mbunge wa Maswa, mabwawa 35 yalishafanyiwa upembuzi yakinifu, leo mnasema mnaangalia inventory ya nchi nzima halafu mtafanya ukarabati. Mimi naomba kwa ajili ya Wana-Maswa, ni lini mtawajali Wana-Maswa ili muweze kuwajengea mabwawa haya na vijiji vya Maswa viweze kupata maji ya kutosha? Kwa sababu katika Mradi wa Ziwa Victoria tuko phase ya pili, tutachelewa kupata maji. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana kwa jinsi ambavyo anawapenda wananchi wake kuhakikisha kwambwanapata maji safi na salama. Pia nishukuru kwamba nilivyofanya ziara Maswa tulikuwa wote, tulitembea mpaka tukaenda mabwawa yote mawili. Mheshimiwa Mbunge tunafuata wataalam wanatushauri nini na bado tunaendelea kuongea nao kwamba kwa nini tusikarabati Old Sola ili liweze kutunza maji wakati haya ya hili bwawa lililopo yakiisha tunaweza tukatumia lile. Wameniambia kwamba hiyo inawezekana lakini kama lile likaweka maji bila kutumika chochote kinaweza kikatokea, kama ilivyotokea kwamba lilibomoka, linaweza likaja kuathiri na hili bwawa ambalo tayari limeshawekewa miundombinu. Nimwambie Mheshimiwa Mbunge siyo kwamba tumeishia hapo, bado wataalam wanajaribu kufanya uchunguzi kuona ni namna gani watafanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ukija kwa upande wa swali la pili, ujenzi wa mabwawa hayo, ni kwamba ndani ya Bunge hili tulishatoa maelekezo kwenye Halmashauri nchi nzima kwamba kila Halmashauri iainishe mabwawa. Pia tumeelekeza kwamba Halmashauri zenyewe zinatakiwa kutenga fedha na kuhakikisha kila mwaka walau wanajenga bwawa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia hivi kwa ujumla kwa sababu sisi Wizara tunafanya kazi ya maji kwa nchi nzima, hatufanyi kwa Halmashauri moja. Kwa hiyo, pamoja na Halmashauri yake na Halmashauri nyingine zilizopo hapa nchini zinatakiwa kutekeleza hilo.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba EFD ni mashine ya kukusanya kodi na kutoa risiti, kwa maana nyingine ni device ya TRA ya kukusanyia kodi, sasa kwa nini Serikali isiwape wafanyabiashara EFD mashine bure?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, EFD ni sahihi ni kwa ajili ya matumizi ya kikodi pia kwa matumizi ya wafanyabiashara wetu ili waweze kujua kumbukumbu sahihi katika kufanya biashara zao. Katika hili ndiyo maana Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwamba EFD zigawiwe bure, lakini tuangalie mfumo mzuri wa kuweza ku-share gharama hizi za kupata mashine hizi za EFD. Kwa hiyo, Serikali inawekeza lakini na wafanyabiashara wetu nao wanawekeza kwa pamoja ili tuweze kujenga Taifa letu.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri kwamba, kwa kuwa kule katika halmashauri ukiwaeleza jambo hili na wao wanatupia mpira kwenye Wizara, wakati Wananchi wa Maswa wanaendelea kupata tabu ya maji na katika Mradi wa Ziwa Viktoria wako phase two, ina maana watachelewa sana kupata maji. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari basi, angalau tushirikiane na ili tuweze kuchagua yale mabwawa muhimu zaidi kwa kutoa huduma kwa wananchi tuanze nayo hata kama ni machache? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe kwanza mfano; Mheshimiwa Bilakwate Halmashauri yake ya Karagwe tayari imeleta mapendekezo ya mabwawa sita na mabwawa hayo tunayafanyia kazi na tunazungumza kati ya halmashauri yake na Wizara ya Maji na Umwagiliaji ili tuweze kuona tunafanya nini kwa kushirikiana kwa sababu Serikali ni hiyo hiyo moja ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Nyongo, Halmashauri yake waanze kufanya kazi kwanza kidogo kule kwao, halafu wawasiliane na sisi tutaona suala la kufanya. Kwa bahati nzuri nimeshatembelea kwenye halmashauri yake na tukaona baadhi ya mabwawa. Basi halmashauri ianze kufanya kazi, Wizara haiwezi kuruka moja kwa moja kuja huko bila yeye mwenyewe. Mapendekezo haya aliyoyazungumza nafikiri wameyasikia, kwa hiyo, wayafanyie kazi, wawasiliane na sisi ili tuweze kufanya kazi.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nashukuru sana kwa kujali hilo.
Ningependa kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri wa maji kwamba kuna mradi ule mwingine wa Ziwa Victoria unaopita hadi maeneo ya Kolandoto kwenda Wilaya ya Kishapu. Nilishawahi kuuliza siku za nyuma kwamba kuna vijiji vya Mwamashindike, Mwabalatulu, Mwakidiga, Lalago hadi Budekwa viko karibu na eneo la Kishapu. Je nini kauli ya Serikali kwa maeneo hayo kupata maji kutoka ule mradi wa Kolandoto kuja maeneo hayo? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa. Katika utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Kishapu tulichokifanya ni kwamba maeneo yote ambayo lile bomba limepita tumetoa matoleo ya kupeleka kwenye vile vijiji ambavyo vipo ndani ya kilometa 12 kila upande. Sasa tumetoa maelekezo kwa Wakurugenzi, kwamba sasa wanapopanga mipango yao ya kupeleka maji kwenye vijiji vyao pale ndipo patakapokuwa chanzo cha kuchukulia maji. Kwa hiyo, mipango ya halmashauri na vipaumbele vyao tumeshawazogezea sasa kwenye lile bomba kubwa. Lakini pia tutaweza kuendelea na bajeti ya Serikali maeneo yale mengine kulingana na bajeti ambayo mmeipitisha hivi karibuni. Tukipata fedha hizo basi tutaendelea nasi kusaidiana na Halmashauri kupeleka maji maeneo mengi jinsi itakavyokuwa inawezekana.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Ninapenda kujua kwamba Maswa tumekuwa na tatizo kubwa sana la maji, kwa kweli hali ni mbaya na inahitajika hali ya dharura kutatua tatizo la maji katika Mji wa Maswa na maeneo yake. Sasa ninaomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, anatuhakikishia vipi kwamba kuna njia mbadala ya kupata maji katika Mji wa Maswa kwa sababu bwawa tunalolitumia limekauka kabisa? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza, nikiri, ni kweli bwawa ambalo Mji wa Maswa ulikuwa unategemea limekauka, na hii inatokana na matumizi yasiyokuwa endelevu ya wafugaji ambao walikuwa wanafuga jirani na lile bwawa kuweza kuzalisha matope na hivyo kufanya lile bwawa kujaa matope na maji kukauka. Kwa hiyo, Serikali tumetenga bilioni 1.1 katika Halmashauri ya Maswa, sasa katika fedha zile wanaweza wakatumia sehemu ya fedha hiyo katika kutafuta mpango wa dharura ili kuhakikisha kwamba wananchi wa pale wanapata maji.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa ujumla, Mkoa wa Simiyu, tunao mpango mkubwa wa kupeleka maji kutoka Ziwa Victoria kupeleka Bariadi na wilaya hizo zote ambao unafadhiliwa na KfW pamoja na Global Climate Fund, huu ni Mfuko wa Mazingira Duniani, kwahiyo fedha hizo, Euro milioni 100 na Euro milioni 25 tayari tumezipata. Sasa hivi tunakamilisha tu usanifu wa kina na muda si mrefu tutatangaza tenda ili tuweze kuujenga mradi ule, huo ndio utakuwa jibu la Mkoa huu wa Simiyu kuliko hivi visima ambavyo kwa muda mfupi vinakuwa vinakauka.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona, naomba niulize swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuna mfuko wa NEDF ambao Mheshimiwa Waziri ameutaja yaani National Entrepreneur Development Fund, kwa mwaka huu pesa hizo hazijatoka. Napenda kupata kauli ya Serikali, je, ni lini hizo shilingi bilioni 2.5 zitatolewa ili ziweze kuwawezesha Watanzania wanaotaka kufungua biashara ndogondogo au kufungua viwanda vidogo vidogo waweze kuwezeshwa na kufanya hivyo? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko wa NEDF kama mlivyoona taarifa ambayo imekuja pekee ni mfuko ambao unawachangamsha wawekezaji ukitoa mikopo mbalimbali. Katika mwaka wa fedha tunaomaliza tulitengewa shilingi bilioni 2.4, pesa hizo hazijatoka, lakini mwaka huu haujaisha. Nina imani hizo pesa zitakuja katika mwaka huu wa fedha na nimemkumbusha Waziri wa Fedha kwamba fedha hizo Wabunge wanazihitaji haraka wazipeleke Majimbo. Nina imani kabla jua halijazama pesa hizo zitapatikana.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba EFD ni mashine ya kukusanya kodi na kutoa risiti, kwa maana nyingine ni device ya TRA ya kukusanyia kodi, sasa kwa nini Serikali isiwape wafanyabiashara EFD mashine bure?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, EFD ni sahihi ni kwa ajili ya matumizi ya kikodi pia kwa matumizi ya wafanyabiashara wetu ili waweze kujua kumbukumbu sahihi katika kufanya biashara zao. Katika hili ndiyo maana Mheshimiwa Rais alitoa maelekezo kwamba EFD zigawiwe bure, lakini tuangalie mfumo mzuri wa kuweza ku-share gharama hizi za kupata mashine hizi za EFD. Kwa hiyo, Serikali inawekeza lakini na wafanyabiashara wetu nao wanawekeza kwa pamoja ili tuweze kujenga Taifa letu.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza kabisa napenda kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri. Nina maswali mawili tu madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba ujenzi unaendelea, lakini unaendelea kwa kasi ndogo sana.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba wanatoa fedha kwa wakati na kuhakikisha ujenzi huo unaendelea kwa haraka ili ukamilike, kwa sababu watumishi wanapata shida sana kusafiri kutoka Bariadi hadi Ligangabilili?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Serikali ina mpango gani juu ya kuikaribisha National Housing (Shirika la Nyumba la Taifa) kwenye Mkoa wa Simiyu kuweza kujenga nyumba za National Housing katika mkoa nzima yaani katika wilaya zake zote tano ili kuweza kuwasaidia wafanyakazi kupata makazi mazuri ya kuweza kuishi? Ahsante sana.
NABU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwa ajenda ya kasi ndogo ya utendaji wa kazi naomba nichukue concern hiyo, tutafanya follow up kuangalia ni kinachoendea. Nilifika pale Itilima, ni kweli changamoto kubwa ilikuwa ni tatizo la fedha. Tukaja kufanya uhangaikaji katika ofisi yetu ndiyo maana tukapata zile fedha nyingine zikaenda kule, ili kuweza kuongeza speed ya ufanyaji wa kazi pale. Vilevile tutawasiliana na wenzetu wa Itilima ili kuangalia kuna kitu gani ambacho kinakwaza. Nia ni kuongeza speed ya utendaji wa kazi ili hatimaye wananchi na hasa watumishi wa Itilima waweze waweze kukaa katika mazingira rafiki.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la National Housing kuweza kukaribia katika Mkoa wa Simiyu kwa ajili ya kujenga nyumba; ni wazo nzuri, na niwashukuru sana wenzetu wa National Housing wamekuwa wakishiriki ujenzi wa nyumba katika maeneo mbalimbali. Hata hivyo ninaamini kwamba tutapata maelekezo vizuri juu ya nini cha kufanya kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambayo ni Wizara yenye dhamana katika eneo hilo, hasa katika Mkoa wa Simiyu.
Mheshimiwa Spika, mara nyingi sana wanaambiwa kwamba watenge maeneo maalum kwa ajili ya kuwakaribisha National Housing. Hata hivyo kuna maeneo mengine National Housing walijenga nyumba lakini matumizi ya zile nyumba imekuwa ni changamoto kubwa na sana katika Halmashauri zetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tuchukue kama ni challenge nyingine katika upande wetu vilevile, kwamba endapo National Housing wanakuja kuwekeza basi lazima nisiamasishe Halmashauri tuwe tayari kuhakikisha kwamba tunazitumia nyumba hizo, kwa sababu fedha hizi zisipotumika vizuri tutatengeneza gharama kubwa kwa Serikali yetu. Kwa hiyo, ni wazo zuri Mheshimiwa Nyongo na mimi kama TAMISEMI nitalichukua jambo hili, nitaongea na dada yangu Mheshimiwa Angelina, Naibu Waziri wa Ardhi tuangalie namna ya kufanya ili wananchi wa Simiyu waweze kufanya kazi kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa Simiyu.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI:
Mheshimiwa Spika, Ahsante sana. Napenda kujibu swali la nyongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri alivyojibu majibu yake mazuri kuhusiana na suala la National Housing.
Kwa Mkoa wa Simiyu tayari National Housing wana maeneo waliyopewa katika Wilaya mbili, Wilaya ya Busega pamoja na Wilaya ya Bariadi. Tatizo lililoko katika wilaya zingine ni kwamba bado hawajawa tayari kutenga maeneo.
Mheshimia Spika, kwa maelekezo ambayo pia Mheshimiwa Rais alitoa kwamba National Housing ili waweze kujenga na waweze kutoa nyumba zao kwa bei nzuri lazima Halmashauri husika iwe imeshatenga eneo ambalo halina changamoto kwa maana kwamba litahitaji fidia, litahitaji miundombinu. Kwa hiyo, wao wafanye maandalizi tayari viwanja waweke National Housing watakwenda kujenga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili pia, kuna Wilaya zaidi ya 30 ambazo National Housing wamejenga na nyumba zile zinaharibika, ikiwemo Mkoa wa Rukwa, nyumba zimejengwa lakini watu hawajaingia wala hawajapanga. Kwa hiyo, wakati mwingine ku-pull up resources katika maeneo mengine inakuwa ni ngumu; na katikati hapa walisimama kwa ajili ya kuendeleza eneo la Iyumbu. Kwa hiyo halmashauri yoyote itakayokuwa tayari National Housing wataweza kuja, lakini tuwaombe pia mfanye maandalizi yale ya msingi ili National Housing waweze kushiriki.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, swali langu dogo tu la nyongeza ni kwamba kwa kuwa masharti ya mikopo kwenye mabenki na SACCOS nyingi ambazo kwa kweli watu wengi wamekopa na wameshindwa kulipa madeni na yamewasababishia umaskini mkubwa. Je, hamuoni kwamba kuna haja Serikali sasa mkatazama namna nyingine ya kuwapatia walimu hawa mikopo ya masharti nafuu ili waweze kujenga nyumba zao za kudumu? Swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, mna mpango gani wa kuiwezesha Halmashauri ya Maswa kama tulivyoongea siku za nyuma, kwamba Halmashauri na zenyewe ziwe na uwezo au zijengewe uwezo wa kuchukua mikopo ili mikopo hiyo kupitia halmashauri iwasaidie walimu hao kujenga nyumba zao za bei nafuu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli mikopo mingine inayotokana na taasisi za benki ina changamoto nyingi sana, lakini kwa utaratibu wa sasa wa kuwasaidia wafanyakazi kuna suala la mortgage financing ambalo Bunge hili hili lilipitisha sheria humu ndani kuwawezesha watumishi mbalimbali waweze kupata fursa ya mikopo kupitia fedha wanazochangia katika mifuko yao ya Hifadhi ya Jamii.
Mheshimiwa Spika, katika hili naomba niwapongeze Utumishi Housing ambao wamefanya kazi kubwa sana katika maeneo mbalimbali hivi sasa. Tunaona wazi kwamba matangazo yao yametoka, sasa naomba tuwaambie watumishi wa Serikali, tutumie dirisha hili vizuri ili tuweze kupata nyumba katika maisha yetu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la kuziwezesha Halmashauri mbalimbali hasa Halmashauri ya Maswa, kupata mikopo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba inafanya uwekezaji; kuhusiana na jambo hili mara nyingi sana ofisi yetu huwa inapokea vibali mbalimbali vya kutaka halmashauri kufanya uwekezaji katika eneo fulani. Hata hivyo mara nyingi sana ofisi yetu huwa inapitia haswa yale maombi kuangalia ili jambo likishapitishwa, likapatiwa kibali ambapo lisije likawa mzigo mkubwa sana kwa Halmashauri hiyo kiasi cha kushindwa kujiendesha.
Kwa hiyo, mawazo mazuri yanakaribishwa, na ofisi yetu ina wataalam watafanya analysis lile jambo linalofanyika basi Halmashauri hiyo haitawekwa nyuma kuhakikisha kwamba inapewa kibali ili ifanye uwekezaji katika halmashauri yake.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO Mheshimiwa Spika nashukuru kwa majibu ya Serikali, na niwapongeza Serikali kwa kuanza kufanya mradi huu kwa kuweka taa za barabara kuu za Mji wa Maswa. Ninachosikitika ni kwamba mradi huu umekwenda nusunusu sasa naomba Mheshimiwa anipe majibu ya kweli wameweka taa 18

Je, wana mpango wa kuweka taa ngapi ambazo zitatosha kuanzia Mwigumbi kwenda njia panda.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, wananchi wa Maswa wanapata shida barabara hiyo zinapopita gari kwa kasi kubwa watu wanapata ajali na wengine wanapoteza maisha na kuna mpango wa kutengeneza bypass road kuzunguka Mji wa Maswa.

Je, barabara hiyo nayo itajengwa lini? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba katika barabara zote za sasa ambazo zinatengenezwa imekuwa ni sehemu ya mkataba kwamba pale ambapo barabara zinapita kwenye Miji, moja ya eneo ambalo lazima lishughulikiwe na Wakandarasi ni kuweka taa za barabarani ikiwemo Mji wa Maswa. Taa sizopungua 60 zitaweka katika Mji wa Maswa ili kukamilisha Mji wote kwenye barabara ile kuu, swali la kwanza.

Mheshimiwa Spika, bypass road ya Maswa itajengwa kulingana na upatikanaji wa fedha ipo kwenye mpango na itajengwa mara tu Serikali itakapokuwa imepata fedha ahsante.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, swali la kwanza, ni jepesi tu; ni lini ujenzi unaanza, basi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kama Serikali ya Ujerumani imeweza kutoa fedha kwa ajili ya upembuzi yakinifu, inakuwaje Serikali inasuasua kutoa fedha kwa ajili ya usanifu wa kina? Hivi hata hao wanatoa fedha za ufadhili katika hatua hizi za awali hatuoni kama tunawa-discourage kwa kitendo cha Serikali kusuasua kutoa fedha za kuendeleza mradi huu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hayo tu.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimesema barabara hii itaanza mara fedha itakapopatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimhakikishie katika swali lake la pili, kuhusu kwamba Serikali inasuasua. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi hii Barabara inapita Maswa – Lalago – Mwanhuzi – Sibiti – Hydom – Mbulu – Karatu. Katika baadhi ya barabara, hii tayari kama mlivyosikia jana kwenye bajeti, kipande cha Mbulu – Haidom kitaanza kujengwa. Pia Mheshimiwa Waziri jana amesema barabara hii itatangazwa siku za karibuni ambayo ni sehemu ya hii barabara kwa fedha za Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, hata hicho kipande ambacho sasa tutafanya ni design and build, yaani ni kufanya usanifu na ujenzi, basi hela ikipatikana hata kipande hiki cha Lalago – Maswa kitajengwa. Ahsante.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachotokea Tarime hata Maswa kinatokea hicho kwamba Hospitali ya Maswa inazidiwa kwa wagonjwa na imekadiriwa kwanza kuwa Hospitali ya Wilaya, lakini inahudumia zaidi ya Wilaya moja. Kuna wagonjwa wanatoka Itilima, wagonjwa wanatoka Wilaya ya Meatu na wagonjwa wa Wilaya ya Maswa. Hospitali inaonekana kama ya Wilaya lakini inazidiwa kwa sababu watu wengi wanakwenda pale.

Kwa hiyo nilikuwa naomba aji-commit Mheshiwa Naibu Waziri je, na Maswa atai-consider na yenyewe iweze kuongezewa hadhi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameongea kuhusiana na Hospitali ya Halmashauri ya Maswa ni hospitali ambayo ni kongwe, lakini ina hudumia wananchi wengi wa ndani ya Halmashauri ya Maswa, lakini pia na Halmashauri zingine kama Itilima na Meatu. Lakini naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali iliona hilo na imelifanyia kazi. Kwanza kwa kujenga Hospitali ya Halmashauri katika Halmashauri ya Wilaya ya Itilima ili kuhakikisha wananchi wa Itilima ambao walikuwa wanalazimika kufika Maswa sasa watatibiwa Itilima, lakni pia imeboresha sana hospitali ya Halmshauri ya Meatu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hayo bado tunatambua kwamba kuna kazi ya kufanya katika Hospitali ya Halmashauri ya Maswa na ni muhakikishie tunaji-commit kwamba tutaendelea kuhakikisha tunaboresha miundombinu, vifaa tiba na upatikanaji wa wataalam ili tuhakikishe hospitali ile inatoa huduma bora zaidi. (Makofi)
MHE. STANSALUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuwa Magereza nyingi zipo katikati ya mji kwa mfano Mji wa Maswa ipo katikati ya mji na majengo na maeneo yao yanaingiliana sana na makazi ya watu na maeneo hayo yanaonekana kuwa ni potential hata kwa uwekezaji mwingine.

Je, ni lini Serikali itaamua basi kujenga Magereza nje ya miji kwa mfano Maswa tumeshatoa na eneo na kuwapa Magereza ili wajenge nje ya mji na kuachia maeneo ya katikati ya mji kwa ajili ya uendelezwaji wa shughuli zingine za kibiashara? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nyongo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa asili zamani huko kidogo maeneo haya yalikuwa pembeni ya miji, lakini kadri miji inavyokua tumejikuta sasa wakati mwingine maeneo haya ya Magereza na hata majeshi yakiwa katikati ya miji, jambo hili sio la kulijibu kwa haraka haraka kwa sababu ni mpango mkubwa unaohusisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Magereza au vyombo kama hivyo ambavyo vina changamoto kama hiyo.

Mheshimiwa Spika, wacha tulichukue tuone namna tunavyoweza kulifanya lakini si jambo jepesi kwa haraka kuhamisha gereza kwa mara moja na miundombinu yake, uwekezaji uliopo pale ni mkubwa lakini ni hoja ambayo kwa kweli Mheshimiwa Mbunge acha tuichukue tuitafakari.
MHE. STANSALUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kuwa Magereza nyingi zipo katikati ya mji kwa mfano Mji wa Maswa ipo katikati ya mji na majengo na maeneo yao yanaingiliana sana na makazi ya watu na maeneo hayo yanaonekana kuwa ni potential hata kwa uwekezaji mwingine.

Je, ni lini Serikali itaamua basi kujenga Magereza nje ya miji kwa mfano Maswa tumeshatoa na eneo na kuwapa Magereza ili wajenge nje ya mji na kuachia maeneo ya katikati ya mji kwa ajili ya uendelezwaji wa shughuli zingine za kibiashara? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nyongo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwa asili zamani huko kidogo maeneo haya yalikuwa pembeni ya miji, lakini kadri miji inavyokua tumejikuta sasa wakati mwingine maeneo haya ya Magereza na hata majeshi yakiwa katikati ya miji, jambo hili sio la kulijibu kwa haraka haraka kwa sababu ni mpango mkubwa unaohusisha Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Magereza au vyombo kama hivyo ambavyo vina changamoto kama hiyo.

Mheshimiwa Spika, wacha tulichukue tuone namna tunavyoweza kulifanya lakini si jambo jepesi kwa haraka kuhamisha gereza kwa mara moja na miundombinu yake, uwekezaji uliopo pale ni mkubwa lakini ni hoja ambayo kwa kweli Mheshimiwa Mbunge acha tuichukue tuitafakari.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na ningependa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwanza fedha hizi zimekuwa zikitolewa na Halmashauri, lakini hatuoni ni namna gani zinavyorudishwa ili kuweza kukopeshwa watu wengine; je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha inaweka mkakati thabiti wa kuhakikisha kwamba hizo fedha zinavyorudi basi wapewe na watu wengine ili waweze kupatiwa mikopo hiyo na kuweza kujiendeleza katika biashara?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; je, Serikali haioni umuhimu sasa wa kutoka kwenye asilimia nne kwa wanawake, nne kwa vijana na mbili kwa walemavu kuongeza asilimia walau ziwe 15 ili kila kundi lipate asilimia tano tano? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, Mbunge wa Maswa Mashariki kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba fedha hizi asilimia kumi ambazo zimekuwa zinatolewa kwa vikundi vya wajasiriamali katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa zimewekwa kwa mujibu wa sheria na kKanuni ili ziwe ni fedha ambazo zinazunguka kwa maana ya revolving fund. Kwa maana kila vikundi ambavyo vinakopeshwa vinapaswa kutekeleza shughuli hizo za ujasiriamali na kurejesha fedha zile ambazo zilikopwa bila riba yoyote ili ziweze kutumika pia kuwakopesha vikundi vingine na hatimaye kuendelea kuwajengea uchumi mzuri wana vikundi katika vikundi hivi vya ujasiriamali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kumekuwa na changamoto ya urejeshaji wa fedha hizi kwenye baadhi ya vikundi vya ujasiriamali vinavyokopeshwa. Na sheria ya sasa imeweka utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba tunakwenda kufungua akaunti maalum kwa ajili ya fedha hizi za mikopo ya asilimia kumi na kuhakikisha kila kikundi cha ujasiriamali kitarejesha fedha hizo na zionekane zinarejeshwa na kukopeshwa kwenye vikundi vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuwaelekeza Wakurugenzi wote wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha wanalisimamia kwa karibu sana suala la mikopo na marejesho na sisi kama Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Serikali kwa ujumla tutakwenda kufanya kaguzi kuona fedha zilizokopeshwa zinarejeshwa na zinaendelea kukopeshwa katika vikundi vingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; tumeweka asilimia kumi kutokana na mazingira ya fedha za mapato ya ndani kuwa yana majukumu mengi sana; sote tunafahamu asilimia 40 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, asilimia 60 kwa Halmashauri za Mijini kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini pia kuna shughuli zingine nyingi. Wazo hili ni zuri la kufikiria kuongeza asilimia 15 lakini tutakwenda kulifanyia tathmini na kuona kama linawezekana kutekelezwa lakini kwa sasa tunaendelea na asilimia kumi kwa sababu tumeangalia vigezo mbalimbali ili kuziwezesha Halmashauri kuendelea na shughuli zake. Nakushukuru sana.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; Wilaya ya Maswa nayo ina ranchi kubwa takribani ekari 12,000 Ranchi ya Shishiu pale Maswa na Mheshimiwa Waziri analifahamu hilo.

Je, wana mpango gani wa kuwagawia wananchi wa Maswa watumie ranchi hiyo kwa ajili ya matumizi ya ufugaji maana hatuoni Serikali inafanya juhudi gani katika ranchi hiyo? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Ulega, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa majibu yake mazuri kwa Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na mawazo ya wananchi kuona kwamba maeneo ya Wizara ya Mifugo ambayo ni pamoja na ranchi na eneo ambalo analizungumza Mheshimiwa Nyongo lenyewe sio ranchi Ni holding ground, kwamba linapokuwa hivyo basi wananchi wapewe au wafanye shughuli zinginezo. Tunakubaliana kwamba tunafanya tathmini ya maeneo yote tuliyonayo ili tuone ni kwa namna gani yanaweza yakatumiwa vizuri zaidi.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa eneo la Shishiu, Halmashauri ya Wilaya ya Maswa wameleta andiko na mpango wao kuonesha ni kwa namna gani wanataka kutumia hilo eneo. Wameeleza wanataka eneo dogo, sisi tumewarudishia tukawaambia leteni mpango wa kutumia eneo lote la Shishiu kwa ujumla wake halafu tutaona ni kwa namna gani sasa mnakwenda kulitumia halafu tuweze kuwapa nafasi ya kulitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe tu Waheshimiwa Wabunge na wananchi maeneo ya Wizara ya Mifugo ambayo yapo wazi, tunataka tuyatumie kikamilifu kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe, lakini sekta binafsi ili iweze kuwekeza vizuri kwenye hayo maeneo na yaweze kutumika kwa tija zaidi, ahsante. (Makofi)
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza niishukuru sana Serikali kwa kuingia mkataba na mkandarasi huyu ili ujenzi uanze tarehe Mosi, Julai, kwa hilo kwanza napongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, ili niweze kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza, ni kwamba swali la kwanza; mikataba mingi ya ujenzi inasainiwa, lakini ujenzi unapopita maeneo yao, watu wanakuwa hawajalipwa compensation ili ujenzi ule uanze. Je, Serikali imekwishalipa compensation kwa wale watu wa sehemu ambako mradi huo unapita ili mradi huo uanze?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; mkandarasi huyu waliyepatiwa wa CHICO Construction ndio huyu huyu aliyejenga barabara ya kilometa 50 kutoka Mwigumbi kwenda Maswa. Barabara hii hata kabla haijakabidhiwa ilikuwa tayari imekwishaanza kupata mashimo na kuharibika. Mkandarasi huyo sasa hivi anafanya mobilization ku-bypass ili aanze kukarabati barabara ambayo hata bado hajaikabidhi. Je, Serikali ina uhakika gani kwamba baada ya kumpa mkandarasi huyu kazi hiyo ya bypass atajenga kwa kiwango kinachostahili? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nyongo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, utaratibu wa Serikali ni kwamba barabara haiwezi kuanza kujengwa kama wananchi hawajalipwa fidia katika eneo hilo. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kabla barabara haijaanza kujengwa, wananchi watalipwa fidia na baada ya hapo ndiyo ujenzi utaendelea; hilo namuondolea wasiwasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, anauliza mkandarasi ambaye amepewa barabara hii, M/S CHICO, kwamba alijenga barabara kutoka Mwigumbi kwenda Maswa na imeharibika. Bahati nzuri mwenyewe Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba barabara hii haijakabidhiwa, utaratibu ni kwamba ukipata kazi, unafanya kazi yako, kabla hujakabidhi kuna muda wa matazamio na lolote likitokea, kama kuna sehemu imeharibika, unapaswa kutengeneza kwa gharama zako. Ameshaelekezwa maeneo yote ambayo yameharibika ayarekebishe ili aendelee na kazi nyingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, kwamba huyu tutamfuatilia na kumsimamia kwa ukaribu, kazi lazima ikamilike. Kama kuna mahali kuna shida tutawasiliana mara kwa mara na Mheshimiwa Mbunge ambaye yuko karibu na wananchi wake, ili fedha ya Serikali ifanye kazi ambayo imekusudiwa. Ahsante.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani na wewe mwenyewe ni shahidi, usanifu umefanyika toka mwaka 2017 mpaka leo tunakwenda miaka mitano, sita bado Serikali inatafuta fedha ya kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami. Hivi kweli Serikali mko serious na ujenzi wa barabara hii? Mheshimiwa Flatei alitaka mpaka kupanda juu ya meza, hivi mnawaambia nini wananchi wa maeneo haya, Serikali mna mpango wa kujenga barabara hii lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili Mheshimiwa Waziri wananchi wa Maswa Mjini wanahitaji taa za barabarani kwa mujibu wa maelekezo yako Mheshimiwa Naibu Waziri taa 60 mmetuwekea taa 18 tu mwaka jana, mna mpango gani wa kumalizia taa zilizobaki katika mji wa Maswa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Stanslaus Haroon Nyongo Mbunge wa Maswa Mashariki kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali iko serious kuijenga barabara hii ambayo nimeitaja inayoanzia Lalago, Mwanuzi, Hydom, Mbulu hadi Karatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ninaomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika eneo la Mwanuzi-Sibiti kwenye bajeti hii tumetenga kuanza na ujenzi na zimetengwa billion 5 na tumetoa kibali lianze kwanza kujengwa daraja linaloitwa Itembe. Lakini katika barabara hiyo ambayo ni muendelezo kipande cha Mbulu Hydom tayari tumeshatangaza barabara kilomita 23 na tunaomba kipande chote kile kitangazwe, kwa hiyo muda wowote tutatangaza kilomita zote 50 ikiwa ni muendelezo wa hiyo barabara kuhakikisha kwamba yote inakamilika. Kwa hiyo, Serikali iko serious na ndio maana kazi zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili naomba nimuhakikishie kwamba tuliahidi tutakamilisha hizo taa 60 na nitoe wito ama nitoe maagizo kwa Meneja wa Mkoa wa Simiyu kuhakikisha kwamba zoezi hili linakamilika kama tulivyoahidi kama Serikali, ahsante. (Makofi)
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana, mimi nishukuru tu kwamba majibu ni mazuri, lakini siyo majibu ya swali la msingi.

Swali la msingi linauliza ni lini barabara hii inaanza kujengwa?

Kwa hiyo swali langu mimi la kwanza la nyongeza ni lini barabara hii inaanza kujengwa? Na swali la pili ni lini barabara hii inaanza kujengwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante na napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, Mbunge wa Maswa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwenye swali la msingi ni lini Serikali itajenga barabara kutoka Sibiti hadi Salama, Sayaka, Kisamba nimejibu kwamba ili uanze kuijenga barabara lazima ifanyiwe upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, na katika hiyo barabara aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge kuna eneo ambalo tumesema kilometa 71 ipo kwenye mpango wa EPC na tayari taratibu zimeshaanza.

Kwa hiyo, ni kwa maandalizi ya kuijenga na vipande ambavyo vimebaki kutoka Mwandoya Junction ambapo ni Goboko kwenda Kisesa hadi Itilima mkandarasi ameshapatikana kwa ajili ya kuanza kuifanyia usanifu, hayo yote ni maandalizi ya kuijenga kwa kiwango cha lami na baada ya kuikamilisha ndipo sasa barabara hiyo tutajua gharama za ujenzi na tutaanza kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wilaya ya Maswa hasa katika Mji wa Maswa hatujawahi kujengewa Kituo cha Polisi toka tumepata uhuru mwaka 1961: -

Je, ni lini Serikali itajenga kituo chake katika Wilaya ya Maswa na nyumba za maaskari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Nyongo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba kweli ziko wilaya hasa Wilaya kongwe kama Maswa hazina vituo vya polisi kwa maana ya ngazi ya OCD. Wizara ina mpango wa kuzijengea vituo vya polisi vya ngazi ya wilaya, wilaya zote ambazo hazina vituo hivyo kwa kutegemea upatikanaji wa fedha. Nami nafahamu wilaya hii kwa sababu pia ina mapori kule na hifadhi, wanahitaji kituo hiki, hivyo tutaipa kipaumbele katika mpango huo. (Makofi)
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba kwa mfano sisi pale katika Mkoa wa Simiyu tuna Pori la Maswa na ni pori kubwa na ni maarufu. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutangaza mapori haya kimataifa ili yaweze kutumika kwa maana ya kukaribisha watalii, vilevile kuhakikisha kwamba wananchi wa maeneo haya wananeemeka na mapori haya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli katika Halmashauri ya Maswa na Mkoa wa Simiyu kuna Pori maarufu la Maswa na kwamba Serikali imekuwa na mkakati wa kuhakikisha kwamba inatangaza mapori haya ili watalii waendelee kuja na Serikali yetu iendelee kupata mapato. Ndio maana hivi sasa tunaongea Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan anaendelea kuitangaza Royal Tour ili tuhakikishe watalii zaidi wanaendelea kuongezeka katika hifadhi zetu lakini maeneo ya kitalii ikiwepo Pori la Maswa. Kwa hiyo nimhakikishie kwamba mpango wa Serikali ni huo na utahakikisha kwamba wananchi wanaoishi maeneo ya jirani pia wananufaika na mpango huo, ahsante.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Swali langu kwa Mheshimiwa Waziri ni moja tu kwamba: Kwa kuwa mnakwenda kujenga sasa vyuo kwa wilaya zote, ina maana ya mahitaji ya walimu wa ufundi yanakwenda kuongezeka: Mna mpango gani maalum kama Wizara wa kuzalisha walimu wa kwenda kufundisha elimu ya ufundi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Nyongo, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli ujenzi wa vyuo hivi; vile 25 na hivi 63 na hivi vya mikoa unakwenda kuongeza uhitaji wa walimu kwenye eneo hili. Naomba nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge, kwanza tuna chuo chetu ambacho kinafundisha walimu wa masuala haya atakayekwenda kufundisha maeneo haya ya vyuo vya ufundi pale Morogoro. Vile vile, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Nyongo, tunakwenda kufanya maboresho ya mitaala pamoja na sera yetu ya elimu. Tutakwenda ku-convert vyuo vyetu vile vya ualimu tulivyokunavyo zaidi ya 35 ili tuingize component au kada ya ufundi mle ndani ili tuweze kupata hiyo supply ya walimu kwenye maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie vile vile Mheshimiwa Nyongo kwamba, Mheshimiwa Rais tayari alishatoa kibali cha kuajiri watumishi au walimu zaidi ya 571, ambao tunaendelea na mchakato na mpaka kufika sasa walimu 171 tayari tumeshaajiri kwa ajili kuanza kutoa mafunzo kwenye vyuo 25 ambavyo ujenzi wake umekamilika.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri, je, Serikali ina mpango gani wa kutambua, kwa sababu hii teknolojia ya viuadudu ni teknolojia ya kuangamiza mbu. Mbu ni kiumbe aliyeumbwa na Mungu kuishi duniani.

Je, Serikali imefanya mkakati gani kwamba teknolojia hii ikitamalaki mbu wote watakuwa wamekwisha yaani hatutakuwa na mbu. Je, Serikali imeshafanya utafiti kutambua umuhimu wa mbu kuwepo duniani?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli anachosema Mheshimiwa Nyongo, anazungumzia kweli unapomuondoa kiumbe yoyote ndani ya ikolojia kuna madhara yake kwenye ikolojia. Kwa sababu sehemu mbalimbali duniani wamekuwa wakifanya hilo na wakatokomeza mbu wanaoeneza malaria na haijawahi kutokea tatizo kwenye ikolojia ambalo limeweza kuleta madhara ya kibinadamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri aendelee kuiamini hii sayansi inayoenda kutumika kwa sababu moja, sisi tunaenda kumtegea mbu pale ambapo anazaliwa kwa maana ya kumuondoa pale ambapo anazaliana, lakini anapokosekana hapa ndiyo tunatumia alichosema dada yangu Mheshimiwa Ikupa kwa maana ya kunyunyuzia.

Mheshimiwa Naibu Spika, anaposhindikana eneo hilo tunatumia net, tunaenda kutumia hizo mbinu zote. Nataka kumhakikishia kwamba kitakachoenda, ndiyo maana tunataka ipate ithibati kupitia Shirika la Afya Duniani kwa maana ya WHO ili kuhakikisha hayo mambo yote unayoyasema ya ikolojia na mambo mengine yamezingatiwa, ahsante.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini ni kwamba mkopo unaotolewa na NHIF ni wa shilingi milioni 200 na utaifanya hospitali yetu kulipa kiasi cha shilingi milioni 6,500,092 kwa mwezi, katika miezi 36, na itakuwa imelipa jumla ya shilingi milioni 237, pamoja na riba ya asilimia 11.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haioni nia njema ya Wilaya ya Maswa ya kukopa NHIF kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la X–Ray ili Serikali itoe fedha ambayo si mkopo kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo la X–Ray na wananchi wapate huduma?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni lini Serikali vilevile itajenga Kituo cha Afya cha Kata ya Sangamwalugesha katika Kijiji cha Sangamwalugesha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Nyongo kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa miundombinu ya huduma za afya inatumia fedha za Serikali Kuu na fedha zinazotokana na makusanyo ya ndani, zikiwemo fedha za uchangiaji wa huduma za afya lakini pia na za Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niwapongeze sana Halmashauri ya Maswa na nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge; kwa sababu yeye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii na amekuwa mfano mzuri kuonesha tunaweza tukatumia fursa za mikopo ya NHIF, tukaboresha miundombinu na hatimaye tukatoa huduma bora zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuhakikishie pamoja na kwamba tutakatwa shilingi milioni 6,500,000, bado watakuwa na uwezo wa kuendelea kujiendesha. Pia, jengo litakalojengwa litaongeza mapato ya Hospitali yetu hii ya Maswa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili kuhusiana na hiki kituo cha afya, naomba tulipokee tukafanyie tathmini, tuone kama kinafiti kwenye vituo vya afya vya kimkakati ili tuweze kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho cha afya. Ahsante.
MHE. STANSALAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, kutokana na jibu la swali la msingi, kwamba tayari barabara hii imeshasainiwa mkataba. Naomba kuiuliza Serikali baada ya kusaini mkataba ni muda gani Mkandarasi huyu anaanza kujenga hiyo barabara ya Karatu – Haydom – Maswa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, pamoja na barabara nyingi ambazo ziko takribani sita, ziko kwenye EPC+F, baada ya kusaini nilijibu hapa kwamba, wakandarasi wameendelea kuoneshwa hayo maeneo na barabara hizi zinasimamiwa na makao makuu.

Mheshimiwa Spika, kinachofanyika sasa ikiwepo na hiyo barabara ambayo inapita kwenye Jimbo la Mheshimiwa Mbunge, ni kuwaonesha wakandarasi, wakandarasi kuzigawa zile barabara kwenye vipande (lots) zaidi ya nne na kutafuta wakandarasi wengine ambao watasimamiwa na huyo mkandarasi mkubwa kwa ajili ya kujenga hizo barabara. Kutakuwa na vipande visivyopungua vinne katika kila barabara, kwa maana ya makambi, kutafuta maeneo ambayo yana raw materials, kwa maana ya kokoto na changarawe, tayari wako wanapita na kujitambulisha kwenye hizo barabara. Kwa hiyo, mchakato unaendelea, ahsante.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni kwamba maghala mengi yamejengwa maeneo ambayo mikoa inazalisha chakula, tunakubaliana nayo. Lakini pale kuna mikoa mingine uzalishaji wa chakjula ni kidogo sana na mvua ni za shida. Inapotokea shida ya chakula kunakuwa tena kuna gharama ya kusafirisha; gharama ya fedha na gharama ya muda kutoka maeneo yanayozalisha chakula kwenda kwenye maeneo yasiyozalisha chakula.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka maghala vile vile katika maeneo ambayo mikoa inazalisha kidogo chakula kama Mkoa wa Simiyu na hasa maeneo amabayo yana shida ya chakula? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti yetu ambayo inamalizikia tumetenga shilingi 25 kwa ajili ya ujenzi wa maghala na tumeangalia maeneo yote. Kwa mfano katika Mkoa wa Simiyu hivi sasa kupitia mradi wa TANIPAC wa sumu kuvu tumebadilisha matumizi ya ghala lile ili ibaki kuwa sehemu ya ghala kuhudumia Mkoa wa Simiyu na mikoa Jirani ambao uzalishaji wake si mkubwa sawa na mazao ya chaklula ili inapotokea changamoto ya chakula cha msaada basi tuweze kukipeleka kwa uharaka zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tumezingatia pia jiografia hiyo na uzalishaji katika maeneo husika.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, majibu ya Serikali ni mazuri sana na Mkoa wa Simiyu umepewa fedha kwa ujumla kama walivyopewa Mikoa mingine. Namuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa umuhimu wa Mkoa wa Simiyu kwa sababu ya zao la pamba, kwa sababu kuna njia mbovu sana kwa mfano sasa hivi tunakwenda kusafirisha mazao ya pamba njia ni mbaya sana kutoka vijijini.

Je, Mheshimiwa Naibu Waziri uko tayari sisi kwa kushirikiana na TARURA tulete hesabu ya kipekee kwa ajili ya kupambana na tatizo hili ili muweze kutujengea barabara mbovu katika Mkoa wa Simiyu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nyongo la kuleta maombi ya kipekee; hivi sasa Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI imeteua timu ya kufanya mapitio ya namna ya kutoa mgao wa fedha za barabara kwenye Halmashauri zetu kote nchini kwa kuangalia umuhimu wa maeneo, kuangalia masuala ya kilimo yaliyokuwepo hapo, upitwaji wa magari kwa wingi na kadhalika.

Kwa sasa TARURA ilirithi mfumo ambao ulikuwa katika Road Fund ya namna ya mgawanyo wa fedha hizi zinazopelekwa, lakini baada ya timu hii kumaliza itawasilisha taarifa yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI na baada ya kuwasilisha taarifa hiyo, watakaa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, pamoja na TARURA kuona ni namna gani sasa mgawanyo wa fedha utaendana kutokana na mazingira yaliyoko katika maeneo mbalimbali hapa nchini ikiwemo kule Jimbo la Maswa anakotoka Mheshimiwa Nyongo.

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa mustakabali huo huo kwa jinsi zinavyotokea ajali nyingi si baharini tu hata pale panapotokea barabara inapokutana na reli kuna ajali nyingi sana zinatokea na kusababisha madereva wa treni sasa hivi wanapiga horn usiku kucha na kusababisha watu kutokulala hususani pale treni inapopita ili kuepusha ajali za barabarani zinazotokea. Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka automatic gates katika kila barabara na reli inapokatiza ili kuondoa ajali na kutokupiga horn usiku zinazowafanya watu kukosa usingizi?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nyongo, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwa na changamoto kubwa sana kati ya maeneo ambapo barabara inapita na reli inapita. Kwa kutambua hilo, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Shirika letu la Reli Nchini, tumetangaza tenda kwa ajili nya kuweka mifumo mipya automatic systems ambayo itakuwa ni gate way inajifunga na kufunguka automatic. Vile vile, tenda hii mwisho wa ku–submit ni kesho.

Kwa hiyo, wale wote ambao wako interested na ni international tender, wanakaribishwa kuomba ili tuweze kutengeneza mifumo yote na maeneo yote ya mapitio kati ya barabara na reli, ahsante.
MHE. STANSALAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Gereza la Maswa kama majibu ya Serikali yanavyosema ni Gereza kongwe la siku nyingi na ukarabati inawezekana ukatumia gharama kubwa, na Magereza hii ipo katikati Maswa Mjini;

Je, Serikali ipo tayari tuwapatie kiwanja nje ya mji na lile gereza mkabadilisha ikiwezekana na magereza mengine, yale magereza ya mjini mkayafanya kuwa business complex mkapata vyanzo zaidi vya ndani?

Je, mna mpango gani na zile nyumba za wafanyakazi pale Maswa ambazo nazo nazo zina hali mbaya?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nikiri, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba, Magereza ya mjini hasa ile ya Maswa ni kongwe na limechakaa sana. Nikubaliane na yeye tu baada ya Bunge hili ninatarajia kufanya ziara Mkoani Simiyu.

Pamoja na mambo mengine nitatembelea eneo la Maswa. Kama atakuwa na nafasi tukaenda wote tuone namna ambavyo tunaweza tukalifanyia ukarabati Gereza hili au kukubaliana mpango wake wa kupata eneo jingine la kujenga magereza.

Mheshimiwa Spika, kuhusu nyumba tunavyofanya ukarabati wa magereza ni pamoja na majengo yenyewe ya magereza, kwa maana ya mahabusu na vyumba wanavyokaa wafungwa, pamoja na nyumba za watumishi wakiwemo askari. Kwa hiyo, tutakapofanya ukarabati maeneo yote mawili yatazingatiwa, nashukuru.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza ninakubaliana na majibu ya Serikali, wamefanya analysis vizuri lakini jinsi bei inavyopanda katika soko la dunia kama Serikali ilivyoeleza, hata gharama za ulimaji au za kilimo zinapanda vile vile.

Je, kwa nini basi Serikali isiangalie namna ya ku-subsidize hili zao la pamba kwamba mkulima anapolima ukatengeneza bei fulani ambayo kama itashuka katika bei ya dunia basi mkulima huyo aweze kuuza kwa bei ambayo imepangwa hata kabla hajaenda kwenye kilimo, kwa sababu analima kwa gharama kubwa wakati wa kuvuna bei inakuwa imeshuka na inawaumiza sana wakulima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Mmesema wenyewe mtakuja na kitu kinaitwa price stabilization fund, mtatunga sheria mtaileta Bungeni.

Je, ni lini sheria hiyo itatungwa ili sisi wadau wa pamba tuweze kuchangia katika sheria hiyo na tuje na sheria ambayo ni nzuri kwa mkulima wa pamba nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, cha kwanza nikubaliane vile vile na maoni ya Mheshimiwa Mbunge ya kuhakikisha tuna-subsidize katika zao la pamba katika kuhakikisha tunamsaidia mkulima. Sisi kama Serikali jambo hili tumelipokea. Tunachofanya ni tathmini, tutatafuta fedha ili kuhakikisha jambo hili linafanikiwa na kuwa lenye mantiki kwa faida ya wakulima wote wa pamba nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lini sheria hiyo tutaleta, nafikiri kwa sababu tupo katika mchakato wa kuanzisha huu mfuko wa kinga ya bei. Tutakapomaliza huu mchakato ninaamini kabisa kwamba kabla hatujafika mwaka 2025 jambo hili litakuwa limekamilika na limeanza kufanyiwa kazi.