Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Ahmed Ally Salum (11 total)

MHE. AHMED A. SALUM aliuliza:-
Majibu ya Serikali ya Swali Na.1 la tarehe 6 Septemba, 2016 yanapingana na ahadi ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Magufuli aliyoitoa wakati akiwa kwenye kampeni katika Jimbo la Solwa:-
(a) Je, kwa nini Serikali inapingana na ahadi ya Mheshimiwa Rais?
(b) Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Hospitali hiyo ya Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Solwa, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa ahadi zote za Mheshimiwa Rais unafanyika kupitia mpango wa bajeti iliyotengwa kila mwaka. Hivyo, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali haipingani na agizo la Mheshimiwa Rais na kwamba Hospitali hiyo itajengwa kama agizo lilivyotolewa. Serikali itaendelea kuweka kipaumbele na kutenga bajeti kuhakikisha ujenzi unaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ilivyoelezwa katika jibu la msingi la Swali Na.1 la tarehe 9 Septemba, 2016, azma ya Serikali ni kuhakikisha tunakamilisha ujenzi wa Hospitali ile, ambapo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 zimetengwa shilingi milioni 40 kutokana na ukomo wa bajeti kwa ajili ya kuendelea na ujenzi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga kutekeleza ahadi hiyo ya Mheshimiwa Rais ndani ya kipindi hiki cha utekelezaji wa Ilani, ambapo tunatarajia kuongeza nguvu ya kibajeti kwa mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. AZZA H. HAMAD (K.n.y. MHE. AHMED ALLY SALUM) aliuliza:-
Miradi ya maji ya World Bank katika Jimbo la Solwa imesimama kwa
sababu ya Wakandarasi kutokulipwa fedha zao kwa muda mrefu sasa:-
Je, ni lini Serikali itawalipa Wakandarasi fedha zao ili miradi hiyo ikamilike.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji,
naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Jimbo la
Solwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli miradi mingi ya maji ikiwemo miradi ya
Jimbo la Solwa ilisimama kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha.
Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji mpaka sasa imeshatuma fedha
kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kiasi cha shilingi bilioni 1.17 kwa ajili
ya kuwalipa Wakandarasi kulingana na hati zao za madai walizowasilisha. Kwa
sasa wakandarasi wote wanaojenga miradi ya maji katika Halmashauri ya
Shinyanga Jimbo la Solwa wanaendelea na kazi katika Vijiji vya Mendo,
Nyashimbi, Mwanamadilana na Mwakitolyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutuma fedha katika
Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Shinyanga kwa kadri fedha
zitakavyopatikana ili kuhakikisha miradi yote inakamilika kama ilivyokusudiwa.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE (K.n.y MHE. AHMED A. SALUM) aliuliza:-
Majengo mengi yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi katika Jimbo la Solwa kama vile vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na zahanati yako katika hatua za mwisho kukamilika.
Je, kwa nini Serikali isione umuhimu wa kukamilisha majengo hayo ili yaweze kutoa huduma?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Solwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Solwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga wamejenga kwa nguvu zao vyumba vya madarasa 37, nyumba za walimu 33 na zahanati 38 ambazo zipo katika hatua mbalimbali.
Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri imetenga jumla ya shilingi milioni 695.3 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa majengo yaliyoanza kwa nguvu za wananchi katika sekta ya elimu na afya. Hadi sasa Halmashauri imeshapokea shilingi 420,881,000 ambazo zimepelekwa katika ukamilishaji wa miundombiinu ya elimu na afya.
Vilevile Serikali imeongeza fedha za ruzuku ya maendeleo kutoka shilingi bilioni 1.2 zilizotengwa katika Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/2017 hadi shilingi bilioni 1.7 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 sawa na ongezeko la asilimia 42 kwa ajili ya kutekeleza miradi kwa kuzingatia vipaumbele vya wananchi. Kulingana na muongozo wa asilimia 50 ya fedha hizo zinatakiwa kutumika katika miradi ngazi ya Halmashauri na asilimia 50 zinatakiwa kutekeleza miradi hiyo katika ngazi ya vijiji.
MHE. EZEKIEL M. MAIGE (K.n.y. MHE. AHMED A. SALUM) aliuliza:-

Waziri Mkuu alipofanya ziara katika Mkoa wa Shinyanga aliahidi ujenzi wa Vituo viwili vya Afya katika Jimbo la Solwa:-

Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Solwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 inayoelekeza kuwa na Kituo cha Afya kila Kata sambamba na utekelezaji wa ahadi mbalimbali za viongozi wa Kitaifa. Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga yenye Jimbo la Solwa ilipewa kipaumbele na kutengewa shilingi milioni 900.0 kwa ajili ujenzi na ukarabati wa Kituo cha afya Tinde, kilichogharimu shilingi milioni 400 na Kituo cha Afya Samuye kilichogharimu shilingi milioni 500. Vituo hivyo vimekamilika na vimeanza kutoa huduma kwa wananchi. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ni miongoni mwa Halmashauri 67 zilizoidhinishiwa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Fedha zote zimepokelewa na ujenzi unaendelea.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Ahmed Ally Salum Mbunge wa Solwa kuwa ahadi za viongozi zitaendelea kutekelezwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. AHMED A. SALUM aliuliza:-

Katika Jimbo la Solwa tayari kuna maboma 158 ikiwemo shule za msingi, sekondari na afya na tayari tumeomba fedha ili kukamilisha maboma hayo:-

Je, ni kiasi gani cha fedha Jimbo hilo limepata ili kukamilisha maboma hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Solwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha 2018/ 2019, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 29.9 kwa ajili ya kukamilisha maboma 2,392 ya shule za sekondari ambazo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga imepatiwa kiasi cha shilingi milioni 87.5 kwa ajili ya kukamilisha maboma saba ya shule za sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea na ukarabati/ujenzi wa vituo vya afya na zahanati 352 kwa gharama ya shilingi bilioni 184.6 ambapo kipaumbele ni ukamilishaji wa maboma yaliyoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi. Ukarabati wa vituo 352 unahusisha ukamilishaji wa maboma 199 ya vituo vya afya na zahanati.

Katika Halmashauri ya Wilaya Shinyanga, Serikali imefanya ukarabati wa Kituo cha Afya Samuye na Tinde kwa gharama ya shilingi milioni 900. Vilevile, katika mwaka wa fedha 2019/2020 kupitia mapato yake ya ndani Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga imetenga kiasi cha shilingi milioni 140 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya zahanati.
MHE. AHMED A. SALUM aliuliza:-

Usanifu na upembuzi yakinifu wa barabara ya kutoka Mwanza – Solwa – Bulige kwa kiwango cha lami umekamilika:-

Je, ni lini mradi huu utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Solwa, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara ya Mwanangwa – Misasi – Salawe – Solwa – Kahama yenye urefu wa kilometa 150 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia Mikoa ya Mwanza na Shinyanga. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami ilikamilika Desemba, 2017 kwa gharama ya shilingi milioni 798.8.

Mheshimiwa Spika, kipaumbele cha Serikali sasa ni kuunganisha Makao Makuu ya Mkoa na nchi jirani kwa barabara za lami zilizoainishwa kwenye Shoroba za Maendeleo (Development Corridor). Barabara nyingine ikiwemo ya Mwanangwa – Misasi – Salawe – Solwa – Kahama itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuifanyia matengenezo barabara hii ili ipitike majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2019/2020 kiasi cha shilingi bilioni 1.6 zimetengwa.
MHE. LUCY T. MAYENGA (K.n.y. MHE. AHMED A. SALUM) aliuliza:-

Bwawa la Ishololo katika Kata ya Usule na Misengwa katika Kata ya Musengwa ni mabwawa ambayo ujenzi wake haujakamilika kwa muda mrefu sasa; na kwa kuwa, tumeshaomba maombi maalum ili tupate fedha za kukamilisha miradi hii miwili:-

Je, Serikali inatoa tamko gani katika kukamilisha miradi hii?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Jimbo la Solwa, lenye sehemu kuu mbili kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Skimu ya Masengwa yenye eneo la ukubwa wa hekta 325 ilijengwa chini ya mradi shirikishi wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji mwaka 2004 kwa ujenzi wa banio na mfereji. Hata hivyo, skimu hiyo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji ya umwagiliaji hususan kipindi cha kiangazi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto hiyo, katika mwaka 2007/2008, Ofisi ya Umwagiliaji Kanda ya Mwanza ilifanya upembuzi wa awali na kupata sehemu ya kujengea bwawa. Katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kupitia upya upembuzi wa awali na kufanya upembuzi wa kina wa Mradi wa Umwagiliaji wa Masengwa utakaohusisha ujenzi wa bwawa ili kupata gharama halisi ya ujenzi kwa sasa. Serikali itaendelea kutafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa bwawa mapema iwezekanavyo katika mradi wa umwagiliaji Masengwa baada ya kazi ya upembuzi yakinifu kukamilika.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa ujenzi wa Bwawa wa Ishololo uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini ni mojawapo ya miradi iliyokuwa ikitekelezwa kupitia Mradi wa Uwekezaji katika Kilimo katika Wilaya yaani DASIP. Miradi hiyo ilikuwa inagharamiwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika kuanzia mwaka 2006/2007 hadi mwaka 2013/2014 ambapo jumla ya shilingi Tshs. 572,552,001.79 zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa Tuta la Bwawa ambao ulifikia asilimia 26.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mradi huo kutokamilika kwa wakati, Wizara katika mwaka 2016 ilipitia upya mpango kabambe wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji ambapo mradi huo ni mojawapo ya miradi kabambe itakayotekelezwa katika Awamu ya Kwanza. Aidha, Serikali itatuma timu ya wataalam kufanya tathmini ya mahitaji na gharama za kuendeleza mradi huo kwa sasa ili kuanza ujenzi wa mradi huo ikiwemo ujenzi wa bwawa.
MHE. AHMED ALLY SALUM Aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa skimu ya Umwagiliaji iliyopo Kata ya Isholo, Wilayani Shinyanga utakamilika baada ya kusimama tangu mwaka 2014?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum Mbunge wa Jimbo la Solwa kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo chini ya Programu ya kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) kupitia Mpango wa Kuendeleza Kilimo Wilayani (DASIP) ambao ulianza mwaka 2006 na kumalizika Disemba, 2014 umejenga skimu mbalimbali za umwagiliaji ikiwemo mradi wa umwagiliaji Ishololo. Kazi zilizokuwa zimefanyika katika mradi wa Umwagiliaji Isholo ni ujenzi wa tuta la bwawa ambao ulifikia asilimia 26.

Mheshimiwa Spika, kutokana na mradi huu kuwa miongoni mwa miradi ambayo haikukamilika chini ya mpango tajwa kufuatia fedha iliyotengwa kutotosha kumaliza kazi zote, katika mwaka 2016, baada ya Wizara kupitia upya Mpango Kabambe wa Umwagiliaji, mradi huu umepangwa katika vipaumbele na umebainisha njia nzuri ya kumalizia ujenzi wa skimu ya Ishololo.

Mheshimiwa spika, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kuendeleza ujenzi wa skimu hii katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP 2020-2025). Aidha, Tume inaendelea kutafuta fedha kutoka Vyanzo mbalimbali vya Fedha ili kukamilisha ujenzi wa mradi huo katika mwaka wa fedha 2021/2022 na hivyo kuwawezesha wakulima wa Ishololo kunufaika na skimu hiyo.
MHE. AHMED A. SALUM aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Mwanangwa – Mwakitolyo hadi Bulige Wilayani Kahama kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 – 2025?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salim, Mbunge wa Solwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Mwanangwa – Mwakitolyo hadi Bulige yenye urefu wa kilomita 118.8 ni sehemu ya barabara itokayo Mwanangwa – Misasi - Salawe – Solwa - Kahama yenye urefu wa kilomita 148.8. Serikali tayari imeanza ujenzi kwa awamu ambapo kilomita 5.65 kuanzia Kahama kuelekea Solwa na sehemu ya mita 450 katika mji wa Bulige zimekamilika kwa kiwango cha lami. Katika mwaka wa fedha 2022/2023, kiasi cha Shilingi milioni 750.62 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa kilometa 1.2. Ahsante.
MHE. SANTIEL E. KIRUMBA K.n.y. MHE. AHMED A. SALUM aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa kiwango cha lami wa Barabara ya Mwanangwa – Mwakitolyo hadi Bulige utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Solwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza ujenzi wa Barabara ya Mwanangwa – Mwakitolyo hadi Bulige yenye urefu wa kilometa 148.8 kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Jumla ya kilometa 5.65 za sehemu ya Kahama kwenye barabara hii zimejengwa kwa kiwango cha lami na mita 540, sehemu ya Bulige imejengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, aidha, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Serikali imetenga shilingi milioni 750.62 kwa ajili ya ujenzi wa kilometa 1.2, sehemu ya Solwa na Bulige ambapo mkandarasi tayari amepatikana na ameshakabidhiwa mradi ili kuanza kazi. Ujenzi umepangwa kukamilika mwezi Septemba, 2023, ahsante.
MHE. DKT. CHRISTINA C. MNZAVA K.n.y. MHE. AHMED A. SALUM aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa skimu ya umwagiliaji Kata ya Ishololo wilayani Shinyanga utakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K. n. y WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ahmed Ally Salum, Mbunge wa Jimbo la Solwa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa ujenzi wa skimu ya umwagiliaji Ishololo wenye ukubwa wa hekta 600 ni mojawapo ya miradi ambayo ilikuwa ikitekelezwa kupitia mpango wa kuendeleza kilimo wilayani (District Agricultural Sector Investiment Projects). Kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB). Ufadhili wa mpango huu ulifikia kikomo tarehe 31/12/2013 kabla ya mradi huo kukamilika. Wakati mpango wa utekelezaji wa DASIP unafikia kikomo, Utekelezaji wa Mradi wa Ishololo ulikuwa umefikia aslimia 23.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya mapitio ya usanifu katika mradi wa Ishololo ili kupata gharama halisi za kukamilisha mradi huo. Ukarabati wa mradi huo utapangwa katika Mwaka wa Fedha 2024/2025.