Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Dr. Raphael Masunga Chegeni (29 total)

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, utalii ili uweze kuendelea vizuri na uweze kuboresha Pato la Taifa ni pamoja na ushirikishwaji wa wananchi wanaoishi kando kando ya Hifadhi hizi za Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nina mgogoro sasa hivi wa wafugaji zaidi ya ng‟ombe 5000 kwa vijiji vya Kijereshi na Nyamikoma katika Jimbo la Busega ambao wamekamatwa kwa sababu ya askari wa Game Reserves kuwasukumizia kwenye hifadhi ili waweze kutoza fedha hawa wafugaji. Hii mifugo ina zaidi ya siku tatu imefungiwa kwenye pori. Hivi kweli kama tunataka ushirikishaji mzuri na uhifadhi wa maliasili zetu.
Je, Serikali inachukua hatua gani sasa kuruhusu hiyo mifugo, kwa sababu ng‟ombe hawana tatizo, ili waweze kuachiwa…

MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba ninaomba tamko la Waziri wa Maliasili kuhusiana na mifugo hii ambayo imeingizwa kwenye hifadhi kinyume cha utaratibu na kwa nini imeendelea kufungiwa kule isiachiwe? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa…

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Nakushukuru kwa kunipa nafasi kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Chegeni, Mbunge wa Busega, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, wanavijiji wanaopakana na Mbuga ya Serengeti katika eneo la Busega na vijiji hivyo ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja, wameingiza ng‟ombe zaidi ya 6000 katika eneo lao na ng‟ombe hao wamekamatwa na Askari. Jana usiku nimetoa maagizo kwamba ng‟ombe hao waachiwe na wanavijiji wachukue ng‟ombe zao bila kuchelewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kusisitiza kwa wafanyakazi wa mbuga ya Serengeti kuwaachia ng‟ombe hao mara moja. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, tunatambua kwamba Serikali ina mzigo mkubwa sana kuhusiana na masuala ya madai ya walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuuliza kwamba kuna zaidi ya 3,000 ambao wamestaafu mwaka 2014 na mwaka 2015, mpaka sasa hivi hawajalipwa mafao yao. Je, ni lini Serikali angalau mafao ya watu ambao wameshastaafu tayari wanahitaji walipwe warudi majumbani kwao watalipwa pesa hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS (TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna Walimu wamestaafu, nami naomba nikiri kwamba hata katika Ofisi yangu kuna baadhi ya walimu walifika pale moja kwa moja kuleta madai yao. Kwa mfano, kuna mwalimu mmoja alikuwa akifundisha pale Bahi. Walimu wengi waliokuwa na changamoto, walikuwa katika Mfuko wa PSPF.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Serikali imetoa maelekezo katika Mfuko wa PSPF kwamba haraka iwezekanavyo walimu wote waliokuwa wanadai, wahakikishe stahili zao zimelipwa, kwa sababu Serikali imefanya mchakato mkubwa sana kuiwezesha PSPF katika madeni iliyokuwa inadai kwamba iweze kupata mafungu ya kutosha ilimradi PSPF iendelee kulipa madeni na Serikali imetimiza hilo.
Sasa naomba nitoe agizo kwamba Mamlaka zinazohusika katika hii mifuko zihakikishe kwamba Walimu wote ambao waliokuwa wanadai waweze kupata stahili yao. Siyo jambo jema kutokuwalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano, mwalimu mmoja kutoka pale Morogoro alizimia kabisa kwa kudondoka kwasababu hakupata mafao yake. Ndiyo maana tumetoa maelekezo mazito na ni imani yangu kwamba Mfuko wa PSPF kwa sababu umeshaanza kupata mafungu yale yaliyokuwa yanadai Serikalini, iwalipe walimu wetu ilimradi waendelee kuishi maisha mazuri.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza, napenda nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake na kama alivyosema kwamba nafuatilia, ni kweli nimefuatilia hii fedha imeshafika huko Busega na imeshafanya kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Mheshimiwa Naibu Waziri kasema kwamba, makusanyo yanazidi kuimarika na kwa kuwa, Busega ni moja ya Wilaya ambazo ni mpya na miundombinu bado ina matatizo hususan barabara. Barabara ya Mwamanyiri kwenda Badugu, Barabara ya Kisamba – Nyaruhande – Nyangiri na Barabara ya Mkula – Kijereshi – Lamadi. Je, kwa kuwa, makusanyo yanaimarika; Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa barabara hizi sasa zinaboreshwa ili ziende sambamba na bajeti jinsi inavyoimarika?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa, Mikoa Mipya ikiwemo Simiyu, Katavi, Geita, Njombe na Mkoa mpya wa Songwe, ina matatizo sana ya miundombinu na kwa kuwa, bajeti ambazo zimekuwa zikitengwa za Mikoa mama ni kubwa kuliko bajeti za mikoa mipya. Je, Serikali haioni kuna haja sasa kwa mikoa mipya hii na wilaya nyingine mpya zipewe kipaumbele cha kibajeti ili zipate mafungu ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri kwamba, hivi sasa kwa dhamira tuliyonayo kwa Serikali hii ya Awamu ya Tano, nafurahi sana kufanya kazi katika Wizara hii. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa, lazima tuimarishe barabara zote, hizi ambazo amezisema Mheshimiwa Dkt. Raphael Chegeni na nyingine zote za wilaya zote na halmashauri zote Tanzania nzima. Tuna dhamira hiyo na naamini tutafikia malengo haya kwa namna tulivyodhamiria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa suala la Mikoa mipya, naomba nichukue nafasi hii kuielekeza Bodi ya Barabara Nchini pamoja na TANROAD kuangalia kwa makini sana wanavyoweka migawo ya fedha za matengenezo. Wazingatie mahitaji mahsusi yaliyoko katika mikoa hii ambayo Mheshimiwa Dkt. Raphael Chegeni, Mbunge wa Busega, ameitaja pamoja na mikoa mingine ambayo nayo ina mazingira mahsusi kwa maana ya mazingira magumu ya usafiri.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, katika ziara yake Mkoani Simiyu Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelekezo, kuna mgogoro mkubwa wa hifadhi na wananchi wa Wilaya za Busega, Wilaya ya Bariadi, Wilaya ya Itilima na Wilaya ya Meatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama Waziri Mkuu alitoa maelekezo na maagizo kwamba, Mawaziri wanne wakutane mara moja, leo ni miezi mitatu imepita hakuna kinachoendelea.
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri lini sasa mtatii agizo la Waziri Mkuu la kukutana na kutatua migogoro hii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali kupitia Waziri Mkuu akiwa Mkoani Simiyu alitoa maelekezo. Maelekezo aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri Mkuu akiwa Simiyu yamekwishaanza kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tunayo taarifa iliyoandaliwa ya undani wa orodha ya migogoro yote inayohusika katika vijitabu ambavyo tayari vimeshagawiwa kwa Waheshimiwa Wabunge wote, nia ya Serikali imekwishaelezwa mara kadhaa hapa kwamba umefika wakati sasa baada ya kukusanya taarifa za awali tunakwenda kukusanya Wizara zote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kila mmoja anafahamu, Waheshimiwa Wabunge wanafahamu na wananchi wote kwa ujumla wanafahamu kwamba sasa tuna vikao muhimu vya bajeti ambavyo vinakamilika mwisho wa mwezi wa sita, mara tu baada vikao vya bajeti tunakwenda kutekeleza ahadi hiyo ya Serikali ya kwenda kupitia upya migogoro yote hiyo kwa kushirikisha Wizara zote zinazohusika, lakini baada ya kukamilisha jukumu hili lililoko mbele yetu la Bajeti ya Taifa.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, pamoja na kazi nzuri aliyofanya katika Jimbo la Rorya, naomba tu nimuulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile ahadi ya Serikali kupitia REA III itakamilisha mradi kabambe wa kuweka umeme katika Jimbo la Rorya kuanzia tarehe 1 Julai, 2016. Je, Waziri anawahakikishiaje wananchi wa Rorya kwamba katika REA III, vijiji vyote vilivyobakia kupata umeme vitapata umeme huo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa vile Mpango wa REA III uko mpaka Jimbo la Busega na kuna Kituo cha Afya cha Lukungu pale Lamadi hakina umeme na kimeshapatiwa tayari vifaa kutoka Shirika la AMREF. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kunihakikishia kwamba kupitia REA III Kituo hiki cha Afya cha Lukungu na chenyewe kitapata umeme huo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Chegeni aliyeuliza kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge wa Rorya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa REA II tunatarajia itakamilisha kazi zake mwisho wa Juni, 2016. Nichukue nafasi hii, siyo kwa Jimbo la Rorya tu lakini na kwa Wabunge wengine, nimhakikishie Mbunge wa Rorya kwamba vijiji vyote ambavyo vilikuwa katika REA Awamu ya II ambavyo havitakamilishwa, pamoja na kwamba tunataka vikamilishwe, vitaingizwa katika REA Awamu ya III. Ni mpago wa Serikali kwamba vijiji vyote hapa nchini ambavyo havijapata umeme katika REA Awamu ya II vitapatiwa umeme katika REA Awamu ya III inayoanza Julai, 2016. Nirekebishe kidogo swali la Mheshimiwa, amesema tarehe 1 Julai siyo kukamilisha, tarehe 1 Julai sasa ndiyo tunaanza REA Awamu ya III itakayoendelea kwa miaka mitatu, minne hadi mitano, ile Awamu ya II ndiyo itakamilika Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na Jimbo la Busega kupatiwa umeme wa uhakika REA Awamu ya III, ni kweli viko vijiji vya Mheshimiwa Mbunge wa Busega, Mheshimiwa Dkt. Chegeni ambavyo vilikuwa viunganishwe umeme kwenye REA Awamu ya II lakini havijapata umeme ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Lukungu katika Mji wa Lamadi. Tunatambua eneo la Lamadi ni eneo la kibiashara kwenye Jimbo la Mheshimiwa wa Busega, eneo hilo litapatiwa umeme pamoja na vituo vingine na Kituo cha Afya cha Lukungu kitapatiwa umeme kwenye REA Awamu ya III.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimwia Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri kwanza nimpongeze amekuwa anatoa majibu marefu na mazuri.
Kwa kuwa viwanda vya pamba au vinu vya pamba katika Wilaya ya Busega vingi havifanyi kazi kwa mfano, kule Ngasamo na Nasa; na kwa sababu Waziri amesema kwamba, ana mkakati wa kuvifufua viwanda hivi, Je, kupitia sera hii mpya ya viwanda kwa Serikali ya Awamu ya Tano, viwanda hivi vitakuwa ni sehemu ya mkakati huo?
WAZIRI WAVIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 02 Mei nimezindua mkakati unaitwa C to C (cotton cloth); ukiusoma ule mkakati unaanzia kwa mzalishaji wa pamba, azalishe kwa tija. Pamba ikiwepo ginnery zitafufuka, ginnery zilikufa kwa sababu pamba haikuwepo, kwa hiyo ni mchakato mzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie kama alivyosema hapa Mheshimiwa Ndassa. Ijumaa nitakuwa na wadau wenyewe wa pamba Mwanza ambapo Wakuu wa Mikoa wote watashiriki na Bodi ya Mazao itashiriki, tutayajadili yote hayo. Nipeni information zote zinazotakiwa kwa siku ya leo kesho naanza safari nitakuwa Mwanza yote hayo nitayafanya tu, ningependa viwanda vyote vifanye kazi ikiwemo kile cha Mzee Gulamali cha Manonga.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na matatizo yaliyozungumzwa ya watu wa Kijiji cha Kitunda ambayo kwa karibu sana yanafanana na watu wa Jimbo la Busega, ambako kule Busega tuna Ziwa Victoria, hawa wana Bahari. Sasa hivi usafiri wa majini ni tatizo na Waziri mwenye dhamana wakati ule alitembelea Kijiji cha Nyamikoma katika Wilaya ya Busega na akaahidi ujenzi wa gati, lakini mpaka sasa hivi sijajua Serikali inamefikia wapi? Je, Mheshimiwa Waziri anaweza akawahakikishia wananchi wa Busega kwamba, lile gati la Nyamikoma litajengwa ili kusaidia usafiri kwa wananchi wa Jimbo la Busega na Majimbo mengine jirani kama Mwibara, Bunda na Ukerewe?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, tuna maeneo mengi ambayo yameainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi na Mheshimiwa Dkt. Raphael Chegeni anafahamu kwamba, katika aliyoyaeleza yamo. Nimhakikishie kile kilichoko katika Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi, ni wajibu wetu na ni lazima tukitekeleze katika kipindi hiki cha miaka mitano ambacho tumeahidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe Mheshimiwa Dkt. Raphael Chegeni tulitafakari kwa undani kuchunguza katika kila kituo ambacho amekiorodhesha tuone. Hatimaye tumpe majibu kipi tunaanza lini na kipi kitafuata lini na hatimaye apate ratiba kamili ya utekelezaji wa ahadi hiyo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Kwa kweli nimsifu sana kwa kazi kubwa anayofanya ya kufuatilia maslahi ya watu wako wa Jimbo la Busega. Ahsante sana.
MHE. DKT. RAPHAEL M.CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na kwa kuwa Mkoa wa Simiyu ni moja ya mikoa mipya, tuna tatizo kubwa sana la kutokuwa na Hospitali ya Rufaa. Kwa vile Mheshimiwa Nyongo alikuwa ameomba kwamba, Hospitali ya Maswa ipewe hadhi hiyo ya kuwa hospitali ya rufaa, lakini Mkoa wa Simiyu tuliamua kwamba Bariadi ndiyo inafaa kuwa Hospitali ya Rufaa. Sasa kwa kuwa Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo, ni lini ujenzi huu wa kukamilisha Hospitali ya Rufaa kwa Mkoa wa Simiyu na mikoa mingine mipya ikiwemo Mikoa ya Songwe, Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Geita pamoja na Simiyu yenyewe, lini hii mikoa mipya itasaidiwa kupata hospitali za rufaa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa katika Wilaya mpya vilevile ndani ya mikoa hii mipya ikiwemo na Wilaya ya Usega, tuna tatizo la kutokuwa na Hospitali za Wilaya na sisi katika Wilaya ya Busega tumeiteua Hospitali ya Mkula kwa mkataba wa miaka miwili kuwa hospitali teule ili iweze kutoa huduma kwa wananchi wa Wilaya ya Busega waweze kupata huduma za Kiwilaya. Lini mchakato huu wa Serikali utakamilika? Tumeshapeleka maombi Wizarani sasa ni muda mrefu lakini hatujapata majibu. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kukiri wazi kwamba, kwa mtazamo wake wa Hospitali ya Bariadi ambayo Serikali mwaka huu tunajielekeza kupeleka 1.4 billion kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa. Hapa maana yake, ule ujenzi uendelee na ni mtazamo mzuri, hata wao kule wanaona kwamba inastahili iwe Hospitali ya Kanda. Kwa hiyo, kikubwa zaidi tutaendelea kuipa nguvu hiyo Hospitali ya Bariadi, lengo kubwa ni kuwa hospitali inaweza kuhudumia ukanda wote ule. Pia suala zima la ujenzi wa Hospitali ya Mkoa, huu ni mpango mkakati wa Serikali yetu ya Awamu ya Tano kwa sababu tunajua tuna mikoa mipya ambayo, tumeianzisha kama alivyosema kuna Songwe na mikoa mingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nini kinachohitajika kufanyika? Ni kwamba katika mwaka wa fedha, kwa sababu huu ndiyo mwaka wa kwanza wa Serikali ya Awamu ya Tano, imani yangu ni kwamba katika mwaka wa fedha unaokuja niwaombe sasa Waheshimiwa Wabunge, kwa umoja wetu na katika vikao vyetu vile vya kisheria, vikao vyetu vya Madiwani, hali kadhalika vikao vyetu vya RCC, jambo hili liwe kipaumbele ili mradi mwisho wa siku na sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutakuwa tunakusanya mikakati yote ya mikoa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za mikoa. Hata hivyo, katika hili hatutosita kwa sababu lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba, kila mkoa unakuwa na hospitali yake ya mkoa na baadaye tunakuwa na hospitali za Kanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo katika swali la pili kwamba Busega hamna hospitali ya Wilaya, ni kweli na kwamba wanatumia hospitali ya Mkula kama ni hospitali teule, lakini bahati mbaya kibali bado hakijapatikana. Hivyo, tutawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Afya, lengo kubwa ni kupata kibali, lakini hata hivyo mpango mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba kila wilaya inapata hospitali ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumekwenda mbali zaidi, kwa sababu sehemu zingine coverage ya Wilaya ndani yake kuna Halmashauri kadhaa. Sasa tunasema kwamba, ikiwezekana kila Halmashauri iwe na hospitali yake, kwa hiyo huo ndio mpango wa Serikali. Imani yangu kubwa ni kwamba, tutaungana na mpango huu wote kwa pamoja kusukuma juhudi za ukusanyaji wa kodi ili tupate fedha za kutosha, mwisho wa siku maamuzi yetu ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya na Mikoa yaweze kufikiwa. Hivyo, Mheshimiwa Chegeni endelea na spidi hiyo hiyo, nadhani kila kitu kitakuwa sawasawa.

NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda tu kuongezea majibu ya nyongeza kuhusu swali la pili la kibali cha Hospitali ya Mkula, kuwa district designated hospital, kwa ajili ya Wilaya ya Busega. Tayari Mheshimiwa Raphael Chegeni, Mbunge wa Jimbo hilo amewasilisha jambo hili Wizarani kwetu na amenikabidhi barua zake mimi mwenyewe hapa Bungeni juzi tu, hata siku tatu hazijapita, ili niweze kufuatilia suala hili. Namwahidi kwamba nitawakabidhi wataalam suala hili, ili waweze kufika maeneo ya pale Mkula, bahati nzuri napafahamu vizuri, wakafanye ukaguzi, wajiridhishe kama inakidhi vigezo na hatimaye Wizara ya Afya iweze kuipa kibali cha kuwa Hospitali Teule ya Wilaya.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini inafahamika kabisa kwamba vyama hivyo vya wafanyakazi vinakuwa vinachukua matakwa na mahitaji ya wafanyakazi wenyewe. Na kwa kuwa Serikali imekuwa ikiwasaidia sana waweze kuingia katika vyama hivi na Serikali hapa imetoa agizo kwamba itawachukulia hatua waajiri ambao wanawazuia kujiunga na vyama hivi.
Je, Serikali inatoa tamko gani kwa sababu baadhi ya wafanyakazi wanakuwa wamefanya kazi lakini wanakuwa na madai yao mbalimbali ambayo hawajalipwa na Serikali. Kwa mfano, Chama cha Walimu Tanzania kina madai mengi sana Serikalini lakini madai hayo bado hayajalipwa. Je, kupitia bajeti hii, Serikali itatoa tamko la kuwalipa walimu madai yao na malimbikizo yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tamko Serikali itasema nini, naomba nirudie katika majibu yangu ya msingi ya kwamba Serikali kupitia Sheria Namba 6 ya mwaka 2004 imeendelea kutoa msisitizo kuwataka waajiri wote kuruhusu wafanyakazi wajiunge katika vyama vya wafanyakazi. Na jambo hili ni la kisheria na Kikatiba, na vilevile sisi Tanzania tumekubaliana na ile ILO Convention Namba 87 ambayo inazungumza kuhusu uhuru wa wafanyakazi kujiunga katika vyama vyao.
Kwa hiyo, nichukue tu fursa hii pia kuwataka waajiri kwa kutoa tamko tena ya kwamba wahakikishe kwamba wanawaruhusu wafanyakazi wao wote kujiunga na vyama vya wafanyakazi kwa sababu hii ni haki yao ya kimsingi ya kushirikiana kama ambavyo imesemwa kwenye sheria na kwenye Ibara 20 ya Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongezea katika majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri,katika Ofisi ya Waziri Mkuu. Ni kwamba, katika suala zima la madai ya walimu, tumezungumza kwamba sasa hivi Ofisi ya Rais - TAMISEMI inafanya uhakiki wa madai yote. Lengo letu kubwa ni kuhakikisha kwamba walimu wote ambao wanadai, na si walimu peke yake bali katika kada mbalimbali, katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha unaokuja basi madai yote tuweze kuya-address; kila mtu afanye kazi kwa morale katika mazingira yake ya kazi.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa waathirika wengi wa ulemavu, kama alivyosema Mheshimiwa Amina Mollel, katika migodi hii wanapata matatizo mengi sana wanapojikuta kwamba wanapoteza viungo vyao au wanapata ulemavu wakiwa kazini; na kwa kuwa waajiri wengi na hasa migodi hii wamekuwa hawalipi fidia wafanyakazi hawa wanaopata matatizo, na Sheria Namba 20 ambayo inaanza kutumika kuanzia mwezi ujao Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba ndiyo itaanza kushughulikia masuala haya.
Je, kwa wale waajiri ambao wamekaidi kwa muda mrefu, Serikali inatoa tamko gani ili kusudi wafanyakazi hawa ambao wameumia wakiwa kazini waweze kupata fidia zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la msingi Mheshimiwa Mbunge anauliza Serikali inachukua hatua gani au inatoa tamko gani kwa waajiri wote ambao wanakaidi kuwafidia wafanyakazi ambao wameathirika kutokana na magonjwa yanayotokana na kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi, Sheria Namba Nane ya mwaka 2008 ambayo imeunda Mfuko wa Fidia kwa wafanyakazi kupitia kifungu cha tano cha sheria hiyo itaanza kufanya kazi tarehe 1 Julai, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kubwa na maudhui ya Sheria hii ni kuhakikisha kwamba wafanyakazi wote wale ambao wamepata occupation diseases wanatibiwa kupitia mfuko huu; na wale ambao watakuwa wamepata ulemavu uliosababishwa na shughuli za kazi na wenyewe wanaweza kufidiwa au kupata mataibabu kutokana na aina ya ugonjwa walioupata kutokana na ripoti ya madaktari Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Serikali sasa inafanyaje? Katika mazingira haya kumtaka mwajiri atimize wajibu wake uko utaratibu ambao uko kwa mujibu wa sheria ambao umewekwa ya kwamba waajiri wote watatakiwa kwanza kuwasilisha michango yao kwa mujibu wa sheria ambapo Sekta Binafsi watatakiwa kuchangia asilimia moja ya wage bill ya kila mwezi, na katika sekta ya umma vilevile asilimia 0.5. sasa kwa wale ambao watakaidi kuchangia maana yake ni kwamba kwanza sheria inasema watatozwa fine ya riba ya asilimia 10 ya kile ambacho wamekichelewesha, lakini pili watapelekwa pia mahakamani na wakithibitika kwamba wameshindwa kuwasilisha michango hiyo adhabu ni kuanzia shilingi milioni 50 au pia kifungo kisichopungua miaka mitano mpaka kumi cha mkuu wa taasisi hiyo.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Napenda kuuliza swali moja.
Katika hii Mikoa na Wilaya mpya, nyingi zina matatizo ya kutokuwa na shule za kidato cha tano na sita. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuzisaidia hizi Wilaya mpya ikiwepo Busega, ambayo mpaka leo hii hatuna shule ya A-Level? Mheshimiwa Waziri anaweza kunipa mkakati gani wa Serikali kusaidia hizi Wilaya na Mikoa mipya?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba yapo baadhi ya maeneo makubwa hadi Wilaya nzima ambako hakuna shule ya kidato cha tano na sita, lakini nilisema hapa kwamba sekta ya elimu imekuwa decentralized na kwa hiyo maana ya decentralization ni kwamba mipango yote inapangwa kuanzia kule chini na ikiletwa kwetu ni kwa ajili ya kuona tu kwamba tunaipokea na kukubaliana na wadau kama ambavyo tunavyosema kwamba Halmashauri ndizo zinazomiliki shule hizi na kwa kufanya hivyo tunaamini kwamba ndiyo sera ile ya D by D inapokuwa imetekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninamsihi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kama wao wataanzisha jambo hili wakalikamilisha, wakileta kwetu hatuna pingamizi kama watakuwa wameziteua shule watakazodhani zinaweza zikawa ni rahisi kuzifanya ziwe high school.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali madogo mawili. Kwa kuwa Chama cha Mapinduzi kinaongoza kwa kuwa na utaratibu unaoeleweka na wa kidemokrasia ndani ya chama chake tofauti na baadhi ya vyama ambavyo vimekuwa havina uongozi wa demokrasia iliyoshamiri. Je, Serikali kupitia kwa Msajili wa Vyama anaweka utaratibu gani ili kuhakikisha demokrasia ndani ya vyama inatekelezwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa nchi yetu iko kwenye vyama vingi na baadhi ya wanasiasa wanagomea mijadala ndani ya Bunge kitu ambacho ni kuwanyima haki wananchi ambao wamewachagua ili waje kuwawakilisha ndani ya Bunge. Je, Bunge hili linazidi kuchukua hatua gani dhidi ya kitendo hiki cha kutowatendea haki wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza limeulizwa, Serikali kupitia Msajili wa Vyama vya Siasa inahakikisha vipi demokrasia inakuwepo katika vyama vya siasa. Vyama vya siasa vipo kwa mujibu wa sheria ambayo imevianzisha lakini vilevile vyama hivi vinasimamiwa na Msajili wa Vyama ambaye kazi yake kubwa ni kuratibu shughuli zote za vyama na amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba vyama vyote vinatii sheria ambayo imeviunda lakini na Katiba ya nchi ambayo inaelekeza masuala mbalimbali ya kiuongozi katika vyama hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa nafasi ya Msajili wa Vyama vya Siasa yeye siku zote ndiye amekuwa mlezi wa vyama hivi na popote pale ambapo kumekuwa kuna shida ya masuala ya kidemokrasia ndani ya vyama amekuwa akichukua hatua stahiki kwa maana ya kukutana na wadau na kuweka mambo sawasawa katika vyama hivi. Kwa hiyo, tunaendelea kuamini kwamba kwa nafasi ya Msajili ataendelea kuvilea vyama hivi na kuhakikisha demokrasia inakuwepo katika vyama vya siasa kama ambavyo vimeanzishwa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili limeulizwa kwamba kama Serikali tunachukua hatua gani sasa kwa namna ambavyo hali inaendelea hapa Bungeni ambapo baadhi ya wenzetu wanatoka nje na hivyo wananchi kukosa uwakilishi kupitia uongozi wao humu ndani. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari jambo hili lilishatolewa ufafanuzi mara nyingi sana na wewe Naibu Spika ulishatoa maelekezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nisirudie maneno mazuri ambayo umekwishayatoa, lakini msimamo unafahamika kwamba wote tumeingia humu ndani kwa ajili ya kutetea na kuwasilisha maslahi ya watu wetu. Kwa hiyo, ndugu zangu Watanzania wenzetu huko nje wanaona ambao wamebaki kutetea maslahi yao na ambao wametoka.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda niipongeze Serikali kupitia Mradi huu wa REA I, II na III. Kwa kuwa kuna Kata ya Badugu yenye vijiji vya Mwaniga, Manala, Badugu yenyewe na Busani mpaka leo wanaona nguzo za umeme zimepita tu, lakini hawajapewa transfoma. Je, Mheshimiwa Waziri ananihakikishia kwamba vijiji hivi vitapata umeme sasa kuanzia Julai?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa vijiji vya Nyakaboja vilivyoko kwenye njia kuu ya kwenda Musoma, Vijiji vya Mngasa, Kalago na Lukungu ambako kuna kituo cha afya mpaka leo hakuna umeme. Je, Mheshimiwa Waziri vilevile atanihakikisha kwamba vijijni hivi ambavyo vinatoa na huduma za Hospitali ya Lukungu pamoja na Hoteli ya Serenity na Speke Bay ambazo zinaingiza mapato kwa nchi hii, vitapatiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Kata ya Badugu kupatiwa umeme, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba vijiji vyote vya Kata ya Badugu, kama anavyojua Mheshimiwa mwenyewe ni kwamba maeneo yote ya Nyamikoma, Nyakaboja, Nyakungula pamoja na yale yote ambayo yanaunganishwa Kata ya Badugu yatapatiwa umeme kwenye awamu hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, vijiji vya Kata ya Badugu ambavyo vimebaki ambavyo vinajumuisha maeneo ya Nyamanara, Nyamikoma, Nyazikungura pamoja na maeneo mengine ya Lamadi yatapatiwa umeme kwenye transfoma itakayofungwa kuanzia Julai, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu umeme kwa vijiji ambavyo vinaungainisha hospitali ya Lukungu pamoja na hoteli ya Serenity iliyopo Lamadi, nimhakikishie Mheshimiwa Dkt. Chegeni kwamba vijiji vyote vilivyobaki ambavyo ni vijiji 16 vitapatiwa umeme. Awamu ya kwanza ya REA kwenye Jimbo la Busega tulipeleka vijiji 22 na katika Awamu ya II ya REA kwenye Jimbo hilo hilo la Busega tumepeleka vijiji 18 na Awamu ya III ya REA kwenye Jimbo hilo hilo tunapeleka vijiji 19 vyote vilivyobaki. Vijiji hivyo ni pamoja na Ng‟wanangi, Ng‟wanale, Vijiji vya Lamadi vilivyobaki vyote vitawaka umeme kwenye Jimbo la Busega.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante sana. Napenda nishukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa muuliza swali ametoka Bungeni humu na ameliacha swali hili, mimi naomba niulize kama ifuatavyo:- (Makofi)
Mheshimiwa Waziri, kwa kuwa wananchi wa Luchelele wamekuwa kwa muda mrefu sana wakiahidiwa kuhusu suala la fidia; na pale Luchelele kulikuwa na mpango mpaka kujenga kiwanja cha golf ambacho mpaka leo hii imekuwa ni hadithi; na hii mara kwa mara tunaambiwa kuna fidia italipwa, imechukua muda mrefu. Sasa Serikali imefikia wapi kwa suala la fidia ili kweli wananchi wa Luchelele walipwe fidia yao na Serikali iendelee na mpango wake wa Luchelele kama ilivyopangilia?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Wilaya ya Nyamagana inapanuka kuelekea sehemu za Luchelele na kwa kuwa mipango mingi kule inafanyika. Je, Serikali kupitia Wizara yako, ina mkakati gani kuhakikisha kwamba ile Luchelele na St. Augustine yote inaendelezwa kwa mpango na masharti ya Mpango Mji wa Jiji la Mwanza?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika majibu yangu ya awali nilisema kwamba wananchi hawa watalipwa fidia na taarifa zilizopo kama nilivyosema ni kwamba kuna mkopo kutoka CRDB. Status ya mkopo huo ni nini na tumefikia wapi mpaka sasa? Ni kwamba walipoleta ile request, katika ile shilingi bilioni sita, CRDB walikuwa wameweka commitment yao kuwakopesha shilingi bilioni 5.5. Kwa hiyo, ilivyokuja ile request TAMISEMI, ikaonekana kwamba deni linalodaiwa ni tofauti na mkopo watakaoweza kupata.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ikatakiwa clarification, ni jinsi gani pesa nyingine itaweza kupatikana hapo? Wakaandikiwa tena barua, Mkurugenzi wa Nyamagana ambayo ni barua ya tarehe 5 Mei, 2016 kumwambia kwamba alete mchanganuo huo sasa, ile tofauti ya shilingi bilioni 2.5 ambayo inatakiwa ku-top up na ile ambayo inatoka CRDB, kuona italipwa vipi na utaratibu wake utakuwaje?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wakaleta hiyo feedback tena katika Ofisi ya TAMISEMI lakini hawakuambatanisha ule muhtasari wa vikao vilivyokubaliana hilo. Kwa hiyo, ofisi yetu imepeleka hiyo barua tena. Lengo ni kuleta zile attachments za makubaliano ya kikao ili mradi ofisi ya Rais, TAMISEMI iendelee na process ya kuhakikisha jambo hili linakamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili kuhusu mikakati ya kuendeleza Wilaya ya Nyamagana; kama nilivyosema watu wa Nyamagana mpango wao mkubwa ni kuhakikisha maeneo hayo yanapimwa. Tunajua wazi kwamba Jiji la Mwanza ni kubwa sana, ndiyo maana katika suala zima la uendelezaji wake, tunaelekeza hizi Halmashauri na Manispaa zetu ziweze kuweka utaratibu mzuri wa mipango miji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana watu wa Jiji la Mwanza, kwa sasabu kwa utashi wao mzuri na mawasiliano mazuri wamesababisha Jiji la Mwanza libadilike. Kwa kushirikiana na LAPF wametengeneza center nzuri sana ya kibiashara. Ni imani yangu kubwa sana kwamba mpango ule walioufanya LAPF na mikakati yao ya upimaji katika eneo la Nyamagana kuelekea maeneo haya ya Luchelele itaendelea. Lengo kubwa ni kulibadilisha Jiji la Mwanza liendelee kuwa bora, katika suala zima la kuendeleza Kanda ya Ziwa ya nchi yetu.

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza namshukuru Naibu Waziri kwa majibu mazuri, lakini nilitaka kuongezea tu katika majibu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la uendelezaji wa Mji wa Mwanza kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameuliza, Jiji la Mwanza pamoja na Majiji mengine kama 14 yako kwenye utaratibu wa kupanga Miji yao kwa maana ya kuwa na master plan; na Jiji la Mwanza ni mojawapo na master plan yake inaandaliwa na wameshirikishwa vizuri. Kwa hiyo, hata hawa ambao wako Luchelele wamekuwa considered katika ile master plan ambayo iko katika process ambayo inaandaliwa. Baada ya muda mfupi nadhani kwenye mwezi Juni hii itakuwa imekamilika na watakuwa katika utaratibu mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika suala la fidia siyo Luchelele peke yake, ni maeneo mengi labda kwa kutumia fursa hii pia niseme Wizara imejipanga katika kuhakikisha tunawakumbusha wale wote ambao Mashirika na Taasisi mbalimbali ambazo zinadaiwa wakimewo wenzetu wa Airport Dar es Salaam na maeneo mengine na hata yale yaliyochukuliwa na Jeshi. Tunawaandikia ili kuwakumbusha zile fidia waweze kuzilipa kwa sababu zimekuwa za muda mrefu na kadri zinavyokaa ndivyo jinsi gharama ya Serikali inavyokuwa kubwa hasa katika kupitia katika Mashirika yenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutalizingatia na tutaendelea kulifuatilia na watu wa Mwanza, Luchelele na maeneo mengine watafidiwa.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na kwa Serikali yetu kwa mpango mzuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu kwa kweli ni mradi ambao una tija kubwa sana kwa wananchi wa maeneo husika katika Wilaya ya Busega, Wilaya ya Itilima, Bariadi, Maswa na Meatu. Kwa kuwa mradi huu utakapopita vijiji ambavyo vipo umbali wa kilomita 12, kushoto na kulia mwa bomba kuu, vitapata huduma ya maji: Je, Serikali ina mpango gani kwa vijiji ambavyo vipo nje ya mradi huu kupatiwa maji ili waweze kunufaika na mradi wa namna hii? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa Ziwa Victoria lina maji mengi sana na mikoa mingi ina matatizo ya maji, kwa nini Serikali isiwe na mpango mwingine kabambe; baada ya Mkoa wa Simiyu kupata maji, basi Mkoa wa Singida na wenyewe upate maji na mpaka Dodoma nao waweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kwa kunipa pongezi; lakini pili, vijiji vinavyotarajiwa kunufaika na mradi huu ambavyo vipo umbali wa kilomita 12 kutoka katikati ya bomba ni vijiji 223.
Swali lake namba moja ameuliza, vijiji ambavyo vipo nje ya zile kilomita 12; nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, baada ya mradi kukamilika huwa tuna utaratibu wa kuendelea kutoa fedha kwenye mamlaka zilizo karibu na hilo bomba ili ziweze kuendeleza kupeleka maji kwenye maeneo ambayo hayakupitiwa na huo mradi. Kwa hiyo, tutaendelea kufanya hivyo kama ambavyo tumeshaendelea kufanya kwenye mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Shinyanga.
Swali la pili, Ziwa Victoria lina maji mengi; ni kweli lina maji mengi. Kuna utaratibu gani wa kupeleka maji kwenye maeneo ambayo hayajapata maji ikiwemo pamoja na Mkoa wa Singida?
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tayari tuna mradi tumepata Dola milioni 265 na mwaka wa fedha unaokuja tunasaini mkataba kwa ajili ya kupeleka maji ya Ziwa Viktoria, Nzega, Mkoa wa Tabora hadi Igunga.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tumesema kwamba sasa hivi tutaanza kufanya utafiti, upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kupeleka maji pia katika Mkoa wa Singida ambao ni mkoa kame na hauna maji ya kutosheleza kule chini. Kwa hiyo, tunaendelea kufanya tafiti ili kuhakikisha kwamba maji yanawafikia wananchi wote.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, napenda tu kuuliza swali dogo kwa Mheshimiwa Waziri.
Kwa kuwa Bodi ya Pamba muda mwingi iko Dar es Salaam na Makao Makuu yako Dar es Salaam, na kwa kuwa Mkoa wa Simiyu ndio Mkoa unaoongoza kulima pamba hapa nchini. Je, Serikali inatoa tamko gani kwa wakulima ambao wamekuwa wakipata mbegu hizi na dawa ambazo haziwasaidii na wala hawapewi fidia. Ni lini Bodi hii itahamia karibu na Mikoa ambayo inazalisha pamba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi ameshatoa agizo la Bodi ya Pamba kuhamia Mwanza na kwa taarifa tulizonazo ni kwamba wanatakiwa wawe wamehama kabla ya tarehe 10 mwezi huu.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili. Swali la kwanza, kwa kuwa hizi zana haramu, yaani nyavu pamoja na zana nyingine zinatengenezwa na viwanda vilivyoko hapa nchini na zinaagizwa kuingia hapa nchini na wafanyabiashara: Je, Serikali inachukua hatua gani kwa hao watu ambao wanaleta zana haramu hapa nchini? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa wavuvi haramu hasa ni watu ambao wanajitafutia riziki zao, wengi wamenyang’anywa zana zao na kuchomwa moto ili kuitikia agizo la kisheria la nchi: Je, Serikali ina mpango gani kuwasaidia hao wananchi ambao maisha yao yote yanategemea uvuvi lakini kwa sasa hawawezi kufanya kwa sababu wanakiuka sheria? Wanasaidiwaje kupata mikopo angalau waweze kuendesha maisha yao, lakini pili kufundishwa namna endelevu ya kufanya uvuvi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haijaishia tu katika kukamata makokoro na zana nyingine haramu zinazotumika katika uvuvi, lakini vile vile kuhakikisha kwamba, pale yanapotengenezwa na yanapotokea, vilevile wanaohusika wanakamatwa.
Waheshimiwa Wabunge, kama mtakumbuka, ni karibuni tu meli iliyoingia katika bandari ya Dar es Salam ilishikwa ikiwa imebeba zana mbalimbali za uvuvi zikiwepo zana za kutengeneza makokoro na nyavu ndogo ambazo inaaminiwa zingeweza kutengeneza mpaka nyavu 20,000. Huo ni mfano tu wa kuonesha kwamba siyo tu tunakamata wavuvi, lakini vile vile hata viwanda na hata katika kuingiza vile vile tunadhibiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, ifahamike tu kwamba, ugumu unaotokea ni kwamba zana za uvuvi au vifaa vinavyotumikia kutengeneza zana za uvuvi vile vile zinatumika kutengeneza vitu vingine ambavyo ni halali. Kwa mfano nyavu, siyo kwamba unakuta hasa kwamba ile bidhaa inayotoka kiwandani ni haramu; inaweza ikawa inatumika kwa ajili ya vitu vingine ambavyo vinaruhusiwa kisheria. Kwa hiyo, kidogo inaleta shida, lakini pale tunapobaini moja kwa moja kwamba ni kifaa au ni zana ambayo inaenda kutumika kufanya uvuvi haramu au kutengeneza zana za uvuvi haramu, tunachukua hatua.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, ni kuhusu msaada gani Serikali inatoa kwa wavuvi wadogo? Nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Wizara hii, imeweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba wavuvi wadogo wanaweza kupata mikopo kupitia katika Benki yetu ya Kilimo, lakini vile vile kuna mikopo ambayo inapatikana kwa ajili ya pembejeo kupitia Mfuko wa Pembejeo. Tayari Benki ya Uwekezaji ambayo nayo ina fursa kwa ajili ya mikopo na Wizara pia inakopesha vikundi mbalimbali vya wavuvi. Kwa hiyo, kuna fursa mbalimbali kwa vikundi na wavuvi ambao watahitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiacha fursa zilizopo kwa ajili ya kutoa mikopo, Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri mbalimbali imeendelea kutoa elimu kuhusu uvuvi endelevu na uvuvi bora kwa kupitia vikundi mbalimbali vya Beach Management Unit na tayari katika maeneo mengi ya nchi yetu, elimu hii imetolewa, lakini kama nilivyosema tunatoa elimu kupitia vyombo vya habari kama television na tunaamini imesaidia sana kupunguza tatizo la uvuvi haramu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunavyofahamu, uvuvi haramu ni kama uhalifu mwingine. Hata watu wakiwa na elimu namna gani, bado mara nyingi kuna tabia ya wahalifu kuendelea kuwepo, lakini Serikali itaendelea na jitihada za kupambana na uvuvi haramu.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna wilaya nyingi mpya ambazo zina matatizo sana ya hata kutokuwa na Hospitali za Wilaya. Na kwa kuwa majibu yake anasema kwamba kuna fedha ambazo zimetengwa, je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kunihakikishia kwamba katika Wilaya ya Busega kituo cha Nasa hizo fedha zitapatikana lini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Dkt. Chegeni unafahamu na wewe kule kwako umenikaribisha, nakushukuru sana. Hicho kituo cha afya ulichokisema
miongoni mwa maeneo ambayo yana changamoto, na akina mama wanapata shida kubwa sana kupata huduma za upasuaji. Nilikueleza wazi kwamba katika kipindi cha huu
mwaka tutafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kwamba tunajenga jengo la upasuaji kama nilivyosema katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuwa na imani,
kwamba Serikali kwa kupitia Wizara ya afya tuna mkakati mpana sana kuhakikisha kwamba tunapelekea huduma katika maeneo hayo na Mungu akijaalia kabla ya mwezi wa sita tunaweza tukaenda kuweka jiwe la msingi sawa sawa
na kituo cha afya cha Malya kule kwa ndugu yangu Ndassa.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya
Mheshimiwa Waziri, Halmashauri nyingi zina mapato kidogo na kwa vile baadhi ya vyanzo vya mapato Serikali Kuu
imevichukua, kwa hiyo, ina maana kwamba baadhi ya Halmashauri hazitaweza kulipa Wenyeviti kwa mujibu wa
majibu ya Mheshimiwa Waziri alivyosema hapa. (Makofi)
Je, Serikali ina mpango gani mbadala kuhakikisha kwamba Wenyeviti wote, regardless wanatoka kwenye
Halmashauri ipi na wenyewe waweze kupata malipo kama haya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuna wakati mwingine marejesho yanakuwa siyo rafiki sana, ndiyo maana katika utaratibu wa sasa inawezekana Wabunge wengine watauliza kwamba property tax imechukuliwa imeenda Serikali Kuu, tunafanyaje na haijaridi? Hili hata Waziri wa Fedha baadaye akija ku-table bajeti yake hapa katika mjadala mpana baadaye, itaonekana ni jinsi gani tutafanya. Lengo letu ni kuziwezesha Halmashauri zetu cha kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu changamoto hii hata Waheshimiwa Wabunge wengine wanaweza
wakasimama baadaye wakasema hata Madiwani wengine wamekopeshwa kwenye mabenki, wanataka kupelekewa mahakamani, ndiyo maana nasema katika mchakato huu mpana, mara baada ya kurekebisha sheria, kwa sababu sheria ile itakuja hapa mtaona kwamba Waziri mwenye dhamana atakuwa anapata fursa ya kuhakikisha Halmashauri zinaenda vizuri, kwa sababu zimewekwa kwa mujibu wa Katiba, Ibara ya 145 na utelekezaji wake Ibara ya 146.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Waziri mwenye dhamana amepewa mamlaka hiyo kwa utaratibu wa sheria
za nchi Sura namba 287 na 288 ile ya vijijini na ile ya miji. Kwa hiyo, katika kurekebisha Sheria ya Fedha, itamsaidia sana Waziri mwenye dhamana kufanya maamuzi hayo mwisho wasiku kwa kuangalia jiografia ya Halmashauri hizi ambapo zenyewe zinatofautiana katika nguvu ya kimapato.
Halmashauri ya Ilala huwezi ukafananisha na Halmashauri ya Kakonko kwa mwalimu wangu pale, hizi zinatofautiana. Kwa hiyo, Waziri mwenye dhamana atakuwa anapata nafasi nzuri kuiangalia nchi kwa upana wake na kuangalia hizi Halmashauri, Madiwani na Wenyeviti ili kazi iende vizuri.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuweza kuniona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri
ya Mawaziri na Naibu Waziri, kwa Wilaya ambazo ni mpya na Mheshimiwa Naibu Waziri amezungumzia suala la Busega kwamba alikuta pale matatizo ya watumishi, je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia Wilaya hizi mpya ambazo zimeanzishwa zenye uhaba wa ikama ya watumishi? Vilevile pili baadhi ya watumishi walio wengi hawajalipwa mafao yao. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu pale awali ni kwamba tutajitahidi Halmashauri hizi mpya ambazo zimeanzishwa na bahati nzuri Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi) amezungumza wazi kwamba tuna hizi ajira mpya ambazo zinakuja lengo kubwa ni kuziba mapengo yote yaliyokuwepo katika maeneo yetu. Ofisi yetu imeshaanza kufanya tathmini ya kujua ni watumishi wangapi wanahitajika katika Halmashauri gani ili kuziba haya mapengo yaliyopo. Kwa hiyo, mtani wangu Mheshimiwa Dkt. Chegeni ondoa hofu zoezi hili litaweza kujibu matatizo ya watumishi katika Jimbo na Halmashauri yako ya Busega.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, suala la zao la pamba na usindikaji wake au kuongeza thamani ni suala la msingi sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Busega kuna vinu ambavyo ni vya viwanda vya Pamba kama cha Ngasamo na Sir Ginnery. Maeneo yote haya yamekuwa na viwanda ambavyo vimesimama, havifanyi kazi na hivyo kupelekea wananchi wengi na wakulima wa pamba kushindwa kuuza pamba yao kwa bei yenye kuongeza thamani. Je, Mheshimiwa Waziri ana mkakati gani? Pamoja na suala la Manonga na kwingineko ambako kuna viwanda ambavyo havifanyi kazi vizuri, kama Serikali kuna namna gani ya kuweza kuboresha viwanda hivi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, chanda chema huvikwa pete. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wanaotoka kwenye eneo la pamba, nenda kwenye mkakati wa pamba mpaka mavazi, ukurasa wa 91 majibu yote yako pale. Tutaweza kufaidika na pamba kama zamani, soko litakapokuwa linaweza kuvuta (the demand pull) na mojawapo ya mambo ya kufanya ni kuongeza ufanisi katika zao la pamba. Mwaka 2016 kwa kutumia ways and measures baada ya ku-control watu wasichafue pamba, nyie ni mashuhuda bei imepanda kidogo, tutaendelea na nikuahidi Mheshimiwa Mbunge tukitoka hapa nitakupa huo ukurasa namba 91 nilikuja nao nilijua itajitokea uone mambo mazuri. The productivity, pamba ina tatizo kwa sababu hakuna tija katika uzalishaji.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Lamadi ni mji ambao kijiografia unapanuka kwa kasi sana; na kwa kuwa Lamadi hiyo hiyo imeshakidhi vigezo ambavyo Mheshimiwa Waziri amevizungumza hapa, Wizara ya Ardhi imeshapima viwanja pale, miundombinu ya maji ipo, barabara zipo na Mheshimiwa Rais alipokuja alivutiwa sana na mji ule na akasema kwamba angependa uwe mji wa kibiashara, ufanye biashara kwa saa 24 kwa siku.
Je, Serikali haioni kwamba kama kuna kitu kinaitwa
hati ya dharura basi itumike kuufanya Mji wa Lamadi Mji mdogo ili kusudi iweze kuchochea maendeleo kwa wananchi badala ya kuendelea kuuacha hivi hivi ambapo baadaye unaweza ukaleta matatizo makubwa zaidi?
Swali la pili, kwa kuwa ukiangalia katika barabara inayotoka Mwanza kwenda Musoma, mji pekee ambao unakua zaidi ni Lamadi, Serikali haioni kwamba kuendela kuuachia kutangaza Halmashauri ya Mji Mdogo wa Lamadi itazidi kuleta matatizo makubwa zaidi kwa wananchi na kusababisha mpangilio ambao baadaye itakuwa ni tatizo kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Dkt. Chegeni mjukuu wa Mzee Mchengerwa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, alivyosema kupeleka hati
ya dharura kwamba Mji wa Lamadi utangazwe kwa hati ya dharura, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Chegeni tulifika pale kwako Lamadi na mimi najua expansion ya mji ule unavyokua kwa kasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa zaidi ni kwamba kilio hiki tumekisikia na bahati nzuri Mheshimiwa Rais ameshaweka commitment pale alipokuwa site na bahati mbaya tulivyoangalia kuna baadhi ya changamoto ndogo ndogo ambazo zipo kuufanya mji ule tuutangaze rasmi. Naomba niseme kwamba jambo hili tunalichukua kwa pamoja, baadaye tujadiliane miongoni mwa zile changamoto zilizokuwepo tuziweke sawa ili mradi tuweze kufikia katika mpango ambao unastahiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika jambo lingine kuhusu kuutangaza rasmi, Mheshimiwa Chegeni naomba tutakapokaa baadaye vizuri na bahati nzuri na Mheshimiwa Waziri wangu wa Nchi hapa yupo na amekusikia naye jambo hilo analiangalia kwa karibu zaidi tutafanya utaratibu wa kuona jinsi gani tufanye ili commitment ya Mheshimiwa Rais ameiweka pale basi mwisho wa siku waone kwamba kulikuwa na Dkt. Chegeni amepigania Mji wa Lamadi umeweza kupatikana na kuufanya mji wa kibiashara uweze kuendana na hadhi kwa kadri tutakavyoweza kuutangaza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kilio chako tumekisikia, tutaakaa pamoja, tutajadiliana pamoja nini tufanye sasa cha haraka kwa mustakabali wa Mji wa Lamadi ambao unakua kwa kasi. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ujenzi, nina swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa baadhi ya makampuni haya kwa muda mrefu sana yamekuwa yakifanya udanganyifu na hasa katika miamala ya simu pamoja na muda wa maongezi kwa wateja na kwa kuwa Serikali tayari imeshaanza kudhibiti suala hili. Je, Serikali haioni kwamba ni busara na ni vyema kuendelea kudhibiti makampuni yote haya ya simu yaweze kulipa kipato sahihi na kutokuwanyonya wananchi katika suala la miamala ya simu pamoja na muda wa maongezi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana naye na ndivyo tunavyotaka kufanya na tunavyoEndelea kufanya kwa kutumia huu mtambo wa TTMS na makampuni yote hatutaacha hata moja tutayaingiza katika mfumo huu na kuhakikisha mapato yao yote yanayopatikana tunayafahamu na tunapata haki yetu.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu, hoja ya swali la Mheshimiwa Kishimba ni kwamba kumekuwa na utaratibu wa kumtahini mwanafunzi kwa mtihani wa mwisho na wakati mwingine unakuta mwanafunzi pengine zile siku za mwisho anakuwa na matatizo ambayo yanamfanya ashindwe kufaulu vizuri.
Je, Serikali haioni kwamba kuna haja ya kuangalia maendeleo ya mwanafunzi huyu ili kusudi maendeleo yake yawe ni sehemu ya mtihani wake wa mwisho ili kuondoa mchanganyiko huu?
Swali la pili, kwa vile kumekuwa na wizi wa mitihani mara kwa mara na hii inachangiwa kwa sababu wanafunzi wanajiandaa kwenda kushinda mtihani badala ya kujua namna ya kujibu mtihani.
Je, Serikali inatafuta mbinu gani mbadala za kuwasaidia vijana badala ya kukariri kufanya mtihani, wafanye mtihani kwa kuelewa namna ya kushinda mtihani?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, Serikali imekuwa ikifanya hivyo kwa kutumia matokeo endelevu yaani mwanafunzi amekuwa akipimwa katika muda wake anaokuwa darasani, vilevile hata wale wanaofanya shughuli za vitendo, kwa mfano wale wanaosoma masomo ya ufundi wamekuwa wakienda kwenye mazoezi wanafuatiliwa na pia shughuli za vitendo zimekuwa zikichangia asilimia 30 niliyosema katika mitihani ya mwisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile mtihani wa mwisho ni kweli ndiyo unakuwa na nafasi kubwa zaidi kwa ajili ya hiyo asilimia 70; endapo mwanafunzi amepata tatizo siku ya mwisho ya mtihani, taarifa huwa zinatolewa na kuweza kuangalia kwamba alikuwa kwenye mazingira gani. Wakati mwingine mwanafunzi anashauriwa asifanye mtihani kama hali yake kwa mfano itakuwa ni ya ugonjwa ili aweze kurudia na kufanya mtihani wakati mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa wizi kwa kiwango kikubwa Serikali imeweza kudhibiti tatizo hilo, nanyi mtakuwa mashahidi katika kipindi hiki, hasa toka tumeingia halijawahi kutokea tatizo la wizi wa mitihani. (Makofi)

WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri na ningependa kuweka msisitizo kwenye suala la wizi wa mitihani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kulihakikishia Bunge lako kwamba Serikali imedhibiti suala la wizi wa mitihani na kinachotokea ni udanganyifu katika mitihani, ambapo baadhi ya Walimu ama huwa baada ya kufungua zile karatasi za mitihani wanaenda pembeni wanawaandalia wanafunzi majibu na kuyapeleka katika chumba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Serikali imekuwa pia makini katika kuhakikisha kwamba inaangalia kwa karibu usimamizi wa mitihani na wote ambao wanakuwa wanajihusisha na udanganyifu katika mitihani hatua zimekuwa zikichukuliwa na zitaendelea kuwa zinachukuliwa.(Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa viuatilifu hivi kwa kweli imekuwa ni hasara kubwa sana kwa wakulima, na kwa kuwa wakulima wa Jimbo la Bariadi na Jimbo la Busega katika msimu huu wamelima sana zao la mahindi lakini limeshambuliwa na funza, kitu ambacho kimesababisha watapata uhaba wa chakula, je, Serikali inachukua hatua gani za makusudi ili watu hao wanaoingiza viatilifu ambavyo havifai na viko chini ya viwango wanadhibitiwa na wanapewa adhabu kali?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye maelezo yangu ya awali; kama Mheshimiwa Mbunge anawafahamu watu au makampuni ambao wameingiza viuatilifu ambavyo haviko katika ubora unaotakiwa kisheria tutawachukulia hatua. Hata leo hii hii akinipa list yao tutaanza kufanyia kazi na kuchukua hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuwafungia na kuwaondolea leseni ya kuagiza na kuuza viuatilifu lakini vile vile kuwapeleka Mahakamani kwa sababu ni kinyume cha Sheria kuuza dawa na viuatilifu ambavyo havina ubora.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza, lakini sambamba na hiyo nakushukuru sana kwa kuweza kunipa pongezi kwa swali langu la ki-CPA. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Naibu Waziri amejibu vizuri, lakini kodi hii inasema ni road licence na yeye anasema ni kodi ya usajili wa gari ya mwaka kwa hiyo ni vitu viwili tofauti. Kwa hiyo, napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri, je, haoni kwamba kodi hii kwanza inakusanywa kimakosa kwa sababu jina leke liko tofauti na lilivyo na pili haoni kwamba ingekuwa bora zaidi tungeikusanya kwa kutumia matumizi ya gari barabarani ili kuongeza kama mapato yake?? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kuna baadhi ya watu sasa wanasumbuliwa barabarani, kwa kudaiwa madeni ya gari ambayo pengine ina muda mrefu haifanyi kazi ipo nyumbani na wanadaiwa kwamba lazima alipe kodi hiyo. Je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kuna haja ya kutoa tamkoili watu wasisumbuliwe barabarani na traffic, polisi, pamoja na TRA juu ya suala hili la kulipa kodi hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kiutaalamu kodi hii au ada hii haitwi road licence, kama Sheria inavyosomeka pamoja na kanuni zake, zinasomeka The Road Traffic Motor Vehicles Registration, kwa hiyo hii ni motor vehicle ni ownership kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi. Sio kwamba inalipiwa kwa matumizi yake barabarani, kwa hiyo, sheria inasema hivi, lakini kwa lugha zetu za mtaani tunaiita hivyo. Lakini kimsingi hii ni ownership na sio sheria ya kutumia ni ada ya kutumia gari barabarani, hapana.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, ada hii ya leseni ya gari ya mwaka hutozwa kwa kila gari kulingana na ukubwa wa engine ya gari na kwa sasa kwa jinsi ilivyo sheria hii haitoi fursa ya kusamehe ada hii ambayo haikulipwa huko nyuma.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi kwamba ipo katika kanuni zetu sehemu ya nane kifungu cha 32 mpaka 34 inamuelekeza owner wa vyombo vya moto jinsi ya kufanya utaratibu upi afuate kama chombo chake hakitumii tena, haki-own tena ili aweze kwenda kwa registrar ambaye ni Katibu Mkuu Hazina ili aweze sasa chombo chake kuwa deregister na hataweza kudaiwa tena ada hiyo.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema hii ni sheria lakini kama Serikali tumesikia kilio cha Wabunge wengi pamoja na wananchi tunalifanyia kazi, tunaifanyia kazi sheria pamoja na kanuni zake kuona jambo hili linafika mwisho ambao ni mzuri kwa Serikali yetu pamoja na wananchi wetu.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri katoa majibu mazuri sana, lakini mimi nina concern moja kubwa kwamba hawa tembo madhara yao ni makubwa sana katika Wilaya ya Busega ambayo inapakana na Wilaya za Bunda na Serengeti. Maelezo ya Mheshimiwa Waziri katika majibu yake amesema kwamba hawa tembo wanazidi kudhibitiwa, lakini mwishoni amesema kwamba tembo wameongezeka zaidi, sasa sijaelewa kwamba sasa kwa vile wameongezeka zaidi madhara yatakuwa makubwa kwa wananchi. Serikali sasa kupitia Wizara yake ina mkakati gani kuwaokoa wananchi ambao wanasumbuliwa na tembo kwa kusababishiwa hasara kubwa zaidi?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, huko nyuma nchi yetu ilikuwa na tembo wengi sana, wanafika 110,000, hivi sasa hatua tuliyofikia hapa wanyama hawa walipunguzwa sana na ujangili wakafika chini ya 10,000. Sasa hivi ndiyo idadi hiyo inaanza kukua na tunaanza kuwaona. Katika eneo lile la Serengeti na eneo la Maswa tunafanya utafiti kuangalia kama tunaweza kujenga uzio wa kuwatenganisha watu, mashamba yao na hifadhi. Tunafanya mazungumzo na wawekezaji wakubwa hapa nchini kwetu na mazungumzo yanaelekea vizuri. Sikupenda nifike mahali ninasema jambo hili, lakini Serikali inalichukulia jambo hili kwa uzito mkubwa sana na ndiyo maana tunafanya utafiti wa uwezekano wa kujenga uzio wa kilometa 140 tuone kwamba italeta afueni kiasi gani katika kuwadhibiti wanyama hawa.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo yamejikita katika kuelezea uhalisia wa mifuko hii na changamoto zilizopo, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwanza, kwa vile inaonekana wazi kwamba watumishi wengi na hasa wanachama wa mifuko hii wanapokuwa wameachishwa kazi au wametorokwa na waajiri wao wanahangaika sana kuweza kujikimu katika maisha yao na hiyo sio hiari yao isipokuwa wameachishwa kazi au wametorokwa na waajiri. Sasa Serikali haioni kwamba kuna haja hawa watu ambao wanapata dhahama hii, wasaidiwe kuchukua mafao yao ili wajikimu katika maisha yao wakati wakitafuta kazi zingine za kuweza kujipatia kipato?
Swali la pili, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kabisa kwamba mifuko hii ina changamoto nyingi sana, ikiwa ni pamoja na gharama za uendeshaji ambayo inakula mifuko ya wanachama hawa, lakini pili kutokana na kwamba mifuko hii imekuwa mingi mno na utitiri ambao mafao yao hata hayana tija kwa wanachama wenyewe.
Je, ni lini sasa Serikali, kufuatia kauli ya Mheshimiwa Rais siku ya sherehe ya Mei Mosi Moshi katika Mkoa wa Kilimanjaro alipotaka Serikali ilete hoja hapa Bungeni, Muswada wa kuweza kuigawa mifuko hii kutoka utiriri huu na kubakiwa na angalau mifuko miwili tu ambayo itakuwa na sekta ya umma au na sekta binafsi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba ni lini Serikali itatii maagizo ya Mheshimiwa Rais kwa kuleta Muswada hapa Bungeni ili tuweze kurekebisha suala la mifuko hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la kwanza naomba tu nirudie majibu yangu ya msingi ya kwamba katika kuliangalia suala hili la fao la kujitoa kama lilivyokuwa linaitwa, sisi kama Serikali na kupitia maazimio ya Bunge hili mwaka 2012 ambayo ilisema Serikali iangalie utaratibu mzuri wa kushughulika na suala hili la fao la kujitoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kama nilivyosema tayari tumekwishaanza maandalizi ya kuja na utaratibu mwingine mbadala ambao utamfanya mfanyakazi wa Kitanzania yule ambaye ataachishwa kazi na hajafikisha umri huo wa miaka 60 wa kuchukua mafao yake, tuone namna ya kuweza kuliweka sawa na kumsaidia asipate shida katika muda huu wote wakati bado anasubiria kupata ajira nyingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo kwa sababu jambo hili linakuja Bungeni, nimuombe tu Mheshimiwa Mbunge avute subira. Muda sio mrefu tutawasilisha mapendekezo yetu hayo na ninyi kama Wabunge mtapata nafasi za kuweza kuchangia na kutushauri vema sisi kama Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lke la pili; ni lini tutatii maagizo ya Mheshimiwa Rais ya kuunganisha mifuko hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge ya kwamba sisi baada ya tamko la Mheshimiwa Rais kazi hiyo imefanyika mara moja na katika majibu yangu ya msingi nimesema tayari tumeshakutana na wadau, tumezungumza namna bora ya kuunganisha mifuko hii na muda sio mrefu tutatoa pia taarifa sehemi ambayo tumefikia na tutawapa pia the way forward ya namna ambavyo mifuko hii itakuwa. Hivyo Mheshimiwa Mbunge vuta subira tu, hii yote iko katika mipango na agizo la Mheshimiwa Rais tumelitii na tumelitekeleza. (Makofi)
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Maswali Namba 75 na swali Na 76 yanafanana lakini Mheshimiwa Naibu Waziri katika majibu yake ambayo ni mazuri sana amesema kwamba palipo na wananchi na kama wamehamasika na wameshajitolea kuanza kazi za ujenzi wa vyuo kama hivi, Serikali iko tayari kuweza kuwapa mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bunge lililopita, Serikali iliwakubalia wananchi wa Wilaya ya Busega kutenga eneo kwa ajili ya kuanzisha Chuo cha Ufundi Stadi (VETA). Je, wazo hili la Serikali bado liko palepale au limebadilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema mwenyewe, kama tayari kuna ahadi thabiti ya Serikali kuhusiana na chuo chake cha VETA Busega, leo hii haiwezi ikabadilika. Kwa hiyo, tuendelee na majadiliano tokea tulipoacha kutoka kwa wenzetu ili tuone namna bora ya kutekeleza ahadi hiyo. (Makofi)