Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Njalu Daudi Silanga (6 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naitwa Njalu Silanga, Mbunge wa Jimbo la Itilima, maarufu Mtemi unakotoka. Kwanza nianze kuwashukuru wapigakura wangu wa Jimbo la Itilima kwa kuweza kuniamini kuwawakilisha katika Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaunga hoja ya Mheshimiwa Rais kwa hotuba nzuri aliyoizungumzia hasa inalenga vijana kupata ajira, amezungumzia suala la viwanda, nchi yetu imekuwa na viwanda vingi, viwanda vingine bado vinafanya kazi na vingine vilisha-expire.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Mheshimiwa Rais wasaidizi wake wakiifuatilia vizuri, na wakitekeleza kwa kasi wanayoifanya ni imani yangu tunaweza tukatoka hapa tulipo tukapiga hatua nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia viwanda ni lazima miundombinu yote iwe kamili, ninamshukuru Mheshimiwa Muhongo leo amejaribu kutoa ufafanuzi kuhusu mambo ya umeme. Viwanda vikubwa nchini lazima umeme uwepo saa zote, kwa sababu kiwanda kinapoendeshwa umeme ukikatika mwekezaji atakuwa na gharama kubwa sana.
Mheshimwa Mwenyekiti, jambo jingine ni lazima sasa Serikali ifike muda itenge maeneo maalum kwa ajili ya viwanda, na tunapozungumza viwanda maji yawepo na barabara ziwepo za kutosha hasa kule mali ghafi inakopatikana, utakuta maeneo mengi mali ghafi zipo lakini haziwezi kufika katika sehemu husika kwa sababu ya barabara hazipitiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, kwenye Jimbo langu ninakotoka nashukuru sana Mheshimiwa Rais amempandisha Mheshimiwa Mbarawa kuwa Waziri wa Ujenzi, alipokuja kilometa kumi tulitumia saa mbili kufika tunakokwenda, kwa kweli ni hali tete na mbaya sana. Haya maeneo yote yakishawekewa utaratibu mzuri, miundombinu ikakaa vizuri, basi katika haya yote tunayoyazungumzia, yanaweza yakatekelezwa vizuri na yakaleta matunda kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni kuimarisha kilimo ili viwanda tunavyovizungumza hivi viweze kuzalishwa katika maeneo husika ili mali ipatikane ya kutosha. Ukiangalia nchi yetu inatumia gharama kubwa sana hususani kwenye kipindi hiki cha njaa, lakini ukifuatilia kwa undani zaidi, utakuta ni Serikali haitekelezi wajibu wa kupeleka fedha au kuimarisha watendaji kwa maana ya Maafisa Kilimo katika maeneo husika zikaweza kuzalishwa malighafi za kutosha katika maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia Nyanda za Kusini, utakuta mbolea inaenda muda muafaka, pembejeo zinaenda muda mufaka, lakini leo tunakotoka katika Majimbo yetu, unaweza ukakuta tunavyoongea mpaka leo hata pembejeo hazijafika katika maeneo husika, tayari mkulima yule ataathirika tu kwa namna nyingine na ataanza kulia Serikali. Basi ifike muda muafaka mambo haya yaweze kutiliwa nguvu na kufanyiwa kazi haraka iwezekanavyo, ili wananchi waweze kufaidika na kasi ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu Mheshimiwa Rais alipokuwa akifanya kampeni, alitoa ahadi mbili, barabara ya kutoka Budalagujiga kwenda Mwabasabi, kwenda Nanga na akatoa ahadi ya tatizo la machungio katika vijiji vinavyoishi kando kando mwa mpakani, vijiji hivyo ni Nyantugutu, Pijulu, Mwaswale, Mwamtani na Kuyu, vyote hivyo kuna changamoto kubwa katika maeneo husika. Ningeiomba Serikali kwa ahadi ya Mheshimiwa Rais, nayo iweze kufanyiwa kazi ili wanachi hao waweze kuendelea kuamini na kasi ya utekelezaji ya awamu ya tano.
Mheshimwa Mwenyekiti, tunayo changamoto nyingine, kuna bwawa katika Kijiji cha Habia, limejengwa mwaka 2006. Takribani ya milioni 700 hadi 800 zimeshapotea pale, hakuna chochote kinachoendelea, ukiuliza wakandarasi walitoka Dar es Salaam, hela ile imepotea ukifika pale kwenye site unaletewa kitabu na mtu amebaki pale, kuendelea kusubiri Serikali inasema nini. Nimuombe Waziri wa Maji, jambo hili alitolee majibu, kwa sababu wananchi wa eneo hilo, walitoa eneo lao, lakini hakuna faida yoyote wanayoipata na matokeo yake watu wanapoteza maisha katika eneo lile husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe Serikali ya Chama cha Mapinduzi iendelee na kasi iliyonayo, kwa kutekeleza ahadi wanazozisema na kuzifanyia kazi papo kwa hapo. Nimpongeze sana Mheshimiwa Jenista Mhagama, alikuja katika Wilaya yetu, siku hiyo hiyo akaelezwa kilio cha wananchi na akatoa majibu na hivi sasa wananchi wale walipata alichokiahidi mahindi tani 400, hongera sana Mama, chapa kazi. (Makofi)
Ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya, alitembelea katika kituo chetu cha Nkoma, nadhani hatua zimeshachukuliwa na inaendelea kufanyiwa kazi, hongera sana endelea na moto huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya na Mkoa wetu wa Simiyu ni mpya, bado hatujaungana na Mikoa mingine kwa maana ya lami, ninaomba sasa kilometa 52 zinazotoka Bariadi kwenda Maswa - Migumbi nazo basi Mkandarasi apatikane ili wananchi waweze kuuza mazao yao kwa bei nzuri zaidi. Ukizingatia Wilaya yetu na Mkoa wetu, ni miongoni mwa Wilaya zinazolima kwa wingi sana. Mfano hivi sasa tunavyozungumza choroko zimeshaanza kuuzwa lakini barabara ni mbovu, kwa hiyo mwananchi ataendelea kupata bei za chini. Lakini yote haya yakiwekwa vizuri tunaweza tukafanya kazi kubwa na nzuri zaidi ikawa na matunda na majawabu ya haraka zaidi iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa uvumilivu uliouonesha leo, kweli umedhihirisha kwamba wewe ni Mtemi, umevumilia vya kutosha na hatimaye umetoa majibu, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga hoja ya Hotuba ya Mheshimiwa Rais
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nianze kumshukuru Waziri wa Viwanda na Biashara kwa hotuba yake nzuri ambayo imeelekeza changamoto za Watanzania. Nitaanza na ku-declare interest kwa maana ya kwamba ni mmiliki wa kiwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumzia viwanda tunazungumzia viwanda vya aina gani? Sisi wakulima wa pamba tunakotoka tulikuwa na viwanda 77 leo vimebaki 40 na hivi 40 na vyenyewe vipo katika hali tete. Nini mpango wa Serikali kuvisaidia viwanda hivi ili viweze kufanya kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumza na ukifuatilia suala la viwanda kwanza malighafi yenyewe haipo ni kwa sababu Serikali haijaweka kipaumbele kwa mazao yanayozalishwa hapa nchini ili yaweze kuwa na bei kubwa. Kwa mfano, pale Morogoro tunacho Kiwanda cha Ngozi baada ya Serikali kuzuia ngozi zetu zisisafirishwe bei zimeshuka. Leo bei ya kilo moja ya ngozi ya ng‟ombe ni shilingi 400 lakini enzi zile wakati wanasafirisha ilikuwa ni shilingi 1,500, ya mbuzi ilikuwa shilingi 1,000, ya kondoo ilikuwa shilingi 800, leo unazungumzia ya kondoo shilingi 100 kwa kilo na ya mbuzi unazungumzia shilingi 200, kwa jinsi hii tunalindaje viwanda vyetu vya ndani? Ifike mahali sasa Serikali ijaribu kuangalia kwa undani na kwa umakini zaidi ili kuhakikisha mali tunayoizalisha hapa nchini inakuwa na viwanda vya kuzalisha vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile ione ni jinsi gani ya kuongeza bei, hili jambo kwa kweli linanipa taabu. Unakuta mazao yetu ya ndani kodi inaongezwa, mfano kama pamba. Mashudu yana kodi, mafuta yana kodi lakini mali inayotoka nje inakuwa haina kodi, unategemea hii mali itapanda kwa utaratibu upi? Ukizungumzia zao la pamba, zao la pamba linajumuisha vitu vingi, utachukua mapumba yale makapi, utachukua mbegu zake utauza lakini kwa hali iliyopo ukigusa kila kitu kina kodi kwa sababu sisi soko la nje hatuli-control hatuwezi kuongeza bei na mkulima bei yake ikiongezeka ni sehemu ya kichecheo kwa wakulima kuweza kuzalisha kwa mwaka unaofuata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya Wizara ya Kilimo imezungumza, kwa mwaka 2004 nchi ilizalisha robota 700,000 lakini leo tunazungumzia uzalishaji wa tani 150,000, ni tayari nchi imeingia hasara kwa aina gani? Tumekosa dola lakini vilevile tumekosa ajira kwa vijana wetu. Mimi niiombe sana Serikali, Waziri atenge muda wa kukutana na wenye viwanda hawa ili aweze kuzungumza nao wamwambie ni changamoto za aina gani wanazokabiliana nazo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani nchi inazungumza kila siku masuala ya viwanda lakini bado kuna watu ambao wana viwanda lakini wameshindwa kuviendesha kwa sababu ya mambo mengi. Tuna kiwanda pale Arusha kipya na kizuri kabisa lakini kimeshindwa kufanya kazi. Hata huyu Mchina ambaye yuko pale Shinyanga amefungua Kiwanda cha Nyuzi pamoja na Kiwanda cha Oil Mill haviwezi kufanya kazi kwa sababu ya malighafi na gharama inakuwa kubwa. Kwa hiyo, ifike mahali tuangalie ni jinsi gani tunataka kuwasaidia Watanzania lakini tuangalie ni jinsi gani tunataka tusimamie mazao yetu ya ndani ili kuyaongezea thamani ili wakulima wetu waweze kupata bei zilizokuwa nzuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mambo mengi ambayo yanasababisha tushindwe kusonga mbele. Ukiangalia mfano mwaka huu tumekosa pamba na mtu anayehusika na viwanda anapaswa sana kusimama kwa sababu ni sehemu yake ili viwanda vyake viweze kufanya kazi. Mwaka huu tuna maeneo mengi ambayo yamesababishiwa hasara na baadhi ya wataalam wa TPRI kwa sababu ya kuleta dawa mabovu hivyo hatuna pamba ya kutosha. Hili jambo lazima Waziri wa Viwanda aliangalie kwa umakini zaidi na kuhakikisha wanakuwa wamoja ili wasukume gurudumu la maendeleo kuhakikisha nchi yetu tunaipeleka mahali tunakokusudia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto nyingine kwenye suala la viwanda. Viwanda vyetu lazima tukubali, kwanza suala la umeme bado halijakaa vizuri, lazima ongezeko la umeme wa kutosha liwepo. Kiwanda unakiendesha ndani ya miezi miwili, lakini ndani ya miezi hiyo miwili utalipa miezi mitatu inayofuata, kama ni bili ya shilingi milioni 100 utalipa miezi mitatu mfululizo, tayari pale yule mwenye kiwanda hawezi kuendelea atasimama tu hivyo hivyo na mwisho wa siku nchi yetu itaingia kwenye matatizo makubwa sana.
Niiombe sana Wizara inayohusiana na jambo hili ilishughulikie kwa umakini zaidi na kuona jinsi gani sasa tunasonga mbele na kauli mbiu ya Mheshimiwa Rais inayosisitizia suala la viwanda. Viwanda vina changamoto na lazima Mheshimiwa Waziri aingie ndani zaidi, ajifunze zaidi najua ni mtaalam na jinsi anavyojibu yuko shapu kama Mbunge wa Kishapu akiweka mambo yake vizuri tunaweza tukapiga hatua kubwa sana lakini bila kufanya hivyo tutazungmza hapa miaka mitano itaisha na viwanda havitaenda ni kwa sababu mambo hayako wazi tunaelewa kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu walioendelea, kuna nchi kama Bangladesh, ina sehemu tu ya viwanda, kiwanda kimoja kina wafanyakazi 25,000, kila kitu kipo na masaa yote kinafanya kazi lakini sisi Tanzania hapa hatujajipanga vizuri. Hata hivyo, kwa kasi hii ya Awamu ya Tano naamini imejiwekea utaratibu mzuri. Niwaombe sana Waziri wa Kiwanda pamoja na Waziri wa Nishati na Madini muweke kasi kwenye mambo ya umeme kwa sababu viwanda vyetu vina fail, vinaunguza vitu kutokana na mambo mengi. Yote haya tukiyazingatia na kuyachukulia maanani tutapiga hatua na nchi yetu itabadilika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mambo magumu sana ambayo tunayaona lakini mambo mepesi sana tukishirikiana na wananchi wetu, tunavyo viwanda vya SIDO. Mfano mimi kwenye Jimbo langu pale Luguru, maana Mwenyekiti wewe ni Mtemi kule, kuna Kiwanda cha SIDO kipo siku nyingi tu. Kile tayari kikitengenezewa utaratibu kinafanya kazi maana majengo tunayo zile teknolojia zipo zinabadilika kila siku tu ni kwenda kutoa zilizokuwepo unaweka mitambo mingine kazi inaendelea, lakini bado sasa tunazunguka na tunazungumza sana. Kama tunataka vijana wawe na ajira ni pamoja na vitu kama hivi tukiviwekea kipaumbele tunaweza tukapiga hatua na nchi yetu tukaipelekea pale panapokusudiwa. (Makofi)
Suala lingine ni alizeti. Sasa hivi pamba inaenda inashuka lakini alizeti sasa nayo imeingia kwenye soko. Nimuombe Waziri wa Viwanda ajaribu kuangalia na kutoa ushauri kwenye Wizara ya Kilimo kwa sababu ni wamoja wanaweza wakaungana wakafanya kazi ya pamoja ili kusudi kuhakikisha Taifa letu sasa linapiga hatua. Kwenye alizeti, niishauri Serikali tuna mifumo kwenye nchi hii mingi sana, mkiingiza bodi na kadhalika tayari lile soko litashuka. Leo mwenzangu wa Singida amezungumzia ni walimaji wazuri sana ni kwa sababu hakuna bodi pale ukiingiza tu bodi lazima patakuwa na tatizo, itaanza kushuka na kadhalika. Tuyaangalie sana hizi bodi wakati mwingine yanaliingiza Taifa kwenye matatizo na migongano isiyokuwa na maana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nianze kwanza kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi nzuri wanayoifanya kwa kuweza kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi na wananchi wanaipokea kwa asilimia mia moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naishukuru Wizara ya TAMISEMI kwa kazi kubwa na kwa muda mfupi walioifanya na kuonesha kwa wananchi kwa kuchukua hatua kwa wale wanaofuja fedha za Serikali. Naiomba Wizara hii ijaribu kuangalia maeneo mapya hususan Wilaya ya Itilima, ni Jimbo jipya na Wilaya mpya, takribani miaka 20 liko upinzani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli, wananchi hawa wameweza kufanya kazi kubwa ya kutekeleza Sera za Serikali ya Awamu ya Tano. Serikali ya Awamu ya Tano inasema kila kijiji kuwe na zahanati. Tunavyozungumza hivi, tunazo Zahanati 29 na zahanati nane ziko katika hatua za mwisho. Naiomba Wizara iweze kuleta fedha za kumalizia hizo zahanati ziweze kufanya kazi, ukizingatia Wilaya yetu ya Itilima ni Wilaya ambayo haina Hospitali ya Wilaya. Tunategemea sana hizo zahanati zitapunguza kasi katika maeneo ya Maswa pamoja na Wilaya ya Bariadi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuipongeza tu Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa inayoifanya, vilevile na Waziri Mkuu kwa kazi kubwa anayoifanya pamoja na wasaidizi wake. Nataka niwaambieni ndugu zangu, Awamu ya Tano imewagusa Watanzania wote na haya tunayoyazungumza na wao wanasikia. Kwa kweli, kazi inayofanywa, kila mtu anaiona na anaitazama. Ni sehemu pekee kwa muda mfupi wameweza kutekeleza majukumu makubwa na ya msingi kwa kuleta mabadiliko makubwa katika awamu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumzia suala la madawati, Awamu ya Tano imezungumza kwa mapana sana. Tunaozunguka vijijini unakuta shule moja ina wanafunzi 939, ina madawati 36! Unategemea pale tunatengeneza Taifa la aina gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baada ya Awamu ya Tano kugundua na kutoa maelekezo, bado wenzetu wanaendelea kulalamika, lakini hoja ni nzuri ni kuhakikisha Watanzania, watoto wetu, wanapata maisha bora na elimu iliyo bora. Vilevile itapunguza gharama kwa wazazi wetu kununua mashati pamoja na sketi kwa ajili ya watoto wetu watakapokuwa na madawati bora, natarajia na elimu itakuwa nzuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe ushauri, kwenye 50%, kwenye suala la shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Wengi wamesema, lakini ikumbukwe, lazima tujenge uwezo katika maeneo yetu ya vijiji. Shilingi milioni 50 tutakapozipeleka bila kuwa na elimu ya kutosha, zile fedha zitapotea na hazitaleta impact yoyote katika maeneo husika. Taasisi moja ipo katika maeneo ya Halmashauri inaitwa Idara ya Maendeleo ya Jamii; wale watu wangefanya kazi ya kutoa elimu kwa wananchi kabla fedha zile hazijafika waweze kujua jinsi ya kuzitumia, kuliko kumpelekea mtu lundo la shilingi milioni 50 katika kijiji kimoja, halafu zile fedha zitapotea na hazitakuwa na hadhi yoyote katika maeneo husika. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo, zile fedha ni nyingi zinaweza zikasaidia na zikatoa umaskini katika maeneo husika. Maeneo yako katika tabaka mbalimbali. Maeneo mengine kuna Vyama vya Ushirika, kuna ma-godown, maeneo mengine wanalima korosho, pamba na kadhalika. Ile fedha ikitolewa na Tume ya Ushirika ikiboreshwa vizuri, ni imani yangu ile fedha inaweza ikawa mtaji mkubwa katika vijiji husika na ikaleta maendeleo makubwa sana kama wenzangu walivyochangia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya machache, nashukuru sana, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja ili Watanzania waweze kufaidika na hii Awamu ya Tano. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naipongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa kazi nzuri wanayoifanya wakiongozwa na Mheshimiwa Profesa Muhongo, Naibu wake, Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na watalaam wake wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Wizara ya Nishati na Madini, katika Jimbo langu la Itilima, Makao Makuu ya Wiliya, REA phase two, haikuweza kuweka umeme katika maeneo ya nyumba za viongozi wa Wilaya ikiwemo nyumba ya Mkurugenzi na nyumba ambayo Viongozi wa Kitaifa hufikia pamoja na kituo cha mafuta kilichojengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naombe Wizara ya Nishati na Madini ione umuhimu kwenye REA phase three iweze kuzambaza umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ya Makao Makuu ya Tarafa ipo miradi ya maji ya Serikali iliyowekezwa inahitaji umeme. Mfano Tarafa ya Kinamweli Kijiji cha Nzezei tunao mradi wa maji ambao uko tayari, unafanya kazi kwa kutumia jenereta ambayo inaleta gharama kubwa kwa wananchi pamoja na kituo cha afya cha Zagayu ambacho kinatoa huduma ya afya katika Vijiji 18 pamoja na Wilaya jirani ya Maswa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa ya Kanadi katika Kijiji cha Migato ni center kubwa ambayo inaweza kuongeza mapato makubwa kwenye nchi yetu pamoja na ajira kwa vijana; inahitaji umeme. Kuna baadhi ya Vijiji ambavyo havina umeme katika Jimbo langu la Itilima kama ifuatavyo:-
Tarafa ya Kinang‟weli, Kijiji cha Nhobola, Sunzara, Kidula, Ngwamnemha, Sawida, Isegwe, Mahembe, Kinang‟weli, Isegwa, Lulung‟ombe, Kabale, Sasago, Mlimani, Kashishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa ya Itilima, Gambasuga, Dasina, Musoma, Ng‟wabagwa, Ng‟wangwita, Ikangalipu, Tagaswa, Nseme, Magazo, Nkololo, Mwalushu, Ng‟wamanhu, Ng‟wagwita, Dasina B, Banamhala, Bugani, Isakang‟wale.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa ya Kanadi ambavyo havina umeme ni kama ifuatavyo; Chimwamiti, Shishasi, Ng‟wakatale, Mtobo, Mwabalah, Pijulu, Nkuyu, Ngailo, Migoto, Simiyu, Lali, Madilana, Mhunze, Ngwabulugu, Ngailo, Lali, Nyatugu, Senani Ng‟waogama, Ng‟wangutugu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba hoja yetu niliyosema, Mheshimiwa Waziri aweze kutupatia hitaji hilo muhimu kwenye eneo langu la Jimbo la Itilima.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kuipongeza Wizara hii ya Maliasili na Utalii kwa kazi nzuri wanayoifanya wakiongozwa na Profesa Jumanne Maghembe pamoja na watalaam wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri na yenye ubora wanayoifanya katika kulinda maliasili ya nchi yetu, ambacho ni kivutio cha utalii ndani na nje ya nchi yetu Tanzania na ndicho kichocheo cha maendeleo ya Taifa letu. Natambua Wizara hii ni ngumu na ina changamoto nyingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara hii itazame vizuri kwenye maeneo ya mipaka ya Hifadhi ya Wanyamapori (game reserves), kwani kumekuwa na malalamiko makubwa kwa Maafisa wa Wanyamapori ikiwa ni pamoja na vitendo vya uovu kwa wananchi kwa kuwatoza faini zisizo kwenye utaratibu wa kawaida wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Maofisa wamekuwa wakiwaswaga ng‟ombe na kuwaingiza ndani ya hifadhi hata kama watakuwa nje ya hifadhi. Nashauri Serikali kupitia Wizara hii iweze kutatua kero hii kubwa inayosumbua wafugaji wengi hapa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia katika hotuba ya Bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kukupongeza kwa kazi nzuri unayoifanya ambayo Watanzania wote na Wabunge wa CCM tunaamini kazi yako ni nzuri sana, kama jina lako lilivyo Tulia, uendelee kutulia kama ulivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza ku-declare interest kwenye upande wa viwanda. Nianze kusema tunapozungumza katika Serikali yetu ya Awamu ya Tano kuhusiana na suala la viwanda kwa ujumla. Tunavyo viwanda, tulikuwa navyo vingi vya pamba pamoja na viwanda vya nyuzi. Katika Bajeti ya Waziri wa Fedha, ukiitafakari na kuifuatilia ni nzuri sana imeonesha maeneo mbalimbali. Nizungumzie suala la pamba na wafugaji pamoja na samaki katika Kanda yetu ya Ziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kodi iliyopunguzwa ni shilingi 450,000 ukurasa wa 89 na shilingi 250,000, lakini vilevile tunategemea sisi watu wa pamba bei ya soko liko nje, tunajaribu kuangalia mali ambayo iko hapa nchini ambayo wanunuzi wake wako hapa, tayari moja kwa moja panakuwa na kodi kubwa. Mfano mashudu unapoyapa kodi tayari unaongeza gharama kubwa na anayefanya hii biashara ya mashudu ni mtu mdogo wa kawaida, muuza kuku na wafugaji wadogo wadogo, tayari wanaongeza bei ya pamba inaongezeka kupata bei nzuri angalau mkulima, ni kwa sababu control hatuna ya bei ya soko la pamba. Niiombe Serikali ijaribu kuangalia sana kwa mapana zaidi kuhusiana na suala zima la viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye upande wa alizeti, ukipita barabara ya kutoka Singida unaenda Shinyanga utakuta wananchi wameshaji-organise pale wanauza mafuta yale. Lakini Serikali lazima ifike mahali itazame ni namna gani iwasaidie na hawa wakulima wadogo wadogo ili ile mali iweze kuzalishwa vizuri zaidi, iingizwe kwenye soko, i-compete na masoko mengine, lakini hivi sasa inaangaliwa tu, hakuna jitihada ambazo naona kama zinafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile lazima tujipange kuangalia viwanda vyetu vidogo vidogo; mfano viwanda vya SIDO, mimi kwangu kule kwenye Jimbo langu la Itilima ninalo eneo kubwa la SIDO, lakini sijawahi kuona Serikali imekuja kutembelea na kupata mawazo katika eneo lile husika lakini kila siku tu tunakutana tunazungumzia viwanda. Niombe sana Serikali ya Awamu ya Tano iweze kufanya kazi hiyo ili iwafikie wahusika tuweze kuboresha viwanda vyetu na wananchi waweze kupata bei nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia habari ya viwanda na vingine. Wenzetu wanaoendelea kwa kasi sana mfano kama Wachina, ziko Benki za Maendeleo ambazo zina-finance wawekezaji, lakini leo nchi yetu hii ukiitazama vizuri sana utakuta gharama ziko kubwa, mtu akitaka kuingiza kiwanda lazima atachajiwa kodi na anaenda kuwekeza zaidi ya miaka miwili, mitatu ndiyo ataanza kupata profit. Moja kwa moja inakuwa ni gharama kubwa katika uendeshaji na hawezi kuendesha kiwanda hicho husika kwa asilimia 100, matokeo yake ni hasara hata fit katika competition ya biashara katika nchi zingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumzia kuimarisha uwekezaji wetu wa ndani, mimi niiombe Serikali iweze kujua na kufuatilia ni kwa nini wawekezaji wetu wa ndani kila mwaka wanashuka chini, lazima kuna sababu za msingi ambazo zinasababisha. Ukiangalia nchi yetu wakati inapata uhuru, Mwalimu Nyerere yuko nayo kuna vitu vingi ambavyo viliachwa katika nchi hii. Kulikuwa na Musoma, kulikuwa na Mwanza MWATEX, kulikuwa na Tabora, kulikuwa na Urafiki, kulikuwa na Mbeya; zote zile hazifanyi kazi lakini kila mwaka tunapokutana tunaposikia bajeti, tupo wadogo mpaka tumeingia humu Bungeni tunasikiliza mipango, mipango. Ningeomba sasa kwa sababu Waziri wa Fedha ni Mpango, mipango hii sasa ifanane na jina lake, aweke mipango mizuri ili tutoke hapa tulipo tusonge mbele kuleta maendeleo katika nchi yetu na Taifa letu kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumzie suala la Benki ya Kilimo. Serikali imefanya jambo jema la kuhakikisha inaweka Benki ya Kilimo, sasa tuiombe nayo hii Benki pamoja na msimamizi wa Serikali ambaye ni Waziri wa Fedha awahamasishe sasa watoke mjini waende vijijini. Waende kwenye mikoa ambayo inazalisha siyo kuja kuendelea kulalamika na kuomba fedha hata zile ambazo Serikali imeshatenga bado hazijafanyiwa kazi. Tukifanya hivyo tutakuwa tunawajenga wakulima wetu kuweza kujua jinsi ya matumizi mazuri ya benki na vitu vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie katika suala zima la ufugaji. Lazima tufika mahali tutambue kwamba ufugaji ni nini na unaingizaje pato katika nchi yetu. Tunapozungumzia ufugaji nao wanahitaji watengenezewe mazingira ambayo ni mazuri na ni salama ya kuweza kunufaika na maeneo yetu.
Tunatambua kabisa katika nchi yetu tunaamini kabisa kwamba tunahitaji hifadhi na kadhalika, juzi Mheshimiwa Waziri wa Maliasili alikuwa anajibu swali langu alisema vijiji vinavyopakana na kandokando ya hifadhi zinapata asilimia 25 ya fedha zinazotozwa, siamini kama zile fedha kweli zinaenda tofauti na hela tu ndogo, nitaomba Mheshimiwa Waziri nitamtafuta kwa muda wake anielekeze ni jinsi gani kwa sababu naamini hela zinazokuja ni kidogo sana wala haziwezi kuwasaidia wananchi katika maeneo hayo wanayoishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze Benki ya Maendeleo. Benki ya Maendeleo ndiyo uti wa mgongo wa nchi yetu. Kama tunataka tujenge viwanda na kama tunahitaji tuwekeze katika maeneo mbalimbali, hii benki ikiwezeshwa na ina wataalam inaweza ikafanya kazi kubwa, nzuri ya kuingiza fedha nyingi bila kutegemea kodi tu kwa sababu itazungusha na wale watu wawekezaji watakuja kukopa katika benki yetu hii na itaweza kuzalisha fedha nyingi katika kuleta uchumi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho niishauri Serikali, hii kodi ambayo imewekwa kwenye mabenki, ninavyoiona inaweza ni nzuri kwa sababu tunahitaji tupate kodi, lakini kwa mtazamo wangu na muono wangu na kuishauri Serikali tunaweza tukajikuta tunapoteza deposite nyingi kwenye mabenki kwa sababu kodi itakayotozwa ni hela nyingi sana. Sasa hivi kama una wafanyakazi 300, ukipeleka kwenda kufanyiwa malipo kila mfanyakazi mmoja ni shilingi 3,000 kwa hiyo utakuta watu hawaweki hela kwenye benki wataamua kutumia njia zingine, tayari nchi itaanza kuyumba katika hali ya kiuchumi. Niombe hilo nalo waweze kuliangalia ni jinsi gani ili waliboreshe vizuri zaidi na lengo letu ni kupata mapato mengi ya kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie katika Kanda, mfano Kanda ya Ziwa iangalie ni viwanda gani vinavyohitajika katika maeneo yetu. Leo hivi sasa tunazungumza bei ya pamba haieleweki na wakulima nao wanasubiri wauze waweze kupata fedha zile, lakini kila mwaka zao hili linadorora, ukifuatilia zaidi zao hili linaingiza fedha nyingi sana kwa mwaka, mwaka jana tumepata dola bilioni 6.4, lakini hakuna kipaumbele kinachowekwa na Serikali kuhakikisha kwamba hawa wakulima wa zao la pamba tunawasiadiaje kuongeza hizi gharama, matokeo yake zinaongezwa tu kodi katika maeneo husika na imefika mahali Serikali hata ruzuku ya pembejeo haipeleki, kwa mwaka wa jana haikupeleka hata senti moja, wakulima wenyewe wanaendelea kujiendesha. Niiombe Serikali ijaribu kuangalia namna gani kuhakikisha inatatua tatizo la bei ya pamba katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho tukitaka tuende vizuri, zao hili la pamba linaweza likajiendesha vizuri sana, zikipungua kodi ambazo hazina msingi, ambazo zinazosababisha kuongezeka kwa bei, kwa sababu hatuwezi tukasema kwamba tuzuie kodi, lakini lazima tuangalie kwamba inaingiza kiasi gani kwenye nchi dola za kigeni na asilimia kubwa nchi inatumia fedha za kigeni nyingi, kwa sababu mahitaji mengi hatunayo hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iangalie ni jinsi gani itasaidia katika eneo hili ili tupunguze malalamiko katika maeneo na ipunguze hizi kodi ambazo hazima maana. Kweli naiomba Serikali suala kabisa la mashudu watoe kodi haina sababu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja kwa asilimia 100.