Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Njalu Daudi Silanga (15 total)

MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza:-
Sekta ya Afya hutenga fedha za Mfuko wa Pamoja (HSBF) kwa ajili ya kununua dawa, vifaa tiba na kadhalika:-
(a) Je, Serikali imejipanga vipi kuboresha mfumo wa manunuzi ili kupunguza mlolongo mrefu wa manunuzi uliopo sasa wa Halmashauri kutoa fedha, kisha kusubiri mpaka MSD itafute mzabuni mwingine?
(b) Mgao unaotolewa kutoka MSD kwenda vituoni ni kwa vituo vyenye fedha tu; Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa vituo vyote vinapata dawa kwa wakati ili kuhudumia wananchi wake?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijajibu swali, naomba nitumie nafasi hii kwa heshima na taadhima kuwashukuru Wabunge wenzangu wote wa CCM kwa kunipa kura nyingi, nami nawaahidi sitowaangusha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Jimbo la Itilima, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha mfumo wa ununuzi wa dawa, vifaa, vifaatiba na vitendanishi, Wizara inaomba Halmashauri kuwasilisha mapema maombi ya kununuliwa dawa na vifaa hivyo, ili MSD iweke kwenye mpango wake wa mwaka mzima wa manunuzi. Pia MSD imeingia mkataba, yaani frame work contracts na washitiri ili kupunguza mlolongo mrefu wa manunuzi ya dawa kwa sasa, mikataba hii, itasaidia Halmashauri kupata dawa katika muda mfupi zaidi.
Pia, MSD imeingia mkataba na washitiri wa ndani, yaani prime venders ili waweze kusambaza dawa pale ambapo zitakosekana katika maghala ya bohari ya dawa MSD. Idadi ya washitiri wa ndani kwa sasa imefikia 13 na juhudi zinafanyika kuongeza idadi hiyo ili kuimarisha utoaji wa huduma za dawa nchini. Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, pia imewasilisha mapendekezo ya kufanya mapitio ya Sheria ya Manunuzi, ili dawa ziweze kununuliwa kwa muda mfupi zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mgao wa dawa unaotolewa kutoka MSD kwenda vituoni, Serikali imetoa maelekezo kwamba, vituo vyote vya umma vipatiwe dawa bila kujali kama vina deni MSD. Pale Wizara inapopata mgao wa fedha kutoka Hazina madeni hayo hulipwa, pia Wizara yangu imeagiza Halmashauri kutumia vyanzo mbadala vya mapato kama vile Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) makusanyo ya papo kwa papo na fedha toka Bima ya Afya (NHIF), zitumike kununulia dawa ili kuziba pengo la bajeti toka Serikali Kuu. Fedha zingine ni za Mfuko wa Pamoja, (Health Basket Fund), ambapo asilimia 67 inatakiwa itumike katika kununulia dawa, vifaa, vifaatiba na vitendanishi. Vyanzo vyote hivyo vikitumika na kusimamiwa vizuri, vitapunguza sana pengo la bajeti kutoka Serikali Kuu.
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza:-
Mkandarasi katika barabara ya kutoka Mwegusi - Maswa tayari ameshapatikana na yuko eneo la kazi.
Je, ni lini barabara ya kutoka Maswa - Itilima - Bariadi itapatiwa mkandarasi kwa ajili ya kuunganisha kipande hicho cha barabara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Itilima kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Maswa – Itilima hadi Bariadi ni sehemu ya mradi wa barabara kuu ya Mwigumbi - Maswa - Bariadi hadi Lamadi yenye urefu wa kilometa 171. Mradi huu umegawanywa katika sehemu kuu tatu; sehemu ya Mwigumbi hadi Maswa - kilometa 50.3, sehemu ya Maswa hadi Bariadi - kilometa 48.9; na sehemu ya Bariadi hadi Lamadi - kilometa 71.8. Mradi huu wa barabara ya kutoka Mwigumbi - Maswa - Bariadi hadi Lamadi unatekelezwa kwa awamu kwa kugharamiwa na Serikali kwa asilimia mia moja.
Mheshimiwa Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Bariadi hadi Lamadi - kilometa 71.8 umekamilika. Ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Mwigumbi hadi Maswa - kilometa 50.3 unaendelea kutekelezwa. Aidha, kwa sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa sehemu ya Maswa hadi Bariadi yenye urefu kilometa 48.9 ambapo ujenzi utaanza baada ya fedha kupatikana.
MHE. KISWAGA B. DESTERY (K.n.y. MHE. NJALU D. SILANGA) aliuliza:-
Mheshimiwa Rais kwenye kampeni za uchaguzi aliahidi kupanua mpaka wa Game Reserve iliyoko Maswa:-
Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Itilima, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Pori la Akiba Maswa lilianzishwa kisheria kwa Tangazo la Serikali Namba 270 la mwaka 1962. Pori hilo ni sehemu muhimu ya uhifadhi wa baioanuai katika mfumo wa ikolojia ya Serengeti ambayo inatoa mchango muhimu kwa viumbe mbalimbali wanaopatikana katika maeneo hayo ikiwemo kutunza vyanzo vya maji kwa mahitaji ya binadamu na shughuli za kiuchumi hususan utalii. Kwa muda mrefu tokea kuanzishwa kwa pori hili, wananchi wa vijiji husika wamekuwa wakinufaika na pori hili kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi, upatikanaji wa ajira na mgao wa fedha ambapo asilimia 25 ya mapato yatokanayo na shughuli za uwindaji wa kitalii hutolewa kwa Halmashauri ya Wilaya husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Pori la Akiba la Maswa limefanyiwa marekebisho ya mpaka mara tano katika jitihada za kutatua changamoto ya mahitaji ya ardhi kwa wananchi wanaoishi jirani na pori hili. Hata hivyo, uamuzi wa kumega ardhi ya pori hili kwa kurekebisha mipaka mara kwa mara haujaweza kukidhi haja ya kumaliza tatizo hili kwa namna endelevu.
Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo kikuu cha changamoto hii ni ukosefu wa mpango wa matumizi bora ya ardhi ambapo wananchi huendelea na utamaduni wa kumiliki idadi kubwa ya mifugo inayozidi uwezo wa maeneo ya malisho na kilimo cha kuhamahama. Uzoefu umeonyesha kuwa umegaji wa ardhi kwa namna ulivyofanyika siku za nyuma si suluhu endelevu ya tatizo la migogoro kati ya hifadhi na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika swali namba 332 la tarehe 8 Juni, 2016 linalohusu marekebisho ya mipaka ya Hifadhi ya Moyowasi na wananchi, Wizara yangu itaorodhesha maombi haya katika orodha ya maeneo yanayopakana na hifadhi yatakayoshughulikiwa kimkakati na Serikali kwa kushirikisha wadau wote muhimu ikiwa ni pamoja na wananchi, Wizara ya Maliasili na Utalii, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, TAMISEMI, Maji, Nishati na Madini na Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara yangu inaendelea kusisitiza kwamba utekelezaji wa azma ya Serikali ya kujibu kero za wananchi kuhusu changamoto za mahitaji ya ardhi utazingatia uwepo wa sheria, kanuni na taratibu na pia kuweka mbele maslahi ya Taifa.
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza:-
Halmashauri ya Itilima ni mpya iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria, lakini mpaka sasa hivi haijapata fedha za kutosha kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya Wilaya.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuipatia Halmashauri hiyo fedha za kutosha kwa ajili ya maendeleo yake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Itilima, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2016 Halmashauri ya Wilaya ya Itilima ilikuwa imepokea shilingi bilioni 5.04 kati ya shilingi bilioni 8.2 zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwa ni asilimia 61.5 ya bajeti yote ya maendeleo kwa mwaka wa fedha 2015/2016.
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka 2016/2017 Halmashauri hiyo imetengewa shilingi bilioni 10.4 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo sawa na ongezeko la asilimia 26.8 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016. Upelekaji wa fedha katika Halmashauri za Serikali za Mitaa hufanywa kwa kuzingatia hali ya makusanyo ya Serikali kila mwezi. Hivyo, naomba kutoa wito kwa taasisi za umma na sekta binafsi kuweka mkazo katika kuimarisha makusanyo ya kodi na ushuru mbalimbali ili kujenga uwezo wa Serikali katika kutoa huduma kwa wananchi.
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza:-
Mradi wa Maji wa Mwalushu ulianza kutekelezwa tarehe 19 Januari, 2014 na vituo vyote 28 vimejengwa, mabomba yamelazwa na matenki mawili yamekamilika, lakini mradi huo hautoi maji mpaka sasa kutokana na Mkandarasi kutolipwa fedha zake:-
Je, ni lini Serikali itatoa pesa ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Jimbo la Itilima, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli, Mradi wa Maji wa Mwalushu ulianza kujengwa mwaka 2014 na kwa sasa umefikia asilimia 70 ya utekelezaji. Mradi huu unagharimu kiasi cha shilingi bilioni 1.2 na umelenga kuwahudumia jumla ya watu 2,051 kwa kutumia vituo 29 vya kuchotea maji. Kwa sasa kazi zilizobakia ni ufungaji wa umeme, ujenzi wa tenki la chini ya ardhi na ununuzi wa pampu.
Mheshimiwa Spika, hadi mwezi Januari, 2017 Mkandarasi wa mradi huu tayari amekwishalipwa jumla ya shilingi milioni 701. Wizara itaendelea kumlipa Mkandarasi madai yake kadri atakavyowasilisha kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Itilima. Aidha, Mkandarasi anatarajia kukamilisha kazi zilizobaki ifikapo mwezi Aprili, 2017.
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza:-
Halmashauri ya Wilaya ya Itilima ni mpya na haina Hospitali ya Wilaya.
Je, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo ili wananchi wa Wilaya hiyo waweze kupata huduma za afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Itilima kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa jumla ya ekari 30 zimepatikana kwa gharama ya shilingi milioni 30 ili kupata eneo la ujenzi wa hospitali ya Wilaya. Katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri imetenga jumla ya shilingi milioni 159.6 kutoka mapato ya ndani na shilingi milioni arobaini na tano kutokana na ruzuku ya maendeleo (CDG) kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri imetenga kiasi cha shilingi milioni 371.16 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD). Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 169.9 zinatokana na mapato ya ndani na shilingi milioni 201.2 ni fedha za maendeleo kutoka Serikali Kuu (CDG).
MHE. MASHIMBA M. NDAKI (K.n.y. MHE. NJALU D. SILANGA) aliuliza:-
Wilaya ya Itilima ni mpya na ina eneo kubwa linalovutia kwa ajili ya makazi na shughuli za kilimo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuunganisha miundombinu ya barabara ya Migato, Nkuyu, Longalombogo, Laini, Bulombeshi na Bumera ili kuvutia watu kufanya biashara za mazao katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Jimbo la Itilima, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuunganisha maeneo ya Migato, Nkuyu, Longolombogo, Laini na Bulombeshi kwa uboreshaji wa mtandao wa barabara kama ifuatavyo:-
Barabara ya Bumera - Bulombeshi na Bumera - Gaswa - Sagata - Laini ya kilometa 20, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 imefanyiwa matengenezo ya sehemu korofi kwa kunyanyua tuta na kuweka changarawe kilometa 3 na kujenga Kalavati 9 katika barabara ya Bulombeshi – Bumera - Gaswa. Katika bajeti ya mwaka 2017/2018 zimetengwa shilingi milioni 99.6 kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum urefu wa kilometa sita na matengenezo ya kawaida urefu wa kilometa nane katika barabara ya Bumera - Gaswa - Laini.
Barabara ya Migato - Ndoleleji - Nkuyu yenye kilometa 22.9, mwaka wa fedha 2016/2017 imefanyiwa matengenezo katika maeneo korofi kwa kiwango cha changarawe na kujenga makalvati matatu katika barabara ya Migato - Ndoleleji yenye urefu wa kilometa 6.5.
Lagangabilili - Muhuze - Migato mpaka unapofika Longolombogo yenye kilometa 40, kwa mwaka wa fedha 2015/2016 barabara hiyo imefanyiwa matengenezo katika kipande cha Lagangabilili - Muhuze - Migato kilometa 11 na kujenga makalvati kumi. Katika bajeti ya 2016/2017 yamejengwa makalvati sita na kuwekwa changarawe baadhi ya maeneo korofi yenye urefu wa kilometa 15. Aidha, katika bajeti ya 2017/2018, jumla ya shilingi milioni 49.18 zimetengwa kwa ajili ya kufanya matengenezo mbalimbali katika barabara hii.
MHE. KISWAGA B. DESTERY (K.n.y. MHE. NJALU D. SILANGA) aliuliza:-
Maeneo mengi yamefanyiwa utafiti na kampuni za kigeni kwa muda mrefu bila kufikia hatua ya kufungua migodi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuzifutia leseni kampuni hizo na kuwapatia wachimbaji wadogo wadogo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Kwanza kabisa na mimi kwa sababu nimesimama hapa kwa mara yangu ya kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii kufika hapa leo. Vilevile nimshukuru pia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa kuniamini na kuniweka katika Wizara hii mpya. Vilevile nimshukuru Mheshimiwa Spika, Wabunge wote na Wajumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara kwa malezi yao mazuri na kunifikisha hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga lililoulizwa na Mheshimiwa Kiswaga ambaye ni Mbunge wa Magu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na kanuni zake inatambua umiliki wa leseni za utafutaji mkubwa wa madini na uchimbaji mdogo wa madini inayotolewa kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na Sheria ya Madini ya mwaka 2010 kama ilivyorekebishwa mwaka 2017, leseni za utafutaji wa madini aina ya metali, viwandani na nishati (makaa ya mawe na urani) hutolewa kwa muda wa miaka minne ya awali na kuhuishwa kwa mara ya kwanza kwa miaka mitatu na mara ya pili kwa miaka miwili. Hivyo leseni ya utafutaji mkubwa wa madini ya aina hizo hubaki hai kwa kipindi cha miaka tisa. Aidha, leseni za utafutaji wa madini na vito na ujenzi hutolewa kwa mwaka mmoja na haziwezi kuhuishwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iwapo mmiliki wa leseni atashindwa kuendesha shughuli za utafutaji wa madini, leseni yake hufutwa kwa mujibu wa Sheria ya Madini ya mwaka 2010 na Marekebisho yake ya mwaka 2017. Aidha, katika kipindi cha mwaka 2014/2015 hadi 2016/2017 jumla ya leseni 423 za utafutaji wa madini zilifutwa ambapo mwaka 2014/ 2015 zilifutwa leseni 2013, mwaka 2015/2016 zilifutwa leseni 155 na mwaka 2016/2017 zilifutwa leseni 65.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la leseni lililofutwa hutathminiwa na Wakala wa Jiolojia yaani Geological Survey of Tanzania (GST) kwa ajili ya kutengwa kwa wachimbaji wadogo endapo litaonekana kuwa na mashapo yenye tija. Katika kipindi cha mwaka 2014/2015 hadi 2016/2017 jumla ya maeneo 19 yenye ukubwa wa jumla takriban hekta 69,652.88 yalitengwa kwa wachimbaji wadogo katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, Serikali itaendelea kufuatilia na kujadiliana na kampuni zilizomiliki leseni za utafutaji wa madini ili kuona uwezekano wa kuachia baadhi ya maeneo yanayofaa kwa uchimbaji mdogo.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO (k.n.y MHE. NJALU D. SILANGA) aliuliza:-
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015, Mheshimiwa Rais aliahidi kujenga nyumba za watumishi katika Makao Makuu ya Wilaya ya Itilima katika Kijiji cha Langabidili. Je, ni lini ahadi hiyo itaanza kutekelezwa?
NABU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Itilima kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Itilima ni kati ya Wilaya tano zinazounda Mkoa wa Simiyu. Wilaya hii ilianzishwa mwaka 2012 kwa GN Na. 73, na Halmashauri yake ilianzishwa mwezi Mei, 2013 kwa GN Na. 47. Wilaya ya Itilima imezaliwa kutoka katika Wilaya ya Bariadi na kuunda Mkoa wa Simiyu wenye Wilaya tano na Halmashauri sita. Watumishi wa Halmashauri wanalazika kuishi Bariadi Mjini na kusafiri umbali wa kilometa 33 kila siku kutoka Bariadi hadi Makao Makuu ya Wilaya kwa ajili ya kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na usumbufu na gharama za usafiri Serikali ilitoa shilingi milioni 500 kwa mwaka wa fedha 2014/2015 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za watumishi na kulipa fidia maeneo ya wananchi. Hadi sasa ujenzi wa nyumba nne unaendelea katika hatua za mwisho.
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali ilitenga shilingi milioni 230 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nne za wananchi. Aidha, Serikali imetoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji. Ujenzi unaendelea na unatekelezwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2017/ 2018, Serikali imetenga shilingi milioni 250 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nyingine nne za watumishi. Serikali itaendelea kutenga fedha kidogo kidogo kwa kadri zitakavyopatikana ili kuweza kukamilisha nyumba za watumishi.
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza:-
Shirika la Nyumba lilianzishwa kwa ajili ya kusaidia watumishi wa umma pamoja na wananchi wenye maisha ya chini na Mkoa wa Simiyu ni mpya ambapo tayari kuna watumishi wengi ambao hawana nyumba za kuishi ikiwemo Wilaya za Itilima na Busega:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga nyumba katika Mkoa mpya wa Simiyu pamoja na wilaya zake kwa kutumia Shirika la Nyumba?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Itilima, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Nyumba la Taifa lilipokea maombi ya ujenzi wa nyumba kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Itilima mwaka 2014. Baada ya kupokea maombi hayo shirika liliendelea na hatua nyingine za maandalizi ikiwa ni pamoja na kuandaa mpango wa kina wa matumizi ya ardhi, kuandaa michoro ya nyumba na kukadiria gharama za nyumba husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika liliingia makubaliano na Halmashauri ya Wilaya ya Itilima ya kujenga jumla ya nyumba 14 tarehe 2 Julai, 2005. Kati ya nyumba hizo 13 za Wakuu wa Idara na moja ni ya Mkurugenzi wa halmashauri. Utekelezaji mradi huu ulipangwa kuanza mara moja baada ya halmashauri kulipa kiasi cha shilingi bilioni 400 ikiwa ni awamu ya kwanza ya malipo ya nyumba husika. Hata hivyo, Halmashauri ya Itilima haijafanya malipo hayo hadi sasa na hivyo kuchelewesha kuanza kwa mrai huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzipongeza Halmashauri za Momba, Busekelo, Mlele, Mvomero, Monduli, Uyui, Kongwa na Geita na nyingine kwa ushirikiano ambao umewezesha watumishi wao kujengewa nyumba na Shirika la Nyumba la Taifa. Natoa wito kwa halmashauri zote uhitaji wa nyumba kuwasilisha maombi ya kujengewa nyumba na Shirika la Nyumba ili maombi hayo yaweze kufanyiwa kazi na kuwapatia makadirio ya gharama za ujenzi ili kazi hiyo iweze kufanywa na Shirika la Nyumba.
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza:-
Tanzania ni nchi yenye mazao ya biashara kama pamba, korosho, tumbaku na kahawa. Zao la pamba linazidi kuporomoka kutoka wastani wa ekari moja kilo 400 hadi kilo 120 kwa ekari moja ikilinganishwa na nchi kama China ekari moja kilo 2,000, India kilo 1,500, Burkina Faso kilo 1,200 na wastani wa uzalishaji wa dunia ni kilo 1,200 kwa ekari moja:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kunusuru zao hilo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Jimbo la Itilima, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza Mkakati wa Kuendeleza Zao la Pamba unaoratibiwa na Bodi ya Pamba Tanzania kwa lengo la kuhakikisha kuwa tija na uzalishaji wa pamba nchini vinaongezeka. Kutokana na utekelezaji wa mkakati huo, uzalishaji wa pamba msimu 2017/2018 unatarajiwa kufikia zaidi ya tani 600,000. Aidha, mafanikio hayo yanatokana na upatikanaji wa mbegu bora, viuatilifu, huduma za ugani, uchambuaji na uongezaji thamani wa zao hilo.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeanzisha Mkakati wa Kuzalisha Pamba hadi Mavazi kwa maana ya (Cotton to Clothing Strategy 2016-2020) ambao unatarajia kuongeza uzalishaji wa pamba kutoka wastani wa kilo 600 hadi 700 kwa ekari kwa sasa na kufikia kilo 1,800 kwa ekari ifikapo mwaka 2020.
Mheshimiwa Spika, aidha, mkakati huo unalenga kuongeza utengenezaji wa nyuzi kutoka wastani wa tani 30,000 kwa mwaka hadi kufikia tani 90,000 ifikapo mwaka 2020 pamoja na kuongeza mauzo ya bidhaa za pamba nje ya nchi kutoka wastani wa Dola za Marekani milioni 30 hadi kufikia milioni 150 kwa mwaka 2020.
Mheshimiwa Spika, ili kufanikisha ongezeko la tija na ubora wa pamba, Serikali imechukua hatua ya kuimarisha mfumo wa uzalishaji wa mbegu za pamba ambapo kuanzia msimu 2018/2019, maeneo yote yanayolima pamba yatatumia mbegu aina ya UKM08 na kuachana kabisa na mbegu aina ya UK91 ambayo haina ubora. Aidha, aina mpya ya mbegu za pamba UK171 na UK173 zilizoidhinishwa mwezi Januari, 2018 zinaendelea kuzalishwa kwa wingi na zitaanza kuwafikia wakulima kuanzia msimu wa kilimo cha pamba wa 2021/2022. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. STANSLAUS H. NYONGO K.n.y. MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya kutoka Sibiti – Kisesa – Itilima – Bariadi
– Salama - Sayaka hadi Kisamba kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga Mbunge wa Itilima kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Sibiti hadi Mwandoya Junction ama Loboko ni sehemu ya barabara ya Karatu – Mbulu – Hydom – Sibiti – Lalago – Maswa yenye urefu wa kilometa 389 ambayo imepangwa kujengwa kupitia utaratibu wa Engineering, Procurement, Construction & Financing (EPC + F).

Mheshimiwa Spika, sehemu ya Mwandoya Junction hadi Kisesa – Itilima – Bariadi yenye urefu wa kilometa 100, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina inaendelea na sehemu ya kutoka Bariadi – Salama hadi Magu kupitia Ng’haya (kilometa 76) ipo katika hatua ya manunuzi ya kumpata Mhandisi Mshauri kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Ahsante.
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Kituo cha Askari Wanyamapori katika Wilaya ya Itilima na maeneo yanayozunguka Pori la Akiba Maswa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Jimbo la Itilima, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara imekamilisha ujenzi wa Kituo cha Askari Wanyamapori katika Wilaya ya Itilima mwezi Oktoba, 2022. Kituo hicho kipo katika Kijiji cha Longalombogo ambapo kitakuwa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi na Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) na kitahudumia zaidi ya vijiji tisa vikiwemo Longalombogo, Nding’ho, Lung’wa, Nyantugutu, Mbogo, Shishani, Pijulu, Ng’walali na Mwamakili.
MHE. SIMON S. LUSENGEKILE K.n.y. MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Mahakama ya Ardhi chini ya Muhimili wa Mahakama?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Itilima kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa utatuzi wa migogoro ya ardhi unaanzia katika ngazi ya Mabaraza ya Ardhi ya Vijiji na Mabaraza ya Kata ambayo yote yana mamlaka ya kufanya usuluhishi. Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya ndiyo yenye jukumu la kutatua migogoro ya ardhi nchini ambapo ikiwa mtu hakuridhika na uamuzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba ya Wilaya atakata rufaa kwenda Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwepo wa Mahakama ya Ardhi napenda kumfahmisha Mheshimiwa Mbunge kuwa katika Mahakama Kuu kuna Divisheni maalum ya Mahakama Kuu, Kitengo cha Ardhi. Hata hivyo, Serikali inaendelea kufanya maboresho katika Marabaza ya Ardhi ili kuangalia namna bora ya kuyawezesha ikibidi ihamishiwe katika Muhimili wa Mahakama, ahsante.
MHE. NJALU D. SILANGA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga madaraja katika Mto Garamoha, Isolo, Nyagokolwa, Mbogo na Mhuze Wilayani Itilima?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Njalu Daudi Silanga, Mbunge wa Jimbo la Itilima, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2022/2023, TARURA iliajiri Mhandisi Mshauri ambao ni Chuo cha Ufundi Arusha kufanya uchunguzi wa kijiolojia katika Mto Garamoha ambapo kazi hiyo imekamilika kwa gharama ya shilingi milioni 35. Kwa sasa TARURA inaendelea na usanifu wa daraja hilo kwa lengo la kupata gharama halisi za utekelezaji wa ujenzi wake.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mto Isolo kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 41 kwa ajili ya kujenga daraja la mawe sehemu ya kwanza ya Mto Isolo. Ujenzi wa daraja la pili katika Mto Isolo usanifu wake utafanyika katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa kutumia wataalam wa ndani wa TARURA.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Mto Mbogo, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 40 katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya usanifu wa ujenzi wa daraja kwa tekinolojia ya upinde wa mawe lenye ukubwa wa mita 15 ili kupata gharama halisi. Mto Mhuze umetengewa shilingi milioni 30 kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa kijiolojia ili kuwezesha kusanifu kwa daraja hilo.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa madaraja katika Mto Garamoha, Isolo, Mbogo na Mhuze utaendelea baada ya kukamilika kwa usanifu ili kupata gharama halisi za ujenzi.