Supplementary Questions from Hon. Njalu Daudi Silanga (14 total)
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, kwa vile, Halmashauri yangu ya Wilaya ya Itilima imeweza kulipa MSD zaidi ya milioni 120, hivi sasa tunavyozungumza vituo hivyo havijaweza kupata dawa, vituo hivyo ni Mwaswale, Nangale, Chinamili, Nkoma, Sunzura na Sawida. Je, ni lini sasa vituo hivyo vitapata dawa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante. Ni kweli tumepokea fedha za dawa kutoka Mfuko wa Pamoja kutoka kwenye vituo walivyovitaja vya Mwaswale ambapo tuna milioni 17.7, Lugulu milioni 16.2, Nyamalapa milioni 13.8, Chinamili milioni 13 na vituo vingine takribani zaidi ya shilingi milioni 50. Vituo hivi vitapata dawa kutoka kwa wale washitiri wa ndani (prime venders) ambao nimewazungumzia, nimesema mpaka sasa tuna Washitiri 13 na tunaendelea kufanya jitihada za kuongeza Washitiri wengine. Lengo likiwa ni kupunguza time ya Washitiri hawa ku-supply dawa kwenye vituo hivi. Washitiri tulionao kwa sasa kwa faida ya Waheshimiwa Wabunge wote ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, tunao Astra Farmer, Jill Came, Salama Pharmacy, Anuther, Planet Farmer, Bahari Pharmacy, Samiro Pharmacy, Hashi Pharmacy, Pyramid, Mac Medics, Shukuru, Abakus na Philips. Washitiri hawa wanatusaidia kwa kiasi kikubwa kuziba pengo pale ambapo kwenye Bohari ya Taifa ya Dawa hatuna dawa na tuna fedha kutoka Halmashauri basi Halmashauri zinapokosa dawa zinapaswa kuandikiwa kibali maalum kutoka kwenye Bohari ya Dawa ya Kanda na kwenda kununua dawa hizo kwa Washitiri hawa wa ndani ambao wana mikataba na MSD.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo likiwa ni kuhakikisha Halmashauri zetu zinanunua dawa kwa watu waliothibitishwa na dawa ambazo zina viwango vya ubora vinavyohitajika.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Lini sasa kauli ya Serikali hiyo barabara kipande cha kilometa 48 kitakamilika?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la awali kwamba tunatafuta fedha ili kuanza kujenga barabara hii na mara tutakapopata fedha tutaanza kujenga barabara hii. Kutaka commitment ya Serikali kuhusu lini tutamaliza nadhani ni mapema mno. Naomba wananchi watuvumilie na Mheshimiwa Mbunge mtuvumilie tukipata fedha tutaanza kujenga na tutawajulisha wakati huo lini tutaweza kukamilisha.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa vile swali la msingi la Busokelo linafanana na la Wilaya yangu mpya ya Itilima. Kwa vile Halmashauri ya Wilaya ya Itilima ishatenga eneo la hekari 40 na tayari mipango yote inaendelea. Je, Serikali iko tayari kusaidia baadaye watakapokamilisha mpango huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, wameshatenga eneo ekari 40, Serikali inasemaje katika hili? Serikali inachokisema ni kwamba mkimaliza mipango yenu wekeni katika Mpango wa Bajeti ya 2017/2018 kama kipaumbele cha ujenzi wa hospitali. Na ninaomba nikwambie itakapofika katika mchakato huu wa bajeti, kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa sababu sera yetu kubwa ni kujenga hospitali kila Halmashauri badala hata ya kujenga Hospitali kila Wilaya. Kwa hiyo kwa huu mpango mkiuanza sisi kazi yetu ni kusukuma tu.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge naomba uondoe hofu, ni kwamba wekeni katika mpango, nia yetu ndani ya miaka mitano watu waone kwamba, Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuleta mabadiliko katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.
Nataka kuuliza swali la nyongeza. Katika ziara ya Mheshimiwa Rais, alipita katika Kijiji cha Budarabujiga aliyeko madarakani Mabasabi na Ikindilo, aliahidi kivuko pamoja na barabara hiyo, ni lini itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi ya kivuko, ahadi kama ya barabara, ahadi zote kama nilivyosema awali na ninajua na nyie watani zangu huko Wasukuma mambo mengi sana mmeahidiwa huko hasa katika suala zima la maboti na maeneo mbalimbali.
Mimi imani yangu kubwa ni kwamba, Dkt. John Pombe Magufuli ndani ya miaka hii mitano atafanya mambo ya mfano sana ambayo hatujawahi kuyaona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na haya yanajielekeza jinsi gani amejipanga Serikali yake katika ukusanyaji wa mapato, kwa mara ya kwanza mnaona rekodi kubwa katika ukusanyaji wa mapato kutoka kukusanya kwanza bilioni 600 mpaka bilioni 800, sasa tunaanza kukusanya one point something trillion, sio jambo la mchezo! Na mnaona jinsi gani pesa wakandarasi waliokuwa wamesimamisha miradi yao sasa wakandarasi wako site wanaanza kufanya kazi kwa ajili ya umakini wa ukusanyaji wa kodi.
Kwa hiyo, naomba niwaambie, mkakati huu unaoenda wa kukusanya fedha katika Serikali maana yake utaenda sambamba na kuhakikisha zile ahadi zote na miundombinu iliyokusudiwa inaweza kutekelezwa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante.
Kwa kuwa bajeti ya 2015/2016 Serikali imeweza kupeleka asilimia 61.5 katika Wilaya ya Itilima; je, kulingana na makusanyo ya Serikali hivi sasa tunavyoona ina kasi kubwa ya kukusanya fedha nyingi, iko tayari kufidia asilimia 38.5 ya fedha ili kukamilisha miradi iliyobakia kwa 2015/2016? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa bajeti ya mwaka 2016/2017 ya Wilaya ya Itilima ina shilingi bilioni 10, hadi sasa Serikali inaweza ikaniambia katika quarter hii ya kwanza imepeka kiasi gani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema pale awali kwamba katika Wilaya ya Itilima, Halmashauri ya Itilima katika kipindi kilichopita imepelekewa asilimia 61 na hili ni kutokana na hali mbalimbali tulipotoka katika kipindi cha mwaka wa fedha uliopita.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo naomba nikuhakikishie kwamba Serikali itahakikisha kwamba inasukuma juhudi kubwa sana, fedha zinazokusanywa zinapelekwa kwa wananchi ndiyo maana hivi sasa ukiangalia kwamba hata kuna miradi ile ambayo ilikuwa imepitiliza mwaka especially miradi ya maji Serikali imekuwa ikitoa nguvu ya kutosha kupeleka fedha katika maeneo hayo lengo kubwa ni kutekeleza miradi hiyo.
Mheshimiwa Spika, ni kweli katika bajeti ya mwaka wa fedha mwaka huu kwa mfano, wenzetu wa Itilima bajeti yao ya mwaka sasa hivi ni shilingi bilioni 10.2 lakini nikiri wazi kwamba katika katika hii bajeti ya maendeleo bado hakuna fedha yoyote ya maendeleo iliyoenda isipokuwa ni fedha za OC tu ambazo kiujumla wake katika Halmashauri mbalimbali tumepeleka hivi sasa karibuni shiingi bilioni 6.2 na Halmashauri ya Wilaya ya Itilima kwa OC ya mwezi wa Julai imepelekwa milioni 39, lakini lengo kubwa la Serikali kuhakikisha fedha iliyokusanywa iweze kupelekwa katika miradi ya maendeleo ili kukidhi yale makisio ya bajeti ya mwaka huu wa fedha yaweze kutekelezeka vizuri.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa, Halmashauri tayari ilishatoa certificate Wizarani: Ni lini sasa fedha hizo zitaenda ili kusudi wananchi wa Nkoma na Mwalushu, takriban 14,000 waweze kupata huduma iliyo sawa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Itilima inayo mabwawa 17; mabwawa haya yana upungufu wa miundombinu: Serikali iko tayari sasa kukutana na Wataalam wa Halmashauri yangu ya Itilima ili watakapoleta maombi waweze kuyashughulikia hayo mabwawa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, tumeshaweka utaratibu kwamba tutatoa fedha kwa kuwasilisha certificate. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mara tu certificate itakapofika, fedha tunazo na kutokana na Mfuko wa Maji, Mheshimiwa Waziri wa Fedha amekuwa anatupatia fedha kila wakati. Kwa hiyo, fedha ipo, ila wakati mwingine tunachelewa kwa sababu ya uhakiki; lazima tuhakikishe kwamba certificate hiyo ni ya kweli na kwamba ikienda iende ikalipe malipo ambayo ni ya halali.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la mabwawa 17; sasa hivi tayari bwawa moja tumemaliza ukarabati Bwawa la Habia, ambalo ni fedha zilizotolewa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Wizara imeshaagiza kwamba ikiwezekana kila mwaka kila Halmashauri itenge fedha na kujenga bwawa moja. Pia tuko tayari kukaa pamoja na Halmashauri ya Itilima ili kuangalia ni jinsi gani tunaweza tukashirikiana katika utekelezaji wa hayo mabwawa 17.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante na ahsante kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri yetu ya Itilima kwa mwaka wa fedha 2017/2018 tulikaa na kupitisha katika bajeti makadirio ya shilingi bilioni 1.6 na kipaumbele chetu tukaweka shilingi milioni 650 iwe ndiyo sehemu ya ujenzi wa hospitali hiyo. Nataka kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni kigezo gani kilichotumika kutoka kwenye shilingi milioni 600 na kurudi shilingi milioni 179?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Halmashauri yetu ya Itilima ina changamoto nyingi katika maeneo yetu, na tayari Halmashauri yangu kushirikiana na wananchi eneo tumeshalipata na tayari tumeshafyatua tofali zaidi ya 15,000 na hivi sasa tumekuwa tukitegemea mapato ya ndani yataweza kusaidia kusukuma uendeshaji wa jengo hilo pamoja ikiwa na zina ahadi ya Mheshimiwa Rais? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hoja inayozungumzwa na Mheshimiwa Njalu ni hoja ya msingi, na jambo hili Mheshimiwa Njalu alilizungumza mara kadhaa wakati tulipokuwa tukibadilishana mawazo, lakini jambo hili tulivyokuwa tukilifuatilia ilikuwa ni kuhusu mchakato na ilipofika decision ya mwisho, juzi nilikuwa naongea na Mkurugenzi wa Itilima kwamba nini kilijiri mpaka imefikia hapo; imeonekana kwamba baada ya kikao kile cha mwisho cha Baraza la Madiwani kulikuwa na makubaliano kutokana na fedha iliyotengwa kwamba milioni 169 iliekezwe katika suala hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo ndiyo manaa Serikali Kuu ikaongeza shilingi milioni 200 na zaidi. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge anajua kwamba haja ya suala zima la Hospitali ya Wilaya sisi kupitia Ofisi yetu hata katika commitment tuliyoweka kwa ajili ya eneo lako la Itilima ukiangalia katika maeneo ambayo tunakwenda kuboresha vituo vya afya Itilima nako tutapeleka takribani shilingi milioni 700 Mungu akijaalia kwa lengo tu kubwa la kuhakikisha kwamba wananchi wa Itilima wanapata hospitali.
Kwa hiyo, jambo hili ni la msingi na sisi Serikali tunalichukulia kwa uzito wake mkubwa sana. Jukumu letu kubwa ni kuwasaidia wananchi wako wa Itilima ambao Mheshimiwa Mbunge unawapigania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kuongeza fedha katika kuhakikisha kwamba ujenzi huu ambao unaendelea katika maeneo mbalimbali, kama tulivyosema katika bajeti ya mwaka huu wa fedha 2017/2018 katika fedha zile za CDG tumeziweka katika mafungu ambayo yatamalizia miradi mbalimbali ambayo ime-stuck katika sekta ya afya na sekta ya elimu. Jukumu letu kubwa ni kuweza kuongeza nguvu za wananchi ili hii miradi iliyoanza iweze kumalizika, kwa hiyo, Mheshimiwa Njalu naomba uwe na imani kwamba Serikali yako iko nawe kuhakikisha kwamba maendeleo katika jimbo lako ambalo ni jimbo jipya yanaweza kufanikiwa kama ilivyokusudiwa.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ni kweli kulingana na uchache Halmashauri ya Wilaya ya Itilima haukuweza kupata shilingi milioni 400 kwa wakati. Tuliweza kujenga nyumba nne kwa kutumia utaratibu kwa kutumia mikataba ya halmashauri na Naibu Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Kandege alikuja kufungua hizo nyumba. Je Waziri atakubaliana nami kuangalia utaratibu mpya na wa masharti ya ujenzi wa nyumba za watumishi hapa nchini?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, miji mingi nchini imekuwa ikikua kwa kasi bila mpangilio. Je, Wizara iko tayari kushirikiana na halmashauri hapa nchini ili kuweka upimaji ikiwemo Wilaya ya Itilima na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Njalu tukutane huko nje tufahamishane namna gani mahitaji yake namna gani anaweza tukajenga hizo nyumba, lakini ajue Shirika la Nyumba limewekwa kwa mujibu wa sheria lazima lifanye biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama tulivyokubaliana kwamba wangekuwa wanatenga pesa halafu tunawajengea nyumba. Shirika la Nyumba ujenzi wake wa gharama za ujenzi ni nafuu kuliko contractor yoyote, Shirika la Nyumba ni contractor wa daraja la kwanza. Hata hivyo, kwa kujua ni Shirika la Nyumba la Serikali gharama za ujenzi ni nafuu na ubora wa nyumba zake ni mzuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, labda tujadiliane huko nje kitu gani wamekwama badala ya kujenga nyumba 13 wanataka wajenge ngapi halafu tujue namna ya kushirikiana. Kwa kweli hatuwezi kujenga nyumba bila kupewa pesa Shirika la Nyumba haliwezi kwa sababu itabidi likope fedha benki liende kujenga nyumba zao. Kwa hiyo naomba Mheshimiwa Njalu kwa hili la nyumba tuwasiliane baadaye ili tuone jambo gani wamekwama, tuweze kushirikiana.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili upimaji kabla ya kupima Mji wa Itilima lazima ifanywe master plan na bahati nzuri Bariadi wameshafanya master plan. Kama tatizo ni utaalam, sisi tuko tayari kuwaazima Wataalam wa Mipango Miji wawasaidie Itilima namna ya kuandaa master plan, halafu baada ya master plan then sasa lije zoezi lingine la upimaji na upangaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa kama halmashauri yoyote haina Wataalam wa Serikali wa upangaji na upimaji wasipate tatizo. Serikali imeshasajili makampuni ya upangaji na ya upimaji ya Wataalam wabobezi ambao tumewasajili na tumewapa ruksa ya kufanya kazi hizi kama wenzao wa ujenzi wanavyofanya kazi nyingine za ujenzi wa barabara na majengo.
Mheshimiwa Naibu Spka, kwa hiyo, halmashauri kama haina Wataalam isikae ikisubiri Wataalam wa Serikali tunayo makampuni ambayo yanaweza kuwasaida wananchi wa Itilima kupanga mji wao, kupima hadi umilikishaji. Kwa hiyo, tunaweza tukawasaidia Wataalam, lakini pia halmashauri inaweza ku-engage Wataalam binafsi kampuni binafsi wakafanya kazi hiyo. Kwa hiyo, yote mawili yanawezakana kufanywa kwa Itilima.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Spika, kwanza ahsante sana kwa kunialika kwenda kuona ngoma, niko tayari kwenda huko. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kwanza kumpongeza Naibu Waziri wa Kilimo kwa majibu yake mazuri aliyonijibu. Hivi sasa maeneo mengi yameonekana kuwa na ugonjwa wa mbegu hii UKM08. Je, Serikali inatoa tamko gani kwa wakulima wa zao la pamba kwa maeneo ambayo yanaathirika na ugonjwa huu Fusarium hasa ikizingatia kwamba viuatilifu vinavyokuja havifikii viwango na kusababisha mashamba mengi kuharibika?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Naibu Waziri ameelezea kwamba kuna mkakati mzuri kwa mwaka 2016/2017 ekari moja imeweza kuzalisha kilo 300 lakini kwa mwaka 2016/2017 wastani ambao tumeweza kukusanya kwa nchi nzima kwa maana kwa mikoa 17 na wilaya 56 ni takribani kilo milioni 120. Kwa hiyo, atakubaliana nami kwamba zao la pamba linazidi kuporomoka. Ukigawanya kwa wastani katika zao zima kwa nchi nzima ni Mkoa mmoja tu wa Simiyu wenye kuzalisha kilo 70,000 na mikoa 16 ndiyo unaigawanya. Kwa hiyo, kama Wizara iko shughuli ya kufanya kuhakikisha zao hili linaongezeka kwa uzalishaji. Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, awali kabisa, naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifuatilia sana juu ya zao zima la pamba na hasa ukizingatia na yeye pia ni mfanyabiashara wa zao hili la pamba.
Mheshimiwa Spika, nikija kwenye maswali yake mawili madogo ya nyongeza kwa ufupi kabisa na kwa pamoja ni kwamba zao la pamba kama zao la pamba na mbegu, sisi kwenye zao la pamba zile mbegu huwa inachukua muda mrefu sana na ukizingatia kwamba mbegu hizo tunazosema utafiti unafanyika muda mrefu muda wa karibu sana na kwa haraka ambao unaweza ukafanyika ni ile miaka mitano. Kwa maana hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote wajue kabisa kwamba suala zima la utafiti huwa linachukua muda mrefu na muda mfupi ambao unaweza ukafanyika ni kipindi cha miaka mitano.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake lile la pili la nyongeza kwamba kwa nini kilimo hiki cha zao la pamba kimeporomoka, ni kweli kwamba wakulima walikuwa hawafuati zile kanuni bora za kilimo cha pamba. Nichuke fursa hii kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu amekuwa ni champion, amekuwa akihamasisha na akiwaeleza hata Wakuu wa Mikoa juu ya ufuatiliaji wa zao zima la pamba.
Mheshimiwa Spika, vilevile amemuagiza hata Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI kuboresha suala zima la ugani. Pia kama Serikali tumejipanga kuhakikisha kwamba katika msimu wa 2018/2019, tutaboresha zao la pamba kutoka hiyo tani 300,000 kwa ekari hadi tani 600,000 kwa kuzingatia hayo maelezo ambayo nimesema ili wakulima wote nchini waweze kuhakikisha kwamba wanafuata kanuni bora za kilimo cha pamba. Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Pamoja na Serikali kuendelea kutatua mgogoro wa hifadhi, uko mgogoro mkubwa kando kando ya mapori yetu wanyama wakali tembo kusababisha vifo kwenye maeneo ya Mwalali, Kuyu na Matongo. Serikali ina mkakati gani sasa kutatua mgogoro mkubwa huu kwa sababu tembo wanaendelea kuzaliana, na wanaleta madhara makubwa katika maeneo yetu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nikiri kwamba baada ya Serikali kuongeza juhudi za ulinzi wa hifadhi na kudhibiti majangili, limekuwepo tatizo la wanyama wengi sasa kuanza kuvamia maeneo ya vijiji na maeneo mengi ambayo taarifa tumezipokea ni kwamba, wanyama kama tembo na wanyama wengine wamevamia mashamba na kuna maeneo ambayo wamesababisha vifo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ambayo Wizara imechukua, kwanza tumeimarisha kikosi chetu cha ulinzi lakini tunaelekea sasa kuanzisha vituo maalum kwa ajili ya ulinzi kwenye kanda. Katika maelekezo ambayo tumeyatoa, maeneo mbalimbali tuliyokwenda tumezielekeza halmashauri zote ambazo zinapakana na maeneo ya hifadhi kuhakikisha kwamba katika maombi yao ya watumishi wanaajiri Maafisa Wanyamapori ambao wataweza kufika kwenye maeneo yenye migogoro kabla sisi askari wetu hawajafika.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nawashukuru Wizara kwa majibu mazuri ambayo umeyatoa kulikana na utekelezaji wa kazi waliyoifanya. Nina swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa jukumu kubwa la Wizara ni kuhakikisha wanatoa elimu kwenye maeneo yanayopakana na kandokando ya hifadhi kama vijiji alivyovitaja, lakini kupitia taasisi yake, TAWA aliweza kutoa fedha kwa ajili ya kuanzisha Shule ya Sekondari katika Kijiji cha Nkuyu, Kata ya Nkuyu kwa kushirikiana na wananachi. Sasa Wizara iko tayari kukamilisha ile Sekondari?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Njalu Silanga, Mbunge wa Itilima kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli tuliwahi kuweka mradi kwenye shule hiyo aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge na tukajenga madarasa manne; nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaenda kumalizia yale maeneo ambayo yamebaki ili shule hii iweze kufanya kazi.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa niulize swali dogo la nyongeza. kwa kuwa Mji wa Makambako ni mji mkubwa unaokuwa kwa kasi na unaunganisha nchi ya Zambia na nchi jirani ya Congo. Ni utaratibu upi wa haraka utakaofanyika kuhakikisha hayo majibu ya Mheshimiwa Waziri yatakamilika kwa muda muafaka ili wananchi wa Makambako wapate huduma iliyo bora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Mji wa Makambako upo katika Tier III katika mradi huu wa TACTIC. Tier One, ndiyo sasa wakandarasi wamepatikana, michakato imekamilika na wanakaribia kusaini mikataba ya kuanza kazi na wale wa Tier II design ya miradi ndiyo inafanyika hivi sasa tunavyozungumza, na tayari wale consultants wamepatikana. Hii Tier III ambayo Mji wa Makambako upo, nayo wanapatikana wataalam kwa ajili ya kuangalia Master Plan na feasibility study ya mji ule. Kwa hiyo, muda siyo mrefu mradi huu utaanza pale katika Mji wa Makambako.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na jinsi walivyojibu katika swali la msingi. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa katika Daraja la Mto Garamoha ni daraja linalounganisha Kata tatu, Kata ya Mwaswale, Nkuyu na Ndolelezi na daraja lile hupelekea kipindi cha mvua wananchi kushindwa kupita katika eneo hilo kwenda kupata huduma katika Kata ya Sagata. Sasa kwa kuwa fedha ni kiasi kidogo cha bajeti ya TARURA kwa nini Serikali isiweke kwenye fedha za maendeleo ili kusudi wananchi waweze kujengewa daraja hilo?
Swali la pili, kwa kuwa katika Kata ya Mwaswale kuna barabara ambayo TARURA wamejenga kutoka Makutano hadi Mwakubija lakini bado kilomita 51 za kutoka Mwakubija kwenda Sopalodge. Serikali sasa haioni umuhimu wa kufungua barabara ya kutoka Mwakubija kwenda Sopalodge kwa ajili ya kwenda kufanya shughuli za kiutalii katika Wilaya hii ya Itilima? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Silanga swali lake la kwanza kuhusu fedha iliyotengwa kwa ajili ya daraja hili la Mto Garamoha, tutaangalia katika utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024 tuone fedha hii iliyotengwa kwa ajili ya ujenzi wa daraja hii inakwenda mara moja ili kuweza kujenga daraja hili kuweza kutoa huduma kwa wananchi wa maeneo aliyoyataja Mheshimiwa Silanga.
Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la kujenga barabara hii ya kilometa 51 kutoka Maswale kuelekea Sopalodge. Barabara hii tayari ujenzi wake ulikuwa umeshaanza hapo awali na kwa sasa hii barabara inapita katika Pori Tengefu la Maswa katika maeneo ya Nyasosi kuelea Sopalodge ambapo barabara kufika Nyasosi pale wameishia pale na bado hizo kilometa 51. Kwa sababu barabara hii ni muhimu sana ambayo inafupisha wananchi wa maeneo haya badala ya kuzunguka kilometa 250 wanakuwa wanaenda chini ya kilometa 100 kufika katika maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, tutaendelea kuipa kipaumbele kadri ya upatikanaji wa fedha ili tuweze kujenga barabara kuanzia Gwalali kuelekea Makutano hadi kufika Mwakibija na kuelekea kule Sopalodge.
MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Tatizo lililoko Karatu linafanana kabisa na tatizo lililoko Wilaya ya Itilima. Zaidi ya zahanati 10 tumepata vibali lakini hatuna watumishi kada ya afya, nini kauli ya Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Njalu, Mbunge wa Jimbo la Itilima kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Itilima ni moja ya halmashauri nchini zenye upungufu mkubwa zaidi wa watumishi ukilinganisha na halmashauri nyingine.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika ajira za watumishi wa sekta ya afya ametoa kipaumbele katika Halmashauri na Mikoa yenye upungufu mkubwa zaidi wa watumishi ikiwemo Mkoa wa Simiyu na ikiwemo Halmashauri ya Itilima.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama ambavyo ajira zilizopita wamepata kipaumbele cha watumishi wengi, mara fursa za ajira zitakapojitokeza tutahakikisha tunapeleka watumishi wengi zaidi Itilima ili wapate kutoa huduma bora za afya kwa wananchi, ahsante.