Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Luhaga Joelson Mpina (22 total)

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii. Kwa kuwa barabara ambayo ameitaja Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Meatu Mheshimiwa Leah Komanya ni barabara ambayo pia inaungana na barabara ya kutoka pale Mwabuzo ikaenda Kabondo, Itinje, Mwandwitinje mpaka Mwaukoli na inaunganisha na zote hii inatoka Bariadi nyingine inatoka Meatu zinaenda zote Mkoa wa Tabora na Wilaya ya Igunga.

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu mapendekezo haya yote tuliyapeleka kwa pamoja kama ambavyo Naibu Waziri wa Ujenzi amejibu, sasa anaweza kunihakikishia kwamba haya maombi yote yanafanyiwa kazi kwa pamoja na muda mfupi ujenzi utaanza wa barabara hizi sasa kuwa za mkoa na baadaye ujenzi kuanza mara ili kuondoa changamoto zilizopo kwa sasa kutokana na TARURA kushindwa kumudu kukidhi mahitaji yake?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mpina, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, naomba nitumie Bunge lako Tukufu kumwagiza Meneja wa Mkoa wa Simiyu, Shinyanga na Mwanza na maeneo yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wameshaleta mapendekezo kwenye maeneo haya, wafanye kazi ya tathmini haraka iwezekanavyo, wawasilishe majibu Wizarani na sisi kama Serikali tuweze kuchukua hatua ili maeneo hayo yaweze kutengenezwa kwa haraka na wananchi wote waweze kupata huduma ya barabara. Ahsante. (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijauliza swali langu la nyongeza nimeshindwa kujizuia kumpongeza Dkt. Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kwa kura zote kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mwenyezi Mungu ambariki ili atekeleze haki za Watanzania hapa Bungeni. Baada ya hayo, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa majibu haya yaliyotolewa, mrai wetu huu wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere hauwezi kukamilika kama mkataba ulivyosema. Tulipokuwa kwenye Kamati ya Bajeti mwezi wa 11 Waziri alikuja mbele ya Kamati akaieleza kwamba sababu za mradi huu kuchelewa ni Mkandarasi kukaidi dizaini iliyowekwa na wataalam ya kujenga mahandaki matatu kwa ajili ya kuchepusha maji, lakini badala yake alijenga handaki moja, jambo ambalo lilimfanya achelewe sana kukamilisha kazi hiyo, kwa hiyo ndiyo sababu kubwa ya msingi; na sababu za UVIKO-19 zilikataliwa; na majibu haya yako kwenye Hansard za Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tena wamekuja na majibu mengine, wanasema kwamba ni kuchelewa kwa mitambo ya kubebea ile milango ya vyuma (hoist crane system), ndiyo iliyochelewa kufika na mradi huu kuchelewa kwa sababu ya UVIKO-19.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu majibu haya yanakanganya, kwenye Kamati chini ya Hansard waliyakataa majibu hayo kwamba hayana ukweli wowote na wakasema kwamba majibu sahihi ni kwamba huyo alikuwa mzembe na kwamba watam-penalize kwa ucheleweshaji atakaoufanya wa kuchelewesha mradi huu ambao unacheleweshwa na Watanzania. Sasa Mheshimiwa Waziri atuambie; Kamati ni sehemu ya Bunge, na hapa wamekuja na majibu mengine, na ushahidi wa Hansard upo. Nini majibu ya Serikali ya kuchelewesha mradi huu, kwa sababu majibu mawili tayari yametolewa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni kuhusu katakata ya umeme inayoendelea na mgao wa umeme unaoendelea hivi sasa. Mwanzo tulielezwa kwamba sababu ya mgao wa umeme unaoendelea sasa hivi ni kwa sababu ya matengenezo ambayo hayakufanyika kwa miaka mitano, ndiyo maana wako kwenye maintenance. Baada ya muda mfupi tena tukaambiwa kwamba ni kwa sababu ya mabwawa yanayotumika kufua umeme kukauka na yamekauka kwa sababu ya mifugo pamoja na ukaidi wa binadamu. Sasa hivi tena, wakati huo huo TANESCO nao wanasema kwamba hakuna mgao wa umeme, baadaye TANESCO wanatangaza mgao wa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hebu tuelezwe na Serikali; kwa sababu suala la katakata ya umeme na mgao wa umeme hivi sasa linaathiri sana Watanzania; viwanda vinafungwa, wananchi wako kwenye dhiki kubwa, huduma za afya zimevurugika, huduma za maji zimevurugika. Kwa ujumla Taifa liko kwenye hali ngumu ya ukosefu wa umeme…

MWENYEKITI: Umeeleweka Mheshimiwa, umeeleweka.

MHE. LUHAGA J. MPINA: …tupate majibu sahihi ya Serikali ni nini kinachosababisha hali hii ya kukatikakatika kwa umeme kuendelea?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nianze na swali la kwanza, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, mradi kwa mujibu wa mkataba unatarajiwa kukamilika tarehe 14 Juni, 2022. Wazungu wanasema do not cross the river before you reach there. Muda utakapofika kama mradi hautakamilika hatua za kisheria za kimkataba zitachukuliwa kwa aliyesababisha ucheleweshaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, lilikuwa linajitegemea, liliulizwa kwa nini maji hayakujazwa kufikia mwezi Novemba na sababu za kueleza kwamba cranes na milango vilichelewa kwa sababu ya UVIKO ni sababu pekee ya kuchelewesha kuziba diversion channel iliyokuwa inachepusha maji. Kwa hiyo maelezo hayo hayahusiani na mradi mzima, kwamba mradi umechelewa. Kama nilivyosema, muda wa kukamilisha mradi bado haujafika na tutakapofikia mto tutaivuka kutokana na mazingira yatakayokuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba hakuna taarifa zinazokinzana, isipokuwa taarifa zote hizi kwa pamoja zitashughulikiwa kulingana na muda utakavyokuwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, kuhusu kukatika kwa umeme; kwanza niombe kutoa maelezo ya Serikali, kwamba TANESCO haikatikati umeme, hakuna mtu ambaye ameajiriwa kwa ajili ya kukata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mifumo ya umeme ina-respond kulingana na mazingira. Kikubwa zaidi kinachotokea ni kwamba pale ambapo mitambo yetu inazidiwa na matumizi yenyewe automatically inakata umeme. Sasa tunapokwenda kuangalia tatizo ni nini, tukilibaini basi tunawasha. Miongoni mwa tatizo ambalo limekuwa likitokea ni kwamba, mara nyingi mitambo inapokuwa imepata mzigo mkubwa ikakata umeme na wale watumiaji nao wenyewe wanazima vifaa vyao.

Kwa hiyo sisi tukirudi kwenye mtambo wetu tukawasha unakubali kuwaka kwa sababu mitambo inakuwa haipo. Sasa wale wenzetu wakiwasha tena inakata tena. Kwa hiyo pengine inaonekana kama kuna mtu anakata na kuwasha, lakini ni system yenyewe ina-respond. Tunachokifanya ni kuhakikisha kwamba tunaongeza nguvu zetu za mitambo ili kuweza ku-capture sasa mahitaji tuliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie kidogo suala la kwamba tulisema maji, sasa tukasema gesi. Ni kwamba tulitarajia kuwa kwenye marekebisho ya mtambo yetu ya kufua gesi ambayo inazalisha sehemu kubwa sana ya umeme hapa nchini tuiongeze kwa sababu sasa tuna uwezo wa kuongeza megawatt takriban 290, twende tukarekebishe kwenye visima vyetu vya gesi ili sasa tuweze kupata gesi nyingi zaidi kwa sababu ya kutokuwa na hali nzuri ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niseme. Ule mgao au matarajio makubwa ya mgao tuliodhani tutakuwa nao hatutakuwa nao; na sababu kubwa za kutokuwa na mgao huo ni tatu. Jambo la kwanza, tumekaa pamoja na wataalam, kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwamba mgao usiwe mkali kiasi kile, tukabaini kwamba tunaweza tukapata ile gesi iliyokuwa kwa wenzetu wa PAET ambao ndio watakaokwenda kurekebisha mitambo yao, tukapitisha baadhi ya kiwango kidogo cha gesi kupitia mitambo yetu ya TPDC na hivyo kufidia upungufu wa gesi ambao tungeupata. Hiyo imekuwa ni sababu ya kwanza, kwamba lile pengo kubwa ambalo tungelipata kwa kutokuwa na gesi tutalipunguza kupitia gesi na kuichepusha kwa kupitia njia ya TPDC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo tunaliona, sisi sote ni mashahidi kwa sasa, hali yetu ya mabwawa imeanza kurudi katika hali nzuri na hivyo itaweza kutusaidia kujazia sasa kwenye maeneo ambayo yanatakiwa yapate umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, umeme ni supply and demand. Tulitarajia kwamba kutakuwa kuna mahitaji makubwa sana ya umeme. Kuna kitu kinaitwa load flow analysis. Yulipoifanya load flow analysis tulibaini kwamba kile tulichokitaratjia kitahitajika sicho ambacho kitahitajika. Baada ya kuwa tunahitaji takriban 280 hadi 300 tunaona zitakazohitajika ni kama megawatt 100, ambazo katika mfumo wa kawaida huwa hazipo hapa na pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nitoe kauli ya Serikali, ule mgao ambao tuliutarajia utakuwepo kwa makali yale na ukubwa ule hautakuwepo na tutahakikisha kwamba watu wanaendelea kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho niseme, katika kipindi hiki ambako kutakuwa na mgao mdogo au kutokuwepo kwa umeme katika maeneo mbalimbali tutaitumia vizuri nafasi hiyo ili kufanya mambo kadhaa yanayoboresha mfumo wetu. Mojawapo ni kuhakikisha tunapunguza mzigo katika njia za umeme tunazoziita feeder, zile ambazo zimezidiwa kutoa sehemu moja kwenda sehemu nyingine, kukatia miti na mapori ambayo yamekuwa yakiangukia maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kuboresha vituo vyetu vya kupoza umeme. Kama jana tulifanya cha Muhimbili, leo tunafanya pale Kunduchi na kesho kutwa watafanya pale Ubungo ili kuhakikisha kwamba tutakaporudi katika hali ya kawaida baada ya wiki moja ama mbili, tunarudi katika hali nzuri ambayo itakuwa bora kwa watu wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nasikitika sana kwa majibu haya yaliyotolewa na Serikali. Kipindi cha miaka minne toka mwaka 2018 mpaka leo Serikali inazungumzia suala la tathmini, inazungumzia suala la upembuzi yakinifu, miaka minne! Wananchi wa Simiyu wamechoka na hizi danadana za Serikali, leo tunataka tuambiwe nini sababu zilizozuia mradi huu kujengwa ili tujue, kwa sababu huwezi kutuambia hadi miaka minne unazungumzia tathmini, unazungumzia upembuzi yakinifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni nchi yetu imekuwa ikiagiza bidhaa za nguo kutoka nje ya nchi kutokana na ukosefu wa viwanda kama hivi, tunaagiza bidhaa za nguo kutoka nje tunatumia fedha nyingi za kigeni kuagiza bidhaa za nguo nje ya nchi. Lakini pia wananchi wa Tanzania wanateseka kwa kukosa soko zuri la pamba kwa sababu ndani ya nchi hakuna viwanda na kugeuka kuwa soko la wakulima wa nchi zingine kwa kununua bidhaa zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ajira zetu tunazi-export kila leo; Serikali ituambie ni lini Serikali itachukizwa na mambo haya na kuingia kwenye uwekezaji wa viwanda vya pamba ili wakulima wa pamba waweze kupata bei nzuri na tuweze kunufaika na valua addition la zao la pamba? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mbunge kwa swali lake zuri la nyongeza na ni kweli akisikitika ana haki ya kusikitika, lakini kiukweli ilikuwa ni lazima taasisi yetu ya TIRDO ifanye upembuzi yakinifu wa kuhakikisha kwamba kinachokwenda kufanyika je, kinaweza kuleta manufaa tarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile ikumbukwe kwamba kuna mifuko kama mitano ambayo ilikuwa ichangie kwenye ujenzi huo; kwa maana ilikuwa kwanza ni kuhakikisha hii mifuko inakubaliana na module operant pamoja na kufanya hayo mambo mengine, lakini kimsingi ilionekana vilevile katika upembuzi yakinifu ndiyo maana utaona upembuzi wa kwanza ulionesha tunahitaji shilingi bilioni 59.4 kujenga. Lakini wakati wakifanya mchakato wakaona kwamba kuna uwezekano wa kuokoa hizo shilingi bilioni 51.

Sasa labda Mheshimiwa anasema ni lini tutamalizana na jambo hilo, labda Mheshimiwa Mbunge nikuombe kitu kimoja kabla ya tarehe 15 Machi, 2022 tayari kitaitishwa kile kikao ambacho kitaelezea muafaka wa hili jambo na Mheshimiwa Mbunge tutawaalika Wabunge wa Mkoa wa Simiyu ili tuweze kukubaliana way forward kwa pamoja.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya CAG ya mwaka 2019/2020 na mwaka 2020/2021 kesi hizo nilizozitaja zimesajiliwa katika Mabaraza yetu; Baraza la Rufani za Kodi (TRAT) na Bodi ya Rufani za Kodi (TRAB) zilisajiliwa kesi hizi zenye thamani ya trilioni 360 na hivyo kama majibu ya Serikali kwamba hakuna kesi ya trilioni 360 wakati kwa mujibu wa Taarifa ya CAG hizi kesi zilikuwa zimesajiliwa na Mabaraza haya; hizi kesi zipo wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, zipo taarifa za uhakika kwamba katika mwaka huu wa fedha Serikali iliamua kupokea shilingi bilioni 700 kupitia katika hizo kesi za shilingi trilioni 360 na katika kipindi cha Disemba, 2021 na Februari, 2022 Serikali ilipokea fedha hizo na kuzifuta kesi zenye thamani ya shilingi trilioni 360. Kwa nini Serikai iliamua kupokea fedha bilioni 700 badala ya shilingi trilioni 360 kama madai halali ya nchi? (Makofi)
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake aliyoyaleta, lakini naomba niweke kumbukumbu sawa; jambo hili hata jana nimeona limejadiliwa kwa kirefu sana na nitakuomba unipe dakika ili niweze kuliweka sawa.

Mheshimiwa Spika, jambo hili liko namna hii, ni kweli anachosema Taarifa ya CAG ya mwaka 2019 ilisema hivyo na Taarifa ya CAG ya mwaka 2019 maana yake ni ukaguzi wa vitabu vya mwaka 2018 (mwaka unaofuatia nyuma yake) lakini kilichofanyika ni kipi?

Mheshimiwa Spika, baada ya mzozo kujitokeza kati ya kesi ya Acacia pamoja na Serikali, Acacia aliuza jambo lile kwa Barrick na Rais wa wakati ule, Rais Magufuli aliunda timu ya kufanya makubaliano na hawa watu mwaka 2017/2018 na makubaliano hayo yaliendelea kwenye mjadala, yakaisha tarehe 24 Januari, 2020 na sherehe hizi zilifanyika Ikulu mbele ya Rais Magufuli na shamrashamra kubwa na Tanzania tukakubali kuachilia shilingi trilioni 360 tumalize shauri lile na tukaunda Kampuni ya Twiga na nchi nzima tunasheherekea kampuni ile kwamba ina ubia wa asilimia 16 kwa Serikali na asilimia 84 kwa Barrick.

Mheshimiwa Spika, na mambo mengine yaliyokubaliwa kwenye makubaliano hayo la kwanza ni lile la ubia kwamba Serikali tutakuwa na asilimia 16 na wao watabakiza asilimia 84.

La pili, wao walikuwa na kesi na sisi ya dola bilioni 2.7 wakafuta kesi hiyo; la tatu, tukakubaliana kwamba watatoa dola milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ambayo hata kwenye briefing ndio Mbunge wa Kahama aliyekuwa anaiulizia, tukakubaliana hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, si hilo tu, tukakubaliana kwamba watakuwa wanatoa dola sita kwenye kila wakia ya dhahabu na tukakubaliana kwamba watatoa dola milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa maabara ya madini.

Kwa hiyo, haya yalikuwa sehemu ya frame work agreement ile ambayo ilikubalika na baada ya hapo tukawa tumeshamaliza yale mashauri yakiwemo na mengine ambayo yaliyokuwa yanahusisha mjadala kwenye makubaliano yale yaliyokuwa yanafanyika.

Mheshimiwa Spika, sasa baada ya kuwa imeshafanyika hivyo, kilichofanyika kingine ilikuwa ni kuanza kupokea gawio baada ya kuwa jambo lile limeshafungwa tangu mwaka 2020, kama lilishafungwa tangu mwaka 2020 kilichofuatia mwaka 2021 tulipokea gawio, mwaka 2022 tumepokea gawio na dola milioni 300 ambazo ndio kama bilioni 700 ilikuwa sehemu ya makubaliano kwenye mjadala uliofanyika na sherehe ile ilifanyika Ikulu, mbele ya Rais Magufuli. (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, kwanza nasikitika kwamba swali limeuliza shilingi trilioni 360 lakini limejibiwa shilingi trilioni 4.21. Hata hivyo, ninayo maswali mawili ya nyongeza: -

La kwanza, kwa nini Serikali iliamua kukubali kupokea shilingi bilioni 700 kutoka katika kesi za malimbikizo ya makampuni ya madini maarufu “makinikia” badala ya shilingi trilioni 360 ambayo ni madai halali katika nchi yetu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, nini kilichowafanya TRA washindwe kukusanya malimbikizo ya kodi yasiyo na kesi ya shilingi trilioni 7.54 na kusababisha ongezeko hili la malimbikizo ya kodi kufikia asilimia 94.6 lakini wakati huo huo uwezo wa TRA wa kukusanya malimbikizo hayo umekuwa ukishuka kila wakati na kufikia asilimia 10 tu na wakati huo TRA ikijivuna kwamba inaongeza makusanyo ya kodi?

SPIKA: Mheshimiwa Mpina kwanza nipate ufafanuzi; swali linazungumzia kesi 1,097; shilingi trilioni 360 na hizo Dola za Kimarekani milioni 181.4.

Mheshimiwa Naibu Waziri jibu linazungumzia mashauri kuwa 854 ambayo thamani yake ni shilingi trilioni 4.21 na dola za Kimarekani milioni 3.48. Haya ndiyo mashauri yaliyopo ambayo Serikali inayajua ambayo ni tofauti na ya Mbunge au mmechagua kati ya yale ambayo yapo, mmeamua kuyajibia haya ambayo mmeleta majibu? Nataka kuelewa kwanza hapa. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Hayo ni mashauri ambayo yapo na Serikali tunayatambua.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, naona umesimama. Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, ufafanuzi wa hiyo sehemu ya kwanza, halafu nimpe fursa ya kujibu yale maswali mawili.
WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, kwenye suala la msingi lile la shilingi trilioni 360; moja, Serikali haijakubali tu kimya kimya, haijakubali kupokea fedha hizo kwa maana ya kuacha shilingi trilioni 360, isipokuwa kilichofanyika, utakumbuka Serikali ilipeleka complain against makampuni hayo ya madini na baada ya complains zile kupelekwa…

SPIKA: Ngoja Mheshimiwa, twende kwa mtiririko mzuri. Ninachotaka kuelewa, swali la Mheshimiwa Mpina linazungumzia kesi 1,097; jibu linazungumzia kesi 854 na thamani ambayo Mheshimiwa Mpina anazungumzia ni shilingi trilioni 360, serikali inasema ni shilingi trilioni 4.21. Mimi nataka kuelewa ili nitoe mwongozo vizuri wa majibu hapa, namna Serikali ijibu. Haya majibu ambayo Serikali mmetoa, ni kwamba ndiyo kesi zilizopo ama idadi ni hii aliyotaja Mheshimiwa Mpina na kiasi cha fedha ni hiki alichotaja Mheshimiwa Mpina?

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, pana utofauti. Ile kesi kubwa aliyoiongelea ya Shilingi trilioni 360 ni ya upande wa makinikia. Hii ya mashauri ambayo yanaenda kwenye shilingi trilioni nne, ni ya mashauri ya kesi nyingine ambazo ziko TRAB na TRAT ambazo ndiyo Serikali inaendelea kuyafanyia kazi moja baada ya nyingine.

Kwa hiyo, pana mambo ya aina mbili na lingine limeongezeka ya yale yasiyo ya kesi na lile linakuwa la tatu. Kwa hiyo yameunganishwa pamoja.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza suala la kuvunja sheria hapa halipo kwa sababu tayari hawa wananchi wameshashinda kesi mahakamani na Mahakama ikawapa ushindi na ikaamuru mifugo yao warejeshewe.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; Waziri wa Maliasili na Utalii wakati anahitimisha bajeti yake alisema mifugo hiyo itarudishwa mara moja; na Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokutana na kikao cha wafugaji wote nchini aliagiza mifugo hiyo wairejeshwe lakini sasa hivi…

SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa Mpina ulishatoa maelezo marefu sana.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, swali ninaloliuliza hapa orodha ipo Wizarani na Waziri anayo orodha kwa nini anakwepa hapa kuwalipa hao wafugaji wanyonge ambao wameshashinda kesi mahakamani na kutudanganya hapa kwamba hiyo orodha hana?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu kwenye swali la msingi ni kwamba mpaka sasa hatujapata orodha ya wafugaji ambao wanalalamika hawajarejeshewa mifugo yao. Kama ambavyo nimeeleza kwamba kesi inapopelekwa mahakamani sisi tunapeleka vielelezo tu lakini kesi inabaki kuwa ni chini ya hakimu, DPP na sisi tunakuwa kama mashahidi, kwamba tumekamata mifugo hii, baada yah apo hakimu ndio anayetoa hukumu. Aidha, hukumu inakuwa ni kurejeshewa hiyo mifugo kwa faini au mifugo kutaifishwa.

Nimesema endapo kama kuna mfugaji ambaye ana kesi ambayo inatudai sisi Wizara ya Maliasili na Utalii basi waje wizarani tutakaa pamoja tuichambue hiyo kesi na tutaweza kutekeleza kama Serikali.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Moja; Serikali ina makakati gani wa dharura wa kudhibiti biashara holela, uingiaji wa mikataba mibovu na usimamizi hafifu wa sheria ambazo kasoro hizo zinasababisha ajira nyingi za Watanzania kupotea?

Mbili; kwa nini Serikali isiachane na utaratibu wa sasa hivi wa baadhi ya ajira kupatikana kwa njia ya uteuzi na badala yake ajira zote zikapatikana kwa njia ya ushindani, ajira za Viongozi na ajira za Watendaji, Mawaziri, Wakurugenzi na Makatibu Wakuu na Watendaji wengine wote wa Serikali ili kuiwezesha Serikali kupata Viongozi wenye uwezo usiotiliwa mashaka katika nafasi mbalimbali za Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, (KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Kisesa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameeleza ni mkakati gani ambao Serikali imeendelea kuchukua kwa ajili ya kuhakikisha kwamba hakuna mikataba mobovu pia utumiaji mzuri wa fedha ambazo zinaenda kwenye maeneo ya uwekezaji ili kuweza kulinda ajira za Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayofuraha kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba tayari Serikali kupitia vyombo vyake muhimu imekwisha kuanza kuchukua hatua na mtakumbuka Mheshimiwa Rais katika nyakati zote amekuwa akichukua hatua katika kuimarisha vyombo vyetu vinavyosimamia sheria, ikiwemo Mahakama lakini pia Polisi, TAKUKURU kwa maana ya PCCB (Prevention and Combating Corruption Bureau) ambayo inapambana na maswala ya rushwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua nyingine Serikali imeendelea kuweza kuchukua hatua kwa wale ambao wamekuwa wakiingiza katika mikataba mobovu, hatua mbalimbali zimekwisha kuchukuliwa na Serikali tayari ina Mahakama maalum kuchukua hatua kwenye masuala ya rushwa. Kwa mfano, tunayo Mahakama ambayo inasimamia masuala ya makosa ya kiuchumi, ambayo hii mojawapo ni kudhibiti haya ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyasema.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake pili ameeleza kwamba ajira kwa nini zisipatikane kwa njia ya ushindani badala ya uteuzi jinsi ilivyo. Kwa sasa, Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inaeleza namna na mfumo wa uendeshaji wa Serikali na inatambua uwepo wa ajira ambazo zinapatikana kwa utaratibu ambao Mheshimiwa Mbunge ameusema wa ushindani lakini pia zipo ajira zinazopatikana kwa njia ya uteuzi kulingana na provisions zilizopo katika Katiba, zipo pia ajira ambazo zinapatikana kwa utaratibu wa kuomba ama kuzipata.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo katika kupanua wigo wa ajira, Serikali imekwisha kuchukua mikakati ya kuhakikisha tunatafuta ajira ndani na nje ya nchi. (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Moja, kwa nini Wizara na TRC waliacha bei ya ushindani ya shilingi bilioni 9.1 kwa kilometa moja ya standard gauge na kuamua kumpa kampuni ya CCECC kwa shilingi bilioni 12.5 kwa kilomita moja ya standard gauge na kuisababishia hasara Serikali ya shilingi trilioni mbili ambayo ni kinyume na matakwa ya single source kama alivyoeleza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Ni kwa nini Serikali isivunje huo mkataba baina ya TRC na CCECC wa ujenzi wa kipande cha Tabora - Kigoma kwa sababu hata hiyo Lot III, Lot IV anayoi-refer CAG ameshatuambia kwamba tayari walikiuka utaratibu wa sheria. Kwa nini Serikali isifute huu mkataba wa kinyonyaji?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu bei ya ushindani, bei zilizopo ni tofauti sana na zilizotumika miaka ya 2017 wakati nchi inaanza ujenzi wa standard gauge. Kila kitu kimebadilika, hususan katika suala la asilimia zaidi ya 65 ya SGR, inatumia chuma. Bei ya Soko la Dunia ya chuma, imeongezeka kwa robo tatu ya gharama yake. Pia mwaka 2017 bei ya mafuta ilikuwa takribani shilingi 1,900, sasa hivi imekwenda mpaka shilingi 3,000 na kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo gharama anazolinganisha Mheshimiwa Mpina, ziko tofauti sana na gharama za leo. Hata hivyo, hapa tumesema katika jibu letu la msingi kwamba tumeokoa takribani shilingi bilioni 632.74. Katika nchi za Afrika Mashariki, sisi Tanzania peke yake, kwa gharama ya ushindani, ndiyo tumeweza kuwa na kiwango kidogo zaidi cha kutengeza kilomita moja kwa dola za Kimarekani milioni nne, wakati nchi jirani na hata ukisoma ripoti ya Benki ya Dunia, ni zaidi ya dola za Kimarekani kwa kilomita moja milioni 7.69. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nihakikishie Watanzania na Bunge lako tukufu kwamba hakuna hasara yoyote, zaidi tumeokoa fedha hizi ambazo nimezitamka hapa. Engineering estimate zilikuwa dola za Kimarekani bilioni 3.006 sawa na shilingi trilioni 7.2, nasi tumesaini mkataba wa shilingi trilioni 5.2. Maana yake tumeokoa tena shilingi trilioni mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, kwa nini mkataba usivujwe? Huu makataba hatuwezi kuuvunja kwa sababu kwanza ni wa gharama nafuu; na pili, ni mkataba na CCECC. Ukiangalia rank za Makampuni yote duniani, perfomance ya kampuni hii, inaonesha kufanya vizuri, ni ya 10 kwa mwaka 2021, na ni ya 11 kwa mwaka 2022. Kwa hiyo, hata kipande kile cha kutoka Isaka - Mwanza ambacho ni kilomeeta 341, wana asilimia zaidi ya 30. Kwa hiyo, wanafanya vizuri na ndiyo maana tuliwapa mkataba huu wa kutoka Tabora kwenda Kigoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu hayo mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kwa kuwa tathimini iliyofanywa na Wizara Novemba 2021 ilibaini kwamba jumla ya bilioni 83 za bidhaa za dawa pamoja na bidhaa za afya zilikuwa zimeibiwa.

Je, Serikali ilichukua hatua gani na imechukua hatua gani kwa hao watumishi ambao wamefanya ubadhilifu wa dawa hizo kwa ajili ya wananchi kwa ajili ya kutolea huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa, uwezo wa Bohari ya Dawa (MSD) kusambaza dawa pamoja na bidhaa nyingine za afya ni asilimia 59 tu. Hii inatokana na malimbikizo ya madeni ambayo ni zaidi ya bilioni 259, lakini pia mtaji wa bilioni 593. Je, Serikali inatoa tamko gani kumaliza matatizo haya, ili kuiwezesha taasisi yetu ya MSD kuwa na uwezo mkubwa wa kusambaza dawa pamoja na bidhaa nyingine za afya kwa maslahi ya wananchi wetu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimshukuru Mbunge mwenzangu kwa swali lake zuri, lakini swali la kwanza ni kwamba, wamechukuliwa hatua gani wale walioonekana kufanya ubadhiriru wa bilioni 83. Moja, sisi kama wataalam wa Wizara ya Afya tulifanya kazi yetu na kuona kwamba, kuna dalili za upotevu wa bilioni 83.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi yetu iliyofuata ni kukabidhi kwenye taasisi yetu ya TAKUKURU ambayo ina wataalam wa kujua sasa ili kufuata sheria na taratibu na haki za watumishi wa umma, tumepeleka kule wanafanya uchunguzi. Miezi miwili iliyopita walituambia kwamba, wako kwenye hatua za mwisho sasa kuweza kubaini specifically ni nani kafanya nini na ni nini kimefanyika ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua. Hilo ni swali lake la kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, ni kweli kwamba, Waheshimiwa Wabunge fedha wanazopitisha hapa bilioni 200 kwa ajili ya vifaa tiba na dawa ni fedha za vituo vyetu kwenye majimbo yetu. Maana yake tukipitisha hapa kwenye bajeti tunapitisha pesa kwa ajili ya vituo vyetu. Vituo vyetu vikipata pesa zinapelekwa MSD, maana yake ni nini? MSD tulitegemea i- operate kama bohari ya dawa, lakini ina-operate kama procurement entity.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hilo la kwamba, wapewe mtaji, nafikiri liliibuka wakati wa bajeti yetu na Wizara ya Fedha wamelichukua na wiki iliyopita tulikutana kujadili kuona namna gani MSD wanaweza wakapatiwa mtaji, ili sasa tukiwapitishia fedha hapa Bungeni, basi vituo vyetu vikiomba dawa MSD wakutwe tayari walishanunua dawa hizo. Hilo ni suala la kulichukua tu ili kuondoa ucheleweshaji uliopo.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Kwa kuwa chanzo kikubwa cha migogoro ya wananchi na wanaoishi katika maeneo ya hifadhi na wahifadhi ni mipaka pamoja na alama zinazoonekana, lakini pia ni pamoja na kuzuia matumizi mseto katika maeneo ya WMA kinyume na mikataba iliyofungwa katika uanzishaji wa WMA hizo: Je, Serikali ina mkakati gani mahususi wa kuondoa changamoto hizo ili kuwezesha wananchi kuishi kwa ushirikiano mwema na wahifadhi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kimsingi Serikali inatamani sana kuimaliza hii migogoro, lakini tunatambua kwamba mahitaji ya ardhi sasahivi ni makubwa, wananchi wanaendelea kuongezeka na kila mtu anatamani kumiliki ardhi. Ardhi iliyobaki ni ardhi iliyohifadhiwa ambayo ni inasimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii na utalii. Kwa hiyo, kumekuwa na hizi changamoto za hapa na pale na mara nyingi wananchi wanasema ni migogoro, lakini sisi tunasema siyo migogoro kwa sababu, maeneo yana mipaka yake, yana ramani zake, yana GN zake. GN zipo na zinajulikana, isipokuwa pale ambapo kunakuwa na sintofahamu ya mpaka, tunaenda kuufafanua kwa kuweka vigingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naendelea kuwaomba wananchi kwamba sisi tunaendelea kuongezeka, lakini ardhi ni ile ile. Tuendelee kuheshimu haya maeneo kwa mustakabali mzima kabisa wa Serikali na kwa vizazi vinavyokuja. Tunatunza haya maeneo siyo kwa sababu tu yameangaliwa, tunatunza kwa sababu tunaendelea kuongezeka.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Kwa kuwa, Serikali imeendelea kukaidi na kukiuka sheria katika uingiaji na usimamizi wa mikataba ya uziduaji ambayo ni madini gesi na mafuta na pamoja na matakwa yale ya TEITI lakini pia kuna matakwa ya Sheria Kifungu 12 cha (The Natural Wealth and Resources (Permanent Sovereignty) No. (5) Act, 2017) ambayo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa swali.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ambayo inataka mikataba yote iletwe hapa Bungeni. Kwa nini Serikali inaendelea kukiuka matakwa haya ya kisheria? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali haina mpango wala haifanyi maksudi kwamba lazima sheria iliyowekwa ikiukwe. Sheria zote zinasimamiwa na Serikali na Wabunge wote nasi Watendaji wote wa Serikali tumeapa kusimamia sheria ya nchi na Katiba ya nchi, kwa hivyo kama kuna ambayo haitekelezwi ni suala lingine la kuangalia tu mikakati ya Serikali ya kujisimamia na kuhakikisha kwamba sheria zinatekelezwa kwa mujibu wa jinsi zilivyotungwa lakini hakuna utaratibu wowote wa kwamba Serikali inakusudia na inavunja sheria yeyote.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa, Serikali kupitia TARURA, Mkoa wa Simiyu iliahidi kujenga Daraja la Mto Sanjo linalounganisha Itilima na Meatu na Daraja la Mto Sanga linalounganisha Maswa na Meatu kwa muda mrefu. Je, ni lini Serikali itatimiza azma yake hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itatimiza azma ya kujenga madaraja haya katika mito hii miwili aliyoitaja Mheshimiwa Mpina, inayounganisha kati ya Wilaya ya Itilima na Wilaya ya Maswa, lakini kuna mingine ambayo ametaja pia ya Wilaya ya Meatu anakotoka yeye Mheshimiwa Mpina. Tutaangalia katika bajeti hii ambayo tunaenda kuitekeleza 2023/2024 na kuona ni kiasi gani kimetengwa na nitakaa na Mheshimiwa Mpina kuweza kuona tunaanza vipi kwa haraka kadri ya fedha iliyotengwa ya ujenzi wa madaraja haya mawili.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Kwanza niipongeze sana TRA kwa hatua walizozichukua kuongeza uwezo wa kukagua hii miamala ya transfer pricing, ikiwemo ununuzi wa Kanzidata ya Orbis na kuiwezesha Serikali kupata mapato stahiki. Sasa ninayo maswali mawili ya nyongeza:-

Swali la kwanza; hizo hatua ambazo amezizungumza Mheshimiwa Naibu Waziri zimesaidia kwa kiwango gani kuongeza mapato ya Serikali?

Swali la pili; ni kauli gani Serikali inatoa juu ya ongezeko kubwa la taarifa shuku juu ya fedha haramu ambapo miamala ya usafirishaji wa fedha kwa njia ya kielektroniki na fedha taslimu imeongezeka kutoka trilioni 123 hadi trillioni 280 mwaka wa 2023. Sasa ishara hii inaonesha kwamba, kuna ongezeko kubwa la rushwa, ufisadi, transfer pricing, elicit financial flow, capital flight, sasa haya matukio haya kwa ongezeko hilo la hizi takwimu Serikali inatoa kauli gani kama FIU ilivyotoa taarifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote kabla ya kujibu maswali naomba kumpongeza Mheshimiwa Mpina pamoja na Wabunge wengine kwa namna wanavyopigania kuona kwamba, ukusanyaji wa mapato unapatikana kwa ufanisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza, kwa kweli, hatua hizi zimesaidia kwa kiasi kikubwa sana. Ndiyo maana inadhihirika hata hivi karibuni tumeona TRA wamevunja rekodi katika ukusanyaji wa mapato hapa nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kupitia TRA Serikali imeimarisha mifumo ambayo itadhibiti mianya yote ya rushwa na hata njia nyingine za ukwepaji wa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hayo, Serikali kupitia TRA imeongeza rasilimali watu kwa kiasi kikubwa sana na hata hivi karibuni nafasi 524 zimetangazwa na mchakato unaendelea.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri, pamoja na hayo Serikali imekwenda mbali sana, iko sasa hivi kwenye FATAF (Financial Action Task Force), anti-money laundering, anti-terrorism financing, Serikali iko vizuri sana. Mimi niko kwenye kikao cha European Union na tumeona namna European Union wanavyoisifia Serikali ilivyodhibiti utakatishaji pesa na ku-finance terrorism katika Taifa letu.

Mheshimiwa AG.

MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, nilitaka tu kuongeza ya kwamba, kwa mujibu wa Sheria ya Anti-Money Laundering, taarifa shuku zinapowasilishwa kwa FIU, baada ya kufanyiwa analysis hupelekwa na kufanyiwa kazi na vyombo vyenye dhamana ya kuchunguza na baadae kuchukua hatua za kisheria. Kwa hiyo, taarifa ambazo zimekwishatolewa kwa sasa zinaendelea kufanyiwa kazi na vyombo vyenye dhamana hiyo vilevile. (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Kwa kuwa Serikali katika Jimbo la Kisesa ilishaahidi kujenga mnara katika Kata za Isengwa, Mbugabanya, Mwabusalu, Mwakisandu, Lingeka na Mwabuma: Ni lini Serikali itatimiza azma yake hiyo ili kuboresha mawasiliano katika kata hizo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, Mbunge wa Jimbo la Kisesa, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge alileta kata sita ambazo zilikuwa na changamoto, na kweli nasi tukajiridhisha kuna changamoto hiyo. Baada ya kupitia na kuangalia bajeti yetu, Mheshimiwa Rais ameridhia kupeleka fedha za ujenzi wa minara katika Kata za Mwabuma, Isengwa pamoja na Mwabusalu ambapo watoa huduma wa Airtel na TTCL watakwenda kujenga. Kata nyingine ambazo zimebaki, tunazipokea kama Serikali, fedha zitakapopatikana tutahakikisha kwamba tunafikisha huduma ya mawasiliano, ahsante sana.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa hili tatizo la ajira ni tatizo kubwa sana hapa nchini hivi sasa. Je, kwanini Serikali isifanye tracer study na kuandaa database ya vijana wote wanaohitimu mafunzo ili kuweza kuwatambua, kuweza kuwafuatilia na kujua namna nzuri ya kuwapatia ajira Serikalini pamoja na sekta binafsi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwanini Serikali isiandae mfumo mzuri wa kuwakopesha hawa vijana, wale wanaotaka kuingia kwenye ujasiriamali hata walau mtaji wa Milioni 20 wa kuanzia na wakajidhamini kwa vyeti vyao vya vyuo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mweyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kumekuwa na tatizo la ajira lakini kwa sehemu kubwa Serikali imeweza kulifanyia kazi Serikali ya Awamu Sita ya Mama Samia Suluhu Hassan. Tumekuwa na mikakati mingi ya kuweza kuhakikisha tatizo hili linapungua, mojawapo kwanza amefungua private sector kwa kubadilisha sheria pamoja na sera. Sambamba na hilo katika maeneo mengi vijana sasa wameanza kupata ajira kwenye miradi mikuwa ya maendeleo, lakini sambamba na hilo wameendelea kutoa ajira katika Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili katika kutafuta kanzidata, ni kweli tumekuwa katika kila nafasi ambazo zinatolewa kwa ajili ya ajira majina yale ambayo wamekuwa waombaji tumekuwa tukiyachukua kupitia kitengo cha ajira TAESA ili kuweza kupata takwimu sahihi za vijana ambao wamemaliza Vyuo Vikuu. Sambamba na hilo hatuwaachi hivyo, kumekuwa na mafuzo mbalimbali ya kuwapa internship, wapo vijana ambao wamepelekwa TRA na taasisi nyingine nyingi za Serikali kuweza kupata mafunzo ya uzoefu kazini sambamba na kuanzisha pia utaratibu wa kuwauhisha wale ambao wamehitimu kwenye vyuo mbalimbali vikiwemo vya VETA na FDC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hilo hilo tumekwishakuanza kufanya, tumemaliza manpower survey kuweza kujua, lakini tunaenda kwenye hatua mbili sasa ya kufanya labour survey kuweza kujua idadi ya vijana ambao wanaweza kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili kuhusiana na mikopo, Serikali hii imekuwa ikitoa mikopo ya Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan tena kwa upendo mkubwa, ukiangalia hakuna kijana yoyote ambaye hapati mkopo, kumekuwa na scheme za utoaji mikopo katika elimu. Kwa mfano, kwa Shule za Msingi, tumekuwa tukitoa elimu bila malipo, lakini akimaliza sekondari anaenda Chuo Kikuu anakutana na bodi ya mikopo ambayo inampa mikopo, akitoa Chuo Kikuu, anapokuja nje anaenda kwenye Halmashauri zetu tunatoa mikopo ya 4:4:2 kwa maana ya asilimia Nne (4) kwa wanawake, asilimia Nne (4) kwa vijana na asilimia Mbili (2) kwa watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo tumekuwa na scheme nyingine za makubaliano na mabenki mbalimbali kuweza kushusha riba na kutoa mikopo ikiwemo benki hizo za kilimo ambazo tayari zimekwishaanza kutoa na yalikuwa ni maelekezo mahususi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kuweza kuhakikisha katika kila Halmashauri wanatenga maeneo maalum ya vijana kwa ajili ya kufanya kilimo na wanapewa mikopo kupitia Benki lakini pia Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge pia Mheshimiwa Luhanga Mpina ambaye ndiye muuliza swali kama mtapitisha bajeti ya Wizara ya Kilimo, kule kuna mpango wa building the better tomorrow ambao unaenda kugusa vijana zaidi ya Milioni Moja katika kuhakikisha wanatengenezewa scheme za maeneo ya kilimo kwa maana ya block farming na wajibu wa Wizara ya Kilimo, itakuwa ni kuandaa kwanza maeneo hayo lakini pili kutafuta fecha kwa ajili ya kuwapa vijana hao na kuweka miundombinu na tatu ofisi ya Waziri Mkuu itakuwa wajibu wa kuweza kuratibu shughuli hizo. Kwa hiyo, Mheshimiwa hayo tumeyaona kwa kweli vijana wakae tu mkao wa kula na watoe ushirikiano kwa Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan inawaona na inawaangazia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya hapo Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan hivi juzi, ametoa zaidi ya Shilingi Milioni 10 kila Mkoa kwa ajili ya wamachinga. Kwa hiyo, vijana wengi wako kwenye eneo hilo, ahsante. (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa usambazaji na ugawaji wa mbolea katika msimu wa kilimo 2022/2023 uligubikwa na changamoto nyingi ikiwemo wakulima kuuziwa mbolea feki, mbolea nyingi kutoroshwa lakini wakulima wengi kupelea mbolea na kusababisha hasara kubwa.

Je, katika msimu huu wa kilimo 2023/2024 Serikali imejipanga vipi kutatua changamoto zilizojitokeza mwaka jana na kuleta hasara kubwa kwa wakulima?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Luhaga Mpina, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba tulivyoanza mfumo wa ruzuku kulikuwa na changamoto. Changamoto zilikuwa nyingi, tulikuwa na changamoto ya mfumo wa distribution lakini vilevile changamoto ya waagizaji wa mbolea kuamini kuwa Serikali itawalipa, changamoto ya watu kutokuwa waaminifu. Nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote, mkifanya tathimini ya mwaka jana na mwaka huu changamoto zilizokuwepo mwaka jana nyingi zimetatuliwa na Serikali na tutaendelea kuboresha mfumo wa ruzuku kila siku kwa sababu changamoto zinajitokeza mpya kila kukicha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwaka huu tumekumbana na changamoto ya baadhi ya wafanyabiashara kwenda kuanza kutafuta njia ya kutorosha mbolea. Kwa sababu wameshindwa kuiba ndani ya mfumo, wameshindwa kuingiza takwimu hewa, sasa wameanza kutaka kutorosha katika boarder, Mkoa wa Songwe na Mkoa wa Kigoma imetusumbua sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nilitaarifu Bunge lako tumewakamata wafanyabiashara ambao walikuwa wanataka kutorosha mbolea kwa njia ya barabara na sasa hivi wamepandishwa Mahakamani kwa makosa ya uhujumu uchumi. Niendelee kuwaambia Watanzania na wakulima kwamba Serikali itaendelea kuboresha mfumo, hatutouacha mfumo wa ruzuku kwa sababu tunaamini kwamba tuna wajibu wa kuwasaidia wakulima wadogo na tutaendelea kukabiliana na changamoto zinazojitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hauwezi kufananisha changamoto za mwaka jana na mwaka huu. Mwaka huu hakuna changamoto ya usambazaji, tumeusisha vyama vya ushirika, tumeusisha halmashauri husika katika usambazaji wa mbolea, tumeendelea kuujenga mfumo kwa kutumia wenzetu wa eGA kuongeza security kwenye mfumo wetu ili kupunguza matatizo yaliyokuwepo mwaka jana. Kwa hiyo naamini kwamba tutaendelea kuuboresha mfumo wetu siku zinavyozidi kwenda. (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa sababu kubwa ya kushuka kwa bei ya pamba ni makato makubwa yanafanywa na Bodi ya Pamba, ambapo mwaka 2021 kwa kilo moja walikata shilingi 400; mwaka 2022 walikata shilingi 300 kwa kilo moja; na mwaka huu 2024 napo watakata.

Je, ni nani anayeruhusu viwango hivi kukatwa na kusababisha wananchi kupata bei ndogo ya pamba?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ninafahamu Mheshimiwa Mpina anatambua kwamba kuna makato ambayo yapo katika kanuni, kuna makato ambayo wakulima wanakubaliana wao wenyewe na kuna makato ambayo yapo kisheria. Kwa hiyo sisi ambacho tunakipokea ni kwamba, panapotokea malalamiko kila baada ya msimu wa zao ambalo linakuwa limelimwa ama limefanyiwa biashara, Wizara tunakuwa tunapitia na kuangalia yale makato. Yale ambayo tunaona yanamuumiza mkulima tunashauri Bunge lako Tukufu tunayaondoa. Kwa hiyo sisi jambo hili tuseme tumelipokea na baada ya huu msimu utapokwisha basi tutapitia yale makato yote na kuangalia yale ambayo yanawaumiza wakulima.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa usambazaji na ugawaji wa mbolea katika msimu wa kilimo 2022/2023 uligubikwa na changamoto nyingi ikiwemo wakulima kuuziwa mbolea feki, mbolea nyingi kutoroshwa lakini wakulima wengi kupelea mbolea na kusababisha hasara kubwa.

Je, katika msimu huu wa kilimo 2023/2024 Serikali imejipanga vipi kutatua changamoto zilizojitokeza mwaka jana na kuleta hasara kubwa kwa wakulima?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Luhaga Mpina, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikiri kwamba tulivyoanza mfumo wa ruzuku kulikuwa na changamoto. Changamoto zilikuwa nyingi, tulikuwa na changamoto ya mfumo wa distribution lakini vilevile changamoto ya waagizaji wa mbolea kuamini kuwa Serikali itawalipa, changamoto ya watu kutokuwa waaminifu. Nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote, mkifanya tathimini ya mwaka jana na mwaka huu changamoto zilizokuwepo mwaka jana nyingi zimetatuliwa na Serikali na tutaendelea kuboresha mfumo wa ruzuku kila siku kwa sababu changamoto zinajitokeza mpya kila kukicha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwaka huu tumekumbana na changamoto ya baadhi ya wafanyabiashara kwenda kuanza kutafuta njia ya kutorosha mbolea. Kwa sababu wameshindwa kuiba ndani ya mfumo, wameshindwa kuingiza takwimu hewa, sasa wameanza kutaka kutorosha katika boarder, Mkoa wa Songwe na Mkoa wa Kigoma imetusumbua sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nilitaarifu Bunge lako tumewakamata wafanyabiashara ambao walikuwa wanataka kutorosha mbolea kwa njia ya barabara na sasa hivi wamepandishwa Mahakamani kwa makosa ya uhujumu uchumi. Niendelee kuwaambia Watanzania na wakulima kwamba Serikali itaendelea kuboresha mfumo, hatutouacha mfumo wa ruzuku kwa sababu tunaamini kwamba tuna wajibu wa kuwasaidia wakulima wadogo na tutaendelea kukabiliana na changamoto zinazojitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hauwezi kufananisha changamoto za mwaka jana na mwaka huu. Mwaka huu hakuna changamoto ya usambazaji, tumeusisha vyama vya ushirika, tumeusisha halmashauri husika katika usambazaji wa mbolea, tumeendelea kuujenga mfumo kwa kutumia wenzetu wa eGA kuongeza security kwenye mfumo wetu ili kupunguza matatizo yaliyokuwepo mwaka jana. Kwa hiyo naamini kwamba tutaendelea kuuboresha mfumo wetu siku zinavyozidi kwenda. (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri kwa kweli ya Naibu Waziri lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, maboresho aliyoyasema Mheshimiwa Naibu Waziri ni makubwa. Je, hayo maboresho yametusaidia kuongeza kaguzi kiasi gani ikilinganishwa na kaguzi zilizokuwepo ambayo ilikuwa ni asilimia 1.2 kati ya makampuni 504 yanayojihusisha na miamala ya transfer pricing?

Swali la pili, Je, maboresho hayo yaliyofanywa na TRA yametuwezesha kuokoa fedha kiasi gani zilizokuwa zinapotea kutokana na kukosekana uwezo ndani ya nchi wa kukagua miamala ya transfer pricing?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina, kama ifuatavyo:-

Maboresho hayo ambayo tumefanya kupitia TRA yameongeza asilimia 4.5, mwaka uliopita kabla kufanya maboresho hayo ilikuwa tuko asilimia 1.2 lakini sasa tuko asilimia 4.5 kwa hiyo ni hatua kubwa sana ambayo tumepiga.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni suala la kitakwimu naomba tumpelekee kwa maandishi. (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa kuwa gharama za matibabu ya figo watu wanapoenda kusafisha damu ni kubwa sana, takribani shilingi 540,000 kwa wiki; na kwa maana hiyo ni takribani shilingi 2,160,000 kwa mwezi, gharama ambazo ukweli ni kwamba wananchi wetu wanashindwa ku-afford na wengi wanapoteza maisha. Sasa haya mambo mengine ya bima tunajiandaa na bima na nini na Bunge hili lilishawahi kutoa msamaha mwingi katika maeneo mengi, kwa nini wagonjwa hawa wasitibiwe bure na tukatoa msamaha katika hili eneo na tukafidia kwa ajili ya maeneo mengine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia Mheshimiwa Mbunge, kwa kweli wazo lake lina nia njema, lakini nataka kuwaambia, juzi hapa tumeonesha kuna zaidi ya shilingi bilioni 70.4 zimesamehewa kwenye eneo hilo ambalo Mheshimiwa analisemea. Tutaendelea kuchakata, kwa sababu sasa hivi tunaenda kwenye michakato ya bajeti na vitu vingine, watupe muda tuone. Kwa sababu, tunaweza kuahidi hapa, tukaahidi na isiweze kutekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Afya ameshafanya kazi kubwa sana ya kukaa chini na wataalamu wetu. Hizi huduma za figo zinaenda kushuka sana kwa sababu tumeshapata watu wanaoweza kutoa madawa na vile vifaa vinavyotakiwa kutoa huduma hiyo kwa bei rahisi zaidi na huduma hizo zitaenda kushuka sana. Haitakuwa kama bei aliyokuwa anaisema Mheshimiwa Mpina hapo.
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa kuwa Serikali iliweka mkakati wa kukarabati mitambo na njia za umeme, ili kumaliza tatizo la katakata ya umeme na migawo ya umeme.

Je, tangu programu hiyo ilivyoanza mwaka 2022 Serikali imeweza kupunguza kwa kiasi gani katakata na migawo ya umeme inayoendelea wakiwemo wananchi wangu wa Jimbo la Kisesa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII K.n.y. NAIBU WAZIRI MKUU NA WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo haya ya teknolojia huwezi kuwa na uhakika wa asilimia mia moja. Mambo haya ya umeme tatizo linaweza kutokea wakati wowote, unaweza kufanya matengenezo leo, kesho likatokea tatizo umeme ukakatika. Niombe tu aendelee kuiamini Serikali kwamba, tutajitahidi kwa kadiri ya uwezo wetu kuhakikisha tunaondokana na matatizo haya. (Makofi)
MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nimerejea Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la nyongeza, kwa kuwa tuna vijiji zaidi ya 6,000 hapa Tanzania havina zahanati. Je, Serikali ina mkakati gani wa haraka sana wa kuhakikisha kwamba wananchi hawa wanapata huduma za matibabu kwa kujenga zahanati na kumalizia zahanati ambazo wananchi walishajitolea kwa nguvu kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii ina thamini sana huduma za afya kusogezwa karibu na wananchi na ndio maana kupitia mpango wa maendeleo ya Afya ya Msingi tuliainisha maeneo yote ya vijiji na mitaa yenye sifa ya kujenga vituo vya afya. Katika miaka hii mitatu ya fedha tangu mwaka 2021/2022 mpaka sasa Serikali imeshapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa jumla ya maboma 1,254 ya zahanati nchini kote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba tunahakikisha vijiji vyote vyenye sifa ya kupata zahanati vinaendelea kujengewa zahanati, lakini mitaa yote yenye sifa ya kupata zahanati pia inaendelea kujengewa zahanati hizo kwa awamu.