Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mashimba Mashauri Ndaki (52 total)

Mapendekezo ya Mpango wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali katika Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili nami nichangie kwenye hoja hii ambayo iko mbele yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jina langu naitwa Mashimba Ndaki, natoka Maswa Magharibi. Nachukue nafasi hii pia kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa neema zake na uwezo wake ambao umeniwezesha kufika kwenye Bunge lango Tukufu. Pia nachukue nafasi hii kuwashukuru wananchi na wapigakura wangu wa Jimbo la Maswa Magharibi kwa kunipa kura nyingi ambazo hazikuwa na maswali; na hata wapinzani wetu walinyoosha mikono. (Makofi)
Nawashukuruni sana wapigakura wa Jimbo la Maswa Magharibi, kama nilivyokuwa nikiahidi na kama nilivyokuwa nikisema, niko hapa kuwawakilisha, kuwatumikieni na tutafanya kazi pamoja, tumeshaanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii pia kumpongeza sana Rais Mheshimiwa John Pombe Magufuli kwa namna ambavyo ameshaanza kazi baada ya kulihutubia Bunge hili. Tunamtia moyo kwamba sisi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tuko pamoja naye, tutasaidiana naye ili ndoto ambayo anayo kwa ajili ya Watanzania iweze kukamilika. Tunajua anayo ndoto kubwa na inaeleweka mpaka inatisha upande ule wa pili. Tutakusaidia Mheshimiwa Rais kama Wabunge ambao tumeaminiwa na wananchi kwa kipindi hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri ambao wameshateuliwa na kuanza kazi zao. Kazi yenu ni njema, endeleeni, msikatishwe tamaa na maneno ya wachache wetu ambao wao siku zote ni kukatisha tamaa tu. Kazi yenu ni njema, tuko pamoja. Mahali ambapo mtahitaji msaada wetu, kuweni na uhakika mtaupata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najua kwa namna ambavyo mmeanza kwa kasi wengi hawapendi; na hasa hii slogan ya hapa kazi tu, wengine wanajaribu kuipotosha na kusema yasiyokuwepo kwenye hiyo slogan, hata hivyo, endeleeni! Hata ninyi mliofunga mageti, mimi nawapongeza. Wenzetu wanasema eti mngeanza kwa kujengea watu uwezo. Unamjengea mtu uwezo wa namna ya kuja kazini kwa muda uliopangwa! Unataka kumjengea mtu uwezo kwamba atoke saa ngapi kazini anapofika! Hii itakuwa nchi ya namna gani? Endeleeni, chapeni kazi, tuko pamoja! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nijielekeze sasa mchango wangu kwenye hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango. Mapendekezo yake ni mazuri na yana kitu ukisoma unaona kabisa kwamba nchi yetu sasa inaelekea wapi. Mheshimiwa Waziri, hongera sana kwa mapendekezo haya na Mpango huu ambao umeuleta mbele yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni tofauti sana ukisoma na maoni ya wenzetu. Nimesoma sana ndani yake, huwezi kusema utapata kitu hapa cha ushauri. Sijui kama Mheshimiwa Waziri amesoma na kwamba labda kapata chochote, kwa sababu imejaa malalamiko, manung’uniko, hakuna ushauri wowote ndani yake, ina maneno tupu, wala hakuna takwimu. Sasa sijui kama upinzani wako serious kama wanakuja na vitu vya namna hii Bungeni na wanataka kweli kuongoza nchi hii na kuifikisha mahali pazuri. Wapinzani ninyi ni watu wazuri sana, lakini kuweni serious…(Makofi)
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Taarifa imefika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka sasa nichangie tu kwa haraka haraka katika mapendekezo haya ambayo yako mbele yetu. Kuhusiana na suala la viwanda, naunga mkono kwamba sasa tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda. Nakubaliana kabisa na hayo yaliyoandikwa lakini nataka tu kuweka angalizo kwamba bado tunavyo viwanda kwenye nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mapendekezo ya Mpango sijaona mazingira mazuri yanayojengwa kwa ajili ya viwanda ambavyo tayari vipo na vinajikongoja au vinapata shida kwa sababu ya changamoto mbalimbali.
Kwa hiyo, nilikuwa nasihi kwamba wakati tunatengeneza na kuimarisha Mpango huu kuelezwe bayana kwenye Mpango ni kwa namna gani mazingira yataboreshwa ili viwanda vilivyopo na ha ta hivyo vitakavyokuja viweze…
MWENYEKITI: Muda umekwisha.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika azma ya Serikali kuwa nchi ya viwanda na hatimaye kuwa na uchumi wa kati lazima Serikali ije na mkakati wa kulitumia Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo (SIDO) kwa mapana zaidi. Kwa hali ilivyo sasa hivi SIDO ina ofisi na kutoa huduma kwenye Makao Makuu ya Mikoa tu na Mikoa mingine haina, hali hii inafanya wananchi wanaotaka huduma kufuata huduma za SIDO Makao ya Mkoa ambako ni mbali. Lazima SIDO iwezeshwe ili iweze kufuata watu na kuwapa huduma huko wanakoihitaji. SIDO isogeze huduma katika Wilaya, Kata na hata vijijin na kwenye miji mingine midogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado mazingira ya kufanya ama kuanzisha biashara katika nchi yetu siyo rafiki kwa wafanyabiashara na wawekezaji. Mwananchi akitaka kufanya biashara hapo hapo anafuatiliwa na TRA na vyombo vingine vya utozaji kodi. Kwa wawekezaji vilevile mwananchi huyu mara hii amepata wapi mapato au faida ili alipe kodi wakati mtaji amekopa na anatakiwa aanze kurejesha? Serikali itengeneze mazingira rafiki kwa kuwawezesha wananchi wafanye biashara na uwekezaji kwa uhuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuwa sustainable kwenye viwanda lazima pia wanasiasa na private sector waaminiane. Sasa hivi bado kuna kutokuaminiana kati ya wanasiasa au Serikali kwa upande mmoja na sekta binafsi kwa upande mmoja. Serikali iweke mazingira ya kuaminika kwa sekta binafsi ikiwa ni pamoja na kuwa-assure wawekezaji wa nje na wa ndani kwamba waliwekeza mali yao itakuwa salama, haitataifishwa ama mazingira ya uwekezaji yasiwe yanayobadilika badilika sana kuashiria risk kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia kwenye hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Nichukue nafasi hii kwanza kabisa kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kushughulikia kwa sehemu kubwa sana suala la ushirika kwenye maeneo yetu kwa sababu wakati huo ushirika ulikuwa umekufa kabisa. Mwaka jana wakati anasisitiza mimi binafsi nilikuwa na wasiwasi kama unaweza ukafanya jambo lolote lakini kwa kweli alijitahidi sana na watu walielewa ushirika umefanya jambo zuri kwa mwaka huu ulioisha na naamini mwaka huu tunaouanza utafanya vizuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri katika Ofisi ya Waziri ya Mkuu, Mheshimiwa Jenista kwa kutusaidia kwenye Wilaya yangu na kwenye Jimbo langu alitupa pesa tukaanzisha Kiwanda cha Kuchambua Mpunga pamoja na ku-grade. Tumefanikiwa na tumeweza, vijana wanaendelea, wamepata ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimshukuru kwa sababu aliweka mbegu kwenye Kiwanda cha Chaki na chenyewe sasa kimeota, kimekuwa kiwanda kikubwa, tumepata mabilioni kutoka Serikalini, mjenzi tayari amekwishaanza kujenga. Kwa hiyo, nawashukuru sana Ofisi ya Waziri Mkuu kwa uwezesho mkubwa ili vijana wetu waweze kupata ajira, kujiongezea kipato na kuendesha maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumze mambo mawili tu. Jambo la kwanza nataka kuzungumza juu ya ajira hizo hizo za vijana. Uchumi wetu kwa sehemu kubwa unaendeshwa na sekta isiyo rasmi. Sekta isiyo rasmi ina utawala uchumi wetu kwa asilimia kama 60 hivi. Katika sekta hii isiyo rasmi sehemu kubwa wanaofanya kazi huko ni vijana maana nguvu kazi ya vijana kwenye Taifa hili ni kama asilimia 56 na asilimia 70 wako kwenye sekta isiyo rasmi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii inapoendelea kuwa kubwa namna hii siyo afya sana kwa uchumi wetu kwa sababu wataalam wa mambo ya uchumi wanasema sekta isiyo rasmi kama ni kubwa tuhesabu kwamba nchi hiyo itaendelea kuwa katika hali ya umaskini kwa sababu sekta isiyo rasmi haina mchango mkubwa unaoweza kueleweka kwa Serikali na hata kwa uchumi wa nchi hiyo. Kwa hiyo, sekta hii isiyo rasmi lazima tuendelee kufanya juhudi kuipunguza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali ili kurasimisha biashara za baadhi ya watu lakini pia kujenga ujuzi kwa vijana ili waweze kujiajiri watoke kwenye sekta hii isiyo rasmi wawe rasmi zaidi. Pia nashukuru pia kwa mpango wa Serikali ambao sasa umekwishaanza wa kugawa vitambulisho vya Sh.20,000 ili wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo wadogo waweze kusajiliwa lakini hii ni hatua ya kwanza tu ili waweze kwenda hatua ya pili ambayo sasa itawafanya wajulikane na waweze kutoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sekta hii isiyo rasmi, sasa wanaingia vijana ambao wamemaliza vyuo vikuu na vyuo mbalimbali kwa sababu ya kukosa nafasi za ajira maeneo mengine. Sekta hii inapoingiliwa na watu waliosoma namna hii, lazima sasa kama Taifa tuanze kuangalia ni kwa namna gani tunafanya kwa kasi kuipunguza sekta hii ili iwe rasmi watu hawa ambao Taifa limewasomesha waweze kuchangia sawasawa kwenye uchumi wa nchi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, vinginevyo tukiendelea kuiacha ikaendelea kuwa kubwa kwa wimbi kubwa la wasomi wanaoingia kwenye sekta hii, kwanza wakiingia huko kwa sababu mambo yake mengi hayajaeleweka vizuri watachanganyikiwa na kwa hiyo itakuwa ni chanzo cha vurugu au cha kukosesha amani nchi yetu kwa sababu wao wana-higher expectation. Tunaposoma chuoni tunaamini kwamba ukitoka hapo basi utakuwa umeukata sasa wakikutana na sekta isiyo rasmi ambayo haijaeleweka vizuri inaweza ikawapunguzia amani zaidi na hivyo kuwaongezea msongo wa mawazo na hatimaye kupelekea kutupeleka kwenye mahali ambapo hatutaki kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nataka kushauri pia vijana wetu wengi wanaomaliza vyuo vikuu hata kama ajira zipo wanashindwa kuajiriwa kwa sababu ya kukosa uzoefu. Suala hili limekuwa tatizo kubwa kweli. Nashauri Serikali kwa nini isije na mpango wa kujengea uwezo vijana wetu wanaomaliza vyuo wote wapate uzoefu wa mambo waliyoyasomea huko chuoni kupitia programu ambayo itakuwa ni ya kujenga uzoefu ya kiserikali. Siyo hii ambayo mtu anakuwa chuoni anaenda practical sijui miezi miwili, mitatu, no, akimaliza chuo kikuu aende Internship Programme ya muda wa mwaka mmoja au miwili ajenge uzoefu, aweze kuajiriwa nafasi za ajira zinapotokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunakutana na watu mbalimbali, mashirika mbalimbali ya kimataifa na taasisi zingine zisizo za kiserikali zinasema tunashindwa kuwaajiri vijana wanaotoka chuoni kwa sababu kwanza uzoefu hana lakini pia ujuzi wa kazi ile ambayo wangeweza kumpa hana, sasa atapataje uzoefu na ujuzi huo? Serikali ikija na mpango wa kila mwanafunzi anapomaliza chuo aende kwa Afisa Utumishi wa Wilaya, Idara au wa chombo chochote cha Serikali akae hapo, gharama zinaweza kuwa za mzazi au mlezi ili ajengewe uwezo awe na uzoefu na ujuzi wa lutosha ili aweze kuajirika nafasi za ajira zinapopatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tukiendelea na utaratibu tulio nao sasa mtu amalize chuo kikuu, ana matarajio makubwa, anafikiri atapata kazi, akienda kwenye interview anaonekana hana uzoefu, anarudishwa aende nyumbani akafanye nini? Kwa hiyo, nashauri Serikali kwamba ni muhimu sasa ije na Internship Programme ambayo itawawezesha vijana hawa wapate uzoefu na ujuzi wa mambo waliyoyasomea na hasa kazini ili waweze kuajirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nataka nizungumze na pengine litakuwa jambo la mwisho, ni suala la viwanda. Ni hivi, wawekezaji wa nje tunawahitaji sana lakini pia wawekezaji wa ndani nao tunawahitaji sana. Nadhani hawa wa ndani tunawahitaji zaidi kwa sababu wao pia wanatuona sisi kama Watanzania wenzao. Najua wawekezaji wa nje ni wazuri lakini wanatuona sisi kama soko lakini pia kama chanzo cha malighafi ili kutengeneza semi-processed commodity waweze kwenda kumalizia kwenye viwanda vyao kule nyumbani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumze tu juu ya viwanda vya nguo. Ni kweli tuna kauli mbiu inayosema ‘pamba hadi nguo’ lakini ni kauli mbiu tu inaungwa mkono na Sera ipi ya Viwanda vya Nguo? Hatuna Sera ya Viwanda vya Nguo! Naelewa tuna Sera ya Viwanda lakini Sera mahsusi kwa ajili ya Viwanda vya Nguo haipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, amesema Mheshimiwa mama Kilango jana hapa, nchi hii ina uwezo mkubwa wa kuzalisha pamba nyingi na hivyo kwa pamba hii tungeweza kuajiri watu wengi zaidi kama tungeangalia kwa ndani kwanza badala ya kuangalia soko la nje. Habari ya pamba ingeweza kujenga uchumi wetu vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa mama Malecela jana ametuambia Bangladesh ambayo ilikuwa nchi maskini sana hailimi pamba lakini imeajiri watu wake asilimia 85 kupitia pamba ambayo inazalishwa sehemu nyingine. Sasa sisi ni zaidi maana tuna watu milioni sita ambao wameajiriwa kwa kulima pamba kwenye nchi hii ambapo pamba yao inaweza ikatengeneza ajira zingine milioni tatu na kitu au mpaka nne. Kwa hiyo, pamba inaweza ikaajiri watu milioni kumi katika nchi hii ikiwa tutafanya juhudi za makusudi kuwaunga mkono wale waliowekeza kwenye viwanda vya pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini tusiwe na mpango kama ule tulionao kwenye sukari? Mbona viwanda vya sukari vimeweza kutu-sustain. Viwanda vya sukari vinazalisha sukari kwa nchi hii, hatuzalishi sukari kwa kuuza nje lakini tunazalisha sukari kwa ajili yetu Watanzania na tumevilinda kwa namna mbalimbali kwa kuzuia sukari isiingie hapa. Viwanda vya pamba hatujavilinda kwa namna hiyo, tumeacha soko huria hata kwa vitu ambavyo vinaweza vikatengenezwa hapa kwa kutumia pamba yetu na viwanda hivyo vikatengeneza ajira kwa ajili ya watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana tutafute ni kwa namna gani tunaweza kuongeza uzalishaji wa pamba lakini kuongeza viwanda vinavyochambua na kutengeneza nguo zinazotokana na pamba kutoka kwenye pamba yetu badala ya kuangalia tu kuuza pamba iliyo ghafi kwenda nje. After all tunapoiuza kule nje kilo moja kwa wenzetu inazalisha mashati matatu sisi hapa mkulima wa kwangu kule Maswa anapata Sh.1,200 tu lakini yule tuliyemuuzia pamba kule nje ananiletea shati, shati moja hapa nitanunua kwa Sh.40,000 mara tatu ni Sh.120,000. Tumetengeneza ajira kwake, tumemuongezea kipato yeye, sisi ambao tumezalisha tumeachwa hatuna kitu. Kwa hiyo, nafikiri Serikali ianze sasa kuwa na mkakati na mazao haya ambayo hasa ni ya Kimkakati tuone ni kwa namna gani tunaweza kuyalinda yakaajiri watu wetu wengi baadaye yakatupa kipato cha kutosha kwenye nchi yetu na watu wetu wakapata ajira wakafurahia matunda ya uhuru wa nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka niseme hayo mambo mawili tu kwa leo, nitazungumza mambo mengine nitakapopata nafasi nyingine hasa kuhusiana na viwanda vya nguo hapa nchini. Viwanda vya nguo vya hapa nchini kwa kweli hatujavitendea haki kwa sababu hatuvilindi, vinajipigania vyenyewe lakini ukijaribu kuangalia waliowekeza ni wazawa, ni Watanzania ambao wanaajiri Watanzania, wanatupatia kipato na tunapata namna ya kuendesha maisha yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020
MHE. MASHIMBA M. NDAKI – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA BAJETI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa tena nafasi ili niweze kuhitimisha hoja yangu ambayo iliwekwa Mezani kwako asubuhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya Kamati ya Bajeti imechangiwa na Wabunge tisa; Mheshimiwa Dkt. Sware Semesi, Mheshimiwa Mbaraka Dau, Mheshimiwa Jitu, Mheshimiwa Adadi Rajabu, Mheshimiwa Mussa Mbarouk, Mheshimiwa Martha Umbulla, Mheshimiwa Shally Raymond, Mheshimiwa Joseph Kakunda na Waziri wa Fedha na Mipango - Mheshimiwa Dkt. Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye hoja zilizosemwa na Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu muda wangu ni kidogo sana hapa. Mheshimiwa Dkt. Sware aliongelea kuhusu VAT kwenye miradi ya World Bank, kuiwezesha NFRA, uwekezaji kwenye Sekta ya Kilimo na uwekezaji kwenye Shirika la TTCL.

Mheshimiwa Mwenyekiti, masuala yote hayo tumeyazungumza kwenye Kamati na pia kwenye taarifa yetu tumeyaonesha. Kwa mfano, kipengele cha 12 - Mapendekezo ya Kamati; 12:3, 12:5 NFRA ukurasa ule wa saba kipengele cha 3:2 na Sekta ya Kilimo tumeizungumza sana hasa ukurasa ule wa saba kipengele cha 3:1.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inawezekana kuwa ukuaji wa uchumi ungechochewa zaidi na Sekta ya Kilimo, lakini pia sekta ambazo Serikali imewekeza zaidi zinachangia kwa sehemu kubwa sana kwenye kilimo. Kwa mfano, Sekta ya Ujenzi inachangia kwa sehemu kubwa sana kwa sababu mimi naamini sekta hizi huwezi kuziweka peke yake zikawa na faida kwenye uchumi, lakini zina faida kilimo pia kwa sababu ya namna ya mwingiliano wa kilimo pamoja na sekta ambazo Serikali iliwekeza sana. Hata hivyo, bado kuna umuhimu kwa Serikali kuwekeza zaidi kwenye suala hili la kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbaraka Dau aliongelea masuala ya TRA kufikia shilingi trilioni 1.9, nami naungana naye kuipongeza TRA kwa sababu kwa kweli wamefika kiwango ambacho ni kikubwa na kwa kweli ni cha kupigiwa mfano. Huwezi kudharau jambo hili. Shiligi trilioni 1.9 ni kiwango kikubwa, ingawa kweli bado jitihada zinatakiwa kufanyika, lakini ni kiwango kikubwa kabisa ambacho tunahitaji kutambua. Nasi kama Kamati tumetambua hilo na kwa kweli wamefanya jitihada mno. Kwa muda wa nusu mwaka makusanyo ya nchi kwa ujumla ni asilimia 95 nukta, sikumbuki sawa sawa lakini ni asilimia 95. Sasa makusanyo ya namna hii kwa mtu yeyote kwa kweli lazima apongeze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Dau amezungumzia upotevu wa mapato yasiyo ya kodi, lakini bado Kamati inaendelea kusisitiza pia kwamba kuhusiana na suala hili na tunatambua kwamba mapato kweli yanapotea hasa kwenye bandari zinazoitwa bubu; sasa kwenye Kamati pia tulisisitiza sana kwamba suala hili liangaliwe vizuri kwa sababu ni muhimu sana kuziangalia hizi bandari bubu. Bahati nzuri mwaka 2019 tulipitisha bajeti ya kumruhusu Waziri anayehusika na Wizara hii kuweza kuzitambua bandari bubu. Kwa hiyo, ni suala tu la Serikali sasa kuona ni kwa namna gani wanaweza wakazitambua baadhi ya bandari bubu ili kuweza kupunguza upotevu wa mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Dau alizungumzia pia ukusanyaji wa kodi ya majengo, naye alisema hakuwa ameona kwenye taarifa yetu, lakini kwa kweli kwenye taarifa yetu suala hili tulizungumza na kwenye mapendekezo kipengele kile cha 12:9 tulilitaja vizuri na naamini Mheshimiwa Dau atakuwa ameona pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia alizungumza juu ya mfumo wa stamps za kieletroniki (ETS). Kamati inaipongeza Serikali sana kwa kuja na mfumo huu madhubuti ambao tunaweza kusema umetoa real time data, yaani kwa makusanyo yanayokusanywa kwa wakati ule ule na lakini pia kuziba mianya ya upotevu wa mapato. Mfumo huu umeonyesha matokeo chanya na hivyo Serikali haina budi kuangalia sehemu nyingine pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuanza na mfumo huu mwanzoni kabisa, Kamati ilitaarifiwa kwamba Serikali wanaanza na vinywaji vile vikali, lakini wanaendelea kuweka ETS kwenye viwanda vile vinavyozalisha vinywaji baridi; maji, soda na kadhalika. Nadhani pia Serikali wataangalia ili kwenda kwenye bidhaa zaidi ya hizo za vinywaji peke yake kwa sababu katika Kamati tuliona pia pengine labda wanaweza wakaenda mpaka kwenye cement na bidhaa nyingine ili mradi tu kuhakikisha kwamba kodi inayotokana na bidhaa hizo ambazo tunaweza kuweka ETS, basi kodi hiyo ipatikane kwa urahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia alizungumza juu ya mchango wa hisani ya jamii (social responsibility). Mheshimiwa Dau alisema kule kwake kuna mtu mmoja anachangia shilingi milioni mbili nadhani kwa mwaka na alikuwa anaona pengine hicho ni kiwango kidogo. Sasa ipo Sheria ya Mapato Na. 332 ambayo inazungumza juu ya suala hilo. Kwa hiyo, ni muhimu sheria hii ikafuatwa ili kwamba wananchi wanaozunguka eneo hilo ambalo mwekezaji yupo na wenyewe waweze kufaidika na kitu hiki kwa sababu kipo kwenye sheria zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mchangiaji mwingine ni Mheshimiwa Jitu Soni, yeye aliongelea kuhusu masuala ya Sekta ya Kilimo na Blue Print. Kamati inaipongeza Serikali kwa hatua iliyochukua hasa katika kuondoa tozo mbalimbali ikiwa ni pamoja na zile alizokuwa akizitaja Mheshimiwa Jitu. Bado tunasisitiza Blue Print kwa sababu bado ipo kwenye mchakato wa kufanyiwa kazi, basi Serikali iharakishe kufanyia kazi suala hili ili wananchi na wafanyabiashara kweli wawe na mazingira mazuri ya kufanyia biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia alizungumzia kuhusiana na Serikali ione umuhimu wa kusimamia Sekta ya Kilimo na kuondoa vikwazo vya kikodi katika sekta hii. Suala hilo limezungumzwa pia na Wabunge wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la TTCL ambalo Mheshimiwa Waziri pia amelizungumzia. Tunashukuru kwamba Serikali imekubali kwamba TTCL inahitaji kuwezeshwa. Kwa kweli inahitaji kuwezeshwa hasa katika suala la minara. Tunashukuru kwamba Serikali inakubaliana na pendekezo tuliloliweka kwa sababu tayari wameshakutoa ruhusa ili waweze kukopa kama Mheshimiwa Waziri alivyosema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi pia tulikubaliana kwamba TTCL hawapaswi kununua minara mitumba, baada ya maelezo yanayohusiana na sheria tuliyoiweka sisi wenyewe. Kwa hiyo, hatukubaliani na suala hilo, lakini bado tunasisitiza kwamba Serikali ione umuhimu wa kuiwezesha TTCL ili iweze kufanya kazi zake vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Balozi Adadi Rajab ameongelea masuala ya miradi ya Liganga na Mchuchuma na pia mradi wa General Tyre. Tumesisitiza kwenye taarifa yetu kuhusiana na miradi hii ya kimkakati ambayo ipo kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kwamba miradi hii basi Serikali iharakishe namna ya kuitekeleza kwa haraka iwezekanavyo kwa sababu ina tija na ina faida kwa nchi yetu. Kwa hiyo, Serikali iangalie tu ni kwa namna gani inaweza ikaharakisha uanzishwaji wa miradi hii ili iweze kuwasaidia wananchi na kulisaidia Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tu na reservations zetu kwenye mradi wa General Tyre ule wa Arusha kwa sababu tuliona ni kama mipango yake haiendi sawa sawa na pengine wawekezaji waliokuwa wameshapatikana tayari, Kamati ilikuwa inaona kama wawekezaji hao hawajawa serious kiasi cha kutosha kuweza kuanzisha au kufufua kiwanda hiki cha General Tyre. Kwa hiyo, tulitoa tahadhari kwa Serikali kwamba iwe makini inapokaribisha hawa wawekezaji ili kuona kama wanaweza wakafanya kazi hiyo au watashindwa kufanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbarouk aliongelea masuala ya mapato na vyanzo vya Halmashauri kwa mazingira ya biashara. Ni kweli tumekubaliana, lakini mapato na vyanzo vya Halmashauri amezungumzia; lakini ukijaribu kuangalia kuhusu mapato ya Halmashauri kwenye taarifa ambayo tumewasilisha mbele yako, mapato ya Halmashauri yamepanda. Sasa sijaelewa Mheshimiwa Mbarouk anapozungumza mapato au vyanzo vya mapato ya Halmashauri alikuwa anamaanisha mapato ya aina gani? Kuhusu suala la mazingira ya biashara tunakubaliana naye kwa sababu pia tumelizungumza kwenye taarifa yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Martha Umbulla aliongelea masuala ya Deni la Taifa, mfumuko wa bei na NFRA. Mimi nakubaliana naye na sisi tumezungumza kwenye taarifa yetu kwamba suala la Deni la Taifa inabidi liangaliwe kwa sababu ukuaji wake ni ule wa nje. Ni wale wakopeshaji wa nje, sio wakopeshaji wa ndani. Sasa wakopeshaji wa nje wana mambo yao. Sasa ni vizuri kuliangalia kwa makini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mfumuko wa bei tulizungumza pia tukashauri Serikali iangalie mfumuko wa bei pamoja na riba zinazotolewa na mabenki yetu ili kuona uwiano wa hivi vitu viwili kama tunaweza kubadilisha au kusahihisha riba zinazotolewa na mabenki yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la NFRA Mheshimiwa Mama Umbulla tunakubaliana kabisa kwamba NFRA lazima iwezeshwe kifedha na kimtaji kwa sababu hivyo ilivyo sasa hivi inakua ni ngumu sana wao kununua chakula au mahindi hasa wakati mahindi yamekuwa kwa wingi kwa wakulima wetu, hasa ukizingatia kwamba suala la chakula ndiyo linalosaidia kupunguza mfumuko wa bei zaidi linapokuwa ni zuri. Sasa likiachwa linaelea, siyo vizuri sana kwa sababu italeta shida kwenye mfumuko wa bei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Shally Raymond aliongelea mwenendo wa riba pamoja na gharama za mabenki. Mheshimiwa Joseph Kakunda, aliongelea mfumo wa uwajibikaji wa watumishi Serikalini uangaliwe namna ya kuwa na huo mfumo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Kakunda alizungumzia juu ya utokaji wa fedha za mfuko wa jimbo zipangiwe mwezi Januari. Yaani kazi zake zipangwe mwezi Januari, zikija tu ziende kwenye miradi moja kwa moja. Suala hili nadhani linahitaji mjadala mkubwa, kwa sababu ni kweli zikija zinaweza zikaenda kwenye miradi, lakini nadhani mfuko wa Jimbo kazi yake ni kuchochea au kuhamasisha maendeleo, sio kumaliza miradi iliyoanzishwa na Halmashauri husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kmahitaji ya Jimbo yanabadilika mara kwa mara, sasa yakipangwa moja kwa moja kuanzia Januari halafu yaje yatekelezwe mwezi wa Kumi au wa Kumi na Moja pesa zinapokuja, inaweza kabisa wakati huo ikawa mahitaji yamebadilika yamekuwa mengine na kwa hiyo utekelezaji wake ukawa ni mgumu. Kwa sababu mfuko huu uko chini ya Waheshimiwa Wabunge, nadhani wanaelewa maana yake, pesa zake hizi zinapokuja kwenye Majimbo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Kakunda ndio alikuwa wa mwisho kuchangia. Labda suala la VAT kwenye miradi linafanyiwa kazi na Serikali na Serikali imekubali…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia Mheshimiwa.

MHE. MASHIMBA M. NDAKI – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA BAJETI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kumaliza hoja yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali maoni, ushauri na mapendekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti. Ahsante sana. (Makofi)

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nimshukuru tena Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu na kuhitimisha ama kutoa mchango wangu kwa hoja iliyokuwepo jana na leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru wewe binafsi sana, sana, kwa kutuongezea mjadala wetu jana, pamoja na kwamba ulisaidiwa kidogo jioni, lakini pia umeendelea leo, lakini nikushukuru sana wewe pia kwa kuongoza mjadala vizuri. (Makofi)

Nimshukuru pia Mheshimiwa Naibu Spika, Wenyeviti wa Bunge, kwa uwezo na umahiri wao kuliendesha Bunge letu, lakini pia nichukue nafasi hii kumshukuru na kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Majaliwa, pamoja na Waheshimiwa Mawaziri ambao wamekuwa wakikaimu nafasi yake wakati hayupo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu amekuwa makini sana katika kusimamia shughuli za Serikali, aidha napenda kuwashukuru sana, sana Waheshimiwa Wabunge wote ambao mlipata nafasi kuchangia hotuba yetu, lakini hata wale ambao hamkupata nafasi mmechangia, kwa sababu katika hili ni Wabunge 48 wamechangia kwa kuzungumza na Wabunge watatu, wamechangia kwa kuandika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, changamoto za Wizara yangu kwa kweli ni nyingi na dalili yake kwamba changamoto ni nyingi ni uchangiaji wa Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wengi na wewe imekulazimu angalau kupunguza dakika za Mbunge kila mmoja kuchangia. Sasa inaonesha ni kwa namna gani sekta hizi mbili ya mifugo na uvuvi ni sekta muhimu na za msingi sana kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kusema ukweli sekta hizi zinabeba watu wengi, lakini pia wengi wao kipato chao siyo kile cha juu, ni kipato cha chini na cha kati kidogo. Kwa hiyo, ni sekta ambazo kwa kweli zina umuhimu mkubwa na ndiyo maana zinapojadaliwa kweli zinavuta hisia za watu wengi.

Mheshimiwa Spika, nipende kushukuru sana, ushauri wa Kamati yetu ya Kilimo, Mifugo na Maji, ushauri wao ulikuwa mzuri sana na niahidi tu kwamba tutauzingatia wote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu michango ni mingi sana na mimi nimechanganywa na makaratasi mengi ya wasaidizi wangu hapa yaani wana majibu karibu yote ya Waheshimiwa Wabunge, sasa niseme tu kwamba Waheshimiwa Wabunge hoja zenu, maoni yenu na mapendekezo yenu tutayazingatia katika utekelezaji wa bajeti yetu ya mwaka 2021/2022 na tutatoa majibu kwa njia ya maandishi kwa kila hoja ambayo imezungumzwa na kila Mheshimiwa Mbunge, wale walioandika, pamoja na wale waliopata nafasi ya kuzungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mimi hapa niseme mambo machache tu ambayo nadhani si muhimu sana kuliko mengine, lakini nadhani kwa sababu ya muda wetu yale nitakayoweza kusema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na suala la ushirikishwaji hafifu wa wadau wakati wa kutunga sheria, kanuni na taratibu, inawezekana kwa sababu kama kawaida sekta hizi ni pana hasa kwenye upande wa uvuvi, ukisema uvuvi ukanda wote wa bahari, zaidi kilometa 1,400 ni ukanda mrefu na watu ni wengi. Ukija Ziwa Victoria ni kubwa watu ni wengi, nenda Ziwa Tanganyika, nenda Ziwa Nyasa ni watu wengi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ushirikishwaji unaweza usionekane sana ingawa watalaam wetu kwakweli wamekuwa wakijitahidi sana wanapofanya utafiti juu ya jambo linalotaka kufanyiwa mabadiliko au linalotaka kufanyiwa marekebisho, wamekuwa wakijitahidi kupita kwenye maeneo ya wadau ili kupata taarifa zao ili kupata maoni yao.

Mheshimiwa Spika, lakini niseme tu kwamba Wizara itajitahidi, tutajitahidi kuhakikisha ya kwamba kila mdau anayehusika kwenye masuala ya uvuvi, kila mdau anayehusika kwenye masuala ya mifugo kama tunataka kutunga sheria ama kubadilisha ama kupitia upya lazima tutawashirikisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna wakati tulienda Mafia tukakutana na wavuvi walisema hiyo changamoto na kwa sababu changamoto kule ilikuwa ni kubwa zaidi, tuliamuru watafiti na watalaam wetu warudi tena kule na walirudi wakaenda kushirikisha wadau wetu mbalimbali ili kusudi tu tuweze kupata majibu ya changamoto ambazo zinawakabili wavuvi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye suala la wavuvi kuhitaji elimu kutoka Wizarani badala ya kuwachomea zana zao za uvuvi. Hili suala ni la msingi sana na tumeliona baada ya kufanya mikutano na wavuvi, tulifanya mkutano mkubwa na wadau wa uvuvi Dar es Salaam, tukafanya mkutano mkubwa na wadau wa uvuvi Mwanza, tumeliona na hawa wadau wengi wanakuwa hawana habari na mambo mengi yanayotokea ndani ya Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na hivyo tumeamua ndani ya Wizara kuanzia Katibu Mkuu wangu anayehusika na Uvuvi na watendaji wake, Wakurugenzi pamoja na Wakuu wa Idara, Wakurugenzi wa Taasisi zilizo chini ya Uvuvi wote tumeamua sasa twende kwa hawa wadau, kujaribu kuzungumza nao na kuwaelimisha juu ya sheria tulizozipitisha na kanuni tunazozitunga na kuzipitisha ili wazifahamu. Kwa sababu wadau wengi wanakuwa hawazifahamu, kwa hiyo, tumekubaliana kwamba tutatoa elimu juu ya sheria, kanuni na taratibu zilizoko, lakini pia tutatoa elimu juu ya tozo mbalimbali ambazo zinapitishwa na Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia tutatoa elimu juu ya tafiti mbalimbali tunazozifanya sisi ngazi ya Wizara ili kuhakikisha tu kwamba tuko kwenye ukurasa mmoja na wadau wetu badala ya kwenda tu na kuwachomea nyavu zao, badala ya kwenda tu na kuwalaumu, badala ya kwenda tu na kupora labda mitumbwi yao, hapana; lazima tuwape elimu halafu ndio tuweze kuanza kushughulika nao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutashirikiana pia na wadau wengine wanaoshiriki kwenye mazao ya uvuvi kama TASAC ili ya kwamba tuone ni kwa namna gani elimu inaweza ikafika mapema.
Lakini kulikuwa na suala la wavuvi wa Ziwa Tanganyika waruhusiwe kutumia taa za solar zenye watts 200 badala ya watts 50 kwa chombo. Serikali tuliruhusu matumizi ya taa kumi zenye watts tano kwa kila moja kwenye uvuvi wa dagaa katika Ziwa Tanganyika na hii inatokana na utafiti uliofanyika pia hatufanyi vitu hivi bila kuwa na utafiti bila kuwa na taarifa kamili zinazohusiana na utaalam wa jambo fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utafiti unaonesha kwamba mwanga wa taa hizo kumi kwa watts tano unafika kina cha mita 150. Sasa ukisikiliza maoni ya Waheshimiwa Wabunge hapa, wanasema ni chini ya hapo, lakini utafiti wetu unaonesha hivyo. Ongezeko la mwanga halina tija sana kutokana na sababu kuwa zaidi ya kina cha mita 150 hakuna samaki kwa kuwa hakuna hewa ya oxygen kule chini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa mimi sijaelewa vizuri labda kwa sababu tutahitaji kuzungumza na kukutana na wadau, tutaelewa vizuri wanachokimaanisha labda kina maana gani. Kwa hiyo, tutaendelea kuwatembelea wavuvi wetu walioko Ziwa Tanganyika, tuelimishane nao juu ya habari hii ya taa na ingawa pia wengine wana maoni kwamba taa za solar pia zisitumike, yaani kuna wakati maoni mbalimbali yanakuja na yanafika mahali yanatuletea shida kidogo.

Mheshimiwa Spika, suala la lingine lilikuwa linahusu kuruhusu uvuvi wa kambamiti uanze Disemba hadi Mei; Mheshimiwa Mpembenwe nadhani alizungumza suala hili.

Mheshimiwa Spika, uvuvi wa kambamiti kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo unaruhusiwa kufanyika kuanzia mwezi Machi hadi Septemba kila mwaka kwa Kanda ya Kaskazini inayohusisha Wilaya za Bagamoyo, Pangani, Chalinze na kuanzia mwezi Aprili hadi Agosti kila mwaka kwa Kanda ya Kusini inayohusisha Wilaya za Mkuranga, Kibiti pamoja na Kilwa. Aidha, kipindi kilichobaki kimeachwa ili kambamiti waweze kuzaliana na kukua.

Mheshimiwa Spika, maamuzi haya yamefanyika baada pia ya taarifa za utafiti wa kisayansi na kuzingatia uendelevu wa rasilimali za kambamiti. Hayo ndiyo tuliyoyazingatia katika kuangalia ni kipindi kipi ukanda ule wa Kaskazini wavue na ni kipindi kipi ukanda huu wa Kusini wavue. Kwa hiyo, hayo ndio tuliyoyazingatia, lakini ni baada ya kufanya utafiti.

Mheshimiwa Spika, tutaendelea kufanya utafiti na kuona kama maoni ya Waheshimiwa Wabunge ndio valid kwa sasa ili tuweze kuamua pia. Sisi hatuko stagnant sana, hatuko rigid sana kiasi kwamba tunashirikiana, tunasikiliza kile kilio cha wavuvi wetu, cha wadau wetu kuhakikisha kwamba tu tunakwenda pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende kwenye mifugo; muda wetu ni mchache, lakini nizungumzie kuhusiana na uhaba wa miundombinu ikiwemo majosho, mabwawa, visima na minara. Niseme tu kwamba kwa kweli uhitaji ni mkubwa na kwa namna ambavyo Waheshimiwa Wabunge mmechangia, mmeona pia namna fungu letu lilivyo. Sasa kwa sababu uhitaji ni mkubwa kwa mwaka huu wa fedha hatutaweza kukamilisha kila jambo walilohitaji Waheshimiwa Wabunge tulifanye kuhusiana na miundombinu ya mifugo. Tutafanya kwa sehemu lakini sehemu zingine tutafanya kwa miaka inayokuja.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, tumeweza kujenga majosho 12 tu, mengine 59 yanaendelea kujengwa, tuna majosho 199 yamekarabatiwa na majosho 111 yanaendelea kukarabatiwa. Kwenye mpango wetu wa mwaka huu tumesema tutajenga majosho 129; kwa hiyo, tutaangalia tutaanza na mahali ambapo majosho hayapo kabisa. Tutawapa kipaumbele mahali ambapo ng’ombe wako wengi, lakini pia majosho hakuna. Kwa hiyo, tutaangalia hilo lakini miaka inayofuata tutaendelea kwenda kwenye maeneo mengine pia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kuhusiana na mabwawa; mabwawa pia tunayo kidogo kwa mwaka huu wa fedha ambao ninaomba sana Waheshimiwa Wabunge mtupitishie tuna mabwawa matano. Sasa tutayagawaje kwa Wabunge na majimbo 260 na kitu, hiyo pia ni changamoto yetu nyingine. Lakini nawaombeni tu kwamba tukubaliane maeneo ambayo yatapata mabwawa basi ukipata moja, ninaomba tu tushirikiane, siku nyingine tutapata nyongeza kwa kadri ambavyo tutakuwa tumepata fedha.

Ndugu yangu Mheshimiwa Nicodemus Maganga alisema tutachukua shilingi asipopata, lakini nimhakikishie tu kwamba mpango wetu ni kila mmoja aweze kupata kulingana na fedha tulizonazo. Lakini niombe tu kwamba ikiwa hautafanikiwa kupata kwa mwaka huu, kuna mwaka utafanikiwa kupata. Kabla ya 2025 unayoihofia, tutakuwa tumekupa malambo au mabwawa ambayo tutatuliza wapiga kura wako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie kuhusiana na upatikanaji wa malisho, jambo hili pia limechangiwa na Wabunge wengi. Sasa Wizara tunaendelea kuboresha malisho. Mheshimiwa Naibu Waziri wangu amelizungumza kidogo, lakini mpango wetu ni kwamba tunataka mashamba ya Serikali na mashamba ya Taasisi za Serikali, tuyape mbegu kama ambavyo Naibu Waziri amezungumza tuwape mbegu waweze kupanda. Taasisi zetu za utafiti pia tutazipa mbegu waweze kupanda na wakishapanda tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo kuwaleta wafugaji wetu waweze kujifunza kwenye maeneo haya ambayo tumesema tutapanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumesema tutaenda Halmashauri 20 ili ziwe na mashamba darasa ya malisho, sasa Halmashauri hizi 20 bado ni pungufu, haziwezi kuenea kwenye maeneo ambayo wafugaji wetu wametawanyika. Lakini ninaomba sana, sana maeneo ambayo tutafika na malisho na mbegu hizi za malisho, basi wafugaji walioko kwenye maeneo hayo wajifunze namna ya kustawisha malisho ili tuweze kuwa na malisho ya kutosha. Lakini pia tunataka tuhamasishe wadau wetu Serikali za Mitaa na wao maeneo wanayotenga wajaribu pia kupanda mbegu ambazo sisi tutakuwa nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme tu kwamba kuna Halmashauri ambazo zimetenga maeneo ya wafugaji vizuri, lakini kuna Halmashauri zimetenga maeneo ya wafugaji na maeneo ya wakulima, lakini kwa upendeleo sana ambao sio mzuri na upendeleo huu umeleta mgongano kwenye baadhi ya Halmashauri. Utakuta eneo la Halmashauri zima, limepewa wafugaji asilimia 70, wakulima asilimia 30 wakati idadi ya wafugaji na wakulima iko sawa, sasa utakuta lazima maeneo kama haya kutakuwa tu na ugomvi.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninawasihi sana Halmashauri zetu kwamba tunapopanga maeneo ya malisho tuzingatie pia uwiano wa watu walioko kwenye Wilaya yetu, tuzingatie pia uwiano wa shughuli za kimaendeleo zinazofanyika kwenye Halmashauri zetu hizo, vinginevyo tutaendeleza ule ugomvi. Lakini nafurahi kusema kwamba kuna Wilaya ambazo zimeamua zitaanza kutenga maeneo na kufanya kama ranchi.

Mheshimiwa Spika, nawaunga mkono Halmashauri za namna hiyo na ninawaombeni Halmashauri za namna hii badala ya kuomba fedha za miradi ya kimkakati za kujenga stendi, za kujenga sijui vitu gani basi pelekeni kwenye ranchi hizi mlizotenga. Hizi ranchi zinaweza zikawapa fedha nyingi kuliko mnavyoweza kutarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kifupi tu niseme sisi ranchi tunakodisha kwa hekari moja shilingi 3,500; sasa ukikodisha wafugaji wengi kwenye ranchi mtakazokuwa mmetenga, wafugaji wengi ukawa na hekari za kutosha ni chanzo kimojawapo cha mapato ya Halmashauri zenu. Badala ya kung’ang’ania na miradi ya stand, miradi ya masoko sijui na miradi ya namna gani, utakuwa umetatua tatizo la kipato cha Halmashauri yako, lakini utakuwa umeondoa mgogoro kati ya wakulima na wafugaji au wafugaji pamoja na wawekezaji wengine wanaotaka kutumia ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika suala la kuongeza upatikanaji wa huduma za ugani na vitendea kazi, hili suala pia limezungumzwa sana na Waheshimiwa Wabunge, ni kweli tutaendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI ambao ndio wanahusika hasa kwenye ajira za Maafisa Ugani wetu hasa wale wote wa uvuvi pamoja na wale wa mifugo. Lakini tutaimarisha mifumo yetu ya huduma za ugani kiganjani ikiwemo m-kilimo ambao ni mfumo unaosaidia kufikisha elimu ya ufugaji bora wa samaki, ufugaji bora wa mifugo kwa wadau wetu mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaendelea kufanya hivyo. Lakini tumesema kwenye taarifa yetu tutawezesha safari hii kununua pikipiki 300, ambazo tutazigawa kwenye maeneo ambayo tunaona ni critical kwenye baadhi ya halmashauri. Mahali ambapo wafugaji au shughuli za ufugaji ziko nyingi, tutagawa pikipiki ili kuweza kuwasaidia hawa watu wetu pia waweze kusafiri na kukutana na wadau wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda niende sasa nizungumze kidogo kuhusiana na suala la NARCO, wewe umetoa mchango wako juu ya jambo hili.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Bahati mbaya muda umeisha, lakini basi nakupa bonus dakika tano umalizie.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, basi nakushukuru sana ahsante sana, nikushukuru sana. Mengine sasa tutatoa majibu kama nilivyosema kwa maandishi, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, naomba sasa kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANO YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Na mimi nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kukubali bajeti nzuri namna hii ije hapa Bungeni. Pia niwapongeze wapishi, Mheshimiwa Waziri, Dkt. Mwigulu Nchemba na Eng. Hamad Masauni kwa namna ambavyo walipika na hatimaye kutuletea hapa. Lakini pia nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Kamati ya Bajeti ambao walitoa maoni mazuri sana kuhusiana na bajeti hii; uchambuzi wao kwa kweli umejitosheleza nami nawashukuru sana. Lakini niwashukuru pia Wabunge wote waliochangia hata wale ambao hawakuchangia lakini wametoa mawazo yao kwa namna moja ama nyingine, lakini hasa wale ambao walichangia sekta ya mifugo na uvuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na hoja za Kamati, mojawapo ilikuwa ni Serikali iweke mazingira bora na kuhamasisha wananchi kufuga samaki. Suala hili la ufugaji wa samaki ni suala jipya. Tunakubali kwamba tutaendelea kufanya kazi hilo na Serikali tumejiandaa vizuri. Moja, tumeandaa miongozo mbalimbali inayoongoza suala lenyewe la ufugaji wa samaki, tuna miongozo ya namna ya kufuga au kutunza vifaranga; tuna miongozo ya namna ya kufuga samaki kwenye mabwawa; tunamiongozo ya namna ya kufuga samaki kwenye vizimba; na miongozo mbali mbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunajitayarisha vizuri kwa sababu wavuvi wetu hasa wanaotaka kufuga samaki kwenye vizimba wanapata shida hasa kwenye suala la environmental impact assessment Pamoja na NEMC. Sasa sisi tumesema tutagharamia na tutafanya kama Wizara, strategic environmental assessment kwenye maeneo ya upande hasa wa ziwa na bahari na maeneo yanayokubalika, halafu tutawajulisha wanaotaka kufuga samaki ili waweze kufuga samaki kwenye maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala hili la kufuga samaki pia tumesema tuanzishe vituo vipya viwili, vitakavyowezesha wananchi wetu kujifunza. Tuna vituo vipya vitano viko kule Lindi, Ruvuma, Mwamapuli pale Igunga, Kingorwila Morogoro na kule Chato na tumesema tunaongeza vituo vyangine viwili kule Mtwara na Dar es Salaam. Hivi vituo viwili vitakuwa ni special kwa ajili ya watu wa mwambao, kwa sababu mfugaji wa samaki kwa vizimba vya mwambao na kule ziwani tofauti kidogo, kwa hiyo tumeona tuanzishe vituo viwili. Mwaka wa fedha unaokuja vituo hivyo vitafanya kazi na wananchi walioko kwenye maeneo hayo watakwenda kwenye vituo hivyo ili waweze kujifunza namna ya ufugaji bora wa samaki jinsi ulivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumesema vile vile tutaendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa wafugaji wa samaki wa mabwawa na vizimba na maeneo mengine. Wataalam wetu wapo tayari kwenda na kutoa utaalam, mafunzo ili kwamba suala hili liweze kueleweka vizuri na wananchi waweze kuchukua hii kama fursa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu, suala la kufuga samaki ni suala rahisi sana na vijana ambao wako huko wanajaribu kuangalia wafanye kazi gani, wanaweza kuanza na hili kwa sababu hili ni eneo oevu sana na linaweza kuwapa kipato kizuri cha kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine ambalo Kamati walitushauri walisema Serikali iweke mazingira yatakayowezesha usafirishaji wa mazao ya uvuvi. Tumejitahidi sana kwenye eneo hili, moja ya jitihada tulizofanya ni kupunguza tozo. Tulisema kwenye bajeti yetu tulipokuwa tunasoma hapa, tumepunguza tozo za aina mbalimbali ambazo tulizitaja kwenye bajeti yetu, sipendi kuzirudia hapa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo tulilizungumza na Kamati, ni Serikali iendeleze mapambano dhidi ya uvuvi haramu na kudhibiti utoroshaji wa mazao ya uvuvi, suala hili ni suala endelevu. Naomba Waheshimiwa Wabunge waelewe na wananchi ewelewe kwamba, uvuvi haramu haukubaliki kwa namna yoyote ile. Tunaendelea nalo lakini kwa namna ambayo itakuwa ni shirikishi zaidi. Tumezitayarisha halmashauri zetu pamoja Kamati za Ulinzi za Wilaya na za Mikoa, ili zishiriki kwenye jambo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili lilikuwa likichukuliwa kama ni suala la ngazi ya Wizara peke yake, lakini safari hii tunatakata twende pamoja kama Serikali moja. Kwa hiyo ndio maana mtaanza kuona Wakuu wa Wilaya wanasaka makokolo na Wakuu wa Mikoa wanatafuta wavuvi haramu na kuwapa adhabu kwa mujibu wa sheria. Sasa tunataka Serikali kwa ujumla tulivalie njuga suala hili ili ijulikane kwamba ulinzi wa rasilimali za mazao ya samaki ni wetu sisi wote. (Makofo)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye masuala ya mifugo. Kamati walitushauri kwamba jitihada zaidi ziongezwe kupambana na magonjwa ya mifugo, hili ni suala ambalo pia ni endelevu, sisi tunaendelea kama Wizara. Moja tunajengea uwezo kituo chetu kinachozalisha chanji cha TVI kipo pale Kibaha, tumetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.4 kwa ajili ya kuzalisha chanjo zaidi. Pia Wizara tumetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya kujenga majosho katika maeneo ya wafugaji, hasa maeneo ambayo mifugo yetu mingi ipo. Kwa hiyo, tutajenga majosho kwenye maeneo ya Waheshimiwa Wabunge ili tujaribu kupunguza namna za magonjwa zinazosababishwa na kutoogesha mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tutanunua dawa za kuogesha hiyo mifugo. Tumetenga pesa kiwango fulani na tutafanya ukarabati wa clinic zetu mahali popote zilipo, tumetenga kiasi cha pesa kwenye bajeti yetu ili kwamba tuhakikishe angalau tuna clinic za mifugo kwenye maeneo yetu kuweza kutibu mifugo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo tumesema tutalifanya ni suala linalohusiana na mambo ya ugani. Kamati ilitushauri kwamba tuweke mazingira wezeshaji ya ufanyaji kazi kwa Maafisa Mifugo ili waweze kuzungukia mashamba na mifugo. Tulisema pia kwenye bajeti yetu, kwamba kwenye bajeti hii tumetenga kiasi cha pesa tutanunua pikipiki 300, kwa ajili ya Maafisa Mifugo ili waweze kutembea na kuwafikia wafugaji popote watakapokuwa. Mbali ya kuwanunulia vifaa hivi, pia tutafanya mafunzo rejea kwa ajili ya maafisa hawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yaliyozungumzwa na ushauri uliotolewa ni mwingi. Niseme tu kwamba ushauri wote na hoja zilizotolewa tumezichukua tutazijibu kwa maandishi, ziko nyingi; kuna bajeti ya mifugo na uvuvi ni ndogo tumechukua, naomba tu watupe nafasi kwa bajeti hii tuliopewa waone tunafanya nini kwa mwaka ujao na si sasa hawatakuwa na sababu za kumdai Mheshimiwa Rais kutoongezea bajeti baada ya kufanya kazi ambazo tumepangiwa mwaka huu watakapotupitishia bajeti yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kusafirisha na kuuza mazao ya mifugo na samaki bado kweli ni kidogo tunakubali na tunataka tuongeze sasa uzalishaji kwenye sekta hizi zote mbili. Utagundua kwamba kazi zote tulizozitenga kuzifanya zinalenga kuogeza tija na uzalishaji kwenye masuala haya mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ulinzi na usalama kwa wavuvi na wafugaji. Suala hili linaihusu Serikali nzima na tutashirikiana na Kamati za Ulinzi za Wilaya na za Mikoa ili tuhakikishe ya kwamba wavuvi wanapokuwa baharini au wanapokuwa kule ziwani, wako salama na vifaa vyao na vyombo vyao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala lingine la miundombini ya mifugo, nimetaja baadhi. Pia lipo suala la mchango wa uvuvi kwenye pato la Taifa. Nadhani hili litaelezwa kwa kirefu sana na litaongelewa vizuri zaidi naMheshimiwa Waziri au Naibu Waziri wa Fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu zao la mwani ambalo linastawi kwenye mwambao wa pwani kuanzia Mtwara, Lindi, Dar es Salaam, Pwani kwenda mpaka Tanga. Suala hili tumelichukua vizuri na sisi kwenye bajeti ijayo tumetenga pesa mahususi kwa ajili ya zao la mwani kuhusiana na uzalishaji wake, soko lake na kuhusiana hasa akinamama wanaozalisha suala hili tuwatafutie vifaa vinavyoweza kuvuna zao hili kwa wingi. Kwa hiyo suala hili pia tumeliwekea maanani sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kuna suala la Ranchi za Taifa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushUkuru sana na naunga mkono hoja.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa nakupa dakika moja, malizia Ranchi za Taifa.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Ranchi za Taifa, tumelichukua na najua Waheshimiwa Wabunge hapo walishauri sana juu suala hili, lakini hata kwenye hoja hii limezungumzwa sana, tumelichukua na tunafanya tathmini, wategemee transformation kubwa kwenye Ranchi zetu za Taifa. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze pia kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri Profesa Ndalichako na Naibu Waziri mama Engineer Stella, lakini pia nimpe pole kufiwa na mama yake, Mungu aendelee kumtia nguvu katika wakati huu mgumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye kujadili hotuba ya Mheshimiwa Waziri na nianze na eneo la ada elekezi. Nilikuwa najiuliza kuna tatizo gani mpaka tuanze na ada elekezi? Tatizo hili linamgusa nani? Na nilikuwa najiuliza, wanaopeleka kwenye shule hizi za binafsi ni akina nani? Si Mawaziri, sio Makatibu Wakuu, sio Makamishna, sio Wabunge na watu wengine wakubwa wakubwa?
Sasa Mheshimiwa Waziri anapoileta hapa au tunapoiona, mimi najiuliza pia je, hii sio conflict of interest? Kwa sababu wanaopeleka watoto kwenye shule hizi ambazo sasa zinatakiwa zipewe ada elekezi ni watu walio na uwezo mkubwa kifedha. Na kama tutakubali ada elekezi kwa shule hizi za binafsi maana yake tunatafuta unafuu wa wakubwa na kama watapata unafuu hawa wakubwa kwenye shule hizi za binafsi basi tusahau shule zetu za Serikali kuboreshwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za Serikali ni nyingi kuliko shule za binafsi. Kama zingekuwa ni bora zingeweza kuchukua watoto wote wanaofaulu kwenda sekondari, kidato cha kwanza mpaka cha nne, kidato cha tano mpaka cha sita na hizi shule za binafsi zingekosa wateja. Lakini sasa kwa nini shule hizi za binafsi zinachukua watoto wetu? Ni kwa sababu shule zetu za Serikali tunazitelekeza, miundombinu yake mibovu, walimu wachache, ndiyo hawa hatuwalipi vizuri, ndiyo hawa ambao Wabunge wanalalamika hapa hawapandishwi madaraja na ndiyo hawa ambao wakitaka pesa ya nauli kwenda likizo hapewi. Lakini kwenye shule hizi hayo yote wanapewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini huyu mwalimu asifundishe vizuri? Kwa nini huyu anayemiliki shule binafsi anapolipa pesa hii asitengeneze miundombinu mizuri ya madarasa? Nyumba za walimu na mambo mengine? Kwa hiyo. Mheshimiwa Waziri mimi ningekuomba tu ungekuja na mkakati mahsusi kwa ajili ya kuboresha shule zetu za Serikali, tunazo kuanzia ngazi ya kata, kata zote zina sekondari, vijiji vyote vina shule za msingi. Sasa hizi zinatakiwa ziboreshwe. Tuwe na walimu ambao wako motivated, tuwe na madarasa yanayotosha, tuwe na vitabu vinavyotosha, mazingira kwa ujumla kwenye shule zetu yawe bora. Hizi shule za binafsi watapunguza wenyewe ada zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu kama shule za Serikali zimekuwa nzuri, zinatoa kile wanachotaka wazazi naniatapeleka mtoto wake shule ya binafsi akalipe laki tano, akalipe milioni au ngapi? Sasa nimesikia kwenye majibu ya Mheshimiwa Waziri alipokuwa anaulizwa swali wakati mmoja kwenye Bunge hili, akasema; tunatafuata namna ya kuzitofautisha hizi ada kulingana na shule hizi za binafsi. Sasa nikawa najiuliza pia tunataka kurudi kule kwenye matabaka ambayo Mwalimu Nyerere aliyakataa? Kuna shule za wenye hela, shule za wasio na hela, shule za weusi, shule za weupe. Mimi nafikiri itatuletea matatizo. Suala la ada elekezi tungeliacha, kwa walioamua kuanzisha hizo shule waziendeshe kwa gharama hizo watakazoweza, kama wanashindwa wazifunge.
Niende kwenye suala lingine la pili. Elimu ya msingi bure. Naipongeza Serikali yangu kwa mkakati wake wa elimu bure. Elimu bure imesaidia kuchukua watoto waliokuwa wanafichwa kwa sababu ya michango mbalimbali na ada mbalimbali zilizokuwepo kwenye shule za msingi na shule za sekondari na matokeo yake kwenye shule za msingi uandikishaji umeongezeka. Sisi kwenye Mkoa wetu wa Simiyu uandikishaji ni 123%; kwenye Wilaya yangu ya Maswa asilimia 130 na kitu. Watoto wengi wameandikishwa na hivyo tunaamini watoto wengi watapata elimu kuanzia ya msingi na hata ya sekondari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sasa kutokana na kuongezeka huku kuna tatizo la miundombinu kwenye shule zetu za msingi na shule zetu za sekondari. Hatuna madarasa ya kutosha, hatuna nyumba za walimu za kutosha, hatuna vyoo vya kutosha. Aidha, kwenye shule za sekondari maabara zetu hazijakamilika na mahali pengine bado yameanzishwa tu maboma yakaishia hapo na Serikali ilipoanzisha tena mchango wa madawati ndio basi kabisa habari ya maabara imesahauliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa ninamsihi Mheshimiwa Waziri kwamba hebu tujaribu kuja na mkakati unaoeleweka kuhusiana na mapungufu haya.
Waheshimiwa Wabunge, wengi wameelezea habari ya mapungufu haya kwa hiyo, hiki ni kielelezo kwamba, kila mahali kuna tatizo kubwa la upungufu wa madarasa, nyumba za walimu, ofisi za walimu, vyoo; upungufu huu ni mkubwa. Tunajitahidi na Halmashauri zetu, lakini ni vizuri Wizara hii kwa sababu, ndio Wizara mama na ndio yenye kuelekeza ubora wa elimu kwenye nchi yetu waje na mkakati ni kwa namna gani tunatatua tatizo hili kwa sababu, tumekazana na habari ya madawati, lakini najiuliza madawati haya yanawekwa wapi? Juani kwenye mti? Kwa sababu madarasa hayapo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule yangu moja ina darasa la kwanza mpaka la saba ina madarasa matatu tu, shule ya Zawa! Lakini tunapeleka madawati pale ambayo tumechangishana kule. Najiuliza tunaenda kuyaweka wapi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, walimu wetu ambao pia wana madai chungu nzima kama walivyosema wenzangu hawana nyumba za walimu na hasa kwenye Jimbo langu shida ni kubwa sasa matokeo yake napata allocation ya walimu anakaa miaka mitatu anaomba uhamisho ahame kwa sababu, nyumba za walimu hazipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ni vizuri Serikali ikaja na mkakati ni kwa namna gani mkakati unaoeleweka ni kwa namna gani unatatua mapungufu haya ambayo tumeyataja hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga…
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue pia nafasi hii kukushukuru kunipa nafasi ili niweze kuhitimisha hoja ambayo tumekuwa nayo toka asubuhi. Lakini nikushukuru sana kwa usimamizi wa Bunge lako hili Tukufu; lakini pia nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge ambao wamechangia hoja hii toka asubuhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge ambao wamechangia hoja hii ni 22 kwa sababu ni wengi siwezi kuwataja kwa majina; lakini hawa wamechangia kwa kuzungumza lakini pia wapo waliochangia kwa maandishi Wabunge watatu; pia nitambue mchangiaji na hotuba ya Mwenyekiti wangu wa Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji wamechangia kwa sehemu kubwa sana juu ya bajeti yetu hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu muda ni mchache nadhani nitatumia muda huu kufafanua hoja chache tu kwa sababu ya muda. Na hoja nyingi ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge tutazijibu kwa maandishi lakini nichukue nafasi hii kuwapongeza sana Wabunge ambao wamechangia kwa maandishi au kwa kuzungumza kwa sababu yote waliyoyazungumza ni masuala yaliyokuwa yanalenga kutuelekeza, kutushauri lakini kutoa mapendekezo ambayo yakifanyiwa kazi yamkini kazi yetu ya mwaka wa fedha ujao 2022/2023 ikawa kazi njema na ikaendelea kuwasaidia watanzania na ikaendelea kuleta tija kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa nchi yetu, mama Samia Suluhu Hassan kwa kutuongezea bajeti lakini pia kwa kujali sana sekta hizi za uzalishaji kwa sababu safari hii sekta za uzalishaji karibu zote zimeongezewa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, nianze sasa kujibu hoja moja moja kwa kifupi lakini kama nilivyosema tutajibu kwa maandishi kwa kueleweka vizuri na Wabunge wote ambao hoja zao wamezitoa zitajibiwa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya Mheshimiwa Mariam Ditopile kuwawezesha wavuvi wadogo, limekwisha kusemwa na Mheshimiwa Naibu Waziri, tutafanya hivyo. Tuna mpango wa kuwapa boti 320 tena zaidi lakini boti hizi zitakuwa ni special sana; zitakuwa na GPS, Fish hold, vifaa vya ubaridi, Fish finder, hizi boti zinauwezo wa kubeba tani 1.5.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri hebu rudia; boti ngapi?

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni boti 320.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Tunza umeisikia hiyo? Haya endelea bwana. (Makofi/Vicheko)

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kupitia TAFIRI tumefanya utafiti kutambua maeneo yanayofaa kwa uvuvi na program tunaikamilisha ili kutumia kitu kinaitwa lango la simu ili kuwezesha wavuvi kupata taarifa za maeneo ya uvuvi moja kwa moja kwenye simu zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mariam pia alikuwa ana hofu juu ya upungufu wa samaki kwenye viwanda vyetu. Kupungua kwa rasilimali za uvuvi katika Ziwa Viktoria, hususan samaki aina ya sangara, kunatokana na sababu mbalimbali na suala kubwa kabisa lililosababisha mojawapo ni uvuvi haramu. Sasa alitaka kujua mkakati wetu wa kudhibiti uvuvi haramu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli, kuanzia mwaka uliopita umekuwa ule wa kushirikisha wadau wote wa uvuvi. Ni kweli tumefanya kazi kubwa kupitia operations tulizozifanya, lakini kufanya operations peke yake tuligundua kwamba haitoshi, tukaona ni vizuri tushirikishe wadau wote kuanzia wavuvi wote wanaovua kwenye maziwa na kwenye bahari, lakini pia kuzishirikisha Serikali zetu za Mitaa, Halmashauri zetu pamoja na Serikali za Mikoa zihusike moja kwa moja kwenye masuala haya ya kudhibiti uvuvi haramu, kwa sababu Serikali ni moja. Haiwezi kuwa ni Serikali inayotoka Dodoma kwenda kudhibiti uvuvi haramu kule Bunda au Rorya ni mbali sana wakati kuna Serikali pia kule.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mkakati wetu ulikuwa ni huo wa kufanya zoezi hili liwe shirikishi, Serikali nzima ihusike, pia wadau wote wahusike ili tuweze kudhibiti uvuvi haramu kwenye nchi hii. Tunajua wote samaki ni rasilimali inayomsaidia kila Mtanzania. Samaki hawa wakitusaidia leo tu kesho wasitusaidie ni bahati mbaya sana maana kesho watakuwepo watoto wetu, wajukuu zetu, na wanadamu wengine watakuwepo, sasa watakuta nini kama hatushirikiani kwa pamoja kudhibiti rasilimali hizi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kutoa elimu, pia tumeendelea kufanya maboresho ya kanuni zetu ili tuweze kudhibiti sawasawa suala hili, tumeendelea pia kutoa elimu ya uvuvi endelevu kwa jamii za wavuvi.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda ambavyo vimefungwa siyo lazima sana kwamba vilifungwa kwa sababu, sangara hawapo. Vingine vimefungwa kwa sababu ya management, matatizo ya ki-management, vingine kwa sababu ya matatizo ya uendeshaji, na kadhalika. Si sawa sana kusema viwanda vimefungwa kwa sababu, sangara walikuwa kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, biashara ya dagaa kwenye Ziwa Tanganyika. Mheshimiwa Naibu Waziri ameieleza vizuri sina sababu ya kuirudia, lakini nieleze labda kuhusiana na kuongeza thamani ya dagaa na kupunguza upotevu wa mazao ya dagaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika Ziwa Viktoria, Serikali kupitia mradi au kupitia pesa za mkopo wa masharti nafuu ambazo tumezitangaza leo asubuhi sisi kupewa pia, tumetenga fedha kwa ajili ya kununua mitambo ya ukaushaji wa mazao ya uvuvi kwa kila Mkoa ili kuongeza thamani na kupunguza upotevu wa mazao. Kwa ukanda wa bahari Mheshimiwa Naibu Waziri ameeleza namna ambavyo mradi wetu wa IFAD bado upo, tunazo zaidi ya Bilioni Thelathini na Sita kwa ajili ya kazi hiyo kwa upande wa ukanda wa bahari wote. Kwa hiyo, tutafanya kazi hii kwa upande wa dagaa ili kusudi tuweze kupunguza upotevu wa mazao ya samaki, hususan dagaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala la leseni za Bahari Kuu kuwa ni kubwa. Suala hili lilianzishwa na Mheshimiwa Simai. Kwa mujibu wa Kanuni ya Usimamizi na Uendelezaji wa Uvuvi wa Bahari Kuu ya mwaka 2021 bei za leseni za uvuvi wa bahari kuu kwa meli za Kitanzania zilipunguzwa kati ya asilimia 70 hadi asilimia 86 ikilinganishwa na bei za leseni kwa meli za kigeni. Mfano, uvuvi wa mishipi ni Dola 8,000 tu kwa mwaka kwa wazawa, ikilinganishwa na dola 50,000 kwa wageni. Kwa hiyo, utaona zimepunguzwa kwa sehemu kubwa sana hizi bei za leseni ambazo Mheshimiwa Mbunge alikuwa akizitaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya suala la mwani imeelezwa vizuri na Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini kulikuwa na suala lililosemwa na Kamati kuhusu biashara ya mwani inakua kwa kasi na inatekelezwa na wanawake, Wizara iandae mpango wa kuwaelimisha na kuwawezesha wakulima wa mwani mbinu bora za kilimo hicho. Sasa Mamlaka ya Serikali za Mitaa kwa mwaka wa 2021/2022 tumetoa mafunzo ya uzalishaji na uhifadhi wa zao la mwani kwa wakulima 4,569 katika Mikoa ya Tanga, Lindi na Mtwara, pia Wizara tumewezesha wakulima wa mwani katika Mikoa ya Tanga na Lindi kwa kuwapatia kamba zenye thamani ya shilingi milioni 20. Mwaka wa 2022/2023 Wizara tutaendelea kuhamasisha na kuwawezesha wakulima 2,000 ili waweze kutumia teknolojia bora za uzalishaji na uongezaji thamani wa zao la mwani katika Mikoa ya pwani. Vilevile kujenga vichanja 10 vya kukaushia mwani katika Halmashauri za Wilaya za Mtwara, Lindi, Lindi DC, Lindi MC, Kilwa, Mkuranga, Mafia, Bagamoyo, Pangani, Tanga, Mkinga na kadhalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu muda wangu unakimbia sana niende nigusie pia masuala machache yanayohusiana na mifugo. Kulikuwa na suala la udhibiti wa magonjwa ya mifugo ambalo Mheshimiwa Kenneth Nollo alilisema. Kwa mwaka wa 2021/2022 Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, sekta ya mifugo tumejenga majosho 192, na ninadhani kwenye taarifa yetu yapo, kwa gharama ya Shilingi 3,458,000,000 katika Halmashauri 45 kwenye Vijiji vyenye mifugo mingi zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa 2022/2023 Wizara tutajenga tena majosho mengine 406 yenye thamani ya shilingi 7,304,441,000 yakiwemo majosho 128 kwa gharama ya shilingi 2,304,441,000 kwa fedha za ndani na majosho 278 kwa kiasi cha shilingi 5,000,000,000 fedha za nje, majosho haya yatajengwa katika maeneo ya malisho kwa lengo la kupunguza magonjwa yaenezwayo na kupe. Kwa hiyo, kazi hii tunaendelea kuifanya na kwa mwaka huu unaokuja tutaifanya kwa sehemu kubwa sana. Waheshimiwa Wabunge kila mmoja angehitaji majosho mahali ambapo kuna ng’ombe kwenye Jimbo lake, nadhani safari hii tutajitahidi angalao kila Mbunge kupata josho moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala la ufugaji wa punda na kufungwa kwa kiwanda cha punda kule Shinyanga. Mheshimiwa Khadija Aboud alisema Serikali ihamasishe kufanya kazi hiyo. Kwa kifupi ni kwamba, nchi nyingi duniani zimepiga marufuku biashara hii ya nyama ya punda. Zimepiga marufuku kwa sababu ya uzalianaji wa punda, punda wanazaliana kwa nadra sana. Punda anaweza kuchukua miaka mitatu ili aweze kuzaa na baada ya kuzaa hapo anaweza akachukua miaka mingine sita au zaidi ili aweze kuzaa. Kwa hiyo, punda hawaongezeki kama ng’ombe wanavyoongezeka au kama wanyama wengine wanavyozaliana. Kwa hiyo, bila kuwa na tahadhari tunapowatumia kama kitoweo basi wanaweza wakatoweka kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, punda wanatumika pia kwa shughuli nyingine za uzalishaji. Siyo nyama tu na ngozi na vitu vingine, wanatumika pia kwa njia za uzalishaji. Kulikuwa na suala lingine la ufugaji katika ranch za Taifa. Hili suala limezungumzwa sana, lakini kwa uzito sana limezungumzwa na Mheshimiwa Mwijage, Mheshimiwa Dkt. Kikoyo na Waheshimiwa wengine wamelizungumza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niseme pengine kwamba Kampuni yetu ya Ranchi za Taifa - NARCO inamiliki ranchi 14 na inazitumia. Inawezekana isiwe kwa uwezo wake uliopo, lakini nadhani ni vizuri tungeenda taratibu kwenye suala hili kwa sababu Serikali imeweka maeneo hayo kama buffer areas ili wakati Serikali itahitaji ardhi kwa jambo mahsusi ambalo linahusu maslahi ya nchi yetu inaweza wakati wowote ikaenda kwenye ranch. Sasa tukisema ranch hizi zipo tu halafu sasa tuzitumie kama tutakavyotaka, mimi naamini tunaweza kuonekana kama hatujatumia vizuri rasilimali hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ya Ranch ya Mwisa na Kagoma, Mheshimiwa Dkt. Kikoyo na Mheshimiwa Mwijage nimewasikia na hoja yenu nimeichukua, lakini pia Mheshimiwa Mwijage alihitimisha vizuri sana baada ya kusema Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara ya Mifugo, Wizara ya Ardhi, tukutane chini ya Waziri Mkuu ili tuweze kulizungumza suala hili. Nami naunga mkono hoja hiyo kwamba ni vizuri tuzungumze suala hili na mamlaka za nchi ili tuone tunalimalizaje, kwa sababu tukiendelea kuzungumza NARCO pamoja na Waheshimiwa Wabunge wawakilishi wa wananchi, tunaweza tusifikie muafaka ambao utakuwa mzuri sana kwa sababu ninaposikia Mheshimiwa Dkt. Kikoyo anasema hata Ranch ya Mwisa na Kagoma hazipo kwa mujibu wa sheria, basi nadhani linakuwa suala zito kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nadhani tutakutana ili tuweze kuzungumza, nami naamini tutafikia muafaka sawasawa, tutafikia muafaka mzuri ili kwamba rasilimali hizi ranch, pia wananchi wetu na wenyewe wakae kwa amani, wakae kwa starehe kwenye hayo maeneo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja ya Kamati ya Bunge kutokana na umuhimu wa vitalu katika kuzalisha mifugo bora zoezi la kupanga vitalu lizingatie manufaa ya kufuga kisasa badala ya kuchunga. Tunauchukua ushauri huo na mimi wakati wote nimekuwa nikikutana na wafugaji na kuwaeleza kwamba, ndugu zangu lazima tuanze sasa kufikiria kufuga badala ya kuchunga. Kwa sababu, tumechunga miaka yote hii, lakini tija bado haijaonekana kwetu wafugaji wenyewe, pia hata kwa Taifa lenyewe. Sasa tunayo haja ya kufanya mabadiliko, kuna haja ya kuboresha ili tuingie kwenye kufuga mifugo. Wafugaji wetu siyo wagumu sana ndiyo maana kwenye hotuba yangu, kama mmesoma vizuri, hii mliyokuwa mnanisikiliza hapa ni summary lakini hotuba ndefu ilikuwa kwenye vishkwambi vyetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama mmenisoma vizuri nimesema kwa mwaka huu wa fedha 2022/2023 nitaanza kampeni kwa kukutana na wafugaji, hawa ambao tunawaita ni wachungaji, tuelimishane juu ya kufuga kwa tija, tuelimishane juu ya kufuga kibiashara, tuelimishane ni kwa namna gani tunaweza kutumia rasilimali hizi za mifugo zikanufaisha familia na zikanufaisha Taifa letu. Kwa hiyo, tutafanya kampeni kubwa, pia zaidi ya kampeni tutatumia viongozi walioko ngazi kuanzia ya Kijiji mpaka ngazi ya Mkoa ili tuweze kuelewana, mbali na hivyo tutaendelea pia kutenga maeneo ili kwamba, tuwe sasa na maeneo maalum ya kufugia mifugo yetu ikiwa ni pamoja na wafugaji wenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu suala hili linataka kuachwa kwa Serikali kana kwamba, Serikali ina ardhi kibao imelala mahali, sasa ikipungua itaenda ichukue impe mtu aende aweze kufuga, Hapana! Wafugaji pia tuna ardhi na maeneo ambayo mifugo yetu ipo, maeneo hayo tunaweza kuanza kuyaboresha, tukiondoka hapo ndiyo tuende kwenye maeneo ya wazi. Na maeneo haya ya wazi pia yako chini ya Halmashauri. Tumezungumza na Halmashauri nao wayaboreshe, siyo kuyaacha kama yalivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ziko Halmashauri nyingi ambazo zimetenga maeneo kwa ajili ya malisho, lakini bado maeneo hayo hayajaboreshwa, hayana miundombinu stahiki inayotakiwa, majosho, maji, na kadhalika. Sasa tuchukue hatua sisi wote wadau kwenye suala hili la mifugo, kuanzia wafugaji wenyewe. Ndiyo maana tunasema lazima tuanze sasa utaratibu wa kupanda malisho, suala la malisho haliepukiki kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi, lakini kutokana na tunavyoongezeka Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, binadamu tunapoongezeka shughuli zetu za kiuchumi zinaongezeka pia. Sasa zinapoongezeka lazima ardhi itapungua ile ambayo utachunga huria, sasa lazima tuanze kufikiria kuwa na mashamba ya malisho yanayomilikiwa na wafugaji wenyewe. Ndiyo maana kwenye mashamba yale 100 ambayo tutayaanzisha ambayo tumeita ni mashamba darasa, haya mashamba tutayakabidhi kwa mfugaji mmoja-mmoja na baadaye tutatathmini ni mfugaji yupi anaelekea kwenye kufuga kiuendelevu. Badala ya kuyaweka kwenye taasisi za Serikali tutawapa wafugaji na hawa wafugaji ndiko wafugaji wengine watakwenda kujifunza namna ya kulima na kutunza hayo mashamba ya malisho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, masuala ni mengi, huduma za ugani, Mheshimiwa Nollo pia anasema Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo ni vya zamani. Nakubaliana na wazo hilo ni kweli…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa bado una dakika mbili.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ooh, nakushukuru sana. Ahsante sana kwa kunipa muda, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2023
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia taarifa za Kamati zetu hizi mbili, Kamati ya TAMISEMI pamoja na Kamati ya Utawala Katiba na Sheria. Niende moja kwa moja kwenye kuchangia kwa sababu muda wetu ni mdogo, nitachangia mambo mawili, kwanza ni Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na la pili nitachangia linalogusa pia TAMISEMI juu ya kugawa maeneo ya utawala wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuipongeza Serikali kwa kuifanya sasa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ifanye kazi pande zote za Muungano (Tanzania Bara na Zanzibar), kwa mujibu wa marekebisho ya Sheria yake Namba 8 ya Mwaka 2006 inaifanya sasa Tume hii iweze kufanya kazi maeneo yote mawili ya Muungano au ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tume hii ya Haki za Binadamu iko Kikatiba na kwenye Katiba ukurasa wa 108 na 109 majukumu ya Tume hii yametajwa yako mengi na mimi niyataje machache. Moja, ni kufanya shughuli za kupokea malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu. Jingine ni kufanya uchunguzi juu ya mambo yanayohusu uvunjaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora. Jingine ni kama ikibidi kufungua mashauri Mahakamani ili kuzuia vitendo vya uvunjaji wa haki za binadamu na jingine ni kuchunguza mienedo ya mtu yeyote anaehusika au taasisi yeyote inayohusika na masharti ya Ibara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu haya ukiyaangalia ni majukumu makubwa, majukumu mazito na ni majukumu yenye upana wake. Ukiangalia nchi yetu kwa kuiangalia Tanzania Bara na Zanzibar nayo ni kubwa sana. Sasa kwa majukumu haya ambayo Tume hii imepewa napata shida kuona utendaji kazi wao kama unaridhisha ili wananchi waweze kufikiwa na Tume hii ya Haki za Binadamu. Kusema ukweli ufikiaji au utendaji kazi wa Tume hii hauwapati wanachi wetu kwa ujumla wake. Moja, ni kwa sababu Tume hii ina Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti na Makamishna na Wasaidizi wa Makamishna halafu wako Dodoma Makao Makuu ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa watumishi kwanza ni wachache lakini pia hawapo kwenye Mikoa na Wilaya zetu. Sasa kama wako Dodoma haya malalamiko yaliyosemwa kwenye majukumu yao wanayapata kwa njia ipi. Kama wanayapata wanawezaje kuwafikia hao wanaolalamika kuzingatia uchache walionao na vifaa wanavyovitumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa kweli nataka kuishauri Serikali kwamba kama tumekubali kuwa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora basi Tume hii iwezeshwe kwa namna ya watumishi tuwe na watumishi mpaka kwenye Mikoa au Wilaya ili wananchi wetu wanapopatwa na madhila yanayohusiana na kuvunja kwa haki za binadamu wawe na mahali ambapo wanaweza kupeleka pa karibu zaidi, kuliko mwananchi kutokea Wilayani kwangu kule Maswa alete hoja yake hapa Dodoma, sasa nashindwa kuelewa itatatuliwa saa ngapi, malalamiko hayo yatatuliwa saa ngapi, shida hizo zitatatuliwa saa ngapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani assumption iliyokuwepo tulipokuwa tunaweka Tume hii ni kwamba Tume hii labda inahusika na viongozi tu lakini kuvunjwa kwa haki za binadamu hakufanywi na viongozi peke yao hata raia wanavunja haki za binadamu. Pia mambo mengine yanatokea kule kwenye maeneo yetu ambako hakuwezi kuonekana kwa urahisi. Kama Tume hii ingejulikana ipo na inafanya kazi kushughulikia matatizo haya, malalamiko hasa ya uvunjaji wa haki za binadamu, Tume hii ingeweza kupunguza sana kitu ambacho mwenzangu aliyenitangulia amesema malalamiko ya wananchi ambayo viongozi wetu wanakutana nayo wanapokuwa wanafanya mikutano yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali kwamba Tume hii kwanza iongezewe watumishi, Watumishi wake wasifanye kazi kutokea Dodoma peke yake waende Mikoani na Wilayani, pia waongezewe rasilimali fedha. Rasilimali fedha kama haijaongezwa hawawezi kufika huko kwenye maeneo yetu. Jambo la tatu miundombinu kama majengo na vifaa vya TEHAMA viweze kupatikana kwa Tume hii ili waweze kufanya kazi yao vizuri na kuwahudumia wananchi wetu vinginevyo kwa rasilimali chache na kwa uchache wa watumishi waliopo hii Tume itabakia kwenye Katiba na itabakia kwenye maandishi yetu lakini utendaji kazi wao hatuwezi kuuona kama wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende suala la pili la kugawa maeneo ya utawala wa nchi yetu. Naelewa kwa sababu suala hili limekuwa likizungumzwa hapa na Waheshimiwa Wabunge kwa njia ya maswali ya nyongeza na Serikali imekuwa ikijibu hapa kwamba pengine upatikanaji wa fedha utakapokuwepo suala linaweza likatazamwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ni kubwa. Nchi yetu sisi ni kubwa kiasi kwamba unaweza ukajumlisha nchi nne za Afrika Mashariki Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi, bado hujapata eneo la ukubwa wa nchi yetu. Sasa nchi yetu kwa sababu ni kubwa mimi sihesabu kama ni balaa kwa nchi yetu kuwa kubwa, tuhesabu kama ni fursa! Siyo kosa kosa nchi yetu kuwa kubwa. Inavyoelekea ni kwamba tunaona sasa kama ni tatizo, mimi sioni kama ni tatizo, ni fursa na tukijielekeza vizuri bado tunaweza kufanya nchi yetu ikatawalika vizuri na suala la utawala bora na lenyewe likaenda sawa sawa lakini kwa kugawa maeneo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kugawa maeneo ya nchi yetu, wilaya kubwa kama Kilosa ambayo ni zaidi ya Mkoa wa Kilimanjaro, wilaya kubwa kama ya Maswa yenye square kilometers zaidi ya 3,000, ni kubwa; sasa maeneo kama haya kuyahudumia kwa watu walioko kule ni shida sana. Ni tabu sana kwa Mkuu wangu wa Wilaya, Mkurugenzi na watumishi wengine waliopelekwa na Serikali kule kuhudumia eneo kubwa lililo pana namna hii, haya maeneo yagawiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunashindwa kuyagawa, basi kwa neno lile la Tawala za Mkoa, kwa kuwa na mkoa au kuwa na wilaya ili tuwe na DC, basi tugawe kwa upande huu wa pili, Serikali za Mitaa. Tugawe ziwe halmashauri mbili na maeneo ya vijiji yale makubwa ambayo yanafanana na kata na yenyewe yagawiwe angalau tuwe na halmashauri mbili kwenye eneo la halmashauri moja ambayo ni kubwa na vijiji au kata. Kwa sababu utakuta kata nyingine ni sawa na tarafa kabisa, lakini imeachwa kuwa kata moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tugawe halmashauri, tugawe kata na vijiji. Haya maeneo yakigawiwa, ndiyo maeneo muhimu kwa wananchi wetu kufikishiwa huduma kule kwa ukaribu sana. Tunaweza kufikiria kugawa kuwa na Mkuu wa Mkoa na kuwa na Mkuu wa Wilaya baadaye lakini kuwa na Mkurugenzi na kuwa na Mtendaji wa Kata, kuwa na Mtendaji wa Kijiji ni suala ambalo tunaweza kulifikiria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza kufanya hata kwa awamu kuliko tukiacha maeneo kama yalivyo. Maeneo mengine hayafikiwi kabisa na huduma za Umma, hayafikiwi kabisa na watumishi wa Serikali kwa sababu ya ukubwa wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine tumekuwa tukilalamika hapa kwamba rasilimali fedha zinazoenda kule labda hazisimamiwi vizuri, lakini tatizo mojawapo ni ukubwa wa haya maeneo. Tunapeleka miradi mingi. Kwa mfano, mradi uliopelekwa kijiji changu kimoja kinaitwa Mwandu, kilomita 120 kutoka Makao Makuu ya Wilaya, sasa huyu DC na Mkurugenzi, Afisa Elimu, Afisa Kilimo atafika saa ngapi kule na kusimamia kazi ya mradi au pesa zilizopelekwa kule ukizingatia pia vifaa kama magari na pikipiki na vyenyewe bado ni pungufu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa haya maeneo tukiyagawa itakuwa ni karibu kuyahudumia, mtu anaweza kwenda hata kwa pikipiki bila matatizo yoyote. Mtu anaweza akaenda hata kwa pick-up bila shida yoyote, mgongo usimuume kwa sababu mwendo atakaoenda ni mfupi. Kama maeneo yatabaki makubwa namna hii, bado watumishi wataendelea kupata shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzuri wa kuyagawa haya maeneo, itarahisisha usimamizi wa shughuli na miradi ya Serikali.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mashimba Ndaki, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Jumanne Sagini.

TAARIFA

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naelewa fikra alizonazo Mheshimiwa Ndaki ya kupendekeza kuyagawa haya maeneo zaidi, lakini naomba kumpa taarifa zaidi kwamba mpaka mwaka 2012 Mkoa wa Shinyanga ulikuwa unaibeba Mkoa karibu wote wa Simiyu. Serikali kwa kutambua hayo, iliweza kuugawa Mkoa wa Shinyanga na baadhi ya Wilaya za Shinyanga zilizokuwa tatu zikagawanyika tukapata halmashauri sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri atambue kwamba juhudi zimekuwa zikifanyika, lakini haitakuwa na tija sana iwapo utagawa bado ukashindwa kuweka miundombinu stahiki kuiwezesha Serikali kutimiza wajibu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kumpa hiyo taarifa.

MWENYEKITI: Ahsante; Mheshimiwa Ndaki taarifa hiyo unaipokea?

MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa sehemu; natambua Mkoa wangu wa Simiyu ulimegwa kutoka Mkoa wa Shinyanga mwaka 2012, lakini hiyo haizuii kugawa wilaya kubwa kuwa halmashauri mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwa na wilaya kubwa kama ya Maswa, anaifahamu Mheshimiwa Sagini, kubwa, lakini ni halmashauri moja. Huyu Mkurugenzi atatoka damu kifuani kufuatilia miradi kwenye kata zake 36 na vijiji karibu 140 kwenye wilaya hiyo. Tutampa shida bure. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba hapa ni kwamba, sawa Serikali imefanya juhudi kubwa, lakini bado tunahitaji kuyagawa haya maeneo hata kama ni kwa awamu. Mwaka huu basi halmashauri hizi kubwa tuzigawe ziwe halmashauri mbili. Halmashauri tano kubwa tuzigawe, halmashauri tano nyingine mwaka unaofuata tuzigawe…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa kwa mchango wako.

MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu siku ya leo. Naanza kwa kusema naunga mkono hoja iliyoko mbele yetu, Hoja ya Wizara ya Mipango na Uwekezaji, pamoja na Hoja ya Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hasa kwenye Jimbo langu la Maswa Magharibi kwenye mradi mmoja wa maji. Mheshimiwa Rais ametupatia fedha kwenye maeneo mengi; elimu, afya, kilimo na barabara, na vitu vingi tumepewa. Pia namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kipekee kabisa kwenye mradi huu wa maji kwenye jimbo langu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Mkoa wetu wa Simiyu tuna mradi mkubwa wa kutoa maji Ziwa Victoria kwa Wilaya zote tano, lakini kwenye Wilaya ya Maswa upande mmoja ndiyo ulikuwa ule mradi wa maji unaishia. Kwa hiyo, ule upande wa pili ambao mimi niko, hatukuwa na chanzo cha maji kutoka Ziwa Victoria, lakini nachukua nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kuwa juzi juzi mkataba wa kutoa maji Ziwa Victoria kuyaleta kwenye Mji wa Malampaka na hatimaye Mji wa Malya na Vijiji vilivyo karibu umesainiwa, na mkandarasi yuko site. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa sababu, ameniondoa kwenye uyatima wa maji ya Ziwa Victoria kwenye Jimbo langu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wa Wizara hizi mbili. Hawa mimi naweza kusema tuwaite Singida Boys. Kwa kweli, wamejitahidi, wameweka juhudi kubwa kwenye mpango na kwenye bajeti yenyewe. Juhudi mliyoweka ndani yake kwa kweli matunda yake tumeyaona na ni kazi nzuri. Pia nawapongeza Manaibu wao, Mheshimiwa Chande, Naibu Waziri wa Fedha; Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, mdogo wangu, Naibu Waziri wa Nchi kwenye Wizara ya Mipango na Uwekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini mambo haya mliyoyapanga yakitekelezwa tunaweza kabisa kupiga hatua pamoja na ushauri wa Waheshimiwa Wabunge watakaotoa. Naamini kabisa sisi kama nchi tutapiga hatua ya kimaendeleo zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza na kilimo kwa sababu na mimi ni mtu wa kilimo na jimbo langu lote kazi kubwa wanayofanya wananchi wangu ni kilimo. Naanza kwanza kwa kuishukuru Serikali kwa miradi ya umwagiliaji kwenye jimbo langu; Mradi wa Umwagiliaji wa Masela, Mradi wa Umwagiliaji wa Bukangilija, naambiwa unapata fedha kwenye bajeti hii tunayoijadili. Basi namshukuru sana Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Bashe, kwa kufikiria kupata miradi ya namna hiyo kwenye Jimbo langu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa letu kwa sababu, mpaka leo Watanzania tulivyo tunapata chakula kutoka kwenye kilimo, mpaka leo tunapata malighafi za viwandani kutoka kwenye kilimo, pia tunapata fedha za kigeni kutoka kwenye kilimo, na tunapata ajira kubwa ya Watanzania kutoka kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kikubwa sana ambacho kwenye taarifa za Waheshimiwa Mawaziri tunaojadili hoja zao wametaja mchango wa sekta ya kilimo kwenye ukuaji wa pato la Taifa kuwa ni mkubwa kuliko mchango mwingine wowote. 26.5% ni mchango mkubwa sana, lakini tujaribu kuangalia sasa kibajeti sekta hii kwa upana wake kwa maana ya kilimo cha mazao na mambo mengine, lakini ukaleta mifugo pia, na uvuvi. Bajeti iliyopangwa hapa ni ndogo sana. Nimejaribu kufanya hesabu, ni kama asilimia nne tu ya bajeti ambayo tunaijadili hapa ndiyo inaenda kwenye kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Taifa nilidhani tungefikiria kukipa kilimo rasilimali fedha nyingi zaidi kuliko maeneo mengine kwa sababu mchango wake ni mkubwa. Kwa kuweka asilimia nne tuliyoweka sasa hivi na huku nyuma ilikuwa ipo chini asilimia tatu na kidogo, lakini bado mchango wake kwenye ukuaji wa Taifa ni asilimia kubwa zaidi, 26.5%. Sasa tungeongeza asilimia nne nyingine kwa mfano, nadhani mchango wa sekta hii ungekuwa ni mkubwa zaidi na hivyo sekta hii ingeweza kuchangia zaidi kwenye fedha za kigeni, kwenye ajira za Watanzania, kwenye chakula kwa ajili yetu kama Watanzania, pia kwenye viwanda kwa malighafi za viwandani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani kama Taifa tuanze kufikiria huko tunapoelekea mbele, tunafanyaje na sekta hii ambayo inatupatia maziwa mengi zaidi kwa kuipa majani kidogo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie juu ya suala la bei za mazao. Mwenzangu Mheshimiwa Kapinga aliyemaliza kusema kabla yangu anashukuru kwa ajili ya bei za mazao anayolima kwenye eneo lake, lakini mimi bei ya zao la pamba kwenye eneo langu bado ni kidogo. Kusema kweli bei za mazao yetu ya kilimo tunabahatisha, kwa sababu tunategemea soko lile la nje. Sasa soko likiwa zuri bei zinapanda, soko likiwa chini, basi bei zinaanguka. Sasa ndivyo ilivyofanyika kwa zao la pamba. Mwaka huu bei ni shilingi 1,060 imepandapanda kidogo nimeambiwa ni shilingi 1,200 mpaka 1,300 sasa hivi kwa sababu ya ushindani bei, lakini bado ipo chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa tunaloambiwa ni kwamba kwa sababu tunauza mazao yetu nje, tunategemea soko la nje. Sasa hii ni sababu kongwe mno kwa Taifa letu. Toka zamani tunaambiwa ni kwa sababu ya kuanguka kwa bei ya soko la dunia, basi mazao yetu pia yanaanguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sasa Serikali ikaja na mpango wa namna ya kuwazawadia wakulima wa nchi hii ambao wanatusaidia katika mambo mengi. Kuna haja ya kuja na Mfuko wa Kilimo ambao ndani yake tutakuwa na Mfuko wa Fidia ya Bei za Mazao za Wakulima wa nchi hii. Kwa sababu tusipofanya hivyo, tutaendelea kuishi na soko la dunia. Sasa ili tuishi nalo vizuri, sisi kama nchi tufikirie namna ambavyo tunaweza kuwazawadia wakulima wetu kuliko kuiachia dunia ifikirie namna ya kuwazawadia wakati ndio hao wanatulisha, wanatupatia ajira na wanatupatia fedha za kigeni. Kwa mfano, tuna Mfuko wa Reli, REA, Maji, tumeshindwaje kuwa na Mfuko wa Sekta ya Kilimo? Mimi nadhani inawezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nitoke hapo kwenye kilimo niende kwenye suala la pili. Sekta isiyo rasmi katika nchi yetu sijaona imetajwa sana kwenye mpango, na hata kwenye bajeti. Sekta isiyo rasmi kwenye nchi yetu kwa mujibu wa utafiti wa Timu yetu ya Takwimu ya Taifa inachukua 46% ya shughuli zinazofanywa na Watanzania. Sasa hii ni kubwa mno na kwa Mkoa wa Dar es Salaam 58% ya kaya zilizopo Dar es Salaam zinajihusisha na sekta isiyo rasmi. Nini maana yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba, hii sekta isiyo rasmi haijasajiliwa, hatujaitambua sana na pengine shughuli zake zinaweza kuwa zina mtaji mkubwa. Kwa mfano, utafiti uliofanyika Dar es Salaam mwaka 2019 unaonesha kwamba, mtaji uliowekezwa kwenye sekta isiyo rasmi kwa Dar es Salaam ni shilingi bilioni 901.7. Hizo ni pesa nyingi. Hii ni fedha ya kutosha kabisa. Sasa bado tunapokuwa na sekta isiyo rasmi kubwa namna hii, siyo afya kwa uchumi wetu na kwa mapato ya Taifa letu kwa sababu kuna mapato ambayo hatuyapati kutoka kwenye mtaji mkubwa wa namna hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nafikiri Serikali ije na sera zinazovutia sekta isiyo rasmi, iwe rasmi. Serikali ije na sheria na taratibu zilizo rahisi za usajili wa biashara hasa mpya ili kwamba sekta hii isiyo rasmi ambayo inahusisha gereji, bodaboda na vitu vingi mbalimbali ambavyo tunaona kama vina faida ndogo, lakini ni kubwa vikijumuishwa kwa pamoja. Sekta hii isiyo rasmi iwe rasmi na iweze kuchangia mapato ya Taifa letu kama ambavyo sisi wote tunatamani tuwe na kipato kikubwa kama Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mikakati ya kimsaada kwa ajili ya mafunzo na mikopo kwenye sekta hii. Mikakati mingine ni pamoja na motisha za kikodi. Motisha za kikodi zinaweza zikafanya hawa watu wanaokimbia kuwa rasmi wakaja wakawa rasmi. Sasa tofauti na ilivyo sasa hivi, mtu akionekana tu kidogo ana biashara yake ndogo tayari halmashauri na TRA wanaenda pale. Sasa tuje na motisha za kikodi ambazo zitasababisha hawa watu wapende kuwa rasmi badala ya hali walionayo ya kutokuwa rasmi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala lingine la tatu juu ya ajira. Ajira bado ni tatizo kwenye nchi yetu. Watoto wetu wengi wanaomaliza vyuo hawajaajiriwa na kwa hili kila mmoja hapa ni mwathirika kama familia na pia kama Taifa. Takwimu nilizonazo zinaonesha ajira za kudumu zimeajiri Watanzania 18% tu, ajira za muda wa kati zimeajiri Watanzania 10%, pia ajira za muda mfupi zimeajiri Watanzania wengi zaidi kama 72%. Sasa hizi ajira za muda mfupi ni ajira ambazo hazina uhakika kwa sababu ni miezi mitatu, sita au mwaka mmoja.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ni juu yetu kuhakikisha sekta zile zinazoajiri watu wengi zinapata rasilimali fedha ya kutosha ili ziweze kutengeneza ajira ya kutosha kwa ajili ya watu wetu. Naona Mwenyekiti umewasha microphone yako. Vinginevyo tutazungumza habari ya ajira, lakini kama tusipokuja na mkakati ambao ni sahihi kwa ajili ya kutibu tatizo la ajira, bado tutaendelea kulia na hili tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ahsante sana kwa kunipa nafasi, nakushukuru sana na nirudie tena kusema naunga mkono hoja iliyopo mbele yetu. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia Wizara hii ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nichukue nafasi hii kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kufanya na kwa presentation nzuri waliyofanya asubuhi ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie mambo mawili au matatu kama muda utatosha. La kwanza, ni majengo ya zahanati na vituo vya afya. Ilani ya Chama cha Mapinduzi imesema tunajenga Zahanati kila Kijiji na tunajenga Vituo vya Afya kwenye kila Kata. Maana yake, haya ni majengo ili huduma za afya ziweze kutolewa kwenye majengo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa najaribu kuangalia hotuba ya Mheshimiwa Waziri sikuona kiuwazi sana mpango mahsusi juu ya jambo hili la Vituo vya Afya kwenye Kata na Zahanati kwenye Vijiji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma pia hotuba ya Waziri wa TAMISEMI, lakini na kwenyewe sikuona kwa uwazi sana. Jambo hili linazungumzwa vizuri na mkakati mahsusi umewekwa ili kuhakikisha kweli tuna zahanati kwenye kila kijiji na tuna vituo vya afya kwenye kila kata. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma hizi za afya zinatolewa kwenye majengo yenye viwango maalum; siyo kila jengo tu linaweza kuwa zahanati au kituo cha afya. Sasa kama hatujazungumza kwa uwazi hapa; na kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi jambo hili tulilizungumza sana kwa wapiga kura wetu na wengine tumehamasisha, wameanzisha maboma na mengine yamekwisha, yaliyofikia kwenye lenta, yapo mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najiuliza, nikirudi naenda kuwaambia nini wananchi wangu sasa ambao tayari wana maboma yamekwisha, bado kuezekwa? Yapo maboma mengi kwenye Jimbo langu la Maswa Magharibi yamekwisha bado kuezekwa tu, lakini kwenye mpango wa Mheshimiwa Waziri wa Afya na hata kwenye mpango wa Waziri wa TAMISEMI sijaona. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwamba wakati Mheshimiwa Waziri anakuja kuhitimisha, atuambie angalau mpango mkakati ni upi kuhusu zahanati kwa kila Kijiji na kituo cha afya kwa kila kata, vinginevyo, watu wetu tutawakatisha tamaa. Nina maboma mengi kwenye Jimbo langu na nilichokuwa nawaambia wapiga kura wangu ni kwamba Serikali watatusaidia kuyamaliza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, liko boma kwenye Kijiji cha Bukangilija, liko boma Kijiji cha Nyabubinza, liko boma Kijiji cha Mwanubi, liko boma Kijiji cha Mwang‟anda; yako maboma mengi! Sasa kama hayapo kwenye mpango huu, kwa kweli nasikia baridi kwamba nitakapokutana na watu wangu itakuwaje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa akijumuisha hotuba yake, basi atuambie mpango mahsusi hasa kwa ajili ya kila kijiji kuwa na zahanati yake, kila kata kuwa na kituo cha afya, ni upi hasa ili tuweze na sisi kuwa na matumaini kwa wapiga kura wetu pia? Kwa hiyo, hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, ni suala la ubora wa huduma za afya kwenye maeneo yetu. Nashukuru kwamba wamefanya uhakiki Wizara, kwenye hotuba ya Waziri ameelezea; wamefanya uhakiki na kutathmini na walikuwa wanavipa vituo vya afya au zahanati, zile zinazotoa huduma za afya alama za nyota ya kwanza mpaka ya tano. Sasa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukijaribu kuangalia, vituo hivi vinavyotoa huduma ya afya karibu asilimia 87 vilipata nyota kati ya sifuri (0) na moja (1).
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kuonesha kwamba huduma zinazotolewa kwenye vituo vya afya na kwenye zahanati bado ni duni sana. Ukweli tunaufahamu kwa sababu tunatoka kwenye maeneo hayo. Sasa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri sikuona pia mpango mkakati ni upi kuhakikisha kwamba hizi huduma zinakuwa bora kwenye hivyo vituo ambavyo wao wamevihakiki. Sijaona mpango mkakati ni upi ili kufanya huduma hizi ziwe bora kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake, huduma zinazopatikana kwenye zahanati au vituo vya afya, maana maeneo haya ndiyo yanayotoa huduma za msingi za afya kwenye maeneo yetu, siyo nzuri. Nina Kituo changu cha Afya cha Mwasai kinahudumia Kata tatu; Kata ya Masela, Kata ya Seng‟wa na Kata ya Isanga. Kituo hiki cha Afya kina Nurse mmoja na Clinical Officer mmoja; watu wawili ndio wanaofanya kazi pale, vifaa tiba pale havitoshelezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipata mfadhili kwenye hicho Kituo cha Afya akatuletea vifaa vya upasuaji, viko kwenye container mpaka leo. Tukiuliza kwa nini havifanyiwi kazi, wataalam wanatuambia hakuna Daktari pale. Hii inaonekana kwamba watumishi kwenye zahanati na kwenye vituo vya afya ni pungufu sana. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri watutazame kwa jicho la pekee wa maeneo hasa ya vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu nina vituo vya afya viwili; Kituo kingine kinaitwa Malampaka na chenyewe ni hivyo hivyo, kina container la upasuaji lakini limekaa tu, halifanyiwi kazi, vifaa vipo vimekaa tu. Tatizo ni kwamba hakuna mtaalam. Pia pale kuna tatizo la ziada kwamba hakuna jengo la upasuaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu Serikali wakiwa wazi na kutuambia tunatatuaje haya matatizo ili huduma za afya kwenye maeneo yetu ziwe angalau bora? Waheshimiwa Wabunge wengi wamesema, maeneo mengi yanayoonekana ni mazuri ni kuanzia kwenye wilaya, mkoa na kuendelea juu, lakini ukishuka chini huduma za afya siyo nzuri sana. Kwa hiyo, tunaomba Serikali itoe kipaumbele kwenye maeneo haya ili watu wetu pia ambao ndio wengi wapate huduma zinazotosheleza kwa ajili ya afya zao ili waweze kufanya na kujitafutia maendeleo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, ni huduma za ugonjwa wa saratani. Saratani imekuwa tatizo kwenye nchi yetu sasa hivi. Nilikuwa najaribu kuangalia takwimu sikuzipata vizuri, lakini inavyoelekea tatizo la saratani linaongezeka, maana watu wanaotoka kwenye maeneo yetu ni wengi; wanapochunguzwa wanakutwa na saratani, lakini huduma za matibabu au huduma za kupunguza ukali wa tatizo hili zipo tu Ocean Road, Dar es Salaam. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Serikali ifikirie ni kwa namna gani inaweza ikawa na huduma za matibabu kwenye Kanda au Mikoa ili kutuletea huduma hii ya matibabu kwa ugonjwa huu karibu na wananchi wetu? Vinginevyo ni ghali mtu wa kutoka kule Kijiji changu cha mwisho Jija atafute usafiri aende Maswa Shinyanga, baadaye apande basi mpaka Dar es Salaam akatafute matibabu, ni ghali sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunaomba Serikali inapojibu itueleze mpango wake ni upi hasa ili kuwapunguzia wananchi wake adha za kupata matibabu hasa kwa ugonjwa huu ambao sasa unakuja juu kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa ni hayo kwa siku ya leo, lakini nimalizie kwa kuwapongeza hawa…
MWENYEKITI: Ahsante, muda wetu ndiyo huo.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi pia niweze kuchangia Hali ya Uchumi na Bajeti ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Naibu wake pamoja na wasaidizi ambao amefanya nao kazi bega kwa bega na hatimaye kutuletea kitu kamili na kilichoiva vizuri cha namna hii kwenye Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze Serikali kwa nia yake ya dhati kutaka kutuelekeza kwenye kujitegemea kama Taifa, kwa sababu ukiangalia bajeti ilivyotengenezwa, na hata maelezo yake ambayo yamesomwa na Mheshimiwa Waziri kwa kweli yanaonesha dhamira ya Serikali kujitegemea na yanaonyesha ya kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kabisa kupeleka maendeleo kwa wananchi baada ya kutenga asilimia 40 ya bajeti yake kwenye fedha za maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kutoa mchango wangu kwa kuangalia mambo mawili tu kwenye hali ya uchumi. Jambo la kwanza ni lile la kujitegemea kwa kuimarisha viwanda kwa ajili ya uchumi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, uwezeshaji wa suala hili unategemea uwekeshaji na tunapozungumza juu ya uwekezaji huu maana yake tunamzungumza mtu mwenye mtaji wa hapa ndani na mwenye mtaji wa nje ya nchi yetu. Lakini nadhani ni jambo moja tu ambalo limewekewa nguvu sana katika kuhakikisha kwamba tunapokuwa na uchumi wa viwanda tunatengeneza ajira na hatimaye tuweze kukusanya kodi, huo ni upande mmoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna upande wa pili ambao naona kama tunausahau kidogo; kuwawezesha hawa Watanzania, hasa wakulima wetu wadogo wadogo ili na wenyewe wajumuishwe kwenye harakati hizi za kuinua uchumi wetu wa viwanda kwa wao pia kushiriki, si tu kuzalisha malighafi, sio kuwa vibarua au kulipwa mishahara au kuajiriwa kwenye viwanda au kwa wawekezaji; lakini wao pia kushiriki kama wawekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimejaribu kuangalia ninaona kuna pengo kubwa sana. Wazalishaji wetu wadogowadogo, hasa wakulima wanaunda nguvukazi ya asilimia 65 na kutokana na taarifa mbalimbali, wanatuzalishia malighafi za viwandani, wanatuzalishia chakula.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye harakati zetu hizi za kujenga uchumi wa viwanda tunawaangalia kama waajiriwa peke yake, hatujawaangalia kama watu ambao wanaweza wakaja pamoja na wao pia wakashiriki kama wawekezaji, wakaendelea kuzalisha kama ambavyo wameendelea kuzalisha toka uhuru wa nchi hii. Wamezalisha wametupa chakula, wamezalisha wametupa malighafi za viwandani, wamezalisha wametupa mazao ambayo tukiuza nje tunapata fedha za kigeni. Sasa nilikuwa najaribu kuangalia Serikali imeweka mkakati gani jumuishi ili na wao waweze kushiriki kwenye uwekezaji huu ambao tunataka nchi yetu tuwekeze halafu hatimaye tuwe nchi ya kipato cha kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, ushirika wa wakulima hawa wadogo wote tunafahamu umekuwa hauna nguvu sana ni dhaifu sana. Mimi nilikuwa nafikiri kama ungetiliwa nguvu ungekuwa una nguvu za kutosha kuweza kutumika kuwafanya hawa wazalishaji wadogo wadogo ili wao wawe wawekezaji kwenye maeneo yao. Wamekuwa wawekezaji kwa muda mrefu sasa Serikali inatengeneza mazingira na kuweka mkakati gani ili kuwafanya hawa watu badala ya kutoa tu nguvu zao, badala ya kufanywa kama wafanyakazi na wenyewe wawe wawekezaji kwa namna ambavyo wamekuwa wawekezaji toka mwanzo?
Kwa hiyo nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri atakapojumuisha ajaribu kutufafanulia, kwamba hawa wakulima wadogo wadogo hasa wakulima wadogo wadogo wa wa vijijini wana wekewa mazingira ya namna gani ili na wenyewe waendele kuwa wawekezaji wadogo wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ni suala la thamani ya shilingi yetu, zimetajwa sababu zinazofanya shilingi yetu iendelee kuporomoka. Moja ni kuimarika kwa dola ya Kimarekani, lakini lingine ni kuchelewa kupatikana kwa fedha za kigeni hasa kwenye bajeti yetu, pia mapato kidogo ya fedha za kigeni. Lakini kuna moja ambalo tunaona na wachangiaji wengine wamekuwa wakilitaja hapa, la hawa watoa huduma pamoja na bidhaa kutaka kupata malipo kwa njia ya dola, halijatajwa hata kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala hili pia limekuwa kero kwa wananchi hasa wa kawaida na wananchi wengine kwamba ukitaka kununua bidhaa au ukitaka kununua huduma ulipe kwa dola. Suala hili nalo linasababisha thamani ya shilingi yetu kushuka. Kwa hiyo na lenyewe Mheshimiwa Waziri angetusaidia ni kwa namna gani Serikali inakuja na uamuzi uliothabiti na ulio wazi, kwa sababu sheria ipo inayozuia jambo hili lakini bado linaendelea.
Mheshimiwa naibu Spika, suala lingine la tatu ni hili linalohusiana na shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Naipongeza Serikali kwa sababu imeanza kwa kutenga shilingi bilioni 59 ili kwamba ziende kwenye vijiji zaidi ya 1000 kwenye nchi yetu yote. Hapa bado kuna kizungumkuti kwa sababu Serikali inasema itapeleka pesa hizi kwenye SACCOS, sasa najaribu kujiuliza hizi SACCOS ambazo zitapelekewa hizi pesa Serikali inazifahamu na kama inazifahamu hizi SACCOS ziko kila kijiji? Maana vijiji vingine havina SACCOS, hii hela itapelekwa kwa nani? Kwa taasisi ipi ili iweze kuzitoa hizi pesa kama mikopo kwa watu wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nilikuwa na mapendekezo kwenye jambo hili. Mimi nilikuwa nafikiri badala ya kutegemea SACCOS ambazo hatujazitathmini na hatujui kama ziko kila kijiji, kwamba badala ya kufanya hivyo tungeunda Bodi za Mikopo za Vijiji vile ambavyo vitapelekewa hizi pesa. Bodi hii ya mkopo iwe ndiyo inasimamia hizi pesa kujaribu kuzigawa au kuzitawanya kwenye vikundi au kwa watu ambao wako kwenye vikundi ili kupata hii mikopo lakini kwa riba nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa napendekeza kwamba hizi fedha ziwe ni revolving au ziwe za mzunguko; kwa sababu mpaka sasa hivi hatujaelewa kwamba zitakuwa ni za namna gani, maana zikienda kwenye SACCOS hauziiti tena za mzunguko.
Kwa hiyo, nilikuwa nafikiri ziwe za mzunguko, na hizi pesa zibaki kwenye kijiji husika zisiende kwenye vijiji mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nilikuwa napendekeza kwamba usimamizi wa hizi bodi ufanywe na Maafisa Maendeleo wa Kata na Maafisa Maendeleo wa Wilaya zetu na hizi shilingi bilioni 59 wakati wakuzigawa hii mara ya kwanza vijiji vitakavyopewa viwe pilot, lakini kila Jimbo lazima liwe na kijiji au kimoja au viwili ili tujue kila Jimbo performance ya mpango huu unafananaje, vinginevyo …
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango.
Napenda tu kumtia moyo Mheshimiwa Waziri kwamba kuwa Waziri wa Mipango na Fedha kwenye nchi inayoendelea kama Tanzania ni kazi. Na mimi nakutia moyo tu kwamba kazi hii unaiweza na ninakuamini utatuvusha kabisa na pia ukizingatia mashauri na maelekezo ambayo Waheshimiwa Wabunge wanakupa kwenye michango yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kuzungumzia kilimo. Uchumi wa viwanda ambao tunautamani, unategemeana sana na hali yetu ya kilimo. Kwenye taarifa ambazo tumezisoma, hali yetu ya kilimo imepungua sana. Uzalishaji wa mazao ya nafaka umepungua na uzalishaji wa mazao ya biashara umepungua. Kwenye taarifa na hotuba ya Mheshimiwa Waziri inasema mwaka huu kilimo chetu kimeanguka mpaka kwenye asilimia 2.3. Kwenye mazao ya nafaka kilimo chetu kimepungua kutoka asilimia 3.4 kuja asilimia 3.2; pia tumepunguza uzalishaji kwenye mazao ya biashara, mazao kama pamba, kahawa na katani yamepungua sana uzalishaji wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu ambazo zimetajwa mojawapo ni hali ya hewa, kwa sababu kilimo chetu kinategemea hali ya hewa. Tunaposema hali ya hewa, maana yake ni mvua ambayo tunategemea kudra za Mwenyenzi Mungu. Tatizo lingine linalotajwa kwenye maelezo ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2016/2017 ni upungufu au kukosekana kwa masoko ya mazao yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumesahau pia yako matatizo mengi yanayokikumba kilimo chetu ambayo sijaona kama yameshughulikiwa au yamekuwa addressed vizuri kwenye mpango wa mwaka huu 2016/2017. Mojawapo ni bei za mazao hasa mazao ya biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, bei za mazao ya biashara zimekuwa ndogo kwa wakulima ambao ni wakulima wadogo wadogo kiasi kwamba wamekata tamaa kulima mazao hayo. Kule kwenye Jimbo langu tunalima pamba na tulikuwa tunalima pamba kwa wingi kweli; lakini pamba imeendelea kushuka uzalishaji wake, mwaka jana imeshuka, mwaka juzi ilishuka na mwaka huu itakuwa ni mbaya zaidi kwa sababu najua wakulima wa pamba hawakulima pamba nyingi kwa sababu bei waliyokuwa wanatarajia ni kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashangaa hata sasa Serikali haijatoa bei elekezi itakuwa ni shilingi ngapi kwa zao la pamba. Kwa hiyo, mwakani pia tutegemee zao hili litapungua sana kiuzalishaji kwa sababu wakulima wanalima kwa kutegemea bei waliyopata mwaka 2015. Sasa mwaka huu kutakuwa na pamba kidogo sana. Kwa hiyo, uzalishaji katika kilimo utaendelea kuwa chini. Sasa nilikuwa naiomba Serikali wajaribu kuangalia, najua ya kwamba kuna tozo zilizokuwepo, Mheshimiwa Waziri wa Kilimo alituambia zitaondolewa, sasa hatujui zikiondolewa zitakuwa zimepandisha bei za mazao haya kwa wakulima kwa kiasi gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri ikaeleweka mapema, tozo zilizoondolewa ili wakulima hawa watiwe moyo kulima haya mazao; vinginevyo mazao ya kilimo, hasa ya biashara ambayo tunayategemea kwa muda mrefu yataendelea kupungua. Kwa hali hiyo, malighafi ambazo tunazitegemea kwa viwanda hazitakuwepo, mazao ambayo tunategemea kuyauza nje na yenyewe yatapungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, hiyo ni sababu nyingine, lakini sababu ya pili tumepuuza kilimo cha umwagiliaji. Nchi hii ina hekta nyingi, mamilioni ya umwagiliaji ambayo yanaweza yakatumia kilimo cha kumwagilia, yakatuzalishia mazao ya nafaka na mazao ya biashara, lakini hatujaweka nguvu ya kutosha hapo, ndiyo maana hata bajeti ya Kilimo, hata tulipendekeza iongezwe lakini sijaona kama imeongezwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo ambalo linalimwa kwa kumwagiliwa kwa sasa ni asilimia moja tu, lakini hiyo asilimia moja inatupa mazao ya nafaka kama asilimia 26 hivi. Kwa hiyo, utaona Kilimo cha Umwagiliaji kina uhakika namna gani kutupa mazao tunayotaka, kama tungeongeza nguvu kidogo tu, tukatoa bajeti ya kutosha, tukawa na sehemu nyingi za kumwagilia, tungeweza kupata mazao mengi ya biashara na ya nafaka kwa ajili ya nchi yetu. Sasa tumepunguza bajeti yake na sijui umwagiliaji utafanyika kwa kiasi gani. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu nyingine ambayo imefanya kupungua kwa mazao ya kilimo au kudorora kwa kilimo chetu ni pembejeo mbalimbali tunazopeleka kwa wakulima. Tunapeleka kwa kuchelewa na wakati mwingine tunapeleka kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, safari hii tumeweka bajeti kidogo mno na ndiyo hicho ambacho tulikuwa tunapigania hata kwenye Kamati kwamba bajeti ya pembejeo iongezwe, haijaongezwa mpaka leo. Kwa hiyo, tutegemee pia mwakani kilimo chetu kitakuwa ni kidogo sana. Mazao tutakayovuna yatakuwa kidogo sana kwa sababu ya tatizo la pembejeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lingine lililokuwepo hapo ni utafiti. Serikali inapeleka fedha COSTECH, lakini kwa nini pesa hizi zisiende moja kwa moja kwenye Taasisi za Utafiti za Mazao ya Kilimo? Kwa nini zisiende moja kwa moja kule, zinapitia COSTECH? Kwa nini zisiende moja kwa moja Uyole, Ukiriguru, Seliani kule Arusha? Kwa nini zisiende moja kwa moja mpaka zipitie COSTECH?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tusipoangalia haya mambo, yataendelea kufanya kilimo chetu kipungue uzalishaji wake mwaka hata mwaka. Kilimo kikipungua tusahau sasa uchumi wa viwanda kwa sababu malighafi nyingi inatoka kwenye kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba wakati Mheshimiwa Waziri anajaribu kujumuisha, atuambie ni mikakati gani sasa ipo angalau kupandisha hadhi ya kilimo kinachoendelea kudorora mwaka hadi mwaka? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka kuzungumzia ni kodi kwenye vifaa vya ujenzi. Kwenye bajeti hii kuna kodi kwenye nondo na vifaa vingine vya chuma vimewekewa kodi na sababu inayosemwa ni kwamba tunataka tulinde viwanda vyetu vya ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, sina uhakika Serikali imefanya utafiti kiasi gani kuona kwamba viwanda vyetu vya ndani vinaweza vikazalisha nondo za kutosha, vinaweza vikazalisha vifaa vingine vya ujenzi vya kutosheleza mahitaji. Kuna mwamko mkubwa sasa hivi wa wananchi wetu kujijengea nyumba bora na suala la nyumba bora liliwekwa pia hata kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Chama cha Mapinduzi walisema tutahamasisha wananchi wetu kujenga nyumba bora lakini pia kwa kuwezesha vifaa kupatikana kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunapoweka kodi na ushuru kwenye vifaa vya ujenzi, tutegemee watu wetu kuendelea kuishi kwenye nyumba za majani, tutegemee watu wetu kuendelea kuishi kwenye nyumba za tembe, tutegemee mazingira ambayo tunapiga kelele kila wakati kwamba lazima yawe mazuri na yenyewe yaendelee kuharibika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi ya kutoa mchango wangu kwa njia ya maandishi. Aidha, nimpongeze Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa kazi ngumu lakini nzuri wanayoifanya. Mchango wangu utajielekeza kwenye mambo yafuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya hifadhi; kwa takwimu nilizonazo, Tanzania ina eneo la uhifadhi ambalo ni asilimia 38 ya eneo lote la nchi. Hili ni eneo kubwa sana na nchi yetu ni moja ya nchi iliyo na eneo kubwa sana la uhifadhi duniani. Wakati wa uhuru nchi yetu ilikuwa na watu karibu milioni kumi tu, lakini hivi leo watu tunakaribia milioni 50. Eneo la makazi ya watu haliongezeki, watu wakiongezeka na shughuli zao za kiuchumi, kijamii nazo zinaongezeka na kwa sababu shughuli hizi zinafanyika kwenye ardhi, lazima maeneo ya uhifadhi yatalazimika kutumiwa na watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu kwa Serikali ni kwamba Serikali iangalie upya maeneo ya uhifadhi kwa kuyapunguza ili yatumike kwa shughuli za watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mapato ya utalii na idadi ya watalii; mapato yatokanayo na utalii bado ni madogo. Nakubaliana na hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba juhudi kubwa zinafanyika ili kufikisha kipato kitokanacho na utalii hapo kilipo. Kama nchi yetu ni ya pili kwa kuwa na vivutio bora vya utalii duniani baada ya Brazil, kwa nini mapato yetu kama nchi yakabaki kidogo namna hii? Mheshimiwa Waziri ni vyema akatoa maelezo juu ya jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mapato yetu ni kidogo kwa sababu idadi ya watalii wanaotembelea maeneo yetu ya utalii ni wachache. Ni kweli watalii wamekuwa wakiongezeka mwaka hadi mwaka, lakini ongezeko hili ni dogo kuwezesha kutupatia mapato makubwa ambayo yanatokana na utalii. Ninamtaka Mheshimiwa Waziri atueleze ana mkakati gani mpya wa kuongeza idadi ya watalii na hatimaye kutuongezea mapato kama nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la migogoro ya wafugaji na hifadhi; ipo migogoro kati ya wafugaji na Hifadhi za Taifa kwa sababu wafugaji wanapopata matatizo ya malisho na maji wanatafuta malisho na maji kwenye hifadhi. Nakubali huku ni kuvuruga sheria, lakini wafugaji hawa wanapovunja sheria kwa kuingiza mifugo yao kwenye hifadhi, Serikali nayo kwa kutumia wafanyakazi wake nao wavunje sheria kwa kuua ng‟ombe ama mifugo yao? Nao pia wavunje sheria kwa kuchoma nyumba za wanavijiji, wafugaji ambao wanaishi kando kando ya hifadhi? Wafanyakazi hao nao waombe rushwa kutoka kwa wafugaji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima Serikali i-balance, hapa sheria zifuatwe, lakini with a human face. Umefika wakati sasa maeneo ya wafugaji yatengwe na kuwekewa miundombinu muhimu inayohitajika ikiwepo utatuzi wa tatizo la malisho ya mifugo ya wafugaji. Serikali ikae kitako kwa kuhusisha Wizara zinazohusika ili kutatua migogoro hii na nchi ipate mabadiliko ambayo wananchi wanayahitaji. Wizara na Serikali ziache kufanyakazi kwenye silo, Serikali ni moja lazima ije na mkakati wa pamoja ili kuondoa udhia huu kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kunisaidia ujenzi wa mabweni mawili ya shule ya sekondari Malampaka. Haya ni nyongeza ya mabweni mengine yaliyojengwa baada ya Waziri wa Elimu kutoa fedha pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakati wa kuwa na refa wa ubora wa elimu wa kitaifa ambaye atakukwa huru kufuatilia ubora, usimamizi na uendeshaji wa shule zetu za msingi na sekondari. Huyu atasimama katikati ya shule binafsi na shule za Serikali. Refa huyu atafanya the playing ground kuwa leveled kati ya shule ya Serikali na shule binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati muafaka sana Serikali ije na mapendekezo ya kuunda chombo hiki ili kisaidie kuendesha shule zetu za msingi na sekondari kwa usawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni upungufu wa walimu na vitabu katika Wilaya yangu ya Maswa hususani Jimbo langu la Maswa Magharibi. Katika shule za msingi tuna upungufu wa walimu 727. Shule za sekondari tuna upungufu wa walimu 108 wa masomo ya sayansi na walimu 88 wa masomo ya sanaa hasa kiingereza. Naiomba Serikali wakati wa kugawa walimu wanapoajiriwa iangalie maeneo yaliyo na upungufu mkubwa ili yapewe kipaumbele kama ilivyo Wilaya yangu ya Maswa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia tuna upungufu wa vitabu vya masomo ya sanaa upande wa sekondari. Vitabu vya darasa la nne kwa mtaala mpya havipo kabisa mkoa mzima wa Simiyu. Naiomba Serikali itatue changamoto hii ili watoto wetu wapate elimu bora si bora elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vyuo vyetu vya maendeleo ya jamii bado vinaweza kutoa ujuzi na utalaamu tunaouhitaji ili kuendeleza masuala ya ufundi kwa watoto wetu. Hata hivyo vyuo hivi vina miundombinu iliyochakaa sana. Moja ya vyuo hivyo ni Chuo changu cha Maendeleo ya Wananchi cha Malampaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wizara iangalie ni kwa namna gani chuo hiki kinaweza kukarabatiwa na kupatiwa vifaa vya kufundishia pamoja na kuongezewa walimu. Vilevile naomba Serikali iangalie upya mitaala ya kufundishia ya vyuo hivi. Kwa maoni yangu mitaala iliyopo ni ya zamani haiendani na mazingira tuliyo nayo sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Fedha na Mipango kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nachukua nafasi hii kukushukuru kunipa nafasi tena ili na mimi niweze kutoa mawazo yangu juu ya Wizara hii ya Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaendelea nataka mimi pia kama ambavyo amezungumza mzungumzaji aliyepita, nikutie moyo kwamba kazi unayofanya ni njema, hauna sababu za kunyong‟onyea au kujisikia upweke, sisi tupo. Wote tumetumwa na wananchi ili kuja kuwasemea hapa Bungeni. Kwa hiyo, timiza wajibu wako kama ambavyo inakupasa kufanya na sisi tutakuwa pamoja na wewe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nijielekeze sasa kwenye kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri lakini nianze na ukurasa ule wa 40, Msajili wa Hazina. Msajili wa Hazina anayo kazi kubwa ya kusimamia rasilimali za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali kwa ujumla. Kazi yake hii ni kubwa na muhimu sana kwa Taifa, inabeba vitu vingi, mashirika na taasisi za Serikali uangalizi wake uko chini yake. Nilikuwa najaribu kujiuliza, je, huyu mtu ana wafanyakazi wa kutosha? Tena wawe wa kada mbalimbali kwa sababu, mashirika na taasisi hizi za Serikali ni nyingi lakini pia zina sekta mbalimbali tofauti-tofauti.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa najaribu kuangalia bajeti yake aliyowekewa na kulinganisha na ukubwa wa kazi ambayo amepewa, naona kama haitoshelezi. Mwanzoni niliona kama ni kubwa, iko shilingi 160,181,000,000 nikaona kama ni kubwa lakini nilipoingia kwa undani nikakuta ndani yake shilingi milioni kama 150 hivi ni kama social responsibilities kwa mashirika yaliyo chini ya huyu Msajili wa Hazina. Nikaona ukiondoa pesa za maendeleo anabaki na hela kidogo sana za uendeshaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu hii imepewa kazi kubwa sana. Mheshimiwa Rais alipokuwa akihutubia Bunge hili alisema kuna mashirika ya umma yaliyouzwa ambayo tathmini yake inabidi ifanyike, mengine yarudishwe, mengine yaangaliwe kama yalipouzwa yanaendelea kufanya shughuli zile ambazo zilikuwa zimekusudiwa au la. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, nimeona tu mashirika ambayo wameandika Kiswahili cha kileo, uperembaji ni kama 55 tu lakini pia hatujaona kwa kina kwamba haya 55 ndiyo yanayofanya kazi, ndiyo yaliyofilisika, ndiyo yaliyobadilisha matumizi au yana hali gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, nilipokuwa najaribu kuangalia bajeti nikaona kwa sababu labda ya bajeti kuwa ndogo ndiyo maana Msajili wa Hazina hajaweza kufanya kazi yake ipasavyo kuweza kutupa taarifa zilizo kamili kama wananchi ili tuweze kufahamu. Kwa sababu kama ni ahadi ya Rais kwamba mashirika haya ya umma mengine yatarudishwa Serikali au yataangaliwa yauzwe upya au mengine yatafanyiwa mpango mwingine, tungetakiwa sisi kama wananchi kujua hatua iliyofikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Waziri anapohitimisha Wizara yake hii pengine tutapenda kujua kuna hali gani ya mashirika na mali za Serikali chini ya Msajili wa Hazina.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni ufuatiliaji na tathmini. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri pia nilipokuwa najaribu kuangalia ufuatiliaji na tathimini haujapewa uzito ule unaostahili. Asilimia 40 ya bajeti ya nchi yetu mwaka tunaouendea itakuwa ni bajeti ya maendeleo. Kama hatuna mkakati na mpango unaoeleweka juu ya ufuatiliaji na tathmini tunaweza kujikuta tuna miradi ambayo iko chini ya kiwango, haiko sawa na thamani ya fedha iliyopangiwa au haijakamilika sawasawa. Kwa hiyo, kipengele hiki cha ufuatiliaji na tathmini ni muhimu sana kikieleweka kwamba kipo na kwamba kinafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri zetu huko tulikotoka miradi mingi inayotoka Serikali Kuu haina fedha ya ufuatilliaji na tathmini. Kwa hiyo, wanapoagizwa kufuatilia miradi hii ili waweze kutoa taarifa Serikalini wanashindwa kufanya hivyo kwa sababu hakuna bajeti mahsusi kwa ajili ya jambo hili kwa hiyo wanahangaika wanabaki tu sasa kujikusanyakusanya wenyewe kwa fedha yao lakini wana malalamiko makubwa. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri anapokuwa anahitimisha pia ajaribu kuangalia suala la ufuatiliaji na tathmini liwekewe uzito unastahili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni uwezo wa mashirika chini ya Wizara hii, yapo mashirika chini ya Wizara hii lakini nizungumzie tu shirika moja la TTCL. TTCL bado inaendelea kupata ruzuku ya Serikali. Najiuliza TTCL ni Kampuni ya Simu kama ambavyo makampuni mengine ya simu yalivyo, inashindwaje kuingia kwenye ushindani kama yanavyoshindana makapuni mengine na yenyewe ikatupatia faida kama Shirika letu la Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukijaribu kuangalia taarifa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri unaona kabisa kwamba TTCL bado haijasimama pamoja na kutiwa nguvu na vitu vingine.
Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri anaposimama hapa kujibu hoja atuelezee mashirika yaliyo chini ya Wizara hii hasa yale ambayo ni mzigo kuna sababu gani ya kuendelea nayo? Kwa nini mengine tusiyaache tukaendelea na mashirika ambayo yanaweza yakatoa faida kwa Serikali?
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho kimezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge wengine ni Sheria ya Manunizi. Kweli kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri hajataja kitu chochote lakini sheria hii pia ilipigiwa kelele kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais alipokuwa anafungua Bunge hili. Tulitegemea kwamba tungepata majawabu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri kwamba hatua tulizonazo ni zipi sasa kuhusianana na sheria hii. Tunapeleka fedha nyingi kuanzia mwakani kwenye Halmashauri na sehemu zingine lakini Sheria ya Manunuzi imebaki ile ile inayotunyonya, ile ile inayolalamikiwa. Kwa hiyo, tungependa Mheshimiwa Waziri atueleze Sheria hii ya Manunuzi italetwa lini hapa Bungeni ili tuweze kuirekebisha na miradi itakayofanyika ifanyike kweli kuonesha value for money ambayo imetumika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze la mwisho juu ya Benki ya Wakulima ambayo imeundwa hivi karibuni. Benki hii imepewa shilingi 60,000,000,000 lakini bado wanalalamia wakati kuna benki nyingine wamepewa kama shilingi 20,000,000,000. Mfano TIB Corporate hata kwenye hotuba ya Waziri amesema hawa watu wameweza kuvuta amana zingine sasa hii TADB yenyewe imeshindwaje kuvuta amana zingine na inashindwaje hata kufika tu maeneo ambayo wakulima wapo? Kwa sababu ukijaribu kuangalia benki hii bado iko Dar es Salaam kama walivyozungumza wazungumzaji wengine, naona kama hatutaweka nguvu inayoeleweka mwelekeo wake hii pia inaweza ikawa benki tu ambayo ina jina la Benki ya Wakulima lakini wakulima haiwasaidii. (Makofi)
Kwa hiyo, naomba sana tuwasaidie wafanyakazi walioko kwenye benki hii ili kuweza kufikia maeneo yetu ya vijijini ili wawaguse wakulima kama lilivyo jina la benki yao. Vinginevyo tutakuwa tuna Benki ya Wakullima kama tulivyokuwa na Benki ya Wakulima Vijijini CRDB au TRDB zamani lakini isiweze kuwasaidia wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, yangu yalikuwa ni hayo lakini Mheshimiwa Waziri atakaposimama kuhitimisha hoja yake basi naamini tutapata majibu na majawabu ya hoja hizi nilizozungumza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili nami pia niweze kuchangia mapendekezo haya ya Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kama ambavyo Mheshimiwa Mapunda amesema. Nilidhani kwamba tungekuwa na rejea ambayo inatuelekeza ni kwa namna gani angalau tumejaribu kufanya kwa mwaka huu ambao unaelekea mwishoni, ingekuwa nzuri sana; lakini sasa tumekosa hiyo. Wakati nasoma haya mapendekezo nikawa najiuliza, hivi inakuwaje mtu anafikiria kuoa mke wa pili wakati huyu wa kwanza hata hajamwoa? (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unamwita mke wa pili au mke wa kwanza? Sasa kwa kweli hiyo tu ndiyo imeleta shida kwenye mapendekezo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ni vizuri kama ndiyo taratibu zetu, kanuni zetu au sheria zetu, basi ni vizuri kuzibadilisha ili tupate angalau matokeo ya miezi sita ya mpango ule uliopo kwenye mwaka, halafu tuweze kuangalia sasa tunapendekeza nini. Vinginevyo inakuwa ngumu kweli kweli kuchangia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kitu cha pili kabla sijatoa mchango wangu. Cha pili ni kwamba, mwaka 2015 tulipokuwa kwenye uchaguzi kila mtu alikuwa anaimba mabadiliko. Mabadiliko ni rahisi kuyaimba lakini yana tabia moja ambayo siyo nzuri wakati mwingine. Mabadiliko yana tabia ya kumtoa mtu kwenye comfort zone yake. Sasa inaelekea Serikali hii ya Awamu ya Tano, kwa sababu imevaa njuga za mabadiliko, watu wengi hatufurahii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli kwamba kama tunataka mabadiliko, ni lazima tutoke kwenye comfort zone tuliyokuwa tumezoea. Haiwezekani ukataka kwenda Peponi au Mbinguni bila kufanya ibada. Ibada nyingine ni mara tano kwa siku, nyingine inabidi uache kula na kunywa, lengo tu ufike Peponi au Mbinguni.
Sasa kuna vitu ambavyo sisi kama wananchi na Serikali yetu kama kweli tunataka mabadiliko yaliyo ya maana, vitu vingine inabidi tuvisahau na vitu vingine inabidi tuviache kwa sababu tunataka mabadiliko. Hatuwezi kufikia mafanikio ikiwa tutataka tukae kwenye raha ile tuliyokuwa nayo miaka 50 iliyopita. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge ni lazima tulielewe hilo hata tunapojadili hali ngumu za maisha zinazowakabili watu wetu, tujue kuwa hiyo ndiyo hali halisi ya kutaka mabadiliko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha pili ni kwamba humu Bungeni kuna kitu ambacho mimi sijakipenda sana kinatugawa Wabunge. Kuna kitu kinasemwa na Wabunge wengi wewe huwajui wapiga kura, wewe hukupigiwa kura, kuna mtu hakupigiwa kura humu ndani?
MBUNGE FULANI: Ndio.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Hapana. Mimi naamini kila Mbunge amepigiwa kura hapa, kura zetu zinatofatiana idadi tu, Mheshimiwa Mpango amepigiwa kura moja akawa Mbunge. Mimi nimepigiwa kura makumi elfu nikawa Mbunge, wenzetu wa Viti Maalum wamepigiwa kura kadhaa ni Wabunge, sasa tunapofika humu na kuanza kugawanyana wewe hujapigiwa kura, wewe huwajui wapiga kura, kila mtu anajua mpiga kura wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kutahadharisha tu ni kwamba Mheshimiwa Mpango kura yako wewe ni moja ukapata Ubunge, lakini nyuma ya kura moja kuna kura mamilioni ya Watanzania yaliyompa kura aliyekupa wewe kura. Kwa hiyo, aliyekupa kura anatarajia mamilioni ya kura za Watanzania waliompigia waguswe kupitia wewe. Wewe ni Mbunge kabisa halali wa kupigiwa kura, ni Mbunge halali na Uwaziri wako ni halali, lakini kumbuka kuna kura nyingi huko nyuma ya kura yako zinataka kuguswa na wewe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende kwenye kuchangia mapendekezo. Kitu cha kwanza mapendekezo yanasema kufungamanisha maendeleo ya uchumi na maendeleo ya watu, ninakubaliana nayo, lakini ili maendeleo ya watu yaonekane yamefungamanishwa na maendeleo ya uchumi lazima ionekane kwamba katika huduma zile za kijamii ambazo zinagusa watu wengi, wananchi wetu wanazipata kwa urahisi kwa gharama nafuu, wanazipata wanapozihitaji. Hali ilivyo, wakati huu kwa kweli haiko namna hiyo, kwa sababu mpango ambao tuko nao sasa hivi haujawahi kutekelezwa kikamilifu kiasi cha kugusa maeneo yanayogusa wananchi wengi, kwa mfano afya, elimu na mambo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapotaka kukuza uchumi wetu ili ufungamane na maendeleo ya watu lazima tufanye juu chini katika mapendekezo haya tufanye juhudi zile zinazogusa wananchi wetu hasa wanyonge. Tusipofanya hivyo hatutafungamanisha maendeleo ya uchumi wetu unakua ndio, lakini watu wetu watabaki kwenye hali zile zile, kwa hiyo ni ushauri wangu wa kwanza huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine tunatakiwa tuwe na miradi ya kielelezo ndiyo, lakini miradi ya kielelezo kutoka mwaka juzi, kutoka miaka ya nyuma sana mpaka tunaendelea na kuendelea nayo nadhani pia hii sio mpango mzuri, sio utaratibu mzuri. Nimejaribu kuangalia mapendekezo ya mpango huu, mimi nikawa nafikiri ningekuta kuna mradi angalau mmoja wa kielelezo wa umwagiliaji lakini hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napendekeza ni vizuri na ni muhimu sana tukaangalia kwa sababu tumekwishakupewa taarifa, hali ya hewa ya mwaka tunaoundea sio nzuri. Watu wa hali ya hewa wametuambia, lakini pia mabadiliko ya tabia nchi yanatueleza hivyo, hali sio nzuri ya mvua zitakazonyesha baadae, lakini tuna eneo na maeneo makubwa ambayo yangeweza kumwagiliwa yakatupa chakula na mazao ya biashara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mapendekezo haya unaona vitu vingine tu lakini jambo la umwagiliaji ambalo lingetupa maji ya uhakika halijawekewa msimamo, ambalo lingetupa mazao kila wakati, halijawekewa mpango, sasa tunafanyaje? Nahisi habari hii ya kuwa na umwagiliaji mkubwa ni ya muhimu sana kuwekwa kwenye mpango kwa sababu tuna vyanzo vya maji vingi, maziwa matatu makubwa na mito mikubwa tunayo hapa nchini kwetu, hilo ni la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni uvuvi wa bahari kuu, hatujaona humu kama kwenye mpango kunapendekezwa kitu chochote. Mheshimiwa Rais ameimba wakati wa kampeni anasema anashangaa kwa nini ukanda wetu wa Pwani hakuna hata kiwanda kimoja cha samaki, hakuna. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunashangaa hatuna meli ya kuvua hata moja ambayo ingeweza kununuliwa na Serikali kwa bei ambayo iko chini ya bei ya Bombardier, inawezekana kabisa tukinunua meli moja tunaweza tukawa na uvuvi mkubwa kwenye bahari kuu. Lakini kwenye mapendekezo haya unaona tu uvuvi umetajwatajwa tu kifupi kifupi tu lakini hakuna seriousness yoyote ambayo unaiangalia na kuiona iko humo ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu cha tatu ambacho nimekikosa ni mazao yetu makuu ya biashara kwenye mpango, kwenye mapendekezo hayapo, lakini ukijaribu kuangalia takwimu mazao yetu makuu ya biashara korosho, tumbaku, kahawa, pamba mazao haya uzalishaji wake unapungua kila mwaka, uko chini lakini kwenye mapendekezo hakuna kitu chochote kinachotajwa angalau mkakati kuonyesha ya kwamba tuna mkakati wa maana kupandisha uzalishaji wa mazao haya ili tuweze kupata hela nyingi za kigeni, lakini pia watu wetu waweze kujipatia kipato kwa sababu ndio wengi wanaolima mazao haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nipendekeze pia kwamba mapendekezo haya ya mpango yajaribu kuangalia mazao makuu ya biashara tunafanyaje juu ya haya ili kwamba kuweza kupandisha kipato cha wananchi wetu. Mengi ya mazao haya tunauza yakiwa ghafi, kwenye mapendekezo ya mpango hakuna dalili zozote ya kuyageuza ili angalau tuyauze yakiwa na value added, hakuna, sasa tunafanyaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilitaka kusema hayo machache tu nashukuru sana kwa kunipa nafasi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wengine wamechangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri ambayo imejaa uzalendo na ukweli ndani yake, kwa sababu nilipokuwa nikisoma hakuna chembechembe za ushilawadu ndani yake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze mchango wangu kwa ukurasa namba 16 unaosema asilimia 56 ya nguvu kazi ya Taifa ni vijana, wengi wa vijana hawa wameajiriwa kwenye sekta isiyo rasmi na ni wengi kweli zaidi ya asilimia 70 katika nchi yetu na kwa wakati huu kundi hili linazidi kuongezeka maana mwanzoni lilikuwa na vijana wachache, lakini hasa ambao wana elimu ya darasa la saba, kidato cha nne na wengine kidato cha sita, lakini sasa hivi linaingiza kundi la vijana wasomi ambao pia wamemaliza hata chuo kikuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kundi hili linaanza kuwa muhimu sana wakati huu na tusipoangalia kama Serikali basi tutakuwa tunapoteza nguvu kazi nyingi kwa sababu wanajiunga kwenye kundi la sekta isiyo rasmi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta hii isiyo rasmi ina changamoto nyingi. Moja ni udogo wa mtaji, mitaji yao ni kidogo sana. Pili, ni tija ndogo kwenye uzalishaji wanaohusikanao, pia wana matumizi duni sana ya teknolojia pia utaratibu wa wao kujisajili na kuwa kwenye sekta rasmi ni mrefu sana Kiserikali unawakwaza. Kodi ambazo zinatozwa kwenye kundi hili si rafiki sana kuwafanya waondoke kwenye sekta isiyo rasmi kuingia kwenye sekta iliyo rasmi, kubwa kabisa ni kwamba kundi hili lina ukosefu wa mahali pa kufanyia shughuli zake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshuhudia mara nyingi watu hawa wamekuwa wakiondolewa, wakikaa mahali fulani kidogo wanaondolewa, aidha inatolewa amri na Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa. Wote tumeshuhudia kipindi kilichopita namna ambavyo kundi hili la wafanyabiashara, wale wasio rasmi, walivyofurushwa kule Mwanza na Dar es Salaam mpaka Mheshimiwa Rais mwenyewe akaingilia kati. Kwa kuangalia matatizo haya waliyonayo hatujaonesha kama Taifa kwamba tunataka kulipunguza kundi hili la sekta isiyo rasmi ili liingie kwenye sekta iliyo rasmi, hivyo mchango wake katika Taifa hili kiuchumi na kimapato umekuwa
mdogo sana kwa sababu siyo rahisi sana kulifuatilia kundi hili kwa mifumo rasmi iliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali iangalie upya mfumo wake ili kulifanya kundi hili litoke katika sekta isiyo rasmi liingie kwenye sekta rasmi ambayo itatoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa nchi yetu, vinginevyo tukiliacha namna hii na kundi hili linaendelea kukua basi tutakuwa na kundi kubwa. Tunapokuwa na kundi kubwa limekaa kwenye sekta isiyo rasmi, wataalam wa uchumi wanasema bado kundi hilo litabaki kwenye hali ya umaskini.
(Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naisihi Serikali ije na mkakati au sera mpya kwa sababu sera iliyopo inayolihusu kundi hili, ile ambayo nimeiona ni ile ya mwaka 1994. Sasa kama ipo nyingine labda sijaiona, lakini kama ni ya zamani kiasi hicho basi Serikali ni vizuri ije na sera mpya, sera hiyo iainishe ni kwa namna gani inalitoa kundi hili kutoka kwenye sekta isiyo rasmi kuliingiza kwenye sekta iliyo rasmi ili kundi hili pia liweze kulipa kodi kwa Serikali na liweze kutoa ajira kwa wananchi walio wengi kwa sababu likibaki kwenye kundi hili la sekta isiyo rasmi haliwezi kutoa ajira tunazozitegemea na hatuwezi kupata mapato ya kutosha kwenye kundi hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo nataka niliongelee ni suala la taarifa zinazotoka kwenye Taasisi za Serikali. Mwaka jana mwezi wa Oktoba mwanzoni au mwezi wa Septemba mwishoni, Tanzania Meteorological Agency (TMA) walitoa taarifa yao kuhusiana na hali ya mvua
ya vuli na mwelekeo wa mvua za masika zitakavyokuwa. Taarifa hii ilitolewa kipindi kile cha Oktoba na Disemba na wakatahadharisha pia kwamba kipindi cha masika Novemba mpaka Aprili pia ni wakati wa mvua za masika lakini mvua zitakuwa ni kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hizi sikuona kama zinaratibiwa vizuri na kutumiwa vizuri na watu walioko Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kiasi kwamba sasa tulipofika kwenye mvua za vuli, mvua za vuli kweli zilikuwa ni chache, maeneo mengi yalikuwa ni makavu na maeneo mengi yanayotumia mvua za vuli kulima walipolima hawakuotesha na wengine waliootesha mazao yalikauka kwa sababu kipindi cha mvua kilikuwa kifupi sana. Hata hivyo, kipindi cha mvua za masika pia kilichelewa sana mvua maeneo mengine zimenyesha Februari na Januari mwishoni, matokeo yake wakulima walipopanda mvua tena zimekuja kukatika hapa katikati. Sasa matokeo yake tumekuwa na mavuno kidogo katika maeneo mengi ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua na tunakumbuka kweye Bunge hili kwamba Bunge lililopita, Waziri wa Kilimo alikuja na takwimu akasema Wilaya kama 55 hivi zina upungufu mkubwa wa chakula, lakini hatukuona hatua zinazochukuliwa na Serikali kuanzia pale TMA walipotangaza
hali za mvua kutopatikana zile za vuli na hata hizi za masika. Hatukuona hatua zinazochukuliwa na Wizara ya Kilimo ili kuwatahadharisha wakulima na kuwatayarisha waweze kujitayarisha na jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naona shida hapa kwamba, taarifa zinatoka hukohuko Serikalini, Taasisi ni ya Serikali, zinakuja huku upande mwingine hazitumiki vizuri. Sasa ninaiomba Serikali wawe na uratibu mzuri wa taarifa zinazotoka hasa zinazotusaidia wanyonge kama wakulima
huko kijijini. Vinginevyo tusipopata tahadhari ya namna hii tunaendelea na mambo tukijua mambo yatakuwa kawaida na kumbe kule mbele tunakutana na hatari. Kwa hiyo, niiombe Serikali wawe wanaratibu vizuri taarifa zinazotoka kwenye taasisi zake ziweze kuwa za manufaa kwa wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka jana inasema fedha zilizoombwa ni shilingi bilioni 236 na kuendelea, lakini mwaka 2017/2018 fedha zilizoombwa ni shilingi bilioni 171. Fedha ya Matumizi ya Maendeleo 2016/2017 ni shilingi bilioni 165 lakini mwaka 2017/2018 ni bilioni…
Ooh! Ahsante, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi nitoe mchango wangu kwenye Wizara hii ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayofanya kwenye Wizara hii, mapinduzi makubwa yamefanyika kwa muda huu wa mwaka mmoja ambao amekaa hapo. Tumeona kwenye hotuba yake hapa vitu vingi
vimefanyika vikubwa vikubwa ambavyo siku za nyuma vingechukua labda miaka mingi sana lakini kwa muda mfupi amejitahidi. Nichukue nafasi hii kwa kweli kumpongeza sana kwa juhudi anazoendelea nazo. Naamini kwa muda atakaokuwepo kwenye Wizara hii mabadiliko makubwa yatakwenda kutokea kwa sababu ni mama anayejitahidi sana; ni mama anayejali na ni mama kwa kuongea anamaanisha, lakini pia vitendo vyake tunaviona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii pia kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu mwaka jana nilipeleka maombi ili kunisaidia kwenye shule yangu mojawapo ili iweze kupata kibali hatimaye iwe A-Level. Alinisaidia akanipa kama shilingi milioni 100 na zaidi, tukajenga bwalo na mabweni ya wanafunzi tayari yamekamilika na mwaka huu tumepata kibali cha kuingiza watoto wa kidato cha tano. Ahsante sana Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze kutoa mchango wangu kuhusiana na ukaguzi wa shule kwenye maeneo yetu. Ukaguzi wa shule ni muhimu sana kwenye nchi yetu na kwenye shule zetu kwa sababu kwa huo ndio tunaelewa ubora wa elimu yetu inayotolewa huko mashuleni. Hata hivyo, Kitengo cha Ukaguzi kuanzia huko Taifa mpaka huku chini Wilayani kina hali sio nzuri sana. Nichukue mfano wa kitengo hiki kwenye Wilaya yangu ya Maswa. Wilaya yangu ya Maswa kitengo hiki hakina miundombinu inayotakiwa ili kiweze kufanya kazi yake vizuri. Kwanza wako kwenye kaofisi kamoja ambapo wamejibana, lakini pia vifaa hawana, wana gari moja ambalo limezeeka sana na ni gharama kubwa kulifanyia maintenance.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukichukua hali iliyoko kwenye kitengo hiki, vifungu au mafungu ya fedha yanayopelekwa kwenye ukaguzi wa elimu ni kidogo sana kiasi kwamba hawawezi kwenda field na kukikuta gari bovu kama ilivyo kwenye Wilaya yangu ndiyo hali inakuwa ngumu kabisa. Hawawezi kufanya maintenance, hawawezi kununua mafuta, hawana posho ya kujilipa wanapokwenda kukagua kwa hiyo, ubora wa elimu kwenye maeneo yetu unakuwa ni wa mashaka mashaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe Kitengo cha Ukaguzi kwa shule zetu, shule za msingi hata shule za sekondari kiboreshewe mazingira yake. Wapewe usafiri unaowezekana kusafiri kwenda kwenye shule kukagua, wapewe vifaa vinavyohitajika, wapewe posho yao, wapewe mafuta, kama hawapewi watafanyaje kazi hizi, itakuwa ni ngumu sana. Gari lililopo pale kwenye Wilaya yangu halina matairi, halifanyiwi maintenance, hawa watu wapo tu pale ofisini. Pamoja na kwamba wako wachache lakini wangeweza kujitahidi angalau basi kuzitembelea baadhi ya shule ili waangalie ubora wa elimu inayotolewa pale, hilo ni jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka nizungumzie ni hii Tume ya Walimu, sijui kama iko sehemu ngapi, kama iko kwenye Wizara yake, Wizara ya Utumishi au Wizara ya TAMISEMI. Hii Tume ya Walimu na yenyewe ina matatizo lukuki. Hawa Tume inatakiwa akituhumiwa mwalimu waende kwenye eneo la kazi la yule mwalimu, lakini hawaendi kwa sababu pia wanapokea pesa kidogo. Wakienda pia wanatakiwa baada ya kubaini mashtaka aliyonayo warudi waje wafanye kikao ofisini (kikao cha Tume), lakini hawawezi kufanya vikao vyao vya Tume kwa sababu pia hawana fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, matokeo yake unakuta mwalimu ametuhumiwa, ameandikiwa mashtaka wamemtembelea lakini hawawezi kumwita kuja kufanya naye kikao kwa sababu fedha hazipo kwenye Tume hii ya Walimu na kwa hiyo, mwalimu huyo anakaa analipwa nusu mshahara kwa sababu anapotuhumiwa anasimamishwa analipwa nusu mshahara muda mrefu. Kwenye Wilaya yangu ya Maswa kuna walimu kama wawili, watatu hivi, wamekaa sasa kama mwaka nzima hawajasikilizwa, wanaendelea kulipwa nusu mshahara. Kwa kweli naomba sasa Wizara hii ya Elimu iweke mpango madhubuti ya kuimarisha Tume hii ya Utumishi ya Walimu ili iweze kuwasaidia walimu hasa wale

wanaopata matatizo na kama mtu kesi yake haieleweki basi imalizwe mapema halafu aendelee kufanya kazi yake vinginevyo kwa mafungu wanayopewa hawawezi kufanya kazi yao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni majibu wanayosubiri walimu ambao Tume imekwishapeleka hoja zao huko Makao Makuu wanasuburi muda mrefu sana. Wengine wanaposubiri hata barua zinaporudi ili aje arudishwe kazini inachukua muda mrefu mno, lakini ana barua ambayo iname-clear mashtaka yake lakini bado kurudishwa kazini inakuwa ni ngumu sijui utaratibu huu unakuwaje. Maana inakuwa pale kwa Afisa Utumishi anaambiwa subiri, subiri, subiri. Nashauri utaratibu huu uangaliwe upya ili tuwarahisishie walimu hawa wanapopata matatizo lakini pia matatizo yao yapogundulika hayapo basi warudishwe kazini haraka iwezekanavyo na stahili zao waweze kupewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande mwingine nataka nizungumzie kuhusiana na FDC. FDC kuanzia mwaka jana Mheshimiwa Waziri alituambia zimerudi kwenye Wizara yake. Hivi FDC (Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi) huko kwenye maeneo yetu vina hali siyo nzuri sana. Nichukue mfano wa Chuo cha Maendeleo ya Wanachi cha Malampaka kule kwenye jimbo langu kina miundombinu ambayo imezeeka sana. Mheshimiwa Waziri hiki Chuo cha Maendeleo ya Jamii kimetoka kilipokuwa middle school kikageuzwa kikawa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi. Kwa hiyo, majengo yake ni ya zamani sana, yamechakaa lakini haya hajakarabatiwa na samani zilizoko pale na zenyewe ni za zamani sana zingine zimevunjika, hazina thamani kama jina lake lilivyo. Hivi vyuo kwa sababu vimerudishwa kwake Mheshimiwa Waziri basi naomba aviangalie kwa maana ya kuvipatia vitanda na samani. (Makofi)

Mwenzangu ananikumbusha hapa, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Malya pia kina matatizo yale yale. Hiki chuo nachokizungumza cha Malampaka kina walimu wawili tu na kinatakiwa kiwe na walimu 26; hakuna usafiri na vifaa vya kujifunzia.

Sasa naomba Mheshimiwa Waziri anapojumuisha ajaribu kuviangalia hivi vyuo pia kwa sababu vimerudi kwake basi viweze kuwasaidia wananchi wetu huko tuliko. Maana vyuo hivi ndiyo mkombozi sasa kwa watoto wetu wale wanaomaliza form four wale wanaomaliza darasa la saba ili wajifunze elimu ya kiufundi na elimu mbalimbali iweze kuwasaidia kwenye maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimazilie kwa kusema ahsante sana kwa kunipa nafasi lakini pia naendelea kumshukuru pia Mheshimiwa Waziri kwa sababu amefanya juhudi kubwa sana kwa kweli hasa kwenye shule yangu ya sekondari ya Malampaka, tuna hali nzuri sasa hivi na tunaanza A-level, lakini kama alivyomtuma Katibu wake Mkuu alipofika pale aliahidi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Nianze kwa kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi pamoja na timu yao yote ya Wizara kwa namna ambavyo wanafanya kazi zao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze sana kwa sababu ya kuja na mpango mzuri hasa unaohusiana na mbolea. Kuna mambo mengi yamesemwa kuhusiana na mbolea lakini mimi nataka tu kutahadharisha mambo mawili au matatu. Mpango wenyewe ni mzuri wa kununua mbolea kwa pamoja, ni mpango mzuri sana. Mambo matatu tu ninayotaka yaweze kufanyika kwa wakulima wangu waliopo Maswa na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla, moja ni bei. Najua mtatoa bei elekezi kwa sababu wale wauzaji wasije wakavuka pale, kwa hiyo, naomba bei iwe nafuu, kama itakuwa nafuu hakuna shida.

Pili, ni kufika kwa wakati, mbolea hiyo ifike kwa wakati kwa wakulima wetu, isipofika kwa wakati kama walivyochangia Wabunge wengine itakuwa haina maana sana.

Lakini la tatu kwenye mbolea, nataka tu kusema kwamba mbolea hii sasa ipatikane maeneo yote, siyo ukanda fulani tu upewe mbolea na ukanda mwingine usipate mbolea. Kwa sababu sasa tutakuwa na uhakika wa kuipata mbolea hii na inapatikana kwa wote basi ipatikane kwa wakulima wote nchi nzima. Hongereni sana kwa mpango huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze kwa kutoa tozo hizo ambazo zilikuwa zimerundikwa kwenye kilimo. Waheshimiwa Wabunge tozo hizi zilikuwa zinakwamisha mambo mawili, moja ni bei za mazao kwa ajili ya wakulima wetu zilikuwa zinakuwa chini kwa sababu tozo nyingi zipo pale. Pia zilikuwa zinakwamisha uwekezaji kwenye sekta hii ya kilimo, mifugo na uvuvi. Kwa hiyo, tunawapongeza sana kwa jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niwapongeze pia kwa kusimamia vizuri ushirika, ulishaanza kulegalega na kwenda tenge, lakini kwa ujio wenu naona sasa mambo yanaanza kurekebishwa kwa sababu wale walafi wa pesa mnaanza kuwachukulia hatua. Hongereni sana na endeleeni na maeneo mengine ambayo yamebakia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nawapongeza ni la pembejeo, mmesimamia vizuri habari ya pambejeo, ule wizi uliokuwa ukifanyika mmeusimamia vizuri na mpo imara katika hilo. Nataka muendelee kusimamia namna hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka sasa niishauri Serikali kwenye eneo la kilimo hasa kwenye uwekezaji. Uwekezaji kwenye kilimo umekuwa ni mdogo sana. Kwa muda wa miaka mitano iliyopita uwekezaji upande wa ukuaji wa kilimo ni mdogo sana. Kwa muda wa miaka mitano iliyopita kilimo kimekua kwa wastani wa asilimia 2.8, ni asilimia ndogo, lakini ukilinganisha ukuaji wa watu kwenye nchi yetu ni asilimia 2.7. Sasa ukijaribu kulinganisha ukuaji wa kilimo na ukuaji wa idadi ya watu karibu ni ule ule. Sasa ukikumbuka kwamba ukuaji wa kilimo ndiyo ukuaji wa kipato chetu maana yake ni kwamba kipato cha Watanzania wengi ambao wanaajiriwa kwenye kilimo hakijakua kwa kiasi kinachoweza kusemwa ni kikubwa, haujakua sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mfululizo wa ukuaji wa kilimo umekuwa ukiendelea kushuka kila wakati, kila mwaka umekuwa ukishuka. Mwaka 2014 kilimo kilikua kwa asilimia 3.4, mwaka 2015 asilimia 2.3 na mwaka 2016 asilimia 2.1. Sasa ukuaji huu ni mdogo sana. Tunapoendelea na ukuaji wa kilimo ukiwa mdogo hivi ni hatari kwetu kwa sababu bado tunategemea kilimo lakini pia ni hatari kwa Sera ya Viwanda ambayo Serikali yetu inaiendesha sasa hivi maana yake malighafi kutoka viwandani itakuwa ni kidogo na matokeo yake vile viwanda ambavyo Mheshimiwa Mwijage anaalika wawekezaji kila wakati na siku mbili zilizopita alikuwa akituelezea hapa kwamba ameweza kuanzisha viwanda vingi, vinaweza kuwa na hatari ya kufungwa baadaye kwa sababu ya vitakosa malighafi kwasababu ya ukuaji mdogo kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri Serikali iendelee kuwekeza kwenye kilimo kwa sehemu kubwa sana lakini pia Serikali hii iendelee kuhamasisha wawekezaji wengine hasa sekta binafsi ili iweze kuchangia kwa sehemu kubwa kwenye kuwekeza kwenye kilimo. Vinginevyo kama tukiitegemea Serikali yenyewe tu hatutafika kukamilisha kuwa na malighafi zitakazotosha kwa viwanda vile ambavyo tunategemea vianzishwe kwenye Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokuwa tukitembelea Mkoa wa Shinyanga na Mwanza tulikuta kiwanda cha nyuzi cha pale Shinyanga kinachotumia raw materials (malighafi), pamba kwa wingi kimesimamisha uzalishaji wake. Tatizo mojawapo ilikuwa ni kwamba wamepungukiwa na pamba kwenye kiwanda chao. Kwa hiyo, tuongeze uwekezaji kwenye kilimo ili tuhakikishe kwamba malighafi nyingi zitakazopatikana zinatumika kwenye viwanda vyetu ambavyo vimekwisha kuanzishwa tayari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia ni umuhimu wa umwagiliaji kwenye nchi yetu. Nimekuwa nikizungumza habari ya umwagiliaji sana, lakini ni muhimu sana kwa wakati huu kwa sababu ya mabadiliko ya tabianchi ambayo tunafahamu sasa hivi mazingira ya dunia yamebadilika, kumeongezeka joto na mambo mengine na ukame unaongezeka. Sasa tusipotia nguvu kwenye umwagiliaji tutakuwa bado tunarudi nyuma kwa sababu kilimo cha kutegemea mvua hakitoshelezi mahitaji yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha umwagiliaji kina faida nyingi, moja mkulima atalima muda wote kwa hiyo atakuwa na ajira mwaka mzima. Vilevile wawekezaji wanaokuja kuwekeza kwenye viwanda watakuwa na uhakika wa kupata malighafi wakati wote wa uzalishaji wa viwanda vyao. Pia umwagiliaji unatusaidia wakulima kwa sababu badala ya kulima mara moja utalima mara mbili ama mara tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna fursa kubwa sana kwenye suala la umwagiliaji kwenye nchi yetu. Takwimu tulizonazo zinasema tuna hekta milioni 29 zinazofaa kwa umwagiliaji lakini eneo linalomwagiliwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kutoa mchango wangu kwenye bajeti hii ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kutuletea bajeti nzuri lakini pia niwashukuru sana watendaji wao wakuu, Katibu Mkuu pamoja na timu yao hiyo nyingine iliyopo ofisini. Wamefanya kazi nzuri na wametuletea bajeti ambayo kila Mtanzania aliposikia alifurahia na alipongeza. Kwa hiyo, nawapongeza sana sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niwapongeze pia TRA kwa makusanyo yao mazuri ambayo kupitia hayo yametusaidia kufanya mambo makubwa kwa mwaka huu unaoisha na naamini hata kwa mwaka ujao tunaweza kuendelea kufanya mambo makubwa zaidi. Tumelipa mishahara sisi wenyewe, tumelipia reli sisi wenyewe, tumelipia ulinzi na usalama wa nchi yetu sisi wenyewe, tumelipia ndege ingawa watu wanazidharau lakini tumelipa sisi wenyewe, kwa hiyo imetusaidia kujitegemea kama nchi kwa kiasi kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu kwa watu wa TRA ni kwamba waweze tu kuongeza kujenga mazingira mazuri kwa walipa kodi wetu ili makusanyo yao yaweze kuongezeka. Wafanye juu chini kuwafanya walipa kodi wetu wajisike fahari kulipa kodi yao, waone kwamba wanastahili kulipa, waelewe kwamba kulipa kodi ni ustaarabu lakini wataona hivyo baada ya wao TRA pia kujenga mazingira mazuri kwa ajili yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia naomba kodi za TRA zieleweke, mtu akitaka kuanza biashara fulani ajue kabisa atatakiwa kulipa kodi zipi. Kuwe na namna za kodi elekezi ambazo TRA wanakuwa nazo ili mimi nikitaka kufanya biashara nijue TRA watachukua hela yao kiasi gani hapa. Unajua wafanyabiashara wanataka mambo yao yajulikane, yawe wazi na wanataka uhakika ili atakapoingia kwenye biashara aweze kupata faida anayoitarajia. Uchumi wetu unakua, kwa hiyo lazima pia TRA wajenge mazingira ya biashara kukua, ya kilimo kukua na uchumi wetu kuendelea kupanda vinginevyo makusanyo yao yanaweza yasiwe endelevu sana kama biashara na kilimo havikui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie pia upande wa ajira pamoja na mzunguko wa fedha, hivi vitu vina uhusianao sana. Fedha au pesa inazo tabia nyingi lakini tabia mojawapo ni kwamba pesa ni adimu, money must be scarce or limited in supply na pesa inazunguka kwa mtu ambaye anafanya kazi, pesa haizunguki tu kwa zamu kwamba ni zamu yako imefika, inazunguka kwa mtu ambaye anafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naisihi Serikali itengeneza mazingira ya watu kufanya kazi ili kwamba waweze kupata pesa. Naiomba Serikali waanze kufikiria miradi ambayo itazalisha au itatoa mazao kwa haraka, inatoa faida kwa haraka, hiyo nayo watie nguvu hapo ili kwamba watu wafanye miradi kama hiyo waweze kupata pesa. Miradi ambayo tunaita ni quick wins au low hanging fruits ili watu waweze kujiingiza huko na kupata hela mzunguko wa pesa uweze kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi kama hiyo ni kama wachimbaji wadogo, viwanda vidogo vidogo vikitiwa nguvu na moyo vinaweza vikafanya mzunguko wa fedha ukawa mkubwa kwa sababu wengi wataingia huko. Pia miradi mikubwa ya kielelezo ambayo nchi yetu imekwishakuianza iajiri Watanzania. Najua kandarasi kubwa wamepewa watu wa nje lakini tuwe na utaratibu ambao hata nadhani sheria zetu unaukubali kwamba Watanzania waajiriwe wengi kwenye miradi hii, wanaweza kuajiriwa wale watu wakubwa wakubwa kule juu kidogo lakini hapa katikati na huku chini waajiriwe Watanzania ili waweze kupata pesa iweze kuzunguka hapa nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia NGO’s zilizoko kwenye nchi yetu hii walazimishwe waajiri Watanzania. Hizi NGO’s nazo wanapokuja hapa wanalazimisha kuleta watu wao kutoka nje. Nafikiri umefika wakati sasa kazi hizo zinazofanywa kwenye NGO’s zifanywe na Watanzania kwa sababu tuna ujuzi na weledi wa kutosha kufanya kazi hizi ili pesa zinazokuja kwa sababu wanazileta kwa lengo la kusaidia umaskini wetu, basi umaskini wetu uwe ni fursa isiwe ni kitu ambacho ni balaa au kinatupita pembeni. Watanzania wengi waajiriwe kwenye hizi NGO’s kuanzia chini, katikati na hata juu ili pesa zinazokuja zizunguke hapa na zitusaidie kweli kama wanataka kuondoa umaskini kwenye nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kazi za makampuni makubwa ya hapa nchini pia yapewe kazi kubwa kubwa. Nimesikia juzi Mheshimiwa Makamu wa Rais anasema wakandarasi wanaweza wakapata kazi isiyozidi shilingi bilioni 10, nadhani hili ni jambo zuri kwa sababu hawa wakandarasi wa ndani wakipewa pesa kama hiyo itafanya izunguke hapa ndani na kufanya mazunguko wa fedha uwe mkubwa hapa nchini kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala la kukuza viwanda kwenye nchi yetu. Kwanza nipongeze kabisa hotuba ya Mheshimiwa Waziri hasa kwa upande wa viwanda vinavyozalisha mafuta ya kula kwamba wameweka tozo/ushuru kwenye mafuta ghafi yanayoingia kutoka nje hasa yanayotokana na mawese. Hongera sana kwa jambo hili kwa sababu tozo hii ilikuwa imeondolewa hapo nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba tozo hii iongezwe badala ya asilimia 10 aliyoiweka Mheshimiwa Waziri iwe asilimia 15 ili kulinda viwanda vyetu vya mafuta ya kula hapa ndani lakini pia kulinda wafanyabiashara wetu. Kwa sababu hata hayo mafuta wanayosema wanaingiza mafuta ghafi lakini ukiyachunguza asilimia ya mafuta ghafi ni kama 10 tu, asilimia 90 ya mafuta haya yako kamili kabisa. Kwa hiyo, ili tuweze kujenga viwanda vyetu, ushuru kwa bidhaa zinazotoka nje lazima uongezeke ili tuweze kulinda viwanda vyetu hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nizungumzie suala la wastaafu hasa wale wanaopata pesa zao kupitia Hazina, walio na account zao Benki ya Posta. Hawa wana dirisha la kupata mikopo huko Benki ya Posta lakini wanapoomba mikopo yao nyaraka zinachelewa sana kutoka Hazina tofauti na nyaraka au na wale ambao walikuwa kwenye Mifuko ya PSPF na LAPF.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri awafikirie hawa wastaafu maana na wenyewe bado maisha yanaendelea, kwa hiyo tuwasaidie wale wanaopata hela zao kutoka Hazina wakiomba mikopo kupitia Benki hii ya Posta wapewe mikopo yao mapema, hiki kisingizio cha nyaraka zinachelewa nadhani hakina sababu ya kuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kama muda wangu pia utakuwa haujaisha niongelee suala la …

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kurejea kidogo kwenye Kitabu cha Wakristo kinachoitwa Biblia, Kitabu Kitakatifu kwenye Kitabu cha Nehemia, Sura ya 1-4. Nehemia alianza kazi ya kujenga ukuta wa Yerusalemu. Wakati ameanza kujenga ukafika ngazi fulani walitokea watu waliokuwa wakiitwa akina Sanbalati na Tobia wakaanza kusema ukuta wenyewe anaojenga hata mbweha akipanda hapo unaanguka mara moja. Kwa hiyo, wakaanza kumdhihaki, kumdharau na mambo mengine mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu kumwambia Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Rais mwenyewe wajenge ukuta wa Yerusalemu, ni wakati wao sasa wa kujenga ukuta wa Yerusalemu bila kujali makelele yanayopigwa na akina Tobia na Sanbalati, kwa sababu wakiwasikiliza hawataweza kufanya cha maana kwenye nchi hii, lakini huu ni wakati waou Mungu amewapa wafanye kazi ambayo iko mbele yenu kwa ajili ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa maana wakiendelea kuwasikiliza hawatafanya kitu; wakinunua ndege watasema ndege yenyewe wananunua kwa cash wangekopa, wakikopa watasema wanaongeza deni la Taifa, wanaongeza mzigo kwa wananchi, wakijenga viwanda watasema viwanda vyenyewe vinavyojengwa ni mashine za kusaga unga na kadhalika, kwa hiyo, wakiwasikiliza watawatoa kwenye reli. Nawaambia viongozi wangu kwamba ni wakati wao mzuri, wajenge Taifa hili na wako kwenye mwelekeo mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Kwanza, niende kwenye huduma za jamii hasa upande wa maji. Mkoa wa Simiyu tuna mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria; leo ni kama miaka mwili mradi huu ulishapitishwa lakini mgogoro upo kwenye eneo litakalowekwa tanki kubwa ambalo litasambaza maji kwenye Mkoa wa Simiyu kuanzia Wilaya ya Bariadi, Itilima, Meatu na Maswa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahali ambapo kutajengwa tenki hilo ni mahali ambapo kuna madini ya nickel, kizungumkuti kiko hapo. Mheshimiwa Rais aliwahi kuja Mkoa wa Simiyu, akasema tenki lijengwe kwenye Mlima Ngasamo mahali ambapo mwekezaji anataka kuchimba nickel, lakini bado uamuzi wa kujenga tenki hilo haujafanyika. Sasa sielewi tumsikilize nani Mheshimiwa Rais, mwekezaji au nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasikia kibali kinatafutwa kutoka kwa Kamishna wa Madini, sasa huyu Kamishna wa Madini anakaa nchi gani kwamba ameshindwa kuandika kibali ili mkandarasi aweze kuanza? Maana najua mkandarasi alishatafutwa, amepatikana na pesa zipo lakini kazi haifanyiki leo ni kama mwaka mmoja na zaidi mradi huu haujaanza. Naomba sana mradi huu wa maji sasa uanze na kama ni kibali kinachotakiwa kutolewa kutoka kwa huyo Kamishna wa Madini, basi kifuatiliwe haraka kipatikane ili mradi uweze kuanza na sisi watu wa Mkoa wa Simiyu tuweze kupata maji yaliyo safi na salama na ya uhakika zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la huduma za kiuchumi lakini niende moja kwa moja kwenye awamu ya tatu ya Mradi ya REA. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati Mheshimiwa Kalemani pamoja na Naibu wake kwa sababu wanajitahidi sana kuhakikisha kwamba REA awamu ya tatu inafanya kazi yake kama ilivyotarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nina tatizo kidogo kwenye Wilaya yangu ya Maswa mkandarasi aliyepangwa Mkoa wa Simiyu ambaye pia yupo Wilaya ya Maswa amepewa kilomita kidogo kulinganisha na vijiji alivyonavyo. Utakuta kwenye vijiji anapokwenda kuweka umeme anaweka kitongoji kimoja kwa sababu anasema kijiji hiki nimepewa kilomita moja na nusu au kilomita mbili, kwa hiyo, inatosha kupeleka umeme kwenye kitongoji kimoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imezua ugomvi kwenye vijiji vyetu, kitongoji kimoja kinapata umeme vitongoji vinne kwenye kijiji hicho havipati umeme. Wananchi kwenye vijiji vinavyobaki wanauliza wao ni wananchi wa nchi gani? Wanauliza wao ni wananchi wa wapi mbona kitongoji kimoja tu kinapata umeme?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana mikataba hii ambayo Wizara ya Nishati wameingia na wakandarasi hawa hebu iangaliwe upya, vinginevyo itaacha ugomvi mkubwa kwenye vijiji vyetu kwa sababu maeneo machache tu yatapata umeme na maeneo mengine yatakuwa hayajapata umeme sasa inatuletea ugomvi sisi viongozi tunakuwa kama tumewabagua watu wetu. Kwa hiyo, naomba sana suala hili liweze kuangaliwa hasa kwenye REA awamu ya tatu hii inayoendelea lirekebishwe kwa haraka ili kwamba kama umeme unaenda kwenye kijiji basi uende kwenye vitongoji vyote. Hii habari ya kilomita mbili kwenye kijiji haitusaidii itatuletea ugomvi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye eneo la sekta binafsi lakini upande wa wafanyabiashara. Nashukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu amekwishakutana na wafanyabiashara wa nchi hii na kuzungumza nao kujaribu kutatua changamoto ambazo wanazo. Najua hakika ya kwamba kuanzia Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais mwenyewe wana nia nzuri kabisa na wafanyabiashara, lakini tatizo liko kwa watendaji wa Serikali katika kutekeleza maelekezo na kazi wanazotakiwa kuzifanya ili biashara ziweze kwenda kwenye nchi hii. Watendaji wa Serikali sijui hawaelewi kitu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi wafanyabiashara kutoka kwenye Wilaya yangu wanafanya biashara ya ng’ombe wanavusha ng’ombe kutoka kwetu kwenda Dar es Salaam wamefika hapa Dodoma wanasimamishwa halafu wanaulizwa leseni yenu iko wapi, leseni wanaionesha, kisha wanaulizwa mwenye leseni yuko wapi, mwenye leseni hayupo tunawapiga faini Sh.500,000. Sasa najiuliza mwenye leseni ya kupeleka ng’ombe Dar es Salaam naye apande kwenye gari ambalo limepakia ng’ombe? (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vitu ambavyo kwa kweli havieleweki kwa hawa watendaji wetu. Huyo mwenye kufanya hiyo biashara na mwenye leseni ana watu wake wanaowasafirisha wale ng’ombe na yeye mnataka apande kwenye hilo roli?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Afya.

Kwanza niwashukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii pamoja na Naibu wake kwa kutupeleka mbele kwenye suala la afya kwenye nchi yetu. Wakati tunaanza Bunge hili kulikuwa na kelele za upatikanaji wa dawa, dawa zilikuwa hazipatikani kwenye zahanati, vituo vya afya na hata hospitali zetu, lakini leo tuna asilimia kama 80.

Pia kulikuwa na kelele za upatikanaji wa dawa za chanjo wakati tunaanza Bunge hili leo hatusikii kelele hizo zikiwapo, nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake. Kiwango cha chanjo kwenye nchi yetu kimepanda mpaka asilimia 90 na kwa Afrika kama taarifa yao ilivyosema tuko watatu baada ya Rwanda na Zambia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwapongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa ujenzi wa miundombinu pamoja na upatikanaji wa vifaa na vifaa tiba. Niwashukuru sana kwa ajili ya kuniletea vifaatiba kwenye kituo changu cha afya cha Malampaka, tumepata vifaatiba vizuri vya kisasa vingi vinatosheleza pia tumepata pesa za kutosha kuweza kujenga wodi pamoja na majengo mengine, tunawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la upungufu wa watumishi wa afya sasa hivi kwenye nchi yetu ni mkubwa. Taarifa ya kamati inasema tuna upungufu wa asilimia 48, hiki ni kiwango kikubwa sana na hiki kinaenda mpaka kwenye maeneo yetu. Mkoa wa Simiyu tuna wataalam wenye ujuzi ambao wanaweza wakahudumia wagonjwa wachache sana. Kwa taarifa nilizonazo ni kwamba mwaka 2012 wakati mkoa unaanza tulikuwa na wataalam wenye ujuzi asilimia 2.6, lakini mwaka 2016 wameongezeka kidogo asilimia 4.8. Sasa ukijaribu kuangalia kiwango hiki ni kidogo sana. kwa Wilaya yangu ya Maswa ina upungufu wa watumishi wa afya 525, uhitaji ni 726 na waliopo ni 201 tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo upungufu huu ni mkubwa Sana na nilkuwa nasihi kwamba Serikali sasa iangalie tatizo hili kama tatizo kubwa linaloikumba nchi yetu na lishughulikiwe kwa pamoja Wizara ya Utumishi, Wizara ya Afya pamoja na Wizara ya TAMISEMI. Vinginevyo lishughulikiwe kama ambavyo tumeshughulikia tatizo la upatikanaji wa walimu kwa shule zetu. Suala hili lazima lifanyiwe hivyo vinginevyo watu wetu watakuwa wanaangamia kwa sababu ya kukosa huduma kwenye vituo hivi ambavyo tuna bidii kubwa ya kuviboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala lingine ambalo halijazungumzwa kabisa; kuhusu uzazi wa mpango. Uzazi wa mpango sijaona hata kwenye hotuba ya Kamati hata hotuba ya Mheshimiwa Waziri mwenyewe. Hata hivyo najaribu kuangalia kwa mbele kwamba idadi ya watu inaongezeka kwa kasi sana. Nchini mwetu sasa inakadiriwa kuwa na watu kama milioni 58 na tunavyoendelea mpaka mwaka 2022 pengine tutakuwa watu milioni sitini na kitu; na kwa kuangalia vizuri watoto watu walio chini ya umri wa miaka 15 kwenye nchi yetu ni nusu ya Watanzania. Sasa utaona Watanzania hawa watu wazima wanahudumia watu wengi kiasi gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa mchango wangu kwa Wizara hii kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni upi hasa mkakati wa Wizara kuhakikisha viwanda vyetu vya ndani vilivyojengwa, vinavyojengwa na vitakavyojengwa baadae vinalindwa ili viweze kukua na kuweza kuhimili ushindani wa viwanda vya wenzetu wa Ulaya, Asia na Amerika ambao viwanda vyao vimejiimarisha? Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri hakuna mahali popote alipotaja kulinda viwanda dhidi ya ushindani usio haki kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenye viwanda vya nguo, nyama, maziwa, nyanya na kadhalika wanalalamika juu ya ushindani usio haki unaotokana na waagizaji wa bidhaa toka nje kutolipa kodi stahiki kwa Serikali kwa sababu waagizaji hao wana-under declare ama kwa kushirikiana na watumishi wasio waaminifu wa TRA wanafanya under-valuation ya bidhaa walizoagiza na hivyo kulipa kodi isiyo stahiki. Nini nafasi ya Tume ya Ushindani katika hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukumbuke kuwa sisi bado ni nchi changa sana, tusipokuwa na mkakati wa uhalisia wa kulinda viwanda vyetu, tusahau kabisa kuwa na uchumi wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naitaka Serikali ilete mpango mkakati wa kulinda viwanda vyetu ili ndoto ya Tanzania ya viwanda iweze kukamilika na kukuza uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Waziri, lakini lazima uzingatie kulinda viwanda vyetu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Kilimo
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami pia niweze kuchangia hoja hii ya Mheshimiwa Waziri iliyo mbele yetu. Nianze kwa kusema kwamba siungi mkono hoja ikiwa suala la bei ya pamba halitakaa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unafahamu vizuri kazi ya kulima inakuwaje. Kama kazi ya kulima zawadi yake ndiyo hii tunayoipata kutoka Serikalini basi nadhani tuhamasishe watu wetu waache kulima. Mwaka jana bei ya pamba ilikuwa Sh.1,200, mwaka huu kama alivyosema ndugu yangu ni Sh.1,100 sababu hazieleweki, haijajulikana kwa nini bei imeshuka? Kuna mambo mengi hapa ambayo yanasikika, moja ni kwamba Sh.33 zinabaki sijui ushirika, Sh.12 zinaenda kuimarisha sijui Chama Kikuu cha Ushirika, Sh.55 zinaenda wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapofika kwenye masuala yanayogusa watu wengi ni muhimu sana Serikali iwe sikivu sana. Ni vuzuri tuelewane hapa, bei ya pamba kama ilivyotajwa na ndugu yangu Mheshimiwa Ndassa ndivyo ilivyo kwa nini kuondoa Sh.100 kwa wakulima? Si ingebaki angalau Sh.1,200 kama ilivyokuwa mwaka jana, kwa nini tumeiondoa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutataka majibu yaliyo sahihi, lakini jibu lililo sahihi ni kurudisha Sh.100 kwa wakulima wa pamba. Majibu mengine mbali na hayo hayataeleweka na hayaeleweki. Ndugu yangu Mheshimiwa Ndassa amesema vizuri, mazao haya makuu ya pamba, korosho na mazao mengine ni siasa kwenye nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema juu ya ununuzi wa pamba mwaka huu. Msimu wa pamba umekwisha kuanza tarehe 1 Mei, 2018 lakini hakuna tone la pamba iliyonunuliwa mpaka sasa. Kwenye Jimbo na Wilaya yangu hakuna pamba iliyonunuliwa na sababu ni kwamba, umekuja utaratibu mpya wa kununua kupitia ushirika. Ushirika ni mzuri, lakini ulifanya vibaya siku za nyuma na watu hawauamini tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa badala ya Serikali kuhangaika na mafunzo na kuwajengea uwezo watu wetu na ushirika wenyewe ili waelewe dhana mpya ya ushirika kwamba itawasaidiaje wananchi wetu, wamekuja moja kwa moja na kuiweka kwenye utekelezaji. Nadhani ni kosa kwa sababu kama watu walishauona ushirika ni mbaya unapotaka kuanzishwa upya ni muhimu sana kuwaelimisha wananchi waweze kuelewa. Kwa hali ilivyo mimi sijui tutaishia wapi msimu huu wa pamba kwa sababu kama pamba haijanunuliwa, haijaenda kwenye ghala la ushirika, sasa sijui itaenda lini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo hayo utaratibu uko hivi, pamba ikusanywe kwenye ghala la ushirika, ghala lenyewe la ushirika kwenye kijiji liko moja na kijiji kina vitongoji zaidi ya kimoja, vitatu, vinne hadi vitano na vingine viko mbali, lakini wakati wa ununuzi wa watu binafsi pamba ilikuwa inanunuliwa mahali karibu na mwenye pamba, maghala yalikuwa mengi. Sasa safari hii ghala liko moja na mahali pengine maghala hayo ya ushirika yaliyopo yamechakaa hayana hadhi ya kuhifadhi pamba, sijui tutafanyaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tatizo lingine kuna utaratibu wa wakulima kulipwa pesa yao kupitia benki. Kwa nini iwe ni lazima? Nafikiri suala la kulipwa kupitia benki ni zuri kama ni kwa hiyari, kwa sababu hii pesa ni ya mkulima. Mimi nauza pamba yangu leo, nina mgonjwa, nina matatizo mtoto wangu hajaenda shule sijanunua uniform za shule, halafu nipeleke pamba yangu nisubiri siku mbili, tatu, nne bado sijalipwa. Halafu ikilipwa niende benki iliyo Makao Makuu ya Wilaya kilometa mia moja na kitu, saa ngapi nakamilisha mahitaji yangu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili linapaswa kuangaliwa vizuri. Halafu ushirika unafanyika kama wakala, wao wanakusanya pamba ya mkulima halafu mnunuzi anakuja pale na pesa yake au pesa yake anawapa watu wa ushirika. Hivi kuna mnunuzi gani binafsi atapeleka pamba yake kwa mshirika ambaye anajulikana alikuwa …

TAARIFA . . .

MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naikubali kabisa taarifa yake. Kwa sababu hao viongozi waliochaguliwa nina habari wengine wametoa rushwa sijui kwa kutarajia kupata kitu gani. Kwa hiyo, ni walewale waliokuwa wameharibu ushirika kule nyuma ndiyo wamerudi.
(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini pamba haijapelekwa sokoni mpaka leo ni kwa sababu wanunuzi na wenyewe wamerudisha mikono nyuma kwa sababu hawana imani na watu wa ushirika waliopewa dhamana ya kuchukua pamba na pesa kwa wanunuzi. Mnunuzi huyu atamwaminije mtu ambaye hajamchagua? Atamwaminije ampe bulungutu la mamilioni ya pesa eti amnunulie pamba wakati hamjui? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama utaratibu wa kununua uko hivyo basi wanunuzi binafsi wapeleke watu wao kwenye gulio pamba ilipo, muuzaji aje pale auze pamba yake alipwe hela yake aondoke lakini mtu atakayekuwepo pale ni yule aliyeaminiwa na mnunuzi wa pamba. Vinginevyo ushirika tuendelee kuujenga upya bado haujapokelewa vizuri kwa sababu ya historia yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya pamba kuwa chini inasababishwa na vitu vingi mojawapo ni soko la hapa ndani ni dogo sana. Takwimu zinaonesha asilimia 20 mpaka asilimia 30 ndiyo tunaweza kutumia hapa ndani. Viwanda vyetu vya pamba vinashindwa kushindana kwa sababu ya ushindani usio haki wa nguo nyingi kutoka Uchina, Malaysia, Uturuki na mahali pengine. Sasa tutapandishaje mazao ya wakulima wetu nchi hii kama hatulindi viwanda vilivyoko kwenye nchi hii? Viwanda vya nchi hii havilindwi vinaachwa tu na wakati mwingine vinashindanishwa na mtu ambaye ana nguvu kuliko yeye, lazima vitakufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka huu zao la pamba limelimwa kwa wingi sana. Tunamshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu hata Mheshimiwa Waziri wa Kilimo mweyewe kwa kuhamasisha hivyo, lakini wakulima wetu wamelima pamba hii kwa taabu sana na ndiyo maana nasema kama bei ya pamba hairudi Sh.1,200 siwezi kuunga mkono hoja hii.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kutoa mchango wangu kuhusiana na hoja hii iliyoko mbele yetu.

Kwanza kabisa napenda niwapongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri ambayo wanafanya kwenye Wizara hii ya Fedha. Nimegundua kwamba Waziri wa Fedha kwenye nchi kama ya kwetu ni kazi kweli kweli lakini Mheshimiwa Waziri na Naibu wake pamoja na watalaam wake wanajitahidi sana kufanya kazi ili kuonesha kwamba Taifa hili na nchi hii tunataka kwenda mahali, hongereni sana Mheshimiwa Waziri. Utapata majina mengi sana, bahili, msimamo mkali na mambo mbalimbali, lakini ninavyojua Waziri wa Fedha lazima awe bahili na lazima awe na msimamo vinginevyo mambo hayatakwenda. Hawezi kuwa Waziri wa Fedha ambaye ni Waziri anayegawa gawa tu, Waziri anayetewanywa tu, haiwezekani. Kwa hiyo, hongereni sana na endeleeni kuchapa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja iliyo mbele yetu ambayo naiunga mkono, nilikuwa najaribu kuangalia mambo ambayo yameandikwa humu, nataka nizungumze mambo machache tu.

Mheshimiwa Spika, kipengele cha kwanza ambacho nakiona ni nakisi ya bajeti yetu. Kwenye kitabu chako Mheshimiwa Waziri umesema mwaka 2016/2017 nakisi ya bajeti yetu ilikuwa asilimia 1.5, lakini mwaka 2017/2018 nakisi ya bajeti yetu imeongezeka imefika aslimia 2.1. Sasa kuongezeka kwa nakisi hii siyo kuzuri sana, labda niseme tu kwamba nakisi ya bajeti inapoongezeka maana yake ni kwamba matumizi ya Serikali ni makubwa kuliko kipato chake maana yake tuna kipato kidogo, matumizi yetu ni makubwa.

Mheshimiwa Spika, sasa kama matumizi ni makubwa maana yake Serikali, lazima itafute namna ya kufidia pesa zilizopungua na namna mojawapo ambayo Serikali huwa wanafanya ili kufidia pesa zilizopungua ni kukopa kwenye benki zetu. Sasa nakisi ikiwa kubwa maana yake Serikali italazimika kukopa kwenye mabenki au maeneo mengine lakini hasa kwenye benki. Sasa Serikali ikienda kukopa kwenye benki maana yake inaanza kushindana na sekta binafsi kukopa na wakishinadana hawa watu tunajua matokeo yake.

Mheshimiwa Spika, riba ya benki itapanda lakini pia kwa sababu Serikali ni mkopaji mzuri, kuna uwezekano mkubwa kabisa sekta binafsi ikapata pesa kidogo za kukopa kutoka kwenye benki. Sasa kama engine ya uchumi wetu ni sekta binafsi na Serikali inakopa kiasi kikubwa kutoka kwenye benki. Utakuta kwamba mitaji ya sekta binafsi itapungua kwa hiyo, uwekezaji kwa ujumla utapungua kwa sababu watu binafsi hawawezi kukopa kutoka benki zetu kwa sababu wanashindana na Serikali iliyo na urahisi wa kukopa kwa sababu inaaminika zaidi.

Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana kwamba suala la nakisi ya bajeti yetu Mheshimiwa Waziri uliangalie namna linavyokuwa na inawezekana kwa viwango inavyotakiwa haijawa kubwa sana lakini kama litaendelea kukua, nakisi hii itaendelea kukua, italeta shida huko baadae. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la Ofisi ya Mipango ambalo limezungumziwa pia na wenzangu wengine. Ofisi ya Mipango ni ya muhimu sana kwenye Wizara ya Fedha lakini wenzangu na sisi kwenye Kamati tumependekeza ni vizuri ikiwa chini ya Rais. Ninavyojua ni kwamba mipango inatangulia haya mambo ya bajeti kwa sababu bajeti maana yake unaweka pesa kwenye mipango sasa kama mipango tutaipa kisogo, nashindwa kuelewa kama tunaweza kuwa na bajeti zilizo nzuri au zilizo sawa sawa. Kwa hiyo, ninasihi kabisa kwamba Ofisi ya Mipango na lile Fungu la Mipango Namba 66 ni vizuri likarudishwa, ili ya kwamba tuwe na Ofisi ya Mipango iliyo imara, Ofisi ya mipango ambayo ni forward looking itakuwa inaona mambo kwa mbali ya nchi yetu kuliko tukiwa tu na kaofisi kamipango ambako kamefichwa mahali na pengine hakana autonomize sana.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilikuwa naomba kwamba, ofisi ya Mipango na fungu lake likae sawasawa na kama tulivyopendekeza basi ibaki Ofisi ya Rais ili tuwe na mipango iliyo sawa sawa na kwamba baada ya kuwa na mipango sasa tunaweza kuwa na bajeti zinazotabirika na tunaweza kuwa na shughuli ambazo zinaeleweka. Lakini tukiweka nguvu tu kwenye matumizi au kukusanya kodi sasa pesa tukizipata tunazipeleka wapi? Maana hatuna mipango ambayo imewekwa sawa sawa.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la tatu la malipo kwa watoa huduma na wakandarasi. Wenzangu pia wamelizungumzia suala hili kwa kweli lina shida kidogo hasa kwenye malipo yake. Kuna ukawizaji mkubwa sana wa kulipa watoa huduma na wakandarasi hasa wa ndani na hii ina athari kubwa tu, hasa wa ndani. Ninaelewa umuhimu wa kuhakiki madeni hasa yanapofika kuwa ni madeni ya muda mrefu, ni muhimu sana kuyahakiki kama Wizara nawapongeza ni sawa myahakiki kwa sababu lazima ujiridhishe na kile unacholipa.

Mheshimiwa Spika, wazungu wanasema in God we trust, in money we audit. Kwa hiyo, lazima tuhakikishe malipo yanayolipwa yanaridhisha, yana thamani ya pesa tunazotaka kulipa. Kwa hiyo, juu ya suala la uhakiki mimi nawaunga mkono kabisa, lazima mhakiki kabla hamjalipa malipo. Lakini tuwalipe basi hao watu baada ya kuhakiki. Maana sasa huu uhakiki unapochukua baada ya mwaka mmoja, miaka miwili kwa kuwa unakuwa uhakiki ambao hauaminiki aminiki au na wahakiki hawa basi na wenyewe wapelekewe wahakiki wengine kwa sababu vinginevyo kwa kweli watu haturidhiki kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia namna tunavyolipa haya madeni ya wakandarasi na watoa huduma. Kwa nini tusilipe watoa huduma na wakandarasi wengi angalau, badala ya kumlipa mtu mmoja, mkandarasi mmoja mnalipa bilioni 200 na pengine huyo mkandarasi ana ushirika na mtu wa nje, sehemu kubwa pesa inatoroka kwenda nje haizunguki hapa ndani.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Spika, nami nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili kuweza kutoa mchango wangu kwenye hoja hii iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, pamoja na Naibu wake pia niwapongeze Watendaji walioko ofisini kwao, Katibu Mkuu pamoja na wote walioko ofisini kwa kufanya kazi kwa juhudi kubwa na hatimaye kutuletea bajeti ambayo ni nzuri kwa kweli na ni bajeti ambayo inaleta matumaini makubwa kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, bajeti hii ni nzuri kwa sababu moja imeweka vizuri kodi ambazo zilikuwa zinasumbua hasa wakati huu tunapotaka kujenga uchumi wa viwanda. Hakuna kodi iliyoongezeka kuzidi kiwango hata mahali ambapo kodi zimeongezeka na hasa wazalishaji wetu wa ndani, bajeti hii imewaangalia vizuri kwa kweli. Wasiwasi wangu tu ni huu utambulisho wa electronic tax stamp, sijaelewa sawasawa kama kweli haina matokeo ambayo ni hasi kwa mlaji na wazalishaji. Tutajifunza huko mbele, tutaona pengine haitakuwa na matokeo haya. Lakini vinginevyo kama ina matokeo chanya basi tutakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuzungumzia mapato yetu ya ndani. Mapato yetu ya ndani yanaendelea kuongezeka lakini ongezeko kubwa liko kwenye kodi. Mapato yasiyotokana na kodi bado ni madogo sana, bajeti iliyopita kutokana na hotuba hizi zilizosomwa hapa, mapato yasiyo ya kodi ilikuwa trilioni 1.7 na mwaka huu ambao bajeti yake tunaijadili mapato yasiyotokana na kodi yanakadiriwa yatakuwa trilioni 2.16. Sasa kitakachokusanywa bado hatuelewi.

Mheshimiwa Spika, mapato haya siyo makubwa sana na mapato haya yanatakiwa kuwa makubwa kwa sababu ni lazima sasa yaweze ku-supplement mapato yanayotokana na kodi. Mapato yanayotokana na kodi bado ni madogo kwa sababu uchumi wetu unatawaliwa na sekta isiyo rasmi kubwa sana, kwa sababu sekta isiyo rasmi ni kubwa basi hatupati kodi ya kutosheleza huko. Sasa lazima tutafute namna ya kongeza mapato yasiyo ya kodi. Tunaweza kuyaongeza kwa namna mbili tu ambazo napendekeza hapa.

Mheshimiwa Spika, moja ni kufanya Ofisi ya TR isimamie vizuri makampuni na taasisi za Serikali ambazo zinazalisha. Kusema ukweli TR anatakiwa awezeshwe kiasi cha kutosha kabisa ili aweze kusimamia vizuri mahali ambapo Serikali ina stake, kwenye kampuni ambazo Serikali ina stake, TR asimamie vizuri kuhakikisha tunapata mapato ya kutosha kule. Pia taasisi zingine na ikiwezekana taasisi ambazo hazizalishi au ni mzigo kwa Serikali basi tuweze kuondokana nazo, kwa nini kuendelea kuzipa ruzuku, kuendelea kuzipa pesa wakati hazizalishi na haziongezi mapato yoyote kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jambo la pili ambalo kama nchi tumeendelea kulizungumza kwa muda mrefu, suala la uvuvi kwenye Bahari Kuu. Inasemekana tunapoteza shilingi trilioni moja kila mwaka kwa sababu ya kutoweka maanani uvuvi kutoka kwenye Bahari Kuu. Sasa Serikali imekuwa na maelezo tofauti kwamba wanafanya upembuzi yakinifu ili kutengeneza bandari ya uvuvi, lakini huu mwaka ni wa tatu niko kwenye Bunge lako bado upembuzi yakinifu unaendelea.

Mheshimiwa Spika, sasa nadhani umefika wakati kwamba sasa tuanze uvuvi wa Bahari Kuu ili utusaidie kutuongezea mapato yasiyo ya kodi. Vinginevyo tutaendelea kuimba wimbo wa namna hii, bado tutakuwa na mapato chini tutakuwa na mapato duni na hivyo tunapotaka kufika 2020 au 2025 tuwe na uchumi wa kati itatuchelewesha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la pili, suala la maji. Suala la tozo ya maji kwenye mafuta. Suala la maji ni muhimu sana kwenye nchi yetu kwa sababu mbili pia. Kwanza maji tunayataka sisi kama binadamu kwa matumizi yetu mbalimbali, lakini pia maji tunayataka kwa ajili ya kilimo chetu. Kilimo chetu kwa sababu ya kutegemea mvua kimekuwa kilimo cha chini, kimekuwa kilimo ambacho hatuna uhakika hata tukilima kama tunaweza kuvuna. Tukiweka nguvu kubwa kwenye maji tuna uhakika na kilimo na tuna uhakika wa kuwapatia watu wetu maji ambayo wanahangaika usiku na mchana mahali pengi.

Mheshimiwa Spika, mimi natoka kijijini kabisa, kijiji changu tunachota maji kilomita saba kwenda, kilometa saba kurudi. Sasa suala la maji ni suala kubwa na ni suala muhimu sana kwenye nchi yetu. Tuliomba Serikali iongeze shilingi 50 kwenye maji. Serikali inasema haiwezi kuongeza kwa sababu itaongeza mfumuko wa bei. Mfumuko wa bei unaoongezwa na mafuta ni wakati mafuta yamepanda bei huko tunakoyanunua, lakini kwa muda wa miaka miwili sasa na huu ni wa tatu nadhani, mafuta hayajaweza kupanda sana kwenye soko la dunia kiasi kwamba yakipanda, pengine tukiyanunua kwa gharama ya juu kule hapa tutajiletea inflation (mfumuko wa bei) imported inflation, lakini mafuta hayajapanda sana huko kwa wenzetu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Spika, nami nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili kuweza kutoa mchango wangu kwenye hoja hii iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, pamoja na Naibu wake pia niwapongeze Watendaji walioko ofisini kwao, Katibu Mkuu pamoja na wote walioko ofisini kwa kufanya kazi kwa juhudi kubwa na hatimaye kutuletea bajeti ambayo ni nzuri kwa kweli na ni bajeti ambayo inaleta matumaini makubwa kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, bajeti hii ni nzuri kwa sababu moja imeweka vizuri kodi ambazo zilikuwa zinasumbua hasa wakati huu tunapotaka kujenga uchumi wa viwanda. Hakuna kodi iliyoongezeka kuzidi kiwango hata mahali ambapo kodi zimeongezeka na hasa wazalishaji wetu wa ndani, bajeti hii imewaangalia vizuri kwa kweli. Wasiwasi wangu tu ni huu utambulisho wa electronic tax stamp, sijaelewa sawasawa kama kweli haina matokeo ambayo ni hasi kwa mlaji na wazalishaji. Tutajifunza huko mbele, tutaona pengine haitakuwa na matokeo haya. Lakini vinginevyo kama ina matokeo chanya basi tutakwenda vizuri.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuzungumzia mapato yetu ya ndani. Mapato yetu ya ndani yanaendelea kuongezeka lakini ongezeko kubwa liko kwenye kodi. Mapato yasiyotokana na kodi bado ni madogo sana, bajeti iliyopita kutokana na hotuba hizi zilizosomwa hapa, mapato yasiyo ya kodi ilikuwa trilioni 1.7 na mwaka huu ambao bajeti yake tunaijadili mapato yasiyotokana na kodi yanakadiriwa yatakuwa trilioni 2.16. Sasa kitakachokusanywa bado hatuelewi.

Mheshimiwa Spika, mapato haya siyo makubwa sana na mapato haya yanatakiwa kuwa makubwa kwa sababu ni lazima sasa yaweze ku-supplement mapato yanayotokana na kodi. Mapato yanayotokana na kodi bado ni madogo kwa sababu uchumi wetu unatawaliwa na sekta isiyo rasmi kubwa sana, kwa sababu sekta isiyo rasmi ni kubwa basi hatupati kodi ya kutosheleza huko. Sasa lazima tutafute namna ya kongeza mapato yasiyo ya kodi. Tunaweza kuyaongeza kwa namna mbili tu ambazo napendekeza hapa.

Mheshimiwa Spika, moja ni kufanya Ofisi ya TR isimamie vizuri makampuni na taasisi za Serikali ambazo zinazalisha. Kusema ukweli TR anatakiwa awezeshwe kiasi cha kutosha kabisa ili aweze kusimamia vizuri mahali ambapo Serikali ina stake, kwenye kampuni ambazo Serikali ina stake, TR asimamie vizuri kuhakikisha tunapata mapato ya kutosha kule. Pia taasisi zingine na ikiwezekana taasisi ambazo hazizalishi au ni mzigo kwa Serikali basi tuweze kuondokana nazo, kwa nini kuendelea kuzipa ruzuku, kuendelea kuzipa pesa wakati hazizalishi na haziongezi mapato yoyote kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jambo la pili ambalo kama nchi tumeendelea kulizungumza kwa muda mrefu, suala la uvuvi kwenye Bahari Kuu. Inasemekana tunapoteza shilingi trilioni moja kila mwaka kwa sababu ya kutoweka maanani uvuvi kutoka kwenye Bahari Kuu. Sasa Serikali imekuwa na maelezo tofauti kwamba wanafanya upembuzi yakinifu ili kutengeneza bandari ya uvuvi, lakini huu mwaka ni wa tatu niko kwenye Bunge lako bado upembuzi yakinifu unaendelea.

Mheshimiwa Spika, sasa nadhani umefika wakati kwamba sasa tuanze uvuvi wa Bahari Kuu ili utusaidie kutuongezea mapato yasiyo ya kodi. Vinginevyo tutaendelea kuimba wimbo wa namna hii, bado tutakuwa na mapato chini tutakuwa na mapato duni na hivyo tunapotaka kufika 2020 au 2025 tuwe na uchumi wa kati itatuchelewesha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la pili, suala la maji. Suala la tozo ya maji kwenye mafuta. Suala la maji ni muhimu sana kwenye nchi yetu kwa sababu mbili pia. Kwanza maji tunayataka sisi kama binadamu kwa matumizi yetu mbalimbali, lakini pia maji tunayataka kwa ajili ya kilimo chetu. Kilimo chetu kwa sababu ya kutegemea mvua kimekuwa kilimo cha chini, kimekuwa kilimo ambacho hatuna uhakika hata tukilima kama tunaweza kuvuna. Tukiweka nguvu kubwa kwenye maji tuna uhakika na kilimo na tuna uhakika wa kuwapatia watu wetu maji ambayo wanahangaika usiku na mchana mahali pengi.

Mheshimiwa Spika, mimi natoka kijijini kabisa, kijiji changu tunachota maji kilomita saba kwenda, kilometa saba kurudi. Sasa suala la maji ni suala kubwa na ni suala muhimu sana kwenye nchi yetu. Tuliomba Serikali iongeze shilingi 50 kwenye maji. Serikali inasema haiwezi kuongeza kwa sababu itaongeza mfumuko wa bei. Mfumuko wa bei unaoongezwa na mafuta ni wakati mafuta yamepanda bei huko tunakoyanunua, lakini kwa muda wa miaka miwili sasa na huu ni wa tatu nadhani, mafuta hayajaweza kupanda sana kwenye soko la dunia kiasi kwamba yakipanda, pengine tukiyanunua kwa gharama ya juu kule hapa tutajiletea inflation (mfumuko wa bei) imported inflation, lakini mafuta hayajapanda sana huko kwa wenzetu.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Mimi labda nianze kwa kusema machache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, sisi kama nchi lazima tufikirie kujitegemea zaidi hapa ndani kwetu kuliko kutegemea watu wengine. Wakati wa kuanza kufikiria kujitegemea ni wakati huu. Sasa kama fikra zetu bado zitaendelea kudhani kwamba kuna mtu atatusaidia ili kama nchi tuweze kusonga mbele kimaendeleo mawazo hayo hayapo kwa ulimwengu wa sasa. Kwa sababu hata waliokuwa wakitusaidia na kutuonea huruma zamani mazingira yao yamebadilika sana. Yamebadilika kwa kiasi kikubwa na wao wakati huu wanaanza kufikiria nani atawasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kwamba lazima tuanze kuwaza kujitegemea wenyewe badala ya kufikiria kwamba kuna mtu atatusaidia kututoa hapa tulipo. Ukisikiliza mazungumzo yanayosemwa bado tunafikiri sana kwamba labda tuko miaka ya 1970, miaka ya 1980, wakati ambapo tulikuwa tunalelewa tu mpaka asilimia 60 ya bajeti zetu zilikuwa zinategemea misaada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nakumbuka wakati Mzee Mwinyi anachukua madaraka nchi ilikuwa kwenye hali isiyo nzuri, mbaya. Mzee Mwinyi alitoa hotuba wakati fulani akasema, baada ya kupata urais nimekuta kwenye chungu cha Hazina hakuna kitu. Sasa nimejaribu kutembea Ujerumani, Marekani na nchi mbalimbali kote huko wananiambia nenda kakubaliane na IMF au World Bank.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unaweza kuona ni kwa namna gani ikiwa unataka kusaidiwa kila wakati masharti utakayoongezewa, utakayopewa ili uyatimize kupata huo msaada ni masharti ya namna gani. Sasa katika dunia ya leo masharti yameongezeka zaidi, zaidi ya kukubaliana na World Bank, zaidi ya kukubaliana na IMF, kuna masharti mengine ambayo hayaruhusu kabisa tabia, mienendo na tamaduni za Kitanzania. Sasa tukiendelea kufikiria kwamba lazima tu tusaidiwe ili tutoke hapa tulipo basi mimi nachelea kusema inawezekana tukaamua kuuza uhuru wetu, uhuru unaotunza utamaduni wetu, uhuru unaotunza mienendo na desturi na mila zetu, tukauza ili tupate hiyo misaada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, misaada tunaihitaji, lakini iwe katika misingi ile inayokubalika katika utamaduni na mila zetu, ndiyo maana hata kwenye kipindi tunachokijadili, kwenye taarifa hii, bado kuna misaada tuliyopata kutoka kwa wasamaria wema, misaada ambayo haikuambatana na masharti ambayo ni hasi kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye ukurasa wa 29 wa taarifa ya Kamati ya Bajeti tulitarajia tungeweza kupata misaada ya trilioni 2.6, lakini tulipata bilioni 878. Mimi niseme kama tulipata misaada ya namna hii basi ndiyo misaada iliyokuwa haina masharti ya kutufanya tuuze uhuru wetu, tulipata, si kwamba hatukupata kabisa kama wenzetu wanavyoweza kusema. Misaada tunapata, lakini ni ile ambayo wanakubaliana na masharti yetu sisi pia, sio tu tuuze kila kitu, tukubali kila kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu habari ya mikopo hiyo kila mtu anakopa. Mtu binafsi anakopa, nchi inakopa na unakopa kwa kulinganisha na hali yako ya kulipa. Sasa ukiona hali yako ya kulipa haiendi sawasawa basi unakwepa huo mkopo kwa hiyo, kama nchi kwa kweli, lazima tufikirie kujitegemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi niseme tu kwamba ninamuunga mkono sana Mheshimiwa Rais anaposema tujitegemee, lazima Watanzania tuamue kujitegemea. Anasema tutaumia kidogo, lakini tutakwenda. Kwa hiyo, ni lazima tukubali na sisi ndani ya Bunge lako ndio watu wanao…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa…

MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na Naibu wake kwa utumishi wao wa unyenyekevu, kujituma na usikivu katika kutekeleza majukumu yao. Nimpongeze sana pia Mheshimiwa Rais kwa kutoa kipaumbele cha juu kabisa kwenye suala la elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa Mheshimiwa Waziri kunitengea fedha za kukarabati upya Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Malampaka. Naomba sasa ramani za majengo yatakayokarabatiwa zipelekwe kwenye Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Malampaka ili ujenzi na ukarabati uanze mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshasubiria kwa muda mrefu sasa ramani hizi hazikamiliki na sababu ya kweli ya kuchelewesha ramani hizi bado haijajulikana. Naomba sana mchakato huu uharakishwe ili ukarabati wa chuo hiki uweze kuanza na hatimaye kuwafaidisha wananchi wa Maswa na Jimbo la Maswa Magharibi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na naomba kuwasilisha.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Spika, niipongeze sana Wizara hii na Mheshimiwa Waziri kipekee na Naibu Mawaziri wake kwa kazi nzuri wanayofanya ili kuunganisha nchi yetu kwa barabara, reli na kimawasiliano, hongereni sana.

Mheshimiwa Spika, barabara yangu ya Ikungu - Malampaka ilitengewa bajeti ya shilingi milioni 800 ili iweze kujengwa kwa kiwango cha lami mwaka wa fedha 2018/ 2019 lakini ujenzi huu haujaanza mpaka leo. Katika bajeti ya 2019/2020, Wizara imetenga shilingi milioni 300 kwa ajili ya barabara hii. Je, ni lini sasa barabara hii itaanza kujengwa ikiwa tumebakia na mwezi mmoja tu mwaka wa fedha 2018/ 2019 uishe? Barabara hii ni muhimu sana kwa ajili ya kuunganisha na bandari kavu ya Malampaka ambayo itakuwa ni lango la bidhaa na biashara kwa Mikoa ya Simiyu, Mara na maeneo ya Kenya.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami ulilenga kuboreshwa kwa barabara na kurahisisha usafiri ili uwe wa haraka zaidi na kufanya watu na usafirishaji mizigo ifike mapema zaidi na hatimaye kuchochea shughuli za uchumi ziende kwa kasi zaidi. Cha kushangaza muda wa kusafiri kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza umebaki kuwa ni uleule kama wakati ule ambapo barabara hazikuwa za lami. Mabasi yalikuwa yanatoka saa 11.00 alfajiri Dar es Salaam kabla ya lami na kufika Mwanza saa 5.00 au saa 6.00 usiku. Sasa tuna barabara za lami lakini muda unaotumika kwa mabasi kusafiri bado ni uleule na wakati mwingine ni zaidi.

Mheshimiwa Spika, sasa barabara za lami zimetusaidiaje ikiwa hazijapunguza muda tuliokuwa tunapoteza barabarani? Ni shughuli ngapi za kiuchumi zinachelewa? Ni fedha kiasi gani zinapotea kwa kupoteza muda barabarani? Wizara hii inafanya kazi nzuri lakini tafuteni ufumbuzi wa tatizo hili.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi pia niweze kuchangia Wizara hii ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais, kwa kuwa na ndoto kubwa ya Tanzania ya Viwanda ifikakapo 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niwapongeze Mheshimiwa Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kutafsiri ndoto hii vizuri kwa watendaji wa Serikali walioko chini yao. Kwa kweli, mambo yakienda hivi, tunaweza kufikia ndoto hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nizungumze mambo machache tu ambayo Serikali lazima iyaangalie tunapotaka kufikia ndoto hii ya Tanzania ya Viwanda ifikapo mwaka 2025. Hatuwezi kuwa na viwanda imara ikiwa hatuwezi kuvilinda. Viwanda vinavyoanzishwa kwenye nchi yetu lazima vilindwe. Hakuna nchi ambayo imetamani kuwa nchi ya uchumi wa viwanda, halafu ikaviacha viwanda vyake bila kuvilinda kwa sababu vingeweza kufa. Hivyo hivyo, nasi kama nchi, lazima tuwe na juhudi za makusudi kulinda viwanda vyetu ili viweze kusimama, kukua na kuimarika. Vinginevyo tusipovilinda, itakuwa ngumu kufikia ndoto ya Mheshimiwa Rais ya Tanzania ya Viwanda mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba tunaweza kuvilinda viwanda vyetu kwa njia za kikodi na utawala. Tusipofanya hivyo, nimesema Tanzania ya Viwanda hatuwezi kuipata haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda vyetu vingi vimeanzishwa lakini havifanyi kazi kwa uwezo wake kamili. Tulikuwa na viwanda vya nguo 33 mwaka 1992 lakini leo tuna viwanda vitano vinavyofanya kazi lakini navyo kwa chini ya kiwango. Ni kwa sababu viwanda hivi vimeachwa wazi vishindane na mabwana wakubwa walioanzisha viwanda vya nguo muda mrefu kama India, China, Uturuki na nchi zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bila kulinda viwanda vyetu vya nguo itakuwa ni ngumu, lakini tukivilinda viwanda hivi, vinaweza vikatupatia ajira kwa wakulima wetu, ajira kwa watu wetu, kwa maana ya wafanyakazi viwandani lakini pia vinaweza vikaongeza kipato kwa ajili ya taifa letu kwa maana ya kulipa kodi. Tusipofanya hivyo hatutafanikiwa kabisa (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimejaribu kuona namna alivyotoa hotuba yake Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, sijaona kama kuna sera makusudi ya kulinda viwanda vyetu ili viweze kukua. Kwa namna vilivyo sasa hivi, viko kwenye kiwango cha chini sana, ni viwanda ambavyo tunaweza kuviita ni vichanga. Sasa tukivi-expose kwenye mashindano haya makubwa, havitaweza kukua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hotuba ya Waziri, amesema viwanda vyetu vya chuma vina uwezo wa kuzalisha tano milioni moja, lakini vinazalisha tani laki mbili na arobaini, mwisho hapo. Sasa tatizo ni nini? Tatizo ni kwamba vinashindanishwa na viwanda vya chuma vilivyostawi na kuimarika muda mrefu vya Wachina.

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda hivi visipolindwa, haviwezi kukua na vikiendelea kufanya kazi kwa uwezo wa chini namna hii, gharama zake ni kubwa, matokeo yake wananchi wetu wanaendelea kununua nondo na vifaa vingine vya chuma kwa bei ya juu. Lazima tulinde viwanda vyetu, lazima tuvilinde viwanda vya nguo, chuma na viwanda vinavyoinukia sasa hivi. Tusipofanya hivyo, kuwa na Tanzania ya Viwanda, itakuwa ni ndoto 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia vivutio vya uwekezaji kwenye viwanda. Vivutio hivi vya uwekezaji kwa viwanda, lazima vile vinatabirika. Mwaka jana tulipitisha sheria kuvilinda viwanda vinavyozalisha madawa, ni jambo zuri sana, lakini tusiishie kulinda viwanda vinavyozalisha madawa tu lazima twende pia kwenye viwanda vingine. Lazima tuweke vivutio vinavyoeleweka, vinavyotabirika, vitakavyokuwa vya muda mrefu ili hawa wawekezaji watakapokuja hapa ndani, wawe na uhakika ya kwamba vivutio hivi vitakuwa ni vya kudumu na hivyo wanaweza wakafanya biashara hapa ndani vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye suala la Mradi wa Mchuchuma na Liganga. Mradi huu wa Mchuchuma na Liganga ni wa muda mrefu sana. Kwa kweli niungane na wengine wote waliosema kwamba imechukua muda mrefu na inabidi sasa juhudi za makusudi zifanyike ili tuwe na mradi huu mapema iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka kutoa tahadhari…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, kengele ya pili imeshagonga.

MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, muda ni mdogo sana. (Makofi)
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasoi ili niweze kuchangia mapendekezo pamoja na muongozo wa Mpango wetu wa Mwaka wa 2020/2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ambayo tuanajadili kwenye kikao chako hiki ni mapendekezo ambayo yamepitia pia kwa wadau wengine na kupitia hatua mbalimbali hatimaye kuja kwenye Kamati ya bajeti lakini pia mwishoni yamekuja kwenye Bunge lako hili Tukufu ili pia Waheshimiwa Wabunge waweze kutoa mapendekezo yao ili kuboresha mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa mwaka 2020/2021. Kwa hiyo, hapa tunajielekeza kwenye kuboresha mapendekezo haya na kupendekeza mambo mengine ambayo Waheshimiwa Wabunge wanadhani kwamba ni muhimu yakawemo ndani ya mpango wa maendeleo wa Mwaka unaokuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha pili ni mwongozo; tunaoujadili ni mwongozo huo wa mapendekezo na mwongozo unatoa tu muelekeo kwa namna gani Wizara, Taasisi na Mashirika ya umma, halmashauri zetu na watu wengine wa Serikali wanaongozwa katika kupanga, katika kubajeti, katika kutekeleza na kufuatilia na hatimaye kutoa taarifa kwa mipango watakayoitekeleza mwakani. Nilitaka nianze na huo ufafanuzi ili kwamba tuweze kuelewana tunapokwenda pamoja na Waheshimiwa Wabunge. Kwa hiyo, hapa hatujadili mpango wenyewe haujafika ni mapendekezo.

Mheshgimiwa Mwenyekiti, sasa nizungumze mambo machache ambayo naamini na ni mawazo yangu. Mengine tumeyazungumza kwenye Kamati ya bajeti lakini mengine ni mawazo ambayo ninadhani pia ni muhimu kuyazungumza mbele ya Bunge lako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni changamoto ya mzao yetu ya kilimo; nakumbuka mwaka jana tulikuwa na changamoto ya masoko ya zao la korosho mpaka Mheshimiwa Rais aliingilia kati, Korosho zikaanza kununuliwa, zikanunuliwa lakini zikakaa muda mrefu bila kuuzwa nje ya nchi mahali ambapo tunauza kwa wingi ikiwa ghafi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna changamoto ya zao la pamba mwaka huu; mwaka huu pia tumepata changamoto hiyo kwasababu soko la pamba kwenye soko la Kimataifa lilianguka kwa hiyo bei ikawa ya chini lakini bado tunaishukuru Serikali kwasababu iliweka bei ambayo ingekuwa na faida kwa wakulima sasa kukatokea kutoelewana hapo kati ya wakulima pamoja na wanunuzi wa zao hilo la pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna changamoto hapa kubwa ya masoko ya mzao yetu. Nilikuwa naomba kwamba katika mapendekezo ya mpango huu, hebu Serikali ijielekeze katika kutatua changamoto hii. Tunapozungumza bado kuna wakulima wa pamba hawajalipwa pamba yao kwenye maeneo mengi ya maeneo wanayolima pamba. Sasa tatizo ni soko la zao hilo sasa ni muhimu sasa Serikali ikachukua hatua tangu mapema kuhakikisha kwamba masoko ya mzao yetu ya kilimo yanatengenezwa mapema ili wakati wakulima wetu wanapovuna basi waweze kuuza mazao yao bila matatizo, bila shida, bila kurupushani na bila wao kuhangaika. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana tufanye hivyo na tutaboresha masoko ya mazao yetu hata hapa ndani ikiwa tutakubaliana na usemi wa Serikali ya Awamu ya Tano kwamba tuwe na viwanda vinavyochakata mazao yetu badala ya kuyauza yakiwa ghafi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kuna soko la bidhaa; soko hili lipo, limesajiliwa na lina watumishi lakini hatujaona likitumika sawa sawa. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana kwenye mapendekezo haya basi soko la bidhaa lionekane sasa linafanyakazi yake iliyopangwa kufanyika ya kuuza mazao yetu ya kilimo. Sasa inavyoonekana sasa hivi ni kama halijawa na uwezo mkubwa wa kufanya kazi hiyo sasa ni vizuri kwenye mapendekezo ya mpango huu, mapendekezo yangu ni kwamba lipewe uwezo wa kufanyakazi iliyopangiwa lifanye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili nililotaka kuzungumzia ni mapato yetu hasa yale yanayokusanywa na TRA; tunaipongeza TRA kwa kuongeza mapato kutoka bilioni 800 Mwaka 2016 hadi trilioni 1.3 sasa trilioni 1.3 imeendelea hivyo kwa muda sasa wa miaka miwili tunakwenda mitatu haiongezeki zaidi ya hapo sasa ninachohisi ni kwamba inawezekana TRA wamefika mahali ambapo pengine hawawezi tena kwenda zaidi ya hapo lakini nakumbuka dhana ya uchumi wa viwanda. Kiwanda kikiwa kikubwa kikawa na malighafi nyingi, wafanyakazi wengi, mashine nyingi namna ya kukitawala inakuwa ngumu maana kunatokea kitu kinachoitwa diseconomies of scale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inawezekana kwa TRA kitu kama hiki pia kimetokea sasa TRA ni kubwa. Sasa mapendekezo yangu ni kwamba, mapendekezo haya tunayojadili yatambue kwamba TRA ni kubwa na pengine inatakiwa sasa muundo wake utengenezwe upya kwa namna ya kuwa na Kanda badala ya kuwa na mikoa na wilaya kama ilivyo sasa hivi ili management ya TRA ya juu iweze kuwasiliana na watu wachache badala ya kuwasiliana na watu mikoa 26 na wilaya sijui 100 na ngapi, huyo mkuu wa TRA inamuwia vigumu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, muundo wake ubadilishwe na utakapobadilishwa utawezesha hawa watu wa kwenye Kanda kuwafikia kwa urahisi watu wa Mkoani, watu wa Wilayani na hivyo kuongeza mapato ya Serikali au mapato yanayotokana na kodi vinginevyo itakuwa bado ni ngumu kwasababu TRA imekuwa ni kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzoefu tulioupata mwezi wa tisa, mwezi wa juzi, TRA wamekusanya trilioni 1.740 sasa hiyo inawezekana ikawa ya kipindi tu, ikawa ni event, tusiporekebisha mambo kadhaa wa kadhaa lakini inawezekana kabisa makusanyo yetu kwa vyanzo tulivyonavyo hatujakusanya kiwango cha kutosha lakini ikiwa tutarekebisha muundo wake kwa viwango au kwa kodi zilizopo sasa hivi inawezekana tutakusanya kiwango kikubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kuzungumzia ni deni la Serikali; deni la Serikali limekuwa likiongezeka na nakublaiana na maelezo ya Mheshimiwa Waziri pia kwamba deni hili bado ni himilivu lakini Mwezi Agosti tumeambiwa denoi hili kuwa Trilioni 49, Mwezi Agosti mwaka huu lilikuwa trilioni 52 limeongezeka sasa ni himilivu kwasababu ya vigezo mbalimbali ambavyo Waheshimiwa Wabunge pia wanavifahamu humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nilichokuwa naomba kwenye mpango huu tunaoujadili, ni kwamba thamani ya shilingi yetu iendelee kuwa imara pia. Mpango uhakikishe thamani ya shilingi yetu inaendelea kuwa imara vinginevyo ikitikisika kidogo tu deni hili linaweza likaongezeka bila hata kuongeza kukopa ikiwa shilingi yetu itakuwa dhaifu dhidi ya sarafu ya nchi zingine hasa zile tunazofanyanazo biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa naomba sana kwenye mpango huu ambao tunaupendekeza, Serikali ihakikishe thamani ya shilingi yetu inakuwa imara, inaimarika dhidi ya Dola ili ya kwamba tusipate shida. Kuna usemi unaosema “wenzetu nchi zilizoendelea wakipata kikohozi sisi huku tunalazwa” maana yake ndiyo hiyo kwamba shilingi yao ikiimarika na ya kwetu ikawa dhaifu tunapata shida. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kwmaba kwenye mpango huu tunaoujadili, Serikali ihakikishe shilingi yetu ni imara, imeimarika na kwmaba inakwenda vizuri dhidi ya sarafu zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na hayo machache ya kusema jioni ya leo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Kamati hizi mbili Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji pamoja na Kamati ya Ardhi na Maliasili.

Mheshimiwa Spika, niwapongeze sana Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati zote mbili kwa kufanya kazi yao vizuri na hatimaye kutuletea taarifa hii hapa Bungeni. Pia niwapongeze sana Mawaziri wanaohusika na sekta hizi nne kwa sababu ya kazi wanazofanya tunaona kazi wanayofanya na kwenye maeneo yetu tunaziona.

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie suala moja tu la ushirika hasa wa mazao. Ushirika ni kitu kizuri na umekuwa kitu kizuri toka wakati wa kupigania uhuru wa nchi yetu. Imekuwa kiunganishi cha watu wetu na hata kwenye nyakati za uhur, Mwalimu Nyerere pamoja na wenzake walitumia ushirika ili kuweza kuwaunganisha Watanzania na hatimaye kudai haki yetu ya uhuru.

Mheshimiwa Spika, pia ushirika umekuwa kitu kizuri kwa sababu umeliletea Taifa hili sifa nyingi sana. Wakati wa miaka ya 1968 Ushirika ulionekana ndiyo chanzo kikubwa na kizuri kwa mapato yanayotokana na mazao. Katika Afrika sisi Tanzania tulikuwa wa kwanza na wakati huo kwa dunia nzima, kwa mambo ya Ushirika sisi tulikuwa namba tatu, baada ya Israel na Denmark. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hii ni kuonesha tu kwamba ushirika ni jambo zuri na jambo tunaloendelea nalo mpaka leo. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu amelishupalia jambo hili na miaka miwili iliyopita ushirika umefufuka kwenye maeneo yetu. Hata hivyo, nataka niseme mambo machache ambayo ni kikwazo katika kuendelea kukua kwa ushirika.

Mheshimiwa Spika, la kwanza ni uongozi katika ushirika huu. Suala hili la uongozi ni katika ngazi zote za ushirika kuanzia kile Chama cha Msingi kwenda kwenye Wilaya na Mkoa, kuna matatizo ya kiuongozi sana. Hii ni kwa sababu viongozi waliopatikana kwenye ushirika huu ni wale viongozi tuliowarithi kutoka kwenye ushirika ule ambao ulikuwa umeharibika. Wengi wao tumewachukua na kuwaleta kwenye ushirika mpya ambao tumeuanzisha kwa mujibu wa Sheria ya Ushirika ya mwaka 2013. Sasa hawa watu walioko kwenye ushirika sasa hivi walikuwa na matarajio yao kinyume kabisa na matarajio ya ushirika unavyopaswa kuwa. Kwa hiyo, hawa ndio wamekuwa tatizo kubwa kwa sababu wanachojali ni maslahi yao binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naomba sana, hebu Serikali ijaribu kuangalia muundo wa kiungozi wa ushirika wetu kuanzia ngazi ya chini mpaka mkoa. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji) SPIKA: Ahsante sana Mheshimia Mashimba Ndaki, umeeleweka. (Makofi)

MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru sana kunipa nafasi ili nami niweze kutoa mchango wangu kuhusiana na hoja hii iliyo mbele yetu ya Waziri wa Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango pamoja na Naibu Waziri wake kwa sababu ya nguvu na akili walizoweka kwenye kuandaa bajeti ya mwaka huu. Kusema ukweli wameweka nguvu na akili kubwa, lakini pia wametoka na kitu ambacho ni cha manufaa na kina leta matumaini kwa Watanzania wengi sana. Kwa hiyo niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri Mheshimiwa Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote wa Wizara hii, kwa kuja na bajeti ambayo inatoa matumaini makubwa kwa Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, mapinduzi ya viwanda ya nchi ya Uingereza yalisababishwa na mambo mawili tu. Cha kwanza ni nishati, na hiyo ilikuwa ni nishati ya makaa ya mawe. Halafu cha pili mapinduzi kwenye usafiri na uchukuzi, na njia kubwa iliyokuwapo ni njia ya reli. Mambo hayo mawili yalisababisa Waingereza wakafanya mapinduzi ya viwanda na wakaanza kuzalisha bidhaa nyingi. Mpaka ilipofika mwaka wa 1884 na kuendelea wakaanza kutafuta masoko ya bidhaa zilizokuwa zikilizalishwa kwenye viwanda vyao.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakaanzia Ulaya wakafika mpaka kwetu Afrika na huku wakaona ili waunze bidhaa zao vizuri lazima watutawale; lakini chanzo ilikuwa ni nishati ya umeme walioyoipata kwa njia iliyokuwa rahisi lakini pia mambo ya usafiri, uchukuzi na mambo mengine. Kwa hiyo tunaponzungumza nchini kwetu juu ya kuzalisha umeme wa kutosha bado tupo sahihi. Nchi yetu tunapozungumza reli ya kisasa na kuboresha njia za usafiri nyingine zote, barabara na viwanja vya ndege pamoja nakuwa na ndege zetu bado tupo sahihi. Mheshimiwa Rais yupo sahihi, wasaidizi wake wanaomshauri, Makamu wa Rais Mheshimiwa Waziri Mkuu na Mawaziri wengine wote tupo sahihi na tupo kwenye njia sahihi. Kwa hiyo ninaamini baada ya miaka michache hawa wanaopotosha na kubeza watakuja kukubali ya kwamba tulipata kiongozi kwenye miaka hii ambaye alitupeleka mahali kulipokuwa sahihi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kutoa ushauri kwa mambo mawili au matatu. La kwanza ni kuhusu Shirika letu la TPDS. Shirika hili limeboreshwa sana sasa hivi, limeunda kampuni mbili zingine, yaani kampuni inayoshughulika na gesi na kampuni nyingine inashughulika na mafuta. Shirika hili limepewa majukumu mbalimbali lakini jukumu mojawapo ni kuhakikisha kwamba linaendeleza matumizi ya gesi kwenye nchi yetu. Kwa kutimiza jukumu hilo, shirika hili limeweza kupeleka gesi kwenye viwanda 41 na lipo mbioni kupeleka gesi kwenye viwanda vingine 14.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini si hivyo tu shirika hili pia limeweza kuunganisha kwenye magari zaidi ya 200 ili yaweze kutumia gesi pamoja na petrol; sasa magari haya ni mengi sana. Pamoja na mambo hayo shirika hili limeweza pia kuunganisha gesi kwenye baadhi ya kaya katika jiji la Dar es Salaam ili gesi hiyo iweze kutumika majumbani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba sana Serikali ijaribu kuangalia kulipa nguvu shirika hili ili liweze kuendelea na mpango wake hasa ule wa kutumia gesi kwenye magari kwa sababu mpango huu una faida kubwa kwa nchi yetu. Kwa mfano magari haya 200 kama yangekuwa ni ya serikali. Serikali ingeweza kuokoa pesa nyingi kwa sababu kwa mujibu wa maelezo yao kutoka Dar es Salaam kuja hapa Dodoma mtungi unaoweza kutumika kwa gari linalotumia petrol ni mtungi wa kil 15 ambao unagharimu kama shilingi 40,000 au na kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa maana yake kutoka Dar es Salaam kuja hapa Dodoma unaweza kufika kwa shilingi sana nyingi 50,000 balada ya shilingi 150,000 mpaka shilingi 200,000. Kwa hiyo ikiwa shirika hili litawezeshwa likajenga vituo vya kuweka gesi hapa Dodoma na pengine Manyoni au Singida na mahali pengine Shinyanga au Mwanza, mtu anaweza akatoka Dar es Salaam mpaka Mwanza akatumia gesi, kitu ambacho kitamgharimu hela kidogo mpaka kufika Mwanza. Na kwa maana hiyo nchi inaweza ikaokoa hela nyingi sana za kigeni ambazo tunatumia kununua mafuta petrol na diesel.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nchi inaweza ikaokoa hali zetu za mazingira kwa sababu gesi ni rafiki ya mazingira. Kwa hiyo nilikuwa nashauri kwamba shirika hili liwezeshwe na liweze kugharimia au liweze kutoa gesi kwenye magari mengi zaidi. Mimi nilikuwa nashauri pengine Serikali ingefikiria sasa kuleta magari yake yanayotumia njia mbili, njia mojawapo iwe ya gesi ili kwamba magari hayo mengi ya Serikali yatumie gesi badala ya kutumia petrol au diesel, hilo ni jambo la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ambalo nataka kushauri; sasa hivi dunia yetu inaendeshwa kimtandao. Kuna kitu ambacho kinaitwa Digital Economy, na duania yote sasa mwelekeo ni huo. Sasa ukijaribu kuangalia sisi tunatumia mifumo hii kwa uchache sana. Naelewa serikali imeweka mifumo ya TEHAMA mbalimbali, inayo, lakini bado hatujamia fursa hii kwa ukamilifu wake. Kuna mambo mengi ambayo yanatumiwa kwenye uchumi huu wa ki-dijitali. Kwa mfano siku hizi kuna mikopo unaweza ukapata kwa kupitia simu yako ya mkononi, lakini pia kuna namna nyingi zinatumika kuanzisha mitandao mbalimbali ambayo kupitia mitandao hiyo watu wanalipa pesa na wanapata bidhaa zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa nashauri kwamba sisi kama nchi hebu tunanze kufikiria kuchukua hii fursa ambayo iko wazi sasa hivi kwanza kwa kuwa na sera ya TEHAMA. Kwa sababu sera ya TEHAMA pia hatuna; tuwe na sera ya ICT halafu baada ya hapa tuwe na sheria zitakazotu-guide namna ya uwendeshaji wa uchumi huo ambao dunia inakimbia haraka kuelekea huko.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa nashauri kwamba sasa sisi kama nchi tunapopanga mipango yetu ya uchumi tuanze kufikiria jambo hili ambalo hatuwezi kuliepuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie jambo la tatu kuhusiana na masoko ya mazao yetu; jambo ambalo limezungumza na Wabunge wengine. Mwaka jana Serikali ilifanya uamuzi mzuri, Wizara ya Kilimo ikanunua korosho kutoka kwa wa kulima kwa bei nzuri lakini korosho ile hatujaweza kuiuza kwa sababu shida ni masoko. Pia sasa hivi tupo kwenye msimu wa kuuza pamba, pamba yetu sasa hivi inapelekwa tu kwenye magodauni ya vyama vya mashirika lakini hakuna mnunuzi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mashimba Ndaki kengere ya pili imeshagonga.

MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia sehemu ya hotuba ya Mheshimiwa Rais ambayo aliitoa tarehe 13 Novemba, 2020. Kabla ya hapo nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mungu kwa kuniwezesha kurudi tena kwenye nyumba hii ambayo kwa kweli, sio rahisi kurudi, lakini kwa nguvu za Mungu basi anatuwezesha kurudi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kukishukuru Chama Cha Mapinduzi pamoja na wapiga kura wangu wa Jimbo la Maswa Magharibi kwa kunipa imani tena kurudi ndani ya nyumba hii, lakini nichukue nafasi hii kwa kipekee sana kumshukuru sana Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli kwa kuniamini kwamba, naweza kumsaidia kazi kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais na niahidi tu kwamba, sitamwangusha, nitafanya kazi kwa bidii, maarifa, nguvu zangu zote na akili zangu zote ili kusudi tu kusudi ambalo analiona linatakiwa kutimizwa na Wizara hii basi liweze kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilipewa malengo makubwa mawili kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais. La kwanza, ni kuhakikisha kwamba, sekta hizi mbili zinachangia kwa sehemu kubwa kuondoa umaskini wa Watanzania wanaoshughulika na mifugo na uvuvi, lakini la pili kuhakikisha sekta hizi zinachangia kwa sehemu kubwa kwenye pato la Taifa na la mwisho kuhakikisha sekta hizi zinachangia kwenye ajira kwa Watanzania, kitu ambacho kimekuwa adimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulipewa pia kwenye hotuba hiyo lengo dogo mahususi hasa kuhusiana na uvuvi wa bahari kuu kwamba, sasa uvuvi wa bahari kuu uchangie kwa mwaka bilioni 352 badala ya kuchangia kwa wastani wa bilioni 3.3 kwa mwaka. Sasa hayo ndio malengo makubwa yaliyoko kwenye hotuba ya Mheshimiwa Rais. Sasa pamoja na kwamba, tungependa sana kufikia malengo hayo, lakini kuna changamoto ambazo Waheshimiwa Wabunge katika michango yao hapa wamekuwa wakiziainisha, lakini pia ziko changamoto nyingine ambazo hazijaweza kuainishwa na Waheshimiwa Wabunge, lakini tumeziona katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi tulipoingia hapo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa uvuvi lipo suala la uvuvi haramu. Uvuvi haramu unapunguza rasilimali ya uvuvi katika nchi yetu bila mpangilio wowote. Kwa hivyo, uvuvi haramu unapaswa kupigwa vita kwa namna yoyote ile na kila Mtanzania ili tuweze kulinda rasilimali hii na tuweze kuirithisha hata kwa wenzetu watakaokuja baadaye. Sasa ili kuondoa uvuvi haramu sisi tumekuja na mbinu shirikishi tukitaka kuwashirikisha wadau wote wanaohusika na uvuvi, ili kuhakikisha kwamba, tunakubaliana ni kwa namna gani kwa pamoja tuweze kuondoa uvuvi haramu ambao ni hatari kwa rasilimali hii ya uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, liko suala la tozo mbalimbali ambazo Waheshimiwa Wabunge pia wamezitaja. Tumeliona na tumeliangalia, kwa sehemu kubwa limefanyiwa kazi suala la tozo, lakini tutaendelea kuliangalia suala la tozo zinazotozwa kwa leseni za biashara na tozo nyingine zinazotozwa zinakwaza wavuvi wetu. Tutaliangalia kwa upande wa juu, lakini niombe pia Wizara ya TAMISEMI, Mamlaka za Serikali za Mitaa, waangalie pia na wao kwa upande wao tozo wanazotoza kwa upande wa uvuvi ili tuwaondolee mzigo mzito wavuvi wetu kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine katika uvuvi ni suala la uvuvi kwa bahari kuu. Tumejipanga vizuri na suala hili, Mheshimiwa Rais alishasema kwenye hotuba yake, kuna mpango wa meli zile nane; nne Bara na nne Zanzibar, lakini kwa Bara pia tumepata msaada mwingine wa meli moja kutoka Japan kwa hiyo zitakuwa tano. Kwa hiyo, tutakuwa na meli tano zitakazoanza kuvua kwenye uvuvi wa bahari kuu, lakini pia shirika letu au Mamlaka yetu ya Uvuvi wa Bahari Kuu imeimarishwa sasahivi ina staff wanaofanya kazi. Mwaka jana Sheria ya Uvuvi wa Bahari Kuu ilipitishwa, sasa hivi tunamalizia Habari ya kanuni zake tuipitishe ili tuweze kuanza kushughulika na uvuvi wa bahari kuu ambao kusudi lake ni kuleta bilioni 352 kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, katika upande wa mifugo. Tumejipanga kwa habari ya miundombinu ili kuweza kuhakikisha kwamba, miundombinu ya uvuvi inakamilika katika maeneo ya wavuvi. Hii ni pamoja na malambo au mabwawa, minada, majosho na mambo mengine yanayotakiwa na wafugaji, ili kusudi tu waweze kuboresha mifugo yao ili iweze kuwa na afya bora na afya njema ili iweze kuleta tija kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la malisho; katika suala hili pia tumejipanga vizuri kama Wizara, tumepanga kwamba tuwe na hekta milioni moja na nusu kufikia mwisho wa mwaka huu, lakini ndani ya miaka mitano tunataka kufikia malisho ya hekta milioni sita. Kwa hiyo, tumepanga ili kufikia lengo hilo, kwanza kwa kushirikiana na zile…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umeisha.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kutoa mchango wangu kwenye Mpango wetu wa tatu kwenye mipango ya miaka mitano ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, sekta yetu ya mifugo na uvuvi ni sekta ya uzalishaji, na Waheshimiwa Wabunge wamejikita sana kuchangia michango mingi inayohusiana na sekta hii ilikuwa inalenga changamoto ambazo zinakabili sekta yetu ya mifugo na uvuvi. Kwahiyo Waheshimiwa Wabunge mimi nichukue nafasi hii kuwashukuru sana kwasababu mmeelezea changamoto ambazo zinakabili sekta ya mifugo na uvuvi ili isiweze kuzalisha sana kama ambavyo inategemewa; lakini pia mmeshauri kwa namna gani sekta hii iendeshe mambo yake ili iweze kuwa na tija kubwa kwa Taifa na iweze kuchangia kwa sehemu kubwa kwenye uzalishaji kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, sasa changamoto nyingi zilizoelezewa na Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Wabunge kama wanane hivi wamechangia kwenye sekta hii; moja ya changamoto waliyochangia Waheshimiwa Wabunge ni changamoto ya miundombinu hasa inayohusiana na mifugo ndio michango mingi imetoka hapo. Miundombinu inayohusiana na mifugo juu ya afya ya mifugo lakini pia juu ya miundombinu wezeshi ili kufanyabiashara ya mifugo iwe rahisi. Pia juu ya afya ya wanyama au afya ya mifugo yako masuala ya majosho, yako masuala ya malambo, visima, yako masuala ya kliniki za mifugo ndio hayo ambayo yanakwaza na yametajwa kwa sehemu kubwa na Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, nipende tu kulihakikishia Bunge lako kwamba sisi pia Wizara ya Mifugo na Uvuvi tumewasikia na tutajitahidi kwa kadri itakavyowezekana kwa kadri ambayo tutakuwa tukipata fedha kwa kadri ambavyo tutakuwa tukipata rasilimali fedha kutoka kwa Serikali au kutoka kwa wadau wengine, tutajitahidi sana kumaliza au kupunguza matatizo ya miundombinu kwenye sekta hii ya mifugo.

Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti ya mwaka ujao ambayo Waheshimiwa Wabunge mtatupitishia, tumeweka ujenzi wa majosho, malambo, kliniki na visima ili kuhakikisha kwamba afya ya mifugo yetu inakuwa bora ili mifugo yetu nayo iwe bora kuwezesha kutupa nyama bora na fedha nyingi ukilinganisha na leo. Tuondokane na ule usemi ambao hata Mheshimiwa Rais aliusema: “Mfugaji anakonda na ng’ombe mwenyewe au mfugo wenyewe nao unakonda”

Mheshimiwa Spika, sasa angalau mwakani tumeweka bajeti ya majosho 129, tutaomba Waheshimiwa Wabunge mtusaidie kutupitishia. Pia tumeweka bajeti ya malambo na visima kadhaa; tumeweka bajeti ya clinic kadhaa, tunaomba Waheshimiwa Wabunge mtusaidie ili angalau tuweze kusukuma mbele uzalishaji katika Sekta ya Mifugo na Uvuvi uweze kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo linakwaza uzalishaji ambao limetajwa na Waheshimiwa Wabunge hasa upande wa uvuvi ni juu ya Sheria yetu ya Uvuvi ya mwaka 2003. Napenda kuliambia Bunge lako sheria hii ya mwaka 2003 ilifanyiwa marekebisho mwaka 2009, lakini ikatengenezewa pia Kanuni zake mwaka 2009. Mwaka 2020, Kanuni zinazoongoza utekelezaji wa sheria hii zilifanyiwa tena marekebisho. Kwa hiyo, tumeendelea kufanya marekebisho ya Kanuni zetu ili kuwarahisishia wavuvi waweze kuvua samaki wale ambao wanatakiwa na wale ambao wao pia wavuvi wetu watajipatia fedha au kipato.

Mheshimiwa Spika, lakini tumeendelea pia kufanya mapitio ya Kanuni zetu, mwaka huu tulikutana na baadhi ya Wabunge na nikawaeleza kwamba tunafanya tena mapitio ya hizi Kanuni tujaribu kuona baada ya kuzitumia wavuvi wamesema ni Kanuni ipi ambayo bado inaendelea kukwaza. Kwa hiyo, tunaendelea kupitia tena Kanuni zetu na nimewaagiza TAFIRI waanze kufanya utafiti na walishaanza kufanya ili watuletee ni Kanuni zipi ambazo zinakwaza uvuvi kwenye bahari, maziwa na hata sehemu nyingine ili tuzifanyie marekebisho kusudi tu uzalishaji kutoka kwenye sekta ya uvuvi uweze kuongezeka. Niseme tu kwamba marekebisho haya yanaendelea na lengo lake ni kuboresha ili kwamba uzalishaji kwenye sekta ya uvuvi uweze kuongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati watu wetu wanapita kule na kujaribu kuangalia vipimo au kupima nyavu zetu zinazotumika ili pengine kuangalia ni nyavu zipi zinatumika kwenye uvuvi haramu, kulikuwa na kipimo kinaitwa match gauge na kingine ni vernier caliper. Match gauge ilikuwa inawapunja wavuvi wetu, wavuvi wakalalamika na wakaja Ofisini kwangu tukarekebisha hiyo hali. Sasa tunatumia vernier caliper badala ya match gauge ili kupima nyavu ipi inafaa kwa ajili ya uvuvi. Kwa hiyo, utagundua malalamiko mengi yanayohusiana na kukamatwakamatwa wavuvi wetu yamepungua sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuanzia Januari, 2021 hadi Februari, 2022 pamoja na Taarifa ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa Kipindi cha Januari 2021 hadi Januari 2022
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nichukue nafasi hii kukupongeza kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi sana na Waheshimiwa Wabunge, ila nikutakie mema kwenye kazi zako kama Naibu Spika wa Bunge letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kuwashukuru sana Wajumbe wa Kamati yetu ya Kilimo, Mifugo na Maji, kwa ushauri wao na maelekezo yao mengi ambayo sio kwenye taarifa hii tumeyasikia, lakini pia kila wakati tunapokutana nao wanatupa maelekezo, wanatupa mapendekezo, wanatupa maoni ambayo ni ya kujenga kwa kweli, wao hawakai kwenye mstari wa kukosoa tu kama Serikali, lakini pia wanaonesha changamoto tulizonazo, lakini pia na kutuonesha njia ya kutoka kwenye hizo changamoto. Namshukuru sana Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati na Makamu Mwenyekiti pamoja na Wajumbe wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa ambacho kimezungumzwa kwenye taaarifa ni upatikanaji wa fedha lakibi bajeti ya Wizara yetu ya Mifugo na Uvuvi. Nipende kukubaliana na maoni ya Kamati, kwamba inawezekana kweli hapa tunachangamoto kubwa lakini wote tumekwisha kusikia commitment ya Serikali kuhusiana na sekta hizi za uzalishaji, kilimo, mifugo, uvuvi, maliasili na sekta zinazozalisha. Tumemsikia Mheshimiwa Rais mwenyewe alipokuwa akihutubia Bunge kwamba tunataka kuangalia na kuona ni namna gani tunaziwezesha sekta hizi za uzalishaji ili ziweze kujikita sawasawa kwenye kuzalisha ajira, lakini kuzalisha mazao yale ambayo yanazalishwa na hizi sekta. Lakini pia Mheshimiwa Rais amerudia jambo hili tulipokuwa kwenye ziara pamoja naye Mkoa wa Mara kwamba sasa ni zamu ya kuziangalia sekta hizi za uzalishaji kuona ni kwa namna gani zinapewa kipatumbele kibajeti ili ziweze kuzalisha na kutoa mchango wake unaotakikana kwa Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara ya Mifugo na Uvuvi, pia tumekuwa na jitihada hizo tukisaidiana kwa karibu sana na Wizara ya Fedha na Mipango. Hivi karibuni tumekwisha kupeleka maandiko yetu yote mawili la mifugo pamoja na andiko la uvuvi kuonesha ni kwa namna gani tunataka pesa kwenye components mbalimbali ili tukipatiwa zile pesa tuweze kuzalisha kwa wingi, tuweze kuzalisha ajira zinazotakiwa, lakini sekta hizi ziweze kutoa mchango wake mkubwa ambao kwa kweli unategemewa na Watanzania kwa ujumla.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninaamini kama maandiko haya tuliyopeleka na tuliyoji-engage pamoja na Wizara ya Fedha yatakapopita, tunaamini mchango wa sekta yangu ya Mifugo na Uvuvi itaweza kutoa mchango wake unaotakiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna maeneo mengi ambayo nisingependa kuyataja hapa ambayo tumeyaainisha kwa upande wa mifugo, lakini pia hata upande wa uvuvi tumeainisha na baadae kukubaliana na hivi karibuni tu kuna dalili njema sana kuhusiana na malisho ya mifugo yetu, Serikali ya China iko tayari na imekwisha iko kwenye hatua za mwisho kutupatia dola za Kimarekani milioni tatu kwa ajili ya malisho ya mifugo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, huo ni mfano mmoja tu wa jambo ambalo tayari Wizara ya Fedha na sisi tumeji-engage pamoja na kwamba kuna dalili nzuri ya jambo hilo kutokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia bado kuna mambo yanayohusiana na mabwawa, bado kuna mambo yanahusiana na maji, na suala la maji pia bado tuna engage pamoja na Wizara ya Maji, kwa sababu na wenyewe wana fedha za maji, lakini sisi pia tunatafuta fedha za maji pamoja na kwamba tumeshauriwa na Bunge lako kwamba angalau kuwe na namna ya kupanga pamoja, lakini tunakaa pamoja na Wizara ya Maji ili kwamba miradi yetu ya maji iliyopo Wizara ya Mifugo na itakayokuwepo Wizara ya Maji isiweze kuingiliana au tusiweze kuiweka mahali pamoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Serikali iko na commitment ya kutosha kuhusiana jambo la kubajeti kuhusiana na sera hizi...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa muda wako umekwisha malizia malizia sekunde kumi.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana, lakini nilihakikishie tu Bunge lako kwamba Serikali imekwisha kuona kwamba kuna haja ya kuongeza bajeti kwenye sekta hizi za uzalishaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2022
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili pia niweze kuchangia mapendekezo, maoni na maazimio ya Kamati yetu ya Kilimo, Mifugo na Maji. Kwanza nianze kwa kuishukuru sana Kamati yetu chini ya Mwenyekiti Dkt. Ishengoma na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Maige. Tunawashukuru sana kwa ushauri wao na kwa maelekezo ambayo wameendelea kutupa kama Wizara, lakini pia tunawashukuru sana kwa kututia moyo na kuendelea kufanya kazi hii vizuri katika mazingira ambayo tunakuwepo.

Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana pia Wajumbe wa Kamati. Wajumbe wa Kamati kila tulipokutana nao walikuwa very positive na sisi na walikuwa wakitushauri mambo ambayo yanaweza kuleta tija kwenye Wizara ya Mifugo na Uvuvi, tunawashukuru sana.

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutuongezea bajeti hasa kwa mwaka huu wa 2022/2023. Bajeti yetu pia iliongezwa kwa asilimia 62, mwaka uliopita ule tulikuwa na bajeti ya shilingi bilioni 168 mwaka huu tuna bajeti ya shilingi bilioni 269. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais na sisi tunaahidi kwamba, kwa fedha hii tutafanya yale yote yanayowezekana kutokana na bajeti hii, yaweze kukamilika ili mwaka unaokuja aweze kuvutika na pengine kutuongezea bajeti kufikia bajeti ile ambayo tulikuwa tunaihitaji.

Mheshimiwa Spika, nianze na suala hili la uduumavu wa samaki na niseme kidogo. Suala hili sio tu Kamati ililiona, lakini pia sisi kama Wizara tuliliona hasa kuhusiana na Bwawa la Mtera. Sasa sababu ni moja tu ambayo inaonekana hadharani kwamba, kuna uchafuzi wa mazingira kuzunguka bwawa lile, lakini sisi tukasema hatuwezi kuchukua sababu hiyo moja ndio ikawa sababu ya kudumaa kwa samaki walioko kwenye Bwawa la Mtera. Kwa hiyo, tumeenda mbali zaidi na kuiagiza Taasisi yetu ya Utafiti inayoitwa TAFIRI ili ifanye utafiti, iangalie kama kuna sababu nyingine na hatua zinazoweza kuchukuliwa ili kuondokana na tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika, sasa nataka niwahakilishie Watanzania kwamba suala la udumavu nimezungumza na Kamati, lakini Kamati ikifanya reference na Bwawa la Mtera. Kwa hiyo, samaki wengine wanaotoka kwenye maeneo ya bahari na maji matamu au maji baridi wako salama na Watanzania wakila samaki bado wanabaki ni salama.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la ajira, ambalo limezungumziwa na Wabunge wengi, lakini mmojawapo Mheshimiwa Thea Ntara. Alizungumza akitaka kujua ni kwa namna gani sekta hii kwa sababu ni ya uzalishaji pia, inatengeneza ajira. Sekta ya Mifugo na Uvuvi, imejiandaa kutengeneza ajira kwa kadiri itakavyowezekana na kwa kadiri ambavyo tunapata fedha kutoka Serikalini. Kwa wakati huu tuna vituo atamizi vinavyoshughulika na masuala ya mifugo pekee nane na tuna vijana 240 kwenye hivyo vituo tayari kunenepesha mifugo na kuiuza. Lengo la vituo hivi vya kifugaji ni kujaribu kubadilisha fikra za wafugaji wetu waweze kufuata vijana hawa namna watakavyokuwa wakifuga ili tuongeze tija na tufuge kibiashara upande wa mifugo.

Mheshimiwa Spika, pia upande wa uvuvi, tuna vijana 200 sasa hivi wako kwenye vituo vyetu atamizi vya binafsi 14 na vituo atamizi vya Serikali viwili, ambavyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu wako kule kujifunza ufugaji wa samaki na wakitoka pale hawa ni wafugaji wa samaki moja kwa moja. Tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu anatuunga mkono na kwa kuwapa allowance vijana wale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia kwenye uvuvi tuna vizimba ambavyo tayari vinaanza hivi karibuni. Kuna wanufaika zaidi ya 1,800 na kitu. Miongoni mwa wanufaika hao watakuwemo vijana. Kwa hiyo, ajira kwa vijana sekta hii pia tunaitengeneza kupitia shughuli hizi ambazo Wizara imepangiwa.

Mheshimiwa Spika, niendelee na suala la Serikali kujenga mabwawa kwa kushirikiana. Suala hili hata tulipofika mbele ya Kamati tuliwaeleza kwamba sisi Wizara tatu; Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Maji, tayari tuko kwenye mazungumzo na wataalam wetu wameshatengeneza memorandum of understanding ili turatibu kwa pamoja. Tuweze kufanya kwa pamoja hizi kazi za kuchimba mabwawa, tuwe na design inayoeleweka, tuwe na viwango vinavyofanana ili Serikali inapotaka kujenga bwawa la mifugo, lakini litatumika pia kama chanzo cha maji ya binadamu na chanzo cha maji wakati mwingine kwa ajili ya umwagiliaji. Kwa hiyo, tayari Serikali tuko kwenye mchakato na tukikamilisha tutasaini memorandum of understanding, halafu suala hili litafanyika kwa pamoja kwa uratibu mzuri na changamoto ambazo zimetajwa na Waheshimiwa Wabunge pengine zitapungua kama sio kuondoka kabisa.

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la malisho kwa mifugo yetu ambalo limezungumzwa pia na Waheshimiwa Wabunge. Sasa hivi tumetengeneza sera au mfumo wa mabadiliko wa Sekta ya Mifugo. Moja ya suala ambalo tunalizungumza kwenye mabadiliko haya ni namna gani malisho yatapatikana kwa mifugo yetu hapa nchini. Kwa hali ilivyo…

SPIKA: Sekunde 30.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kwa hali ilivyo sasa hivi, wafugaji wetu wanategemea maeneo ya malisho ya jumla. Sasa kwenye mfumo na mabadiliko haya tunayokuja nayo, tunataka wafugaji wenyewe wamiliki maeneo ambayo watakuwa wanalisha mifugo yao. Wamiliki wenyewe na tutasaidiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwapa hati kwa ajili ya maeneo hayo ya malisho.

Mheshimiwa Spika, pia tunataka maeneo yaliyotengwa yote kwa kufuata ule mpango wa matumizi bora ya ardhi, maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya ufugaji tuyasajili halafu tuyatangaze kwenye gazeti la Serikali ili yalindwe kisheria, badala ya hali ilivyo sasa hivi wakati maeneo hayo yanapotengwa yasipolindwa mtu yeyote anaweza akaja na kuyachukua. Kwa hiyo, tuko na mpango huo na tutaendelea kuwaelimisha wafugaji wetu ili waweze kuelekea kwenye mwelekeo huo na tunahisi tukienda pamoja na wafugaji wetu tutapunguza migogoro inayosababishwa na ukosefu au upungufu wa malisho kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda…

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kunipa nafasi ili niweze kuchangia bajeti ya mwaka 2023/2024. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uimara wake katika kukuza uchumi wa nchi yetu kwa kuendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo inaendelea kwenye nchi yetu, lakini pia kuanzisha miradi mingine kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze kwa ajili ya kuendelea kuhakikisha nchi yetu inakuwa salama na nchi yetu inaendelea kutawaliwa huku akijali sana utawala bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango kwa kututayarishia Bajeti hii ambayo kusema ukweli kama itakwenda kutekelezwa kama ambavyo imesomwa hapa baada ya marekebisho ya Waheshimiwa Wabunge nadhani itakuwa ni Bajeti tulivu na Bajeti ambayo ninaamini itapeleka nchi yetu mbele kwa mwaka ujao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze pia Waheshimiwa Mawaziri wote chini ya Kiongozi na Jemedari wao Mkuu Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza majukumu yao ya msingi kuhakikisha nchi yetu na Watanzania kwa ujumla wanapata maendeleo kwa kusapotiwa na Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia suala moja tu siku ya leo na jambo lenyewe ninalotaka kuzungumzia ni bei za mazao hasa mazao ya kilimo. Nataka kuzungumzia jambo hili kwa sababu mazao yetu ya kilimo ni muhimu sana kwa nchi yetu, ni muhimu sana kwa wananchi, ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Bashe kwa ubunifu wake na namna ambavyo anaendelea kutekeleza shughuli zinazohusiana na mambo ya kilimo kweye sekta yake. Serikali imefanikiwa kutoa ruzuku kwa mbolea, tunaipongeza sana lakini Serikali imefanikiwa kutoa viuatilifu kwa ajili ya wakulima wanaohitaji viuatilifu hivyo maeneo mbalimbali. Sisi kwa upande wetu tumepata viuatilifu kwa ajili ya zao la pamba na tumepewa bure, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais lakini tunampongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuongeza Bajeti ya Kilimo mwaka uliopita na hata mwaka ambao tunajadili Bajeti yake. Mwaka uliopita bajeti ilikuwa shilingi bilioni 920 hivi, mwaka huu ni shilingi bilioni 970. Tunaamini kama fedha hizi zitatolewa na Serikali zikaenda kutekeleza miradi ya maendeleo inayohusiana na kilimo tunaamini tutapiga hatua na pengine tutafikia lengo la kukuza uchumi kwa 5% badala ya 3% ambayo tumefikia sasa hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la kufanya haya ni nini? Lengo la kufanya haya ni kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na mimi naamini kwa hatua hizi ambazo zinachukuliwa na Serikali uwezekano mkubwa kabisa wa kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo upo. Inawezekana kabisa tukaongeza kwa sehemu kubwa sana. Sasa mazao yetu haya ya kilimo ni muhimu sana kwa mambo mbalimbali. Moja; yanaendelea kuajiri Watanzania. Pili; yanaendelea kutupatia kipato kama Watanzania, asilimia kama 65 tunapata maisha yetu kutoka kwenye mazao ya kilimo, kutoka kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao haya ya kilimo pia ni muhimu kwa sababu haya ndiyo yanayotuletea fedha za kigeni hapa nchini kwetu. Tulikuwa na nakisi ya Serikali juu ya uagizaji na uuzaji wa mazao yetu nje kiasi cha dola milioni 5,000 hivi lakini mazao ya kilimo yametusaidia sana kutuletea fedha za kigeni ili kupunguza nakisi yetu kati ya biashara na nchi zingine. Hii inatusababisha tuwe na mfumuko wa bei kidogo pia tuwe na fedha za kigeni zinazotosheleza kununua mahitaji yetu mbalimbali tunayoyahitaji kutoka kwa wenzetu nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano mwaka wa 2021 korosho imetuletea dola milioni 226.9, ongezeko kutoka dola 159 mwaka 2021. Katani mwaka 2021 imetuletea 127, mwaka wa 2022 imetuletea 178.5, pamba imetuletea dola 103.4 mwaka wa 2022 ongezeko kutoka dola milioni 81.3. Kwa hiyo, mazao haya yana umuhimu mkubwa sana kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunapokuja kwenye bei wanazolipwa wakulima wetu hapa ndani ya nchi kusema ukweli bado kwenye eneo hili hatujafanya vizuri. Malipo wanayopata wakulima wetu ni malipo kidogo ukilinganisha na nguvu wanayoiweka kwenye hicho kilimo, ukilinganisha na gharama wanayoiweka kwenye hicho kilimo, ukilinganisha na muda wanaotumia ili kuvuna hayo mazao na hii wakati mwingine inaweza kuwa ni kwa sababu zilizo nje ya uwezo wa Serikali au nje ya uwezo wa mkulima wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la bei linatatulika, mwaka 2020/2021 bei ya korosho kwa mfano, korosho mkulima aliuza kati ya shilingi 3,400 mpaka 3,600 mwaka 2020/2021 lakini 2021/2022 mkulima ameuza korosho yake bei ya shilingi 1,400 mpaka shilingi 1,800 anguko kubwa sana hili karibu linakaribia nusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkulima wa pamba 2021/2022 bei aliyouzia pamba yake ni shilingi kati ya 1,560 mpaka 2,200 bei ilikuwa nzuri lakini msimu huu 2022/2023 bei ya pamba ni shilingi 1,060 na hatujui kama itakwenda kupanda, anguko la nusu zaidi ya nusu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hii inakatisha tamaa wakulima wetu, inakatisha tamaa wasilime tena msimu ujao lakini pia inafanya wawe na kipato kidogo na inawafanya waendelee kuwa wanyonge kwenye nchi ingawa mchango wao, mchango wa mazao wanayozalisha ni mkubwa na unaisaidia na kuifaidisha nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naomba Serikali iingilie kati kwenye bei za mazao haya kwa kuanzisha price stabilization fund. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naona umewasha kinanii chako, naomba nimalizie tu nusu dakika. Ianzishe price stabilization fund ili kuwasaidia wakulima hawa bei za mazao yao zinapoanguka na hili siyo wazo geni ni wazo linalofanywa na nchi zilizoendelea na maeneo mengine. Kwa hiyo, sisi hapa tunaweza kufanya hivyo pia tena kwa kuwachaji wakulima wakati bei za mazao haya zinapokuwa ziko juu lakini pia Serikali inaweza ikaweka ruzuku ili kufidia bei zinapoanguka. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ahsante sana.

MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja hii ya Mheshimiwa Bashe, Waziri wa Kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa nchi yetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa uthubutu wake kuweza kuongeza bajeti kwenye Wizara hii ya Kilimo ambayo ni uti wa mgongo wa Watanzania wote. Lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Bashe na Naibu wake Mheshimiwa Mavunde kwa namna ambavyo wamepangilia na kujitayarisha kufanya kazi kwa ajili ya Watanzania wote wanaoshughulika na kilimo kitaalam kabisa. Hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala moja tu ambalo mimi nataka kutoa ufafanuzi nalo ni suala la wafugaji kuingiza mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima, mashamba ya mahindi ama mazao mengine. Suala hili limezungumzwa kwa uchungu, sauti, inayoeleweka na Mheshimiwa Alexia Kamguna, Mbunge wa Viti Maalum, Morogoro. Nipende kusema tu, hakuna sheria ya nchi yetu inayoruhusu wafugaji waende kuchunga kwenye mashamba ya wakulima ambao wamelima mazao yao. Hakuna sheria ya namna hiyo. Hata sheria zinazotuongoza kutenga maeneo ya kufugia hazisemi hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi pia nimewahi kuchunga mifugo, ilikuwa marufuku kwenda kupeleka ng’ombe kwenye shamba la mtu la mahindi au mazao mengine na kulisha; ukifanya hivyo ukirudi nyumbani utapata adhabu kali; na familia yenye ng’ombe iliyokuwa inafanya hivyo, inachukua ng’ombe wake inakwenda kulisha mashamba ya watu wengine ilikuwa inajulikana kama familia ya watu wenye dharau, wasio na heshima na hivyo ilitengwa kwa namna fulani, hata ikiwa na mabinti wazuri kiasi gani, mabinti wale walikuwa hawaolewi kwa sababu wanatoka katika familia yenye dharau. Hata ikiwa na vijana wa kiume wazuri jinsi gani, vijana wale hawawezi kuoa kwenye kile kijiji, wataoa kijiji cha mbali ambako hawajulikana kwamba wanadharau na familia yao inadharau kwa sababu inatabia ya kupeleka mifugo yake kwenye mashamba ya watu wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, vitendo hivi havikubaliki. Niombe tena wafugaji popote mlipo, nchi yetu inaruhusu tuishi mahali popote ili mradi tusivunje sheria za nchi. Sasa wafugaji acheni kupeleka mifugo yenu kwenye mashamba ya wakulima, hairuhusiwi kwa sheria zetu; sisi Wizara ya Mifugo na Uvuvi miongozo yetu inakataa. Tuna miongozo ya malisho na rasilimali za vyakula vya mifugo. Hakuna mahali tumetaja mifugo ikale mazao ya wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana sana sana, tunaendelea kutoa elimu kama Wizara ili kuwaelimisha wafugaji waelewe na wasipeleke mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe sana viongozi, ngazi za Serikali za vijiji, Kata, ngazi za wilaya waangalie jambo hili. Jambo hili linatokea na wenyewe wapo pale. Wakulima wanapigwa, wanadhulumiwa mazao yao, kusema kweli ni kama kitendo cha kuhujumu uchumi; kwa sababu tunafahamu, mkulima ametegemea amelima hekali zake tatu, amefikia mahali pa kuvuna, halafu mifugo inaachiwa inakula mazao yote. Maana yake huyo mkulima kwa mwaka mzima atakuwa hana kipato, chakula, kwa hiyo hana namna ya kuishi mpaka mwaka mwingine utakapokuja. Kusema kweli tabia hii siyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie tu kwa kusema kwamba, wafugaji tufuge kileo, tufuge kwa kuelewana na wenzetu wanatumia ardhi ileile. Tufuge na wenzetu anaofanya shughuli za kiuchumi, tuziheshimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nakushukuru sana, sisi kama Wizara tutaendelea kutoa elimu kwa wafugaji ili waweze kuelewa kwamba jambo hili ni baya. Nitakwenda Mkoa wa Morogoro, nitatembelea mahali ambapo wafugaji wapo wengi tuelimishane, tuelezane ni namna gani tunaweza kushi na Watanzania wengine vizuri kuliko kuendeleza migogoro ya namna hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kukushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya Katiba na Sheria. Nianze kwa kukupongeza kwa kukaa kwenye kiti hicho; umependeza na naamini utatutendea haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue pia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake na nia yake njema juu ya nchi yetu juu ya masuala ya utawala bora, mambo ya sheria pamoja na Katiba. Nimpongeze sana pia Mheshimiwa Waziri Pindi Chana, Naibu wake pamoja na timu yao kule chini kwa usimamizi mzuri juu ya Wizara hii, wanafanya kazi nzuri sana. Sisi kama Kamati tumepata ushirikiano mzuri kutoka kwao kwenye mambo mengi tuliyokutana, kuanzia kwenye kutembelea miradi mpaka kwenye kujadili bajeti zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze pia Mheshimiwa Jaji Mkuu na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu ambaye yuko humu ndani, pia Mtendaji Mkuu wa Mahakama Mheshimiwa Ole Gabriel, mtumishi wa Mungu. Pia niwapongeze sana timu zote zinazoongoza Mafungu ya Katiba na Sheria. Kwa sababu kwa kweli kazi yao ni nzuri sana, wamehusika sana katika kutuelimisha kama Kamati ili tujue kila fungu linahusika na nini na majukumu na kazi zao. Wamekuwa na bidii sana ya kukutana na Kamati ili kutuelimisha na sisi kwa sehemu kubwa tumeelewa na ndiyo maana nimegeuka kuwa mwanasheria mzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze sana Serikali kwa kuanzisha Vituo Jumuishi vya Mahakama (ICJ). Vituo hivi kwa kweli vinatufaa sana sisi wananchi kwa sababu vina mambo mengi. Ukikuta kituo kinaitwa kituo maana yake hapo kuna Mahakama ya Mwanzo, kuna Mahakama ya Wilaya, kuna Mahakama ya Mkoa, kuna Mahakama Kuu na wakati mwingine Mahakama ya Rufaa inaweza ikatumia vituo hivi jumuishi kufanya sessions za Mahakama ya Rufaa. Niipongeze sana Serikali kwa approach hii. Naamini wananchi wataendelea kupata haki zao kwa karibu na gharama nafuu kuliko ilivyokuwa hapo mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumetembelea vituo hivi Mwanza, Njombe, hapa Dodoma na mahali pengine, vituo hivi vimejengwa vimekamilika kabisa na ni vituo ambavyo vinajitosheleza. Niiombe tu Serikali iongeze watumishi kwenye vituo hivyo, mahakimu wa Mahakama za ngazi zote hizo wawepo kwenye vituo hivyo ili kwamba wananchi wetu wakienda pale waweze kuhudumiwa na mambo yao yaweze kuishia hapo badala ya kusafiri kuelekea mbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze pia Serikali kwa ajili ya Wakili Mkuu wa Serikali kwa kuokoa fedha nyingi za Serikali, hasa kwenye mashauri haya ya nje na hata haya ya ndani. Niipongeze sana Serikali kwa sababu kupitia Wakili Mkuu wa Serikali, Serikali imeokoa fedha nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alipokuwa anasoma hotuba yake, tumesikia alivyotaja mabilioni na matrilioni ya fedha yaliyookolewa, lakini sisi pia kwenye Kamati na hata taarifa yetu imetaja kwamba, Wakili Mkuu wa Serikali ameokoa fedha nyingi sana za Serikali ambazo zingepotea kama isingekuwa weledi na utaalam wa ofisi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niombe ofisi hii iweze kuongezewa wafanyakazi ili wawepo wafanyakazi wa kutosha, pia mafunzo juu ya masuala ya upatanishi (arbitration). Nadhani ni field mpya kwetu kama tunaweza kuanza kuwa na chuo cha kwetu hapa, tukafundisha wataalamu wa kutosha kuhusiana na jambo hili, litakuwa jambo jema. Kama hatuna, basi kama kuna vyuo kule nje, basi wataalam wetu wapelekwe wajifunze juu ya masuala haya ili watuwakilishe vizuri sisi Serikali. Dunia ya leo ya utandawazi na tunapokaribisha uwekezaji mwingi namna hii na unapofurika kuja Tanzania, tunahitaji ofisi hii ifanye kazi yake vizuri ikiwa na wataalamu walio na weledi kwenye mambo mbalimbali ili Taifa letu tusipate hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo nizungumze mambo mawili na la tatu nitamalizia la Jimbo langu. La kwanza, ni mchakato wa kupata haki baada ya kushinda kesi, Mheshimiwa OIelekaita amezungumza kidogo. Mchakato huu kusema kweli baada ya mchakato wa kesi kuisha na mtu anatakiwa sasa apewe haki yake, mchakato ni mrefu sana. Inabidi afungue tena kesi kwa Msajili wa Mahakama kupata hiyo haki yake, aweke tena wakili kama ana uwezo wa kufanya hivyo au aanze kusafiri kupata haki yake aliyopata mahakamani kwenda mahakamani tena. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mlolongo wote huu naambiwa uko kisheria, lakini hii sheria si inaweza ikabadilishwa? Kwa sababu kusema ukweli mlolongo huu unawanyima haki wananchi wetu wengi mno. Kwanza, wananchi wetu akishashinda kesi hajui kama kuna mambo ya kukazia hukumu na hata huo utaratibu akielezwa wa kukazia hukumu, utaratibu wake na namna ambavyo upo kisheria ni mrefu mno, kiasi kwamba inaingiza gharama na inakatisha tamaa na wananchi wetu wengi wameshindwa kupata haki yao na wengine hata wameaga dunia hawapo, lakini haki yao walishinda mahakamani kwa sababu tu ya kipengele hiki cha kutokukazia hukumu ili kupata haki yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana Serikali ijaribu kuangalia sheria inayoongoza masuala haya ni sheria ya namna gani, iletwe hapa Bungeni tuweze kuirekebisha. Kama pengine labda tu ni bureaucracy za kimahakama, sasa utaratibu huo unaweza kufupishwa? Tukizungumzia masuala ya kidijiti ambayo Mheshimiwa Mwenyekiti wetu ameyazungumza vizuri. Masuala ya kidijiti yakienda vizuri huu utaratibu unaweza ukafupishwa ili mtu apate haki yake? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najiuliza, mimi nimeshinda kesi, ng’ombe wangu walikamatwa kwenye hifadhi, nikashinda kesi. Hivi Mahakama inashindwa nini sasa wakati huo huo kwa sababu imeniona nina haki, inashindwa nini kunipa haki wakati huo huo? Mpaka tena nianze utaratibu mwingine, nikasajili, nitafute mtu wa kunisaidia, kwa kweli utaratibu huu si mzuri sana na nadhani sisi kama Wabunge tunahitaji kuuangalia upya na kama ni sheria, iletwe hapa Bungeni tuibadilishe ili utaratibu huu uweze kutoa haki kwa watu wetu mara mtu anaposhinda kesi mahakamani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ninalotaka kuzungumzia ni juu ya documentation za ushahidi. Ushahidi unapokwenda mahakamani, unatakiwa upeleke documents ambazo ni original. Kwa mfano, kama ni mkataba, nina kesi na ndugu yangu hapa Mheshimiwa Mpembenwe, labda za madai, nipeleke mkataba wangu ambao ni original, nipeleke malipo yangu ambayo nilifanya original. Sasa, kama nina kazi nazo zingine zinasimama kwa sababu hizi documents ziko kule mahakamani. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ndaki, muda wako umeisha, hitimisha.

MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ooh! Ahsante naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kwanza ili niweze kuchangia miswada hii miwili iliyowekwa mbele yetu; Muswada wa TARI na wa TAFIRI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kuleta miswada hii miwili ambayo itasaidia. Sisi kama wawakilishi wa wananchi tuna matumaini kwamba inaweza ikatusaidia sana huko tunakofanya kazi na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nianze tu na maelezo na maoni yangu ya jumla kuhusiana na miswada yote miwili. La kwanza ni kuhusiana na TAFIRI na TARI; upande wa TAFIRI muswada wake unasema utakuwa na Deputy Director General na upande wa muswada ule wa TARI wenyewe utakuwa tu na Director General, hayupo Deputy Director General.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimejaribu kuangalia na kulinganisha hizi taasisi mbili ukubwa wake, na kuona kwamba ukiangalia TARI ni kubwa kuliko TAFIRI kwa maana ya idadi ya watu na kwa maana ya taasisi zake pia. TARI ina taasisi 16, TAFIRI itakuwa na taasisi nne, lakini TAFIRI ina Deputy Director General ambaye kwenye muswada wake wamesema atafanya kazi kama zile atakazokuwa akifanya Director General.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nilikuwa ninasita kidogo hapa kwa sababu taasisi hizi ukiziangalia ni taasisi za kitaalamu, na ni taasisi ambazo zinatakiwa zitoe mazao yatakayotusaidia sisi kama nchi kitaalam. Sasa kuzijaza na watu kama TAFIRI kuiweka na watu wawili ambao hata ujuzi wake na weledi na uwezo wao ni kama unalingana naona kama ni kuipa mzigo TAFIRI kubeba watu wawili viongozi wakubwa badala ya kuiacha tu na Director General peke yake.
Pia hili linasababisha kubebesha watu wetu mzigo kwa sababu, hizi taasisi zinapata ruzuku kutoka kwa Serikali. Na ruzuku inapatikana kutokana na kodi ambazo wananchi wa nchi hii wanatoa. Sasa kwa nini tusiwe tu na Director General kwa TARI kama walivyoainisha kwenye sheria, lakini pia kwa TAFIRI tuwe na Director General tu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu Deputy Director General hatuna sababu ya kuwanaye kwa sababu mimi naona ni kama tu tunaongeza mzigo kwa taasisi hii ambayo ni ndogo, itakuwa na taasisi nne na wafanyakazi wake watakuwa wachache, lakini chini ya Mkurugenzi Mkuu, pia wapo wakurugenzi wengine ambao wanaweza wakamsaidia kazi nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ni suala la succession plan wakurugenzi watakaokuwa chini ya Mkurugenzi Mkuu wanatosha kabisa kuwa succeeded kupata cheo cha Mkurugenzi Mkuu baadaye. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hiyo ni observation yangu ya kwanza. Nilikuwa naomba kwamba, Mheshimiwa Waziri atakapokuwa ana-conclude atuambie ni kwa nini sasa TAFIRI inakuwa na Deputy Director halafu TARI ambayo ni taasisi kubwa inakuwa na Director peke yake? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine nililotaka kusema la jumla ni matokeo ya tafiti kutokana na sheria hizi tunazopitisha. Tuna matatizo makubwa kwenye sekta za kilimo na uvuvi kwa ujumla. Tuna matatizo ya masoko, tuna matatizo ya mbegu, ya viuatilifu na matatizo mengine mbalimbali ambayo tunayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilidhani kwamba, kwa kuwa na taasisi hizi ambazo sasa, kwa mfano TARI ni taasisi itakayokuwa huru ambayo itatoka kuwa Idara ya Wizara, itakuwa taasisi inayojitegemea vivyo hivyo TAFIRI; kwamba sheria hii sasa ingeainisha tafiti zitakazofanyika, matokeo yake yanaweza yakafikaje kwa wadau; kwa wakulima kwa mfano tutapata faida gani za moja kwa moja kutokana na kuwa na Taasisi hii ya Kilimo kisheria? Faida zinazotokana na upatikanaji wa masoko, mbegu zilizo bora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni tumepata matatizo ya mbegu za mazao mbalimbali, mazao ya biashara lakini pia mazao ya chakula; tuna matatizo makubwa hapa. Sasa mimi nlitegemea sheria hizi mbili tunazotaka kuzipitisha zingeainisha ni kwa namna gani tafiti zake zinawafikia walengwa kwa muda unaotakiwa, lakini pia zinatoa matokeo ambayo yanagusa wananchi wetu. Mimi natoka sehemu wanayolima pamba, kuna wakati wakulima wetu wanapewa mbegu za pamba ambazo hazioti, lakini zinapitia kwa hawa talaam na zimepitia hii michakato yote hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mimi nilikuwa najaribu kuangalia sheria hii sasa inatusaidiaje sisi kama wawakilishi wa wakulima kupata mbegu bora, masoko kwa ajili ya mazao yetu? Tumezungumza hapa siku chache zilizopita kuhusiana na mazao ambayo yanaozea kwenye mashamba ya wakulima wetu. Sasa tafiti hizi zinatusaidiaje? Kwa sababu tunapitisha hizi sheria lakini sasa zitagusaje watu wetu kihalisia kuliko tu kuziacha kitaalam namna hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo nimejaribu kulilinganisha kwenye sehemu zote mbili, kwenye muswada wa TAFIRI na TARI ni kipengele kile cha kukopa na kuwekeza. Kipengele hiki cha kukopa na kuwekeza mapendekezo ya Kamati yamesema vizuri kwamba kukopa na kuwekeza kwa taasisi ya TAFIRI kwa mfano Kamati wamesema ni muhimu kwamba Msajili wa Hazina aweze kuhusishwa. Lakini upande wa ule Muswada wa Kilimo haujasema chochote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa napendekeza kwamba pia huu Muswada wa Kilimo pia useme wazi kwamba Msajili wa Hazina anahusishwaje inapokuja suala hasa la kuwekeza. Kwa sababu mali hizi ni taasisi za Serikali na mwenye kujua mali na thamani yake kwa upande wa Serikali ni Msajili wa Hazina. Kwa hiyo, nilikuwa naomba kwamba kwa upande huo pia kipengele upande wa TARI wamuhusishe Msajili wa Serikali ili kujua uwekezaji unaowekwa ni kiasi gani na anaweza kuufuatilia kwa namna gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipengele cha mwisho ni sehemu ya tano ya muswada ule wa TARI kipengele kile cha nane kinasema kwenye uwakilishi wa bodi atakuwepo mwakilishi mmoja kutoka kwa wakulima. Kwa nini awe mmoja na wasiwe wawili kama ambavyo Kamati imependekeza? Mimi nashauri kwamba wawe wawili kama ambavyo Kamati imependekeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwenye kipengele cha tisa wamependekeza pia awepo mwakilishi mmoja kutoka kwa wale wa wawakilishi wa Agri-business Organizations. Mimi pia hapo nilikuwa napendekeza wawepo wawakilishi wawili, kwa sababu ukizingatia pia maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani hao wanaokuwa ni members wa Bodi kwenye TARI wengi wao ni wafanyakazi kwenye Serikali. Sasa tukiwa na wawakilishi pia wanaoongezeka kutoka kwa wakulima na hawa wanaowakilisha watu wanofanya shughuli zinazohusiana na kilimo lakini za kibiashara na wenyewe wakaongezeka tutaweka uhusiano ambao utakuwa ni mzuri kwenye Bodi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwangu yalikuwa ni hayo, nakushukuru sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2018
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana, na mimi nichukue nafasi hii kuchangia hoja iliyo mbele yetu, lakini mwanzo kabisa nauna mkono hoja hii iliyopo mbele yetu.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya Bunge lako ni kutunga sheria, na sheria ziko mbele yetu, nilikuwa nasihi kwamba tujielekeze katika kutunga sheria ili watu na wananchi wa nchi yetu waone faida ya sisi kuwemo humu ndani, lakini tukianza kukwepa jukumu hili na kulisukuma kwa mtu au kikundi cha watu basi tutakuwa tunakwepa jukumu letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Muswada huu uliopo mbele yetu ni Muswada ambao concept yake haijulikani sana kwa watu wengi, kwa sababu hiyo pengine ndiyo maana tunapochangia humu ndani tunaonekana kama hatuelewi muelekeo vizuri au ni kwa namna gani. Kwa hiyo, nataka niseme tu kwamba hii Public Private Partnership ni tofauti sana uwekezaji wake na uwekezaji ule wa binafsi tunaoita private investment ni tofauti kabisa, ni tofauti na uwekezaji mwingine ambao umetajwa hapa ambao ni joint venture ni tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Public Private Partnership ni uwekezaji ambao kimsingi Serikali ilitakiwa kuwekeza, kwa sababu mwenye jukumu la kutoa public goods na public services ni Serikali, sasa kwa sababu Serikali haiwezi kuwa na rasilimali zote, kutoa public goods na public services kwa wananchi wake kwa wakati mmoja, ndiyo maana sasa Serikali imekuja na muswada huu ili kushirikiana na sekta binafsi, lakini sekta binafsi hii itoe public goods au public services. Kwa hiyo, nia yake ukijaribu kuangalia msingi wake ni kwamba siyo kwa sababu uwekezaji huu unataka kuweka faida, kupata faida kubwa hapana! Lengo kubwa kabisa ni kutoa huduma kwa umma wa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni tofauti na private investment ambapo anakuja Ndugu Dangote, Ndugu Mengi, ndugu nani anasema naweka kiwanda mahali fulani, nataka kuzalisha bidhaa fulani kwa kuuza ili nipate faida. Kwa hiyo, iko tofauti kidogo sasa tu napochangia hapa na kuvijumlisha vyote hivi kwamba ni kitu kimoja siyo sahihi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema kwamba hii sheria Serikali inalenga ipate nyongeza ya rasilimali kutoka sekta binafsi ili iweze kuwahudumia wananchi wake vizuri zaidi. Ndiyo maana hata uwekezaji wake unawekewa masharti kwa sababu usitake sana kuwaumiza wananchi wake, ndiyo maana wakati mwingine kwa mfano, kwenye solicited projects, Serikali inaweka ruzuku au inachangia pesa ili kusudi mwananchi atakayepata ile huduma asiumizwe, kwa sababu ilikuwa ni jukumu la Serikali kufanya hivyo, lakini kwa sababu ya rasilimali zake kuwa kidogo inaona ishirikiane na huyu wa sekta binafsi atoze pesa kidogo na yeye apate pesa kidogo, lakini ikiwa atatoza pesa kiasi kikubwa wanaweza kukubaliana huko baadae kwamba badala ya kuwatoza hivi wananchi wangu watoze hivi, mimi kiasi hiki nitachangia kwa sababu ni jukumu la Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo suala hili tunataka kulifanya gumu tena kama tulivyolifanya mwaka 2010 na kama tulivyolifanya mwaka 2014 tuliporekebisha hiyo sheria ya mwaka 2010, leo kwa sababu Serikali imekuwa wazi natarajia tungetunga sheria ambayo itavutia upande wa pili wa sekta binafsi iungane na Serikali ili tupate rasilimali za kutosha, lakini naona hapa ni kama watu wana…, sielewi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu sasa kitu kingine kwamba kwa sababu muswada huu tutaupitisha hapa, ninaomba Serikali iweke mpango mkakati wa namna ya kutambulisha dhana hii ya PPP kwa watumishi wake na kwa wananchi kwa ujumla kwa sababu hii ni fursa, hata wananchi hawajui kwamba kuna vitu vinaitwa PPP ambapo unaweza ukashiriki na Serikali, ukafanya kitu cha kimaendeleo ukahudumia watu, lakini wewe pia ukafidika.

Naomba sana kwamba uwepo uwezo wa namna fulani ya kuwajengea uwezo watumishi wa Serikali na wananchi pia waweze kufahamu vizuri dhana hii ya PPP wakishafahamu waweze kujua ni kwa namna gani wanaweza wakafanya manunuzi ya miradi hii yote ya aina mbili unsolicited na ile solicited, waweze kujua kwa uwazi kabisa ili waweze kushiriki kikamilifu kufanya kazi na Serikali yao kwa manufaa ya wananchi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye sheria yenyewe kifungu cha 10 ambacho Wabunge wengine pia wamechangia. Serikali inasema kwenye unsolicited project kwamba haitatoa guarantee kwa mtu ambaye atakuja na wazo lake na anataka kufanya unsolicited project. Naungana na Serikali kwamba ni sawa kwa sababu huyu mtu anapokuja na wazo lake alilobuni kimsingi Serikali haikujitayarisha na hilo wazo, ana wazo la kwake mwenyewe na yeye ameshaona fursa wala siyo Serikali iliyoona, ndiyo maana ukijaribu kuangalia masharti yale yanasema mradi ule uwe unique, maana yake hakuna mwingne kwenye eneo ambalo mradi huu unataka kuwekwa, huyu mtu asishindane na watu wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na kutotoa guarantee lakini hata uhakikisho kwamba wewe na wazo lako hili, Serikali tunakuhakikishia moja, mbili, tatu ili uweze kufanikiwa kwenye wazo lako hili. Sasa nilikuwa naomba Serikali ifikirie kutoa assurance ya mtu huyu kwa wazo lake zuri alilokuja nalo pengine wa kutoka hapa ndani au wa kutoka nje, lakini toa assurance kwamba miundombinu, kwa mfano umeme, barabara, maji, ardhi, Serikali itamsaidia, lakini ikimwaacha tu hivi ubunifu wake ule anaweza kukata tamaa na pengine ubunifu ule ungeweza kulisaidia lile eneo ambalo ubunifu wake atauweka au ataisaidia nchi kwa ujumla kwa sababu ubunifu wake ungeweza kugusa mahali pengi pa nchi yetu, badala ya kumwacha tu kwamba sasa wewe endelea na pesa zako na watu wako na kila kitu cha kwako mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali ifikirie kutoa assurance ni tofauti na kutoa guarantee, ni tofauti sana! Naomba kwamba Serikali ifanye hivyo angalau kwa miundombinu au kwa mazingira wezeshi yatakayomwezesha yule mtu akamilishe wazo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwenye Kifungu cha 5 cha Sheria hii….

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Sheria ya Fedha ya Mwaka 2019
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nawashukuru pia Waheshimiwa Wabunge wenzangu kukubali kwamba na mimi nizungumze angalau kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali kwa kukubali mambo mengi ambayo kwenye Kamati ya Bajeti tulipendekeza kwenye Muswada na kwa kweli wamejitahidi kuyafanyia kazi. Wamekubali kutoongeza ushuru wa bidhaa kwa ile wanayoongeza kila mwaka asilimia tano, lakini pia wamekubali kwamba wafanyabiashara wanapoanza kufanya biashara na wawekezaji basi wapewe kipindi cha miezi sita mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumze mambo machache tu, la kwanza ni Sheria yetu ya Bajeti na inaposomwa pamoja na Sheria ile ya Public Finance Management; ni kwamba Bunge lako linaanza kushughulika na bajeti mwezi wa Nne na kuendelea, lakini Wizara ya Fedha inaanza kushughulika na masuala ya bajeti na kikodi mwezi wa 12 na kuendelea na matokeo yake kunakuwa na mismatch ya namna fulani ya kushughulikia jambo lile lile. Sasa nadhani kuna haja ya kuangalia ili ku-harmonize hizi sehemu kama mbili au tatu zinazoshughulikia bajeti; Bunge, Wizara au Serikali lakini pia na wenzetu wa Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Fedha anakutana na wenzetu wa Afrika Mashariki kipindi ambacho Bunge lako Tukufu halijakutana na kuzungumza au na kuona kile kitakachozungumzwa na Waziri wa Fedha kule Afika Mashariki. Sasa haya mambo nadhani yanahitaji kuwekwa sawa sawa ili kwamba tuweze kutembea pamoja na kwamba inapofika sasa tunashughulikia suala la bajeti ya nchi yetu hasa Bunge lako kuanzia mwezi ule wa Nne na kuendelea, basi kuwe na vitu ambavyo tumeshakubaliana tayari kupunguza mivutano ambayo inaweza kuwepo na wakati mwingine inaleta sintofahamu isiyo na sababu. Hilo lilikuwa la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nataka nizungumzie suala la vitambulisho vya Wajasiriamali. Naishukuru Serikali, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuwa pro-active na kufanya jambo hili sasa litekelezwe kwenye nchi yetu pamoja na kwamba upo upungufu ambao umekuwepo, lakini angalau sasa linatekelezwa, wajasiriamali wanasajiliwa ili baadaye waweze kulelewa na hatimaye waweze kufanya biashara kubwa. Kitu kimoja tu ninachotaka kushauri kwa Serikali ni kwamba vitambulisho hivi sasa viboreshwe. Kwa hivi vilivyo haviko tofauti sana kati ya kitambulisho cha mjasiriamali huyu na huyu, kwa sababu hakina hata jina yaani kimeandikwa tu “Kitambulisho cha Mjasiriamali”.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kiwe na jina lakini pia kiwe na picha ya huyo mjasiriamali, lakini pia kiwe na ujasiriamali huo anayofanya huyo mtu. Kama ni Mama lishe iandikwe mama lishe, kama ni muuza mitumba, kiandikwe muuza mitumba, vinginevyo hivi vitambulisho kwa hali vilivyo havijakaa sawa sawa, kwa sababu wanachofanya sasa wananchi wetu ni kupeana hivi vitambulisho. Wewe unacho kitambulisho? Sina, lakini unataka kwenda kuuza kwenye gulio? Ndiyo. Haya chukua hiki hapa cha kwangu. Wanapeana namna hiyo kwa sababu havijatofautishwa sana. Hilo ni suala lingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la tatu, nataka nizungumzie suala la under valuation na under invoicing hasa ya bidhaa za nguo zinazotoka nchi za nje hasa maeneo mawili ya China na India. Kwa India tumepata taarifa kutoka kule kwenye Kamati kwamba angalau sasa kuna namna ambayo wanafanya kwa sababu wameshasaini memorandum of understanding suala hili la under valuation na under invoicing halipo kwa upande wa bidhaa za nguo zinazotoka India, lakini bado kwa bidhaa zinazotoka China bado hawajafikia maamuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa suala hili linaumiza viwanda vyetu vya pamba hapa ndani kwa sababu bidhaa zinatoka China zinauzwa kwe bei ya chini, zinaleta ushindani usio sawa. Kwa hiyo bidhaa zetu za nguo zinazozalishwa na viwanda vyetu zinakutana na ushindani usio sawa na vinashindwa kupata soko kwenye soko letu la ndani. Hivyo, naomba sana TRA, Wizara ya Fedha kwa ujumla walifanyie kazi suala hili ili angalau sasa tupandishe matumizi ya pamba ndani ya nchi tuepukane na habari ya kuuza pamba yetu nyingi nje ya nchi tunapokutana na bei imeshuka chini na kwa hiyo tunalazimika kushusha chini bei kwa wakulima wetu, kitu ambacho kwa utaratibu wa kuongeza kipato cha wakulima wetu, hakikubaliki. Kwa hiyo, naomba kwamba jambo hili lifanyiwe kazi haraka ili tuongeze matumizi ya pamba hapa ndani na pamba yetu tunajua itapanda bei tu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia linavyozungumzwa na wenzetu suala la pamba, lakini sisi tunaotoka kwenye pamba sasa hivi tunalishughulikia, Mheshimiwa Waziri Mkuu anazo taarifa na ameshatupa taarifa ya kwamba analishughulikia kwa ukaribu sana na bei wala haijaanguka. Bei ni ile ile ya 1,200 haijateremka kwa wakulima wetu, sasa wenzetu wanalichukua vinginevyo, lakini tunajua wana nia gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yangu yamekwisha nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ubia Baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi wa Mwaka 2023
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi na mimi niweze kusema kidogo juu ya sheria zilizoko mbele yetu. Mimi ninajikita hasa kwenye uchambuzi wa sheria mabadiliko ya mbalimbali Sheria mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kweli ya kushughulikia masuala na hoja za nchi yetu. Kila mmoja ni shahidi, anaona jinsi ambavyo Rais wetu anahangaika anakimbia huku na kule ili kuhakikisha tu kwamba masuala ya nchi yetu yanakwenda sawasawa. Mambo mengine na kelele zingine zinazopigwa Mawaziri wapo wazishughulikie ili Mheshimiwa Rais tumpe nafasi ya kushughulikia hoja na masuala ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze pia Mawaziri wanaohusiana na Sheria hizi tunazozijadili leo. Mheshimiwa Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa usikivu wao hata wakati walipokutana na kamati mablimbali. Kwa kweli tunawashukuru sana kwa sababu walikuwa wasikivu na ushauri wa kamati ulizingatiwa ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kidogo tu juu ya huduma za habari, hasa kipengele cha mwisho alichomalizia kuchangia Mheshimiwa Nusrat. Mheshimiwa Nusrat anasema kwamba, ukomo wa juu au ukomo pia wa chini ungeachwa wazi, lakini ni vizuri kukumbuka kwamba mahakama inaendeshwa na watu. Na kwa sababu inaendeshwa na watu kwenye utoaji haki kikatiba kila mtu anakuwa yuko sawa mbele ya Sheria. Sasa tukiacha wazi namna hiyo kama ambvyo ameshauri inawezekana kabisa mtu mwingine akapewa adhabu kubwa, mtu mwingine akapewa adhabu ndogo kwa kosa lile lile moja. Kwa hiyo kuwafanya watu hawa mbele ya Sheria waonekane wanahaki tofauti tofauti. Kwa hiyo, nadhani kwa namna ambavyo Kamati sisi tulishauri lakini pia namna ambavyo sheria ilikuwa imekaa bado haina makosa au matatizo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende upande wa Bohari ya Dawa. Upande wa Bohari ya Dawa, Ibara ya 27 inapendekeza kuondoa sekta binafsi kwenye wajumbe wa bodi. Ni maoni yetu na maoni yangu kwamba sekta binafsi ndiyo inakuwa injini ya kuendesha uchumi wetu. Na kwa sababu Bohari ya Dawa ina namna mbili, inatoa huduma lakini pia lazima na yenyewe ifikirie kuendesha kibiashara; ikiwa na mjumbe mmoja wapo kutoka sekta binafsi lingekuwa ni suala ambalo lina tija sana kwenye bodi. Huyu angeleta ubunifu wa kufanya biashara, huyu angeleta uzoefu, na huyu angeleta ujuzi ambao ungewasaidia bodi kuweza kufanya taasisi hii ifikirie pia kuendeshwa kibiashara badala ya kuendesha tu kama bodi ya kutoa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye Sheria hii kipengele cha (f) wametaja baadhi ya watu watakao alikwa kuja kwenye bodi lakini haisemi watu hawa wanatoka kwenye sekta ipi. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiri kwamba Bohari ya Dawa hasa board members wao mmoja wapo atoke kwenye sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika,lakini pia, kwenye Sheria ya reli Ibara ile ya 44 inafuta kifungu kidogo cha (22)(3) ambacho pia kilikuwa kinaacha wazi kuacha Wakurugenzi pamoja na Mkurugenzi Mkuu, kwamba wanaweza wakatoka kwenye sekta binafsi, kwamba sasa wanatoka kwenye mlolongo ule wa kiserikali per se. Lakini lengo letu hapa pia ni kufanya reli iwe ya kibiashara zaidi. Kwa hiyo tungeacha wazi kifungu hiki pia, kwamba muendeshaji wa Shirika letu la Reli kuanzia Mkurugenzi Mkuu na Wakurugenzi wengine wanaweza wakatoka kwenye sekta binafsi au wakatoka kwenye wigo ulio nje ya Serikali badala ya kutaka kila mtumishi wa Serikali hasa Wakurugenzi mbalimbali wa idara ya reli kwamba watoke ndani ya Serikali. Hii nayo ingeweza kuongeza ujuzi na ubunifu kwenye Shirika la Reli na hivyo kufanya Shirika la Reli lifanye shughuli zake kibiashara zaidi kama ambavyo mwelekeo wa sasa ulivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, yangu yalikuwa ni hayo machache naunga mkono hoja. Ahsante sana.
The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Act, 2023
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kunipa nafasi na mimi niweze kusema kidogo juu ya sheria zilizoko mbele yetu. Mimi ninajikita hasa kwenye uchambuzi wa sheria mabadiliko ya mbalimbali Sheria mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake ya kweli ya kushughulikia masuala na hoja za nchi yetu. Kila mmoja ni shahidi, anaona jinsi ambavyo Rais wetu anahangaika anakimbia huku na kule ili kuhakikisha tu kwamba masuala ya nchi yetu yanakwenda sawasawa. Mambo mengine na kelele zingine zinazopigwa Mawaziri wapo wazishughulikie ili Mheshimiwa Rais tumpe nafasi ya kushughulikia hoja na masuala ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze pia Mawaziri wanaohusiana na Sheria hizi tunazozijadili leo. Mheshimiwa Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kwa usikivu wao hata wakati walipokutana na kamati mablimbali. Kwa kweli tunawashukuru sana kwa sababu walikuwa wasikivu na ushauri wa kamati ulizingatiwa ipasavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kidogo tu juu ya huduma za habari, hasa kipengele cha mwisho alichomalizia kuchangia Mheshimiwa Nusrat. Mheshimiwa Nusrat anasema kwamba, ukomo wa juu au ukomo pia wa chini ungeachwa wazi, lakini ni vizuri kukumbuka kwamba mahakama inaendeshwa na watu. Na kwa sababu inaendeshwa na watu kwenye utoaji haki kikatiba kila mtu anakuwa yuko sawa mbele ya Sheria. Sasa tukiacha wazi namna hiyo kama ambvyo ameshauri inawezekana kabisa mtu mwingine akapewa adhabu kubwa, mtu mwingine akapewa adhabu ndogo kwa kosa lile lile moja. Kwa hiyo kuwafanya watu hawa mbele ya Sheria waonekane wanahaki tofauti tofauti. Kwa hiyo, nadhani kwa namna ambavyo Kamati sisi tulishauri lakini pia namna ambavyo sheria ilikuwa imekaa bado haina makosa au matatizo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende upande wa Bohari ya Dawa. Upande wa Bohari ya Dawa, Ibara ya 27 inapendekeza kuondoa sekta binafsi kwenye wajumbe wa bodi. Ni maoni yetu na maoni yangu kwamba sekta binafsi ndiyo inakuwa injini ya kuendesha uchumi wetu. Na kwa sababu Bohari ya Dawa ina namna mbili, inatoa huduma lakini pia lazima na yenyewe ifikirie kuendesha kibiashara; ikiwa na mjumbe mmoja wapo kutoka sekta binafsi lingekuwa ni suala ambalo lina tija sana kwenye bodi. Huyu angeleta ubunifu wa kufanya biashara, huyu angeleta uzoefu, na huyu angeleta ujuzi ambao ungewasaidia bodi kuweza kufanya taasisi hii ifikirie pia kuendeshwa kibiashara badala ya kuendesha tu kama bodi ya kutoa huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye Sheria hii kipengele cha (f) wametaja baadhi ya watu watakao alikwa kuja kwenye bodi lakini haisemi watu hawa wanatoka kwenye sekta ipi. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiri kwamba Bohari ya Dawa hasa board members wao mmoja wapo atoke kwenye sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika,lakini pia, kwenye Sheria ya reli Ibara ile ya 44 inafuta kifungu kidogo cha (22)(3) ambacho pia kilikuwa kinaacha wazi kuacha Wakurugenzi pamoja na Mkurugenzi Mkuu, kwamba wanaweza wakatoka kwenye sekta binafsi, kwamba sasa wanatoka kwenye mlolongo ule wa kiserikali per se. Lakini lengo letu hapa pia ni kufanya reli iwe ya kibiashara zaidi. Kwa hiyo tungeacha wazi kifungu hiki pia, kwamba muendeshaji wa Shirika letu la Reli kuanzia Mkurugenzi Mkuu na Wakurugenzi wengine wanaweza wakatoka kwenye sekta binafsi au wakatoka kwenye wigo ulio nje ya Serikali badala ya kutaka kila mtumishi wa Serikali hasa Wakurugenzi mbalimbali wa idara ya reli kwamba watoke ndani ya Serikali. Hii nayo ingeweza kuongeza ujuzi na ubunifu kwenye Shirika la Reli na hivyo kufanya Shirika la Reli lifanye shughuli zake kibiashara zaidi kama ambavyo mwelekeo wa sasa ulivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, yangu yalikuwa ni hayo machache naunga mkono hoja. Ahsante sana.
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali za Sekta ya Sheria wa Mwaka 2023
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia sehemu chache sana kuhusu Miswada hii miwili. Kusema ukweli kama ambavyo amechangia mchangiaji wa kwanza, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuleta mabadiliko ya sheria za nchi yetu kwa ajili ya ustawi wa wananchi. Pia, niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mwanasheria Mkuu, kwa usikivu wao wanapokutana na Kamati yetu ya Utawala, Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Spika, utagundua kwamba marekebisho ambayo Kamati tulishauri, mapendekezo tuliyoshauri kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Waziri wa Sheria, mengi yamekubaliwa na Serikali. Kwa hiyo, utaona hata uchangiaji wetu umefilisika sana kwa sababu mengi yamekubaliwa.

Mheshimiwa Spika, labda niseme mambo machache kwenye Sheria ile ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali, kifungu cha 7, kunaongeza kifungu cha 14B ambacho kwa kifupi niseme kuna mtu anaitwa License Authority anapewa mamlaka ya kufuta leseni ya biashara ya mtu na kwamba huyo Afisa, wasiwasi wa Kamati na wasiwasi wangu ni kwamba, huyu Afisa anaweza akafuta leseni bila sababu za msingi. Kwa hiyo, yalikuwa ni maoni yetu sisi kama Kamati kwamba, pengine sababu za kufuta hiyo leseni zinazopendekezwa na huyo Afisa, zingeweza kuwekwa kwenye sheria ili tusiwe na mchanganyiko na pengine labda upendeleo wa namna fulani kwenye kufuta leseni ya mtu. Maoni yetu ilikuwa ni kwamba, masharti au sababu za kufutwa zingeweza kuelezwa kwenye sheria.

Mheshimiwa Spika, kipengele kingine ni Kifungu cha 8 ambacho kinafuta Kifungu cha 17 cha sheria iliyokuwepo na kukiandika upya, hakuna matatizo hapo. Kulikuwa na shida ya uwepo wa Polisi uliokuwa unaashiria matumizi ya nguvu wakati tunafuatilia leseni hizi zinapoisha muda wake. Bahati nzuri nimesikia Serikali imekubali mapendekezo ya Kamati kwamba, uwepo wa Polisi hautokuwepo.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na ushauri mmoja hapa kwamba, sasa hivi tunakwenda kwenye mifumo hii ya kidijitali. Sasa kama tukienda kwenye mifumo ya namna hii, kwa nini tusitengeneze mfumo ambao mtu anaweza akau-manage akiwa ofisini kwake. Hawa wote waliopewa leseni wakawa kwenye mfumo huo, inaonesha leseni yake inanza tarehe ngapi, inaisha tarehe ngapi na kwa hivyo wote ambao leseni zao zinakwisha, huyu mtu anaangalia kwenye mfumo, halafu anawasiliana nao na kuwaambia kuwa leseni yako imekwisha, kwa hiyo inabidi uhuishe upya kwa njia ya kimfumo, badala ya kuwa na watu wanaanza kufuatilia moja kwa moja kule, ili tukapunguza matumizi ya watu kwenye mifumo ya namna hiyo.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na suala lingine kwenye sheria mbalimbali hasa zile za sekta ya sheria hasa kwenye sehemu ya13 Ibara ya 48. Kulikuwa kunaongeza kipengele cha 4A kifungu cha 1 na 2. Ilikuwa inamaanisha kabla sheria haijatungwa, utaratibu wa kutunga sheria unajulikana mpaka inapofika hapa Bungeni, lakini kwenye utaratibu huo ilikuwa inaongeza masharti ya Tume ya Marekebisho ya Sheria nayo kuingia kwenye mchakato huo.

Mheshimiwa Spika, naona wakati wa maelezo, Mheshimiwa Waziri ameeleza kana kwamba alikubali ushauri wa Kamati na kama amekubali kwenye suala hili ni sawa, kwa sababu tulikuwa na wasiwasi kwamba, ikiwa itafanyika hivyo, kutakuwa na ucheleweshaji wa mchakato mzima wa utungaji wa sheria, kwa sababu inabidi tafiti kubwa zifanywe na Tume ya Kurekebisha Sheria, halafu utaratibu mwingine ndiyo uweze kufuatwa.

Mheshimiwa Spika, pia tuliona hii Tume ya Kurekebisha Sheria haina rasilimali watu wa kutosha, vifaa vya kutosha na rasilimali fedha za kutosha kuweza kufanya kazi hiyo iliyokuwa inaongezwa kwenye Tume hiyo. Kwa hiyo, tukaona pengine majukumu hayo yangeweza yasitekelezwe kabisa au yakatekelezwa lakini kwa kuchelewa sana na hivyo tukawa na sheria zinazoendelea kuumiza watu na hatua hazichukuliwi. Hata hivyo, kwa sababu Serikali imekubali nadhani sio suala tena la kujadili.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, ya kwangu yalikuwa ni hayo. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 4) wa Mwaka 2023
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia sehemu chache sana kuhusu Miswada hii miwili. Kusema ukweli kama ambavyo amechangia mchangiaji wa kwanza, nachukua nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuleta mabadiliko ya sheria za nchi yetu kwa ajili ya ustawi wa wananchi. Pia, niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mwanasheria Mkuu, kwa usikivu wao wanapokutana na Kamati yetu ya Utawala, Katiba na Sheria.

Mheshimiwa Spika, utagundua kwamba marekebisho ambayo Kamati tulishauri, mapendekezo tuliyoshauri kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Waziri wa Sheria, mengi yamekubaliwa na Serikali. Kwa hiyo, utaona hata uchangiaji wetu umefilisika sana kwa sababu mengi yamekubaliwa.

Mheshimiwa Spika, labda niseme mambo machache kwenye Sheria ile ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali, kifungu cha 7, kunaongeza kifungu cha 14B ambacho kwa kifupi niseme kuna mtu anaitwa License Authority anapewa mamlaka ya kufuta leseni ya biashara ya mtu na kwamba huyo Afisa, wasiwasi wa Kamati na wasiwasi wangu ni kwamba, huyu Afisa anaweza akafuta leseni bila sababu za msingi. Kwa hiyo, yalikuwa ni maoni yetu sisi kama Kamati kwamba, pengine sababu za kufuta hiyo leseni zinazopendekezwa na huyo Afisa, zingeweza kuwekwa kwenye sheria ili tusiwe na mchanganyiko na pengine labda upendeleo wa namna fulani kwenye kufuta leseni ya mtu. Maoni yetu ilikuwa ni kwamba, masharti au sababu za kufutwa zingeweza kuelezwa kwenye sheria.

Mheshimiwa Spika, kipengele kingine ni Kifungu cha 8 ambacho kinafuta Kifungu cha 17 cha sheria iliyokuwepo na kukiandika upya, hakuna matatizo hapo. Kulikuwa na shida ya uwepo wa Polisi uliokuwa unaashiria matumizi ya nguvu wakati tunafuatilia leseni hizi zinapoisha muda wake. Bahati nzuri nimesikia Serikali imekubali mapendekezo ya Kamati kwamba, uwepo wa Polisi hautokuwepo.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na ushauri mmoja hapa kwamba, sasa hivi tunakwenda kwenye mifumo hii ya kidijitali. Sasa kama tukienda kwenye mifumo ya namna hii, kwa nini tusitengeneze mfumo ambao mtu anaweza akau-manage akiwa ofisini kwake. Hawa wote waliopewa leseni wakawa kwenye mfumo huo, inaonesha leseni yake inanza tarehe ngapi, inaisha tarehe ngapi na kwa hivyo wote ambao leseni zao zinakwisha, huyu mtu anaangalia kwenye mfumo, halafu anawasiliana nao na kuwaambia kuwa leseni yako imekwisha, kwa hiyo inabidi uhuishe upya kwa njia ya kimfumo, badala ya kuwa na watu wanaanza kufuatilia moja kwa moja kule, ili tukapunguza matumizi ya watu kwenye mifumo ya namna hiyo.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na suala lingine kwenye sheria mbalimbali hasa zile za sekta ya sheria hasa kwenye sehemu ya13 Ibara ya 48. Kulikuwa kunaongeza kipengele cha 4A kifungu cha 1 na 2. Ilikuwa inamaanisha kabla sheria haijatungwa, utaratibu wa kutunga sheria unajulikana mpaka inapofika hapa Bungeni, lakini kwenye utaratibu huo ilikuwa inaongeza masharti ya Tume ya Marekebisho ya Sheria nayo kuingia kwenye mchakato huo.

Mheshimiwa Spika, naona wakati wa maelezo, Mheshimiwa Waziri ameeleza kana kwamba alikubali ushauri wa Kamati na kama amekubali kwenye suala hili ni sawa, kwa sababu tulikuwa na wasiwasi kwamba, ikiwa itafanyika hivyo, kutakuwa na ucheleweshaji wa mchakato mzima wa utungaji wa sheria, kwa sababu inabidi tafiti kubwa zifanywe na Tume ya Kurekebisha Sheria, halafu utaratibu mwingine ndiyo uweze kufuatwa.

Mheshimiwa Spika, pia tuliona hii Tume ya Kurekebisha Sheria haina rasilimali watu wa kutosha, vifaa vya kutosha na rasilimali fedha za kutosha kuweza kufanya kazi hiyo iliyokuwa inaongezwa kwenye Tume hiyo. Kwa hiyo, tukaona pengine majukumu hayo yangeweza yasitekelezwe kabisa au yakatekelezwa lakini kwa kuchelewa sana na hivyo tukawa na sheria zinazoendelea kuumiza watu na hatua hazichukuliwi. Hata hivyo, kwa sababu Serikali imekubali nadhani sio suala tena la kujadili.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, ya kwangu yalikuwa ni hayo. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani wa Mwaka 2023.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafsi hii kukushukuru wewe kunipeleka kwenye Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria angalau nimeanza sasa kuwa mwanasheria. Kwa muda wa mwaka mmoja huu ambao nimekuwepo huko, naanza kuelewa vifungu vya Sheria vinakaaje na unaweza kuvijadili kwa namna gani. Nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu pamoja na Naibu wake. Kwa kweli niseme Mheshimiwa Waziri kwa jinsi ilivyo ngozi yake na sura yake, hata moyo wake uko hivyo. Ni mweupe, yuko wazi kwenye Kamati mjadala haukuwa rahisi rahisi. Ulikuwa ni mgumu lakini hatukuweza kuona kama anabadilika sura au sasa anasema naondoka nakwenda, hapana. Hivyo hivyo anavumilia halafu anajua tu kwamba tutafika mahali tutaelewana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri na sisi alituweka huru kabisa kujadili Miswada hii na ndiyo maana tukafikia hatua hii ambayo kwa Taarifa ambazo zimesomwa na Mwenyekiti wetu nadhani tumejitahidi kufanya kazi kwa uwazi lakini pia kizalendo sana.

Mheshimiwa Spika, vilevile, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuja na hizi R nne kwa sababu msingi wa Sheria hizi ni zile R nne za Mheshimiwa Rais. Reconciliation (Maridhiano) tukubaliane, sasa wengine wanatafsiri vibaya, maridhiano sio kila kitu utapata wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utakavyopata wewe na mwenzako apate. Unaona. Vilevile, resilience (kuvumiliana) tuvumiliane kwa sababu tuko tofauti tofauti. Itikadi tuko tofauti na mambo mengine. Sasa tuvumiliane tunapotaka kwenda kama nchi. vilevile, reformed (mabadiliko) tufanye mabadiliko kwa sababu yanahitajika yafanyike na ndiyo maana ya Sheria hizi kuja hapa. Lazima tufanye mabadiliko ili tufike mahali ambapo nchi yetu inataka kwenda. Pia, tunapofanya haya mabadiliko, sasa tukubali kujenga upya (rebuilding). Tukubali kujenga upya nchi yetu kwa sababu hii nchi ni yetu sisi wote. Tutafaidika watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, sasa baada ya utangulizi huo, nianze kama nilivyofundishwa kujadili Miswada hii. Nitaanza na Muswada huu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. Kwenye Ibara ile ya 28(8) kulikuwa na suala hilo. Hapana, nianze na Ibara ya 19, Ibara ya 20(1), hii ibara inazungumzia juu ya kadi kupotea, kadi kufutika au kadi kuharibika. Kwa kweli hapa kulikuwa na tozo na ada lakini Serikali kwa usikivu wake wamesema hiyo wameiondoa. Kwa hiyo, hakuna ada hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wadau wetu walipokuja kutoa maoni kwenye Kamati kwa kweli walizungumza sana juu ya suala la kutoa ada au pesa ili upate kitambulisho kipya. Sasa, Serikali imekubali na ndiyo maana nasema kwa kweli Serikali ni sikivu sana na Mheshimiwa Waziri alitusikiliza vizuri.

Mheshimiwa Spika, niende kwenye ibara ya 23(2) kwenye kukata rufaa. Sheria hii au Muswada huu ulikuwa unasema, “Ukataji wa rufaa kwa ajili ya kukataliwa maombi ni lazima iwe mahakama ya wilaya”. Hata hivyo, Serikali wamekubali kwamba sasa tunaweza kukata rufaa katika Mahakama za mwanzo ambazo ziko karibu na wananchi na ziko karibu na wapiga kura wetu. Kwa hiyo, hawatalazimika kusafiri umbali mrefu kwenda wilayani na wakati mwingine kupoteza pesa kwa sababu lazima uwe na nauli ili ufike na wilaya zetu tunazifahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ibara nyingine ni ya 28 (8). Sasa Kamati tulionesha wasiwasi juu ya kifungu hiki. Kifungu hiki “kinasema uhalali wa mwenendo chini ya kifungu hiki hautahojiwa kwa sababu tu Afisa mwandikishaji alisikiliza na kuamua pingamizi aliloweka yeye mwenyewe na katika hali yoyote ile utaratibu katika uchunguzi wowote chini ya Kifungu hiki utaanza katika hatua ambayo Afisa mwandikishaji atakapohitaji uthibitisho wa sifa zilizopo za mtu ambaye pingamizi limewekwa dhidi yake”.

Mheshimiwa Spika, sasa tulionesha wasiwasi juu ya kipengele hiki kwa sababu ikiwa kitatumika vibaya na huyu Afisa mwandikishaji, akikitumia vibaya na kwa sababu uamuzi wake utakuwa ni wa mwisho. Kwa hiyo, tulionesha wasiwasi kwamba kipengele hiki kingeweza kubadilishwa. Sasa sijasikia kama Serikali wameleta mabadiliko kwenye kifungu hiki na labda ufafanuzi zaidi tutaupata kutoka kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, niende tena kwenye kifungu kingine. Mtanivumilia kwa sababu mimi ni mwanasheri mwaka mmoja. Kifungu kingine ni kifungu cha 88(1) kinasema “Endapo mwenendo wa upigaji kura katika kituo chochote unakatizwa au kuzuiliwa kwa ghasia au vurugu wakati kuna wapiga kura waliobaki ambao hawajamaliza utaratatibu…” na maneno mengine ynanaendelea hapo.

Mheshimiwa Spika, sasa hapa pia sisi kama Kamati tulionesha wasiwasi juu ya sababu zilizoandikwa hapo. Upigaji wa kura kuzuiliwa kwa ghasia au vurugu maana yake Sheria inataja mambo mawili tu, ghasia ama vurugu. Lakini uchaguzi pia unaweza ukasimamishwa au ukakatizwa na majanga makubwa ambayo yanaweza yakatokea wakati uchaguzi unaendelea. Kwa mfano kipindupindu kimelipuka au janga lolote lile limeingia kwenye nchi kama tulivyokuwa na COVID wakati ule. Sasa tulidhani kwamba Sheria ingefafanua vizuri zaidi ikaingiza majanga mengine au mambo mengine ambayo yanaweza yakafanya uchaguzi ukawa umekatizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kifungu hicho niende tena kwenye kifungu kingine cha 107 kwenye Sheria hiyo hiyo. Hii Sheria inasema wasimamizi wa uchaguzi wa Tume watahakikisha nyaraka zote ambazo kifungu hiki zinatumika zinatekeketezwa baada ya kupita kipindi cha miezi sita. Sisi tuliona kipindi cha miezi sita ni kifupi sana na mashauri mengine ya uchaguzi yanakwenda miaka miwili, mitatu. Sasa kama ni kipindi cha miezi sita yanatekeketezwa, sasa ushahidi ule hautakuwepo.

Mheshimiwa Spika, sasa tulishauri, pengine Serikali wangetumia njia za kisasa zaidi. Wangetumia TEHAMA ili kupunguza mizigo ya makaratasi na vitu vingine na kuhakikisha kwamba uhifadhi wake unakuwa salama zaidi. Kwenye hii Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ninaishia hapo.

Mheshimiwa Spika, kwenye Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kulikuwa na suala la kwanza lilikuwa ni la jina. Kwa kweli tunaishukuru Serikali imekubali kwamba, Tume hii ya Uchaguzi itaitwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ilikuwa huru kwa kweli kwa sababu Sheria Mama inasema hii Tume ya Uchaguzi itakuwa ni idara huru. hata Muswada wenyewe kwenye Ibara ya 6(1) inasema Tume hii itakuwa huru. Sasa, tulikuwa hatuoni sababu ni kwa nini sasa tusiweke neno “Huru” kwenye jina la Muswada huu wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi? Tunashukuru kwamba Serikali ilikubali.

Mheshimiwa Spika, kipengele kingine ambacho kwenye Sheria hii tulipata shida kidogo “Rais atatoa Mwenyekiti na Makamu…” hiki kimekwishakuwa resolved kwa sababu Serikali imesema Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti kuna utaratibu ambao utawekwa kuhakikisha kwamba na wenyewe wanapita katika maeneo ili Rais anapopelekewa anapelekewa watu ambao watakuwa wako sahihi kabisa.

Mheshimiwa Spika, mwisho ni kifungu cha 18 kwenye Sheria hii ya Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi. 18(1) inasema “kutakuwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi atakayeteuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Tume.” Nadhani na yenyewe imezingatia kwa namna fulani. Kwa sababu, wakati wadau wamekuja walikuwa na malalamiko juu ya wajumbe wa Tume, walikuwa na malalamiko juu ya Mkurugenzi wa uchaguzi kwamba anateuliwa na Rais tu. Lakini Sheria imeweka wazi sasa na inasema, baada ya kupendekezwa na tume maana yake baada ya kupitia mchakato fulani ndipo Rais atapelekewa ili aweze kuteua Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, nadhani nimekuwa nguli kiasi cha kutosha. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi wa Mwaka 2023.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafsi hii kukushukuru wewe kunipeleka kwenye Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria angalau nimeanza sasa kuwa mwanasheria. Kwa muda wa mwaka mmoja huu ambao nimekuwepo huko, naanza kuelewa vifungu vya Sheria vinakaaje na unaweza kuvijadili kwa namna gani. Nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu pamoja na Naibu wake. Kwa kweli niseme Mheshimiwa Waziri kwa jinsi ilivyo ngozi yake na sura yake, hata moyo wake uko hivyo. Ni mweupe, yuko wazi kwenye Kamati mjadala haukuwa rahisi rahisi. Ulikuwa ni mgumu lakini hatukuweza kuona kama anabadilika sura au sasa anasema naondoka nakwenda, hapana. Hivyo hivyo anavumilia halafu anajua tu kwamba tutafika mahali tutaelewana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri na sisi alituweka huru kabisa kujadili Miswada hii na ndiyo maana tukafikia hatua hii ambayo kwa Taarifa ambazo zimesomwa na Mwenyekiti wetu nadhani tumejitahidi kufanya kazi kwa uwazi lakini pia kizalendo sana.

Mheshimiwa Spika, vilevile, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuja na hizi R nne kwa sababu msingi wa Sheria hizi ni zile R nne za Mheshimiwa Rais. Reconciliation (Maridhiano) tukubaliane, sasa wengine wanatafsiri vibaya, maridhiano sio kila kitu utapata wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utakavyopata wewe na mwenzako apate. Unaona. Vilevile, resilience (kuvumiliana) tuvumiliane kwa sababu tuko tofauti tofauti. Itikadi tuko tofauti na mambo mengine. Sasa tuvumiliane tunapotaka kwenda kama nchi. vilevile, reformed (mabadiliko) tufanye mabadiliko kwa sababu yanahitajika yafanyike na ndiyo maana ya Sheria hizi kuja hapa. Lazima tufanye mabadiliko ili tufike mahali ambapo nchi yetu inataka kwenda. Pia, tunapofanya haya mabadiliko, sasa tukubali kujenga upya (rebuilding). Tukubali kujenga upya nchi yetu kwa sababu hii nchi ni yetu sisi wote. Tutafaidika watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, sasa baada ya utangulizi huo, nianze kama nilivyofundishwa kujadili Miswada hii. Nitaanza na Muswada huu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. Kwenye Ibara ile ya 28(8) kulikuwa na suala hilo. Hapana, nianze na Ibara ya 19, Ibara ya 20(1), hii ibara inazungumzia juu ya kadi kupotea, kadi kufutika au kadi kuharibika. Kwa kweli hapa kulikuwa na tozo na ada lakini Serikali kwa usikivu wake wamesema hiyo wameiondoa. Kwa hiyo, hakuna ada hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wadau wetu walipokuja kutoa maoni kwenye Kamati kwa kweli walizungumza sana juu ya suala la kutoa ada au pesa ili upate kitambulisho kipya. Sasa, Serikali imekubali na ndiyo maana nasema kwa kweli Serikali ni sikivu sana na Mheshimiwa Waziri alitusikiliza vizuri.

Mheshimiwa Spika, niende kwenye ibara ya 23(2) kwenye kukata rufaa. Sheria hii au Muswada huu ulikuwa unasema, “Ukataji wa rufaa kwa ajili ya kukataliwa maombi ni lazima iwe mahakama ya wilaya”. Hata hivyo, Serikali wamekubali kwamba sasa tunaweza kukata rufaa katika Mahakama za mwanzo ambazo ziko karibu na wananchi na ziko karibu na wapiga kura wetu. Kwa hiyo, hawatalazimika kusafiri umbali mrefu kwenda wilayani na wakati mwingine kupoteza pesa kwa sababu lazima uwe na nauli ili ufike na wilaya zetu tunazifahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ibara nyingine ni ya 28 (8). Sasa Kamati tulionesha wasiwasi juu ya kifungu hiki. Kifungu hiki “kinasema uhalali wa mwenendo chini ya kifungu hiki hautahojiwa kwa sababu tu Afisa mwandikishaji alisikiliza na kuamua pingamizi aliloweka yeye mwenyewe na katika hali yoyote ile utaratibu katika uchunguzi wowote chini ya Kifungu hiki utaanza katika hatua ambayo Afisa mwandikishaji atakapohitaji uthibitisho wa sifa zilizopo za mtu ambaye pingamizi limewekwa dhidi yake”.

Mheshimiwa Spika, sasa tulionesha wasiwasi juu ya kipengele hiki kwa sababu ikiwa kitatumika vibaya na huyu Afisa mwandikishaji, akikitumia vibaya na kwa sababu uamuzi wake utakuwa ni wa mwisho. Kwa hiyo, tulionesha wasiwasi kwamba kipengele hiki kingeweza kubadilishwa. Sasa sijasikia kama Serikali wameleta mabadiliko kwenye kifungu hiki na labda ufafanuzi zaidi tutaupata kutoka kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, niende tena kwenye kifungu kingine. Mtanivumilia kwa sababu mimi ni mwanasheri mwaka mmoja. Kifungu kingine ni kifungu cha 88(1) kinasema “Endapo mwenendo wa upigaji kura katika kituo chochote unakatizwa au kuzuiliwa kwa ghasia au vurugu wakati kuna wapiga kura waliobaki ambao hawajamaliza utaratatibu…” na maneno mengine ynanaendelea hapo.

Mheshimiwa Spika, sasa hapa pia sisi kama Kamati tulionesha wasiwasi juu ya sababu zilizoandikwa hapo. Upigaji wa kura kuzuiliwa kwa ghasia au vurugu maana yake Sheria inataja mambo mawili tu, ghasia ama vurugu. Lakini uchaguzi pia unaweza ukasimamishwa au ukakatizwa na majanga makubwa ambayo yanaweza yakatokea wakati uchaguzi unaendelea. Kwa mfano kipindupindu kimelipuka au janga lolote lile limeingia kwenye nchi kama tulivyokuwa na COVID wakati ule. Sasa tulidhani kwamba Sheria ingefafanua vizuri zaidi ikaingiza majanga mengine au mambo mengine ambayo yanaweza yakafanya uchaguzi ukawa umekatizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kifungu hicho niende tena kwenye kifungu kingine cha 107 kwenye Sheria hiyo hiyo. Hii Sheria inasema wasimamizi wa uchaguzi wa Tume watahakikisha nyaraka zote ambazo kifungu hiki zinatumika zinatekeketezwa baada ya kupita kipindi cha miezi sita. Sisi tuliona kipindi cha miezi sita ni kifupi sana na mashauri mengine ya uchaguzi yanakwenda miaka miwili, mitatu. Sasa kama ni kipindi cha miezi sita yanatekeketezwa, sasa ushahidi ule hautakuwepo.

Mheshimiwa Spika, sasa tulishauri, pengine Serikali wangetumia njia za kisasa zaidi. Wangetumia TEHAMA ili kupunguza mizigo ya makaratasi na vitu vingine na kuhakikisha kwamba uhifadhi wake unakuwa salama zaidi. Kwenye hii Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ninaishia hapo.

Mheshimiwa Spika, kwenye Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kulikuwa na suala la kwanza lilikuwa ni la jina. Kwa kweli tunaishukuru Serikali imekubali kwamba, Tume hii ya Uchaguzi itaitwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ilikuwa huru kwa kweli kwa sababu Sheria Mama inasema hii Tume ya Uchaguzi itakuwa ni idara huru. hata Muswada wenyewe kwenye Ibara ya 6(1) inasema Tume hii itakuwa huru. Sasa, tulikuwa hatuoni sababu ni kwa nini sasa tusiweke neno “Huru” kwenye jina la Muswada huu wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi? Tunashukuru kwamba Serikali ilikubali.

Mheshimiwa Spika, kipengele kingine ambacho kwenye Sheria hii tulipata shida kidogo “Rais atatoa Mwenyekiti na Makamu…” hiki kimekwishakuwa resolved kwa sababu Serikali imesema Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti kuna utaratibu ambao utawekwa kuhakikisha kwamba na wenyewe wanapita katika maeneo ili Rais anapopelekewa anapelekewa watu ambao watakuwa wako sahihi kabisa.

Mheshimiwa Spika, mwisho ni kifungu cha 18 kwenye Sheria hii ya Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi. 18(1) inasema “kutakuwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi atakayeteuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Tume.” Nadhani na yenyewe imezingatia kwa namna fulani. Kwa sababu, wakati wadau wamekuja walikuwa na malalamiko juu ya wajumbe wa Tume, walikuwa na malalamiko juu ya Mkurugenzi wa uchaguzi kwamba anateuliwa na Rais tu. Lakini Sheria imeweka wazi sasa na inasema, baada ya kupendekezwa na tume maana yake baada ya kupitia mchakato fulani ndipo Rais atapelekewa ili aweze kuteua Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, nadhani nimekuwa nguli kiasi cha kutosha. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Ahsante sana. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa Mwaka 2023
MHE. MASHIMBA M. NDAKI: Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafsi hii kukushukuru wewe kunipeleka kwenye Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria angalau nimeanza sasa kuwa mwanasheria. Kwa muda wa mwaka mmoja huu ambao nimekuwepo huko, naanza kuelewa vifungu vya Sheria vinakaaje na unaweza kuvijadili kwa namna gani. Nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge na Uratibu pamoja na Naibu wake. Kwa kweli niseme Mheshimiwa Waziri kwa jinsi ilivyo ngozi yake na sura yake, hata moyo wake uko hivyo. Ni mweupe, yuko wazi kwenye Kamati mjadala haukuwa rahisi rahisi. Ulikuwa ni mgumu lakini hatukuweza kuona kama anabadilika sura au sasa anasema naondoka nakwenda, hapana. Hivyo hivyo anavumilia halafu anajua tu kwamba tutafika mahali tutaelewana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Waziri na sisi alituweka huru kabisa kujadili Miswada hii na ndiyo maana tukafikia hatua hii ambayo kwa Taarifa ambazo zimesomwa na Mwenyekiti wetu nadhani tumejitahidi kufanya kazi kwa uwazi lakini pia kizalendo sana.

Mheshimiwa Spika, vilevile, nichukue nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuja na hizi R nne kwa sababu msingi wa Sheria hizi ni zile R nne za Mheshimiwa Rais. Reconciliation (Maridhiano) tukubaliane, sasa wengine wanatafsiri vibaya, maridhiano sio kila kitu utapata wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, utakavyopata wewe na mwenzako apate. Unaona. Vilevile, resilience (kuvumiliana) tuvumiliane kwa sababu tuko tofauti tofauti. Itikadi tuko tofauti na mambo mengine. Sasa tuvumiliane tunapotaka kwenda kama nchi. vilevile, reformed (mabadiliko) tufanye mabadiliko kwa sababu yanahitajika yafanyike na ndiyo maana ya Sheria hizi kuja hapa. Lazima tufanye mabadiliko ili tufike mahali ambapo nchi yetu inataka kwenda. Pia, tunapofanya haya mabadiliko, sasa tukubali kujenga upya (rebuilding). Tukubali kujenga upya nchi yetu kwa sababu hii nchi ni yetu sisi wote. Tutafaidika watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, sasa baada ya utangulizi huo, nianze kama nilivyofundishwa kujadili Miswada hii. Nitaanza na Muswada huu wa Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani. Kwenye Ibara ile ya 28(8) kulikuwa na suala hilo. Hapana, nianze na Ibara ya 19, Ibara ya 20(1), hii ibara inazungumzia juu ya kadi kupotea, kadi kufutika au kadi kuharibika. Kwa kweli hapa kulikuwa na tozo na ada lakini Serikali kwa usikivu wake wamesema hiyo wameiondoa. Kwa hiyo, hakuna ada hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wadau wetu walipokuja kutoa maoni kwenye Kamati kwa kweli walizungumza sana juu ya suala la kutoa ada au pesa ili upate kitambulisho kipya. Sasa, Serikali imekubali na ndiyo maana nasema kwa kweli Serikali ni sikivu sana na Mheshimiwa Waziri alitusikiliza vizuri.

Mheshimiwa Spika, niende kwenye ibara ya 23(2) kwenye kukata rufaa. Sheria hii au Muswada huu ulikuwa unasema, “Ukataji wa rufaa kwa ajili ya kukataliwa maombi ni lazima iwe mahakama ya wilaya”. Hata hivyo, Serikali wamekubali kwamba sasa tunaweza kukata rufaa katika Mahakama za mwanzo ambazo ziko karibu na wananchi na ziko karibu na wapiga kura wetu. Kwa hiyo, hawatalazimika kusafiri umbali mrefu kwenda wilayani na wakati mwingine kupoteza pesa kwa sababu lazima uwe na nauli ili ufike na wilaya zetu tunazifahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Ibara nyingine ni ya 28 (8). Sasa Kamati tulionesha wasiwasi juu ya kifungu hiki. Kifungu hiki “kinasema uhalali wa mwenendo chini ya kifungu hiki hautahojiwa kwa sababu tu Afisa mwandikishaji alisikiliza na kuamua pingamizi aliloweka yeye mwenyewe na katika hali yoyote ile utaratibu katika uchunguzi wowote chini ya Kifungu hiki utaanza katika hatua ambayo Afisa mwandikishaji atakapohitaji uthibitisho wa sifa zilizopo za mtu ambaye pingamizi limewekwa dhidi yake”.

Mheshimiwa Spika, sasa tulionesha wasiwasi juu ya kipengele hiki kwa sababu ikiwa kitatumika vibaya na huyu Afisa mwandikishaji, akikitumia vibaya na kwa sababu uamuzi wake utakuwa ni wa mwisho. Kwa hiyo, tulionesha wasiwasi kwamba kipengele hiki kingeweza kubadilishwa. Sasa sijasikia kama Serikali wameleta mabadiliko kwenye kifungu hiki na labda ufafanuzi zaidi tutaupata kutoka kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Spika, niende tena kwenye kifungu kingine. Mtanivumilia kwa sababu mimi ni mwanasheri mwaka mmoja. Kifungu kingine ni kifungu cha 88(1) kinasema “Endapo mwenendo wa upigaji kura katika kituo chochote unakatizwa au kuzuiliwa kwa ghasia au vurugu wakati kuna wapiga kura waliobaki ambao hawajamaliza utaratatibu…” na maneno mengine ynanaendelea hapo.

Mheshimiwa Spika, sasa hapa pia sisi kama Kamati tulionesha wasiwasi juu ya sababu zilizoandikwa hapo. Upigaji wa kura kuzuiliwa kwa ghasia au vurugu maana yake Sheria inataja mambo mawili tu, ghasia ama vurugu. Lakini uchaguzi pia unaweza ukasimamishwa au ukakatizwa na majanga makubwa ambayo yanaweza yakatokea wakati uchaguzi unaendelea. Kwa mfano kipindupindu kimelipuka au janga lolote lile limeingia kwenye nchi kama tulivyokuwa na COVID wakati ule. Sasa tulidhani kwamba Sheria ingefafanua vizuri zaidi ikaingiza majanga mengine au mambo mengine ambayo yanaweza yakafanya uchaguzi ukawa umekatizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kifungu hicho niende tena kwenye kifungu kingine cha 107 kwenye Sheria hiyo hiyo. Hii Sheria inasema wasimamizi wa uchaguzi wa Tume watahakikisha nyaraka zote ambazo kifungu hiki zinatumika zinatekeketezwa baada ya kupita kipindi cha miezi sita. Sisi tuliona kipindi cha miezi sita ni kifupi sana na mashauri mengine ya uchaguzi yanakwenda miaka miwili, mitatu. Sasa kama ni kipindi cha miezi sita yanatekeketezwa, sasa ushahidi ule hautakuwepo.

Mheshimiwa Spika, sasa tulishauri, pengine Serikali wangetumia njia za kisasa zaidi. Wangetumia TEHAMA ili kupunguza mizigo ya makaratasi na vitu vingine na kuhakikisha kwamba uhifadhi wake unakuwa salama zaidi. Kwenye hii Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ninaishia hapo.

Mheshimiwa Spika, kwenye Muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kulikuwa na suala la kwanza lilikuwa ni la jina. Kwa kweli tunaishukuru Serikali imekubali kwamba, Tume hii ya Uchaguzi itaitwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ilikuwa huru kwa kweli kwa sababu Sheria Mama inasema hii Tume ya Uchaguzi itakuwa ni idara huru. hata Muswada wenyewe kwenye Ibara ya 6(1) inasema Tume hii itakuwa huru. Sasa, tulikuwa hatuoni sababu ni kwa nini sasa tusiweke neno “Huru” kwenye jina la Muswada huu wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi? Tunashukuru kwamba Serikali ilikubali.

Mheshimiwa Spika, kipengele kingine ambacho kwenye Sheria hii tulipata shida kidogo “Rais atatoa Mwenyekiti na Makamu…” hiki kimekwishakuwa resolved kwa sababu Serikali imesema Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti kuna utaratibu ambao utawekwa kuhakikisha kwamba na wenyewe wanapita katika maeneo ili Rais anapopelekewa anapelekewa watu ambao watakuwa wako sahihi kabisa.

Mheshimiwa Spika, mwisho ni kifungu cha 18 kwenye Sheria hii ya Muswada wa Sheria ya Tume ya Uchaguzi. 18(1) inasema “kutakuwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi atakayeteuliwa na Rais baada ya kupendekezwa na Tume.” Nadhani na yenyewe imezingatia kwa namna fulani. Kwa sababu, wakati wadau wamekuja walikuwa na malalamiko juu ya wajumbe wa Tume, walikuwa na malalamiko juu ya Mkurugenzi wa uchaguzi kwamba anateuliwa na Rais tu. Lakini Sheria imeweka wazi sasa na inasema, baada ya kupendekezwa na tume maana yake baada ya kupitia mchakato fulani ndipo Rais atapelekewa ili aweze kuteua Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Taifa.

Mheshimiwa Spika, nadhani nimekuwa nguli kiasi cha kutosha. Nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Ahsante sana. (Makofi)