Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mashimba Mashauri Ndaki (8 total)

MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:-
Barabara ya kutoka Maswa Mjini kupitia Kijiji cha Njiapanda mpaka Mwigumbi inajengwa kwa kiwango cha lami na barabara hii inaendelea kutoka Kijiji cha Njiapanda kupitia Mji Mdogo wa Malampaka mpaka Mwabuki. Barabara hii ni ya muhimu sana kwa shughuli za kibiashara, kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Maswa Mjini, Mji Mdogo wa Malampaka na Wilaya ya Maswa kwa ujumla na inaunganisha Mkoa wa Simiyu na Mwanza kwa upande wa Wilaya ya Kwimba:-
Je, Serikali ina mpango wa kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami kutoka Njiapanda mpaka Mwabuki?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa barabara ya kutoka Kijiji cha Njiapanda – Malampaka - Mwabuki na imeendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali kwa kiwango cha changarawe ambapo katika mwaka wa fedha 2014/2015 barabara hii ilitengewa kiasi cha shilingi milioni 561.225 kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum, matengenezo ya kawaida pamoja na ujenzi wa madaraja matatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, matengenezo hayo yalihusisha eneo la kutoka Jojiro - Nyamilama na Kijiji cha Mwankulwe ambacho kina jumla ya kilometa 20 na madaraja matatu. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 barabara hii imetengewa jumla ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida na matengenezo ya muda maalum ambapo TANROADS Mkoa wa Mwanza imefanya ukarabati kutoka Mwabuki - Jojiro pamoja na kipande cha kutoka Kijiji cha Mwankulwe hadi Malampaka ambacho kina jumla ya kilometa 120. Mpango wa kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami kutoka Njiapanda - Mwawabuki utategemea upatikanaji wa fedha.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:-
Bwawa la maji la Kijiji cha Mwamihanza limejaa mchanga hivyo kukauka mapema hasa ifikapo nyakati za kiangazi. Je, Serikali ina mpango gani wa kulikarabati bwawa hilo pamoja na miundombinu inayopeleka maji kwa wananchi wa Kijiji cha Mwamihanza na vijiji jirani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, bwawa la maji katika Kijiji cha Mwamihanza, Wilayani Maswa lilijengwa na Serikali mwaka 1970 kwa lengo la kutoa huduma ya maji kwa wananchi na mifugo katika Kijiji cha Mwamihanza na vijiji vya jirani, na limekuwa likihudumia wakazi 1,518 na mifugo 3,578. Bwawa hili limejaa mchanga kutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu zikiwemo shughuli za kilimo na mifugo eneo la catchment baada ya mradi wa maji kusimama kwa muda mrefu bila kufanya kazi kwa kushindwa kuendeshwa na wananchi kutokana na gharama kubwa za uendeshaji wa matengenezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Bwawa la Mwamihanza ni chanzo muhimu kwa wananchi wa Kijiji cha Mwamihanza na vijiji vya jirani, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Maswa imeweka ukabarati wa bwawa pamoja na miundombinu katika mpango wa bajeti wa miaka mitatu ambapo ukarabati utafanyika kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 kupitia vyanzo vya fedha za ndani za Halmashauri na fedha za Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji ya Awamu ya Pili.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali ina mpango wa kubadilisha mitambo ya kusukuma maji, inayotumia diesel, ili itumie nishati ya jua kwa lengo la kupunguza gharama za uendeshaji kwa wananchi na kufanya mradi uwe endelevu. Aidha, Serikali imeanza kuvijengea uwezo vyombo vya watumia maji, ili viweze kudumu kuendesha miradi ya maji na kuifanya kuwa endelevu.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:-
Nchi yetu kwa sasa ina wataalam wengi katika sekta mbalimbali kama vile uhasibu, uchumi, uongozi, menejimenti, udaktari, utawala na kadhalika.
Je, Serikali haioni haja sasa kwa ajira zote kwenye NGOs na taasisi binafsi nchini kupewa Watanzania na kuacha mpango uliopo sasa wa kuruhusu wageni kuajiriwa hasa kwenye nafasi za juu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, wageni wanaajiriwa nchini kwa kuzingatia Sheria ya Ajira ya Wageni Namba Moja ya mwaka 2015. Kabla ya kutoa kibali cha kazi kwa mgeni kamishna wa Kazi anatakiwa kujiridhisha kuwa nafasi anayoombewa mgeni ni adimu na mwajiri amefanya juhudi za kutafuta Mtanzania wa kuajiriwa katika nafasi hiyo. Aidha, sheria inamtaka mwajiri kutengeneza mpango wa kurithisha ujuzi na kuhakikisha mgeni anayeombewa kibali anarithisha utaalamu huo kwa Mtanzania ili muda wa kibali utakapokwisha Mtanzania huyo aweze kuchukua nafasi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kuwa utaratibu wa utoaji vibali vya ajira kwa wageni unazingatiwa ipasavyo kwa kutumia sheria na miongozo iliyopo. Kwa hali hiyo, Serikali itaendelea kuona haki inatendeka kwa mujibu wa sheria ili Watanzania waendelee kupata ajira katika NGOs na taasisi binafsi.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:-
Maeneo mengi ya Mkoa wa Simiyu na Mikoa mingine kama vile Dodoma, Singida, Shinyanga na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Tabora na Mwanza yanapata mvua za masika hafifu sana, hivyo kuathiri kwa kiasi kikubwa shughuli za kilimo katika Mikoa hiyo:-
Je, Serikali ina mpango gani mkubwa wa kujenga mabwawa kwa ajili ya kilimo katika maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Jimbo la Maswa Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ilikwishaainisha maeneo yote nchini yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji na kuandaa mpango kabambe wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji wa mwaka 2002. Hata hivyo, kutokana na mabadiliko ya tabianchi na matumizi ya ardhi, Wizara kwa kushirikiana na Serikali ya Japan inafanya mapitio ya mpango huo ili uhusishe ujenzi wa mabwawa madogo, ya kati na makubwa kwa nchi nzima yakiwemo maeneo yanayopata mvua hafifu za masika. Vilevile mpango huo utahusisha matumizi ya maji ya maziwa makuu, ikiwemo Ziwa Viktoria, kwa ajili ya umwagiliaji wa kutumia teknolojia zinazotumia maji kwa ufanisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupitia mpango huo inatarajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2017/2018. Kukamilika kwa mpango huo kutawezesha kufanyika kwa usanifu wa miradi ya mabwawa kwenye maeneo yenye mvua hafifu yaliyotajwa pamoja na maeneo mengine yenye uhaba wa mvua. Katika mpango huo Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji itaanza ujenzi wa mabwawa makubwa ya kimkakati ya Kidunda, Ndembela na Farkwa.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:-
Serikali imekamilisha mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Mji wa Ngudu na vijiji vilivyo karibu na Mji huo Wilayani Kwimba, mradi huu unatoa maji ya uhakika kuliko miradi ya visima vifupi ambavyo ni vya msimu, lakini Mji Mdogo wa Malampaka na vijiji vingine vya karibu kama Jihu, Bukigi, Muhida, Lali, Nyabubinza na Mwang’horoli ambavyo vipo karibu na Mji wa Ngudu havijaunganishwa kwenye mradi huo.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuunganisha Mji Mdogo wa Malampka na vijiji vya Jihu, Bukigi, Muhida, Lali, Nyababinza na Mwang’horoli katika mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetekeleza mradi wa maji safi kutoka Ziwa Victoria kwenda katika Mji wa Ngudu na vijiji vilivyopo kandokando ya bomba linalopeleka maji katika Mji wa Ngudu. Vijiji hivyo ni Runele, Ngatuli, Nyang’onge, Damhi na Chibuji. Mradi huu ulihusu ulazaji wa bomba kilomita 25 na sehemu nyingine ya bomba lilitumika bomba la zamani la mradi wa visima uliojengwa miaka ya 70. Bomba hilo ni la kipenyo cha inchi nane na kulingana na usanifu halitoshi kupeleka maji kwenda Malampaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji inatekeleza miradi ya maji Malampaka, Sayusayu, Mwasayi, Njiapanda na Sangamwalugesha, ambapo miradi hii imekamillika na wananchi wanapata maji.
Aidha, miradi ya maji ya Lalagomandang’ombe na Jija inaendelea kujengwa na ujenzi umefikia asilimia 50. Serikali pia imekamilisha usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa miradi ya maji ya Mwabulimbu, Mwamanenge, na Badi ambao utahudumia vijiji vitatu vya Muhiba, Jihu na Badi yenyewe. Ujenzi wa miradi hii utafanyika katika awamu ya pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeandaa mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda kwenye Miji ya Sumve, Malampka na Mallya. Hadi sasa taratibu za kumpata mtaalamu mshauri atayefanya usanifu wa mradi huo zianendelea. Hivyo, baadhi ya vijiji alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge vitajumuishwa katika mradi huo. Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni mbili kwa ajili ya mradi huo.
MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:-
Serikali imekamilisha mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Mji wa Ngudu na vijiji vilivyo karibu na mji huo Wilayani Kwimba. Mradi huo unatoa maji ya uhakika kuliko miradi ya visima vifupi ambavyo ni vya msimu. Lakini Mji Mdogo wa Malampaka na vijiji vingine vya karibu kama Jihu, Bukigi, Muhida, Lali, Nyabubinza na Mwang’honoli ambavyo vipo karibu na Mji wa Ngudu havijaunganishwa kwenye mradi huo.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuunganisha Mji Mdogo wa Malampaka na vijiji vya Jihu, Bukigi, Muhida, Lali, Nyabubinza na Mwang’honoli katika mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria ili kuwapatia wananchi maji ya uhakika?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mradi wa maji safi toka Ziwa Victoria kwenda katika Mji wa Ngudu na vijiji vilivyopo kandokando ya bomba linalopeleka maji katika mji huo. Vijiji hivyo ni Runele, Ngatuli, Nyang’onge, Damhi na Chibuji. Mradi huu ulihusu ulazaji wa bomba kilometa 25 na sehemu nyingine ya bomba lilitumika bomba la zamani la mradi wa visima uliojengwa miaka ya 1970. Bomba hilo ni la kipenyo cha inchi nane na kulingana na usanifu halitoshi kuendeleza zaidi kwenda Malampaka.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji…

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji imetekeleza Miradi ya Maji ya Malampaka, Sayusayu, Masayi, Njiapanda na Sangamwalugesha ambayo imekamilika na wananchi wanapata maji. Miradi ya Maji ya Lalago, Mandang’ombe na Jija inaendelea kujengwa na ujenzi umekamilika kwa asilimia 65. Serikali pia imekamilisha usanifu na uandaaji wa makabrasha ya zabuni kwa Miradi ya Maji ya Mwabulimbu, Mwamanenge na Badi ambao utahudumia vijiji vitatu vya Muhiba, Jihu na Badi yenyewe. Ujenzi wa miradi hii utafanyika katika Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza miradi hii kwa awamu, hivyo, kwa vijiji ambavyo havipo katika awamu hii tunaomba Mheshimiwa Mbunge awasiliane na halmashauri husika ili viwe katika kipaumbele katika awamu zinazokuja.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:-
Shamba la malisho lililopo katika Kata ya Shishiyu Wilayani Maswa linamilikiwa na Serikali lakini halitumiki ipasavyo:-
Je, Serikali Kuu haioni haja ya kulirejesha shamba hilo kwa Halmashauri ya Wilaya ili lipangiwe matumizi mengine?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo cha kupumzishia mifugo (holding ground) cha Shishiyu kina ukubwa wa hekta 4,144 na ni kati ya vituo 28 vilivyotengwa nchi nzima kwa mujibu wa Sheria ya Magonjwa ya Wanyama Na. 17 ya mwaka 2003 kwa ajili ya kukusanya na kupumzisha mifugo inayotoka minada mbalimbali kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa kabla ya kusafirisha mifugo hiyo kwenda katika viwanda vya kuchinja na kuchakata nyama au kusafirisha kwenda nje ya nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, uwepo wa vituo vya kupumzishia mifugo ni hitaji la Kimataifa katika biashara ya mifugo. Zipo sheria mbalimbali za Kimataifa zinazolazimisha uwepo wa maeneo haya, yanayolenga utoaji huduma unaozingatia viwango ambazo zinasimamiwa na Shirika la Afya ya Wanyama ulimwenguni - OIE na makubaliano ya Kimataifa ya afya ya wanyama na mimea (Sanitary and Phytosanitary (SPS) chini ya Shirika la biashara la Kimataifa (WTO).
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili pia hutumika kama kituo cha karantini kwa ajili ya kuchunguza magonjwa, hususan yale ya milipuko yanapojitokeza hasa kutokana na Kanda ya Ziwa kuwa na mifugo mingi na baadhi ya mikoa katika Kanda hii inapakana na nchi jirani hivyo ni rahisi ka magonjwa ya wanyama ya milipuko kujitokeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kuna mwingiliano mkubwa wa wanyama wafugwao na wanyama pori kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Pori Tengefu la Maswa kutokana na umuhimu wa kituo hiki kwa ajili ya biashara ya mifugo ndani na nje ya nchi. Hivyo, siyo vema kubadilisha matumizi na madhumuni ya kuanzishwa kwa kituo hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, eneo hili litaendelea kubaki chini ya usimamizi wa Serikali Kuu kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili eneo hili liweze kutumiwa na wadau wote waliopo kwenye mnyororo wa kuongeza thamani (value chain) ya mifugo na mazao yake.
MASHIMBA M. NDAKI aliuliza:-
Mabonde ya mpunga katika Vijiji vya Masela, Bukangilija na Mwatigi katika Wilaya ya Maswa yanaweza kuzalisha mpunga mwingi kuliko ilivyo hivi sasa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga mabwawa na mifereji ya umwagiliaji katika maeneo hayo ili kuwawezesha wakulima kuongeza tija katika uzalishaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mashimba Mashauri Ndaki, Mbunge wa Maswa Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ina mikakati ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji nchi nzima ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Maswa imekuwa ikiendekeza scheme za umwagiliaji zinazotumia teknolojia ya kuvuna maji ya mvua kwa kujenga mabanio ya kuchepusha maji na mfumo wa mifereji ya umwagiliaji katika mashamba. Kwa maeneo ambayo yemeonekana yanafaa usanifu wa kina hufanyika na kisha ujenzi wa mabwawa ya kuhifadhi maji kwa ajili ya umwagiliaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Wilaya ya Maswa ipo miradi mbalimbali ya umwagiliai inayotumia mifumo mbalimbali ikiwemo miradi ya umwagiliaji ya Masela, Bukangilija na Mwatigi. Kwa mradi wa Masela wenye eno la hekta 450 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji ulifanywa usanifu wa mwanzo wa ujenzi wa mabwawa na mifereji. Kwa sasa Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kufanya usanifu wa kina ili ujenzi wa bwawa na mifereji ufanyike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa umwagiliaji wa Bukangilija wenye hekta 307 ulijengwa mwaka 2004 kupitia Mpango wa Kuendeleza Kilimo Wilayani (DADPS) hivyo miundombinu yake imechaka na inahitaji ukarabati mkubwa. Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya ukaratabati wa mradi huo kwa upande wa bonde la Mwatigi lenye ukubwa wa hekari Mwaka 2013 chini ya ufadhili wa World Food Program ulichimbwa mfereji mkuu lakini miundombinu mingine haikujengwa hivyo fedha zitahitajika kukamilisha ujenzi wa mradi huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji itaendelea kufanya usanifu wa awali ili kuangalia uwezekano wa ujenzi wa mabwawa katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo maeneo yaliyotajwa. (Makofi)