Answers to supplementary Questions by Hon. Mashimba Mashauri Ndaki (21 total)
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kipekee zaidi namshukuru Mungu kwa fursa hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali la msingi nimeuliza sehemu ya Serikali kama ruzuku. Nikiri kwamba nimepokea majibu ya Serikali, lakini naomba sasa niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mtakubaliana na mimi kwamba kuku wa kienyeji ndio mradi wa chini kabisa wa mwananchi yeyote kumudu Tanzania. Kila kaya ingepata kuku wa kienyeji tungeboresha hata chakula chetu sisi wenyewe na pia miradi kwa akinamama. Nimeambiwa hapa kwamba bei ya ruzuku ni shilingi 1,400/= na shilingi 1,500/= naomba niseme kwamba hiyo ndio bei ya kibiashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Serikali kama Serikali inatoa ruzuku gani ili kila kaya ipatiwe vifaranga hivi vya kienyeji ambavyo pia Serikali inatakiwa kutoa elimu, vifaa vya kulishia kuku hawa, vyakula vya kulishia ikiwemo starter, growers na pia dawa za kuku hawa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa swali hili nimekuwa nikiliuliza kwa awamu zote na sasa ni mara ya tatu niko Bungeni na jibu linajibu kwamba wako wanafanya utafiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, miaka 15 ya utafiti kwa nchi ambayo ina Chuo cha Kilimo na Mifugo kama ilivyo SUA ni jambo ambalo halikubaliki. Swali, ni lini sasa Serikali itawezesha Wabunge wote Viti Maalum wakafanye miradi hii ya kuku wa kufuga kwenye mikoa yao? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, lakini pia, nichukue nafasi hii kumshukuru sana mama yangu Mama Raymond kwa swali lake hili ambalo ameendelea kuliuliza kila wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza kwamba Serikali inatoa ruzuku gani, ili bei ya vifaranga hao tunaowauza angalao iwe chini kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba hiyo bei ya shilingi 1,400/= na shilingi 1,500/= kuna ruzuku ndani yake, kwa sababu bei ya kifaranga ni shilingi 2,200. Sasa badala ya kuuzwa shilingi 2,200 Serikali kwa kushirikiana na kampuni nilizozitaja wanatoa ruzuku ili kwamba wahitaji wa vifaranga hawa wawapate kwa bei ya shilingi 1,400 na shilingi 1,500. Kwa hiyo, ni kwamba Serikali pamoja na wadau wake tunatoa ruzuku. Sasa kama bei ya shilingi 1,400 na shilingi 1,500 bado ni kubwa, hilo linaweza kuwa ni suala lingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la pili kama ulivyoelekeza, basi tutaona ni kwa namna gani Wabunge wa Viti Maalum tuwapeleke Naliendele mahali ambapo tunafanya utafiti, ili waelezwe kitaalamu utafiti huo unachukua muda gani na kwamba utaisaidia nchi hii baada ya muda gani. Nadhani itakuwa ni suala la msingi sana, nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wakati anajibu swali la msingi nilitaka tu nimkumbushe kwamba nimeuliza swali hili mwaka juzi nikiwa humu ndani ya Bunge na Serikali ilijibu kwamba itafanyia kazi, sasa amekuja na majibu mengine kwamba ataangalia.
Je, sasa yuko tayari kuingiza Halmashauri ya Itigi ambayo ina wafugaji wengi ambao ni wapya na wameingia maeneo ambayo tunayo kwa sababu ya fursa ya malisho kuingiza kwenye suala zima la malambo ili wapate sehemu ya kunyweshea mifugo yao?
Lakini lini Mheshimiwa Waziri upo tayari kuambatana na mimi kwenda kujionea uhalisia wa wafugaji walivyo wengi katika Jimbo hili la Manyoni Magharibi, kwa maana ya Halmashauri ya Itigi angalau katika mnada mmoja tu wa Mitundu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Massare, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo Wilaya ya Manyoni na Halmashauri ya Itigi inavyotunza wafugaji walioko kwenye Wilaya hiyo, tunalazimika sisi, kama Wizara kujali sasa kwenye bajeti ijayo na kutekeleza suala la kujenga lambo kwenye Wilaya yake ya Halmashauri ya Itigi. (Makofi)
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba lambo ambalo tumesema tutaangalia kwenye bajeti, kimsingi tutachimba lambo kwenye halmashauri yako kwa sababu, tunaelewa una wafugaji wengi na mifugo ni wengi kwenye wilaya yako.
Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya suala lake la pili la mimi kwenda kwenye halmashauri yake na jimbo lake, ili kwenda kujionea hali halisi, niko tayari nitafanya hivyo ili tuweze kuona hali halisi na kwa pamoja tuweze kutathmini na kuona ni kitu gai tunaweza kuwasaidia wafugaji wetu walioko Wilaya ya Manyoni na Halmashauri ya Itigi. (Makofi)
MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; Wilaya ya Maswa nayo ina ranchi kubwa takribani ekari 12,000 Ranchi ya Shishiu pale Maswa na Mheshimiwa Waziri analifahamu hilo.
Je, wana mpango gani wa kuwagawia wananchi wa Maswa watumie ranchi hiyo kwa ajili ya matumizi ya ufugaji maana hatuoni Serikali inafanya juhudi gani katika ranchi hiyo? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana lakini pia nimshukuru sana Mheshimiwa Ulega, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa majibu yake mazuri kwa Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, kumekuwa na mawazo ya wananchi kuona kwamba maeneo ya Wizara ya Mifugo ambayo ni pamoja na ranchi na eneo ambalo analizungumza Mheshimiwa Nyongo lenyewe sio ranchi Ni holding ground, kwamba linapokuwa hivyo basi wananchi wapewe au wafanye shughuli zinginezo. Tunakubaliana kwamba tunafanya tathmini ya maeneo yote tuliyonayo ili tuone ni kwa namna gani yanaweza yakatumiwa vizuri zaidi.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa eneo la Shishiu, Halmashauri ya Wilaya ya Maswa wameleta andiko na mpango wao kuonesha ni kwa namna gani wanataka kutumia hilo eneo. Wameeleza wanataka eneo dogo, sisi tumewarudishia tukawaambia leteni mpango wa kutumia eneo lote la Shishiu kwa ujumla wake halafu tutaona ni kwa namna gani sasa mnakwenda kulitumia halafu tuweze kuwapa nafasi ya kulitumia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe tu Waheshimiwa Wabunge na wananchi maeneo ya Wizara ya Mifugo ambayo yapo wazi, tunataka tuyatumie kikamilifu kwa kuwashirikisha wananchi wenyewe, lakini sekta binafsi ili iweze kuwekeza vizuri kwenye hayo maeneo na yaweze kutumika kwa tija zaidi, ahsante. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante; kwa kuwa katika swali la msingi majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ilikuwa kwamba lengo la Shamba la Nangaramo ni kusambaza mitamba, lakini katika maeneo mengi yenye mashamba haya mitamba hiyo imekuwa ndama wake wanauzwa kwa shilingi 1,500,000 na hivyo wananchi kushindwa kumudu gharama za kununua ndama.
Je, Serikali haioni haja ya kuondoa kabisa hayo mashamba na kwa vile lile lengo la msingi la kusambaza mitamba halijafanikiwa? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; kuhusiana na bei ya mitamba, hiyo ni biashara; na ndama au ng’ombe wanaouziwa wananchi bei yake inajumlisha gharama za kumtunza yule ng’ombe pamoja na gharama zingine zote.
Mheshimiwa Spika, sasa huwezi kumnunua ng’ombe ambaye Mheshimiwa Mbunge anamuita ni ndama, actually ni ng’ombe kwa sababu huyo ng’ombe anaponunuliwa kwetu anakuwa yupo tayari kubeba mimba ili aweze kuzaa. Sasa sio ndama kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge amemuita na pengine tutaangalia utaratibu ambao unapelekea mpaka kufikia gharama za namna hiyo, tuone kama tunaweza taratibu za gharama zikapungua tuweze kuwauzia kwa bei ambayo ni reasonable. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitangaze tu kwamba kwa Shamba la Nangaramo tayari tumewauzia wananchi walio karibu na shamba hilo mitamba 14 wameweza kununua na shamba letu kwa sababu linazalisha sio mitamba mingi sana, inatafutwa na wana order kubwa mpaka sasa hivi wanasubiria. Sasa suala la bei tutaliangalia tuone ni kwa namna gani inaweza kupungua ili wananchi waweze kununua mitamba mingi zaidi. (Makofi)
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa majibu mazuri ya Serikali. Kwa kuwa wanawake wa Kigoma wanaojishughulisha na uvuvi wanahitaji kujengewa uwezo katika mnyororo wa thamani na kuongezewa pia mitaji. Je, ni lini Serikali italeta mradi huu ili uweze kuwanufaisha wanawake wa Mkoa wa Kigoma wanaojishughulisha na shughuli za uvuvi. (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Kigoma, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Kigoma na Ukanda wote wa Ziwa Tanganyika, tuna mradi unaoitwa Fish for ACP ambao unajumuisha Ukanda wote wa Ziwa Tanganyika. Lengo la mradi huu ni kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi kwenye Ziwa Tanganyika ikiwemo dagaa, migebuka na mazao mengine ya uvuvi yaliyoko kwenye Ukanda wa Ziwa Tanganyika. Mradi huu unalenga kuongeza ubora, unalenga kupunguza upotevu wa mazao ya uvuvi unaotokea kwenye mialo na kwenye masoko yalioko kwenye ukanda huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tayari, Serikali inaendelea na utekelezaji wa mradi huu na mwaka huu tutaendelea; na miaka mingine tutaendelea mpaka ukanda uliye...
NAIBU SPIKA: Ahsante kwa majibu mazuri.
MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nataka nijue sasa commitment ya Serikali kwa Kata zilizobaki, kwa maana katika majibu ya msingi inaonesha kwamba kuna Kata moja tu imejengewa majosho na Jimbo la Singida Magharibi ni moja ya Majimbo ambayo yana wafugaji wengi sana: -
Je, Serikali lini itakwenda kutekeleza ujenzi wa majosho katika Kata za Igelansoni, Makilawa, Mwaru, Igombwe pamoja na Minyuge?
Swali la pili: Je, Waziri yuko tayari kuongozana nami Mbunge akajionee namna wafugaji wanapata adha kulingana na changamoto ya magonjwa katika mifugo yao kutokana na kutokuwepo kwa majosho?
WAZIRI MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Elibariki Kingu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, natambua ya kwamba uhitaji wa majosho nchini ni mkubwa na kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi tumeelekezwa kuweka josho kwenye kila Kijiji kilicho na mifugo. Kwa hiyo, kwenye mpango wetu wa Wizara, mwaka huu fedha tutakaouanza tumeweka pia mpango wa kuendelea kujenga majosho kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini. Sasa tutatoa kipaumbele kwenye maeneo aliyoyataja Mheshimiwa Kingu; Gelansoni, Iyumbu, Igombwe na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, juu ya suala la kuambatana naye ili twende kukutana na wafugaji wake. Niko tayari kufanya hivyo na pengine kama tutapata wakati, weekend mojawapo tunaweza kuambatana ili tukutane na hao wafugaji.
MHE. MICHAEL C. MWAKAMO: Mheshimiwa Spika, kwenye Jimbo la Kibaha Vijijini kwenye Kata ya Magindu, Ruvu, Gwata na Dutumi kuna wafugaji wa kutosha lakini majosho hakuna: Je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kunipatia sehemu ya majosho aliyoyataja kwamba yapo kwenye bajeti? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwakamo, Mbunge wa Kibaha kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tutapanga vizuri kwenye majosho ambayo Serikali itatupa fedha kwa mwaka wa fedha ujao ili kuhakikisha kwamba Jimbo la Kibaha pia linapata majosho, yanaweza yasiwe yote lakini angalau maeneo yaliyo muhimu yenye wafugaji wengi, tutaongea pamoja na Mheshimiwa Mbunge ili tuone kwamba maeneo hayo yanapata majosho pia.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Tatizo la majosho lipo maeneo mengi. Halmashauri ya Mji wa Bunda, nadhani mjomba unajua kuna wafugaji wengi, lakini kuna malambo ambayo hayako kwenye hali nzuri; Kinyambwiga, Gushigwamara, Kisangwa pamoja na Rwabu: Ni lini mtayakarabati hayo malambo ili wananchi wa Bunda waweze kupata huduma ya kulishia mifugo yao?
Mheshimiwa Spika, ahsante.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nilishafika Bunda, nilishayaona hayo malambo, tulishaenda na Mheshimiwa Getere tukazunguka tukaona maeneo ya malambo ambayo yameharibika. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwenye mwaka ujao 2023 tuna mpango wa kukarabati malambo mengi kidogo. Pia tuna mpango wa kujenga malambo mapya, yatakuwa mengi, zaidi ya manne ambayo mlitupa bajeti ya mwaka huu. Kwa hiyo, tutafikiria kuangalia wananchi na wafugaji wa Bunda ili tuone malambo yao ambayo yameharibika ni kwa namna gani tutaweza kuyakarabati.
MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Changamoto ya majosho iliyopo kwenye Singida Magharibi ni sawa na changamoto iliyopo kwenye Jimbo la Igunga, kwenye Kata ya Kinikinila, Isakamaliwa, Mamashimba, Kilungu pamoja na Igulubi: -
Je, ni lini Wizara itatatua changamoto hii, ukizingatia Jimbo la Igunga ni miongoni mwa majimbo yenye mifugo mingi nchini?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Nicholaus Ngassa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Igunga na Wilaya ya Igunga kwa ujumla tulipangia mwaka huu wa fedha kwamba tungeweza kujenga majosho zaidi ya matano, lakini majosho matatu hatukuweza kuyajenga kwa sababu hatukupata ushirikiano mzuri na Ofisi ya Mkurugenzi.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninaamini kwenye bajeti ijayo, kwa sababu pia tumetenga majosho kwa Wilaya ya Igunga, tutapata ushirikiano wa kutosha na kwa hivyo maeneo aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge tutayapangia kujenga majosho. Tupate ushirikiano wa kutosha ili kwamba majosho yatakayopangwa kwa wilaya hiyo basi yaweze kukamilishwa.
MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Jimbo la Singida Mashariki ni miongoni mwa majimbo yenye wafugaji wengi sana, na Mheshimiwa Waziri alishawahi kuniahidi majosho takribani matatu kwenye Kata za Siuyu, Ulyapiti, pamoja na Isuna.
Sasa ni nini kauli yake kwa mwaka huu wa fedha?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, namtafutia majibu.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Vijiji vya Ombiri, Muungano, Golopaguma, Dalayi navyo vina matatizo makubwa ya majosho kwa ajili ya mifugo. Na ikumbukwe kwa Mkoa wa Dodoma Wilaya ya Chemba ndiyo yenye mifugo mingi. Naomba kujua commitment ya Serikali sasa ni lini tutaenda kujenga majosho kwenye vijiji hivyo? Ahsante sana.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Wilaya na Mkoa wa Dodoma kwa ujumla una mifugo mingi sana. Kwa mwaka huu wa fedha tunaoenda nao angalau kila wilaya tulikuwa tumewapangia majosho si chini ya manne, tuliwapa upendeleo kidogo. Sasa safari ijayo tutaangalia pia hasa kwa Jimbo la Mheshimiwa Mbunge wa Chemba, tuone ni kwa namna gani tunaweza kupanga kujenga majosho mengine ili Mheshimiwa Mbunge na wafugaji wake waweze pia kufaidika.
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa hadi leo ni mwaka wa kumi na mbili niko Bungeni na sijawahi kutembelewa na Waziri wa Mifugo katika jimbo langu, je, Waziri atakuwa yuko tayari kutembelea jimbo langu kuja kuongea na wafugaji ikiwemo na changamoto hizo za majosho na mambo mengine?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Nyanghwale, Mbunge ambaye pia ana wafugaji wengi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, niko tayari kumtembelea Mheshimiwa Mbunge na jimbo lake. Najua wapo wafugaji wengi na kwa hiyo kumkosa Waziri wa Mifugo au msaidizi wake itakuwa ni tatizo. Sasa niko tayari kufanya hivyo kipindi hiki cha bunge tunaweza kutafuta wikiendi mojawapo twende au baada ya Bunge ili ya kwamba tuweze kukutana na wafugaji wake tutatue matatizo na changamoto zilizoko zinazohusiana na mifugo.
MHE. DUNSTAN L. KITANDULA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa, naomba niulize swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Waziri ulipokuja kutembelea mnada wa Hororo, mojawapo ya changomoto tuliyoizungumza ni ukarabati wa lambo la Ng’ombeni. Je, ahadi iko pale pale, kwamba litakarabatiwa?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kitandula kama ifuatavyo: -
Ahadi yetu Mheshimiwa Mbunge iko pale pale, na tutafanya hiyo kazi mpaka ikamilike ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa mnada huo. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge kuwa na uhakika kwamba sisi kazi hiyo tulishaanza kuifanya na kwa hivyo tutaikamilisha kama ambavyo tumepanga. Ahsante sana.
MHE. SYLVIA F. SIGULA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Wizara, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; uchumi wa vijana wengi wa Mkoa wa Kigoma unategemea sana uvuvi, na sasa hivi tunashukuru kwa sababu tumeanza usafirishaji wa samaki kutoka ndani kwenda nje. Lakini kumekuwa na changamoto, pamoja na kuwa na hiki chuo bado kuna tatizo kubwa la ubora wa samaki wetu kukidhi kwenye masoko ya nje na ndani na chuo hiki kinatoa kozi moja.
Je, Serikali haioni sasa ni muda mwafaka wa kuongeza kozi ya fish processing, quality assurance and marketing ili tuweze kupata wataalam wengi wa kusimamia ubora wa samaki wetu ili kupunguza hasara kwa wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; je, Waziri yuko tayari kuongozana na mimi au Mbunge wa jimbo husika kwenda katika chuo hiki kuona hizi changamoto yeye mwenyewe? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Sigula, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua umuhimu wa vijana kuingia katika tasnia hii ya uvuvi hasa vijana wa Mkoa wa Kigoma kwa sababu ya mazingira waliyonayo ya Ziwa Tanganyika. Chuo chetu hiki cha Kibirizi kiko kwenye eneo dogo na sisi kama Wizara tunachukua hatua za makusudi kutafuta eneo lingine kwenye Manispaa hiyo hiyo ya Kigoma ili tuweze kukipanua chuo hiki kiweze kutoa mafunzo zaidi kwa vijana hawa ikiwa ni pamoja na kozi aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la kufika Kigoma ili kuweza kuona mazingira halisi, niko tayari kuambatana naye.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa bado uhamasishaji unaendelea, lakini wavuvi wetu wengi hawa wadogo wanakosa elimu na zana kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao, lakini vilevile wanakosa taarifa za kutosha za masoko yanayoweza ku-determine bei ya bidhaa zao wanazozalisha. (Makofi)
Nini sasa mkakati wa Serikali kuhakikisha kwamba wanasaidia jamii hii hasa kwenye eneo la Ukerewe ili wavuvi wetu waweze kunufaika na shughuli zao za uvuvi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuzingatia mazingira ya Ukerewe kama eneo maalum la uvuvi; nini sasa mkakati wa kujenga mwalo kwenye eneo la Kakukuru kwenye Wilaya yetu ya Ukerewe? Nashukuru sana. (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili kwa pamoja ya Mheshimiwa Joseph Mkundi, Mbunge wa Ukerewe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina mpango mkakati wa namna ya kuwasaidia wavuvi wetu hapa nchini ili kuwasaidia wawe na zana bora, lakini pia waweze kuongeza uzalishaji wa mazao ya samaki hapa nchini. Mojawapo ya mkakati ni kwenye bajeti ya mwaka ujao tuna mpango wa kununua boti 320 kwa nchi nzima ili tuweze kuzikopesha kwa wavuvi wadogo wadogo na wavuvi wa kati waweze kuwa na uwezo wa kuvua katika maji marefu upande wa bahari, lakini pia upande wa maziwa yetu. Lakini pia tuna mpango wa kuboresha mialo yetu yote na kuijenga katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuboresha masoko madogo madogo ya wavuvi wetu kwa kujenga vichanja ili mazao yale yanayotolewa baharini au ziwani yaweze kupata mahali pa kuanikwa vizuri, lakini yaweze kuwa bora na kuweza kupata bei iliyo nzuri kwenye soko letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala lake la pili, Serikali imepanga kukarabati mwalo wa Kakukuru kwenye Wilaya ya Ukerewe ili kwamba mwalo ule uwe bora, ili kwamba wavuvi wa Wilaya ya Ukerewe wapate mahali ambapo wanaweza wakashusha mavuvi yao vizuri na kwa urahisi zaidi. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kunipa nafasi.
Mikoa ya Kigoma, Rukwa na Katavi ni mikoa ambayo inamiliki Ziwa Tanganyika, kwa bahati mbaya sana mikoa hii yote hakuna sehemu Serikali imewekeza viwanda vya kuchakata samaki.
Ni lini Serikali itapeleka viwanda kwenye maeneo ya mikoa hiyo ili kuepukana na wizi unaofanywa na nchi jirani kwenye maeneo ya kwetu? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kakoso kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi kwa sasa imefaulu kumpata mwekezaji ambaye amejenga kiwanda cha kuchakata mazao ya uvuvi kwenye Mji wa Sumbawanga. Kiwanda hiki hivi karibuni kitaanza uchakataji wa mazao ya uvuvi, lakini pia Serikali inaendelea kuhamasisha wawekezaji kutoka sekta binafsi ili pia kuwekeza kwenye maeneo ya ukanda mzima wa Ziwa Tanganyika kuanzia Kigoma kuja Mkoa wa Katavi mpaka Rukwa.
Kwa hiyo, Serikali tunaendelea na uhamasishaji na wawekezaji wakipatikana tutawapeleka kwenye ukanda wa Ziwa Tanganyika ili waweze kuwekeza zaidi. (Makofi)
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuuliza swali dogo la nyongeza; kwa kuwa mnada wa Upili wa Olokii miundombinu yake imeharibika sana, mizani imekufa, hakuna maji na Wizara ndio inakusanya fedha zote katika mnada huo wa Upili.
Ni lini Serikali itakarabati mnada huo ili kuhakikisha kwamba huduma nzuri na bora inapatikana kwenye mnada huo wa Olokii? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, Serikali kwenye bajeti ya mwaka ujao imetenga shilingi bilioni 21.2 kwa ajili ya kukarabati minada yake ya Upili na minada ya mipakani yote, ili kuweza kuwarahisishia wafugaji ambao wanapeleka mifugo yao kwenye minada hiyo. Kwa hiyo, miongoni mwa mnada ambao Mheshimiwa Mbunge anausema utafanyiwa ukarabati kupitia bajeti hii. (Makofi)
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi.
Mheshimiwa Waziri mwaka jana ulikuja Kirando na ukaona kwamba ule mwalo uliokuwa umewekwa na Serikali umezama. Nini mpango wa Serikali wa kujenga soko ambalo nilikuonesha kwamba eneo tayari tumeliandaa pale Kirando? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, nilifika Kirando na kweli mwalo ule tuliukarabati na kujenga miundombinu mbalimbali lakini umezama. Lakini ahadi yetu Mheshimiwa Mbunge iko pale pale kwamba tutaujenga upya Mwalo wa Kirando kwa kutumia bajeti ambayo tayari tumetengewa na Serikali, ili kuhakikisha kwamba ubora tuliokuwa tunautaka utokee kwenye mwalo huo unaendelea kuwepo.
Kwa hiyo, tutaendelea na juhudi kwa mwaka wa fedha ujao kuweza kukarabati miundombinu iliyoko hapo, ili pia kuweza kuwasaidia wavuvi wetu hasa eneo la Kirando ambao wanavua kwa wingi sana. (Makofi)
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru; Mkoa wa Mara ulikuwa na viwanda vinne vya kuchakata Samaki, lakini vyote vimekufa kimebaki kimoja tu cha Musoma Fishing Process kwa sababu ya changamoto mbalimbali ikiwepo ukosefu wa miundombinu rafiki wa uwanja wa ndege ambao ungeweza kusafirisha mazao ya samaki kwenda nje na sasa tunasafirisha malighafi kwenda Nairobi ili yaweze kuchakatwa yatoke nje.
Sasa ningetaka kujua mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kwamba inatatua changamoto mbalimbali ili viwanda vyetu vile vifufuliwe na kuweza kuuza mazao ya samaki na sio malighafi ya samaki? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, ni kweli kwamba viwanda vilikuwepo kwenye Mji wa Musoma na ukanda wote wa Ziwa Tanganyika upande wa Mkoa wa Mara na sasa kiwanda kimoja kinaendelea kufanyakazi. Lakini nitoe tu ufafanuzi kwamba viwanda vingi pia havifanyikazi kwa sababu ya matatizo ya kiuendeshaji, matatizo ya kimenejimenti ya wenye viwanda wenyewe. Sababu sio moja tu kwamba miundombinu inayohusiana na kuongeza masoko na kadhalika ndio inayosababisha hiyo. Viwanda vingi vya wawekezaji hasa vya samaki vimekumbwa na tatizo la uendeshaji wa viwanda hivyo, matatizo ya kimenejimenti. Kwa hiyo, Serikali kama Serikali tuko tunazungumza nao na kuona ni kwa namna gani viwanda vile vinaweza vikafufuliwa au basi kuvikabidhi kwa wawekezaji wengine binafsi ili viweze kuendelea kufanyakazi. Kwa sababu…
MHE. FURAHA N. MATONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Ni lini Serikali itajenga chanja za kuanika dagaa Kanda ya Ziwa ili wafanyabiashara hasa akinamama walioko kule waweze kupata masoko lakini pia waweze kupata faida katika biashara zao wanazozifanya? (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana mwaka wa fedha ujao unaoanza tarehe 1 Julai, Wizara na Serikali kwa ujumla tumekubaliana na Benki ya Wakulima – TADB kutoa mikopo kwa wavuvi na kwa wafugaji. Kwa hiyo, ninaamini Mheshimiwa Furaha atahamasisha wananchi na hasa wanawake katika Mji wa Mwanza ili waweze kujitokeza na kupata fursa hii ambayo wavuvi wote wanayo katika nchi yetu, lakini pia wavuvi ambao watakuwa wako kwenye vikundi na wale wavuvi ambao watakuwa wanaweza kufanya shughuli hii binafsi binafsi. (Makofi)
MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua mpango na kazi kubwa ya Serikali ni pamoja na kuweka mazingira mazuri na mazingira wezeshi kwa wavuvi hasa kuimarisha masoko kwa sababu baada ya bidhaa kupatikana ndio ukuaji wa viwanda kwenye maeneo mengine.
Nilitaka nijue Mpango Mkakati wa Serikali mlionao kushughulikia na kukimbilia soko la mpakani kati ya Tanzania na Kenya kuweka soko pale la samaki kwa ajili ya maboresho na ukuaji wa viwanda hivyo ambavyo vinazungumzwa vya Musoma. Nataka nijue Mpango Mkakati wa Serikali mlionao. (Makofi)
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, nimshukuru sana Mheshimiwa Chege kwa ufuatiliaji wake hasa kuhusiana na masoko ya mazao ya uvuvi kuelekea kwenye nchi jirani ya Kenya. Tumeliona tatizo hilo na tuna mpango sasa wa kuweka utaratibu hasa kwenye mpaka ule wa Sirari ili kwamba wavuvi wanapopeleka mazao yao kwenda nchi ya Kenya au mpakani wasipate usumbufu ambao walikuwa wakiupata huko nyuma. Kwa sasa tutaweka utaratibu ambao utawasaidia wavuvi hawa kulipa tozo mbalimbali ambazo wanatakiwa kulipa za halmashauri lakini pia za Serikali Kuu, kwa urahisi zaidi ili waweze kulipata soko la nchi jirani ya Kenya ambalo mara nyingi kwa kweli linawapa bei iliyo nzuri.
Kwa hiyo, tutashirikiana na wenzetu walioko pale mpakani upande wa Wizara nyingine Wizara ya Fedha na Mipango na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (Uhamiaji) ili kuweka urahisi utakaowafanya wavuvi wetu waweze kulipata soko la nchi jirani kwa urahisi zaidi. Ahsante sana. (Makofi)