Supplementary Questions from Hon. Dr. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (4 total)
MHE. MWANNE I. MCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba niulize maswali madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa hivi karibuni kulikuwa wawekezaji kutoka China ambao walitarajia kufika Mkoa wa Tabora tarehe 22 na safari yao kuahirishwa Air Port baada ya kuwa na dosari ndogo ndogo za visa. Je, ni lini sasa wawezekezaji hao ambao wataanzia kusimamia na kuangalia maeneo ya Kiwanda cha Tumbaku pamoja na Manonga safari yao itakamilika?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili, kwa kuwa Kiwanda cha Nyuzi kina historia ndefu na mpaka sasa hivi ninavyosema kiwanda hicho hakifanyi kazi na wameondoa mitambo yote ambayo ilikuwepo pale. Je, Serikali iko tayari kufuatilia mitambo hiyo ambayo imeng‟olewa pale?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na Kiwanda cha Manonga kwamba kulikuwa na Wachina wanakuja, wameishia Air Port kwa sababu ya masuala ya Immigration na mambo mengine, ni lini sasa watakuja. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kuwasiliana nao ili kuona lini watakuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini suala la pili kuhusiana na Kiwanda cha Nyuzi kwamba Serikali iko tayari kufuatilia sasa kuhakikisha kwamba kinafanya kazi. Nimhakikishie kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Serikali iko tayari kufuatilia na kuhakikisha kwamba kinafanya kazi.
MHE. MWIGULU L. NCHEMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Ujenzi wa barabara ya Singida, Sepuka, Ndago, Kizaga kwa kiwango cha lami ni ahadi ya Mheshimiwa Rais na ipo kwenye ilani ya uchaguzi ukurasa wa 56. Kwa kuwa upembuzi yakinifu katika barabara hii ulishafanyika na Mheshimiwa Naibu Waziri alishafanya ziara kukagua masuala yote katika barabara hiyo ni lini sasa ujenzi kwa kiwango cha lami utaanza katika barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mbunge nakupongeza sana kwa sababu nimefuatilia kweli barabara hii muhimu na niseme tu ni mwaka wa fedha uliopita ndiyo tulikuwa tunaendelea kufanya kazi ya usanifu wa kina kwa ajili ya Ujenzi wa lami wa barabara hii. Mheshimiwa Mbunge vuta subira kwa sababu tunakwenda kwa hatua baada ya kukamilisha hili zoezi ambalo tulikuwa tunalifanya sasa tunatafuta fedha ili tuweze kuijenga kwa kiwango cha lami barabara hii muhimu.
MHE. MWIGULU L. NCHEMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri.
Mheshimiwa Naibu Spika,kwa kuwa Watanzania wanapokwenda nje ya nchi sasa hivi wanatumia scarf, t-shirt za bendera za Taifa na tai kama hizi, ile Mwigulu style na wanatambuliwa kuwa ni Watanzania.
Kwa nini Serikali isiidhinishe tu kwamba scarf, tai za Taifa na bendera za Taifa ndiyo itakuwa vazi la taifa kwa sababu nchi hii hawawezi wakavaa uniform ili kutambulisha kwamba lile ndiyo Vazi la Taifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu yeye amekuwa mzalendo kwelikweli katika kuhamasisha masuala ya utamaduni nchini Tanzania, lakini vilevile kama amabvyo ametaka kujua kwamba vazi ambalo amekuwa akilitumia yeye binafsi mara nyingi, kwa maana ya vazi la tai ambayo ina bendera ya Taifa, kwanini sisi kama Wizara tusilirasimishe rasmi liweze kuwa Vazi la Taifa.
Niseme kwamba kwa sababu kwa sasa hivi kuna mchakato ambao tumeshauanzisha na tumeshaufufua ambao ni mchakato mpya, lakini pia niseme kwamba maoni ambayo ameyatoa tunayachukua na tutayafanyia kazi ili tuangalie kama kuna huo uwezekano. Ahsante sana.
MHE. MWIGULU L. NCHEMBA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Kibaya, Urughu - Mtekente - Mtowa na Sheluwi ni moja ya barabara inayobeba uchumi wa Iramba na katikati ya Mtekente na Mtowa pana daraja la kisasa sana limejengwa.
Je, kwa nini Wizara ya Ujenzi isiipandishe barabara hii kufuatana na umuhimu wake ili iwe chini ya TANROADS iweze kujengwa kwa kisasa na iweze kusaidia wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, ni kweli Waheshimiwa Wabunge watakubaliana na mimi kwamba tumekuwa na chombo hiki TARURA na dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba TARURA inafanya kazi nzuri na kweli nitumie nafasi hii niwapongeze TARURA kwa sababu wameanza vizuri maeneo mengi, wanafanya vizuri na kumekuwa na mchakato wa kuzitambua barabara zetu kwa nia dhabiti ya kuweza kuziboresha.
Mheshimiwa Spika, nimuombe Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu wa kupandisha barabara uko kisheria na kama saa nyingine itapendeza watumie nafasi hiyo kwa vikao walivyonavyo ili waweze kuleta mapendekezo na sisi kama Serikali tutazama kwa namna hiyo kwa mujibu wa taratibu zilizokuwepo ili kama itakidhi kupandishwa basi Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana atafanya hivyo. Lakini kimsingi ni kwamba TARURA ipo kwa ajili ya kuboresha barabara zetu na nifahamishe tu kwamba itaenda kujenga barabara zetu mpaka kiwango cha lami.