Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Mussa Ramadhani Sima (15 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, napongeza sana juhudi zinazofanywa na Mheshimiwa Waziri katika kuboresha na kutatua migogoro ya wafugaji na wakulima. Niiombe Wizara mambo yafuatayo:-
(1) Ije na mfumo mpya wa pembejeo ili kuondoa upotevu wa fedha na itasaidia kutathmini hali ya kilimo nchini.
(2) Mkoa wa Singida ni maarufu kwa kilimo cha alizeti na vitunguu, naiomba Wizara ituletee mbegu bora ili tukidhi bidhaa ghafi nchini.
(3) Cattle holding ground iliyoko Singida Mjini takribani kilomita tano toka centre, naiomba Wizara itupatie heka 21 ambayo ni sehemu ya eneo hilo ili tuweze kutengeneza Trading Area na kuboresha Mji wetu wa Singida, ukizingatia eneo limepitiwa barabara kuu.
(4) Naiomba Wizara iwasaidie wafanyabiashara wa ngozi kupata soko la uhakika la ndani na nje ya nchi, hasa Afrika Mashariki kwani sasa hivi soko hakuna na bei imeshuka kutoka 2000 kwa kilo mpaka 100 kilo. Wizara ije na mpango maalum wa kuboresha suala hili.
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017- Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nami nimshukuru Mwenyezi Mungu lakini kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kutoa mchango wangu katika Bunge hili, nichukue fursa hii kuwashukuru wananchi wangu wa Jimbo la Singida Mjini walionipa ridhaa hii na mimi niwaahidi utumishi uliotukuka.
Pia nichukue fursa hii kushukuru Chama changu cha Mapinduzi, lakini pia niishukuru Kamati yangu ya Viwanda na nimpongeze pia Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji wake mzuri ambapo mambo mengi ambayo na mimi niliyatarajia sasa nimeyaona yakiwa humo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye kuchangia hoja ya viwanda. Nianze na EPZA kwa maana ya pale Kurasini, eneo lile ni muhimu sana na niipongeze sana Serikali kwa uwekezaji mkubwa ambao unaendelea pale. Mambo yaliyomo mule ni mengi sana na nimejifunza vitu vingi mle ndani na ni vizuri sana Watanzania wakajua kwamba leo hii Serikali yetu kwenda kwenye viwanda wala haijakosea. Kuna uwekezaji mkubwa na pale wanatengeneza jeans ya grade A, suruali ile inauzwa Marekani, Uingereza na German, ina-compete kwenye soko la Kimataifa. Hali kadhalika pale wanatengeneza mpaka ATM card mpaka voucher tunayoweza kuitumua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hoja yangu ni nini hapa? Hatuwezi kuendelea kuwa-entertain wawekezaji halafu wakawekeza na sisi tukabaki tu kutumika. Niiombe Serikali ifike mahali tuwe na mpango wa ku-adopt teknolojia kutoka kwa wenzetu hawa wageni lakini isitoshe ku-adopt kama inawezekana kuinunua teknolojia ifike mahali tuinunue teknolojia. Baada ya huo muda wakiweza kuondoka na sisi tuweze kuendesha hivyo viwanda ambavyo vipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine ni la ajira. Tumezungumzia kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi asilimia 40% ya ajira. Nataka jambo hili tuliweke wazi. Tunao vijana zaidi ya 800,000 wanaingia mtaani kila mwaka na wote hawa tunazungumzia ajira. Hapa palihitaji ufafanuzi mpana kidogo. Najua utafiti ulifanyika ndani ya chama changu na Serikali yangu wanajua kabisa kwamba ajira hii inawezekana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka tuliweke vizuri, ni vizuri tukaliweka katika mazingira ambayo yanaeleweka. Tunayo service industry, tuna kiwanda cha huduma, kote huku unakokuona hotelini, kwenye masoko, usafirishaji, mazingira haya yote yanazungumzia ajira ya Watanzania. Hoja yangu hapa ya msingi ni lazima sasa Serikali ijikite kwenda kuangalia mikataba ya hawa Watanzania wanaoajiriwa kwenye haya maeneo. Ni namna gani wanafaidika na namna gani wanaweza kujikimu kwenye maisha yao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo wenzangu walizungumza awali lazima Serikali ijikite kwenye agro-product. Tuna kila sababu sasa ya kuwekeza zaidi kwa wakulima wetu ambao tunajua kila mkoa sasa hivi unazalisha na hiyo ago-product itatusaidia sasa kuboresha viwanda vyetu. Connectivity ionekane ya mkulima, ya mchuuzi na mtumiaji, hii pia inaongeza wigo wa ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja ya kulinda viwanda vyetu vya ndani. Amejaribu kuizungumza Mheshimiwa Waziri namna ya kulinda viwanda vyetu vya ndani, mimi nilitaka nishauri na lazima tuliweke wazi. Ufafanuzi hapa ulitakiwa uwekwe bayana, tunapovipeleka viwanda vyetu vya ndani kwenye tenders kwa maana kwamba tumetangaza tender na vyenyewe vinakwenda ku-compete, kazi ile ni ngumu sana. Tunatakiwa katika asilimia 100% tuwape kwanza viwanda vya ndani asilimia 40% halafu asilimia 60% waingie kwenda ku-compete na viwanda vingine vya nje, hapa tutakuwa tumeweza kulinda viwanda vyetu vya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe mfano mdogo, tuna Kiwanda cha TANALEC kinachotoa transformer bora East Africa na sisi Serikali mle ndani ni wabia. NDC wana 10% lakini TANESCO wana 20%, sisi ni wabia, maana yake sisi ni member wa Bodi ya TANALEC lakini kwa bahati mbaya sana tunaagiza transformer kutoka India. Ukiagiza transformer kutoka India, wenzetu Serikali ya India inatoa ruzuku ya 10% kwenye viwanda vyake vya ndani, kwa hiyo, uzalishaji unakuwa mkubwa inafikia mahali wanatafuta masoko kwa cheap price. Kwa hiyo, ukija ukiwaingiza TANELEC kwenda ku-compete wenzetu wanakuwa chini halafu hawa wa TANALEC wanakuwa wako juu na ukizingatia TANALEC wako Tanzania na sisi tunamiliki percent ya TANALEC. Kwa hiyo, niwaombe sana tunapokwenda kuhakikisha tunalinda viwanda vyetu vya ndani ni lazima tuzingatie mambo haya ya msingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine, tuna kiwanda cha Urafiki, tuna asilimia 49% pale kwenye kiwanda kile na Wachina wana asilimia 51%, ndiyo wasemaji wakubwa wa kiwanda, lakini uzalishaji wa pale ni hafifu na Kamati imeeleza pale kuna madeni ya kutisha. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Waziri tufike mahali kama ambavyo tumeshauri sisi ndiyo tu-hold share ya Kiwanda cha Urafiki. Sasa leo tunavaa khanga na vitenge kutoka China lakini tuna Kiwanda cha Urafiki, niombe sana Serikali iliangalie suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mahali siku za nyuma tulijaribu kulinda viwanda, niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge, tuna Mufindi Paper Mills. Kiwanda hiki cha Mufindi kinatumia rasilimali za Tanzania na ikumbukwe miaka ya nyuma 2007 cubic meter moja walikuwa wanauziwa nusu ya bei badala ya 28,000 wanauziwa 14,000 na bado ile pulp wanaisafirisha kwenda Kenya na wakitoka Kenya importation ya huku tumewapunguzia mpaka 10% Serikali inaingia hasara. Wakenya hawana misitu, misitu iko Tanzania. Kwa hiyo, niiombe Serikali iende ikaliangalie hili, hili jambo ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niende moja kwa moja nizungumzie sekta ya ngozi. Mheshimiwa Waziri amezungumzia sekta ya ngozi hapa kwamba wataiangalia na wataboresha mpaka kufikia kiwango cha wet blue. Wet blue jamani ni sawa na kutengeneza raw material, ni sawa na kutengeneza ghafi. Leo hivi viwanda vilivyopo vya wet blue tunazungumzia temporary turning maana yake ni sawa na mtu anakwenda kwenye harusi unamuogesha tu halafu anaenda hana viatu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi leo tumepeleka fedha kwenye SIDO nimeona pale, zaidi ya shilingi bilioni sita lakini tunasafirisha ngozi hatuwezi kwenda huko. Mheshimiwa Waziri ni shahidi maghala yamejaa ngozi. Niombe sana Serikali sasa ichukue hatua ya haraka kuhusu suala hili. Vile viwanda ni temporary, umezungumzia viwanda nane hakuna viwanda nane Mheshimiwa Waziri, kama vinazidi sana ni vinne na bado ni temporary kwa hiyo Tanzania bado hatuna viwanda hivyo. Niombe sana jambo hili liangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nishukuru tumezungumzia habari ya regulatory bodies, tu-harmonise vifanye kazi kwa pamoja kuondoa mlolongo mrefu ambao hauna tija. Jambo lingine tumezungumzia model, nimeona kwenye kitabu hapa, wenzetu wa Vietnam, China, Korea Kusini na wengine wote walianzia hapa tulipo. Kwa hiyo, niombe sana tuangalie hili tabaka la kati kwa maana ya middle class ndiko mahali ambapo tunatakiwa kujikita zaidi kuhakikisha kwamba Watanzania wanaweza kujikimu na maisha yao juu ya uwepo wa viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tunapozungumzia SIDO lazima tuweke connection na VETA. Hivi vitu lazima vihusiane, SIDO na VETA. Hatuwezi kuishia tu SIDO, VETA inafanya nini ili iweze kutusaidia? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Waziri jambo la mwisho kwamba sasa wakati umefika kama tumeamua Tanzania iwe nchi ya viwanda, tuwe na siku ya viwanda Tanzania. Jambo hili litawarahisishia wafanyabiashara na wenye viwanda kukutana na kujadili changamoto wanazokutana nazo hata kila mwaka, hata kila baada ya miezi sita, jambo hili litatusaidia sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niende mbali zaidi. Leo wenzetu wa Rwanda wanazalisha alizeti. Singida sisi ni maarufu sana kwa alizeti na bahati mbaya sana sijaona kama tunaenda kuanzisha kiwanda cha alizeti Singida, niombe sana suala hili liangaliwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia sisi Singida ni wafanyabiashara wazuri sana wa vitunguu. Mheshimiwa Waziri karibu sana tuje tuanzishe soko la Kimataifa pale Singida ili tuweze kuwasaidia wananchi wa pale. Rwanda leo wameweka 25% ya kodi hata Kenya wenyewe nao wanaweka lakini sisi tukitaka kuweka hapa mpaka tukaulize East Africa. Mheshimiwa Waziri naomba agenda hii uilete vizuri ili tuweze…
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, natanguliza pongezi kwa kuteuliwa kwake Mheshimiwa Waziri na hongera kwa uwasilishaji mzuri, naomba nizungumzie mambo machache yafuatayo:-
Kwanza, Serikali ilitoa waraka wa responsibility allowance, lakini mpaka sasa haijaanza kutekelezwa ili kuwawezesha viongozi wetu kwenye Idara ya Elimu.
Pili, kumekuwa na tatizo kubwa sana la madeni ya walimu, Serikali lazima ije na Mpango wa kukomesha madeni ya walimu.
Naomba soko huria la vitabu lidhibitiwe kuendana na mitaala ya elimu. Nashauri kuwe na formality moja nchi nzima ya vitabu.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nichukue fursa hii kukushukuru, lakini pia nimpongeze sana Mheshimiwa Profesa Sospeter Muhongo kwa uwasilishaji wake mzuri, lakini kwa kazi yake. Hakuna ubishi kwamba mzee huyu kwa kweli ana-fit kwenye nafasi yake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na umeme; katika Jimbo langu la Singida Mjini ninavyo vijiji 13 na mitaa 13 ambayo haina umeme. Katika taarifa yake Mheshimiwa Waziri, imeonesha wazi kwamba kutakuwa na KV 400 zinapita Singida kwenda Shinyanga, lakini pia kwenda Namanga. Nimuombe sana tusiwe watazamaji, lakini tusiwe watu wa kupisha mradi unapita unaenda kwa wengine na sisi tuwe sehemu ya mradi. Naomba Mheshimiwa Waziri utushirikishe na ikiwezekana sasa vijiji vyangu vyote hivi nilivyovitaja na mitaa viweze kupatiwa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeguswa kidogo na suala la vinasaba. Kabla sijaendelea na mimi nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuweka vinasaba ambavyo vimetusaidia kwa kiasi kikubwa sana; vimepunguza uchakachuaji wa mafuta kwa asilimia kubwa na kama haitoshi vimedhibiti mafuta ya magendo (smagling product). Vinasaba hivi vimedhibiti pia on transit product. Yale mafuta yanayopita hapa kwenda nchi za jirani vimedhibiti, lakini pia hata yale mafuta ambayo yanasamehewa kodi, vinasaba hivi vimetusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama haitoshi vimeongeza makusanyo ya kodi na vimeleta ushindani kwa wafanyabiashara wa mafuta nchini. Nikuombe sana na niwaombe Waheshimiwa Wabunge na wananchi tufike mahali tuiunge mkono Serikali, tuwe waadilifu na kama haitoshi kwa wale wafanyakazi wetu ambao tunawatuma kwenda kubeba mafuta haya sasa wawe makini na kazi hii kwa sababu Serikali kwa kweli ina mkono mrefu na nikuombe Mheshimiwa uifanye kazi yako vizuri, nakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nigusie suala la madini. Kwa kweli, kwa Mkoa wangu wa Singida tunayo madini mengi sana na ya kutosha, lakini hali tuliyonayo pale haifanani na yale madini tuliyonayo pale. Nataka niiombe Serikali sasa iwaangalie wale wachimbaji wadogo waweze kupewa fedha na kama haitoshi, wachimbaji wadogo wale waweze kupewa elimu, kwa maana sasa waendane na teknolojia ya uchimbaji ya sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tatizo ninaloliona pale, naliona tatizo kubwa moja, GST. Mamlaka ya GST siyaoni, GST wanavyoonekana kwa sasa kazi yao haina meno. GST wakati umefika sasa wafanane kama EWURA kwa sababu, na wao nao ni wakala, wapewe hatimiliki. Sasa hivi makampuni yote tunayoyaona makampuni makubwa ndio ambayo yanafanya utafiti na wakishamaliza utafiti ule hawako tayari kutupa hali halisi ya madini tuliyonayo pale kwenye maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejionea, nitoe mfano wa Shanta Company Limited pale Singida walitoa eneo la Mwintiri kwa wachimbaji wadogo, lakini eneo lile wachimbaji wadogo wameshindwa kuliendeleza kwa sababu hawana utafiti, hawajapewa ramani nzima ya eneo lile lililopo pale. Sasa kwa hali hii ni lazima Serikali ije na mpango kama ni sheria, kama ni nini, ije tuweze kuisimamia. GST wapewe mamlaka wawe mawakala ambao wanaweza kusimamia raw data na sio watu wa kupewa processing data. Huu sio wakati wa processing data. Wawe ni watu ambao wana raw data na wawekezaji wote wanaokuja waanzie GST, hii inaweza kutusaidia sisi na wale wachimbaji wetu wadogo walioko kule wanaweza kupata mwelekeo wa kuchimba madini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kama ambavyo alitangulia msemaji mmoja tuko naye kwenye Kamati ya Viwanda na Biashara alizungumzia namna ambavyo TANELEC, kiwanda ambacho sisi tuna hisa, kiwanda ambacho kimefika mahali sasa Serikali imekitelekeza. Mimi nizungumzie upande mdogo wa REA. REA waliwapa kazi Symbion, Symbion wamekwenda kuomba kutengenezewa transfoma TANELEC, hivi tunavyozungumza zimetengenezwa transfoma za zaidi ya shilingi bilioni mbili zimekaa pale. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia kama Kamati transfoma ambazo Symbion walizi-order ziko pale TANELEC, kwa hiyo, wametuingizia hasara Serikali. Nikuombe Mheshimiwa Waziri na kuna taarifa kwamba ulifika pale na ukatoa maagizo. Na sisi tukuombe ifike mahali sasa hawa watu wanaopewa tender, tender hizi lazima ziangalie kwanza viwanda vya ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka wakati nachangia kwenye viwanda nilitoa ushauri kwamba kabla hatujaenda kwenye kutangaza tenda ya kuingiza viwanda vyetu kwenye tender ni lazima kwanza ikiwezekana 40% ibaki kwetu, 60% waende wakashindanishwe kwenye tender, hali hii itatusaidia sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia wenzetu wa Symbion wanaagiza transfoma kutoka India. Na nilitoa mfano siku ile wenzetu kule wanatoa ruzuku kwenye viwanda vya ndani 10% kwa kila kiwanda. Uzalishaji unakuwa mwingi kwa hiyo, wanatafuta sehemu ya dumping, sasa sisi hatuwezi kuendelea kuwa dumping place. Niombe sana na sisi sasa tufike mahali tuone umuhimu wa viwanda vyetu vya ndani, hali hii itatusaidia kuhakikisha kwamba Tanzania inakuwa nchi yenye viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Singida Mjini tumejaaliwa kuwa na chanzo cha umeme ambacho ni upepo na mpaka sasa sioni juhudi za Serikali kuhakikisha kwamba rasilimali hiyo ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia tunaweza kuitumia ipasavyo, sioni. Maana tunakoelekea tunaelekea kwenda ku-misuse rasilimali ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niuone mpango wa Serikali wa kuhakikisha rasilimali ile iliyojitokeza kwenye eneo letu la Singida Mjini ya umeme wa upepo, Serikali inakuja na mpango wa kuwekeza ama kutafuta wawekezaji. Na kwa bahati nzuri tayari walishajitokeza wawekezaji, kwa bahati mbaya sijajua wameishia wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wako Wind East African Company walijitokeza, lakini kama haitoshi wako Power Pull nao walijitokeza. Sasa niiombe Serikali, kama wawekezaji walijitokeza na wameonesha nia, kama kuna mahali tunaweza kuwa-support basi tuwa-support waje wawekeze umeme pale Singida. Tunajua umuhimu wa umeme kwenye maeneo yetu, sisi tumejaaliwa hilo na maeneo yetu tuna uzalishaji mkubwa sana. Tunauhitaji umeme huu kwa kasi kubwa, utatusaidia kuinua uchumi wetu hasa kwa maeneo yale ya Kisasida ambayo tayari pale tuna uzalishaji na ndio tuna kilimo cha umwagiliaji cha mboga mboga.
Mheshimiwa Waziri nikuombe sana ifike mahali, sisi ndugu zetu wa Singida Mjini pale tunakutakia kila la heri, tunakuomba ufike ili uweze kutuwezesha na sisi kuweza kuupata huu umeme na uchumi wetu uweze kukua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya na mimi nimalizie kwa kumshukuru sana Mheshimiwa Rais, kwa kweli kumteua baba huyu ametusaidia sana sisi. Ameionesha dhamira ya dhati ya nchi yenye viwanda kwamba inawezekana kwa sababu tayari tuna uwezo wa kupata umeme kwa kila eneo. Baada ya kusema haya, naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji na mikakati mizuri inayomkomboa Mtanzania wa hali ya chini. Niombe mambo machache.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama za upimaji ardhi zipungue zaidi ili kumuwezesha mwananchi kuweza kumiliki ardhi. Niiombe Serikali itusaidie kupima ardhi ya maeneo yaliyo pembezoni ya Singida Mjini, karibu kata nane, mfano, Mwankoko, Uhamaka, Kisaki na kwingine ili kuwezesha mwananchi kukoposheka na kuinua uchumi wa maeneo hayo, hali hii itatusaidia kuwa na mpango mzuri wa ujenzi na makazi.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri kwa uwasilishaji mzuri. Kwa kuwa Serikali kupitia Wizara hii ilitoa agizo la kuwauzia MPM miti kwa nusu ya bei, that is cubic meter 1 – 14,000 badala ya 28,000 tangu mwaka 2007 mpaka sasa hivi Serikali inaingia hasara isiyopungua shilingi bilioni 2.8 kila mwaka. Naomba Wizara ije na mkakati wa kuondokana na tatizo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa karatasi inatengenezwa Kenya, lakini misitu iko Tanzania na bado importation ya karatasi ina punguzo la kodi la asilimia10 badala ya asilimia 25 ninaiomba Serikali ije na mpango wa kuhimiza viwanda vyetu kama MPM kutengeneza karatasi badala ya mifuko peke yake na tuongeze kodi ya importation iwe asilimia 25.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru, lakini nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri.
Niende moja kwa moja katika Wizara hii ya Maji, nadhani umefika wakati sasa Serikali ijielekeze na ielekeze nguvu zake zote pale. Nimeona wametutengea shilingi bilioni mbili point nne, niombe sana kama walivyoomba wenzangu kwamba, fedha hizi sasa ifike wakati zije zote, ili tuweze kukamilisha miradi yetu ya maji iliyoko pale katika Jimbo la Singida Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niishukuru Serikali kwa mradi wa maji mkubwa ambao uko pale katika Kata yangu ya Mwankoko. Changamoto kubwa iliyopo pale, mradi ule uko pale, lakini wananchi wa Mwankoko hawafaidiki na ule mradi ulioko pale. Kama hiyo haitoshi, wananchi wale walipisha ule mradi kwa maana kwamba, sasa walipaswa kulipwa fidia; uthamini umefanyika mara ya kwanza zaidi ya milioni 800 hawakulipwa! Umekwenda umefanyika mara ya pili, sasa hivi tunazungumzia bilioni moja na milioni 500 hazijalipwa mpaka sasa! Nilitarajia kuziona kwenye makabrasha haya ambao Mheshimiwa Waziri ametuletea au kwenye kitabu hiki kwamba, shilingi bilioni moja point tano wananchi hawa sasa wanakwenda kulipwa fedha zao za fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri wakati anakuja kuwasilisha awaeleze wananchi wa Mwankoko kwamba, watalipwa fedha zao lini, ili kuondokana na hii adha ambayo inaendelea sasa. Na unafahamu kabisa kuchelewa kulipa zaidi ya miezi sita maana yake unakoelekea sasa wafanye uthamini wa tatu tunaenda kuzungumzia shilingi bilioni tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini uko mradi mwingine wa maji ambao uko eneo la Kisaki unaitwa mradi wa ILAO. Kwa bahati mbaya sana pale nako kuna zaidi ya shilingi bilioni tatu wananchi wanatakiwa walipwe, kwa ajili ya fidia wamepisha mradi wa maji wa ILAO. Vimechimbwa visima viwili pale Kisaki, vile visima viwili kwa hali iliyoko sasa tunakoelekea maana yake wananchi watakosa maji! Kisima kimoja kilikuwa kinatoa maji cubic metre 250 kwa saa na sasa zinashuka mpaka zimeenda 170 kwa muda wa mwaka mmoja! Kwa mwaka mwingine unaofuata, miaka miwili maana yake wananchi wa eneo lile wanaotegemea maji ya Mradi wa ILAO watakosa maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, anapokuja ku-wind up lazima atueleze kwamba, kwa namna gani sasa wananchi hawa tunaweza kuwakomboa na hii adha ambayo inajitokeza kwenye hili eneo la Kisaki. Kwa sasa wananchi wa eneo lile hawafaidiki na ule mradi! Wanalinda mradi, wanalinda maji na visima vilivyoko pale, lakini wao hawapati maji! Niiombe sana Serikali ifike mahali iwaonee huruma wananchi ambao wamepisha eneo lile kwa ajili ya mradi wa maji na wao wafaidike na yale maji, lakini waweze kulipwa fidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uko mfumo wa maji taka. Nimwombe Mheshimiwa Waziri, tunayo maabara ya maji, sasa hebu zipewe nguvu hizi maabara za maji zitusaidie kuchunguza kwa sababu tukiacha sasa mfumo wa maji taka huu ukaenda holela hatutakuwa na uhakika na maji ambayo tunayapata sisi kwenye eneo lile! Bahati nzuri tayari tumekwishakaa, tumeandaa mradi mzuri ambao umeshafanyiwa upembuzi yakinifu kwa ajili ya mfumo wa maji taka, unahitaji fedha. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, tunahitaji fedha, sisi tumeshajiwekea utaratibu mzuri juu ya ule mfumo wa maji taka, ili tuondokane na hili tatizo ambalo liko pale katika Jimbo la Singida Mjini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamezungumzia juu ya Wakala; Wakala wa Maji Vijijini nadhani ndiyo suluhu. Pia Waheshimiwa Wabunge wameonesha hapa Mheshimiwa Waziri fedha atazipata wapi, fedha hizi wameeleza kwenye mafuta, tuongeze pale kama wanavyofanya EWURA shilingi 50, tuweke 50 nyingine, lakini kama haitoshi wamekwenda kwenye simu! Wala hakuna tatizo hatuhitaji kulijadili jambo hili! Nimwombe Mheshimiwa Waziri aliweke mezani, fedha zipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, ninaporudi mimi kule Jimboni swali hili linakuwa swali gumu sana; wananchi wangu hawana maji, tumewatengea shilingi bilioni mbili point nne! Bilioni mbili hizi tunaomba zifike, ili tuweze kuzisimamia na hizi fidia ambazo nimezizungumza za Mwankoko naomba nazo pia ziweze kuletwa.
MWENYEKITI: Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nichukue fursa hii kukushukuru sana, lakini nikupongeze kwa ukakamavu ambao unauonesha hapa Bungeni, Mungu akubariki sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri na ama hakika Watanzania sasa wanasubiri kuona mabadiliko ambayo tumewaahidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, niende moja kwa moja kwenye hoja, nianze na reli ya kati. Tunajenga reli ya kati kwa standard gauge lakini liwe jambo jema sana tuzingatie vituo vyote. Nafahamu pale Singida itapita Manyoni, Itigi na kuendelea mbele, lakini reli ya kati ilikuwa inakwenda mpaka Singida Mjini. Sehemu pekee ambayo ndiyo sehemu ya kibiashara iko pale mjini. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri katika vituo vyake asiache kituo cha Singida Mjini, almaarufu reli yetu ile tulikuwa tunaiita Kamnyampaa maana yake ndiye mzee mwenyewe yule. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili, kwenye bajeti tumezungumzia ongezeko la kodi ya mitumba kutoa 0.2 mpaka 0.4. Ni lazima tuwe wakweli, Watanzania bado hatujawa na maandalizi ya kutumia viwanda vyetu vya ndani, ya kutumia nguo zilizoko ndani badala ya kutumia mitumba ambayo ni bei rahisi. Leo hii ukitazama vizuri sisi wote tunatumia sana mitumba kuliko nguo za dukani. Tukiongeza kodi maana yake tunaongeza thamani ya mitumba. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Waziri amezungumza kuna tatizo la kiafya na mambo mengine. Mpaka tunafikia umri huu kwa kweli wajibu wa Serikali ni kuwaelimisha Watanzania juu ya afya kuliko kuongeza kodi. Kama hiyo haitoshi, tumezungumzia ngozi, kwamba Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji itakuja na mpango madhubuti wa ku-deal na sekta ya ngozi, ni mpango gani huu? Tunazungumzia sekta ya ngozi wakati hatuna viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda hivi vinavyozungumzwa hapa vyote hivi vinatengeneza wet blue, ni temporary turning, ndivyo viwanda tulivyo navyo. Viwanda vinavyofanya finishing, utazungumzia Himo na Moshi Tanneries kule, viwanda viwili haviwezi kukidhi haja ya kutengeneza bidhaa kwa Watanzania wote milioni 50. Tunazungumzia sekta ya ngozi ambayo leo ngozi inaoza kwenye ma-godown, tuna tani karibu 5,000 zinaoza, halafu tunasema tutakuwa na mpango madhubuti. Nilitarajia mpango madhubuti ni kufungua milango, tuondoe ile kodi ya zaidi ya asilimia 80 ya exportation ili hawa watu waweze kuuza ngozi yao East Africa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeua kiwanda cha Mwanza Tanneries kwa sababu ya ukaribu wa ziwa, kitu ambacho siyo kweli. Hebu twende tukaangalie ile Jinja Tannery, ni mita 200 tu pale lakini kiwanda kinafanya kazi, leo tunaendelea kuua viwanda. Kwa hiyo, niombe Mheshimiwa Waziri, kwenye suala hili la ngozi, huu mkakati madhubuti unaozungumzwa ni vizuri ungeletwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni miongoni mwa wajumbe wa Kamati ya Viwanda na Biashara na nimeshiriki kwenye kikao cha wadau, wachuuzi wa ngozi na wale wenye viwanda vya ngozi, hakuna majibu thabiti yaliyotolewa ni namna gani tuna-deal na viwanda vya ngozi. Leo hii ngozi inaoza, ngozi imeshuka bei imefika mpaka Sh.100, inatupwa, lakini tunasema tumempa Waziri sasa aje na mkakati. Mheshimiwa Waziri wa Fedha, hakuna mkakati na kama upo uletwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la mafuta, tumeweka asilimia 10 kwenye importation ya crude palm oil, lakini mafuta yaliyoko ndani leo bado VAT inatutesa. Nilitarajia kuiona Serikali sasa inaondoa VAT katika bidhaa inayosindikwa. Tumendoa VAT katika bidhaa ambayo haisindikwi lakini mkulima yule yule ambaye analima alizeti, anaipeleka kiwandani, ikishatoka pale inalipiwa kodi asilimia 18, maana yake utakuwa hujamsaidia. Kwa hiyo, niombe sana tuondoe VAT pia kwenye mafuta yetu haya ya alizeti ambayo tunayatumia sasa, tutakuwa tumemsaidia mkulima wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wa Kenya kwenye mashudu wameondoa VAT na sisi tunategemea sana haya mashudu yatusaidie. Niombe na sisi tuondoe VAT kwenye mashudu. Hii nayo itasaidia wakulima wetu wadogo wadogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini na mimi nichangie kwenye zile shilingi milioni 50 ambazo Serikali inazitoa vijijini. Kuna mambo mawili hapa, tunazungumzia shilingi milioni 50 vijijini lakini hatuzungumzii shilingi milioni 50 kwenye mitaa. Kama sababu kwamba vijiji vina mamlaka ya kisheria, yawezekana mnatutofautisha hapo, mimi nina mitaa 50 na vijiji 20, sasa tunakwenda kuleta mgawanyiko katika jamii ambayo inaongozwa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Kama sababu ni kwa sababu vijiji vina mamlaka ya kisheria, basi ni vizuri sasa na mitaa hii ipewe mamlaka hayo hayo na wenyewe wapewe mgawanyo huo sawa, unless otherwise tuzungumzie shilingi milioni 50 vijijini kwenye vijiji na mitaa, hapo tutaelewana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini shilingi milioni 50 hii, wenzangu wamejaribu kuchangia nami naomba nishauri, tujifunze katika yale mabilioni ya Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, tusije tukazalisha mgogoro ambao hatukuutarajia. Tumekwenda na nia njema ya kuwakomboa Watanzania, lakini namna ya kwenda kusimamia zoezi hili la shilingi milioni 50 linaweza likawa mwiba mchungu sana kwetu hapo kesho.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niombe, kama tutashindwa kuanzisha Community Bank basi ni vizuri tutumie NMB kwa maana iko kila halmashauri, tuweke dawati litakalo-deal na hii shilingi milioni 50 li-act kama Community Bank. Tukiweka dawati pale NMB tayari usimamizi wa fedha zile utakuwa uko salama. Sisi wanasiasa tuwe sehemu ya kuwahamasisha watu wetu kuanzisha vikundi na kwenda kufungua akaunti, lakini watakaotoa elimu hiyo wawe ni watu wanao-deal na fedha, jambo hili litakuwa limetuokoa na tunaweza kwenda vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie usajili wa pikipiki. Asilimia 50 ya Watanzania leo wanatumia usafiri wa pikipiki. Vijana wetu leo wote unaowaona wamejiajiri kwenye usafiri wa pikipiki. Wanaolipa kodi na wanaochangia matibabu leo ni hao hao waendesha boda boda lakini tumeongeza thamani ya usajili wake kutoka Sh. 45,000 mpaka Sh. 95,000. Nilitarajia kuona utapungua badala ya kuongezeka.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunazungumzia Watanzania kupata ajira, wako ambao tayari wamejiajiri. Ni lazima tuwatengenezee mazingira bora ili waweze kuboresha sehemu zao hizo za kazi. Naomba jambo hili pia nalo tulitafakari kwa kina tuone ni namna gani tunaweza kuwasaidia hawa waendesha boda boda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie na property tax. Nichukue fursa hii kuipongeza sana Serikali kwa hatua madhubuti ambazo wameamua kuchukua kwenye property tax. Yawezekana tukalitazama kwamba halmashauri zetu sasa zinakwenda kufa kwa sababu sehemu hii maalum imechukuliwa na TRA, la hasha! Ule mpango ambao tumejiwekea, kwenye Halmashauri yetu katika zile bilioni tatu ambazo tutakusanya ndani ni pamoja na property tax.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyofahamu kwenye mpango huu kile kiasi ambacho tumekipanga TRA kwa maana Serikali itatuletea kama kilivyo, sasa silioni tatizo la property tax hapa, kwa sababu kama tumekubali kukusanya shilingi milioni 100 kwenye property tax Serikali inatuletea zile shilingi milioni 100, imetupunguzia mzigo. Kwa hiyo, nichukue fursa hii kuipongeza kwa dhati Serikali kwa hatua hii ambayo wamechukua kwa kweli property tax itatusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nipongeze sehemu nyingine, tumeweka kodi ya asilimia 10 kwenye importation ya karatasi. Awali wakati nachangia kwenye viwanda nilisema, Mufindi Paper Mills walipewa jukumu la kutengeneza karatasi na si mifuko, lakini wamekuwa wakisafirisha pulp na kupeleka Kenya badala yake karatasi huku kwetu inaingia bure. Leo Serikali imeweke asilimia 10, naipongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kuja na mpango huu mzuri wa maendeleo, yapo maeneo ambayo Serikali imefanya vizuri sana:-
(1) Elimu bure licha ya changamoto inayojitokeza. Elimu ya juu hususani mikopo naiomba Serikali itatue changamoto hiyo.
(2) Afya ya mama na mtoto mpango huu umewekwa vizuri sana.
(3) Tulipitisha bajeti ya sh. 50,000,000 kila Kijiji naomba isomeke kila Kijiji na kila Mtaa.
(4) Ongezeko la bajeti ya maendeleo toka trilioni 11.5 mpaka trilioni 13.1 hali hii itatusaidia kuharakisha maendeleo.
(5) Mkakati wa ukusanyaji mapato ikiwa ni pamoja na udhibiti wa upotevu wa mapato.
Naiomba Serikali ipunguze utitiri wa tozo na kero kwa wananchi itawapa unafuu wa kufanya biashara na kuinua pato la Taifa. Serikali iboreshe huduma za maji, afya, umeme, barabara pia na reli.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha za Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zilizo chini yake pamoja na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba nzuri ya bajeti imegusa kila nyanja ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu, pamoja na kazi inayofanywa na Serikali kwenye sekta hii zipo changamoto nyingi lakini niiombe Serikali kuja na mpango mahsusi wa kuondokana na madeni ya walimu. Niiombe Serikali kuja na mpango wa teaching allowance ili iwe motisha kwa walimu
kama inavyotoa kwa viongozi yaani responsibility allowance.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maji; naishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajali wananchi wa Jimbo la Singida Mjini. Naomba nizungumzie miradi ya vijijini 10 inayofadhiliwa na Benki ya Dunia changamoto kubwa inayojitokeza katika Jimbo la Singida Mjini ni kuwa miradi yote imekamilika
akini wananchi hawapati maji tatizo kubwa ni kwamba umefanyika uchakachuzi mkubwa katika ujenzi wa miundombinu ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Singida Mjini tumejaliwa rasilimali ya vyanzo vya umeme:-
(i) Umeme wa upepo na makampuni mawili yaliyojitokeza ni:-
(a) Power pool
(b) Wind East African Company.
(ii) Umeme wa jua (solar power) na kampuni ya Synohydro ya China wamejitokeza kuzalisha umeme huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba TANESCO ipunguze urasimu katika kutoa PPA na pia TANESCO inapaswa kuyaacha makampuni kuzalisha umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi milioni 50 kila kijiji, naiomba Serikali yafuatayo; kwanza isomeke shilingi milioni
50 kila kijiji na kila mtaa ili kutoa fursa kwa majimbo ambayo hayana vijiji bali ni mitaa kama Singida Mjini na pia fedha hiyo itoke mapema.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, aliyetuwezesha leo tupo hapa, lakini nichukue fursa hii pia kumshukuru sana na kumpongeza Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya, niwapongeze pia nimpongeze Waziri Mheshimiwa Ummy na Naibu Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mambo machache ya kuzungumza, jambo la kwanza ndani ya Singida Mjini leo tunajenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Mheshimiwa Ummy alifika pale na alitoa maagizo na nimshukuru sana. Naomba nisisitize, tunayo changamoto kubwa ya Hospitali ya Wilaya ya Singida Mjini, eneo kubwa ambalo tunalitegemea ni ile hospitali ya Mkoa tuliyonayo iweze kuhamia iende Hospitali ya Rufaa ambayo ipo Mandewa na ile hospitali ya Mkoa iwe hospitali ya Wilaya. Ninamuomba sana Mheshimiwa Ummy wakati ana wind up atusaidie kutoa tamko hili ili tuweze kuharakisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mandewa na ile hospitali ya Mkoa iliyopo pale iwe Hospitali ya Wilaya. Tutakuwa tumetatua tatizo kubwa sana Singida Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, nizungumzie zoezi la damu salama. Niipongeze Serikali inatumia gharama kubwa leo na katika mpango huu wa damu salama imetusaidia sana. Mkoa wa Singida, tangu Juni , 2016 mpaka Februari, 2017 wamekusanya unit takribani 2,300, bahati mbaya sana Singida Mjini zilikusanywa unit 12 tu, changamoto kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mazingira mengine inaonesha kabisa Singida Mjini tunawanyonya wenzetu wa Halmashauri zingine kwa ajili ya kutumia zile damu salama. Naiomba Serikali ifanye tathmini na iweze kusimamia zoezi hili kikamilifu kwa kila Halmashauri ili tujue tatizo lipo wapi. Kwa sababu kama unakusanya unit 12 maana yake watu waliochangia damu ni watu 12 tu. inawezekana mwamko ni mdogo au yawezekana watendaji wetu Serikalini wanashindwa kufanya kazi hii vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ikifanyika tathmini itatusaidi kuweza kupata damu salama kwa wingi, zoezi hili litatusaidia sana. Niombe sana Serikali iweze kulisimamia jambo hili kwenye maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue fursa hii kuishukuru Serikali, imetupatia fedha za dawa na mpaka sasa ni takribani milioni 200 tumepata Singida Mjini fedha za dawa, nimpongeze sana Dada yangu Ummy. Karibu asilimia 93 ya fedha za dawa zilizokuja Singida Mjini, asilimia 93 siyo jambo dogo Serikali inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ninayoipata mwananchi anapokwenda kupata huduma na akaambiwa dawa hamna, nami nasimama kwenye majukwaa kuwaambia kwamba Serikali imeleta fedha za dawa asilimia 93, ninakosa ni mazingira gani ninaweza kuwaeleza, matokeo yake itanilazimu sasa na mimi nigeuke kuwa muuguzi au kuwa daktari au kuwa mhasibu ili niweze kusimamia fedha hizi namna zinavyoweza kutumika. Kwa hiyo, niiombe Serikali, tunapotoa fedha na mkatuachia tu tuendelee kuratibu jambo hili sisi wawakilishi wa wananchi mnatupa mtihani mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninaona kwenye vitabu tumepata fedha na kweli fedha zimefika, lakini hakuna dawa. Mwananchi anapokwenda akakosa dawa huwezi kueleza, utaeleza kitu gani? Tuna kila sababu sasa ya kusaidiana ni namna gani tufanye kuweza kusimamia utekelezaji wa hizi fedha zinazoletwa. Kama dawa zimenunuliwa ni lazima tujue dawa zipo na wananchi wetu wasipate matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiomba Serikali Watumishi wetu wanapata wakati mgumu sana, leo tumefika mahali call allowance hamna, extra duty hamna, kazi ni kubwa. Daktari anamaliza shughuli zake, nurse anamaliza shughuli zake lakini ataitwa kwa sababu ni wito na atakuja, atakapokuja kufanya ile kazi halipwi, wanayo madeni makubwa sana watumishi wetu.

Ninaiomba sana Serikali iweze kulisimamia jambo hili, hatuna tatizo hilo, tuna tatizo tu la Menejimenti linalosababisha watumishi wasiweze kupata fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itaua morali ya watumishi. Sisi tunapokaa nao, unapozungumza nao, unafanya mikutano unaona kuna mahali wanajitoa wao kufanya kazi lakini sisi tumeshindwa kuweza kutimiza kile ambacho walistahili kupewa ni haki yao. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kazi nzuri inayoendelea. Katika sera ya zahanati kila kijiji/mtaa na kituo cha afya kila kata, pia hospitali ya wilaya na mkoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Singida Mjini kwa asili ya mji ulivyo karibu kata nane za mjini zinategemea Hospitali ya Mkoa. Hivyo ninaiomba Serikali kuharakisha kuanza kazi kwa Hospitali ya Rufaa ili Hospitali ya Mkoa ihamie kwenye Hospitali inayojengwa sasa hivi na eneo/majengo ya Hospitali ya Mkoa yatumike kama Hospitali ya Wilaya, tutakuwa tumemaliza tatizo la Singida Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu damu salama, mpango huu ni mzuri sana na unasaidia sana wananchi hususani Singida Mjini. Changamoto inayojitokeza hapo ni kama ifuatavyo:-

(i) Mwamko mdogo kwa wananchi kuchangia damu;
na
(ii) Halmashauri hazitengi bajeti kwa ajili ya zoezi hilo
hususan Singida Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwezi Juni, 2016 hadi Februari, 2017 Halmashauri ya Manispaa ya Singida imekusanya unit 12 tu out of 2300 za mkoa mzima. Hivyo tunaishi kwa kutegemea Wilaya nyingine au tunatumia damu isiyo salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali ifanye tathmini kwenye jambo hili. Pia Mganga Mkuu wa Mkoa awe na mamlaka ya kuisimamia Halmashauri katika kutekeleza jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fedha za dawa, ninaishukuru sana Serikali kwa kutoa fedha Singida Mjini takribani shilingi 203,100,000 ambayo ni sawa na asilimia 93. Tatizo tunalolipata dawa hazionekani, nakosa majibu ya kuwaambia. Naiomba Serikali itusaidie kusimamia upatikanaji wa dawa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii kukushukuru. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema aliyetuwezesha leo tuko hapa kujadili Bajeti hii ya Elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika mchakato mzima wa kazi ambayo tumempatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Mawaziri; nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Elimu kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Hakuna ubishi kwamba Serikali inafanya kazi kubwa na mchango wake ni mkubwa sana kwenye eneo hili la elimu, hakuna ubishi kwenye hilo. Sina sababu ya kuelezea mafanikio ya elimu ambayo yapo na kila Mtanzania anajua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma kitabu hiki cha Bajeti ya Elimu. Nina Shule kongwe ya Sekondari ya Advance ya Mwenge. Katika ukarabati ambao Serikali inaufanya sasa hivi, lakini shule yangu ya Mwenge haipo kwenye ukarabati huo. Nataka nimweleze Mheshimiwa Waziri, shule hii mwaka 2016 ilifaulisha kwa asilimia 93, licha ya kwamba miundombinu hiyo hiyo tunaendelea nayo lakini Walimu wangu wanafanya kazi kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mkoa wa Singida, ni Manispaa ya Singida Mjini pekee ambayo haina Shule ya Sekondari ya Kidato cha Tano na sita na ndiyo tunaitegemea Shule ya Sekondari ya Mwenge na ndiyo Shule ya Kitaifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka nilieleze hili bayana ili Mheshimiwa Waziri aone umuhimu wa ukarabati wa shule hii kongwe ya Mwenge Sekondari. Kwa mazingira haya haya, sisi Singida Mjini tunalazimika sasa kuanza ujenzi wa shule nyingine za Advance ili kuweza kuwapunguzia mzigo wazazi na vijana ambao wanafaulu kwenda shule za sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukipewa fedha hii, ikikarabatiwa Shule hii ya Mwenge Sekondari itatusaidia katika mazingira ya kuanzisha hata Mwenge Day kwa sababu tunao uwezo huo. Yataongezwa madarasa, tunaanzisha advance ya Mwenge Day. Mheshimiwa Waziri nakuomba sana utupunguzie mzigo wazazi, nasi tuwe na kauli ya kuweza kuzungumza kwa wananchi waone umuhimu wa uwepo wa Advanced Level Singida Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shule hii inao wazabuni mle ndani, wanadai zaidi ya shilingi milioni 500 na hao wazabuni ndio tunawategemea kutuchangia kwenye maabara na kwingine kwenye ujenzi kwa namna yoyote ile. Sasa Serikali lazima ione umuhimu wao, itusaidie na hao wazabuni wakilipwa wataendelea kutusaidia kwa kadri watakavyojaaliwa. Namwomba Mheshimiwa Waziri na hili nalo aliwekee umuhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Jimbo la Singida Mjini, Kata ambazo hazina Sekondari, wameanza kujenga na tayari Kata yangu moja ya Unyanga wamejenga Sekondari, inahitaji usajili Mheshimiwa Waziri. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri; tumeshakamilisha majengo ya maabara, naomba sana Shule hii ya Unyanga nayo iweze kupata usajili na tuweze kuwapa morale wazazi wa kuweza kuendelea kuchangia elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuzungumzie juu ya elimu bora (quality education). Hakuna ubishi kwamba Serikali inafanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha tunafikia malengo ya kuwa na elimu bora. Tayari tunayo elimu bila malipo, tayari kuna Responsibility Allowance inatolewa kwa ajili ya viongozi wetu, Wakuu wa Shule, Walimu Wakuu na Waratibu; hakuna ubishi kwenye hili. Katika mazingira haya haya, ziko changamoto ambazo hatuwezi kuziepuka ili kufikia malengo hayo. Hii ina-create gap kati ya wale viongozi kwa maana ya Walimu Wakuu, Waratibu wa Shule na Walimu wa kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu anayeingia darasani leo hakuna allowance yoyote anayoipata, lakini kiongozi anayemwongoza, anayo allowance. Serikali lazima ioneshe ni namna gani inam-promote na huyu Mwalimu anayeingia darasani ili tuweze kufikia quality education. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia kulipa madeni ya Walimu yasiyokuwa ya mishahara. Sasa hayo yaliyokuwa na mishahara ni nani aliyasababisha na ni nani ataenda kuwalipa? Naomba Serikali isibague, tunahitaji kulipa madeni yote na tuondokane na mpango huu wa Walimu kuendelea kudai, inashusha morale ya kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mwalimu leo haendi likizo, fedha ya likizo haipo. Mwalimu anahamishwa, hapewi fedha ya uhamisho, haipo. Mwalimu anawezaje kufanya kazi fedha ya matibabu haipo? Naiomba Serikali ilete fedha kwa wakati Walimu waweze kwenda likizo, Mwalimu anayehamishwa apewe fedha, tuondokane na mpango huu wa madai. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la madaraja. Habari ya madaraja miaka mitatu, sijui OPRAS, kila kitu kimeletwa hapa, lakini hakina msaada kwa Mwalimu. Walimu lazima wapandishwe madaraja kwa wakati. Hii ndiyo motisha yetu sisi Walimu wala hatuna kitu kingine. Serikali inapaswa izingatie. Kama tumeamua kwenye Open Performance Appraisal System, basi tuamue. Habari ya kukaa miaka mitatu na yenyewe haitimiii, jambo hili linatupa mzigo mkubwa sana. Naiomba Serikali iliangalie vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inapaswa iangalie teaching allowance, hatuwezi kuepuka. Huwezi kutoa allowance kwa Walimu hawa ambao ni viongozi, subordinate wao ukawaacha. Hatuwezi kuepuka hili! Serikali lazima ije na mpango huu, itusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mamlaka ya Nidhamu; tunazungumzia elimu bora. Tumeunda Tume ya Utumishi ya Walimu hapa kwa Sheria Na. 25 ya Mwaka 2015, wameizungumza Kambi ya Upinzani pale. Ni ukweli usiofichika, tumefuta Mikoa, Halmashauri, tukapeleka Mamlaka ya Nidhamu hii Tume ya Utumishi kwenye Wilaya. Leo watumishi watatu kwenye Wilaya ambayo ina Halmashauri mbili, wameshindwa Walimu 1,200 watawezaje Walimu 3,000? Mamlaka ya Nidhamu haijapewa kipaumbele. Niiombe Serikali iliangalie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hiyo mamlaka, TSC kwenye Ofisi zao haina vitendea kazi, haina fedha, haina chochote. Sasa unatarajia inawezaje kusimamia jambo hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, tujue umuhimu wa quality education, tunahitaji kuwashirikisha wadau wote wakiwemo TSC. Kama inashindikana, tuwape semina Waratibu na Walimu Wakuu waweze kuifanya kazi hii kwa pamoja ili tuhakikishe kabisa kama tunazungumzia uadilifu kwenye utumishi uwe ni uadilifu ambao unawagusa watu wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TSC kama imeshindikana, tuirudishe sheria hapa ili tuweze kuirekebisha. Leo wale maafisa wa TSC wanafanya kazi, hawana vyeo. Haieleweki mishahara yao ikoje, wanafanyaje kazi hii? Naomba sana Serikali iliangalie jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho ni community participation. Serikali ina kila sababu ya kuwashirikisha wazazi na wananchi kuweza kushiriki kwenye hili. Baada ya kuanzisha elimu bila malipo, wengi wamerudi nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kila sababu ya kuanzisha programu maalum ambayo itainua ubora wa elimu. Training; kutoa mafunzo maalum kwa ajili ya wazazi. Tutoe mafunzo maalum kwenye Kamati za Shule, tutoe mafunzo maalum kwa Walimu; hii itatusaidia kufikia malengo ambayo tumeyakusudia ya kuwa na elimu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kuiomba Serikali ione elimu ndiyo kila kitu. Tusipomwangalia Mwalimu huyu kama stakeholder namba moja, hatuwezi kufanikiwa malengo ya kufikia elimu bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja ya Serikali.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali imeendelea kupunguza tatizo la maji nchini. Singida Mjini katika bajeti ya mwaka 2016/2017 tulipewa shilingi bilioni mbili mpaka sasa hivi fedha hizo hazijaja. Naiomba Serikali ituletee fedha hizo tuweze kukamilisha miradi ya maji iliyopo. Bajeti hiyo ya mwaka 2016/ 2017 Serikali pia iliahidi kutupatia fedha za fidia shilingi bilioni tatu kwa wananchi wa eneo la Irao - Kisaki waliopisha mradi wa maji mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi ya vijiji kumi vya maji vinavyofadhiliwa na Benki ya Dunia, miradi hii imejengwa Singida Mjini bahati mbaya wananchi hawana maji mpaka sasa hivi. Naomba Serikali ije ifanye tathimini ya miradi hiyo na hatua za kinidhamu zichukuliwe kwa waliohusika kukwamisha miradi hiyo.
Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari za Mwaka 2016
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa kutambua umuhimu wa Muswada wa Mabadiliko ya Tasnia ya Habari kuelekea kuwa muhimili wa nne. Kifungu cha (7), wajibu na haki ya media lengo ni kuimarisha National Security. Kifungu cha 8(1) kwamba kutakuwa na leseni ya kuchapisha ama kuuza. Hiyo itasaidia kuongeza uwajibikaji, kufanya tathmini kila mwaka, ni source ya revenue na pia itaongeza uadilifu.
Kifungu cha 14(2) kuhusu sifa za Director General, naomba tuongeze awe na uzoefu usiopungua miaka mitatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha (1) kuhusu Mfuko wa Mafunzo ya Habari, mafunzo ya wanataaluma ya habari, kukuza na kuendeleza program na kuongeza utafiti. Naipongeza Serikali kwa kifungu hiki kwani kitasaidia kuwafanya wanahabari waende na wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kifungu cha 23 kuhusu Baraza Huru la Habari; mwanahabari aliyethibitishwa atakuwa mwanachama, utakuwa na uwezo wa kujisimamia, italetea haki ya wanahabari. Vile vile Baraza hili litakuwa na uwezo wa kuishauri Serikali na kusimamia vyema tasnia ya habari.