Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Yahaya Omary Massare (36 total)

MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Ili Mtu au Kampuni iweze kufanya biashara ya Mazao ya Misitu anapaswa kusajiliwa:-
(a) Je, ni kwa nini usajili huu hufanywa kila mwaka?
(b) Je, Serikali haioni kwa kufanya hivyo kunaongezea walipa kodi mzigo?
(c) Je, usajili huu hauwezi kufanywa pale tu mtu au Kampuni inapoanza biashara kwa mara ya kwanza na anapoendelea aweze kuhuisha badala ya kusajiliwa upya kila mwaka.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, lenye sehemu (a), (b) na (c), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, usajili wa wafanyabiashara wa mazao ya misitu hufanywa kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Sura 323, kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002, Kifungu cha tano (5) na Kifungu cha 108 na Kanuni zake za mwaka 2004, Kanuni ya 54 kwa kuzingatia kiasi cha mazao ya misitu cha kuvuna mwaka hadi mwaka, ambacho hutegemea uwezo na ndicho kigezo cha kutambua idadi ya wafanyabiashara wa mazao ya misitu watakaopewa vibali vya kuvuna ili kuepuka kuwa na idadi kubwa ya wateja kuliko uwezo wa msitu kuvunwa katika mwaka husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, usajili wa kila mwaka husaidia kutekeleza mipango endelevu ya usimamizi kwa ajili ya kupanga kiwango kinachotakiwa kuvunwa kwa mwaka. Aidha, utaratibu huu hutoa fursa kwa wafanyabiashara wapya kuingia kwenye soko hivyo kuweka mipango mizuri zaidi ya kutambua mahitaji yao kulinganisha na uwezo wa misitu iliyopo. Vile vile kutoa fursa kwa wananchi wengi zaidi kushiriki na kunufaika na uvunaji wa rasilimali za Taifa, mazao ya misitu ikiwa ni sehemu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa zoezi la usajili huambatana na ada mahsusi, wafanyabiashara waone kuwa hii ni fursa kwao kuchangia pato la Taifa kupitia biashara wanazozifanya, utaratibu ambao unafanana na masharti ya biashara nyingine zinazofanyika hapa nchini.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Kila Mtanzania ana haki ya kupata habari wakiwamo wananchi wa Itigi.
Je, kwa nini wananchi wa Itigi na maeneo ya jirani wananyimwa haki ya msingi kutokana na Kituo cha Redio Mwangaza kuzuia masafa ya redio nyingine ikiwemo Redio ya Taifa TBC na TBC FM?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inatambua kuwa kila Mtanzania ana haki ya kupata habari wakiwemo wananchi wa Itigi. Upatikanaji wa matangazo yanayotolewa katika masafa ya mawasiliano ya FM hutegemea na ukaribu wa mahali kilipo kituo cha utangazaji husika. Itigi iko umbali mkubwa kutoka vituo vya utangazaji vinavyoweza kusikika katika eneo hilo. Kwa sasa Itigi ni moja ya maeneo ambayo mawasiliano ya vituo vya utangazaji vilivyo mbali hayapatikani vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Itigi ni Wilaya iliyoko Mkoa wa Singida takribani umbali wa kilometa zaidi 150 kutoka mji wa Dodoma na kama kilometa 100 toka Singida Mjini ambako vituo vingi vya redio vinarushia matangazo yake. Hii inafanya redio nyingi kutosikia vizuri eneo kubwa la Wilaya ya Itigi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, uwekezaji wa redio za FM ikiwemo TBC umefanyika katika miji ya Singida na Dodoma ambapo kitaalam mawimbi ya redio hufifia na kusababisha kutokuwepo na usikivu mzuri wa redio katika eneo la Itigi toka miji hiyo. Vilevile Redio Mwangaza imesimika mitambo ya kurusha matangazo (booster stations) Itigi katika kujikwamua na tatizo la usikivu usio wa uhakika toka Dodoma kwa kuzingatia masharti ya leseni katika eneo la Itigi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuhimiza TBC kusimika mitambo ya kurusha matangazo kwa ajili ya wakazi wa Itigi ili waweze kupata haki yao ya kupata habari.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano katika kampeni zake za uchaguzi alipokuwa Itigi aliombwa na wananchi wa Itigi kuwajengea barabara ya kuingia Mji wa Itigi yenye urefu wa kilometa 8.3 na akakubali.
Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kama ilivyoahidiwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya kuingia Mji wa Itigi (Itigi access road) yenye urefu wa kilometa 8.3 iko chini ya Halmashauri ya Mji wa Itigi. Hata hivyo, ujenzi wa barabara hii utatekelezwa wakati wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara kuu ya Makongorosi - Rungwa - Itigi hadi Mkiwa yenye urefu wa kilometa 413.
Mheshimiwa Naibu Spika, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Makongolosi -Rungwa - Itigi hadi Mkiwa umekamilika na kwa sasa Serikali inatafuta fedha za kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wakati wa kampeni aliahidi kuvirudisha Serikalini viwanda vyote vilivyobinafsishwa, lakini havifanyi kazi.
Je, ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa ahadi hiyo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa agizo la Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, la kuhakikisha viwanda vilivyobinafsishwa vinafanya kazi, lilianza kutekelezwa mwezi Novemba, 2015.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ya kwanza ilikuwa ni Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwataka wote waliopewa viwanda katika mtindo huo kutoa taarifa ya kina ya utendaji wa viwanda hivyo. Timu ya wataalam kutoka Wizara ya Viwanda na Ofisi ya Msajili wa Hazina walifuatilia na wanaendelea kutathmini kwa kutembelea kiwanda baada ya kiwanda, ili kutafuta ufumbuzi wa matatizo yanayosababisha kiwanda kutokufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya taratibu hizo hapo juu, Wizara yangu inaendelea na zoezi la kuchambua mikataba ya mauzo kwa viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo ama havifanyi vizuri au vimesimama uzalishaji kabisa. Uchambuzi huo unafanyika kwa kushirikiana na Ofisi ya Msajili wa Hazina pamoja na Wizara za kisekta ambazo ni Maliasili na Utalii, Nishati na Madini, Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Uchambuzi huo unaangalia hali ya umiliki, wajibu wa mwekezaji, wajibu wa Serikali, utekelezaji wa mkataba wa mauzo, hali ya sasa ya kiwanda na hivyo kutoa mapendekezo ya hatua stahiki. Zoezi hili linaenda sambamba na ulinganishaji wa taarifa za uwekezaji katika viwanda vilivyobinafsishwa zilizowasilishwa kwenye Ofisi ya Msajili wa Hazina na wamiliki wa viwanda hivyo kama nilivyoeleza hapo awali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, tathmini ya hali ya viwanda nayo inaendelea kufanyika kwa ushirikiano wa Ofisi ya Msajili wa Hazina ambapo viwanda 45 tayari vimefanyiwa tathmini. Kati ya viwanda hivyo, viwanda vinne vimeonesha dalili kuwa wawekezaji wa sasa hawana uwezo wa kuvifufua hivyo, kuwa na uwezekano wa Serikali kutafuta wawekezaji wengine. Taarifa ya tathmini itakapokamilika itawasilishwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kupata maoni ya kisheria katika njia muafaka ya kutwaa viwanda hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua nyingine ambayo tumeichukua katika kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ni Serikali kukitwaa kiwanda cha chai Mponde (Mponde Tea Estate Limited) kilichopo Lushoto – Tanga, ambacho mwekezaji amekiuka makubaliano ya kimkataba. Kiwanda hicho kilitwaliwa tarehe 29 Januari, 2016 na tayari mazungumzo kati ya Serikali na Mfuko ya Hifadhi ya Jamii wa Local Authority Provident Fund – LAPF yanaendelea. Mazungumzo hayo ni matokeo ya maagizo ya Mheshimiwa Rais kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza katika sekta ya viwanda.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Barabara ya Mkiwa – Rungwa - Makongorosi ni ya udongo na nyakati za mvua barabara hiyo inaharibika sana kiasi cha kutopitika kabisa:-
Je, Serikali ina Mpango gani wa kuitengeneza barabara hiyo kwa lami ili kuwaondelea kero wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi hususan wa Kata za Mwamagembe, Rungwa na Kijiji cha Kitanula.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mkiwa - Rungwa - Makongorosi ni sehemu ya barabara kuu ya kutoka Mbeya – Chunya – Makongorosi - Rungwa - Itigi hadi Mkiwa yenye urefu wa kilomita 413. Kati ya hizo kilometa 219 zimo katika mtandao wa barabara Mkoa wa Singida na sehemu kubwa ikiwa katika Jimbo la Manyoni Magharibi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa kiwango cha lami kwa sehemu ya Mbeya hadi Chunya kilometa 72 umekamilika. Barabara ya Mkiwa - Rungwa hadi Makongorosi ni ya changarawe na hupitika kipindi chote cha mwaka isipokuwa sehemu korofi katika maeneo ya Kintanula na Mwamalugu katika Mkoa wa Singida ambazo husumbua wakati wa kipindi cha mvua nyingi kutokana na hali ya kijiografia na udongo unaoteleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Nchini TANROADS imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami barabara hiyo. Katika bajeti ya mwaka 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 5.848 kwa ajili ya kuanza sehemu ya barabara sehemu ya Mkiwa – Itigi - Noranga ambazo ni kilometa 57. Tumetenga shilingi bilioni 8.848 kwa ajili ya kuanza ujenzi sehemu ya Chunya -Makongorosi ambayo ni kilometa 43. Aidha, zabuni kwa ajili ya kazi hizi zinatarajiwa kuitishwa mwezi huu Novemba, 2016.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Tanzania ni nchi yenye misitu mingi na Sheria ya Usafirishaji wa Mazao ya Misitu inazuia kusafirisha zaidi ya sentimeta15 au inchi sita.
Je, Serikali imepata hasara kiasi gani kwa kuruhusu usafirishaji wa sentimeta 20 sawa na inchi nane ili kujenga uwezo wa kiushindani na nchi nyingine katika soko?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massarem, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu cha 50 cha Kanuni za Sheria ya Misitu kinakataza kusafirisha magogo nje ya nchi. Sheria hiyo pia hairuhusu kuuza nje ya nchi mbao zote zenye unene unaozidi inchi sita, uamuzi ambao azma yake kubwa ni kutoa fursa ya kukuza viwanda ndani ya nchi na kupanua wigo wa ajira kwa vijana nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kwa mujibu wa sheria, Serikali hairuhusu usafirishaji wa mbao zenye unene wa sentimeta 20 sawa na inchi nane ni dhahiri kwamba haiwezi kuwa na takwimu za hasara iliyoipata kwa kuruhusu usafirishaji wa mbao za unene huo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Tanzania imejaaliwa kuwa na almasi na madini ya aina mbalimbali kwa wingi ikiwemo gypsum;
(a) Je, ni busara kwa viwanda vyetu humu nchini kuagiza gypsum kutoka nje ya nchi?
(b) Je, Serikali haioni kuwa huo ni ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za Watanzania?, na
(c) Serikali inachukua hatua gani kukomesha utaratibu huu ili kutunza fedha zetu chache za kigeni na kulazimisha ajira kwa Watanzania katika machimbo ya gypsum hususan Itigi?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI, alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, lenye sehemu (a), (b), na (c), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kujenga uchumi endelevu na hasa uchumi wa viwanda, ni busara viwanda vyetu kutumia malighafi zilizopo nchini tukilenga zaidi upatikanaji ajira kwa Watanzania, kuimarisha urari wa malipo (balance of payment) kupunguza mfumuko wa bei na uhifadhi wa fedha za kigeni (Foreign currency retention).
Mheshimiwa Spika, viwanda vyetu hapa nchini hutumia aina mbili ya jasi yaani anhydrate (calcium sulphate) inayotumika katika viwanda vya saruji na food grade calcium sulphate inayotumika katika viwanda vya vyakula na vinywaji. Madini ya jasi yanayotumika katika viwanda vya ujenzi hupatikana hapa nchini katika maeneo ya Kilwa (Rufiji), Makanya (Same), Tanga na Itigi wakati yanayotumika kwenye viwanda vya vyakula na vinywaji hayapatikani nchini hivyo kulazimika kuyaagiza kutoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, Serikali inahimiza na kuhamasisha watumiaji wa malighafi za ndani ili kuzalisha bidhaa za viwandani na kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini. Ni kwa mtazamo huo Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imesitisha uingizwaji wa jasi itumikayo katika viwanda vya saruji kutoka nje ya nchi kuanzia tarehe 10 Agosti 2016.
Mheshimiwa Spika, vile vile Serikali inaendelea kufuatilia na kuhakikisha wachimbaji wanafuata masharti ya leseni walizopewa. Aidha, Serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kulinda viwanda vya ndani na hatimaye kutengeneza ajira nyingi kupitia sekta hii. Katika kufanya hivyo, Serikali pia inazingatia mahitaji na uwezo wa uzalishaji wa ndani ili kulinda walaji wa Tanzania na mitaji ya wawekezaji.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Shamba la Kampuni iliyokuwa ikiitwa Tanganyika Packers lenye ekari 45,000 katika Halmashauri ya Itigi limetelekezwa kwa muda mrefu na wananchi wa kata nne (4) na vijiji 12 wamekuwa wakilitumia kwa kilimo na ufugaji:-
(a) Je, ni lini Serikali itapendekeza kwa Mheshimiwa Rais kufutwa kwa hati hiyo?
(b) Je, ni lini Serikali italirudisha rasmi shamba hilo kwa Halmashauri ya Itigi ili lipangiwe matumizi kwa ajili ya wakulima na wafugaji?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, shamba lenye hati namba 15467 na ukubwa wa ekari 45,000 lililopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi lilimilikishwa kwa Kampuni ya Tanganyika Packers Limited mwaka 1955 kwa muda wa miaka 99 kwa matumizi ya ufugaji (cattle holding).
Mheshimiwa Naibu Spika, shamba limezungukwa na Vijiji vitatu vya Kitaraka, Doroto na Kaskazi ambavyo wananchi wake kupitia uongozi wa vijiji wamekuwa wakikodishwa maeneo ya kilimo na ufugaji kutokana na shamba hilo kutoendelezwa na Mwekezaji kwa muda mrefu. Baada ya Mwekezaji kushindwa kutimiza masharti ya uendelezaji wa shamba hili, Serikali ililitaifisha shamba hili pamoja na majengo yaliyokuwa ndani yake na kuliweka chini ya uangalizi wa msajili wa Hazina. Aidha, kwa nyakati tofauti kupitia vikao vya viongozi na wananchi, Serikali imekuwa ikikataza wananchi kuvamia shamba hili kwa kuwa ni mali halali ya Serikali kwa ajili ya mipango ya uwekezaji lakini wananchi wamekuwa wakikaidi makatazo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa, shamba hili ni mali halali ya Serikali hivyo wananchi waliovamia na kufanya maendelezo ndani ya shamba hili ni kinyume na taratibu na hivyo wasitishe shughuli zao mara moja. Serikali inaendelea kuandaa mpango wa uwekezaji utakaoleta tija ya maendeleo kwa Taifa hasa kwa wananchi wanaozunguka shamba hili.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inatambua juhudi zinazofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Itigi katika kuleta maendeleo kwa wananchi wake. Tayari walishaleta maombi Serikalini kwa Msajili wa Hazina kwa lengo la kutaka kuingia ubia na Mwekezaji ili kuliendeleza shamba hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inayafanyia kazi maombi hayo na itatoa taarifa kamili baada ya kukamilisha tathmini ya faida na hasara zitakazotokana na uwekezaji unaopendekezwa. Natoa rai kwa viongozi wa Serikali za Vijiji na Kata kuacha kugawia wananchi eneo hilo kwa mtindo wa kuwakodisha kwa kuwa kufanya hivyo ni kinyume na taratibu za sheria ya nchi.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Katika Mpango wa Kilimo Kwanza Serikali ilihamasisha Watanzania kuongeza uzalishaji katika kilimo ili Serikali itoe mikopo ya matrekta kwa wingi.
(a) Je, kumekuwa na mafanikio kiasi gani kwa mazao ya biashara na chakula?
(b) Kama kumekuwa na mafanikio, je, kuna utaratibu gani wa kuendeleza mpango huo kwa wananchi wanaohitaji kukopeshwa matrekta wakiwemo wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninamshukuru sana Mungu. Vilevile ninamshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kunipa dhamana hii. Ninakushukuru sana wewe binafsi kwa kunilea vyema na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Kilimo naomba nijibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Mpango wa Kilimo Kwanza umekuwa na mafanikio katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara nchini ambapo uzalishaji wa jumla wa mazao ya biashara katika msimu wa 2016/2017 umeongezeka kufikia tani 881,583 ikilinganishwa na tani 796,562 mwaka 2015/2016. Aidha, uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka hadi kufikia tani 16,172,841 kwa msimu wa 2015/2016.
Mheshimiwa Spika, uzalishaji wa mazao ya chakula kwa Mkoa wa Singida umeongezeka kutoka tani 453,097 mwaka 2013/2014 hadi tani 481,452 kwa mwaka 2015/2016. Aidha, uzalishaji wa mazao ya biashara umeongezeka kutoka tani 184,066 mwaka 2012/2013 hadi tani 293,873 kwa mwaka 2015/2016. Uzalishaji wa mazao ya chakula katika Wilaya ya Manyoni umeongezeka hadi kufikia tani 42,554 kwa mwaka 2015/2016 ambapo uzalishaji wa mpunga umeongezeka kutoka tani 1,342 mwaka 2011/2012 hadi kufikia tani 6,212 mwaka 2015/2016. Alizeti uzalishaji umeongezeka kutoka tani 4,464 mwaka 2010/2011 hadi tani 21,871 mwaka 2016/2017, na ufuta umeongezeka kutoka tani 2,285 mwaka 2010/2011 hadi kufikia tani 8,874 kwa mwaka 2015/2016.
• Mheshimiwa Spika, jumla ya matrekta 18,774 yanafanya kazi nchini ambapo kati ya matrekta hayo, matrekta makubwa ni 11,500 na matrekta madogo ya mkono ni 7,274. Aidha, Wilaya ya Manyoni ina matrekta makubwa 32, matrekta madogo ya mkono 39 na wanyamakazi 14,782 ambapo kilimo cha kutumia maksai ni maarufu katika Wilaya ya Manyoni.
Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada za Serikali Kuu katika kuhakikisha wakulima wanapata zana bora za kilimo, halmashauri za wilaya pia zimeelekezwa kuhamasisha wakulima kujiunga au kuanzisha vyama vya akiba na mikopo (SACCOS) ambavyo vitakopesha wanachama wake au kuwadhamini kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha kwa ajili ya kununua matrekta na zana zake.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Sasa hivi baadhi ya watumishi wa Halmashauri kama vile Wakurugenzi na wengine wanapostaafu hupatiwa kadi ya bima ya afya pamoja na familia zao.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia kadi kama hizo watumishi na viongozi wa Serikali waliostaafu kabla ya utaratibu huo kuanzishwa ikizingatiwa kuwa wengi wao walilitumikia Taifa hili kwa uadilifu na uaminifu mkubwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua mchango wa wastaafu waliowahi kuwa watumishi na viongozi wa Umma katika maendeleo ya Taifa hili. Kwa sababu utaratibu wa kuwapatia bima ya afya wastaafu waliowahi kuwa viongozi na watumishi wa Umma ni kupitia Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Sura Namba 395, Toleo la Mwaka 2015 kwa kuzingatia vigezo na masharti yafuatayo:-
(i) Mstaafu husika lazima awe alikuwa mwanachama mchangiaji wa mfuko kabla ya kustaafu.
(ii) Mstaafu awe amefikisha umri wa kustaafu kwa hiari miaka 55 au kwa lazima au miaka 60.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kupitia utaratibu huu, wanachama wastaafu wanaokidhi masharti na vigezo vilivyoainishwa, hupatiwa bima ya afya inayomuwezesha kupata huduma za matibabu yeye mwenyewe pamoja na mwenza wake hadi mwisho wa maisha yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia uhitaji wa huduma za afya na changamoto za upatikanaji wa huduma hizi kwa wastaafu na wananchi wengine walio nje ya utaratibu huu, mfuko umeweka utaratibu wa kujiunga kwa hiari kupitia utaratibu wa mwanachama binafsi.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alipotembelea Itigi alitoa ahadi ya kusaidia mradi wa maji katika Mji wa Itigi:-
Je, Serikali imetekeleza kwa kiasi gani ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tayari Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa maji katika Mji wa Itigi ambao ni ahadi ya Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete. Mradi huu utahusisha Vijiji saba (7) vya Itigi - Mjini, Mlowa, Zinginali, Majengo, Tambuka-reli, Kihanju na Songambele. Kazi zilizofanyika hadi sasa ni utafiti wa vyanzo vya maji yaani (hydrogeological investigation) pamoja na uchimbaji wa visima saba.
Mheshimiwa Spika, kati ya visima saba (7) vilivyochimbwa visima vinne (4) vilipata maji ya kutosha kwa kiasi cha mita za ujazo 3,048 kwa siku ikilinganishwa na mahitaji ya sasa ya mita za ujazo 1,248 kwa siku. Aidha, kazi ya usanifu wa miundombinu ya maji itakayojengwa umekamilika katika Vijiji sita vya Mlowa, Zinginali, Songambele, Tambukareli, Itigi Mjini na Majengo. Kwa upande wa Kijiji cha Kihanju usanifu huo unaendelea. Taratibu za kumpata Mkandarasi wa kujenga miundombinu katika vijiji sita (6) zitaanza hivi karibuni.
Mheshimiwa Spika, mradi huu utatekelezwa kwa awamu tatu; Awamu ya kwanza inahusisha utafiti wa vyanzo vya maji na uchimbaji wa visima ambayo imekamilika. Awamu ya pili inahusisha usanifu wa msambazaji wa maji ambapo umekamilika katika vijiji sita na uandaaji wa makabrasha ya zabuni na manunuzi ya wakandarasi wa ujenzi. Awamu ya tatu itahusisha ujenzi wa miundombinu ya maji.
Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa mradi huu kunatarajiwa kuboresha hali ya upatikanaji wa maji kutoka asilimia 47 ya sasa kufikia asilimia 85 kwa wakazi wa Mji huo, pia itawezesha kuanzishwa Mamlaka ya Maji ya Mji wa Itigi.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Je, ni lini Vijiji vya Jeje, Kashangu, Idodyandole, Mbugani, Aghondi, Mabondeni, Kitopeni, Ipande, Muhanga, Damwelu, Kitaraba, Kazikazi, Kintanula na Rungwa vitapatiwa umeme katika Mradi wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kupeleka umeme katika vijiji vyote vya Tanzania Bara ambavyo havijafikiwa na miundombinu ya umeme ili vifikiwe na umeme ifikapo mwezi Juni, 2021.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Manyoni Magharibi lina vijiji vipatavyo 39 ambapo vijiji 11 vimefikishiwa miundombinu ya umeme. Vijiji 10 vya Kamenyanga, Kayui, Jeje, Songa Mbele, Njirii, Kashangu, Idodyandole, Sanjaranda, Ziginali na Ipanga vimewekwa katika mradi wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza. Utekelezaji wa mradi huu umekwishaanza na mkandarasi anayefanya kazi hii katika Mkoa wa Singida aitwaye CCCE-ETERN Consortium anatarajia kukamilisha kazi Juni, 2019. Kazi za ujenzi zinajumuisha ujenzi wa kilometa 22.4 za njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 na kilometa 36 za njia za umeme wa msongo kilovoti 0.4/0.23, ufungaji wa transfoma 18 na uunganishwaji wa wateja 662. Gharama ya mradi huu ni shilingi bilioni mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji 18 vilivyobaki vikiwemo vya Mbugani, Aghondi, Maondeni, Kitopeni, Ipande, Muhanga, Damwelu, Kitaraba, Kazikazi, Kitamula na Rungwa vitaanza kupelekewa umeme kupitia mradi huu mzunguko wa pili kuanzia Julai, 2019 na kukamilika Juni, 2021.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Mjasiliamali au mtu yeyote anapokata mti anatakiwa achukue 70% ya kile anachokilipia:-
• Je, ni lini recovery rate ya 30% ya mbao ilifanyiwa utafiti?
• Je, ni taasisi gani ilifanya utafiti huo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mauzo ya miti ya Serikali kwa ajili ya kuvuna hufanyika baada ya kufanya tathmini ya ujazo wa miti kwa kupima unene na urefu wa miti inayotarajiwa kuuzwa. Ujazo huu hauhusishi ujazo wa matawi, majani na mizizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti zilizowahi kufanywa na wataalam wetu wa misitu kati ya mwaka 1996 hadi 1999 wakati wa kutekeleza Mradi wa FRMP (Forest Resource Management Programme), zilibainisha kuwa mteja anaweza kupata mbao kati ya asilimia 60 – 70 ya ujazo wa mti uliopimwa kama atachakata magogo hayo kwa kutumia mashine zenye ufanisi wa kiwango cha juu ambazo ni frame saw au band saw. Mashine hizi hupatikana kwenye viwanda vikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika viwanda vidogo vidogo na vya kati ambavyo hutumia mashine zenye ubora wa chini kiwango cha uzalishaji ni kati ya asilimia 20 - 43 ambapo wastani ni asilimia 30 ya ujazo wa mti. Utafiti huu ulifanywa kati ya mwaka 2005 na 2007 na wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Chuo cha Viwanda vya Misitu cha Moshi (FITI). Teknolojia duni, uelewa mdogo na usimamizi hafifu ndiyo chanzo cha kuwa na ufanisi huo mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia utafiti huo na ufanisi wa teknolojia iliyopo sasa ya msumeno wa mkono na msumeno wa duara (circular saw) hauwezi kuzalisha mbao zenye ujazo wa zaidi ya asilimia 30 ya ujazo wa mti uliopimwa. Kiwango cha asilimia 30 kitaalam tunakiita recovery rate.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano wakati wa kampeni aliwaahidi wananchi wa Itigi katika Jimbo la Manyoni Magharibi kusaidia kupunguza gharama kubwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, pia kulipa mishahara yote ya watumishi, mgao wa dawa kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD), vifaa tiba na kuongeza Madaktari Bingwa:-
• Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo?
• Je, Serikali haioni kuwa kwa sasa ni bora kujenga hospitali ya Serikali katika Halmashauri mpya ya Itigi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika utoaji wa huduma za afya, Serikali inatoa ruzuku ya fedha kwa ajili ya kulipia mishahara ya watumishi pamoja na ruzuku ya dawa na vifaatiba. Jumla ya watumishi 50 wa Hospitali ya Mtakatifu Gaspar wanalipwa mishahara na Serikali ambao ni Daktari Bingwa mmoja, Daktari (MD) mmoja, Mteknolojia Maabara Mmoja, Madaktari Wasaidizi Wawili, Tabibu Wawili na Wauguzi 43.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mgao wa dawa na vifaatiba kutoka Bohari Kuu (MSD) unaendelea kutolewa na Serikali. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, kupitia MSD Serikali ilitoa dawa zenye thamani ya shilingi milioni 105.674 na mwaka wa fedha 2017/2018 hospitali ilipatiwa dawa zenye thamani ya shilingi milioni 114.671.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Itigi katika bajeti ya mwaka 2018/2019, imetengewa jumla ya shilingi milioni 600 kama ruzuku ya miradi ya maendeleo ili kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Eneo la ujenzi wa hospitali lenye ukubwa wa ekari 50 limeshatengwa katika Kijiji cha Kihanju, Kata ya Tambukareli.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-

Mji wa Itigi unakua kwa kasi na umeme umeenda vijiji vya Lulanga, Itagata, Ukimbu, Chabutwa, Mtakuja, Makale na Mitundu ambapo ni kilomita 71; kwenda Itigi hadi Mwamagembe ni zaidi ya kilomita 130:-

(a) Je, Serikali haioni ni vema sasa kuipa TANESCO hadhi ya Kiwilaya katika Wilaya ya Itigi?

(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza watumishi wa Shirika la Umeme katika Jimbo la Manyoni Magharibi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuleta ufanisi katika kuwahudumia wananchi wa Mji wa Itigi katika Jimbo la Manyoni Magharibi mwaka 2003 TANESCO ilianzisha Ofisi ndogo ya Itigi kwa lengo la kuongeza huduma za umeme kwa wananchi. Aidha, TANESCO imekuwa ikifungua ofisi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wateja wake katika maeneo mbalimbali nchini. Vilevile Ofisi hizo zimekuwa zikipandishwa hadhi kutoka ofisi ndogo hadi kuwa Ofisi za Wilaya na Mkoa za TANESCO kwa kuzingatia mahitaji ikiwa pamoja na kukua kwa shughuli za uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa TANESCO imefungua ofisi katika Mji wa Itigi kwa ajili ya kuwahudumia wateja katika hadhi ya ofisi ndogo. Hata hivyo, TANESCO imeanza taratibu za kupandisha ofisi hiyo hadhi ili kuwa ofisi ya TANESCO ya Kiwilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya TANESCO Itigi inasimamiwa na Techinician na watumishi wengine 11. Katika mwaka wa fedha 2018/2019, TANESCO inatarajia kuongeza watumishi wengine watano pamoja na Mwandisi ili kuwahudumia wateja wa maeneo yote ya Itigi ikiwa ni pamoja na wateja kutoka Vijiji vya Lukanga, Itagata, Ukimbu, Chabutwa, Mtakigi, Makle, Mitundu na Mwamagembe.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-

Wananchi wa Manyoni Magharibi kwa kushirikiana na Serikali kupitia miradi mbalimbali ikiwemo TASAF wamejenga zahanati katika Vijiji vya Gurungu, Sanjaranda, Kitopeni, Ipande, Doroto, Itagata, Kalangali, Makale, Mwamagembe na Kintanula, lakini mpaka sasa zahanati hizi hazina Waganga:-

Je, ni lini Serikali itazipatia zahanati hizo Waganga, ili wananchi wapate huduma kufuatana na sera yake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika kwa Mwaka wa Fedha 2017/ 2018 na 2018/2019 Serikali imeajiri watumishi 8,444 wa afya katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa ambapo watumishi 46 walipangwa kwenye vituo vya afya na zahanati katika Jimbo la Manyoni Magharibi. Zahanati za Gurungu, Sanjaranda, Kitopeni, Ipanda, Doroto, Itagata, Kalangali, Makale, Mwamagembe na Kitanula zimepatiwa Waganga na wataalam mbalimbali wa afya ambao wanatoa huduma hadi hivi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu ya vituo vya afya vya kutolea huduma za afya sambamba na kuajiri wataalam wa afya kwa awamu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-

Ipo ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kilometa nane oinayopita katikati ya Mji wa Itigi.

Je, ni lini sasa barabara hii itaanza kujengwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Mhehsimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kukamilisha usanifu wa barabara inayopita katikati ya Mji wa Itigi yenye urefu wa takribani kilometa nane. Usanifu huo umefanywa kama sehemu ya usanifu wa barabara ya Mkiwa - Itigi - Rungwa - Makongolosi yenye urefu wa kilometa 413 uliosimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania yaani TANROADS. Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara inayopita katikati ya Mji wa Itigi kwa kiwango cha lami itakayojengwa chini ya mradi wa ujenzi Mkiwa -Itigi - Rungwa - Makongolosi ili kufungua fursa za kiuchumi na kijamii katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuza:-

Je, ni lini Serikali itaifanya Halmashauri ya Itigi kuwa Wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Massare Mbunge wa Manyoni Mangharibi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza wakati majibu swali la Bunge Na. 287 kuhusu pendekezo la kugawa Mkoa wa Tanga, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa Serikalli inatambua umuhimu wa kuanzisha maeneo mapya ya utawala kwa ajili ya kusogeza huduma karibu na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele cha kuhakikisha maeneo yalianzisha hivi karibuni yanaboresha na kuendelezwa kwa miundombinu na huduma mbalimbali zikiwemo Ofisi, makazi ya viongozi na watendaji, huduma za afya, elimu, maji, mawasiliano, barabara na umeme ili wananchi waanze kunufaika na huduma zinazotolewa na Serikali kupitia mamlaka hizo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-

Eneo la mbuga linalozunguka Mji wa Itigi linafaa sana kwa kilimo cha mazao mbalimbali kama mahindi, alizeti, choroko na dengu, lakini eneo hili linajaa maji na kufanya kilimo kuwa kigumu. Je, Serikali ipo tayari kusaidia wananchi wanaolima katika eneo hilo kwa kuwajengea mifereji ya kuongoza maji yasiingie mashambani?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, eneo la mbuga linalozunguka Mji wa Itigi limekuwa likijaa maji pale mvua zinapokuwa juu ya wastani ambapo historia inaonesha kuwa bonde hili lilijaa maji kipindi cha mwaka 1997/1998 wakati wa mvua za Elnino na katika msimu wa 2015/2016 baada ya miaka tisa tangu wakati wa mvua za Elnino mwaka 1997/1998.

Mheshimiwa Spika, Serikali inalichukua suala la Mheshimiwa Mbunge na itatuma wataalam wa kilimo na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa ajili ya kwenda kufanya utafiti na tathmini ya kina ya maji kujaa kwenye mashamba ya wakulima. Utafiti na tathmini hiyo itakapokamilika tutakuja na mikakati na mapendekezo stahiki yatakayosaidia kutatua changamoto ya kujaa maji mashambani na kuwasaidia wakulima wa eneo la mbuga linalozunguka Mji wa Itigi ili kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima hao.
MHE. YAHAYA O. MASSARE Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga malambo katika Halmashauri ya Itigi kwa ajili ya wafugaji kunyweshea maji mifugo yao?
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI Alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, inategemea ifikapo mwaka 2025, tutaongeza idadi ya malambo na mabwawa ya maji ya mifugo kutoka 1,384 hadi 1,842 na visima virefu kutoka 103 hadi 225. Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Wizara inakamilisha ujenzi wa mabwawa matatu ya Chamakweza kule Chalinze, Kimokouwa, Longido na Narakauo, Simanjiro pamoja na ujenzi wa visima virefu viwili cha Usolanga, Iringa na Mpapa, Manyoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa 2021/2022 Wizara imepanga kutekeleza ujenzi wa mabwawa matano yenye thamani ya shilingi bilioni 1.6 na visima virefu sita vyenye thamani ya shilingi milioni 560 kwa maeneo yenye changamoto ya ukame na uhitaji mkubwa wa maji hapa nchini. Wizara itaangalia uwezekano wa kuingiza Halmashauri ya Itigi katika mpango kutegemeana na bajeti tutakayokuwa tumeipata kwa mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge, Madiwani na Wakurugenzi katika Halmashauri zetu, ikiwemo Halmashauri ya Itigi, kutenga na kutumia asilimia 15 ya mapato ya ndani yatokanayo na mifugo kujenga miundombinu muhimu kwa mifugo, ikiwa ni pamoja na mabwawa, majosho, malambo, visima, minada na kadhalika.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya kuwasaidia Wananchi wa Mji wa Itigi kuweza kuvuna maji katika Mbuga inayozunguka Mji huo?
NAIBU WAZIRI MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Itigi ni miongoni mwa miji miwili iliyopo katika Wilaya ya Manyoni. Mji huu unakadiriwa kuwa na wakazi wapatao 32,000. Serikali imeendelea kutekeleza ahadi iliyoitoa kwa kuwasaidia wananchi wa maeneo yanayozunguka Mji wa Itigi kuweza kuvuna maji ambapo imekamilisha utambuzi wa awali wa maeneo ambayo yanafaa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa katika Mji wa Itigi na katika Kijiji cha Kayui, Kata ya Magandu, Kijiji cha Muhanga, Kata ya Ipande pamoja na Kjiji cha Kaskazi, Kata Kitaraka ambayo yameonekana yanafaa kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa. Katika mwaka wa fedha 2021/ 2022, Serikali itakamilisha usanifu wa kina na kuainisha ukubwa wa mabwawa yatakayojengwa kuanzia mwezi Januari, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, katika mwaka wa 2020/2021 katika kuimarisha hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Mji wa Itigi Serikali imekamilisha ujenzi wa mradi wa maji mkubwa unaohudumia vijiji sita vya Songambele, Mlowa, Majengo, Tambukareli, Zinginali na Itigi. Mradi huu umekamilika mwezi Disemba, 2020 na kugharimu shilingi bilioni
2.64. Mradi umewezesha upatikanaji wa maji katika Mji wa Itigi kufikia asilimia 80.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itawapatia wananchi wa Kijiji cha Kintanula Kata ya Mwamagembe katika Jimbo la Manyoni Magharibi mawasiliano ya uhakika ya simu?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote unatekeleza miradi minne katika Kata mbili za Jimbo la Manyoni Magharibi. Miradi hiyo inatekelezwa katika Kata za Mgandu ambapo kuna miradi miwili na Idodyandole miradi miwili. Utekelezaji wa miradi yote miwili katika Kata ya Mgandu na mradi mmoja katika Kata ya Idodyandole umekamilika. Utekelezaji wa mradi mmoja katika Kata ya Idodyandole katika Kijiji cha Mbugani bado unaendelea.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) itakifanyia tathmini Kijiji cha Kintanula Kata ya Mwamagembe na hatimaye kijiji hiki kitaingizwa katika orodha ya vijiji vitakavyojumuishwa katika zabuni zitakazotangazwa katika mwaka wa fedha 2021/2022.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -

(a) Je, kwa nini TANESCO imewaondoa watumiaji wadogo wa umeme chini ya unit 75 katika Vijiji vya Itigi, Majengo, Ziginali, Tambukareli, Songambele na Mlowa kuwa Mitaa badala ya Vijiji?

(b) Je, ni lini wanavijiji hao watarudishwa katika matumizi ya watumiaji wadogo kwa kuwa hivi ni Vijiji na si Mitaa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Agizo la kurekebisha bei la EWURA Na. 2016-010 la Mwaka 2016, kupitia masharti Namba (h) na (i) inaelekeza TANESCO, kuwaunganisha wateja wapya wa majumbani walio maeneo ya vijijini katika kundi la D1 yaani Domestic 1. Kupitia mfumo wa njia moja ya umeme na wateja walio katika kundi la D1 watahamishiwa kwenda T1 ambayo ni Tariff 1. Endapo manunuzi yao katika kipindi cha miezi mitatu mfululizo yatazidi wastani wa unit 75 kwa mwezi.

Mheshimiwa Spika, wateja wa Itigi walihamishiwa kwenda kundi la T1 kwa kuwa wapo Itigi mjini. Kwa sasa, TANESCO inaendelea kuchambua hali ya ununuzi wa umeme kwa wateja hawa. Kwa lengo la kubaini waliokidhi vigezo vya kuwa kwenye kundi la D1 kwa mujibu wa Agizo la EWURA. Zoezi hili linatarajia kukamilika ifikapo tarehe 30 Novemba, 2021. Baada ya zoezi hili kukamilika wanaostahili kuwa kwenye kundi la Tariff D1 watapelekwa kwenye kundi hili Disemba, 2021.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -

Je, ni lini Mtambo wa matangazo ya TBC Taifa na TBC FM utafungwa katika Mji wa Itigi ili Wananchi wapate matangazo hayo muhimu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare Mbunge wa Manyoni Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenekiti, Serikali kupitia Shirika lake la Utangazaji la Taifa (TBC) mkakati wake ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya matangazo ya redio nchi nzima ifikapo Mwaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya Mwaka 2022/2023 TBC imepanga kuwasilisha maombi katika Bunge lako tukufu kuidhinishiwa kiasi cha shilingi bilioni saba zitakazotumika mahsusi kwa ajili ya upanuzi wa usikivu katika Wilaya 14 nchini ikiwemo Wilaya ya Manyoni. Mkakati ni kuhakikisha kuwa wananchi wanaoishi katika wilaya ambazo hazipati matangazo ya TBC Taifa na TBC FM zinapata ifikapo mwaka 2025.

Mheshimiwa Mwenekiti, TBC imeendelea kuboresha usikivu katika maeneo ambayo hayana usikivu ama usikivu wake ni hafifu. Miradi inayotekelezwa kwa Mwaka wa fedha 2021/2022 ni katika Wilaya na maeneo 24 ya nchi ikiwemo maeneo ya mpakani ambayo ni Ngara, Karagwe, Kasulu, Tanganyika, Same na Nkasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengine ni Kilombero/Mlimba, Kahama, Sikonge, Bunda, Ngorongoro, Uvinza, Makete, Ruangwa, Kyela, Morogoro Vijijini/Kisaki, Kilwa, Serengeti, Songwe, Njombe, Simiyu, Unguja na Pemba. Miradi hii iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji na inatarajiwa kukamilika yote na kuzinduliwa ifikapo Julai, 2022. Miradi hii ikikamilika usikivu wa TBC utafikia asilimia 83, ahsante sana. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kuvuna maji katika Mji wa Itigi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali inaendelea na ukarabati wa mabwawa mawili ya Rungwa na Muhanga yenye thamani ya zaidi ya milioni 460 yenye ukubwa wa kati katika Wilaya ya Manyoni ili kuongeza uvunaji wa maji ya mvua yatakayonufaisha wananchi katika Wilaya hiyo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -

Je, kuna mkakati gani kudhibiti tembo wanaovamia Vijiji vya Doroto, Kitaraka, Kamenyanga, Gurungu, Muhanga na Njirii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kunusuru maisha na mali za wananchi katika Vijiji vya Doroto, Kitaraka, Kamenyanga, Gurungu, Muhanga na Njirii-Manyoni. Aidha, Wizara imeanza kuimarisha Kituo cha Askari cha wanyamapori kilichopo Kijiji cha Doroto kwa kuongeza Askari, vitendea kazi na kutoa Elimu kwa wananchi juu ya mbinu rafiki za kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -

Je, Serikali haioni ni kuwakandamiza Wananchi wa Itigi kwa kuondoa Miji kwenye bei ya kuweka umeme kutoka shilingi 27,000 hadi shilingi 320,000?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI aljibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali haikandamizi mwananchi yoyote, bali inawajali na kuwaunganishia huduma ya umeme kwa gharama zenye ruzuku ndani yake. Kati ya mwaka 2008 na 2013, gharama za kuunganisha umeme zilikuwa shilingi 455,104.76 ndani ya mita 30; shilingi 1,351,883.52 ndani ya mita 70; na shilingi 2,001,421.60 ndani ya mita 120 kwa maeneo ya Mijini na Vijijini. Gharama hizi ndizo zilizokuwa zinaakisi gharama halisi za kuunganisha umeme wa njia moja.

Mheshimiwa Spika, Mwaka 2013, Serikali ilipunguza kwa kuweka ruzuku gharama za kuunganisha umeme kuwa shilingi 320,960.00 ndani ya mita 30, shilingi 515,617.52 ndani ya mita 70 na shilingi 696,669.64 ndani ya mita 120 kwa maeneo ya mijini. shilingi 177,000.00 ndani ya mita 30, shilingi 337,739.60 ndani ya mita 70 na shilingi 454,654.00 ndani ya mita 120 kwa maeneo ya vijijini.

Mheshimiwa Spika, kuanzia mwezi Januari, 2022 bei imerejea kwenye gharama za mwaka 2013 kwa maeneo ya mijini na shilingi 27,000 kwa maeneo ya vijijini. Gharama hizi zina ruzuku ya Serikali ndani yake. TANESCO inabaini eneo la miji na vijiji kwa kutumia Sheria ya Mipango Miji Namba 8 ya mwaka 2007.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kupanda Hifadhini mazao yanayofuatwa na wanyama waharibifu kutoka Hifadhi za Rungwa, Muhesi na Kizigo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na changamoto ya ongezeko la matukio ya wanyamapori kuingia kwenye makazi ya watu na kusababisha madhara kwa wananchi na mali zao. Changamoto hiyo imesababishwa na uanzishwaji wa shughuli za binadamu kwenye shoroba, maeneo ya mtawanyiko wa wanyamapori na maeneo ya pembezoni mwa hifadhi. Maeneo hayo hutumiwa na wanyamapori wanaohama kutoka katika mfumo mmoja wa ikolojia kwenda mfumo mwingine kwa ajili ya kutafuta maeneo ya malisho, maji, mazalia, ulinzi na mapumziko kwa nyakati tofauti.

Mheshimiwa Spika, kutokana na sababu hiyo ya kiikolojia, upandaji wa mazao katika hifadhi za wanyamapori hauwezi kuzuia wanyamapori kuhama kutoka mfumo mmoja wa ikolojia kwenda mfumo mwingine.

Vilevile upandaji wa mazao hifadhini ni ukiukwaji wa sheria za uhifadhi kwa kuwa wanyamapori wanaishi katika mazingira asilia ambapo mimea mingine ambayo siyo ya asili hairuhusiwi ndani ya hifadhi.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -

Je, ni lini ukarabati utafanywa katika njia ya umeme kutoka kituo kikubwa kuelekea Ikungi, Manyoni, Itigi, Mitundu hadi Mwamagembe?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Singida umeunganishwa na Gridi ya Taifa kutoka katika kituo cha kupoza umeme kilichopo Mkoani Dodoma kupitia njia ya kusafirisha umeme za msongo wa kilovolti 220 na 400 hadi kituo cha kupoza umeme cha Singida. Kwa kutumia msongo huo mkubwa, Serikali kulingana na upatikanaji wa fedha imepanga kujenga kituo kikubwa cha kupoza umeme Wilayani Manyoni ili kuondoa changamoto za umeme kusafiri umbali mrefu.

Mheshimiwa Spika, matengenezo ya njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kilovolti 33 kutoka kituo kikubwa cha kupoza umeme cha Singida kuelekea Manyoni, Itigi, Mitundu hadi Mwamagembe tayari yanaendelea na katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga kiasi cha shilingi 471,000,000.00 kwa ajili ya matengenezo ya njia hiyo. Vilevile mkandarasi wa njia ya reli ya SGR atakapomaliza ujenzi eneo la Kintinku, TANESCO itaunganisha njia ya umeme kutoka Wilaya ya Bahi kwenda Manyoni, hivyo kuimarisha upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-

Je, kuna mpango gani kuvuna/kuwahamisha Tembo kutoka katika Pori la Rungwa, Muhesi na Kizigo ambao wanaingia katika Vijiji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakiri kuwepo kwa changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu wakiwemo tembo. Kwa sasa Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Udhibiti Wanyamapori Wakali na Waharibifu wa Mwaka 2020/2024. Wizara inaendelea kufanya yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, ni kutoa elimu juu ya kujikinga na wanyamapori wakali na waharibifu; pili, kujenga vituo vya askari wanyamapori ili kusogeza huduma karibu na wananchi; na zaidi ya hapo ni kufunga mikanda (GPS collars) tembo kwa kuanzisha timu maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuwashirikisha wananchi kwa kutoa mafunzo kwa askari wa vijiji ili kuongeza nguvu ya kudhibiti tembo katika maeneo ya wananchi, nakushukuru.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -

Je, kuna maamuzi mengine baada ya Kamati ya Mawaziri nane kurudisha kwa wananchi wa Itigi shamba la Kampuni ya Tanganyika Packers?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, shamba la iliyokuwa Kampuni ya Tanganyika Packers ni kituo cha kupumzishia mifugo kinachojulikana kwa jina la Kitaraka Holding Ground. Shamba hili linamilikiwa na Serikali tangu tarehe 1 Mei, 1955 na linatambulika kwa Na. 35 na Hati ya Kumiliki Ardhi Na. 15467 inayotaja ukubwa wa shamba kuwa ni ekari 45,000 (hekta 18,218.623) kwa ajili ya malisho na kutunzia mifugo (cattle holding ground).

Mheshimiwa Spika, Kamati ya Mawaziri nane wa kisekta ya kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 haijarudisha kwa wananchi wa Itigi shamba la iliyokuwa Kampuni ya Tanganyika Packers. Serikali imeelekeza ifanyike tathmini ya kina ya shamba la Kitaraka ili kubaini hali halisi kwa sasa kwa ajili ya kuwezesha Serikali kufanya uamuzi wa kumaliza mgogoro uliopo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Mkiwa – Itigi hadi Rungwa inayounganisha Mkoa wa Mbeya na Singida utaanza kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza ujenzi wa barabara ya Makongolosi – Rungwa – Mkiwa kwa awamu. Taratibu za manunuzi ya mkandarasi wa kazi za ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sehemu ya Noranga – Itigi eneo la Mlongoji yenye urefu wa kilometa 25 zipo katika hatua za mwisho za kusaini mkataba. Aidha, Serikali inaendelea na taratibu za manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa kujenga sehemu ya kilometa 31.9 kati ya Itigi Kitongoji cha Mlongoji na Mgandu kwa kiwango cha lami. Kwa sehemu iliyobaki Serikali inaendelea kutafuta fedha za ujenzi. Ahsante.
MHE. ABEID R. IGHONDO K.n.y. MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -

Je, ni malambo/mabwawa mangapi yatajengwa katika Halmashauri ya Itigi kwa ajili ya kunyweshea Mifugo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya mifugo katika maeneo mbalimbali hapa nchini, ikiwemo katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi. Aidha, mwaka 2021/2022 Serikali ilikamilisha ujenzi wa bwawa la kunyweshea mifugo katika Kijiji cha Mhanga Halmashauri ya Wilaya ya Itigi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya mabwawa na visima kwa ajili ya maji ya mifugo nchini ni makubwa. Hivyo, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ujenzi wa mabwawa na kuchimba visima katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Itigi. Kulingana na upatikanaji wa fedha, vilevile, ili kukabiliana na upungufu uliopo, na nitoe wito kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kuhamasisha wafugaji na wadau wengine kuwekeza katika miundombinu ya maji ya mifugo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza: -

Je, lini Tume ya Umwagiliaji itatimiza ahadi yake ya kuvuna maji ya mvua katika Mbuga inayozunguka Mji wa Itigi ili kuepusha mafuriko?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu spika, katika Mwaka wa Fedha 2023/24, Serikali kupitia Tume ya Taifa ya imetenga fedha kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kuweza kuchimba na kujenga mifereji ya kuongoza maji kutoka bonde linalozunguka Mji wa Itigi na kuelekeza maji hayo mashambani.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, utekelezaji wa ujenzi wa mifereji hiyo utasaidia kuepusha mafuriko yanayojitokeza katika Mji wa Itigi.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA K.n.y. MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-

Je, lini Serikali itachimba Bwawa la Umwagiliaji katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi baada ya Bwawa la Itagata kutofanya kazi kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imepanga kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Bwawa la Itandamilomo lililopo ndani ya Halmashauri ya Itigi ili kupata gharama halisi za ujenzi. Bwawa hilo litatumika kwa kiasi kikubwa katika kuchochea kilimo cha umwagiliaji kupitia mbuga kubwa iliyopo katika Kata za Kitaraka, Itigi Mjini, Tambukareli, Itigi Majengo, Sanjaranda, Ipande, Aghondi na Idodyandole katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi.

Mheshimiwa Spika, Bwawa la Itagata lililopo katika Halmashauri ya Itigi linafanya kazi na Serikali itaendelea kulifanyia maboresho kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:

Je, lini Serikali itachimba visima vya maji kwenye Vijiji vya Kayui, Kalangali, Makale na Mwamagembe – Manyoni?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na zoezi la utafiti wa maji ardhini pamoja na uchimbaji wa visima virefu katika Wilaya zote za Mkoa wa Singida ikiwemo Wilaya ya Manyoni, kupitia programu mbalimbali ikiwemo programu maalum ya uchimbaji wa visima 900.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Wilaya ya Manyoni, Serikali imekamilisha uchimbaji wa visima katika vijiji vinne vya Makale, Jeje, Idodyandole na Mtakuja ambapo kazi ya upimaji wingi wa maji (pumping test) katika visima hivyo inaendelea. Aidha, kazi ya uchimbaji wa visima katika maeneo mengine ya Wilaya hiyo ikiwemo vijiji vya Kayui, Kalangali na Mwamagembe unaendelea ambapo unatarajia kukamilika Oktoba, 2024.