Supplementary Questions from Hon. Yahaya Omary Massare (111 total)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002, ilizuia usafirishaji wa mazao ya misitu ambayo hayajachakatwa ikiwemo asali, mbao na hata wanyamapori. Naomba kuuliza swali langu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kufanya zuio hilo Serikali imeruhusu kusafirisha mbao ya sentimita 15 tu unene na wakati huo wadau na masoko yanahitaji zaidi ya sentimita 15. Je, Serikali iko tayari sasa kuwaruhusu wafanyabiashara ambao wanafanya export ya mbao hizi, wakiwemo wafanyabiashara wa mitiki, pine na mbao za miche ya asili angalau wafikie katika sentimita 20 ili nao wapate tija na kushindana na wafanyabiashara wenzao katika masoko?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika Jimbo langu la Manyoni Magharibi na Wilaya nzima ya Manyoni, imezuia uvunaji wa mbao na mazao ya misitu kwa ujumla, Je, Serikali sasa ipo tayari kushirikiana na Halmashauri yangu mpya ya Itigi uvunaji uendelee, badala ya watu sasa kuiba ili walipe kodi za Serikali na maduhuli na pia kusaidia pato la Halmashauri wakati misitu ipo?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa Sheria ambayo ameitaja Sheria Namba 14 ya mwaka 2002, Serikali iliweka utaratibu kwa uvunaji wa mazao mbalimbali ya misitu kama alivyoyataja na kwa uchache ni pamoja na miti ya mitiki, pamoja na ya pine, napenda kusisitiza kwamba pale ambapo Sheria ipo na ilikwishawekwa na Serikali, ni wajibu wetu kufuata masharti ya Sheria hiyo katika kipindi chote ambacho Sheria hiyo bado imesimama.
Mheshimiwa Naibu Spika, iwapo kuna mawazo mengine mapya ambayo ni mazuri, ya kujenga kwa maslahi ya Taifa, basi ni budi kufuata utaratibu wa kawaida wa kisheria kuweza kurekebisha sheria ili kuweza kunufaika na mawazo mapya kama yapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, uvunaji wa mazao ya misitu katika Jimbo la Manyoni Magharibi na Wilaya Manyoni kwa ujumla ulizuiliwa kwa sababu za msingi za uhifadhi. Pale unapoendelea kuvuna unatakiwa uvune ukizingatia sharti la uvunaji endelevu, kama utaendelea kuvuna bila kuzingatia masharti ya uvunaji endelevu, ukakiuka masharti sustainability maana yake ni kwamba utakosa kila kitu kwa sababu misitu hiyo inaweza kupotea kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunapokea maoni yake na kwamba sasa tutakwenda kufanya utafiti wa kisayansi kwenda kuangalia kama zuio hilo sasa limepitwa na wakati, inawezekana msitu huo sasa umeweza kupata hadhi ambayo inawezekana kabisa tukaendelea kuvuna badala ya kusimamisha kama tulivyosimamisha hapo awali. Tutaongozwa na utafiti wa kisayansi ili tuweze kuona kwamba, sasa tunaweza kuendelea kuvuna.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni haki ya kila mwananchi hasa Mtanzania kupitia kodi zao kusikiliza redio ya Taifa hasa TBC. Je, ni lini Serikali sasa itaweka booster yake ya TBC katika Mji Mdogo wa Itigi ili na wananchi wale wasikie redio yao ya Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuambatana na mimi kwenye gari yake yenye redio nzuri ili atakapofika Itigi asikie matatizo yaliyoko pale?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba usikivu wa redio hasa Redio ya Taifa pale Itigi siyo mzuri lakini hii imetokana na mabadiliko ya teknolojia kutoka Mediam Waves (MW) kwenda FM. TBC kwa sasa inamalizia zoezi la kufanya uchambuzi wa kuangalia mahali ambapo tunatakiwa kuweka booster na maeneo mengine tunalazimika kupeleka mtambo. Sasa ni lini usikivu utaboreka, ni pale utaratibu huu wa kufanya uchambuzi utakapokamilika na ni hivi karibuni kwa sababu tupo mwishoni kabisa, upembuzi ukimalizika tutaamua sasa Itigi tunaweka mtambo au booster.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mimi kama Waziri wa Habari nipo tayari kuambatana naye na yeye anajua kwamba Singida ni nyumbani kwetu. Najua usikivu pale ni mbovu ndiyo maana tunafanya kila liwezekanalo kazi hii ikamilike mapema tuweze kuongeza usikivu wa Redio ya Taifa kwenye eneo la Mheshimiwa Mbunge.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Naomba nimuulize swali dogo tu Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa swali la msingi linafanana sana na Jimbo langu la Manyoni Magharibi ambapo kuna zahanati tatu tu. Je, ni lini Serikali itaanza kujenga vituo vya afya katika Kata za Idodyandole, Aghondi, Sanjaranda, Majengo, Tambuka Reli, Kitaraka, Mgandu, Kalangali, Mwamagembe na Ipande?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu Jimbo la Mheshimiwa Mbunge ni sehemu ambazo zimegawanyika na wana changamoto ya resources lakini suala la ujenzi wa hizi zahanati kama nilivyosema ajenda yetu ileile. Bahati mbaya mwaka huu tulikuwa na mchakato mpana wa vikao vyetu vya Bunge na vikao vya bajeti vya Halmashauri havijaenda vizuri, lakini niwaombe tunapoanza Bunge hili la Awamu ya Tano sisi Wabunge tuwe ndiyo wa kwanza kubainisha vipaumbele vya maeneo yetu na ujenzi huu wa zahanati maana yake unaanzia kwetu sisi, Mbunge unaangalia priority yako iko katika maeneo gani.
Mheshimiwa Naibu Spika, imani yangu kubwa ni kwamba, michakato ile itakapoanza katika vikao vyetu ikifika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, jukumu letu ni kusukuma sasa mambo haya yaweze kwenda vizuri. Najua wazi kwamba Mheshimiwa Mbunge wangu wa Manyoni ni kweli ana changamoto kubwa, lakini namuahidi kwamba mwaka huu ni wa kwanza tulikuwa na changamoto kubwa sana lakini mwaka unaokuja tutakaa pamoja; kama Wabunge tutakuwa katika mikutano yetu katika Halmashauri na sisi Ofisi ya TAMISEMI tutashirikiana vizuri zaidi kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya afya hususani kupata zahanati na vituo vya afya katika maeneo hayo aliyoyaeleza.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Mkiwa - Itigi, Rungwa - Makongorosi aliyoitaja Mheshimiwa Waziri ni barabara inayopita katikati ya Mji wa Itigi wenye vijiji vya Songambele, Majengo na Itigi Mjini na kwa majibu haya, maana yake barabara hii imeshushwa daraja. (Makofi)
Swali, wakati sheria inabadilika kutoka mita 45 kuja mita 60, wananchi hawa waliwekewa alama za “X” kwamba wasiendeleze maeneo yale. Sasa kwa majibu haya; je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaweza kutamka kwamba wale wananchi waendelee na ujenzi? (Makofi)
Pili, Naibu Waziri anaweza kuthibitishia wananchi wa Itigi kwamba itakapoanza kujengwa kilometa 35 za kwanza na kipande kile kitakajengwa pamoja nacho? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimechanganyikiwa nimechanganyikiwa kidogo kwa sababu swali la pili linapingana au linakinzana na swali la kwanza; kwa sababu swali la kwanza tumemwambia tunajenga hiyo barabara wakati tunajenga hiyo ya kutoka Rungwa - Makongorosi hadi Mkiwa. Kwa maana nyingine, lile eneo ambalo limewekewa “X” ni lazima liendelee kubakiwa kuwekewa “X”. Sasa tumemaliza kufanya upembuzi yakinifu, hatua zinazofuata ni za kulipa fidia na kuanza ujenzi baada ya kutafuta hizi fedha na kupatikana.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili sijui nijibu vipi kwa sababu nadhani la pili linajibu kwa hili la kwanza, kwa sababu tunajenga hili eneo na tutajenga. Tunachokifanya ni tunatafuta fedha.
Kwa hiyo, naomba sana asiwaambie watu wajenge hilo eneo. Maeneo ambayo yamewekewa “X” maana yake ni kwamba katika upembezi yakinifu imeonekana hapo ndiyo barabara itapita. Tafadhali sana, usiwahimize wakajenga, hilo eneo libakie ili tutakapopata fedha tuweze kujenga.
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, siyo kwamba tutajenga na hiyo, tunajenga kupitia hapo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona ili niulize swali dogo tu la nyongeza, kwa kuwa swali la msingi wananchi wa Morogoro linafanana sana na wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi hususan Mji mdogo wa Itigi. Je, ni lini Serikali itasaidiana na Halmashauri yangu kuhakikisha Vijiji vya Rungwa, Kintanula, Kalangali, Mitundu, Kingwi, Dodiandole, Mbugani, Mabondeni, Njirii, Gurungu, Majengo, Songambele, Kitalaka, Kihanju na Tambuka Reli vitapatiwa maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kushirikiana na Halmashauri zote nchini kwa kuzipangia bajeti ili ziweze kutekeleza miradi ya maji. Hilo limeshafanyika, katika Mwaka wa Fedha unaokuja Serikali imehakikisha Halmashauri zote inazipatia fedha kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zilizotolewa kwanza ni kuhakikisha kwamba miradi iliyokuwa inaendelea inakamilika, baada ya hapo ndipo wanakwenda sasa kwenye miradi mipya. Kwa hiyo, kwa mujibu wa swali lake Serikali tayari inashirikiana na Halmashauri, sasa ni wajibu wake Mheshimiwa Mbunge, kwa sababu na yeye ni Diwani, kukaa katika kikao cha Madiwani na uongozi wa Halmashauri ili waweze kupanga bajeti kwa hela iliyotengwa ili hivyo vijiji viweze kufikiwa. Kama fedha haitatosha basi mwaka ujao wa fedha wataleta maombi, tutatenga fedha nyingine.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida pamoja na Mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa mikoa masikini ambayo inahitaji usaidizi wa Serikali. Sasa Mheshimiwa Waziri yuko tayari kusaidia wananchi wa mikoa hii ya Dodoma na Singida kwa ushawishi wake mkubwa na weledi wake kufanya basi angalau kiwanda kimoja kiwekezwe katika Mkoa wa Singida, hususan katika Jimbo la Manyoni Magharibi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kutembelea wananchi wa Itigi ili kujionea fursa zilizopo ili kushawishi wawekezaji waweke kiwanda katika eneo la Itigi? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kama niko tiyari kuwekeza Singida na Dodoma? Niko tiyari. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namba mbili ni kutembelea Itigi.Ninapaswa kutembelea Singida kwenye Jimbo la Mheshimiwa Kingu, kuna mradi wa maziwa, tutapanga twende wote.
Lakini nichukue fursa hii kuwaeleza kwamba ukanda huu una fursa ya maziwa, una fursa ya viwanda vya mafuta jamiii ya alizeti na una fursa ya sekta ya ngozi. Hapa Dodoma Wizara yangu imetengewa ekari 200 na ninayo pesa tayari ya kutengeneza cluster ya ngozi.
Kwa hiyo, hii ni sehemu ambayo ni potential na kwa kutumia ngozi tutatoka; mnajua idadi ya ng‟ombe tulio nao. Kwa hiyo, Dodoma tunaweza kutengeneza viatu tukavika Afrika.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niulize swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, matatizo yaliyopo huko Korogwe yanafanana sana na matatizo yaliyopo katika Jimbo la Itigi; kuna shamba lililokuwa la Shirika la Tanganyika Packers lipo katika eneo la Kitaraka, lilitelekezwa na shirika hili baada ya shirika hili kufilisika mwishoni mwa miaka ya 1980.
Mheshimiwa Spika, wananchi wa maeneo yale katika vijiji vya Kitaraka, Kaskazi Stesheni, Doroto, Majengo, Tambukareli, Kihanju na Sanjaranda wamelitumia shamba lile kulima na linawasaidia sana kupata mahitaji yao ikiwemo mazao ya chakula pamoja na mazao ya biashara, lakini kuna taarifa kwamba Serikali ina mpango wa kulibinafsisha shamba lile kwa wawekezaji.
Je, ni nini kauli ya Serikali kwamba haitaonesha inaleta mgogoro na wananchi ambao shamba lile sasa linawanufaisha wananchi wengi sana wazawa na wananchi wa nchi hii kuliko kuweka mwekezaji, ni nini kauli ya Serikali juu ya suala hilo?
NAIBU WAZIRI ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli anachokizungumza kwamba wananchi wamekuwa wakilitumia lile shamba na ametaja vijiji vinavyohusika. Naomba nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwamba nia ya Serikali ni njema na kama kuna hatua ya kuweka mwekezaji vilevile pia itakuwa ni kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa Jimbo lake.
Mheshimiwa Spika, tunachotaka afahamu ni kwamba Serikali haiko pale kunyang’anya wananchi ardhi na kuwaacha wakiteseka. Kitakachofanyika ni kwamba watakaokuwa wa kwanza kufikiriwa ni wale wananchi walioko pale na kwa sababu shamba lile lilikuwa linamilikiwa na Serikali tangu awali kwa maana hiyo Serikali kulipangia matumizi mengine ni sahihi. Tutakachofanya kabla halijapewa mwekezaji lazima yale maridhiano ya awali katika kukubaliana namna ya kuweza kufanya ile kazi yaweze kukubalika kwa sababu wao pia wanatambua hawako pale kihalali kulingana na umiliki wa shamba lile.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona ili niulize swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa askari hawa ambao wanatekeleza kufanya nchi hii iwe na amani kuhakikisha wahalifu wanakuwa hawafanyi vizuri wako katika Jimbo langu la Itigi na wanakaa katika nyumba ya railway ambayo ni mbovu sana. Kituo kile kiko katika nyumba za railway; Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwaboreshea Kituo cha Polisi na Mheshimiwa Waziri anajua kabisa kituo kile ni kibovu na hakifai na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi wamejitahidi kwa nguvu zao wameshindwa. Nini kauli ya Serikali na je, itawasaidia wananchi wa Halmashauri ya Itigi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, natambua mazingira ya kituo kilichopo Itigi na Mheshimiwa Mbunge amekuja mara kadhaa kulielezea jambo hilo na ameandika na barua ya kiofisi na nimemwahidi kwamba kwa hatua ambazo wameshazifanya wao, akiongoza yeye mwenyewe jitihada hizo na sisi kama Wizara tutawaunga mkono na binafsi nitafika katika Jimbo lake kuweza kuongeza nguvu kwa kuona mazingira yaliyopo na hatua ambazo zimeshachukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge, nimhakikishie, awahakikishie na vijana wetu kwamba jambo hilo ameshalifikisha na sisi tutalichukulia hatua zinazostahili kwa kulipa uzito unaostahili.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwa kuwa katika barabara hii korofi kipindi chake cha kuharibika sasa kimekaribia, kipindi cha mvua ambacho katika maeneo ya Lulanga, Itagata, Ukimbu, Mitundu, Kiombo, Mwamaluku, Mwamagembe, Kintanula hadi Rungwa udongo huo aliousema ni mbaya na ukarabati uliofanyika kipindi cha nyuma ulikuwa haukidhi kiwango. Je, sasa Serikali iko tayari kufanya marekebisho ya kutosha katika kipindi hiki kabla mvua hazijaanza?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; katika ujenzi wa kipande hiki cha kilometa 57 ambacho Meshimiwa Naibu Waziri amekisemea hapa, watakapoanza wanatarajia ni muda gani utachukua kukamilika? Maana yake wananchi wanahamu kubwa ya kuona barabara ya lami katika kipande hiki nikiwemo mimi Mbunge wao.
Mhesshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba, baada ya Bunge hili nitakuwa na safari ya kuipitia barabara hii. Nitamjulisha Mheshimiwa Mbunge tarehe kamili nitakapokuwa katika eneo lake ili tusaidiane kutambua kwa karibu zaidi na kwa macho siyo kuandikiwa tu, hatimaye tuhakikishe tunaposimamia hatua za marekebisho ambazo Mheshimiwa Mbunge anazihitaji tuweze kuzisimamia vizuri.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu lini tutakamilisha, nimwombe Mheshimiwa Mbunge ajue dhamira ya Serikali hii ya kuikamilisha hii barabara, aone kama ambavyo tumejibu katika swali la msingi maeneo ambayo tayari tumeyakamilisha na tupo katika kuendelea kukamilisha maeneo yaliyobaki. Naomba atuamini, kusema ni lini huwa naogopa sana kwa kazi hizi za ujenzi ambazo zina process, lazima upate hela na hatimaye ujihakikishie kipande gani kinakamilika kwa wakati gani. Naomba aniwie radhi kwamba hiyo kazi ya kusema lini hasa siyo rahisi sana. Kikubwa tuna dhamira ya dhati na tutakamilisha kujenga hii barabara kama ambavyo kwenye Ilani imeeleza. Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niulize swali dogo tu kwa kifupi. Kwa kuwa matatizo yaliyopo huko Kyerwa yanafanana sana na yaliyopo katika Jimbo langu la Manyoni Magharibi katika Mji wa Itigi ambao hauna maji kabisa toka nchi hii imepata uhuru. Je, sasa Serikali iko tayari kusaidiana na Halmashauri ya Itigi ili wananchi wa Itigi Mjini pale wapate maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali imeahidi kupeleka maji katika Mji wa Itigi na mpango huo upo. Kwa hiyo, tunaendelea kufuatilia utekelezaji wa yale mambo ambayo tulishakubaliana kwa mwaka huu tunafanya nini. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira, Serikali itahakikisha kwamba Mji wa Itigi unapata maji.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa
kunipa nafasi. matatizo yaliyopo huko Segerea yapo pia katika Jimbo langu la
Manyoni Magharibi katika Halmashauri ya Itigi kuna msitu unaitwa Chaya Open
Area, ni kitalu cha uwindaji ambacho muda mrefu hakina Mwekezaji. Sasa
Serikali inataka kuondoa wananchi ambao wamekaa pale kwa ajili ya kulima na
wanafuga vizuri sana. Je, Serikali inaweza ikaona umuhimu wa wananchi wale
kuendelea kutumia Chaya Open Area ambapo ni eneo ambalo halina kabisa
faida kwa ajili ya uwindaji?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika,
anazungumzia eneo la Chaya na anatoa maoni kwamba pengine Serikali ilitoe
sasa eneo hili kwa ajili ya matumizi ya kibinadamu kwa wananchi wa eneo hilo
na wanaozunguka eneo hilo. Tumejibu swali hili mara nyingi kama Serikali
kwamba tunayo changamoto kama Taifa ya kwamba katika maeneo kadhaa
wananchi wamepata au wameonekana kuwa na uhitaji wa maeneo kwa ajili ya
matumizi ya kibinadamu yakiwemo makazi, kilimo pamoja na ufugaji. Kama
Serikali tumekwishasema kwamba jambo hili linatakiwa lishughulikiwe kisayansi na
kitaalam. Huwezi kuzungumzia juu ya uhaba wa ardhi juujuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wakati huu tunavyoendelea tayari Serikali
imekwishaunda Kamati ya Kitaifa inayohusisha Wizara nne ambayo inapita katika
maeneo yote ya nchi hii kuangalia kwa uhalisia kabisa wapi kweli kuna uhaba
wa ardhi na wapi kweli ardhi tungeweza kuitumia kwa namna bora zaidi. Kamati
hii itasaidia baadaye Serikali iweze kuja kusema kwamba eneo hili ni kweli
linaweza likabadilishwa matumizi na eneo lingine liendelee kubakia kutumika
kwa namna ambayo sote tutakubaliana tukiwa tunaongozwa na Serikali
kwamba matumizi hayo ya hivi sasa ni matumizi ambayo yana tija zaidi kwa
Taifa.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii adhimu ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo langu la Manyoni Magharibi kuna vijiji vya Mbugani, Agondi, Mabondeni, Kitopeni, Ipande, Muhanga, Damwelu, Kitalaka, Kaskazi Stesheni, Kintanura, Lungwa na Kalangali havina umeme. Je, Serikali inaweza kutoa tamko kwamba REA Awamu ya Tatu wananchi wa vijiji hivi watafikiwa na umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa, nakupongeza sana juzi uliniletea orodha ya vijiji vyako vyote, kwa hiyo vijiji vyako vyote Mheshimiwa Mbunge ulivyotaja katika Awamu ya Tatu vyote vitapitiwa na umeme, na nikuhakikishie kwamba kufikia mwezi Machi kama ambavyo tumeeleza, vijiji vyote kwa nchi nzima wakandarasi watakuwa site ikiwa ni pamoja na Jimbo lako la Manyoni Magharibi.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika,
ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niulize swali dogo la nyongeza. Matatizo yaliyoko huko Lulindi yapo katika Jimbo la Manyoni Magharibi, kuna barabara kutoka Idodyandole kwenda Ipangamasasi, kuna tawi la Mto Kizigo imekuwa ni
korofi sana na kwa nguvu ya Halmashauri hatuwezi kujenga;
Je, Mheshimiwa Waziri anaweza akatuahidi angalau kwa maneno kwamba Serikali kupitia TANROADS itatusaidia katika kipande hicho kidogo cha daraja?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba tupewe muda mfupi tu, hatutahitaji muda mrefu tutakuja kutoa taarifa ya barabara ambazo tunapendekeza zipandishwe hadhi na nyingine zikasimishwe kwa TANROADS.
Naomba tu nitoe tahadhari, inaonekana maombi ni mengi sana na tukipeleka barabara nyingi sana TANROADS uwezo wao kwa sababu kifedha haiongezeki sana kulinganisha na mzigo tunaowapa, tusije tukaishia nazo zikawa za sub standard kwa sababu kazi ni kubwa na uwezo
ni mdogo.
Kwa hiyo, nilitaka tu nitoe tahadhari hiyo lakini tutakuja kutoa taarifa hivi karibuni ni zipi zitapandishwa hadhi na zipi zitakasimiwa kwa TANROADS.
Mheshimiwa Spika, naomba tupewe muda kidogo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa matatizo yaliyoko huko Mbulu yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo Itigi katika Jimbo la Manyoni Magharibi, ni kwamba Itigi ni eneo kubwa sana, lipo katika Wilaya ya Manyoni. Kutoka mwanzo wa Tarafa ya Itigi hadi mwisho kuna zaidi ya kilometa 200 na ni Tarafa moja tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba kuuliza swali dogo tu la nyongeza kwamba Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuigawa Tarafa hii ya Itigi kuwa Tarafa nyingi kwa sababu ya eneo na jiografia ni eneo kubwa sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuko tayari, lakini kwanza lazima mchakato huu uanze katika suala zima la vijiji, itakuja katika vikao vya Ward Council, vitakuja katika vikao vya full council, vitakuja DCC, RCC vitafika kwetu, then Waziri mwenye dhamana, kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa, Sura ya 287 kifungu cha 10 ambacho kinafanya variation ya haya maeneo, atachukua jukumu hilo la kufanya hivyo.
Kwa hiyo, ndugu yangu wa Itigi wala usiwe na hofu katika hilo, anzeni mchakato, sisi Serikali tuko kwa ajili ya
kutekeleza hayo ambayo mtayafanya.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Matatizo yaliyopo huko Busokelo yapo pia katika
Halmashauri ya Wilaya ya Itigi. Katika Wilaya ya Manyoni kuna Halmashauri ya Manyoni na Hamashauri ya Itigi; Halmashauri ya Itigi square kilometer zinakidhi na maombi yamekuwa yakipelekwa kila mara na toka mwaka 1980 Serikali imekuwa ikiwaahidi wananchi wa Itigi kwamba watapatiwa Wilaya kamili.
Je, sasa ni lini Serikali itaipa Halmashauri ya Itigi kuwa Wilaya kamili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ukiangalia Manyoni, lazima tufahamu juhudi kubwa ya Serikali iliyofanya pale, mwanzo ile yote ilikuwa inaitwa Wilaya na Halmashauri ya Manyoni. Hapa katikati ndiyo tukapata Halmashauri mpya ya Itigi na wewe Mheshimiwa Mbunge unafahamu hata suala zima la upelekaji wa fedha ndiyo kwanza tumepeleka kwa ajili ya kujenga miundombinu ya Halmashauri ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili ninafahamu
kwamba, siku ile nilikuwa na Mkuu wa Wilaya pale na alisikitika katika hilo alisema kwamba mafuta anayoyatumia ni kwamba, akiamua kuzunguka eneo lake matufa yanaisha kwa sababu Manyoni ukijumlisha na Itigi ni eneo kubwa sana.
Naomba niseme japokuwa maombi hayo inawezekana mwanzo yalikuja yalidondoka kwa sababu yalishindwa kupata sifa, hizo sifa sasa hivi zikikamilika basi naomba mfanye ile michakato ya kisheria kama inavyokusudiwa kuanzia katika ngazi za Ward DC, Baraza la Madiwani, DCC, RCC na ikifika katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI
na Waziri wangu yuko hapa, hawezi kushindwa kufanya maamuzi sahihi kwa kadri anavyoona jambo hilo linafaa kwa maslahi mapana ya wananchi wa Itigi.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii, pia nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Lakini pamoja na majibu hayo mazuri nina maswali madogo tu ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ya Maliasili kupitia TFS imekuwa ikitoa vibali vya kuvuna mazao ya misitu. Mvunaji anaanzia vijijini, Wilayani kwenye kanda na hadi Wizara, lakini kabla ya kuruhusiwa kuvuna mazao ya misitu, Serikali imekuwa ikiwasajili wadau hawa na kuwatoza pesa kila mwaka. Vilevile kumekuwepo na tatizo kubwa la Wizara hii kuwa ikishatoa vibali hivi inachukua muda mfupi tu kuvifuta kama ilivyokuwa mwaka huu ambapo vilitolewa vibali zikiwemo approval za…
… kutoka nchi za nje na baadae vilifutwa na Mheshimiwa Waziri, sasa swali.
(a) Je, ni lini Serikali itaacha utaratibu huu mbaya na ambao unawatia hasara wadau wao?
(b) Serikali haioni sasa ni vyema isitoe approval hizi hadi ijiridhishe kwamba wananchi na wadau hawa wakipewa vibali hivyo watafanya kazi kwa mwaka mzima kuliko kama hivi wanatoa na kufanya kazi kwa miezi miwili tu na kuwasimamisha?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufupi suala la uvunaji wa maliasili linatokana na ukweli kwamba nia na dhamira ya Serikali ni kuliwezesha Taifa hili kuweza kutekeleza mipango yake yote ya maendeleo kwa kutumia rasilimali za Taifa hili ikiwemo maliasili. Jambo la msingi ni kwamba tunatakiwa kutumia maliasili hizo kwa namna ambayo ni endelevu. Kwa hiyo, udhibiti haumaanishi kwamba rasilimali hizi au maliasili hizo zisitumike kabisa, hapana, nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba tunafanya matumizi endelevu ili tuweze kuendana hata na malengo ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kuhusu swali lake moja kwa moja la utaratibu wa utoaji wa vibali, huo ni utaratibu ambao utatuwezesha kutoa fursa kwa kila mwananchi ya kuweza kushiriki katika uvunaji wa raslimali hizo. Lakini ikiwa kwamba, utaratibu huo unaonekana pengine una kasoro basi kwa kuwa ulikuwepo kwa mujibu wa sheria basi…
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anayo fursa ya kufuata utaratibu wa kawaida wa kuleta maoni ili tuweze kupitia upya sheria hiyo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niulizes swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, matatizo yaliyopo huko Mbeya Vijijini yanafanana kabisa na matatizo waliyonayo wakulima wa Itigi. Wakulima wa Itigi wanalima mazao mbalimbali yakiwemo mazao ya biashara na mazao ya chakula, lakini wanategemea sana Kampuni hii ya Tanganyika Packers ambalo limetelekezwa na sasa wanalitumia. Mheshimiwa Naibu Waziri alifika pale na aliona hamasa ya wananchi kutaka shamba lile lirejeshwe kwa wananchi kupitia Halmashauri yao.
Je, ni lini sasa Wizara hii italirudisha shamba lile kwa wananchi kwa sababu kampuni hii inayolimiliki ilishafilisika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati wa ziara yangu Itigi, niliona changamoto ya ardhi waliyokuwanayo wananchi, pamoja na kuwepo na shamba ambalo ni kama limetelekezwa na hivyo kuhitaji jitihada za kuangalia namna ya kuwapatia.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari mchakato wa kuangalia namna ya kuligawa shamba hilo unaendelea. Wizara yangu kwa kushirikiana na Msajili wa Hazina inatayarisha waraka wa kwenda Baraza la Mawaziri ili hatimaye shamba hilo liweze kugaiwa kwa utaratibu ambao utaonekana unafaa ikiwa ni pamoja na kugawa kwa wafugaji na wakulima wa Itigi.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo yaliyoko huko Buchosa yanafanana kabisa na matatizo yaliyoko Itigi katika Halmashauri mpya ya Itigi. Wakati Halmashauri hii inaanzishwa ilipata watumishi kutoka Halmashauri mama ya Manyoni ambayo hata nayo ilikuwa na watumishi wachache na hivi tunavyozungumza Halmashauri ya Itigi pia imekutana na janga hili la vyeti fake, kuna baadhi ya watumishi ambao wameondoka, je, Serikali iko tayari sasa itakapotoa ajira kutuletea watumishi wa kutosheleza katika Halmashauri mpya ya Itigi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naomba kujibu swali la Mheshimiwa Massare kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunatambua upo upungufu na kama ambavyo tumekuwa tukieleza humu ndani, mwaka kesho tunatarajia kuajiri zaidi ya watumishi wapya 52,436. Jana tu pia tayari Mheshimiwa Rais alishaagiza, tumetoa kibali cha watumishi wapya 15,000 kwa ajili ya kwenda kuziba pengo la watumishi ambao wamekutwa na vyeti vya kughushi, lakini vilevile kuweza kuziba ikama na tutaendelea kufanya hivyo kila mara itakapobidi.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo tu la nyongeza. Kwa kuwa, matatizo ya maji yaliyoko huko Maswa Mashariki yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika Halmashauri ya Itigi na shida kubwa iko kwa wafugaji katika suala zima la kunywesha mifugo yao. Sasa Serikali kwa maana ya Wizara ya Maji iko tayari kukubaliana na mapendekezo ya Halmashauri ya Itigi kwa ajili ya kuchimba malambo tu madogomadogo katika vijiji vyake?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufupi kabisa ni kwamba, Mheshimiwa Mbunge tuko tayari kushirikiana na halmashauri yake kuhakikisha tunachimba mabwawa madogo madogo kwa ajili ya mifugo. Kwa hiyo, tuendelee kuwasiliana.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Matatizo yaliyopo huko Itilima yapo pia katika Halmashauri mpya ya Wilaya ya Itigi. Wananchi wa Itigi wanaitegemea sana Hospitali ya Mission ya Mtakatifu Gaspari hawana hospitali ya wilaya. Je, Sasa Serikali iko tayari kusaidia Halmashauri ya Itigi kujenga nayo hospitali ya Wilaya ili iondokane na gaharama kubwa wanazotumia wananchi wake ambao ni wapiga kura wetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Itigi kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kuna changamoto, lakini mara nyingi ndugu zangu nilikuwa nikisema hapa kwamba hili suala la ujenzi wa hospitali, ujenzi wa vituo vya afya mara nyingi michakato hii inaanza kule site chini. Hata hivyo niseme kwamba kwa kesi ya Itigi Mheshimiwa unakumbuka kwamba umeuliza swali hili mara kadhaa na ndiyo maana kutokana kwamba umeliuliza swali hili mara kadhaa, hata Serikali sisi kupitia ofisi yetu iliona lazima iipe kipaumbele Itigi kwa sababu hakuna Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipokwenda kutembelea pale Itigi tulikuta kituo cha afya ambacho hali yake si shwari, tukasema tunaanza na hapa. Ndiyo maana muda si mrefu ujao tutakwenda kujenga centre ya upasuaji kubwa sana na kujenga wodi zingine. Lengo kubwa ni kukiboresha kile Kituo cha Afya cha Itigi angalau kiweze kutoa huduma ambayo inalingana lingana japo na hospitali ili wananchi wa Jimo lako waweze kupata huduma vizuri.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa madini haya ya jasi
(gypsum) yako mengi sana katika nchi hii hasa Itigi, Msagali maeneo ya Mpwapwa na maeneo mengine. Baadhi ya nchi ambazo zinatuzunguka hazina madini haya ya jasi ikiwemo Congo, Rwanda na Burundi. Je, Serikali itasaidiana na wajasiriamali na wachimbaji wadogo hawa wa jasi kuwapatia masoko katika nchi hizi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa viwanda vya cement vinatumia malighafi hii ya jasi kutengenezea cement lakini sasa kuna baadhi ya viwanda ambavyo vimewekezwa nchi hii vinaagiza clinker moja kwa moja kutoka nchi za Ulaya na Asia. Je, Serikali sasa iko tayari kuhakikisha viwanda vya cement ambayo vitawekwa baadaye vinafanya processing hapa hapa nchini ikiwemo kujenga matanuru ambayo jasi itatumika? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, kuhusu kusaidia wawekezaji waweze kutosheleza viwanda vya ndani na ku-export jasi hiyo ni sehemu ya shughuli yangu. Mheshimiwa Mbunge tutakutana tuwa-organize vijana tuweze kuwaongoza kwenda sokoni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuagiza clinker kutoka nje napenda niliambie Bunge lako Tukufu kwamba, uwezo uliosimikwa wa viwanda vya Tanzania vyenye uwezo wa kuzalisha cement tani milioni kumi na laki nane kwa mwaka tuna uwezo wa kujitosheleza clinker. Hata hivyo, jambo moja la kufurahisha, wenye viwanda vyote 11 walikutana Dar es Salaam chini ya Uenyekiti wa Dkt. Meru, Katibu Mkuu wangu na wakakubaliana wao kwamba watapeana clinker yenye viwango na yenye bei nzuri. Hakuna haja ya kuagiza nje wakati clinker inapatikana hapa.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona. Matatizo yaliyoko huko Singida Magharibi yanafanana kabisa na yaliyoko katika Jimbo la Manyoni Magharibi, na sisi tumeanza kujenga zahanati nyingi.
Je, Serikali iko tayari sasa kuiongezea mgao Halmashauri ya Itigi ili iweze kufunika maboma ambayo tayari tumeshayaanza katika vijiji vya Mbugani, Mnazi Mmoja, Tulieni na vijiji vingine vingi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli anachoshuhudia Mheshimiwa Mbunge kwamba tulipofika pale Itigi katika Halmashauri ya Itigi, lakini bahati mbaya wao hawana Hospitali ya Wilaya. Ndiyo maana mpango wa Serikali ni kuhakikisha kwamba Halmashauri ile ambayo kwa jiografia yake mara nyingi wanatumia kile Kituo cha Kanisa kama ndiyo sehemu kubwa ya utoaji huduma ya afya, Serikali hatutasita kutoa ushirikiano.
Mheshimiwa Spika, katika ule mpango ambao fedha ambazo tumetenga; na Halmashauri hiii tutaipa kipaumbele. Kwa hiyo, Mkurugenzi ahakikishe yale maboma yaliyoanzwa kujengwa, yamemilika. Hata hivyo, kuna mpango kwamba, tutaisaidia Itigi as a special case kuona ni jinsi gani wananchi wa Manyoni Magharibi wataweza kupata huduma nzuri.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali madogo mawili:-
Kwa kuwa, dhamira ya Serikali hii ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha wananchi wake wanajitegemea hasa katika suala la chakula, pia kuhakikisha wananchi hawavamii hifadhi zilizotengwa kwa ajili ya kuhifadhi wanyama na misitu ya hifadhi. Pia kwa kuwa eneo langu la Itigi eneo wananchi ni asilimia 35 tu, asilimia 65 ni eneo ambalo limetengwa kwa ajili ya hifadhi ya Wanyamapori ya Rungwa, Muhesi na maeneo mengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, shamba hili ndiyo shamba lenye rutuba na ndiyo shamba ambalo lina kiwango kizuri cha kufanya wananchi waweze kunufaika na kujitegemea kwa chakula na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo alipokuja Itigi katika mkutano wake wa hadhara na wananchi aliwaambia na kuwahakikishai wananchi kwamba shamba hili sasa litarudishwa kwa wananchi;
Je, Mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo na shamba hili liko kwenye Wizara ya Kilimo, aliwadanganya wananchi wa Itigi kwamba atawarejeshea shamba hili?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Kampuni hii ya Tanganyika Packers ilishafilisika, haipo kisheria na ilishafutwa, je, sasa Serikali iko tayari kutekeleza yale ambayo Mheshimiwa Rais alipokuja Itigi alisema kwamba atawasaidia wananchi wa Itigi shamba hili ili liwanufaishe jamii nzima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa nilipofika Itigi nilitoa ahadi kwamba Serikali itachukua hatua kuhakikisha kwamba shamba analolizungumzia litarudi kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimfahamishe Mbunge kwamba utaratibu huo umeshaanza kwa sababu Wizara ambayo awali ndiyo ilikuwa inamiliki hilo shamba imeshawasilisha taarifa kwa Treasury Register ili utaratibu wa kurudisha utaratibu kwa wananchi na hasa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi iweze kufanyika. Kwa hiyo, naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo uwongo, hatukudanganya lakini mchakato unaendelea.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi ni wananchi ambao nao wanapenda kitoweo cha samaki. Kwa kuwa hatuna bwawa wala ziwa.
Je, Serikali iko tayari kushirikiana nami Mbunge wao na vikundi vya vijana na akina mama wa Itigi kuweza kuanzisha mabwawa ya samaki?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafurahi kusikia kwamba Mheshimiwa Mbunge anataka kuhamasisha vijana wake wa Jimbo la Manyoni Magharibi ili kuwekeza katika ufugaji wa samaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimfahamishe tu kwamba Wizara iko tayari kushirikiana naye ili mradi afuate utaratibu ambao unatakiwa nao ni kwa kupitia Halmashauri ambayo yeye mwenyewe ni Diwani.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niulize swali la nyongeza, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu haya mfuko huu unatambua tu viongozi na watumishi wa umma, lakini watumishi wa sekta za kisiasa kama Wabunge na viongozi wengine hawapo katika mfumo huu. Je, Serikali sasa iko tayari kuwaingiza watumishi wa kisiasa wakiwemo Wabunge katika utaratibu huu ambao unafikia miaka 55 au 60 waweze kupatiwa kadi za afya na wawe ni wanachama?
Mheshimiwa Naibu Spika, na kama Serikali inakubali, je, ni lini utaratibu huu utaanza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge ndio wanatunga sheria na nataka nimuombe sana Mheshimiwa Massare, kama jambo hili kwa umuhimu wake alipitishe katika Tume ya Utumishi wa Bunge lijadiliwe halafu sasa lifikishwe Serikalini kwa taratibu nyingine kufuatwa. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Kwa kuwa, matatizo yaliyoko Mpwapwa yanafanana sana na matatizo yaliyopo katika Jimbo langu la Itigi. Watu wanaenda kilometa nyingi sana kufuata maji hasa katika vijiji vya Rungwa, Kintanula, Kalangali, Mitundu, Chabutwa na Mabondeni;
Je, Serikali itasaidiaje kutatua tatizo hili katika Jimbo la Manyoni Magharibi;
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha program ya utekelezaji wa maendeleo ya maji, iliyodumu kuanzia mwaka 2006/2007 mpaka 2015. Sasa hivi tumeingia katika program ya pili. Huu ni mwendelezo wa kuhakikisha kwamba wananchi wa Tanzania wanapata huduma ya maji iliyo safi na bora, na kusogeza huduma ya maji iwe karibu ili akina mama wasitumie muda mrefu kupata maji.
Mheshimiwa Yahaya Masare nikuhakikishie kwamba tunaendelea na kama ambavyo umeona katika Bajeti ya mwaka huu tumehakikisha kwamba kila Halmashauri imetengewa fedha, tutaendelea kupeleka wataalam na tutasimamia tuhakikishe kwamba fedha hii inatumika. Sheria ndogo ndogo imepitishwa tumeweka value for money, tuhakikishe kwamba hela iliyopelekwa inafanya kazi nzuri na kuhakikisha wananchi wanapata maji.
Hivyo, nikuhakikishie kwamba tutatenga fedha kila mwaka, kuhakikisha kwamba wananchi wako wa maeneo hayo mpaka ya Rungwa wanapata maji.
MHE. QAMBALO W. QULWI: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi tena naomba niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la kupandishwa
hadhi kituo hiki limekwisha kujadilikwa katika mamlaka zilizopo pale wilayani na hata mkoani, kwa hiyo kama ni suala la mamlaka iliyobaki kushughulikia jambo hili ni mamlaka iliyoko juu ya hizo mbili. Je, ni lini sasa timu hiyo ya ukaguzi
itatumwa ili upandishwaji hadhi wa kituo hiki uweze kukamilika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa safari ya kuelekea kupata Hospitali ya Wilaya ya Karatu imeanza, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kutenga fedha katika bajeti ya kuanzia mwaka huu na kuendelea ili miundombinu michache iliyobakia iweze kukamilika? Ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nili-cross check mpaka jana kuangalia taarifa hizi status zikoje, lakini kwa
taarifa nilizozipata kule inaonekana mchakato ulikuwa haujakamilika vizuri. Kwa hiyo, naomba tushauriane tu, tutaangalia jinsi gani tutafanya ili wenzetu wa Halmashauri ili kama lile jambo limekwama halijafika katika mamlaka husika, hasa katika Wizara ya Afya waweze kufanya hivyo ili
Waziri wa Afya aweze kufanya maamuzi, nadhani jambo hilo litakuwa halina shida kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Wizara kuweza
kutenga fedha, ni kweli, na unakumbuka nilikuja pale jimboni kwako na nilitoa maelekezo kadhaa ambapo nilikua sijaridhika na kufika pale nilikuta watu wamefunikwa mablanket ambayo yametolewa store baada ya kusikia Naibu Waziri anakuja pale; kwa hiyo nimegundua changamoto
mbalimbali pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mchakato wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya tutaendelea kufanya hivyo. Naomba niwasihi hasa ndugu zetu wa Halmashauri, anzeni mpango huo sasa kuanzia bajeti zenu za Halmashauri ikifika kwetu sisi
Wizarani jambo letu kubwa liwe ni ku-compile vizuri na kufanya taratibu vizuri ili mchakato wa ujenzi wa hospitali ufanyike. Hoja yako ni hoja ya msingi na bahati nzuri eneo lile ni eneo la kitalii lazima tuwekeze vya kutosha tuwe na hospitali yenye maana pale hata mgeni akija aweze kupata
huduma nzuri.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, matatizo yaliyopo huko Masasi, yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika Mji wa Itigi wenye vijiji saba vya Kihanju, Songambele, Tambukareli, Majengo, Ziginari, Itigi Mjini na Mlowa, hakuna kabisa mtandao wa maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tulishaandika barua kwa Wizara kuomba wataalam wa Wizara waje watufanyie upembuzi yakinifu na Wizara ikatujibu kwamba haina wataalam kwa sasa na kwamba tushirikiane na Mkoa, na tukaandika barua ya kuomba kiasi kidogo tu, shilingi milioni 40 kwa ajili ya kutusaidia bajeti ili wataalam hawa wa Mkoa na wale wa Halmashauri waweze kufanya upembuzi yakinifu ili tuwapatie maji wananchi wa Itigi.
Je, ni lini sasa Serikali itaisaidia Halmashauri ya Itigi hizo hela kidogo tu ambazo zitafanya nasi tupate mchanganuo wa kujua ni nini tunahitaji ili Wizara iweze kutupa pesa za kujenga miundombinu ya maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa kuhusu fedha za uendeshaji au kufanyia usanifu wa kazi kwenye Halmashauri yake, katika hii bajeti ya shilingi bilioni 237 tuliyoitoa, kazi yake kubwa kwanza ni kujenga miundombinu kama ipo lakini pia fedha hizo zinatumika kwa usanifu, usimamizi na kadhalika; lakini pia na uendeshaji wa ofisi ni fedha hiyo hiyo. Kwa hiyo, katika bajeti ambayo Halmashauri yake ya Itigi imetengewa kwa mwaka 2017/2018 naomba watumie sehemu ya hiyo fedha ili waweze kufanya hiyo kazi ambayo Mheshimiwa Mbunge anaizungumzia. Kama wanaleta maombi, maana tutawapa hizo fedha, lakini tutakata kwenye allocation ambayo wametengewa kwa mwaka 2017/2018.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo yaliyopo huko Wilaya ya Ulyankulu yanafanana kabisa na matatizo yaliyoko katika Jimbo langu la Manyoni Magharibi. Jimbo la Manyoni Magharibi ni Tarafa ya Itigi ambayo ina upana mkubwa, eneo moja mpaka eneo lingine ni kilometa 219, ni jimbo kubwa kuliko majimbo mengi. Tumeshapeleka na kupitia taratibu zote hadi RCC kuiombea Itigi kuwa Wilaya lakini hadi leo Serikali imekuwa kimya. Je, Serikali inasema nini kuhusu jambo hili la Wilaya ya Itigi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli. Kwanza awali hata hili eneo la Itigi tulikuwa hatujapata Halmashauri kamili na ndiyo maana mchakato wa kwanza ulikuwa ni kupata Halmashauri. Suala hili najua Mheshimiwa Massare umelizungumza mara nyingi tangu uchaguliwe kuwa Mbunge. Naomba nikuhakikishie kwamba tutafanya verification katika ofisi yetu kuona hizi document ziko katika process gani. Kama hali haijawa sawa sawa tutatoa maelekezo kwa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kwamba ikamilishe zile taratibu ningine zote ambazo zitakuwa zimepungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nakumbuka kwamba Mheshimiwa Mbunge tulifika pale Itigi na kweli ukiangalia jiografia hata aliyekuwa Mkuu wa Wilaya wa kule ambaye sasa hivi ndiye Mkurugenzi wetu Mkuu wa TIC alikuwa anapata changamoto kubwa sana kui-manage ile Wilaya ya Manyoni. Kwa hiyo, Mheshimiwa Massare naomba nikuhakikishie kwamba mambo haya yote yakikamilika, Ofisi ya Rais (TAMISEMI) itakapojiridhisha, haitasita kufanya maamuzi kwa maslahi mapana ya eneo lako husika.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mji wa Itigi wenye Kata tatu za Majengo, Itigi Mjini na Tambukareli na vijiji saba vya Kihanju, Songambele, Tambukareli, Majengo, Ziginali, Itigi Mjini na Mlowa havina kabisa huduma ya maji toka nchi hii ipate uhuru na hata kabla ya wakati huo ikitawaliwa na mkoloni na kwa kuwa Halmashauri yetu inafanya juhudi na tumeandika barua kwa Wizara ya Maji kuomba Mhandisi wa Wizara hii aje atushauri namna gani ya kuweka miundombinu ya maji na kwa kuwa hadi leo hatujapata majibu.
Mheshimiwa Spika, nini kauli ya Serikali kwamba dhamira ya Serikali ikoje kuwasaidia wananchi wa Itigi na wenyewe wapate huduma hii ya maji kwa kuleta Mhandisi aweze kutushauri namna ya kuweka miundombinu ya maji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nikuhakikishie kwamba kutokana na utaratibu uliowekwa na Wizara ya Maji na Umwagiliaji Awamu ya Tano ya kuhakikisha kila Halmashauri inatengewa bajeti, tumeendelea kutenga bajeti kwa kila Halmashauri ili waweze kutekeleza miradi ya maji katika Halmashauri zao kwa sababu wapo karibu na wanaelewa matatizo yanayowazunguka.
Mheshimiwa Spika, nakiri ni kweli Mheshimiwa Mbunge uliniambia kwamba barua kuomba wataalam kutoka Wizara ya Maji inawezekana imeshakuja tayari lakini nitaifuatilia. Tatizo kubwa ambalo liko kwenye Halmashauri yako ni kukosa wataalam wenye weledi na tuliongea na kushauriana kwamba sasa ulete barua ili tuweze kukusaidia wataalam ama tukuchukulie wataalam kutoka Mamlaka ya Maji ya Singida au Makao Makuu ili wakasaidiane na wataalam wa Halmashauri yako kuhakikisha kwamba tunafanya usanifu wa haraka na ulio bora na utekelezaji uendelee. Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba tutakupatia wataalam Mheshimiwa Mbunge.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo tu la nyongeza. Matatizo yaliyoko huko Uyui yapo pia katika Jimbo la Manyoni Magharibi. Halmashauri ya Wilaya ya Itigi kuna mabwawa madogo yale malambo madogo ambayo yamepasuka na mengine yamefukiwa na maji likiwemo la Kaskasi stesheni, Mkalamani Itigi Majengo, pamoja na la Muhanga. Je, Serikali iko tayari na sisi kutusaidia fedha kidogo katika Mfuko huo ili na sisi kama halmashauri tuweze kurekebisha mabwawa haya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Mheshimiwa Mbunge ame-pose hilo swali hapa sasa hivi na hatujui kwamba mabwawa hayo assessment imefanyika na inahitaji gharama kiasi gani na hatujui kama Halmashauri imeweka kipaumbele gani katika hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kwamba kwa sababu suala la mabwawa hayo ni jambo la msingi; naomba tuwaagize wenzetu wa Halmashauri ya Itigi, kwamba sasa wataalam wa maji waweze kwenda katika eneo hilo wafanye tathmini ya mabwawa hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni kwa sababu mabwawa haya yakijengwa yataisaidia jamiii katika eneo letu; tujue kwamba kama Serikali tunajipanga vipi kurekebisha mabwawa hayo mara baada ya kupata bajeti halisi na tuweze kuliweka katika mipango ya maendeleo ya bajeti katika Halmashauri ya Itigi.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami niulize swali dogo la nyongeza. Kuna ahadi nyingi tuliwaahidi wananchi wetu wakati tukiomba kura ikiwemo Mheshimiwa Rais kuahidi wananchi wa Itigi kuwajengea barabara ya lami inayoingia katika Mji wa Itigi kilometa nane. Je, ni lini sasa Wizara hii itatekeleza ahadi hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuna ahadi nyingi ambazo zilitolewa wakati wa kampeni na yeye mwenyewe Mheshimiwa Mbunge alitoa ahadi zake na Mheshimiwa Rais alitoa ahadi katika maeneo ambayo alienda kuomba kura. Katika kipindi ambacho aliomba na kutoa ahari ahadi utekelezaji wake ni ndani ya miaka mitano. Upo utaratibu ambao umewekwa mahsusi ili kuhakikisha kwamba ahadi zote ambazo zilitolewa na Mheshimiwa Rais zitaenda kutekelezwa. Naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, Ilani ya CCM inatekelezwa ndani ya miaka mitano na sisi ni waungwana tukiahidi huwa tunatekeleza.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, naomba nimuulize swali dogo tu la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, matatizo yaliyopo huko Mkoani Kigoma yapo pia katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, kuna uhaba mkubwa wa watumishi, vituo vya afya na zahanati wakati mwingine vina mtumishi mmoja. Je, Serikali iko tayari sasa baada ya kuajiri kuleta watumishi katika Halmashauri ya Itigi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, katika wale watumishi watakaokwenda kuajiriwa hakika tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba sehemu ambayo kuna upungufu mkubwa ikiwa ni pamoja na jimbo lake tunawapeleka.
Mheshimiwa Spika, wakati Mheshimiwa Susan anaongea, aliongelea kuhusiana na baadhi ya vituo kufungwa na sisi Wabunge ni mashuhuda Mheshimiwa Waziri wa Utawala Bora alitoa tamko tukiwa humu ndani ya Bunge kwamba kama kuna eneo lolote Mbunge anajua kwamba kituo kimefungwa kwa sababu ya kukosekana watu wa kutoa huduma pale apeleke maombi ili isitokee hata sehemu moja eti tumefunga kituo kwa sababu hakuna mtu wa kutoa huduma ya afya kwa eneo husika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niendelee kuwasihi Waheshimiwa Wabunge kama kuna maeneo ambayo tumejenga na Mheshimiwa Bobali alisema jana, ni fursa hii tuhakikishe kwamba hakuna kituo cha afya hata kimoja au zahanati yetu hata moja ambayo inajengwa ikakamilika ikaacha kutumika eti kwa sababu hakuna watu wa kutoa huduma.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo yaliyopo huko kwenye jimbo Mheshimiwa Mgimwa yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika jimbo langu ambapo Serikali imeonesha nia njema ya kujenga skimu ya umwagiliaji katika Bwawa la Itagata. Sasa kwa kuwa bwawa hili lilikuwa lilishaanza kuvuja na ile pesa ya kujenga skimu Serikali; maana ya Wizara ilituambia tutoe ili tuwape wale wakandarasi wa umwagiliaji kutoka Wizarani wa kuziba mabwawa; sisi pesa tumeshalipa.
Je, Serikali sasa iko tayari kurudisha ile pesa haraka ili na sisi certificate iliyioko kwenye halmashauri tuweze kumlipa mkandarasi katika Skimu ya Umwagiliaji ya Itagata? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, kwanza nimpongeze kwa jinsi anavyofuatilia shughuli za ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya umwagiliaji na kweli Bwawa la Itagata limekamilika. Naomba Mheshimiwa Mbunge baada ya kikao hiki leo tukutane ili tuweze kuangalia jinsi ya kukupa hiyo fedha muende mkakamilishe miradi mingine inayoendelea.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambaye ameonesha dhamira ya kweli ya Serikali ya Awamu ya Tano kuwatua ndoo kichwani akinamama, nina maswali madogo mawili.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; wananchi wa Itigi kwa sasa wananunua maji ndoo moja Sh.1,000 hususani akinamama. Je, sasa Serikali, Mheshimiwa Waziri anaweza akawaambia nini wananchi wa Itigi ambao wanamsikiliza na kumwona katika TV muda huu, kwamba mradi huu utatangazwa lini, kwa kuwa kila kitu kimeshakamilika na wananchi wa Itigi tunataka kumsikia leo anasema nini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, yuko tayari sasa kwenda kuongea na wananchi wa Itigi kwamba mradi huu tunauanzisha lini katika kipindi cha mwezi huu?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Kama majibu ya msingi ambavyo yameelezwa na Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba utekelezaji wa miradi unakwenda katika awamu tatu na awamu zote sasa zimekamilika, tunakwenda kwenye utekelezaji. Pia tuna utaratibu ambao tunachimba visima na kufunga pampu za mkono wakati tunasubiri mradi mkubwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama shida iko namna hiyo watu wananunua ndoo moja Sh.1,000 namwomba Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane, kwa sababu bajeti yake ipo, tutachimba visima vya haraka na kufunga pampu ili wananchi waachane na hilo la kununua maji ndoo Sh.1,000.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili; nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba niko tayari kuongozana naye kwenda Itigi tukaongee na wananchi huko baada ya bajeti yangu. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri yenye kutia moyo wananchi wa Jimbo la Manyoni Magharibi, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Kalangali kimepitiwa na umeme ukaenda kutua kijiji cha pili cha Mkoa wa Tabora, Kijiji cha Kipili. Wananchi wa Kalangali wanasononeka sana na kupitwa na umeme huu. Je, sasa Wizara hii iko tayari kuingiza kijiji hiki katika mzunguko huu wa kwanza, Awamu ya Tatu ya REA?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Waziri wa Wizara hii alipokuwa Naibu Waziri alikuja Itigi na alifanya mkutano mzuri sana na wananchi. Sasa yuko tayari kwenda kufanya mkutano na wananchi wa Rungwa kuwahakikishia kwamba Awamu ya Tatu mzunguko wa pili umeme utaenda hadi Rungwa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza lilihusu Kijiji cha Kalangali ambapo kwa maelezo yake kijiji hiki kimepitiwa na miundombinu ya umeme ambayo imeelekea Mkoa wa Tabora na wananchi wa kijiji hiki hawajapa umeme huo.
Napenda nikubali maelezo ya Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa kuna maelekezo ya Serikali maeneo yote yaliyopitiwa na miundombinu ya umeme mkubwa na ambayo hayajapata umeme yapatiwe. Kwa kuwa kazi katika kijiji hiki ni kushusha transfoma na kuwaunganisha wateja, napenda nimthibitishie nitatoa maelekezo kwa mkandarasi na REAwafanyie kazi kijiji hiki na kipatiwe umeme katika awamu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ombi la Mheshimiwa Waziri kufanya ziara katika Wilaya ya Itigi, Kijiji cha Rungwa, naomba nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ombi hilo limekubaliwa na ziara itafanyika kama ilivyo utaratibu wetu kutembelea maeneo mbalimbali. Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Waziri, Serikali imedhamiria kufanya kazi nzuri sana hasa katika Jimbo langu, imejenga bwawa na inajenga scheme ya umwagiliaji katika Bwawa la Ikagata, lakini kuna fedha kiasi cha shilingi milioni 180 na zaidi za scheme ya umwagiliaji ziliazimwa kwa ajili ya kuziba bwawa hili ambalo lilikuwa linavuja.
Je, ni lini Serikali itarudisha fedha katika mradi ule ili Mkandarasi aweze kulipwa, amalizie kazi hii ambayo dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano na Wizara yenu iko na nia njema kwa wananchi wa Jimbo langu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda kwa ufupi tu nimwombe Mheshimiwa Mbunge baada ya Bunge saa saba mchana tuweze kukutana ili niweze kupata maelezo vizuri zaidi ili nami niweze kuhakikisha kwamba nalisimamia hili jambo liweze kukamilika kwa wakati. Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo yaliyoko huko Mbalizi yanafanana kabisa na yaliyoko katika Halmashauri ya Itigi ambapo shamba la Tanganyika Packers eka 45,000 ambalo lipo pale kwa miaka mingi limetelekezwa na Serikali imekuwa na kauli tata juu ya shamba hili wakati tukiliomba lirudishwe kwa wananchi au kuanzishwe mradi mwingine, kwamba litarudishwa, baadae Serikali inasema italichukua. Sasa nini kauli sahihi ya Serikali kwa shamba la Tanganyika Packers ambalo limeachwa na limetelekezwa kwa muda mrefu katika Halmashauri ya Itigi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nisisitize kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, kwamba maeneo kama lile la Tanganyika Packers Mbeya na maeneo mengine ya aina hiyo Serikali haina nia ya kubadilisha matumizi ya msingi yaliyokusudiwa kwa ajili ya kuendeleza maeneo hayo katika sekta ya viwanda.
Kwa hiyo, maeneo hayo ni lazima yaendelee kutengwa na kutunzwa kwa ajili ya maendeleo ya sekta ya viwanda. Kwa hiyo, maeneo hayo ni ya uwekezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ndugu yangu Mheshimiwa Yahaya naomba tushirikiane na Halmashauri ya Wilaya ya Itigi kuhakikisha kwamba eneo hilo linaendelea kulindwa na miongoni mwa maeneo ambayo ni ya halmashauri ya wilaya ambayo mnatakiwa myalinde kikamilifu kwa ajili ya sekta ya viwanda na uwekezaji kwa ujumla ni eneo hilo, kwa hiyo, naomba sana tushirikiane katika hilo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize maswali madogo mawili ya nyongeza pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, tofauti ya majibu haya kwamba kuna asilimia 60 na 70 na kuna asilimia 30, wadau hawa wanapita katika njia moja na wanachukua vibali sehemu moja na wakaguzi wa vizuia, wanakagua bila kujua huyu katoka kwenye mashine ya kisasa au mashine ya kizamani. Kwa mpango huo, inamaanisha kwamba kuna mwanya mkubwa sana wa rushwa, kuna mtu atatoka na asilimia 60 na mwingine asilimia 30. Je, sasa Serikali inakuja na mkakati gani uliobora kabisa kuepusha watumishi ambao sio waaminifu kufanya kazi ambayo imenyooka kwa dhamira iliyopo sasa ya Awamu hii ya Tano kwamba tunataka wananchi watendewe haki?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini sasa Serikali itaona njia bora zaidi ya kusaidia wadau hawa wajasiriamali, wale ambao wana mashine za kizamani waweze kuwezeshwa na kupata mashine hizi za kisasa ili kuondoa mkanganyiko huu ambao unasababisha mwanya mkubwa wa rushwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Omary Massare, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza kwa sababu yeye ni mdau mkubwa sana wa mazao yatokanayo na misitu na kwa kweli amekuwa akifanya kazi nzuri sana na amekuwa mshauri mzuri sana katika masuaa mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mkakati ambao Wizara imeweka, Serikali kwa kweli imeweka mkakati mkubwa wa kuhakikisha tunawahamasisha wananchi wote wahakikishe wanapata teknolojia za kisasa, mashine ambazo ni bora kwa sababu hizi mashine zingine kwa kweli zinafanya upotevu mkubwa sana na hasara ni kubwa. Katika suala hilo ndiyo maana tumeweka mkazo kwamba wale wote ambao wanakuwa na zile mashine ambazo zinapoteza sana kwa kweli hawaruhusiwi. Pale ambapo itabainika kwamba baadhi ya watumishi wetu katika maeneo kadhaa wanaruhusu hizo mashine zitumike kwa rushwa basi tunaomba mtusaidie kututajia majina ili hatua kali ziweze kuchukuliwa kwa watumishi wa aina hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu namna ya kuwasaidia Watanzania hawa, kwa kweli ziko njia nyingi za kuwasaidia Watanzania lakini nitumie nafasi hii kuwahamasisha kwamba wajaribu kutafuta mikopo ya aina mbalimbali. Kuna aina nyingi za mikopo sasa hivi, kuna ile mikopo inayotolewa na Halmashauri, kuna mifuko mingi inatoa mikopo basi wachukue mikopo ili waweze kupata mashine ambazo ni bora ambazo zitawafanya wapate mazao mengi zaidi kuliko mashine ambazo ziko hivi sasa. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali. Kwa kuwa matatizo yaliyopo huko Ileje yanafanana kabisa na yaliyopo katika Jimbo la Manyoni Magharibi, Halmashauri ya Itigi. Mvua zinazonyesha maji yake yanapotea na ni dhamira ya Serikali ya kuwatua akinamama ndoo kichwani. Je, sasa Serikali iko tayari basi kujenga angalau bwawa moja tu katika mwaka ujao wa fedha katika Halmashauri ya Itigi?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iko tayari na katika huu mpango kabambe uliokamilika tumeainisha kwamba maeneo mengi tutajenga mabwawa tuweze kuvuna maji ili wananchi wasipate shida ya maji ya kunywa, pia umwagiliaji hata mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze kwamba Bwawa la Itagata kwenye jimbo lake tumekamilisha kujenga. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami niulize maswali mawili madogo ya nyongeza. Nishukuru majibu mazuri ya Serikali yenye dhamira ya kuona sasa wananchi wanapatiwa huduma ambazo zinakidhi. Kwa kuwa, Serikali imeona busara hii na kutoa ruzuku kwa Hospitali hii ya Mtakatifu Gaspar lakini gharama zake ni juu sana na sasa Serikali imeona ni vizuri ianze kujenga hospitali ya Wilaya katika Halmashauri ya Itigi.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, katika kutekeleza Ilani ya CCM tunazo changamoto ambapo Serikali imetuletea pesa za kujenga kituo cha afya lakini gari la Kituo cha Afya ni dogo, wakati huo huo kuna Kituo cha Afya cha Mitundu ambacho ni kilometa zaidi ya 100 kutoka kituo cha afya kwenda Hospitali ya Wilaya ya Manyoni iliyopo sasa. Je, Serikali iko tayari kutoa gari la wagonjwa kusaidia kituo kile ili kupunguza gharama za wananchi wetu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kituo cha Afya Rungwa ambacho kiko zaidi ya kilometa 200 kimeshakamilika. Je, Serikali iko tayari sasa kukifungua kituo hiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza anaongelea juu ya suala zima la upungufu wa magari kwa maana ya ambulance kwa ajili ya kituo cha afya alichokitaja ambacho anasema kipo karibia kilometa 100. Ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba inapunguza adha kwa wananchi hasa wagonjwa, ndiyo maana gari zinapopatikana zimekuwa zikitolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pale magari yatakapokuwa yamepatikana tutaanza kupeleka maeneo yenye uhitaji mkubwa hasa yale ambayo yanahitaji kutembea umbali mrefu. Naamini na hicho alichosema Mheshimiwa Mbunge nasi pia tutazingatia.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili anaulizia juu ya utayari wa Serikali kufungua kituo cha afya kilichokamilika. Essence ya kujenga kituo cha afya ni ili kiweze kutoa huduma kwa wananchi. Serikali kama mambo yote yamekamilika tuko tayari kuzindua kituo hicho cha afya. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati, ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, dhamira ya wananchi lakini dhamira ya Serikali ya kupeleka umeme vijijini kwa maana ya REA utekelezaji wake umekuwa mdogo na unasuasua sana. Katika Jimbo langu kuna vijiji vya Kashangu, Jeje, Idodyandole, Ipangamasasi, Mbugani, Agondi, Mabondeni, Kitopeni, Ipande, Muhanga, Damwelu, Kitalaka, Kaskazi Station, Kintanula na Rungwa havina umeme. Je, nini kauli ya Serikali kwa wananchi wa vijiji hivi wategemee lini kupelekewa umeme? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa umeme wa Mkoa wa Singida unakwenda hadi katika Wilaya ya Manyoni pamoja na Itigi lakini hatuna substation ipo station moja tu kubwa kule Singida. Je, Serikali iko tayari sasa kuweka substation Itigi kwa ajili ya kuboresha miundombinu hii ya umeme? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Massare, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi. Kwanza, nimpe pole kwa ajili ambayo aliipata na namwombea kwa Mwenyezi Mungu ampe afya njema. Pamoja na changamoto hiyo ya afya Mheshimiwa Massare ameendelea kulitumikia Jimbo lake hususani katika sekta ya nishati.
Mheshimiwa Naibu Spika, maswali yake mawili ya nyongeza, la kwanza lilijielekeza katika utekelezaji wa mradi huu wa REA III. Katika Wilaya ya Manyoni REA III, mzunguko wa kwanza kuna vijiji 30 na Jimbo lake lina vijiji 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge mkandarasi yupo anaendele na kazi katika maeneo ya Manyoni Mashariki katika Vijiji vya Majengo, Selia, lakini kwa kuwa, yeye Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo lake la Manyoni Magharibi ameuliza utekelezaji, nataka nimtaarifu hata asubuhi hii nimeongea na mkandarasi, ameshaanza kupeleka vifaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka pia, nilitaarifu Bunge lako Tukufu kutokana na utatuzi wa changamoto ambazo zilikuwa zinaukabili mradi. Mradi vizuri, sasa hivi unaendelea vizuri kwa sababu, mpaka sasa tunavyozungumza mpaka Januari vijiji takribani 5766 vimeshapata umeme kutokana na utekelezaji wa mradi huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge ameulizia juu ya ujenzi wa substation katika eneo la Itigi Manyoni:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimtaarifu Mheshimiwa Mbunge kwamba, Singida tuna substation. Kutokana na mipango ya Serikali na ujenzi ulioanza wa line ya Kv 400 kutoka Singida mpaka Namanga, Serikali ina mpango wa ku-upgrade Kituo cha Singida. Kwa hiyo, nataka nimtaarifu kwamba, kutokana na matengenezo yatakayoendelea tutakipandisha hadhi Kituo cha Singida, ili kuhimili umeme mkubwa utakaosafirishwa mpaka Namanga, hivyo ni wazi kwamba, Mkoa mzima wa Singida kuhusu changamoto ya labda pengine usafirishaji wa umeme haitakuwpo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba tu Mheshimiwa Mbunge aendelee tu kuiunga mkono Serikali, mipango ya kupandisha hadhi substation ya Singida inaendelea. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niulize swali la nyongeza. Dhamira njema ya Serikali imeleta mradi mkubwa wa kusambaza maji katika Mji wa Itigi. Wakandarasi walipewa ruhusa ya kuanza mradi ule bila pesa. Je, Serikali iko tayari sasa kuwalipa certificate zao ambazo tayari wamesha-raise katika Wilaya hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya, lakini tunatambua maeneo ya Itigi ni moja ya maeneo yenye changamoto kubwa sana ya maji. Nasi kama Wizara ya Maji tukaona haja sasa ya kuutekeleza mradi ili wananchi waweze kupata maji. Sisi kama Wizara hatutakuwa kikwazo kwa Wakandarasi wenye uwezo na wenye sifa na wanaotekeleza kazi zao vizuri kuwalipa kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutamlipa certificate yake ili Wakandarasi waendelee na kazi.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza. Matatizo yaliyoko huko kwenye Shamba la Efatha Mkoa wa Rukwa yanafanana kabisa na matatizo yaliyoko katika Halmashauri ya Itigi shamba lililokuwa linamilikiwa na shirika ambalo limekufa la Tanganyika Packers. Serikali haitoi tamko la moja kwa moja, liko chini ya Msajili wa Hazina, lakini hakuna mwekezaji aliyejitokeza hadi leo hii.
Je, Serikali imekubali sasa kulirudisha shamba hili kwa wananchi kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Itigi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli suala analolizungumzia Mheshimiwa Massare ni la muda mrefu, lakini naomba tu nimpe uhakika kwamba masuala yote ambayo yanasimamiwa na Msajili wa Hazina alishaanza kuyapitia na kuweza kuona mashamba yale au uwekezaji ambao ulikuwepo na ukakwama uko chini ya Hazina sasa hivi, anapitia shamba moja baada ya lingine na akishakamilisha basi anaweza kutoa nini kitawezakufanyika. Hatuwezi kusema sasa hivi kwamba tunalirudisha kwa wananchi wakati Msajili wa Hazina bado anafanyia kazi mashamba hayo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii nami niulize swali la wanariadha ambao nao Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa ambayo ilikuwa inafanya vizuri sana katika riadha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jimbo ninalotoka mimi kulikuwa na wanariadha miaka ya nyuma, lakini hata mimi mwenyewe nilikuwa mwanariadha. Kwa kuwa ili wanariadha na vijana ambao wapo shuleni waweze kupata hamasa ya michezo ni pamoja na vyombo vya habari ikiwemo TBC kusikika katika maeneo mbalimbali. Je, ni lini sasa Serikali itafanya TBC isikike katika eneo la Itigi ambapo haisikiki kabisa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie fursa hii kuweza kumpongeza Mheshimiwa Massare kwa sababu swali lake la usikivu wa TBC amekuwa akiuliza karibu kila Bunge, lakini niseme kwamba ni suala la kibajeti na kwa kuwa hili ni Bunge la Bajeti kwa mwaka huu tutaangalia namna gani ambavyo tutaboresha usikivu katika eneo lake la Itigi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali na tumeona kweli Serikali sasa imeonesha nia ya kupunguza kadhia hii ya watumishi wa kada ya afya. Nina maswali madogo mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, dhamira ya Serikali, lakini na wananchi katika Jimbo la Manyoni Magharibi, Halmashauri ya Itigi ni kujikwamua, wameanza kutumia nguvu zao katika kujenga zahanati na vituo vya afya katika vijiji vyao, lakini nguvu zao zinaonekana kuisha. Je, Serikali iko tayari sasa kuwasaidia wananchi wa vijiji ambao wameanza kujenga zahanati kwa nguvu zao?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, katika swali ambalo niliuliza mwaka jana kipindi kama hiki majibu ya Serikali ilikuwa yameonesha kwamba na Hansard iko hapa ninayo kwamba, Serikali ilikuwa imetenga milioni 600 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, lakini hadi tunapozungumza leo hii bajeti nyingine ya Wizara ya TAMISEMI ilishasomwa, hospitali hii bado hatujaletewa pesa. Je, Serikali iko tayari sasa basi kupeleka hizi pesa ambazo iliahidi na wananchi walisikia kwamba zitapelekwa katika Halmashauri ya Itigi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na nimpe pole sana kwamba, alipata ajali mbaya hivi karibuni, lakini pamoja na kwamba, alikuwa na machungu ya maumivu aliweza kuwakumbuka wananchi wake wa Manyoni na akaanza kuandika swali hili ambalo nalijibu hapa leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nijibu maswali ya nyongeza mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba, sisi Serikali tunahimiza wananchi na wenyewe Waheshimiwa Wabunge wamekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha wananchi kushiriki kujenga vituo vya afya na zahanati na kuna maboma mengi.
Naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, jitihada na nia ya Serikali iko palepale, kadri ambavyo uwezo utapatikana tutapeleka fedha za maboma, lakini pia kupeleka wataalam na vifaa tiba ili kuweza kuboresha huduma za wananchi wetu katika maeneo yao na hii itakuwa ni kwa nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, anauliza habari za hospitali yake ya Itigi; naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutaendelea kuliangalia hili kulingana na uwezo wa Serikali. Kama mwaka huu bajeti hii haikupelekwa katika eneo lake la Hospitali ya Itigi kama alivyotaja Mheshimiwa Mbunge, basi tunalichukua kulifanyia kazi ili wakati ujao aweze kupata fedha na kuweza kupata huduma na kuboresha hospitali yake ya wilaya.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante, pamoja na majibu ya Serikali ambayo kidogo yana ukakasi, nina maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, barabara hii ya Mkiwa - Rungwa hadi Makongolosi imekuwa ikitengewa pesa kwa muda mrefu toka nimeingia katika Bunge hili na hata Mheshimiwa Rais aliwahi kusimama katika mkutano wa hadhara akiwaambia wananchi wa Itigi kwamba sasa inajengwa na mkandarasi alipatikana lakini hatujui kilichotokea.
Sasa je, Serikali hususani Wizara hii ambayo inayohusika na barabara hii ambayo inahusika na TANROADS, Wizara ya Ujenzi, wako tayari sasa kusema mbele ya Bunge lako tukufu ni lini wataanza kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami kilometa 56.9 ambazo zimetajwa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, barabara hii inapita katikati ya Mji wa Itigi, mji wa kibiashara na wananchi wanajishughulisha katika kuhangaika kutafuta maisha yao vizuri, barabara hii sasa imegeuka mto inapitisha maji. Je, ni lini Serikali itafanya haraka kukarabati barabara hii kwa dharura?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, tumemsikia Mheshimiwa Mbunge na kama nilivyosema kwenye jibu la msingi ni kwamba tumeshafanya usanifu na tutawasiliana na wenzetu wa TANROADS tuangalie namna bora ya haraka zaidi kuweza kurekebisha hali hii katika Jimbo lake. Lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama sasa anavyozungumza Mji wa Itigi unapitisha maji; naomba nimuagize Meneja wa TANROADS Mkoa wa Singida na Wilaya hii afanye tathmini ili alete maombi tuone hatua ya haraka zaidi ya kuweza kurekebisha hali hii ili maji yasiweze kupita katika eneo hili na huduma ziweze kuendelea. Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Matatizo yaliyoko huko Tumbatu yako pia katika Jimbo la Manyoni Magharibi, maeneo ya Kintanula, Kalangali, Mnazi Mmoja, Tulieni, Mbugani na baadhi ya maeneo ya Jimbo langu hayana mawasiliano mazuri ikiwemo Itagata na Lulanga. Je, Mheshimiwa Waziri anawahakikishiaje wananchi hao wa Jimbo la Manyoni Magharibi mawasiliano yatapatikana hasa katika Kijiji cha Kintanula lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahaya Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Massare na Waheshimiwa Wabunge wengine wote ambao wana changamoto za mawasiliano kwenye majimbo yao kwamba kuna tenda ambazo tulitangaza, tenda kwa ajili ya kata 521 nchi nzima ambazo zitategemewa kuhudumia vijiji 122 na hizo tender zilifungua tarehe 3 Oktoba na sasa hivi tuko kwenye taratibu za kuwa wa-award tender kutoka kwa watoa huduma mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Massare na Waheshimiwa Wabunge wengine wote ambao wana changamoto za mawasiliano kwenye majimbo yao kwamba kuna tenda ambazo tulitangaza, tenda kwa ajili ya kata 521 nchi nzima ambazo zitategemewa kuhudumia Vijiji 122 na hizo tenda zilifungua tarehe 3 mwezi wa 10 na sasa hivi tuko kwenye taratibu za kuwa wa-award tenda kutoka kwa watoa huduma mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Massare na Waheshimiwa Wabunge wengine tunaweza kukaonana wakati wowote mezani kwangu pale nikawaonyesha Vijiji ambavyo tayari vimeshakuwa awarded, vile ambavyo bado havijawa awarded kwa ajili ya kwenda kuwekewa huduma za mawasiliano tunategemea mwezi wa kwanza kutakuwa na awamu nyingine kwa ajili ya kumalizia Vijiji vichache vitakavyokuwa vimebakia.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa fursa hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, majibu haya Serikali ni mazuri na yana dhamira njema ya kuijenga nchi hii ifikie katika malengo mazuri. Lakini kuna majibu ya swali kama hili ambao niliuliza mwaka 2016 kama 2016/2017 na bahati nzuri kwenye hansard ninalo lilipata majibu ambao yalionyesha matumaini kwamba kuna siku Halmashauri ya Itigi inaweza kuwa Wilaya. Lakini kwa kuwa Halmashauri ya Itigi ni engeo ambao lina ukubwa wa Squire kilometa 17,000 ni sawa sawa baadhi ya mikoa ambao ipo katika nchi hii na ni tarafa moja.
Je, sasa Serikali ipo tayari kuwa tuachane na suala la kuongeza Wilaya tuondoe walau tuongeze tarafa ambazo hazitakuwa na ghamara kubwa za uendeshaji ikiwemo ofisi ya Wakuu na nini au madiwani?
La pili, katika eneo langu kuna kijiji kinaitwa Mitungu ambacho nacho kina eneo kubwa ukubwa wa eneo ni mkubwa sana lakini wananchi ni wengi. Kutoka katikati ya kijiji mpaka pembeni ni kilometa 40 upande mmoja na upande wa pili hivyo hivyo.
Je, Serikali iko tayari kufanya kazi nzuri kama nazofanya Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani ambaye anatamka jambo na linafanyiwa kazi na haraka unapata matokeo. Je, kwenye kijiji hiki kimoja tu ambacho tunataka kugawanywa angalu kupata vijiji viwili kina watu zaidi elfu 30 Serikali ipo tayari angalu kusaidia na kunipa uwezekano wa mwaka 2020 kuona wepesi katika eneo hili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Mheshimiwa Mbunge tunakusudia na kutengependa apate wepesi mwaka 2020 na kwa kazi nzuri anayoifanya kuwasemea wananchi wake wa Manyoni tunaamini kwamba wataendelea kumwani na kumunga mkono.
Mheshimiwa Naibu Spika, ameuliza maswali mawili ya nyongeza kwa uchungu na akionyesha ukubwa wa nchi ulivyo na ameonyesha namna ambavyo alishapata majibu ya matumaini hapa Serikali inafanya tathimini kutoka mwaka hadi mwaka. Baada ya kufanya tathimini ya kuangalia maeneo ambayo bado yanazidi kuimarishwa kwa maana ya Ofisi na vitendea kazi vingine miradi ya maendeleo iliyopo na uwezo wa Serikali ndio maana tukaja na jibu la namna hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo amezungumza hapa kwanza maeneo haya yanafanya uchanguzi kwa mfano vijiji vya mwaka huu tayari timu yetu imeshatembelea maeneo mbalimbali kuangalia maeneo ya migoro mahali ambapo ilikubadilisha GN wameshafanya kazi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tulipokee hili tuendelee kushauliana tuone kama haitaingiza gharama kubwa Serikalini. Kama ambavyo tunajua tukiongeza maeneo itakauwa gharama zaidi tutaona namna ambavyo kama kuna wepesi wa kuifanya ile kazi ili hawa wananchi waweze kupata huduma karibu. Lakini nawaomba waendelee kuwahimiza nia ya Serikali ni njema sana na Wabunge watakubaliana na sisi kwamba kwa kweli kama unaanzisha maeneo mapya na kati ya hapa kuna watu ambao wadai ofisi za mikoa kuna ofisi za wilaya, Ofisi za Wabunge, Ofisi za kata vijiji na mitaa kwa kweli ukiangalia huo ukubwa na wingi wa shughuli hiyo unahitaji tutulie kuimalisha maeneo ambayo kweli tunayo sasa ili tuweze kuongeza baadaye ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Niishukuru Serikali kwa majibu mazuri, lakini pamoja na majibu haya mazuri sana ya Serikali nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Itigi ni eneo ambalo lina mbuga na ardhi ni nzuri na kama ilivyoonesha kwenye historia kwamba Serikali imekiri kweli kwamba, maji huwa yanajaa.
Sasa je, Serikali iko tayari sasa pamoja na kutuma Tume ya Umwagiliaji wataalam hawa waangalie namna iliyo bora ya kuyavuna maji haya ili yaje kuwa msaada wakati wa kiangazi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Wananchi wa Itigi na maeneo jirani wanalima sana zao la dengu na kwa kuwa Bodi ya Mazao Mchanganyiko imekuwa haizingatii sana mazao haya ambayo yanapatikana maeneo ambayo ni machache kama Shinyanga na kwetu Itigi na maeneo ya Tabora suala la dengu.
Je, sasa Serikali iko tayari kufanya juhudi za makusudi kusaidia wananchi hawa wanaolima dengu kupata masoko ya uhakika badala ya kupunjwa na walanguzi ambao huwa wanakuja kila mwaka na bei inakwenda chini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza anataka kujua kwamba, Serikali kama iko tayari kutuma wataalam wake kwa ajili ya kwenda kufanya tathmini ya kina kule.
Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ipo tayari na ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimesema kwamba kupitia swali lako hili, natoa maelekezo kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Kanda ya Dodoma kwenda haraka iwezekanavyo katika hii mbuga ya Itigi ili kwenda kufanya tathmini ya kina ili tuone namna gani bora ya kuweza kuvuna maji haya ya mvua yanayosababisha hasara kubwa kwenye hili bonde kwenye kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anataka kujua Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko. Ni kweli Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kwa mujibu wa sheria ambayo tumeikabidhi kusimamia mazao zaidi ya 35 ikiwemo zao la alizeti na kwamba Serikali tupo tayari kama ulivyoona sasa hivi tupo katika majadiliano ya kina na wenzetu wa India na Vietnam ambao ni wanunuzi wakubwa kwa ajili ya kuingia mkataba maalum wa kuuza mazao haya ya mikundekunde kwa sababu wao ndiyo walaji wakubwa ili tusije kuhangaika na soko huko baadae.
Mheshimiwa Spika, tunafahamu kwa sababu wenzetu wameweka ban kwenye suala hili la kuingiza kiasi cha dengu na mazao haya ya mikundekunde, sasa tunataka tuingie makubaliano hayo ili tutengeneze soko la uhakika na la bei nzuri kwa wakulima wetu.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niulize swali dogo la nyongeza. Katika Jimbo la Manyoni Magharibi ambako mimi natoka kwa maana ya Halmashauri ya Itigi kuna vijiji 15 na vitongoji kadhaa bado havijafikiwa umeme. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anasemaje juu ya vijiji vyangu ni lini vitapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Massare, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Singida ni kati ya mikoa ambayo imejengewa kituo kikubwa kabisa cha kupoza umeme na kipo kingine kinachoongezwa kikubwa pia kwa ajili ya kupitisha umeme kutoka Iringa kupita Singida kwenda Arusha kwa ajili ya kwenda nje ya nchi ambapo ni Arusha kwenda Kenya.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Singida ni mkoa ambao hauna matatizo ya umeme na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo machache ambayo kwake bado hayajapata umeme, yataendelea kupelekewa umeme kwa kupitia taasisi yetu ya TANESCO, lakini kwa kupitia awamu mbalimbali ikiwemo REA awamu ya tatu, mzunguko wa pili, ambao kwa sasa unaendelea kwa sababu umeme tunao wa kutosha na tunao uwezo wa kupeleka lakini ni kwa awamu kwa awamu kama nilivyotangulia kusema.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wakati anajibu swali la msingi nilitaka tu nimkumbushe kwamba nimeuliza swali hili mwaka juzi nikiwa humu ndani ya Bunge na Serikali ilijibu kwamba itafanyia kazi, sasa amekuja na majibu mengine kwamba ataangalia.
Je, sasa yuko tayari kuingiza Halmashauri ya Itigi ambayo ina wafugaji wengi ambao ni wapya na wameingia maeneo ambayo tunayo kwa sababu ya fursa ya malisho kuingiza kwenye suala zima la malambo ili wapate sehemu ya kunyweshea mifugo yao?
Lakini lini Mheshimiwa Waziri upo tayari kuambatana na mimi kwenda kujionea uhalisia wa wafugaji walivyo wengi katika Jimbo hili la Manyoni Magharibi, kwa maana ya Halmashauri ya Itigi angalau katika mnada mmoja tu wa Mitundu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Massare, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, la kwanza, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa namna ambavyo Wilaya ya Manyoni na Halmashauri ya Itigi inavyotunza wafugaji walioko kwenye Wilaya hiyo, tunalazimika sisi, kama Wizara kujali sasa kwenye bajeti ijayo na kutekeleza suala la kujenga lambo kwenye Wilaya yake ya Halmashauri ya Itigi. (Makofi)
Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba lambo ambalo tumesema tutaangalia kwenye bajeti, kimsingi tutachimba lambo kwenye halmashauri yako kwa sababu, tunaelewa una wafugaji wengi na mifugo ni wengi kwenye wilaya yako.
Mheshimiwa Naibu Spika, juu ya suala lake la pili la mimi kwenda kwenye halmashauri yake na jimbo lake, ili kwenda kujionea hali halisi, niko tayari nitafanya hivyo ili tuweze kuona hali halisi na kwa pamoja tuweze kutathmini na kuona ni kitu gai tunaweza kuwasaidia wafugaji wetu walioko Wilaya ya Manyoni na Halmashauri ya Itigi. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Spika, matatizo yaliyopo kule Liwale, Nachingwea yanafanana kabisa na yaliyopo katika Jimbo la Manyoni Magharibi Mkoa wa Singida kuunganishwa na Mkoa wa Mbeya kwa barabara inayotoka Mkiwa, Itigi hadi Rungwa.
Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Massare Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana nami kwamba katika bajeti tuliyopitisha barabara hii ya kuanzia Mkiwa kwenda Rungwa, Lupa hadi Makongorosi, imetengewa bajeti kuanza kwa kiwango cha lami. Na sisi kama Wizara tunategemea muda wowote barabara hii iweze kutangazwa kwa ajili ya ujenzi, kwa sababu ni kati ya barabara chache ambazo zimebaki ambazo ni barabara kuu, trunk, yaani kuunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Mbeya.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba taratibu zote za manunuzi zimeshakamilika, tunachosubiri ni kutangaza hiyo tender kwa sababu fedha imeshapitishwa na Bunge lililopita kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Wizara ya Maji ina dhamira njema na wananchi wa Jimbo langu la Manyoni Magharibi. Kuna visima ambavyo vimeahidiwa na Wizara katika Vijiji vya Jeje, Njirii, Kamenyanga, Itagata, Ukimbu, Chabutwa, Makale na Kalangali na Itagata, je, ni lini wataenda kuchimba visima hivi?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Kubwa nimuombe Mheshimiwa Mbunge baada ya dakika chache nakuja kuwasilisha bajeti yangu ya Wizara ya Maji na bajeti yetu imesikiliza ushauri wa Waheshimiwa Wabunge. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tumezingatia maelekezo yako katika kuhakikisha wananchi wako tunawachimbia visima. Ahsante sana.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niulize maswali madogo mawili ya nyongeza. pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali juu ya upatikanaji wa maji katika maeneo yetu hasa Mji wa Itigi ambapo mimi ndio Mwakilishi wao.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahadi hii ya kuvuna maji katika Mji wa Itigi, ni swali la pili nauliza katika Bunge hili, Bunge lililopita niliuliza swali kama hili. Majibu yalikuwa tunajiandaa, dalili inaonesha kwamba watafanya.
Je, ni lini sasa uvunaji huu utaenda kufanya katika Mji wa Itigi na maeneo ambayo umeyataja ya Kayui, Muhanga na Kaskazi kujenga mabwawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, Lakini swali la pili, nashukuru pia Serikali kwa kukamilisha mradi mkubwa wa maji katika Mji wa Itiga ambao una manufaa makubwa kwa wananchi lakini unawatua akina mama ndoo kichwani. Lakini gharama za kuunganisha maji yale kwenda ndani ni gharama kubwa sana. kwa hiyo, mtu wa kijijini kwa shilingi 200,000 ni hela nyingi. Je, Serikali ipo tayari kupunguza gharama za uunganishaji maji ili wananchi wanufanike na mradi huu mkubwa ambao Mbunge wao amehangaika nao kuupata na wizara imesaidia? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, uvunaji huu wa maji tunautarajia kuutekeleza katika mwaka wa fedha ujao kwa maana mwaka 2021/2022. Mheshimiwa Mbunge ahadi hii imekuwa ikitolewa toka huko awali lakini kwa sasa hivi kama tulivyokuwa tumeendelea kuongea RUWASA imekuwa ni mkombozi, RUWASA imekuwa ni chachu ya mageuzi ya utekelezaji wa miradi ndani ya Wizara. Hivyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge ili sasa linaingia kwenye utekelezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusiana na gharama za uunganishaji, hili nalo limekuwa ni tatizo sugu. Hata hivyo, kama tulivyomsikia Mheshimiwa Waziri wakati wa uwasilishaji wa bajeti, ni suala ambalo tayari lipo katika uangalizi mkubwa ambapo tunahitaji kuona wananchi wanaenda kupata nafuu kubwa katika uunganishwaji wa huduma ya maji sio tu katika Mji wa Manyoni bali kwa Tanzania nzima.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, naomba commitment ya Serikali au itusaidie Serikali kuona namna iliyobora hasa kwa mbegu ambayo inaitwa Hysun inauzwa shilingi 35,000 kwa kilo mbili.
Je, Serikali sasa ipo tayari kuingiza ruzuku kwa mbegu hii ili uzalishaji wa mafuta uwe bora zaidi katika Mkoa wa Singida na mikoa mingine ambayo inalima alizeti?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri kwamba gharama ya mbegu za highbred za alizeti ni kubwa sana na sio rahisi mkulima wa kawaida kuweza kuzinunua. Kwa hiyo, mpango wa Wizara ya Kilimo kwa mwaka ujao wa fedha baada ya kupitishiwa bajeti yetu hapa ni kwamba tukimaliza mkutano wa kukutana Singida na wazalishaji wote wa viwanda vya kulizisha mafuta mpango wetu ni kutengeneza subsidy, ruzuku ili bei ya mbegu hizo kwa utaratibu tutakaoweka kwa wasambazaji ili wakulima bei yao iweze kupungua.
Kwa hiyo huo ni sehemu mpango wetu na tunaamini tutautumia katika mwaka ujao wa fedha ili kuweza kupunguza bei ya mbegu za alizeti.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wananchi wa Kintanula ni walinzi shirikishi wa hifadhi kubwa kabisa ya Rungo Mhesi Kizigo ambayo ipo pale na wanasaidia kupambana na majangili kwa njia ya mawasiliano. Sasa kupitia mnara huu, wananchi hawana mawasiliano sasa. Ili kuepusha ajali nyingi ambazo zinatokea za watu kuanguka juu ya miti na kuvunjika mgongo na wakati mwingine viuno; je, Serikali inasemaje? Ni lini itakwenda kukamilisha mradi huu ili wananchi hao pia wanufaike na mradi huu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kuna mnara ambao unajengwa pale katika Kijiji cha Mhanga, ulisimama Kitongoji cha Jirimli, ulikuwa unajengwa na Halotel. Sasa Serikali ipo tayari kuzungumza na Halotel ambao walisimamisha ujenzi wa mnara huu ili waendelee? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika swali langu la msingi, Kijiji hiki kitaingizwa katika utaratibu wa kufanyiwa tathmini ili tujiridhishe ukubwa wa tatizo na kujua kama tunahitaji kwenda kuweka mnara au tunaenda kuongeza tu nguvu ya mnara uliopo ili uweze kuhudumia wananchi wa pale.
Mheshimiwa Spika, pia lengo la Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote ni kufikisha mawasiliano kwa wananchi wote. Kwa hiyo, hilo ni jukumu la Serikali, nasi Serikali tumejipanga kwa ajili ya kuhakikisha kwamba vijiji ambavyo vinahitaji mawasiliano kikiwemo na Kijiji ambacho Mheshimiwa Mbunge amekitaja, kitakuwepo ndani ya mkakati wa Kiserikali wa kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata mawasiliano.
Mheshimiwa Spika, pia kuhusu masuala ya Halotel; katika ujenzi wa minara, wakandarasi wengi ambao wanapewa tender za ujenzi wa minara hii ni kwamba wamekumbana na changamoto nyingi katika kipindi hiki ambacho tulikuwa tuna Covid 19, lakini pia katika baadhi ya vibali ambavyo walikuwa wanaomba, vingine vilichelewa kwa sababu ambazo zilikuwa nje ya uwezo wao. Sasa Serikali imejipanga kwamba katika vipengele ambavyo vinahusisha na vibali ambavyo Serikali moja kwa moja inahusika, tunaenda kuhakikisha kwamba tunashirikiana na wenzetu ambao wanatoa vibali ili vibali vile vinatoka kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Iko nia ya Serikali ya kujenga barabara ya kutoka Mkiwa kwenda Noranga kilometa 56.9 ambayo ilikuwa imetangazwa mwaka 2017, na sasa hivi katika bajeti iliyopita alisema kwamba wataitangaza. Je, ni lini sasa barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Massare kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara iliyotajwa ni barabara ambayo imepata kibali na taratibu zote zimekamilika; muda wowote itatangazwa kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami. Mheshimiwa Mbunge tumeongea naye mara kadhaa, pamoja na Mbunge wa Chunya Mheshimiwa Kassaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii inatarajiwa kutangazwa muda wowote kwa sababu imeshapata kila kitu na imekamilika, kwa maana ya kutangazwa. Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Kwanza, naomba niipongeze Serikali kwa kutangaza barabara ambayo nilikuwa naipigania hapa Bungeni kwa muda mrefu ya kipande cha kilometa 25 kutoka Itigi kuelekea Noranga. Sasa, je, Serikali iko tayari kuongeza kipande kingine katika bajeti ijayo ya 2021/2022 angalau kufanya urefu uwe wa kutoshatosha? Barabara hii ni ndefu, ina kilometa 219.
NAIBU SPIKA: Unamaanisha bajeti ya 2022/2023 au? Kwa sababu hii si ndiyo tumetoka kuijadili sasa hivi?
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, hapana, namaanisha bajeti iliyotangazwa ni hii ambayo inaishia Juni. Je, kuanzia Julai 2021/2022, Serikali iko tayari kuongeza kipande kingine ili barabara hii iweze kufanya vizuri zaidi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahaya Massare kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zilizotangazwa zimetangazwa kwa bajeti ambayo tunaendelea kuitekeleza kabla ya tarehe 30 Juni na barabara anayoisema pia tumeitengea fedha kwa bajeti tutakayoanza kutekeleza Julai. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaendelea na ujenzi kwa kipande kinachoendelea mpaka barabara itakapokamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo bajeti tuliyotangaza ni kwa mwaka huu tunaoendelea nao kabla ya Juni, 30, lakini tumetenga pia fedha kwa ajili ya bajeti tunayoanza 2021/2022. Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.
Kwa kuwa dhamira ya Serikali ni kupeleka umeme katika vijiji vyote katika nchi ya Tanzania nzima ikiwemo na vitongoji, lakini kuna changamoto katika Wilaya ya Manyoni feeder ya Manyoni kutoka Singida ambayo inahusisha Wilaya ya Ikungi, Wilaya ya Manyoni na Halmashauri ya Itigi, umeme wake una katikakatika mara kwa mara, na ipo dhamira njema ya Serikali ya kujenga vituo vya kupozea umeme katika Mkoa wa Singida vipo vitatu ikiwepo Manyoni, Mitundu katika Jimbo langu na Iramba; je, ni lini ujenzi wa vituo hivi unaanza?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa mgunge wa Singida kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba yapo baadhi ya maeneo ambayo umeme wake unakuwa haufiki vizuri kwa sababu ya laini kuwa ni ndefu, lakini Mkoa wetu wa Singida ni mkoa mmojawapo wenye kituo kikubwa sana cha kupoza umeme pale mjini, na umeme unatokea pale kuelekea maeneo ya jirani, na tunao umeme wa kutosha kuweza kuhudumia maeneo yote. Ni kweli tunatarajia kuweka vituo vyengine vya kupoza umeme katika maeneo yetu ya Singida, mchakato wa kutafuta wazabuni na maeneo sahihi ya kuweka unaendelea, kabla ya mwaka huu haujaisha Waheshimiwa Wabunge wataona maendeleo katika maeneo yao na ikiwemo kwenye Jimbo lake ambapo tunatarajia kuweka kituo cha kupoza umeme kwa ajili ya kuweza kusambaza umeme kwa karibu zaidi katika maeneo yake.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, lakini yapo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Singida eneo ambalo linaathirika sana na ukatikaji wa umeme ni eneo la Itigi, lakini na Manyoni wao wanaita feeder ya Manyoni na kila Jumamosi au Jumapili ya wiki lazima umeme ukatike. Sasa je, ni lini zoezi hili litakoma kukatwa katwa umeme katika Halmashauri ya Itigi?
Mheshimiwa Spika lakini pili tunachangamoto ambayo imetokea sasa wakati wenzetu wanaendelea na wakandarasi wa REA nchi nzima katika wilaya ya Manyoni hakuna mkandarasi. je, ni nini tatizo na ni lini mkandarasi wa REA III atapatikana katika Halmashauri za Manyoni na Itigi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Massare kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, naomba nianze na swali la pili la Mkandarasi wa REA. Ni kweli kwamba Serikali ilitangaza kazi za kutengeneza umeme wa vijijini na maeneo mengi yakawa yamepata wakandarasi, lakini maeneo Matano yalibaki bila kupata wakandarasi ikiwemo Singida kwa maeneo ya Itigi na Manyoni ni mojawapo.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa taarifa kwenye Bunge lako Tukufu kwamba Ijumaa ya wiki iliyopita, Mkandarasi anayeitwa TungTang amesaini mkataba wa kupeleka umeme katika Wilaya zetu za Itigi na Manyoni na
tumemwambia aripoti kazini Jumatatu ijayo wakati sisi ofisini Serikali ikiwa inaendelea kukamilisha utaratibu wa malipo ya awali.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kusema kwamba, lot ya Singida iko pamoja na lot ya Shinyanga, Tanga na Arusha. Wakandarasi wote hawa tunatarajia waanze kuripoti katika maeneo yao ya kazi kuanzia Jumatatu ya wiki ijayo.
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la kukatikakatika kwa umeme, nianze kwa kusema kwamba tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo inaonekana wazi kabisa kwamba kuna mabadiliko makubwa ambayo yamefanyika katika Wizara ya Nishati, lakini katika Shirika letu la TANESCO na tunatarajia kabisa kwamba katika kipindi kifupi kijacho wenzetu ambao wamepewa dhamana sasa TANESCO wataenda kukidhi yale mahitaji ambayo Watanzania wanayatarajia.
Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu, bajeti ya TANESCO sasa imewekewa mechanism ya kuhakikisha inaongezeka kwa kuziba ile mianya iliyokuwa ikiachia mapato yavuje ili kuweza kupata nguvu zaidi sasa ya kuimarisha maeneo hayo ya kukatika kwa umeme. Kukatika kwa umeme kunasababishwa na sababu nyingi nyingi, lakini zile ambazo ziko ndani ya uwezo wetu tunahakikisha kwamba tunazifanyia kazi ili tatizo hilo liweze kwisha, siyo kwa Itigi na Manyoni peke yake, lakini kwa nchi nzima. Naomba kuwasilisha.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Kituo cha Afya cha Itigi ambacho kinahudumia watu wengi katika Mji wa Itigi kama hospitali, je, Serikali ni lini itapeleka X-ray katika kituo hiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahaya Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa vituo hivi vya afya unaendana na uwekaji wa vifaa tiba zikiwemo mashine hizi za X-ray na ununuzi wa mashine hizi unakwenda kwa awamu kwa kadri ya bajeti zetu. kwa hivyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunatambua kwamba Kituo cha Afya cha Itigi kina uhitaji mkubwa wa X-ray na kinahudumia wananchi wengi, hivyo tutaendelea kutafuta fedha ili tupate mashine ya X-ray kwa ajili ya kuboresha huduma za afya katika Kituo cha Afya cha Itigi. Ahsante. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii ili niulize swali dogo tu la nyongeza. Ni lini sasa mkandarasi ambaye majuzi tu
Mheshimiwa Naibu Waziri alituambia hapa katika Bunge lako Tukufu kwamba anaanza kazi katika Halmashauri za Wilaya za Manyoni na Itigi ataanza kazi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahaya kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliwaelekeza wakandarasi wa lot hizo nne ambazo zilikuwa zimebakia, waripoti katika vituo vyao vya kazi wiki hii inayokwisha leo na ilikuwa ni kwenda kuangalia maeneo ya kupata go down za kutunza vifaa vyao na kuwasiliana na Waheshimiwa Wabunge.
Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa Mbunge hajawasiliana na mkandarasi wake, naomba nitakapotoka hapa mimi mwenyewe nimuunganishe naye. Wiki inayokuja tunatarajia waanze kwenda kwenye maeneo hayo kwa ajili ya survey na kuanza kazi ambazo wameshasaini mikataba tayari. Nashukuru.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii nami niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itupe ufafanuzi kidogo; pamoja na ufafanuzi uliotolewa wa shilingi 27,000 katika vijiji lakini kabla ya hapo kulikuwa na bei tatu; kulikuwa na 320,000; 177,000 kwenye vimiji vidogo kama Itigi na 27,000 kwa vijiji. Sasa wametoa wale wa 177,000 wamewapeleka kwa 320,000; vijiji ambavyo vimeungana vijiji vitatu vinne kwa kuwa tu vina kasoko basi vinaonekana ni mji vilipe 320,000/-. Je, Serikali iko tayari sasa kukubaliana na bei zilizokuwa kabla ya kurudi 27,000 na kuwa 177,000 kwa miji midogo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali zuri kutoka kwa Mheshimiwa Massare. Ni kweli hata kabla ya hapa tayari sisi kama Wizara kwa niaba ya Serikali tumeshapata mapendekezo na maoni na maombi mbalimbali ya ku-vary hizi gharama ambazo tuko nazo sasa. Na wengine wakaenda kwenye kupendekeza kwamba hata mtumishi wa Umma anavyolipwa posho anapoenda kwenye jiji, manispaa au wilaya, zile posho anazopewa zinatofautiana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Serikali niseme tumelipokea na tutakwenda kulifanyia kazi ili kuangalia uhalisia wa maisha tunayoishi sasa na gharama ambazo Serikali inaweza ikazitoza ili wananchi waweze kupata huduma hii ya umeme kwa gharama nafuu ambayo inamfikia kila mtu. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana nikupongeze kwa kupata nafasi hii. naomba niulize sasa swali dogo la nyongeza: -
Mheshimiwa Spika, matatizo yaliyopo huko Hanang’ yanafanana kabisa na katika Halmashauri ya Itigi, ambayo ina Tarafa moja. Halmashauri ya Itigi ilikosa pesa za ujenzi vituo vya afya vya tarafa kwa sababu, ni tarafa moja, lakini ina kata 13. Je, sasa Serikali iko tayari kuiangalia kwa jicho la kipekee angalau tukapata kituo kimoja hapa karibuni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahaya Massare, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kujibu kwenye swali la msingi; kigezo cha ujenzi wa vituo vya afya ni tarafa, lakini pia kata za kimkakati. Kwa hiyo, pamoja na kwamba, Itigi kuna tarafa moja, lakini bado wana sifa ya kupata vituo vya afya kupitia tathmini ya kata za kimkakati.
Kwa hiyo, naomba nilichukue hili na nitawsiliana na Mheshimiwa Yahaya ili tuweze kuona kata zipi za kimkakati tuzipe kipaumbele kwenye awamu zinazofuata za ujenzi wa vituo vya afya. Ahsante. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Naomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Serikali ina dhamira njema sana ya kupeleka umeme vijijini na kwa kuwa Mkandarasi wa Wilaya ya Manyoni ambapo kuna majimbo mawili; Manyoni Mashariki na Manyoni Magharibi ambapo mimi nipo, Mkandarasi wake alichelewa kuanza kazi na toka ameripoti hatuoni kitu kinachoendelea: Je, Serikali iko tayari kumhimiza aanze kazi haraka?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Massare kama ifuatavo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inawahimiza sana Wakandarasi wote kukamilisha kazi zao kwa wakati kwa mujibu wa mkataba na tunaamini hakuna atakayechelewa na atakayechelewa hatua madhubuti zitachukuliwa kwa mujibu wa mkataba.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii, lakini nisikitike swali nimeulizia Itigi lakini wamejibiwa watu wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeuliza usikivu wa Itigi kwa sababu maalum, sisi Itigi hatusikii kabisa redio, ni kwa sababu redio Mwangaza waliweka mnara wao pale mtambo, kwa hivyo redio nyengine hazisikiki kabisa ikiwemo TBC, na swali hili ni mara ya 3 nauliza ndani ya Bunge hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niulize Mheshimiwa Waziri aniambie Manyoni ni sehemu ya Itigi, Manyoni wanasikia TBC, Itigi hatusikii kabisa, sasa huo mtambo mtakaoufunga mwakani huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli mnatuahirishia miaka yote hii, Mheshimiwa Nape yupo hapa ulipokuwa Waziri wa Habari ulijibu swali hili ukatuambia mtatusaidia kutufungia mtambo pale sasa leo tunajibiwa tu watafunga na Manyoni na Ngara na wapi, hebu naomba comitment ya Serikali, sisi Itigi hatusikii kabisa redio, wananchi wetu hawana pesa ya kununua tv, hata Mheshimiwa Rais akihutumia hawamsikii kupitia viredio vyao.
Sasa ni lini mtatufungia kamtambo hako? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare Mbunge wa Manyoni Magharibi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya matangazo ya TBC, changamoto ni mbili ya kwanza ni uhafifu wa usikivu na pili inawezekana usikivu haupo kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa changamoto ya Manyoni kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi, nimesema kwamba katika mwaka wa fedha ujao kuna Wilaya 14 ambapo Manyoni ikiwa moja ya Wilaya ambazo zinakwenda kutatuliwa changamoto za usikuvu wa mawasiliano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vilevile nafahamu kabisa kwamba changamoto hii imekuwa ya muda mrefu lakini ni lazima pia tutume wataalamu wetu wakajiridhishe na ukubwa wa tatizo ili tujue tatizo ni kwamba hakuna mawasiliano au mawasiliano ni hafifu, ili tuweze kuchukuwa hatua stahiki ili kuhakikisha kwamba Itigi inapata mawasiliano ya TBC. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Swali langu nimeulizia Mji wa Itigi ila imejibiwa vijijini. Basi, sasa je, Serikali ipo tayari sasa kuvuna maji katika Mji wa Itigi ili kujenga bwawa linaoitwa Mkalamani ambalo lipo palepale Mjini Itigi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, kujibu swali lake la nyongeza la kuvuna maji katika Mji wa Itigi.
Mheshimiwa Spika, Mji wa Itigi ni moja ya Miji ambayo upatikanaji wake wa maji unaendelea vizuri kwa sasa ni zaidi ya asilimia 70. Kwa hiyo, kwenye masuala ya uvunaji wa maji tunazingatia zaidi maeneo ambayo maji yanapatikana kwa shida zaidi, lakini pale itakapobidi basi tutafanya hivyo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Wakati wenzetu wanakwenda kwenye mfumo wa 4G Jimboni kwangu baadhi ya Vijiji havina kabisa mawasiliano ikiwepo Kijiji cha Mhanga, Kintanula na Kijiji cha Lulanga.
Je, ni lini sasa Serikali itatimiza ahadi yake ya muda mrefu ya kupeleka minara katika vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Masare kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge tunawasiliana mara kwa mara na hivi vijiji tayari kilichokuwa kinasubiriwa ni tenda kutangazwa na tenda tayari imeshatangazwa Tarehe 20 Oktoba. Hivyo, tunasubiri mchakato huu ukamilike ili utekelezaji wa mradi huu uanze mara moja. Mimi pamoja na Mheshimiwa Mbunge bahati nzuri tumeshafika katika eneo lake na vijiji ambavyo amevitaja mimi binafsi nimeshafika katika maeneo hayo, kwa hiyo nimhakikishie kwamba hilo ninalifahamu kabisa na Serikali itaenda kutekeleza. Ahsante sana.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi.
Je, Serikali ina mpango gani wa barabara ya kuunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Simiyu kupitia Daraja la Sibiti?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Singida na Mkoa wa Simiyu kupitia Daraja la Sibiti hivi ninavyoongea barabara zote tatu ziko kwenye kukamilisha usanifu wa kina kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami kuanzia Ulemo kwenda Sibiti, lakini pia kuanzia Iguguno kwenda Sibiti wakandarasi wako tayari wanafanya usanifu kwa ajili ya maandalizi ya kujenga kwa kiwango cha lami kuunganisha hiyo mikoa miwili, ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ipo dhamira ya Serikali ya kuunganisha mikoa yote kwa barabara za lami. Mkoa wa Singida ni miongoni ni mwa mikoa ambayo haijaunganishwa na mikoa mingine ukiwemo Mkoa wa Simiyu na Mkoa wa Mbeya.
Je, dhamira ya Serikali ya kujenga barabara ya Mkiwa – Itigi – Rungwa hadi Makongorosi imefikia wapi kuanza kujengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Massare, Mbunge wa Itigi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara hii ni barabara kuu ambayo inatoka Mkiwa – Itigi - Rungwa hadi Makongorosi – Chunya. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii ni kati ya barabara 22 ambazo ziko kwenye maandalizi ya kuanza kujengwa kwa kiwango cha lami kuanzia Mkiwa kwenda Manyoni mwaka huu wa fedha kilometa 50. Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi. Serikali iliahidi Bwawa la Mhanga katika Halmashauri ya Itigi na wakaanza ujenzi, lakini ukasimama: Je, Waziri yuko tayari kwenda nami kuona utekelezaji wa ahadi hii nzuri ya Serikali ili wananchi wawaone aweze kusukuma malizio lile lambo ambalo linajengwa pale Muhanga?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishe kaka yangu Mheshimiwa Massare, niko tayari kwenda Itigi. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Serikali imekuwa ikiahidi mara nyingi kujenga Kituo cha Polisi Itigi ambacho wanatumia majengo chakavu ya reli, angalau kituo cha daraja C. Sasa, je, ni lini?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Massare Mbunge wa Itigi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uchakavu wa kituo kilichopo, tutafanya tathimini kuona kiwango cha uchakavu; na kama eneo hili halitoshi tuko tayari kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge ili eneo lipatikane la kutosha kwa ajili ya kujenga kituo chenye hadhi ya Wilaya ya Itigi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshiniwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kituo cha Doroto ambacho kimetajwa kwenye majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ni kituo kikubwa ambacho kinasimamia Game Reserve ya Muhesi lakini hakina gari: Je, Serikali ipo tayari sasa kupeleka gari jipya kabisa katika kituo hiki?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili: kuna wananchi ambao walifariki kutokana na wanyama hao wakali katika Kijiji cha Nyabutwa katika Kata ya Mgandu na maeneo mengine mazao ya watu yaliliwa: Je, ni lini Serikali itawalipa kifuta jasho na kifuta machozi kwa ajili ya kuwafariji wananchi hao kutokana na matukio hayo ya wanyama wakali?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yahaya Omari Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nimtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeshapokea magari 59 ambayo yatasambazwa kwenye vituo vilivyo na athari ya wanyamapori wakali na waharibifu, hivyo nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba priority itapelekwa katika Kituo hiki cha Doroto.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili lingine la kifuta machozi na kifuta jasho, tulikuwa na changamoto kidogo ya fedha na kufanya tathmini na tayari tumeshakamilisha. Hivyo, wakati wowote tutaanza kulipa wathirika wa changamoto hii. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Ipo ahadi ya Serikali ya kujenga Kituo cha Polisi Itigi. Kwa muda mrefu, majengo wanayotumia polisi sasa ni ya reli na ambayo reli sasa wanajenga. Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake ya kujenga Kituo cha Polisi daraja B Itigi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua kweli Itigi ulikuwa Mji Mdogo lakini sasa unakua kwa kasi na unahitaji Kituo cha Polisi na ndio maana tayari tumeshamtuma Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida ili kufanya uhakiki wa uwepo wa kiwanja, ukubwa wake ili kuleta mahitaji na michoro iweze kuandaliwa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho. Kwa hiyo Mheshimiwa niko tayari kufuatilia jambo hilo ili kuona kwamba linatekelezwa ili Mji wa Itigi uweze kupata Kituo cha Polisi kama alivyoomba cha daraja B.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Kipo Kituo cha afya Rungwa ambacho tunaendelea na ujenzi na hakijasajiliwa kama kituo cha afya na watumishi ni wa zahanati. Je, sasa Serikali iko tayari kupeleka watumishi kwa Kituo hiki cha Afya cha Rungwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahaya Massare, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kituo hiki cha afya ambacho kinaendelea na ujenzi baada ya kukamilika tutafanya mpango wa kuhakikisha kwamba tunapeleka watumishi ili kianze kutoa huduma za afya. Ahsante. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu haya marefu ya Serikali na historia ambayo hapa haitusaidii sana, dhamira ya Serikali pamoja na kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere pamoja na kuweka mahela kwenye mafuta ya petroli ambao watumiaji wa petroli wala hawahusiki na umeme huu vijijini.
Je, ni lini sasa Serikali itaangalia namna iliyo bora ya kupatana na wananchi ambao wanahitaji kuweka umeme kama wanashindwa kupunguza bei ili wapatane naye basi alipe sehemu ya gharama na gharama nyingine azilipe polepole kulingana na makubaliano watakayokubaliana, Serikali iko tayari kufanya jambo hili?
Mheshimiwa Spika, pili, kulikuwa na bei wakati huo Mheshimiwa hapa amejibu amesema ilikuwa shilingi 177,000 na shilingi 27,000 huko vijijini kabisa, vijiji miji ambayo kama Itigi ambao wameiondoa sasa katika ile laki moja na sabini saba kuja laki tatu ishirini. Je, Serikali iko tayari kurudisha vile vijiji miji ambavyo kutokana tu kupimwa eti tayari ni mji! Je, wako tayari sasa kuturejeshea katika ile bei ya shilingi 177,000?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yahaya Massare, Mbunge wa Manyoni, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kulipa gharama za kuunganishwa umeme awamu kwa awamu au taratibu, tumeshaanza kuufanyia mkakati na majadiliano yanaendelea kuona namna bora ya kuweza kufikia azma hiyo. Changamoto kubwa ni kwamba gharama za bidhaa zinabadilika mara kwa mara, kwa hiyo mtu akilipa kidogo kidogo kwa muda ambao tutakuwa tumekubaliana, akamalize ndani ya muda huo labda pengine itatusaidia, lakini akichukuwa muda mrefu na pengine kushindwa kumaliza ndani ya ule muda tuliokubaliana, tutajikuta huduma hii inakuwa ni changamoto kwa kuitekeleza.
Mheshimiwa Spika, tayari wataalam wetu wa TANESCO wanaendelea kuangalia namna bora ya kuweza kupunguza hizi gharama za kuunganisha umeme kwa awamu moja kwa wateja wetu ili kuweza kufika azma ya kuwaunganishia wananchi wote umeme, lakini hasa kwenye maeneo ya mijini kwa sababu gharama za vijiji tayari zimepunguzwa.
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la pili, wenzetu wa TANESCO walishirikiana na wenzetu wa TAMISEMI kubaini na maeneo gani ya miji na ni maeneo gani ya vijiji na gharama ya vijijini ikabaki kuwa shilingi 27,000 na gharama za mijini zikasemwa hizi gharama nyingine ambazo tayari Serikali imeweka ruzuku ndani yake. Hata hivyo, Serikali ya Awamu ya Sita ni sikivu kwa wananchi itaendelea kufanya kazi kuendelea kuona namna ambayo inaweza ikawafikishia huduma bora Watanzania hata kwa kufanya majadiliano mengine ya kuona maeneo gani ipeleke kwa gharama gani kwa ajili ya kufikisha azma ya wananchi wote kupata umeme.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na napenda niongezee kidogo kwamba ni dhahiri kwamba yapo maeneo ya miji, kwanza tafsiri yetu ya miji na vijiji inatokana na sheria ya TAMISEMI, lakini dhahiri kwamba yako maeneo ya miji na majiji manispaa ambayo yako pembezoni yana sifa zote za maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri tumebaini maeneo hayo na tumekubaliana na maombi ya Waheshimiwa Wabunge wengi pamoja na kwamba maeneo hayo yapo kwenye mipaka na miji na majiji lakini ukienda ukiona ni dhahiri kabisa kwamba yana sifa za maeneo ya vijiji kwa maana ya mazingira na hali ya kipato.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo katika bajeti ya Wizara ya Nishati tutatoa maelezo na utaratibu wa kuzingatia uhalisia wa maeneo haya katika kupanga bei ya kuunganisha. Ahsante. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti; iko dhamira ya Serikali ya kujenga hospitali za halmashauri 28 katika bajeti ambayo tunaimaliza sasa. Je, lini hospitali hizi zitapelekewa fedha, ikiwemo hospitali ya Halmashauri ya Itigi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Massare, Mbunge wa Manyoni kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali zote za halmashauri zote ambazo zimeanza ujenzi na vituo vyote vya afya ambavyo vimeanza ujenzi kwa fedha ya Serikali mpango wa Serikali ni kuendelea kupeleka fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa hopitali hizo. Ndiyo maana kwenye mwaka ujao wa fedha tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 69.95 kwa ajili ya ukamilishaji wa hospitali zile 59, ikiwemo hii ambayo Mheshimiwa Massare ameisema. Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi. Sheria zilizopo sasa Tanzania mabasi na malori yanatembea mchana na malori ndiyo yanayotembea usiku lakini duniani kote mabasi yanatembea muda wote, malori yanatembea mchana mwisho saa 12:00. Je, ni lini na sisi Tanzania tutakwenda na utaratibu ambao uko duniani ili twende na wenzetu katika maendeleo?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa
Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahaya Massare kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, lengo ni kuhakikisha kwamba shughuli za uchumi zinaendelea kufanyika nyakati zote. Tunaamini kabisa kwamba mabasi na malori na magari yote yakiweza kutembea masaa 24 yatachangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, hivyo siyo suala la kusema yupi ni bora kuliko mwingine lakini changamoto ambayo nimeizungumza ni kwamba lazima tutakapofanya hivyo tuzingatie usalama wa wananchi wa nchi yetu na tumegundua kwamba mabasi na malori ndiyo ambayo ni visababishi vikubwa vya ajali. Nitatoa mfano wa ajali zilizotokea hivi karibuni ajali ambayo imetokea pale Tanga hivi karibuni ambayo iliua takribani Watanzania 20 ilikuwa ni kati ya lori na basi tena nyakati za usiku. Ajali iliyotokezea hapa Kongwa halikadhalika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba concern ya Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wengine kuona kwamba huduma hizi zinaweza kuimarishwa na kutoa nafasi kwa wananchi wetu kuweza kutoa mchango wao katika uchumi wa nchi yetu kwa ufanisi zaidi tumezipokea na tutazifanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza mikakati hiyo imeshaanza na tuvute subira pale ambapo wataalam wetu watatushauri utaratibu bora zaidi wa kufanya basi tuweze kuruhusu mabasi hayo yaweze kutembea muda wote.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, wananchi wa Itigi baada ya kuliwa mazao yao na hawa wanayama wanategemea kile kidogo ambacho Serikali imekiweka kwenye sheria ikiwemo kifuta machozi na kifuta jasho;
Je, ni lini sasa watamalizia kulipa wananchi ambao wameliwa mazao yao miaka miwili iliyopita?
Mheshimiwa Spika, swali la pili Serikali imegawa pori kubwa la akiba la Rungwa, Muhesi na Kizigo kuwa mapori yanayojitegemea. Rungwa peke yake, Muhesi peke yake na Kizigo peke yake. Muhesi imepakana sana karibu na vijiji vingi vya Itigi;
Je, ni lini sasa wataongeza askari wa wanyamapori ili angalau waweze kuwadhibiti hawa wanyama wanapotoka kule kuingia kwenye makazi ya watu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hivi karibuni mwezi wa tatu tumemaliza kulipa kifuta jasho na kifuta machozi katika Wilaya ya Manyoni hususan katika maeneo ya Vijiji vya Njiri, Rungwa, Sanjaranda na Itigi Mjini ambao walipata madhara makubwa ya wanyamapori wakali na waharibifu. Hivyo nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge, kwamba kwa sasa hivi tumeshafanya tathmini kwa wale ambao wamebaki tutawalipa katika mwaka huu wa fedha.
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la askari, tumeshaomba tayari kuongezewa tena kwa mwaka huu askari waajiriwa ambao tayari tumeshapata kibali tunaamini kwenye maeneo ambayo yana changamoto za wanyama wakali na waharibifi tutaendelea kuongeza nguvu na vituo kujengwa ili angalau tupunguze athari hii ya wanyama wakali na waharibifu.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi.
Je, sasa Serikali ni lini itasaidia hospitali za Mikoa nazo kutoa huduma hii ya saratani, kwa sababu sasa hivi inatolewa katika Hospitali za Kanda tu na hospitali kubwa kama ile KCMC, Bugando na Ocean Road tu?
Swali la pili, kwa kuwa magonjwa yasiyokuwa ya kuambukizwa ukiwemo ugonjwa wa kisukari, pressure pamoja na magonjwa mengine; Je Serikali sasa ina mkakati gani wa kutoa elimu ya kutosha hasa Wilayani ambako wagonjwa hawa ndiyo wanakotokea ili kuondoa rufaa nyingi kwa ajili ya hospitali kubwa kama Muhimbili?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, moja ndiyo maana Serikali sasa hivi, Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa fedha na amehakikisha hospital zote za Mikoa zina CT scan, maana yake sasa kwenye hospitali zetu za Mikoa wanaweza kucheki na kugundua mapema saratani kabla haijakua.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna mkakati mahsusi wa kuwasomesha Wataalam kwa ajili ya kuwapeleka ngazi za Mikoa na kuweza kutoa huduma hiyo. Kwa sasa tunapima lakini tunashirikiana kwa kutumia telemedicine ili kuwasiliana na hospitali zetu za Kanda na Mikoa.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kata ya Idodyandole, Kata ya Gondi na Kata ya Ipande ni kata kubwa sana, na tulileta mapendekezo: Je, lini Serikali itatoa pesa kwa ajili ya kituo hiki cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kwa bahati nzuri, ni hivi karibuni tu Mheshimiwa Massare ameleta orodha hii ya kuomba vituo hivi vya afya na Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kwenda kujenga kituo cha afya kipya katika maeneo ambayo ameyataja.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Manyoni inapata umeme kutoka Singida na kutoka Singida – Ikungi – Manyoni lakini Itigi – Mitundu hadi Mwamagembe, kutoka kituo kikubwa kinachopoza umeme ni karibu kilometa 400. Serikali ilikuwa na mpango wa kujenga vituo vya kupoozea umeme substation katika Mkoa wa Singida ikiweo Iramba na hiki cha Manyoni ambacho amekitaja kwenye majibu na cha Mitundu.
Je, ni lini sasa wanaenda kujenga vituo hivi katika Mkoa wa Singida? (Makofi)
Swali la pili, nguzo za zege sasa hivi tunaziona katika maeneo mengi zikiwekwa, njia hii ndefu ya kutoka Singida kama nilivyoitaja na umbali wake kutoka Manyoni lakini kutoka Itigi kwenda Mitundu mpaka Mwamagembe kilometa ni nyingi. Ni lini wataweza kuweka sasa nguzo za zege kwa sababu maeneo haya kuna maeneo chepe chepe, maeneo ya misitu lakini maeneo yenye acid yanakula sana nguzo hizi za miti.
Je, ni lini sasa Serikali itaanza kufanya hilo zoezi ili kufanya maisha yawe mazuri, umeme ni maisha. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, mojawapo ya sababu ya umeme kukatika katika maeneo mengi ni kusafiri kwa umbali mrefu. Serikali kupitia TANESCO ilifanya upembuzi yakinifu na kubaini mahitaji ya vituo vya kupooza umeme takribani 88 katika Halmashauri zetu zote, imetafuta fedha kupitia mradi wetu wa Gridi Imara na tukapata karibia shilingi trilioni nne na shilingi bilioni mia mbili ambazo zitakuja kwa awamu nne. Awamu ya kwanza tumepata shilingi bilioni 500 na tutajenga vituo 15 katika Wilaya mbalimbali. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Massare pamoja na Waheshimiwa wengine kwamba itakapofika miaka mitano, sita ijayo baada ya mradi wa Gridi Imara kukamilika, kila wilaya tunatarajia iwe na kituo cha kupoaza umeme ili umeme usisafiri umbali mrefu na kuweza kukatika katika humo njiani.
Mheshimiwa Spika, sasa vituo alivyovitaja vya Iramba, Mkalama na maeneo mengine vitajengwa pia katika awamu hizo kulingana na wale ambao wana hali ngumu zaidi kufuatia wenye hali nzuri kidogo.
Mheshimiwa Spika, kwenye eneo la nguzo za zege ni kweli Serikali inafanya jitihada za kuhakikisha inabadilisha nguzo za miti kuweka za zege katika maeneo chepe chepe, yenye wadudu waharibifu na maeneo ya mapori ambapo hatuwezi kuingia mara kwa mara kufanya marekebisho. Maeneo aliyoyasema ni ya kipaumbele na tutaenda kuyatazama ili tuyaweke kwenye mpango wa kuyabadilishia kutoka nguzo za mbao kuweka za zege ili umeme upatikane kwa wakati wote katika maeneo hayo na maeneo mengine pia. Ninakushukuru.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Ipande Kijiji cha Mhanga, Kata ya Sanjalanda Kijiji cha Gurungu, Kata ya Mgandu Kijiji cha Itagata na Kata ya Wamagande Kijiji cha Kitanura hakuna mawasiliano kabisa. Nini kauli ya Serikali kuwapelekea wananchi hawa minara ya mawasiliano ya simu?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Tanzania ya sasa ni Tanzania ya Kidigitali, hatutahitaji mtanzania yeyote aachwe nyuma, kwa hiyo naomba nipokee changamoto hizi ili tupeleke wataalam wakaangalie ukubwa wa tatizo ili tupeleke huduma ya mawasiliano na watanzania wote washiriki katika uchumi wa kidigitali, ahsante sana.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Katika Jimbo langu la Manyoni Mgharibi Halmashauri ya Itigi kuna vijiji vya Mhanga, Tulieni, Mnazi na Vijiji Itagata na Vijiji vya Lulanga havina mawasiliano kabisa. Je, Serikali iko tayari sasa kuingiza katika mpango ujao wa bajeti vijiji hivi navyo vipate huduma ya minara.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira kuu ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inafikisha huduma ya mawasiliano. Kwa sababu ameiomba Serikali kama iko tayari, Serikali tuko tayari kuhakikisha kwamba tunaingiza katika mpango ujao wa kuhakikisha kwamba tunafikisha huduma ya mawasiliano, nakushukuru sana.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana:-
Mheshimiwa Spika, katika jimbo ambalo mimi ndio mwakilishi wao, Halmashauri ya Itigi, kuna skimu moja tu. Je, Serikali sasa iko tayari kuyatumia Mabonde ya Ipalalyo na Bonde la Mnazi kwa ajili ya kutengeneza skimu nyingine?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, tupo tayari na tutashirikiana na Mheshimiwa Mbunge kwa ajili ya kufanya hilo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Kwa kuwa wanyama hawa wamekuwa wanashambulia watu na tatizo ni upungufu wa Askari: Je, ni lini Serikali itaongeza askari katika Kituo cha Doroto ambacho ni Makao Makuu ya Game Reserve ya Muhesi?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Kuna waathirika wengi wamevamiwa, wengine wameuawa, mashamba yao yameliwa na tembo, au wanyama wakali wameuawa: Je, ni lini mtalipa watu wetu hawa katika Jimbo langu katika Halmashauri ya Itigi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, najibu maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunakiri kwamba kuna upungufu wa askari ambao wanatakiwa walinde kwenye maeneo haya. Nimwambie tu Mheshimiwa kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ndani ya mwezi huu tutahakikisha kwamba tunapeleka Askari katika kituo cha Doroto ili kuhakikisha kwamba shughuli za ulinzi wa wananchi dhidi ya wanyama wakali zinaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie tu kwamba tayari Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan imeshaachia kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wote walioathirika na athari za wanyamapori wakiwemo tembo wanapatiwa fidia zao na kupatiwa malipo yao, nakushukuru.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Serikali imenunua magari ya kuchimba maji katika kila Mkoa na yako chini ya DDCA. Je, ni lini yatakuwa chini ya Wahandisi wa maji wa Mikoa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare kuhusiana na magari ya uchimbaji visima kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwa sasa hivi magari haya yako chini ya DDCA tayari taratibu za ndani za kiwizara zinaendelea wakati wowote mambo yote yatakaa sawa kwa RMs wa Mikoa yote.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini kuna swali nauliza.
Mheshimiwa Spika, wale Mawaziri nane walikuja kufanya nini? Leo tunapokuja kusema kwamba Serikali haikuelekeza, haya kama huo ni mgogoro, je tutautatua lini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana; jambo la kwanza kwenye ile Kamati ya Mawaziri nane ambayo ilizunguka maeneo mbalimbali nchini, kila eneo lilikuwa linapelekewa taarifa kuhusiana na mahitaji ya eneo husika, sasa katika shamba la Kitaraka Holding maamuzi ya Serikali ambayo Kamati ya Mawaziri nane iliyatoa pale ni kwamba sasa ifanyike tathmini ambapo katika ile tathmini tutajua lile shamba wananchi wameingilia kwa kiwango gani ili sasa tuweze kumega sehemu ya lile eneo kuwakabidhi wananchi na sehemu ya eneo ibaki katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa ajili ya kazi ambayo ilikuwa inaifanya hapo awali.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sasa hivi kinachofanyika, Kamati ya Mawaziri tulikaa na Mheshimiwa Waziri ikaundwa tume maalum ambayo inafanya hiyo tathmini na baada ya hiyo tathmini kukamilika sisi tutakwenda katika eneo hilo kwenda kutoa maamuzi ya mwisho kwa ajili ya wananchi. Kwa hiyo, hiyo ndio kazi kubwa ambayo imefanyika.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Katika Jimbo langu la Manyoni Magharibi vitongoji ambavyo viko underline havidi vitano.
Je, Serikali iko tayari sasa kutoa jibu la uhakika kwamba vitongoji katika Jimbo langu navyo vitapatiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye swali la msingi tunatafuta mbinu mbadala ambayo itatuwezesha kupata mradi utakaofikia vitongoji 15 vilivyo underline na visivyo underline kwenye Majimbo yote.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi hii naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko dhamira ya Serikali ya kutoa ajira kwa vijana hasa kupitia vitalu nyumba, lakini vitalu nyumba hivi ni ghali sana. Je, Serikali iko tayari sasa kuweka ruzuku katika vitalu nyumba ili vijana wengi waweze kujiajiri kupitia eneo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Massare, kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumekuwa na programu ya kutoa elimu kwa ajili ya vijana kujifunza utengenezaji wa vitalu nyumba na tumekwishakufanya katika Halmashauri zaidi ya 82 na katika hayo maeneo ilikuwa wajibu wa kwanza ni kuhakikisha kwamba elimu inatolewa, lakini pia fedha na gharama zote zinaratibiwa na Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan kupitia ofisi ya Waziri Mkuu. Ni kweli kitalu nyumba kimoja kilikuwa kinagharimu zaidi ya karibia shilingi milioni 12, baada ya kuliona hilo na kwa ushauri mzuri wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria na muuliza swali Mheshimiwa Massare akiwa mjumbe tulitembelea Zanzibar na tuliweza kuona kwamba kuna uwezekano wa kutengeneza vitalu nyumba bila kutumia mabomba ya chuma na kutumia tu vitu vya asili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumekwishakuanza kuwa-engage wataalam kuweza kutusaidia zaidi namna gani watashusha gharama na kutafuta wadau wengine ambao watasaidia katika kuweza kuwapa mikopo vijana hawa katika maeneo haya. Kwa kweli eneo hili limeonekana linapokelewa vizuri na vijana, tutahakikisha kwamba kwa ushirikiano na ushauri ambao mnautoa tutaufanyia kazi kila wakati. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana na ninashukuru sana kwa majibu mazuri ya Serikali ambayo yana dhamira njema ya kuunganisha Mikoa ya Singida na Mbeya kwa barabara ya kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, sasa kwa maelezo yake Mheshimiwa Naibu Waziri; ni lini sasa huyu mkandarasi atafika Itigi ili wananchi nao waanze kufurahia matunda mazuri ya nchi yao?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mkoa wa Singida unaunganishwa na Mkoa wa Simiyu kwa barabara ya vumbi kupitia Daraja la Sibiti. Je, ni lini sasa na barabara hii nayo itaweza kuanza ujenzi wa kiwango cha lami? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza Serikali inapokea pongezi za Mheshimiwa Mbunge kwa kuanza ujenzi wa barabara hii. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wakati nakuja hapa Bungeni tayari mkandarasi wako wanasainiana mkataba na mara baada ya kufanya kazi hii naamini mkandarasi ataanza kukusanya vifaa ili kuweza kwenda kuanza hii kazi. Kwa sababu baada ya kusaini mkataba kazi inayofuata ni mobilization na kuanza kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa swali lake la pili la kuunganisha Mkoa wa Singida na Simiyu; barabara hii aliyoitaja ambayo inapita Daraja la Sibiti tayari imeshakamilishwa kwa kufanyiwa usanifu wa kina. Daraja limeshajengwa; nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pia kwamba katika mwaka huu wa fedha tumeongeza kilometa za kujenga barabara za lami ambazo zinaingia kwenye Daraja la Sibiti mpaka kilometa 25. Na Serikali katika bajeti inayokuja nina hakika tutaanza kwa awamu kujenga vipande vya barabara za lami ili kuunganisha Mikoa ya Singida na Simiyu kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi hii; kwa kuwa halmashauri nyingi hazina zimamoto, je, Serikali ipo tayari kujipanga upya sasa badala ya kutoka katika sehemu moja za Wilaya na Manispaa na Majiji kwenda katika Halmashauri zetu au kukasimu madaraka ya zimamoto katika Halmashauri ili kuweka wigo mpana wa namna ya kuzima moto katika maeneo yetu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahaya Massare, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kama nilivyosema kwenye jibu la msingi zipo halmashauri ambazo hazina kabisa huduma hizo, lakini ipo mikoa pia ambayo haina huduma hizo, ndiyo maana tukasema kulingana na mipango yetu na bajeti tutaanza na mikoa ambayo haina kabisa huduma za zimamoto na ukoaji tukiendelea kuimarisha uwezo huo kwenye mamlaka kubwa kama manispaa, miji na majiji baadaye tutaendelea kupanua huduma hizi kwenda Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo zipo vijijini. Nashukuru.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, iko dhamira ya Serikali ya kujenga vyuo hivi vya VETA katika Halmashauri zetu.
Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Halmashauri ya Itigi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Massare, Mbunge wa Itigi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza tufanye marekebisho, vyuo hivi havijengwi kwenye Halmashauri, vyuo hivi vinajengwa katika Wilaya. Kwa hiyo, zipo Wilaya ambazo zina Halmashauri zaidi ya moja, kwa hiyo, naomba nifanye marekebisho madogo kwenye eneo hilo kwamba hatujengi kwenye Halmashauri, lakini tunajenga katika Wilaya. Kwa hiyo, nimuonde wasiwasi Mheshimiwa Mbunge katika Wilaya ya Itigi napo vilevile tutafikia eneo hili kuhakikisha kwamba tunajenga chuo katika eneo hilo kwa sababu ni Wilaya muhimu kujengewa chuo.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, ni lini Serikali itapeleka vifaatiba katiba Halmashauri ya Itigi ambapo tumejenga zahanati na vituo vya afya lakini vifaa tiba na watumishi ni haba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Katika mwaka wa fedha uliopita, Halmashauri ya Itigi pia imepata vifaatiba, pia mwaka huu wa fedha, bajeti hii ambayo inatekelezwa, tutapeleka vifaatiba na fursa za ajira zitakapojitokeza, tutahakikisha tunatoa kipaumbele kwa watumishi ili Halmashauri ya Itigi iweze kupata huduma bora za afya. Ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ipo dhamira ya Serikali ya kupeleka umeme vijijini kote na umeme kufika maeneo ya mbali kabisa kutoka Mkoa wa Singida ambako ndio sub-station kubwa ilipo eneo la Rungwa, lakini umeme unafika ukiwa faint na Serikali ilikuwa na dhamira ya kujenga kito cha kupoza umeme kwa maana ya sub-station katika eneo la Mitundu. Je, Serikali inaanza lini kujenga kituo cha kupoza umeme Mitundu, ili kusaidia wananchi, ili waweze kujiwezesha na viwanda vidogo vidogo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Massare, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli mpango huo upo, na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunatafuta fedha na pili, mchakato huo wa upatikanaji wa fedha ukikamilika basi tutaanza kujenga kituo hiki cha kupoza umeme, ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni juzi tu tumepitia Sheria ya Bima ya Afya, je, katika sheria hii, ita-consider mtoto ambaye anazaliwa kwa kadi ya mama yake kutumia angalau kwa miezi mitatu wakati wazazi wanajipanga kumtengenezea bima huyu mtoto aliyezaliwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili; Serikali ilishawahi kutoa tamko kama hili kwamba imeelekeza hospitali, wazazi wanapojifungua watumie bima za mama zao lakini hili halifanyiki. Nini kauli nyingine ya Serikali kwa sababu jambo hili linajirudia, Serikali inasemaje katika hili?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kujibu maswali mawili mazuri ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Moja; anasema je, sheria iliyopo sasa ambayo tulipitisha juzi kwamba inaenda ku-accommodate, labda nisisitize tu, kwamba siyo tu sheria tuliyoipitisha juzi kuanzia sasa ni kwamba, watoto wanaozaliwa hospitali ambao wazazi wao wana kadi zao za bima, watibiwe na wapate huduma kwa sababu ambazo nimezielezea hapa inawezekana ku-track vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, akaseme je, tunafanya nini kuhusu ambao sasa wanakwenda kwenye vituo vyetu na tayari tulitoa tamko lakini bado hayo matatizo yanaendelea. Waheshimiwa Wabunge wenzangu ninawaomba pia nawaasa Watanzania wenzangu na ninawaasa Watumishi wa Mfuko wa Bima ya Afya na hospitali zote Tanzania kwamba sasa hivi tukisikia hilo na likitokea na Mheshimiwa Mbunge ukikutana na kitu kama hicho naomba utuletee na mtu huyo ambae amesababisha hayo atachukuliwa hatua mara moja palepale. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Halmashauri ya Itigi haijachimbiwa visima katika bajeti mbili zilizopita na gari la Mkoa wa Singida limekuwa likienda huku huku mara Msomera mara wapi? Sasa lini Serikali itakwenda kuchimba visima katika Halmashauri ya Itigi, katika Jimbo langu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahaya Massare, Mbunge wa Itigi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hili eneo ambalo linatakiwa likachimbwe visima lipo kwenye mpango na kwa sababu gari lipo pale Mkoani tunarajia likimaliza upande umoja liliopo litakwenda katika maeneo haya na maeneo yote ambayo yanatakiwa kuchimbwa visima, visima vitachimbwa.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Polisi waliopo Itigi wana mgogoro na Shirika la Reli ambalo linajiimarisha sasa na Wizara yake imekuwa na ahadi nyingi kujenga Kituo cha Polisi Itigi, Mheshimiwa Naibu Waziri, mara nyingi tumeongea kuhusu hili. Je, ni lini sasa mtaenda kujenga Kituo cha Polisi kwa ajili ya Polisi wazuri ambao wapo katika Halmashauri ya Itigi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua na nimshukuru kwa kweli Mheshimiwa Mbunge, kwa namna anavyofuatilia umuhimu wa kuwa na Kituo cha Polisi chenye hadhi ya Wilaya eneo la Itigi. Nimuahidi tu kwamba kwa vile Eneo la Itigi tayari tumeliweka kwenye mipango yetu avumilie pale Wizara ya Fedha itakapokuwa imetupatia fedha kwa ajili ya kujenga Kituo hicho cha Polisi tutakuwa tumemaliza kabisa mgogoro huo. Nashukuru. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali hili niliuliza Bunge la Kumi na Moja na majibu ya Mheshimiwa Omary Mgumba yalikuwa hivi hivi kwamba wataenda, akiwa Naibu Waziri wa Wizara hii. Sasa leo na mwaka huu kuna El-nino, wanatuambiaje watu wa Itigi kwamba tufe kwa sababu Serikali haitimizi ahadi? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Halmashauri ya Itigi ina scheme moja tu ya umwagiliaji na ambayo haifanyi kazi vizuri. Je, Serikali inaweza kuniahidi mbele ya Bunge lako Tukufu, kwamba wataenda kutekeleza angalau mradi mmoja wa scheme ya umwagiliaji kwa ajili ya wananchi wa Itigi wakati Wizara hiyo imepata fedha nyingi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Massare, Mbunge wa Manyoni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haina nia ya kuona wananchi wa Itigi wanakufa kwa sababu ya mafuriko. Jukumu letu sisi kama Wizara ya Kilimo ni kuhakikisha kwamba tunawajengea miundombinu itakayowasaidia wao kwenye kulima, lakini vilevile itaongeza pato ya Halmashauri ya Mji wa Itigi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kilichoahidiwa katika Bunge la Kumi na Moja na ambacho hakikutekelezwa, ilikuwa ni kwa sababu ya changamoto za kifedha. Sasa hivi fedha tunayo, ndiyo maana mwaka huu tumetenga fedha na tunakwenda kulifanyia kazi. Kwa hiyo, nimwondoe shaka Mbunge kwamba, jambo hilo litafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ujenzi wa Mradi Halmashauri ya Itigi iko sehemu ya mipango yetu, kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Halmashauri ya Itigi ina skimu moja tu na haifanyi kazi vizuri. Je, Serikali sasa ipo tayari kutuongezea angalau skimu nyingine?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo tayari kuongeza skimu katika Halmashauri ya Itigi na ipo katika mipango yetu. Ukiangalia katika mpango wa Tume ya Taifa, Itigi kuna schemes ambazo zimeongezeka pale, ahsante.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, naomba niulize Serikali maeneo ya kwangu maeneo ya Muhanga, Gurungu, Turieli na Mnazi Mmoja pamoja na Kitanula hakuna kabisa mawasiliano, je, Serikali ipo tayari kupeleka minara katika maeneo haya ili wananchi nao waweze kufaidi matunda ya nchi yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Yahaya kuwa tupo tayari kuleta mawasiliano maeneo haya na tayari michakato ya kuja kufanya tathmini tupo mwishoni kuja kufika maeneo haya yote.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Wilaya ya Manyoni ina majimbo mawili. VETA inayoendelea kujengwa katika Manyoni iko katika Jimbo la Manyoni Mashariki. Unawaambiaje watu wa jimbo langu eneo la Itigi kuhusu ujenzi wa shule ambayo mmeitaja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nikijibu swali dogo la Mheshimiwa Massare ni kwamba Mheshimiwa Massare anajua na tulishazungumza suala hili na alikuja ofisini na akaangalia orodha ya shule zitakazokwenda kujengwa za ufundi na Wilaya ya Manyoni, ilikuwa Manyoni imekosewa, Manyoni Kaskazini na Manyoni Kusini tukarekebisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Massare, shule yake ya Ufundi ipo, tumeshafanya marekebisho mwanzoni kulikuwa na typing error. Shule ile itakwenda kujengwa katika jimbo lake kama vile alivyoshauri yeye mwenyewe na kazi hii itaanza Julai mwaka ujao wa fedha. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, Serikali ilitupa karatasi tukajaza vituo vya kimkakati, je, ni lini vituo vya Halmashauri ya Itigi vitaletewa fedha ili tujenge kituo cha kimkakati cha afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Waheshimiwa Wabunge waliorodhesha maeneo ya kujenga vituo vya afya vya kimkakati ikiwemo katika Halmashauri ya Manyoni pale Itigi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kujenga vituo hivyo vya afya.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, gari lililonunuliwa na Serikali na Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kuchimba maji katika mikoa yote ikiwemo Mkoa wa Singida, magari hata hayatulii sehemu moja na usimamizi wake umekuwa haueleweki. Je, Serikali imejipangaje ili miradi ya maji katika vijiji na katika maeneo yetu iweze kufanyika vizuri?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Massare, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan Suluhu Hassan aliagiza magari ya kuchimbia visima na hii ilikuwa ni fursa kubwa sana kwa Watanzania. Kwa hiyo nitumie fursa hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maji, kuwaelekeza ma-RM wote nchini kuhakikisha kwamba haya magari hayakupelekwa kwa ajili ya kwenda ku-park, yamepelekwa kwa ajili ya kwenda kufanya kazi ili Watanzania wapate maji na nitafuatilia ili kuona utekelezaji unaendaje. Ahsante sana.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali lakini nina maswali madogo mawili. Swali la kwanza; uchimbaji wa visima katika Halmashauri yangu ya Itigi katika Wilaya ya Manyoni, maeneo ya Kayui na Mtakuja wamechimba, lakini maji hamna kabisa. Je, Serikali iko tayari sasa kuajiri wataalam wazuri wa surveyors ambao kabla ya uchimbaji waweze kutuainishia kabisa kwamba hapa tukichimba tutapata maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali ipo tayari sasa kwenda kuchimba kisima katika eneo la Kalangali ambapo kuna shida kubwa na tunajenga sasa hivi Sekondari ya Ufundi ya Amali?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza sana Mheshimiwa Massare kwa kazi kubwa anayoifanya na ufuatiliaji wa miradi ndani ya Jimbo lake. Kama ambavyo nimejibu katika jibu la msingi, baada ya kuchimba visima tunaanza kupima wingi wa maji kwa maana ya pumping test na baada ya kujiridhisha maji hayo hayatokuwa yanatosha, basi tutaangalia eneo lingine. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Wizara ya Maji inao wataalam na vifaa vya kutosha kuhakikisha kwamba kazi hii tunaifanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande swali la pili kuhusu Kalangali, ninatumia fursa hii kumwelekeza RM Mkoa wa Singida, ahakikishe anaangalia kipaumbele cha Mheshimiwa Mbunge kuhakikisha kwamba, akaanze na eneo hili ili liweze kuhakikisha kwamba lina upatikanaji wa maji ambapo itaweza kusaidia katika maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, Halamshauri ya Itigi, Kituo cha Polisi Itigi, Polisi wa Itigi wanakaa kwenye majengo ya Reli na Reli wanajiimarisha pia yamechakaa sana.
Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kujenga kituo cha polisi katika Halmashauri ya Itigi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Massare kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema tunajenga vituo vya polisi kwa kutumia bajeti ya Serikali, Mfuko wa Tuzo na Tozo lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama kituo chake mwaka wa fedha huu hakipo basi tutakitengea fedha kwenye mwaka wa fedha 2025/2026 ili tujenge kituo cha polisi katika eneo lake la Itigi, ahsante sana.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, mvua za El-Nino zimenyesha kwa kiwango kikubwa katika Halmashauri ya Itigi, Barabara ya Itigi – Damweru haipitiki kabisa, ilikuwa imejaa maji na sasa maji yameanza kukauka, lakini Barabara ya Kalangali kwenda Tulieni imeharibika kabisa haipitiki.
Je, Serikali iko tayari kutuongezea pesa za kutosha kurudisha miundombinu hii ili watu wafanye maisha yao ya kawaida?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa barabara zetu hizi na hasa za wilaya na kama nilivyotangulia kusema kipaumbele cha Serikali katika kipindi hiki ni kuhakikisha inaunganisha mawasiliano ya barabara kwenye maeneo ambayo mawasiliano yamekatika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itatafuta fedha na itatumia taratibu za dharura kuhakikisha inaunganisha mawasiliano kwenye maeneo ambayo yameathirika sana na mvua na mawasiliano yamekatika katika kipindi hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kwa uendelevu Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu hii ili iweze kuwa miundombinu imara ambayo inapitika kwa misimu yote na mwaka mzima.
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Serikali imedhamiria kupeleka umeme vijijini kote nchini ikiwemo kwenye jimbo langu ambako vijiji vingi vinapatiwa umeme. Ni lini mtaanza kutekeleza kupeleka umeme katika vitongoji 15 katika Jimbo la Manyoni Magharibi, Halmashauri ya Itigi, ambavyo tulileta hapa?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa swali kuhusu vitongoji 15. Kama nilivyosema mapema wiki hii, tupo katika hatua za mwisho za kumalizia, ili kuweza kuwapata wakandarasi katika maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, suala la kupeleka umeme kwenye vitongoji, ambako tuko mwishoni kumalizia, ni suala ambalo ni la kipaumbele kwenye Serikali ya Awamu ya Sita. Ndiyo maana hata mwaka wa fedha unaokuja, 2025, tumetenga fedha nyingine, kwa ajilai ya kuanza mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji 20,000 ambapo kwa mwaka wa fedha 2025 tutapeleka umeme kwenye vitongoji 4,000. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tunalifanya jambo hili kwa kasi kuhakikisha kwamba tunaanza kupeleka umeme vitongojini. Kwa jimbo la Mheshimiwa Mbunge, tutahakikisha pia kazi inaanza na vitongoji 15 vinapatiwa umeme huku tukisubiri mradi wa 2024/2025 ambao unaanza kupeleka umeme kwenye vitongoji 20,000, ahsante. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Wilaya ya Manyoni ina majimbo mawili. VETA inayoendelea kujengwa katika Manyoni iko katika Jimbo la Manyoni Mashariki. Unawaambiaje watu wa jimbo langu eneo la Itigi kuhusu ujenzi wa shule ambayo mmeitaja? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nikijibu swali dogo la Mheshimiwa Massare ni kwamba Mheshimiwa Massare anajua na tulishazungumza suala hili na alikuja ofisini na akaangalia orodha ya shule zitakazokwenda kujengwa za ufundi na Wilaya ya Manyoni, ilikuwa Manyoni imekosewa, Manyoni Kaskazini na Manyoni Kusini tukarekebisha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Massare, shule yake ya Ufundi ipo, tumeshafanya marekebisho mwanzoni kulikuwa na typing error. Shule ile itakwenda kujengwa katika jimbo lake kama vile alivyoshauri yeye mwenyewe na kazi hii itaanza Julai mwaka ujao wa fedha. (Makofi)
MHE. YAHAYA O. MASSARE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza; umeme ni maisha na sasa watu wanatumia umeme kufanya mambo yao yaende vizuri, sasa lakini kutoka shilingi 320,000 kwa vijiji ambavyo ni vidogo, ambavyo wamevionesha kama ni vijiji mji.
Je, Serikali ipo tayari sasa vile vijiji vidogo vilivyokusanyika pamoja kama vijiji vya Itigi ambavyo ni vijiji saba kwa pamoja, Kijiji cha Mitundu, viwalipe 27,000?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; wananchi wanapolipa hizo gharama za kuunganishiwa umeme Serikali inachukua muda mrefu sana. Je, Serikali inasemaje, ni muda gani mahsusi, mtu akishalipia umeme anakuwa anajua kwamba atafungiwa mita? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maswali mawili ya nyongeza.
Swali la kwanza kuhusiana na gharama kwenye maeneo ya vijiji mji, Serikali tumeshaanza kufanya mapitio kwenye maeneo ambayo tunadhani yanatakiwa kupunguziwa gharama kutoka 320,960 hadi shilingi 27,000.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa tumeshaainisha maeneo 1,500 na kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge hiki Kijiji alichokisema na vijiji vingine vya Itigi pia vimepitiwa. Tutaenda kufanya mapitio zaidi ili kuona kama hicho Kijiji ambacho Mheshimiwa Mbunge amekitaja kinaweza kuingia katika mapitio haya.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na kuunganisha umeme tunaendeleza kuboresha huduma kuhakikisha wananchi wanaunganishiwa umeme kwa wakati. Suala la kuunganisha umeme lina sehemu mbili yaani mwananchi kufanya wiring na sisi kisha kupeleka huduma ya kuunganisha umeme. Tuendelee kuwasisitiza wananchi pale ambapo huduma ya umeme inafika kwenye maeneo yao waweze kufanya wiring kwa wakati na sisi tutaendeleza kuboresha huduma ili kuhakikisha huduma ya kuunganisha umeme kwa wananchi inakuwa ya haraka na ya uhakika, ahsante.