Primary Questions from Hon. Athumani Almas Maige (37 total)
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Kilimo cha tumbaku katika Mkoa wa Tabora katika Jimbo la Tabora Kaskazini kinakabiliwa na matatizo ya pembejeo, madeni ya wakulima, viongozi wabovu wa vyama vya ushirika, ukosefu wa wanunuzi, wanunuzi watatu kupanga bei, matatizo haya yanachangiwa na mapungufu ya Sheria ya Ushirika ya Tumbaku:-
(a) Je, ni lini Serikali italeta Sheria za Ushirika na Tumbaku katika Bunge lako tukufu ili zifanyiwe marekebisho?
(b) Kilimo cha tumbaku ni kazi ngumu inayoathiri afya za wakulima. Je, kwa nini Serikali kupitia Bodi ya Tumbaku isiwaagize wanunuzi kuwalipa wakulima posho kwa kufanya kazi inayoathiri afya zao?
(c) Je, ni lini Serikali itatafuta wanunuzi wengine wa tumbaku hasa kutoka China ili kuondoa ukiritimba wa wanunuzi watatu wa tumbaku waliopo sasa nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia mapendekezo ya wadau Bunge lako tukufu lilifanya mabadiliko ya Sheria ya zamani ya Ushirika Namba 20 ya mwaka 2003 hivi karibuni inakuja na sheria mpya ya ushirika namba sita ya mwaka 2013 ambayo utekelezaji wake umeanza. Aidha, endapo kutakuwa na haja ya kufanya tena mapitio au marekebisho ya sheria hiyo kwa kuzingatia maoni ya wadau Serikali haitasita kufanya hivyo. Kuhusu Sheria ya Tumbuka Na. 24 ya mwaka 2001 Wizara kwa sasa inapitia upya ikiwa ni pamoja na kukusanya maoni ya wadau ili ikilazimu iletwe Bungeni kwa nia ya kufanyiwa marekebisho kulinga na hitaji la sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa hakuna sheria, kanuni au utaratibu wowote unaolazimaisha makampuni ya ununuzi wa tumbaku kulipa posho au fidia kwa wazalishaji Serikali inawashauri wadau wa tumbaku kupitia baraza lao kujadili suala hili ili kama wakiona umuhimu wa kutungiwa sheria Serikali ianze kulifanyia kazi.
Aidha, kwa sasa vifaa vya kinga kwa maana ya gloves, gum boots na mask kwa wakulima wa tumbaku vinaingizwa kwenye gharama za uzalishaji wa tumbakuhivyo kuwa sehemu mjengeko wa bei. Wakulima au Vyama vya Msingi wanashauriwa kununua vifaa hivi mara wapokeapo malipo baada ya kuuzwa kwa tumbaku yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikifanya jitihada za dhati za kuongeza ununuzi wa zao la tumbaku ili kuongeza ushindani na hatimaye kuwezesha wakulima kupata bei nzuri. Aidha, kwa sasa kuna jumla ya makampuni manne ya ununuzi wa tumbaku nchini ambayo ni Alliance One Tabacco Tanzania Ltd., Tanzania Leaf Tobacco Company Ltd., Premium Active Tanzania Ltd. pamoja na Japanese Tobacco International Leaf Services.
Mheshimiwa Naibu Spika, licha ya uwezo wa makampuni haya nchini, Serikali bado inaendelea na jitihada za kutafuta wanunuzi wengine wa tumbaku kutoka nchini China na Vietnam ambao baadhi yao wameonyesha nia ya kununua tumbaku ya Tanzania.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Sehemu kubwa ya Jimbo la Tabora Kaskazini, Uyui haina maji chini ya ardhi na hivyo wananchi hawawezi kupata maji kwa kuchimba visima. Wananchi wanaipongeza Serikali kwa kubuni mradi wa kuleta maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria kupitia Shinyanga, Kahama, Nzega mpaka Isikizya na maeneo mengine ya Mkoa wa Tabora.
(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi huo ili wananchi wa jimbo la Tabora Kaskazini katika vijiji vya Isikizya, Upuge, Majengo na Kanyenye wapate huduma ya maji?
(b) Kwa kuwa bomba hilo la maji litatoa maji kwa umbali wa kilometa 25 kuwafikia wananchi wachache. Je, Serikali haioni kuna sababu ya kuanzisha mradi wa kuchimba mabwawa na kukinga maji ya mvua kama chanzo kingine cha maji kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naona baada ya kupitisha bajeti jana watu wameridhika na maji.
Kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliai naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea na utekelezaji wa mradi wa maji wa kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka katika Miji ya Tabora, Igunga, Nzega na Sikonge pamoja na vijiji 89 vilivyopo ndani ya kilometa 12 kwa kila upende kutoka bomba kuu, vikiwemo vijiji vya Isikizya, Upuge na Majengo. Kwa sasa taratibu za kupata wakandarasi wa ujenzi mradi huo zinaendelea ambapo ujenzi wa mradi unategemewa kuanza mwaka wa fedha 2016/2017. Aidha, kijiji cha Kanyenye utekelezaji wake utajumuishwa katika mipango ya Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuendelea kuboresha huduma ya maji Serikali itaendele akutenga fedha pamoja na kutafuta vyanzo vingine vya maji ikiwemo ujenzi wa mabwawa na kuweka utaratibu kupitia Halmashauri husika kuvuna maji ya mvua kwa maeneo yote ambayo hayatapitiwa na mradi pamoja na yale yenye shida kubwa ya maji.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Makao Makuu ya Wilaya ya Uyui yapo Isikizya eneo ambalo halina miundombinu, nyumba za kuishi na huduma rafiki kwa wafanyakazi. Shirika la Nyumba la Taifa limejenga nyumba Isikizya na lilipendekeza kuuza nyumba hizo kwa Halmashauri ya Uyui na kumaliza malipo ndani ya miaka mitatu lakini Halmashauri haina uwezo wa kumaliza malipo ndani ya miaka mitatu. Hivyo wafanyakazi wa Halmashauri wanaendelea kuishi katika nyumba za kupanga Mjini Tabora:-
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuchangia ununuzi wa Nyumba za Shirika la Nyumba (NHC) ili wafanyakazi wa Halmashauri ya Uyui wahamie Isikizya?
(b) Shirika la Nyumba ni wadau wa maendeleo ya makazi na kwa kuwa Serikali ina nia ya kusaidia uanzishwaji wa Makao Makuu ya Wilaya ya Uyui, je, kwa nini Serikali isishawishi Shirika la Nyumba kuongeza muda wa kuuza nyumba zake kutoka miaka mitatu hadi kumi ili kuwezesha Halmashauri kulipa polepole?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016, Halmashauri ya Wilaya ya Tabora/Uyui ilitenga shilingi milioni 174.6 kwa ajili ya ununuzi wa nyumba tatu za watumishi ambazo zimejengwa na Shirika la Nyumba la NHC ili watumishi wa Halmashauri hiyo wahamie Isikizya yalipo Makao Makuu ya Halmashauri. Vilevile katika mwaka wa fedha 2016/2017, zimetengwa shilingi milioni 150 kutokana na mapato ya ndani kwa ajili ya ununuzi wa nyumba zaidi za watumishi.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa kifungu 14 (1) cha Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimepewa mamlaka ya kukopa katika taasisi mbalimbali za ndani au kuingia mikataba ya
NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT)
8
manunuzi baada ya kupata kibali cha Waziri mwenye dhamana. Hata hivyo, katika kufanya hivyo Halmashauri zinapaswa kuzingatia uwezo uliopo katika kurejesha mkopo husika. Hivyo, Halmashauri inashauriwa kununua nyumba za NHC kwa kuzingatia uwezo uliopo katika bajeti iliyotengwa kwa mwaka 2016/2017.
MHE. ALMASI A. MAIGE aliuliza:-
Sehemu kubwa ya Jimbo la Tabora Kaskazini, Uyui halina maji chini ya ardhi na hivyo wananchi hawawezi kupata maji kwa kuchimba visima, hivyo Serikali ikabuni mradi wa kuleta maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria kupitia Shinyanga, Kahama, Nzega mpaka Isikizya na maeneo mengine ya Mkoa wa Tabora.
(a) Je, ni lini Serikali itatekeleza mradi huo ili wananchi wa Jimbo la Tabora Kaskazini katika vijiji vya Isikizya, Upuge, Majengo na Kanyenye wapate huduma ya maji?
(b) Kwa kuwa bomba hilo la maji litatoa maji umbali wa kilometa 25 kushoto na kulia na kuwafikia wananchi wachache; je, Serikali haioni kuna sababu ya kuanzisha mradi wa kuchimba mabwawa na kukinga maji ya mvua kama chanzo kingine cha maji kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa Mradi wa Kutoa maji Ziwa Victoria kupeleka katika Miji ya Tabora, Igunga, Nzega na Sikonge pamoja na vijiji 89 vilivyopo ndani ya kilometa 12 kwa kila upande kutoka bomba kuu. Kwa sasa taratibu za kupata wakandarasi wa ujenzi wa mradi huo zinaendelea ambapo ujenzi wa mradi unategemewa kuanza mwezi Disemba, mwaka huu wa 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, bomba kuu la kutoa maji Ziwa Victoria litahudumia vijiji vilivyopo ndani ya kilometa 12 kila upande. Aidha, Serikali itaendelea kubuni vyanzo vingine vya maji ikiwemo ujenzi wa mabwawa ya uvunaji maji ya mvua na uchimbaji wa visima virefu ambapo katika mwaka wa fedha 2016/2017 imetenga kiasi cha shilingi milioni 754.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika vijiji vya Halmashauri ya Uyui.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Kufunguka kwa mawasiliano ya barabara za Tabora, Nzega, Tabora - Manyoni na Tabora - Kigoma kumeleta maendeleo ya kukua kwa Mji wa Tabora na kuongezeka shughuli za uwekezaji na ujenzi wa nyumba za makazi na biashara:-
Je, ni lini Serikali italeta Msajili wa Hati za Viwanja Tabora ili aweze kuidhinisha hati za viwanja kwa wakazi na wawekezaji kwa kuwa kwa sasa huduma hizo hazipo Mkoani Tabora?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Msajili wa Hati Msaidizi ameshateuliwa kwa kuzingatia Kifungu Na. 4 cha Sheria ya Usajili wa Ardhi, Sura Na. 334. Tangazo la uteuzi lilitolewa katika Gazeti la Serikali la tarehe 16, Desemba, 2016, Toleo Na. 52.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Msajili Msaidizi ameshawasili kituoni. Aidha, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu mpaka sasa Wizara imeshapeleka Wasajili wa Hati katika Ofisi zote za Kanda. Rai yangu kwa Halmashauri zote nchini ni kuongeza kasi ya upimaji, upangaji na umilikishaji wa ardhi ili wananchi waweze kupatiwa hati za umiliki wa maeneo yao.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Hivi karibuni wakati Mheshimiwa Rais akifungua majengo ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PPF aliongelea wazo la kuunganisha Mifuko ya Jamii iliyopo sasa NSSF, PPF, GEPF na LAPF na kufanya ama mifuko miwili au hata mmoja tu kama ilivyo katika nchi nyingine.
(a) Je, mchakato huu sasa umefikia wapi?
(b) Je, Serikali ina malengo ya kuunda mifuko mingapi baada ya muungano huo wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athumani Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ina jumla ya Mifuko Saba ya Hifadhi ya Jamii. Kati ya mifuko hiyo, mitano ni ya pensheni ambayo ni NSSF, LAPF, PSPF, GEPF na PPF, mmoja ni wa fidia kwa wafanyakazi na mmoja ni wa bima ya afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzishwa kwa mifuko mitano ya pensheni hapa nchini kumetokana na historia ya mfumo wa kiuchumi ambayo nchi yetu imepitia tangu uhuru mpaka sasa. Mifuko hii ilipokuwa inaanzishwa ililenga kutoa huduma za hifadhi ya jamii katika sekta mbalimbali kama vile watumishi wa umma, mashirika ya umma, polisi na sekta binafsi.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa kuunganisha Mifuko ya Jamii umefikia hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa tathmini na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (actuarial evaluation) ambayo pamoja na mambo mengine imetoa mapendekezo kuhusu namna bora na mambo muhimu ya kuzingatiwa katika zoezi la kuunganisha mifuko. Aidha, wadau mbalimbali wameshirikishwa wakiwemo vyama vya waajiri na wafanyakazi ili kutoa maoni na mapendekezo Serikalini kwa maamuzi. Kimsingi Serikali imefikia hatua nzuri ya mchakato huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mpaka sasa Serikali haijafanya uamuzi rasmi wa idadi ya mifuko itakayobaki baada ya kuiunganisha mifuko iliyopo hivi sasa. Hata hivyo, Serikali itazingatia maoni na ushauri wa wadau ili kufanya uamuzi muafaka wa idadi na aina ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inayotakiwa kuwepo kwa kuzingatia uwepo na mahitaji ya sekta binafsi na sekta ya umma.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Mahakama ya Mwanzo katika Kata ya Upuge, Wilaya ya Uyui, imetelekezwa zaidi ya miaka kumi na kusababisha miundombinu yake kuanza kuharibika.
• Je, ni kwa nini Mahakama hii imetelekezwa?
• Je, ni kwa nini majengo ya Mahakama hiyo yasitumike na Idara nyingine za Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA - K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimekuwa nikisema hapa Bungeni, uhaba na uchakavu wa majengo ni moja ya changamoto zinazokabili Mahakama katika sehemu nyingi nchini. Wizara yangu ipo bega kwa bega na Mahakama ya Tanzania katika kukabiliana na hali hii ikiwa ni pamoja na changamoto nyingine zinazoikabili Mahakama ukiwepo upungufu wa watumishi.
Mheshimiwa Spika, ni kweli jengo la Mahakama ya Mwanzo Upuge ni chakavu lakini halijatelekezwa kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge. Jengo hili linaonekana kutelekezwa kutokana na ukweli kwamba siku za nyuma lilikuwa halitumiki. Hata hivyo, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa jengo hilo kwa sasa linafanya kazi, yupo Hakimu na huduma za kimahakama zinatolewa kama kawaida. Kwa sasa tathmini inafanyika ili kulifanyia matengenezo jengo hilo kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kazi.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Sekta binafsi ya ulinzi ilianzishwa mwaka 1980 ikiwa na kampuni mbili tu na ikiwa haina miongozo yoyote.
• Kwa kuwa sasa sekta hii ina kampuni zaidi ya 850 nchini kote, je, Serikali italeta Sheria ya Sekta Binafsi ya Ulinzi ili pia kuanzisha mamlaka ya sekta binafsi ya ulinzi?
• Je, Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) ina mpango gani wa kushirikiana na Chama cha Sekta Binafsi ya Ulinzi ili kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athumani Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba sekta ya ulinzi binafsi imekuwa sana hapa nchini na kwamba Serikali inatambua umuhimu wa sekta hii na ilishaanza maandalizi ya kuwasilisha Muswada wa Sheria ya Makampuni Binafsi ya Ulinzi. Katika kufanikisha jambo hili Wizara ya Mambo ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliandaa walaka kupeleka Baraza la Mawaziri kwa hatua za awali. Ili kukamilisha hatua hii yanahitajika maoni ya wadau kutoka pande mbili za Muungano. Serikali imeweka utaratibu wa kupata maoni kutoka katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na mara yatakapopokelewa waraka huu utawasilishwa mapema iwezekanavyo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Inspekta Jenerali wa Polisi imekuwa ikishikiana na sekta binafsi ya ulinzi katika nyanja mbalimbali. Kwa mujibu wa Sheria ya Jeshi la Polisi na Polisi Wasaidizi Namba 322 Rejeo la mwaka 2002. Jeshi la polisi limekuwa likitoa mafunzo kwa makampuni binafsi ya ulinzi, kufanya ukaguzi kuchukua alama za vidole kwa watumishi, kutoa vitambulisho na kutoa ushauri kwa makampuni hayo ili kuboresha na kuhakikisha huduma ya ulinzi inatolewa katika viwango vinavyostahili.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Katika Kijiji cha Majengo, Kata ya Ikongolo, TASAF ilijenga bwawa kubwa la kukinga maji ya mvua kwa madhumuni ya umwagiliaji na matumizi ya vijiji vyote vinne vya Kata ya Ikongolo, lakini bwawa hili lilivuna maji kwa mwaka mmoja tu na kisha kwa masikitiko makubwa bwawa hilo lilipasuka kingo yake moja na maji yote yakatoka:-
(a) Je, wataalam wa Serikali wamegundua ni kwa nini bwawa hilo limepasuka kingo yake kuu?
(b) Kwa vile bwawa hilo lilileta shughuli nyingi za kiuchumi kwa wananchi kwa kilimo cha umwagiliaji, je, ni lini Serikali itaanza harakati za kuziba mpasuko uliotokea katika kingo za bwawa ili wananchi waendeleze shughuli zilizosimama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora kaskazini lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kubomoka kwa tuta (Embarkment) la Bwawa karibu na sehemu ya kupumulia (spillways) katika Kijiji cha Majengo kulitokana na athari za mvua nyingi zilizonyesha msimu wa mwaka 2013/2014.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa bwawa hilo, Serikali imeidhinisha shilingi milioni ishirini kwa ajili ya ukarabati wa bwawa hilo ambao utahusisha ujenzi wa njia ya kuchepusha maji (spillways). Fedha hizo zitatokana na ruzuku ya maendeleo kwa Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Barabara ya Tabora – Mambali – Bukumbi – Shitage - Tulole mpaka Kahama ipo katika mpango wa Serikali wa kujenga barabara za lami nchini:-
(a) Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza?
(b) Kumekuwa na mvutano wa wapi barabara hiyo ingepita baada ya kufika Mambali, mapendekezo ya Bodi ya Barabara ya Mkoa ni kuwa barabara hiyo ipite Bukumbi, Shitage, Tulole na kuunga Kahama; Je, Serikali inatoa msimamo gani baada ya mapendekezo hayo ya Bodi ya Mkoa wa Tabora?
(c) Je, ni lini kipande cha barabara hiyo kitachukuliwa na TANROADS?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ambayo ipo katika mpango wa kujengwa kwa kiwango cha lami ni ya Tabora – Mambali – Itobo - Kagongwa - Kahama yenye urefu wa kilometa 180. Barabara hii ipo katika hatua za mwisho za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambapo kazi ya usanifu inafanywa na Mhandisi Mshauri NIMETA Consult na inatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Julai mwaka 2018. Baada ya kazi ya usanifu kukamilika Serikali itatafuta fedha ili kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kupandishwa hadhi kwa barabara ya Mambali – Bukumbi - Shitage na Tulole tayari sehemu ya barabara ya Mambali hadi Bukumbi yenye urefu wa kilometa 28.5 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na TANROADS na sehemu ya Bukumbi - Mhulidede kilometa 24.7 imekasimiwa kufanyiwa matengenezo na TANROADS kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018.
Mheshimiwa Spika, sehemu ya Mhulidede – Tulole kilometa 21 imeanza kuhudumiwa na TANROADS kuanzia mwaka huu wa fedha 2017/2018 na kufanya barabara yote ya Mambali – Bukumbi – Mulidede - Tulole - Kahama kuhudumiwa na TANROADS. (Makofi)
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Halmashauri ya Wilaya ya Uyui inajulikana kwa jina la zamani la Tabora District Council (TDC) jina ambalo linagongana na jina la Manispaa ya Tabora (Tabora Minicipality). Wilaya kupitia Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa alileta maombi ya kubadili jina la Halmashauri kutoka Tabora District Council (TDC) na kuwa Halmashauri ya Uyui na Halmashauri imeomba kubadili jina la Jimbo la Tabora Kaskazini na Jimbo la uyui ikibeba jina la Wilaya na jina la eneo la kijiografia Uyui kwa sababu, hakuna tena Tabora Kaskazini, Kusini wala Magharibi:-
(a) Je, ni lini jina la Halmashauri litabadilishwa kuwa Halmashauri ya Uyui?
(b) Je, ni lini Jimbo la Tabora Kaskazini litaitwa Jimbo la Uyui?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Maige, naomba kwanza dakika moja tu nielezee furaha yangu; leo nimeamka saa 10:00 usiku kwa ajili ya kujiandaa kuja kujibu maswali, lakini furaha yangu kubwa ni kwa sababu Simba Sports Club baada ya kupata ubingwa sasa naamini Watanzania watapata wawakilishi kwenye michezo ya kimataifa ambao hawatatupa pressure kwa sababu vijana hawa wanajua kucheza vizuri sana mpira wa miguu, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya maelezo hayo…
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge a Tabora Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mhesimiwa Mwenyekiti, maombi yenye mapendekezo ya kubadili jina la Halmashauri ya Wilaya ya Tabora kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui sawa sawa na jina la Wilaya ya Uyui ambayo yamepitishwa na vikao vya kisheria vya Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Kamati ya Ushauri ya Mkoa yameshapokelewa na yako katika hatua za kupata ridhaa. Nawaomba wadau wote wa suala hili wawe na subira wakati Serikali inapomalizia mchakato huo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Ibara ya 75 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mapendekezo ya kubadili jina la jimbo yaliyoridhiwa na baraza, wilaya na mkoa yanatakiwa kuwasilishwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo ndio yenye mamlaka ya uamuzi. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Hivi karibuni Serikali kupitia JKT imeanzisha tena mafunzo ya vijana wa kujitolea na wale wa mujibu wa sheria waliomaliza kidato cha sita au kutoka vyuo hapa nchini.
• Je, ni kweli kuwa JKT wanachukua wanafunzi kwa mujibu wa sheria kutoka katika shule na vyuo vya Serikali tu?
• Je, Serikali haioni kuwa vijana kutoka shule na vyuo binafsi wanahitaji pia mafunzo muhimu ya uzalendo na kujiendeleza kiuchumi?
• Je, ni vijana wangapi kwa mujibu wa sheria kwa mwaka 2017/2018 wamechukuliwa na JKT katika shule na vyuo binafsi nchini?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wa mujibu wa sheria huchukuliwa moja moja kutoka shule za Serikali na binafsi bila kuhusisha vyuo. Vijana kutoka vyuo vya Serikali na binafsi hujiunga na mafunzo ya JKT kwa utaratibu wa kujitolea ambapo utaratibu wa kuwapata hupitia katika usaili unaofanyika ngazi za Wilaya na Mikoa ambapo unahusisha pia vijana wengine wenye sifa bila kujali shule aliyotoka.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaona umuhimu wa kuchukua vijana kutoka shule na vyuo binafsi kwa ajili ya mafunzo katika Jeshi la Kujenga Taifa, ndiyo maana uteuzi wa vijana unahusisha shule zote za Serikali na binafsi. Vijana ambao ni wahitimu wa vyuo vya Serikali au binafsi huingia JKT kwa utaratibu wa kujitolea kama nilivyosema awali.
c) Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana waliojiunga na JKT kutoka shule binafsi idadi yao ni 7,076 ambapo kati yao wavulana ni 5,432 na wasichana ni 1,644. Idadi hiyo ni kati ya vijana 20,000 walioitwa kujiunga na mafunzo kwa mujibu wa sheria kwa mwaka 2017/2018.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Zahanati ya Migungumalo, Kata ya Usagari Uyui ilijengwa kwa maandalizi ya kuwa Kituo cha Afya na kufunguliwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa tarehe 25/11/1997 na kuahidi kuwa zahanati hiyo itakuwa Kituo cha Afya cha Kanda ya Magharibi.
(a) Je, Serikali ina mipango gani ya kuikuza zahanati hiyo ili iwe Kituo cha Afya kutokana na mahitaji na huduma zinazotolewa kuwa juu ya uwezo wa zahanati?
(b) Kwa kuenzi kazi na juhudi za Rais Mstaafu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, kufika mpaka Usagari kufungua zahanati; je, Waziri yuko tayari kumwomba Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano kuja kuzindua Kituo cha Afya baada ya kuipandisha hadhi Zahanati hiyo ya Migungumano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa Zahanati ya Migungumalo inahudumia wananchi na inatoa huduma za kiwango cha juu. Zahanati hii imeendelea kutengewa fedha kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwa wananchi kupitia Mfuko wa Pamoja wa Afya, fedha za matumizi mengineyo, fedha za Benki ya Dunia (RBF), Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na fedha za dawa kupitia Bohari ya Dawa (MSD). Lengo la Serikali ni kuendelea kuiwezesha zahanati hiyo iendelee kutoa huduma nzuri zaidi kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, miundombinu iliyopo kwa sasa katika Zahanati ya Migungumalo haikidhi vigezo vya kutoa huduma za afya kwa ngazi ya kituo cha afya. Kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kujenga vituo vipya na kuboresha vituo vya afya vilivyopo nchi nzima ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wagonjwa zikiwemo huduma za dharura na upasuaji.
Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali inaendelea na ujenzi wa vituo cha afya 210 kikiwemo Kituo cha Afya cha Upuge ambacho kimepokea shilingi milioni 500 ili kukiwezesha kutoa huduma za dharura na upasuaji. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri ya Wilaya ya Tabora/Uyui imetengewa shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ambayo ikikamilika itahudumia wananchi wengi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na Serikali ya Wilaya, Halmashauri na viongozi wa Kata ya Usagari ili waanze juhudi za kujenga Kituo cha Afya cha Kata ya Usagari na ikiwezekana waanze juhudi za kujenga zahanati katika kila kijiji kama sera ya afya inavyoelekeza. Serikali iko tayari kuunga mkono nguvu za wananchi katika kumalizia ujenzi huo utakaofanyika chini ya uratibu wa halmashauri, ofisi ya Mbunge na ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Kuja kwa Mheshimiwa Rais au kiongozi mwingine wa kitaifa itategemea sana na aina ya miradi itakayokamilika. (Makofi)
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Kituo cha mafunzo ya Wanyamakazi na utengenezaji wa zana za kilimo katika Kata ya Upuge, Wilayani Uyui, Mkoani Tabora kimechakaa sana na hakifanyi kazi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kukifufua Kituo muhimu sana kwa mafunzo na zana zake vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athumani Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2002/2003 hadi 2006/2007, ilikarabati vituo sitini na nane vya mradi wa wanyamakazi katika mikoa kumi na nane nchini kikiwemo Kituo cha Upuge kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya na kupewa zana kwa ajii ya kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wakulima. Zana hizo ni pamoja na plau, majembe ya palizi, majembe ya matuta, tindo (rippers) na mikokoteni kwa ajili ya kutoa mafunzo na kufanya maonesho kwa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la ukarabati huo ni kuvifanya vituo hivyo kuendelea kutoa mafunzo kwa wakulima katika maeneo yao kwa kushirikiana na Maafisa Ugani waliopatiwa mafunzo juu ya wanyamakazi kwa ajili ya kufundisha wakulima katika vijiji. Aidha, eneo linalolimwa na wanyamakazi limeongezeka kutoka asilimia ishirini hadi asilimia ishirini na nne hivyo, kupunguza matumizi ya jembe la mkono kutoka asilimia sabini hadi asilimia 62.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufikia lengo la kuongeza uzalishaji na tija, Wizara ina jukumu la kusimamia upatikanaji wa Zana za Kilimo, utoaji mafunzo yahusuyo Zana za Kilimo, udhibiti wa ubora wa zana zinazoingia nchini kwa kushirikiana na CAMARTEC, utafiti na huduma za ugani, pamoja na kuainisha zana mbalimbali kwa matumizi ya mashamba kabla na baada ya kuvuna.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Wanyamakazi cha Upuge kwa sasa kina maksai ishirini na mbili na eneo lenye ukubwa wa hekta themanini kwa maana ya (ekari 200), hivyo, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Uyui inakusudia kufanya ukarabati wa zana hizo na kuanza kutoa mafunzo kwa Maafisa Ugani ishirini na Wakulima mia moja katika msimu wa 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara ya Kilimo inaishauri Halmashauri ya Wilaya ya Uyui kukitumia Kituo cha Upuge kwa mafunzo na uzalishaji wa mazao ya kilimo ili kupata fedha zitakazosaidia kumudu gharama za kuendesha kituo hicho. Wizara ya Kilimo inasisitiza kuwa Halmashauri za Wilaya zote nchini ni lazima zisimamie na kuendeleza vituo vya wanyamakazi vilivyopo katika Halmashauri zao.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Serikali imeanzisha sera nzuri ya viwanda nchini ili kukuza uchumi wa viwanda na maendeleo kwa wananchi.
(a) Je, Serikali haioni upungufu wa mafundi mchundo na mafundi sadifu kuwa ni kikwazo cha ufanisi wa sera ya viwanda?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuziimarisha shule za ufundi za Moshi, Ifunda, Tanga na Mtwara ili kuwaandaa na kuwapatia mafundi sadifu kufanikisha sera ya viwanda nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa mafundi mchundo (technicians)na mafundi stadi (artisans)katika kutekeleza azma ya Serikali ikifikia uchumi wa kati kupitia viwanda ifikapo mwaka 2025. Hadi kufikia Desemba 2018, kulikuwa na vyuo vya ufundi stadi 449 nchini ambavyo vilidahili wanafunzi 119,184 kujiunga katika fani mbalimbali za ufundi ili kuwa na wataalam wa kutosha kuendana na mageuzi ya viwanda nchini. Vilevile, kupitia programu ya taifa ya kukuza ujuzi kwa vijana, jumla ya vijana 10,858 wamefaidika na mafunzo mbalimbali ya ujuzi katika fani za useremala, uashi, terazo, uchongaji vipuri, ufundi umeme, ufundi bomba, uchomeleaji, ushonaji, upishi, huduma za hoteli, ufundi magari na kutengeneza viatu vya ngozi. Mikakati hiyo inakusudia kuwa na wataalam wa kutosha ili kufanikisha utekelezaji wa sera ya viwanda.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kuborsha mazingira ya elimu nchini ikiwemo ukarabati wa shule na miundombinu ambapo kupitia mradi wa lipa kulingana na matokeo (EP4R) kati ya mwaka wa fedha 2015/2016 hadi Desemba, 2018 Serikali imetumia jumla ya shilingi bilioni 11.2 kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe za ufundi. Shule zilizokarabatiwa ni shule ya Sekondari Moshi kwa shilingi bilioni 2, Ifunda shilingi bilioni 2.8, Tanga shilingi bilioni 1.8, Musoma shilingi bilioni 1.2, Bwiru Wavulana shilingi milioni 825 na Iyunga shilingi milioni 978. Lengo la Serikali ni kuhakikisha shule hizo za ufundi zinaimarishwa ili kuwa na wataalam watakaoshiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa viwanda.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Waajiri wamekuwa wakilipa Tozo ya Maendeleo ya Ujuzi kwaWafanyakazi (SDL) ya asilimia 4.5 ya mshahara kwa kila mfanyakazi ambayo ililengwa kupelekwa VETA kwa lengo la kuendeleza ujuzi:-
(a) Je, ni asilimia ngapi ya tozo hiyo inapelekwa VETA?
(b) Je, nilini Serikali itarejesha VETA katika Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuleta uwiano wa mantiki kuwa VETA inaendeleza ujuzi wa wafanyakazi?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika,kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige,lenge sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Tozo ya Kuendeleza Ujuzi, (Skills Development Levy-SDL)ni kodi inayokusanywa na Mamlaka ya Mapato nchini chini ya Sheria ya Kodi ya Mapato na Sheria iliyoanzisha VETA, Sheria Na.1 ya mwaka 1994 iliyorejewa mwaka 2006. Mwajiri anayeajiri wafanyakazi wanne au zaidi anapaswa kulipa tozo hii ambayo ni asilimia 4.5 ya malipo ghafi. Kiwango cha SDL inayopokelewa VETAni theluthi moja ya pato la SDL ambayo ni asilimia 33 ya tozo hiyo.
(b) Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ilianzishwa ili kuwezesha nguvu kazi kubwa nchini kupata stadi stahiki za ajira kulingana na mabadiliko ya mfuko wa kiuchumi, kisiasa na kijamii. Majukumu makuu matano (5)ya VETAni kusimamia, kuratibu, kugharimia, kutangaza na kutoa mafunzo ya ufundi stadi.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2006VETA ilihamishiwa katika iliyokuwa Wizara ya Elimuna Mafunzo ya Ufundi Stadi, kwa sasa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kulingana na mahitaji ya wakati huo. VETA hufanya shughuli zake kwa kufuata sera na mipango ya Serikali ya muda mrefu na mfupi ili kuhakikisha wakati wote kunakuwa na nguvu kazi za kutosha na yenye ujuzi stahiki kuchangia katika maendeleo ya kiuchumi.Kwa mantiki hiyo, suala la VETA kuwa Wizara gani, itategemea mahitaji ya Serikali kulingana na wakati husika.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Serikali inatekeleza mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria na kuyapeleka Mkoa wa Tabora katika Miji ya Igunga, Nzega, Manispaa ya Tabora, Sikonge, Isikizya na Urambo:-
(a) Je, ni vijiji gani vya Mashariki vya Jimbo la Tabora Kaskazini – Uyui vitapatiwa maji kutokana na mradi huo?
(b) Kwa vile ni idadi ndogo tu ya vijiji kati ya 82 vya Jimbo la Tabora Kaskazini ndiyo vitapatiwa maji na mradi huo: Je, Serikali ina mpango gani wa kuvipata maji vijiji vyote katika Jimbo la Tabora Kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenye Miji ya Tabora, Igunga na Nzega pamoja na vijiji zaidi ya 102 vilivyopo umbali wa kilomita 12 kila upande kutoka bomba kuu. Vijiji vilivyopo Jimbo la Tabora Kaskazini katika mradi huu ni 26 ambavyo ni Igoko, Isikizya, Ikonolo, Mswa, Itobola, Isenegenzya, Majengo, Ikongolo, Kanyenye, Kiwembe na Kalemela,
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali imeanza kutekeleza miradi katika miji 28 kupitia mkopo wa Dola za Marekani milioni 500 kutoka Benki ya Exim ya India. Mradi huo utapeleka maji katika Miji ya Sikonge, Urambo, Kaliua na baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Uyui kwa kutoa maji Ziwa Victoria. Mpaka sasa vijiji vilivyotambuliwa wakati wa usanifu wa kupeleka maji Sikonge, Urambo na Kaliua ni 14 ambavyo ni Kasisi B, Ilalongulu, Mpenge, Isenga, Ngokolo, Ulimakafu, Mabama, Tumaini, Maswanya, Chali Ndono, Itinka, Tulieni na Utemini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kwa miradi yote miwili itahudumia jumla ya vijiji 40 vya Jimbo la Tabora Kaskazini. Serikali itaendelea kutenga na kutoa fedha ili kuhakikisha vijiji vyote vilivyobaki vinapata huduma ya maji.
MHE. ALMAS A. MAIGE Aliuliza:-
Mradi wa REA III(1) unatekelezwa katika Jimbo la Tabora Kaskazini kwa kasi ndogo na mpaka sasa ni vijiji vitatu tu kati ya vijiji 82 ndiyo vimewashwa umeme.
(a) Je, Serikali inachukua hatua gani kumfanya mkandarasi akamilishe kuwasha umeme katika vijiji vyote 18 vya REA III(1)?
(b) Kwa vile kwa makosa Mradi wa REA III(1) unarudiwa kupelekwa katika Kijiji cha Upuge, Kata ya Upuge ambako umeme ulishapelekwa na REA III. Je, ni lini sasa umeme utapelekwa katika Kata ya Ikongolo ambako ni Kata jirani na Kata ya Upuge?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almasi Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa kufikisha umeme katika vijiji vyote nchini vikiwemo vijiji vya Jimbo la Tabora Kaskazini. Katika Jimbo la Tabora Kaskazini, Vijiji 18 vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA III(1) unaoendelea kutekelezwa na Mkandarasi Kampuni ya JV Pomy Engineering Company Limited, Intercity Builders Limited na Octopus Engineering Limited. Ili kuhakikisha mkandarasi anakamilisha kazi za kuwasha umeme katika vijiji 18 vinavyofanyiwa kazi, Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na TANESCO wameimarisha usimamizi wa kazi za kila siku za mkandarasi na kumtaka mkandarasi kuwa na vifaa kwa ajili ye ujenzi wa mradi kutoka ndani ya nchi.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Vijiji vya Kata ya Ikongolo vinavyojumuisha Kanyenye, Kiwembe na Majengo vitapelekewa umeme kupitia utekelezaji wa Mradi wa REA III(2) utakaoanza mwezi Januari, 2020. Kazi ya kupeleka umeme katika vijiji vya kata hizo utahusisha ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa kilovolt 33 yenye urefu wa kilometa 36.14, njia ya umeme wa msongo wa kilovolti 0.4 yenye urefu wa kilometa 20.28, ufunguaji wa transfoma tisa za KVA 50 na KVA 100 pamoja na kuwanungnishia umeme wateja wa awali 614 na gharama ya mradi huu ni shilingi bilioni 2.29.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Miaka iliyopita Serikali ilikuwa na nia ya kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia katika shule za msingi na za upili.
(a) Je, nini kilitokea kwa Serikali katika kutekeleza nia yake hiyo nzuri?
(b) Je, ni lini Serikali itaanza kutumia Kiswahili kama lugha ya kufundishia katika shule za msingi na za Upili ili kukuza uelewa wa wanafunzi katika masomo yao?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKONOLIJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, suala la lugha ya kufundishia na kujifunzia ni suala la kisera kama ambavyo limeanishwa katika aya 3.219 na 3.220 ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014. Sera hiyo inabainisha matumizi ya lugha mbili za kufundishia na kujifunzia ambazo ni Kiswahili na Kiingereza na kwa sasa lugha ya Kiswahili inatumika kufundishia katika ngazi ya elimu ya awali na elimu ya msingi, vyuo vya ualimu ngazi ya cheti na vyuo vya ufundi stadi.
(b) Mheshimiwa Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali bado inaendelea kutumia lugha ua Kiingereza katika kufundishai na kujifunzia katika ngazi ya elimu ya sekondari, vyuo vya kati na vyuo vikuu na hii ni kutokana na umuhimu wa lugha hiyo katika masuala ya kitaifa, ya kikanda na kimataifa kwa ajili ya mawasiliano na biashara ili kuwajengea wanafunzi ufahamu na umahiri katika lugha hiyo.
MHE. ALMASI A. MAIGE aliuliza:-
Wilaya ya Uyui haina Mahakama ya Wilaya na ina Mahakama moja tu ya Mwanzo inayotumia chumba kidogo katika jengo la Mkuu wa Wilaya ya Uyui baada ya kutelekeza Mahakama ya Mwanzo ya Upuge:-
(a) Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya ya Uyui?
(b) Je, ni kwa nini Serikali ilitelekeza Mahakama ya Mwanzo ya Upuge pamoja na majengo yake katika Kijiji cha Upuge?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Almasi Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uhaba wa majengo ni moja ya changamoto kubwa inayoikabili Mahakama ya Tanzania, Mahitaji ya majengo ya kuendeshea shughuli za mahakama hapa nchini ni makubwa, Kwa msingi huo, mahakama imejiwekea utaratibu wa kujenga majengo haya kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya Uyui ni miongoni mwa majengo ya Mahakama za Wilaya 33 yaliyopangwa kuanza kujengwa mwezi June, 2020 kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, kwa sasa mahakama ipo katika hatua za mwisho kukamilisha mchakato wa awali ili ujenzi wa majengo hayo uanze kwa muda kama ilivyo katika mpango wa mahakama.
Mheshimiwa Spika, Serikali haikulitelekeza jengo la Mahakama ya Mwanzo Upuge, sababu kubwa ilikuwa ni uchakavu wa jengo lenyewe ambalo halikuwa rafiki kuendelea kutumika kuendeshea shughuli za mahakama. Hata hivyo, tunatoa shukrani zetu za dhati kwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Uyui kwa kutuwezesha kupata ofisi kwa ajili ya kuendelea kutoa huduma za Mahakama ya Mwanzo Upuge wakati tukiendelea na taratibu za ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ambayo pia itakuwa na Mahakama ya Mwanzo katika jengo moja.
MHE. INNOCENT S. BILAKWATE (K.n.y. MHE. ALMAS A. MAIGE) Aliuliza: -
Wananchi wa Jimbo la Tabora Kaskazini wamejitolea kujenga Vituo vya Afya katika Kata za llolangulu, Mabama, Shitagena na Usagari katika Kijiji cha Migungumalo: -
Je, Serikali ipo tayari kuanza kuchangia miradi hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua mchango mkubwa wa wananchi katika ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya kote nchini. Hivyo, Serikali ina dhamira ya dhati ya kuchangia nguvu hizo za wananchi katika kukamilishaji vituo hivyo ili vianze kutoa huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa ukarabati na ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini ikiwemo kukamilisha maboma ya majengo ya kutolea huduma za afya yaliyojengwa na wananchi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa, ambapo ujenzi wake ulisimama kwa kukosa fedha. Hadi kufikia Septemba 2020 jumla ya shilingi bilioni 315.31 zimetumika kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Mheshmiwa Naibu Spika, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 27.75 kwa ajili ya kukamilisha maboma 555 ya zahanati nchini yakiwemo maboma manne (04) katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora ili kuunga mkono jitihada za wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua na kuthamini michango na nguvu za wananchi na itaendelea kuchangia nguvu za wananchi katika kujenga na kukarabati miundombinu ya kutolea huduma za afya nchini kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ALMAS A. MAIGE Aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya ya Uyui?
NAIBU WAZIRI YA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi ni mara ya kwanza kusimama hapa baada ya uteuzi, nipende tu kutumia nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu lakini vilevile kumshukuru Mama yangu Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini katika nafasi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria nipende kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Mahakama ya Tanzania kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya uhaba na uchakavu wa majengo na miundombinu ya Mahakama. Katika maeneo mengi Mahakama imekuwa ikitumia majengo ya kuazima kutoka taasisi nyingine na kupangisha ili kuweza kutoa huduma kwa wananchi. Aidha, katika baadhi ya Wilaya wananchi wamekuwa wakipata huduma za Mahakama ya Wilaya katika Wilaya za jirani.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wa Tabora Wilaya tatu; Uyui, Kaliua na Sikonge hazikuwa na Mahakama. Hivyo, wananchi wa Wilaya hizo wamekuwa wakipata huduma katika Wilaya za jirani ambapo Wilaya ya Uyui na Sikonge wanahudumiwa na Wilaya ya Tabora na Wilaya ya Kaliua wanapata huduma za Mahakama Wilayani Urambo. Mwaka 2020 Mahakama ilianzisha Mahakama ya Wilaya za Uyui na Kaliua katika Majengo ya Ofisi za Wakuu wa Wilaya ili kusogeza huduma karibu na wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, utatuzi wa changamoto hii ya majengo inafanyika kwa awamu kadiri bajeti inavyoturuhusu. Katika mipango yake, Mahakama ya Wilaya ya Uyui itajengwa mwaka wa fedha 2022/2023 kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, Mahakama ya Wilaya ya Kaliua itajengwa mwaka wa fedha 2021/2022 na tayari zabuni imetangazwa. Vilevile Mahakama inaendelea kukamilisha ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Sikonge, pamoja na ukarabati mkubwa wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Hakimu Mkazi Tabora.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwapatia maji wananchi walio katika Vijiji ambavyo havifikiwi na Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria katika Jimbo la Tabora Kaskazini?
WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Tabora Kaskazini lina kata 19 na vijiji 82. Katika utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria kwenda katika Miji ya Nzega, Igunga na Tabora jumla ya vijiji 20 vya Jimbo la Tabora Kaskazini ambavyo ni Ibushi, Igoko, Isikizya, Ikonola, Ikonola, Mswa, Itobela, Ibelamilundi, Isenegezya, Mtakuja, Majengo, Kalemela, Saw Mill, Imalampaka, Magiri, Kinyamwe, Lunguya, Upuge, Kasenga na Mhogwe vimenufaika na mradi. Aidha, Serikali imekamilisha utekelezaji wa miradi mitatu ya mtandao wa bomba inayonufaisha vijiji vinne vya Kilungu, Milumba, Migungumalo na Ishihimulwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali iko kwenye hatua za awali za utekelezaji wa miradi sita itakayonufaisha vijiji kumi na mbili vya Makazi, Ugowola, Ndono, Mbiti, Kalola, Ufuluma, Nzubuka, Izugawima, Ibiri, Mayombo, Nsimbo na Kagera. Katika Mpango wa bajeti ya fedha 2021/2022, Serikali imepanga kutekeleza miradi mitano itakayonufaisha vijiji vinane vya Ikongolo, Kanyenye, Kiwembe, Kongo na miji 28 kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 500 kutoka Benki ya Exim India ambao utanufaisha vijiji 14 na hivyo kufanya jumla ya vijiji 58 vya Jimbo la Tabora Kaskazini kupata huduma ya maji.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza:-
Kituo cha Afya Upuge kinahitaji jengo kwa ajili ya mashine za mionzi yaani x-ray na ultra sound: -
Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya mashine hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athumani Maige, Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Uyui shilingi milioni 500 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa Kituo cha Afya Upuge. Ujenzi wa majengo manne ulifanyika na majengo yote yanatumika. Serikali inatambua uhitaji wa jengo la x-ray na ultra sound katika kituo hicho. Serikali imekwishatoa ramani za majengo ya mionzi kwa Halmashauri zote nchini ikwemo Halmashauri ya Wilaya ya Uyui.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, Serikali inaielekeza Halmashauri kutenga fedha za mapato ya ndani ili kuanza ujenzi huo kwa awamu kuanzia mwaka wa fedha 2022/2023. Serikali itaendelea kuboresha majengo ya x-ray na ultra sound kote nchini.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza: -
(a) Je, ni wakulima wangapi wadogo wadogo wamepata mikopo kutoka Benki ya Kilimo ili kukuza tija kwa wakulima hao?
(b) Je, riba za Benki ya Kilimo zinatofauti gani na riba za Benki za Biashara katika kumsaidia mkulima mdogo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -
(a) Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Julai, 2021 Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imekwishatoa mikopo yenye jumla ya shilingi bilioni 281.74 kwa ajili ya kuendeleza miradi ya kilimo, ufugaji na uvuvi nchini. Mikopo hiyo imewanufaisha wakulima 1,514,695 vikiwemo vyama vya wakulima 151 hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, sambamba na utoaji wa mikopo ya moja kwa moja, Benki ya Maendeleo ya Kilimo inasimamia Mfumo wa Dhamana kwa Wakulima Wadogo (Smallholder Credit Guarantee Scheme – SCGS) unaolenga kuchagiza mabenki na taasisi za fedha kuongeza ukopeshaji katika sekta ya kilimo. Hadi kufikia mwisho wa mwezi Juni 2021, SCGS ilitoa udhamini wa mikopo kwa wakulima wadogo 11,244, vikundi vya wakulima 181 na SMEs 43 waliopata mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 89.92 kutoka benki 9 washiriki katika uendeshaji wa mfuko wa SCGS.
(b) Mheshimiwa Spika, kwa upande wa riba, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) imeweka utaratibu wa kutoza riba kwa kiwango cha asilimia 10 kwa kuzingatia uwezo wa wazalishaji wa madaraja tofauti katika sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi. Kwa maana hiyo, mikopo inayotolewa kwa wakulima wadogo hutozwa riba nafuu isiyozidi asilimia 10 na kwa masharti nafuu ya urejeshwaji wake yanayozingatia misimu ya mavuno na mauzo ya mazao.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Tabora – Mambali – Ishihimulwa – Shitage – Muhulidede kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Tabora – Mambali – Bukumbi – Ishihimulwa – Shitage – Muhulidede yenye urefu wa kilomita 109.4 ni sehemu ya barabara inayounganisha mikoa ya Tabora na Shinyanga. Sehemu ya barabara kutoka Tabora hadi Bukumbi yenye urefu wa kilometa 84 ni barabara ya mkoa. Kutoka Bukumbi hadi Muhulidede yenye urefu wa kilometa 25.4 ni barabara ya wilaya iliyokasimiwa kwa Wakala wa Barabara (TANROADS) kuanzia mwaka wa fedha 2018/2019.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya barabara hii kutoka Tabora hadi Mambali yenye urefu wa kilomita 56, imefanyiwa usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Kazi ya usanifu ilikamilika mwezi Aprili, 2020. Baada ya kukamilika kwa usanifu na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza kazi za ujenzi kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sehemu ya barabara iliyobaki ya kutoka Mambali – Bukumbi hadi Muhulidede yenye urefu wa kilomita 53.4, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuifanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha kuwa barabara hii ya Tabora - Mambali – Bukumbi hadi Muhulidede inapitika vizuri majira yote, katika mwaka wa fedha 2021/2022, jumla ya Shilingi milioni 443.989/= zimetengwa kwa ajili ya kuifanyia matengenezo mbalimbali. Ahsante.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza: -
Je ni lini Serikali italeta Bungeni Muswada wa Sheria ya Kampuni Binafsi za Ulinzi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Athuman Almasi Maige, Mbunge Wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa Sheria inayosimamia Makampuni Binafsi ya Ulinzi na kwa sasa Waraka wa Baraza la Mawaziri kuhusu mapendekezo ya kutunga Sheria ya Huduma za Sekta Binafsi ya Ulinzi umekamilika na utawasilishwa katika Baraza la Mawaziri kwa ajili ya maamuzi baada ya kupata maoni ya kina ya wadau wa pande zote mbili za Muungano juu ya rasimu ya sheria hiyo. Baada ya kukamilika kwa hatua hizo Muswada wa Sheria hiyo utaletwa Bungeni.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE auliza: -
Je, Serikali ni lini italeta Bungeni Muswada wa Sheria ya Kampuni Binafsi za Ulinzi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwepo kwa Sheria inayosimamia kampuni binafsi za ulinzi. Kwa sasa Waraka wa Baraza la Mawaziri kuhusu mapendekezo ya kutunga Sheria ya Huduma za Sekta Binafsi za Ulinzi umekamilika, na utawasilishwa katika Baraza la Mawaziri kwa ajili ya Maamuzi baada ya kupata maoni ya kina ya wadau wa pande zote mbili za Muungano juu ya rasimu ya sheria hiyo. Baada ya kukamilika kwa hatua hizo, Muswada wa Sheria hiyo utawasilishwa Bungeni. Nashukuru sana.
MHE. ATHUMANI A. MAIGE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itabadilisha mtambo wa kutengeneza hewa ya Naitrojeni Kituo cha Afya Upuge na kuleta mtambo wa hewa ya Oksijeni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Athumani Almas Maige, Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Upuge kilifungiwa mtambo wa kutengeneza vacuum mwaka 2012 kwa ajili ya huduma za dharura na upasuaji. Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 imefanya tathmini ya mitambo hiyo na matengenezo madogo ya kuzibua njia ya hewa yatafanyika ili iweze kutumika.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 katika mwaka wa fedha 2021/2022 imepanga kununua mitambo 10 ya kuzalisha hewa ya Oksijeni . Mitambo hiyo itazalisha hewa na kusambaza kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ikiwemo Kituo cha Afya cha Upuge ambacho kimefungiwa mfumo wa kupokea na kutawanya hewa ya Oksijeni. Ahsante.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza: -
Je, ni lini Barabara ya Manoleo hadi Kituo cha Afya Upuge itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Manoleo - Kituo cha Afya Upuge yenye urefu wa kilometa 22.10 imesajiliwa kwa jina la Nyambele – Upuge – Muhogwe - Magiri ambapo kutokana na umuhimu wake imeendelea kutunzwa kwa kuwekewa kipaumbele kwenye bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na umuhimu wa barabara hii, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe kilometa 13 na kujenga makalavati saba, ambapo ipo hatua ya uandaaji wa nyaraka za zabuni kwa ajili ya kumpata Mkandarasi. Ujenzi unatarajiwa kuanza mwezi Mei, 2023.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili Barabara ya Nyambele – Upuge – Muhogwe – Magiri yenye urefu wa kilometa 22.10 iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Aidha, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali itatenga shilingi milioni 91.8 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida kilometa 15, ujenzi kwa kiwango cha changarawe kilomita mbili na kunyanyua tuta na kujenga makalvati mawili, ahsante.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga barabara ya mkato kutoka Kigwe B hadi Magiri Uyui ili kuchepusha magari makubwa kupita Tabora Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara ya mkato kutoka Kigwa B mpaka Magiri - Uyui Serikali imekuwa ikifanya matengenezo ya mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa barabara hiyo inapitika wakati wote.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024, Serikali itatenga shilingi milioni 125 kwa ajili ya kufanya matengenezo ya muda maalum ya kilomita Saba kwa kuziwekea changarawe na kujenga kalavati moja ili iweze kuendelea kupitika muda wote na kutoa huduma kwa wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, TARURA itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuendelea kuifanyia matengenezo na kujengwa kwa kiwango cha lami kadri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itajenga vyumba maalum vya kuweka mitambo ya x–ray na ultra sound katika Kituo cha Afya Upuge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha wa 2017/2018, Serikali ilitenga Shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ukarabati wa Kituo cha Afya Upuge kwa kujenga jengo la wazazi, jengo la maabara, jengo la kuhifadhia maiti, nyumba ya mtumishi na njia ya kupita wagonjwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika vituo vya afya nchini kwa kuendelea kujenga majengo ya kutolea huduma muhimu ikiwemo huduma za mionzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kujenga vyumba maalum vya kuweka mitambo ya X– Ray na Ultra Sound katika Kituo cha Afya Upuge kadri fedha zitakavyopatikana.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza:-
Je, ni minara mingapi ya mawasiliano ya simu itasimikwa Uyui kati ya minara 780 itakayojengwa nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP), Serikali imeainisha kata tisa zilizopo Uyuyi ambazo zimepatiwa watoa huduma (Airtel, Halotel na TTCL) hivyo kufanya idadi ya minara tisa itakayojengwa na tunatarajia vijiji 26 vilivyopo katika kata hizo vitanufaika na huduma baada ya kukamilika kwa ujenzi wa minara hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wilaya ya Uyui ni miongoni mwa Wilaya zinazonufaika na Miradi ya Mawasiliano kupitia UCSAF, ambapo idadi ya minara 28 imejengwa na imekamilika katika kata 25 zilizopo wilayani humo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha na kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa upande wa Jimbo la Tabora Kaskazini, Kata za Igulungu, Kalola, Ufuluma, Nsimbo na Upuge zimefanyiwa tathmini na sasa Serikali kupitia UCSAF inamtafuta mtoa huduma atakayefikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo hayo.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itachimba visima katika Shule ya Sekondari Ndono Uyui?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nia ya Serikali ni kuona maji yanapatikana kwa ajili ya matumizi ya jamii, maendeleo ya kiuchumi na mazingira. Shule ya Sekondari Ndono ilikuwa na changamoto ya maji, na katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imepeleka maji shuleni hapo kupitia kisima kilichopo katika Zahanati ya Kijiji cha Ndono na sasa wanafunzi wanapata maji safi na salama. Aidha, Serikali imeanza maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa bomba la maji kutoka mradi wa Ziwa Victoria kwenda Wilaya za Urambo na Kaliua ambapo wananchi wa Kijiji cha Ndono ikiwemo wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Ndono wataongezewa upatijanaji wa huduma ya maji.
MHE. RASHID A. SHANGAZI K.n.y. MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Viwanda vya Mbolea nchini ili Wakulima waongeze tija?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA, alijibu: -
Mheshimwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na Mpango wa Kuratibu Uwekezaji wa Viwanda vya Mbolea Nchini. Matokeo ya uratibu huo ni pamoja na Kiwanda cha Mbolea cha Minjingu na ujenzi unaoendelea wa Kiwanda cha Mbolea cha Itracom Fertilizer Limited, Jijini Dodoma. Nakushukuru.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaipatia Hospitali ya Wilaya ya Uyui gari la wagonjwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imepeleka magari mawili ya kubebea wagonjwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Uyui mwezi Februari, 2024. Magari hayo yamepangwa katika Hospitali ya Wilaya Uyui na Kituo cha Afya Igalula.
Mheshimiwa Spika, magari hayo yanatumika kutoa huduma kwa mfumo wa Kaskedi ambapo Vituo vya Afya vya Loya, Tura, Upuge na Mabama pamoja na zahanati ambazo hazina magari ya kubebea wagonjwa vitahudumiwa.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Shitage – Uyui kilichoanza kujengwa kwa nguvu za wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na kituo cha afya katika Kata ya Shitage. Aidha, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Uyui imetenga shilingi milioni 350 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Vituo vya Afya vya Mabama, Loya, Tuura pamoja na Zahanati za Ibela, Mbiti, Izugawima, Gilimba na Magir.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2025/2026 Serikali kupitia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Uyui itatenga bajeti kwa ajili ya ukamilishaji wa Kituo cha Afya cha Shitage, ahsante.