Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Athumani Almas Maige (77 total)

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana pia kuniruhusu na mimi niulize swali la pili la nyongeza.
Mheshimiwa Waziri wa viwanda na Biashara amejibu majibu mazuri sana, kwa ujumla lakini ningependa na mimi kujua kwamba suala la viwanda vilivyobinafsishwa limekikumba kiwanda chetu cha Nyuzi cha Tabora. Ningependa Mheshimiwa Waziri aniambie ana mkakati gani hasa wa Kiwanda cha Nyuzi Tabora ambacho kilikuwa kinasaidia wakulima wote wa Pamba katika Kanda ya Ziwa Magharibi? Ahsante sana.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kiwanda cha Nyuzi Tabora mmiliki wa Kiwanda hicho ameshaitika wito kwa Msajili wa Hazina, madai yake yeye anasema nyuzi zake hazina soko.
Kwa hiyo, tunashirikiana naye ili tuweze kupata soko la nyuzi zake lakini tuweze kuona kiwanda kile kinafanya kazi. Nyuzi zake zilikuwa zinakosa soko, mtu anakuambia kiwanda hiki nyuzi hazina soko na hayo niliyowaeleza bidhaa kutoka nje ndiyo mojawapo ya mambo yaliyokuwa yanatuumiza. Kwa hiyo, tuko nae bega kwa bega, wataalam wanafanyia kazi, na nitakuja kuleta mrejesho kwa watu wa Tabora ili kusudi kiwanda chenu kiweze kufanya kazi vizuri.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kuniruhusu niliulize maswali mawili ya nyongeza licha ya majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, soko la tumbaku duniani limeendelea kupungua haraka na kwa hivyo hivi karibuni wakulima tumbaku Tabora watakosa mahali pa kuuza tumbaku. Je, Serikali haioni ni muhimu kuanzisha mazao mengine ya biashara kama ufuta, karanga na alizeti?
Swali langu la pili, matatizo ya wakulima wa tumbaku sasa hivi yanatokana na usimamizi mbovu au mdogo unaotekelezwa na bodi yetu ya tumbaku. Hawana uwezo wa hela na hawa vilevile rasilimali watu na kweli kuacha zao la tumbaku liluke luke kama vile kuku hana kichwa.
Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuiboresha Bodi ya Tumbaku au kuboresha kitu kingine mamlaka mengine ya kusimamia zao la tumbaku ili wakati huu tunahangaika na tumbuka lakini wakulima wawe na hali nzuri ya mauzo ya tumbaku? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, moja kabisa nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba soko la tumbaku linaendelea kuleta changamoto siku hadi sikuhii ni kwa sababu kama mnafahamu Waheshimiwa Wabunge tumbaku ndiyo zao la pekee ambalo hata yule mtumiaji anapiga vita toka siku ya kwanza anapoanza kuitumia. Mnafahamu kwenye tumbaku zote kwenye pakiti za tumbaku imeandikwa tobacco is dangerous to your health, kwa hiyo, imefanya watumiaji wengi wa tumbaku kujiondoa duniani na hasa wale wanaotoka Ulaya Magharibi na Marekani. Soko la tumbaku siku hizi limehamia kwa kiasi kikubwa katika Bara la Asia hasa China lakini nikubaliane naye kwamba ni soko ambalo tunaendelea kupata changamoto katika ununuzi wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nakubaliana nay eye kabisa kwamba njia mojawapo ya kuwafanya wananchi wetu wasiweze kupata mdororo wa uchumi ni kuwashauri kutoweka mayai kwenye kapu moja na kuzalisha mazao mengine ambayo nayo yana tija hususan mazao ya karanga na alizeti ambayo yanaendana vizuri kabisa na hali ya hewa na udongo wa Mkoa wa Tabora.
Kwa hiyo, Serikali imekuwa ikiwahamasisha wananchi siyo wa Tabora tu wasijiingize kwenye kilimo cha zao moja kwa sababu tumeona athari za wananchi kufanya hivyo lakini wajaribu kulima azao mengi iwezekanavyo ili pale zao moja linapopata changamoto waweze kuwa na uchumi wasije wakapata matatizo. Kwa hiyo, nakubaliana naye kabisa kwamba Serikali tutachukua hili na tutafuta namna ya kufanya uhamasishaji wa wananchi kuingia kwenye kilimo kingine lakini huku tukiendelea kutafuta masoko ya tumbaku kwa sababu niseme siyo kwamba masoko hayapo moja kwa moja, ni suala la kutafuta masoko mengine kwa hiyo tutaendelea kufanya hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la nyongeza la usimamizi wa tumbaku, nakulibaliana naye kabisa kwamba bodi yetu ya tumbaku imekuwa na changamoto nyingi sana hususan katika eneo la fedha, lakini vilevile katika eneo la rasilimali watu. Kwa sasa Wizara inajitahidi kusaidia katika kutatua changamoto hizi na tayari mwaka huu kama mnavyoona kidogo soko la tumbaku limeweza kuendeshwa vizuri kwa sababu bodi wamepata baadhi ya fedha, lakini tutaendelea kuboresha hali katika bodi yetu na wazo lake kuhusu kutafuta njia mbadala kama bodi haijafanikiwa nimueleze tu kwamba Serikali inalichukua hili tuangalie kama Bodi ya Tumbaku ikishindwa kufanya kazi labda kama tunaweza tukatafuta kitu kingine ili mradi kwamba tunajua kwamba hata hicho kingine nacho fedha na itahitaji rasilimali watu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mwisho kabisa mimi nimshukuru Mheshimiwa Almas Maige amenifundisha mengi sana katika eneo hili la tumbaku, ni mtu ambaye nakaa naye kabisa ni mzoefu, kwa hiyo, nitaendelea kumuomba ushauri ili tuweze kuleta ufanisi kwa wakulima wetu wa tumbaku si wa Tabora tu, lakini vilevile tunafahamu changamoto zilizopo Chunya, Mpanda, tunafahamu zilizoko Namtumbo, zote Wizara inashughulikia, nashukuru.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kuniruhusu nami niulize swali la nyongeza kwa niaba ya wakulima wa tumbaku. Kwa vile sheria hii ya ushirika pamoja na sheria ndogo Na. 42 iliyounda Bodi ya Tumbaku zimeendelea kuwa na upungufu mkubwa, ni lini Serikali italeta sheria hizo mbili hapa katika Bunge lako ili zifanyiwe marekebisho na kwa faida ya wakulima na zao la tumbaku nchini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Sheria ya Ushirika kufanyiwa marekebisho pamoja na ile inayounda Bodi ya Tumbaku, nimwambie kuwa Sheria ya Tumbaku ndiyo imepitishwa tu karibuni haina hata miaka mitatu, imeanza kufanya kazi tu mwaka 2015 pamoja na kwamba ilipitishwa kuanzia mwaka 2013.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kuna maeneo ambayo yanahitaji marekebisho, itabidi tufuate utaratibu wa kawaida na hatimaye sisi kama Wizara tutahakikisha kwamba inakuja Bungeni. Vivyo hivyo kwa sheria inayounda Bodi ya Tumbaku, tukipata mawazo kutoka kwa wadau mbalimbali kwamba inahitaji kufanyiwa marekebisho tutafanya utaratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni vigumu kwa sasa kumwambia kwamba, tutaileta kwenye Bunge hili lini kwa sababu bado kama Wizara hatujapata malalamiko makubwa au mapendekezo kutoka kwa wadau mbalimbali ya kuweza kurekebisha.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Moja, kwa vile umethibitisha kweli kwamba hakuna maji chini Uyui Kaskazini; je, Serikali iko tayari sasa kuanzisha mradi kabambe wa kuchimba mabwawa katika eneo hilo?
Swali la pili, katika kijiji cha Majengo kuna chanzo kizuri cha maji ambacho watu wanateka maji kila siku kwa kuchimba kwa mikono. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kwenda na mimi na Wataalam wake wa maji kuangalia eneo hili kama inaweza kuchimbwa visima virefu ili yapatikane maji ambayo ni salama badala ya haya maji ambayo hayana usalama? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza ameuliza mabwawa, mabwawa ndiyo sera ya Wizara ya Maji. Maeneo yote ambayo yana matatizo ya ukame na yanapata mvua tumeamua kumaliza tatizo la maji, moja kwa kuvuna maji kutoka kwenye mapaa ndiyo maana tumeagiza Halmashauri ziweke utaratibu kila wanapopitisha michoro ya nyumba wahakikishe kwamba wanaainisha uvunaji wa maji ya mvua.
Pili, ni sera yetu kwamba tuna hakikisha na tayari tumeshaagiza kila mwaka, kila Halmashauri wahakikishe wanafanya usanifu wa bwawa moja na kuleta maombi ya pesa ili tuweze kuwapa wajenge mabwawa kuhakikisha tunamaliza matatizo ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili linalohusu eneo la Majengo, Mheshimiwa amesema kwamba watu wanafukua maji na maji wanayapata. Ikolojia ya ardhi huwa ni ngumu, lakini kwa sababu umetueleza hili naomba nikuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutalifanyia kazi, lakini niagize Halmashauri husika waende katika hilo eneo wakaangalie halafu watupe taarifa ili tuweze kuona tunalifanyia nini.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa uwezo wa kifedha wa Halmashauri ya Tabora ni mdogo sana na haiwezi kununua nyumba hizo zote kwa ajili ya mahitaji ya wafanyakazi wake. Je, Serikali inaweza kuidhamini Halmashauri ya Uyui ili iweze kukopa kwa muda mrefu kutoka Shirika la Nyumba?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Halmashauri ya Uyui ni mpya bado na ina changamoto nyingi sana, je, Serikali haioni umuhimu wa kuibeba Halmashauri hii ili iweze kutatua matatizo yake au changamoto ambazo zinaikabili na hasa tatizo hili la nyumba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Shirika la Nyumba limejenga pale nyumba za kutosha takribani nyumba 49 kama sikosei na katika bajeti ya mwaka huu wameweza kutoa gharama za ujenzi wa nyumba tatu. Suala la kuidhamini, kwa sababu Serikali ikidhamini lazima kuwe na utaratibu wa kurejesha na Mheshimiwa Mbunge alifika ofisini kwangu na timu yake na kwa analysis ya mapato yao ya ndani hata kama wakikopa zile nyumba watahitaji siyo miaka mitatu takribani miaka 10 ili kurejesha mkopo huo, kwa hiyo, hili ni suala la negotiation kati ya Halmashauri na Shirika la nyumba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Shirika la Nyumba lilikuwa linasema kwamba, ni lazima iwe ndani ya miaka mitatu lakini ukiangalia uwezo wa Halmashauri ya Uyui kulipa katika miaka mitatu haiwezekani unless otherwise wakubaliane kulipa ndani ya miaka kumi. Kama wakikubaliana ndani ya miaka kumi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI haitosita kuangalia jinsi gani itafanya ili watumishi wale waweze kupata nyumba. Hata hivyo, lazima Halmashauri hii iangalie jinsi gani itaweza kulipa lakini ndani ya miaka mitatu kwa Uyui hawawezi kulipa lile deni.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala zima la kuibeba Halmashauri hii, naomba niseme wazi, jukumu letu kubwa ni kuhakikisha Halmashauri zote zinafanya kazi vizuri. Japo changamoto ya bajeti ni kubwa lakini tunaendelea na harakati mbalimbali za kukamilisha majengo yaliyokuwepo pale Uyui ili Halmashauri mpya ya Uyui ifike muda sasa isimame vizuri, watumishi wote wapate mazingira rafiki ya kufanya kazi na wananchi wapate huduma.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
La kwanza, kwa vile Serikali imebuni mradi huo ambao utatusaidia sana sisi Wana-Uyui hasa Tabora Kaskazini, je, Serikali sasa iko tayari kuviorodhesha vijiji ambavyo vitakuwa katika mradi huo ili vijiji ambavyo havitakuwa ndani ya mradi tuvishughulikie kuvipatia maji?
Swali la pili kuhusu mradi wa Malambo ya maji, je, Serikali sasa iko tayari kutoa ahadi kwamba iko tayari kuanza utafiti wa wapi malambo hayo yatachimbwa? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nitaanza na swali la pili kuhusu mpango wa Serikali kujenga mabwawa, kwanza naomba nitoe taarifa kwamba kulingana na survey ambayo tumeifanya, tuna mabwawa 3,000 ambayo yameshajengwa hapa nchini kwetu. Katika hayo, asilimia 50 yanafanya kazi na asilimia 50 hayafanyi kazi.
Kwa hiyo, mpango tulionao ni kuhakikisha kwamba haya asilimia 50 ambayo hayafanyi kazi tunayafanyia ukarabati. Pamoja na hiyo, Bunge la Bajeti lililopita tulielekeza kila Halmashauri wahakikishe kila mwaka wanasanifu bwawa moja na wanaleta ili tuweze kutenga fedha kuhakikisha kwamba kila Halmashauri kila mwaka inajenga bwawa moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kuhusu ni vijiji gani ambavyo vimeainishwa kwenye huu Mradi wa Kutoa Maji Ziwa Victoria kupeleka Tabora? Maeneo yatakayopitiwa na mradi huu ni pamoja na Kata ya Upuge; ambayo ni Kijiji cha Upugwe, Muhogwe, Lungunya na Kasenga vitapata maji.
Kata ya Magiri ambayo ni kijiji cha Magiri, Imalampaka, Kalemela vitapata maji. Kata ya Isikizya; ambapo kijiji cha Ilalwasimba, Isikizya, Igoko, Ibushi vitapata maji. Kata ya Ibelamailundi; kijiji cha Ibelamailundi, Mtakuja, Itobela, Isenegeja vitapata maji na pia Kata ya Ilolangulu; ambapo Kijiji cha Kasisi „A,‟ Ngokolo na Isenga vinatarajiwa kupata maji kupitia katika mradi huu. (Makofi)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na pongezi zangu kwa niaba ya Wanauyui na Tabora wa ujumla kupeleka Msajili wa Hati, nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, kwa vile kuna upungufu mkubwa sana wa idara mbalimbali za ardhi pale ikiwemo ya upimaji na mipango: Je, Serikali iko tayari kupeleka tena wataalam hao ili wafanye kazi na Msajili huyu wa Hati?
Swali la pili; kwa vile kabla ya kupelekwa Msajili huyu wiki moja iliyopita, kwa miaka mingi iliyopita Hati za Tabora zimekuwa zinasajiliwa katika Ofisi nyingine za Kanda, Dodoma na Mwanza: Je, Serikali sasa iko tayari kurudisha kumbukumbu ya Hati zetu zote pale Tabora? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameuliza kuhusu upungufu wa wataalam wa idara nyingine, ametaja mipango miji, kama tuko tayari kupeleka.
Mheshimiwa Spika, naomba nilihakikishie Bunge lako kwamba kwa sasa katika kipindi hiki ambacho pia tunatakiwa kama Wizara zote au Serikali kuhamia Dodoma, baadhi ya Wataalam ambao wako Makao Makuu tutawasambaza katika kanda ambazo zina upungufu, kwa sababu, maeneo mengi ni karibu yanao wataalam wa kutosha, lakini ni machache likiwepo la Tabora ambao hawana wataalam hao. Kwa hiyo, tutawapeleka katika Kanda ili kuendelea kuziimarisha kama tulivyoahidi.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili, amesema Hati zilizoko Mwanza na maeneo mengine ambazo ni za Tabora; naomba nimhakikishie tutafanya utaratibu wa kuhakikisha hati hizo zinarudi katika ofisi husika kwa sababu tayari Msajili ameshapatikana, basi anao wajibu pia wa kuhakikisha anatunza Hati za Maeneo ambayo anayasimamia na yeye wa Kanda ya Tabora ana Mikoa zaidi ya minne.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Barabara hii ambayo sasa hivi iko chini ya plan ya kujengwa kwa kiwango cha lami imekuwa na matatizo sehemu zile za Kizengi ambako madaraja yake ni mabovu na ikitokea dharura yoyote gari moja likazimikia barabarani magari mengine hayapiti. Je, katika kipindi hiki cha kungojea Serikali ina mpango gani wa kupanua Daraja lile la Kizengi?
Mheshimiwa Spika, pili, barabara hii inaunganisha Mikoa ya Dodoma, Singida na Tabora lakini hatuoni uharaka wa kujenga barabara hii. Je, Serikali sasa inaweza kutuambia ni lini hasa ujenzi huu utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Almas Maige kwamba tulichokisema, ile sentensi ya mwisho, kwamba TANROADS itaendelea kuifanyia matengenezo barabara hii ili iweze kupitika majira yote hii ni pamoja na madaraja. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi, matengenezo haya yanahusisha na madaraja.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili, nimhakikishie kwamba taratibu tumezianza na tutaanza kujenga hii barabara mara baada ya kukamilika evaluation na tukampata mkandarasi.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Ni lini Serikali itarudisha mitaala ya shule za upili ili iweze kuzalisha mafundi mchundo na mafundi sadifu kama ilivyokuwa zamani watu hawa walizewa kujitegemea? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi binafsi nikiwa ni mnufaika katika eneo hilo niliweza kutembelea katika shule nyingi ambazo zinatoa mafunzo ya ufundi, ikiwemo Ifunda, Mtwara, Bwiru na kadhalika. Lakini kitu nilichojifunza ni kwamba zile shule baada ya kuzichanganya na wanafunzi ambao wanasoma kidato cha tano na cha sita imejikutwa kwamba kwa upande wa ufundi ni kama vile ufundi haupo. Vilevile baada ya kuwa VETA ina uwezo wa kuingiza wanafunzi moja kwa moja katika masomo ya ufundi sanifu.
Kwa hiyo, ilionekana lile eneo kama linakuwa reduntant, sasa baada ya hapo tuliita timu kutafakari namna gani tunaweza tukaendelea na shule hizo. Jambo tuliloliona ni kwamba kwa hali ya sasa ambayo elimu imeongezeka na shule nyingi zinatoa wanafunzi wanaofaulu vizuri mpaka kidato cha nne, tunafikiria kwamba hizo shule zirejeshwe katika kutoa mafunzo ya ufundi sanifu, lakini baada ya kujenga shule ambazo zitawachukuwa wale waliokuwa wanasoma kidato cha tano na sita ili kusiwe na upungufu katika eneo hilo, kwa hiyo hali halisi ndio hiyo.
MHE. ALMASI A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru sana kuniruhusu kuuliza swali. Kituo cha Afya cha Upuge ndiyo peke yake Hospitali ya Wilaya Jimboni kwangu, hakuna hospitali kabisa isipokuwa Kituo kile cha Upuge na hakina wataalam wa dawa za usingizi, wanaitwa anesthesia kitaaluma, kwa hiyo, hatuwezi kufanya operesheni. Je, Serikali inafikiria nini kupeleka mtaalam wa dawa za usingizi ili operesheni zifanyike? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kituo cha Afya cha mtani wangu pale, katika idadi ya wataalam ambao tutawaajiri hapa katikati kutokana na nafasi nyingi zilizotolewa na Mheshimiwa Rais tutaangalia mahitaji halisi ya kituo hiki then tutawapa kipaumbele ili mradi wampate mtaalam huyo wa usingizi.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza ninaomba Bunge lako Tukufu litambue kwamba nina maslahi katika mifuko yote hii ya hifadhi ya jamii.
Swali langu la kwanza ni kwamba mifuko hii inatofautiana katika kukokotoa mafao ya wafanyakazi wanaoacha kazi au wanaostaafu. Kwanza mifuko inakokotoa kutokana na gross salary mapato yote ya mfanyakazi; pili inakokotoa kutokana na basic salary.
Mheshimiwa Naibu Spika, nini msimamo wa Serikali, ni kuhusu basic salary au gross income ya mfanyakazi?
Swali la pili, fao la kujitoa baadhi ya mifuko hii saba iliyotajwa inaitangaza kama ni fao kwa wafanyakazi wanaoacha kazi na mifuko mingine ni marufuku kabisa kulipa mafao kabla ya miaka 60. Je, ni nini msimamo wa Serikali? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Naibu Spika, nitayajibu yote kwa ujumla kwa sababu yanaingiliana. Kuhusu kukokotoa, kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa mwaka 2014 ambao ulianza kufanya kazi tarehe 1 Julai wenye vipengele 15 umeainisha namna ya ukokotoaji wa mafao kwa wafanyakazi ambao wamestaafu. Nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba mfumo uliowekwa kupitia SSRA ndiyo ambao unatumika na ndiyo ambao umeridhiwa mpaka hivi sasa, lakini kama kuna mapendekezo ya namna bora ya kuboresha, Serikali bado tupo tayari kuweza kusikiliza na kuona namna bora ya kuweza kuwasaidia wafanyakazi wetu ili wapate mafao ambayo wataweza kuwafanya wamudu maisha ya dunia ya leo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu sana kwamba Mheshimiwa Mbunge ni mdau mkubwa na ana mchango mkubwa sana katika eneo hili na nimpongeze kwa kazi kubwa ambayo ameifanya, naamini kabisa kwamba anayo nafasi kama Mwenyekiti wa ATE kushirikiana kwa pamoja wakaleta mapendekezo yao ili tuone namna bora ya kuweza kufanya. (Makofi)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu niulize maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuuliza maswali, naomba nieleze yafuatayo, kwa mara ya kwanza nasema Serikali imeshindwa kujibu swali Bungeni.

Hakuna Mahakama, Mahakama haifanyi kazi miaka kumi iliyopita na majengo yote pamoja na nyumba za wafanyakazi milango imetolewa yote na madirisha yamechukuliwa. Mimi nimefanya kazi ya kupeleka umeme pale kwenye Mahakama ile na Kituo cha Afya, hakuna Mahakama pale.
Mheshimiwa Spika, naomba sasa niulize maswali yangu mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, ni kwa nini Mahakama ile imetelekezwa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, ni kwa nini majengo ya Mahakama hiyo yasitumike na Idara nyingine za Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA - K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, katika utaratibu wa ufanyaji kazi wa kimahakama shughuli kubwa inayofanywa katika Mahakama ni suala zima la usikilizaji wa mashauri na uamuzi. Nakubalina na Mheshimiwa Mbunge kwamba ni kweli Mahakama ya Mwanzo ya Upuge ni chakavu sana, lakini shughuli za kimahakama zinaendelea wakati tunaendelea kujipanga kama Serikali ili baadaye tufanye ukarabati mkubwa wa kuweza kurahisisha ufanyaji kazi wa Mahakama.
Mheshimiwa Spika, tarehe 12/06/2017 kazi za Mahakama zilianza kufanyika kupitia katika baadhi ya ofisi pale katika Halmashauri na mpaka navyozungumza hivi sasa tayari mashauri 50 yalishawasilishwa pale Mahakamani na mashauri 41 yalishafanyiwa uamuzi. Pia pale katika Mahakama ya Upuge yupo Hakimu, mwanzoni tulikuwa tuna Hakimu anaitwa Bumi Mwakatobe ambaye alikuwa anatembelea, lakini sasa hivi yupo Hakimu wa kudumu anaitwa Jacqueline Lukuba ambaye yuko muda wote pale. Kwa hiyo, kuhusu suala la kwamba wananchi wanakosa fursa ya kupata huduma za kimahakama, wananchi wa Wilaya ya Uyui wanapata huduma hii kama ambavyo nimeisema hapo.
Mheshimiwa Spika, nimuahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba nafahamu changamoto tulizonazo kubwa ni kuhusiana na masuala ya bajeti katika Mahakama, lakini tunaendelea na ukarabati wa Mahakama zetu za Mwanzo na Mahakama za Wilaya, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba pindi utaratibu utakapokamilika tutafanya marekebisho makubwa katika Mahakama hii ili wananchi wa Uyui waweze kufaidika na huduma za Mahakama.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza.
Kwa vile matatizo haya ya afya katika Wilaya ya Kakonko yanafanana sana na ukosefu wa Hospitali ya Wilaya ya Uyui na Wilaya ya Uyui tumejitahidi kupitia Halmashauri kujenga hospitali lakini tumeishia kwenye OPD na tungeomba Serikali ituambie; je, inaweza kutuongezea hela ili tuweze kumalizia OPD yetu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli pale hawana Hospitali ya Wilaya na wameanza programu ya ujenzi wa OPD, lakini sasa hivi tunafanya needs assessment katika maeneo yote ambayo majengo yalianza bado hayajakamilika. Ndiyo maana katika harakati zetu sasa hivi tunakamilisha Kilolo, Mvomero lakini tunaenda kule Siha ninaamini kwamba Uyui. Naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mchakato tunaofanya hivi sasa na wataalam wangu pale ofisini tutaangalia nini tufanye, lengo kubwa tuikamilishe hospitali yetu ya Uyui na wale Wanyamwezi wa Tabora pale waweze kupata huduma kama Wanyamwezi wengine hapa Tanzania. (Makofi)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kuniruhusu niulize maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri, mimi nasikitika sana Serikali haisemi kwamba mimi ndiye niliyeleta Muswada Binafsi wa Sekta ya Ulinzi Binafsi (Private Security Industry Bill) wa mwaka 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa je, Serikali iko tayari kunilipia kunirudishia gharama hata nusu ya ghalama niliyoitumia katika utafiti huo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, na la pili, kwa kuwa mchakato wa kuipata sheria hii ya sekta ya ulinzi binafsi unakuwa mrefu sana, je, Serikali sasa iko tayari kutunga GN ambayo itatumika wakati huu wa mpito kwa sababu makampuni haya yalianzishwa bila GN wala sheria yoyote?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI):
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na swali lake la kwanza, awali napenda kuchukua furusa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Maige kwa mchango mkubwa sana ambao amekuwa akiutoa katika sekta binafsi ya ulunzi na hivyo kama Serikali tunathamini sana mchango wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Mheshimiwa Maige kuwasilisha muswada wake binafsi hapa Bungeni majibu ya Serikali yalikuwa kwamba Serikali itafanya kazi hiyo, kwa maana ya kuleta muswada huo ili ujadiliwe mbele ya Bunge na sheria hii iweze kutungwa.
Kwa hiyo, nimuombe tu Mheshimiwa Maige kwamba ile kazi kubwa aliyoifanya aichukulie kama ni sehemu ya mchango wake kwa Taifa hili; na yeye kama akiwa mzalendo namba moja basi aone kama ni mchango wake katika kusaidia Serikali katika kukamilisha utungwaji wa sheria hii. Ninafahamu sana kwamba Mheshimiwa huyu ni mzalendo, itakuwa ni sehemu ya mchango wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, la juu ya GN, katika majibu yangu ya msingi nimesma taratibu za utungwaji wa sheria zinaelekea kukamilika na hivyo namshauri Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tumeshapitia kote huko, hatua hii ilibaki atupe nafasi Serikali kuwasilishwa muswada huu ili sheria hii itungwe na baadaye zitakuja hizo GN zingine kwa ajili ya ku-regulate maswala ya ulinzi katika sekta binafsi.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, siridhiki kabisa na majibu aliyotoa Mheshimiwa Naibu Waziri, na huu ndio mzaha ambao hatupendi Wabunge. Milioni 20 mimi ninazo mfukoni hapa, si ningetengeza bwawa hilo? Halitengelezeki kwa milioni 20 bwawa hilo, Bwawa kubwa na limepasuka. Nataka kujua na alisema kwamba itatokana na ruzuku, nani anatoa ruzuku, hatujui; lakini hela zinakwenda kwa nani, hatujui; mkandarasi nani atafanya hiyo kazi hatujui, jibu hili si sahihi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sitaki tena kuomba mwongozo baadaye lakini ningependa Waziri anijibu vizuri, kwamba hizo hela zitatoka wapi na hela hizo hazitoshi, lakini je, lini hela zitapatikana? Hiloni swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tangu mwaka 2014/2015, 2016/2017, leo miaka mingapi? Barabara imejaa miti iliyoota, nani atatengeneza hiyo barabara ya kwenda kwenye bwawa kwa sababu haipitiki? Nataka kujua pia je, barabara ile itatengenezwa na nani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu milioni ishirini; mara nyingi kila mtu ana taaluma yake. Maana yake ma-engineer kama wamefanya assessment; kwa sababu ni ile sehemu iliyobomoka tu. Kama Mbunge anahisi kama shilingi milioni ishirini haitoshi; katika hili naomba niseme kwamba; kwa sababu bwawa limevunjika katika spillways; ngoja tupeleke hizo fedha halafu tuone nini kitaendea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakapofanya assessment; kama mtaalam wa maji, mabwawa, engineer amefanya assessment na amesema ni milioni ishirini, lakini Mheshimiwa Mbunge anasema haitoshi, aah, tutaangalia maana huyo mtu inawezekana qualifications zake hazimtoshi kukaa katika nafasi hiyo, ndiyo maana ameleta assessment ya milioni ishirini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili maana yake si kwa sababu yuko Jafo hapa; kwa sababu kuna mtu alifanya designing na assessment ya bwawa lilivyopasuka na amesema milioni ishirini. Isipotosha maana yake watu hawa ndio watakaokuwa wanakwamisha shughuli za maendeleo katika maeneo yetu, hatutaweza kuvumilia. Naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwa sababu nina safari ya kwenda Kaliua na Urambo nitapita kwenda kutembelea bwawa hilo na kuangalia hali halisi ikoje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini fedha hizi zitatoka katika Local Government Capital Development Grant kutoka TAMISEMI, naomba asihofu fedha hizo zitakwenda. Kuhusu suala la barabara kufika katika eneo lile naomba niseme kwamba hiki ni kipaumbele cha Halmashauri yenyewe kadri inavyosema kwamba bajeti yake inajenga barabara katika eneo gani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu naamini kwamba tutafika site tutakwenda kuiona hiyo barabara, basi waweke kipaumbele kama barabara hiyo ambayo haipo katika mpango lazima iwekwe katika mpango ili wananchi waweze kufika katika eneo hilo.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa vile kipande cha barabara hiki cha Mambali – Bukumbi – Shitage - Mhulidede mpaka Kahama kupitia Tulole ni muhimu sana kiuchumi kwa sababu ya biashara ya mikoa miwili hiyo; Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami?
Swali la pili, ni lini uchambuzi yakinifu na usanifu utaanza kwa ajili ya barabara hiyo? Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kufuatilia hii barabara, barabara hii ambayo anaizungumza kutoka Mambali – Bukumbi- inakwenda mpaka Mhulidede ni barabara ambayo inapakana na Jimbo la kwangu kule Ushetu. Kwa vile amekuwa akifuatilia barabara hii imewezesha hata kile kipande cha kilometa 21 nilichokitaja kwenda Tulole hadi Kahama Mjini ili kuleta ulinganifu na kuleta maana kimeanza kuhudumiwa.
Mheshimiwa Spika, namwomba tu Mheshimiwa Mbunge kwamba avute subira, Serikali imefanya juhudi kubwa sana kuunganisha mikoa na mikoa na kuunganisha mikoa na nchi jirani. Kwa vile kazi inaendelea vizuri nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa maeneo ya Bukumbi, Mhulidede, Mambali na majirani zake kule upande wa Bukene kwamba baada ya kazi nzuri ya kuunganisha mikoa sasa nguvu kubwa itaelekezwa kuunganisha barabara hizi ambazo zinaunganisha wilaya na mikoa.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge avute subira baada ya kuwa kazi nzuri ya kuunganisha mikoa na nchi za jirani ikikamilika basi zoezi la usanifu kwa kipande hiki cha barabara kutoka Mambali ambacho kimsingi kitapunguza umbali wa mtu anayetoka Tabora kwenda Kahama kwa takribani kilometa 50.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuvute subira tutakuja kufanya usanifu na kuweza kujenga barabara hii. Usanifu utaanza baada ya kuwa tumejipanga vizuri na kuhakikisha kwamba, sasa tunafanya muunganiko wa sehemu hii ya barabara.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri ambayo yako sawasawa na matakwa ya Wanauyui, DCC pamoja na RCC. Hata hivyo, nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa vile Serikali na wadau wengine wote wamekuwa wanalipa fedha zilizotakiwa kwenda Halmashauri ya Uyui, I mean Tabora District Council, zimekuwa zinalipwa halmashauri au manispaa; je, Serikali sasa itakuwa tayari kusaidia hela zote ambazo zimelipwa manispaa na manispaa wakazitumia, ili ziweze kurejeshwa katika Halmashauri ya Uyui?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa vile maelekezo ya Serikali ni kwamba, tukae sasa Baraza la Madiwani, DCC na RCC tuombe kubadilishiwa jina la Tabora Kaskazini ambalo halina Mashariki, Kusini wala Magharibi liweze kuwa Jimbo la Uyui. Je, Serikali, yeye Waziri ataunga mkono jambo hili ili liweze kupita haraka kama ambavyo tunapendekeza sisi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza, kuhusu mkanganyiko wa jina, nataka nimwambie Mheshimiwa Maige na wadau wote wa Mkoa wa Tabora na nchi nzima kwamba hakuna mkanganyiko wowote wa jina; kwa sababu Halmashauri ya Manispaa ya Tabora hailingani kwa vyovyote vile na Halmashauri ya Wilaya ya Tabora, kwa hiyo, hakuna tofauti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utendaji, wale watendaji wa Serikali wanaokosea kupeleka fedha za Halmashauri ya Wilaya ya Tabora wakazipeleka kwenye Halmashauri ya Manispaa ya Tabora wamefanya makosa. Kwa hiyo, fedha zote ambazo zimekwenda Manispaa ya Tabora ambazo ni za Halmashauri ya Wilaya ya Tabora zinatakiwa zipelekwe Halmashauri ya Wilaya ya Tabora na kama kuna fedha zilikwenda kimakosa zirejeshwe haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa mwenyekit, katika swali lake la pili; sisi katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kwa sababu hatuna mamlaka na jina la jimbo, tunawaunga mkono Halmashauri ya Wilaya ya Tabora ambao pengine baada ya muda mfupi ujao itakuwa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui. Wakipendekeza jina Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwamba, jina la Tabora Kaskazini sasa libadilishwe sisi tutawaunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana leo ya Waziri wa Ulinzi ndugu yangu Mheshimiwa Mwinyi nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa vile idadi inayochukuliwa kwa mwaka ni ndogo sana ukilinganisha na idadi ya wanafunzi wanaomaliza shule form six na vyuo. Je, Serikali haioni umuhimu wa kupanua kiasi idadi ya wanafunzi hawa ili wapate mafunzo ambayo tunafikiri kwamba ni ya maadili na uzalendo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa vile vijana wengi wanaotoka baada ya mafunzo kutoka JKT husahau au kuacha mafunzo mazuri na maadili waliyofundishwa kule JKT. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwafuatilia vijana hawa ili wasisahau mafunzo na kuacha maadili mazuri ya wananchi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Almas Maige kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu idadi ndogo ya vijana tunaowachukua kwa mujibu wa sheria, ni kweli kwamba wahitimu sasa hivi wanazidi 60,000, lakini uwezo wetu wa kuchukua inakadiriwa kuwa ni kama 20,000 peke yake. Kwa hiyo iko mikakati ya kuhakikisha kwamba tunaongeza idadi ya vijana wanaochukuliwa kwenda JKT kwa kuboresha miundombinu katika kambi tulizonazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaendelea kuziboresha ili ziweze kuchukua vijana wengi zaidi na ni matumaini yetu kwamba kila mwaka tutaendelea kuongeza idadi. Hata hivyo, hivi karibuni tu tumefungua kambi mpya tano katika Mikoa ya Rukwa kule Milimbikwa na Ruwa, Mpwapwa Dodoma, Makuyuni Arusha, Itaka pamoja na Kibiti. Kwa hivyo ni mategemeo yetu kwamba, kwa kuongeza kambi hizi mpya idadi ya vijana tunaoendelea kuwachukua itaongezeka ili hatimaye wote wanaomaliza form six waweze kujiunga kwanza na JKT kabla hawajaanza vyuo vikuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la kufuatilia vijana ili wasisahau maadili nadhani hili ni wazo zuri. Mpaka sasa hivi hakuna mkakati wa kuwarudisha tena lakini tunalipokea tutaangalia njia bora zaidi ya kulifuatilia.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana na mimi kuniruhusu niulize swali la nyongeza katika suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuhusu raia wageni kushiriki mambo ya ndani ya nchi yetu katika Jimbo la Mchinga inafanana sana na hali ilivyo katika kambi za wageni katika Mikoa ya Kigoma na Tabora hasa Ulyankulu na Katumba. Katika maeneo hayo wageni wamekuwa wengi wanafanya maamuzi kwa ajili ya Watanzania waliopo pale. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaangalia wakimbizi wale wasifanye maamuzi yanayohusu Watanzania? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. ANTONY P. MAVUNDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria za nchi yetu zimeweka wazi namna ambavyo wageni wataingia nchini na shughuli zao zote zinaratibiwa kwa mujibu wa sheria. Inapotokea kuna wageni wowote wameingia nchini wanafanya mambo kinyume na sheria tafsiri yake ni kwamba wanavunja sheria za nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu limeletwa hapa Bungeni, tunalipokea na tutalifanyia kazi kuhakikisha kwamba wageni wote waliopo huko wafuate sheria za nchi yetu na pia tunawaagiza maafisa wetu wa Serikali kuhakikisha kwamba wanalifuatilia jambo hilo ili waweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushuru sana kuniruhusu niulize hili la nyongeza, lakini kwanza nianze na shukurani kubwa sana, Mheshimiwa Waziri wa Nishati alikuja jimboni kwangu kuzindua REA III. Naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri kwa nini mkandarasi hajaanza kazi kwenye barabara ile ya kuja nyumbani kwangu, kijiji cha kwetu Kasenga, Majengo, Ikongolo, Kanyenye na Nzubuka?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Maige kwa swali lake la nyongeza. Kwanza nikubaliane na Mheshimiwa Maige, ameshafanya vijiji kumi na viwili kwenye jimbo lake lakini vijiji vya barabara ndiyo anaendelea navyo. Kwa hiyo, ni shauku ya Mheshimiwa Maige na wananchi kwamba vijiji vyote vingepatiwa umeme kwa siku moja. Nimhakikishie Mheshimiwa Maige kwamba hivi sasa anaendelea na Kijiji cha Lipogolo na kuna Kitongoji kinaitwa Kwa Muni ndipo anakosimika nguzo. Kwa hiyo, niungane na Mheshimiwa Mbunge kwamba ameshamaliza vijiji vya ndani sasa ameanza kufanya kazi katika vijiji vya kandokando mwa barabara. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Maige vijiji vyake kumi na moja vilivyobaki, vyote vitapelekewa umeme katika round hii ya kwanza.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nami niulize swali la nyongeza kuhusu REA. REA haikupita kabisa katika vijiji vya Kanyenye, Majengo, Ikongolo, Kiwembe, Zumbuka na Igulawima, tukategemea kwamba REA Namba Tatu itatusaidia hilo, lakini sasa mkandarasi haonekani. Lini mkandarasi ataonekana katika vijiji hivyo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Almas juu ya lini Mkandarasi atafika katika maeneo yake kutekeleza mradi katika vijiji alivyotaja?
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme, kwa kweli Wakandarasi kwa sasa hivi wako site na kwa kuwa kupitia Bunge lako na kupitia Wizara ya Fedha na Benki Kuu kwamba zile pesa shilingi bilioni 268 Letter of Credit zimefunguliwa pamoja na dola milioni 52. Kwa hiyo, nataka niseme wakandarasi wote hawana kisingizio tena waende site, wafanye kazi ili miradi hii ikamilike kwa wakati na hakutakuwa na msalie Mtume. Ahsante. (Makofi)
MHE. ALMAS. A MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naipongeza sana Serikali kwa fedha ambazo imetupatia kwa ajili ya Kituo cha Upuge na fedha ambazo zinapelekwa kwenye zahanati hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo naomba niseme ukweli kwamba methali ya kwamba mzigo mzito mpe Mnyamwezi, hatuitaki tena kwa sababu inatukandamiza. Tunasema mzigo mzito punguza, beba mwenyewe. Kwa sababu tumegundua kwamba kumbe mzigo mzito ni kutokuwa na vituo vya afya, kutokuwa na barabara huko kwetu, hatutaki tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunataka Bunge hili lielewe kwamba Wilaya yote ya Uyui ina kituo kimoja tu cha afya, sidhani kama kuna Wilaya nyingine hapa Tanzania iko namna hiyo, lakini vilevile hakuna tena hospitali ya Wilaya katika Wilaya nzima. Kwa hiyo, vituo vya afya vilivyopo, zahanati hizi ndiyo tunazoomba zipanuliwe ziweze kuwa vituo vya afya. Kwa hiyo, wananchi wa Kata ya Usagari, wamechanga shilingi milioni 50 wakiwa na lengo la kupanua kituo kile kiwe kituo cha afya na maeneo yapo. Tunaona ni bora kuongezea kuliko kujenga upya…
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali, je, Serikali iko tayari kubadili msimamo wake ili hela za wananchi, shilingi milioni 50 na Mfuko wa Jimbo wa shilingi milioni 10 watuongezee tupanue kituo kile kiwe kituo cha afya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, samani swali langu la pili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; kwa kujua hali ilivyo kule Jimboni kwangu kwamba hakuna kituo cha afya, hakuna zahanati bora zaidi ya hiyo ya Migungumalo; je, Serikali iko tayari kutusaidia kujenga kupandisha Zahanati za Ilolanguru na Ufuluma ili vitumike kwa muda kama vituo vya afya?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la mtani wangu Mnyamwezi wa Tabora kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata maombi yake Mheshimiwa Maige. Hata hivyo naomba nikiri wazi kwamba Mbunge huyu amekuwa mpiganaji sana wa eneo lake. Hata siyo muda kwa kazi kubwa anayofanya, hata jina la Halmashauri yake muda si mrefu sana litabadilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu kwamba kutokana na changamoto, ndiyo maana tuliwapa fedha kuimarisha Kituo cha Afya cha Upuge ambacho sasa hivi kinaenda vizuri, lakini hata katika bajeti ya mwaka 2018/2019 kutokana na shida kubwa waliyokuwa nayo tumewapa takriban shilingi bilioni 1.5 watajenga Hospitali ya Wilaya. Vilevile kabla ya tarehe 15 mwezi wa saba katika Jimbo la Igalula tutapeleka fedha nyingine kwa ajili kuimarisha kituo cha afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba wananchi wa jimboni kwako tutafanya kila liwezekanalo ili kama kuna vituo ambavyo vinatakiwa tuvipe hadhi, tutaangalia nini tufanye, lengo letu kubwa kama Serikali ni kuhakikisha kwamba Wanyamwezi wa Tabora wanapata huduma ya afya vizuri kama wengine. (Makofi)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kuniruhusu niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Jimbo la Tabora Kaskazini lina vyanzo vichache sana vya maji, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kusafiri na mimi kwenda kutembelea chanzo kikubwa cha maji pale Kijiji cha Majengo Ikuza ili kuona kama kinafaa kugawa maji kwenye vijiji vya karibu vya Kanyenye, Ikongolo, Kiwembe na Majengo yenyewe?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, niko tayari na tayari nimeshazungumza naye, majukumu hayo nimemkabidhi Mkurugenzi wa Mamlaka wa Maji ya Tabora ili aende akatembelee eneo lake na kutumia chanzo hicho cha maji ili Jimbo lake lipate maji safi na salama.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya mdogo wangu Mheshimiwa Waziri Dkt. na pamoja na kunikaribisha Ofisini kwake na kulijadili suala hili nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, kwa vile kituo hiki kina mfanyakazi mmoja tu. Huyu mfanyakazi mmoja atafundisha wanyama yeye, atatengeneza zana za kilimo yeye na hili ndio ninalosema suala la mzigo mzito kumpa Mnyamwezi hebu tuache, mzigo mzito wapunguze wabebe wenye mzigo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni umuhimu wa kuongeza wataalam kituoni pale ili waweze kufundisha na kutengeneza vifaa vingi au zana za kilimo kwa ajli ya wanyamakazi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, je Serikali ina mpango gani sasa wa kupeleka mitambo mipya baada ya kupata umeme ili waweze kutengeneza zana za kilimo kwa ajili ya wakulima wangu jimboni kaskazini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akifuatilia suala hili kwa kipindi kirefu na pia ameweza kufika hata ofisini kwetu kwa ajili tu ya wananchi wake wa kule Upuge pale Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nikija katika maswali madogo mawili ya nyongeza ni kweli kabisa kwamba kituo hiki cha Upuge kina mtaalam mmoja, lakini kama Serikali kama Wizara ya Kilimo tulishatoa vituo vyote hivi vya zana za kilimo kwenye halmashauri zote nchini. Kwa maana hiyo nihase halmashauri zote nchini kuhakikisha kwamba zinatilia mkazo vituo vya zana vya kilimo ili viweze kufanya kazi kwa ufanisi.
Mhesimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine katika swali lake la pili la nyongeza, ni kweli kulikuwa hakuna umeme na kwa sababu umeme umeshapatikana, Wizara yangu nitatuma wataalam kwenda pale Upuge kufanya assessment kabla ya mwezi wa Nane, kwa sababu kuna mashine zingine pale hazijawahi kutumika kama ile ya vipuri vile vya kuchongea. Nakushukuru.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana nami kuniruhusu niulize swali la nyongeza kwenye swali hili 496. Kwa vile Jimbo zima la Tabora Kaskazini lina kituo kimoja tu cha afya na Mheshimiwa Rais alipopita katika Jimbo langu aliambiwa tatizo hili na akachangia shilingi milioni 10 ili kujenga Kituo cha Afya pale Mwagelezi na Mbunge akachangia shilingi milioni tano. Je, Serikali iko tayari kutuongeza hela ili kituo kile kikamilike? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kwa dhati kabisa nipongeze juhudi ambazo Mheshimiwa Mbunge amekuwa akizifanya kwa kushirikiana na wananchi wake. Jana tumepokea barua yake ambayo inaonesha jinsi ambavyo amechangia kutoka Mfuko wa Jimbo na pia katika kutoka vyanzo vyake katika suala zima la kuhakikisha afya inaboreshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie, kwa jitihada na nguvu ambazo ameanzisha pamoja na wananchi wake, kwa kadri nafasi itakavyoruhusu na bajeti ikiruhusu hakika hatutasahau kuhakikisha kwamba tunapeleka huduma ya afya. Kama ambavyo amekuwa akisema kwamba siku hizi mzigo mzito humbebeshi Mnyamwezi unampunguzia unataka kila mtu abebe wa kwake, naomba nimhakikishie kwamba ni azma ya Serikali kuhakikisha kwamba huduma ya afya Uyui inaboreshwa. (Makofi)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru sana na mimi niulize swali moja dogo la nyongeza kuhusu suala la tumbaku. Tumbaku ndiyo siasa na ndio uchumi wa Mkoa wetu wa Tabora. Tatizo kubwa ni masoko, mwaka jana hapa mpaka tukapewa majina ya wazee wa tumbaku na akinamama wa tumbaku, sisi Wabunge wa Tabora. Swali, je, Serikali imefanya nini ili kutafuta masoko mengine ya tumbaku ili sisi tuuze tumbaku yetu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue fursa hii hata yeye Mheshimiwa Mbunge pia kumpongeza; kama alivyosema kwamba ni kweli tumbaku ni maisha kwa wananchi wote wa Mkoa wa Tabora na maeneo yote yanayolima tumbaku. Hata hivyo, kama Serikali tumejipanga. Sasa hivi tuna kampuni nne na tayari tumeshaanza kufanya mazungumzo na tumeongea na nchi ya Vietnam nao pia wamekubali kununua tumbaku yetu. Katika msimu huu wameahidi kabisa kwamba watanunua tani 1000 za tumbaku. Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa amjibu mazuri ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini umeona kwamba kuna utata wa maneno fundi sadifu na fundi mchundo na hilo limekuwa tatizo la elimu yetu. Fundi mchundo niartisan na Serikali imefanya vizuri sana lakini fundi sadifu ambaye ni Full Technician Certificate (FTC) holders ndio tuna upungufu mkubwa. Technical field inafanya kazi, ma-engineer wanawatelemshia hawa watu wa fundi sadifu na fundi sadifu wanawateremshia watu wa artisans.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo limekuwa tatizo, kuna gap kubwa kati ya wahandisi (engineers) wanaofanya kazi na kwenda kuunganisha huku chini nafasi katikati imepotea. Baada ya hapo nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya sana kazi ya kuanzisha Shule za Kata, zimeenea maeneo yote ya vijijini na kata. Je, Serikali sasa haioni umuhimu wa kuzifanya baadhi ya Shule za Kata ziwe shule za ufundi ili kumwaga mafundi katika ngazi za vijiji na kata ili kuijenga sera hii ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali imeamua kujenga VETA na kwa kuwa Jimbo langu la Tabora Kaskazini hakuna chuo hata kimoja cha VETA. Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Chuo cha VETA katika Jimbo la Tabora Kaskazini.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwanza kuna vyuo vya ufundi ambavyo vinasimamiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia lakini pia kuna shule hizi za ufundi ambazo zimekarabatiwa kama nilivyotaja na tunaomba tupokee wazo lake tulifanyie kazi, tukiona linafaa itafanyiwa kazi na kutekelezwa ili kuongeza na kupunguza gap ambalo amelizungumza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili ameuliza kama kuna kuna uwezekano wa kuanzisha Chuo cha VETA katika Jimbo lake la Tabora Kaskazini, tunaomba tulipokee ni wazo jema likifanyiwa kazi atapata majibu kwa wakati muafaka. Ahsante.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kuniruhusu na mimi niulize swali moja la nyongeza kuhusu tumbaku kwa sababu tumbaku Tabora ndio siasa yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vyama vingi vya msingi vimekufa au vimesinzia au havifanyi kazi kutokana na mfumo wa zamani uliokuwepo na hasahasa utoroshaji wa tumbaku, kukwepa madeni kupitia vyama vya IF. Sasa mfumo mzuri umewekwa na kwamba madeni yamedhibitiwa. Je, Serikali kupitia Benki ya Kilimo haiwezi kuwadhamini wanachama hawa wa vyama sinzia ili vilime tumbaku kwa mkakati wa kulipa madeni?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Maige, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze kwa ufatiliaji wake wa karibu wakulima wake wa tumbaku. Swali la Mheshimiwa Maige ni kwamba TADB inawasaidiaje wakulima kupitia vyama vya msingi. Jibu ni kwamba Serikali inaendelea kufanya jitihada kwanza ya kufufua vyama vya msingi viweze kuzingatia utawala bora (good governance) kwani kwa kipindi cha nyuma vyama vya msingi baadhi ya viongozi walikuwa siyo waadilifu kwa hiyo fedha nyingi zilikuwa zinapotea kwa njia hiyo kwa sababu walishindwa kuzisimamia vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mkakati wa Serikali wa kuboresha ushirika na kuhakikisha vyama vya msingi vinakuwa na viongozi waadilifu basi tumhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakaa na TADB na kuangalia ni namna gani tunaweza tukaratibu jambo hili ili wakulima kupitia vyama vya msingi waweze kupata mikopo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, ni majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia. Je, yupo tayari kufuatana na mimi kwenda kuangalia eneo ambalo tayari Wilaya ya Uyui tumeliweka kwa ajili ya VETA?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, sina shida ya kuandamana na Mheshimiwa Mbunge na akipenda vilevile anaweza akawa na Wabunge wa Viti Maalum wa Mkoa husika wakati wa kutembelea eneo hilo. kwa hiyo, tukitoka tutapanga ili tuweze kutembelea huko.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza. La kwanza, kwa vile tozo hii ya asilimia 4.5 ya mshahara wa mfanyakazi ni kubwa kuliko tozo zote duniani. Siyo Afrika tu, dunianina hapa Afrika Mashariki tozo hii inatozwa asilimia 1.2 Kenya tu, tena kwa ajili ya sekta moja ya utalii. Swali la kwanza, je, Serikali haioni umuhimu wa kupunguza tozo hii ili kufanya utendaji wa biashara hapa nchini uwe rahisi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, hapa Tanzania tunafanya biashara au kazi kwa utatu, yaani Serikali, Wafanyakazi na Waajiri,VETA kuwa chini ya Wizara ya Elimu, imetutoa katika mfumo huo. Je, Serikali haioni sasa ni muhimukurudisha VETA chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambako kuna Kazi, Ajira na Mafunzo.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Almas Maige kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kuhusu kwamba SDL tunayotoza sisi ni kubwa kuliko zote zinazotozwa duniani, siwezi kuwa na uhakika kuhusu hilo. Hata hivyo, concern au hoja ya kupunguza kodi hiyo au tozo hiyo tayari imeshawasilishwa Serikalini. Hata juzi wakati wa Maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Chama cha Waajiri Tanzania waliileta kwa msisitizo mkubwa na Mheshimiwa Rais aliitolea maelekezo kwamba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayehusika na masuala ya Kazi na Ajira ajaribu kuwakutanisha utatu ule ambao Mheshimiwa Maige ameusema, yaani Serikali, Wafanyakazi na Waajiri ili waweze kujadiliana wapate muafaka kuhusu namna bora ya kuratibu tozo hii.

Mheshimiwa Spika, watakapokutana, itabidi sasa jambo hilolipelekwe kwenye kikosi kazi kinachohusiana na mambo ya kodi, yaani ile Tax Reform ili waweze kujadili na ikiwezekana mapendekezo yaweze kutolewa na ikibidi sheria ije Bungeni irekebishwe ili sasa tuwe na tozo ambayo imekubalika na pande zote.

Kuhusiana naswali lake la pili kwamba kwa nini VETA isihamishiwe Ofisi ya Waziri Mkuu ambaye ndiye hasa inahusika na masuala ya ajira. Kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, Serikali ni ileile. Kwa hiyo, kuhusu kwamba jambo fulani linatakiwa liwe wapi wakati fulani, ni masuala ya maamuzi tu ya muda na inategemea sana kwa wakati huo, kwamba umuhimu au mahitaji yanahitaji iwekwe wapi. Kwa vyovyote vile, masuala ya ufundi stadi ni suala la elimu vilevile. Kwa hiyo, siyo kwamba kuna shida ikiwepo kwenye Wizara ya Elimu, lakini kama tunavyosema, itaendelea kubadilika kulingana na maamuzi ya Serikali kwa wakati husika.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza, naomba nitoe kwa dhati kabisa shukrani kubwa kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, kwa miradi mingi aliyoweka katika Jimbo langu. Naomba niitaje hapa kwa niaba ya Bunge ili lielewe miradi gani ipo Jimboni kwangu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, upo Mradi wa Maji ya Ziwa Victoria ambao ni sehemu ya shilingi bilioni 600; Kituo cha Afya cha Upuge, shilingi milioni 850; Hospitali ya ngazi ya Wilaya Isikizye shilingi bilioni mbili; Kituo cha VETA kinachojengwa Isikizye, sasa ni shilingi bilioni tano; Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Magharibi mabilioni na umeme wa REA wa vijiji 18 mabilioni ya shilingi. Naomba salamu hizi na pongezi zimfikie Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Je Serikali ina mpango gani kupelekea maji vile vijiji 42 vilivyobakia? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili: Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka wataalam wa maji ili kuchunguza vyanzo vya maji katika vijiji vya Kata za Ufuluma, Shitage, Nsimbo, Bukumbi, Makazi na Igulungu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri aliyekuja kufuatilia mradi huko kwetu, nasi tumemwekea binti aende akaoe. Karibu sana Mheshimiwa Aweso. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, lakini nashukuru kwa zawadi aliyonipa. Nataka nimhakikishie mimi beberu, siyo jogoo la pasaka bwana, nipo tayari. (Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kama Serikali ambacho nataka kusema ni kwamba tumejipanga vizuri katika kuhakikisha tunaondoa kabisa tatizo la maji katika Mkoa wa Tabora. Tuna mradi mkubwa zaidi ya shilingi bilioni 600. Pamoja na hayo, kutokana na mapenzi makubwa na mahaba ya Mkoa wa Tabora, tumeshapeleka shilingi 8,345,000,000/= katika kuhakikisha tunaendelea kutatua tatizo la maji na fedha hizi tutatekeleza kwa kutumia wataalam wetu wa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, sisi kama Wizara ya Maji tupo tayari kupeleka wataalam kufanya usanifu kwa vijiji ambavyo havijapata maji ili viendelee kupata huduma hii muhimu sana ya maji. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya kitaalam kuhusu uUwanja wa Ndege wa Ipole nilitaka kujua sasa, je, lini uwanja unaopendekezwa katika mapori ya Ugala utamalizika?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nina swali la pili, Serikali ina mpango gani wa kuyatangaza maeneo ya Kwihara pamoja na yaliyokuwa makazi ya Marehemu Mirambo kwa ajili ya utalii? Ahsate sana.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Almas, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kumpongeza Mheshimwia Almasi pamoja na kwamba ameuliza kwa niaba ya Mheshimiwa Joseph Kakunda, pia amekuwa ni mshauri mzuri na mdau mzuri sana wa mambo ya utalii. Kama nilivyojibu kwenye jibu letu la msingi ni kwamba tulisitisha ujenzi wa Uwanja wa Ndege ya Ipole kutokana na ushauri wa kitaalam tuliopata kutoka Wizara ya Mawasiliano. Tulielekeza Wilaya kuangalia eneo lingine ambalo linafaa kwa ajili ya ujenzi. Kwa bahari mbaya eneo lote linalozunguka maeneo hayo ni ardhi oevu na ni eneo ambalo ni chepechepe yaani wetland na imekuwa vigumu kupata eneo ambalo tunaweza tukajenga uwanja kwa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika Hifadhi mpya ya Ugala tunavyo viwanja viwili vidogo vya ndege, kiwanja cha Siri na kiwanja cha Muhuba ambavyo vipo kama takribani kilometa 100 kutoka uwanja wa Ipole ulipokuwa. Kwa sasa Wizara yetu imebadilisha hadhi ya Pori la Akiba la Ugala na kuwa Hifadhi ya Taifa, tumeelekeza TANAPA kuboresha viwanja hivyo ili viweze kutumika wakati wote kwa huduma ambazo zilikuwa zimekusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili ni mpango wa kuyatangaza makazi au maeneo ya kale ya Mtemi Mirambo. Kama tulivyofanya nchi nzima tumeelekeza maeneo mengi ya mali kale kuchukuliwa na Taasisi zetu zote zinazofanya utalii nchini. Eneo hili la Mirambo kama tulivyofanya kule Iringa tutawaelekeza TANAPA kuwekeza pale utaalam na nguvu ili kuhakikisha kwamba tunayahusisha katika product ya utalii kuwawezesha watalii wanaotua Tabora na maeneo mengine ya Mkoa wa Tabora kuyafahamu maeneo haya ya historia.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nami niulize swali la nyongeza katika swali la 79 linalohusu maji. Naishukuru sana Serikali yangu, imetuletea maji kutoka Ziwa Victoria na inachukua kata 10 za Jimbo langu, lakini kuna kata zinazobaki zaidi ya nane hazipati maji:-

Je, Serikali ina mpango gani kupeleka maji kwenye kata ambazo hazipati maji ya mradi wa Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge na nimeshafika pale Uyui, lakini ninachotaka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, Serikali imefanya jitihada kubwa sana zaidi ya shilingi bilioni 600 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi mkubwa utakapofika katika Jimbo lake la Uyui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa naaka nimhakikishie maji yatafika Uyui na maeneo ambayo hayana maji tutahakikisha yale maji yaweze kufika na wananchi wake waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri na juhudi kubwa inayofanywa na Waziri wa Nishati ninayo maswali mawili ya nyongeza.

(i) Kwa vile katika mradi huu wa REA III uliokuwa na vijiji 18 katika Jimbo langu ni vijiji vinne tu ndiyo vimepata umeme mpaka sasa. Je, ni lini vijiji vyote 18 vitapata umeme?

(ii) Kwa kuwa Jimbo langu lote la Tabora Kaskazini lenye vijiji 82 ni vijiji saba tu ndiyo vimepata umeme. Napata wasiwasi kama kweli umeme utaenea karibu vijiji vyite 82. Je, Serikali inawahakikishia wananchi wa Jimbo la Tabora Kaskazini kwamba vijiji vyite 82 vitapata umeme?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya swali la msingi la Mheshimiwa Almas Maige, lakini zaidi nimpongeze sana Mheshimiwa Maige anavyofuatilia masuala ya umeme katika Jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya mwaka 2015 Jimbo zima la Tabora Kaskazini halikuwa na kijiji chochote chenye umeme lakini kwa juhudi kubwa alizofanya Mheshimiwa Maige kufuatilia upatikanaji wa umeme hadi sasa tuna zaidi ya vijiji saba vina umeme. Kwa hiyo, nipende kumpongeza Mheshimiwa Maige lakini niwaombe wananchi wa Jimbo la Tabora Kaskazini wawe na imani na Serikali kwa sababu vijiji vyote 82 vitapelekewa umeme ifikapo mwezi Juni, 2021.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maswali yake mawili ya nyongeza kuhusiana na vijiji 18 ni lini vitapate umeme?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa mkandarasi anaendelea na vijiji vingine pamoja na kwamba ameshawasha vijiji saba alivyotaja Mheshimiwa Mbunge lakini tarehe 25 mwezi huu, mkandarasi atawasha vijiji vingine vine ikiwemo Kijiji cha Ibushi, Kagera ya Nsimbo, Majengo ambako Mheshimiwa Mbunge unatoka kwenye Kata ya Ikongolo pamoja na Mputi navyo vitawashwa umeme tarehe 25 mwezi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 15 mwezi ujao vijiji vingine vitawashwa umeme ikiwemo Kijiji cha Mkalya, Mpenge pamoja na Ngokoro. Kwa hiyo niwape taarifa wananchi ambavyo Mheshimiwa Mbunge anavyofanya kazi vijiji vyote vya Tabora Kaskazini vitapelekewa umeme ifikapo Juni mwaka 2020/2021.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri wa Elimu amejibu kwa kutumia sera, lakini swali langu mimi hapa lilitumia sheria na bahati nzuri sana amelielezea vizuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa Kiswahili kimekuwa na kuwa moja ya lugha mashuhuri sana Duniani ambayo chimbuko lake ni Tanzania. Je, Serikali haioni umuhimu wa Kiswahili kutumika sasa kuwa lugha ya kufundishia katika elimu yetu kwa ngazi zote? Swali la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa Kiswahili sasa kimekuwa na kuwa bidhaa muhimu sana ya kuuza nchi za nje na hivyo kuingiza hela kupitia walimu wa Diaspora. Je, Serikali ina mpango gani wa kukikuza Kiswahili na kukiuza nje ya nchi? (Makofi)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante ningependa kumjibu Mheshimiwa Almas Maige maswali yake ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kuhusiana na lugha ya Kiswahili ambayo hakika ni ligha adhimu na imeendelea kushika kasi, suala la kutumia lugha hiyo kufundishia kama nilivyoeleza katika majibu yangu ya msingi lugha hiyo inatumika katika kufundisha katika shule za elimu ya awali, msingi na vyuo vya ualimu ngazi ya kati na bado Serikali inaona kuna umuhimu wa kutumia lugha ya kiingereza kama ambavvyo nilisema katika majibu yangu ya msingi na ndio maana ukiangalia hata Waheshimiwa Wabunge wengi humu ndani wanawapeleka watoto wao kwenye english medium kwa sababu wanatambua umuhimu wa lugha hiyo, kwa hiyo Serikali itaendelea kutumia lugha zote kama ambavyo imeelezwa katika sera ya elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kukuza Kiswahili, kwanza nshukuru kwamba lugha yetu ya Kiswahili imeendelea kupendwa na baadhi ya nchi wamekuwa wakiomba Tanzania kuweza kufundisha lugha ya Kiswahili katika nchi zao kama vile Sudan Kusini, Afrika ya Kusini pamoja na nchi nyingine. Kwa hiyo ni lugha ambayo Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba tunaimarisha na suala la lugha ya Kiswahili sio suala tu la kujua kuzungumza, lakini pia lina suala la usanifu wa lugha ya Kiswahili, kwa hiyo tutaendelea kuhakikisha kwamba tunaimarisha ili fursa zinazojitokeza Watanzania waweze kunufaika zaidi. (Makofi)
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kijiji cha Migungumalo, Kata ya Usagari, Marehemu Mheshimiwa Benjamin William Mkapa alizindua zahanati ndogo na aliahidi kwamba pale patajengwa kituo cha afya ili iwe hospitali kubwa ambayo atakuja kuifungua tena. Nilipoingia madarakani tumeanzisha kujenga kituo kile na kwa uchungu sana nilikuwa nimepanga kwenda kumwambia Mheshimiwa Benjamin Mkapa kwamba sasa ajiandae kuja kufungua kituo kile na bahati mbaya Mheshimiwa Mkapa amefariki, Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Nimeshamwambia Mheshimiwa Rais juu ya suala hilo…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Maige, swali lako la nyongeza?

MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu, kwa vile kituo kile tunakijenga kwa nguvu za wananchi, je, Serikali ina mpango gani wa kukimalizia kituo hicho ili heshima ya Marehemu Benjamin Mkapa ihimidiwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Jimbo la Tabora Kaskazini kwa kuchangia maendeleo na kuanza ujenzi wa kituo hicho cha afya ambacho lengo ni kupandisha hadhi ya zahanati kuwa kituo cha afya. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Maige kwamba katika bajeti ya Serikali ya kwenda kukamilisha majengo ya zahanati na vituo vya afya ambayo imetengwa katika mwaka huu wa fedha katika halmashauri yake na katika jimbo lake, jumla ya vituo vinne vimetengwa na jumla ya shilingi milioni 200 zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo eneo hilo la kituo hicho cha afya ambacho ilikuwa ni ahadi ya Mheshimiwa Rais, basi tutakwenda pia kuona namna gani tunashirikiana katika bajeti hii, lakini pia katika bajeti zinazofuata, ili tuweze kukikamilisha kiweze kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwanza niishukuru Serikali kwa majibu mazuri kwamba na matumaini kwamba tutajengewa Mahakama yetu mwaka 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini je, kwa kipindi hiki ambacho Mahakama ya Wilaya ya Uyui iko ndani ya chumba kidogo sana katika jengo lile la DC. Je, Serikali ina mpango gani wa kutafuta jengo kubwa ili kutatua tatizo hilo la jengo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa vile yako majengo ya Mahakama ya awali ya Mwanzo ya Upuge yametelekezwa na ni makubwa yana nyumba za wafanyakazi na sasa kuna umeme wa REA, lakini pia kuna maji ya Ziwa Victoria na barabara nzuri; je, Serikali haioni ni busara kuanza kutumia majengo yale ya Mahakama ya Mwanzo ya Upuge kwa shughuli za Mahakama ya Wilaya ya Uyui?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria nipende kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maige kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza hili la kutumia chumba kidogo hili tutalifanyia kazi haraka sana, nadhani mamlaka zinanisikia huko ni muhimu kuanza kufanya tafiti ili kujua tunaweza tukapata chumba wapi kikubwa ambacho kinaweza kikatoa huduma hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hii Mahakama ya Mwanzo Upuge nitaifuatilia kwa karibu kuona inaanza kazi mara moja kwa sababu kwanza, tunasema tunaupungufu wa vyumba halafu kumbe kuna nyumba zingine zimekaa hazifanyi kazi, kwa hiyo nadhani hili tumelichukua na tutalichukulia hatua haraka sana, ahsante.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli sijapata majibu mazuri namna hii katika Serikali hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, namshukuru sana. Nawapongeza sana Wizara ya Maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo nina maswali madogo tu mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vile vijiji vitano alivyovitaja Ikongolo, Kanyenye, Kiwembe, Kongo na Hurumbiti ni bakaa ya mradi wa Ziwa Viktoria na hela zake zipo shilingi bilioni 25. Je, lini mradi huu wa kumalizia vijiji hivyo vitano utaanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa vile wananchi wangu wa Jimbo la Tabora Kaskazini wanahitaji mafunzo na elimu kuhusu matumizi ya maji hayo, lakini vilevile kuhusu utunzaji wa miundombinu ya maji, je, lini elimu hiyo kwa wananchi itaanza kutolewa? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge Mzee wangu Almas Maige kwa kazi kubwa na nzuri hasa ya kuwapigania wananchi wake wa Tabora kuhakikisha maji tunayatoa Ziwa Viktoria na kuyapeleka Tabora, Igunga, Nzega. Historia itakukumbuka mzee wangu, Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake kwamba lini tutatekeleza mradi katika vijiji vitano, nataka nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, sisi Wizara ya Maji si Wizara ya Ukame, vijiji vile vitano vilivyobaki tunakwenda kuvikamilisha mara moja ili wananchi waweze kupata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa kuhusu suala zima la elimu katika eneo lile la Tabora, Wizara ya Maji tumetekeleza mradi mkubwa sana wa zaidi ya bilioni 600 katika Mji wa Tabora, Igunga, Nzega. Pasipo elimu kwa wananchi inawezekana wakahujumu miundombinu ya maji. Hii ni kazi yetu sote Mheshimiwa Mbunge, mimi Waziri wa Maji na Waheshimiwa Wabunge wote kuhakikisha kwamba tunatoa elimu ya kulinda na kutunza vyanzo na miundombinu ya maji ili kuhakikisha wananchi hawa wanaenda kuvilinda na kuvitunza, ili miradi hiyo iwe na manufaa kwa vizazi vya sasa na vya baadaye. Ahsante sana.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa Jimbo la Tabora Kaskazini na Tarafa mbili na kata 19 na lina kituo kimoja tu cha afya; je, ni lini Serikali itaunga mkono juhudi za Mbunge na wananchi za kujenga vituo vya afya katika Kata za Mabama, Usagari, Chitage ikiwa ni pamoja na kukiinua hadhi kituo cha Lolangulu? Swali la kwanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa hospitali mpya ya Wilaya ya Uyui imevunja rekodi ya kuwapa referral wagonjwa kwenye kituo cha afya tena kwa bodaboda.

Je, Serikali lini itapeleka gari la wagonjwa la kubebea wagonjwa katika zahanati nyingine zote katika Jimbo langu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi Serikali kwa kuthamini afya za wananchi wa Halmashauri ya Uyui na Jimbo la Tabora Kaskazini imepeleka fedha ndani ya miaka mitatu zaidi ya bilioni 3.4 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Vituo vya Afya vitatu ambavyo vinatoa huduma, lakini ni kweli kwamba tunahitaji gari la wagonjwa katika Hospitali ya Halmashauri na Serikali imeshaweka mipango madhubuti kabisa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ya kutafuta magari ya wagonjwa kwa ajili ya Hospitali zetu za Halmashauri lakini pia kwa ajili ya vituo vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nimhakikishe Mheshimiwa Maige kadri mipango hii inavyoendelea kutekelezwa tutahakikisha tunapata gari la wagonjwa kwa ajili ya Hospitali ya Halmashauri, lakini pia kwa ajili ya vituo vya afya, lakini tunaamini kwamba tunahitaji kuwa na vituo vya afya katika kata zetu zote kama Sera na Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi yanavyoeleza likiwemo jimbo hili la Tabora Kaskazini kwa maana ya Halmashauri ya Uyui. Naomba nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kila mwaka tunaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka ujao wa fedha tumetenga fedha kwa ajili ya vituo vya afya 221, lakini tutaendelea kutenga fedha ili kuhakikisha jimbo hili pia linapata vituo vya afya.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini bado nina maswali ya nyongeza, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, je, Serikali inaweza kutoa ruzuku ambayo zamani ilikuwa ikitoa kwa wakulima kwa mazao mbalimbali sasa iende kwenye Benki ya Kilimo halafu benki isimamie na kutoa mikopo hiyo kwa riba ndogo sana? Kilimo hakiwezi kukopeshwa zaidi ya asilimia 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, hivi karibuni Benki Kuu imetangaza fedha za kusisimua uchumi trilioni moja.

Je, haiwezekani Benki Kuu ikapeleka sehemu ya fedha hiyo kwenye Benki ya Kilimo ili yenyewe isimamie kwa kuwakopesha wakulima kwa riba ndogo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Almas Maige kwa pamoja, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na ruzuku ya shilingi trilioni 1 ambayo urejeshaji wake utakuwa ni wa riba asilimia 3 ni mkakati maalumu ikiwa ni moja kati ya hatua tano ambazo BoT imeziweka kwa ajili ya mabenki yote nchini. Kwa hiyo, TADB ni moja kati ya mabenki ambayo yanapaswa kutumia fursa hiyo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba TADB ni miongoni mwa mabenki kadhaa ambayo tayari yameshapeleka maombi hayo kwa ajili ya kupatiwa fedha hizo kwa ajili ya kutekeleza malengo na mikakati yake ikiwemo dhima kubwa ya kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais kuhakikisha kwamba riba zinapungua kwa kiwango kisichozidi asilimia 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, kuna jitihada mbalimbali ambazo kama Serikali inachukua za kuhakikisha kwamba tunaiongezea uwezo TADB pamoja na benki nyingine zilizo chini ya mamlaka ya Serikali ili ziweze kupata mitaji ya kutosha pamoja na zenyewe kuwa na utaratibu wa kubuni njia za kujiwezesha kuongeza ukwasi ili waweze kutoa mikopo zaidi na kusaidia sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na sekta nyingine mbalimbali nchini.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, Jimbo la Tabora Kaskazini vijiji 58 vitapata maji ya Ziwa Victoria. Swali, Je, Serikali ina mpango gani kuchimba visima virefu katika maeneo ambayo bomba la Ziwa Victoria halipiti?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maige Mbunge wa Tabora kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu fika mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria umeweza kufika katika Mkoa wa Tabora. Lakini kwa maeneo ambayo mradi huu hauwezi kufika kwa sababu, bomba kuu linapopita ni kilomita 12 kulia na kushoto wanaweza kunufaika moja kwa moja.

Maeneo ambayo yako ndani zaidi mpango wa Serikali ni kuchimba hivi visima virefu na tayari Serikali imeviandaa visima zaidi ya 500 kwa ajili ya nchi nzima. Hivyo niweze kumtoa hofu Mheshimiwa Maige na yeye ataweza kuingia katika mgao wa visima hivi. Lengo ni kuona kwamba wananchi wenye imani kubwa kwa Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan wanaweza kuhudumiwa na kutuliwa ndoo kichwani. (Makofi)
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri kweli ya Serikali, lakini je, barabara hii ambayo imengojewa kwa muda mrefu sana na Serikali inaendelea kutafuta fedha. Je, wananchi wa Jimbo langu wasubiri mpaka lini ili barabara hii ianze kujengwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kipande kile cha Mambari – Bukumbi, Shitaga na Ishihimulwa, je, ni lini Serikali itaweka katika bajeti fedha za kufanyia usanifu wa ujenzi wa barabara hii? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge aone jitihada za Serikali, ni mwaka jana tu 2020, tumekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa maana, ya maandalizi ya kuanza kujenga kwa kiwango cha lami kilomita hizo 56. Hata hivyo, barabara iliyobaki tumekiri kwamba bado haijafanyiwa upembuzi na Serikali inatafuta fedha.

Kwa hiyo, Mheshimiwa avute subira, Serikali ina mpango na ndio maana tayari tumeshaanza hatua na fedha itakapopatikana tutaanza ujenzi kwa kiwango cha lami. Kipande kilichobaki hadi Muhulidede kitafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. ATHUMANI A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kuniruhusu na mimi niulize swali la nyongeza. Barabara ya Tabora - Mambali ambayo ufanisi wake umekwishafanyika siku nyingi, lini itaanzwa kujengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maige, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Tabora - Mambali tulishakamilisha usanifu wa kina na fedha tumetenga; na Serikali inaendelea kutafuta fedha kuijenga hii barabara yote kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Katika Kituo cha Afya cha Ukuge ulijengwa mtambo mkubwa uliokusudiwa kutengeneza oxygen kwa ajili ya Kanda yote ya Magharibi, lakini bahati mbaya mtambo ulipowashwa, ukawa unatengeneza nitrogen.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuchukua mpango huo unaotengeza nitrogen ili watuletee unaotengeneza oxygen?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, alichokielezea kuhusu huo mtambo ili Serikali ichukue najua suala hili linahusu zaidi Wizara ya Afya. Kwa hiyo, kwa niaba ya Wizara ya Afya, tuseme tumelipokea hilo na Serikali italifanyia kazi. Ahsante sana.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Je, Serikali inakiri kuwa muda wa miaka sita tangu ichukue Muswada huu ni mrefu sana kutoletwa Bungeni?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, wakati tunajadili kupata maoni ya Muswada huu tuligundua kwamba kipengele kile cha kubeba silaha Upande wa Zanzibar kisingekubaliwa. Je, tukiongeza maneno “isipokuwa Zanzibar” katika kipengele kile kitafanya Muswada huu uamke na kuletwa Bungeni?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu mawali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maige kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, uandaaji wa sheria, hasa hizi ambazo zinahitaji ushirikishwaji mpana wa jamii hususani kwenye hili ambalo linahusu pande mbili za Muungano ni jambo ambalo miaka sita huwezi ukasema ni muda mrefu sana. Ni muda mrefu lakini ili tupate sheria itakayokubalika kwa pande zote na wadau wote tunaomba Mheshimiwa atuvumilie tuweze kulikamilisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu maoni ya kubeba silaha upande wa Zanzibar kwamba kuna changamoto pengine hicho kipande kiondolewe, naomba Mheshimiwa asubiri michakato ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar na Baraza la Mawaziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaweze kukamilisha kazi yake tuweze kuwasilisha Muswada huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Uyui iko kwenye chumba kidogo sana tulichopewa na Ofisi ya DC.

Je, ni lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya ya Uyui? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nipende kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kutoka Uyui kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyoeleza katika jibu la msingi, ni kwamba sasa hivi Mahakama ya Tanzania imeendelea katika shughuli za ujenzi wa Mahakama mbali mbali hapa nchini. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge, tuwasiliane baada ya kipindi hiki ili niweze kumuweka katika kumbukumbu zilizo sahihi juu ya lini tunaenda kuanza ujenzi katika eneo lake. Ahsante.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Barabara ya Tabora - Mwambali imeshafanyiwa usanifu tangu mwaka 2020, lakini mpaka leo haijaanza kujengwa. Ni lini barabara hii itaanza kujengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu baadhi ya maswali, barabara zote ambazo tayari zimefanyiwa usanifu na ambazo zipo katika mpango wa Serikali ni kwamba sasa hivi kitu kimoja ambacho tunakitafuta ni fedha ili tuanze kuzitekeleza. Kwa hiyo, ninaamini kwamba mara fedha itakapopatikana, basi na hii barabara itaanza kujengwa. Ahsante sana.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali.

Kituo cha Afya cha Upugi kilikarabatiwa kwa hali ya juu sana na kuletewa mitambo ya kisasa, lakini hela zilipungua kwa kujengea jengo la mashine ya x-ray na ultrasound. Huu mwaka wa nne zile mashine hazijafunga.

Je, lini Serikali itajenga jengo la kuweka mashine ya x-ray na ultrasound katika Kituo cha Upugi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Almas Maige, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ikipeleka fedha katika ujenzi wa miundombinu ya huduma za afya, kwanza tunapeleka kwa awamu. Awamu ya kwanza, majengo ya OPD, majengo ya maabara ya mama na mtoto; lakini awamu ya pili tunatenga majengo mengine ya Vipimo ya x-ray, ultrasound na wodi, lakini kwa taarifa ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitoa kwamba fedha hazikutosha kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya x-ray na ultrasound, nimhakikishie kwamba Serikali kwa maana ya fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri na Serikali Kuu tutakaa tuone wapi tunapata fedha ili tuweze kukamilisha majengo hayo, ahsante. (Makofi)
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Sisi tuna mradi wa Skimu ya Shitage, iligharimu fedha nyingi sana, haifanyi kazi. Lini ahadi ya Mheshimiwa Waziri ya kutengenezwa hiyo skimu itatekelezwa ili wananchi wapate faida ya mradi ule?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Maige, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema pale awali, tunafahamu kwamba kilimo cha umwagiliaji ndicho kilimo hasa ambacho kitamkumboa mkulima wa Tanzania. Kwa umuhimu huo, tumeamua kwa dhati kabisa kuipitia hii miradi yote ikiwemo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameisema. Nimwondoe hofu ya kwamba tumejipanga kuhakikisha miradi hii inafanya kazi.

Kwa hiyo, katika eneo lake pia tutapita na hivi sasa tunaendelea kutafuta fedha na mtaona kwenye bajeti yetu inayokuja, nguvu kubwa hivi sasa imewekwa kwenye Tume ya Umwagiliaji kuwawezesha ili tuweze kufanya kilimo cha umwagiliaji. (Makofi)
MHE. ATHUMANI A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Katika kituo hicho pia kuna mtambo mkubwa wa kufua nguo ambao screen yake au kisomeo kiliharibika wakati mtambo unapelekwa kwenye site: Je, Serikali iko tayari kuleta spare nyingine ili kituo kile kiweze kufanya kazi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; katika kituo kile pia kuna mtambo mkubwa wa X-Ray ambao haufanyi kazi kwa sababu hakuna jengo la kufunga mtambo ule: Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kusafiri na mimi kwenda huko Upuge ili tukaone ufumbuzi wa kupata jengo jipya la kufunga mionzi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mtambo wa kufua nguo ambao umeharibika naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutafanya tathmini ya mahitaji kwa maana ya gharama, lakini tutaona kati ya fedha ya mapato ya ndani na kutoka Serikali Kuu ipi inaweza ikatumika kuhakikisha mtambo huo unafanya kazi au tunanunua mtambo mwingine.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na Jengo la X-Ray, kwamba X-Ray ipo lakini hakuna jengo, naomba tulichukue suala hili tukalitazame. Pia nitoe wito kwa Halmashauri ya Tabora kuanza kuona uwezekano wa kutenga fedha za mapato ya ndani kwa ajili ya kujenga jengo la X-Ray, kwa sababu tayari kuna mtambo na wana mapato ya ndani, wanaweza wakatenga kwa awamu kujenga jengo hilo ili tuweze kutoa huduma hiyo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo niko tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge tukapitie eneo hilo. Ahsante.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kuniruhusu niulize swali moja la nyongeza.

Je, lini Serikali itakamilisha miradi ya maji kutoka Ziwa Victoria katika vijiji vya Mogwe, Ikongolo, Majengo, Kiwembe, Mbiti na Muswa?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge pamoja na Makamu Mwenyekiti wangu wa Kamati, Serikali imefanya jitihada kubwa ya kuyatoa maji katika Ziwa Victoria na kuyaleta katika Mji wa Tabora, Igunga na Nzega. Kazi iliyobaki ni kufanya tu usambazaji.

Nataka nimhakikishie usambazi huo tutaufanya katika vijiji ambavyo amevitaja ili katika kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma ya maji safi na salama.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Waziri kwa majibu mazuri ya Serikali; nina maswali mawili ya nyongeza.

Je, Serikali iko tayari kukipa kipaumbele kipande kile cha kilomita nne kutoka barabara kuu ya Nzega kwenda kituoni ili kiweze kufikika wakati wa dharura?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Je, Serikali sasa iko tayari kumalizia kipande cha barabara kinachotokea pale kituo cha afya kwenda Kijiji cha Kasenga, Majengo, Ikongolo, Ipuge; vilevile vijiji vya Izugawima, na Nzuguka ili wananchi wa vijiji vile waweze kupata huduma haraka kwenye Kituo cha Afya cha Upuge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Jimbo la Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iko tayari kuipa kipaumbele barabara hiyo ya kilomita nne ili kuweza kusogeza huduma za jamii kwa wananchi. Nimwelekeze Meneja wa TARURA wa Halmashauri ya Uyuwi kuhakikisha kwamba wanatenga fedha kwenye eneo hilo, kwa maana ya kuipa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa kuwa barabara hii ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja, ambayo inaunganisha kituo cha afya na vijiji kadhaa alivyovitaja ni muhimu kuwawezesha wananchi kupata huduma za afya Serikali iko tayari kuipa kipaumbele barabara hii ili iweze kujengwa na kupitika vizuri. Ahsante.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Waziri ni lini Serikali itaanza kujenga kwa lami barabara ya Tabora Mambari ili kuunganisha Tabora Magharibi na Mashariki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Almas Maige kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa barabara hii unategemeana na upatikanaji wa fedha na tutaangalia katika bajeti hii ambayo imepitishwa ambapo ninyi Bunge hili Tukufu limeiidhinishia TARURA matumizi uya fedha ya zaidi ya Bilioni 830, kwa ajili ya kuweza kukarabati barabara mbalimbali nchini mwetu kwenye Majimbo yetu ikiwemo Jimbo la Mheshimiwa Almas Maige, kwa hiyo tutaliangalia na kuweza kulifanyia kazi.
MHE. ALMASI A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu nami niulize swali la nyongeza kwa swali hili 226. Lini Serikali itaendeleza na kumalizia vituo viwili katika Kata za Usagali na Shitage? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kumalizia vituo vya afya hivi ambavyo amevitaja Mheshimiwa Mbunge na kadiri pale bajeti itakavyoruhusu, basi tutakwenda kuvimalizia.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, majibu yaliyotolewa na Serikali yamejielekeza kwenye barabara ndogo iliyokuwepo wakati swali langu lilikuwa ni kutaka barabara kubwa ili malori yasipite mjin,i (barabara ya pete), kwa hiyo nina maswali mawili ya nyongeza.

Je, Serikali iko tayari kujenga barabara ya pete kutoka Kigwa B kwenda Magiri ili kuepusha magari makubwa yanayokwenda Burundi na Rwanda kupita Mjini na kuharibu barabara za Mjini?

Swali la pili, kwa vile Miji yote inayojengwa sasa ina barabara za pete pamoja na Jiji letu la Dodoma na Mji mdogo wa Nzega. Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga barabara za pete kuzunguka Mji wa Tabora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iko tayari kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami kadiri ya upatikanaji wa fedha, lakini tayari katika bajeti hii ya 2023/2024 TARURA imetenga fedha ya kufanya upembuzi yakinifu kujua gharama jumla itakuwa ni kiasi gani kwa ajili ya ujenzi wa lami wa barabara hii. Hivi ilivyo sasa bado ina uwezo wa kubeba malori na ndiyo maana tunaifanyia periodic maintenance.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kuhusu barabara za pete (ring roads); Serikali iko tayari kujenga barabara ya pete (ring road) katika Mji wa Tabora, tunashirikiana na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi kuweza kuona tunaanzaje mchakato wa kufanya feasibility study ili Mji huu wa Tabora uweze kupata barabara hiyo ya pete.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri hayo ya ndugu yangu Mheshimiwa Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; je, Serikali haijali kuona mashine zile zimekaa kwenye makasha ya kusafirishia kwa miaka saba kuwa zinaweza kuharibika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Serikali ina ushauri gani juu ya wagonjwa wanaokaa kusubiri huduma za x-ray mashine na ultrasound ili kufanyiwa upasuaji, ukizingatia kuwa hata katika hospitali ya Wilaya iliyoko kilomita tano tu kutoka Upuge nako huduma hizi hazipatikani kwa sababu mtumiaji wa mashine hizo hayupo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Maige kama ifuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inajali sana na ndiyo maana kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi fedha ilitengwa kwa ajili ya ujenzi wa majengo yaliyokuwapo mwanzo, lakini nimtoe shaka Mheshimiwa Mbunge ndani ya wiki hii nitaomba mbele ya Bunge lako tukufu, niongozane naye na wataalam wa afya kufika katika Kituo cha Afya cha Upuge na kuona ni namna gani tunaweza kuchukua hatua kwa sababu haikubaliki miaka saba vifaa hivi vikakaa bila kutumika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili nirejee kwenye jibu langu la kwanza katika maswali yake ya nyongeza. Tutatatua changamoto hizi tukiwa site palepale na Mheshimiwa Maige, lakini nikiwa katika ziara hiyo kwa sababu kuna Mbunge mwingine wa Tabora ambaye alizungumzia basi tutatembelea pia Kituo cha Afya cha Misha kuhakikisha tuone changamoto zilizopo na kuhakikisha tunazitatua. (Makofi)
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na Serikali imetoa majibu mazuri sana, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; Kata ya Ibili ilikuwepo katika mradi wa kwanza ambao ulikuwa ujengewe mnara, je, imeondolewa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; wananchi wategemee lini mradi huu wa kata tano utaanza?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Ibili imo katika Mradi wa Tanzania ya Kidigitali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipengele cha pili, kama ambavyo nimesema katika jibu langu la msingi, Serikali kupitia UCSAF tunamtafuta mtoa huduma na mchakato utakapokamilika basi mtoa huduma atafika maeneo hayo kwa ajili ya kupata eneo na baadaye atapata vibali na kuanza shughuli ya ujenzi wa mnara huo kwa ajili ya wananchi wa Tabora Kaskazini. Ahsante.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mahitaji ya jengo la X–Ray katika Wilaya ya Maswa, linafanana kabisa na Kituo cha Afya cha Upuge. Kuna mitambo pale kwa miaka mitano ipo kwenye mabox, X–Ray Mashine na Ultrasound. Lini Serikali itajenga jengo? Kwa sababu mitambo hii itaoza, ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kwanza kumuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI; kwamba Serikali ilishapeleka mashine ya X–Ray, ilishapeleka Ultrasound, na wao kupitia mapato ya ndani wana uwezo wa kujenga jengo la X–Ray na Ultrasound ili wananchi waanze kupata huduma hizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni wajibu wao, na nitoe wito, kwamba wanatakiwa kuweka kwenye bajeti haraka iwezekanavyo, na ikiwezekana kwenye mapitio ya bajeti mwezi Desemba wananchi waanze kupata huduma za X-Ray na Ultrasound. Ahsante.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Wilaya ya Uyui ni mpya na hatuna Mahakama, tunatumia chumba kidogo sana; je, lini Serikali itajenga Mahakama ya Wilaya ya Uyui?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na naomba nijibu swali la Mheshimiwa Maige, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mpango wetu wa kujenga Mahakama za Wilaya ni pamoja na kukarabati ambazo ni chakavu, naomba nipokee Mahakama hii ya Uyui nita-check na Mheshimiwa Mbunge tuone tuiweke kwenye mpango ili tuweze kukarabati pia.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano katika Kata ambazo Jimbo la Tabora Kaskazini hakuna mawasiliano; Igulungu, Chitage, Bukumbi na Chese?

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Athuman Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa, tunakiri kwamba Tabora Kaskazini ina changamoto kubwa sana ya mawasiliano; na katika mradi wetu huu kwa bahati mbaya sana haikuwezekana. Hata hivyo, tayari tumeshachukua kata tano za Tabora Kaskazini ambazo tunakwenda kuzifikishia huduma ya mawasiliano ndani ya mwaka huu wa fedha, ahsante sana.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, haya ndio majibu bora kabisa ya Serikali, natoa pongezi kwa Mama Samia Suluhu Hassan lakini pia Waziri Aweso na Waziri Prisca Mahundi. Niliomba maji haya kwa ajili ya shule hiyo na nimepewa na wanafunzi pale na jamii yote niipongeze Serikali sana sana, naomba nitoe shukrani zangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina swali moja tu la nyongeza. Shule hii ina wanafunzi 1500 na ni wengi sana kwa hiyo bill ya maji, ankara imekuwa kubwa sana. Je, Serikali inaweza kutoa ruzuku sehemu ya ankara hii ili wote wapate maji, sasa wanafunzi wanachangia maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Awali ya yote nipende kupokea pongezi za Mheshimiwa Mbunge lakini na yeye pia ni kupitia jitihada zake kama mwenyewe anavyosema, alikuja ofsini tuliweza kuongea kwa pamoja na maombi yake tumeyafanyia kazi. Kuhusiana na kuona mradi huu unabaki kuwa endelevu suala la bill shuleni na wanafunzi wote waweze kupata maji kila siku, Mheshimiwa Mbunge nimelipokea tutalifanyia kazi kwa pamoja.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kunipa mimi ruhusa ya kuuliza swali la mwisho la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Chitage na Kata ya Usagari Mbunge kwa kushirikiana na wananchi tunajenga vituo vya afya.

Je, Serikali ina mpango gani wa kutusaidia kumalizia vituo hivyo vya Chitage na Usagari Mikungumalo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kwanza kumpongeza Mheshimiwa Almas Maige yeye pamoja na wananchi wake kuweza kujitoa kuanza ujenzi wa vituo hivi vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vilevile nimtake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora kufika katika vituo hivi vya afya ambavyo vimeanza kujengwa kwa nguvu ya wananchi na kufanya tathmini na kuona vile vigezo ambavyo vinahitajika kwa ajili ya kusajili kituo cha afya kama wanakidhi hawa wananchi wa Mheshimiwa Maige na wawasilishe taarifa hiyo Ofisi ya Rais TAMISEMI ili tuviweke katika mipango yetu ya utafutaji wa fedha katika Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kweli kuniruhusu na mimi niulize swali la nyongeza. Mahakama ya Wilaya ya Uyui inafanyakazi katika chumba kidogo kilichoazimwa kutoka kwa DC. Je, lini Serikali itajenga jengo la Mahakama ya Uyui?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maige Mbunge wa Uyuwi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kule tuna mradi tayari unaendelea na tutafuatilia kuona unakamilika lini.
MHE. ALMAS A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kuniruhusu niulize swali la nyongeza.

Kituo cha Afya cha Upugi kiko kilometa nne kutoka barabara kubwa ya Tabora - Nzega. Mheshimiwa Rais alipopita pale wananchi walimuomba awawekee barabara ya lami kwa sababu wagonjwa wakizidiwa kutoka kituo cha afya kwenda mjini inakuwa taabu sana. Je, Serikali iko tayari kuanza kujenga barabara hiyo ya kilometa nne?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKAO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Almas Maige, Mbunge wa Tabora Kaskazini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iko tayari kwa ajili ya kutekeleza maeneo yote yenye utata wa barabara ikiwemo eneo ambalo amelianisha Mheshimiwa Mbunge, isipokuwa kwa sasa tunatafuta fedha ili tuzitenge katika bajeti ili tuanze utekelezaji. Ahsante.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kuniruhusu na mimi niulize swali la nyongeza.

Ni lini Serikali itamalizia Kituo cha VETA kinachojengwa pale Iskizya, Uyui muda mrefu hakijakamilika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Maige, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge katika fedha tulizozipata za UVIKO-19 zaidi ya bilioni 20 zilipelekwa kwenye maeneo ya vyuo vile 25 vilivyokuwa vinaendelea na ujenzi. Na ujenzi huo unaendelea, kama kutatokea mapungufu machache sisi kama Wizara tutakwenda kukamilisha eneo hilo la ujenzi. Kwa hiyo, nimuondoe wasiwasi ndani ya kipindi hiki kifupi kijacho tunakwenda kukamilisha ujenzi katika chuo kile cha Uyuwi. Nakushukuru sana.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kweli kuniruhusu na mimi niulize swali la nyongeza. Mahakama ya Wilaya ya Uyui inafanyakazi katika chumba kidogo kilichoazimwa kutoka kwa DC. Je, lini Serikali itajenga jengo la Mahakama ya Uyui?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Maige Mbunge wa Uyuwi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kule tuna mradi tayari unaendelea na tutafuatilia kuona unakamilika lini.

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, Wilaya ya Uyui Makao Makuu yake ni Isikizya, kilometa 35 kutoka Tabora Mjini, na lipo tatizo kubwa kweli la umeme. Watumishi pale; DC na Wakurugenzi hawafanyi kazi kutwa nzima, umeme unakatika zaidi ya mara tano kwa siku; je, Serikali ina mpango gani wa kuweka umeme wa kudumu pale Isikizya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almas Maige, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tayari Serikali tumechukua hatua katika Halmashauri ya Uyui na katika Mkoa mzima wa Tabora. Tumechukua hatua na tuna mradi unaendelea wa kujenga vituo vya kupooza umeme na line za kusafirisha umeme. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, baada ya mradi huo kukamilika ndani ya miezi 18, tatizo la kukatikakatika kwa umeme unaotakana na line ndefu kutoka Tabora Mjini mpaka Uyui mpaka kwenye Jimbo la Mheshimiwa Sitta tutakuwa tumelipunguza.

Mheshimiwa Spika, pia nimwelekeze Meneja wa TANESCO Mkoa wa Tabora ahakikishe ratiba wanazozipanga zinazingatia maeneo ambayo yanatoa huduma kwa wananchi hususan maeneo ambayo yanatoa hospitali, vituo vya afya pamoja na shule na maeneo mengine ambayo yanatoa huduma kwa wananchi, ahsante.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nina swali moja tu la nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, kwa vile makosa haya ya ukatili wa kijinsia sasa yanaendana na makosa ya kuporomoka kwa maadili.

Je, Serikali haioni haja ya kuboresha sheria hii iliyopo sasa ili kuchanganya tiba ya makosa haya yanayotokana na kuporomoka kwa maadili? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba nijibu swali la nyongeza kuwa Serikali inaona haja ya kuboresha sheria hizi, hivi sasa tupo katika mchakato wa kupitia taarifa maalum ya masuala ya maadili.

Mheshimiwa Spika, utakumbuka katika Bunge hili tulizungumza sana kuhusu masuala ya maadili, masuala ya mahusiano ya jinsia moja. Nimeshaunda timu maalum pale Wizarani na wanaandaa taarifa kuona namna gani sheria hizi tuendelee kuziboresha. Kwa hiyo, haja ya kuboresha ipo na ndiyo jukumu la msingi la Bunge. Kazi ya Bunge ni kutunga sheria, kazi ya Bunge ni kurekebisha sheria, kwa hiyo, suala la kuangalia kama ipo haja au haipo kwa kweli, nichukue nafasi hii kusema tu kwamba, hilo ndilo jukumu la msingi kabisa la Wizara yangu na tunaendelea kuangalia namna gani tuendelee kuziboresha sheria zetu.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuulize Mheshimiwa Waziri; je, ni lini barabara ya Mambali – Bukumbi – Shitage – Mulibede mpaka Ushetu itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Barabara aliyoitaja Mheshimiwa Maige itajengwa kwa awamu na tayari mameneja wa mikoa ikiwepo Mkoa wa Tabora kama ilivyopangwa kwenye bajeti wapange ama watangaze kwa kiasi kile ambacho kimepangwa kwenye bajeti kuanza kuijenga barabara hiyo.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Ni lini Serikali italipa fidia kwa wananchi waliochukuliwa maeneo yao hivi karibuni katika Kata ya Mabama, Wilaya ya Uyui? (Makofi)

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata Mabama nafikiri huu ni mgogoro ambao unakuja kwa sasa hivi, kwa hiyo sisi tutakachokifanya ni kupata uhakika na baada ya kupata uhakika kama kweli wananchi eneo lao limevamiwa, basi taratibu zitafanywa za uhakiki na kama wanastahili fidia watalipwa fidia yao.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ina mpango gani wa kulipa fidia kutokana na madhara wanayopata raia kwa vitendo vya baadhi ya watumishi wabaya wa TFS? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Almasi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, masuala yote ya haki za binadamu yanatekelezwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zilizopo. Nimhakikishie Mheshimiwa Almasi, pale watumishi wetu watakapokuwa wamefanya makosa chini ya sheria hizo, fidia stahiki zitatolewa kwa mujibu wa sheria iliyopo. (Makofi)
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, ni lini Serikali itapeleka gari la usimamizi wa huduma katika Halmashauri ya Uyui ambayo ina majimbo mawili Tabora Kaskazini na Igalula?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kutokana na jiografia kati ya vituo hivi vya afya, mfumo wa kutumia gari moja la Kaskedi hautofanya kazi vizuri, je, ni lini Serikali itapanga kupeleka magari mawili katika Kituo cha Afya cha Upuge na Kituo cha Afya cha Mabamba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, magari 70 yaliyokuwa yamebaki ya usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za afya tayari yameingia nchini na Serikali inaendelea na utaratibu wa kuyatoa magari haya bandarini na hatua nyingine za usajili wa haya magari. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba magari haya yakitoka, Halmashauri ya Uyui na yenyewe itapata gari moja.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kwamba kama Serikali ilivyotenga pesa kununua magari ya kusafirishia wagonjwa na kuweza kuyaleta katika jimbo lake. Nimhakikishie kwamba Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuongeza magari ya wagonjwa kwa ajili ya kuhudumia katika Vituo vya Afya vya Upuge na Mabamba kama alivyoomba. (Makofi)
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Katika Kata ya Bukumbi wananchi na Mbunge tumejenga kituo kizuri cha afya. Lini Serikali itapeleka magari au pikipiki, kwa ajili ya usafiri wa hawa askari?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani alikuwa anaulizia swali kituo cha polisi na siyo cha afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maige, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali mpaka sasa imetoa pikipiki 105 kwa ajili ya vituo vya polisi katika maeneo mbalimbali nchini na kwa jinsi ya upatikanaji wa fedha, Serikali itatoa pikipiki kwa ajili ya kuhudumia vituo vya kata, kama alivyotaja Mheshimiwa Mbunge Maige.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, kwa kuwa kituo hiki cha Shitage kinachojengwa kwa kutumia nguvu za wananchi kimechukua muda mrefu, vilevile, kwa kuwa kituo kipo mbali kwa umbali wa kilometa 120 mpaka kituo kingine cha afya na kitahudumia kata tatu ambazo ni Shitage, Igulungu na Bukumbi; je, Serikali haioni kwamba umefika muda sasa wa kujenga kituo hiki ili kitoe huduma kwa hizi kata tatu?

Swali la pili, kwa vile kituo hiki cha Shitage Mheshimiwa Waziri anasema inategemea fedha za ndani za mwaka 2025/2026 zianze kujenga kituo hiki, wananchi wamechoka; haoni kwamba ni mbali sana kufikiria kujengewa tena kwa fedha za ndani za Halmashauri mpaka mwaka 2025/2026 ni mbali sana. Je, haoni umuhimu wa kumaliza kituo hiki sasa hivi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua kuwa kituo hiki cha Shitage kiko mbali na kinahudumia takribani kata tatu na ndiyo maana imeweka kipaumbele cha kutenga fedha katika bajeti ijayo ya mwaka 2025/2026 kwa ajili ya kukamilisha kwa sababu katika mwaka huu wa fedha na mwaka ujao wa fedha tunakwenda kukamilisha vituo viwili vya afya na zahanati nne.

Mheshimiwa Spika, pili, mwaka 2025/2026 siyo mbali kwa sababu safari ni hatua na tumekwishaanza ujenzi wa vituo vingine hivyo tutakamilisha ujenzi wa kituo hicho muda huo ukifika, ahsante.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Tabora Kaskazini, kata mbili ambazo ni Kata ya Igulungu, Kijiji cha Mbeya ambako kuna zahanati hakuna kabisa mawasiliano, lakini pia Kata ya Ibiri hakuna mawasiliano; je, ni lini Serikali itajenga minara katika kata hizo mbili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Almas Maige, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kata hizi mbili jana tuliongea na Mheshimiwa Maige na tayari watendaji wanashughulikia. Katika mwaka ujao wa fedha tutafanya baadhi ya maeneo ili kuhakikisha mawasiliano yanakaa vizuri.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Je, ni lini Serikali itanunua magari, kwa ajili ya vituo vya afya vya Mabama na Upuge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha, Serikali itaendelea kuagiza magari haya ya kusafirishia wagonjwa (ambulance), kwa ajili ya kusambaza katika maeneo tofauti-tofauti katika vituo hivi vya kutolea huduma ya afya. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, kwa kuzingatia vipaumbele na upatikanaji wa fedha Serikali italeta magari haya katika vituo ulivyovitaja.
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, kwa vile biashara yote ya tumbaku inalipwa kwa dola, kwa nini wakulima wanalipwa kwa shilingi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, tumbaku inafanyika kwa dola na kinachofanyika ni kwamba transaction inapotoka kwa mnunuzi kwenda kwenye vyama vikuu vya msingi huwa vinafanyika kwa dola. Inapotoka kwenye transaction kutoka katika vyama vya msingi baada ya makato yote ambayo wakulima wanakuwa walikopa katika msimu wa kilimo, ile difference inayobaki wakulima wanalipwa kwa shilingi kulingana na thamani ya fedha ya siku hiyo husika. Hicho ndicho ambacho kinafanyika sasa. Ahsante sana.

SPIKA: Sasa huyo anayebadilishia hapo katikati ni nani kama mkulima huwa anapata pembejeo kwa dola na yule mnunuzi ananunua kwa dola, nani anayembadilishia mkulima hapo ghafla kwamba yeye ndiyo apewe shilingi?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ni Chama Kikuu cha Msingi (TCJE) ambao sasa wao ndiyo wameingia mikataba na wakulima kwa sababu zile account za wakulima ni za shilingi. Kwa hiyo wao wanachokifanya wana-convert ile thamani ya dola ya siku hiyo; yaani kwa mfano labda mkulima thamani yake labda ni dola 100 kwa hiyo wanakwenda kuangalia katika thamani ya bei ya shilingi ya dola kwa siku hiyo kama ni 2,500, kwa hiyo watalipwa ile shilingi 250,000/=, lakini hiyo inatoka kwenye Chama cha Msingi, Chama Kikuu cha Ushirika kwenda kwa mkulima.