MHE. ELIBARIKI I. KINGU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza swali langu; sasa hivi pamekuwa na utaratibu ambapo Serikali inapopeleka fedha za maendeleo kwenye Halmashauri hasa fedha zinazopelekwa kuanzia miezi ya Machi, Aprili na Mei, fedha hizi zinapokuwa hazijatumika zote pamekuwa na utaratibu wa miaka mingi mwaka wa fedha unapoisha zinarudishwa hazina na hivyo kuathiri sana utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi. Natoa mfano Jimbo la Singida Magharibi na Majimbo mengi Tanzania tumepokea fedha za ujenzi wa vituo vya afya, hosteli na mabweni lakini fedha hizi zimepokelewa kuanzia mwezi wa Aprili na Mei ni wazi itakapofika mwisho wa financial year fedha hizi zitakuwa hazijatumika zitarudi Hazina na hatujui zinakwenda kutumika namna gani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, je, Serikali ya Chama cha Mapinduzi, Serikali yangu haioni umuhimu wa kusitisha mpango huu na kuruhusu fedha hizi ambazo tayari zinawagusa wananchi wanyonge zisirudi Hazina zaidi sana ukawekwa mpango wa kuzi-monitor? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kingu, Mbunge wa Singida Magharibi, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, najua jambo hili lilizungumzwa hapa na wewe mwenyewe ulionesha interest kubwa lakini na pia kuitaka Serikali ilifanyie kazi. Nashukuru leo limerudi tena naomba kutoa ufafanuzi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hasssan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inapeleka fedha nyingi sana sasa hivi kwenye Halmashauri kwa ajili ya maendeleo. Upelekaji huu ni wakati wote, toka tulipoanza mwanzo wa mwaka wa fedha na tutaendelea kupeleka mpaka mwisho wa mwaka wa fedha ili kuwafanya wananchi waweze kupata maendeleo kupitia miradi inayolengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni kweli tuliliwekea sheria ambazo zinataka fedha inapofika angalau tarehe 15 ya mwezi wa Juni wa mwisho wa mwaka wa fedha kama Halmashauri haijamudu kufanya matumizi lazima zirudi halafu tuliweka utaratibu wa kama Halmashauri imepelekewa fedha na wamefika muda wa mwisho wa kushika fedha na kutaka kuzirudisha, waweze kuandika barua ya kuonesha kwamba mpaka tarehe hii bado tuna fedha ambazo hazijatumika kwa sababu ya taratibu za manunuzi labda kwa sababu pia kwenye taratibu za manunuzi unapotengeneza mradi unalipa kadiri hatua fulani inavyofikiwa.
Kwa hiyo, inawezekana kuna miradi ambayo inafikiwa mwezi Juni tarehe 15 ipo kwenye hatua labda ya lenta na haijakamilisha kwenye finishing. Utaratibu huu unawezesha pia Wizara ya Fedha kuzirudisha fedha hizi kwenda kwenye Halmashauri ingawa kuna changamoto ambayo Mheshimiwa Mbunge ameionesha hapa na Waheshimiwa Wabunge wote tumeshuhudia kwenye maeneo yetu.
Mheshimiwa Spika, nini Serikali inafanya kweli hili; niliwaagiza Wizara ya Fedha kubadilisha utaratibu na kufanya maboresho kwenye Kanuni zetu ili kuweka Kanuni ambayo angalau inaweza kuruhusu miezi kadhaa baada ya mwaka wa fedha wa bajeti ili fedha zile ziweze kukamilisha kazi hiyo. Ingawa kwenye hili, hatutahitaji mwanya wa wazembe kukaa na fedha bila kuzitumia akitegemea ataongezewa muda. Pamoja na Kanuni hiyo ambayo tutaiboresha lakini bado tutaweka kipengele kinachombana mwajiri/mtendaji wetu kule kuhakikisha kwamba kila fedha inayoingia lazima itumike kwa kipindi kinachotakiwa kwa sababu wengine wanaweza kukaa na fedha mpaka miaka miwili, sasa hilo hatutaruhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutaangalia ni miezi mingapi inaweza kutufaa ambayo itaingia mwaka wa pili wa fedha ili fedha hii iweze kukamilisha miradi hiyo lakini kwa barua vilevile inaonesha kwamba amepata fedha tarehe fulani labda ndani ya Juni yenyewe na mradi umeshaanza kutekelezwa upo hatua fulani na lazima tukakague tuone kama kweli fedha ile imebaki na inatakiwa itumie kufikia kipindi hicho, huyo tutamridhia. Vinginevyo hatutaruhusu mtendaji yeyote akae na fedha kwa uzembe tu halafu ategemee kupata offer ya kuongezewa miezi mingine, hao watachukuliwa hatua kali ili tuweze kujenga nidhamu ya matumizi ya fedha kwa sababu wananchi wanahitaji miradi na kuona fedha inatumika vizuri na Waheshimiwa Wabunge kama Wenyeviti wa Kamati za Maendeleo kwenye Jimbo ni lazima na ninyi mridhike kwamba fedha iliyokwenda imetumika kwenye mradi kusudiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali inafanya maboresho hayo na tutatoa taarifa katika kipindi hikihiki cha Bunge ili muondoke hapa mkiwa na uhakika kwamba fedha iliyotumwa kwenye maeneo yenu inaweza kutumika lakini pia imepata fursa ya kutumika kipindi kijacho cha fedha. Ahsante sana. (Makofi)