Contributions by Hon. Dr. Hamisi Andrea Kigwangalla (37 total)
Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Masuala ya UKIMWI na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Hoja ya kwanza ambayo nitaanza nayo ni ya viroba kwa sababu nilielekezwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu niongoze kikosi kazi cha Serikali cha kushughulikia suala hili ambacho kilihusisha Wizara na taasisi mbalimbali za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka hivi tunavyoongea suala hili linaelekea ukingoni na pengine baada ya miezi mitatu viroba vitapigwa marufuku kabisa katika nchi hii na wala sio suala la kusema viroba vitaruhusiwa kuuzwa labda kwenye maeneo maalum kama bar ama kwenye vioski na vitu kama hivyo na vitoke kwenye maduka ya kawaida, tunaelekea kwenda ku-ban kabisa (total ban) ya matumizi ya viroba katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia suala la usagaji na mambo ya ushoga, nalo tumelishughulikia sana ndani ya Serikali na mimi mwenyewe nimeongoza kikosi kazi cha kufanya tathmini ya suala hili. Hivi tunavyoongea kuna taasisi mbalimbali ambazo zilikuwa zinajihusisha na uhamasishaji wa vitendo vya ushoga zipo katika uchunguzi na nyingine tumezifutia usajili na hazifanyi kazi katika nchi yetu. Tutaendelea kuchukua hatua dhidi ya watu wote wale ambao watapingana na tamaduni zetu ambazo zinalindwa na sheria ambayo tuliipitisha hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hapa kuna Wabunge wameniletea taarifa za shoga mmoja maarufu kwa jina la James Delicious ambaye anajiuza kwenye mitandao. Namuagiza Katibu Mkuu afuatilie taarifa hizi ili shoga huyu aweze kuchukuliwa hatua haraka iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la tatu kwamba watumiaji wa dawa za kulevya huku tunawakamata lakini kwa upande mwingine tunawapa tiba. Hii inajulikana kama public health approach kwamba hatuwezi kuwakamata watu wanaotumia na tukawachukulia hatua badala yake tuna jukumu la kibinadamu la kuwahudumia kama wameamua kufuata huduma kwenye vituo vya kutolea huduma. Kwa hiyo, suala la udhibiti lina sheria na taratibu zake, lakini pia suala la kuhudumia waliothirika lina taratibu zake kwa mujibu wa sheria na kanuni mbalimbali za afya za kitaifa na za kimataifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la watumishi kwenye sekta ya afya, ni kweli tunakiri upungufu kwa sababu katika miaka miwili iliyopita, kwa tathmini tuliyoifanya mwaka 2016 tulipaswa kuwa na watumishi wapatao 179,509 lakini tunao 90,000 tu sawa na 51%. Kwa hiyo, tuna upungufu mkubwa, tunaufahamu na tunaendelea kuushughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine lililojitokeza ni suala la Ocean Road Cancer Institute kuwa na vifaa vilivyochakaa. Suala hili tunalifahamu na tayari Serikali imeweka kipaumbele cha kipekee kwenye taasisi hii inayotibu magonjwa ya saratani na hivi ninavyoongea hapa, bajeti ya dawa kwenye kituo hiki imepanda kutoka shilingi milioni 700 mwaka uliopita mpaka shilingi bilioni saba mwaka wa fedha ambao unaendelea. Mpaka kufikia Disemba tayari Ocean Road walikuwa wamepatiwa bajeti ya shilingi bilioni tatu na sasa hivi upungufu wa dawa kwa kweli umepungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, tumeongeza idadi ya vitanda kutoka 40 mpaka 100 kwa wagonjwa wanaopokea tiba ya saratani kwa njia ya dawa na hivyo msongamano umepungua sana. Kwa sasa Serikali ina mikakati ya kuanzisha huduma za tiba ya saratani kwenye vituo vingine mbalimbali kwenye kanda nne za nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, KCMC kufikia Disemba walianzisha huduma ya tiba kwa dawa (chemotherapy), lakini Bugando mwezi Machi wataanza kutoa tiba ya mionzi kwa mara ya kwanza toka tupate uhuru ya ugonjwa wa saratani ambayo ilikuwa haijawahi kutolewa hata siku moja nje ya Kituo cha Ocean Road.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Hospitali yetu ya Kanda ya Rufaa ya Nyanda za Juu Kusini, pale Mbeya na yenyewe kufikia Julai itaanza kutoka huduma za tiba ya sarani kwa njia ya mionzi pale pale ili ku-off load mzigo wa wagonjwa ambao wangelazimika kuja mpaka Ocean Road kwa ajili ya kupata tiba hiyo. Sasa watapata kule kule Nyanda za Juu Kusini na tutaendelea kushusha huduma hizi karibu zaidi na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kulikuwa kuna hoja ya makazi ya wazee kwamba yamechakaa. Hili tunalifahamu na tulishalichukulia hatua. Hivi sasa tunavyoongea hapa vituo kumi vya kuhudumia wazee vinafanyiwa ukarabati kwenye maeneo ya majiko na vyoo, lakini pia tutavipelekea bajaji kwa ajili ya kuwasaidia wazee waweze kupata huduma za kupelekwa hospitali na maeneo mengine kirahisi zaidi.
Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa hii. Awali ya yote napenda nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema na mwenye kurehemu kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu ili nami niweze kujibu hoja mbalimbali za Waheshimiwa Wabunge wenzangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba ufikishe kwa Mheshimiwa Spika salamu zangu za masikitiko makubwa lakini pia nikuunganishe na wewe kwenye salamu hizo za pole pamoja na Waheshimiwa Wabunge wenzetu wote kwa misiba mbalimbali iliyotukuta. Tukianza na msiba wa aliyekuwa Spika wa Bunge la Tisa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samuel John Sitta, lakini pia Wabunge wenzetu Mheshimiwa Hafidh Ali Tahir na Mheshimiwa Dkt. Elly Marco Macha. Kwa wote hawa naomba Mwenyezi Mungu azilaze roho zao mahali pema peponi. Amina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitumie nafasi hii kwa namna ya kipekee kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kunipa ushirikiano na kunishirikisha kwa ukaribu katika utekelezaji wa jukumu hili la kusimamia na kuiongoza Wizara hii. Pia naomba nimshukuru mke wangu mpenzi Dkt. Bayum Kigwangalla na watoto wetu Sheila, Hawa na H.K Junior kwa kunitia moyo na kunivumilia wakati wote ninapokuwa mbali na familia yangu nikitekeleza majukumu mbalimbali ya kila siku ya ujenzi wa Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii, lakini pia kwa kipekee nimshukuru Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa uongozi thabiti mnaotoa kila siku na ushirikiano mnaotupa katika kutekeleza majukumu yetu tuliyopewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niishukuru kwa dhati Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano mkubwa wanaonipatia siku hata siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwapongeza watumishi wote wa Wizara yetu ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakiongozwa na Katibu Mkuu Idara Kuu ya Afya, kaka yangu Dkt. Mpoki Ulisubisya na Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii ndugu yangu mama Sihaba Nkinga pamoja na wafanyakazi wote wa sekta za afya na maendeleo ya jamii nchini kwa kazi yao nzuri na iliyotukuka ambayo wamekuwa wakiifanya kila siku katika kuboresha maisha ya Watanzania wenzetu. Nawaomba sana tuendelee kufanya kazi kwa ushirikiano huu, lakini pia kwa uadilifu mkubwa ili kufikia malengo yetu tuliyopewa na kufikia malengo ya Taifa kadri tunavyotarajiwa na Watanzania wenzetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa maandishi na kwa kusema hapa Bungeni. Michango yenu kwa hakika inalenga kuboresha huduma za afya na maendeleo ya jamii zinazotolewa na kusimamiwa na Wizara yetu. Kama mlivyoona ndugu zangu, hoja zilizotolewa ni nyingi lakini muda tuliopewa hautoshi kujibu hoja zote, hivyo majibu ya kina ya hoja moja baada ya nyingine tutayawasilisha kwa maandishi na Waheshimiwa Wabunge wote mtapatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naomba sasa nijibu hoja chache ambazo nimepewa nizizungumzie katika maeneo mbalimbali kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, naomba kuzungumzia kuhusu mfumo wa afya (health system). Kwa hakika mfumo wa afya tangu tumepewa majukumu haya na Watanzania mwaka 2015 umeendelea kuimarika kwa kasi ya ajabu. Mafanikio haya ya kuimarika kwa mfumo wa afya yaani (health system) hayawezi kuzungumziwa bila kuutambua na kuuthamini mchango mkubwa wa viongozi wetu wakuu wanaoongozwa na Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambaye hata kabla hajatuteua sisi kwenye nafasi hizi alionesha nia yake ya dhati ya kutaka kuleta mabadiliko kwenye Sekta ya Afya kwa kuanza kusimamia sekta hii yeye mwenyewe kwa ziara zake maarufu za kushtukiza alizozifanya Hospitali ya Taifa Muhimbili na matokeo yake sote tunayafahamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kiongozi wetu Mkuu mwingine Mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa champion wa mambo yote yanayohusu akinamama lakini pia afya ya uzazi salama ambapo pia amekuwa karibu sana na Wizara hii akitupa mwongozo, maelekezo na ulezi wa kila siku katika utekelezaji wa majukumu yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile, Mheshimiwa Waziri Mkuu naye amekuwa mstari wa mbele kwenye utekelezaji wa majukumu ya sekta hii na tumemwona kila alipofika kwenye mkoa wowote ule kwenye nchi yetu amekuwa akitusaidia kufanya usimamizi wa moja kwa moja yeye mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimelisema hili kwa sababu linatokana na utafiti ambao umefanywa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya TWAWEZA, ambapo katika utafiti huo matokeo waliyatoa mwaka jana katikati, wameonesha kwamba mfumo wa afya umeimarika kutokana na takwimu za sauti za wananchi ambao waliwahoji. Kwa msingi huo mafanikio haya kazi yetu sasa ni kuendelea kuyalinda lakini pia kuendelea kusonga mbele siku hata siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja ya pili ninayopenda kuzungumzia inahusu rasilimali watu. Mfumo wa afya una vitu vikubwa vitatu; cha kwanza ni rasilimali watu; cha pili ni vifaa, vifaa tiba, dawa, vitendanishi; lakini cha tatu ni miundombinu ya kutolea huduma za afya. Eneo la muhimu kuliko yote katika muktadha wa kutoa huduma bora za afya ni eneo la rasilimali watu. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia suala hili kwa uchungu kuanzia kwenye mambo ya udahili, ajira kwa watumishi kwenye sekta hii pamoja na motisha, yote haya yanahusu eneo la rasilimali watu. Kwa kuwa ni wengi waliochangia, nawatambua wachache tu, wengine naomba mjue kwamba katika majibu ya hoja kwa ujumla wake mtapata majibu ya kina na majina yenu yatakuwa yamewekwa humo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, michango ambayo napenda kuifafanua kwa ujumla wake kwa sababu muda hautoshi ni mchango wa Mheshimiwa Devotha Minja, Mheshimiwa Susan Lyimo, Mheshimiwa Mussa Sima, Mheshimiwa Juliana Shonza na Mheshimiwa mama Anna Makilagi. Kwa pamoja wamezungumzia mambo ya motisha na mambo mbalimbali, lakini pia kuna Waheshimiwa Wabunge wengine wamezungumzia mambo ya fukuza fukuza ambayo imekuwa ikifanyika na naomba nizungumzie hili la mwisho nililolisema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sisi kama Wizara ya Afya hatupendezwi sana na fukuza fukuza isiyofuata utaratibu kwa sababu sisi tuna jukumu la kusimamia sekta hii na katika kusimamia sekta hii tunafahamu hatuwezi kutimiza malengo yaliyopo kwenye Sera ya Afya ya Taifa bila kuwa na rasilimali watu ambayo ina motisha ya kutosha. Ni kwa msingi huo, mara kwa mara tumeshuhudia Waziri wa Afya akitolea msimamo thabiti suala hili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, rasilimali watu kwenye sekta ya afya ni ina gharama kubwa sana, kuanzia kwenye training kuja kwenye ajira, gharama za kuwalipa mishahara, gharama za kuwapa motisha, gharama ya kumhudumia daktari mmoja ni kubwa sana ukilinganisha na wataalam kwenye sekta nyingine. Wataalam hawa wanatoa huduma kwa kiwango cha hali ya juu sana na mara nyingi, nje ya muda wao wa kawaida wa kufanya kazi. Kwa namna yoyote ile, watumishi wa Sekta ya Afya wanapaswa kutiwa moyo na sio kudhalilishwa kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge mmekuwa mkisema hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na sisi kwenye sekta hii tunasema tutaendelea kulinda maslahi ya watumishi wa Sekta ya Afya kama hawatofukuzwa au kusimamishwa kazi kwa taratibu za kimaadili ambazo sisi Wizara ya Afya tunazisimamia. Kuna taratibu za kiutawala hayo hatutayaingilia, lakini kwa mambo yote yanayohusu uadilifu wa watumishi kwenye sekta ya afya, mabaraza yote ya kitaaluma yako chini ya Wizara yetu na hivyo mtu yoyote yule awe kiongozi anayesimamia eneo lake la utawala ni lazima afuate utaratibu wa kisheria ambao unasimamiwa na Wizara yetu. Tunahitaji staha kwa wataalam hawa ili waendelee kupata moyo wa kuwahudumia Watanzania wenzetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo hili la rasilimaliwatu tumepata mafanikio makubwa sana katika miaka ya hivi karibuni. Miaka iliyopita takriban 15, (miaka hiyo na mimi nilikuwa nasoma udaktari Chuo Kikuu) tulikuwa tunahitimu si zaidi ya 100 kwa nchi nzima; lakini leo hii kwa mwaka tuna uwezo wa kuzalisha Madaktari takriban 1,100 kila mwaka unaopita. Pia Wauguzi tu kwa mfano miaka hiyo ya 2000 mpaka 2005, tulikuwa tuna uwezo wa kuzalisha Wauguzi wasiozidi 3,500; leo hii ninavyozungumza hapa tuna uwezo wa kuzalisha Wauguzi wapatao 13,562, hii ni idadi kubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto inayokuja, kwa bahati mbaya hatuisimamii sisi kwenye sekta yetu na tunaendelea na mazungumzo na wenzetu ili tuweze kuipatia ufumbuzi, ni changamoto ya kuwa-absorb kwenye mfumo wa afya wataalam wote ambao tunawazalisha. Hii changamoto si yetu peke yetu, ni changamoto sana sana unaweza ukasema ya kitaifa kwa sababu inahusiana na ukomo wa bajeti, jambo ambalo linahusiana na ukuaji wa uchumi wetu. Kwa hivyo hatuwezi kumnyooshea kidole mtu yeyote yule kati yetu kwa sababu ni jambo ambalo wakati mwingine liko nje na uwezo wetu wa kibinadamu, kwa sababu kama hakuna pesa za kuwalipa mishahara, unafanya nini hata kama unatamani kuwaajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, pamoja na mafanikio makubwa tuliyoyapata kwenye eneo la production ya heath care workers lakini tuna changamoto kubwa sana ya absorption ya health care workers kwenye health system ya nchi yetu. Changamoto hii tutaendelea kuitatua taratibu kama ambavyo Waziri anayehusika na Manejimenti ya Utumishi wa Umma amesema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wengi wanapotaka kupata watumishi kwenye maeneo yao wanazungumzia kupata watumishi kutoka Wizara ya Afya; lakini wanasahau kwamba bajeti ya watumishi hawa iko kwenye dhamana ya watumishi ambao ni Accounting Officers kwenye maeneo yao; Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala, Wakurugenzi wa Halmashauri na Wakurugenzi wa Hospitali mbalimbali, wote hawa wanapaswa kupanga bajeti kwa ajili ya kuajiri rasilimali watu kwenye sekta ya afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kazi yetu ni kuzalisha, kuwasajili, kuangalia wanafanyaje kazi, kuangalia uadilifu wao na takwimu za rasilimali watu kwenye sekta ya afya nchini lakini si kuajiri. Kibali cha kuajiri kipo kwa wenzetu wa Menejimenti ya Utumishi wa umma lakini pia mishahara ipo
kwa wenzetu wa Hazina. Bajeti ya kuwaajiri ipo kwa Wakurugenzi wetu wa Halmashauri. Kwa hivyo, napenda kutumia jukwaa hili kuwaomba Waheshimiwa Wabunge waanze kwanza wao wenyewe kwenye Halmashauri zao kupanga bajeti ya kuajiri rasilimaliwatu ya kutosha kwenye maeneo yao kabla ya kuja kuomba sisi tuwasaidie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine kwenye eneo hili la rasilimali watu ni changamoto ya retention ya health care workers. Changamoto ya kuhakikisha rasilimali watu kwenye sekta hii inabaki kwenye eneo husika, haiondoki kwa sababu tunaona sasa hivi Madaktari hao wachache tulionao kwa zaidi ya asilimia 70 wapo kwenye maeneo ya mijini tu, maeneo ya vijijini hakuna. Wakati wanapangwa na Wizara ya Afya pale mwanzoni ukifuatilia kuna tracer studies mbalimbali zinazofanyika ambazo zinafuatilia wafanyakazi walihitimu wapi, walihitimu lini na walipelekwa wapi na sasa wako wapi imeonekana kwamba wengi wanaopelekwa kwenye maeneo ya pembezoni wanahama kutoka huko, wanahamia kwenye maeneo ya centre; wanahamia kwenye Wilaya za Mjini ama kwenye miji mikubwa ama kwenye hospitali kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni changamoto ambayo inasababishwa na kuwepo kwa imbalances za kijiografia ambazo zinajitokeza kwenye mfumo wa afya, ambapo kuna baadhi ya maeneo ni lucrative, ni ya kijani zaidi kuliko maeneo mengine. Sasa kwa msingi huo ni lazima waajiri, kwa maana ya Wakurugenzi ama Wakurugenzi wa Hospitali ama wa Halmashauri ama Makatibu Tawala, wanapowaajiri ni lazima watengeneze package ya kutoa motisha kwa rasilimali watu kwa maeneo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala ambalo nataka kulizungumzia limeshazungumziwa na Mheshimiwa George Simbachawene, linahusu ugatuaji wa madaraka (decentralization by devolution) na hili limezungumziwa na Waheshimiwa Wabunge wengi, Mheshimiwa Lwota, Mheshimiwa Restituta Mbogo, Mheshimiwa Jasmine Tiisekwa, Mheshimiwa Bashe, Mheshimiwa Makilagi na Mheshimiwa Shally Raymond, naomba niliache hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maendeleo ya jamii. Kwenye suala la maendeleo ya jamii mambo makubwa yaliyozungumziwa hapa jambo la kwanza ni la training. Waheshimiwa Wabunge pamoja na Kamati wamechangia kwamba Vyuo vya Maendeleo ya Jamii tuvihamishe kutoka kwetu tuvipeleke Wizara ya Elimu. Jibu la hoja hii ni fupi tu, kwamba vyuo hivi sio vyuo vikuu ni vyuo vya kada za kati ambazo zinahitajika kwa ajili ya kuendeleza Sekta yetu ya Maendeleo ya Jamii na hivyo si lazima vikae kule kwenye Wizara ya Elimu, japokuwa mitihani yote ambayo inatolewa na vyuo hivi inatolewa na Taasisi ya NACTE lakini pia vinasimamiwa na NACTE ambayo ni Taasisi iko chini ya wenzetu wa Wizara ya Elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa tuliyonayo kwenye eneo hili ni namna ya kuwaajiri – absorption kama nilivyosema pale mwanzoni. Tunao watumishi wengi ambao tunawazlisha kila siku wataalam kwenye eneo hili lakini namna ya kuwaajiri ni changamoto. Nitoe rai kwa Waheshimiwa Wabunge na viongozi wote wanaosimamia maendeleo kwenye mikoa na wilaya kuweka bajeti ya kuajiri wataalam hawa, lakini pia kuweka bajeti kwa ajili ya kuwapa vitendea kazi na kuwapa maeneo ya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshaeleza kwamba Sera yetu ya Maendeleo ya Jamii inataka kwa uchache wawepo wawili kwenye kila Kata, wasikae kwenye ofisi kuu pale Wilayani, wakae kwenye kata, wapewe vyombo vya kufanyia kazi ili waweze kutekeleza majukumu yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la nne linahusu huduma za tiba kwenye Hospitali za Muhimbili, MOI, Ocean Road, Kitengo cha Psychiatric kimezungumziwa pamoja na kitengo cha moyo JKCI pamoja na KCMC na Bugando.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nitazungumzia moja tu la tiba ya saratani. Tiba ya saratani wakati tunaingia kwenye majukumu haya zilikuwa haziridhishi kwa kiasi kikubwa sana, lakini mikakati ambayo imewekwa imeanza kuboresha huduma kwenye eneo hili kwa kasi ya ajabu. Kwa sababu kwa mfano, tiba ya chemotherapy ilikuwa mtu anapaswa kusubiri kwa miezi zaidi ya mitatu, leo hii tumeweza kupunguza waiting time kutoka hiyo zaidi ya miezi mitatu mpaka kufikia wiki tano hadi sita tu na tunakusudia kufikia mwisho wa mwaka huu tuweze kushusha waiting time mpaka kufikia kati ya wiki mbili mpaka wiki nne mgonjwa awe ameshapata tiba anayostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, hakukuwa na baadhi ya vifaa vya kutolea tiba ya mionzi. Vile vilivyokuwepo vimekuwa ni vya zamani sana na sasa tayari tumepewa bajeti na tuko katika mchakato wa kununua mashine mpya ya linear accelerator pamoja na CT simulator kwa ajili ya kutoa tiba ya mionzi, ambao tuna uhakika mwisho wa mwezi huu utakamilika. Tuna malengo ya mbali zaidi ya kununua mashine nyingine ya kisasa ambayo katika ukanda huu wa maziwa makuu hakuna hata nchi moja imefunga mtambo huo unaoitwa Pet CT ambao nao lengo lake ni kufanya uchunguzi na kubaini kwa uhakika zaidi yaani kufanya dermacation ya eneo ambalo limeathiriwa na cells ambazo ni malignant ambazo zina cancer.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuna mambo makubwa mawili yanafanyika pale ambayo ni state of the art, ni ya kisasa sana, na hii ni upandikizaji wa kifaa cha usikivu kinachojulikana kama cochlea implant. Hizi ni operations mpya ambazo zitaanza kufanyika pale na zitatusaidia kupunguza idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaanza kufanya operation za kupandikiza mafigo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hii pia itatusaidia kupunguza wagonjwa kwenda nje ya nchi. Hili ni jambo ambalo Mheshimiwa Rais alilizungumza wakati anazindua Bunge hapa hapa Bungeni la kupunguza idadi ya wagonjwa wanaoenda kutibiwa nje ya nchi kwa kuboresha huduma za rufaa ndani ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo napenda kuzungumzia ni hospitali za rufaa za mikoa. Hili lingeweza kwenda sambamba na lile la decentralization by devolution ambalo nimeliruka kwa sababu limeelezewa.
Waheshimiwa Wabunge wengi na hususan Wajumbe Kamati yetu ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, wamekuwa wakitamani sana, huduma za afya zisimamiwe moja kwa moja na Wizara ya Afya Makao Makuu, yaani kama Sectorial Ministry. Sisi tunadhani na tunaamini kwa dhati kabisa kwamba mfumo uliopo sasa ndio mfumo mzuri zaidi wa kuhudumia wananchi kwenye sekta hii ya afya hapa nchini, kwa sababu wananchi kwa kupitia mfumo huu wanakuwa na sauti ya moja kwa moja kwenye huduma zinazotolewa kwenye vituo vya afya kule chini mpaka kufikia ngazi ya hospitali ya wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoki-plan na kufikiria ndani ya Serikali kwa sasa ni angalau kama tutaweza tutenganishe mifumo miwili ya kutoa huduma za afya. Bado ipo katika fikra, kwamba mfumo wa afya ya msingi yaani kutoka zahanati, kituo cha afya mpaka ngazi ya hospitali ya wilaya usimamiwe na wenzetu wa TAMISEMI kupitia mamlaka zao za Serikali za Mitaa, lakini hospitali za mkoa kwa sababu ni hospitali za rufaa uje kwenye fungu 52, yaani Wizara ya Afya usimamiwe huku pamoja na huduma nyingine za rufaa. Ni wazo ambalo tunalifikiria ili ku-accommodate mapendekezo mbalimbali ambayo yamekuwa yakitolewa na Waheshimiwa Wabunge.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii na naomba kuunga mkono hoja ya Waziri wa Afya.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa hii na mimi nichangie kwenye hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango. Kwanza, nianze kwa kuiunga mkono hoja hii, lakini pili kwa kumpongeza yeye mwenyewe binafasi na Naibu wake kwa kuleta mpango huu mzuri ambao unatoa dira ya namna ambavyo Serikali itatekeleza majukumu yake kwenye mwaka unaokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, naomba nitoe ufafanuzi kwenye maeneo machache ambayo yamegusa sekta ya maliasili na utalii kwa ujumla wake. Lakini kabla ya kufanya hivyo, nitumie nafasi hii kuwashukuru viongozi wetu wa juu wa Serikali kwa miongozo mbalimbali na maagizo ambayo wamekuwa wakitupa toka wametupa dhamana ya kusimamia sekta hii. Mimi naomba niwape uhakika tu wao pamoja na wananchi wa nchi yetu kwamba sintowaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ambalo nimeona limejitokeza kwa kiasi kikubwa na ambalo ninaomba nianze kwa kulitolea ufafanuzi kabla sijafika mbali ni suala la kwamba Waziri mpya wa Maliasili na Utalii ameanza kazi kwa kufukua makaburi. Naomba niseme tu kwamba mimi siyo mashuhuri sana kwa ufukuaji wa makaburi, lakini ukiwa Waziri halafu ukawekwa kwenye Wizara ambayo wiki ya kwanza tu hata kabla hujaanza kazi kila mtu anasema umekalia kuti kavu, ni lazima kabla hujaanza kufanya kazi uliyopewa uanze kwanza kwa kusafisha nyumba yako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo, tumeanza kazi ya hygiene kwenye Wizara hii na kazi hii haitakoma mpaka pale ambapo mitandao yote ya watu ambao wako ndani ya Wizara hii wanashiriki kwenye vitendo vya ujangili, wanashiriki kwenye hujuma na wamekuwa wakitajwatajwa kwenye kashfa mbalimbali za rushwa, tutashughulika nao kwanza. Tukimaliza kuing’oa hii mitandao sasa tutaanza kazi kubwa na pana na ya maana zaidi kwa nchi yetu ya kuendelea kuongeza idadi ya watalii, lakini pia kuongeza idadi ya vivutio, pia kuendelea na kazi ya uhifadhi wa rasilimali hii adimu tuliyonayo kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tutafanya hivyo kwa kuwekeza kwenye kanda nyingine kama Kanda ya Kusini kwa maana ya diversification ambapo kwa sasa tutaelekeza nguvu zetu huko ili kuifungua corridor ya Kusini kiutalii. Serikali imepata fedha, shilingi bilioni takribani juu kidogo ya 300 kwa ajili ya kutekeleza mradi mkubwa wa kuifungua Kanda ya Kusini kiutalii na ninaomba hapa nitambue mchango mkubwa wa Waziri wa Fedha na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango na timu yake, kwa kazi kubwa waliyofanya ya kuandika andiko la mradi huu na hatimaye kufanikisha zoezi la kupata fedha hizi zaidi ya bilioni 300 kwa ajili ya kufungua corridor mpya ya Kusini kitalii na ninaona kwa kweli yuko busy kutekeleza mpango wake ule uliopita na sisi tunamshukuru. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla hatujafika kuanza kutekeleza hii mipango yote mizuri, nilisema ni lazima tuanze kusafisha. Katika kusafisha naomba niseme sikusudii kufukua makaburi ya Mawaziri wazuri waliopita hapo wakapata ajali mbalimbali za kisiasa kama akina Mheshimiwa Maige, Mheshimiwa Kagasheki na Mheshimiwa Maghembe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nianze kwa kuzungumzia Waziri mmoja ambaye wenzetu hawa wa Upinzani walimsema sana alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii na huyu si mwingine ni Mheshimiwa Lazaro Nyalandu. Ninataka niseme tu kwamba rafiki yangu, Mheshimiwa Nassari alizungumza kwa mwembewe nyingi sana hapa Bungeni kwamba kama Dkt. Slaa…
(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Unajua ukiwa unaishi kwenye nyumba ya vioo, usianzishe vita ya mawe, kuna wengine kwa wale mliokuja wapya humu Bungeni mnatakiwa mjifunze mazingira ya humu ndani, kuna watu wanaguswa na kuna watu hawaguswi. Mimi ni katika watu wasioguswa na huwa sipendi mambo ya kipuuzi kabisa hata siku moja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu amesema nimeanza kazi kwa kuanza kufukua makaburi sasa sitaki kuwakumbusha yaliyotokea huko nyuma lakini naomba tu niwape uhakika kwamba mimi huwa sichezewi chezewi. Mtu aliyesema nimeanza kazi hii kwa kufukua makaburi na mimi nasema leo nafukua moja na ninaanza kufukua hilo moja kwa maelezo yaliyotolewa na Wabunge hawa wa Upinzani kwenye Bunge lililopita. Walisema Mheshimiwa Lazaro Nyalandu kazi yake ni kustarehe kwenye mahoteli ya kitalii, kazi yake ni kutembea nchi za mbali huko Marekani wapi na warembo, wakasema alitembea alienda Marekani na Aunty Ezekiel.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakasema Ndugu Lazaro Nyalandu anatumia helikopta za wawaekezaji kwa shughuli zake binafsi za kisiasa na Mheshimiwa Nassari alisema kwamba kama yeye kama Dkt. Slaa angeshinda Urais mwaka 2015 na akampa yeye Uwaziri wa Mambo ya Ndani kwa siku moja tu, angeanza kwa kushughulika na Mawaziri wa hovyo kama Mheshimiwa Lazaro Nyalandu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa leo ninaeleza kwamba kwa nini Mheshimiwa Nassari alikuwa sahihi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Nassari alikuwa sahihi kwa sababu wakati Waziri Nyalandu akistarehe kwenye Hoteli ya Serena pale Dar es Salaam akitumia helikopta ya mwekezaji wa TGTS, mezani kwake…….
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, nilichokuwa nataka kusema ni tu kwamba wakati Mheshimiwa Nyalandu Nyalandu akivinjari kwenye Hoteli ya Serena ambapo alikuwa akifanyia kazi zake za Waziri wa Maliasili na Utalii kwenye hoteli ile na akapewa chumba akawa anaishi pale kwa muda wote ule, mezani kwake kulikuwa kuna GN yaani tamko la Serikali kuhusiana na kitu kinachoitwa concession fees kwenye mahoteli ambayo yako ndani ya mbuga ya Serengeti.
KUHUSU UTARATIBU . . .
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Bobali mimi mzoefu humu ndani, wewe unadhani mimi najibu hoja, mimi sijibu hoja mimi nachangia, mwenye hoja yuko pale Waziri wa Fedha na Mipango. Muwe mnajifunza nishasema mimi huwa sichezewi chezewi. Kwa sababu najua Kanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kuchangia, ninachokisema ni kwamba wakati Mheshimiwa Nyalandu akifanya yote hayo kulikuwa kuna mambo makubwa mawili ambayo napenda tu kuyatolea mfano hapa.
Moja; mezani kwake kama Waziri wa Maliasili na Utalii kulikuwa kuna concession fees ambayo ilikuwa imependekezwa na TANAPA na gazeti likatengenezwa likisubiri signature ya Waziri ili Serikali ianze ku-charge concession fees kwenye mahoteli ya kitalii. Hilo lingeongeza mapato na kwa mwaka huo wa 2014 tungeweza kukusanya bilioni 16 lakini Waziri yule hakusaini hiyo GN mpaka anaondoka madarakani, maana yake Mheshimiwa Nyalandu aliikosesha Serikali mapato ya takribani bilioni 32, hilo ni moja na ni jambo ambalo watu wa mahoteli walipinga na baada ya watu wa mahoteli kupinga, Serikali ikashitakiwa Mahakamani, Serikali ikapata ushindi mahakamani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, Waziri alikuwa hana lolote lile la kuamua kwa sababu kuna amri ya Mahakama kwamba Serikali iko sahihi na i-charge concession fees, lakini Waziri yule hakusaini kwa miaka miwili mpaka anatoka madarakani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo kama haya ukiniambia nafukua makaburi mniache tu niendelee kufukua lazima nifukue kwa sababu bila kuweka mambo sawa, bila kujua kwa nini Mheshimiwa Nyalandu hakusaini, bila kujua Mheshimiwa Nyalandu alikuwa anashirikiana na akina nani na je, alikuwa anashirikiana nao wapo ama wameondoka? Huwezi kufanya kazi yako vizuri. Ndiyo maana hata Mawaziri watakaowekwa pale wataendelea kutolewa tu, wataendelea kukalia kuti kavu tu, sasa mimi siko tayari kukalia kuti kavu, hata nikikaa miezi mitatu nitakuwa nimeinyoosha hii sekta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili napenda kuzungumzia mahusiano ya kutatanisha aliyokuwa nayo Waziri wa Maliasili na Utalii Ndugu Nyalandu na wawekezaji wa taasisi maarufu inajulikana kama Friedkin Family Foundation ni billionea kutoka nchi ya Marekani ambayo ilikuwa ina Makampuni yanayofanya kazi mbalimbali za utalii hapa na bado yapo mpaka sasa. Moja inaitwa Mwiba Holdings, nyingine inaitwa Winged to Winrose na nyingine inaitwa Tanzania Game Trackers Safaris. Kampuni zote hizi, Kampuni ya TGTS ilipewa vitalu zaidi ya vitano ambazo ingepaswa kupewa kwa mujibu wa sheria maana yake ni kwmba hapo kuna mazingira ya kutatanisha, kuna mambo hayako sawa na bado Kampuni hii ipo na inafanya kazi kwenye sekta hii, ukisema nisifufue makaburi utakuwa unanionea, ni lazima nijue kwa nini waliopewa vitalu zaidi ya vitano? Kwa nini wanaendelea kuwinda?
Kampuni ya Mwiba Holdings ina tuhuma za ujangili kwamba Kampuni inawinda, inafaya kazi za utalii lakini imekamatwa na nyara za Serikali na hizi Kampuni zote zinamilikiwa na mtu mmoja anaiywa Tom Friedkin ambaye ni rafiki wa Ndugu Nyalandu na Waziri huyu kama nilivyosema huko nyuma alikuwa akifanya kampeni za Urais kipindi kile tulijaribu na sisi kuomba ridhaa ya Chama kugombea Urais, alikuwa akifanya kampeni zake, akizunguka na helkopta ambayo inamilikiwa na Kampuni ya huyu Ndugu Tom Friedkin. Sasa katika mazingira kama hayo, Waziri wa Maliasili na Utalii, GN ya kusaini kuhusu kudai concession fee iko mezani kwao hausaini na unaka kwenye hoteli...
T A A R I F A . . .
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, zama zinabadilika na uongozi pia unabadilika. Kwenye Wizara ya Maliasili na Utalii sasa hivi kuna Waziri ambaye anaweza kumchukulia hatua Ndugu Nyalandu, kwa hivyo kama ndiyo kilio chako Ndugu Haonga mimi nitaagiza hapa TAKUKURU pamoja na Jeshi la Polisi wayasikilize haya ninayosema, wachukue Hansard, wakafanye uchunguzi ili waweze kumchukulia hatua Ndugu Nyalandu wala hilo halisumbui. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ndiyo kiu yako na wewe kama mwananchi na kama Mbunge kwamba kwa nini Nyalandu hajafika mahakamani, mahakama bado zipo na jinai haiishi muda, jinai hata miaka 100 ipo tu, kwa hiyo vyombo vinavyohusika vichukue hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo Ndugu Nyalandu alikuwa akitumia helicopter za Kampuni za huyu Ndugu Tom Friedkin kufanya kampeni zake za Urais lakini pia kufanya kampeni zake za ubunge Jimboni. Katika mazingira kama hayo, dada yangu Devotha Minja ukisema nisifukue makaburi utakuwa unanionea bure tu. Mniache nifukue haya makaburi, tuweke sawa nchi, tumsaidie Mheshimiwa Rais ndiyo kazi tuliyopewa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu, vitalu vya uwindaji kabla ya Ndugu Nyalandu vilikuwa vikitolewa kwa makampuni mbalimbali na muda wa kuwinda ulikuwa ni katika kipindi cha miezi mitatu tu, kati ya Julai mpaka Oktoba ili kuwapa nafasi wale wanyama kupumua na pia kuzaliana, lakini...
T A A R I F A . . .
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea na mchango wangu, Ndugu Nyalandu alivyopewa tu kiti cha Waziri wa Maliasili na Utalii alichokifanya bila huruma yoyote ile, bila uzalendo wowote ule alianzisha mchakato wa kubadilisha...
MWENYEKITI: Ahsante.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2017 na Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019; na Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii. Labda nianze kwanza kwa kumkumbusha Mheshimiwa Selasini, wale anaowasema wale ndiyo shemeji zake wakubwa maana dada zake wana rangi ambayo inavutia sana makabila ya wale anaowasema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo hata nyumbani kwangu leo nimeondoka asubuhi nimewaaga wajomba zake. Kwa hivyo, haya mambo hayawezekani katika nchi yetu. Sisi ni wamoja na hata Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe ana wajomba zako wa kutosha, Mheshimiwa Mwigulu, Mheshimiwa Makamba and the list goes on and on! Huwezi kuzungumza ukabila Tanzania. Tuachane na haya mambo ya hovyo hovyo, hayatusaidii kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, naomba nianze kuchangia kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshiimwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa jinsi ambavyo anaendelea kutoa dira na mwelekeo wa Taifa letu katika kuboresha maisha ya Watanzania na kuleta ustawi wa Watanzania wote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nichangie hoja iliyotolewa na Mheshimiwa Richard Phillip Mbogo kuhusiana na uvunaji wa mazao ya maliasili kutoonekana kuchangia kikamilifu katika pato la Taifa letu. Alipenda kujua sababu hasa ni nini?
Mheshimiwa Spika, Sekta ya Misitu inachangia pato la Taifa kwa kiwnago cha asilimia 3.5 tu! Kinaonekana ni kiwango kidogo sana na hata sisi tunaosimamia sekta hii tunaona kwamba kiwango hiki ni kidogo, lakini kiukweli kiwango hiki hakipaswi kuonekana kidogo ila kinachosababisha kikubwa ni formula ya mfumo wa fedha kwa namna ambavyo mchango wa Sekta ya Misitu unakokotolewa, lakini mchango wa Sekta ya Misitu na mazingira kwa ujumla ni mkubwa sana kwenye uchumi wa Taifa letu kuliko ambavyo inasemwa kwamba ni asilimia 3.5 tu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ku-mention mambo machache tu, Sekta ya Misitu inachangia kwenye upatikanaji wa maji, umeme na kwenye kilimo. Ukitaka kuitazama kwa upana wake utaona kwamba kama Watanzania zaidi ya asilimia 70 wanategemea kilimo kama shughuli yao ya msingi ya kiuchumi na kama kilimo kinategemea maji ya mvua na kama mvua zinatokana na uwepo wa misitu iliyohifadhiwa, maana yake kwa kiasi kikubwa sana uchumi wa Tanzania wa watu wetu walio wengi unategemea kwa kiasi kikubwa misitu ambayo inahifadhiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia, wanyama kuanzia ng’ombe au zaidi ya milioni 36 ambao Mheshimiwa Mpina kila siku hapa anajivunia nao wanategemea maji yanayotokana na uhifadhi wa vyanzo vya maji ambavyo ndiyo hiyo misitu inayohifadhiwa. Uzalishaji wa umeme, miradi ya umeme ambayo kila siku Mheshimiwa Dkt. Kalemani hapa anajivunia na Waheshimiwa Wabunge kila siku mnaomba umeme kwa ajili ya wannachi wetu. Ule umeme unaozalishwa kutokana na maji ukirudi kinyumenyume utakuja kugundua unatokana pia na uhifadhi wa misitu ambao tunaufanya katika Wizara yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, ukitaka kukokotoa vizuri ukaangalia hizo factor zote utaona wazi kabisa kwamba Sekta ya Misitu inachangia kwa kiasi kikubwa sana kwenye uchumi wa nchi yetu kuanzia kwenye kuzalisha umeme, kilimo, mifugo, samaki, uhifadhi wa wanyamapori kwa sababu kwenye hii misitu pia tunahifadhi wanyamapori. Sasa ni nani ambaye ana formula ya kiuchumi ya kuangalia umuhimu wa misitu katika uhifadhi wake wa bioanuai ambao unafanyika. Kwa kweli utaona ni kwa kiasi kidogo sana formula inayotumika na wenzetu wa Wizara ya Fedha kukokotoa umuhimu wa misitu inavyotumika.
Mheshimiwa Spika, pia misitu inatusaidia sana kuondoa madhara ambayo yangejitokeza kutokana na uwepo wa hewa ya ukaa. Kama tungekuwa hatuna misitu maana yake hewa ya ukaa ingeongezeka duniani na mazingira yangeharibika maradufu na maradufu. Kwa hivyo, kwa kuhifadhi misitu tunaweza kupunguza ongezeko la hewa ya ukaa angani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vile vile kwenye misitu tunapata asali, uyoga, dawa na tunapata hewa ya oxygen ambayo sisi sote tunaivuta. Sidhani kama formula za kiuchumi zinaangalia hadi oxygen ambayo tunavuta kila siku ambayo inatokana na uwepo wa misitu ambayo inatusaidia ku-control hewa ya ukaa hapa duniani.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, kwa kweli mchango wa misitu katika uchumi na katika pato la Taifa hauwezi kuwa ni hiyo asilimia 3.5 tu ambayo inazungumzwa na wanatakwimu za kiuchumi. Sisi tunaamini ingepaswa kuwa kubwa zaidi ya hiyo lakini kwa sababu ya formula inayotumika mchango wake unaonekana kuwa ni huo wa asilimia 3.5 ya pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, hoja ya pili nilipenda kuzungumzia ilitolewa na Mheshimiwa Magdalena Sakaya ambaye alisema kwamba utumiaji wa mazao ya misitu nchini kwa kutengeneza samani badala ya kuagiza kutoka nje ya nchi ambapo tunapoteza chanzo cha mapato.
Mheshimiwa Spika, tunakubaliana na yeye, lakini bado sana teknolojia ya wazalishaji wetu hapa ndani imekuwa duni kwa kiasi kikubwa na mazao mengi yanayotokana na uvunaji wa misitu bado hayajatumika kikamilifu kwa matumizi mengine mbalimbali ikiwemo hiyo ya kutengeneza samani za maofisini na majumbani, lakini pia kutengeneza briquette kwa ajili ya mikaa na matumizi mengine mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali imekuwa ikitoa maagizo mbalimbali mara kadhaa kuhusu taasisi mbalimbali za Serikali kuanza kutumia samani za hapa ndani na mfano mzuri ni kwenye Bunge lako ambapo tunatumia samani zinazotokana na mazao ya misitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia mwaka huu kadri ambavyo Ilani ya Uchaguzi inatuelekeza tutenge asilimia 10 ya mazao ya misitu kwa ajili ya viwanda vya ndani, tunafanya hivyo. Huu ni mwaka wa pili sasa tumekuwa tukifanya hivyo, tunatenga uzalishaji kwenye misitu kwa asilimia 10 kwa ajili ya viwanda hususan katiak mashamba yetu ya Longuza na mashamba ya Mtibwa.
Mheshimiwa Spika, hoja ya mwisho ambayo napenda kuchangia inatokana na mchango alioutoa Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe hapa Bungeni kuhusiana na kwamba VAT imepunguza kasi ya ukuaji wa Sekta ya Utalii hapa nchini. Introduction ya VAT inaweza ikasemwa kwamba imepunguza kasi ya ukuaji wa Sekta ya Utalii lakini sisi tunapenda kuona kwamba bado ni mapema mno kufanya tathmini ya aina yoyote ile kama introduction ya VAT imeathiri ukuaji wa sekta ama la!
Mheshimiwa Spika, hatupingi wala hatukubali, lakini tunaona tu kwamba muda wa kufanya tathmini bado hautoshi na sisi tunaona sababu za ku-introduce VAT kwenye Sekta ya Huduma za Utalii ilikuwa ni ya maana sana, kwamba sekta hii kwa muda mrefu imekuwa ikionekana kama vile ni sekta ipo na haizalishi sana kwa ajili ya Watanzania.
Mheshimiwa Spika, sasa, ili Watanzania wa kawaida waweze kufaidika na Sekta ya Utalii ni lazima Sekta ya Utalii itozwe kodi ili hizo kodi ziende kutumika kutekeleza miradi ya kijamii ambayo itawagusa wananchi wengi, hilo ni jambo la kwanza. Pia, ni lazima wananchi wawezeshwe kushiriki katika Sekta ya Utalii ili nao wapate kipato kutokana na sekta yenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa kwa bahati mbaya sana, sekta hii kwa miaka mingi imekuwa ikiwa controlled na wawekezaji kutoka nje ambapo mawakala wapo nje ya nchi na baadhi ya mawakala wapo ndani. Malipo kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakifanyika nje ya nchi na kwa hivyo hapa Tanzania tunakuwa hatupati chochote. Pia wafanyabiashara wa Tanzania walikuwa wachache kwa miaka mingi.
Mheshimiwa Spika, sasa tulichokifanya katika miaka hii ni kutanua wigo wa kuwavutia wawekezaji wa ndani nao washiriki kwenye biashara ya utalii ili pia tuweze kupata kodi. Pia tunapo-introduce VAT maana yake walau tunapunguza economic leakage ambayo ilikuwa inasababishwa kwa mapato ya utalii kubaki nje na kutokuingia hapa ndani kwa sababu tunachaji kwenye huduma ambazo ziko hapa ndani. Kwa kufanya hivyo, tunakuwa tuna uhakika sasa ule mchango mkubwa ambao unaonekana kwa sekta pana ya utalii wa asilimia 17.6 kuwa na faida kwa wananchi wa kawaida. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja na ahsante.
Makadilio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Maliasili na Utalii
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii niweze kuhitimisha hoja yetu ya Wizara ya Maliasili na Utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze kwa kutumia fursa hii kukushukuru wewe mwenyewe pamoja na Mheshimiwa Mtemi John Chenge, Mbunge na Mwenyekiti wa Bunge kwa kutuongoza vyema kwenye mjadala huu toka tulipoweka mezani mapema jana. Pia nitumie fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote kwa kujadili hotuba ya Wizara yangu kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Mheshimiwa Spika, nitumie pia nafasi hii kumshukuru sana Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii pamoja na Kamati yake yote kwa kuchambua, kujadili na kutoa maoni na ushauri kwenye maeneo mbalimbali yaliyohusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara yetu kwa mwaka wa fedha 2017/2018 na pia kutoa maoni kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2018/2019. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile ninawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango ya maandishi lakini pia kwa michango ya kusema hapa Bungeni moja kwa moja. Kimsingi Wizara yetu imepokea uchambuzi, maoni na ushauri wao. Niwahakikishie tu kwamba tutauzingatia kwa kina na kwa uzito wake katika utekelezaji wa majukumu yetu katika siku zinazokuja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia binafsi niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wenzangu kuwa kwa kweli siku mbili za kukaa hapa mbele zimekuwa ni somo kubwa sana kwangu kwenye kazi hii ya dhamana ya Wizara ya kuwa kama Waziri kwenye Wizara ambayo nimepewa na Mheshimiwa Rais niweze kuwatumikia Watanzania wenzangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, japokuwa michango mingine nikiri ilikuwa mikali kweli kweli, lakini nilifarijika kwamba michango hii imenipika vizuri zaidi na ninaamini baada ya leo nitakuwa Waziri mzuri zaidi kuliko ilivyokuwa juzi kabla sijasimama mbele ya Bunge lako tukufu na kutoa hoja ya Wizara yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaamini michango ya Waheshimiwa Wabunge imenipitisha kwenye tanuru ambalo linazidi kuongeza uwezo na umahiri wangu wa kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye sekta hii nyeti, kwenye uchumi na maendeleo ya Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo wahenga waliwahi kusema kwamba ili dhahabu iweze kung’ara vizuri ni lazima ipite kwenye tanuru lenye moto mkali na mimi ninashukuru sana kwa fursa ya kupita mbele ya tanuru la Bunge lako tukufu ambapo nimepikwa na kuiva vizuri zaidi tayari kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo kwenye sekta hii nyeti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wabunge waliochangia kwenye Wizara yetu jumla walifika 99 kati yao waliochangia kwa kuongea moja kwa moja hapa Bungeni ni 42 na 57 walichangia kwa maandishi.
Mheshimiwa Spika, naomba niwahakikishie tu kwamba maoni yao tumeyapokea na pamoja na hoja ambazo zimetolewa ufafanuzi na Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria na Mheshimiwa Naibu Waziri na nyingine ambazo nitazifafanua mimi mwenyewe hapa, naomba kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba hoja nyingine tutawasilisha majibu yake kwa maandishi kwa sababu hatutaweza kufafanua maeneo yote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maeneo yaliyoguswa na Kamati yetu ni pamoja na utekelezaji wa miradi ya maendeleo, migogoro ya mipaka na ushirikishaji katika zoezi la uwekaji vigingi, ukokotoaji wa takwimu za idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania, utozaji wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), uwindaji wa kitalii, biashara ya wanyamapori hai, utangazaji wa utalii, ukusanyaji wa mapato, mgongano wa Sheria za Uhifadhi na sheria nyingine, hali ya jumuiya za hifadhi za wanyamapori, uingizaji mifugo kwenye maeneo ya hifadhi, uharibifu wa misitu na matumizi mseto ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia baadhi ya hoja ambazo zimewasilishwa na Waheshimiwa Wabunge ziligusa maeneo ya biashara ya wanyamapori hai, mradi wa umeme wa Rufiji, kurejesha Wizara ya Maliasili na Utalii sehemu ya uvuvi ili kuendeleza utalii wa fukwe, migogoro ya mipaka na ushirikishaji katika zoezi la uwekaji vigingi, mgogoro wa Pori Tengefu la Loliondo, kuendeleza utalii Kusini mwa Tanzania, wanyamapori wakali na waharibifu, uwindaji wa wenyeji, ulinzi wa maeneo ya mapito, mtawanyiko na mazalia ya wanyamapori, tozo ya pango kwenye hoteli zilizopo kwenye maeneo ya hifadhi na kodi na tozo mbalimbali kwenye sekta ya utalii.
Mheshimiwa Spika, nyingine ni kubaini na kuendeleza vivutio vya utalii, ushirikishaji kwenye uhifadhi wa maliasili, malikale na utalii, biashara ya mazao ya misitu, uwezo wa kusimamia uhifadhi wa maliasili, malikale na utalii, matumizi ya nishati ya kuni na mkaa, utangazaji utalii, maeneo ya hifadhi yaliyopoteza sifa kwa mfano Pori Tengefu la Wembele, uingizaji mifugo kwenye maeneo ya hifadhi, uendelezaji wa maeneo ya malikale na historia ya utamaduni wa makabila mbalimbali, kuimarisha mikakati ya uhifadhi wa vyanzo vikuu vya maji kwenye Mto Ruaha na mito mingine, matumizi mseto eneo la Hifadhi ya Ngorongoro na changamoto ya utawala bora.
Mheshimiwa Spika, nitaomba nitumie fursa hii sasa kutoa ufafanuzi kwenye baadhi ya maeneo mahususi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mchungaji Peter Msigwa, rafiki yangu na mtani wangu alinipiga sana hapa jana. Napenda kutumia sehemu moja kuanza kufafanua kwenye hoja yangu kwamba mimi ni kiongozi kijana, ningepaswa kuwa visionary zaidi, lakini yeye alikuwa anasema mpaka jana alikuwa hajaona chochote kipya ambacho kimeletwa na Waziri huyu kijana. Kwanza mimi sio kijana, labda nina sura tu ya ujana, lakini nilishavuka ujana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kuleta kwenye attention ya Mheshimiwa Msigwa pamoja na Waheshimiwa Wabunge wenzangu wote mambo machache kadhaa ambayo katika kipindi hiki cha miezi nane tumeweza kuyabuni ya kuyaanzisha na mengi yapo katika hatua mbalimbali. Pengine ndiyo maana watu wengi sana wamekuwa wakishangaa hata Mawaziri wenzangu kwamba mbona Wizara ya Maliasili safari hii inapita taratibu fulani hivi ukilinganisha na miaka takribani mitatu mfululizo iliyopita?
Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba tumebadilisha sana namna ambavyo tuna-approach mambo kwenye Wizara hii toka tulipoteuliwa na zaidi tunatumia mbinu ya ku- engage wadau. Mbinu ya kushirikisha wadau pamoja na waathirika wa maamuzi mbalimbali ambayo tumekuwa tukiyafanya (multisectoral stakeholders engagement). Tunafanya sana mambo yetu kwa kushirikisha wadau.
Mheshimiwa Spika, baadhi ya mambo ambayo tumeanza kuyafanya ni pamoja na kubuni Tamasha la Urithi wa Mtanzania ambalo litafanyika kila mwaka hapa nchini na kwenye maeneo yote yale ambapo Watanzania ama marafiki zetu wanaweza kupenda kufanya ambapo litafanyika mwezi Septemba wa kila mwaka.
Mheshimiwa Spika, Tamasha hilo tumelipa jina la Urithi Festival. Tuliteua Kamati ya wadau mbalimbali wa media, tasnia za utamaduni, mambo ya urithi na utalii na kuwashirikisha kubuni wazo la kuwa na tamasha ambalo litautambulisha utamaduni wetu sisi kama Watanzania kwamba tuna lugha yetu ya Kiswahili, lugha zetu za asili za makabila zaidi ya 120 tuliyonayo, mila na desturi zetu, historia yetu kama Taifa na Muungano wetu wa kipekee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna mambo mengi ambayo tunaweza tukaelezea kuhusu Tanzania zaidi ya kuwa na aina moja tu ya urithi ambao ni urithi wa asilia, kibailojia (natural heritage) ambayo ni ya wanyamapori, uoto na uwanda, tunaweza tukazungumza pia kuhusu utamaduni wetu kuhusu mila na desturi, historia yetu na mambo kama hayo. Kwa hiyo, tumeamua ku-designate na kuutambua mwezi Septemba kama Mwezi wa Urithi wa Mtanzania na kilele chake itakuwa ni Tamasha la Urithi Festival ambalo litafanyika kila mwaka na tutaanza kulitekeleza mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika mwezi huu, mambo mengi yatafanyika ikiwemo matamasha ya ngoma za jadi, michezo ya kuigiza, matamasha ya muziki wa kizazi kipya, matamasha ya muziki wa dansi, matamasha ya filamu, matamasha ya hotuba, ngonjera na vitu vingine mbalimbali ambavyo tumekuwa tukivifanya kama Watanzania.
Mheshimiwa Spika, pia katika mwezi huu kutapikwa vyakula vya Kitanzania, menu maalum ya vyakula vya asili vya Mtanzania kwenye mahoteli yote ya kitalii. Kwa hiyo, ndiyo maana tumesema tuna-engage wadau wa sekta hii ili waweze ku-absorb na kukubaliana na mawazo haya, waweze kushiriki kwenye tamasha hili kikamilifu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia katika mwezi huu mavazi yatakuwa ni ya Kitanzania, kama utapenda kuvaa vazi la asili ya kimwambao, vazi la Kiswahili kama alivyopendeza Mheshimiwa Mtolea na Mheshimiwa Masoud, basi utavaa hivyo na kwenye mahoteli wanaweza wakavaa hivyo. Kama utapenda kuvaa vazi la Kimasai, utavaa hilo; kama utapenda kuvaa vazi la vitenge (African prints) utavaa vitenge ama khanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, basi kwenye mahoteli yote ya kitalii, Balozi zetu, Ofisi za Serikali kutakuwa kuna mavazi ya aina hiyo kuanzia tarehe moja Septemba na lengo ni kuutambulisha utamaduni wetu, lakini pia tutapamba maeneo mbalimbali ya nchi na taswira mbalimbali za Utanzania wetu. Lengo ni kusherehekea Urithi wa Mtanzania na mwezi Septemba tumeamua kufanya hivyo. Hili ni katika mojawapo ya mawazo tuliyokujanayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia lengo letu kufanya hivi, ni kuhakikisha tunaweka fungamanisho (linkage) la utalii wa wanyamapori (wildlife), maeneo asilia na utalii wa utamaduni. Lengo ni kuongeza mazao ya utalii ili watalii wawe na shughuli nyingi wanazoweza kuja kuzishuhudia Tanzania. Matamasha ya namna hii yanafanyika South Africa na Brazil.
Mheshimiwa Spika, kuna watu wanafahamu Tamasha la Samba huko kwenye nchi za kule Amerika ya Kusini, ni maarufu sana duniani na watu wanakwenda kule kipindi hicho cha tamasha hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kusudio la kuwa na tamasha hili ni kitu kama hicho ambacho kinafanyika nchi kama za Brazil na Mexico ambapo kuna mwezi wa urithi wa nchi zao kama huu tunaozungumza hapa. Hili ni katika mojawapo ya mawazo tuliyonayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, tumekuja na wazo la kuhuisha mifumo ya kukusanya mapato na mifumo ya taarifa katika Wizara ya Maliasili. Tunatengeneza mfumo mmoja unaojulikana kama MNRT Portal ambapo ifikapo Julai Mosi mfumo huu utaanza kutumika. Malengo ni kukidhi matakwa ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi lakini pia kukidhi matakwa ya maagizo mbalimbali ya viongozi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Rais hapa alipokuwa anazindua Bunge hili alisema ni lazima tubuni mbinu ya kukusanya mapato kisasa ili kuhakikisha mapato hayavuji katika sekta ya utalii. Pia ni kukidhi matakwa ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano tulioupitisha hapa mwaka 2016 kwamba tutumie mifumo ya kielektroniki kukusanya mapato ili kuongeza tija katika ukusanyaji, lakini pia ili kuongeza urahisi wa mtu kufanya malipo ndani ya Serikali hususan sisi kwenye sekta yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumetengeneza mfumo mmoja ambao ndiyo walikuwa wanauzungumza Waheshimiwa Wabunge hapa, hata leo alizungumza Mheshimiwa dada yangu na shemeji yangu, Mheshimiwa Lucy Owenya kwamba kuwe kuna dirisha moja. Sasa dirisha tunalolitengeneza ndiyo huu mfumo wa kielektroniki. Kwa hiyo, ukitaka kulipa chochote kile kwenye sekta ya utalii, kila Idara ya Serikali tutakuwa tumetengeneza fungamanisho ambapo unaweza ukalipa kupitia kwetu na wao wakapata pesa zao ili kuongeza urahisi wa kufanya biashara kwenye sekta ya utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia kumekuwa kuna malalamiko mengi kwamba watalii wanalipa kwa mawakala huko nje ya nchi na sisi hapa pesa haziingii, lakini mtalii anakuja, alishalipia kule, hapa anahudumiwa na pesa inabaki kule nje. Ili kuondoa hiyo, tuliona tukitengeneza mfumo mmoja wa malipo wa kielektroniki ambao pia utakuwa una applications mbalimbali zikiwemo za kwenye simu, zikiwemo za kwenye mtandao tunaweza ku-capture malipo yanayofanyika nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, pia tutaweza ku-capture taarifa, Kamati yetu ilizungumzia suala la taarifa, tutaweza ku- capture taarifa kwa sababu mfumo huu tutaufungamanisha na mifumo ya Uhamiaji.
Mheshimiwa Spika, nafikiri kila mtu anafahamu jitihada zinazoendelea kule Wizara ya Mambo ya Ndani kutengeneza e-visa na e-migration systems ambazo zitakuwa zimefungwa kule, lakini sisi tutazifungamanisha na mfumo wetu ili tuweze kukusanya taarifa sahihi na kwa wakati katika sekta ya utalii. Kwa hiyo, tunakoenda, changamoto kama hizi za takwimu kutokuwa sahihi hazitakuwepo tena. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo tumefanya na tunaendelea kulishughulikia ni suala la kuhuisha maeneo ya makumbusho pamoja na maeneo ya mambo ya kale kwani yamekuwa katika hali duni. Tumeona mfano mzuri wa utekelezaji wa mpango huu kwenye eneo la Oldivai Gorge ambapo Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro imeingia ubia na Idara ya Mambo ya Kale, pamoja Taasisi ya Makumbusho, wamejenga kituo kizuri sana cha makumbusho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, model hii tumeona tu- amplify kwa sababu Idara ya Mambo ya Kale inapata bajeti ndogo, lakini ina maeneo nyeti yenye thamani kubwa sana kidunia ya kiutalii, tumeona tuwaunganishe na taasisi zetu nyingine ambazo zinafanya shughuli mbalimbali na zinaingiza kipato kikubwa ili waweze kuyaboresha yale maeneo ya mambo ya kale na maeneo ya makumbusho kwa ubia na hatimaye tuweze kuyatangaza kwa pamoja ukilinganisha na maeneo ya Hifadhi za Taifa za maeneo ya Mapori ya Akiba na Mapori Tengefu ili tuweze kupata wageni wengi zaidi watakaokuwa wanatembelea maeneo ya mambo ya kale na maeneo ya makumbusho.
Mheshimiwa Spika, bahati nzuri mkakati huu uko vizuri na tumeingiza kwenye bajeti hii. Kwa hiyo, kuanzia mwezi wa Saba, taasisi hizi ambazo zinauwezo mkubwa wa kipesa, zitaanza kufanya uendelezaji kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, eneo la makumbusho pia litaboreka na lengo ni kuongeza product za utalii (tourism products), mazao ya utalii, kwa sababu sasa hivi utalii kwa zaidi ya asilimia 80 umejikita zaidi kwenye utalii wa mambo ya wanyamapori. Sasa tunavyotanua wigo kufanya matamasha, lakini pia kuongeza makumbusho na kuboresha maeneo ya mambo ya kale, maana yake tunaongeza mazao ya utalii. Lengo letu tunapoongeza mazao ya utalii ni kumtaka mtalii anapoingia nchini akae muda mrefu zaidi.
Mheshimiwa Spika, sasa hivi wastani wa mtalii kukaa hapa nchini ni kati ya siku tisa mpaka kumi. Tunataka tunavyoongeza hizi tourism products mtalii a-spend muda zaidi. Kadri anavyozidi kukaa hapa nchini ndivyo anavyozidi kutumia zaidi dola zake na ndivyo anavyozidi kuacha pesa hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaongeza mazao haya ili kuongeza kipato cha Serikali. Pia kadri maeneo ya vivutio yanavyoongezeka, wananchi pia wanaoishi jirani na maeneo haya nao wanapata shughuli za kufanya, watauza baadhi ya vifaa, watauza souvenirs wataweza na wenyewe kushiriki katika uchumi mpana wa utalii.
Mheshimiwa Spika, kwenye Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano tulioupitisha mwaka 2016 palizungumzwa kutokuwepo kwa linkage kati ya sekta ya utalii na maendeleo ya watu; na ndiyo maana pengine malalamiko yanakuwa mengi dhidi ya sekta hii kwa sababu pengine kuna baadhi ya jamii zinazozunguka maeneo yaliyohifadhiwa hazioni faida ya moja kwa moja ya uwepo wa maeneo haya.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kadri tunavyozidi kufungamanisha sekta ya utalii na maendeleo ya watu ndivyo ambavyo hata hii migogoro ambayo inajitokeza sasa tunarajia itazidi kupungua. Pamoja na mambo mengine mengi ambayo ningeweza kuyasema, lakini kwa faida ya muda nisiyaeleze yote kwa upana, naona muda nao unanitupa mkono, inatosha tu kutaja maeneo ya misitu ya asili ambayo ilipoteza hadhi kwenye Halmashauri, kwenye vijiji tumeiwekea mkakati wa kuifufua, mkakati wa kuitengea maeneo kwa ajili ya mkaa, Mheshimiwa Naibu Waziri amefafanua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia tumeanzisha utaratibu mpya wa kutengeza utambulisho wa Mtanzania (destination branding) ambapo tumetengeneza slogan ya Tanzania Unforgettable kwa kutumia wadau mbalimbali waliobobea katika eneo hili la kufanya branding. Bila shaka mmeona hata kwenye mabegi tumewapa ndiyo tunaanza hivyo kuitangaza brand yetu. Pia tutatoa print materials mbalimbali, tutatumia mitandao kuitangaza brand yetu kuanzia sasa na Tanzania kwa kweli kwa jinsi ilivyo na vivutio ambavyo ni unmatched au unparalleled, kwa hakika mtu akija hapa ataondoka na unforgettable experience. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunakusudia kuanzisha Mamlaka ya Utalii wa Fukwe, limezungumzwa hapa suala la fukwe, ni katika mambo mapya ambayo tunakusudia kuyafanya na hivyo tuta- harmonize mahusiano yetu kwenye ku-manage hizi fukwe pamoja na zile marine parks ambazo kwa sasa ziko chini ya Idara ya Fisheries iliyopo Wizara ya Mifugo ili iwe package moja kwenye hiyo sheria mpya ambayo pengine tutaileta hapa Bunge siku za usoni.
Mheshimiwa Spika, pia tuanzishe Jeshi Usu ili kuimarisha ulinzi wa maliasili zetu, lakini pia kuhuisha sheria za TAWA, TFS na kutunga kanuni mbalimbali kama kanuni za shoroba, kanuni za buffer zone, kanuni za maeneo ya mtawanyiko wa wanyamapori, lakini pia kufanya mabadiliko makubwa kwenye Kanuni za Jumuiya za Hifadhi ya Wanyama Pori (WMAs). Yote haya ni mambo ambayo tunayafanyia kazi; na tunayafanyia kazi kwa speed kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo tunalifanya kwa sasa ni kufungua corridor ya Kusini. Tunakusudia kwa kweli kufungua corridor ya Kusini na mikakati mwezangu ameigusia kidogo, nisiirudie kuelezea jambo hili.
Mheshimiwa Spika, vilevile naomba nitumie nafasi hii kumshukuru na kumpongeza Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuridhia maombi yetu kadhaa ambayo tumempelekea ya kutaka kupandisha hadhi baadhi ya maeneo ili tukae kimkakati zaidi katika kufungua corridor nyingine kiutalii. Alizungumza Mheshimiwa Mbatia hapa. Kwa sababu tunakusudia kufikia hao watalii 8,000,000 katika miaka takribani saba iliyobakia ili tuweze kufikia malengo ya kukusanya mapato ya dola za Marekani bilioni 16 kufikia mwaka 2025, ni lazima pia tufungue maeneo mapya ya utalii. Kwa sababu maeneo ya Kaskazini yameanza kuwa exhausted, watalii wamekuwa wengi sana kiasi kwamba hata maintenance ya barabara inakuwa ngumu, kila baada ya mwezi inabidi mfanye repair ya barabara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wakati tuna vivutio vingi na vyote vina wanyama wale wale, kwa hiyo, tunafungua maeneo mengine. Hapa nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kukubali kupandisha hadhi mapori ya akiba ya Burigi, Biharamulo, Kimisi, Ibanda na Chifu Rumanyika badala ya kuwa na Mapori ya Akiba, sasa tunaanzisha mchakato rasmi wa kuyapandisha hadhi ili yaende yakawe National Parks. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, watu wa Kanda ya Kaskazini Magharibi, mama yangu Mheshimiwa Profesa Tibaijuka na mdogo wangu Mheshimiwa Innocent Bashungwa, wakae mkao wa kula, utalii unakuja Ukanda wao. Tuna-take advantage ya kiwanja cha ndege cha Chato, lakini pia kwenye bajeti hii tumeweka mkakati wa kuchonga barabara zinazoingia kwenye mapori haya ya akiba ambayo sasa tunaanzisha mchakato wa kuyapandisha hadhi yaende yakawe National Parks ili tuifungue corridor hii ya Kaskazini Magharibi kiutalii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia tunasubiri majibu mengine kama Mheshimiwa Rais ataridhia kupandisha hadhi baadhi ya mapori yaliyopo Ukanda wa Kati na Magharibi ili tuifungue corridor ya kati Magharibi kwa maana ya kutokea hapa Dodoma kwenda Tabora kupita Katavi tuunganishe na Kigoma iwe nayo ni circuit nyingine ya kiutatalii. Mapori ninayoyazungumzia ni mapori kama Swagaswaga, Mkungunero, Rungwa, Mhesi lakini pia mapori ya Ugala kwenda mpaka mapori ya Kigosi Moyomosi ili nayo tuchague baadhi yake tuyapandishe hadhi yawe National Parks ili tuyajengee miundombinu na yenyewe yaweze kuanza kutumika kwa kasi zaidi kwa shughuli mbalimbali za utalii.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nachukua fursa hii adhimu kwa kweli kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutujibu maombi yetu hayo na bahati nzuri majibu yamekuja kwa wakati muafaka, barua nimeipokea jana kwamba Mheshimiwa Rais ameridhia tuanze mchako wa kuyapandisha hadhi mapori hayo ya akiba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine jipya ambalo tumekuja nalo ni kushirikisha jamii. Sisi tuna falsafa kwenye Wizara yetu kwa sasa kwamba uhifadhi endelevu ni uhifadhi shirikishi jamii na hapa tunamaanisha kwamba kwenye kila changamoto ni lazima tuzungumze na jamii na ndiyo maana nilikuwa tayari kuzungumza na wananchi wa Momela kwa mdogo wangu, rafiki yangu Mheshimiwa Joshua Nassari, lakini pia nilizungumza na Mheshimiwa John Heche.
Mheshimiwa Spika, bahati mbaya sana, Waheshimiwa Wabunge hata ukiwatendea wema namna gani, wakija hapa ndani wanakupiga tu. Hawazungumzi yale mema dhidi ya watu wao. Kwa mfano, Mheshimiwa Heche juzi tu hapa watu wake zaidi ya 100 walikuwa wamekamatwa wamewekwa ndani kwenye operation ambayo ilikuwa inaendelea kule. Sisemi operation ilikuwa haramu, hapana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, operesheni ilikuwa halali, imefanyika vizuri, wananchi wameshirikishwa, ushahidi upo, kuna ushahidi wa picha, kuna ushahidi wa video, kuna ushahidi wa mihutasari ya mikutano ya kushirikisha wananchi. Katika vigingi ambavyo vilifikia idadi ya 147 kwa plan iliyokuwepo, siku wananchi wake wanafanya mgomo zoezi lisiendelee pale Kegonga, kulikuwa kumeshawekwa beacons zaidi ya asilimia 90.
Mheshimiwa Spika, zilibaki beacons 13 tu katika beacons 147. Kama kweli zoezi halikuwa shirikishi toka mwanzo, vijiji vingine vyote zaidi ya kumi vingekataa. Kilikataa kijiji kimoja tu cha Kegonga kwenye Kata hiyo ya Nyandugu ambapo wao walitaka kufanya vurugu na walidhani kwamba kulikuwa hakuna ushirikishwaji na kuna mtu mmoja pale alihamasisha vurugu hizo kutokea.
Mheshimiwa Spika, mimi pamoja na kufuatilia na kupata ukweli wa jambo lenyewe, nikatumia busara, nikasema kwamba ni vema hawa watu nitumie busara ya kuzungumza na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama.
Mheshimiwa Spika, wewe kiongozi mzoefu unafahamu changamoto ninayoweza kuipata katika mazingira kama hayo, wakati Mkuu wa Wilaya na Kamati yake ya Ulinzi na Usalama inaendesha operation, Mkuu wa Mkoa amefanya ziara, amebariki operation iendelee, kuna timu nzima pale ya vyombo vya Ulinzi na Usalama vipo pale vinaendesha operation, halafu mimi Waziri ambaye ninashikiria sheria ambao inasimamiwa sasa na Serikali yetu kule kwenye Local Government, ninapofanya uamuzi wa kumwambia Mkuu wa Wilaya sitisha hiyo operation yako, siyo katika maslahi ya umma, na mimi Waziri mwenye sheria, naona kwa sasa haiendi sawa. Hebu sitisha mpaka nije mimi mwenyewe. Ni mazingira magumu sana.
Mheshimiwa Spika, nilikwenda extra mile kwa sababu ya urafiki wangu mimi na Mheshimiwa John Heche kwamba amenieleza hili jambo kwa hisia kali, na mimi ni Waziri, na mimi ni Mbunge mwenzake, hebu ngoja intervene kusimamisha hiyo operation na hatimaye tutatafuta suluhu mimi mwenyewe nikienda site. Nikasitisha zoezi lile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikamwomba zaidi Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambapo tayari charge sheets zilikuwa zimeandikwa kwa watu wale zaidi ya 100 na wako ndani kwamba Mheshimiwa naomba hao watu hebu watoe ili nijenge mahusiano mema na hao watu, nitakapokuja niweze kuzungumza nao vizuri wakiwa hawana kesi. Nikamshawishi Mkuu wa Wilaya na akaacha kufungua hizo kesi na waendesha mashitaka walikuwa njiani wanatoka Mkoani kwenda pale na wako kambi pale wanaendelea kuandika hayo mashtaka ili wawapeleke Mahakamani, lakini nikasitisha na zoezi la kwenda Mahakamani. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, bado ukiwa Waziri wa Wizara hii, utapata lawama sana. Watu watasema beacon imechimbiwa chini ya uvungu, beacon imechimbiwa kanisani, imechimbiwa msikitini. Mambo mengi haya yanayosemwa kwa kweli nimekuwa nikiyafuatilia toka nimekaa kwenye kiti hiki, mengi nimekuwa nikiona siyo ya kweli.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, beacon yenye urefu wa kunishinda mimi, zaidi 6.4 feet haiwezi kukaa kwenye uvungu wa kitanda. Hizo ni beacon ndefu, lakini pia ziko beacon fupi ambazo zinanifika mimi hapa. Kwenye picha zilizokuwa zinarushwa hapa nafikiri mliona, beacons zote nilizozitembelea zinanifika hapa. Haiwezi kukaa chini ya uvungu wa kitanda. Hicho kitanda labla ni double decker ambacho chini hakina kitanda. Kwa vitanda vya ndugu zetu huko vijijini tunakotoka, ni vifupi chini. Kwa hiyo, maneno mengi yanasemwa ili kujenga hoja kwamba Wizara ya Maliasili na Askari ambao ni barbaric kweli kweli, ambao hawajali masilahi ya watu.
Mheshimiwa Spika, naomba kwanza niseme falsafa hiyo sasa tumeifuta kwenye Wizara hii. Tunashirikiana vizuri na wananchi, na mimi kama kiongozi mkuu kwenye Wizara hii napenda kushirikisha wananchi, napenda kuwa-engage wadau. Hata Mheshimiwa Heche huna haja ya kusema hapa kwa sababu kwanza nimeshakuhakikishia kwamba tutakwenda kule kwenye Jimbo lako tukaone hali halisi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia wewe umesema maneno mazito hapa kwamba Gibaso, boundary ile ni hard line, wananchi hapa, hifadhi hapa. Huwezi kuweka buffer zone kwenye eneo la wananchi, ni simple logic! Nikienda nikikuta hali iko hivyo, niko radhi kumshawishi Mheshimiwa Rais tufanye variation ya mipaka, niko radhi kufanya hivyo.
Kwa hiyo, mambo ya namna hiyo hayapaswi kuzua mjadala hapa kwa sababu mimi mwenyewe nitayafanya kwa mikono yangu. Nitafika maeneo husika na nitahakikisha tunaweka sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia tumeanzisha pale TTB studio ya TEHAMA ambayo itaenda kutumika kwa ajili ya ku-monitor mawasiliano kila mahali kwenye mtandao neno Tanzania litakapotokea kwenye mjadala. Lengo letu ni kukusanya takwimu na kuwajua watu wanaozungumzia kuhusu Tanzania wanapatikana wapi, ni wa umri gani na tufanye nini ili kuweza kuwavutia kuja kutalii katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze la vigingi dakika mbili tu. Naomba sana Bunge lako tukufu lisisitishe zoezi hili. Nasema kwa sababu ifuatayo kubwa moja.
Mheshimiwa Spika, tunaweka vigingi ili tujue nani na nani wameingia ndani ya eneo la hifadhi. Kama ni hifadhi imeingia ndani ya eneo la wananchi tujue. Halafu mahali palipo na mgogoro tunatatua. Kwa mfano nilikwenda Kimotorok kwa ndugu yangu Mheshimiwa Millya, nikafika pale, nikajionea, kweli kuna vigingi, kuna makanisa yako ndani ya hifadhi na kituo cha afya kimo ndani ya hifadhi. Katika maeneo kama haya, mimi binafsi niko radhi kumshawishi Mheshimiwa Rais turekebishe mipaka, vitu kama hivi vitoke. Kwa sababu ni eneo ukakuta labla ni la kilometa moja, ni eneo dogo tu ambalo tunaweza tuka-coincide tukasema hili tulirudishe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mchakato wake utaanza, lakini ni lazima Waziri uanzishe huo mchakato. Kama mipaka haijawekwa au vigingi havijawekwa nitajua kipi na kipi kimeingia na kipi kipo ndani na kipi kipo nje? Kwa hiyo, zoezi liendelee, Waheshimiwa Wabunge mtupe ushirikiano na wananchi wenzetu watupe ushirikiano tukamilishe zoezi la kuweka vigingi, lakini tukijua kwamba hiyo siyo final, hiyo siyo hatua ya mwisho.
Mheshimiwa Spika, askari wanaolinda hizi hifadhi wasisumbue wananchi wala wasitumie nguvu kulazimisha vigingi kuwekwa ama kuwaondoa katika hatua hii ya kwanza. Wananchi wabaki katika maeneo hayo, tutatatua mgogoro mmoja baada ya mwingine kwa kufuata harama za vigingi ambazo zitakuwa zimeshawekwa. Naomba hili pia niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge wenzangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo bila kuchukua sana muda wako, nitakwenda Arumeru mimi mwenyewe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii. Pia nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii pia na naomba nitoe mchango wangu kwanza kwa kuunga mkono hoja iliyowekwa mbele yetu na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na kuwahakikishia kwamba kwa kuwa tunafanya kazi vizuri na kwa ukaribu, tutaendelea kushirikiana kuhakikisha mapendekezo yaliyotolewa na Kamati yao tunayafanyia kazi kwa wakati muafaka na kwa namna ambayo wenzetu Wajumbe wa Kamati na Bunge litaridhia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nianze kwanza kwa kuchangia kuhusu mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kufufua Shirika la Ndege, kujenga viwanja vya ndege nchini na namna ambavyo unaungana moja kwa moja na jitihada za kukuza utalii katika Taifa letu. Jana zilizuka hoja nyingi kuhusu Uwanja wa Ndege wa Chato na unaweza ukazielezea kiurahisi sana kama utazungumzia Mkakati wa Serikali ya Awamu ya Tano wa kufungua kiutalii Circuit ya Magharibi na Kaskazini Magharibi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mkakati huu unaenda sambamba na mkakati wetu wa kufanya ukarabati na utanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Nduli, kilichopo pale Iringa na kujenga viwanja vingine viwili vya ndege pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ambayo kwa sasa ni hifadhi ya saba kwa ukubwa duniani na kwa Afrika inashika namba nne na kwa Tanzania ni hifadhi ya kwanza kwa ukubwa. Ndipo mahali pekee kwa haraka haraka ukienda kutembelea unaweza ukawaona predators wakiwa in action. Unaweza ukaona simba wakikimbiza mbogo, wakikamata na kula ni matukio ya kawaida kabisa ukiwa pale Ruaha National Park.
Mheshimiwa Spika, sambamba na mkakati huu, katika Awamu ya Tano tunakusudia kufungua pia Circuit ya Kusini kwa upande wa Selou kwa maana ya kujenga Kiwanja kingine cha Ndege cha kiwango cha sakafu ngumu Kaskazini mwa Pori la Akiba la Selou maeneo ya Matambwe, uzuri wewe ni mwenyeji sana kule ili kufungua utalii wa picha upande huo. Mikakati yote hii kwa ujumla wake inaenda sambamba na mikakati inayotekelezwa na Serikali ya kufufua Shirika la Ndege la Taifa kwa kununua ndege lakini pia kufungua safari za moja kwa moja kwenye masoko mbalimbali ya utalii na kuyaunganisha na Jiji letu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikianza na jitihada zetu za kupandisha hadhi Mapori ya Akiba ya Burigi, Biharamulo, Kimisi, Ibanda na Rumanyika kwenda kwenye hadhi ya National Park, muda si mrefu tutafikisha mbele yako mapendekezo ya Serikali baada ya kukamilisha mchakato ambao tupo katika hatua za mwisho ili tupate ridhaa ya Bunge lako Tukufu kupandisha hadhi Mapori haya matatu na kuyaunganisha kuwa National Park moja ya Burigi Chato National Park, ambako itachukua yale maeneo yaliyokuwa Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi na Kimisi, pia kupandisha hadhi Pori la Akiba la Ibanda ili kuwa Ibanda National Park na Pori la Akiba la Rumanyika ili kuwa Rumanyika National Park.
Mheshimiwa Spika, Circuit hii itakamilika kwa kuunganisha na Hifadhi ya Taifa ya Rubondo ambayo iko ndani ya Ziwa Victoria na Hifadhi ya Taifa ya Saanane na tutaweza kuiunganisha na Circuit ya Magharibi pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Mahale na Hifadhi ya Taifa ya Gombe. Pia ndani ya Serikali tuko katika mchakato kuona kama tunaweza tukapandisha hadhi eneo la kiini cha Pori la Akiba la Moyowosi, Kigosi na Ugala pale pembezoni mwa mto ili pia yawe Hifadhi ya Taifa na tuweze kufanya utalii wa picha. Circuit hiyo sasa itakamilika kwa upande mmoja. Vilevile Circuit ya Kusini tutaweza kuiunganisha vizuri kwa kuwa na ndege ambazo zitaweza kutua na kufanya safari zake za kawaida kila siku kwenye maeneo ya Msambe, kama nilivyosema, upande wa Kaskazini Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, pia katikati ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi pamoja na hiyo Circuit ya Kaskazini ya pori la akiba la Selou.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ukiangalia kwa undani sana unaweza ukaona tunapowekeza kwenye ndege na viwanja vya ndege ni kama vile tunatupa pesa nyingi sana kwenye jambo ambalo pengine haliwagusi wananchi moja kwa moja. Nimesikia michango ya Waheshimiwa Wabunge, hususan wanaotokea ng’ambo ya pili katika eneo hilo na mimi napenda kupingana nao na pengine kuwapa maelezo kwamba sekta ya utalii inachangia kuingiza pato la Taifa kwa asilimia 17.6 na ndiyo sekta inayoongoza kwa kuingiza fedha za kigeni hapa nchini kwa asilimia 25 ya fedha zote za kigeni zinazoingia nchini. Pia sekta hii inachangia Dola za Kimarekani bilioni 2.4 katika uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, Utafiti wa Benki ya Dunia wa mwaka 2014 ulisema kama nchi yetu itafanya vizuri katika eneo la maliasili na utalii kufikia mwaka 2025 tutaweza ku- tap kutoka kwenye sekta hii mapato yanayofikia Dola za Kimarekani bilioni 16,000. Kipindi hicho inakadiriwa kwenye taarifa hiyo kubwa kabisa inayohusu Hali ya Uchumi wa Tanzania ya Benki ya Dunia, kwamba watalii kwa mwaka huo watakuwa wamefikia kiasi cha milioni 8 leo hii tuko hapo karibia milioni 1.5.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, utaona Waheshimiwa Wabunge wengi wanachangia kwamba pengine jitihada za kutangaza vivutio hazijafanyika ipasavyo, pengine tunahitaji kujipanga zaidi; tunakubaliana nao lakini pia Serikali imeshachukua hatua nyingi sana katika kutangaza vivutio vyetu na ndiyo maana idadi ya watalii inaongezeka mwaka hata mwaka. Mwaka jana tu Mheshimiwa Waziri Mkuu alitufungulia channel maalum ya utalii (Tanzania Safari Channel) tumepokea mapendekezo ya Kamati kwamba tujitahidi kuifanya iweze kuonekana nje ya nchi na ndizo jitihada ambazo kweli kwa sasa tunaendelea kuzifanya ili iweze kuonekana kwa wingi zaidi nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pamoja na kwenda kwenye show mbalimbali ambazo tunawakilishwa na Bodi yetu ya Utalii bado tuna mikakati mingine mahsusi ya kukuza sekta ya utalii kwa kutumia watu mashuhuri wanaokuja hapa nchini. Pia kutangaza kwenye michezo kutangaza, vituo vya mabasi na treni kule nje, ni mikakati ambayo tunaiwekea hatua mbalimbali za utekelezaji. Pia kuweka mabango makubwa katika maeneo yote ambayo ni mageti ya kuingia katika nchi yetu kuanzia viwanja vya ndege na hata pale maeneo ya bandarini; tuna mradi huo ambao tuko katika hatua ya kuutekeleza na muda si mrefu kila sehemu utakuwa ukizunguka ukiangalia hivi unaona simba, tembo na kadhalika. Hata kwenye ile round about kubwa ya hapa Dodoma tunakusudia kuweka television kubwa kabisa ambayo itakuwa inaonesha live kila kinachoendelea ndani ya creator. Kwa hivyo, tukifanikiwa kufanya hilo, kila atakaye kuwa anaingia katika Jijini la Dodoma ataweza kuona vivutio vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, napenda pia kuzungumzia kuhusu Mradi wa REGROW ambapo wenzetu wanadhani kwamba unasuasua lakini pia Kamati yetu imezungumzia sana kuhusu ucheleweshaji wa utekelezaji wa mradi huu. Mradi huu unatekelezwa kwa mkopo kutoka Benki ya Dunia ambapo nchi yetu inakopeshwa Dola za Kimarekani milioni 150. Fedha hizi ni nyingi na ni mkopo na mkopo maana yake ni lazima ulipwe.
Mheshimiwa Spika, nilipoteuliwa kuwa Waziri kwenye Wizara hii nilisoma lile andiko la mradi na nikaona kwamba haukukaa zaidi kibiashara. Kwa sababu ukiuangalia unaona haujahusisha ujenzi wa barabara kutoka Nduli Airport pale Iringa kwenda mpaka kwenye geti la Msambe kuingia Ruaha National Park, hakuna mradi wa kuukarabati Uwanja wa Ndege wa Nduli lakini pia ulikuwa ujenge viwanja vidogo vidogo vya hadhi ya changarawe katika maeneo yote hayo ambayo nimeyazungumzia ya Circuit hii ya utalii ya Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wewe ni Mhifadhi unafahamu, kila mkitaka kukarabati viwanja vya changarawe lazima mchukue material humo humo ndani ya hifadhi yenyewe maana mnazidi kuharibu mazingira lakini pia mnajenga mwaka huu baada ya mwaka mmoja mnaanza ukarabati. Nikasema mradi ulipokuwa designed haukukwa commercially sound kwa kiasi kikubwa, kwa hivyo, tukasema lazima tuufanye huu mradi uwe wa kibiashara. Ili kuufanya mradi ule uwe wa kibiashara tuliona ni lazima pajengwe viwanja vya ndege ambavyo vina sakafu ngumu ambavyo vinaendana na uhifadhi wa mazingira kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, tukasema badala ya viwanja 15 bora tupate vinne (4) ambavyo vitadumu kwa muda mrefu, havihitaji ukarabati lakini pia vitatuwezesha tupate watalii ambao kwa sasa wanatukwepa kutokana na masharti mbalimbali yaliyopo katika bima zao za maisha ama bima zao za flight. Mfano, wazee wanaokuja Tanzania hapa ambao wako zaidi ya miaka 65 ni asilimia 5 tu ya watalii wote lakini hili ndilo kundi kubwa ambalo linasafiri duniani kwa ajili ya kupumzika; wazee ambao wako kwenye pensheni, wana pesa za kutosha, wana bima za maisha wanahitaji kwenda kupumzika katika maeneo mbalimbali. Hawa wote wanakwenda Kruger National Park kule South Africa kwa sababu wenzetu wana uwanja wa ndege ambao una sakafu ngumu na sisi tunaishia kupata asilimia 5 tu.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, tukijenga Viwanja vya Ndege kwa sasa maana yake tutaweza kupata hii segment ya soko la watalii ambao wana bima za maisha. Sababu ni moja tu, bima nyingi za maisha zinawataka watalii lazima wasafiri kwenye ndege ambayo ina injini mbili, ma-pilot wawili lakini pia atue kwenye sakafu ambayo ni ngumu, ambapo ikitokea ajali ataweza kulipwa hiyo bimavinginevyo hawezi kupata hiyo bima. Kwa hiyo, sasa tukaona ni bora ili kuufanya mradi uwe commercially viable tujenge viwanja vichache lakini vyenye sakafu ngumu tuweze kupata wageni hao. Kwa hivyo, tuliweka mguu tukasema hapana lazima mabadiliko yafanyike katika mradi huu ili mradi uwe commercially viable, tuongeze idadi ya watalii na pia tupate pesa kwa ajili ya kulipa deni ambalo linatokana na mradi wenyewe.
Mheshimiwa Spika, pia ikatokea maneno kidogo ambayo sasa hivi tungeweza kuyatatua kwamba tutatekeleza mradi katika eneo la Selou, kwa hivyo, tusiutekeleze kule Selou kwa sababu kuna uharibifu wa mazingira. Sisi tukasema hapana mradi utatekelezwa maeneo yote ama usitekelezwe kabisa kwa sababu hatuwezi kutekeleza nusu nusu tukaiacha segment ya mradi ambayo ipo katika Pori la Akiba la Selou. Bahati nzuri Benki ya Dunia sasa hivi wamekubali kwamba tutekeleze mradi na tutekeleze pia mradi wetu wa kufufua umeme katika Bonge la Mto Rufiji. Kwa hivyo, kwa sasa tumebaki tuna negotiate kwenye eneo hili moja la viwanja vya ndege.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo napenda kuzungumzia ni kuhusu uwindaji wa kitalii. Uwindaji wa kitalii umekumbwa na dhoruba nyingi sana tangu mwaka 2008 mpaka leo. Uzuri wewe ulikuwepo Bungeni na ulikuwa kwenye Kamati inayosimamia maliasili hivyo unafahamu kilichotokea, sina haja ya kurudia hapa.
Mheshimiwa Spika, wakati mimi nateuliwa kuwa Waziri kwenye Wizara hii nilikuta mapato yameshuka mpaka chini ya bilioni 10 kwa mwaka sasa hivi tumeweza kuyapandisha mpaka zaidi ya bilioni 40 na mwaka huu tunakusudia kuweka bajeti zaidi ya bilioni 60. Mapinduzi ambayo tumeyafanya kwenye sekta ya uwindaji wa kitalii ambayo mashuhuri yanajulikana kama Hunt More for Less yatatupeleka kuifufua sekta ya uwindaji wa kitalii na kupata mapato makubwa zaidi kuliko ilivyo sasa na pengine uwindaji wa kitalii nao ukachangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja ya Kamati. (Makofi)
Azimio la Bunge la Kuridhia Ubadilishaji Hadhi Mapori ya Akiba ya Biharamulo, Burigi, Kimisi, Ibanda na Rumanyika – Orugundu kuwa Hifadhi za Taifa
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, Mhifadhi, ahsante kwa fursa hii, Nashukuru kwanza kwa kukubali hoja hii iletwe hapa kwenye Bunge lako Tukufu, lakini pili kwa mchango ambao umeutoa hapa. Japokuwa umenirushia nondo kwelikweli ukijua kabisa ni Daktari Bingwa wa Afya ya Jamii, lakini najifunza haraka.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote kwanza nianze kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Awamu ya Tano kwa kukubali ushauri wetu mbalimbali ambao tumekuwa tukiupeleka kwake, hususan jambo moja kubwa ambalo mwezi Januari, tarehe 15 alilifanyia uamuzi, kwamba, uhifadhi katika Awamu ya Tano ubadilike kidogo tutoke katika misingi ya uhifadhi ya zamani ambayo ilikuwa inajikita kwenye dhana ya command and control zaidi kwa maana ya kutumia law enforcement zaidi tuhamie kwenye uhifadhi ambao unahusisha maendeleo ya jamii, unafaidisha watu, kwa maana fupi community based conservation.
Mheshimiwa Spika, imefika mahali Mheshimiwa Rais ametoa ridhaa yake, lakini pia ametoa mwongozo ambao sasa unatupa dira ya kuweza kutekeleza azma pana tuliyonayo ya kuichora upya tasnia ya uhifadhi hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, mambo mengi yamekuwa yakizungumziwa katika nchi yetu kuhusu uhifadhi, lakini mengi yamekuwa yakikwama kwa sababu, wewe bahati nzuri ni Mhifadhi unafahamu ni jinsi gani sheria za uhifadhi zilivyo rigid, sheria hizi ni ngumu sana. Ukiwa Waziri wa Maliasili na Utalii unataka kufanya ubunifu kwenye maeneo haya utapata tabu sana kwa sababu, ni lazima upate ridhaa ya
Mheshimiwa Rais, Baraza la Mawaziri limshauri, akupe ridhaa yake, uje upate ridhaa ya Bunge, halafu mrudishie tena Mheshimiwa Rais ndio sasa kitu kitokee. Kwa hivyo, unaweza ukawa Waziri ambaye pengine unapata tabu sana kufanya innovation kwenye eneo ambalo umepewa kusimamia kwa sababu ya rigidity ambayo ipo kwenye sheria mbalimbali za uhifadhi.
Mheshimiwa Spika, kwa hatua tuliyofikia na mwongozo ambao Mheshimiwa Rais ameutoa sasa tunafarijika kwamba, tunaweza kusonga mbele na kufanya ubunifu katika maeneo mbalimbali ambayo tunakusudia kuyafanyia kazi. Mheshimiwa Rais ameturuhusu turekebishe mipaka ya maeneo ya uhifadhi na hii ni mojawapo ya jitihada ambazo tunafanya.
Mheshimiwa Spika, katika eneo hilo, kwa mfano, kuna baadhi ya misitu ya reserve, tutaikata tutarudisha kwa wananchi ili kupunguza pressure kwenye maeneo haya ya Hifadhi za Taifa, ndiyo ile dhana ya community based conservation itafanya kazi ipasavyo. Kwanza lazima tutatue changamoto za wananchi, wananchi wanahitaji maeneo kwa ajili ya kuchunga, makazi, kilimo na uchimbaji wa madini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maeneo kwa kiasi kikubwa katika mikoa ile yalikuwa yamehifadhiwa, kama si Mapori ya Akiba basi ni misitu ambayo inaifadhiwa kwa mujibu wa sheria, Misitu ya Halmashauri ama misitu ya Serikali Kuu. Kwa hiyo, katika kuchora upya ramani ya uhifadhi katika mikoa ile, tutaweza kufikia azma ya kuwapa wananchi maeneo ambayo watayatumia kwa shughuli hizo mbalimbali ambazo wamekusudia. Jambo hilo tu peke yake lilihitaji kwa kweli ridhaa ya Mheshimiwa Rais mwenyewe wala siyo uamuzi wa Waziri wa Maliasili na Utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba ya kwako yote niyachukue kama ushauri na tutayafanyia kazi. Hili la kuhamisha wanyama tunalifahamu na tayari kazi hiyo imeshaanza kufanyika. Nikuhakikishie tu kwamba nimefanya ziara mara tatu katika Mapori haya ya BBK katika maandalizi ya kuleta hoja hii ya Azimio ya Kuyapandisha hadhi kwenda kuwa Hifadhi za Taifa, maeneo yale yame-recover kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge ambao tulifanya nao ziara mwaka jana ni mashahidi, tulikutana na makundi makubwa ya tembo yakihama kutoka Burigi na kuhamia upande pili wa barabara ambao ni upande wa Hifadhi wa Kimisi na pia kuna makundi makubwa ya nyati yapo katika maeneo haya. Vilevile wawekezaji ambao wamefika kufanya survey kwa ajili ya kuja kuwekeza pale ambapo tutatoa fursa ya kufanya hivyo wameanza kupigana vikumbo, kuwania maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuwekeza. Hii ni dhahiri kwamba hata kama private sector nao wanafikiria kuwekeza mle ni dhahiri kwamba maeneo haya yana vivutio ambavyo vitaleta tija katika kukuza utalii katika eneo husika. Kwa hiyo, tutafanya kazi ndogo za kuhamishia wanyama kama ambavyo umetushauri ambao hawapatikani kwa sasa.
Mheshimiwa Spika, lakini kufafanua tu kidogo hili la Ngorongoro Conservation Area Authority tayari tumeshawapa maeneo mengi. Maeneo hayo ya Kolo, Miambani na Mapango ya Amboni. Wiki iliyopita nimesaini administrative directive ambayo sasa ni Waraka wa kisheria kuyahamisha kutoka taasisi moja kuyapeleka taasisi nyingine. Ngorongoro ana maeneo kadhaa ambayo yana urithi wa kiutamaduni ama yana hadhi ya kuwa Geopark kwa sababu ana maeneo mawili ambayo yana hadhi hiyo na yametambuliwa na UNESCO. Kwa hiyo, tumeona tumuongeze pia Mapango ya Amboni, Michoro ya Miambani na Irrigation Scheme ya jadi pale Engaruka, zote hizi atakuwa akizisimamia na kuziendeleza, kwa hiyo, naye Ngorongoro tumempa mzigo.
Mheshimiwa Spika, lakini pia taasisi zote za uhifadhi tumezipa mizigo mingine ya kuendesha maeneo mbalimbali ya mali kale. Maeneo ya Kalenga tumempa TANAPA kwa sababu yapo karibu na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, maeneo ya Isimila tumempa TANAPA, Nyumba ya Mwalimu Nyerere ile ya pale Magomeni tumempa TANAPA na Kilwa, Songo Mnazi tumewapa TAWA. Tumewagawia haya maeneo ili kukamilisha hizi circuit.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, ndugu yangu Mheshimiwa Msingwa asiwe na wasiwasi, hiki kichwa kilichokalia hapa ikifika mwaka 2020 tufanye tathmini pamoja na utaona tofauti. Kwa sababu kuna mambo mengi tunayafanyia kazi na kwa hakika yataichora upya ramani ya uhifadhi wa nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuunganisha na hoja tu ya Mheshimiwa Nsanzugwanko katika eneo hilo, tunapoelekea kuichora upya ramani ya uhifadhi nchini, pamoja na kupandisha hadhi haya Mapori ya Akiba matano kwenda kuwa Hifadhi za Taifa pia tunakusudia kupandisha hadhi kiini cha mapori ya akiba mengine matatu katika ikolojia hiyo hiyo moja. Pori la Akiba la Kigosi tunachukua kiini tunapandisha kinakuwa national park, tunaacha eneo la nje linabaki kuwa game reserve. Pori la Akiba Moyowosi tunapandisha hadhi kiini pamoja na ile Ramsar site inakuwa national park, pembezoni tunaacha inabaki kuwa game reserve. Pori la Akiba Ugala tunapandisha hadhi eneo la kiini ile satellite area tunaiacha inaendelea kuwa game reserve, tunaunganisha na misitu ya hifadhi ambayo ipo katika maeneo hayo ambayo tunaipandisha hadhi pia inakuwa natural reserves.
Mheshimiwa Spika, malengo yetu ni kuichora upya ramani ya uhifadhi. Pembezoni kabisa mwa misitu ya hifadhi tunarekebisha maeneo ya vijiji, tunakata ardhi ya misitu tunawarudishia wananchi ili wawe na ardhi ya kutosha. Tunaweka alama za kudumu na baada ya kuweka alama za kudumu sasa tunasisitiza na kuimarisha ulinzi wa maliasili hizo kwamba zisivamiwe. Pamoja na kupunguza maeneo hayo lakini pia kuna maeneo mengine ambayo tutayapandisha hadhi na maeneo mengi mapya tutayaazisha kwa sababu ya umuhimu wake kiuhifadhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, eneo la Wembele na Nyahua Mbuga ni the only connection kati ya hifadhi zilizoko Kusini; kwa maana ya ecosystem ya Ruaha, Rungwa kuja kuunga kwenye hifadhi zilizopo Kaskazini kupitia Nyahua, Wembele mpaka kutokea Maswa Game Reserve. That’s the only connection ambapo wanyama wanatoka Kusini wanakuja Kaskazini, wanatoka Kaskazini wanaenda Kusini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile maeneo muhimu kama hayo niliyosema connection kati ya Burigi, Biharamulo na Kimisi ukiunganisha na Kigosi Moyowosi kwenda mpaka Mahale, Katavi National Park mpaka Gombe, hiyo pia ni ikolojia moja. Kwa hivyo, kuna maeneo ambayo tunayapandisha hadhi, kwa mfano misitu iliyopo kule Uvinza, Masito East, Masito West, Misitu ya Tongwe East, Tongwe West tunaiunganisha na North East Mpanda yote tunaipandisha hadhi na tunahifadhi katika ngazi ya Kitaifa ama ngazi ya Halmashauri za Wilaya ili kuwe na uhakika wa corridor ambazo zinapitika mwaka wote. Kwa sasa hivi maeneo mengine hayo niliyoyataja ni general land, kwa hiyo, wanaweza kufanya lolote sasa tunaamua kuyahifadhi kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lengo letu ni kutimiza hilo nililolisema la kuichora upya ramani ya uhifadhi. Vijiji ambavyo kwa mfano vipo katikati ya kiini cha maeneo yaliyoifadhiwa tunavihamisha, tunavikatia maeneo pembezoni ili kuwa na uhakika kule ndani pako salama na maisha ya huko kwenye hifadhi yanabaki kuwa salama na wanyama hawatolewi katika njia yao ya kila siku na matokeo yake kuvamia vijiji vya watu na kusababisha migogoro ambayo ulikuwa unaizungumzia.
Mheshimiwa Spika, tunafanya hivi kwa msingi mmoja, sisi watoto wa Tanzania tukitembea nchi za nje huko tunajivuna sana kwamba tunatoka Tanzania. Katika mambo ambayo tunajivuna nayo ni urithi wa maliasili ambao tunao na urithi huu unatambulika kimataifa na sisi ni miongoni mwa nchi ambazo zimetenga eneo kubwa la ardhi yake kwa ajili ya kuhifadhi maliasili mbalimbali ambazo ni urithi kwa sisi tunaoishi leo na vinavyokuja hapo baadaye.
Mheshimiwa Spika, huu ni urithi wa kipekee, ni unique feature ya nchi ya Tanzania na ni urithi ambao unaweza kujizalishazalisha, unaweza kuji-renew haushi. Ni utajiri ambao haufilisiki kama tutaweza kuuhifadhi na kuutunza na ni utambulisho wa nchi yetu nje ya mipaka ya nchi yetu. Kwa hiyo, jukumu la uhifadhi kwa kweli tunalichukua katika viwango vya juu sana na katika umuhimu wa kipekee na ndiyo maana tumeona tuichore upya ramani ya hifadhi zetu hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, ni kweli TANAPA inaongezewa mzigo lakini inategemea unalinganisha TANAPA na kitu gani. Uongozi wa Jenerali Waitara na Mkurugenzi wetu, Ndugu Kijazi ni dhabiti na imara. Mimi kama Waziri najiridhisha katika taasisi ambazo nimepewa kuzisimamia TANAPA ina viwango vya juu sana vya utendaji na ndiyo maana kila mtu hapa anawamwagia sifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, TANAPA wana hifadhi 16 tu, kati ya hizo tano (5) kweli zinajiendesha na zinatoa faida ambayo inasaidia kuendesha hifadhi nyingine. Ukitaka kulinganisha sasa TANAPA ambaye ana hifadhi 16 na TAWA ambaye ana hifadhi zaidi ya 100, utaona migogoro kwa kiasi kikubwa na hizo operesheni zinazozungumziwa hapa zililazimika kufanyika si kwa sababu ya uzembe wa TANAPA, hapana, kwa sababu TANAPA analinda vizuri maeneo yake, ni kwa sababu kulikuwa na uzembe chini Wizara ya Maliasili na Utalii na mamlaka za Serikali za Mitaa na wakati huo TAWA ilikuwa haijaazishwa. Kwa hiyo, kuhamisha baadhi ya majukumu kutoka TAWA kuyapeleka TANAPA mbali na sababu ambazo tumezisema wakati tunatoa hoja yetu ya msingi ni jambo ambalo pia linapunguza mzigo kwa TAWA lakini pia linaimarisha ramani ya uhifadhi hapa nchini.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaona pengine ni vyema kwa maeneo ambayo yana umuhimu wa kipekee tukayapeleka TANAPA ili yakapata ulinzi wa kutosha. Kwa mfano, Moyowosi hatuchukui hifadhi yote, tunachukua kiini tu tunampa TANAPA, nje ya kiini tunamuacha TAWA aendele kusimamia. Lengo letu ni moja, kuongeza idadi ya men in the boots, ya askari ambao wako katika eneo husika.
Mheshimiwa Spika, tunafanya hivi siyo tu kwa sababu za ulinzi wa maliasili iliyoko pale lakini kwa sababu za ulinzi mpana wa nchi yetu. Kwa sababu mapori haya yamekaa katika eneo ambalo ni conflict zone; kuna wakimbizi na wahalifu wanaotoka katika nchi za jirani. Kwa hiyo, tunavyoongeza men in the boots kwenye maeneo haya maana yake pia tunaimarisha ulinzi katika nchi yetu, kwa sababu patrol na miundombinu itakuwa mingi na maeneo haya yatabaki kuwa salama. Linakuwa ni jambo la ajabu sisi tunazuia watu wetu wasitumie maeneo haya kwa shughuli zao za kila siku halafu watu wa nchi nyingine wanakuja kuyatumia, ni jambo ambalo halikubaliki kidogo. Kwa hiyo, tumeona bora tuyahifadhi na tuyalinde kwa nguvu zaidi kuliko ilivyokuwa hapo awali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hoja nyingi wamezizungumzia Mheshimiwa Mabula na Mheshimiwa Kanyasu naomba nisizirudie, labda niseme moja hii ya REGROW na Sungura Wawili. Mradi wa REGROW upo pale pale, fedha zimeshaingia ndani ya Serikali. Nilifafanua hapa siku tatu au nne zilizopita, tunachokifanya ni kuendelea kupatana na wenzetu ili mradi ule uwe na tija zaidi. Kuna haja gani ya kujengewa viwanja vya ndege vya changarawe kwa pesa ya mkopo ambayo nchi yetu italipa wakati tuna uwezo wa kuwataka wanaotukopesha watujengee kiwanja ambacho ni cha hard surface (sakafu ngumu) ili kiweze kudumu zaidi. Tunaona economically hai-make sense kuwa na project ambayo itakuwa ya muda mfupi kiasi hicho, halafu project yenyewe si rafiki kwa mazingira.
Mheshimiwa Spika, kwa sababu ukitaka kufanya ukarabati wa kiwanja cha changarawe maana yake ni lazima uchukue material humo humo ndani ya hifadhi, kwa hiyo, pia it is not environmental friendly. Kwa hiyo, tunaona bora tujenge kiwanja cha ndege ambacho ni cha sakafu ngumu na ndilo jambo pekee ambalo tumebaki tukizungumza na watu wa World Bank. Pesa wameshatoa, ruhusa ya kuendelea na mradi imeshatoka na Mradi wa Kukuza utalii Kusini unaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na mradi huo, tumepata pesa pia baada ya kuonyesha nia ya kuyapandisha hadhi Mapori ya Akiba kuwa National Park kutoka Global Climate Facility ambao watatupa pia dola za Kimarekani milioni 100 ambazo zitatusadia kufanya maboresho katika Mapori haya ya Akiba kwa sababu na wao wameona kwamba sisi wenyewe tuna nia ya kufanya hivyo. Malengo yetu ni kutimiza azma ya Ilani ya Uchaguzi ambayo sasa imedumu takribani miaka 10 ikizungumzia jambo moja; Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano sasa mwaka wa tisa huu wanazungumzia jambo moja kubwa nalo ni diversification ya kijiografia ya vivutio vya utalii hapa nchini, haiwezekani tuka-concentrate watalii kwenye kanda moja tu ya nchi yetu, tufungue kanda nyingine. Ndiyo maana tunafungua Circuit hii ya Kusini na Kaskazini Magharibi. Lengo letu ni ku-diversify geographical shughuli za utalii katika nchi yetu ukiacha Circuit ya Zanzibar.
Mheshimiwa Spika, pia tunafungua circuit ya utalii wa fukwe katika ukanda wa fukwe utakaoanzia Bagamoyo kwenda mpaka Tanga. Sasa hivi tuko katika mipango ya awali, tunachora ramani na ile water front yote tunaiwekea mkakati. Pia water front ya Kilwa sambamba na kutambua umuhimu wa kipekee wa magofu yaliyopo pale Kilwa Kisiwani pamoja na jitihada zinazoendelea za kuifungua Circuit ya Kusini pale kuunganisha la Selous National Park kwa upande ule wa nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, tunaichora upya ramani ya utalii na uhifadhi katika nchi yetu na hii ni moja ya jitihada.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa fursa hii, naunga mkono hoja na naomba kutoa hoja.
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selous kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. awali ya yote nianze kwa kukupongeza wewe na mfumo mzima wa taasisi yetu ya Mhilimi wa Bunge kwa kukubali hoja hii iingie hapa Bungeni siku ya leo lakini pia zaidi kwa kutoa ushauri, mchango na mapendekezo mbalimbali ambayo yanalenga katika kuboresha utekelezaji wa majukumu ya usimamizi ambayo Serikali imepewa na Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, pili; nimpongeze Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa uamuzi wake wa kuamua kubadili matumizi ya sehemu ya eneo la Pori la Akiba la Selou kuwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere. Na niwashukuru Waheshimiwa Mawaziri wenzangu wote pamoja na Serikali kwa ujumla, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushauri na mwongozo katika kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais la kuleta hoja hii hapa Bungeni siku ya leo.
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo naomba pia niwashukuru watendaji wote wa Wizara yetu wakiongozwa na Katibu Mkuu Prof. Adolf Mkenda kwa kuendelea kutupa ushauri wa kiufundi ambao umetuwezesha kufikia hatua hii.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba nitoe ufafanuzi kwenye maeneo machache ambayo yamechangiwa na Waheshimiwa wabunge lakini pia niwaahidi kwamba kwa yale ambayo sintoweza kuyagusa, hususan yaliyoletwa kwa maandishi na hata mengine ambayo yamechangiwa kwa kusema hapa Bungeni, basi tutayazingatia katika kutekeleza maagizo haya baada ya azimio hili kufanikiwa kupitishwa na Bunge.
Mheshimiwa Spika, jambo ambalo naona kubwa na limejitokeza sana ni suala la kwa nini eneo lote la square kilometer 50,000 za Pori la Akiba la Selous lisigeuzwe kuwa eneo la uhifadhi maalum la Nyerere. Niliona alitoa taarifa hapa Mheshimiwa mchangiaji mmoja kwamba pengine huu mfumo ulivyo kwa sisi kupandisha hadhi sehemu tu ya ikolojia nzima una maana yake. Japokuwa pia hata kama tungetaka kuutazama mfumo huo wa conservation area tukaunganisha na maeneo mengine pia ingeweza kufaa tu. Lakini kwa sasa tunaona mapendekezo haya ambayo yanatokana na maelekezo ya Mheshimiwa Rais inafaa zaidi kwa hivyo ambavyo tumeyaleta na tunaomba Waheshimiwa Wabunge wapitishe mapendekezo haya kama yalivyo kwa sababu zifuatazo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza; ni ukweli kwamba Hifadhi za Taifa kwa mfumo wa ikolojia ambao upo katika nchi yetu, huwa zinakuwa zimefichwa na maeneo yenye hadhi nyingine za uhifadhi katika mzingo wake. Kwa maana ya kwamba kama kuna Hifadhi ya Taifa katikati kwenye kiini ambayo inatengeneza kiini cha ikolojia hiyo basi pembezoni mwake kunakuwa aidha na mapori ya akiba, mapori tengefu, misitu ya hifadhi ama maeneo ya jumuiya za uhifadhi za wananchi. Na haya maeneo mengine yanafanya kama vile buffer ya hiki kiini ambacho kinakuwa ni Hifadhi ya Taifa. Na huu ndio muundo ambao utaupata katika ikolojia zote.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, hata ikolojia maarufu zaidi hapa nchini na duniani kote kwa ujumla wake ikolojia ya Serengeti kuna mapori ya akiba kama ya Ikolongo, Gurumeti, Pori la Akiba la Maswa, Poli Tengefu la Loliondo, kuna eneo la Hifadhi ya Ngorongoro; yote haya yanaizunguka ikolojia pia Lake Natroni kwa kule juu yote haya yanaizunguka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. Kwa hivyo, kunakuwa kuna maeneo mengi ambayo yapo katika hadhi tofauti tofauti za uhifadhi ambapo katikati yake ndio kunakuwa kuna Hifadhi ya Taifa.
Mheshimiwa Spika, na muundo huu haupo kwa bahati mbaya, muundo huu unatuwezesha kuwa na uhakika wa kuwa na hifadhi ya Taifa katika kiini lakini pia unasaidia matumizi mengine kufanyika katika maeneo ambayo yana hadhi nyingine tofauti, kwa mfano kama ni kwenye mapori ya akiba na mapori tengefu na kama kuna wanyamapori basi inaruhusiwa kuwinda wale wanyama lakini pia kama ni maeneo ya misitu basi hapo itaruhusiwa kuvuna ile misitu ili iweze kutumika.
Mheshimiwa Spika, hii ni kwa sababu malengo ya nchi yetu sio kuwa na maeneo ya hifadhi na kuwa nayo tu, malengo ya nchi yetu ni kuwa na maeneo ya hifadhi lakini pia kuyafanya maeneo haya yatusaidie katika kupambana na umasikini. Yatupe kipato ambacho kitatusaidia kutekeleza miradi mingine. Kwa hivyo, tunaangalia siku zote tunafanya trade off kwamba eneo hili tutafaidika zaidi tukifanya nini, tukifanya utalii wa picha ama tukifanya utalii wa picha na uwindaji ama tukivuna miti. Kwa hivyo hivyo ni vigezo katika vigezo ambavyo vinatufanya tuamue eneo gani liwe nini kama Taifa na ni muundo ambao umedumu kwa muda mrefu na haujawahi kutuangusha.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, tunaomba kwa kweli muundo huu tuendelee kuulinda na hata kwenye hii Hifadhi ya Taifa ya Nyerere kuna jumuiya za uhifadhi wa wanyamapori ambazo zipo zinazunguka hifadhi hii; kuna misitu kama alisema Mheshimiwa Mchengerwa na Mheshimiwa Bobali ambapo wanavuna miti wale hawavuni miti Selous, wanavuna miti kwenye misitu ya hifadhi ambayo ipo pembezoni mwa Selous. Kwa hivyo, ni vitu kama hivyo kwamba hii maliasili tunaitumia kwa kuvuna, tunapovuna tunauza tunapata faida kama nchi inatusaidia kuhifadhi maeneo yenyewe lakini pia inatusaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo barabara, shule, afya na vitu vinginevyo.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, hata pale Selous inapozunguka watu wengi hudhani kwamba miti inavyovunwa pale ama mikaa inayochomwa pale basi imetoka Selous kwa sababu wananchi katika nadharia yao wanadhani eneo lote lile tu kwa sababu tu ni msitu basi lote ni Selous, hapana pembezoni mwa Selous kuna hifadhi za misitu hususan katika eneo hilo la Wilaya ya Liwale lakini pia ukipanda kwa juu zaidi kuna jumuiya ya hifadhi ya wanyamapori, jumuiya ya Gonabis ipo pale kutoka kule Wilaya za Kibiti mpaka kule eneo la Kisarawe. Lakini pia kwa upande wa huku utakuta kuna Hifadhi ya Misitu ya Udzungwa, kuna Kilombero Pori Tengefu la Kilombero ambalo alikuwa analizungumzia Mheshimiwa Suzan Kiwanga.
Mheshimiwa Spika, na hapa labda niseme kidogo kwa sababu amelizungumza kwa kirefu kwamba wale Sheshe wanapaswa kuwa katika Pori Tengefu la Kilombero na kwa sasa katika ramani mpya ya kutengeneza hii ikolojia ya huku kusini upya, tumeamua kupandisha hadhi Pori Tengefu la Kilombero ili sasa liende likawe Pori la Akiba la Kilombero yaani iwe Kilombero Game Reserve. Na sababu kubwa ni pamoja na kuhifadhi hao Sheshe. Walikuwa zaidi ya 40,000 mwaka 1990 leo hii wamebaki 4,000 tu na hao Kampuni ya Kilombero North Safaris wanasaidia sana katika kutoa ulinzi kwa hao Sheshe ambao wamesalia.
Mheshimiwa Spika, pia Kilombero ilikuwa mashuhuri kwa makundi makubwa ya Nyati na Tembo ambayo sasa hivi huyaoni tena. Kwa hivyo, tumekusudia kwa kweli kwa dhati kuimarisha ulinzi katika eneo hili. Pia naomba ifahamike kwamba Milima ya Udzungwa, Milima ya Mahenge na Milima ya Mbalika kwa ujumla wake ndiyo inatusaidia kupata Bonde la Kilombero ambalo linafanya kazi kama chujio la kupeleka maji katika Mito hiyo ya Luwegu pamoja na Mto Kilombero kutengeneza Mto Ulanga ambao unaenda kutengeneza hilo Bonde la Stiegler ambalo tunakusudia kuzalisha umeme takribani megawati 2115.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, uhifadhi wa eneo hili upstream huku Kilombero ni muhimu sana na kwa maana hiyo tumeamua kupandisha hadhi eneo hili lakini pia Milima ya Mahenge na misitu yake, Milima ya Mbalika na misitu yake na maeneo ya jirani ambayo bado hayana watu tunayapandisha hadhi kuwa Pori la Akiba la Kilombero. Pia tunatoa sehemu kubwa kutoka 6,500 square kilometer mpaka kubakisha 2,500 za kiini cha bonde kurudisha kwa wananchi kwa ajili ya kupunguza presha ili waweze kuishi kihalali na waweze kufanya shughuli zao za kilimo na ufugaji katika eneo ambalo sasa litakuwa halali kuliko ilivyo hivi sasa ambapo wanahesabika kama wavamizi.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, tumeangalia sana suala hilo kwa ujumla wake na haswa kwa faida hizo kubwa za kiuhifadhi lakini pia faida pana zaidi za kitaifa za kuzalisha umeme katika Bonde la Mto Rufiji.
Mheshimiwa Spika, pia ilijitokeza kwa kina sana hoja ya TANAPA kubebeshwa mzigo. Na sisi tunaona lakini tofauti ya maeneo yanayohifadhiwa na kusimamiwa na TANAPA na yale yanayohifadhiwa na kusimamiwa na TAWA kwa kweli ni matumizi tu, umuhimu wa maeneo haya ni uleule bioanuai iliyopo kwenye maeneo haya ni ileile na pengine wakati mwingine mapori ya akiba yanaweza yakawa yana bioanuwai nzuri na nyeti zaidi kuliko hata Hifadhi za Taifa.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, hii lugha ya kwamba tunapandisha hadhi ni lugha tu rahisi lakini kimsingi hatupandishi hadhi, tunachokifanya tunabadilisha matumizi ya eneo kwamba eneo hili matumizi yanaruhusiwa, eneo hili matumizi ya resource iliyopo pale hayaruhusiwi.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, maeneo haya ni muhimu sana na kwa takwimu za haraka haraka TAWA ambayo kwanza ni taasisi changa sana inasimamia takribani maeneo yenye ukubwa wa kilomita za mraba 250,000 wakati TANAPA inasimamia eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 60,000 baada ya kuongeza na hizi hifadhi mpya tatu.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, ukiangalia pia bajeti ya TANAPA per square meter ni kubwa sana, ni zaidi ya asilimia 157 katika standard ambazo zimewekwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhifadhi wa Bioanuai (ICUN) wakati TAWA wapo kwenye asilimia 83, kwa hivyo bado hawajafikia hata ile asilimia 100 ya per square meter ya eneo ambalo wanapaswa kusimamia. Ngorongoro wameshafika zaidi ya per square meter kwa asilimia 600 zaidi.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, ukipiga hesabu hizo unaona kabisa kwamba kwa kweli mgawanyo wa resources ambazo zinapatikana per square meter ya eneo ambalo linahifadhiwa bado unaipa disadvantage kubwa sana taasisi hii ambayo bado ni changa pia ya TAWA.
Mheshimiwa Spika, hivyo, katika uelekeo wetu wa mbele, tunaona kwamba ili kuondoa hii fragmentation ya mgawanyo mbovu wa rasilimali katika taasisi ambazo zinafanya kazi ileile ambayo ina umuhimu uleule, tunakusudia ndani ya Serikali bado tunaendelea na mchakato wa ndani kufanya kidogo amalgamation ambayo tutamtenga TANAPA atabaki peke yake na tutamchukua TAWA tutamuunganisha na Ngorongoro kutengeneza taasisi moja yenye nguvu lakini pia itakuwa ina nguvu ya rasilimali ili iweze kusaidia ku-balance kidogo uwiano per square meter wa uhifadhi kwa maana ya kipimo cha rasilimali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, tunafikiria kufanya hivyo, hatukusudii kuunganisha zote kwa pamoja, tunaona pia itatuletea changamoto lakini kwa sasa tunakusudia walau kuunganisha TAWA na Ngorongoro ili tuweze kugawanya resources ziende zikasaidie zaidi kuimarisha uhifadhi.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, kwamba nani ana mzigo mkubwa zaidi, na kwamba tunamuongeze mzigo TANAPA, mwenye mzigo mkubwa zaidi ni TAWA. Na hata hivyo, kwamba TAWA maeneo yake yanachukuliwa, ni kweli yanachukuliwa lakini pia maeneo ya mapori ya akiba pia yanaongezeka; kwa mfano hapa nimetaja Pori la Akiba la Kilombero linaongezeka na linaongezeka ukubwa pia kwa zaidi ya square kilometer 5,000, sasa hivi lina square kilometer 2,500, hicho kiini ambacho bado kipo hai.
Mheshimiwa Spika, lakini tunapoongeza na hii milima na misitu ambayo ipo hapa jirani katika Pori la Akiba la Kilombero litakuwa na zaidi ya square kilometer 7,500. Kwa hivyo, litakuwa eneo kubwa sana na eneo lote hili linaweza likatumika kwa shughuli za uwindaji na shughuli nyingine za matumizi ya rasilimali.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, tunaongeza pia mapori ya akiba mengine ambayo yapo katika pipeline katika hatua mbalimbali ndani ya Serikali ikiwemo eneo la Wamimbiki, Lake Natron na Wembele tumesema hapa asubuhi kwenye swali. Maeneo yote haya pia tunaongeza kule magharibi eneo la Luganzo Tongwe, tunatengeneza pori la akiba, haya maeneo ni makubwa sana na yataenda kuimarisha shughuli za uwindaji wa kitalii ambao unasimamiwa na Taasisi ya TAWA na kama tutafanikiwa kupitisha mapendekezo yetu kama yatakuja hapa Bungeni basi tutakuwa na hiyo taasisi moja mpya ambayo itasimamia maeneo yote ya hifadhi za wanyamapori nje ya maeneo ya Hifadhi za Taifa.
Mheshimiwa Spika, swali lingine ambalo limejitokeza sana ni eneo la Mradi wa REGROW, Mheshimiwa Naibu Waziri amefafanua hapa kiasi fulani. Nilipenda tu kuongeza kwamba Mradi wa REGROW ambao unalenga kukuza utalii kanda ya kusini, ni mradi wa kuhifadhi lakini pia kukuza shughuli za utalii. Kwa hivyo, tunachokifanya katika Pori la Akiba la Selous kubadilisha matumizi ya sehemu ya eneo hilo kuwa Hifadhi ya Taifa ni katika jitihada hizohizo za kuimarisha uhifadhi lakini pia kukuza utalii. Kwa hivyo, Benki ya Dunia hawajasema neno lolote lile kwamba watasitisha utekelezaji wa mradi huu katika eneo hilo na wanaunga mkono kwa sababu malengo yapo palepale.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, kuna suala la UNESCO kwamba hatujawaarifu UNESCO kwamba pengine tutapoteza hadhi ya kuwa eneo la Urithi wa Dunia, hapana. Eneo hili bado ni mali ya Serikali na kwa kuwa lipo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, linasimamiwa na msimamizi mmoja kwa maana ya administration yake na msimamizi huyu ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, hizi taasisi zote zinafanya kazi kusimamia mali ambazo zipo chini ya Wizara ambazo ziko chini ya custodian wake mkuu ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara. Kwa hivyo, iwe katika hadhi ya pori la akiba ama Hifadhi ya Taifa bado msimamizi/mmiliki ni yuleyule mmoja ambaye amepewa dhamana ya kusimamia naye ni Katibu Mkuu. Kwa hivyo, UNESCO hawatoweza kubadili kutunyang’anya hiyo hadhi kwa sababu tumepandisha tu hadhi ya kiuhifadhi zaidi tumebadilisha matumizi sasa inakuwa Hifadhi ya Taifa kwa sababu eneo ni lilelile na simamizi ni yuleyule. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hii ni kwa mujibu wa kanuni za UNESCO ile kanuni ya 172 ambayo inaeleza namna kama nchi itaamua kubadilisha mipaka ya usimamizi katika eneo lake ama itaamua kumbadilisha msimamizi. Taratibu ambazo zitapaswa kufuatwa na nchi yetu ni kupeleka taarifa ya mabadiliko hayo ya matumizi ambayo tumeifanya na wala hakuna shida yoyote kwa sababu hatubadilishi mipaka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo napenda kulizungumzia ni eneo la mifugo, kwanza hakuna makazi wala mifugo ndani ya Pori la Akiba la Selous. Mifugo ambayo inaonekana ipo katika ukanda huo wote, ipo katika maeneo mengine nje ya Pori la Akiba la Selous na haya ni maeneo ambayo pia yanahifadhiwa katika hadhi nyingine mbalimbali tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kuna mifugo mingi sana katika eneo la Kisarawe na pale ilipo inavamia kwenye Hifadhi ya Jumuiya ya Gonabis ambayo ni WMA ya wananchi. Na tumeona sasa ili kupunguza presha katika ikolojia hiyo yote basi tutamega sehemu ya hifadhi hii ya Jumuiya ya Wanyapori ya Gonabis na kuwapa wananchi ambao ni wafugaji lakini tuta-restrict matumizi badala ya kuruhusu wajenge makazi na waishi humo ndani ya WMA tutawaruhusu katika kipindi fulani fulani cha mwaka waweze kuingiza Mifugo yao katika eneo ambalo tutaliwekea mipaka ili waweze kuchunga. Lengo ni kupunguza pressure katika ikolojia hiyo nzima ili wananchi pia waweze kupumua, wafugaji nao kupata mahitaji yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu miundombinu, hii ni habari njema kwa Waheshimiwa Wabunge na wananchi wenzangu wote wanaotokea mikoa ile, kwa sababu tunavyoenda kuweka mkakati wa kutengeneza Hifadhi ya Taifa pale, miundombinu ni jambo la lazima. Ilivyokuwa zamani ili ufike Selou njia rahisi zaidi ilikuwa ni kuruka kwa ndege hizi ndogo ambazo ni gharama kubwa sana lakini utalii wa picha kwa kiasi kikubwa unahitaji miundombinu mbalimbali ikiwemo usafiri wa reli, Mheshimiwa Rais tayari yuko katika mkakati wa kufanya mazungumzo lakini pia kutekeleza mradi wa kuboresha reli ya TAZARA, kwa hivyo, itakuwa ni njia mojawapo ya kufika katika eneo hili.
Mheshimiwa Spika, pia kuna barabara tayari Mheshimiwa Rais alishaagiza ijengwe kwa kiwango cha lami. Katika mradi huu, Serikali sasa itajipanga kuhakikisha Selou na Nyerere National Park panafikika kirahisi zaidi kuliko ilivyo sasa kwa sababu watalii wa picha wakiwemo wa ndani ni rahisi zaidi kufika kwa njia ya barabara kuliko hizi ndege ndogo ambazo ni gharama kubwa.
Mheshimiwa Spika, pia kupitia mradi REGROW tutajenga viwanja vya ndege vidogo vidogo visivyopungua vitano. Vilevile kwa sasa tunafanya utafiti ili tuweze kujenga kiwanja kimoja cha ndege kikubwa eneo la Kisaki, nje kidogo ya hifadhi ya Taifa ya Nyerere ili iwe ni rahisi kufika katika eneo hili. Kwa hivyo, Waheshimiwa Wabunge wenzangu hizo ni fursa ambazo zitakuja kwa kupata hifadhi mpya ya Taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu kwamba utalii utaporomoka, hapana. Utalii hauwezi kuporomoka ndiyo utakua sasa kwa kasi zaidi kwa sababu tunaenda kuwekeza kwa nguvu zaidi.
Mheshimiwa Spika, mapato ya TAWA, nimeshajibu hayatashuka. Labda moja ambalo napenda kulifafanua tena, naona na muda umenitupa mkono ni kuhusu wafanyakazi, Mheshimiwa Mlinga ameliongea kwa uchungu sana naomba nilifafanue.
Mheshimiwa Spika, wafanyakazi hawa ni wa Serikali kwa ujumla wake, kwa mujibu wa Kanuni za Utumishi wa Umma, kwamba yuko kwenye taasisi gani ni jambo moja lakini jambo lingine ambalo ni la ukweli sana ni kwamba kwa kuwa ni watumishi wa Serikali stahiki zao zote za msingi kwa mujibu wa taratibu za Serikali ziko pale pale. Kwa hiyo, kama yupo kwenye parastatal ambayo inatoa zaidi ya kile ambacho kinatolewa na Serikali, hiyo ni bahati yake lakini kwamba wabaki palepale ni jambo ambalo linaweza likafikiriwa, naomba nilichukue tuone kama kwa mujibu wa sheria linaweza likatekelezeka. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata kama likishindikana pia siyo jambo baya kwa sababu kuna maeneo mapya mengi ambayo yanaanzishwa na yanapandishwa hadhi kuwa Mapori ya Akiba na yako chini ya TAWA na watumishi watakaotoka katika eneo hili wanaweza kwenda kuanzisha hayo maeneo mapya. Pia sisi kama Serikali tunaona tunavyozidi kufanya maboresho ya taasisi hii mpya ya TAWA ndivyo ambavyo mapato yake yanakua na pengine katika hatua fulani na wao wataweza kufikia hatua hiyo ya kulipwa vizuri zaidi kama ambavyo leo wafanyakazi wa TANAPA wanalipwa.
Mheshimiwa Spika, wewe mwenyewe ni shahidi wakati mnaanza kazi kwenye maeneo haya ya uhifadhi mlikuwa mnavaa ‘chachacha’, vijana wadogo wadogo kama Mlinga pengine hawakuwahi kuziona, lakini enzi hizo kulikuwa hata viatu hakuna, sare za kuvaa kulikuwa hakuna na hata waliokuwa TANAPA walikuwa hawapati hayo mahitaji. Hata TAWA wakati inaanza hata sare pia walikuwa hawana lakini leo hii watumishi wote wa TAWA wana sare nzuri, wanavaa viatu vizuri, wanalipwa vizuri, wanapata stahiki zao vizuri, japokuwa katika kiwango cha chini. Kwa hivyo, kadri TAWA inavyoendelea kuimarika ndivyo ambavyo na wao watazidi kuboreshewa maslahi yao.
Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa fursa hii na naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa fursa hii, na nianze kwanza kwa kukushukuru wewe mwenyewe Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimshukuru sana Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wenyeviti wote, na mahsusi Mwenyekiti Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu ambaye, ninyi nyote kwa pamoja mmeshiriki katika kutuongoza vizuri katika mjadala huu wa Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Pia kipekee niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa kujadili hotuba ya Wizara yetu ya Maliasili na Utalii kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ninamshukuru sana Mheshimiwa Kemilembe Julius Lwota, Mbunge ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa kuchambua na kujadili utekelezaji wa bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2019/2020; lakini pia, kwa kutoa maoni kuhusu makadirio na mapato ya matumizi kwa mwaka wa fedha wa 2018/2019. Vilevile ninamshukuru Mheshimiwa Mchungaji Peter Simon Msigwa Mbunge, na Naibu wake Mheshimiwa Catherine Ruge, ambao ni wasemaji kwa upande wa Wizara ya Maliasili na Utalii kutoka Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninawashukuru pia, Waheshimiwa Wabunge wote kwa namna ya kipekee kwa kutoa michango mbalimbali ya kuongea hapa Bungeni lakini pia michango ya maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imepokea na kuchambua michango kutoka Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Waheshimiwa Wabunge. Jumla ya Waheshimiwa Wabunge 68 kwa ujumla wao, wamechangia ambapo 36 wamechangia kwa kuongea hapa Bungeni na 32 wamechangia kwa maandishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwahakikishia kuwa maoni na ushauri wote uliotolewa na Wabunge utazingatiwa kwa dhati kabisa katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, zimetolewa hoja nyingi mbalimbali na kwa faida ya muda naomba nisizirudie, lakini ninaomba nitoe ufafanuzi kwenye maeneo machache, na ninaomba Waheshimiwa Wabunge waniruhusu nifanye hivyo kwa faida ya muda.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hoja zote zilizotolewa hapa, hoja ambayo tunaona tuipe uzito sana katika kuitolea ufafanuzi kwa sababu inagusa maeneo mengi ya Waheshimiwa Wabunge, lakini pia wananchi kwa ujumla wake ni hoja ya nigogoro ya mipaka baina ya mamlaka za maeneo mbalimbali yaliyohifadhiwa na wananchi wanaozunguka maeneo hayo. Ushauri umetolewa, maombi yametolewa na Waheshimiwa Wabunge kwamba pengine ile Kamati ambayo Mheshimiwa Rais aliyoiunda Januari 15 mwaka 2019, baada ya kukamilisha kazi yake inge-share ripoti ya kazi hiyo na Bunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, ufafanuzi pamoja na kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu aliutoa hapa juzi, na naona pia jana imejitokeza na leo imejitokeza, naomba tu niwape comfort Waheshimiwa Wabunge kwamba mchakato huu kwanza, kama alivyosema Mheshimiwa Waziri Mkuu, uliagizwa na Mamlaka ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na hivyo kazi tuliyotumwa mimi pamoja na Mawaziri wenzangu wengine saba ilikamilika na tumeshawasilisha ripoti kwa aliyetutuma, na ndio utaratibu wa kiutendaji. Sasa Mheshimiwa Rais atashauriwa na Baraza lake la Mawaziri na hatua zitakapo anza kuelekezwa kwamba zichukuliwe ni wazi Waheshimiwa Wabunge watapata mrejesho. Hata hivyo niwatoe hofu kwamba tumefanya sample ndogo ya maeneo wamezungumza Waheshimiwa Wabunge wengi, kwa sababu nafahamu wengi wangetamani tufike kila eneo ndipo waone kwamba tunashughulikia migogoro ya maeneo yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, Naomba niwape comfort Waheshimiwa Wabunge kwamba kazi iliyofanyika imefanyika kwa kikamilifu na ni kazi ambayo ilipewa uzito mkubwa sana na Serikali na si kazi ambayo ilianza Januari 15, kuna kazi nyingine zilishafanyika huko nyuma. Kuna Tume mbalimbali zilishaundwa, tumechambua taarifa zote hizo lakini tukaona haitoshi tukaona pia tuchukue maoni kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge na tukapata maoni yenu, mapendekezo yenu na maombi sehemu nyingine na yote haya, tumeyafanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tukaona haitoshi tukawaita Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa, wa Wilaya, Wakurugenzi wote wa halmashauri zote hapa nchini wakaja pia wakazungumza na Kamati yetu, nao wakatuelezea migogoro mingine ambayo ipo katika maeneo yao na yote hiyo tumeifanyia kazi na kimsingi kuna migogoro ambayo mahsusi tumeipatia mapendekezo kadhaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo kwenye maeneo mengi zaidi, tumeweka tu principle ambayo itatumika kufanya maamuzi tunavyoelekea mbele. Kwa hivyo hata kama mgogoro haukuwepo katika migogoro ambayo tumeipitia, na hiyo itakuwa ni bahati mbaya sana, basi itaguswa na hiyo principle ambayo tutaitumia katika kufanya utekelezaji; na hii sasa, ni mpaka pale ambapo Mheshimiwa Rais atakubaliana na mapendekezo ambayo tumeyapeleka.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini walau linaloleta faraja kubwa kwa Waheshimiwa Wabunge na kwa wananchi ni jambo moja, na hili ni spirit ya Mheshimiwa Rais. Azma ya Mheshimiwa Rais ilikuwa ni kupunguza manung’uniko, kero na migogoro kwa upande wa wananchi kuliko hata kwa upande wa hifadhi; japokuwa aliweka angalizo kwamba tuhakikishe tunalinda hifadhi hizi, tuhakikishe pia tunalinda ikolojia hizi ambazo tunazo kwa namna yoyote ile. Kwamba tutatue migogoro lakini tuhakikishe pia uhifadhi unaendelea na shughuli za utalii zinaongezewa tija. Kwa hivyo mambo yote yamezingatiwa katika uchambuzi wetu na mapendekezo yako vizuri. Kwa hivyo comfort iliyopo ni kwamba kwenye maeneo yale yenye kero, kwa kweli spirit na muongozo wa Mheshimiwa Rais ulikuwa ni kwamba wananchi wapate ahueni; na hilo ndilo tulilolizingatia katika mapendekezo yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa kuwa bado kazi ni mbichi naomba niishie hapo nisije nikajikuta naanza kuelezea baadhi ya migogoro ilhali hatujapewa muongozo na aliyetutuma; lakini walau muwe mna-comfort hiyo kwamba migogoro baada ya mapendekezo haya kupitishwa na Mheshimiwa Rais pengine tutaipunguza kwa kiasi kikubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Maelekezo mengine yote ya ushirikishwaji wa wananchi tunayapokea kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge na ndivyo ambavyo tumekuwa tukifanya; labda tutaweka msisitizo zaidi kwamba wananchi washirikishwe kwa kiasi kikubwa katika kupitia mipaka na katika zoezi zima la kuweka vigingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna maelezo pia ambayo yalitolewa kwenye ripoti ya Kamati, lakini pia Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, pia Mheshimiwa Sakaya, Mheshimiwa Catherine Magige, Mheshimiwa Yussuph Hussein pia alizungumzia leo na Waheshimiwa wengine wamezungumzia eneo la Ngorongoro. Naomba hapa nielezee tu kwamba, eneo hili ni katika maeneo ya urithi wa dunia ambao unatambulika na UNESCO. Pia ni eneo nyeti kidogo kiuhifadhi ma unyeti wake kwa kiasi kikubwa unajengwa na msingi kwamba ni eneo pekee ambalo matumizi mseto ya ardhi yanaruhusiwa kwamba kuna matumizi ya uhifadhi wa wanyamapori katika eneo hilo lakini pia shughuli za mwananchi zinaruhusiwa, wananchi wanaishi sambamba na wanyamapori.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na changamoto nyingi ambazo zimejitokeza kutokana na model hii na ukweli unazidi kujibainisha pale ambapo tunaona dhahiri kwamba idadi ya watu toka mwaka 1959 inapotangazwa ambapo walikuwepo 8,000 imeongezeka sana leo hii tuna watu takribani 93,000 katika eneo lile lile. Pia idadi ya mifugo imeongezeka, shughuli za utalii pia zimeongezeka kulikuwa kuna lodge chini ya sita leo hii tunazo lodges zaidi ya 10 katika eneo hilo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo shughuli za utalii zimeongezeka, shughuli za watu zimeongezeka pia wananchi wanaopita katika eneo la Ngorongoro kwenda Serengeti na kwenda Mkoa wa Mara upande wa pili pia wameongezeka. Kwa hivyo kulikuwa kuna haja ya Serikali kwa kweli kukaa chini kutathmini na hatimaye kuja na mapendekezo kwamba nini kifanyike katika eneo hili nyeti sana la kiuhifadhi la Ngorongoro. pia kwa kuzingatia ukweli kwamba per square meter eneo la Ngorongoro ndio hifadhi pekee ambayo inaingiza pesa nyingi zaidi kuliko hifadhi zote Afrika Mashariki na Kati, per square meter. Kwa hivyo, ni eneo fulani ambalo kiuchumi ni muhimu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tumefanya kazi hiyo, niliunda Kamati mimi kama Waziri mwaka jana mwezi Machi, Kamati imetuletea ripoti wiki iliyopita na ina mapendekezo kadhaa. Mapendekezo tunaona yakikubaliwa na wananchi na wadau wote yatakuwa mazuri yatasaidia ku-balance mahitaji ya makundi yote ambayo yanatumia ardhi ya Ngorongoro wakiwemo wananchi pia sisi wahifadhi na shughuli za utalii kwa ujumla wake kwa sababu tunapendekeza na kama Serikali itakubali kwa maana ya kupitia Baraza la Mawaziri, basi sisi tunapendekeza kwamba eneo la Ngorongoro kwa kuwa linazidi kupata athari kubwa ya mazingira ni lazima tuchukue hatua mahususi kama zifuatazo; kwamba katika eneo lile kuna shughuli ambazo zinahusiana na uhifadhi 100%. Eneo kwa mfano la crater, kuna craters tatu pale almost, ya Embakai pamoja na hiyo Ngorongoro Crater ni lazima maeneo haya yalindwe. Pia kuna msitu wa Kaskazini ni lazima eneo hili lilindwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunavyoona sisi pengine matumizi katika maeneo haya nyeti na maeneo mengine ambayo yana wanyamapori wengi kama Ndutu pengine yawe limited kwa ajili ya wanyamapori.
Vilevile tunaona kwamba mle ndani kuna makazi ya wananchi, wananchi wale hawaruhusiwi kulima, hawaruhusiwi kujenga nyumba za kudumu, kwa hivyo maisha yao yanakuwa magumu sana. Ukitaka kujenga shule alizungumza Mheshimiwa Catherine Magige ni mpaka wapate kibali, wakitaka kujenga zahanati ni mpaka wapate kibali, kwa hiyo wanakuwa wanapata adha kubwa sana kuleta maendeleo katika maisha yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi pia tunaona hii si sawa, jamii ya wananchi wa Ngorongoro ina haki kama jamii ya wananchi wa Iringa, jamii ya wananchi wa Moshi, ya kujiendeleza. Hatuwezi kusema jamii hii itabaki kuwa duni toka enzi na enzi mpaka leo tunaona kwamba lazima tuipe fursa pia ya kujiendeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, jamii hii hairuhusiwi kulima katika eneo lile tunalazimika kuwapa chakula kidogo ili kuwasaidia, lakini jamii pia nayo imebadilika sana, leo hii jamii ya Ngorongoro sio wafugaji 100%, kwa kiasi kikubwa pia kuna watu wanahitaji kulima kuna watu wengine mle zaidi ya asilimia 25, hawana ngombe hata mmoja kwa hivyo siyo wafugaji, hawana mfugo hata mmoja, kwa hivyo siyo wafugaji. Je, hawa watu wanaishije, huwezi kusema wanaishi kwa kutegemea maziwa na nyama peke yake, kwa hivyo tumeona tugawe sehemu kadhaa tutengeneze vijiji proper vijiji ambavyo wananchi wataruhusiwa kufanya shughuli zozote zile za uendelezaji, wataruhusiwa kumiliki ardhi, wataruhusiwa kufanya shughuli za kiuchumi nyingine kama sehemu nyingine yoyote ile ya nchi, kwa sababu kwa sasa hivi wanahesabika wako ndani ya hifadhi. Kwa hivyo wamekuwa limited kufanya shughuli kadhaa ambazo zinatambulika na lazima zifanyike kwa kibali maalum. Kwa hivyo, tunaona tutaanzisha sasa vijiji mahususi katika eneo hili ambavyo vitakuwa haviingiliani sana na uhifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tutabakisha maeneo ambayo yatatumika kwa ajili ya shughuli za uhifadhi mseto ambapo wanyapori watapita humo na wananchi wataishi katika maisha yale ya kizamani ya kimila ya kiasili ya kimasai kama ambavyo iko sasa. Kwa hivyo tutaweka maeneo hayo matatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo tunaona kwamba eneo lile bado ni finyu sana ni lazima tu-annex maeneo ya jirani ambayo yana uhifadhi pia yana mila zinazofanana na watu wa pale ili eneo liwe kubwa zaidi ili wananchi tutakapokuwa tunawahamisha kwenye maeneo yale nyeti tuwasogeze pembeni hapo waweze kukaa. Sasa tutaweka mfumo ambao utatoa motisha kwa watu ambao watakubali kuhama wao wenyewe katika eneo moja kwenda eneo linguine, lakini pia tutaweka masharti magumu kwa watu ambao watataka kuendelea kubaki katika eneo hilo. Lengo letu ni kutotumia nguvu katika kuendelea kuhakikisha hifadhi ya eneo la Ngorongoro inabaki kuwa endelevu kwa vizazi na vizazi vinavyokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kulitolea ufafanuzi ni suala la hifadhi mpya ambazo tumeziongeza kwa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na hizi ni yale yaliyokuwa mapori ya akiba matano na ninayo furaha kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba mchakato ambao tuliupitisha hapa Bungeni kwenye Bunge lililopita kupitia azimio la kupandisha hadhi mapori ya akiba haya matano kuwa hifadhi za Taifa umekamilika, Mheshimiwa Rais ameshaandika tangazo kwenye gazeti na muda si mrefu litakuwa liko public.
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa mkononi ninayo hati ambayo inatoka kwa Mheshimiwa Rais ambapo akitangaza hifadhi tatu mpya za Taifa ambazo kama Mheshimiwa Bernadetha Kasabago Mushashu alivyopenda tumwambie majina ya hifadhi hizo maana yake anasikiasikia tu. Naomba nimpe taarifa rasmi sasa Mheshimiwa Bernadetha Kasabago Mushashu kwamba Mheshimiwa Rais ameamua kutangaza Hifadhi ya Taifa ya Burigi - Chato National Park, Hifadhi ya Rumanyika - Karagwe National Park na hifadhi ya Taifa ya Ibanda - Kyerwa National Park. Kwa hivyo hizo ndio hifadhi mpya tatu ambazo zinaingia katika orodha ya hifadhi za Taifa na zitakuwa chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa ya Ngorongoro.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nitamke kwamba Wizara ya Maliasili na Utalii ilianza mchakato wa kuunda mfumo wa kukusanya takwimu na taarifa mbalimbali kutoka kwa watalii wa kielektroniki, pia mfumo wote wa shughuli zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia wizara yenyewe kama makao makuu lakini pia na taasisi zote zitafanyika kwa njia ya mtandao na tumejenga mfumo mpya kabisa ambao utakuwa mmoja tu na utakuwa chini ya Wizara na taasisi zote watapewa windows kwa ajili ya kufanya shughuli zao ujulikanao kama MNRT Portal.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu umeshaanza kutumika kwenye baadhi ya taasisi na taratibu tunaendelea kusambaza kwenye taasisi nyingine na utakapokamilika changamoto ya takwimu itapungua sana na mfumo huu mwisho wa siku utafika mpaka kwa wadau, watu wanaofanya biashara ya tour, wale tour operators, watu wa mahoteli, wote watakuwa na huu mfumo na watafanya kazi zao kwa kutumia mfumo huu wa kielektroniki ambapo utakuwa unaoana na mifumo mingine kwenye taasisi zingine zote ambazo zinahusika na kuwachaji tozo wadau mbalimbali wa utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, tutakuwa tuna link ya OSHA tutakuwa tuna link ya BRELA, tutakuwa tuna link ya TRA, utaunganishwa na kufungamanishwa na mifumo yote ya Serikali na hivyo itakuwa ni rahisi kulipa tozo, ni rahisi kuletewa invoice na itakuwa ni rahisi kufanya booking na package za wageni wanaokuja katika kampuni yako. Kwa hivyo tunaamini mfumo huu utapunguza kwa kiasi kikubwa sana business process ambazo zinafanywa na taasisi mbalimbali zilizopo chini ya Wizara yetu pamoja na wadau wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Waheshimiwa Wabunge wa kutoka Kusini ambao wanasema hii ndio kusini proper wamezungumzia sana kuhusu mradi wa Regrow kutokuwa na impact kubwa sana katika Mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara. Wameongea kwa uchungu sana kuhusu Mji Mkongwe wa Mikindani, Mji Mkongwe wa Kilwa Kisiwani, hifadhi ya Selou kwa upande wa Mkoa wa Lindi nami nawaelewa. Naomba niseme nimechukua concern yao na nitaifanyia kazi kwa ukaribu sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuanzia napenda pia niwape taarifa tu kwamba Mji Mkongwe wa Mikindani pia tumeshausajili kwenye urithi wa dunia na kila mwaka tunafanya Tamasha la Mji Mkongwe wa Mikindani, pia Mji Mkongwe wa Kilwa nao tuko katika mchakato wa kuusajili ili nao uwe katika orodha ya miji ambayo ni urithi wa dunia. Pia tuko katika mpango wa kuendeleza utalii wa fukwe na kwa sasa tutaanza na fukwe za Kigamboni na Bagamoyo. Kwa kuanzia tumeshaandika andiko, liko tayari na katika hatua ya pili sasa tutazungumzia fukwe za ukanda huu wa kusini hii ya Lindi na Mtwara.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu fukwe ya Mnazibay tunafahamu fukwe ya Kisiwa cha Mafia ni katika fukwe bora kabisa duniani na zinapendeza kwa kweli madhari yake na hilo halina mjadala, halibishaniwi, ni ukweli usiopingika, lakini tunakwenda kwa awamu. Katika awamu ya kwanza tunaona kwanza tufanye kazi kubwa ya kuwekeza kwenye utalii wa fukwe katika Jiji la Dar es Salaam na hapa tumeangalia sana uwepo wa miundombinu. Ili uwe na product ya utalii ambayo inafanya kazi kimkakati ni lazima uwe karibu na uwanja wa ndege wa Kimataifa. Ili kuwe kuna uwezekano wa zile long-haul flight kufika na kushusha wateja na wateja kufika kwenye kivutio kwa haraka zaidi kuliko kuwa na stop nyingine tena kwamba achukue local flight kwenda kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, tumeona katika kukuza fursa ambayo inakuja na utalii wa fukwe, utalii wa mikutano na utalii wa meli, tuwekeze kwanza katika Jiji la Dar es Salaam. Huu ni mradi mkubwa sana ukianza huu mradi, dunia nzima itatikisika kwa sababu idadi ya watalii itaongezeka kwa kiasi kikubwa sana. Pia ni concern ya Waheshimiwa Wabunge kwamba tuongeze idadi ya watalii hapa nchini. Utalii wa Tanzania kwa kiasi kikubwa kwa sasa ni utalii unaoendana na mazingira asilia, utalii wa nature, utalii wa wanyamapori kwa kiasi kikubwa zaidi ya asilimia 80 na utalii huu pia umejikita katika circuit moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iliona katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa mwaka 2016 – 2021, tufanye diversification, tutanue wigo wa vivutio vya utalii ili tutengeneze mazao mengine ya utalii, mojawapo ni hili zao la utalii wa utamaduni ndio maana nazungumzia Mji Mkongwe wa Mikindani, Mji Mkongwe wa Kilwa, Mji wa Bagamoyo na vivutio vingine vya malikale kama vile Isimila, Kalenga na historia ya nchi yetu kupitia Machifu na vitu vingine. Sasa hiyo ni aina moja ya zao la utalii ambalo ni lazima sisi kama Serikali tuwekeze.
Mheshimiwa Naibu Spika, zao lingine kubwa na muhimu la utalii ambalo ni lazima tuwekeze kama tunavyoelekezwa na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano ambao tuliupitisha hapa Bungeni ni utalii wa fukwe na lingine ni utalii wa mikutano na lingine ni utalii wa maze yaani cruise ship.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa sisi tumeona tuanze kwa Dar es Salaam tuunganishe haya mazao yote kiurahisi zaidi na pale tayari tuna advantage ya uwanja wa ndege wa kimataifa ambao upo pale na sasa hivi unafanyiwa uendelezaji mkubwa na Serikali, ujenzi umevuka asilimia 99. Kwa hivyo muda si mrefu tutakuwa tuna uwanja wa ndege mzuri zaidi, tuna shirika la ndege ambalo linafanya kazi vizuri. Sasa tukiunganisha na vivutio vya fukwe vilivyopo pale Dar es Salaam na vivutio vya utamaduni itakuwa rahisi sana kupata faida na tija ambayo itakuja na hizi product. Kwa hivyo sasa hivi wenzetu wa TPA ambao tuko nao katika uendelezaji wa mradi wa utalii wa cruise ship, utalii wa meli tunajenga gati maalum kwa ajili ya cruise ship tourism na hii itatusaidia sana kuongeza watalii. Kwa tathmini niliyofanya na wataalamu tunaweza tukapata zaidi ya trilioni tatu kwa utalii wa cruise ships.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo utalii wa meli tu peke yake unaweza ukaleta trilioni tatu. Huu utalii tulionao leo unatuletea trilioni sita. Kwa hivyo kwa haraka haraka tu unaona kwamba kama ni matunda yanayoning’inia chini zaidi, lower hanging fruits maana yake cruise ship tourism ni lazima tuwekeze kwa haraka sana. Kwa hivyo, tunawekeza katika eneo hili na tayari tunarudisha uanachama wa nchi yetu katika yale mashirika ya kimataifa yanayohusika na cruise ship tourism ili tuwe katika mikakati ya kupanga, kufanya marketing mapema ili tutakapokamilisha ujenzi wa gati hili maalum kwa ajili ya cruise ships watalii waanze kuingia nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni utalii wa mikutano; utalii huu tukiwekeza vizuri kama ambavyo majirani zetu wamefanya tuna uwezo wa kupata zaidi ya trilioni mbili kutokana na mikutano ambayo itavutiwa hapa nchini. Eneo lingine ni huo utalii wa fukwe ambao kwa ujumla wake tunakusudia kuanzisha eneo maalum la utalii pale Kigamboni na eneo la Bagamoyo ambapo tutajenga kumbi kubwa za mikutano na hapa nazungumzia mikutano ambayo watu zaidi ya 5,000 wanaweza wakaingia na wakafanya mikutano kwa wakati mmoja. Sizungumzii ukumbi kama ule tulionao sasa wa AICC, nazungumzia project kubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuko katika hatua za kufanya andiko la mradi huu, hatua ya awali ya utafiti imekamilika, sasa tuna proposal ambayo itakwenda kwa Makatibu Wakuu, baadaye Baraza la Mawaziri na mradi huu ukipitishwa tutaanza kuutekeleza. Uzuri tuna uwezekano mkubwa sana wa kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi huu. Huu ni awamu ya kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya pili tutakwenda kwenye fukwe za Maziwa pia tutakwenda kwenye fukwe zilizopo Mafia, Kilwa, Mtwara na maeneo ya Tanga mpaka Pangani kuunganisha na hiyo Bagamoyo niliyoisema. Kwa hivyo eneo hili kwa kweli tunalipa kipaumbele cha hali ya juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ni hoja ya hoteli zilizokuwa chini ya Shirika la Utalii Tanzania (Tanzania Tourist Corporation) ambalo lilivunjwa na baadaye mahoteli 17 yakauzwa kwenye sekta binafsi. Katika hoteli hizi kuna hoteli, nilipoteuliwa kwa kweli nilipewa maelekezo ya namna ya kuzifanyia tathmini hoteli hizi zote ili tuweze kuona ni zipi bado ziko viable na zipi ambazo haziko viable ili tuweze kuvunja mikataba, tuzirudishe ndani ya umiliki wa Serikali na hatimaye tuweze kuzikodisha kwa waendeshaji wengine.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika tathmini iliyofanyika takribani hoteli 10 zilionekana zina changamoto mbalimbali za kimkataba na katika hizi 10 ilionekana hoteli nne tayari zimekiuka moja kwa moja masharti ya mikataba ya mauziano baina yake na Serikali. Hizi ziko chini ya kampuni moja inaitwa Hotels and Lodges Limited na hizi nazungumzia hoteli kama Seronera Wildlife Lodge, Ngorongoro Wildlife Lodge na Kilimanjaro Wildlife Lodge na ile ya Mafia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa tuko katika hatua mbalimbali ndani ya Serikali ili kufanya uchambuzi wa nyaraka ambazo zipo, tukishirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wizara ya Fedha na wiki ijayo tutakaa kikao cha mwisho ili kufikia maamuzi ya nini itakuwa hatma ya hoteli hizi nne ambazo moja kwa moja zimeshakiuka masharti ya mkataba ili tuweze kuchukua hatua ya kuzirejesha Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo lilizungumziwa hapa na limezungumziwa na wachangiaji wengi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Peter Msigwa, Mheshimiwa Grace Kiwelu na wachangiaji wengine lilihusu biashara ya wanyamapori hai nje ya nchi. Biashara hii kwa ndani ya nchi bado inaruhusiwa na actually tunahamasisha iweze kufanyika pia tunawahamasisha wadau mbalimbali waanzishe ranch kwa ajili ya kufuga wanyamapori kwa sababu kuna uhitaji mkubwa wa wanyamapori. Pia nyara ambazo zinaweza zikatumika kwa ajili ya shughuli mbalimbali hapa ndani ya nchi pia kuvutia wawekezaji kutoka nje waje hapa ndani ya nchi wawekeze kwenye viwanda vya Nyara pia ufugaji wa wanyamapori na hatimaye tuweze kuindeleza biashara hii na iweze kuleta tija kwa Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili sasa ni biashara hii ya wanyamapori nje ya nchi. Kwa sehemu ya kwanza kwa sasa hivi tunafanya mabadiliko ya Kanuni ambapo tutaruhusu hata mabucha ya nyamapori katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa ajili ya matumizi ya wananchi. Kwa sababu tunafahamu wananchi kimila lakini pia hata wengine tu kwa upenzi tu wanapenda kutumia nyamapori kwa matumizi ya chakula ili kupata protein na tumeamua kuanzisha mabucha kwa ajili ya kutoa fursa hiyo kwa wananchi. Kwa hivyo hii inapaswa iende sambamba na wananchi kuanzisha mashamba (ranch) kwa ajili ya kufuga wanyama pori. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ni lile la kupeleka nje ya nchi. Kwa nje nchi kwa kweli mimi huwa sipendi kumung’unya maneno, biashara hii imekoma. Mheshimiwa Peter Msigwa ananiangalia vizuri, naomba uniangalie vizuri na usome midomo yangu; biashara ya wanyama pori hai nje ya nchi haitofanyika mimi nikiwa Waziri wa Maliasili na Utalii. Sababu ziko wazi tu, nilipokuwa Mbunge hapa tulikuwa naye Mheshimiwa kaka yangu Mchungaji Peter Msigwa, kaka zetu waliokuwa Mawaziri wa Wizara hii walishambuliwa sana kuhusu wanyamapori hai. Mara twiga ameenda, mara pundamilia, mara nyani, mara nini! Kwa hivyo Mheshimiwa tulikuwa tunasema na mimi nilikuwa mmojawapo nikirusha mawe na hata rafiki zangu nao walikuwa moja wapo ya watu waliokuwa wakilalamikia sana jambo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nilipoteuliwa nikakuta wameshazuia na mimi nikasema hii haitofunguliwa mimi nikiwa Waziri. Kwa hivyo hii tumeifunga hatutosafirisha. Mapendekezo ya Mheshimiwa Msigwa ni kwamba pengine kuna mijusi, kuna ngedere kwenye mashamba ya watu, kuna kwereakwerea; na pia hata Mheshimiwa Adadi Rajab naye analalamikia vipepeo kwamba tungeweza kuwaruhusu wananchi wanaofuga wanyama hawa wao wenyewe wasafirishe nje ya nje, ama waliopo kwenye maeneo ya wazi wachukuliwe wasafirishwe nje ya nchi. Tungeweza kufanya hiyo, lakini hatutaki kuweka hiyo principle, kwamba tunaruhusu baadhi ya wanyamapori na tunakataza baadhi ya wanyamapori. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Tumeamua tu kufunga milango ya wanyamapori ambao ni urithi wa kiasili wa Watanzania kutoka nje ya nchi, hawatatoka. Hata chawa hatatoka, hata kunguni hatatoka, kwa hivyo size ya mnyama haita-matter. Hakuna mnyamapori hai atatoka mipaka ya Tanzania kihalali, kwa njia ya biashara kwenda nje ya nchi eti kwa sababu tunataka kipato, hapana. Nimesema anayetaka kufanya biashara ya nyara afuge, aendeleze hizo nyara zake hapa, azitengeneze hapa, atengeneze hizo bidhaa hapa, auze bidhaa hizo nje ya nchi. Anayetaka kufuga ili waje watazamwe, aanzishe zoo yake hapa na sisi tutamuunga mkono, afanye hiyo biashara ya Zoo hapa, kana ana wageni awatoe huko kwao awalete hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini biashara hii ya watu kununua wanyama hapa kwenda kuweka kwenye ma-zoo huko; kwa mfano vipepeo, kule Marekani kuna zoo kubwa sana wamejaza mle vipepeo ambao wanatoka Amani Nature Reserve hapa Muheza kwa kaka yangu Mheshimiwa Adadi, na watu wanaingia kwa gharama kubwa kwenda kuwaona pale. Sisi wazo letu ni kwamba, hawa vipepeo kwa sababu ni mahsusi na ni pekee kwa hapo tu Amani Nature Reserve hawapatikana sehemu nyingine yoyote ile duniani, vipepeo wa aina ile, basi ni bora na nilishaagiza Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ashirikiane na wale wananchi ambao wanafuga vipepeo pale tujenge Museum ya kwetu pale. Tujenge Zoo tuwaweke wale vipepeo pale kiwe kivutio kimojawapo cha utalii katika eneo lile, kwa sababu tayari watu wanapenda kwenda kutembea kwenye Msitu wa Amani na kwenda kuoga kwenye yale maporomoko yaliyoko pale kwenye mito ile iliyoko pale. Watalii wengi wanaenda pale na wengine wanaenda kutembea kwenye ule msitu, ni kivutio tayari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tuongeze tu product nyingine ya utalii kwa kuanzisha zoo pale tuweke hao vipepeo na watu waende wakawaone pale. Kwa hivyo wale wananchi ambao wanafuga na maisha yao wanayaendesha kwa kupata kipato kutokana na vipepeo, basi watakuwa wanawapeleka pale kwenye museum kila baada ya muda wanawapeleka pale na watu wanakuja kuwaona na wananchi wale wanapata faida inayotokana na vipepeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu wale wafanya biashara wakati zuio linatolewa mwaka 2016 mwezi Mei, walikuwa wameshalipa fedha kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali kutoka Serikalini. Tayari tathmini hii imefanyika, uhakiki umefanywa na Wizara ya Fedha na hao wananchi watarejeshewa fedha zao ambazo walikuwa wameshalipa ndani ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kulitolea ufafanuzi ni eneo la uwindaji wa kitalii. Biashara ya uwindaji wa kitalii kwa kweli ilikuwa inafanya vizuri mpaka mwaka 2008/2009 na baadaye biashara hii ikaanza kuanguka. Sababu za kuanguka ni nyingi lakini tatu mahsusi ambazo napenda kuzisema hapa ni pamoja na kuvamiwa kwa maeneo yanayotumika kwa ajili ya uwindaji wa kitalii na wananchi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kibindamu, zikiwemo kilimo, ufugaji pamoja na makazi. Hiyo imekuwa iki- discourage sana wawekezaji katika sekta hiyo lakini pia hata wawindaji wanaokuja kuwinda katika maeneo hayo; kwa sababu wawindaji hawa ni watu wanapenda wayakute haya maeneo katika uasilia wake. Sasa wakikuta mle ndani kuna ng’ombe anaona sasa hili tena siyo pori hiki tayari kimeshakuwa kijiji siyo tena pori kwa ajili ya uwindaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu nyingine ilikuwa ni zuio ambalo lilifanywa na nchi za nje, huko ambako ni masoko yetu makubwa kama Marekani kupitia ile U.S Fish and Wildlife Service ya Marekani pamoja na Scientific Review Group ya Umoja wa Ulaya; kwamba nyara za simba na tembo zisiingizwe katika nchi hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama wawindaji wanakuja huku kuwinda halafu kiu yao ni kupata hizo nyara za wanyamapori kama nyara za simba na tembo; nchini kwao kule kama haziruhusiwi kuingia maana yake hata wao kuja kuwinda huku haina maana tena kwa sababu kinachowafanya waje kuwinda ni wao kupata hizo nyara. Kwa hivyo lile zuio kule limetusumbua sana katika biashara hii. Kingine ni wanaharakati ambao wanapinga uwindaji wa wanyamapori.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo haya mambo makubwa matatu yalisababisha kwa kiasi kikubwa sana biashara hii kuanguka hapa duniani na si Tanzania peke yake. Kwa hivyo mapato yalishuka lakini pia changamoto zikawa nyingi kwa hawa waendeshaji wa biashara hii, kwa maana ya zile kampuni za Hunting Operators, matokeo yake sasa wakarudisha maeneo mengi Serikalini; na wakati mimi nateuliwa kuwa Waziri kwenye Wizara hii nilikuta vitalu takribani 81 viko wazi. Kwa hivyo biashara kwa kweli ilikuwa imeanguka kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tumefanya jitihada kama Serikali kwa kushirikiana na wadau hao kufanya mageuzi mbalimbali katika sub sector hii. Mojawapo likiwa ni kuzungumza na United States Fish and Wildlife Service pamoja na hii Taasisi ya Nchi za Ulaya inayojulikana kama Scientific Review Group ili waweze kuruhusu nyara ziingizwe katika nchi zao kutoka nchi za Afrika na kwa sababu lobbying iliyofanywa na Serikali za nchi za Afrika imekuwa kubwa, zaidi ni kuwaelimisha kwamba uwindaji si kitu ambacho kinapunguza population ya wanyama huku Afrika lakini ni kitu ambacho kinasaidia kupata mapato ambayo yanatuwezesha kulinda maeneo haya. Kwa sababu gharama ya kuyahifadhi na kuyalinda ni kubwa mno, haya maeneo ni makubwa sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania 1/3 ya maeneo yetu ni hifadhi, kwa maana ya asilimia takribani 33 ni hifadhi. Kuyalinda maeneo haya halafu kama hayaingizi fedha ni mzigo mzito sana kwa Serikali, lakini tumeyalinda kwa faida yetu, kwa faida mbalimbali ya kiikolojia lakini pia kwa faida za vizazi kutoka nchi mbalimbali ambavyo vinakuja kutumia maliasili hizi. Sasa jukumu la kuzilinda haliwezi kuwa la kwetu peke yake, kwa hivyo kuwaomba watusaidie tupate fedha kwa ajili ya kulinda na yenyewe inakuwa too much kuombaomba. Kwa hivyo ni bora tufanye biashara kwenye maeneo haya ili mapato yatumike kurudi kuendelea kuyahifadhi maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo elimu ya namna hii imezunguka sana huko Ulaya, huko Marekani na baadhi ya states za kule Marekani wameweza kuruhusu nyara ziingizwe katika hizo states zao. Baadhi ya nchi za Ulaya wametuelewa na wenyewe wameweza kufungulia nyara ziweze kuingia katika hizo nchi zao, kwa hivyo mafanikio tumeanza kuyapata kwa kiasi kikubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tumepitia kwa ujumla wake; niliunda Kamati mwaka jana mwezi Machi; ambayo imepitia sekta yote hii ya uwindaji wa kitalii na imetuletea ushauri. Kamati ilikuwa ndani yake ina wadau na hatimyae wameleta ushauri kwamba kuna mambo kadhaa ambayo tuyafanyie mojawapo likiwa ni hilo la lobbying lingine likiwa ni eneo la kufanya marketing vizuri zaidi, lakini pia lingine likiwa ni kuvutia professional hunters ambao hawa ni wawindaji bingwa ambao wana elimu na ujuzi mahsusi kwa ajili ya kuwindisha wageni waje Tanzania ili kufanya kazi ya uwindaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo walipendekeza tupunguze tozo ambayo tunawachaji hao wawindaji bingwa kutoka nchi nyingine, wengi wanatoka nchi ya Afrika ya Kusini na nchi ya Zimbabwe na wachache kidogo Botswana pale. Kwa hiyo tumefanya mabadiliko hayo kwenye kanuni, tumerekebisha hizo tozo mbalimbali, tumerekebisha tozo za wanyama, za kuuza nyara, top fees, game fees na kwa kiasi kikubwa haya mabadiliko kwa kweli tuliyaita hunt more for less; gharama za kuja kuwinda Tanzania zimepungua sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hata vitalu vyenyewe tumeona tuvibadilishe category. Tulikuwa tuna category tano, sasa tumezishusha zimebaki category tatu, lakini pia tumeona tuongeze muda wa kumiliki kitalu badala ya kuwa na miaka mitano tunapeleka kitalu daraja la kwanza na kwa daraja la pili mtu ataweza kuwinda kwa miaka kumi katika eneo lile. Pia kwa daraja la tatu tumesogeza muda badala ya miaka mitano tumepeleka mpaka miaka 15.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo kwa mtu ambaye atashiriki kwenye biashara hii akapata kitalu atakuwa na uhakika ile tunayoizungumza kila siku, akina Mheshimiwa Msigwa anazungumzia hapa, stability ndiyo hiyo tunayoizungumza. Kwamba mtu atakuwa na kitalu kwa miaka 10 ama kwa miaka 15 bila kuingiliwa na Serikali as long as analipa tozo mbalimbali ambazo anapaswa kulipa. Kwa hivyo ataweza hata kuendeleza kujenga kambi nzuri, kambi za kudumu kwa muda wote huo akiwa na uhakika kwamba kwa miaka 10 ata- operate kitalu chake bila shida yoyote ile, kwa hivyo anaweza hata akapanga safari za miaka 10 za wageni wake. Kwa hivyo hayo ndiyo mageuzi ya hunt more for less ambayo tumeyafanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na mageuzi hayo, inakuja issue ya kuanzisha utaratibu wa kugawa vitalu kwa njia ya mnada. Tumeona tuweke utaratibu wa kugawa vitalu kwa njia ya mnada wa kielektroniki, mnada ambao utawafaidisha watu wa ndani ya nchi lakini pia hata wa nje ya nchi. Lengo ni kuongeza ushindani ili tupate bei kubwa zaidi kwa kila kitalu ambacho tutakiuza, lakini pia lengo ni kuweka uwazi zaidi, kuongeza more transparency ambayo ilikuwa ikilalamikwa sana. Ilikuwa ukiwa Waziri wa Maliasili na Utalii siku ya kwanza ukipiga hodi Wizarani, basi kuna makampuni mawili yatakutembelea hapo na yatakapoondoka yatakuachia briefcase zenye dollar za kutosha. Sasa huo utamaduni tulikuwa tunasikia hizo hadidhi, kwa hiyo mimi nilipoingia pale nikasema hapana, mimi sitaki kukutana na wafanya biashara tutaweka utaratibu ambao ni wazi, utaratibu ambao utatoa haki kwa kila mtu na mimi sitaki kuwa na contact na mfanya biashara. Wao wakutane na mnada kwenye mtandao wa-bid na atakayeshinda ndiyo ameshinda, hakuna haja ya kumjua Waziri ili uweze kupata kitalu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo huo uwazi pia tunaamini utavutia sana wawekezaji kwa sababu watakuwa na uhakika wa kupata kitalu kama amefika ile bei ambayo tunaitarajia. Kwa hivyo haya ni mageuzi ambayo nilipenda kuyasema, na kwamba si kwamba matamko ya Waziri yameweza kutikisa biashara hii. Leo hii nafikiri mmeona bajeti yetu inavyoenda vizuri hakuna malalamiko sana kutoka kwa wadau, wadau wameridhika na wadau wenyewe wanatusifia. Ukienda kuangalia kwenye mitandao hotuba zao wanazotoa wanasifia, wanasema Wizara sasa iko stable, biashara imekuwa nzuri zaidi kuliko kipindi chochote kile katika historia ya Wizara ya Maliasili na Utalii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata ninyi wenyewe ni mashahidi, bajeti yetu imefika hapa Wabunge wengi wamechangia, wametupa pongezi tunawashukuru, tunazipokea lakini kiukweli credits hizi ziende pia kwa wadau wetu kwa sababu wamekuwa wakitupa ushauri na sisi tulikuwa tunatega masikio vizuri, tunajaribu kuielewa biashara na tunajaribu kufanya maamuzi ambayo yana faida kwa Serikali na faida pia kwenye sekta yenyewe kwa ujumla wake. Hiyo imesaidia sana hata migogoro humu na Waheshimiwa Wabunge imekuwa midogo kwa sababu tumejifunza sana kusikiliza na kufanya maamuzi ambayo yanakubalika na wadau wote. (Mkofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, uhifadhi na ulinzi wa maeneo ya wanyamapori tumeuimarisha sana. Nilisema jana katika hotuba yangu hapa, kwamba tumeunda Jeshi Usu, tumefanya transformation kubwa sana katika eneo hili sasa tuna Jeshi Usu imebakia tu Mheshimiwa Rais kuwavisha vyeo wale Makamishna. Kwa hivyo leo hii sisi kwa mfano TANAPA mmezoea kumuita Mkurugenzi Mkuu Kijazi, leo hii yule ni Kamishna wa Uhifadhi ni Conservation Commisioner (CC), ndiyo cheo chake si tena Mkurugenzi Mkuu. Hivyo hivyo kwa TAWA, TFS, kwa Ngorongoro, wale ni Makamishna wa Uhifadhi ni Conservation Commissioners. Kwa hivyo hii ni matokeo ya mabadiliko makubwa tuliyoyafanya ya kuji-transform kutoka kwanye mfumo wa kiraia kwenda kwenye mfumo wa Jeshi Usu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru sana Majenerali ambao ni Wenyeviti wetu wa Bodi za Taasisi hizi, lakini pia Major General Milanzi ambaye alikuwa Katibu Mkuu wetu wakati mimi nateuliwa kuwa Waziri kwa sababu walitupa sana inputs za kuweza kutufikisha kukamilisha mchakato wa kuwa Jeshi Usu na wanaendelea kulilea jeshi hili mpaka litapokuwa imara. Tunatoa mafunzo kwa watu wetu, tunaimarisha Kikosi Kazi cha Taifa dhidi ya ujangili ambacho kinafanya kazi kubwa na nzuri sana ya kizalendo ya kuimarisha ulinzi lakini pia kufanya ufuatiliaji wa majangili. Sasa hivi kwa kweli ukitembea, alisema jana Mheshimiwa Catherine Magige, ukitembea huko utakutana na wanyamapori wanazunguka kila kona. Wanyamapori juzi wamezunguka pale Mvomero, mara mwezi uliopita tulisikia wako pale Morogoro Mjini kabisa, wamekuwa kila sehemu wanaenda wana amani hakuna mtu anayeweza kuwa-shoot na kuweza kupata nyama kwa sababu tunafuatilia kwa ukaribu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiwa jangili ukikutwa na nyara ya Serikali utapata kifungo tu, hakuna namna utakwepa. Vitendo vya rushwa tumevidhibiti kwa kiasi kikubwa kwa sababu kikosi kazi kina watu kutoka vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama. Kila mmoja anamwogopa mwenzake, hakuna mtu anayeweza kuthubutu kuchezacheza na kesi ya ujangili hata kidogo. Ujangili wa misitu tumeudhibiti kwa kiasi kikubwa; alizungumza Mheshimiwa Dkt. Sware Semesi, kwa kweli tuko vizuri sana. Hata kwenye eneo la biashara ya mbao naona muda umeniishia ningefafanua zaidi lakini tuko vizuri sana, tumedhibiti sana ujangili wa mazao ya misitu na tunafanya mabadiliko makubwa sana kwenye sekta ya misitu kwenda kwenye hiyo mamlaka ambayo umeizungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kubadilisha mfumo mzima wa kupata mkaa kwa ajili ya matumizi kwenye majiji makubwa, namna ya kuufungasha mkaa, namna ya ku-cross check, namna ya kuvuna, namna ya matanuri yale yatakayokuwa yote haya tumeshafanyia kazi na tumeshatunga Kanuni. Kimsingi tuko katika hatua sasa za utekelezaji tu wa mageuzi haya. Tumefanya mabadiliko makubwa sana kwenye eneo hilo nilipenda nigusie hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa kweli uhifadhi na ulinzi wa maeneo haya umeimarika sana na nadhani kuliko kipindi chochote kile katika historia ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi tuna uhakika kwamba tembo akifa ataoza hapo na tutakuta meno ya tembo yako pale pale. Imejitokeza mara kadhaa, imejitokeza kule Loliondo tembo walipata ugonjwa karibu tembo sita walipata kamlipuko fulani nafikiri ilikuwa ni bacillus anthracis na wote wakafa pale na meno ya tembo yote tuliyakuta intact kwenye mizoga ya tembo. Hakuna mtu aliyeenda kuyaokota ili afanye biashara. Kwa hivyo leo hii kesi ambazo tunahangaika nazo ni za meno ya tembo ya zamani, hakuna kesi mpya, fresh cases za mtu ambaye emeenda ame-shoot tembo leo ama ame-shoot faru leo ni za kuhesabu. Yaani sijapata repoti ya hizo kesi zaidi ya mwaka; kwa hiyo ninaweza nikasema ni negligible, kwa hivyo kazi ya ulinzi imeimarika sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Eneo la Masoko. Tumejiimarisha sana katika kutangaza vivutio vya utalii hapa nchini na mkakati wetu wa kwanza ni kama nilivyosema ni kuongeza mazao ya utalii, kufanya geographical diversification kwenda kwenye maeneo mengine zaidi ya utalii, lakini pia kutumia mbinu za kisasa zaidi kujitangaza ikiwemo kutumia mitandao na kutumia watu mashuhuri. Tumeanzisha Tanzania Safari Channel na itakwenda kimataifa Waheshimiwa Wabunge msifikirie itakuwa local, na productions zake zita-improve. Mheshimiwa Sugu alitupiga mawe hapa asubuhi, productions zake zita-improve sana, tutafanya production tofauti na hizo unazoziona leo. Haya ni material ya zamani lakini ni material tutakayoyatoa baadaye na hususan tutakapoanza kwenda global yatakuwa mazuri zaidi, yako kimkakati zaidi na yatakidhi matakwa ya ulichokuwa unakisema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kutumia watu mashuhuri, Mbwana Samatta ni balozi wetu wa utalii alizungumza Mheshimiwa Molel. Ni balozi wa utalii tumeshamteua na hiyo kazi anayofanya ni sisi ambao tunashirikiana naye kumwelekeza namna ya kutumika vizuri. Kwamba Bendera ya Tanzania ionekane, ataje Tanzania mara nyingi, azungumze Kiswahili mara nyingi, awaalike wachezaji wenzake mashuhuri kuja Tanzania lakini pia hata Timu yenyewe ya KRC Genk tupo katika mazungumzo nao ili kuwaalika waje wacheze mechi hapa kama ambavyo Simba jana imecheza na Sevilla na mitandao yote ya kula Spain inazungumzia inataja neno Simba, inataja neno Tanzania. Ndicho tunachokitaka, more visibility, tuonekane zaidi, ndicho tunachokitaka kwa kutumia michezo. Tumefadhili AFCON, tumeshiriki AFCON, tume-brand uwanja wa Taifa, ni mambo mengi tumeyafanya katika eneo hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hizo kuna roadshows ambazo ziko targeted ambazo tunazifanya katika nchi mbalimbali za kimkakati kama China, Australia, Russia, India, pamoja na Israel na ndiyo maana mnaona wageni hawa wanakuja kwa China peke yake mwaka huu tutafanya roadshows takriban tatu, tumefanya roadshow moja hiyo iliyofanyika mwaka jana October, tutafanya nyingine mwezi Juni, tutafanya nyingine mwezi Novemba. Lengo letu kwa China peke yake tuweze kupata watalii wasiopungua 500,000 ndani ya miaka miwili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunivumilia, naomba nihitimishe tu kwanza kwa kukushukuru wewe mwenyewe kwa kunivumilia, lakini pia kwa kunipa fursa hii na naomba nimalizie tu kwa kutoa hoja.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 - Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa hii. Naomba nichangie kidogo Hoja hii ya Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia kwenye maeneo mawili, eneo la kwanza linahusu hoja ambayo ipo katika kitabu cha Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani kwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, ambapo kwenye ukurasa wa 17 na kuendelea anazungumzia kuhusu uteuzi wa wanajeshi, ama wanajeshi ambao bado ni wanajeshi au wanajeshi waliostaafu kwenye nafasi mbalimbali za kiuongozi kama wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msemaji huyu wa Kambi Rasmi ya Upinzani anazungumzia kwamba hii ni sawasawa na dhana ya politicization of the Army. Napenda kupingana naye kwa sababu politicization of the Army haipo katika zama hizi kwenye nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema haipo kwa sababu kinachofanyika kwa sasa kimsingi ni kwamba Mheshimiwa Rais anatumia mamlaka yake ambayo yamekuwa provided for kwenye Katiba yetu kuteua watu ambao anaona watafaa kwenye maeneo mbalimbali ya uongozi na kuwapa madaraka ya kumsaidia kazi ya kuongoza nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna maeneo yamekaa kimkakati (strategic regions) kama Kigoma ni mpakani, Kagera pamoja na maeneo ya Ruvuma. Maeneo ambayo yamekaa kimkakati kwa maana ya kiulinzi zaidi Mheshimiwa Rais anaona watu ambao wana inclination ya kijeshi aidha ni wanajeshi au ni wanajeshi wastaafu wanafaa kwenda kumsaidia kuongoza katika maeneo yale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri anayofanya.
T A A R I F A . . .
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kitabu hakuna mahali ambapo wanaelezea mwanajeshi hata mmoja ambaye ameteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Mkuu wa Mkoa ambaye amekiuka taratibu anazozizungumza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi, tunachokiona ni kwamba Mheshimiwa Rais amewateua watu ambao anaona watafaa kumsaidia kutekeleza majukumu yake ya kuongoza nchi yetu na kulinda mipaka yetu na kuleta amani ndani ya nchi na kusaidia kuleta amani kwa watu ambao wanatuzunguka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huo nashindwa kuelewa wanatoa wapi dhana kwamba Jeshi letu linakuwa politicized. Kwa sababu hawezi leo hii Mheshimiwa Waitara kuweka Mezani hapa hata photocopy tu ya kadi ya mwanajeshi hata mmoja ambaye amejiunga na CCM, hawezi kuweka Mezani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachoweza kuzungumzika ni kwamba anahisi kwa sababu kwenye Katiba ya CCM ukiwa Mkuu wa Mkoa ama Mkuu wa Wilaya unakuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi anahisi na hao wanajeshi pengine baada ya kuteuliwa kushika haya mamlaka mbalimbali kama Mkuu wa Wilaya ama Mkuu wa Mkoa basi wanaingia kwenye vikao vya Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna ushahidi wowote wa hilo na naweza kusema kwamba kwa sababu Ilani inayoongoza Taifa letu ya mtu ambaye amechaguliwa na wananchi, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ni ya Chama cha Mapinduzi na ili ilani hii isimamiwe na chama ambacho kinaongoza dola ni lazima wale ambao wamepewa nafasi ya kusimamia utekelezaji wa ilani hiyo waweze kutoa taarifa ndani ya chama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama italazimika Mkuu wa Mkoa kwenda kutoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi kwenye Kamati ya Siasa na yeye ni mwanajeshi, atakwenda kutoa taarifa hiyo. Kwa sababu huwezi kutenganisha uongozi wa nchi hii ambao Chama cha Mapinduzi kimepewa dhamana na wananchi kupitia kura kwa kumchagua Mheshimiwa Rais anayetokana na Chama cha Mapinduzi na utendaji wa kila siku wa chama, haiwezekani, ni dhana ambayo haipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kwamba, Chama cha Mapinduzi kilimsimamisha Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Rais akachaguliwa na wananchi na baada ya kuchaguliwa sasa anatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama chake, watu aliowateua ni lazima waende wakakieleze chama nini wanafanya kwenye nafasi mbalimbali walizopewa kwenye maeneo yao. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Awali ya yote napenda nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia afya njema na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu ili niweze kujibu hoja mbalimbali za Waheshimiwa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, nakuomba uje mbele hapa.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Pili, napenda kutumia nafasi hii kwa heshima na taadhima ya hali ya juu kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniamini na kunipa nafasi ya kuwatumikia wananchi wa Tanzania katika Sekta ya Afya na Maendeleo ya Jamii kama Naibu Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namshukuru sana Mheshimiwa Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kusimama kidete kuhakikisha ndoto za wananchi wa Tanzania za kupata maendeleo endelevu zinafikiwa. Vilevile namshukuru kwa namna ya kipekee bosi wangu Madam Boss Lady Waziri wa Afya na Binamu yangu Mheshimiwa Ummy Ally Mwalimu kwa kunipa ushirikiano wa hali ya juu katika jukumu hili nililopewa na Mheshimiwa Rais la kumsaidia kusimamia na kuongoza Wizara hii nyeti nchini kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa shukrani za kipekee kwa wananchi wa Jimbo langu la Nzega Vijijini kwa kuniwezesha kufika hapa nilipo. Pia namshukuru sana Mke wangu mpenzi Dkt. Bayoum na watoto wetu Sheila, Hawa na HK Junior, nafahamu Mama Sheila uko hapa kunipa support. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile nakushukuru wewe mwenyewe kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge hili, lakini pia kwa namna ya kipekee kumpongeza Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti wote wa Bunge kwa uongozi madhubuti mnaotoa na ushirikiano mnaotupa katika kutekeleza majukumu yetu hapa Bungeni. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namshukuru Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na Waheshimiwa Wabunge wote kwa ushirikiano wanaonipatia katika kutekeleza majukumu yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwapongeza watumishi wote wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakiongozwa na Katibu Mkuu Idara Kuu ya Afya, Dkt. Mpoki Ulisubisya na Katibu Mkuu Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Mama Sihaba Nkinga na wafanyakazi wote wa Sekta za Afya na Maendeleo ya Jamii kwa kazi yao nzuri wanayofanya na naomba tuendelee kufanya kazi kwa uadilifu, uaminifu na uhodari wa hali ya juu ili tuweze kufikia malengo, tusimwangushe Mheshimiwa Rais pamoja na Wabunge wenzetu, Madiwani na wananchi wote wanaotutegemea sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa maandishi na kwa kusema hapa Bungeni, kwa hakika michango yao inalenga kuboresha huduma za afya na maendeleo ya jamii nchini.
Kama mlivyoona Waheshimiwa Wabunge hoja zilizotolewa ni nyingi sana, lakini muda tuliopewa hautoshi kujibu hoja zote, nafahamu Mheshimiwa Waziri atajibu kwa mapana na marefu, lakini nami nimeona nichangie kwenye hoja hii angalau kwa kutoa ufafanuzi kwenye maeneo machache kama ifuatavyo na majibu ya kina ya hoja zote ambazo zimetolewa hapa yatawasilishwa Bungeni kwa Waheshimiwa Wabunge kwa maandishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja kuu ambayo imejitokeza hapa ni hoja ya namna ya ku-finance mfumo mzima wa afya. Kuna namna nyingi ambazo nchi mbalimbali duniani zinagharamia mifumo yake ya kutoa huduma za afya kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mfumo wa kutumia kodi, kuna mfumo wa kutumia pesa za wanaotaka huduma kulipia huduma hizo hospitalini kuna mifumo ya kulipia huduma kabla hujatumia. Hapa nazungumzia mifumo ya Bima ya Afya, mifumo ya kuchangia namna hiyo na Tanzania kwa kiasi kikubwa mfumo wetu unategemea zaidi pesa kutokana na kodi. Tuna asilimia takribani 25 ya watu ambao wanachangia kwa pesa kutoka mifukoni mwao pale ambapo wanahitaji kupata huduma za afya kwenye vituo vya kutolea huduma hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kiasi kidogo sana, kuna asilimia takribani 27 ya Watanzania ambayo inafaidika kwa mifumo mbalimbali ya Bima ya Afya iliyopo katika nchi yetu. Suala hili limejitokeza kwenye michango ya Mheshimiwa Seif K. Gulamali, Mheshimiwa Zitto Kabwe, Mheshimiwa Joseph Mbilinyi (Sugu), Mheshimiwa Ester Bulaya, Mheshimiwa Lazaro Nyalandu, Mheshimiwa Taska R. Mbogo na Mheshimiwa Halima A. Bulembo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wengine ni Mheshimiwa Dua William Nkurua, Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mheshimiwa Godfrey W. Mgimwa, Mheshimiwa Agnes M. Marwa, Mheshimiwa Kunti Yusuph Majala, Mheshimiwa Zuberi M. Kuchauka, Mheshimiwa Allan J. Kiula, Mheshimiwa Amina S. Mollel, Mheshimiwa Stella Ikupa Alex, Mheshimiwa Hamidu H. Bobali, Mheshimiwa Ahmed M. Shabiby, Mheshimiwa Susan L. Kiwanga na wengine watanisamehe kama sikuwataja majina yao hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kiasi kikubwa wengi wamechangia suala la Bima ya Afya ama kwa namna moja ama nyingine gharama za huduma za afya nchini. Jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hususan ya Awamu ya Tano, ambayo inatafsiri Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, chama ambacho kimeshinda uchaguzi wa mwaka 2015 inasema kwamba: “Kufikia mwaka 2020 tutakuwa tumetoa bima ya afya kwa Watanzania wote na bima hiyo ya afya itakuwa ni ya lazima.” Sasa kuitafsiri Ilani ya Uchaguzi, sisi tuliopewa dhamana ya kutoa uongozi kwenye sekta hii, tayari tumeanza kufanyia kazi azma hiyo ambayo inaelekezwa na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua tulizochukua mpaka leo na Waheshimiwa Wabunge ni kwamba tuna mikakati ya aina mbili, kwanza tuna mkakati wa muda mrefu na mkakati huu ni wa kuelekea kuwa na mfumo mmoja wa bima ya afya nchini, mfumo ambao utakuwa ni wa lazima, mfumo ambao utataka kila Mtanzania awe na aina mojawapo ya kuchangia huduma kabla ya kutumia yaani mifumo kama ya Bima ya Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu ili hili lifanikiwe, ni lazima tuunganishe Mifuko na hili amelisema vizuri Mheshimiwa Zitto Ruyagwa Kabwe, lakini pia Wabunge wengine wamelichangia. Sasa ili kufanikisha hili, tayari tumeanza mchakato wa ndani ya Serikali kwanza kuhakikisha tuna mkakati wa kugharamia huduma za afya yaani National Health Financing Strategy, pia kuhakikisha tunaandaa mapendekezo ya sheria ya Single National Health Insurance ambayo tutaiwasilisha Bungeni ili iweze kupitishwa na Wabunge ianze kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchakato wote huu ukikamilika tunaamini itakuwa imeshapita takribani miaka miwili hadi mitatu ili sheria hiyo iweze kuanza kufanya kazi kama itapita kwenye Bunge hili. Tayari ndani ya Serikali tumeanza mchakato huo, tuna National Health Financing Strategy pia tayari tumeshaanza kuandaa Muswada huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchakato ndani ya Serikali tayari umekwishaanza na matarajio yetu ni kwamba kwenye Bunge la Septemba kama kila kitu kitaenda sawa, tutaweka mezani kwenye Bunge lako Tukufu, Muswada wa Single Health Insurance mchakato huo utaanza. Hata hivyo, kwa kutambua ucheleweshaji ambao unaweza ukajitokeza ili sheria hii iweze kuanza kufanya kazi wakati sisi tumeweka malengo ndani ya Chama cha Mapinduzi kwamba kufikia Mwaka 2020 takribani asilimia 80 ya Watanzania wawe na Bima ya afya ya aina moja ama nyingine, tumeona tuanze kutekeleza mpango wa haraka na wa muda mfupi wa kufanya maboresho ya lazima kwenye mfuko wa kuchangia huduma za afya wa CHF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuanze kutekeleza hayo kwa sababu hatufanyi mabadiliko yoyote yale ya kisheria, tayari tuna Sheria ya CHF ya mwaka 2001, pia tuna sheria ya National Health Insurance Fund ambazo zinaishi na zinafanya kazi, tutafanya maboresho ya ki-program ya kiutekelezaji hapa na pale ili wananchi waweze kupata huduma bora zaidi za afya haraka zaidi wakati tukijipanga kutekeleza mpango huo ambao utakuja kwenye hiyo Sheria ya Single National health Insurance ambayo itaweka ulazima kwamba kila Mtanzania ni lazima awe na bima ya afya. Mabadiliko ambayo tunayafanya kwenye CHF iliyoboreshwa, siyo mabadiliko ya ajabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nafahamu Waheshimiwa Wabunge miongoni mwetu tunaweza tukawa ni beneficiaries wa mabadiliko hayo ambayo yameanza kufanyiwa kazi na taasisi mbalimbali ambazo zinafanya kazi kwa ukaribu na Wizara yetu katika baadhi ya mikoa hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto mbalimbali za kwenye CHF kama vile changamoto ya portability kwa maana ya kuhama na card ya CHF kutoka kwenye ngazi moja ya huduma kwenda kwenye ngazi nyingine itapatiwa ufumbuzi, maana hapa tunazungumzia kwenye maboresho haya mtu akiwa na card ya CHF kutoka kijijini aweze kupata huduma za afya kutoka kwenye ngazi ya zahanati, ngazi ya kituo cha afya, ngazi ya hospitali ya Wilaya mpaka kufikia ngazi ya hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa niseme, tayari kwenye yale malalamiko ya D by D sitalieleza kwa upana sana hilo Mheshimiwa Waziri alifafanua. Tayari tumeanza mchakato wa ndani ya Serikali kutafuta namna ya kuzichukua hospitali za mikoa na kuziweka chini ya Wizara ya Afya, ili mfumo wa rufaa uwe chini ya Wizara ya Afya lakini mfumo wa afya ya msingi ubaki chini ya TAMISEMI.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa kuna mantiki kubwa sana. Chini ya TAMISEMI kuna uwakilishi wa wananchi na uwakilishi huo wa wananchi ni lazima. Hatuwezi kuwa na haki na usawa kwenye nchi kama wananchi hawashirikishwi kwenye kufanya maamuzi mbalimbali. Huu ndiyo msingi wa falsafa ya D by D, ugatuaji wa madaraka maana yake tunashusha nguvu za kufanya maamuzi kwenye mikono ya wananchi kwenye Halmashauri zetu, kwenye Kata, Kwenye Vijiji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi ku-defeat the whole purpose ya kuwa na D by D kwa kutaka kufanya mabadiliko tu makubwa ya kiutendaji kwenye mfumo wa afya, lakini kwenye hospitali za mikoa uwakilishi wa wananchi haupo ndiyo maana tumesema hizi tunaweza tukazihamisha kutoka TAMISEMI tukazipeleka chini ya Wizara ya Afya na mfumo wa rufaa kwa ujumla wake ukawa chini ya Wizara ya Afya na ukafanya kazi vizuri zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwenye maboresho ya CHF tutaweza kumpatia huduma Mtanzania kutoka ngazi ya Zahanati mpaka ngazi ya hospitali ya Rufaa ya Mkoa. Tayari mchakato huu umekamilika na card zitakuwa ni za kielektroniki, tunasubiri mchakato ndani Serikali wa kufanya maamuzi ukamilike tuweze ku-launch mradi huu mkubwa wa maboresho ya CHF.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Susan Lyimo alizungumzia kwamba mimi ni Balozi wa Wanawake kwa nini sikukemea kauli iliyotolewa humu ndani? Naomba nimhakikishie tu kwamba Ubalozi wangu uko pale pale na dhamira yangu ni safi. Yaliyotokea ndani ya Bunge kwa bahati mbaya sana yalitokea wakati sipo, lakini tayari utaratibu wa Kibunge ulishalifanyia kazi suala hilo na hivyo siwezi kuliingilia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kupandisha hadhi vituo. Waheshimiwa Wabunge wote ambao mna vituo mnataka vipandishwe hadhi, andikeni barua kwa Waziri wa Afya na kesho mnikabidhi, nita-assign Idara Maalum ya Ukaguzi iliyoko chini ya Wizara yetu ipite kwenye Majimbo yenu ikague hospitali, zahanati na vituo vya afya vyote na kisha imshauri Mheshimiwa Waziri wa Afya kama kweli kuna haja ya kuvipandisha hadhi ama la. Naomba mtekeleze hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu taasisi ya Saratani ya Ocean Road, tuna mpango kabambe wa kufanya maboresho makubwa kwenye taasisi hii, hili ni jambo ambalo limewagusa Waheshimiwa Wabunge wengi hata sisi linatugusa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka kwa mara ya kwanza Mheshimiwa Waziri wa Afya alipotembelea hospitali ya Ocean Road alitoa machozi jinsi alivyokuta wagonjwa wale wanapata madhila makubwa kwenye huduma za afya. Tayari tumejipanga kununua mashine mpya ya LINAC ambayo tutaifunga kwenye jengo jipya ambalo amelizungumzia Mheshimiwa Rashid Ally Abdallah. Hata hivyo, pia tumetenga bilioni saba kwa ajili ya dawa, kwa hivyo yale matatizo ya chemotherapy aliyokuwa anayazungumzia kwenye mwaka wa fedha unaokuja yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi wa uhakika.
Mheshimiwa Susan Mgonokulima alizungumzia kuhusu viroba, namwagiza hapa Mkurugenzi Mkuu wa TFDA aende akafanye uchunguzi wa kitaalam wa kemikali na kiwango cha alcohol kilichomo kwenye viroba kwenye viwanda mbalimbali vya viroba nchini na aniletee taarifa ndani ya siku 14. Mheshimiwa Mwakibete na Mheshimiwa Joseph Mbilinyi (Sugu) CT- Scan kwa ajili ya hospitali ya Rufaa ya Mbeya, tayari tumeshatoa maelekezo nilipokuwa nimefanya ziara pale Mbeya Rufaa takribani miezi miwili iliyopita ili muweze kupatiwa CT Scan machine.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, na mimi nianze kwa kuunga mkono hoja ya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2017/2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuchangia naomba kwanza niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote, kwa kutoa michango yao kwenye mambo mbalimbali yanayohusu uboreshaji wa huduma za afya nchini. Niwahakikishie tumesikiliza kwa makini na tutayafanyia kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi napenda kutoa mchango wangu kama ifuatavyo; kwamba wakati tunaomba kura mwaka jana sisi wa Chama cha Mapinduzi tulizungumzia sana kuleta mabadiliko ya kweli kwenye nchi yetu, na tulipoweka mkakati huu wa kuzungumzia kuleta mabadiliko ya kweli, siyo tu mabadiliko kama waliyozungumzia wenzetu, tulijua wazi kwamba mabadiliko yanakuja na maumivu, na tulijua wazi kwamba mabadiliko yatakuja tu kama kutakuwa kuna uwajibikaji na watu watafanya kazi ipasavyo. Pia tunatambua kuwa mabadiliko ni lazima yatokee, kwa sababu kama kuna kitu kina uhakika wa kubadilika basi ni mabadiliko yenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, toka Serikali ya Awamu ya Tano imeingia madarakani, Rais wetu Dkt. John Pombe Magufuli, amepata heshima kubwa sana kwenye duru za Kimataifa kwa kuimarisha mifumo ya uwajibikaji kwenye nchi yetu, lakini pia kwa kurejesha nidhamu ya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwongozo anaoutoa Mheshimiwa Rais, umetuwezesha sisi wa Wizara ya Afya kuboresha huduma kwa kiasi kikubwa sana kiasi kwamba utafiti wa TWAWEZA ambao uliwasilishwa takribani miezi miwili iliyopita umeonesha kwamba sekta ya afya inatoa huduma bora, na hii ni kwa mujibu wa utafiti wa sauti za wananchi ambapo wananchi wametoa feedback hiyo, kwamba huduma za afya zimeboreka kwa sababu ya uwajibikaji wa Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo napenda kuchangia ni kuhusu nia njema ya Serikali kwenye eneo la kuongeza upatikanaji wa dawa nchini. Nia hii inajionyesha wazi kwa Serikali kutenga bajeti ya shilingi bilioni 251.5 ambayo imeanza kutekelezwa mwezi julai mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti hii shilingi bilioni 70 ndani yake zitakwenda moja kwa moja kununua dawa kwa ajili ya kupeleka kwa wananchi, na mpaka sasa Wizara ya Afya imekwisha pokea shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kununua kuanza kupeleka…
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye eneo la dawa Serikali pia inaimarisha upatikanaji wa dawa za chemotherapy yaani dawa ya huduma za kansa kwa tiba ya kemikali ambapo mwaka huu tuna shilingi bilioni saba ukilinganisha na shilingi bilioni moja iliyekuwepo mwaka jana. Kwahiyo naomba Waheshimiwa Wabunge watuamini tuna nia njema ya kuboresha huduma za afya nchini, na kufikia mwezi wa 12 tunaahidi tutakuwa tumewezesha upatikanaji wa dawa wa asilimia 85 ukilinganisha na asilimia 63 tuliyonayo kwa sasa.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Pia namshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kutupa fursa na sisi tutoe michango yetu kwenye hoja aliyoiweka mezani. Nampongeza zaidi yeye na Mawaziri waliopo kwenye Wizara yake kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kufanya na kwa miongozo mbalimbali ambayo wamekuwa wakitupa katika utekelezaji wa majukumu haya mazito tuliyopewa na Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitambue michango mingi ya Waheshimiwa Wabunge iliyotolewa kwenye sekta ya maliasili na utalii. Niseme tu kwamba michango yote tumeipokea, tunaifanyia kazi na zaidi maelezo ya kina tutayatoa wakati wa hotuba yetu ya bajeti ili kuwekana vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, naomba nitoe ufafanuzi kwenye mambo machache yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa lililojitokeza katika michango mbalimbali ya Waheshimiwa Wabunge ambalo napenda kulitolea ufafanuzi ni hoja iliyotolewa na Mheshimiwa Chegeni, Mheshimiwa Njalu, Mheshimiwa Gimbi na Waheshimiwa Wabunge wengine kuhusiana na migogoro ya wafugaji na Hifadhi za Taifa. Naomba hapa nizungumzie pia jambo zima linalohusiana na zoezi la mipaka na utatuzi wa migogoro hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia maelekezo ya Serikali yaliyopitia kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye mipaka yote ya maeneo yaliyohifadhiwa tumeweka vigingi (beacons) ambazo zinayatambua maeneo ya hifadhi na kuonesha maeneo ya vijiji yanaishia wapi. Mpaka sasa tumefanikiwa kuweka takribani vigingi 27,942 sawa na asilimia 79 ya malengo tuliyojiwekea ya kuweka vigingi katika maeneo yote yaliyohifadhiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi hii kubwa ambayo imefanyika, bado kuna changamoto zinajitokeza. Changamoto ya kwanza kubwa ambayo tunaipata ni kwamba kuna wananchi walikuwa wakiishi katika maeneo ya hifadhi ama wakifanya shughuli mbalimbali katika maeneo ya hifadhi wakiamini ni maeneo ya vijiji. Pamoja na mwongozo aliotupa Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba beacon ziwekwe tu kwanza halafu baadaye tutazungumza na wananchi nini litakuwa suluhisho kwa yale maeneo ambayo tayari wamekuwa wakiyatumia na sisi tumekuwa tukifanya hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hapa naomba nitumie fursa hii kuwaondoa wasiwasi Waheshimiwa Wabunge wote pamoja na wananchi kwa sababu tunafanya kazi sasa baada ya zoezi la kuweka vigingi kukamilika ya kupita kwenye maeneo hayo ambayo yanaonekana aidha vigingi vimeingia kwenye maeneo ambayo wananchi wamekuwa wakiyatumia ama kwenye yale maeneo ambapo hifadhi imeingia ndani zaidi kuliko ambavyo ilikuwa kabla hatujafanya zoezi la uhakiki wa mipaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi hiyo tumeanza kuifanya na tunaifanya sisi wenyewe, mimi na mwenzangu Mheshimiwa Naibu Waziri hatua kwa hatua tunakwenda kwenye eneo moja baada ya lingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, migogoro mingine unakuta eneo ambalo limehifadhiwa na linatumika kwa matumizi ya shughuli mbalimbali za kibinadamu ni dogo sana. Kibinadamu tumeanza kufikiria kufanya variation ya mipaka yetu na kuyaacha nje maeneo haya ili wananchi waweze kuyatumia kama tunaona kiikolojia hakuna madhara yoyote yale yatakayojitokeza ili tupunguze migogoro ambayo tumekuwa tukiipata baina ya wahifadhi na wananchi ambao ni majirani zetu kwenye maeneo yaliyohifadhiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hilo, kuna maeneo mengi ambayo yalitangazwa kama maeneo ya hifadhi ambayo yamekuwa yakitumika kwa muda mrefu sasa kwa shughuli mbalimbali za kibinadamu. Maeneo haya tumeshaamua kuyaachia, baadhi ya maeneo hayo yana Ranchi za Taifa, viwanja vya ndege na vijiji ambavyo vimetangazwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, katika ile ripoti tuliyopewa na wataalam wa tume iliyoundwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, tayari kuna maeneo takribani 14 tumeyaachia lakini pia kuna maeneo mbalimbali kama alivyozungumza ndugu yangu Mheshimiwa Vuma tumepewa miongozo na viongozi wetu wakuu kwa mfano Mheshimiwa Rais alisema tuachie eneo la msitu wa kule Kagera Nkanda na tumeshaamua kuachia eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kinachofanyika sasa ni kufanya variation ya mipaka ili tuweze kutangaza rasmi lakini hatuna taarifa za wananchi kunyanyaswa katika maeneo ambayo tayari tumekwishatoa mwongozo wa kuyaachia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo hivyo kuna maeneo ya Mkungunero, kuna baadhi ya maeneo ambayo tumeona kwamba tunapaswa kufanya variation ya mipaka na kuyaachia ili wananchi ambao waliokuwa wanayatumia kwa muda mrefu waendelee kuyatumia kwa sababu hata kama kwa mujibu wa sheria siyo eneo lao, lakini wao wanaamini ni eneo lao. Kwa hivyo, mgogoro hautakwisha kwa sababu wahifadhi wataendelea kuamini kwamba wananchi wamevamia eneo lao, wakati na wananchi wanaendelea kuamini kwamba ni eneo lao hata ukiwaambia nini hawakuelewi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, katika jitihada za usuluhishi ambazo tunazifanya ni pamoja na kukubali kuachia baadhi ya maeneo au kubadilisha baadhi ya maeneo. Kwa mfano, kule Utete tumeachia eneo la Msitu wa Kale na tunafanya sasa taratibu za kurekebisha ili lirudi kwa wananchi lakini tumewaomba Halmashauri watupe eneo lingine lililopo mbali zaidi na mipaka ya mji ili tuweze kulihifadhi ku-compensate kwa eneo ambalo tumeliachia, kwa hivyo jitihada hizo zinaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni kuhusu migogoro baina ya wanyamapori ambao wanatoka katika maeneo ya hifadhi na kwenda kwenye maeneo ya wananchi. Kwanza hapa changamoto kubwa ambayo inajitokeza ni kwamba wananchi wengi katika miaka ya hivi karibuni wamekuwa wakifanya shughuli zao za kibinadamu aidha kwenye shoroba ambazo ni mapito ya wanyamapori ama kwenye maeneo ya karibu sana na buffer zone, eneo kinga la maeneo yaliyohifadhiwa ambazo ni mita 500 tu. Wanyama hawajui mipaka ambayo tuliojiwekea sisi binadamu wamekuwa wakitoka kwenda kwenye maeneo ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, tunatoa elimu ya wananchi kuzungusha mizinga ya nyuki kwenye maeneo ya mashamba yao kwa sababu wanyama kama tembo huwa wanaogopa uwepo wa mizinga ile na kurudi kwenye maeneo yaliyohifadhiwa ili wananchi waweze kuepukana na migogoro ambayo inayosababishwa na wanyama hao.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunazidi kujenga madungu ama observation towers kwenye maeneo ya jirani na maeneo wanayoishi wananchi hususani maeneo korofi kwa mfano kule Itilima ambako juzi kumetokea maafa na kule Bunda kwenye Vijijji vya Kihumbu, Hunyali na Maliwanda ili askari wetu waweze kuwa-track wanyamapori aina ya tembo ambao wamekuwa wakizoea kwenda maeneo ya vijiji na kuweza kuwarudisha kwa kutumia teknolojia za kisasa kama teknolojia ya kutumia drones kwenye maeneo ya mipaka…
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili nami nitoe mchango wangu kwenye Bajeti Kuu ya Serikali kufuatia hotuba ya hoja ya bajeti ambayo iliyowasilishwa na Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba Madelu wiki iliyopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ameendelea kutoa uongozi uliotukuka katika taifa letu kwa muda huu mchache ambao ameanza kufanyakazi kama Rais. Kama ingekuwa kwenye mchezo wa mpira tungesema mama anaupiga mwingi sana kwa jinsi ambavyo anachukua hatua nyingi mbalimbali ambazo ni sahihi kwa nyakati sahihi. Nasema hivyo, kwa mfano hili ambalo amelizungumza Mheshimiwa Sanga (Jah People); kwamba mama jana tu ametoka kuzungumza kwamba riba kwenye mabenki ishuke na isiwe zaidi ya asilimia 10, hilo tu peke yake ni jambo kubwa sana kwenye kuchochea ukuaji wa uchumi katika taifa letu, hilo tu na mengine mengi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia hatua mbalimbali ambazo zimewekwa kwenye bajeti ya mwaka huu zinaonesha wazi kwamba mama ana dhamira ya dhati kabisa ya kutaka kukuza uchumi, kuchochea ukuaji wa uchumi, kutoa ajira nyingi pamoja na kuboresha huduma za kijamii kwa watu wetu; na kwa hili nina kila sababu ya kumpongeza Mheshimiwa Mama yetu Samia Suluhu Hassan. Lile alilolisema Mheshimiwa Sanga kwamba watu waache kufikiria mambo mbalimbali nadhani halipo. Mama anafanyakazi nzuri na sidhani kama kuna mtu ambaye atajaribu kukiuka utaratibu ambao tumejiwekea kwenye chama chetu, kuvuta fomu ya kuomba nafasi yoyote ile ya juu mwaka 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo kwa wale Wabunge wenzangu tuendelee kupambana majimboni, kwa wale ambao ni Mawaziri wapo kwenye front bench waendelee kupambana majimboni, waendelee kuchapa kazi wamuache mama afanyekazi kwa sababu anafanyakazi nzuri, na hakuna sababu ya kutikisa Taifa kwa uchaguzi ama kwa fununufununu zisizo na maana katika kipindi hiki ambacho mama anafanya mabadiliko makubwa katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ya kwanza baada ya utangulizi ni kwamba, taifa ili liendelee linahitaji mambo mengi, lakini katika mambo makubwa ambayo taifa linapaswa kuyatumia kama chachu ya kuleta maendeleo ni pamoja na maliasili zake (natural resources). Natural resources zinapaswa kuwa chanzo cha taifa lolote lile kuendelea. Sisi tumejaaliwa gesi lakini pia tumejaaliwa dhahabu. Pia taifa ili liendelee linapaswa kutumia nguvu kazi yake, kwa maana ya watu wake. Sasa haya mambo mawili ninayaona katika uchumi wetu bado hatujaya-exploit fully, hatujayatumia ipasavyo kuweza kuturusha kwenda mbele kwa kasi zaidi katika uchumi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, na nasema hivyo kwa sababu bado hatujaweza kutumia uchumi unaotokana na maliasili zetu kama dhahabu, kwa maana ya kuongeza thamani; jana tumefurahi kuona mama amezindua kiwanda kikubwa kule Kanda ya Ziwa cha kufanya refinery ya dhahabu, ni uelekeo sahihi; lakini tunaweza tukafanya vizuri zaidi ya hapo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tunapaswa tuongeze speed ya uwekezaji kwenye sekta ya gesi ili maliasili ya gesi ambayo tumejaaliwa tuweze kuitumia kwa faida, kwa maana ya kuongeza thamani ili kutengeneza mbolea na baada ya kutengeneza mbolea hiyo gesi itaenda kuwa chachu ya kukua kwa uchumi wa mkulima ambaye atatumia ile mbolea. Kwa hiyo tuna haja pia ya kuwekeza kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mbali na hivyo jambo lingine kubwa ambalo linakosekana katika uchumi wetu ni mfungamanisho (linkage) kati ya sekta ya kilimo na sekta ya viwanda; hapa tuna changamoto kubwa, na changamoto hii inasababishwa kwanza na viwango viwango vikubwa vya kodi, lakini pili kuwepo kwa regulation ya hali ya juu na Serikali kuingilia kwa kiasi kikubwa sana kwenye utendaji wa sekta ya kilimo, kitu ambacho kinasababisha biashara iwe ina imbalances nyingi kutokana na kanuni nyingi ambazo zinatungwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo ili tuweze kuendelea na kuendeleza watu wetu ambao ni zaidi ya asilimia 65 na ambapo zaidi ya milioni 40 wanategemea sekta ya kilimo ni lazima tufanye value addition, tuongeze thamani kwenye mazao yanayolimwa na wakulima wetu. Sasa tukiweza kuongeza thamani ya mazao maana yake tutakuwa tumeongeza vyanzo vya mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa hivi ilivyo uchumi wetu Pato la Taifa linachangiwa kwa kiasi cha asilimia 25 mpaka 27 na watu zaidi ya milioni 40. Kwamba wale asilimia 65 ambao wanategemea shughuli za kilimo wanaokaribia milioni 40 ya Watanzania wote wanachangia kwenye Pato la Taifa kwa asilimia takriban kati ya 25 mpaka 27 tu. Sasa hawa ni watu ambao kwanza hatuwatozi kodi, kwa sababu hakuna mchungaji anayetozwa kodi ya mifugo zaidi ya milioni 30 ambayo tunajivunia kuwa nayo, lakini pia wakulima hawatozwi kodi. Sasa ili tuweze kupata kipato kutokana na hawa watu zaidi ya milioni 40 ni lazima kuwe kuna namna ambavyo kuna value addition kwenye ile shughuli kubwa ya kiuchumi wanayoifanya ili sasa kule ndiko tukapate kodi, kwa sababu kwenye mazao hatutozi kodi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ushauri wangu ni kwamba, tunakoelekea huko itafutwe namna ya hawa watu zaidi ya milioni 40 kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye Pato la Taifa. Tutaweka kodi gani, maswali hayo wataalam wanaweza wakayatazama, lakini kwamba tutafanya nini kuna uwezekano mkubwa, kama tutafanya value addition kwa kuwezesha ujenzi wa viwanda ambavyo vinafungamanisho la moja kwa moja na shughuli ya kilimo, mifugo na uvuvi, basi kule kwenye viwanda tutapata kodi ambayo itasaidia kuchangia kwenye uchumi wa taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye fungamanisho napenda kutoa mfano, amezungumza Mheshimiwa Mbunge mmoja hapa wakati anachangia, kwamba kulikuwa kuna kongamano jana la alizeti pale Singida; na nina-declare interest, mimi nina kiwanda cha kusindika mafuta ya alizeti. Nilikijenga mwaka 2009 huko kabla sijaingia kwenye siasa. Tangu nimekijenga kiwanda hicho mpaka leo hatujawahi kufikisha uzalishaji wa mafuta kwa zaidi ya tani walau elfu 10, na kiwanda kikubwa ambacho kwa mwaka mmoja kinaweza kikafanya volume ya tani elfu 10.
Mheshimiwa Naibu Spika, sababu kubwa, ya kwanza tunafeli kwa sababu hakuna raw materials hakuna malighafi ya kuingiza kiwandani. Kwa hiyo tunaendelea kuhamasisha watu wawekeze kwenye uchumi wa viwanda, lakini watu wakiwekeza kwenye uchumi wa viwanda hakuna malighafi ya kupeleka kwenye viwanda. Sasa kwanini inakosekana malighafi ilhali Watanzania zaidi ya milioni 40 ni wakulima? Maana yake hapo kuna miss match, hapo kuna gap kubwa ambalo sisi kama Serikali tunapaswa kuliziba, tunapaswa kulifanyia kazi. Kwamba ni namna gani wakulima wetu watazalisha na hatimaye wanachokizalisha kiingie kwenye viwanda ambavyo vinajengwa? Kwa hivyo tunahitaji kufanyia kazi jambo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sababu kubwa nyingine ya pili ni kwamba, kwenye uchumi wa viwanda ukishakuwa tu mfanyabiashara kwenye nchi yetu unakuwa labeled kwamba huyu anataka kuwaibia wakulima, ana lengo baya na wakulima, anawaminya wakulima. Dhana hiyo inasababisha kwa kiasi kikubwa sana kutokushamiri kwa uwekezaji kwenye eneo la viwanda, lakini pia mahusiano hasi kati ya Serikali wakulima na wafanyabiashara; jambo ambalo kama lingerekebishwa, na ni jambo tu la mindset, basi tungeweza ku-unlock potential kubwa sana ambayo ipo kwenye uchumi ambao unategemea zaidi kilimo, kwa maana ya kufanya backward linkage kati ya kilimo na viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine kikubwa ambacho ningependa kukisema ni kwamba tax rate, kiwango cha kodi kama Mheshimiwa Mwigulu ataenda ku- review mchumi mmoja anaitwa Arthur Laffer akasoma ile Laffer Carve ataweza kutusaidia sana kama taifa kutunga viwango vya kodi ambavyo ni rafiki kwenye kukua kwa uchumi pamoja pia kwenye kuongeza kipato cha Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimalizie tu kwanza kwa kumpongeza kwa hotuba nzuri ambayo aliiwasilisha hapa; kiukweli hotuba yake ilikuwa kama muziki kwenye masikio ya Waheshimiwa Wabunge wakati akiiwasilisha na…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Haya, ahsante sana…
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALA: …ana-deserve credit zote japo kuwa Mheshimiwa Mwigulu ni Yanga hilo ndilo tatizo alilonalo tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwashukuru na ninaunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Mungano na Mazingira kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nami naomba nichangie kwenye jambo hilohilo la kuzalisha umeme kwenye Mto Rufiji na nitachangia zaidi katika muktadha wa uhifadhi na ikizingatiwa kwamba mradi huu unatekelezwa kwenye eneo la Hifadhi ya Pori la Akiba la Selous ambalo lipo chini ya Usimamizi wa Wizara yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na umuhimu na uthamani wa kipekee ambao unawekwa kwenye Pori la Akiba la Selous, lakini naomba Bunge lako Tukufu na Watanzania wote kwa ujumla watambue kwamba Selous ni rasilimali ya Taifa na rasilimali zina sifa moja ili ziwe rasilimali; zinapaswa kuleta manufaa kwa wananchi, zinapaswa kuleta manufaa kwa binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba tutambue kwamba rasilimali ambazo tumejaliwa kama urithi katika nchi yetu haziwezi kututenganisha na mahitaji ambayo sisi tunahitaji kuyapata kutokana na rasilimali ambazo tumepewa kama zawadi. Kwa hiyo, ni lazima tuwianishe uwepo wa rasilimali na maendeleo ya watu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna schools of thought mbalimbali, kuna watu wanaoamini kwamba rasilimali zihifadhiwe kama zilivyo mpaka mwisho wa dunia, lakini wanasahau kwamba na sisi binadamu ni sehemu ya dunia, ni sehemu ya ikolojia na tuna mahitaji yetu na kwa maana hiyo ni lazima na sisi tutumie rasilimali hizi. Kitu cha msingi cha kuzingatia ni kuhakikisha kwamba tunatumia rasilimali kwa uendelevu wake bila kuziharibu, bila kuathiri bionuwai nyingine iliyopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilihakikishie Bunge lako Tukufu hapa kwamba Serikali kupitia Wizara yetu imezingatia matakwa ya uhifadhi endelevu wa rasilimali iliyopo kwenye Hifadhi ya Taifa ya Pori la Akiba la Selous. Tumefanya hivyo kwanza kwa kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa kufuata misingi ya utekelezaji wa miradi. Ndiyo hiyo Environmental and Social Impact Assessment anayoizungumzia Mheshimiwa Naibu Waziri wa Nishati. Hilo ni hitaji la kwanza la lazima na tumesema itafanyika kwa haraka na ikamilike kabla utekelezaji wa mradi haujaanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili, Waziri wa Maliasili na Utalii nimeunda kikosi kazi cha Wataalam kutoka Taasisi za TAFIRI TAWIRI, TITISA na Taasisi nyingine zinazohusika na maliasili ili wafanye utafiti wa kina wa kuangalia bionuwai iliyopo katika eneo husika. Utafiti huu utatuwezesha kujua kuna species gani zipo katika eneo la utekelezaji wa mradi na tufanye nini tuweze kuzihifadhi zisipotee na nini kitatokea kama tutafanya mradi huu kwa zile species zilizopo pale. Je, species zilizoko pale ni endemic kwa maana pale ni makazi yao ya kudumu ama ni species hizi ambazo exotic ambazo zimekuja kuhamia kwa kufuata mahitaji mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiweza kuzitambua hizo species na mahitaji yake na kujua kama endemic ama ni exotic tutaweza kujua tufanye nini ili kuokoa zisipotee na ndiyo kazi ambayo sisi Wizara yetu tunafanya kuhifadhi bionuwai mbalimbali za wanyama pamoja na mimea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo kuna timu ya Wataalam iko site, inakusanya mbegu za wanyama, samaki na mimea na kila aina ya bioanuwai iliyoko pale na kuzitunza kwa ajili ya matumizi ya baadaye. Pia tumehakikisha kwenye design ya mradi kutabaki na Oxbow Lakes, maziwa ya asili yaliyoko pale, lakini pia tunaongeza maziwa mengine ambayo yatasaidia kuweka uhai wa viumbe hai ambavyo viko katika eneo lile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali iko macho na sisi wahifadhi tuko macho hatutokubali Pori la Akiba la Selou lishuke hadhi yake kwa sababu ya utekelezaji wa mradi huu. Madhara yanaweza yakajitokeza, lakini mpaka sasa hakuna anayejua ni nini kitatoke kwa sababu hakijatokea. Kwa hivyo, nyingi zinazozungumzwa hapa kwa mfano mchango wa Dkt. Sware ni nadharia tu, ni theory’s tu ni rhetoric hakuna ushahidi wa nini kitatokea kwa hakijatokea na uharibifu haujafanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo tunachokifanya kwa sasa ni kujipanga kupunguza madhara yanayoweza kutokea endapo mradi utatekelezwa ndicho tunachojipanga. Kuna nadharia kwamba joto litaongezeka kwa sababu ya utekelezaji wa mradi, kuna nadharia kwamba flow ya mto itabadilka kutokana na utekelezaji wa mradi. Zote ni nadharia, huwezi kuwa na uhakika kwamba zitaathiri mto pamoja na wanyamapori kwa namna gani, sambamba na hilo. (Makofi)
T A A R I F A . . .
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yake siipokei na sipokei kwa sababu za kisayansi kama yeye ni Dkt na mimi ni Dkt. vilevile na mimi ni mwanasayansi, nampa sababu ya kisayansi kama yeye ni daktari anaamini kwenye sayansi,, tusikilizane kama yeye ni daktari na anaamini kwenye sayansi nampa sababu ya kisayansi, hakuna haja ya kubishana kwa kelele, tulieni msikie sayansi. Anachokisema kinaweza kikatokea ndiyo ninachosema kwamba ni nadharia, ni theory hakijatokea bado kwa sababu mradi haujatekelezwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kuna kitu kitakachojitokeza ni kwamba wanyama, mimea wana kitu kinaitwa adaptation, kwenye mabadiliko yanayojitokeza. Kwa hivyo mazingira yatakapobadilika wale wanyama wanabadilisha tabia zao wanaweza waka-adapt kwenye mazingira mapya yaliyojitokeza. Kwa hiyo,hiyo ni sababu ya kisayansi na nina uhakika anaifahamu. Kwa hivyo hatuna haja ya kubishana sana kwa sababu hii ni sayansi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, awali ya yote nianze kutoa mchango wangu kwanza kwa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, mama Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea shilingi trilioni 1.3. Lakini pili niseme tu ukweli, nilihamasika kuchangia kwenye Mpango huu, awali sikuwa na mpango huo baada ya kauli yako jana, kwamba hizi shilingi trilioni 1.3 zilizoletwa na Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan zimeichangamsha nchi. Ni kwa nini na sisi tusiweke Mpango wetu wenyewe kwenye Bajeti inayokuja wa kutenga shilingi trilioni 1.3 au shilingi trilioni1.5 ya kwetu wenyewe kwenye Bajeti? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo hili kwa kweli lilinifikirisha sana na ndipo nikaona niombe kuchangia, ili kuweka msisitizo kwenye jambo hilo. Maana yake ulilisema juu juu hivi halafu likaishia pale nikasema pengine nitoe mawazo yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiukweli nakubaliana sana na hili wazo na ninasema hivi kwa sababu, ninaona kuna haja ya kufanya hivyo kutokana na mambo kadhaa ambayo nitayataja. Mojawapo kwanza ni affirmative action kwamba tutakuwa tuna Mpango mahsusi wa nini tufanye na fedha yetu wenyewe. Kwa ajili ya kusambaza keki ya Taifa kila kona ya Nchi yetu kwa maana ya kwenye majimbo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, tutakuwa na sababu mahususi za kitu gani fedha hizi ziende zikafanye. Lakini la tatu, tuna stress kubwa sana kwenye uchumi wetu kutokana na namna tulivyoendesha mambo yetu hapo nyuma. Lakini pia kutokana na kuingiliwa na mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19. Kwa hivyo, uchumi umeathirika sana, uchumi una-undergo stress kubwa sana. Kwa ambao ni wahangaikaji, wajasiriamali wenzangu huko mtaani watakubaliana na mimi, hali si shwari kwenye uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili tuweze kurudi kwenye mzunguko mzuri ni lazima Serikali ifanye mambo kadhaa. Mojawapo kiukweli ni kutoa nafasi za ajira kwa wingi zaidi ili watu waweze kuajiriwa. Ama iongeze mishahara, ama iongeze posho kwa maana ya ku-pump fedha kwenye jamii, ili mzunguko uwepo kule watu waweze kutumia uchumi uweze kukua tena. Lakini uchumi wetu kabla ya Covid na kabla ya miaka hii kadhaa hapa nyuma ulikuwa unakua kwa kiwango cha asilimia 7. Sasa hivi unakua kwa kiwango cha asilimia 4 hivi kwenda kwenye asilimia 5 hapo. Maana yake hatuko vizuri sana kwenye economic growth na ili uchumi uweze kukua ni lazima tufanye juhudi za makusudi kabisa za kusukuma fedha kwa wanachi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo hii inaweza ikawa ni njia mojawapo ya kusukuma fedha kwa wananchi. Lakini mbali na hivyo nimeona kwamba tunaweza tukatumia mradi huu wa shilingi 1.3 trilioni ambao umeingia, kama chachu ya sisi wenyewe kuamka tu na kuanza kutenga fedha kwa ajili ya miradi ambayo inaenda kuwagusa watu. Hususani kufuatia stress ambayo imeufika uchumi wetu na mambo yafuatayo ningependa kushauri yafanyike. Kwamba, katika hizi fedha ambazo tumegawiwa sasa hivi kwenye Majimbo yetu, ni lazima kutengenezwe mfumo mzuri wa usimamizi wa matumizi ya fedha hizo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima kutengenezwe mfumo mzuri wa ufuatiliaji, mfumo mzuri wa tathmini na mwisho wa siku mfumo wa kupima matokeo. Na sasa kuanzia hapo kwa sababu, hizi fedha zitakwenda mpaka mwisho wa bajeti hii tuliyonayo sasa. Kwenye bajeti itakayokuja Serikali ituletee Mapendekezo ya namna ambavyo tutapata pengine shilingi trilioni 1.5 nyingine sasa ambayo tutakwenda nayo kwenye mwaka ule utakaofuata. Na hii itakuwa ni kama vile measure ya ku-stimulate ukuaji wa uchumi baada ya janga la CORONA ambalo limeupiga uchumi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama tutakuwa tumeweka mifumo mizuri ya usimamizi, ufuatiliaji na tathmini kutokana na hii shilingi trilion 1.3 tuliyopewa sasa hivi maana yake mwakani tutaendelea tu na Mpango ule. Ambao utakuwa mzuri zaidi kwa ajili ya kutia chachu ukuaji wa uchumi tena na kuhakikisha kuna mzunguko kwenye maisha ya watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo ni lazima tuweke mfumo ambao utawezesha kitu kama pay for performance yaani kama vile performance basic financing. Kwamba, tukiweka vigezo sasa hivi na fedha zimeshakwenda, wale watakaofanya vizuri basi wata-enjoy hiyo shilingi 1.5 trilioni ambayo itakuja kwenye bajeti ijayo. Kwa hivyo mfumo kama huu utapendeza sana kama utafanyiwa kazi, utaandaliwa na hatimaye utatekelezwa. Kwa sababu, linaweza likawa ni jambo la kudumu kwamba, tunatenga fedha kwa ajili ya miradi mahususi kila mwaka kwenye bajeti yetu sisi wenyewe na wala sio kusubiria mikopo ama fedha za wafadhili. Kwa hivyo mfumo kama huu wa kulipa kwa matokeo unaweza ukafikiriwa kutumika kwenye matumizi ya hizi fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili ambalo napenda kulizungumzia, kutokana na stress ambayo imeukumba uchumi wetu, ni lazima mbali na hayo ambayo tayari nimekwisha kuyasema Serikali ifikirie kuweka ahueni kwa wajasiriamali na wahangaikaji. Nchi nyingine tumeona makampuni ambayo yamefeli kulipa mikopo either ile mikopo ikichukuliwa na Serikali kupitia special purpose vehicles, ama yanapewa ahueni kwamba malipo ya marejesho kwa kipindi fulani yatasimamishwa ili hizi biashara ziweze kukua ili ziweze ku-thrive tena kufuatia kuanguka kwa uchumi ambako kumesababishwa na Covid-19. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa sisi kwetu tunaweza tukafanya mambo machache kadhaa ambayo napenda kuyasema. Kwa mfano, kwenye sekta ya utalii ili tuweze kuvutia watu kuja hapa nchini Tanzania inasemwa sana kwamba, ni nchi ambayo ina gharama kubwa kuja kuitembelea basi gharama hizo tunajua zinasababishwa na nini. Ni parking fee za ndege, landing fee za ndege, kodi kwenye jet fuels zote hizi tunaweza, tukatafuta namna ya kwenye bajeti inayokuja pengine tukazishusha chini ili kushusha gharama ya watu kuja Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, na tukazitangaza hizi bei mpya mwisho wa siku tukavutia watalii wengi zaidi kuja hapa Tanzania. Lakini pia, tukavutia wawekezaji wengi zaidi kuja Tanzania. Hiyo nayo inaweza ikawa ni njia mojawapo ya kuweza ku-catalyze economic growth kufuatia janga la UVIKO-19.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, ili ku-stimulate pia growth ya biashara hapa nchini ni lazima tu-consider baadhi ya malipo kwa mfano, pay as you earn, skills development levy. Tukayasimamisha kwa kipindi fulani ili kuyafanya makampuni yetu ambayo yana madeni makubwa ambayo yanashindwa kuendesha shughuli zake, kwa sababu, kipato kimeshuka kutokana na mzunguko kuwa duni yakaweza ku- thrive katika kipindi hiki kigumu ambacho tunapitia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, Serikali inaweza ikaangalia katika Mpango wake namna ya kufanya stimulus, kwenye biashara za hapa nchini ili kuvutia uwekezaji. Lakini pia ili kuwalinda wale wawekezaji ambao wanajikongoja katika kipindi tulichonacho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, Serikali inaweza ikasaidia ni namna gani benki za biashara zifanye kwa wale wafanyabiashara ambao pengine wameshindwa kulipa mikopo. Badala ya kufilisiwa na mali zao kuuzwa ama kufunga biashara basi mikopo ile ikasimamishwa kwa kipindi fulani, ikapelekwa mbele ikafanyiwa restructuring. Halafu biashara zile zikaruhusiwa ziendelee na mwisho wa siku zika-thrive zikachangamka na uchumi ukachangamka kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo, nilikuwa napenda nitoe ushauri huo kwamba, ni lazima Mpango huu ambao umeletwa hapa tuutolee mawazo yetu ukafikiria namna fulani ya kuweka stimulus kwenye economic growth ya nchi yetu. Na jambo la mwisho ambalo napenda kuzungumzia linahusu uwepo wa baadhi ya miradi ambayo inasemekana imekuwa over costed. Kwamba, anakuja mtu ame-tender labda shilingi 100 anaonekana ni tenderer mmoja, sasa na huyo mmoja anashindwa kupewa ile tender wana re-advertise inapotangazwa kwa mara ya pili anakuja tenderer mwingine. anasema mradi ule badala ya shilingi 100 labda yeye ata-tender kwa shilingi 150 anapewa mradi, akishapewa mradi anarudi kumtafuta yule aliyekuwa ame- tender kwa shilingi 100 anampa ile kazi aende akafanye yeye anakula shilingi 50 bila kufanya kazi yoyote ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuna kila haja ya Serikali kuichunguza na kuifuatilia sana miradi yetu na namna tender za miradi mikubwa zinavyofanya. Kwa sababu, kumekuwepo na taarifa za over costing ya miradi kutokana na tenderers kupewa miradi kwa style hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021
MHE. DKT. HAMISI A. KINGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii na niwapongeze Wenyeviti wa Kamati zote tatu pamoja na Wajumbe wao kwa kazi kubwa waliyofanya ya kutuletea taarifa zilizosheheni uchambuzi wa kina juu ya mambo mbalimbali yanayohusu mustakabili mwema wa Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, nitaanzia pale alipoishia Mheshimiwa Simon Msonge kuhusiana na KADCO kuweka taarifa sawa tu. In fact KADCO ilipokuwa inaingia Mwaka 1998 Mwezi Julai wakati wanasaini mkataba ilikuwa imeshasajiliwa kama kampuni yenye malengo ya kwenda kuendesha Kiwanja cha Ndege Kilimanjaro miezi mitatu kabla lakini kwenye mkataba wake na Serikali Taasisi hii ya KADCO ilikuwa inapewa mkataba wa miaka ishirini na tano, Concession’s Agreement (mkataba wa uendeshaji), lakini mkataba huo utaweza kuhuishwa kila baada ya miaka 15, lakini hauna kiwango cha fee au charge yeyote ile ambayo KADCO itaenda kulipa Serikali. Kampuni hiyo baada ya kusajiliwa miezi kadhaa baadaye ikaiuzia Serikali ya Tanzania asilimia 24 ya hisa. Kwa hiyo Serikali akawa sehemu ya hiyo kampuni ya KADCO.
Mheshimiwa Spika, pamoja na masharti hayo ya ajabu ya mkataba huo, mkataba ambao kimsingi haukuweka vifungu vya ukomo, kampuni hiyo ya KADCO pamoja na Serikali kushindwa kuivunja kwa sababu hakukuwa na ukomo baada ya maamuzi ya Baraza la Mawaziri mwaka 2009, Serikali ika-resort kununua zile hisa za wanahisa wengine ambao walikuwa Kampuni ya South Africa ilikuwa inaitwa SAIF ilikuwa kampuni ya Uingereza ilikuwa inaitwa Mott MacDonald International, lakini pia kulikuwa na kampuni ya Tanzania ya Inter-Consult ambayo ilikuwa na hisa asilimia 4.6 tu wakati wale Mott MacDonald walikuwa na zaidi ya asilimia 41, nawale SAIF walikuwa wana asimilia 30. Serikali ikakopa pesa takribani bilioni 12.5 (5.3 USD) ikanunua zile hisa za wale wanahisa.
Mheshimiwa Spika, maamuzi ya Baraza la Mawaziri yalikuwa yanaelekeza kwamba zile hisa zikinunuliwa hasahasa uendeshaji ya Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro utapelekwa chini ya mikono ya TAA.
Mheshimiwa Spika, katika hali ya kusikitisha ni kwamba mpaka leo kile kiwanja kinaendeshwa na Kampuni ya KADCO. Sasa ukijiuliza kama maamuzi ya Baraza la Mawaziri yalikuwa kwamba baada ya zile hisa kununuliwa na Serikali ikakopa Benki ya CRDB 5.3 milion USD na TAA wale wakalipa kufikia mwaka 2014 wakawa wamemaliza lile deni, kwa nini bado kuna KADCO mpaka leo? Hupati majibu. Hata hivyo, KADCO wale wanaendesha ile kampuni ambayo asilimia mia inamilikiwa na Serikali kupitia TR msajili wa Hazina na mkataba wao ulihuishwa tena mwaka 2008 kwa sababu katika ule mkataba wa awali mkataba una uhai wa miaka 25, lakini ikifika miaka 15 unahuishwa tena, kwa hivyo ulihuishwa tena mwaka 2008 kabla hata ya ile miaka 15.
Mheshimiwa Spika, sasa kwenye hili unaona wazi kwamba jinsi ilivyoanzishwa hii KADCO na jinsi ilivyokuja kumpa Serikali asilimia 24 na jinsi baadaye Serikali ilivyokuja kununua zile hisa pale mwanzoni na jinsi ambavyo hii KADCO mpaka leo bado inaendelea kuendesha na kusimamia shughuli za uendeshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kilimanjaro, kuna harufu kubwa ya upigaji kwamba KADCO ni dili tupu. KADCO inanuka rushwa, inanuka mipango na hatuelewi wale waanzilishi walikuwa akina nani? Kwa nini walianzisha kampuni hii na akina nani halisi walio nyuma ya hii KADCO ambao mpaka leo wanaendelea kuipa mafao na mafanikio ambayo haipo kihalali?
Mheshimiwa Spika, wafanyakazi wake waliajiriwa na private company, lakini mpaka leo bado wapo wanakusanya mapato pale, hatujui yanaenda wapi, CAG hajui yanaenda wapi. Kama wana mkataba wa Concession Agreement tulimhoji Katibu Mkuu alipokuja mbele ya Kamati yetu, akasema KADCO inaendelea kuendesha ule uwanja kwa sababu kuna Concession Agreement ambayo ilisainiwa mwaka 1998. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukamwambia sasa hiyo Concession Agreement inabaki kwa masharti yapi? Kwa sababu mkataba wa ukodishwaji maana yake kuna kiwanja cha pesa ambacho unalipa. Kwa hivyo sasa wale KADCO hawalipi chochote Serikalini, lakini wanakusanya na kile wanachokikusanya wanakipeleka wapi na wanakusanya kwa Mkataba upi au kwa makubaliano yapi? Unakosa majibu. Walishindwa kujibu, tukawapa muda watuletee na mpaka leo hawajawahi tena kuleta majibu ya ziada. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Kingwangalla nalinda muda wako. Hebu nisaidie, hii KADCO inaitwa KADCO kule BRELLA ni nani mmiliki halali wa hii Kampuni kwa sasa? Ni nani mmiliki? Bado ni wale waliokuwepo ambao walishalipwa ile asilimia 100 iliyolipa Serikali ama kuna mahali hapo imebadilika imekuwa ya Serikali? Yaani kwamba nikienda BRELLA leo nitawakuta wale wamiliki au naikuta Serikali?
MHE. DKT HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi KADCO inamilikiwa na Serikali ya kwa asilimia mia moja chini ya Msajili wa Hazina toka huo mwaka 2010.
SPIKA: Sasa, samahani nakuuliza wewe kwa sababu unaonekana unazijua sana hizo taarifa na mimi nataka nizijue. Kama Serikali ilishanunua hii Kampuni maana yake ni ya Serikali.
MHE. DKT HAMISI A. KIGWANGALLA: Ndio.
SPIKA: Ni mahali gani inatokea tena kurejea kwa wale watu ambao walikuwepo tangu mwanzo?
MHE. DKT HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika…
SPIKA: Nataka kuelewa tu siyo kwamba wewe ndiyo Serikali, maana hii sasa ni ya kwetu sisi, hii ni taarifa ya Kamati, kwa hiyo nataka nifahamu vizuri.
MHE. DKT HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, nakuelewa vizuri na actually huo mkanganyiko unaoupata wewe na ndiyo mkanganyiko alioupata CAG na ndiyo mkanganyiko tulioupata sisi na ndiyo maana tunaona kwamba hakuna haja ya kuendelea…
SPIKA: Labda swali langu la mwisho. Kama Serikali imeshalipa asilimia mia moja huo mkataba unatambuliwaje mpaka kuna maswali ya kuhuishwa wanahuisha kitu gani ambacho hakipo? Kwa sababu Serikali si ilishanunua asilimia moja? Sasa, ni mkataba gani tena unaoendelea mpaka unahitaji kuhuishwa tena na ukasema haujaisha, haujaisha vipi, wakati…
MHE. DKT HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, Mkataba ulisainiwa Mwaka 1998, ilipofika mwaka 2008 kukawa na hoja kwamba KADCO wameshindwa kufanya uendelezaji kadri ulivyokuwa mkataba wa awali wa mwaka 1998 na hivyo Mkataba ule uvunjwe. Sasa katika kikao cha Baraza la Mawaziri ikaonekana kwamba waende waka-negotiate ili kuvunjwa ule mkataba. Wale KADCO ambao ni wabia wa Serikali kwa kipindi kile cha awali wakakataa kuvunja ule mkataba, walipokataa kuvunja ule mkataba ndipo Serikali sasa ikaamua kununua zile hisa za wale wanahisa wengine ambazo nimesema alikuwepo Mott MacDonald International alikuwa na asilimia 41, alikuwepo SAIF alikuwa na asilimia 30, alikuwepo Inter-Consult Limited alikuwa na asilimia 4.6 na Serikali alikuwa na asilimia 24. Kwa hivyo Serikali akawalipa wale ili waondoke.
Mheshimiwa Spika, kabla ya mkataba ule Serikali kuamua kununua zile hisa mwaka 2009, mwaka mmoja nyuma 2008, mkataba ule wa awali wa concession agreement ile ikahuishwa upya mwaka mmoja kabla, kwa hivyo inapaswa kuisha mwaka 2023. Leo hii wanasema wanaendelea kuitumia KADCO kuendesha Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro kwa kutumia concession agreement. Sasa concession agreement na nani? Kama KADCO ni mali ya Serikali kwa asilimia 100, Serikali inampa kampuni nyingine tena ambayo ni ya kwake haki ya kutekeleza majukumu ambayo yangepaswa kutekelezwa na TAA.
Mheshimiwa Spika, wakati huohuo kwenye maamuzi ya Baraza la Mawaziri, maamuzi yalisema hivi categorically kabisa, very explicitly kwa lugha ya kisheria kwamba, share za KADCO za wale wabia binafsi zinunuliwe na Serikali na sikishanunuliwa na Serikali Uwanja wa Ndege wa KIA urudishwe chini ya TAA ili auendeshe kama ambavyo anaendesha viwanja vingine vyote vya ndege, ikiwemo kiwanja kikubwa zaidi hapa nchini cha Dar-es-Salaam, lakini hilo halijawahi kufanyika toka 2010 mpaka leo. Sababu wanayosema ni kwamba, kinachofanya wasiiondoe KADCO ni concession agreement ambayo ilisainiwa wakati Serikali akiwa kwenye ubi ana wadau wa sekta binafsi hao niliowataja. Kwa hivyo, ndiyo mkanganyiko tunaousema.
Mheshimiwa Spika, unachokiona kwa kuwa, kule kwenye KADCO wanakusanya mafao na yale mafao sasa hayaji kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina yanaenda kwenye ile kampuni ya KADCO, ndiyo tunasema kuna harufu ya kwamba, pengine hii KADCO inawanufaisha baadhi ya watu ambao wako nyuma yake, ndiyo maana hawataki kuiondoa. Nafikiri nimejieleza vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakwenda kwenye hoja yangu ya pili. Napenda kuzungumzia suala la mradi mkubwa wa kimkakati wa reli ya kisasa (SGR). Kulitokea hoja hapa nafikiri ilikuwa Bunge la Bajeti ambapo ilionekana kuna utata kwenye namna tenda ya awamu ya tano ya mradi wa SGR ilivyotolewa kwa njia ya single source kwa kampuni inayotokea nchi ya marafiki zetu Republic of China. Ikaonekana kwamba, majibu yaliyotolewa hapa ni kwamba single source kwenye phase five ya SGR imefanya tumepata Mkandarasi kwa gharama nafuu sana na hii ni reli iliyokuwa inatoka Tabora kwenda Kigoma.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge waliochangia ile hoja, nakumbuka, walisema huyo aliyepewa ni yule ambaye ametekeleza awamu ya tatu ambayo inatoka Mwanza mpaka Isaka, kule kwenye ile lane hajafanya kazi yoyote mpaka sasa, huu takribani ni mwaka wa pili hajafanya chochote. Kwa hivyo inakuwaje ameongezewa kipande cha Tabora kwenda Kigoma, hiyo ndiyo hoja iliyokuwepo.
Mheshimiwa Spika, sasa mimi hoja yangu ni kwamba, mwezi Agosti mwaka huu TRC wametangaza awamu ya sita ambayo inatoka Uvinza kwenda Gitega, nchi jirani ya Burundi kupitia Msongati. Wametangaza open tendering process competitive bidding ushindani unaruhusiwa, kwa maana hiyo wamerudi kwenye kile ambacho walikikataa. Sasa kama single sourcing ambayo wameitumia kwenye kipande cha kutoka Tabora kwenda Kigoma imetupa ahueni kwa nini kwenye awamu hii ya sita wamerudi tena kwenye ushindani wakati mwanzoni walisema ushindani haulipi?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nilipenda kuhoji suala hilo na pengine kuomba Bunge lako Tukufu liridhie kufanya uchunguzi maalum wa namna zabuni zote za mradi huu mkubwa wa kimkakati zilivyotolewa ili tuwe na majibu yaliyo clear bila kutubabaisha-babaisha. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia napenda kuzungumzia eneo la pili kwenye mradi huu wa SGR. Pale Dar-es-Salaam reli ya SGR inapaswa kuingia bandarini na ifahamike kwamba, kwenye biashara ya uchukuzi kwa njia ya reli kinacholipa zaidi ni mizigo ni cargo, hata sio abiria. Kwa hivyo, cargo kwa kiasi kikubwa inapaswa kuchukuliwa bandarini moja kwa moja ili kwanza kuongeza efficiency ya bandari, lakini pili kule kuna mapato makubwa zaidi ukilinganisha na mapato ya abiria.
Mheshimiwa Spika, sasa miradi hii ya SGR inavyotolewa inatolewa kwa njia ya design and build. Kwamba, anayebuni ule mradi anafanya usanifu wa ule mradi ndiye ambaye atajenga mradi husika. Ilikuwaje Serikali ikaingia mkataba wa kujenga reli ambayo ilianzia pale juu, pale station, kuja mpaka Morogoro na ikafuata awamu ya pili kuja mpaka Makutupora bila kuweka link ya kuingia bandarini (port link)?
Mheshimiwa Spika, kwamba, walikuwa wanawaza nini? Mkandarasi ame-design reli halafu hajaifikisha bandarini, halafu sasa hivi wanaanza mchakato wa kutangaza kipande cha kutoka pale station kuingia bandarini na kinawasumbua kidogo kwenye design. Kwa hivyo, nilipenda kulizungumzia hilo kwa sababu linaleta utata namna ambavyo reli itakuja ku-land kule bandarini kwa sababu, bandarini ni chini na hapa station ni juu. Sasa inasumbua magari yapatika wapi? Nafasi kule ndani inasumbua itakuwaje? Sasa ilikuwaje waka-design mradi wa kuendeleza bandari na huku juu waka-design mradi wa SGR bila kuweka link ya moja kwa moja ya hivi vitu viwili, pia bila kuweka link ni namna gani watu wataingia na kutoka bandarini kwa miguu, kwa magari na kwa treni kwa njia nyingine zozote zile ambazo zinapaswa kutumika?
Mheshimiwa Spika, design ya miradi mikubwa kama hii inapaswa kufuata njia ambayo inaitwa multi-modal designing. Kwamba, unapo-design logistics za sehemu lazima ufanye consideration ya aina zote za usafiri na uchukuzi zitakazopita katika eneo hilo. Iwe kama kuna urahisi wa kufika kwa ndege, kufika kwa helicopter, kufika kwa baiskeli, kufika kwa miguu, kufika kwa trams, kufika kwa gari, magari ya abiria, magari binafsi, ni lazima uweke consideration ya mambo hayo.
Mheshimiwa Spika, sasa bandari yetu na hii SGR vilipodizainiwa (design) mradi wa kutanua bandari ulivyodizainiwa (design) na mradi wa SGR walivyo-design hawakufanya hiyo multi modal kind of designing. Kosa hili pia unaliona kwenye mradi wa BRT. BRT imekuwa designed kwa gharama kubwa sana ukilinganisha na BRT nyingine ambazo zimejengwa katika nchi mbalimbali duniani, sisi ya kwetu inaendana na nchi moja tu ya Colombia.
Mheshimiwa Spika, walipo-design wanamwaga zege ya takribani nchi 10/12. Ni zege nzito sana kiasi kwamba, wangeweza kwa hapa juu kuweka provision ya tram, yaani treni nyepesi ya kupita mijini. Hapo inapaswa kuzingatiwa kwamba, Jiji la Dar-es-Salaam kwa sensa ya juzi limekutwa na watu karibu 5.6 million. Kwa siku watu wanao-move, wanao-commute katika jiji la Dar-es-Salaam wapo kati ya Laki Nne mpaka Laki Tano.
Mheshimiwa Spika, sasa usafiri huu wa BRT ndani ya muda mfupi tu utapoteza mantiki yake, hautaweza kuwasafirisha watu kutoka eneo moja kwenda jingine kwa ufanisi ambao ulitarajiwa wakati wa designing kwa sababu, kwanza designing ilifanyika zaidi ya miaka 20 iliyopita wakati huo Jiji la Dar-es-Salaam lilikuwa lina wakazi waliokuwa wanakadiriwa 4.3 million, leo hii imeshafika hapo, kama tunaenda hivi kwa trend hii, miaka 30 ijayo population ya Dar-es-Salaam ita-double pengine tutakuwa na wakazi zaidi ya Milioni 12. Hapo maana yake ni nini, kama hukufanya multi modal designing, ukaweka provision ya barabara za juu, ukaweka provision ya trams kwenye hiyo BRT hapohapo, maana yake huo mradi ni white elephant. Na tumekopa, kwenye hii awamu ya kwanza, Dola 150,000 za Kimarekani na ambazo tunazilipa Watanzania kupitia kodi zetu. Kwa hivyo, tunatarajia wataalamu wetu wanapo¬-design hii miradi wasitutie hasara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na hili napenda kuchangia kuhusu uendeshaji sasa wa hiyo lane ambayo sisi tumekopa, kama nchi. Juzi hapa nimeona kwenye vyombo vya habari kwamba, BRT ile lane inakodishwa kwa kampuni ya nje. Bahati mbaya sana BRT is not rocket science. Siyo sayansi ya kurusha roketi kwenda mwezini ama kwenda kwenye sayari nyingine, ni kitu rahisi sana, lane iko pale unaweka basi juu yake, Dereva analiendesha, linasimama kwenye vituo vyote, watu wanapanda na kushuka. Kwenye sehemu ya tiketi unaweka tu mfumo, ukishaweka ule mfumo immediately unaanza ku-charge. Leo hii analetwa mwekezaji wan je kuja kuendesha BRT, mwisho wa siku akipata faida anaondoka na pesa zake zote kupeleka nje ya nchi. Nini maana ya local content tunayoizungumza kila siku? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunao waendeshaji wakubwa wa mabasi hapa Tanzania na mabasi yanaenda sehemu mbalimbali. Mtu anaendesha mabasi 50 hadi 100 yanatoka Dar-es-Salaam yanakwenda Bara kwenye Mikoa mbalimbali na wanaweza hizo operations. Kuna u-special gani kwenye kuendesha mabasi katika Jiji la Dar es Salaam? Hiyo ni nukta ya kwanza. Nukta ya pili, Dar es Salaam kulikuwa kuna usafiri dedicated wa UDA mpaka mwaka 1983 ambapo Serikali iliamua kuwaruhusu waendeshaji binafsi kwa sababu UDA ilionekana kushindwa kubeba mzigo wa uchukuzi katika Jiji la Dar es Salaam. Baada ya waendeshaji binafsi kuingia, mwanzo wa daladala kuingia, leo hii Dar-es-Salaam tuna mabasi takribani 7,000 yanayochukua watu kutoka sehemu moja kwenda nyingine na yanamilikiwa na takribani watu 5,000 mbalimbali.
SPIKA: Dakika moja, malizia, kengele ya pili ilishagonga.
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, pamoja na ajira ambazo zinatolewa kwa wanaoagiza yale mabasi kuyaleta hapa nchini, wanaofanya ukarabati wa mabasi kwa maana ya gereji na mafundi gereji, lakini pia Mama Lishe wanaouza chakula kwa hao makondakta, ma-tanboy, pamoja na mafundi wanaofanya kazi kwenye hizo gereji, sheli mbalimbali ambazo zinapata watu wenye daladala wanaweka mafuta, zote hizi kwa ujio wa BRT maana yake hizi ajira zote zinakufa. Na hizi ajira zikifa ni takribani ajira 20,000 mpaka 30,000 hizi ajira zikifa tulitarajia basi walao yale mafao ya uwekezaji tulioufanya kwenye BRT basi yabaki hapa nchini na yasichukuliwe na mtu ambaye anatoka nje ya nchi.
Mheshimiwa Spika, kwa nini Serikali haikuweka utaratibu wa kumlazimisha operator atakayetoka nje atakapokuja hapa nchini basi lazima awe na partnership ya lazima na kampuni ambayo leo hii inaendesha BRT? kwa nini hayakuwekwa hayo masharti? (Makofi)
SPIKA: Haya, ahsante sana.
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.
Azimio la Bunge Kuhusu Pendekezo la Kuridhiwa Mkataba Baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Dubai kwa Lengo la Kuanzisha Ushirikiano wa Kiuchumi na Kijamii katika Uendelezaji wa Maeneo ya Bandari Nchini
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na mimi nitoe maoni yangu kwenye hoja hii muhimu sana iliyoko mbele yetu.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha mchakato huu wa mageuzi makubwa ya kiutendaji kwenye Bandari yetu ya Dar es Salaam na bandari nyingine hapa nchini. Haya ni mambo ambayo yalikuwa yamekwama kwa muda mrefu yalihitaji mtu mwenye uthubutu, mtu ambaye atakuwa tayari kutupiwa mawe ilimradi mambo makubwa kama haya yaweze kutokea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nimpe moyo Mheshimiwa Rais wetu na Mheshimiwa Waziri na timu nzima iliyolifikisha jambo hili hapa tulipofika kwamba wasikatishwe tamaa na watu ambao wanakusudia kutukwamisha, kwa sababu miongoni mwa wanao tukwamisha wengine siyo raia wa nchi yetu. Nilisikia clip moja inazunguka mtu ambaye alikuwa anajaribu kutaka kutukwamisha siyo hata Mtanzania, lakini pia wengine wanaotaka kutukwamisha ni wanasiasa kutoka upande wa upinzani, badala ya kuchangia hoja ambayo ni mkataba wanaleta hoja nyingine za ajabu ajabu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niseme hapa kwamba Mheshimiwa Rais Samia hawezi kuwa mtu wa kwanza kupigwa mawe pale ambapo alithubutu kufanya jambo kubwa. Mambo haya yalianza toka Awamu ya Kwanza walisemwa viongozi wakuu. Mzee Mwinyi alisemwa miaka ile ya 1990 alipokuwa anaamua kuikwamua nchi kutoka kwenye mfumo wa centrally planned economy uliokuwepo wakati huo na kutuleta kwenye mfumo wa soko huria, aliambiwa amelikanyaga na kulichana Azimio la Arusha, aliziba masikio akasonga mbele. (Makofi)
Mzee Mkapa alipokuwa anaamua kutekeleza yale ambayo yaliamuliwa na Rais aliyemtangulia ambaye ni mzee wetu Mzee Mwinyi naye aliambiwa anauza mashirika ya umma, kelele zilikuwa nyingi lakini aliziba masikio akasonga mbele hakurudi nyuma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata Mzee Magufuli hapa juzi alipokuwa anataka kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere alipigwa vita sana, walikuwepo wenzetu upande wa upinzani, lakini naye aliamua kuziba masikio na akasonga mbele. Leo hii karibu tuanze kupata umeme megawati zaidi ya 2,150. (Makofi)
Kwa hiyo, mtu yeyote yule siku yoyote ile atakayoamua kufanya jambo zuri lenye manufaa atarajie atapingwa, atarajie atapigwa vita, hakuna watu ambao watakuwa tayari kumuunga mkono moja kwa moja kwa sababu nyingi mbalimbali mojawapo ni woga wa mabadiliko na nyingine ni woga wa kitu ambacho hawakijui. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kupingwa, kukosolewa sio mambo ya ajabu ni mambo ya kawaida, kwa hiyo napenda kumtia moyo Mheshimiwa Rais, lakini pia Mheshimiwa Waziri na timu nzima ya Wizara hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya maneno hayo ya utangulizi ninapenda nijikite moja kwa moja kwenye kile kifungu cha 23 ili kujaribu kujibu hofu mbalimbali ambazo zililetwa, lakini kabla ya kifungu cha 22 labda nianzie kile cha nane ambacho kinahusu haki za ardhi (land rights). Kifungu hiki hakiendi kummilikisha ardhi huyu mwekezaji anayekuja, kinaenda kumpa haki za kutumia ardhi na sisi katika sheria zetu za ardhi hapa nchini, haturuhusiwi hata sisi wenyewe tuliozaliwa hapa haturuhusiwi kumiliki ardhi, tunapewa tu haki ya kutumia ardhi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hata huyu mwekezaji anapokuja atapewa haki ya kutumia ardhi na haki atakayopewa yeye itapitia TIC kwa sababu sio mzawa. Kwa hiyo, atapata derivative rights, atapewa masharti ya namna ya kutumia ardhi atakayoitaka na ndio ataishia pale, lakini sio kumilikishwa ardhi.
Kwa hiyo, wanaowadanganya Watanzania huko nje kwamba ardhi yetu inauzwa na anapewa mwarabu wa Dubai waache tabia hiyo kwa sababu ni upotoshaji ambao haujengi Taifa, ila unaenda kutukwamisha kufanya mambo yetu ya maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini lingine ambalo napenda kulisema linahusu upotoshaji ambao umewekwa kwenye eneo la kipindi cha mkataba na termination. Walikuwa wanasema kwamba tunauza kipande cha ardhi ya Tanzania kwa miaka 100, kwanza hakuna hicho kitu kwenye mkataba huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia mkataba huu unaweka ukoma kwenye hicho hicho kifungu cha 23; wengi wanatia mashaka kwenye kile kifungu kidogo cha (4) ambacho bahati nzuri Mheshimiwa Naibu Spika amekifafanua vizuri sintokirudia, lakini mimi napenda kutia msisitizo kwenye kile kifungu cha kwanza kwamba kifungu 23(1) inasema kwamba mkataba huu utaendelea kufanya kazi mpaka pale mambo kadhaa yatakapojitokeza. Moja ni shughuli za mradi zitakapoisha, lakini la pili ni mikataba ile midogo midogo ya utekelezaji itakapomaliza muda wake. (Makofi)
Sasa kama ile itamaliza muda wake na shughuli za mradi zitakuwa zimeisha automatically huu mkataba mama utakuwa hauna kazi, utakuwa umekufa, hautokuwepo tena. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kusema kwamba mkataba huu hauna mkomo sio sahihi, kwa sababu sisi tuwe makini tu kwenye ile mikataba midogo midogo ambayo Serikali wataenda kusaini huko mbele kwa maana ya Hosting Government Agreement ama Concession Agreement na hapo mimi na mapendekezo yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, kwamba Serikali watakapoenda kujadili na hatimaye kupatana juu ya HGAs pamoja na Concession Agreements wawe makini kwenye kipindi kwenye mkataba. Wasizidishe miaka 30, naona imekuwa kama consensus hapa Wabunge wengi wamejadili hivyo na mimi napenda kuungana na wanaopendekeza miaka kati ya 25 ama 30. Kwa maana ya kwamba ikipita hicho kipindi cha miaka hiyo 30 maana yake kama hatujasaini mkataba mwingine na wala hakuna mkataba mwingine ambao uko hai maana yake hii IGA inakuwa imekuwa imekufa automatically. Hata kama itakuwepo haijafutwa lakini itakuwa imekufa kwa sababu ya hichi kifungu cha 23(1). (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia napenda kupendekeza kwamba watakapoenda kusaini ile mikataba ya utekelezaji hizo Hosting Government Agreement pamoja na Concession Agreement, wawe makini wasije wakasaini mikataba ya kumpangisha kutumia ardhi, wasaini mikataba zaidi zaidi inayojielekeza kwenye kumpa haki ya usimamizi wa miradi husika, kwa maana ya kwamba sisi tubaki na haki za kumiliki ili mitambo, kumiliki hizo facilities ambazo watakuwa wamejenga, lakini tumpe tu mikataba ya operations, usimamizi, marekebisho kwa miaka hiyo atakayotaka na hapo tutakuwa tumelinda sana maslahi ya Tanzania kwenye mikataba hiyo, kuliko tukisema tunaenda kumpa aidha mikataba ya upangishaji kama tenant agreements ama CMS agreement.
Mheshimiwa Spika, jambo la tatu ninalopenda kupendeza wakawenalo makini kwenye Bandari ya Dar es Salaam ukiangalia miradi iliyopo kwenye appendix I, phase one unaona pale kuna shughuli ambazo Serikali yetu imeshakopa pesa nyingi na zimekwishafanyika sema kuna mapungufu ya hapa na pale ambayo yanaenda kutekelezwa na mkataba huu. Sasa pale maana yake kuna uwekezaji wa Serikali. Kwa hiyo, mapendekezo yangu ni kwamba iundwe kampuni ya pamoja kati ya DP World na TPA ambayo Serikali itakuwa ina hisa zake na mwisho wa siku kabla ya kuunda hiyo kampuni utakuwa tumeshafanya valuation, tutakuwa tumefanya uthamini wa mali iliyoko pale. Kwa hiyo tutakapoenda kufunga naye mkataba tutapata share za kutosha kwa hiyo DP World ataendesha ndio, lakini na sisi tutakuwa wabia kwenye mkataba wa kuendesha Bandari ya Dar es Salaam kuliko kusema tunamwachia moja kwa moja. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na hiyo naweza nikapendekeza pia hio kampuni mpya itakayoundwa baina ya DP World na TPA iweze kuwa listed kwenye Soko la Hisa, ili katika ile local content Watanzania wengi zaidi waweze kununua hisa na waweze kupata matunda yanayotokana nan uwekezaji wa kimkakati katika Taifa letu. (Makofi)
(Kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa kengele ya pili imeshagongwa, shukrani sana.
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kushukuru kwa kunipa nafasi, lakini pia nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu na watendaji wote wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kazi nzuri wanaoendelea kufanya. Pamoja na pongezi hizo niliona na mimi nisimame nitoe mchango wangu kidogo kwenye Wizara hii hususani pale ambapo michango ya baadhi ya Wabunge wenzangu ilipojielekeza kwenye kujaribu kuangalia kipi ni kipaumbele muhimu zaidi kati ya kuwekeza kwenye kununua bombardier, ama kuwekeza kwenye kutoa huduma za maji kwa wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia sana katika muktadha wa maendeleo, unaweza ukapata changamoto kwamba kipi kianze na unaweza ukaingia kwenye mtego wa hadithi ya kuku na yai kwamba kipi kinaanza? Kuku ama yai ama yai ama kuku na matokeo yako unaweza kujikuta unashindwa kufanya uamuzi. Lakini kwa wale tuliopata bahati ya kusoma masomo ya kuweka vipaumbele (priority setting) na masomo ya usawa tunakubaliana kwamba cha msingi zaidi ni namna tu ya kuweka utaratibu wa kuweza kufikia malengo unayoyakusudia, na wale usiingie kwenye mtego wa kuamua kipi kianze kuku ama yai na vitu kama hivyo. Kwa hivyo, kweli hili la kwamba tunanunua bombadier ama tunawekeza kwenye maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kwanza napenda nilihakikishie Bunge lako tukufu kwamba sekta ya maji ni katika sekta zinazopewa kipaumbele cha hali ya juu katika nchi yetu na kuna uwekezaji mkubwa unafanyika kwenye sekta hii na hata hili linadhibitika kwenye bajeti ya mwaka huu kuna zaidi ya bilioni mia sita tisini na saba zimetengwa kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia ukisoma ukurasa wa saba wa kitabu cha Mheshimiwa Waziri utaona anaeleza kwamba malengo kwenye sera ni pamoja na kuwa asilimia 85 ya vijiji vya Tanzania vinapata maji safi na salama kufikia mwaka 2020; na kwamba mpaka leo hii utekelezaji umeshavuka lengo la asilimia 85 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 85.2. Japokuwa kuna mapungufu madogo madogo kwenye hiyo miradi, na kwamba kati ya utekelezaji huu wa kiwango hiki cha asilimia 85 ni asilimia 58.7 tu ndio ambao wanaweza kupata maji kutokana na miradi mbalimbali iliyotekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokiona hapa ni kwamba, zifanyike jitihada za makusudi za kuongeza tija na ufanisi kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji, lakini si kwamba hakuna uwekezaji unaofanywa kwenye sekta ya maji na hivyo hatuwezi kufananisha uwekezaji kwenye ununuzi wa bombardier against ule wa kuwekeza kwenye huduma za maji hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo napenda kusema kwamba hakuna makosa yaliyofanyika kwenye kuwekeza kununua ndege za bombardier na ninampongeza Mheshimiwa Rais, kwa uamuzi huu mahususi wa kuamua kuifufua sekta ya Utalii kwa kuwekeza kwenye ununuzi wa bombardier.
Ninachopenda kumalizia kwenye mchango wangu ni kwamba Mheshimiwa Rais anapaswa apongezwe.
KUHUSU UTARATIBU . . .
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Ninachojaribu kusema ni kwamba napenda kutumia nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuamua kwa dhati kabisa na kwa pesa zetu wenyewe kulifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kuwekeza kwenye ununuzi wa ndege za bombardier na dreamliner na pengine na airbus ziko njiani zinakuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyozungumza hapa, wenzetu wa Ethiopia wamenunua ndege kumi, wameweka order za bombardier kumi kwa ajili ya kuendelea kujitanua na kuboresha sekta yao ya utalii na sisi hatuwezi kubaki nyuma. Tanzania inaongoza kwa kushika nafsi ya pili kwa vivutio vya maliasili duniani lakini bado hatujavitumia ipasavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapungufu tuliyo nayo ni pamoja na kuwa na miundombinu mibovu, ni pamoja na kukosa national career ambayo ingeweza kusafirisha watalii kutoka kwenye nchi zao kuja hapa ndani, lakini pia kuwatoa hapa ndani kutoka kwenye kituo kimoja kwenda kituo kingine.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo jitihada za kufufua Shirika la Ndege la Taifa zinapaswa kuungwa mkono na sisi Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi. Hivyo nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa jitihada hizo, na sisi wa sekta ya utalii tunafurahia sana lakini tuna kereka sana watu wanavyoitupia mawe idea hii ya Mheshimiwa Rais ya kuwekeza kwenye manunuzi ya bombardier.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tunafarijika sana na jitihada zinazofanywa na wenzetu kwenye sekta nyengine kama sekta ya ujenzi, kwa kufungua barabara shirika la reli pamoja na kujenga viwanja vya ndege. Zote hizi zinaenda kutia chachu ya kukua kwa sekta ya utalii ambapo katika nchi hii ipo katika sekta ya utalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa fursa ya kusema siku hii ya leo hapa Bungeni. Awali ya yote, nianze kwanza kwa kumshukuru na kumpongeza anayofanya Mheshimiwa Rais wetu Dkt Samia Suluhu Hassan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitatembea na ile hashtag aliyoanza nayo juzi Mheshimiwa Nape Moses Nnauye, kwamba “Nasimama na Mama.” Kwa hivyo, kama wewe ni Mtanzania na unaipenda nchi yetu na huna mahala pengine pa kwenda zaidi ya kuishi hapa Tanzania, basi kama upo kwenye Mtandao wa Kijamii na una jambo lolote lile la kusema hata kama ni picha yako nzuri tu, umevaa vizuri umeamua kuji-post, basi weka hashtag ifuatayo; “Nasimama na Samia”. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu kama wewe ni Mtanzania, una kila sababu ya kusimama na Mama, una kila sababu ya kumshukuru Mheshimiwa Rais wetu, Dkt Samia Suluhu Hassan, kwa sababu anafanya kazi nzuri. Lazima utakubaliana na mimi kwamba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, amechukua uongozi wa Taifa letu katika kipindi kigumu sana, katika kipindi kigumu kihistoria ambapo kwa mara ya kwanza Taifa letu limepoteza Rais aliyepo madarakani na kuisimamisha nchi katika amani. Kwa utulivu uliopo sasa ni lazima tukiri kwamba Mama huyu ana uwezo wa kiuongozi wa kipekee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, sisi kama Watanzania ni lazima tusimame naye, unapofurahi, unapoji-post kwenye mtandao kwa amani na utulivu bila kuingiliwa, andika hashtag “Nasimama na Mama.” Kwa sababu, tayari hata kama mengine yote yasipokuwepo, unayo sababu ya uwepo wa amani na utulivu ambao una-enjoy na ambao unakuwezesha kusimama na Mama katika Mitandao ya Kijamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, Wabunge wote wenye Mitandao ya Kijamii tuandike leo “Nasimama na Mama” kama hashtag yetu. Wana-CCM wote zaidi ya milioni 10 tuliopo katika nchi hii leo tu-post tuandike hashtag “Nasimama na Mama.” Watanzania wote wazalendo popote pale walipo kama wataingia mtandaoni wana jambo lolote lile la kusema leo hashtag yetu iwe “Nasimama na Mama.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimbo la Nzega Vijijini walishatoa msimamo wao alipofanya ziara pale kwamba wao hawana mambo mengi ya kuomba, lakini wanatoa shukrani nyingi zaidi kwa miradi ya maendeleo aliyotuletea. Mheshimiwa Rais Dkt. Samia, toka ameingia madarakani ameporomosha zaidi ya bilioni 100 kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo kwenye jimbo langu tu katika kipindi cha miaka mitatu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye sekta ya elimu, sisi pale Nzega kipaumbele chetu cha kwanza ni elimu, kipaumbele chetu cha pili ni elimu, kipaumbele chetu cha tatu ni elimu na kwenye elimu ametuletea miradi ifuatayo katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita tumepata:-
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, shule mpya mbili za sekondari katika kata mpya ambazo zilikatwa mwaka 2015 zaidi ya shilingi bilioni 1.2; Mbili, madarasa mapya yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 2.0; Tatu, mabweni yenye thamani zaidi ya shilingi milioni 100; Nne, mabwalo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200; Tano, tumepata shule za msingi mpya mbili; na Sita, kwenye miradi ya shule shikizi tumepata shilingi milioni 849. kama wewe ni Mwanazega Vijijini mwenzangu na upo kwenye Mtandao wa Kijamii na hii miradi imekigusa kijiji chako ama kata yako uki-post leo andika “Nasimama na Samia”. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la afya, ambacho ni kipaumbele cha pili cha muhimu katika Jimbo la Nzega Vijijini. Tumepata vituo vipya kabisa vya afya viwili; pale Inagana kituo kimekamilika na miezi mitatu iliyopita tumeletewa zaidi ya milioni 300 kwa ajili ya dawa na tumeletewa watumishi. Kituo cha Afya cha Inagana kwenye Kata ya Magengati leo kinatoa huduma zote ikiwemo huduma za upasuaji wa dharura na huduma za kumtoa mtoto tumboni mambo ambayo hayakuwepo toka tupate uhuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, pale kwenye Kituo cha Afya Lusu tayari tunatoa huduma za upasuaji, tuna ambulance mpya, kila kitu kinaenda vizuri hakuna shida. Wananchi wa Kata za Kimkakati za eneo hilo wanapata huduma zote ikiwemo huduma za kumtoa mtoto tumboni na huduma za upasuaji wa dharura. Pale Nata tumepata Kituo kipya kabisa cha Afya, mwaka 2021 alipofanya ziara, Rais Dkt. John Pombe Magufuli, mimi binafsi niliahidi milioni tano na nikatoa na Mheshimiwa Rais akaahidi milioni 10 na akatoa. Alipoingia Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan akaona jitihada tulizoanza nazo, akaleta milioni 400 kituo cha afya kikakamilishwa na leo wananchi wa Kata ya Nata na kata za jirani wanapata huduma zote muhimu za afya ikiwemo huduma za upasuaji wa dharura na huduma za kumtoa mtoto tumboni. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, kama wewe ni Mwananata, Mwanalusu, Mwanamwasala umeguswa na miradi iliyoletwa na Serikali ya Mama, Mheshimiwa Dkt. Samia na kama upo kwenye mitandao leo nakutaka mimi Mbunge wako ukiandika chochote kwenye Mitandao ya Kijamii andika “Nasimama na Samia” hiyo ndiyo hashtag yetu kwa siku ya leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mama, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan pia mwaka mmoja uliopita ametuletea shilingi bilioni moja kwa ajili ya kujenga hospitali mpya ya wilaya katika halmashauri yetu. Hospitali hiyo imeanza kujengwa, baadhi ya majengo yamekamilika na huduma zimekwishaanza kutolewa angalau zile huduma za wagonjwa wa nje.
Mheshimiwa Naibu Spika, maboma ya zahanati, kwa kiasi kikubwa yamekamilishwa, bado tuna ombi moja tu, tunaomba hapa kwa sababu, maboma ni mengi kwenye Sekta ya Elimu na Sekta ya Afya na hatuwezi kuyamaliza kwa kutumia fedha za ndani. Mheshimiwa Waziri Mchengerwa, tunaomba atuombee basi tupatiwe kiasi chochote tuendelee kukamilisha majengo ya zahanati katika jimbo letu. Kwa maana mahitaji ni zaidi ya shilingi bilioni 2.0 lakini tumepokea shilingi milioni 190 tu katika kipindi kilichopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo ya huduma za kijamii kama elimu, huduma za afya, huduma za kiuchumi kama kusafirisha mazao kutoka vijijini kuyapeleka sokoni hayawezi kufanikiwa kama hakuna barabara. Katika awamu hii bahati nzuri mimi na wewe tumeingia Bungeni humu zamani, zamani kidogo. Miaka ile tunaingia unakuta halmashauri nzima unapata milioni 400, milioni 300 kwa mwaka, lakini leo katika awamu hii ya Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambapo kwa ujumla wake bajeti ya barabara vijijini imekuwa kutoka zaidi ya milioni 600 mpaka zaidi kidogo ya trilioni 4.2. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa halmashauri yetu tu, kwa Jimbo langu la Nzega Vijijini, tumepokea shilingi bilioni 4.0 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za vijijini. Kwa hivyo, kama wewe ni mfanyabiashara ama ni mkulima unayekuja Nzega Vijijini kuchukua mazao ama unalima mazao yako unayapeleka sokoni na unapita kwenye barabara za Jimbo la Nzega Vijijini lazima ukubaliane na mimi kwamba kuna mkono thabiti, imara wa Mama, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Basi kama upo kwenye Mtandao wa Kijamii wowote ule unaoutumia leo andika hashtag “Nasimama na Samia”. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tuna vijiji 28 tu vinavyopata umeme wa REA. Katika kipindi cha miaka hii mitatu ya Mama Samia Suluhu Hassan tumepokea zaidi ya shilingi bilioni 23 kwa ajili ya kujenga umeme kwenye vijiji vyote vya jimbo letu. Kwa hiyo, kama wewe upo kule Nzega Vijijini unapata umeme na upo kwenye mtandao basi leo andika “Nasimama na Samia”. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye maji, Mheshimiwa Rais Samia, amefanya maajabu makubwa katika Jimbo letu la Nzega Vijijini. Tulikuwa hatuna maji ya bomba hata sehemu moja kwenye jimbo hili, leo hii zaidi ya 76% ya vijiji katika jimbo langu wanapata maji ya bomba, kwa sababu Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, imetenga na kuleta kwa vitendo katika jimbo letu zaidi ya shilingi bilioni 19.3 kwenye miradi ya maji vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, kama leo hii wewe ni Mwananzega Vijijini mwenzangu na unakunywa maji yanayotokana na miradi iliyojengwa katika eneo letu na upo kwenye Mitandao ya Kijamii, kuanzia leo tembea na hashtag ya “Nasimama na Samia.” (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na sifa zote hizi ambazo tunamtolea Mheshimiwa Rais wetu, nina ombi moja kwa Waziri Mchengerwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kigwangalla, muda wako umekwisha umechangia vizuri, ahsante.
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja, nasimama na Samia. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Madaktari, Madaktari wa Meno na Wataalam wa Afya Shirikishi wa Mwaka 2016
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri wa maelezo ya awali juu ya muswada huu. Mimi ninaomba nichangie kwenye maeneo machache hususan yaliyogusiwa na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge na mengine atakuja kumalizia mwenyewe Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, labda nianze na hili moja la mwisho la Mheshimiwa Dkt. Godwin Mollel ambalo linahusu ugonjwa usiojulikana kuingia hapa na Madaktari wa Afrika nzima kuitwa na kwamba wote hawa, vichwa vyote hivi vya Madaktari Bingwa walioko hapa Afrika wakashindwa mpaka aje mzungu.
Mheshimiwa Dkt. Mollel na wewe kama daktari nadhani hii ni dharau kubwa sana kwa wanataaluma wenzetu na sisi wenyewe tukiwa kama wanataaluma wa taaluma ya udaktari na wengine tumebobea kwenye fani mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani siyo sahihi sana kwa wanataaluma wa Kiafrika kuji-belittle to that extent (kujidogosha kwa kiasi hicho). Kwa mfano, kwa taaluma hiyo ya mlipuko wa ugonjwa mpya kuingia nchini, mimi peke yake tu hapa nipo ndani ya hili Bunge ni mbobezi kwenye eneo hilo. Kwa hiyo, ukianza kuzungumzia magonjwa kama haya ya mlipuko na usalama wa afya nikupe tu taarifa kwamba Tanzania ni pathfinder country kwenye issue za global health security (usalama wa afya wa Kimataifa) kwa sababu tumekuwa nchi ya kwanza kufanyiwa joint evaluation committee ya namna ya utayari wetu kwenye mwitikio wa magonjwa ya mlipuko ambayo pengine hayajulikani ni magonjwa yapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo sisi ni wa kwanza duniani kufanyiwa joint external evaluation na tuka-pass vigezo vyote kwa alama za juu sana, kwa namna tunavyoweza kuitikia ukitokea ugonjwa wa mlipuko. Kwa mfano, ukilipuka ugonjwa wa Ebola ama ukaibuka ugonjwa wa Dengue ama ukaibuka ugonjwa wa Chikungunya, tuko vizuri sana. Labda nikukumbushe tu kwenye microbiology lazima ulisoma kirusi kinachojulikana kama chikungunya virus ambacho pia kinasababisha ugonjwa wa milipuko katika hizi homa za kutoka damu (hemorrhagic fevers). (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Chikungunya virus aligundulika hapa Afrika na wanasayansi waliogundua Chikungunya virus walikuwa ni Waafrika wenyewe, wala hawakuwa wazungu na ni Profesa mmoja wa kutoka Chuo Kikuu cha Makerere kule Uganda. Pia ugonjwa wa Zika imegunduliwa na wanasayansi wa Afrika wala siyo wazungu. Kwa hiyo, kujidogosha na kuwadogosha wanataaluma wa Kiafrika sio jambo jema na tunapaswa kujikubali katika maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ninalopenda kuzungumzia ni suala linalohusu uwekezaji wetu kwenye sayansi na teknolojia inayohusiana na tiba. Kwanza, tuna uwekezaji mkubwa sana katika nchi yetu kwa sasa, mfano mzuri ili tusiende mbali hata Mheshimiwa Mbarouk amezungumzia ni eneo la tiba ya magonjwa ya moyo. Tanzania kwa sasa tumeanza kupokea wagonjwa wa magonjwa ya moyo wanaopewa rufaa kwenye nchi za jirani kama Malawi, Zambia na nchi nyingine kuja kutibiwa Tanzania. Na sisi tumeanza kuwa kama India, kama Apollo kwa sababu tunapokea wagonjwa kutoka nchi nyingine wanakuja kutibiwa Jakaya Kikwete Cardiac Institute. Tunapaswa kutambua hilo na kujipongeza lakini pia kusema mambo mazuri ambayo yanafanywa na wanasayansi wetu Wataalam wetu kwenye sekta ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo naomba nitumie nafasi hii kuwapongeza sana Wataalam wote wa magonjwa ya moyo walioko pale Muhimbili kwa ubunifu wanaoufanya, pia kwa kutoa huduma za kibingwa zaidi kwenye eneo la magonjwa ya moyo, kwa sababu wametusaidia sana kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa kutibiwa nje ya nchi hususan watoto wadogo ambao mara nyingi wanapata magonjwa ya moyo ya kuzaliwa nayo (congenital heart anomalies).
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa msingi huo siyo kwamba hatujafanya uwekezaji, pia hapa Dodoma tumefanya uwekezaji mkubwa kwenye eneo la vifaatiba katika hospitali inayojulikana kama Benjamin Mkapa Ultra Modern Hospital, pigia mstari Ultra Modern. Tukizungumzia Ultra Modern tunamaanisha ni ya kisasa zaidi. Benjamin Mkapa kuna CT Scan ambayo haipo nchi zote za Afrika Mashariki na Kati ila ipo Tanzania tu na huu ni uwekezaji wa kipekee na ni wa kupigiwa mfano. Lakini pia Muhimbili National Hospital, tumewekeza kwa kununua pia CT Scan nyingne mpya na ya kisasa zaidi kuliko zote zilizopo katika nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati. Huu ni uwekezaji wa kupigiwa mfano na ninaomba Mheshimiwa Mbunge atambue hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaendelea kuwekeza kwa kuanzisha huduma nyingine mpya za kibingwa zaidi katika hospitali zetu nchini. Kwa mfano, katika Hospitali za Taifa Muhimbili tumeanzisha huduma ya kufanya upandikizaji wa vifaa vya usikivu (cochlear implants). Kwa hiyo, tunafanya cochlear implantation kuliko nchi zote za hapa Afrika Mashariki na Kati. Kwa msingi huo, tutaanza kupokea wagonjwa wa rufaa pia kutoka nchi nyingine kuja hapa Tanzania kupata huduma ya cochlear implantation. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaanza pia huduma za kupandikiza figo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, tunaweka sawa Kanuni ya namna ya kuendana na suala hili lakini utaalam upo, vifaa vipo na uwezo upo na tuko tayari kuanza, sasa tunaweka taratibu za kisheria na kikanuni vizuri ili tuanze kupandikiza figo kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili. Yote haya yatapunguza kwa kasi kubwa idadi ya wagonjwa wanaoenda nje ya nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa napitia idadi ya wagonjwa wanaoenda nje ya nchi, nilishangaa sana ile ripoti kukuta katika eneo la magonjwa ya moyo namba ziko zero zero ukilinganisha na miaka miwili au mitatu iliyopita. Kwa hiyo, tunapiga hatua na ni hatua kubwa na tunapaswa tujitambue na tujikubali sisi wenyewe kabla wengine hawajatukubali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kumridhisha Mheshimiwa Dkt. Godwin Mollel pamoja na Watanzania wenzangu wote kwa ujumla, ni kwamba Serikali inafanya kazi kubwa kwenye eneo la uwekezaji kwenye vifaa vya kisayansi na teknolojia mbalimbali za kutolea tiba.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Dkt. Mollel kwamba tumefanya uwekezaji mkubwa kwenye eneo la vifaa vya kufanya uchunguzi lakini pia kutolea tiba ya mionzi katika hospitali ya Taifa ya Kansa pale Ocean Road Cancer Institute na tunavifunga muda siyo mrefu, tumeshatoa zabuni, tumeshaingia mkataba na suppliers na majengo yako tayari, sasa tunaanza kufunga vifaa hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatukuishia hapo tu, tunaenda kufunga mashine mpya inayojulikana kama PET-Scan ambayo itakuwa ina uwezo wa ku-localize ugonjwa ulipo; kutambua eneo na mipaka ya ugonjwa wa saratani ili kutoa tiba mahususi kwenye eno hilo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili napenda kulisema hapa kwa sababu Tanzania idadi kubwa ya wagonjwa ambao tunawapeleka kwa rufaa nje ya nchi huko India kwa kiasi kikubwa ni wagonjwa wa saratani na wagonjwa wa moyo. Kwenye eneo la moyo nimeeleza tulivyofanikiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye eneo la saratani bado tunahitaji kuwapeleka wagonjwa wetu nje kwa ajili ya hiki kipimo tu cha PET-Scan. Sasa kwenye bajeti hii tumewekeza takribani shilingi bilioni 15 kwa ajili ya kufanya ununuzi wa kifaa hiki. Kitakuwa ni kifaa cha kwanza katika nchi zote za Afrika Mashariki na Kati ukitoa South Africa pamoja na Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Tanzania, ukitoa Afrika Kusini, sisi tutakuwa wa pili kuwa na PEP-Scan na kutoa huduma za localization ya lesion mbalimbali za saratani. Kwa msingi huo, tunafanya mapinduzi makubwa kwenye huduma za afya hapa nchini na ninaomba Mheshimiwa Mbunge na Waheshimiwa Wabunge wote pamoja na Watanzania watambue na kuthamini jitihada hizi kubwa zinazofanywa na awamu ya tano kwenye eneo hili la uwekezaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kujibu hoja nyingine iliyopo kwenye taarifa ya wenzetu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Kuhusu hili suala analolisema Mheshimiwa Msemaji kwamba nchi yetu inaongoza zaidi kwa kufuata maoni ya watu na wanasiasa badala ya ukweli wa kisayansi. Hii siyo kweli. Naomba nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba pamoja na uhuru wa kutoa maoni, pamoja na kwamba kwa vyovyote vile lazima uamuzi wowote uwe ni maoni ya mtu yeyote yule, lakini kinacho-matter hapa ni nani hasa anayetoa maoni hayo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Serikali ya Awamu ya Tano, kuna vichwa vimesheheni taaluma mbalimbali za
kisayansi. Kuna maprofesa, madaktari, kuna wabobezi kwenye taaluma za sheria, taaluma za Utawala; hakuna upungufu hata kidogo ya uwezo wa kitaalamu. Hakuna upungufu hata kidogo ya uwezo wa kutafsiri takwimu ama ripoti, ama uwezo wa kufanya utafiti ama kuongoza Wizara husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa namna yoyote ile, uongozi tulionao kwenye Serikali ni uongozi wa watu wenye taaluma za hali ya juu. Wamefika katika vilevile kwenye fani zao, wana uzoefu wa kutosha, ni wabobezi wa kutosha na sina shaka na maoni ya wabobezi hawa wakati wanafanya maamuzi, kwa sababu kwa vyovyote vile maamuzi yao yatakuwa yamejikita kwenye facts za kisayansi kama anavyosema na kwenye ukweli kama ulivyo. Ndiyo maana huoni changamoto kubwa sana za kufanya maamuzi. Ndiyo maana unaona sekta ya afya inaenda vizuri kwa sababu tuko vizuri. Mimi peke yangu tu hapa nina degree nne. Sasa kuwa na degree nne siyo mchezo shehe!
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye eneo utendaji, Makatibu Wakuu wengi utaona Mheshimiwa Rais anateua wabobezi kwenye fani zao; Maprofesa, Madaktari, wanataaluma za sheria, taaluma za utawala na fani nyingine; ni wabobezi wa kutosha. Kwa hiyo, hata kama wakitoa maoni, nina uhakika maoni yao kwa vyovyote vile yatakuwa mazuri na yamejikita kwenye fani mbalimbali ambazo wamebobea kitaaluma.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo amelisema kwenye taarifa yake ambalo siyo la kweli, ni kwamba kuna viashiria vya kupungua wataalamu wa afya nchini. Hapana, siyo kweli. Wataalamu wa afya wameendelea kuzalishwa kwa wengi zaidi ukilinganisha na huko tunakotoka. Tunakiri kuwepo kwa changamoto ya uwezo wetu wa kibajeti wa kuwaajiri wote ili kuwa-absorb kuingia kwenye system, lakini siyo kwenye eneo la production of health care workers.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la production tuna uzalishaji wa kutosha. Miaka kumi iliyopita tulikuwa
tunazalisha wakati mimi na wewe tunahitimu. Miaka 20 iliyopita, madaktari tulikuwa tunazalishwa tusiofika 200. Changanya Dentists na Medical Officers, tulikuwa hatufiki 200. Medicine unakuta labda wako 100 na Dentists unakuta labda wako 30 ama 20.
Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ninavyozungumza hapa, madaktari wanaozalishwa kila mwaka hapa nchini ni 1,100 kwa mwaka. Kwa hiyo, ongezeko hili ni kubwa sana ukilinganisha na miaka 10 mpaka 15 iliyopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Nyongo anazungumzia kuhusu degree za Muhimbili. Ni kweli kuhitimu Muhimbili haikuwa jambo rahisi, kulikuwa kuna ugumu wake na ugumu ule ulilenga kwenda kuzalisha madaktari ambao tunawaamini na ni salama zaidi kwa ajili ya kuwahudumia wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sisi tuliosoma pale, hili halitukwaza; kinyume chake, tuliongeza bidii ya kujisomea na kufanya mazoezi ili tuweze kuwa Madaktari bora zaidi. Ndiyo maana leo hii ukiona nashusha vitu hapa, ujue nilibatizwa kwa moto, sikubatizwa kwa maji. Ndiyo maana leo hii ni daktari bora, nalihudumia Taifa kwa nafasi niliyopewa na Mheshimiwa Rais. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto tunayoipata sasa ni wenzetu wa sekta ya elimu ku-regulate hivi vyuo ili kutoa quality ile ile ambayo inatoka kwenye Chuo Kikuu cha Muhimbili. Hapo sasa sisi tunakuja na solution kwenye mapendekezo ambayo tutayaleta huko mbeleni ya sheria nyingine ya kutunga mtihani wa Kitaifa kwa watu wote wanaohitimu kwenye vyuo vingine mbalimbali ili ku- standardize qualifications zote za wataalamu hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, wewe umesoma IMTU, kama una “A” au C shauri yako, sisi hatuitambui. Hiyo ni ya kitaaluma, una digrii yako; lakini ili uguse mgonjwa wetu, ni lazima tukupe mtihani na mtihani huu ni wa Kitaifa na ufaulu. Kwa hiyo, tunachokifanya sasa ni kuandaa hayo mapendekezo ya sheria hii ambayo itaweka usawa wa wanataaluma wanaohitimu kwenye vyuo mbalimbali nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbarouk alizungumzia kuhusu madaktari kuwa na huruma na uzalendo. Mimi kama daktari sina shaka na hili kwa kweli, wataalamu wetu kwenye sekta ya afya wanafanya kazi kubwa sana, wanajitoa sana na mara nyingi pamoja na kujitoa huko, pamoja na uzalendo mkubwa walionao, hawapati hata hayo malipo ambayo wangestahili kuyapata; lakini wanajitoa na wanaendelea kuhudumia wananchi kwa uzalendo wa hali juu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wachache wanaweza wakawa na changamoto mbalimbali labda za rusha, lugha mbaya; hatuwezi kusema watu wote watakuwa sawa, hivyo sisi sasa kupitia sheria hii ambayo tunaitunga, tunaweka utaratibu wa malalamiko haya kufika kwenye Baraza na wachache ambao wanatia doa watahukumia kwa mujibu wa code of conduct ambazo zinaanzishwa sasa kwa sheria hii kwenye Ibara ya 59 ambapo madaktari na wataalamu wote ambao wanaguswa na sheria hii watapaswa ku- observe codes of ethics mbalimbali ambazo zitatungwa hapo baadaye baada ya sheria hii kupita. Huko nyuma hatukuwa na sheria ambayo inatengeneza code of ethics. Kwa hiyo, tunakoelekea sasa tutaboresha haya mambo yote ya malalamiko, ya uwezo mdogo, lugha chafu, rushwa na makosa mengine yote ya kitaaluma yatahukumiwa sasa kwa mujibu wa sheria kwa sababu tumeweka kipengele hicho.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho ninalopenda kuzungumzia ni hili linalohusu Madaktari Wasaidizi na kada nyingine hizi za chini ambalo lilipelekea kuleta sintofahamu kwa kiasi fulani.
Napenda tu kutoa historia kwamba kwanza tunawatambua na kuwathamini sana Madaktari Wasaidizi (AMO’s) na hatuna mgogoro wowote ule na wala sheria hii haina lengo lolote lile la kwenda kuwapunguzia mamlaka ama kuwafuta ama kuwafanya waonekane irrelevant, kwamba hawafai, hapana.
Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni Jeshi letu la Askari wa Miguu na wanafanya kazi kubwa huko tunakotoka kwenye Majimbo yetu na kazi yao tunaithamini kwa kiasi kikubwa na wala hatuwafuti na hatuwezi kuwafuta kwa sababu wanahitajika na madaktari hawa wapo dunia nzima, siyo Tanzania peke yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, Mheshimiwa Waziri atalimalizia hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri; Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama na Mheshimiwa Angella Jasmine Kairuki, Naibu Mawaziri pamoja na Watendaji wote wa Ofisi hii ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kupongeza hotuba nzuri iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kutoa ufafanuzi kwenye maeneo machache ambayo Waheshimiwa Wabunge waligusia katika sekta ya maliasili na utalii na kwa kuwa muda hautoshi naomba nijibu bila kuwatambua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni eneo la migogoro ya ardhi. Msimamo wa Serikali kwa sasa kwa migogoro yote ya mipaka, matumizi maeneo ya hifadhi ambayo yapo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii tupo katika Kamati ambapo Januari 15 mwaka huu Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliunda Kamati ya Mawaziri kutokana Wizara nane ambao wamepita maeneo yenye migogoro, wamechambua taarifa mbalimbali na sasa tuko katika hatua za mwisho za kuandaa ushauri ambao tutaufikisha kwa Mheshimiwa Rais. Pindi atakapotoa maagizo yake tutarudi kinyumenyume kurekebisha mipaka accordingly ili kutatua migogoro hiyo na huo ndio mtazamo wetu. Kuna maeneo yamezungumziwa ya Kilombero, Serengeti, Grumet, kuna pembeni ya Mto Rubana, yote kwa ujumla wake jibu letu ni hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kuzungumzia ni kukuza utalii wa fukwe. Limezungumziwa jambo hili kwa kiasi kikubwa; Mheshimiwa Mbaraka Dau na wengine, naomba niwahakikishie kwamba Serikali ya Awamu ya Tano kwa sasa imejipanga ipasavyo kukuza utalii wa fukwe na tutaanza kwa kuwekeza katika maeneo ya Ziwa Victoria, eneo la Chato, lakini pia fukwe za Bahari ya Hindi eneo la Saadan likihusianisha visiwa vilivyopo katikati ya Bahari ya Hindi, lakini pia kisiwa cha Mafia. Mafia kuna vivutio vya pekee kuna whale sharks ambacho ni kivutio cha Kimataifa na watalii ambao ni high end wanapenda kuogelea pamoja na hao papa nyangumi ambao wanapatikana sehemu mbili tu duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapaangalia Mafia kwa jicho la kipekee na tunakusudia kuweka mkakati mahususi sambamba na kujenga maeneo ya vivutio vya fukwe, vivutio vya mikutano yaani kwa ajili ya kuendeleza conventions tourism lakini vivutio vya michezo kwa maana kuendeleza sports tourism. Michezo tunayoingalia kwa sana ni michezo kama ya gofu, tennis, michezo ya baiskeli ya kimataifa ambayo tunaamini kwa pamoja itakuza sana utalii wa fukwe ukilinganisha na utalii wa mikutano.
Sambamba na hilo tumetengeneza maeneo matatu ya kukuza utalii, hivyo kama nilivyosema eneo la Chato ambapo hifadhi za Taifa ambazo Bunge hili Tukufu katika Mkutano uliopita wa Bunge lilipandisha hadhi hifadhi za Burigi, Biharamulo na Kimisi pamoja na nyingine, eneo lile tunakushudia kuendeleza utalii wa fukwe pamoja na utalii wa mikutano. Eneo lingine ni hili la Saadan, pamoja na ufukwe wote Bagamoyo, Pangani mpaka Tanga na ukiunganisha na hivyo visiwa nilivyovitaja. Eneo lingine ni hili la Kilwa tukiunganisha Kilwa Kisiwani pamoja na ufukwe wote kuanzia Kilwa mpaka Mtwara. Kwa hivyo eneo la utalii wa fukwe kwenye bajeti yetu tutakayoisoma hapa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri kwa mchango wako.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, nianze kwanza kwa kuwapongeza Wenyeviti wa Kamati zote mbili ambao wametoa hoja hapa Bungeni leo hii. Lakini niishie palepale alipoishia Mheshimiwa Mpina kwamba Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, aliteuliwa na Mwenyezi Mungu mwaka 2015 kuja kuwafuta machozi Watanzania. Na yeye kwa mamlaka aliyopewa na Mwenyezi Mungu akaunda Serikali ambayo ina mtazamo huo na ambayo inaendelea na zoezi la kuwafuta machozi Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenye Sekta ya Uhifadhi – wewe ni shahidi – Serikali ya Dkt. Magufuli imewafuta machozi wafugaji ambao walikuwa na migogoro mikubwa na maeneo ya hifadhi. Imewafuta machozi wakulima ambao walikuwa wanaishi bila amani ndani ya mipaka ya nchi yao kwa kuwa wamejikuta wapo katika maeneo ya hifadhi.
Mheshimiwa Spika, leo hii migogoro baina ya wananchi na sisi wahifadhi imepungua sana, na yote hii ni kutokana na utendaji na uongozi mahiri wa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli. Mheshimiwa Rais ametutuma twende kwa niaba yake tukawafute machozi hawa wananchi. Hatuwezi kukaa ofisini tukategemea tutaweza kutatua migogoro inayowasibu wananchi bila kufika site. Iwe tutaonekana ni watendaji na sio watunga sera ama wasimamizi wa sera, potelea mbali, Cha muhimu tumewafuta machozi wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika miaka hii minne ya uongozi wa Dkt. Magufuli, mapato kwenye Sekta ya Utalii yamekua kutoka trilioni 3.8 mwaka 2015 mpaka trilioni zaidi ya 6.5 mwaka 2018. Idadi ya watalii imeongezeka kutoka milioni moja mwaka 2015 mpaka milioni moja na nusu mwaka 2018, matarajio yetu ni kwamba tutakapokuwa tunatoa takwimu za mwaka 2020 ambapo Mheshimiwa Rais, Dkt. Magufuli na Serikali yake watakuwa wanamaliza muhula wa kwanza wa uongozi wa taifa letu, tuwe tumefikisha idadi ya watalii milioni mbili.
Mheshimiwa Spika, na mafanikio haya yamechangiwa na vitu vingi, na mtu atakayebeza kwa kiongozi wa aina yangu sipaswi kumjibu hata kidogo kwa sababu nitaanza ku-question uwezo wake, uelewa wake na uzoefu wake kwenye sekta hii, jambo ambalo kwa heshima niliyonayo na ninayopenda kumpa Mbunge mwenzangu, sipendi kulifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika miaka hii minne ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli, tumeweza kudhibiti mapato yanayotokana na Sekta ya Utalii kwa kiasi kikubwa kwa kupitia kutengeneza mfumo fungamanishi wa kukusanya mapato ujulikanao kama MNRT Portal ambayo sasa inaendelea kuwekezwa kwenye taasisi zote ambazo zinakusanya mapato kwenye Sekta ya Uhifadhi na Utalii kwa ujumla wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia tumeweza kuendeleza na kukuza jitihada zetu za kutangaza vivutio vya utalii ikiwemo kutumia maonesho maarufu kama Karibu Kili Fair, Karibu Kusini ambayo ilifana sana, kwao na Mheshimiwa Mch. Msigwa kule, na sasa tunaanzisha maonesho mapya ya Kanda ya Ziwa yajulikanayo kama GLITE (Great Lakes International Tourism Expo) ambayo yatakuwa yakifanyika Mwanza kwa mara ya kwanza mwaka huu mwezi wa sita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini sambamba na hiyo tumekuwa tukitumia watu mashuhuri kutangaza vivutio vya utalii. Watu mashuhuri wapo ndani ya nchi na nje ya nchi, kwa malengo ya kukuza utalii wa ndani lakini pia wa nje ya nchi. Wamedhihakiwa hapa wasanii ambao tumekuwa tukiwatumia kutangaza vituo vya utalii. Sipaswi kuwajibia lakini ninapenda nieleze kwa ufupi tu concept ya kutumia influencers ama watu mashuhuri kwenye kutangaza katika zama hizi za sasa.
Mheshimiwa Spika, mfano msanii mmoja kama Diamond Platnumz, Nasibu Abdul. Ana wafuasi milioni 8.6 kwenye akaunti yake moja ya Instargram, anajulikana Tanzania kwa kiasi kikubwa, anajulikana Afrika Mashariki, Afrika yote na nchi mbalimbali huko duniani, na hivi ninavyozungumza hapa anafanya tour ya kutangaza muziki wake, kuuza muziki wake nchi za Ulaya, baada ya kumaliza tour nchi za Afrika.
Mheshimiwa Spika, mtu huyu anafuatiliwa kwa ukaribu sana na kwa raha za vijana ambao ni chini ya miaka 35, anafuatiliwa kwa ukaribu kuliko hata mimi na Mheshimiwa Mch. Msigwa. Maana yake akiweka kivutio cha utalii ama experience ambayo ameipata akiwa kwenye kivutio fulani cha utalii maana yake takribani watu milioni 8.6 wana fursa ya kufikiwa na huo ujumbe, na huo ujumbe atakaouweka katika ukurasa wake utadumu kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na kizazi ambacho tunaki-target katika zama za sasa, hususani ukiwa kiongozi visionary ni kwamba tunawatazama watoto wetu, wadogo zetu na vizazi vitakavyokuja kwa sababu sisi hatuna tradition ya kwenda kutalii, hatuna tradition ya safari na vitu kama hivyo. Sasa ili tuweze kuwafikia kizazi hicho, hatuwezi kupenyeza ujumbe wa vivutio tulivyonavyo kwenye television, kwenye magazeti na all these other traditional media, ni lazima tutumie new media ambapo ndipo watoto wetu, wadogo zetu wapo huko.
SPIKA: Malizia Mheshimiwa Waziri.
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, tukubaliane tu kwamba watoto wa sasa hivi wanatumia mitandao ya kijamii kupata taarifa zaidi kuliko chombo chochote kile kingine cha habari. Kwa hiyo, kwa maana nyingine wanawafuatilia hawa watu mashuhuri. Kwa hiyo, tukiwatumia hawa tuna uhakika taarifa zitafika kwa walengwa kwa haraka zaidi na kwa uhakika zaidi kuliko tukitangaza kwa kutumia njia hizi ambazo tumezizoea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ninaunga mkono Hoja za Kamati zote mbili. Ahsante. (Makofi)
Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba Kigosi Kuwa Hifadhi ya Taifa Kigosi pamoja na Azimio la Kuridhia Mapendekezo ya Ubadilishaji wa Hadhi Sehemu ya Eneo la Pori la Akiba la Igalla Kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mto Ugalla pamoja na Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu Zebaki (Minamata Convention on Mercury)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa hii ya kufafanua maeneo machache ambayo yamechangiwa na Waheshimiwa Wabunge wenzangu na pili niwashukuru wachangiaji wote na kimsingi niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa kiasi kikubwa wameunga mkono hoja ambayo imewekwa mezani kwako. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia zaidi niwashukuru Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati kwa ushirikiano mkubwa waliotupa wakati tulipokuwa tukifanyia kazi azimio hili, lakini pia niwapongeze sana na niwashukuru Kambi ya Upinzani Bungeni pia kwa kuunga mkono hoja hii kwa kiasi kikubwa na niwahakikishie tu kwamba mashaka yaliyopo, wasiwasi mdogo uliopo tutaushughulikia kwa uungwana na ustaarabu wa hali ya juu tukizingatia mapendekezo ya Waheshimiwa Wabunge wenzetu ambao wamechangia hapa Bungeni, tunafahamu Mheshimiwa Magdalena Sakaya amezungumzia uwezekano wa uwepo wa watu katika maeneo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwahakikishie tu kwamba Mheshimiwa Rais anawapenda sana Watanzania, anajali maslahi yao na anayahudumia kwa karibu sana mahitaji ya Watanzania wote ikiwemo hawa Watanzania ambao kipindi ambapo ulinzi ulilega kwenye maeneo haya ya hifadhi walivamia na ndio maana mwezi Januari 15 Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli alitupa maelekezo mimi pamoja na Mawaziri wengine saba tukafanya kazi kubwa sana ya uchambuzi wa maeneo yenye migogoro na maeneo yote haya tuna mapendekezo mahususi ambayo tumeyafikisha kwake na wakati atakapotupa mwongozo namna ya kuyamaliza basi tutarudi kwa Waheshimiwa Wabunge na kwa wananchi kuwapa mrejesho, lakini pia kufanyia kazi maelekezo ambayo tutakuwa tumepewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwamba tuko makini na nia ni njema na migogoro yote iliyopo katika maeneo yanayohifahiwa kwa kweli tutaishughulikia kiuungwana sana na sote ni mashahidi maeneo ya hifadhi kwa sasa yametulia kwa kiasi kikubwa, wananchi wanaishi vizuri na maeneo ya hifadhi na askari wetu, hakuna tena ile pigapiga, kamata kamata haipo tena.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu pia kufafanua kwamba changamoto ambazo zimetolewa katika eneo la mzigo ambao anabebeshwa TANAPA tunazifahamu na Serikali imekwishaanza kuzifanyia kazi, mwaka huu tulifanya kazi kidogo bahati mbaya haikukamilika kama ambavyo tunatarajia, kwa hiyo tutaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Wizara ya Fedha ili tuweze kuona walau kuna namna ambayo tunaisaidia TANAPA na uhifadhi kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na mwisho kabisa nisema tu kwamba baada ya mchakato wa kupandisha/kubadilisha hadhi maeneo haya matatu kwa maana ya Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Hifadhi ya Taifa Mto Ugalla na Hifadhi ya Taifa ya Kigosi Tanzania itafikisha Hifadhi za Taifa 22. Pia tukichanganya na marine parks mbili ile ya Mafia Ruvuma Estoary Marine Park pamoja na ile ya Mafia kule tukichanganya na hii ya Mnazibay tutakuwa nazo jumla parks zipatazo 24 na hivyo Tanzania itakuwa ndio nchi yenye hifadhi nyingi zaidi hapa Barani Afrika. Kwa sasa kuna nchi ya Kenya ambayo ina hifadhi 23 ukichanganya hifadhi za nchi kavu na hifadhi za kwenye maji, lakini Tanzania tulikuwa nazo hizo 16, baada ya kupandisha na kubadilisha hadhi maeneo yote haya sasa Tanzania tutakuwa tuna hifadhi 24. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwambe anauliza hizi zina maana gani? Maana yake kubwa ni kwamba hii itakuwa ni selling point ya muhimu sana kwamba sisi ni nchi yenye hifadhi nyingi, kwa hiyo, kiuhifadhi itatupa credit, lakini pia kibiashara itatupa credit kwa sababu ni selling point kwenye marketing kuna punch line. Kwa hiyo, tukisema kwamba sisi tuna nyingi zaidi kuliko wengine tunaonekana sisi ni vinara na hivyo ni bora zaidi kuliko wengine na hivyo itatusaidia kuuza kirahisi zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na nukta yangu ya mwisho nimpongeze sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa mwongozo ambao amekuwa akiutoa kutuwezezesha kufikia hatua hii. Kwetu sisi wahifadhi hii ni hatua kubwa na nyeti na hizi Hifadhi za Taifa sio tu zitasaidia kupata mapato lakini zinaweka mustabali wa maisha ya watu wetu. Nchi yetu imekuwa degraded kwa kiasi kikubwa, eneo la malisho ya mifugo limeharibika kwa zaidi ya asilimia 31, kiasi cha mvua kimepungua sana na sababu ni hii encroachment ya wananchi kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na hii ilikuwa inatishia kuleta njaa miongoni mwa watu wetu ambao sisi Waheshimiwa Wabunge tunawatetea hapa kila siku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hatua hizi anazochukua Mheshimiwa Rais za kumaliza migogoro, lakini pia kubadilisha hadhi baadhi ya maeneo ili kuyahifadhi vizuri zaidi ili kuyapa ulinzi mkubwa zaidi, ili kuweza kuyatumia kibiashara zaidi kwa kweli ni hatua ambazo zitaandika jina la Mheshimiwa Rais Magufuli kwa wino wa dhahabu kwa vizazi na vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na kwa maazimio yote mawili naomba kutoa hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo
MHE. DKT. HAMIS A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa kuwa leo ni mara yangu ya kwanza kuzungumza katika Bunge lako Tukufu, toka tumalize miaka mitano iliyopita ambayo pia nilipata heshima ya kuwa Mbunge wa Jimbo la Nzega Vijijini, naomba nianze hotuba yangu kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai. Pili kwa kuwashukuru wanachama wenzangu wa Chama cha Mapinduzi wa Jimbo la Nzega Vijijini na wananchi wenzangu wote wa Jimbo la Nzega Vijijini kwa kunipa heshima ya kuwa Mbunge wao kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Mheshimiwa Spika, pili nikushukuru wewe mwenyewe kwa kunipa fursa ya kuzungumza katika hoja hii ya Waziri wa Kilimo siku hii ya leo. Jambo la kwanza ambalo napenda kulizungumzia linahusiana moja kwa moja na uelekeo wa kilimo cha umwagiliaji kwenye Taifa letu.
Mheshimiwa Spika, Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla wake limejaliwa kuwa na bahati ya kuwa na maji mengi ya baridi, siyo maji ya chumvi. Ukienda katika nchi ya Israel utakuta kule wanafanya treatment ya maji ya chumvi kuyafanya yawe ya baridi ili waweze kumwagilia, lakini sisi hatuna haya ya kufanya hivyo katika mito mirefu na maziwa makubwa duniani, 10 bora duniani, Tanzania imeajliwa kuwa nayo sita. Kwa hiyo, katika vyanzo vya maji baridi Tanzania tuna mtaji mkubwa ukilinganisha na nchi zote ambazo zinatuzunguka na hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nalisema hili kwa sababu naamini tunapoelekea tutashuhudia zaidi vita nyingi zikisababishwa na ukosefu wa maji baridi kuliko vita hizi za mafuta na gesi ambazo tumezishuhudia katika kipindi tulichopita, wanaziita water wars. Sasa ili tusiende huko, lakini pia tuweze kuitumia resource ya maji ambayo tumejaliwa by virtual of being Tanzanians na kuwa na hii land scape nzuri ni lazima kwanza tujipange kuhifadhi vyanzo vya maji hususani maji baridi.
Mheshimiwa Spika, la pili, ni lazima tupange kufanya matumizi endelevu na yenye faida kwa vizazi na vizazi vya nchi yetu. Sababu kubwa ni moja, leo hii tunawekeza kwenye kilimo, watu wetu tunawahamasisha walime ambao ni zaidi ya asilimia 70, lakini mwisho wa siku hatupati yield ya kutosha kwa ajili ya ku-sustained chakula cha ndani, lakini pia kwa ajili ya kuuza nje, wakati tuna vyanzo vya maji baridi vya kutosha kuliko nchi zote zinazotuzunguka hapa jirani.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo nataka niishauri Serikali kwamba katika Awamu hii ya Tano iliyopita na sasa tumeingia ya Sita, bahati nzuri Rais aliyeko sasa alikuwa sehemu ya Awamu ya Tano, imefanyika miradi kabambe mikubwa ya kihistoria ambayo inaweka legacy ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kiasi kikubwa sana. Napenda kuishauri Serikali iwekeze kwenye kilimo cha umwagiliaji kama legacy ya Serikali ya Awamu ya Sita, tutoke kwenye kilimo cha kutegemea mvua, kwa sababu kilimo cha kutegemea mvua kimesha-prove kwamba hakiwezi kutupeleka popote.
Mheshimiwa Spika, wakati sisi tunazaliwa na kukua pale Nzega, kiwango cha mvua kilikuwa kinazidi milimita za ujazo 2,000. Leo hii kiwango cha mvua kipo kati ya milimita za ujazo 600 mpaka 900. Ni kiwango ambacho hakiwezi kuivisha mazao ya mahindi mpaka kufikia mwisho na kuvuna. Kwa maana hiyo wananchi wetu ambao walizoea kulima kilimo cha kutegemea mvua wanalima mahindi leo hii wakiendelea na utaratibu huo wa kulima mahindi, hawawezi kuvuna. kwa hiyo, ni lazima sasa tubadilishe utaratibu, twende kwenye kilimo cha umwagiliaji na cha uhakika Zaidi.
Mheshimiwa Spika, kwa nini nazungumzia huu unapaswa kuwa ni mradi kabambe ambao utaweka legacy ya Serikali ya Mheshimiwa Mama Suluhu Hassan ya Awamu ya Sita ni kwa sababu, vyanzo vya maji tulivyonavyo; Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa, Ziwa Victoria na mito yote ambayo inatengeneza haya maziwa na inayoingia baharini, kama tukitumia ipasavyo na tukitumia mabonde tuliyojaaliwa na Mwenyezi Mungu tunaweza kuwa godown la chakula la Ukanda huu wa Afrika na hata kupeleka nchi nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wazo langu ni kwamba, leo hii tunajadili sana, kila Mbunge akisimama anazungumza naomba maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, kuna baadhi ya vijiji havina maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Kwa nini tusiwe hapa Bungeni Wabunge tunajadili kuletewa maji kwa ajili ya umwagiliaji, kwamba tujenge mabomba makubwa ambayo mtu mrefu kama mimi naweza nikatembea ndani yake kutoka Ziwa Victoria, kutoka Ziwa Tanganyika, kutoka Ziwa Nyasa tuyatawanye mpaka huku Dodoma, Dodoma kuna ardhi nzuri, lakini hakuna maji, mvua ni chache. Kama tukileta maji kutoka Ziwa Victoria ama maji kutoka Ziwa Tanganyika maana yake yatapita mikoa yote ya huko Magharibi mpaka kufika hapa Dodoma na tutamwagilia na tutalima kwa uhakika, hata wale wafugaji wanaohamahama hawatakuwa na haja ya kuhama kwenda maeneo mengine ambayo yana vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wazo hili linaweza kuonekana ni wazo gumu kutekelezeka, lakini ni wazo ambalo linawezekana. Kama Israel leo hii wana-treat maji chumvi kuyapeleka kuwa maji baridi ili wafanye kilimo cha umwagiliaji kwenye nchi ambayo ni kame, kwa nini sisi tushindwe kutumia maji baridi ambayo tayari tunayo, arable land ambayo tunayo, tunakwama wapi?
Mheshimiwa Spika, mfano kule kwetu, kuna bonde maarufu sana linaitwa Bonde la Isagee, nimeona Wizara wanatujengea pale godown, kijijini kwangu Puge, ulipita pale na lile godown likijengwa pale maana yake liko kwenye catchment area ya walimaji wazuri wa nafaka ikiwemo mpunga na mahindi. Hata hivyo, kilimo kinachofanyika pale kwa kiasi kikubwa kinatoka kwenye hili bonde la Isegenhe kwa nini bonde kama lile lisipate maji ya uhakika kutoka kwenye mito na maziwa ya maji baridi ambayo yanatuzunguka hakuna sababu kwa nini…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. DKT. HAMIS A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa fursa hii ya kuchangia asubuhi hii ya leo.
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Kalemani na Naibu wake pamoja na Wizara kwa ujumla wake kwa kazi nzuri wanayofanya kwenye Wizara yao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mchango wangu utakuwa na sehemu mbili, sehemu ya kwanza napenda kuchangia kuhusu uchumi wa gesi kwa sababu imekuwa bahati mbaya sana hatuzungumzii tena uchumi wa gesi katika nchi yet una nilidhani kwamba uchumi wa gesi pengine ungekuwa neema. Miaka ya 2010 wakati naingia hapa Bungeni tulizungumza sana kuhusu uchumi wa gesi.
Mheshimiwa Spika, kipindi kile matarajio kwenye uchumi huu wa gesi yalikuwa bei zingefika takribani dola 16 kufikia mwaka 2020 ilikuwa ni kipindi cha miaka kumi, lakini leo tunavyozungumza hapa bahati mbaya sana bei zimeshuka badala ya kwenda mbele kwenye hiyo dola 16 tuliyokuwa tunafikiria per one British Thermal Unit, leo hii bei zimeshuka mpaka dola nane. Ukitazama bei ya gesi kwenye soko la Japan, Korea ya Kusini na Ulaya unaona bei zinashuka tu badala ya kupanda na hapo nimeangalia takwimu za kabla ya mwaka 2020 ambapo hapa duniani tulikuwa hatujakumbwa na baa la COVID 19 maana yake tungetarajia pengine bei zingekuwa zinapanda badala ya kushuka. Sasa ukiweka na impact ya COVID 19 maana yake bei zitazidi kushuka.
Mheshimiwa Spika, lakini nimetazama makadirio ya bei kwa miaka 15 inayokuja yatakuwaje. Miaka 15 inayokuja bei ya milimita moja ya BTU ya gesi itakuwa dola 14 tu. Hii kwa sisi wana mazingira inatupa mtazamo tofauti kwamba pengine kizazi kinachokuja cha watoto na wajukuu zetu hakitozungumza aina ya nishati ambazo tunazizungumza leo, kwa sababu tungetarajia pengine gesi ingezungumzwa miaka kumi na tano, ishirini ijayo kama ndiyo source pekee ya energy lakini bahati mbaya haitokuwa hivyo. Kwa hivyo, sisi kwa bahati mbaya sana tusipoitumia ipasavyo gesi yetu leo, hii resource ya gesi tuliyoipata leo itapotea bure na haitokuja kuwa na faida yoyote ile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nalisema hili kwa kutoa ushauri kwa Serikali kwamba tufikirie kwa namna yoyote ile kuanza kuitumia gesi tuliyojaliwa na Mwenyezi Mungu leo badala ya kudhani kwamba tunaweza tukafaidika sana huko mbele kuliko ilivyo sasa. Hii ni kwa sababu hata yale matarajio tuliyokuwa nayo miaka kumi na moja iliyopita hayakuwa. Kwa hivyo, tunakoenda huko mbele tunaweza tukajikuta hatupati faida yoyote kutokana na hii gesi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba tutazame zaidi faida tutakayoipata kutokana na uwekezaji kwenye sekta ya gesi kwa kutazama zaidi value chain impact ya gesi kwenye uchumi, lakini pia kwa kutazama zaidi local content kwamba tunafaidikaje, wananchi wanafaidikaje kwa uwepo wa uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya gesi kuliko kuwaza zaidi kupata mapato ama mgao kutoka kwenye ile actual gesi inayopatikana.
Mheshimiwa Spika, miaka kumi na moja iliyopita tuliokuwepo hapa Bungeni tuliona kilichotokea na pengine miaka kumi na moja inayokuja siku za mbele tutajaliwa kuwepo wengine bado wadogo tu, tutaweza kuyaona haya na tutakumbushana hapa ndani kwamba wakati huo uchumi wa gesi hautokuwa na maana yoyote ile kama tusipoamua leo ku-tap into the potential that the gas economy is going to bring to our country na badala yake tukawaza zaidi mapato. Nalisema hili kutokana na sheria tulizozitunga miaka miwili, mitatu iliyopita hapo ambazo zinazidi kuweka ugumu kwenye majadiliano ya uwekezaji kwenye sekta ya gesi badala ya kuzitazama zile PSA kibiashara zaidi, kuzitazama kwa mawanda mapana zaidi ya impact ya gesi kwenye value chain ya uchumi wetu, kwenye local content ya uchumi wetu tutajikuta tunapitwa na wakati. Hakuna uwekezaji utakaotokea na hatutokuja kupata faida ya hii gesi ambayo tumejaliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya kulizungumza hilo, naomba kumshukuru Mheshimiwa Waziri Dkt. Kalemani, miezi miwili iliyopita alikuja pale Jimboni kwetu Nzega Vijijini na akatuzindulia mradi katika Kata ya Isanzu wa kuweka umeme vijijini. Bahati mbaya sana alisema baada ya siku kumi umeme ungewaka leo imepita miezi miwili umeme haujawaka. Kwa hiyo, namuomba ahadi aliyoitoa kwa wananchi wale itekelezwe na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sambamba na Kijiji cha Isanzu kuna Kata nyingine kama za Tongi, Mizibaziba bado hazijawa na umeme na zote hizi walishafanya tafiti na zinahitaji kupata umeme.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Awali ya yote nianze kwa kukupongeza wewe na Mheshimiwa Naibu Spika kwa kuchaguliwa kwa asilimia zote na Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa viongozi wetu katika mhimili huu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, nampongeza Mwenyekiti wangu wa Kamati kwa uwasilishaji mzuri wa ripoti. Nina mambo mengi ya kuzungumza, lakini nitaomba kwanza nianze na hili moja tu, na sidhani kama muda utanitosha.
Mheshimiwa Spika, ni kwamba mnamo Aprili 6, 2020 CAG aliwasilisha Taarifa ya Ukaguzi wa Fedha za Serikali Kuu kwa Mwaka Unaoishia 30, Juni, 2020. Katika uwasilishaji wake, CAG hapa Bungeni alinitaja kwa jina na nafasi niliyokuwa nashika mpaka kufikia mwaka 2020, Desemba - nafasi ya Waziri wa Maliasili na Utalii, akinihusisha na hatua mbalimbali za upungufu wa kiutendaji uliotokea kwenye Wizara niliyokuwa naisimamia.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, CAG alisema mimi nikiwa kiongozi pale, na alinitaja kwa jina; na leo nimejiridhisha kwa kupitia ripoti hizo, kwamba niliidhinisha matumizi ya Tamasha la Urithi (Urithi Festival) shilingi bilioni 2.085 na haikuwa kweli. Hata leo ukienda kutazama kwenye vitabu utaona siyo sahihi, kwa sababu kwanza wakati tamasha hili linaandaliwa na hata linafanyika, mimi nilikuwa nimelazwa hospitali kufuatia ajali niliyoipata tarehe 4, Agosti, 2018 na tamasha lilifanyika mwezi mmoja baada ya hapo, mimi nikiwa nimelazwa Muhimbili. Akasema mimi niliidhinisha wapewe Clouds Media, wapewe TBC, wapewe Wasafi, pesa za kufikia kiwango cha zaidi ya shilingi bilioni mbili, taarifa ambayo haikuwa kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivyo hivyo, CAG alitamka hapa Bungeni wakati akiwasilisha kwamba mimi nilifanya safari binafsi kupanda Mlima Kilimanjaro mnamo Septemba, 2019 na safari ile ilitumia pesa za TANAPA na NCAA kwa kufuata maelekezo yangu, jambo ambalo pia halikuwa kweli, kwa sababu safari hiyo ilikuwa ipo katika mpango wa marketing wa Wizara na mambo yote haya yalikuwa yako katika Mpango wa Tanzania Unforgettable ambao ulikuwa unatekelezwa na Wizara…
SPIKA: Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, ili twende vizuri kwenye huu mjadala wa taarifa zetu hizi mbili za Kamati, maana nilikuwa najaribu kufuatilia, maana hivi vitabu ninavyo hapa na kwenye kompyuta. Hii taarifa unayoizungumzia, ipo kwenye ipi kati ya hizi taarifa mbili? (Makofi)
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, kwa ajili ya kurahisisha rejea yako, unaweza ukapitia Ripoti ya Mwaka ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu ukaguzi…
SPIKA: Sasa ngoja. Leo tunajadili taarifa za Kamati za Bunge mbili ili zituongoze kwenye Bunge letu kufanya maamuzi fulani ambayo tutayapeleka kama maazimio ya Bunge kwa Serikali ili wayafanyie kazi.
Sasa nataka kuelewa vizuri, ili tuelewane tunaendaje na huu mjadala? Maana naona ulipoanzia mwanzoni na hapa ulipofika sasa, ni “taarifa ile siyo kweli, taarifa ile siyo kweli na taarifa ile siyo kweli,” mpaka hapa nilipokusikiliza. Sasa sijajua muda wako wa kuchangia umeamua kutumia nafasi yako kukanusha taarifa ile au umeamua kutumia muda wako kuchangia kwenye hoja hizi zilizo mbele yetu, ili Bunge baadaye liamue kwamba linaielekeza nini Serikali cha kufanya? Hicho ndicho ninachotaka kuelewa ili Kanuni zetu zituongoze vizuri tunakotaka kwenda.
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, sawa. Nashukuru na bila shaka unanitunzia muda wangu, maana yake nina dakika tano tu.
Mheshimiwa Spika, nilikuwa naorodhesha hii mifano kwa sababu Kamati ya PAC imechambua taarifa zinazoishia Juni, 2020. Kwenye taarifa hiyo ambayo inaishia Juni, 2020 ndimo mimi nilitajwa, lakini katika proceeds za kazi za Kamati, hayo madai ya CAG hayaingii kwenye hii ripoti kwa sababu waliyatupilia mbali kwa kuwa yalikuwa ni ya uongo.
SPIKA: Sawa. Nimekuelewa vizuri Mheshimiwa.
Waheshimiwa Wabunge, nadhani maelezo ya Mheshimiwa Dkt. Dkt. Kigwangalla sote tumeyasikia hapa na mimi nimeyasikia. Nafikiri zitumike njia sahihi zinazotakiwa kukanusha Taarifa ya CAG. Kwa sababu sisi hapa ndani tunafahamu Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali inapoletwa hapa ndani tunaipeleka kwenye Kamati ikafanyiwe kazi. Sasa ikiwa ile taarifa inazo taarifa ambazo siyo za kweli, basi lazima tutumie njia iliyo sahihi.
Kwa sababu mimi niliyekaa hapa mbele mkiniweka katika mazingira kwamba niishike ile taarifa nianze kusema nani ni mkweli na nani siyo mkweli, ili niseme Taarifa ya CAG siyo kweli ama ni kweli, lazima zote mbili niwe nazo na niwe na vielelezo. Kwa sababu hapa, yaani Bunge lina Taarifa moja tu ya CAG.
Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, taarifa ya kukanusha uko huru kabisa kuileta kwa Spika kwa maandishi ili ifanyiwe kazi kwa utaratibu mzuri. Ukisema hapa ndani utalielekeza Bunge kuliambia kwamba kipengele hiki cha Taarifa ya CAG siyo kweli kwa sababu wewe umesimama kutoa maelezo hapa, utakuwa unaniweka mimi katika mazingira ambayo; sijaiona mimi taarifa yako ambayo inakanusha zaidi ya maelezo unayoyatoa sasa.
Kwa kuwa taarifa niliyonayo mimi ni ile ya CAG, basi nakuruhusu ulete maelezo yako ya kukanusha ile taarifa ili ifanyiwe kazi kwa utaratibu ulio wa kawaida. Sote tunafahamu Kanuni zetu haziruhusu Mbunge kuchafuliwa na mtu yeyote wala mtu mwingine yeyote kuchafuliwa na Mbunge.
Kwa hiyo, kama Mheshimiwa Mbunge hujatendewa haki na ile taarifa, wewe ulete malalamiko yako kwa njia ya kawaida kabisa na yatafanyiwa kazi na Bunge hili. Wala usiwe na wasiwasi, unalindwa kabisa. Ila kutumia muda huu wa kuzijadili hizi taarifa za Kamati hapo ndipo ambapo wewe sasa utakuwa unazikosea taratibu zetu za Bunge.
Kwa hiyo, ama uchangie kwenye hizi au kama ni hayo yako ya kuilalamikia ile taarifa na kueleza namna ambavyo siyo sahihi, utumie njia za kawaida ambazo unaruhusiwa kabisa Kikanuni. Kama ni hayo tu ulikuwa nayo, niite mtu mwingine, halafu wewe kama nilivyotoa maelezo, una nafasi ya kumletea Spika malalamiko yako ili yafanyiwe kazi.
Haya, ahsante sana. Waheshimiwa Wabunge, ameonesha ishara ya kuonesha kwamba pengine atachukua hizo hatua nyingine, lakini kwa sasa hana mchango mwingine zaidi ya huo aliokuwa anazungumza kuhusu yeye na ofisi ambayo aliwahi kuihudumia.
Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, hali ya kiuchumi ya familia nyingi za kitanzania zinafanana sana na kesi ya mtoto aliyetolewa mfano na Mheshimiwa mtoa hoja. Pia kesi ya mtoto ya mtoa hoja inafanana sana na kesi za watoto wengi ambao wapo katika majimbo yetu. Hii imenifanya nisimame hapa kwa sababu nimejitazama mimi mwenyewe ninatoka wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi ni mtoto wa Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi enzi hizo, na ninakumbuka kipindi hicho wakati mimi nafaulu vizuri sana Form Six masomo yangu ya PCB, mama yangu mzazi ndio alikuwa mlezi wangu pekee na alikuwa hajalipwa mishahara yake ya karibu miaka miwili hivi.
Mheshimiwa Spika, nikitafakari hali ya mtoto ambaye amefaulu kwa Division One, kama ambavyo mimi nilikuwa nimefaulu kwa Division One kipindi namaliza na mzazi wangu hana uwezo; na nikitazama mazingira ya watoto wengi wa kitanzania; naona kuna haja ya suala hili kutazamwa kwa umakini zaidi kuliko linavyotazamwa sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa nini nasema hivyo? Tunaelewa Wizara ya Elimu wanafanya kitu kinaitwa means tests ili kuwapata watoto ambao watapata sifa za kupewa mkopo na Serikali. Tunafahamu kama Taifa, tunapata changamoto ya kuongezeka kwa wahitaji wa mkopo kutoka kwenye Bodi ya Mikopo kila mwaka, kwani kila mwaka wanaongezeka.
Mheshimiwa Spika, sasa hatutarajii siku moja population itashuka kwa sababu ukitazama namba zilizotangazwa jana za sensa utaona pengine miaka 30 ijayo idadi ya jana itakuwa ime-double. Pengine tukawa na watu zaidi ya milioni 120. Sasa nini Serikali ifanye kama suluhisho la kudumu? Ni lazima ufanyike mchakato wa wazi wa njia za kupata wahitaji na wanufaika wa mfuko huu wa Bodi ya Mikopo, pia ipatikane namna ya kuwasaidia hawa ambao wanafikisha zile sifa ambazo zinahitajika. Vinginevyo, tutatengeneza bomu kubwa sana la watoto pamoja na wazazi wao ambao watakuwa wanailaumu Serikali maisha yao yote.
Mheshimiwa Spika, you can imagine mtoto ambaye amefaulu kwa division one kama ambaye ametolewa mfano na mtoa hoja, akikosa fursa ya kwenda kusoma Udaktari kama ambavyo alikuwa ametamani, you can imagine hiyo scenario crisis ambayo inajitokeza kwake na familia yake, lakini namna ambavyo watoto wengi watakufa moyo kutokana na hiyo. Pia yatatokea maswali ambayo tutapaswa kuyahoji kwamba je, tunatenda haki kwa watoto wa Taifa letu? Kwa sababu elimu ni haki ambayo inatolewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Spika, pia kupata mkopo ni haki ya watoto ambao wamefaulu na wanakidhi vigezo. Tusipotoa haki hiyo kama Taifa, maana yake tunatengeneza kundi la watu ambao wataacha kuamini katika Katiba, wataacha kuamini katika Sheria, wataacha kuamini katika Serikali, wataacha kuamini katika Bunge, wataacha kuamini kwenye kitu chochote kile ambacho kiko morally right. Kwa sababu kama nimefanya kila kitu vizuri, nimefanya kila kitu sawa, nisipopata haki, kuna haja gani ya kuwa mtu mwema katika dunia hii? Ndiyo maswali ambayo watoto wengi na wazazi wengi watajiuliza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wewe ni msomi wa Sheria, anaisema vizuri sana Mwanafalsafa Tom Tyler kwenye kitabu chake cha “Why People Obey the Law” ambacho alikiandika mwaka 1990, kwamba uhalali wa maamuzi yanayotolewa na viongozi, uhalali wa sheria zinazotungwa na Mabunge ya Mataifa utapatikana tu endapo sheria hizo, endapo Serikali zao, endapo Mabunge yao yatatoa haki kwa wananchi na wananchi wataona haki imetolewa na wata-enjoy matunda ya haki ambayo inatolewa na sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ili mifumo yetu ya Utawala Bora, ili Katiba yetu, sheria zetu ziendelee kuaminiwa, kuthaminiwa na kutumainiwa, ni lazima tutoe haki kwa watu wa Taifa letu. Haki ya msingi kabisa ambayo mwanadamu yoyote anapaswa kuipata, basi ni haki ya kupata elimu. Kuna haja gani ya kuzaa mtoto ukamlea vizuri, ukampa miongozo, akaenda shule, akasoma vizuri, na akafaulu, akakosa fursa ya kwenda kusoma masomo ya Chuo Kikuu kwa sababu nchi yake imeshindwa kumwekea mfumo mzuri wa namna ya kupata msaada wa kulipiwa ada na gharama nyingine za masomo yake?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, pamoja na kwamba tunaelewa Serikali ina mzigo mzito wa kukidhi gharama za kusomesha watoto wa Taifa letu, ni lazima tuweke mfumo kwanza wa wazi; pili, unaokubalika; tatu, unaotekelezeka, wa kuwafikia wahitaji na wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya kati na hata elimu ya juu.
Mheshimiwa Spika, ilivyo sasa, mfumo tulionao hautoi haki kwa watu wengi na hivyo ninaunga mkono hoja ya mtoa hoja kwamba jambo hili liangaliwe upya na mwisho wa siku tupate suluhisho la kudumu, ahsante. (Makofi)
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Kuhusu Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kutofuata Maelekezo ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, nakushuru kwa kunipa fursa hii nami nichangie hoja ya Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, nimemsikiliza vizuri sana msomaji wa taarifa mbele yetu. Katika taarifa hiyo imeonekana wazi kabisa kwamba Waziri mwenyewe kwa kauli yake kama alivyonukuliwa na muwasilishaji akisema kwamba anajukumu la kuisimamia bodi lakini pili bodi haijakaidi maelekezo yake. Pia on Hansard Waziri huyo huyo hapa mbele ya Bunge lako Tukufu, jambo lililopelekea mpaka ukatoa maelekezo aende kwenye Kamati akahojiwe.
Mheshimiwa Spika, pia on Hansard, Waziri huyo huyo hapa mbele ya Bunge lako tukufu, jambo lililopelekea mpaka ukatoa maelekezo aende kwenye Kamati akahojiwe na Kamati iwasikilize watu wote, iweze kutuletea taarifa ambayo leo tunaijadili hapa; ulimsikia na tulimsikia sote hapa ndani on Hansard akisema kwamba Bodi imeweka resistance kubwa, imekataa maelekezo yake na pengine kuna kitu kilichofichika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hizi ni kauli tata za Waziri huyu huyu mmoja; moja, ndani ya Bunge, ndani ya Kumbukumbu Rasmi za Bunge; pia kauli nyingine kwenye Kamati na kauli zake zinapingana hata saa 72 hazijapita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, ni dhahiri kwamba Waziri amelidanganya Bunge lako Tukufu kwa kusema uongo ndani ya Bunge. Pia uongo aliousema Mheshimiwa Waziri hapa Bungeni, umeleta taharuki ndani ya Bunge, ndani ya Umma wa Watanzania na zaidi kwa watoto ambao wanasikiliza Bunge kwa matumaini makubwa juu ya hoja yao ya msingi kwamba ni namna gani Serikali yao itawapatia mikopo waendelee na masomo yao ya elimu ya juu. Kwa hiyo, Waziri hakuwa makini na taarifa ambayo alikuwa anaipeleka kwenye jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika utangulizi huo, naomba Waziri aliombe radhi Bunge lako Tukufu; pili, awaombe radhi wananchi kwa kusababisha taharuki kubwa iliyojitokeza; tatu, nilikuwa naomba Waziri mwenyewe ajitathmini kama anatosha kuwa mwakilishi wa Rais kwenye usimamizi wa sekta hii. Kama hii ndiyo taswira anayoipeleka mbele ya Bunge Tukufu na kwa Umma, ajitathmini kama bado ana hadhi na uhalali wa kuendelea kumsaidia Mheshimiwa Rais kwenye nafasi hiyo. Kama akiona hawezi, ampe fursa Mheshimiwa Rais aweke mtu mwingine anayeweza kumsaidia vizuri kwa sababu yeye ni dhahiri ameshindwa kusimamia sekta yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ni jambo la kuiaibisha Serikali kuona kwamba Mheshimiwa Waziri anatamka mbele ya Bunge; kwenye Kumbukumbu Rasmi, ndani ya vyombo vya habari vyote na Umma wote ukimsikiliza kwamba taasisi anayoisimamia imekaidi maelekezo yake. Hata kama ingekuwa imekaidi, nisingetarajia Waziri wa Serikali kuja kulalamika ndani ya Bunge. Kuna machinery za kiutendaji na kiutawala ndani ya Serikali yenyewe za namna ya kuchukua hatua dhidi ya watu wanaokaidi viongozi wao wa juu, watu wanaokaidi maelekezo yanayotolewa na Serikali, kuna namna za kiutawala za kushughulika na mambo hayo na siyo kuja kulalamika Bungeni.
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Kigwangalla, kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Getere.
T A A R I F A
MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri samahani. Nilitaka Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla a-declare interest kwamba alipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii alikuwa na mgogoro na Katibu Mkuu wake ambaye kwa sasa ni Waziri wa Elimu. (Makofi)
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa mwongozo huo. Kiukweli namshukuru pia Mheshimiwa Getere kwa kulileta hili. Sina maslahi yoyote kwenye jambo hili, lakini kiuhalisia ni kwamba tumefika hapo tulipofika kwa sababu Mheshimiwa Waziri ametumia, yaani kufanya personal attack dhidi ya Bodi ya Mikopo kuja kulidanganya Bunge, kwamba Bodi imemgomea na vitu kama hivyo, badala ya kutafuta suluhu ya tatizo la msingi ambalo ni bajeti ndogo kwenye mikopo ya elimu ya juu.
Mheshimiwa Spika, ni utaratibu huo ambao ulipelekea kwenye hilo ambalo umekuwa ukilisema kwamba yeye anapenda migogoro, ugomvi na ku- attack watu binafsi badala ya kufanya kazi.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa hii nami nitoe mchango wangu kidogo kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa letu kwa mwaka mmoja unaokuja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika dunia ya sasa tunayoishi, viongozi wa zama zetu sisi, tutapambana na changamoto nyingi. Ukisoma taarifa ya Benki ya Dunia wanaweka changamoto 20, of course ndani yake humo yapo na yale mambo ambayo sisi hatuyakubali hapa kwetu, lakini katika yale mambo ambayo sisi tunayakubali, angalau nizungumzie matatu makubwa katika hizo changamoto. Ya kwanza ikiwa ni mabadiliko ya tabia nchi, pili ni umasikini uliokithiri, na ya tatu ni ile inayohusiana na njaa. Amezungumza vizuri sana Mheshimiwa Reuben Kwagilwa changamoto inayohusiana na kukosekana na uhakika wa chakula mezani miongoni mwa watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi tatu zinahusiana kwa ukaribu sana, moja, baada ya nyingine; zina connectivity ya ukaribu sana. Kwa mfano, changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi inapelekea kukosa uhakika wa chakula kwa watu wetu ambao wanategemea kilimo cha jembe la mkono. Hii moja kwa moja inaenda kusababisha mfumuko mkubwa sana wa bei (inflation). Amezungumza Mheshimiwa Kwagilwa, sina haja ya kurudia. Kwa sababu umasikini uliokithiri ambao unapimwa na Benki ya Dunia kwa kigezo kipya cha Shilingi 5,052/= kwa siku ambacho kimetangazwa juzi tu; maana yake ni umasikini wa kukosa kukosa mahitaji ya kawaida, ya lazima ya kila siku (basic needs). Watu wengi wanakuwa wamekosa mahitaji yao ya msingi kama vile malazi ya uhakika, chakula cha uhakika na mavazi yenye heshima na staha inayostahili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda katika hizo changamoto tatu zilizopo hapo, nijikite zaidi kwenye changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi. Katika zama tunazoishi kumekuwa na ongezeko kubwa sana la idadi kubwa sana ya watu katika Taifa letu, na juzi zimetangazwa figures mbalimbali za Sensa ya Watu na Makazi na ukizitazama kwa jicho la kisayansi utaona kwamba idadi ya watu, miaka thelathini ijayo itakuwa ime-double. Kama sensa safari hii inatangaza watu milioni 61, maana yake tutakuwa tumefika watu zaidi ya milioni 120 ifikapo mwaka takribani 2050 na kitu au 2060 huko. Hili lina-pose a very huge challenge kwa uongozi wa sasa na uongozi unaokuja kuhusiana na uhakika wa maisha yetu hapa nchini na duniani kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siku za hivi karibuni nimeona kuna clip moja inazunguka kwenye mitandao ya kijamii ya watu ambao wanaendesha bodaboda wakiwa wamepakia mkaa. Ukiona zile bodaboda na kulikuwa kuna mtu alikuwa anaongea kwenye hiyo clip akizungungumzia suala la mkaa akisema Ruvu hiyo, Ruvu hiyo. Pale unajifunza mambo kadhaa yafuatayo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza, ni kwamba tuna changamoto kubwa ya nishati ukanda wa Pwani. Nami nikaamua kwenda kutazama figures kwa sababu nakumbuka niliwahi kufanya kazi katika Wizara ya Maliasili na Utalii, na niliwahi ku- commission utafiti wa mahitaji ya mkaa hapa nchini. Nilipoenda kutazama figure zangu, kwenye ripoti ambayo niliwahi kuletewa huko nyuma katika mapito yangu, nilishtuka sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jiji la Dar es Salaam peke yake, kwanza katika nchi kwa ujumla wake kwa mwaka mzima tunatumia tani 1,895,248 za mkaa na asilimia 50 ya tani hizi za mkaa zinatumika katika Jiji la Dar es Salaam. Kwa sababu wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kwa zaidi ya asilimia 95 wanatumia mkaa. Hii ni biashara kubwa sana ambayo sidhani kama tunaitilia maanani sana kama nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya mkaa kwa utafiti wa mwaka 2014 uliofanywa na Benki ya Dunia kwa hapa Tanzania ilionesha ni biashara ya Shilingi bilioni moja ya Kimarekani. Kwa utafiti niliou-commission mimi nikiwa Waziri kipindi hicho, kwa mwaka volume ya biashara ya mkaa ilikuwa ni ya shilingi trilioni 2.5 za Kitanzania. Kama asilimia 50 ya biashara hii iko kwenye Jiji la Dar es Salaam maana yake unazungumzia pesa inayozunguka zaidi ya shilingi trilioni 1.2. Kwa wakati ule tulikadiria kwamba kutokana na kiwango cha kukusanya mapato cha shilingi 250 kwa kila kilo ya mkaa inayokusanywa na Serikali kwa maana ya Wakala wa Huduma na Misitu, tungeweza kukusanya shilingi bilioni 575 kama biashara ya mkaa ikiwa properly regulated, ikasimamiwa vizuri, badala ya check points zilizopo sasa hivi ambazo ni kama tu zinahalalisha tu watu ambao tayari wameshafanya uharibifu kwenye misitu, kama ikiwa regulated, namna nzuri ya kuvuna na kukusanya mapato tunaweza tukatumia fedha hizi kwenda kuwekeza kwenye uzalishaji wa mkaa huu wa clean energy kama vile briquettes, hizi tofali zinazotengenezwa kwa pumba za mpunga na vitu vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaweza kutumia pesa hizi kwenda kuwekeza kwenye utumiaji endelevu wa misitu (sustainable use of our forest resources), lakini bahati mbaya sana tunakusanya chini ya Shilingi bilioni 30 kwa mwaka kutokana na mkaa. Hilo lilikuwa ni jambo langu la kwanza ambalo nilipenda kulizungumzia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nilipenda kuzungumzia suala la kuanzishwa kwa mfuko wa kuhifadhi bei za mazao; sijui kama nimetafsiri Kiswahili kwa usahihi, lakini nazungumzia Price Stabilization Fund; kwamba kama Taifa tunahitaji kuwa na mfuko maalum wa kudhibiti bei za mazao hapa nchini. Pia mfuko huu utatuwezesha kununua chakula pindi chakula kipo chini kwa uhakika zaidi na kukigawa kwa wananchi kipindi ambapo chakula kimepungua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilisema pale awali kwamba changamoto kubwa hapa nchini kwetu kwa watu wetu wa kawaida ni chakula na mahitaji ya msingi tu, wala watu wetu hawataki mambo makubwa sana. Sasa kama tutaweka utaratibu mzuri wa chakula, na pia ili tuwe na utaratibu mzuri wa kuhifadhi chakula, maana yake tunahitaji utaratibu mzuri wa kuhifadhi mazingira, kwa sababu watu wetu wanalima kwa jembe la mkono na wanategemea zaidi kilimo cha mvua za Mwenyezi Mungu. Sasa kama hakuna mvua kutokana na uharibifu wa mazingira, maana yake hatutaweza kupata chakula cha kutosha katika Taifa letu.
Kwa hiyo, nilikuwa napenda kumshauri Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango katika mapendekezo yake aliyoyaleta atazame sana eneo la mabadiliko ya tabia nchi, na eneo la kuanzisha Price Stabilization Fund ili bei za mazao zikishuka, mfuko unaweka pale, wakulima wanapata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano kwenye korosho tuliwapa matumaini wakulima wa korosho, bei zikapanda mpaka zikafika zaidi ya shilingi 2,600. Kawaulize, leo wanauza korosho yao kwa shilingi ngapi? Ni chini ya shilingi 2,000. Kwenye pamba tuliwapa matumaini wakulima wa pamba na wafanyabiashara wa pamba kwamba pamba inakwenda mpaka shilingi 2,000; kawaulize mwaka huu wameuza pamba yao kwa Shilingi ngapi; na kama wanunuzi walikuwepo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ambacho kitaweza kututoa kwenye hii changamoto ya kutatua matatizo ya wakulima kila mwaka ni kuwa na mfuko...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, ahsante kengele ya pili.
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2021 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa fursa hii ya kuchangia kwenye mpango na Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/2023. Awali ya yote nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan na Serikali yake kwa kuja na bajeti nzuri ya kimkakati, na mikakati iliyopo ndani ya bajeti hiyo inaendana na nyakati tulizopo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiisoma bajeti Kuu ya Serikali, ukatazama namna ambavyo Serikali inaenda kupunguza kodi, namna ambavyo Serikali inaenda kuwekeza kwenye miradi ya kimkakati, utaona moja kwa moja kwamba taswira na umbile la bajeti hii ni taswira ya kwenda kufanya economic recovering kufuatia kuanguka kwa uchumi wa Kitaifa na Kimataifa kulikosababishwa na mambo makubwa mawili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza likiwa, kuanguka na kudorora kwa uchumi kulikosababishwa na mlipo wa ugonjwa wa Covid-19 mwaka 2019 ambapo madhara yake tunayapata mpaka leo. Jambo la pili, mdororo wa uchumi na changamoto tunazopitia leo hii zinafanana na zile za mwaka 1979 na 1980 ambao ulisababishwa na mapinduzi ya kule Iran ya wale Ma-shaah wa Iran ambapo mafuta kutoka Iran hayakuweza kuingia kwenye Soko la Kimataifa kirahisi na hivyo gharama za mafuta kwa maana ya force refuels zika-double.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sasa hivi pia kumetokea mgogoro baina ya nchi ya Ukraine na Urusi ambapo hususan Urusi ni nchi ya pili kwa uzalishaji mkubwa wa mafuta na ni nchi ya kwanza kwa uzalishaji wa gesi. Kwa maana hiyo, kudorora kule kwa uchumi tunakokupata sasa hivi na kupanda kwa bei za mafuta kumesababishwa na mgogoro huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya changamoto za kiuchumi zilizotokea mwaka 1980 ama ukitazama changamoto za kiuchumi zilizotokea mwaka 1930 na miaka iliyofuatia kufuatia the great depression, utaona sera za kiuchumi ambazo Serikali za nchi mbalimbali zilichukua zilikuwa ni za supply side economics, kwa maana ya sera ambazo proponents wake ni wachumi kama akina John Bernard King ambao walikuwa wanazungumzia kwanza kuhusu Serikali kuongoza uchumi kwa maana ya kufanya Government intervention na kuachana na sera za kwamba Serikali haitoshikilia chochote kwenye uchumi, itauacha uchumi wenyewe ujiendeshe na mwisho wa siku kimbunga kikipita basi bahari itatulia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sera hizi ninaziona moja kwa moja kwenye bajeti hii ya mwaka 2022, na pia naziona sera hizi kwenye mchakato mzima wa kuendesha uchumi wa Taifa letu katika kipindi cha mwaka mmoja cha uongozi wa Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, ambapo mambo yanayofanyika ni pamoja na kwanza kupunguza viwango vya kodi. Tumeona kodi zimepunguzwa maeneo mengi, na la pili ambalo tunaliona ni kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati kwa maana ya kwamba Serikali inaachia fedha ilizonazo, inazipeleka kwenye jamii kwa kutekeleza miradi mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, tunaona Serikali ikichukua mikopo kutoka sehemu mbalimbali na hata sasa hivi ukisoma hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Fedha na mipango, unaona tayari wako katika negotiation ya mkopo wa zaidi ya Shilingi trilioni moja kutoka Benki ya Dunia. Wapo katika negotiation ya mkopo wa zaidi ya Shilingi trilioni mbili kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), lakini na pia unaona zile fedha za shilingi trilioni 1.3 za UVIKO ambazo zote zinakuja kuingia katika uchumi wa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa napenda kuishauri Serikali iendelee katika trajectory hiyo hiyo, wasisikilize kelele za watu wanaosema tunakopa sana kwa sababu hao hawawatakii mema wananchi wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, na kwanini nalisema hili, anasema, John Bernard King kwamba katika zama kama hizi ambapo unataka kuchochea ukuaji wa uchumi kufuatia mdororo, ni lazima Serikali iingilie, ni lazima Serikali ichukue hatua za muda mfupi, hatua za dharura za kuwakomboa wananchi wa kipato cha chini dhidi ya ukali wa maisha unaosababishwa na mdororo wa kiuchumi. Hatua zenyewe ni pamoja na kuhakikisha tunaongeza ajira kwa kuongeza uwekezaji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, bila Rais wetu na Serikali yake kutoka nje, kuboresha mahusiano ya Kimataifa, kurudi ndani kuboresha mifumo na misingi ya utawala bora, hatuwezi kukopesheka, hatuwezi kuvutia wawekezaji kutoka nje kuja kuwekeza katika uchumi wetu, na hatimaye kuzalisha ajira, kuzungusha fedha katika mzunguko wa uchumi wetu, na mwisho wa siku tutaanguka vibaya sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, napenda kuwaambia Serikali kama ambavyo alifanya Ronald Regan miaka ya mwanzo ya 1980 na sera zake zikajulikana maarufu sana kama Reganomix na ambazo mimi pia nimezifuatilia kwa ukaribu na nimeandika katika kitabu changu cha Kigwanomix, napenda pia kuendelea kuwaomba watu wa Serikali wakae katika mtiririko huo huo wa kutanua uchumi wetu kwa kufanya uwekezaji lakini pia kuboresha mahusino ya Kimataifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hizi hatua zote ambazo zinachukuliwa na Mheshimiwa Rais nimeziweka katika makundi 10. Ukizitazama kwa undani wake unaweza ukaziita Samianomix kama ambavyo kule Marekani mwaka 1980 waliziita sera za Rais wa wakati huo Bwana Ronald Regan, Reganomix. Kwa hiyo, nami napenda kuzitaja hatua ambazo zinachukuliwa ni pamoja kupunguza viwango vya kodi, kufuta baadhi ya mipango isiyo na tija kama hii ambayo ameisema Waziri wa Fedha wakati anasoma bajeti yake; kupunguza magari, lakini pia gharama za kusimamia magari ya watumishi wa umma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ya tatu, kupunguza matumizi ya Serikali kama ambavyo tunaona Waziri wa Fedha alipohutubia, kupunguza riba kwenye benki zetu kama ambavyo tunaona kwenye benki katika kipindi cha Mheshimiwa Mama Samia, baadhi ya benki zimeshusha viwango vya riba mpaka asilimia tisa. Pia kuendelea kukopa mitaji kutoka nje ili kuleta katika uchumi wetu; sita, kuboresha utawala bora na uhusiano wa Kimataifa kama ambavyo tunaona, Rais ana-reach out kwenye Mataifa mbalimbali, kama ambavyo tunaona Rais ameweza kuitangaza Tanzania vizuri sana kupitia Royal Tour.
Mheshimiwa Naibu Spika, na hapa napenda nitoe mapendekezo kwamba Waziri wa Maliasili na Utalii akatazame mkakati ambao tulianza kuufanya kipindi mimi nikiwa pale Wizarani wa kutangaza vivutio vya Utalii kwenye michezo hususan Soka la Ulaya. Hii ni katika mikakati ambayo itaungana na Royal Tour katika kuvutia wawekezaji na wageni kuja kutembelea Tanzania. Ni mkakati ambao utaendana na Samianomix.
Mheshimwia Naibu Spika, la saba ni kutekeleza miradi ya kimkakati kwa kutumia fedha za nje badala ya kutumia fedha za ndani. Kwa hiyo, ni katika ile ambayo ameisema Waziri wa Fedha hapa EPC+F.
Mheshimiwa Naibu Spika, namba nane ni kuendelea kuwekeza kwenye sekta ambazo zinagusa watu wengi ikiwemo sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kama ambavyo bajeti inasema; tisa, ni kuboresha huduma za jamii kama ambavyo tumekuwa tukifanya; na kumi, kuwekeza zaidi kwenye miradi ya kimkakati kwa mfano miradi ya gesi, aliongea vizuri sana Mheshimiwa Prof. Muhongo, sina haja ya kurudia. Siyo tu kwenye gesi wameanza na LNG plant, waende kwenye miradi ya mbolea ambayo inatokana na gesi, waende kwenye miradi ya madawa ambayo inatokana na gesi, na tukifika hapo, tutakuwa tumeweza kuchomoka katika mtanziko tulioingia kutokana na changamoto nilizozisema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, muda umeniishia, ningeweza kuongea mengi zaidi. Nashukuru kwa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Taarifa ya Kamati Maalum iliyoundwa Kuchunguza Mgogoro wa Ardhi kati ya Mwekezaji kwenye Shamba la Malonje na Vijiji Vinavyolizunguka Shamba hilo Kikiwemo Kijiji cha Sikaungu katika Jimbo la Kwela
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa fursa ya kuchangia asubuhi ya leo. Awali ya yote narejesha shukurani zangu za dhati kwa Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aliyetujalia uhai, na aliyetuwezesha kukutana hapa siku ya leo tukiwa wazima wa afya.
Mheshimiwa Spika, pili, nakupa shukurani Mheshimiwa Spika, kwa kunipa fursa ya kuwa Mjumbe wa Kamati hii na kazi yetu haikuwa rahisi sana, lakini kwa uhakika, kwa namna ulivyokuwa umeweka mchanganyiko mzuri kwenye Kamati, haikutushinda. Tumeifanya kazi hiyo kwa weledi wa hali ya juu, na kwa uaminifu na uzalendo uliopitiliza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naunga mkono mapendekezo yote yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati yetu na ninaomba niwashawishi Waheshimiwa Wabunge wenzangu waunge mkono mapendekezo hayo kama yalivyo ama wayaboreshe zaidi, kama watakavyoona inafaa.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa mchango wangu ili kutia msisitizo tu kwamba pendekezo la kwanza ambalo tumelitoa mbele ya Bunge lako Tukufu linazingatia maslahi ya kila mdau kwenye eneo husika. Sababu ya kupendekeza hivyo ni ukweli na uhalisia wa kwamba kumekuwa na gaps ambazo zimetufikisha kwenye mgogoro huu kutoka kila upande. Kuna matobo upande wa Serikali ambayo ndiyo mengi zaidi, lakini pia kuna matobo upande wa wananchi, lakini pia kuna matobo upande wa mwekezaji.
Mheshimiwa Spika, sasa bila kurudi kwenye drawing board na kuanza upya mchakato wa namna ya kukidhi maslahi ya kila mdau katika eneo lile hatuwezi kutatua mgogoro huo. Ndiyo maana Kamati baada ya kutafakari kwa kina, lakini pia baada ya kuangalia taarifa mbalimbali kufika uwandani tuliona tuisaidie Serikali kwa kuipa ushauri kwamba ianzie kwanza kwa kufuta umiliki wa shamba hilo kwa kila mwenye umiliki katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, mwekezaji anamiliki eneo lake lifutwe, baadhi ya watu waliopewa blocks wanamiliki hati zao zifutwe, Gereza la Mollo linamiliki hati yake ifutwe, vijiji vimepimwa juu ya ardhi ya kawaida (general land) navyo hizo hati zifutwe ili sasa upimaji ufanyike upya bila makosa kwa kuzingatia mahitaji, uwezo wa uwekezaji, shughuli wanazofanya watu na pia kwa kuzingatia maslahi ya watu wote waliopo katika eneo hilo. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumetenda haki, lakini pia tutakuwa tumetatua mgogoro kwa kiasi kikubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika upungufu mkubwa uliopo pale kwa upande wa Serikali, kwa mfano, shamba limekuwa likiongezeka ukubwa kutoka mwaka hadi mwaka kutokea enzi za aliyekuwa mwanzishaji wa hilo shamba alikuwa anaitwa Bwana George Damm, Mzungu huyu Mlowezi mwaka 1930. Akaja mke wake akaongeza ukubwa mwaka 1955, wakaja NACO ambao ni Shirika la Serikali mwaka 1967 wakaongeza ukubwa, wakaja tena NARCO wakaongeza ukubwa mwaka 1973. Shamba limekuwa likikua kwa kiasi kikubwa sana mpaka likafikia ekari 47 na ushee.
Mheshimiwa Spika, katika hatua zote hizo za kuongeza ukubwa wa shamba na kubadilisha ardhi ya vijiji vya asili kutoka kubwa ardhi ya vijiji kwenda kuwa general land hakukuwahi kuwa na ushirikishwaji wa wananchi, hakukuwahi kufuatwa taratibu za kubadilisha ardhi ya kijiji kwenda kuwa ardhi ya kawaida (general land). Sasa kama taratibu hazikuwahi kufuatwa toka awali uhalali hauwezi kupatikana leo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapa hata ukitazama wanafalsafa mbalimbali wanaozungumzia kuhusu haki za binadamu wanasema hata siku moja matokeo hayawezi kuwa halali kama mchakato wa kuyatengeneza hayo matokeo hakuwa halali. Hapa napenda kumnukuu Tom Taylor ambaye ni mbobezi wa Falsafa ya Sheria anazungumzia kuhusu msingi wa uwepo wa haki. Kwa hiyo, Kamati kwa kutafakari kwa kina, tulifikia kushauri kwamba kwa kuwa mchakato wa kulianzisha shamba lenyewe pale awali na hii inatokana na hadidu rejea ya kwanza uliyotupa hakukuwa halali, basi matokeo yote yanayokuja huku mwisho hayawezi kupata uhalali. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hivyo, ndiyo maana tukapendekeza pale kwenye maazimio kwamba basi turudi kule mwanzo tutengeneze kwanza uhalali wa shamba lenyewe. Baada ya kutengeneza uhalali, sasa basi watu wote kwa kuzingatia mambo yaliyotokea, uwekezaji walioweka na uendelezaji walioufanya wapatiwe vipande vipande katika shamba husika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baadaye vilikuja vikapimwa Vijiji vya Sikaungu, Msanda Muungano na vingine vinavyozunguka pale na vikapewa hati vimekuja kupewa hati juu ya ardhi ya general (ardhi ya shamba) shamba tayari lina hati ambayo ni general land ama ardhi ya kawaida. Vijiji vikaja vikapimwa juu vikawa super reimposed juu ya general land ambayo haikubaliki kisheria na hivyo mgogoro tena wa kisheria unatokea.
Mheshimiwa Spika, ndiyo maana wananchi wa Sikaungu hata walipogawia eka zile 1,000 walikataa. Wakasema hizi eka 1,000 zipo kwenye ardhi ya kijiji chetu kwa sababu wana hati. Sasa mtu ana hati ya kijiji, kijiji kimesajiliwa, kijiji kimepimwa na hilo shamba limo katika ardhi yake ya kijiji. Yeye anasema ni eneo lake kwa nini agawiwe tena wakati ni eneo lake. Kwa hiyo, huwezi kutatua mgogoro katika mazingira hayo. Ni lazima ufute hati inayosajili kijiji, hati inayotoa mipaka ya Kijiji, na pia ufute hati inayoweka mipaka ya shamba. Ukishafanya hivyo sasa ndio utapima useme kijiji kitaishia hapa na shamba litaanzia hapa, ukifanya hivyo sasa utatua mgogoro.
Mheshimiwa Spika, kwa hali ilivyo leo hii wananchi wanaamini eneo ni la kwao lipo ndani ya kijiji na kweli wana hati na wana usajili wa kijiji chao halali kabisa. Mbali na hivyo wananchi hawa wana haki nyingine ya msingi ya kiasili (customary rights) za kumiliki hilo eneo kwa sababu ni nyumbani kwao ni mahali pa asili yao.
Mheshimiwa Spika, siku zote tunafanya makosa makubwa sana katika nchi hii kuamini kwamba tunaweza tukaenda sehemu tu, tukapima ardhi, tukaanzisha hifadhi ama tukapima ardhi tukaanzisha shamba kwa maendeleo sawa. Sawa kabisa hakuna anayekataa, lakini hatupati haki ya kuchukua ardhi ya asili ya wananchi. Hatupati hiyo haki. Tutaipata hiyo haki kama tutafuata taratibu na taratibu zimewekwa na sheria na sheria inataka kwanza Mheshimiwa Rais, apewe atoe ridhaa yake kwamba tunabadilisha ardhi ya kijiji kuwa ardhi ya general kwa shughuli za maendeleo…(Makofi)
SPIKA: Malizia Mheshimiwa dakika 10 zimeshaisha.
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, sawa namalizia.
Mheshimiwa Spika, pili, tunapata uwezekano wa kufanya hivyo baada ya hiyo ridhaa ya Mheshimiwa Rais, kutolewa, itolewe notice ya siku 90, wananchi wakubali ardhi yao kuchukuliwa ama isichukuliwe. Wananchi nao wakitoa ridhaa, sasa ndiyo unabadilisha ardhi. Sasa hili shamba toka enzi za George Damm mpaka miaka hii mchakato wa namna hiyo hakuwahi kufanyika. Hivyo, hakukuwahi kuwa na ridhaa ya mamlaka zinazopaswa. (Makofi)
SPIKA: Haya. Ahsante sana.
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa fursa hii ya kuchangia kwenye Hotuba ya Waziri wa Maji mdogo wangu Mheshimiwa Aweso. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya uhai na fursa ya kutukutanisha hapa siku ya leo tukiwa wazima wa afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili nitumie fursa hii kwa namna ya Kipekee kabisa kumpongeza Mheshimiwa Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kazi nzuri anayoendelea kuifanya kwa kila sekta hususan kwenye Sekta hii ya Maji. Alipokuwa Makamu wa Rais alidhamiria na akaweka wazi dhamira yake ya kumtua ndoo mama kichwani. Ikawa neema Rais akawa ndiyo yeye na ameisimamia azma yake ya kumtua ndoo ya maji mama kutoka kichwani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu alipopata fursa ya kuongoza Taifa letu, upatikanaji wa maji kwa wastani kwa sisi wenye majimbo ya vijijini haukuzidi 45%. Kwa Jimbo langu mahususi upatikanaji wa maji ulikuwa ni wa wastani wa 43%. Hata hivyo leo nasimama hapa kuongea, Jimbo la Nzega Vijijini tunapata maji kwa kiwango cha 79%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nimepata fursa ya kuwa Mbunge kwa mara ya kwanza mwaka 2010, upatikanaji wa maji katika Jimbo lote la Nzega ukichanganya na Nzega mjini ya sasa ulikuwa ni wastani wa 23%. Nilifika kwenye Kijiji kimoja kinaitwa Kabale pake kwenye Kata ya Nata, wananchi wakati wa kampeni waliniletea chupa ya maji wanayotumia yenye rangi kama juice ya watermelon (juice ya tikiti maji). Leo hii watu wa Kabale wanakunywa maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii ninapozungumza hapa watu wa Kabale wanapata maji yanayotiririka kutoka bombani wala siyo maji ya kisima. Watu wa Kabale wapo kilometa takribani tatu kutoka kwenye Mradi mkubwa uchimbaji wa dhahabu uliokuwepo pale Nzega maarufu kama The Golden Pride Project. Hata hivyo, pamoja na kuwa kwenye rasilimali kubwa ya namna hiyo, hawakuwa hata na maji ya kutumia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii dhahabu imeondoka yamebaki mashimo lakini ameingia Rais mwenye nia thabiti ya kuleta maendeleo na ustawi wa watu. Watu wa Kabale wanapata maji safi na salama yanayotiririka kutoka bombani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana mdogo wangu Mheshimiwa Aweso kwa kazi nzuri na kubwa anayoifanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais wetu. Maana Mheshimiwa Rais anahitaji paratroopers kama Mheshimiwa Aweso ili azma yake ya kumtua mama ndoo ya maji kichwani iweze kutimia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, japokuwa jukumu hili naona linachukua nguvu na nafasi ya ujana wa Mheshimiwa Aweso lakini hakuna namna ni lazima usimame imara uende ukaitende. Mheshimiwa Aweso ulikuja hapa Bungeni ulikuwa kijana mdogo handsome mwembamba. Leo hii una kipara, mvi na unazeeka kwa sababu ya kutatua kero za maji na kwa sababu ya kumsaidia Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kutimiza azma yake. Kwa kweli kwa pamoja wewe Mheshimiwa Aweso na viongozi wote akiwemo Katibu Mkuu wetu mpya Bi. Mwajuma Waziri, tunawapongeza sana kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya. Hatuna malalamiko mengi, tuna shukrani zaidi lakini tunawaombea dua pamoja na Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wanazunguka huko wanamsema vibaya sana Mheshimiwa Rais, amenyamaza kimya na hawajibu. Hata hivyo, mimi napenda leo kumuombea dua Mheshimiwa Rais na ninafahamu wananchi wa Kata ya Kigandwa ambao hawakuwa na maji wakati anapita na wewe Mheshimiwa Aweso ukaahidi na ukapeleka mradi wa shilingi bilioni mbili leo hii wanapata maji, wanamuombea dua Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakina mama wa Kabale ambao hawakuwa na maji walikuwa wanakunywa maji yenye rangi ya watermelon wanamuombea dua Mheshimiwa Rais, wanakuombea dua wewe Mheshimiwa Aweso, wanawaombea dua viongozi wote wa Wizara yetu ya Maji. Pia, hao hawana malalamiko na wala hawasikilizi kelele na vurugu zinazofanywa na viongozi wapuuzi wanaozunguka huko kumtukana na kumlaumu Mheshimiwa Rais wetu. Tunataka mpate nguvu na mjue sisi tuko nyuma yenu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwakani mwaka 2025 tunamuombea dua Mheshimiwa Rais wetu aweze kupita kwa kura nyingi za kishindo. Kwa sababu kwa hili la maji, sadaka aliyoitoa ni kubwa sana na akina mama wataendelea kumuombea dua, watamsimamia, watampigania na sisi tutakuwa nyuma ya akina mama ambao amewatua ndoo ya maji kichwani, kwenda kumuombea dua na kumpigania ili kuhakikisha anapata ushindi wa kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nimeona watu wa Pangani wako hapa. Mheshimiwa Aweso, watu wa Pangani kama wananisikiliza, wakulinde, wakulee, wakupiganie na wakatae mchwa wanaopita kwenye Jimbo lako wakupe kura za kishindo mwakani ili uendelee kutimiza majukumu yako. Mimi ninaamini Mheshimiwa Rais hatokutoa kwenye Wizara hii. Ninakuombea dua ubaki hapo uendelee kutufanyia kazi njema ambayo unaifanya. Vilevile, namuombea mdogo wangu Mheshimiwa Engineer Kundo katika msafara huo huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, muda ni mdogo sana lakini namshukuru sana Mheshimiwa Aweso na viongozi wote wa Wizara kwa kuitikia maombi yetu tuliyomuomba Mheshimiwa Rais katika ziara yake aliyopita mwezi Oktoba mwaka 2023 kwenye maeneo matatu tu ambayo yalikuwa yamebaki hayana mradi wowote ule wa maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nasimama hapa kuzungumza maeneo hayo yote yana miradi. Mradi wa Kigandu unatekelezwa na juzi engineer wangu wa maji Ndugu Ntulo, amepeleka mradi kwenye eneo lingine na leo kwenye bajeti hii kuna kisima kirefu kwenye Kata ya Mwasala ambazo hazikuwa na maji.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja na ahsante kwa nafasi hii.
MUswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu wa mwaka 2021 (Toleo la Kiingereza)
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii na awali ya yote nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema kwa kutujalia uhai, lakini pia kwa kutuwezesha kukutana hapa siku ya leo tukiwa wazima, bukheri wa afya.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nitachangia kwenye maeneo mawili tu, vifungu viwili; kifungu pendekezwa cha 18 kwenye muswada na kifungu cha 19 kwenye muswada.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu cha 18 kinaenda kubadilisha kifungu cha 30 kilichokuwepo kwenye sheria ya awali, ile sheria ya mwaka 1973 ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2002 ambapo mapendekezo ya marekebisho yaliyopo kwenye muswada, kama yalivyowasilishwa na Serikali, yanaenda kupandisha viwango vya mali kutoka assets za shilingi milioni 100 ama zaidi kwenda kwenye shilingi milioni 300 au zaidi, lakini pia gross turnover ya shilingi milioni 50 hadi shilingi milioni 150; kwamba wafanyabiashara wote ambao watakuwa wana-assets za zaidi ya shilingi milioni 300 ama gross turnover ya zaidi ya shilingi milioni 150 watawajibika kwa mujibu wa sheria kuajiri wahasibu ambao wana CPA ama wahasibu wale wakaguzi wa hesabu ambao wamesajiliwa kama CPA PP (Certified Public Accountant in Public Practice).
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi ninadhani pamoja na Serikali kuleta mapendekezo ya marekebisho ambayo yanaongeza viwango kutoka milioni 100 mpaka 300, kutoka milioni 50 mpaka milioni 150 bado viwango hivi ni vidogo sana na ningependelea Serikali watazame jambo hili katika muktadha tofauti kidogo. Kwamba, bado milioni 300 ni ndogo sana kuwa ni mali za mfanyabiashara, kuna wafanyabiashara kwa mfano kwenye nature ya biashara kama ya dawa (pharmacy); kama kibanda kile ni mali yake na ana warehouse hizo assets tu peke yake zinaweza zikafika hata milioni 200, lakini pia dawa, ule mzigo alioweka mle ndani, unaweza ukazidi milioni 200 hata milioni 300.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ukichanganya vyote hivi vitazidi milioni 500, milioni 600 kama mtaji na hivyo, kumtaka lazima awe na mhasibu nadhani ni kumuongezea cost za uendeshaji. Ni kumuongezea gharama za uendeshaji na usimamizi wa biashara yake ambazo pengine hazihitaji kwa sababu kuna uwezekano mkubwa, mfano mimi binafsi ni Daktari wa Tiba, mke wangu ni Mfamasia ama ni daktari kama ilivyo sasa, mtoto wetu akawa mfamasia, tukaamua kufungua biashara ya pharmacy na tukakaa sisi wenyewe kama familia pale, hatuhitaji mhasibu. Na sisi wala hatuhitaji mifumo complicated, tunahitaji mfumo rahisi wa computer ambapo tunaweka data za mauzo, data za stock na tukitoka jioni tunafunga ofisi yetu tunarudi nyumbani, mhasibu wa nini hapo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kutikana na nature ya biashara yetu, kutokana na mtaji, kutokana na gross turnover ambayo tunapata tutalazimika kuweka mhasibu wakati sisi hatuhitaji mhasibu.
Kwa hiyo, mapendekezo yangu ni kwamba, hata hivi viwango vinavyopendekezwa vya assets za thamani ya milioni 300 ama gross turnover kwa mwaka ya shilingi milioni 150 yarekebishwe na viwango hivi viongezwe pengine kutoka milioni hiyo 300 inayopendekezwa kwenda mpaka kati ya bilioni moja na nusu hadi bilioni mbili na kutoka milioni 150 mpaka bilioni moja kwa kiwango cha chini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hii itafanya requirement, uhitaji wa kuwa na mhasibu kwenye organization kuwa wa maana zaidi kwa sababu, hii ni biashara kubwa. Na pengine bilioni moja ni mtaji mkubwa na hivyo, mtu anayeendesha biashara ya kuzungusha bilioni moja kiukweli anahitaji mhasibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini mfano mkulima ana shamba ekari 500 ama ekari 1,000 ana matrekta mawili, ana power tillers, ana ma-godown hapo site yake, ana mashine ana harrow, ana planters kwa ajili ya kupandia, ana mashine ya kupulizia dawa, ukiangalia assets base ya huyu mfanyabisahara ambaye ni mkulima kimsingi na Wabunge wengi nafahamu hapa ni wakulima, utakuta uwekezaji kwa maana ya lile shamba, ma-godown, pamoja na hizo farm implements ambazo anatumia kufanya shughuli ya kilimo inazidi bilioni moja.
Sasa turnover anaweza akalima ekari 100 ama akalima ekari 200 na mwisho wa siku pengine bei zimeanguka kama zilivyoanguka mwaka huu bei za baadhi ya nafaka hapa nchini, mauzo yake yakawa chini ya shilingi milioni 200/
300. Ukimtaka huyu mtu lazima awe na mhasibu ni kumuwekea masharti ambayo yanamuongezea gharama za uendeshaji ambazo pengine hazihitaji sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, tunapotunga sheria ni lazima tuwe makini sana kwa sababu kuja kurekebisha ni kazi na sidhani kama Ndugu yangu Mheshimiwa Mwigulu atakapoanza kusimamia utekelezaji wa sheria hii hatopata kelele endapo viwango vitakuwa chini. Maana yake wanaofanya biashara ya mabeli ya mtumba wana zaidi ya milioni 300 wanayozungusha wote watatakiwa wawe na wahasibu, wanaofanya biashara ya maduka ya jumla wote watatakiwa kuwa na wahasibu na sidhani kama kwa sasa tunahitaji kelele hiyo katika siasa za nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili nililopenda kuzungumzia ni kifungu cha 19 cha muswada ambacho kinaenda kubadilisha sheria hii iliyopo sasa kwa kuongeza kifungu cha 30A, 30B na 30C, ambayo hii inahitaji kuwe na mawasilisho ya audited financial statement kwenda NBAA kwa ajili ya record. Kwamba, kila mhasibu anayekagua hesabu za taasisi ama za mfanyabiashara mmoja lazima azichukue zile hesabu na awajibike kuziwasilisha NBAA kila mwaka kadiri anavyofanya biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kutaka uwajibikaji, pamoja na kutaka ku-enhance transparency, kuweka uwazi zaidi kwenye biashara, hiki ni kifungu hatarishi sana kwa ustawi wa biashara hapa nchini na kwa nini nasema ni hatarishi?
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kifungu ambacho kitaenda kufanya biashara nyingi sana zikwame kupata mikopo kwenye bank zetu. Sitaki kuongea sana mambo ambayo yako unethical, lakini nadhani hata kukiweka hiki kifungu chenyewe ni completely unethical, ni kinyume kabisa na maadili ya confidentiality kwa maana ya siri kati ya mhasibu na directors wa kampuni ambayo ameenda kuikagua, kwamba mhasibu anawekewa kifungu hapa ambacho kinamtaka alazimike kupeleka hesabu za mteja wake NBAA wakati yeye ana-non disclosure agreement na mteja wake kwamba, asitoe siri ya zile hesabu ambazo anaenda kumkagua huyu mhasibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu hiki kinaleta hatari gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, kifungu hiki…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Malizia Mheshimiwa, kengele ya pili imeshagonga.
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, eeh, muda umeisha? Ahsante naomba nimalizie tu hapa dakika moja tafadhali.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu Serikali wanapo-introduce kifungu hiki lengo lao ni kutaka kuweka uwazi zaidi, lakini pia lengo lao ni kutaka kuwadhibiti wale wahasibu ambao wanatengeneza hesabu mbili-mbili kwenye kampuni moja. kwamba, kuna hesabu zinazoenda benki, lakini pia kuna hesabu zinazoenda TRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hakuna asiyejua kwamba kumekuwepo na hii practice toka kabla ya uhuru na itaendelea kuwepo kwa sababu hii ni practice ambayo inawafanya wafanyabiashara warekebishe hizo hesabu kwa kuzi-doctor in some way ili waweze kukopesheka. Hii ni siri ambayo ipo na tunaifahamu na sidhani kama wazee wetu mwaka 1973 walipokuwa wanaenda kukitunga hiki kifungu hawakuwa wanajua hii practice ipo; walijua, lakini waliamua kunyamaza wakaacha hiyo environment ya biashara ifanye kazi kama inavyofanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu wazee wetu walijua kwamba, saa nyingine ukikuta jinni limefunikwa kwenye chupa, basi usilifungulie. Hujui wazee waliolifungia humo ndani walikuwa na nia gani.
NAIBU SPIKA: Haya, ahsante sana Mheshimiwa. Hoja yako imeeleweka, ahsante sana.
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Fedha wa Mwaka 2020 (Toleo la Kiingereza)
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa fursa hii. Nami naomba nitoe mchango wangu kidogo kwenye Sheria ya Fedha ya Mwaka 2021.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu wa kwanza utahusiana na Sheria ya Ushuru wa Barabara na Mafuta, Sura 220 hususan yale mapendekezo yanayowekwa kwenye kifungu cha nyongeza cha 4A(a). Kimsingi hapa nakubaliana sana na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya Bajeti yote kwa ujumla wake lakini napenda tu kuweka msisitizo kwamba pengine imefika wakati sasa Serikali kwa kuzingatia umuhimu wa barabara za vijijini kiuchumi na kijamii ikafanya maamuzi mahsusi na ya haraka kabisa ya kuanzisha Mfuko wa Barabara Vijijini. Naamini hili litakuwa ni kiini cha kuleta mabadiliko makubwa katika namna ambavyo TARURA itafanya kazi yake kwa tija na kwa ufanisi kwenye kujenga barabara za vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili halihitaji kusisitizwa sana kwa sababu umuhimu wa barabara unajulikana kiuchumi lakini pia kijamii. TARURA uwezo wake umeonekana kuwa mdogo sana sana kifedha lakini pia hata kiufanisi kutokana na kwamba bado ni taasisi mpya, changa na inahitaji Serikali iwekeze nguvu zake kwa kiasi kikubwa ili iweze kutufikisha kwenye malengo tuliyokusudia wakati tunaanzisha TARURA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuanzisha Mfuko maalum wa Barabara Vijijini itasaidia hivi vyanzo vyote mbalimbali vya mapato ambavyo ni kwa malengo ya kuboresha ujenzi wa barabara vijijini basi pesa hizi ziende kule moja kwa moja badala ya kuingia kwenye Mfuko Mkuu Hazina ambapo tuna mashaka pengine kunaweza kukawa na ucheleweshwaji lakini pia kunaweza kukawa na urasimu mkubwa. Tunaona ni vyema tuungane na mapendekezo ya Kamati ya Bajeti kwamba uanzishwe Mfuko Maalum wa Barabara Vijijini na hili liwe ni jambo la kipaumbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Marehemu Benjamin Mkapa Mungu amrehemu alianzisha huu Mfuko wa Barabara ambao leo hii umetuletea faida kubwa sana katika ujenzi wa barabara hapa nchini. Mimi napenda na Mama yetu naye Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aanzishe Mfuko wa Barabara Vijijini na hii iende ikawe legacy yake kwa sababu nchi inasonga mbele sio kwamba inarudi nyuma ama inabaki pale pale, hatuwezi kubaki na mambo yale yale machache ambayo yalifanywa na viongozi waliotangulia. Ni wakati kwa sisi kama Bunge kusimama kwa nia ya dhati kabisa kumshauri Mheshimiwa Rais wetu naye aweke legacy yake kwenye eneo la ujenzi wa barabara vijijini jambo ambalo sisi Wabunge na wananchi linatugusa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo napenda kuchangia ni kuhusiana na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290 kuhusiana na mabadiliko ambayo yalikuwa yameletwa na Serikali kwenye Muswada ambapo produce cess ingepaswa kuondolewa halafu mapato yake ikawa kama shirika ama kampuni imelipa service levy basi hiyo itoshe kuwa ndiyo kodi pekee ambayo ingetozwa kwa shirika husika. Hili ni jambo lenye hatari kubwa sana hususan kwa zile Halmashauri ambazo zinategemea kupokea mapato yake kutokana na mazao zaidi kuliko kitu kingine chochote kile. Halmashauri zenye mazao ya pamba, tumbaku, korosho, chai na kahawa kwa kiasi kikubwa sana zinategemea produce cess kama chanzo kikuu cha mapato ya kuendeshea shughuli zake. Hivyo, naomba jambo hili kwa kweli lisitishwe na lisipite kama ambavyo nimeona pia Kamati ya Bajeti wamependekeza kwamba Serikali isite kwa sasa basi na mimi naungana nao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu nalopenda kuchangia linahusu Sheria ya Kodi ya Majengo, Sura 289 ambapo Serikali imekuja na mapendekezo mazuri sana ambayo yanaelekea kuanza kutoza Kodi ya Majengo kwa kutumia LUKU za umeme. Hili ni jambo zuri lakini jambo hili bado halijaeleweka vizuri, lina mashaka na wasiwasi mkubwa kutoka miongoni mwetu Waheshimiwa Wabunge lakini pia hata kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo kama msamaha ambao unawekwa na Sheria ya Majengo kwenye kifungu chake cha 7 kuna baadhi ya makundi ambayo yanapewa exemption ya kutotozwa Property Tax. Pia kuna vijiji na maeneo mengine vinapewa msamaha wa kutotozwa Property Tax. Tutakapoanza kutoza kwenye LUKU inaweza ikaleta tafrani namna ambavyo itakuwa inatozwa kwa sababu baadhi ya nyumba ambazo zina LUKU na ukizingatia mafanikio makubwa ambayo tumepata kwenye umeme wa vijijini maana yake watu wengi wamepata access to electricity na kwa maana hiyo wameweka umeme kwenye nyumba zao na hivyo, wote hawa tukisema tunawatoza tutajikuta tunapata changamoto kwenye namna ya kuwabagua wale wa vijijini hususan vijiji ambavyo vinapewa msamaha na Sheria ya Majengo lakini pia yale makundi mbalimbali kama wazee wenye umri wa miaka zaidi ya 60 ambao pia wanapewa msamaha kwenye Sheria hiyo ya Majengo kwenye kifungu cha 7, kutakuwa na changamoto kubwa sana ni namna gani tutawabagua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali ifanye utaratibu wa kurekebisha Mfumo wa LUKU hususan mfumo wa TEHAMA ili uweze kubaini na kutambua makundi pamoja na maeneo ambayo yanapewa msamaha. Vinginevyo hili jambo litatuletea political catastrophe kwenye majimbo yetu ambapo wazee na watu wa vijijini wanaweza wakajikuta wanatozwa kodi kinyuma kabisa cha sheria na ikaleta usumbufu mkubwa. Kwa hivyo, kabla ya kuanza kuitekeleza, Serikali wawe makini sana kwenye kurekebisha mfumo wake wa ki-electronic hususan unaohusiana na LUKU. Ni jambo zuri lakini lazima tuliendee kwa tahadhari kidogo ili lisituletee changamoto. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la nne ambalo napenda kulizungumzia ni kwamba kwenye sheria nimeona kuna mapendekezo ambapo Serikali ingependelea Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali aende akakague mashirika na kampuni ambapo Serikali ina hisa hata ambazo ziko chini ya asilimia 50. Hili pia naona kama ni jambo ambalo haliendani kabisa na mifumo ya uendeshaji wa makampuni (corporate governance systems) kwa sababu kwenye corporate governance wenye mamlaka ya kuamuru nani akakague wapi ni Bodi ya Wakurugenzi wa Kampuni husika. Bodi ya Wakurugenzi inakuwa formulated kwa kiasi kikubwa kutokana na wabia ambao wana nguvu kubwa kwenye hiyo kampuni kwa maana ya kuwa na shareholding power kubwa kuliko wale ambao ni minority shareholders.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, kama Serikali ni minority shareholder kwenye kampuni haiwezi kuelekeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali akaenda kukagua kwenye kampuni ambako kuna majority shareholders ambao ndiyo wanaunda Bodi ya Wakurugenzi na ndiyo ambao wanaimiliki na kuiendesha kampuni husika. Kwa hivyo, hili ni jambo ambalo pia napenda kupendekeza Serikali ikaridhia likaondolewa kwenye sheria ili kutoleta tafrani lakini pia kutokuathiri utendaji wa kiutawala bora ambao tunaenda nao katika nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tano nalopenda kuzungumzia linahusu Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 hususan kwenye yale mapendekezo ya Serikali ya kutoza asilimia 2 kwenye mauzo ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi. Kwenye ile sheria wanasema kama ni kampuni au ni shirika litatozwa asilimia 2 ya mazao ambayo itanunua lakini kama ni AMCOS ama ni Ushirika haitatozwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutoza kupitia kampuni hata kama kampuni hailipi moja kwa moja tozo hii itamfikia yule muuzaji kule mwisho kwa maana ya mkulima ama Chama cha Ushirika. Hata tunapoamua kwamba tusitoze kwa AMCOS tukiamini kwamba ni wakulima wetu ama kwa cooperative union, bado tunapotoza kwenye kampuni automatically tumetoza hadi kule kwa mkulima. Kwa hiyo, ni jambo ambalo linapaswa pia kutazamwa. (Makofi)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, muda wako umekwisha. (Makofi)
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Uwekezaji Tanzania wa Mwaka 2022
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa fursa hii. Nilitaka tu kumpa taarifa Mheshimiwa Ramadhan kwamba na mimi hii suti niliyovaa leo, hii blazer, imeshonwa na kijana wa Kitanzania anaitwa Mtani Nyamakababi, lakini pia nitakayovaa kesho imeshonwa na Sheria Ngowi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenda kwenye hoja ni kwamba tunatunga Sheria ya Uwekezaji katika zama ambapo mataifa mengi duniani yametunga sheria zinazofanana na hii ya kwetu, lakini pia tunatunga sheria hii tukizingatia kwamba sheria inayohusiana na uwekezaji kwa kiasi kikubwa ni sheria ambayo inapaswa kuweka mazingira ya kufanya biashara na mazingira ya kuvutia mitaji ndani ya nchi vizuri zaidi. Sasa kwa masikitiko makubwa sheria hii haiendi kutufikisha mahali pa tofauti sana na tulipo sasa, hayo ni masikitiko yangu.
Mheshimiwa Spika, na ninasema hivyo kama tutajilinganisha na nchi za hapa jirani tu, tukiacha zile za mbali, tukijilingaisha na Rwanda kwa mfano, walipotunga sheria yao ya uwekezaji waliunda chombo kinaitwa RDB (Rwanda Development Board). Rwanda Development Board ni One Stop Centre kwa uhalisia wake, sio kwa maneno ni One Stop Centre; ukifika pale utasajili kampuni yako, utajisajili kwenye kodi, utajisajili kwenye taasisi kama OSHA, kwenye taasisi kama NSSF, taasisi zote za compliance utazikuta pale RDB na utaondoka na documents zote pale, utalipa fees zote pale, tozo zote pale, unaondoka pale na makaratasi yako unaenda kufungua ofisi unaanza biashara, lakini sheria yetu hii ambayo tunaenda kuitunga leo haijaweka mazingira hayo ya kuwa One Stop Centre kwa uhalisia wake, hilo ni jambo linalosikitisha.
Mheshimiwa Spika, mikakati ya maendeleo kwenye dunia inataka pale ambapo wewe umechelewa kuingia kwenye jambo basi siku unayoingia uingie vizuri zaidi, uwe tofauti na wale ambao waliingia miaka mitano nyuma. Sasa sisi tunapoenda kutunga sheria ambayo wala haizifikii sheria za nchi nyingine ambazo zilitungwa miaka mitano, miaka kumi hapo nyuma ni jambo la kusikitisha kidogo.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Silicon Valley ya kule Marekani ni technological hub. Ni sehemu ambapo wanafanya incubation ya wagunduzi na wavumbuzi wa teknolojia za kisasa, lakini China alipoimarisha uchumi wake na akaanza kufanya utafiti (research and development), akaanzisha mji wake kuufananiaha na ule wa Silicon Valley. Alipokuja kujenga mji unaitwa Shenzhen, amejenga mji mzuri na wa kitofauti sana ambao unatoa challenge kubwa sana kwa Silicon Valley ya kule Marekani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hata sisi tunapoenda kutunga sheria yetu leo tulipaswa kutunga sheria ambayo itazishinda kwa vivutio sheria ambazo zimeshatangulia za majirani zetu tu hapa, hata tusijilinganishe na watu wa mbali sana, majirani zetu kama Mauritius wana sheria nzuri za uwekezaji, majirani zetu kama Kenya, majirani zetu kama Rwanda nimewataja, wana sheria nzuri sana za uwekezaji ambazo zinaweka mazingira rahisi sana ya kufanya biashara. Kwa sababu unapotunga sheria ya kuvutia uwekezaji vitu vikubwa viwili ni key, cha kwanza ni urahisi wa kufanya biashara kwenye hiyo nchi, lakini cha pili, kutabirika kwa mifumo na miundo ya kisheria yaani legal framework yote iwe inatabirika katika hiyo nchi.
Mheshimiwa Spika, sasa sisi sheria yetu kwa mfano pamoja na masharti mazuri yaliyowekwa kwenye Blue Print for Regulatory Reforms kwenye biashara na uwekezaji ningetarajia vile vivutio na yale masharti mazuri yaliyowekwa kwenye blue print yangeingizwa kwenye general provisions za hii sheria, lakini sheria hii haikufanya hivyo. Hilo ni jambo ambalo nimelishangaa kidogo nilipokuwa naipitia hiyo sheria kabla ya kuja kuchangia hapa kwamba tumeweka masharti mazuri sana kwenye blue print, lakini hatujayaweka kwenye sheria, kwa nini? Sielewi! Ningetarajia kwa kweli nione masharti yale yamewekwa kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Spika, lakini pia kama tungetaka kupata mafanikio yanayotusababishia kutimiza hayo malengo makuu mawili niliyoyasema ya easy of doing business na predictability basi tungepaswa kuipa hadhi kubwa zaidi hii TIC, kwa sasa hivi ni Kituo cha Uwekezaji, lakini kama tungetaka kuipa nguvu zaidi hii TIC tungeweza kufanya mambo mawili, tungeipa mamlaka kamili kuifanya authority ama tungeipa mamlaka kamili kwa kuifanya kuwa commission. Na kufanya hivyo tungeweza kuwataka sasa, kwa mujibu wa sheria, TRA wakaleta afisa wao pale mwenye mamlaka kamili akawa anatumia sheria ya TRA kutokea pale TIC kwa hivyo, akawa anafanya mambo yote kutokea pale TIC.
Mheshimiwa Spika, BRELA wangeleta mtu wao pale, Afisa ambaye anakasimiwa mamlaka na yule Mkurugenzi Mkuu wa BRELA anakuja kukaa hapa TIC. Afisa mkubwa, siyo junior ambaye akishapokea maombi ya wawekezaji aondoke na mafaili ayapeleke tena BRELA na yule wa TRA ayapeleke tena TRA na yule wa NSSF ayapeleke tena NSSF. Tungetarajia hizi ofisi zote; OSHA na wengine wote ambao wanahusika na masharti ya compliance wawekwe pale TIC.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo ingekuwa ni commission na pengine hao maafisa wanaohusika na compliance wangekuwa ni makamishna ambao wangekaa pale na wangekuwa na mamlaka kamili ambayo yanakasimiwa na zile sheria nyingine. Hapo tungesema tumefanya mabadiliko makubwa na hivyo tumejenga Shenzhen ambayo ni ya kisasa ukilinganisha na Silicon Valley ile ya Marekani.
Mheshimiwa Spika, pia tungetaka kuongeza mamlaka, kwa hiyo mamlaka mpya ambayo naifikiria kichwani, basi hata uwekezaji kwenye madini, kwenye kemikali hatarishi, ungepaswa kusimamiwa na mamlaka hiyo.
Mheshimiwa Spika, Vile vile vivutio vyote ambavyo vinatolewa nje ya mamlaka hii vingepaswa kutolewa kwenye mamlaka hii. Badala yake leo hii tuna ile Kamati inaitwa NISC, ambayo nafikiri Mheshimiwa Waziri Mkuu ndiye Mwenyekiti wake, ingepaswa kujadili mambo mengine lakini siyo kujadili vivutio vya uwekezaji. Mambo yote ya vivutio tungeyaweka sehemu moja, kwamba kuna miradi inayokwenda kujadiliwa tena NISC ama kuna Waziri fulani anajadili miradi yake kwenye eneo lake au sekta yake, naye anatoa vivutio vyake, hapana. Vivutio vyote tungevichukua tukavilundika kwenye hiyo mamlaka na ikafanya kazi.
Mheshimiwa Spika, la mwisho, ...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)
Muswada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi wa Mwaka 2022
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa fursa hii. Nilitaka tu kumpa taarifa Mheshimiwa Ramadhan kwamba na mimi hii suti niliyovaa leo, hii blazer, imeshonwa na kijana wa Kitanzania anaitwa Mtani Nyamakababi, lakini pia nitakayovaa kesho imeshonwa na Sheria Ngowi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwenda kwenye hoja ni kwamba tunatunga Sheria ya Uwekezaji katika zama ambapo mataifa mengi duniani yametunga sheria zinazofanana na hii ya kwetu, lakini pia tunatunga sheria hii tukizingatia kwamba sheria inayohusiana na uwekezaji kwa kiasi kikubwa ni sheria ambayo inapaswa kuweka mazingira ya kufanya biashara na mazingira ya kuvutia mitaji ndani ya nchi vizuri zaidi. Sasa kwa masikitiko makubwa sheria hii haiendi kutufikisha mahali pa tofauti sana na tulipo sasa, hayo ni masikitiko yangu.
Mheshimiwa Spika, na ninasema hivyo kama tutajilinganisha na nchi za hapa jirani tu, tukiacha zile za mbali, tukijilingaisha na Rwanda kwa mfano, walipotunga sheria yao ya uwekezaji waliunda chombo kinaitwa RDB (Rwanda Development Board). Rwanda Development Board ni One Stop Centre kwa uhalisia wake, sio kwa maneno ni One Stop Centre; ukifika pale utasajili kampuni yako, utajisajili kwenye kodi, utajisajili kwenye taasisi kama OSHA, kwenye taasisi kama NSSF, taasisi zote za compliance utazikuta pale RDB na utaondoka na documents zote pale, utalipa fees zote pale, tozo zote pale, unaondoka pale na makaratasi yako unaenda kufungua ofisi unaanza biashara, lakini sheria yetu hii ambayo tunaenda kuitunga leo haijaweka mazingira hayo ya kuwa One Stop Centre kwa uhalisia wake, hilo ni jambo linalosikitisha.
Mheshimiwa Spika, mikakati ya maendeleo kwenye dunia inataka pale ambapo wewe umechelewa kuingia kwenye jambo basi siku unayoingia uingie vizuri zaidi, uwe tofauti na wale ambao waliingia miaka mitano nyuma. Sasa sisi tunapoenda kutunga sheria ambayo wala haizifikii sheria za nchi nyingine ambazo zilitungwa miaka mitano, miaka kumi hapo nyuma ni jambo la kusikitisha kidogo.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Silicon Valley ya kule Marekani ni technological hub. Ni sehemu ambapo wanafanya incubation ya wagunduzi na wavumbuzi wa teknolojia za kisasa, lakini China alipoimarisha uchumi wake na akaanza kufanya utafiti (research and development), akaanzisha mji wake kuufananiaha na ule wa Silicon Valley. Alipokuja kujenga mji unaitwa Shenzhen, amejenga mji mzuri na wa kitofauti sana ambao unatoa challenge kubwa sana kwa Silicon Valley ya kule Marekani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hata sisi tunapoenda kutunga sheria yetu leo tulipaswa kutunga sheria ambayo itazishinda kwa vivutio sheria ambazo zimeshatangulia za majirani zetu tu hapa, hata tusijilinganishe na watu wa mbali sana, majirani zetu kama Mauritius wana sheria nzuri za uwekezaji, majirani zetu kama Kenya, majirani zetu kama Rwanda nimewataja, wana sheria nzuri sana za uwekezaji ambazo zinaweka mazingira rahisi sana ya kufanya biashara. Kwa sababu unapotunga sheria ya kuvutia uwekezaji vitu vikubwa viwili ni key, cha kwanza ni urahisi wa kufanya biashara kwenye hiyo nchi, lakini cha pili, kutabirika kwa mifumo na miundo ya kisheria yaani legal framework yote iwe inatabirika katika hiyo nchi.
Mheshimiwa Spika, sasa sisi sheria yetu kwa mfano pamoja na masharti mazuri yaliyowekwa kwenye Blue Print for Regulatory Reforms kwenye biashara na uwekezaji ningetarajia vile vivutio na yale masharti mazuri yaliyowekwa kwenye blue print yangeingizwa kwenye general provisions za hii sheria, lakini sheria hii haikufanya hivyo. Hilo ni jambo ambalo nimelishangaa kidogo nilipokuwa naipitia hiyo sheria kabla ya kuja kuchangia hapa kwamba tumeweka masharti mazuri sana kwenye blueprint, lakini hatujayaweka kwenye sheria, kwa nini? Sielewi! Ningetarajia kwa kweli nione masharti yale yamewekwa kwenye eneo hili.
Mheshimiwa Spika, lakini pia kama tungetaka kupata mafanikio yanayotusababishia kutimiza hayo malengo makuu mawili niliyoyasema ya easy of doing business na predictability basi tungepaswa kuipa hadhi kubwa zaidi hii TIC, kwa sasa hivi ni Kituo cha Uwekezaji, lakini kama tungetaka kuipa nguvu zaidi hii TIC tungeweza kufanya mambo mawili, tungeipa mamlaka kamili kuifanya authority ama tungeipa mamlaka kamili kwa kuifanya kuwa commission. Na kufanya hivyo tungeweza kuwataka sasa, kwa mujibu wa sheria, TRA wakaleta afisa wao pale mwenye mamlaka kamili akawa anatumia sheria ya TRA kutokea pale TIC kwa hivyo, akawa anafanya mambo yote kutokea pale TIC.
Mheshimiwa Spika, BRELA wangeleta mtu wao pale, Afisa ambaye anakasimiwa mamlaka na yule Mkurugenzi Mkuu wa BRELA anakuja kukaa hapa TIC. Afisa mkubwa, siyo junior ambaye akishapokea maombi ya wawekezaji aondoke na mafaili ayapeleke tena BRELA na yule wa TRA ayapeleke tena TRA na yule wa NSSF ayapeleke tena NSSF. Tungetarajia hizi ofisi zote; OSHA na wengine wote ambao wanahusika na masharti ya compliance wawekwe pale TIC.
Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo ingekuwa ni commission na pengine hao maafisa wanaohusika na compliance wangekuwa ni makamishna ambao wangekaa pale na wangekuwa na mamlaka kamili ambayo yanakasimiwa na zile sheria nyingine. Hapo tungesema tumefanya mabadiliko makubwa na hivyo tumejenga Shenzhen ambayo ni ya kisasa ukilinganisha na Silicon Valley ile ya Marekani.
Mheshimiwa Spika, pia tungetaka kuongeza mamlaka, kwa hiyo mamlaka mpya ambayo naifikiria kichwani, basi hata uwekezaji kwenye madini, kwenye kemikali hatarishi, ungepaswa kusimamiwa na mamlaka hiyo.
Mheshimiwa Spika, Vile vile vivutio vyote ambavyo vinatolewa nje ya mamlaka hii vingepaswa kutolewa kwenye mamlaka hii. Badala yake leo hii tuna ile Kamati inaitwa NISC, ambayo nafikiri Mheshimiwa Waziri Mkuu ndiye Mwenyekiti wake, ingepaswa kujadili mambo mengine lakini siyo kujadili vivutio vya uwekezaji. Mambo yote ya vivutio tungeyaweka sehemu moja, kwamba kuna miradi inayokwenda kujadiliwa tena NISC ama kuna Waziri fulani anajadili miradi yake kwenye eneo lake au sekta yake, naye anatoa vivutio vyake, hapana. Vivutio vyote tungevichukua tukavilundika kwenye hiyo mamlaka na ikafanya kazi.
Mheshimiwa Spika, la mwisho, ...
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)