Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Selemani Jumanne Zedi (19 total)

MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza:-
Kata za Semembela, Isagenhe na Kahama ya Nhalanga hazina kabisa mawasiliano ya simu za mkononi:-
Je, ni lini Kata hizi zitapatiwa huduma hii muhimu ya mawasiliano ya simu za mkononi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Seleman Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia zabuni zinazotolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Kata ya Kahama ya Nhalanga ilijumuishwa katika Zabuni ya Awamu ya Kwanza B (Phase 1B) ya mradi chini ya Kampuni ya Mawasiliano ya Simu za Mkononi ya Airtel kwa ruzuku ya Dola za Kimarekani 32,000. Utekelezaji wa mradi ulianza rasmi Aprili, 2014. Kazi ya ujenzi wa mnara imeanza na inatarajiwa kukamilika mwezi Februari, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Zabuni ya Awamu ya Pili A (Phase 2A), Kampuni ya Mawasiliano ya Simu za Mkononi ya MIC kwa maana ya Tigo imepewa jukumu la kupeleka huduma za mawasiliano ya simu za mkononi katika Kata ya Isagenhe kwa ruzuku ya Dola za Kimarekani 66,309. Utekelezaji wa mradi huu ulianza mwezi Aprili, 2015. Survey ya mradi imefanyika na utekelezaji upo katika hatua ya manunuzi ya vifaa vya mnara. Aidha, ujenzi wa mnara unatarajiwa kukamilika kabla ya kwisha mwaka huu wa fedha 2015/2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Semembela imejumuishwa katika mchakato wa awamu ya tatu ya mradi wa mawasiliano vijijini ambapo zabuni yake inatarajia kutangazwa ndani ya mwaka huu wa fedha 2015/2016. Pia kampuni ya Viettel kwa maana ya Halotel itaanza kujenga mnara wa mawasiliano ya simu mapema mwezi Mei, 2016.
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza:-
Je, Serikali kupitia REA inachukua hatua gani kwa Mkandarasi CHICCO ambaye ameshindwa kukamilisha utekelezaji wa Mradi wa Kupeleka Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II) katika vijiji vya Mwangoye, Mbutu na Mambali?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkandarasi CHICCO kutoka China alishinda zabuni ya usambazaji wa umeme vijijini REA Awamu ya Pili katika Mkoa wa Tabora. Ni kweli kwamba mkandarasi huyu alianza kazi kwa kusuasua hali iliyosababisha Wakala wa Nishati Vijijini kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kumwandikia barua ya kutoridhishwa na kazi na kuongeza usimamizi wa kufuatilia utendaji wake. Hatua nyingine iliyochukuliwa ni pamoja na kumtaka mkandarasi huyo kuongeza kampuni nyingine (sub-contractor) ili kuharakisha shughuli za ujenzi wa mradi huo. Utekelezaji wa kazi hiyo wa mkoa mzima unaendelea ambapo kazi imekamilika kwa asilimia 82 na mradi unatarajiwa kukamilika mwishoni wa mwezi Juni, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme vijiji vya Mambali, Mbutu pamoja na Mwangoye inaendelea na imefikia utekelezaji kama ifuatavyo:-
(i) Kijiji cha Mambali kazi ya kupeleka umeme imekamilika kwa asilimia 100 na wateja wapatao 49 wameunganishiwa umeme.
(ii) Kijiji cha Mwangoye kazi ya kujenga njia ya umeme imekamilika. Taratibu za ufungaji wa transfoma zinaendelea na umeme unatarajiwa kuwashwa mara baada ya kukamilika kwa ufungaji wa transfoma hizo.
(iii) Kijiji cha Mbutu hakikuwepo kwenye mradi huu hata hivyo mkandarasi CHICCO alipewa kazi ya ziada na mradi unaendelea. Mkandarasi amemaliza kazi ya upembuzi yakinifu na sasa yupo katika hatua za mwisho za kukamilisha michoro ya kiuhandishi kabla ya kuanza utekelezaji wa mradi wa umeme katika kijiji hiki.
MHE. HUSSEIN M. BASHE (K.n.y MHE SELEMANI J. ZEDI) aliuliza:-
Ujenzi wa vyumba vya upasuaji katika vituo vya afya vya Bukene na Itobo umekamilika na kwamba vifaa vyote kwa ajili ya kutoa huduma ya upasuaji vimeshafunguliwa ikiwa ni pamoja na vifaa vya kuhifadhia damu na mashine za kufulia. Je, ni jambo gani linazuia huduma za upasuaji kuanza katika vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli vituo vya afya vya Itobo na Bukene vimepata vifaa vyote vinavyohitajika kwa ajili ya upasuaji ambavyo vimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, kinachokwamisha shughuli za upasuaji kuendelea katika kituo cha afya cha Itobo ni kukosekana kwa Mtaalam wa usingizi baada ya aliyekuwepo kusimamishwa kazi kwa tuhuma za rushwa. Mkoa kwa kushirikiana na Halmashauri umepanga kumhamisha Mtaalam huyo kutoka sehemu nyingine ili huduma za upasuaji ziweze kuendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa kituo cha Bukene mbali na mtaalam wa usingizi, kinachokwamisha ni ukosefu wa maji ya uhakika na tayari Halmashauri inafanya marekebisho hayo. Halmashauri imetakiwa kuhakikisha upungufu huo unaondolewa mapema ili huduma hizo muhimu zianze kutolewa na kuwaondolea adha wagonjwa kufuata huduma hiyo Nzega Mjini.
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza:-
Ukosefu wa nyumba za walimu katika maeneo ya vijijini unasababisha Walimu kuhama maeneo hayo na hivyo kusababisha upungufu mkubwa wa Walimu, pia Halmashauri nyingi hazina uwezo wa kujenga nyumba za Walimu za kutosha kwa kutumia fedha zao za ndani.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga nyumba za Walimu wa shule za msingi vijijini hasa ikizingatia kuwa vijijini hakuna nyumba ambazo Walimu wanaweza kupanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi Mbunge wa Jimbo la Bukene kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa nyumba za Walimu kupitia bajeti zilizotengwa katika kila mwaka. Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi bilioni 13.9 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba 1,157 kwa shule za msingi na shilingi bilioni 11.1 zimetengwa kujenga nyumba 661 kwa shule za sekondari nchini. Aidha, kupitia mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES II), Serikali imepanga kujenga nyumba za Walimu 183 katika shule za sekondari kwenye Halmashauri mbalimbali zenye uwezo wa kuchukua familia sita kwa kila nyumba.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Nzega katika mwaka wa fedha 2016/2017 imetengewa shilingi milioni 486.3 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za Walimu kwa shule za msingi na sekondari.
MHE. SEIF K. S. GULAMALI (K.n.y. MHE. SELEMANI J. ZEDI) aliuliza:-
Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Tabora (RCC) mwaka 2014 ilikubali ombi la wananchi wa Wilaya ya Nzega la kutaka kuanzishwa kwa Wilaya mpya ya Bukene hasa ikizingatiwa kuwa Jimbo la Bukene lina vigezo vyote vinavyohitajika kwa uanzishwaji wa Wilaya na ombi hili lilipelekwa TAMISEMI ili kufanyiwa kazi.
Je, Serikali imefikia wapi katika utekelezaji wa maamuzi ya RCC ya kuomba uanzishwaji wa Wilaya mpya ya Bukene?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Mkoa wa Tabora uliwasilisha maombi ya kuanzishwa kwa Wilaya ya Bukene baada ya kupitishwa na Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika tarehe 29 Mei, 2015. Kikao hicho kilijadili pendekezo la kuanzisha Mkoa mpya wa Ngega sambamba na kuanzisha Wilaya mpya ya Bukene. Aidha, tarehe 26 Februari, 2016 Katibu Tawala Mkoa wa Tabora aliandikiwa barua yenye Kumb. Na. BD. 310/365/31 ya tarehe 26/02/2016 ili kufanyia kazi mapungufu yaliyobainishwa katika maombi hayo. Tayari mkoa umefanyia kazi upungufu huo na kuwasilisha taarifa kwa barua ya tarehe 11 Aprili, 2016.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchambuzi wa kina unafanyika sambamba na maombi ya maeneo mengine. Aidha, timu ya wataalam imefanya zoezi kubwa la uhakiki wa vigezo na taratibu (physical verification) kwa maeneo mbalimbali nchini ili kuweza kumshauri Mheshimiwa Rais kuhusu mapendekezo hayo kwa kuzingatia Ibara ya 2(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
MHE. MOSHI S. KAKOSO (K.n.y MHE. SULEIMAN J. ZEDI) aliuliza:-
Serikali imejitahidi sana kupeleka umeme vijijini jambo ambalo litaongeza ajira kutokana na uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo vya kusindika mazao ya kilimo maeneo ya vijijini kama vile usindikaji wa mafuta ya alizeti, kukoboa na kupaki mpunga na kusaga na kupaki unga wa mahindi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa vijijini kupata elimu, mitaji na masoko ili shughuli za kuanzisha usindikaji wa mazao ya kilimo kiwe tija?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Suleimani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Zedi kwa kutambua juhudi za Serikali za kupeleka umeme vijijini ambao ni kichocheo muhimu katika uanzishwaji wa viwanda vidogo vya usindikaji wa mazao ya kilimo.
Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa viwanda katika kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi, Wizara yangu kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) inatekeleza mkakati wa Wilaya moja, bidhaa moja (One District, One Product – ODOP) ambao SIDO kwa kushirikiana na wadau katika Halmashauri walichagua bidhaa moja katika Wilaya kwa lengo la kuiendeleza. Kwa upande wa Bukene wao walichagua zao la mpunga.
Mheshimiwa Spika, hivyo, SIDO ina jukumu la kutoa huduma mbalimbali ikiwemo mafunzo juu ya usindikaji mazao ya kilimo, kuendeleza teknolojia rahisi za uongezaji thamani mazao ya kilimo na kuandaa maonesho ya kikanda ili kuwasaidia wajasiriamali waweze kupata masoko ya bidhaa zao.
Mheshimiwa Spika, aidha, kupitia Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Ujasiriamali (National Entrepreneurship Development Fund) wananchi wa vijijini wamekuwa wakikopeshwa fedha kwa masharti nafuu ili waweze kuanzisha miradi midogo na ya kati kwa lengo la kujipatia ajira na kuongeza kipato.
Mheshimiwa Spika, tunatambua tatizo la SIDO kutowafikia wananchi walio wengi zaidi vijijini kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa rasilimali fedha na mtandao wa shirika kuishia ngazi ya Mkoa katika Mikoa yote ya Tanzania Bara. Hivi sasa changamoto hizo zitatazamwa kwa kina katika hatua ya kupitia upya sheria iliyoanzisha shirika hilo kwa lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi wa shirika katika kuhudumia jasiriamali ndogo na za kati nchini.
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza:-
Barabara ya kuanzia Tabora - Mabali – Bukene – Itobo hadi Kahama ni muhmu sana kwa shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Jimbo la Bukene na barabara hii ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Je, ni lini barabara hii yenye urefu wa kilometa 149 itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Tabora – Mambali - Itobo yenye urefu wa kilometa 115 ni sehemu ya mradi wa barabara ya Tabora – Mambali - Itobo hadi Kagongwa Wilayani Kahama yenye urefu wa kilometa 180, inayounganisha Wilaya ya Tabora, Nzega na Kahama. Kwa sasa barabara hii inafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mkataba wa kazi hiyo ulisainiwa tarehe 14 Septemba, 2017 na ni wa miezi 15. Kazi hii inafanywa na Mhandisi Mshauri M/s Nimeta Consult kwa gharama ya shilingi milioni 789.205. Hadi sasa jumla ya shilingi milioni 608 zimeshatolewa kwa ajili ya kazi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii utaanza baada ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika kulingana na upatikanaji wa fedha. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza:-
Kwa mujibu wa Sera ya Usambazaji wa Maji kutoka bomba kuu litakalotoa maji ya Ziwa Victoria kutoka Kahama hadi Tabora Mjini, ni kwamba vijiji vyote vilivyo ndani ya kilometa 12 toka bomba kuu vitaunganishwa na maji.
Je, ni vijiji vingapi vya Jimbo la Bukene ambavyo vimo ndani ya kilometa 12 vitaunganishwa maji kutoka bomba kuu hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa naiba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Jimbo la Bukene kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kupitia Kahama una lenga kuwapatia huduma ya maji wakazi wa Miji ya Tabora, Uyui, Nzega na Tinde pamoja na vijiji 89 vilivyopo ndani ya eneo la kilomita 12 kila upande wa bomba kuu la Mradi wa KASHWASA. Mradi huu ni wa malengo ya muda mrefu ya kuwapatia huduma ya maji ya uhakika wananchi wapatao milioni 1.1 wa maeneo hayo. Ujenzi wa mradi umegawanyika katika Awamu Mbili. Awamu ya Kwanza itahusisha kupeleka maji katika Miji ya Tabora, Igunga, Uyui, Nzega na Tinde. Kazi zitakazotekelezwa katika awamu hiyo ni pamoja na ujenzi wa bomba kuu kutoka Kijiji cha Solwa, ulazaji wa mabomba na ukarabati wa mitandano ya usambazaji maji katika miji hiyo. Awamu ya Pili mradi itahusu kupeleka maji katika Mji wa Sikonge kutoka Ziwa Victoria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Jimbo la Bukene lililopo katika Halmashauri ya Nzega Vijijini, jumla ya vijiji vitatu vya Iboja, Ilagaja na Chamipulu vitapata huduma ya maji kupitia bomba kuu la kutoa maji Ziwa Victoria kutoka Kijiji cha Solwa kwenda Nzega. Kwa vijiji vingine ambavyo vipo umbali zaidi ya kilometa 12, Serikali itaendelea kutekeleza miradi ya maji katika vijiji hivyo kwa kutumia vyanzo vingine vya maji. Kazi hii itaendelea kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2017/2018 ambapo Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.8 kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Nzega kwa ajili ya kazi hiyo. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza:-
Kata ya Bukene Wilayani Nzega inaundwa kwa Kijiji kimoja tu chenye wakazi zaidi ya 7,600 jambo ambalo linakwamisha uharakishaji wa huduma za maendeleo kwa wananchi. Tulishafuata taratibu zote za kuomba Kijiji cha Bukene kigawanywe ili kupata Kijiji kingine kipya:-
Je, Serikali haioni kuwa siyo sahihi kuwa na Kata inayoundwa na Kijiji kimoja?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, taratibu za kuzingatiwa wakati wa kuanzisha au kupandishwa hadhi maeneo ya utawala zimeelezwa katika Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287 na (Mamlaka za Miji) Sura 288, Toleo la 2002. Sambamba na taratibu hizo upo mwongozo uliofanyiwa marekebisho mwaka 2014 unaofafanua vigezo vya kuzingatiwa katika kuanzisha maeneo hayo ili kuepusha uanzishwaji holela wa maeneo ya utawala yasiyokuwa na sifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vipo vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa katika kuanzisha vijiji. Mapendekezo ya kugawanywa kwa Kijiji cha Bukene kilichopo katika Kata ya Bukene, Halmashauri ya Wilaya ya Nzega hayajawasilishwa rasmi kwa kuzingatia taratibu zilizopo kisheria ikiwa ni pamoja na kujadiliwa na kupitishwa katika vikao vyote vya kisheria ambavyo ni Serikali ya Kijiji, Mkutano Mkuu wa Kijiji, Kamati ya Maendeleo ya Kata, Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Kamati ya Ushauri ya Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kipaumbele cha Serikali kwa sasa siyo kuanzisha maeneo mapya ya kiutawala bali kuimarisha maeneo ya kiutawala yaliyopo ili yaweze kutoa huduma stahiki kwa wananchi.
MHE. SELEMAN J. ZEDI aliuliza:-

Je, ni lini ujenzi wa barabara ya Tabora – Mambali – Itobo - Kagongwa yenye urefu wa Kilometa 149 utaanza kujengwa kwa kiwango cha lami? Kwani ni ahadi ya Mheshimiwa Rais na pia imo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2015 - 2020.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Uchukuzu na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo:-



Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza kutekeleza mpango wa ujenzi wa barabara ya Tabora – Mambali – Itobo–Kagongwa yenye urefu Kilometa 149 kwa kuanzia na hatua ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wameingia mkataba na Mhandisi Mshauri NIMETA Consult Ltd. kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Tabora – Mambali – Itobo – Kagongwa kwa gharama ya shilingi milioni 789. Hadi sasa Mhandisi Mshauri amekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na kazi ya usanifu wa kina itakuwa imekamilika kufikia Juni, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara baada ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, gharama za ujenzi pamoja na maandalizi ya nyaraka za zabuni kukamilika, Serikali itatafuta fedha za kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii. Aidha, wakati kazi ya usanifu ikiendelea, Wizara kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) itaendelea kutenga fedha za matengenezo mbalimbali kwa barabara hii ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. Jumla ya shilingi 345 zimetengwa katika mwaka wa fedha 2018/ 2019 kwa ajili ya kazi hiyo. Ahsante.
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza:-

Kijiji cha Sojo katika Kata ya Isugule, Wilayani Nzega patajengwa Kituo kikubwa (coating yard) cha kuandaa mabomba yote ya mradi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani, Tanga ambapo Kituo hicho kitakuwa na wafanyakazi zaidi ya 2,000; kutokana na ongezeko hilo la idadi ya watu mahitaji ya huduma za Jamii yatakuwa makubwa:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Kituo kidogo cha Polisi katika Kijiji cha Sojo ili kuhakikisha usalama kwa wananchi na mali zao?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Jeshi la Polisi iliona umuhimu wa kuwepo kwa Kituo cha Polisi katika Kijiji cha Sonjo ambapo ndipo kitakapojengwa kituo cha kuandaa mabomba ya mafuta toka Uganda kuja Tanzania. Aidha, juhudi mbalimbali zimekwishaanza ambapo Uongozi wa Polisi Mkoa wa Tabora kwa kushirikiana na Uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Nzega wanaendelea na utaratibu wa kupata eneo la kujenga Kituo cha Polisi kitakachokuwa na hadhi ya daraja ‘C’ ambacho kitakuwa na Askari kuanzia kumi na tano (15), pia eneo la ujenzi wa nyumba za kuishi askari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa wananchi wa Sonjo wanapata huduma ya Polisi katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Nzega.
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza:-

Je, Serikai haioni umuhimu wa kuajiri Wafamasia angalau katika kila Kituo cha Afya nchini ili kuimarisha usimamizi na mtiririko wa upatikanaji dawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Jimbo la Bukene, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa ikama wa watumishi wa afya, Mfamasia anapaswa kuwepo katika ngazi ya Hospitali. Kwenye ngazi ya Vituo vya Afya na Zahanati, ikama inaelekeza kuwepo kwa Mteknolojia wa Dawa au Mteknolojia Msaidizi wa Dawa. Kada hizi ni muhimu kuwepo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kuimarisha uratibu na usimamizi wa bidhaa za afya.

Mheshimiwa Spika, kuanzia Mei, 2017 hadi Februari, 2021 Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeajiri Wafamasia 79, Wateknolojia wa Dawa 313 na Wateknolojia wa Dawa Wasaidizi 160. Serikali inatambua changamoto ya uhaba wa Wataalam hawa, ambapo katika mwaka wa fedha 2021/ 2022 imepanga kuajiri watumishi 10,467 wakiwemo Wafamasia na Wateknolojia wa Dawa watakaopelekwa kwenye Hospitali za Halmashauri, Vituo vya Afya pamoja na zahanati kote nchini.
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza:-

Je, Serikali imefikia hatua gani katika mradi wa kutoa maji kutoka Nzega Mjini, tenki la Ushirika hadi Bukene ambapo vijiji 20 na vitongoji zaidi ya 100 vitanufaika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imekamilisha kazi ya usanifu wa mradi wa kutoa maji katika tenki la Ushirika Mjini Nzega kwa ajili ya kuhudumia watu zaidi ya 79,485 katika vijiji 20 na vitongoji vyake. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 kiasi cha fedha shilingi bilioni mbili kimetengwa na utekelezaji wa mradi huu utaanza, ambapo utahusisha kulaza mabomba ya kusambaza maji umbali wa kilometa 176, kujenga matenki matano ya kuhifadhi maji ya ujazo wa lita 100,000, lita 150,000, lita 250,000 na lita 300,000 na kujenga vituo vya kuchotea maji 83.
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza: -

Je, ujenzi wa barabara ya Tabora – Mbambali – Bukene – Itobo hadi Kahama umefikia hatua gani baada ya kutengewa fedha kwenye bajeti mwaka 2020/2021?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na utayarishaji wa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Tabora – Mbambali – Bukene – Itobo yenye urefu wa kilometa 114. Kazi hii ilitekelezwa na Mhandisi Mshauri NIMETA Consult ya Tanzania na ilikamilika Aprili, 2020 kwa gharama ya shilingi milioni 790.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya shilingi milioni 1,000 sawa na bilioni moja zimetengwa kwa ajili ya kuanza maandalizi ya ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, aidha, wakati Serikali inaendelea na maandalizi ya kuanzia ujenzi wa barabara hii, Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Ahsante. (Makofi)
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Jengo la Wodi za kulaza Wagonjwa pamoja na kupeleka mashine ya X-ray katika Kituo cha Afya Itobo kilichopo Jimbo la Bukene?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Jimbo la Bukene, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imepeleka shilingi milioni 250 katika Kata ya Itobo kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kituo hicho ili kiweze kuwa na uwezo wa kutoa huduma za upasuaji. Ujenzi wa majengo hayo umeanza na unatarajiwa kukamilika ifikapo 30 Aprili, 2022.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa vituo hivi vya afya unafanyika kwa awamu. Hivyo, baada ya awamu hii ya kwanza ya ujenzi kukamilika, Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo mengine ikiwemo wodi katika Kituo cha Afya cha Itobo. Aidha, mashine za X-ray zitaendelea kununuliwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga minara ya mawasiliano ya simu katika Kata ya Karitu na Ikindwa – Bukene?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) iliifanyia tathmini Kata ya Ikindwa iliyopo katika Wilaya ya Nzega na kubaini kuwa ina changamoto ya upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu na hivyo kata hiyo imejumuishwa katika zabuni iliyotangazwa tarehe 24 Oktoba, 2022 kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Kata ya Karitu, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa wote itaifanyia tathmini kata hiyo ili kubaini mahitaji ya mawasiliano na kuiingiza katika zabuni zitakazotangazwa na Mfuko katika awamu zifuatazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza: -

Je, ni nini kinachelewesha ujenzi wa barabara kutoka kutoka Tabora – Mambali – Bukene hadi Kangogwa ilihali ilishatengewa bajeti?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (ENG.GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninapenda kujibu Swali la Mheshimiwa Selemani Jumanne Zedi, Mbunge wa Bukene, kama ifuatavyo: -

Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Tabora – Mambali – Bukene hadi Kagongwa yenye urefu wa KM 114 umekamilika mwaka 2020. Baada ya kukamilika kwa usanifu na gharama za ujenzi kwa kiwango cha lami kujulikana, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi. Aidha, Serikali imejenga kilometa 9.6 kwa kiwango cha lami kutoka Tabora Mjini kuelekea Mambali.

Mheshimiwa Spika, wakati Serikali ikiendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami, Wizara yangu kupitia TANROADS imeendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika wakati wote. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya Shilingi Milioni 1,200 zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo. Ahsante.
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza: -

Je, ni lini Kituo cha Afya Bukene kitapatiwa mashine ya x- ray na ultrasound?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Seleman Jumanne Zedi, Mbunge wa Jimbo la Bukene, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Afya Bukene kinatoa huduma za kiuchunguzi ambapo kwa sasa kina mashine ya Ultrasound. Aidha, kituo hiki hakina miundombinu ya jengo la kuwezesha utolewaji wa huduma za X-Ray. Serikali itaendela kutenga bajeti kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya afya pamoja na ununuzi wa mashine za uchunguzi ikiwemo X-Ray na Ultrasound kwa ajili ya vituo vya huduma nchini ikiwemo Kituo cha Afya cha Bukene, ahsante.
MHE. SELEMANI J. ZEDI aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kuipandisha hadhi Zahanati ya Kijiji cha Sojo ili kiwe Kituo cha Afya na kuweza kuhudumia wananchi na watumishi wa Mradi wa Bomba la Mafuta?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Selemani Jummane Zedi, Mbunge wa Jimbo la Bukene kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Sojo ni moja kati ya vijiji saba vya Kata ya Igusule yenye wakazi 23,237. Kata hii ina zahanati moja iliyopo katika Kijiji cha Sojo ambayo inaendelea kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kwenye Kata ya Igusule.