Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Musa Rashid Ntimizi (22 total)

MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.
Wananchi wa Jimbo la Igalula hususani Kata ya Loya na Halmashauri yetu imefanya kazi kubwa sana kujenga kituo hicho cha polisi na nguvu kwa sasa imetuishia na kazi kubwa imefanyika. Serikali kupitia Wizara haioni umuhimu wa kusaidia nguvu hizi za wananchi katika kumalizia kituo hiki cha polisi na kiweze kuanza kufanya kazi? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata ya Igalula na Kata ya Kigwa kuna vituo vya polisi ambavyo vingeweza kutoa huduma katika Kata ya Loya kipindi hiki hatuna kituo kituo cha polisi katika Kata ya Loya. Tatizo letu kubwa lililopo pale katika vituo hivi viwili vya polisi havina usafiri. Je, Wizara haioni umuhimu wa kuvipa usafiri vituo hivi vya polisi ili viweze kuendelea kutoa huduma katika maeneo ambayo hayana vituo vya polisi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali bado inaendelea na juhudi zake za kuhakikisha kwamba inajenga vituo mbalimbali katika nchi yetu. Kwa hiyo basi, pamoja na juhudi zilizofanywa na wananchi, nimwombe Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na Serikali na kuona kwa namna gani tunaweza tukakamilisha kituo hiki. Nina uhakika kabisa wananchi kwa juhudi walizozifanya bado kuna nafasi ya kuendelea kushirikiana na Serikali ili kukamilisha ujenzi huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili amezungumzia tatizo la usafiri. Ni kweli vituo vingi havina usafiri lakini Serikali katika bajeti yake ya mwaka huu inajipanga kuhakikisha kwamba inanunua magari mengi ili kuweza kuvipatia vituo mbalimbali usafiri na tutaangalia kituo kimojawapo kati ya alivyovisema tutaweza kukipatia usafiri.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na nia nzuri ya Serikali ya kumpunguzia mkulima wa tumbaku makato mengi ambayo yanafanya mkulima huyu asipate tija ya zao la tumbaku, kuna shida ya makato ya mkulima yanayotokana na ujenzi wa ma-godown ambayo ma-godown yale yalijengwa kwa mkataba wa CRDB na kupatikana mkandarasi kwa kupitia CRDB. Ma-godown yale hayana tija yamedondoka mpaka sasa hayafanyi kazi lakini mkulima wa tumbaku anaendelea kukatwa mpaka sasa. Je, Serikali inasema nini kuhusu hili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama anavyosema Mheshimiwa Mbunge kwamba kumekuwepo na changamoto nyingi za makato ambayo yanaendelea kufanya bei anayopata mkulima katika zao laki kuwa ndogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikijaribu kupitia hizi tozo ili tuweze kuona namna ya kuzipunguza, tunafahamu changamoto anayoizungumzia ya maghala na katika wiki hii Mheshimiwa Waziri wa Kilimo aliitisha kikao cha Bodi ya Tumbaku, kikao ambacho kilikaa kwa masaa sita na moja kati ya masuala ambayo bodi imeelekezwa kuifanyia kazi ni hili la ma-godown madeni ambayo wakulima wanaendelea kulipa kila wakati na katika kikao kile wameelekezwa kuleta jibu haraka iwezekanavyo. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hili linafanyiwa kazi na tutapata jibu sahihi muda siyo mrefu.
MHE. MUSSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru pia kwa juhudi nzuri za Mheshimiwa Waziri anazozifanya katika kuhakikisha kwamba Mikoa ambayo inalima mazao mbalimbali, inakuwa na uwezekana wa kupata viwanda vya ku-process hayo mazao. Mkoa wetu wa Tabora una zao la tumbaku, na juhudi ambazo anazifanya Mheshimiwa Waziri tunaziona;
Je, Mheshimiwa Waziri anatuelezaje kuhusu uwezekano wa kupata mwekezaji wa kuja kuweka kiwanda katika cha kuchakata kuchakata zao la tumbaku katika Mkoa wetu wa Tabora?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ambayo ninayahangaikia sana ni kuweza kupata viwanda Tabora. Kwa sababu ameniuliza kuhusu tumbaku nitajibu tumbaku lakini siku nyingine nitakueleza na viwanda vingine ambayo viko kwenye pipe line. Tumehangaika, tumewapata Wachina tunawashawishi wakatengeneze kiwanda cha ku-process tumbaku pale, lakini panapo majaliwa ya Mwenyenzi Mungu, huenda mwisho wa mwezi huu au mwezi ujao nikaenda Vietnam, nakwenda mahsusi kutafuta kiwanda cha tumbaku na kukipeleka Tabora, kwa hiyo nahangaika jambo la muhimu watu wa Tabora muiombee Serikali hii ili kusudi tuchape kazi.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri na majibu yanaleta matumaini kwa hawa askari wetu, lakini nilikuwa na maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, je, katika mpango huu wa Serikali wa kujenga nyumba za askari wetu, Wilaya yetu ya Uyui itaangaliwa kwa macho mawili? Kwa sababu Halmashauri yetu ya Tabora kwa maana ya Uyui imetumia zaidi ya shilingi milioni 300 kujenga kituo kile cha polisi, kwa sasa kama nilivyosema kwenye swali la msingi askari wetu hawana makazi ya kukaa wanakaa kwenye nyumba za mabati.
Lakini la pili, Serikali ina wajibu wa kuwapatia makazi bora askari wetu, ukiangalia nchi nzima askari wetu wanakaa katika nyumba za kupanga mitaani kwa sababu hakuna makazi ya askari wetu.
Je, Serikali inawalipa posho ya makazi askari hawa au ina mpango gani wa kuwalipa posho za makazi askari hawa kwa sababu wanakaa nyumba za kupanga uswahilini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ni swali ambalo limekuwa likiulizwa takribani kila siku katika Bunge hili na kila Mbunge amekuwa akiuliza kwamba nyumba zitajengwa katika eneo lake, vituo vitajengwa katika eneo lake. Nimekuwa nikijibu na vitajengwa lini, likiwemo suala la Mheshimiwa Mbunge la Uyui. Na nimekuwa nikijibu swali hili mara nyingi kwa mfumo ambao umezoeleka hapa, lakini naomba leo nije na jibu lingine kidogo ambalo litakuwa ni mbadala ambayo yale najibu. Si kwa majibu ya majibu ambayo nilikuwa nimejibu mwanzo yatakuwa hayamo, majibu ambayo nilikuwa nimeyajibu mwanzo yataendelea kubakia vilevile kwamba tunaendelea kujenga kadri ya hali ya uwezo wa bajeti utakaporuhusu ukiachilia mbali programu ambazo tayari ziko mezani.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jibu ambalo nataka niongezee sasa hivi ni kwamba nilikuwa naomba nitoe wito kwa Waheshimiwa Wabunge kwamba katika fedha za Mfuko wa Jimbo ambazo tunapata basi tuweke kipaumbele kuhakikisha kwamba tunaimarisha makazi ya askari kwa yale maeneo ambayo bado ujenzi wake haujakuwa katika ratiba za hivi karibuni pamoja na vituo vya polisi. Kwa hiyo, pamoja na nyongeza hiyo na hili lingine lilikuwa kama ni ushauri nilitaka nitoe Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kimsingi ni kwamba ujenzi wa nyumba 4,136 unahusisha mikoa 17, lakini wamechukua mikoa miwili ya Zanzibar. Kimsingi Mikoa ya Zanzibar ni mitano kwa hiyo inakuwa takribani 20. Sasa labda Mheshimiwa Ntimizi, mimi na yeye tukae baadaye tuone kama katika Wilaya yake ya Uyui, katika Awamu ya Kwanza unaingia ama kama haimo katika awamu ya kwanza basi tuweze kushirikiana mimi na yeye kuhakikisha tunaingiza katika Awamu ya Pili ya ujenzi wa nyumba hizo 4,136.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini swali lake la pili alikuwa ameuliza ni kwamba je, kuna utaratibu wa kuwalipa askari posho wale ambao hawakai katika nyumba za Serikali, ni kweli upo utaratibu huo, na kuna posho ya pango, ni asilimia 15 ya mshahara.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Shida ya maji ya Kilindi inafanana na shida ya maji katika Jimbo letu la Igalula. Tuna mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria unaokuja katika wilaya zote za Mkoa wa Tabora, lakini mradi huu hauleti maji katika Jimbo letu la Igalula. Je, Wizara haioni umuhimu wa kuchepusha mradi ule kuleta katika Jimbo letu la Igalula ili kuondoa matatizo ya maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, usanifu wa sasa wa mradi wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria kuleta Tabora hauwezi kufikisha maji hayo katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge kule Igalula. Baada ya mradi kukamilika na kwa sababu tuna mradi mwingine wa kutoa maji Mto Malagarasi, maji yakishakuwa mengi basi baadaye tutaangalia jinsi ya kusanifu na kuyatoa maji hayo kuyapeleka hadi Jimbo la Mheshimiwa Mbunge kule Igalula.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Tatizo la barabara hii ya Kilombero linafanana na tatizo la barabara yetu ya Tabora - Itigi. Kipande cha Chaya - Nyahua kilomita 89 ambacho kinaifanya barabara hii mpaka sasa isiweze kupitika na tunaelekea katika kipindi cha mvua.
Barabara hii ni muhimu sana kwa sisi wakazi wa Tabora, Katavi na Kigoma. Tunaomba Serikali ituambie ni lini barabara hii itatengenezwa ili kufungua barabara hii na kusaidia wakazi wa mikoa hiyo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Musa Ntimizi anafahamu kwamba mwezi wa Kumi na Moja ndiyo tutakuwa na kikao na Kuwait Fund kuhusu hii barabara. Labda kwa maana ya taarifa kwa wananchi wa kule nao wajue ni kwamba tunatarajia kupata fedha kutoka Kuwait Fund kwa ajili ya kukamilisha hiki kipande ambacho kimebakia kati ya Chaya na Nyahua; na kikao cha kupata hiyo commitment kitafanyika mwezi ujao mwezi Novemba.
MHE. MUSSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru wewe na pia kwa kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri; lakini katika majibu yake Serikali imekiri kwamba wanunuzi hawa wa tumbaku wana muungano wa ukiritimba katika kupanga bei na kiasi cha tumbaku cha kununua. Wanapenda kuangalia gharama za mkulima katika kuzalisha zao lake ndipo wapange bei, lakini sisi hatujui wao wanauza shilingi ngapi katika Soko la Dunia. Je, ni hatua gani Serikali inachukua katika kumsaidia mkulima huyu wa tumbaku katika kupata bei nzuri?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Serikali ililitangazia Bunge kwamba kupitia WETCU wana mpango wa kufufua Vyama 64 vya Wakulima wa Tumbaku ambapo wanachama wa vyama vile walichangishwa sh. 100,000/= kila mmoja katika kufanikisha zoezi hilo, lakini leo WETCU na makampuni wamewanyima wakulima hawa pembejeo, lakini vile vile wanasema kwamba soko la kununua tumbaku ile hakuna. Wakulima tayari wameshalima na utaratibu wote wameshamaliza na hawajui watauzia wapi tumbaku hiyo. Je, Serikali inawaambia nini wakulima hawa wa tumbaku ambao tayari sasa wemeshalima tumbaku yao na wanasubiri mauzo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba biashara ya tumbaku inaendeshwa kwa cartel; kuna makampuni machache duniani ambayo ndiyo yanaamua kila kitu, yanaamua kiasi, lakini vile vile yanaamua bei. Ni kweli vile vile kwamba mara nyingi kampuni zinazonunua tumbaku zenyewe hazina tabia ya kuonesha faida na gharama zao lakini wanataka wakulima na wazalishaji waoneshe.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikiendelea na majadiliano na haya makampuni na kwa sasa makampuni hayo yamekubali kutuonyesha gharama zao pamoja na faida wanazopata ili tuweze kulinganisha wakati wa kuamua bei dira. Kwa hiyo, kuanzia msimu unaokuja, Serikali vile vile sasa na wadau wengine watafahamu upande wa pili wa hali halisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na wakulima ambao wamelima tumbaku lakini hawajawekwa kwenye utaratibu wa ununuzi, kauli ya Serikali ni kwamba tumbaku inazalishwa na inauzwa kwa kupitia Vyama vya Ushirika, ni kilimo cha mkataba. Ni vigumu sana kumhakikishia mkulima soko kama hakukuwa na makubaliano kabla ya kilimo. Kwa hiyo, tunaendelea kuwakumbusha wakulima kwamba ni vizuri wapitie utaratibu wa Vyama vya Ushirika ili kuweza kuingia mkataba na makampuni yanayonunua tumbaku kwa sababu ni zao ambalo hupati bei nje ya utaratibu wa kawaida.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tutaendelea kuboresha mfumo ikiwa ni pamoja na kuboresha Vyama vya Ushirika kwa sababu changamoto kubwa iliyopo katika zao la tumbaku ni kwa sababu vyama vingi vya ushirika vina madeni. Mkoa wa Tabora ni Mkoa wa mfano kabisa, kwa hiyo, mara nyingi sana imetokea kwamba wakulima wengi hawataki kuuza kwenye mfumo wa Vyama vya Ushirika kwa sababu vyama vinadaiwa. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya Vyama vya Ushirika.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri lakini pia pamoja na Serikali kutoa maelekezo kwa TIC kuhusu kunadi fursa hiyo kwa wawekezaji kuja kujenga kiwanda hiki Mkoani Tabora lakini wawekezaji wa Philip Morris wanaozalisha sigara duniani wanatarajia kuja kujenga kiwanda hiki mkoani Morogoro. Pamoja na kwamba Serikali kupitia Halmashauri yetu ya Nzega, Tabora Manispaa na Wilaya ya Uyui tulishatoa maeneo kwa ajili ya kiwanda hiki kuja kujengwa Tabora, lakini bado tunasikia Philip Morris wanakuja kujenga kiwanda hiki Mkoani Morogoro.
Je, Serikali haioni kwamba haiwatendei haki wana Tabora ambao ndiyo watoka jasho wakubwa katika zao hili la tumbaku? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali dogo la pili, Serikali imekiri asali bora na nyingi inazalishwa katika Mkoa wa Tabora hususani katika Jimbo la Igalula. Kwa nini Serikali kwa makusudi makubwa kabisa isingesaidia uongezaji wa thamani wa zao hili la asali kwa maana ya kupata utaalamu na packaging ili kusaidia kipato cha wana Igalula na nchi kwa ujumla? Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI (K.n.y. WIZARA YA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji pamoja na majibu mazuri yaliyotolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ntimizi kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli Kampuni ya Philip Morris wamekwishaanza ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani ya tumbaku pale Morogoro. Wawekezaji wanazo sababu na vigezo wanavyovitumia katika kuchagua maeneo ya mahali gani wawekeze. Kazi ya Serikali mara zote imekuwa ni kuwashawishi na kuwashauri lakini hatufiki mahali tukawalazimisha kama wao wanaamini kwamba sehemu fulani ndipo patakapowapa tija katika uwekezaji wao. Kwa hivyo, Philip Morris pamoja na kushauriwa kwamba wakajenge kiwanda hicho Tabora wao waliamua kuendelea kuwekeza hapo Morogoro. Tukiwalazimisha wanaweza wakaamua kwenda kujenga kiwanda hicho nchi nyingine ambayo pia inazalisha tumbaku. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini baada ya kuona hilo, Chama Kikuu cha Ushirika cha Tumbaku Mkoa wa Tabora (WETCU) katika mkutano wao mkuu waliamua kwamba na wao wawekeze kwenye kiwanda cha kuongeza thamani tumbaku. Mpaka leo wamekwishapata eneo kule Urambo na limepimwa. Sasa hivi wanafanya tathmini ili walipe fidia kwa wananchi walioko pale. Wakishawaondoa wale wananchi walio kwenye eneo hilo, ujenzi wa kiwanda cha kuongeza thamani katika mkoa wa Tabora Wilaya ya Urambo utaanza kufanyika mara moja kupitia Chama hiki cha Msingi cha Ushirika cha WETCU.
Mheshimiwa Spika, swali la pili la nyongeza la Mheshimiwa Ntimizi lilihusu wananchi kueleweshwa namna bora ya kusindika na kufungasha asali. Hili jambo linaendelea, viko vikundi na kupitia Halmashauri vikundi hivi vimekuwa vinaendelea kupatiwa mafunzo ya namna hii na SIDO Mkoa wa Tabora na wao wamekuwa wakijihusisha na hili jambo la kuwafundisha wananchi namna bora ya usindikaji wa asali ili iweze kuwa na ushindani katika soko la ndani na soko la Kimataifa.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Moja ya matatizo ya Walimu wetu ni kukosa makazi katika maeneo wanayofundishia katika vijiji vyetu. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inajenga nyumba za kutosha kwa Walimu wetu ili kuwapa motisha kufundisha vizuri katika maeneo yetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la kuimarisha miundombinu hasa kwa Walimu, ni kweli tumekuwa na changamoto ya nyumba, ndiyo maana hata baadhi ya Watumishi wengine wakishaajiriwa wanakumbana na changamoto kubwa sana ya makazi. Ndiyo maana toka mwaka 2016 katika Sekta ya Elimu tulitumia fedha nyingi takriban shilingi bilioni 64 kujenga miundombinu ya madarasa, vyoo na nyumba za Walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulifanikiwa katika Shule ya Sekondari; mpango wa MMES II tumejenga nyumba takriban 283. Hata hivyo, naomba nishukuru sana Waheshimiwa Wabunge na wadau mbalimbali. Tumeshiriki kwa pamoja kujenga nyumba katika maeneo mbalimbali, lakini hata hivyo, katika mpango wa Serikali, mwaka huu tutaenda kushirikiana tena na wadau na fungu letu la Serikali kuhakikisha tunaongeza idadi ya nyumba. Lengo kubwa ni Walimu wetu na wataalam mbalimbali ambapo sio kada ya Walimu peke yake, waweze kupata makazi bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua hii bado ni changamoto kubwa, lakini naomba tushirikiane kwa pamoja, na Serikali imeweka nguvu za kutosha kuhakikisha kwamba tunajenga nyumba za Walimu na wa kada nyingine katika maeneo mbalimbali.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nazungumzia shule hizi ambazo tunazijenga kutokana na umbali wa shule mama. Kuna maeneo ni zaidi ya kilometa 20 watoto wanatembea, hata hawa kuanzia darasa la nne mpaka darasa la saba wanatembea zaidi ya kilometa 20 kwenda na kilometa 20 kurudi, tunasababisha wasichana kukatisha masomo yao kutokana na kupata mimba, lakini pia tunasababisha wavulana kuona hakuna umuhimu wa kwenda kusoma kwa sababu ya umbali wa shule hizi.
Je, kwa nini sasa Serikali haioni umuhimu wa kutumia kigezo hicho kuzisajili shule hizo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili Mheshimiwa Waziri amesema moja ya sababu ya vigezo vinavyoweza kufanya shule hizo zisisajiliwe ni kutokuwa na ofisi za Walimu Wakuu na kadhalika kama alivyovitaja. Baadhi ya shule zetu nyingi hizo tunazoziita za satellite zimeshajengwa kwa asilimia zaidi ya 80 zimekamilika lakini bado hazisajiliwi. Wakaguzi wakija wanatoa kila siku sababu mpya. Kwa nini shule hizi ambazo zimetimiza zaidi ya 80% ya vigezo zisijaliwe? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ni lengo la Serikali kuhakikisha kuwa wanafunzi wote wanaotakiwa kusoma wanasoma, kwa hiyo shule hizi zinapoanzishwa ni vema kukawa na ushirikishwaji vizuri. Kwa mfano kuanzisha shule katika maeneo ambayo yanatambulika rasmi, kama ni vijiji ni vijiji rasmi isiwe ni yale maeneo ambayo watu wanaenda labda pengine kwa shughuli za kilimo za msimu tu halafu wakasema kwamba wanaanzisha shule kwa sababu shule inatakiwa iwe endelevu.
Sasa kama kuna shule ambazo zimeanzishwa kwa mujibu wa kamati za shule zinatambua na kwa jinsi ambavyo wananchi walioko huko ni wengi wa kutosha na kuna hiyo miundombinu ya kutosha na bado haijasajiliwa, basi mimi nashauri wafuate tataribu na mimi nitakuwa tayari kusaidia kama hizo shule zinakidhi vigezo husika.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Wakati tunasubiri utaratibu wa kupata maji hayo ya uhakika ya hiyo progamu ya pili ya maji hayo kutoka Ziwa Victoria, je kwa sasa Serikali ina utaratibu gani wa haraka wa kusaidia kutatua maji katika Jimbo la Igalula?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri atakuwa tayari baada ya Bunge hili kwisha, kuambatana na mimi kwenda katika Jimbo la Igalula kuona shida kubwa ya maji ya wananchi wa Jimbo la Igalula? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Musa Ntimizi kaka yangu, Mbunge kwa namna ya kipekee anavyowapigania wananchi wake wa Igalula.
Mheshimiwa Spika, mkakati wetu, pamoja na ujenzi wa bomba la kutoka Ziwa Victoria mpaka Uyui na maeneo mengine, lakini moja ya mkakati wetu kama Wizara, Serikali na Mheshimiwa Rais nia yake ya kuwatua akinamama ndoo kichwani, tumetenga bajeti katika kila Halmashauri na Halmashauri ya Igalula imetengewa fedha katika bajeti hii ya 2017/2018. Kwa hiyo, mkakati wetu ni kusimamia kwamba wanatengenezewa visima vya haraka ili wananchi wetu wa Igalula waweze kupata maji.
Mheshimiwa Spika, kukamilika kwa mradi huu wa Ziwa Victoria kutatupa fursa sisi kama Wizara kuangalia namna gani wananchi wa Igalula wanaweza kunufaika kupitia hili bomba kuu. Hii ni kwa sababu Waswahili wanasema unapokuwa karibu na waridi lazima unukie, nataka niwahakikishie wananchi wa Igalula watanufaika na maji kutokana na ukaribu wa bomba hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la mimi kwenda katika Jimbo la Igalula, nipo tayari baada ya Bunge Mheshimiwa Mbunge kushirikiana naye kuhakikisha kwamba nakwenda kuzungumza na wananchi wa Igalula. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini shida ya ya maji Longido ni sawasawa na shida ya maji iliyopo Jimbo la Igalula. Maeneo mengi ya Jimbo la Igalula maji chini hayapatikani kwa urahisi, visima vingi vimechimbwa lakini havitoi maji na kusababisha kupotea fedha nyingi za Serikali; lakini yako maeneo mengi ambayo yanaweza yakachimbwa mabwawa na yakasaidia upatikanaji wa maji katika Jimbo la Igalula.
Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti umeshafanyika, upembuzi yakinifu na usanifu katika Kata ya Goweko na Igalula umeshafanyika, lakini mpaka sasa miradi hii haijafanyika na miradi hii ilikuwa kwenye bajeti ya Serikali ya mwaka 2016/2017, lakini mpaka sasa hakuna kinachofanyika. Sasa naomba kujua miradi hii ni lini itatekelezwa? Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru. Moja tu, ukimwona mtu mzima analia ujue kuna jambo. Sasa mpaka Mheshimiwa Ntimizi analia maana yake Igalula kuna hali mbaya sana katika suala zima la maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara ya Maji na kwa kuwa, sisi si Wizara ya ukame, tupo tayari kushirikiana nae katika kuhakikisha tunawachimbia mabwawa ili wananchi wake waweze kupata maji kwa wakati. Ahsante sana.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la Halmashauri ya Chamwino linafafana na tatizo la Halmashauri ya Tabora Uyui. Tuna zaidi ya miaka kumi tumeamia Isikizya, lakini jengo la Halmashauri yetu lina zaidi ya miaka mitano halijakamilika kutokana na kutoletewa pesa.
Je, ni lini Serikali itatusaidia ili kumalizia ujenzi wa jengo hilo. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema mwanzo ni kwamba maombi haya ya Halmashauri yako katika maeneo mbalimbali na ni kweli Mheshimiwa Mbunge nimefika kwako Uyui tulikuwa pamoja siku ile, kikubwa zaidi tutaangalia kipindi hiki kutokana na bajeti zilizotengwa katika mahali ambapo pesa ambazo hazijapelekwa basi tutafanya harakati ziwezekanazo mradi tuweze kupeleka fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile niweze kusema kwamba commitment ya Serikali ni kuhakikisha kwamba kama tulivyofanya mwaka huu hivi sasa tumepeleka takriban bilioni 30 kwa Halmashauri mpya na Halmshauri mbalimbali kwa hiyo tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo kuwezesha mpango huu wa Serikali ambao tumeupanga katika bajeti zetu. (Makofi)
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Moja ya matatizo ya Walimu wetu ni kukosa makazi katika maeneo wanayofundishia katika vijiji vyetu. Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba inajenga nyumba za kutosha kwa Walimu wetu ili kuwapa motisha kufundisha vizuri katika maeneo yetu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala zima la kuimarisha miundombinu hasa kwa Walimu, ni kweli tumekuwa na changamoto ya nyumba, ndiyo maana hata baadhi ya Watumishi wengine wakishaajiriwa wanakumbana na changamoto kubwa sana ya makazi. Ndiyo maana toka mwaka 2016 katika Sekta ya Elimu tulitumia fedha nyingi takriban shilingi bilioni 64 kujenga miundombinu ya madarasa, vyoo na nyumba za Walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulifanikiwa katika Shule ya Sekondari; mpango wa MMES II tumejenga nyumba takriban 283. Hata hivyo, naomba nishukuru sana Waheshimiwa Wabunge na wadau mbalimbali. Tumeshiriki kwa pamoja kujenga nyumba katika maeneo mbalimbali, lakini hata hivyo, katika mpango wa Serikali, mwaka huu tutaenda kushirikiana tena na wadau na fungu letu la Serikali kuhakikisha tunaongeza idadi ya nyumba. Lengo kubwa ni Walimu wetu na wataalam mbalimbali ambapo sio kada ya Walimu peke yake, waweze kupata makazi bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua hii bado ni changamoto kubwa, lakini naomba tushirikiane kwa pamoja, na Serikali imeweka nguvu za kutosha kuhakikisha kwamba tunajenga nyumba za Walimu na wa kada nyingine katika maeneo mbalimbali.
MHE. MUSSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwanza nipongeze kazi nzuri ya kuboresha mazingira ya kutolea afya katika maeneo yetu kwa nchi nzima. Kutokana na shida kubwa ya afya iliyopo katika maeneo yetu tuliyokuwa nayo, Serikali ije na mpango mahususi wa kuhakikisha kwamba zile nguvu za wananchi katika maeneo yote waliyojenga maboma ya zahanati na nyumba za wauguzi, inawasaidia kumaliza maboma hayo. Je, Serikali lini itafanya hilo ili kumaliza shida ya afya katika maeneo yetu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, mpango mahususi wa Serikali upo na ndiyo maana katika bajeti hii ambayo tunakwenda kumaliza, jumla ya vituo 208 vinaenda kujengwa, lakini pia katika bajeti ambayo ndiyo tunaomba Waheshimiwa Wabunge leo wapitishe, nina uhakika kwamba ikipitishwa jumla ya shilingi bilioni 100.5 inaenda kutumika kwa ajili ya kujenga Hospitali za Wilaya 67 katika Halmashauri zetu. Hiyo yote inaonesha dhamira ya Serikali kwamba ina nia ya kuhakikisha kwamba tatizo la afya linaondolewa.
MHE. MUSSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Pia nashukuru majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri kama alivyosema na kutupongeza wananchi, Mkurugenzi na mimi kwa nia nzuri ambayo tumeionesha ya kushirikiana na Jeshi la Polisi katika uhakikisha kero za ujambazi na usalama wa wananchi wetu zinatekelezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kituo hiki kimekamilika takribani miaka mitatu sasa na hayo marekebisho ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyasema kama Mbunge nilikwishatoa fedha kwa maana mifuko ya simenti na nondo kurekebisha ile Amari ili kituo hiki kiweze kuanza kazi, takribani mwaka mmoja uliopita. Je, ananihakikishia vipi Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba kituo hichi sasa kitaenda kufunguliwa haraka kutokana na mahitaji yake?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini (b) Wilaya yetu ya Uyui ni Wilaya kubwa katika Mkoa wa Tabora ina majimbo mawili ya Igalula, Tabora Kaskazini lakini katika majibu yake amesema tuna magari matatu ambayo kwa kweli hayakidhi haja ya mahitaji ya Wilaya yetu. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kutuletea magari pamoja na mgao mkubwa wa mafuta ili kuweza kutoa huduma zilizo bora katika Wilaya yetu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue fursa hii kuendelea kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa jitihadi zake ambazo amekuwa akizifanya katika kuhakikisha kwamba kituo hiki kinakamilika haraka. Ni sahihi kabisa Mheshimiwa Mbunge kama ambavyo nimesema awali kwamba, amechangia katika kukamilika ujenzi wa Kituo cha Loya, ni jambo jema. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi kwamba, si dhamira ya Serikali kuona jitihada zake na wananchi ambao wametumia nguvu zao kujenga kituo hiki ziende bure bure kwa kuchelewesha kukitumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi ni kwamba, tatizo lililopo ni kwamba tunahitaji kukamilisha Lockup pamoja na amari ili ziwe katika hali nzuri kabla ya matumizi. Jambo hilo tunatarajia kulikamilisha katika muda mfupi sana ujao. Nitahakikisha kwamba nitakapotoka hapa nitafuatilia ili katika kipindi cha mwezi mmoja tuweze kukamilisha vitu hivyo viwili na kituo hiki kianze kutumika mara moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na magari, ni sahihi kwamba katika Wilaya ambazo zina changamoto za magari mojawapo ni Wilaya ya Uyui katika Mkoa wa Tabora. Ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba maeneo yote ikiwemo Wilaya ya Uyui hasa kulingana na ukubwa wa kijiografia wa Wilaya ile yanapata magari ya kutosha zaidi ya yale magari matatu ambayo nimeyazungumza katika jibu langu la msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu ambacho tunaweza kusema kwamba sasa hivi kinatukwaza au kinatukwamisha kutekeleza hilo ni kwamba bado mgao huo haujafanyika kutokana na changamoto mbalimbali ambazo zinakabili programu zima ya uletaji wa magari yaliyodhamiriwa kuletwa katika Serikali. Changamoto hizo zitakapopata ufumbuzi na magari hayo yatakapokuwa tayari kugawiwa, basi nina uhakika basi Mkoa wa Tabora ikiwemo Wilaya ya Uyui na Wilaya nyingine kama Nzega haina gari hata moja zitapewa kipaumbele.
MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa Serikali inafanya vizuri sana kwenye umeme vijijini lakini bado tuna tatizo kubwa kwenye umeme mjini ikiwemo Singida Mjini yapo maeneo ambayo hayana umeme. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kutuletea umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge Sima. Pamoja na Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini tulifanya ziara katika Mkoa wa Singida na katika Wilaya ya Singida Mjini tuliona hilo tatizo. Kwa hiyo, nataka niseme ni kweli Serikali inatambua tatizo la uwepo wa ukuaji wa maeneo ya mijini na changamoto ya upatikanaji wa nishati kwa hiyo, inakuja na mpango wa Peri-Urban ambao utapeleka umeme katika miji inayokua kuanzia mwaka wa fedha 2018/2019.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Katika mkakati wa kupunguza vifo vya mama na mtoto Jimboni Igalula tumeanzisha ujenzi wa vituo vya afya vitano kwa nguvu za wanachi na Mbunge ambapo tumefikia katika hatua ya boma. Je, Serikali ina mpango gani kusaidia nguvu hizi za wananchi ukizingatia hatuna kituo hata kimoja cha afya katika Jimbo la Igalula? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze Naibu Waziri kwa majibu mazuri sana, yale ya wali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali hili la Mheshimiwa Ntimizi, kwanza naomba nimpongeze Mbunge huyu, katika kazi ambayo ameifanya ni kuhamasisha wananchi wake kujenga vituo vya afya vipya lakini bado havijajengwa. Nikiri wazi kwamba amefika ofisini kwangu na kuweza kuweka kipaumbele katika suala zima la Jimbo lake. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama tulivyoongea ofisini kwetu jinsi gani tutafanya ofisi yetu isaidie katika suala zima maeneo yale tupate vituo vya afya hasa tukianza na vituo vya afya viwili, jambo hili ni commitment ya Serikali, tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo ili wananchi wa eneo lile la Jimbo la Igalula waweze kupata huduma ya afya.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Kwanza nitoe shukrani za dhati kwa ziara ya Mheshimiwa Waziri, alipokuja Jimboni kwangu nilimweleza shida ya umeme katika bwawa la maji na sasa tayari transforma imefungwa na umeme unawaka. Nashukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nina masikitiko kidogo, REA awamu ya kwanza, ya pili na ya tatu katika Jimbo la Igalula lenye vijiji takriban 98 ni vijiji sita tu ndivyo vimepata umeme katika Jimbo la Igalula; na katika vijiji hivyo sita ni baadhi tu ya maeneo ya vijiji ambavyo vimepata umeme maeneo mengine hayajapata umeme. Kwa mfano, katika Kata ya Igalula, yenye vijiji sita ni kijiji kimoja tu ndiyo kimepata umeme. Je, Serikali haioni usambazaji wa umeme katika Jimbo la Igalula unasuasua na hauridhishi?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Waziri alikuja kwenye ziara katika Jimbo la Igalula, alitembelea Kata ya Miswaki, Loya na Lutende. Alijionea hali ya uzalishaji mpunga mkubwa katika eneo lile na halmashauri ilivyowekeza mashine za kisasa za kukoboa mpunga katika eneo lile; akaahidi kupeleka umeme katika kata hizo tatu za Lutende, Loya na Miswaki. Je, ni lini zoezi hili litakamilika na wananchi wa kule waweze kupata umeme? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri, kama ambavyo ameeleza kwenye kusoma majibu ya Mheshimiwa Mbunge. Pili, nimpongeze sana Mheshimwa Ntimizi anavyofuatilia maendeleo ya nishati katika Jimbo lake. Sambamba na hilo nipokee shukrani alizotupatia kwa kupeleka maji katika Kata yake ya Igalula na wananchi zaidi ya 1,000 wanapata maji kupitia mradi huo.
Mheshimiwa Spika, na sasa nijielekeze katika maswali yake mawili ya nyongeza. Swali la kwanza ni kuhusiana na vijiji vitano vya Igalula. Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge, hivi mkandarasi sasa hivi yuko katika kijiji cha pili katika Kata ya Igalula na vijiji vyote vitano katika Kata ya Igalula vitapelekewa umeme kupitia mradi huu unaoendelea hivi sasa.
Mheshimiwa Spika, suala la pili; Mheshimiwa Mbunge ni kweli nilitembelea kata ya Lutende, Miswaki pamoja na Loya. Ni maeneo ambayo yana makazi mengi na yana uchumi mzuri. Nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge, Mradi huu wa kupeleka umeme katika kata hizo tatu tutautoa katika Jimbo la Manonga, Kata ya Simbo na mkandarasi ameshaanza kazi; ingawa kutoka Simbo kuelekea Lutende ni kilometa 20 lakini wakandarasi wameshaanza kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, kutoka Lutende kwenda Miswaki ni kilometa 27, kutoka Miswaki kwenda Rorya ni kilometa 13 na kuna jumla ya vijiji 14. Nimpe taarifa kwamba transfoma 17 zimeshapelekwa katika kata hizo tatu na wananchi wa kata hizo watapatiwa umeme ndani ya miezi sita ijayo. (Makofi)
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya kutia matumaini ya Mheshimiwa Naibu Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kama nakumbuka Wizara iliahidi kutoa orodha ya vijiji vyote vitakavyotagazwa na kufunga minara katika majimbo yetu nchi nzima. Swali langu ni lini orodha hii tutapatiwa Waheshimiwa Wabunge ili tuwe na nafasi ya kushauri yale maeneo ambayo tunadhani ni muhimu zaidi kupata mawasiliano? Hapo ikiwemo na Bariadi katika Jimbo unalotoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, maeneo mengi service provider hawa wanapenda kujazana katika maeneo ya centers tu, wanakimbia kupeleka minara katika maeneo ya vijiji vyetu ambako ndiyo kuna shida kubwa ya mawasiliano na population ni kubwa sana. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwalazimisha service providers kwenda kuweka minara katika maeneo yetu ya vijijini ili wananchi wetu waweze kupata mawasiliano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Musa Rashid Ntimizi, Mbunge wa Igalula, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyoshughulika kuhakikisha jimbo lake wananchi wanapata huduma ya mawasiliano. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine wote kwamba Serikali inahakikisha kwamba mawasiliano yanapatikana kwa uhakika katika majimbo yote nchi nzima. Hivi navyozungumza nimekwishazungumza tena mara nyingine kwamba tumefikia asilimia 94 ya wananchi kuwasiliana na tutahakikisha kabla ya mwaka ujao kuisha asilimia 100 ya wananchi wa Tanzania wanapata mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza, Mheshimiwa Mbunge orodha ya mwanzo nitaitoa kesho ya vijiji zaidi ya 600 ambavyo tunategemea kupeleka minara ya mawasialiano kwa ajili ya wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anataka kujua kwa nini watoa huduma wanarundikana sehemu moja. Kama nilivyowahi kuzungumza hapo awali hawa watoa huduma za mawasiliano ni wafanyabiashara na mfanyabiashara kawaida anatafuta sehemu ambako atapata biashara nzuri, hawawezi kupeleka sehemu ambako hakuna mvuto au ambako wakiwekeza pesa yao haitarudi. Ndiyo maana Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imekuwa ikitoa ruzuku kwa haya makampuni waweze kupeleka mawasiliano mpaka vijijini ambako kabisa wananchi hawawezi kununua huduma za mawasiliano kwa jinsi ambavyo watoa huduma wanataka. Ndiyo maana sasa tumeanzisha Mfuko wa Wawasiliano kwa Wote ili uweze kuziba hilo gap na kufanya wananchi waweze kuwasiliana nchi nzima.
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini nina maswali madogo mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kumekuwa na kawaida ya hawa service providers pamoja na ruzuku wanayopata kutoka Serikalini kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote wamekuwa wanajikusanya kwenye maeneo ambayo tayari kuna mawasiliano badala ya yale madhumuni ya kupeleka mawasiliano kwenye maeneo ambayo hayana mawasiliano. Mfano katika jibu lake la swali langu, katika Kata ya hiyo ya Tura, Kijiji cha Karangasi, tayari kuna mawasiliano lakini bado tena kumepelekwa mtandao mwingine, lakini yapo maeneo ambayo hayana mawasiliano. Je, kwa nini sasa hawa Service Providers wasipeleke mawasiliano kwenye maeneo yale ambayo hayana mawasiliano?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Kata ya Mmale yote haina mawasiliano; je, ni lini Serikali itapeleka mawasiliano katika Kata hiyo ya Mmale? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge wa Tura kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, hoja yako uliyoizungumza ni kweli, kwamba service providers, watoa huduma za mawasiliano walikuwa wanajirundika kwenye maeneo machache, maeneo ambayo yana biashara kubwa au yana population kubwa ya watu. Baada ya kuliona hili, Bunge hili hili liliamua kuunda Mfuko wa Masiliano kwa Wote. Maana yake nini, ni kwamba ule Mfuko sasa unaenda kwenye maeneo yale ambayo, hawa wanaofanya biashara tu bila kujali utu wa mwanadamu Mtanzania, kwamba sasa tuwalazimishe waende kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfuko huu tayari, sasa hivi tunaenda maeneo yote bila kujali kwamba kuna faida kubwa na ndiyo maana hata kwenye maeneo anayoyahitaji Mheshimiwa Mbunge sasa, baada ya kutangaza hii tenda tutahakikisha kata zote, maeneo yote ili mradi yana Watanzania yanapata huduma ya mawasiliano. (Makofi)
MHE. MUSA R. NTIMIZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, kwanza kabisa kwa masikitiko makubwa napenda kupokea majibu yasiyoleta matumaini ya kupata maji kwa wananchi wenzangu wa Jimbo la Igalula.

Mheshimiwa Spika, Waziri ni shahidi, amekuja Jimboni kwangu na Mheshimiwa Makamu wa Rais tulizungumzia kero hii ya maji, alikuja Mheshimiwa Waziri Mkuu na alikuja Mheshimiwa Rais alitoa ahadi kwamba maji ya Ziwa Victoria yatakuja katika Jimbo la Igalula. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Waziri amesema Jimbo la Igalula vijiji vyake viko zaidi ya kilometa 30 linapopita bomba la maji, lakini naomba nikwambie linapojengwa tenki kubwa linalopeleka maji Sikonge na Urambo ambapo ni takribani kilometa 100 na zaidi liko kilometa 18 toka Jimboni kwangu. Lakini wananchi wa Jimbo la Igalula hawapati maji ya ziwa Victoria.

Mheshimiwa Waziri ajiweke katika nafasi yangu aone namna gani tabu napata Majimbo yote ya Mkoa wa Tabora yanapata maji ya Ziwa Victoria kasoro Jimbo la Igalula tu. Lakini ndani yake kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais. Je, Wizara itatekeleza lini ahadi hii ya Mheshimiwa Rais? La kwanza. (Makofi)

Lakini la pili amezungumzia miradi ya Tura, Nsololo na Loya ambayo usanifu wake umeshafanyika muda mrefu na documents zimeshafika Wizarani muda mrefu lakini haipo katika financial year 2018/2019 pamoja na shida kubwa ya maji tuliyokuwa nayo katika Jimbo la Igalula. Je, Waziri ananiambia nini na wananchi wa Jimbo la Igalula leo wanasikia wanataka kusikia kauli ya Waziri? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji kwanza nataka nimtoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kiukweli sisi kwa Mkoa wa Tabora tumeona ni eneo ambalo limekuwa na changamoto kubwa sana na ndiyo maana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametupa zaidi ya shilingi bilioni 600 katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji katika Mkoa wa Tabora kuyatoa maji Shinyanga na kuyapeleka katika Mkoa wa Tabora, lakini kupeleka mpaka Kaliua pamoja na Urambo kwa Mama yetu Sitta.

Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge subira yavuta heri. Tumeanza utekelezaji wa awamu ya kwanza na hatuna kikwazo chochote, nataka nimuhakikishie baada ya maji kufika Tabora tutamhakikishia kwamba tunayapeleka katika eneo lile na ahadi ni deni, tutahakikisha tunatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kumtua mwanamama ndoo kichwani.

Lakini kuhusu suala zima la kibali kuhusu suala la utekelezaji ama usanifu wa Loya, Mheshimiwa Mbunge nataka nimhakikishie naomba baada ya saa saba tukutane na wataalam wetu ili hili jambo tulifanye kwa haraka ili wananchi wake waweze kupata huduma hii muhimu. Ahsante sana. (Makofi)