Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Hussein Mohamed Bashe (4 total)

MHE. HUSSEIN M. BASHE aliuliza:-
Wakati wa kampeni za Uchaguzi Jimbo la Nzega Mjini tarehe 14/10/2015, Mheshimiwa Rais aliahidi kuwa majengo yanayotumiwa na mkandarasi wa barabara ya Nzega – Tabora na majengo ya TANROADS yatakabidhiwa kwa Halmashauri ya Mji wa Nzega ili yaweze kutumika kwa ajili ya Chuo cha VETA:-
(a) Je, Serikali imefikia hatua gani kutekeleza ahadi hiyo ili majengo hayo yakabidhiwe katika Halmashauri ya Nzega?
(b) Je, Serikali ipo tayari kuwaambia wananchi wa Nzega lini chuo hicho kitaanzishwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe, Mbunge wa Nzega Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Nzega na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora zimeandaa na kuwasilisha Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano maombi ya majengo ya kambi iliyokuwa inatumika wakati wa ujenzi wa barabara ya Nzega - Puge kwa ajili ya kutumia kambi hiyo kama chuo cha VETA.
Mheshimiwa Naibu Spika, kulingana na mkataba wa ujenzi wa barabara, majengo ya mkandarasi ni mali yake na hayarejeshwi Serikalini. Majengo aliyokuwa anatumia Mhandisi Mshauri ndiyo yaliyorejeshwa kwa mwajiri, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Wizara bado inayafanyia kazi maombi ya kuyakabidhi majengo hayo kwa Halmashauri ya Mji wa Nzega kwa kuzingatia taratibu za uhamisho wa mali za Serikali kutoka taasisi moja kwenda taasisi nyingine. Aidha, uamuzi wa lini Chuo cha VETA kitaanzishwa, utategemea upatikanaji wa majengo hayo na uamuzi wa mamlaka inayohusika na kutoa vibali vya kuanzishwa kwa Vyuo vya VETA.
MHE. HUSSEIN M. BASHE aliuliza:-
Wakati wa kampeni za uchaguzi Mheshimiwa Rais aliahidi ujenzi wa daraja la Nhobola na daraja la Butandula pamoja na barabara inayounganisha Kijiji hicho na Kijiji cha Mbogwe:-
Je, ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa ahadi ya ujenzi wa madaraja hayo pamoja na barabara zake?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA): alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimwia Hussein Mohamed Bashe, Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua za awali za ujenzi wa daraja la Nhobola na Butandula zimeshafanyika kufuatia kukamilia kwa upembuzi yakinifu (feasibility study), usanifu wa awali (preliminary design) na usanifu wa kina yaani (detailed design) ili kujua gharama za ujenzi wa madaraja yote mawili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa usanifu huo daraja la Nhobola linatarajiwa kugharimu shilingi milioni 589.8 ambazo zitahusisha ujenzi wa barabara yenye kilomita 5.1 kuunganisha kati ya Mbogwe na Nhobola. Ujenzi wa daraja la Butandula utagharimu shilingi milioni 245.57 na utahusisha matengenezo ya sehemu zote korofi zenye urefu wa kilomita 16.2 katika vipande vya barabara ya Ijanija-Butandula, Butandula-Izegwa, Mwangoye na Butandula-Uchama. Kwa kuwa hatua hiyo imekamilika, Halmashauri itaweka katika mpango wa bajeti yake ili kupata fedha hizo na kuanza ujenzi wa madaraja hayo yote mawili.
MHE. HUSSEIN M. BASHE aliuliza:-
Halmashauri ya Mji wa Nzega haina shule hata moja ya kidato cha tano na sita na hivyo kuwafanya wanafunzi wengi kulazimika kwenda kusoma nje ya Mji wa Nzega; lakini Mbunge kwa jitihada zake amejenga vyumba viwili pamoja na bweni katika shule ya sekondari Bulende kwa ajili ya kidato cha tano na sita.
(a) Je, Serikali ipo tayari kuanzisha masomo kwa kidato cha tano kuanzia mwaka huu wa 2016;
(b) Je, ni lini Serikali itajenga vyumba vya madarasa ya kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari Chief Itinginya ili angalau kuwe na shule mbili za kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe, Mbunge wa Nzega Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri ya ukarabati wa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya Sekondari ya Bulende, na sasa anaendelea na ujenzi na hosteli, Mheshimiwa hongera sana kwa kazi hii nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha shule ya Sekondari ya Bulende inapata sifa ya kuwa ya kidato cha tano, Serikali imetenga shilingi milioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa bweni katika bajeti ya mwaka 2016/2017. Ili shule iweze kusajiliwa kuwa ya kidato cha tano na sita inapaswa kuwa na miundombinu ya kutosha kama vyumba vya madarasa, mabweni, samani, bwalo la chakula, vyoo pamoja na uwepo wa walimu wa masomo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri inapaswa kuwasilisha maombi ya usajili wa shule katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Ufundi ambao watatuma wataalam kukagua miundombinu ya shule kabla ya kutoa kibali. Mpango wa Serikali ni kuhakikisha miundombinu ya kutosha inajengwa kwa kushirikisha nguvu za wananchi katika shule ya Sekondari ya Chief Itinginya ili kukidhi na kusajili kuwa ya kidato cha tano.
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri imepanga kutenga bajeti katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari ya Chief Itinginya.
MHE. HUSSEIN M. BASHE aliuliza:-
Je, ni lini Serikali inakusidia kuanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya kilometa 10 ndani ya Mji wa Nzega kama ambavyo Mheshimiwa Rais aliahidi wakati wa kampeni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hussein Mohamed Bashe, Mbunge wa Jimbo la Nzega Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hatua za awali za utekelezaji wa ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga kilometa 10 za barabara kwa kiwango cha lami zimeshaanza, ambapo kazi zilizofanyika ni upembuzi yakinifu, usanifu wa kina, kuandaa michoro na makisio ya kazi za ujenzi wa kilometa 10. Mtandao huo wa barabara utajengwa katika Kata ya Nzega Mjini Mashariki, sawa na kilometa tano na Nzega Mjini Magharibi kilometa tano zilizobaki.
Mheshimiwa Spika, gharama za kutekeleza mradi huo ni shilingi bilioni 5.2 ambazo zitahusisha ujenzi wa mitaro ya barabara na makalavati ikiwemo mitaro mikubwa katika eneo la Samora, ujenzi matabaka ya barabara ya changarawe na ujenzi wa mtabaka mawili ya lami nyepesi.
Mheshimiwa Spika, makisio ya gharama hizo yatazingatiwa katika bajeti ya Halmashauri kwa mwaka 2017/2018 kwa ajili ya kuanza utekelezaji kwa awamu.