Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Joseph George Kakunda (13 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kabla sijachangia naomba niwashukuru sana wananchi wa Sikonge kwa kuniamini kuwa Mbunge wao kwa mara ya kwanza. Naomba niwatoe wasi wasi, wasiwe na wasiwasi wowote hapa kazi tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaingia katika hotuba, naomba nieleze kwamba nikiwa Mbunge nilifadhaika sana siku Mheshimiwa Rais alipotoa hotuba yake. Wakati Mheshimiwa Rais anaingia humu ndani, zilizuka fujo ambazo zilinifanya ninyong‟onyee kwa muda, nikishangaa
kwa sababu sikutegemea hadi wenzetu wakatoka wakisusia, hawakutaka kumsikiliza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini leo...
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Leo nimefarijika kuona badala ya kumsikiliza siku ile Mheshimiwa Rais, leo wenzetu wamesoma vizuri hotuba yake na wakisimama wanamsifu bila vurugu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ustaarabu huu uliooneshwa leo Watanzania wanauona na sisi Wabunge wote kwa ujumla naomba tuuzingatie ustaarabu huu siku zote, ili kama kuna hoja ijibiwe kwa hoja badala ya vurugu ambazo zinatufanya sisi wote tupoteze heshima yetu nje ya
Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nije kwenye hotuba. Kiwango cha commitment kilichooneshwa na Mheshimiwa Rais katika hotuba yake ni cha hali ya juu sana. Ni kiongozi ambaye yuko tayari kwa kauli na vitendo kupambana na vikwazo vyote ambavyo kwa muda mrefu vimekua vikimsababishia Mtanzania kero nyingi katika juhudi za kujikwamua kutoka kwenye umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, matumaini ya sasa ya Watanzania ikiwemo Wanasikonge ni makubwa mno, kwamba, baada ya miaka 10 ya Mheshimiwa Dkt. Magufuli akiwa Rais uwezekano wa kufikia malengo ya Dira ya Maen deleo ya Taifa ifikapo mwaka 2025 si wa kutilia
shaka tena, kinachotakiwa kila mtu kutimiza wajibu wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Rais ya tarehe 20/11/2015 na utendaji wake wa Rais na Serikali yake hadi sasa, umeongeza matarajio ya wananchi kuhusu kufanikiwa katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, kuboresha ukusanyaji wa mapato ya Serikali, kudhibiti
matumizi, kuimarisha uadilifu, uaminifu na uzalendo na vyote hivi vinaashiria matokeo makubwa katika kupunguza umaskini. Ili tufanikiwe katika yote hayo, yale majipu ambayo Mheshimiwa Rais aliyaahidi kuyatumbua, majipu makubwa, majipu madogo na hata vijipu uchungu, vyote lazima vitumbuliwe bila kuona huruma. Mheshimiwa Rais ameahidi na tayari utekelezaji unaendelea, tunamshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Sikonge walifurahishwa sana na hotuba ya Rais na wamekaa mkao wa hapa kazi tu, wanatimiza majukumu yao hususani katika sekta ya kilimo kwa kulima sana mashamba ya tumbaku na mazao ya chakula, kutengeneza mizinga kwa ajili
ya asali na nta na kutumia fursa nyingine zozote zilizopo kupambana na umaskini.
Wanakumbuka ahadi nzuri zinazojenga matumaini za Mheshimiwa Rais kwamba Serikali itawaboreshea zaidi mazingira ya kufaidika na jasho lao.
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo ningependa kukumbusha kwa sababu yako katika hotuba ya Mheshimiwa Rais, la kwanza, linalohusu eneo langu, kuondoa kero kwenye zao la tumbaku kwa kumwezesha mkulima apate pembejeo kwa urahisi na kwa muda muafaka
na kwa bei nafuu kwa kutumia mfumo rahisi ambapo mkulima kupitia Chama chake cha Msingi, akae kitako na mnunuzi ili waingie mktaba wa mnunuzi kukopeshwa pembejeo au pembejeo zitolewe kwa mkulima wakati wa msimu wa malipo kabla kilimo hakijaanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia mfumo wa malipo uboreshwe kuondoa malipo kuchelewa kwa zaidi ya miezi mitatu na Serikali imlinde mkulima asiibiwe wakati wa kubadilisha viwango vya fedha kutoka kwenye dola ya Kimarekani kwenda kwenye shilingi ya Kitanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye kilimo kuna mambo mengi sana ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi. Watu wa Ushirika wanahitaji kuwasaidia wakulima katika maeneo mengi, COASCO ambao ni auditors wa ushirika ni tatizo kubwa, wamekuwa siyo wa kweli, ni bora tu
kuwaondoa ili mfumo wa ukaguzi ubaki chini ya ukaguzi wa ndani wa Halmashauri na CAG, hili litatusaidia.
Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mengi mno kwenye kilimo yatazungumzwa na wengine, naomba wakulima waonewe huruma, wasaidiwe na Serikali pamoja na wadau kuondokana na adha wanazozipata.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningependa nilizungumzie ni kuboresha uhusiano kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi, kwa mfano, mfugaji wa nyuki ni rafiki mkubwa sana wa misitu kwa sababu yeye anategemea kuweka mizinga yake kwenye misitu, kwa nini mfuga nyuki aonekane adui kwenye hifadhi eti tu kwa sababu tu anatumia mzinga wa gome la mti! Kwa nini Serikali isitoe elimu na huu ni ushauri kwa wafuga nyuki, ili watumie mizinga ya kisasa itakayofanya hatimaye wawe na uhuru wa kuingia hifadhini kwa sababu watakuwa
wamesajiliwa, hata wavuvi wadogo wadogo nao wanahitaji kusaidiwa kwa elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo napenda kuzungumzia kama kukumbusha kwa sababu liko kwenye hotuba, ni miundombinu. Barabara za lami na sisi tunahitaji kuunganishwa na Mikoa mingine kama Tabora - Katavi, Tabora – Mbeya - Singida, Tabora – Kigoma, kuboresha reli ya kati, miradi ya umeme vijijini na mitandao ya simu. Wilaya yangu ya Sikonge karibu 70% ya maeneo ya makazi hayajaunganishwa na mitandao ya simu. Ni muhimu sana kwenye awamu hii suala la mtandao lishughulikiwe kwa jicho kamilifu. Naomba maeneo yote yaliyo nyuma kwa miundombinu yapewe kipaumbele na Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine Serikali iendelee kuwekeza kwenye elimu. Katika Wilaya yangu kuna maeneo 49 ambayo yanahitaji shule mpya kabisa za msingi. Katika maeneo 19 wananchi wamejenga madarasa, Halmashauri haina fedha za kukamilisha, kwa hiyo, Serikali
Kuu bado tunaomba iendelee kuwekeza kwenye elimu ya msingi, siyo kwamba MMEM ilikwisha, basi hakuna uwekezaji mpya unao endelea, tunaomba tuendelee kuwekeza kwenye elimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kwenye afya tuna upungufu mkubwa sana wa zahanati, watumishi na dawa, vyote viendelee kuwa katika mipango ya Serikali. Kwenye maji tuna matumaini makubwa na mradi wa Ziwa Victoria, tunaomba ukamilike.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, naomba nimalizie kwa kusisitiza kuhusu barabara ya lami kutoka Tabora-Ipole-Mpanda. Tunaomba fidia ilipwe mapema, barabara ijengwe mapema kuondoa adha wanayoipata wananchi amabo ni watumiaji wa barabara hiyo.
Design yake ifanyiwe mapitio ili tuta la barabara ya lami liwe juu…
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kakunda muda wako umekwisha.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, namalizia, yaongezwe madaraja na makalvati…
NAIBU SPIKA: Naomba ukae tafadhali…
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: ...ili barabara itakayojengwa iwe ya kudumu. Naomba kuwasilisha, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Haizuiliki kuzungumzia masuala ya kisera ya Wizara ya Afya ambayo wamesema kwamba kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata iwe na kituo cha afya. Sera wanaimiliki wao, TAMISEMI kazi yao ni kusimamia na kuratibu utekelezaj wa sera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo langu kubwa ni ceiling ambazo Serikali huwa inailazimishia mikoa. Kwetu sisi Tabora kwenye ceiling ya TAMISEMI ambayo ndiyo tumepitisha bajeti, kwenye sekta yote ya afya ni shilingi bilioni 19 kwa mkoa mzima. Kama tunataka kutekeleza sera inavyotaka kila kijiji kiwe na zahanati na kila kata iwe na kituo cha afya, kwenye Wilaya ya Sikonge peke yake tunahitaji vituo vya afya 18 vipya na zahanati mpya 41. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo langu linakuja, nimewauliza watalaam wa afya kule kwangu, ili ujenge kituo cha afya kwa mujibu wa miongozo ya Wizara ya Afya, majengo, vifaa, wataalam na kila kitu unahitaji zaidi ya shilingi bilioni mbili. Ili ujenge zahanati kwa mujibu wa miongozo ya Wizara ya Afya kwa kila kitu unahitaji zaidi ya shilingi milioni 500. Ina maana kwa Sikonge tu tunahitaji zaidi ya shilingi bilioni 65, tutazipata wapi na tutakamilisha lini ikiwa Serikali inatupangia ceiling ya shilingi bilioni tatu kwenye wilaya yetu? Kwa hiyo, hilo ni tatizo kubwa na tusije tukaiacha hivyo hivyo, Serikali kwa ujumla wake inatakiwa ilifanyie kazi suala hili ili kusudi kweli sera hii iweze kutekelezeka, hilo lilikuwa la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu Maafisa wa Maendeleo ya Jamii. Zamani hawa tulikuwa tunawaita Mabwana na Mabibi Maendeleo. Taarifa ya Waziri kule mwisho kwenye majedwali inaonyesha kabisa kwamba Wilaya ya Sikonge tuna Maafisa Maendeleo ya Jamii 14 na wote wako Makao Makuu ya Wilaya. Katika kata zangu 20 hakuna Afisa Maendeleo ya Jamii ambaye yuko kwenye kata. Nashauri Serikali iachane na maneno, wakati wa utekelezaji ndiyo huu, hapa kazi tu, tuhakikishe kwamba hawa Mabibi na Mabwana Maendeleo wanafika kwenye kata ili kusudi waweze kuhamasisha maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, ni kuhusu Vyuo vya Maendeleo ya Jamii na Vyuo vya Wananchi hivi (FDCs). Tumeambiwa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba tuna Vyuo tisa vya Maendeleo ya Jamii nchi nzima. Napendekeza vyuo hivyo viboreshwe zaidi ili vifikie hatua ya kutoa diploma na hata digrii ili kusudi tusomeshe watu wengi zaidi kwenye hii fani ya maendeleo ya jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu hivi Vyuo vya Wananchi (FDCs - Folk Development Colleges), kama tulivyokuwa tunazungumza siku tunajadili hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na hata siku ya kujadili Wizara ya Viwanda, tunahitaji watu wengi, tunahitaji staff, tunahitaji nguvu kazi ambayo itaajiriwa kwenye viwanda vidogo vidogo, kama hivi Vyuo vya Maendeleo ya Jamii vitaendelea kufundisha elementary sijui kushona nguo, kitu ambacho hata fundi cherehani wa mtaani anaweza akakifanya, naomba hivi vyuo vibadilishwe viwe VETA za maendeleo ya jamii ili kusudi viweze kusaidia uchumi wetu na maendeleo ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la nne ambalo nataka kuchangia ni ukatili wa kijinsia. Kwa mwaka mmoja tu 2015, kwenye hii hotuba ya Mheshimiwa Waziri aliyotupatia, inaonekana Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Morogoro, Pwani na Tanga imeongoza katika ukatiri wa ngono, hiyo mikoa mitano. Wana matukio zaidi ya 300 ya ukatili wa ngono, hii mikoa niliyoitaja. Mikoa ambayo ina matukio chini ya 100 ni Mkoa wa Simiyu peke yake, hii ni hatari!
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nchi iwe na programu maalum ya elimu dhidi ya ukatili wa ngono, hilo ni suala la aibu sana, linatakiwa lipatiwe programu maalum kabisa. Sijaiona hiyo programu kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri, naomba sana suala hili lizingatiwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine kwenye haya matukio ni mashambulio ya kudhuru mwili na matusi. Haya mambo ni mabaya na yanasababisha chuki katika jamii na familia nyingi. Imeonekana Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, Morogoro tena na Rukwa ina matukio zaidi ya 1,000, hii ni hatari. Mikoa yenye matukio chini ya 100 ni Dodoma, Kilimanjaro, Lindi, Mara, Mwanza, Mbeya, Pwani, Ruvuma na Simiyu tena. Hivi kule Mara walitumia mbinu gani kupunguza matatizo haya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, napendekeza Mheshimiwa Waziri apeleke timu Mkoa wa Mara kuchunguza kuona hivi wale watu, kwa sababu wanaaminika wana hasira sana, wamepunguzaje haya matukio ya kushambuliana ili elimu ile iweze kutumika kwenye mikoa mingine hasa hii ambayo ina matukio mengi ili kupunguza matatizo haya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tano ambalo nataka kuchangia ni uchangiaji wa halmashauri kwenye Mfuko wa Wanawake - WDF. Katika halmashauri ambazo zimetajwa kwenye hotuba ya Waziri ni Halmashauri moja tu ya Iringa ndiyo imeonekana imechangia kwa asilimia 100. Kuna Halmashauri kama ya Kinondoni, Kigoma Ujiji, Sumbawanga, Tabora Manispaa, Misungwi, Mwanza na nyingine nyingi ziko chini ya asilimia 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hatua gani ambayo Serikali inachukua sasa kuhakikisha kwamba watu wanaboresha michango yao angalau inafika zaidi ya asilimia 50 na kuendelea. Kuna baadhi ya halmashauri mchango wao ni chini ya asilimia moja, hii ni serious. Naomba suala hili liweze kuchukuliwa kwa umakini wa hali ya juu kwa sababu hawa wanaotekeleza ni waajiriwa wa Serikali, wanatakiwa waheshimu miongozo inayotolewa na Serikali, wasiendelee kufanya kinyume na utaratibu ambao umeelekezwa na Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo nataka kuchangia ni suala la wazee. Naomba Serikali isimamie kikamilifu utekelezaji wa maelekezo yake ya kisera. Kwa mfano, suala la huduma bure za afya kwenye hospitali za Serikali na vituo vya afya na zahanati kwa wazee lisibaki kwenye maneno wala kwenye makaratasi. Najua Waziri wa Afya alitoa Circular mwezi Februari lakini imeendelea kutoheshimika kwenye maeneo yaliyo mengi hapa nchini. Naomba sana ufuatiliaji wa karibu uwepo ili hiyo Circular iweze kutekelezwa isibaki kwenye karatasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wakati mgombea wetu wa Urais alizungumzia kuhusu pesheni ya wazee. Hili ni suala ambalo ukizunguka kwenye vijiji unaulizwa na wazee, bwana tuliambiwa kuhusu pesheni imefikia hatua gani? Naomba Mheshimiwa Waziri atakaposimama aweze kulitolea maelezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho, kuna Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake na Mfuko wa Vijana, sawa, lakini wazee wanauliza Mfuko wa Wazee vipi? Kwa maana ya hawa wazee waliostaafu, Mfuko wa Wazee Serikali inatufikiriaje sisi? Kwa sababu Mheshimiwa Waziri wa Afya ndiyo anahusika na masuala ya wazee, naomba wazee wangu wa kule Sikonge wasikie leo anazungumza kuhusu Mfuko wa Wazee atauanzisha lini? (Makofi)
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Wataona baadaye usiku. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ya kwangu yalikuwa ni hayo lakini naomba nimalizie kwa vituko vya kisiasa. Ukistaajabu ya Mussa walisema utaona ya Firauni. Kule Uganda kilitokea kituko kimoja kikubwa sana jana lakini nisingependa kukieleza kwa kina kila mtu anajua. Kwa hiyo, kumbe Tanzania sisi tuna afadhali katika demokrasia na ni mfano wa kuigwa. Wenzetu wamefikia katika hali mbaya, naomba tuwaombee ili kusudi nchi ile iendelee kuwa na amani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba kuunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naenda moja kwa moja kwenye hoja.
Naomba nimuunge mkono Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri, lakini nimwambie kwamba Barabara ya Tabora - Itigi - Manyoni kilometa 260, ambayo ameipangia shilingi bilioni 79 hizi za Serikali hazitatosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwepo Kuwait wakati tunazungumza na Kuwait Fund kuhusu kupata fedha kwa ajili ya barabara hii na walisema ikikamilika barabara ya Kilwa the next road itakuwa ni hii barabara ya Tabora - Itigi - Manyoni. Kwenye hotuba yake amegusia kidogo tu kuhusu hayo mazungumzo, lakini hajasema commitment ya Kuwait Fund ikoje, naomba wakati ana-windup atupatie commitment ya Kuwait Fund ikoje? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, barabara ya Makongorosi - Rungwa - Itigi hadi Mkiwa; hii barabara imeamuliwa kujengwa tangu miaka kumi iliyopita, ninaomba isifike miaka 20 barabara hii bado inajengwa, ninaomba sana. Hayo mawili yanamtosha Mheshimiwa Waziri kuyafuatilia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu cha tatu kiwanja cha ndege cha Tabora, amepanga pale shilingi bilioni 7.8; kiwanja cha ndege cha Tabora kilianza kujengwa mwaka 1919, hadhi yake ya sasa hivi iko nyuma sana ukilinganisha kwamba pale Tabora ndiyo makao makuu ya Western Brigade ya Jeshi. Ninaomba sana Serikali iweke kipaumbele kwenye kiwanja cha ndege cha Tabora; kwanza, hizo fedha shilingi bilioni 7.8 zilizopangwa zionekane kwa macho zimetumika, kusiwe na uchakachuaji wa aina yoyote Mheshimiwa Waziri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu reli ya kati. Reli ya kati madhara yake ni makubwa sana kama haitajengwa. Kusafirisha mafuta kwa njia ya barabara petrol, diesel, mafuta ya taa, ni gharama kubwa sana na hii ndiyo inasababisha bei ya vitu hivi kuwa kubwa, inaathiri sana maisha ya watu wetu. Naomba sana kipaumbele, kwa njia yoyote ile Serikali ifanye lolote inaloweza kufanya hii reli ya kati lazima ijengwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo napenda kuchangia ni kuhusu bandari. Upo mradi unaoendelea pale, ule mradi unaoendelea wa kuboresha bandari kwa kushirikiana na Benki ya Dunia na Serikali ya Uingereza ninaomba usimamiwe vizuri, ili hatimaye meli kubwa ziweze ku-dock pale na ziweze kushusha shehena kubwa sana, ili tusiathirike kibiashara. Bandari yetu ina potential kubwa sana ya kusaidia uchumi wa nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ambalo napenda kuzungumzia ni mitandao. Kwetu kule tuna shida ya mitandao kwenye kata nyingi sana, lakini hasa kwenye kata za Kilori, Kipili, Kitunda na Majojoro, ninaomba sana wakati Waziri anaposimama aweze kuzungumza commitment ya Serikali kuhusu kuboresha mitandao kwenye Wilaya yangu ya Sikonge. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri.
Naomba niende moja kwa moja kwenye masuala machache, sasa hivi Wizara inafanya mapito makubwa ya sera ya ardhi na tunaona huko mikoani inaendelea. Naomba kwa hatua hii Wizara isifanye makosa waliyofanya mwanzoni pale. Baada ya sera ya mwaka 1995 waliandaa sheria halafu baadae ndiyo wakaja kuandaa mkakati wa kutekeleza sheria. Kilichokuwa kinatakiwa ni kwamba baada ya sera unaandaa mkakati wa Taifa ambao unakwenda sambamba na programu ya Kitaifa ya kutekeleza sera, halafu ndiyo unakuja unamalizia na sheria. Kwa hiyo, naomba safari hii wazingatie huo mfuatano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye utekelezaji wa sera tunahitaji mambo mawili makubwa, kwanza awareness ya wadau wote waielewe sera, lakini pili tunahitaji rasilimali, rasilimali watu hiyo ni ya kwanza kabisa na rasilimali fedha. Kwa miaka mingi fedha ambayo imekuwa ikitengwa au inaombwa na Wizara hii imekuwa ni kidogo mno. Ndiyo maana Wizara hii ina upungufu mkubwa wa Maafisa Ardhi, Maafisa Mipango Miji, Wapima, Wathamini, Wachora Ramani, Wakadiriaji Majengo na kadhalika. Kwa kifupi ina nguvukazi kidogo sana, sidhani kama hiyo nguvukazi inaweza kutekeleza sera kama wanavyotaka. Vilevile rasilimali fedha imekuwa inapangwa kidogo sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana ukiangalia taarifa kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri viwanja vilivyopimwa mwaka huu 2015/2016 ni 112,000 tu angalau wangepima 400,000 ingekuwa ni afadhali kwa nchi yetu. Kati ya hivyo viwanja 112,000 viwanja 38,700 vyote vimepimwa Dar es Salaam na Pwani ambayo ni asilimia 35, huu ni upungufu mkubwa sana. Hati miliki zilizosajiliwa 25,000 tu angalau wangekuwa na uwezo wa kusajili hati 100,000 kwa mwaka ingetusaidia kama nchi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama trend ni hii ina maana kwamba hata hii mipango kabambe ya majiji, manispaa na miji yetu inayoandaliwa haitaweza kutekelezeka kwa sababu ya ufinyu wa rasilimali fedha na upungufu wa rasilimali watu. Naomba sana Wizara ijipange ili kwenye mwaka mwingine unaokuja baada ya mwaka ujao (2017/2018), waje na mkakati wa maombi ya fedha za kutosha ili utekelezaji ufanyike vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna upungufu wa nguvu kazi au upungufu wa uwezo wa kutumia fedha. Katika mwaka huu wa fedha walipanga kutumia shilingi bilioni 3.45 kwa ajili ya miradi ya maendeleo wamepata shilingi bilioni 3.43 ambayo ni sawasawa na asilimia 99, lakini hotuba ya Waziri inatuambia wametumia milioni 745 tu ambayo ni asilimia 21. Ina maana hata kama tukiwapa pesa kumbe uwezo wa kutumia fedha yaani ile absorption capacity inavyoelekea kwa Wizara hii ni ndogo sana, sasa sijui watajipangaje. Mheshimiwa Waziri atakaposimama atueleze vizuri wamejipangaje, hivi uwezo wa kutumia fedha tufanyaje, sisi Wabunge tumsaidie vipi ili Wizara hii iwe na uwezo wa kutumia fedha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu mwingine ni Shirika la Nyumba la Taifa, utekelezaji wake nao ni mdogo sana. Mahitaji ya nyumba kwa nchi yetu ni 200,000 kwa mwaka, lakini wao wamepanga kujenga nyumba 5,000 tu kwa mwaka ukilinganisha na nyumba 200,000 yaani ni upungufu mkubwa sana. Mahitaji ya jumla ya nchi yetu sisi tunahitaji nyumba 3,000,000, tutafikia lini malengo haya?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Naomba niseme kwamba wapinzani wamewasilisha malalamiko ya mtu mmoja bila ya kuleta bajeti mbadala ya upinzani. Hawa ni sawa sawa tu na Mbunge mmoja amesimama pale amechangia, lakini kusema hiyo ni hotuba ya upinzani kama bajeti mbadala hiyo ni bajeti hewa. Niliamini kama kweli ingekuwa ni Serikali kivuli basi ingewasilisha bajeti mbadala, mfano kama ameona shilingi trilioni 29.5 ni nyingi sana wao wanapendekeza trilioni ngapi? Tungesikia kutoka kwao, naamini Watanzania wamewaelewa hawa ndugu nadhani tuwaache kama walivyo na hawapo hapa Bungeni kwa sababu wamedharau. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kimkakati bajeti yetu ni nzuri sana, na vyanzo vya mapato vya bajeti hivi vinakusanyika vizuri. Kwa mfano kuondoa kodi ya majengo (property tax) kutoka kwenye Serikali za Mitaa ambazo kwa pamoja zilikuwa na uwezo wa kukusanya kati ya asilimia tano hadi 10 tu ya fedha ya kodi yote ambayo inaweza kukusanywa ni jambo la kupongeza sana. TRA kama watajitahidi, kama ninavyowafahamu mimi, wanao uwezo mkubwa wa kukusanya kati ya asilimia 50 hadi 70 ya potential. Ina maana wanaweza wakakusanya hadi trilioni 1.8 ambayo ukilinganisha na pato la zamani la shilingi bilioni 300 ina maana tutakuwa tumepiga maendeleo makubwa sana kwa hiyo naipongeza sana Serikali kwa uamuzi huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano wa pili, makusanyo ambayo yalikuwa ya retention yalikuwa yanatumika vibaya sana kwa hiyo kwa sasa hivi itakuwa ni fursa ya mapato hayo kutumika vizuri.
Suala lingine zuri tumepunguza mikopo ya nje kwa trilioni 0.03 kulinganisha na mwaka jana kwa ajili ya kupunguza utegemezi, kwa hiyo, hilo ni jambo lingine la kupongeza sana Serikali. Angalizo pekee hapo ni kwamba tumeongeza mikopo ya ndani kwa trilioni 1.34 hatua hii ni nzuri, lakini Wizara ya Fedha itahitaji udhibiti na ufuatiliaji wa karibu sana, kwa sababu riba za mikopo ya ndani zipo juu sana Wizara ya Fedha na Benki Kuu wakizembea kidogo tu tutatumbukia kwenye mizozo isiyo na tija inayoweza kusababisha sintofahamu kupitia matokeo hasi kama mfumuko wa bei. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, maoni ya upinzani dhidi ya bajeti ya Serikali yana ukakasi wa hasira ya kugomea Bunge bila sababu za msingi. Kwa nini tuandikie mate na wino upo? Wanazo Halmashauri kadhaa ambazo wanaziongoza hivi huko kwenye Halmashauri zao wamesamehe ushuru wote na tozo zote? Badala yake wameongeza ushuru na kodi kwa hiyo ina maana kwamba hapa wanakuja kufanya mchezo wa maigizo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana Watanzania waelewe kwamba sisi Wabunge wa CCM tuko hapa kuwawakilisha na tuko makini katika kazi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Serikali kwa kuweka vipaumbele vya kujenga uchumi wa viwanda kwenye bajeti hii mpya. Katika vipaumbele hivyo nashauri Serikali ikamilishe maandalizi muhimu yanayotakiwa kwenye sekta wezeshi ili kuhakikisha kwamba bajeti hiyo itatekelezeka vizuri sana. Kwa mfano kule kwetu kuna barabara ya kutoka Chunya hadi Itigi na barabara ya Ipole hadi Rungwa, barabara hizo mbili ni barabara muhimu sana kwa kwetu kwa uchumi wa viwanda, tunaomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji wa Ziwa Victoria ni mradi mmoja wezeshi ambao ni muhimu sana. Miradi ya umeme vijijini, zahanati, vituo vya afya, shule ni miradi wezeshi ambayo tunaomba sana fedha ambazo zimepangwa kwa mwaka ujao ziweze kutolewa zote zitumike zote kwa ufanisi. Na vilevile pale ambapo kutakuwa na upungufu mwaka 2017/2018 tusisahaulike kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kusimamia utekelezaji wa mpango na bajeti napenda kujua ni shilingi ngapi zimewekwa kwa ajili ya monitoring and evaluation? Kwa sababu haiku wazi kwenye Bajeti hii. Bila monitoring and evaluation tutapata matatizo makubwa. Kwa mfano Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amepangiwa shilingi bilioni 34, kwa mtazamo wangu fedha hizo ni ndogo sana. Tunamtarajia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Ofisi yake iimarishwe zaidi ili afanye kazi vizuri zaidi. Tunahitaji awe na uwezo mkubwa wa kufanya ukaguzi wa kitaalamu au technical audit ambapo haiitaji wahasibu na wakaguzi wa ndani peke yake. Inahitaji wahandisi, wakadiriaji wa majengo, wachumi na wataalamu wengine wengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunahitaji ofisi hii iweze kuimarishwa kwa nguvu kazi na uwezo wa kufanya kazi. Sasa hii pesa iliyowekwa hapa ni ndogo sana, kwa hiyo tunaomba sana ifikiriwe mara mbili ili kusudi bajeti hiyo iongezwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo napenda kusisitiza ni bajeti ya utafiti. Kwenye sekta karibu zote ni bajeti ndogo sana imepangwa. Utafiti duniani kote ni jukumu la Serikali, kwa hiyo inatakiwa bajeti ya utafiti hasa kwenye mazao ya biashara na chakula iongezwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kuchangia ni kwamba, Serikali imekiri hapa kwamba kuna ugumu wa kukusanyaji wa mapato kwenye sekta isiyo rasmi. Sasa Serikali imejua tatizo inatakiwa ikamilishe sasa sehemu muhimu ya namna gani ya kutatua tatizo hili, kwa sababu tunahitaji kukusanya mapato kutoka kwenye sekta isiyo rasmi. Nashauri Serikali iweke kipaumbele cha kuisajili sekta yote isiyo rasmi ili kuijua vizuri na kurahisisha Serikali kukusanya mapato yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nafurahi kusikia kuwa deni letu la Taifa bado ni himilivu, na ili kudhibiti deni letu Wizara ya Fedha inatakiwa kuwa macho sana na madalali wa mikopo ya miradi mikubwa ambao hujiita transaction agents, ambao hujifanya wanasaidia nchi kupata mikopo mikubwa kutoka kwenye Serikali rafiki za nchi nyingine. Kama watu hao wasipodhibitiwa hatimaye tutakuwa na mikopo yenye gharama kubwa sana maana nao huwa wanatoza tozo.
Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yetu mikubwa kama ya reli, bwawa la Kidunda, bomba la mafuta, itaathirika kwa kuiingiza nchi kwenye gharama kubwa zaidi kama hatutawadhibiti hao transaction agents. Naomba sana Serikali iwe makini.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nina wasiwasi na bajeti ndogo sana kwenye sekta ya ardhi kukidhi kazi muhimu za kupima viwanja nchi nzima, lakini hasa hasa lile swala ambalo Mheshimiwa Waziri Mkuu alikubali hapa, kwamba inatakiwa iteuliwe Kamati ya Kitaifa ambayo itaunganisha Wizara zaidi ya nne kwa ajili ya kufanya kazi ya kubaini maeneo yote ambayo yanahitaji kuongezwa ili kusudi wakulima na wafugaji wapate maeneo mengi zaidi ya kufanya shughuli zao. Hii bajeti iliyoko kwenye sekta ya ardhi ambayo ndiyo ingegharamia kazi hiyo hakuna.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sana Serikali ifikirie mara mbili, kazi hiyo ni ya muhimu sana kwa maendeleo ya taifa. Na kwa ajili ya kuliweka taifa letu katika amani na utulivu ni muhimu sana mapori ya akiba ambayo yamekosa sifa mpaka sasa hivi yako mengi sana hapa nchini hii timu inatakiwa iende ikafanye ukaguzi na kuleta mapendekezo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ambalo ningependa kulitolea maoni yangu, ni kukata kodi gratuity ya Wabunge. Sidhani kama kulikuwa na ulazima wa kuleta suala hilo mwaka huu, lakini vilevile si dhani kama kuna ulazima wa kukata hiyo gratuity. Najua, inaletwa ili kusudi makato yaanze kufanyika kuanzia mwezi wa saba unaokuja.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Ofisi ya Mbunge ni Taasisi inayojitegemea, na ina majukumu mengi sana kwenye jamii, na wananchi wanaitegemea, na fedha hizi nyingi huwa hazitumiwi na Mbunge binafsi, fedha nyingi huwa zinakwenda kwenye jamii, Mbunge huwa anachangia miradi mbalimbali. Kwa hiyo, mimi naomba sana...
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kakunda muda wako umekwisha.
Naomba kuunga mkono hoja, ahsante sana.
Azimio la Bunge Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja kwamba Bunge lako Tukufu liridhie mkataba wa Kimataifa wa kudhibiti matumizi ya dawa na mbinu za kuongeza nguvu michezoni.
Mheshimiwa Naibu Spika, tumechelewa sana kama nchi na kwa kweli nchi yetu ya Tanzania kulinganisha na nchi ambazo zimetajwa kwenye hiyo orodha ya nchi saba ni kama aibu. Naomba sana leo hii turidhie na tuingie kwenye zile nchi ambazo zipo makini kwenye hili suala. Wanamichezo wengi wa Tanzania inawezekana wameathirika kutokana na matumizi ya hizi dawa. Ingawa mkataba huu una udhaifu wa kutokutoa viwango sawa vya udhibiti wa dawa kiasi ambacho kuna baadhi ya nchi wanaruhusu matumizi ya bangi, wanaona ni sawasawa tu, lakini kwa kweli tukiingia sisi inabidi tuwe na orodha ndefu zaidi kuliko ile orodha ambayo ipo kwenye huu mkataba ili kusudi Watanzania wote wanaoshiriki michezo na Watanzania ambao wako mitaani waweze kuishi wakiwa na afya njema; tuwalinde wote siyo tuwalinde wana michezo peke yao, Kwa sababu hata waliopo mitaani kesho wanaweza wakawa wanamichezo tukiwahamasisha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko faida nyingi ambazo tutazipata kutokana na kutekeleza huu mkataba. Kwanza tutapata elimu; elimu ambayo kwa wana michezo na makocha wa michezo kuhusu makosa ya kutumia dawa hizo na madhara yake itasaidia sana kuweza kuokoa kundi na hasa la vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tutapunguza, tutazuia usafirishaji wa biashara ya vifaa na dawa ambazo zimezuiliwa, pia tutadhibiti matumizi kwa kuboresha njia mbalimbali za uchunguzi na vipimo kwenye maabara na inawezekana na sisi tukapata maabara yenye ithibati ya Kimataifa ya kuchunguza na kupima matumizi kama hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Kamati ambayo Mheshimiwa Hafidh ameipendekeza iwe inatoa adhabu kali sana kwa watakaogundulika kutumia hizo dawa, kwa sababu bila adhabu kali matumizi ya dawa hizo yataendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivyo, ni wajibu wa Serikali na wadau kufadhili na kusimamia mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ambao utahakikisha utekelezaji sahihi wa kanuni zilizopo kwenye mkataba huo ili kuhakikisha kwamba matumizi ya dawa zote zilizoainishwa na ambazo sisi kama Taifa tutaziongeza yanadhibitiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Azimio hili la Bunge linaweza kusaidia nchi yetu kupata mafanikio kimichezo na kuondokana na sifa ya kuwa kichwa cha mwendawazimu, kwa sababu baadhi ya dawa kama bangi na mirungi na hata dawa za kusisimua misuli kwa wale ambao wanapenda sana kucheza michezo ile mingine ya usiku, nadhani zinaweza kusababisha afya kuathirika na nguvu zao kimichezo kupungua na viwango vyao vya michezo kupungua. Kwa hiyo, inabidi tuchukue hatua kali. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa nimalizie mchango wangu kwa kusema kwamba, kama nchi hizi hatua kali ambazo tutazichukua lazima ziandikwe kwenye sheria, kama hazijaandikwa kwenye sheria zikabaki tu kwenye kanuni ndogo ndogo sijui za Vyama vya Michezo tutakosa nguvu ya kuweza kutekeleza. Kwa hiyo, inatakiwa ziingie kwenye sheria zetu kama nchi, Mheshimiwa Waziri wa Sheria ashiriki kuhakikisha kwamba sheria inatungwa ambayo itatoa udhibiti na makosa ya matumizi ya hizo dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwa nini nasema hivyo? Wapo wachezaji wengi sana wamecheza mpira kwa muda mfupi na wakaathirika; wamecheza mpira mwaka mmoja mtu anakuwa nyoronyoro kabisa. Nasikia pale Kariakoo kuna matatizo makubwa sana ndiyo maana wachezaji wengi wa Yanga huwa wanacheza kwa muda mfupi mpira, sasa hiyo inatakiwa ifuataliwe, siyo wote ni baadhi yao na hata wachezaji wa Simba!
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta mchezaji mzuri anatoka mkoani akifika pale mjini mwaka mmoja, miwili tayari amepoteza kiwango chake, angalau wale ambao huwa wanatoka katika nchi za nje kidogo wanajua mantiki ya hizo dawa; huwa wanacheza kwa muda mrefu sana, kwa mfano yule Mkongo, anaitwa nani yule, yule wa Yanga ana umri wa miaka karibu 40 lakini anacheza mpira mpaka sasa hivi. Mwenzangu ameonesha wasiwasi kwamba huenda inawezekana labda anatumia lakini naamini yule hatumii ndiyo maana amecheza mpira kwa muda mrefu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mifano ya wachezaji kama Joseph Kaniki ambaye alikamatwa na dawa za kulevya kule Ethiopia na wachezaji ngumi ambao walisafirishwa na marehemu Shaban Mwintanga ambao walikamatwa kule Mauritius ni mifano ya aibu ambayo hatutegemei tuendelee kuipata katika nchi yetu ili kusudi hata sisi tujenge jina kwenye nchi nyingine kwamba sisi ni nchi ambayo ipo makini. Ni lazima uchunguzi wa kina uwe unafanywa kwa mfano kama timu inasafiri kwenda nje ya nchi, kabla hawajatoka nje ya nchi uchunguzi ufanywe wa kina kwamba hawana dawa na wanaporudi vile vile uchunguzi ufanyike wa kina kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii. Ahsante sana.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa Fedha 2017/2018
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Dkt. Mpango kwa uwasilishaji wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo. Nampongeza kwa kutuletea vipaumbele vilevile kama vilivyokuwa mwaka 2016/2017 kujenga msingi wa uchumi wa viwanda, kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara na usimamizi wa utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni commitment ya kuendelea kutekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo ya nchi na hii inaonesha kielelezo cha uendelevu wa mIpango yetu, kielelezo cha sera zinazotabirika na kielelezo cha mipango imara. Kwa hiyo, namshukuru sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimefurahi alipoonyesha katika kitabu hiki cha mapendekezo mkakati wa ufuatiliaji na tathmini chini ya uratibu wa Tume ya Mipango ambao umewekwa vizuri sana. Napongeza lakini natoa rai kwamba yale mazuri ambayo yalikuwa yanatekelezwa na ule Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, yaingizwe katika huu Mpango wa Ufuatiliaji na Tathmini ili kuboresha zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti nimeshituka kidogo niliposoma tathmini ndogo iliyoko kwenye kitabu cha mapendekezo hasa kuhusu hali ya viwanda ya sasa (status). Tuna viwanda vikubwa 1,322, tuna viwanda vidogo 47,921, takwimu ni nzuri. Hata hivyo tatizo nimeliona kwenye viwanda vikubwa vya uzalishaji yaani manufacturing industries viko 998; lakini kati ya hivyo 998 asilimia 53 ya viwanda hivyo viko katika mikoa mitatu tu ya Dar es Salaam, Arusha na Kagera. Sasa hii mimi nimeona kwamba kwa kweli uwiano wa uwekezaji katika viwanda vya uzalishaji nchini hauko vizuri. Naomba huko tuendako ili kusudi hii status iweze kubadilika, huko tuendako tuzingatie uwiano wa maendeleo ya nchi yetu kwa kuzingatia kwamba viwanda vya uzalishaji vinahitajika hata katika mikoa ambayo sasa hivi haina hivyo viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, labda nije sasa kwenye miradi ya kipaumbele. Nimeisoma, ni mizuri na ninatoa maoni kidogo katika miradi ya kipaumbele kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, reli ya kati kwa kiwango cha Kimataifa au standard gauge ni mradi muhimu sana. Juhudi ambazo zimeshaanza za kutafuta fedha kwa ajili ya mradi huu naomba zisilegezwe; zifuatiliwe kwa ukamilifu wake ili kusudi hii reli ijengwe kama ambavyo inaonekana katika mapendekezo. Umuhimu wake unaonekana kutokana na matokeo ya kiuchumi yatakayopatikana. Kwanza, ujenzi wa reli ya kati utashusha gharama za usafiri na usafirishaji ambazo ndizo kiini kikubwa cha kupanda gharama za maisha. Mfano, gharama za kusafirisha mbolea, gharama za kusafirisha mafuta ya petrol na diesel zitapungua kwa kiasi kikubwa na hivyo kupunguza bei ya petrol, bei ya diesel na bei ya pembejeo na hiyo itasababisha maisha yawe nafuu kwa wananchi. Kwa hiyo, mradi huo ni muhimu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bado tunahitaji barabara za lami, viwanja vya ndege, tunahitaji kuboresha barabara za changarawe na hili niliwekee msisitizo kwenya maeneo yangu ya Jimbo. Barabara ya Tabora – Ipole – Mpanda ambayo sasa hivi inajengwa, mkazo uwekwe, barabara ile ikamilike kwa ajili ya kunganisha Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Katavi. Barabara ya Ipole - Rungwa inaunganisha Mkoa wa Tabora na Mkoa wa Mbeya. Naomba katika kipindi hiki cha mwaka 2017/2018 ianze kujengwa; na barabara ya kutoka Chunya – Itigi – Mkiwa, kipindi cha mwaka 2017/2018 barabara hii nayo ikamilike kwa sababu hapo kuna uchumi mkubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria ni muhimu sana. Imetajwa miradi ya maji kwa ujumla jumla, sasa mimi nakwenda kwenye specific ili Mawaziri husika wa sekta husika wazingatie wakati watakapokuwa wanaweka maoteo ya bajeti rasmi kwa ajili ya kuingia kwenye rasimu ya mpango wenyewe, naomba sana mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria ufike Sikonge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, status ya sasa hivi wametangaza kandarasi tatu. Kuna lot inatoka Solwa mpaka Nzega; kuna lot inatoka Nzega mpaka Igunga; na kuna lot inatoka Nzega mpaka Tabora Mjini. Ile lot ya kutoka Tabora Mjini mpaka Sikonge haijatangazwa. Naomba wakati wa bajeti utakapofika, Waziri wa Maji asimamie hilo ili lot ya kutoka Tabora Mjini mpaka Sikonge ionekane kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018; vinginevyo kwa kweli tutakuwa hatuwatendei haki wananchi wa Sikonge. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona mapendekezo ya jumla kuhusu afya; lakini nilitegemea kuona mkakati wa kujenga zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata, unakuwa wazi katika huu mpango. Nimesoma maelezo, yako jumla jumla sana, naomba tuwe specific; zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata ni sera ya Serikali na ni sera ya nchi yetu. Kwa hiyo, naomba sana iwe specific.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni kuhusu mpango kwenye sekta ya kilimo. Sisi Sikonge hatuwezi kuzungumzia kilimo bila kuzungumzia tumbaku. Status ya sasa hivi kwa mwaka 2016/2017; hawa ndugu zetu makampuni yanayonunua tumbaku, yameshusha makisio kwa zaidi ya asilimia 50, maana yake nini? Maana yake ni kwamba kijiji ambacho kilikuwa na wakulima 300 wa Tumbaku mwaka huu hawataweza kulima wote 300, watalima labda wakulima 100. Ina maana wengine hata wakilima hawana pa kuuza.
Naomba sana Serikali kwanza kwa mwaka huu iwe macho kuhusu haya makampuni ili yafanyike marekebisho ya makusudi, lakini kwenye mpango wa 2017/2018 matatizo kama yaliyotokea mwaka huu naomba yasijitokeze kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mwongozo wa Uandaaji wa Bajeti ya mwaka 2017/2018, naunga mkono na ninaipongeza Serikali kwa kuendelea na vigezo vya asilimia 40 kwamba itumike kwa ajili ya miradi ya maendeleo na asilimia 60 kwa ajili ya matumizi ya kawaida. Kwa kweli huo ndiyo msingi ambao utaendeleza pale ambapo tumeanza mwaka 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono vigezo hivyo vikuu vya ugawaji wa rasilimali kwa sababu nchi yetu itaendelea kuweka uzito unaostahili kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vigezo vikuu vya OC, napendekeza viwe ni pamoja na idadi ya miradi ya maendeleo inayosimamiwa na taasisi husika ili miradi hiyo utekelezaji wake usimamiwe vizuri na ulingane na thamani ya fedha itakayotumika. Kama idadi ya miradi ya maendeleo haitakuwa miongoni vya vigezo vya kugawa OC, basi tutakuwa tunatekeleza miradi ambayo haisimamiwi vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile upo umuhimu wa kupitia upya vigezo vya kisekta ili kulingana na wakati uliopo ziandaliwe; maana yake hivi vigezo ambavyo viko kwenye hivi vitabu viliandaliwa kipindi kirefu sana, mwaka 2005/2006.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana vigezo hivyo vifanyiwe mapitio ili vilingane na wakati wa sasa. Mfano, ruzuku katika sekta ya maji kwa sasa inahitaji kigezo cha idadi ya watu tu wanaokaa vijijini, lakini kwa sasa hivi kuna wakazi wengi katika Miji Mikuu ya Wilaya na Miji Midogo ambayo ndiyo imejitokeza hivi karibuni. Mimi naomba vigezo hivi vifanyiwe mapitio ili kusudi vilingane na mahitaji ya wakati wa sasa maana yake ni vya muda mrafu sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yangu yalikuwa ni machache tu, ni hayo, nawapongeza sana Serikali, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Mkataba wa Ubia wa Uchumi baina ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye mada ya leo. Nilipokuwa ninausoma mkataba hisia zikanipeleka kwenye historia. Miaka takribani mia moja iliyopita na zaidi walikuja wazungu na mikataba, lakini kabla ya kuja wazungu na mikataba wazungu walisitisha biashara ya utumwa na katika tangazo la kusitisha biashara ya utumwa ukisoma verses zilizokuwemo mle ni pamoja na kusema kwamba hii nguvu kazi ambayo tulikuwa tunaichukua tunaisafirisha ibaki kulekule ili izalishe kwa ajili ya viwanda vyetu. Baada ya hapo walifungua mashamba makubwa, mashamba yale yalikuwa ni kwa ajili ya kuzalisha malighafi zilizokuwa zinahitajika kwenye viwanda na wakati ule ndiyo ilikuwa mapinduzi ya viwanda yanafanyika Ulaya. Kwa hiyo, dalili zote za mfanano wa mikataba ya wakati ule imo kwenye huu mkataba, kwa hiyo mkataba huu una harufu ya ukoloni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yamezungumzwa mengi na wenzangu na mimi nirejee kwamba hakuna mkataba mbovu ambao nimewahi kuushuhudia kama huu kuanzia mwanzo tu. Pale kwenye kurasa za mwanzo kabisa ukisoma jinsi nchi zetu zilivyoorodheshwa, zimeorodheshwa kama block moja kwa moja, lakini walivyokuja kuorodhesha nchi zao wakaorodhesha moja moja halafu baadaye wakasema and the EU, hii aliisema mwanzoni kabisa Mheshimiwa Lugola. Mimi kuanzia hapo tu nilipata wasiwasi na nikapata wasiwasi zaidi hata wataalam wetu ambao walikuwa wanakwenda ku-negotiate tangu miaka ile ya 2007 mpaka juzi, nilipata wasiwasi kama kweli walikuwa wanajiandaa vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, viwango vilivyomo humu vya terms kwa asilimia zaidi ya 80 ni vya ukandamizaji, kutukandamiza sisi na mengine yamo humu yanalazimisha kwamba tukisaini mkataba huu ndiyo tutapata hata masuala ya development cooperation. Sasa suala hili limenisumbua sana kama ambavyo limewasumbua Wabunge wengine, ninaomba niunge mkono wale wote ambao wametoa wito, Serikali isikubali kusaini mkataba huu mpaka pale marekebisho makubwa yatakapokuwa yamefanyika ikiwemo kuruhusu nchi mojamoja kujitoa wakati wowote inapoona kuna hatari. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ningezungumza mengi lakini mengi yameshazungumwa itakuwa ni kurudia, ninaomba niishie hapo, wote tuunge mkono kukataa kukataa mkataba huu. Ahsante sana.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwenye Kamati
ya Miundombinu naunga mkono hoja, taarifa yao ilikuwa nzuri sana. Nakubaliana nao hoja
kwamba kuzorota kwa huduma za reli kumesababisha utegemezi kwenye barabara kwa
usafirishaji wa abiria na mizigo. Na hiyo ina matokeo mabaya sana kwa upande wa uchumi
wetu, kwa sababu barabara zetu zinaharibika kwa haraka, tunaongeza gharama za ukarabati,
uhimilivu wa barabara unapungua kutoka miaka 20 hadi miaka mitano na gharama za usafiri
na usafirishaji kwa ujumla zinaadhiri uchumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano lita moja ya petroli au dizeli kwa wastani inauzwa
kama shilingi 2,000; lakini kama mafuta yale yangekuwa yanasafirishwa kwa njia ya reli isingefika
bei hiyo ingekuwa labda shilingi 1000, shilingi 800 au shilingi 1200; na hiyo ingekuwa na matokeo
mazuri kwa uchumi. Kwa hiyo naomba kutoa wito Serikali isilale, ifanye mbinu zozote zile hata
kama gharama ni kubwa ijengwe reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa. Hiyo itakuwa ni
ukombozi mkubwa sana kwa Taifa letu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, wakati mbinu hizo za kujenga reli zinafanyika, wasiache
kuendelea kujenga barabara za lami na barabara za changarawe hasa vijijini ili kusudi
kuwezesha gharama zetu za usafiri na usafirishaji kupungua. Kwetu kule Sikonge kuna barabara
muhimu ambazo nataka nizitaje hapa, barabara ya changarawe ya Tutuo - Izimbili - Usoke,
barabara ya changarawe ya Sikonge - Mibono - Kipili naomba ziangaliwe kwa macho mawili.
Barabara hizi tunadhani huwa kuna mchezo unafanyika. Kwa mfano barabara ya Sikonge -
Mibono - Kipili kila mwaka hupangiwa fedha kwamba itatengenezwa kutoka Sikonge mpaka
Kipili, lakini wakifika Mibono wanaacha, kila mwaka. Naomba mwaka huu imepangiwa milioni
862 ifike Kipili.
Naomba Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi aifikirie sana hiyo Wizara, na akubaliane na mimi
kwamba barabara ile itobolewe mwaka huu ifike Kipili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ambalo napenda kulizungumzia, suala la kusema
Bandari ya Tanga na Mtwara zinajiendesha kwa hasara huo ni uongo uliopitiliza. Serikali ifanye
uchunguzi kubaini sababu kwa nini bandari hizi zijiendeshe kwa hasara wakati potential ni
kubwa? Kwa mfano wafanyabiashara wa pale Tanga Mjini kwa nini wapitishie mizigo
Mombasa? Ina maana kuna matatizo hapo kwenye bandari ya Tanga. Kwa hiyo, naomba sana
uchunguzi ufanyike ili watakaobainika hatua zichukuliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la nne suala la mawasiliano. Zinatumika fedha nyingi za mfuko
wa mawasiliano vijijini, lakini kunakuwa na wababaishaji upande wa mitambo ambayo
inawekwa. Inakuwa wananchi hawapati coverage ambayo tunaitaka kwenye mawasiliano,
mtambo unawekwa lakini coverage inakuwa ndogo sana. Sasa mimi naomba Wizara
inayohusika; kule kwetu kuna kata za Kipili, Kirumbi, Kilori, Kitunda, Ngoywa, Ipole, Kiloleli, Igigwa,
Nyahuwa na Mole, hakuna mawasiliano ya uhakika licha ya kwamba kuna minara. Mimi
naomba sana Wizara inayohusika ifuatilie matumizi ya fedha za mfuko wa mawasiliano vijijini, je,
zilitumika kihalali au kulikuwa na ubabaishaji, ili kusudi hatua zichukuliwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kabisa kwenye umeme…
NAIBU SPIKA: Muda umekwisha Mheshimiwa.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Naibu Spika ahsante naunga mkono hoja.
Muswada wa Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo, wa Mwaka 2016
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami pia, nitoe pongezi nyingi sana kwa Serikali, hasa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Tizeba, kwa kuleta Muswada huu katika kipindi hiki muhimu kabisa. Sheria ya Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya mwaka 2016 pamoja na ile ya Uvuvi ni Miswada muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nilikuwa nasema mara nyingi kwamba kazi za msingi za Serikali duniani kote kwenye Sekta ya Kilimo ni tatu kubwa; na katika kazi hizo tatu, ya kwanza kabisa ni utafiti; halafu ya pili ni kuwasaidia wakulima wapate mikopo, pembejeo, vifaa vya kilimo cha kisasa na ya tatu kuwalinda wakulima wapate jasho lao halali; wasinyonywe na wafanyabiashara wenye mbinu chafu ambao lengo lao ni kupata faida peke yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kazi hii ya msingi ambayo ni ya utafiti, naomba Serikali kama ambavyo imeleta Muswada huu, itoe kipaumbele cha kutosha kwa taasisi hii ya utafiti ili kusudi sheria hii ijitosheleze na taasisi ya utafiti itakapoanza kazi zake, ifanye kazi zake kwa ufanisi unaotegemewa. Kwanza, tafiti zifanyike; pili, taarifa za utafiti zitumike kwa ajili ya maendeleo; mafunzo kuhusu matumizi ya taarifa za utafiti yasiwe kwa wataalam peke yao, bali yafikishwe mpaka kwa wadau wakiwemo wakulima; masuala ya teknolojia yawekewe umuhimu wa kipekee na yasimamiwe vizuri ili teknolojia itumike kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii na teknolojia ni sehemu ya utafiti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wananchi wetu watabaki kutumia teknolojia zile zile za miaka yote; za tangu mwaka 1947 hatutafika popote. Vile vile bila utafiti kuhusisha masoko, mafanikio ya kilimo yatakuwa kidogo sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sina sababu ya kuchukua muda wako mrefu sana kujadili kitu ambacho ni kizuri sana. Nimepitia sheria yote, miundo ya usimamizi iko vizuri na mambo mengi sana yamewekwa vizuri na Kamati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naipongeza vile vile Kamati kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kushauri. Pia naipongeza Serikali kwa mambo mengi ambayo Kamati imeshauri wameyaweka kwenye schedule of amendment. Kwa hiyo, kwa kweli, nawapongeza sana kwa hatua hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipengele kimoja ambacho ningependa kukitilia umuhimu wa kipekee ni source of financing. Vyanzo vya fedha vya taasisi hii ni kama vimefichwa. Naomba Serikali iweke wazi; kama nilivyosema, jukumu la kwanza kabisa la Serikali la msingi kwenye Sekta ya Kilimo ni Utafiti; ni lazima kuwe na Mfuko utakaosaidia tafiti za kilimo na Serikali itoe mchango mkubwa wa kibajeti kwenye Mfuko huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwa na taasisi huru kusiifanye taasisi hiyo iachwe kama yatima, iwe ndiyo kisingizio cha kutoipangia bajeti inayotosha kwa sababu wataachiwa wadau, wakiwemo wakulima kwamba sasa mazao yao yakatwe makato ili kusudi kuipa fedha Taasisi ya Utafiti. Naomba hili liwe wazi kabisa, Serikali ikubali kuweka Mfuko Maalum wa Utafiti na yenyewe ichangie zaidi ya asilimia 90 ya bajeti kwa ajili ya Mfuko huo na wadau wengine wataongeza pale ambapo patabaki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusu uwakilishi wa wakulima kwenye vyombo vya usimamizi, umetajwa vizuri, napongeza sana; lakini kama sifa za wale wakulima watakaowakilishwa hazitaainishwa vizuri kwenye sheria, basi unaweza ukawa na mwakilishi ambaye mchango wake ni hafifu. Kwanza, mwakilishi lazima ajue maana ya utafiti na awe na uzoefu nao ili kusudi mchango wake uwe mzuri kwenye vikao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ambalo napenda nizungumzie hapa ni uhusiano wa taasisi hii tunayoanzisha na taasisi nyingine zinazosimamia utafiti hapa nchini. Kamati ilizungumza sana kuhusu uhusiano na COSTECH, nami naongezea hapa, uhusiano kati ya taasisi hii tunayoanzisha na NIMR. Najua NIMR inasimamia tafiti za afya, lakini kuna baadhi ya mambo yanayohusu tafiti za afya yanahusu kilimo. Kwa mfano, kuenea kwa malaria inawezekana ikawa na uhusiano wa karibu sana na maendeleo ya kilimo, kwa sababu, malaria wale wakulima wanakolima ni kwenye maji na kwenye maji ndipo kunapozalishwa mbu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upo uwezekano tafiti zikagongana kati ya tafiti za afya na tafiti za kilimo. Kwa hiyo, uhusiano ni muhimu sana uwekwe vizuri kwenye hii sheria kwamba watahusianaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile COSTECH, ukisoma vizuri Sheria ya COSTECH, inaonesha kwamba, COSTECH ndiyo msimamizi mkuu wa tafiti zote, ukiacha zile za afya ambazo zinasimamiwa na NIMR. Kwa hiyo, mtafiti yeyote kwa mfano anayetoka nje akija Tanzania hapa kama anafanya utafiti; ukiwemo utafiti wa kilimo, lazima ajisajili COSTECH na afanye mtihani wa COSTECH, afaulu, ndiyo aruhusiwe kwenda kufanya utafiti wake. Kwa hiyo, ni muhimu sana uhusiano ukaelezwa vizuri kwenye sheria ili kusudi hapo baadaye kusiwe na mgongano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina uzoefu wa kutosha katika hili kwa sababu nilifanya kazi Umoja wa Mataifa, UNDP na niliona kwamba COSTECH ndiyo msimamizi mkuu wa tafiti zote, ukiacha zile za afya ambazo zinasimamiwa na NIMR. Kwa hiyo, uhusiano wa taasisi hizi ambazo tunazianzisha, hii ya kilimo na ile ya uvuvi na COSTECH pamoja na NIMR ni muhimu sana ukaoneshwa vizuri kwenye sheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu pili, la mwisho ni uhusiano wa taasisi hizi za Sekta ya Kilimo na Sekta nyingine wezeshi za kilimo. Mfano, huwezi kuendesha utafiti unaohusu kilimo cha umwagiliaji bila kuhusisha Sekta ya Maji. Sekta ya Maji ndiyo inabeba dhamana ya rasilimali za maji. Kwa hiyo, ni muhimu sana uhusiano ukawa vizuri kwenye sheria ili kusudi kusiwe na migongano na sekta nyingine wezeshi. Ushirikiano uwekwe vizuri na hasa kuwahusisha kwenye Kamati ndogo ndogo zitakazoundwa na kwenye Bodi na kwenye vyombo vingine vya usimamizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mambo mengine, sheria imekaa vizuri. Natoa pongezi na naunga mkono Bunge hili lipitishe sheria ili zianze kutumika haraka iwezekanavyo. Ahsante sana.