Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Questions to the Prime Minister from Hon. Joseph George Kakunda (2 total)

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kuniona. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu; katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na migogoro mingi sana baina ya wafugaji na wakulima kwa upande mmoja, kugombea maeneo; lakini pia baina ya wakulima, wafugaji na maliasili, kwa upande mwingine. Hii ni katika maeneo mengi ya nchi. Sasa kwa kuwa katika Ilani ya Uchaguzi yako maelekezo kwamba Serikali itapima maeneo mapya kwa ajili ya wakulima na wafugaji hususan kuongeza eneo la wafugaji kutoka hekta milioni moja hadi milioni tano:-
Swali, je, ni lini Serikali itateua Kamati ya Kitaifa ambayo itapitia maeneo yote na kutoa mapendekezo yatakayotekelezwa ili kuondoa migogoro hii na watu waendelee kuishi kwa amani? Hii kazi inahitaji msaada zaidi. Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kakunda Mbunge wa Sikonge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri kwamba sasa hivi tunayo migogoro mingi sana ya wafugaji na wakulima, lakini pia hata migogoro ya ardhi yenyewe tu baina ya jamii zetu; mtu mmoja mmoja lakini pia na jamii na jamii. Migogoro hii tumefika wakati sasa tunatakiwa kuitafutia ufumbuzi. Jambo ambalo amelieleza Mheshimiwa Mbunge ni miongoni mwa mikakati ambayo sisi tunayo pia.
Mheshimiwa Spika, moja, tumeanza kutafuta njia sahihi ya kuondoa migogoro ya ardhi na hii inatokana na kuongezeka kwa matumizi na mahitaji ya ardhi na thamani ya ardhi. Pili, kumetokana na matatizo makubwa yaliyojitokeza kwenye maeneo yale ya mipaka kutokana na mahitaji ya kupanua eneo; kuongezeka kwa mifugo mingi; lakini wakati mwingine ni utendaji wa hovyo tu wa Watendaji wetu wa Serikali ambao tumewapa dhamana kwenye maeneo yale. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia tunao wawekezaji ambao wanaingia kinyemela kwenye maeneo yetu na wanapoingia kule wanajichukulia ardhi na kuongeza maeneo bila ridhaa ya wananchi wenyewe na kusababisha migogoro mingi. Kwa hiyo, jukumu la Serikali ambalo pia Mheshimiwa Mbunge amesema, ni kweli tuliamua tuunde task force inayounganisha Wizara tatu; Wizara ya Ardhi yenyewe, Wizara ya Maliasili, pamoja na Wizara ya Kilimo ili tuweze kubaini mipaka yote, tuweze kubainisha maeneo haya ili kila mmoja ajue anakaa wapi na vinginevyo, kwa kupima maeneo haya na kuweka mipango bora ya matumizi ya ardhi yanayobainisha maeneo ya wafugaji, wakulima, viwanda na maeneo ya makazi ya kawaida. Kwa hiyo, task force hii kwanza tumezipa Wizara zenyewe majukumu.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Maliasili ituambie kwenye maeneo yale na ukomo wake, wanaishia wapi. Wizara ya Kilimo nayo watuoneshe wananchi wanaishia wapi na kilimo wapi baadaye sasa tumwite Waziri wa Ardhi wakae pamoja, tuweze kuweka mipaka mipya. Hii ikiwemo na kuongeza maeneo ya wafugaji kama ambavyo sasa tumeamua wafugaji wote sasa kuwatengea maeneo, kutumia ranch zetu za Taifa na mkakati huu ni ule wa kuboresha mifugo yetu.
Mheshimiwa Spika, wananchi wanaofuga kawaida, watakuwa wanapeleka mifugo yao kwenye maeneo ambayo tumewatengea kama ranch ambayo mimi mwenyewe nimetembea; nimekwenda Mkoa wa Kagera kuona kule Misenyi, Karagwe lakini pia nimekwenda na Ngara. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ufumbuzi wetu ni kuwapeleka wafugaji kwenye maeneo yale, tunataka tuwamilikishe kwenye zile blocks. Wafugaji wote wenye mifugo mingi wakae kwenye maeneo yale ili sasa waweze kulisha, kuogesha, wanenepeshe, waweze kuuza maeneo ya nje. Huku vijijini kutakuwa na ngā€˜ombe hawa wachache ambao watakuwa wanaenda ranch kwa kuwapa maeneo hayo ya wafugaji, baada ya kuwa tumeweka mpango bora wa matumizi.
Kwa hiyo, Tume ile itakapoundwa, tutaileta maeneo hasa yenye migogoro. Simiyu nimekwenda nimeona migogoro mingi, kwa hiyo, maeneo kama hayo yatapata kipaumbele katika kuanza na zoezi hili.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba hatimaye imehuishwa Sera ya Elimu ambayo ilizinduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2014 lakini mpaka inahuishwa tena haikuwahi kutekelezwa kwa sababu ilikosa nguvu ya sheria. Sasa kwa mahuisho haya yaliyofanyika sasa hivi, je, Serikali imejipanga lini kuleta Sheria ya Elimu mpya Bungeni ili kuyapa nguvu haya mahuisho ambayo yamefanyika?
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kakunda, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli hata Sera ya mwanzo tulipokuwa tunatekeleza tulikuwa na Sheria inasaidia, inaongoza utekelezaji wake, lakini kutokana na mabadiliko haya tumegusa maeneo yanayohitaji mabadiliko ya kisheria pia ili Sera hii iweze kutekelezeka; na kwa kuwa tunaelekea kwenda kuizindua na Wizara ya Elimu inaendelea na mchakato wa kusimamia maboresho ya Sera hii mpaka kuzinduliwa na utekelezaji wake, tutaendelea kubaini maeneo muhimu ya kubadilisha Sheria ili tuweze kutunga Kanuni ili ziweze kuwezesha urahisi wa utekelezaji wa Sera hii. Kwa hiyo Wizara ya Elimu imejipanga, inaendelea na mchakato na nimetoa wito hapa na nimeeleza kwamba, bado tunaendelea kutoa elimu kwa njia mbalimbali, kushirikisha wadau wote. Kwa hiyo hii hatua tunayoendelea nayo ya kila hatua itakuwa inabaini kadiri ya mahitaji ya mabadiliko ya sheria na kutengenezea kanuni za usimamizi wa utekelezaji wa sera hiyo, ahsante sana. (Makofi)