Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to Primary Questions by Hon. Joseph George Kakunda (36 total)

MHE. BONIPHACE M. GETERE (K.n.y. MHE. AMINA N. MAKILAGI) Aliuliza:-
Wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma katika Kata za Etaro, Ifulifu, Nyegina na Nyakatende wanakabiliwa na taizo la maji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia wananchi wa kata hizo maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Amina Makilagi naomba kwanza nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais kwa imani kubwa aliyoionyesha kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais , TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Nassor Makilagi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wananchi katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma katika Kata za Itaro, Ifulifu, Nyegina na Nyakatende wanakabiliwa na tatizo la maji kwa sababu mahitaji halisi ya maji katika kata hizo ni lita 953,550 wakati uzalishaji wa maji katika vyanzo vilivyopo ambavyo ni visima sita katika Vijiji vya Keimba na Kabegi kwenye Kata ya Ifulifu, Kijiji cha Mkikira katika Kata ya Nyegina na Vijiji vya Kigera, Nyegina na Kamguruki katika Kata ya Nyakatende vinazalisha lita 5,100 kwa siku pamoja na mradi wa maji ya bomba katika Kata ya Nyegina unazalisha lita 50,000 kwa siku na hivyo kufanya jumla ya lita zinazozalishwa kwa sasa kuwa 55,100 tu ambazo ni asilimia sita ya mahitaji.
Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kuboresha huduma za maji kwenye eneo hilo, Serikali inakamilisha ujenzi wa mradi mkubwa wa maji utakaohudumia wakazi wa Manispaa ya Musoma pamoja na wakati wa Kata za Nyamkanga, Bukabwa na Busimwa katika halmashauri ya Wilaya ya Butiama na wakazi kwenye Kata za Etaro, Nyegina na Nyakatende katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Hadi sasa Serikali imeshapeleka shilingi milioni 900 kwenye Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma, ambayo inasimamia utekelezaji wa mradi huo.
Mheshimiwa Spika, kazi ambazo zimeshatekelezwa hadi sasa ni kupima njia ya bomba, kuchonga barabara kuelekea Mlima Balima kutakakojengwa tenki lenye ujazo wa lita milioni mbili ambalo litasambaza maji kwa mtiririko kupeleka huduma za maji safi na salama katika kata nilizotaja. Aidha, taratibu za ununuzi wa mabomba yenye urefu wa kilometa 35 zimekamilika.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA aliuliza:-
(i) Je, Serikali ina mkakati gani mahususi katika kuboresha mazingira ya kujifunza katika shule za umma za sekondari nchi nzima ikiwa ni pamoja na ukarabati wa majengo, madarasa, mabweni na maabara?
(ii) Je, kwa nini Serikali isione umuhimu wa kuifuta kazi Bodi na Menejimenti ya Mamlaka ya Elimu Tanzania na kuiunda upya kwa sababu imeshindwa kusimamia ubora wa elimu nchini?
(iii) Je, Serikali ina mpango gani wa kuzifufua shule zilizokuwa za watoto wenye vipaji maalum?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zainab Athuman Katimba, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), refu sana, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali za kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika shule za umma za sekondari nchini. Kupitia Mpango wa Maendeleo ya Elimu ya Sekondari (MMES II) ulianza kutekelezwa mwaka 2004 hadi mwezi Disemba 2016, jumla ya shule za sekondari 792 zimejengwa na kukarabatiwa miundombinu yake na kuwa shule kamili kwa gharama za shilingi bilioni 123.8.
Aidha, katika kipindi hicho jumla ya maabara 6,287 sawa na asilimia 60.52 ya lengo zimekamilika kati ya maabara 10,387 zilizohitajika. Kupitia Mpango wa Lipa kwa Matokeo kwa mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya shilingi bilioni 21.9 zimeidhinishwa kwa ajili ya upanuzi wa shule 85 za sekondari na shule 19 za msingi. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya vyumba vya madarasa 320, mabweni 155 yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 80 kila moja na matundu ya vyoo 829 yatajengwa.
(b) Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Elimu Tanzania huchangia katika kukuza ubora wa elimu nchini kupitia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya elimu kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi chuo kikuu. Changamoto iliyopo ni upatikanaji wa fedha za kutosha kuwezesha kutekeleza miradi mingi zaidi kama inavyotarajiwa na wananchi katika maeneo mengi nchini.
(c) Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuzikarabati shule kongwe 89 zikiwemo shule nane za wanafunzi wenye vipaji maalum kupitia Mamlaka ya Elimu Tanzania na Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R). Mradi huu utakaogharimu jumla ya shilingi bilioni 89 hadi kukamilika unatekelezwa kwa awamu. Hadi kufikia Julai, 2017 jumla ya shule kongwe 43 zimekarabatiwa na shule 20 zitakarabatiwa katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA aliuliza:-
Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Morogoro umekamilika lakini haina umeme wala maji:-
Je, ni lini Serikali itapeleka umeme na maji katika hospitali hiyo ili ianze kutumika na kupunguza msongamano wa wagonjwa katika Hospitali ya Rufaa ya Morogoro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dokta Christine Gabriel Ishengoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 100 kwa ajili ya mifumo ya umeme na maji katika Hospitali mpya ya Wilaya ya Morogoro. Ifikapo tarehe 15 Novemba, 2017, Sh.25,240,969.33 zitakuwa zimelipwa kwa ajili ya kuingiza umeme hospitalini hapo. Hadi sasa TANESCO wameshaweka nguzo na mfumo wa umeme katika jengo la hospitali, kazi iliyobaki ni kufunga transfoma ili umeme uweze kuwashwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa miundombinu ya maji hospitalini hapo utakaogharimu shilingi milioni 50 unaendelea. Kati ya hizo, shilingi milioni 21 zimeshapelekwa kulipia kazi zinazoendelea. Mifumo ya huduma ya maji itakuwa imekamilika ifikapo mwishoni mwa Januari, 2018.
MHE. ANNA R. LUPEMBE aliuliza:-
Kijiji cha Mtisi katika Kata ya Sitalike hakuna eneo la kilimo:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapa wananchi hao maeneo kwa ajili ya kilimo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Richard Lupembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Mtisi kilichopo katika Kata Sitalike, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo kina eneo la ardhi lenye jumla ya hekta 1,066.86. Kati ya hizo, hekta 1,043.86 ni sehemu ya Hifadhi ya Msitu wa Msaginya unaomilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS). Maana yake ni kwamba, jumla ya kaya 589 zenye wakazi 3,416 wa kijiji hicho wamebakia na eneo la hekta 23 tu wanaloruhusiwa kulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mahitaji ya ardhi ya kilimo katika kijiji hicho ni hekta 919.4, Halmashauri ya Wilaya ya Nsimbo, ifikapo mwishoni mwa Novemba, 2017, itakuwa imewapatia ardhi wakazi hao kutoka katika Kijiji cha Stalike (Makao Makuu ya Kata ya Sitalike) chenye ardhi ya ziada hekta 2,950.
MARWA R. CHAHA (K.n.y. MHE. SABREENA H. SUNGURA) aliuliza:-
Akiwa katika Kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 Mheshimiwa Rais aliahidi ujenzi wa barabara ya lami (Kasulu Road) ili kufungua Mji wa Ujiji:-
Je, ni lini Serikali itatoa fedha kwa ajili ya ujenzi huo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Sabreena Hamza Sungura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania aliahidi ujenzi wa kilomita10 za barabara kwa kiwango cha lami ndani ya Manispaa ya Kigoma Ujiji. Kutokana na ahadi hiyo, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji imeamua kujenga barabara ya Ujiji
– Bulenga - Bangwe yenye urefu wa kilomita 7.5 ambapo usanifu umekamilika na itagharimu shilingi bilioni 11.6 ambapo ujenzi unaweza kuanza mwaka wa fedha 2018/2019 na barabara ya Ujiji hadi Daraja la Mngonya yenye urefu wa kilomita 2.5, hivyo kufanya jumla ya kilomita10 ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ili uunganishe na ile barabara ya kutoka Kasulu lazima upembuzi yakinifu na usanifu wa barabara hiyo ufanyike kuunganisha kutoka Daraja la Mungonya hadi barabara Kigoma - Kasulu katika eneo la Msimba lenye urefu wa kilomita tatu. Kipande hicho cha kutoka Daraja la Mngonya hadi Msimba hakijafanyiwa upembuzi yakinifu. Kwa hiyo, Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma inashauriwa kuweka kipaumbele na kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara kutoka Daraja la Mto Mngonya hadi Msimba kwa kiwango cha lami.
RUTH H. MOLLEL aliuliza:-
Maboresho ya utendaji wa Serikali za Mitaa yalilenga kuimarisha na kujenga uwezo wa Serikali za Mitaa kujiendesha kwa kuwapatia rasilimali watu na fedha za kutosha kutekeleza Sera ya Ugatuaji wa Madaraka.
Je, Serikali ina lengo gani kuimarisha Serikali za Mitaa ziweze kujiendesha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ruth Hiyob Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ibara za 145 na 146 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mamlaka za Serikali za Mitaa ni mamlaka shirikishi za kisheria na kidemokrasia zilizoanzishwa kwa kwa lengo la kuwashirikisha wananchi katika shughuli zote za maendeleo, huduma za jamii, utawala bora, utekelezaji wa sheria, ulinzi na usalama kwa kuzingatia kanuni za uwazi na uwajibikaji.
Mheshimiwa Spika, tangu mwaka 1999 Serikali imetekeleza programu mbalimbali za kuboresha utendaji katika ngazi ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Miongoni mwa programu hizo ni Programu ya Maboresho ya Serikali za Mitaa iliyolenga kuimarisha miundo na mifumo ya Mamlaka za Serikali za Mitaa ili zijiendeshe na kuwahudumia wananchi kwa ufanisi. Aidha, Programu ya Maboresho ya Usimamizi wa Fedha imeimarisha na kuinua uwezo wa Halmashauri katika kukusanya mapato na kudhibiti matumizi.
Mheshimiwa Spika, katika kuziimarisha zaidi Mamlaka za Serikali za Mitaa, bajeti ya ruzuku ya maendeleo kwa Halmashauri imeongezeka kutoka shilingi bilioni 49 mwaka 2008 hadi shilingi bilioni 249 mwaka 2017. Aidha, kuanzia mwaka 2015, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeruhusiwa kwa mujibu wa sheria kuajiri watumishi wake wa kada 22 za ngazi za chini ikiwemo Watendaji wa Vijiji baada ya kupata kibali cha kuajiri. Ahsante.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE aliuliza:-
Wilaya za Kakonko, Buhigwe na Uvinza ni Wilaya mpya ambazo hazina Hospitali za Wilaya.
Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali za Wilaya katika Wilaya hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Josephine Johnson Genzabuke, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko imeidhinishiwa jumla ya shilingi milioni 500 kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya. Ujenzi wa hospitali hiyo unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 1.5 hadi kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza imetenga eneo la ekari 80 na imekamilisha michoro ya jengo la Hospitali ya Wilaya. Halmashauri imeshauriwa kuweka kipaumbele na kutenga bajeti katika mwaka wa fedha 2018/2019 ili kuanza ujenzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Buhigwe inaendelea na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya kwa kuanza na jengo la wagonjwa wa nje, utawala na maabara unaogharibu shilingi milioni 450. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 Halmashauri imetengewa shilingi milioni 500 kuendelea na ujenzi. Kazi hii inatekelezwa na SUMA JKT na kazi inaendelea. Ujenzi wa hospitali unafanyika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha na unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 6.4 hadi kukamilika.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y MHE. YOSEPHER F. KOMBA) aliuliza:-
Ni dhamira ya Serikali kutekeleza mpango wa elimu bure kuanzia chekechea hadi kidato cha nne, lakini mpango huu una changamoto ambazo zisipotatuliwa zitasababisha kushuka kwa ubora wa elimu.
(a) Je, ni nini tamko la Serikali juu ya wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza kwa kigezo cha kutofaulu kwa kiwango cha kianzia alama 100 na kuendelea?
(b) Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha ujenzi wa maabara unakamilika kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yosepher Ferdinand Komba, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, tamko la Serikali ni kwamba mwanafunzi anahesabiwa kufaulu mtihani wa Taifa wa darasa la saba endapo atapata alama kuanzia 100 hadi 250 katika masomo yote aliyoyafanya. Hata hivyo, wanafunzi walio na alama chini ya 100 huhesabika kuwa ni miongoni mwa waliokosa sifa za kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, wanafunzi walioshindwa kufikia alama 100 na kuendelea, hushauriwa kujiunga na mfumo usio rasmi wa Elimu Masafa (Open Distance Learning) unaosimamiwa na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, vyuo vya ufundi au shule za sekondari za binafsi. Wanafunzi wanaojiunga na mfumo huo wa elimu hawamo katika utaratibu wa utekelezaji wa mpango wa elimu msingi bila malipo, lakini wanafunzi wanaosoma katika utaratibu huo watakaofaulu mtihani wa Taifa wa kidato cha nne huchaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika shule za Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la (b); ujenzi wa maabara katika Halmashauri zote unaendelea ili kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia masomo ya sayansi. Kati ya maabara 10,387 zinazohitajika nchini, ujenzi wa maabara 6,287 sawa na asilimia 60.5 ya mahitaji umekamilika.
Nazikumbusha Halmashauri zote kukamilisha mapema ujenzi unaoendelea kwa kushirikisha wadau na nguvu za wananchi.
MHE. REHEMA J. MIGILLA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaondoa vikwazo kandamizi kwa walimu wanaotaka kuhama vituo vyao vya kazi kwa hiari yao kutokana na sababu mbalimbali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rehema Juma Migilla, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna vikwazo kandamizi kwa walimu wanaotaka kuhama vituo vyao vya kazi kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kufuata wenza wao au ugonjwa. Hata hivyo, katika kuhamisha mwalimu, Serikali inazingatia ikama ili kutoathiri taaluma kwa kuhakikisha wanafunzi wanaendelea kufundishwa masomo yote kwa mujibu wa mitaala ya elimu iliyoidhinishwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Mheshimiwa Naibu Spika, hitaji hilo ndiyo husababisha katika baadhi ya maeneo walimu kusubiri apatikane mwalimu mbadala kwanza kabla ya kutolewa kibali cha uhamisho ili wanafunzi wasikose haki yao ya kusoma masomo husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba uhamisho wa mtumishi wa umma ni haki yake endapo atazingatia utaratibu uliowekwa. Ndiyo maana kuanzia Julai, 2017 hadi sasa Serikali imetoa vibali vya uhamisho kwa walimu 2,755 nchi nzima. Aidha, taratibu za kutoa vibali vya uhamisho kwa walimu wengine walioomba uhamisho zinaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nachukua nafasi hii kuwaelekeza walimu nchi nzima na watumishi wengine wote kuzingatia utaratibu na waache kutumia viongozi mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge kuwaombea uhamisho. (Kicheko)
MHE. JASSON S. RWEIKIZA aliuliza:-
Maeneo mengi ya Bukoba Vijijini kama vile Kata za Ruhunga, Kibirizi, Izimbya, Mugajwale, Rukoma, Kikomelo na nyingine yana tabu kubwa sana ya upatikanaji wa maji na kilio hiki kimekuwa cha muda mrefu sana:- Je, ni kwa nini Serikali haichukui hatua ya kuwasaidia wananchi hao.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli hali ya upatikanaji wa huduma za maji kwenye maeneo aliyoyataja bado ni changamoto. Hata hivyo, kwa uhalisia hali hiyo ni tofauti na maeneo mengi ya Halmashauri ya Bukoba Vijijini ambako Serikali imekamilisha hivi karibuni miradi 18 ya maji kwenye Kata za Nyakibimbili, miradi mitatu (3); Kyamulaile, miradi mitatu (3); Kemondo, miradi mitatu (3); Buteragunzi, miradi minne (4); Rubole, mradi mmoja (1); Karabagaine, mradi mmoja (1); Rubafu (mradi mmoja (1); na Mikoni, miradi miwili (2) iliyogharimu shilingi 3,552,117,690 inayohudumia wakazi 61,279; hali hiyo imeinua upatikanaji wa maji hadi kufikia asilimia 64 ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wote wa Bukoba Vijijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya upatikanaji wa maji itapanda zaidi hadi kufikia asilimia 75 ifikapo mwezi Juni, 2018 kutokana na kukamilika kwa miradi ya Rukoma, Ubwera, Katoma na Kibirizi inayogharimu Sh.2,235,274,135 na itakayohudumia wakazi 18,449.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa kuna visima 75 vinavyofanya kazi kwenye Kata ya Rukoma, Ruhunga, Butulage, Mgajwale, Izimbya, Katoro, Rubale, Kaibanja, Kishogo, Kasharu, Maruku na Kikomero; na vyanzo vingine 90 vya maji kwenye Kata za Nyakato, Buhendagabo, Katerero na Bujugo. Serikali itatekeleza miradi ya maji kwenye Kata za Ruhunga, Mugajwale, Izimbya na Kikombero ambako kwa sasa wakazi wake wanahudumiwa na visima 23 vyenye uwezo wa kuhudumia watu 7,500 kati ya wakazi 11,794 waliopo katika Kata hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia awamu ya pili ya utekelezaji wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa Mwaka 2018/2019 imetenga shilingi bilioni 2.5 endapo Bunge litaridhia ili kuboresha zaidi upatikanaji wa huduma za maji Bukoba Vijijini ikiwemo maeneo yaliyotajwa na Mheshimiwa Mbunge.
MHE. CECIL D. MWAMBE (K.n.y MHE. UPENDO F. PENEZA) aliuliza:-
Je, Serikali imeweka mikakati gani kuimarisha huduma za umeme, maji, afya na elimu katika maeneo ya vijijini ili kuongeza uzalishaji katika maeneo hayo na kuzuia wimbi la watu kukimbilia mijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Upendo Furaha Peneza, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza uzalishaji katika maeneo ya vijijini kwa kuimarisha huduma za umeme, maji, afya na elimu kwa lengo la kuzuia wimbi la watu kukimbilia mijini Serikali inatekeleza mikakati ifuatayo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, kuendelea kuboresha miundombinu ya shule za msingi na sekondari kwa kujenga na kukarabati madarasa, vyoo, maabara, mabweni, nyumba za walimu, mabwalo, maktaba kwa kuzingatia mahitaji ya shule husika. Pia kujenga shule mpya katika maeneo ambayo shule za msingi na sekondari ziko mbali. aidha, mkakati wa madawati kwa kila shule, mkakati wa kujenga maabara kwa shule za sekondari na ajira mpya kwa walimu wapya wa michepuo ya sayansi ni miongoni mwa mikakati mahususi ya kuboresha sekta ya elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, kuendelea kuboresha miundombinu kwenye sekta ya afya ambapo kwa mwaka huu wa fedha pekee Serikali inajenga na kukarabati vituo vya afya 183 kwa gharama ya shilingi bilioni 81 vitakavyokamilika ifikapo tarehe 30/4/2018; ambapo shilingi bilioni 35.7 zimetolewa kwa ajili ya vifaa tiba. Ili kuongeza upatikanaji wa dawa Serikali imeongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015/2016 hadi shilingi bilioni 260 mwaka huu wa fedha 2017/2018 ambazo zimesaidia sana kuongeza upatikanaji wa dawa mijini na vijijini. Pia kipaumbele maalum kimewekwa kuhusu kuongeza watumishi wa afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika sekta ya nishati vijiji 7,873 kati ya vijiji 12,545 vya Tanzania Bara vitapatiwa umeme kuanzia mwaka huu wa fedha 2017/2018 hadi 2021. Umeme utasambazwa hadi kwenye maeneo yote ya shule, zahanati, vituo vya zfya, hospitali, mitambo ya maji, viwanda vidogo vidogo, viwanda vya kati na viwanda vikubwa.
Aidha, huduma za maji zitaboreshwa zaidi kupitia utekelezaji wa awamu ya pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji. Serikali pia itaendelea kuimarisha barabara vijijini ili kupunguza gharama za usafiri na usafirishaji hasa wa mazao kwenda kwenye soko.
MHE. ALLY S. UNGANDO aliuliza:-
Maeneo ya Kibiti, Bungu, Jaribu Mpakani na Nyamisati katika Jimbo la Kibiti yanakuwa kwa haraka sana na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu.
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kupanga mipango miji?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuweka mitandao na kuchonga barabara za mitaa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ally Seif Ungando, Mbunge wa Kibiti lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti kwa mujibu wa Sheria Namba 8 ya Mipango Miji ya mwaka 2007 imeandaa Mpango Kabambe (Master Plan) wa Mji Mdogo wa Kibiti ili kuwa dira ya upangaji na uendelezaji wa mji huo ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Kibiti. Kazi hiyo imepangwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Februari, 2018 na kuwasilishwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kuidhinishwa na kusajiliwa. Michoro hiyo itakuwa na jumla ya viwanja 360 ambapo kati ya hivyo, viwanja vya matumizi ya makazi ni 205, makazi na biashara 82, viwanja vya matumizi ya umma 25, makazi maalum (housing estate) nane , viwanda vidogo 20 na maeneo ya wazi 20.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa miundombinu zikiwemo barabara ndani ya Mji Mdogo wa Kibiti utaanza kutekelezwa baada ya kuidhinishwa kwa michoro ya mipango miji na Wizara yenye dhamana na Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA aliuliza:-
Wilaya ya Karagwe ina walimu ambao bado wanadai malimbikizo ya mishahara, walimu hawa hupandishwa madaraja bila ya kurekebishiwa mishahara yao kitu ambacho kimekuwa ni kero kubwa kwa walimu wa Karagwe na maeneo mengine nchini.
(a) Je, Serikali inawaambia nini walimu hawa na imefikia wapi kutatua kero zao?
(b) Je, Serikali imefikia wapi katika kuhakikisha Teachers Service Commission (TSC) inapata rasilimali watu na fedha ili iweze kutetea maslahi ya walimu nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa, Mbunge wa Karagwe lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikilipa madeni ya malimbikizo ya mishahara ya walimu kila mwezi kupitia akaunti zao za benki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia tarehe 30/6/2017 Serikali imelipa kiasi cha shilingi bilioni 14.236 kwa walimu 18,865 kati ya shilingi bilioni 69.461 ilizokuwa ikidaiwa hadi kipindi cha 2015/2016 ambapo walimu 12,284 ni wa shule za msingi na 6,581 ni wa shule za sekondari wakiwemo walimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe 105 waliolipwa jumla ya shilingi 110,555,836.70. Serikali itaendelea kuongeza kiasi inacholipa kwa mwezi ili kumaliza kabisa deni hili kwa muda mfupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TSC, Serikali imeendelea kuimarisha Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) kwa kuipatia Ofisi za Makao Makuu, Ofisi za Wilaya pamoja na kuipatia samani na watumishi katika ofisi hizo. Kwa mfano, Ofisi ya TSC Wilaya ya Karagwe yupo Katibu wa Wilaya na Maofisa wawili. Katika mwaka huu 2017/2018 TSC imepewa kibali cha nafasi za ajira mpya 26 na mwaka ujao 2018/2019 nafasi 43 endapo Bunge litaridhia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo ni kukamilisha ikama iliyoidhinishwa inayohitaji watumishi wasiopungua sita na wasiozidi nane kwa kila Wilaya. Hadi Desemba, 2017 TSC imepewa shilingi bilioni 1.247 za matumizi mengine ukiacha mishahara kati ya shilingi bilioni 4.622 zilizotengwa mwaka huu 2017/2018. Bajeti ya mishahara ikijumlishwa na hiyo Bajeti ya Matumizi Mengineyp (OC), TSC kwa mwaka 2017/2018 imetengewa jumla ya shilingi 12,422,291,495.
MHE. FLATEI G. MASSAY aliuliza:-
Mradi wa Maji wa Hydom umechukua muda mrefu kumalizika na wananchi wanasubiri maji huku muda wa mkataba na mkandarasi ukiwa umeisha.
Je, kwa nini Serikali isimfukuze mkandarasi huyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji wa Mji wa Haydom ulianza kutekelezwa mwaka 2014 lakini kutokana na changamoto ya fedha utekelezaji ulisimama mwaka 2015/2016. Hata hivyo, pamoja na mkataba wa mkandarasi kuisha muda wake, napenda nimsifu na kumshukuru Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya Mheshimiwa Chelestino Mofuga na Mkurugenzi wa Halmashauri Ndugu Hudson Kamoga kwa kufanya kikao kati yao na mkandarasi chini ya Uenyekiti wa Katibu Mkuu wa Wizara ya maji Profesa Kitila Mkumbo tarehe 2/11/2017, ambapo muafaka wa mkandarasi kuendelea kutekeleza mradi huo unaotarajiwa kukamilika mwezi Aprili, 2018 ulipatikana. Kwa maana hiyo, wakazi wa vijiji vya Haydom na Ng’wandakw vinavyounda Mji wa Haydom wenye wakazi 17,406 wataanza kupata maji baada ya mradi huo kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, nyongeza yangu kuhusu taarifa tulizozipata usiku wa leo zinazohusu changamoto za Mkandarasi zinazohitaji utatuzi wa haraka namwomba Mheshimiwa Flatei Massay na mwenzangu Naibu Waziri wa Maji tukutane hapa Bungeni baada ya kipindi cha asubuhi ili tupate utatuzi wa haraka wa mradi huo. (Makofi)
MHE. PROF. NORMAN A. S. KING aliuliza:-
Mwaka 2013 Serikali ilianza kutekeleza mradi wa maji wa Kata za Kinyika na Matamba katika Wilaya ya Makete lakini mradi huo haukufanikiwa kutokana na Serikali kutoa maelekezo ya kulaza mabomba ya inchi 2.5 na 4 badala ya inchi 8 kwenye mradi wa kilometa 18; mradi wa maji wa Tarafa za Magoma na Bulongwa ulijengwa muda mrefu wakati idadi ya watu ikiwa ndogo lakini sasa idadi ya watu na matumizi vimeongezeka.
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa Tarafa ya Matamba?
(b) Je, ni lini Serikali itakamilisha mradi wa maji wa Tarafa ya Bulongwa ili Kata za Bulongwa, Kipagalo na Luwumbu ziweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Norman Sigalla King, Mbunge wa Makete lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa maji wa Kata ya Matamba na Kinyika unaosambaza huduma za maji kwenye vijiji tisa ulianza kujengwa mwaka 2007 na ulikamilika mwaka 2014. Kabla ya ujenzi kuanza usanifu wa mradi huo ulilazimika kubadilishwa ili kutumia bomba la inchi 4, 2 na 1.5 badala ya bomba la inchi 8 kulingana na fedha zilizokuwepo kwani gharama za mradi kwa usanifu wa awali zilikuwa kubwa zaidi. Kutokana na ongezeko la watu kutoka 12,019 mwaka 2007 hadi 17,686 kwa sasa mradi huo haukidhi mahitaji. Ili kukidhi mahitaji Serikali inakamilisha usanifu wa mradi utakaotoa maji Mto Misi ambapo ujenzi unatarajiwa kuanza mwaka 2018/2019.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba mradi wa maji Bulongwa na Magoma unaohudumia vijiji 14 uliojengwa mwaka 1984 haukukidhi mahitaji ya sasa na miundombinu yake ni chakavu. Serikali imeanza ukarabati wa mradi ambapo hadi sasa bomba jipya kwa umbali wa kilometa nne limelazwa na linahudumia Vijiji vya Unyangogo, Iniho na Mwakauta. Mchakato wa kumpata mkandarasi atakayetekeleza awamu ya pili ya ukarabati huo unaendelea ili kukarabati bomba kwa umbali wa kilometa mbili. Ukarabati wa mradi mzima unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 30, 2018.
MHE. GODFREY W. MGIMWA (K. n. y. MHE. SUZANA C. MGONOKULIMA) aliuliza:-
Tangu kutangazwa sheria ya kuzitaka Halmashauri zote nchini kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya wanawake na vijana.
Je, ni nini kinaifanya Serikali kutokuwa na taarifa ya mfuko huo kujua una kiasi gani cha fedha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Suzana Chogisasi Mgonokulima, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, chimbuko la maelekezo yanayozitaka Halmashauri zote nchini kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa ajili ya mikopo ya wanawake asilimia tano na mikopo ya vijana asilimia tano ni Azimio la Bunge la Agosti 1993, chini ya kifungu cha 17(1) cha Sheria ya Exchequer and Audit Ordinance ya mwaka 1961; likiazimia kuanzishwa kwa Mifuko Maalum ya Mikopo kwa Vijana na Wanawake kwa kuchangiwa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya kila halmashauri kila mwaka. Baada ya azimio hilo Serikali ilitoa maelekezo mahsusi kwa Halmashauri zote nchini kutenga fedha hizo kuanzia mwaka wa fedha 1993/1994.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na changamoto kadhaa za kiutekelezaji ambazo zimekuwa zikisababisha utekelezaji wa azimio hilo usifikie asilimia 100. Miongoni mwa changamoto hizo ni kutofikia viwango vya makusanyo ya ndani vilivyopangwa kwa mwaka husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano katika mwaka wa fedha 2016/2017 jumla ya shilingi 665,414,828,000 za mapato ya ndani zilipangwa kukusanywa na Halmashauri zote nchini; lakini mapato halisi yaliyokusanywa ilipofika mwisho wa mwaka yalikuwa ni shilingi 544,897,803,696 tu. Kutokana na ukusanyaji kutotabirika na hivyo kutofikia viwango tarajiwa, badala ya kiasi cha shilingi bilioni 56.8 kukopeshwa wanawake na vijana kama ilivyokuwa imetengwa, ni shilingi 17.5 tu sawa na asilimia 31, ndizo zilizotolewa.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwakumbusha wakurugenzi wa halmashauri zote 185 Tanzania Bara kwamba kutotoa asilimia 10 ya mapato ya ndani ni tabia ambayo husababisha waandikiwe deni kwenye taarifa za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kupitia Bunge lako Tukufu, naagiza kuanzia sasa ni lazima kila Halmashauri itoe asilimia 10 ya mapato halisi ya ndani kama ilivyoelekezwa na Serikali ili kutokusababisha madeni ya aina hiyo.
MHE. ESTER A. MAHAWE aliuliza:-
Takwimu zinaonesha upungufu mkubwa wa matundu ya vyoo zaidi ya 200,000 katika shule mbalimbali za sekondari na msingi.
(a) Je, nini mkakati wa Serikali wa kumaliza tatizo hilo?
(b) Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka wa kuja na mkakati mbadala kama ilivyofanya wakati wa kumaliza tatizo la madawati na maabara nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuna upungufu wa matundu ya vyoo 276,198 kwa shule za msingi na 20,534 kwa shule za sekondari. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya matundu ya vyoo 6,708 kwa shule za msingi na 2,071 kwa shule za sekondari yamejengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya tathmini ya kina tumebaini kuwa zinahitajika jumla ya shilingi bilioni 646.822 kumaliza tatizo hilo. Wizara yangu imetoa maelekezo kwa halmashauri zote kwamba katika Bajeti ya mwaka 2018/2019, fedha za ruzuku ya maendeleo ambazo ni jumla ya shilingi bilioni 55.2 endapo zitapitishwa na Bunge, sehemu kubwa ya fedha hizo ielekezwe kwenye kipaumbele cha miundombinu ya elimu ikiwemo vyoo kwenye shule zote ambazo tayari wananchi watakuwa wamechangia nguvu zao.
Uamuzi huo utatoa nyongeza kubwa sana kwenye Bajeti ya shilingi bilioni 19.97 ambayo imetengwa chini ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mahsusi kwa ajili ya matundu ya vyoo katika shule za msingi na shule za sekondari. Mkakati wa Serikali ni kutumia fedha hizo kumalizia kazi za ujenzi ambazo zitakuwa zimeanzishwa na wananchi.
MHE. JOSEPH K. MHAGAMA aliuliza:-
Idadi ya watu nchini inazidi kuongezeka, ongezeko hili linaenda sambamba na ongezeko la mahitaji ikiwemo ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwajengea uwezo wakulima na wafugaji ili waendeshe shughuli zao katika maeneo madogo lakini kwa tija kubwa na kuwaondolea adha wanazozipata?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Kizito Mhagama, Mbunge wa Madaba kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali huwajengea uwezo wakulima na wafugaji nchini kupitia elimu na ushauri wa kitaalam ambao hutolewa na Maafisa Ugani walioko kwenye Kata na Vijiji vya Halmashauri zote nchini. Hadi Desemba, 2017 tunao Maafisa Ugani 13,532. Kati ya hao Maafisa Ugani 8,232 ni wa kilimo cha mazao, 4,283 ni wa mifugo, 493 ni wa uvuvi na 524 ni wa ushirika.
Elimu ya kilimo na ufugaji bora hutolewa kupitia mashamba darasa 11,213 nchi nzima kwa wakulima na wafugaji wakubwa na wadogo, vikundi vya ushirika vya miradi ya umwagiliaji kwa njia ya mitaro na njia ya matone (drip irrigation) na vikundi vya ushirika vya ufugaji wa kisasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia awamu ya pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo itakayoanza kutekelezwa mwaka ujao 2018/2019 Serikali inaandaa mradi wa kilimo cha kutumia vitalu nyumba (green house) utakaotekelezwa kwa kila halmashauri kujenga vitalu nyumba visivyopungua viwili ili kusambaza teknolojia mpya ya kilimo yenye uwezo mkubwa wa kuzalisha shehena ya mazao mengi katika eneo dogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati mingine ni pamoja na kufanya sensa mahsusi ya kuwatambua wakulima wadogo na wakubwa, kuwasajili, kujua uwezo wao na kujua mahitaji yao ya mbegu, mbolea na madawa. Zoezi hilo limeanza na mazao ya kahawa, tumbaku, korosho, chai na pamba kwa mazao ya biashara; pamoja na mazao ya mahindi, mpunga, ngano na muhogo kwa upande wa mazao ya chakula. Takwimu hizo zitasaidia utekelezaji wa mikakati ya kuongeza uzalishaji kwa kuhakikisha pembejeo za kilimo zinawafikia wakulima mapema ili zitumike kwa wakati stahiki wa kilimo kwa lengo la kuongeza tija.
MHE. GRACE V. TENDEGA aliuliza:-
Kuna uhaba wa nyumba za kuishi walimu licha ya juhudi za wananchi kujenga nyumba za walimu wa shule za msingi na sekondari; walimu hao pia wanahitaji kujenga nyumba zao wenyewe za kudumu.
Je, ni lini Serikali itaweka utaratibu wa kutoa mikopo kwa walimu ili wajenge nyumba zao binafsi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Grace Victor Tendega, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa upo uhaba wa nyumba za walimu katika shule za msingi na sekondari ndiyo maana imekuwa ikijitahidi kila mwaka kujenga nyumba za walimu. Katika mwaka huu wa fedha 2017/2018 Serikali kwa kushirikiana na wananchi, imekamilisha ujenzi wa nyumba 274 za walimu na hivyo kufikisha idadi ya nyumba 14,640 kati ya nyumba 67,711 zinazohitajika kwenye shule za sekondari. Aidha, nyumba 290 za walimu zimejengwa kwenye shule za msingi na hivyo kufikisha idadi ya nyumba 45,638 kati ya nyumba 175,930 zinazohitajika. Takwimu hizo zinabainisha kwamba familia za walimu 52,071 katika shule za sekondari na familia za walimu 130,300 kwenye shule za msingi zinaishi kwenye nyumba za kupanga au nyumba zao binafsi. Ni wazi kwamba mahitaji ya nyumba za walimu ni makubwa mno.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imedhamiria kuendelea kuweka kipaumbele cha kujenga nyumba za walimu za kuishi familia mbili, nne au sita ambazo ni za gharama nafuu kulinganisha na gharama za kujenga nyumba za kuishi familia moja. Kipaumbele cha juu kitaendelea kuwekwa kwenye maeneo yenye mazingira magumu ya kupata nyumba za kupanga hasa maeneo ya vijijini.
Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa mikopo kwa ajili ya Walimu kujenga nyumba zao binafsi ni kama ulivyo kwa watumishi wengine wa Serikali, ambapo mtumishi anaruhusiwa kukopa kwenye taasisi au benki yenye mkataba maalum na mwajiri kwa kujaza fomu ili akatwe marejesho ya mkopo kutoka kwenye mshahara ambapo makato ya mkopo hayatakiwi kuzidi theluthi mbili ya mshahara na mkopo wote kulipwa kwa kipindi cha kati ya miezi 36 (miaka mitatu) hadi miezi 300 (miaka 25) kulingana na masharti ya taasisi husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, miongoni mwa taasisi zinazotoa mikopo ya nyumba kwa watumishi wa Serikali wakiwemo walimu ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Kampuni ya Nyumba za Watumishi (Watumishi Housing Company), Benki ya Afrika (Bank of Africa – BOA) kupitia mpango wake wa WEZESHA, mabenki kadhaa mengine kama NMB, CRDB, Azania na kadhalika na kampuni nyingine kama vile T-Mortgage yanayolenga zaidi kuwakopesha watumishi wa kipato cha chini na cha kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili watumishi wakiwemo walimu wapate mikopo ya kujenga nyumba binafsi kwenye maeneo watakayochagua wao, inatakiwa Wakurugenzi wa Halmashauri wawasiliane na taasisi zinazokopesha ili waingie makubaliano maalum yatakayowawezesha watumishi wa Halmashauri wanaotaka mikopo ya kujenga nyumba binafsi wakiwemo walimu kupata mkopo.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-
Bwawa la Lukuledi ambalo huhudumia Kata za Lukuledi, Mpanyani na Chikinja ni muhimu sana kwa wananchi.
Je, Serikali itafanya lini ukarabati wa bwawa hilo kwa sababu kiwango cha maji kinapungua kwa kujaa mchanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali kupitia Wakala wa Uchimbaji Visima na Mabwawa (DDCA) inaendelea na kazi ya usanifu wa kina wa miundombinu ya Bwawa la Lukuledi lililojengwa mwaka 1954 ambalo ukarabati wake utakapokamilika litahudumia wananchi wapatao 11,544 kwenye vijiji vya Lukuledi A, Lukuledi B, Mraushi, Mkolopola, Ndomoni na Naipanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, usanifu huo unahusisha mabwawa mengine mawili yenye uwezo wa kuhudumia wananchi 15,746. Mabwawa hayo ni Bwawa la Mihima litakalohudumia vijiji vya Mihima, Muungano na Mpanyani na Bwawa la Chingulungulu litakalohudumia vijiji vya Chingulungulu, Namatutwe na Namalembo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la usanifu huo ni kubaini gharama zitakazohitajika kukarabati mabwawa hayo matatu yenye uwezo wa kuzalisha na kusambaza huduma ya maji kwa wananchi wapatao 27,290.
MHE. HAMIDU H. BOBALI aliuliza:-
Je, Serikali imefanya tathmini juu ya ubora na changamoto zilizopo katika shule za sekondari za kata nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la kitafiti la Mheshimiwa Hamidu Hassan Bobali, Mbunge wa Mchinga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwaka 1995 hadi 2005 ni kipindi ambacho tafiti, tathmini, mikakati na mipango mingi katika sekta ya elimu, ikiwemo Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Elimu (ESDP) inayotekelezwa kupitia Mpango wa Elimu ya Msingi (MMEM) kuanzia mwaka 2000 na Mpango wa Maendeleo wa Elimu ya Sekondari (MMES) kuanzia mwaka 2004 ilianzishwa.
Mipango hiyo ndiyo chimbuko la maamuzi ya kuanzisha Shule ya Sekondari kila Kata ili kuhakikisha watoto wengi zaidi waliokuwa wanakosa nafasi za masomo ya sekondari, licha ya kufaulu mitihani ya darasa la saba kwa sababu tu ya uchache wa shule wanapata nafasi hizo. Hadi mwezi Oktoba, 2017 tulikuwa na shule za sekondari za kata 3,103 zilizokuwa na wanafunzi 197,663 ambapo kama zisingekuwepo wangeikosa elimu ya sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, tathmini mbili za Serikali zilizochambua kwa kina sekta ya elimu kupitia Tume ya Profesa Mchome ya mwaka 2013 iliyochambua sababu za ufaulu hafifu wa wanafunzi kwenye mitihani ya mwaka 2012 ya kidato cha nne na Kamati kuhuisha na kuoanisha Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995, Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo mwaka 1996, Sera ya Taifa ya Elimu ya Juu ya mwaka 1999 na Sera ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa Elimu ya Msingi mwaka 2007 iliyoongozwa na Mwalimu Abubakar Rajab mwaka 2013, ndizo zilizobaini na kuishauri Serikali kuanzisha sera mpya moja ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014.
Mheshimiwa Naibu Spika, sera mpya imetoa maelekezo mahususi kuhusu namna ya kuboresha elimu ya awali, elimu ya msingi, elimu ya sekondari, elimu ya ufundi na elimu ya juu. Mitaala imesharekebishwa, ikama, vifaa, samani na miundombinu vyote hivi vinaendelea kuboreshwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa shule mpya, ujenzi wa madarasa, vyoo, maabara, mabweni, maktaba, nyumba za walimu, ofisi ya walimu, mabwalo na majengo ya utawala unaoendelea nchi nzima kwa kushirikiana na wananchi; kuboresha upatikanaji wa vitabu vya kiada na ziada katika shule za sekondari pamoja na juhudi za Serikali kuhakikisha walimu wa kutosha wanapatikana hasa wa masomo ya sayansi na hisabati, ni uthibitisho wa namna Serikali ilivyo na dhamira ya kuinua ubora wa elimu.
MHE. SALMA R. KIKWETE aliuliza:-
(a) Kwa kuwa elimu ni haki ya kila mtoto, je, Serikali inawasaidiaje watoto wenye usonji ili nao wapate elimu?
(b) Je, Walimu wanaofundisha watoto hao wanatosheleza kwa mujibu wa ikama?
(c) Kwa kuwa watoto hao wana mazingira tete, je, Walimu wao wana utaalam wa kutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Salma Rashid Kikwete, Mbunge wa Kuteuliwa, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, usonji ni ulemavu ambao huathiri mfumo wa mawasiliano katika ubongo, mahusiano na utambuzi. Wanafunzi wenye usonji wamekuwa wakifundishwa na Walimu watalaam wa ulemavu wa akili waliopatiwa mafunzo kazini. Hadi sasa tuna wanafunzi 1,416 wenye usonji na Walimu 157 walio katika shule 18 za msingi nchini. Walimu hao ni wachache na hawatoshi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wapo Walimu waliopata taaluma hiyo kwenye Chuo cha Patandi, lakini hawako kwenye shule maalum, nasisitiza tena agizo langu nililolitoa kwenye Mkutano wa Kumi kwamba Halmashauri zote ziwahamishie Walimu hao kwenye shule zenye wanafunzi wenye ulemavu ikiwemo wenye usonji ifikapo mwezi wa Desemba, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, utoaji wa elimu maalum nchini kwa wanafunzi wenye ulemavu wasioona, viziwi, albino, usonji, viziwi–wasioona, walemavu wa akili, walemavu wa viungo, uoni hafifu, wenye vipawa na vipaji pekee pamoja na wenye matatizo ya ujifunzaji utaendelea kupewa kipaumbele. Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia ikiwemo miundombinu, vifaa maalum kwa mahitaji maalum, kutoa mafunzo zaidi kwa Walimu pamoja na kugharamia kwa ujumla elimu msingi bila malipo kwa wanafunzi wote ikiwemo wenye mahitaji maalum.
MHE. PAULINE P. GEKUL aliuliza:-
Kata ya Sigino na Vijiji vyake vyote katika Jimbo la Babati Mjini haina kabisa maji safi na salama:-
Je, ni nini mkakati wa Serikali wa kuipatia maji safi na salama Kata hiyo pamoja na Vijiji vyake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Pauline Philip Gekul, Mbunge wa Babati Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba vijiji vyote vinne katika Kata ya Sigino ndani ya Halmashauri ya Mji wa Babati vyenye wakazi 11,895 havina huduma ya maji safi na salama. Hata hivyo ziko hatua mahsusi zinazoendele. Mnamo tarehe 29 Mei, 2017, Halmashauri ya Mji wa Babati ilisaini mkataba wa Sh.487,470,000 kujenga mradi wa maji katika Kijiji cha Imbilili ambao ulipangwa kukamilika tarehe 30 Juni, 2018 lakini Mkandarasi Black Lion Limited amebainika kuwa na uwezo mdogo kwani hadi sasa ametekeleza kazi kwa asilimia saba tu. Naishauri Halmashauri ambapo Mheshimiwa Pauline Gekul ni Diwani, itathmini haraka hali hiyo na ichukue hatua haraka kwa manufaa ya wananchi.
Mheshimiwa Spika, hatua nyingine kubwa inayoendela ni utekelezaji wa mkataba kati ya Halmashauri na Mkandarasi Maswi Drilling Company Limited kuchimba visima virefu katika Vijiji vya Sigino, Singu na Haraa kwa shilingi milioni 94.5 ambao umefikia asilimia 25 na utakamilika tarehe 30 Juni, 2018. Usanifu na ulazaji wa mabomba yakayosambaza huduma za maji safi na salama kwa wananchi utaanza mwaka 2018/2019 kwa kutumia Sh.611,137,000 ambazo zimetengwa kutekeleza mradi huo. Ahsante.
MHE. HAWA S. MWAIFUNGA aliuliza:-
Kiwango cha elimu katika Mkoa wa Tabora kimeshuka sana, Mkoa umefanya vibaya katika mtihani wa darasa la saba, kidato cha nne na cha sita. Kufanya vibaya kunatokana na changamoto mbalimbali kama walimu, upungufu wa madawati na idadi kubwa ya wanafunzi katika madarasa.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kero hizi zinatatuliwa ili kurejesha hadhi ya elimu Mkoa wa Tabora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. GEORGE J. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Subira Mwaifunga, ambaye ni mtoto wa shangazi yangu na Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto zilizotajwa katika swali, si kweli kwamba kiwango cha elimu kimeshuka sana Mkoani Tabora kwa kufanya vibaya kwenye mitihani. Takwimu zinathibitisha hali tofauti kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja, katika mitihani ya darasa la saba ya mwaa 2016 kiwango cha ufaulu kilikuwa asilimia 71.35 ambapo Mkoa wa Tabora ulishika nafasi ya 10 kitaifa, lakini mwaka 2017 ufaulu ulipanda hadi asilimia 73.61 na Mkoa ukaendelea kushika nafasi ya 10 kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, katika mitihani ya kidato cha nne ya mwaka 2016 kiwango cha ufaulu kilikuwa asilimia 71 ambapo Mkoa wa Tabora ulishika nafasi ya 10 kitaifa, lakini mwaka 2017 ufaulu ulipanda hadi asilimia 84 na Mkoa kushika nafasi ya 3 Kitaifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kwa upande wa kidato cha sita, ufaulu mwaka 2016 ulikuwa asilimia 97.8 na Mkoa wa Tabora ulishika nafasi ya 11 kitaifa. Kwa mwaka 2017 pamoja na takwimu kuonesha kuwa ufaulu ulikuwa asilimia 87, nafasi ya mkoa kitaifa ilipanda hadi nafasi ya 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka yote miwili mfululizo, Mkoa wa Tabora umekuwa juu ya wastani wa ufaulu kitaifa, hilo ni jambo la kujivunia. Kwa hali hiyo hatuwezei kusema kiwango cha elimu katika Mkoa wa Tabora kimeshuka bali kimepanda. Serikali ina kila sababu ya kumpongeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mheshimiwa Aggrey Mwanri na viongozi wote wa Mkoa wa Tabora wakiwemo viongozi wa wilaya zote na hamashauri zote kwa juhudi zao zilizowezesha matokeo hayo mazuri.
MHE. DKT. STEVEN L. KIRUSWA aliuliza:-
Ubora wa elimu wanayopata watoto wa jamii ya kifugaji wanaosoma shule za kutwa vijijini unaathiriwa sana na umbali mrefu wanaotembea wanafunzi kutoka makazi yao (maboma) hadi shuleni.
(a) Je, ni kwa nini Serikali isijenge mabweni katika baadhi ya shule zilizo kwenye vijiji vyenye mtawanyiko mkubwa wa maboma?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wananchi wa Longido kujenga vyumba 177 vya madarasa, nyumba 291 za walimu na matundu 561 ya vyoo?
(c) Je, Serikali imepanga lini kuziba upungufu wa walimu 234; Waratibu Elimu Kata 18 na maafisa ngazi ya Wilaya 12 katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali refu la Mheshimiwa Dkt. Steven Lemomo Kiruswa, Mbunge wa Longido, lenye vipengele (a), (b) na (c) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua changamoto inayowakabili watoto wa jamii ya kifugaji ndivyo maana katika kipindi cha kuanzia Julai, 2017 hadi Aprili, 2018 imekamilisha ujenzi wa bweni la wasichana na matundu 14 ya vyoo na inaendelea na ujenzi wa bweni la wavulana na nyumba tatu za Walimu katika Shule ya Msingi Sinya.
Vilevile nyumba ya Walimu two in one na madarasa matatu yanaendelea kujengwa katika Shule ya Msingi Kitumbeine ambao yatakamilika Juni, 2018.
Aidha, katika Shule ya Msingi Longido, ujenzi wa vyumba nne vya madarasa uko katika hatua ya msingi. Shule hizo tatu zina uwezo wa kuhudumia wanafunzi 1,323. Utekelezaji huo unafanyika ili kuwapunguzia adha watoto wa jamii ya kifugaji ambao kwa wastani hutembea zaidi ya kilometa 15 kutoka nyumbani hadi shuleni.
Aidha, ujenzi wa madarasa 24 kwenye Shule za Ranch, Imatiani Sokoni, Olmoti, Olmolog na Engurusai vimekamilika wakati ujenzi wa madarasa 18 katika shule mbalimbali unaendelea. Ujenzi wa bweni katika Shule ya Msingi Ngerenyai umekamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 515. Kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo, vyumba vya madarasa na nyumba za walimu. Serikali kwa kushirikisha nguvu za wananchi na wadau itaendelea kujenga mabweni kwenye maeneo ya wafugaji na maeneo mengine yenye uhitaji kadri ya upatikanaji wa fedha utakavyowezekana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Longido ina Kata 18 ambazo kwa sasa Kata zote zina Maafisa Elimu Kata. Katika ngazi ya Halmashauri ya Wilaya kuna upungufu wa Afisa Elimu vielelezo baada ya aliyekuwepo kuhamishwa kwenda Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC). Serikali itaziba pengo hilo hivi karibuni, sambasamba na kupunguza upungufu wa walimu katika Shule za Msingi na Sekondari.
MHE. MWITA M. WAITARA (K.n.y MHE. JOHN W. HECHE) aliuliza:-
Mazingira ya ufundishaji kwa Walimu walio wengi nchini ikiwemo Wilaya ya Tarime yamekuwa siyo rafiki, ambapo Walimu wamekuwa wakibebeshwa mzigo wa gharama za vifaa vya kufundishia kama maandalio ya somo, chaki na kadhalika:-
Je, matumizi haya yatarekebishwaje katika mfumo huu wa elimu bure ulioanzishwa na Serikali ya Awamu ya Tano.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kwa ruhusa yako, nimpe pole Mheshimiwa John Heche na wote ambao wamefiwa, Serikali ipo pamoja nao katika misiba hiyo.
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa John Wegesa Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini, ambapo marekebisho yake madogo naomba yaingie katika Hansard kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kupitia Waraka wa Elimu Na.5 wa mwaka 2015, uliotoa mwongozo wa Serikali kuhusu Elimu Msingi bila malipo, majukumu ya Serikali, jamii, wazazi, walezi, wakuu wa shule, Kamati au Bodi za shule, yamefafanuliwa vizuri sana kwenye Waraka huo. Miongoni mwa majukumu ya Serikali ni kutoa ruzuku ya uendeshaji wa shule, inayogharamia chakula kwa wanafunzi wa bweni, ununuzi wa vitabu vya kiada na ziada, vitambulisho, mitihani endelezi, mitihani ya Taifa, shughuli za michezo, maandalio ya somo, chaki na vifaa vingine. Hivyo siyo sahihi kwa Walimu kutumia fedha zao kugharamia maandalio ya somo na vifaa kama chaki.
Mheshimiwa Spika, nawaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri, Maafisa Elimu wote wa ngazi zote na Walimu Wakuu kusimamia vizuri Mpango wa Utoaji Elimu Msingi bila malipo kama ulivyofafanuliwa katika waraka nilioutaja, kuanzia sasa Walimu wasikubali kubebeshwa mizigo ya gharama isiyowahusu.
MHE. MARTIN M. MSUHA aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya mapitio ya mipaka ya baadhi ya maeneo kama vile mikoa, wilaya na majimbo ya uchaguzi kwani baadhi ya mipaka ya maeneo hayo yana muingiliano unaoleta ugumu wa utoaji wa huduma za jamii?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuligawa Jimbo la Mbinga Vijijini kwa kuzingatia ukubwa wake wa kata 29?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Martin Alexander Mtonda Msuha, Mbunge wa Mbinga Vijijini, lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kufanya mapitio ya mipaka kwa baadhi ya mikoa, wilaya na majimbo ya uchaguzi hasa yenye muingiliano unaosababisha ugumu wa utoaji wa huduma za jamii. Hata hivyo, zoezi hilo ambalo linaweza kusababisha mapendekezo ya maeneo mapya ya utawala au kuyahamisha mengine litafanyika baada ya kukamilisha miundombinu ya majengo ya ofisi, majengo ya huduma mbalimbali na vifaa katika mikoa, wilaya na halmashauri mpya zilizoanzishwa tangu mwaka 2012.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Ibara ya 75 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imepewa mamlaka ya kuyagawa majimbo ya uchaguzi kwa kuzingatia vigezo vya idadi ya watu, jiografia, hali ya mawasiliano, ukubwa wa jimbo na uwezo wa ukumbi wa Bunge. Ili jimbo ligawanywe Tume hutoa tangazo kuhusu nia hiyo. Baada ya tangazo, mapendekezo hujadiliwa katika vikao vya halmashauri, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Mkoa na hatimaye huwasilishwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo hutangaza Jimbo jipya baada ya kupata kibali cha Rais.
MHE. ALMAS A. MAIGE aliuliza:-
Halmashauri ya Wilaya ya Uyui inajulikana kwa jina la zamani la Tabora District Council (TDC) jina ambalo linagongana na jina la Manispaa ya Tabora (Tabora Minicipality). Wilaya kupitia Ofisi ya Katibu Tawala Mkoa alileta maombi ya kubadili jina la Halmashauri kutoka Tabora District Council (TDC) na kuwa Halmashauri ya Uyui na Halmashauri imeomba kubadili jina la Jimbo la Tabora Kaskazini na Jimbo la uyui ikibeba jina la Wilaya na jina la eneo la kijiografia Uyui kwa sababu, hakuna tena Tabora Kaskazini, Kusini wala Magharibi:-
(a) Je, ni lini jina la Halmashauri litabadilishwa kuwa Halmashauri ya Uyui?
(b) Je, ni lini Jimbo la Tabora Kaskazini litaitwa Jimbo la Uyui?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu swali la Mheshimiwa Maige, naomba kwanza dakika moja tu nielezee furaha yangu; leo nimeamka saa 10:00 usiku kwa ajili ya kujiandaa kuja kujibu maswali, lakini furaha yangu kubwa ni kwa sababu Simba Sports Club baada ya kupata ubingwa sasa naamini Watanzania watapata wawakilishi kwenye michezo ya kimataifa ambao hawatatupa pressure kwa sababu vijana hawa wanajua kucheza vizuri sana mpira wa miguu, ahsante sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya maelezo hayo…
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Almas Athuman Maige, Mbunge a Tabora Kaskazini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mhesimiwa Mwenyekiti, maombi yenye mapendekezo ya kubadili jina la Halmashauri ya Wilaya ya Tabora kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui sawa sawa na jina la Wilaya ya Uyui ambayo yamepitishwa na vikao vya kisheria vya Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya na Kamati ya Ushauri ya Mkoa yameshapokelewa na yako katika hatua za kupata ridhaa. Nawaomba wadau wote wa suala hili wawe na subira wakati Serikali inapomalizia mchakato huo.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Ibara ya 75 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mapendekezo ya kubadili jina la jimbo yaliyoridhiwa na baraza, wilaya na mkoa yanatakiwa kuwasilishwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambayo ndio yenye mamlaka ya uamuzi. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA aliuliza:-
Mwaka wa 2014/2015, Jimbo la Magu halikupatiwa Walimu wa shule za msingi na bado kuna uhaba wa Walimu:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta Walimu Magu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniventura Desderius Kiswaga, Mbunge wa Magu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Magu inao Walimu wa shule za msingi 1,281 kati ya Walimu 2,002 wanaohitajika, hivyo kuna upungufu wa Walimu 821. Kati ya Walimu 1,276 wa shule za msingi walioajiriwa mwezi Disemba, 2017, Halmashauri ya Wilaya ya Magu ilipangiwa Walimu 56 ambao wameripoti kwenye shule zilizokuwa na uhitaji mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Walimu 77 ambao ni miongoni mwa Walimu wa ziada wa masomo ya sanaa katika shule za sekondari za Halmashauri ya Wilaya ya Magu wamehamishiwa shule za msingi. Vile vile katika Mwaka wa Fedha 2017/2018, Serikali imepanga kuajiri Walimu 10,130 wa shule za msingi nchi nzima ili kukabiliana na uhaba wa Walimu katika maeneo mbalimbali; na Halmashauri ya Magu nayo itapangiwa Walimu hao. (Makofi)
MHE. GEORGE M. LUBELEJE aliuliza:-
Jimbo la Mpwapwa lina tarafa mbili, yaani Tarafa ya Mpwapwa na Tarafa ya Mima, lakini tangu kuanzishwa kwa Tarafa ya Mima hakuna miundombinu yoyote iliyojengwa kama vile Ofisi ya Tarafa na vyumba vya watumishi:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Ofisi ya Afisa Tarafa na za watendaji wengine wa ngazi ya tarafa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa George Malima Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Afisa Tarafa wa Tarafa ya Mima hajajengewa ofisi, anatumia Ofisi ya Afisa Mtendaji wa Kata ya Mima kutekeleza majukumu yake. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga Sh.50,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi ya Afisa Tarafa huyo itakayojengwa katika Kijiji cha Mima.
MHE. COSATO D. CHUMI (K.n.y. SAUL H. AMON) aliuliza:-
Jimbo la Rungwe ambalo lina kata 29 lina vituo viwili tu vya afya ambavyo ni Masukulu na Ikati; wananchi wa Kata ya Mpuguso na Isongole kwa nguvu zao wameanzisha ujenzi wa vituo vya afya:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia kumaliza ujenzi huo ili kuwapunguzia adha ya kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu katika Hospitali ya Wilaya ambayo baadhi ya maeneo ni takriban kilometa 50 na usafiri usio wa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Saul Henry Amon, Mbunge wa Rungwe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea na uboreshaji wa vituo vya afya 208 nchi nzima ili kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wagonjwa karibu na wanapoishi. Katika Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe, Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 1, yaani mwezi Septemba, 2017 ilipeleka Sh.500,000,000 kwenye Kituo cha Afya cha Ikuti kwa ajili ya kujenga jengo la wagonjwa wa nje (OPD), chumba cha upasuaji, wodi ya watoto, wodi ya akina mama wajawazito, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la kufulia la kisasa, mtambo wa oxygen na kukarabati miundombinu ili kuhakikisha huduma za upasuaji wa dharura kwa mama wajawazito na huduma nyingine zinapatikana katika Kata ya Ikuti badala ya kufuata huduma hizo kwenye hospitali ya wilaya ambayo iko mbali. Aidha, mwezi Aprili, 2018 Serikali imepeleka Sh.500,000,000 kwenye Kituo cha Afya cha Masukulu ili kujenga na kukarabati miundombinu itakayoboresha huduma kama ilivyo kwa Kituo cha Afya cha Ikuti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha 2018/2019, Kituo cha Afya cha Mpuguso kimetengewa shilingi milioni 100 kutoka kwenye mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya kumalizia jengo la wagonjwa wa nje (OPD). Sambamba na kuitaka halmashauri itenge fedha za mapato ya ndani ili kuendeleza ujenzi kwenye Kituo cha Afya cha Mpuguso na kuanza ujenzi kwenye Kituo cha Afya cha Isongole, napenda kutoa ahadi kwamba Serikali itavipa vituo hivyo kipaumbele cha juu ili ikiwezekana vikamilike mwakani.
MHE. EDWARD F. MWALONGO aliuliza:-
Watendaji wa Vijiji ni kada muhimu sana katika kuwahudumia wananchi walio vijijini:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia mafunzo ya mara kwa mara watumishi hawa ili kuboresha utumishi wao na utoaji huduma kwa wananchi walioko vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Edward Franz Mwalongo, Mbunge wa Njombe Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watendaji wa Vijiji kama walivyo watumishi wengine wa umma wanapaswa kupewa mafunzo mara kwa mara ili kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi. Mafunzo yanayotolewa kwa Watendaji wa Vijiji hujumuisha masuala ya utawala bora, mapambano dhidi ya rushwa, mapambano dhidi ya UKIMWI mahali pa kazi, maadili ya utumishi wa umma pamoja na majukumu yao katika utumishi wa umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia ruzuku ya maendeleo kwa Serikali za Mitaa ambayo inajumuisha Mpango wa Mafunzo kwa watumishi wa kada mbalimbali, Watendaji wa Vijiji 1,840 walipewa mafunzo katika mwaka wa fedha 2016/17. Kuanzia Julai 2017 hadi Aprili 2018 kwa mwaka huu unaoendelea, Watendaji wa Vijiji 1,543 wamepewa mafunzo. Mpango huu ni endelevu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutumia fursa hii kuziagiza halmashauri zote nchini kuweka kipaumbele na kutenga bajeti ya mafunzo kwa kada hii muhimu na kuanzia mwakani tutaanza kufuatilia utekelezaji wa agizo hili ili kuhakikisha kuwa limezingatiwa na halmashauri zote wakati wa bajeti.
MHE. TASKA R. MBOGO aliuliza:-
Wabunge wa Viti Maalum ni sawa na Wabunge wengine wa Majimbo kwa sababu hakuna tofauti ya kiapo cha Wabunge wa Majimbo na wale wa Viti Maalum.
Je, ni kwa nini Wabunge wa Viti Maalum hawaingii kwenye Vikao vya Kamati ya Fedha za Halmashauri zao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Taska Restituta Mbogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, imeundwa kwa mujibu wa Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287, kifungu cha 75 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji), Sura ya 288 kifungu cha 47 pamoja na kifungu cha 40(2)(c) cha Kanuni za Kudumu za Halmashauri za mwaka 2014 na Kanuni za Kudumu za Mamlaka za Serikali za Mitaa kifungu 41(1) zinazotaja Wajumbe wa kuingia kwenye Kamati ya Fedha na Mipango kuwa ni Meya au Mwenyekiti wa Halmashauri ambaye atakuwa Mwenyekiti; Naibu Meya au Makamu Mwenyekiti, Mbunge au Wabunge wa Majimbo wanaowakilisha Majimbo katika Halmashauri hiyo; Wenyeviti wa Kamati za Kudumu katika Halmashauri; Wajumbe wengine wasiozidi wawili watakaopendekezwa na Mwenyekiti au Meya na kupigiwa kura na Baraza la Madiwani la Halmashauri, mmoja kati yao akiwa mwanamke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wa Viti Maalum hawaingii kwenye vikao vya Kamati za Fedha za Halmashauri kwa sababu hawajatajwa kwenye orodha ya Wajumbe iliyoainishwa na kifungu cha 41(1) na kifungu cha 40(2) cha Kanuni za Kudumu za Mamlaka za Serikali za Mitaa za Mwaka 2014, zinazofafanua mahitaji ya Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287, kifungu cha 75 na Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Miji) Sura ya 288 kifungu cha 47.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-
Serikali imeanzisha Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC)
kwa lengo la kutatua matatizo ya walimu.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha Tume hiyo ili ifanye kazi kikamilifu kama ilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) imeanzishwa kwa Sheria ya Utumishi wa Walimu Namba 25 ya mwaka 2015 na kuanza kutekeleza majukumu yake rasmi tarehe 1Julai, 2016 kupitia Ofisi za Tume zilizopo katika Wilaya 139 za kiutawala ambazo zinasimamiwa na Makatibu Wasaidizi wa Wilaya. Majukumu ya tume yameainishwa katika kifungu cha 5 cha Sheria hiyo ambayo ni pamoja na kusimamia mikataba ya ajira za walimu, kuwapandisha madaraja na kuchukua hatua za kinidhamu, ikiwemo kusikiliza rufaa kutoka ngazi za chini, kuwatambua na kutunza kumbukumbu za walimu wa shule za msingi na sekondari, kusimamia mafunzo ya walimu walio kazini, kufanya tafiti mbalimbali zinazohusu utumishi wa walimu na kutathmini hali ya utumishi wa walimu na kusimamia maadili ya utumishi wa walimu.
Mheshimiwa Spika, huu ni mwaka wa pili tu wa uhai wa Tume hiyo ambayo bado ni changa. Mikakati mahususi ya Serikali ili kuiimarisha zaidi Tume hiyo ni ifuatayo:-
• Kuendelea kuipatia fedha ili iweze kutimiza majukumu yake ipasavyo. Mfano katika mwaka wa fedha 2018/2019 Bunge limeiidhinishia Tume ya Utumishi wa Walimu shilingi 12,515,260,520 kati ya hizo shilingi 7,893,115,025 ni za mshahara na shilingi 4,622,145,495 ni za matumizi mengineyo, ili Tume ipate vitendea kazi kama magari, samani za ofisi na pia kugharamia vikao vya mashauri ya nidhamu na vifaa.
• Kuipatia ofisi na watumishi wa kudumu, mfano, hadi sasa inao Makatibu Wasaidizi wa Wilaya 138 ambao wameshajengewa uwezo na mwaka ujao 2018/2019 wataajiriwa watumishi 45 wapya na wengine 145 watahamishiwa kwenye Tume kama uhamisho wa kawaida. Uimarishaji wa Tume hiyo utaendelea kufanyika ndani ya wigo wa sheria iliyoanzisha Tume hiyo.
MHE. NASSOR SULEIMAN OMARY aliuliza:-
Uhakiki wa vyeti feki umeathiri wafanyakazi wengi na wengine wamepoteza ajira zao:-
Je, ni wafanyakazi wangapi wamepoteza ajira zao sekta ya elimu pekee?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Nassor Suleiman Omar, Mbunge wa Ziwani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017 na 2017/2018, Serikali ilifanya uhakiki wa vyeti vya watumishi wa umma ili kubaini waliokuwa na vyeti halali na waliokuwa na vyeti vya kughushi. Katika uhakiki huo, jumla ya Walimu 3,655 walibainika kuwa na vyeti vya kughushi, hivyo walipoteza sifa za kuendelea kuwa watumishi wa umma.
MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:-
Je, ni kwa kiasi gani Serikali inasimamia suala la asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri kwa ajili ya vijana na akina mama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuhakikisha halmashauri zote nchini zinatenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. Katika Mwaka wa Fedha 2016/2017, jumla ya shilingi bilioni 56.8 zilitengwa na halmashauri zote nchini na jumla ya shilingi bilioni 17.5 sawa na asilimia 31 zilitolewa kwa vikundi vya wanawake na vijana. Katika mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya shilingi bilioni 61.6 zilitengwa na hadi kufikia Februari, 2018 jumla ya shilingi bilioni 15.6 sawa na asilimia 27 zilikuwa zimetolewa, ambapo jumla ya vikundi 8,672 vya wanawake na vijana vilipatiwa mikopo. Katika mwaka wa fedha 2018/ 2019, shilingi bilioni 53.8 zimetengwa kwa ajili ya Mfuko wa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu katika halmashauri zote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza uwajibikaji katika kutenga na kupeleka fedha za Mfuko wa Wanawake na Vijana kwa vikundi husika, Serikali itaweka utaratibu katika Sheria ya Fedha (Finance Bill) ya mwaka 2018/2019 utakaohakikisha kwamba halmashauri zote zinatekeleza kikamilifu agizo hilo. (Makofi)