Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Joseph George Kakunda (6 total)

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:-
Barabara ya Ipole - Mpanda yenye urefu wa kilometa 359 iliyoko kwenye mpango wa kujengwa kwa lami iko kwenye hali mbaya sana kutokana na kuharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha, maji maji yamejaa kuvuka barabara na maeneo mengine yanatitia kiasi kwamba mabasi ya abiria na magari ya mizigo yanapata shida kupita na wananchi wa Tabora, Sikonge na Katavi nao wanataabika sana na barabara hiyo.
(a) Je, Serikali inachukua hatua gani za dharura za muda mfupi kuwasaidia wananchi wa Tabora, Sikonge, Katavi na maeneo mengine wanaoathirika na tatizo hilo?
(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kufanya mapitio ya haraka ya usanifu wa barabara hiyo ili kunyanyua zaidi tuta na kuongeza madaraja na makalvati ili kudhibiti maji ya mvua yasiharibu barabara mpya itakayojengwa?
(c) Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa lami na kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, lenye sehemu (a), (b) na (c), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli mwezi Januari hadi Machi mwaka 2016 Mikoa ya Tabora na Katavi ilipata mvua nyingi na sehemu ya barabara ya Tabora, Ipole, Koga hadi Mpanda kuharibika, hususan Mto Koga kujaa maji na kupita juu ya daraja la Koga. Hali hii ilisababisha barabara ya Tabora - Mpanda, sehemu ya Ipole hadi Nyonga, kufungwa kwa muda Serikali ilichukua hatua za haraka za kuifanyia matengenezo ya dharura barabara hii baada ya mafuriko kupungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, barabara mbadala ya Tabora - Uvinza hadi Mpanda, ilipatiwa pia matengenezo ya dharura ili Mkoa wa Katavi usijifunge kabisa. Kwa kuwa maji yamepungua, hatua nyingine ambazo zimechukuliwa ni pamoja na kuruhusu magari madogo na mepesi kuanza kutumia barabara ya Tabora hadi Mpanda. Serikali itafanya mapitio ya usanifu wa kina, wakati wa utekelezaji wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Tabora hadi Mpanda. Ujenzi wa barabara hii unategemea kuanza katika mwaka wa fedha 2016/2017 chini ya ufadhili wa Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:-
Mradi wa REA unaendelea kutekelezwa katika vijiji 24 katika Jimbo la Sikonge lakini mradi huo ulisimamia kwa muda mrefu ambapo baadhi ya maeneo nguzo zilizoachwa barabarani zimeanza kufukiwa na mchanga kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha:-
(a) Je, Serikali itakamilisha lini mradi huo kwa Awamu ya Kwanza na Pili?
(b) Je, Awamu ya Tatu ya utekelezaji wa mradi huo itahusisha vijiji gani katika Wilaya ya Sikonge na ni lini utaanza na kukamilika?
(c) Je, Serikali haioni umuhimu wa kufikisha umeme wa REA kwenye mitambo ya kusukuma maji ya Ityatya, Uluwa, Makazi, Igumila, Majojolo na Kiyombo ili kupunguza gharama za dizeli ambazo zimekuwa zikiathiri upatikanaji wa maji kutokana na gharama kubwa za uendeshaji mitambo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Sikonge ilijumuishwa kwenye REA Awamu ya II ambayo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2016. Kazi ya kupeleka umeme Wilaya ya Sikonge inajumuisha pia ujenzi wa umeme wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 166.44 lakini pia ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa 58.06. Kazi hii pia itajumuisha ufungaji wa transfoma 28 za ukubwa mbalimbali pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 1,704.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huo ambao unatekelezwa kupitia mkandarasi CHICCO umekamilika kwa asilimia 88 hadi sasa. Ujenzi wa njia ya msongo wa kilovoti 33 umekamilika kwa asilimia 86 na ujenzi wa msongo wa kilovoti 0.4 umekamilika kwa asilimia 89.3, lakini pia transfoma 15 zimeshafungwa na wateja 228 wameunganishiwa umeme. Kazi hii imegharimu shilingi bilioni 6.42.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa Mradi wa Kusambaza Umeme Vijijini REA, Awamu ya III, unatarajiwa kuanza mwezi Julai, 2016. Mradi wa REA Awamu ya III unakusudia kupeleka umeme katika vijiji vyote vilivyobaki vya Mheshimiwa Mbunge pamoja na shule, zahanati na vituo vya afya. Kadhalika, kazi hii itajumuisha kupeleka umeme kwa wananchi wapatao 1,510. Kazi hii inagharimu pia jumla ya shilingi milioni 4.33.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya kupeleka umeme kwenye pampu za kusukuma maji alizozitaja Mheshimiwa Mbunge za Ityatya, Makazi na Uluwa itafanywa na REA Awamu ya III. Kazi ya kupeleka umeme kwa vijiji na pampu hizi itahusisha ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilometa tisa, lakini pia ufungaji wa transfoma tatu pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 141. Kazi hii itagharimu shilingi milioni 317.14. Aidha, pampu za maji za Igumumila, Kiyombo na Magolo zitafanyiwa tathmini kubaini mahitaji yake ili na zenyewe ziweze kupatiwa umeme haraka iwezekanavyo.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:-
Kati ya mwaka 1954 na 1957 kulifanyika zoezi la upimaji wa maeneo ya Hifadhi za Misitu, Mapori ya Akiba na Hifadhi katika Wilaya ya Sikonge ambapo kulikuwa na wakazi takribani 16,000 na ng’ombe wapatao 2500. Kwa sasa wakazi wameongezeka hadi kufikia takribani 300,000 na ng’ombe wapo takribani 200,000 lakini eneo la kuishi, kulima na malisho ya mifugo na shughuli nyingine za kiuchumi ni lile lile la asilimia 3.7 ya eneo lote la Wilaya huku eneo la Hifadhi likibaki asilimia 96.3 na hali hii inasababisha migogoro kati ya wakulima, wafugaji na warina asali dhidi ya Maafisa Maliasili.
(a) Je, ni lini Serikali itawaongezea wakazi wa Wilaya ya Sikonge eneo la kuisha, kulima na kulishia mifugo kutoka asilimia 3.7 hadi angalau asilimia 25 ya eneo lote la Wilaya?
(b) Je, Serikali haioni kuwa kuongeza eneo la Wilaya hiyo kwa asilimia 25 kutaepusha migogoro iliyopo sasa na hivyo wananchi watatekeleza shughuli zao kwa amani na utulivu huku wakilinda mazingira pamoja na hifadhi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, lenye sehemu (a) na
(b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na takwimu za Taasisi ya Takwimu ya Taifa (The National Bureau of Statistics) na Sensa ya mwaka 2012, Wilaya ya Sikonge ina ukubwa wa kilometa za mraba 27,873 na idadi ya watu wapatao 179,883. Aidha, maeneo ya hifadhi za misitu na wanyamapori yana ukubwa kilometa za mraba 20,056.94 sawa na asilimia 72 ya eneo lote la Wilaya, hivyo kufanya eneo la makazi na shughuli nyingine za binadamu kuwa sawa na asilimia 28.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi za misitu na mapori ya akiba katika Wilaya ya Sikonge ni muhimu kwa uhifadhi na maendeleo ya sekta nyingine, ikiwa ni pamoja na kuwa vyanzo vya mto Ugalla, ziwa Sagara, Nyamagoma na ardhi oevu ya Malagarasi - Moyowosi. Kwa mantiki hiyo, kugawa maeneo haya na kuruhusu shughuli za kibinadamu kutahatarisha upatikanaji wa rasilimali za maji kwa ajili ya shughuli za uvuvi, kilimo, ufugaji, matumizi ya nyumbani na mengineyo kwa kiasi kikubwa. Muhimu zaidi ni mchango mkubwa wa misitu hiyo katika hali ya hewa na udhibiti wa mabadiliko hasi ya tabianchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, imethibitika kwamba kilimo cha kuhama hama, ikiwa ni pamoja na utumiaji wa maeneo makubwa ya ardhi; ufugaji wa kuhama hama ukijumuisha uingizaji wa mifugo katika maeneo yaliyohifadhiwa, ni matumizi mabaya ya rasilimali ardhi na yasiyo na tija kwa Taifa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi nitumie nafasi hii kuwakumbusha na kuwaomba wananchi kwa kushirikiana na uongozi wa Halmashauri za Wilaya husika, kuchukua hatua za makusudi kuandaa na kutekeleza mipango ya matumizi bora ya ardhi; hatua ambazo zitasaidia kuondoa changamoto za mahitaji ya ardhi katika Wilaya zote nchini ikiwa ni pamoja na Wilaya ya Sikonge iliyoko Mkoani Tabora.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakiboresha Chuo cha Maendeleo ya Jamii yaani FDC Sikonge ili kilingane na Vyuo vya VETA kwa kuogeza idadi ya walimu na mafunzo yanayotolewa?
NAIBU WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya vyuo 55 vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) kuhamishiwa katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia mwaka 2016/2017 Wizara imeanza kufanya tathmini kwa vyuo vyote ili kujua mahitaji halisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutimiza azma hiyo, katika bajeti ya maendeleo kwa mwaka fedha 2017/2018 zimetengwa kiasi cha shilingi bilioni 12 kwa ajili ya kukarabati majengo na miundombinu ya baadhi ya Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi. Wizara pia katika bajeti ya maendeleo ya mwaka 2017/2018 imetenga shilingi bilioni 10 kupitia Mradi wa Kukuza Stadi za Kazi (ESPJ) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia na ambao utadumu kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2017 imepanga kuviboresha kwa awamu vyuo hivyo 55 vya Maendeleo ya Wananchi, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Sikonge kitatembelewa ili kuona uwezekano wa kukiboresha.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itakifanyia tathmini ya kina (ex-post evaluation) Kituo cha Vijana cha TULU kilichopo Sikonge?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Vijana cha TULU kinamilikiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge chini ya usimamizi wa Serikali ya Mkoa wa Tabora. Kilianzishwa mwaka 2014 kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata mafunzo na stadi za ujuzi mbalimbali kama vile ujasiriamali, kilimo pamoja na ujenzi wa makazi bora. Baadaye vijana waanzilishi wa kituo hiki walikisajili kama asasi isiyo ya kiserikali (NGO) ijulikanayo kama Pathfinder. Baada ya kituo hiki kusajiliwa kama NGO, ilibainika kuwanufaisha vijana wachache tofauti na malengo yaliyokusudiwa ambayo ni kuwanufaisha vijana walio wengi ndani na hata nje ya Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Spika, kutokana na kituo hiki kuendeshwa kwa maslahi ya vijana wachache, Serikali iliamua kuchukua hatua ya kubadili usajili wa kituo hiki kutoka kwenye NGO na kuwa kituo cha vijana kitakachosimamiwa na Serikali kwa lengo la kunufaisha vijana wengi zaidi. Aidha, nyaraka muhimu zimewasilishwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya kubadilisha usajili huo wa awali. Baada ya maamuzi hayo kukamilika, Serikali itafanya tathmini ya kina ili kubainisha matumizi na programu mbalimbali zitakazotolewa katika kituo hiki.
MHE. JOSEPH G. KAKUNDA aliuliza:-
Upembuzi yakinifu kwa ajili ya kuijenga kwa kiwango cha lami barabara ya Ipole - Lungwa ulianza miaka mingi iliyopita na hii ni sehemu ya barabara kuu (trunk road) inayounganisha makao makuu ya Mkoa wa Mbeya. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 barabara hiyo imetengewa shilingi 350,000,000 kwa ajili ya kumalizia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Je, ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Joseph George Kakunda, Mbunge wa Sikonge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ikiwa ni pamoja na uandaaji wa nyaraka za zabuni kwa barabara ya Ipole hadi Lungwa yenye urefu wa kilometa 172 inaendelea. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 jumla ya shilingi milioni 1,211 zimetengwa na katika mwaka wa fedha wa 2017/2018, tunashukuru mmezipitisha shilingi milioni 435 kwa ajili ya kukamilisha kazi hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu, usanifu wa kina pamoja na maandalizi ya nyaraka za zabuni na gharama za mradi kujulikana, Serikali itaanza kutafuta fedha za ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Ipole hadi Lungwa.