Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Joseph George Kakunda (17 total)

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri, lakini hili tatizo la hizi kata limekuwa la muda mrefu na hasa ukizingatia kwamba kata zenyewe ziko pembezoni mwa Mji wa Musoma. Nataka kuuliza ni lini haya maji yatawafikia hizo kata kwa sababu wamekuwa na usumbufu wa muda mrefu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, pamoja na matatizo ya mji wa Musoma pia kuna matatizo makubwa ya Mji wa Bunda na hasa Jimbo la Bunda ninakotoka mimi. Kuna kata saba zina matatizo makubwa ya uhaba wa maji ambazo ni Unyali, Kitale, Mgeta, Mihingo, Nyamaghunta na Salama; nilitaka kumuomba tu Waziri ni lini atafika? Nimuombe tu afike kwenye hizo kata saba za Jimbo langu ili aweze kujionea hali halisi ya uhaba wa maji katika jimbo hilo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; ni kweli kwamba, ni muda mrefu, lakini nimuahidi kwamba, mara mradi huu ambao umeanza kutekelezwa utakapokamilika wakazi hawa watafaidika na maji hayo. Swali la pili kuhusu Bunda; naomba nimuahidi Mheshimiwa Mwita Getere kwamba mara baada ya Mkutano huu wa Bunge nitatembelea Mkoa wa Mara na nitafika Bunda. Ahsante sana.
MHE. ZAINAB A. KATIMBA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali na niseme ninatambua jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika kuboresha elimu. Nina maswali mawili ya nyongeza.
Je, Serikali ina mkakati gani katika mabweni haya 155 ambayo inatarajia kuyajenga katika mwaka wa fedha 2017/2018 kuhakikisha kwamba, inazingatia kipaumbele katika ujenzi wa mabweni katika shule zetu za kata?
La pili, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha Mamlaka ya Elimu ya Juu Tanzania ambayo inaonekana inapata changamoto kutokana na kutokuwa na fedha za kutosha, inatengewa fedha za kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutekeleza mkakati wa kujenga mabweni kwa kushirikiana na Halmashuri na wananchi, kama ambavyo tumekuwa tukifanya na hivi natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge wote kule kwenye maeneo yao ambako kuna ujenzi wa mabweni, basi wasaidie kuwahamasisha wananchi washiriki kikamilifu kwenye mkakati huu, lengo ni kuhakikisha kwamba, tunakamilisha ifikapo mwezi Juni mwakani, kama ambavyo tumejipanga.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, tutaweka fungu maalum kwenye bajeti kwa ajili ya kuisaidia taasisi ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja pamoja na taasisi nyingine ambazo zinasaidia maendeleo ya elimu nchini. Ahsante sana.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Majimbo ya Longido na Ngorongoro ni majimbo ambayo yapo kwenye mazingira magumu sana na upatikanaji wa huduma za afya si wa uhakika. Wilaya ya Ngorongoro haina hospitali ya wilaya, Wilaya ya Longido imetengwa kwenye bajeti lakini utekelezaji bado. Je, ni lini Serikali itaweka mkazo kwenye majimbo haya ambayo kwa kweli yana mazingira magumu ya kijiografia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyosema mwenyewe kwamba Majimbo ya Longido na Ngorongoro yapo katika mazingira magumu na Wilaya ya Longido hakuna hospitali na Wilaya ya Ngorongoro tayari iko katika bajeti. Naomba ushirikiano wake mara fedha ambazo zipo kwenye bajeti zitakapopelekwa, ashiriki kikamilifu katika kusimamia ili matumizi ya fedha zile yawe mazuri kama ambavyo ilikusudiwa. Mwaka ujao wa fedha tushirikiane naye kuhakikisha kwamba Longido nao tunawawekea bajeti. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
MHE. EMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tabora Manispaa tuna tatizo kubwa la msongamano wa wagonjwa katika Hospitali Teule ya Kitete na kwa kuzingatia hilo, Tabora Halmashauri kwa kushirikiana na Madiwani pamoja na wananchi wengine tumetenga eneo kwa ajili ya kujengwa Hospitali ya Wilaya ambayo mpaka sasa hivi ujenzi wake unasuasua kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Je, Serikali inajipanga vipi katika kusaidia uwezeshaji wa kuweza kujenga hospitali hiyo ya wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimshukuru Mheshimiwa Mwakasaka pamoja na Waheshimiwa Madiwani katika Manispaa ya Tabora kwa kutenga eneo la kujenga Hospitali mpya kwenye Manispaa ya Tabora ambayo itakuwa Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa msingi huohuo, kwa kuzingatia kwamba Hospitali ya Kitete ni kweli imezidiwa na mzigo maana yake ndiyo hospitali pekee ya rufaa ya mkoa, Serikali inaahidi na namwomba ushirikiano wake, wakati tutakapokuwa tunaweka kwenye bajeti tushirikiane ili tuweze kupitisha kwa pamoja. Ahsante sana.
MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, pia nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Sasa naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa ni sera na mpango wa Serikali kila wilaya kuwa na hospitali, je, ni lini ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Vijijini utaanza licha ya jitihada nyingi za Serikali?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ni lini ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mvomero utakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) : Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba ni sera ya Serikali kujenga hospitali moja kila wilaya na napenda nimhakikishie Mheshimiwa Dokta Ishengoma na Waheshimiwa Wabunge wote kwamba Serikali itaendelea kuwezesha ujenzi wa hospitali moja kila wilaya kwa awamu. Katika Mkoa wa Morogoro tumeanza na Manispaa ya Morogoro na tutaendelea na wilaya nyingine kwa awamu zinazofuata. Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wangu, katika sehemu ya pili ya swali lake Mheshimiwa Dokta Ishengoma kuhusu Hospitali ya Mvomero na bahati nzuri tulikuwa pale Mvomero tukabaini baadhi ya upungufu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeshatenga fedha ya kumalizia jengo lile baada ya kuona upungufu ule na imani yangu ni kwamba kabla ya mwezi Januari hospitali ile itakuwa imekamilika ili wananchi wa Mvomero waweze kupata huduma vizuri. (Makofi)
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Mkoa wa Katavi ni kimbilio la wananchi wengi ambao wamekosa ardhi ya kilimo na wakati huohuo ardhi iliyopo Mkoa wa Katavi asilimia themanini imemilikiwa na misitu ya Serikali kiasi kwamba wananchi walio wengi wamekosa kupata nafasi ya kufanya shughuli zao za kiuchumi kupitia sekta ya kilimo hasa katika kata za Sibwesa, Kasekese, Katuma, Bulamata ambako kuna migogoro mingi ya ardhi. Je, Serikali imejipanga vipi kutatua kero ya ukosefu wa ardhi ili wananchi waweze kuitumia ipasavyo kujikwamua kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyozungumza katika Mkoa wa Katavi sehemu kubwa ya ardhi ni misitu na maeneo ya hifadhi. Ni lengo la Serikali kuendeleza maeneo hayo katika msingi wa kuendeleza misitu na hifadhi kwa ajili ya ustawi wa mazingira lakini vilevile kwa ajili ya kuendeleza ile hali nzuri ya hewa ikiwemo mvua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba katika halmashauri na vijiji vyote tuendelee kuhakikisha kwamba kila kijiji kinakuwa na mpango ardhi wa eneo lake ambao unaainisha maeneo ya kulima, maeneo ya kuishi kama kijiji, maeneo ya mifugo na malisho ili kusudi tuwe na mipango endelevu ya maisha yetu. Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo ndilo jibu langu.
MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Wilaya ya Siha kwenye Kata Ngarenairobi na Ndumeti wananchi hawana maeneo ya kulima pamoja na makazi, wamekaa kwenye mabonde wakati wamezungukwa na heka zaidi ya elfu hamsini na sita za Serikali lakini kukiwepo na mashamba makubwa sana ya ushirika ndani ya Wilaya ya Siha ambayo hayatumiki kama inavyotakiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumwomba Waziri kama atakuwa tayari kufuatana na mimi baada ya Bunge hili tukatizame mazingira ya Wilaya ya Siha na huko Ndumeti pamoja Ngarenairobi na maeneo mengine tuweze kuamua namna ya kupanga hiyo ardhi kubwa sana iliyoko Siha kwa matumizi ya wananchi kwa ajili ya kilimo, makazi lakini vilevile kutenga maeneo ya viwanda na uwekezaji mwingine kwa ajli ya Serikali na sera iliyopo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa la Siha na maeneo kama hayo ni uwekezaji mkubwa ambao unafanywa na wananchi wachache. Kwa hiyo, tungependa tupate kwanza mpango wa Halmashauri yake halafu ndiyo tuweze kuufanyia kazi. Ahsante sana.
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wananchi wa Kijiji cha Mtisi wanapata shida sana, hawana kabisa eneo la kilimo. Nafikiri umeona kabisa hapa jinsi gani eneo la hifadhi ni kubwa zaidi kuliko eneo la kilimo na kaya zimeonekana hapa. Naishukuru Serikali imepanga kuwapa ardhi Novemba mwishoni lakini wananchi wa Mtisi wanahitaji kulima sasa, sasa hivi ndiyo kipindi cha maandalizi ya kilimo, wanatakiwa waandae mashamba yao. Je, Serikali haioni ni vema kubadilisha hii Novemba mwishoni wafanye Novemba hii mwanzoni ili wananchi wale waweze kupata maeneo ya kilimo waweze kupata chakula ndani ya familia zao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, ndani ya Kata hii ya Sitalike kwenye Vijiji vya Matandalani na Igongwe kutokana na ardhi ndogo wako ndani ya ramani toka 1972, lakini Serikali ilienda kuwabomolea nyumba zao na mpaka leo hii imekuwa tafrani, wala hawaelewi hatma ya maisha yao. Je, Serikali ina mpango gani na wananchi wa Matandalani na Igongwe? Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kwenda kwenye Kata ya Sitalike kuona adha hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kurejea majibu yangu ya swali la msingi katika kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Anna Lupembe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimesema kwamba ifikapo mwishoni lakini hadi sasa kazi za kuwapatia ardhi wananchi hao zinaendelea. Hadi jana kaya 200 zilikuwa zimeshatambuliwa na zilikuwa zimeshatengewa eneo maalum. Kwa hiyo, bado zoezi hilo linaendelea ile mwishoni mwa Novemba ni kumalizia kazi, kazi itakuwa imekamilika. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi wowote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la pili amesema kwamba wananchi wa Kijiji cha Matandalani na Igongwe walibomolewa nyumba ni kwa sababu walikuwa kwenye hifadhi. Natoa wito kwa wananchi ambao wako kwenye maeneo ya hifadhi kwamba wanatakiwa waondoke wenyewe badala ya kusubiri kuondolewa kwa nguvu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa shida hiyo iliyopo kule Matandalani na Igongwe na Halmashauri ya Nsimbo kwa ujumla, nilipita juzi lakini niko tayari kwenda tena kama matatizo yataendelea kuzidi kuwepo.
MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri anasema ujenzi unaweza kuanza mwaka 2018/2019, unaweza kuanza. Sasa wananchi wa Mji wa Ujiji na Kasulu kwa ujumla wanataka kupata uhakika, yaani ile commitment ya uhakika kwamba utaanza 2018 au unaweza maana ukisema unaweza, unaweza usianze.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika Mji wa Mugumu tulipewa kilomita mbili mwaka wa fedha uliopita lakini kilomita mbili hizi tumetangaza mara tatu hazijapata mkandarasi kwa sababu ya kilometa chache. Je, Wizara iko tayari kwa mwaka ujao wa fedha kutuongezea kilomita iwe rahisi kwa ajili ya wakandarasi kufanya mobilization?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tumesema kwamba ujenzi unaweza ukaanza kwa sababu bajeti haijapitishwa na Bunge. Naomba Mheshimiwa Mbunge tushirikiane naye kupitisha kwanza bajeti ndiyo ujenzi uweze kufanyika vinginevyo kama Bunge halitapitisha bajeti hiyo, ujenzi hauwezi kuanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili amesema kwamba wamepata ugumu kupata mkandarasi kwa sababu ya ufupi wa barabara ya kilomita. Ningemwomba Mheshimiwa Mbunge amshauri Mkurugenzi wake wa Halmashauri aweze kutembelea Halmashauri za jirani ambazo zimeweza kujenga hizo hizo kilomita mbili na zimepata wakandarasi. Ahsante sana.
MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, ili hawa watumishi wa Serikali za Mitaa waweze kutoa huduma kwa ufanisi wanahitaji kupata mafunzo ya mara kwa mara ili kuboresha utendaji wao. Kwa kuwa kwa muda mrefu mafunzo yamesimamishwa, tunategemeaje hawa watumishi waweze kutoa huduma ipasavyo? Hilo swali la kwanza.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, viongozi ambao wako karibu sana wananchi ni Watendaji wa Kata na Mitaa pamoja na Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Kata, ndio wapo karibu sana na wananchi na ndio ambao wanatoa huduma karibu kabisa na wananchi. Watendaji wanapata mshahara lakini Wenyeviti hawapati chochote. Je, Serikali ina mpango gani kwa ajili ya kuwamotisha Wenyeviti ili waweze kutoa huduma vizuri kwa wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Spika, katika maeneo ambayo yamejengewa uwezo kwa hali ya juu kabisa ni hili eneo la Serikali za Mitaa. Kuna programu nyingi sana za kisekta zimeendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa nyakatii mbalimbali. Kuna Programu kwa mfano ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo, Programu ya Kuendeleza Sekta ya Maji, zote hizi zimekuwa na mafunzo mbalimbali kwa watendaji wa Serikali za mitaa kwa ajili ya kuimarisha uwezo wao, hasa hasa zile kada za fedha, ununuzi na wahandisi. Serikali inatoa commitment ya kuendelea kutoa mafunzo mara fedha zinapopatikana.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu posho za Wenyeviti wa Serikali za Vijiji na Vitongoji. Mwongozo uliopo ni kwamba kila Halmashauri inatakiwa iboreshe makusanyo yake ya ndani, iongeze makusanyo yake ya ndani na mwongozo uliopo ni kwamba asilimia 20 ya mapato yake ya ndani yanatakiwa yatumike kwa ajili ya posho na agizo ambalo limetolewa na kusisitizwa na Serikali ni kwamba wale ambao wanachelewesha kulipa posho za wenyeviti wa vijiji na vitongoji sasa itabidi wachukuliwe hatua.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wa Wilaya ya Kakonko kwa sasa wanapata huduma katika Kituo cha Afya cha Kakonko na kituo hicho kimezidiwa kwa sababu msongamano wa watu ni mkubwa. Kituo hicho kinahudumia wananchi kutoka hadi Mkoa jirani wa Kagera kwa maana ya wananchi wa Nyakanazi, Kalenge pia na wakimbizi kwa sababu katika Wilaya ile kuna kambi za wakimbizi, Waziri amesema kwamba mwaka 2017/2018 zimetengwa shilingi milioni 500.
Je, Waziri yupo tayari sasa kutokana na jinsi wananchi wanavyopata shida pamoja na waganga na wauguzi kwa sababu watu wakiwa wengi waganga nao wanachanganyikiwa, yupo tayari kufuatilia hizo shilingi milioni 500 ziweze kwenda mara moja Kakonko kwenda kuwasaidia wananchi? (Makofi)
Swali la pili; kwa wakati huu ambapo Wilaya ya Uvinza haina Hospitali ya Wilaya, wananchi wanapata huduma katika vituo vya afya na zahanati, lakini vituo hivyo vya afya pamoja na zahanati havina watumishi wa kutosha.
Je, katika mgao huu wa wafanyakazi ambao wataajiriwa kwa sasa, Serikali iko tayari kabisa kupeleka watumishi wengi wa kutosha kwenda kusaidia katika Wilaya ya Uvinza ambayo haina Hospitali ya Wilaya? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Genzabuke kwa jinsi ambavyo anafuatilia huduma hasa kwa wanawake katika Mkoa wa Kigoma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali lake la kwanza, napenda kumthibitishia kwamba fedha hizo ambazo zimetengwa kwenye bajeti ya 2017/2018 nitazifuatilia na kuzisimimamia mimi mwenyewe binafsi kuhakikisha kwamba zimekwenda haraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika swali la pili, wiki hii iliyopita tumekamilisha upatikanaji wa watumishi 2,008 ambao sasa hivi wanaendelea kugawanywa katika Halmashauri mbalimbali. Leo hii nitahakikisha kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza imepata watumishi wa kutosha angalau kwa mahitaji ya asilimia 50. (Makofi)
MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Sera ya Elimu Bure imewasaidia baadhi ya wazazi wasio na uwezo kuandikisha watoto shuleni, lakini wakati huo huo bado kuna michango kadhaa inayoendelea kwa baadhi ya shule na michango hii imerudisha nyuma morali ya wazazi kuchangia kwa juhudi katika maendeleo mbalimbali ya shule.
Je, Serikali ipo tayari sasa kutoa elimu kwa wananchi kwamba sera ni elimu bila ada na siyo elimu bure ili kuwafanya wananchi waweze kuchangia kwa nguvu kama ilivyokuwa zamani? (Makofi)
Swali la pili, shule za Sekondari za Keni, Shimbi na Bustani katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo ni shule ambazo zimejengwa kwa mtindo wa ghorofa kwa sababu ya uhaba wa ardhi katika Wilaya ya Rombo na sasa zina muda karibu wa zaidi ya miaka 10 wananchi wameshindwa kuzikamilisha.
Je, Serikali ipo tayari katika bajeti ijayo katika bajeti
ijayo kuzipokea hizi shule na kuzikamilisha ili kuweza kuunga mkono nguvu za wananchi katika jitihada zao za kufanya maendeleo mengine kama kumalizia maabara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS – TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubalina na Mheshimiwa Selasini kwamba kuna michango ambayo inaruhusiwa. Lakini michango ile ina utaratibu kwamba ili kusudi mchango uweze kukubalika kisheria ni lazima Kamati ya Shule au bodi ya shule iwe imeujadili na kupeleka kwa wadau ambao ni wazazi, wakipitisha wanaomba kibali kwa Mkuu wa Mkoa, wakipata kibali basi hapo wanaweza wakaendelea na kuchangishana. Huo ni utaratibu ambao ni mzuri, namshauri Mheshimiwa Mbunge autumie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa swali lake
la pili, sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na Wizara ya Elimu tupo tayari kukaa na Mheshimiwa Mbunge ili tuweze kujadili namna ambavyo tunaweza tukaboresha utaratibu wa kuzikamilisha hizi shule ambazo anazizungumzia. (Makofi)
MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naomba niulize swali dogo la nyongeza.
Hivi karibuni Naibu Waziri wa Elimu ametoa kauli akisema watoto wakitaka kuolewa wawe na cheti cha kumaliza form four, wakati huo huo Serikali ilisema wale wanafunzi ambao wanapata ujauzito wakiwa shuleni wasiendelee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ningependa nipate
kauli ya Serikali katika mkanganyiko huu, nini hasa ni kauli ya Serikali sahihi. Vipi wanafunzi ambao wanapata mimba wakiwa shuleni na hawaendelei kwa mfumo wa shule, lakini na kauli ya Waziri ya kusema anayetaka kuolewa awe na cheti cha form four? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS – TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) -MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa majibu sahihi kwa Mheshimiwa Waitara pamoja na Watanzania wote waliopata mkanganyiko kuhusu kauli hiyo ni kwamba, nilisema Sera Mpya ya Elimu ya mwaka 2014 huko tunakoelekea inabadilisha mfumo wa sasa wa elimu kwenda kwenye mfumo mpya ambao utahitaji mtoto aanze chekechea mwaka mmoja, asome shule ya msingi miaka sita, shule ya sekondari miaka minne na hii itakuwa ni lazima kwa yeyote atakayeanza darasa la kwanza hadi amalize form four. Kwa hiyo, nikasema kwamba tutakapofika wakati huo, kithibitisho muhimu kwamba huyu mtoto sasa amemaliza form four ni school leaving certificate, wakati huo siyo leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ndugu yangu Mheshimiwa Waitara huo ni ufafanuzi sahihi kabisa wa sera mpya. Sasa hivi tunaandaa utaratibu na maandalizi ikiwepo pamoja na miundombinu ili tuweze hatimae kuitekeleza hiyo sera muda utakapofika. Kwa hiyo, usiwe na mkanganyiko ndugu yangu Waitara. (Makofi)
MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mzuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi kuna tatizo limejitokeza, kuna Waraka unasema walimu wa arts ambao wamezidi katika shule za sekondari wanahamishiwa shule za msingi. Huu uhamisho unakuwaje ilhali Rais wetu alisema walimu wasihamishwe mpaka pale fungu lao litakapopatikana.
Je, hao walimu wameshaandaliwa mafao yao ya uhamisho ili waende kwenye vituo vyao vipya huku tayari Wizara imeshasema mpaka itakapofikia tarehe 15 Februari walimu hawa wawe wamefika vituoni kwao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, napenda kujua, huu uhamisho wa kuwatoa walimu wa arts kutoka sekondari kuwapeleka primary unaweza kuathiri ufundishaji wa wanafunzi wa huko primary. Je, Serikali imeandaa induction course kwa ajili ya walimu hawa ili waweze ku-coup na ufundishaji wa walimu wa primary? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): MheshimiwaMwenyekiti, swali la kwanza kwa wale wanaohusika ambao wamepata Waraka Rasmi wakiusoma vizuri watagundua kwamba maelekezo yaliyomo katika Waraka ule ni kwamba uhamisho unafanyika kutoka kwenye shule ya sekondari kwenda kwenye shule ya msingi ambayo iko karibu na eneo hilo, siyo kumtoa kwenye Wilaya moja kumpeleka Wilaya nyingine. Uhamisho ule ni wa ndani ya kata kwa hiyo hauna gharama za uhamisho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ule uhamisho kutoka shule za sekondari kwenda primary umezingatia kwanza kipaumbele kwa wale walimu ambao walijiendeleza, zamani walikuwa walimu wa shule ya msingi wakajiendeleza wakapata diploma na degree hatimaye wakahamishiwa katika shule za sekondari.
Kwa hiyo, kuwarejesha kwenye shule za msingi ambazo wana uzoefu nazo hakuhitaji induction course ya aina yoyote. Kwa hiyo, hicho ndiyo kipaumbele ambacho kimewekwa na kimezingatia walimu wa diploma na walimu wa degree ya kwanza. Ahsante.
MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nitoe masikitiko makubwa sana kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, ambapo tarehe 8 Juni, 2016 niliuliza swali kuhusu vijiji na kata hizo hizo na aliyekuwa Naibu Waziri na sasa ni Waziri mwenye dhamana TAMISEMI alinipa majibu ambayo yalikuwa yanaeleza kwamba vijiji hivyo vimetengewa bajeti ya shilingi milioni 49.5 ambayo itatekelezwa mwaka 2016/2017. Mpaka sasa hivi hakuna kinachoendelea, ni Bunge hili hili ambalo linatoa majibu hayo na leo tena nimepewa asilimia hiyohiyo 49.5 kwamba itatekelezwa 2018/2019. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu, ni lini Serikali itapeleka pesa kwa wananchi hawa, toka mwaka 1995 mpaka leo ni upembuzi yakinifu unafanyika, ni lini hawa wananchi watapata maji? (Makofi)
MheshimiwaMwenyekiti, swali la pili, ni kwa nini hawakufanya upembuzi wa kina wakati bajeti ilitengwa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye jibu langu la msingi, ni kweli kwamba usanifu wa kina haukufanyika ule wa zamani, lakini kwa sasa tunatarajia usanifu kina utafanyika mwaka 2018/2019 kwa ajili ya utekelezaji wa kumaliza kabisa matatizo ya maji kwenye maeneo hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ambalo lilikuwa ndiyo la kwanza, ni kwamba kazi ambazo zimefanyika kuanzia 2016 mpaka Desemba, 2017 nimesema hapa kwamba tumejenga visima sita katika Kata za Magulilwa, Luhota, Maboga na Mgama. Hii kazi imefanyika na taarifa hizi zimetoka kule kule kwenye Halmashauri yake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, taarifa za kina zaidi namuomba sana tushirikiane naye baada ya kikao hiki ili tuweze kushauriana vizuri namna bora ya kuhakikisha kwamba tunamaliza matatizo ya wananchi kwenye maeneo hayo.
MHE. MAFTAHA A. NACHUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Kakunda, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kumekuwa na malalamiko mengi sana kwa Wakazi wa Dodoma wakiwemo Wabunge na Taasisi mbalimbali za Kiserikali kwamba ili waweze kupata huduma ya ardhi Manispaa ya Dodoma, basi kuna mzunguko mkubwa sana na mlolongo mkubwa sana.
Je, Serikali ipo tayari hivi sasa kufanya uchunguzi maalum na kuchukua hatua kwa kuwa, sasa Manispaa ya Dodoma ni Mji Mkuu kwamba tunahitaji huduma hizi ziende kwa haraka? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, zipo Taasisi za Serikali ambazo zinahamia Dodoma hivi sasa, zinataka kujenga ofisi zao hapa Dodoma, lakini bado kumekuwa na urasimu mkubwa sana taasisi hizo kupewa ardhi pale Manispaa.
Je, Serikali ipo tayari hivi sasa kuweka utaratibu maalum ili Taasisi hizi za Kiserikali ama Taasisi za Umma ziweze kupewa maeneo ya kuweza kujenga ofisi zao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Maftaha Abdallah Nachuma na ndiyo maana wakazi wa Kusini wanamwita mashine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mlundikano wa kazi uliokuwepo katika kipindi hiki cha awali cha utekelezaji wa majukumu mapya ya kuunganisha majukumu ya iliyokuwa Manispaa ya Dodoma na ile iliyokuwa CDA ndio umefanya kuwe na baadhi ya malalmiko katika hatua za awali za utekelezaji wa kazi, kwa sababu kulikuwa na migogoro mingi sana ya viwanja, mahitaji ya kubadilisha mikataba mingi sana na hapo hapo kuna mahitaji ya kuendelea kupima maeneo mapya. Kwa hiyo, haya matatizo ambayo Mheshimiwa Maftaha ameyataja ni matatizo ya mpito tu ambayo yatarekebishwa hivi karibuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa swali lake la pili, hadi sasa Manispaa imepima viwanja 1,288 na ambavyo tayari hati zake zimetayarishwa. Maeneo ambayo ni Mji Maalum wa Serikali yamepimwa viwanja 147, ikiwemo Ikulu, Wizara zote zimepatiwa hati na vilevile taasisi za umma na viwanja vya mabalozi 64.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nakuonesha hati ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni hii hapa, tayari imepatikana na ipo Ofisini. Wizara zote zina hati kama hii. Taasisi zote za umma ambazo zinahitaji ardhi, waende Manispaa pale watapewa hati zao ambazo zitawawezesha kupata maeneo ya kuweza kujenga ofisi zao haraka sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile katika maeneo ya Nala wamepima viwanja 922 na kiwanja cha michezo cha Nzuguni kimepimwa, kile ambacho tulipata msaada kutoka Morocco na viwanja 218 katika maeneo mengine.
Waheshimwa Wabunge na wananchi kwa ujumla wanakaribishwa waombe viwanja Manispaa na mimi kama msimamizi wa Manispaa hiyo, nawaahidi kwamba watakuwa wamepata hati kabla ya mwisho wa mwezi huu wa pili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo limepimwa viwanja vya Serikali ni hili hapa na naweza nikalionyesha Waheshimiwa Wabunge waweze kuliona. Kazi imefanyika vizuri. (Makofi)
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Dodoma sasa hivi ni Makao Makuu ya nchi na Manispaa wameongezewa jukumu lingine la ardhi ambalo lilikuwa la CDA, lakini kuna upungufu mkubwa wa vitendea kazi pale Manispaa hasa ile Idara ya Ardhi pamoja na watendaji ni wachache kiasi kwamba ukienda pale bado kuna watu wengi wanakaa kwenye foleni kwa muda mrefu.
Serikali sasa kwa kutambua kwamba Dodoma ni Makao Makuu, imejipangaje kuhakikisha kwamba Manispaa ya Dodoma inawezeshwa kwa vitendea kazi, miundombinu pamoja na watendaji wa kutosha ili wafanye kazi kwa weledi na kwa haraka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kupata nguvu kazi ya kutosha kutoka kwenye ile iliyokuwa CDA, ni kweli kwamba bado kuna mahitaji ya watumishi na baadhi ya vitendea kazi na hivyo vinafanyiwa kazi mpaka mwezi wa sita, matatizo mengi yatakuwa yamekamilika.