Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mwantakaje Haji Juma (13 total)

MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza:-
Jeshi la Wananchi la Tanzania (JWTZ) limekuwa tegemeo kwa nchi hususan katika masuala ya kiulinzi nchini:-
Je, ni lini Serikali itawapatia nyumba bora za makazi askari wa Jeshi hilo, hasa ikizingatiwa nyumba zilizopo hazitoshi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ina nia ya kuliboresha Jeshi kwa vifaa, zana na miundombinu ikiwa ni pamoja na nyumba za makazi ya wanajeshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali imechukua hatua ya kupunguza mahitaji makubwa ya nyumba kwa wanajeshi kwa kuanzisha mradi wa ujenzi wa nyumba 10,000.
Awamu ya kwanza ambayo utekelezaji wake umeshaanza, zinajengwa nyumba 6,064 katika kambi mbalimbali nchini. Katika awamu ya pili tunatarajia kujenga nyumba 3,034 kwa ajili ya askari wa ngazi ya kati na Maafisa. Pamoja na mradi huu, Serikali itaendelea kutenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya ukarabati wa nyumba zilizopo ili kupunguza uhaba wa makazi kwa wanajeshi.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza:-
Zanzibar vipo vikundi vya VICOBA ambavyo usajili wake ni lazima waje Tanzania Bara kufanya usajili:-
(a) Je, ni lini Serikali itaanzisha Ofisi Tanzania Zanzibar ili kuweka unafuu kwa wananchi wa Zanzibar?
(b) Je, gharama za usajili wa VICOBA ni kiasi gani?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Bububu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, VICOBA ni vikundi ambavyo vimekuwa vikiundwa na wananchi ili kupambana na changamoto ya ukosefu wa huduma ya kifedha, hususan wananchi wa kipato cha chini na wale waishio mbali na huduma rasmi za kifedha. Vikundi hivi kwa sehemu kubwa vimekuwa vikiundwa na kusimamiwa na taasisi zisizo za Serikali kama vile NGOs, CBOs na kadhalika. Kwa maana hiyo, taratibu za uratibu, uhamasishaji, usajili na malezi ya vikundi hivyo hufanywa na NGO‟s au CBO‟s.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali haina mwongozo maalum kwa sasa kwa usajili wa vikundi vya VICOBA. Hivyo basi, baadhi ya vikundi vya VICOBA kutoka Zanzibar hufuata usajili Tanzania Bara ili kukidhi matakwa ya taasisi zinazowaongoza, hususan NGOs na CBOs. Aidha, kwa kutambua mchango mkubwa wa vikundi hivyo katika kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira na huduma za kifedha katika baadhi ya maeneo na makundi maalum, Serikali imetoa fursa kwa vikundi hivyo kusajiliwa BRELA pamoja na Halmashauri za Wilaya.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Zanzibar Ofisi za Ushirika zinasajili VICOBA kama Vyama vya Kuweka na Kukopa vya Awali kwa makubaliano kwamba, VICOBA hivyo vitakua na hatimaye kubadilishwa kuwa SACCOS kamili.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha mapitio ya marekebisho ya Sera ya Huduma Ndogondogo za Kifedha na Sheria yake Tanzania Bara na Sera ya Huduma Ndogondogo za Kifedha kule Zanzibar zinazotarajiwa kuweka mwongozo rasmi wa usajili wa VICOBA na uendeshaji wake. Mapendekezo ya marekebisho ya sera yanasubiri kupangiwa tarehe ya kujadiliwa na kupitishwa na Baraza la Mawaziri wakati wowote kuanzia sasa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za usajili wa vikundi vya VICOBA zinatofautiana kutegemeana na mamlaka zinazowasajili. Mfano, ada ya usajili chini ya NGOs ni sh. 150,000 na Halmashauri za Wilaya ni kati ya sh. 30,000 na sh. 70,000. Viwango vya ada ya usajili chini ya Halmashauri za Wilaya vinatofautiana kwa kuwa hakuna mwongozo maalum, kama nilivyosema hapo awali, unaopaswa kuzingatiwa na Halmashauri zote.Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kwa upande wa BRELA ada za usajili zinatofautiana kulingana na mtaji wa kikundi husika. Mfano ada ya usajili kwa kikundi chenye mtaji usiozidi sh. 5,000,000 ni sh. 10,000; kati ya sh. 5,000,000 na 10,000,000 ni sh. 20,000 na kati ya sh. 10,000,000 na sh 50,000,000 ni sh. 50,000.
MHE. KHADIJA NASSIR ALI (K.n.y MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA) aliuliza:- Zanzibar kumekuwa na matukio ya uhalifu yanayojitokeza mara kwa mara. Je, Serikali ina mpango gani wa kuzuia vitendo vya uhalifu visijitokeze Zanzibar?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Bububu kamaifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mipango ya muda mfupi, kati na mrefu wa kukabiliana na wahalifu na uhalifu ndani ya mipaka ya nchi yetu. Mikakati iliyopo ni pamoja na:- (i) Kuwajengea uwezo wa utendaji kazi askari wote ili wawe na uwezo wa kubaini, kupeleleza na kufuatilia mitandao ya kiuhalifu hapa nchini. (ii) Kufanya misako na doria za miguu, pikipiki na magari ili kubaini na kuzuia hali zozote za kihalifu zinazoweza kujitokeza. (iii) Kuimarisha ulinzi maeneo ya mipaka yote ikiwemo ya maji ili kuzuia uhalifu. (iv) Kuimarisha kikosi cha kuzuia na kupambana na madawa ya kulevya cha polisi sambamba na madawati ya Mikoa na Wilaya kwa kushirikiana na Mamlaka ya Taifa ya Kudhibiti Dawa za Kulevya.
(v) Kuimarisha ushirikiano baina ya Jeshi la Polisi na taasisi nyingine nchini hasa vyombo vya ulinzi na usalama. Mheshimiwa Mwenyekiti, yakifanyika haya pamoja na mambo mengine vitendo vya uhalifu na wahalifu vitapungua nchini ikiwemo na Zanzibar.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza:-
Kumekuwa na wimbi la mabweni na hata shule kuungua moto, hususan Tanzania Bara. Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti hali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Bububu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kulikuwa na wimbi la shule kuungua moto na mwaka 2016 pekee kuanzia mwezi Januari hadi Disemba nchi ilikuwa na janga kubwa la kuunguliwa na shule za sekondari 29, zikiwemo mbili zisizo za Serikali na shule za msingi mbili ikiwemo moja isiyo ya Serikali.
Matukio hayo yalitokea mfululizo na hata shule nyingine kukumbwa na tatizo hilo zaidi ya mara moja. Mbaya zaidi, katika mwezi wa Agosti, 2016 kasi ya matukio ya shule kuungua moto iliongezeka ambapo kati ya tarehe Mosi hadi 12 Agosti, 2016 jumla ya shule za sekondari za Serikali tano ziliungua. Tumeshukuru Mungu mwaka 2017 matukio haya ya moto hayajatokea tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa hakuna uhakika wa chanzo halisi cha matukio haya moto yanayojitokeza. Hata hivyo, inadhaniwa kuwa chanzo cha moto hususan katika shule kongwe ni hitilafu ya umeme iliyotokana na uchakavu wa miundombinu na hujuma kutoka kwa watu na vikundi visivyo na nia njema.
Mheshimiwa Naibu Spika, majanga ya moto katika shule zetu yanaweza kudhibitiwa ikiwa wote kwa pamoja tutashirikiana kutambua na kudhibiti viashiria na vyanzo ambavyo huleta majanga hayo. Serikali imetoa maelekezo kwa Mikoa, Halmashauri na wadau wengine wa elimu ili kudhibiti majanga ya moto mashuleni ikiwa ni pamoja na uundwaji wa Kamati za kukabiliana na majanga katika ngazi ya Halmashauri na katika ngazi za shule husika kwa kushirikisha wadau muhimu wa elimu katika ngazi mbalimbali.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza:-
Tanzania imeweka nafasi maalum za uwakilishi wa wanawake katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa makundi ya walemavu, wasomi, vijana na wanawake:-
Je, ni lini Serikali itatunga sheria itakayozilazimisha taasisi za Serikali kutenga nafasi maalum za ajira kwa Watu Wenye Ulemavu ili nao wasiendelee kujisikia kama wategemezi katika jamii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma Mbunge wa Bububu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ni kielelezo cha utu. Kufanya kazi kunamwezesha mwanadamu kujitegemea hivyo kupata heshima katika jamii. Kutokana na hilo Serikali imefanya jitihada za kutunga Sera ya Taifa ya Maendeleo na Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu ya Mwaka 2004 kwa lengo la kuleta maendeleo, haki na heshima kwa watu wenye ulemavu. Aidha, mwaka 2010 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya Watu wenye Ulemavu Na. 9 ya Mwaka 2010. Sheria hii inatoa mwongozo wa kisheria wa namna ya kutoa huduma mbalimbali kwa watu wenye ulemavu ikiwemo ajira.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa upande wake imeendelea kusimamia utekelezaji wa Sheria hii kwa kuziagiza Taasisi za Serikali na Binafsi kuajiri watu wenye lemavu wenye sifa sawia kila inapohitajika, hivyo tumeendelea kufanya kaguzi kwa kuwatumia Maafisa Kazi ili kuhakikisha kuwa utekelezaji wa sheria hii unafanyika ipasavyo. Aidha, Serikali imeendelea kusimamia upatikanaji wa ujuzi na sifa linganifu kwa watu wenye ulemavu ili waweze kuajirika na kujiajiri kiurahisi kwa kutoa mafunzo kupitia vyuo vya ufundi na vyuo vingine kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na jamii kuamini kuwa watu wenye ulemavu hawawezi kufanya baadhi ya kazi imepelekea baadhi ya waajiri kutowaajiri Watu Wenye Ulemavu. Hivyo naomba nichukue nafasi hii kuagiza waajiri wote nchini kuzingatia sheria kila inapotokea nafasi za ajira zinazoweza kufanywa na Watu Wenye Ulemavu na wamefikia viwango vya sifa zinazotakiwa naomba tuwape kipaumbele.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza:-
(a) Je, ni lini Serikali itawapatia gari lingine Kituo cha Polisi Magharibi ‘A’ ili kupunguza matumizi ya magari binafsi kwa Jeshi la Polisi?
(b) Je, Serikali imejipanga vipi kupunguza uhalifu unaojitokeza mara kwa mara?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Bububu lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua tatizo la upungufu wa vitendea kazi katika Jeshi la Polisi hususan magari ya doria kote nchini ikiwemo Bububu. Kwa kuzingatia umuhimu wa doria katika kudhibiti masuala ya usalama wa raia, Serikali inaendelea kuongeza idadi ya magari na vitendea kazi vinginevyo kadiri hali ya uchumi inavyoruhusu. Mpango ya Jeshi la Polisi ni kupeleka gari moja katika Wilaya ya Magharibi ‘A’ mara baada ya kupokea magari mapya katika siku za hivi karibuni.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeendelea kutekeleza jukumu lake la msingi la ulinzi wa raia pamoja na mali zao ili kuhakikisha wananchi na mali zao wanakuwa katika hali ya usalama. Katika kutekeleza jukumu hilo ipo mikakati mbalimbali ambayo imetekelezwa ikiwa ni pamoja na kufanya doria na operesheni za mara kwa mara, kutoa elimu kwa jamii ili kuwajengea uwezo wa kutambua matendo yanayoashiria uhalifu na kutoa taarifa polisi kwa lengo la kuchukua hatua kabla uharibifu kufanyika. (Makofi)
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza:-
Kituo cha Polisi Bububu ni kikongwe sana na pia kimechakaa sana na kinahitaji ukarabati mkubwa. Je, ni lini kituo hicho kitafanyiwa ukarabati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, na mimi naomba niungane na Waheshimiwa wengine kumshukuru Mwenyezi Mungu kukujalia kuungana na sisi leo ukiwa mzima. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Bububu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uchakavu wa vituo vya polisi vikongwe nchini kikiwemo Kituo cha Polisi cha Bububu. Jeshi la Polisi lina mpango wa kuvikarabati vituo hivyo kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Aidha, ukarabati wa vituo hivyo vya Polisi kikiwemo Kituo cha Polisi Bububu utafanyika ili kuboresha mazingira ya kazi kwa askari wetu ili kuwawezesha kutoa huduma bora kwa wananchi. (Makofi)
MHE. FAKHARIA SHOMAR KHAMIS (K.n.y. MWANTAKAJE HAJI JUMA) aliuliza:-
(a) Je, ni lini Serikali itawapatia mtaji na kuwawezesha kiuchumi wananchi wengi ambao wamejiunga katika vikundi vya uvuvi?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia vifaa vya kisasa ili kuondokana na vifaa haramu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Bububu, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeweka mazingira mazuri kwa wavuvi kupata mikopo ya masharti na riba nafuu kutoka katika Benki ya Maendeleo ya Kilimo na kupitia Dirisha la Kilimo katika Benki ya Rasilimali. Mikopo hiyo itawezesha wavuvi kununua zana bora za uvuvi. Pia, Serikali inaendelea kuwahimiza wavuvi kujiunga katika vikundi na kuanzisha Vyama vya Ushirika vya Msingi, Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) na VICOBA ili waweze kukopesheka na kuweza kununua zana na vyombo bora vya uvuvi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hairuhusu matumizi ya vifaa haramu kwenye uvuvi kwa mtu yeyote kwa mujibu wa Sheria ya Uvuvi Na. 22 ya Mwaka 2003 na Kanuni zake za mwaka 2009 na sheria nyingine za nchi. Aidha, Serikali imefuta Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwenye injini za kupachika, nyuzi za kushonea nyavu, nyavu za uvuvi na vifungashio kwa kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2011 na Sheria ya Mamlaka ya Mapato ili kuwasaidia wavuvi kupata zana za uvuvi kwa bei nafuu. Pia, Serikali inaendelea kuwahamasisha wavuvi kujiunga kwenye Mifuko ya Huduma za Kijamii ukiwemo Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambao umeanzisha utaratibu unaojulikana kam Wavuvi Scheme ili kuwawezesha wavuvi kupata huduma za kijamii zinazotolewa na mfuko huu, kama vile huduma za afya pamoja na kupewa malipo ya uzeeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatoa ruzuku kwenye injini za kupachika ambapo Kikundi/Chama cha Ushirika cha Wavuvi kinatakiwa kuchangia asilimia 60 na Serikali asilimia 40 ya gharama. Aidha, Serikali inahamasisha sekta binafsi kujenga viwanda vya kutengeneza boti na zana bora za uvuvi ili kuwezesha wavuvi kuzipata kwa bei nafuu na kwa urahisi. (Makofi)
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza:-
Zipo benki zinazotoa mikopo ya kilimo hususan Benki ya Kilimo Tanzania:-
Je, kwa upande wa Zanzibar ni wananchi wangapi wanaofaidika na mikopo ya kilimo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti,kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Bububu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya wananchi walionufaika na mikopo inayotolewa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania kwa wananchi wa Zanzibar hadi kufikia tarehe 31 Julai, 2018 ni 3,000. Kati ya hao wanaume ni 1,800, wanawake 900 na vijana wa kike na kiume ni 300. Aidha, jumla ya mikopo iliyotolewa kwa idadi hiyo ya wananchi wa Zanzibar hadi kufikia tarehe 31Julai, 2018 ni shilingi bilioni 6.50.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza:-

Wananchi wengi wamekuwa wakiathirika kisaikolojia:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga vituo vya ushauri nasaha.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Bubu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwa wananchi wengi wamekuwa wakiathirika kisaikolojia kutokana na matukio na changamoto mbalimbali za maisha ikiwemo magonjwa, umaskini wa kipato, kufiwa, ukosefu wa ajira, kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji, ukatili na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwapatia huduma watu walioathirika kisaikolojia imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kuhakikisha uwepo wa wataalam wa kutosha wa kutoa huduma ya ushauri wa Kisaikolojia. Kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Serikali imeajiri Maafisa Ustawi wa Jamii katika Halmashauri zote 185, kwa baadhi ya Halmashauri nyingine Maafisa hao wako hadi katika ngazi ya Kata. Lengo la Serikali ni kuwa na Maafisa Ustawi wa Jamii hadi ngazi ya Kata katika Halmashauri zote ili wananchi waweze kufikiwa na kupata huduma kwa urahisi na kwa haraka ili kuwaondolea athari zitokanazo na matatizo ya kisaikolojia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha wananchi wenye matatizo ya kisaikolojia wanaata huduma zenye kiwango cha ubora, Serikali imeandaa mwongozo wa utoaji msaada wa kisaikolojia wa kijamii kwa watoto walio katika mazingira hatarishi na vijana wa mwaka 2014 (The National Guideline for Psychosocial Care and Support Services for MVC and Youth 2014), na mwongozo wa Utoaji wa Msaada wa Kisaikolojia na Jamii (The National Guideline for Provision of Psychosocial Care and support Services of 2019) pamoja na taratibu za uendeshaji (Standard Operating Procedure (SOP). Pia Maafisa Ustawi wa Jamii na Wataalam wengine wameendelea kujengewa uwezo katika eneo hili la utoaji wa Msaada wa Kisaikolojia na Kijamii ili waweze kutoa huduma bora na kwa weledi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua fursa hii kusisitiza wananchi watumie wataalam wetu wa Ustawi wa Jamii waliopo katika Ofisi ya Halmashauri ili waweze kupata huduma za ushauri wa kisaikolojia. Aidha, Serikali itaendelea kuajiri wataalam kadri inavyowezekana ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hii muhimu.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakifanyia ukarabati Kituo cha Polisi Bububu ambacho ni chakavu sana?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI Alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Jimbo la Bububu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uchakavu wa Kituo cha Polisi Bububu na tayari tathmini kwa ajili ya ukarabati imefanyika mwezi Mei, 2021 na fedha kiasi cha shilingi 33,172,200 zinahitajika kwa ajili ya kubadilisha paa, mfumo wa umeme, mfumo wa maji taka na maji safi, pamoja na kupaka rangi. Aidha, Serikali inatafuta fedha za ukarabati wa kituo hicho ikiwa ni pamoja na vituo na makazi ya askari ya maeneo mengine ambayo yanafanyiwa tathmini kwa ajili ya ukarabati. Ahsante.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatoa mafunzo kwa makundi ya vijana na wanawake wanaopata mikopo ili waweze kujiwezesha kiuchumi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKAO NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma Mbunge wa Jimbo la Bububu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Kanuni ya 23 ya Kanuni za Utoaji na Usimamizi wa Mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu Wenye Ulemavu pamoja na marekebisho yake, Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeelekezwa kutenga fedha kutoka katika fedha za marejesho ya mikopo hiyo kwa ajili ya kuwajengea uwezo pamoja na ufuatiliaji wa shughuli za vikundi kwa vikundi vilivyokubaliwa kupata mikopo.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 jumla ya vikundi 6,317 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika halmashauri zote nchini vimepatiwa mafunzo kuhusu masuala ya uongozi, usimamizi wa fedha, uendeshaji wa miradi na utoaji wa taarifa.
MHE. MWANTAKAJE HAJI JUMA aliuliza:-

Je, lini Kituo cha Polisi Bububu pamoja na nyumba za Askari vitafanyiwa ukarabati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantakaje Haji Juma, Mbunge wa Jimbo la Bububu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi imepanga kukarabati Kituo cha Polisi cha Bububu kwa awamu. Kwa awamu ya kwanza Serikali inakarabati hanga la kuishi familia 18 za askari ambalo linagharimu shilingi 19,358,450 na kwa sasa umefikia katika hatua ya umaliziaji. Baada ya awamu hii, Serikali imepanga kutumia shilingi 46,000,000 kukarabati kituo hicho pamoja na nyumba za askari katika mwaka wa fedha 2024/2025, nakushukuru.