Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Oliver Daniel Semuguruka (3 total)

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Kwanza kabisa napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa mahali hapa katika Bunge lako Tukufu. Pia napenda kumpongeza Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayozidi kuifanya. Mimi binafsi namwombea kwa Mwenyezi Mungu aendelee kumpa nguvu tele aendelee kutumbua majipu. Ewe Mwenyezi Mungu msaidie Rais wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa kazi nzuri wanazozifanya kwa kulitumikia Taifa letu kwa moyo wa dhati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia napenda kuwashukuru akinamama wa Mkoa wa Kagera kwa kunipigia kura nyingi za kutosha ili niweze kuwawakilisha katika Bunge lako Tukufu. Nawaahidi kwa moyo wangu wa dhati sitowaangusha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze moja kwa moja katika mchango wangu katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambayo ni Wizara nyeti inayotegemewa na watu wengi. Mkoa wa Kagera tumebarikiwa kuwa na ardhi nzuri yenye rutuba na hali ya hewa nzuri yenye mvua za kutosha. Mkoa wa Kagera kilimo kimekuwa cha kusuasua kwa sababu ya teknolojia duni pamoja na pembejeo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kagera pembejeo hazifiki kwa wakati, unakuta mkulima ameshaandaa shamba lake kwa muda mrefu lakini kupata mbolea au mbegu bora kwa muda unaotakiwa imekuwa ni changamoto kwani mbolea haifiki wala mbegu. Kwa hiyo, naomba Serikali yako Tukufu iweze kuliangalia hilo. Pia kuna miundombinu mibovu ya usafiri wa mazao kutoka shambani hadi kwenye masoko, hilo pia naomba liangaliwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Kagera tuna zao kuu ambalo ni mgomba (ndizi). Zao hilo limevamiwa na ugonjwa unaitwa mnyauko hasa kwa Wilaya za Ngara, Karagwe, Muleba na Bukoba Vijijini. Ugonjwa huo wa mnyauko umeshambulia sana migomba. Tunaomba Wizara husika iweze kuangalia jinsi itakavyoweza kutusaidia kutibu ugonjwa huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wangu wa Kagera umebarikiwa kuwa na mazao makuu mawili ya biashara nayo ni kahawa na miwa. Kuhusu kahawa masoko yamekuwa ya kusuasua, imefika hatua wakulima wanapata shida, wanaanza kukata tamaa ya kulima zao la kahawa kwa kukosa soko. Unakuta wanaanza kufanya magendo ya kwenda kuuzia nchi jirani ili wapate unafuu wa bei. Tunaomba Wizara husika iangalie zao letu la kahawa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu zao la miwa, Mkoa wa Kagera pia umebarikiwa kuwa na Kiwanda kikubwa cha Sukari. Hata hivyo, nashauri wale wakulima wadogo wadogo waweze kusaidiwa kuwapa mashamba darasa ili waweze kuungana na wale wenye mashamba makubwa ili tuweze kupata viwanda vya kutosha vya sukari.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba niongelee kuhusu mifugo. Mkoa wa Kagera una mgogoro kati ya Ranchi ya Kitengule na wananchi. Wananchi hawana sehemu ya kufugia mifugo yao, tunaiomba Serikali kushughulikia mgogoro huo haraka iwezekanavyo. Kagera tuna mifugo ya kutosha, inakadiriwa kuwa na ng‟ombe wanaofugwa wapatao 550,070, ng‟ombe wa asili wanakadiriwa kuwa 528,632 na ng‟ombe wa maziwa 21,438, mbuzi wafugwao wanakadiriwa kuwa 593, 607, mbuzi wa asili wanakadiriwa kuwa 583,202 na mbuzi wa maziwa 10,405. Wanyama wengine ni kondoo 53,061 na nguruwe 44,402. Ikitumiwa vizuri na Serikali itasaidia sana ukuaji wa uchumi Mkoa wa Kagera na Taifa kwa ujumla. Kwani itachochea ujenzi wa viwanda vya mazao ya mifugo na kutoa fursa za ajira kwa wananchi walio wengi hususani vijana.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kuongelea upande wa uvuvi. Usalama wa wavuvi siyo mzuri katika Mkoa wetu wa Kagera. Maharamia wanavamia sana wavuvi wanaokuwa ziwani wakivua samaki. Tunaomba Serikali iweke doria ili wavuvi wetu waweze kuwa katika security. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu leseni, nashauri wasitoze zaidi ya mara moja. Unakuta mvuvi yupo Bukoba Mjini akiamua kwenda Muleba akifika pale kuna leseni tena anatakiwa alipie. Tunaomba leseni iwe moja ili waweze kuzunguka kwa unafuu zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali yako iangalie kuhusu nyavu. Wavuvi wadogo hawana makosa kununua hizo nyavu, washughulikiwe wale wanaoziingiza ili wapate zinazokubalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba Serikali yako kwa hiyo shilingi milioni hamsini ambayo inatarajiwa kutolewa iangalie na wavuvi. Hiyo shilingi milioni hamsini imezungumziwa sana upande wa akinamama na vijana lakini kwa wavuvi sijasikia. Naomba pia wavuvi wakumbukwe, wana vikundi vyao nao wagawiwe hela hiyo ili waweze kujiongeza katika uchumi wao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haya machache naunga mkono kwa asilimia mia moja bajeti ya Wizara ya Kilimo iweze kupita.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kunipatia nafasi. Awali ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii na kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa najikita katika Sheria ya Mtandao iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu mwaka jana. Naona hii sheria haijafahamika vizuri kwa wananchi, nilikuwa naomba Serikali iweze kufuatilia kwa undani zaidi utumiaji wa hii Sheria ya Mitandao. Je, ni lini Wizara yako itatoa elimu ili watu waielewe hii Sheria ya Mitandao, maana mitandao inatumika ndivyo sivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba pia kuhusu simu. Ni lini simu zitakuwa na rate moja? Kwa mfano, mtandao wa Vodacom au Airtel na Tigo kuwa na rate moja? Nilikuwa naomba pia Serikali iweze kulingalia hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mkongo wa Taifa umeenea nchi nzima, lakini internet inasumbua sana, baadhi ya maeneo ni shida. Unaweza uka-download kitu kwa muda wa masaa mawili, document. Labda una haraka sana ya kwenda sehemu unataka document uwasilishe sehemu, lakini inakuwa ni shida, nini maana ya kuweka Mkongo wa Taifa zima?
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia network kwa vijijini imekuwa shida sana. Mtu unaenda vijijini unabeba simu tatu, atleast, upate communication. Unabeba labda simu ya Vodacom, Airtel na TTCL, hapo pote unatafuta communication. Nilikuwa naomba pia, hili iweze kuliangalia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najikita moja kwa moja katika SUMATRA. Mara nyingi tunasikia SUMATRA ikidhibiti nauli za mabasi na treni, lakini kwenye nauli za ndege hakuna kudhibiti, ukiuliza unaambiwa inategemea soko kwa kuwa ni huria. Mbona basi ni huria na inazidhibitiwa? Unakuta ndege, kila ndege ina nauli yake, unakuta FastJet ina nauli yake, ATCL ina nauli yake, kila ndege ina nauli yake. Tulikuwa tunaomba na hili nalo muweze kuangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa Kagera Airport. Kagera tuna Kagera Airport, lakini pia Ngara tuna uwanja wa ndege unaitwa Luganzo Airport. Huo uwanja wa Luganzo ulishasahaulika kabisa, hata hauongelewi katika Ilani ya CCM sijawahi kuona. Ule uwanja ulitumika sana kipindi cha wakimbizi, ndege zote za UN tulikuwa tunatumia pale. Na mimi ni mmoja wapo nilikuwa nafanya kazi UN, ndio tulikuwa tunatumia hata kuleta mizigo, cargo zote za wakimbizi zilikuwa zinatumia huo uwanja, lakini uwanja umesahaulika kabisa. Tunaomba Wizara hii iweze kuangalia ule uwanja wa Luganzo kama Serikali inaweza ikaanza kuutumia ili hata wawekezaji wa ndege waweze kutumia ule uwanja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, najikita pia katika ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma. Watumishi wa umma wana tatizo la makazi kutokana na uhaba wa nyumba za Serikali. Unakuta mtumishi wa Serikali amehamishwa kutoka kituo kimoja kwenda kingine, anakaa hotelini muda mrefu sana, hapa hela za Serikali zinazidi kutumika. Kabla ya kuhamishwa kwa nini asitafutiwe nyumba ili Serikali kuweza kuangalia hizo hela zisiende bure. Nyumba hazina hadhi bora kwa…
MWENYEKITI: Ahsante.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naunga mkono hoja asilimia mia moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna matatizo mengi kwa wananchi hasa wakazi wa maeneo ya karibu na hifadhi. Wananchi wanataka kulima na kufuga, maeneo wanayoishi yamejaa, hayawatoshi. Wanaona kuna eneo jirani miaka yote lipo wazi na lina rutuba nzuri ya kilimo, wanaingia kulima na kufuga, wanakamatwa na kufunguliwa mashtaka ya uvamizi wa Hifadhi ya Taifa. Nini maana ya neno hifadhi ya Taifa maana isijekuwa inatumika sivyo. Hifadhi haina zuio lolote la mipaka inayojulikana kwa kijiji ikiwamo vibao vya kutambulisha hifadhi au fence.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hifadhi haina hata wanayamapori; kama ni hifadhi ya ardhi kwa wananchi kuitumia baadae basi ijulikane ni kwa matumizi yapi na hiyo baadae labda ndio imefika sasa kwa maana hifadhi nyingi za aina hiyo zimetengwa tokea ukoloni na zingine ni zaidi ya miaka 40. Je, Serikali ina mipango gani ya kutambulisha maeneo ya uhalisia wa leo na mwaka ulioanza kuwa hifadhi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utalii; utalii unajulikana kwa matangazo. Tanzania ni nchi ya pili duniani kwa vivutio vya utalii ya kwanza ikiwa ni Brazil, lakini ni nchi inayopata watalii wachache sana kulinganisha na nchi zenye vivutio vichache. Watalii milioni moja tu wakati vivutio kibao, amani na utulivu inakuwaje nchi kama Misri yenye tatizo la usalama inapata watalii zaidi ya milioni ishirini kwa mwaka? Nchi kama Mauritania yenye vivutio vichache mno nayo inatushinda? Je, Wizara kweli inafanya matangazo? Makampuni ya utalii yanajihusishaje na kuuza utalii? Tunayo kweli makampuni ya utali maarufu ya kimataifa? Tunahitaji kuona utalii ukitangazwa kila kona.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Ndege ni zao kubwa la utalii. ATCL haipo Kimataifa; ni nini mipango ya Serikali kufanya biashara ya utalii na ATCL kwa makampuni ya utalii kuwa na hisa ATCL? Ushauri wangu kwa Wizara ni kuhamasisha bidhaa za Tanzania hasa kazi za mikono kuuzwa kwenye maduka ya airports kubwa kama London - Heathrow, Schiphol - Amsterdam, Frankfurt - German na kadhalika. Jina Tanzania lionekane kila sehemu, linakuza hamu ya watu kuja kufanya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia unaweza kufanya mikakati ya kuandaa vijana 100 kwenye miji mikubwa yenye watalii na kumvalisha nguo zenye maandishi ya Tanzania huku wakishikilia mabango na kuzunguka mitaani. Vijana hao wanalipwa ujira mdogo tu. Wizara ihakikishe jina Tanzania linasikika kila kona ya dunia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kodi zinazotozwa kwenye hotels za kitalii ni kubwa au ni hotels zenyewe maana hotels ni ghali sana ikiwemo chakula. Watalii wengi wanaokuja nchini ni wale ambao wamejibana kwa muda mrefu hivyo kutokuwa na pesa nyingi kutosheleza matumizi makubwa. Tuweke bei nafuu kuvutia watalii kuja nchini kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.