Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Oliver Daniel Semuguruka (14 total)

MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:-
Mkoa wa Kagera umezungukwa na nchi za Rwanda, Burundi na Uganda na mipaka ya nchi hizo imekuwa adhabu kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera, kwani hali ya usalama wa raia na mali zao umekuwa mashakani kutokana na kuvamiwa na majambazi toka nje ya Tanzania wakishirikiana na baadhi ya Watanzania wasio na uzalendo na Taifa lao.
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuimarisha ulinzi katika mipaka hiyo ili wananchi wa Mkoa wa Kagera waweze kuishi kwa amani na utulivu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yako matukio ya ujambazi katika mikoa ya pembezoni ikiwemo Kagera ambapo watu toka nchi jirani wanaingia na silaha kali za kivita na kufanya unyang‟anyi wa mali za wananchi. Hii inatoka na mkoa huu kupakana na nchi ambazo zimekosa amani na kuzalisha wahamiaji haramu kuingia nchini kwetu kwa njia za panya na tukizingatia kwamba mipaka yetu imezungukwa na mapori makubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama inafanya mikakati ya kutekeleza yafuatayo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, vyombo vya ulinzi na usalama vinafanya operesheni za pamoja katika mipaka yetu; vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi yetu na nchi ya jirani vinafanya operasheni za pamoja na kubadilishana taarifa mbalimbali za uhalifu na wahalifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vyombo vya ulinzi na usalama hufanya misako ya kushitukiza katika mapori yote yaliyoko Kagera, Kigoma na maeneo yote ya mipakani, kwani ndiyo maficho ya uhalifu; hufanya doria na polisi kusindikiza magari katika baadhi ya maeneo tete; Kamati za Ulinzi na Usalama za maeneo husika zinafanya vikao vya ujirani mwema ili kuwaelimisha wananchi juu ya kutoa taarifa kwenye Mamlaka za Serikali husika wanapoona wageni wasiofahamika wanaingia ama kutoka katika maeneo yao.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:-
Upungufu wa dawa katika Hospitali mbalimbali za Serikali nchini umeleta athari kubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera na Wilaya zake zote:-
Je, Serikali inakiri uwepo wa upungufu wa dawa nchini? Kama inakiri hivyo, inawaambia nini wananchi kuhusu tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kulitaarifu Bunge
lako Tukufu kuwa mojawapo ya vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni kuboresha upatikanaji wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa umma hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza azma hii, Serikali ya Awamu ya Tano ilichukua juhudi za makusudi kwa kuongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 katika mwaka wa fedha wa 2015/2016 hadi kufikia shilingi bilioni 251.5 katika mwaka wa fedha 2016/2017. Aidha, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa hadi kufikia mwezi Aprili, 2017 jumla ya sh. 112,198,920,456/= zilishatolewa na kupelekwa Bohari ya Dawa ili kuviwezesha vituo vya kutolea huduma za afya vya umma kupata mahitaji yake ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia ongezeko hilo la fedha, hali ya upatikanaji wa dawa nchini imeimarika na kumbukumbu zilizopo Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto zinaonesha kuwa hali ya upatikanaji wa dawa nchini imeimarika kwa kufikia asilimia 83. Kadhalika, hadi kufikia tarehe 15 mwezi Januari, 2017 Mkoa wa Kagera pekee umepokea kiasi cha sh. 4,150,767,216/= kupitia Fungu Namba 52, yaani Wizara ya Afya, kwa ajili ya kununulia dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi.
MHE. ALEX R. GASHAZA (K.n.y. MHE. OLIVER D.
SEMUGURUKA) aliuliza:-
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngara kuna matatizo makubwa sana ya maji kiasi kwamba wananchi wa maeneo hayo wanaona kuwa kupata maji ya bomba ni kama ndoto isiyowezekana na wamekuwa wakilipishwa gharama ya maji hata kwa wateja ambao hawapati kabisa huduma ya maji kwa kipindi cha mwezi husika ikiambatana na shilingi 1,500 kila mwezi kwa ajili ya mita ya maji.
(a) Je, Serikali inakubaliana na tozo ya shilingi 1,500 ya lazima kwa malipo ya mita?
(b) Je, Serikali inawaambia nini wananchi wanaotozwa bili za maji wakiwa hawajapata huduma ya maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika uendeshaji wa mamlaka na utoaji bora wa huduma ya maji, tozo ya shilingi 1,500 ilipitishwa na EWURA mwaka 2011 kwa mchanganuo ufuatao:-
(i) Shilingi 500 service charge; na
(ii) Shilingi 1,000 meter rent.
Mheshimiwa Naibu Spika, tozo hii iliendana na bei ya maji inayotumika hadi sasa. Kutokana na tarrifs mpya za EWURA ambazo zimeondoa tozo hiyo kwa sasa Mamlaka ya Maji Mjini Ngara inaandaa andiko la mpango wa biashara (business plan) litakalowasilishwa EWURA kwa ajili ya mapitio ya bili hiyo na kupata bili mpya ya maji inayoendana na wakati uliopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na malalamiko yaliyopo kuhusu baadhi ya wananchi kupelekewa ankara wakati hawapati huduma ya maji, Wizara itafuatilia kwa kina kujua kama ni kweli tatizo hilo lipo na endapo itabainika hatua stahiki zitachukuliwa.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:-
Katika maeneo ya Bugarama, Wilaya Ngara kuna Mgodi wa Kabanga Nickel uliodumu kwa miaka 30 sasa na kampuni mbalimbali zimekuwa zikiendesha shughuli zake kwenye mgodi huo na kuondoka tangu mwaka 1970 wakidai kuwa wanafanya utafiti huku bei ya Nickel katika soko la dunia akishuka.
Je, wananchi wa Ngara hususan maeneo ya Bugarama watanufaika na uwepo wa rasilimali hiyo iliyopo kwenye maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kampuni ya Kabanga Nickel inamiliki mradi wa utafutaji madini ya Nickel katika eneo la Kabanga chini ya leseni namba moja ya mwaka 2009 iliyotolewa tarehe 02 Mei, 2009. Kampuni hiyo inaendelea kufanya utafiti wa kina ili kubaini kama mradi huo unaweza kuendelezwa kwa faida zaidi. Hivi karibuni bei ya madini ya Nickel ilishuka ghafla kutoka dola za Marekani 11 kwa pound mwaka 2010 hadi dola za Marekani 4 kwa pound kwa mwaka 2014. Kutokana na hali hiyo, kampuni inatarajia kuendeleza shughuli za uchimbaji mara baada ya bei hiyo kuimarika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi tarehe 4 Aprili, 2017 bado bei ya Nickel katika soko la Dunia ilikuwa dola 4.45 kwa pound ikilinganishwa na bei ya dola 11 mwaka 2009 mradi ulipokuwa ukifanyiwa upembuzi yakinifu. Mgodi unatarajiwa kutoa ajira 1,455 wakati ujenzi ukiendelea na wakati wa uzalishaji itaajiri Watanzania 800. Mradi utakapoanza kupata faida mambo yatakayofanya wananchi wanufaike ni pamoja na kulipa service levy, kutoa huduma za Maendeleo pamoja na ajira hapa nchini. Kadhalika tutajenga miundombinu kwa ajili ya kusaidia jamii.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:-
Mkoa wa Kagera unazalisha matunda ya aina mbalimbali kama vile ndizi, nanasi, parachichi, embe na kadhalika. Kwa kuwa kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Tano ni kuhakikisha uchumi wa viwanda nchini.
Je, Serikali inaweza kuweka wazi mikakati madhubuti iliyoandaliwa ya ujenzi wa viwanda vya kusindika matunda katika Wilaya ya Ngara, Karagwe na Bukoba katika kipindi cha kuanzia mwaka 2016/2020?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhima ya Mpango wa Pili wa Miaka Mitano ni kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya kiuchumi na maendeleo ya watu. Katika mpango huu imebainishwa wazi kuwa ni jukumu la sekta binafsi kujenga viwanda na Serikali ibaki na jukumu la kuweka mazingira bora ya uwekezaji na ufanyaji biashara. Pia katika mpango huo tunalenga kuanzisha viwanda vinavyotumia malighafi zitokanazo na mazao ya wananchi, viwanda vinavyoajiri watu wengi na viwanda vinavyozalisha bidhaa zinazotumika kwa vingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumueleza Mheshimiwa Oliver Semuguruka, Wabunge wote wa Kagera na Wana Kagera wote kwa ujumla kuwa Serikali inasimamia mikakati ifuatayo katika ujenzi wa viwanda vinavyosindika matunda Mkoani Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ni kuimiza Serikali ngazi ya Kijiji, Kata na Wilaya kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mbili, kuhakisha maeneo hayo yanawekewa miundombinu wezeshi na saidizi; tatu, kupitia SIDO kutoa mafunzo ya kusindika malighafi za shamba ikiwemo matunda; nne, kujenga majengo ya viwanda (industrial sheds) ambapo wajawasiamali watapata mafunzo ya kuchaka na kusindika mazao yao ya shamba; na tano kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuchangamkia uwekezaji Mkoa Kagera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa mwitikio ni mzuri kwani viwanda vinavyosindika matunda vimeanza kujengwa, hii ni pamoja na kiwanda cha Mayawa kilichopo Bukoba Mjini, kiwanda cha kusindika nyanya kilichoko Ibwera kinachomilikiwa na Mheshimiwa Dkt. Samsoni Rweikiza Mbunge wa Bukoba vijijini, kiwanda cha mvinyo wa ndizi cha Salum Said Seif kilichoko Mulemba na kiwanda cha mvinyo cha ndizi kilichopo Karagwe kwa kutaja baadhi.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:-

Barabara ya Kyaka – Kasulu hadi Benako Ngara imeishia Bugene:-

Je, ni lini barabara hiyo ya lami itajengwa hadi Benako?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel Semguruka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kyaka – Bugene – Kasulo (Buneko) yenye urefu wa kilometa 178 ni barabara kuu na inahudumiwa na Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa barabara hii kiuchumi na kijamii iliamua kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Awamu ya kwanza ilihusisha sehemu ya barabara toka Kyaka hadi Bugene (Nyakahanga) yenye urefu wa kilometa 59.1. Sehemu hiyo tayari imekamilika kujengwa kwa kiwango la lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, awamu ya pili inahusisha sehemu ya barabara kutoka Bugene hadi Kasulo (Benako) yenye urefu wa kilometa 118.9. Sehemu hii kwa sasa inafanyiwa upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na uandaaji wa nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Kazi hii ipo katika hatua za mwisho chini ya Mhandisi Mshauri LEA International Ltd ya Canada ikishirikiana na LEA International Ltd ya Asia Kusini. Kazi hii inagharamiwa na Jumuiya ya Nchi za Afrika Mashariki na itajengwa kupitia mradi huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati sehemu hiyo ikisubiriwa kujengwa kwa kiwango cha lami, Wizara itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kufanyia matengenezo mbalimbali ili kuhakikisha kuwa barabara hii inapitika vizuri majira yote. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 jumla ya shilingi milioni 650.371 zimetengwa kwa ajili ya matengenezo mbalimbali ya barabara hiyo.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:-

Kivuko kilichopo Bukoba Vijijini Kyanyabasa hakikidhi viwango kabis:- Je, ni lini Serikali itaweka kivuko au daraja litakalokidhi viwango?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Kivuko cha MV Kyanyabasa kinachotoa huduma kati ya Buganguzi na Kasharu eneo la Kyanyabasa katika Mto Ngono kilinunuliwa mwaka 2005 na kina uwezo wa kubeba abiria 50 na magari madogo mawili kwa pamoja. Kivuko hiki kilifanyiwa ukarabati mkubwa mwaka 2016 na kinaendelea kutoa huduma kwa wananchi wa Bukoba bila matatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuendelea kutoa huduma nzuri na zenye viwango, Serikali katika mwaka wa fedha 2020/2021, imejipanga kukifanyia maboresho makubwa ikiwa ni pamoja na kuweka viti na paa kwa ajili ya abiria kujikinga na mvua na jua; kuweka taa kwa ajili ya kutumika kuvusha abiria kwa dharura nyakati za usiku na ukarabati utakaohusisha kubadilisha milango pamoja na kupaka rangi.

Mhehimiwa Naibu Spika, kivuko kilichopo kwa sasa kinatosheleza kutoa huduma inayohitajika kwa wananchi wa eneo hilo. Hivyo, hakuna haja ya kujenga daraja kwa sasa. Serikali itaangalia uwezekano wa kujenga daraja siku za usoni pale itakapohitajika.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:-

Wilaya ya Karagwe ina Sekondari moja tu ya kidato cha Tano na Sita ambayo ni Bugene Sekondari.

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Sekondari za Nyabionza na Kituntu ili ziwe shule za kidato cha Tano na Sita?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepeleka kiasi cha shilingi milioni 190 katika shule Nyabionza kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili na mabweni mawili. Aidha, ujenzi na ukarabati wa maabara tatu, bweni moja la wasichana, maktaba, bwalo na jiko unaendelea kwa kutumia mapato ya ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe. Vilevile Shule ya Sekondari Kituntu, imepokea jumla ya shilingi milioni 52.5 ambazo zinatumika kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili na bweni moja ambalo liko katika hatua ya umaliziaji. Kadhalika, halmashauri inaendelea na ujenzi wa maktaba moja, bweni moja la wavulana, madarasa mawili, bwalo la chakula na jiko kwa kutumia mapato ya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli hizi za ujenzi wa miundombinu ni maandalizi ya kuzipandisha hadhi shule hizo mara tu zitakapokamilika ambapo zitasajiliwa na kupangiwa wanafunzi wa kidato cha tano.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ya ujenzi wa Barabara ya Bugene kupitia Pori la Kimisi hadi Benaco kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kutekeleza ahadi ya Rais ya ujenzi wa barabara ya Bugene kupitia Pori la Kimisi hadi Benaco kwa kiwango cha lami ambapo upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Bugene – Kasulo – Kumunazi yenye urefu wa kilometa 128.5 ulikamilika mwaka 2019. Taratibu za manunuzi ya Mkandarasi wa ujenzi wa sehemu ya Bugene – Burigi Chato National Park yenye urefu wa kilometa 60 zipo katika hatua ya mwisho kwa kutumia fedha za ndani. Katika mwaka wa fedha huu wa 2021/2022 shilingi bilioni tatu zimetengwa kwa ajili ya kazi hiyo.

Aidha, Serikali imewasilisha Benki ya Maendeleo ya Afrika maombi ya fedha za ujenzi kwa sehemu iliyobaki ya Burigi Chato National Park hadi Kumunazi yenye urefu wa kilometa 68.5. Ahsante.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA K.n.y. MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafungua Matawi ya Benki ya Kilimo katika Wilaya za Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oliver, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Kilimo (TADB) imefanikiwa kufungua matawi katika kanda tano ambazo ni Kanda ya Kati, Dodoma; Kanda ya Mashariki, Dar es Salaam; Kanda ya Magharibi, Tabora; Nyanda za Juu Kusini, Mbeya na Kanda ya Ziwa, Mwanza ambayo inahudumia Mkoa wa Kagera na wilaya zake. Aidha, Benki ipo katika hatua za mwisho za kufungua Ofisi ya Kanda ya Kusini, Mtwara na hatua za awali za kufungua Ofisi ya Kanda ya Kaskazini, Arusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kukamilisha ufunguzi wa Ofisi za Kanda, TADB itaangalia uwezekano wa kufungua ofisi katika mikoa na ikiwezekana wilaya, lakini hili litazingatia uwezo wa benki wa kifedha ikiwa ni pamoja na faida na ukuaji wa mtaji. Ahsante.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga njia mbili katika barabara ya Bandarini hadi Rwamishenye na CRDB mpaka Njiapanda ya Kashai ili kuondoa msongamano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Bandarini – Rwamishenye yenye urefu wa kilomita 4.6 inafanyiwa usanifu wa kina ulioanza tarehe 22 Machi, 2022 kwa ajili ya kuwa Barabara ya njia mbili. Kazi ya usanifu inafanywa na Mhandisi Mshauri Luptan Consult Ltd kwa gharama ya Shilingi Milioni 70.05 na kazi inategemewa kukamilika mwezi Mei, 2022. Kazi za ujenzi zitaanza mara baada ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, usanifu wa barabara ya CRDB – Njiapanda ya Kashai yenye urefu wa kilomita 0.5 itaanza mara tu kazi ya usanifu wa kina wa barabara ya Bandarini – Rwamishenye utakapokamilika na fedha za usanifu zitakapopatikana.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga stendi kuu ya mabasi Bukoba Mjini?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti wa Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018, 2018/2019 na 2019/2020 Serikali ilipeleka jumla ya shilingi milioni 835.95 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi mpya ya mabasi katika eneo la Kyakailabwa Kata ya Nyanga. Fedha hizo zilitumika kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kuingilia stendi kwa kiwango cha lami, ujenzi wa vyoo, ujenzi wa mabanda matatu ya abiria na kituo cha polisi umekamilika. Aidha, ujenzi wa eneo la maegesho ya mabasi na malori upo hatua ya changarawe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 imejumuisha mradi wa stendi hiyo kwenye Mpango wa TACTIC awamu ya pili. Ahsante.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kukitangaza vya kutosha Kivutio cha Maporomoko ya Maji Rusumo ili kuchangia pato la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kushirikiana na Halmashauri za Wilaya kubaini vivutio mbalimbali vya utalii nchini kwa lengo la kuongeza wigo wa mazao ya utalii, katika kutekeleza hilo mwaka 2021 wataalam wa Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ngara walibaini vivutio vya utalii na fursa mbalimbali za uwekezaji na shughuli za utalii katika Mkoa wa Kagera.

Mheshimishiwa Spika, miongoni mwa vivutio vilivyobainishwa ni Maporomoko ya Maji ya Mto Rusumo ambayo yanatoa fursa ya uendelezaji wa shughuli za utalii. Hata hivyo, tathmini ya awali iliyofanywa na watalaam wa Wizara imebaini kwamba kiasi kikubwa cha maji ya maporomoko hayo kimechepushwa kwa ajili ya uzalishaji wa umeme na hivyo kupunguza mvuto wa utalii wa maporomoko pekee.

Mheshimishiwa Spika, kwa mujibu wa ushauri wa watalaam, mara baada ya kukamilika kwa mradi wa uzalishaji wa umeme na kukabidhiwa Serikalini, tathmini mpya itafanyika ili kuunganisha utalii wa maporomoko ya maji na utalii wa uzalishaji wa umeme. Endapo tathmini hiyo itaonesha uwezekano wa eneo hilo kutumika kama kivutio cha utalii wa maporomoko ya maji na utalii wa uzalishaji umeme, Serikali itajielekeza kwenye kufanya maboresho ya miundombinu katika maporomoko hayo na kuyatangaza ndani na nje ya nchi kwa lengo la kuvutia watalii kutembelea katika kivutio hicho.

Mheshimiwa Spika, kupitia Bunge lako tukufu niendelee kuwahamasisha Watanzania wenzangu kuwa na utamaduni wa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii. Aidha, nitoe wito kwa Mheshimiwa Mbunge, uongozi wa Mkoa na wadau wengine kwa ujumla kuhamasisha uwekezaji wa huduma ikiwemo huduma za malazi na miundombinu mbalimbali katika vivutio vya utalii vilivyopo katika Mkoa wa Kagera.
MHE. OLIVER D. SEMUGURUKA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga kingo za Mto Kanoni unaopita katikati ya Mji wa Bukoba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oliver Daniel Semuguruka, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Halmashaurii ya Manispaa ya Bukoba mwezi Februari, 2022 ilitumia shilingi milioni sita kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kusafisha, kupanua na kuongeza kina cha Mto Kanoni.

Mheshimiwa Spika, ili kuondoa changamoto hiyo Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 imejumuisha mradi wa ujenzi wa kingo za Mto Kanoni kwenye Mpango wa TACTIC Awamu ya Pili unaotarajiwa kuanza mwezi Januari, 2023, ahsante.